Search This Blog

Sunday, 22 May 2022

TAHARUKI - 4

 







    Simulizi : Taharuki

    Sehemu Ya Nne (4)

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    KUMBE wakati ule ndiyo walikuwa wakipambana na Frank Mumba, ambaye alifanikiwa kuwashinda na kutokomea gizani na gari lao, kurudi Hilton Hotel, alikopanga chumba. Hivyo basi, Wibo hakuchelewa, akatoka nje na kupanda gari lake jingine , aina ya Opel, na haraka sana akalitia moto na kuliondoa kwa kasi kuelekea katika nyumba ile iliyokuwa maficho yao ya kutesea watu wanaowahisi kuingilia mambo yao . Ni nyumba ambayo haikuwa mbali sana , ni kama kilo meta tatu hivi kutoka pale.

    Alitumia dakika kumi tu kufika hasa ukizingatia hakukuwa na usumbufu wowote wa magari barabarani. Akalipaki gari na kushuka hata bila kulifunga mlango, na kuuendea mlango wa kuingilia mle ndani, ambao ulikuwa wazi. Wibo akachomoa bastola yake na kuanza kuingia kwa tahadhari kubwa huku mtutu wa bastola ameuelekeza juu, na pia akitembea kiupande kwa kutanguliza mguu mmoja mmoja, wa kulia na wa kushoto.

    Baada ya kuufikia mlango, akachungulia kidogo mle ndani. Akawaona, Kim, Mark na Rodger, wakiwa wamekaa chini huku wakiugulia maumivu baada ya kupata kipigo kile kitakatifu. Ndipo alipoingia kwa kishindo na kushuhudia kile kilichotokea!

    “Ni nini kinachoendelea?” Wibo akawauliaza huku bastola ikiwa wai mkononi mwake!

    “Mh, ni hatari bosi!” Kim akasema huku akifuta damu mdomoni kwa kutumia kiganja cha mkono!

    “Hatari ya nini?” Wibo akaendelea kuuliza huku akiiweka bastola yake kibindoni.

    “Kumbe Frank ni mtu hatari sana !”

    “Hakika ni mpelelezi hatari!” Akaongeza Mark.

    “Ukweli amefuzu kimedani...” Rodger naye akaongeza.

    “Msiniambie kuwa amewashinda!”

    “Ndiyo hivyo bosi, ametushinda! Ukweli hatukutegemea kama ni mtu mkali namna hiyo!”

    “Yuko wapi sasa?”

    “Ametoroka!”

    “Shenzi sana , hamfai! Watu watatu mnashindwa na mtu mmoja?” Wibo akaendelea kusema kwa hasira huku akipunga ngumi yake hewani!

    “Oh, ilikuwa hatari bosi, ni kitendo cha sekunde moja tu, jamaa akawa anapepea baada ya kutusambaratisha!”

    “Kwa hivyo mna maana tuhesabu tumeshindwa? Hapana, nyanyukeni haraka tumfuatilie kule hotelini alikofikia!”

    “Sawa bosi!” Akasema Kim. CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “ Hilo ni muhimu bosi...” akaongeza Rodger.

    Mark hakusema kitu zaidi ya kuushika mdomo wake ulikuwa unavuja damu kutokana na kipigo! Kamwe hakujua kuwa kwa mara ya mwisho kipigo kile alikipata lini!

    Wote watatu, Kim, Mark na Rodger wakanyanyuka na kumfuata Wibo, ambaye alikuwa amechukia mithili ya nyati aliyejeruhiwa. Kamwe hakupenda mtu yule hatari apone, na siri ile ifichuliwe endapo atakuqwa amewataarifu polisi. Baada ya kutoka nje, ndipo walipokuta lile gari lao, aina ya Ranger Rover walililofika nalo pale, halipo sehemu walipolipaki.

    “Mh, gari liko wapi?” Kim akauliza!

    “Na gari halipo?” Wibo akauliza huku akizidi kuchanganyikiwa!

    “Halipo, tulikuwa tumelipaki hapa nje!”

    “Bila shaka ameondoka nalo yule mwanaharamu!” Rodger akasema.

    “Ama kweli ni mshenzi!”Mark akasema huku amekunja ngumi ya hasira!

    “Ok, tusipoteze muda, tuondoke, najua hatafika nalo mbali. Atalitelekeza mahali, alichotaka ni kutoroka nalo tu, hii London hawezi kutoka kirahisi!” Wibo akawaambia.

    Wote wakapanda gari la Wibo, ambaye aliliondoa kwa mwendo wa kasi kuelekea Hilton Hotel. Hata hivyo baada ya kufika karibu na hoteli ile, wakalikuta gari lile, Rangr Rover, likiwa limetelekezwa kando ya barabara, karibu na bustani ya Harde Park , umbali wa mita mia moja kutoka ilipo hoteli ile.

    “Gari hili hapa!” Wibo akawaambia.

    “Ni kweli, amelitekeza hapa...” Kim akasema.

    “Hakumna muda wa kupoteza, shukeni mpande gari hilo !” Wibo akatoa amri!

    Wote watatu wakashuka na kuingia ndani ya lile gari, Ranger Rover, na safari ikaendelea kama kawaida, hadi walipofika hotelini. Walipoingia ndani katika chumba namba 222, hawakukuta mtu, ulikuwa ni muda mfupi tu, tokea Frank Mumba na Scola walipoondoka na kuelekea katika nyumba ile ya siri, mtaa wa High Hilborn, kwa ajili ya kujificha.

    “Huyu mshenzi ametoroka!” Wibo akasema kwa hasira kali!

    “Sijui kakimbilia wapi!”

    “Bila shaka kwa mpelelezi mwenzake, Bown Lambert!” Kim akasema bila kuwa na uhakika!

    “Usiseme hivyo!” Wibo akamkatiza na kuongeza. “Hawezi kukimbilia huko, itakuwa amejichimbia sehemu nyingine!” Wibo akaendelea kusema.

    “Bosi, unaonaje tukimvamia Brown, labda tunaweza kumpata?” Rodger akasema.

    “Huwezi kumvamia Brown kirahisi, anamtandao mkubwa, ambao utatuvurugia mpango mzima tulioumaliza tayari. Sisi tunataka kumpata Frank, ambaye ndiye kuiungo kikuu cha Brown!”

    “Sawa bosi...”

    “Cha muhimu, tuondoke hapa na kuanza operesheni ya kumsaka jiji zima, mpaka apatikane!” Wibo Eze akaendelea kutoa amri. Wote wakapanda kwenye magari yao na kuanza safari ya kumsaka Frank Mumba, mpaka apatikane kabla hakujapambazuka!

    Ni hatari sana !

    *******

    Nyumbani kwa mpelelezi Brown Lambert, alikuwa amelala usingizi usiku ule, na upande wake wa pili, mke wake, Prisila Donaldson, naye akiwa ni mwanamke mrembo, mwenye asili ya Afrika vilevile, alikuwa amelala. Mara mlio wa simu yake ya mkononi iliita. Bw, Brown akashtuka kutoka usingizini. Ni simu iliyokuwa kando ya kitanda alichokuwa amelalia, ukiwa ni utaratibu wake aliozoea kuiweka pale. Akaichukua na kuangalia namba za mpigaji, ambazo aliona ni za mpelelezi, Frank Mumba, kutoka nchini Tanzania .

    “Haloo Frank…”

    “Haloo Brown…”

    “Nipe habari…”

    “Mambo mazito!”

    “Fafanua mshirika…”

    “Jamaa wameniwahi!” Frank akamwambia na kuendelea. “Nimekurupushana nao baada ya kuniteka nyara!”

    “Mh, unasema walikuteka nyara?” Bw. Brown akauliza huku akinyanyuka kutoka kitandani.

    “Ndiyo, kumbe jamaa walikuwa wananifuatilia kuanzia mwanzo nilipokuwa nakuja hapa Uingereza. Walikuwa wamemtuma mtu anifuatilie baada ya kuhisi kwamba mimi na wewe ni washirika…” Frank alimweleza matukio yote, kuanzia mwanzo hadi mwisho na jinsi Scola alivyompeleka pale kwenye maficho ya siri katika mtaa wa High Hilborn. “…Hiyo naomba uje ili tupange kinachoendelea kwani mkufu umeshafikishwa nchini Ufaransa na wakora walioupora…” Frank akamaliza kusema.

    “Sawa Frank, nimekuelewa. Ni lazima tuufuatilie mkufu huo huko Paris , hivyo wewe jiandae mimi nakupitia hapo mafichoni, ambapo nimeshapafahamu, kisha tuondoke mara moja!” Bw. Brown akamwambia kwa msisitizo! CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Unasema tunaondoka usiku huu?” Frank akamuuliza!

    “Ndiyo, tutaondoka usiku huu huu!”Brown akasema.

    “Tiketi za ndege je?”

    “Usihofu…nitapitia kukata tiketi kwenye ofisi za Wakala wa Air Frace, ambazo hufanya kazi kwa muda wa saa 24. Cha muhimu ni kukuta umeshajiandaa, unanisubiri!”

    “Sawa, nitafanya hivyo!”

    Baada ya kumaliza kuwasiliana na Frank, Bw. Brown akaelekea ndani ya bafu lilokuwa mle ndani na kujimwagia maji ili apate nguvu. Alitumia kama dakika tano tu, na alipomaliza, akavalia nguo zake maalum za kikazi, kisha akachukua zana zake za kazi, ambazo alizitia ndani ya begi lake. Halafu akamuaga mke wake Prisila kwa kumpiga busu la shavu, halafu akatoka nje haraka haraka kwa kukimbizana na muda.

    Brown akaliendea gari lake aina ya Ford Fomoco lililokuwa sehemu ya maegesho. Akapanda na kulitia moto, kisha akaliondoa kuelekea kule alipokuwa mwenzake, Frank Mumba, ndani ya maficho aliyopelekwa na mwanadada, Scola Eze. Hakika hakutegemea kama watu wale wangeweza kumtambua Frank mapema namna ile kiasi cha kutaka kumdhuru!

    Brown akaliendesha gari lile kwa mwendo wa kasi akiwa na nia ya kumuwahi Frank, kwani alikuwa na wasiwasi kuwa mtandao wa wezi wa ule mkufu wanaweza kumfuatilia Frank baada ya kujua kuwa alikuwa ametoroka mikononi mwao. Wangemsaka usiku ule mpaka wampate! Na hiyo itasababisha upelelezi wao ukwame na mkufu ule utoweke mikononi mwao! Kamwe hakupenda kitu kama kile kitokee!

    Brown akapitia kwenye ofisi ya Wakala wa Shirika la Ndege la Ufaransa, zilizoko katika mtaa wa Havard Avenue 416 A, ambazo hufanya kazi kwa muda wa saa 24. Baada ya kufika, hakupoteza muda akalipaki gari na kushuka haraka, kisha kuelekea ndani ya ofisi ya kampuni hiyo ya ndege, ambapo alikata tiketi za watu wawili, katika ndege iliyokuwa inaondoka alfajiri, kuelekea, Paris , Ufaransa.

    Baada ya kukata tiketi, Brown akaeleke garini na kuondoka kumfuata Frank, ambaye muda wote alikuwa akiwasiliana naye na kumwambia akae tayari!





    Mara baada ya kumaliza kuwasiliana na Brown, Frank Mumba alifungasha mzigo wake, ambao ni begi dogo, lakini lililokuwa na uwezo wa kubebe vitu vya kumtosha katika kazi yake.Tuseme kulikuwa na nguo na zana nyingine za upelelezi, ambazo zilikuwa zimehifadhiwa ndani ya mifuko midogo, ambayo hata wale watu waliotumwa na Wibo Eze hawakuweza kuiona baada ya kumwingilia chumbani na kupekua hilo begi lake.

    Kulikuwa na bunduki fupi aina ya ‘Uzi,’ iliyotengenezwa nchini Israel , bastola aina ya ‘Wimbley,’ visu vidogo, mikasi na mabomu ya mkono, yenye umbile dogo, lakini yaliyoweza kulete madhara makubwa punde yanapolipuka. Ni vitu ambavyo kwa mtu wa kawaida asingewezxa kuvifahamu kama siyo askari.

    Wakati Frank alipokuwa anamsubiri Brown, pia, aliona ni vyema amjulishe mwanadada, Scola Eze, juu ya safari yao ile ya kuelekea nhini Ufaransa kuufuatilia ule mkufu wa thamani. Akachukua simu yake na kupiga namba za simu yake ya mkononi ambapo alimpata Scola katika laini, lakini wakawasiliana kwa wasiwasi mkubwa!

    “Frank!” Scola akasema!

    “Sema Scola!” Frank akamwambia.

    “Hali mbaya sana !”

    “Kwa nini?”

    “Kaka Wibo, amegundua kuwa umetoroka baada ya kuwashinda nguvu watu wake. Hivyo basi, amewaamuru wakusake ndani ya jiji zima baada ya kukukosa kule hotelini!”

    “Kwa hivyo unaniambiaje sasa?”

    “Naomba usiondoke hapo mafichoni!”

    “Ah, mimi naondoka muda siyo mrefu Scola…”

    “Unakwenda wapi?”

    “Naelekea Ufaransa…hivyo tutawasiliana zaidi..”

    “Unakwenda na nani?”

    “Nakwenda na mwenzangu, ambaye yuko njiani kuja kunichukuwa!”

    “Mhimize awahi, kwani jamaa wanaendesha msako mkali…Oh!” Scola akaendelea kusema kwa msisitizo!

    “Hawatupati…”

    “Haya…safari njema…” CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alipomaliza kuwasiliana na Scola, Frank akachukuwa mzigo wake na kutoka nao nje ili kumuwahi Brown. Mara gari lile aina ya Ford Fomoco likasimamishwa nje ya geti la nyumba ile, na Frank akagundua kuwa ni mshirika wake, Brown. Akachomoka pale mafichoni akiwa na mzigo wake na kuingia ndani ya gari lile, na kabla ya kuongea chochote, akaliondoa gari kwa mwendo wa kasi kwa kuufuata mtaa ule mdogo.

    Kisha Brown akauacha mtaa ule na kuliingiza gari kwenye barabara kuu, ambayo ilikuwa na magari machache tu yaliyokuwa yanapita. Ni barabara kuu iliyokuwa inaelekea kwenye Uwanja wa Ndege wa Heathrow, jijini London .

    “Tunakwenda uwanja wa ndege,” Brown akamwambia Frank.

    “Mambo yote tayari?” Frank akamuuliza.

    “Kila kitu tayari…tiketi ninazo…”

    “Hakuna tatizo tuwahi, kwani wale ni watu hatari sana , wanaweza wakatuharibia kazi yetu na tuukose mkufu tunaoutafuta!” Frank akamwambia Brown.

    Lakini wakati wakiwa katika barabara ile kuu kuelekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Heathrow, waliona magari mawili yaliyokuwa yakiwafuata nyuma yao kwa mwendo wa kasi sana .

    “Umeona?” Brown akamuuliza Frank.

    “Ndiyo, nimeona, tuna mkia…”

    “Sasa?”

    “Dawa yao ndogo hawatuwezi!”

    Magari yaliendelea kufukuzana huku Brown naye akiongeza mwendo. Gari la kwanza aina ya Audi, lilikuwa na watu wa kazi wa Wibo Eze, ambao ni Mark, Rodger na Kim, ambao hapo mwanzo Frank alikuwa amewasambaratisha ndani ya ile nyumba ya mateso waliyokuwa wamempeleka. Hakika walikuwa na hasira sana baada ya kumuaona adui yao aliyewatoka kirahisi, na waliapa kuwa wangemkamata tu, wangemkatakata vipande vya nyama kwa kutumia msumeno! Ndiyo, ni adhabu iliyokuwa inamfaa!

    Gari la pili lilikuwa ni aina ya Opel, ambalo Wibo Eze ndiye aliyekuwa analiendesha akilifuatia nyuma lile Range Rover. Alikuwa akitaka kuona watu wale wanakamatwa mara moja na kuwafuta katika uso wa dunia kabla hawajawatibulia mipango yao Na Wibo mwenyewe ndiye aliyewazindua baada ya kuwatembelea na kuwakuta wamesambaratishwa, na mateka wao ametoroka! Basi, Wibo naye akawa sambamba nyuma yao akifuatilia mpaka pale atakapojua hatima yake!

    Mbio za kufukuzana ziliendelea hadi gari walilokuwemo Brown na Frank likafika kwenye makutano ya barabara kuu. Ni barabara moja wapo iliyokuwa inatumika kupitisha magari makubwa ya kubeba mizigo, na pia palikuwa na taa za kuongoza magari . Kwa muda ule taa nyekundu ilikuwa inawaka kwa kusimamisha magari yanayotokea upande ule magari yale yaliyokuwa yanafukuzana.

    Hata hivyo magari yale hayakuonyesha dalili zozote za kusimama, na honi ikasikia upande wa pili, ambapo lori kubwa la mizigo lilikuwa linatokea huku limewasha taa zake kuashiria hatari. Dereva wa gari kubwa akauma meno yake na kuiona ile hatari iliyokuwa inawakabili kwa kutokea kwa ajali ile mbaya, kwani hakuweza kushika breki za ghafla ukizingatia lile lilikuwa ni gari kubwa lililobebe shehena ya mizigo!

    “Brown, unaliona hilo lori?” Frank akamuuliza baada ya kuliona limewawashia taa ya hatari!

    “Ndiyo, naliona…”

    “Sasa…utaliwahi kweli?”

    “Nitapita hapohapo!” Brown akasema huku akiuma meno na kupangua gea, halafu akaongeza mafuta! Tairi zikatoa mlio mkali wa msuguano!

    Gari lao likafanikiwa kupita huku limebakiza kama mita tatu tu ligongwe na lori lile la mizigo! Na baada ya kufanikiwa kupita, Brown akaongeza mwendo na kuwakwepa wale waliokuwa wanawafukuza. Lakini kivumbi kilikuwa kule nyuma, yale magari mawili, Opel na Range Rover, yaliyokuwa yanawafukuza, yalishindwa kusimama kujibamiza katika lile lori, na kishindo kikubwa cha mvunjiko wa vioo na mpondeko wa mabati!kikatokea! Magari yakakokotwa huku yakiwa yamepondeka vibaya sana ! Watu wote waliokuwa ndani yake walibanwa na mabati na kufanya wafe papo hapo, akiwemo Wibo Eze!

    Ukweli ni kwamba wote walifia pale na kufanya kuwa ajali mbaya sana na ya kutisha. Kwani pia lile lori kubwa baada ya kuyakokota yale magari nalo liliserereka na kwenda kupinduka upande wa pili wa barabara huku likimuacha dereva akiwa amejeruhiwa vibaya, kwani kebini ya mbele yote iling’oka na kwenda kuangukia umbali wa mita tano! Muda siyo mrefu magari ya polisi na kikosi cha uokoaji yakafika huku yakipiga ving’ora na kuanza kutoa msaada.

    Ajali ile ya kutisha iliweza kushuhudiwa na wapelelezi wale, Brown na Frank, lakini hawakusimama zaidi ya kuongeza mwendo kuelekea uwanja wa ndege kuiwahi ile ndege iliyokuwa inaondoka alfajiri ile kuelekea Paris , Ufaransa.

    Hakika walikuwa wamepania!



    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ********

    Hakika ulikuwa ni usiku wa hekaheka nzito. Na Scola Eze hakuwa na raha kabisa tokea kaka yake, Wibo Eze alipoanza msako kabambe wa kumtafuta Frank Mumba, aliyekuwa amefanikiwa kuwatoroka watu wale waliokuwa wamemteka nyara na kumpeleka katika nyumba ya mateso. Ndipo alipompigia simu Frank na kumweleza juu ya kusakwa kwake, ingawa alikuwa ameshamficha katika maficho ya muda.

    Hata baadaye Frank alipojulisha kwa simu kuwa yuko mbioni kwenda uwanja wa ndege kwa safari ya kuelekea Paris , Ufaransa, Scola aliamua kumfuatilia ili kuhakikisha katika nyumba ile aliyokuwa amemwacha. Roho yake ilikuwa nzito sana akihofia maisha ya Frank, hivyo akaondoka na lile gari, Ford Munstang, na kuelekea katika nyumba ile ya maficho, ambayo hata kaka yake alikuwa haijui kama ilikuwa ya kwake, kwani aliimiliki kwa siri sana , ukizingatia naye alikuwa ni mtu wa mtandao!

    Scola alipofika katika nyumba ile, alikuta Frank Mumba ameshaondoka kitambo na kuiacha nyumba hiyo kama ilivyokuwa mwanzo. Hivyo hakupoteza muda, akaligeuza gari na kuliondoa kwa kasi kutoka ndani ya ua wa nyumba ile na kumfuatilia Frank aliyemuaga kuwa anaelekea uwanja wa ndege. Kwa muda ule alikuwa kama mtu aliyekuwa amechanganyikiwa, na alikuwa akiendesha gari lile kwa mwendo wa kasi sana kwa kuifuata barabara ile kubwa iliyokuwa na uwezo wa kupitisha magari manne pande mmoja, kwa wakati mmoja.

    Lakini kwa usiku ule magari yalikuwa machache na kumpa fursa ya kutamba barabarani. Baada ya kufika kwenye makutano ya barabara, penye taa za trafiki, ndipo Scola alipoikuta ile ajali mbaya, iliyohusisha yale magari matatu, lori kubwa la mizigo na yale magari mawili, Opel na Range Rover, yaliyokuwa yanatumiwa na kaka yake, Wibo Eze na wapambe wake, Mark, Rodger na Kim. Haraka Scola akasimamisha gari kando ya barabara na kushuka kuelekea sehemu ile ilipotokea ajali. Askari polisi na vikosi vya uokoaji walikuwa wameshafika na kuzungushia utepe wa rangi ta njano, kuzungukia eneo la ajali. Walikuwa wakiangalia uwezekano wa kuwachomoa waliokuwa ndani ya magari yale mawili.

    Scola alifanikiwa kuyaona magari hayo mawili ambayo yalikuwa yamekokotwa na lile lori na kugota kwenye ukingo wa barabara. Ndiyo, yalikuwa ni yaleyale, moja la kaka yake na wapambe wake ambao walikuwa wameachana muda siyo mrefu, wenyewe wakiapa kumsaka Frank Mumba! Hakika Scola alichanganyikiwa hasa kwa jinsi magari yale yalivyokuwa, kwani ilikuwa siyo rahisi kwa mtu yeyote kutoka hai. Yalikuwa yamepondeka vibaya kama karatasi iliyokuwa imekunjwa na haifai kutumika tena zaidi ya kutupwa jalalani.

    Wakati huo askari wa Usalama Barabarani walikuwa wakichukua maelezo ya dereva mmoja, ambaye alishuhudia ajali ile ikitokea. Alieleza jinsi magari yale yalivyokuwa yanafukuzana kwa mwendo wa kasi, ambapo gari jingine lilifanikiwa kupita na yale mengine kujibamiza ubavuni mwa lori, ingawa dereva wa lori alijaribu sana kuwapa ishara ya kupiga honi kuwa wasimame.

    Basi, Scola akabaki amesimama pale akiangalia taratibu za uokoaji. Alikuwa na masikitiko makubwa ya kumpoteza kaka yake, Wibo Eze, kwenye ajali ile mbaya. Umati wa watu waliokuwa wamejaa baada ya ajali ile kutokea hawakujua kilichokuwa kinaendelea, kwamba watu wale waliokufa kwenye ajali ile walikuwa ni watu waovu tu, waliokuwa wanafukuzana ili kutekeleza uovu wao. Lakini mwanadada Scola hakuwa na lakufanya zaidi ya kusubiri maiti itolewe na kupelekwa London General Hospital , kwa gari maalum la wagonjwa, halafu ashughulike na masuala ya msiba, ikiwa ni pamoja na kuwataarifu ndugu zao walioko nchini Nigeria .

    Hakika kinara cha uhalifu kilikuwa kimeondoka kama masikhara!

    ********

    Wakati mtafutano wa nguvu ukiendelea jijini London, nchini Uingereza, baina ya wapelelezi mahiri, Frank Mumba, Brown Lambert na wakora, Wibo Eze na kundi lake, kule nchini Angola, katika ufukwe mwanana wa Futungo de Bellas, mawimbi ya bahari yalikuwa yakipiga taratibu mchanga na mawe katika ufukwe ule, kimbilio la warembo mashuhuri kwa mapumziko ya wiki na likizo, katikati ya jiji la Luanda, Mji Mkuu wa Jamhuri ya Angola.

    Kando ya ufukwe ule, makazi ya Rais wa Angola , yanayojulikana kama Ikulu, yalikuwa yamejengwa umbali wa mita mia moja hivi kukiwa kumezungushiwa uzio madhubuti. Ni makazi ambayo yalikuwa yamefichwa na vivuli vya miti iliyopandwa kimpangilio na kufanya mandhari ya pale ipendeze sana . Na tafsiri ya jina la ufukwe ule kwa lugha ya kireno ni kimbilio la Warembo, kwa walivyoukatia watu wenye fedha, ambao huwa wanakwenda kuziteketeza kwa matumizi bila huruma!

    Kwenye mchanga pale ufukweni mwa Bahari ya Atlantiki, Bilionea wa Kireno, Miguel da Silva, alikuwa amejilaza pembeni mwa mwanadada mrembo aliyeumbwa akaumbika, aliyejulikana kwa jina la Vivian Moreno. Kilichokuwa kinaendelea pale ufukweni mwa bahari ilikuwa ni raha mustarehe. Walikuwa wanaponda raha na kusahau kama kulikuwa na kitu kinachoitwa kifo!

    Utakumbuka saa ngapi? CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Vivian Moreno, msichana chotara aliyezaliwa na mama, raia wa Angola na baba raia wa Ureno, alizaliwa na kukulia nchini Ureno kabla ya kurejea kuishi nchini Angola , na mama yake, baada ya baba yake aliyekuwa akijishughulisha na biashara za dawa za kulevya, kufungwa kifungo cha maisha nchini humo. Kiumri, Vivian alikuwa na umri wa miaka 21 na alipofika nchini Angola na kugundua kuwa alikuwa mrembo wa nguvu, aliamua kuutumia urembo wake ili kuhakikisha yeye na mama yake wanaishi katika hali nzuri bila shida.

    Ndipo Vivian alipojikuta akimnasa, bilionea, Miguel da Silver, mtu mzima mwenye umri wa miaka 54. Ni usiku wa jana yake ndipo Miguel alipokea simu kutoka Paris , nchini Ufaransa, ikimtaarifu kuwa Edmond Balle na Hamis Kangwe walikuwa wameifanikisha ile kazi ile kazi waliyokuwa wamepewa, ya kuupora mkufu wa almasi, uliokuwa ndani ya kasri ya Malkia, ambao yeye Miguel alikuwa anausaka kwa udi na uvumba, na kwa kutumia gharama yoyote. Hakika ilikuwa ni furaha ilioje kwa upande wa bilionea yule, kwani kwa kiasi fulani aliona kuwa mambo yake ni lazima yatanyiooka kama alivyopanga!

    Pia, aliambiwa kuwa vijana wale walikuwa wameshaufikisha mkufu ule jijini Paris, na kuukabidhi kwa haramia la kimataifa, aliyewahi kuitikisa Paris na Kinshasa, Mokili wa Ngenge! Na sasa kilichokuwa kinasubiriwa, ni yeye kwenda nchini Ufaransa na kukabidhiana mkufu ule baada ya yeye kukabidhi kitita cha fedha kwa upatikanaji wake. Miguel alijiamini sana, na fedha alikuwa nazo, kwani ni mtu aliyekuwa anamiliki migodi ya almasi, hivyo fedha hazikuwa tatizo kwake!

    Ufukweni, Futungo de Bellas, Miguel alikuwa amepumzika na kimwana Vivian akijipongeza kwa ushindi ambao utamfanya awe bilionea mara dufu pindi akiutia mkufu huo mikononi mwake. Wakati huo, Vivian alikuwa amevalia nguo za kuogea, chupi aina ya bikini na sidiria, ambavyo vyote viliwezesha kuyaonyesha maumbile yake kwa ujumla. Ni umbile lililowasumbua wanaume wengi wakware. Wote wawili walikuwa wamelala kwenye vitanda vile vya ufukweni huku wakitomasana kimahaba.

    “Vivian mpenzi…” Miguel akaita kwa sauti ndogo kama iliyotokea tumboni.

    “Mpenzi wangu…” Vivian akaitikia huku akimwangalia kimahaba.

    “Napenda kukuambia jambo.”

    “Jambo gani?”

    “Nakujulisha kwamba kesho ninakwenda safari…”

    “Safari ya wapi?”

    “Ninakwenda Paris, Ufaransa.”

    “Oh, vizuri sana,” Vivian akasema na kuendelea. “Nakutakia safari njema, na ufike salama.”

    “Nashukuru sana mpenzi, sijui nikuletee zawadi gani?”

    “Chochote utakachopenda mpenzi…”

    “Chochote tu, hakina jina?”

    “Utakachoona kinakupendeza, hata mimi kitanipendeza mpenzi...”

    “Ok, basi nitakuletea unachopendelea mpenzi, ambacho nakijua.”

    “Nitashukuru sana.”

    Miguel na Vivian waliendelea kukaa pale ufukweni huku wakipunga upepo hadi walipotosheka. Ndipo walipoondoka kwa kutumia gari lao la kifahari, aina ya Hammer la rangi nyeusi, walilofika nalo pale, na kuelekea katika maskani yao, yaliyoko eneo la uzunguni, jijini Luanda, ambako palikuwa na jumba la kifahari la bilionea yule. Pia, ni eneo maarufu ambalo hukaa watu wenye uwezo mkubwa wa kifedha, ambalo lilizungukwa na mandhari ya kupendeza iliyozungukwa na miti ya kila aina.



    Eneo zima la makazi ya Miguel, lilikuwa na ukubwa wa ekari zipatazo ishirini hivi, kukiwa na hilo jumba na vitu vingingine kama , mabwawa ya ya kuogelea, farasi na wanyama wengine wadogo wadogo. Akiwa ni mtu mwenye fedha nyingi, Miguel alikuwa akimiliki ndege yake binafsi aina ya Folkker Jet Engine, iliyokuwa maalum kwa familia yake tu. Ilikuwa imetengenezwa kwa mfano wa nyumba kwa ndani, kwani iligawanywa katika sehemu mbalimbali, kama chumba cha kulala chenye kitanda kikubwa, sebule iliyokuwa na makochi. Meza, jokofu dogo, runinga, simu na huduma nyinginezo. Chumba kingine kilikuwa ni cha marubani waliokuwa wanairusha ndege ile, ambao walikuwa wanajitegemea peke yao .

    Ndege ile ya gharama kubwa, Miguel aliinunua ili kujidhihirishia utajiri wake, kutoka nchini Marekeni, na ambayo pia ilikuwa inamilikiwa na watu wachache sana , kwani gharama zake zilikuswa kubwa sana . Na ilikuwa inarushwa na marubani wawili, raia wa Afrika ya kusini, wenye asili ya kikaburu. Basi, ndege hiyo ndiyo aliyotegemea kusafiri nayo kwenda Ufaransa, kukutana na Mokili wa Ngenge, ili wakabidhiane ule mkufu wa thamani ulioporwa katika kasri ya Malkia, nchini Uingereza!

    Baada ya kufika tu, Miguel na Vivian waliingia ndani na kuoga tena upya kuyaondoa yale maji ya bahari waliyokuwa wameyaoga mwanzoni kule ufukweni. Walipomaliza wakaendelea na ratiba nyingine, ikiwemo ya Miguel kujiandaa kwa ajili ya safari ile ya kwenda Ufaransa…

    ********

    Baada ya mbio za kufukuzana na hatimaye msafara wa akina Wibo Eze kupata ile ajali mbaya, Brown lambert na Frank Mumba walifanikiwa kufika kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Heathrow, jijini London . Baada ya kufika, Brown alikwenda kulihifadhi gari lake sehemu yenye usalama, ambapo angelikuta punde atakaporudi. Na huo ni utaratibu aliokuwa anautumua Brown mara nyingi sana wanapokuwa katika hekaheka zile, kwani hakutaka adui zake wampate.

    Kisha Brown na Frank, wakaelekea sehemu ya kusubiria abiria, ambapo walifanya taratibu zote na kuingia ndani ya ndege. Hawakupata usumbufu wowote, kwani vitambulisho vyao vilionyesha kuwa walikuwa ni wapelelezi wa kimataifa waliokuwa kazini. Walipomaliza kuingia ndani ya ndege, basi mioyo yao ikatulia baada ya kuona azma yao imefanikiwa kwa kuponea kushambuliwa na wale watu waliokuwa wanawafukuza kwa magari mawili! CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ilipotimu saa moja na dakika kumi za asubuhi, ndege ile kubwa aina ya Boeing 747 ya Shirika la Ndege la Ufaransa, iliruka kutoka pale kuelekea, Paris , Ufaransa. Ukweli ni kwamba ilikuwa ni lazima Brown na Frank Mumba waupate ule mkufu wa thamani uliokuwa mikononi mwa maharamia. Na safari ile ya kwenda Ufaransa ilikuwa ni ya kuchosha, lakini wapelelezi wale hawakujali sana zaidi ya kutaka kuikamilisha kazi ile ya aina yake inayofanywa na wapelelezi wengi wanaowania ile zawadi nono iliyoahidiwa na malkia!

    Baada ya saa kadhaa za kuelea angani ndege ile ilitua salama kwenye Uwanja wa Ndege wa Charles de Gaulle, jijini Paris . Baada ya kuegeshwa katika sehemu yake, abiria wote wakashuka na kuelekea katika sehemu ya ukaguzi, isipokuwa wapelelezi, Brown Lambert na Frank Mumba, ambao walipitia katika sehemu maalum ya wageni mashuhuri, kwa sababu walikuwa na vibali vya kumiliki silaha wakiwa kazini.

    Lakini wakati Brown na Frank wakiwa katika eneo lile la ‘VIP’ waliweza kuiona ile ndege ya kifahari aina ya Folkker Jet Engine, iliyokuwa imetua, na ilikuwa inaelekea sehemu ile waliyokuwa wao, halafu ikapaki. Ndege ile ilikuwa ni kivutio kwa upande wao, kwa sababu ilikuwa na namba za usajili wa nchi ya Angola . Hivyo basi hawakuondoka pale hadi ndege ile ilipopaki, wakabaki wakiangalia kilichokuwa kinaendelea ukizingatia wao walikuwa ni wapelelezi, hiyo ni lazima kila wanachokitilia mashaka wakichunguze.

    Kutoka upande wa Mapokezi, alitokea mtu mmoja aliyekuwa ameshiba, akionekana ni mtu aliyekuwa na fedha. Mtu yule alikuwa amevalia mavazi ya kiutamaduni yaliyoshonwa kwa kitenge cha waksi na kumfanya apendeze sana . Halafu akaiendea ile ndege kwa mwendo wa madaha. Mtu yule alikuwa ni Mokili wa Ngenge, aliyekuwa amekwenda kumpokea bilionea Miguel da Silver, aliyewasili na ndege ile. Mlango ukafunguliwa na Miguel akashuka chini na kwenda kukutana na Mokili Ngenge. Na yeye alikuwa amevalia mavazi ya gharama, suti nyeusi, ya vipande vitatu.

    Baada ya kufikiana, wakakumbatiana kwa muda, halafu Mokili akamchukua Miguel na kumuongoza hadi sehemu ile lilipokuwa limepaki gari lake la kifahari aina ya Mercedes Benz lenye milango sita. Wakapanda na kuondoka katika eneo lile la uwanja, huku nyuma wakifuatiliwa na gari moja aina ya Chevrolet, iliyokuwa imewabeba walinzi wa Mokili wa Ngenge. Hakika alikuwa ni mmoja wa watu mashuhuri sana jijini Paris .

    Frank Mumba na Brown walishuhudia yote yaliyokuwa yakitendeka, hivyo wakajua kuwa Miguel alikuwa amefika pale kwa ajili ya kukabidhiwa ule mkufu wa thamani na Mokili. Hata hivyo hawakuwa na sababu yoyopte ya kuwafuatilia, kwani kama walivyokuwa wamelekezwea nyumbani kwa Mokili, mtaa wa Mtakatifu Dennis, ambao ni maarufu sana jijini Paris . Wakionekana kama abiria wa kawaida tu, walikodi teksi na mkumwambia dereva awapeleke sehemu ambayo Brown alikuwa anafikia mara kwa mara afikapo Paris .

    Ni katika nyumba moja iliyokuwa katika makazi ya watu wa kipato cha chini, ambayo ilikuwa imezungukwa na uzio pamoja na miti mingi iliyofanya ijifiche, au tuseme hakuna mtu aliyeifuatilia. Upande wa mbele palikuwa na geti kubwa la chuma kama zilivyokuwa nyumba nyinine. Baada ya kufika, wakaingia ndani ya nyumba ile ambayo haikuwa na watu kwa muda ule. Hawakupoteza muda, Frank na Brown wakaanza kuandaa silaha zao za kazi pamoja na kuvalia nguo nyingine na hata sura za bandia zilizowafanya wabadilike sana tofauti na zilivyokuwa mwanzo

    Walipokuwa tayari, Brown na Frank wakatoka katika eneo hilo bila kushtukiwa na mtu yeyote, halafu wakakodi teksi, iliyowapeleka kwenye kampuni ya magari ya kukodi, ambayo mtumiaji huwa analioendesha mwenyewe. Nia yao ilikuwa ni kupata gari zuri la kuweza kukabiliana katika hekeheka ile!

    ********

    Wakati huohuo, upande mwingine, ndani ya nyumba moja chakavu iliyoko kwenye mtaa mdogo ulioko ndani ya jiji la Paris , kulikuwa na kikao cha watu watano waliokuwa wakipanga mikakati yao ya kazi iliyokuwa inawakabili. Nyumba ile ambayo ilikuwa haina wakaazi, ni moja ya nyumba ambazo zilitakiwa kuvunjwa na kujengwa nyumba nyingine za kisasa, hivyo watu wale waliona kama ni kichaka cha kupangia mambo yao maovu, ili kuukwepa mkono wa dola!

    Watu wale, walikuwa ni vijana wa kizungu, Giovan, ambaye ndiye kiongozi, Goppa, Chriss, Papadou na Dimitros. Walikuatana pale baada ya kuitwa na kiongozi wao, ambaye alikuwa ameamua kuifanyia kazi taarifa ile ya kuibwa kwa mkufu ule wa thamani. Lakini yeye aliamua kwamba, waupate kwa staili ya aina yake, ambayo ni ya kutumia nguvu kuuchukua mikononi mwa walioupora kule Uingereza, kwani mpango ule naye alikuwa anauelewa ingawa ni kwa juu juu, kutoka kwa wapambe wa Mokili wa Ngenge!

    Vijana wote wanne, walikuwa wamekaa makini na kuyafungua masikio yao kumsuikiliza kiongozi wao, Giovan, aliyekuwa anawapa maelekezo ya kazi hiyo iliyokuwa inawakabili. Ni kazi nzito ya kuhakikisha mkufu ule wa thamani unapatikana kwa gharama yoyote! Ilikuwa ni kujitoa mhanga na kuuchukua kutoka mikonononi mwa watu washenzi, ambao pia hawakupenda uchukuliwe kibwege!

    Giovann alikohoa kidogo na kusafisha koo lake, halafu akawaambia kwa sauti ndogo lakini kavu, “Jamani, tumekutana hapa tena, ili kupanga mkakati wetu wa mwisho…”

    “Ndiyo mkuu…” wote wakaitikia. CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Habari tulizozipata ni kuwa, mkufu ule umeshaletwa hapa Paris , baada ya kuibwa kule Uingereza. Na umeletwa na vijana wa tajiri, Mokili wa Ngenge, ambaye ameuchimbia ndani ya jumba lake linalolindwa na ulinzi mkali…” akanyamaza kidogo huku akiendelea kuwaangalia.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog