Search This Blog

Sunday, 22 May 2022

MKANDA WA SIRI - 1

 







    IMEANDIKWA NA : HALFANI SUDY



    *********************************************************************************



    Simulizi : Mkanda Wa Siri

    Sehemu Ya Kwanza (1)

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Utangulizi.



    Chifu Abdullah anaingia katika kazi ngumu kuliko zote alizowahi kuzifanya katika maisha yake, kazi ya kuusaka mkanda wa siri uliopotea kimaajabu katika kasri yake. Alishindwa kuulinda, sasa anausaka kwa nguvu. Msako wa mkanda unazikutanisha pande mbili zenye taaluma za juu katika mambo ya uhalifu.

    Mkanda unatembea toka kwenye mkono huu kwenda katika mkono mwengine, pande zote mbili zinautafuta mkanda kwa nguvu na akili kila unapopita. Wengi wanajeruhiwa, wengi wanaumizwa, wengi wanakufa, sababu kuu ni Mkanda wa Siri.

    Jeshi la Polisi nalo linaingia kazini kusaka wahalifu, bila kujua wahalifu hao wana uhusiano mkubwa na Mkanda wa Siri. Haiwi kazi rahisi kuupata mkanda, mkanda unazua kizaazaa kwa maana sahihi ya neno kizaazaa. Hivi ndani ya mkanda wa siri kuna nini cha siri?



    Tusome wote..



    Magomeni:

    Saa 10:10 A.M



    FOLENI ilikuwa imeshamili katika mitaa mingi ya Jiji la Dar es salaam. Kilikuwa ni kipindi cha mvua, na kama ilivyoada katika Jiji hili.....sikuzote mvua huambatana na foleni.

    Katika barabara ya Morogoro kulikuwa na foleni hasa. Magari yalikuwa yameshonana sana, kila dereva akitafuta namna japo tu ya kusogea hata hatua moja mbele. Lakini hakukuwa na uwezekano huo hata chembe.

    Katika barabara hiyohiyo ya Morogoro, maeneo ya Magomeni ilikuwepo gari moja ya kifahari aina ya Range Rover Vogue. Gari hiyo nzuri, nyeusi na ya thamani ilikuwa ni miongoni mwa gari zilizokwama kabisa kutokana na foleni ya siku hiyo iliyosababishwa na mvua. Dereva wa gari hiyo alikuwa ni kijana wa kiume. Kijana mtanashati, kijana ambaye nae alikumbwa na foleni hiyo akiwa anaelekea sokoni Kariakoo. Kufanya 'shopping'.

    Baada ya kukaa muda mrefu, Kijana alinyoosha mkono wake hadi katika kitufe cha redio. Akaiwasha. Akijua labda redio itamburudisha kidogo ama kumpunguzia walau kidogo maumivu ya ile adha ya foleni. Kijana alitulia tuli kitini huku mikono yake yote miwili ikiwa imeushikilia sukani wa gari yake. Masikio yakisikiliza redio.



    "Habari iliyotufikia hivi punde.....meli iliyokuwa inatoka huko Zanzibar kuelekea jijini Dar es salaam yazama, meli hiyo iitwayo MV donors ilizama wakati....."



    Redio iliyofunguliwa na yule kijana iliendelea kuongea. Lakini kwa bahati mbaya haikuwa inasikilizwa na yule kijana. Kijana alihisi kama anapigiwa kelele tu na ile redio. Habari ile ya kuzama meli ya MV donors ilimchanganya sana.



    *****

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Zanzibar:

    Saa 7:07 A.M



    Gari moja ndogo aina ya Toyota vitz ilikuwa inatembezwa kwa mwendo wa kawaida kurejea katika makazi ya dereva wa gari hiyo. Gari ilikuwa imetoka bandarini kumsindikiza mgeni wa mmiliki wa gari hiyo. Dereva wa gari hiyo alikuwa kijana wa makamo. Alikuwa anaendesha gari huku akiufatiza wimbo wa mwanamuziki 50 Cent uitwao In da club ukiosikika katika redio ya gari yake. Alikuwa anaendesha, anaimba huku akicheza kwa kutingisha kichwa. Hakika alikuwa na furaha sana.



    Katikati ya bahari.

    Saa 9:30 A.M



    Meli ya MV donors ilikuwa katikati ya bahari. Abiria ndani ya meli hiyo walikuwa na furaha sana. Wakifurahia kusafiri majini. Wakifurahia kwenda kuonana tena na ndugu zao. Baada ya mwendo wa robo saa hali ya hewa ya baharini ilibadilika! Lilitolewa tangazo kuwa abiria wachukue tahadhari kwa kuvaa 'life jackets' Mtangazaji aliwapa imani kuwa hali itakuwa sawa muda si mrefu.

    Msichana mmoja, alikuwa ndani ya meli hiyo. Alikuwa ametulia tuli kitini kaupakata mkoba wake. Msichana huyo ndiye aliyetoka kusindikizwa na yule kijana aliyekuwa anarudi kwake na ile gari aina Toyota vitz. Tangazo la tahadhari lilirudiwa tena katika meli ile. Tangazo lililopenya katika masikio yote mawili ya yule msichana. Abiria wote hawakulipa uzito unaostahili lile tangazo. Eti wakiamini maneno ya Mtangazaji 'hali itakaa sawa muda si mrefu' Lakini siyo kwa yule msichana. Msichana alisikia kitu cha ziada katika sauti ya Mtangazaji. Sauti ya Mtangazaji iliambatana na hofu!



    Hali ya bahari iliendelea kuchafuka. Kila dakika zilivyokuwa zinayoyoma. Lakini yule msichana aliendelea kutulia tuli kitini. Alifungua begi lake dogo la mkononi, akachambuachambua katikati ya nguo zake, akatoa mkanda wa video. Ilikuwa ni ile mikanda mikubwa ya video, ya kizamani. Akauangalia ule mkanda kama dakika saba. Akatingisha kichwa, ishara ya kusikitika. Akapekua tena katika begi lake, akatoa mfuko wa nailoni, maarufu kama mfuko wa rambo. Akaufungua ule mfuko wa nailoni akauweka ule mkanda wa video, akauangalia mfuko kwa tuo. Msichana akasikitika tena. Akapekua tena begi lake, akatoa mfuko mwengine wa nailoni, akauvesha juu ya ule mfuko wa awali. Mkanda sasa ukawa ndani ya mifuko miwili ya rambo. Alihakikisha hautoi hata nafasi ndogo ya kupitisha hewa. Alivyothibitisha kwa kuubonyezanyeza akaurudisha ule mkanda katikati ya begi lake. Akaendelea na utulivu wake kitini.

    Bahari iliendelea kuchafuka!

    Haikuielewa kabisa ile kauli ya matumaini toka kwa Mtangazaji,

    'Hali ya hewa itakuwa sawa baada ya muda mfupi' Sasa meli ilianza kutingishika kwa nguvu!

    Abiria ndani ya meli walianza kutapika ovyo. Wengine walianza kuvaa 'life jacket' kwa pupa, kama walivyoambiwa na Mtangazaji, lakini kwa bahati mbaya hazikutosha. Abiria mia mbili, 'life jackets' sabini. Zingetosha vipi? Abiria wengi sana walikosa kuvaa mavazi yale muhimu, ambayo yangewasaidia sana endapo lingetokea lolote! Miongoni mwa watu waliokosa 'life jacket' alikuwa ni yule msichana. Msichana mzuri, aliyeuficha uzuri wake ndani ya vazi la baibui na hijab nyeupe. Huku chini akivaa viatu vya wazi maarufu kama mmasai. Yeye alitulia tuli kitini. Akisubiri kitakachotokea mle ndani ya meli. Meli ilianza kuingiza maji ndani. Maji yalianza kupenya katika chumba cha injini. Taratibu maji yalisambaa katika meli mzima. Kumbe maji yaliingia muda kidogo, na hiyo ndio sababu ya sauti ya Mtangazaji kuambatana na hofu! Maji sasa yalitamalaki meli mzima. Yule msichana alivyoguswa na maji ya bahari miguuni mwake. Sasa ndio aliona ukubwa wa hatari waliyokutana nayo!



