Search This Blog

Sunday, 22 May 2022

MKANDA WA SIRI - 5

 







    Simulizi : Mkanda Wa Siri

    Sehemu Ya Tano (5)

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ilikuwa usiku wa manane akiwa amelala mbele ya duka moja pale Tandika. Alihisi kupapaswa na mtu mapajani, mwanzoni alidhani ni ndoto, lakini baada ya kuhisi akizidi kupapaswa ghafla alifumbua macho, ndipo alipokutana na vitu viwili kwa mpigo. Alikutana na Kisu kirefu pamoja na sura ya kutisha ya Dula Mbabe. Mbabe wa Tandika. Jamaa alikuwa anataka kumbaka Binunu, Binunu sio kwamba hakuwa tayari kubakwa tu, pia hakuwa amewahi hata kufanya mapenzi kwa hiyari yake. Sasa ataingiaje katika ulimwengu wa mapenzi kwa mtindo wa kubakwa? Kilichofuatia baada ya pale kilitikisa jiji zima la Dar es salaam. Kichwa cha Dula Mbabe kiliokotwa Temeke Sudani, kiwiliwili kisicho na miguu cha mtu asiyejulikana kiliokotwa mbele ya Temeke hospitali huku miguu ikiokotwa katika dampo la Yombo. Polisi hawakupata shida kujua kwamba viungo vile ilikuwa ya mtu mmoja, Dula Mbabe. Jambazi waliyekuwa wanamsaka kwa muda mrefu bila mafanikio. Hawakujishughulisha kumsaka muuaji, walijua itakuwa ni kisasi toka kwa majambazi wenzie baada ya kudhulumiana mali za wizi.

    Huo ndo ulikuwa mwanzo wa Binunu kuuwa...

    Sababu kuu ya kuwa mkatili kiasi kile ni kwamba, Binunu alianza kuwa mtoto wa mtaani akiwa na umri mdogo sana, na kwa kiasi kikubwa mtaa ndio uliobadiri akili na vitendo vya Binunu. Hata mpango wa kwenda kuvamia kasri ya Abdullah ili kuupora mkanda ni yeye ndiye alikuwa ameupanga. Mpango wa kutumia spray za ocer na foner, huku yeye akiziita kwa ujumla spray zile kama OcaFona. Richard alishangaa sana uwezo wa akili wa Binunu katika kupanga. Alikuwa ameshafanya operesheni kadhaa na watu tofautitofauti, watu mahiri katika medani, lakini hii waliifanya kwa ufanisi mkubwa zaidi, walipata walichokitaka bila kutumia nguvu, na mipango ya Binunu ikienda sawa kwa asilimia mia. Alimkubali sana mwanamke yule na kufikia hatua ya kumwamini na kumpa mkanda wa siri kwenda nao Dar akamkabidhi Martin. Lakini kwa bahati mbaya kabisa meli ya MV Donors ikiwa na Binunu pamoja na mkanda ilizamishwa kwa hila za Malolo katikati ya bahari Hindi. Ajari ilikuwa mbaya sana, kuliko ajari yoyote ya meli iliyowahi kutokea katika kisiwa cha Zanzibar. Ajari ilikuwa na madhara kwa Binunu pia, alijigonga vibaya katika kisogo na kupoteza kumbukumbu pamoja na kuchanganyikiwa. Pamoja na ujasusi wake wote lakini Binunu akili ilimpaa. Kama alikuwa na akili angalau za kuweza kujuta basi labda angejuta kiuwendawazimu kwa kitendo chake cha kujiingiza katika operesheni ile. Ni kudra za Mwenyezi Mungu tu ndizo zilizomuokoa Binunu. Alisukumwa na maji ya bahari yaliyompeleka hadi ufukweni. Na nusu saa baadae aliokotwa na wavuvi wawili, na baada ya muda mrefu wa kushauriana wavuvi wale waliamua kumpeleka katika uwanja wa Maisala. Huku wakilichukuwa wao begi dogo likiloning'inia mgongoni mwa Binunu. Begi lenye mkanda wa siri lilichukuliwa na wavuvi huku Binunu akicheka kiuwendawazimu. Na kutokea yote yaliyotokea...



    SASA leo Binunu aliyebadilishwa na mtaa alikuwa ana kwa ana na Chifu, mtu aliyeamini kuwa ndiye aliyewaua wazazi wake wapendwa miaka kumi na saba iliyopita. Na taswira mbaya ya wazazi wake ilimjia tena kichwani mwake. Aliwaona wakiwa hawana uhai wamelaliana chini. Huku damu za baba yake mzazi zikuwa zimemtampakaa mama yake mzazi, ilikuwa ni taswira mbaya sana ya kusikitisha ambayo Binunu aliishuhudia akiwa na umri mdogo. Kumbuka mama yake alikuwa ametoka kubakwa kabla hajauwawa. Taswira ambayo haikuthubutu kutoka katika ubongo wake kwa muda wa miaka kumi na sababu. Na taswira ile mbaya ya wazazi wake ilimpandisha hasira maradufu. Kwa haraka alinyoosha mikono yake yote miwili na kumkaba shingoni kwa nguvu. Huku kidole gumba cha mkono wa kulia akikikandamiza katika koromeo la Chifu. Chifu macho yalimtoka pima!

    Mkono wa kulia wa Chifu ukaushika mkono wa kushoto wa Binunu, na mkono wa kushoto wa Chifu ukaushika mkono wa kulia wa Binunu. Akijaribu kuitoa mikono ya Binunu shingoni mwake, lakini hakuweza!

    Mikono ya Binunu ilikuwa imara, haikusogea hata chembe. Na kilitokea kitendo cha ghafla. Binunu alimpiga Chifu kichwa takatifu katikati ya utosi wake!

    Chifu hakukitegemea kabisa kitendo kile, Binunu alimstukiza sana, wakati yeye akihangaika kuitoa ile roba pale shingoni, Binunu alifanya kitu kingine.

    Chifu alichanganyikiwa.

    Na muda uleule, Utosi wa Chifu ulivimba kitu kinachoitwa nundu. Chifu naye hakukubali. Hakuwa tayari kudhalilishwa kiasi kile, tena na mwanamke. Aliacha kuushika ule mkono wa kushoto wa Binunu na kuutumia kurusha ngumi ya nguvu kuelekea katika shavu la kushoto la Binunu. Yule mwanamke aliyekulia mtaani aliikwepa ngumi ile kwa ustadi mkubwa sana, huku akiutoa mkono wa kulia katika shingo ya Chifu na kuutumia kurusha ngumi yake ya nguvu, ngumi iliyompata Chifu bara'bara katika mbavu upande wa kushoto. Jamaa alitoa mguno mdogo wa maumivu. Binunu alitanua mikono yake yote miwili mithili ya mtu anayetaka kupaa angani na kuibamiza kwa nguvu zake zote katika kichwa cha Chifu. Mkono wa kulia ulitua katika sikio la kushoto la Chifu na mkono wa kushoto ulitua katika sikio la kulia la Chifu. Masikio yote mawili ya Chifu yalipatwa na pigo lile. Alisikia mivumo mibaya masikioni mwake kutokana na pigo lile liitwalo Malaika.



    "Ni sababu gani iliyokufanya uwaue wazazi wangu?" Binunu aliuliza kwa sauti kubwa yenye ghadhabu.

    Chifu alikaa kimya.

    Alikuwa anamtazama tu yule mwanamke. Siyo kama alikaa kimya kwa jeuri ama kiburi, la hasha alikuwa hajasikia chochote alichoulizwa. Bado masikioni mwake kulikuwa na mivumo kutokana na pigo baya la Malaika alilopigwa. Binunu alihisi jamaa hataki kujibu swali lake. Hasira zilizidi kumpanda. Alirudia tena kupiga pigo lilelile la Malaika. Ni mivumo ya vuuuu vuuuu iliendelea maradufu katika masikio yote ya Chifu. Chifu alibaki mdomo wazi, chozi la uchungu la kiume lilimdondoka sakafuni.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Saa 9: 04 A.M

    Katika kisiwa cha Pemba bado wakina Malkia walikuwa wanamsubiri Ayoub. Hawakutaka kutoka pale mpaka waonane nae na kuongea nae. Bado walikuwa na imani kwamba pale ndipo kwenye jibu la mkanda wa siri.



    Baada ya masaa mawili, Ayoub alikuwa anarejea katika kibanda chake. Akiwa amebeba mfuko wa rambo uliosheheni samaki wabichi. Akiwa umbali kama wa mita miamoja aliwaona watu wanne wakiwa wamekaa mbele ya kibanda chake. Kati ya watu wale alimfahamu mtu mmoja tu.



    "Wale wengine ni kina nani?" Ayoub alijiuliza kimoyomoyo.



    Hakuwa na miadi na wageni kwa siku ile. Ayoub aliendelea kwenda katika kibanda chake bila kujua kwamba alikuwa anaisogelea hatari. Kwa mwendo wa taratibu Ayoub aliendelea kuelekea katika kibanda chake dhaifu. Kibanda alichokitengeneza kwa dharura tu baada ya kuhama kwa lazima katika nyumba aliyokuwa amepanga awali. Alitembea huku akiwa na mashaka mengi sana ndani ya moyo wake. Moyo ulikuwa unamdunda pasi na kawaida. Ni mara ya tatu sasa katika maisha yake moyo kumdunda namna ile....Hakuwahi kudundwa na moyo kiasi kile tangu siku ile alivyouwawa baba yake na siku aliyovamiwa chumbani kwake na watu wasiojulikana. Matukio mawili ambayo yamebaki kuwa kitendawili kwake hadi leo. Hakujua vyanzo vyake, hakujua sababu zake. Matukio ya kutisha ambayo yalimtoa Ayoub katika hali aliyokuwa nayo akiwa mtoto, hali ya ucheshi, na matukio hayo yalimtengeneza Ayoub katika hali aliyonayo sasa, hali ya ukimya na upole.

    Na hapo ndipo wakina Malkia nao walimuona....



    Wakina Malkia walivyoona mtu anaelekea pale wote walisimama wima. Wakijua mtu wa kulifumbua fumbo lao lililodumu mwezi mzima alikuwa amewasili. Mtu muhimu kwa mustakabali wa mkanda uliowapotea kimaajabu. Na sasa walikutana.



    "Wageni wako hawa Mwenyekiti" Yule mvuvi aliyewapeleka pale alisema baada ya salamu.



    "Ahaaa, nashukuru sana kaka" Ayoub alisema huku akiziangalia kwa zamu sura za wageni zilizopo mbele yake. Alijaribu kuziuliza kumbukumbu zake lakini zilimjibu kwamba hakuwahi kukutana na sura kama zile tangu azaliwe.



    "Karibuni sana wageni wangu" Ayoub alisema kwa sauti ya upole yenye kuonesha ukarimu ndani yake.



    "Naitwa Angel Michael, huyu anaitwa Maziku Donge na huyu anaitwa Jackson Fued..." Malkia aliwatambulisha wenzake na yeye mwenyewe kwa majina ya uwongo huku akiwaonesha kwa vidole wenziwe wakati wa utambulisho.

    Huku wote wakimwangalia yule jamaa kwa pamoja.



    "Nashukuru sana kuwafahamu... Mimi kwa majina ninaitwa Ayoub...Ayoub Mbembati, ni mwenyekiti wa BMU ya hapa...karibuni sana" Ayoub alisema kwa sauti yake ya upole.



    "Ayoub Mbembatiii!" Wote walisema kwa pamoja kwa taharuki, kasoro yule mvuvi aliyewasindikiza. Mstuko dhahiri ulionekana kwa wageni wale watatu. Walianza kuangaliana kwa muda.

    Hawakuyaamini masikio yao.

    Mstuko na taharuki ile ilipokewa kwa namna tofauti na yule mvuvi msindikizaji pamoja na Ayoub mwenyewe. Kwanini wageni washangae namna ile kwa kusikia tu jina la Ayoub. Kuna tatizo...tatizo gani sasa?



    Mdundo wa hofu wa moyo wake ulioanza pindi tu alipowaona kwa mbali wageni wale ulimthibitishia Ayoub kwamba ulikuwa sahihi, na wale wageni hawakuwa watu wema. Hawakuwa wema kwa vipi, hakujua, alichojua ni kutafuta namna ya kujiokoa. Ilimfunukia kwamba pale hapakuwa mahali salama.



    "Ayoub Mbembati..." Malkia alitamka kwa sauti ndogo ya kuchoka. Lilikuwa jina ambalo hakutaka kulisikia kabisa kwa wakati ule. Jina lile lilikuwa na thamani, tena thamani kubwa sana miezi miwili iliyopita, lakini siyo sasa. Sasa halikuwa na thamani kabisa.



    *****



    Kule Kisarawe hali ilikuwa ngumu sana kwa Chifu Abdullah. Binunu alikuwa amechachamaa kwa jazba na hasira. Ulikuwa ni wakati mgumu sana kwa Chifu. Pengine ingekuwa enzi zake asingeweza kunyanyaswa kiasi kile na yule mwanamke, lakini sasa umri ulikuwa umemtupa mkono. Binunu alitumia vizuri udhaifu huo wa Chifu. Alikuwa ameshampiga mabao ya masikio mara tano sasa. Chifu alikuwa hawezi kabisa kujitetea. Kichwa chote kilikuwa kinamuuma vibaya sana. Na Binunu hakuwa na dalili kabisa ya kuacha kumpiga kwa namna ileile, sehemu ileile, kwa nguvu ileile. Na Chifu aliona asipojitahidi kujibu anachoulizwa atakufa kifo kibaya. Atakufa akiwa kiziwi. Pamoja na maumivu makali na mivumo isiyoisha masikioni mwake lakini sasa alijitahidi kumsikiliza ili amjibu.



    "Kwanini uliwauwa wazazi wangu?" Binunu aliuliza kwa ukali huku akitambua kuwa Chifu alikuwa hasikii. Na kweli Chifu hakusikia, lakini alijibu. Chifu aliona mdomo wa Binunu jinsi ulivyokuwa unacheza.

    Alimuelewa.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "M..ka...nda!" Chifu alisema kwa sauti ya kukatakata. Binunu alisikia vizuri sana jibu la Chifu. Na muda uleule alikumbuka sauti ya kukwamakwama ya baba yake siku ile wakati anakata roho. Jinsi ikivyokwamakwama na kumwambia kuwa mkanda anao Ayoub.



    "Inamaana mkanda tulioenda kuuiba kwenye kasri juzi ndio mkanda alioniambia baba miaka kumi na saba iliyopita kuwa upo kwa Ayoub?" Binunu alijiuliza kimoyomoyo...huku akikumbuka tukio lile na kudhani limetokea juzi tu, kumbe ulikuwa mwezi sasa umepita.

    Na kumbukumbu hiyo ilimzidisha hasira maradufu.

    Binunu alipandwa na hasira maradufu huku akiwa hailewi kabisa mambo yale yalivyokuwa yanatokea. Sasa alipata kitendawili kipya kabisa kichwani mwake...Hakuelewa kwanini sasa kina Martin walikuwa wanauhitaji ule mkanda. Mkanda wa siri uliosababisha kifo cha wazazi wake wapendwa. Mikono ya Chifu ilikuwa imeziba masikio yake yote mawili, ikizuia mapigo yale ya hatari sana kutoka kwa Binunu. Binunu sasa aligairi, hakufanya kama alivyofanya awali. Alibadili kitendo...

    Alimshika Chifu shingoni kama alivyomshika awali, kwa kasi Chifu nae aliacha kuziba masikio na kuipeleka mikono yake juu ya mikono ya Binunu.



    "Na hii ni kwa niaba ya baba!" Binunu alitamka maneno hayo huku akimpiga Chifu kichwa takatifu, kichwa cha nguvu mara mbili ya kile alichompiga awali.

    Chifu alijaribu kukwepesha kichwa chake, lakini kasi ya Binunu kupeleka kichwa kile ilikuwa ni zaidi ya kasi ya Chifu aliyoitumia kukwepa.

    Kilimpata!

    "Na hiyo kwa niaba ya mama..khabithi wewe!" Binunu alisema huku akipiga ngumi ya nguvu kwa mkono wake wa kulia, ngumi iliyotua katikati ya uso wa Chifu. Chifu aliinama chini huku akiwa ameshika uso wake kwa viganja vyake vyote viwili. Binunu alikuwa amempiga palepale kilipotua kichwa.

    "Na hiyo kwa niaba ya mzee Mbembati...baradhuli mkubwa wewe!" Teke kali toka kwa Binunu lilimpata bara'bara katikati ya miguu yake. Kumbuka Chifu alikuwa uchi wa mnyama. Teke lile lilimrusha juu Chifu na kumpelekea kwenda kujigonga vibaya sana ukutani. Chifu alilala chali akiwa hoi bin taaban. Pumzi zake zilikuwa zinatoka kwa mbali sana. Alikuwa anapigania hewa ili aweze kuishi. Bila wasiwasi wowote Binunu alimsogelea taratibu Chifu, mguu wake wa kulia alimuwekea Chifu kifuani na kuanza kumkandamiza kwa nguvu. Madonge makubwa ya damu yalitoka mdomoni mwa Chifu. Alikuwa anatapika huku sura yake ikiwa imechakaa vibaya sana. Sura ikiwa haina matumaini ya kuishi. Binunu alinyanyua juu ule mguu wake wa kulia na kuurejesha chini kwa kasi sana na nguvu kubwa, mguu ulitua palepale ulipotua awali, katika kifua cha Chifu. Chifu alitapika madonge ya damu huku akiunguruma mithili ya Simba mzee. Binunu hakuwa na huruma hata kidogo, hakumhurumia Chifu, sasa alinyanyua juu mguu wake wa kushoto na kupiga katika sehemu za siri za Chifu, kumbuka Chifu alikuwa uchi wa mnyama.

    Na pigo lile lilitua vizuri sana.

    Chifu alitoa ukelele mkali, na kuanza kulia mithili ya mtoto mdogo. Binunu aliinama pale chini na kumshika Chifu shingoni. Alilishika koromeo la Chifu kwa vidole vyake viwili, kidole gumba na kidole cha shahada. Na kuanza kulivuta. Macho yalimtoka pima Chifu mithili ya kijusi aliyebanwa na mlango. Maumivu akiyoyapata Chifu yalikuwa hayana mfano, na kwa bahati mbaya kwake alishindwa kabisa kujitetea, msaada pekee kwake ulikuwa ni kupiga makelele, alikuwa anapiga tu makelele yasiyo na maana yoyote kwa Binunu. Binunu alilibinya lile koromeo la Chifu, kitendo kilichofanya amlize Chifu apendavyo. Yule mwanamke akalivuta bwana koromeo. Alilivuta kwa nguvu nia yake ni kulitoa nje!. Roho ya Chifu haikutaka kukaa tena katika mwili ule uliokuwa unapitia katika mateso makali sana. Roho haikuweza kuvumilia maumivu yale. Roho ya Chifu iliruka juu na kwenda kuzimu. Chifu alikata roho akiwa anapitia maumivu makali sana, maumivu ambayo hakuwahi kuyafikiria hata siku moja, maumivu makali ilikuwa kama anachunwa ngozi akiwa hai.



    Binunu aliingia ndani, alilivua lile gauni. Alijifuta damu za Chifu zilizomtapakaa mwilini kwa kutumia lilelile gauni, sasa alivaa suruali ya jeans nyeusi na tshirt ya bluu, chini alivaa raba nyeusi zilizomkaa vema bila hata kujua nguo zile za nani. Alitoka nje ya nyumba ile na kutokomea kusikojulikana.



    *****



    "Wewe kumbe ndo Ayoub Mbembati..?" Malkia aliuliza kwa sauti yake ya uchovu. Sauti isiyokuwa na matumaini yoyote. Walikuwa wamecheza mchezo uitwao pata...potea.



    "Ndio mimi Angel, mimi ndiye Ayoub...kwani kuna tatizo gani?" Ayoub alijibu kwa sauti yenye mashaka na kumalizia kwa kuuliza swali. Hakuna aliyenyanyua mdomo wake kumjibu Ayoub. Wote walitazamana tena, kisha wakatikisa vichwa vyao kwa masikitiko. Hali iliyozidi kumchanganya Ayoub pamoja na yule mvuvi msindikizaji. Wakina Malkia hawakuwa na la ziada pale, haikuwa na maana yoyote kujibu swali la Ayoub. Kumbukumbu mbaya zilipita vichwani mwao.



    Wewe kumbe ndo Ayoub Mbembati..?" Malkia aliuliza kwa sauti yake ya uchovu. Sauti isiyokuwa na matumaini yoyote. Walikuwa wamecheza mchezo uitwao pata...potea.



    "Ndio mimi Angel, mimi ndiye Ayoub...kwani kuna tatizo gani?" Ayoub alijibu kwa sauti yenye mashaka na kumalizia kwa kuuliza swali. Hakuna aliyenyanyua mdomo wake kumjibu Ayoub. Wote walitazamana tena, kisha wakatikisa vichwa vyao kwa masikitiko. Hali iliyozidi kumchanganya Ayoub pamoja na yule mvuvi msindikizaji. Wakina Malkia hawakuwa na la ziada pale, haikuwa na maana yoyote kujibu swali la Ayoub. Kumbukumbu mbaya zilipita vichwani mwao.



    ***



    Yaliyotokea miaka kumi na saba iliyopita..

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    SIKU ile Mzee Issa alivyopigwa risasi na akiwa katika harakati za kukata roho, kwa sauti ya kukatakata aliyoitoa akiwa anapitia katika maumivu makali, alimwambia mwanae mpendwa Binunu kuwa mkanda upo kwa Ayoub. Baba Binunu kwa kauli ile alikuwa anamlenga Binunu pekee lakini kwa bahati mbaya sana kauli ilisikiwa na watu wote pale sebuleni. Kauli yenye thamani sana ilisikiwa na masikio mabaya pia, masikio yasiyopaswa kabisa kuisikia kauli ile kulingana na unyeti wake. Ndipo msako wa kina Chifu ulipobadili mwelekeo. Badala ya kuusaka mkanda wa siri kama walivyokuwa wanafanya awali, sasa walianza kumsaka Ayoub kwa udi na uvumba....wakiamini kuwa Ayoub ndiye mwenye mkanda kama alivyosema baba yake Binunu kumwambia mwanae wakati anakata roho. Wakina Chifu hawakuhangaika kabisa na yule mtoto, hawakumfanya chochote, walimuacha akilia huku akizilalia maiti za wazazi wake. Na ndio kosa kubwa waliolifanya kina Chifu, walisahau kwamba umuuwapo nyoka lazima utenganishe kichwa na kiwiliwili. Wao waliondoka na jina tu la mtu muhimu kwao, huku wakimuacha hai mtoto Binunu. Na kama walidhani ni kazi rahisi kumpata Ayoub kisha kuupata mkanda, basi walikuwa wamejidanganya sana.

    Hiyo haikuwa kazi rahisi hata kidogo.



    Walitumia miaka kumi na saba kumtafuta bila kujua huyo Ayoub anakaa wapi, ingawa kwasasa walikuwa na maelezo mengi sana kuhusu maisha ya Ayoub huko nyuma lakini hawakujua kabisa kwasasa Ayoub anaishi wapi. Na hata hao waliowaleza wakina Chifu maisha ya Ayoub ya awali hawakujua kwa sasa Ayoub yuko wapi. Baada ya kupita miaka hiyo ndipo upelelezi wa kina Chifu ulipowafikisha mahali alipo Ayoub na mkanda wa siri. Naaam, kina Chifu walifika katika kisiwa cha Unguja. Ni kweli kuwa Ayoub alikuwa na mkanda mahali fulani katika chumba alichopanga huko Unguja. Siku zote tangu aupate mkanda ule aliutunza mahali pa siri, mahali alipokuwa anapajua yeye pekee, lakini ulikuwa humohumo katika chumba kidogo alichopanga. Na katika miaka yote hiyo alikuwa bado hajaungalia mkanda una nini ndani yake, hakujua ni vitu gani vilivyopo katika mkanda ule vilivyosababisha madhila makuu kwa baba yake na yule mzungu. Ingawa hakuwa na video lakini hiyo haikuwa sababu ya kutouangalia mkanda ule. Yeye hakutamani hata kidogo kuuangalia. Alikuwa hapendi hata kuliangalia kava tu la mkanda ule kwakuwa ulikuwa unamrejeshea kumbukumbu mbaya sana za nyuma. Picha mbaya na ya kutisha aliyoiona wakati baba yake anakata roho ilimjia pindi tu aukumbukapo mkanda ule. Na alikuwa anapata HOFU kuu moyoni. Kabla hajahamia katika kibanda akaacho sasa ambacho ndipo walipomkuta wakina Malkia, Ayoub alikuwa amepanga mjini Unguja. Sababu iliyomfanya ahame kwenye nyumba hiyo ya Unguja ilitokea mwezi mmoja uliopita.



    Siku hiyo, Ayoub alikuwa anarejea nyumbani kwake toka matembezini saa nne usiku. Alikuwa anarudi nyumbani kwake akiwa hana wasiwasi wowote ule. Historia mbaya ya mambo yote yaliyotokea miaka kadhaa iliyopita ilikuwa imeanza kufutika kichwani mwake. Alifungua mlango wa chumba chake na kuingia ndani, alipiga hatua za taratibu kuifata swichi ili awashe taa iliyopo mle chumbani kwa lengo la kupata mwanga. Lakini hakuifikia swichi......Kitu ambacho hakuwa anakifahamu kabla..yeye alidhani yuko peke yake mle chumbani, kumbe haikuwa hivyo, hakuwa peke yake, kulikuwa na wageni walioingia kwa siri sana ndani ya chumba chake saa mbili kabla ya yeye hajarejea toka matembezini. Ayoub alikuwa chumba kimoja, tena gizani na wageni wabaya na wenye lengo baya sana. Ndani ya kiza kinene katika chumba cha Ayoub kulikuwa na wageni wawili walioingia bila hata kukaribishwa na mwenyeji wa chumba kile. Namna waliyoitumia kuingia mle ndani walikuwa wanaijua wao wenyewe. Wageni hao wasio rasmi, mmoja alikuwa anaitwa Peter Kissali na mwengine alikuwa anaitwa Malolo Abdallah.



    Peter alikuwa amekaa juu ya kitanda kilichochakaa kilichokuwa kinamilikiwa na mmiliki wa chumba kile. Wakati mgeni mwengine, Malolo alikuwa amekaa katika kiti pekee cha mbao ambacho kilikuwepo katika kona moja ya chumba kile. Kutokana na giza la kutisha Ayoub aliingia bila kuhisi kabisa kama kuna watu chumbani mwake mpaka pale alivyosemeshwa na sauti asiyoijua wakati akielekea kuwasha swichi ya umeme.



    "We are in OMS, and now we need M..." Peter alisema kwa lugha ya mafumbo tena kwa lugha ya kiingereza.

    Ayoub sio tu hakuelewa maana ya maneno yale pia hakuelewa kabisa ile sauti iliingia vipi mle ndani. Mstuko alioupata kutokana na kusikia sauti ile hauna mfano. Alistuka sana...hakutegemea kabisa. Alibaki amesimama wima huku akitetemeka kwa woga katikati ya chumba chake.



    "Tuko katika operesheni mkanda wa siri, na sasa tunahitaji mkanda" Malolo aliyatafsiri kwa kiswahili maneno ya kiingereza yaliyoongelewa na Peter.

    Na sasa mstuko wa Ayoub ulizidi maradufu. Ayoub alihisi mambo aliyoyakimbia Kilwa sasa yalikuwa yamemfata Unguja, tena yamesubiri miaka kumi na saba ili yarejee tena.



    "Mkanda wa ....." Ayoub hakumaliza alichotaka kusema.



    "Mkanda aliokupa baba yako mzazi, mzee Mbembati miaka kumi na saba iliyopita huko kwenu Kilwa, ndio huo mkanda ambao tunautaka sisi..." Peter alimalizia maneno ya Ayoub kwa maringo na kujiamini sana.

    Ayoub alibabaika sana!

    "Tumeingia kirafiki, tumekuwa werevu maana tumekusubiri kirafiki pia, na sasa tunaongea kirafiki, tupe mkanda kirafiki, ili tuondoke kirafiki na ubaki kuwa rafiki yetu" Malolo alisema huku akinyanyuka toka kule konani mwa chumba, katika kiti alichokikalia.



    Ayoub alikuwa hana ujanja wowote ule wa kimapambano. Alikuwa sio mtu wa kuzoea misukosuko na mikikimikiki kabisa na hata angekuwa mtu wa hivyo mle ndani alikuwa peke yake, na hakujua maadui zake wako wangapi. Ingawa hadi sasa alikuwa ameshasikia sauti za watu wawili tofauti. Aliongea.



    "Mzee hakuwahi kunambia nikukabidhini ninyi mkanda .." Ayoub alijibu kizembe sana.



    "Hahaha, alikwambia umkabidhi nani sasa?" Peter alicheka kwa dharau huku akimtupia swali Ayoub.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Utatupa hutupi!" Malolo nae alidakia kwa kauli aliyoitoa kimamlaka.

    Ayoub alikaa kimya.



    "Hatujaja kwa shari, usitulazimishe tuondoke kwa shari, tupe mkanda kijana!" Peter aliacha kucheka na kutahadharisha akiwa bado amekaa pale kitandani bila wasiwasi wowote.



    "Niwape ama nisiwape?" Hayo ni mawazo yaliyopita katika kichwa cha Ayoub. Mawazo yaliyopita kwa mtindo wa swali. Ayoub alikuwa anajiuliza mwenyewe, awape mkanda ama asiwape?.

    "Siwapi" Alijijibu pia mwenyewe, kimoyomoyo, akimaanisha kuwa kwa njia yoyote ile hatoutoa mkanda.



    "Utatupa!" Peter alisema kuijibu kauli ya Ayoub ambayo aliisema kimoyomoyo. Ayoub alistuka sana. Kwani lile lilikuwa jibu la jibu lake alilojijibu mawazoni tu. Jamaa alijibu swali lililokuwa linapita kichwani kwake. Ayoub aliona ni jinsi gani kwamba alikuwa na watu hatari sana chumbani mwake. Jinsi gani alivyo karibu na hatari. Watu wenye kuweza kujibu hata vitu vinavyopita kichwani mwake.



    'Na kwa mara ya kwanza Ayoub alijuta kwa kitendo chake cha kutouangalia mkanda ule'



    Lakini pamoja na umahiri mkubwa waliouonesha watu wale ambao hakuzijua hata sura zao kutokana na giza nene lililokuwa mle chumbani, hakukata tamaa. Aliamua kufanya kitu.

    'Hapa nitafute nafasi ya kuufikia mlango ili nikimbie, mbio ndio usalama wangu pekee wa kujiokoa..mbio kali sana za kujiokoa na kifo'



    Ayoub alipiga hatua ndogo sana kwa mguu wake wa kushoto, lengo ni kutaka kurudi nyuma na kutafuta namna ya kujiokoa. Hatua ambayo ilielekea upande ulipokuwa mlango. Ilikuwa hatua ndogo sana ya kimyakimya tena katika giza nene. Lakini cha ajabu mguu ule wa kushoto uliopiga hatua ile haukufika chini. Ulisimamishwa na sauti ya Peter!



    "Unaenda wapi Ayoub, usilete hila yoyote hapa, hila toka kwako inamaanisha unahamu ya KIFO! na bila shaka tutaikamilisha hamu yako dogo" Peter alisema kwa umakini mkubwa huko neno kifo akilitaja kwa sauti kubwa tofauti na yale maneno mengine.



    Mguu wa kushoto wa Ayoub ulikuwa umeganda hewani ukining'inia. Akiwa hajui aurudishe alikoutoa ama akanyage alipotaka kuupeleka. Alikuwa anawaza harakaharaka kichwani mwake lakini hakupata jibu. Atapata vipi jibu wakati alikuwa na mawazo mvuragano. Mawazo ambayo yalienda sambamba na mshangao.



    "Jamaa wana macho aina gani hawa? wamewezaje kuuona mguu wangu katika giza kama hili?" Kwa mwendo wa taratibu Malolo alimfata pale aliposimama Ayoub. Ayoub sasa alimuona japo kwa shida maana macho yake sasa yalianza kuzoea giza. Na hapo ndipo alipoanza kuelewa sababu ya wale jamaa kumuona, walikuwa wamekaa muda mrefu mle chumbani na walikuwa wamelizoea giza. Ayoub sasa alijitahidi kuiangalia sura ya jamaa aliyekuwa anamfata, angalau ajue kama aliwahi kukutana nae sehemu nyingine tofauti na leo, au aihifadhi kichwani ili aitambue siku nyingine kama atapata nafasi ya kufika siku hiyo. Pamoja na jitihada zake zote lakini hakufanikiwa kabisa kuiona sura ya mtu yule. Malolo alizikatisha jitihada za kuona za Ayoub.

    Ghafla, Malolo aliufyatua ule mguu wa kulia uliobaki chini. Ilikuwa kazi rahisi sana kwakuwa Ayoub alikuwa amesimamia mguu mmoja. Ayoub alienda chini mithili ya gunia la mpunga ! Hakujiandaa kabisa na tukio lile na hata angejiandaa angeenda tu chini, aligaragara chini huku akilia kwa uchungu uliochanganyika na majuto.



    "Usijaribu kuleta ujanja wowote hapa kama bado unapenda kuwa mvuvi katika sayari hii...tofauti na hivyo utaenda kuwa mvuvi kuzimu, kama huko kuzimu kuna bahari!" Peter alitahadharisha akiwa bado amekaa palepale kitandani. Kijana Ayoub alikuwa hajazoea kabisa shuruba...yeye alizoea kusumbuana na samaki lakini sio kusumbuana na binadamu wenzake. Akiwa pale chini alikuwa analia huku damu zikimchuruzika mdomoni, na hapo ndipo alifikia uamuzi mgumu sana katika maisha yake, aliamua kuwapa mkanda wale jamaa ili kuokoa maisha yake.

    "Na..wa..pa M..ka..nda..." Ayoub alisema kwa sauti ya kukatakata iliyoonesha kuwa alikuwa anapitia katika maumivu. Alinyanyuka taratibu toka pale sakafuni na kusogelea swichi ya umeme ili awashe taa.



    "Usiwashe taa!" Malolo alisema kwa ukali.

    Lilikuwa katazo zuri la Malolo kwa wakati ule lakini katazo lile liliharibu kabisa ushindi upande wao. Ayoub alichukua kiti alichokuwa amekalia Malolo awali na kupanda darini. Aliutoa mkanda na kuwakabidhi. Alikabidhi mkanda katika mikono mibaya huku mikono yake ikitetemeka na macho yake yakitoa machozi mfululizo.



    'Na kwa mara nyingine tena Ayoub alijuta kwa kitendo chake cha kutouangalia kitu kilichomo katika mkanda ule' Majuto ni mjukuu.



    Jamaa waliuchukua mkanda wa siri mikononi mwa Ayoub na kutokomea nao. Bila kuiona sura ya Ayoub. Bila Ayoub kuziona sura zao. Waliingia na giza, na walitoka na giza.



    Asubuhi ya siku iliyofuata Ayoub alihama ile nyumba bila kupenda, alihama kwa kudhani wale jamaa wangerejea tena na kumdhuru. Hakuonana tena na wale majamaa mpaka baada ya mwezi mmoja. Watu walewale walikuwa wamemfata Ayoub tena kudai mkanda ambao waliuchukua wao wenyewe chumbani kwa Ayoub usiku wa giza kali. Lilikuwa ajabu la nane la Dunia!





    Ulikuwa ni mwezi wa mashaka mazito na upelelezi mkali toka katika jeshi la Polisi kwenda kwa watu wawili. Vikosi vya jeshi la Polisi vikiongozwa na Koplo Baruani viliendelea na msako wao ambao kwa sasa ulielekea kufeli, tunaweza kuuita msako uliofeli wa kumsaka kijana Martin Nguzu, jamaa anayetuhumiwa kumuua mtu ndani ya gari bandarini. Msako huo ulienda sambamba na msako wa kumsaka Mr Na na na, mzungu aliyeacha taharuki kubwa sana katika hoteli ya Grand villa. Koplo Baruani alitumia mbinu zake zote alizofunzwa katika chuo cha upolisi, CCP Moshi, koplo Baruani alitumia pia mbinu za ziada alizotunukiwa na Mwenyezi Mungu. Pamoja na kutumia mbinu hizo mbili alizozipata katika sehemu kuu mbili alizoziamini sana lakini jina la Martin Nguzu lilibaki kuwa kama msamiati mgumu ambao haukuwahi kutokea katika lugha yake adhimu ya Kiswahili. Na kuhusu Mr Na na na, ilikuwa ni sentensi tata yenye utata mwingi sana, ambao kwa mwanafunzi wa kiwango chake cha elimu hakuweza kuutatua utata huo.

    Pengine alichokuwa anakosea Koplo yule kijana pamoja na Jeshi la Polisi kwa ujumla ni kufanya upelelezi ndani ya upande mmoja tu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hawakutilia maanani kabisa kuhusu upande wa pili wa Muungano, kisiwa cha Zanzibar. Upande ambao ndipo yalipokuwa majibu ya maswali yao yote.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ilikuwa umepita mwezi mmoja na wiki kadhaa toka kifo cha Shanta wa bandarini, kijana mbabe kuliko wote bandarini, Mansour. Leo hii ilimkuta Koplo Baruani akiwa nje ya nyumba anayoishi Martin pindi akiwa jijini Dar es salaam. Nusu saa ilimuweka koplo Baruani katikati ya mlango wa nyumba ile, kasimama mithili ya sanamu la pale Posta. Alikuwa anabisha hodi bila ya kujibiwa. Pamoja na jitihada zake za kuisaka nyumba ile hadi kuipata lakini kitu ambacho alikuwa hajakifahamu bado.....Martin alikuwa anaishi nyumba ile mara chache sana akiwa jijini Dar es salaam. Mara nyingi hata akiwa Dar es salaam alikuwa analala katika hoteli mbalimbali. Sababu kuu za kuhamahama zikiwa ni hisia zake, alikuwa anazisikiliza sana hisia zake juu ya mahali pa kulala. Hisia zikimkataza anaacha, hisia zikimwambia anafanya. Koplo Baruani alivyoona kimya baada ya kubisha hodi kwa muda mrefu, aliamua kumtafuta Mwenyekiti wa mtaa wa Magomeni Mapipa ili apate ruhusa ya kuingia katika nyumba ile na kuipekua. Ilimchukua nusu saa nyingine kumpata Mwenyekiti wa mtaa. Na sasa walikuwa watu watano mbele ya mlango wa nyumba ya Martin. Walikuwa Mwenyekiti wa mtaa wa Magomeni, wajumbe wawili, shahidi mmoja na Koplo mwenyewe. Walivunja mlango wa nyumba na kuingia ndani. Ilikuwa ni nyumba ndogo yenye vyumba vitatu, bafu na sebule safi ya kisasa. Walipita chumba kimoja baada ya kingine, kwa umakini na tahadhari kubwa sana walijaribu kupekua kila sehemu waliyoihisi inaweza kuwa na lolote, lakini hawakulikuta hilo lolote. Baada ya saa moja walikaa sebuleni na kujadiliana.



    "Kwani Martin amehamia lini mtaa huu?" Koplo Baruani alimuuliza mzee Nondo ambaye ndiye alikuwa Mwenyekiti wa mtaa wakiwa wamesimama sebuleni.



    "Ana kama miaka mitano sasa kama sikosei.." mzee Nondo alijibu baada ya kufikiria kidogo.



    "Kwani nani alikuwa rafiki yake mkubwa hapa mtaani?" Koplo Baruani aliuliza tena baada ya kuandika maelezo kidogo katika kijitabu chake. "Kwa kweli huyu kijana hajawahi kuwa na rafiki hapa mtaani, alikuwa ni mtu wa kuingia na kutoka, ukimuona leo tarajia kumuona tena baada ya miezi mitatu" Kijana mmoja aliyeitwa kama shahidi katika upekuzi ule alijibu.



    "Mtu anaweza kuishi miaka mitano mtaani bila kuwa na urafiki na mtu yeyote, inawezekana kweli hiyo Mwenyekiti?"



    "Ni ngumu sana Afande, lakini kwa huyo kijana anayekaa nyumba hii ni nyepesi sana, na amelithibitisha hilo, akwambialo Uledi ni ukweli mtupu" Mwenyekiti alijibu.



    Baada ya kuongea hili na lile Koplo Baruani aliagana na watu wale, aliagana nao huku akiahidi kuwa atarejea tena kama atakuwa na sababu ya kurejea, pia aliwaachia namba yake ya simu ya mkononi ili wampigie pindi tu Martin watakapomuona pale mtaani. Naye alichukua namba zao. Koplo Baruani aliondoka huku akiwa bado ana maswali mengi sana juu ya mtu aitwaye Martin Nguzu lakini kwa bahati mbaya sana kwake hakuwa na wa kumuuliza.



    *****



    "Kumbe wewe nd'o Ayoub, Ayoub Mbembati? daaah tumefanya a big mistake, we can call it " the mistake of the year..!" Malolo alisema kwa sauti kubwa, huku moyoni mwake akiwa anatamani Ayoub aseme yeye sio Ayoub Mbembati. Lakini itatokea vipi hiko anachokitamani? Mbele yao alikuwa amesimama mtu, na alikuwa Ayoub halisi, Ayoub Bin Mbembati.



    Ayoub alistuka sana kuisikia sauti ile ikiwa katika mshangao namna ile. Kumbukumbu zake zilirudi kwa kasi sana hadi mwezi mmoja uliopita, wakati alipopata wageni asiowatarajia gizani, na kuporwa mkanda wa siri bila kupenda.



    "Usiwashe taa!" Ayoub badala ya kujibu swali la Malolo, ama kukili maelezo ya Malolo, yeye alikumbuka karipio la kutowasha taa alilopewa chumbani kwake gizani. Na ndipo alipoikumbuka kwamba sauti ambayo ilimpa karipio lile, sauti ambayo ilimkataza kwa nguvu asiwashe taa ya chumbani kwake mwezi mmoja uliopita ilikuwa mbele yake, sauti ileile, sauti yenye kupenda kukaripia wanyonge. Hakuwahi kulisahau karipio la sauti ile ubongoni mwake. Alilikumbuka siku zote zilizofuata baada ya karipio lile. Sauti ile ilikuwa imeshajirudia mara kadhaa katika ndoto alizoota baada ya siku ile, ilikuwa ni miongoni mwa sauti mbaya zaidi kuzisikia katika maisha yake, ilikuwa ni sauti mbaya iliyokuwa inamilikiwa na mtu aliyeondoka na mkanda wa siri katika usiku wa giza. Kamwe hakuthubutu kuisahau ile sauti hasa ikiwa katika mtindo wa kukaripia.



    "Mkanda si mliuchukua nyinyi lakini..." Ayoub aliropoka akiwa katika hali ya kutetemeka. Kauli ile ilisikiwa na wote, kauli ambayo haikueleweka kabisa na yule mvuvi msindikizaji, lakini kauli ilieleweka, tena ilieleweka vizuri sana na wakina Malolo. Wote walitazamana. Waliielewa maana ya kauli ya Ayoub. Ilikuwa inamaanisha kwamba walikuwa wameenda sehemu siyo sahihi. Walishauchukua mkanda toka mikononi mwa Ayoub mwezi mmoja sasa. Na leo wameenda tena.



    "Usiwashe taa!" Peter nae alikumbuka kauli ya Malolo siku ile. Sauti Iliyokuwa inamkataza Ayoub asiwashe taa.

    "Labda angewasha taa siku ile, leo hii tusingesumbuka namna hii..ona sasa tumepotea maboya kizembe sana" Mawazo hayo yalipita kichwani mwa Peter. Na ilikuwa kweli, wasingewasha taa wangekuwa na taswira ya Ayoub vichwani mwao, na wangemtambua Ayoub kabla hawajahangaika na kwenda Pemba, wangemtambua pale tu walipomuona kwenye runinga tangu wakiwa Kisarawe.



    Upande wa Ayoub alikuwa anatetemeka vibaya sana. Aliamini kwamba wale ndio watu aliokuwa nao katika chumba chenye giza, watu hatari sana wenye kusoma hadi mawazo ya mtu yapitayo kichwani.



    "Mkanda walishauchukua sasa wamefata nini tena kwangu, bila shaka leo wamekuja kunimaliza, siku ile walifata mkanda na leo bila shaka wamefata roho yangu! Nina mkosi gani mimi?..." Inawezekana kweli kwamba Ayoub alikuwa na mkosi. Maana alikuwa amepitia na kushuhudia mambo makubwa na mazito sana katika maisha yake. Na bado mambo hayo yalikuwa yanamuandama.



    "Mwendawazimu katuuza aisee..." Peter alisema kwa nguvu. Akiwa na maana kuwa Binunu kawauza kwa kuwaonesha mtu sie, lakini kauli ile ilimstua vibaya sana yule mvuvi msindikizaji.



    "Hapana jamani, huyu ndiye aliyepo katika picha yenu, ni mwenyekiti wetu wa BMU, wala sijawauza, hebu iangalieni vizuri picha yenu halafu mumuangalie na huyu, au labda mniambie mapacha." Mvuvi msindikizaji alilalama.



    "Shut up! Tena funga kabisa mdomo wako mchafu, hatuko katika maigizo hapa, nitakupasua tumbo lako sasahivi na kuutawanya utumbo wako hewani!" Malkia alifoka kwa nguvu huku akirusha mikono yake hewani. Akionesha jinsi atakavyousambaza utumbo wa mvuvi msindikizaji.

    Jamaa aliogopa sana. CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hakutegemea kabisa kama watu wale walikuwa wakali namna ile, Mvuvi hakuweza kujizuia majimaji mepesi yasiiloweshe suruali yake, mkojo mwembamba ulimtoka bila kupenda, mkojo mwembamba ulimtoka bila kujua. Kila mmoja aliuona mkojo ule lakini hakuna aliyeujadili. Na tangu hapo wala hakuthubutu kufungua tena mdomo wake ulioitwa mchafu kuchangia chochote. Ingawa kichwani mwake kulikuwa na swali likilojirudia mara kwa mara.

    "Hawa jamaa ni wakina nani?, na kuna nini kati yao na Mwenyekiti?" Alitamani sana kuuliza lakini wala hakuthubutu kabisa kulitoa swali lile nje ya mdomo wake mchafu, aliliacha likijiuliza ndani ya ubongo wake. Nani anayewaza kutamani kuuona utumbo wake ukitapakaa hewani.



    Sasa Binunu aliingia katika mitaa ya Kisarawe akiwa na akili timamu kabisa. Kila kitu kilichotokea huko nyuma katika maisha yake kabla ya ile ajari mbaya ya meli kilirejea kwa kasi kubwa sana katika akili yake. Kumbukumbu zake adhimu zilizokuwa zimepotea takribani mwezi mmoja sasa zilikuwa zimerejea, kasoro vitu vichache ambavyo vilikuwa vimetokea mara ya mwisho baada ya meli ya Mv Donors kuzama. Hivyo ndivyo vitu pekee ambavyo hakuvikumbuka kabisa. Hakukumbuka baada ya ajari ile mkanda ulielekea wapi?. Alijaribu kukumbuka lakini kumbukumbu zilimgomea kabisa.



    "Nakumbuka nilikaa kwenye kiti, baada ya kama ya saa moja meli ilianza kwenda mrama, kishaaaa.....yes.. lilitolewa tangazo la tahadhari, nakumbuka niliutoa mkanda baada ya tangazo lile na kuuvirigiza katika mfuko wa nailoni. Baada ya muda mfupi maji yalianza kuingia kwenye meli, nilisukumwa vibaya sana na yale maji......halafu, halafu kikatokea nini vileeeee, ah mbona nimesahau, aaah yes nimekumbuka.....nilimuona Ayoub Mbembati akiongea katika runinga....nooo sasa kwenye ile meli nilitokaje? Na mkanda utakuwa uko wapi?"



    Kwa mara ya tano sasa alijaribu kukumbuka matukio yaliyotokea baada ya yeye kuingia katika meli, lakini aliishia kukumbuka hayo tu. Saa mbili sasa zilikuwa zimepita tangu Binunu akae katika msingi wa nyumba isiyoisha karibu na soko la Kisarawe. Alikuwa amekilaza kichwa chake juu ya magoti yake. Alikuwa akijaribu kuwaza upya juu ya mustakabari wa operesheni ya mkanda wa siri.



    "Hii ni operesheni ya ajabu sana kuwahi kuifanya katika maisha yangu. Nilikodiwa na wakina Martin Hisia kufanya OMS bila kujua kuwa OMS ni Operesheni inayonihusu kwa asilimia mia moja. Niliingizwa katika operesheni ya kusaka kitu kinachonihusu kabisa lakini bila kujua. Kumbe ilikuwa ni operesheni ya kusaka kitu kilichopoteza maisha ya baba yangu mzazi. Operesheni ya kusaka kitu kilichoondoka na maisha ya mama yangu mzazi. Wazazi wangu walikufa kikatili sana kwa sababu ya mkanda tukiousaka katika OMS...Mkanda ule sijui utakuwa na nini ndani yake? Yaani Baba alikubali kufa kinyama namna ile lakini si kuuachia mkanda kwa watu wale wabaya, wenye nia mbaya bila shaka. Hivi mkanda huo utakuwa na nini lakini ndani yake?" Binunu sasa aliinua kichwa chake toka magotini na kuangalia mbele. Alikuwa anaangalia mbele lakini alikuwa haoni chochote kile. Alikuwa mbali sana kimawazo.

    "....kwa sasa nina majukumu makuu mawili tu hapa duniani. Na majukumu hayo labda nd'o sababu ya mimi kuendelea kupumua mpaka sasa. Baada ya kuyamaliza majukumu hayo bila shaka nitakuwa nimekamilisha sababu ya mimi kuletwa Duniani. Nitakuwa tayari kufa! Najua ni majukumu mazito sana lakini lazima niyatimize, na hiyo ni kwa ajili ya wazazi wangu waliotokea kuwa wema kwangu kuliko mtu yeyote yule duniani..." Katika macho ya Binunu kulikuwa na majimaji mepesi yanatiririka alipokumbuka juu ya wazazi wake, maji yalishuka kwa kutengeneza michirizi myembamba katika mashavu yake laini.



    Binunu alikuwa analia, na alikuwa analia baada ya miaka mingi sana kupita bila kulia. Hakukumbuka lini mara yake ya mwisho kulia, ingawa alikumbuka kwamba yeye alikuwa ameshawaliza watu wengi sana katika maisha yake. Na mtu wa mwisho alitoka kumliza saa mbili zilizopita.



    "....nina jukumu zito sana la kulipa kisasi kwa wote waliosababisha vifo vya wazazi wangu wapendwa, pamoja na jukumu hilo zito lakini pia nina jukumu lengine zito, jukumu la kuusaka mkanda wa siri popote pale ulipo, kwa njia yoyote ile lazima niupate ule mkanda. Yaani ni LAZIMA!..." Binunu aliwaza huku neno la mwisho akijikuta amelitamka kwa sauti kubwa. Kitu kibaya sana kwake, hakuwa na kumbukumbu kabisa kama kwa mara ya mwisho mkanda alikuwa nao yeye. Alikumbuka mambo ya zamani sana na kusahau ya hivi karibuni.



    Kule visiwani kina Malolo iliwafunukia kwamba walikuwa wamekosea. Walikuwa wameenda kwa mtu asiye sahihi. Lilikuwa ni kosa la kiufundi. Malolo alimpa ishara kwa siri Peter, ishara ile ya siri toka kwa Malolo ilisafiri kwa njia ya siri pia na kufika hadi kwa Malkia. Na wote watatu walielewana. Malkia alimuaga Ayoub akiwa na tabasamu tele usoni mwake. Alikuwa siye Malkia yule aliyemkoromea na kumtisha Mvuvi msindikizaji muda mfupi uliopita. Huyu sasa alikuwa mwanamke mrembo mwenye tabasamu la kirembo sana. Tabasamu lenye kuweza kumpumbaza mwanaume yeyote yule rijali, na kutoa hata asichoambiwa kutoa. Ayoub hakuwa hata na nguvu ya kuagana na watu wale. Ingawa aliliona tabasamu la Malkia lakini hakuwa hata na hisia za kupumbazwa na tabasamu lile ghali. Alibaki mdomo wazi huku akiwatazama tu wageni wake. Wale jamaa hawakujari. Walianza kuondoka huku Ayoub na Mvuvi msindikizaji wakiingalia migongo ya wababe wale watatu hadi ilipopotea katika upeo wa macho yao.

    Ilikuwa ni safari kuelekea Kisarawe.

    Laiti wangejua walichokuwa wanaenda kukutana nacho?



    Ayoub na yule mvuvi msindikizaji sasa walibaki wanatazamana wenyewe, wakiwa hawaamini kabisa kama wamebaki salama, hawakuwa wanaelewa lengo la watu wale kuwaacha. Ulikuwa ni kama mchezo wa kuigiza wakina Steven Marashi na Ruby. Lakini ukweli ni kwamba huu haukuwa mchezo wa kuigiza. Ulikuwa ni mchezo wa kweli, wale majamaa waliondoka huku wakiwa hawajawagusa hata kucha zao wavuvi wale wawili!



    Kisarawe..saa 05:08 P.M

    Wakina Malkia waliwasili katika mji wa Kisarawe mida ya saa kumi na moja jioni. Walikuwa wamerudi tena katika maficho yao ya muda mfupi baada ya kukikosa walichokifata huko Pemba. Malolo alikuwa ndiye katangulia mbele wakati wanaingia ndani, mle sebuleni. Nyuma yake alikuwa anafatiwa na Peter na wa mwisho wa msafara ule wa watu watatu alikuwa Malkia, mwanamke wa kipemba hatari sana!

    Alipofika tu ndani ya sebule Malolo alihisi harufu ya kifo! Harufu ya kifo cha binadamu. Haikuwa shida hata kidogo kwa Malolo kujua kwamba mle ndani kulikuwa na mwili wa binadamu, na ulikuwa unatoa harufu ya kifo. Malolo alikuwa amecheza michezo hatari mingi sana, na kukutana na harufu za vifo mara nyingi sana.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Bloody bastard.." Malolo alisema kwa sauti ndogo sana huku kwa haraka akiitoa bastola yake kiunoni ...mwanaume alikuwa tayari kwa lolote.

    Tayari kuuwa!

    Tayari kufa!

    Ingekuwa mimi au wewe tungerudi nyuma tena kwa hofu kubwa sana, lakini Malolo hakuwa mimi au wewe, yeye alisonga mbele akiwa makini zaidi huku mdomo wa bastola yake ukiwa umetangulia mbele, tayari kwa kuitungua hatari yoyote ile mbele yake.

    Peter na Malkia walisikia sauti ya Malolo ingawa ilisemwa kwa sauti ya chini sana, pia walikiona kitendo kilichofanywa na Malolo. Moja kwa moja wakajua mambo si salama ndani ya nyumba ile, mambo si shwari maskani mwao. Nao wakatoa bastola zao viunoni. Wakati Malkia alitoa bastola moja, aliyoishika imara kwa mkono wa kulia. Peter alitoa bastola mbili toka kila upande wa kiuno chake, mikono yake yote miwili sasa ilishika bastola. Peter alikuwa anangalia kushoto na kulia kila baada ya sekunde moja, sekunde hii akiangalia kushoto, sekunde inayofuata basi aliangalia kulia. Alikuwa anapiga hatua kila baada ya kuridhika kuwa kuna usalama pande zote mbili, hatua ambayo iliruhusu na Malkia nae apige hatua lakini kwa aina tofauti. Yaani Ilipendeza sana kuwangalia. Malkia yeye alikuwa amegeuka nyuma, akiiangalia hatari yoyote itokayo nyuma yao, alikuwa anarudi kinyumenyume lakini kwa tahadhari na umakini mkubwa sana. Huku kupiga kwake hatua kulifuata baada ya hatua ya Peter, ambaye nae aliruhusiwa na Malolo. Kila mmoja alikuwa anamlinda mwenzake huku akiwa anamsaka adui. Kwa mwendo wa kunyata na kwa 'style' ile ya aina yake walifika hadi sebuleni kabisa.

    Malolo ndiye alikuwa wa kwanza kumuona, alikutana uso kwa uso na uso wa Chifu huku mwili wake ukiwa umelala hovyo sakafuni karibu na meza ya runinga. Malkia alikuwa wa mwisho katika msafara ule na kumbuka kuwa alikuwa amegeuka nyuma, lakini cha kushangaza na kustaajabisha alikuwa ndiye wa kwanza kufika katika mwili usio wa uhai wa Chifu pale sakafuni.



    "Chifuuuuuu" Malkia aliita kwa nguvu huku akiutikisa mwili ule lakini Chifu hakuitika. Ataitika vipi wakati hakuwa katika ulimwengu huu? Wale wanaume wawili hawakuzubaa. Walikuwa wanatanguliza bastola zao kabla ya kugeuka kila upande wakiohisi adui anaweza kutokea, vidole vyao vya shahada vikiwa katika triga tayari kwa kuifyatua hatari. Ndani ya mioyo wao walikuwa na uchungu mkubwa sana, walikuwa na hasira kali sana, walikuwa na huzuni kuu. Lakini hawakutaka kuendeshwa na hisia kama Malkia. Ilibidi wazidhibiti hisia zao ili nao wasiingie katika mikono ya adui. Ukweli ni kwamba ilikuwa inawauma sana maana kumkuta Chifu katika hali ile ilikuwa ni habari mbaya sana kwao.



    "Chifu ameuwawa! Chifu, Chifuuu, nakuomba please usife Chifu, usife mpaka nitakapokuletea mkanda niliokuahidiiiiiiii....." Malkia alithubutu kusema kwa sauti yenye majonzi makuu, huku aliutikisa kwa nguvu mwili wa baridi tena uliokuwa mtupu wa Chifu. Ukimya ulikuwepo pale sebuleni uliharibiwa vibaya sana na kelele za majonzi za sauti ya Malkia.



    "Shiiiiiiiiii!" Malolo alimnyamazisha Malkia huku akiwa ameweka kidole chake cha shahada cha mkono wa kushoto katikati ya mdomo wake.



    "Ni hatari sana hiyo" Peter alisema kwa sauti ndogo sana. Malkia alinyamaza kulia kwa sauti, lakini hakunyamaza kulia kwa kutiririsha machozi, machozi yalimmiminika kama mtoto mdogo. Kwa mara nyingine tena Binunu alikuwa analiza mtu siku ile. Jamaa walimwangalia mwanamke yule aliyekuwa anapitia katika machungu makubwa sana lakini hakuna aliyeenda kumbembeleza, wao wenyewe walikuwa hawaijua hatma ya usalama wao mle ndani.



    "Siku nitakayokufa hakika mtazikuta maiti mbili, yangu na ya huyo atakayeniuwa, nachukia sana kifo lazima nipambane sana ili kukiepuka...Chifu hawezi kufa kizembe hata siku moja!" Chifu alishawahi kuwaambia maneno hayo wakina Malolo, na Peter aliyakumbuka pale sebuleni. Na ndipo alipopata cha kufanya, alimpa ishara Malolo, na aliielewa.

    Waliitekeleza.

    Vijana wale wawili walianza kuingia ndani ya nyumba huku wakimuacha Malkia pale sebuleni akiwa ameulalia mwili wa Chifu. Hakika lile lilikuwa PIGO MUJA'RABU kwa Malkia. Walienda kukagua sehemu moja baada ya nyingine ili kuona kama kuna maadui ndani au labda maiti ya pili kama alivyowaahidi Chifu juu ya siku atakayokufa.

    Baada ya nusu saa jamaa walikutana tena sebuleni. Wakiwa idadi ileile, watatu na mwili wa Chifu ukiwa umelala bado sakafuni ukiwa hauna uhai...huku Malkia akiwa pembeni ya mwili ule. Akiwa amekaa kitako, amenyoosha miguu yake, kaupakata ule mdoli uliokuwa unamilikiwa na Binunu, Malkia alikiwa ametoa macho akiwa anashangaa kitu kisichoonekana. Alikuwa anaongea maneno yasiyoeleweka. Amini, usiamini.....Akili ya Malkia haikuweza kustahamili uzito wa kifo cha mtu wa karibu yake sana, mtu aliyekuwa analala nae kitanda kimoja, shuka moja. Wakishirikiana kila wanachopaswa kushirikiana wanandoa. Ama kweli mapenzi ni kitu cha ajabu sana. Malkia alikuwa amestahamili maumivu mengi sana katika maisha yake, maumivu ya kuumiza sana lakini leo hii alishindwa kabisa kuvumilia maumivu ya mapenzi. Mume anauma wewe! CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ugonjwa kama aliokuwa nao Binunu leo hii ulimrudia yeye, na mdoli aupendao Binunu leo hii alikuwa anaupenda yeye. 'What goes around, comes around'

    Daah! Malkia alikuwa amechanganyikiwa katika siku ileile ambayo Binunu alikuwa amerejewa na akili pamoja na kumbukumbu zake za maisha yake ya nyuma.



    MWISHO WA MKANDA WA SIRI SEASON 1

0 comments:

Post a Comment

Blog