Search This Blog

Sunday 22 May 2022

BORN TO DIE - 5

 







    Simulizi : Born To Die

    Sehemu Ya Tano (5)

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Baada ya siku tatu, hali ya nchini Senegal ilikuwa katika vuguvugu kubwa la kutaka kujua mpango wa serikali yao utakwendaje baada ya rais kukubali kukaa chini na kiongozi wa waasi nchini humo.

    Vyombo vya habari vilitangaza taarifa mbalimbali za mkutano ule wa adhara na hadi kufikia mida ya saa nne asubuhi, Rais wa Senegal na Kamanda Bonito walikuwa mbele ya vyombo vya habari wakishiriki kufanya makubaliano ya kugawiana madaraka ili kuiweka nchi katika amani.

    "Leo, ni siku ambayo tumepanga kumaliza tofauti zetu. Tofauti ambazo zinasababisha vifo kwa ambao hawana hatia, tofauti zinazosababisha yatima na watoto wa mtaani kuongezeka. Leo tunataka kumaliza tofauti hizi," Alianza Rais wa Senegal mbele ya vyombo vya habari na umati wa watu mkubwa uliokuwa nje ya jengo la ikulu. Ulinzi ulikuwa mkubwa nje na ndani.



    Wanajeshi wenye silaha nzito walitembea huku na huko katika kuimarisha amani ya eneo lile pamoja na kuwalinda wananchi waliokuwa wametawanyika nje kwa furaha wakisubiri muafaka upatikane.

    "Tupo hawa kuwaambia kinachoendelea hadi sasa ndani ya makubaliano yetu. Mimi pamoja na Kamanda Bonito." Akamtazama Bonito, yule Rais. "Tumeamua kugawana madaraka. Mimi nitakuwa Rais na yeye atachukua Uwaziri Mkuu. Bunge litavunjwa na kuundwa jipya katika usawa ulio wa haki," Kimya kikatanda wakati Rais wa nchi ile anatabanainisha yale waliyoyasaini kwa ajili ya amani. Akaongea mengi Rais wa Senegal lakini kubwa alilogusia ni mgawanyo wa madaraka.

    Baada ya hayo, ruhusa ikatoka kwa ajili ya waandishi wa habari kuuliza maswali.



    "Ni vipi mtu ambaye hana uraia wa nchi hii anaweza kuongoza wananchi asiojua asili yao?" Mwandishi mmoja alimuuliza swali Rais huku akisema Bonito si raia wa Senegal.

    "Katika njaa, kila kilichopo kwa ajili ya kuzuia njaa, basi hicho ni chakula. Haijalishi Bonito ni wa nchi gani, ili mradi anamuda mrefu Senegal, basi huyu ni raia kama wewe. Anaijua lugha yetu na anajua vema kuhusu Senegal. Tumpe nafasi kwa ajili ya amani ya nchi hii." Aliongea kwa sauti ya msisitizo Rais na Bonito alionekana akitikisa kichwa kuafiki maneno yale.

    "Kamanda Bonito, ni jambo gani ambalo linaweza kuwa kauli mbiu katika uongozi wako?" Aliuliza swali mwandishi wa habari mwingine.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Kwanza kabisa, hakuna silaha ambazo zitaruhusiwa kuingia katika nchi hii maana hizo ndiyo sababu kubwa ya sisi kuuana. Wakati sisi tunauana kwa silaha hizo, watengenezaji wanachukua kiasi kikubwa cha pesa kwani majaribio yao yanakuwa sawa. Miili yetu imekuwa majaribio ya silaha zao, miili yetu ni biashara kwao. Nikianza kulitumikia taifa hili, basi tambua rasmi kuwa Afrika itakuwa imetoka kwenye utumwa wa watu wachache." Maneno hayo yalifanya wananchi wengi wapige makofi na hisia fulani kuhusu uraia wa Bonito zikaanza kufutika.

    "Unadhani kutoingiza silaha ndio kutapunguza mfarakano wa nchi hii?" Swali toka kwa mwandishi mwingine.



    "Hapana. Ila suala la silaha litaenda sambamba na kufukuza wanyonyaji ambao wanasababisha ajira za nchi hii kuwa na ukubwa unaolingana na punje ya sukari. Tutaondoa mabepari wanyonyajji wote wa nchi hii. Na badala ya sisi kuwa wanavita kwa kuingia msituni, basi tutasambaza harakati za ukombozi nchi nzima. Uhuru utakuwa mikononi mwetu. Mali ambazo tumeporwa, ni muda wa kuzirudisha mikononi mwetu." Bonito aliongea kwa hisia na wakati huo Rais alikuwa kimya akimtazama kwa kuiba wakati anaongea maneno hayo.

    Waandishi waliandika habari na kuchukua matukio motomoto yaliyokuwa yanaendelea kuchukua nafasi siku ile ya mkutano wa adhara.



    Viongozi wale wawili ambao waliamua kumaliza tofauti zao, walijibu maswali kadha wa kadha huku wakiamini kuwa mwisho wa yale yote itakuwa ni kumaliza mapigano baina ya wao kwa wao. Lakini hawakujua vita ndio kwanza ilikuwa inaanza, vita baina yao na hao wanaowaita wanyonyaji.

    Walipeana mikono ya umoja na kupiga picha kadhaa kama ukumbusho na huo ndio ukawa mwanzo wa safari nyingine ya Bonito kwenye siasa.



    ****



    Ndani ya miezi mitatu, hali ilikuwa tulivu na Bonito alikuwa ni mtu wa kutimiza mengi aliyokuwa anayasema. Nusu serikali aliyoiunda akiunganisha na nusu serikali ya rais wa nchi ile, ilikuwa inaleta changamoto nyingi bungeni na matatizo mengi yalikuwa yanatatuka kwa kutumia serikali hiyo mseto.

    Peter, Vanessa na Al Bashir, walikuwa ni wapelelezi wa siri wa Kamanda Bonito na mara kwa mara walikuwa wanatumwa kazi ngumu kama za mauaji ya wazungu ambao walikuwa wanakataa kuondoka nchini Senegal. Hali ilikuwa tete kwa wale wazungu wawekezaji, walivunjishwa mikataba yao mashirika yao yaliwekwa chini ya wananchi wa Senegal.

    Ajira zikafumuka nchini Senegal kwa kutumia mpango wa kufukuza wawekezaji wanyonyaji. Mambo yakaenda murua na bila kusita wananchi walimshukuru Waziri Mkuu wa nchi ile, Kamanda Bonito Muchakila.



    Wakati hayo yanapamba moto na kupewa kipao mbele, kambi ya Born To Die ilikuwa inaendelea kufanya mazoezi ya siri japo Bonito alimwambia Rais kuwa kambi hiyo imekufa.

    Mazoezi yalikuwa yanaendelea yalikuwa ni mafunzo ya wao wenyewe, hawakuwapa wazungu tenda ya kuwafundisha tena kama hapo mwanzo. Hilo ndilo lilikuwa kosa kubwa kwa Kamanda Bonito, kosa ambalo Vanessa aliliona na alionya mapema sana.

    Rais akiwa kamuachia madaraka Bonito afanye anachotaka, alijikuta hata yeye yupo matatani. Bonito alifunga mipaka mingi ya nchi yake hasa katika kuingiza silaha na vitu vitakavyopoteza amani ya nchi ile. Bonito akayafungia hata mataifa ambayo Rais wa nchi ile alikuwa anayetegemea. Rais akawa matatani na mwisho wake ilikuwa ni kumsukumia mpira Bonito na mataifa yale yakapanga kumuonesha cha moto Bonito.

    Si mataifa hayo pekee, hata yale ambayo yalikuwa yanawasaidia waasi, nao wakaapa kumfundisha Bonito kwa sababu ya alichokifanya.



    ****



    Peter alikuwa kama mbogo katika kufanya harakati za kufukuza wazungu wanyonyaji, alianzisha vikundi mbalimbali vya kiuana harakati na makaratasi mbalimbali yalisambazwa nchi nzima katika uhamasishaji wa kufukuza wazungu. Si kama Al Bashir na Vanessa hawakuwepo, walikuwepo ila ushiriki wao ulikuwa ni wa kawaida sana. Labda sababu asili yao ilikuwa si ya nchi ile, au labda walikuwa hawajazoea amani kama ambayo walianza kuipata. Lakini yale afanyayo Peter, yalikuwa ni katika kulikomboa bara zima la Afrika hasa kama nchi zenye mapigano zingeiga yale ambayo yalikuwa yanatendeka Senegal.



    ****



    Nje ya hapo, Rais wa Senegal aliamua kufanya mambo yake kisirisiri kutokana na shinikizo la wale waliokuwa wanamsaidia. Alitafuta watu wake waaminifu na kuwagawanya katika makundi wafuatilie nyenendo za Bonito.

    Alifanikiwa kiasi kikubwa sana hasa kuigundua kambi ya Born To Die. Na mbaya zaidi alitambua hadi wale ambao walikuwa washirika wake wa karibu. Akatoa taarifa kwa wale washirika wake wengine ambao walitoka barani Ulaya na Amerika.

    Wale mabwanyenye walipopata taarifa, wakawatafuta wale waliokuwa wanasaidia kambi ya Born To Die. Wakawachimba mkwara kabla ya kuungana nao kwa ajili ya kuibomoa kambi ile na kumng'oa Bonito madarakani.



    Mipango ilitisha na inasikitisha kuona watu wema ndio wanapangiwa mabaya. Wale wabaya wanatengenezwa kuwa wazuri. Ni vipi tutafika kama tutaendekeza uoga hata katika madaraka yetu?

    Afrika ni wapi tunaelekea? Ni nani ambaye atatukomboa kutoka katika utumwa wa watu hawa wachache? Kwa nini tusiungane na tujikite katika kuutokomeza utawala ambao unatunyonya? Afrika, kwa nini sisi tuwe watu wa kukanyagwa kwa vitu vyetu badala ya kuwa juu na kuvitetea? Afrika, je? Tupo tayari kuliona bara letu linadidimia kwenye kina cha bahari. Hapana.

    Afrika tusimame na kuungana ili tukomboke kwenye mikono ya hawa wanyonyaji. Tusimame imara na kuutoa huu ukoloni mamboleo, tusimame na tusema utumwa sasa mwisho. Hakuna ambaye atatuzuia, hakuna ambaye atatukataza kulilia nchi zetu. MUNGU yu nasi, Afrika tusimame.



    Ilikuwa ni usiku sana siku hiyo, usiku wa manane wakati kambi ya Kiasi nchini Senegal iitwayo Born To Die, ikiwa haina hili wala lile. Usingizi uliwachukua hadi baadhi ya walinzi wa kambi ile kubwa. Wachache waliobaki hawakufua dafu mbele ya uvamizi mkubwa uliofanywa katika muda ambao wanajeshi wale wamelala fofofo.

    Peter, Vanessa na Al Bashir walikuwa wamelala katika kambi hiyo kama kawaida yao kwani walikuwa hawana pengine pa kulala zaidi ya kwenye kambi hiyo kubwa.

    Makomandoo kumi kutoka bara la Ulaya, Asia na Amerika wakiwa wametumwa na serikali ya jeshi lao kuja kumuadhibu Kamanda Bonito kwa aliyoyafanya, walikuwa nje ya uzio wa kambi ile na silaha zao za hatari katika mapigano. Wakiwa wamejichora usoni kwa rangi maalumu za kijeshi, walikuwa ni watu wa kutoa ishara pekee kwenye maongezi yao.



    Walionesha wazi kuwa wameiva katika mafunzo makali ya majeshi waliyotoka. Walikimbia kwa makini bila kusikika na mtu. Walicheza na hisia za waliolala hata kabla hawajaamka. Walichokuwa wamekuja kukifanya ni kutekeleza agizo la Rais wa Senegal kuhusu kambi ile, walitaka kuibomoa yote na yeyote ambaye ataleta upinzani, basi angeuawa bila kusita.

    Walipanda ukuta wa kambi ile kwa makini kwa kutumia kamba ambazo mbele yake kulikuwa na nanga inayoweza kunasa mahali penye uwezo wa chuma kuingia. Walipanda kwa pamoja na ukiwatazama wakati wapo ukutani utawafananisha na maninja. Walikuwa wanapanda wakiwa sawa na mstari ulinyooka vema wakiwa katika moja ya ukuta wa kambi ile.

    Walipofika kabla ya kudondokea upande wa pili ambao ni ndani, walitazama huku na huko kuona kama kuna walinzi ambao walikuwa macho wazi kulinda ama kwa nia yoyote.



    Na bahati nzuri, ni wanajeshi wakiasi pekee ndio waliokuwepo. Wananchi wengi walirudi mijini kwani amani kiasi chake ilikuwa imepatikana.

    Makomando wale walikimbia kwa pamoja kama wafanyavyo maninja. Walijibanza kwenye ukuta mmoja ambao ulikuwa ni jengo la kambi ile. Kiongozi wa wale mabwana, aliwatawanya wenzake kwa ishara na wakagawana wawili wawili katika makundi matano. Kila kukundi kikaenda upande wake na kazi kubwa ilikuwa ni kupanda mabomu mazito ya masaa katika kambi ile. Walifanya kazi hiyo haraka haraka kabla ya vijana wa kambi ile hawajadamka.

    Siyo kila ambaye yupo ndani basi kapitiwa na usingizi daima. Wakati wale makomando wanafanya yao nje, wapo ambao walisikia mienendo na kila kitu kinachofanyika nje. Watu hao ni Peter na Vanessa. Walikwishanusa harufu ya hatari katika hisia zao, na kilichokuwa kinaendelea kwenye ubongo wao, ni kuanzisha vurumai ili wapone wao au kambi nzima.



    Wakatoka kwenye chumba walimokuwa wanajiegesha kila siku na moja kwa moja wakanyoosha korido ndefu hadi kwenye chumba ambacho Al Bashir na baadhi ya wanajeshi walikuwa wanalala.

    Al Bashir alikuwa katika usingizi mzito sawa na wanajeshi wengine watatu. Peter aliyechukua jukumu la kumuamsha kijana yule, alifanya hivyo na wakati huo Vanessa naye alikuwa anajaribu kuamsha baadhi ya wanajeshi ambao aliwaamini kuwa hawana papara wasikiapo jambo la hatari.

    Walipotoka ndani ya vyumba vile, tayari walishapata wanajeshi kumi ambao walikuwa kimya wakiwasikiliza Peter na Vanessa wanataka kusema nini.

    Peter akiwa na Vanessa walitoa taarifa maalumu kuhusu kuvamiwa na waliwapa uhakika huo baada ya kuwaambia japo wachungulie kwenye madirisha ya vyumba vyao. Baadhi waliwaona wavamizi ambao walikuwa makini kushinda umakini wenyewe, lakini tayari walikwishashtukiwa.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Cha msingi ni sisi kwenda chumba cha silaha na kila mmoja akamate silaha yake tayari kwa mapambano. Wenzetu wakisikia, basi ujue hapa patawaka moto." Peter aliongea na wale wanajeshi wakaafiki kwa kwenda katika chumba ambacho kilikuwa mlemle. Wakachukuwa silaha ambazo hupendelea kutumia na kujiweka sawa kwa ajili ya kupewa amri ya kutoka nje na kuwateketeza wavamizi.

    Huko nje baada ya dakika kumi na tano, wale makomando walikuwa wamesimama kwa pamoja, wameungana tena tayari kwa kuanza safari yao ya kutokomea eneo lile. Wakiwa hawajui kuwa wameshtukiwa, wakawa wanakimbia kwa hadhari hadi kwenye ukuta ambao walidondokea ndani wakati wamekuja. Wakashika kamba na kuanza kupanda ukuta ule kama vile walivyofanya mwanzo.



    Wakiwa katikati ya ukuta, mlio wa risasi usio na sauti kubwa ulisikika toka nyuma kwao na hapohapo komando mmoja alidondoka chini. Wakiwa hawaelewi ni nini cha kufanya kwa sekunde zile, risasi nyingine ikatumwa na komando wa pili akadondoka.

    "Sniper. (Mdunguaji)" Alisikika mwanajeshi mmoja akinong'ona na hapohapo, akaona komando mwingine akidondoka kama wale wa mwanzo wawili.

    Haraka wote kwa pamoja wakajitupa ndani ya uzio ule na kubaki wamelalalia matumbo huku silaha zao wakiziweka tayari kwa lolote.

    Al Bashir akiwa katika dirisha moja la chumba fulani cha kambi ile, alikuwa makini katika kudungua makomando wale. Aliweka silaha yake risasi kumi na kila risasi aliahidi kudondosha mwanajeshi mmoja.



    Wenzake wakakaa pembeni kusubiri ahadi yake kabla hawajatoka nje kupigana nao. Sasa Makomando watatu walikuwa chini na wengine saba wakiwa wamelala chini penye mwinuko kidogo ambao ulimfanya Al Bashir kupoteza shabaha yake.

    "Wamejificha," Aliongea Al Bashir kuwapa taarifa wenzake. Bunduki yake aliyokuwa kaifunga kiwambo cha kuzuaia sauti ilikuwa imeelekea kule wale jamaa walipolala.

    "Tufanyaje sasa." Aliuliza Peter.

    "Hawa watakuwa wametega mabomu na baada ya kumaliza ndio walikuwa wanaondoka. Sasa ni heri tufe wote kwa kujificha humu ama tutoke tupambane nao kisha tukimbie kambi. Lakini kumbuka hawa watu viapo vyao ni vya kufa na kupona. Hawana cha kupoteza kwenye suala kama hili." Aliongea Al Bashir na wote wakaafiki kusubiri dakika kadhaa ili watoke na kupambana.



    Hawakujua kuwa hizo dakika ndizo ambazo wenzao wanazisubiri.

    Kiongozi wa makomando alitoa mawasiliano yake na kuwasiliana haraka na makao makuu kuwaambia kinachoendelea kwenye kambi ile. Na bila kupoteza muda, makao makuu wakawasiliana na Rais wa Senegal. Naye bila kusita, akalipa amri jeshi lake lililokuwa karibu na kambi ile kudumisha usalama kwa wale makomando wa kigeni. Jeshi likaibuka na kuanza kukimbilia kule ambapo kambi ipo.

    Dakika tano zilitosha sana kwa jeshi la serikali ya Senegal kuvamia eneo lile kwa nguvu huku likirusha mabomu na risasi kwa kasi ya ajabu. Peter na kundi lake wakashtuka kusikia hayo, wakaamua kupiga king'ora cha hatari kutahadharisha kambi kuwa wamevamiwa.



    Al Bashir alikuwa yupo dirishani, hakupaparika wala kushtuka wakati ya nje yanaendelea. Aliendelea kuwinda wapinzani wake kwa umakini mkubwa.

    Kiongozi wa makomando wale alielewa njia zote za wadunguaji hivyo alikuwa makini katika kutoa amri za wenzake wanyanyuke. Walitulia pale chini huku wakitazama saa zao. Zilibaki dakika 40 mabomu yalipuke.



    "Tunatakiwa kujua huyu mdunguaji yupo wapi," alishauri kiongozi wa makomando kwa lugha yao ya kikomando.

    "Ndio. Vita vipo hapa, lakini huyu jamaa hatotoka pale hadi atumalize," mwingine aliongea.

    "Wewe wa Urusi, nyoosha juu begi lako tuone risasi itatokea wapi." Aliongea kiongozi na hapohapo komando wa Kirusi alivua begi lake la mgongoni na kulinyoosha juu, na kweli Al Bashir alifyatua risasi ambayo alipiga begi na kusababisha wale makomando watambue ni wapi Al Bashir kajificha.

    "Kwenye lile dirisha yupo huyo mjinga." Aliongea kiongozi wa makondoo wale huku akichungulia kwa makini asijekupigwa risasi na Al Bashir.

    "Naweza kupambana naye," Komando mmoja aliongea na wenzake wote wakakaa kimya na kumuangalia. "Cha msingi ni kunisaidia kuniinua hapa maana ukiinuka tu, unakula risasi. Sasa nachotaka ni mmoja kuzubaisha ili apige risasi yake. Wakati anapiga, mimi nitasimama na hapo ndio itakuwa mwisho wa ngebe zake," Aliongea yule bwana mwenye asili ya Kimarekani.

    "Sasa itabidi mwingine tumvalishe begi mgongoni litakaloziba hadi sehemu ya kisogo. Hapo tutampata kwani huyu bwana analenga sana kichwani na shingoni.



    Tukifanya hivyo, tutampata." Ni maamuzi ya haraka ambayo yalifanywa na Makomando wale na dakika mbili zilizofuata, tayari Komando mmoja alikuwa kavalishwa begi kubwa na akahesabiwa moja hadi tatu. Naye akanyanyuka na kujifanya anakimbilia ule ukuta wa nyuma yake, waliokuwa wanajaribu kuudandia.

    Al Bashir akafanya kosa kufyatua risasi, kwani alimpa nafasi Komando mwingine kuchomoka pale alipo na kuanza kukimbia kwa mtindo wa zigi zaga ili kupoteza shabaha ya Al Bashir.

    Wakati anakimbia, risasi kadhaa zilimkosa na kwa mtindo aliokuwa anakimbia nao, ni wazi alikuwa kafuzu mafunzo ya vitendo.

    Alichomoa pini katika bomu lake alilokuwa kalining'iniza kwenye koti kisha kwa utaalamu uliotukuka, alijirusha sarakasi aina ya mtupu na kujibanza chini ya dirisha ambalo Al Bashir alikuwa kasimama. Kwa haraka akatupia bomu lake ndani ya dirisha lile na mara mlipuko mkubwa ulisikika huku bunduki ya Al Bashir ikidondokea mbele ya Komando yule.

    Komando yule alifyonza na kupukuta mikono yake kwa kazi nzito aliyoifanya.



    Wakati hayo yanajiri, Peter, Vanessa na wanajeshi wa kiasi wengine walikuwa nje wanapambana na jeshi la serikali ya Senegal. Ilikuwa ni vita ya kufa na kupona kwa wanajeshi wa Born To Die na wale wa Senegal. Walipigana, wakatoana damu na kumalizana yote ilikuwa ni katika kuutafuta uhai wao kwa hali na mali.

    "Peter. Tuna kazi nzito. Unajua kuwa wametega mabomu hapa? Sasa itakuwa tatizo yakilipuka," aliongea Vanessa wakati wamejificha na wakizikoki silaha zao kwa ajili ya kurudi kupambana.

    "Ndio. Lakini makomando wote hutega mabomu yao yalipuke baada ya lisaa limoja. Na hapa nadhani tuna dakika ishirini tu. Huko kwa Al Bashir sidhani kama kutakuwa salama. Anacheza na watu hatari sana." Peter aliongea huku akiwa makini na maadui wanaozidi kuongezeka katika kambi ile. Hali ilikuwa tete kwa timu nzima ya jeshi la Waasi na mambo yalizidi kuwawia ugumu wanajeshi wote wa Born To Die. Walianza kurudi nyuma huku wakiendelea kufyatua risasi zao kwa wingi.



    ****



    Baada ya komando yule kufanikisha kumuondoa uhai Al Bashiri kwa kumtupia bomu ndani, alirudi kwa wenzake na kisha wakajikusanya vema huku wakiangaza huku na huko kwa kudumisha ulinzi. Hali ilikuwa tulivu kwao kwani jeshi la serikali liliwavuta wanajeshi wote upande mwingine.

    Makomando wale wakainyanyua miili ya Makomando wenzao na kupanda nayo katika ukuta tayari kwa kuwarudisha nyumbani marehemu wale.

    Huko katikati ya mji, Bonito alikuwa hana hili wala lile kuhusu kuvamiwa kwa kambi yake anayoiongoza. Alilala kwa starehe huku nje ulinzi ukiwa mkubwa kama wa rais wa Amerika. Hakujua kuwa wenzake wanateketea msituni baada ya kutambulika na wanoko kama rais wa Senegal. Akalala kwa raha mustarehe.



    ****



    Kazi ya vita iliendelea kupamba moto katika kambi ile na jambo kubwa ambalo liliwaokoa wanajeshi wengi ni kukimbilia katika ghala la silaha ambalo lilikuwa limesheheni silaha za aina mbalimbali.

    Peter, Vanessa na wanajeshi wengine, walivamia vifaru vikubwa na kuanza kujibu mapigo dhidi ya wale wanajeshi watukutu wa serikali. Pia wanajeshi wengine wa miguu waliweza kunyanyua makombora ya kudungulia magari pamoja na ndege lakini safari hii walikuwa wanapiga katikati ya kundi la watu. Wanajeshi wa serikali wakaanza kupoteza maisha kwa wingi na wengine kuanza kurudi nyuma kwa kasi lakini hali ilizidi kuwa mbaya kwao. Waliuawa bila huruma kwa dakika kumi za mwanzo.

    Wakiwa wanakimbilia porini na baadhi ya wanajeshi kurudi kambini kwa furaha, milipuko mikubwa ikaanza kusikika katika kambi ile ya Born To Die. Ndipo Peter na wenzake waliotambua kuwa kulitegewa mabomu wakakumbuka jambo hilo lakini walikwishachelewa, nusu ya wanajeshi wakiasi walitekea katika milipuko ile ya mabomu.



    Hakuna kilichosalia katika kambi ile zaidi ya wanajeshi wapatao ishirini waliokuwa wanawafukuza wanajeshi wa serikali. Peter akadondosha chozi la uchungu pale alipotoka nje ya kifaru na kushuhudia kambi iliyomlea katika ukubwa wake wote ikiteketea. Akasikitika na sana na.kujikuta akishuka akiwa kakamata bunduki yake nzito aina ya 'min machine gun' ambayo iliungana na mkanda mzito wa risasi nyingi sana. Akashuka na chini na kutazama moto mkubwa uliokuwa unaiapamba kambi ile.

    Akatikisa kichwa kwa masikitiko asiamini kuwa wenzake wengi wameteketea katika jengo lile. Akiwa katika angalia yake ya kule kwenye kambi yao, akajisahau kuwa yupo vitani na pale alipo ni porini na alikuwa anawafukuzia maadui mbali kabisa na eneo lile. Akasahau ilo kabisa, akajikuta anapoteza ngao nyingine muhimu katika maisha yake.

    "Peeeeety." Sauti ya Vanessa iliita kwa nguvu nyuma yake na wakati huo binti yule alikuwa anakimbia kumuelekea yeye. Peter akageuka na kumtazama Vanessa ambaye alikuwa anakuja kwa kasi kwake. Vanessa alimpomfikia Peter akamrumkia na kudondoka naye chini na wakati huo mlio mkali wa risasi ulisikika pembeni yake. Peter akadondoka na Vanessa huku kamkata kiuno chake.



    "I saved you Pitty. Like how I promice you. (Nimekuokoa Pitty, ni kama nilivyokuahidi)" Aliongea Vanessa kwa sauti ya chini na kumfanya Peter atabasamu na kupapasa kiuno cha Vanessa kwa mahaba huku akipandisha mkono wake hadi ubavuni. Mkono wake ukahisi ubaridi mkali wa maji maji, akatazama mkono huo akakutana na damu nyepesi ambayo ilikuwa inachuruzika kwa kasi kutoka katika ubavu wa Vanessa.

    "Umepigwa risasi?" Peter aliuliza kwa hamaki kana kwamba alikuwa haamini kile alichokihisi. Vanessa alitabasamu na kumuangalia yule mvulana jasiri katika mambo mengi.

    "Uliniambia nitakuwa rafiki yako siku ambayo nitakufa kwa ajili yako, nadhani sasa nitakuwa rafiki yako," Vanessa aliongea suala lingine badala ya kujibu lile la Peter.

    Pater akatambua kuwa sehemu ile si salama tena na aligundua kuwa wanajeshi wa serikali watarudi tena kuangamiza kilichosalia licha ya lengo kuu la kuilipua kambi ile likiwa limekamilia.

    Peter akanyanyuka haraka na kutazama huku na huko na aliona wenzake baadhi wakiwa wanapambana na wanajeshi wabishi. Alipoangalia pembeni kule ambapo risasi imetokea alimuona mwanajeshi mmoja aliyekuwa anaua wanajeshi wengine bila ya yeye kuonekana. Mawazo ya Peter yalienda sawa kwa kuamini kuwa yule ndiye aliyemtwanga Vanessa risasi. Akachukua 'min machine gun' na kuanza kummwagia risasi nyingi yule bwana hadi akawa kaka chandarua.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alipomaliza akahamia kwa wale wasumbufu ambao wenzake walikuwa wanawashindwa kabisa. Akazidi kuwatekeza kwa kuwapiga risasi kadiri ya uwezo wake. Alipoachia kifyatulio (trigger) ya bunduki yake, kulikuwa hakuna tena masalia ya wanajeshi eneo lile. Akatupa bunduki ile na kwensa hadi kwa Vanessa pale alipokuwa kalala.

    "Nimeona hasira zako Petty," aliongea Vanessa kwa tabu.

    "Nakupeleka hospitali Vanee," Peter aliongea huku akianza kumnyanyua Vanessa.

    "Hapana Pitty. Kuna kitu nataka nikwambie hapa kabla hatujaenda huko," Vanessa alimkataza Peter zoezi alilotaka kulifanya.

    "Utaniambia njiani tukiwa tunaenda." Peter aliongea tena akianza kumuinua Vanessa lakini binti yule alikataa katu. Peter ikabidi asalimu amri kwa kumweka pembeni ya sehemu ile na kumsikiliza yule mwanadada mrembo ambaye alikuwa akitokwa na damu nyingi sana.



    "Pi.....tty na...kup....enda sana" Sauti ya Vanessa iliongea kwa kukwama kwama na safari hii machozi ya maumivu yalikuwa yakimtoka.

    "Nafahamu Vanee...." Peter hakumaliza kauli yake Vanessa akamkatisha.

    "Nyamaza nikwambie...." Akifoka Vanessa huku machozi yakimtoka. Peter akanyamaza na kumsikiliza. "Nakupenda, lakini ahadi ye.... ye..tu ya ndo....ndo....a nadha...aani ina...fiiii...ka kikom...o ha.....pa," Vanessa alikuwa katika hatua mbaya sana na kila alipokuwa anaongea, alikuwa anatoa pumzi kubwa na kusababisha tobo lililopita risasi kuzidi kumwaga damu. "Lakini una...ku....mb....uuuuka, uli...se...se...ma utaniiiii....mbia wi....wi....mbo siiii....ku mo...moja hivi," Akakumbushia ya nyuma Vanessa na Peter akaafiki kuwa anakumbuka siku hiyo. "Niiii...mbi...e" Peter akatazama juu na chozi likamtoka kila alipowaza shida anazozipata mpenzi wake pale alipo.

    "Ina maana ndio anakufa?" Alijiuliza Peter. "Hapana. Hawezi kufa. Ngoja nimuimbie. Atakubali twende hospitali nikimuimbia." Peter alijishauri haraka na kumtazama Vanessa ambaye alikuwa anasubiri kuimbiwa. Peter akaanza kumuimbia wimbo ambao aliutunga mwenyewe siku za nyuma. Ni wimbo wa mapenzi ambao ulikuwa na maneno mengi ya kujenga mapenzi ambayo wameyaanza. Ulienda hivi:



    " Si kama sauti yako sikuisikia, Vanee, amini kila siku masikio yangu yalikusikia. Si kama macho yangu nilikufumbia, Vanee, mboni zangu kila siku zilikuangalia.

    Akili yangu yote ilikuwaza wee, uoga wangu ukanifanya kwako nife nioze. Nilipodondoka ukiyeniona ni wewee, nakiri hilo Vanee, acha nikupongeze.

    Mapenzi yangu kwako, yalianza hata kabla ya siku ile wewe kunifuatilia. Tabasamu lako, ndilo hasa liliichanganya akili yangu na kubaki tu nakuangalia. Utajiri wako, ulitosha kabisa kuniambia nikikutaka utanikatalia.

    Sikujua kuwa moyo wangu na wako, hakuna ambao hukuumia. Pale tukutanapo, hakika hisia za mapenzi ndizo ziliongea.

    Ooh! Vanee, Vanessa. Nakumbuka nilipokwambia nakupenda. Niliona macho yakijibu, Peter nakupenda pia. Nilijiapiza kuwa siwezi kukutenda, hilo ndilo kwako nililiapia. Popote utakapokwenda, nilijiapiza nyuma kukufuatia. Pale ulipopinda, sikusita ukweli kukuambia, Vanee. "Peter alikuwa akimuimbia msichana yule kwa sauti yake nzuri na kumfanya Vanessa atabasamu tu. Hadi anamaliza mashairi kadhaa ya wimbo ule, Vanessa alikuwa katabasamu bila kuongeza neno hadi alipohakikisha mpenzi wake kamaliza.



    "Kweli unakipaji Pitty," Vanessa aliongea kwa sauti ya chini huku akipalaza kiganja chake cha mkono katika shavu la Peter.

    "Asante Vanee. Haya twende Hospitali mpenzi wangu," Peter aliongea huku akianza kushughulika kumnyanyua.

    "Usihangaike Pitty. Tunza kipaji chako. Usifikirie kuhusu visasi Pitty." Vanessa aliongea lakini Peter alikuwa kama hasikii alichokuwa anaelezwa. Akamnyanyua na kuanza kwenda na Vanessa kwenye gari dogo la jeshi lao ambalo liliachwa na wenzake ambao wengi walikimbia baada ya kupata upenyo huo.

    "Peter," Vanessa aliliita jina la mpenzi wake kwa urefu wakati Peter anaelekea kwenye gari aliloliona mitaa ile.

    Peter akamtazama Vanessa ambaye alikuwa anatoa machozi ya uchungu. "Naondoka mpenzi wangu. Naondoka sasa," Vanessa aliongea huku akianza taratibu kushusha mikono yake toka shingoni kwa Peter.



    "Kwa heri Peter," Vanessa aliposema hayo, mikono na mwili wake ukalegea kwenye mikono kakamavu ya Peter. Peter akasimama na kumtazama mpenzi wake. Alikuwa kafumba macho ambayo yalijaa machozi, na pia alikuwa kanuna mdomoni. Vanessa alikuwa kamuaga Peter na roho yake kutangulia panapostahili. Vanessa hakuwa na uhai tena.



    Lilikuwa ni tendo la ghafla sana kwa Peter na kwa Vanessa pia. Peter hakutegemea kuwa kuna siku atakuja kumpoteza Vanessa katika mikono yake, na Vanessa sidhani kama aliwahi kuota kuwa atafia kwenye mikono ya Peter. Lakini kilichoandikwa na MOLA katika maisha ya kila mmoja wetu, ndicho ambacho kwa uweza wake kitatimia katika maisha haya.

    Peter alibaki kaganda nyuma kidogo ya gari dogo la jeshi. Alikuwa bado kamkamata Vanessa katika mikono yake. Alikuwa bado kamshikilia mpenzi wake wa ukweli, mpenzi toka moyoni kabisa. Ni kama akili yake ilikuwa imeganda kwa kuwekwa barafu. Hakujua kama yupo ndotoni au ni katika uhalisia. Akili yake ilijiuliza mara zaidi ya mia kuwa yule amuonaye ni marehemu Vanessa au yu ndotoni tu na akiamka atakuta Vanessa yupo katika ubavu wake akiwa anakoroma kutokana na usingizi mzito.

    Peter akajikuta mwenye kutamani ile kuwa ni ndoto na si kinyume. Akatamani awe ndotoni na kisha adamke. Akatamani na ndoto hiyo iishie hapohapo alipokuwa anaiota kuwa Vanessa amemuacha, na kuiacha kabisa dunia hii. Akajilazimisha kuamka toka kwenye ndoto ile lakini ilikuwa si ndoto bali ni kweli. Ni kweli Vanessa alikuwa hayupo kiroho katika dunia hii.

    “Noooooo,” Peter alitoa sauti kali ya uchungu baada ya kimya kirefu alichokuwa kakikamata kwa kufikiria mambo kadha wa kadha.

    Akapiga magoti huku bado kamkamata Vanessa mikononi mwake. Akamtazama binti yule mwenye urembo uliotukuka licha ya kuwa komavu kimwili na kifikra.



    “Vanee. Mbona umeondoka mapema sana mama yangu? Mbona umeondoka bila kutimiza ahadi yetu ya mimi na wewe kufunga ndoa? Kwa nini umeondoka Vanessa. Kwa nini umeondoka bila kutimiza ahadi yetu?” Peter alikuwa akiuliza mwili ambao kwa wakati huo ulikuwa ni kama sanamu, haujibu wala kuonesha nia ya kujibu. “Ni kweli umeondoka Vanee? Ni kweli umeniacha katika hali hii? Nitafanya nini bila wewe? Nitaishi vipi bila wewe Vanessa? Ulibaki wewe tu katika dunia hii, lakini sasa umeniacha mpenzi wangu. Umeniacha katika hali mbaya ya mateso ya nafsi na mwili,” Peter alilia kwa nguvu zake zote. Alilia kwa sauti ya juu huku mwanamke ampendaye akiwa katika mikono yake. Peter alitia huruma.

    Alikwishapoteza familia yake yote huko nyuma, baba, mama, kaka na dada. Leo hiyo anapoteza tena mpenzi ambaye walikwisha ahidiana mambo mengi katika maisha yao. Ni halali atie huruma, na ni halali alie kwa uwezo wake wote. Lakini ukweli unabaki kuwa ‘whats goes around, you must comes down’ yaani chochote kitakachojitokeza, unatakiwa utulie. Ni maneno ambayo aliwahi kuambiwa na baba yake kipindi cha nyuma sana, Peter akayakumbuka maneno hayo.

    “Kuna maisha mapya baada ya kifo,” Alikuwa baba yake Peter, Mzee Madira akiwa kakamata jembe la mkono akipalilia mihogo yake ambayo aliipanda kwa ajili ya kudumisha utamaduni wake kuhusu kilimo. Pembeni yake alikuwepo Peter na pembeni ya Peter alisimama kaka yake, Bruno Madira. “There’s a new life after death,” Akarudia tena maneno yale Mzee Madira kwa lugha ya kiingereza, na kichwani kwa Peter yakaingia na sasa akatulia na kumtazama Vanessa ambaye alikuwa hana uhai.



    “Kuna maisha mapya baada ya kifo. Naamini tutakutana tena katika maisha mapya,” Peter aliongea kwa ujasiri maneno hayo ambayo yalikuwa ni nguvu nyingine ya kumnyanyua pale alipokuwa kapiga magoti. “Tukikutana tena, nitakuoa na tutaishi kwa furaha na kwa amani. Utawajua wazazi wangu, na nitawajua wazazi wako. Kwa sasa, acha niende kumaliza walichokianzisha hawa wajinga.” Kwa ujasiri mkubwa Peter alienda kwenye gari lingine kubwa, linalotumika kubebea silaha na lundo la wanajeshi. Akamweka Vanessa kwenye bodi la gari lile na kisha akalimwagia mafuta ya petroli gari lile na kutupia njiti ambayo aliiwasha. Moto ukatanda kwenye gari na kuunguza kila kilichomo mle.

    “Nenda salama Vanessa. Nipo njiani nakuja.” Aliongea hayo huku akipiga ishara ya msalaba.

    Akatoka eneo lile akiliacha gari lile likizidi kuwaka moto kila shemu hadi kwenye injini ambayo ililipuka na sauti nzito ya mlipuko huko ikatanda pori lote. Wakati huo Peter alikuwa kishaondoka kabisa eneo lile na safari yake ilikuwa ni kuelekea katika Jiji la Dakar, huku njiani akiwa makini asikutane na jeshi walilolifukuza toka msituni.



    *****



    Saa kumi alfajiri, Peter alikuwa nje ya geti ya jumba kubwa lenye walinzi wakali. Walikuwa wanamuuliza maswali kadhaa kabla ya kumruhusu aingie ndani.

    “Nawaambia nahitaji kuonana na Kamanda Bonito, kuna jambo la msingi na la haraka.” Alisisitiza Peter mbele ya wale wanajeshi ambao walikuwa hawamjui kabisa.

    “Okay. Tumwambie nani anamuhitaji,” Mmoja wa walinzi aliyekuwa kakamata mbwa mwenye kutoa ulimi nje kwa matamanio, na bunduki yake ya SMG ikiwa mgongoni, alimuuliza Peter.

    “Mwambie Peter toka Born To Die,” Peter alimpa taarifa yule mlinzi na hapohapo yule bwana alienda kwenye kibanda kidogo kilichopo pale. Ndani ya kibanda kulikuwa na mlinzi mwingine. Yule mlinzi mwenye mbwa, akampa maelezo sahihi yule wa kibandani.



    Mlinzi wa kibandani akatoa simu ya mkonge na kupiga namba fulani na uweka sikioni. Baada ya sekunde kadhaa, alikuwa kiongea na mtu wa pili aliyempigia. Na hata baada ya sekunde nyingine kadhaa, alikuwa amekwishapata melezo ya kina toka kwa mtu wa upande wa pili. Akamueleza yule bwana mwenye mbwa.

    Naye mlinzi mwenye mbwa alipomaliza kuelezwa, alimfuata Peter na kuongozana naye hadi getini. Akakaguliwa na kisha akapita moja kwa moja kwenye uzio mkubwa uliozunguka jumba lile la kifahari. Japo lilikuwa ni jumba la kuvutia, lakini macho ya Peter hayakuwa katika kuthaminisha uzuri huo bali akili yake ilifunga na macho pia. Peter alikuwa akiwaza ni maisha gani ambayo anaelekea kuishi baada ya kumpoteza Vanessa.

    Mlinzi aliongozana naye hadi kwenye sebule kubwa ambalo lilikuwepo ndani mle. Akamkaribisha huku akimtazama kwa makini hasa kwa ule muonekano wake wa kichafu uliosababishwa na kutapakaa damu za Vanessa pamoja na vita kali waliyopigana usiku uliopita.



    Dakika chache mbele, Kamanda Bonito aliingia katika sebule lile na kumkuta yule mlinzi akiwa anamtazama Peter kwa makini. Akamuomba atoke kwa sababu yule si kijana wa kumlinda kiasi kile. Mlinzi katoka na kuwaacha wale majemdari wawili peke yao.

    “Nini Peter?” Aliuliza kwa sauti ya kitetemeshi Bonito baada ya kumuona Pater akiwa katika mawazo mazito tangu alipofika pale. Hakumpa nafasi ya kujibu swali lile, akatupa lingine. “Kumetokea nini Peter? Niambie.” Wasiwasi ulichukua nafasi kwenye sauti ya Bonito Muchakila.

    Peter akanyanyua kichwa chake na kumtazama kiongozi wake akiwa katika wahka mkubwa. Akatikisa kichwa kwa masikitiko kisha akajibu maswali ya Bonito.

    “Tumepoteza kambi nzima Kamanda. Nimempoteza Vanessa, nimempoteza na Bashir pia.” Kilio cha maumivu kikafuata kwa Peter. Kamanda Bonito akawa kinywa wazi asijue afanye nini kati ya kumbembeleza kijana yule ama kumuuliza kilichotokea, lakini kubwa lililomfanya asite zaidi, ni kambi yao kuvamiwa. Nani aliyejua ile kambi ilipo? Ikabidi wazo la kubembeleza lipotee na badala yake aulize jambo la msingi.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ilikuwaje Peter?” Peter akajua kuwa kuna jambo anatakiwa kufanya badala ya kulia.

    “Walikuja makomando, wakatega mabomu. Lakini sisi tuliwaona. Bashir akaanza kuwachukua. Ndipo jeshi la serikali likatokea msituni na kuanza vurugu……..” Peter alimuhadithia kila kitu Bonito kwa ufupi.

    “Gascoign. Huyu ni Gascoign tu,” Alibwata Bonito akimshutumu Rais wa Senegal bwana Gascoign Mushede. “Tumekwisha sasa. Hatuna jinsi hapa Pitty.” Aliongeza Kamanda.

    “Hapana. Ni lazima niende huko kwenye matengezo ya hizi silaha. Nataka kwenda kuharibu, nataka kwenda kulipa kisasi kwa Vanessa. Naomba nieleze ni wapi huko,” Peter aliongea kwa sauti kavu huku uso wake ukiwa moja kwa moja kwa Bonito.

    “Peter, unataka kwenda kufa na wewe. Tafadhali, achana na hizo fikra. Nakupa pesa nyingi uende sehemu nyingine, lakini si kwenda huko upatakapo. Utaishia hukohuko,” Bonito alishauri.

    “Haijalishi. Nimepoteza kila kitu katika maisha yangu, siyo mbaya na wao wakapoteza japo kidogo tu. Naomba niambie ni wapi nalipata eneo linalosambaza silaha barani Afrika.”



    “Peter acha ujinga, utaenda kufa…” Peter alinyanyuka toka kwenye kochi na kumdaka Kamanda Bonito koo kwa nguvu, hakujali wadhifa na ukubwa alionao. Alichodhamiria, ndicho alichokitaka.

    “Baba amekufa, Mama amekufa, Kaka amekufa, Dada naye hivyohivyo. Mpenzi wangu kafuata. Kwa sababu ileile. Kwa sababu ya serikali yetu chafu. Mimi nina hasara gani nikifa? Niache nikafe,” Maneno hayo ya mwisho yalienda sambamba na Peter kumuachia koo Bonito ambaye alimtazama kwa makini kijana yule. Akajua anasababu ya kumpa maelezo ya kina. Akasimama pale alipokuwa kajilaza baada ya kukabwa koo, akaelekea kilipo humba chake.

    Baada ya dakika kadhaa, alikuwa amekuja na bahasha pamoja na mavazi mapya ya kijeshi, jeshi la nchi ya Senegal.

    “Najua hawa waliokuwa wanatuletea sisi tu. Wapo Urusi. Kila kitu kipo kwenye hiyo bahasha. Chukua nenda kasome mwenyewe.” Bonito aliongea huku anamkabidhi bahasha ya kaki aliyokuja nayo toka chumbani.



    Peter akaipokea kwa hamasa na kutaka kuifungua, Bonito akamkataza.

    “Huna muda mrefu Pity. Hayo yametokea huko porini, lakini sasa hivi serikali hii ya kijinga itakuwa mlangoni kwangu kwa ajili ya kumaliza walichokianza.” Bonito aliongea kwa upole huku akimtazama Peter na maneno hayo yalizama vema kichwani kwa Peter. Akaiweka bahasha ile ndani ya shati lake chafu. “Chukua na hizi nguo. Pitia Kongo, pale kuna rafiki zangu watakusaidia kukusafirisha hadi katika meli zinazoenda huko Urusi.” Peter akaafiki maneno yale huku akipokea mavazi ya jeshi aliyopewa na Bonito.

    “Nenda. Chochote kitakachotokea, kumbuka umezaliwa kufa. You was Born To Die Pity. Usiogope kifo hata kidogo. Nenda salama Kamanda wangu.” Alimaliza kwa saluti Kamanda Bonito na Peter aliitikia heshima hiyo kwa saluti vilevile.

    Alitoka ndani ya nyumba ile ikiwa tayari ni saa kumi na moja. Haraka akapanda gari lake na kuanza safari nyingine ya kuelekea katika msitu ambao ungempeleka hadi Kongo.



    ****



    Ni kama Kamanda Bonito aliota kuwa Rais angefanya hila zingine za kuja nyumbani kwake baada ya kuimaliza kambi ya born to die. Baada ya Peter kuondoka tu, magari kadhaa ya kijeshi yalifunga breki katika geti la nyumba ya Kamanda Bonito na kwa sekunde kadhaa, walikuwa tayari wameongea na walinzi wa pale.

    Rais akashuka toka garini na kuitazama nyumba ile kwa mbwembwe, akatabasamu na kuanza kuingia katika uzio wa jumba lile.



    Kule ndani, baada ya Peter kuondoka, Kamanda Bonito alikaa kwenye kochi kama mwenye kusubiri jambo fulani. Na kweli baada ya dakika kadhaa, akasikia ving’ora vya gari za polisi. Akacheka kwa sauti ya chini na kutikisa kichwa kushoto, kulia.

    “Umeshida Gascoign. Wewe ndiye mshindi lakini unaingiza taifa katika janga zito ambalo halitakuja kuzimika.” Bonito aliongea hayo wakati huo viatu vilisikika vikipita katika dirisha la sebule lake kuelekea kwenye mlango wa kuingilia.

    Kamanda Bonito Muchakila, akatoa bastola aliyokuwa kaipachika nyuma kwenye nguo yake. Akaitzama bastola ile aina ya revolva, kisha akaibusu. Na sasa sauti ya viatu ilisikika kwenye mlango wa kuingilia pale sebuleni.

    “When one hero dies, five heroes born at the same time of the death. (Pale shujaa mmoja anapokufa, mashujaa wengine watano huzaliwa katika muda uleule ulotokea kifo)”Bonito akaingiza ncha ya mbele ya bastola ile kwenye midomo yake baada ya maneno yale.



    Na pale mlango wa sebule ulipofunguliwa tu! Bonito alifyatua bastola yake na risasi ambayo ilikuwemo, ilipita kinywani kwake na kufumua kisogo chake.

    Kamanda Bonito akawa kajiua kabla ya kuhukumiwa.

    Hata Rais alipofika pale mlangoni na kusikia sauti ya mlio wa bastola, alisita kwanza kuendelea kusogea mbele na kusubiri kusikia jambo lingine. Hakushika kitasa cha mlango wa sebule na badala yake aliita walinzi na askari wake.





    “Toeni kilichomo humo ndani.” Rais aliongea akiwa pale mlangoni bila kuingia ndani. Na baada ya kusema hayo, yeye akaondoka kuelekea nje lilipo gari lake.Wale mabwana walipoingia huku bastola na mitutu yao ya bunduki ikiwa tayari kwa lolote, walikutana na maiti ya Bonito ikiwa imeegamia kwenye kochi huku tobo kubwa likiwa kisogoni kwake. Walisogea kwa hamaki na kushindwa kuelewa ni nini kimetokea ndani ya dakika zile chache pekee. Walishuhudia mkono wake ukiwa na bastola lakini hawakuthubutu kugusa chochote kwa muda ule.



    “Tunaingia tena vitani Senegal.” Aliongea mlinzi mmoja kwa masikitiko baada ya kuutazama mwili wa Bonito kwa muda mrefu.

    Hata wale askari wa Rais walijikuta wakiwa katika masikitiko na hali ya sintofahamu baada ya maneno yale machache ya yule mlinzi. Ni wazi kifo cha Bonito kingeathiri nchi nzima kwa sababu Rais aliyopo, hakuwa na sauti mbele ya nchi zenye mabavu. Na pia kifo cha Bonito, kingezua bunge kuvunjika na viongozi walioteuliwa na Kamanda Bonito, wangeanza kuuawa tena kama wale wa mwanzo. Uasi ungerudi tena katika nchi ile ndogo na masikini.

    Gari la kubeba wagonjwa lilifika katika nyumba ya Bonito sambamba na askari wa upelelezi. Hiyo ni baada ya Rais kuondoka katika eneo lile. Uchunguzi ukafanyika na kugundulika kuwa Bonito kajichukua uhai wake mwenyewe. Maiti akapakizwa kwenye gari maalumu kwa ajili hiyo, na safari ya kuelekea mochwari, ikashika nafasi asubuhi ile.



    ****



    Nchi nzima ya Senegal ilikuwa kimya kusikiliza hotuba ya Rais wao kuhusu kifo cha Bonito. Aliongea kwa uchungu kana kwamba kilichotokea kilimuuma sana. Lakini ukweli ulibaki kuwa, licha ya uchungu katika uso wake, furaha ilitawala katika moyo wake. Hivyo ndivyo binaadamu alivyo, uso hauwakilishi moyo hata kidogo.

    Aliongea mengi kuhusu Bonito. Mengi hayo yalikuwa ni mema aliyoyafanya katika uongozi wake. Yote kwa yote, hakuthubutu kuongelea kuhusu kuvamia kambi ya Born To Die.

    “Tumepoteza shujaa mkbwa katika nchi yetu.” Ni baadhi ya maneno ambayo Rais aliyaongea bila kujua kama yana ukweli ndani yake.

    Aliwafumba wananchi wa nchi ile kwa mengi lakini maneno yake yalikuwa ni ukweli mtupu kama angekuwa na moyo wa ukweli kwenye kifo cha Bonito. “Kwa heri Kamanda Bonito Muchakila.” Ni maneno ya mwisho kuongea Rais Gascoign, na baada ya maneno hayo, akawa kamaliza hotuba yake.



    *****



    Peter akiwa katika safari yake ndefu na ngumu hasa kutokana na wanajeshi wa kisenegal waliotapakaa barabarani na sehemu mbalimbali hasa za maeneo yenye watu wengi, aliweza kufanikiwa kuingia kwenye pori ambalo wanalitumia sana kujificha.

    Alilijua pori lile fika, hivyo hakuwa na wasiwasi juu ya wanyama au wadudu watakaohatarisha maisha yake. Wasiwasi wake ulibakia kwa wanajeshi wa serikali ambao tayari walikuwa wamekwishajua makazi yao yapo wapi.



    Hadi saa tatu za usiku, tangu asubuhi alipoondoka kwa Kamanda Bonito, Peter alikuwa bado hajafika sehemu aliyoikusudia. Ilikuwa ni safari ndefu sana na hatimaye saa nne asubuhi siku inayofuata, alifika katika misitu iliyopo Kongo ambayo Waasi wa nchi ile walikuwa wanaitumia sana katika kufanya mambo yao yakiwemo kujificha.

    Peter akasogeza gari lake lililokuwa limechoka kwa safari ndefu na ngumu. Akalisimamisha gari lake mbele ya nyumba moja iliyojengwa kwa maturubai (hema) na baada ya sekunde kadhaa ya kulisimamisha gari hilo, walitokea wanajeshi watano mbele na nyuma ambao walikuwa wamemuelekezea mitutu ya bunduki.

    “Born To Die.” Peter aliongea maneno hayo akiitambulisha kambi ya waasi ambayo katoka na wanajeshi wale walitua chini silaha zao na kumkaribisha ndani ya hema walilokuwa wamelijenga pale nje.



    “Nahitaji kuonana na Xouma.” Aliongea Peter baada ya kukaribishwa kitini.

    Askari mmoja ambaye alikuwepo kwenye kumkaribisha, alitoka katika hema lile na kwenda katika hema lingine ambalo bila shaka Xouma, kama alivyoitwa na Peter alikuwepo huko.

    Baada ya dakika zipatazo mbili, yule askari aliingia akimtangulia bwana mmoja mrefu na mweusi, aliyevalia mavazi ya jeshi lakini yake yakiwa katika rangi tofauti ya shati la buluu ya kupauka na suruali ya buluu iliyoiva (Dark Blue).

    “Nini kimetokea huko kwenu?” Ndilo swali alilouliza Xouma, kiongozi wa kambi ile ya msituni kwa pale Kongo.

    “Rais kamsaliti Kamanda,” Alijibu Peter kwa masikitiko.

    “Mbona imetangazwa kuwa Bonito kakuta kajiua ndani ya jumba lake?” Swali hilo lililoulizwa kwa mtindo wa kutoa taarifa, likamfanya Peter kutumbua macho kama mtu aliyekabwa na fupa la samaki. “Ina maana hujui hilo?” Xouma alimuuliza Peter baada ya kuona mtu kakabwa na kigugumizi cha ghafla.

    “Nilimuacha mzima kabla sijaanza safari ya kuja huku,” Aligutuka Peter na kujibu kwa hamaniko.



    “Ni maiti kwa sasa.” Aliongea Xouma.

    “Rais mbwa sana yule,” Peter alimtusi Rais wa Senegal.

    “Kwani nini kimetokea?”

    “Nadhani Rais aliitambua kambi yetu ilipo. Juzi tumepambana na jeshi lake lakini mwisho wa siku kambi yote ililipuliwa kwa kusaidiana na Makomando toka mabara ya nje……..” Peter alieleza hadithi nzima toka walipopigana na kupoteza kila kitu na kila mtu akiwepo mpenzi wake Vanessa.

    Akaelezea alipoenda kwa Kamanda Bonito na kuelekezwa kila kitu kuhusu kwenda anapopataka lakini hakueleza lengo la kwenda huko kwa sababu kitaenda kinyume na wale wanajeshi. Sababu kubwa ni kwamba, wale wanajeshi wa Kongo walikuwa washirika wakubwa wa huko Peter anapokwenda.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Una bahati kijana. Kuna meli itakuja kesho kupitia Guinea. Wataleta silaha huku kwa kutumia magari yao. Utapanda magari hayo hadi Guinea ambapo utaenda na hao wanajeshi hadi kwenye meli yao. Watakufikisha sehemu ambapo nawe itabidi uwe mjanja kupanda meli za kwenda huko Urusi. Msaada wetu ni huo.” Aliongea Xouma na Peter aliafiki suala hilo.



    Wakaanza kuongea mengi mengine hadi muda ulipowadia kufanya majukumu huku Peter akipewa nafasi ya kupumzika.

    Akiwa katika chumba cha mapumziko, Peter alianza kuangalia tena makaratasi aliyoewa na Bonito kwa makini zaidi kwani aliweza kuyasoma akiwa ndani ya gari lake lakini si kwa umakini kama muda ule.

    Zilikuwa ramani ambazo alizielewa vema kutokana na elimu ambayo alipewa huko nyuma na baba wa Vanessa, Mzee Gomez.

    Alijua ni wapi pa kuanzia na ni wapi pa kuishia kutokana na ramani ile ambayo ilikuwa ni ya Urusi. Akaikunja na kuiweka chini ya mto.

    Akatoa makaratasi mengine ambayo safari hii yalikuwa ni pesa za Kimarekani lakini zenyewe zilikuwa bado hazijakatwa, zilikuwa kama gazeti. Maelezo ya kuzikata pesa zile, yaliandikwa kwenye karatasi ndogo iliyokuwepo katika bahasha ile. Hazikuwa bandia, bali zilikuwa katika kuingizwa katika mzunguko wa fedha wa dunia hii.



    Akaweka pesa zile ambazo zilikuwa katika dola mia moja.

    Akajilaza chali, akapumua pumzi ndefu na kufumba macho yake. Akajikuta akiwa katika taharuki baada ya kufikiria matukio mengi ambayo yalitokea kwa muda mfupi sana. Hata miaka kadhaa haikuisha jinsi matukio hayo yalivyochukua nafasi katika maisha yake.

    Akakumbuka siku za furaha za maisha yake hasa akiwa na familia nzima. Akamkumbuka sana mdogo wake wa kike na kaka yake pia kwa jinsi walivyokuwa wanapendana na kuelewana. Akakumbuka wazazi wake na kisha akakumbuka jinsi walivyopoteza uhai wao kirahisi rahisi tu.

    Hiyo haikutosha, akakumbuka alivyokimbia mkoa aliokulia na kwenda ugenini. Huko akakutana na Vanessa ambaye alimpenda kwa moyo wake wote. Lakini naye akampoteza kirahisi sana. Matukio yakawa yanajirudia na aliyaona ni kama yametokea kwa siku moja pekee.

    “Maisha yanaenda kasi sana,” Peter alitamka hayo na kujigeuzia uapande wa pili wa kitanda chake, usingizi ukawa mali yake.



    ******



    SEHEMU FULANI, URUSI.



    Peter alikuwa kakamata darubini yake na kutazama wanajeshi kadhaa waliokuwa wanalinda kambi kubwa yenye silaha nzito ndani ya uzio wake. Makombora kadhaa yalielekezwa kwenda juu, na vifaru vilipishana huku wanajeshi wengi wakiwa nyuma yake wakikimbia kwa mbwembwe.



    Akiwa katika mavazi masafi aliyopewa na Kamanda Bonito, aliishusha darubini ile na kuiweka kifuani. Akatazama nyuma alipotoka na kujikuta mwenye kutabasamu bila kupenda.

    “Naenda kumaliza kazi.” Alijisemea Peter huku akirekebisha bunduki yake kwenye mikono imara. Na baada ya kuiweka sawa, akatoa mkanda wa risasi katika begi lake na kupachika katika bunduki ile. Akajifunga mkanda ule wa risasi katika mwili wake. Na baada ya hapo, akaanza kusogea kule ilipokuwepo ile kambi kubwa yenye wazungu wa kutosha.

    Ni siku mbili kama alivyoahidiwa na Xouma, magari ya jeshi yalifika katika nchi ya Kongo na Peter akapata nafasi na kukwea magari hayo na kuelekea Guinea, ambapo pia nchi ile ya kutoka Asia, inasambaza silaha zake. Walipofika Guinea, Peter alipanda Nohari ambayo ilimfikisha hadi pembezoni mwa bahari ya Atlantiki katika kipande cha bahari kiitwacho The Baltic Sea.



    Peter akasoma ramani aliyopewa na Kamanda Bonito na kisha akatafuta uwezekano wa kutoka pale kwa sababu kulikuwa hamna watu wengi sana wanaoweza kukaa hadi usiku. Pesa zikatembea na akapata mtumbwi ambao ulimuingiza katika kijiji kimoja kilichopo huko Urusi.

    Hapo Safari yake ikawa imetimia kwa sababu kijiji hicho ndicho kilikuwa muongozo mzuri wa kufika anapopataka.

    Amekwishafika, kaweka silaha yake vema tayari kwa kupambana. Silaha ambazo alizipata hukohuko Urusi kutokana na pesa zake. Peter ambaye ni Muafrika, kapigana hadi kafika kambi inayosambaza silaha kwa Waasi wa nchi za Bara la Afrika.

    Kijana akaingia katika kambi ile na kuanza kutekeza kila kilichopo kwa bunduki pamoja na mabomu aliyokuwa kayaning’iniza katika mavazi yake. Peter alikuwa ni mwiba kwa wanajeshi wale ambao sidhani kama walitegemea ugeni wa aina ile.



    Alifanikiwa kutekeza silaha kali za maangamizi, lakini mwisho wake alikamatwa na kuwekwa katika chumba kidogo na kuteswa sana kabla kiongozi wa sehemu ile hajafika na kuanza kumuhoji.

    “What is your name? (Jina lako ni nani?)”

    “I don’t know. (Sijui)”

    “Pu pu pu.” Zilisikika sauti hizo kwenye chumba hicho kidogo kilichokuwa na watu watano.

    Sauti hizo zilikuwa ni sauti za kipigo kumwendea Peter aliyekuwa anaulizwa maswali.

    Jamaa hao watano, mmoja ambaye ndiye alionekana mkuu, alikuwa anauliza maswali, wengine wawili wamemshikilia kwa nguvu Peter ambaye alikuwa anaulizwa maswali. Huku wamemkunja mikono kwa nyuma na kufanya kifua na tumbo lake kubetuka vizuri kwa mbele jambo ambalo lilimpa yule jamaa wa tano kumshushia kipigo cha nguvu pale alipokaidi kujibu maswali yao.



    “I am asking you again. If you don’t answer, we will kill you (Nakuuliza tena. Kama usipojibu, tutakuua)” Yule mkuu wao ambaye alivalia mavazi ya kijeshi, tena yale yenye nyota nyingi mabegani na kwenye mifuko ya shati lake, alimpa onyo Peter aliyekuwa anapewa kipigo huku akiwa amechakaa uso kwa damu pamoja na kuvimba vibaya mno.





    Alishapoteza matumaini ya kuishi kwani mwili wake ulikuwa umelegea kiasi kwamba alikuwa anawapa uzito wale waliokuwa wamemshikilia.

    “What is your name (Jina lako nani)?” Jamaa aliulizwa swali.

    “I don’t know Sir (Sijui Mkuu)” Alijibu Peter kwa sauti ya chini iliyokuwa imeishiwa nguvu kabisa.

    Yule mpigaji alivyoona hivyo, alinyanyua ngumi yake tayari kuendelea kuishindilia mwilini mwa Peter.

    “Stop, (Acha)” Yule mkuu alimkataza mpigaji.

    “You are so rude, boy. Very good, (Wewe ni mkorofi, kijana. Safi sana)” Mkuu yule aliongea huku akizunguka zunguka kile chumba kwa tambo.

    “Release him. (Muachieni)”.Aliwaambia wale jamaa waliokuwa wamemshika na wao wakatii amri kwa kumwachia Peter.



    “You all, go outside (Ninyi nyote, nendeni nje)” Aliendelea kuwaamuru wale jamaa waliokuwamo mle ndani, nao wakatoka na kumuacha Peter kalala chini akigugumia kwa maumivu.

    “Okey. Now we're alone. You've to tell me the truth. (Sawa. Sasa tupo peke yetu. Unatakiwa kuniambia ukweli,” Aliongea mkuu yule huku akichutama karibu na pale alipokuwa amelala Peter Madira, kijana kutoka Senegar.

    “I've nothing to tell you (Sina cha kukuambia)” Alijibu Peter kwa sauti ya ukakamavu lakini iliyojaa maumivu.

    “That’s bad boy. So damn bad. (Hiyo mbaya kijana. Tena mbaya sana)” Aliongea yule mkuu huku akisimama toka eneo lile na kwenda kwenye jiko moja la umeme ambapo alikuwa ametenga birika la maji.

    Akachukua birika lile na kwenda nalo kwenye meza iliyokuwamo mle, kisha akamimina maji yale kwenye kikombe na kuchukua kahawa kiasi kwenye kijiko na kuchanganya kwenye maji yaliyo kwenye kikombe.



    Alivuta kiti kwa nyuma na kukikalia, kisha akafunua sahani moja iliyokuwepo mezani pale na kuchukua chapati moja.

    Aliikunja chapati ile na kuanza kuila huku akishushia kwa kahawa aliyoichanganya muda mfupi uliopita.

    Katikati ya ulaji wake, alimtupia jicho Peter aliyekuwa amelala pale chini. Alimwona jinsi anavyomwangalia alavyo, naye akatumia udhaifu huo kuongea naye.

    “Are you hungry? (Una njaa?)” Alimuuliza Peter huku bado anatafuna kipande cha chapati alichokuwa kabwia mdomoni.

    “Come on. Let’s eat. (Njoo. Njoo tule)” Aliongea yule mkuu na kunyanyuka pale kitini na kwenda kwenye kabati moja kuu-kuu la vyombo na kuchukua kikombe kimoja cha plastiki na kwenda nacho mezani.

    “Don’t you want it? (Hautaki?)” Alimuuliza Peter aliyekuwa amelala pale chini baada ya kumwona hajishughulishi kuitikia karibu yake.

    Peter alianza kuinuka pale alipokuwa na moja kwa moja akaelekea kuungana na yule mkuu kwenye meza ile.

    “That's my man. (Huyo ndiye mtu wangu)” Alimsifia wakati ananyanyuka huku yeye akimimina maji kwenye kile kikombe alichokuja nacho mara ya pili.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Peter naye alivuta kiti kiuchovu na kukaa huku akimuelekea yule mwenyeji uso wake. Akapewa kahawa kwenye kikombe kile na kusogezewa sahani ya chapati ili ajilie.

    Alikula kwa taratibu na kistaarabu kuliko alivyotegemea yule mkuu aliyekuwa anamuangalia kwa macho ya kumdadisi mtuhumiwa wake ambaye alikuwa kifua wazi na chini kavaa kombati ya jeshi yenye mabaka ya kijani aliyopewa na Kamanda Bonito.

    “So.Tell me soldier boy. Who're you and who sent you here, (Niambie kijana. Wewe ni nani na nani kakutuma hapa?)” Yule mkuu alimuuliza huku akiweka miguu yake mezani.

    “I am nobody and nobody sent me here. (Mi si kitu na hakuna aliyenituma hapa)” Peter alijibu na kisha aliinamia kahawa yake na kuendelea kuinywa.

    “You act like a taugh guy. Am I right boy? (Unajifanya kijana mgumu sana.Nadanganya kijana?)” Mkuu alimuuliza huku bado miguu yake ikiwa pale mezani anaitikisa-tikisa kwa mbwembwe.

    “No. I just answer your questions. But if you like me to be a tough guy,I'll be. But don’t blame me. (Hapana. Najibu maswali yako. Lakini kama unapenda niwe mgumu, nitakuwa. Lakini usinilaumu)” Peter alijibu huku anasogeza kikombe cha kahawa na sahani mbele kumuelekea yule mkuu.



    “You never answer my questions boy. And don’t try me to make you like before. (Hujanijibu maswali yangu kijana. Na usinijaribu nikufanye kama hapo mwanzo)” Mkuu aliongea huku macho yake kamkazia Peter.

    Pitty alikaa kimya huku naye macho yake anamuangalia yule mkuu ambaye umri kiasi fulani ulikuwa umeenda lakini alikuwa bado mkakamavu.

    Akiwa ndani ya mavazi yake ya nyota, mkuu yule alishusha miguu yake juu ya meza na kusogea mbele zaidi na kumkingia uso yule jamaa.

    “Umetumwa na Hispania? Cuba au Korea?” Mkuu yule alimuuliza kwa lugha ileile ya kiingereza.

    Peter akacheka kwa dharau kisha akamuangalia yule mkuu na kuhisi kama anapoteza dira.



    “Kwa nini ziwe nchi hizo na siyo zile mnazowatengenezea silaha za maangamizi na kuwapa ili muone kama zinafanya kazi ipasavyo? Kwa nini zisiwe zile nchi ambazo mnazichukulia malighafi zake na kujilimbikizia nyie? Kwa nini zisiwe zile nchi ambazo kila siku zinalia na njaa huku zikipoteza watoto wake kwa waume kwa sababu ya vita ambavyo nyie ndio wachonganishi? Kwa nini zisiwe nchi mnazozuga mnatandaza demokrasia, kumbe mnatandaza vita? Kwa nini zisiwe hizi nchi mnazozitupia magonjwa kila kukicha?

    Kwa nini zisiwe nchi hizo na badala yake zikawa nchi ambazo zinatetea msifanye maasi yenu?” Aliongea Peter kwa sauti ya chini iliyoanza kupata ahueni baada ya maumivu kupoa kiasi. Aliongea kwa hasira na msisitizo ndani yake.

    “Kwa hiyo umetokea Afrika,” Aliongea yule mkuu huku akirudisha mgongo wake kwenye kiti na kuweka miguu yake mezani tena na mikono yake akiipitisha shingoni na kuja kukutana nyuma ya kisogo chake.

    “Well, well. Umetoka Afrika. Niambie sasa. Umetoka Kongo, Kameruni au Naijeria. Au labda umetoka Niger au Sudan,” Alizidi kubwabwaja yule mkuu.



    “Nimetokea Afrika. Siwakilishi nchi wala Taifa,” alijibu kwa nyodo na kwa kujiamini.

    “Okey. Sasa ni muda wa kuwa siriasi. Nauliza na unajibu ipasavyo, sawa?” Mkuu alikuja juu sasa na kumtaka Peter awe siriasi kwa akifanyacho.

    “Ni wewe ndiye haupo siriasi. Nipo siriasi hata kwenye kula. Ni vema uwahi kusema ulichokusudia kuliko kuniacha au kuendelea kuniuliza maswali. Sitataja jina langu, wala hutojua nipo hapa kwa ajili gani,” aliweka msisitizo kwa akifanyacho.

    “Utakufa kijana,” Mkuu aliongea huku akiendelea kumwangalia kwa uangalifu.

    “I was BORN TO DIE,” alimjibu mkuu na kumuacha mkuu akiwa kinywa wazi bila kusema neno.

    Maneno yale yalidhihirisha kuwa haogopi wala kuhofia jambo lolote litakalokuja kumtokea mbeleni.

    “Nakuuliza mara ya mwisho. Wewe ni nani na nani kakutuma,” Mkuu aliuliza kwa hasira na mwenye sura iliyokuwa katika hali ya isiyo na utani ndani yake.

    “Go to hell (Nenda kuzimu),” Alijibu kama kumnong’oneza lakini sauti yake ikiwa yenye kiburi na wingi wa ujasiri.

    Mkuu yule alionesha ghadhabu zake moja kwa moja pale alipoepua birika lile lenye maji ya moto na kummwagia Peter kifuani.



    “Damn shit. You stupid,” Peter alitoa ukelele mmoja wa maumivu huku akirudi nyuma na kiti chake.

    “Nakuuliza tena blood foolish, we ni nani na misheni yako ni nini,” Mkuu aliuliza kwa sauti ya juu huku bado hasira zake zikiwa kileleni.

    “I was Born To die. Hata ufanye nini hupati kitu,” alimjibu kwa sauti ya juu na ya maumivu kutoka mwilini mwake.

    Mkuu kuona hivyo,akawaita wale wasaidizi wake na walikuja na kumkamata tena Peter na kumvutia hadi pale mezani na mikono yake wakaiweka juu ya meza.

    Mkuu wa sehemu ile akachukua uma kwenye kabati lililopo mle ndani na kisha akaanza kuirusha rusha na kuidaka huku akizunguka mle ndani huku na huko na maongezi yake yakiwa ya shari zaidi.

    “Unajidai mgumu sana kijana. Leo tutaona. Na utakufa sababu ya ujinga wako,” Mkuu aliongea huku akimwelekea pale mezani na kumuuliza tena maswali yale yale.

    “I was Born To Die (Nimezaliwa kufa)” Alijibu hivyohivyo kila alipoulizwa swali jambo lililompa hasira yule mkuu na kuwaambia wale wasaidizi wake waweke vizuri mkono wa kulia wa Peter.



    Alipoona mkono umekaa sawia, alinyanyua juu ile uma aliyokuwa nayo na moja kwa moja akaituliza kwenye mkono Peter.

    “Aaaagh.You fuckin, you’re hurting me motherf**** (Aaagh. We mjinga unaniumiza (Akatukana),” Alitoa kilio hicho kwa nguvu huku misuli yake ya shingo ikichomoza kwa sababu ya kujikaza wakati ile uma inaingia mkononi.

    “Niambie wewe ni nani?”

    “Nimekwambia sijui, nimezaliwa kufa.” Alijibu huku akilia kwa sauti ya juu.

    “Mpigeni huyu. Mi nitarudi baada ya dakika kumi.” Mkuu aliwapa ruhusa wale wasaidizi na yeye akatoka nje.

    Hapo hapo Peter akaanza kupokea kipigo cha nguvu kutoka kwa wale jamaa watatu.

    Waliompiga kichwani, walimpiga.Waliompiga mateke walimpiga, ili mradi walimpiga hadi akalegea na kushindwa hata kuongea.

    Dakika kumi baadaye, mkuu alirudi na kumkuta Peter kachakaa kwa damu na vimbe mbalimbali zikizidi kuongezeka katika mwili wake.



    “Vizuri sana,” Aliwapongeza wale wasaidizi na kumfuata Peter pale pembezoni mwa kona ya kile chumba alipokuwa amekaa.

    “Sasa niambie. Wewe ni nani?” Swali lilelile liliulizwa.

    Peter akamwangalia usoni na kutabasamu, tabasamu ambalo lililopotoka, lilitoka na michirizi ya damu mdomoni mwake.

    “Unajisumbua tu!. I was Born To Die” Akajibu kwa sauti ya chini na kisha akamtemea mate yalichanganyikana na damu usoni kwa yule mkuu.

    “Big mistake (Kosa kubwa)” Mkuu alitamka na kutoa bastola yake kisha akampiga usoni kwa nguvu kwa kutumia kitako kile cha bastola.

    Uso wa Peter ukachanika lakini ndio kama alikuwa amempagawisha mkuu.

    Akampiga tena upande mwingine wa uso wake napo akapachana. Peter sasa akawa anavuja damu uso mzima zaidi ya mara ya kwanza.



    “Tell me, who're you? (Niambie,wewe ni nani?)” Mkuu aliuliza lakini hakupata jibu bali mihemo ya kasi kutoka kwa Peter Madira.

    “I will kill you, blood foolish.(Nitakuua mpumbavu wewe)” Mkuu alimuonya huku akiikoki bastola yake na kumwekea kichwani.

    “I was Born To Die. I've nothing to loose (Nimezaliwa kufa, sina cha kupoteza)” Alijibu kwa kulegea na taratibu akainamisha kichwa kwa ajili ya kuipokea ile risasi.



    Mkuu naye akaanza kukibonyeza kile kifyatulio cha risasi huku akiwa makini asiifyatue hovyo huenda Peter atasema chochote. Lakini hadi amefikia nusu ya ile triger, hakuna neno lililomtoka yule jamaa.

    Kijana yule akainua kichwa chake na kumtazama kijakazi mmoja mle ndani ambaye alikuwa na rangi nyeusi kama yeye. Peter akatabasamu na midomo yake ikapepesa kwa kunong'ona neno "AFRIKA".

    Kijakazi yule alikuwa anamtazama na wakati huo mkuu wake anafanya maamuzi yake ya mwisho.



    Mkuu naye akaanza kukibonyeza kile kifyatulio cha risasi huku akiwa makini asiifyatue hovyo huenda Peter atasema chochote. Lakini hadi amefikia nusu ya ile triger, hakuna neno lililomtoka yule jamaa.

    Kijana yule akainua kichwa chake na kumtazama kijakazi mmoja mle ndani ambaye alikuwa na rangi nyeusi kama yeye. Peter akatabasamu na midomo yake ikapepesa kwa kunong'ona neno "AFRIKA".

    Kijakazi yule alikuwa anamtazama na wakati huo mkuu wake anafanya maamuzi yake ya mwisho.



    Bila kutegemea, kijakazi alishtuka pale aliposikia mlio wa risasi na kufuatia kwa mwili wa Peter kudondoka. Japo alikuwa ni mmoja wa wale wanajeshi waliyomsulubisha Peter, lakini kitendo kile cha Mkuu wake kumpiga risasi na kumuua Peter, kilimuuma sana.



    Akajiangalia rangi yake, akagundua ni nyeusi. Akakumbuka midomo ya Peter wakati inazungumza neno la mwisho ‘AFRIKA’. Akagundua kuwa naye ni Muafrika kama yule kijana aliyeuawa.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wakati wachache wakipigana kulikomboa bara zima au nchi za Afrika, wapo ambao wanakwamisha jitihada hizi kwa kuondoa wakombozi hawa. Peter ni mfano wa bara zima la Afrika. Si mtu bali Afrika.

    Afrika inadidimizwa na wanyonyaji kwa kufanywa kama jalala la silaha, magonjwa, vita, ujinga, njaa, umasikini na mambo kemkem yanayokwamisha maendeleo ya bara zima.

    Kama Afrika tunataka mabadiliko ya nchi zetu, inatubidi tusimame na kuunga sauti zetu. Tuwe na sauti moja ya mabadiliko, na tuwe na sauti moja ya umoja. Makundi katika madaraka, ndiyo sababu ya kuwapa mwanya watu wachache watutawale hadi watoto wetu.



    Afrika tuamke.



    MWISHO.



0 comments:

Post a Comment

Blog