    Katika chumba cha injini, kulikuwa na mtu mmoja na maiti moja. Jamaa mmoja aliyetambulika kwa jina la Malolo Abdallah alikuwa yuko pembeni ya maiti ya Mhudumu wa kiume wa meli ile. Mhudumu aliyemuuwa kwa kisu muda mfupi uliopita. Malolo aliingia katika meli kwa kazi maalum, na alienda katika chumba cha injini kwa kazi maalum. Ni yeye ndiye aliyetoboa kule chini, kwa kutumia bomu dogo lisilo na mripuko wala sauti! Nia ni kuhakikisha maji yanapenya na kuingia ndani ya meli. Ili watu wote waangamie, ndani ya meli na kuupoteza kabisa kila kitu chao, ukiwemo mkanda wa siri! Kuchafuka kwa hali ya hewa ya bahari kulimsaidia sana Malolo katika kazi yake. Hakuna aliyekuwa makini mle ndani ya meli. Hadi maji yalivyoanza kuingia....nd'o wakastuka. Baada ya kuhakikisha maji yanaingia ndani ya ile meli Kupitia tundu alilolitoboa kwa bomu, Malolo alizama majini na kutokomea.



    Meli ya MV Donors sasa ilizidiwa na maji. Taratibu ikaanza kuzama majini. Nusu ya meli ilikuwa imezama ndani ya maji. Wakati watu wote wakihangaika huku na kule kunusuru roho zao. Ndipo lilipotokea jambo la kustusha sana! Meli ilikatika vipande viwili katikati! Kipande kimoja, kile cha mbele, kiligeuka chini juu, kikaanza kumimina watu vibaya sana. Watu walitoswa majini kilazima! Ilikuwa vyovyote watakavyofikia! Kile kipande cha nyuma kilisimama wima! Watu wakaanza kuserereka kuelekea majini. Hiki ndio kile kipande alichokuwa yule msichana.





    Zanzibar,

    Saa 10:00 A.M



    Yule kijana aliyetoka kumsindikiza yule msichana aliyekuwa ndani ya meli alikuwa amekaa kwenye sofa ya kifahari nyumbani kwake. Meza iliyokuwa mbele yake kulikuwa na chupa tupu tatu za bia aina ya safari, pamoja na ‘glass’ iliyokuwa na bia nusu. Kijana alikunywa sana. Na ilimpasa anywe. Usiku alikuwa ametoka kukamilisha kazi kubwa na ngumu sana. Kazi ya kuhakikisha mkanda wa siri unarejea mikononi mwao. Na kwa fikra zake akijua sasa unakaribia kufika jijini Dar ea salaam. Laiti angejua ya huko baharini.... Kijana aliamua kujipongeza kwa bia, huku akiendelea kusikiliza muziki mwanana katika redio kubwa sebuleni kwake.



    Magomeni,

    Saa 10:00 A.M



    Bado yule kijana alikuwa kwenye foleni. Foleni ilikuwa haitembei hata kidogo. Alijiinamia katika sukani wa gari yake, huku akitafakari ile habari mbaya aliyoisikia redioni. Ajari ya meli. Meli ya MV donors alikuwa amepanda mtu muhimu sana, tena akiwa na mkanda muhimu sana! Mkanda haukupaswa kuwa mikononi mwa mtu yeyote yule. Zaidi yao. Ni yeye aliyemtuma Binunu kwenda visiwani Zanzibar, kuhakikisha mkanda unarudi mikononi mwao. Na kweli, Binunu akishirikiana na Richard walifanya kazi mzito sana. Ingawa kwa shida lakini walirejesha mkanda wa siri mikononi mwao. Eti leo hii mkanda ukiwa unaletwa jijini Dar es salaam, anasikia redioni kuwa meli aliyopanda Binunu imepata ajari. Jamaa alichanganyikiwa sana!

    Aliinuka toka katika usukani aliokuwa ameulalia. Akaangalia nje kupitia dirishani. Mvua ya haja iliendelea kunyesha. Alitukana tusi la nguoni. Sijui alimtukana nani? Lakini alitukana. Alichukua simu yake, akatafuta jina la Richard, akaliona, akabofya kitufe cha kijani, cha kupigia simu na kumpigia Richard Phillipo.

    Richard alikuwa bado yupo sebuleni, akinywa bia huku akimsikiliza 50 Cent, mwanamuziki anayempenda zaidi, wimbo wa 21 Questions sasa ulikuwa unasikika katika spika za redio yake. Ndipo aliisikia simu yake ikiita. Alipunguza sauti ya redio na kuisikiliza simu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Nambie Martin" Richard alisema pindi tu alipopokea simu.



    "Richard mambo yameharibika!" Martin alisema kwa wahka mkubwa.



    "Kivipi Martin, Binunu yuko njiani na mkanda wa siri, nusu saa tokea sasa utakuwa mikononi mwako...neema yaja brother" Richard alisema kwa sauti ya kujigamba.



    "Meli aliyopanda Binunu imezama Richard!" Martin alisema.



    "Unasema!" Richard aliuliza, huku macho yakiwa yamemtoka pima.



    "Meli imezama Richard" Martin alirudia tena. Kwa sauti ya upole sasa.



    "Lahaula!" Aliropoka Richard.



    "Ni mbaya sana kwetu hii, mbaya..mbaya...mbaya sana'a!" Martin alisisitiza



    "Daaah, Tunafanyaje sasa Martin" Richard aliuliza.



    "Kodi boti sasahivi Richard, uende hadi eneo la tukio lazima tumpate Binunu pamoja na mkanda wa siri.....ni lazima!" Martin alisisitiza.



    "Sawa Martin" Sekunde hiyohiyo Richard alitoka nje ya nyumba yake, akaingia kwenye gari na kwa kasi ya haraka alielekea bandarini. Hakuwasha redio ya gari yake safari hii..alisahau kabisa habari za 50 Cent.



    Dakika kumi zilitosha kumfikisha Richard bandarini, na dakika kumi na tano alizitumia kupata boti ya kukodi. Aliipata. Yeye na muendesha boti wakaingia majini kuelekea mahali ilipozama meli ya MV donors.



    Katikati ya bahari ilikuwa ni dhahama! Watu walikuwa wanajitahidi kadri ya wawezavyo kuokoa roho zao. Lakini ilikuwa ngumu sana! Ilikuwa ni vilio na makelele baharini. Pamoja na vilio vyao, lakini haikusaidia chochote, sasa lilizuka balaa jipya. Mvua.... Vilio vyao vilisindikizwa na mvua kubwa sana baharini!



    Takribani dakika arobaini na tano zilimfikisha Richard katika eneo la tukio. Alifika haraka sana kwa kutumia ile boti ya mwendokasi. Alikuwa ameloa tepetepe.....Na kazi ya kumtafuta Binunu akiwa na mkanda wa siri ilianza mara moja. Richard alishuhudia watu wakitapatapa sana majini.. walikuwa wanajitajidi kukiepuka kifo kibaya cha maji, lakini uwezekano wa kuepuka kifo ulikuwa mdogo sana, ilikuwa wako ndani ya maji tena katika kina kirefu na juu yao walikuwa wanamwagikiwa na maji mfululizo, mvua!



    Zaidi ya saa moja sasa tangu ajari itokee hakukuwa na msaada wowote toka Serikalini. Richard ilimjia roho ya ubinadamu na kutamani kuwasaidia lakini hakujua yupi wa kumsaidia, yupi wa kumuacha. Wote walihitaji msaada.



    Zaidi ya saa zima Richard alizunguka eneo lote lile kumtafuta Binunu lakini hakumwona! Na kutomuona Binunu ilimaanisha kutouona mkanda wa siri pia! Richard alichoka, aliamua kuwaokoa watu watatu waliokuwa karibu ya boti yao. Wakarejea nchi kavu.



    Saa 12:05 P.M

    Taarifa za kuzama meli ya MV Donors zilikuwa zimesambaa Tanzania mzima. Redioni, televisheni na katika mitandao ya kijamii kama Facebook, Instagram na WhatsApp watu walikuwa wanazungumzia juu ya ajari hiyo mbaya. Lawama zote zikielekezwa kwa Serikali.



    Kule Magomeni. Foleni sasa ilikuwa inatembea katika barabara ya Morogoro. Gari alilopanda Martin sasa lilikuwa linasogea pia. Mwanzoni alipanga kwenda Kariakoo kufanya 'shopping', lakini sasa aligairi baada ya kusikia taarifa ile mbaya kwake redioni. Aliamua kwenda Posta.... Gari ya Martin ilitembea kwa mwendo wa taratibu mpaka ikafika maeneo ya Jangwani. Foleni ilianza upya! Martin alisonya msonyo mrefu, foleni ilikuwa inamuharibia ama kumcheleweshea kila kitu alichokuwa anapanga katika kichwa chake.



    Pembeni ya gari ya Martin alikuwa amesimama mtu mmoja, mtu aliyekuwa anampigia hesabu Martin muda mrefu sana. Macho ya watu wote hayakuwa makini na yule mtu. Sababu kuu alikuwa Mwendawazimu! Muonekano wake pamoja na mavazi yake vilikuwa vya kiuendawazimu. Mwendawazimu ambaye Martin alitoka nae Ubungo na sasa alikuwa nae Jangwani. Mwendawazimu akiwa na lake moyoni! Martin alipoteza umakini wake kutokana na ile taarifa ya ajari ya meli ya MV Donors, bila hivyo angekuwa ameshatambua kama alikuwa anafatiliwa na yule Mwendawazimu kwa muda na umbali mrefu kiasi kile.

    Ghafla yule Mwendawazimu alifungua mlango wa kati taratibu sana, mlango wa gari ya Martin, aliingia ndani ya gari kimyakimya, alijilaza na kutulia tuli. Hakuna mtu yeyote aliyemuona!



    Martin alikuwa mbali kimawazo. Alifanya makosa ambayo ni aghalabu kufanywa na yeye. Siyo aghalabu tu, hayajawahi kufanywa na yeye. Martin alijisahau 'kulock' milango ya gari yake, alipoteza umakini kiasi kwamba mtu anaingia katika gari yake bila kutambua. Siku zote Martin alikuwa anaishi kwa hisia, lakini leo hisia zake hazikuambua lolote. Ndani ya gari alikuwa yeye na Mwendawazimu! Mwendawazimu alilala katika ile gari ya kifahari. Na foleni ilisogea, utadhani foleni ilikuwa inamsubiri yeye aingie garini. Na Martin aliendesha gari kuelekea Posta.



    Safari ya Martin ilimfikisha bandarini, Posta. Hakupanga safari ya Posta kabla, nia yake kuu ilikuwa kwenda Kariakoo. Kisha nd'o kwenda bandarini kumpokea Binunu. Lakini hakuona umuhimu wa kwenda Kariakoo kufanya 'shopping', kwa hali kama ile iliyotokea. Alienda bandarini moja kwa moja. Martin alishuka ndani ya gari, bila kutambua kwamba alikuwa anamwacha Mwendawazimu ndani ya gari yake. Alivyoshuka chini, alikumbuka 'kulock' milango yote ya gari kwa kutumia 'remote'. Huku akimfungia mwendawazimu ndani ya Range Rover.

    Safari yake ilimpeleka hadi katika ofisi za meli ya MV Donors, hali aliyoikuta, alichoka. Ofisi za MV Donors zilikuwa mithili ya msibani, kulikuwa na watu wengi sana wakilia. Ilikuwa mayowe matupu! Martin akaona pale sio mahali pazuri kukaa. Aliamua kwenda kusubiri ndani ya gari yake. Hakuona sababu ya watu wale kulia, ni yeye pekee ndiye aliyepaswa kulia. Alikuwa amepoteza kitu kikubwa sana....kitu cha thamani sana…Mkanda wa siri! CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Akiwa njiani kuelekea katika gari yake, simu yake ya mkononi iliita. Aliitoa mfukoni harakaharaka na kuiangalia. Richard ndiye aliyekuwa anapiga. Aliipokea.



    "Nambie Richard" Martin aliongea simuni akiwa amesimama.



    "Comrade bilabila aisee" Richard alijibu kwa sauti ya kukata tamaa.



    "Inamaana Binunu hajaonekana!" Martin aliuliza kwa nguvu.



    "Ni ngumu sana kumpata kwa hali ilivyo kule baharini, ni ngumu sana Comrade!" Richard alijibu.



    "Mkanda je?" Martin aliuliza swali lengine. "Binunu nd'o ana mkanda, what do you expect comrade?, obvious kutomuona Binunu ni kutouona mkanda. Kwa sasa tukimtaja Binunu nd'o tunautaja Mkanda and vice versa is true"



    Safari ya Martin ilimfikisha bandarini, Posta. Hakupanga safari ya Posta kabla, nia yake kuu ilikuwa kwenda Kariakoo. Kisha nd'o kwenda bandarini kumpokea Binunu. Lakini hakuona umuhimu wa kwenda Kariakoo kufanya 'shopping', kwa hali kama ile iliyotokea. Alienda bandarini moja kwa moja. Martin alishuka ndani ya gari, bila kutambua kwamba alikuwa anamwacha Mwendawazimu ndani ya gari yake. Alivyoshuka chini, alikumbuka 'kulock' milango yote ya gari kwa kutumia 'remote'. Huku akimfungia mwendawazimu ndani ya Range Rover.

    Safari yake ilimpeleka hadi katika ofisi za meli ya MV Donors, hali aliyoikuta, alichoka. Ofisi za MV Donors zilikuwa mithili ya msibani, kulikuwa na watu wengi sana wakilia. Ilikuwa mayowe matupu! Martin akaona pale sio mahali pazuri kukaa. Aliamua kwenda kusubiri ndani ya gari yake. Hakuona sababu ya watu wale kulia, ni yeye pekee ndiye aliyepaswa kulia. Alikuwa amepoteza kitu kikubwa sana....kitu cha thamani sana…Mkanda wa siri!

    Akiwa njiani kuelekea katika gari yake, simu yake ya mkononi iliita. Aliitoa mfukoni harakaharaka na kuiangalia. Richard ndiye aliyekuwa anapiga. Aliipokea.



    "Nambie Richard" Martin aliongea simuni akiwa amesimama.



    "Comrade bilabila aisee" Richard alijibu kwa sauti ya kukata tamaa.



    "Inamaana Binunu hajaonekana!" Martin aliuliza kwa nguvu.



    "Ni ngumu sana kumpata kwa hali ilivyo kule baharini, ni ngumu sana Comrade!" Richard alijibu.



    "Mkanda je?" Martin aliuliza swali lengine. "Binunu nd'o ana mkanda, what do you expect comrade?, obvious kutomuona Binunu ni kutouona mkanda. Kwa sasa tukimtaja Binunu nd'o tunautaja Mkanda and vice versa is true"



    "Kazi ipo comrade"



    "Tena si ndogo, kazi ngumu kuliko zote tulizowahi kufanya katika sayari hii yaja. Kumtafuta Binunu aliyezama baharini. Kumbuka baharini kuna maji kaka, je Binunu atapona kwa yale maji? Na kuhusu mkanda....Je mkanda hautaharibika ukiingia maji?!



    “Tena maji ya chumvi!" Richard alikazia.



    "Usiseme sana brother, tuamini mkanda uko sehemu fulani salama. Binunu hawezi kuruhusu mkanda uharibike. Yule ni Komando hata ikibidi kuumeza mkanda ataumeza ili kuunusuru. Kwa hali ilivyo nakuja Zanzibar sasahivi" Martin alieleza kwa kirefu.



    "Itakuwa poa sana uje tuongeze nguvu" Richard aliunga mkono hoja ya Martin nae kwenda Zanzibar.



    "Ni njiani Comrade"



    Simu ikakatwa.



    "Martin bwana...Binunu ameze mkanda mkubwa vile" Richard alijiuliza peke yake. Sasa Martin aligairi kuelekea katika gari yake. Alirudi bandarini na kukata tiketi ya boti ya Zanzibar. Kabla hajaondoka aliongea mawili matatu na mtu mmoja pale bandarini, wakati akisubiri muda wa Boti ya Azam Marine kuondoka. Na muda ulipofika Martin alienda Zanzibar bila kujua kuwa anaondoka ilhali alikuwa kamfungia Mwendawazimu katika gari yake!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Zanzibar

    Saa 3:07 P.M



    Martin aliwasili Zanzibar. Akipokelewa na Richard bandarini. Waliongozana hadi katika gari ya Richard.



    "Martin Hisia hali ngumu sana" Richard aliongea pindi tu walipoingia garini. Kwa sauti iliyokosa matumaini.



    "Daah ni kweli Comrade, ila everything will be ok, kwani Wahanga wa ajari wanapelekwa wapi?" Martin alisema huku akiuliza swali.



    "Nafikiri itakuwa katika viwanja vya Maisala" Richard alijibu. "Ok twende huko kwanza as our starting point" Alishauri Martin.



    "Sawa" Richard na Martin walielekea katika viwanja vya Maisala.



    *****



    Katika viwanja vya Maisala hali ilikuwa tete. Ni kweli maiti na wahanga wa ajari ya meli ya MV Donors walikuwa wanapelekwa hapo. Kama alivyofikiria Richard. Hali katika viwanja hivyo ilikuwa ni ya kutisha na kusikitisha sana. Maiti zilikuwa zimelazwa chini katika misururu mirefu, huku ndugu na jamaa wakipita mbele ya maiti hizo wakijitahidi kuwatambua ndugu zao. Kwa pembeni ilikuwa sehemu ya majeruhi. Makelele, vilio na malalamiko yalitawala kiwanjani hapo. Ilikuwa tafrani! Wakina Martin walipofika katika viwanja vya Maisala moja kwa moja walielekea mahali walipohifadhiwa majeruhi. Haikuwaingia akilini hata kidogo kwamba Binunu anaweza kufa kwa ajari ile. Binunu alishawahi kupata mikutuo mikubwa na ya hatari zaidi ya aliyoipata kwenye ajari ile ya meli. Binunu hakuwahi kuwa mtu mzembe tangu azaliwe. Walimuamini sana, na alijiaminisha kwao, kwa vitendo sio kwa maneno. Siku zote Binunu alikuwa ni mshindi. Ukitaka ufanikiwe katika operesheni yako, basi mchukue Binunu...na hiyo ndio sababu ya Binunu kuwemo katika operesheni hii. Operesheni mkanda wa siri!

    Dakika zaidi ya arobaini walizitumia kumsaka Binunu. Lakini dalili zote zilionesha kwamba Binunu hakuwepo kati ya majeruhi wale. Sasa waliamua kuelekea kwenye misururu mirefu ya maiti. Zaidi ya saa moja walitumia kukagua maiti. Lakini hata kwenye maiti hawakufanikiwa kuiona maiti ya Binunu.

    Walichanganyikiwa sana!



    Dar es salaam

    Saa 4:30 P.M



    Saa zaidi ya nne yule Mwendawazimu alikuwa amekaa ndani ya gari ya Martin. Cha ajabu Martin hakurejea. Sasa akaanza kujuta mwenyewe kwa hatua aliyoichukua. Mwendawazimu alijiona amecheza mchezo wa pata potea....na kwa bahati mbaya amepotea!



    "Lazima nitafute namna ya kutoka nje"



    Kitu ambacho hakukijua yule Mwendawazimu Martin hakuwahi kuwa mjinga. Martin alikuwa anaitwa Martin Hisia, Mwendawazimu aliweza kuingia kwenye gari yake kwa kuwa Martin alikuwa katika dimbwi la mawazo. Martin ana hisia zaidi ya mtu yeyote katika sayari ya Dunia. Na hiyo ndio sababu ya kuitwa Martin Hisia kwa watu aliowahi kufanya nao kazi walikubali Martin alikuwa kiboko! Eti aiache gari yake bandarini bila ulinzi? Huyo sio Martin Hisia. Martin alikuwa amempa kijana mmoja kazi ya kulilinda gari lake, hadi atakavyomuelekeza venginevyo. Na hivyo ndivyo kijana Mansour alivyofanya. Alikuwa analiangalia gari la Martin kila baada ya dakika moja. Mwendawazimu alipania kutoka nje ya gari ile. Alijua akilemaa atafia mle. Alijaribu kugusa kioo cha gari ile, kilikuwa kioo cheusi kigumu. Ilihitaji nguvu za ziada kuweza kukivunja. Mwendawazimu alikuwa nazo nguvu hizo, tena hata zaidi ya hizo zikihitajika. Akiwa kwa ndani aliona kila kitu kilichokuwa kinaendelea nje, ilhali watu wa nje hawakuwa wanaona kabisa kilichopo ndani ya gari ile. Ilikuwa 'tinted'. Jamaa hakuwa Mwendawazimu. Alikuwa katika operesheni ya kutekeleza jambo fulani. Jambo ambalo bado alikuwa hajalipatia utatuzi mpaka sasa. Aliishia kufungiwa tu ndani ya gari. Jina lake halisi yule mwendawazimu lilikuwa ni Peter Kissali.

    Mwendawazimu alizungusha macho yake ya kijasusi nje ya ile gari. Alimgundua! Hakika aligundua kwamba lile gari kulikuwa na mtu alikuwa analilinda pale bandarini. Sasa Mwendawazimu alikuwa anataka kufanya kitu bila kushuhudiwa na yule mlinzi.

    Mansour alikuwa ni mtoto wa mjini. Mtu mjanja sana kuliko wote pale Bandarini. Wenyewe walikuwa wanamwita Shanta. Mwanaume asiyechagua kazi ya kufanya. Leo alifanya kazi hii, kesho atafanya kazi ile, ilmradi mkono wake uende kinywani. Mansour alikuwa anajuana na Martin Nguzu kimjinimjini. Alishafanya nae kazi kadhaa, na kulipwa ujira wa maana na Martin. Hivyo baada ya leo hii kupata kazi ya kulilinda gari la Martin alikuwa makini sana kuitazama ile gari mara kwa mara, akijua kuwa endapo atailinda na Martin kuikuta salama gari yake, basi ajiandae kupokea donge nono.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Zanzibar,

    Saa 05:54 P.M



    Kina Martin walikuwa hoi bin taaban. Bado walikuwa katika viwanja vya Maisala lakini hakuna lolote la maana walilovumbua. Pamoja na kupoteza muda wote huo pale uwanjani lakini hawakumuona Binunu, wala kuivuta harufu ya Binunu. Hii ilikuwa ni hatari sana kwa mustakabari wa Mkanda wa siri.

    Sasa walikuwa nje ya viwanja wakiwa wameegemea gari ya Richard, Toyota Vitz. Wakijadiliana.



    Katika kibanda kimoja cha mama lishe, umbali kama wa mita mia moja kulikuwa na mtu amekaa. Akiwa makini kuwafatilia kina Martin tangu walivyowasili katika viwanja vile. Jamaa alikuwa kashika sigara aina ya Portsman mkononi. Ni sigara ya kumi na tatu tangu alivyowasili mahali pale. Malolo alikuwa makini akiwatazama majamaa wale wawili. Huku akitabasamu moyoni mwake. Malolo alikuwa anamkumbuka sana Richard, alikumbuka usiku uliopita walivyovamia nyumbani kwa Bosi wake na kuondoka na mkanda wa siri! Hakumkumbuka tu yule mwanamke wa ajabu. Kwa kushirikiana na mwanaume aliyekuwa anatazamana nae sasa walivyofanya mambo ya ajabu na kushangaza sana, na kufanikiwa kuondoka na mkanda ule. Malolo hakuiona vizuri sura ya huyo mwanamke, kutokana na maluweluwe, yeye alifanikiwa kumuona Richard pekee na kuishia kuitambua tu jinsia ya mshirika wake. Kutofanikiwa kuinasa sura ya yule mwanamke ndio sababu iliyomfanya kuizamisha meli mzima ya MV Donors. Ili kumpoteza yule mwanamke, kuupoteza pia ule mkanda wa siri. Hii inaitwa "Bora tukose wote"



    "Hivi walijuaje hawa kama ule mkanda ulikuwepo sehemu ile?" Malolo alijiuliza mwenyewe kimoyomoyo akiwa pale kibandani alipokaa. Hakukuwa na wa kumjibu moyoni mwake, wa kumjibu alikuwa anatazamana nao, wakiwa wameegemea gari.



    ***

    Bado watu wanaviziana katika viwanja vya Maisala, na Binunu hajapatikana, Dar es salaam Mwendawazimu anajikuta anafungiwa ndani ya gari..



    ILIKUWA jana usiku, usiku wa saa sita. Katika eneo la kasri la Chifu Abdullah Khalifa kulikuwa kimya muda huo. Walinzi kadhaa walikuwa wanaizunguka kasri hiyo na bunduki zao mikononi. Kuhakikisha hali ya usalama katika kasri inakuwa nzuri.

    Malolo Abdallah alikuwa amesimama katikati ya mlango wa Chifu Abdullah, akiwa na bastola mbili kila upande wa kiuno chake, akihakikisha baya lolote lile halimkuti Bwana Abdullah ama Chifu kama walivyozoea kumwita wenyewe. Malolo ndiye alikuwa mlinzi mkuu katika kasri ile.



    Nje ya kasri hiyo kulikuwa kuna vivuli viwili vilikuwa vinaisogelea kasri hiyo. Kivuli cha mwanamke na kivuli cha mwanaume. Vivuli vile vilikuwa vivuli vya Richard Philipo na Binunu Issa. Walikuwa wanainyatia nyumba ile kwa lengo kuu moja tu, kuupata mkanda wa siri. Walikuwa wamejipanga vizuri. Wote wakiwa wamevaa nguo nyeusi za mpira zilizowabana vizuri, na viatu vyepesi vyeusi. Hawakuwa na tofauti yoyote ile na giza. Ilikuwa kama giza tu linasogea. Migongoni mwao walikuwa na mitungi ya gesi, iliyofanana kama mabegi, mitungi nayo ilikuwa meusi...mipira meusi toka mgongoni katika mitungi ilipita juu ya bega la kushoto la kila mmoja na kuziba pua na midomo yao. Viziba pua pia vilikuwa veusi. Walijizuia vizuri pua zako na kupumuua kwa kutumia oksejini iliyokuwa inatokea katika mitungi, migongoni mwao. Walikaribia kabisa katika kasri ya Chifu. Wakaanza kupuliza 'spray' walizoshika mikononi mwao. 'Spray' nne, kila mmoja akishika mbili, moja mkono wa kushoto na nyingine mkono wa kulia. 'Spray' za foner. 'Spray' zenye sumu iletayo usingizi pindi tu mtu aivutapo. Sumu iliyokuwa inaweza kusambaa umbali wa mita mia moja kila upande na kumuathiri mtu yoyote atakayeivuta pasi na kizuio. Ukiivuta tu 'spray za foner' umelala.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Walinzi wa Chifu waliivuta na walilala!



    Binunu na Richard waliingia ndani ya kasri kirahisi. Huku wakiendelea kupulizia zile 'spray' kila hatua waliokuwa wanapiga. Ilikuwa nusa, ulale. Malolo nae aliingia katika mtego huo wakina Binunu. Alilala bila kujijua katikati ya mlango wa chumba cha Chifu. Jamaa walipata nafasi wakaingia hadi chumbani kwa Chifu. Richard na Binunu waliingia hadi chumbani kwa Chifu. Huku wakivuta hewa safi ya oksejini ikitoka katika mitungi yao migongoni. Hawakupata shida kabisa kuingia ndani ya kasri ya Chifu Abdullah, funguo moja tu ilifanya kazi ya kufungua milango yote. Wenyewe wanaiita 'master key'. Milango yote ilisalimu amri kwa kutumia 'master key' moja. Hawakuwa wanaongea katika hiyo operesheni. Ilikuwa ni kimyakimya na kupeana ishara za mikono mara chache sana. Ndipo safari yao ilipowafikisha katika chumba cha Chifu. Wakimwacha Malolo kalala vibaya mlangoni. Chumbani kwa Chifu walimkuta nae kalala usingizi mzito, usingizi uliotokana na spray ya Foner, kazidiwa nguvu kabisa na sumu toka katika 'spray' ile. Binunu alitoa 'spray' nyingine pembeni mwa mtungi wake wa gesi, 'spray' tofauti na zile wakizozitumia awali katika kuingia mle ndani, hii ya sasa ilikuwa inaitwa Ocer. Akampulizia Chifu puani taratibu. Chifu alipiga chafya mara tatu mfululizo. Ishara kwamba alikuwa anazinduka toka usingizini. Sasa akaamka huku akiwa anakohoa kwa nguvu.



    Zile zilikuwa 'spray' maalum kwa kazi za kimafia. Kulikuwa kuna 'spray' ya kulaza iliyokuwa inaitwa Foner, na kuna ya kuamsha iliyokuwa inaitwa Ocer. Lakini ukipuliziwa 'spray' ya Ocer huamki kawaida, inakuamsha ukiwa na maluweluwe, hujitambui! Na kueleza jambo lolote utakaloulizwa bila kujitambua. Na kutokumbuka chochote kama ulieleza kitu hata uamkapo. 'Spray' hizo hutumiwa sana na askari Polisi kwa wale Wahalifu wanaokataa kutoa siri hata baada ya kupewa mateso makali. Hupuliziwa na kutapika kila kitu! Wakiamka huendelea kuficha siri zao bila kujua kama walieleza kila kitu wakiwa hawajitambui.



    Chifu alikaa kitako kitandani. Akiwa anashangaashangaa tu.



    "Chifu Abdullah" Binunu aliita kwa sauti ndogo. Sauti iliyosikiwa vizuri na Chifu. Lakini Chifu alitoa macho tu kuwaangalia wale watu wawili. Haelewi chochote. Hakujibu chochote.



    "Chifu Abdullah....mkanda wa siri umeuweka wapi?" Binunu aliuliza tena bila kujari kama Chifu hakuitika alivyomuita awali.



    Chifu hakujibu, lakini aliangalia sehemu moja katika ukuta. Richard akaelewa. Richard alienda kwenye ukuta, sehemu alipokuwa anapaangalia Chifu. Akapagusa. Palikuwa pagumu sana, hamna dalili ya uwazi wala nafasi ya kuweza kuweka kitu. Richard akamwangalia Binunu. Binunu nae hakuzubaa akamuuliza Chifu.



    "Wanafunguaje pale Chifu kuupata Mkanda wa siri?" Chifu hakujibu, lakini aliangalia swichi ya kitandani 'bed switch'.

    Binunu akaelewa.

    Binunu akaisogelea ile swichi, iliyokuwa inaning'inia pale kitandani. Akaibonyaza. Ukuta ulijifungua mithili ya deki. Kikatoka kitu kama kisahani kikiwa na mkanda.

    Eee bwana wee!

    Richard aliuona vizuri mkanda, Mkanda wa Siri! Akauchukua. Binunu akampulizia Chifu ile 'spray' ya awali..Foner. Chifu alilala tena. Binunu akabonyeza tena ile swichi ya kitandani. Kile kisahani kikazama ndani ya ukuta. Kisha ukuta ukajifunga. Ukawa kama awali. Jamaa wakawa wanatoka nje ya chumba cha Chifu wakiwa na mkanda wa siri mkononi. 'Spray ya Ocer' iliyotumika mle chumbani kumuamsha Chifu kwa bahati mbaya ilifika hadi mlangoni, pale alipolala Malolo. Malolo aliamka! Akiwa na maluweluwe tele, hana nguvu hata kidogo. Alikuwa analazimisha kufungua macho. Macho yalikuwa mazito sana. Yaligoma kabisa kufunguka. Akiwa katika harakati za kufungua macho alisikia watu wakitoka chumbani kwa Chifu. Binunu alikuwa ameshamvuka Malolo pale mlangoni. Malolo alijilazimisha kufungua macho. Yalifunguka! Malolo alifanikiwa kumuona Richard. Akitoka ndani ya chumba cha Chifu. Alijigeuza kwa shida. Alimuona mwengine! Malolo alifanikiwa kuuona mgongo wa mwanamke ukitoka nje. Yeye aliwaona, wao hawakumuona kama anawaona!

    Walinzi wengine waliaamka mnamo saa tisa usiku. Wakiwa hawaelewi kabisa nini kilitokea. Waliendelea kulinda kama ilivyowapasa. Huku wote wakiandamwa na ugonjwa wa kichwa kizito.

    Kule ndani Chifu nae alizinduka. Kuamka tu cha kwanza kufikiria mkanda! Alinyanyuka kitandani akabonyeza swichi ya kitandani. Ukuta ulifunguka. Chifu alinyanyuka na kwenda kuuangalia mkanda katika ukuta. Mkanda haukuwepo! Chifu alipiga makelele!



    “Mkandaaaaaaa!”



    Walinzi wote wa kasri ya Chifu walikimbilia mlangoni mwake haraka. Walinzi wapatao thelathini walikuwa wakinesanesa tu mlangoni. Wamelewa sumu ya ‘foner’. Wote vichwa vizito! Lakini Malolo pekee ndiye aliyeingia ndani. Kidogo yeye alikuwa hana mneso sana. Aliamka zamani kidogo tofauti na wale walinzi wengine. Alimkuta Chifu amechanganyikiwa! Donge zito limemkaba kooni, hajui alie ama acheke. Alijitahidi kusema lolote Malolo amsikie lakini sauti haikutoka. Alithubu kutoa ukelele wa mwanzo tu. Sasa hakuweza kusema chochote. Chifu alikuwa kaacha mdomo wazi mithili ya mbwa! Macho yamemtoka pima! Malolo akaelewa bila kuambiwa.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Mkanda umepotea Chifu?" Malolo aliuliza kibwege. Kwani yeye ndiye alikuwa amewaona japo kwa maluweluwe. Chifu alitikisa kichwa kinyonge, kukubali. Malolo nae alichanganyikiwa. Ingawa alijua kama wamevamiwa lakini hakudhani kama wataweza kuuona mkanda. Uliwekwa sirini. Malolo alijizungusha kwa haraka mithili ya pia, huku akitoa ukelele wa ghadhabu. Ama hakika walipatwa, waliwezwa, walipatikana..!



    Walinzi kule nje akili ziliwarejea. Wote wakaingia ndani ya chumba cha Chifu. Kuutafuta mkanda. Chumba kilijaa...ilikuwa vichekesho, lakini hakuna aliyefikiria kucheka. Huyu kapekua hapa, yule kapekua pale.



    Baadae Ilibidi wakae chini, sebuleni na Chifu kujadiliana, hadi saa kumi na nusu hawakuwa wamepata jibu bado. Zaidi ya kufikiria kuwa lazima mkanda utakuwa umesafirishwa kwenda Dar es salaam. Hilo lilikuwa wazo la Malolo.

    Na nani...hakuna aliyejibu swali hilo. Lakini Malolo alikuwa na taswira usoni mwake. Hakusema.



    Saa kumi na moja asubuhi. Malolo alienda bandarini, akitekeleza kwa vitendo wazo lake kuwa lazima mkanda utasafirishwa kwenda Dar es salaam. Alivyofika bandarini aliambiwa meli moja tu ndio itakayoenda Dar es salaam asubuhi. Nae alikata tiketi meli hiyo. Asubuhi meli ilianza safari. Kama alivyowaza Malolo. Ndani ya meli Binunu alikuwepo akiwa na mkanda, na Malolo alikuwepo akiufatilia mkanda. Akiwa hajui u mikononi mwa nani. Aliitafuta sana sura ya mtu aliyemuona katika maluweluwe. Sura inakuja mara inakata. Kumbuka ‘Ocer’ haikumpata vizuri Malolo. Endapo ingempata bara'bara...isingekuja kabisa taswira ya Richard, ingeondoka jumla. Alijaribu kuitafuta ile taswira aliyaiona kwa maluweluwe, hakuiona. Ndipo alihisi labda yule mwanamke ndiye atakuwa na mkanda. Hakuwa anaijua kabisa taswira ya sura yake. Alibahatika kuona mgongo tu wa yule mwanamke. Meli ilikuwa imejaza hasa. Peke yake Malolo hakuwa na uwezo wa kuteka meli mzima ili kulazimisha mwenye mkanda autoe. Alichofikiria ndicho alichofanya. Aliitoboa meli kwa 'silence bom' ili wakose wote. Hii inaitwa Liwalo na Liwe!



    *****



    Dar es salaam; saa 7:07 P.M

    Jijini Dar es salaam, bado kulikuwa na mviziano kati ya Mansour na Mwendawazimu. Jua lilikuwa limezama na giza sasa lilikuwa limeanza kushika hatamu. Huku Mwendawazimu akiwa bado yuko ndani ya gari ya Martin na Mansour yuko nje ya gari ya Martin. Lakini sasa Mansour alikuwa ameisogelea kabisa na kuegemea boneti ya gari. Peter Kissali au Mwendawazimu alikuwa katika hali mbaya sana mle ndani ya gari. Saa alizokaa mle zilimfanya awe katika hali ngumu sana. Alifikiria sana namna ya kutoka ndani ya gari bila kustukiwa na mlinzi, hakuipata. Kila alichotaka kufanya aliona sicho, au sio wakati wake. Alifikiria hadi alichoka. Uwendawazimu wote ulimuisha!

    Ghafla simu yake iliyokuwa mfukoni ilitoa mtetemo. Aliitoa na kuiangalia kidogo kisha kuipokea.



    "Malolo ndugu yangu nimepatikana!" Peter aliongea kwa sauti ndogo.



    "Uko wapi Peter?" Malolo aliuliza.



    "Nimefungiwa ndani ya gari!" Peter alijibu.



    "Kakufungia nani Peter?" Malolo aliuliza tena, safari hii sauti yake ikiambatana na hofu.

    "Martin, Martin, Martin Hisia kaniweza kweli" Peter aliongea kwa kulalama.



    "You are a man Peter, wewe ni zaidi ya Mwanajeshi Peter, Kumbuka Arusha Peter. Mkumbuke Nunda! Hivi unakumbuka ulifungiwa kwenye banda la Simba peke yako lakini mwanaume ulitoka!. Eti leo hii ushindwe kutoka kwenye Range Rover? Siku zote wewe ni shujaa Peter! Fanya juu chini utoke ndani ya gari, inabidi uje Zanzibar Peter, uje haraka sana, mambo magumu sana huku" Malolo aliongea kwa hisia.



    "Hahaha" Peter aliishia kucheka tu.



    Na simu ikakatwa.



    Maneno ya Malolo yalimkumbusha mbali sana Peter. Alikumbuka magumu mengi waliyoyapitia katika Operesheni zao hatari, likiwemo hii aliyokumbushwa na Malolo. La kufungiwa na Simba bandani. Katika OPS. Malolo alikuwa hatanii ulikuwa ni ukweli mtupu!



    Ilianza kama biashara lakini biashara ikageuka kuwa Operesheni ngumu sana. Walitumwa kwenda kuuza madawa ya kulevya jijini Arusha. Yeye na Malolo. Baada ya kuuza madawa kama walivyoagizwa na Chifu ndipo tamaa ya Pesa ikawapata. Tamaa ya kuyapora tena yale madawa toka kwa yule jamaa waliyemuuzia. Hawakujua kama jamaa alikuwa makini katika kazi yake. Hakwenda peke yake katika hoteli ya Chanaga kufanya biashara, kulikuwa na watu nyuma yake, wakifatilia kila kitu kinavyoendelea. Peter na Malolo hawakulijua hilo. Walimuonesha jamaa bastola!

    Aligwaya.

    Aliwapa pesa pamoja na madawa bila wasiwasi wowote. Walipotaka kutoka nje ya hoteli hawakupiga hata hatua tatu. Walitazamana na midomo mitano ya bastola. Toka kwa watu watano tofauti. Ilikuwa zamu yao wao kugwaya. Zamu yao kuporwa!

    Waliporwa madawa pamoja na pesa kimyakimya. Wakaachwa.

    Kina Malolo nao hawakukubali. Wataenda kumwambia nini Chifu ilhali hawakuwa na madawa wala pesa. Walipanga usiku wawaendee tena wale jamaa. Kuwavamia ili wapate angalau kimoja, pesa ama madawa ya kulevya. Waliyokutana nayo huko....wao wenyewe walikiri kuna watu makatili sana duniani! Na kuipa jina operesheni ile kama Operesheni Pambana na Simba (OPS).



    Ghafla Peter akagutuka toka mawazoni.



    "By any means lazima nitoke humu leo, no sio leo, ni sasahivi! Nilitoka katika OPS nishindwe kwenye ‘OMS’ (Operesheni Mkanda wa Siri)?" Peter alisema hilo neno huku akipiga ngumi ya nguvu katika kioo. Kioo kilisambaratika! CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Makelele ya mvunjiko wa kioo yalifika katika masikio yote mawili ya Mansour.

    Afanalek!

    Mansour hakusubiri hata sekunde moja, alienda wakawaka pale dirishani. Kifua katanguliza mbele, kujitanabaisha kwamba yeye ni mbabe! Bila kujua kwamba alikuwa anaenda kukutana na Mwendawazimu!



    E bwana wee!!!



    Saa Mbili usiku mke wa Chifu alirejea nyumbani. Ni wiki moja na nusu sasa alikuwa ameenda kuwatembelea jamaa zake huko Pemba. Alirudi leo baada ya kupigiwa simu na mumewe na kuambiwa kuwa mkanda umepotea. Baada ya maelezo toka kwa mumewe, Malkia aliitisha mkutano wa walinzi wote. Baada ya mahojiano hakuna mlinzi aliyekuwa na jibu la maana. Wote walikuwa sijui, sijui, sijui, sijui. Aliyejitahidi sana alisema sielewi. Baada ya kumuulizia Malolo aliambiwa kuwa Malolo hajarejea tangu alivyoenda kuufatilia mkanda. Usiku uleule mwanamke yule hatari wa kipemba nae aliingia kazini. Akiwa na mkoba wake mweusi wa begani wenye silaha hatari!

    Malkia alienda kuutafuta mkanda wa siri. Moja kwa moja nae akili zake zilimwambia aende katika viwanja vya Maisala.

    Na alienda!

    Malkia aliwasili katika viwanja vya Maisala usiku uleule.



    *****

    Mbabe Mansour alikaribia katika kioo cha gari ya Martin Nguzu. Alipigwa na butwaa! Kioo cha nyuma cha gari ile ya kifahari hakikuwepo! Alijaribu kuangalia mazingira ya eneo lile labda ataona chochote kitakachoweza kupasua kioo cha gari ile. Hakuona chochote cha maana, eneo zima kuzunguka gari ile kulikuwa kumetulia tuli. Alijaribu kuchungulia ndani ya gari. Kupitia katika kioo cha gari. Kuona labda kitu kilichovunja kioo kile kitakuwa kimeingia ndani ya gari.

    Lilikuwa ni kosa la karne!

    Ndani ya Range Rover Vogue Mwendawazi aliiona ile shingo ya yule mlinzi. Hakuchelewa... Aliivuta kwa nguvu ndani ya gari huku akiinyonga kuelekea upande wa kulia! Ulisikika mlio hafifu kama kijiti kikavu kikivunjika. Kilikuwa ni kitendo cha kama sekunde thelathini tu lakini kilimpeleka Mansour nje ya sayari hii! Peter hakuicha ile shingo ya mlinzi, aliendelea kumvuta ndani Mansour kwa kupitia lile dirisha bovu. Giza lilikuwa upande wake. Lilimsaidia kutoonekana na jicho lolote lile haramu kwake.



    ******



    Zanzibar: Saa 9:30 P.M

    Watu wanne hatari walikuwa katika kiwanja cha Maisala. Martin na Richard wakiwa pamoja. Malolo akiwa pekee, na Malkia akiwa pekee. Malolo bado alikuwa anawafatilia wakina Martin Hisia, na sasa alikuwa anawaona wakitoka nje ya uwanja wa Maisala. Bila shaka kwenda kukaa tena mbele ya gari yao. Malolo nae harakaharaka alitoka nje ya uwanja. Lilipoelekea windo lake. Alivyofika tu nje kina Martin jicho lake moja kwa moja lilitua katika ile gari yao walipokaa awali.

    Hawakuwepo!

    Aliangalia kulia kisha akageuza shingo yake harakaharaka kuangalia kushoto. Kulikuwa na watu wengi lakini sio aliowahitaji. Kina Martin walimpotea katika shabaha yake! Kina Martin walienda mahali pasipojulikana.

    Malolo alichoka!

    Martin Hisia ndiye alihisi kwamba walikuwa wanafatiliwa. Alimwambia Richard kwa siri. Kisha Richard nae aligeuka kwa siri kumwangalia huyo jamaa akiyewafatilia. Sasa wote walimuona yule jamaa. Richard aliikumbuka sura ya yule jamaa, lakini hakukumbuka alimuona wapi. Alijaribu kuvuta kumbukumbu, hazikuja. Ndipo walivyotoka nje, Waliamua kupotea katika macho ya Malolo kwa muda ili kuweza kuziangalia vizuri nyendo zake.



    Na Mwindaji akageuka kuwa mwindwaji.



    Lakini kina Martin walichokuwa hawakijui ni kwamba, walifanikiwa kuyakimbia macho ya Malolo lakini hawakufanikiwa kuyakimbia macho ya Malkia. Malkia aliwaona vizuri sana vijana wale hadi walipoenda kujificha.



    Na ndipo Wawindaji wakawa wanawinda huku wakiwa wanawindwa na Mwindaji.



    Sasa zilikuwa zinatumika akili, hisia, maarifa na ujuzi. Wakati kina Martin Hisia wakimzidi akili Malolo, na Malkia nae aliwazidi akili wakina Martin. Malolo nd'o alikuwa zuzu wa mwisho kwa wakati ule, alikuwa anahangaika kuwatafuta wakina Martin bila mafanikio yoyote.



    *****

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Katikati ya Bahari. Binunu alikuwa anazama pamoja na kile kipande cha meli. Naam, kile kipande alichokuwemo Binunu kilikuwa kinazama majini. Huku watu wakiwa wanaporomoka vibaya sana kuelekea majini. Binunu alibaki amekishikilia imara kile kiti alichokalia. Binunu alikuwa imara!

    Ilikuwa labda king'oke kiti ndipo nae aang'oke. Kile kipande cha meli hakikuwa na huruma, kilikuwa kinazama chote majini huku Binunu akiwa mahali palepale! kaking'ang'ania kiti chake. Alipoona kipande kinazidi kwenda chini. Aliamua kutoka akiwa anaogelea ndani ya maji yaliyokuwepo ndani ya meli. Kile kipande cha meli hakikukoma kuwasulubu wanadamu waliokuwa katika kipande kile. Hali ilikuwa ya hatari sana. Kipande kiliongeza mwendokasi na kujikita chini ya mchanga wa bahari kwa nguvu!

    Kikatulia.

    Kwa bahati mbaya kabisa msukumo wa meli kuelekea mchangani ulimkumba na yeye, Binunu alipoteza uelekeo katika kuogelea kwake. Kasi ya msukumo wa kujigonga kwa meli chini ukichanganya na nguvu ya maji ulimpeleka ndivyo sivyo Binunu. Alikumbwa na vitu vilivyopo ndani ya meli na kwenda kubwagwa katika kiti cha chuma, alijigonga vibaya sana nyuma ya kichwa chake, kisogoni. Maumivu yalisambaa haraka sana mwili mzima. Damu zinamvuja! Akapoteza umakini wa kuogelea. Akanywa funda la maji. Akajaribu kutapatapa, akanywa funda la pili la maji. Akatoa ukelele mdogo wa maumivu na majuto. Kutoa ukelele lilikuwa kosa, akanywa funda mbili za harakaharaka. Akapata maluweluwe, meli ikanesa tena, sasa kipande kilikaa sawasawa chini ya mchanga...lakini kukaa sawa kule kulikuwa na athari kubwa sana kwa Binunu. Maana msukumo ule tena ulimfanya Binunu ajigonge tena katika ukuta wa meli ile. Tena kwa bahati mbaya alijigonga mahali palepale, kisogoni! Alilia kwa nguvu sasa. Maji hayakukisikia kilio chake au labda hayakukielewa.....Bila kutarajia akarushwa kwa nguvu nje ya meli kupitia dirishani.



    Maji yana nguvu sana asikwambie mtu.



    BOTI za Jeshi la Wananchi wa Tanzania pamoja na vyombo mbalimbali vya baharini vya kiraia viliendelea kuopoa maiti pamoja na wahanga wa ajari ile mbaya ya meli. Hadi saa sita ya usiku bado Boti, Mashua, Ngalawa, na Majahazi yalikuwa yanajitahidi kuopoa maiti na wahanga wa ajari.



    Katika viwanja vya Maisala, hadi saa sita ya usiku bado majamaa walikuwa bado wanaviziana. Malkia akiwa kajibanza sehemu ileile, Martin na Richard nao wakiwa bado wamejibanza sehemu ileile. Sehemu mbaya kwao, maana iliruhusu wao kuonwa na Malkia vizuri sana ilhali wao walikuwa hawamuoni. Kwa lugha nyingine tunaweza sema walikuwa wamejianika mbele ya adui!

    Na Malolo nae alikuwa bado anazurura kila pembe kuwatafuta kina Martin. Lakini hakuwaona. Kwa hakika mkanda ulizua mambo. Kwa mahali alipokuwa Malkia alikuwa na uwezo wa kuwafanya chochote atakacho kina Martin. Alikuwa na uwezo wa kuwadungua kwa bastola kirahisi sana. Lakini aliamua kusubiri, kuwadungua haikuwa njia sahihi hata kidogo ya kuupata mkanda, pia hakuwa anajua watu wale wanahusika vipi katika kadhia ile. Yeye aliamua kuwawinda tu baada ya kuona wanawindwa na macho ya Malolo. Kwahiyo Malkia ilimpasa kusubiri na alisubiri. Mababu zetu waliwahi kusema zamani sana, karne na karne zilizopita ...."Subira yavuta heri".



    Msako wa Binunu bado waendelea katika viwanja vya Maisala, na sasa kaongezeka Malikia



    BOTI za Jeshi la Wananchi wa Tanzania pamoja na vyombo mbalimbali vya baharini vya kiraia viliendelea kuopoa maiti pamoja na wahanga wa ajari ile mbaya ya meli. Hadi saa sita ya usiku bado Boti, Mashua, Ngalawa, na Majahazi yalikuwa yanajitahidi kuopoa maiti na wahanga wa ajari.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Katika viwanja vya Maisala, hadi saa sita ya usiku bado majamaa walikuwa bado wanaviziana. Malkia akiwa kajibanza sehemu ileile, Martin na Richard nao wakiwa bado wamejibanza sehemu ileile. Sehemu mbaya kwao, maana iliruhusu wao kuonwa na Malkia vizuri sana ilhali wao walikuwa hawamuoni. Kwa lugha nyingine tunaweza sema walikuwa wamejianika mbele ya adui!

    Na Malolo nae alikuwa bado anazurura kila pembe kuwatafuta kina Martin. Lakini hakuwaona. Kwa hakika mkanda ulizua mambo. Kwa mahali alipokuwa Malkia alikuwa na uwezo wa kuwafanya chochote atakacho kina Martin. Alikuwa na uwezo wa kuwadungua kwa bastola kirahisi sana. Lakini aliamua kusubiri, kuwadungua haikuwa njia sahihi hata kidogo ya kuupata mkanda, pia hakuwa anajua watu wale wanahusika vipi katika kadhia ile. Yeye aliamua kuwawinda tu baada ya kuona wanawindwa na macho ya Malolo. Kwahiyo Malkia ilimpasa kusubiri na alisubiri. Mababu zetu waliwahi kusema zamani sana, karne na karne zilizopita ...."Subira yavuta heri".



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog