Search This Blog

Sunday, 22 May 2022

FUTA MACHOZI MPENZI - 1

 





    IMEANDIKWA NA : NYEMO CHILONGANI



    *********************************************************************************



    Simulizi : Futa Machozi Mpenzi

    Sehemu Ya  Kwanza (1)



    “Unafanya nini hapo binti?” ilisikika sauti ya mwanaume mmoja kutoka katika gari la kifahari, lilikuwa Range Rover SUV ya rangi ya kijivu yenye gharama zaidi ya milioni mia moja.

    “Nasubiri usafiri!” alijibu msichana huyo aliyeulizwa swali, sauti yake ilikuwa nyororo mno, alivaa sketi fupi na laini iliyoyaacha mapaja yake wazi kwa asilimia kubwa.

    “Unauza tuongee biashara?” aliuliza mwanaume huyo.

    “Nani? Mimi? Hapana! Nimetoka kwenye pati,” alijibu msichana huyo huku akionekana kushtuka, hakuamini kama angeulizwa swali kama hilo, ila hakukasirika kwani mavazi yake yalionyesha kama msichana aliyekuwa akijiuza.

    “Sawa. Unaishi wapi?”

    “Manzese Midizini!”

    “Naweza kukusaidia kukupa lifti?”

    “Mmh! Hapana baba! Wewe endelea na safari yako,” alisema msichana huyo huku akionekana kuwa na hofu kubwa.

    “Wala usijali! Mimi si mtu mbaya, ni mtu mwema, si unaona natembea na Biblia, wala usihofu,” alisema mwanaume huyo huku akiitoa Biblia na kumuonyeshea msichana huyo ambaye kidogo akaonekana kuwa huru.

    Msichana huyo alikuwa amesubiri usafiri kwa kipindi kirefu hapo barabarani, alihitaji lifti na usiku huo alikuwa akitoka katika sherehe ya kuzaliwa ya rafiki yake aliyeitwa Zaituni. Huko, hakuwa na raha, kila mwanaume alikuwa akimwangalia yeye, alivalia nguo nyepesi ambayo iliyafanya maungo yake kuonekana vizuri kabisa.

    Alikosa amani, hata alipokuwa akitembea, macho yake yalikuwa huku na kule, aliogopa, hakuwa na amani kabisa mpaka alipoamua kuondoka katika sherehe hiyo. Aliondoka kisiri, hakutaka mwanaume yeyote yule amuone kwani aliogopa kufuatiliwa, hilo akafanikiwa na kufika mpaka barabarani.

    Hakujua ni kwa namna gani angeweza kurudi nyumbani kwao, hakuwa na fedha, hakuwa na usafiri wowote ule, aliogopa na pale alipokuwa moyo wake ulikuwa na hofu ya kubakwa, alihisi muda wowote ule wanaume wangetokea na kumbaka.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kwa sababu Kinondoni ilikuwa sehemu moja iliyokuwa na machangudoa wengi, walipomuona, walihisi kwamba alikuwa mwenzao hivyo hawakutaka kujali sana. Akaondoka mpaka alipofika barabarani, alijitenga na kusimama pembeni kabisa, tena akiwa peke yake.

    Watu waliokuwa wakipita na magari, waliyasimamisha na kushusha vioo, walimwangalia msichana huyo kwa macho yaliyojaa matamanio, walitamani kumpandisha ndani ya gari na kuondoka naye lakini maneno yao yote yalionyesha kuwa walitaka kulinunua penzi lake kwani kwa jinsi alivyoonekana, alikuwa na mvuto wa ajabu.

    “Twende binti! Nina laki moja hapa, haina matumizi yoyote yale,” alisema jamaa mmoja aliyekuwa ndani ya gari yake.

    “Hapana! Wewe nenda tu!”

    “Jamaniiiiiii!”

    “Nimesema nenda tu kaka yangu,” alisema msichana huyo.

    Alikaa hapo mpaka ilipofika saa nane usiku. Mwili wake ulikuwa ukitetemeka, mbali na baridi alilokuwa akilihisi lakini bado hofu kubwa iliutawala moyo wake na kumfanya kutokwa na kijasho chembamba kwa mbali.

    Alimuomba Mungu usiku huo uwe na amani kwani pale aliposimama, hakukuwa na mtu yeyote aliyekuwa akipita, ni magari tu ndiyo yaliyokuwa yakimpita na mengine kumpigia honi mpaka alipokuja huyo mzee ambaye akamchukua na kuondoka naye.

    “Unaitwa nani binti?” aliuliza mzee huyo kwa sauti ya utaratibu.

    “Pamela Ndanshau!”

    “Ooh! Sawa. Mimi naitwa Edward,” alijitambulisha mzee huyo.

    “Sawa. Nimefurahi kukufahamu baba!”

    “Mimi si mkubwa, ni kijana tu Pamela, unaweza kuniita rafiki au mshikaji wa mjini,” alisema mzee huyo huku akiachia tabasamu, japokuwa kichwa chake kilikuwa na mvi nyingi lakini aliukataa ukubwa, kwake, alijiona kuwa kijana wa miaka ishirini.

    Walikuwa wakizungumza mengi, mzee Edward alikuwa mchangamfu, kila wakati yeye ndiye aliyekuwa akitawala mazungumzo ya humo garini. Moyo wake ulifurahi mno, kitendo cha kukutana na msichana mrembo kama alivyokuwa Pamela, kwake ilikuwa ni bahati kubwa.

    Pamoja na kuongeea kwa uchangamfu, bado macho yake hayakutulia, kila wakati alikuwa akiangalia mapaja ya msichana huyo, yalinona, yalimtamanisha mno, kila alipomwangalia pepo la ngono lilimuingia na kumtoka, likamuingia tena na kumtoka.

    “Mmh! Anatamanisha! Mtoto amenona sana! Hivi kwa nini nilizaliwa zamani? Nilitakiwa kipindi kama hiki kuwa kijana,” alijisemea Mzee Edward huku akiendelea kuyaangalia mapaja ya Pamela kisiri.

    Pamela hakuwa na amani, kichwa chake kilikuwa na mawazo, japokuwa mzee huyo alijifanya kuwa mcha Mungu kwa kumuonyeshea Biblia lakini bado hakuwa na amani, alimwangalia, macho yake yalionyesha tamaa kubwa, wakati mwingine alitamani kuteremka na kutembea lakini ilishindikana kabisa.

    Mzee Edward hakuongea naye mambo ya mapenzi, alimuonyeshea wema mkubwa wa kumsaidia kwani pale alipokuwa amesimama, haikuwa sehemu salama, moyo wake ulimwambia ni lazima amsaidie msichana huyo mrembo.

    Hawakuchukua muda mwingi wakafika Manzese Midizini, mzee huyo akasimamisha gari mbele ya nyumba moja iliyoonekana kawaida sana, hakukuwa na mtu, kulikuwa na ukimya mkubwa mahali hapo, Pamela akamshukuru Mzee Edward na kisha kuufungua mlango wa gari kwa ajili ya kuteremka.

    “Pamela...” aliita mzee huyo, Pamela akamgeukia.

    “Abeee...”

    “U msichana mzuri sana, hukutakiwa kuwa mahali pale, tena kwa wakati kama huu, unaishi na nani hapa?” aliuliza mzee huyo.

    “Mama na mdogo wangu!”

    “Sawa. Nitakuja kukuona kesho! Una simu?”

    “Ndiyo!”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Naruhusiwa kuwa na namba yako?”

    Kabla ya kujibu chochote, Pamela akanyamaza na kuangalia chini, alionekana kuwa na hofu. Mzee huyo hakuonekana kama alikuwa mtu mbaya na ndiyo maana tangu alipomsaidia mpaka wanafika hapo, hakumwambia neno lolote la kimapenzi, alimsaidia kama mtu aliyekuwa akihitaji msaada mkubwa.

    Hakuona kama ulikuwa uungwana wa kumnyima namba mzee huyo kwani bila wema wake, inawezekana bado angeendelea kuwa kule barabarani akisubiri lifti kutoka kwa watu wengine, je, ingekuwaje kama angepewa lifti na mwanaume ambaye angemtaka kimapenzi kinguvu?

    “Hii hapa! Andika,” alisema Pamela na kisha kumtajia namba ya simu Mzee Edward, alipoiandika, akachukua bahasha na kumpa Pamela, kwa jinsi bahasha ile ilivyoonekana, ilionyesha ndani kulikuwa na kitu, hakujua kulikuwa na nini ila akahisi kwamba zilikuwa pesa, alipoipokea, akateremka.

    Mzee Edward hakutaka kuondoka mahali hapo mpaka pale ambapo angehakikisha Pamela ameingia ndani. Alibaki mahali hapo, Pamela akaanza kugonga mlango, baada ya dakika chache, kijana mmoja akaufungua mlango na kuingia ndani.

    “Bye...” alisema Mzee Edward kwa sauti, Pamela hakuitikia zaidi ya kumpungia mkono kumuaga. Mzee Edward akawasha gari na kuondoka zake huku akionekana kuwa mwenye furaha tele kukutana na msichana huyo.





    “Pamela! Upo wapi?” ilisikika sauti ya mwanaume kwenye simu, haikuwa sauti ya kawaida, ilikuwa ni sauti ya ukali.

    “Nyumbani baby!” alijibu Pamela kwa sauti ya upole.

    “Jana ulikuwa wapi?”

    “Nilikwenda kwa rafiki yangu Zaituni, si nilikwambia kama kuna sherehe ya siku yake ya kuzaliwa,” alijibu Pamela kwa sauti ya upole kabisa.

    “Wewe mwanamke malaya sana. Mbona hukuniambia wakati unarudi? Au ulipitia kwa mabwana zako? Yaani wewe kila siku umalaya tu, hivi unaona sifa kuwa malaya kukitembeza kwa kila mtu?” aliuliza jamaa huyo kwa sauti ya ukali, alikasirika mno.

    “Hapana mpenzi laki...” alisema Pamela lakini hata kabla hajamaliza sentensi yake, jamaa huyo akakata simu.

