Search This Blog

Sunday 22 May 2022

FUTA MACHOZI MPENZI - 5

 





    Simulizi : Futa Machozi Mpenzi

    Sehemu Ya  Tano (5)



    William alikosa amani, kila alipokaa kichwa chake kilikuwa kikimfikiria msichana Cassey, hakuamini kama kweli alikuwa na mimba yake. Si kwamba hakupenda mtoto, alitamani sana kupata mtoto lakini hakupanga kupata mtoto kwa mtu kama Cassey ambaye kila siku alimuona kuwa mtu wa kupita, wa kumvua sketi na kuondoka zake.

    Nyumbani, hakuonekana kuwa na furaha kabisa, Linda alipokuwa akimuuliza kuhusu hali iliyomsababisha kuwa hivyo, hakumwambia ukweli zaidi ya kumdanganya kwamba alihisi kichwa kikimuuma mno.

    “Pole sana,” alisema Linda huku akienda kumchukulia dawa.

    Kichwa chake kiliyafikiria magazeti ya udaku, aliyaona yakiwa mitaani huku kukiwa na habari yake kwa ukubwa mbele kabisa, hakujua ni mahali gani angeuficha uso wake kwani kila mtu angefahamu kwamba alilala na msichana Cassey na kumpa mimba na wakati alikuwa na mpenzi wake aliyekuwa akijulikana kila kona.

    Hakuacha kumpigia simu Cassey na kumwambia kuhusu kuitoa mimba hiyo. Cassey hakukubali, hakutaka kumsikiliza na wakati mwingine mpaka wakawa wanagombana kisa tu kuambiwa kwamba alitakiwa kuitoa mimba hiyo.

    Wakati mwingine William alimtafuta Cassey na kumuomba sana, hakutaka kuona mimba ile ikiendelea kukua, alitaka itolewe haraka iwezekanavyo na hata kama angehitaji kiasi gani cha fedha alikuwa tayari kumpa lakini mwisho wa siku akubaliane naye.

    “Nilivyokuwa na kiu ya mtoto, halafu wewe unaniambia niitoe mimba hii! Hivi unahisi nitakuelewa William? Siwezi kukuelewa hata kidogo,” alisema Cassey alipokutana na William.

    “Lakini nakuomba sana! Naona aibu sana Cassey, sijajua dunia itaniangaliaje! Nakuomba Cassey!” alisema William huku akionekana dhahiri kuchanganyikiwa.

    “Haiwezekani! Siwezi kuhatarisha maisha yangu kwa ajili ya kukufurahisha wewe, mwanaume unayeonekana hukuwa na mipango thabiti na mimi zaidi ya kunivua nguo, kunichezea na kuondoka zako,” alisema Cassey.

    Hakuubadilisha moyo wake, kila siku alimwambia hivyohivyo kwamba asingeweza kuitoa mimba hiyo. Alimaanisha alichokuwa akikisema, hakuteteleka, alimwambia kweli kwamba jambo hilo lisingeweza kufanikiwa hata mara moja.

    Siku zikaendelea kukatika mpaka Linda alipoanza kujisikia uchungu wa kutaka kujifungua, harakaharaka akachukuliwa na kupelekwa hospitali. Huko, William alikuwa nje akimsikilizia mpenzi wake ambaye alikuwa ndani ya leba akijifungua.

    Watu waliokuwa naye, wagonjwa wengine wakaanza kumpiga picha, kumuona William ilionekana kama bahati, halikuwa jambo la kawaida hata kidogo. Alitokea kupendwa sana, kila kona alipokuwa, watu walimfuata na kumpiga picha na wengine kupiga picha pamoja naye kwani mtandao wake wa MeChat kwa kipindi hicho ndiyo ulikuwa habari ya mjini.

    Siku hiyo, hospitalini hapo William hakuonekana kuwa sawa. Alionekana kuwa na hofu kubwa moyoni mwake. Kichwa chake hakikumfikiria Linda, kilimfikiria Cassey ambaye naye baada ya miezi nane angekwenda hospitalini na kujifungua. Alijua namna msichana huyo alivyompenda, alijua kabisa asingeweza kuvumilia kutunza siri, ilikuwa ni lazima awaambie waandishi wa habari kwamba alizaa na yeye.

    Wakati akiwa mahali hapo huku akiwa na mawazo tele, mara akaanza kusikia sauti ya mtoto ikilia kutoka katika chumba kile. Japokuwa alikuwa na mawazo tele, kidogo tabasamu likaonekana usoni mwake. Wala hazikupita dakika nyingi, mlango ukafunguliwa na kutakiwa kuingia kwa ajili ya kumuona mtoto wake.

    Akapiga hatua mpaka alipokuwa Linda, katika kitanda kingine kabisa na kumpa pole kwa kazi kubwa aliyokuwa nayo, hakuishia hapo, akaanza kumpiga mabusu mfululizo mashavuni mwake kuonyesha furaha kubwa aliyokuwa nayo moyoni mwake.

    “Hongera mpenzi wangu...” alisema William huku akiendelea kummwagia mabusu mfululizo.

    “Nashukuru sana mpenzi! Tumepata mtoto wa kiume,” alisema Linda huku akionekana kuwa na furaha tele.

    William akakifuata kitanda kilichokuwa pembeni na kumwangalia mtoto wake. Alionekana kuwa na sura nzuri, alichukua macho yake lakini sehemu kubwa ya sura yake alichukua kwa mama yake. William akatoa tabasamu pana, hatimaye aliitwa baba kwa mara ya kwanza, hakutaka kuchelewa, hapohapo akampa jina mtoto wake na kumuita William Jr.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mtoto akampa furaha kubwa maishani mwake, kidogo mawazo juu ya msichana Cassey yakaanza kupungua, akajiweka karibu na familia yake kama kujisahaulisha, kila wakati alikuwa akitabasamu, yote hayo yalikuwa ni kupoteza machungu aliyokuwa nayo juu ya msichana Cassey.

    Siku ziliendelea kukatika, baada ya wiki moja ya furaha tele, Cassey akamtumia meseji ya picha William ambayo ilimuonyesha akiwa amesimama, juu hana kitu huku akiwa amelishika tumbo lake na kusindikizia maneno machache yaliyosomeka ‘Am bout to be a baby mama’ akimaanisha kwamba alikuwa akijiandaa kuwa mama mtoto.

    Furaha ya muda mfupi aliyokuwa nayo William ikayeyuka moyoni mwake, hofu ikaanza kumuingia, mwili ukamtetemeka huku kijasho chembamba kikimtoka. Hakuamini kama Cassey angeweza kumtumia picha yenye ujumbe kama huo, hakutaka kukubali, hapohapo akampigia simu.

    “Cassey!”

    “Ndiyo baba watoto!”

    “Kwa nini umenitumia hiyo picha? Hujui kama nina mke?” aliuliza William huku akionekana kukasirika.

    “Una mke au hawara?”

    “We mpumbavu sana. Kwa nini umenitumia picha hiyo?”

    “Tatizo lipo wapi?”

    “Hujaona tatizo hapo?”

    “Sijaona! Au tatizo ni kumuonyeshea mwanaume matunda ya mbegu aliyoipanda?” aliuliza Cassey.

    “Cassey! Nina mtu nyumbani, unalifahamu hilo! Hivi unahisi itakuwaje kama akiiona hii picha?” aliuliza William.

    “Kwa hiyo hunipendi?”

    “Sijamaanisha hivyo!”

    “Umemaanisha nini? Humtaki mtoto wako?”

    “Nisikilize Cassey!”

    “Nijibu kwanza!”

    “Sasa si ndiyo unisikilize...”

    “Kama hunitaki! Ninajiua! Bora nife tu,” alisema Cassey na kukata simu.

    “Halo...halo...halo...” aliita William huku akionekana kuchanganyikiwa kwani hakutaka kabisa kusikia Cassey akijinyonga kisa yeye, alichokifanya ni kuligeuza gari lake na kuanza kuelekea nyumbani kwa msichana huyo kwani kwa jinsi alivyokuwa amemjibu, alijua tu kwamba ni lazima msichana huyo angejiua kama alivyomwambia.

    Aliendesha gari kwa kasi lakini baada ya dakika kadhaa akashangaa kuona foleni kubwa mbele yake, alichanganyikiwa, alijitahidi kupiga honi ili apishwe lakini hakukuwa na mtu aliyekuwa radhi kumpisha kwani kila mtu alionekana kuwa na haraka na mambo yake.

    Ikambidi avumilie huku akimuomba Mungu Cassey asichukue uamuzi wa kujiua kwa ajili yake. Baada ya dakika kumi ndipo magari yaliporuhusiwa na kuondoka mahali hapo.

    Huku akiwa njiani, ghafla simu yake ikaanza kuita, alipoichukua na kuangalia kioo, akakutana na jina la Cassey, harakaharaka akaipokea na kuiweka sikioni.

    “Cassey! Naomba usijiue...” alisema William mara baada ya kupokea simu.

    “Samahani! Bila shaka unamfahamu mwenye simu hii,” alisikika mwanaume kutoka upande wa pili, William akaogopa.

    “Ndiyo!” alisema huku akianza kulengwa na machozi.

    “Pole sana!” alisikika mwanaume huyo.

    “Ya nini?”

    “Mwenye simu hii ame....” alisikia sauti hiyo ikimwambia lakini hata kabla mtu huyo hajamaliza sentensi yake, kwa kuchanganyikiwa, gari la William likaacha njia, kwa kasi ya ajabu likaelekea pembeni ya barabara kulipokuwa na miti mingi, likaanza kuserereka huko kwa kasi huku likipindukapinduka.

    Akajigonga huku na kule, na kwa sababu hakuwa amefunga mkanda, akajikuta akitolewa ndani ya gari kupitia kwenye kioo cha mbele na kutupwa nje ambapo moja kwa moja akaenda na kuligonga bega lake katika mti mkubwa. Hapohapo akatulia, akahisi pumzi zikikata na kuona mtoa roho akianza kumnyemelea.



    Vijana wa Nicholaus hawakuacha kufika hospitalini hapo, walikuwa wakienda na kujifanya kwamba walikuwa na wagonjwa kumbe nyuma ya pazia walikuwa wakifuatilia kila kitu kilichokuwa kikiendelea.

    Kila kona, watu walizungumzia tukio lililotokea kwamba kulikuwa na daktari aliyetaka kumuua mgonjwa kitandani kitu kilichowafanya wagonjwa wengi kuhisi kwamba hawakuwa sehemu salama, hasa katika hospitali hiyo ambayo ilikuwa ikijulikana kila kona kutokana na huduma zake nzuri.

    Madaktari walichukia, walimwambia polisi aliyekuwa akilinda alinde kiuhakika na mwisho wa siku mgonjwa huyo apone na kurudishwa nyumbani huku akiwa salama kabisa.

    Ulinzi uliendelea kama kawaida. Kitu walichokifanya Kibra na vijana wenzake ni kutafuta mavazi ya kipolisi, yaliyofanana na polisi yule aliyekuwa akilinda katika chumba kile ili mmoja aende na kulinda yeye ili iwe rahisi kuingia ndani ya chumba kile.

    Baada ya siku mbili, tayari walipata mavazi ya polisi. Alitakiwa kuvaa kijana mmoja, walichokifanya kilikuwa ni kupanga dili kwamba ni lazima wamchukue msichana mmoja na kwenda kule hospitalini ambapo baada ya kufika ajifanye ameanguka na kuchukuwa na polisi yule.

    Hilo halikuwa tatizo hata kidogo, siku hiyohiyo wakampata msichana huyo na kumpanga na hivyo kuelekea hospitalini huku yule aliyetakiwa kuvaa kama polisi akiwa ameziweka nguo hizo katika mfuko wa plastiki na kuelekea chooni huku akifuatilia kwa kutumia masikio yake.

    Wakati msichana yule akipiga hatua kuelekea katika wodi moja, alipofika karibu na polisi yule akajifanya kuanguka kwa kuzidiwa na ugonjwa kitu kilichowafanya watu wote kushtuka. Haraka sana Melania, mama yake na polisi yule wakamsogelea pale alipoangukia na kisha kumuinua, hakuyafumbua macho yake, akajifanya kuzidiwa hivyo kuanza kumpeleka katika chumba kingine huku wakiongozwa na nesi mmoja.

    Kwa haraka sana jamaa aliyekuwa chooni ambaye tayari alikuwa na mavazi ya kipolisi akatoka chooni kule na harakaharaka kuanza kutembea kuelekea katika chumba kile.

    Watu walimuona lakini walipuuzia kwani kila mmoja aliamini kwamba huyo alikuwa polisi yule aliyekuwa ametoka. Hakutaka kuchelewa, kwa haraka sana akaingia ndani ya chumba kile, akayapeleka macho yake, yakatua kitandani, akamuona Godson akiwa amelala huku amejifunika shuka mwili mzima, hakutaka kuchelewa, akachukua sindano yake na kuanza kumsogelea pale kitandani alipokuwa tayari kwa kumuua.

    “Ni muda wake wa kufa,” alisema mwanaume huyo, harakaharaka akaitoa sindano tayari kwa kumchoma Godson kitandani pale.

    ****

    Ilikuwa ni ajali mbaya, kila aliyeiona alishika kichwa kwa mshtuko mkubwa, hawakuwahi kuliona gari likibingilika kwenye bonde kiasi kile zaidi ya kuangalia kwenye filamu tu.

    Waliokuwa wakipita na magari yao, wakayasimamisha na kisha kuteremka, waliliangalia gari lile lililokuwa bongeni kulipokuwa na miti mingi. Hawakujua kama dereva wa gari hilo alikuwa mzima au la.

    “Mungu wangu!” alisema mwanamke mmoja.

    Wanaume wawili wakaanza kuteremka kule bondeni huku wakimwambia mwanamke yule apige simu katika hospitali iliyokuwa karibu na mahali hapo na kuwaambia kile kilichokuwa kimetokea.

    Wanaume wale walipofika chini, wakavunja mlango na kumtoa William. Hakukuwa na aliyejua kama mtu huyo alikuwa William kwa jinsi alivyokuwa. Kichwa kilikuwa kinatoa damu, alikuwa ametulia tuli na kitu kilichowafanya kugundua kwamba alikuwa hai ni mapigo yake ya moyo yaliyokuwa yakidunda kwa mbali sana.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wakambeba na kumpeleka juu barabarani. Hakuwa akijitambua, walipomfikisha huko, wakamuingiza katika gari la wagonjwa ambalo lilifika mahali hapo kwa haraka sana na kuanza safari ya kuelekea hospitali.

    “Atapona kweli?” alisikika mwanaume mmoja akiuliza, zaidi ya magari kumi yalikuwa mahali hapo.

    “Inawezekana! Ila ameumia sana, yaani mpaka tumeshindwa kumtambua,” alisema mwanaume mmoja ambaye naye alimuona William alivyokuwa akipelekwa kule barabarani lakini hakujua kama alikuwa William kwa jinsi uso wake ulivyochakazwa kwa damu.

    Akapelekwa mpaka katika Hospitali ya Apostal Medical Centre iliyokuwa hapohapo Manhtattan. Walipofika, akateremshwa, akawekwa kwenye machela na kuanza kusukumwa kuelekea katika chumba cha upasuaji.

    Kila mtu aliyemuona, alimuonea huruma kwani kwa hali aliyokuwa nayo, kila mmoja alijua kwamba mtu huyo alikuwa akienda kufa. Walipofika katika chumba hicho, harakaharaka manesi wengine wakaingia na kuanza kumsafisha, walipomaliza, ndipo wakagundua kwamba mtu huyo alikuwa William.

    “Ni William,” alisema nesi mmoja huku akionekana kushtuka.

    “Unasemaje?”

    “Ni William,” nesi huyo alisikia hivyo, harakaharaka akayapeleka macho yake kwa mgonjwa huyo na kumwangalia, kweli alikuwa William.

    Huruma walizokuwa nazo zikaongezeka mioyoni mwao, hawakutegemea kumuona mtu huyo akiletwa hospitalini hapo baada ya kuumia vibaya katika ajali iliyotokea.

    Manesi hayo ndiyo waliosambaza taarifa hiyo kwa watu wengine na ndani ya dakika ishirini tu tayari waandishi wa habari walifika hapo na kutaka kujua ukweli kwani wao waliona kwenye mitandao ya kijamii kwamba mwanaume huyo alikuwa amepata ajali mbaya ya gari.

    “Sisi si wasemaji wa hospitali,” alisema nesi mmoja.

    “Basi sawa. Tunahitaji kuonana na wasemaji,” alisema mwandishi mmoja.

    Wakachukuliwa na kupelekwa katika ofisi ya daktari huyo ambaye aliwapa taarifa kamili kwamba ni kweli William alikuwa amepata ajali mbaya ya gari na hali yake haikuwa nzuri kabisa. Aliwaambia kila kitu huku wakionekana kuwa na hofu kwamba inawezekana mwanaume huyo alikuwa amekufa kwenye ajali hiyo ila walifichwa.

    “Ila taarifa zinasema kwamba amekufa!” alisema mwandishi mmoja.

    “Hiyo ni taarifa ya mitandaoni. Mmekuja kwangu kwa kuwa mnataka kupata taarifa ya hospitali, kwa hiyo nawaambieni hajafa na hatokufa kwa kuwa yupo kwenye mikono salama,” alisema daktari huyo huku akionekana kumaanisha alichokuwa akikizungumza.

    Taarifa hizo ziliendelea kusambazwa na baada ya dakika kadhaa, Linda akapigiwa simu na wazazi wake ambao walitaka kuonana naye.

    “Upo wapi?” aliuliza mama yake.

    “Nyumbani!”

    “Tunakuja!”

    Hawakutaka kumwambia kwenye simu, walijua hali aliyokuwa nayo, kama wangempa taarifa juu ya kilichokuwa kimetokea basi wangeweza kusababisha matatizo mengine.

    Baada ya dakika kadhaa wakafika nyumbani hapo. Kwa jinsi alivyoonekana, Linda hakujua kilichokuwa kimetokea, aliwakaribisha huku akiwa na furaha tele na hivyo kuanza kuzungumza naye huku wakimkazia macho.

    “William alikupigia simu lakini hakuwa amekupata,” alisema mama yake.

    “Mbona simu ipo hewani!”

    “Hatujajua kwa sababu gani. Alitupigia na kutuambia kwamba alijisikia kuumwa kichwa hivyo alipitia hospitali,” alisema mama yake, kidogo Linda akashtuka.

    “Mbona hakuja nyumbani au kumpigia simu dokta wa familia?” aliuliza Linda.

    “Hatujajua! Ila hali yake si nzuri, alisema kichwa kinamsumbua sana,” alisema baba yake.

    Linda alihuzunika, aliwaamini wazazi wake, hakugundua kama alikuwa akidanganywa, walichokifanya ni kuondoka nyumbani hapo na kwenda hospitalini. Hakuwa na mawazo sana, kitu alichokifikiria ni kwamba mume wake alikuwa akiumwa kichwa kweli.

    Hawakuchukua dakika nyingi wakafika hapo hospitalini. Hali aliyokutana nayo ikaanza kumtisha, kulikuwa na idadi kubwa ya watu huku kukiwa na waandishi wengi waliomtia hofu na kuhisi kulikuwa na kitu. Kitendo cha kuteremka kutoka garini, waandishi wakamfuata kwa lengo la kumuhoji.

    “Unajisikiahe?” alimuuliza mwandishi mmoja.

    “Kuhusu?”

    “Kifo cha mume wako,” alijibu mwandishi huyo.

    Hakufuata miiko ya kazi, aliuliza swali ambalo hakuwa na uhakika nalo hata kidogo. Linda akashtuka, hakuamini kile alichokuwa ameulizwa, hakujibu kitu, alibaki amepigwa na butwaa, alimwangalia vizuri mwandishi huyo na ndipo alipopata jibu la watu wengi kukusanyika mahali hapo kwa wingi namna ile.

    Huku akiwa kwenye hali hiyo, mama yake akamvuta na kisha kuondoka naye huku waandishi wa habari wakitaka kuzungumza naye ka kumuhoji baadhi ya maswali kitu ambacho wazazi hao hawakutaka kuona kikitokea.

    Bila kutarajia, machozi yakaanza kumtoka mashavuni mwake, hakuamini kama kweli mpenzi wake, William alifariki dunia. Hakutembea kwa mwendo mrefu ndani ya jengo la hospitali hiyo, akasimama, akaona miguu kuwa mizito, akataka kuanguka, baba yake akamuwahi, akamdaka na kumpeleka kwenye benchi ambapo hapo, Linda akaanza kulia mfululizo huku akilitaja jina la mume wake. Kwa kifupi, alichanganyikiwa.





    Watu waliendelea kumiminika hospitalini hapo huku kila mmoja akitaka kujua undani juu ya ajali iliyokuwa imetokea. Wapo waliohisi kwamba kulikuwa na mchezo ulifanyika, kuna baadhi ya mabilionea walitaka kumpoteza William kwa kuwa tu alikuwa mtu aliyekuja juu kifedha na kulikuwa na kila dalili za kuwapiku katika utajiri wao.

    Hospitalini hapo, hakukuwa na aliyecheka, kila mmoja alionekana kuwa na uso uliokuwa na huzuni tele. Wengi walipata taarifa kwamba William alikufa hivyo walitaka kupata ufafanuzi juu ya mahali ambapo mazishi hayo yangefanyika na hata kanisa ambalo wangelitumia kumuaga sura ya mwisho.

    Dunia ilikuwa kimya, kila mmoja aliyeisikia taarifa hiyo hakuamini kama kweli William alikuwa hai, na kama alikuwa hai hakukuwa na mtu aliyehisi kama mwanaume huyo angeinuka tena kitandani alipolala.

    Madaktari walihangaika mno, walijaribu kuyaokoa maisha yake kwani kadiri dakika zilipokuwa zikienda mbele, mapigo yake ya moyo yalikuwa yakishuka sana hivyo kumuwekea dripu iliyokuwa na dawa ya kushtua zaidi mapigo yake ya moyo.

    Walipambana, aliumia zaidi kichwani, alikuwa ametoka damu lakini kwa wakati huo hawakutaka kushughulika na kichwa, kitu muhimu kilikuwa ni kuhakikisha mapigo yake ya moyo yanarudi na kuwa katika hali ya kawaida kabisa.

    Baada ya kumuwekea dripu zaidi ya nne zilizokuwa na dawa Melphonilyze ambayo ilitumika kushtulia mapigo ya moyo ndiyo kidogo ikamsaidia na hatimaye kuanza kurudi katika hali yake ya kawaida, kilichotakiwa kufanyika ni upasuaji wa kichwa chake tu kuangalia tatizo lilikuwa nini.

    “We must perfom craniotomy surgery,” (ni lazima tumfanyie upasuaji wa kichwa) alisema daktari mmoja aliyekuwa na kibati kilichoandikwa Dr. Pham.

    Hakukuwa na kuchelewa, ili kufanikisha kile walichotaka kukiangalia ilikuwa ni lazima wamfanyie upasuaji wa kichwa kwani walihisi kwamba damu ziliweza kuvilia kwenye ubongo kitu ambacho kingemletea tatizo kubwa zaidi.

    “Play the music,” (washa muziki) alisema Dk. Pham.

    “Which one?” (upi?)

    “Abba’s 1977 While the Music still Goes On,” (While the Music Still Goes On wa Abba wa mwaka 1977) alisema Dk. Pham na daktari mmoja kuwasha muziki.

    Ilikuwa ni kawaida yao katika kila wakati walipokuwa wakikutana na upasuaji mkubwa ilikuwa ni lazima kuwasha muziki na kusikiliza huku wakiendelea kufanya upasuaji huo.

    Muziki huo ukawashwa na kuanza kufanya upasuaji huo. Walikuwa wakizungumza, wakicheka kwani waliamini kwamba upasuaji haukutakiwa kuwa siriazi sana kwa kuogopa kuingiwa na hofu, hivyo hali hiyo ingewafanya kuona kile kilichokuwa kikitokea kuwa cha kawaida sana.

    Upasuaji ukaanza, baada ya kukichana kichwa cha William, wakaanza kutoa kipande cha fuvu ambacho kitaalamu huitwa Bone Flap na kisha kukiweka pembeni kwa ajili ya kuangalia ndani ya ubongo kuona kulikuwa na nini.

    Wakati wakiendelea kufanya upasuaji huo bado walikuwa wakizungumza huku wakikiangalia kichwa hicho kwa makini kabisa ambapo huko wakaliona donge la damu likiwa limeganda katika ubongo wake, tena kwa kujificha ndani ya ubongo kwa mbali.

    “Ooh my God!” (Ohh Mungu wangu) alisema Dk. Pham huku akionekana kushangaa.

    “What is it?” (kuna nini?) aliuliza nesi mmoja.

    “This is brain hemorrhage,” (damu imevuja kwenye ubongo) alijibu Dk. Pham.

    Kila mmoja alishtuka, hawakuamini kusikia kwamba damu ilikuwa imevilia katika ubongo wa William. Hilo lilikuwa tatizo kubwa ambalo kwa watu wengi waliokuwa wakipata tatizo hilo, asilimia themanini walikuwa wakifa kwani damu huwa na kawaida ya kusambaa kwa haraka sana katika ubongo kuliko sehemu nyingine yoyote ile.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Waliogopa, waliuona mwisho wa William ukiwa mikononi mwao kwani hata kama angepona ilikuwa ni lazima kupata matatizo mawili, iwe ugonjwa wa kusahau kila kitu kilichotokea katika maisha yake yote au nusu ya maisha lakini pia ilikuwa ni kupata ugonjwa wa kupooza ambao ungeyatesa maisha yake kitandani.

    Japokuwa walikuwa wakiimba lakini baada ya kugundua hilo, kila mmoja akabaki kimya, wakaanza kuangalia, damu ilikuwa kwenye ubongo na kwa bahati nzuri sana kwa William ni kwamba ilikuwa kama donge moja la damu na si kwamba ilisambaa.

    “We have to remove it without soring a brain,” (ni lazima tuiotoe damu pasipo kuutonesha ubongo) alisema Dk. Pham huku akiliangalia donge lile la damu.

    “We have ten hours to perfom this craniotomy,” (tuna saa kumi za kufanya upasuaji huu wa kichwa) alisema Dk. Pham, na mpaka kipindi hicho, tayari yalikuwa yamepita msaa mawili.

    Upasuaji ulikuwa ukiendelea, Dk. Pham na wenzake hawakutoka ndani ya chumba kile, walijua kwamba nje kulikuwa na watu wengi waliokuwa wakisubiri kuona ni kitu gani ambacho kingetokea ndani ya chumba kile.

    Donge la damu halikutoka kirahisi, kila walipoligusa kwa maana ya kulitoa, lilihama na kuhamia sehemu nyingine kitu kilichowapa usumbufu mkubwa kwani mpaka wanakamilisha kulitoa, tayari walitumia saa sita na hivyo kuanza kurudishia fuvu taratibu.

    Mpaka wanamaliza, walichukua saa kumi na mbili, walichoka, hawakuwa na matumaini kama William angepona kwani kila walipokuwa wakiangalia mashine ya Mult Parameter Monitor mapigo yake ya moyo yalionyesha kushuka kwa ghafla na kupanda.

    “We have to pray for him,” (inabidi tumuombee) alisema Dk. Pham.

    Hawakuwa na jinsi, kadiri walivyomwangalia William kitandani pale walikiri kwamba mwanaume huyo alikuwa akienda kufa. Hali yake ilitisha na kila walipomwangalia, mioyo yao iliwaambia kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wa William kuvuta pumzi ya dunia hii.

    Baada ya kumaliza kusali, wakatoka na moja kwa moja Dk. Pham kuwaita wazazi na Linda ofisini kwake kwa ajili ya kuzungumza nao. Hakuwaficha, aliwaambia ukweli juu ya kila kitu kilichokuwa kikiendelea kwamba kijana wao alikuwa kwenye hali mbaya na kama wasingemuomba Mungu basi angeweza kufariki dunia kitandani hapo.

    “Hatuna ujanja zaidi ya kusali sana, tukishindwa, basi atakufa kwani nisingependa kuwaficha, watu wanaopata tatizo hili, wengi hufa japokuwa kwa William tunajaribu kupambana,” alisema Dk. Pham japokuwa alikuwa akizuiliwa kuwaambia ndugu wa wagonjwa maneno kama hayo lakini hakuwa na jinsi.

    Linda alikuwa akilia, moyo wake ulikuwa ukimuuma mno na alikuwa amebakiza wiki moja kabla ya kujifungua lakini mumewe alikuwa hoi kitandani. Hakutaka kumwangalia hapo alipolala kwani alihisi angeumia zaidi, angelia na hatimaye mimba yake kuharibika.

    ****

    “Mandy! I want to see you,” (nataka nikuone Mandy) alisema Cassey kwenye simu, alikuwa akizungumza na rafiki yake kipenzi.

    “Is there something wrong?” (kuna tatizo huko?)

    Cassey alitaka kuzungumza na rafiki yake kipenzi na ndiyo maana alimpigia simu kwa lengo la kukutana naye na kuzungumza naye mambo mawili matatu.

    Moyo wake ulikuwa ukimuuma, kila alipokuwa akiiona habari ya William kwenye mitandao ya kijamii na televisheni, alijiona kuwa mkosaji kwa kuwa alijua fika kuwa mwanaume huyo alipata ajali baada ya kumwambia kwamba alitaka kujiua.

    Mandy hakuchelewa, ndani ya nusu saa alikuwa ndani ya nyumba ya rafiki yake, Cassey na kuanza kuzungumza naye. Hakutaka kumficha, alimwambia jinsi alivyokuwa akijuta kwa kile kilichotokea na wakati mwingine alijiona kuwa mkosaji mkubwa. Alimwambia kila kitu kilichokuwa kimetokea, tangu siku aliyomwambia William kwamba alikuwa na mimba yake mpaka siku hiyo.

    “Kwa hiyo alipopata ajali alikuwa akikukimbilia wewe?” aliuliza Mandy!”

    “Ndiyo!”

    “Na ulitaka kweli kujiua?”

    “Hapana! Nisingeweza, nilitaka kuona kama anajali. Nimefanya upumbavu mkubwa sana Mandy! Ninajuta, ninajuta kuufanya utoto kama huo,” alisema Cassey huku akilia kama mtoto.

    “Pole sana rafiki yangu!”

    Cassey hakutaka kubaki nyumbani, ilikuwa ni lazima kwenda hospitali kumuona William. Alipokwenda huko na kuteremka, waandishi wa habari wakamsogelea na kisha kuanza kumpiga picha.

    Alikuwa msichana maarufu na ujio wake mahali pale uliwafanya waandishi wa habari kutokutulia na hivyo kutaka kumuhoji maswali machache. Hakujibu kitu, kwa jinsi alivyoonekana tu alionyesha ni jinsi gani alikuwa na mawazo tele na moyo uliojaza maumivu makubwa.

    Alikwenda mpaka ndani ya hospitali hiyo. Alipomuona Linda, moyo wake ulizidi kuchoma kwani alijiona mkosaji kwa kuona kabisa kwamba kile kilichokuwa kimetokea, yeye ndiye alisababisha hali hiyo. Akawafuata pale alipokuwa na kuwapa pole.

    Cassey alikuwa msichana wa kwanza maarufu kufika hospitalini hapo lakini baada ya siku mbili, zaidi ya masupastaa ishirini walifika mahali hapo kwa ajili ya kumpa pole Linda na wazazi kwa kile kilichokuwa kimetokea.

    William aliendelea kuwa kimya kitandani, siku ya kwanza ikapita, hakuzinduka, ya pili ikaingia na hatimaye wiki nzima kukatika lakini bado alikuwa kimya tu.

    Mpenzi wake Linda akajifungua huku akiendelea kuwa kitandani hapo. Hakujua kama alikuwa baba, aliendelea kuteseka huku akiendelea kupumulia mashine ya oksijeni kwani vinginevyo angeweza kufa palepale.

    Baada ya miezi miwili kupita ndipo William akaamka kitandani, akayafumbua macho yake, alipona, kichwani kulikuwa sawa na mapigo yake ya moyo yalikuwa yakidunda kawaida, na hata lile bega lililokuwa limeumia, kidogo alijisikia nafuu.

    “William ameamka,” alisema nesi mmoja baada ya kumuona akifumbua macho, aliamua kumwambia Dk. Pham ambaye alikwenda katika chumba kile, kweli William alikuwa amefumbua macho lakini hakuzungumza kitu chochote kile.

    Wazazi walipopewa taarifa, hawakuamini, hata Linda aliposikia, alitaka kujionea hivyo Dk. Pham kuwaruhusu kumuona mgonjwa huyo aliyekaa kitandani kwa miezi miwili pasipo kuzungumza kitu chochote.

    Walipoingia ndani na kumuona, wakaachia tabasamu pana lakini kwa William alionekana kuwa tofauti kabisa. Alibaki akiwaangalia huku akiwakodolea macho.

    “My husband....”(mume wangu!) aliita Linda, akamsogelea pale kitandani na kumkumbatia.

    “Who are you? Do we know each other?” (wewe ni nani? Tunafahamiana?) aliuliza William huku akimwangalia Linda machoni kwani alionekana kuwa mgeni, mtu ambaye hakuwahi kumuona katika maisha yake. Kwa kifupi, kitendo cha damu kuingia kwenye ubongo wake, ukafuta kumbukumbu zake za miezi kadhaa nyuma kabla ya kuelekea nchini Marekani.

    “Mwanangu....” aliita mama yake.

    “Mama! Huyu ni nani? Nipo wapi? Mbona nipo na Wazungu? Kuna nini mama?” aliuliza William.

    “Mwanangu....”

    “Mama! Ninahitaji kumuona Melania! Nilipanga kuonana naye. Mungu wangu! Nilimkataa Melania, ameumia sana, kwa nini nimemuumiza msichana wa watu! Mama, Melania yupo wapi? Mama nataka nimuone Melania nimuombe msamaha,” alisema William huku akianza kulia. Hakukumbuka kitu chochote kile, hakukumbuka kama alikwenda nchini Marekani kusoma chuo, kitu alichokikumbuka ni mama yake na msichana Melania tu.



    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Polisi walikuwa na akili, walijua fika kwamba ilikuwa ni lazima muuaji arudi tena ndani ya hospitali hiyo na kukamilisha kile alichokitaka kwani mara ya kwanza alipotaka kumuua Godson, hakufanikiwa.

    Walichokifanya katika usiku wa siku hiyo ni kumtaka Dk. Sam amuhamishe Godson ndani ya chumba kile na kumpeleka katika chumba kingine kabisa pasipo madaktari wengine wala wazazi wake kufahamu.

    Hilo likafanyika kwa haraka, hakukuwa na nesi aliyemwambia, daktari aliyemsaidia kumuhamisha Godson ndani ya chumba kile alikuwa Dk. Mshana ambapo wakaifanya kazi hiyo na polisi mmoja kuagizwa kwenda ndani ya chumba kile, alale kitandani, atakaposikia mlango unafunguliwa, basi ajifunike na kushika bastola yake.

    Hilo ndilo lililofanyika kwa siku mbili. Wazazi wake hawakuruhusiwa kumuona kwa kisingizio kwamba hakuwa katika hali nzuri baada ya tukio la kutaka kumuua kufanyika.

    Siku ya kwanza ikapita, ya pili ikaingia na ndipo siku ya tatu vijana wale wakarudi kwa ajili ya kufanya kile walichotaka kukifanya. Mpaka msichana huyo anaanguka, polisi alijua kwamba ulikuwa ni mchezo, alihisi kwamba alifanya hivyo kwa kuwa kuna mtu alitaka kuingia ndani ya chumba hicho, hakutaka kulizuia hilo, alichokifanya ni kumsaidia msichana huyo kisha kumpeleka sehemu.

    Huku nyuma kijana yule akaingia ndani ya chumba kile, akakisogelea kitanda, mgonjwa aliyekuwa kitandani, alijifunika shuka mwili mzima, kijana yule hakujua kama mtu aliyelala alikuwa polisi, akamsogelea na kisha kuchukua sindano yake kwa lengo la kumchoma lakini kabla hajafanya lolote lile, akashtukia akidakwa mkono, shuka likatolewa, akapigwa na mshtuko baada ya kuona mdomo wa risasi ukimwangalia.

    “Tulia hivyohivyo! Ukipiga kelele tu, nakumwaga ubongo,” alisema polisi huyo huku akimwangalia muuaji aliyekuwa akitetemeka.

    “Nisamehe bro!” alisema huku akitetemeka.

    Kabla hajafanya kitu chochote, akampiga pingu kijana yule, mkono mmoja ulifungwa pingu na sehemu nyingine ya pingu kufungwa kwenye kitanda kisha polisi yule kupiga simu.

    “Nimempata!” alisema huku akimwangalia kijana yule kwa hasira.

    “Muulize wenzake walipo tuwafanyie kazi sasa hivi,” ilisikika sauti upande wa pili na hivyo polisi yule kuanza kumuuliza mwanaume yule.

    Alimwambia, hakutaka kumficha kwani aliambiwa kwamba kama angemficha basi ingekuwa hatari zaidi katika maisha yake. Akamwambia kwamba wenzake walikuwa nje, kwenye gari moja, Vitz yenye rangi ya bluu wakiwa wanamsubiri.

    Polisi yule akawapa maelekezo wenzake ambapo wakaelekea huko na kweli kulikuta gari hilo ambapo wakalizunguka na kuwakamata vijana wawili waliokuwa wamebaki ndani ya gari hilo.

    Kule ndani, kijana yule akatolewa, akafungwa pingu mikono yote kwa nyuma na kushikwa na kuanza kutolewa nje. Wazazi wa Godson na Melania walibaki wakishangaa, hawakuamini kile walichokiona, ilikuwaje ndani ya chumba alicholazwa kijana wao watoke wanaume wengine ambao hawakuwa wakiwafahamu?

    “Imekuwaje?” aliuliza baba yake Godson.

    “Huyu ndiye alitaka kumuua mwanao!” alijibu polisi.

    “Mwanangu?”

    “Ndiyo!”

    Vijana wale wakachukuliwa na kupelekwa katika kituo cha polisi na kuambiwa kwamba kitu walichotakiwa kufanya kilikuwa kimoja tu, kumtaja mtu aliyekuwa amewatuma kufanya mauaji hayo.

    Hawakusema, walibanwa sana lakini wakanyamaza, kila walipoulizwa swali hilo walibaki kimya kitu ambacho kwa polisi wa kituo hicho waliona kama wakidharauliwa.

    “Kamuite Kunta Kinte,” aliagiza mkuu wa kituo hicho.

    Ndani ya dakika mbili, kipande cha mwanaume kikaingia, alikuwa mweusi tii kama mtu aliyejipaka masizi, alijazia vilivyo, mikono yake ilikuwa mipana, uso wake ulikuwa mbaya mithili ya sokwe mtu.

    Alisimama mbele ya mkuu wa kituo kile kwa heshima kubwa, alipiga saluti na kuibana mikono yake vilivyo. Akaambiwa kwamba vijana watatu waliokuwa mbele yake hawakutaka kujibu kile walichokuwa wanauliza.

    “Acheni utani,” alisema mwanaume huyo huku akionekana kushangaa.

    “Kweli tena!”

    “Wanakataaje sasa?”

    “Hata sisi tunashangaa!”

    “Eti ni kweli mmekataa kujibu maswali?” aliuliza mwanaume yule huku akiwaangalia lakini vijana wale walikuwa kimya.

    “Naombeni dakika tano tu! Watasema kile tunachotaka kukifahamu!” alisema mwanaume huyo, hakutaka kuwachukua wote, akamchukua kijana mmoja na kuingia naye kwenye chumba kilichoandikwa ‘Usipige Kelele’ mlangoni.

    Ndani ya chumba hicho kulionekana kutokuwa sehemu salama, kulikuwa na michirizi ya damu, nyundo, mapanga, fimbo, beseni la maji, plaizi, taulo, kiti kilichokuwa na tundu kubwa sehemu ya kukalia na vitu vingine vingi kwa ajili ya kuwatesea watu waliokuwa makaidi.

    Mlango ukafungwa na kilichosikia ndani ya dakika moja ni kelele za maumivu makali kutoka kwa kijana yule. Alikuwa akipiga kelele huku akimwambia mwanaume huyo kwamba alikuwa tayari kumwambia mtu aliyekuwa amewatuma.

    “Najua utaniambia, ila sitaki uniambie sasa hivi, kwanza tuendelee kufanya mazoezi ya kijeshi,” alisikika mwanaume huyo lakini kijana yule alisisitiza kwamba alikuwa tayari kumwambia juu ya mwanaume aliyekuwa amewatuma kufanya mauaji yale.

    Baada ya dakika kadhaa, wakasikia jina la Nicholaus likitajwa. Mwanaume huyo akaridhika, akafungua mlango na kisha kumtoa kijana huyo ambaye alipotolewa ndani ya chumba kile, akalala chini, mwili ulitapakaa damu na hata kusimama hakuweza.

    “Mleteni mwingine!” alisema mwanaume huyo huku akichukua sigara yake na kuiwasha.

    Wote watatu walipoingizwa ndani ya chumba hicho, kwa jinsi walivyopewa mateso, walimtaja mtu aliyekuwa amewatuma kufanya mauaji yale. Jina la Nicholaus likatajwa na kila mmoja hivyo walichotakiwa kufanya ni kuhakikisha kwamba mwanaume huyo anapatikana haraka iwezekanavyo.

    ****

    Kila mtu alikuwa akimshangaa William, hakuwa akikumbuka kitu chochote kile na kila alipokuwa akizungumza, alizungumza kuhusu msichana Melania tu. Walimshangaa, alisahau kila kitu, hakumkumbuka mtu yeyote katika maisha yake zaidi ya watu wawili ambao alikuwa nao kwa karibu sana alipokuwa nchini Tanzania, mama yake na msichana huyo.

    Mkewe alikuwa akilia, hakuamini kama mumewe alimsahau kwani kila alipomwangalia, hakuonekana kumkumbuka hata kidogo na kila wakati alikuwa akimuuliza kwamba alikuwa nani na kwa nini alikuwa mahali hapo.

    “Mama! Nataka kuondoka! Nataka niende nikamwambie Melania kwamba anisamehe, labda ndiye mwanamke wangu sahihi, mama naomba nikaonane na Melania,” alisema William huku akiinuka kitandani pale.

    Kila kitu alichokiona kilikuwa kipya, hakujua sababu iliyomfanya kuwa mahali hapo, na hata alipoambiwa kwamba alikuwa nchini Marekani, alishangaa, alifikaje na wakati alikuwa nchini Tanzania?

    “Marekani? Nimefikaje?” aliuliza William.

    “Ulikuja!”

    “Hapana! Sikuwahi kuja Marekani! Mama! Hivi tuna hela kiasi gani za kuja nchini Marekani? Nilikuwa na mpango wa kuhack barua pepe ya Chuo Cha Harvard lakini sikuwahi kufika! Sasa nimefikaje? Mama! Nataka nikachukue hela, jana nimewachezea mchezo mchafu sana wale watu wa benki, ngoja nikaangalie kama hela imeingia,” alisema William.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Maneno yote hayo alikuwa akiyazungumza harakaharaka. Hakutaka kubaki humo ndani, akatoka. Hakuijua sehemu yoyote ile, alikuwa akishangaa, nje, akakutana na waandishi wa habari na kuanza kumpiga picha.

    Hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea, alishangaa, wakati mwingine alihisi kama alikuwa akiota kwani hakuwahi kufikiria kama angefika nchini Marekani, na kitu kilichomshangaza zaidi ni jinsi alivyokuwa akipigwa picha.

    “Who are you?” (nyie ni wakina nani?) aliuliza William huku akishangaa.

    Alichokifanya daktari ni kuwatuma watu wamchukue William na kisha kumpeleka ndani. Hilo likafanyika, baada ya kupelekwa ndani na kuambiwa atulie, Dk. Pham akawaita wazazi na Linda kwa ajili ya kuzungumza nao.

    Akawaambia kwamba hawakutakiwa kushangaa kile kilichokuwa kikiendelea kwani ndiyo hali iliyomkuta William hivyo walitakiwa kukubaliana naye na baada ya miezi michache hali yake ingerudi kama kawaida kama alivyokuwa na angekumbuka kila kitu.

    “Kwa hiyo tufanye nini?”

    “Nendeni naye Tanzania! Naamini akifika huko, mazingira atakayokutana nayo yanaweza kumsaidia kukumbuka, kwa hapa Marekani, ni vigumu sana kutokea,” alisema Dk. Pham huku akiwaangalia.

    Hicho ndicho walichokifanya, baada ya siku mbili wakaondoka na kurudi nchini Tanzania. Marekani, kila mmoja alishangaa, hawakuamini kama ajali ile aliyoipata William ingemfanya kuwa kwenye hali ile ya kupoteza kumbukumbu zake.

    Ndani ya ndege alikaa na mkewe, Linda, alikuwa akimuongelesha lakini William hakusema kitu chochote kile, hakumfahamu, ndiyo kwanza alikuwa amemuona na kila alipotaka kumkumbusha, alimnyamazisha kwa kumwambia anyamaze kwani hawakuwa marafiki.

    “Lakini nata...”

    “Wewe mwanamke nimesema nyamaza. Tangu hospitalini unanifuatilia tu, nimesema nyamaza na sitaki uniongeleshe kitu chochote kile,” alisema William huku akimwangalia Linda.

    Linda aliumia lakini hakuwa na jinsi. Safari iliendelea na baada ya saa ishirini na mbili, ikatua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere ambapo wakateremka na kuchukua teksi ambayo iliwapeleka mpaka nyumbani kwao.

    Walipofika William alionekana kukasirika kwani kila walipokwenda, Linda alikuwa pamoja nao. Alimchukia, kila alipomwangalia na mtoto yule aliyekuwa amemshika ambaye alionekana kuwa mdogo wa miezi miwili, moyo wake ulimkasirisha mno na wakati mwingine alitamani hata kumfukuza.

    Linda hakutaka kumuacha William, aliamini kwamba kuna siku kumbukumbu zake zingerudi na kuanza kukumbuka kila kitu kilichotokea. Nchini Tanzania, kila mtu alimshangaa, alikuwa kijana mdogo mwenye sura mbaya lakini kila mmoja alikuwa akimfahamu.

    Watu hawakukauka nyumbani kwake, walifika hapo na kuanza kumpiga picha kitu kilichomshangaza, kwa nini apigwe picha na wakati hakuwa mtu maarufu au kiongozi wa nchi?

    “Mama! Nini kinaendelea? Mbona sielewi kitu chochote kile? Yaani nashangaa watu wanakuja na kunipiga picha kana kwamba mimi ni maarufum” aliuliza William huku akimwangalia mama yake.

    “Mwanangu! Wewe ni maarufu sana!”

    “Maarufu! Kivipi?” aliuliza William.

    Kwa msaada wa maelezo, Linda akaanza kumwambia William kila kitu kilichokuwa kimetokea, siku ya kwanza alipofika Marekani mpaka alipopata ajali mbaya ya gari. Hakuamini, alibaki akimsikiliza Linda, hakumuelewa kabisa hasa pale alipomwambia kwamba alikuwa mpenzi wake.

    Alimwangalia, hakumkumbuka hata kidogo, alishangaa kwani maishani mwake hakufikiria kuwa na msichana wa Kizungu. Hakukumbuka kitu chochote kile, hata alipomwangalia William Jr hakuwa akimfahamu kabisa, kwake alimuona kuwa mtoto wa kigeni na si wake.

    “Na huyu ni mtoto wako,” alisema Linda huku akimwangalia William usoni, kama kulia, alilia sana lakini hakukuwa na kitu kilichobadilika.

    “Mtoto wangu?”

    “Ndiyo!”

    “Sijawahi kuwa na mtoto. Kwanza sijawahi kuwa na demu,” alisema William huku akimwangalia Linda.

    Alimaanisha, alichokuwa akikisema kwake kilionekana kuwa sahihi kabisa. Hakukumbuka kama alikuwa na msichana, hakupendwa kwa kuwa alikuwa na sura mbaya, alimwangalia Linda, alipomwambia kwamba alizaa naye, alishangaa kwani hakuwahi kufikiria kupendwa na msichana mzuri kama alivyokuwa Linda.

    Wakati hayo yakiendelea ndipo alipofungua televisheni na kuona habari ambayo ilimshtua sana, ilikuwa ni ya harusi ya mtoto wa bilionea, Melania na kijana aliyejulikana kwa jina la Godson.

    Akashtuka, alichokikumbuka ni jana tu alitoka kuzungumza na msichana huyo kwenye mgahawa, iweje leo tangazo litokee na kuona kwamba msichana huyo alikuwa akitarajia kuolewa.

    Alihuzunika moyoni mwake, alihisi kwamba Melania alimwambia kwamba alitaka kuwa naye kwa ajili ya kumuumiza tu na ndiyo maana kesho yake harusi yake ilikuwa ikitangazwa.

    Hakutaka kubaki nyumbani, siku iliyofuata alikuwa kanisani. Humo, alikuwa gumzo, kila mtu alikuwa akimwangalia, hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea, watu walimshangaa na hawakujua sababu iliyomfanya kurudi nchini Tanzania ghafla namna hiyo na wakati alikuwa mtu maarufu sana.

    Kanisani, watu hawakutulia, kila mtu alimsogelea, hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea kwani alijiona kuwa mtu wa kawaida, hakuwa maarufu, sasa ilikuwaje watu waendelee kukusanyika mbele yake kiasi kile?

    “William! Pole sana kaka! Nimesikia majanga uliyopata miezi miwili iliyopita,” alisema mwanaume mmoja aliyekaa karibu naye, William akashangaa kwani aliamini kwamba hakukuwa na mtu aliyekuwa akimfahamu, huyo alimfahamu vipi?

    “Unanifahamu?” aliuliza William huku akionekana kushangaa.

    “Sasa nisikufahamu wewe kaka? Kila mtu anakufahamu! Mpaka rais,” alisema kijana huyo.

    “Hapana! Hakuna mtu anayenifahamu!”

    “Wewe huoni jinsi watu wanavyokushangaa?”

    “Kwa nini wananishangaa? Au kwa sababu mimi mbaya?”

    “Hapana! Ni kwa sababu wewe ni maarufu,” alijibu kijana huyo.

    Haikuwa mara ya kwanza kuambiwa hivyo, aliambiwa mara kadhaa kwamba yeye alikuwa maarufu na hakujua umaarufu wake ulitokana na nini. Aliendelea kukaa kwenye kanisa lile mpaka maharusi walipoanza kuingia. William akasimama, akaanza kumwangalia Melania, uso wake ulikuwa kwenye furaha kubwa, siku hiyo msichana huyo alionekana kuwa mrembo sana.

    Melania alipokutanisha macho yake na William, alishangaa, ilikuwaje mwanaume huyo kuwa kanisani kipindi hicho na wakati alikuwa nchini Marekani akiendelea na maisha yake?

    Hakuzungumza kitu zaidi ya kumuonyeshea tabasamu na kisha kuelekea mpaka mbele ya kanisa lile ambapo huko, harusi ikafungwa na kuwa mke wa Godson.

    “Melania....Melania...” aliita Godson huku akimfuata msichana huyo aliyekuwa akijiandaa kuingia ndani ya gari la maharusi.

    “William! Mbona upo hapa?” aliuliza Melania.

    “Nimekuja kwenye harusi yako. Jana tulipoagana, nikajikuta nikiwa Marekani,” alisema William.

    “William! Upo sawa?”

    “Ndiyo! Hivi kwanza niambie kuhusu yule jamaa!”

    “Jamaa gani?”

    “Niliyemfutia picha zako!”

    “Ni stori ndefu, ila kwa kifupi ni kwamba amekamatwa na polisi. Amefikishwa mahakamani na kufungwa miaka mitano kwa sababu alitaka kumuua mume wangu,” alisema Melania.

    “Mume wako?”

    “Ndiyo! Huyu hapa!”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Alitaka kumuua kivipi? Mbona unanichanganya! Si alikuwa nchini Australia! Au walikutana huko?” aliuliza William huku akimwangalia Melania aliyebaki akiwa na mshangao.

    Wakati wakizungumza hayo, waandishi wa habari walikuwa wakiwapiga picha tu. Wengi walishangaa kitendo cha William kuwa nchini Tanzania na wakati alikuwa nchini Marekani.

    Harusi ikafungwa, alifurahi kwa sababu alipomkataa Melania alimwambia kwamba kuna siku angepata mwanaume sahihi na si yeye. Akaondoka kanisa, akasimama kituoni na kupanda daladala.

    Alishangaa, watu waliendelea kumwangalia, waliopata taarifa za kupoteza kumbukumbu zake walimuonea huruma kwani alipokuwa akijiangalia, alijiona kuwa mtu wa kawaida sana ambaye hakuwa na umaarufu wowote ule.

    Ndani ya daladala kila mtu alitaka kupiga naye picha. Kuonana na William halikuwa jambo jepesi hata mara moja, alikuwa mtu wa kuishi Marekani, bilionea mwenye pesa ndefu ambaye alitakiwa kufanya kila kitu alichotaka kukifanya.

    Alipofika nyumbani, alishangaa kumkuta Linda akilia, hakujua ni kitu gani kilimliza, alimsogelea na kuanza kumbeleza huku akimlaumu Mungu kwa sababu gani alikuwa akipitia maisha hayo.

    “Pole sana,” alisema William.

    “Nashukuru!”

    “Hivi unarudi lini kwenu?” aliuliza William.

    “Unasemaje?”

    “Unarudi lini kwenu? Nashangaa umekuja na kukaa hapa, hakuna mtu anayekufahamu, upoupo tu, hivi unaishi wapi? Naona tumekuja wote lakini sikujui! Huwezi kuondoka hata kwenda kuishi hotelini dada yangu?” aliuliza William maswali yaliyomfanya Linda kulia sana.

    “Unataka niondoke?”

    “Ndiyo! Ikiwezekana hata sasa hivi! Wewe nenda tu kwani hapa hakuna mtu anayekujua,” alisema William na kuelekea chumbani kwake, akaingia humo na kutulia kitandani. Sauti pekee aliyokuwa akiisikia kutoka sebuleni ni ya Linda tu aliyekuwa akilia kama mtoto, japokuwa mama yake alijaribu kumbembeleza lakini mwanamke huyo hakunyamaza.

    “Mama muache asepe! Unamng’ang’ania unamjua? Kung’ang’ania watu utakuja kung’ang’ania majini,” alisema William kwa sauti, akajifunika shuka na kuziba masikio yake kwani hakutaka kabisa kuisikia sauti ya Linda wala mtoto wake, William Jr ambaye alikuwa akilia tu kana kwamba alikuwa akifahamu kilichokuwa kikiendelea.



    Moyo wa msichana Cassey ulikuwa kwenye hali mbaya, alikosa amani na kila alipokaa kichwa chake kilimfikiria William. Aliumia kwani alijua kwamba yeye ndiye alikuwa chanzo cha mwanaume huyo kupata ajali hiyo kwani kama asingemwambia kuwa anataka kujiua, basi asingemfuata na hivyo kupata ajali mbaya iliyopoteza kumbukumbu zake.

    Alijisikia hukumu moyoni mwake, wakati mwingine alikuwa akikaa peke yake nyumbani kwake na kulia kwa maumivu makali, alikosa raha, akakosa amani maishani mwake, kitu pekee alichokuwa akikifikiria kwa wakati huo ni William tu.

    Alikuwa na siri kubwa moyoni mwake, hakutaka mtu yeyote afahamu kitu chochote, si hao tu bali hata William hakutaka afahamu ukweli. Alimwambia kwamba alikuwa na mimba ya mwezi mmoja lakini ukweli ni kwamba hakuwa na mimba, alitaka kumfanya mwanaume huyo awe karibu naye, kwani aliamini kila mwanaume alihitaji mtoto, alidhani kwamba angefurahi lakini mwisho wa siku mwanaume huyo akabadilika na kuhitaji aitoe mimba ile.

    Aliumia zaidi moyoni mwake, alijuta kumdanganya William kwani pamoja na ubaya wa sura yake, lakini moyoni mwake alikuwa mwanaume pekee aliyekuwa akimpenda kwa moyo wa dhati.

    Hakutaka kubaki nchini Marekani, ilikuwa ni lazima amuone William na ikiwezekana amuombe msamaha kwa kumdanganya kwani ukweli ni kwamba hakuwa na mimba kama alivyomwambia.

    Siku mbili zilizofuata, akafanya hatua zote za usafiri na alipopata vibali akaanza safari ya kuelekea nchini Tanzania kwa kutumia ndege yake binafsi. Njiani, mawazo yake yalikuwa kwa William, hakujua angemwambia nini, hakujua kama mwanaume huyo hakuwa na kumbukumbu zake, hakukumbuka kitu chochote kile kilichotokea siku chache zilizopita maishani mwake.

    Alipofika Tanzania, akaelekea katika Hoteli ya Serena. Alijua kwamba William alikuwa akijulikana sana, hivyo alichokifanya ni kumuuliza mhudumu ambaye alimwambia kwamba alimfahamu sana William na hakukuwa na Mtanzania ambaye hakumfahamu mtu huyo.

    “Everybody knows him. He is a superstar,” (kila mtu anamfahamu! Jamaa ni staa sana,) alisema mhudumu.

    “So, you know where he lives?” (kwa hiyo unajua anapoishi?)

    “Yeah!”(ndiyo)

    Akahitaji kupelekwa huko, alichokifanya ni mhudumu ni kumwambia Cassey kwamba lingekuwa jambo jema kama angezungumza na uongozi wa hoteli hiyo kwa ajili ya ruhusa na hivyo msichana huyo kufanya hivyo.

    Mhudumu akaruhusiwa na hatimaye kuanza kwenda Tabata alipokuwa akiishi William. Hawakuchukua muda mrefu sana wakafika, nje kulikuwa na waandishi wa habari ambao walitaka kuingia humo kuzungumza na William lakini mlinzi aliwaambia wasubiri, hivyo wakafanya hivyo.

    “Nimemleta mgeni wa William,” alisema kijana yule aliyekuwa mhudumu.

    “Siyo mwandishi huyo?”

    “Sasa mwandishi kutoka gazeti gani kaka? Au udaku la Marekani!” alihoji mhudumu huyo kiutani.

    Wakaruhusiwa na kuingia ndani. Mapigo ya moyo wa Cassey yalikuwa yakidunda mno, walipofika sebuleni, wakakutana na mama yake William aliyekuwa akimbembeleza Linda aliyekuwa akilia huku akiwa na mtoto wake.

    Hakujua ni kitu gani kilitokea na kitu cha kwanza kabisa kilichomjia kichwani mwake ni kwamba inawezekana William alikuwa amefariki dunia. Nguvu zikamuisha, akajikuta akisimama palepale mlangoni aliposimama.

    Akakaribishwa, akakaa kochini na kuanza kujitambulisha. Linda alimfahamu, alikwishawahi kutambulishwa mara kadhaa na William hivyo hakushtuka kumuona msichana huyo amefika mahali hapo.

    “What the hell is going on?” (kitu gani kinaendelea?)

    Linda akaanza kumwambia kila kitu kilichotokea kwamba ajali mbaya aliyoipata William ilimsababishia kupoteza kumbukumbu zake. Cassey hakutaka kuliamini hilo, alichomwambia ni kwamba alitaka kuonana na William ili kuzungumza naye.

    Hilo halikuwa tatizo, mama yake William, Bi Sophia akamchukua na kumpeka chumbani alipokuwa William ambaye alikuwa amelala. Akaamshwa na macho yake yalipotua kwa Cassey alibaki akimshangaa, hakumfahamu msichana huyo na hakujua kama katika maisha yake aliwahi kuonana naye.

    “Wewe ni nani?” aliuliza William huku akionekana kushangaa.

    “Umenisahau?”

    “Sijakusahau, bali sikujui kabisa,” alijibu William.

    “Naitwa Cassey!”

    “Ndiye nani na unahitaji nini?” aliuliza William huku akimwangalia msichana huyo.

    Cassey akabaki kimya kwa muda, hakuamini kwamba William alimsahau hata yeye mwenyewe. Kwa jinsi walivyokuwa na majibu ya William yalivyotoka ilionekana kama walikuwa wakiigiza lakini mwenzake alikuwa akimaanisha, hakumkumbuka na hakujua alifika mahali hapo kufanya nini.

    “Mimi ni mpenzi wako! Kumbuka nilikwambia nina mimba yako,” alisema Cassey na kumfanya William kushtuka.

    “Una mimba yangu?”

    “Ndivyo nilivyokwambia!”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mbona sikufahamu! Tulishawahi kukutana kabla?”

    “Ndiyo!”

    “Wapi?”

    “New York!”

    William hakujibu kitu, alibaki akimwangalia Cassey, hakumkumbuka kabisa, alimshangaa kwa sababu mpaka kipindi hicho hakuwahi kuwa na rafiki Mzungu, sasa ilikuwaje mtu kama Cassey amfuate na kumwambia maneno hayo na wakati hakuwahi kuwa karibu na Mzungu?

    Akamfukuza kwani alimuona muongo na kulikuwa na kitu alichokihitaji. Cassey hakuamini, alikuwa akifukuzwa na mwanaume ambae kila siku alimwambia kuwa alikuwa mwanamke wake wa ndoto. Moyo wake uliumia lakini hakuwa na jinsi, akaondoka zake kurudi nchini Marekani.

    Hali ya William haikubadilika, bado aliendelea kuwa na mawazo kila siku, mambo yaliyokuwa yakitokea hakuamini, kila alipokaa, alifuatwa na waandishi wa habari na kuambiwa maneno mengi kuhusu umaarufu wake.

    Hakujua sababu ya waandishi kumuuliza hivyo kwani kitu alichokikumbuka, hakuwa maarufu bali mtu wa kawaida sana. Kwenye mitandao ya kijamii, alikuwa akizungumziwa yeye tu.

    Ukiachana na tovuti ya Global Publishers, Jamii Forum na nyingine nyingi, pia alikuwa akizungumziwa mpaka katika tovuti za nchini Marekani, Uingereza na nchi nyingine.

    Alishangaa, watu hao walimjuaje, na kama alikuwa maarufu, umaarufu wa nini kwani aliyakumbuka maisha yake yote, hakuwahi kuona kama kuna siku aliwahi kuwa mtu maarufu.

    “Mimi ni maarufu? Eti nina mtandao! Sasa mtandao gani tena?” alijiuliza William pasipo kupata jibu.

    Linda hakutaka kuendelea kubaki nchini Tanzania, kama kuumia, aliumia sana, kama kulia alilia sana lakini hakukuwa na kitu kilichobadilika. Alichokifanya baada ya siku mbili ni kurudi nchini Marekani huku akiwa na majonzi tele. Alisimiamia biashara za mpenzi wake, akaunti zake zote kwa kuamini kwamba kuna siku angerudiwa na kumbukumbu na kukumbuka kila kitu kilichotokea.

    William aliendelea na maisha yake nchini Tanzania, hakujua sababu ya waandishi kumtafuta sana, kila alipokaa, alifuatwa na watu na kuhitaji kupiga naye picha. Alishangaa, aliambiwa kwamba alikuwa mtu maarufu kitu ambacho kila siku alipingana nacho.

    Baada ya kukaa Tanzania kwa wiki mbili, akaalikwa ikulu kwa ajili ya kuonana na rais, alishangaa, hakuwahi kufikiria kitu kama hicho. Alijiona kuwa mtu wa kawaida, sasa ilikuwaje mpaka aitwe na rais na wakati hakuwa amefanya jambo lolote lile.

    Mualiko huo ulitakiwa kufanywa baada ya siku mbili, alikuwa kwenye presha kubwa, kila alipokuwa akilifikiria jambo hilo, mapigo yake ya moyo yalimdunda kupita kawaida.

    Siku hizo zilipotimia, akaelekea huko huku akiwa na mama yake. Akakutana na waandishi wa habari wengi, wote walikuwa wamealikwa, alipoteremka kwenye gari, akaanza kupigwa picha mfululizo.

    Kila kitu kilichokuwa kikiendelea kilimshangaza sana, hakujua sababu, aliambiwa kwamba alikuwa mtu maarufu lakini hakujua umaarufu wake ulikuwa ni wa nini.

    “Au ndiyo natengenezwa kuwa mrithi wa Kanumba? Au labda natengenezwa kuchukua mikoba ya Diamond Platnumz. Lakini mbona sijui kuimba wala kuigiza! Kwa nini wanataka niwe mtu maarufu?” alijiuliza lakini akakosa jibu.

    Akakaribishwa ikulu kwa heshima kubwa, hakuamini kama ingetokea siku ambayo angeingia ndani ya ikulu hiyo. Alikaa kwenye kochi kubwa huku akionekana kutokujiamini kabisa. Alitetemeka, hiyo ndiyo ilikuwa siku yake ya kwanza kufika humo.

    “Mama! Sijiamini kabisa,” alisema William huku wakiwa sebuleni wakimsubiri rais.

    “Jiamini mwanangu! Nilishakwambia kwamba wewe ni mtu maarufu!” alisema mama yake.

    “Umaarufu gani?”

    “Umetengeneza mtandao!”

    “Mtandao? Mama! Sijawahi na wala kufikiria kutengeneza mtandao hata siku moja. Sasa iweje niwe nimetengeneza mtandao? Mimi ni mtaalamu wa kompyuta ila si mtaalamu wa kutengeneza mtandao,” alijibu William, walikuwa kama wakinong’ona.

    Baada ya dakika kadhaa, rais akafika sebuleni hapo, kitu cha kwanza akamuonyeshea tabasamu pana William na kisha kumsogelea na kumkumbatia.

    Kwa muonekano aliouonyesha rais huyo ulionyesha kabisa kwamba alikuwa akimfahamu kabla kitu kilichomfanya William kumshangaa kwani hakujua kama rais huyo alikuwa akimfahamu hata kidogo.

    “Kumbe unanifahamu?” aliuliza William.

    “Yeah! Nakujua sana. Kwa nini umeniuliza hivyo?” aliuliza rais, alionekana kutokujua tatizo alilokuwa nalo William.

    “Siamini kama unanijua kwani sijawahi kulifanyia taifa kitu chochote kile.”

    “Hahah! William! Umeibadilisha dunia, kila mtu anakishangaa kichwa chako, hivi kina uwezo gani?” aliuliza rais.

    “Kawaida. Ila...daah! Mbona mnanichanganya sana,” alisema William.

    Rais mwenyewe alikuwa akishangaa mpaka pale alipoambiwa kwamba William alipata ajali na alipoteza kumbukumbu zake hivyo hakuwa akikumbuka kitu chochote kile.

    Alipoambiwa hivyo, kidogo hata mazungumzo yake yakabadilika na kuanza kuzungumzia habari nyingine kabisa. Hayo ndiyo yalikuwa maisha yake, mpaka mwaka mmoja unapita, hakuwa amekumbuka kitu chochote kile, hakujua mpenzi wake, Linda alikuwa katika hali gani, hakujua kuhusu mtandao wake, kila kitu kilichokuwa kikiendelea, kwake yalikuwa maisha mapya.





    “Mamaaaa....mamaaaa...Linda...Linda mpenziiiiii....” ilisikika sauti kutoka chumbani kwa William, saa ya ukutani ilikuwa ikionyesha kwamba tayari ilifika saa nane usiku.

    Alikuwa akipiga kelele kama mtu aliyechanganyikiwa, akainuka kitandani na kuanza kukimbia huku na kule chumbani mule. Alikishika kichwa chake, aliendelea kupiga kelele, aliona kama matukio yalikuwa yakijirudia kichwani mwake, alichanganyikiwa, hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea.

    Alijiona akiwa ndani ya gari, aliendesha kwa kasi na baada ya muda fulani akapata ajali, alichanganyikiwa, alichokuwa akikiona ilikuwa ni vigumu kuamini kama kilikuwa kichwani mwake kwani aliona kama picha mbele yake kitu kilichomfanya kupiga kelele mno.

    Mama yake akatoka chumbani kwa kasi na kwenda chumbani kwa William, akamkuta akiwa kitandani huku akipiga kelele, akamfuata na kumuuliza tatizo la kupiga kelele lakini hakutoa jibu lolote zaidi ya kulitaja jina la Linda tu.

    “Nini kimetokea?” aliuliza mama yake, alionekana kuchanganyikiwa kwani alihisi tayari mtoto wake alikuwa kichaa.

    “Linda mama! Linda yupo wapi?” aliuliza William.

    Mama yake hakuamini, ulikuwa umepita mwaka mzima tangu William apate ajali na kusahau kila kitu, alikumbuka kwamba mara ya mwisho Linda kuwa huko ni mwaka uliopita na miezi kadhaa, alikataa kumuona na kusema kwamba hakuwa akimfahamu, sasa ilikuwaje leo hii aanze kumuulizia na wakati alimfukuza.

    Hakugundua kama kijana wake alikuwa amerudiwa na fahamu. Alibaki akimwangalia kwa mshangao mkubwa, alikuwa akibubujikwa na machozi kwani kitendo cha William kumkumbuka Linda kilionekana kuwa na mafanikio makubwa kwenye afya yake.

    “Mama! Linda! Mama! Linda yupo wapi? Kwa nini nipo hapa! Hapa ni wapi?” aliuliza William huku akionekana kushangaa huku na kule.

    Alitulia kwa muda na jinsi chumba kile alivyokiangalia akagundua kwamba alikuwa chumbani kwake. Alichanganyikiwa, hakujua ni kitu gani kilitokea kwani kumbukumbu zake zilikumbuka tukio la mwisho la kupata ajali lililokuwa limetokea.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hakujua ni kitu gani kilitokea mpaka kuwa ndani ya chumba kile. Hakutaka kuamini kama kweli pale alipokuwa palikuwa chumbani kwake, nchini Tanzania katika Mtaa wa Tabata.

    Akatoka ndani na kwenda nje, akamkuta mlinzi ambaye naye alibaki akimwangalia, alizisikia zile kelele na kuangalia kwa makini mule ndani, alitaka kujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea.

    “Hamis! Nimefikaje hapa?” alimuuliza mlinzi huku akimwangalia kwa kumshangaa.

    “Mbona upo kila siku!”

    “Kila siku? Inamaana kila kitu kilichokuwa kinatokea nchini Marekani kilikuwa ni ndoto?” aliuliza William.

    “Hapana!”

    “Sasa imekuwaje nipoi hapa? Linda yupo wapi?” aliuliza William, wakati Hamis akitaka kujibu, mama yake akatokea na kumkonyeza kwamba hakutakiwa kujibu kitu chochote kile.

    “William, njoo ndani!” alisema mama yake huku akimshika mkono.

    “Mama! Nataka uniambie ukweli! Kwa nini nipo hapa? Nani anasimamia mtandao wangu?” aliuliza William huku akiendelea kupigwa na mshangao.

    Mama yake akamchukua na kuelekea naye ndani, aliona jinsi kijana wake alivyokuwa amechanganyikiwa. Walipofika ndani, wakakaa kochini na kuanza kuzungumza, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumuuliza alikumbuka kitu gani cha mwisho.

    “Nilipata ajali jana!” alijibu William.

    “Jana? Hapana! Ni mwaka na miezi kadhaa imepita! Baada ya hapo unakumbuka nini?”

    “Sijajua nini kiliendelea,” alisema William.

    Mama yake hakutaka kumficha, akaanza kumuhadithia kila kitu kilichotokea baada ya yeye kupata ajali. Alimsikiliza kwa makini, moyo wake uulimuuma, maneno aliyokuwa akiongea mama yake yalimshtua sana, hakuamini kama kweli yeye ndiye aliyemfukuza Linda.

    Alihisi kabisa kitu chenye ncha kali kikiuchoma moyo wake. Linda alimpenda, alihisi maumivu mazito baada ya kujiuliza ni maumivu makali kiasi gani aliyoyasikia mwanamke huyo.

    “Mama! Mimi nilimfukuza Linda?” aliuliza William, hakuamini alichokuwa amekisikia.

    “Ndiyo! Ulimfukuza. Na pia kuna mwanamke mwingine!” alisema mama yake.

    “Yupi?”

    “Anaitwa Kesi...”

    “Cassey! Ilikuwaje? Mungu wangu! Nakumbuka nilipata ajali nikiwa namfuata huyu msichana,” alisema William huku akionekana kukumbuka kila kitu.

    “Naye alikuja ila ukamfukuza.”

    “Mungu wangu! Nilimfukuza na Cassey pia?”

    “Ndiyo!”

    “Mama! Haiwezekani! Ni lazima nirudi Marekani!”

    William hakutaka kuishia hapo, kitu cha kwanza kilikuwa ni kuingia kwenye mtandao wake wa MeChat kuona unaendeleaje. Hakuamini, kulikuwa na zaidi ya watu milioni mia tano waliokuwa wakiutumia. Moyo wake ulikuwa na furaha tele, hakuamini kama aliweza kutengeneza kitu kilichokuwa na watumiaji wengi kiasi hicho.

    Hakutaka kuchelewa, alizikumbuka namba za mpenzi wake, Linda hivyo kuchukua simu na kumpigia. Siku ikaanza kuita, iliita na kuita na mwisho wa siku kupokelewa na sauti ya Linda kusikika upande wa pili.

    ****

    Moyo wa Linda ulikufa ganzi kwani mauamivu aliyokuwa akiyasikia yalizoeleka na hivyo kuwa si maumivu tena. Aliumia, hakuamini kama kweli alifukuzwa na William na hakutaka kumuona tena.

    Alijua kwamba mwanaume huyo alikuwa akiumwa lakini hilo hakutaka kulijali, alihisi kwamba alikuwa mzima na kile alichokifanya kilikuwa cha makusudi kabisa.

    Alirudi nchini Marekani na kuendelea na maisha yake. Huko, aliendelea kusimamia kampuni za William na masuala yote ya kifedha kwa kuamini kwamba kuna siku mumewe angerudi tena.

    Mtoto wao, William Jr aliendelea kukua kama kawaida. Maisha bila William yalikuwa magumu mno kwa Linda lakini alivumilia huku kila siku akimuombea William kwa Mungu kwamba afya yake itengemae na kukumbuka kila kitu katika maisha yake.

    Baada ya mwaka na miezi mitatu, akapigiwa simu mchana wa siku moja. Alipoiangalia simu ile, code zilionyesha kwamba ilitoka Tanzania na kitu alichojua ni kwamba mama yake William alikuwa amemkumbuka hivyo kumpigia kama siku nyingine japokuwa kwa siku hiyo namba ilikuwa tofauti.

    “Nani anaongea?” aliuliza mara baada ya kupokea simu.

    “William!” alisema William kitu kilichomfanya Linda kuishiwa nguvu za miguu, akakaa vizuri kwenye kiti.

    “William?” aliuliza.

    “Ndiyo mpenzi! Ninakumbuka kila kitu! Naomba unisamehe mpenzi kwa nilichokufanyia,” alisema William huku akiwa na huzuni tele.

    “Nimekukumbuka mpenzi! Nimelia sana kwa ajili yako! Nimeumia kwa ajili yako mpenzi!” alisema Linda huku akianza kulia kilio cha kwikwi.

    “Ninakuja hukohuko. Ninakuja kukuona mpenzi! Ninakuja kuishi na wewe na kufunga ndoa,” alisema William.

    Siku iliyofuata, akakodi ndege kuelekea nchini Marekani. Hakukuwa na tatizo la viza kwani Wamarekani walimuona kama mwenzao kwa sababu alikuwa na kazi kubwa aliyokuwa akiifanya chini ya CIA.

    Taarifa ikapelekwa nchini Marekani kwamba William alikuwa njiani kuelekea huko. Walichokifanya CIA ni kuwasiliana na mkewe na kumwambia kwamba hakutakiwa kumwambia mtu yeyote juu ya ujio wa William.

    Ndani ya ndege William alikuwa na mawazo tele, hakuamini kilichokuwa kikiendelea katika maisha yake. Wakati mwingine alibaki na kuyafikiria maneno ya mama yake kama kweli alimfukuza Linda nyumbani.

    Mbali na mwanamke huyo pia akamkumbuka Cassey, alijiuliza juu ya mimba aliyokuwa nayo kama alijifungua salama au la. Safari iliendelea na baada ya saa ishirini na saba, ndege ikaanza kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa JFK jijini New York.

    Akateremka, kulikuwa na maofisa wengi wa CIA waliokuwa wakimsubiri, hakukuwa na mwandishi wa habari, mbali na maofisa hao pia alikuwepo Linda aliyekuwa na mtoto William Jr, alipomuona mpenzi wake, akaanza kumsogelea na kumkumbatia kwa furaha.

    “Hatimaye umeruudi mpenzi!” alisema Linda huku akilia.

    “Nimerudi kuanza maisha mapya na wewe. Futa Machozi Mpenzi! Kila kitu kilichopita, naomba ukisahau,” alisema William.

    Waliendelea kukumbatiana, hakuridhika, akambeba William Jr, kila alipomwangalia macho yake yalijaa machozi kwani alihisi mapenzi mazito yakiongezeka kwa familia yake hiyo.

    Hawakukaa sana wakachukuliwa na kuingia ndani ya gari ambapo safari ya kuelekea nyumbani ikaanza. Wakaelekea huko, ndani ya gari walikuwa wakizungumza mambo mengi. William hakutaka kukumbuka kilichotokea, akaanza maisha yake na Linda, kwa kipindi hicho alihitaji sana kuwa karibu na familia yake.

    Baada ya siku mbili kupita akampigia simu Cassey na kumuuliza kuhusu ujauzito. Kwanza msichana huyo akafurahi kusikia kwamba William amerudiwa na kumbukumbu zake na kitu alichomuongezea ni kwamba hakuwa na mimba, alimwambia vile kwa sababu alitaka kujua ni kitu gani kingetokea.

    “Wewe mpumbavu sana, ulinitisha mno,” alisema William huku akitoa kicheko, naye Cassey akaanza kucheka.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nilijua kwamba ungechanganyikiwa. Hujachelewa, umewahi sana. Ninafunga ndoa wiki mbili zijazo. Ungependa uwepo?” aliuliza Cassey.

    “Haina shida. Niandalie kadi yangu na Linda, baada ya kwako, yangu itafuata,” alisema William, wakazungumza mambo mengine na kukata simu.

    Maisha yakabadilika, akaendelea kuingiza fedha, mtandao wake wa MeChat uliendelea kumuingizia fedha, akawa bilionea na ndani ya miaka miwili akawa juu zaidi ya Mtandao wa Facebook, aliendelea kupendwa huku kila siku akifanya kazi za CIA za siri na kufanikiwa kuwapa Wamarekani siri za majeshi ya Urusi, silaha zao, Wachina, Wakorea na nchi yoyote ambayo ilikuwa adui mkubwa wa Marekani.

    Na la kuongezea zaidi, yeye ndiye mtu aliyehusika kuzidukua kompyuta za Tume ya Uchaguzi Marekani kwa kuyabadilisha matokeo ya Marekani kwa kumpa Donald Trump badala ya Hillary Clinton.



    MWISHO

0 comments:

Post a Comment

Blog