Search This Blog

Sunday, 22 May 2022

TAHARUKI - 1

 





    IMEANDIKWA NA : PATRICK J. MASSAWE



    *********************************************************************************



    Simulizi : Taharuki

    Sehemu Ya Kwanza (1)



    TARATIBU habari hizo zilianza kama mzaha. Zikaendelea kuvuma kidogokidogo, na mwishowe zikaanikwa hadharani. Ama hakika, zilikuwa ni habari za kushtukiza na kushangaza sana, zilizowaacha watu vinywa wazi, na kujiona kama walikuwa wakiota ndoto za mchana kweupe! Ni habari ambazo zilikuwa zimeenea na kutangazwa katika vyombo vingi vya habari duniani kote, hususan magazeti na televisheni. Hasa karibu magazeti yote ya nchini Uingereza, kulikotokea tukio hilo la aina yake, yalitangaza habari hizo, na kuzipa uzito wa hali ya juu.



    Ni kwamba mkufu wenye thamani kubwa, uliotengenezwa kwa madini ya almasi, ambao uliokuwa umehifadhiwa ndani ya Kasri la Malkia wa Uingereza, ulikuwa umeibwa na watu wasiofahamika. Hata hivyo, habari hizo hazikuwaingia akilini watu wenye akili timamu, ambao waliona kama ulikuwa ni mchezo wa kuingiza uliobuniwa ili kuwafurahisha watu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Iweje wale watu waliohusika na wizi huo, waweze kuingia ndani

    ya jumba lile la kifalme, ambalo lililokuwa na ulinzi mkali kwa muda wote wa saa ishirini na nne? Pia, lilikuwa limezungukwa na uzio madhubuti, ambao siyo rahisi kwa mtu yeyote kuweza kuruka, na kila pembe zilikuwa zimetegeshwa kamera za usalama zikiwa zinaimarisha ulinzi!



    Kila mtu alizungumza lake. Wengine walisema kuwa ile ilikuwa ni njama iliyokuwa imepangwa na walinzi wenyewe katika kuuiba. Wengine wakadai kuwa mkufu ule ulitenegenezwa kwa madini ya almasi tupu, ulikuwa umechukuliwa na mizimu kwa njia ya ajabu, kwa vile nao ulikuwa umeporwa na wazungu kutoka katika ardhi ya waafrika miaka mingi iliyopita. Hivyo basi, mizimu ilikuwa imeurudisha ulipotoka. Alimradi kila mmoja alisema yake. Lakini hakuna aliyekuwa na uhakika na anachokisema!



    Serikali ya Uingereza haikukaa kimya, ikatangaza tenda kubwa kwa vikundi vyote vya upelelezi, wakiwemo wale wa Scotland Yard, na hata wa kujitegemea, ili wafanye upelelezi wao wa kina, na kuhakikisha mkufu ule unapatikana haraka iwezekanavyo, na ikiwezekana wahusika wapatikane. Dau nono likatangazwa na Serikali ya Uingereza, kwa atakayefanikiwa kuurejesha mkufu huo katika hali yake ileile!



    Majasusi mahiri, na wapelelezi wa kujitegemea kutoka katika nchi mbalimbali duniani, hasa mashirika, kama (FBI) wa Marekani, (KGB) wa Urusi, (BBI) Shirika la Binafsi la Upelelezi, na wengineo walijitokeza kwa wingi na kichangamkia tenda ile. Wakaingia mitaani na kuanza msako wa nguvu kuwapata wahusika wale ambao bado walikuwa hawajafahamika walipokimbilia!



    Nchini Tanzania , habari zile nazo zilipokelewa kwa hisia tofauti. Watu walikuwa wakikaa katika makundi, hususana kwenye vijiwe vya kahawa vilivyosheheni mitaani na hasa katikati ya jiji la Dar es Salaam, wakiijadili taarifa ile. Watu hawakubanduka katika runinga au redio zao, kusikiliza taarifa ya habari kutoka katika Shirika la Habari la Uingereza, lililokuwa likiielezea taarifa ile kwa kina.



    Ukweli ni kwamba walikuwa wamechanganyikiwa!

    Kama ujuavyo tena, kila mmoja alizungumza lake aliloona linafaa, hata kama lilikuwa ni la uongo. Na hata habari za mpira za timu kubwa za hapa nchini, au nchi za nje, hazikushabikiwa sana baada ya habari zile kutapakaa. Kila mmoja alitaka alizungumzie na kuonekena kama analijua tukio zima lilivyotokea!

    Hakuna aliyejua chochote, ni siri kubwa!



    ********



    Kama kawaida, ndani ya jiji la Dar es Salaam, asubuhi hiyo palipambazuka vizuri. Mabasi ya daladala yalikuwa yakiingia kwa wingi katikati ya jiji, na baadhi ya abiria walioshuka, walikuwa wakikimbilia katika meza za wauza magazeti ya siku ile, ambayo mengi yalikuwa na vichwa vya habari vinavyohusiana na tukio lile la wizi wa mkufu ule wathamani. Wengine walikuwa wakinunua na wengine wakisoma vichwa vya habari na kuwakinga waliotaka kununua!



    Basi, asubuhi hiyo, kwenye kijiwe maarufu cha kahawa, kilichoko eneo la Posta Mpya, katika kona ya makutano ya Barabara ya Azikiwe na Garden, mkabala na Hoteli ya Embassy, wateja walikuwa wamejaa wakinywa kahawa kwa kijana mmoja muuza kahawa maarufu, aliyekuwa anauza kahawa katika eneo hilo wanapokuta watu wa kila aina. Huo ulikuwa ni utaratibu wao wa kila siku kukutana pale kabla ya kuelekea katika shughuli zao za kikazi na mihangaiko mingine.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wateja walikuwa wamekaa kwenye mabenchi ya mbao, na vikombe vyao vya kahawa mikononi wakinywa taratibu huku wakiendelea na mazungumzo yao , ambayo kila wanapokutana asubuhi, huwa wanazungumza. Mjadala ulikuwa mkali sana , watu wakibishana juu ya kuhusu kuibwa kwa mkufu ule wenye thamani kubwa ndani ya Kasri la Malkia!



    “Jamani ee, mmezisikia habari za kuibwa kwa mkufu wa thamani ndani ya jumba la Malkia kule Uingereza?” Mteja mmoja alisema kwa sauti kubwa huku akijisogeza vizuri pale kwenye benchi.

    “Ndiyo, tumezisikia, inashangaza sana …” akaongeza mwingine huku akiiangalia kahawa ya moto iliyojaa kwenye kikombe chake.

    “Hivi jamani, hebu tujiulize, inawezekana mtu akaingia ndani ya jumba hilo na kuiba?” Muuza kahawa akauliza na kuongeza. “Au walinzi walikuwa wamelala usingizi wa pono?”



    “Ni vigumu sana ,” mteja mwingine akasema kwa kujiamini na kuendelea. “Lakini nasikia eti waliohusika na wizi huo, ni watu wachawi mahiri, na waliokubuhu, ambao walijigeuza Panya, halafu wakaingia mle ndani bila kushtukiwa na walinzi. Na baada ya kuingia, wakatoka na mkufu huo! Sasa walikoelekea hapajulikani, biashara mbele kwa mbele!”



    “Ahahaaa!....Ahahaaa! Wateja wakaangua kicheko cha nguvu baada ya mada ile kutolewa!



    “Unasema walijigeuza Panya?” Akauliza mteja mwingine huku akiangua kicheko cha nguvu kiasi cha kufanya kikombe cha kahawa kimtoke mkononi!



    “Ndiyo manaake, sasa unafikiri waliingiaje? Watu wajanja sana , hii ni sayansi ya aina yake! Sayansi ya giza !” Aliyetoa mada ile akaendelea kusema kwa msisitizo kana kwamba zilikuwa habari za kweli!



    “Inawezekana ikawa kweli…basi tuendelee na kahawa yetu, ya Malkia wa Uingereza tuachane nayo. Tunaweza tukakamatwa na kuisaidia polisi sasa hivi! Mashushushu wametapakaa kila kona!” Mteja mwingine akasema.



    “ Hilo neno…maana imekuja mambo ya Panya tena. Una uhakika?” Akasema mtu mmoja wa makamo mwenye upara.



    “Nina uhakika! Kwani nyie amsikilizi vyombo vya habari?” mtu yule akazema kwa msisitizo!



    “Haya, kama ni kweli basi, tuendelee na mada nyingine...” mteja mwingine akawaambia.



    “Poa, tuendelee na mambo ya mpira sasa, kuhusu dirisha dogo la usajili...” mtu mwingine mnazi wa timu moja pinzani akasema!

    Wateja wote wakamsikiliza na kuuendesha mjadala kichinichini bila ya kupaaza sauti zao kama ilivyokuwa mwanzo, kwani kila mmoja alitaka aseme ili aonekane ndiye anayejua zaidi kwa kile kilichotokea!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ni hadi wateja wale walipotosheka, na kila mmoja akaondoka na kuendelea na shughuli nyingine. Muuza kahawa akamaliza biashara yake na kuondoka na birika lake la kahawa, na kijiwe kikabaki cheupe. Lakini ukweli ukabaki kuwa mkufu ule wa thamani ulikuwa umeibwa na unatafutwa kwa udi na uvumba!



    Habari ndiyo hiyo!



    ******



    Ufukwe wa Coco ni moja ya fukwe nzuri zenye mandhari ya kuvutia, zilizosheheni miti ya minazi iliyokuwa na kivuli, pamoja na mchanga mweupe, kando ya Bahari ya Hindi, eneo la Oysterbay, jijini Dar es Salaam . Ufukwe ule huvutia watu wengi, wakiwa katika rika mbalimbali, kwenda kujiburudisha kwa kula, kunywa, na kuogelea baharini, hasa siku za mwisho wa wiki. Ukweli ni kwamba palifaa sana kwa kuondoa uchovu baada ya kazi za wiki nzima.



    Basi, siku hiyo ya Jumamosi tulivu, ikiwa hali ya hewa ni nzuri na mawimbi ya bahari yakivuma na kugonga katika miamba iliyoenea eneo lote la ufukwe, alionekana kijana mmoja mtanashati, akishuka kutoka ndani ya gari dogo, jipya, aina ya Nissan March. Gari lile lenye rangi ya bluu iliyokolea, lilikuwa limepaki katika maegesho ya magari muda siyo mrefu, likitokea katikati ya jiji.Baada ya kushuka, kijana yule alifunga mlango wa gari na kuondoka kwa mwendo wa taratibu kuelekea ufukweni.



    Katika mkono wake wa kushoto, kijana yule alikuwa amebeba mfuko mdogo tu, ambao ndani yake kulikuwa na kitabu kikibwa cha hadithi, pamoja na kamera ndogo ya kisasa. Akafika katika mti mmoja wa mnazI uliokuwa na kivuli kizuri, kisha akakaana chini katika mchanga ule laini. Hata hivyo, kabla hajaamua la kufanya, kijana yule alivuta pumzi ndefu na kuzishusha. Halafu akayatupa macho yake kuelekea baharini, ambapo watu walipokuwa wanaogelea.



    Lakini baadaye akatoa kile kitabu cha hadithi na kufungua kurasa kadhaa, tayari kwa kuanza kusoma, kwa kuanzia sehemu ile aliyokuwa amekomea punde tu alipokuwa ameacha kusoma tangu alipoanza kukisoma kitabu kile chenye riwaya ya kusisimua, inayohusiana na mambo ya upelelezi. Na kila aanzapo kusoma, kamwe hapendi kabisa mtu yeyote amsumbue na kumkatisha, ndiyo maana anapendeleea kwenda sehemu za ufukweni.



    Alikuwa ni kijana, Frank Mumba, ambaye alikuwa na mazoea ya kufika pale mara kwa mara, ukiwa ndiyo utaratibu wake aliojipangia kila anapopata nafasi. Ilikuwa ni starehe yake aliyokuwa ameiweka hasa ukizingatia alikuwa ni mtu wa kusafiri sana , kiasi cha kukosa muda. Ndiyo tuseme kuwa kazi ilikuwa inachukuwa muda mwingi kuliko mapumziko, kitu ambacho alikuwa ameshakizoea.Vilevile alikuwa bado hajaoa, na kuwa na mke wa kumuondolea upweke.



    Ni mara nyingi Frank Mumba alishinwa kuelewa mara moja kitu kilichokuwa kinamshawishi awe anapendelea kufika katika ufukwe wa Coco. Lakini ni kwamba moyo wake ndiyo uliomshawishi awe anakwenda kujipumzisha, akijipatia kinywaji, na hata kujisomea kitabu cha riwaya. Kimakazi, Frank Mumba alikuwa anaishi eneo la Survey, Chuo Kikuu, katika nyumba yake, iliyoko kando tu ya Barabara ya Sam Nujoma.



    Ni nyumba ndogo ya kifamilia, iliyojengwa mjengo wa kisasa, iliyozungukwa na ukuta madhubuti na geti kubwa upande wa mbele. Pia, kwa upande wa ndani palikuwa na nafasi ya kutosha hata kupaki magari matatu. Alikuwa anaishi na mdogo wake tu, ingawa umri wake wa miaka 36 ulikuwa unamsuta. Lakini sababu za kufanya achelewe sana kuoa, kwa vile alikuwa ni mtu wa kusafiri sana, katika nchi mbalimbali na kukosa hata muda wa kupumzika!



    Yeye akuwa ni mtu wa kazi tu!



    Kitaaluma, kijana, Frank Mumba alikuwa ni Mpelelezi wa Kujitegemea wa Kimataifa, taaluma aliyoisomea baada ya kupitia katika vyombo ya usalama, likiwemo Jeshi la Polisi nchini. Alikuwa amepitia mafunzo mbalimbali ndani na nje ya nchi, hasa nchini Uingereza, katika Chuo cha Scotland Yard, alikofuzu taaluma yake ya upelelezi. Pia, alihudhuria kozi kadhaa, nchini Marekani, chini ya Shirika la Upelelezi la Marekani.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya kufanya kazi katika Jeshi la Polisi nchini kwa muda wa miaka kadhaa, aliamuanakuacha kazi kwa hiari yake mwenyewe, na kujiajiri, kutokana na ushawishi wa rafiki yake, kijana Brown Lambert, mpelelezi mashuhuri wa kimataifa, mwenye asili ya Afrika, aliyekuwa na makazi yake jijini London. Kwa msaada wa rafiki yake huyo, ndipo Frank Mumba alipojiongezea ujuzi; hasa katika sanaa ya mapigano na kutumia silaha za aina mbalimbali, pamoja na mafunzo magumu ya kijeshi aliyoendelea kuyapata nchini Uingereza, na kwingineko. Mafunzo yake yaliufanya mwili wa Frank Mumba ujengeke kimazoezi, kiasi cha kuogopwa na mhalifu yeyote aliyemsogelea karibu.



    Basi, huyo ndiye Frank Mumba aliyekuwa amefika katika ufukwe wa Coco siku ile ya Jumamosi, katika kuiburudisha akili yake. Hivyo, akaendelea kujisomea kitabu chake, huku upepo mwanana uliombatana na harufu ya bahari, ukivuma kutoka baharini ukimpuliza na kumpa burudani ya pekee. Na hicho ndicho kilichomfanya awe anapenda kufika pale.



    Wakati Frank anaendelea kusoma kitabu kile, simu yake ya mkononi iliyokuwa mfukoni mwake iliita. Akaitoa na kuangalia namba za mpigaji. Akaachia tabasamu jepesi baada ya kuzisoma namba zile na jina la mpigaji. Alikuwa ni rafiki yake mkubwa, Brown Lambert, ambaye walikuwa hawajaonana kwa kipindi cha mwezi mmoja hivi, katika pilikapilika zao za kikazi, kwani naye alikuwa amechukuwa likizo fupi ili kupumzika na familia yake, ambayo nayo ilikuwa haionani naye mara kwa mara. Kisha Frank akabonyeza batani na kumsilikiza:



    “Haloo, Bw. Brown…” Frank alimwambia.



    “Haloo Frank…”upande wa pili ukasema na kuendelea. “Habari za hapo Tanzania…”



    “Habari ni nzuri, sijui huko Uingereza…”



    “Huku ni nzuri…” Bw. Brown akasema na kuongeza. “Je, una habari mwenzangu?”



    “Habari gani?” Frank akamuuliza.



    “Ina maana hufuatilii habari za ulimwengu ukiwa kama mpelelezi?” Bw. Browan akamuuliza.



    “Ninazifuatilia sana…lakini habari ni nyingi. Sasa sijui ni habari ipi unayoisema, ambayo inahitajika kufanyiwa upelelezi”



    “Ok, ngoja nikupashe…” Brown akamwambia kwa nia ya kumwelezea vizuri juu ya habari hiyo.



    “Nipashe ndugu yangu.”



    “Kuna tenda ya nguvu imetolewa hapa nchini Uingereza. Ni kwamba, watu wasiojulikana wameingia katika Kasri ya Malkia (Buckingham Palace), jijini, London na kuiba mkufu wa thamani kubwa uliokuwa umehifadhiwa humo. Ni mkufu wa almasi, uliokuwa umehifadhiwa kwa muda mrefu sana, katika sehemu nyeti kama kumbukumbu, lakini watu wajanja wakauchukuwa kwa nia mbaya. Hivyo, Malkia ametangaza zawadi nono kwa atakayefanikiwa kuurejesha, upo?”



    “Ndiyo, nakupata,” Frank akasema na kuendelea. “Na kama habari ndiyo hizo, nimezisikia katika vyombo mbalimbali vya habari, vya ndani na nje, lakini sikutilia maanani, ukizingatia hawakutaja kama kuna zawadi yoyote itakayotolewa…”



    “Basi, ndiyo hivyo. Nataka kama kawaida yetu, wewe ukiwa mtu wangu wa karibu, ambaye tumefanya kazi nyingi, tushirikiane katia sakata hili. Sasa natumaini umenielewa ninachoongea.”



    “Ndiyo, nimekuelewa sana…”



    “Kama umenielewa, fanya haraka, jiandae kwa safari na uje hapa London, na kama kawaida yetu na tuianze kazi mara moja” CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hakuna tatizo, nitajiandaa kuanzia muda huu. Nitegemee hapo London muda wowote mambo yatakapotengamaa…”



    “Ok, tutaongea mengi baada ya kufika.”



    “Hakuna shaka, bai…”



    Baada ya kumaliza mazungumzo yao, mapigo ya moyo wa Frank Mumba yaliendelea kupiga kwa kasi na kubaki amekikamata kile kitabu alichokuwa anasoma. Hakuwa na hamu ya kuendelea kusoma tena mara baada ya kuzipata habari zile za kusisimua. Ni habari ambazo humfanya ajione kama mtu aliyekuwa katika ulimwengu mwingine! Mwili wake ulikuwa umeshazoea kuwa na pilikapilika nyingi sana, hiyo anapokuwa ameutuliza, anajiona kama kuna kitu lkilichokuwa kimepungua.



    Ni kuuchangamsha kwa kazi!



    Frank Mumba hakuendelea kukaa tena pale ufukweni, akayazungusha macho yake pande zote za ufukweni na kuangalia jinsi watu

    walivyokuwa wanaifurahia wikiendi. Hata hivyo, alinyanyuka na kuchukua ule mkoba wake mdogo, na kukiingiza kile kitabu chake, halafu akaelekea lilipo gari lake kwa mwendo wa taratibu. Na alipolifikia gari lake, akapanda na kuondoka kwa safari ya kurudi nyumbani kwake, Survey, kwa mwendo wa taratibu akiiwazia ile kazi ya kukata na shoka.



    Muda huo ilikuwa imetimu saa kumi na mbili na robo za jioni.



    ********



    Ulikuwa ni wizi wa aina yake, wa mkufu wenye thamanui kubwa kutoka ndani ya kasri la Malkia, jijini London , nchini Uingereza. Ni mkufu ambao wote ulitengenezwa kwa madini ya almasi ya thamani kubwa, na ulikuwa ni mkufu wenye historia kongwe na pia thamani kubwa kuliko mikufu yote ya kihistoria iliyohifadhiwa kwenye chumba cha kumbukumbu ya utawala wa kifalme wa Uingereza ndani ya kasri hiyo ya kifalme.



    Mkufu huo haukuwa mali ya nchi ya Uingereza, bali ulikuwa umeibwa na wafanyabiashara mashuhuri wa Kireno, enzi zile kule Angola , katika karne ya 17. Halafu baada ya kuuiba, wao wakaenda kuuza kwa wafanyabiashara wa Uingereza, waliokuwa wakisafirisha watumwa kutoka Afrika Magharibi. Hivyo, ndivyo mkufu huo ulivyoingia katika kasri ya kifalme huko London . Hakika ulikuwa ni kumbukumbu tosha ya karne!



    Hata hivyo, mmiliki halali wa mkufu huo, alikuwa ni mwanamama, Malkia, Nziga Mbadi, aliyeishi katika eneo lililojulikana kwa jina la Bike, katika nchi ya Angola, zama zile za kale. Wafanyabiashara wale wa Kireno, walikula njama na mganga mmoja wa kienyeji, ambaye aliemfuata Malkia Nziga Mbadi, na kumlaghai kwamba mizimu ya mababu ilimtuma apewe mkufu ule wa thamani kubwa ili apate kuupeleka kwao. Malkia yule aliyeamini mambo ya mizimu ya mababu, hakubisha baada ya kuambiwa vile, aliuvua ule mkufu ule mkufu na kumkabidhi mganga yule wa kienyeji, ambaye hatimaye alikwenda kuuza kwa wafanyabiashara wa Kireno, kwa kupewa bunduki moja aina ya ‘Gobore’. Hatimaye Wareno wale baada ya kuupata, waliuuza ule kwa wafanyabiashara maarufu wa Uingereza, wakiongozwa na mmoja wao, kinara, Bw. Peterson Bell.



    Hata hivyo, baada ya kusafiri na kufika na mkufu ule, katika Bandari ya Dover , nchini Uingereza, ili apate sifa, Bw. Peterson Bell, aliuzawadia ukoo wa kifalme wa Uingereza mkufu ule alioutapeli kwa Malkia wa Kiafrika. Lakini sasa mkufu ule wa thamani kubwa na tena wa kihistoria, baada ya kudumu na kuhifadhiwa kwenye kasri ya Malkia kwa mamia ya miaka, hatimaye ulikuwa umetoweka katika mazingira ya kutatanisha; kwa kuibwa na maharamia wa kimataifa, tena wazoefu!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ndipo utawala wa Uingereza ulipotangaza zawadi nono kwa atakayefanikiwa kuurejesha mkufu ule kutoka kwa watu wale walioupora. Na wataalamu wa minada ya kuuza vitu vya kale na vya kihistoria, walikaa na kutathmini gharama za mkufu ule, ambapo baada ya kupitia, walitoa taarifa kwamba ulikuwa na thamani ya Paundi za Uingereza, Milioni 675. Na mtu angefanikiwa kuurejesha, angepewa kitita cha Paundi milioni 450!



    Tayari wapelelezi mbalimbali wa kujitegemea na mashirika yao , walikuwa wakimezea mate kitita hicho, ambao wengi wao kisiri, walikuwa wameshajitosa kwenye kinyang’anyiro cha kuusaka mkufu huo kwa udi na uvumba, tokea tangazo hilo lilipotolewa hadharani.



    Mbali ya mashirika ya upelelezi kujitokeza, pia, kulikuwa na wakora wengine waliojipenyeza ili kuusaka mkufu huo, ili wafaidike na hilo donge nono. Alimradi kila mmoja aliahangaika kivyake!



    Hapo ndipo mpelelezi mashuhuri wa kujitegemea, Bw. Brown Lambert, mwenye asili ya Afrika, anayewahi kufanyia kazi kwenye Kikosi cha Scotland Yard, alipoamua kujitosa katika hekaheka za kuusaka mkufu huo wa thamani, kwa kupitia shirika lake binafsi la upelelezi, lilojulikana kama, Brown Bureau of Investigation (BBI) Shirika lile halikuwa na uhusiano wowote na lile la Marekani, la Federal Bureau of Investigation (FBI) Isipokuwa herufi za majina yao ndizo pekee yake zilizotokea kulandana, ingawa yote yalikuwa ni mashirika ya upelelezi.



    Ni mara nyingi, shughuli zote za upelelezi, za Brown Lambert zilifanikishwa na Mpelelezi wa Kimataifa kutoka nchini Tanzania , kijana, Frank Mumba, akiwa ni mpelelezi anayejiamini na asiyekuwa na uoga dhidi ya wale aliokuwa anafuatilia nyendo zao. Ndiyo maana akiwa jijini Dar es Salaam , Brown alimpigia simu na kumwita aende jijini London haraka ili wakaifanye kazi ile iliyokuwa na malipo ya donge nono!





    ********

    Frank Mumba na Brown Lambert walikutana kwa mara ya kwanza nchini Nigeria , ndani ya jiji la Lagos , katika mtaa wa maarufu wa Victoria, ikiwa wote wawili wakiwa kazini. Walikuwa wamepewa kazi ya kuchunguza kadhia ya kutoweka kwa mabilioni ya fedha kutoka kwenye benki moja ya kigeni, iliyokuwa na tawi lake jijini Lagos . Waliifanya kazi ile kwa ufa nisi mkubwa na kufanikiwa kuwapata wahusika wa wizi ule, na sheria ikachukuwa mkondo wake.



    Tokea pale, Frank na Brown wakawa na urafiki mkubwa, na ukawa mwanzo wa kushirikiana katika biashara za kuchunguza uhalifu, kila wanapopata miadi ya kulipwa donge nono. Hakika ni kazi ambayo ilihitaji kuwa na ujasiri wa hali ya juu, uk izingatia wakati mwingine ilihitaji kupambana na wahalifu wakubwa wa kimataifa, waliokuwa na mtandao mkubwa wa kihalifu, hasa ule wa ‘Mafia!’



    Mara nyingi, Frank Mumba hakuzifungia macho tenda hizo kwa sababu pamoja na kwamba ni kazi za hatari, zilimlipa vizuri. Alikuwa tayari ametajirika akiwa katika umri mdogo, kwa kuwa na vitega uchumi vingi ndani ya jiji la Dar es Salaam, na kwingineko.



    Pia, alikuwa amefungua ofisi yake ya kushughulikia mambo ya upelelezi, ambapo alikuwa amewaajiri vijana wengine kadhaa wa kumsaidia na mara nyingi aliwapatia mafunzo ya uhakika, ili kutimiza lengo lake la kuwapata vijana mahiri katika taaluma ile ya upelelezi.



    Ofisi yake ilikuwa inafanya kazi ya upelelezi makini sana , ambao kwa namna moja ama nyingine kwa upande wa Jeshi la Polisi, hususan Idara ya Upelelezi, walikuwa wakiuendesha taratibu bila msingi wowote.



    Ni kitendo kilichokuwa kinalalamikiwa kutokana na watuhumiwa wengi kushinda kesi mahakamani, wakati ni kweli walikuwa wametenda kosa, na ushahidi ulikuwepo! Huo ulikuwa ni udhaifu mkubwa katika upelelezi!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kitendo kile kiliwafanya wafanyabiashara wakubwa wa kimataifa waliopenda kufanyiwa upelelezi katika nchi za nje, wamtumie, ambapo kwa Jeshi la Polisi kungekuwa na urasimu mkubwa kumpata mpelelezi wa kushughulikia matatizo hayo. Basi urasimu huo, uliwafanya watu wengi kumtumia mpelelezi, Frank Mumba,

    na mara nyingi alifanikiwa kwa kiwango cha hali ya juu kiasi cha kujiongezea sifa. Ni sifa zilizozagaa hapa nchini Tanzania , na nchi za nje, kwa kushirikiana na Brown Lambert, mpelelezi aliyebobea!





    ********

    Anga lote lilikuwa shwari siku hiyo. Mnara mrefu na mashuhuri wa Eiffel, uliojengwa kwa vipande vya vyuma, ambao ni fahari kubwa ya alama ya jiji la Paris , nchini Ufaransa, na dola ya Wafaransa, uliweza kuonekena wazi wakati ndege kubwa aina ya Boeing 747 ya Shirika la Ndege la Ufaransa, iliyotokea Hearthrow, jijini London , ilipotua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Charles De Gaulle, jijini Paris .



    Ndani ya ndege ile, abiria, vijana wawili, wote wakiwa wanaume watanashati, walionekana wakiyatupia macho yao pande zote na kuonekane wazi nyuso zao zikionyesha furaha kwa kufanikiwa kwao kusafiri kutoka jijini London, na kufika, Paris , nchini Ufaransa salama. Watu hao, walikuwa ni Edmond Balle, raia wa Nigeria , na Hamisi Kengwa, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Hamisi na Balle, waliwasili Paris wakiwa na ‘mzigo maalum,’ ambao uliwafanya wawe wageni maalum, kwa Bw. Mokili wa Ngenge, raia wa Kongo, ambaye naye alikuwa amefika pale uwanjani kuwapokea.



    Hakika safari ya kuwafikisha nchini Ufaransa, kutokea Uingereza, ilikuwa ya mashaka kidogo ukizingatia jinsi kulivyokuwa na ulinzi mkali baada ya mkufu ule kuibwa.



    Na mpaka wanapopanda ndege, na hatimaye inaruka angani, walishukuru sana, kwani palikuwa panafanyika upekuzi wa hali ya juu kwa kila mtu aliyetiliwa mashaka, hususan watu wenye asili ya Afrika. Hivyo iliwabdi Hamisi na Kengwa, wawe watu wa kujificha sana , tangia walipoupora mkufu ule yapata wiki moja iliyopita.



    Tuseme walikuwa wakihama mtaa huu, mara mtaa ule, na pia wakijipaka madawa maalum yaliyowasaidia wasiweze kuonekana na binadamu wa kawaida, na hata kamera na mitambo ya usalama iliyotapakaa katika maeneo mengi.



    Ndege ile ilituia salama uwanjani, na abiria wakaanza kushuka, wakiwemo Hamisi Kengwa na Edmond Balle. Baada ya kushuka, wakaelekea sehemu maalum ya kukutana na Mokili wa Ngenge, aliyekuwa anawasubiri. Mokili alikuwa ameshahonga fedha,

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Faranga milioni nne za Ufaransa kwa wafanyakazi wote waliokuwa zamu ya siku ile pale uwanjani, kiasi kwamba ingawa walijua mzigo uliokuwa umebebwa na watu wale wawili, Hamisi na Balle, lakini hawakuweza kuwakamata kwa sababu walishapokea kitita cha fedha. Waliwaachia hadi walipotoka nje ya ya jengo la uwanja na kwenda kukutana na Mokili Ngenge, sehemu ya Mapokezi, wanapofikia wageni mashuhuri (VIP). Hakika Mokili wa Ngenge alikuwa amejiandaa ipasavyo.



    Gari likaingizwa ndani hadi sehemu ya maegesho katika uwanja mkubwa, mbali kidogo na ilipokuwa nyumba. Sehemu ile, palikuwa na magari mengine sita, ya kifahari yaliyokuwa yamepaki na kuuonyesha utajiri wake. Mokili, Hamisi na Balle wakashuka wakiwa na mzigo wao, halafu wakaelekea ndani ya jumba lile la kifahari, ambalo halikutofautiana na Ikulu ya Rais wa nchi. Jumba lote lilikuwa kimya kabisa, hasa ukizingatia famili yake ilikuwa imesafiri kwenda nchini, Jamhuri ya Kidemkrasi ya Kongo.



    Hamis na Edmond walifika eneo lile na kumkuta Mokili akiwa amejaa tele ndani ya chumba cha mapokezi ya wageni mashuhuri. Alipowaona, akasimama kutoka kwenye sofa lile alilokuwa amekalia.



    “Karibuni sana …” Mokili aliwaambia huku akiwapa mkono kila mmoja.



    “Ahsante sana bosi..” Hamisi akasema huku akiunda tabasamu pana.



    “Ahsante bosi…” Balle naye akasema huku akiwa na furaha. Kwa ujumla wote wawili walikuwa na furaha, na kila mmoja akiwa amebeba Briefcase, lakini ile iliyokuwa na’mkufu’ wa thamani, ilibebwa na Balle.



    “Naona mambo mazuri,” Mokili akawaambia.



    “Mambo mazuri...” wakasema wote.



    “Ok, twendeni kwenye gari,” Mokili akawaambia.

    “Sawa,” wakaitikia.



    Wote wawili wakamfuata Mokili nyuma, hadi walipofika katika eneo la maegesho ya magari, alikopaki gari lake la kifahari, aina ya Mercedes Benz, la rangi nyeusi, lenye milango sita. Ndani yake alikuwepo dereva akiwasubiri Baada ya kulifikia, wakapanda na kuondoka eneo lile la uwanja wa ndege, kuelekea katika makazi ya Mokili wa Ngenge. Kwa ujumla wote walikuwa wamenyamaza kimya, kila mmoja akitafakari lake, hadi walipofika katika himaya ya Mokili, mtaa wa Mtakatifu Dennis, jijini Paris .

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Gari likaingizwa ndani hadi sehemu ya maegesho katika uwanja mkubwa, mbali kidogo na ilipokuwa nyumba. Sehemu ile, palikuwa na magari mengine sita, ya kifahari yaliyokuwa yamepaki na kuuonyesha utajiri wake. Mokili, Hamisi na Balle wakashuka wakiwa na mzigo wao, halafu wakaelekea ndani ya jumba lile la kifahari, ambalo halikutofautiana na Ikulu ya Rais wa nchi. Jumba lote lilikuwa kimya kabisa, hasa ukizingatia famili yake ilikuwa imesafiri kwenda nchini, Jamhuri ya Kidemkrasi ya Kongo.



    Baada ya kuingia, wakaelekea ndani ya chumba maalum cha kupumzika wageni, ukizingatia walikuwa wametoka safari ndefu iliwabidi kupumzika kwanza. Wakahudumiwa vinywaji wanavyopendelea pamoja na chakula, huku muda wote ule mkoba uliokuwa na ule mkufu ukiwa jirani yao , kamwe hawakupenda kumkabidhi kwanza kabla ya maongezi maalum, ikiwa ni pamoja na kukabidhiana kitita cha fedha za kuikamilisha kazi ile ya hatari!



    Na baada ya kupumzika zaidi ya saa nzima hivi, ndipo Mokili wa Ngenge alipowakaribisha ndani ya chumba kingine, ambacho kilikuwa kama chumba cha mikutano. Palikuwa na meza kubwa na ndefu, ambayo pande zote kulikuwa na viti vipatavyo kumi. Wote wakakaa tayari kwa maongezi mengineyo. Ule mkoba uliokuwa na mzigo wakauweka juu ya meza, wakawa wanaukodolea macho.



    “Mmefanya kazi kubwa sana !” Mokili Ngenge akawaambia huku akiwaangalia kwa zamu.



    “Ni kweli bosi, lakini ilikuwa ni kazi ngumu na ya hatari sana . Mtu kuingia katika kasri ya Malkia na kuupora mkufu, si jambo dogo hasa ukizingatia kuna mitambo ya ulinzi na kamera zimewekwa kila pembe!” Balle akasema.



    “Si mchezo, kama siyo ile dawa tuliyojipaka na dawa na kuzuia tusiweze kuonekana, basi saa hizi tungeongea mengine!” Hamisi naye akasema.



    “Yote nafahamu, kazi mliyofanya ni kubwa, ndiyo maana nawapongeza sana …” Mokili akawaambia.



    “Na sisi tunashukuru bosi, hebu chukua mzigo wenyewe uuangalie, na utuakatie chetu tuondoke...” Balle akamwambia Mokili.



    Mokili akauchukuwa ule mkoba na kuukagua kabla hajaufungua. Baada ya kuridhika ndipo alipoufungua kwa kutumia namba maalum, ukafunguka. Mokili akauona ule mkufu wenye thamani kubwa, ambao aliutoa na kuuangalia kwa takriban dakika kumi!

    Akaridhika huku akikenua meno yake!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mambo safi sana !” Mokili wa Ngenge akaema huku akiurudisha tena mkufu ule ndani ya mkoba kama ulivyokuwa mwanzo.



    Mokili wa Ngenge akaumiliki yeye ule mkufu, akipanga kuuhifadhi na kumsubiri mteja wake, tajiri, bilionea wa Kireno, Bw. Miguel da Silva, aende kuuchukua. Halafu akanyanyuka kivivu na kuelekea ndani ya chumba maalum akiwa na ule mkoba, ambapo aliuhifadhi ndani ya kasiki liliojengewa ukutani, na pia hufunguliwa na ufunguo maalum. Kisha baada ya kuuhifadhi, akatoka tena kwenda kuungana na watu wake, Hamisi Kengwa na Edmond Balle, tayari kwa kumaliziana malipo.



    “Naona ni muda muafaka wa kumaliziana malipo...” Mokili akawaambia.



    “Ni kweli bosi, ni muhimu tumalizane, kwa vile huko nje kumeshanuka! Tunatafutwa kishenzi!” Hamisi akamwambia.



    “Waingereza wamecharuka! Wametoa donge nono kwa mtu atakayeweza kutoa taarifa kwa walioiba mkufu huo!” Balle naye akasema.



    “ Hilo naelewa, kwani vyombo vyote vya habari ulimwenguni, vinatangaza tukio hili. Lakini mimi ni mtu wa aina yake, hawawezi kunipata, nyie niachieni mchezo huu, nitaucheza mimi!”



    “Hakuna shaka, mchezo tunakuachia wewe!”



    Mokili akachomoa mabunda ya fedha, kiasi kile walichokuwa wamekubaliana, halafu akawakabidhi Hamisi na Balle. Kilikuwa ni kasi kikubwa cha fedha, kiasi cha shilingi milioni mia tatu walichokubaliana hapo awali walipokutana katika kupanga mpango ule wa hatari. Hamisi na Balle waliridhika baada ya kukabidhiwa, kisha wakaaga na kuondoka wakiwa wamepewa usafiri wa kuwafikisha wanapokwenda.



    Wale watu hatari, Hamisi Balle na Edmond Balle, hawakuonekana tena! Baada ya kupewa kitita chao cha fedha ya kutakata, wakapotea labisa kila mmoja kivyake, ili kukwepa mkono wa dola, endapo wangetafutwa! Wakamwacha Mokili wa Ngenge, akipanga kumpigia simu, Bilionea, Miguel da Silva, ili kumjulisha kuwa mzigo ulikuwa umepatikana!



    ********

    Mokili wa Ngenge alikuwa mtu mashuhuri na wa kuheshimika sana katika mtaa maarufu wa Mtakatifu Dennis, jijini Paris . Ni mtaa unaokaliwa na wakazi wengi wenye asili ya Afrika, wakitokea katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo , Kenya , Uganda , Tanzania , Ghana , Sierra Leon, Gambia , Benin , Nigeria na kwingineko Barani Afrika. Hata watu hao walivyofika kule, walijua wenyewe katika mihangaiko yao ya kutafuta maisha kwa ujumla.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Umashuhuri wa Mokili wa Ngenge, ulitokana na utajiri wa biashara kubwa nzito, alizokuwa akiziendesha nchini Ufaransa. Ni kitu ambacho kilifanya Mokili aogopewe hata na Wafaransa wenyewe aliokuwa anaishi nao katika ardhi yao . Hakika ni Mokili huyu ambaye akishirikiana na mtu mmoja, Mnigeria, Wibo Eze, ambapo waliopanga njama zote zilizofanikisha kuibwa kwa mkufu ule wa thamani, uliotengenezwa kwa almasi tupu, kutoka ndani kasri ya Malikia, Buckingham Palace !



    Walikuwa watu hatari!



    Wibo Eze, pia, alikuwa pia ni mtu anayeheshimika sana kwenye mtaa wa Porchester Terrace, jijini London , eneo la Baywater. Vilevile naye alikuwa na makampuni makubwa aliyokuwa anayamiliki na kumfanya aheshimiwe na wazungu, hasa ukizingatia alikuwa katika ardhi yao .



    Magari yote aliyokuwa akitembelea sehemu mbalimbali nchini Ufaransa, yalikuwa ya kifahari. Pia, aliokuwa anamiliki majumba makubwa, likiwemo lile alilokuwa anaishi katika mtaa wa Porchester Terrase. Ni jumba lililokuwa limezungukwa na uzio madhubuti na kukiwa na ulinzi mkali siku zote.



    Mokili wa Ngenge, rafiki yake mkubwa Wibo Eze, alikuwa ni mmoja wa watu waliopora utajiri wa nchim ya Kidemokrasia ya Kongo, na kwenda kujilimbikizia mapesa mengi katika mabenki makubwa mashuhuri ya Ulaya. Vilevile, Mokili alikuwa akimiliki Studio mashuhuri jijini Paris , ambapo karibu wanamuziki wengi wa Kongo, walizalishia kazi zao na kufanikiwa. Mara nyingi, Mokili aliwa akisafiri hadi nchini Kongo, ambapo alikuwa akisaka vipaji vipya vilivyochomoza vya wanamuziki wadogo.



    Ni Studio iliyojulikana kwa jina la Mokili Production, iliyokuwa ikiongoza kwa kwa kupromoti na kuuza muziki wa Kiafrika, Barani Ulaya na Amerika, na kufanya ufahamike kwa kiasi fulani.



    Pamoja na biashara ya muziki, pia, Mokili alikuwa akimiliki shirika dogo la ndege za kukodi, lililokuwa likendesha shughuli zake katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, kutoka uwanja wa ndege wa eneo la Ndiji, jijini Kinshasa , kwenda katika miji mingine ya nchi ile, kama, Mbadaka, Lubumbashi, Kisangani , Goma, Matadi, Mbuji Mayi , Bukavu na mingine ya nchi jirani.



    Biashara ya madini ya thamani kutoka barani Afrika, haikumuacha Mokili nje kama ilivyo kwa rafiki yake, Wibo Eze mwenye shughuli zake katika jiji la London .



    Lakini mbali ya kuwa na biashara halali, Mokili na Wibo walikuwa na siri nzito iliyowaunganisha pamoja kiasi cha kuwafanya marafiki wakubwa wasioweza kutenganishwa. Ukweli ni kwamba wote walikuwa wahalifu wa kimataifa, wakijihusisha na hujuma nzito ambazo baada ya kufanikisha walilipwa donge nono la fedha kutoka katika magenge makubwa ya wahalifu wa kimataifa duniani.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Basi, ndiyo safari hii walipopata kibarua ambacho kingewalipa donge nono kupita yote waliyowahi kulipwa katika shughuli zao za uhalifu wa kimataifa. Kilikuwa kibarua cha kusugua kichwa hasa mpaka waweze kufanikiwa, na kwa vile ni watu ambao hawakupenda kushindwa, au kukata tama, wakaamua kujaribu! Ni kuiba mkufu wa thamani uliohifadhiwa miaka mingi, ulioko ndani ya kasri ya Malkia wa Uingereza!





    ITAENDELEA 

0 comments:

Post a Comment

Blog