    Moyo wake ulinyong’onyea, aliumia moyoni mwake, mwanaume aliyekuwa amempigia simu aliitwa Dickson. Huyo alikuwa mwanaume wake wa kwanza, hakuwahi kubadilisha mwanaume yeyote zaidi ya huyo.

    Alimpenda sana Dickson, walikaa kwenye uhusiano kwa miaka zaidi ya mitano huku mwanaume huyo akiwa kila kitu kwake. Walipeana ahadi nyingi kwamba wangeona na kujenga familia pamoja, maneno hayo yalimchanganya Pamela na kuamua kumpa moyo wake Dickson.

    Baada ya kukaa kwenye mahusiano kwa kipindi fulani, Pamela akapata ujauzito kitu ambacho hakumficha Dickson, akamwambia ukweli lakini tofauti na mategemeo yake, Dickson akamwambia kwamba ule ujauzito haukuwa wake, hivyo hakuutambua.

    Pamela alihuzunika, hakuwa na mwanaume mwingine zaidi ya huyo, hakuwahi kumvulia nguo mwanaume yeyote na kufanya naye mapenzi, mwanaume ambaye aliwahi kumfanyia hivyo alikuwa Dickson tu na ndiye aliyempa mimba lakini mwisho wa siku mwanaume huyohuyo alimwambia kwamba mimba haikuwa yake.

    Dickson akakaa na kujifikiria, akaona kwamba kwa kadiri muda unavyokwenda, mimba ile ingeongezeka na yeye hakuwa tayari kuzaa na Pamela, alichomwambia ni kutoa mimba ile.

    “Nitakufa...” alisema Pamela.

    “Hutoweza kufa! Wewe toa tu!”

    “Sina hela, wewe mwenyewe si unajua tulivyo masikini!” alisema Pamela.

    “Nitakupa hela.”

    “Basi sawa!”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/-

    Wakakubaliana, baada ya siku mbili, tayari Dickson akapata kiasi cha fedha kilichohitajika na hatimaye mimba kutolewa. Hilo ndilo alilolitaka, hakumjali sana Pamela, kwake alikuwa mwanamke wa starehe, mapenzi yalikwisha moyoni mwake na kitu pekee kilichokuwa kimebaki ni mazoea tu.

    Wakati yeye akichukulia mazoea katika mapenzi hayo, kwa Pamela ilikuwa balaa, moyo wake ulikufa na kuoza kwa Dickson, usiku hakulala vizuri, alichanganyikiwa kwa penzi lake na muda wote alikuwa akimuhitaji lakini mwanaume huyo hakujali.

    Hakuwa anapokea simu, aliwasiliana na Pamela siku ambayo alihitaji kufanya hivyo. Mawazo yalimuendesha, mwili wake ukapungua kiasi kwamba kila mtu alimshangaa.

    Siku ambazo Dickson alipojisikia kufanya mapenzi, aliwatafuta wanawake wake wengine, walipomwambia kwamba walikuwa kwenye siku zao, akamtafuta Pamela ambaye hakuwa na kinyongo, alimpenda sana Dickson hivyo kama kawaida akaitanua miguu yake tena.

    Hayo ndiyo yalikuwa maisha yake, yalimuumiza lakini hakuwa na jinsi, alitamani kuendelea kuwa na mwanaume huyo kwa sababu alimpenda kwa moyo wa dhati. Siku zikakatika mpaka alipopata mimba ya pili.

    Alishangaa, hakujua iliingiaje na wakati alikuwa akitumia mpira, hakujua kama wakati wa kufanya mchezo huo, katikati Dickson alikuwa akiutoa mpira na kufanya bila mpira. Akili yake ilichanganyikiwa mno, hakujua ni kitu gani alitakiwa kufanya, alimwambia Dickson ambaye naye alibaki akishangaa tu, hakutaka kukubali kama hiyo ilikuwa mimba yake.

    “Haiwezekani! Hii ni mara ya pili, utakuwa na mwanaume mwingine,” alisema Dickson huku akionekana kuchukia.

    Hiyo mimba nayo ikatolewa, mwili wake ulichoka hata kabla hakuwa mke wa mtu. Huo ndiyo ukawa mwisho wa kuwa na Dickson, moyo wake ulimuuma lakini hakuwa na jinsi kwani alimpenda kupita kawaida.

    Aliendelea kukaa nyumbani, baada ya mwaka mmoja, Dickson akamrudia tena, akamuomba msamaha, ilikuwa vigumu kwa msichana huyo kukubali lakini mwisho wa siku akaamua kumsamehe kwa sababu alimpenda, hivyo mapenzi kuanza tena.

    Mpaka anakutana na mzee Edward, ilikuwa imepita wiki moja tangu kurudiana na Dickson, hakuwa na mapenzi makubwa kwa Dickson lakini alishindwa kumuacha kwa sababu tu alihisi moyo wake ukimpenda mno.

    “Nilijua tu wewe malaya! Ulikwenda kutembea na mabwana zako huko halafu unamsingizia Zaituni,” alisema Dickson kwenye simu.

    “Nisamehe mpenzi...”

    “Hebu toka huko! Nisamehe inasaidia nini,” alisema Dickson na kukata simu.

    Japokuwa mapenzi yalikuwa ni furaha lakini kwa Pamela yalikuwa ni sawa na kuishi kwenye tanuru la moto. Hakukuwa na siku ambayo aliyafurahia mapenzi aliyokuwa nayo kwa Dickson, kila siku alijiona akipitia katika maumivu makubwa lakini bado msimamo wake ulikuwa ni kumshikilia huyo Dickson ambaye hakuonekana kujali chochote kile.

    Tangu alipomlalamikia na kukata simu, Dickson hakutaka kupiga tena, kwake, alijua kwamba Pamela hakuwa akipindua, hata kama angemkuta amelala na wanawake, bado msichana huyo angemsamehe na kufanya kile alichokitaka.

    Mapenzi mazito ya Pamela yakawa kama fimbo ya kumchapia, hakujua msichana huyo alijisikiaje, hakujua ni kwa jinsi gani aliumia moyoni mwake, kitu alichokijali ni kwamba alipotaka penzi alipewa bila kinyongo chochote kile.

    Wakati yeye akiringa, wakati akimuona Pamela hakuwa na thamani yoyote ile ndicho kipindi ambacho Mzee Edward akaingia kwa nguvu zote. Mzee huyo akatokea kumpenda Pamela, kwake alionekana kuwa msichana wa tofauti, mwenye uzuri wa ajabu ambao uliutikisa mtima wa moyo wake.

    Baada ya kupewa namba ya simu, siku iliyofuata akampigia simu Pamela na kuzungumza naye. Hakutaka kumficha, alimwambia kwamba alimpenda na alitaka kumfanya mwanamke mwenye furaha kuliko wanawake wote aliowahi kuwa nao.

    “Na mkeo je?” aliuliza Pamela.

    “Mke wangu anaumwa sana Pamela. Sidhani kama atapona,” alijibu mzee huyo.

    “Mmh! Sasa si ndiyo muda wa kumfariji!”

    “Pamela! Siwezi kukuficha kitu chochote. Ninampenda sana mke wangu, nimekuwa naye tangu nilipokuwa masikini mpaka leo hii! Ninamthamini zaidi ya mtu yeyote katika dunia hii. Kila siku nimekuwa nikimlaumu Mungu kwa kumlaza mke wangu kitandani kwa mwaka mmoja na nusu. Kila nikimwangalia, nahisi atakufa, ninaumia kwa mawazo na ndiyo maana niliamua kutafuta msichana ambaye ataniondolea mawazo, ikitokea mke wangu akafa, basi nimuoe yeye,” alisema mzee huyo, wakati akiyazungumza hayo, sauti yake ilitoka na kwikwi kuonyesha kwamba aliumizwa na kilichokuwa kikiendelea.

    “Pole sana mshikaji wangu,” alisema Pamela, jina hilo likamfurahisha mzee huyo, akaachia tabasamu pana.

    “Nashukuru sana! Naomba nikuone leo,” alisema mzee huyo.

    “Leo?”

    “Ndiyo!”

    “Mmh!”

    “Kuna nini? Mbona unaguna jamani?

    “Nitakwambia! Ngoja nicheki ratiba yangu,” alisema Pamela.

    “Sawa. Nakupenda Pamela!”

    “Ahsante!” alisema msichana huyo na kukata simu



    Moyo wake uliumizwa vya kutosha, ulijeruhiwa mno, ulikosa amani na kila siku ulikuwa ukipitia katika maumivu makali. Alichoka, alilia usiku na mchana na ndiyo maana mzee Edward alipomwambia kwamba alikuwa tayari kumpa furaha akahisi kitu cha tofauti ndani ya moyo wake.

    Hakuhitaji mapenzi, kitu alichokihitaji ni furaha tu, hakutaka fedha, hakutaka mali, kitu ambacho alikihitaji kuliko kitu chochote ni furaha ambayo Dickson alishindwa kumpatia kwa kipindi kirefu.

    Baada ya kujifikiria kwa saa kadhaa, akamwambia mzee huyo kwamba alikuwa tayari kwenda naye sehemu kama alivyoomba kitu kilichomfurahisha mzee huyo na hivyo baada ya saa mbili, wakaonana.

    Pamela akakutana na mzee huyo katika mgahawa wa Jumanji uliokuwa Msasani, hapo walizungumza sana, kwa jinsi alivyoonekana Pamela hakuwa na furaha, hilo lilimfanya mzee Edward kukosa amani na hivyo kumuuliza sababu ya kuwa hivyo.

    Pamela hakuficha, alimwambia ukweli kile kilichokuwa kimetokea, alimwambia jinsi moyo wake ulivyokuwa na majeraha kutokana na yale aliyokuwa akifanyiwa na mpenzi wake. Maneno hayo yalimpa uhakika mzee huyo kwamba angemchukua Pamela kwani alimuahidi kitu ambacho alikihitaji kila siku katika maisha yake, FURAHA.

    “Unampenda?” aliuliza mzee huyo.

    “Ukweli wa moyo wangu unampenda ila sihitaji kuwa naye na sijui nitamtoa vipi moyoni mwangu,” alisema Pamela huku akionekana kuwa na huzuni mno.

    “Huwezi kumtoa kama hutomuingiza mtu mwingine. Ili huyo atoke, ni lazima mwingine aingie kwani ndani ya moyo hakuwezi kukaa watu wawili,” alisema mzee huyo.

    “Najua hilo!”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Naomba niwe nawe. Nakuahidi huyo kiumbe atatoka na tutakuwa mimi na wewe, wewe na mimi,” alisema mzee huyo.

    Walizungumza mambo mengi, kwa sababu msichana huyo alihitaji sana furaha katika kipindi hicho, akakubali kuwa na Mzee Edward na hivyo uhusiano mpya kuanza. Kama alivyosema mzee huyo ndivyo alivyofanya, alimpenda sana Pamela na kila wakati alikuwa akiwasiliana naye na kutaka kujua anaendeleaje.

    Kitendo cha mzee huyo kuwa karibu naye kila wakati kikamfanya kuanza kumuingiza taratibu na kumuondoa Dickson ambaye kila alipokuwa akipiga simu kazi yake ilikuwa ni kulalamika tu na kumpa vitisho vya kumuacha kwa mara nyingine.

    Pamela hakujali, hakutaka kusikia kitu chochote kile, vile vidonda vilivyokuwa moyoni mwake vikaanza kupona na ile furaha ambayo ilikuwa imepotea kwa kipindi kirefu ikaanza kurudi moyoni mwake.

    Akabadilika, mama yake akamshangaa, haikuwa kawaida kuliona tabasamu la binti yake lakini kipindi hicho, kila wakati msichana huyo alikuwa akitabasamu tu. Mama yake hakutaka kukaa kimya, akamuuliza, alitaka kujua siri kubwa ya tabasamu lile.

    “Nina furaha tu mama,” alisema Pamela.

    “Sawa. Najua una furaha! Ila furaha ya nini?” aliuliza mama yake.

    “Nitakwambia mama!”

    “Kwa nini usiniambie sasa hivi?”

    “Na kwa nini nikwambie sasa hivi? Mambo mazuri hayataki haraka mama,” alijibu Pamela huku akiwa na tabasamu pana.

    Ndani ya miezi mitatu ya mahusiano ya kimapenzi, mzee huyo hakumwambia Pamela kuhusu kufanya mapenzi, kwake, kuwa karibu na msichana huyo ilikuwa ni furaha tele. Wakati mwingine alikuwa akimuita hotelini, huko walikaa na kuzungumza huku msichana huyo akiwa amekiegemea kifua chake, hakumvua nguo zake zaidi ya kuendelea kupiga stori mpaka walipoondoka.

    Pamela akajihisi vibaya, akahisi kwamba mzee huyo alikuwa na matatizo mwilini mwake, haikuwa kawaida kuwa na mwanaume na kukaa naye kwa kipindi kirefu bila kufanya mapenzi na wakati alikuwa akimgharamia kwa kila kitu.

    “Hakuna tatizo! Ila kufanya mapenzi ni maamuzi, kupanga wote wawili,” alisema mzee Edward.

    “Ila tatizo nini mpenzi?”

    “Pamela! Tatizo kubwa ni mke wangu! Ananifanya nijisikie vibaya sana. Nilikwambia kwamba ninampenda, kufanya mapenzi na wewe nahisi kama nitamsaliti,” alisema mzee huyo ambaye hakutaka kabisa kuficha juu ya penzi alilokuwa nalo kwa mkewe.

    “Pole jamani! Mungu atamponya tu!”

    Siku zikaendelea kukatika huku akiishi nyumbani kwao Manzese. Baada ya miezi mitano ya mahusiano ya kimapenzi na mzee huyo, Pamela akapangiwa jumba kubwa maeneo ya Kijitonyama na kutakiwa kukaa huko.

    Hakuamini siku ambayo alichukuliwa na mzee huyo na kuonyeshewa jumba hilo, alimkumbatia mzee huyo na kulia kifuani mwake. Kutoka Manzese, kwenye nyuma ya kimasikini mpaka katika jumba hilo kwake ilionekana kuwa ndoto kubwa.

    Mbali na jumba hilo, akanunuliwa gari, akafunguliwa biashara mbili ambazo alitakiwa kuziendesha yeye mwenyewe. Mpaka kufikia kipindi hicho hakutaka kumficha mama yake, akamwambia ukweli kuhusu mzee Edward.

    “Unasemaje?”

    “Ndiyo hivyo mama! Ananipenda, nipo naye kwa miezi sita,” alijibu Pamela.

    “Huyo anataka kukuchezea tu halafu akuache,” alisema mama yake ambaye alionekana kuwa na hofu kubwa.

    “Mama! Tupo kwenye uhusiano kwa miezi sita, hakuwahi kuniomba penzi! Tunakaa wote hotelini, chumbani lakini hataki kufanya mapenzi,” alisema Pamela, mama yake hakuamini, akauliza mara mbilimbili na jibu likawa hilohilo.

    Mwanamke huyo akataka kuonana na mzee Edward, hilo halikuwa tatizo, mzee huyo alipopewa taarifa hiyo akaonana na mwanamke huyo. Alimchangamkia, akamwambia kabisa mama Pamela kwamba alimpenda mno binti yake, hakujali umri wake, alitamani sana kuwa naye ila kuna baadhi ya vitu hakuwa akivifanya kwa sababu ya mke wake aliyekuwa hoi kitandani.

    “Bora umekuwa mkweli! Kwa hiyo una malengo gani na Pamela?” aliuliza mama yake.

    “Ninataka kuishi naye! Ninataka kumpa furaha maishani mwake, najua moyo wake umekata tamaa ya kuishi, najua ameumizwa sana, huu ni wakati wa kubadilisha kila kitu, ninahitaji kumpa furaha moyoni mwake,” alijibu mzee huyo.

    Mama Pamela akaridhika na mzee huyo, hakuwa na jinsi zaidi ya kutoa ruhusa. Kwa kitendo cha kuwa karibu na Mzee Edward, akaamua kabisa kumuacha Dickson, alijua namna ambavyo mwanaume huyo angemtafuta sana, alichokifanya ni kubadilisha namba ya simu kitu kilichomaanisha kwamba hakutaka kuwasiliana naye tena katika maisha yake.

    Mapenzi yakanoga, Mzee Edward hakutaka kumficha mkewe, alijua kwamba alikuwa mgonjwa kitandani, alimjali lakini aliamua kumpa ukweli kuhusu msichana aliyekuwa amempata.

    Hilo halikumuumiza mwanamke huyo, alimpenda sana mume wake, kwa miaka yote hiyo ya kuishi pamoja, hawakuwa wamepata mtoto japokuwa walikuwa matajiri wakubwa, Mzee Edward hakuwa na tatizo bali tatizo kubwa lilikuwa kwa mkewe aliyekuwa ameharibika mfuko wa uzazi.

    Kwa kipindi chote hicho, mzee huyo hakutaka kumsaliti mkewe, alijua kwamba hakuweza kushika mimba lakini hilo halikumfanya kutembea nje ya ndoa yao, aliendelea kumjali na kumpenda kila siku.

    Kitendo cha kumwambia kwamba alipata msichana ambaye aliamini kwamba angempa furaha, mwanamke huyo akafurahia, hakuumia, akamuita mumewe na kumkumbatia kisha kumbusu mdomoni.

    “Sina muda mwingi wa kuishi mume wangu! Nahisi huu ndiyo mwisho wa safari yangu, nitakufa siku yoyote ile, ila naomba kabla sijafa nifanyie kitu kimoja,” alisema mwanamke huyo kwa sauti ndogo.

    “Bila shaka mke wangu!”

    “Naomba nimuone mwanamke uliyeamua kumchukua na kumsaidia,” alisema mwanamke huyo kitandani pale.

    Mzee Edward hakuwa na jinsi, alitaka kumfurahisha mke wake katika siku za mwisho za uhai wake, alichokifanya ni kuondoka na aliporudi, alikuwa pamoja na Pamela, alimtambulisha kwa mke wake kwamba ndiye msichana aliyeamua kuwa naye kwa ajili ya kumpa furaha.

    Mwanamke huyo alifurahi, alimshukuru Mungu kuonana na Pamela na baada ya siku tatu, akafariki dunia kitandani hapo kitu kilichomfanya Mzee Edward kuwa na maumivu makali moyoni mwake.

    Msiba ukafanyika, mzee huyo alihuzunika na kulia, katika kipindi chote alichoishi na mke wake, waliishi kwa upendo mkubwa, alimpenda na kumthamini na kwake alikuwa kila kitu katika maisha yake. Wakamzika katika makaburi ya Kinondoni na baadaye kuamua kuishi na Pamela kitu kilichompa amani na furaha msichana huyo.



    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Oya! Umemuona yule mtoto?” aliuliza jamaa mmoja aliyekuwa kwenye daladala, alikuwa akizungumza kwa sauti ya chini kuhakikisha abiria wengine hawasikii.

    “Mtoto gani?”

    “Yule aliyebebwa na yule mwanamke!”

    “Duuh! Huyu binadamu au nyani?” aliuliza jamaa huyo aliyeambiwa amwangalie mtoto huyo.

    “Shiiiiii....atasikia..” alisema jamaa huyo.

    Mwanamke mmoja masikini aliyevalia kitenge kilichochakaa kilichokuwa juu ya dela kuukuu alikuwa ndani ya daladala moja iliyokuwa ikitoka Gongo la Mboto kuelekea Makumbusho.

    Mwanamke huyo aliyeonekana kupigwa na maisha alikuwa amembeba mtoto wake ambaye alikuwa gumzo ndani ya daladala hiyo kutokana na ubaya wa sura yake. Kila abiria alimshangaa, alitisha, watu wengi walihisi mwanamke huyo alimbeba nyani mpaka pale mtoto alipoanza kulia na kugundua kwamba alikuwa binadamu.

    Aliwashangaza watu wengi, hawakujua tatizo lilikuwa nini mpaka mtoto huyo kuwa na sura mbaya namna ile. Wapo waliokuwa wakicheka na wengine kujisikia vibaya, japokuwa mara nyingine aliwasikia abiria wakimcheka mtoto wake, alinyamza lakini moyo wake ulikuwa na maumuvu makubwa mno.

    Hilo ndilo lililomtesa, tangu alipomzaa mtoto huyo, kila kitu kilionekana kubadilika. Mumewe ambaye naye alikuwa masikini alipoona mkewe amezaa mtoto mbaya namna ile, akaamua kumkimbia na kumuacha peke yake akiteseka.

    Maisha yalimpiga, hakuwa na kazi yoyote zaidi ya kuuza genge katika Mtaa wa Tandale kwa Tumbo alipokuwa akiishi. Mtoto wake alikuwa gumzo kila kona, wengi walipenda kumwangalia na kumcheka kwa jinsi alivyokuwa na sura mbaya.

    Watoto na watu wazima mitaani walimtumia mtoto huyo kuwa tusi kwa wengine kwani kila aliyeambiwa ana sura mbaya kama mtoto huyo alichukia na kupigana. Mama wa mtoto huyo alidharaulika, na si kwa sababu alikuwa masikini, pia kwa sababu ya ubaya wa sura ya mtoto wake.

    Mpaka anateremka katika kituo cha Tandale Kwa Tumbo, watu walikuwa wakimwangalia, gumzo humo ndani lilikuwa ubaya wa sura ya mtoto yule ambaye kila alipokuwa akilia, ubaya wake uliongezeka na kumtisha kila mmoja.

    Hayo ndiyo yalikuwa maisha yake, yalimuumiza lakini hakuwa na jinsi. Wakati mwingine alikuwa akimuuliza Mungu kwa nini aliamua kumpa mtoto wake sura mbaya kiasi kile lakini hakupata jibu lolote lile.

    Ilipombidi kulia, alilia sana lakini kamwe hakutaka kumtelekeza mtoto wake, aliamini kwamba Mungu alikuwa na makusudi yake, kwa nini mtoto huyo asingepewa Bakhresa? Kwa nini mtoto huyo asingepewa Mengi? Kwa nini Mungu aliamua kumpa yeye mtoto huyo na wakati alijua kwamba alikuwa masikini? Alijua Mungu alikuwa na sababu ambayo ndiyo iliyomfanya kusubiri na kuona ni kitu gani kingetokea.

    Maisha yaliendelea kumpiga kila siku, alipambana, alikuwa radhi kukosa chakula lakini si kwa mtoto wake ambaye aliendelea kukua zaidi na zaidi na alipofikisha umri wa miaka mitatu, akamuanzisha shule ya chekechea.

    Siku ya kwanza kufikishwa shuleni hapo, watoto wengine wakaanza kulia, walimuogopa, walimkimbia kitu kilichomfanya kumuumiza mno moyoni mwake. Machozi yalimtoka mbele ya mwalimu, kwa sababu watoto wengine walikuwa wakiogopa, akaamua kuondoka naye, hakutaka kumpeleka shule tena, aliona ni bora angekaa naye nyumbani tu.

    Mtaani, mtoto huyo aliyeitwa William alionekana kuwa kituko, watoto wenzake hawakutaka kucheza naye kwa sababu walimuogopa mno. Yeye mwenyewe hakujua ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea, hakujua kama sura yake ndiyo iliyokuwa ikiwatisha watoto wengine.

    Siku zikaendelea kukatika, miezi ikasonga mbele na alipofikisha umri wa miaka minne, mama yake, Sophia akakutana na mwanaume mmoja, hakumfahamu, ilikuwa mara yake ya kwanza kumtia machoni.

    Mwanaume huyo alikuwa akipita mtaani kwao, alikuwa ameshika brifukesi, alionekana kuwa na haraka mno ya kuelekea ofisini kwake. Alipokaribia na genge la Sophia, akamwangalia mwanamke huyo na mtoto aliyekuwa pembeni yake, ghafla akasimama na kugeuka na kumfuata mwanamke huyo.

    Sophia alishangaa, hakumjua lakini kwa jinsi alivyokuwa akimfuata, uso wake ulikuwa kwenye tabasamu pana kana kwamba alikuwa akimfahamu mwanamke huyo, alipomfikia, akamsalimia na kisha kuinama na kumwangalia William.

    “Huyu ni mtoto wako?” aliuliza mwanaume huyo aliyevalia nadhifu.

    “Ndiyo!”

    “Aisee! Una bahati sana,” alisema mwanaume huyo.

    “Nina bahati! Ya nini?” aliuliza Sophia huku akimshangaa mwanaume huyo.

    “Una mtoto mzuri sana,” alisema mwanaume huyo huku akiachia tabasamu.

    Alichokuwa akikisema, alimaanisha kutoka moyoni, uso wake ulikuwa na tabasamu pana na kila Sophia alipomwangalia mwanaume huyo, aliona tabasamu lile ambalo lilitoka kwa dhati kutoka moyoni mwake.

    “Unamaanisha nini?”

    “Huyu mtoto ni mzuri! Ana akili sana!” alisema mwanaume huyo.

    “Ana akili?”

    “Ndiyo! Ni mtoto mwenye uwezo wa ajabu sana. Unalijua hilo?” aliuliza mwanaume huyo huku akiendelea kumwangalia William, kwake, mtoto huyo alionekana wa tofauti.

    “Unamaanisha nini!”

    “Mtoto wako ni mzuri, ana akili sana, nahisi Mungu aliamua kukupa huyu mtoto kwa makusudi yake, usimlalamikie Mungu. Hajawahi kuumba mtu mbaya, kila anapokaa na kumwangalia mtoto wako, anajisifia kwamba ametengeneza kitu kizuri sana kiasi kwamba anaweza kuwa sehemu na kujisifia kwamba miongoni mwa watu aliopatia kuwaumba, wa kwanza huyu mtoto,” alisema mwanaume huyo maneno yaliyomchanganya sana Sophia.

    “Sijajua unamaanisha nini?”

    “Kuna siku utajua namaanisha nini! Ninachotaka ujue ni kwamba Mungu kila anapomwangalia mtoto wako, anajivunia kwa kufanya kazi nzuri,” alisema mwanaume huyo, alipomaliza, akasimama, akachukua shilingi elfu kumi kutoka mfukoni mwake na kumkabishi Sophia kisha kuondoka mahali hapo.

    Moyo wake ukawa na furaha, hakuamini kile alichokisikia kutoka kwa mwanaume huyo. Moyo wake ulikata tamaa, kila alipomwangalia mtoto wake, alimlaumu Mungu kwa kumpa mtoto mwenye sura mbaya kama aliyokuwa nayo.

    Akamuinamia William na kumkumbatia. Moyo wake ulikuwa na faraja ambayo hakuwahi kuisikia tangu alipomzaa mtoto huyo. Mume wake alimkimbia kwa sababu ya William, alipoteza ndugu zake kwa sababu ya mtoto huyo, kwake, ndiye alikuwa faraja yake na hakujua sababu iliyomfanya Mungu kumchagua mto to huyo na kuwa uzao wake.

    “Ninakupenda mwanangu! Nakupenda sana,” alisema Sophia na kumkumbatia mtoto wake huku machozi ya furaha yakimtoka machoni na kutiririka katika mashavu yake.

    Maneno yale yakamtia nguvu ya kusonga mbele, alimuona mtu huyo kama malaika ambaye aliyatabiri maisha ya mtoto wake hapo baadaye. Nguvu yake ya utafutaji ikaongezeka na kila siku alihakikisha anakuwa karibu na mtoto wake huyo.

    Miaka ikakatika na alipofikisha miaka saba akaamua kwenda kumuanzisha Shule ya Msingi ya Hekima iliyokuwa hapohapo Tandale. Japokuwa hakuwa amesoma chekechea lakini aliamini kwamba Mungu angempa nguvu mtoto wake kusonga mbele na kufanya vizuri shuleni hapo.

    Wanafunzi wengi walimshangaa, mbele ya macho yao alionekana kuwa kituko kiasi kwamba wanafunzi wa darasa la saba wakaamua kumuita jina la Zinjathropus, jina ambalo kwa kipindi hicho hakujua lilikuwa na maana gani.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kila kona, aliitwa kwa jina hilo, hakujua wanafunzi hao walimaanisha nini, alilipenda kwa sababu lilionekana kuwa jina zuri la Kiingereza au Kigiriki, hivyo kwake ikawa sifa kubwa.

    Hakuwa amesoma chekechea lakini yeye ndiye alikuwa mwanafunzi wa kwanza kujua kusoma vizuri na kuandika. Walimu walimshangaa mno, hakuonekana kuwa mwanafunzi wa kawaida.

    Alipenda hesabu, alipenda kuzifanya kila wakati, uwezo wake haukuishia kwenye hesabu tu, alifanya vizuri katika masomo yote kitu kilichomfanya Sophia kusikia faraja kila siku katika maisha yake.

    Miaka ikakatika, ikasonga mbele, akaingia darasa la saba. Mpaka kufikia hapo, alijulikana na wanafunzi wote wa shule za msingi zilizokuwa katika Wilaya ya Kinondoni. Alikuwa ndiye kichwa chao, katika mitihani yote iliyokuwa ikijumlisha shule zote za Wilaya ya Kinondoni, yeye ndiye alikuwa akifanya vizuri.

    Hakuliacha jina la Zinjathropus, alitambua kwamba alikuwa mbaya wa sura, alilipenda jina hilo ambalo aliendelea kukua nalo huku kwenye kila daftari lake akiliandika jina hilo kwa ukubwa zaidi na kuonekana.

    “Kwa nini umelipenda jina hili?” alimuuliza rafiki yake, Omari.

    “Kwa sababu ni zuri na linaendana nami! Si unaona nilivyo mbaya,” alisema William huku akitoa tabasamu lililoufanya ubaya wake kuongezeka maradufu.

    “Hapana! Huendani nalo! Unatakiwa kuitwa Bill Gates!”

    “Kwa nini?”

    “Kwa sababu wewe ni genius sana! Badilisha jina, jiite Bill Gates,” alisema Omari.

    “Hapana! Nalitaka jina hilihili,” alisema William huku akimwangalia Omari.

    Siku zikaendelea kukatika, japokuwa alikuwa na sura mbaya shuleni hapo lakini wanafunzi wengi walikuwa wakimfuata wakitaka kufundishwa masomo mbalimbali. Kwa William hilo halikuwa tatizo, alikuwa mtu wa kujitolea kiasi kwamba aliwafanya wanafunzi wengi kumpenda kwa kile alichokuwa akikifanya shuleni hapo.

    Walimu walimpenda, walimtaka kila mwanafunzi kuiga kile alichokuwa akikifanya, uwezo wake uliendelea kuwashangaza watu wengi na kulifanya jina la Zinjathropus kukua kila siku na hata kulifunika jina lake la William.

    Baada ya kukaa kwa miezi kadhaa na kuingia darasa la saba, mitihani ya taifa ikafanyika, hakuonekana kuwa na hofu, aliamini kabisa kwamba alikuwa akienda kufanya vizuri katika mitihani hiyo.

    “Zinjathropus aongoza Tanzania...” aliisikia sauti hiyo kichwani mwake, sauti ililolifanya tabasamu pana kuonekana usoni mwake.



    Moyo wa mzee Edward ulikuwa kwenye majonzi mazito, kila alipokaa alikuwa akimkumbuka mke wake, alimpenda kwa mapenzi ya dhati, hakutaka kumuona akiondoka mikononi mwake lakini Mungu aliamua kumchukua na kumpumzisha.

    Faraja pekee kwa kipindi hicho alikuwa msichana Pamela tu, alimpenda msichana huyo, akamfanya kuwa karibu naye na kila wakati walikuwa wakizungumzia mambo yao mbalimbali likiwemo la kuishi pamoja.

    Hilo halikuwa tatizo, kwa kipindi hicho Pamela alikuwa radhi kwa kila kitu, alimpenda mzee huyo kwa sababu alifanikisha kuirudisha furaha yake kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma kabla hajakutana na Dickson ambaye alimuonyeshea upande mwingine wa furaha kwamba kulikuwa na huzuni kubwa.

    Baada ya kumuoa na kuishi pamoja, Pamela akapata ujauzito. Hilo lilikuwa jambo la furaha sana, hakutaka kumficha mumewe, akamwambia kwamba alikuwa mjauzito kitu kilichomchanganya mzee huyo.

    “Unasemaje?” aliuliza huku akionekana kuchanganyikiwa kwa furaha.

    “Nina mimba!”

    “Unasema una nini?”

    “Mimba!” alijibu Pamela huku akiachia tabasamu pana.

    Mzee Edward akamsogelea Pamela na kisha kumkumbatia. Moyo wake ulikuwa na furaha kupita kawaida. Katika maisha yake yote, hakukuwa na kitu alichokuwa akikitamani kama mtoto.

    Alitafuta mtoto kwa miaka mingi, tangu alipokuwa bilionea, katika kipindi chote hicho alikuwa akimtafuta mtoto kwa mke wake lakini mwanamke huyo alikuwa na tatizo la kutoshika mimba na kumsaliti hakutaka kabisa.

    Mungu alisikia kilio chake. Kuanzia siku hiyo hakutaka kumuona Pamela akitoka kwenda kazini. Akawatafuta wasichana ambao walifanya biashara hiyo kwa kuogopa kwamba shetani angeweza kujiinua na kumuua mke wake katika ajali.

    Alimchunga kama nyuki wamchungavyo malkia wao, kila siku alikuwa akirudi nyumbani, kwa sababu alitarajiwa kupata mtoto hata kazi zake alizifanya kwa uhakika, alijitoa na kuufanya utajiri wake kuwa mkubwa.

    Hakuridhika, alikuwa na kila kitu, akamuhamisha mkewe kutoka Masaki alipokuwa akikaa na kumpeleka Osterbay ambapo alinunua nyumba huko huku mama yake Pamela akimuacha Kijitonyama.

    Alitamani kumuona mkewe akiwa kwenye maisha yenye furaha, akimlinda kwa sababu alikuwa akitarajia kumletea mtoto, kitu ambacho alikuwa akikitamani sana.

    “Nahisi kama naota,” alisema Mzee Edward, wakati huo Pamela alitimiza miezi sita, tumbo lilikuwa kubwa na kila siku Mzee Edward alipokuwa akiliangalia, alitamani kulia.

    “Kwa nini?”

    “Hatimaye nakwenda kuitwa baba! Hii ni heshima kubwa sana. Mke wangu! Umenipa heshima ambayo siamini kama kuna siku ningeweza kuipata. Kuwa na utajiri pasipo kuwa baba, bora uwe masikini tu,” alisema mzee huyo, muda wote uso wake ulikuwa kwenye tabasamu pana.

    Miezi tisa ilipotimia, Pamela akajifungua salama mtoto wa kike na kumpa jina la Melania ambalo kila siku lilikuwa kichwani mwa Mzee Edward. Melania akaongeza mapenzi katika maisha yao, kila siku mzee Edward alikuwa akimbeba mtoto huyo, kwa kumwangalia, alikuwa mtoto mzuri mno, alichukua sura ya mama yake na kila mtu aliyekuwa akimwangalia alikiri kwamba mtoto huyo angekuwa mzuri mno miaka ya baadaye.

    “Ni katoto kazuri sana jamani! Hata kakitabasamu, mweee...kazuri hako,” alisema msichana mmoja, rafiki wa Pamela aliyekwenda kumtembelea mzazi huyo.

    “Kweli kabisa. Natamani ningekuwa na katoto kama haka jamani! Kazuri sana,” alisema msichana mwingine.

    Kila wikiendi walikuwa wakitoka na kwenda kwenye maduka ya watoto kununua nguo na vitu vingine vya watoto. Maisha yalibadilika, mtoto Melania alibadilisha kila kitu ndani ya maisha yao.

    Mzee Edward alijipanga, akapanga maisha ya mtoto wake, hakutakiwa kupata tabu zozote maishani mwake, alitaka kumpa elimu bora, maisha mazuri ambayo yangeufanya uzuri wake kuongezeka maradufu.

    Miezi ikasogea, miaka ikakatika, Melania alipofikisha umri wa miaka miwili akaanza masomo ya chekechea katika shule ya matajiri ya Victoria Nursery School ambapo ndani yake kulikuwa na watoto wengi wa matajiri na viongozi mbalimbali wakiwemo watoto wa mawaziri.

    “Jamani! Huyu Melania ni mzuri sana, atakuja kuwa mrembo mno hapo baadaye,” alisema Mwalimu Bertha alipokuwa akimwangalia Melania.

    “Kweli kabisa. Kana uzuri wa ajabu sana. Hivi amechukua kwa mama yake au?” aliuliza mwalimu Thomas, yeye mwenyewe alipokuwa akimwangalia Melania, alithubutu kusema kwamba katika maisha yake aliwahi kumuona mtoto aliyekuwa na sura nzuri mno.

    “Amechukua kwa mama yake! Naye ni mzuri huyo..” alisema mwalimu Bertha, kila alipokuwa akimwangalia Melania, alitamani kama angekuwa mtoto wake.

    Siku zikaendelea kwenda mbele, Melania akaendelea kukua, watoto wengi waliokuwa hapo shuleni walipenda kucheza naye kwa sababu tu alikuwa mzuri wa sura. Kila siku baba yake alipokuwa akifika shuleni hapo, kitu cha kwanza alitaka kupata taarifa kama kulikuwa na watoto waliokuwa wakipenda kucheza na mtoto wake.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Yupo mmoja, huyu anaitwa Nicolaus...” alijibu mwalimu.

    “Ndiye anapenda kucheza na binti yangu? Walimu kuweni makini! Hivi vitoto siku hizi vinajifanya kuwa na mambo ya kizungu sana,” alisema mzee huyo, alionekana kuwa na wivu kupindukia kwa mtoto wake.

    Miaka ikakatika, baada ya kufika darasa la sita, uzuri wa Melania ukaongezeka zaidi, akavunja ungo, mwili ukanawiri, nyonga zikatanuka na sauti yake kuwa nyororo iliyowavutia wavulana waliokuwa wakimwangalia. Mbali na sifa hizo, kifua chake kikaanza kujaa, kila aliyemwangalia, alikuwa akimtamani sana.

    Mvulana aliyekuwa karibu naye alikuwa Nicolaus, huyu alikuwa mtoto wa Waziri Mkuu, Bwana Antony Makunga. Alimpenda sana Melania, kila alipokuwa akimwangalia, aliuona uzuri wa msichana huyo.

    Kulikuwa na wavulana wengi waliokuwa wakimpenda Melania lakini cha kushangaza, hakukuwa na yeyote aliyekuwa tayari kumfuata msichana huyo na kumwambia ukweli juu ya alivyokuwa, uzuri uliokuwa ukiwavutia mno.

    Hata Nicolaus mwenyewe alikuwa mkimya, alimuogopa msichana huyo, japokuwa alikuwa rafiki yake lakini hakutaka kumwambia ukweli juu ya hisia kali za kimapenzi alizokuwa nazo kwa msichana huyo.

    Alimpenda sana, moyo wake ulikuwa kwenye mapenzi mazito, wakati mwingine alishindwa hata kulala na alipokuwa akifanikiwa kulala, muda wote ndoto zake zilikuwa kwa msichana huyo lakini hakuufungua mdomo wake kumwambia ukweli.

    Mapenzi yalimtesa na kumtesa, alipokuwa akimuona Melania akizungumza na wavulana wengine, alihisi kitu chenye ncha kali kikiuchoma moyo wake, alisononeka na siku nzima alikuwa akiugulia na maumivu makali.

    “Melani!” alimuita msichana huyo.

    “Nikuulize kitu?”

    “Niulize tu Nico!”

    “Daah! Au subiri nitakuuliza siku nyingine!”

    “Jamani! Niulize leo...”

    “Nitakuuliza tu!” alisema Nicolaus.

    Alitaka kumuuliza kama msichana huyo alikuwa akimpenda kama alivyokuwa akimpenda au la. Kila alipotaka kumuuliza swali hilo, mapigo yake ya moyo yaliongezeka na kudunda kwa nguvu kana kwamba moyo ulitaka kuchomoka.

    Melania alimuomba sana amuulize lakini kijana huyo hakumuuliza, akapotezea na kupanga siku nyingine ya kumuuliza.

    Wakati Nicolaus akiwa anateseka moyoni mwake, hivyo ilikuwa kwa Melania. Alimpenda kijana huyo, kila alipokuwa akimwangalia, moyo wake ulikiri kwamba mvulana huyo alikuwa na sura nzuri kuliko wavulana wengi hapo shuleni.

    Siku hiyo ambayo Nicolaus alisema kwamba alitaka kumuuliza kitu, alitega sikio lake, alitaka kusikiliza kile alichotaka kuuliza mvulana huyo lakini akanyamaza na kuahirisha kitu kilichomfanya kuumia mno.

    Naye hakulala kwa raha usiku, mwili wake ulipevuka, matamanio ya kufanya mapenzi yalimkamata na mtu pekee aliyeona kwamba alistahili kumvua nguo zake hakuwa mwingine zaidi ya Nicolaus ambaye kila siku alikuwa na hofu ya kumwambia jinsi alivyokuwa akijisikia.

    “Hivi nimwambie mimi au? Atahisi nini? Kweli msichana amtongoze mvulana! Nitaonekanaje? Kweli ni tamaduni yetu hii?” alijiuliza bila kupata majibu.

    Siku zikaendelea kukatika mpaka walipomaliza darasa la saba na kuingia kidato cha kwanza. Hakukuwa na aliyemwambia mwenzake, kila siku walikuwa pamoja lakini wote waliogopana.

    Walipoingia kidato cha tatu, Nicolaus hakutaka kukubali, kama kuteseka, aliteseka sana kwa ajili ya penzi hilo, alichokifanya ni kujitoa mhanga, akaupiga konde moyo wake na kumuita msichana huyo.

    “Melani!” alimuita.

    “Abee!”

    “Naomba nikwambie kitu kimoja!”

    “Kitu gani?” aliuliza Melania, tabasamu lilikuwa usoni mwake, Nicolaus akashusha pumzi nzito, mapigo ya moyo yakaanza kudunda kwa nguvu.

    “Nakup....” alisema na kisha kunyamaza.

    “Unasemaje?”

    “Melania! Ninakupenda sana! Nilitamani nikwambie hili tangu zamani! Nimeshindwa kuvumilia. Kwa kipindi chote, miaka yote hiyo nimekuwa nikikupenda sana, nimeshinda nahisi leo ndiyo siku yenyewe. Ninakupenda sana Melania,” alisema Nicolaus huku akimwangalia msichana huyo usoni, kwa aibu, akaanza kuangalia chini.

    “Nimesikia!” alijibu Melania baada ya ukimya wa sekunde kadhaa.

    “Kwa hiyo?”

    “Kuhusu?”

    “Nataka uwe mpenzi wangu! Nataka uwe msichana wangu pekee!” alisema Nicolaus, wakati huo aliupiga moyo wake konde, alikuwa tayari kwa kila kitu.

    “Naomba nikajifikirie...”

    “Sawa,” alijibu Nicolaus harakaharaka, hakutakka hata kuuliza sababu za kumfanya msichana huyo kwenda kujifikiria na wakati jambo hilo lilikuwa la kumalizana kwa kuwa hisia zilikuwa moyoni na si nyumbani, ila kutokana na hofu, akamkubalia harakaharaka.



    Hakujua ni kitu gani alitakiwa kumwambia Nicolaus, ni kweli alikuwa akimpenda lakini hata naye alikuwa akimuogopa. Usiku mzima ulikuwa ni kujifikiria ni jibu gani alilotakiwa kumpa kijana huyo aliyekuwa akilisubiria kwa hamu kubwa.

    Asubuhi ilipofika, akaelekea shule. Alipofika huko, hakutaka kuonana naye, hakutaka kumpa upenyo wa kuzungumza naye kwani alimpenda lakini hakuwa tayari kumwambia kwa mdomo wake.

    Nicolaus hakulalamika, moyo wake haukuwa ukijiamini kabisa, ni kweli alikuwa akilisubiri jibu hilo kwa nguvu zote lakini naye aliogopa kumfuata msichana huyo na kumuuliza kuhusu jibu lake.

    Siku zikakatika, ukaribu wao ukapungua kwa kuogopana kwani muda huo mioyo yao ilikuwa na kitu cha tofauti kabisa, hakukuwa na urafiki tena bali kilichokuwa kikiibuka kilikuwa ni mapenzi ya dhati.

    Mwaka huo ukapita na kuingia kidato cha nne. Mwaka huo wa mwisho ndiyo ambao Nicolaus akalikumbushia lile jibu alilotakiwa kupewa na moja kwa moja msichana huyo kukubaliana naye na hivyo kuanza uhusiano wa kimapenzi uliotakiwa kuwa siri kubwa.

    Wakawa wapenzi, wakapenda sana, kila siku walikuwa pamoja, walionyesheana ni kwa jinsi gani walikuwa wakipendana. Wakati uhusiano huo ukiendelea, mama yake Melania, Pamela akapata mtoto wa pili wa kiume na kumpa jina la James ambaye aliiongeza furaha iliyokuwa katika familia hiyo.

    Maisha yaliendelea kama kawaida. Wanaume hawakuwa mbali na Melania, walimpenda kwani alikuwa msichana mrembo ambaye kila mmoja hakuamini kama katika maisha yake angekutana na msichana mrembo kama alivyokuwa Melania.

    Japokuwa walikuwa kwenye uhusiano wa dhati, Melania hakutaka kufanya mapenzi na Nicolaus. Kila siku mwanaume huyo alipomwambia wakafanye, msichana huyo alikuwa akitoa sababu nyingi kwamba yupo bize na wangefanya siku nyingine.

    Hilo likamuumiza sana Nicolaus, kila alipomwangalia mpenzi wake, jinsi alivyonawiri mwili wake ulimsisimka, mapigo yake ya moyo yalimdunda kwa nguvu kwani alitamanisha na kuvutia kuliko kawaida.

    “Kama hataki si bora nimbake tu,” alisema Nicolaus huku akionekana kushikwa na mhemko mkubwa kwa msichana huyo.

    Hilo ndilo alilolipanga, hakutaka kuona akiendelea kula kwa macho na wakati msichana huyo alikuwa mpenzi wake. Walikuwa wakifanya mambo mengi, wakishikana hapa na pale, wakibadilishana mate lakini kufanya mapenzi lilionekana kuwa suala gumu sana.

    “Kwa hiyo hutaki?” aliuliza Nicolaus.

    “Si kwamba sitaki baby!”

    “Kumbe?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nataka ila muda bado!”

    “Kwa hiyo mimi niendelee kuwa mpenzi mtazamaji tu?” aliuliza Nicolaus.

    “Simaanishi hivyo!”

    “Kumbe unamaanisha nini? Sasa kama hatufanyi mapenzi, kitu gani kitatutambulisha kwamba mimi na wewe ni wapenzi? Kuna utofauti gani wa mimi na kaka yako au wewe na dada yangu?” aliuliza Nicolaus huku akionekana kupagawa.

    “Utofauti upo, tunabadilishana mate, hiyo ni ishara mojawapo ya kwamba sisi ni wapenzi,” alijibu Melania.

    “Hiyo haijatosha. Au unatembea na jamaa fulani halafu kwangu unanikazia?” aliuliza Nicolaus.

    “Hapana! Wasiwasi wako tu!”

    Kabla hajapanga kumbaka msichana huyo, mara kwa mara Melania alikuwa akifika nyumbani kwao na kuingia mpaka chumbani kwake lakini baada ya kuwa na wazo la kumbaka, tayari kukawa na ugumu kwa msichana huyo kufika nyumbani kwao.

    Mara kwa mara alikuwa akimwambia Melania afike nyumbani kwao lakini msichana huyo aligoma, ni kama alikuwa ameshtukia kile kilichotaka kutokea huko. Nicolaus hakutaka kubaki kimya, kila siku ilikuwa ni lazima amkumbushe kwamba alitaka kuzungumza naye nyumbani kwao.

    Uhusiano huo uliendelea mpaka walipomaliza kidato cha nne na kusubiri matokeo ya kuingia kidato cha tano. Hawakuwa na hofu, walijua kwamba wangefaulu kwani shule waliyokuwa wakisoma ilikuwa miongoni mwa shule bora zilizokuwa zikifaulisha sana ingawa ilikuwa ni ya watoto wa matajiri tu.

    Walisubiri nyumbani huku kila mmoja akifikiria lake. Nicolaus, alikuwa akifikiria kufanya mapenzi na Melania na wakati msichana huyo alikuwa akifikiria kuhusu elimu yake ya kidato cha tano na sita.

    Waliendelea kuwasiliana. Kila siku kwa Nicolaus iilikuwa ni malalamiko tu, alimtaka mpenzi wake wafanye mapenzi lakini msichana huyo alikataa katakata na kumwambia kwamba alitakiwa kusubiri hadi ndoa. Ilimuuma, hakuwa na jinsi, kwa sababu aliambiwa asubiri, akafanya hivyo.

    Wakafaulu vizuri na kuingia kidato cha tano. Wakati wakijiandaa kusoma kidato cha tano Tanzania, baba yake Nicolaus akaamua kumsafirisha mtoto wake aelekee nchini Australia katika Jiji la Melbourne kuendelea na masomo ya chuo katika Chuo cha Monarch kilichokuwa jijini humo.

    “Mpenzi! Nitakuwa muaminifu katika kipindi chote nitakachokuwa huko,” alisema Nicolaus.

    “Na mimi pia nitakuwa mwaminifu katika kipindi chote nitakachokuwa huku,” alisema Melania.

    Wakaagana na Nicolaus kupanda ndege na kuelekea nchini Australia. Huku nyuma Melania alikuwa na mawazo tele, kila siku alikuwa akiwasiliana na Nicolaus na kumwambia namna alivyokuwa akimpenda.

    Alikosa furaha, kila alipokuwa akilala usiku picha ya mwanaume huyo ilikuwa ikimjia kichwani mwake. Miaka ikakatika, miaka miwili ikapita na kuanza masomo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

    Alifurahi kuingia chuoni humo. Siku za kwanza alikuwa gumzo, kila mwanaume aliyekuwa akimwangalia alitokea kumpenda. Alikuwa mtoto wa bilionea mkubwa, mwenye kampuni nyingi na hata maisha yake hapo chuoni yalionyesha kwamba alikuwa mtoto wa bilionea.

    Alikuwa akiendesha gari la thamani kuliko hata maprofesa wenyewe. Kila alipokuwa akiingia chuoni, wote walikuwa wakilishangaa gari lake ambalo dukani lilikuwa ni zaidi ya milioni mia moja na hamsini.

    Hakujali, kwake, fedha ilikuwa kawaida sana. Hakuwa mtu wa matanuzi, alipendwa na watu wengi kwa kuwa alikuwa mcheshi na kutokana na uzuri wake ilikuwa vigumu kugundua kwamba mpaka kipindi hicho hakukuwa na mwanaume aliyemuingia kimwili.

    Wakati akiwasiliana na Nicolaus kwa kipindi chote ndipo akamwambia kwamba alitarajiwa kurudi nchini Tanzania kwa ajili ya likizo fupi. Melania akafurahi sana, hakuamini kama kweli kipindi hicho angemuona mpenzi wake kwa mara nyingine.

    Akajipanga kumpokea kwa mapenzi mazito. Baada ya kuwasiliana kwa siku kadhaa hatimaye mwanaume huyo akaingia Tanzania. Walipoonana, hakuonekana kuwa kawaida, yale mapenzi ambayo aliyaona kwa mpenzi wake kipindi cha nyuma hayakuwa kama kipindi hicho.

    Melania alishangaa, alimfahamu Nicolaus, alipokuwa na furaha, alimjua vilivyo na hata alipokuwa amebadilika, aliweza kuligundua hilo. Hakujua tatizo lilikuwa nini. Hilo lilimchanganya kichwani mwake, wakati mwingine alihisi kwamba kwa sababu alishindwa kufanya naye mapenzi basi ndiyo maana aliamua kubadilika namna hiyo.

    Hakuwa akizungumza naye hata kwenye simu, muda mwingi mwanaume huyo alimwambia kwamba alichoka. Alipokuwa akichati naye katika Mtandao wa Allo, ulionyesha kwamba meseji zilikuwa zikisomwa lakini hazikuwa zikijibiwa.

    “Nicolaus, tatizo nini mpenzi?” aliuliza msichana huyo.

    “Hakuna tatizo!”

    “Niambie ukweli! Sipendi kukuona ukiwa kwenye hali hii! Wewe niambie tatizo nini?” alisema Melania, wakati huo walikuwa wakizungumza kwenye simu.

    “Hutaki hata tufanye mapenzi! Sawa, umenifanya kula kwa macho, lakini hata kunionyeshea umbo lako mpenzi,” alisema Nicolaus.

    “Kwa hiyo hilo ndilo linalokufanya kuhuzunika namna hiyo jamani?”

    “Ndiyo! Umeumbika lakini hunipi hata nafasi ya kukuona, kweli mpenzi unanifanyia hivi!” alilalamika Nicolaus.

    “Basi subiri!”

    Baada ya dakika kadhaa, picha kadhaa zikaingia katika simu ya Nicolaus, akazifungua na kuanza kuziangalia. Zilikuwa picha za utupu za msichana huyo, alijipiga pasipo kuwa na aibu yoyote ile.

    Hakuogopa, alimwamini sana Nicolaus, kumtumia picha za utupu tena zilizoonyesha sura yake hakuona kuwa na tatizo lolote lile. Nicolaus alipozipata picha hizo, akakenua, moyo wake ukawa na furaha sana.

    “Sasa amekwisha...” alisema Nicolaus.

    Kuanzia kipindi hicho, hakutaka kuwasiliana tena na Melania. Ndiyo kwanza akaondoka kurudi nchini Australia huku moyo wake ukiwa na furaha tele. Kiukweli alikuwa na kazi kubwa na picha hizo, kitendo cha kutumiwa tu, lilikuwa kosa kubwa kwa msichana huyo.



    “Una akili sana Zinjathropus...umepata masomo yote mia,” alisikika kijana mmoja akimwambia William.

    “Unasemaje?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Umepata masomo yote mia! Nimetoka kuangalia matokeo, wewe mtu umetisha sana,” alisema kijana huyoi.

    Matokeo ya darasa la saba yalitoka, kama ambavyo alitegemea, William aliweza kufanya vizuri na kupata alama za juu kabisa kwenye masomo hayo. Mama yake hakuamini, alipoambiwa mara ya kwanza alihisi kwamba watu walikuwa wakimdanganya.

    Alifahamu kwamba mtoto wake alikuwa na uwezo mkubwa ila si kwa kufanya vizuri kwa kiasi hicho. Akaelekea shuleni kwenda kuhakikisha kwa macho yake. Hakukukuwa na kitu kilichobadilika, kama alivyokuwa ameambiwa ndivyo alivyokutana nayo huko shuleni.

    Moyo wake ulifarijika, kitendo cha mtoto wake kufanya vizuri namna ile kukamfanya kumkumbuka mwanaume yule ambaye alikutana naye kwa mara ya kwanza na kumwambia kwamba alizaa mtoto aliyekuwa na uwezo mkubwa.

    Furaha ikamzidi na machozi kuanza kumtiririka, palepale shule alipokuwa, akapiga magoti chini na kumshukuru Mungu. Alidharaulika sana, alisemwa sana lakini mwisho wa siku Mungu akataka kuuonyesha ulimwengu kwamba hakuwa anakosea katika kazi yake, kila kitu alichokiumba alikuwa na makusudi nacho.

    Kila mtu aliyemuona Wiliam alikuwa akimpongeza kwa kazi nzuri aliyoifanya. Kwa kuwa alifaulu kwa kiasi kikubwa akapelekwa katika Shule ya Sekondari ya Tabora Boys. Huko, hakuacha kufanya vizuri, alikuwa moto wa kuotea mbali kiasi kwamba kila mwanafunzi alikuwa tegemeo lake kwani kazi yake ya kufanya vizuri ilikuwa ni zaidi ya mwanafunzi yeyote aliyewahi kusoma katika shule hiyo.

    Siku zilikwenda mbele na miaka kukatika. Baada ya kumaliza kidato cha nne, akarudi nyumbani. Hakutaka kukaa tu, kwa sababu moyo wake ulianza kupenda kompyuta, akaanza kujifunza namna ya kutumia kompyuta.

    Marafiki zake ndiyo waliomfundisha. Kila siku alikuwa akionana na marafiki hao na kumuonyeshea namna ya kutumia kompyuta. Aliipenda, alimwambia mama yake jinsi alivyokuwa akipenda kompyuta ila hakuweza kununuliwa kwani mama yake hakuwa na fedha za kutosha.

    Hilo lilimuuma sana, aliuchukia umasikini, alikuwa na nguvu za kutosha, pamoja na kuwa na uwezo mkubwa darasani, kila siku alikuwa akiondoka nyumbani na kwenda Tandale Sokoni ambapo huko alibeba mizigo na ilipofika jioni, alirudi nyumbani na kuigawa fedha aliyoipata kwa matumizi ya nyumbani na nyingine akiiweka kwa ajili ya kununua kompyuta.

    Alifanikiwa kukusanya kiasi ambacho kikamfanya kununua kompyuta iliyokuwa ya kawaida tu. Hapo ndipo alipoanza kufanya mazoezi nyumbani. Uwezo wake mkubwa ukamfanya kugundua mambo mengi. Kila siku alikuwa akiingia katika mitandao mingi, alikuwa akijifunza mambo mengi kuhusu kompyuta.

    Uwezo wake uliweza kuwashangaza hata marafiki zake ambao ndiyo waliomfundisha kompyuta, akaanza kuvijua vitu vingi sana. Alijifunza na kujifunza, kompyuta ikawa kichwani mwake, hakuwa amesoma chuo lakini kwa kuwa alijifundisha sana kupitia video mbalimbali, akaweza kutengeneza mpaka tovuti yake.

    “Unajua kutengeneza tovuti?” aliuliza rafiki yake kwa mshangao.

    “Ndiyo! Unafikiri kazi kubwa Hemedi? Ni ndogo mno, kama kumlisha mtoto mwenye njaa,” alijibu William.

    “Umejifunza wapi?”

    “Utundu tu! Nataka niijue sana kompyuta kuliko kitu chochote kile,” alisema William.

    Kichwa chake kilikuwa kikifikiria kompyuta, kila siku ilikuwa ni lazima kujifunza jambo jipya., Hakuwa amesomea kompyuta lakini uwezo wake ukawafanya hata watu waliokuwa wamejifunza kumpyuta kumshangaa kwani hawakuwahi kukutana na mtu aliyekuwa na uwezo mkubwa kama aliokuwa nao William.

    Hata alipotakiwa kuendelea na masomo ya kidato cha tano, hakutaka, alipenda kompyuta hivyo kumwambia mama yake kwamba alitaka kusoma kompyuta kwa kuwa aliipenda sana.

    Mama yake alilalamika sana lakini hakuwa na la kufanya. Huo ndiyo ulikuwa uamuzi wa mtoto wake, akaungana naye katika uamuzi huo aliokuwa ameufanya.

    “Unaamini kwamba kompyuta itakupa pesa?” aliuliza mama yake.

    “Ndiyo mama! Itanipa pesa sana. Kuna mambo fulani najifunza kuhusu codes,” alisema William.

    “Ndiyo kitu gani hicho?”

    “Hahah! Mama haya mambo ya kompyuta magumu sana. Ngoja nijifundishe zaidi halafu nitakwambia siku nyingine,” alisema William.

    Alichokifanya ni kukutana na wataalamu wa IT ambao alizungumza nao mambo mengi na kuwaonyeshea kile alichokuwa akikifahamu yeye. Watu hao walimshangaa hasa waliposikia kwamba hakuwa ameingia darasani kusoma kompyuta hata kidogo.

    “Unajua kuhusu C++?” aliuliza jamaa mmoja.

    “Yeah! Ya kitoto sana hiyo!” alijibu William.

    “Java?”

    “Nayo naijua yote,” aliwaambia.

    “Sasa umekuja kwetu tukufundishe nini na wakati kila kitu unakijua?” aliuliza jamaa mmoja huku akionekana kushangaa.

    “Hakuna mengine?”

    “Mmh! Mpaka hapo utakuwa umesoma mengi. Hizi WhatsApp zinatengenezwa na Java, hizi Facebook na nyingine zinatengenezwa na Java, sasa kama wewe unaijua Java, kuna umuhimu gani wa kusoma?” aliuliza jamaa huyo.

    “Kwa hiyo naweza kuiba hela benki?”

    “Hahaha! Utaweza? Washikaji wameweka codes ngumu sana. Ukizijua utafanikiwa,” alisema jamaa huyo.

    “Basi poa. Nitatengeneza virus hatari sana, halafu nitamtuma aende akavuruge data za kompyuta zao,” alisema William huku akiwaangalia vijana hao ambao walibaki wakimshangaa tu.

    “Tunakutaki kila la kheri kaka!”

    Hakutaka kuzungumza sana, aliijua kompyuta, kichwa chake kilikuwa hatari katika kufahamu mambo mengi kwenye kompyuta. Alikuwa katika familia masikini, aliamini kwamba mama yake hakuwa na fedha na ilikuwa ni lazima kupambana mpaka kufanikiwa kupata fedha.

    Alichokifikiria hapo ni kuwa mwizi wa mtandaoni (scammer). Alijua kwamba angefanikiwa katika hilo. Usiku wa siku hiyo akataka kuiba hela na kuziingiza kwenye akaunti yake ya benki, alipotaka kufanya hivyo, akakumbuka kwamba hakuwa na akaunti benki.

    “Basi nitaziingiza kwenye simu yangu!” alisema na kuanza kazi.

    Ilikuwa kazi kubwa, alihangaika usiku kucha akifanya kazi hiyo. Hakutaka kulala, alikuwa akicheza na codes za benki ya Tanzanian Bank ambayo ndiyo iliyotumiwa na watu wengi kipindi hicho.

    Codes zake zilikuwa ngumu, alijitahidi kucheza nazo, alicheza nazo na kucheza nazo lakini akachemka kwani watu waliokuwa wameziweka codes hizo walionekana kuwa hatari sana.

    Hakuridhika, hakuamini kama kulikuwa na kushindwa mbele yake, alichokifanya ni kutengeneza virusi wake hatari na kuvipa jina la Wirus. Alivitengeneza kwa siku mbili, kila alipokuwa akimaliza na kuvijaribu, vilionekana kuwa vyepesi kuuliwa.

    Hakutaka kukata tamaa, wiki nzima kazi yake kubwa ilikuwa ni kutengeneza virusi hivyo na baada ya wiki moja na nusu kumalizika, akafanikiwa kutengeneza virusi hao, baada ya hapo akavituma kwenye kompyuta za benki hizo.

    Virusi wakaingia, wakafunga mafaili yote muhimu, yakapotea na ndiyo naye akatumia mwanya huohuo kuiba kiasi cha milioni mia tano na kukiingiza kwenye simu yake. Kilikuwa kiasi kikubwa mno, alijua kwamba angeshtukiwa, alichokifanya ni kuchukua virusi walewale na kuviingia katika kompyuta za Shirika la Simu la Tritel alilokuwa akilitumia, alipofanikiwa, akafuta kumbukumbu, virusi wakala baadhi ya mafaili na kuvuruga data za kompyuta hizo, fedha hazikuonekana kama ziliingizwa katika simu hiyo, alipomaliza. Akatulia na kuweka miguu kitandani.

    “Mimi ni milionea,” alijisemea huku akiangalia salio kwenye akaunti yake ya simu. Mwisho wa kuweka fedha ilikuwa ni milioni mbili, ila kwa sababu alikuwa mtu hatari sehemu hizo, shilingi milioni mia tano zilikaa kwenye simu yake, kilichobaki kilikuwa ni kutumia tu.

    ****CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “What do you want Kattie?” (unahitaji nini Kattie?)

    “I want to see you,” (nahitaji kukuona)

    “You wanna see me?” (unahitaji kuniona?)

    “Yeah!”

    “Right now?” (sasa hivi?)

    “Yeah!”

    “I got no time to see yo right now, I will call you right back,” (sina muda wa kukuona sasa hivi, nitakupigia baadaye) alisema Nicolaus na kukata simu.

    Moyo wake ulikuwa kwenye furaha tele, tangu alipokwenda nchini Australia kuanza masomo katika Chuo cha Monarch kilichokuwa katika Jiji la Melbourne, wanawake wengi wakatokea kumpenda.

    Alikuwa mchangamfu, alipenda kuzungumza na watu wengi, wanawake walichanganyikiwa naye na kila wakati walipenda kuwa karibu yake. Hakuwaambia wanachuo kwamba alitokea nchini Tanzania, aliwaambia kwamba alitokea nchini Marekani na ndiyo maana hata lafundi yake alikuwa akizungumza kama Mmarekani.

    Wazungu, hasa waliokuwa nchini Australia waliwapenda Wamarekani weusi, walipenda jinsi walivyokuwa wakizungumza na muda mwingi walikuwa wakitaka kuwa karibu nao. Nicolaus alilifahamu hilo, alijua kwamba kama angesema kuwa ametoka barani Afrika basi angedharauliwa na baadhi ya watu na ndiyo maana alipofika, akawaambia kwamba alitoka nchini Marekani na ndiyo maana alizungumza kama Mmarekani mweusi.

    Wanawake wakaanza kumshobokea, hakutaka kuwaacha, alijua kwamba kama angediriki kufanya mapenzi na Mzungu hasa kutoka nchini humo ingempa nafasi ya kuishi kwa amani kama raia wa nchi hiyo, hivyo kila msichana aliyemwambia kwamba alikuwa akimpenda, usiku wa siku hiyo alilala naye.

    Hakumfikiria Melania, hakukumbuka kama alikwishawahi kukutana na msichana aliyekuwa na jina hilo. Wakati mwingine hakuwa akiwasiliana naye, alipokuwa akitumiwa meseji alijibu kwa kujisikia.

    Msichana huyo aliumia lakini hakutaka kulalamika, alihisi kwamba inawezekana masomo ndiyo yalimfanya mwanaume huyo kuwa bize kwa kiasi hicho.

    Baada ya kuhangaika sana, baada ya kulala na wanawake wengi wa Kizungu hatimaye penzi lake likaishia kwa msichana mwenye sura ya kirembo, huyu aliitwa Kattie. Siku za kwanza hakutaka kabisa kuwa naye, msichana huyo alijitahidi sana kuzungumza naye, kumsalimia lakini Nicolaus akajifanya kuwa bize ila mwisho wa siku akajikuta akiingia mikononi mwake.

    Kattie hakutaka kumuacha Nicolaus, kwake alimuona kuwa mwanaume mwenye bahati sana huku akili yake ikimwambia kwamba mwanaume huyo alikuwa ametoka nchini Marekani. Mapenzi yakawa motomoto na hata msichana huyo alipokuwa akirudi nyumbani kwao jijini Sydney walikuwa wakiwasiliana na Nicolaus kwenda huko.

    “Nataka unioe,” alisema msichana huyo.

    “Lini?”

    “Tutakapomaliza chuo. Ila hukuniambia Marekani unaishi sehemu gani,” alisema msichana huyo.

    “Naishi Brooklyn, karibu na lile daraja kubwa,” alisema Nicolaus.

    “Ooh! Nimefurahi kujua!”

    Mahusiano yakanoga, siku ziliendelea kukatika, miaka ilipokatika na kutakiwa kufunga chuo ndipo akaanza kumkumbuka msichana Melania. Mapenzi aliyokuwa nayo kwa msichana huyo yaliondoka moyoni mwake, mapenzi ya Wazungu yakamchanganya kupita kawaida.

    Alikumbuka jinsi msichana huyo alivyoutesa moyo wake, alimtaka sana kimapenzi, tena kwa kipindi kirefu lakini alikataa. Aliumia moyoni, kama yeye alikuwa ameumia, naye akataka kumuumiza kama alivyokuwa amemuumiza.

    Alichokitaka ni kumuomba picha zake za utupu ili azisambaze katika mitandao ya kijamii. Alichokifanya ni kujifanya ameyarudisha mapenzi hayo kwa msichana huyo huku akimchombezachombeza kuhusu picha hizo.

    Melania alikataa kwa kuwa aliogopa, aliona jinsi wanawake wenzake walivyokuwa wakiteseka mara baada ya picha zao kuvuja mitandaoni, wengine waliamua kujiua kwa sababuu waliona kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wao, walionekana kama vituko katika jamii, hivyo alipinga sana suala hilo.

    Wakati Nicolaus aliporudi Tanzania na kumwambia msichana huyo kuhusu picha zake, Melania hakuwa na jinsi, alimpenda mpenzi wake na hivyo kumtumia picha hizo ambapo baada ya kuzipata, akaondoka na kurudi nchini Australia.

    “Upo wapi?” aliuliza Melania katika mtandao wa Allo, baada ya kumpigia simu na kumkosa.

    “Nipo Australia!”

    “Mbona ghafla na hukuniaga?”

    “Kwa sababu sipendi kuaga watu! Una shida yoyote?” aliuliza Nicolaus swali ambalo liliendana na emoji ya kucheka mpaka machozi katika mtandao huo.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog