Search This Blog

Sunday, 22 May 2022

UFUKWE WA MADAGASCAR - 2

 







    Simulizi : Ufukwe Wa Madagascar

    Sehemu Ya Pili (2)

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



     Niliendelea kusota na hatimaye nikatokezea kwenye sehemu ya lile gogo iliyokuwa juu ya yale maji ya ule mto. Kwa kweli nilishikwa na furaha isiyoelezeka huku nikiweka kituo kidogo sehemu ile, nikivuta hewa na kusambaza oksijeni ya kutosha kwenye mapafu yangu na kuhema ovyo kama shujaa aliyetoroka kifo. Hata hivyo sikutaka kujidanganya kuwa pale nilikuwa sehemu salama hasa nilipowakumbuka wale watu hatari niliyowatoroka kule darajani muda mfupi uliopita. Hivyo mara baada ya kuvuta hewa ya kutosha nikaendelea na safari yangu ya kuzidi kuukwea ule mti. Muda mfupi baadaye nikawa nimefanikiwa kutoka kabisa kwenye ule mto na kuifikia sehemu ya nchi kavu kando ya ule mto kwenye shina la ule mti. Kwa kweli nilijisikia furaha sana kwani japokuwa nilikuwa bado nikisikia maumivu makali kutokana na yale majeraha yaliyosababishwa na mawe hatari ya ule mto lakini sehemu kubwa ya maumivu yale ilikuwa imemezwa na kitendo kile cha kufanikiwa kuinusuru roho yangu.

     Nikiwa pale juu ya shina la ule mti nikaanza kuyachunguza vizuri mandhari yale. Ule mto ulikuwa mkubwa na mpana na kwa sehemu ile ulikuwa umekatisha katikati ya msitu wenye miti mirefu na mikubwa. Ingawaje nilipochunguza vizuri kwa mbali niliweza kuyaona makazi ya watu hali iliyonitanabaisha kuwa eneo lile halikuwa mbali sana na mji mdogo. Nikageuka na kutazama kule nyuma ule mto ulipokuwa ukitokea huku nikitarajia kuliona lile daraja nilipowatorokea wale watu lakini sikuliona kwani matawi makubwa ya miti mirefu iliyokuwa kando ya ule mto iliukinga upeo wa macho yangu vilevile niligundua kuwa katika eneo fulani ule mto ulikuwa umekunja kona na kushika uelekeo wa pale nilipokuwa. Hivyo haraka nikagundua kuwa nilikuwa nimesafirishwa umbali mrefu na yale maji ya ule mto kutoka kwenye lile daraja ingawa sikuweza kufanya makadirio ya haraka ya umbali ule.

     Baridi ilikuwa ikinipiga kwa vile sikuwa na nguo yoyote ya kunisitiri mwilini na yale majeraha ya mawe mgongoni na pajani yalikuwa yakiendelea kuvuja damu taratibu na kwa kweli hali ile sikuipenda lakini vilevile sikuwa na namna ya kukabiliana nayo. Niliitazama saa yangu ya kijasusi mkononi aina ya BBE-HD Spywatch isiyoweza kuingiza maji na yenye ujazo wa 8GB. Inayoweza kurekodi sauti na picha lakini vilevile yenye uwezo wa kunasa sauti ya tukio lolote lililopo umbali wa mita nane na pia inayotoa utambulisho wa hali joto ya mwili na mazingira na uelekeo wa pande za dunia. Dakika chache zilikuwa zimesalia kabla ya kutimia saa mbili asubuhi, majira ya saa ile yalionesha hivyo. Njaa ilikuwa ikinuuma ingawa nilijitahidi kwa kila hali kuipuuza. Jambo muhimu la kwanza nililokuwa nikilifikiria ni juu ya namna ya kupata nguo za kujisitiri mwilini na baada ya hapo mambo mengine yangefuatia.

     Nikiwa pale juu ya shina la ule mti mawazo mengi yakawa yakipita kichwani mwangu na kabla sijaamua nifanye nini mara nikashtushwa na mtikisiko wa kichaka hafifu chenye nyasi ndefu kilichokuwa ng`ambo ya ule mto. Nikageuka na kukitazama kile kichaka kwa makini na hapo nikaona kiashiria cha mjengeo wa kiumbe hai. Sikutaka kusubiri...



    ...nikaona kiashiria cha mjengeo wa kiumbe hai. Sikutaka kusubiri zaidi hivyo haraka nikashuka kwenye shila la ule mti kisha kwa tahadhari nikanyata nikipotelea kwenye ule msitu uliopakana na ule mto kwa kasi ya mjusi pori. Huku nikifanya hivyo pasipo kutengeneza kiashiria chochote cha uwepo wangu eneo.

     Mara baada ya kuingia kwenye ule msitu sikwenda mbali badala yake nikajibanza nyuma ya mti mmoja mkubwa uliokuwa kando ya ule mto ambao uliniwezesha kuona vizuri ng’ambo ya ule mto kwenye lile eneo ulipotokea ule mtikisiko wa kile kichaka. Muda mfupi uliofuata mara nikawaona watu wanne wakijitokeza kwenye kile kichaka kilichokuwa ng`ambo ya ule mto. Kuona vile nikasogea karibu ili niweze kuona vizuri watu wale ni akina nani. Taswira iliyonasa machoni mwangu ikapelekea moyo wangu upoteze utulivu kabisa.

     Amanda alikuwa ameongozana na Meja Pascal Karibwami, Staff Surgent Anatole Nkunda na Koplo Adolphe Sahinguvu huku wote wakionekana katika nyuso zenye hasira na mikononi mwao wameshika bastola. Walipofika kando ya ule mto wakasimama huku wakionekana kushauriana jambo fulani. Nilipomtazama Meja Pascal Karibwani nikagundua kuwa uso wake ulikuwa umefura kwa hasira bila shaka kutokana na ule uzembe uliofanywa na askari wake kiasi cha kunipa mwanya mzuri wa kutoroka.

     Wakiwa wamesimama ng’ambo ya ule mto mara nikawaona wakiyatazama yale maji ya ule mto kwa makini kama waliokuwa wakitarajia kuniona nikiibukia maeneo yale. Lakini maji ya ule mto yaliendelea kuwasuta huku yakisafiri taratibu kwa mzizimo wa aina yake hali iliyonipelekea nitabasamu kidogo. Kisha nikamuona Meja Pascal Karibwani akizungumza jambo fulani ambalo sikuweza kulisikia huku akinyoosha kidole chake kuwaelekeza wale askari wake katika lile gogo la ule mti uliotumbukia kwenye ule mto, ambalo dakika chache zilizopita nilikuwa nimekaa pale juu ya shina lake. Tukio lile likanipelekea nianze kushikwa na mashaka juu ya maamuzi ambayo yangefuatia baada ya pale.

     Kulikuwa na majadiliano fulani ya kina kati ya Meja Pascal Karibwami na wale askari wake huku kila mmoja akionekana kutoa hoja yake kwa kina kwa kadiri alivyohisi kuwa huwenda ingekuwa na msaada mkubwa katika kunikamata tena. Nikiwa bado nimejibanza nyuma ya ule mti nikaendelea kuwatazama wale watu kwa utulivu huku nikisubiri hatima yao ingawa kwa namna moja au nyingine nilikuwa na kila sababu ya kuamini kuwa mimi ndiye niliyekuwa ajenda yao kubwa katika maongezi yale. Baada ya muda mfupi mara nikahisi kuwa yale maongezi yao ni kama yalikuwa yamefika ukomo na sehemu iliyosalia ilikuwa ni ya utekelezaji wa mkakati.

     Nikiwa bado nimejibanza nyuma ya ule mti kando ya ule mto mara ghafla nikawaona wale watu wakigeuka tena na kulitazama kwa makini gogo la ule mti mkubwa ulioangukia mle ndani ya ule mto. Huku Meja Pascal Karibwami akionekana kuwaelekeza wale askari wake juu ya jambo fulani ambalo liliwapelekea wote wageuke vizuri na kuutazama kwa makini ule msitu uliokuwa ng’ambo ya ule mto ambao mimi nilikuwa nimejibanza nyuma ya ule mti nikiwatazama kwa makini.

     Haukupita muda mrefu mara nikamuona yule mwanajeshi kauzu matata aliyejitambulisha kwangu hapo awali kwa cheo cha Staff Surgent Anatole Nkunda akijirusha kujitosa kwenye ule mto na kuanza kuogelea taratibu akiuvuka ule mto kwa kulifuata lile gogo la ule mti uliotumbukia mtoni. Tukio lile haraka likanipelekea nianze kuhisi nini ambacho kilikuwa kinaelekea kutokea baada ya pale na kwa vile sikuwa muumini mzuri wa kitu kinachoitwa bahati sikutaka kuondelea kusubiri.

     Taratibu nikauacha ule mti niliokuwa nimejibanza nyuma yake kisha kwa tahadhari ya hali ya juu nikaingia ndani zaidi ya ule msitu nikitokomea huku tayari nikiwa na wazo jipya kichwani mwangu. Wazo lililofufua tumaini na kunipa furaha isiyoelezeka kutoka katika sakafu imara ya moyo wangu. Nafsi yangu ikanitanabaisha kuwa ile ndiyo ingekuwa nafasi nzuri ya kujiokoa vizuri mbali na wale watu hatari katika mtindo nilioupa kauli mbiu ya perfect get away ya mshangao wa aina yake.

     Mara nilipouacha ule mti na kutokomea kwenye ule msitu nikaanza kutimua mbio za kijeshi nikiupangua ule msitu kwa kasi ya ajabu kurudi kule kweye lile daraja nilipowatoroka wale watu kwa kujitosa mtoni huku nikiwa uchi wa mnyama kama nilivyozaliwa. Hata hivyo niligundua haraka kuwa ule msitu ulikuwa bado haujaathiriwa sana na shughuli za kibinadamu vinginevyo mtu yeyote ambaye ningekutana naye katika ule msitu nikiwa katika hali ile ya uchi asingesita kunipa mgongo na kutimua mbio huku akidhani kuwa mimi ni mwendawazimu kama siyo kiumbe kutoka sayari nyingine.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

     Ndani ya muda mfupi tu hatimaye nikawa nimelifikia tena lile daraja lililokuwa na kuzuizi cha yale mawe ambapo muda mfupi uliopita nilikuwa nimejitosa kwenye ule mto mkubwa uliokuwa ukitatisha chini yake wakati nilipokuwa nikiwatoroka wale watu hatari. Nilipolifikia lile daraja nikajibanza kwenye mti mmoja uliokuwa jirani na eneo lile huku nikichunguza kwa makini hali ya usalama ya eneo lile. Sikumuona mtu yeyote na lile gari la jeshi TDI-Discover lilikuwa bado limeegeshwa palepale kama nilivyokuwa nimeliacha wakati ule nilipotoroka. Kitu cha kushangaza zaidi ni kuwa hata yale mawe ya kizuizi yaliyokuwa kule mbele ya lile daraja bado yalikuwa hayajaondoshwa yote hali iliyonipelekea nifahamu kuwa lile tukio la kutoroka kwangu lilikuwa limewachanganya sana wale watu kiasi cha kutokushughulika tena na kile kizuizi cha yale mawe.

     Nikiwa nimeridhishwa vizuri na usalama wa eneo lile taratibu nikayaacha yale maficho ya kwenye ule mti na kunyata kwa tahadhari nikienda kwenye lile gari. Muda mfupi uliofuata nikawa nimelifikia lile gari hivyo hali bado ilikuwa shwari. Nilipochungulia sehemu ya mbele ya lile gari nikaliona lile begi langu na kunifanya nijisikie furaha. Haraka nikafunga milango ya nyuma ya lile gari kisha nikaelekea kule mbele ambapo nilifungua mlango wa dereva na kuingia ndani. Nilipochunguza mle ndani haraka nikagundua kuwa funguo ya lile gari haikuwepo mahala pake. Hata hivyo hali ile haikunitatiza sana kwani haraka nikaibomoa ile swichi ya injini iliyokuwa chini ya usukani wa lile gari na kisha kutafuta nyaya mbili muhimu ambazo nilipozigusisha mara moja shoti ndogo ya umeme ikapiga na kuipelekea injini ya lile gari kuwaka. Sikutaka kupoteza muda hivyo haraka nikafanya jitihada za kuondoka eneo lile.

     Bila kupoteza muda nikaligeuza lile gari kwa fujo na kushika uelekeo wa kurudi kule tulipotoka huku mwendo wangu ukiwa wa kasi isiyoelezeka. Macho yangu mara kwa mara yakawa yakitazama kwenye vioo vya ubavu wa lile gari hadi ile taswira ya madhari yale nyuma yangu ilipotokomea kabisa machoni mwangu. Baada ya mwendo mrefu wa safari yangu hatimaye nikajiridhisha kabisa kuwa hakukuwa na gari lolote lililokuwa likinifuatilia nyuma yangu. Hata hivyo sikutaka kujidanganya kuwa bado nilikuwa salama kwa kuendelea kulitumia lile gari la jeshi la wananchi wa Burundi. Hivyo wakati nikiendelea na safari yangu macho yangu yakawa makini kutazama huku na kule na kwa kufanya vile mara nikaiona barabara moja ya vumbi iliyokuwa ikichepukia upande wa kulia. Pasipo kujishauri nikapunguza mwendo na kuingia upande wa kulia nikiifuata barabara ile ya vumbi.

     Ilikuwa ni barabara nyembamba ya gari iliyosongwa na nyasi hafifu na vichaka vya miti. Nilipochunguza vizuri nikagundua kuwa ile barabara ilikuwa ikielekea mashambani. Baada ya mwendo mfupi nikawa nimepata maegesho mazuri chini ya mti mkubwa wa mwembe uliozungukwa na vichaka hafifu vya miti na nyasi.

     Yalikuwa ni mazingira tulivu na sehemu isiyokuwa na dalili zozote za uwepo wa watu. Nilipoegesha gari chini ya ule mwembe nikalichukua lile begi langu kutoka kwenye siti ya abiria upande wa kushoto ambapo alipokuwa ameketi Meja Pascal Karibwami pale awali. Ndani ya lile begi kulikuwa na nguo zangu chache hivyo haraka nikajifuta vizuri mwilini kwa kitambaa changu cha leso. Nilipomaliza nikachukua kisanduku kidogo cha huduma ya kwanza kilichokuwa ndani ya lile gari na nilipokifungua nikakuta vifaa vyote muhimu vya huduma ya kwanza kama; mikasi midogo, mabunda ya pamba safi, bandeji, vidonge vya kutuliza maumivu, spiriti, gv na vifaa vingine muhimu vya huduma ya kwanza.

     Kupitia vifaa vile nikaanza kujitibu lile jeraha la kwenye paja langu la mguu wa kushoto lililotokana na yale mawe hatari ya kwenye ule mto niliyojitosa nikiwatoroka wale watu. Wakati nikijitibu nikawa ni kama niliyeamsha maumivu makali mwilini. Hata hivyo sikuwa na namna ya kuepukana na kadhia ile.

     Hatimaye nikamaliza kujitibu lile jeraha vizuri na kujifunga bandeji imara iliyoukamata vyema msuli wangu wa paja. Nilipomaliza nikaanza kujitibu yale majeraha ya maongoni. Maumivu yalikuwa makali mno wakati nilipojimwagia dawa nyingi kwenye yale majeraha na kuyasafisha kwa pamba safi niliyoibana vyema kwa ncha ya makasi. Hatimaye nikamaliza zoezi lile na kuyafunga yale majeraha kwa bandeji. Kisha nikachukua vile vidongea vya kutuliza maumivu na kumeza tembe mbili. Kutoka katika lile begi langu nikachukuwa suruali ya jeans ya rangi ya samawati, fulana ya rangi ya kijivu na kofia nyeusi ambapo nilizivaa zile nguo. Zile buti zangu ngumu za ngozi zilikuwa kwenye mfuko mweusi wa nailoni uliokuwa pale mbele hivyo haraka nikazivaa zile buti miguuni.

     Nilipojitazama kupitia kwenye kioo cha mbele kilichokuwa chini ya paa la lile gari nikaridhishwa vizuri na muonekana wangu. Nilipochunguza vizuri mle ndani ya lile bagi langu la mgongoni nikafurahi sana kukuta zile nyaraka zangu zote muhimu zikiwa salama pamoja na kile kiasi cha fedha nilichotokanacho jijini Kigali nchini Rwanda. Kwa kweli kichwa changu kilikuwa kimepata utulivu wa hali ya juu huku nikiwa bado siamini vizuri kama nilikuwa nimefanikiwa kukiponyoka kifo zile dakika chache zilizopita.

     Hatimaye nikaanza kufanya upekuzi wa kina ndani ya lile gari katika namna ya kuchunguza kama ningebahatika kupata silaha yoyote ya kuanzia harakati zangu pale jijini Bujumbura nchini Burundi. Mungu mkubwa kwani baada ya upekuzi wa kina ndani ya lile gari kwenye droo moja iliyokuwa kwenye dashibodi ya lile gari nikaikuta bastola moja aina ya SP-21 Barak Silenced na magazini zake mbili zilizojaa risasi. Nikaichukua ile bastola na kuisunda kibindoni kisha nikaichukua ile ramani yangu ndogo ya kukunja ya kijasusi na kuitia mfukoni. Sasa nilikuwa tayari kuanza harakati na nilipojitazama tena kupitia kile kioo cha mle ndani cha chini ya paa la lile gari pale mbele nikagundua kuwa sura yangu ilikuwa imerejewa na uhai.

     Sikuwa na sababu ya kuendelea kukaa zaidi eneo lile hivyo haraka nikawasha gari na kugeuza nikirudi kwenye ile barabara ya lami kwa kupitia tena kwenye ile barabara hafifu ya vumbi iliyosongwa na nyasi ndefu na vichaka vya hapa na pale. Baada ya muda mfupi tu nikawa nimeifikia tena ile barabara ya lami. Kabla ya kuingia kwenye ile barabara ya lami nikasimama kwanza nikichunguza hali ya usalama wa eneo lile. Sikumuona mtu yeyote eneo lile wala gari la doria hivyo mambo bado yalikuwa shwari. Hivyo bila kusubiri zaidi nikatia moto gari na kuingia kwenye ile barabara ya lami ambapo nilishika uelekeo wa upande wa kulia nikizidi kutokomea mbali na kule nilipotoka.

     Nilipofika mbele kidogo nikaiacha ile barabara baada ya kuhisi kuwa mbele yake kulikuwa na dalili za uwezekano wa uwepo wa maandamano kama zilivyokuwa sehemu mbalimbali za jiji la Bujumbura. Hivyo nikaingia upande wa kushoto kuifuata barabara nyingine ya lami na nilipochunguza kupitia ile ramani yangu ndogo ya kijasusi nikagundua kuwa nilikuwa kwenye barabara iliyokuwa pembezoni mwa ufukwe wa Ziwa Tanganyika katika eneo lililofahamika kwa jina la Muha. Kwani wakati nikiendelea na safari yangu kwa mbali upande wa kushoto niliweza kuona mandhari nzuri ya Ziwa Tanganyika na hapo nikakumbuka kuwa hata ule mto niliyojitosa huwenda ulikuwa ukitapisha maji yake katika ziwa lile. Kwa kweli nikajikuta nikimshukuru tena Mungu kwa kuniepushia mbali na janga lile.

     Nilichokuwa nimepanga kichwani mwangu kwa muda ule ilikuwa ni kufika katikati ya jiji la Bujumbura kwani nikiwa pale ningekuwa na nafasi nzuri ya kuanza harakati zangu. Ile barabara niliyoingia haikuwa na msongamano mkubwa kwani magari yalikuwa machache sana huku yakipita kwa ustaarabu. Kwa kweli niliomba nisikutane na kizuizi kingine chochote mbele yangu. Nikiwa naendelea na safari yangu katika baadhi ya maeneo nilikutana na vijana wengi waliojazana kwenye Toyota Pickup ambapo walinipungia mikono kwa furaha na hapo nikajua kuwa kitendo cha wale vijana kuliona lile gari la jeshi huwenda walikuwa wakidhani kuwa mimi ni mwanajeshi wa jeshi la Burundi. Kwa vile hadi wakati ule jaribio la mapinduzi ya kijeshi lilikuwa likiendelea nchini Burundi. Hata hivyo nikafanya hisani kwa kuwapungia mkono huku usoni nikiumba tabasamu jepesi hadi pale nilipopishana nao huku kila mmoja akiendelea na hamsini zake.

     Sikupenda kuendelea na harakati zangu kwa kutumia lile gari la jeshi la wananchi wa Burundi kwa vile niliona kuwa lingekuwa ni jambo la hatari sana kwa usalama wangu. Hasa baada ya suala la amani nchini Burundi kuzidi kuwa tete. Hivyo wakati nikiendelea na safari yangu nikawa nikiyatembeza macho yangu huku na kule nikitafuta sehemu nzuri ambayo ningelitelekeza lile gari bila ya mtu yeyote nyuma yangu kufahamu kuwa ningekuwa nimeshika uelekeo upi baada ya pale. Niliipita hoteli ya kifahari ya La Bamba iliyokuwa upande wa kulia huku nikiendelea kuiona mandhari nzuri ya Ziwa Tanganyika kwa upande wa kushoto kwangu. Nikaendelea na safari yangu hadi pale nilipokutana na barabara ya Avenue du Cercle Nautique. Nilipoyafikia makutano yale nikapata wazo kuwa pale ndiyo ingekuwa sehemu nzuri ya kulitelekeza lile gari la jeshi kwa vile niliona kuwa ingekuwa vigumu kwa mtu yeyote kuweza kufahamu kuwa ningekuwa nimeshika uelekeo upi baada ya pale. Hivyo nilipofika pale nikaingia upande wa kuchoto wa ile barabara sehemu yenye kichaka hafifu cha kuelekea kwenye ufukwe wa Ziwa Tanganyika. Kisha nikaligueza lile gari na kulitelekeza eneo lile katika uelekeo wa lile gari kutazama kule nilipotoka. Nilipomaliza nikafunga vioo na milango ya lile gari na kushuka chini. Nilipolichunguza vizuri eneo lile sikumuona mtu yeyote na hali ile ikanipa faraja kubwa kuwa hila yangu ilikuwa bado haijashtukiwa.

     Jua la asubuhi lilikuwa tayari limekwisha chomoza vizuri na miale hafifu ya jua lile iliponifikia mwilini ikazidi kuvipa uhai viungo vyangu. Begi langu dogo la shanta likiwa mgongoni nikaanza kutembea taratibu nikiliacha eneo lile na kuendelea na safari yangu nikiifuata ile barabara.

     Kwa mujibu wa ile ramani yangu ndogo ya kukunja ya kijasusi ni kuwa kutoka pale kulikuwa na mwendo mrefu endapo ningeamua kutembea kwa miguu hadi kuifikia kona ya barabara ya Avenue du 13 Octobre. Iliyokuwa kando ya kituo cha mzungo wa maji wa Bujumbura ujulikanao kama Cercle Nautique de Bujumbura kwa upande wa kushoto katika ufukwe wa...



    ...Ziwa Tanganyika. Ambapo mara baada ya kufika kwenye kona ya barabara ile kwangu ingelikuwa ni jambo rahisi kuweza kupata usafiri wa kunifikisha ninapotaka katikati ya jiji la Bujumbura.

     Nikiwa naendelea kutembea kwa miguu kandokando ya barabara ile nikapishana na magari matatu. Magari mawili yakiwa ni madogo na ya kawaida na gari moja lilikuwa ni lori la jeshi la wananchi wa Burundi lililokuwa limewabeba wanajeshi wengi waliovaa sare zao na bunduki zao mikononi.

     Hata hivyo kupitia kofia yangu ya kapero iliyonikinga vyema usoni nikajitahidi kwa kila hali kuuficha uso wangu wakati wale wanajeshi kwenye lile lori walipogeuka na kunitazama nilipokuwa nikipishana nao. Hata hivyo hawakusimama na hali ile ikawa salama kwangu. Hatimaye nikaifikia ile kona ya barabara ya Avenue du 13 Octobre huku nikiwa nimetembea kwa muda usiopungua nusu saa.

     Nilipofika kwenye kona ya ile barabara nikajisikia faraja kidogo baada ya kukutana na pilika pilika hafifu za watu wa eneo lile. Kulikuwa na watu wengi kiasi watembea kwa miguu na hata idadi ya magari nayo ilikuwa imeongezeka barabarani. Hata hivyo hali ya utulivu katika barabara ile ilitosha kunitanabaisha kuwa hali ya usalama jijini Bujumbura nchini Bujumbura bado ilikuwa tete.

     Mara nilipoingia kwenye ile kona barabara ya Avenue du 13 Octobre nikaiacha ile kona na kushika uelekeo wa mbele zaidi ambapo muda mfupi baadaye nilikuja kukutana na barabara ya Avenue de La Plage. Nikiwa naendelea kutembea kando ya barabara ile magari kadhaa yakawa yakinipita huku mara kwa mara nikijaribu kusimamisha teksi bila ya mafanikio. Jambo lile kwa kiasi fulani lilinishangaza sana kwani hali kama ile ilikuwa ni vigumu sana kuiona jijini Dar es Salaam ampao wasaka tonge hawalali usiku na mchana kutafuta mkate wa kila siku. Sehemu ambapo hata takataka za jiji tayari zimegeuka dili katika kujipatia kipato cha kujikimu kwa baadhi ya wakazi wake. Kwani zile teksi nilizojitahidi kuzisimamisha zilikuwa zikinipita bila kisimama ingawa ndani yake hazikuonekana kuwa na abiria.

     Baada ya mwendo mrefu wa miguu hatimaye nikawa nimekifikia kituo kimoja kikubwa cha kujazia mafuta kilichokuwa upande wa kushoto wa ile barabara huku nyuma yake kikiwa kimepakana na ufukwe wa Ziwa Tanganyika. Nilipokifikia kile kituo cha kujazia mafuta nikawa nimeingiwa na tumaini baada ya kuziona teksi kadhaa zikiwa zimeegeshwa kando yake.

     Mzee mmoja dereva wa teksi mwembamba mrefu na mwenye mvi nyingi kichwani akawahi kunisomea ramani mapema kabla ya wenzake wakati nilipokuwa nikikaribia maegesho yale ya taksi. Bila kupoteza muda mara tu nilipoifikia ile teksi ya yule mzee nikafungua mlango wa nyuma na kuingia ndani. Yule mzee dereva wa ile teksi kuona vile na yeye akafungua mlango wa dereva wa ile teksi yake na kuingia mle ndani huku akigeuka na kunitazama katika uso wa tabasamu la kibiashara. Nilipomchunguza yule mzee nikagundua kuwa umri wake ungekuwa ni kati ya miaka sitini na tano na sabini na mbili. Mtu ambaye asingeona umuhimu wowote wa kukimbia vita kwani kwa hesabu ya Mungu kwa umri wa miaka ya kuishi binadamu hapa duniani basi huwenda mzee yule alikuwa amebakiwa na miaka michache sana ya kuishi duaniani. Lakini bado alikuwa imara na mwenye siha njema na nilipomtazama usoni macho yake yakanitanabaisha kuwa yalikuwa yamehifadhi historia ndefu ya jiji la Bujumbura na vichochoro vyake.

    “Ou vas-tu jeune homme?”. Unaelekea wapi kijana?. Yule mzee akaniuliza huku akinikata jicho la udadisi na hapo nikatabasamu tu mbele yake kabla ya kumwambia.

    “Me prendre pour le centre-ville”. Nipeleke katikati ya jiji. Ombi langu likampelekea yule mzee anitazame kwa mshangao kidogo kisha kwa utulivu akaniambia.

    “Il est pas très sûr d?y aller maintenant”. Siyo salama sana kwenda katikati ya jiji kwa sasa.

    “Je besoin d?un endroit agréable pour le petit dejeuner”. Nahitaji sehemu nzuri kwa ajili ya kufungua kinywa. Nikamwambia yule mzee dereva wa teksi kwa utulivu hali iliyompelekea anitazame kwa utulivu kama mtu afikiriaye jambo fulani kisha akaniambia huku akitabasamu.

    “Je vais vous prendre pour Havana Club. Il est un endroit agréable et sécuritaire”. Nitakupeleka Havana Club. Ni sehemu nzuri na yenye usalama.

    “Oui!”. Sawa!. Nikamuitikia yule dereva wa teksi pasipo kufanya mapatano ya kiasi cha pesa ambacho angenitoza hadi sehemu ilipokuwa hiyo Havana Club.

     Muda uleule ile teksi ikayaacha yale maegesho yake kando ya kile kituo cha kujazia mafuta na kuingia kwenye ile barabara ya Avenue de La Plage tukielekea mbele kuifuata Hotel Restaurant Tanganyika Lake View. Hata hivyo hatukuifikia hoteli ile kwani tulipofika mbele kidogo tukakunja kona upande wa kulia na kuanza kuifuata barabara ya Rue des Swahili. Ilikuwa ni barabara pana iliyoonekana kufanyiwa ukarabati wa mara kwa mara.

     Mbele ya ile barabara kulikuwa na vijana wengi waliokuwa wakiandamana kuunga mkono jaribio la mapinduzi ya kijeshi lililokuwa likiendelea nchini Burundi. Mapinduzi yenye lengo la kuing?oa madarakani serikali ya rais Pierre Nkurunziza. Wale vijana walikuwa wakipambana kikamilifu na polisi wa kutuliza ghasia waliokuwa wakitumia mbwa, maji ya kuwasha na mabomu ya mzchozi kuwatawanya waandamanaji wale. Zoezi lile lilionekana kuwa gumu kwelikweli kwani wale vijana walikuwa wakijibu mashambuli kwa kurusha mawe na silaha nyinginezo za jadi.

     Tuliendelea mbele kuifuata ile barabara na tulipoona kuwa zile vurugu kati ya wale vijana waandamanaji wa wale polisi wa kutuliza ghasia zikiongezeka yule dereva akaamua kuiacha ile barabara ya Rue des Swahili na kuingia upande wa kushoto akifuata barabaraya Rue Karuzi Halafu baada ya safari fupi hatimaye tukaja kuyafikia makutano ya barabara ya Avenue Ntahangwa na barabara ile ya Rue L?Lmbo. Tulipoyafikia yale makutano yule dereva wa teksi akaingia upande wa kulia akiifuata barabara ya Rue L?Lmbo. Hata hivyo hatukwenda mbali sana katika barabara ile kwani tulipofika mbele kidogo yule dereva akaiacha ile barabara na kuingia tena upande wa kushoto akiifuata barabara ya Rue du Tanganyika. Tulipoingia kwenye barabara ile nikakumbuka kugeuka nyuma na kutazama kama kungekuwa na gari lolote nyuma yetu likitufungia mkia. Sikuliona gari lolote hivyo hali ya usalama bado ilikuwa shwari.

     Kama zilivyokuwa nchi nyingine nyingi masikini za dunia ya tatu za Afrika nchi ya Burundi nayo haikuwa tofauti kabisa wakati nilipoichunguza mitaa mingi ya jiji la Bujumbura na kuiona hali ya makazi yake. Sehemu kubwa ya jiji la Bujumbura ilikuwa na makazi duni ya watu wengi na machache ya daraja la kati.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

     Tulipofika kwenye pembe ya ile barabara ya Reu du Tanganyika tukaingia upande wa kulia tukiifuata barabara nyingine ya Reu des Pecheurs. Tulipoingia kwenye barabara ile haraka nikagundua kuwa tulikuwa tumeingia kwenye barabara iliyokuwa ikikatisha katikati ya makazi ya watu waliokuwa na afya ya kutosha kiuchumi kwani barabara ile ilikuwa imepakana na nyumba za kisasa zenye kuta na mageti makubwa ya uzio mbele yake na pia ilikuwa ni barabara yenye utulivu wa hali ya juu.

     Baada ya safari ya kitambo kifupi hatimaye tukaja kukutana na barabara kubwa ya kisasa ya Boulevard du 1er Novembre kwa upande wa kushoto. Tulipoyafikia makutano yale ghafla akili yangu ikawa ni kama iliyopigwa shoti kali ya umeme hatari wenye nguvu nyingi na hivyo kuzipelekea shughuli za mwili wangu kusimama kwa ghafla kama niliyepigwa kumbo na ugonjwa hatari wa kiharusi.

     Nilikuwa nimeyakumbuka vizuri maelezo ya Amanda wakati ule tulipokuwa tukisafiri wote kuja jijini Bujumbura wakati aliponiambia kuwa angefikia kwenye nyumba moja iliyokuwa kwenye mtaa wa Boulevard du 1er Novembre jijini Bujumbura. Kisha nikakumbuka kuwa mara tu niliporudiwa na fahamu kwenye ile nyumba ya ghorofa niliyotekwa na wale watu hatari wakishirikiana na Amanda kabla ya kuwatoroka. Nilikuwa nimemuuliza Amanda kuwa pale ni wapi na Amanda alikuwa amenieleza kuwa pale kwenye ile nyumba ya ghorofa tulikuwa kwenye mtaa wa Boulevard du 1er Novembre.

     Kwa kweli nilijikuta nikiitazama barabara ya mtaa ule huku hisia zangu zikasafiri kilometa nyingi katika ufikirivu wangu kabla ya hisia zangu kuchotwa na jinamizi la matukio yote niliyoyashuhudia hadi kufikia pale. Hata hivyo kipo kitu kimoja cha ajabu kilichokuwa kimenishangaza. Mandhari ya barabara ile ya Boulevard du 1er Novembre hayakuelekea kufanana walau hata chembe na yale mazingira ya lile jumba la ghorofa lililojitenga kule msituni nilipotekwa na Amanda na wale watu wake hatari. Boulevard du 1er Novembre ilikuwa ni barabara pana ya kisasa yenye sifa zote sawa na zile barabara nyingine za kisasa za jiji la Bujumbura. Barabara ile ikipakana na makazi ya kisasa yenye nyumba nyingi za ghorofa na ofisi chache zenye nidhamu kiuchumi na nilipozidi kuichunguza sikuweza kuona dalili zozote za uwepo wa msitu au nyumba iliyojitenga kama ile niliyotekwa.

     Nikiwa nimegeuka nyuma na kuendelea kushangaa mandhari yale dereva wa ile teksi akaingia upande wa kulia akiifuata ile barabara ya Boulevard du 1er Novembre huku upande wa kushoto tukiliacha jengo zuri la ghorofa la hoteli ya Old Presidential Palace na mbele kidogo mgahawa wa kisasa wa Snack La Fantasia. Tulipofika mbele kidogo ya ile barabara tukakutana na makutano mengine ya barabara Chaussée P.L.Rwagasore.

     Tulipofika kwenye makutano yale tukauvuka ule mzunguko wa barabara na kuingia barabara ya Chaussée P.L.Rwagasore huku mwendo wetu wa gari ukizidi kuongezeka. Tulipishana na magari mengi katika barabara ile hata hivyo hatukufika mbali sana mara nikamuona yule dereva wa teksi akipunguza mwendo na mbele kidogo akaingia upande wa kushoto akiifuata barabara fupi ya Reu de la Victoire. Ilikuwa ni barabara pana lakini fupi iliyopakana na ofisi za kisasa na makazi yanayopendeza yenye utulivu.

     Mwisho wa barabara ile tukaingia upande wa kulia kuifuata barabara kubwa ya Boulevard de I?Uprona. Ilikuwa ni barabara pana ya kisasa iliyopakana na migahawa ya kisasa na ofisi mbalimbali za mashirika yenye afya kiuchumi. Hatukusafiri kwenda mbali sana katika barabara ile mara nikamuona yule dereva wa teksi akipunguza mwendo na hatimaye kusimama mbele ya mgahawa mkubwa wa kisasa wenye kuta safi za vioo juu yake kukiwa na bango kubwa jeupe lenye maandishi ya rangi ya kahawa yakisomeka HAVANA CLUB. Chini ya bango lile kukiwa na maandishi madogo yanayosomeka More than just a venue.

     Mara baada ya ile teksi kusimama mbele ya mgahawa ule kwa sekunde kadhaa nikayatembeza macho yangu kwa utulivu nikiutazama mgahawa ule na tukio lile likaipelekea akili yangu ishikwe na mduwao hafifu. HAVANA CLUB ulikuwa ni mgahawa wa kisasa wenye kila kionjo cha zama za leo. Nilifurahi sana kwani dereva wa ile teksi alikuwa amenifanyia uchaguzi mzuri kwa kunileta katika mgahawa ule.

     Dereva wa ile teksi akayarudisha tena mawazo yangu mle ndani ya teksi pale alipovunja ukimya kwa kunidai pesa kwa ajili ya ile huduma ya usafiri. Alikuwa amenitoza pesa nyingi kwa kunipiga cha juu hata hivyo kwa kuwa nilikuwa na uzoefu mkubwa na madereva wa teksi wa mijini sikutaka kutia upinzani wowote badala yake nikafungua pochi yangu kutoka mfukoni na kutoa kiasi kile cha pesa na kumpa yule dereva huku nikitabasamu. Wakati yule dereva akizihesabu zile pesa mimi nikalichukua lile begi langu dogo la mgongoni kando yangu kisha nikafungua mlango wa nyuma wa ile teksi na kushuka.

     Muda mfupi uliofuata ile teksi ikaondoka nyuma yangu ikitokomea mitaani na hivyo kunipa nafasi nzuri ya kuvaa begi langu dogo la shanta mgongoni huku nikipiga hatua zangu kwa utulivu kuelekea kwenye mlango wa mbele wa HAVANA CLUB. Hata hivyo wakati nikitembea kuelekea kwenye Club ile nikawa nikiyatembeza macho yangu kwa makini kupeleleza mandhari yale.

     Kulikuwa na magari machache yaliyokuwa yameegeshwa kwenye eneo la maegesho ya magari la Club ile na nilipoyachunguza vizuri magari yale haraka nikagundua kuwa mengi yalikuwa ni magari ya watu wenye vipato vya kueleweka. Baadhi ya magari yale yalikuwa ni ya kubebea watilii mbugani na mengine yalikuwa ni ya maafisa wa umoja wa mataifa waliokuwa wakisimamia suala la amani nchini Burundi. Kupitia yale magari nikahisi kuwa huwenda watu wale walikuwa mle ndani ya mgahawa wakijipatia chakula, vinywaji au starehe yoyote iliyokuwa ikipatikana ndani ya Club ile.

     Kulikuwa na watu wachache waliokuwa wamesimama nje ya Club ile wakiendelea na mazungumzo yao. Watu wale wakageuka kidogo kunitazama wakati nilipokuwa nikiufikia mlango wa mbele wa ile Club hata hivyo sikuwatilia maana badala yake nikaendelea na hamsini zangu.

     Mara tu nilipoufikia ule mlango wa mbele wa HAVANA CLUB nikausukuma taratibu na kuingia ndani na hapo nikajikuta nikikabiliana na macho ya watu waliokuwa wameketi mle ndani wakiendelea na starehe zao. Watu wale haraka wakageuka kidogo na kunitazama na macho yao yaliponizoea wakageuka na kuendelea na hamsini zao kana kwamba mtu waliyekuwa wakimsubiri mle ndani hakuwa mimi na hali ile ikanifurahisha kwani sikupenda kuendelea kuzatamwa na kugeuka kivutio.

     Hatimaye nikaurudisha ule mlango mkubwa nyumba yangu kisha taratibu nikaanza kupiga hatua zangu kwa utulivu nikikatisha katikati ya ukumbi mkubwa wa ile Club katika namna ya kutafuta sehemu nzuri ya kukaa na wakati nikitembea nikawa nikiyatembeza macho yangu taratibu kuwatazama watu waliokuwa mle ndani. Tathmini yangu ya haraka ikanieleza kuwa idadi kubwa ya watu waliokuwa mle ndani ya ile Club walikuwa ni wageni wa kutoka nje ya nchi ya Burundi na zaidi kabisa nje ya bara la Afrika. Kulikuwa na wazungu wengi huku wakiwa wameyaweka mabegi yao chini pembeni ya viti walimoketi. Wazungu wale walikuwa wakijipatia vinywaji na vyakula huku wakiendelea na maongezi yao na nilipowachunguza nikagundua kuwa wengi wao walikuwa ni watalii wa kutoka nchi za ulaya hususan Ufaransa na bara la Marekani kutokana na lugha walizokuwa wakizungumza. Waafrika wenzangu kama...



    ...Waafrika wenzangu kama mimi walikuwa wachache sana labda kutokana na gharama za juu za huduma zilizokuwa zikitolewa mle ndani.

     HAVANA CLUB ilikuwa ni Club ya kisasa kabisa yenye kila kionjo cha daraja la kimataifa kama Snack-Bar Pizzeria, ukumbi mkubwa wenye meza nyingi za mchezo wa Pool table. Ukumbi mwingine mkubwa kwa ajili ya kujipatia vyakula vya kimataifa wenye meza ndefu za kisasa zilizozungukwa na viti vizuri vya sofa vyenye foronya laini pamoja na ukumbi mwingine mkubwa wenye jukwaa zuri linalotazamana na viti vingi vya kisasa kwa ajili ya kufanyia matamasha ya muziki na mikutano mbalimbali. Kila ukumbi ulikuwa imejitenga na hivyo kutengeneza mgawanyo mzuri wa starehe tofauti zenye utulivu zinaweza kufanyika kwa wakati mmoja.

     Nilikuwa nimetokezea kwenye sehemu ya Bar ya ile Club na lile halikuwa lengo langu kwani njaa ilikuwa ikiniuma sana. Hivyo akili yangu yote ilikuwa imejikita kwenye kupata mlo wa nguvu na baada ya hapo mengine yote yangefuatia.

     Mtu yeyote ambaye angekuwa akizifuatilia kwa karibu nyendo zangu mle ndani isingemuwia vigumu kunigundua kuwa nilikuwa mgeni wa mandhari yale na ile ndiyo ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kabisa kufika pale kwa namna hatua zangu zilivyokuwa zikipwaya katika kufanya maamuzi ya haraka ya uelekeo wangu. Muziki laini ulikuwa ukisikika taratibu mle ndani na hivyo kuzikonga vizuri nyoyo za watu waliokuwa mle ndani.

     Ule ukumbi ulikuwa mkubwa pengine wenye uwezo wa kumeza watu wasiopungua mia tano kwa wakati mmoja bila bugdha yoyote huku ukiwa na meza nyingi ndogo fupi na pana zilizozungukwa na makochi mazuri ya sofa laini. Katika baadhi ya meza zile watu walikuwa wameketi kwa utulivu huku wakijipatia vinywaji na japokuwa tayari ilikuwa imetimia saa nne asubuhi lakini taa nzuri zenye mwanga hafifu zilikuwa zikiendelea kuangaza mle ndani. Runinga pana zilizokuwa zimetundikwa ukutani mle ukumbini zilikuwa zimejikita katika kurusha taarifa mbalimbali za jaribio la mapinduzi ya kijeshi lililofanyika jijini Bujumbura huku mara kwa mara picha za vijana waliokuwa barabarani wakiandamana kuunga mkono mapinduzi yale na kuishinikiza serikali iliyoko madarakani iachie ngazi zikirushwa.

     Nilimaliza kukatisha katikati ya ukumbi ule na nilipokuwa mbioni kuifikia kaunta ya vinywaji upande wa kulia nikauona mlango mkubwa uliokuwa wazi lakini uliofunikwa kwa pazia zuri na jepesi. Juu ya mlango ule kulikuwa na kibao cheusi chenye maandishi meupe yakisomeka kwa lugha ya kifaransa Salle à manger yenye maana ya Dining Hall kwa lugha ya kiingereza ama ukumbi wa chakula kwa lugha ya kiswahili. Chini ya maandishi yale kulikuwa na maelezo mengine ya kifaransa yakisomeka Vous êtes les bienvenus yenye maana ya Wote mnakaribishwa sana.

     Sikuona sababu ya kuuliza hivyo nikashika uelekeo wa upande wa kulia nikipotelea kwenye ule mlango. Mara tu niliposogeza pazia refu la ule mlango nikajikuta nikitazamana na ngazi chache za kuelekea sehemu ya chini ya lile jengo na hapo nikaanza kuzishuka zile ngazi taratibu. Nilipofika chini ya zile ngazi nikauona mshale mdogo mweupe uliochorwa ukutani ukielekeza upande wa kushoto. Nilipoufuata ule uelekeo mbele kidogo upande wa kulia nikaiona korido nyembamba inayotazamana na milango minne na upande wa kushoto kulikuwa na mlango mmoja uliokuwa wazi ukifanana na ule wa awali ukiwa umefunikwa kwa pazia jepesi. Juu ya mlango ule kulikuwa na kibao kingine cheusi chenye maandishi meupe kama yale ya awali na hapo nikajua kuwa ule mlango ndiyo uliokuwa wa kuelekea kwenye ukumbi wa chakula. Hivyo bila kupoteza muda nikashika uelekeo ule na kutokomea mle ndani.

     Hatimaye nikajikuta nimetokezea kwenye ukumbi mkubwa wa kisasa wenye madirisha makubwa ya vioo yaliyofunikwa na mapazia safi marefu yaliyosogezwa kando kidogo kuruhusu mwanga wa jua kupenya kwa urahisi kutoka nje na kuangaza mle ndani. Utulivu wa mandhari yale ulikuwa wa hali ya juu uliomezwa na sauti ya muziki laini wa kubembeleza unaoweza kuacha kumbukumbu ya muda mrefu kwa mtu yoyote baada ya kuondoka eneo lile. Sauti ile tamu ya muziki ilikuwa ikirushwa kutoka katika spika zilizokuwa maeneo fulani kwenye kona za ukumbi ule.

     Kulikuwa na wahudumu wa kike warembo waliokuwa wakihudumia wateja wachache waliokuwa mle ndani wameketi kwenye meza nzuri za mbao ya mti wa jacaranda na viti vifupi vyenye foronya laini. Nilipoyatembeza haraka macho yangu mle ndani nikagundua kuwa idadi ya watu wengi waliokuwa mle ndani walikuwa ni wazungu wapenzi na familia zao. Upande wa kulia wa ule ukumbi kulikuwa na mlango na dirisha dogo la jikoni na mle ndani nikawaona wapishi katika mavazi yao ya kazi.

     Mara tu nilipoingia mle ndani watu wote wakageuka kunitazama kabla ya kuendelea na hamsini zao na hapo nikaanza kuzitupa hatua zangu kwa utulivu nikitafuta sehemu nzuri ya kuketi mle ndani. Kwa kufanya vile nikaiona meza moja iliyokuwa imejitenga kwenye kona ya ukumbi ule. Muda mfupi uliofuata nikawa nimeifikia meza ile ambapo nilivuta kiti na kuketi.

     Nikiwa nimeketi kwenye ile meza nikasogeza pazia na kupitia ukati msafi wa kioo cha dirishani nikaweza kuyaona mandhari tulivu ya kuvutia nje ya ukumbi ule. Kulikuwa na nyasi nzuri za rangi ya kijani kibichi zilizopakana na maua ya rangi tofauti ya kuvutia na nyasi zile zilikuwa zimepandwa kuzunguka mabwawa matatu ya kuogelea kando yake kukiwa na viti vya kupumzikia kwa waogeleaji vyenye miavuli mizuri ya kujikinga na miale ya jua. Katika viti vile baadhi ya wazungu walikuwa wameketi na wengine wakiogelea huku wote wakiwa katika mavazi ya kuogelea na bikini nzuri zenye mvuto wa aina yake. Kando ya mabwawa yale kulikuwa na bustani nzuri ya miti yenye viti visivyohamishika katika mandhari tulivu.

     Msichana mrembo mhudumu wa ukumbi ule wa chakula akayarudisha mawazo yangu mle ndani wakati alipokuja na kusimama mbele ya ile meza niliyoketi huku tabasamu la kibiashara likivinjari usoni pake. Nilipoyainua macho yangu kumtazama mhudumu yule kwa sekunde kadhaa macho yangu yakajikuta yakipumbazwa na uzuri wake.

     Alikuwa msichana mzuri na mrembo sana ambaye kamwe sikuwahi kumuona msichana wa namna ile katika pitapita zangu. Japokuwa alikuwa amevaa sare za kazi lakini bado uzuri wake haukuchujuka hata chembe. Nywele zake nyeusi za kibantu alikuwa amezikata vizuri katika mtindo wa Lowcut na hivyo kumpelekea aonekane mzuri wa asili. Macho yake makubwa na meupe yaliyozungukwa na kope ndefu na nyeusi, pua yake ndefu ya kihabeshi, mdomo wake wa kike wenye kingo pana kiasi na vishimo vidogo mashavuni vinavyochomoza haraka kila anapotabasamu vikazidi kuzisulubu vibaya hisia zangu.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

     Kidani cha asili chenye herufi V kilikuwa kimenasa vyema kwenye shingo yake ndefu na kupotelea katikati ya kichochoro hafifu kilichofanyika katikati ya matiti yake makubwa kiasi yenye chuchu imara zilizotuna na kuisumbua kidogo blauzi yake. Mkono wake wa kushoto alikuwa amevaa saa nzuri ndogo ya kike iliyotengenezwa kwa namna ya kupendeza na hivyo kuongeza ziada nyingine katika uzuri wake. Sketi yake nyeusi fupi iliyoishia juu ya magoti ilikuwa imenasa vyema kwenye kiuno chake chembamba kilichoshikilia mzigo mkubwa wa makalio yake imara yaliyoimarisha vizuri minofu ya mapaja yake yaliyotuna kama chura na kumpelekea aonekane kama aliyeficha vipande vya mikate mfukoni. Niseme pia rangi yake ng’avu ya maji ya kunde ilikuwa ni kigezo kingine kilichotumika kumruhusu auteke moyo wangu bila pingamizi lolote na hivyo kunifanya nisahau hata kile kilichonifikisha mle ndani.

    “Bien venu frère, je ne sais pas qu?est-ce que tu veux qu?on t?apporte?”. Karibu kaka sijui ungependa kuagiza nini?. Yule mhudumu akaniuliza kwa sauti tulivu iliyotuama vyema kwenye sakafu ya mtima wangu na hivyo kunipelekea kwa sekunde kadhaa nikose neno la kuongea kutokana na kupumbazika na uzuri wake. Baada ya kitambo kifupi hatimaye nikavunja ukimya huku nikitabasamu.

    “Je demande d?abord la soupe de poisson à la rouille que je chauffe un peu la vendre, et après je vais comander un forte repas”. Naomba kwanza uniletee supu ya samaki nipashe tumbo joto halafu baadaye mlo wa nguvu. Nikamwambia yule mhudumu baada ya kusoma orodha ya vyakula iliyokuwa juu ya ile meza nikiipitia kwa utulivu.

    “Il y a autre chose?”. Kuna kingine chochote?. Yule msichana mrembo mhudumu akaniuliza na baada ya kufikiri kidogo na kuitazama tena ile orodha ya vyakula pale mezani nikavunja ukimya.

    “Amaine moi du vin de la Navette de Marseille”. Naomba uniletee na mvinyo mwepesi wa Navette de Marseille. Yule mhudumu akaitikia kwa kutikisa kichwa chake huku akitabasamu na wakati alipokuwa akijiandaa kuondoka eneo lile nikakumbuka kumuuliza kitu, lengo langu likiwa ni kutaka kuisikia sauti yake nyororo ya kumtoa nyoka pangoni.

    “?a va prendre combien de temp?s?”. Itachukua muda gani?.

    “Juste maintenant”. Sasa hivi. Yule mhudumu akaniambia huku akitabasamu.

    “Jai faim, je serais contant si tu le fait rapidement”. Nina njaa sana hivyo nitashukuru ukinifanyia haraka. Nikamwambia yule mhudumu huku nikimkonyeza kidogo kwa jicho langu la kushoto na kumpelekea azidi kutabasamu.

    “Ne t?enfait pas”. Ondoa shaka. Yule mhudumu akaniambia kisha akageuka na kuanza taratibu kuondoka eneo lile na wakati akitembea akili yangu ikajikuta ikizidi kupumbazika na mtikisiko maridhawa wa mzigo wa makalio yake chakaramu.

     Nikaendelea kumtazama msichana yule kwa utulivu hadi pale alipotokomea kwenye kaunta ya jikoni ya ukumbi ule wa maakuli huku nikijisikia faraja ya kipekee kabla ya mawazo yangu kuhamia kwenye tafakuri nyingine.

     Sasa nilikuwa nimeingia rasmi jijini Bujumbura nchini Burundi tayari kuanza kazi niliyotumwa na idara yangu ya ujasusi jijini Dar es Salaam. Nikiwa bado nimeketi kwenye ile kona nikaanza kukumbuka misukosuko yote niliyopitia tangu nilipoanza safari yangu kutokea jijini Kigali nchini Rwanda jioni ya jana. Kisha nikakumbuka namna nilivyomuokoa Amanda na hatimaye kupambana kikamilifu na wale watekaji wa msituni kule njiani. Kwa kweli sikuwa nimetarajia kabisa kuwa Amanda angekuja kunisaliti pamoja na fadhila zote zile nilizomfanyia. Hata hivyo ule haukuwa wakati wa kumlaumu Amanda badala yake niliona kuwa zilipaswa kujilaumu mwenyewe kwa kitendo cha kumwamini sana mtu nisiyemfahamu vizuri.

     Baada ya muda mfupi kupita mara nikamuona yule dada mhudumu akirudi pale nilipoketi huku mikononi akiwa amebeba sinia kubwa lenye staftahi huku lile tabasamu lake la kibiashara usoni likikataa kabisa kwenda likizo. Yule mhudumu alipofika pale kwenye meza yangu akainama kwa utulivu akilitua lile sinia juu ya ile meza mbele yangu na kitendo kile cha kuinama kidogo kikapelekea kile kidani chake kilichojificha katikati ya mfereji wa matiti yake kitoke mafichoni na kuning?inia kifuani mwake na hivyo kunipelekea niweze kukiona vizuri.

     Kilikuwa kidani kizuri cha madini yanayong?ara sana nisiyoyafahamu chenye herufi V. Hata hivyo msichana yule mhudumu hakuonekana kupendezwa na tukio lile la kuponyokwa kwa kidani chake kile kilichonipa nafasi nzuri ya kuyachungulia matiti yake yenye mvuto wa kipekee. Hivyo haraka akakichukua kile kidani na kukirudishia katikati ya matiti yake kisha akaitengeneza vizuri blauzi yake huku akiona aibu kidogo mbele yangu.

     Nikamtazama usoni mrembo yule huku nikitabasamu tukio lile likampelekea atabasamu kidogo kwa aibu huku akiyakwepesha macho yake pembeni yasikutane na yangu na tabia yake ile ya heshima ikazidi kupeleka nuru njema moyoni mwangu. Yule dada mhudumu hatimaye akaanza kuitoa ile sahani ya supu na glasi ya mvinyo mwepesi kutoka kwenye lile sinia na kuviweka mbele yangu huku akikwepa kunitazama usoni.

    “Do you speak Swahili?”. Nikamuuliza yule mhudumu wakati alipokuwa akiendelea na kazi yake pale mezani. Japokuwa Burundi ni nchi inayotumia lugha ya kifaransa kama lugha rasmi ya ofisini lakini kiswahili haikuwa lugha ngeni katika nchi zilizo katika ukanda wa maziwa makuu na vilevile katika sehemu kama pale HAVANA CLUB ambapo wageni mbalimbali wa kimataifa walikuwa wakifika. Hivyo lisingekuwa jambo la kustaajabisha kwa wafanyakazi wa mle ndani kujua kuzungumza angalau lugha mbili au tatu za kimataifa katika namna ya kurahisisha utoaji wao wa huduma hivyo swali langu bado lilikuwa na mantiki. Swali langu likampelekea yule msichana anitazame kwa bashasha zote huku akitabasamu na hapo nikajua kuwa huwenda lile swali lilikuwa limemfurahisha sana.

    “Unataka nini?”. Hatimaye yule mhudumu akaniuliza huku macho yake meupe makubwa na legevu yakinitazama usoni na tabasamu lake usoni likaashiria kuwa urafiki wetu ungedumu kwa muda mrefu zaidi.

    “Napenda kufahamu hiyo herufi V kwenye kidani chako shingoni ina maana gani?”. Swali langu likampelekea yule mhudumu azidi kuchanua tabasamu lake usoni na hali ile ikazidi kunitia faraja moyoni mwangu.

    “Herufi V ni herufi ya mwanzo ya jina langu”. Hatimaye akanijibu huku akijichelewesha pale mezani kama aliyekuwa na kiu ya kutaka kuzidi kunisikia.

    “Vanessa, Vaileth, Verdiane, Vicky, Victorie...”. Nikajaribu kuotea huku nikiangua kicheko hafifu.

    “Veronica”. Yule mlimbwende akanikatisha kabla sijamaliza kuotea huku akiangua kicheko hafifu kilichopelekea vile vishimo vya mashavuni mwake vionekane waziwazi bila kificho na hivyo yale meno yake meupe yaliyopangika vizuri kuongeza ziada nyingine katika uzuri wake. Loh! Veronica alikuwa msichana mzuri mno kuwahi kumuona maishani mwangu hata Amanda hakufua dafu mbele yake.

    “Jina lako tamu kama asali na hakika uzuri wako umelitendea haki”. Nikachombeza utani huku nikiangua kicheko hafifu.

    “Mh! nashukuru, na wewe je unaitwa nani?”. Veronica akaniuliza na nikiwa tayari nimejiandaa kukabiliana na swali la namna ile nikamdanganya huku nikitabasamu...



    “Naitwa Gilbert”

     “Hii ni mara yako ya kwanza kufika hapa HAVANA CLUB?”. Veronica akaniuliza huku akijitia kupangapanga lile bakuli la supu na ile glasi ya mvinyo mwepesi.

    “Hujakosea ingawa nimetokea kuipenda sana Club hii”

     “Ni kweli kwani nilipokuona tu kwa mara ya kwanza wakati ulipokuwa ukiingia humu ndani nikajua kuwa wewe ni mgeni wa mahali hapa”. Veronica akaongea huku akinitazama na hapo nikajichekesha kidogo kabla ya kumuuliza.

    “Umejuaje?”

     “Kwanza sura yako ni ngeni kabisa machoni mwangu na wateja wanaofika hapa wengi huwa nawafahamu na istoshe nilikuona ukibabaika kidogo kama mgeni wa mazingira haya wakati ulipokuwa ukiingia”. Veronica akaniambia na kwa kweli nilimuona ni msichana mjanja na mwerevu kiasi cha kuweza kunishtukia mapema.

    “Mh! au labda Club yenu haipendi wageni?”. Nikachombeza utani na hapo nikamsikia Veronica akiangua kicheko cha dhahiri.

    “Naomba unisamehe kaka sikuwa na maana hiyo”. Veronica akaongea kwa utulivu baada ya kicheko chake kufika ukomo. Kitambo kifupi cha ukimya kikafuatia huku Veronica akijitahidi kunisogezea karibu staftahi ile na ukaribu wake ukanipelekea niisikie harufu nzuri ya manukato yake aliyojipaka mwilini. Bila kupoteza muda nikavunja ukimya nikimuuliza kwa sauti ya chini ambayo isingeweza kumruhusu mtu yeyote jirani na eneo lile kunisikia.

    “Vipi shemeji yangu hajambo?”. Swali langu likampelekea Veronica anitupie jicho la hisia kisha taratibu akatikisa kichwa chake kuonesha kuikataa hoja ile huku tabasamu lake bado lingali usoni mwake.

    “Wewe ni mtanzania?”. Veronica akaniuliza huku dhahiri nikifahamu kuwa alikuwa akitia jitihada za kuyahamisha maongezi yangu.

    “Ndiyo”

     “Watanzania wengi tabia zenu zinafanana”. Veronica akaniambia huku akitabasamu.

    “Mh! kwani watanzania tabia zetu zipoje?”

     “Wacheshi na marafiki sana”

     “Mh! labda kwa kuwa wewe ndiye umesema basi naamini itakuwa kweli”. Nikaongea huku nikiangua kicheko hafifu kilichomfanya Veronica azidi kutabasamu.

    “Unakaa wapi hapa jijini Bujumbura?”. Hatimaye nikavunja tena ukimya na kumuuliza Veronica.

    “Nakaa nyumba namba 37 kwenye jengo la shirika la nyumba la taifa kando ya barabara ya Boulevard de I?ndependence, nyuma ya uwanja wa mpira wa miguu wa Prince Rwagesore Stadium”. Veronica akaniambia huku akiitazama saa yake ya mkononi.

    “Huwa unatoka saa ngapi kazini?”

     “Saa mbili usiku mara baada ya mwenzangu anayenipokea zamu kufika”. Veronica akaniambia kwa sauti tulivu huku akionesha jitihada za kutaka kuondoka baada ya kumaliza kazi yake ya kuniandalia maakuli pale mezani.

    “Naomba ruhusa yako ya kuja kukutembelea usiku wa leo kama hutojali”. Nikaongea kwa utulivu huku nikimtazama Veronica machoni katika namna ya kutaka kupata hakika na jibu ambalo lingemtoka mdomoni.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Karibu sana”. Hatimaye Veronica akaniambia huku akiniaga kwa tabasamu maridhawa huku akichukua lile sinia aliloletea zile staftahi na kuondoka zake.

     Kwa sekunde kadhaa nikabaki nimeganda kama sanamu huku nikimtazama Veronica namna alivyokuwa akiondoka eneo lile na hatimaye kutokomea kabisa kwenye ile kaunta ya ule ukumbi wa chakula.

     Mara baada ya Veronica kutoweka machoni mwangu nikavuta lile bakuli la supu karibu yangu na kuanza kujipatia mlo. Kwa kuwa nilikuwa na njaa sana ile supu nilifakamia kwa kasi ya ajabu hivyo baada ya muda mfupi lile bakuli lilikuwa tupu. Nikasubiri kidogo ule mlo ushuke vizuri tumboni kisha taratibu nikashushia na ule mvinyo mwekundu wa kifaransa wa Navette de Marseille na wakati ule mvinyo ukishuka taratibu kooni mwangu akili yangu nayo ikaanza kuchangamka na kuanza kufikiria ni wapi pa kuanzia kazi nzito iliyokuwa mbele yangu.

     Nilipomaliza kupata ule mlo Veronica akaja pale mezani mara moja kuondoa vile vyombo na kusafisha ile meza. Alipomaliza nikamuagiza aniletee kuku wa kurosti kwa vitunguu saumu pamoja na ugali wa dona wa kuweza kunipa nguvu mwilini. Halafu nikamwambia aniongezee glasi nyingine ya mvinyo mwekundu.

     Veronica aliponiletea ule mlo na kuondoka nikaanza kula taratibu huku nikipata wasaha mzuri wa kuichukua ile ramani yangu ndogo ya kijasusi ya kukunja kisha nikaifungua na kuanza kuipitia taratibu huku nikiendelea kujipatia ule mlo pale mezani.

     Kupitia ile ramani yangu ndogo ya kijasusi ya kukunja niliweza haraka kufahamu sehemu ulipokuwa uBalozi wa nchi yangu Tanzania kwa pale jijini Bujumbura nchini Burundi. Ofisi za uBalozi wa Tanzania pale jijini Bujumbura zilikuwa umbali mfupi baada ya kuyavuka makutano ya barabara ya Avenue de Gihungwe na barabara ya Avenue du 18 Septembre. Kutoka pale HAVANA CLUB hadi zilipokuwa ofisi zile za uBalozi wa Tanzania nchini Burundi hapakuwa na umbali mrefu sana ingawa pia isingefaa kutembea kwa miguu kwani mitaa mingi ya jiji la Bujumbura kwa wakati ule ilikuwa imezingirwa na askari waliokuwa wakijitahidi kudumisha hali ya usalama baada ya lile jaribio la mapinduzi ya kijeshi kufanyika.

     Akili yangu hatimaye ikajikita kwenye hoja nyingine juu ya aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Burundi Meja jenerali mstaafu Adam Mwambapa na kwa kweli bado sikuweza kupata hoja yoyote juu yake. Meja jenerali mstaafu Adam Mwambapa kama cheo chake kinavyojieleza vizuri siyo tu alikuwa kiongozi na mwakilishi mzuri wa serikali ya Tanzania nchini Brurundi lakini vilevile alikuwa kiongozi mstaatu wa kijeshi mwenye elimu ya juu ya masuala ya kijeshi na mbinu zote za mapigano ya medani za kivita.

     Kiongozi wa namna yake kusikika ametekwa au kutoweka katika mazingira ya kutatanisha halikuwa jambo la kulichukulia mzaha hata kidogo. Kwa kweli nilishindwa kabisa walau kuhisi nini ambacho kingekuwa kimejificha nyuma ya tukio lile la kutoweka kwa mwakilishi wa nchi na kiongozi yule mkubwa wa kijeshi. Huku nikiamini kuwa kama ni kweli kuwa Meja jenerali mstaafu Adam Mwambapa angekuwa ametekwa basi mtekaji huyo asingekuwa mtu mmoja na badala yake kingekuwa labda ni kikundi cha siri cha wanajeshi na wanajeshi hao walipaswa kuwa ni watu waliofuzu vizuri katika masuala ya kijeshi. Fikra zile zikanipelekea nianze kuhisi hatari na ugumu wa kupambana na watu hao hatari endapo harakati zangu zingenikutanisha nao, iwe kwa bahati mbaya au kwa makusudi.

     Hatimaye nikamaliza kupata mlo wangu wa nguvu katika mgahawa ule kisha nikachukua simu yangu kutoka mfukoni na kuandika ujumbe mfupi wa kumfahamisha Brigedia jenerali Ibrahim Gambari kuwa tayari nilikuwa nimefika jijini Bujumbura nchini Burundi. Ule ujumbe ulipoenda nikazima simu yangu na kuitia mfukoni.

     Wazo fulani lilikuwa limenijia akilini. Sikutaka kufanya mizunguko yangu huku nikiwa na mzigo wowote hivyo Veronica alipokuja pale mezani kuondoa vyombo akanipa karatasi ndogo yenye bili ya ile huduma ya chakula na vinywaji. Nikaipokea ile karatasi na kuipitishia macho kisha nikafungua wallet yangu ndogo kutoka mfukoni na kuhesabu kiasi kile cha pesa na kulipa. Halafu nikachomoa noti mbili za faranga za Burundi ambazo nilimpa Veronica kama ahsante kwa kunihudumia vizuri pale mgahawani. Veronica akapokea noti zile kwa furaha na kabla sijaondoka nikamuomba nimuachie lile begi langu dogo la shanta kwa kisingizio kuwa nilikuwa na mizunguko mingi jijini Bujumbura hivyo kutembea na begi lile kwangu ingekuwa usumbufu. Veronica akanikubalia ombi langu bila kusita hivyo nikaagana naye kwa miadi ya kuonana naye tena baadaye.

     Saa yangu ya mkononi ilionesha kuwa ilikuwa ikielekea kutimia saa tano na robo asubuhi wakati nilipokuwa nikitoka nje ya lile jengo la HAVANA CLUB na kuelekea kando ya eneo lile sehemu kulipokuwa na maegesho ya teksi.

     Jua tayari lilikuwa limechomoza vizuri na hivyo kupelekea joto hafifu kuongeza ziada nyingine ya hali ya hewa ya jiji la Bujumbura. Jaribio lile la mapinduzi ya kijeshi lenye lengo la kuing?oa madarakani serikali ya rais Pierre Nkurunziza lilikuwa limeacha taharuki ya aina yake na kutengeneza hali ya hofu kwa raia wa nchini Burundi. Hofu ile ya kudorora kwa hali ya usalama nchini Burundi ilikuwa imepelekea raia wengi kuanza kuyakimbia makazi yao na kuelekea nchi za jirani kama mkoani Kigoma nchini Tanzania, Rwanda na D.R. Congo kuyanusuru maisha yao. Hivyo kwa wakati ule mitaa mingi ya jiji la Bujumbura ilikuwa mbioni kubaki ukiwa kwa kukimbiwa na watu. Hata hivyo hali ile haikuwa kwa wakazi wote kwani wapo baadhi ya raia waliokuwa wamejifungia majumbani mwao huku wakisubiri kuona hatima ya mapinduzi yale.

     Dereva wa teksi kijana anayeelekeana na umri wangu, mrefu, mweusi na mwenye sura yenye bashasha zote za kirafiki akawahi kunifungulia mlango wa mbele wa teksi yake wakati nilipokuwa mbioni kuyafikia yale maegesho ya teksi nje ya HAVANA CLUB. Hata hivyo sikukubaliana na mpango wake badala yake nikazunguka na kufungua mlango wa nyuma wa teksi ile na kuingia ndani. Yule dereva wa teksi kuona vile haraka akaufunga ule mlango alionifungulia kisha haraka akazunguka na kufungua mlango wa dereva wa ile teksi na kuingia ndani na kabla hajageuka nyuma na kuniuliza uelekeo nikavunja ukimya na kumwambia.

    “Prends moi à l?ambassade de Tanzanie”. Nipeleke ulipo uBalozi wa Tanzania. Yule dereva akanitazama kidogo na kutikisa kichwa chake katika namna ya kuashiria kuwa alikuwa amenielewa na nilipomchunguza nikajua kuwa hakuwa mtu wa maneno mengi.

     Muda uleule ile teksi ikayaacha yale maegesho na kuingia upande wa kulia kuifuata barabara ya Boulevard de I?Uprona. Hata hivyo kabla hatujafika mwisho wa barabara ile mara nikamuona yule dereva akikata kona kuingia upande wa kulia na kuifuata barabara ya Avenue de la Mission. Ilikuwa ni barabara kama zilivyokuwa barabara nyingine za mitaa ya jiji la Bujumbura kutokana na muonekano wa mandhari yake. Tofauti pekee niliyoiona ni kuwa barabara ile haikuwa na msongamano wa waandamanaji na ilikuwa ikikatisha katikati ya majengo marefu ya ghorofa yenye ofisi za kisasa za watu binafsi na ofisi za mashirika mbalimbali ya serikali ya Burundi.

     Baada ya safari fupi hatimaye tukawa tumefika mwisho wa ile barabara na hapo nikamuona yule dereva akipunguza mwendo na kuingia upande wa kushoto akifuata barabara pana ya Chaussée P.L. Rwagasore. Ilikuwa barabara pana zaidi kama zile za masafa marefu na hata idadi ya magari katika barabara ile ilikuwa kubwa na magari yale mengi yalikuwa ni ya jeshi la wananchi wa Burundi huku yakiwa yamebeba wanajeshi. Nikageuka kuyatazama magari yale ya jeshi kwa utulivu huku mawazo mengi yakipita kichwani. Hata hivyo nilipogeuka nyuma kutazama sikuliona gari lolote likitufungia mkia na hali ile ikanitia faraja.

     Barabara ya Chaussée P.L. Rwagasore mbele yake ingekuja kukutana na barabara nyingine ya Boulevard de I?Independence. Hata hivyo kabla hatujayafikia makutano yale mara nikamuona tena yule dereva wa ile teksi akipunguza mwendo na hatimaye kuingia upande wa kulia akiifuata barabara ya Avenue du Commerce. Hata hivyo hatukusafiri sana katika barabara ile kwani kule mbele ile barabara ilikuwa imefungwa na polisi wa Burundi waliokuwa wakipambana kikamilifu na waandamanaji. Hivyo yule dereva akaingia upande wa kushoto kuifuata barabara ya Avenue du Marche na hapo mwendo wetu ukaongezeka. Yule dereva alikuwa mtu mjanja sana na anayeijua vizuri kazi yake kwani nilipomchunguza nikagundua kuwa alikuwa akiepuka zile barabara zilizokuwa na msongamano wa magari na zile zilizokuwa na waandamanaji wa kuunga mkono lile jaribio la mapinduzi la kijeshi.

     Nikiwa kwenye ile siti ya nyuma ya ile teksi uchunguzi wangu ukanitanabaisha kuwa majengo mengi muhimu ya serikali kama posta, benki, hospitali na vituo vya redio kwa wakati ule yalikuwa chini ya ulinzi mkali wa jeshi la wananchi wa Burundi. Wanajeshi wale wakionekana kuyazingira majengo yale na bunduki zao mikononi.

     Tulipoyafikia makutano ya barabara ya Avenue de L?Enseignement na ile barabara ya Avenue du Marche nikamuona tena yule dereva akipunguza mwendo na kuingia barabara ya Avenue de L?Enseignement upande wa kulia na hapo nikaliona jengo la Banque de Crédit de Bujumbura upande wa kulia. Hata hivyo kwa wakati ule benki ile ilikuwa imefungwa huku ikionekana kulindwa kikamilifu na wanajeshi waliokuwa wamelizingira jengo lile kikamilifu.

     Tukaendelea na safari yetu na kabla ya kuifikia barabara ya Rue de La Sciénce yule dereva akapunguza tena mwendo na kuingia upande wa kushoto akiifuata barabara ya Boulevard Patrice Lumumba. Kitendo cha kuingia kwenye barabara ile kikanipelekea nilione jengo la Galerie du Progres upande wa kulia kwenye barabara ya Rue du Progres na jengo refu la ghorofa la benki ya biashara ya Kenya kiasi cha umbali wa hatua chache kabla ya kuyafikia makutano ya barabara ya Boulevard Patrice Lumumba na barabara ya Avenue Pierré Ngendandumwe.

     Mwendo wetu ukiwa siyo wa kubabaisha tulipofika mbele kidogo upande wa kulia tukaipita barabara ya Avenue Des Eucalyptus kisha barabara ya Avenue du Palmier upande wa kulia na ile barabara ya Avenue Des Non Aligens upande wa kushoto. Tulipoyafikia makutano ya barabara ya RN 7 nikamuona yule dereva akiufuata mzunguko wa barabara wa RN 7 na hapo haraka nikajua kuwa yule dereva wa teksi alikuwa akifanya ujanja wa kuongeza mizunguko ili hatimaye anitoze pesa nyingi kwani vinginevyo angeweza kupunguza urefu wa safari ile kwa...



    ...kuchepukia upande wa kulia ambapo mbele yake angekuja kukutana na ile barabara ya Avenue du 18 Septembre ambapo tungeshuka na barabara ile hadi sehemu lilipokuwa jengo la ofisi za ubalozi wa Tanzania nchini Burundi. Hata hivyo sikutia neno lolote kwani pamoja na hila ya yule dereva kwangu ilikuwa ni starehe nyingine ya utalii wa maeneo mbalimbali ya jiji la Bujumbura.

     Tulipoufikia ule mzunguko wa barabara ya RN 7 yule dereva akauzunguka mzunguko ule na kushika uelekeo wa upande wa kushoto akiifuata barabara ya Boulevard du Japan. Ilikuwa barabara pana yenye njia mbili upande wa kushoto na njia nyingine mbili upande wa kulia. Ilikuwa ni barabara yenye matunzo mazuri na miongoni mwa barabara za kisasa kabisa jijini Bujumbura. Barabara ile ikipakana na majengo marefu ya ghorofa yenye ofisi za mashirika ya kimataifa kama shirika la wakimbizi duniani UNHCR-United Nations High Commissioner for Refugees, shirika la afya duniani WHO-World Health Organisation na ofisi za wizara ya haki na sheria za nchini Burundi. Kwa hakika ilikuwa ni barabara yenye ustaarabu na utulivu wa hali ya juu kama vile zilivyokuwa barabara nyingi za eneo la Upanga lililopo jijini Dar es Salaam nchini Tanzania.

     Mara tu tulipoingia kwenye ile barabara dereva wa ile teksi akapunguza mwendo na kuendesha gari taratibu na kwa kufanya vile nikagundua kuwa kutoka pale hatukuwa mbali sana na ofisi za uBalozi wa Tanzania jijini Bujumbura. Nilipogeuka kutazama upande wa kulia nikaliona jengo kubwa la kanisa la katoliki la Regina Mundi Cathedral. Tukaendelea na safari ile na mbele kidogo tukaja kukutana na barabara ya Boulevard de la Liberte.

     Mara tu tulipoyapita makutano yale upande wa kushoto nikaliona jengo la shule ya Ubelgiji la jijini Bujumbura-Ecole Belge de Bujumbura. Hatukufika mbali sana katika safari yetu mara nikamuona yule dereva wa teksi akipunguza mwendo na kisha kuwasha taa za gari za upande wa kulia akiashiria kuwa alikuwa akijiandaa kuchepukia barabara ya Avenue du 18 Septembre kwani mbele kidogo ya barabara ile upande wa kushoto kabla ya kuyafikia makutano ya barabara ya Avenue du 18 Septembre na barabara ya Avenue de Gihungwe ndiyo lilipokuwa jengo lenye ofisi za uBalozi wa Tanzania jijini Bujumbura nchini Burundi. Sikupenda teksi ile ikanishushie mbele kabisa ya lile jengo la uBalozi hivyo kabla yule dereva hajakata kona kuifuata barabara ile haraka nikavunja ukimywa kwa kumwambia.

    “Laissez-moi ici, s?il vous plaît”. Niache hapa tafadhali. Kauli yangu ya ghafla ikampelekea yule dereva azidi kupunguza mwendo kisha akageuka kidogo na kunitazama kama mtu aliyeshikwa na mshangao. Hata hivyo hakutia neno badala yake akazidi kupunguza mwendo zaidi na hatimaye kusimama mbele ya ofisi moja ya mawasiliano iliyokuwa kwenye ile kona. Sikutaka kupoteza muda hivyo haraka nikamuuliza yule dereva gharama za usafiri hadi pale na aliponiambia pasipo mabishano nikachomoa noti kadhaa kutoka katika wallet yangu mfukoni na kumpa kiasi kile cha fedha kisha nikamshukuru huku nikifungua mlango na kushuka. Muda uleule mara nikaiona ile teksi ikigeuza na kushika ule uelekeo wa kule tulipotoka.

     Ile teksi ilipotoweka kabisa machoni mwangu nikaanza kupiga hatua zangu kwa utulivu nikikatisha mbele ya zile ofisi za mawasiliano kuelekea barabara ya Avenue du 18 Septembre na nilipoingia tu kwenye ile barabara nikagundua kuwa ilikuwa ni barabara iliyochangamka kidogo kwa pilikapilika za magari. Labda kutokana na kwamba ile ilikuwa ni barabara iliyokuwa imepakana na majengo yenye ofisi nyeti za serikali ya Burundi na mashirika makubwa ya kimataifa. Wakati nikitembea upande wa kulia wa ile barabara nikauona mgahawa mmoja wa kisasa wa La Belle Fille Restaurant baada ya kuipita ofisi ya shirika la Bima la Burundi. Upande wa kushoto wa barabara ile kulikuwa na bustani ya wazi ya maua kabla ya kulipita jengo la benki ya wanawake ya Burundi.

     Nilikatisha mbele ya bustani ile ya wazi na nilipolivuka lile jengo la benki ya wanawake ya Burundi nikapita mbele ya jengo refu la ghorofa lililokuwa likitumika kama makao makuu ya ofisi za ukusanyaji kodi na mapato za serikali ya Burundi. Baada ya kulipita jengo lile hatimaye nikajikuta nikikabiliana na ofisi za uBalozi wa Tanzania nchini Burundi. Mbele ya ofisi zile za Balozi kulikuwa na bustani nzuri ya miti na maua ya kupendeza yaliyokatiwa vizuri na katikati ya bustani ile mbele ya lile jengo kulikuwa na milingoti sita yenye bendera za nchi za Afrika ya mashariki zilizokuwa zikipepea kwa utulivu.

     Kwa tathmini ya haraka nilipozichunguza ofisi zile za Balozi ya Tanzania nchini Burundi nikagundua kuwa kwa wakati ule zile ofisi zilikuwa mbioni kuzidiwa na pilikapilika za watu waliokuwa wamefika pale kufuata huduma. Upande wa kushoto nje ya zile ofisi kulikuwa na magari mengi yaliyoegeshwa. Idadi kubwa ya magari yale yalikuwa ni ya watu binafsi na machache yalikuwa ni ya mashirika ya kimataifa kama UNHCR, UNCEF, Amnesty International na magari ya mashirika mbalimbali makubwa ya habari duniani kama THE REUTERS, CNN, BBC na mengineyo. Nje ya ofisi zile pia niliwaona watu wengi wakiwa na mabegi yao kama wasafiri na hapo nikajua kuwa watu wale walikuwa kwenye pilikapilika za kufuata taratibu za uhamiaji kabla ya kuondoka nchini Burundi kufuatia hali ya usalama wa nchi ile kuzidi kuwa tete.

     Hatimaye nikafika nje ya ofisi zile na hapo nikaanza kujipenyeza katikati ya lile kundi kubwa la watu nikielekea ndani ya zile ofisi za Balozi kuelekea eneo la mapokezi.

     Mara tu nilipoingia nikagundua kuwa msongamano wa watu mle ndani ulikuwa mkubwa sana huku watu wale wakiwa wamepanga foleni kwenye mistari minyoofu kufuata huduma kwenye kauta kubwa yenye maafisa uhamiaji wanne waliokuwa wamependeza katika sare zao za kazi. Maafisa uhamiaji wale walikuwa ni wanaume watatu na dada mmoja ambaye haraka macho yetu yalipokutana akashikwa na hamaki huku tabasamu la hakika likichomoza usoni mwake. Msichana yule nilimfahamu kwa jina la Hidaya Kijuu afisa uhamiaji mwenye cheo cha Sajenti. Miezi miwili iliyopita Hidaya alikuwa amefunga ndoa na rafiki yangu kipenzi wa jeshi la wananchi wa Tanzania Kanali Mbinde Mtimkavu jijini Dar es Salaam ambapo sherehe yao ya kufana ilifanyikia kwenye ukumbi wa jeshi wa Lugalo.

    “Kha! shemeji…!” Hidaya alikuwa wa kwanza kuniita kwa uchangamfu wa hali ya juu huku ameshikwa na furaha isiyoelezeka.

    “Hakika ndiyo mimi shemejio. Mh! kweli waswahili hawakukosea pale waliposema milima haikutani lakini binadamu hukutana”. Nikaongea kwa utulivu huku usoni nikiumba tabasamu na nilipoifikia ile meza ya kaunta alipokuwa Hidaya nikaiegemeza mikono yangu huku nikipambana vikali na macho ya chuki kutoka kwa watu waliokuwa kwenye mstari wa foleni ya kumfikia Hidaya baada ya kuhisi kuwa nilikuwa nataka kuwazidi maarifa kwa kukwepa kupanga foleni. Wale maafisa wengine wa uhamiaji wakageuka kunitazama kwa makini huku dhahiri wakionekana kushindwa kunielewa. Hata hivyo niliwasalimia na wote wakaitikia na kugeuka wakiendelea na hamsini zao.

     Hata hivyo Hidaya alikuwa mjanja sana kwa kushtukia kuwa maongezi yetu eneo lile yangeweza kusababisha kero kwa wale watu waliokuwa wamepanga foleni ya kutaka huduma kwenye kaunta yake. Hivyo haraka akanionesha ishara kuwa nizunguke nyuma ya ile kaunta na kwenda kumsubiri kwenye ukumbi mdogo wa kuta za vioo uliokuwa ndani ya lile jengo. Bila kupingana na wazo lake nikafanya vile na nilipokuwa nikiizunguka ile kaunta nikawaona maafisa wengine uhamiaji wa ofisi zile za uBalozi wakiwa ndani ya ofisi zao wametingwa na kazi. Wengine wakichambua taarifa kutoka kwenye majalada yaliyozizunguka meza zao na wengine wakifanya uhakiki wa taarifa kwenye kompyuta. Hata hivyo hakuna aliyejisumbua kunitazama wakati nilipokuwa nikipiga hatua zangu kwa utulivu katikati ya korido pana kuelekea kwenye ukumbi mdogo uliozungukwa na kuta kubwa za vioo uliokuwa upande wa kushoto wa lile jengo la ofisi zile za ubalozi.

     Nyuma ya ile kaunta kulikuwa na meza na viti vilivyokaliwa na maafisa wengine wawili wa kike waliokuwa makini kuwahudumia watu na upande wa kulia kwenye kona ya ile kaunta kulikuwa na korido nyingine pana iliyokuwa ikitazamana na milango ya vyumba vitatu vya ofisi iliyokuwa wazi. Huku nje ya korido ile kukiwa na foleni nyingine ya watu katika mabenchi marefu, watu wale wakisubiri kuingia kwenye zile ofisi. Ile korido niliyoingia ilikuwa ikitazamana na milango mitatu ya ofisi na mwisho wa korido ile kulikuwa na ngazi za kuelekea ghorofa ya juu.

     Hatimaye nilipofika katikati ya ile korido nikauona ukumbi mdogo wa mikutano wenye jumla ya viti kumi na mbili vilivyoizunguka meza moja ndefu ya umbo mstatili. Ukumbi ule ulikuwa umezungukwa na kuta kubwa za vioo na mapazia marefu ambayo kwa wakati ule hayakuwa yamefungwa.

     Taratibu nikausukuma mlango wa kile chumba na kuingia ndani ya ule ukumbi huku nikiyatembeza macho yangu taratibu kutathmini mandhari yale. Ukiondoa ile meza kubwa ya mikutano iliyozungukwa na viti kumi na mbili na runinga pana iliyokuwa upande wa kulia wa kile chumba. Ukutani hakukuwa na ziada nyingine mle ndani zaidi ya utulivu wa hali ya juu. Nilipourudishia ule mlango nyuma yangu nikatembea taratibu nikiizunguka ile meza kisha nikavuta kiti kimoja na kuketi. Nikiwa pale nikaanza kumkumbuka vizuri Meja jenerali mstaafu Adam Mwambapa, Balozi wa Tanzania nchini Burundi ambaye taarifa zilizoifikia idara ya ujasusi jijini Dar es Salaam zilikuwa zimeeleza kuwa alikuwa ametekwa na watu wasiofahamika.

     Dakika tano zilipokuwa mbioni kutokomea tangu nilipoingia mle ndani ya kile chumba mara nikauona mlango wa kile chumba ukifunguliwa kisha Hidaya akaingia mle ndani huku akiwa katika uso wenye tabasamu la kirafiki. Hidaya alipoingia mle ndani akaanza kuzunguka kile chumba huku akishusha mapazia katika namna ya kuyazuia macho ya watu wanaopita nje ya kile chumba kututazama wakati tukiendelea na maongezi yetu. Hidaya alipomaliza kufungua yale mapazia akaelekea ukutani na kuwasha taa iliyoleta nuru ya kutosha mle ndani kisha akaja na kuvuta kiti akiketi mbele yangu. Nilipomtazama mara moja sikuona tashwishwi yoyote usoni mwake ingawa alijitahidi kwa kila hali kutabasamu. Hidaya alikuwa msichana mzuri na mrembo mwenye umbo lenye mvuto wa aina yake lakini vilevile mcheshi na anayethamini sana utu.

    “Habari za jijini Dar es Salaam Tibba?”. Hidaya akavunja ukimya akiniuliza kwa sauti nyepesi ya kubembeleza huku akinilegezea macho kabla ya kuangua kicheko hafifu cha kimahaba. Nilimfahamu vizuri Hidaya kuwa utani ilikuwa hulka yake na kwa kuwa nilikuwa nimemzoea wala sikuona tatizo lolote badala yake nikajikuta nikiangua kicheko cha furaha na kicheko kile kilipokuwa mbioni kufika ukomo nikavunja ukimya.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kweli kaka yangu Mbinde kapata mke. Sipati picha angekufanya nini kama muda huu angekuwa humu ndani amejibanza sehemu fulani halafu akufume unanifanyia upuuzi huo”. Nikamwambia Hidaya na kitendo cha kumuona haraka akigeuka na kuyatembeza macho yake kwa hofu mle ukumbini kikanipelekea niangue kicheko kingine.

    “Mh! umenitisha sana na kaka yako jinsi alivyo na wivu ningetoka mkuku humu ndani bila ya kupenda kabla hajanifikia”. Hidaya akaongea huku akiendelea kucheka kisha akasogeza kiti vizuri na kuvaa uso wa kazi.

    “Dar es Salaam ni kwema kama ulivyokuacha shemeji”. Nikaongea kwa utulivu huku tukitazamana pale mezani na hapo Hidaya akanitazama kidogo kama anayefikiri kitu cha kuongea na hatimaye akavunja ukimya akiongea kwa sauti dhaifu inayopwaya.

    “Hapa mambo si shwari Tibba”

     “Nafahamu na ndiyo maana nimekuja hapa Hidaya. Chifu amenigusia juu ya kutekwa kwa Balozi wetu hata hivyo maelezo yake hayakuwa na ziada yoyote nje ya maelezo yaliyokuwa kwenye faksi aliyotumiwa kutoka hapa”. Nikaongea kwa utulivu huku nikimtazama kwa makini msichana yule mwanausalama machachari.

    “Jana usiku Chifu alinidokeza juu ya ujio wako kwa njia ya simu na kwa kweli nilifurahi sana niliposikia kuwa ni wewe ndiye uliyekabidhiwa jukumu hili. Kwani kwa vile ninavyokufahamu najua kazi itafanyika kwa weledi wa hali ya juu na majibu yatapatikana haraka ingawa pia sitarajii kuwa kazi itakuwa nyepesi”. Hidaya akaongea kwa sauti tulivu na nilipomtazama usoni nikagundua kuwa mzaha ulikuwa mbali kabisa na nafsi yake.

    “Ina maana Chifu alikuwa akifahamu kuwa wewe upo huku?”. Nikamuuliza Hidaya kwa udadisi huku nikimtazama usoni kwa makini.

    “Ndiyo alikuwa akifahamu na ni yeye ndiye aliyependekeza niletwe hapa”

     “Una muda gani tangu uhamishiwe hapa kikazi?”. Nikamuuliza Hidaya huku mawazo mengi yakipita kichwana mwangu.

    “Mwezi mmoja na nusu” Hidaya akanijibu huku akinitazama kwa makini.

    “Sasa mbona Chifu hakuwahi kunidokezea juu ya uwepo wako hapa jijini Bujumbura?”

     “Huwenda alitaka kukufanyia surprise kwa vile anajua sisi ni marafiki wa muda mrefu kama chanda na pete”. Hidaya akaongea kwa uchangamfu huku akiumba tabasamu hafifu usoni mwake. Kitambo kifupi cha ukimya kikapita huku kila mmoja akiwaza lake na ukimya ule ulipokuwa mbioni kushika hatamu nikawekeza kwenye hoja ya msingi.

    “Nini kinachoendelea hapa Burundi?”

     “Baadhi ya raia wa kawaida, wanasiasa na wanajeshi hawaitaki serikali iliyopo madarakani”

     “Kwa nini?” nikamuuliza Hidaya kwa shauku na hapo nikamuona akinitazama kidogo kwa mshangao.

    “Taarifa zinaeleza kuwa rais wa Burundi ndugu Pierre Nkurunziza anajaribu kuipindisha katiba ya nchi hii ili aweze kugombea kiti cha urais kwa mhula wa tatu na ambapo inasemekana kuwa mpango huo ni kinyume cha katiba”

     “Kweli aliyesema kuwa Afrika ni bara la giza hakuwa amekosea. Hivi hii Afrika imeingiliwa na mdudu gani kiasi kwamba kila kiongozi anayeingia madarakani aone ugumu wa kutoka wakati inapofikia wakati wa kufanya hivyo?”...



    “Kweli haya ni maradhi ya aina yake kwani hata wale viongozi wanaoona aibu na kuondoka madarakani kwa mujibu wa katiba ukizitazama vizuri nyuso zao kwa makini utagundua kuwa mioyo yao bado inatamani kuendelea kubaki madarakani ila tu ni kwamba mazingira ya kuendelea kubaki madarakani hayaruhusu”. Hidaya aliongea kwa masikitiko.

    “Unavyosema ni kweli kabisa Hidaya ingawa wapo baadhi ya viongozi wa Afrika ambao wamewafanyia mambo mengi mema na mazuri raia wao kiasi kwamba raia haohao wakaamua kuendelea kuwabakiza madarakani waendelee kuwaongoza kwa muda mrefu kutokana na wananchi wao wanavyowaamini na kufurahishwa na uongozi wao. Lakini kitu cha kushangaza ni kuwa viongozi wa namna hiyo wamejikuta wakipokea fadhila hizo kwa kiasi cha kupitiliza kiasi kwamba baadaye wanapotakiwa kuachia madaraka ya nchi huanza kuchukia na kuikataa hali hiyo na badala yake hutengeneza mikakati mikali ikibidi kumwaga hata damu za raia wasio na hatia kama siyo kuwashughulikia wapinzani wao kwa mbinu chafu ili tu waendelee kubaki madarakani na kula maisha na familia zao pamoja na ndugu jamaa na marafiki.

     Kuna mifano mingi tu ya viongozi wa Afrika waliokaa madarakani kwa kipindi kirefu sana kiasi kwamba ilipofika wakati wa wananchi kuwataka waachie madaraka wao hawakuwa tayari kufanya hivyo kwa ridhaa yao.

    “Ni kweli Tibba” Hidaya akaongea kwa utulivu huku akitikisa kichwa kuonesha kunielewa.

    “Blaise Compaoré aliyekuwa rais wa Burkina Faso aliingia madarakani kwa kufanya mapinduzi ya kijeshi mwaka 1987. Mapinduzi ambayo yaliing?oa madarakani serikali ya rais wa wakati huo ndugu Thomas Sankara ambapo aliuwawa katika mazingira yasiyoelezeka. Baada ya miaka 27 ya ungozi wa rais Blaise Compaoré hatimaye wananchi wa Burkina Faso wakaonesha kutosheka naye wakimtaka aachie madaraka. Hata hivyo hakuwa tayari kufanya hivyo badala yake akajaribu kubadili katiba ili awanie urais kwa mhula mwingine. Wananchi kuona hivyo wakakasirika na kuingia mitaani wakiandamana na kupinga uhuni huo. Matokeo yake nguvu ya umma ikamshinda hivyo akalazimika kukimbilia nchi jirani ya Ivory Coast huku serikali ya mpito ikishikiliwa na jeshi.

     Rais wa Equatorial Guinea ndugu Teodoro Obiang Nguema Mbasogo amekaa madarakani kwa muda wa miaka zaidi ya 35 tangu alipotwaa madaraka kwa mapinduzi ya kijeshi na kuapishwa kuwa rais mwaka 1982.

     José Eduardo dos Santos, rais wa nchi ya Angola amekaa madarakani tangu mwaka 1979, ikiwa ni miaka minne baada ya nchi hiyo kupata ukombozi. Wakati akisifiwa kwa sera yake nzuri ya kuinua sekta ya mafuta nchini humo, bado amekuwa akishutumiwa vikali kwa kuongoza serikali inayonuka rushwa. Wakati asilimia sabini ya raia wa nchi hiyo wakiishi chini ya dola mbili kwa siku moja mtoto wake wa kike aitwaye Isabel kupitia mianya ya kisiasa amekuwa mmoja wa matajiri wakubwa akitambulika kama bilionea mwenye umri mdogo barani Afrika.

     Rais Robert Mugabe ni kiongozi mwingine aliyekaa madarakani kwa zaidi ya miaka 34 huku akiendelea kukosolewa vikali na serikali za nchi za magharibi. Lakini vilevile amekuwa akipendwa sana na raia wengi wa bara la Afrika kwa misimamo yake mikali ya kuzituhumu serikali za nchi za magharibi kwa kupenda kuingilia mambo ya serikali za nchi nyingine zikiwemo nchi za Afrika.

     Paul Biya rais wa Cameroon na yeye amekaa madarakani kwa miaka zaidi ya 32 hadi sasa tangu mwaka 1982 na amekuwa akijificha katika siasa za chama kimoja tangu miaka ya themanini na hatimaye kuachana na siasa za chama kimoja mapema miaka ya tisini chini ya shinikizo la kimataifa. Hata hivyo chaguzi nyingi zinazomrudisha madarakani zimekuwa zikihisiwa kuwa siyo za haki huku akiendelea kuboresha mahusiano mazuri na nchi ya Ufaransa.

     Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda amekuwa madarakani tangu mwaka 1986 baada ya kuanguka kwa tawala za Iddi Amin Dada na Milton Obote. Hata hivyo amekuwa miongoni mwa viongozi walio mstari wa mbele kupinga vitendo vya kishoga lakini vilevile anasifika kwa kuinua vizuri uchumi wa nchi ya Uganda na kutengeneza mipango kabambe ya kupambana na ugonjwa hatari wa UKIMWI nchini kwake.

     Kiongozi mwingine wa Afrika ni Brigedia Omar al-Bashir wa Sudan ambaye aliingia madarakani mwaka 1989 kwa mapinduzi ya kijeshi yasiyo ya kumwaga damu. Amekaa madarakani kwa zaidi ya miaka 25 na amechaguliwa mara tatu kuendelea kushika madaraka katika chaguzi tatu zenye kukosolewa vikali na wapinzani na umoja wa mataifa. Mwaka 2009 Omar al-Bashir alikuwa ndiye kiongozi wa kwanza wa Afrika kushtakiwa kwenye mahakama ya ICC kwa tuhuma za mauji ya halaiki, ubakaji na utesaji wa watu katika jimbo la Darfur.

     Idriss Déby rais wa Chad yeye pia amekaa madarakani kwa zaidi ya miaka 23 tangu mwaka 1990 alipoipindua madarakani serikali ya rais wa wakati huo ndugu Hissene Habré katika mji mkuu wa nchi hiyo uitwao N?Djaména.

     Kiongozi mwingine ni Isaias Afwerki rais wa Eritrea ambaye na yeye amekaa madarakani kwa zaidi ya miaka 23 tangu nchi hiyo ilipopata uhuru wake mwaka 1993. Eritrea ni nchi ya mrengo wa chama kimoja tu cha siasa. Chama cha siasa cha rais Afwerki kiitwacho People?s Front for Democracy and Justice (PFDJ) ndiyo chama pekee kinachoruhusiwa kushiriki shughuli za siasa za nchi hiyo. Ndugu Afwerki amekuwa akikosolewa vikali kwa kushindwa kukuza demokrasia nchini mwake. Serikali yake imekuwa ikipambana vikali na wakosoaji wake huku akivifungia vyombo binafsi vya habari vinavyokinzana na utawala wake.

     Mwingine ni ndugu Yahya Jammeh rais wa Gambia ambaye hadi sasa amekaa madarakani kwa zaidi ya miaka 20 tangu alipoanza kuitawala nchi hiyo tangu mwaka 1994 akiwa mwenyekiti wa chama chake cha siasa cha Armed Forces Provisional Ruling Council (AFPRC)

     Denis Sassou Nguesso rais wa jamhuri ya Kongo ni miongoni mwa marais waliokaa muda mrefu madarakani katika nchi yake. Hadi wakati huu amekaa madarakani kwa muda wa zaidi ya miaka 17 tangu kuanguka kwa utawala wa rais Pascal Lisouba nchini humo. Hii ni sehemu tu ya viongozi wa Afrika wenye kasumba ya kupenda kung?ang?ania madaraka”. Nikaweka kituo na kumtazama Hidaya nikitaka kupata hakika kama alikuwa akiyasikiliza maelezo yangu kwa makini na kitendo cha kumuona akinitazama kwa utulivu kikanijulisha kuwa tulikuwa pamoja.

    “Mh! Tibba kweli wewe ni mdadisi. Umeyajulia wapi mambo yote hayo?”. Hidaya akaniuliza kwa shauku huku akinitazama kwa makini.

    “Haya ni mambo tunayopaswa kuyafahamu sisi wote Hidaya kwani ukichunguza utagundua kuwa matatizo ya nchi za Afrika kwa kiasi kikubwa yanafanana. Ingawa mimi binafsi wakati mwingine naona kuwa tatizo siyo kwa kiongozi kukaa muda mrefu madarakani kwani anaweza kufanya hivyo kutegemeana na katiba ya nchi husika kama itamruhusu kufanya hivyo na siyo kubadili katiba ili izidi kumuweka zaidi madarakani. Raia wengi hawana matatizo na serikali inayokaa madarakani muda mrefu kama serikali hiyo itawaletea maendeleo na kukidhi haja ya shida zao. Lakini pale unapokuta kiongozi wa nchi na serikali yake ni mzigo kwa raia, serikali inanuka rushwa huku ikiandamwa na utabaka wa kidini au ukabila na hakuna maendeleo yoyote hapo ndiyo ubaya wa viongozi wa Afrika unapoonekana waziwazi”. Nikaweka kituo huku nikiviminyaminya vidole vyangu mkononi.

    “Kwa muda mfupi wa mwezi mmoja na nusu tangu nilipofika hapa jijini Bujumbura nimegundua kitu?”. Maelezo ya Hidaya yakaamsha upya hisia zangu na hapo nikamkata jicho la shauku kabla ya kimuuliza.

    “Kitu gani?”

     “Suala la ukabila”

     “Bado sijakuelewa?”. Nikamuuliza Hidaya huku nikimtazama kwa makini.

    “Burundi ni miongoni mwa nchi chache za barani Afrika zenye makovu ya ukabila na katika nadharia hiyo hali ya kuaminiana kati ya wenyewe kwa wenyewe huwa ni tete. Hii nchi inaundwa na watu wa makabila matatu. Kabila la Wahutu ndiyo kubwa kuliko makabila mengine huku likichukua kiasi cha asilimia themanini na tano ya idadi ya raia wote wa Burundi. Asilimia kumi na nne ya sehemu iliyosalia inachukuliwa na watu wa kabila la Tutsi na hivyo kupelekea asilimia moja iliyosalia kuchukuliwa na kabila dogo kabisa la Watwa. Hata hivyo msuguano mkali upo katika haya makabila mawili makubwa.

     Kwa mfano ikitokea serikali inaongozwa na mhutu basi ujue hapo idadi kubwa ya watutsi hawataunga mkono serikali hiyo kinaga ubaga kwa vile aliyeko madarakani siyo wa mrengo wao. Vilevile ikitokea kuwa serikali iliyopo madarakani inaongozwa na mtutsi basi hapo ujue wahutu wengi watahisi kuwa uongozi uliopo madarakani hauwatendei haki na ndiyo maana kumefanyika mapinduzi mengi ya kijeshi katika nchi hii”. Hidaya akaweka kituo akinitazama na macho yetu yalipokutana nikagundua kuwa macho yake yalikuwa na uchovu mwingi kama mtu aliyepoteza usingizi kwa muda wa siku mbili mfululizo.

    “Unadhani jeshi la wananchi wa Burundi limefanikiwa kuchukuwa udhibiti wa maeneo yote ya serikali?”. Nikamuuliza Hidaya katika namna ya kuzidi kumdadisi.

    “Mh! bado hali ni tete kwani inavyoonekana ni kama mpango wa jaribio hili la mapinduzi ya kijeshi hapa Burundi ulikuwa haujaratibiwa vizuri na kupata ushawishi wa kutosha kutoka kwa viongozi waandamizi wa jeshi. Kwani baadhi ya askari watiifu kwa serikali ya rais Pierre Nkurunziza wameonekana wakipambana kikamilifu kudhibiti mapinduzi haya dhidi ya askari wenzao waasi wanaotaka kuing?oa serikali iliyoko madarakani na hivyo kupelekea hali ya usalama wa hapa Burundi kuzidi kuwa tete”

    Maelezo ya Hidaya nilikuwa nimeyapata vyema hivyo nikaanza kuyatembeza macho yangu mle ndani taratibu huku mawazo mengi yakipita kichwani mwangu juu ya hali ile ya usalama ilivyokuwa pale nchini Burundi. Nilitamani kumuelezea Hidaya juu ya masaibu yote yaliyonikuta tangu nilipotoka jijini Dar es Salaam hata hivyo sikuona kama ule ungekuwa wakati mwafaka hivyo hatimaye nikavunja tena ukimya.

    “Kupitia maelezo yako inaonekana kuwa kuna mpasuko mkubwa ndani ya jeshi la wananchi wa Burundi?”

     “Naweza kusema hivyo kwani ukiwasikiliza raia wa hapa Burundi kwa makini utagundua kuwa wapo baadhi yao wasiobariki hata kidogo jaribio la mapinduzi haya ya kijeshi huku wakidai kuwa rais Pierre Nkurunziza anakiuka sheria kwa kuvunja katiba ya nchi inayomtaka kukaa madarakani kwa vipindi vya mihula miwili tu tofauti na yeye anavyotaka kuwania urais kwa mhula wa tatu. Lakini vilevile wapo raia wa Burundi wanaoona kuwa kitendo cha rais Pierre Nkurunziza kuwania tena urais hajafanya kosa lolote na wala hajaibaka katiba ya nchi. Watu hao wanao muunga mkono rais Nkurunziza wakitumia kigezo kuwa mwanzoni rais Pierre Nkurunziza alisimikwa madarakani na sheria ya bunge la Burundi lakini kwa sasa anayo haki ya kikatiba ya kuwania urais kama walivyo wagombea wengine wa vyama pinzani na kama ukichunguza kwa makini utagundua kuwa kuna namna ya ukweli juu ya madai haya. Hata hivyo bado naweza kusema kuwa mambo ya hapa nchini Burundi tuwaachie warundi wenyewe”. Hidaya hatimaye akaweka kituo huku akinitazama kwa utulivu kama mtu aliyezongwa na fikra nyingi kichwani.

    “Mambo ya Burundi kuwaachia warundi wenyewe ni jambo jema zaidi kwani hakuna nchi inayoruhusiwa kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine kwa mujibu wa sheria za kimataifa. Lakini ni lazima ufahamu kuwa hali yoyote ya machafuko ya kisiasa na umwagaji damu utakaotokea hapa nchini Burundi yana athari kubwa kwa nchi nyingine za jirani ikiwemo Tanzania. Kwa mfano tangu kufanyika kwa jaribio la mapinduzi haya ya kijeshi hapa Burundi kumekuwa na wimbi kubwa la wakimbizi wa kutoka hapa nchini Burundi wanaovuka mpaka na kuingia nchini Tanzania katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu iliyopo mkoani Kigoma. Matokeo yake ni kuwa kumekuwa na uharibu mkubwa wa mazingira unaofanywa kutokana na ukataji mkubwa wa miti ya asili inayotumika kama chanzo cha nishati ya kupikia chakula katika kambi hiyo na mfumuko mkubwa wa magonjwa ya kuambukiza kama kipindupindu na homa ya matumbo.

     Lakini vilevile serikali yetu imekuwa ikitumia fedha nyingi katika kutoa misaada mbalimbali kwa wakimbizi hawa kwa kuzingatia utu wa binadamu na hivyo kupunguza kasi ya maendeleo kwa taifa katika nyanja mbalimbali. Hivyo kama kutakuwa na namna ya kufanya katika kuzuia hali ya machafuko ya kisiasa hapa nchini Burundi mimi naona ni jambo jema zaidi alimradi namna hiyo ya kuzuia machafuko hayo ifanyike kwa weledi wa hali ya juu na ushirikiano wa majadiliano ya pamoja baina ya pande mbili zenye kutofautiana, wakuu wa nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo nchi ya Burundi ni mwanachama hai pamoja na viongozi wakubwa wa umoja wa Afrika wenye ushawishi katika masuala ya kisiasa”CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

     “Idara yetu ya ujasusi ina mpango gani juu ya hili jaribio la mapinduzi ya kijeshi la hapa nchini Burundi?”. Hidaya akaniuliza kwa udadisi.

    “Hadi wakati huu bado sijasikia chochote na naamini kuwa hatuwezi kusikia chochote hadi hapo mkutano wa viongozi wa nchi hizi za Afrika Mashariki utakapofika tamati jijini Dar es Salaam. Kilichonileta hapa ni kumtafuta Balozi wetu hadi hapo atakapopatikana au hatima yake kujulikana”. Nikamwambia Hidaya kwa msisitizo.

    “Chifu tayari amekwishanieleza kila kitu juu ya safari yako ya kuja hapa Burundi wakati nilipoongea naye usiku wa jana”. Hidaya akaniambia kwa utulivu na hapo nikamtazama kwa udadisi nikizichunguza vizuri hisia zake na nilipotaka kutumbukiza hoja mpya mara nikakumbuka kumuuliza jambo katika namna ya kutaka kupata hakika.

    “Nani aliyeko nyuma ya mpango huu wa mapinduzi ya kijeshi hapa Burundi?”

     “Kiongozi mmoja mwandamizi wa jeshi la wananchi wa Burundi aitwaye Meja jenerali Godefroid Niyombare. Taarifa zinaeleza kuwa Meja jenerali Godefroid Niyombare akiwa na...



    ...viongozi wengine wa kijeshi akiwemo aliyekuwa waziri wa ulinzi wa Burundi kupitia kituo kimoja binafsi cha redio kiitwacho FRANCE 24 walitangaza mapinduzi hayo ya kijeshi. Muda mfupi baada ya kutangazwa kwa mapinduzi hayo ya kijeshi yenye lengo la kuing?oa madarakani serikali ya rais Pierre Nkurunziza raia wengi waliingia mitaani kusherehekea mapinduzi hayo huku wanajeshi wengi wakionekana kulinda ofisi za serikali kikiwemo kituo cha kurushia matangazo cha redio ya taifa. Wakati huo rais Pierre Nkurunziza akiwa jijini Dar es Salaam Tanzania kuhudhuria mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika Mashariki ambapo suala la mustakabali wa amani ya hapa nchini Burundi likiwa ndiyo kipaumbele namba moja.

     Taarifa zinaeleza kuwa mara baada ya kutangazwa kwa mapinduzi hayo ya kijeshi rais Pierre Nkurunziza alijaribu haraka kurudi hapa Burundi lakini ndege yake ilisemekana kugeuzia angani na kurudi nchini Tanzania. Shirika la habari la AFP la nchini ufaransa Agence France-Presse liliripoti kuwa wanajeshi waasi walikuwa tayari wameuteka uwanja wa ndege wa kimataifa wa hapa Bujumbura”.

    Maelezo ya Hidaya yalikuwa yameongezea ziada nyingine katika ufahamu wangu ingawa pia hayakuwa na msaada mkubwa katika harakati zangu. Hatimaye nikapiga mwayo hafifu wa uchovu na kunyoosha viungo vyangu na nilipotulia nikaiegemeza vizuri mikono yangu juu ya ile meza na kutumbukiza hoja mpya katika maongezi yale.

    “Taarifa kupitia Fax iliyotumwa katika ofisi kuu ya idara yetu ya ujasusi jijini Dar es Salaam kutoka hapa inaeleza kuwa Balozi wetu wa hapa Burundi Meja jenerali mstaafu Adam Mwambapa ametekwa. Una mfahamu mtu aliyetuma taarifa hiyo?”. Nikamuuliza Hidaya kwa utulivu huku nikimtazama usoni kwa makini. Swali langu likampelekea Hidaya alegeze kidogo uso wake na kutabasamu kisha akakohoa kidogo kusafisha koo lake na hatimaye kuvunja ukimya.

    “Ndiyo namfahamu na mtu huyo ni mimi”. Jibu la Hidaya likapelekea fikra zangu zimezwe na mduwao wa aina yake huku kwa sekunde kadhaa nikimtazama katika namna ya kutoamini maneno yale. Loh! hatimaye nikashusha pumzi taratibu na kuulegeza uso wangu huku nikiliruhusu tabasamu jepesi kuchomoza usoni mwangu kisha nikasogeza kiti changu vizuri na kuketi.

    “Kwa kweli sikuwahi kufikiria kama mtu aliyetuma Fax ile ungekuwa ni wewe Hidaya. Mh! Kweli Chifu alikuwa na maana kubwa kukuleta hapa”. Nikaongea huku nikiangua kicheko hafifu kisha kicheko kile kilipofika ukomo nikaendelea.

    “Hata hivyo ni matumaini yangu kuwa huwezi kutuma Fax yenye ujumbe mzito kama ule ukiwa katika namna ya kufanya mizaha yako kama tulivyokuzoea. Hili ni jambo nyeti sana Hidaya na naamini kuwa ulifanya uchunguzi wa kutosha wa kujiridhisha kabla hujaamua kutuma Fax ile”

     “Mh! Tibba yaani hata kama napenda kufanya mzaha lakini siwezi kufanya mzaha katika jambo nyeti kama hili”. Hidaya akaongea kwa kusononeka huku akionekana kutopendezwa na kauli yangu. Hata hivyo nikatabasamu kidogo kulainisha maongezi yetu kisha nikamchombeza Hidaya utani kwa kumkonyeza tukio ambalo lilimpelekea na yeye atabasamu kidogo. Utulivu uliporejea mahala pake nikavunja ukimya.

    “Nataka kufahamu kuwa ni mazingira gani yaliyokufanya uamini kuwa Balozi Adam Mwambapa ametekwa”. Swali langu likampelekea Hidaya aupishe utulivu kidogo huku akionekana kufikiri jambo kisha akaniambia.

    “Ilikuwa ni muda wa saa nane, usiku wa kuamkia siku ya jana, muda mfupi baada ya tukio la jaribio la mapinduzi ya kijeshi kufanyika hapa Burundi. Asubuhi ya siku ile ya kuelekea mapinduzi haya Balozi Adam Mwambapa hakufika hapa ofisini kwake kama ilivyozoeleka pasipo kutanguliza taarifa yoyote jambo ambalo lilikuwa siyo la kawaida. Ilipofika saa tano asubuhi wafanyakazi wa hapa sote tukaingiwa na wasiwasi kwani ile haikuwa hali ya kawaida na kwa kuwa taratibu za kazi yangu nazifahamu vizuri niliamua kupiga simu ya nyumbani kwake”

     “Balozi Adam Mwambapa anaishi wapi hapa jijini Bujumbura?”. Nikamuuliza Hidaya huku nikimtazama usoni kwa makini.

    “Chausée P.L. Rwagasore nyumba namba 26. Nadhani kadiri utakavyoendelea kukaa hapa Bujumbura utaizoea vizuri mitaa ya jiji hili”. Hidaya akaweka kituo huku akinitazama kama ambaye alikuwa akitarajia kusikia swali lingine kutoka kwangu.

    “Wakati unasiliana na Balozi Adam Mwambapa wewe ulikuwa wapi?”

     “Niliwasiliana naye nikiwa hapa ofisini kupitia simu ya mezani ya idara yangu”. Jibu la Hidaya lilikuwa la kweli na la hakika.

    “Baada ya hapo nini kilifuata?”

     “Baada ya miito kadhaa hatimaye simu ya nyumbani ya Balozi Adam Mwambapa ikapokelewa na kwa kweli tukio lile lilinitia faraja sana moyoni.

    “Nani aliyepokea hiyo simu?”

     “Alikuwa ni Balozi Adam Mwambapa mwenyewe na baada ya kumuuliza kama kulikuwa na tatizo lolote lililompelekea kutokufika ofisini siku ile akaniambia kuwa nisiwe na wasiwasi wowote kwani alikuwa akijiandaa kwenda kuhudhuria mkutano wa dharura ulioandaliwa na viongozi waandamizi wa serikali ya Burundi hapa jijini Bujumbura.

     Maelezo ya Hidaya yakawa yamenishtua kidogo na kunipelekea nianze kuunda hoja za kila namna kichwani mwangu ingawa nilipomtazama Hidaya sikuweza kuona tashwishwi yoyote usoni mwake.

    “Balozi Adam Mwambapa alikwambia kuwa huo mkutano wa dharura ungefanyikia wapi?”

     “New Parador Residence. Ni hoteli moja yenye ukumbi wa kisasa wa mikutano na huduma ya malazi uliopo kando kidogo ya hili jiji la Bujumbura”

    Maelezo ya Hidaya yakanipelekea nimtazame kwa utulivu huku nikiiruhusu taarifa ile kupenya vizuri kwenye fikra zangu.

    “Balozi alikueleza kiini cha mkutano huo?”

     “Ingawa alikuwa hajapewa maelezo ya kutosha juu ya mkutano huo lakini aliniambia kuwa taarifa za awali zilieleza kuwa mkutano huo ulikuwa ukihusiana na hali tete ya usalama wa hapa nchini Burundi baada ya jaribio la mapinduzi ya kieshi kufanyika”

     “Nani aliyeitisha mkutano huo?’’. Nikamuuliza Hidaya kwa udadisi ingawa sikuwa na hakika kama angeweza kuwa na jibu moja la hakika.

    “Hilo hakunidokeza labda kwa sababu nilisita kuendelea kumuuliza na hiyo ni baada ya kuona kuwa majibu yake yalikuwa ya mkato sana kama mtu mwenye haraka”. Hidaya akaongea huku akijitahidi kuvuta kumbukumbu kichwani mwake.

    “Sasa ni kitu gani kilichokupelekea uamini kuwa Balozi Adam Mwambapa amatekwa?”. Baada ya kufikicha macho yangu kwa vidole na kupiga mwayo hafifu wa uchovu nikamuuliza Hidaya huku nikimtazama kwa makini.

    “Saa nane ya usiku ule ambao asubuhi yake niliwasiliana na Balozi Adam Mwambapa nilishtushwa kutoka usingizini na mlio wa simu ya mezani iliyokuwa sebuleni kwangu”. Hidaya akaendelea kuongea huku akionekana kuzidi kuvuta kumbukumbu hata hivyo nilimkatisha.

    “Simu kutoka kwa nani?”

     “Ilikuwa ni simu ya kutoka nyumbani kwa Balozi Adam Mwambapa na mzungumzaji alikuwa ni Balozi Adam Mwambapa mwenyewe”. Hidaya akaweka kituo na hapo nikamtazama kwa shauku kama nyoka aliyeona kifaranga cha kuku. Maelezo yale yalikuwa yameanza kunivuta hivyo nikaegemeza vizuri mikono yangu pale juu mezani huku nikimtazama Hidaya kwa makini.

    “Una hakika kuwa sauti ya mzungumzaji kwenye hiyo simu uliyopokea ilikuwa ni ya Balozi Adam Mwambapa mwenyewe?”. Nikamuuliza Hidaya katika namna ya kutaka kupata hakika.

    “Nina hakika kabisa kwani sauti ya Balozi Adam Mwambapa ni vigumu kuisahau kama ilivyo kwa mlio wa risasi. Hidaya akanitanabaisha akichombeza utani.

    “Mara baada ya kuipokea hiyo simu Balozi Adam Mwambapa alikueleza nini?”

     “Sauti yake ilikuwa imetawaliwa na kitetemeshi cha hofu na mashaka wakati aliponieleza kuwa maisha yake yalikuwa hatarini kwani nyumba yake ilikuwa imevamiwa na watu wasiojulikana na hivyo alikuwa akiomba msaada wa haraka”. Maelezo ya Hidaya yakawa yameamsha hisia mpya nafsini mwangu hivyo taratibu nikauruhusu utulivu kichwani mwangu huku nikitafakari kwa kina juu ya maelezo yale.

    “Walinzi wake walikuwa wapi wakati yeye akivamiwa?”

     “Sikukumbuka kumuuliza swali hilo kutokana na haraka”. Jibu la Hidaya likanipelekea nishikwe kidogo na mshangao huku nikimkodolea macho. Hatimaye nikamuuliza.

    “Kwa hiyo unataka kuniambia kuwa tangu ulipowasiliana na Balozi Adam Mwambapa asubuhi ile hiyo simu ya saa nane usiku ilikuwa ni ya mara yenu ya pili kuwasaliana?”. Nikamuuliza Hidaya huku nikimtazama kwa makini.

    “Ndiyo’’. Hidaya akanijibu kwa hakika huku akinitazama.

    “Nini kilifuata baada ya hapo?’’

     “Nilimdadisi Balozi Adam Mwambapa kwa kumuuliza kuwa ni kipi kilichokuwa kimempelekea ahisi kuwa alikuwa amefanyiwa uvamizi”

     “Jibu lake lilikuwaje?’’ nikamuuliza Hidaya kwa shauku.

    “Alinieleza kuwa nyumba yake ilikuwa imezingirwa na wavamizi hao wasiojulikana na nje kulikuwa na majibizano ya risasi kati ya walinzi wake na wavamizi hao”. Hidaya akaweka kituo akinitazama kama mtu afikiriaye jambo hali iliyonipelekea na mimi nianze kuibua maswali mengi kichwani mwangu juu ya maelezo yale ambayo sasa nilikuwa nimeanza kuhisi uzito wake.

    “Baada ya hapo Balozi Adam Mwambapa alikueleza nini?”. Hatimaye nikamuuliza Hidaya baada ya kuhisi kuwa ukimya ulikuwa mbioni kushika hatamu mle ndani. Hidaya akageuka kwa utulivu kunitazama kisha akaendelea.

    “Hiyo ndiyo ilikuwa mara yangu ya mwisho kuisikia sauti ya Balozi Adam Mwambapa kwani wakati nilipokuwa nikijiandaa kutia neno ghafla sauti yake ilitoweka hewani ingawa simu ile haikukatwa. Nikiwa naendelea kusikilizia kupitia simu ile kwa mbali niliweze kuisikia sauti ya Balozi Adam Mwambapa ikilalamika na hatimaye kukoma kabisa na kisha kufuatiwa na sauti ya milio kadhaa ya risasi ambayo nayo pia haikudumu sana”. Hidaya akaweka kituo tena kama mtu afikiriaye jambo kwa kina na nilipomtazama usoni nikagundua kuwa uso wake ulikuwa umejawa sana na simanzi na hapo nikajua kuwa alikuwa amehuzunishwa sana na tukio lile la kutekwa kwa Balozi Adam Mwambapa.

     Sasa nilianza kushawishika juu ya maelezo ya Hidaya yaliyokuwa kwenye ile Fax aliyoituma jijini Dar es Salaam kwenye ofisi kuu ya idara ya ujasusi ikielezea juu ya tukio la kutekwa kwa Balozi wetu wa Tanzania nchini Burundi Meja jenerali mstaafu Adam Mwambapa. Kwa kweli nilimeza fundo kumbwa la mate baada ya kuhisi kazi ngumu ya hatari iliyokuwa mbele yangu.

    “Sasa baada ya hapo ikawaje?. Hatimaye nikavunja ukimya na kumuuliza Hidaya kwa utulivu huku nikimtazama.

    “Niliendelea kuiweka ile simu sikioni huku nikiita katika namna ya kutarajia kumpata mtu yeyote hususani miongoni mwa wale watekaji apokee simu ile na kuongea dhumuni za uvamizi ule. Lakini hilo halikutokea kwani muda mfupi uliofuata ile simu upande wa pili ilikatwa kabisa na sikuweza kusikia chochote.

     Hofu ikiwa imenishika hatimaye nikairudishia ile simu mahala pale kisha nikaamka kutoka kitandani na kujiandaa haraka. Nilipomaliza kujiandaa nikatoka nje na kufunga mlango wa nyumba kisha nikawasha gari langu na kuelekea mtaa wa Boulevard du 28 Novembre nyumba namba 26 sehemu yalipokuwa makazi ya Balozi Adam Mwambapa”

    Mara hii nikamtazama Hidaya na kumuona kuwa ni msichana jasiri sana kwa kitendo cha kuthubutu kuhatarisha maisha yake kwa kutembea mitaani usiku wa manane katika jiji lisilokuwa na usalama.

    “Ulipofika nyumbani kwa Balozi Adam Mwambapa hali ilikuwaje?”. Nikamuuliza Hidaya kwa shauku huku nikimtazama kwa makini.

    “Sikufanikiwa kufika kwani mapema tu nilipoanza safari yangu nikagundua kuwa mbele yangu nilikuwa nikielekea kukabiliana na kifo”

     “Kwanini unasema hivyo?”

     “Kwa sababu barabara nyingi za jiji la Bujumbura kwa wakati ule zilikuwa zimetawaliwa na majibishano ya risasi kati ya wanajeshi waasi na wale wanajeshi wanaoiunga mkono serikali ya rais Pierre Nkurunziza. Kwa hiyo unaweza mwenyewe kuhisi hali ya usalama ilikuwaje kwa wakati huo”. Hidaya akaniambia huku akinikata jicho la hadhari.

    “Kwa hiyo uligeuza na kurudi nyumbani?”...

    “Hapana sikurudi nyumbani kwani hata kama ningerudi nyumbani bado nisingeweza kupata usingizi kutokana na hali yenyewe ya mambo ilivyokuwa. Kutoka nyumbani kwangu hadi hapa ofisini umbali wake siyo mrefu sana hivyo nikawa nimepata wazo la kupenyapenya mitaani na kuja hapa.

    “Walinzi wa hapa ofisini waliponiona waliingiwa na wasiwasi hata hivyo niliwatoa hofu kwa kuwaambia kuwa kulikuwa na jambo la dharura lililokuwa limejitokeza na hivyo nilikuwa nimelazimika kufika hapa usiku ili kulifanyia kazi. Sikukabiliana na upinzani wowote hivyo nikafungua ofisi na kuingia ndani ndiyo nikaketi na kuandika ile Fax na hatimaye kuituma makao makuu ya idara yetu ya ujasusi jijini Dar es Salaam”

    Maelezo ya Hidaya yakawa yameniingia vizuri na kwa mara nyingine nikajikuta nikimpongeza kwa kuwa msichana jasiri, mzalendo na mwenye kujali.

    “Ulitoa taarifa kwa vyombo vya usalama vya hapa Burundi?”. Nikamuuliza Hidaya kwa udadisi.

    “Hapana! kwani baada ya kufikiri sana niliona kuwa hilo lisingekuwa jambo jema”

     “Kwa nini?”

     “Jaribio hili la mapinduzi ya kijeshi hapa nchini Burundi limepelekea hali ya kutoaminiana sana tena kwa baadhi ya maafisa katika vyombo vya usalama. Hivyo niliona kuwa taarifa kama hii ya kutekwa kwa Balozi Adam Mwambapa huwenda kwa baadhi ya maafisa usalama wa hapa wangeipa uzito unaostahili huku wengine wakihisi kuwa ni kama niliyekuwa nimeenda kutoa taarifa za uchochezi baina ya nchi na nchi au baina ya makundi hasimu. Vilevile sikutaka serikali ya Burundi ijihusishe kwa namna yeyote katika suala hili kwa kigezo kuwa katika mazingira nisiyoyaelewa huwenda ushahidi wa tukio hili la kutekwa kwa Balozi Adam Mwambapa ungetoweshwa na vyanzo vyake vyote muhimu vya upelelezi kufutiliwa mbali na hivyo kazi yote kuwa ngumu”. Hidaya akaweka kituo baada ya kumaliza kutoa maelezo yake na kwa kweli alikuwa amenifurahisha sana kiasi cha kulipelekea tabasamu langu jepesi lichomoze usoni taratibu kama miale ya jua la asubuhi.

    “Niseme kuwa umefanya uamuzi mzuri wa busara kwa kuto kutoa taarifa hizi kwa chombo chochote cha usalama cha hapa nchini Burundi kwani hata Chifu amesisitiza kuwa jambo hili lifanyike kwa weledi na usiri wa hali ya juu. Vinginevyo serikali yetu inaweza kulaumiwa kwa kutokuwa makini na usalama wa maafisa wake”. Nikasisitiza kisha baada ya kufikicha macho kidogo nikamuuliza Hidaya.

    “Kuna mtu mwingine yeyote anayefahamu habari hizi za kutekwa kwa Balozi Adam Mwambapa katika ofisi yenu?”CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

     “Hapana nimelazimika kutengeneza taarifa ya uongo inayotanabaisha kuwa Balozi Adam Mwambapa amepata dharura ya kikazi hivyo hatokuwepo hapa ofisini kwa siku kadhaa. Sikupenda mtu yeyote wa hapa ofisini afahamu juu ya suala hili katika hatua ya awali kama hii”. Hidaya akaniambia kwa hakika pasina kuujutia uamuzi wake na kwa kweli hata mimi nilikuwa nimependezwa na uamuzi wake.

    “Chifu analifahamu hilo?”. Nikamuuliza Hidaya katika namna ya kutafuta uhalali

    “Wazo hili limetoka kwake na nimekuwa nikimfahamisha kwa ukaribu kila kitu kinachoendelea hapa nchini Burundi tangu kutokea kwa jaribio hili la mapinduzi ya kijeshi”

     “Umefanya vyema sana”. Nikamwambia Hidaya kisha nikakohoa kidogo kusafisha koo kabla ya kuendelea.

    “Niseme tukio la kutekwa kwa Balozi wetu Adam Mwambapa limenishtua na kunishangaza sana kwani hadi sasa nikifikiria bado sioni sababu yoyote walau ya kuhisi tu inayoweza kuhalalisha tukio la kinyama kama hili”

     “Hata mimi nimeshindwa kuelewa kinachoendelea Tibba”. Hidaya akasisitiza huku akitikisa kichwa chake katika namna ya kuonesha kusikitishwa na tukio lile.

    “Nitajitahidi kufanya kila liwezekanalo katika kuhakikisha kuwa Balozi wetu Adam Mwambapa anapatikana na yeyote aliyehusika na kitendo hiki cha kiharamia ataijutia nafsi yake”. Maelezo yangu yalikuwa ya hakika na kwa namna moja au nyingine yalionekana kumfurahisha sana Hidaya kiasi cha kumpelekea atabasamu na uzuri wake kujidhihirisha vizuri usoni mwake.

    “Kuwa mwangalifu sana Tibba kwani huwenda hali ikawa tofauti kabisa na vile unavyofikiria”. Hidaya akaniambia na kupitia sauti yake tulivu ya kike niliweza kuhisi huruma aliyokuwa nayo juu yangu. Hata hivyo nilimtoa wasiwasi kwa kumwambia.

    “Ondoa shaka Hidaya naamini kuwa Mungu atanisaidia”. Kitambo kifupi cha ukimya kikapita huku kila mmoja akionekana kuzama kwenye tafakuri na wakati hali ile ikiendelea mara nikakumbuka kumuuliza Hidaya.

    “Kuna mtu yeyote aliyefanikiwa kufika nyumbani kwa Balozi Adam Mwambapa baada ya tukio la kutekwa kwake?”

     “Hakuna mtu yeyote aliyefika kwani ni kama nilivyokueleza kuwa hakuna mtu mwingine anayefahamu juu ya tukio hili hapa ofisini isipokuwa mimi peke yangu na Balozi Adam Mwambapa huko alipo. Hidaya akaongea kwa msisitizo na kwa hakika nilimuelewa vizuri. Ukimya kiasi ukapita baina yetu huku kila mmoja akionekana kuzama tena katika fikra zake na kwa kweli tukio la kutekwa kwa Balozi Adam Mwambapa lilikuwa limenishangaza sana.

     Kwa namna moja au nyingine niliamini kuwa watu hao ambao walihusika katika kumteka Balozi Adam Mwambapa walikuwa ni watu wenye uwezo na maarifa ya juu ya medani za kijeshi kwa vile Balozi Adam Mwambapa alikuwa ni kiongozi mstaafu wa jeshi mwenye maarifa ya juu sana ya mapambano. Ingawa bado sikuweza kuhisi lengo la watekaji hao.

     Mwanzoni nilihisi kuwa huwenda watekaji hao walikuwa na lengo la kujiingizia fedha haramu endapo wangejitokeza na kudai malipo kwa ajili ya kumwachia Balozi Adam Mwambapa. Lakini ni kitendo cha kuona kuwa muda unaenda pasipo watekaji hao kujitokeza na kudai fedha kilizidi kunitia mashaka. Ukimya ule ulipokuwa mbioni kushika hatamu Hidaya akaibua hoja.

    “Umefikia kwenye hoteli gani hapa jijini Bujumbura?’. Swali la Hidaya likanipelekea nitabasamu kidogo kabla ya kuvunja ukimya.

    “Mwenyeji wangu ameniambia kuwa anakaa nyumba namba 37 kwenye jengo la shirika la nyumba la taifa kando ya barabara ya Boulevard de I?ndependence. Nyuma ya uwanja wa mpira wa miguu wa Prince Rwegasore Stadium hapa jijini Bujumbura”

     “Mh! mara hii tu ushapata mwenyeji wa kufikia kwenye jiji usilolijua?”. Hidaya akaniuliza huku akiangua kicheko cha kimbea na kuubinua mdomo wake.

    “Mwenyeji wangu anaitwa Veronica. Toto zuri la kirundi lenye vigezo vyote vya kuupoza vyema mtima wangu”. Nikaongea kwa utulivu huku nikiliruhusu tabasamu hafifu kuchanua usoni mwangu. Hidaya akaangua kicheko hafifu cha udaku huku akipiga makofi dhaifu ya kimbea.

    “Mh! Tibba kwa mambo hayo tu mimi sikuwezi. Najua mtoto wa watu atakuwa amebabaishwa na uzuri wako tu vinginevyo huna lolote zaidi ya kumdanganya”

     “Sasa Hidaya nifanyeje wakati mzabuni wa kunipikia chakula kitamu cha kirundi na kunipa huduma nyingine za kimwili na za kiroho keshashinda tenda hiyo moyoni mwangu tena kwa kiwango cha juu”. Nikaongea kwa utulivu huku nikiangua kicheko hafifu na bila shaka Hidaya nilikuwa nimemfikisha mahala pake kwani suala la utani ilikuwa hulka yake hali iliyompelekea azidishe kicheko huku mkono wake mmoja shavuni na mdomo wake kuachama kwa mshangao.

    “Mh! Tibba kweli umeshindikana bora utafute mmoja wa kuoa utakayetulia naye kama mimi ya kaka yako. Tambua kuwa umri unaenda huo!”. Hidaya akaniambia huku machozi ya kicheko yakikaribia kubisha hodi machoni mwake.

    “Kwani kuoa mwisho miaka mingapi wenzangu mliopo kwenye ndoa?”. Nikamchombeza tena utani.

    “Shauri yako!. Wewe kazi yako kuwachezea warembo na kuwaacha kwenye mataa. Yaani kama ndiyo ningekuwa mimi wala nisingekubaliana na huo upuuzi wako”. Hidaya akaongea huku akiyabetua mabega yake.

    “Mh! jamani kwani nimemdanganya au tumekubaliana. Kama atanifaa basi huwenda nikatangaza nia kabisa na wewe ukiwa kama wifi yake mwandamizi basi naamini kuwa hapata haribika jambo”. Maneno yangu yakamuacha Hidaya akiendelea kuangua kicheko cha udaku huku kichwani nikianza kupanga namna ya kuanza rasmi harakati zangu pale jijini Bujumbura. Kile kicheko cha Hidaya kilipokuwa mbioni kukoma akageuka na kuniambia.

    “Chifu aliniambia nikuandalie sehemu nzuri ya malazi pamoja na silaha”

     “Wala usisumbuke Hidaya mimi nitalala kwa mrembo Veronica na kuhusu silaha tayari nimekwishaipata moja ya kuanzia kazi”. Maelezo yangu yakapeleka mshangao wa aina yake usoni kwa Hidaya na hapo kile kicheko chake kikakoma kabisa.

    “Khe! Hiyo silaha umeipata wapi?”. Hidaya akaniuliza huku kanitumbulia macho kwa mshangao.

    “Nimeipata huko njiani nilipotoka”. Jibu langu likatosha kabisa kumfahamisha Hidaya nini nilichokuwa nikimaanisha hivyo haraka akamezea na kubadili mada.

    “Sasa ungependa nikusaidie nini kwa sasa?”

     “Nahitaji usafiri wa uhakika usiokuwa na rekodi ya kesi yoyote ya barabarani”. Nikaongea kwa utulivu huku nikimtazama Hidaya usoni.

    “Kuhusu hilo ondoa shaka. Nyuma ya hili jengo kuna gari moja jeusi aina ya Peugeot 504. Utalitumia kwa muda wote utakao kuwa hapa jijini Bujumbura. Chifu alinifahamisha juu ya hilo mapema wakati tulipozungumza kwa simu hivyo tayari nilikuwa nimekuandalia gari”. Hidaya akaongea kwa utulivu.

    “Nashukuru sana Hidaya”

     “Sema kingine” Hidaya akaniambia huku akinitazama kwa shauku.

    “Ofisi ya Balozi Adam Mwambapa ipo wapi katika hili jengo?’’. Nikamuuliza Hidaya huku nikiitazama saa yangu ya mkononi.

    “Nje ya chumba hiki kuna korido. Ukitoka nje upande wa kushoto mwisho wa korido hiyo utaziona ngazi. Panda hizo ngazi kuelekea ghorofa ya pili na utakapomaliza kupanda hizo ngazi utajikuta ukitazamana na korido pana inayotazamana na milango ya vyumba vya ofisi mbalimbali. Wewe nyoosha moja kwa moja hadi mwisho wa hiyo korido utauona mlango mkubwa wa kijivu. Mlango huo ndiyo wa kuelekea ofisi ya Balozi Adam Mwambapa na juu yake kuna kibao kidogo cheusi chenye maandishi meupe kinachotanabaisha cheo chake”. Maelezo ya Hidaya nikayashika vyema hivyo nikasogeza kiti changu nyuma na kusimama.

    “Ofisi yake ipo wazi?”. Nikamuuliza na hapo nikamuona Hidaya haraka akijipapasa mifukoni na baada ya muda mfupi akawa amepata funguo moja na kunikabidhi mkononi. Nikaipokea ile funguo na kuitia mfukoni kabla ya kumuuliza.

    “Maafisa wenzako hawawezi kunisumbua?”

     “Usijali nitawataarifu kuwa wewe ni fundi wa mashine ya kudurufu iliyopata hitilafu ofisini kwa Balozi”. Uongo wa Hidaya ukanifanya niliruhusu tabasamu hafifu kuchomoza usoni mwangu kwani Hidaya alikuwa msichana mjanja sana na mwerevu.

    “Ngoja nikachunguze huwenda nikapata chochote cha kunisaidia”. Hatimaye nikamwambia Hidaya huku nikimkonyeza kichokozi tukio lililompelekea aangue kicheko kama ilivyokuwa kawaida yake.

    “Usijali Tibba uwanja sasa ni wako unaweza kucheza utakavyo. Ukihitaji msaada wowote usisite kunijulisha mimi nitakuwa pale mapokezi nikisaidiana na wenzangu kuhudumia watu”. Hidaya akaniambia huku na yeye akisogeza kiti chake nyuma na kusimama. Nilipousukuma ule mlango na kutoka nje Hidaya tayari alikuwa nyuma yangu akanipiga ngumi hafifu ya kichokozi mgongoni kisha akashika uelekeo wa upande wa kulia kuelekea ile sehemu ya mapokezi. Nikasimama kidogo nikitabasamu huku nikimtazama Hidaya namna alivyokuwa akitembea kwa mikogo kisha nikaanza kuzitupa hatua zangu taratibu kuelekea mwisho wa ile korido sehemu kulipokuwa na ngazi za kupanda kuelekea ghorofa ya juu ya lile jengo.

     Nilitembea kwa utulivu huku mawazo mengi yakipita kichwani mwangu na nilipozifikia zile ngazi nikaanza kuzipanda na kwa kuwa nilikuwa mgeni wa mazingira yale mara kwa mara nilijikuta nikisimama na kuweka kituo nikitazama huku na kule. Baada ya muda mfupi hatimaye nikamaliza kuzipanda zile ngazi na hapo nikajikuta nikitazamana na korido pana yenye sakafu imara ya tarazo inayotazamana na milango minne. Milango miwili ilikuwa upande wa kushoto na milango miwili mingine ilikuwa upande wa kulia na mwisho wa korido ile kulikuwa na mlango mkubwa wa rangi ya kijivu.

     Kabla ya kukatisha katika korido ile nikageuka na kutazama mwisho wa ngazi zile upande wa kushoto. Kupitia dirisha jembamba la kioo lililokuwa upande ule niliweza kuona mandhari tulivu ya lile jengo yaliyozungukwa na miti mirefu ya kuvutia na bustani nzuri ya maua. Vyote vikiwa ndani ya uzio wa ukuta wenye sistimu maalum ya umeme wa kuzuia wezi. Nje ya ukuta ule niliyaona majengo mengine ya ghorofa yenye nyungo za runinga na minara ya mawasiliano juu yake.

     Nikiwa nimeridhika na uchunguzi wangu wa awali nikaanza kutembea taratibu nikikatisha katikati ya korido ile kuelekea kwenye ule mlango mkubwa wa kijivu uliokuwa mwisho wa ile korido. Kwa kufanya vile nikapata wasaha mzuri wa kuitazama ile milango iliyopakana na ile korido kwa upande wa kulia na kushoto. Kwa kufanya vile nikaweza kuiona ofisi ya afisa mahusiano, ofisi za afisa mkuu anayeshughulika na masuala ya vibali vya ukaaji na pasi za kusafiria pamoja na ofisi ya afisa mkaguzi kupitia utambulisho uliokuwa juu ya milango ile. Hatimaye nikaufikia ule mlango wa kijivu uliokuwa mwisho wa ile korido na kupitia kibao cheusi juu ya mlango ule chenye maandishi meupe nikatambua kuwa ile ilikuwa ni ofisi ya Balozi Adam Mwambapa kama Hidaya alivyokuwa amenielekeza hapo awali.

     Nilipoufikia ule mlango nikakishika kitasa chake na kujaribu kuufungua. Ule mlango ulikuwa umefungwa hivyo sikutaka kutia ufundi mwingine badala yake nikaingiza mkono mfukoni na kuchukua ile funguo niliyopewa na Hidaya. Nilipoupachika ule ufunguo kwenye lile tundu la kitasa na kuuzungusha kabari yake ikafyatuka na hapo nikakizungusha kidogo kile kitasa na kuusukuma ule mlango kwa ndani. Ule mlango ukafunguka na hapo kwa tahadhari nikausukuma na kuingia mle ndani kabla ya kuurudishia nyuma yangu.

     Taswira iliyojengeka machoni mwangu ilikuwa ni ya mandhari tulivu ya ofisi ya kisasa yenye vitu vyote muhimu. Upande wa kushoto kulikuwa na dirisha pana la kioo dirisha hilo lilikuwa limefunikwa kwa mapazia mawili marefu ya rangi ya kijivu. Nilipoyatembeza macho yangu kwa utulivu juu ya lile dirisha nikaziona picha mbili zilizotundikwa ukutani. Picha moja ilikuwa ni ya Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania na picha nyingine ilikuwa ni ya Balozi Adam Mwambapa akiwa katika suti nadhifu nyeusi, shati la kijivu na tai nyeusi. Macho yake tulivu katika sura yake ya umbo duara, pua pana ya kibantu na mdomo uliozungukwa na ndevu zilizokatiwa vizuri vikiongeza ziada nyingine katika wajihi wake.

     Kando ya dirisha lile kulikuwa na meza kubwa ya ofisini yenye majalada mengi juu yake. Bendera ndogo mbili, moja ya taifa la Tanzania na nyingine ya taifa la Burundi. Kitabu kidogo cha katiba ya nchi ya Tanzania. Kidau cha wino, mhuri na kichupa kidogo chenye wino mweupe wa kufutia maandishi.

     Nyuma ya meza ile kulikuwa na kiti kikubwa cha ofisini yenye foronya laini na kiti kile kilikuwa kimetundikwa koti jeusi la suti. Niliendelea kuyatembeza macho yangu kwa utulivu mle ndani na upande wa kulia wa ile meza nikaliona kabati kubwa nadhifu la mbao lenye droo sita. Sakafu ya ofisi ile ilifunikwa kwa zulia maridadi jekundu huku katikati likiwa na mstari mpana wenye rangi za bendera ya taifa la Tanzania.

     Upande wa kushoto kulitundikwa saa kubwa ya ukutani ya mshale na pembeni ya saa ile kulikuwa kalenda moja kubwa. Kando ya dirisha lile mle ndani kulipangwa seti moja ya makochi mazuri ya ngozi laini ya sofa yaliyoizunguka meza ya kioo yenye umbo duara na chini ya meza ile kulikuwa na magazeti na majarida kadhaa tofauti ya huko siku za nyuma. Kando ya makochi yale kulikuwa na rafu kubwa ya vitabu na majalada yaliyopangwa kwa ustadi wa hali ya juu. Kiyoyozi makini kilichokuwa mle ndani kiliendea kusambaza hewa safi.

     Ofisi ilikuwa ya kistaarabu sana yenye samani za kisasa na iliyopangiliwa vizuri ama kwa hakika muonekano wake uliendana kabisa na ule wa hadhi ya ofisi ya balozi. Runinga kubwa ya ukutani iliyounganishwa na chaneli tofauti za kimataifa iliyokuwa ukutani mle ndani ilikuwa imezimwa na katika kona mbili za ile ofisi kulikuwa na maua mazuri ya asili katika vyungu vyake maalum vya udongo, kazi nzuri ya mfinyanzi.

     Nikiwa nimeridhishwa na mandhari nzuri ya ofisi ile yenye hadhi ya juu taratibu nikaanza kutupa hatua zangu nikianza uchunguzi kwenye yale magazeti na majarida yaliyokuwa chini ya ile meza ya kioo mle ndani iliyozungukwa na ile seti ya makochi ya sofa. Nilipofika kwenye ile meza nikaanza kufanya upekuzi. Hata hivyo nilipomaliza upekuzi wangu sikuambulia chochote cha maana kwani yale magazeti na majarida yalikuwa ni ya kawaida kabisa tena matoleo ya siku za nyuma. Hatimaye nikaiacha sehemu ile na kuhamia kwenye ile rafu ya mbao yenye vitabu na majalada chungu mzima nikaanza kufanya upekuzi wangu kwa makini huku nikipekua kila kitabu na jalada na maeneo yote muhimu katika rafu ile. Hata hivyo nilimaliza zoezi lile pasipo kuambulia chochote cha maana kwani vile vitabu na yale majalada vilikuwa ni nyaraka za wazi za sera za mahusiano ya kimataifa. Ajenda za vikao na mikutano iliyofanyika huko siku za nyuma pamoja na masuala ya sheria za kimataifa sera na mipango.

     Hatimaye nikaiacha ile rafu na kuelekea kwenye lile kabati lenye droo sita lililokuwa upande wa kushoto wa ile ofisi. Nilipofika nikaanza kuzifungua zile droo moja baada ya nyingine na kuanza kufanya upekuzi makini na kwa vile droo zile hazikuwa na vizuizi vyovyote kazi ilikuwa rahisi tu. Hata hivyo ndani ya droo zile hapakuwa na kitu chochote cha maana zaidi ya picha za Balozi Adam Mwambapa akiwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa wa Burundi. Picha zile zilikuwa zimepigwa katika maeneo tofauti yenye hadhi ya juu baadhi kwenye hoteli za kifahari na nyingine Ikulu ya Burundi. Hatimaye nikazifunga zile droo na kuhamishia upekuzi wangu kwenye ile meza ya ofisini.

     Nilianza upekuzi kwa kupekua jalada moja baada ya jingine juu ya meza ile lakini pia sikuambulia kitu chochote katika ukomo wa upekuzi wangu hivyo nikahamishia upekuzi wangu kwenye droo tatu za meza ile ya ofisini. Mle ndani ya droo sikuambulia kitu chochote cha maana zaidi ya pini za majalada, gundi ya maji, kalamu mbalimbali za wino na karatasi mbili za kaboni zilizokuwa zimekunjwa vizuri na kuhifadhiwa vyema ndani ya bahasha ya kaki. Hakukuwa na kitu kingine cha maana ambacho kingeweza kunisaidia katika harakati zangu hivyo hatimaye nikazifunga zile droo kama nilivyozikuta. Kisha kwa makini nikayapanga vyema yale majalada pale juu ya meza huku akili yangu ikifikiria upya juu ya nini cha kufanya.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

     Nikiwa katika hali ile mara nikapata wazo fulani wakati nilipolitazama lile koti la suti lililotundikwa kwenye kile kiti cha ofisini. Nikasogea karibu na kulichukua lile koti na kuanza kulipekua mifukoni na wakati nikifanya vile pua yangu ikajikuta ikisumbuliwa kidogo na harufu nzuri ya manukato ya gharama yaliyopuliziwa kwenye koti lile. Lilikuwa ni koti zuri la suti lenye vifungo vinne la brandi ya daraja la kwanza kwa ubora na sikuwa na mashaka yoyote kuwa koti lile la suti lilikuwa ni la Balozi Adam Mwambapa. Hata hivyo nilipomaliza upekuzi wangu sikuambulia kitu chochote cha maana zaidi ya pakiti moja ya sigara aina ya Marlboro iliyokuwa na sigara mbili ndani yake pamoja na kibiriti kimoja cha gesi na hapo nikahitimisha kuwa Balozi Adam Mwambapa alikuwa mvutaji wa sigara. Hatimaye nikalirudishia lile koti la suti mahala pake huku akili yangu ikianza kuhisi kushindwa.

     Mwishowe nikasimama na kuitia mikono yangu mifukoni kwa utulivu huku nikianza upya kuishughulisha akili yangu. Pembeni ya ile meza ya ofisini chini yake kulikuwa na mashine ndogo ya digital ya kurudufu, printer, scanner na mashine moja ya fax. Nilijaribu kuifanyia upekuzi mashine moja baada ya nyingine nikijaribu kupekua karatasi zilizokuwa ndani yake nikichunguza kama ningeweza kupata kitu chochote muhimu cha kunisaidia. Sikupata kitu chochote cha kunisaidia na kwa kutaka kujiridhisha zaidi nikaiwasha ile kompyuta ya pale mezani ili kuchunguza kama kungekuwa na nyaraka zozote zilizokuwa zimefanyiwa kazi kupitia ile mashine ya kurudufu, printer, scanner na ile mashine ya fax. Hata hivyo jitihada zangu ziligonga mwamba kwani ile kompyuta ilikuwa imefungwa kwa password inayofahamika na mtumiaji pekee wa ile kompyuta ambaye bila shaka alikuwa ni Balozi Adam Mwambapa. Nikaanza kuhisi kuwa upekuzi wangu ulikuwa hauelekei kuniletea manufaa yoyote hivyo nikaizima ile kompyuta na kuanza kutembeatembea mle ndani katika namna ya kufikiri zaidi nini cha kufanya.

     Nikiwa katika hali ile mara wazo fulani likawa limenijia kichwani baada ya kuikumbuka ile simu ya mezani iliyokuwa pale juu ya ile meza ya ofisini mle ndani. Nilipoikaribia ile meza na kuichunguza ile simu kwa utulivu nikagundua kuwa mfumo wa mawasiliano wa ile simu ulikuwa ni ule wa kizamani unaotumia sistimu ya Landline. Hali ile ikanipa matumaini hivyo nikakichukua kiwambo cha ile simu na kukiweka sikioni katika namna ya kujaribu kama ile simu ilikuwa ikitumika au lah!. Kwa kufanya vile nikagundua kuwa ile simu bado ilikuwa ikitumika.

     Wakati nilipokuwa nikikirudisha kile kiwambo cha simu mahala pake ghafla nikashtuka baada ya kuuona ule mlango wa ile ofisi ukifunguliwa. Tukio lile likapelekea haraka niupeleke mkono wangu mafichoni kuikamata bastola yangu lakini kitendo cha kumuona Hidaya akiingia mle ndani kikabadili dhamira yangu na hapo nikahitimisha kwa kuweka kile kiwambo cha simu mahala pake huku uso wangu ukitengeneza tabasamu la kirafiki...



    “Vipi Tibba?”. Hidaya akawahi kuniuliza huku akiurudishia vizuri ule mlango kabla ya kuanza kutembea taratibu kuja pale niliposimama.

    “Poa”. Nikamwitikia Hidaya huku nikimtazama kwa sura ya kirafiki.

    “Nimehisi kuwa pengine ukahitaji msaada wowote kutoka kwangu”

     “Unaweza kuzungumza na opareta wa hii simu na kumuomba akupe orodha ya simu zote zilizoingia na kutoka kwa muda wa wiki mbili zilizopita?’’. Ombi langu likampelekea Hidaya anitazame kidogo kwa mshangao kabla ya kuniambia.

    “Unadhani hiyo itasaidia kitu?”

     “Sina hakika”. Nikamwambia Hidaya huku nikitabasamu.

    “Okay! basi nipe dakika chache tu naelekea idara ya mawasiliano”. Hidaya akaniambia kisha pasipo kusubiri wazo jingine kutoka kwangu muda uleule nikamuona akielekea mahali ulipokuwa mlango wa ile ofisi kisha akaufungua na kutokomea nje. Kwa sekunde chache zilizofuata nikaendelea kuutazama ule mlango wa ile ofisi kwa utulivu huku akili yangu ikiwa mbali kabisa na eneo lile. Hatimaye nikageuka na kuelekea dirishani.

     Nilipofika pale dirishani nikasogeza pazia pembeni na kupitia ukuta msafi wa kioo nikaweza kuona vizuri mandhari ya nje ya lile jengo. Ile ofisi ilikuwa ikitazamana na ile barabara iliyokuwa ikikatisha mbele ya lile jengo la ubalozi wa Tanzania nchini Burundi na baada ya kuvuka ile barabara upande wa pili kulikuwa na jengo lingine refu la ghorofa. Kwa dakika kadhaa nikatulia pale dirishani huku nikilitazama jengo lile refu la ghorofa kumi na mbili na kujiuliza kuwa lilikuwa likitumika kwa shughuli gani. Nikaendelea kulichunguza lile jengo kwa utulivu huku mikono yangu nikiwa nimeigemeza pale dirishani. Chini ya lile jengo kulikuwa na magari machache yalioegeshwa katika sehemu ya maegesho ya magari ya lile jengo. Nilipoyachunguza vizuri yale magari yaliyoegeshwa pale chini nikagundua kuwa yote yalielekea kuwa ni ya watu binafsi kutokana na utambulisho wa namba zake.

     Vyumba vingi vya lile jengo la ghorofa lililokuwa upande wa pili wa ile barabara vioo vyake vilikuwa vyeusi na vinavyoakisi vizuri taswira ya vitu vya nje na hivyo kutomruhusu mtu yeyote kuona mle ndani kwa urahisi. Hata hivyo bado kulikuwa na vyumba vichache katika ghorofa ya sita na ya nane ambavyo vioo vyake havikuwa vyeusi kama ilivyokuwa kwa vile vingine. Hivyo kwa kuendelea kununua muda huku nikimsubiri Hidaya arudi kule alipoenda nikapeleka macho yangu kutazama vile vyumba ambavyo vioo vyake havikuwa vyeusi na kwa kufanya vile nikaweza kuona japo kwa shida kidogo ndani ya vile vyumba vya lile jengo. Baadhi ya vile vyumba vya lile jengo madirisha yake yalikuwa yamefunikwa kwa mapazia hivyo sikufanikiwa kuona kitu chochote mle ndani. Lakini vile vyumba ambavyo madirisha yake yalikuwa hayajafunikwa kwa mapazia niliweza kuona vifaa vya ofisini kama meza na viti vyake, makabati ya kutunzia nyaraka, rafu za chuma, kompyuta na vitu vingine vidogovidogo vya kiofisi.

     Ndani ya vile vyumba nikawaona baadhi ya wafanyakazi wakiwa wanaendelea na shughuli zao. Wengine wakiwa wameinamia kompyuta zao mezani na wengine wakipitia taarifa kwenye majalada ya ofisini. Alimradi kila mmoja alikuwa amezama kwenye hamsini zake na hakuna aliyekuwa akitazama pale dirishani nilipokuwa nimesimama jambo ambalo lilinipa uhuru wa kuwatazama vizuri wale watu.

     Niliendelea kuvichunguza vyumba vile vya ofisi huku macho yangu taratibu yakihama kutoka kwenye floo moja ya ghorofa na kuhamia kwenye floo nyingine ya ghorofa za jengo lile. Hatimaye macho yangu yakaweka kituo kwenye chumba kimoja kilichokuwa kwenye kona ya kushoto ya floo ya nane ya lile jengo baada ya kumuona mwanaume mmoja akiwa amesimama kando ya pazia la chumba kile lililofunguliwa nusu na kuachwa wazi. Ingawa kulikuwa na umbali mrefu kiasi kutoka pale dirishani niliposimama hadi lilipokuwa lile jengo la ghorofa lakini bado niliweza kuona vizuri ndani ya kile chumba. Mtu yule mrefu alikuwa amelisogeza kidogo pazia la chumba kile huku akinitazama kwa makini pale dirishani nilipokuwa nimesimama. Macho yangu yakaweka kituo kumtazama vizuri yule mtu na nilipomchunguza kwa makini nikagundua kuwa mkononi alikuwa ameshika kitu ambacho sikuweza kukiona vizuri kutokana na vile alivyokuwa amesimama pale dirishani.

     Macho yangu yakiwa yameweka kituo kumtazama kwa makini yule mtu pale dirishani taratibu fikra zangu zikaanza kuzama kwenye tafakuri ya kina nikijiuliza kuwa yule mtu ni nani alikuwa akifanya nini pale dirishani. Hata hivyo sikufika mbali kwenye uchunguzi wangu kwani mara moja moja mawazo yangu yakahamishwa haraka na tukio la mlango wa ile ofisi kufunguliwa. Nilipogeuka na kutazama pale mlangoni nikamuona Hidaya akiingia huku mkononi akiwa ameshika karatasi yenye maelezo fulani. Uso wangu ukaumba tabasamu la kirafiki huku nikimkaribisha Hidaya kwa ishara halafu haraka nikageuka pale dirishani na kurudia kutazama tena kwenye kile chumba alichokuwa amesimama yule mtu kwenye lile jengo la ghorofa lililokuwa upande wa pili wa ile barabara.

     Hata hivyo uchunguzi wangu ule wa mara ya pili ukanipelekea nijikute nikikabiliana na mshtuko usioelezeka. Yule mtu kwenye kile chumba cha ghorofa la upande wa pili wa ile barabara hakuwepo tena pale dirishani kama alivyokuwa amesimama pale awali na pazia nalo lilikuwa limerudishiwa vizuri pale dirishani kiasi cha kuninyima upenyo wa kuweza kuona ndani ya kile chumba. Kwa sekunde kadhaa akili yangu ikashikwa na mduwao huku hisia mbaya zikaanza kuutafuna mtima wangu taratibu. Hata hivyo sikukata tamaa badala nikaendelea kutazama pale dirisha huku nikitarajia kuona lile pazia la kile chumba likifunguliwa na yule mtu kujitokeza tena. Baada ya kitambo kirefu kupita nafsi yangu ikaniambia kuwa nilikuwa nikijifariji bure tu kwani jambo lile lisingewezekana kutokea. Moyo wangu ukajifunza haraka kukabiliana na hali ile na nilipofanikiwa kuumeza vizuri mshtuko wangu nikageuka na kumtazama Hidaya aliyekuwa tayari amefika na kusimama kando yangu huku usoni nikiumba tabasamu hafifu la kirafiki.

    “Samahani Tibba utanisamehe kwa kuchelewa kidogo”. Hidaya akavunja ukimya hata hivyo sikuona kama alikuwa amechelewa sana kama mwenyewe alivyojinasibisha.

    “Usijali Hidaya kwanza nilidhani kuwa ni zoezi ambalo lingechukuwa muda mwingi zaidi ya huu ulioutumia”. Nikaongea kwa utulivu na hapo Hidaya akasogea karibu zaidi na kunionesha ile karatasi aliyoishika mkononi. Ilikuwa ni karatasi yenye rekodi zinazo onesha muda na siku ambazo ile simu ya mezani ya mle ofisini kwa Balozi Adam Mwambapa ilikuwa imetumika kupigwa na kupiga kwenda maeneo tofauti ya ndani na nje ya nchi ya Burundi kwa muda wa wiki mbili zilizopita. Kabla ya kutazama vizuri rekodi zile nikarudishia kwanza lile pazia na kufunika vizuri lile dirisha kisha nikaipokea ile karatasi mkononi mwa Hidaya na kuanza kuzipitia kwa makini rekodi zile za opareta wa idara ya mawasiliano.

     Kulikuwa na simu chache zilizoingia na kutoka kwa kipindi cha juma moja lililopita na nilipochunguza kwa makini nikagundua kuwa mawasiliano yale yalikuwa yamefanyika baina ya ofisi ile ya balozi wa Tanzania nchini Burundi na kurugenzi ya mahusiano ya kimataifa ya Ikulu ya Burundi. Mawasiliano mengine yaliyofanyika yalikuwa ni baina ya ofisi ya waziri wa mambo ya nje wa nchi ya Burundi na Ikulu ya Tanzania jijini Dar es Salaam.

     Kupitia rekodi zile nikatafakari na kujiridhisha kuwa aina yoyote ya mawasiliano ambayo yalikuwa yamefanyika baina ya ofisi ile ya balozi wa Tanzania nchini Burundi na zile idara nyingine za serikali kwa vyovyote yalielekea kuwa ya kawaida na yalikuwa ni ya taratibu za kiutendaji za ofisi ile hivyo sikuyatilia mashaka yoyote.

     Juma la pili hadi kuelekea jaribio la mapinduzi ya kijeshi nchini Burundi kwa kupitia rekodi zilizokuwa kwenye ile karatasi nikagundua kuwa kulikuwa na mawasiliano mengi yaliyokuwa yamefanyika kupitia ile simu ya mezani ya mle ndani ofisini kwa Balozi Adam Mwambapa. Simu za kuingia na za kutoka. Hata hivyo nilipojaribu kufuatilia mawasiliano yale yalipoishia nikagundua kuwa mawasiliano yale mengi yalikuwa ni yenye mwelekeo wa kikazi kutokana na ofisi ambazo yalikuwa yamefanyikia.

     Hata hivyo wakati nikiendelea kuchunguza mara nikagundua kuwa kulikuwa na sehemu moja iliyonivuta na kuamsha upya hisia zangu ambapo simu ile ya mezani ya mle ndani ofisini ilikuwa imetumika kufanya mawasiliano. Sehemu hiyo ilikuwa ni katika hoteli moja maarufu ya kimataifa iitwayo Le Tulip Hôtel Africaine iliyokuwa ikimilikiwa na mfanyabiashara mmoja wa kifaransa iliyopo pembezoni kidogo mwa jiji la Bujumbura.

     Nilipoendelea kuchunguza zaidi nikagundua kuwa muda wa siku mbili zilizopita kabla ya kuelekea kwenye jaribio lile la mapinduzi ya kijeshi nchini Burundi simu ile ya mezani mle ndani ofisini kwa Balozi Adam Mwambapa ilikuwa imetumika kufanya mawasiliano mengi zaidi kuelekea Le Tulip Hôtel Africaine kuliko sehemu nyingine yoyote hali iliyopelekea kuibuka kwa maswali mengi kichwani mwangu.

    “Vipi Tibba kuna jambo lolote umelishuku?”. Swali la Hidaya likanipelekea nigeuke kidogo na kumtazama huku uso wangu ukishindwa kuonesha tashwishwi yoyote. Nilimfahamu Hidaya kama mwanausalama makini na msichana aliyekuwa akiipenda sana kazi yangu ya ujasusi lakini hata hivyo sikuona kama kulikuwa na haja ya kumuelezea kila jambo juu ya hisia zangu katika tukio lile.

    “Mh! kwa sasa ni mapema sana kuzungumza lolote. Nadhani kuna mambo mawili matatu nitahitajika kwanza kuyafanyia kazi ambayo huwenda yakanipa mwelekeo sahihi juu ya nini kilichojificha nyuma ya tukio hili la kutekwa kwa balozi wetu Adam Mwambapa”. Nikaongea kwa utulivu huku nikimshika Hidaya begani ingawa fikra zangu zilikuwa mbali kabisa na eneo lile.

    “Nakuombea sana mafanikio katika harakati zako Tibba ili wale wote waliohusika na tukio hili wakione cha mtema kuni. Vilevile hii iwe fundisho kwa wengine wanaofikiria kufanya kitu cha namna hii”. Hidaya akaongea kwa utulivu ingawa maneno yake yalionekana dhahiri kuhifadhi chuki na hasira dhidi ya kitendo kile cha utekaji.

    “Kutekwa kwa Balozi Adam Mwambapa ni pigo kubwa la kiusalama na udhalilishaji kwa taifa letu. Kamwe vitendo vya namna hii haviwezi kuvumilika kokote ulimwenguni”. Hidaya akaongea kwa gadhabu huku akimeza funda la mate kulitowesha donge kubwa la hasira lililomnasa kooni. Kitambo kifupi cha ukimya kikafuatia huku kila mmoja akijitahidi kuidhibiti vyema hasira iliyokuwa ikifurukuta nafsini mwake. Ukimya ule ulipokuwa mbioni kuota mizizi mle ofisini nikageuka na kumtazama Hidaya kwa utulivu kando yangu kabla ya kamuuliza.

    “Nijuavyo mimi ni kuwa balozi anapaswa kukaa kwenye nyumba yake iliyopo kwenye hili jengo. Sasa imekuwaje Balozi Adam Mwambapa akakaa nje ya eneo hili?”. Swali langu likampelekea Hidaya atabasamu kidogo kama mtu mzima aliyeulizwa swali la kitoto.

    “Nyumba ya balozi inafanyiwa ukarabati hivyo serikali iliamua kukodi nyumba ya nje itakayotumika kama makazi yake hadi hapo ukarabati huo utakapokamilika”. Hidaya akaongea kwa hakika huku akinitazama.

    “Nyumba ya balozi iko wapi kwenye hili jengo?”

     “Juu ghorofa ya tatu”

     “Naweza kuikagua?”

     “Hakuna chochote unachoweza kupata”. Hidaya akaongea huku akiyabetua mabega yake.

    “Kwanini unasema hivyo?”CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

     “Ndani ya nyumba ya balozi kwenye hili jengo hakuna kitu chochote. Mafundi tu ndiyo wanaondelea na ukarabati”. Jibu la Hidaya likanipelekea nimtazame kwa kitambo huku nikitafakari. Ukimya ule ulipokuwa mbioni kushika hatamu nikanyanyua mkono kuitazama saa yangu ya mkononi halafu kama niliyeshtukia kuwa muda ulikuwa ukisonga nikavunja ukimya.

    “Noamba uniruhusu niondoke Hidaya kwani tukiendelea kukaa humu ndani hatutapata majibu”. Kama ambaye ameshtushwa na wazo langu Hidaya akageuka haraka na kunitazama kwa shauku.

    “Unaelekea wapi Tibba?”. Hidaya akaniuliza kwa sauti ya upweke.

    “Boulevard du 28 Novembre nyumbani kwa Balozi Adam Mwambapa”

     “Kuwa mwangalifu sana Tibba kwani yeyote aliyehusika na kitendo hiki haelekei kuwa ni mtu wa kawaida”. Hidaya akanionya.

    “Usijali Hidaya nitakuwa mwangalifu. Utakapoongea na Chifu utamueleza kuwa tumeonana mengine tutaendelea kufahamishana pale itakapobidi”. Nikamwambia Hidaya nikishikana naye mkono wa kuagana huku tabasamu langu la kikazi likiumbika vizuri usoni mwangu. Hidaya hakusema neno lolote badala yake akaingiza mkono wake mfukoni na kutoa kadi ndogo ambayo alinikabidhi mkononi.

    “Ukihitaji msaada wowote utanitafuta kupitia hii kadi”. Hidaya akaniambia kwa utulivu na bila kusema chochote nikaichukua ile kadi na kuipitishia macho kisha nikaitia mfukoni.

    “Ahsante sana Hidaya”. Nikamwambia Hidaya huku nikimshika tena begani katika namna ya kumtoa hofu juu yangu kisha nikaanza kuzitupa hatua zangu kwa utulivu nikielekea kwenye ule mlango wa ile ofisi.

    “Kila la kheri Tibba”

     “Ahsante Hidaya tutaonana Mungu akipenda”

    Nikaendelea kutembea kwa utulivu huku nikiwa na hakika kuwa macho ya Hidaya yalikuwa nyuma yangu yakinisindikiza. Hata hivyo sikugeuka nyuma badala yake nilipoufikia ule mlango wa ile ofisi nikaufungua na kutoka nje.

     Akili yangu ikiwa imeanza kupata afya njema huku matendo yangu yakiwa yameanza kutawaliwa na hisia sikuona sababu ya kuendelea kupoteza muda wangu kwenye ofisi ile. Hivyo mara baada ya kutoka kwenye ile ofisi ya Balozi Adam Mwambapa nikaurudishia ule mlango nyuma yangu na kuanza kukatisha kwa utulivu kwenye ile korido kuelekea kwenye zile ngazi za kushukia ghorofa ya chini.

     Muda mfupi baadaye nilikuwa nikikatisha kwenye ile kaunta ya mapokezi kuelekea nje na wakati nikifanya vile nikagundua kuwa idadi ya watu waliokuwa wakihitaji huduma kwenye ofisi zile ilikuwa imeongezeka maradufu na hivyo kupelekea msongamano mkubwa wa watu eneo lile. Nilipofika pale mapokezi nikatumia dakika chache kuwaaga wale maafisa uhamiaji ambao pale awali nilikuwa nimesalimiana nao kisha nikapenya katikati ya kundi la watu na kutoka nje.

     Kitendo cha kumkumbuka yule mtu aliyekuwa akinitazama kupitia dirisha la kile chumba kilichokuwa kwenye kona ya lile jengo la ghorofa lililokuwa upande wa pili wa ile barabara iliyokuwa ikikatisha mbele ya ofisi zile za ubalozi wa Tanzania nchini Burundi kikawa kimenikumbusha kuwa mwangalifu.

     Kulikuwa na msongamano mkubwa wa watu na magari nje ya ofisi zile za ubalozi waliofika kufuata msaada wa kidiplomasia na nilipowachunguza watu wale nikagundua kuwa wengi wao walikuwa ni raia wa nchini Tanzania waliokuwa wakiishi na kufanya kazi nchini Burundi. Nyuso zao zilionekana dhahiri kushikwa na hofu na mashaka juu ya hatima ya usalama wa maisha yao baada ya lile jaribio la mapinduzi ya kijeshi kufanyika...



    Niliishusha vyema kofia kuufunika uso wangu wakati nilipokuwa nikikatisha katikati ya kundi kubwa la watu lililokuwa pale nje ya ofisi zile za ubalozi nikielekea upande wa kushoto wa lile jengo. Hata hivyo wakati nikifanya vile macho yangu yalikuwa makini zaidi kuzichunguza sura za watu na mijongeo yao. Nilipofika kwenye kona ya lile jengo nikaingia upande wa kushoto nikielekea eneo la nyuma la ofisi zile sehemu kulipokuwa na maegesho ya magari ya wafanyakazi.

     Muda mfupi uliofuata nikawa nimefika nyuma ya lile jengo la ubalozi na baada ya kuyatembeza macho yangu kwa utulivu huku na kule mara nikawa nimeliona gari moja dogo na madhubuti la mtindo wa kizamani aina ya Peugeot 504 kama Hidaya alivyokuwa amenielekeza hapo awali. Gari lile jeusi lilikuwa na vioo vyeusi vinavyoweza kumuwezesha mtu aliyeko ndani kuweza kuona nje pasipo usumbufu wowote huku mtu aliyeko nje akishindwa kuona mle ndani. Gari lile lilikuwa limefungwa magurudumu mapya na madhubuti yanayoweza kuhimili vizuri mikikimikiki na rabsha za aina yeyote katika barabara korofi. Lile gari lilikuwa limeegeshwa kwenye eneo maalum lenye utambulisho wa cheo cha balozi huku kando yake kukiwa na kibao kidogo cheupe chenye maandishi meusi yanayosomeka “This Parking Lot Is Reserved For The Ambassador Only” na hivyo kupelekea gari lile kuonekana limejitenga na magari mengine yaliyokuwa yameegeshwa eneo lile.

     Moyoni nikamshukuru sana Hidaya kwa kunifanyia maandalizi motomoto ya kazi yangu. Muda mfupi uliofuata nikawa nimelifikia lile gari kisha baada ya kujaribu kufungua mlango wa dereva nikafanikiwa kiulaini kwani mlango ule ulikuwa haujafungwa hivyo nikaingia mle ndani. Mara tu nilipoingia mle ndani nikakumbuka kuwa sikuwa nimechukua funguo ya lile gari kutoka kwa Hidaya lakini mara moja tu nilipochungulia kwenye swichi iliyokuwa chini ya usukani nikajikuta nikitabasamu baada ya kuiona funguo ya gari ikiwa mahala pake. Hapakuwa na muda wa kuendelea kupoteza zaidi hivyo nikafunga mlango na kuvaa mkanda wa siti. Dakika chache zilizofuata nikaitoa ile gari kwenye maegesho na kuzunguka nikielekea kule upande wa mbele wa lile jengo la ubalozi kwenye geti la kutokea. Kitu kilichonishangaza ni kuwa walinzi wa ofisi zile hawakunisimamisha na hapo nikahidi kuwa huwenda Hidaya tayari alikuwa amenisafishia njia.

     Muda mfupi uliofuata nikawa tayari nimetoka kwenye lile eneo la ofisi za ubalozi wa Tanzania nchini Burundi na kuingia barabarani. Mshale wa mafuta kwenye dashibodi ya lile gari ulionesha kuwa lile gari lilikuwa na mafuta ya kutosha kiasi cha kufanikiwa kunitoa wasiwasi kuwa mizunguko yangu isingekwamia njiani jambo ambalo lilinifurahisha sana.

     Sikutaka kupita kwenye ile barabara niliyopita pale awali hivyo mara baada ya kuingia kwenye ile barabara iliyokuwa ikikatisha mbele ya zile ofisi za ubalozi nikashika uelekeo wa upande wa kushoto halafu baada ya mwendo mfupi wa safari yangu nikachepuka tena na kuingia upande wa kulia nikiifuata barabara ya Avenue de Gihungwe. Haikuwa barabara yenye msongamano mkubwa wa magari hivyo mwendo wangu ulikuwa wa kuridhisha. Nilipoitupia macho saa yangu ya mkononi nikagundua kuwa ilikuwa ikielekea kutimia saa nane mchana. Jua lilikuwa limeshamiri japokuwa hali ya hewa ya joto la jiji la Bujumbura haikuwa kama ile ya jiji la Dar es Salaam nchini Tanzania.

     Hatimaye nikaupeleka mkono wangu mafichoni kuipapasa bastola yangu na nilipojiridhisha kuwa bado ilikuwa mahali salama nikafyatua kofia ya kujikinga na jua juu yangu kisha nikabandika ile ramani yangu ndogo ya kijasusi ili nisisumbuke sana wakati nitakapohitaji kuitazama.

     Wakati nikiendelea na safari yangu nikagundua kuwa mitaa mingi ya jiji la Bujumbura iliyokuwa na ofisi za serikali kwa muda ule ilikuwa ikilindwa na wanajeshi watiifu wa serikali ya Rais Pierre Nkurunziza. Wanajeshi wale walikuwa wamesambaa kila kona katika namna ya mkakati wa kuzima maandamano ya raia waliokuwa wakiipinga serikali iliyopo madarakani lakini vilevile katika kuhakikisha kuwa vitendo vya uvunjifu wa amani vinakomeshwa mara moja na nchi inarudi katika hali yake ya usalama haraka iwezekanavyo.

     Nilipoendelea kuchunguza nikagundua kuwa kulikuwa na vikwazo vingi vya barabarani vilivyowekwa kwa makusudi na wanajeshi watiifu wa serikali katika namna ya kurahisisha upekuzi wa magari yaliyokuwa yakiingia na kutoka jijini Bujumbura tangu kutokea kwa jaribio lile la mapinduzi ya kijeshi. Lengo kubwa likiwa ni kuzuia mamluki wa jaribio lile la mapinduzi ya kijeshi kuingia au kutoroka jijini Bunjumbura. Hata hivyo gari langu halikusimamishwa barabarani kizembezembe na ile ilitokana na nembo ndogo ya kidipromasia yenye utambulisho wa ubalozi wa Tanzania nchini Burundi iliyokuwa imebandikwa ubavuni mwa lile gari. Hali ile ikanipelekea nikitabasamu huku moyoni nikimpongeza Hidaya kwa kuniandalia mazingira mazuri ya ufanyaji wa kazi yangu.

     Baada ya safari fupi mbele kidogo nikaiacha ile barabara Avenue de Gihungwe na kuingia upande wa kushoto nikiifuata barabara ya Boulevard De la Liberte. Ilikuwa barabara pana yenye kiasi kikubwa cha magari na iliyokuwa ikikatisha katikati ya majengo marefu ya ghorofa yenye ofisi za kimataifa zenye utulivu wa hali ya juu na nje ya majengo yale magari machache yalionekana kuegeshwa katika maeneo maalum ya maegesho. Nikaendelea mbele na safari yangu huku nikifanya tathmini nzuri ya barabara ile iliyoonekana kuwa na watu wachache watembea kwa miguu.

     Baada ya mwendo mfupi wa safari yangu mbele kidogo nikaiacha barabara ile na kuchepukia upande wa kulia nikiifuata barabara ya Avenue Des Euphorbes lakini mara moja nikajikuta nikishikwa na mshtuko. Mara tu baada ya kuingia kwenye barabara ile kupitia vioo vya ubavuni vya gari langu nikawa nimeliona gari moja jeupe aina ya Landcruiser Hardtop likiwa kiasi cha umbali usiopungua mita mia moja nyuma yangu. Ingawa sikuwa na hakika kama gari lile lilikuwa likinifungia mkia au lah! lakini akili yangu ilianza kupoteza utulivu taratibu kadiri nilivyokuwa nikiendelea kulitazama gari lile kupitia vile vioo vya ubavuni vya gari.

     Nilikuwa nimepanga kuwa mara nitakapofika mbele ningeingia barabara ya RN 7 na baada ya kuuvuka mzunguko wa barabara hiyo ningeingia upande wa kushoto kuifuata barabara ya Boulevard du 28 Novembre ambapo mbele yake ningechepuka tena na kuingia kwenye barabara za mitaa mingine ambazo hatimaye zingekuja kunikutanisha na ile barabara kuu ya Chaussée P.L.Rwagasore hadi kwenye nyumba namba 26 yalipokuwa maskani ya Balozi Adam Mwambapa. Lakini kitendo cha kuliona lile gari jeupe Landcruiser Hardtop nyuma yangu kikanipelekea nibadili uelekeo.

     Hivyo nilipoifikia ile barabara ya RN 7 sikuingia upande wa kulia kuifuata ile barabara badala yake nikakatisha na kuingia barabara ya Avenue des Chênes. Kitendo cha kuingia kwenye barabara ile kikalipelekea lile gari jeupe Landcruiser Hardtop nalo likatishe kwenye ile barabara ya RN 7 na kushika uelekeo wangu japokuwa lilikawia kidogo baada ya kusubiri magari machache yakatishe kwanza kwenye barabara ile. Tukio lile bado lisingekuwa kigezo cha kuniridhisha kuwa sasa nilikuwa nimefungiwa mkia hata hivyo kwa namna nyingine ile ilikuwa ni ishara mojawapo ya kunitahadharisha kuwa nilipaswa kuwa makini na mienendo yangu.

     Mara hii nilijikuta nikilitazama lile gari kwa utulivu wa hali ya juu katika namna ya kutafuta hakika kama nilikuwa nikifungiwa mkia na lah!. Hivyo baada ya mwendo mfupi wa safari yangu nikaiacha barabara ile na kuchepuka upande wa kushoto nikiifuata barabara ya Avenue Des Mimosas. Niliendelea kuendesha gari katika barabara ile huku kijasho chepesi kikianza kunitoka usoni. Moyo wangu nao ukawa umeanza kupoteza utulivu hata hivyo kwa kila hali nilijitahidi kupambana kikamilifu na hali ile.

     Akili yangu ikiwa mbioni kupoteza utulivu sasa nilikuwa makini sana kulichunguza lile gari kupitia vile vioo vya ubavuni. Hata hivyo lile gari halikujitokeza mapema hadi pale nilipokuwa mbioni kufikia mwisho wa barabara ile. Nilipenda kutafuta hakika juu ya hisia zangu hivyo nilipofika mwisho wa barabara ile nikachepuka upande wa kulia nikiifuata barabara ya Avenue Des Non Aligens. Ilikuwa barabara pana iliyokuwa ikikatisha katikati makazi ya watu na hapakuwa na msongamano mkubwa wa magari katika barabara ile hivyo niliamua kuongeza mwendo. Kwa kufanya vile haukupita muda mrefu mara nikaliona lile gari Landcruiser Hardtop jeupe likiingia kwenye ile barabara na kushika uelekeo wangu.

     Bado sikutaka kujipa hakika kuwa lile gari lilikuwa likinifungia mkia hivyo kwa kutafuta hakika zaidi baada ya safari ndefu katika barabara ile hatimaye mbele nikaja kukutana na barabara ya Avenue Pierre Ngendandumwe. Nilipoifikia barabara ile nikakunja kona na kuingia upande wa kulia nikiifuata barabara ile kwa utulivu lakini vilevile nikipunguza mwendo wangu kwa kasi. Ilikuwa ni barabara yenye pilikapilika nyingi za magari na watembea kwa miguu hivyo hali ile niliipenda kwa jambo moja kwani lingekuwa ni jambo rahisi kwangu kufanya uchunguzi juu ya lile gari nililohisi kuwa lilikuwa likinifungia mkia.

     Haukupita muda mrefu mara nikaliona lile gari Landcruiser Hardtop jeupe likiingia kwenye ile barabara na kufuata uelekeo wangu. Kitendo kile kikanipelekea nitabasamu kidogo baada ya kuridhishwa vizuri na tathmini za hisia zangu. Sasa nilihitimisha kuwa lile gari Landcruiser Hardtop jeupe nyuma yangu lilikuwa kazini kunifungia mkia kama nilivyokuwa nimehisi pale awali.

     Nilipofika mwisho wa ile barabara ya Avenue Pierre Ngendandumwe nikachepuka na kuingia upande wa kushoto nikiifuata barabara ya Avenue de Muramvya halafu nilipofika mbele kidogo nikachepuka na kuingia upande wa kulia nikiifuata barabara ya Avenue D?Octobre. Nilipoingia kwenye ile barabara nikaongeza mwendo lakini lile gari jeupe Landcruiser Hardtop halikuniacha nifike mbali nyuma yangu na badala yake nikaliona likiongeza mwendo kunifuata.

     Sikutaka mtu au watu waliokuwa ndani ya lile gari jeupe Landcruiser Hardtop nyuma yangu wafahamu nilipokuwa nikielekea. Hivyo mara tu nilipoyapita makutano ya barabara ya Avenue des Travailleurs mbele kidogo nikaingia barabara ya Boulevard du 28 Novembre na kushika uelekeo wa upande wa kulia na hivyo kushika uelekeo wa kurudi kule nilipotoka.

     Kitendo cha kuingia kwenye ile barabara ya Boulevard du 28 Novembre kikanipelekea niongeze mwendo zaidi huku akili yangu ikisumbuka katika kutafuta namna ya kukabiliana na lile gari lililonifungia mkia nyuma yangu. Baada ya kufikiri kwa muda hatimaye nikawa nimepata wazo kuwa mara baada ya kuufikia ule mzunguko wa barabara wa RN 7 ningeshika uelekeo wa upande kushoto nikiifuata barabara ya Chaussée de Gitega kuelekea eneo liitwalo Muha lililojitenga kidogo na makazi ya watu. Nikiamini kuwa nikiwa huko ningeweza kukabiliana vizuri na mtu au watu waliokuwa ndani ya lile gari. Hata hivyo mawazo yangu yalikatishwa haraka na kizuizi cha barabarani kilichokuwa katika makutano ya barabara ya Boulevard du 28 Novembre na barabara ya Avenue de Muramvya.

     Haraka nikapunguza mwendo wa gari baada ya kumuona askari jeshi mmoja akijitokeza na kusimama katikati ya barabara ile akinioneshea ishara kwa mkono wake kuwa nisimame huku mkono wake mmoja akiwa ameikamata vyema bunduki yake SMG. Kwa kweli lilikuwa ni tukio la kushtukiza lakini vilevile lililoichanganya vibaya akili yangu hasa pale nilipokumbuka kuwa nyuma yangu nilikuwa nikifuatiliwa na lile gari jeupe Landcruiser Hardtop. Wakati nikipunguza mwendo kichwani nikawa nikipiga akili namna ya kujinasua kutoka katika kadhia ile bila kupoteza muda. Hata hivyo ni kama hila yangu ilikuwa imeanza kushtukiwa kwani haraka niliwaona wanajeshi wengine wawili wakiongezeka katikati ya barabara ile na kusimama nyuma ya kizuizi kikubwa cha barabarani huku nao wakiwa na bunduki zao mikononi. Loh! hila zangu ni kama zilikuwa mbioni kugonga mwamba.

     Hata hivyo nikapunguza mwendo taratibu huku nikijitahidi kukabiliana na hali ile na nilipochunguza nyuma kupitia vioo vya ubavuni vya lile gari langu nikaliona lile gari jeupe Landcruiser Hardtop likitimua mbio kunikaribia. Hali ile ikapelekea kijasho chepesi kianze kunitoka maungoni. Wakati nilipokuwa nikikikaribia kile kizuizi mbele yangu nikagundua kuwa kulikuwa na magari mengine manne yaliyokuwa yamesimamishwa kando ya ile barabara yakipekuliwa na wajeshi wengine.

     Hatimaye nikakifikia kile kizuizi cha barabarani na kusimama hata hivyo sikushuka kwenye gari badala yake nikashusha kioo cha dirishani kwangu na kutengeneza tabasamu la kirafiki. Wanajeshi wawili haraka wakalizingira gari langu. Mwanajeshi mmoja akaja dirishani hata hivyo hakunisemesha neno zaidi ya kunionesha tabasamu lake la kirafiki baada ya kuiona ile nembo ya ubavuni mwa gari langu iliyokuwa ikilitambulisha lile gari kuwa ni mali ya ubalozi wa Tanzania nchini Burundi. Nikawaona wale wanajeshi wakilizunguka gari langu kama ambao wanachunguza chunguza mle ndani kisha yule mwanajeshi aliyesimama pale mlangoni akanifanyia ishara kwa kichwa kuwa niendelee na safari yangu. Nikatabasamu kidogo na kumuaga yule afande kwa kumpungia mkono kisha nikatia moto gari na kuondoka eneo lile na wakati nikiondoka kupitia vioo vya ubavuni vya gari langu nikawaona wale wanajeshi wakilisimamisha lile gari jeupe Landcruiser Hardtop lililokuwa nyuma yangu likinifukuza.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

     Tukio la lile gari Landcruiser Hardtop jeupe kusimamishwa na wale wanajeshi kwenye kile kizuizi nyuma yangu likanipelekea nitabasamu kwani niliamini kuwa ule ndiyo ungekuwa wakati wangu mzuri wa kulitoroka lile gari na kuendelea na harakati zangu. Hata hivyo hilo halikutokea badala yake muda mfupi uliofuata nikajikuta nikishikwa na mshangao kwani wakati nilipokuwa mbioni kuuzunguka ule mzunguko wa barabara wa RN 7 upande wa kushoto nikaliona lile gari jeupe Landcruiser Hardtop likiingia kwenye ule mzunguko wa barabara kunifuata nyuma yangu. Kwa kweli nilipatwa na mshtuko wa aina yake kiasi cha moyo wangu kupoteza kabisa utulivu. Hatimaye hisia zangu zikanitanabaisha kuwa nilikuwa mbioni kukabiliana na hatari.

     Sikutaka hatari ile inifikie hivyo mara baada ya kuuvuka mzunguko ule wa barabara haraka nikaingia barabara ya Chaussée de Gitega na kuongeza mwendo. Ilikuwa barabara pana ya lami iliyokuwa ikielekea mbali na jiji la Bujumbura isiyokuwa na pilika za magari wala watembea kwa miguu. Barabara ile ilikuwa ikikatisha katikati ya vichaka hafifu na miti mirefu ya kivuli na hivyo kupelekea utulivu wa hali ya juu safarini. Nikiwa katika mwendo mkali njiani nikapishana na malori mawili ya mizigo na gari moja la mtu binafsi. Sikuwa na shaka yoyote kuwa madereva wa magari yale waligeuka kunishangaa baada ya kupishana na mimi huku nikiwa katika mwendo kasi usioelezeka.

     Kwa mujibu wa ramani yangu ndogo ya kijasusi iliyokuwa kwenye ile kofia ya kujikinga na jua juu yangu ni kuwa kule mbele kidogo mara baada ya kulipita jengo la kiwanda cha kuchapisha magazeti. Upande wa kulia ningevuka daraja kubwa na baada ya kulivuka daraja lile barabara ile ingekatisha katikati ya makazi ya watu. Sikupenda kuyafikia makazi yale ya watu kabla ya mpango wangu kukamilika.

     Wakati nilipokuwa mbioni kulipita lile jengo la kiwanda cha kuchapisha magazeti mara nikaliona lile gari jeupe Landcruiser Hardtop likichomoza kwa kasi nyuma yangu huku likiwa limewasha taa kali za mbele. Nilielewa haraka nini maana ya tukio lile hivyo na mimi nikaongeza mwendo zaidi. Hata hivyo dereva wa lile gari Landcruiser Hardtop jeupe nyuma yangu alikuwa mwepesi wa kuishtukia haraka hila yangu hivyo hakunipa nafasi. Kufumba na kufumbua lile gari jeupe Landcruiser Hardtop likawa tayari limenifikia kando yangu ubavuni. Nikageuka haraka kulitazama lile gari na hapo wasiwasi ukaniingia mara baada ya kukiona kioo cha dereva wa lile gari kikishushwa chini kwa haraka. Wakati nikiendelea kushangazwa na tukio lile mara nikauona mtutu wa bastola ukipenyezwa katika upenyo wa dirisha lile na kuelekezwa kwangu.

     Hapakuwa na muda wa kuendelea kusubiri nini ambacho kingetokea baada ya pale hivyo haraka nikaminya breki kuliruhusu lile gari linipite mbele yangu. Muda uleule nikasikia mlio mkali wa risasi iliyonikosa shabaha na kufanikiwa kuparaza boneti ya gari langu na kusababisha cheche kali. Sikuiruhusu risasi ya pili kunifikia hivyo haraka nikaichomoa bastola yangu kutoka mafichoni kisha mkono wangu mmoja ukiwa umeshika usukani nikairuhusu risasi moja kufanya kazi. Hata hivyo risasi ile ikapoteza shabaha kidogo na kukichangua vibaya kioo cha mbele cha lile gari. Risasi ya pili niliyoifyatua haraka ikakichangua vibaya kioo cha mlango wa dereva wa lile hali iliyompelekea yule dereva wa lile gari kuinama chini ili kulipisha shambulizi lile makini...

    Nilipokuwa nikijiandaa kufyatua risasi ya tatu dereva wa lile gari akawa mwerevu wa kushtukia mapema hila yangu hivyo akaliwahi gari langu na kuligonga ubavuni. Mtikisiko uliotokea ukapelekea bastola yangu iniponyoke mkononi na kuangukia kwenye siti ya abiria kushoto kwangu. Nilifahamu kuwa ule ungekuwa mchezo hatari kwani lile gari jeupe Landcruiser Hardtop lilikuwa na nguvu zaidi kuliko gari langu hivyo haraka nikawa nafikiria namna ya kufanya. Nilipotazama kule mbele nikagundua kuwa tulikuwa tumelikaribia lile daraja la mto mkubwa uliokuwa ukikatisha eneo lile. Wakati nikiendelea kufikiria nini cha kufanya lile gari jeupe Landcruiser Hardtop likawa tayari limenifikia tena na kunipiga kumbo ubavuni kiasi cha kufanikiwa kunihamisha barabarani na kunisogeza kwenye uchochoro hafifu wenye nyasi fupi uliokuwa kando ya ile barabara.

     Tukaendelea kufukuzana huku nikijitahidi kwa kila hali kulirudisha gari langu barabarani hata hivyo sikufanikiwa haraka mpango wangu ingawa sasa niliweza kulikwepa lile gari kila lilipokuwa likitia bidii kunipiga kumbo. Dereva wa lile gari alipoona hila yake inaelekea kushindwa akachungulia kidogo dirishani kunitazama na hilo likawa kosa kubwa kuwahi kufanywa na binadamu yule. Nilikuwa tayari nimeichukua ile bastola yangu na kaimata vyema kwa mkono wangu wa kushoto na safari ile sikufanya tena makosa kwani risasi moja niliyoiruhusu baada ya kuvuta kilimi cha bastola yangu ikapenya katikati ya paji la uso wa yule dereva na kukifumua vibaya kichwa chake.

     Tukio lile likalipelekea lile gari lianze kupoteza uelekeo huku likiyumbayumba ovyo barabarani. Wakati tukio lile likiendelea mara nikamuona mtu mwingine aliyekuwa amekaa kwenye siti ya abiria kando ya yule dereva akisogea pale kwa dereva na kujitahidi kuudhibiti usukani wa gari. Hata hivyo hakufanikiwa kwani muda ule tulikuwa tayari tumelifikia lile daraja la ule mto mkubwa na sikutaka kuichezea nafasi ile. Hivyo haraka nikakanyaga pedali ya mafuta na kuanza kulifuata lile gari kushoto kwangu. Yule dereva wa lile gari jeupe Landcruiser Hardtop alikuwa tayari ameulalia usukani wa lile gari huku uhai ukiwa mbali na mwili wake na yule msaidizi wake ndiyo kwanza alikuwa akiukaribia ule usukani wa gari. Hivyo kumbo moja la nguvu la gari langu pasipo upinzani wowote lilitosha kabisa kuliondosha lile gari barabarani. Muda ule mara nikayaona magurudumu ya mbele ya lile gari jeupe Landcruiser Hardtop yakiparamia vibaya ukingo wa lile daraja tukio lililoambatana na mayowe kadhaa ya hofu kutoka kwa watu waliokuwa mle ndani ya lile gari ambao idadi yao sikuweza haraka kuifahamu.

     Magurudumu ya lile gari Landcruiser Hardtop yalipoupanda ule ukingo wa lile daraja nikaliona lile gari likipiga sarakasi mara mbili zaidi hewani. Tukio lile likapelekea mlango mmoja wa lile gari ufunguke na mtu mmoja mwenye sare za kijeshi kuchomoka toka mle ndani. Haraka nikapunguza mwendo kushuhudia ajali ile ya kutisha. Muda uleule lile gari likatumbukia kwenye ule mto na kutengeneza mshindo wa aina yake eneo lile. Yule mtu aliyechomoka kwenye mlango wa lile gari akapiga yowe la hofu huku akisema maneno fulani nisiyoyaelewa wakati akiwa angani lakini hatimaye na yeye akatumbukia kwenye ule mto umbali wa hatua chache kutoka pale lilipotumbukia lile gari. Taratibu nikaendesha gari langu huku nikishuhudia tukio lile hadi pale nilipovuka lile daraja kisha nikaegesha gari langu kando ya ile barabara na kushuka nikielekea kule mtoni.

     Hapakuwa na mtu yeyote eneo lile wala magari yaliyokuwa yakikatisha kwenye ile barabara kwa wakati ule na hali ile ilinipa uhuru. Kwa dakika kadhaa nikasimama kando ya ule mto nikiitazama kwa makini ile sehemu ya mto lilipokuwa limetumbukia lile gari na yule mtu pasipo kuona chochote. Hata hivyo yale maji ya mto kwa sehemu ile yalionekana kutibuka sana. Kufuatia mvua za masika zilizokuwa zikiendelea kunyesha nchini Burundi ule mto ulikuwa umefurika sana kiasi cha kuelekea kutapisha maji kwenye kingo zake. Sikuwa na mashaka yoyote kuwa ule mto ulikuwa na kina kirefu sana kwani pamoja na lile gari kutumbukia kwenye ule mto lakini bado sikuweza kuona dalili zozote za uwepo wa lile gari mle mtoni na badala yake yale maji ya mto yaliendelea kusafiri kwa utulivu huku sauti ya mzizimo wake ikituama vyema masikioni mwangu.

     Nikiwa bado nimesimama kando ya ule mto nikaendelea kutazama kwenye ule mto sehemu ambayo lile gari lilikuwa limetumbukia. Muda ukazidi kusonga pasipo kuona dalili zozote za kuibuka kwa mtu watu au lile gari huku maroli mawili ya mizigo yakipita juu ya lile daraja na kuendelea na safari. Hatimaye nikakata tamaa kabisa ya kuliona lile gari lililotumbukia kwenye ule mto au wale watu waliokuwa mle ndani. Kulikuwa na kila dalili kuwa mvua kubwa ingenyesha muda mfupi baadaye kwani hali ya hewa ilikuwa imebadilika ghafla na wingu zito lilikuwa limeanza kutanda angani.

     Nikiwa sasa nimekata tamaa ya kuambulia chochote mwisho nikaamua kuanza kuondoka taratibu eneo lile. Lakini ghafla wakati nikianza kuondoka nyuma yangu kwenye ule mto nikashtushwa na sauti mtu akipiga yowe kuomba msaada. Nikageuka haraka na kutazama kwenye ule mto ile sauti ilipokuwa ikitokea na hapo nikajikuta nikishikwa na mshtuko. Mwanaume mmoja alikuwa akijitahidi kuogelea kutoka kwenye lile eneo la mto lile gari jeupe Landcruiser Hardtop lilipokuwa limetumbukia huku akiomba msaada. Yule mtu alikuwa hodari sana wa kuogelea akiogelea kwa jitihada zake zote kuelekea kwenye ukingo wa ule mto kwa kihoro kikubwa kama mtu akimbiaye kifo.

     Tumaini la kukipata kile nilichokuwa nikikitarajia likafufuka upya moyoni mwangu na hapo nikaanza kutimua mbio nikirudi kumfuata yule mtu kwenye ukingo wa ule mto.

     Mwanzoni nilidhani kuwa mtu yule huwenda angekuwa ndiye yule aliyechomoka mlangoni wakati lile gari lililotumbukia mtoni lilipokuwa likipiga sarakasi hewani lakini wakati nikimkaribia nikagundua kuwa hakuwa yeye. Hata hivyo nilipomchunguza vizuri yule mtu nikamkumbuka kuwa alikuwa ndiye yule aliyekuwa akinitazama kupitia dirishani wakati alipokuwa kwenye kile chumba cha jengo la ghorofa lililokuwa likitazamana na lile jengo la ghorofa lenye zile ofisi za ubalozi wa Tanzania nchini Burundi muda mfupi uliopita.

     Yule mtu akaendelea kuogelea kwa bidii zake zote hadi alipofika kwenye ukingo wa ule mto huku akiwa hajiwezi kwa hali. Nikawahi kumfikia na kumshika mkono hata hivyo sikumtoa kutoka kwenye yale maji mengi ule ya mto hivyo akawa anaeleaelea tu kwenye ule ukingo. Bila shaka yule mtu hakuwa amenitambua haraka kuwa mimi ni nani kwani macho yetu yalipokutana nikaiona hofu iliyomwingia haraka usoni mwake kiasi cha kutaka kurudi kule alipotoka. Hata hivyo hakufanikiwa kwani tayari nilikuwa nimemkwida shingoni na nilipomchunguza vizuri nikamuona kuwa alikuwa amening?iniza kamera shingoni.

    “Wewe ni nani?” Nikamuuliza kibabe pasipo kutaka kufahamu kama alikuwa akifahamu kuzungumza kiswahili au lah!. Kupitia ile kamera shingoni mwake nikajikuta nikimkumbuka vizuri yule mtu kwani wakati alipokuwa akinitazama kupitia kwenye lile dirisha la kile chumba kilichokuwa kwenye kona ya lile jengo la ghorofa lililokuwa likitazamana na zile ofisi za ubalozi wa Tanzania nchini Burundi. Nikakumbuka kuwa mtu yule alikuwa ameshika kitu fulani mkononi ambacho kutokana na ule umbali sikuwa nimekiona vizuri kitu kile. Lakini sasa kumuona mtu yule akiwa amening?iniza kamera shingoni nikapata hakika kuwa nilikuwa nimepigwa picha kadhaa wakati nilipokuwa nimesimama kwenye lile dirisha la ofisi ya Balozi Adam Mwambapa. Yule mtu alikuwa amevaa suruali ya kijivu na shati jeusi na umri wake haukuelekea kuzidi miaka arobaini. Mweusi na mrefu lakini mwenye macho yaliyohifadhi kila hila nafsini mwake.

    “Naitwa Jean-Baptiste Nibizi”. Yule mtu akajitambulisha kwa kujiamini kana kwamba alikuwa ni mtu maarufu sana Jijini Bujumbura ambaye ni mimi tu ndiye ambaye nilikuwa simfahamu na lafudhi ya kiswahili chake ilikuwa ni ya kirundi.

    “Mna shida gani na mimi?”. Nikamuuliza yule mtu huku nikizidi kumkwida shati lake shingoni.

    “Sina shida yoyote na wewe”. Yule mtu akaongea kwa unyonge hata hivyo nikamchangamsha kwa kumzaba makofi mawili ya nguvu usoni.

    “Sasa kwa nini mnanifuatafuata kila niendako?”

     “Siyo mimi ni wale mimi nimelipwa tu pesa kwa ajili ya kuchukua picha zake”. Maelezo ya yule mtu yakanipelekea nimtazame kwa mshangao kidogo huku nikishindwa kumuelewa vizuri.

    “Wale akina nani?”. Hatimaye nikamuuliza.

    “Wale watu niliokuwa nao ndani ya lile gari”. Yule mtu akaongea kinyonge.

    “Mlikuwa wangapi mle ndani ya gari?”

     “Tulikuwa sita na mimi wa saba”

     “Nipe kamera yako”. Nikamwambia yule mtu huku nikizidi kumkwida hata hivyo yule mtu hakuonesha upinzani wowote badala yake taratibu akaanza kuivua ile kamera yake kutoka shingoni na wakati akiendelea na zoezi lile nikaendelea kumhoji.

    “Nani aliyekulipa pesa kwa ajili ya kuchukua picha zangu?’’. Yule mtu hakufanikiwa kujibu swali langu badala yake ghafla nikamuona akitoa macho na kuacha mdomo wake kama mjusi alikanyagwa na gurudumu la baiskeli tumboni kisha nikaanza kuona damu nyepesi ikimtoka yule mtu puani na mdomoni. Wakati nikiendelea kushangazwa na hali ile mara nikamsikia yule mtu akipiga yowe hafifu la kukata kauli na hapo nikaliona tundu dogo linaloanza kuvuja damu upande wa kushoto wa kifua chake. Haikuniwia vigumu kufahamu kuwa tundu lile linalovuja damu lilikuwa limetokana na shambulizi la risasi hali iliyonipelekea nishikwe na hofu. Yule mtu akaniponyoka mkononi na kuanza kuzama taratibu hata hivyo haraka nikawahi kuupelekea mkono wangu kuichukua ile kamera yake shingoni. Sikufanikiwa na katika muda mfupi tu nikatambua kuwa lile zoezi lisingewezekana kwani mkanda wa ile kamera ulikuwa tayari umefyatuliwa na yule mtu kabla sijaifikia hivyo ile kamera ikawahi kuangukia kwenye maji ya ule mto na kupotea. Nikashawishika kumvuta yule mtu na kumtoa nje ya ule mto hata hivyo wazo lile nikaliweka kando pale nilipojiridhisha kuwa tayari yule mtu alikuwa amekufa. Risasi ya mwisho iliyotoka mafichoni kusikojulikana ikaniparaza kidogo begani na kuacha tundu kwenye shingo ya yule mtu. Hivyo sikuwa na namna tena ya kumuokoa yule mtu badala yake nikamwachia haraka mikononi tukio lililompelekea asombwe haraka na maji ya ule mto huku mimi nikiruka na kujibanza kwenye kichaka kilichokuwa kando ya ukingo wa ule mto.

     Nikiwa nimejibanza kwenye kile kichaka nikaikamata vyema bastola yangu mkononi huku nikiyatembeza macho yangu huku na kule pasipo kumuona mtu yeyote eneo lile. Kwa kweli tukio lile lilinishangaza sana kwani bado sikuweza kufahamu haraka kuwa yale mashambulizi ya risasi yalikuwa yakitokea upande gani. Hata hivyo haraka nikagundua kuwa pale kwenye kile kichaka bado sikuwa sehemu salama kwani risasi kadhaa ziliendelea kuniandama eneo lile kiasi cha kuelekea kutishia usalama wangu. Hali ile ilipoelekea kuzidi kutishia usalama wangu nikajitupa chini na kuanza kutambaa taratibu nikihamia kwenye kichaka kingine kilichokuwa jirani na eneo lile.

     Zile risasi zikaendelea kurindima kwenye kile kichaka na kwa kuwa mipigo yote ilikuwa ya kimyakimya nikajua kuwa kwa vyote bunduki iliyokuwa ikitumika katika shambulizi lile ilikuwa imefungwa kiwambo maalum cha kuzuia sauti. Swali likabaki kuwa shambulizi lile lilikuwa likifanywa na nani na mtu huyo alikuwa amejificha wapi eneo lile. Niliendelea kujibanza kwenye kichaka huku nikijipa utulivu na kutazama huku na kule eneo lile. Muda mfupi uliofuata zile risasi zikakoma na eneo lile likamezwa na utulivu wa hali ya juu. Hata hivyo nikaendelea kujipa subira.

     Kwa kufanya vile mara nikajikuta nikivutiwa na taswira ya kichuguu kidogo kilichokuwa kimechomoza kwenye pembe ya nguzo moja ya lile daraja chini yake. Nilipoendelea kuchunguza vizuri nikagundua kuwa kile hakikuwa kichuguu kama nilivyokuwa nimedhani ila kilikuwa kichwa cha mtu aliyekuwa akijitahidi kuchungulia kwa makini pale kwenye kile kichaka cha awali nilipokuwa nimejibanza. Nilipomchunguza vizuri yule mtu haraka nikamtambua kuwa alikuwa ni yule mwanajeshi aliyechomoka mlangoni wakati ile Landcruiser ilipokuwa ikipiga sarakasi na kutumbukia mtoni. Mkononi alikuwa ameshika bastola. Sasa nilifahamu kuwa yule mtu alikuwa amefanikiwa kuogelea na hatimaye kujiokoa kutoka kwenye ule mto.

     Sikutaka kufanya papara ya namna yoyote badala yake nikajipa utulivu katika namna ya kumwaminisha yule mtu kuwa shambulizi lake lilikuwa limezaa matunda kwenye kile kichaka nilichokuwa nimejibanza pale awali. Yule alipoona kuwa hakuna mtikisiko wowote kwenye kile kichaka akajiaminisha kuwa tayari alikuwa amenilaza chini hivyo akajitokeza kwa uhuru zaidi nyuma ya ile nguzo ya daraja huku akitazama tazama huku na kule. Sikutaka kumuacha aendelee kutabaruku zaidi hivyo nikaikamata vyema bastola yangu na kumchapa risasi ya begani na hapo bila kupenda akaiachia ile bastola yake mkononi na kuangukia mtoni.

     Yule mtu akapiga yowe kali la maumivu na kujishika begani huku akishangaa kuwa shambulizi lile lilikuwa limetokea uelekeo gani. Muda ule nikawa tayari nimekijaza vizuri kichwa chake kwenye jicho langu hiyo yule mtu hakupata nafasi ya kuomba maji kwani risasi yangu moja ikamchakaza vibaya na hapo akaanguka na kutumbukia kwenye ule mto akisombwa na maji.

     Niliendelea kujibanza kwenye kile kichaka kwa muda mrefu katika namna ya kujiridhisha na hali ya usalama wa eneo lile hadi pale nilipohakikisha kuwa hali ilikuwa shwari ndiyo nikatoka kwenye yale maficho kwa tahadhari na kuelekea kule nilipokuwa nimeegesha gari langu. Manyunyu hafifu ya mvua yalikuwa yameanza kuanguka kutoka angani wakati nilipoitazama saa yangu ya mkononi na kugundua kuwa ilikuwa ikielekea kutimia saa kumi na moja kasoro robo jioni. Sikuwa na muda wa kupoteza hivyo mara tu nilipoingia kwenye gari nikaanza safari ya kurudi mjini huku jina la Jean-Baptiste Nibizi likianza kutawala fikra zangu.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

     Mambo yote yaliyotokea kwenye ule mto yalikuwa kama kipande cha mkasa katika filamu ndefu nisioufahamu mwisho wake. Sikuweza kufahamu watu wale waliokuwa wakinifuatilia kwenye lile gari jeupe Landcruiser Hardtop lililotumbukia mtoni walikuwa ni akina nani na walikuwa na shida gani na mimi. Hata hivyo niliamini kuwa hadi kufikia wakati ule uwepo wangu jijini Bujumbura nchini Burundi ulikuwa ukifahamika na watu fulani nisiowafahamu. Nilimkumbuka yule mtu aliyejitambulisha kwangu kwa jina la Jean-Baptiste Nibizi wakati aliponiambia kuwa alikuwa amelipwa pesa kwa ajili ya kunipiga picha kwa siri na hapo nikahisi kuwa kulikuwa na mtu au kikundi cha watu waliokuwa wakitengeneza mikakati michafu katika kuhakikisha kuwa nauwawa mapema kabla harakati zangu hazijafika kokote. Nilitaka kufahamu kuwa watu hao wangekuwa akina nani hata hivyo nilitambua kuwa kwa wakati ule hilo lisingewezekana hivyo nikaendelea na safari yangu huku mawazo mengi yakipita kichwani mwangu.

     ______

     Kama ilivyokuwa kwa viongozi wengi wa bara la Afrika kupenda kuishi kwenye maeneo ya mijini yenye hadhi ya juu kiuchumi na kiusalama. Makazi ya balozi wa Tanzania nchini Burundi Meja jenerali mstaafu Adam Mwambapa nayo pia yalikuwa katika eneo zuri la kifahari lenye majumba makubwa ya kisasa ya watu wakwasi yaliyokuwa yamezungukwa na kuta ndefu za uzio na mageti makubwa yenye vifaa vyote vya usalama vya kuwahakikisha wakazi wake usalama wa hali ya juu.

     Eneo la Chausée P.L.Rwagasore jijini Bujumbura lilikuwa limezungukwa na makazi ya kisasa ya viongozi wa kitaifa na wa kimataifa. Vitongoji vyake vilikuwa vimeunganishwa kwa barabara nzuri za lami zenye taa za barabarani. Pilika za watu na magari zilikuwa hafifu sana huku ustaarabu wa kisomi ukionekana kuzingatiwa kwa asilimia zote. Kwa mbali ukiwa barabarani ungeweza kumuona mtu mmoja mmoja au wawili katika sehemu za kupumzikia za majengo yale ya ghorofa kwa juu wakinywa kahawa na kusoma vitabu na magazeti. Sehemu nyingine ungeona nguo zikiwa zimeanikwa kwenye sehemu maalum za kuanikia nguo. Mahali fulani ghorofani ungeweza kuwaona wapenzi wakiwa wamesimama wakitazama mandhari nzuri ya kupendeza nje ya nyumba zao za kifahari nyakati za jioni. Kwengineko si ajabu sana ungezisikia sauti kali za mbwa wakibweka ndani ya mageti yale...



    Lakini kufuatia jaribio lile la mapinduzi ya kijeshi nchini Burundi taratibu za maisha ya kawaida ya wakazi wake zilikuwa zimebadilika. Majumba mengi ya kifahari katika eneo lile la Chausée P.L. Rwagasore yalionekana kubaki ukiwa kutokana na wakazi wake wengi kufunga majumba yao na kuondoka wakihofia kutokea kwa mapigano na umwagaji damu kati ya vikosi vya askari watiifu kwa serikali ya Rais Pierre Nkurunziza na vile vya waasi wanaotaka kuing?oa serikali iliyoko madarakani.

     Mvua kubwa ilikuwa imeanza kunyesha na giza nalo lilikuwa limeanza kuingia wakati nilipokuwa nikiegesha gari langu barabara ya mtaa wa pili mbele ya supermarket ndogo iliyokuwa imefungwa kwa wakati ule. Kisha nikachukua koti refu jeusi la mvua ambalo Hidaya alikuwa ameniandalia mle ndani ya gari na kulivaa. Bastola yangu ikiwa nyuma kiunoni nikashuka na kufunga mlango wa gari nikianza kutembea kuelekea mtaa wa pili yalipokuwa makazi ya Balozi Adam Mwambapa.

     Pamoja na hofu kubwa ya kutokea kwa machafuko ya kisiasa nchini Burundi lakini mvua ile kubwa ya masika ilikuwa imechangia barabara nyingi za kitongoji kile kukimbiwa na watu. Hivyo wakati nikitembea nikajihisi kama kiumbe pekee niliyekuwa nimesalia kwenye sayari ya peke yangu. Sikuweza kuona gari wala mtu katika barabara za kitongoji kile ingawa hali ile haikutosha kunihakikishia kuwa nilikuwa katika mazingira salama.

     Niliendelea kutembea nikizipita nyumba mbili za ghorofa upande wa kushoto hata hivyo nyumba zile zilikuwa na giza kana kwamba hazikuwa na wakazi wake kwa wakati ule. Nilipofika mbele nikaingia upande wa kulia nikiifuta barabara pana ya lami iliyokuwa ikipakana na maduka makubwa ya kisasa na ofisi ndogo ya posta. Nilipofika mwisho wa barabara ile nikachepuka na kuingia upande wa kushoto nikizipita ofisi za shirika moja la mtandao wa simu na duka moja kubwa la pombe za kisasa. Kwa kufanya vile nikajikuta nikitazamana na barabara tulivu ya mtaa wenye majumba ya kifahari yaliyozungukwa na miti mirefu na kuta zenye usalama wa uhakika. Barabara ya mtaa ule ilikuwa tulivu mno huku ikimulikwa na taa nzuri zenye mwanga mkali na hivyo kunifanya nijihisi kama niliyekuwa nikionekana vizuri na mtu yeyote aliyekuwa mafichoni akinitazama. Kwa mbali niliweza kuzisikia sauti kali za mbwa waliokuwa wakibweka katika nyumba za jirani na eneo lile bila sababu za msingi.

     Kwa mujibu wa maelezo ya Hidaya ni kuwa nyumba namba 26 aliyokuwa akiishi Balozi Adam Mwambapa ilikuwa ikipakana na nyumba ya makamu wa mahakama ya kikatiba ya nchini Burundi jaji Sylvere Nimpagaritse ambaye kupitia taarifa za awali zilizorushwa na kituo kimoja cha matangazo ya redio cha jijini Bujumbura zilikuwa zimeeleza kuwa jaji Sylvere Nimpagaritse alikuwa tayari ametoroka nchi na kukimbilia nchini Rwanda kwa kile alichodai kuwa yeye pamoja na majaji wenzake walikuwa wametishiwa maisha baada ya mahakama ya kikatiba kushinikizwa kumpitisha Rais Pierre Nkurunziza kugombea urais kwa muhula wa tatu kinyume na katiba.

     Kulikuwa na miti michache ya vivuli kandokando ya barabara ile iliyofanikiwa kutengeneza giza hafifu hivyo kwa kukwepa kuonekana kwa urahisi nikachepuka na kuanza kupita chini ya miti ile.

     Nyumba ya jaji Sylvere Nimpagaritse ilikuwa kiasi cha umbali wa hatua ishirini mbele yangu. Ilikuwa nyumba nzuri ya kifahari iliyozungukwa na miti mizuri ya vivuli na sehemu za wazi zenye bustani nzuri ya maua na nyasi za kijani kibichi zilizokatiwa vizuri. Ukuta wake kuizunguka ile nyumba ulikuwa mfupi na wenye nakshi za hapa na pale kiasi cha kumruhusu mtembea kwa miguu kuweza kuona mle ndani kwa shida kidogo. Taa zote za ile nyumba zilikuwa zimezimwa na hivyo kupelekea mandhari yake kutawaliwa na giza. Hata hivyo kupitia taa za barabarani zilizokuwa juu ya nguzo ndefu niliweza kuona sehemu tu ya mandhari yale ingawa uwepo wa giza na ukimya wa nyumba ile haikuwa kigezo tosha cha kunifanya niamini kuwa nyumba ile haikuwa chini ya uangalizi makini wa wanausalama wa nchi ya Burundi.Nilipoipita ile nyumba nikapunguza mwendo na kuanza kutembea kwa tahadhari huku mara kwa mara nikigeuka nyuma na kutazama kama kungekuwa na mtu yeyote aliyekuwa akinifuatilia. Hali bado ilikuwa shwari hivyo nikazidi kufarijika.

     Nyumba ya Balozi Adam Mwambapa ilikuwa umbali wa hatua chache mara baada ya kuipitia ile nyumba ya jaji Sylvere Nimpagaritse kwani nyumba zile mbili zilikuwa zikipakana na kutenganishwa na ukuta mrefu.

     Hatimaye nikawa nimelifikia geti kubwa jeusi la ile nyumba aliyokuwa akiishi Balozi Adam Mwambapa hata hivyo ukuta mrefu uliofungwa sistimu maalum ya umeme wa kuzuia wezi juu yake haukuniwezesha kuona mle ndani. Nilipolifikia lille geti nikasimama na kushawishika kubonyeza kitufe cha kengele kilichokuwa pembeni yake lakini kitendo cha kuona viashiria vichache kuwa nyumba ile ilikuwa gizani kikanipelekea nighairi kwanza mpango wangu. Awali ya yote nilitaka kufahamu kwanza hali ya usalama wa eneo lile hivyo nikaachana kwanza na lile geti na kutembea kwa utulivu kandokando ya ukuta wa ile nyumba chini ya vivuli vya miti katika namna ya kufanya tathmini ya mazingira yale. Lakini vilevile nilitaka kuvuta uwepo wa kiumbe hai chochote ambacho kingekuwa eneo lile kikinitazama.

     Hatimaye nikafika mwisho wa ukuta wa ile nyumba pasipo kuhisi uwepo wa mtu yeyote eneo lile. Hali bado ilikuwa shwari na kwa mbali niliendelea kuzisikia sauti za mbwa waliokuwa kwenye nyumba za jirani na eneo lile wakibweka japo nyumba zote za eneo lile zilikuwa zimetawaliwa na ukimya wa aina yake. Nilipoitazama saa yangu ya mkononi nikagundua kuwa ilikuwa tayari imetimia saa moja na robo usiku. Mvua kubwa bado ilikuwa ikiendelea kunyesha.

     Baada ya kuridhika na tathmini yangu kwa tahadhari nikarudi tena kwenye lile geti mara hii nikiwa na dhamira moja tu ya kuingia mle ndani ya ile nyumba. Nilipolifikia tena lile geti nikasimama huku nikigeuka na kuyatembeza macho yangu huku na kule katika namna ya kujiridhisha na hali ya usalama wa eneo lile. Hali bado ilikuwa shwari na sikuweza kuhisi kitu chochote katika geti la nyumba ya jirani upande wa pili wa barabara lililokuwa likitazamana na lile geti la nyumba ya Balozi Adam Mwambapa. Hivyo nikaisogelea swichi ya kengele iliyokuwa ukutani kando ya lile geti na kubofya kitufe chake. Ile kengele ikaita kwa muda mrefu na hatimaye kukata pasipo mwitikio wa aina yoyote kutoka mle ndani. Takio lile likanipelekea nirudie kubofya tena ile swichi kwa mara mbili zaidi huku nikitarajia mtu yeyote kujitokeza na kunisikiliza lakini hilo halikutokea. Ile kengele ikaendelea kuita tena kwa muda mrefu pasipo mwitikio wowote kisha ikakata. Nikarudia zoezi lile kwa mara kadhaa kabla ya kujiridhisha kuwa nilikuwa nikipoteza muda wangu bure.

     Mwishowe nikaamua kuachana na ile swichi ya kengele badala yake nikausogelea mlango mdogo wa lile geti huku bastola yangu tayari ikiwa mkononi. Lakini wakati nilipokuwa nikitaka kufanya vile mara nikashtushwa na sauti ya muungurumo wa gari lililokuwa likija upande ule hivyo nikachepuka na kujibanza kwenye kona moja ya lile geti nikiliacha kwanza lile gari lipite. Lilikuwa gari dogo aina ya Mitsubishi Wagon ya rangi nyekundu na dereva wa gari lile alipita kwa mwendo kasi uliomnyima fursa ya kutazama vizuri pale nilipojibanza na hali ile kwa kweli ilinitia faraja sana. Nikasubiri lile gari litokomee kabisa mbali na eneo lile na hapo kwa tahadhari nikausogelea tena ule mlango mdogo wa lile geti. Nilipofika nikakishika kitasa na kuusukuma ndani ule mlango taratibu kwa tahadhari ya hali ya juu. Ule mlango ulikuwa wazi tofauti kabisa na matarajio yangu na hali ile ilinishangaza sana.

     Bastola yangu ikiwa mkononi sikutaka tena kurudi nyuma hivyo nikaendelea kuusukuma ule mlango taratibu katika namna ya kuuzuia usipige kelele na kumshtua mtu yoyote ambaye angekuwa mle ndani. Hatimaye nikaingia mle ndani na kuurudishia nyema yangu.

     Kabla ya kufanya mjongeo mwingine wowote nikatulia pale getini nikiyatembeza macho yangu kupeleleza mandhari ya ile nyumba. Ilikuwa nyumba kubwa ya kisasa lakini siyo ya ghorofa yenye madirisha makubwa ya kisasa na baraza kubwa mbele yake iliyopangwa seti moja ya makochi ya sofa. Nje ya nyumba ile upande wa kushoto kulikuwa na banda la wazi la kuegeshea magari na nilipochunguza nikaona kuwa kulikuwa na magari matatu ya kifahari. Gari la kwanza lilikuwa ni Landcruiser V8 jeupe. Gari la pili lilikuwa ni Toyota Lexus RX ya rangi nyeusi na gari la mwisho lilikuwa ni Mercedes Benz E-class jeusi lenye milango sita ambalo niliamini kuwa lilikuwa ndiyo gari lililokuwa likitumiwazaidi na Balozi Adam Mwambapa kwa shughuli za kiofisi.

     Sehemu nyingine ya mandhari ya nyumba ile ilizungukwa na miti mirefu na mikubwa ya kivuli hata hivyo matawi makubwa ya miti ile usiku ule yalikuwa yametengeneza vichaka vya giza la kutisha. Niliendelea kuitazama ile miti mikubwa kwa utulivu huku hisia zangu zikinieleza kuwa mtu yeyote mwenye hila angeweza kujibanza nyuma ya miti ile na kuitimiza adhma yake mbaya. Sehemu ya mbele ya ile nyumba ilikuwa imezungukwa na bustani nzuri ya maua ya kupendeza na katikati ya bustani ile kulitengenezwa njia nzuri ya kutembea kwa miguu kwa vitofali vidogo vinavyovutia. Njia kubwa ya gari ilikuwa imetengenezwa kwa ufundi mkubwa ikianzia sehemu ya getini hadi mbele ya ile nyumba inayomruhusu dereva ageuze gari pasipo kurudi nyuma.

     Kwa sekunde kadhaa niliendelea kusimama pale getini huku nikiupisha utulivu kichwani mwangu na kitendo cha kuona taa zote za ile nyumba zikiwa zimezimwa kikaongeza ziada nyingine katika hisia zangu kuwa mle ndani ya ile nyumba hapakuwa na mtu yeyote hasa baada ya lile tukio la kutekwa kwa Balozi Adam Mwambapa. Lakini vilevile uwepo wa giza zito lililosababishwa na ile miti mikubwa iliyoizunguka ile nyumba ukanipelekea nihisi kuwa hali ile ingeweza kutumika vizuri na adui mwenye hila katika kutimiza adhma yake.

     Hatimaye nikaondoka pale getini na kuzidi kusogea upande wa kulia wa lile geti sehemu kulipokuwa na kibanda cha mlinzi. Bastola yangu ikiwa imetulia vyema kwenye kiganja cha mkono wangu wa kushoto hatimaye nikakifikia kile kibanda cha mlinzi na kuanza kuchunguza mle ndani. Jambo lililonishangaza ni kuwa mlango wa kile kibanda ulikuwa wazi ingawa mle ndani kulikuwa na giza. Kwa tahadhari nikasogea karibu zaidi na kile kibanda na kuanza kuchunguza mle ndani huku mtutu wa bastola yangu ukitangulia mbele tayari kwa rabsha zozote.

     Hatua moja tu niliyoitupa mbele yangu kuukaribia mlango wa kile kibanda ikapelekea pua yangu ijikute ikikabiliana na harufu nzito ya uvundo na hapo nikahisi mambo hayakuwa shwari. Hata hivyo sikusita badala yake nikausukuma mlango wa kibanda kile taratibu kwa mkono wangu mmoja huku mkono mwingine ukiidhibiti vizuri bastola tayari tayari kufanya shambulizi endapo mambo yangebadilika. Sikukutana na upinzani wowote kama nilivyodhani hapo awali lakini ile harufu ya uvundo sasa ilikuwa kali zaidi. Hapakuwa na dalili zozote za uwepo wa kiumbe hai mle ndani hisia zangu zikanitanabaisha vile hata hivyo kwa kutaka kujiridhisha zaidi nikachukua tochi yangu ndogo ya kijasusi aina ya Penlight yenye umbo kama la kalamu ndogo na kumulika mle ndani.

     Taswira iliyojengeka machoni mwangu kwa sekunde kadhaa ikapelekea shughuli za mwili wangu zisimame kwa sekunde kadhaa huku moyo wangu ukiwa umepoteza kabisa utulivu. Miili ya askari wawili ilikuwa mle ndani ya kile kibanda. Askari mmoja alikuwa ameketi kwenye kiti mdomo wazi huku macho yake yakitazama juu. Mkononi alikuwa ameshika kiwambo cha simu ya mezani ambayo haraka nilipoichunguza nikahisi kuwa umauti ule ulikuwa umemfika wakati alipokuwa katika harakati za kufanya mawasiliano ya kuomba msaada. Nilipozidi kumchunguza askari yule nikagundua kuwa kulikuwa na matundu mawili ya risasi upande wa kulia wa shingo yake. Matundu yale ya risasi yalikuwa yamevuja damu nyingi na damu hiyo ilikuwa imetiririka na kuangukia sakafuni ikisambaa ovyo na kuganda.

     Mlinzi wa pili alikuwa amelala chali sakafuni huku macho na mdomo wake vikiwa wazi na hivyo kumpelekea aonekane kama aliyekuwa akitazama kitu fulani kwenye dari ya kibanda kile. Mkono wake wa kulia ulikuwa umetuwama vyema juu ya bunduki yake SMG huku akionekana ni kama aliyekuwa katika harakati za kujibu shambulizi la adui wakati risasi mbili zilipomfumania vibaya na kutengeneza matundu mawili yanayovuja damu katika pafu lake la upande wa kulia.

     Sasa nilifahamu kuwa harufu ile kali ya uvundo ilikuwa ikitokana na kule kuganda na kuanza kuoza kwa ile damu nyingi sakafuni. Loh! ulikuwa ni unyama wa aina yake kwani wale walinzi walikuwa wameuwawa kama kuku. Kwa sekunde kadhaa nikatulia nikijitahidi kukabiliana na taswira ile ya kusikitisha kabla ya kumeza fundo kubwa la mate kuipooza hasira iliyofurika vibaya kifuani mwangu. Hatimaye nikaanza kufanya upekuzi mle ndani hata hivyo nilimaliza upekuzi wangu pasipo kuambulia kitu chochote cha maana hivyo nikaamua kutoka nje ya kile kibanda.

     Nikiwa nje ya kile kibanda nikaanza kutembea kwa tahadhari kuizunguka ile nyumba katika namna ya kupata uhakika wa hali ya usalama wa eneo lile. Giza zito lililofanywa na matawi makubwa ya miti ya vivuli iliyoizunguka nyumba ile likanipa nafasi nzuri ya kufanya mjongeo makini wa utulivu kama kivuli nikitoka mti mmoja na kuhamia mti mwingine. Nilikuwa na hakika kuwa mtu yeyote ambaye angekuwa eneo lile basi angehitaji kuwa na uzoefu wa hali ya juu wa mienendo ya sampuli ile ili kugundua uwepo wangu eneo lile.

     Wakati nikikatisha chini ya miti ile nikagundua kuwa upande wa kulia wa ile nyumba kulikuwa na bwawa kubwa la kuogelea lililozungukwa na vitanda vizuri vya kujipumzisha chini ya miamvuli mikubwa ya kivuli. Nikaendelea kusogea zaidi na kisha kujibanza katika mti mmoja mkubwa uliokuwa jirani na lile bwawa la kuogelea huku nikiyapa macho yangu utulivu wa kufanya uchunguzi wa mazingira yale. Ingawa kulikuwa na giza zito na mvua bado ilikuwa ikiendelea kunyesha lakini kupitia mwanga uliopenya juu ya ukuta wa uzio ukitokea kwenye nyumba ya ghorofa iliyokuwa ikipakana kwa nyuma na ile nyumba ya Balozi Adam Mwambapa niliweza kupata muono hafifu wa ndani ya lile bwawa la kuogelea.

     Kulikuwa na kitu cheusi mfano wa kipisi cha gogo kilichokuwa kikielea kwenye maji ya lile bwawa. Mawazo yangu yakasimama kwa sekunde kadhaa wakati akili yangu ilipokuwa ikikazana kufikiri katika namna kutafuta tafsiri nzuri ya kitu kile kilichokuwa kikielea kwenye yale maji mengi ya lile bwawa la kuogelea. Kwa kufanya vile taswira ya Balozi Adam Mwambapa ikatumbukia katika fikra zangu haraka na kuibua mshtuko uliomezwa haraka na simanzi. Hata hivyo nikaitowesha haraka taswira ile kichwani mwangu kwa mwanga mkali na mwembamba wa kurunzi yangu ndogo ya kijasusi.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

     Maiti ya mlinzi mwingine wa eneo lile ilikuwa amevimba vibaya huku ikielea juu ya maji ya bwawa lile kama mzoga wa kiboko kwenye bwawa lenye kina kirefu. Nikazima kurunzi yangu haraka na kushusha pumzi taratibu huku nikiyafikicha macho yangu na kumeza funda kubwa la mate kuupooza mtima wangu. Hatimaye nikayaacha maficho yale na kuendelea na uchunguzi wangu nikikatisha katika giza zito lililosababishwa na ile miti mikubwa ya kivuli iliyopandwa kuizunguka ile nyumba.

     Kwa muda mfupi tu niliyoshuhudia maiti tatu za walinzi wa ile nyumba ya Balozi Adam Mwambapa nilikuwa na kila sababu za kuyaamini vizuri maneno ya Hidaya kuwa Balozi Adam Mwambapa alikuwa ametekwa. Kwa kweli nilisikitika sana japokuwa sikuweza kufahamu lipi lilikuwa lengo la wa watekaji hao. Kwa mtazamo mwingine ni kuwa Balozi Adam Mwambapa alikuwa ni mwakilishi wa shughuli zote za Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania na serikali yake nchini Burundi.

     Hivyo niseme kuwa Balozi Adam Mwambapa alikuwa kiungo muhimu cha mahusiano baina ya nchi ya Tanzania na Burundi lakini vilevile alikuwa kiongozi mstaafu wa nafasi ya juu sana katika jeshi la wananchi wa Tanzania. Hivyo siyo tu kwamba alikuwa akizifahamu vizuri siri na mbinu nyingi za mikakati ya jeshi la wananchi la Tanzania lakini vilevile alikuwa amelitumikia jeshi hilo kwa miaka mingi ya maisha yake. Kwa hiyo nyadhifa zile mbili muhimu za uongozi wa ndugu Adam Mwambapa akiwa kama kiongozi mkubwa mstaafu wa jeshi la wananchi wa Tanzania na hatimaye kushika wadhifa wa kisiasa kama balozi wa Tanzania nchini Burundi...



    zilikuwa zimeniweka njia panda katika kuhusisha utekaji wake na sababu za kijeshi au za kisiasa. Bado sikuweza kuona mwanga wowote katika fikra zangu hivyo nikaendelea mbele na uchunguzi wangu. Nikauacha ule mti uliokuwa kando ya lile bwawa la kuogelea na kupotelea kwenye giza zito lililokuwa chini ya ile miti iliyokuwa eneo lile.

     Mvua kubwa bado ilikuwa ikiendelea kunyesha na hivyo kunipelekea nitembee kwa tahadhari ya hali ya juu. Wakati nikiikaribia kona moja ya ile nyumba nikashtuka tena baada ya kukiona kitu fulani cheusi kisichoeleweka kikiwa kimelala ardhini umbali mfupi mbele yangu. Hali ile ikanipelekea tena niikamate vyema bastola yangu mkononi na kusogea karibu zaidi ya eneo lile huku macho yangu yakiwa makini kutazama pale chini.

     Mbwa mmoja mkubwa aina ya German shephered alikuwa ameuawa kwa risasi moja ya kichwani. Nilimgundua haraka baada ya kuinama na kumchunguza kwa makini mbwa yule. Kwa sekunde kadhaa nikaupisha utulivu kichwani mwangu huku kwa makini nikiyatembeza macho yangu taratibu kulichunguza eneo lile. Kulikuwa na alama za buti za jeshi kadhaa zilizokanyaga chini eneo lile hata hivyo nilipochunguza kwa makini nikagundua kuwa alama zile zilikuwa ni za mtu mmoja. Nilipoendelea kuchunguza vizuri alama zile nikagundua kuwa zilikuwa zimepotelea kwenye nyasi laini zilizopandwa kuizunguka ile nyumba. Hivyo nikahitimisha kuwa alama zile za buti za jeshi zilikuwa ni za mmoja wa watu waliohusika katika kumteka Balozi Adam Mwambapa.

     Hatimaye nikauacha ule mzoga wa mbwa na kupotelea tena gizani chini ya ile miti iliyokuwa kando ya ile nyumba. Nyuma ya ile nyumba kulikuwa na tenki moja kubwa la maji na kando ya tenki lile kulikuwa na karo kubwa la kuoshea vyombo na kufulia pembeni ya sehemu maalum ya kuanikia nguo ambayo kwa wakati ule haikuwa na nguo. Nilipoendelea kuchunguza nikakiona kibanda kidogo kando ya eneo lile na niliposogea karibu na kukichunguza kibanda kile nikagundua kuwa kile kibanda kilikuwa kikitumika kama makazi ya mbwa wa ile nyumba.

     Mwishowe nikaifikia sehemu ya nyuma ya ile nyumba na kuanza kupanda ngazi chache za varandani kuelekea mlango wa nyuma wa nyumba ile. Ilikuwa ni wakati huo pale nilipouona tena mzoga mwingine wa mbwa mkubwa kama yule wa awali ukiwa umelala kwenye sakafu ya ile varanda. Kando ya yule mbwa kulikuwa na michirizi kadhaa ya damu kutoka kwenye jeraha la risasi lililokuwa kifuani kwa yule mbwa. Nikasimama kidogo kuupeleleza mzoga ule kabla ya kuendelea na safari. Hatimaye nikaufikia mlango wa nyuma wa ile nyumba na kusimama kwa utulivu nikitazama huku na kule katika namna ya kuchunguza hali ya usalama wa eneo lile. Hali bado ilikuwa shwari na sikuona dalili zozote za upinzani katika harakati zangu hivyo nikausogelea ule mlango wa nyuma wa ile nyumba na kuanza kuuchunguza kwa makini.

     Jambo la kustaajabisha ni kuwa ule mlango wa nyuma wa ile nyumba ulikuwa umefungwa kwa funguo na geti lake la grili lilikuwa limefungwa kikamilifu kwa kufuli kubwa la Sorex. Kushughulika na lile kufuli na kuufungua ule mlango niliona ni kazi ambayo ingenipotezea muda mwingi hivyo nikaamua kutafuta mbadala wa namna rahisi zaidi ya kuingia mle ndani. Pembeni ya ile varanda kulikuwa na dirisha moja upande wa kushoto. Nilipolisogelea lile dirisha na kuchunguza kwa utulivu nikagundua kuwa lile lilikuwa ni dirisha la sehemu ya jiko la ile nyumba kwani pamoja na kwamba pazia la lile dirisha lilikuwa limefunika kwa ndani lakini kupitia uwazi mdogo pembeni ya dirisha lile niliweza kuona mle ndani kwa msaada wa kurunzi yangu yenye mwanga mkali.

     Nikajaribu kulifungua lile dirisha kwa hila lakini sikufanikiwa kwani lile dirisha lilikuwa limefungwa ndani kwa komeo. Hivyo hatimaye nikaamua kuvunja kioo cha lile dirisha kwa pigo moja la kitako cha bastola yangu mkononi. Kile kioo kilipovunjika nikapenyeza mkono na kufyatua komeo kulifungua lile dirisha. Muda mfupi uliofuata nikawa nimefanikiwa kulifungua lile dirisha na kuingia mle ndani ya kile chumba cha lile jiko nikitabaruku.

     Kwa dakika chache nikatulia mle ndani ya kile chumba cha jiko huku macho yangu yakiusindikiza kwa utulivu mwanga mkali na mwembamba wa kurunzi yangu mkononi. Kile chumba cha jiko kilikuwa kimezungukwa na makabati ya vyombo yaliyojengewa vizuri ukutani na upande wa kushoto wa chumba kile kulikuwa na sinki kubwa la kuoshea vyombo lililopakana na ukuta msafi wa marumaru nyeupe. Nilipomulika chini nikaiona sakafu imara ya tarazo kabla ya kuizima kurunzi yangu.

     Hatimaye nikaufikia mlango wa kile chumba cha jiko na kuufungua taratibu katika utulivu wa hali ya juu. Ule mlango ulipofunguka nikajikuta nimetokezea kwenye korido pana lakini fupi kuelekea upande wa kulia. Kabla ya kuendelea mbele zaidi nikasimama katikati ya ile korido gizani huku nikiupima vizuri utulivu wa mle ndani. Sikusikia sauti ya kitu chochote mle ndani hivyo hali bado ilikuwa tulivu. Nikaamua kuiwasha kurunzi yangu mkononi na kumulika huku na kule katika namna ya kutaka kupata picha kamili ya mazingira yale kisha nikaizima tena. Hatua chache mbele ile korido ilikuwa imepinda kona kuelekea upande wa kushoto.

     Nikaifuata ile korido kwa utulivu na nilipofika mwisho nikaziona ngazi chache za kushuka chini. Bila kusita nikaanza kuzifuata zile ngazi nikishuka chini kwa tahadhari huku bastola yangu ikiwa mkononi na baada ya safari fupi nikajikuta nimetokezea kwenye ukumbi mdogo wenye meza iliyozungukwa na viti kumi na mbili. Ile meza ilikuwa katikati ya ule ukumbi mdogo na upande wa kulia kulikuwa na sinki moja lililokuwa kwenye kona. Sinki lile lilikuwa limepakana na rafu kubwa ya vyombo iliyojengewa vizuri ukutani.

     Niliposogea karibu na ile meza upande wa kulia nikaliona dirisha kubwa lakini pazia la dirisha lile lilikuwa limesogezwa kando. Nikasogea pale dirishani kwa utulivu na kutazama nje kisha nikawasha tena kurunzi yangu na kuanza kumulika mle ndani. Kupitia mandhari yale haraka nikatambua kuwa ule ulikuwa ni ukumbi wa kulia chakula wa ile nyumba na hapakuwa na kitu chochote cha maana eneo lile hivyo nikaendelea mbele zaidi na uchunguzi wangu.

     Nilipofika kwenye kona moja iliyokuwa upande wa kushoto wa ule ukumbi nikauona mlango na mlango ule ulikuwa umefunguliwa nusu hivyo sikuishika pale badala yake kwa tahadhari nikaingia mle ndani. Kwa kufanya vile nikajikuta nimetokezea kwenye sebule pana yenye umbo duara. Mara baada ya kuingia mle ndani nikasimama kando ya ile sebule na kuanza kumulika kwa kurunzi yangu mkononi nikiyapeleleza mandhari yale.

     Ilikuwa sebule kubwa yenye samani zote muhimu za kisasa. Kulikuwa na seti mbili za makochi ya sofa ya kifahari yaliyopangwa katika mtindo wa kuizunguka ile sebule. Sakafuni kulikuwa na zulia zuri la rangi nyekundu huku katikati ya sebule ile kukiwa na meza fupi ya kioo yenye umbo la pembe tatu. Upande wa kulia wa ile sebule kwenye kona kulikuwa na runinga pana iliyofungwa ukutani huku chini yake kukikiwa na meza fupi nyeusi yenye sistimu ya muziki, deki moja ya Dvd na kinyago kidogo cha askari shupavu akipuliza tarumbeta. Nilipomulika ukutani nikaziona picha mbalimbali za Balozi Adam Mwambapa akiwa katika hafla tofauti za majukumu ya kiserikali jijini Bujumbura. Upande wa kushoto wa ile sebule kwenye kona nyingine kulikuwa na meza fupi ya mapambo iliyotenganisha jokofu na feni. Pembeni ya meza ile kulikuwa rafu kubwa iliyopangwa vitabu na majalada mengi na juu ya rafu ile kulikuwa na vinyago vya kiafrika vilivyopangwa kwa ustadi wa hali ya juu. Kutoka pale nilipokuwa nimesimama upande wa kulia nikauona mlango mkubwa wa sebuleni ile katikati ya madirisha mapana ya vioo yaliyofunikwa kwa mapazia marefu. Kulikuwa pia na mlango mwingine upande wa nyuma wa ile sebule na nilipochunguza nikagundua kuwa ule ulikuwa ni mlango wa kuelekea kwenye vyumba vya kulala vya ile nyumba.

     Nilitaka kupata tathmini ya kina juu ya lile tukio la kutekwa kwa Balozi Adam Mwambapa mle ndani ya ile nyumba hivyo ikanibidi nisogee katikati ya ile sebule na kuanza kumulika kwa ile kurunzi yangu mkononi. Taswira iliyojengeka machoni mwangu ni kuwa kulikuwa na uharibifu mkubwa uliofanywa pale sebuleni kupitia mashambulizi ya risasi. Baadhi ya makochi ya sofa yaliyokuwa pale sebuleni yalikuwa yametobolewa vibaya kwa risasi. Kioo cha dirisha moja kilikuwa kimevunjika. Kabati kubwa la pale sebuleni upande wake mmoja ulikuwa umevunjwa na simu ya mezani iliyokuwa juu ya stuli ndefu kando ya kochi mojawapo la pale sebuleni ilikuwa imepigwa chini na kuvunjika vipandevipande. Mpangilio wa samani za pale sebuleni ukanitanabaisha kuwa kulikuwa kumetokea varangati la kukata na shoka wakati watekaji walipovamia nyumba ile.

     Kwa kweli hali ya pale sebuleni ilikuwa segemnege. Nikiwa nimesimama katikati ya ile sebule nikajikuta nikivutiwa na nyaraka za kiofisi zilizokuwa kwenye kabati la pale sebuleni. Hivyo nikaanza kuzitupa hatua zangu kwa utulivu kulifikia lile kabati. Mle ndani kulikuwa na giza zito. Nilitamani kuwasha taa ya pale sebuleni hata hivyo nafsi yangu ilinionya kuwa kwa kufanya vile huwenda ningeweza kuyavuta macho ya adui ambayo yangekuwa jirani na eneo lile.

     Hatimaye nikawa nimelifikia lile kabati na kwa msaada wa kurunzi yangu mkononi nikaanza kufanya upekuzi. Nilipovichunguza vile vitabu nikagundua kuwa vilikuwa ni vitabu vya kiofisi vinavyohusu masuala mbalimbali ya mahusiano ya kimataifa hivyo nikaachana navyo na kuanza kuchangamkia majalada yaliyokuwa yamepangwa sehemu ya chini ya lile kabati. Nikayapekuwa yale majalada kwa utulivu moja baada ya lingine hata hivyo nilimaliza zoezi lile pasipo kupata kitu chochote cha kunisaidia katika harakati zangu kwani ndani ya majalada yale niliambulia kukuta na ajenda za vikao vilivyopita, barua za kiofisi zilizoegemea masuala ya utendaji, vimemo vya hapa na pale na barua tofauti za mialiko ya kitaifa.

     Mwishowe nikaachana na yale majalada na kuanza kufanya upekuzi katika droo za chini za lile kabati. Droo ya kwanza ilikuwa imejaa matoleo ya zamani ya magazeti mbalimbali ya nchini Burundi na mengine ya nchi za jirani. Droo ya pili ilikuwa na bahasha moja kubwa ya kaki yenye vyeti mbalimbali vya utumishi bora alivyowahi kutunukiwa balozi Adam Mwambapa wakati wa utumishi wake. Hivyo bado hapakuwa na taarifa zozote za maana za kuweza kunisaidia.

     Wakati nikifungua droo ya tatu ya lile kabati ili niendelee na upekuzi wangu ghafla hisia fulani zikanijia akilini na kuniletea maradhi ya hofu. Moyo wangu ukapiga kite kwa nguvu na hapo nikaanza kuhisi kijasho chepesi kikianza kushuka mgongoni kabla ya koo langu kukauka. Nilihisi kuwa kulikuwa na mtu aliyesimama hatua chache nyuma yangu ingawa sikuweza kuthibitisha jambo hilo kwa haraka badala yake nikaikamata vyema bastola yangu mkononi na kugeuka nyuma yangu taratibu. Sikufanikiwa kwani muda ule nikahisi chuma baridi kikitekenya kisogo changu.

    “Tupa bastola yako chini komredi’’. Sauti nzito ya kiume yenye lafudhi mbovu ya kiswahili cha kirundi ikanionya kutoka nyuma yangu. Kwa sekunde kadhaa nikajikuta nimeganda kama sanamu huku maamuzi yangu yakiwa njia panda.

    “Jitahidi kidogo kuwa msikivu komredi huu siyo wakati wa kuleta hila. Nimesema tupa bastola yako chini’’. Ile sauti nyuma yangu ikarudia kunionya na mara hii sikuhisi mzaha wowote hivyo taratibu nikaiweka chini bastola yangu huku nikishindwa kabisa kuamini kama nilikuwa nimejiingiza mtegoni.

    “Wewe ni nani?”. Nikauliza kwa sauti ya kupwaya huku nikigeuka taratibu na kutazama nyuma yangu hata hivyo sikufanikiwa badala yake nikajikuta nikikabiliana na maumivu makali ya kofi zito la sikioni lililonipelekea nianze kuhisi kichefuchefu.

    “Tulia hivyohivyo kenge mkubwa wewe”. Yule mtu akaendelea kunitahadharisha huku akisogea karibu na kuipiga bastola yangu mbali na eneo lile.

    “Mko wangapi?’’. Yule mtu akaniuliza huku akinipekuapekua maungoni na namna ya upekuaji ule ulikuwa na kila namna ya kunidhalilisha.

    “Tuko watatu”. Nikaamua kudanganya pasipo kufahamu kuwa uongo ule ungekuwa na madhara gani huko mbeleni.

    “Muongo wewe sasa hao wenzako wako wapi?’’. Yule mtu akaniuliza kwa kisirani huku akinipekua kwenye mifuko ya nyuma ya suruali yangu huku akinipapasa makalio yangu. Kwa kweli tukio lile lilinipandisha sana hasira hata hivyo sikuwa na namna ya kufanya kwani ule mtutu wa bastola ya yule mtu ulikuwa bado ukinitazama kisogoni nyuma yangu.

    “Sasa kama mimi ni muongo mbona unawaulizia hao wenzangu?”. Nikamuuliza yule mtu nyuma yangu hata hivyo sikujibiwa badala yake nikajikuta nikishushiwa kipigo cha nguvu cha ngumi kavu mgongoni na mbavuni hali iliyonipelekea nianze kuhisi kichomi huku nikihema ovyo.

    “Jibu vizuri swali nililokuuliza na usilete mambo ya siasa”. Yule mtu akamalizia kwa kunizaba kofi moja la shingoni na nguvu ya mkono wake iliyotumika ikanitanabaisha kuwa nilikuwa nimeingia kwenye mikono ya binadamu mbabe mwenye nguvu za ajabu aliyekomaa mwili wake kama mti wa mninga. Kisha yule mtu akanikwida shingoni na kunigeuza katika namna ya kunifanya nimtazame. Mbele yangu alikuwa amesimama mwanaume mrefu kunizidi mimi na mweusi kama lami huku akiwa amenyoa upara na kukipelekea kichwa chake kilichosongwa na mishipa mingi ya damu iliyosambaa ovyo kama mizizi ya mmea wa mhindi kionekane vizuri. Ile njemba ilikuwa kipande cha mtu chenye misuli imara ya nguvu. Kifuani alikuwa amevaa fulana mchinjo ya jeshi iliyokibana vyema kifua chake kiasi cha kunipelekea nidhani kuwa fulana ile ingetatuka muda mfupi ujao. Yule mtu chini alikuwa amevaa suruali ya kombati na miguuni alikuwa amevaa buti ngumu za jeshi. Mkononi alikuwa ameshika bastola ambayo haraka nilipotazama kwa kurunzi yangu nikagundua kuwa ilikuwa ni aina ya 22 Caliber Revolver na hapo matumaini ya kutoka salama kwenye himaya ya mtu yule yakapotea kabisa.

    “Wenzako wako wapi?’’. Yule mtu akaniuliza huku akikunja sura kama aliyeona chembe ya mavi kwenye sahani ya wali hotelini.

    “Nimewaacha mjini”. Nikaongea kwa utulivu huku akili yangu ikianza kufanya kazi. Yule mtu akanitazama kwa utulivu kama ambaye anafikiri jambo kisha akaniuliza.

    “Mbona tumeambiwa kuwa umekuja peke yako?”. Swali la yule mtu likanifanya niyapeleke macho yangu kumtazama usoni huku dhahiri nikionesha kushtushwa na maelezo yake...



    ...“Mmeambiwa na nani?”. Nikamuuliza yule mtu hata hivyo hakunijibu badala yake muda uleule yule mtu akanikwida shingoni na kiunoni kisha akaninyanyua juu juu na kunibwaga vibaya kwenye lile kabati. Lile kabati likapasuka vipandevipande na kupelekea vitabu na yale majalada kutawanyika ovyo sakafuni. Nikapiga yowe kali la maumivu huku nikijitahidi kuwahi kusimama lakini ilikuwa kazi bure kwani yule mtu aliniwahi kabla sijasimama akanikwida tena na kuninyanyua juu. Nikijitahidi kujitetea kwa kila namna nikirusha ovyo miguu na mikono lakini bado haikunisaidia kitu kwani lile jitu likanibeba mzegamzega na kwenda kunibwaga tena kwenye ile meza fupi ya kioo iliyokuwa pale sebuleni. Japokuwa nilijitahidi kwa kila namna kujihami lakini lile jitu lilikuwa na nguvu nyingi kama roboti hivyo likanibwaga juu ya ile meza kama furushi. Ile meza ikapasuka vipandevipande na baadhi ya vioo vyake vikanichanachana mikononi. Nikapiga tena yowe huku maumivu makali yakisambaa mwilini huku nikianza kuingiwa na hofu ya kudhibitiwa kikamilifu. Lile jitu likaangua kicheko cha dhihaka na kujipigapiga kibabe kifuani kama sokwe mtu.

     Nikiwa nimeanza kuhisi hatari ambayo ingenikaribia endapo ningeendelea kuruhusu mashambulizi yale zaidi nikakumbuka haraka ule upande ambao bastola yangu ilikuwa imetupwa na teke la lile jitu. Hivyo nikajiviringisha kwa kasi sakafuni kuelekea ule upande ilipoangukia bastola yangu. Hata hivyo sikufanikiwa kwani lile jitu ni kama tayari lilikuwa limeshtukia dhamira yangu hivyo likaniwahi kwa kunitandika teke makini la tumbo lililonitupa kando kama paka mwizi. Sikuona tena kama kungekuwa na namna nyingine ya kujiokoa kutoka kwenye mikono matata ya lile dubwana hivyo nikawahi kujikaza na kusimama huku hasira za kudhibitiwa zikiwa zimenipanda kichwani kama mbogo aliyejeruhiwa.

     Lile jitu jeusi liliponifikia nikawahi kulitupia mapigo manne ya ngumi kavu za tumbo. Jambo la kushangaza ni kuwa lile jitu halikutia jitihada zozote za kujitetea badala yake likanyanyua mikono yake juu huku likiangua kicheko cha dharau na kutikisa kichwa chake kibabe katika namna ya kunionesha kuwa mapigo yangu hayakuwa yamefua dafu. Nikiwa katika hali ya kushangazwa na tukio lile jitu likanizaba kofi moja zito likitumia mgongo mkavu wa kiganja chake. Pigo lile likanipelekea nijihisi kama niliyepigwa na kipande cha mbao kavu ya mpingo. Nikarushwa na kutupwa sakafuni huku nikihisi maumivu makali yasiyoelezeka. Kwa kweli hali yangu ilizidi kuwa mbaya na kabla sijafikiria namna ya kufanya nikaliona lile jitu likinifuata pale chini. Sasa nilikuwa makini zaidi kwani nilianza kuona hatari kubwa ya kukamatwa mzimamzima kama siyo kupoteza maisha kabisa endapo ningeendelea kupokea mkong?oto wa lile dubwana. Hivyo nikajipanga kujihami zaidi kwa kufanya mashambulizi ya nguvu na yenye tija.

     Lile jitu likionekana kunogewa na mtindo wake mmoja wa kuninyanyua juu na kunibwaga chini kama mcheza miereka mara aliponifikia pale chini akainama tena ili aninyanyue na kunibwaga. Mara hii hakufanikiwa kwani niliwahi kujibetua na kumtandika pigo moja takatifu la teke la kidevu lililompelekea ajing?ate ulimi na kuangua kilio kama mtoto mdogo huku akijishika mdomoni. Nikawahi kusimama wakati lile jitu likiendelea kupepesuka na hapo nikampelekea mapigo matatu makini ya chapuchapu ya kareti shingoni na tumboni kwake hata hivyo sikufua dafu kwani yule mtu aliyakwepa mapigo yangu kama mchezo akiyapangusia mbali.

     Nikabadili mtindo wa mapigano nikitumia Kung fu na hapo nikatupa mapigo matatu makini. Hong Cha, Lei tai na Tang Soo Do hata hivyo bado sikuweza kufua dafu kwani yule mtu alikuwa mpiganaji wa kiwango cha juu huku akionekana kuwa makini sana kuzisoma nyendo zangu. Hata hivyo nilikuwa nimelipunguza kasi kwa kiasi kikubwa kiasi cha kumpelekea atumie wake muda mwingi kujihami badala ya kushambulia. Miaka sita ya mafunzo yangu ya kijasusi niliyokuwa nimeyapata nchini China katika chuo kimoja cha sanaa ya juu ya mapigano Martial Arts. Mafunzo ambayo nilikuwa nimehitimu vizuri katika alama za juu sana kiasi cha kuridhisha kuweza kukabiliana na aina yoyote ya mpiganaji. Hivyo nilipoona mapigo yangu hayaelekei kuniletea majibu ya haraka nikaamua kubadili tena namna ya upambanaji nikitumia mtindo mwingine wa mapigano wa Kung fu uitwao Zui quan au pia mtindo huo ukifahamika kama Drunken first. Mtindo mzuri wa mapigano wenye mapigo hatari kama ule wa Cao guojiu unaonifanya nionekane kama mlevi aliyechanganyikiwa huku lengo langu kubwa likiwa ni kushambulia sehemu laini za mwili wa lile dubwana huku nikimpotezea umakini katika malengo yake.

     Wakati nikilikaribia tena lile jitu nikagundua haraka kuwa lilikuwa limeshtukia hila yangu ingawa halikuweza kufahamu vizuri mikakati niliyokuwa nayo. Hivyo lile jitu likaanza kutupa ngumi mfululizo kichwani mwangu lakini mara hii ilikuwa ni kazi bure kwani nilizikwepa ngumi zake kwa ulaini pasipo kutumia nguvu kubwa mwilini huku nikisogea huku na kule na kama mlevi lakini wakati huo nikiendelea kumdokoa taratibu sehemu laini za mwili wake kama mbavuni, tumboni, shingoni na kichwani.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

     Lile jitu likaanza kuchanganyikiwa huku likishindwa kuelewa namna ambavyo ushindi ulivyokuwa ukihamia kwangu taratibu. Lile jitu lilipoona kuwa hali inazidi kuwa mbaya likawa linajitahidi kunikwepa na kukaa mbali na mimi huku likifuatilia nyendo zangu kwa makini na kwa hakika ile ilikuwa mbinu makini iliyoninyima nafasi nzuri ya kulifikia lile jitu kirahisi. Hivyo lile jitu likawa likinishambulia zaidi kwa mateke.

     Teke la kwanza lililorushwa na lile jitu niliwahi kuliona mapema hivyo nikainama chini kidogo na kuliacha likikata upepo bila mafanikio lakini wakati nikifurahia utundu wangu teke lingine likaja na kukibamiza vibaya kifuani kiasi cha kufanikiwa kunitupa nyuma huku nikiyumbayumba ovyo. Pigo lingine la teke makini la Side-snap kick nikawahi kulipangua lakini lile jitu lilikuwa na nguvu nyingi kwani pamoja na kufanikiwa kulipangua lile pigo lakini bado nilihisi maumivu makali sana mikononi huku nikipepesuka na hatimaye kuanguka chini. Lile jitu kuona vile likapata matumaini ya kuibuka na ushindi hivyo likawahi kunitandika teke lingine la mtindo wa mapigano ya kijapani liitwalo Mae geri hata hivyo nilikuwa makini kuwahi kujiviringisha kando ya eneo lile. Hata hivyo lile jitu halikunipa nafasi ya kutabaruku badala yake akanifuata na kutupa teke lingine ambalo haraka nililikwepa kwa kujitupa kando sakafuni kisha nikaizungusha miguu yangu chini kwa mtindo wa mapigano wa kibrazil itwao Capoeira nikilichota lile jitu mtama maridadi wa kiufundi uliompaisha hewani kabla ya kutua sakafuni kwa matako na hapo tusi zito likamponyoka mdomoni.

     Lile jitu likawahi kusimama lakini nikiwa tayari nimejiandaa kwa tukio lile nikawahi kujibetua kwa sarakasi ya Sama soti kisha nikamchapa pigo moja takatifu la Flying kick na kumtia udhaifu mkubwa kifuani na kichwani kwake. Pigo lile likapelekea lile jitu lirudi kinyumenyume na kupepesuka ovyo huku likipiga mayowe ya hofu. Sikutaka kumkawiza hivyo nikaruka tena hewani na kumchapa pigo lingine la teke la kijapani liitwalo Mikazuki geri ambalo lilikata mzizi wa fitina kwani lile jitu hatimaye likaanguka chini kama mti wa mbuyu na kuvikalia bila kupenda vile vipande vya kioo cha ile meza kilipasuka pale chini sakafuni. Lile jitu likaguna kwa maumivu makali hata hivyo likajikaza na kuwahi kusimama kama Zombi kisha likajipukuta na kujiweka sawa halafu likaanza kunifuata kwa hasira kama Mbogo. Nikajitahidi kulikwepa bila mafanikio na liliponikaribia likatupa pigo moja makini la Kung fu kifuani kwangu lililonisababishia maumivu makali sana. Nikapepesuka na kurudi nyuma na hilo likawa kosa kubwa kulifanya kwani lile jitu likanichapa pigo la teke matata la kijapani liitwalo Yoko geri shingoni na kama nisingefanya jitihada za haraka za kulipoza pigo lile huwenda lingenivunja shingo kama siyo kunisambaratisha kabisa. Lile jitu kuona vile likanogewa na matunda ya kazi yake hata hivyo mara hii bahati haikuwa kwake kwani lilipotupa pigo lingine la teke nikawahi kulidaka na hapo nikapata nafasi nzuri ya kumtandika teke la korodani lililomsababishia maumivu makali na kumpelekea abweke kama mbwa mwizi huku akirukaruka kama aliyekanyaga kaa la moto wakati huo mimi nikijirusha upande wa pili.

     Tukio lile likawa limelipandisha hasira sana lile jitu kwani nililiona likikimbia haraka kuelekea upande ule ile bastola yake ilipoangukia hata hivyo niliwahi kulizuia kwa kulisukumia kochi moja la pale sebuleni kwa mguu wangu. Lile jitu kuona vile likaanza kuokota vitu na kuanza kunirushia kwa hasira na kwa kuwa sote tulikuwa gizani ikaniwia vigumu kuvikwepa vitu vile hivyo nikawa nikihaha huku na kule. Kumbe lile jitu lilikuwa likinifanyia hila kwani wakati nikifikiria namna ya kufanya katikati ya giza lile mara nikajikuta tayari nimeenea kwenye kabari yake matata. Nikajikuta nikifurukuta bila mafanikio kwani lile jitu lilizidi kuikaza vizuri mikono yake na kuninyima kuvuta hewa kwa urahisi. Sikutaka kufa kifo laini cha kondoo anayechinjwa huku ameinamisha shingo mwenyewe hivyo nikaamua kuanzisha purukushani na mikikimikiki ya kuvuruga malengo. Hata hivyo lile jitu halikuniachia kwani mikono yangu sasa lilikuwa limeibana kisawasawa na kwa kuwa lile jitu lilikuwa na nguvu nyingi hali ikazidi kuniwia ngumu lakini hatimaye nikapata ufumbuzi.

     Nilikusanya nguvu za kutosha kisha nikalitandika kichwa cha nguvu lile jitu nyuma yangu na kuupasua vibaya mwamba wa pua yake. Lile jitu likapiga yowe kali la maumivu huku likiniachia bila kupenda na hapo nikageuka na kulitupia pigo kali la kareti shingoni lililolipelekea lile jitu lipepesuke. Ulikuwa ni wakati mzuri wa kufunga kazi hivyo nikatupa ngumi mbili kavu tumboni mwake na kisha kuhitimisha ngwe ile kwa pigo makini la Jeet Kune Do, a very nice finishing kick la kichwani. Lile jitu likapiga yowe kali la maumivu wakati lilipojipigiza kichwa chake ukutani kisha likaanguka chini na kutulia kimya. Nilipolisogelea karibu kulichunguza nikagundua kuwa tayari lilikwisha kata roho huku shingo yake ikiwa imevunjika na damu ikimtoka puani na mdomoni.

     Kwa sekunde kadhaa nikabaki nimesimama nikilitazama lile jitu huku nikitweta ovyo na kijasho chepesi kikinitoka usoni. Kwa kweli nilikuwa nimechomoka na ushindi mwembamba wa pambano kali la kukata na shoka. Hatimaye nikalisogelea lile jitu pale chini na kuanza kulipekua mifukoni. Sikupata kitu chochote cha maana zaidi magazine moja ya bastola iliyojaa risasi.

     Sasa nilikuwa na hakika kuwa uwepo wangu pale jijini Bujumbura ulikuwa ukitambulika rasmi na kikundi cha watu hatari ambao kwa namna moja au nyingine nisingesita kuwahusisha moja kwa moja na lile tukio la kutekwa kwa Balozi Adam Mwambapa. Nikalikumbuka lile gari jeupe Landcruiser Hardtop lililokuwa likinifuatilia nyuma yangu muda mfupi baada ya kutoka kwenye lile jengo la ubalozi wa Tanzania nchini Burundi ambalo ndani yake kulikuwa na wanajeshi. Kisha nikalitazama lile jitu pale chini ambalo lilikuwa limevaa sare za jeshi na hapo nikatambua kuwa nilikuwa nikielekea kukabiliana na watu wa namna gani katika safari yangu ya kijasusi.

     Sikuwa na muda zaidi wa kuendelea kupoteza eneo lile hivyo haraka nikaanza kuitafuta bastola na ile kurunzi yangu ndogo ya kijasusi kule ilipoangukia. Ndani ya muda mfupi nikawa nimefanikiwa kuipata ile bastola na ile kurunzi hivyo nikawa nimevirudisha tena kwenye himaya yangu. Nilipomaliza nikaelekea tena kwenye lile kabati na kumalizia upekuzi wangu kwenye zile droo za chini pasipo kuambulia kitu chochote cha maana. Sikuona dalili za kupata kitu chochote cha kunisaidia pale sebuleni hivyo nikaikamata vyema bastola yangu mkononi na kuelekea vyumbani nikipitia kwenye mlango uliokuwa nyuma ya ile sebule mara baada ya kupanda ngazi chache za eneo lile. Wakati nikiendelea na safari ile nikajipa umakini zaidi hasa baada ya kulikumbuka lile tukio la uvamizi nililofanyiwa na lile jitu muda mfupi uliopita.

     Ule mlango ulikuwa wazi hivyo mara baada ya kumaliza kuzipanda zile ngazi chache kutokea pale sebuleni nikajikuta nimetokezea kwenye korido pana iliyokuwa ikitazamana na milango minne. Milango miwili upande wa kushoto na milango miwili mingine upande wa kulia huku mlango mmoja ukiwa mwisho wa ile korido. Mara baada ya kuingia kwenye ile korido nikasimama kwa sekunde kadhaa nikimulika kwa kurunzi yangu mkononi katikati ya giza nene lililokuwa limetanda kwenye ile korido. Sikuona kiashiria chochote cha uhai kwani ile korido ilikuwa imemezwa na utulivu wa hali ya juu. Sauti pekee iliyosikika ilikuwa ni ile ya mvua kubwa iliyokuwa ikianguka juu kwenye paa la ile nyumba. Nikiwa nimeanza kuridhishwa na hali ya utulivu wa mle ndani nikaanza kujongea taratibu nikielekea chumba cha kwanza cha kwenye ile korido kilichokuwa upande wa kushoto. Muda mfupi uliofuata nikawa nimefika na nilipojaribu kuufungua mlango wa kile chumba nikagundua kuwa ule mlango haukuwa umefungwa hivyo nikausukuma taratibu na kuingia mle ndani.

     Chumba kilikuwa kipana chenye nafasi ya kutosha. Upande wa kushoto kulikuwa na kabati kubwa la nguo la ukutani hata hivyo niliposogea karibu na kulichunguza vizuri lile kabati sikuona kitu chochote ndani yake zaidi ya suruali moja ya kiume iliyotundikwa kwenye ufito mwembamba huku ikionekana kutelekezwa kwa muda mrefu kwa namna ilivyokuwa imeshika vumbi. Pembeni ya kabati lile kulikuwa na meza ndogo ya mbao yenye miguu mitatu iliyochongwa vizuri kando ya kochi moja la sofa. Nilipogeuka na kutazama katikati ya kile chumba nikaona kitanda kikubwa cha futi sita kwa sita kilichotandikwa shuka safi za rangi ya nyeupe. Kando ya kitanda kile kulikuwa na meza ndogo yenye droo mbili na juu ya meza ile kulikuwa na taa ndogo ya Lampshade. Nikaisogelea ile meza ndogo na kuzichunguza zile droo mbili hata hivyo sikuona kitu chochote mle ndani hivyo nikazifunga na kutazama sehemu ya chini ya kile kitanda ambako pia sikuona kitu chochote cha maana. Nikaendelea kupeleleza sehemu nyingine za kile chumba nikitarajia kupata kitu chochote cha kunisaidia katika harakati zangu. Sikupata kitu chochote mle ndani hivyo hatimaye nikaelekea kwenye mlango wa kile chumba na kutoka nje.

     Chumba cha pili kukifanyia uchunguzi kwenye ile nyumba kilikuwa ni kile kilichokuwa kikitazamana na kile cha awali ambapo haraka nilipokichunguza nikagundua kuwa kilikuwa kikitumika kama stoo. Ndani ya kile chumba kulikuwa na vifaa vya kutunzia bustani na mazingira kwa ujumla kama jembe, reki, panga, buti za mvua na vifaa vingine vidogo vidogo. Kulikuwa pia na magunia matatu ya mpunga yaliyopangwa vizuri mle ndani na ziadi ya vile sikuona kitu kingine chochote cha maana.

     Chumba kilichofuata mbele upande ule wa kulia wa ile korido kilikuwa ni chumba cha mazoezi kutokana na vifaa vya kufanyia mazoezi vilivyokuwa mle ndani huku sakafu yake ikiwa imefunikwa kwa zulia zuri la rangi nyekundu. Hivyo mle ndani bado hapakuwa na kitu chochote cha maana katika harakati zangu. Hatimaye nikakiacha kile chumba na kutoka nje nikielekea kwenye chumba kingine cha upande wa pili kilichokuwa kikitazama na kile nilichotoka.

     Nilipoingia ndani ya kile chumba haraka nikagundua kuwa mazingira yake hayakuwa tofauti sana na ya kile chumba cha mwanzo. Hata hivyo niligundua kuwa kile chumba kilikuwa kikitumika na mwenyeji wake kutokana na mandhari ya mle ndani ingawa nilipochunguza...

    vizuri sikuona dalili zozote za uwepo wa mtu mle ndani. Hata hivyo sikukata tamaa badala yake nikafanya upekuzi wa hapa na pale ambao pia haukuniletea manufaa yoyote hivyo mwishowe nikaamua kutoka nje ya kile chumba mikono mitupu.

     Chumba kilichosalia kilikuwa ni kile ambacho mlango wake ulikuwa mwisho ukitazamana na ile korido. Nikausogelea mlango wa kile chumba kwa tahadhari huku bastola yangu ikiwa mkononi. Nilipofika karibu nikagundua kuwa mlango wa kile chumba ulikuwa nusu wazi hivyo nikanyata taratibu na kuingia mle ndani. Mara baada ya kuingia mle ndani ya kile chumba kwa sekunde kadhaa nikasimama kando ya ule mlango huku nikiupima utulivu wa mle ndani. Kupitia mwanga hafifu wa taa za nyumba za jirani kwa mbali niliweza kuona mapazia marefu na mepesi ya madirisha mawili ya kile chumba yakipepea kwa utulivu na hivyo kuiruhusu miali hafifu ya ule mwanga kupenya madirishani na kuingia mle ndani. Nikayatembeza macho yangu taratibu mle ndani nikichunguza kama kungekuwa na mjongeo wowote wa kiumbe hai mle ndani. Hali bado ilikuwa tulivu lakini haikunipelekea niamini kuwa nilikuwa sehemu salama.

     Nikiwa nimeikamata vyema bastola yangu mkononi pamoja na ile kurunzi ndogo kwa tahadhari nikaanza kukatisha katikati ya kile chumba nikielekea upande mmoja wenye dirisha. Wakati nikifanya vile ghafla nikashtushwa na sauti hafifu ya mtu akikohoa mle ndani. Haraka nikageuka kwa tahadhari huku bastola yangu ukiwa tayari kufanya kazi. Ile sauti ya mtu anayekohoa ikasikika tena na mara moja nikagundua kuwa ilikuwa ikitokea kwenye kona moja ya kile chumba iliyokuwa upande wa kulia. Haraka nikawasha kurunzi yangu na kumulika kwenye ile kona na nilichokiona mbele yangu kikanishtua kama siyo kunifedhehesha.

     Kijana mdogo alikuwa ameegemea kwenye kona ya chumba kile huku akihema kwa tabu sana. Alikuwa amevaa suruali nyeusi ya kitambaa na fulana nyeupe hata hivyo ile fulana ilikuwa imelowa damu chapachapa. Yule kijana alikuwa amejishika tumboni kwa mikono yake miwili katika namna ya kupambana na maumivu makali ya tumbo. Bado kulikuwa na kila dalili uhai machoni mwake hivyo nikamsogelea taratibu pale chini kwenye kona alipoketi na wakati nikimsogelea haraka nikagundua kuwa kulikuwa na michirizi ya damu iliyotokea kwenye mlango wa kile chumba hadi pale chini yule kijana alipokuwa ameketi. Sasa nilifahamu kuwa ile michirizi ya damu ilikuwa imetokana na jeraha lililokuwa kwenye sehemu ya tumbo la yule kijana. Loh! ile damu ilikuwa nyingi sana. Hatimaye nikamfikia yule kijana kwa tahadhari kisha nikainama na kumchunguza huku nikishindwa kuelewa kilichomsibu. Katika hali nisiyotarajia yule kijana akafumbua macho ghafla kisha akiniongelesha kwa sauti hafifu akinisihi.

    “S?il vous plaît ne me tuez pas’’. Tafadhali usiniue. Namna ya uzungumzaji wa kifaransa cha yule kijana haraka ukanitanabaisha kuwa yule kijana alikuwa mtanzania mwenzangu.

    “Wewe ni mtanzania?”. Nikamuuliza yule kijana kwa shauku. Yule kijana akanitazama kwa mshangao kabla ya kutabasamu kisha akanijibu kwa sauti hafifu huku akijitahidi kumeza funda la mate.

    “Ndiyo!”. Yule kijana akanijibu kwa sauti dhaifu huku nikishangazwa na tabasamu lake katikati ya hali ile mbaya ya kiafya aliyokuwanayo. Nilipomchunguza vizuri yule kijana tumboni nikakiona kisu kikubwa kikiwa kimezama tumboni mwake na hivyo sehemu ya mpini tu wa kisu kile kubaki nje.

    “Tafadhali naomba unipeleke hospitali vinginevyo nitafia hapa”. Yule kijana akinisihi kwa sauti hafifu iliyopoteza matumaini hata hivyo nilipomtazama kwa makini nikagundua kuwa endapo ningemchukua na kumuwahisha hospitali ni dhahiri kuwa nisingefikanaye mbali. Kulikuwa na kila dalili kuwa yule kijana angekufa katika muda mfupi sana kuanzia pale kutokana na kizidiwa na maumivu makali na damu nyingi aliyopoteza katika lile jeraha tumboni mwake. Roho yake ni kama ilikuwa ikining?inia kwenye uzi mwembamba sana wa pamba chakavu ambao muda wowote ungekatika. Hata hivyo sikutaka kumkatisha tamaa badala yake nikampa matumaini.

    “Ondoa shaka wala hautakufa kwani nimefika hapa kukusaidia”. Nikaongea kwa utulivu huku nikikiegemeza kichwa chake mkononi mwangu huku nikimsogelea karibu ili nimsikie vizuri.

    “Jina lako nani?”. Nikamuuliza

    “Naitwa Sundi”. Yule kijana akaongea kwa sauti dhaifu ya mkoromo.

    “Wewe ni mfanyakazi wa humu ndani?”. Nikamuuliza.

    “Ndiyo”. Sundi akaitikia kwa sauti dhaifu iliyonipelekea nitege sikio langu karibu zaidi na mdomo wake.

    “Balozi Adam Mwambapa yuko wapi?”. Nikamuuliza yule kijana na bilashaka swali langu lilisababisha mshtuko mkubwa usoni mwake kiasi cha kunipelekea nishindwe kumuelewa badala yake nikamuona akinishika mkono wangu taratibu huku akitabasamu. Hata hivyo nilishangazwa sana na machozi mepesi yaliyoanza kutiririka mashavuni mwake pasipo kusema neno lolote. Macho yangu yakaweka kituo kumtazama na hapo nikajikuta nikiingiwa na simanzi kwani sikuwa nimeona ishara yoyote ya furaha kiasi cha kumpelekea yule kijana atabasamu katika hali ile.

    “Tafadhali naomba uniambie Balozi Adam Mwambapa yuko wapi?”. Nikarudia kumuuliza Sundi huku taratibu nikimpigapiga mgongoni katika namna ya kumtia moyo. Sundi akanitazama tena katika hali ya kukata tamaa kabla ya kuzungumza kwa tabu.

    “Sifahamu alipo”. Jibu la Sundi likanipelekea nimtazame kwa mshangao hata hivyo haraka niligundua kuwa hali yake ilikuwa ikizidi kuwa mbaya kwani macho yake yalikuwa yakizidi kubadilika kwa kupoteza muono huku akihema kwa tabu kama mwanariadha wa mbio ndefu aliyekata tamaa na ushidi.

    “Naomba unipe maji ya kunywa. Nasikia kiu sana’’. Hatimaye nikamsikia Sundi akinisihi kwa tabu huku akinishika mikononi wangu na kunivuta karibu yake. Ile ilikuwa ni ishara mbaya sana katika uhai wa Sundi kutokana na ile hali mbaya ya afya aliyokuwa. Sasa kinywa chake alikuwa amekiachama kama ishara ya kuhitaji maji ya kunywa kutokana na kiu kali ya ghafla aliyokuwa nayo. Ni dhahiri kuwa kifo kilikuwa kikimuhitaji Sundi kuliko wakati wowote wa maisha yake na uzoefu ukanikumbusha kuwa endapo ningempa maji mara baada ya kuyanywa hiyo ndiyo ingekuwa safari yake ya mwisho katika sayari hii. Hata hivyo nilifahamu kuwa bila kumpa Sundi maji ya kunywa basi asingeweza kuzungumza tena katika sehemu ndogo iliyosalia ya uhai wake. Hivyo taratibu nikaanza kujitoa mikononi mwake nikipanga kwenda kumchukulia maji ya kunywa kwenye ule ukumbi wa kulia chakula uliokuwa kando ya ile sebule. Hata hivyo wakati nikiwa katika harakati zile mara nikamuona Sundi akinizuia nisiondoke na nilipomtazama usoni nikagundua kuwa kulikuwa na jambo fulani alilotaka kuniambia. Hivyo nikasogea karibu yake zaidi huku nikimtazama usoni kwa shauku.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ukitoka hapa mtafute Padri Aloysius Kanyameza”

     “Nitampata wapi?”. Nikamuuliza Sundi kwa shauku hata hivyo hakunijibu badala yake akaendelea kunitazama kwa utulivu huku akitoa sauti hafifu ya mkoromo kinywani kwake. Nilipomtazama Sundi haraka nikagundua kuwa alikuwa katika hatua za mwisho kabisa za uhai wake. Nikajaribu kumtikisa kidogo na kumuita mara kadhaa lakini Sundi hakuitika badala yake hata ile sauti yake ya mkoromo hafifu ikafifia taratibu na hatimaye kukoma kabisa huku ameacha wazi macho yake akinitazama. Moyo wangu ukapiga kite kwa nguvu na nilipojaribu kupitisha mkono wangu mbele ya macho yake sikuona ishara yoyote ya mjongeo wa macho yake. Macho yake yakaendelea kunitazama kwa utulivu na hapo nikajua kuwa hakukuwa na uhai tena nafsini mwake. Kwa kweli roho iliniuma sana huku moyoni nikishikwa na simanzi isiyoelezeka. Sundi alikuwa amekufa kifo cha maumivu makali mno kwa pigo moja madhubuti la kisu kikubwa kilichozamishwa tumboni mwake pasipo namna yoyote ya utetezi.

     Nikameza fundo kubwa la mate huku nikiyafinya macho yangu katika namna ya kukabiliana na simanzi kubwa nafsini mwangu. Sikuwa na namna tena ya kufanya katika kuukoa uhai wa Sindi hivyo nikamfumba macho na mdomo wake huku taratibu nikimkaza sakafuni. Nikasimama kwa masikitiko huku nimejishika kiuno katika namna ya kukata tamaa sana na aina ile ya unyama. Sikuwa na shaka yoyote kuwa Sundi alikuwa ameuwawa wakati alipokuwa katika harakati za kumsaidia Balozi Adam Mwambapa wakati watekaji walipokuwa katika harakati zao ingawa kwa namna moja au nyingine hisia dhidi ya tukio lile zilikuwa zimeshindwa kabisa kukamilika kichwani mwangu.

     Kwanza nilijiuliza ni kwanini kisu ndiyo kilikuwa kimetumika kuupokonya uhai wa Sundi badala ya risasi kama ilivyokuwa kwa wale walinzi na wale mbwa kule nje ya nyumba. Pili nilishindwa kabisa kuelewa kuwa ni kwa nini Sundi alitabasamu wakati nilipokuwa nikimuuliza kuhusu Balozi Adam Mwambapa ingawa kicheko na tabasamu lake vilikuwa vimechanganyikana na majuto, uchungu na kilio kisichokuwa na uwiano na furaha yake ya kuigiza. Tatu nilikumbuka kuwa michirizi ya damu kutoka kwenye lile jeraha la kisu tumboni kwa Sundi ilikuwa imeanzia mlangoni ndani ya kile chumba ikielekea kwenye kona ya kile chumba hadi pale umauti ulipomfika muda mfupi uliopita akiwa mkononi mwangu.

     Kwa mtazamo wa awali ni kuwa kifo cha Sundi kilikuwa kimefanyika ndani ya kile chumba na siyo nje hivyo hali ile ilimaanisha kuwa muuaji wa Sundi alikuwa ndani ya kile chumba cha Balozi Adam Mwambapa wakati alipokuwa akitekeleza mpango wake. Maswali mengine yakaendelea kuibuka kichwani mwangu wakati nilipokuwa nikizidi kufikiria. Kama Sundi alishambuliwa akiwa mle ndani ya kile chumbani cha Balozi Adam Mwambapa nilitaka kufahamu kuwa Balozi Adam Mwambapa alikuwa wapi wakati tukio lile lilipokuwa likifanyika mle ndani. Ni kweli kuwa watekaji walikuwa tayari wamefanikiwa kumteka Balozi Adam Mwambapa wakati mmoja wao alipofanikiwa kumhadaa Sundi atoke chumbani kwake na kuingia chumbani kwa Balozi Adam Mwambapa huku akijifanya kuwa yeye ni Balozi Adam Mwambapa. Uongo uliompelekea muuaji huyo atimize adhma yake pasipo upinzani wowote?. Kwa kweli sikupata penyenye yoyote katika hisia zangu. Labda huwenda ningepata chochote cha kunisaidia katika kujibu maswali yangu kichwani kutoka kwa lile jitu hatari nililotoka kupambana nalo kule sebuleni. Lakini sasa jitu lile tayari lilikuwa limepoteza maisha baada ya kupambano nalo vikali hivyo uwezo wa taarifa kunifikia kwa wakati ule ulikuwa ndani ya mipaka.

     Wakati nikiendelea kufikiri nikajikuta nikiyakumbuka maelezo ya Sundi wakati aliponitaka nikamtafute Padri Aloysius Kanyameza. Sikutaka kuyachukulia maelezo ya Sundi kama maneno yamtokayo mtu kinywani pale anapokuwa katika hatua za mwisho za kukabiliana na kifo katika namna ya kuweweseka. Nilikuwa na kila sababu ya kuamini kuwa pamoja na jeraha kubwa la kisu tumboni mwake lakini jeraha lile lisingekuwa kigezo cha kuikoroga akili ya Sundi na kumpelekea anieleze jambo asilolifahamu. Hivyo kwa namna moja au nyingine niliamini kuwa Sundi alikuwa akifahamu jambo fulani la siri lenye kuhusiana moja kwa moja na lile tukio la kutekwa kwa Balozi Adam Mwambapa. Hivyo kwa mtazamo mwingine ni kuwa Padri Aloysius Kanyameza angekuwa hatua muhimu sana katika upelelezi wangu ingawa sikufahamu ni wapi ambapo ningeweza kumpata kiongozi huyo wa kiroho pale jijini Bujumbura.

     Muda haukuwa rafiki kwangu vilevile sikutaka kabisa kuamini kuwa lile jitu nililopambana nalo mle ndani lilikuwa peke yake hivyo kwa namna moja au nyingine niliamini kuwa kitendo cha lile jitu kuchelewa kurudisha mrejesho kwa wenzake ingeweza kuwa ni ishara mbaya ya kuwafanya wenzake hao waje na kunikuta mle ndani kabla sijapiga hatua nyingine muhimu katika harakati zangu. Hivyo hararaka nikaanza kufanya upekuzi mle ndani.

     Kile chumba kilikuwa kikubwa na chenye nafasi ya kutosha. Upande wa kushoto na wa kulia wa chumba kile kulikuwa na madirisha mapana yenye nondo na vioo yaliyofunikwa kwa mapazia marefu na mepesi. Upande wa kulia ukutani kulikuwa na kabati kubwa la nguo la mbao na kando ya kabati lile kulikuwa na meza nzuri nyeusi ya kioo. Juu ya meza ile kulikuwa na seti moja ya runinga kubwa Flat screen katikati ya spika mbili za sistimu ya muziki wa Home threatre. Kwa kurunzi yangu ndogo mkononi nikamulika kwa utulivu kwenye kabati lile na hapo haraka nikagundua kuwa upekuzi wa ovyo ulikuwa umefanyika ndani ya lile kabati. Lile kabati lilikuwa limefunguliwa na kuachwa wazi. Nguo za mle ndani zilikuwa zimepekuliwa na kutawanywa ovyo. Droo za ndani za lile kabati zilikuwa zimevunjwa na vitu vilivyokuwa mle ndani vilikuwa vimetawanywa ovyo kila mahali. Katika droo ya chini kabisa ya lile kabati niliona jozi tatu za viatu vya ngozi vya aina tofauti. Mwishowe sikuona kama kungekuwa na tija yoyote ya kufanya upekuzi katika kabati lile hivyo nikageuka na kuchunguza upande wa kulia wa kile chumba.

     Kulikuwa na kitanda kikubwa cha futi sita kwa sita chenye nakshi nzuri za kupendeza hata hivyo kitanda kile kilikuwa kimevurugwa. Shuka zake zilikuwa zimetawanywa ovyo na mito yake ya kuegemea ilikuwa imetupwa sakafuni. Taratibu nikakizunguka kitanda kile na kuanza kuchunguza kwa makini kabla ya kuliondoa lile godoro na kutazama chini yake. Sikuona kitu chochote cha maana hivyo nikahamishia uchunguzi wangu kwenye droo mbili zilizokuwa upande wa kushoto wa kitanda kile. Nilipozifungua zile droo ndani yake sikuona kitu chochote na hapo hisia za awali zikanitanabaisha kuwa kulikuwa kumefanyika upekuzi wa kina mle ndani.

     Hatimaye nikiacha kile kitanda na kuelekea upande wa kushoto wa kile chumba. Mara baada ya kuupita ule mlango wa kile chumba upande wa kushoto nikauona mlango mwingine lakini mlango ule ulikuwa wazi. Niliposogea karibu na kuchunguza mle ndani kwa mwanga wa kurunzi yangu nikagundua kuwa ule ulikuwa mlango wa kuelekea kwenye chumba kidogo cha maliwato. Nikaingia mle ndani kwa tahadhari na kuanza kumulika kwa utulivu hata hivyo sikuona kitu chochote cha maana zaidi ya choo kimoja cha kukaa cha marumaru nyeupe na beseni kubwa la kuogea. Mle ndani ukutani kulikuwa kumening?inizwa mataulo mbalimbali na zaidi ya pale sikuona kitu kingine chochote cha kunivutia hivyo hatimaye nikaamua kutoka nje ya kile chumba...



    Upande wa kushoto wa kile chumba kulikuwa na seti moja ya makochi ya sofa nadhifu na ya kisasa juu ya zulia zuri lenye rangi za ngozi ya Pundamilia. Katikati ya makochi yale kulikuwa na meza ndogo ya mbao yenye umbo la nusu duara. Niliposogea karibu na meza ile na kuchunguza juu yake nikaona kibakuli kidogo cha majivu ya sigara, kibiriti kioja cha gesi, kasha tupu la miwani ya macho na simu ya mezani. Nikaitazama kwa makini ile simu ya mezani huku kichwani nikianza kuvuta picha namna Balozi Adam Mwambapa alivyokuwa katika harakati za kutumia simu za mle ndani katika kufanya mawasiliano na Hidaya wakati watekaji walipovamia ile nyumba. Hatimaye nikashawishika kuchukua kiwambo cha ile na kukiweka sikioni huku nikitumia kitambaa changu kidogo cha leso nikikwepa kuacha alama za vidole vyangu eneo lile. Nilipojaribu kubonyeza tarakimu kadhaa za ile simu ya mezani haraka nikagundua kuwa mawasiliano ya ile simu yalikuwa yamekatwa. Nilikuwa nikitarajia jambo la namna ile hivyo sikushangaa.

     Muda ulikuwa ukienda na dakika nazo zilikuwa zikiyoyoma hivyo hatimaye nikairudisha ile simu mahala pake na kuanza kutembea kwa utulivu nikielekea sehemu ya mbele ya kile chumba. Nilipokaribia dirishani upande wa kushoto nikaona ua kubwa zuri kwenye chungu cha udongo na kando ya ua lile kulikuwa na kiti kimoja cha kupumzikia kilichokuwa kikitazamana na lile dirisha. Pembeni ya kile kiti kulikuwa na meza fupi ya mbao yenye droo mbili na juu ya meza ile kulikuwa na chupa moja tupu ya kahawa na kikombe cha dongo pembeni yake.

     Bastola yangu ikiwa imetuama vyema mkononi nikajaribu kuvichunguza vitu vile kwa makini kabla ya kuhamia kwenye droo mbili za ile meza ndogo iliyokuwa pembeni ya kile kiti cha kupumzikia. Haraka nilipoanza upekuzi wangu nikagundua kuwa zile droo za ile meza nazo zilikuwa zimefunguliwa na kuachwa wazi huku zikionekana zimefanyiwa upekuzi. Watekaji bila shaka walikuwa wamechukua vielelezo vyote ambavyo vingeweza kusaidia katika kupatikana kwa Balozi Adam Mwambapa. Hivyo sikutaka kuendelea kupoteza muda wangu eneo lile badala yake nikahamia kwenye sefu mbili za chumba zilizokuwa kwenye kona ya upande wa kulia wa kile chumba. Hatimaye nikazifikia zile sefu na kuanza kuzichunguza kwa makini. Sefu ya kwanza haikuwa na kitu ndani yake. Ile sefu nyingine ilikuwa wazi huku ikionekana kuwa kulikuwa na upekuzi uliokuwa umefanyika ndani yake. Nilipoendelea kuchunguza mle ndani nikaona kuwa kulikuwa na nyaraka muhimu za kiofisi zikiwemo barua za siri zenye maelekezo fulani kuhusu masuala ya kiutendaji ya kibalozi kutoka ikulu ya Tanzania ya jijini Dar es Salaam.

     Nilipoendelea kuichunguza vizuri ile sefu kwa chini nikagundua kuwa droo zake mbili zilikuwa zimevunjwa na nilipochunguza kwa makini ndani ya zile droo nikagundua kuwa kulikuwa na harufu nzuri ya pesa nyingi iliyohifadhiwa mle ndani kwa muda mrefu. Harufu ile ya pesa ikanipelekea niamini kuwa kulikuwa na kiasi kikubwa cha fedha iliyoibwa kutoka kwenye droo zile za sefu. Hali ile ikanivuta kuzidi kufanya uchunguzi zaidi na kwa kufanya vile nikaokota noti moja ya dola mia ya kimarekani. Nikaichunguzi kwa makini noti ile kabla ya kuitia mfukoni. Kwa muda mfupi uliosalia nikawa nimefanikiwa kufanya upekuzi kwenye vipenyo vyote muhimu vya ile nyumba huku nikiwa sijaambulia kitu chochote cha maana. Hatimaye nikaamua kutoka nje ya ile nyumba lakini safari hii nikiutumia ule mlango wa mbele ambao niligundua kuwa ulikuwa haujafungwa kwa funguo. Sasa nilikuwa na kila sababu ya kuamini kuwa Balozi Adam Mwambapa alikuwa ametekwa na kikundi fulani cha watu wasiofahamika kwa sababu wanazozijua wao.

     Mvua bado ilikuwa ikiendelea kunyesha wakati nilipokuwa nikitoka nje ya ile nyumba na kukatisha kwenye giza zito chini ya miti mikubwa ya kivuli iliyopandwa kuizunguka ile nyumba. Kwa kuhofia usalama wangu eneo lile sikutaka kuwasha ile kurunzi yangu mkononi badala yake nikaitia mfukoni na kuikamata vyema bastola yangu mkononi nikielekea kwenye geti la ile nyumba kutoka nje.

     Mara tu nilipotoka nje ya lile geti nikakumbuka kuitazama saa yangu ya mkononi na hapo nikagundua kuwa nilikuwa nimepoteza muda mwingi ndani ya ile nyumba. Sikutaka kurudi kule nilikoegesha gari langu kwa kuufuata uelekeo ule niliokuja nao. Hivyo mara tu baada ya kutoka nje ya lile geti nikashika uelekeo wa upande wa kulia wa barabara ya lami iliyokuwa ikikatisha mbele ya ile nyumba kwa kuambaa ambaa na ukuta wa uzio wa ile nyumba. Muda ulikuwa umesonga sana na utulivu katika ile barabara na eneo lile lote kwa ujumla ulikuwa umeongezeka. Sauti pekee zilizokuwa zikisika zilikuwa ni sauti za mbwa waliokuwa wakibweka kutoka nyumba za jirani na eneo lile.

     Niliendelea kutembea kwa mwendo wa tahadhari kandokando ya ule ukuta huku mara kwa mara nikigeuka na kutazama nyuma kama kungekuwa na mtu yeyote aliyekuwa akinifuatilia. Sikumuona mtu yeyote hivyo hali bado ilikuwa shwari. Nilipofika mwisho wa ule ukuta nikasimama kutathmini hali ya usalama wa eneo lile na niliporidhika nikachepuka na kuvuka barabara upande wa pili. Nikiwa upande wa pili wa ile barabara nikaendelea kutembea chini ya miti iliyokuwa pembeni ya barabara ile yenye giza hafifu huku jina la Padri Aloysius Kanyameza likianza upya kuzitekenya fikra zangu huku nikijaribu kuwaza ni kwa namna gani mtumishi huyo wa kiroho alikuwa ametumbukia kwenye mkasa huu wa hatari wenye matukio ya aina yake. Jibu sikulipata ingawa hisia zangu zilinitanabaisha kuwa nilikuwa nimejiingiza kwenye mkasa hatari.

     Niliendelea kutembea chini ya miti ile ya kando ile barabara pembeni ya kuta ndefu zilizopandwa kuyazunguka majumba makubwa ya kifahari huku mara kwa mara nikigeuka nyuma katika namna ya kujihakikishia usalama wangu.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

     Ilikuwa ni wakati nilipokuwa nikikaribia kuifikia kona ya barabara ile pale nilipoona mwanga wa taa za gari ukianza kuchomoza kwenye ile kona mbele yangu kasha ukafuatia muungurumo wa gari. Haraka nikawahi kujibanza kwenye kona moja ya ukuta wa eneo lile sehemu iliyokuwa na giza zito lililofanywa na matawi ya mti. Nikiwa nimejibanza kwenye ile kona muda uleule mara nikaliona gari dogo aina ya LandRover likichommoka kwenye ile kona na kuingia kwenye ile barabara. Mwendo wa lile gari ulikuwa wa kasi mno kiasi cha kunitahadharisha kuwa mambo hayakuwa shwari. Nilipolichunguza vizuri lile gari nikagundua kuwa lilikuwa ni gari la jeshi na nyuma yake kulikuwa na wanajeshi sita huku mikononi wakiwa wameshika bunduki zao.

     Muda mfupi uliofuata lile gari likanipita kwa kasi kama gari la kikosi maalum cha uokozi wa majanga ya moto likielekea kule nyuma nilipotoka. Nikiwa bado nimejibanza kwenye ile kona nikaendelea kulitazama lile gari namna lilivyokuwa likitimua. Mara nikaliona lile gari likipunguza mwendo kule mbele na kitendo kile kikawapelekea wanajeshi watatu waruke kwa mbwembwe kutoka nyuma ya lile gari na namna ya urukaji wao ulitosha kunifahamisha kuwa kulikuwa na jambo la hatari. Nilipoendelea kuchunguza nikagundua kuwa wale wanajeshi walikuwa wameruka kutoka kwenye lile gari wakiwa wamebakisha hatua chache kabla ya kuifikia ile nyumba aliyokuwa akiishi Balozi Adam Mwambapa.

     Wale wanajeshi waliporuka mara nikamuona mmoja wao akienda kujibanza mwanzo wa ukuta wa ile nyumba upande wa kushoto. Mwingine nikamuona akiuzunguza ule ukuta kwa nyuma na yule mwingine aliyesalia akaenda kujibanza kwenye kona ya ule ukuta iliyokuwa upande wa kulia. Mara baada ya wale wanajeshi watatu kuruka lile gari LandRover likaongeza tena mwendo kuendelea na safari na lilipofika mbele ya geti la ile nyumba ya Balozi Adam Mwambapa nikaliona likipunguza tena mwendo. Kwa kufanya vile nikawaona wanajeshi wengine watatu wakiruka kutoka nyuma ya lile gari katika mtindo wa kibabe kisha wakijiviringisha barabarani kama ninja kila mmoja akishika uelekeo wake kuizingira ile nyumba. Wale wanajeshi walipomaliza kuruka lile gari LandRover halikusimama badala yake likaongeza kasi mbele ya ile barabara na hatimaye kutokomea mitaani.

     Nikiwa bado nimejibanza kwenye kona ya ule ukuta mara nikawaona wale wanajeshi walioruka kutoka kwenye lile gari LandRover wakielekea kwa tahadhari kwenye geti la ile nyumba ya Balozi Adam Mwambapa huku wakiwa wamezishika vyema bunduki zao mikononi. Haukupita muda mara nikawaona wale wanajeshi wakiusukuma mlango mdogo wa lile geti na kuingia mle ndani. Kwa kweli moyo wangu ulipoteza utulivu kabisa huku damu ikinichemka mwilini hali iliyopelekea kijasho chepesi kianze kunitoka sehemu mbalimbali za mwili wangu. Nafsi yangu ikanitanabaisha kuwa nilikuwa nimepishana na hatari muda mfupi uliopita. Nilikuwa na kila sababu ya kuamini kuwa kuwa wale wanajeshi walikuwa na ushirika na lile jitu hatari nililotoka kupambananalo vikali na hatimaye kufanikiwa kuliangamiza ndani ya ile sebule ya Balozi Adam Mwambapa muda mfupi uliopita.

     Nilitamani sana kuendelea kujibanza eneo lile ili niweze kuwapeleleza vizuri wale wanajeshi walioshuka kwenye lile gari na kuivamia nyumba ya Balozi Adam Mwambapa lakini mara moja nafsi yangu ikanionya kuwa lile lingekuwa jambo la hatari sana. Nilikuwa na kila sababu ya kuamini kuwa mara baada ya wale watu kunitafuta na kunikosa mle ndani ya ile nyumba wasingekubaliana na hali ile na badala yake wangeamua kupanua mipaka ya operesheni yao zaidi wakinisaka katika vipenyo na kona zote za kitongoji kile hivyo endapo ningeendelea kuzubaa eneo lile wangenifikia na kunikamata.

     Kwa kweli sikutaka wale wanajeshi wanifikie hivyo kwa tahadhari nikayaacha yale maficho na kuondoka eneo lile nikiambaa na zile kuta za uzio wa zile nyumba zilizokuwa zikipakana na ile barabara ya lami. Nilipofika mwisho wa ile kona nikaingia upande wa kushoto nikiifuata barabara pana ya lami iliyokuwa ikikatisha katikati ya makazi ya watu.

     Mvua kubwa bado ilikuwa ikiendelea kunyesha na hivyo kupelekea barabara ile kumezwa na upweke wa kifo. Sikuweza kumuona mtu yeyote wakati nilipokuwa nikitembea kandokando ya barabara ile huku mara kwa mara nikigeuka kutazama nyuma. Kulikuwa na nyumba chache zilizokuwa zikiwaka taa katika mtaa ule huku nyumba nyingi zikionekana kutawaliwa na giza. Ilifikia wakati nikawa nasikia milio ya risasi kwa mbali hata hivyo sikuweza kufahamu kwa hakika kuwa sauti zile za majibishano ya risasi zilikuwa zikitokea maeneo gani. Hata hivyo nilijipa tahadhari kwa kuwa makini kutokana na hali ya machafuko ya kisiasa iliyokuwa ikiendelea nchini Burundi.

     Niliendelea kutembea kwa tahadhari kando ya barabara ile na nilipofika mbele nikaona kuwa kulikuwa na barabara nyingine iliyokuwa ikichepuka kuingia upande wa kushoto. Nilipofika eneo lile nikaingia upande wa kushoto kuifuata ile barabara. Niliendelea kutembea katika barabara inayokatisha katikati ya majumba makubwa ya kifahari yaliyozungukwa na kuta kubwa za uzio zenye sistimu maalum za umeme wa kuzuia wezi juu yake. Kulikuwa na utulivu wa hali ya juu katika kitongoji kile hali iliyonipelekea nijihisi mpweke.

     Ile barabara ilikuwa ikikatisha mbele ya mageti makubwa ya nyumba za kifahari zilizokuwa eneo lile hivyo nilipofika mbele kidogo nikachepuka na kuifuata barabara nyingine iliyokuwa ikiingia upande wa kulia. Barabara ile ilikuwa ikikatisha kati ya jengo la benki ya biashara ya Burundi na kituo kimoja binafsi cha urushaji wa matangazo ya redioni.

     Kwa mujibu wa ramani yangu ndogo ya kijasusi ni kuwa mbele ya barabara ile kulikuwa na barabara nyingine ya mtaa iliyokuwa ikikatisha kwa mbele. Upande wa kushoto mbele ya ile barabara ndiyo kulikuwa na ile supermarket ndogo ambayo mbele yake nilikuwa nimeegesha lile gari langu.

     Hata hivyo wakati nilipokuwa mbioni kuifikia ile barabara mara nikashtushwa na muungurumo wa gari lililokatisha haraka na kuingia kwenye ile barabara niliyokuwa nikitembea. Haraka nikawahi kuchepuka na kujibanza kwenye uchochoro mwembamba uliokuwa baina ya ukuta wa nyumba moja na nyingine na nilipochungulia kutazama nikaliona lile gari LandRover ambalo lilikuwa limenipita kwenye ile kona muda mfupi uliopita baada ya kutoka kwenye ile nyumba ya Balozi Adam Mwambapa kule nyuma nilipotoka. Hata hivyo lile gari halikuwa katika mwendo kasi kama lilivyokuwa pale awali wakati likinipita. Nikiwa bado nimejibanza kwenye ule uchochoro nikaendelea kulitazama lile gari na kwa kufanya vile nikawaona wanajeshi wawili wakiwa wameketi sehemu ya mbele ya lile gari. Sehemu ya nyuma ya lile gari hapakuwa na mtu na hali ile ilinishangaza sana.

     Lile gari likaendelea na safari yake kwa mwendo wa taratibu na wa tahadhari na lilipokaribia kwenye kile kichochoro nilichojibanza mara nikaliona likipunguza mwendo na hatimaye kusimama. Tukio lile likanipelekea niingiwe na hofu. Nilipogeuka haraka kutazama nyuma ya kile kichochoro hofu ikaniingia zaidi baada ya kugundua kuwa mwisho wa kile kichochoro kilikuwa na ukomo baada ya kuuona ukuta mrefu wenye seng?enge juu yake. Hivyo kule nyuma hapakuwa na sehemu ya kutokea endapo ningeamua kukifuata zaidi kile kichochoro. Nikiwa katika hali ile ya kutafakari nini cha kufanya mara nikauona mlango wa mbele wa lile gari ukifunguliwa kisha mtu mmoja akashuka huku mkononi akiwa ameshika bastola. Tukio lile likanipelekea nigeuke tena kutazama nyuma ya kile kichochoro huku akili yangu ikifanya kazi ya ziada ya kujihakikishia usalama wangu.

     Nikiwa katika hali ile ya taharuki mara nikagundua kuwa chini ya ule ukuta mwisho wa kile kichochoro kulikuwa na pipa moja chakavu la taka. Sikuwa na namna nyingine ya kufanya hivyo kwa haraka nikalifuata lile pipa na pasipo kujishauri nikaufungua mfuniko wake na kuingia mle ndani kisha nikajifunika kwa ule mfuniko. Lile pipa lilikuwa na takataka chache na nilipolichunguza nikagundua kuwa lilikuwa likitumika kuchomea takataka hata hivyo sikuwa na budi kuvumilia harufu mbaya ya masalia ya takataka zilizokuwa mle ndani ingawa bado hewa safi kidogo iliweza kupenya kupitia matundu machache yaliyofanywa na kutu kwenye mfuniko wa lile pipa.

     Muda mfupi baada ya kuingia mle ndani ya lile pipa mara nikauona mwanga mkali wa kurunzi ukimulika juu ya ule mfuniko wa lile pipa huku ule mwanga ukisindikizwa kwa sauti ya hatua hafifu za mtu akiingia kwenye kichochoro kile. Sikuona kama kuna namna nyingine ya kufanya katika kuepuka kadhia ile. Hivyo nikiwa ndani ya lile pipa nikaikamata vyema bastola yangu mkononi tayari kukabiliana na rabsha yoyote ambayo ingejitokeza mbele yangu.

     Kupitia matundu machache ya kutu yaliyokuwa pembeni ya lile pipa ule mwanga wa kurunzi ya yule mtu mkononi ukaniwezesha kuangalia kule nje. Nilimuona mtu mmoja mrefu mweusi kichwani akiwa amevaa kofia ya bereti na fulana aliyoichomekea vizuri kiunoni kwenye suruali yake ya kombati na buti ngumu za jeshi miguuni huku mkononi akiwa ameshika bastola. Yule mtu alikuwa mrefu sana huku misuli ya shingo na mikono yake ikiwa imetuna kwa ukomavu. Mwonekano wake ukanitanabaisha kuwa alikuwa ni mtu anayependa matata.

     Yule mtu akaendelea kutembea kwa tahadhari akilikaribia lile pipa huku akiendelea kumulika mulika huku na kule kwenye kile kichochoro. Mwenzake bado alikuwa amebaki ndani ya lile gari akisubiri. Yule mtu akaendelea kutembea kwa tahadhari akilikaribia lile pipa nililokuwa nimejibanza ndani yake na kadiri yule mtu alivyokuwa akizidi kulikaribia lile pipa ndivyo moyo wangu ulivyokuwa ukizidi kupoteza utulivu huku kijasho chepesi kikinitoka.

     Hata hivyo wakati nikiwa bado mle ndani ya lile pipa la taka jambo moja likatokea na kunifurahisha sana. Ilikuwa ni wakati yule mtu alipokuwa amesaliwa na hatua chache kabla ya kulifikia lile pipa mara nikasiki akiitwa na yule mwenzake aliyekuwa amebaki kwenye lile gari kule barabarani huku yule mwenzake akilalamika kuwa walikuwa wakipoteza muda wao bure eneo lile. Yule mtu aliyekuwa akilikaribia lile pipa kusikia akiitwa kukamfanya asite kuendelea na safari ya kulifikia lile pipa nililojibanza badala yake akasimama na kulitazama lile pipa kwa makini kama mtu aliyehisi kitu fulani mle ndani ya lile pipa. Hata hivyo yule mtu hakupiga hatua zaidi badala akautembeza ule mwanga wa kurunzi yake mkononi kumulika chini ya lile pipa na huwenda alipoona mabaki ya takataka yaliyoangukia nje ya lile pipa kukampelekea azipuuze hisia zake. Hatimaye nikamuona yule mtu akiitia bastola yake kiunoni huku akimulikamulika eneo lile kabla ya kuamua kugeuza na kurudi kwenye lile gari kule barabarani mwenzake alipokuwa akimsubiri. Baada ya muda mfupi kupita mara nikasikia mlango wa lile gari ukifungwa kisha dereva wa lile gari akatia moto na kuondoka akitokomea mbali na eneo lile.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

     Kwa sekunde kadhaa nikiwa ndani ya lile pipa nikajikuta nikimezwa na mduwao usioelezeka huku nikishindwa kabisa kuamini kuwa nilikuwa nimesalimika na mkasa ule hatari. Hata hivyo niliendelea kujibanza ndani ya lile pipa hadi pale niliporidhika kuwa lile gari lilikuwa limetokomea mbali na eneo lile ndiyo nikauondoa ule mfuniko wa lile pipa na kutoka.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog