IMEANDIKWA NA : HALFANI SUDY
*********************************************************************************
Simulizi : Balaa
Sehemu Ya Kwanza
(1)
KILWA KIVINJE, mwaka
1989.
Ilikuwa tarehe kumi na tano, mwezi wa nne,
mwaka elfu moja mia tisa themanini na tisa. Ilikuwa usiku wa manane, usiku wenye
kiza kinene, usiku ulioandamana na mvua kubwa sana, na radi iliyotoa sauti kali
na za kutisha sana pamoja na miale yenye mwanga wa
kuogopesha.
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Usiku huo ulikuwa
ni usiku muhimu sana, kwa Don Genge pamoja na kundi lake hatari sana. Usiku huo
wa tarehe 15 mwezi wa 4 mwaka 1989 katika chumba cha kuhifadhia maiti, katika
hospitali ya wilaya ya Kilwa, maarufu kama Kinyonga, iliyopo katika mji wa Kilwa
Kivinje, mkoa wa Lindi, kulikuwa na mkutano wa siri.
Don Genge
akishirikiana na madaktari mahiri wa hospitali ya Kinyonga, pamoja na manesi
wenye roho nyeusi, roho mbaya kabisa, roho zisizokuwa na chembe ya huruma hata
kidogo, roho zinazojari pesa na kusahau utu, walikuwa wanaendelea na kikao chao
cha Siri, kilichofanyika katika chumba cha siri, kikiwahusisha watu wanaojua
kutunza siri.
Katika kikao hiko cha Siri.
alikuwepo Don Genge mwenyewe ambaye ndiye alikuwa mwenyekiti wa kikao, Dokta
Zaidi Kilumba, mganga mkuu wa hospitali hiyo, Dokta Sharifa Juma, daktari bingwa
wa upasuaji wilayani Kilwa, Dokta Tamaa Karimu, daktari aliyekuwa ndiye mkuu wa
chumba hiko cha kuhifadhia maiti, kulikuwepo pia na watu sita, walinzi wa Don
Genge, walikuwa walinzi mahiri, walinzi makini, wenye kujua kupigana aina zote
za mapigano. Walinzi waliopitia vyuo mbali mbali duniani, waliojifunza aina
mbali mbali za kuuwa na kufuzu kwa kiwango cha juu sana, waliopitia mateso
makubwa sana katika mafunzo hayo, mateso ambayo si rahisi kuvumilika kwa
binadamu wa kawaida, ndio, walipitia mateso katika mafunzo, mateso ambayo
yamewafanya wawe imara sana leo hii, kutokana na mateso hayo sasa wana uwezo
mkubwa sana wa kutesa, kumtesa mtu yeyote yule na kusema chochote
watakachomuuliza, hata kama aliapa kiapo cha damu kutosema, vijana hao sita
walikuwa wanajulikana kama SIX KILLERS, na majina yao walipewa kwa namba,
kulikuwa na one, two mpaka six, namba zilizotolewa kutokana na ubora wao katika
mapigano, ubora wao katika kujua mambo.
Katika kikao hiko cha siri
walikuwepo pia manesi watano, manesi ambao walikuwa na umuhimu mkubwa sana
katika mpango huu wa siri, manesi walioapa kuzitunza siri, kuzitunza siri
vifuani mwao zikatulia tuli katika mioyo yao
mibaya.
Ulikuwa mkutano muhimu sana kwao, labda
ungeweza kufanyika sehemu nyingine tofauti na chumba hiki cha kuhifadhia maiti.
Lakini sehemu zingine zote waliona siyo sahihi kwao, wakihofia siri zao kuwa
hadharani. Waliamua kufanya kikao chao hiki katika chumba hiki, wakiamini ni
sehemu salama sana, chumba ambacho kingekuwa ndio ofisi yao ya muda katika
kutekeleza mambo yao hayo ya kinyama, mambo ya siri sana, yaliyohitaji sehemu ya
siri na kuhusisha watu wenye kujua kutunza siri kama
hawa.
"Naamini wote tumekula kiapo hapa, kile
kiapo kinaitwa kiapo cha moto, kiapo kisichofutika hata mmoja wetu atakapokufa.
Kiapo kile tulichokula inamaana tutaitumikia kazi hii katika siku zote za maisha
yetu, na hata tukifa. Kazi tulionayo ni nyepesi, na kwa kuwa nyinyi ni watu
makini naamini itakuwa nyepesi zaidi. Kazi yetu ni kuhakikisha hakuna maiti
inayoenda kuzikwa kaburini kutoka katika hospitali hii ikiwa na moyo, lazima
tuhakikishe kila maiti inayotoka katika chumba hiki, cha kuhifadhia maiti haina
moyo.
Kwa siku tuna mkataba wa kupeleka mioyo ya watu kumi na mbili.
Najua ni idadi ndogo sana hiyo, kwa hospitali kubwa kama hii, hospitali
inayohudumia wilaya nzima.
Wote tunajua maiti zote za hospitali hii
zinapitia humu, na ndio maana Dr Tamaa Karimu ukajumuishwa katika mpango huu"
Mwenyekiti Don Genge aliacha kuongea, alitulia ili Kuhakikisha kila neno
aliloongea linapenya na kunasa vizuri katika vichwa vya watu wale. Mle ndani
kulikuwa kimya, kulikuwa na utulivu mkubwa sana, baada ya kimya cha kama dakika
moja Don Genge aliendelea.
"Lakini inawezekana ikatokea siku
hawajafariki watu kumi na mbili, na hivyo tukashindwa kupata idadi ya mioyo
tunayoihitaji, Dr Zaidi Kilumba ndio maana ukajumuishwa katika jopo hili, wewe
ni mganga mkuu katika hospitali hii, lakini kazi yako hapa itakuwa ni
Kuhakikisha mioyo tunayoihitaji inapatikana kila siku, na ikiwezekana izidi,
kazi yako kama mganga mkuu ni Kuhakikisha watu kumi na mbili au zaidi ya kumi na
mbili wanakufa kila siku katika hospitali yako, isipofikia idadi hiyo itabidi
uhakikishe unawauwa wewe, hapa sitaki kukufundisha utawauwa vipi, wewe ni
daktari, kwa kuwa unajua kuwatibu, bila shaka na kuuwa unajua pia" Alipofika
hapo Don Genge alitulia tena. Ili maneno hayo yazame na kujikita vizuri katika
bongo za watu wale.
Baada ya muda mfupi aliendelea
tena.
"Najua kazi hii inahitaji kufanya upasuaji, kuzipasua maiti ili
kutoa hiyo mioyo inayohitajika, Dr Sharifa Juma ndio maana upo hapa, kazi yako
ni Kuhakikisha unazipasua maiti kumi na tano kila siku na kuzitoa mioyo. Najua
kazi yako ni ngumu na inahitaji wasaidizi, ndio maana kuna hawa madada watano,
watakusaidia kila utakapohitaji msaada." Don alitulia tena, Akafungua chupa yake
ya maji na kunywa funda tatu kwa pupa, bila kujari kama alikuwa katika chumba
cha kuhifadhia maiti. Kuingia tu katika chumba kile kulihitaji ujasiri mkubwa,
hili la kunywa maji lilihitaji uwe kichaa kidogo. Chumba cha maiti chenye harufu
ya ajabu ya dawa zilizopuliziwa maiti ili zisiharibike halafu unywe maji, ama
hakika zilihitaji ukichaa, ukichaa kama wa Don.
"Kanuni za kazi hii ni
mbili tu, kutunza siri na ushirikiano. Kila mmoja wetu lazima atunze siri, huu
ni mpango hatari kwa hiyo unahitaji usiri mkubwa mno, pia lazima tushirikiane
ili kuweza kufanikisha Mpango huu, ushirikiano uwe ndio nguzo yetu kuu. Bila
ushirikiano hakuna litakalofanyika. Mwisho kabisa, tutahakikisha akaunti ya kila
mmoja wenu inajazwa pesa nyingi sana kila siku mtakapotukabidhi mzigo wetu. Pesa
ambazo hamjawahi hata kuwaza kuwa nazo, hapo sisemi sana, mtajionea
wenyewe..."
Alipofika hapo Don Genge alitulia,
alitembeza macho yake taratibu kwa kila mtu mle ndani. Wote walikuwa kimya, Don
Genge alivua miwani yake, akaanza kuipangusa vumbi kwa kutumia shati, ingawa
haikuwa na vumbi hata kidogo. Wanajopo wote walimwangalia Don Genge, sasa
ilikuwa zamu yake kuangaliwa.
"Nadhani tumeelewana" Don alisema huku
akiendelea kuifuta miwani yake.
"Ndio" Wanajopo wote waliitikia. Kila
mmoja kwa sauti yenye hisia tofauti. Wengine hisia za uwoga na wasiwasi, wengine
hisia za majonzi, wengine hawakuwa na hisia yoyote, wao waliona wanaenda kufanya
jambo la kawaida tu.CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Good, napenda sana
watu majasiri kama ninyi, hii nchi imeshaoza, kila mmoja anakula kutokana na
urefu wa kamba yake. Acha viongozi wafisadi kwa kupitia mikataba wanayosaini,
mikataba ya kijinga kama ya chifu Mangungo. Nasi lazima tufisadi kwa nafasi
yetu. Nchi haina mwenyewe hii, kila mmoja anakula anapopata nafasi ya kula" Don
aliongea maneno hayo ili kuhalalisha wanachotaka kufanya. Wote mle ndani
walisahau kwamba, ubaya haulipwi kwa ubaya, njia bora ya kulipa ubaya ni
kumfanyia wema kwa aliyekufanyia ubaya, ili nafsi imsute, ili
ajifunze.
Kikao kilifungwa saa tisa alfajiri. Kila mmoja alitoka
katika kikao kile na dhamira moja tu, Kuhakikisha mioyo kumi na tano inapatikana
kila siku, kwa njia yoyote
ile.
**************
Yusuph
Shaweji, alikuwa ni daktari kijana sana katika kituo cha afya Kilwa Masoko.
Marafiki zake walizoea kumwita Dr Yusha, wakichukua herufi ya kwanza ya jina
lake, na herufi ya kwanza ya jina la baba yake.
Dr Yusha alikuwa
daktari mwadilifu sana, mwadilifu kwa madaktari wenzake, mwadilifu kwa wagonjwa.
Alikuwa ni daktari mwenye weledi na kazi yake. Daktari mwenye kuheshinu miiko na
maadili ya kazi yake.
Usiku ule wa tarehe 15/ 4/
1989, wakati Don Genge, madaktari pamoja na manesi wa hospitali ya wilaya ya
Kilwa Kivinje, wakipanga mpango wao ule hatari, Dr Yusha alikuwa katika ukumbi
wa Sillent in, katika sherehe ya ndoa yake, baada ya kufunga ndoa mchana wa siku
ile. Ilikuwa ni siku ya furaha sana kwa Dr Yusha kutimiza ndoto ile adhimu
katika maisha yake, ndoto iliyodumu katika moyo wake kwa muda mrefu sana. Kuoa
ilikuwa ni ndoto yake, kumuoa Nasra, Ilikuwa ni ndoto yake kubwa
sana.
Wakiwa katikati ya sherehe, katikati ya
furaha, wakati Mc wa sherehe ile akitangaza kuwa ulikuwa wakati wa kulishana
keki maharusi, ndipo Dr Yusha akipoisikia simu yake ikiita kwa mbali katika
mfuko wa koti lake.
Katikati ya sherehe ya ndoa
yake Dr Yusha aliitoa simu yake.
"Haloo Dr,
mwanangu anaumwa sana, nahitaji msaada wako sana" Bila salamu sauti ilianza
kuongea, Ilikuwa ni kama sauti ya kizee ama sauti ya mtu aliyechoka kutokana na
madhila makubwa. Sauti ikiyotoka kwa hisia kali, ikiomba
msaada.
Pamoja na kelele za muziki pale ukumbini, pamoja na kelele za
watu pale ukumbini, lakini sauti ile iliyochoka ilipenya japo kwa shida katika
spika ya simu ya Dr Yusha, na kutua kwa shida vilevile katika sikio lake la
kushoto la Dr Yusha.
"Upo wapi?" Dr Yusha aliuliza
kwa sauti kubwa kidogo.
"Hospitali Kivinje"
"Ngoja nimpigie
Dr Kilumba, tuone atawasaidiaje?"
"Dr Kilumba na Dr Tamaa wote
tumejaribu kuwapigia, hawapatikani kwenye simu zao kaka yangu" Ulikuwa mtihani
mkubwa sana kwa Dr Yusha. Pamoja ya kuwa hospitali ya Kivinje hakikuwa kituo
chake cha kazi, lakini alijiona ana dhima ya kusaidia wagonjwa popote pale. Sasa
alikuwa anawaza, aendelee na sherehe ya ndoa yake au aende Kivinje kumsaidia
mgonjwa.
"Nakuja baada ya nusu saa" aliijibu ile
simu.
Mtihani mwengine ukafata, atatokaje katika ukumbi ule ilhali
yeye ndiye bwana harusi. Upande mwengine wa shilingi maadili ya kazi na kiapo
cha udaktari vilikuwa vinamsulubu kwa zamu.
Dr Yusha aliamua kwenda
kumsaidia mgonjwa kwa njia yoyote ile.
Aliangaza mle ukumbini,
alipigwa na butwaa, ukumbi mzima ulikuwa unamwangalia yeye. Ukumbi ukimshangaa.
Dr Yusha akatulia kwa sekunde kadhaa, ndipo aliposikia, kumbe mshereshaji wa
sherehe alikuwa amemwambia akakate keki iliyokuwa mbele ili akamlishe mkewe,
Nasra, wakati yeye alikuwa busy na simu.
"Ndugu
bwana harusi tunaomba uje ukate keki na kwenda kumlisha mkeo mpendwa "
Mshereshaji alikuwa anayarudia kwa mara ya tano maneno hayo. Wakati Dr Yusha
akiwa mbali kwa mawazo, ya kumfikiria mgonjwa. Dr Yusha alikuwa anawaza, akakate
keki ama aende Kivinje kumsaidia mgonjwa.
Alikuwa anafikiria kwa
kina, kumlisha mkewe mpendwa Nasra ile keki tamu aende kuokoa uhai wa
mgonjwa.
Nasra, mwanamke aliyekuwa anampenda kuliko kitu chochote
hapa duniani alikuwa analia. Hakuelewa kabisa mumewe kakumbwa na
nini.
Dr Yusha alinyanyua mguu wake wa kulia taratibu na kuelekea
kwenye meza iliyowekwa keki, ghafla simu yake iliita tena....BALAA.
Dr
Yusha alisita sasa, akakosa msimamo thabiti, akaanza kuitoa simu yake kwenye
koti....
Akaiangalia simu yake. Ilikuwa namba
ileile iliyompigia mwanzo, Dokta Yusha alijishauri kidogo, aipokee ama
asiipokee....simu iliita mpaka ikakata. Akaitia tena mfukoni. Ukumbi mzima
ulikuwa kimyaa, watu wote wakiwa hawaelewi kinatokea nini. Dr Yusha alipiga
hatua nyingine ya kivivu kwa mguu wa kushoto kuifuata meza ya keki. Hatua
ilivyotua chini, na simu iliita kotini.
Dr Yusha aliitoa kwa
haraka.
Akaipokea.
"Uhai wa Mtoto wetu unakutegemea wewe,
tunaomba uje kutusaidia baba" Ile sauti ya mwanzo sasa ilikuwa inalia. Sauti ile
iliyosikika katika hali ya huruma ilipenya hadi katika moyo wa Dokta Yusha.
Badala ya kuelekea kwenye keki, alielekea katika mlango wa ukumbi ule.
Aliitafuta gari yake harakaharaka, akakumbuka funguo hakuwa nayo yeye. Alitafuta
pikipiki ya kulipia (bodaboda).
"Kivinje faster" Alisema huku
akiipanda.
Mwenye ile pikipiki hakuwa na cha kuuliza, aling'oa ile
pikipiki kwa kasi, akaishika barabara inayoelekea Kilwa Kivinje. Jamaa alikuwa '
faster' kweli.
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Dokta Yusha aliacha
taharuki kubwa sana kule ukumbini. Watu wote walibaki midomo wazi, wengi
wakiamini Dokta Yusha amechanganyikiwa. Kwa bahati mbaya hakutokea mtu hata
mmoja aliyepata wazo la kumzuia Dokta Yusha. Ilikuwa ni kama ukumbi mzima
wamepigwa na ganzi.
Nasra, mke wake kipenzi Dokta
Yusha alikuwa hakamatiki, alikuwa hashikiki. Analia kwa sauti na kugaragara
chini. Ama hakika kilimuumiza sana kitendo kile. Aliona amepata aibu, aibu mbele
ya wazazi wake, aibu mbele ya rafiki zake, aibu aibu aibu. Kwa mara ya kwanza
alimchukia Dokta Yusha, kwa moyo wake wote alimchukia mwanaume yule wa maisha
yake.
Wazazi wa Dokta Yusha nao walikuwa katika hali ya huzuni na
masononeko makubwa. Hakika mtoto wao aliwaaibisha sana, tena katika sherehe ya
ndoa yake, mbele ya umati mkubwa. Sherehe ile ya ndoa, iliyotangazwa sana,
iliyogharimu pesa nyingi sana, ilikomea kati, kwa bwana harusi kutokomea na
pikipiki, kusikojulikana, balaa !
Dakika kumi
zilitosha pikipiki aliyopanda Dokta Yusha kufika hospitali, Kilwa Kivinje. Dokta
Yusha aliruka kabla ya ile pikipiki haijasimama na kukimbilia kuingia ndani ya
hospitali ile. Akiacha yule dereva wa pikipiki hajamlipa. Sasa ule mshangao wa
watu wa kule ukumbini, ulihamia kwa mwendesha pikipiki. Dokta Yusha alifika hadi
wodini, alikuta hali ya wodi shwari, hakuna mgonjwa yeyote aliyekuwa mahututi.
Alienda mapokezi, hakukuwa na mtu yeyote usiku ule, alijaribu kuipiga ile namba,
ilikuwa haipatikani, Balaa!
Sasa ule mshangao aliowaachia watu kule
ukumbini, mshangao alioondoka nao na kumletea mwendesha bodaboda, sasa ulimvaa
mwenyewe kwa kasi. Hakumwona kabisa mmiliki wa ile sauti iliyompigia simu, pale
hospitali.
TANO, ni miongoni mwa walinzi wa Don
Genge. Yeye ndio alipewa kazi ya kusafisha njia, ili mpango wao uendelee kama
ulivyopangwa. Kusafisha njia ilikuwa inamaanisha kung'oa magugu yote, ambayo
yangeweza kuwa kikwazo kwa mpango wao. Mmoja wa gugu ambalo walipanga kuling'oa
ni daktari huyu kijana.
Walipanga kumuuwa Dokta Yusha !
Ni
Tano ndiye aliyepiga simu ile, lengo ni kumleta Kivinje ili amuue. Bila kujua
Dokta Yusha aliingia katika mtego huo hatari. Tangu Dokta Yusha alivyowasiri kwa
pupa na pikipiki, mpaka sasa, Tano alikuwa makini nae kila anapokwenda. Lengo ni
kupata sehemu sahihi ya kuweza kumuuwa Dokta
Yusha.
Baada ya Dokta Yusha kutomuona mgonjwa
aliyeitiwa, na simu ya mtu aliyempigia kuzimwa. Alikaa chini na kutafakari
kilichotokea. Kila kitu kilijirudia katika kichwa chake kama filamu, sasa akaona
ukubwa wa kosa alilolifanya. La kukimbia katikati ya sherehe ya harusi yake.
Ukubwa wa kosa uliongezeka zaidi kwa kuwa hakukuwa na mgonjwa kweli pale
hospitali...
Dokta Yusha sasa alikumbuka hali
atakayokuwa nayo mke wake kipenzi Nasra kwa tukio lile baya alilolifanya.
Alikumbuka pia huzuni atakayokuwa kawaachia wazazi wake wapendwa kule ukumbini
baada ya kuondoka bila kuaga. Alijiona kafanya kosa kubwa
sana.
Ghafla, majimaji mepesi yalitiririka katika mashavu yake, Dokta
Yusha alikuwa analia. Kwa kosa kubwa alilolifanya usiku
ule.
Wakati Dokta Yusha akiwaza yale, na chozi la
uchungu kumdondoka pale hospitali. Muuaji namba tano alikuwa hatua chache sana
na pale alipokaa Dokta Yusha, akifikiria jinsi ya kumuua. Aliona kumuua kwa
risasi itazua tafrani kubwa pale hosptali, alipanga kumuuwa Dokta Yusha kwa
mikono yake ama kwa kisu. Alihisi njia hizo ni salama zaidi. Sasa alikuwa
anasubiri Dokta Yusha afanye kosa lolote
lile.
Kule Kilwa Masoko, hali ile ya taharuki na
huzuni iliendelea mle ukumbini.
Baada ya saa moja watu wote waliamua
kurudi majumbani kwao. Huku kila mmoja akiliongelea kwa aina yake tukio la
kukimbia kwa bwana harusi katikati ya sherehe. Wapo waliolifanya kama hadithi
nzuri ya kufurahisha, wapo waliolifanya kama hadithi mbaya ya kusikitisha na
kuhuzunisha.
Watu wa mwisho kurudi nyumbani katika usiku ule wa
sherehe ya harusi ni familia mbili zilizokumbwa na kisanga kile cha kuajabisha,
familia ya Dokta Yusha na familia ya Nasra. Waliweka kikao kidogo mlemle
ukumbini kulizungumzia tukio lile. Kikao kilichoisha bila maelewano yoyote.
Walijaribu kumpigia Dokta Yusha, simu iliita tu bila kupokelewa. Sasa familia
zile mbili wakiwa na Bi harusi walikuwa wanarudi nyumbani, katika gari mbili
tofauti, wakiwa na huzuni na simanzi tele. Huku wanawake wachache ndani ya
familia zile walikuwa wanalia, wakiongozwa vizuri na Bi harusi,
Nasra.
Katika gari aliyopanda Nasra, kulikuwa na
watu watano, Kulikuwemo na dereva, baba yake Nasra, mzee Mpaukha, mama yake
Nasra, mama Mpaukha, na mpambe wa Bi harusi, rafiki yake kipenzi Nasra, Hasina
Omary.
Dereva wa gari ile, alikuwa anaitwa Musa. Dereva wa siku
nyingi sana wa familia ya mzee Mpaukha.
Musa alikuwa amelewa sana
pombe, pombe ambayo aliinywa vilivyo na marafiki zake mle ukumbini. Pombe
ilimfanya apoteze umakini pale katika sukani na kuleta balaa kubwa
sana.
Walitoka vizuri pale ukumbini, lakini gari lilivyokamata lami
mwendo ulibadirika. Musa akawa anaendesha gari bila umakini wowote, siku zote
pombe haziongopi.
Hakukuwa na mtu aliyekuwa makini na mwendo ule,
wakati Musa alikuwa amelewa pombe, watu wengine wote waliobaki walikuwa wamelewa
na kitendo alichokifanya Dokta Yusha kule ukumbini. Gari zima walilewa kwa aina
mbili tofauti. Kila mmoja alikuwa amekaa mkao wa kuchoka katika siti
yake.
Gari wakati inakata kona ya kuelekea nyumbani kwa mzee Mpaukha,
dereva ilimshinda. Ilikuwa kona kali sana, iliyomshinda kabisa Musa, gari
liliacha njia na kujisweka kwenye kapori kadogo....ilikuwa balaa
!
Gari ilijipiga kwa nguvu sana katika mti mkubwa kule kwenye kapori.
Kishindo kikuu kilisikika.
TANO, baada ya
kushindwa mpango wake wa kumuua Dokta Yusha usiku ule. Alirudi mafichoni kwa
wenzake kujipanga upya. Usiku wa siku uliofuata kundi lile hatari la SIX KILLERS
walikuwa na kazi kuu mbili.
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kwanza Kuhakikisha
utoaji wa mioyo kwa maiti zilizokuwepo katika chumba cha kuhifadhia maiti
unafanyika bila wasiwasi wowote.
Pia kuhakisha
Dokta kijana anayejifanya ana morali ya kazi, Dokta Yusha
anauwawa.
Kwa kushirikiana na wale madokta wasiokuwa na maadili ya
kazi waliamini watafanikiwa katika malengo yao hayo
mawili.
Jioni ya siku ile familia ya Dokta Yusha,
ilikwenda hospitali kuwaangaalia wenzao. Yalikuwa majonzi makubwa sana baada ya
kusikia mama Mpaukha alikuwa amefariki. Na ndugu wengine wa Mzee Mpaukha nao
waliwasiri, na waliamua kuuchukua mwili wa mpendwa wao usiku wa siku ile ili
kwenda kufanya maandalizi ya mazishi.
Hadi muda
huo, madaktari wakuu katika hospitali hiyo walikuwa hawajulikani walipo. Nia yao
ilikuwa ni kukaa mafichoni muda mrefu ili idadi ya watu watakaofariki
waongezeke, ili mradi wao wa kupata mioyo kumi na tano kila siku ukamilike.
Walijua wasipokuwa kazini wao, wagonjwa wengi
watakufa.
Saa nne kamili usiku, mganga Mkuu wa
hospitali ya wilaya ya Kilwa, ndugu Zaidi Kilumba, Daktari Mkuu wa upasuaji
Dokta Sharifa Juma, Mkuu wa chumba cha upasuaji, Dokta Tamaa Karimu, wale manesi
watano, na kundi zima la SIX KILLER waliwasiri katika eneo la hospitali ile, kwa
magari aina mbili tofauti. Madokta na manesi walipanda gari yao na lile kundi
hatari walipanda gari yao. Walitofautiana kufika eneo la hospitali kwa dakika
kumi tu, wakitangulia wale madaktari. Walikuwa wamekuja kufanya kazi ya kutoa
mioyo ya maiti, wakifuatiwa na gari la kundi la hatari la Six Killers waliokuja
kulinda hali ya usalama pale hospitali, na kumuua daktari aliyeonekana kizuizi
kwa kazi yao, Dokta Yusha.
Wale madaktari
waliposhuka tu pale hospitali, walilakiwa kwa furaha na bashasha kubwa sana toka
kwa Dokta Yusha. Lakini wao hawakuonesha kabisa sura za furaha, haikuwa kama
ilivyo kawaida yao kila walipokuwa wanakutana hapo kabla. Madaktari wale
walionesha sura zilizoonesha dharau na kiburi.
Madaktari wote watatu
walikataa kushikana mkono na Dokta Yusha wakati wa kusalimiana ! Waliuacha mkono
wa Dokta Yusha ukielea hewani.
"Hivi wewe hiki ni
kituo chako cha kazi, au unataka kutuaminisha kwamba wanaopanga vituo hawana
akili?" Dokta Sharifa alimuuliza swali kwa dharau Dokta Yusha.
Dokta
Yusha hakujibu swali lile, alitumbua macho kuonesha mshangao wake. Aliwaangalia
kwa zamu madaktari wale. Wote walionesha kutojari kabisa mshangao
wake.
"Au unahamu.....?" Dokta Kilumba nae aliuliza swali lililoelea
hewani, bila kutanabaisha Dokta Yusha alikuwa na hamu ya nini.
"Mbona
siwaelewi ndugu zangu" Dokta Yusha aliongea kwa sauti ndogo iliyokuwa ikiashiria
kutoelewa kinachoendelea.
"Naitwa Tamaa Karimu, unaitwa Yusuph
Shaweji, sina undugu na wewe na wala sijawahi kuwa na undugu Na wewe, labda hawa
wenzangu ndio ndugu zako"
"Nani, mimi nitakuwa na ndugu kama huyo?"
Dokta Sharifa alirukia kwa mtindo wa swali.
"Lazima niwe makini, kuna
kitu kinaendelea" Dokta Yusha alijionya mwenyewe
kimoyomoyo.
Wakati wanaongea na Dokta Yusha, lile
kundi la wauaji walikuwa wamejipanga vizuri kule katika chumba cha kuhifadhia
maiti. Tayari kwa kulinda usalama ili wale madaktari waje kufanya mchezo wao
hatari. Mchezo wa kutoa mioyo ya maiti ! Pale walikuwa wanamchanganya tu Dokta
Yusha ili kupoteza umakini wake, na kuwapa nafasi kundi la Six killers wajipange
vizuri kule katika chumba cha kuhifadhia maiti.
Na walifanikiwa
!
Lile anguko la Mwanasheria lilimpeleka moja kwa
moja kule kwenye kibonde kidogo lilipoingia gari la Mzee Mpaukha, na kujikuta
ameulalia mwili wa mpambe wa Bi harusi,
Hasina
Omary.
"Mamaaaaaa"
Mwanasheria alipiga kelele kali sana.
Akiwa amemlalia Hasina, macho yake mbele yake alikutana na picha mbaya sana.
Picha ya kutisha.
"Ni nini hii, inamaana tumekufa
wote" Mwanasheria alijiuliza mwenyewe. Pombe haziongopi kabisa, Mwanasheria
alijiona kama na yeye alikuwemo katika ile gari iliyopata ajari, na sasa watu
wote wamekufa, akiwemo na yeye. Yalikuwa mambo ya ajabu
sana.
Alijiinua taratibu toka katika mwili uliojeruhiwa vibaya sana,
mwili wa Hasina, akasimama wima, huku akiwa anayumbayumba, Mwanasheria
aliangalia vizuri eneo lote lile la ajari. Japo kwa shida kutokana na giza na
kwa macho ya ulevi, lakini alitambua vizuri madhara makubwa yaliyotokea mahali
pale.
"Ni nini hii?" Alijiuliza mwenyewe
Mwanasheria. Mara akili zake za kilevi zilimtuma kufanya kitu. Alitoa simu yake
mkononi na kupiga simu, alipiga simu kwa Robert, alikuwa ni rafiki yake
kipenz.
"Hallo Robert" Aliongea kwa sauti ya
kilevi.
"Nambie Mwanasheria, mbona usiku sana" Robert aliongea kwa
sauti iliyoonesha alikuwa anatoka usingizini.
"Tumepata ajari rafiki
yangu"
"Ajari ?"
"Ndio wenzangu wote wamekufa nimebaki mimi
peke yangu"
"Ulikuwa na kina nani"
"Siwajui"
Pombe
zilimfanya Mwanasheria ajione kama naye alikuwemo katika ile
ajari.
"Sehemu gani imetokea hiyo
ajari?"
"Mtaroni"
"Come on Mwanasheria be
serious"
"Kweli my friend"
"Ulikuwa unatoka wapi
mwanasheria?"
"Kilabuni"
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Robert alitoa
msonyo mrefu na kukata simu. Akihisi Mwanasheria alikuwa katika maruweruwe yake
baada ya kunywa pombe za kutosha.
Upande wa
Mwanasheria, ulibaki na mshangao, kwanini rafiki yake kipenz Robert kamkatia
simu wakati yeye anamueleza jambo muhimu na zito sana.
Mwanasheria
alianza kupiga kelele, na maneno ajari na balaa yakisikika mara kwa mara katika
kelele zake.
Majirani na lile eneo walisikia walisikia vizuri sana
kilio kile cha Mwanasheria, lakini nani katika mji ule alikuwa hamjui
Mwanasheria, nani angekithamini kilio cha mlevi yule, kila mtu alipuuzia kilio
cha mlevi, Mwanasheria. Lakini Mwanasheria hakupuuza, alizidi kupiga
kelele...
Kule hospitali Kivinje hali ya mviziano
iliendelea. Baada ya Dokta Yusha kukaa pale kwa muda mrefu, bila simu yake
kupigwa, bila kumuona aliyempigia simu, aliamua kuondoka. Huku kichwani alikuwa
anawaza, atamwambia nini Nasra na kumuelewa, atawaambia nini wazazi wake.
Alitoka nje na kumkuta dereva wa ile pikipiki amesinzia, alimuasha na
kupanda.
Wakaondoka.
Wakati wanaondoka walipishana na gari
moja lililoingia kwa kasi sana mle hospitali, almanusra
liwagonge.
Walipofika Singino, simu ya Dokta Yusha iliita, kuangalia
namba ni ya ile sauti ya kizee iliyompigia
mwanzo...
Sasa, akawa anajishauri, apokee ama
asipokee ile simu.
"Hebu simamisha pikipiki kidogo" Dokta Yusha
alimwambia dereva wa pikipiki ile kwa sauti kubwa. Pikipiki
ikasimamishwa.
Dr Yusha aliipokea simu ile na kuisikia sauti ileile
ikimsisitiza aende Kivinje kumsaidia mgonjwa wake.
"Mbona nimetoka
hapo hospitali muda huu?" Dokta Yusha aliuliza kwa sauti yenye
kukereka.
"Tupo huku nyuma, karibu na jengo la kuhifadhia
maiti"
"Sasa mbona nilipofika niliipiga hii simu ilikuwa
haipatikani"
"Simu iliisha chaji, yaani hapa nimeilazimisha tu
kuiwash..."
Simu ikakatika.
Dokta Yusha aliamini kweli, simu
ya yule jamaa haikuwa na chaji, maana ndomana hata sasa ilizimika kutokana na
tatizo hilo.
"Turudi hospitali" Alimuamuru yule dereva pikipiki. Yule
kijana aligeuza pikipiki haraka, yeye alikuwa kazini, na aliamini ujira wake
unaongezeka kila inavyoongezeka safari.
Kule
Kivinje, Tano alikuwa hajafanikiwa Mpango wake, hadi Dokta Yusha anapanda
pikipiki na kuondoka, hakuiona nafasi sahihi ya kumuua daktari yule kijana.
Wakati Dokta Yusha anaondoka Tano alijishauri, amfate Dokta Yusha na kumuua
njiani ama afanyaje. Mwishowe aliamua kumrudisha tena Dokta Yusha kwa kutumia
ile simu. Na alifanikiwa, Dokta Yusha alikuwa njiani anarudi.
Tano
alijificha nyuma ya jengo la kuhifadhia maiti la Hospitali ile, na kisu chake
mkononi. Akisubiri kwa hamu ujio wa Dokta Yusha. Daktari wakiyeamini angekuwa
kikwazo katika Mpango wao walioupanga usiku wa siku
ile.
Muda mfupi baadae, Pikipiki aliyopanda Dokta
Yusha iliwasiri pale Hospitali. Dokta Yusha alishuka kwenye ile pikipiki. Siyo
kwa haraka sana kama mwanzo. Akawa anaelekea upande wa kushoto kilipo chumba cha
kuhifadhia maiti cha Hospitali ile.
Dokta Yusha
alikaribia kabisa kile chumba cha kuhifadhia maiti.
Ghafla, alisikia
kelele kali sana zikitoka kule mapokezi.
"Uwiiiiiiii, jamani
tusaidieni, tumeamua vibaya saaaaana, tusaidieni, madaktariiiiii,
tunakufaaaa...." Zilikuwa kelele kali sana. Kelele ambazo zilisababisha Dokta
Yusha abadiri uelekeo. Toka kwenye kifo kurudi katika uhai. Dokta Yusha alitimka
mbio kurudi kule mapokezi, alikosikia makelele ya mtu akiomba msaada. Alipofika
pale alimtambua vizuri sana mpiga kelele, alikuwa Mwanasheria, mlevi maarufu
sana Kilwa Masoko. Taratibu alianza kupunguza mwendo akijua Mwanasheria yupo
katika makelele yake ya kawaida ya pombe. Lakini kadri ya alivyokuwa anamsogelea
Mwanasheria, umakini wake uliongezeka.
Mwanasheria alitapakaa damu
mwili mzima, huku kundi dogo la watu likiwa limemzunguka. Dokta Yusha
alijitahidi kupenya kundi la watu wale na kumfikia mlevi
yule.
"Vipi Mwanasheria?" Baada ya kumkaribia
Dokta Yusha lilimtoka swali.
Mwanasheria alimwangalia Dokta Yusha na
kumtambua.
"Tumepata ajari Dokta, sote tumekufa" Mwanasheria alitoa
kauli iliyomchekesha kila mtu.
"Come down Mwanasheria, wewe
hujafa"
"Nimekufa Dokta, nimekufaaaaaa" Alisema kwa sauti kubwa
sana.
Dokta Yusha aliona pale hawawezi kuelewana.
"Hao
wenzako wako wapi?"
"Wapo humo Dokta" Mwanasheria alisema huku
akionesha kwa kidole chumba kulichokuwa karibu na pale walipokaa.
Kwa
mwendo wa taratibu Dokta Yusha alielekea kule chumbani. Alikutaba na
balaa.
Mwili wa kwanza kuuona ni wa rafiki yake kipenzi, mke wake
kipenzi, Nasra. Alienda mbele ya mwili ule uliolazwa vibaya sakafuni na
kuuinamia. Dokta Yusha aliona ufa mkubwa sana katika kichwa cha mpenzi wake ,
pale alipojigonga na jiwe baada ya ile ajari ya kizembe kutokea. Aligusa upande
wa kushoto wa kifua cha Nasra, mapigo ya moyo yalikuwa yanapiga kwa mbali sana.
Akajua kosa lolote litasababisha ampoteze mke wake.
Alinyanyuka
taratibu, huku chozi likimdondoka na kuufata mwili wa pili, alikuwa ni mkwewe,
mama Mpaukha. Hakuhitaji kumgusa sehemu yeyote kutambua kama mkwewe kipenz
alikuwa amefariki. Aliusogelea mwili wa tatu, mwili wa Alex. Dereva wa Mzee
Mpaukha. Alimuona na damu nyingi sana, huku mabaki ya vioo yakiwa yamebaki
katika mwili ule. Ilikuwa ni picha mbaya sana kuiangalia. Akausogelea mwili wa
nne, wa Hasina, mpambe wa bibi harusi. Aliona mbonyeo mkubwa katika upande wa
kulia wa kichwa kile. Pale alipojigonga na kioo Wakati Musa alipojaribu kukata
kona ile kali. Mwisho aliusogelea mwili wa Mzee Mpaukha, mwili ambao haukuwa na
tofauti sana na mwili wa dereva Musa. Nao mahali ya vioo yalikuwepo katika mwili
ule.
"Balaa" Dokta Yusha alijisemea
mwenyewe.
"Jamani tunakufaaa" sasa ndio alizisikia
kelele za Mwanasheria kule mapokezi.
Dokta Yusha alitoka nje
kumwangalia Mwanasheria alikuwa ameumia sehemu gani. Alimfikia Mwanasheria na
kumkagua mwili mzima. Mwanasheria hakuwa na jeraha lolote zaidi ya zile damu
zilizompakaa. Dokta Yusha akawaza labda Mwanasheria kaumia ndani kwa ndani.
Wakati akimwangalia Mwanasheria ndipo alipomuona Fred kwa mbali, rafiki yake wa
siku nyingi. Na ndiye alikuwa mpambe wake wa harusi siku
ile.
"Vipi Fred"
"Ebana wameumia vibaya
sana, afadhali nimekuona, nimewafata madaktari mpaka nyumbani kwao, hawapo,
sijui wameenda wapi?"
"Kwani kilitokea nini Fred?" Dokta Yusha
aliuliza kwa sauti yake yenye kwikwi.
"Mimi kanipigia simu huyo jamaa
anayelia, muda mfupi tu nilipofika nyumbani kutoka kwenye sherehe, sijui hata
namba yangu aliitoa wapi, yeye alikuwa analia tu, huku akisema wote wamekufa.
Alinielekeza mahali ilipotokea ajari. Nilienda haraka kwa gari, na kukuta
familia ya Nasra wamepata ajari mbaya sana ya gari aisee, majeruhi wako ndani
huko" Fred alisema bila kujua kama Dokta Yusha kashaingia mle ndani na kujionea
mwenyewe athari za ajari ile.
Kule nyuma ya chumba
cha kuhifadhia maiti, Tano alikuwa anasubiri ujio wa Dokta Yusha. Alikuwa
amejiandaa vema kumuua Dokta Yusha pindi atakapotokea tu. Alijibanza konani na
kisu chake mkononi. Hakujua kabisa kuwa kwa wakati ule Dokta Yusha alikuwa
amesahau kabisa habari ya simu ya mtu yule.
Tano alisubiri na
kusubiri.
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alfajiri, mji wa
Kilwa Masoko, waliamka na habari kuu mbili.
Habari ya kwanza ilikuwa
ni kutokea kwa ajari katika kona inayoelekea mtaa wa Lumumba. Vijiwe vyote
vinavyojadiri habari ngumu waliijadiri sana habari hiyo. Habari iliyohusisha
ajari mbaya waliyoipata familia ya Mzee
Mpaukha.
Habari ya pili ni kukimbia kwa bwana
harusi katikati ya sherehe. Habari iliyopambwa na kusimuliwa vizuri sana na
mafundi wa kusimulia. Tena wengine hawakuwepo hata katika ile sherehe yenyewe
lakini ndio walikuwa wasimuliaji wakubwa. Vijiwe vyote vya waambea waliipa sana
'airtime ' habari hii ya bwana harusi kukimbia katikati ya sherehe kuliko habari
ile ya ajari.
Kule Kilwa Kivinje majeruhi wote
sasa walikuwa wodini. Dokta Yusha alifanya kazi kubwa sana usiku ule. Yeye
mwenyewe alifanya kila kitu kuhakikisha majeruhi wote wanapata huduma. Na ile
maiti ya mama Nasra ilipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti na kusubiri
taratibu zingine za mazishi ziendelee.
Hadi
Asubuhi, Dokta Mkuu wa hospitali ya Kinyonga, Zaidi Kilumba, Dokta Mkuu wa
upasuaji Sharifa Juma, na Dokta anayesimamia chumba cha kuhifadhia maiti, Dokta
tamaa Karimu walikuwa hawajawasiri kazini, na wala simu zao zilikuwa
hazipatikani.
Hospitalini walikuwa wanafanya kazi manesi,
wakishirikiana kwa ukaribu mkubwa na Dokta
Yusha.
Hadi saa sita mchana, majeruhi wale wanne
walikuwa hawajapata fahamu. Hali ilikuwa tete. Dokta Yusha alifanya kazi kama
punda, huku akimshukuru Mungu kwa kuwa alikuwa na likizo kwa ajili ya mapumziko
ya ndoa yake.
Madaktari wengine katika hospitali ile, hawakuwa na ari
kabisa ya kufanya kazi.
Saa kumi na mbili jioni,
kazi ya Dokta Yusha ilianza kuleta mafanikio. Mzee Mpaukha alirudiwa na fahamu.
Alifumbua macho taratibu akiwa mbele ya nesi aliyekuwa karibu na kitanda
chake.
"Niko wapi hapa?"
"Tulia baba,
uko sehemu salama"
Nesi alimjibu huku akiweka
vizuri dripu ya maji ilikuwa inaingia mwilini kwa Mzee Mpaukha.
Mzee
Mpaukha, alifumba macho na kutafakari. Matukio yote yaliyotokea usiku uliopita
yalijirudia mithili ya sinema. Tangu wakiwa ukumbini hadi gari lao lilivyoacha
njia.
"Tunakufaaaaaaa!"
Mzee
Mpaukha alitoa ukelele mkubwa akiwa pale kitandani. Ukelele huo uliokuwa na
faida ndani yake. Ukelele ule alifika moja kwa moja katika masikio ya Musa, na
kumuamsha Musa, dereva wake, toka katika usingizi mzito aliolala kuja duniani.
Musa naye aliunga kumsaidia Mzee
Mpaukha
".....kufaaaaaaa"
Nesi sasa
akakimbia kwa kasi kwenda katika kitanda cha Musa. Huku akimshukuru Mungu kwa
kuweza kuwaamsha wagonjwa wawili kwa mpigo, tena katika njia ya
ajabu.
Nusu saa baadae, Dokta Yusha aliwasiri,
alipatwa na furaha isiyo na kifani kukuta wagonjwa wake wawili wamerejewa na
fahamu. Ilikuwa faraja kubwa sana kwake. Asilimia hamsini ya kazi alikuwa
amefanikiwa. Walipoteza fahamu wagonjwa wanne, wawili walikuwa wamerejewa na
fahamu zao na kubaki wawili...
TANO, baada ya
kushindwa mpango wake wa kumuua Dokta Yusha usiku ule. Alirudi mafichoni kwa
wenzake kujipanga upya. Usiku wa siku uliofuata kundi lile hatari la SIX KILLERS
walikuwa na kazi kuu mbili.
Kwanza Kuhakikisha
utoaji wa mioyo kwa maiti zilizokuwepo katika chumba cha kuhifadhia maiti
unafanyika bila wasiwasi wowote.
Pia kuhakisha
Dokta kijana anayejifanya ana morali ya kazi, Dokta Yusha
anauwawa.
Kwa kushirikiana na wale madokta wasiokuwa na maadili ya
kazi waliamini watafanikiwa katika malengo yao hayo
mawili.
Jioni ya siku ile familia ya Dokta Yusha,
ilikwenda hospitali kuwaangaalia wenzao. Yalikuwa majonzi makubwa sana baada ya
kusikia mama Mpaukha alikuwa amefariki. Na ndugu wengine wa Mzee Mpaukha nao
waliwasiri, na waliamua kuuchukua mwili wa mpendwa wao usiku wa siku ile ili
kwenda kufanya maandalizi ya mazishi.
Hadi muda
huo, madaktari wakuu katika hospitali hiyo walikuwa hawajulikani walipo. Nia yao
ilikuwa ni kukaa mafichoni muda mrefu ili idadi ya watu watakaofariki
waongezeke, ili mradi wao wa kupata mioyo kumi na tano kila siku ukamilike.
Walijua wasipokuwa kazini wao, wagonjwa wengi
watakufa.
Saa nne kamili usiku, mganga Mkuu wa
hospitali ya wilaya ya Kilwa, ndugu Zaidi Kilumba, Daktari Mkuu wa upasuaji
Dokta Sharifa Juma, Mkuu wa chumba cha upasuaji, Dokta Tamaa Karimu, wale manesi
watano, na kundi zima la SIX KILLER waliwasiri katika eneo la hospitali ile, kwa
magari aina mbili tofauti. Madokta na manesi walipanda gari yao na lile kundi
hatari walipanda gari yao. Walitofautiana kufika eneo la hospitali kwa dakika
kumi tu, wakitangulia wale madaktari. Walikuwa wamekuja kufanya kazi ya kutoa
mioyo ya maiti, wakifuatiwa na gari la kundi la hatari la Six Killers waliokuja
kulinda hali ya usalama pale hospitali, na kumuua daktari aliyeonekana kizuizi
kwa kazi yao, Dokta Yusha.
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wale madaktari
waliposhuka tu pale hospitali, walilakiwa kwa furaha na bashasha kubwa sana toka
kwa Dokta Yusha. Lakini wao hawakuonesha kabisa sura za furaha, haikuwa kama
ilivyo kawaida yao kila walipokuwa wanakutana hapo kabla. Madaktari wale
walionesha sura zilizoonesha dharau na kiburi.
Madaktari wote watatu
walikataa kushikana mkono na Dokta Yusha wakati wa kusalimiana ! Waliuacha mkono
wa Dokta Yusha ukielea hewani.
"Hivi wewe hiki ni
kituo chako cha kazi, au unataka kutuaminisha kwamba wanaopanga vituo hawana
akili?" Dokta Sharifa alimuuliza swali kwa dharau Dokta Yusha.
Dokta
Yusha hakujibu swali lile, alitumbua macho kuonesha mshangao wake. Aliwaangalia
kwa zamu madaktari wale. Wote walionesha kutojari kabisa mshangao
wake.
"Au unahamu.....?" Dokta Kilumba nae aliuliza swali lililoelea
hewani, bila kutanabaisha Dokta Yusha alikuwa na hamu ya nini.
"Mbona
siwaelewi ndugu zangu" Dokta Yusha aliongea kwa sauti ndogo iliyokuwa ikiashiria
kutoelewa kinachoendelea.
"Naitwa Tamaa Karimu, unaitwa Yusuph
Shaweji, sina undugu na wewe na wala sijawahi kuwa na undugu Na wewe, labda hawa
wenzangu ndio ndugu zako"
"Nani, mimi nitakuwa na ndugu kama huyo?"
Dokta Sharifa alirukia kwa mtindo wa swali.
"Lazima niwe makini, kuna
kitu kinaendelea" Dokta Yusha alijionya mwenyewe
kimoyomoyo.
Wakati wanaongea na Dokta Yusha, lile
kundi la wauaji walikuwa wamejipanga vizuri kule katika chumba cha kuhifadhia
maiti. Tayari kwa kulinda usalama ili wale madaktari waje kufanya mchezo wao
hatari. Mchezo wa kutoa mioyo ya maiti ! Pale walikuwa wanamchanganya tu Dokta
Yusha ili kupoteza umakini wake, na kuwapa nafasi kundi la Six killers wajipange
vizuri kule katika chumba cha kuhifadhia maiti.
Na walifanikiwa
!
Usiku uleule wa saa nne, familia ya Mzee Mpaukha
walijipanga kwenda kuchukua mwili wa mpendwa wao kule chumba cha kuhifadhia
maiti. Walikuwa wanamsubiri Dokta Yusha tu ili waende kuchukua mwili wa
marehemu. Walikuwa wameshaongea na Mkuu msaidizi wa mhifadhi wa chumba cha
maiti. Bila kujua Mpango hasi uliokuwemo katika chumba kile.....Balaa
!
Alivyotoka kuongea na madaktari wale
waliombadirikia, Dokta Yusha moja kwa moja alienda wodini. Hali aliyoiacha
wodini ndiyo aliyoikuta. Hadi muda ule. Ni Mussa na Mzee Mpaukha tu ndio
waliorejewa na fahamu. Dokta Yusha alisogea hadi kitanda alicholazwa mke wake
kipenz, Nasra, alikaa pembeni ya kitanda kile. Huku akimwangalia mkewe aliyekuwa
amefumba macho. Akiwa amehama kabisa katika Dunia hii. Mwanamke aliyekuwa nusu
mfu kwa sasa. Aliangalia jinsi dripu ikivyotiririka taratibu katika mishipa
laini ya Nasra.
Wakati Dokta Yusha akiwa pale na
mkewe, Dokta Kilumba aliingia mle wodini. Alisogea taratibu hadi pale kitandani
alipokuwa amekaa Dokta Yusha. Taratibu Dokta Yusha aliacha kuiangalia ile dripu
na kumwangalia Dokta Kilumba. Dokta waliyetoka kugombana naye punde tu kule
nje.
Dokta Kilumba alipofika pale naye hakuongea. Alikaa pale
kitandani, karibu kabisa na Dokta Yusha, kiasi kwamba magoti yao yaligusana.
Hali ya ukimya iliendelea kama dakika tatu, ndipo Dokta Yusha alikiharibu kimya
hiko.
"Vipi Dokta, mbona umekuja kimya kimya
halafu hauongei ?"
"Tusamehe Dokta, haikuwa dhamira yetu hali ile
itokee"
"Msijari mambo ya kawaida tu kupishana
kauli"
Baadae walielewana. Na kuanza kuongea mambo
mbalimbali.
Dokta Kilumba alikuja kuongea na Dokta Yusha kwa dhamira
maalum. Dhamira mbaya kabisa. Ni kuchelewasha muda kwa Dokta Yusha kwenda kule
chumba cha kuhifadhia maiti kuchukua maiti ya mama Mpaukha. Kwa kuwa na maiti ya
mama Mpaukha ilikuwa katika orodha ya maiti zilozotakiwa kutolewa moyo siku ile
!
Kule nje familia ya Mzee Mpaukha walikuwa
wanamsubiri Dr Yusha atoke wodini kuangalia hali za wagonjwa, ili waende naye
kwenda kuchukua maiti yao kule katika chumba cha kuhifadhia
maiti.
Bila kujua lengo la Dokta Kilumba, Dokta
Yusha aliendelea kuongea nae. Alifurahi sana kuelewana na daktari yule Mkuu,
alijua itakuwa rahisi sana kuwasimamia wagonjwa wake kwa kuelewana na Dokta
yule.
Kule katika chumba cha maiti hali ilikuwa ya
kutisha. Ilihitaji mtu jasiri kuangalia kilichokuwa kinaendelea. Mioyo kumi na
nne toka katika maiti kumi na nne ilikuwa imeshapatikana tayari, na kuhifadhiwa
katika deli moja kubwa jekundu!
Sasa ilikuwa zamu ya kutolewa moyo wa
kumi na tano, ili kukamilisha idadi yao ya siku ile. Kisha baada ya hapo
wakachungulie katika akaunti zao kitaongezeka nini. Waliikumbuka sana ahadi ya
Don Genge.
Hali ndani ya chumba cha kuhifadhia
maiti ilikuwa ya utulivu sana. Kila mtu akifanya kazi yake kwa umakini mkubwa.
Utafikiri walikuwa katika operesheni moja muhimu sana ya kuokoa maisha ya mtu.
Kumbe walikuwa wanafanya vitendo vya kinyama
sana!
Dokta Sharifa alikuwa ameshika kisu maalum
kwa ajili ya upasuaji, mbele yake kulikuwa na kitanda kidogo kikichotumika
kulaza zile maiti wakizozitoa mioyo!
Dokta
Sharifa alikuwa anapasua maiti na kutoa moyo kisha kuishona tena miili ya
marehemu. Wale manesi walikuwa wanafanya kazi ya kubeba maiti na kuzileta pale
kitandani, kisha kuzirejesha katika sehemu zao baada ya kufanyiwa upasuaji na
kushonwa na Dokta Sharifa. Dokta wa kike katili !
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Dokta Tamaa yeye
alikuwa anasimamia kazi kama inaenda vizuri, ndiye alikuwa Mkuu kwa muda ule,
wakati Dokta Kilumba hakuwepo.
Nje kulikuwa na
ulinzi imara. Walinzi wote sita wakiwa na bunduki, walikuwa wamekizunguka chumba
cha kuhifadhia maiti , tayari kwa kupiga mtu au kitu chochote kitakachosogelea
chumba kile. Walikuwa makini, Kuhakikisha hawafanyi kosa lolote la
kiufundi.
Manesi wawili walienda kufungua kabati
moja la kuhifadhia maiti. Walivuta droo taratibu. Sura ya maiti yule ilikuwa
inaonekana vizuri. Sura tulivu kabisa, sura ya kipole, sura isiyokuwa na hatia
yoyote, sura ya mama Mpaukha. Wale manesi wawili waliitoa maiti ile na kuilaza
vizuri kwenye machela. Waliisukuma machela ile kuelekea pale alipokuwa Dokta
Sharifa, ili Dokta afanye kazi ile ya kikatili !
Kazi ya kuutoa moyo
mwili ule, mwili wa mkwe wa Dokta Yusha.
Mwili wa
mama Mpaukha ukawekwa katika kile kitanda maalum kwa kazi hii ya
kikatili!
Dokta Sharifa alinyanyua mkono wake wa kulia ulioshika kisu
juu, akakielekeza kile kisu katika upande wa kushoto katika kifua laini cha
marehemu mama Mpaukha, akichana
taratibu.
Kilikuwa ni kitendo cha kikatili sana,
lakini daktari yule wa kike alikuwa anakifanya bila wasiwasi wowote.
Alikizungusha kile kile kisu kwa mtindo wa duara, kisu maalum kilichokuwa
kimezama vizuri katika nyama za kifua cha mama yule. Alipoona imetosha aliingiza
mkono wake wa kulia, aliokuwa amevaa gloves, alichezesha mkono wake kama dakika
moja katika shimo baya alilolijenga pale kifuani, na kutoka na moyo uliozungukwa
na damu!
Aliuweka pembeni kwenye sahani ya chuma moyo ule, na kuanza
kuushona mwili ule, mwili usiokuwa na moyo kwa
sasa.
Kule wodini 'story' zilinoga kati ya Dokta
Yusha na Dokta Kilumba. Walikuwa wanasimuliana mambo mbalimbali kuhusu fani yao
ya utabibu. Bila kujua mambo ya siri yaliyokuwa wanaendelea katika chumba cha
kuhifadhia maiti.
Mara, mjomba wake Nasra aliingia
wodini.
"Samahani Dokta, inabidi tukautoe mwili wa marehemu ili
tukaufanyie maandalizi"
"Sawa, ngoja tumpigie mtu wa chumba cha
kuhifadhia maiti" Dokta Kilumba alidakia ilihal hakuambiwa
yeye.
Alimpigia Dokta Tamaa, na Dokta Tamaa alimjibu kwamba mambo yako
vizuri wakauchukue tu mwili mpendwa wao.
Dokta
Yusha akiongozana na ndugu mwengine walienda kuuchukua mwili ule usiokuwa na
moyo kwa sasa na kwenda nao Kilwa Masoko kwa ajili ya maandilizi ili
wauzike.
Siku ile ya kwanza kundi la Don Genge kwa
kishirikiana na madaktari wale wenye roho mbaya kabisa walifanikisha Mpango wao
ule wa kinyama!
Siku ya pili Asubuhi, ndio ilikuwa
siku ya kuuosha mwili ule tayari kwa kwenda kuuzika. Mshono waliukuta katika
kifua cha mama Mpaukha ulimshangaza kila mtu aliyekuwa mle chumbani wakati
wanauosha mwili ule...
Wakati mwili unaoshwa,
kizaaza kikaibuka!
Mwili wa mama Mpaukha ulikuwa na mshono mkubwa sana
ambao ulikuwa haujapona bado.
Mshono uliowaacha midomo wazi waoshaji.
Pamoja na mshangao wao lakini waoshaji wale walihisi labda jeraha lile ni
mojawapo ya madhara aliyoyapata mama yule katika ajari ile
mbaya!
Wakina mama wale Waliamua kukaa kimya na kuendelea na kazi yao
ya uoshaji kama kawaida.
Mwili wa mama Mpaukha ulioshwa na kwenda
kuzikwa katika makaburi ya Sanga bila uwepo wa mwanae mpendwa, Nasra, bila uwepo
wa mumewe kipenzi, Mzee Mpaukha .
Mama Kindumba,
alikuwa mlevi maarufu wa kike katika mji wa Kilwa Masoko. Kutokana na kupenda
sana kunywa pombe za kienyeji alikuwa na marafiki wengi sana walevi, miongoni
mwa marafiki ni Mwanasheria.
Mama kindumba
alikuwa anakaa jirani sana na familia ya Mzee Mpaukha. Ujirani huo ndio
uliosababisha na yeye apate fursa ya kwenda kuuosha mwili wa mama Mpaukha. Na
Mama kindumba ni miongoni mwa watu waliostushwa sana na ule mshono wa mama
Mpaukha ulikuwepo pale kifuani.
Baada ya kumzika
mama Mpaukha, jioni ya siku ile mama kindumba ilimkuta kilabuni akipata pombe za
kienyeji kama kawaida yake. Kikao kilikuwa kimependeza ingawa mwenyekiti wa
kikao hiko alikuwa hajawasiri bado.
Baada ya muda mfupi Mwenyekiti
aliwasiri huku akiimba wimbo wa bendi ya msondo ngoma. Alikuwa
Mwanasheria.
"Eeeeeeh nilikuwa nakusubiri kwa hamu
Mwana" mama kindumba aliongea kwa nguvu baada ya kumuona
Mwanasheria.
"Kuna nini tena mama kindumba maana nawe huishiwi
michapo"
"Ni kuhusu ile ajari yenu" mama kindumba alisema huku
anacheka.
"Umeanza kuharibu sasa" sauti ya Mwanasheria ilipoa
kidogo.
"Kumbe yule maza alipata bonge la jeraha kifuani. Alichomwa na
chuma nini pale"
"Mama gani tena?" Mwanasheria alihoji.
"Si
jirani yangu tuliomzika leo kule Sanga"
"Acha zako mama, ushalewa
nini, yule mama hakuumia sehemu yoyote. Alikufa bila jeraha"
"We si
ulilewa Mwanasheria utakuwa na kumbukumbu kweli, maza alikuwa na jeraha kubwa
sana kifuani"
"Hamna kitu kama hicho mama"
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ulizuka mbishano
mkubwa sana kati ya mama Kindumba na Mwanasheria. Walevi wengine walibaki kuwa
wasikilizaji tu.
"Tusiandikie mate, ngoja nimpigie
Dokta Yusha tumuulize, halafu naweka sauti ya nje kabisa" Baada ya mzozo mkubwa
Mwanasheria alishauri.
"Simu itakayozua kizaazaa
kipya" tusubiri hiyo kesho tuone!"
Mwanasheria
akatoa simu yake. Akabofyabofya muda mfupi kuitafuta namba ya Dokta Yusha,
aliiona na kuipiga.
Wakati simu ile inapigwa,
Dokta Yusha alikuwa wodini. Akiwahudumia wagonjwa mbalimbali, wakiwemo mkewe
Nasra na na rafiki wa Nasra, Hasina. Mzee Mpaukha na Musa hali zao sasa zilikuwa
vizuri sana.
Akiwa amekaa pembeni ya kitanda cha
mkewe simu yake iliita. Kuangalia kioo cha simu yake kilisomeka Mwanasheria,
alitabasamu. Alitoka nje na tabasamu lake, alikumbuka vizuri sana vituko vya
Mwanasheria. Alitoka nje ya geti ili akaongee na
Mwanasheria.
"Hallo"
"Dokta tuna ubishi
hapa" Mwanasheria alianza kuongea bila hata salamu.
"Ubishi gani
tena?"
"Eti katika ile ajari marehemu alikuwa na jeraha
lolote?"
"Hapana, alifariki kwa mstuko tu"
"Aliumia kifuani
doktaaaa" sauti ya mama kindumba ilisikika katika ile simu kwa sauti
kubwa.
"Hapana, hakuumia!"
"Tafuta mtu yeyote aliyekuwepo
wakati wa kuosha maiti atakwambia" Mama kindumba alisema.
Na simu ili
katika. Bila shaka kwa kuisha salio ama chaji.
Dokta Yusha
alichanganyikiwa sana.
Ingawa taarifa ile ilitoka
kwa walevi lakini Dokta Yusha aliipa uzito unaostahili. Alipanga kuufatilia
ukweli wa taarifa ile na kuujua ukweli wa taarifa hiyo ya
kushangaza.
Tano wa kundi la Six killers bado
alikuwa anafatilia nyendo za Dokta Yusha. Na nia yao ya kutaka kumuuwa Dokta
Yusha bado ilikuwa palepale. Tano alikuwa anapata ugumu sana kwa kuwa Dokta
Yusha alikuwa anakaa wodini muda wote. Wodi yenye wagonjwa muda wote, na kufanya
kazi ya kumuua iwe ngumu sana.
Wakati Dokta Yusha
akiongea na simu ile, Tano alikuwa hatua chache nyuma yake. Alisikia kila kitu
alichoongea Dokta Yusha na Mwanasheria....alilishika kichwani jina la
Mwanasheria.
"Mwanasheria anahitaji kuuwawa!"
Alilipitisha katika kichwa chake.
Kule kilabuni
ubishi bado uliendelea. Huku Mwanasheria akiwa amepata nguvu na kuelekea
kushinda. Ubishi sasa ulipata washiriki zaidi, walevi walianza kuchangia mada,
huku walevi wengi wakimuunga mkono
Mwanasheria.
Tano aliona mambo yao sasa yameanza
kuingiwa na vijidudu vibaya. Na jukumu lake lilikuwa ni kuviondosha vijidudu
vyote. Sasa naye Mwanasheria akaingia katika orodha ya
kifo!
Baada ya kuongea na simu ile toka kwa
Mwanasheria, Dokta Yusha alikuwa na mawazo mengi sana. Kwa uyakinifu mkubwa
aliipima ile taarifa ya Mwanasheria. Akajua kuna kitu. Alikaa pale kitandani
huku akiingalia bandeji kubwa aliyefungwa mkewe kichwani. Kichwa cha Nasra
kiliathirika sana. Huku kukiwa na wasiwasi kama Nasra akiamka atarejewa na
kumbukumbu zake.
Dokta Yusha alichukua simu yake
na kuitafuta namba ya Shangazi yake Nasra. Alijua kwa vyovyote lazima alikuwepo
wakati maiti ya mama Mpaukha inaoshwa. Aliiona namba na kuipiga huku akiwa
anatoka nje ya wodi.
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Hallo
Shangazi"
"Habari Dokta?"
"Safi kwema
Shangazi"
"Tupo tu hivyohivyo"
"Kuna kitu nataka nikuulize
Dokta"
"Kitu gani hiko Dokta"
"Ulikuwepo kati ya watu
waliomuosha marehemu leo?"
"Ndio nilikuwepo"
"Eti marehemu
alikuwa na jeraha lolote?"
"Tena kubwa sana kifuani, aisee bila shaka
ndio litakuwa limesababisha kifo chake lile"
"Sehemu gani
lilikuwepo"
"Juu ya kifua, sehemu unapokaa
moyo!"
Mwili wa Dokta Yusha ulipigwa ganzi. Ni
yeye ndiye aliyepima mapigo ya moyo ya mama Mpaukha, mara tu walipoingia katika
chumba cha matibabu kabla ya mwili ule kupelekwa katika chumba cha kuhifadhia
maiti.
Alikumbuka aliweka kifaa cha kupima mapigo ya moyo sehemu
ileile unapokaa moyo. Hapakuwa hata na mchubuko. Iweje leo aambiwe kuna jeraha
kubwa sana?
"Halo
Dokta....Halloo...unanisikia?"
Shangazi wa Nasra alikuwa anaongea peke
yake simuni. Ingawa Dokta Yusha aliweka simu sikioni lakini alikuwa mbali sana
kimawazo, alikuwa hasikii chochote.
Usiku uleule
Tano alienda Kilwa Masoko. Kummaliza Mwanasheria. Alijua kumuacha hai
Mwanasheria basi habari juu ya kidonda kilichoibuka ghafla katika kifua cha mama
Mpaukha itaendelea kusambaa. Ilikuwa ni lazima kumuuwa Mwanasheria ili kumziba
mdomo milele !
Usiku wa saa nne usiku ulimkuta
Mwanasheria akinywa bia katika baa ya Tiga Tisa. Alikunywa bia nyingi sana.
Tangu saa kumi na mbili jioni alikuwa hapo akipata
ulabu.
Meza ya tatu toka pale alipokaa Mwanasheria
kulikuwa na mgeni. Mgeni aliyewasiri pale majira ya saa tatu usiku. Mgeni huyo
alikuwa makini kwa kila alichokuwa anakifanya Mwanasheria. Mgeni huyo hakuwa
mwengine ila ni Tano wa Six Killers. Alikuwa anamsubiri mwanasheria anyanyuke
ili akamfanye alichotaka kwenda kumfanya.
Saa tano
usiku Mwanasheria alinyanyuka pale kwenye kiti. Tayari kuelekea nyumbani kwake.
Alisogea taratibu kwenye gari yake, alipanda na kuliwasha. Safari kwenda
nyumbani kwake ilianza. Tano naye alitoka pale Tiga Tisa. Alichukua pikipiki
yake na kulifuata gari la Mwanasheria kwa nyuma.
Mwanasheria alikuwa
amelewa hasa. Alipoteza kabisa umakini na hakutambua kabisa kama alikuwa
anafuatwa. Alifika nyumbani kwake na kuingia ndani. Kutokana na ulevi
Mwanasheria alijikuta amelala katika sofa pale
sebuleni.
Tano alipaki pikipiki yake kwa nje.
Alifika hadi mlangoni katika nyumba ile ya Mwanasheria. Kwa bahati mbaya nyumba
ile haikuwa na fensi.
Kwa kutumia funguo malaya alifungua mlango wa
sebule wa Mwanasheria. Ilikuwa ni kazi ndogo sana, kazi iliyodumu kwa dakika
tatu. Alifungua mlango na kumkuta Mwanasheria amelala pale sebuleni kama mzoga.
Alichomoa kisu chake mkononi. Kwa mwendo wa kunyata akawa anamsogelea pale
sofani.
Akamtikisa kidogo, Mwanasheria hakuamka, alikuwa amelewa sana
pombe. Alimtikisa tena. Nia ya Tano ni kumuamsha Mwanasheria ili kumjua mtu wa
pili aliyedakia ile simu wakati yeye anaongea na Dokta Yusha. Lakini Mwanasheria
hakuamka.
Tano aliamua kuua tu, akijipa moyo atamjua tu huyo mtu.
Alirudisha nyuma ule mkono uliishika kisu, kwa nguvu aliungiza katika tumbo la
Mwanasheria, akatoa akaingiza tena. Alirudia mara nne.Mwanasheria akakata roho
akiwa amelewa.
Tano alitoka nje huku akiwa na
furaha tele. Bila kujua kama alimuua mtu asiye sahihi. Yeye alimuua Mwanasheria
wa Halmashauri ya wilaya ya Kilwa, Ndugu Juma Ngozi. Wakati Mwanasheria
aliyeongea na Dokta Yusha, Mwanasheria mlevi alikuwa kilabuni wakati ule,
akinywa pombe na kupigizana kelele na kina mama Kindumba...
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment