Search This Blog

Sunday 22 May 2022

MKONO WA JASUSI - 1

 







    IMEANDIKWA NA : RICHARD MWAMBE



    *********************************************************************************



    Simulizi : Mkono Wa Jasusi

    Sehemu Ya Kwanza (1)



    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Miezi sita iliyopita… Dar es salaam



    “KAMANDA AMATA,” sauti iliita kutoka nyuma yake. Akageuka na kumwona Madam S akiwa na faili moja mkononi. Alikuwa amesimama katika sehemu ya mbele ya nyumba kubwa huko Gezaulole, mkono wake ukiwa na bandeji kubwa. Akageuka na kumtazama Madam S.

    “Yes Mom,” akaitikia na kuitoa miwani yake usoni.

    “Mheshimiwa Rais anakupongeza kwa kazi ulioifanya, anakubali sana uwepo wako hapa nchini na hususan katika idara nyeti kama hii, nimetoka kuzungumza naye sasa hivi, tumekubaliana jambo moja,” akamkabidhi lile faili ambalo juu yake lilikuwa limeandikwa Rhobinson Quebec na chini yake maandishi mazito ‘Wanted’, akatalizama na kumwangalia Madam S.

    “Roho yake tu wala hatumwitaji akiwa hai,” kisha akageuka na kuondoka.







    T.S.A MAKAO MAKUU – 1999



    “Unakunywa chai au kahawa?” Gina alimuuliza swali Amata aliyekuwa ametingwa, macho kodo kompyutani akiperuzi hiki na kile.



    “Swali lako hilohilo kila siku, na jibu langu lilelile kila mara,” akamjibu na wote wakacheka kwa sauti.



    “Nyie kuna nini huko?” Madam S aliuliza akiwa tayari kasimama mlangoni.



    Wote wakasimama kumpa heshima yake, “Karibu Madam, umeingia kama kivuli!” Kamanda akatania.



    “Hata kivuli huonekana, sema kama hewa!” akajibu kisha wote wakacheka tena, “Kamanda Amata, uje ofisini baada ya mambo yako kuna jambo nikueleze na ulifanyie kazi,” akaondoka. Amata akamtazama Gina kisha wakaendelea na vicheko vyao na mabishano ya chain a kahawa.



    “Madam anakuita ofisi, kuna kazi au?” Gina akaanza uchokozi.



    “Hapana, kungekuwa na kazi angenikurupusha na ninyi nyote mngekuwa katka hekaheka ya kupanga kazi hiyo, itakuwa anataka kuniuliza kama nakuoa au la,” Amata akajibu.



    “Mmmmmhh! Hiyo ndoa ya mi na wewe itakuwa ndoano,” Gina akaendeleza mazungumzo na kumpa Amata kikombe cha Kahawa.



    Mbele ya kompyuta hiyo, Amata alikuwa ametingwa bila kuongea na mtu yeyote, hakuna aliyejua ni nini anakitafuta isipokuwa ni yeye peke yake. Alipokuja kumaliza kazi yake na kuinua macho alijikuta peke yake na kahawa iliyopoa mezani. Akainua walkie talk yake na kuita.



    “We, njoo huku, tupo kwenye chumba namba tano,” Gina akamwita Amata hata kabla hajaambiwa lolote.



    §§§§§

    Ndani ya chumba hicho kulikuwa na watu wane, Madam S, Gina, Jasmine na Amata, waliketi wakitazama moja ya muvi nzito ya kipelelezi ambayo kwa roho yako nyepesi huwezi kuitazama mara mbili. Kwao muvi hiyo iliwafunza mengi sana hasa katika ukachero wa ndani na nje.

    Ilikuwa ikionesha hatua thelathini na tisa za Kijasusi, kila mmoja alikuwa katulia kimya akifuatilia muvi hiyo ambayo kwayo ilikuwa na mafunzo mengi sana. Ilipomalizika baada ya dakika tisini, kila mtu alishusha pumzi ndefu na kumtazama Madam S aliyekuwa ameketi kimya mkono wake ukiwa umekuwa egemeo la kidevu chake. Akainuka akawatazama wote.



    “Nakaribia kustahafu mama yenu, umri umenitupa mkono, kaeni tayari kwa lolote kutoka sasa. Kamanda njoo ofisini,”

    Amata akainuka na kumfuata Madam S mpaka ofini kwake, ofisi pana yenye nafasi ya kutosha, ilikuwa na viti sita vya vono safi, meza kubwa ya mpingo iliyochongwa na vijana wa Suma J.K.T ilipendezesha ofisi hiyo. Ukutani kulining’inizwa picha kubwa ya Hayati Baba wa Taifa, na pembeni sana kulikuwa na picha ya mtu mmoja mwenye macho angavu yaliyoonekana kujua mambo mengi sana. Ukiitazama picha hiyo unaweza kuiuliza swali lakini ilikuwa picha. Kamanda Amata ijapokuwa alikuwa ni T.S.A 1 lakini bado katika ofisi hii aliingia mara chache sana. Picha iliyokuwa hapo ilimkumbusha Mogadishu alipokutana na mtu huyo The Chamelleon, alitamani kumwambia Madam S juu ya hilo lakini bado agano lake na marehemu bandia huyo lilikuwa ni kutunza siri.



    Madam S akazunguka nyuma ya meza hiyo, akasimama mbele ya bendera kubwa ya taifa iliyokuwa kulia kwake na kushoto kwake kulikua na nembo kubwa ya T.S.A, nembo iliyobeba ngao ya Taifa na kunakshiwa kwa dhahabu safi kwenye kingo yake, juu yake kulitokeza kichwa cha Twiga ambacho kilitanguliwa na barafu ya mlima Kilimanjaro. Chini kabi say a nembo hiyo herufi tatu yaani T.S.A zilibebwa ju ya mikuki miwili iliyofanya alama ya X.



    “Saa kumi jioni ya leo, kuna kikao nyeti Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, nitakwenda pale, lakini nataka nionane na wewe mara tu nikitoka, kama kuna lolote tofauti nitakushtua, uwe tayari muda wote,” Madam akamwambia akiwa amesimama wima.



    “Yes! Madam, daima nipo tayari,”



    “Kuna kazi kubwa Amata, ngumu sana mbele yako, itakayoweka maisha yako rehani kuliko siku zote, lakini huna budi kuifanya, nasi tutakuwa bega kwa bega na wewe,”



    “Yes, Madam,” akajibu kwa ukakamavu.



    “Sasa nakwenda kuonana na Mheshimiwa Waziri kisha nitakuita kiofisi ili tuone tunafanya nini katika hili, kwa maana hata mimi bado sijui ila nimedokezeaa tu juu yake,” Madam alimaliza maelezo yake.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    §§§§§



    Jioni ya siku hiyo ilimkuta kamanda Amata D.D.C Kariakoo akipata moja mbili baridi, akili yake ilizunguka kama pia, alijikuta akishikwa na donge kubwa la kujua nini kinataka kujiri katika ofisi yao. Alikwishazoea kuwa kazi zote huwa anaambiwa moja kwa moja na Madam S na kuianza muda huohuo lakini alishangaa kwa sasa Madam S anampa dokezo na kumwambia nitakuita baadae.

    Bia ilishuka taratibu lakini haikuleta matata yoyote katika ubongo wa kijana huyo, ilishuka kama maji na kumtaka kwenda haja ndogo mara kadhaa. Muziki wa Kitanzania uliokuwa ukiporomoshwa na bendi ya Msondo ulimfanya japo kupoteza mawazo yake kwa nukta tu na si sekunde. Aliburudika kwa kuimba kidogo lakini mawazo yaliporudi katika lile analolisubiri kwa hamu. Aliitazama saa yake tayari ilitimu saa kumi na moja na nusu jioni, jua lilikuwa limeuacha mji na ukiliangalia lilichwea katika milima ya Pugu. Akanyanyuka na kupenya katikati ya watu, moja kwa moja akatoke kwenye lango la kutokea nje, akateremka ngazi na kuliendea gari lake aliloliegesha jirani kabisa na duka la Mhindi.

    Alipoketi tu kitini simu yake ikaita, akainyanyua na kuichungulia, Chiba, akaifyatua na kuiweka sikioni.



    “Vipi kijana, likizo imeisha?”



    “Aaa ofisi zetu hazina likizo, dili likitokea popote na muda wowote unajiongeza man,” Chiba akajibu.



    “Niambie!”



    “Vipi hali ya hewa hapo ulipo?” Chiba akauliza.



    “Pako shwari nimejificha kibandani, nyunyiza tu,” Kamanda akamwambia.



    “Kaka kuna nini huko? Maana Madam kanambi nirudi, hapa nilipo tayari niko Uwanja wa Ndege wa Mauritius narudi,” Chiba akaeleza.



    “Aaah! Huyu bibi naona anazeeka sasa, mi mwenyewe kanambia nisubiri ataniita,” Kamanda akamjuza.



    “Ok, saa nne zijazo nitakuwa Dar kaka,”



    “Na mtoto wa Ki-Mauritius?” Kamanda akatania.



    “Hapana, mwenyewe tu, hayo nayaacha hukuhuku, over!” Chiba alimaliza kuongea, kwa kusema neno hilo over alimaanisha maongezi yasiendelee.



    “Tuonane Ruvuma mpaka Maputo dakika 500 zijazo, over!” Kamanda akakata simu na kurudisha mahala pake, kisha taratibu akaingiaza barabarani na kuondoka eneo hilo. Daima hakupenda kukaa eneo moja kwa muda mrefu. Alaiingia barabara ya Msimbazi na kuelekea Faya, pale akakunja kulia kufuata barabara ya Morogoro mpaka karibu na Chuo cha Ufundi cha Dar es salaam akakunja kushoto akachukua barabara ya vumbi ya Ally Khan, akapita Zanaki na kuendelea mpaka mgahawa wa Red Carpet, akaegesha gari yake nje na kuteremka, akaangaza macho huku na kule kisha akaufunga mlango huku funguo ya gari akiwa kaiacha ndani.



    §§§§§

    WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA



    “Madam S,” Mheshimiwa Francis Kifaru aliita kwa sauti yake nzito iliyoelemewa na unene uliopita kiasi. Daima alikuwa akiketi kama anayesinzia kutokana na umri uliopitiliza.



    “Wazee kama hawa wastahafu tu, wanang’ang’ania madaraka mpaka wafie maofisini, ndio maana nch haiendelei” Madam aliwaza.



    “Ndio Mheshimiwa,” akaitika.



    “Kama nilivyokuambia, hilo na hao jamaa wametuomba kuwasaidia na si kama tuwaombavyo basi ni zamu yetu, naamini idara yako itafanya vizuri,” Yule Mzee alitoa maelekezo na kumpa Madam S kabrasha lenye karatasi kadhaa ndani yake juu likiwa na maandishi Siri Nzito, akalitazama haraka haraka na kuliweka vyema.



    “Ok, kazi imefika mahala pake na itatekelezwa,” akajibu na kumuaga mzee huyo, kisha akatoka nje.

    Alipoketi garini, akatulia kwanza, “safi sana, sasa kazi ni moja tu, nilikuwa namuwaza sana mshenzi huyu” Madam S akajiwazia huku akiondosha gari yake maegeshoni.



    §§§§§

    Musanda, Pretoria - a.kusini



    DUMISAN SAJAK MBEKHI, kiongozi mkuu wa Idara ya Kijasusui ya Afrika ya Kusini (N.I.A) alitulia tuli kama aliyegandishwa na barafu katika meza yake kubwa hapo ofisini. Giza lilikuwa tayari limeutawala mji huo wa Pretoria mju wenye amani na utulivu katika miji ya Afrika ya Kusini.

    Akiwa bado katika fikra nzito, mlango wa ofisi yake ulisukumwa, na mwanadada mwenye mwili wa kati, sio mrefu sio mfupi aliingia akiwa katika mavazi ya kijeshi, aliposimama mbele ya mwenyeji wake, huku wakitenganisha na ile meza kubwa, aliiachua kofia yake mabegani na kuivaa kichwani pake kisha akasimama kiukakamavu.

    Dumisan akasimama akionekana wazi amefura kwa hasira na kisasi.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Debra, sina haja ya kupoteza muda, nimekuteua wewe kwa kuwa najua wasifu wako jeshini, unapaswa kuondoka usiku huu na ndege ya Uingereza, uende Canada pale kuna mtu unatakiwa ukaitoe roho yake kisha urudi mara moja. Nataka ukamuue na si vinginevyo, nategemea majibu mazuri kutoka kwako, asante.” Dumisan akaketi. Debra akapiga saluti na kutoka katika ofisi ile, hakutakiwa kujibu lolote kwani hiyo ni amri alichotakiwa kufanya ni kutekeleza aliloambiwa tu basi.





    MIEZI MIWILI ILIYOPITA



    ILIKUWA HALI YA SINTOFAHAMU katika machimbo ya dhahabu huko Mashariki mwa Johanesburg, Afrika ya kusini. Katika moja ya mashimo makubwa ya tajiri maarufu, Khumalo, wafanyakazi takribani kumi na tano waliokuwa wakifanya kazi kwa ukaribu sana na mtu huyo aliyeuawa miaka kadhaa nyuma nao waliuawa na maiti zao kukutwa ndani ya mashimo hayo.

    Machimbo ya dhahabu ya The Great Khumalo yalifungwa kwa muda ili kupisha uchunguzi wa mauaji hayo yaliyotokea ndani ya siku moja lakini haikujulikana ni nani hasa aliyeyatekeleza hayo.



     Maneno mengi sana yalisemwa na watu wa ndani na nje ya mgodi huo, lakini bado haikujulikana haswa chanzo cha vifo hivyo.







    “Hatufanyi kazi mpaka tupate majibu ya vifo vya wenzetu,” mmoja wachimbaji aliyekuwa akiongoza mgomo licha ya kufungwa kwa machimbo hayo aliwaambia waandishi wa habari waliokuja kujua kulikoni.



    §§§§§

    Haikuwa kawaida kwa mrithi wa mgodi huo kufika katika mashimo hayo na kufanya lolote, daima alikuwa akituma watu wake wa karibu kwa kuwaunganisha na wale wa mbia wake, mzungu kutoka Canada. Lakini siku hii yeye mwenyewe aliamua kufika katika eneo hilo la machimbo.

    Saa saba na nusu mchana alitua na helkopta katika viwanja hivyo na kulakiwa na mamia ya wafanyakazi wake waliokuwa wakimsubiri kwa hamu, kwa maana kuna wengine kati yao hata walikuwa hawamjui zaidi ya kusikia jina tu.

    Vumbi kali lilikuwa likitimka na kufanya watu wasogee mbali na eneo hilo. Lereti Khumalo, motto wa Milionea marehemu, Khumalo au The great kama alivyopenda kujiita, alikanyaga ardhi ya uwanja huo huku akisindikizwa na wanaume watano waliokuwa kamili kila idara. Aliwekwa kati, mbele kabisa akitangulia mmoja aliyekuwa amebeba bunduki aina ya SR 2 Versek kifuani mwake, mikono yake ikiwa tayari kwa lolote. Nyuma yake walifuata vijana wawili waliovalia suti maridadi kabisa na miwani myeusi kabla ya mwenyewe Lereti ambaye nyuma yake kulikuwa na wengine wawili.



    Kwa hatua za haraka kidogo huku akiwahi kulikwepa lile vumbi, Lereti alipelekwa kwenye ofisi ambayo baba yake alikuwa akiitumia sana kila aendapo kutembelea machimbo hayo. Kelele za watu waliopo nje, wakiwa na mabango, vilimsumbua mwanadada huyo mwenye miaka ishirini na nane tu. Akiwa ndani ta sueuali ya jeans iliyombana sawia, fulana nyeusi ya mikono mirefu na ilimbana shingo au tuiite kaba shingo, kofia pana aina ya pama ilikuwa kichwani kwake, kifuani alining’iniza mkufu wa uzito mkubwa wa madini ya dhahabu.

    Aliketi kitini baada ya kuingia ndani ya ofisi ile na mbele yake kulikuwa na watu wawili waliokuwa na vyeo vya juu katika mgodi huo, mmoja Mwafrika akiwakilisha kampuni ya The Great Khumalo Goldmines na mwinginw Mzungu raia wa Canada anayemwakilisha mbia wake.

    “Watu wanalalamika, ninyi mnajua si kawaida ya mimi kuja huku wala mshirika wangu Robinson Quebec, lakini imenilazimu kwa kuwa machozi ya wapigania uhuru yameugusa moyo wangu, name sikuwa na budi kukiuka makubaliano, niambieni tatizo liko wapi?” Lereti alianzisha mazungumzo.

    “Madam! Kama ulivyosikia, siku tatu zilizopita kuna watu kumi na tano wamepoteza maisha mgodini, na hii ndiyo wachimbaji wote wamegoma na wanataka majibu ya maswali yao,” Yule Mwafrika akajibu.



    “Ok, sasa maswali hayo ni maswali gani?”

    “Sisi hatuyajui, na kwa kuwa tayari kuna wakaguzi wa serikali wamekuja na kuufunga huu mgodi hivyo tunasubiri wo watasema nini,” Yule Bwana akajibu tena.

    Lereti akatulia akiitazama meza, akafikiri jambo, kisha akainua uso wake na kuwatazama watu hao walio mbele yake.

    “Niitieni viongozi wa Wafanyakazi niongee nao, mimi ni mmoja wa wawamiliki wa mgodi huu,” Kawaeleza.

    “No!” Yule Mzungu akang’aka, “Siyo utaratibu, wewe unaongea na sisi na sisi tutaongea nao,” akaongeza.

    “Mmesema, wanataka majibu ya maswali yao, nimewauliza maswali ni yepi mmekiri hamuyajui, sasa mi niaongea nini na ninyi?” Lereti aliongea mpaka akapiga meza kwa ngumi, kisha akanyanyuka na kutoka nje.

    Kelele za watu zilikuwa zimezidi, askari wenye mbwa walitanda kila mahali kuhakikisha hakuna vurugu yoyote itakayotokea eneo hilo. Lereti akasogea karibu na wale watu lakini akazuiliwa na askari wa Kizungu waliokuwa hapo, wakadai kwamba haruhusiwi kufanya anachokifanya.



    “Madam, hawa watu wana hasira na vifo vya ndugu zao, usiwakaribie wanaweza kukudhuru isitoshe wanajua wewe ndio mmiliki wa mgodi huu, japo si kweli,” mmoja wa askri aliyekuwa na jibwa kubwa kabisa alimwambia Lereti. Binti huyo alimtazama Mzungu Yule aliyekuwa na macho kama ya nyau.

    “Pumbavu mkubwa wewe! Unaweza kunambia maneno hayo mimi, eti huu mgodi wa nani, hebu rudia…”

    “Wa Sir. Robinson Quebec,” akamjibu kwa jeuri.

    Lereti alimtazama na kumsonya, kisha akampita kama hamuoni.

    “Madam!” akamwita huku akijaribu kumshika. Lereti akaepa na kupita lakini muda huo na nukta hiyohiyo Yule Yule bwana alichotwa ngwara maridadi kabisa na walinzi wa Lereti na kubwagwa chini.

    Lereti akageuka na kurudi hatua moja mpaka kwa Yule bwana pale chini.

    “Sikiliza we bwege, nakupa onyo la maneno manne tu ya kilugha chenu ‘Don’t do it again’”.

    Akawaendea watu waliosimama hapo, akawatuliza na ukimya ukatawala kana kwamba hakuna mtu eneo hilo. Kisha akaomba megaphone iliyokuwa ikitumika kuwatulizia watu hao. Walipotulia kimya kabisa akaanza kuongea.



    “Ndugu zangu, nimekuja hapa kuwasikiliza kilio chenu, sasa nitaruhusu maswali manne tu, na nitayajibu kwa ufasaha na nitashughuikia matatizo yenu,” akamaliza na kuwapa kipaza sauti wafanyakazi.

    “Swali la msingi hapa ni moja tu, tunataka tujue sababu ya vifo mfululizo vinavyotokea hapa mgodini, mwezi uliopita vijana watano waliokuwa maopareta wa mitambo kule chini walikufa tu na hatukupewa jibu zuri, siku chache baadae kiongozi mkubwa tu katoka ofisi ya nkurugenzi amekufa ghafla ofisini kwake, na msaidizi wake siku chache baadae kapata ajali naye kafa, juzi watu kumi na tano…” alishindwa kumaliza akaanza kuliza na kile kipaaza sauti kikadakwa na mwingine.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Tuna wasiwasi hata sisi tutakufa, maana kila kif kinawagusa Waafrika tu kwani Wazungu hao hawana roho mbona hawafi, tuna wasiwasi labda kuna hujuma inayofanyika hapa mgodini, tuambiwe,” kijana huyo alipokwishakusema hayo watu wote walilipuka kwa furaha na kumshangilia.

    “Mimi nataka nikuulize kimoja tu, hivi ushawahi kujiuliza kuwa kwa nini wote wnaokufa hasa wale waliokuwa ngazi za juu za uongozi ni Washririka wa mareahemu baba yako?”

    Hapo moyo wa Lereti ukapiga kwa nguvu, masikio na akili yake vikafunguka, akakunja sura ya gadhabu au mshangao, hakuwahi kujiuliza kitu kama hicho wala kukifikiri, akatikisa kichwa. Kisha akaomba kipaza sauti.

    “Nimewasikia, nimewasikia, kwa kuwa maswali yenu yote ni sawa na swali moja, naomba kwanza niwape pole waliofiwa najua wapo hapa, na kampuni itatoa rambirambi na kugharamia maazishi ya watu hao, lakini kuhusu vyanzo vya vifo hivyo ninawaahidi nitatafuta wataalamu binafsi watakaofanya uchunguzi na kisha nitawapa majibu bila kuwaicha, sintounda kamati bali nitasimamaia mwenyewe kila hatua ya uchunguzi huo. Mara baada ya serikali kumaliza uchunguzi wao ninawaomba mrudi kazini na majibu mnayoyatka mtayapata…”

    Lereti alimaliza kuongea, na watu hao na kugeuka kuondoka zake akiacha nyuma yake shangwe na hoi hoi zikirindima, moja kwa moja akaelekea kwenye helkopta aliyokuja nayo na kuondoka.



    §§§§§



    Katikati ya watu waliokuwa kwenye kusanyiko hilo la kumsubiri na kumsikiliza Lereti alikuwapo Kachero hatari wa kike kutoka idara ya Kijasusi ya Afrika Kusini, mwanadada Debrah Mbongheni. Alisikiliza kila kilichoongelewa na akiwa katikati ya umati wa watu aliweza kudodosa hili na lile. Debrah aliitazama helkopta ile ikipotelea kwenye upeo wa macho yake, akajitoa katika lile kundi la watu na kuifuata gari yake tayari kwa swala linguine kwani ilo lilikuwa limepita.

    Jioni ya siku hiyo, akiwa hotelini kwake katika vitongoji vya watu weusi huko Johanesburg, aliketi kwa utulivu juu ya kitanda kidogo akiperuzi hili na lile kuhusiana na The Great Khumalo Goldmines LTD, alkuwa akifanya chimbuchimbu kujua historia ya mgodi huo, hali ya umiliki na uendeshwaji wake kwa kupitia mtandao wa siri wa idara za usalama duniani.



    Katika peruziperuzi hizo akjikuta akifika miaka kama mine au mitano nyuma, akasoma jinsi mauaji ya utata yaliyompata bwana Khumalo, hapo Debrah, akili na ufahamu wake vikanasa na kusoma kwa makini kabrasha hilo lililokuwa likimsisimua mwili. Hapa alimsoma mshukiwa wa mauaji Tracey Tasha. Debra akaona hapana, haitoshi, akafungua mtandao wa watu hatari duniani waliowahi kuwapo, baada ya kupita majina kadhaa kama ya kina Carlos The Jackal na wengineo, hapa akakutana na picha ya mwanamke huyo, mwembaba, mrefu, aliyeshupaa mwili, Tracy, akasoma historia yake kwa umakini sana na kugundua kuwa alikuwa ni motto wa kuasiliwa. Ijapokuwa taarifa hiyo haikueleza kwa undani sana ni nani aliyemuasili lakini iliyeleza kuwa Tracy hakusoma shule yoyote duniani, waalimu walikuwa wakija kumfundisha nyumbani na somo alilojifunza zaidi lilikuwa ni lugha, aliweza kuongea kwa ufasaha luga kumi na nne za ulimwengu.

    Debra hakuamini anachokisoma alipoona kuwa kifo ca Tracy kilimfika huko Afrika ya Mashariki, Tanzania.

    “Tanzania?” akajiuliza, akuamini, akavutiwa sana kutaka kujua mwisho wa Tracy ulikuwaje huko Tanzania. Katika kupekuwa sana ndipo alipokuta abari iyo japokuwa haikuwa imeandikwa vizuri lakini alielewa kuwa Tracy aliuawa na Mpelelezi mashuhuri wa Tanzania, Afrika na nje ya mipaka ya Afrika. Hapo Debrah alijikuta akitetemeka na kichwani mwake jina la Amata au Kamanda kama aitwavyo kutokana na kazi yake inayojulikana na watu wachache lilikuwa lijirudiarudia lakini hakuweza kuona hata moja ya picha yake.

    “Amata, T.S.A 1” alijiwazia jina hilo na kisha kujitupa kitandani akifikiria zaidi juu yake.



    DAR ES SALAAM – saa 3:12 usiku



    KAMANDA AMATA alisimama kiukakamavu mbele ya Madam S wakitenganishwa na meza kubwa iliyo katikati yao, mara hii sio ofisi kuu kule Shamba, la, ni ofisi ndogo iliyopo mita chache tu kutoka jengo muhimu kabisa la nchi hii, jengo jeupe.

    Mikononi mwake alikuwa amekamata kabrasha lile ambalo Madam S jioni hiyo alikabidhiwa na Waziri wa Mambo ya Nje.



    “…anatakiwa kuuawa na si vinginevyo. Lakini kabla ya hilo Kamanda, Baraza la Usalama ya Nchi za SADC, kwa imani waliyonayo juu ya utendaji kazi wa mashirika yetu ya ndani ya usalama na kiintelijensia wametukabidhi kazi ya uchunguzi wa pili wa vifo vinavyoendelea kutukia katika moja ya migodi kule Afrika Kusini kama ilivyoandikwa humo. Ndani ya kabrasha hilo utapata taarifa ya uchunguzi uliofanywa na shirika Fulani la Afrika ya Kusini lakini SADC haijaridhika nao, hivyo imeomba kazi hii ifanywe na idara za hapa nchini, yaani nje ya Afrika Kusini, kazi hii ni siri na ombi hili ni siri kubwa.

    Kwa kifupi, uwende Afrika ya Kusini, ukakamilishe zoezi hilo kwa siku chache, kisha kama huyo anayetajwa humo ndiye, basi unatakiwa kuhakikisha ameuawa kwa siri ikishindikana utajua wewe, Afrika imechoka.”



    Kamanda Amata akiwa kalibana kabrasha lile kwa mkono wake mmoja wa kushoto, alimtazama Madam S kwa macho makavu.

    “Kamanda Amata, nategemea utafanya kazi hiyo kwa uaminifu mkubwa kuliko siku zote, unapoona Jumuiya kubwa kama hizi zinakutumia ujue wewe sasa ni zaidi ya T.S.A 1. Uwe makini kwani ukichelea, Makaburu hawana mzaha, maisha yako rehani sasa, nakusubiri kwenye meza hii hii ama ukiwa hivyo ulivyo au ukiwa ndani ya box,” Madam S akamaliza.

    Kamanda Amata akasimama kwa ukakamavu, “Yes, Madam, umesomeka, kazi itafanyika”. Wakapeana mikono, Madam S akazunguka upande wa pili na kumkumbatia Kamanda huku machozi yakimtoka.

    “Nakupenda Amata, nakupenda zaidi ya mtoto au mume wangu,”…







    BAA YA RUVUMA MPAKA MAPUTO – UWANJA WA NDEGE



    CHIBA mara tu baada ya kuiacha ndege iliyomfikisha Tanzania kutoka Mauritius, hakuwa na shughuli nyingine zaidi ya miadi yake ya kwanza na Amata katika baa kubwa ya Ruvuma mpaka Maputo. Aliweka mizigo kwenye gari yake ambayo daima huiacha hapo uwanjani kila anaposafiri na kuitumia arudipo, alipohakikisha usalama upo akaondoka taratibu na kuikata ile barabara kubwa ya Pugu, akachukua uelekeo wa Kalakata huku akipita kwenye madimbwi makubwa ya maji.

    Haikumchukua muda mrefu aliwasili pale anapopataka, akatafuta maegesho mazuri na kuliweka gari lake kisha akateremka. Akaangazaangaza huku na kule, akavuta hatua chache na kulikaribia lango la kuingia ndani ya baa hiyo. “Ukiingia tu meza ya kulia”, aliyakumbuka maneno ya mwisho ya Kamanda Amata alipokuwa akimpa maelekezo juu ya wapi alipo. Hakukosea, moja kwa moja aliiendea meza hiyo na kumkuta mwenyeji wake, lakini badala ya mmoja sasa walikuwa wawili.

    “Karibu kaka, karibu sana,” Amata alimkaribisha Chiba kitini, wakapeana mikono wakiwa wamesimama.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Inaonekana mnapendana sana,” sauti nyembamba ya Yule mtu wa mwingine, mwanamke mrembo aliyejipaka rangi yam domo kama kachinja kuku kwa meno ilimfikia Chiba, akatabasam, kisha akamwangalia Amata.

    “Lete ndovu baridi tafadhali,” Amata akaagiza wakati wakiketi chini wote wawili.

    “Vipi hapo?” Chiba akauliza.

    “Ah, kawaida tu ya kutafuta umbea wa hapa na pale,”

    “Na mi ningeshangaa, maana sampuli yenyewe haina mashiko…” wakacheka pamoja na mara hiyo kinywaji kilifika.

    “Haya mi sasa niwaache,” yule mwanadada akasema.

    “Hpana keti pamoja nasi, wewe ni mtu muhimu kwetu,” Kamanda akamwambia huku akimshika kiuno na kumkalisha kitini.

    “Ndiyo Chiba!” akaanzisha mazungumzo.

    “Mmenikatisha raha zangu we na bibi yako,” Chiba akalalama baada ya kupiga funda moja la bia.

    “Raha utapata mbinguni,”

    “Nimesikia umepata tenda Afrika ya Kusini,”

    “Ndio kaka, kama wewe ulivyonyang’anywa tenda Mauritous,”

    “Ok, kila kitu kipo sawa kaka, fika stesheni ya treni katikati ya jiji la Joh’burg, kijana mrefu mweusi, akiwa katika jeans ya buluu na fulana nyeupe ataketi jirani yako, mpe hii…” Chiba alitoa maelekezo kisha akampa Kamanda kipande cha noti ya shilingi mia tano. “…naye atakupa cha upande wa pili, atavichukua na kukupa begi ambalo ndani yake utakuta maelekezo yote. Kumbuka ni saa kumi na dakika tano keho jioni,” akamaliza na kuinua chupa yake akamimina bia yote tumboni mwake na kushusha chupa tupu.

    “Umesomeka,” kamanda akajibu na kuiweka ile noti katika waleti yake.

    “Nyie mbona siwaelewi?” Yule mhudumu akauiza.

    “Usijali, lete vinywaji vingine,” Akaagizwa.





    DURBAN – saa 3:19 usiku



    LERETI KHUMALO alikuwa fisini kwake mpaka muda huo, akiwa hajui nini anapaswa kufanya. Alishika kabrasha hili akaliweka huko, akachukua hili akalitupia kule, akili yake ilikuwa kama imeruka.

    Akashtushwa na mlango uliofunguliwa ghafla kisha mlinzi wake akaingia ndani na kuufunga nyuma yake.

    “Madam, tunapaswa tukupeleke nyumbani sasa, muda umekwenda,”

    “Hapana, ngoja kidogo,” Lereti akajibu.

    “Kumbuka hili jingo halitakiwi kuwa na mtu kufikia sasa ni hatari kwa mitambo ya usalama,” Yule mlinzi akamwelewesha.

    “Sikiliza Solwezi, kuna jambo linanitatiza sana hasa la hivi vifo kule mgodini, natafuta kampuni ya kukodi kuendesha uchunguzi lakini nashindwa,”

    “Madam, hiyo kazi inabidi uifanye kwa utulivu sana, lakini haupaswi kufanya peke yako, lazima umshirikishe mbia wako,” Solwezi akamweleza.

    Lereti akamtazama kwa jicho kali, “Najua, najua la kufanya lakini hili nataka nifanye peke yangu, kwanza sasa nina mpango wa kuvunja mkataba na ile kampuni hata kama baba yangu ndiye aliyeingia nao, mimi sitaki,” Lereti akaeleza huku akisimama na kufunga mkoba wako, akaacha kila kitu shaghalabaghala na kutoka akitanguliwa na Yule kijana mpana.



    Dakika kumi baadae alikuwa nyumbani kwake, hakupoteza muda, moja kwa moja aliiendea kompyuta yake na kuingia kwenye mtandao na kutafuta shirika binafsi linaloweza kumsaidia katika kazi yake hiyo. Aliperuzi na kuperuzi akakutana na mshirika mengi sana ya Kiafrika na ya Ulaya, lakini katika upembuzi wake bado hakupata linalomridhisha.

    Lereti alikuwa kama kichaa katika hilo, alipitia mashirika makubwa na madogo, akajaribu kutafuta anwani za watu binafsi wanaofanya kazi kama hizo lakini bado alijikuta akigonga ukuta. “Nifanyeje?” alijiuliza bila kupata jibu, akaendelea kupekua na kupekua. Alipochoka, akaondoka zake na kuingia chumba chake cha kulala, akajibwaga katika kitanda kilichompokea kwa upendo, usingizi ulimpaa, saa yake ya ukutani ilikuwa ikiyoyoma, tayari saa tisa ilikuwa inafika nab ado hakuwa kakamilisha kazi yake.

    Lereti alijikuta akilia peke yake, akaitazama picha ya baba yake Mzee Khumalo iliyokuwa juu ya meza yake ya kusomea. “Nakupenda sana baba,”alijisemea, akaiendea na kuichukua mikononi mwake, akaigusa kwa vidole vyake, “Walikuua baba, niliapa kukulipia kisasi, nilifanya hivyo kwa kuhakikisha nakuwa bega kwa began a mtu aliyemuua,” akiwa katika kuwaza hivyo moyo wake ukapiga kwa nguvu akakumbuka tukio lile la kifo cha Tracey Tasha, Lereti akamkumbuka muuaji huyo, akamkumbuka aliyemuua pia, Amata. “Kamanda Amata,” akajisemea kwa sauti ndogo, akjikuta akiruka kwa furaha kama aliyeshikwa kichaa au uendawazimu.



    SIKU ILIYOFUATA

    Lereti aliamka mapema sana ijapokuwa alichelewa kulala, alijiandaa na kusubiri gari yake kufika, kila wakati alikuwa akitazama saa yake na kuona muda kama hauwendi. Walinzi wake tayari walikuwa wamekwishamzunguka na wakati huo gari yake aina ya Lamborghini ilifika na kuegeshwa mahala pake. Akiwa na walinzi wake waliondoka kuelekea kunako ofisi yake.



    KHUMALO TOWER

    Akiwa ofisini kwake Lereti alikuwa ni mwenye furaha, akachukua kitabu chake cha namba za simu na kupekua hapa na pale, kutafuta jina la Kamanda Amata; nia na madhumuni ni kumuomba amsaidie katika uchunguzi huo, kichwani mwake aliona ni yeye tu anayeweza kufanya kitu. Kosa ambao alijilaumu ni kuwa tangu mara ya mwisho akutane na Amata Dar es salaam hakuwahi kuwasiliana naye tena wala kupekuwa kitabu hicho ambacho mawasiliano yake aliyaweka. “Atanielewa?” akajiuliza. Akapiga moyokonde na kuchukua kile kitabu, kabla hajakifunua, katibu wake akaingia ofisini akiwa na mkono wa simu usiotumia waya.

    “Madam, kuna simu yako naomba nikuunganishe,”

    “Inatoka wapi?”

    “Inatoka Canada kwa Sir Robinson,”

    “Ok, iruhusu tafadhali,” Lereti alimwambia mwanadada huyo. Kwa kuwa siku hiyo hakutaka simu za kumsumbua alizidivert zote ili zipite kwa katibu huyo kwanza. Lereti akaweka simu sikioni na kuipokea.

    “Yes, Mr. Robinson…”

    “Hilo swala unalotaka kulifanya la uchunguzi wa vifo sijui nini, litakugharimu, kwa nini hutaki kutekeleza mkataba wetu?” ile sauti ilimwuliza.



    “Kwanza Mr. Robinson nataka tuonane ikiwezekana tusitishe mkataba na niko tayari kukulipa sehemu yako,”

    “Lereti, baba yako alikuwa mfanyabiashara mzuri sana na ninasikitika kwa nini aliuawa mapema, lakini wewe unakuwa jeuri na utaharibu kazi. Sasa sikiliza kama kuna wasiwasi wowote juu ya eneo hilo la mkataba, tukae tena mezani tuwekane sawa. Lakini nakuonya sitaki kusikia swala la kuita kampuni ya uchunguzi kwani ni inyume na mkataba wetu…”



    “…Mr. Robinson, Robinson…” simu ilishakatika. Lereti akashusha pumzi ndefu na kuitua ile simu. Akaegemea kiti chake na kufumba macho kwa nguvu, hasira ziliwaka ndani mwake, “Robinson anataka nini?” akajiuliza. Mara nukushi yake ikapiga kengele, akairuhusu nayo ikaingiza ujumbe mfupi wa maneno machache.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    …Ole wako uanzishe uchunguzi juu ya sakata hilo, utakula jeuri yako, watu wapo kazini…



    “Watu wapo kazini,” akawaza huku akitikisa kichwa, akahisi kuchanganyikiwa na ujumbe ule, jasho jembamba limkamtiririka.

    Akavuta kitabu chake na kukipekuwa, ni muda mrefu tangu akiweke hapo kabatini, akapekua pekua lakini hakuiona anwani ya Amata, akahamanika na kupekuwa tena kwa nguvu kila ukurasa, hakuona anwani ile, akapigwa na bumbuwazi, kurasa ile ilikuwa imechanwa, ilibaki kishina chake tu. Lereti alihisi akili yake ikishikwa na ganzi, “Nani kaondoa hii karatasi?” akawaza huku akihisi kutetemeka mwili.



    §§§§§

    DEBRAH MBONGHENI alijikuta badala ya kufikiri kazi aliyopewa yeye alivutiwa na mtu anayejulikana kama T.S.A 1, Amata.

    Alishusha glasi yake iliyojaa pombe kali na kuituliza chini taratibu. Akili yake ilikuwa ikifanya kazi haraka sana katika kulikabili jukumu alilopewa, aliitathmini hali ya siku iliyopita iliyokuwa pale mgodini, alimkumbuka Yule mwanadada aloyekuja kwa helkopta, alipenda kukutana naye kwa maswala yake ya awali kabla ahajakabiliana na yeyote mwingine. Kwa kuwa alikuwa amempiga picha kwa kutumia miwani yake aliyoivaa, aliitoa ile picha kutoka kwenye memory card yake na kuihamisha kwenye kompyuta yake, kisha akaiingiza kwenye mtandao wa usalama wa N.I.A na kupata habari za mwanadada huyo.

    Lereti Khumalo, Manager katika mgodi wa The Great Khumalo; yalikuwa ni maelezo baadhi kati ya mengi aliyoyapata. Uamuzi uliokuja kichwani mwake, kwanza ni kumwendea mwanadada huyo ili akapate maelezo zaidi. Moyo wake uliingia kitete, akaamua kuondoka eneo hilo na kujiandaa kwa safari hiyo ghafla…







    Ilimchukua saa chache tu Debrah kufika katika mji wa Durban akitokea Johanesburg kwa ndege ya shirika la Afrika Kusini. Jua bado lilikuwa kali kiasi lakini hatuwezi kusema kuwa kulikuwa na joto au baridi ila hali ya hewa kwa ujumla ya kawaida siku hiyo. Akavuta hatua na kufika jengo la mapokezi ambako alipita bila shida na kutokea nje ya uwanja huo mkubwa uliopewa jina la Luis Botha. Tax ilikuwa usafiri pekee uliomfikisha katika ghorofa kubwa lililobeba maandishi 'Khumalo Tower' juu yake, akainua uso kulitazama na kisha akaingia ndanui yake na kupata maelekezo ya wapi mwenyeji wake alipo.



    §§§§§

    LERETI KHUMALO aligutushwa na hodi iliyobishwa mlangoni kwake na mwanadada aliyeficha uso wake kwa miwani nyeusi alijitoma ndani yachumba hicho kikubwa. Lereti akamtazama kwa jicho pembe kutoka pale alipokuwa akiandika kwenye kompyuta yake. “Nani huyu?” akajiuliza.

    Debrah akaketi pa si na kukaribishwa akitazamana uso kwa uso na mwanadada huyo tajiri. Lereti akaacha kuandika na kuisogeza kando kompyuta yake.

    “Karibu sana, nikusaidie nini?”

    “Asante sana,” akajibu Debrah huku akiiondoa miwani usoni mwake, “Nafikiri nipo katika ofisi ya Bwana Khumalo”.

    “Bila shaka, na we mwenzangu ni nani?”

    “Dhudumile Mwambakosi,” akajitambulisha kwa jina la bandia huku akitabasamu.

    “Ndiyo Dhudumile karibu sana,”

    “Asante, mimi nimetokea nchini Lesotho, ni mmiliki wa maduka kadhaa ya vito vya thamani hasa vitengenezwavyo kwa dhahabu na almasi. Kipindi cha nyuma nilikuwa nanunua mara kadhaa madini hayo kutoka kwa Mr. Khumalo, nikaanguka kiuchumi kutokana na hila za Wabia wangu, lakini sasa nimeweza kusimama mwenyewe hivyo nimerudi kutaka kufanya biashara tena na Mr. Khumalo, yeye ananifahamu sana, je ; naweza onana naye?” Debrah akajieleza maelezo ya uongo akiwa na nia ya kuzunguka lakini afike kwenye lengo lake.

    Lereti akatabasamu na kushusha pumzi ndefu, ukimya ukatawala kati yao, nukta kadhaa baadaye kama si sekunde akajiweka sawa na kuanza kuzungumza.

    “Mara ya mwisho ulifanya biashara na Mr. Khumalo mwaka gani au lini?”

    “Takribani miaka saba iliyopita,”

    “Ok. Huwezi kumwona kwa sasa, kwani hayupo katika biashara hii,” Lereti alimweleza.

    Debrah naye akajiweka sawa, sasa akajiweka sawa, akajiegemeza kwenye meza iliyokuwa mbele yake.

    “Ina maana ameiuza kampuni au inakuwaje hapo sijaelewa,” akaeleza.



    “Hajaiuza kampuni ila kwa sasa hayupo kabisa, amekwishakufa miaka mitano iliyopita,” Lereti alieleza kwa sauti ya chini kidogo iliyosikiwa na Debra kwa ufasaha.

    “Poleni sana, sasa nani anaendesha kampuni hiyo? Baada yake,” Debra akarusha swali kwa maana sasa alimfikisha Lereti pale anapotaka na akajua wazi kuwa atapata kile anachokihitaji kiurahisi zaidi.

    “Mimi, mimi ni binti yake pekee na ndiyo mtoto wake wa kwanza, kwa hiyo kama ni biashara inabidi sasa ufanye na mimi,”

    “Sawa nimekuelewa lakini nikuulize swali, ila samahani kwa swali hili, Mbona sikuwahi kusikia kama Khumalo anaumwa au kifo chake kilikuaje?”

    “Aliuawa!” Lereti akajibu kwa mkato na kuinama chini kama anayeangalia kitu fulani.

    “Pole sana Lereti, baba yako alikuwa mtu mwenye roho nzuri sana, alipendwa, mara kadhaa aliwahi kuja Lesotho na kunitembelea katika ofisi yangu,” Debrah aliongea uongo tupu lakini kwa mtu asiyejua uwongo kama Lereti aliona kuwa ni kweli yote anayoambiwa.

    “Sasa Lereti, mi nataka kurudisha tena biashara na kampuni yako, unasemaje?” akaanzisha mazungumzo mengine kwa lengo lilelile.

    “Haina shaka ila kwa sasa kuna matatizo nayashughulikia, nikiyamaliza nitakutaarifu, we niachie mawasiliano yako,”

    “Matatizo?” Debra akauliza.

    “Ndiyo, si unajua kampuni hii inaendeshwa kwa ubia kwa miaka mingi sasa,” Lereti akafunguka.

    “Ndiyo, hata mzee aliwahi kuniambia hilo,”

    “Sasa nataka kusitisha mkataba na huyo mbia ili nfanye kazi mwenyewe,”



    “Umeona kuwa hakuna maslahi au,” Debra akaendelea na uchokozi wake.

    “Hapana kuna matatizo mengi tu katika mkataba wetu, na kwa sasa mgodi umefungwa na serikali kwa muda,”

    “Aaaah ok, nimesikia hiyo habari kumbe ni mgodi wa Khumalo?”

    “Ndiyo, kuna vifo vimetokea mfululizo ambavyo vimeleta utata, swala hili limepelekea serikali kufunga mgodi na kufanya uchunguzi ambao majibu yake wanayo wao mimi bado sijayapata,” Lereti alijikuta anaingea mambo mengi ambayo hasingepaswa kufanya hivyo.

    Mara simu yake ikaita, akanyakuwa mara moja na kuiweka sikioni.

    “ (…) ndiyo niko tayari, nakuja,” akakata ile simu.

    “Dhundumile, nina kikao na wadau fulani, napaswa kuondoka, sasa nitakutafuta baada ya siku tatu, nafikiri mgodi utakuwa umefunguliwa na pia napenda kukukaribisha kama mdau wa marehemu Khumalo hata ukatembelee na kuona kazi inayofanyika,” Kamwambia hayo huku akiwa amesimama wima na mkoba wake ukiwa tayari begani.

    “Asante sana,” Debrah akamshukuru na kumpa mkono kisha akamkabidhi kadi yake ya kibiashara kwa minajiri ya kutafutana baada ya hizo siku tatu.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    §§§§§

    JOHANESBURG - saa 9:30 alasiri.



    KAMANDA AMATA aliteremka kwenye ndege ya shirika la ndege la Tanzania (ATC) iliyomfikisha katika jiji hilo salama salimini na kwa muda muafaka. Haikumchukua muda kupita eneo la ukaguzi na kutoka nje ya uwanja huo.

    Akiwa katika eneo la maegesho ya magari binafsi na Tax aliitazama saa yake ilikuwa yapata saa 9:51. “Siyo mbaya, nimewahi,” akawaza kisha akainua begi lake la wastani na kuvuta hatua chache kuelekea kituo cha treni iendayo kasi ambacho kimejengwa karibu sana na uwanja huo na kuunganisha miji ya Gauteng, Pretoria na Johanesburg yenyewe, akatafuta mahala alipoelekezwa na Chiba, akaketi na kuweka begi lake sakafuni.

    Ilikuwa ni kituo cha treni cha kisasa kabisa, treni iendayo kasi ndiyo iliyokuwa ikitumiwa eneo hili, msafiri akishuka kwenye ndege kama anaelekea Pretoria basi hapo ilikuwa ni mahala pake. Watu walikuwa ni wengi wakisubiri treni hiyo ambayo ilibaki dakika kadhaa kuwasili, “Wenzetu wameendelea bwana,” akajisemea huku akipapasa gazeti alilolinunua uwanjani hapo 'The Mail' alipekuwa habari zilizopo kuanzia juu na kurasa za ndani, habari nyingi zilikuwa za ki-siasa na michezo zaidi ya hapo ni matangazo mengi sana ya biashara.

    Alam kutoka kwenye vipaaza sauti vilivyofungwa eneo hilo la abiria ilitoa mlio wake na kufuatiwa na sauti nyororo ya mwanadada ikitoa taarifa ya kuwasili kwa treni hiyo dakika moja ijayo na kuwaweka watu kuwa tayari kuingia kwani haikai muda mrefu eneo hilo.

    Kamanda Amata alitazama hekaheka za watu waliokuwa wakijiweka tayari kwa safari.

    “Kaka, we hauwendi?” sauti ya kike ilimgutusha Amata kutoka kwenye gazeti lililomteka akili, akageuka na kumwangalia mwanadada aliyekuwa akimwuliza swali hilo kwa lugha ya Kizulu, bila kujiuliza Amata akajibu kwa lugha hiyohiyo pia lakini lahaja ya sentensi yake ilimfanya mwanadada huyo kucheka.

    “Wewe sio Mzulu?” akauliza.

    “Hapana, mimi ni Mtswana,”

    “Umekuja kutembea au?”

    “Yeah, kutembea tu, nipo kama siku tatu mbele,” akamjibu.

    “Karibu sana,” yule mwanadada akamkaribisha Amata.

    “Asante, unaelekea wapi?” akamyupia swali huku akimwangali na macho yake yakanasa kifuani mwa dada huyo.



    “Nakwenda tu kwa rafiki yangu kesho ninarudi,”

    “Oh, vizuri, nitafurahi kupata mwenyeji kama hutojali,” Kamanda akaanza fujo zake.

    “Yeah kwa nini isiwe hivyo? Na we ni mgeni,”

    wakiwa katika kuongea mara treni iliwasili na kusimama mita chache kutoka pale walipoketi, milango ikafunguka na watu wakaanza kuteremka na wengine wakisubiri kupanda. Yule mwanadada akanyanyuka.

    “Kwa heri tutaonana,” akamuaga Kamanda.

    “Sasa nitakupataje mwenyeji wangu hiyo kesho?” akamtupia swali akiwa kama mita moja na nusu hivi. Yule mwanadada akasimama na kugeuk, tabasamu lake lilimwacha Amata hoi pale kwenye kiti.

    “Are you seriuos?” sasa akauliza kwa Kiingereza. Na Amata akajibu kwa kichwa. Hakusita akamtajia namba zake za simu ya mkononi.

    “Nipigie saa kumi na mbili jioni kesho,” akamwambia huku akiikwea treni hiyo na kumpungia mkono kupitia kwenye kioo.

    Nukta hiyo hiyo kamanda Amata alijikuta hayupo peke yake kwa mara nyingine pale kitini. Kijana mwenye sifa zilezile alizotajiwa na Chiba alikuwa ameketi pembeni yake naye akisoma gazeti na mapajani kwake alikuwa amepakata bahasha.

    “Wapo wengi sana hapa Johanesburg,” yule kijana akaongea Kiswahili safi kabisa. Kamanda Amata hakujibu kitu, akaendelea kusoma gazeti lake alilokuwa nalo mikononi.

    “Karibu Joh'burg,” akamkaribisha huku akimpatia kijipande cha noti ya mia tano ya Kitanzania. Kamanda akachomoa cha kwake na kukichukua kile kingine akaviunganisha.

    “Asante sana, nimekaribia,” akajibu. Yule kijana akachukua ile bahasha na kumpatia, naye akaipokea.



    “Kila kitu kipo humo, maelekezo na vingine vyote, nafikiri hakuna swali,” akasimama na kumuaga Kamanda kisha akaingia kwenye treni ileile iliyokua tayari kuondoka. Kamanda Amata akapapasa ile bahasha, na kuhisi kuna vikorokoro vingi ndani yake, akaifungua na kuchungulia akatoa akatoa funguo ya gari iliyoning'iniziwa kijikaratasi chenye ujumbe, 'Maegesho ya Kaskazini,' akanyanyuka na kuipachika kwapani ile bahasha, akanyanyua begi lake na kuelekea mlango mwingine wa kituo kile.

    Alipofika nje akaitazama saa yake ikamwonesha upande upi ni Kaskazini, akafuata uelekeo na kutokea eno kubwa la wazi lililokuwa na gari nyingi zilizoegeshwa hapo. Akabofya rimoti iliyowekwa sambamba na funguo ile, gari moja ndogo. Fupi. Nyeusi yenye sura ya kishari shari ilwaka taa za mbele, akaiendea na kuketi ndani yake nyuma ya usukani.

    Akachukua bahasha nyingine iliyopo ndani ya ile bahasha kubwa akaichana na kukuta pesa, Euro elfu kumi, pesa nyingi sana. Akazitia mkobani. Akafungua dash board ya gari hiyo ya kisasa, ndani yake kulikuwa na pistol moja yenye nguvu semi auto Boberg XR9-S, ilikuwa ni bastola fupi yenye shepu ya kuvutia, yenye uzito wa oz 17.4 pamoja na magazine yake iliyojaa. Kamanda Amata akatabasamu kukamata silaha hii kwa mara ya kwanza, aliisikia tu sifa zake lakini hakuwahi kuitumia na sasa ilikuwa mara ya kwanza kwake, akaifyatua magazine yake na kuikuta imeshiba sawasawa, risasi nane zilikuwa ndani yake, akairudishia na kuiweka sawa. Akaipachika kiunoni mwake upande wa nyuma.



    Akachukua kijiboksi kingine ambacho ndani yake kulikuwa na kitu kama redio ndogo nyeusi yenye akaichukua nkisha akafyatua kijiwaya kidogo na kukipachika sikioni mwake kisha akabofya kitufe kidogo kilicho upande wa juu, kwa ujumla haikuwa redio bali ni chombo maalumu cha kumfikishia mlengwa ujumbe.



    “... karibu Johanesburg, hoteli utakayoitumia ni Hoteli ya 77 chumba namba 320. Gari hii aina ya Kilimanjaro GX 220-TZ itakufaa kwa kazi yako, hakikisha unazoma maelekezo kwa makini. Kazi iliyokuleta ni kufanya uchunguzi juu ya vifo vinavyotokea katika mgodi wa dhahabu wa Khumalo hapa Johanesburg ndani ya saa sabini na mbili. Tumeitupilia mbali taarifa ya uchunguzi kutoka shirika la kipelelezi la Afrika Kusini. Tunaka uifanye kazi hiyo kwa uaminifu na umakini na kama kuna anayehusika awe kutoka ndani au nje auawe kwa siri ili kukomesha kabisa uonevu huu. Kamanda Amata, baraza la usalama la nchi za SADC limekuteua kwa kuwa linaujua uwezo wake na linaamini utaifanya kazi hiyo. Kama utahitaji msaada wowote utawasiliana na mtu mwenye namba hii (…).



    Ujumbe huu unaharibika baada ya dakika moja tu tangu kumalizika kwake, asante, jihadahari na wanawake warembo...”

    Akaichomoa sikioni mwake na kuiweka juu ya kiti akitafakari, mara kile kiredio kikapiga alam, na kutoa maneno “weka mbali kwa usalama wako” huku kikiwaka kijitaa chekundu. Kamanda Amata akaichukua na kuitupa kwenye maua, sekunde kama kumi hivi, ukatokea mlipuko wa wastani ambao haikuwa rahisi kwa mtu wa umbali wa mita tano kusikia, kile kiredio kiliungua chote kikabaki jivu, akakifuata na kukiokota kisha akakitia kwenye ile bahaha na kukitupia chini ya kiti. Alipohakikisha usalama upo akaondoa ile gari na kueleke mjini.



    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    HOTELI 77 ni hoteli ya kifahari ndani ya jiji la Johanesburg, hoteli hii ilikuwa na kila sifa za uzuri na usalama, viongozi wengi wakubwa kutoka nje na matajiri mbalimbali wa dunia ya kwanza walipenda kufikia mahala hapa.

    Kamanda Amata aliingiza gari yake kwenye kibaraza na kuteremka akiiacha ikiunguruma, wahudumu wawili wakaisogelea, mmoja akachukua begi na mwingine akaipeleka maegeshoni.



    “Sipho Mabaso,” akajitambulisha kwa mhudumu aliyekuwa katika dirisha kubwa la mapokezi, akapewa kitabu na kujisajiri kisha akaichukua funguo yake.

    Ndani ya chumba hicho kipana chenye kitanda kikubwa na kochi moja la watu wawili, Kamanda Amata alisimama mlangoni akikitazama chote kwa chati, akipepesa macho kona hii na ile ili kujua kama kuna hatari yoyote inayomsubiri, hakuna. Akafyatua kioo cha saa yake, nyuma ya kioo hicho kilichobeba mishale ya kuonesha wakati kulikuwa na nobu nyingine mbili ndogo, akabonyeza moja wapo kisha akatulia kimya, sekunde kadhaa akaanza kutembea tembea ndani ya kile chumba mpaka maliwato, hakuna kitu. Akajitupa kitandani na kulala chali huku mikono yake akiiweka chini ya kisogo chake, akafumba macho.



    * * *

    “Miss Lereti, kwa sasa hatuwezi kuruhusu Mgodi wako ufanye kazi, kwa kuwa sakata la vifo vilivyotokea bado ni tete, tumewasiliana na mbia wako kupitia wakala wake naye amekubaliana na uamuzi wa serikali juu ya hili,” kijana mmoja aliyevalia suti nadhifu alimweleza Lereti maneno hayo yaliyouchoma moyo wake.

    Kikao cha watu wane kilikuwa kikiendelea katika moja ya ofisi za serikali katika jiji la Durban, agenda kubwa ikiwa ni juu ya mgodi wa dhahabu unaomilikiwa na Khumalo The Great pamoja na mbia wake Robinson Quebec.



    “Mbona mnanichanganya? Yeye Robinson akubaliane na ninyi, yeye ni nani hata mkataba wetu hausemi kuwa yeye ana mamlaka ya kukubali au kukataa jambo kiutoka nje, mamlaka hayo yapo kwa The Great Khumalo LTD na siyo Robinson Dia-Gold LTD,” Lereti aling’aka.



    “Sikiliza Lereti, tunachokifanya hapa siyo kwamba ni uonevu ila mkataba tuliopewa na mbia wako ambao tunao unaonesha tofauti na unavyosema wewe, hata sisi tulikataa kukubaliana naye lakini akatupa mkataba wake na kampuni nyako, huu hapa,” Yule kijana akazungumza na kuweka mezani kabrasha moja ambalo ndani yake lilikuwa na karatasi kadhaa,” Lereti akalichukua na kulipitia haraka haraka; macho yakamtoka, kijasho chembamba kikamvuja, mkataba ule ulikuwa tofauti kabisa na anaoujua yeye, ule ulionesha kinyume. Akafungua kurasa za mwisho na kukuta saini zilizopo ni zilezile, akashusha pumzi ndefu.



    “Huu sio mkataba aliosaini baba yangu,” Lereti akaonge huku akipi ngumi mezani, “Kuna mkono wa mtu hapa, sikubali,” akaongeza.



    “Tupatie mkataba wako kama unao, maana sisi serikalini tunao huu,” Yule kijana akamwambia na wajumbe wakatikisa vichwa vyao. Lereti akampa ishara katibu wake, naye akatoa kabrasha lililofanana vilevile. Yule kijana akalichukua na kutoa karatasi kadhaa ndani yake, akaanza kuzisoma kwa umakini. Alipomaliza akonekana wasi kuwa amehamanika na kile alichokisoma ndani yake, akamtazama Lereti kasha akamtazama mwakilishi wa Robinson Dia-Gold LTD.



    “Nyie watu mbona mnanichanganya?” Yule bwana akauliza.



    “Huu ndio mkataba uliopo, huo mwingine feki, na ni lazima nifungue kesi mahakama ya biashara kwa utapeli wa Robinson anaotaka kuufanya,” Lereti alifura kwa hasira, akongea huku kauma meno.



    “Mheshimiwa, huu ndiyo mkataba ambao kampuni ya Robinson Dia-Gold ilisainiana na The Great Khumalo miaka saba ilipota, na muda wake mpaka uishe ni miaka kumi, sasa huo aliokuja nao Lereti sisi hatuutambui na ni lazima tufungue kesi mahakama ya biashara kwa kutugeuka,” mwakilishi wa Robinson naye alitema cheche zake.



    “Ok, naahirisha kikao, mpaka baada ya wiki moja, hii mikataba yote lazima niiifikishe kwa wahusika wa usajili wa makampuni kasha mtapewa taarifa lakini mgodi hautofunguliwa kwa sasa, mpaka tufikie muafaka,” Yule kijana akawaeleza na kuagana nao.

    Lereti alisimama akionekana wazi kuchanganyikiwa, macho yake yalijaa machozi, akatoka bila kuaga na kuondoka zake.



    *  *  *



    DEBRAH alijiridhisha na hatua ambayo ameianza kwa mahojiano hayo mafupi na Lereti, hakupoteza muda kwa kuwa alikuwa na siku chache tu za kukamilisha swala hilo kadiri alivyoagizwa na boss wake. Jioni hiyo hiyo alipata usafiri wa ndege kurudi Johanesburg kuendelea na shughuli nyingine zilizo sambamba na hilo. Alipofika tu katika chumba alichopanga na kuweka kambi, alioga harakaharaka na kuamua kuchukua hatua ya pili ya uchunguzi wake usiku huo huo. Kwa kuwa kutoka kwa Lereti aliyoyapata yalimpa mwanga kiasi sasa alidhamiria kujua kinagaubaga sababu ya vifo vilivyotokea mgodini. Siku zote walizoea kusikia watu wamefukiwa na si vinginevyo lakini hivi vya mtindo huu vimekaaje. Alijiweka tayari na kutoka nje ya jengo hilo. Safari ya kuelekea hospitali ya rufaa ya Charlote Maxeke iliyopo katika barabara ya Jubilee kitongoji cha Parktown. Aliingia kwenye gari yake aina ya BMW na uondoka kwa kasi iliyopelekea watu waliokuwa katika mgahawa wan je wa hoteli hiyo kushangaa.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Japokuwa alipambana na foleni za hapa na pale lakini dakika thelathini zilimtosha kufika katika hospitali hiyo kubwa katika jiji la Johanesburg. Alipokwishaegesha gari yake, alivuta hatua na kuufikia mlango mkuu uliomwongoza mpaka meza ya mapokezi, hapo akakutana na wahudumu wa hapo. Akaelekezwa kilipo chumba cha kuhifadhia maiti na haraka haraka akaelekea huko. Kama alivyofikiri ndivyo ilivyokuwa alimkuta mhudumu wa chumba hicho akiwa ameketi katika ofisi yake huku akivuta sigara taratibu na miguu yake kaipandisha juu yameza, muziki wa Brenda Fassie ukikijaza chumba hicho, alikuwa kajiachia kana kwamba yuko peke yake.

    Debra akafungua mlango na kuingia ndani yake, Yule bwana akashusha miguu na kuketi vizuri.



    “Enhe, marehemu wako anaitwa nani?” yulw mhudumu akauliza huku akivuta kabrasha lake.



    “Aliyekwambia nina ndugu marehemu ni nani?” Debrah akamtupia swali.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog