Simulizi : Mkono Wa Jasusi
Sehemu Ya Pili (2)
“Aaa bibie kila anayekuja kubisha mlango hapa huwa kamfata ndugu yake, maana hii ndiyo wodi ya mwisho, hapa mgonjwa huja endapo tu kwenye wodi zote wameshindwa, na akifika hapa lazima atoke. Haya niambie kama maiti yako umefata nini huku Kuzimu?” Yule kijana akauiliza na mara hii akasimama lakini kwa kusimama kwake akaonekana wazi kuwa alikuwa kalewa pombe.
“Sikia, kuna miili ile iliyotoka kule mgodini…”
“Ya wale vijana wale, iliyokuja majuzi yaleeeeee,”
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ndiyo, nafikiri imeshafanyiwa uchunguzi sivyo?”
“Aaaa ndiyo tayari muda tu na polisi wamesharuhusu izikwe sasa, kuna ndugu yako pale au bwana ‘ako” Yule mhudumu akazungumza huku akitoka ndani ya ile ofisi, “Haya, njoo huku labda unataka kumbusu.
Debrah alikereka na maneno ya kijana huyo yasiyo na simile, lakini alijuwa wazi si kosa lake, kosa ni kukaa na maiti muda mwingi.
”Sikiliza wewe, nahitaji kuonana na daktari aliyefanya uchunguzi wa hizo maiti,” akamwambia.
Yule kijana akasimama na kumtazama Debrah, “Ndiyo unakuja saa hizi? Keshaondoka, kuna watu walimfuata hapa kama saa nne zilizopita,” akamwambia.
“Ok, anaitwa nani?”
“Anaitwa daktari Emmanueli Nkosizulu,” akajibu huku akirudi ofisini kwake.
“Nahitaji kuonana naye, nina jambo la msingi sana,” akaeleza.
“jambo lenyewe ni juu ya huo uchunguzi? Aaaaa wale si wameuawa wale, mbona haijifichi, wameuawa wale, sijui ndio kafara watu wapate madini mengi, lo, binadamu mna dhambi kweli,” Yule bwana akazidi kubwata huku akiingia ofisini kwake, alipoketi na kugeuka nyuma, Debrah hayupo. “He! Mzuka au? Chumba kina mauzauza hiki!” akajiwazia peke yake.
Debra alitoka na moja kwa moja kuelekea tena mapokezi; kule kupata tu jina la daktari kulimpa hatua moja mbele, sasa aliitaka taarifa yenyewe.
“Samahani dada, nitampataje daktari Emmanuel Nkosizulu?”
“Hayupo kazini, alipata dharula na kuondoka jioni mara tu alipoingia kazini, labda muone nyumbani kwake,” Yule mhudumu akajibu na kuendelea na kuhudumia wateja wengine. Debrah akajiondoa na kurudi kwenye gari yake.
* * *
Breaking News iliyorushwa usiku huo katika kituo cha televisheni cha S.A TV ilimshtua Kamanda Amata akiwa anamalizia kufunga kifungo cha mkono wa shati lake.
…daktari huyo ameuawa akiwa mita chache kabla ya kuingia nyumbani mwake kwa kupigwa risasi kichwani na watu wasiojulikana, shirika la upelelezi la Afrika Kusini limesema litahakikisha linawatia hatiani waliohusika na mauaji hayo…
Kamanda Amata hakuelewa kwanini damu inamchemka mwilini kwa habari hiyo, akaketi kuendelea kuitazama. “Emmanuel Nkosizulu,” alijitamkia jina hilo, kasha akachukua simu yake kubwa na kubofya sehemu Fulani Fulani akaingiza hilo jina katika mitandao ya utambuzi za watu mbalimbali. Sekunde tatu tu maelezo yakaanza kutiririka.
DAKT. EMMANUEL NKOSIZULU
Dr. Emmanuel Nkosizulu, mzaliwa wa Soweto miaka sabini iliyopita, alikuwa mwajiriwa serikali katika kiutengo cha madaktari bingwa wanaofanya kazi hospitali mbalimbali pindi wanapohitajika. Dakatari wa aina hii hujulikana kama ‘flying doctor’. Kituo chake cha kazi kilikuwa ni hospitali ya Charlote Maxeke kama mchunguzi na mwalimu wa madaktari. Serikali ilikuwa ikimtumia sana katika kesi za uchunguzi na vifo vyenye utata.
Siku hiyo daktari huyo alimaliza kufanya uchunguzi wake kwa kuuweka katika maandishi na tayari alikuwa akiuwasilisha kwa wahusika. Kutokana na uchunguzi wa awali kutokubalika, serikali ilimteua Nkosizulu kufanya upya uchunguzi huo, na baada ya kukamilisha kazi yake na kuwapa taarifa polisi kuwa amekamilisha kasha kibali cha kuzika maiti hizo kutolewa, ilimbidi Nkosizulu kuuwasilisha uchunguzi wake kwa wale waliomtuma.
Akiwa ofisini kwake ndipo alipopatwa na ugeni asiyoutarajia, vijana wawili na msichana mmoja wa kizungu, walimwonesha vitambulisho kuwa wao ni maafisa wa usalama na wametumwa kuja kumchukua ili kumpa ulinzi kwa safari yake ya kwenda Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hiyo, akakubali na kuiprinti kazi yake kasha akaisaini chini yake na kugonga mihuri inayotakiwa, akaitia katika faili na kutoka na vijana hao mpaka kwenye gari waliokuja nayo.
“Kwa sababu muda wangu kwenda kule bado saa kadhaa yanibidi nifike nyumbani kwanza,” aliwaambiwa le vijana.
“Sawa, basi tupatie hilo faili kasha utalichukua kwetu ukiwa tayari,” wakamwambia.
“Hapana, hilo aliwezekani, hili litakuwa mikononi mwangu mpaka nitakapolikabidhi kwa mhusika,” akawajibu huku akifungua mlango wa gari yake. Mmoja wa wale vijana akamshika bega.
“Sikia mzee, hilo faili linatafutwa, watu hawautaki huo uvhunguzi wako, sisi tumetumwa kukupa ulinzi pamoja na kuhakikisha hilo faili linafika mahala pake, kwa nini hutuamini?” aliyeonekana kama kiongozi wao, mrefu, mpana aliyevalia suti safi alimweleza hayo Nkosizulu.
“Nyie msijali, wakiiba hili, mimi hii taarifa yote ipo kichwani, kama mnanipa ulinzi nipeni lakini si kuwapa hili faili,” akawajibu.
“Ok, uamuzi ni wako, sasa tutakupeleka nyumbani kwako kasha ukiwa tayari tutakupeleka Wizarani. Hapo ndipo kazi yetu itakuwa imekamilika, Geofrey Jensen utakuwa gari moja na daktari mimi na Cayla tunafuata na gari yetu,” Yule bwana akeleza na kutoa maelekezo. Kasha wote wakaondoka eneo lile, gari ya daktari ikiwa mbele na ile nyingine ikifuata nyuma kwa umbali wa gari tatu kati yao.
* * *
Kamanda Amata akateremka ngazi taratibu na kuiacha hoteli hiyo ya kifahari ikiendelea kupendezeshwa na mianga ya taa ain aina, akaingia katika gari yake na kuketi nyuma ya usukani, akaichukua bastola yake mpya na kuiweka sawa kasha akaipachika kwenye mkanda maalumu ulipita chini ya kwapa lake. Akawasha gari yake nakuondoka eneo hilo.
“Mtaa wa Mamasilowane, kitalu namba 79 M,” alijisemea huku akiiweka ramani ya gari hiyo sawa sawa kuupata uelekeo anaoutaka kwa kutumia GPS inliyofungwa ndani ya gari hiyo ya kisasa, Kilimanjaro GX 220-TZ, iliyotengenezwa na kuboreshwa na wanasayansi wa Tanzania. Aliipita mitaa kadhaa na kuvuka barabara kadhaa kabla hajaufikia mtaa huo wa Mamasilowane. Sauti kutoka katika ile gari ilimpa taarifa kuwa amefika, mbele mita mia tano apinde kushoto, akafanya hivyo baada ya mita hizo alizotajiwa.
Akaendesha taratibu katika mtaa huo ulioonekana kuwa na ukimya wa hali ya juu. Macho yake yalipepesa huku na huko, mbele yake akaona moja ya barabara iliyoingia katika nyumba Fulani imewekwa utepe wa njano, akajua kwa vyovyote hapo ndipo apatakapo, lakini akiwa bado taratibu aliona mtu mmoja akitoka kwenye ile nyumba kwa mwendo wa haraka haraka. Kamanda Amata akapita bila kusimama na kuipita gari Fulani iliyokuwa imeegeshwa jirani na eneo hilo. Alipokuwa mbele kidogo, akawasha kamera iliyofungwa nyuma ya gari yake kwenye tundu la ufunguo wa buti, kutokea ndani aliweza kumuona Yule mtu akiingia kwenye ile gari na kasha ikaondoka.
Amata akaegesha gari yake katika mgahawa mmoja tulivu uliokuwa hapo na kuiruhusu ile gari kupita kwa kasi, kisha akaingiza yake barabarani kuifuatilia. Kwa kutumia kamera ndogo iliyokuwa mbele ya gari lake katikati ya nembo yam lima Kilimanjaro akaipiga picha na kuweza kuzinasa namba zake, akaihifadhi na kuiingiza katika kijimtambo kidogo kilichofungwa ndani ya gari hiyo, ‘Tracking System’. Nembo nyekundu ikaonekana katika ramani iliyopo kwenye kijiluninga ndani ya gari hiyo, ikimwonesha uelekeo wa ile gari ni wapi ilipo, kasha yeye akapunguza mwendo kwa kuwa alijua wapi anaenda.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
KAMANDA AMATA aliendesha gari yake taratibu akifuata barabara kubwa ya Mandela iliyokuwa ikipita katikati ya jiji la Johanesburg, huku akiangalia katika ramani yake uelekeo wa ile gari anayoitaka, hakuwa na haraka. Ndani ya gari yake alikuwa akisikiliza mziki wa jazz uliopigwa na Luis Amstrong huku akiufuatisha kwa mruzi, ilikuwa burudani sana kwake.. baada ya mwendo wa dakika kama thelathini hivi aliingia katika barabara ndogo ya West Street Sandtone, taratibu akaiona ile gari imeegeshwa katika maegesho ya hoteli kubwa ya kisasa yenye hadhi ya nyota tano, hii ni moja ya hoteli kubwa zinazojulikana ulimwengu, hoteli ya Michelangelo.
Naye akaingia katika maegesho ya upande wa pili, akaliweka gari lake vizuri akilitazama lile la wale jamaa. Hakuchelewa sana, aliwakuta bado wako nje wakijadiliana jambo, vijana wawili wa kizungu na mwanadada mmoja wa asili hiyo hiyo. Kati ya vijana hao mmoja wao alikuwa ni mpana mwenye tambo kubwa. Kasha wakavuta hatua kuielekea ile hotel, lakini hawakutumia mlango mkubwa bali walipita mlango mwingine ulioonekana kama duka Fulani kwani kwenye vioo vya mlango huo kulikuwa na masanamu mengi yaliyovalia nguo mbalimbali za kisasa. Kamanda akashuka na bastola yake kwapani, akafikiri mara mbili akaona hapana, akaamua kuiacha kwani sehemu nyingi kama hizo huwa huruhusiwi kuingia na silaha, akachukua miwani yake yenye uwezo wa kuona kitu cha chuma au silaha iliyo ndani ya kitu chochote kisichokuwa cha chuma.
Akachukua baadhi ya silaha zake ndogo ndogo na kuziweka mahala pake mwilini kasha akauendea ule mlango na kuingia ndani.
Ndani ya duka hilo kulikuwa na nguo nyingi za mitindo mbalimbali, za kiume kwa za kike, wadada warembo na vijana mashababi walikuwa wakijaribu nguo mbalimbali. Kamanda Amata akapita kati ya zile stands za nguo lakini jicho lake likiwa linawatazama wale vijana watatu. Wakafika katika mlango Fulani, palikuwa na walinzi wawili wa kizungu waliovalia suti safi nyeusi na kofia aina ya pama kila mmoja, Kamanda Amata akaivaa miwani yake na kuwatazama, kila mmoja alikuwa na bunduki chini ya kwapa lake, akatabasamu. Wale vijana wakafunguliwa mlango na kuingia ndani, kwa jicho la haraka, Amata aliona ngazi ndefu iliyokuwa ikielekea chini, ule mlango ukajifunga. Akavuta hatua na kuwafikia wale walinzi, akafanya kuwapita kama hawaoni, kabla hajaugusa mlango akadakwa mkono na kusogezwa kando.
“Huruhusiwi kwenda huko! Mbwa weusi hawana nafasi huko,” yule mlinzi akamwambia. Kamanda akamwangalia sana kuanzia juu mpaka chini.
“Nani anayeruhusiwa kwenda huko? Na kuna nini?” akauliza.
“Kijana usitake kujua, utapoteza maisha yako ndani ya dakika tu, mtu mweusi haruhusiwi kwenda huko, ondoka haraka,” Yule mlinzi akamwambia.
Amata akamwangalia sana Yule kijana, kasha akamwangalia Yule wa pili wakati huo wote miwani yake ilikuwa ikirekodi video na mzungumzo yao.
“Kuna nini huko?” akauliza na kufanya kama anataka kuchungulia kupitia ule mlango wa kioo.
Akapigwa kikumbo na kurudi nyuma. Mara akamuona Yule mlinzi mmoja akijisjika sikioni ambapo alikuwa amevaa hearphone, akajua tayari alikuwa ameonekana kwenye kamera za usalama. Haikupita dakika ule mlango ukafunguliwa na Yule mwanadada akatoka, akakbidhi kadi Fulani kwa wale walinzi na kuondoka zake. Baada ya Yule bwana kuongea kwa lugha ya ajabu ambayo Kamanda Amata hakuelewa hata neon moja kama si kushika tu, akaushusha mkono na kumtazama Amata.
“Ingia!” akamwambia Amata, mlango ukafunguka.
“Good! Tutaonana kesho muda kama huu, nitakuja,” akawaambia na kuondoka zake. Nje ya hotel ile alimwona Yule mwanamke wa kizungu akiingia kwenye ile gari waliokuja nayo, mara hii akiwa peke yake, bila ya wale wanaume wawili. Kamanda Amata akazungusha akili na kuanza kuambaa na maua kwa maua mpaka usawa wa gari yake, akafungua mlango na kuingia ndani, akasubiri kuona kinachoendelea. Akachukua bastola yake na kuibana kwapani, alipotazama kwenye kioo kikubwa cha mbele akaiona ile gari ikiondoka maegeshoni, akaifuata. Kwa mtindo uleule alikuwa akiitazama kupitia ramani ndogo iliyowekwa katika gari yake. Dakika kumi na tano zilitosha. Safari ikaishia katika mitaa ya William Nicor na Witkopen, Yule mwanadada akachepuka na kuingia katika uwanja mkubwa wa Montecassino. Ndani ya jingo hilo kulikuwa na kila aina ya burudani unayoijua wewe.
Yule mwanamke akashuka kwenye gari yake, akajiweka nywele zake ndefu vizuri, na kuzifunga kwa nyuma, kasha akatoaka na kitu kama briefcase hivi akafunga gari na kuelekea lile jingo. Kamanda Amata akateremka na kujiweka tayari, akarekebisha suti yake na kuvuta hatua kulielekea lile jengo.
? ? ?
DEBRAH alijishika kichwa kwa mikono yake miwili, akili yake iliganda kwa kiasi Fulani hakuju nini kinatokea. “Wameniwahi,” akajisemea wakati akiangalia mwili wa marehemu dakta Emmanueli Nkosizulu ukiingizwa katika gari ya wagonjwa iliyofika eneo la tukio. Alijaribu kutumia macho ya kikachero kung’amua kama muuawaji au swahiba yeyote wa muuaji alikuwepo eneo lile, hakuweza. Akaingia garini na kuondoka polepole eneo lile, akaegesha gari yake katika mgahawa jirani tu na nyumba ya marehemu, akasubiri hali ya hewa itulie.
Saa moja baadae, utulivu ulirudi katika lile eneo, Debrah akatoka kwenye ule mgahawa na kuvuta hatua kwa miguu yake kuilekea ile nyumba ya marehemu, akapita eneo lililotokea mauaji ambapo paliwekwa utepe wa njano, akapita na kuzunguka nyuma ya ile nyumba kubwa, akatazama ukuta ulioizunguka, haukuwa wa kutisha, akaukwea kwa ustadi na kutua ndani yake, akalifuata moja ya dirisha kubwa la upande wa nyuma, akalichezea kwa namna yake na kuingia ndani kwa upande wa chumbani. Nyumba haikuwa na mtu, akanyata hadi kwenye kabati dogo na kupekuwa hapa na pale, hakuna kitu, akaamua kuelekea sebuleni, akaufungua mlango na kutaka kutoka, na muda huohuo akasikia mlango mkubwa wa mbele ukifunguliwa, akarudi ndani na kujibana nyuma ya mlango wa chumbani, akaacha uwazi kidogo na kuchungulia.
Akawaona vijana wawili na mwanamke mmoja mwenye nywele ndefu wakiingia ndani humo.
“Sasa wewe hakikisha unapata tunachohitaji, sisi tunakupa ulinzi nje huku,” Yule mwanadada akamwambia kijana mmoja kasha wao wawili wakatoka nje na kumwacha Yule mmoja ndani akipekuwa huku na kule. Debrah alitulia akisubiri kuona nini anatafuta, baada ya dakika kama kumi hivi akamwona Yule mtu akiwa ameshika kitu kama kompyuta mkononi mwake na kitabu cha kumbukumbu ‘diary’ katika mkono huohuo akiwa ameviweka pamoja. Hakuendelea kuchambua tena, alipita sehemu kama mbili tatu akipekua-pekua lakini hakupata cha maana. Akatoka na kuufunga mlango wa mbele huku akiushika kwa kitambaa maalum.
Debrah akajitokeza sebuleni, akaliendea dirisha la mbele na kuangalia nje, akamwona Yule kijana akiingai kwenye gari na kuondoka.
“Shiit! Wameniwahi kwa mara ya pili,” akasema kwa sauti ndogo, kasha akatokea njia ileile ailuoingilia na kuondoka eneo lile.
“Nitawatia mkononi tu, watanitambua,” akajisemea huku akitembea haraka haraka kuliendea gari lake pale mgahawani, alipokuwa akiingia kwenye maegesho ya mgahawa huo, aliiona gari nyingine ya kijivu ikitoka kasi kuingia barabarani kwa uelekeo uleule ilikokwenda ile ya wale jamaa.
Debra aliwafuata mpaka alipoona gari zile zote zimeingia wapi, akateremka na kuangalia mwisho wake, alipoona wale jamaa watatu walipoelekea akatikisa kichwa, akajua hao ni watu wa aina gani, “Vampaya,” akajisemea na kisha akaingia garini kusubiri.
Simu ndani yagari lake ikaita, akainyanyua na kuipokea, ilikuwa ni kutoka kwa bosi wake huko Pretoria.
“…Debrah, nimetakiwa kusitisha mara moja operesheni hii, hivyo naomba nikuone hapa ofisini ndani ya saa tano zijazo…” sauti ya Dumisan ikamwambia.
Debrah akabaki kama kapigwa shoku ya umeme, macho yamemtoka, akahisi koo nalo limepteza majimaji, akameza funda kubwa la mate.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“…Kwa nini Boss? … Mbona ghafla hivyo? … Unanistisha,” Debrah alilalama.
“Debrah, wewe ni mtu wangu ninayekuamini kati ya wengi, na kesi zote zenye utata na ngumu kama hizi huwa nakupa wewe, lakini hii naomba uiache, njoo ofisini nitakupa maelekezo mengine, ndani ya saa tano tafadhali uwe hapa, sasa ni saa mbili usiku, hakikisha saa saba usiku ikukute hapa, muhimu sana,” simu ikakatika.
Debrah akabaki midomo wazi, alijikuta akitetemeka kwa hasira, akapiga ngumi usukani na kuanza kulia peke yake. Akawasha gari na kuondoka kwa kasi eneo lile akiwa na hasira, hakurudisha chumba cha hoteli, bali moja kwa moja akawahi uwanja wa ndege na kufanikiwa kupata ndege ya saa moja baadae. Akaelekea kwenye mgahawa na kuketi akaitisha kahawa akisubiri muda wa kuondoka.
“Kwa nini? Kwa nini Dumisan?” akjiuliza pasi na majibu. Akaletewa kikombe cha kahawa na kuanza kunywa polepole. Funda la kwanza, funda la pili, akahisi kitu kama bahasha kikitua mezani lakini mbele yake hakukuwa na mtu. Debra akaingiwa na hofu, akaitazama ile bahasha na kugeuka nyuma taratibu. Mtu mmoja mrefu, mwenye mwili wa wastani, aliyevalia suti nyeusi na kichwani pama jeusi, alikuwa mzungu mwenye nywele ndefu kiasi zilizomwagina mabegani mwake. Wakatazamana na Debrah kwa nukta kadhaa.
Macho ya Yule mtu yalimtisha Debrah, yalikuwa kama yap aka, mboni zake zilikuwa na rangi isiyoeleweka, akatabasamu na kuacha meno yake nje. Debrah akapata mshtuko baada ya kuona meno manne marefu kinywani mwa Yule mtu, meno kama ya samba au chui. Yule jamaa akawa anakiyumbisha yumbisha kichwa chake, kasha akaondoka na kumwacha Debrah pale kitini. Debra alimtazama Yule mtu mpaka alipotoka mlangoni na kupotelea nje, akaichuku ile bahasha, na kuigeuza upande wa pili, haikuwa imeandikwa kitu isipokuwa muhuri mwekundu wenye maneno ya lugha ambayo yeye Debrah hakuielewa hata kidogo; akaichana na kutoa kijikaratasi kidogo ndani yake chenye maandishi machache tu.
…Achana na hili unalolifuatilia, liko juu ya uwezo wako, ukibisha utakufa saa la sita kutoka sasa…
Ule ujumbe ukaisha hapo. Debrah akashusha pumzi ndefu na kuikunja ile karatasi akaitia mfukoni. Tangazo la abiri kupanda ndegeni ndilo lililomgutusha na kukuta kahawa ilikwishapoa muda mrefu, akachomoa noti ya Randi kumi na kuiweka chini ya kikombe kasha akaondoka zake.
? ? ?
DURBAN – usiku huohuo.
LERETI KHUMALO alikuwa na kikao kizito na wanasheria wake na wale waliosimamia mikataba ya ubia kati ya The Great Khumalo Goldmines LTD na Robinson Dia – Gold LTD.
Kwa pamoja waliupitia upya mkataba huo wa ubia na kuuona kuwa ndio hasa ambao wa aliusaini miaka saba iliyopita. Taarifa walizozipata za mkataba kutoka kwa Lereti baada ya kile kikao cha mchana uliopita ziliwatia hofu jopo zima.
“Kuna nini hapa?” mmoja akauliza.
“Robinson ataka kutuumiza, lazima tufanye linalowezekana mapema,” mwingine akajibu. Wakati huo wote Lereti alikuwa kimya, macho yake yakiwa yamejawa na machozi, hana la kusema.
“Au Madam unasemaje?” wakamwuliza Lereti.
“Kiukweli mi hapa najisi nitapata ukichaa, mi naona hili swala liende mbele tumfungulie mashtaka huyu bwana kwenye mahakama ya bishara ya Kimataifa,” akajibu.
“Sawa, wazo zuri lakini kwanza lazima tupite kwenye idara husika hapa kwetu,”
“Ndivyo”.
Kikao kiliafikiana kulipeleka mbele swala hilo, kwa ushirikiano wa wanasheria hao waliandika azimio la pamoja la kufanya hilo, walikubali kwa dhati kumsaidia mteja wao wa miaka mingi.
PRETORIA – Afrika ya Kusini
DEBRAH MBONGHENI aliingia ofisini kwa boss wake Bwana Dumisan na kumkuta bado amejaa nyuma ya meza yake. Alipomuona mwanamke huyo akasimama wima, akajua wazi mwanamke huyo lazima ataangusha varangati la maneno kwa kitendo cha kukatishiwa kazi yake.
“Karibu nyumbani Debrah,” akamkaribisha na kumwonesha kiti.
“Asante, Sir, ni nini hiki mnafanya tena? Mnakatisha kazi wakati ndio kwanza damu inanichemka,” akalalama.
“Sikia wewe, kama mimi ndiye nilikutuma basi ni mimi ndiye ninayekurudisha, rudi nyumbani endelea na kazi yako ya kawaida mdogo wangu, achana na hiyo kesi haituhusu,” akamwambia.
“Mi sikuelewi Mkuu!”
“Ndiyo huwezi kunielewa, najua, lakini sasa jifunze kunielewa, ni taarifa kutoka juu sina budi kuitekeleza, je na wewe wapaswa kufanya nini?” akamwuliza.
Debrah akasimama, akampa saluti, kasha akampa ile barua aliyopewa na Yule mtu wa kutisha pale Uwanja wa Ndege.
Dumisan, akaisoma na kuirudia kama mara tatu hivi, kasha akamrudishia Debrah.
“Endelea na majukumu yako ya kawaida,” akamwambia.
“Unajua nini kwenye hili Mkuu?”
“Debrah! Rudi kazini kwako, nimeshakwambia,” akamsisitizia.
Debrah, shingo upande akatoka ofisini kwa Dumisan na kuishia nje ambako alichukua gari yake ya kazini na kuondoka. Kichwani akiwa na mawazo mengi; kila mara alikuwa akijipiga kwenzi kichwani kuashiria kwamba kuna jambo linamsumbua. Japokuwa aliambiwa hasiendelee na kazi hiyo lakini kichwani mwake aliamua kumtafuta Lereti kwa siri; na aliona wazi kuwa kumtafuta mtu huyo si kwa simu, aliona ni bora kufanya analoweza kumfuata ofisini kwake au hata nyumbani kwa kuwa angeweza kutumia muda wake wa ziada.
“Lazima kuna jambo!” akawaza.
§§§§§
MONTECASSINO – Johannesburg
KAMANDA AMATA akamwangalia Yule mwanamke akiingia katika jingo hilo la starehe na lile begi mkononi mwake. Akashuka taratibu na kumfuatilia ndani ya hilo jingo, akamwona alipoingia lakini yeye hakuingia, akarudi mpaka kwenye gari ya Yule mwanamke. Kwa kutumia funguo yake ya siri yenye kufungua kila aina ya loki za gari, aliunyanyasa mlango huo kwa sekunde chache tu, hakutazama mbali, juu ya kiti cha abiria kulikuwa na kadi moja ndogo yenye maneno machache.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
…Montecassino, 9:20 PM…
Ujumbe uliishia hapo, Kamanda akatikisa kichwa, akatazama saa yake, ilikuwa saa tatu na robo, akachengulia hapa na pale, hakuna cha maana. Alipokuwa akitaka kuondoka akakumbuka kitu, akashusha ‘kizuia jua’ cha upande wa dereva, kulikuwa na vikaratasi na kadi kama nne hivi za benki na leseni ya kuendeshea gari, akaichomoa na kuiangalia kwa makini, picha ya Yule mwanadada ilionekana pale, ‘Jesca Gen’ akairudisha na kuipachika palepale.
Ndani ya jingo lile hakuzuiwa na walinzi kama kule Michelangelo, akaingia ndani ya jingo hilo, muziki mkubwa ulikuwa ndani yake, Kamanda Amata akapepesa macho na kumuona Jesca akiwa juu kidogo kwenye viti maalum vilivyoonekana kuwa ni vya ‘wenye pesa’: Pembani yake kulikuwa na watu wawili wote Wazungu, mmoja kijana alikuwa amesimama wima na mikono yake kaishikanisha pamoja chini ya kitovu chake, mwingine mtu mzima, mwenye nywele ndefu, aliketi kochini wakizungumza kitu Fulani na Jesca.
Amata akapita mpaka sehemu wanayouzia vinywaji, pale alikuta wamejaa Wazungu tupu, hakukuwa na Mwafrika hata mmoja, akasimama katikati na kuegemea kaunta hiyo ya kioo. Mmoja wa wale walioketi pale aliyeonekana m-shari hata kwa sura yake akamsukuma pembeni.
“Waafrika wote; kule!” akamwambia.
Amata akamwangalia Yule jamaa, akaegemea tena.
“Nipe Castle baridi,” akaagiza. Alipoletewa akaifungua kwa meno na kuimiminia kinywani nusu nzima, kasha akamtazama Yule jamaa aliyemsukuma. Wakati akifanya hivyo, kwa mbali akamwona Jesca akiachana na Yule mzee, akiwa kamwachia ile briefcase, naye kuteremka na kuchagua moja ya meza iliyokuwa wazi akaketi na kuagiza kinywaji. Amata akatoka taratibi na kwenda pale alipokuwapo mwanadada huyo.
“Naweza kukaa hapa?” akamwuliza. Jesca akamtazama kijana huyu, aliyevalia nadhifu kabisa, mwonekano wake ulikuwa tofauti na kila mmoja ndani ya Ile casino.
“Yeah, karibu sana,” akamkaribisha na kumwonesha siti. Kamanda akaketi na kuweka bia yake juu ya meza.
“Naitwa Spark!” akajitambulisha.
“Jesca,” naye akajitambulisha.
“Cheers!” wakagonga vinywaji vyao na mara hiyo, Kamanda Amata akaona mikono miwili minene iliyoshiba ikiegama mezani.
Akageuka na kukutana na uso na Yule Yule bwana aliyemsukuma kule kaunta.
“Toka ndani ya klabu hii, Mwafrika wewe huwezi kukaa na mwanamke wa Kizungu,” Yule bwana akamwambia. Kamanda akamtazama Jesca.
“Unamjua huyu?” akamwuliza. Jesca akamtazama mtu huyo kasha akarudisha macho kwa Amata.
“Simjui,” Jesca akajibu.
Kamanda akanyanyuka na kumtazama mtu huyo, Yule bwana hakutaka kuongea, watu wakasogea pembeni wakitazama kitakachojiri maana kila mmoja alimjua bwana huyo kwa ubabe wake.
“Toka nje!” akamwamuru Amata.
Kamanda akamwinua Jesca kwa kumshika mkono na kuanza kuondoka naye, mara akahisi maumivu makali begani mwake, kono la Yule jamaa lilitua sawia juu ya began a kushika nyama yake. Amat akageuka ghafla na kumpa konde moja maridadi lililotua mbavuni, kabla hajajiweka sawa, akampa kichwa kizito kilichokwenda na kufurumua damu puani mwake. Yule bwana akamwachi Kamanda na kurusha teke, Amata akakwepa na kudaka mahala penya korodani, akaziminya kwa nguvu zote, Yule bwana macho yalimtoka.
“Usifikiri kila mtu ni wa kumchezea sawa?” alimuuliza huku akiendelea kuminya kwa nguvu, Yule bwana alijaribu kujikukurusha ili kujinasua kutoka kwenye himaya ya Amata lakini wapi; mwisho akatulia tuli na kujibwaga chini mzima mzima, hana uhai. Watu wote wakabaki kimya, Jesca akamshika mkono Kamanda na kutoka naye nje haraka.
“Spark, umefanya kitu kibaya sana,” Jesca akamwambia walipokuwa nje tayari.
“Kitu gani, kumuu Yule mshenzi?”
“Genge lao ni wauaji waliobobea, watakusaka popote,”
“Nawakaribisha,” akajibu huku wakivuka barabara kulielekea gari la Jesca. Ghafla Jesca akamvuta Amata na kumwegemeza kwenye ubavu wa gari akakutanisha midomo yake na ile ya Amata, sekunde kama tano hivi akamwachia.
“So sweet!” kamanda akamwambia.
“No! wamepita hapo nyuma wangekuona ingekuwa shida, ingia garini, au umekuja na gari?” Jesca akaeleza na kuuliza.
“Hapana, sijaja na gari, unataka kunipeleka wapi?”
“Nikuondoshe hapa har…” Jesca kabla hajamaliza akamvuta ndani Amata, akawasha gari na kuondoka eneo hilo. Mwendo wa dakika kama kumi hivi, hakuna aliyekuwa akiongea na mwenzako
Jesca aliegesha gari kwenye jingo kubwa la kibiashara, Eastgate Shopping Centre.
“Hapa panakufaa,” jesca akamwambia.
“Asante sana, wewe unaishi wapi?” Kamanda akauliza.
“Alberton,” akajibu, “Vipi?” akaongeza swali.
“Usingependa niwe mgeni wako leo?”
“Ow Come on Mr Spark,” Jesca akamwamngalia Amata aliyeachia tabasamu pana.
“Au umeolewa, basi twende kwangu kama hutojali,”
“No,” akawasha gari na kuondoka eneo hilo, baada ya kukatisha barabara kadhaa Kamanda aliona bango kubwa liliobeba jina hilo, ‘Aberton’. Katika mtaa tulivu sana Jesca aliendesha gari yake taratibu mpaka katika moja ya jumba kubwa jeupe.
“Huku mbona kuna ukimya sana?” Amata akauliza.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Huku ni White Suburb, wanaishi watu weupe tu, mtu mweusi ukionekana huku unpigwa risasi au utakuwa nyama ya mbwa,” Jesca akajibu.
“Kwa hiyo maisha yangu yako hatarini?”
“Kama utayaweka mwenyewe, kabla ya saa kumi na moja alfajiri uondoke huku,” akamwambia. Jesca akaegesha gari na wote wawili wakaingia ndani.
Ndani ya sebule kubwa kamanda Amata alimkumbatia Jesca, na kumbushu shingoni, lakini Jesca alionesha upinzani kidogo lakini hakuweza kutoka katika himaya ya Kamanda Amata.
“Please, niache, sipendelea mambo haya!” Jesca aling’aka.
“Mmmhh! Jesca,” Amata alimwita taratibu na kumkamata vizuri kasha akaanza kumnyonya ulimi, Jesca akatulia naye akarudisha majibu, kisha akajitoa katika mikono ya Amata.
“Subiri kwanza,” Jesca akamwambia Amata, kasha akaelekea jikoni na kurudi na kinywaji kikali Vodka na glass mbili zenye kiuno mkononi mwake. Akamimina na kumpatia moja Amata, akaipokea na kuiweka pembeni akafanya hivyo na kwa ile nyingine, akamnyanyua Jessca na kumtupia juu ya kochi kubwa, kasha akaja juu yake na kuanza fujo za mahaba, Jesca alibaki kulala mika tu akionesha ushirikiano wa hali ya juu, nusu saa baadaye kila mmoja alibaki kama alivyozaliwa, mihemo na miguno ya mahaba ikafanya muziki mzuri katika sebule hiyo pana.
§§§§
HOTELI MICHELANGELO – JOHANNESBURG – Usiku huo huo
DON ANGELO akashusha glass yake iliyosheheni kinywaji, juu ya bega lake alimweka mjusi mzuri mwenye kung’aang’aa.
“Ni nani Yule kijana mkorofi?” akauliza vijana wake.
“Hatumjui kwakweli,”
“Watu kama wale hawatakiwi kuwa nasi karibu, wengine si wema,” Don akaeleza.
“Anaweza kuwa mpelelezi? Mbona anajiamini sana?” kijana mmoja aliyejazia misuli akauliza.
“Hakuna mpelelezi Afrika anayeweza kuutambua mtandao huu, wakubwa wengi wapo hapa,” akajishika kiganja chake.
Mara hiyo hiyo, simu ikaita, mmoja wa wale vijana akaipokea, akaongea maneno machache, akamletea Don Angelo.
“…ndio… what? Ok!” akakata simu. Akatulia kwa nukta kadhaa na kuchukua kitambaa chake akajifuta jasho kasha akapiga funda moja la maana la kile kinywaji.
“Amefanya mauaji Montecassino!” Don akaeleza kwa kifupi.
“Nani?” Yule aliyejazia misuli akauliza.
“Huyo tunayemwongelea hapa, na inasemekana kaondoka na Jesca pale club, haijulikani kaelekea wapi. Tomsen, nataka uniletee hii habari yote ndani ya dakika tano tu,” Don akatoa oda.
Dakika tano baadae, Tomsen alikuwa amekwishakusanya habari zote juu ya Amata na kuzituma kwa Don kupitia mtandao wao maalum wa mawasiliano.
Wakiwa wameketi katika namna ya mkutano, vijana wale wenye sura za ajabu kwa walivyojiweka walikuwa wanapewa maagizo maalum na Don yaliyotakiwa kufanyiwa utekelezaji wa haraka.
“Anajiita Mr Spark, lakini ni Amata Ric, Agent kutoka T.S.A, yuko hapa kwa niaba ya SADC kuchunguza upya vifo vya mgodini. Rekodi yake ya kijasusi iko juu sana Afrika, mashirika ya nje yanamtambua kwa mbali, lakini hayajaonesha wazi kama wanamkubali kama jasusi la kimataifa,” akawatazama vijana wake,
“Sasa hivi usiku huu yuko nyumbani kwa Jesca, Jesca ametusaliti, kuna kila namna ataweza kutoa siri za mtandao, “Nendeni, mkawalete wote wawili, msiwasumbue kwa starehe zao waacheni wamalize kasha muwatie mkononi, muwalete hapa nataka kuwaona niwafungishe ndoa…”
“Mmmm, you are so sweet Mr. Spark!” Jesca Gen alilalama na kusifu kwa mahaba aliyokuwa akiipata kutoka kwa Amata usiku huo; alisahau kabisa kwamba aliyekuwa akifurahia naye kuibanjua amri ya sita ni mtu mweusi nay eye ni mweupe. Sekunde, dakika na sasa zikakatika wote wawili wakapitiwa na usingizi mzito na kujitupa mmoja huku na mwingine kule. Ukichanganya na pombe kali walizokunywa hakuna aliyejua hata nini kinaendelea duniani.
Majira ya saa tisa hivi, Kamanda Amata aligutuka kutoka usingizini, akamtazama Jesca, alikuwa kalala fofofo hata hajitambui, akajivuta taratibu na kumuacha palepale katika kochi kwa maana hata hawakukumbuka kwenda chumbani. Alisimama kando na kuvaa nguo zake taratibu bila kufanya ukulele wowote, aliipapasa bastola yake, ipo, akaiweka tayari na kuipachika mahala pake, kasha akaiendea meza ndogo iliyokuwa na droo kadhaa, akapekua hapa na pale, akakutana na nakala moja ya ujumbe uliofika kwa njia ya nukushi. Ujumbe huo ulikuwa na taarifa kuhusu Lereti .
“Lereti,” akajikuta akitamka jina hilo kwa sauti ya chini. Hakujua ni muda gani hasa binti huyo atakuwa safarini. Kamanda Amata taratibu akaliendea dirisha kubwa na kulitazama kwa jinsi lilivyo, nakalipachua kifungulio chake na kulisukuma juu kasha akatoka kwa kutumia dirisha hilo.
Taa zilikuwa ziking’aza kila upande wa barabara hiyo, hata ingeanguka sindano ingeonekana, akatembea kwa hadahari kubwa huku mbwa wakibweka hapa na pale, mkono wake ulikuwa ndani ya koti lake, kidole cha shahada katika kifyatulio cha bastola yake, risasi moja ndani ya chemba wakati saba zikisubiri katika foleni ya mauaji muda wowote. Kwa mbali aliona gari inaingia katika barabar hiyo, zilikuwa mbili. Akarudi nyuma taratibu na kujibana mahali kwenye kijumba cha posta ambacho ndani yake kulikuwa na mitambo ya simu. Ile gari ikapita eneo lile ikifuatiwa na nyingine, alipozitupia macho zote mbili zikasimama kwenye nyumba ya Jesca. Macho yakamtoka Kamanda, akatulia palepale ili aone nini kinatokea.
Wale watu wakateremka na kuifuata nyumba ya Jesca, wachache wakabaki nje wakiweka ulinzi na wengine wakaingia ndani ya ile nyumba. Kelele za mbwa wa nyumba nyingine zilikuwa nyingi. Lakini hawakujali.
§§§§§
JESCA GEN alijikuta kazingirwa pale kwenye kochi na watu ambao hakujua hata wameingiaje ndani kwake, si kwamba alikuwa hawajui lakini alikuwa akiwajua wote kwa sura na majina.
“Mpenzi wako yuko wapi?” mmoja akauliza.
“Mpenzi!” Jesca akashangaa.
“Humu ndani haukulala na mwanaume wewe, tena isitoshe mweusi?”
“Si mngemkuta, yuko wapi sasa?” Jesca akang’aka.
Jesca alijua wazi kuwa amekamatika na alijua nini kingefuata kutoka nkwa Boss wao, lakini alipata nguvu baada ya kuona kwamba Kamanda Amata au Spark hayupo ndani ya nyumba ile. Upekuzi wa haraka ukapita lakini kamanda hakupatikana.
“Sawa umetuzidi ujanja lakini asubuhi ufike Michelangelo uonane na Boss,” Yule kiongozi wao akasema hayo na kuamuru waondoke.
Jesca alipiga ngumi mezani kwa hasira, kwanza hakujua Kamanda Amata ameondokaje na wakati gani, hakujua kama alijua kuwa atafuatwa au la, akaliendea dirisha na kuvuta pazia akaangalia zile gari zikiondoka.
§§§§§
Asubuhi ya siku iliyofuata ilimkuta Kamanda Amata katika banda la magazeti, akanunua moja ya magazeti maarufu sana pale Afrika ya Kusini, habari ya juu kabisa iliyokuwa ikisomwa na wengi ilikuwa ni ile ya wakaguzi wa bodi ya migodi ya Afrika kusini kuutembelea mgodi wa Khumalo. Ndani ya habari hiyo aligundua kuwa msafara huo unatokea Pretoria kuelekea Johanesburg mchana wa siku hiyo. Akili ya Amata ikazunguka haraka haraka, akaondoka eneo lile na moja kwa moja akarudi hotelini kwake, akachukua kompyuta yake na kutazama ramani ya wapi ulipo mgodi huo, akapapata, akafunga kompyuta yake, akachukua simu na kuwasha mtambo wa GPS locator akaingiza maelekezo ya anapotaka kwenda, ikajichora njia nzima ya kupita ikimwonesha umbali na vituo atakavyopitia naidadi ya saa atakazotumia.
“Masaa matatu na dakika ishirini na moja,” akajisemea mwenyewe, akaitazama saa yake, ilikuwa yapata saa tatu asubuhi. Akatochukua baadhi ya vifaa vyake muhimu pa si na kusahau silaha zake za kijasusi, kifaa cha kunusa kama eneo lina bomu au la, akavipachika mwilini mwake, akabadili saa na kuvaa saa maalumu inayoweza kupiga picha, kunasa mazungumzo na kurekodi picha jongefu, miwani yake iliyoonekana kama miwani ya jua yenye uwezo mkubwa wa kuona nyuma na kupima umbali kutoka yeye mpaka kitu cha mbele yake, mashine yake ndogo ya kutolea kopi yenye ukubwa wa pakti la sigara, akavisunda vyote katika nguo zake bila kusahau magazine mbili zilizoshiba risasi. Akatoka nje na kusimamaisha taxi.
“Montecassino tafadhali,” akamwelekeza Yule dereva tax naye akampeleka mpaka hapo, wakalipana na Kamanda Amata akaliona gari lake likiwa palepale alipoliacha jana. Akachonoa rimoti yake mfukoni na kuliwasha, likawaka na kubaki likinguruma. Kutoka kwenye kioo cha rimoti ile aliweza kulikagua gari hilo kama lina mtego wowote. “liko safi,” akajisemea kasha akaliendea taratibu na kuingia ndani yake, akaligeuza na kuondoka eneo lile kwa kasi kama kawaida yake. Ndani ya gari aliiseti upya ramani yake iliyokuwa ikimuongoza njia kuelekea huko aendako.
§§§§§CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
LERETI KHUMALO alikuwa ndani ya helkopta yake, safarini kuelekea mgodini ambako bodi ya ukaguzi wa migodi ilipaswa kuukagua mgodi huo kwa dharula, haikuwa imepangwa lakini ilibidi kutokana na hali tete iliyopelekea kufungwa kwake. Kila mara alionekana ametingwa na na simu yake au laptop iliyokuwea juu ya kijimeza kidogo. Walinzi wake watano walitulia kimya pasi na kuongea lolote. Mvumo wa pangaboi za helkopta hiyo ndiyo pekee uliyosikika kutawala ndani humo. Lereti alikuwa akipekuwa mashirika mbalimbali na watu m,balimbali aliyowaona wangefaa kumsaidia katika kazi yake, sikitiko lake kuu lilikuwa ni kukosa mawasiliano na Amata, tangu waachane ni miaka mingi imepita na hakuwahi kuwasiliana naye, mshangao uliokuwa ukimrudia mara kwa mara ni ule wa nani aliyeondoa kipande cha karatasi chenye anwani ya mtu huyo katika kaitabu chake cha kumbukumbu.
“Ningempata Amata, kazi ingekuwa ndogo,” akawaza na kujikuta chozi likimtoka, kwa mkasa huu, Lereti alimkumbuka sana marehemu baba yake na alitokea kumchukia mbia wake Mr. Robinson Quebec.
Saa tano asubuhi, alitua katika uwanja mdogo wa kutua helkopta nje tu ya mgodi huo na kupokelewa na watu kadhaa waliokuwa hapo tayari kwa shughuli hiyo. Aliposalimiana nao, moja kwa moja wakaingia katika ofisi maalum wakiketi na kusubiri ugeni huo kutoka serikalini. Daima Lereti alikuwa kimya akionekana kuwa mwenye mawazo mengi sana. Dakika kumi baadaye ilifika helkopta nyingine ikawaleta wawakilishi wa mbia wake, ambaye yeye daima huwa hapendi kujitokeza, raia wa Canada na aliishi huko. Nao vilevile wakapokelewa na kuungana na Lereti kuwasubiri wageni wao.
“Lereti,” bwana mmoja aliyeonekana kuwa na tumbo kubwa aliita. Lereti akamtazama tu lakini hakujibu kitu.
“Kwa nini mambo haya unayapeleka kienyeji hivi?” akauliza.
“Mambo gani?”
“Si hawa wageni si tunapewa taarifa tu za juu juu kana kwamba hatuna uamuzi katika hili!” Yule bwana akalalamika.
“Sikia Stephan, mi sijaita watu hapa kwa ukaguzi au nini, hata mimi nimepigiwa simu jana juuu ya hili kutoka kwenye bodi sasa nipinge?” Lereti akauliza, Yule bwana akasonya na kugeukia upande wa pili.
§§§§§
KAMANDA AMATA aliuacha mji wa Johanesburg na viunga vyake na kwa mwendo wa kasi alikuwa akielekea huko mgodini. Baada ya mwendo wa saa mbili gari yake ilianza kumpa ishara kuwa amekaribia eneo husika, ilimwambia kwa maneno ya Kiswahili kuwa ‘Bado kilomita sabini,’ akaendelea kukanyaga mafuta na gari hiyo aina ya Kilimanjaro GX 220-TZ ilikuwa ikifanya vitu vyake huku ikimpa maelekezo mbalimbali kumtahadharisha kama mbele kuna kona na ni ya upande gani, kuna mlima au mteremko, kuna kituo cha mafuta au. Aliendelea kukimbizana na muda huku kichwani akipanga na kupangua ni jinsi gani ataingia hapo bila kujulikana.
Akiwa tayari katika eneo la mgodi huo, kilomita takribani ishirini kabla ya kuufikia, alam ndani ya gari yake ikaanza kupiga kelele na sauti ya kike ilisikika ikimtahadharisha kuwa gari yake inaonekana kwenye rada iliyofungwa huko mgodini.
§§§§§
MGODI WA DHAHABU WA THE GREAT KHUMALO
KUTOKA katika chumba cha usalama ndani kabisa ya mgodi huo, sauti ya tahadhari ilisikika, bwana mmoja aliyekuwa akifanya kazi ndani humo, akaseleleresha kiti chake na kufika kwenye luninga moja wapo iliyokuwa ikionesha kitu kinachowakawaka. “Nini hiki?” akajiuliza na kuanza kubofya bofya kompyuta yake hukua akiangalia kwa makini nini kitu gani kinachoonekana hapo, taratibu ile picha ilikuwa inaonekana kwa uzuri zaidi na ndipo alipoiona gari. Akapiga simu kwa walinzi wa nje na wale walio kwenye vidungu juu kabisa ya majengo yao.
Katika orodha ya watu waliotakiwa kufika mgodini hapo hili gari halikuhusika. Walipogundua hilo mara moja ikaamuliwa gari hiyo inayoonekena kwenye rada ilipuliwe, wakaweka tayari mzinga wa kuifumua gari hiyo wasiyoijua.
Lereti na mshirika wake walikuwa wakitazama kwa makini kwenye luninga iliyo ndani ya ofisi hiyo na wao wakiwa washauri wa mwisho kuamua kama gari hiyo ipigwe au la.
“Msiipige gari ambayo hamuijui, je ni vipi kama ni mmoja wa wageni wetu?” Lereti akawauliza.
“Tumehakikisha wageni wetu wote wa siku ya leo wako njiani salama na hili gari au huyu anayekuja hatumtambui, na sheria yetu hapa wewe mwenyewe unaijua,” mkuu wa kitengo hicho alikuwa akiongea kwa simu maalum na Lereti pamoja na mshirika wake.
Stephan akatoa amri gari hiyo ipigwe mara moja, waliporudi kuitazama tena walikuta taarifa kuwa ile gari haionekani, wakahangaika kuitafuta kwa kutumia rada lakini haikuonekana kabisa. Yule mkuu wa kitengo cha usalama, alibaki kapigwa na bumbuwazi, kwa mbinu zote lakini hakuiona ile gari, ikabidi warushe ndege ndogo ya patrol ili iangalie kutoka juu kama wataiona gari ile…
NDEGE NDOGO ya patrol ilizunguka angani lakini haikuweza kuiona ile gari, kila walipojaribu kutumia njia tofauti za kisasa walishindwa kuiona, wakatoa kule mgodini ambako pia walikuwa wakiendelea kuitafuta kwa mitambo yao lakini hawakuiona.
§§§§§
Kamanda Amata aliegesha gari umbali kilomita kama tano hivi kutoka mgodini, akaliingiza gari lake ndani ya vichaka na kulifunika kwa manyasi kulifanya lisionekane kiurahisi. Alipohakikisha limefichika, akaipachika sawia bastola yake na zana nyinginezo, akatokea barabarani na kutazama umbali ule. Kwa mbali aliona maghala makubwa yaliyojengwa kwa mpangilio, akiwa katika kutafakari hayo alisikia muungurumo wa gari, akajibana nyuma ya mti mkubwa kusubiri. Gari kubwa aina ya MAN lilitokea kule upande way ale maghala na kupita kwa mwendo wa taratibu, nyuma kulikuwa na watu watano waliovalia sare maalumu na mikononi mwao walikuwa na bunduki aina ya SMG, walikuwa ni walinzi wa kampuni inayolinda mgodi ule. Lile lori likasimama umbali mfupi tu kutoka pale alipo Amata, wale vijana wakashuka na bunduki zao mikononi. Wakatawanyika kusaka.
“Ni hapa, walisema kilomita tano, ndiyo hapa, tawanyikeni,” amri ikatolewa na wale vijana wakaanza kutafuta huku na kule wasione.
“Huku!” mmoja aliita akifuata alama za matairi ya gari yaliyoelekea porini, wenzake wakamfuata, na wote wakaingia vichakani kutafuta.
“Hivi hiyo gari ina ukubwa gani hata tusiione?” mmoja akauliza akiwa kajishika kiuno. Kamanda Amata alikuwa akitamani kucheka jinsi walivyokuwa wakibishana wenyewe kwa wenyewe. Akawaona wakiwasiliana na wenzao kupitia simu ya upepo. Good! Amata akajisemea kwa sauti ya moyoni. Baada ya mawasiliano hayo, wakakwea kwenye gari lao na lile gari likageuzwa, ndipo Kamanda Amata akaliwahi kwa nyuma na kulidandia huku akihakikisha haonekani na wale waliosimama juu, nyuma kidogo ya kibini ya dereva. Alipohakikisha hawamuoni kwa kuangalia kwao mbele muda wote alijiingiza ndani yake na kujifunika vyema na turubai zito lilikusanywa kwenye kona moja ya lori hilo.
“Kuna lolote?”
“Hakuna lolote,”
Amata alisikia mazungumzo hayo akajua kuwa wapo getini, mara lile gari likaanza kutembea tena mpaka eneo ambako alihisi ni maegesho, akatulia kimya. Kwa kutumia tundu dogo katika turubai hilo aliweza kuona wale vijana wakiteremka na kuondoka eneo lile, akajifunua kidogo na kuangalia vyema, eneo lile lilikuwa na walinzi kwa mbali, akajitoa na kuteremka haraka haraka, akajibana kati ya gari na gari, kisha akapita uvunguni kwa uvunguni mpaka gari ya mwisho, akajibanza kabla ya kujitokeza akiangalia kupitia uvungu wa gari hilo huku na kule, akaona mmoja wa askari akisogea kunako gari lile akamsubiri kwa hamu, alipofika tu pale, akamshika miguu na kumuta ghafla, Yule bwana ajibwaga, kisha Amata akavuti chini ya gari, akampa kichwa kimoja maridadi, akamzimisha. Palepale uvunguni akachukua nguo za Yule mlinzi na na kuzivaa haraka haraka, kisha akajitokeza kutoka uvunguni akiwa tayari kamficha mtu wake kwenye tairi la nyuma.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Akapita moja kwa moja mpaka kwenye lengo kuu la kuingilia ndani ya mgodi ule, akijifanya kuwa ni mmoja wao kumbe la. Akjipenyeza kwa njia anzozijua yeye. Katika moja ya penyopenyo zake Kamanda Amata aliwaona watu kama kumi hivi wakiwa na mazungumzo Fulani ambayo yeye hakuweza kuyasikia, walikuwa wakitembezwa huku na kule na mtu aliyeonekana kama kiongozi wa msafara, akajua kuwa hao ni wale wageni ambao ana taarifa yao na ndiyo waliomfanya aje huku. Akaendelea kuwafuata bila ya wao kujua, wakihamia pale ye anaenda kule akijaribu kupata hasa nini wanachozungumza, alipofika eneo ambalo wako vizuri na aliwaona vizuri, akachomoa kitu kama bastola lakini haikuwa bastola, akachukua kitu kingine akakipachika kwa mbele, akawalenga na kufyatua, kile kidude kikaenda moja kwa moja kwa kasi kikatua kwenye bega la Yule kiongozi wa msafra kikanata kwenye nguo yake.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment