Simulizi : Ufukwe Wa Madagascar
Sehemu Ya Tano (5)
Niligundua kuwa fahamu zangu zilikuwa zimenipotea muda mfupi baada ya kupigwa ngumi moja ya tumbo iliyonipelekea nitapike maji mengi niliyoyameza tumboni na hapo nikaanza tena huhema kwa pupa huku maumivu makali yakisambaa mwilini. Lile jopo la wale makamanda wa jeshi bado lilikuwa mbele yangu nyuma ya ile meza na hapo nikagundua kuwa haukuwa umepita muda mrefu tangu kupotewa na fahamu zangu hadi kuzinduka. Nilikuwa nimelowa chapachapa kufuatia yale maji niliyomwagiwa.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Tueleze Luteni pesa ulizoiba ziko wapi na watu unaoshirikiana nao ni akina nani?”. Yule kamanda akaniuliza huku akinitazama kwa makini usoni.
“Mnadhani nitaukwepesha ukweli kwa kuyageuza maneno yangu. Nimekwisha waambia kuwa sifahamu lolote”. Nikaongea kwa shida huku mawazo mengi yakipita kichwani mwangu. Ukweli ni kwamba moyoni nilishaanza kuhisi juu ya hatari kubwa iliyokuwa ikininyemelea mle ndani. Vile vielelezo vyangu vilikuwa vimenipelekea moja kwa moja niaminike na wale makamanda wa jeshi la wananchi wa Burundi kuwa nilikuwa miongoni mwa wahaini wa serikali na askari mamluki walioingia nchini Burundi kinyemela kwa ajili ya kusadia kufanyika kwa mapinduzi ya kijeshi. Kwa kweli niliishiwa nguvu na kuanza kukata tamaa kwani utetezi wangu ungehitaji ushahidi mkubwa ambao ungeweza kuwashawishi wale makamanda kuwa mimi sikuwa miongozi mwa hao wanamapinduzi wa kijeshi waliokuwa wakisakwa. Ushahidi ambao ili niaminiwe ingelinibidi nizungumze ukweli juu ya misheni yangu yote hadi kufika kwangu pale Burundi.
Labda ningeweza kufanya hivyo lakini maadili ya kazi yangu kamwe hayakuniruhusu. Kwanza sikutaka kuamini kuwa mara baada ya kuzungumza ukweli huo ningeachiwa huru, lah hasha!. Ni dhahiri kuwa baada ya hapo ningeuwawa kama walivyouwawa mahaini wengine. Lakini vilevile kazi yangu ya ujasusi sifa yake moja ni kufanyika katika mazingira ya siri sana kwani hakuna nchi yoyote inayoruhusu kuchunguzwa au kupelelezwa na nchi nyingine kwa sababu za kiusalama. Hivyo endapo ningezungumza ukweli kwa namna moja au nyingine ningeweza kujitenganisha na wingi wa lawama za moja kwa moja kwangu badala yake lawama hizo zingeelekezewa kwa nchi yangu Tanzania iliyonituma na hivyo kuharibu mahusiano mazuri yaliyojengwa kwa muda mrefu. Ingawa kufuatia kukamatwa kwangu nilifahamu kuwa tayari kulishatia dosali mahusiano mazuri yaliyokuwa baina ya nchi hizi mbili lakini niliona nisipalie mkaa suala hilo kwa kuzungumza ukweli. Hivyo nikapanga kushikilia msimamo wangu hata kama ungenigharimu kifo.
“Luteni, mimi naona tukupe kwanza muda wa kutafakari ili baadaye tutakaporudi uweze kuyajibu maswali yetu vizuri”. Yule kamanda akaongea kwa kujiamini huku akiitazama saa yake ya mkononi kama anayekimbizana na muda.
“Muda hauwezi kubadili ukweli kamanda”. Nikaongea kwa hasira nikipingana kikamilifu na hoja ile.
“Muda hauwezi kubadili ukweli lakini unaweza kubadili matokeo”. Yule kamanda akaongea kwa ujivuni huku akiruhusu tabasamu la kihuni usoni mwake kisha nikamsikia akimwambia yule mtu nyuma yangu.
“Mfungue na umuache huru”. Mwanzoni nilidhani kuwa sijasikia vizuri lakini kitendo cha kumuona yule mtu nyuma yangu akianza kunifungua zile kamba mwilini kwenye kile kiti kikanipelekea nistaajabishwe na upendo ule wa mwendo kasi. Wakati yule mtu alipokuwa katika harakati za kunifungua ile kamba mara nikawaona wale makamanda wakisogeza viti vyao nyuma na kusimama kisha pasipo kuzungumza neno wakaanza kuondoka mle ndani kupitia ule mlango tulioingilia.
Yule mtu nyuma yangun alipomaliza kunifungua zile kamba na yeye akaanza kuondoka mle ndani huku akiwa ameongozana na wanajeshi wengine wawili ambao kupitia sare zao niliweza kuwatambua kuwa walikuwa makomandoo wanaonuka ubabe wa kila namna. Wale watu walipotoka mle ndani ule mlango wa kile chumba ukafungwa kwa nje na hapo nikabaki peke yangu mle ndani.
Nikiwa bado nimeketi kwenye kile kiti mawazo mengi yakawa yakipita kichwani mwangu. Maneno ya yule kamanda yalikuwa yakiendelea kuzitaabisha fikra zangu juu mambo yalivyokuwa yakienda. Sasa nilichokuwa nikikifikiria ilikuwa ni kutoroka mapema mle ndani kabla ya wale makamanda hawajarudi mle ndani kunifanyia mahojiano ya awamu ya pili. Taratibu nikaanza kuyatembeza macho yangu kukipeleleza vizuri kile chumba kilichofanana na pango dogo lililochongwa miaka mingi iliyopita kwa ustadi wa hali ya juu. Tatizo likabaki ni kwa namna gani ningeweza kutoroka kwenye kifungo kile kile pasipo kujua ramani ya lile eneo.
Wakati nikiendelea kutafakari ghafla nikashtushwa na sauti hafifu ya mtu anayekohoa nyuma yangu. Baridi nyepesi ya mshtuko wa hofu ikasambaa mwilini, nywele zikanicheza kichwani huku mate yakinikauka kooni. Nikaanza kuhisi jambo la hatari nisilolifahamu lilikuwa likininyemelea taratibu nyuma yangu. Nikapanga kuwa nisigeuke nyuma haraka hata hivyo mawazo yangu yakasalitiwa na hisia na kunipelekea nishindwe kuvumilia na hapo taratibu nikageuka kutazama nyuma.
Kwa sekunde chache nikashikwa na mduwao usioelezeka. Kiasi cha umbali wa hatua moja nyuma yangu alikuwa amesimama mtu ambaye sikuwahi kumuona hapo kabla wala kufahamu kuwa alikuwa ametokea wapi kwa mle ndani. Lilikuwa pandikizi la mtu mweusi na urefu wake ungepelea kidogo kutimia futi saba. Mwili wake ulikuwa imara na ulioshiba misuli ya nguvu. Jitu lile lilikuwa limevaa suruali ya jeshi na buti za jeshi miguuni, kichwani alikuwa amenyoa upara huku kifua wazi na mikono yake alikuwa ameikunjia kifuani. Lile jitu lilikuwa likinitazama kama kiumbe cha ajabu sana kuwahi kuonekana mbele yake. Mara moja nilipomtazama yule mtu mashaka yakaanza kuniingia huku nikianza kunusa harufu ya matata. Nikataka nisimame haraka pale kwenye kiti hata hivyo sikufanikiwa kwani pigo moja la teke la lililoinuliwa na kwa kasi ya umeme na kutua begani mwangu linanirudisha chini na kuniketisha kwenye kile kiti.
“Tulia chini komredi hakuna haja ya kuharakisha mambo”. Lile jitu likanionya huku maumivu makali yakisambaa begani mwangu. Ukubwa wa umbo la lile jitu ukanishangaza sana kama siyo kuniogopesha.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Wewe ni nani na unashida gani na mimi?”. Nikaliuliza lile jitu huku nikigeuka kiwiziwizi kulitazama tena.
“Usijali utanifahamu hapo baadae”
“Una shida gani na mimi?”. Nikauliza kwa udadisi.
“Wakubwa wamenituma nije kukuhoji”
“Wakubwa gani na kwanini wasije wao wenyewe?”
“Wakubwa wangu wa kazi”
“Kwanini wasije wao wenyewe?”
“Wao wanamajukumu mengine muhimu kwa wakati huu”
“Wewe ndiyo hauna majukumu?”. Nikaliuliza lile jitu na kabla sijaendelea lile jitu likanichapa kofi zito la shingoni ambalo maumivu yake yakanipelekea nimeze funda kubwa la mate huku hasira ikinichemka mwilini.
“Maswali mengine yanafaa umuulize mke wako”. Lile jitu likanifokea na sauti yake nzito ikatengeneza mwangwi mkubwa mle ndani kisha likaniuliza.
“Pesa ulizokwapua ziko wapi na watu unaoshirikiana nao kwenye mapinduzi yenu ya kishenzi ni akina nani?”
“Nimekwisha waambia mabwana zako kuwa sifahamu lolote”. Nikafoka kwa hasira na lile jitu halikuweza kuvumilia tusi lile hivyo likarusha teke usawa wa kichwa changu lakini tayari nilikwishaliona pigo lile hivyo nikainama chini kidogo kulipisha likate upepo. Hata hivyo wakati nikifurahia hila ile lile jitu likaniwahi kwa pigo jingine la teke ambalo lilizama kwenye tundu la mgongo wa kile kiti cha mbao na kunitupa chini kama bwege. Nikawahi kusimama lakini mara hii mateke mawili makini ya lile jitu yakafakinikiwa kunilambisha tope kwenye sakafu ya kile chumba na kunisababishia maumivu makali. Lile jitu kuona vile likaanza kujitapa huku likijipigapiga kifuani kama sokwe mtu na kuangua kicheko cha mahoka.
Haraka nikawahi kusimama kisha nikalifuata lile jitu kulikabili na liliponiona nikilifuata likasimama kama sokwe na kunisubiri. Nilipolifikia nikaanza kulichapa mapigo hatari ya chapchap sehemu tofauti nikipanga kuliangusha chini, lakini ni kama nilikuwa nikilitekenya na hivyo kulipelekea liangue kicheko cha dhihaka. Nilipoona lile jitu halikolei mapigo nikalichapa teke moja la korodani. Likawahi kushtukia pigo lile na kuudaka mguu wangu kisha likanikwida kibabe na kuninyanyua juu kama mwana miereka halafu likaanza kukimbia na mimi mle ndani na kwenda kunibwaga kwenye kona moja ya kile chumba, maumivu yale yakanipekea nipige mayowe. Loh! lile jitu lilikuwa na nguvu nyingi kama lililokunywa viagra. Kabla sijasimama likawahi kupenyeza mkono wake mmoja na kuidaka shingo yangu kisha likaninyanyua juu kwa mkono wake mmoja huku likinitazama kwa hasira. Mara hii nikapata wazo muruwa, haraka nikajikunja na kulitandika lile jitu pigo la kifuti cha pua. Pigo lile makini likauvunja mwamba wa pua yake hapo na hapo lile jitu likapiga yowe kali na kunitupa kando haraka kama lililoshika kaa la moto. Lile jitu likaendelea kupiga yowe kali mle ndani na hivyo kupelekea mtetemo mkali mle ndani kiasi kwamba popo waliokuwa mafichoni wakapagawa na kuanza kuyakimbia maficho yao wakizunguka hovyo mle ndani.
Sasa nililiona lile jitu likinijia mzima mzima huku limepandwa na hasira kama mbogo aliyeparazwa na risasi ya kichwa ya muwindaji. Sikuwa na nguvu za kutosha za kukabiliana na lile na lile dubwana hivyo nikavisogelea vile viti nyuma ya ile meza mle ndani na kuanza kulitupia lile jitu. Ilikuwa kama mchezo kwani lile jitu lilivipangua vile viti kwa mikono yake huku vingine vikivunjika vunjika vipande vipande na kusambaratika mikononi mwake. Lile jitu liliponifikia nikaanza kulikwepa nikikimbilia upande huu na ule kama bondia anayetafuta nafasi nzuri ya kutupa konde lake kwa mpinzani. Lile jitu likawa likinifuata kila ninapoelekea mle ndani. Nilipopata nafasi nzuri nikaruka kwa ufundi wa hali ya juu na kujikita ukutani kwa mtindo mzuri wa sarakasi kisha nikajitupa hewani na kulinasa vizuri lile jitu shingoni kwa kabari ya miguu yangu, kabari matata ambayo ili mtu aweze kujinasua angepaswa kujikaza vizuri ili shonde lisimtoke.
Sote takapiga mwereka na kuanguka chini huku lile jitu likilalama kwa maumivu. Baada ya kukurukakara kubwa mle ndani huku lile jitu likijitahidi kujinasua hatimaye likanizidi nguvu na kuikamata miguu yangu vyema na kuindoa shingoni mwake kisha likawahi kunichapa makofi mawili ya mgongoni wakati nilipojaribu kujiviringisha mbali naye. Japokuwa lile jitu lilikuwa na mwili mkubwa lakini wepesi wake ulinishangaza sana kwani wakati nilipokuwa nikisimama nilishangaa nikichotwa mtama kwa ufundi ilionishangaza sana. Nikarushwa hewani huku nikiweweseka kwa pigo lile. Nilipotua chini lile jitu likawahi kunidhibiti kwa kabari matata shingoni mwangu kwa mokono yake imara. Nikajitahidi kufurukuta bila mafanikio nikitupa mikono na miguu yangu huku na kule.
Lile dubwana halikuniachia kirahisi badala yake likaendelea kukaza mikono yake kwa nguvu zote na kunipelekea nianze kuhema kwa shida. Sasa mle ndani kulikuwa na patashika ya aina yake katika kuhakikisha kuwa najinasua mapema kutoka katika kabari ile ya kifo. Sikufua dafu kirahisi kwani lile jitu lilikuwa na nguvu nyingi za kunidhibiti hivyo ni kama nilikuwa napoteza muda wangu bure kwani halikuniachia.
Hali yangu ikaanza kuwa mbaya baada ya kuanza kukosa hewa, nikatanua mapafu yangu bila mafanikio huku mishipa yangu shingoni ikituna na macho yameniwiva kama nyanya. Hofu ya kifo ikaanza kuniingia taratibu. Nikajaribu kulipiga lile jitu kwa kichwa cha kinyumenyume hata hivyo sikufanikiwa kwani lile jitu lilinikwepa kwa wepesi wa ajabu. Nikiwa katikati ya kujinasua mara wazo fulani likanijia. Kufumba na kufumbua nikatupa pigo moja makini la kiwiko cha nguvu kwenye jicho la kulia la lile dubwana. Lilikuwa pigo makini lililoniletea majibu muruwa. Lile jitu likapiga yowe kali mle ndani kiasi cha kuniogopesha hata mimi mwenyewe hata hivyo halikuniachia badala yake likaninyanyua juu na kunitupia ukutani na kunisababishia maumivu makali ya bega. Hata hivyo sikuwa na muda wa kujilegeza kwani roho yangu tayari ilikuwa mnadani. Wale popo mle ndani wakaanza tena kurandaranda wakionesha kushtushwa sana na zile kelele.
Wakati lile jitu likinijia pale chini huku limejifunika jicho kwa kiganja chake mimi tayari nilikuwa nimeliona hivyo nikawahi kujiviringisha kando kulikwepa kisha kwa mtindo mzuri wa sarakasi nikalisindikiza kwa teke makini la mgongoni. Lile jitu likaenda kujibamiza ukutani huku tusi zito likimtoka mdomoni huku mimi tayari nikiwa nimeangukia upande wa pili wa kile chumba. Hata hivyo sikufanikiwa haraka kujipanga kwani tayari lile jitu lilikuwa limenifikia hivyo likanichapa teke matata kifuani na maumivu yake yalikuwa ni kama niliyepigwa na kipande cha jabali kifuani. Nikatupwa nyuma vibaya na kuangukia tope sakafuni. Nilijaribu kusimama haraka lakini lile jitu lilikuwa makini sana hivyo haraka likawa limenifikia na kuanza kunitupia mateke mfululuzo, baadhi nikafanikiwa kuyapangua mengine yakanipata hata hivyo sikuacha kujitetea nikihamia upande huu na ule kumpotezea umakini.
Nilipopata nafasi nzuri nikarukia ukutani na kukita vyema miguu yangu kisha kwa mtindo wa sama soti nikajibetua hewani kulifuata lile jitu kwa pigo makini la kifuti cha kichwa. Lilikuwa pigo hatari sana kiasi kwamba mtu yeyote wa kawaida kama angepona basi angekuwa tayari amerukwa na akili lakini kwa lile jitu hali ilikuwa tofauti kidogo kwani nililiona likirudi kinyumenyume kwa mwendo wa kupepesuka kama mlevi huku akipiga yowe kali kama aliyepigwa kwa nyundo ya mawe kichwani. Lakini hatimaye akasimama na kukitikisa kichwa chake huku na kule kukiweka sawa. Nilipomchunguza nikaona damu nyepesi ikimtoka puani na masikioni na hapo nikajua kipigo changu kilianza kumkolea.
Sikutaka kumkawiza haraka nikainuka kule nilipoangukia ili kumkabili. Pigo langu la kwanza la teke lilimpata mbavuni, pigo la pili likamparaza tumboni, pigo la tatu akaudaka mguu wangu kwa mkono wake wa kushoto kisha akanichota matama ulionirusha vibaya hewani huku nikiweweseka na nilipotua chini akanikita mguu wa mgongo, pigo baya zaidi kuwahi kukutana nalo katika harakati zangu. Nikagugumia kiume kwa maumivu makali, akawahi kurusha teke linipate tumboni lakini niliwahi kujiviringisha kando hivyo pigo lile likakata hewa bila mafanikio na kunipelekea lile jitu lipepesuke hovyo kwa kukosa mhimili. Nikamfuata haraka na kumchapa teke la kifua, akalipangua kwa madaha lakini hakuwa ameshtukia hila yangu kwani wakati akifurahi kwa kulipangusa pigo langu mimi tayari nilikwishaufyatua mguu wangu mwingine, nikamchapa teke la shingo, pigo lililompelekea apige chafya kama aliyenusa ugolo.
Lile jitu kuona vile likapandwa na gadhabu likaanza kunitukana matusi ya kila aina huku likinisogolea taratibu kama linalotaka kunikamata mzimamzima. Nikaanza kulikwepa nikahamia upande huu na ule huku macho yangu yakiwa makini katika kuhakikisha kuwa halinifikii. Mbinu za lile jitu kutaka kunikamata mzimamzima zilikuwa zimeanza kunitahadharisha kwani nilifahamu kuwa lilikuwa na nguvu nyingi mno kiasi kwamba lingeweza kunidhibiti bila usumbufu mkubwa. Mara mbili tatu nikafanikiwa kulikwepa lile jitu hata hivyo wakati nikijiandaa kulikwepa kwa mara nyingine kwenye kona ya kile chumba bahati mbaya nikateleza kwenye tope na kujikuta mikononi mwake. Lile jitu likanikumbatia na kunibana kifua na mikono yangu kwa nyuma kisha likaanza kunibana mbavu kama chatu anayejiandaa kunimeza, maumivu yake yalikuwa makali mno huku nikihisi kichomi. Nikiwa nimeanza kuona hatari ya kupoteza maisha nikakusanya nguvu za kutosha kisha nikalitandika lile jitu kichwa cha nguvu cha kinyumenyume. Pigo lile likauchana vibaya mdomo wake na kuyavunja meno yake mawili huku akijing’ata ulimi vibaya. Hata hivyo lile jitu halikuniachia na mimi kuona vile nikarudia pigo lile kwa mara pili mara hii nikafanikiwa kulivunja vibaya taya lake la kulia. Lile jitu likapiga yowe na kuniachia bila kupenda, nikaangukia upande wa pili huku nikiwa nahema kwa pupa baada ya kukosa pumzi ya kutosha kwa kitambo sambamba na maumivu makali mbavuni.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Loh! sikuwa nimegeuka nyuma haraka kulitazama tena lile jitu wakati lilipochomoa kisu kutoka kwenye mkanda wa kombati yake kiunoni na kunitupia. Nikashtushwa na maumivu makali yaliyonipelekea nipige yowe baada ya kisu kile kuzama mgongoni. Kabla sijajihami vizuri kisu kingine kikazama kwenye mnofu wa paja la mguu wangu wa kushoto na kusambaza maumivu makali mwilini. Nikapiga yowe kali kuomba msaada lakini ilikuwa ni sawa na kazi bure. Pigo la tatu la kisu lilinikuta wakati nikijitupa chini upande wa pili wa ile sehemu hivyo kikazama kwenye mnofu wa msuli wa mkono wangu wa kushoto. Hofu ikaziteka haraka hisia zangu, nikaanza kuona kifo kilikuwa karibu sana kunifikia. Lile jitu lilikuwa na shabaha ya hali juu katika mtindo wa mapigano ya visu hata hivyo mimi nilikuwa mwalimu zaidi yake. Hivyo kabla ya pigo la nne la kisu chake halijanifikia mimi tayari nilikwishawahi kukichomoa kile kisu kwenye mnofu wa mkono wangu wa kushoto kisha kwa shabaha makini nikakitupa kile kisu kwa mtindo wa kininja, kikaenda kuzama tumboni kwa lile dubwana na huku mpini wake ukisalia nje. Lile jitu likapiga mayowe ya kutetemesha lile pango hadi wale popo kuanza kurandaranda hovyo mle ndani. Lile jitu likaushika ule mpini wa kisu tumboni mwake huku macho yamemtoka kama mjusi aliyebanwa na mlango huku limesimama, taratibu damu ikaanza kusambaa kwenye viganja vyake mkononi.
Kwa maumivu makali nikajikaza na kuchomoa kile kisu kilichozama kwenye mnofu wa paja langu huku nikipiga yowe la uchungu kisha nikakizungusha na kukitupa kwa lile jitu. Kile kisu kikazama mbavuni mwa lile jitu lakini mara hii lile jitu liliachama mdomo pasipo kupiga kelele kama mtu mwenye kiu mbaya ya maji karibu na kufa. Kisu cha tatu wakati nikikichomoa mgongonim maumivu yake yakanipelekea nipige kelele za woga kwani damu nyingi ilinitoka na mimi kwa hasira nikakitupa kile kisu kwa lile jitu kwa nguvu zangu zote na hapo kikaenda na kuzama kwenye shingo yake. Mara hii nilisikia mguno hafifu kwani lile jitu halikuwa na nguvu ya kupiga mayowe tena badala yake nikaliona taratibu likianguka chini kama mbuyu uliopigwa shoka la mwisho kuanguka.
Mle ndani kukasikika kishindo kikubwa wakati lile dubwana likaanguka chini kwenye tope, wale popo wakatowekea kwenye maficho yao kisha ukimya ukachukua nafasi yake mle ndani. Nilianguka chini bila kupenda huku nikihema kwa tabu kama mwanariadha wa mbio za masafa marefu katika mstari wa mwisho wa ushindi wake. Yale majeraha ya visu mwilini mwangu yalikuwa yakivuja damu nyingi iliyoniogopesha kama siyo kunikatisha tamaa ya kuendelea kuvuta pumzi ya uhai hapa duniani. Hali yangu ilikuwa ikielekea kuwa mbaya zaidi. Pamoja na ushindi nilioupata sikuwahi kupambana na jitu hatari katika harakati zangu za kijasusi kama lile jitu lenye kila tabia za mnyama. Nilianza kuona kizunguzungu huku wingu zito likianza kutanda kwenye mboni zangu. Nikataka kusimama lakini sikufanikiwa kwani kizunguzungu kilinipelekea nipige mweleka wa aina yake. Hata hivyo akili yangu haikuwa imechoka kiasi cha kushindwa kufikiri juu ya hatima yangu.
Nikiwa pale chini nikaanza kusota taratibu kulifuata lile jitu pale lilipoangukia. Nilipolifikia nikaanza kulipekua lile jitu mifukoni. Kwenye mfuko wa kushoto wa suruali yake ya jeshi nikaikuta bastola aina ya Berreta M9 na magazini mbili zilizojaa risasi. Nikaichukua ile bastola za zile magazini mbili kisha taratibu nikasota kwenye tope hadi katika sehemu moja yenye uchochoro wa jiwe la ukuta wa kile chumba ambapo nilipenyeza mkono wangu na kuificha ile bastola huku nikiugulia maumvu makali sana katika majeraha ya vile visu mwilini mwangu.
Damu nyingi ilikuwa ikiendelea kunitoka kwenye yale majeraha hali iliyonipelekea nizidi kusikia kizunguzungu. Hatimaye nikayaacha yale maficho ya bastola na kusota kwenye lile tope sakafuni kuelekea kwenye ile meza waliokuwa wameketi wale makamanda wa jeshi pale awali. Hata hivyo sikufanikiwa kwani nilikuwa nimepoteza damu nyingi sana na hali yangu ilikuwa mbaya. Kizunguzungu kilikuwa kimenizidi kufuatia kupoteza damu nyingi kwenye yale majeraha mwilini. Sikuweza tena kuendelea na safari yangu baada ya kuona giza zito likitanda kwenye mboni zangu, nguvu zikaniishia taratibu nikajilaza chini bila kupenda. Nilijaribu kufungua kinywa changu ili nipige yowe kuomba msaada lakini sikufanikiwa badala yake sauti yangu mwenyewe ilinirudia masikioni kama sauti ya mwangwi usioeleweka. Hatimaye sikuweza tena kuona chochote mbele yangu na kilichofuata baada ya pale sikuweza kufahamu kinachoendelea.
_____
Fahamu zilinirudia kwa haraka na hapo nikapiga chafya mara tatu kisha nikafumbua macho yangu taratibu nikiyatembeza huku na kule. Mara hii nilishtuka zaidi baada ya kujiona kuwa nilikuwa juu ya kitanda cha chuma chenye godoro kuukuu lenye madoa makavu ya damu bila foronya. Nilikuwa kwenye chumba kidogo bila dirisha, upande wa kulia wa kile kitanda kulikuwa na meza fupi chakavu ya mbao, juu ya meza ile kulikuwa na beseni dogo la aluminium lenye vifaa vyote muhimu vya Tibba kama mikasi, bandeji, dawa ya kukaushia vidonda, vidonge vya kutuliza maumivu, mabomba ya sindano, kisu kidogo cha kupasulia mgonjwa wakati wa oparesheni, koleo, glovu na dawa nyingine ambazo sikuzifahamu. Hata hivyo vitu vile tayari vilikuwa baadhi vimetumika kwa namna vilivyokuwa vimefunguliwa.
Nilipoyapeleka macho yangu kutazama upande wa kushoto hapo nikaona stendi ndefu ya chuma ya kitabibu iliyotundikiwa chupa mbili za dripu, chupa moja ya dripu ya maji na nyingine dripu ya damu. Macho yangu yakapata uhai kidogo na nilipoichunguza milija ya zile chupa za dripu nikagundua kuwa zote sindano zake zilikuwa zimechomekwa kwenye mkono wangu wa kushoto.
Haraka nikataka niinuke na kuketi kitandani lakini hilo lilishindikana kwani miguu yangu na mkono wangu wa kushoto uliotundikiwa dripu ilikuwa imefungwa kwa pingu zilizofungwa kwenye pembe za kile kitanda cha chuma.
“Hapa ni wapi?”. Nikajiuliza huku hofu ikiniingia taratibu. Maumivu makali yakaanza kusambaa mwilini sambamba na kichwa kuuma. Nilipojichunguza vizuri nikagundua kuwa nilikuwa nimefungwa bandeji mkononi, mgongoni na pajani. Loh! na hapo ndiyo nikakumbuka vizuri juu ya mambo yote yaliyonisibu wakati nikipambana na lile jitu lenye nguvu za ajabu na hatimaye kuliangamiza. Hata hivyo nilipopeleleza vizuri nikagundua kuwa mandhari yale yalikuwa tofauti na kule kwenye kile chumba nilichopambana na lile jitu.
Hiki kilikuwa chumba kidogo sana hata paa lake lilikuwa fupi sana. Mle ndani hapakuwa na taa ya umeme isipokuwa taa moja ya kandili iliyokuwa juu ya ile meza ya kitabibu pembeni ya kile kitandani nilicholazwa. Mle ndani hapakuwa na mtu yeyote mwingine. Wakati nikizidi kupeleleza mandhari yale kwa macho nikaanza kusikia njaa kali tumboni.
Fahamu ziliponirudia vizuri nikakumbuka kuwa mara ya mwisho nilikuwa nikisota kuelekea kwenye ile meza ya kile chumba nilichopambana na lile jitu. Nikakumbuka kuwa sikuwa nimefanikiwa kuifikia ile meza pale fahamu zangu ziliponitoka baada ya kuzidiwa na kizunguzungu kikali.
Wakati nikiendelea kuwaza pale juu kitandani mara nikasikia mlango wa kile chumba ukifunguliwa nyuma yangu kisha kukafuatia na sauti ya vishindo vya miguu ya watu ambao idadi yao sikuifahamu haraka hadi pale watu hao waliponifikia pale kitandani na kunizunguka. Sikutaka kujitia kuwa bado sijarudiwa na fahamu kwa vile nilikuwa na njaa sana hivyo nilihitaji chakula vinginevyo matibabu yale yasingekuwa na maana yoyote kwani hali yangu ingezidi kuwa mbaya.
Wale watu walipoingia mle ndani wakakizunguka kile kitanda wakinitazama kwa shauku. Sikutia neno lolote badala yake nikayatembeza taratibu macho yangu kuwatazama na kwa kufanya vile nikamtambua mtu mmoja tu miongoni mwao ambaye alikuwa ni yule daktari mbilikimo aliyekuwa ameongozana na wale makamanda wa jeshi kwenye kile chumba tulichokuwa na mateka wengine pamoja na Kepteni Amadou Coulibary Sidibe. Wale wanaume wengine sura zao zilikuwa ngeni kabisa machoni mwangu na walikuwa wamevaa kiraia ingawa nilipowachunguza vizuri nikajiridhisha kuwa walikuwa ni maafisa usalama wa serikali ya Burundi. Wale maafisa walikuwa na sura za kazi na hakuna hata mmoja kati yao aliyeonekana kuwa rafiki. Wale maafisa usalama wakaendelea kunitazama kwa makini pale kitandani huku wakionekana kuridhishwa na maendeleo ya afya yangu. Hatimaye mmoja wao akageuka na kumuuliza yule daktari mfupi kando yake.
“Tunamuhitaji kwa mahojiano mafupi”. Yule afisa usalama akaongea kwa kujiamini huku akimtazama yule daktari na hapo nikajua mtu aliyekuwa akihitajika kwa mahojiano nilikuwa mimi. Hata hivyo sikutia neno lolote.
“Hali yake bado haijatengamaa vizuri, anahitaji siku moja zaidi”. Tule daktari akajibu huku akizitazama kwa makini zile chupa za dripu.
“Kwanini siku moja zaidi?”’. Afisa usalama mwingine akauliza huku akigeuka na kumtazama yule daktari kwa udadisi.
“Mwili wake bado ni dhaifu na amepoteza damu nyingi mwilini. Siku moja zaidi atakuwa amemaliza dripu zote na kupata afueni kama hali yake haitobadilika”. Yule daktari akaitetea taaluma yake na hivyo kunipelekea nifurahi kimoyomoyo.
“Kesho usiku tutakuwa hapa kumchukua hatuwezi kusubiri zaidi. Huyu mtu anataarifa muhimu tunazozihitaji”
“Sawa!”. Daktari yule akaitikia bila kutia pingamizi huku akigeuka na kunitazama kabla ya kuniuliza.
“Vipi unaendeleaje?”
“Nina njaa sana naomba chakula”
“Vipi kuhusu maumivu ya kichwa?”. Yule daktari akaniuliza huku akiyakagua majeraha yangu mwilini.
“Naombeni chakula tafadhali vinginevyo nitafia humu ndani”. Nikaendelee kuwasihi wale watu. Yule daktari hakusema kitu badala yake akafungua droo ya meza iliyokuwa kando ya kile kitanda mle ndani na hapo akatoa chupa ya chai na kikombe cha bati. Nikamuona akiifungua ile chupa na kisha kumimina uji mwepesi wa moto kwenye kile kikombe cha bati na kunipa. Nikakipokea kile kikombe kwa pupa na kuanza kuunywa ule uji wa kwa papara pasipo kusubiri upoe. Ulikuwa uji wa moto sana, mwepesi na usiokuwa na chumvi wala sukari hata hivyo kwangu ilikuwa afadhali. Nikabugia vikombe vinne na nilipomaliza mdomo wangu ulikuwa umeungua vibaya na kusababisha vidonda.
“Endelea kupumzika zaidi utapata nafuu”. Yule daktari akanisisitiza baada ya kumaliza kunihudumia na hapo yule daktari na wale maafisa usalama wakatoka nje ya kile chumba na kufunga mlango. Mle ndani nikabaki tena mpweke huku mawazo mengi yakipita kichwani mwangu nikawa nikizikumbuka sura za wale maafisa usalama waliotoka kuniona muda mfupi uliopita.
Usiku ule sikuweza kupata usingizi badala yake mawazo yangu yalijikita katika kufikiria juu ya hatima yangu mle ndani. Mwisho wangu niliuona ulikuwa karibu kuliko nilivyofikiria hata hivyo niliendelea kumuomba Mungu. Nikameza funda kubwa la mate na kujilaza vizuri huku macho yangu yakitazama darini.
_____
Asubuhi ya siku iliyofuata yule daktari mfupi alikuja tena kunijulia hali na kuniletea kiamsha kinywa cha uji mwepesi wa mahindi uliokolezwa pilipili za kunikomoa, usiyotiwa chumvi wala sukari. Hata hivyo sikuwa na namna ya kufanya hivyo nikakaza roho na kuunywa uji ule huku nikifahamu kuwa nilihitaji nguvu mwilini ili kukabiliana na mateso makali dhidi ya wale maafisa usalama wa Burundi usiku ule kama walivyoniahidi. Japokuwa mwili wangu bado ulikuwa dhaifu lakini nilikuwa nimepata nafuu kiasi cha kuweza kunipa matumaini.
Wakati nilipoitazama saa ya mkononi ya yule daktari nikagundua kuwa ilikuwa ikielekea kutimia saa moja asubuhi vinginevyo giza la milele la mle ndani bado lingekuwa fumbo kubwa la majira yale kwangu.
Yule daktari akamaliza kunihudumia na kunifunga tena vidonda vyangu halafu wakati akijiandaa kuondoka nikamuona akinitazama kwa kunihurumia sana kama mtu aniambiaye buriani na hali ile ikanizidishia mashaka.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Usiku wa leo utaenda kuhojiwa na pengine huo utakuwa ndiyo mwisho wako”. Yule daktari akanidokeza kwa sauti ya chini ili walinzi wawili makomandoo wa jeshi waliokuwa wamemsindikiza na kuishia nje ya mlango wa kile chumba wasimsikie. Hazikuwa taarifa za kuniogopesha hata kidogo kwa vile wale maafisa usalama walikwisha gusia juu ya mahojiano hayo wakati waliponitembelea siku ya jana. Kitu kilichonivutia ilikuwa ni hali ya huruma ya yule daktari mfupi na namna alivyonitazama.
“Nitaenda kuhojiwa wapi?”. Nikauliza kwa kunong’ona huku nikimkazia macho yule daktari.
“Humu humu ndani lakini sifahamu ni wapi”
“Kwanini unasema baada ya mahojiano hayo ndiyo utakuwa mwisho wangu?”
“Wamepanga kukuua”. Yule daktari akaongea kwa huruma na taarifa ile ikapelekea koo langu likauke kwa hofu.
“Unaweza kuniambia hapa ni wapi?”
“Hata mimi sipafahamu”. Yule daktari akanong’ona na kunishangaza.
“Kwa vipi?”. Nikamuuliza yule daktari kwa mshangao.
“Ninapoletwa humu ndani huwa nafunikwa machoni na ninapoingia humu ndani huondolewa kitambaa machoni ili nisifahamu hapa ni wapi”. Yule daktari akanong’ona huku akimalizia kufunga bandeji kwenye jeraha langu pajani.
“Najitaji msaada wako tafadhali”. Nilinong’ona.
“Msaada gani?”. Yule daktari akaniuliza kwa udadisi.
“Wapelekee ripoti wakubwa zako kuwa hali yangu imebadilika na kuwa mbaya ili leo wasiweze kunihoji nipate nafuu zaidi”. Nilijaribu kumshawishi yule daktari nikipanga kuununua muda wakati nikifikiria namna ya kutoroka lakini haraka daktari yule akatikisa kichwa chake kuonesha kukataa.
“Nina mke na watoto na wote wananitegemea. Sitaki kuiacha familia yangu yatima”. Yule daktari akanong’ona kisha akamalizia kazi yake.
“Muombe Mungu wako”
Yule daktari akaniaga kisha akaelekea mlangoni ambapo aliufungua na kutoka nje. Ule mlango wa kile chumba ulipofungwa nikasikia vishindo vya miguu vikiyoyoma na hatimaye kutoweka kabisa eneo lile na hapo mle ndani kukawa kimya.
_____
Nilikuwa nimepitiwa na usingizi mzito kitandani wakati niliposhtushwa na kelele za kufuli za mlango wa kile chumba zikifunguliwa kwa papara. Nilikuwa nimelala usingizi mtamu kuliko siku zote za maisha yangu, usingizi ulionipelekea niyasahau masaibu yote niliyowahi kupitia. Lakini hofu ya kifo cha kinyama sasa ilikuwa imeziteka haraka hisia zangu baada kushtushwa na kelele za funguo zikitekenya kufuli za mlango wa kile chumba.
Mlango wa kile chumba ulipofunguliwa wanaume saba wakaingia kibabe mle ndani lakini yule daktari mfupi hakuwepo miongoni mwao. Wanaume watatu kati ya wale niliwakumbuka kuwa walikuwa ni wale maafisa usalama walionitembelea siku ya jana. Wanaume wanne waliosalia walikuwa ni wanajeshi makomandoo ambao niliwatambua haraka kufuatia sare zao za kijeshi. Walikuwa wanaume vipande wenye sura za kazi wanaonuka ubabe, yaani watu wanaofurahia vita kuliko amani.
Watu wale walipoingia mle ndani hawakunisemesha kitu badala yake wakanizunguka haraka pale kitandani kisha mmoja wao akaanza kunifungua zile pingu miguuni na mkononi. Wakati zoezi lile likiendelea mara nikamuona komandoo mmoja akichomoa sindano za dripu katika mishipa yangu mkononi pasipo kuzingatia utaalam wa kidaktari na hivyo kunisababishia maumivu makali hata hivyo yule mtu hakuonekana kujali. Yule mwenzake alipomaliza kunifungua pingu makomandoo wawili wakanishika miguu yangu na kunishusha kwa nguvu pale kitandani. Nilipoangua chini wakaanza kuniburuta kibabe kuelekea nje ya kile chumba na wale maafisa wakawa wakifuatia kwa nyuma…
Tulipotoka nje ya kile chumba tukashika uelekeo wa upande wa kulia huku nikiburutwa chini kwa mkono hata hivyo eneo lile lilikuwa na tope jingi ardhini hivyo sikuumia sana mikononi. Baada ya umbali wa kama hatua kumi tukaingia upande wa kushoto tukiifuata korido nyingine yenye majimaji. Nilipogeuka kutazama nyuma sikuweza kuona chochote kwa vile mle ndani kulikuwa na giza zito na kama si mwanga wa kurunzi iliyokuwa mkononi mwa komandoo mmoja nisingeweza kuona kule tuendako. Lilikuwa ni jumba lisiloeleweka pengine lililotelekezwa kwa miaka mingi na kila sehemu mle ndani kulikuwa na unyevunyevu sana. Ni kama lile jumba lilikuwa kwenye chemichemi isiyokauka. Wakati wote safari ile ikiendelea mimi nilikuwa makini kuyachunguza mandhari yale.
Tulishuka ngazi kwenye korido ile na tulipofika chini tukaingia upande wa kulia tena nyuma yetu tukiiacha korido nyingine inayopotelea gizani. Safari yetu ikaendelea hadi tulipofika sehemu yenye mlango mfupi wa chuma upande wa kushoto. Tulipofika eneo lile tukasimama na hapo yule komandoo akagonga pale mlangoni. Haukupita muda mrefu nikamuona mtu fulani akisogeza kidirisha kidogo na kuchungulia kisha akapotea na baada ya muda mfupi ule mlango ukafunguliwa na kuturuhusu kungia mle ndani. Wakati tukipita pale mlangoni nikachunguza na kuwaona askari jeshi wawili katika sare zao na bunduki zao mkononi. Tulipoingia mle ndani ule mlango ukafungwa nyuma yetu na hapo nikaendelea kuburutwa tukikatisha kwenye korido nyingine mbele yetu halafu baada ya mwendo mfupi tukaingia upande wa kushoto kuifuata korido nyingine ambayo ilikuwa fupi ukilinganisha na zile nyingine. Mbele yetu kulikuwa na mlango mwingine na chuma, tulipofika pale mlangoni dirisha dogo la mlango ule likasogezwa kando kisha mtu fulani akachungulia alipotuona akafunga lile dirisha na kufungua ule mlango.
Safari yetu ikaishia mle ndani ya kile chumba, wale watu wakaniburuta hadi katikati ya kile chumba huku ule mlango wa chumba ukifungwa nyuma yangu. Sikuweza kuona chochote mle ndani kwa vile kulikuwa na giza nene lakini baada ya muda mfupi taa za mle ndani ziliwashwa na hapo nikapata kuyaona vizuri mandhari yale. Mara moja nilipoyatembeza macho yangu kuchunguza mle ndani nikagundua kuwa kilikuwa ni kile chumba cha mateso nilichofikishwa siku ile kuhojiwa na wale makomandoo wa jeshi la wananchi wa Burundi. Lakini wakati huu wale makamanda hawakuwepo wala vile viti na meza na badala yake kulikuwa kumeongezwa taa mbili zaidi ili kumulika mle ndani na mwanga wa taa zile ukanisaidia kuona mlango mwingine wa chuma uliokuwa nyuma ya kile chumba. Kuuona ule mlango kukanipelekea nilikumbuka lile jitu hatari nililopambana nalo siku ile baada ya wale makamanda wa jeshi kuondoka. Nikajiridhisha kuwa jitu lile lilikuwa limeingia mle ndani kwa siri kupitia ule mlango wa chuma ambao siku ile sikuwa nimeuona kutokana na mwanga hafifu wa taa moja iliyokuwa mle ndani.
Mandhari ya mle ndani wakati huu yalinitia hofu. Kulikuwa na beseni kubwa lililojaa maji lakini maji yale yalikuwa yamechanganyikana na damu nzito. Pembeni ya lile beseni kulikuwa na kitanda chembamba cha chuma chenye mikanda imara, ukutani nikaona nyororo fupi na pingu za miguuni na mikononi za chuma. Juu ya dari kulining’inizwa vyuma vifupi kama nondo za mm 12 zilizokunjwa na kuchongwa mbele yake kama vyuma vya kuning’inizia nyama buchani. Vyuma vile vilikuwa vimetapakaa damu ambayo sikuwa na shaka ilikuwa damu ya binadamu. Katikati ya kile chumba kulikuwa na bomba refu la chuma lililotoka upande mmoja wa kile chumba hadi upande wa pili ukutani. Nilifahamu vizuri nini maana ya lile bomba na vile vitu vyote mle ndani. Upande wa kulia wa kile chumba nikaona meza, juu ya ile meza nilipotupia macho nikaziona zile nyaraka zangu zote, pia kulikuwa na sinia dogo lenye kisu, waya mwembamba lakini imara, koleo, nyundo na misumali. Kando ya ile meza chini nikaona betri kubwa ya gari yenye umeme wa waltz 250 na vishikizo vyake. Sakafu ya kile chumba ilikuwa imetapakaa damu nzito na nilipochunguza chini nikaona kofia moja ya kiraia aina ya kapelo na kiatu kimoja cha mguu wa kushoto vilivyotelekezwa pale chini niliona alama za mburuto wa mtu kuelekea mlango wa nyuma wa kile chumba na hapo nikahisi kuwa kulikuwa na mtu aliyetoka kuteswa mle ndani muda mfupi kabla ya kupoteza maisha. Kulikuwa na vifaa vingine vya mateso ambavyo labda nisingeweza kuvielezea kwa kuwa havielezeki kwa mtu wa kawaida lakini niseme mandhari ya mle ndani yalitisha sana kama siyo kukatisha tamaa. Sasa mle ndani kulikuwa na jumla ya watu nane mimi nikiwa wa tisa, yaani wale makomandoo wanne, askari jeshi mmoja wa kawaida aliyetufungulia mlango, wale maafisa watatu wa usalama nchini Burundi na mimi.
Nikiwa pale chini nimeketi wale makomandoo wakanizunguka na hapo nikafungwa kamba miguuni na mikononi kisha nikabebwa na kutundikwa kichwa chini miguu juu. Nilimuona afisa usalama mmoja akinisogelea na kunichapa kofi usoni kisha akainama chini na kuanza kunihoji huku nimening’inizwa.
“Tuambie wenzako wako wapi na pesa ulizoiba umezificha wapi?”
“Wenzangu akina nani?”
“Wenzako unaoshirikiana nao kufanya mapinduzi ya kijeshi hapa Burundi”
“Sifahamu chochote kuhusu hayo mapinduzi ya kijeshi unayoyazungumzia”
“Umezificha wapi?”
“Kwa jinsi nilivyo na shida kama ningekuwa na hizo pesa mnazozituhumu nazo nadhani msingefanikiwa kuzipata”. Nikajitetea huku nikimeza funda kubwa la mate kuitowesha hasira kifuani mwangu.
“Luteni Tibba Ganza wa jeshi la wananchi wa Tanzania, nakushauri ulegeze msimamo wako na kuzungumza ukweli kisha uombe msamaha ili tukusamehe. Labda nikwambie hivi, watu wengi wanaoletwa chumba hiki huanza kwa kushikilia misimamo yao lakini tunapoanza kuwashughulikia huishia kuongea ukweli kila kitu huku wanalia na bahati mbaya sana huwa wanalia huku wakiwa na hali mbaya sana za kiafya. Sidhani kama unapenda tufike huko kote?”
“Hata mimi sipendi”. Nikajibu huku nikimtazama yule afisa usalama.
“Kama hupendi tufike huko basi tuambie wewe ni nani, uko hapa Burundi kufanya nini, wenzako wako wapi na pesa ulizoiba ziko wapi?”. Yule mtu akaanza kunishawishi kana kwamba mimi ni mtoto mdogo.
“Sasa nitakujibu kama ifuatavyo, mimi ni mtanzania, nimekuja hapa Burundi kutafuta fursa za uwekezaji kwenye soko la Afrika mashariki na sielewi kwa nini mmenileta hapa. Kuhusu hizo pesa hata mimi natamani kufahamu pesa hizo zilipo”
“Luteni, kama unadhani tumekuleta hapa ili kupoteza muda wetu basi subiri tukuoneshe”. Yule afisa usalama akanionya na kusimama kisha muda uleule nikaanza kushushiwa kipigo cha mateke ya kichwani na wale makomandoo. Kilikuwa kipigo hatari sana kuwahi kukutana nacho na baada ya dakika tano nilikuwa nimechakaa vibaya huku uso wangu wote umetapakaa damu huku nikihema hovyo.
“Mwacheni”. Nikamsikia yule afisa ukiwaambia wale wababe na hapo wakasitisha kipigo huku wakihema kama kuku wenye kiu ya maji.
“Haya tueleze”
“Naomba mnisamehe sitorudia tena”. Nikaongea huku nikigugumia kwa maumivu makali.
“Hutorudia kufanya nini?”
“Sitorudi kuingia nchini mwenu bila kuwasiliana kwanza na nyinyi?”
“Pumbavu…!”. Nikamsikia afisa usalama mmoja akitukana na hapo akawapiga ukope wale makomandoo na hapo kile kichapo kikaanza upya mara hii hali ilikuwa mbaya zaidi. Wale makomandoo wakaendelea kunikong’ota kwa buti zao za jeshi kichwani kiasi kwamba zile buti baada ya muda mfupi zikawa zimelowa damu.
“Tuambie Luteni vinginevyo hawa watu watakuua”. Nikasikia sauti ikininong’oneza sikioni kwa mbali ingawa nilikuwa na hakika ilikuwa sauti kubwa sana kwa vile tu masikio yangu yalikuwa taabani. Nilijaribu kufumbua mdomo ili niwasihi waniache lakini hilo halikuwezekana kwani mdomo wangu ulikuwa mzito sana kama niliyedungwa sindano ya ganzi kabla ya kung’olewa jino. Hali yangu ilikuwa mbaya sana, damu ilikuwa ikinitoka mdomoni na baadhi ya sehemu za kichwa changu zilikuwa zimechanika hovyo na kuvuja damu. Hata nilipofumbua macho yangu kuwatazama wale watu macho yangu yalikuwa yamevimba sana, nikawa naliona lile eneo ni kama linalozunguka angani na wale watu mle ndani ni kama viumbe visivyoeleweka. Kipigo bado kiliendelea na kwa vile nilikuwa nimefungwa kamba miguuni na mikononi nisingeweza kufanya lolote.
_____
Sikufahamu ni wakati gani kile kipigo kilisitishwa dhidi yangu kwa vile labda niseme fahamu zilinipotea kwa muda. Nilizinduka nikiwa nimelazwa juu ya kitanda cha chuma mle ndani nikiwa nimelala kifudifudi huku mikono na miguu yangu ikiwa imefungwa pingu. Yale majeraha ya visu mwilini yalikuwa yametoneshwa na hivyo zile bandeji kuanza kuanza kutengeneza madoa ya damu. Kabla sijashtuka vizuri nikamwagiwa ndoo mbili za maji baridi ambazo kwa hakika zilinipa uchangamfu mwilini, nilichoshukuru ni kuwa nilikuwa sijavuliwa suruali yangu wala viatu miguuni. Hata hivyo sikuelewa ni kwanini nilikuwa nimelazwa kifudifudi pale kitandani kiasi cha kunipelekea nianze kuhisi vibaya juu ya kufanyiwa yale mambo ya Mombasa kama waswahili wasemavyo.
Fahamu ziliponirudia vizuri hakuna aliyenisemesha badala yake nikawaona wale watu wakikisogelea kitanda changu na kukizunguka. Mmoja wa wale maafisa usalama akaja na kusimama mbele yangu kisha nikamuona akifungua mfuko wa shati lake na kutoa picha ndogo na kunionesha.
“Unamfahamu huyu kahaba?”. Swali lile likanipelekea niyatulize macho yangu kwa makini kuitazama ile picha na mara moja tu nilipoitupia macho ile picha akili yangu ikasimama huku baridi nyepesi ikisambaa mwilini. Ilikuwa ni picha ndogo inayotosha kuwekwa kwenye wallet inayomuonesha msichana mrembo ambaye hata kama ungeniamsha kutoka usingizini usikuwa wa manane nisingeshindwa kumkumbuka. Msichana yule alikuwa Amanda na mara hii picha yake iliamsha hisia mpya moyoni mwangu. Hii ilimaanisha kuwa Amanda hakuwa amekufa kama nilivyokuwa nimedhani hapo awali. Niliwaza.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hapana, simfahamu”. Nikajibu huku nikitikisa kichwa kukataa.
“Una hakika?”
“Ndiyo”. Nikajibu kwa kujiamini swali lile la kijinga.
“Picha hii imeokotwa mahali mlipopata ajali ya kugongana na lori la jeshi wewe na wenzako. Tuna amini kuwa mwanamke huyu alikuwa na wewe”
“Simjui”. Nikamjibu yule afisa usalama kwa mkato kiasi cha kumpelekea airudishe ile picha mfukoni mwake.
“Naona umejitolea kufa peke yako huku wenzako wakiendelea kustarehe mafichoni kwa pesa nyingi mlizoiba. Sijawahi kumuona mtu mjinga duniani kama wewe. Itakufaa nini ufe peke yako wakato wenzako wanaendelea na maisha yao vizuri?. Au unadhani utaandikwa kwenye vitabu vya mashujaa wa nchi hii ?. Unadhani famlia yako itakusifia kwa upuuzi huu?”
“Nimesema sifahamu chochote kuhusu huyo mwanamke”. Nikamkata kauli yule afisa usalama na nilichokiona haraka usoni mwake ilikuwa sura ya kinyama ambayo sikuwahi kuiona kwa binadamu yoyote hapa duniani. Nikamuona yule afisa usalama akiwaonesha ishara fulani wale makomandoo na hapo kilichofuatia nilitamani ardhi ipasuke ili niangukie ndani na kupotelea humo. Nilimuona komandoo mmoja akielekea kwenye ile meza ndogo na kufungua droo, aliporudi pale tulipokuwa mkononi alikuwa ameshika mkia wa taa. Ilikuwa ni silaha mbaya sana ya kuchapia binadamu ambayo pindi unapochapwa nao magamba yake makavu huchuna ngozi na kuacha vidonda vibaya vinavyochukiza kutazama, maumivu yake nayo hayaambiliki. Nikafumba macho na kumeza funda kubwa la mate wakati nilipoanza kuchapwa mgongoni na mkia ule. Loh! maumivu yake yalikuwa makali mno huku nikipiga mayowe kama mtoto mdogo. Hata hivyo kipigo kile hakikukoma.
Nilikuwa nimechapwa mara nyingi tena kwa mfululizo bila kituo, hali yangu ilikuwa mbaya sana, mgongo wangu ulikuwa umechunika vibaya kama mnyama aliyeraruriwa na kucha za chui. Majeraha yangu yalikuwa yakivuja damu kiasi kwamba hata ule mkia wa taa ulikuwa chapachapa umelowa damu. Nilikuwa hoi nikihema hovyo kiasi cha kujionea huruma mwenyewe.
“Ongea ukweli Luteni vinginevyo hatuoni sababu ya kukuacha hai huku ukinywa uji wetu wa bure humu ndani. Au unadhani hii ni shule ya chekechea?”. Yule afisa usalama akanishawishi hata hivyo sikumjibu kitu kwani hali yangu ilikuwa mbaya sana.
“Naona bado hataki kutueleza. Endeleeni na kazi”. Nikamsikia yule afisa usalama akiwaambia wale makomandoo na hapo kipigo cha ule mkia wa taa mgongoni kikaendelea huku wale makomandoo wakipokezana, alipochoka mmoja akampa mwenzake alimradi wasinipumzishe. Kwa kweli nilipiga mayowe kiasi cha koo langu kuelekea kukauka lakini hakuna aliyeonekana kujali na wakati ule mkia wa taa ukitua na kuondoshwa mgongoni vipande vya nyama za mgongo wangu vikawa vikianguka eneo lile. Moyo wangu ulikuwa ukienda mbio isivyokawaida, maumivu ya mgongoni sasa yalikuwa yamefikia ukomo, macho yangu yalikuwa mbioni kupoteza muono wake. Mwili wangu wote sasa ulikuwa ukitetemeka kama mlevi sugu wa pombe kali. Sikupiga makelele tena kuomba msaada badala yake nikabaki kimya nikitazama mbele tayari kukabilina na kifo.
“Mwacheni huwenda yupo tayari kutueleza sasa”. Afisa usalama mmoja ambaye alionekana mkimya hapo awali akaingilia na hivyo kupelekea kipigo kile kusitishwa huku wale makamandoo wakihema hovyo.
“Haya tuambie Luteni juu ya maswali yetu tuliyokuuliza”
Nilitamani kuongea lakini sauti haikutoka hivyo nikabaki nimetulia. Wale maafisa usalama walipoona sizungumzi chochote mmoja akaniuliza.
“Luteni, unafahamu kuwa kushiriki kitendo chochote mapinduzi ya serikali halali iliyoko madarakani ya nchi yoyote duniani ni uhaini na malipo yake ni kifo?”
“Nafahamu”. Nikaongea kwa tabu huku mdomo wangu ukichezacheza kwa hofu.
“Wanataka kukuua lakini mimi nimewashawishi wenzangu tusifanye hivyo kwa kuwa wewe si mtu mkaidi sana kama wenzako waliowahi kuletwa hapa”
“Basi naomba mniache niende zangu na mimi sitowashtaki popote”. Nikaongea kwa sauti dhaifu.
“Unadhani hatukufahamu kuwa wewe ni nani?”. Yule afisa usalama akaniuliza kisha nikamuona akimpiga ukope yule askari mmoja komandoo na hapo nikamuona yule askari akiondoka eneo lile kuelekea kwenye mlango wa chuma wa kile chumba. Alipofika pale mlangoni akagonga mara mbili na baada ya kitambo kifupi ule mlango wa chuma ukafunguliwa kisha akaletwa mtu mmoja mbele yangu ambaye ilinichukua muda mrefu kumfahamu. Baada ya kutuliza vizuri mawazo yangu nikamkumbuka vizuri yule mtu. Alikuwa ni yule askari mwenye cheo cha Koplo aliyejitambulisha kwangu kwa jina la Anatole Nkunda, miongoni mwa wale wanajeshi waliotumika na Amanda kuniteka siku ile ya kwanza nilipozinduka na kujikuta kwenye lile jumba na Amanda. Mtu yule alikuwa amechakaa vibaya kwa mateso makali kiasi cha kutamani kurudia kumtazama. Masikio yake yalikuwa yamekatwa, sehemu ya juu ya mdomo wake ilikuwa imekatwa na hivyo kuyapelekea meno yake yaonekane bila kificho kama ya mbuzi anayetafuna nyasi, jicho lake moja lilikuwa limepasuliwa na mikono yake ilikuwa imevimba mno huku kila sehemu ikionekana kuwa na alama za kitu chenye ncha kali.
“Unamfahamu huyo mtu aliyeko mbele yako?”. Yule afisa usalama akaniuliza kwa udadisi.
“Simfahamu”. Nikajibu kwa hakika hata hivyo jibu langu halikunisaidia kitu kwani swali lile lilipoelekezwa kwa yule mtu dhidi yangu majibu yalikuwa tofauti.
“Sajenti Anatole…”. Yule afisa usalama akaita kwa sauti ya amri.
“Ndiyo afande”
“Unamfahamu huyo mtu aliyelala hapo kitandani mbele yako?”
“Ndiyo namfahamu”
“Eleza unamfahamu kama nani?”. Yule afisa usalama akauliza kwa hasira.
“Namfahamu kwa jina la Tibba Ganza kama afisa wa jeshi la ulinzi la Tanzania mwenye cheo cha Luteni”
“Endelea kueleza vinginevyo utakiona cha mtema kuni wewe!”. Yule afisa usalama akafoka kiasi cha kumpelekea yule mtu mbele yangu aanze kutetemeka na kulia kama mtoto mdogo na hivyo kuipelekea sura yake izidi kutisha kumtazama.
“Mtu aliyeko mbele yangu kama nilivyotangulia kumtambulisha jina lake kwenu hapo awali na yeye pia ni mshirika mwenzetu katika mapinduzi ya kijeshi hapa Burundi. Yeye ni mwenzetu na alifika hapa kutusaidia taaluma yake katika kuipindua serikali kwa malipo ya fedha nyingi tu ambazo nusu yake ameshalipwa”
Loh! maelezo ya yule mtu mbele yangu yakasababisha tumbo langu kusokota kama niliyevamiwa na maradhi mabaya ya chango. Yaani ni kama aliyepigilia msumari wa mwisho katika jeneza langu tayari kwa safari ya maziko. Nilikuwa nimesingiziwa vibaya kiasi kwamba sikufahamu haraka nijitetee vipi na badala yake nikabaki mdomo wazi koo likinikauka. Hata hivyo niliona kuwa kukaa kimya na kuuruhusu uongo ule uaminike isingefaa.
“Muongo mkubwa huyu msimuamini maneno yake hata kidogo”. Nikaongea kwa kujiamini.
“Kama unadhani kuwa yeye ni muongo kwanini usijiulize kuwa tumelifahamu vipi jina lako la Tibba Ganza kama siyo yeye aliyetuambia?”. Yule afisa akaniuliza huku akinitazama kwa udadisi.
“Mimi siitwi Tibba Ganza. Nimekwisha waambia huyu mtu anawadanganya bure ili kujitetea mumuone ni mtu mwema. Muulizeni kila kitu yeye ndiye atakuwa anafahamu kuhusu hayo mapinduzi mnayonituhumu nayo”. Nikaendelea kujitetea lakini pigo moja la mkia wa taa mgongoni likaamsha yale maumivu makali hivyo nikasitisha utetezi wangu ambao hata hivyo hapakuwa na matumaini kuwa ungefaa.
“Yote ninayayosema ni ya kweli afande”. Yule mtu akasisitiza na kuniacha na mshangao usiolezeka. Muda uleule nikamuona yule afisa usalama mwenye roho mbaya kushindwa binadamu wote duniani akisogea mbele yangu kwenye kile kitanda nilicholazwa na kufungwa huku tabasamu la kinyama likichanua usoni mwake na hapo nikahisi jambo baya la hatari lilikuwa mbioni kutokea. Yule afisa usalama alipofika mbele yangu akanitazama kinyama kisha akasogeza koti lake la suti kiunoni na kuchomoa bastola yake kisha taratibu akaielekezea kichwani kwangu…
Sikuwa na shaka yoyote kuwa mwisho wangu ulikuwa umewadia na hapo nikaanza kulaani vibaya nafsi yangu huku nikijuta kuitikia wito wa kuja pale Burundi. Kamwe sikuogopa kufa lakini pia sikupenda mwisho wangu uwe laini kiasi namna ile bila kumuacha adui akiwa kilema asiyefaa kwa lolote hapa dunia. Sikuwahi kamwe kufikiria kuwa safari yangu ya kijasusi ingeishia pale tena katika nchi jirani kabisa na nchi yangu Tanzania. Mawazo mengi yakapita haraka kichwani mwangu na kunifanya nijione kuwa ni kijana nisiye na bahati. Mipango yote ya maisha ikatoweka. Nikapitisha sara fupi ya kimyakimya kumuomba Mungu anisamehe dhambi zangu zote nilizozifanya hapa duniani kisha nikameza funda kubwa la mate na kufumba macho.
Muda uleule mara nikasikia sauti mbaya ya mfyatuko wa risasi usiokuwa na kiwambo maalum cha kuzuia sauti lakini kitendo cha kusikia sauti ile kikanipelekea niamini kuwa bado nilikuwa hai hivyo kwa hofu nikafumbua macho yangu taratibu kutazama mbele. Kichwa cha yule mtu aliyekuwa amesimama mbele yangu kilikuwa kimefumuliwa vibaya kwa risasi, ubongo wake ulikuwa umetawanyika hovyo kwenye tope sakafuni. Tayari roho yake ilikuwa imetoweka mle ndani huku kiwiliwili chake kikiendelea kupapatika kama bata aliyepigwa na jiwe kichwani. Hatimaye kile kiwiliwili chake kikatulia bila dalili za uhai ndani yake. Moyo wangu ulikuwa ukienda mbio isivyo kawaida huku macho yangu yakikataa kuamini kile kilichotokea mbele yangu. Sasa nilifahamu dhahiri kuwa kifo cha binadamu kilikuwa ni kitu rahisi kuliko vitu vyote mle ndani. Loh! kihoro kilinishika kwa hofu huku nikianza kufikiri kuwa ningekufa kifo cha namna gani pale ambapo zamu yangu ingefika.
Wakati mawazo mengi yakipita kichwani mwangu mara nikamuona yule afisa usalama akilisogeza koti lake la suti pembeni kiunoni na kuipachika bastola yake kwenye kasha maalum huku tabasamu la kinyama likikataa kwenda likizo haraka usoni mwake na wakati yule afisa usalama akiipachika bastola yake kiunoni macho yangu yakaona kitu kilichoongeza ziada nyingine katika ufahamu wangu. Nilikiona kitambulisho cha kazi cha yule afisa usalama kikiwa kimening’inizwa kifuani pake kwa utepe wa rangi nyeupe ulioiuzunguka shingo yake.
Jina lake aliitwa Etienne Hakizimana, kamanda wa jeshi na afisa wa ngazi ya juu katika idara ya usalama wa taifa ya Burundi iitwayo Service National de Renseignment-SNR. Afisa yule alikuwa akiishi katika nyumba namba 11 eneo la Musaga jijini Bujumbura.
Kupitia maelezo ya kwenye kile kitambulisho kifuani kwa yule afisa usalama sasa nilianza kupata picha juu ya mambo yalivyokuwa. Niliifahamu vizuri idara ya usalama wa taifa ya Burundi kwa vile ilikuwa ni sehemu ya kazi yangu kufahamu idara za kijasusi za mataifa mengi hususani ya nchi za Afrika. Hata hivyo kabla sijakuja Burundi huko siku za nyuma niliwahi kusoma ripoti moja iliyotolewa na shirika za haki za binadamu duniani la Human Right Watch ikielezea juu ya idara ya usalama wa taifa ya SNR jinsi ilivyokuwa ikishutumiwa na vyama vya siasa vya upinzani kwa kuwakamata viongozi wake mara kwa mara, kuwatesa na baadhi yao kuuwawa kwa kisingizio kuwa walikuwa wakihusika na njama za kuipindua serikali.
Niliendelea kuikumbuka vizuri ripoti ile ambayo nilikuwa nimepata wasaha mzuri wa kuipitia siku moja nilipokuwa katika likizo yangu ya kikazi jijini Dar es Salaam. Ripoti ile ilikuwa ikieleza kuwa idara ya usalama wa taifa ya nchini Burundi-SNR, ilituhumiwa pia kushirikiana kwa siri na kikundi cha Imbonerakure. Kwa mujibu wa maelezo ya kwenye ile ripoti ni kuwa Imbonerakure ni kukundi cha vijana chipukizi wa chama tawala kilichopo madarakani nchini Burundi cha CNDD-FDD. Kikundi hicho kikiondokea kuogopwa sana kutokana na kushutumiwa vikali kwa kuhusika na vitendo vingi vya ukiukwaji wa haki za binadamu kama ukamataji na utesaji wa watu wanaosadikika kuikosoa serikali iliyoko madarakani. Maana halisi ya Imbonerakure ikifahamika kama ‘Watu wanaoona mbali’.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kupitia ripoti ile nikakumbuka vizuri kuwa kulikuwa pia na tuhuma nyingine dhidi ya idara ya ujasusi ya Burundi-SNR kuwa ilikuwa na sehemu maalum za siri kwa ajili ya kuwafanyia mahojiano washukiwa tishio kwa serikali sambamba na mateso makali. Nikakukumbuka kuwa sehemu hizo za siri zilikuwa zikifahamika kwa jina la kifaransa kama La Documentation kama ripoti ile ilivyoeleza. Hivyo kwa namna nyingine mateso na kifo zilikuwa miongoni mwa sifa za La Documentation.
“Luteni…”. Yule afisa usalama akaniita kwa utulivu kana kwamba nilikuwa rafiki yake wa siku nyingi hata hivyo sikumuitikia badala yake nikabaki nikimtazama. Pamoja na yote hata hivyo suala lile halikuonekana kumkera, hivyo akaendelea.
“Nilitaka kukuonesha kuwa wewe ni wa thamani sana kwetu ndiyo maana risasi yangu imekukwepa”. Yule afisa akaongea huku akitabasamu kinyama halafu ghafla sote tukakatishwa na kelele za funguo zikitekenya kufuli za ule mlango wa chuma wa kuingilia mle ndani na hapo sote tukageuka kuutazama ule mlango. Muda mfupi ulifuata ule mlango ukafunguliwa na hapo wakaingia vijana wawili waliova kiraia. Ujio wa wale vijana ukaashiria kuwa kulikuwa na jambo fulani la muhimu kwa vile walivyokuwa na haraka. Hata hivyo wale vijana walionekana kufahamiana vizuri na wale maafisa usalama wa SNR mle ndani. Nikawasikia wakisalimiana kwa lugha ya Kirundi na wale maafisa usalama na katika maongezi yao nikawasikia wakijitambulisha kwa lugha ya kifaransa kuwa walikuwa wametumwa na uongozi wa Imbonerakure. Kisha kwa pamoja wakanisogelea pale kitandani.
“Jina lake anaitwa Tibba Ganza, umri wake ni miaka ishirini na nane, ni Luteni wa jeshi la ulinzi la wananchi wa Tanzania. Taarifa zinaeleza kuwa ni komandoo, shushushu na jasusi wa kuogopwa. Amepata mafunzo ya kijasusi kwa nyakati tofauti katika nchi za Cuba, Israel, China na Marekani. Luteni Tibba Ganza pia amewahi kushiriki na kusaidia majeshi ya umoja wa nchi za Afrika katika kukikomboa kisiwa cha Nzuwani kutoka mikononi mwa majeshi ya Muhamad Bakari katika kisiwa cha Comoros. Akiwa katika batalioni ya jeshi la ulinzi wa wananchi Tanzania ameshiriki pia katika mpango wa kulinda amani nchini D.R Congo (Monusco) na nchini Lebanon (Unifil) chini ya mwamvuli wa Umoja wa Mataifa (UN). Kumekuwa na taarifa pia kuwa amekuwa akifanya safari kadhaa nje na ndani ya bara la Afrika katika nchi tofauti kama sehemu yake ya kazi za ujasusi”. Yule kijana wa Imbonerakure akaweka kituo kidogo na kuendelea baada ya kusafisha koo lake kwa kukohoa.
“Hivyo hatuna mashaka yoyote kuwa yupo hapa Burundi kusaidia mampinduzi ya kijeshi”. Taarifa zile zikapelekea kitambo kifupi cha ukimya kifuatie mle ndani huku watu wote mle ndani wakinitazama kwa mashaka kama bomu la nyuklia lililobakiza sekunde chache kulipuka. Ukweli niseme kuwa hata mimi taarifa zile zilikuwa zimenishtua sana na kunikatisha tamaa. Kwanza zilikuwa ni taarifa zenye ukweli mtupu ingawa bado kulikuwa kuna mambo mengi wasiyoyafahamu kuhusu mimi. Lakini vilevile nilikuwa nimeshangazwa sana na namna wasifu wangu ulivyofahamika na watu wale pamoja na kutumia mbinu zangu zote za kuuficha uhalisia wangu. Hii ilimaanisha kuwa kulikuwa na mtu aidha kutoka ofisi yetu ya ujasusi Dar es Salaam au shushushu wa SNR au Imbonerakure jijini Dar es Salaam aliyekuwa akinifuatilia na kuzifahamu vyema habari zangu. Nikaanza kujiuliza maswali chungu mzima kuwa mtu huyo ni nani na ni kwa wakati gani alipokuwa akinichunguza?. Majibu sikupata hata hivyo sikuacha kushikilia msimamo wangu.
“Mimi siye huyo Tibba Ganza mnayemzungumzia”. Nikaendelea kujitetea na kabla sijamaliza yule afisa usalama akanizaba kofi la uso na kunisababishia maumivu makali. Kwa namna moja au nyingine nikaanza kuhisi kuwa Imbonerakure na SNR ndiyo wangekuwa wamehusika katika kumteka balozi Adam Mwambapa kwa sababu wanazozijua wenyewe. Hata hivyo nilianza kukata tamaa juu ya hisia zangu kwani hadi kufikia pale maelezo ya wale watu hayakuwa walau yamegusia hata kwa mbali juu ya balozi Adam Mwambapa na hivyo kunifanya nianze kuamini kuwa balozi hakuwa mle ndani.
“Wakuu wanahitaji mtu huyu atapishwe taarifa zote muhimu anazozifahamu kwa namna yoyote ile kama mkakati wetu wa kuhakikisha kuwa tunalidhibiti vyema jaribio hili la mapinduzi ya kijeshi hapa Burundi”. Nikamsikia kijana mmoja kati ya wale vijana wawili walioingia mle ndani akiwaambia wale maafisa wa SNR na hapo tumbo likazidi kunivuruga.
“Tukiendelea zaidi ya hapa kwa sasa huwenda akapoteza maisha”. Yule afisa usalama mwenye roho mbaya akatoa maoni.
“Roho ni ya kwake mwili ni wetu hivyo kifo siyo hoja kubwa hapa. Tunachohitaji ni taarifa zote muhimu za kuzifanyia kazi haraka kabla ya hii nchi haijaangukia mikononi mwa washenzi”
“Okay! tutajua namna ya kufanya”. Yule afisa usalama mwenye roho mbaya akadakia huku akionekana kutafakari jambo.
“Ni lazima mfanye kazi yenu haraka kwani endapo idara ya ujasusi ya Tanzania ikanusa na kugundua kuwa tunamshikilia mtu wao humu ndani tutakuwa tumechokoza moto”. Yule kijana wa Imbonerakure akaongea kwa msisitizo na hapo nikafurahishwa na hofu yake dhidi ya nchi yangu Tanzania. Nikajihisi furaha kuwa angalau Tanzania inafahamika vizuri kuwa siyo nchi ya kuchezea hususani pale linapokuja suala la ulinzi wa nchi yetu, watu wetu, rasilimali zetu na mipaka yetu. Haukupita muda mrefu wale vijana wa Imbonerakure wakaaga na kutoka mle ndani.
Mara wale vija walipotoka nje ndiyo nilipoingia kwenye mateso makali ambayo kamwe sitoyasahau katika maisaha yangu. Nilimuona yule afisa usalama mwenye roho mbaya pamoja na wale wenzake wakinisogelea pale kitandani.
“Sema ukweli Luteni vinginevyo utakufa kifo cha mateso makali”. Yule afisa usalama akaninong’oneza sikioni kisha akatoa mche mmoja wa sigara kutoka kwenye mfuko wa shati lake na kuitia mdomoni. Alipoiwasha akaanza kuivuta kwa utulivu.
“Tueleze vizuri Luteni. Upo hapa Burundi kufanya nini, wenzako wako wapi, pesa ulizoiba ziko wapi na silaha za kutekeleza mpango wenu wa haramu wa mapinduzi ya kijeshi mmezificha wapi?”. Yule afisa usalama wa SNR akaniuliza na kwa kweli alikuwa bingwa namba moja wa fitina kwa kunibambikizia hoja nzito kana kwamba alikuwa na hakika kuwa nilikuwa mhusika. Sikujibu maswali yale hata hivyo haikunisaidia kitu kwani nikiwa bado nimelala kifudifudi pale kitandani nikamuona yule afisa akiwapa ishara fulani wale makomandoo na hapo mmoja wao akaenda kwenye ile meza ndogo iliyokuwa mle ndani na kufungua droo moja. Aliporudi mkononi alikuwa ameshika mifuko mingi ya nailoni na chupa ya lita moja yenye kimiminika fulani ndani. Sikuweza kuelewa haraka nini kilichokuwa kikiendelea mle ndani hadi pale nilipomuona yule komandoo akiimiminia ile mifuko ya nailoni kile kimiminika ambacho harufu yake sasa ikanigutusha kuwa ilikuwa ni petroli. Yule afisa usalama mwenye roho mbaya akachukua ile mifuko ya nailoni na kuiwasha kwa kiberiti. Ile mifuko ya nailoni ikaanza kuungua taratibu hadi ilipoanza kudondosha ujiuji wake na hapo yule afisa akaihamishia ile mifuko ya nailoni mgongoni kwangu hivyo ule ujiuji ukawa ukiangukia kwenye vidonda vibichi vilivyotokana na kuchapwa vibaya na ule mkia wa taa.
Yalikuwa maumivu makali mno ambayo kwa hakika yaliniacha katika wakati mgumu karibu na kifo kwani ule ujiuji wa nailoni ulipoangukia kwenye majeraha yangu mgongoni uliendelea kuwaka taratibu na hivyo kuyachoma majeraha yangu mgongoni. Muda mfupi uliofuata mle ndani kukawa na harufu ya mnuko wa mchomo wa nyama mbichi ya mgongo wangu huku mahojiano yakiendelea. Nilijitahidi sana kujigeuza pale kitandani lakini kwa kuwa nilikuwa nimefungwa mikono na miguu sikufanikiwa kwa lolote zaidi ya kuambulia kipigo. Hata hivyo niliendelea kushikilia msimamo wangu kuwa mimi siyo Tibba Ganza na hivyo sielewi chochote kilichokuwa kikiendelea. Mateso yalipozidi sikuweza kuhimili tena maumivu yale. Nilianza kuona kizunguzungu kikali kisha sikuweza tena kuona mbele yangu. Nguvu zikanishia, macho yakaanza kufumba taratibu na baada ya pale sikufahamu kilichoendelea.
_____
Fahamu ziliponirudia nikafumbua macho yangu taratibu nikiyatembeza huku na kule na kwa kufanya vile nikagundua kuwa nilikuwa nimening’inizwa kwenye lile bomba la chuma la mle ndani huku nikiwa kichwa chini miguu juu huku na mikono na miguu yangu ikiwa imefungwa kwa kamba. Yale maumivu makali ya mgongoni yakarejea upya na kunipelekea nipige kelele za kuomba msaada. Mara nikawaona wale watu waliokuwa mle ndani wakinisogelea pale niliponing’inizwa na walipofika kwa vile nilikuwa nikisikia kiu sana nikawaomba wanipe maji ya kunywa. Ombi langu likawapelekea waangue kicheko na hivyo kunipelekea nijihisi kuwa huwenda nilikuwa sahihi na akili yangu haikuwa na hitilafu yoyote.
“Tafadhali naomba mnipe maji. Nasikia kiu sana”. Nikawaambia wale watu na mara hii nikamuona yule afisa usalama wa SNR mwenye roho mbaya akinisogelea karibu zaidi kisha nikamuona akishusha zipu ya suruali yake usawa wa kichwa changu na kuanza kunikojolea akinilazimisha kunywa ule mkojo wake kwa vile hawakuwa na maji mle ndani. Ingawa kitendo kile kiliniudhi sana na kunifedhehesha hata hivyo sikuweza kufanya lolote hadi lile kojo la yule afisa lilipofika kikomo huku nikiwa nimelowa kichwani chapachapa.
_____
Sikumbuki kuwa ilikuwa yapata saa ngapi wakati ule mlango wa chuma kuingia mle ndani ulipofunguliwa na kisha wale vijana wawili wa Imbonerakure kuingia mle ndani huku wakiwa wameongozana na kijana barobaro wa miaka ishirini na ushei aliyefungwa kamba miguni na mikononi akiburutwa kama mnyama anayepelekwa machinjioni. Ingawa nilikuwa taabani kufuatia mateso makali ya kunilazimisha nizungumze vitu nisivyovifahamu lakini roho yangu ilikuwa bado haijaucha mwili ingawa niseme kuwa nilikuwa nimechakaa vibaya na kulowa damu mwili mzima.
Baada ya kuona mateso yanaongezeka na kuzidi kuniathiri vibaya nilikuwa nimeamua kujifanya kuwa nimezidiwa kutokana na hali yangu kuzidi kuwa mbaya. Na ama kwa hakika uongo wangu ulikuwa umefanikiwa kuwashawishi wale maafisa usalama wa SNR kuniacha kwa muda huku nikiwa bado nimening’inizwa kwenye lile bomba kichwa chini miguu juu kama popo huku nikihema taratibu kama niliekuwa mbioni kumalizia safari yangu ya uhai hapa duniani.
Kijana aliyeletwa mle ndani alikuwa amenisikitisha kwa jambo moja. Nilipomtazama uzoefu wangu ukanieleza kuwa alikuwa mlaini sana kuweza kuhimili mikikimikiki ya mle ndani. Kijana yule aliponitupia macho na kuniona jinsi nilivyochakaa akaanza kuangua kilio cha hofu kama mtoto mdogo. Nilimuona akiburutwa hadi katikati ya kile chumba na kisha kubwagwa chini kibabe kabla ya kutandikwa teke la tumbo lililompelekea abweke kama mbwa aliyepigwa jiwe.
Kupitia maelezo ya wale vijana wa Imbonerakure kwa wale maafisa usalama wa SNR nikapata kulifahamu jina la yule kijana kuwa alikuwa akiitwa Floribert Ntakirutama, mwanafunzi wa chuo kikuu cha Bujumbura mwaka wa pili akisomea sayansi ya siasa. Maelezo ya wale vijana wa Imbonerakure yalieleza kuwa Floribert alikuwa kituhumiwa kuwa miongoni mwa wanafunzi vinara wachochezi wa maandamano chuoni hapo kuipinga serikali iliyoko madarakani nchini Burundi. Vilevile akituhumiwa kumiliki bunduki ya kivita kwa siri. Sikutaka kuamini mapema kuwa tuhuma zile zilikuwa za kweli lakini maadam ulikuwa umeletwa kwenye kesi ya ngedere na nyani ndiye hakimu basi ulipaswa kusahau kuhusu haki yako. Wale vijana wa Imbonerakure baada ya kumaliza kutia fitina zao kwa wale maafisa usalama mle ndani dhidi ya yule kijana aliyeletwa wakaaga haraka na kuondoka huku wakiwa wameacha vielelezo muhimu vya kumtia yule kijana hatiani.
Ingawa nilikuwa nimeteswa sana kiasi cha kupelekea mtu yeyote mgeni aogope kunitazama lakini nilijikuta nikimuonea huruma yule kijana. Wale maafisa wakamvua nguo yule kijana haraka na kibabe kwa kizichanana chana kisha wakambeba na kwenda kumlaza chali kwenye kile kitanda cha chuma nilichokuwa nimelazwa hapo awali huku akiendelea kulia na kuleta rabsha za hapa na pale ambazo hazikuelekea kusaidia chochote. Kisha yule afisa usalama mwenye roho mbaya nikamuona akienda kwenye lile sinia lililokuwa juu ya meza na kuchukua ule waya mwembamba na koleo. Aliporudi pale kitandani alipolazwa yule kijana akachukua ule waya na kuuzungushia kwenye uume wa yule kijana kisha taratibu akaanza kuukaza ule waya kwa kutumia ile koleo. Nilihisi yalikuwa maumivu makali sana.
Yule kijana akaanza kupiga kelele kama anayechinjwa kwa msumeno huku akilazimishwa kuwataja wenzake na kueleza mahali alipokuwa ameficha bunduki. Yule kijana alipokana kuhusika na tuhuma zile kibano kikaendelea maradufu na hivyo kelele zake kugeuka kero mle ndani. Wale maafisa walipoona zile kelele zinazidi mle ndani yule afisa mwenye roho mbaya akachukua kipande kimoja cha nguo za yule kijana kilichoraruriwa na kumsokomezea yule kijana mdomoni ili asiendelee kupiga kelele. Hivyo wakati wa mateso yule kijana akawa akisokomezewa kile kipande cha nguo mdomoni ili asipige kelele na walipoacha kumtesa wakawa wakiondoa kile kipande cha nguo mdomoni ili aweze kuzungumza.
Mateso makali yakaendelea mle ndani hata hivyo yule kijana aliendelea kushikilia msimamo wake kuwa alikuwa hafahamu chochote. Wale maafisa walipoona yule kijana haelekei kuzungumza chochote pamoja na kuwepo kwa vile vielelezo vichache alivyokutwa navyo wakaamua kumbadilishia mtindo wa mateso. Afisa mmoja akachukua koleo na kuanza kuzibana korodani za yule kijana taratibu huku akimlazimisha azungumze ukweli. Sikuwa na shaka yoyote kuwa yule kijana alikuwa katikati ya maumivu makali sana kwani niliwahi kukabiliana na mtindo ule wa utesaji huko nyuma katika harakati zangu. Yule kijana macho yakamwiva, mdomo ukaanza kumchezacheza, mishipa ya damu mwilini ikamtuna huku jasho jingi likimtoka mwilini. Roho iliniuma sana labda mateso yale yangekuwa yamehamishiwa kwangu walau ningejikaza kustahimili lakini siyo kwa kijana yule mdogo mwenye mwili laini usiofahamu shuruba zozote ngumu. Nilitamani nijinasue kutoka ile sehemu nilipofungwa ili niwashikishe adabu wale watesaji lakini hilo halikuwezekana kwani wale makomandoo wa jeshi la Burundi walionekana kuwa makini sana na nyendo zangu kuliko kiumbe chochote mle ndani. Sikuwahi kuwaona binadamu wenye roho mbaya kama wale na sikuwa na shaka yoyote kuwa hata shetani endapo angekuwa amejibanza sehemu fulani mle ndani angeshangazwa na unyama ule wa roho mbaya.
Wakati yule kijana akiendelea kuteswa na kulazimishwa azungumze ukweli juu ya tuhuma zilizokuwa zikimkabili mimi nilikuwa nimezama kwenye tafakuri nyingine. Mipango yangu kichwani ilishaanza kujikita kwenye kutoroka mle ndani haraka iwezekanvyo kabla ya kifo hakijanifikia. Kulikuwa na matumaini kidogo katika kutekeleza mkakati wangu wa kutoroka. Tumaini hilo lilitokana na bastola moja na magazini mbili niliyokuwa nimeificha katika upenyo mdogo wa baina ya jiwe na jiwe uliokuwa kwenye kona moja ya kile chumba ambayo nilikuwa nimeipata kutoka kwa lile jitu The ghost nililopambana nalo siku ile ya kwanza nilipoletwa kwenye kile chumba cha mateso.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Bastola ile ingeweza kunirahisishia kutoroka kwangu endapo kama nafasi hiyo ingejitokeza na siyo kwa mapambano ya ana kwa ana kwani kufikia wakati ule mwili wangu tayari ulikuwa dhaifu kwa kukosa lishe inayoeleweka na kwa mateso makali ya mle ndani. Hoja ikabaki ni kwa vipi ningeweza kuipata ile bastola ilhali nikiwa nimefungwa namna ile huku wale makomandoo wakinitazama kwa makini?. Sikuona upenyo huo hata hivyo chochote ambacho kingetokea ili kuifikia ile bastola ungehitajika muujiza mkubwa, muujiza ambao ili ukamilike ulitakiwa uzingatie muda. Muda lilikuwa ni suala muhimu sana katika kutoroka, ni muda ambao ndiyo ungeniruhusu kukamilisha mkakati wangu wa kutoroka lakini pia ni muda ambao ungeamua kuhitimisha safari yangu ya maisha ya hapa duniani nikiwa mle ndani.
Hali ya yule kijana mle ndani ilizidi kuwa mbaya kwani ukubwa wa mateso makali yaliyofanyika dhidi yake niseme haikwendana kabisa na uimara wa mwili wake. Hata hivyo jambo lililonishangaza ni kuwa yule kijana pamoja na mateso yote yale lakini aliendelea kushikilia msimamo wake. Wale maafisa walipomuona yule kijana haelekei kuzungumza chochote wakamfungua na kumuondoa kwenye kile kitandani cha chuma kisha wakaenda kumfunga ukutani kwa kutumia zile pingu za ukutani huku wakiwa wameitawanya miguu na mikono yake halafu wakamuondoa kile kitambaa mdomoni. Niliifahamu vyema namna ile ya utesaji hususani kwa muarifu yoyote muoga lakini kwa jasusi mzoefu kama mimi kamwe wasingefanikiwa kupata chochote kutoka kwangu.
Baada ya kile kitambaa kuondoshwa mdomoni mwake yule kijana alianza kuhema hovyo huku akilia na hapo nikamuona afisa mmoja kati ya wale maafisa usalama wa SRN akichomoa bastola kiunoni na kurudi nyuma hatua kadhaa kisha kwa shabaha makini akielekeza ile bastola kwa yule kijana. Kwa aina ile ya utesaji, mtesi angeonesha dhamira ya waziwazi ya kumlenga mtuhumiwa lakini angefyatua risasi kwa kulenga pembeni kidogo ya mtuhumiwa lengo likiwa ni kumtia hofu ya kifo mtuhumiwa ili azungumze ukweli na hicho ndiyo kilichotokea.
Yule afisa usalama wa SNR akaanza kufyatua risasi lakini akilenga kando kidogo ya kichwa cha yule kijana na hivyo kumpelekea yule kijana azidi kuchanganyikiwa huku akipiga mayowe kwa hofu. Hata hivyo bado yule kijana aliendelea kushikilia msimamo wake kuwa alikuwa hafahamu chochote dhidi ya zile tuhuma na ama kwa hakika nilishangazwa sana na msimamo ule. Hatimaye wakabidilishia mtindo wa mateso na hapo nyundo ya nusu kilo ikaanza kutumila katika kumponda viganja vyake. Loh! niseme kuwa ule ulikuwa unyama wa hali ya juu kuwahi kuushuhudia.
Yule kijana akaendelea kupondwa viganja vyake huku akilazimishwa kuongea, hakuongea badala yake aliendelea kupiga mayowe huku akiwasihi wale watu wamuache kwani alikuwa hafahamu chochote. Mayowe ya yule kijana yakahanikiza mle ndani na kutengeneza mwangwi mkubwa unaojiitikia mara tatu hadi nne na zaidi mle ndani hata hivyo wale watu hawakumuacha. Zoezi lile lilivyozidi kuchukua muda sauti ya yule kijana hatimaye ikaanza kufifia taratibu na hatimaye kukoma kabisa na hapo akagueza shingo yake na kuilazia kushoto huku akifumba macho na kukaa kimya.
Sasa mle ndani kukamezwa na ukimya wa mashetani. Nikashindwa kuelewa kama yule kijana alikuwa amekufa au amepoteza fahamu. Hata hivyo wale watu hawakuonekana kujali chochote ingawa zoezi lile lilikuwa limewapelekea waheme kwa pupa kama waliotoka kufukuzwa. Nikabaki nikimuonea huruma yule kijana huku nikikosa lolote la kufanya. Wasiwasi ukaanza kuniingia tena kwani nilifahamu fika kuwa mara baada ya kumalizana na yule kijana wale maafisa wa usalama wa SNR wangehamia tena kwangu na kwa vile mimi ndiye niliyekuwa mtuhumiwa hatari zaidi mle ndani.
_____
Nilizuga kupoteza fahamu lakini hilo halikufanikiwa kwani hila yangu iliondoshwa na uji mwepesi wa moto kwenye kikombe niliomwagiwa tumboni. Nikafumbua macho na kugugumia kwa maumvu makali ya mchomo wa ule uji na hapo yule afisa mwenye roho mbaya akanitemea mate usoni.
“Luteni wacha kulala au unadhani hii ni moja ya zile gesti zenu za kule Sinza Dar es Salaam”. Yule afisa usalama akaniambia huku akinipigapiga kichwani. Alikuwa akijidai kutaka nimfahamu kuwa alikuwa akilifahamu vizuri jiji la Dar es Salaam ingawa nilikuwa na hakika kuwa Sinza tu ndiyo sehemu aliyokuwa ameishika kichwani mwake wakati alipopata bahati ya kufika Dar es Salaam. Nikafumbua macho na kumtazama tu hata hivyo nikajionesha kuwa hali yangu ya kiafya ilikuwa mbaya sana ili nisiingizwe kwenye mpango mpya wa mateso.
“Ngoja tukuchangamshe kidogo”. Yule afisa usalama akaniambia baada ya kuona sizungumzi chochote. Muda uleule nikaanza kushushiwa kipigo na wale makomandoo wakinishambulia kutoka pande zote za dunia kama mpira wa kona. Kwa muda wa robo saa nikawa nimechakaa vibaya sijitambui huku yale majeraha yangu mwilini yakitoneshwa upya na hivyo kunisababishia maumivu makali sana.
“Tafadhali naomba mniache kwani hali yangu ni mbaya sana”. Nikalalamika kwa sauti dhaifu.
“Hatujali juu ya kufa kwako. Kama hutotueleza ukweli utakufa tu”. Mmoja wao akaongea. Kipigo kikaendelea na kwa kweli hali yangu ilizidi kuwa mbaya hata hivyo niliendelea kushikilia msimamo wangu. Kama ni kufa nilikuwa tayari kufa lakini kamwe nisingekiuka miiko ya kazi yangu kwa kuzungumza ukweli.
Wakati kipigo kile dhidi yangu kikiwa kinaendelea mara sote mle ndani tukashtushwa na kelele za funguo zikifungua kufuli za ule mlango wa chuma wa kuingilia mle ndani. Zoezi la kunishambulia likasitishwa kwa muda na wale watu huku wakisubiri kwa shauku ni nani ambaye angeingia mle ndani. Mlango ulipofunguliwa mara nikawaona wale vijana wawili wa Imbonerakure wakiingia mle ndani lakini safari walikuwa wameongozana na kamanda mmoja wa jeshi ambaye sikuwahi kumuona hapo awali. Kupitia sare za jeshi za yule afisa nikamtambua kuwa alikuwa na cheo cha Meja. Jitu refu na jeusi lenye mwili wa shibe ya kuaminika na mazoezi ya nguvu. Wale watu mle ndani wote wakamsalimu kijeshi yule afisa wa jeshi wakati alipokuwa akikaribia pale nilipokuwa nimetundikwa. Yule afisa wa jeshi na wale vijana wa Imbonerakure walipofika pale tulipokuwa wakasimama karibu yangu wakinitazama lakini yule afisa wa jeshi mwenye cheo cha Meja ndiye aliyekuwa akinitazama kwa udadisi zaidi. Kitambo kifupi cha ukimya kikapita mle ndani kabla ya yule afisa kukohoa kidogo akilisafisha koo lake na hatimaye kuvunja ukimya.
“Poleni na kazi wazalendo”
“Ahsante sana afande”. Wote wakaitikia na baada ya yule kamanda kuyatembeza macho yake mle ndani kumtazama kila mtu na kuyasaili vizuri yale mazingira macho yake hatimaye yakaweka kituo kwangu.
“Luteni, nimefurahi sana kusikia kuwa u mgeni wetu rasmi katika uhaini unaoendelea hapa nchini. Nchi yako imekuwa ikihubiri sana juu ya utawala wa haki na demokrasia lakini matendo yenu hayafanani hata kidogo. Nasikia umefika hapo kama mamluki uliyenunuliwa kwa pesa nyingi ili kusaidia kuung’oa madarakani utawala wa mhutu mwenzetu. Wewe ni zaidi ya muuaji na hustahili kuishi. Unataka sisi na familia zetu tukimbilie wapi na tule nini?. Kama mnapenda haki sana kwanini msisubiri sanduku la kura liamue nani mshindi?. Nakuhurumia sana Luteni kwani kifo chako kitakuwa fundisho tosha wale wanaopenda kuingilia mambo yasiyowahusu.
Ndugu zako uliofika kuwasaidia hadi wakati huu wameshindwa vibaya maeneo mengi nchini na taarifa tulizonazo ni kuwa wameshaanza kutoroka hapa nchini lakini hawatafanikiwa kwani vijana wetu wa SNR na Imbonerakure tayari wameishaizunguka mipaka yote ya nchi hii katika kuhakikisha kuwa hakuna hata mmoja anayefanikiwa kutoroka”. Yule kamanda akaweka kituo akikohoa kidogo na taarifa zile zikawapelekea wale watu mle ndani watabasamu kwa furaha. Yule afisa wa jeshi akaendelea.
“Leo ni siku yako ya mwisho ya kukaa humu ndani. Kesho utahamishwa na kupelekwa gereza la Muramvya ambapo utapata nafasi ya kuonana na maafisa wetu wanaokusubiri kwa hamu baada ya kuzisikia taarifa zako”. Yule kamanda akaweka kituo tena na kugeuka pembeni akiwatazama wale maafisa mle ndani.
“Hakuna haja ya kuendelea kumuhoji. Mwacheni apumzike ili apate muda wa kujiandaa na safari ya kesho”. Maneno ya yule kamanda yakapelekea faraja isiyoelezeka moyoni mwangu ingawa nilifahamu kuwa yangekuwa ni mapumziko ya muda mfupi lakini kwangu ilikuwa afadhali kubwa dhidi ya kile kipigo na nikiwa katikati ya furaha ile nikashtukia nikipigwa na kitu kizito nyuma kichwani halafu baada ya pale sikufahamu kilichoendelea.
_____
Nilizinduka baada ya kuhisi kitu fulani kilikuwa kikinipangusa taratibu mgongoni. Nilifumbua macho yangu na kuyatembeza huku na kule na kwa kufanya vile nikagundua kuwa nilikuwa nimerudishwa kwenye kile chumba kidogo mfano wa kaburi kisichokuwa na dirisha na chenye mlango mmoja mfupi wa chuma. Nilikuwa nimelazwa kifudifudi huku mikono na miguu yangu ikiwa imefungwa pingu kwenye kile kitanda kidogo cha chuma kinachomuenea mtu mmoja mwembamba kuweza kulala kwa shida kama ubao wa kupigia pasi nguo.
Kando yangu alikuwa ameketi yule daktari mfupi mbilikimo akinisafisha majeraha yangu kwa maji yaliyochanganywa na delto na kitambaa cheupe ambacho hadi sasa kilikuwa kimebadilika rangi na kuwa chekundu sambamba na maji yaliyokuwa kwenye ndoo ndogo iliyokuwa kando chini ya kile kitanda kutokana na damu nyingi iliyokuwa kwenye majeraha yangu. Maumivu ya mgongoni yalikuwa makali mno na kichwa nacho kilikuwa kikigonga. Yule daktari akanitazama kwa huruma kabla ya kuniambia.
“Pole sana”
“Ahsante”. Nikamuitikia huku nikijaribu kuvuta kumbukumbu juu ya matukio ya mara ya mwisho na hapo nikakumbuka kuwa nilikuwa nimepigwa na kitu kizito kichwani kabla ya fahamu zangu kunitoka.
“Imekuwa kama bahati kuwa bado upo hai. Nilidhani kuwa tusingeonana tena”. Yule daktari akaongea kwa sauti ya chini na kunipelekea nikumbuke kuwa nje ya mlango wa kile chumba kulikuwa na wale askari jeshi makomandoo waliomsindikiza yule daktari.
“Hata mimi nashindwa kuamini kabisa kuwa bado nipo hai. Labda huwenda Mungu ana makusudi na mimi”. Nikaongea kwa utulivu huku nikimtazama yule daktari kama rafiki mwema. Kimya kidogo kikapita mle ndani.
“Niliwasikia wakisema kuwa kesho watakuhamishia gereza la Muramvya”. Yule daktari akaniambia kwa sauti ya chini na ingawa nilikwishazisikia taarifa zile lakini nikajitia kushtuka kana kwamba zilikuwa taarifa mpya kabisa kwangu.
“Umesikia kwa nani?”. Nikamuuliza yule daktari wa mshangao.
“Nimesikia kwa dereva wa gari linalotumika kunileta humu ndani”
“Ulimsikia akisemaje?”
“Kuwa kesho utahamishwa na kupelekwa gereza la Muramvya kwa mahojiano zaidi”. Taarifa zile zikanipelekea nitulize vizuri mawazo yangu na kufikiri. Kwa kweli nilianza kuhisi kuwa kulikuwa na jambo la hatari zaidi huko kwenye gereza la Muramvya kwa vile lilivyoonekana kuwa ni jambo lenye kufurahiwa sana na yule afisa wa jeshi mwenye cheo cha Meja aliyefika kuniona siku ya jana.
“Gereza la Muramvya liko wapi?”
“Umbali wa kilometa themanini kaskazini mashariki ya hapa tulipo”. Yule daktari akaweka kituo kidogo akinitazama na hivyo kusimamisha kwa muda kazi yake ya kuyatibu majeraha yangu.
“Kwanini unadhani wanataka kunihamishia huko?”. Nikamuuliza.
“Wanahofia kuwa huwenda nchi yako ikatuma mashushushu kupeleleza sehemu ulipo. Hivyo wameonelea kuwa ukiwa kwenye gereza hilo siyo rahisi kufahamika”
“Oh! nashukuru sana kwa taarifa hizi”. Nikamshukuru yule daktari huku akili yangu ikizama kwenye tafakuri.
“Endelea kumuomba Mungu wako azidi kukuokoa kwani Muramvya siyo mahala salama. Hakuna aliyewahi kupelekwa huko nikakutanana naye tena barabarani”. Yule daktari akanisihi. Nikayatafakari kwa kina maneno yake na hatimaye kutikisa kichwa katika namna ya kuonesha kuwa nimemuelewa.
“Nina njaa sana”. Hatimaye nikavunja ukimya.
“Nimekuletea chakula”. Yule daktari akaniambia kisha akafungua kabati dogo la mle ndani na kutoa Hotpot ya chakula na alipoifungua ndani nikaona wali wa maharage. Hamu ya kula ikafufuka haraka nafsini mwangu. Kwa kuwa mikono yangu ilikuwa imefungwa yule daktari akaenda kumuita mmoja wa wale makomandoo nje ya mlango wa kile chumba aje anifungue pingu mikononi. Zoezi lile lilipokamilika nikaanza kula chini ya usimamizi wa mitutu ya bunduki za wale makomandoo. Chakula kilikuwa kitamu sana na nilishiba vizuri. Niseme kuwa tangu niletwe mle ndani sikuwahi kupewa chakula cha heshima kama kile. Hata hivyo wakati nikila akili yangu bado ilikuwa kazini na kwa hila nikalisukuma jagi la maji ya kunywa lililokuwa mezani na hivyo jagi lile likaanguka chini na maji yake yakamwagika. Wale makomandoo wakaonesha kukerwa sana na kitendo kile hata hivyo hawakunifanya kitu badala yake nilipomaliza kula nikalala tena kifudifudi pale kitandani na kufungwa pingu mikononi na kwenye kona za kile kitanda. Wale makomandoo waliokuwa wakinilinda wakatoka nje na kumsubiri yule daktari mlangoni ili aendelee na kazi yake.
“Nahitaji msaada wako tafadhali!”. Nikamwambia yule daktari wakati akimalizia kunitibu vidonda vyangu mgongoni.
“Msaada gani?”. Yule daktari akaniuliza huku akinikata jicho la mashaka.
“Nahitaji bastola”. Yule daktari akanitazama kama aliyesikia habari za msiba wa mama yake mzazi.
“Mimi sina bastola na sikushauri uwe na bastola humu ndani kwani hawa watu watakuua hata kabla hujafanya lolote”
“Mimi tayari ni mfu hivyo siogopi kufa”
“Pengine hujui unachozumza. Hawa watu ni zaidi ya wanyama”. Yule daktari akanionya huku akionekana kushangazwa na hoja yangu na hapo nikawahi kumvuta koti lake na kumkazia macho.
“Sina bastola na hata kama ningekuwa nayo nisingekupa. Hilo ni jambo la hatari sana na wakigundua watatuua sote”
“Naomba unisikilize. Nilimwaga yale maji kwenye jagi kwa makusudi”
“Kwanini?”. Yule daktari akaniuliza kwa mshangao baada ya kitambo kifupi cha kunishangaa kupita.
“Nilitaka upate sababu ya kutoka humu ndani na kwenda kunichukulia maji ya kunywa”
“Ili iweje?”. Yule daktari akanishangaza.
“Kwenye pembe moja ya kile chumba cha mateso nimeficha bastola yenye magazini mbili. Naihitaji tafadhali”. Hoja yangu ikampelekea yule daktari azidi kunishangaa hata hivyo maelezo yangu yalionekana kumuingia.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Unataka kutoroka?”
“Sina hakika lakini kama leo ndiyo utakuwa mwisho wangu wa kukaa humu ndani ni muhimu nikafikiria kujiokoa pia”. Nikaongea kwa sauti ya chini na hapo yule daktari akanitazama huku akiitafakari hoja yangu.
“Nitawezaje kwenda kule bila kusindikizwa na walinzi?”
“Hawawezi kukusindikiza na kuniacha mimi kwani mimi ndiye wanayenihofia zaidi”
“Nitaichukua vipi hiyo bastola na kukuletea humu ndani bila kuonekana?”
“Utaiweka kwenye soksi miguuni na hakuna atakayekushtukia. Unachotakiwa kufanya ni kujiamini tu”. Maelezo yangu yakampelekea yule daktari anitazame kwa mashaka huku akionesha kuelekea kuikataa hoja yangu.
“Tafadhali nahitaji msaada wako kama unapenda niendelee kuishi. Nakuomba unisaidie na nikifanikiwa kutoka humu ndani salama nitakupa pesa nyingi”. Nikazidi kumshawishi yule daktari na hapo sura yake ikaanza kuchangamka.
Wakati tukiendelea kuzungumza mara komandoo mmoja akachungulia mle ndani na kwa kuwa muda wote macho yangu yalikuwa pale mlangoni haraka nikaacha kuongea na muda uleule yule daktari akachukua lile jagi la maji na kuelekea nje ya kile chumba. Nilimsikia yule komandoo akimuuliza yule daktari kuwa alikuwa akielekea wapi na yule daktari akamjibu kuwa alikuwa akienda kuchukua maji. Bila shaka hawakumfuata kwani ule mlango wa kile chumba haukufungwa na hapo nikajikuta katikati ya sara ndefu ya kumuombea yule daktari afanikiwe mpango wetu.
_____
Wasiwasi ulianza kuniingia, japokuwa sikuwa na saa yangu ya mkononi lakini nilihisi kuwa muda wa nusu saa tayari ulikwisha yeyuka bila yule daktari kurudi mle ndani...
_____
Wasiwasi ulianza kuniingia, japokuwa sikuwa na saa yangu ya mkononi lakini nilihisi kuwa muda wa nusu saa tayari ulikwisha yeyuka bila yule daktari kurudi mle ndani. Sikuona sababu ya kuchelewa kwake kwa vile hapakuwa na umbali mrefu sana kutoka pale hadi kwenye kile chumba cha mateso. Taratibu hisia mbaya zikaanza kupenya akilini mwangu huku nikijiuliza ni vipi kama daktari yule angekuwa ameshtukiwa na kuonwa akiwa na ile bastola na wale walinzi wa mle ndani?. Kwa vyovyote angehojiwa na katika mahojiano hayo angenitaja na baada ya kunitaja yumkini huo ndiyo ungekuwa mwisho wetu sote mle ndani yaani mimi na yeye. Sasa nilianza kuhisi kuwa huwenda mawazo yangu yalikuwa sahihi na bila shaka yule daktari alikuwa amekamatwa pindi alipokuwa akiichukua ile bastola na kuchelewa kwake kurudi kulitokana na mahojiano baina yake na walinzi wa mle ndani.
Akili yangu ikiwa mbioni kupoteza utulivu nikaanza kufikiria namna ya kujinasua pale kitandani kabla ya wale makomandoo walinzi hawajanifikia. Ingawa mikono na miguu yangu ilikuwa imefungwa kwa pingu pale kitandani lakini kwamwe nisingekubali kufia pale kitandani kama panya aliyewambwa mtegoni. Mara moja nilipoyatupia macho yangu pale mlangoni sikumuona mtu yeyote na ule mlango bado ulikuwa wazi. Sikutaka kuamini kuwa wale walinzi walikuwa wameondoka pale mlangoni. Labda wangekuwa wamesimama kando wakimsubiri yule daktari. Wazo likanijia na hapo nikakohoa kidogo ili mmoja wao aje kuchungulia na nitakapomuona nimuite na kumsihi haja yangu kuwa nilikuwa nimebanwa na haja kubwa hivyo anifungue pingu ili niende msalani.
Nikiwa katika mkakati ule ghafla moyo wangu ukarejewa na tumaini kiasi cha kuzipelekea nywele zangu zinisimame kwa mshtuko. Nilimuona yule daktari akiingia mle ndani huku mkononi ameshika jagi lililojaa maji hata hivyo nilipomtazama usoni nikagundua kuwa hakuwa kwenye utulivu kama nilivyozoea kumuona. Jasho jepesi lilikuwa likimtoka kwenye paji usoni mwake, mikono yake mifupi ilikuwa ikitetemeka ingawaje alijitahidi kwa kila namna asionekane vile. Macho yake yalikuwa katikati ya hofu na ni kama aliyekuwa akijitahidi kumeza kitu fulani kooni mwake, kitu ambacho hata yeye mwenyewe huwenda hakukifahamu. Alipoingia mle ndani nyuma yake akaongozana na askari mmoja komandoo miongoni mwa wale walinzi waliokuwa pale mlangoni. Nikamuona yule daktari akinikata jicho lenye kunionya juu ya jambo fulani nisilolijua. Alipofika akaliweka lile jagi la maji juu ya lile kabati dogo la mle ndani kisha akafungua droo na kutoa vidonge vya kutuliza maumivu kutoka kwenye kopo fupi jeupe.
“Unahitajika kunywa hivi vidonge kwa ajili ya kutuliza maumivu”. Yule daktari akaniambia pasipo kunitazama usoni huku mkono wake mmoja ukimimina maji kwenye bilauli ya bati iliyokuwa pale mezani.
“Mikono yangu imefungwa”. Nikamwambia na hapo yule komandoo akasogea haraka na kunifungua pingu mikononi. Nikainuka na kuketi kisha nikageuka na kuvipokea vile vidonge na ile bilauli ya maji. Nilipovitupia vile vidonge mdomoni nikavisukuma kwa mafunda kadhaa ya maji ya kwenye ile bilauli huku akili yangu ikifanya kazi haraka na macho yangu yakizunguka huku na kule kutafuta upenyo wa kujikomboa mle ndani. Yule daktari mfupi ni kama alikuwa ameishtukia mapema dhamira yangu hivyo akanionya kwa kutikisa kichwa chake upande huu na ule kwa siri kuwa nisijaribu kufanya hila yangu. Nikampuuza lakini kitendo cha kugeuka na kuuona mtutu wa bunduki ya yule komandoo ukinitazama kwa uchu nikajikuta nikighaili hila yangu. Hivyo nilipomaliza kumeza vile vidonge na kunywa maji taratibu nikajilaza pale kitandani na kufungwa tena mikono yangu kwa pingu huku roho yangu ikisononeka kwa kukosekana kwa mazingira mazuri ya kutoroka kwangu. Nilimuona yule daktari akinitazama kama mtu afikiriaye jambo fulani na ukimya wake ukampelekea yule komandoo amuulize.
“Unasubiri kitu gani kingine daktari?”
“Nahitaji kumchoma mmgonjwa sindano ya kukausha vidonda vinginevyo itamchukua muda mrefu kupata nafuu”. Yule daktari kama aliyezinduka kutoka usingizini akaongea na kisha kugeuka akilifungua tena lile kabati dogo la mle ndani.
“Fanya haraka muda wa kuondoka umefika”. Yule komandoo akaongea baada ya kuitazama saa yake ya mkononi kisha nikamuona akiondoka taratibu eneo lile kuelekea nje.
“Umefanikiwa?”. Nikawahi kumuuliza yule daktari mara baada ya yule mlinzi komandoo kutoka nje ya kile chumba.
“Ndiyo”
“Bastola iko wapi?”. Nikamuuliza yule daktari wa shauku na hapo haraka akaivuta juu suruali yake na kuitoa ile bastola na zile magazini mbili kwenye soksi zake miguuni. Hofu ikiwa imefurika nafsini mwake akaniuliza haraka.
“Iweke katikati ya mapaja kwenye nguo yangu ya ndani”. Bila kuuliza mara mbili yule daktari akaniwekea ile bastola katikati ya mapaja yangu na kunifunika vizuri.
“Mbona umekawia sana kurudi?”. Nikamuuliza yule daktari hata hivyo hakunijibu badala yake akaniambia kwa sauti ya chini.
“Ratiba imebadilika utahamishwa jioni hii hii na siyo kesho kama ulivyokuwa umetaarifiwa hapo awali”
“Kumetokea nini na nani aliyekupasha habari hizo?”. Nikamuuliza yule daktari kwa shauku.
“Muda hauniruhusu kuzungumza hayo. Niambie tutaonana wapi?”. Yule daktari akarakisha kuuliza na hapo nikajua kuwa alitaka kupata uhakika juu ya pesa niliyomuahidi.
“Nje kuna walinzi wangapi?”. Nikamuuliza yule daktari huku moyoni nikianza kuona tumaini la kutoroka.
“Saa tano kamili usiku nitakuwa nimejibanza kwenye miti inayopakana na barabara ya Avenue de la Mission nikikusubiri”. Yule daktari akasisitiza huku akili yake ikionekana kuzama kwenye pesa.
“Kama nitafanikiwa kutoroka, muda wa nusu saa kama utapita bila kuniona basi futa machozi huku ukifahamu kuwa bahati haikuwa yangu”. Maelezo yangu yakampelekea yule daktari anitazame kama asiyetaka kusikia habari zile kisha akamalizia kunichoma sindano ya mwisho na kuvirudisha vifaa vyake vya tiba kwenye lile kabati. Yule komandoo akachungulia tena mle ndani na hapo nikatambua kwa nini yule daktari alikatiza maongezi kwa ghafla.
“Kila la kheri”. Hatimaye nikamsikia yule daktari akaninong’oneza sikioni kisha akauchukua mkoba wake mezani na kuelekea nje. Haukupita muda mrefu mlango wa kile chumba ukafungwa na hapo mle ndani kukamezwa na ukimya.
Nikiwa nimelala kifudifudi pale kitandani mawazo mengi yakaanza kupita kichwani mwangu. Kwa kweli nikijikuta nikimshukuru sana yule daktari kwa kufanikisha kupatikana kwa ile bastola ambayo sasa ilikuwa katikati ya mapaja yangu. Hata hivyo niliona kuwa kupatikana kwa ile bastola ilikuwa ni hatua moja tu katika safari yangu ya kutoroka. Vipi kama nimefanikiwa kuipata ile bastola halafu huko mbele nisipate mazingira ya kufanikiwa kuitumia hadi mwisho wa safari nitakapopelekwa?. Kwa namna nyingine kukutwa na ile bastola ingeweza kutafsirika kama kuwa nilikuwa katika harakati za kutoroka na isipokuwa mazingira ya kutoroka huko ndiyo yalikuwa hayajapatikana. Hilo lingekuwa jambo la hatari zaidi kuliko hata kifo chenyewe kwani kwa vyovyote ningehitajika kueleza ni kwa namna gani nimeipata ile bastola wakati hapo awali nilikuwa nimepekuliwa na kuchukuliwa vitu vyangu vyote. Kwa kweli sikuweza kufahamu haraka kuwa ni kwa namna gani ningeweza kuvumilia mateso mengine makali kabla ya kumtumbukiza yule daktari mfupi kwenye hoja ya ile bastola endapo ningepekuliwa tena na kukutwa nayo baada ya kushindwa kutekeleza mpango wangu wa kutoroka.
Sikuwa tayari kufikishwa kwenye gereza la Muramvya lakini vilevile sikuwa tayari kumuingiza yule daktari kwenye mkasa wa kifo baada ya kukutwa na ile bastola. Hivyo akili yangu ikanionya kuwa kutafuta namna yoyote ya kutoroka kabla sijafikishwa kwenye gereza la Muramvya na kukutwa na ile bastola. Hivyo hoja ya kutoroka ikaanza kuchipua kichwani mwangu. Swali likabaki ni kwa namna gani ningeweza kutoroka au kuitumia ile bastola huku mikono na miguu yangu ikiwa bado imefungwa kwa pingu?. Pingu zingeweza kuwa kikwazo kikubwa katika kufanikisha kutoroka kwangu hivyo akili yangu ikaanza kujikita katika kufikiria namna kushughulika na zile pingu mikononi na miguuni.
Nilikuwa nikifahamu aina nyingi za pingu na namna ya kuweza kuzifungua pasipo msaada wa funguo zake utadhani mimi ndiye nilitezitengeneza. Nilipozichunguza vizuri zile pingu nilizofungwa mikononi na miguuni nikagundua kuwa zilikuwa zikifanana kwa muundo. Pingu za namna ile ili kuzifungua ingehitajika kipande kidogo cha waya mwembamba na mgumu kiasi ambao ningeupenyeza kwenye tundu dogo la pingu zile na kuifyatua kabari yake kwa utaalam wa hali ya juu ambao siwezi kukuelezea. Halafu baada ya hapo ningekuwa huru kuendelea na mambo yangu.
Akili yangu ikiwa imeanza kuchangamka kwa makini nikaanza kukichunguza kile kitanda cha mateso nilicholazwa juu yake na kwa kufanya vile nikagundua kuwa kila pembe ya kitanda kile ilikuwa na nyaya nyembamba zilizoshika kutu kama zile zitumiwazo na mafundi ujenzi wakati wa kutengenezea nguzo za zege kwenye majengo. Zile nyaya zilikuwa zimezungushiwa kwenye miguu ya kile kitanda na hapo nikahisi huwenda zilikuwa zikitumika kwenye mateso. Mikono yangu ikiwa imefungwa kwa pingu nikajaribu kuupeleka mkono wangu mmoja kuufikia ule waya hata hivyo kulikuwa na umbali hivyo ilinigharimu kuulazimisha mkono wangu hadi kufikia hatua ya kuchunika vibaya kwenye kiganja changu hata hivyo hilo halikuniondoa kwenye dhamira yangu. Baada ya hangaika ya hapa na pale hatimaye nikaufikia ule waya na kuanza kuukata kwa kuupindapinda huku na kule.
_____
Nilishtushwa na kelele za funguo zikifungua kufuli za ule mlango kwa nje huku nikiwa naendelea na zoezi la kukata ule waya. Sasa niliamini maneno ya yule daktari kuwa ratiba ya kuhamishiwa gereza la Muramvya ilikuwa imebadilika na kuwa ningemishwa jioni ile na siyo siku ya kesho kama ilivyokuwa imepangwa. Ule mlango ulipofunguliwa mle ndani wakaingia wanajeshi nane warefu na imara wenye vimo vinavyoelekeana. Kofia zao nyekundu za bereti kichwani zikanijuza kuwa walikuwa ni askari jeshi makomandoo wa kuogopwa huku mikononi wakiwa wameshika bunduki. Sura zao zilikuwa ngeni kabisa machoni kwangu na hapo nikajua kuwa nilikuwa nimebadilishiwa ulinzi kwa kuwekewa watu makini zaidi na wenye uzoefu na misafala ya watuhumiwa kwenye barabara za halaiki ili endapo kukitokea kashikashi yoyote safarini waweze kunidhibiti vizuri.
Kabla ya wale wanajeshi hawajanifikia tayari nikiwa nimefanikiwa kukata kipande kidogo cha waya na kukitia mdomoni nikikibana chini ya ulimi. Wale makomandoo waliponifikia haraka wakaanza kunifungua zile pingu miguuni na mikononi na wakati wakifanya vile mmoja wao akashtuka baada ya kuuona ule mchubuko mbaya wa pingu mkononi nilioupata wakati nikiulazimisha mkono wangu kuufikia ule waya.
“Naona ulikuwa ukijaribu kutoroka”. Yule komandoo akaniuliza.
“Hapana”CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Usijaribu hata kufikiria kutoroka vinginevyo utajuta”
“Mnataka kunipeleka wapi?”. Nikawauliza wale makomandoo kwa hila huku nikipanga kuwatoa kwenye fikra za kutoroka kwangu.
“Tunakupeleka sehemu nzuri yenye hadhi yako na siyo kwenye shimo la panya kama hili”. Komandoo mmoja akanijibu hukua akipenyeza tabasamu la kinafiki usoni mwake.
“Kwa kweli nitashukuru sana maana hiki chumba hakifai kuishi binadamu”. Nikaongea kwa hila huku nikijidai bwege nisiyefahamu chochote.
Zile pingu zilipofunguliwa mikononi na miguuni nikashushwa chini ya kitanda kisha pingu mbili zikatumika kunifunga miguuni na mikononi na wakati nikishangazwa na uharaka wa matukio yale nikashtukia nikivalishwa mfuko mweusi kichwani. Muda si mrefu nikashtukia nikishikwa miguuni na kuanza kuburutwa kuelekea nje ya kile chumba hata hivyo nikashumkuru Mungu kuwa nilikuwa nikiburutwa huku nimelalia tumbo na mikono yangu kama ngao ya kuzuia mwili wangu usichunike sakavuni.
Safari ya kutoka mle ndani ikawa imeanza na kwa kweli sikuweza kufahamu vizuri jiografia ya mle ndani kwa vile kichwani nilikuwa nimevikwa ule mfuko mweusi. Tulipita kona nyingi zisizo na idadi. Kuna sehemu tulipofika nikahisi kuwa tulikuwa tukishuka chini zaidi, sehemu nyingine ni kama tulikuwa tukipanda juu na kila baada ya umbali fulani kulikuwa na mlango ambao ulipofunguliwa tuliweza kuendelea mbele na safari. Baadhi ya maeneo ya sakafu ya mle ndani yalikuwa na tope jingi linaloteleza vibaya, sehemu nyingine zilikuwa na unyevunyevu na majimaji na zipo sehemu zilizokuwa kavu kabisa. Yalikuwa mazingira ya ajabu ambayo kamwe nisingeweza kuulewa muonekano wake.
Mlango wa mwisho ilipofunguliwa ukatupelekea tutokezee kwenye eneo tulivu lenye hewa safi ya asili na hapo nikahisi kuwa tulikuwa tumetoka nje kabisa ya lile jengo lenye zile mahabusu za kifo. Wakati nikianza kufurahishwa na hewa ile safi ya asili duniani nikashtukia nikibebwa haraka na kwa wepesi wa hali ya juu na kutupiwa juu ya sehemu iliyonipelekea niamini kuwa kilikuwa ni chumba kidogo kilichopakana na ukuta wa nyaya ngumu pande zote ili kumtenganisha mtuhumiwa hatari na dereva wa lile gari kwa upande wa mbele na walinzi wa msafala kwa upande wa nyuma. Kama umewahi kuuona muundo wa magari yanayotumiwa kusafirishia watuhumiwa hatari duniani kama wahaini dhidi ya serikali, magaidi au watuhumiwa wa mauaji ya kimbari na wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya waliokamatwa na vyombo vya dola basi utakuwa wakwanza kunielewa.
Muda uleule nikasikia mlango wa kile chumba nilichutupiwa kwenye lile gari ukifungwa kwa nje kisha nikasikia vishindo vya watu wakipanda na kukaa kwenye sehemu ya nyuma ya lile gari ambao nilihisi kuwa walikuwa ni wale walinzi wa ule msafala na ule mlango ulipofungwa dereva akatia moto gari na hapo safari ikaanza. Nilipoyatega vizuri masikio yangu nikahisi kuwa kulikuwa na magari mengine mawili kwenye ule msafala yenye askari waliotayari muda wote kwa ajili ya kuboreshwa ulinzi wangu. Gari moja lilikuwa nyuma na gari lilikuwa mbele. Mwendo wa msafala ule ulikuwa wa kukatisha tamaa sana kwa mtuhumiwa kufikiria kutoroka kwa vile ulivyokuwa umeshika kasi kama gari la kubebea wagonjwa mahtuti.
Wakati tukiendelea na safari nikajikuta nikiyakumbuka vizuri maelezo ya yule daktari mfupi mbilikimo kuwa gereza la Muramvya lilikuwa umbali wa kilometa zisizopungua themanini eneo la kaskazini mashariki kutoka pale kwenye zile mahabusu nilizokuwa nimefungwa. Nikapiga hesabu kuwa kwa mwendo ule endapo nisingekuwa makini kilometa themanini zingeweza kuyeyuka haraka hata kabla sijafanya lolote. Hivyo nikasubiri safari ile izoeleke na umakini wa wale walinzi wa msafala upungue kisha haraka nianze harakati zangu.
Nikiwa kwenye kile chumba cha mahabusu taratibu nikakitoa kile kipande cha waya kutoka mdomoni ila kwa kuwa ule mfuko mweusi ulikuwa kichwani ule waya haukuweza kuanguka chini hivyo ikanibidi nikibane kile kipande cha waya kwa meno na kukitoa kwa kuutoboa ule mfuko mweusi kichwani mwangu. Kile kipande cha waya kilipoanguka chini nikatulia kidogo hadi pale niliporidhika kuwa hali bado ilikuwa shwari hapo ndiyo nikaanza kupapasa chini kwa mikono yangu iliyofungwa kwa nyuma na pingu. Halikuwa zoezi rahisi kwa vile nilihitajika kukipapasa kile kipande cha waya kwa umakini ili nisishtukiwe. Sikukiona haraka kile kipande cha waya kilichoanguka chini na hivyo kuepelekea kijasho chepesi kuanza kunitoka maungoni. Ilikuwa kama bahati kwani wakati nilipokuwa mbioni kukata tamaa mara nikafanikiwa kukiokota kile kipande cha waya kikiwa kimeangukia pembeni ya eneo lile.
Haraka nikakichukua kile kipande cha ule waya kisha nikaanza kushughulika kwanza na ile pingu ya miguuni. Lilikuwa zoezi gumu kwa vile nilikuwa sioni kutokana na ule mfuko mweusi niliyovalishwa kichwani. Hivyo utaalam wangu ukawa ukitegemegea ufundi wa kupapasa papasa pale chini. Baada ya hangaika hangaika hatimaye nikafanikiwa kuifungua ile pingu ya miguuni. Kazi ikahamia mikononi na hapo ndiyo nilipouna ugumu wa kuifungua ile pingu kwa vile mikono yangu ilikuwa imefungwa kwa nyuma. Lilikuwa zoezi gumu sana na lililohitaji umakini wa hali ya juu na wakati nikiwa mbioni kufanikiwa lile gari huwenda liliingia kwenye shimo dogo la barabarani kati ya mashimo mengi yaliyokuwa kwenye ile barabara mbovu isiyokuwa ya lami. Kwa kuwa sikuwa nimejiandaa kwa tukio kile kipande cha waya kikaniponyoka mkononi wakati nilipotupwa upande mwengine wa kile chumba na kujigonga vibaya kwenye ule waya wa kile chumba. Lile gari lilipotulia tena barabarani nikajisogeza tena kwenye ule upande niliokuwa huku nikiwa nimelala chini. Nilipofika eneo lile nikaanza tena kupapasa papasa pale chini huku nikiwa makini nisishtukiwe hila yangu. Hata hivyo sikifanikiwa kwani tulikuwa tumeingia kwenye barabara mbovu zaidi yenye mashimo na makorongo yaliyotokana na mvua kubwa iliyonyesha hivyo mle ndani kulikosekana utulivu. Muda ukaendelea kwenda na sikuweza tena kukiona kile kipande cha waya. Hatimaye nikaamua kuachana nacho baada ya kuhisi kuwa wale walinzi wangenishtukia.
Pamoja na ile barabara kuwa mbovu lakini hali ile haikupelekea mwendo wa lile gari kupunguzwa. Nilipoyatega masikioni yangu niliweza kuwasikia wale walinzi nyuma yangu kwenye kile chumba wakiwa wamezama kwenye maongezi ya hapa na pale sambamba na mawasiliano ya redio ya upepo yaliyokuwa yakifanyika na watu wengine wa upende wa pili.
_____
Tulikuwa tumesafiri umbali mrefu pengine kwa makadirio huwenda tulikuwa tumefika nusu ya safari ile wakati niliposhtushwa na kupungua kwa mwendo wa lile gari. Hali ikaonekana kunishtua hivyo nikatulia na kuyatega vyema masikio yangu yangu. Kwa kufanya vile nikagundua kuwa tulikuwa tukikaribia sehemu ya makazi ya watu katika kitongoji kilichochangamka kutokana na pilika pilika nyingi za watu. Kutoka na umbali tuliosafiri nikahisi kuwa tulikuwa bado hatujafika mwisho wa safari yetu na hapo ndiyo nikahisi kuwa huwenda lile gari lilikuwa likipunguza mwendo kwa vile kulikuwa na watu wengi eneo lile ili kukwepa kusababisha ajali. Moyo wangu ukalipuka ghafla kadili lile gari lilivyokuwa likipunguza mwendo. Akili yangu ikaanza kufikiri haraka isivyokawaida na sauti fulani ikaniambia kutoka kusikojulikana.
“Ni lazima ufanye kitu fulani Tibba vinginevyo huu ndiyo utakuwa mwisho wako hapa duniani”. Sauti ile ilipojirudia mara tatu kichwani ikafanikiwa kuzitekenya fikra zangu na hapo kijasho chepesi kikaanza kunitoka huku moyo wangu ukianza kwenda mbio. Haraka nikainuka na kuketi kisha nikainama na kuubana ule mfuko mweusi kichwani kwa magoti. Wakati lile gari likipunguza mwendo na kusimama eneo lile ambalo kelele zake zilinipelekea niamini kuwa tulikuwa tukikatisha katikati ya soko kubwa lenye watu wengi na pilikapilika za kila namna. Nilipoubana ule mfuko mweusi kichwani mwangu nikauvuta kwa nguvu zangu zote. Sikufanikiwa kuuvua kwa vile ulikuwa umefungwa kwa kamba na kukazwa kiasi shingoni mwangu lakini ulichanika na kukaicha nje kichwa changu. Haraka nikayatembeza macho yangu kutazama huku na kule kwa kufanya vile kupitia dirisha dogo lenye kioo na wavu mlangoni nikaona watu wengi eneo la soko wengine wakiwa wamepanga bidhaa zao barabarani huku wakizitoa taratibu baada ya kupigiwa honi mfululizo na dereva wa lile gari ili walipishe lile gari.
Nilipogeuka na kuchungulia sehemu ya nyuma ya lile gari kupitia dirisha lingine dogo lililotenganishwa kwa wavu nikawaona wale walinzi wa msafala makomandoo wakiwa wamezikamata vyema bunduki zao huku wamezama kwenye kutazama nje ya lile gari kupitia vioo vya madirishani vya lile gari ambalo sasa niliweza kulitambua kuwa lilikuwa ni gari aina ya Land Rover Tdi jeupe. Haraka nilipoyarudisha macho yangu kukisaili vyema kile chumba nilichokuwa mlangoni nikaiona ile bahasha yenye nyaraka zangu ikiwa imechomekwa kwenye kisaraka kidogo chini ya mkono wa ule mlango. Nikahisi kuwa damu ilikuwa ikinichemka vibaya mwilini huku moyo ukinienda mbio isivyo kawaida. Bila kupoteza muda haraka nikajilaza chini halafu nikajipinda kwa namna ya ajabu sana hadi nilipofanikiwa kuipitisha miguu yangu kwa nyuma na hivyo kuipelekea mikono yangu iliyofungwa pingu kwa mbele. Lilikuwa zoezi gumu kidogo lenye kutoa jasho na kwa mtu yoyote mwenye kitambi asiyekuwa na mazoezi ingelikuwa ni ndoto ya mchana kweupe. Lakini kwa kuwa mwili wangu ulikuwa mwepesi na uliozoea mazoezi makali zoezi lile lilifanikiwa. Hata hivyo wakati nikimalizia zoezi lile komandoo mmoja mlinzi wa ule msafala aliyekuwa nyuma ya kile chumba akachungulia na kuniona. Ni kama aliyekuwa ameshikwa na butwaa kwa kushangazwa sana na kitendo kile. Kabla hajapiga yowe kuwataarifa wenzake mikono yangu iliyofungwa pingu tayari ilikwishazama ndani ya nguo yangu ya ndani katikati ya mapaja kuichomoa ile bastola niliyowekewa na yule daktari mfupi mbilikimo. Huwa sina kawaida ya kukosa shabaha kwa mawindo ya kipuuzi kama yale hivyo risasi moja tu niliyoifyatua na kuipenyeza kwenye lile tundu ikazama mdomoni kwa yule komandoo aliyeachama mdomo kunishangaa. Risasi ile ilipotokezea upande wa pili kichwa cha yule mtu kilikuwa kimefumiliwa vibaya huku ubongo wake ukiwarukia wenziwe.
Sikuwa na muda wa kupoteza hivyo haraka nikaichukua ile bahasha yenye nyaraka zangu na kuibana kwapani, risasi mbili zilizofyatuliwa kunilenga hazikunipata kwani tayari nilikwishajibanza ubavuni kwenye kile chumba sehemu isiyoweza kuonekana na mtu kupitia tundu dogo la dirisha la wavu la kule nyuma. Wakati hayo yakiendelea mara nikasikia wale makomandoo walinzi wa ule msafala wakikazana kufungua ule mlango wa nyuma wa ile sehemu walikoketi na hapo nikajua kuwa walikuwa katika harakati za kushuka kwenye lile gari ile waniwahi.
Nikiwa tayari nimeishtukia dhamira yao nikajionya kuwa bahati ya namna ile isingejirudia mara mbili hivyo kwa nguvu zangu zote nikaupiga mateke mawili ya nguvu kwenye mlango wa kile chumba nilichokuwa. Mlango haukufunguka badala yake nikaliona vumbi la kidongo chekundu likisambaa mle ndani na hapo nikajua kuwa ule mlango ulikuwa umefungwa kwa nje. Risasi moja ikatosha kuisambaratisha kabari ya ule mlango hata hivyo nikamalizia kazi kwa kuurukia ule mlango kwa miguu yangu yote. Mlango ukafunguka bila kupenda huku mimi nikiangukia kwenye tenga kubwa la mchuuzi wa nyanya huku nikiwa kifua wazi na bandeji kubwa yenye pamba iliyofunika mgongo wangu.
Risasi mbili ziliyofyatuliwa na mlinzi wa kwanza wa ule msafala kushuka kwenye lile gari zikanikosakosa kichwani na kupasua matikiti ya mchuuzi wa eneo lile na hivyo kusababisha mtafutano wa aina yake. Watu wakaanza kukimbia hovyo huku na kule eneo lile kila mtu akishika uelekeo wake baada ya ile milio wa risasi kusikika. Kwangu ilikuwa nafasi ya kipekee. Haraka nikageuka nyuma kujibu mashambulizi yenye lengo la kuwapunguza kasi wale walinzi. Risasi yangu ya kwanza ikampata pajani yule mlinzi aliyenifyatulia risasi na risasi ya pili ikampata dereva wa lile gari begani wakati alipokuwa katika harakati za kufungua mlango wa gari ili ashuke. Nikawaona wale walinzi wa ule msafala waliokuwa kwenye lile gari la mbele na lile la nyuma wakiparamiana kwa pupa kuwahi kushuka chini na bunduki zao mikononi. Sikutaka kuendelea kupoteza muda eneo kwani matumizi ya ile bastola ilikuwa kwa ajili ya kujihami na siyo kuendesha mapambano dhidi ya silaha nzito za kivita walizokuwa nazo wale walinzi mikononi. Bila kuchelewa nikaingia kwenye kichochoro kimoja chembamba cha lile soko huku nikitimua mbio zisizo za kawaida.
Lilikuwa soko kubwa sana lenye msongamano mkubwa wa watu na bidhaa. Nilipogeuka nyuma nikawaona makomandoo wawili wa ule msafala wakitimua mbio kunifukuza nyuma yangu na mmoja akainua bastola yake ili anilenge. Kuona vile nikachepukia upande wa kushoto nikishika kichochoro kingine kisha nikafyatua risasi mbili hewani ili kuongeza hekaheka za watu kukimbia hovyo kwa hofu eneo lile. Hila yangu hakika ikafanikiwa kwani si mchuuzi wala mnunuzi aliyesalia eneo lile. Kila mmoja akashika uelekeo wake na mimi kuona vile nikajichanganya kati yao huku macho yangu yakitazama huku na kule. Hatimaye nikavutiwa na shati moja la jeans lililokuwa limetundikwa kwenye kizimba kimoja cha muuza mitumba. Nikakwapua lile shati halafu mbele nilipoingia kichochoro cha upande wa kulia nikavutiwa na suruali ya kodrai na kofia vilivyokuwa vikiuzwa kwenye kizimba kingine cha muuza mitumba aliyeacha baishara yake na kutimua mbio.
Nikaikwapua ile suruali na kofia na kisha nikaingia kwenye bucha moja ambalo muuzaji wake naye alikuwa amekimbia. Muda mfupi baadaye nilipotoka nje ya lile bucha mtu yeyote angehitaji kutuma teknolojia ya hali ya juu sana ili kunitambua. Ile pingu ya mikononi tayari nilikuwa nimeitelekeza buchani na lile shati la mikono mirefu la jeans likayaficha majeraha na ule mchubuko mbaya wa pingu kiganjani huku ule mfuko niliyovishwa tayari nikiwa nimeufungua na kuutelekeza. Ile bahasha yenye nyaraka zangu nikaikunja na kuichomeka kiunoni nikiibana vyema kwa mkanda wa suruali huku nikiwa nimechukua pesa za mauzo yote ya buchani kwa siku ile.
Ile kofia nikiwa tayari nimeivaa kichwani nikatoka buchani na kuchungulia nje. Walinzi wawili makomandoo wa ule msafala wakanipita kwa kasi ya upepo na bunduki zao mikononi wakikifuata kile kichochoro kilichokuwa kikikatisha mbele ya lile bucha kuendelea mbele kama mafala wasiojitambua. Wale walinzi waliponipita bila kuniona nikatoka buchani na kushika uelekeo wa kule nilipotoka huku nikijitia kukimbia kwa hofu kama niliyepagawa na ile milio ya risasi muda mfupi uliopita. Njiani nikapishana na wale makomandoo lakini hakuna aliyenitambua. Bastola yangu ikiwa kiunoni sikuwa na wasiwasi wowote katika maisha yale mapya ya uraiani.
Nilipotokezea kwenye ile barabara yenye ule msafala nikayaona yale magari matatu ya ule msafala bado yakiwa eneo lile lakini bila askari yoyote ndani yake. Nikavuka ile barabara na kuingia kwenye kichochoro cha upande wa pili wa lile soko nikipotelea mle ndani lakini macho yangu yakiwa makini na nyendo za kila mtu machoni mwangu. Lengo langu lilikuwa kuwahadaa wale walinzi wa msafala waliokuwa wakinitafuta kwani nilifahamu kuwa wote wangeelekeza jitihada zao za kunisaka kwenye ule upande wa pili wa lile soko walikoniona nikikimbilia pale awali.
Upande huu wa soko nilioingia haukuwa rabsha zozote wala watu kukimbia hovyo hata hivyo kulikuwa na mikusanyiko midogo ya watu ya hapa na pale wakielezana juu ya lile tukio la kutoroka kwangu na hapo ndiyo nikaamini kuwa habari mbaya husambaa haraka hata kwenye simu isiyokuwa na vocha.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Muda mfupi uliofuata nikawa tayari nimetokezea kwenye barabara kubwa nyingine ya upande wa pili wa lile soko. Sikuweza kufahamu pale ni wapi kwani eneo lile lilikuwa geni kabisa machoni mwangu. Nikiwa makini na nyendo zangu upande wa pili wa ile barabara kando ya baa moja ya daraja la chini kulikuwa na kituo cha waendesha bodaboda. Dereva mmoja wa bodaboda akaniwahi na bila kupoteza muda nikavuka barabara na kupanda ile bodaboda.
“Unaelekea wapi?”. Kijana dereva wa ile bodaboda akaniuliza wakati tukiondoka eneo lile. Sikumjibu haraka hadi tulipoingia kwenye kona ya tatu ya kile kitongoji kilichoonekana kujitenga na jiji la Bujumbura.
“Nipeleke Bujumbura”...
_____
Niliwasili jijini Bujumbura dakika chache zikiwa zimesalia kutimia saa mbili na nusu usiku. Nikamwambia yule dereva wa bodaboda anishushie Boulevard Central, mtaa mmoja wenye pilikapilika nyingi za watu na biashara uliokuwa katikati ya jiji la Bujunbura. Nikashuka na kumlipa dereva wa bodaboda pesa yake kwa huduma ile ya usafiri kama tulivyokuwa tumekubaliana mwanzo wa safari yetu. Lakini wakati yule dereva wa bodaboda alipokuwa akijiandaa kuondoka baada ya ile pesa niliyompa kuitia mfukoni nikakumbuka kumuonya kuwa asahau kabisa kuwa alikutana na mtu kama mimi endapo ingetokea akahojiwa na mtu yeyote kuhusu habari zangu huku nikiwa nimeshika bastola yangu mkononi. Yule dereva huwenda alitaka kutia neno lakini kitendo cha kuiona bastola yangu mkononi haraka akatia mwendo na kupotelea mitaani.
Haraka nikairudisha bastola yangu mafichoni kisha nikavuka barabara upande wa pili. Mtaa wa Boulevard Central ulikuwa umechangamka sana. Kulikuwa na baa nyingi na baa hizo zilikuwa wazi huku muziki ukiendelea kutumbuiza mle ndani. Kulikuwa na magari yaliyoegeshwa kando ya barabara ile. Nilipochunguza zaidi nikaona kulikuwa na maduka mengi yaliyokuwa wazi, vibanda vingi vya wakaanga chipsi na samaki wa kutoka ziwa Tanganyika. Kando ya barabara ya mtaa ule nikawaona pia akina mama wachuuzi wa vitafunwa mbalimbali kama maandazi, chapati, sambusa, kaukau, bagia, mikate ya kumimina na vikolombwezo vingine huku wakiwa wamepanga bidhaa zao juu ya meza zilizomulikwa aidha na vibatari vilivyokuwa vikitoa moshi mweusi au taa za karabai. Idadi ya watu pamoja na bodaboda katika mtaa ule ilikuwa ya kukinaisha kwa wingi wake. Ulikuwa ni mtaa wa aina yake na pilika zile zikanipelekea nisahau kwa muda mambo yote yaliyonisibu huko nyuma. Majengo machache ya ghorofa yaliyotazamana na barabara ile yalionekana kuwa ni kwa ajili ya makazi ya watu binafsi.
Nikatamani niingie kwenye baa moja ya karibu ili nijipatie walau bia mbili baridi lakini haraka nikasita kufanya vile pale nilipokumbuka kuwa tayari taarifa zangu zilishasambaa kila kona ya jiji la Bujumbura. Hivyo ingelikuwa ni sawa na kujikaribisha kwenye matatizo niliyotoka kuyakimbia lakini vilevile afya yangu haikuwa imeimarika vizuri na istoshe muonekano wangu ungeweza kuibua maswali kwa mtu yeyote ambaye angeutumia muda wake kunichunguza kwa makini. Hivyo nikaamua kuachana na mpango ule wa kujipatia kinywaji badala yake nikaingia kwenye kichochoro kilichokuwa baina ya jengo moja la ghorofa na nyumba ya kawaida yenye paa la mtindo wa mgongo wa tembo.
Wakati nikiingia kwenye kile kichochoro nikakumbuka kugeuka nyuma na kutazama kama kungekuwa na mtu yeyote aliyekuwa akinifuatilia nyuma yangu. Sikumuona mtu yeyote hivyo nikaendelea na safari yangu. Kichochoro kile kikanichukua hadi barabara ya mtaa wa pili. Haukuwa mtaa wenye pilika nyingi kama ule niliotoka lakini pia haukuwa umedolola sana. Nilipozidi kuuchunguza nikagundua kuwa ulikuwa ni mtaa wenye nyumba nyingi za kulala wageni za daraja la chini na kati. Mbali na vile niligundua pia kulikuwa na wasichana waliokuwa wakiuza miili yao. Haikuwa sehemu salama kwangu hivyo nikachepukia upande wa kulia nikiifuata barabara ya mtaa wa ule huku lengo likiwa ni kutokezea barabara ya Avenue de la Juenesse. Hata hivyo kabla sijafika mbali nikakumbuka tena kutazama nyuma yangu.
Nikiwa naamini kuwa mambo yalikuwa shwari mara nikajikuta nikishikwa na wasiwasi. Niliwaona wanaume wawili waliokuwa wamesimama nje ya nyumba moja ya kulala wageni eneo lile wakigeuka na kunitazama na namna ya utazamaji wao ukaamsha hisia tofauti kichwani mwangu. Sikuifuata ile barabara hadi mwisho badala yake nikaingia kwenye kichochoro kingine kilichokuwa upande wa kushoto lakini kabla sijaendelea na safari yangu nikajibanza kwenye kona na kuchungulia kule nyuma.
Hisia zangu zilikuwa sahihi kwani niliwaona wale watu wakianza kushika uelekeo ule niliouchukua huku wakikazana kutupa hatua zao. Hasira zikanishika kwa vile nilikuwa hata sijaanza kufurahia matunda ya uhuru wangu tangu nitoroke kwenye zile selo za mauti za Imbonerakure na SNR. Hivyo nikapanga kuwaonesha kuwa mimi siyo mtu wa kufuatiliwa kibwegebwege.
Haraka nikaanza kutimua mbio hadi nilipotokezea kwenye barabara ya mtaa wa tatu kabla ya wale watu hawajaingia kwenye kile kichochoro. Kisha nikashika uelekeo wa upande wa kushoto kuifuata barabara ya lami yenye mashimo mashimo. Nilipofika mbele kidogo nikaingia upande wa kulia nikikifuata kichochoro kingine. Loh! kumbe kichochoro kile kilikuwa kikiishia uani kwenye moja ya nyumba za mtaa ule. Nikataka nigeuze na kurudi lakini nikajikuta nikisita kufanya vile baada ya kuchungulia kwenye kona na kumuona mtu mmoja miongoni mwa wale wanaume wawili akija kwenye kile kichochoro hivyo nikaamua kuendelea mbele na safari yangu.
Nilipofika nyuma ya ile nyumba uani nikaona ukuta na bila kufahamu kuwa nyuma ya ukuta ule kulikuwa na nini nikaukwea haraka ule ukuta na kuangukia upande wa pili. Nilipoanguka upande wa pili wa ule ukuta nikajikuta nimetokezea kwenye eneo la wazi lenye magari mabovu mengi yaliyotelekezwa kwa miaka mingi chini ya miti mikubwa ya vivuli. Nilipozidi kuchunguza nikagundua kuwa eneo lile lilikuwa ni la shule moja ya msingi jijini Bujumbura kwani kwa mbali niliyaona baadhi ya madarasa ya shule ile kando ya barabara ya lami iliyokuwa ikipita magari.
Sikushawishika kuendelea na safari badala nikachagua gari moja bovu na kujibanza. Haukupita muda mrefu mara nikamuona yule mtu akitokezea juu ya ule ukuta kisha akajitupa chini na kuangukia upande ule wa pili. Nikamuona yule mtu akichomoa bastola yake toka kiunoni na kuishika mkononi huku akinyata kwa tahadhari kuja kwenye yale magari mabovu. Nikamsubiri afike eneo la katikati na hapo nikatoka kwenye maficho yangu na kumzungukia kwa nyuma. Nilimkuta akiwa anachungulia sehemu ya mbele ya lori moja bovu aina ya Bedford lililotelekezwa eneo lile juu ya mawe bila magurudumu.
Kama nyoka ashambuliavyo kwa hila nikamchapa pigo moja matata la kareti begani na hivyo ile bastola bastola yake mkononi kumponyoka. Alipogeuka ili anikabili nikamchapa tena mapigo mawili ya kareti sehemu ya moyo kifuani kwake kisha nikamlipua kwa pigo baya la ngumi ya kolomelo. Akapoteza muhimili huku akiweweseka na kaunguka chini. Nikamuwahi kwa kumrukia na hapo tukaanguka wote chini huku tayari nikiwa nimemtia kabari ya shingo kwa miguu yangu. Tulipoanguka pale chini nikajiviringisha naye kama chatu aliyekamata windo lake na kwa kabari ile nikawa nimefanikiwa kuivunja shingo yake na hivyo kupelekea kiwiliwili chake kuangalia mbele huku kichwa chake kikinitazama kwa nyuma. Nikawahi kumziba mdomo ili asipige kelele. Nikasubiri kitambo kifupi cha muda kipite kisha taratibu nikaifungua ile kabari shingoni mwake na kumsukumia kando yangu huku tayari akiwa amekufa. Nilipompekua mifukoni nikamkuta na pakiti moja ya sigara, kiberiti cha kasha, wallet ya ngozi ya kenge yenye pesa kidogo, bastola na magazini moja. Nikachukua zile pesa huku ile wallet nikiitupa. Ile bastola na magazini yake nikavusunda kwenye mkanda wangu kiunoni.
Baada ya kusubiri kwa dakika kadhaa bila kumuona yule mtu mwingine akijitokeza sehemu ile nikaliacha lile eneo na kukatiza kwenye kiwanja cha mpira wa miguu cha ile shule ya msingi ili nipite chini ya ile miti ya kivuli na kutokea barabarani. Hata hivyo ilikuwa ni wakati nilipokuwa mbioni kuuvuka ule uwanja ili niingie kwenye ile miti ya kivuli mara upande wa kulia nikaona kivuli cha mtu kikisogea taratibu eneo lile. Haraka nikachepuka na kujibanza kwenye kona moja ya ofisi za walimu za ile shule. Kwa kufanya vile mara nikamuona yule mtu akiharakisha kuja upande ule niliojibanza. Kuona vile nikachepuka haraka na kwenda kujibanza kwenye kona nyingine huku nikiwa makini kutomshtua mlinzi wa eneo lile.
Sasa niliweza kumuona vizuri yule mtu aliyekuwa akinifuatilia huku akiwa na bastola yake mkononi hata hivyo kabla yule mtu hajanikaribia zaidi mlinzi wa lile eneo akawa tayari amemuona yule mtu mtu hivyo akajitokeza kutoka kwenye maficho yake ili akabiliane naye lakini alikwishachelewa. Risasi za bastola ya yule mtu yenye kiwambo maalum cha kuzuia sauti zikampata yule mlinzi kifuani na kumlaza chini bila kelele. Nikiwa nimeduwazwa sana na unyama ule haraka nikaichomoa bastola yangu kiunoni na kwa shabaha moja makini nikamlenga yule mtu shingoni huku mlio mbaya wa risasi ukisikika eneo lile. Yule mtu hakupata hata nafasi ya kuomba maji, akaanguka chini na kutulia kimya. Haraka nikatoka pale mafichoni na kwenda kumpekuwa mifukoni. Sikupata kitu chochote cha maana hivyo haraka nikaondoka eneo lile nikikatiza chini ya ile miti ya kivuli kuelekea barabarani.
_____
Usiku bado ulikuwa tulivu na nilihisi kuwa muda ulikuwa ukienda haraka kabla ya mipango yangu haijatimia. Sasa nilikuwa makini sana na nyendo zangu huku nikitembea gizani kwa tahadhari. Nilikuwa nimekiacha kitongoji kijulikanacho kwa jina la Mutoyi na kuingia barabara ya Avenue de la Juenesse. Baada ya umbali mrefu wa kutembea kwa miguu upande wa kulia nikawa nimetokezea kwenye barabara ya Chaussee du Peuple Murundi ambapo niliifuata barabara hiyo upande wa kusini huku nikipishana na magari machache ya jeshi na kujibanza hapa na pale. Hatimaye nikafika njia panda ya barabara ya Chaussee du Peuple Murundi na barabara ya Avenue de I’Université. Kufikia pale nikaingia kushoto nikiifuata barabara ya lami tulivu ya Avenue de l’Université. Nikawa nikitembea kandokando ya barabara ile chini ya giza zito lililofanywa kwa matawi ya miti na kila nilipoona gari nikawa nikijibanza na kuliacha lipite. Baada ya mwendo mrefu wa safari ya kutembea kwa miguu hatimaye nikawa nimeyafikia makutano ya barabara ya Avenue de l’Université na barabara ya Avenue de la Mission. Kufikia pale nikachepuka na kuingia barabara ya Avenue de la Mission upande wa kulia.
Mara tu nilipoingia kwenye ile barabara nafsi yangu ikazongwa na hisia mbaya. Barabara ya Avenue de la Mission haikunivutia hata kidogo kwa namna ya mandhari yake. Ingawa ilikuwa ni barabara tulivu ya lami lakini ilitisha sana kutokana na giza zito lililokuwa kwenye barabara ile lilitokana na miti mikubwa ya kivuli iliyopandwa miaka mingi tangu enzi za utawala wa wakoloni kando ya barabara ile. Miti ile sasa ilikuwa mikubwa mno na muonekano wake ulitisha huku matawi yake makubwa yakijifunga kwa juu na hivyo kuifanya ionekane na giza nene kama barabara ya kuelekea kuzimu. Kama siyo miadi ya kuonana na daktari yule mfupi mbilikimo aliyenisaidia katika mpango wangu wa kutoroka katika sero za SNR na Imbonerakure ni dhahiri nisingeyahatarisha maisha yangu kwa kufika eneo lile. Hata hivyo ingawa sikuwa na pesa za kutosha za kumlipa yule daktari kwa msaada wake lakini niliamini kuwa kufika kwangu na kuonana naye lingekuwa ni jambo la kiungwana zaidi halafu baada ya hapo tungepanga namna ya kumlipa pesa kama nilivyomuahidi.
Kulikuwa na jambo jingine lililokuwa likinisukuma kuonana na daktari yule mfupi mbilikimo kwa kuwa alishaonesha urafiki na mimi nilitaka kuitumia nafasi ile vyema katika kumuhoji ili niangalie kama ningeweza kupata fununu zozote juu ya wapi alipokuwa balozi Adam Mwambapa kwa vile niliamini kuwa alikuwa akifahamu siri nyingi kuhusiana na zile selo za SNR na Imbonerakure. Hata hivyo sikuelewa ni kwanini daktari yule alikuwa tayari tuonane eneo lile linalotisha.
Wakati nilipobonyeza kitufe cha saa yangu mkononi kutazama muda nikagundua kuwa bado nilikuwa ndani ya muda. Dakika kumi zilikuwa zimesalia kabla ya kutimia saa tano usiku. Bastola yangu sasa ikiwa mkononi nikajikuta taratibu nikipunguza mwendo kadili nilivyokuwa nikitokomea gizani kwenye barabara ile inayotisha. Kwa mujibu wa maelezo ya yule daktari ni kuwa saa tano usiku angekuwa tayari ameshafika eneo lile na kujibanza kwenye mti mmoja miongoni mwa miti mingi ya eneo lile akinisubiri. Hivyo kwa vile muda wa miadi ulikuwa bado kutimia nikapanga nifanye kwanza uchunguzi wa kujiridhisha juu ya usalama wa eneo lile. Nikamaliza uchunguzi wangu pasipo mashaka yoyote hivyo nikatafuta mti mmoja mkubwa na kujibanza nikisubiri muda wa miadi yetu ufike.
_____CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Haikuwa hadi ilipotimia saa tano na robo usiku wakati nikiwa mbioni kukata tamaa na kuondoka eneo lile mara nikashtushwa na mwanga wa taa za gari lililoingia kwenye ile barabara ya Avenue de la Mission kwa upande wa kusini. Gari lile lilikuwa likitembea taratibu na kwa tahadhari kiasi cha kuyavuta macho yangu. Matumaini yakaanza kufufuka moyoni mwangu, taswira ya yule daktari mfupi na macho yake yenye huruma ikaanza kujengeka taratibu kwenye mboni zangu na hapo nikaanza kuwaza ni kwa namna gani angevunjika moyo baada ya kumueleza kuwa pesa zake sina hivyo anivumilie hadi kesho. Chochote ambacho kingetokea nilikuwa tayari kukabiliana nacho alimradi urafiki wetu usife.
Lile gari likaendelea kutembea taratibu na kadili lilivyokuwa likikaribia eneo lile nikaanza kuingiwa na mshawasha wa kutaka kujitokeza na kusimama barabarani ili yule daktari anione vizuri. Lakini wakati nikiwa katika harakati hizo moyo wangu ukasita huku nikijiuliza vipi kama ningejitokeza barabarani halafu mtu aliyeko ndani ya lile gari asiwe yule daktari badala yake wawe ni miongoni mwa wale maafisa wa jeshi la Burundi waliokuwa wakinitafuta?. Ni dhahiri kuwa ningekuwa nimejipalia makaa ya moto na kujisogeza kwenye hatari. Hatimaye nikaona ni akheri niendelee kujibanza nyuma ya ule mti. Lile gari hatimaye likafika usawa wangu na kunipita. Lilikuwa ni gari aina ya Toyota Land Cruiser ya rangi nyeupe ndani ya lile gari hata hivyo sikuweza kuona ndani ya lile gari kwa vile vioo vyake viliwekwa tinted nyeusi. Lile gari hatimaye likanipita na kuendelea mbele na safari na hivyo kunifanya nianze kuamini kuwa lile gari lilikuwa katika harakati zake kama yalivyokuwa magari mengine ya mijini. Nikaendelea kulitazama lile gari kwa makini namna liliyokuwa likitokomea kwenye barabara ile huku nikijihisi kukata tamaa ya kumuona tena yule daktari kwa vile muda ulivyokuwa umeenda. Nikiwa bado natafakari namna ya kufanya mara macho yangu yakajikuta yakivutiwa kulitazama tena lile gari baada ya kuliona likigeuza mwisho wa ila barabara na kurudi. Mwendo wa lile gari sasa ulikuwa umepungua zaidi huku likiweka vituo vya hapa na pale hata hivyo sikumuona mtu yeyote akishuka kwenye lile gari. Tabia ile ikanishangaza sana na kunipelekea nihisi jambo lisilo la kawaida.
Kiasi cha umbali usiopungua mita hamsini mara nikaliona lile gari likisimama katikati ya barabara ile. Kilipita kitambo kirefu cha ukimya lile gari likiwa bado limesimama nikiwa katikati ya tafakuri mara nikauona mlango wa unaofuata baada ya ule wa dereva ukifunguliwa. Akashuka mwanaume mmoja mfupi ambaye nilipomchunguza nikapata hakika kuwa alikuwa ni yule daktari mfupi mbilikimo niliyekuwa na miadi naye. Hata hivyo hakuwa katika mavazi yake ya kidaktari kama nilivyozoea kumuona badala yake alikuwa amevaa shati na suruali. Yule daktari aliposhuka akatazama huku na kule kisha akafunga ule mlango na kuanza kutembea taratibu kuelekea mbele ya lile gari na namna ya utembeaji wake wa mashaka mashaka alionekana dhahiri kuwa ni mtu mwenye wasiwasi mwingi.
Yule daktari akaendelea kutembea hadi alipofika mbele ya lile gari akasimama katikati ya barabara huku mwanga wa taa za lile gari ukimmulika kwa nyuma. Nikiwa nimejibanza nyuma ya mkubwa kando ya ile barabara niliweza kumuona vizuri wakati alipouinua mkono wake na kujikinga usoni ili aweze kuona vizuri mbele yake huku akitazama huku na kule. Nikahisi huwenda yule daktari alikuwa amesimama mbele ya lile gari huku mwanga wa taa ukimmulika nyuma yake ili niweze kumuona vizuri na kujitokeza kwenye maficho yangu. Hata hivyo sikushawishika kujitokeza kwani utaratibu ule ulikuwa umekiuka makubaliano ya miadi yetu. Yule daktari alikuwa ameniambia kuwa saa tano usiku tayari angekuwa amefika eneo lile na kujibanza kwenye miti ile kando ya barabara akinisubiri lakini hilo lilikuwa halijafanyika kwani pamoja na yeye kuchelewa kufika eneo lile lakini muda huu alikuwa amejianika waziwazi mbele ya mwanga wa taa za lile gari ili nimuone na kumfuata ambapo ilikuwa kinyume na makubaliano yetu hapo awali. Hivyo machale yakawa yameanza kunicheza.
Yule daktari akaendelea kusimama mbele ya lile gari na alipoona hakuna dalili za kujitokeza kwangu akaanza kutembea akielekea mbele ya ile barabara na hivyo kuliacha lile gari nyuma yake huku akiendelea kutazama tazama huku na kule. Mara ghafla nikamuaona akianza kutimua mbio zisizo za kawaida. Lilikuwa tukio la kushangaza na lisiloeleweka lakini haraka akili yangu ikachangamka baada ya kuona ghafla milango ya lile gari ikifunguliwa na kisha wanaume watatu kushuka huku wakiwa na bastola zao mikononi. Kufuatia tukio lile nikajua kuwa yule daktari alikuwa ametangulizwa kama chambo cha kunikamata endapo ningeshawishika kutoka kwenye yale maficho na kumfuata pale alipokuwa amesimama. Hivyo ilikuwa baada ya yule daktari kuona kuwa hakuna matumaini ya uwepo wangu eneo lile ndiyo akaamua kutimua mbio ili kuiokoa roho yake dhidi ya wale watu waliokuwa kwenye lile gari. Wale watu wakaanza kumfukuza yule daktari huku wakimtaka asimame hata hivyo yule daktari hakutii amri badala yake akazidi kuchanganya miguu akielekea gizani kwenye ile miti kando ya barabara. Wale watu walipoona yule daktari haelekei kusimama mmoja wao akafyatua risasi moja hewani kumtahadharisha. Haikusaidia kitu kwani pamoja na hatua fupi za yule daktari lakini kasi yake ilikuwa ya kushangaza sana.
Yule daktari akiwa mbioni kupetelea kwenye giza zito la miti iliyokuwa kando ya ile barabara mara nikamuona mtu mmoja miongoni mwa wale watu watatu waliokuwa wakimfukuza yule akiinua bastola yake ili kumlenga yule daktari. Sikuwa tayari kuvumilia tukio lile hivyo kwa wepesi wa ajabu nikamuwahi yule mtu kwa risasi moja ya kifuani na hapo akaanguka chini na kuvingirika mara kadhaa kabla ya kutulia. Wenzake wakawa wameshangazwa na tukio lile lakini hawakutoa nafasi kwa yule daktari kutoroka kwani muda uleule nikasikia sauti ya mfyatuko wa risasi mbili kutoka kwenye bastola ya mtu mmoja miongoni mwa wale watu wawili waliosalia wakimfukuza yule daktari. Muda uleule nikamsikia yule daktari kule gizani akipiga yowe kali na kutupwa hewani na alipotua chini sikuweza kumuona.Loh! tukio lile likapelekea simanzi ya aina yake moyoni mwangu na hatimaye nikashindwa kabisa kuvumilia.
Niliwatokezea wale watu kwa nyuma wakati walipokuwa wakikaribia ile sehemu alipoangukia yule daktari chini ya mti. Mtu wa kwanza nikamuua kwa kumpiga risasi mbili za mgongoni, mwenzake alipogeuka nyuma risasi yangu moja ikampata begani na nyingine kichwani na hapo wote wakaanguka palepale na kupoteza maisha. Dereva aliyekuwa amebaki kwenye lile gari kuona vile haraka akatia moto gari na kwa kasi ya ajabu akatoweka eneo lile huku nikimkosakosa kwa risasi zangu zilizofanikiwa kupasua taa za lile gari na kioo cha nyuma. Hata hivyo sikufanikiwa kumpata yule dereva hivyo akawa amefanikiwa kunitoroka.
Haraka nikarudi chini ya ule mti alipoangukia yule daktari ili niangalie namna ya kumsaidia. Hata hivyo ilikuwa ni kama ndoto ya mchana kweupe kwani tayari alikuwa marehemu. Risasi moja ilikuwa imempata kiunoni na nyingine ilikuwa imempata shingoni. Ingawa alijitahidi kuhema lakini mapigo ya moyo wake yalikuwa dhaifu sana, majeraha yake yalikuwa yakivuja damu nyingi huku mdomo wake ukiwa wazi na macho yake yakinitazama bila dalili zozote za uhai.
Kwa kweli nilishikwa na huzuni isiyoelezeka kwani nilikuwa nimempoteza rafiki mwingine wa kukumbukwa katika safari yangu ya kijasusi. Msaada wake kwangu ni dhahiri ulikuwa umemsababishia umauti. Nikaendelea kumtazama yule daktari huku nikitokwa na machozi niliyojitahidi kuyazuia bila mafanikio. Niliendelea kumtazama daktari yule huku mawazo mengi yakipita kichwani mwangu na wakati nikiwa katika hali ile nikashtushwa na muungurumo wa gari lililoingia kwenye ile barabara kwa kasi kabla ya taa zake za mbele kumulika. Sikuwa tayari kukabiliana na hatari ya namna nyingine ambayo ingeweza kuhatarisha usalama wangu. Hivyo haraka nikaliacha lile eneo na kupotelea kwenye giza nene lililokuwa chini ya ile mti kando ya ile barabara nikianza kutimua mbio.
_____
Kulikuwa na ukimya wa kuogofya wakati niliporudia kugonga hodi kwa mara ya nne kwenye mlango wa mbele wa nyumba namba 37 iliyokuwa ghorofa ya pili ya jengo la shirika la nyumba la taifa la Burundi katika mtaa wa Bouleverd de l’indepence jijini Bujumbura. Muda ulikuwa umesonga, majira kwenye saa yangu ya mkononi yalionesha kuwa dakika chache zilikuwa zimeyeyuka baada ya kutimia saa saba usiku. Labda ile ingeweza kuwa sababu ya kumfanya msichana mrembo Veronica asiweze kuamka haraka na kunifungulia mlango kwa kuhofia usalama wake usiku wa manane kama ule.
Nikarudia kubisha hodi mara kadhaa lakini ule mlango uliendelea kunitazama bila muitikio wowote kama mfu. Veronica alikuwa wapi usiku ule hata asiweze kunifungulia mlango?. Nikajiuliza huku wivu ukianza kuzitafuna hisia zangu vibaya. Ingawa sikuwa na miadi naye kuwa usiku ule ningefika pale kwake lakini alipaswa kufungua mlango na kunisikiliza kama mgeni mwingine aliyemgongea mlango kwa dhalula. Niliwaza.
Kuendelea kugonga zaidi pale mlangoni kungeweza kuwaamsha majirani au kumvuta mtu yeyote aliyekuwa eneo lile hivyo nikaacha kugonga. Taratibu nikausogelea ule mlango na kutega sikio, mle ndani hapakuwa na dalili zozote za uwepo wa kiumbe hai hivyo nikapachika funguo zangu malaya na kukitekenya kitasa. Mlango ulipofunguka taratibu nikausukuma na kuingia mle ndani huku bastola yangu ikiwa mkononi. Sijui ni kwanini machale yalinicheza lakini niseme kuwa nilikuwa sahihi. Milango yangu ya fahamu ikanigutusha kuwa mle ndani kulikuwa na mtu kama siyo watu.
Wakati nikipambana na hisia zangu mara mkono wangu ukapigwa kwa pigo lisiloelezeka gizani na hapo bastola ikaniponyoka mkononi na nilipotia bidii kuidaka nikajikuta nikichezea pigo moja makini la teke la kifua lililonitupa ukutani huku nikiguna kwa maumivu makali. Nikawahi kusimama na hapo nikajikuta nikikabiliana na pigo lingine la ngumi ya shingoni gizani. Nikapepesuka na kuweweseka nikirudi nyuma lakini ulikuwa mtego kwani nilishangaa nikichotwa mtama na mtu wa nyuma yangu na kupaishwa vibaya hewani. Nilipotua chini nikatua kwenye mkono wa kochi na maumivu yake yalikuwa kama ya jando lisilo na ganzi.
Baada ya kukituliza vizuri kichwa changu nikagundua kuwa nilikuwa nikipambana na watu wawili mle ndani. Kwa kweli nilikuwa nimepanga kupumzika usiku ule na siyo kujiingiza tena kwenye mikiki mikiki ya namna ile lakini kwa vile ulikuwa ni uvamizi wa shari nami nikaona siyo vibaya nikifungua ukurasa mpya wa mapambano.
Sikuwa tayari kuruhusu shambulizi lolote tena hivyo nikajitupa chini na kujiviringisha kwenda upande wa pili wa ile sebule. Wale watu wakanogewa na kunifuata, mmoja nikamchapa teke la shingoni na mwenzake aliponifikia nikamkwepa na kumkita mguu wa tumbo, kisha nikawatoroka tena na kuhamia upande mwingine. Mmoja akaniwahi ili anipige ngumi ya uso nami nikasogea kidogo kumkwepa kisha nikaudaka mkono wake na kuunyonga kwa ufundi wa hali ya juu wa mtindo judo halafu nikaupiga kiwiko cha nguvu na kuuvunja. Yule mtu akapiga yowe la kuchanganyikiwa kama aliyeibiwa wallet yenye pesa na wajanja wa mtaa wa Kongo kule Dar es Salaam. Mwenzake alipokuja kwa kasi ili anishambulie sikumkawiza nikapita naye na kichwa cha uso na kumng’oa meno ya mbele huku mwamba wa pua yake ukipasuka vibaya. Akaanguka chini na kulia kama mtoto mdogo na alipotaka kusimama nikamrudisha chini kwa pigo la teke la korodani. Yule mwenziwe akachomoa bastola ile anilenge lakini alichelewa kwani bastola yangu nyingine tayari ilikuwa mkononi hivyo nikamchapa risasi mbili za kifua. Mwenzake kuona vile akasimama na kuanza kutimua mbio hata hivyo kabla hajaufikia ule mlango wa sebule risasi yangu moja ikamshona mgongoni na ilipotokea upande wa pili ikaacha tundu kubwa linalovuja damu kwenye moyo wake. Hatimaye mle ndani kukarejewa tena na utulivu.
Kwa sekunde kadhaa nikatega masikio yangu mle ndani kusikilizia chochote. Bado hali ilikuwa shwari hivyo nikaanza kunyata taratibu nikivikagua vyumba vya mle ndani kwa msaada wa kurunzi yangu ndogo mkononi. Sikumuona mtu yeyote mwingine na Veronica hakuwepo mle ndani, jambo ambalo lilinishangaza sana. Nikarudi sebuleni na kuwachunguza vizuri wale watu. Mshtuko ukanijia haraka baada ya kuzitambua sura zao vizuri. Walikuwa ni wale wanajeshi wenye ushirika na Amanda walioniteka siku ile ya kwanza kufika jijini Bujumbura. Mmoja alikuwa ni yule mwenye cheo cha Koplo akiitwa Adolphe Sahinguvu na mwingine alikuwa ni yule mwenye cheo cha Meja akiitwa Pascal Karibwami. Nikashindwa kuelewa ni kwa namna gani wale watu waliweza kuyatambua maficho yale ya siri.
Kwa kweli sikuweza kuelewa nini kilichokuwa kikiendelea hata hivyo wasiwasi juu ya Veronica haukuniacha. Veronica alikuwa wapi na ilikuwaje hadi wale watu wakafika pale?. Nikajiuliza pasipo kupata majibu. Nikatamani nitoke mle ndani na kwenda kutafuta hoteli ya kulala hadi kesho kutakapopambazuka ndiyo niamue nini cha kufanya lakini haraka nikajionya kwani usiku ule ungeweza kuwa hatari zaidi katika maisha yangu kwa vile nilivyokuwa nikisakwa mitaani kama shilingi ya mjerumani.
HIvyo nikaona kuwa sehemu salama ya kulala ingefaa iwe ni palepale nyumbani kwa Veronica lakini hoja ikabaki ningewezaje kulala mle ndani na ile miili ya wale watu?. Mara wazo likanijia haraka, nikaisogelea simu ya mezani juu ya stuli iliyokuwa kando ya kochi moja pale sebuleni na kunyanyua mkonga wake. Baada ya kubonyeza vitufe kadhaa simu ile ilikuwa ikiita upande wa pili. Ile simu haikusubirishwa kwani mwito wake mmoja tu ikapokolewa.
“Hujambo Hidaya?”
“Tibba…”. Sauti ya kike upande wa pili wa ile simu ikaita kichovuchovu lakini kwa mshangao.
“Ndiyo mimi. Samahani kwa kukutoa usingizini”. Nikaongea kwa utulivu.
“Khe! Tibba…!. Ulikuwa wapi na yepi yaliyokusibu?”
“Naomba utume watu waje kuiondoa miili ndani ya nyumba namba 37 Boulevard de l’independence. Tutaongea vizuri nikija kesho ofisini kwako kukuona. Nilimaliza kuongea na kwa vile nilimfahamu vizuri Hidaya namna alivyokuwa mdadisi nikawahi kukata simu kabla maswali yake hayajageuka kikao.
Muda wa nusu saa baadaye vijana wanne walifika na kuindoa ile miili mle ndani. Walikuwa ni vijana wa kitanzania lakini vilevile makachero waliokuwa wakifanya kazi katika ubalozi wa Tanzania pale Burundi. Walipoondoka nikaingia bafuni kuoga na nilipotoka nikapitiliza kitandani. Haukupita muda mrefu usingizi ukanichukua...
Sauti ya mtu aliyekuwa akigonga mlango ilinishtu kutoka katika usingizi mzito uliokuwa umenichukua kwa muda mrefu. Haraka nikatupa blanketi pembeni na kutega masikio yangu vizuri. Nilikuwa sahihi kwani sasa niliweza kuisikia vizuri ile sauti ya mgongaji, nikawaza mgongaji angekuwa nani na hapo akili yangu ikamuwaza Veronica huku nikitamani awe yeye. Hata hivyo nikajiuliza vipi endapo angekuwa siyo yeye?. Nikajiuliza huku nikishuka kitandani haraka na kuketi pembeni.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilipoitupia macho saa yangu ya mkononi nikashtuka kuwa ilikuwa ikielekea kutimia saa tatu asubuhi. Nikagundua kuwa nilikuwa nimelala kwa muda mrefu kufuatia uchovu wa siku ya jana na kwa vile nilikuwa sijalala kwenye mazingira rafiki ya usingizi kama yale kwa kipindi kirefu tangu nilipokamatwa na kuswekwa kwenye zile sero za SNR.
Miale ya jua la asubuhi iliyokuwa imepenya dirishani na kutuama pale kitandani nilipolala tangu kulipopambazuka ni dhahiri kuwa joto lake lilikuwa limeamsha homa hafifu mwilini mwangu, homa ambayo bila shaka ilitokana na majeraha mabaya niliyokuwa moyo mwilini. Mgongaji akaendelea kugonga mlangoni na mara hii niliweza kuitofautisha sauti ile na ile ya magari na bodaboda zilikuwa zikipita kwenye barabara iliyokuwa nyuma ya lile jengo.
Haraka nikaupenyeza mkono wangu chini yam to mmoja wa kuegemezea kichwa uliokuwa pale kitandani kuichukua bastola yangu kisha nikasimama na kuvaa shati haraka bila kufunga vifungo. Muda mfupi uliofuata tayari nilikuwa kwenye mlango wa sebule ya ile nyumba huku nikiwa makini kutomshtua mgongaji. Taratibu nikainama na kuchungulia kwenye tundu la funguo kwenye kitasa cha ule mlango huku bastola yangu ikiwa tayari mkononi. Nikakiona kiuno cha msichana aliyevaa suruali ya jeans nyeusi na blauzi ya rangi ya hudhurungi hapo hofu ikanipungua huku taswira ya Veronica ikijengeka taratibu kwenye mboni zangu.
Bila kusita nikakitekenya kitasa kwa funguo kuifyatua kabari yake kisha taratibu nikaufunguo ule mlango huku mkono wangu ulioshika bastola ukiwa mafichoni nyuma ya mlango. Mlango ulipofunguka macho yangu yakatia nanga kwenye umbo zuri la msichana mzuri na mchangamfu lakini makini kuliko hata chui jiko. Hidaya akanitazama kwa utulivu huku akitabasamu kabla ya tabasamu lake halijageuka kicheko cha kirafiki. Loh! sikuwahi kumuona Hidaya akiwa amependeza namna ile. Alikuwa amevaa kofia nyekundu ya kapelo, nyusi zake alikuwa amezitinda vizuri na kuzipaka wanja, kope zake zilikuwa zimerembwa vyema na hivyo kuyapelekea macho yake makubwa meupe yaonekane vizuri na kupendeza, kingo za mdomo wake zilikuwa zimekolea lips shine ya kijivu na hivyo kuongeza ziada nyingine katika utamu wake. Shingoni alikuwa amevaa kidani ambacho sikuweza kukitazama kwa makini kwa vile taswira ya matiti yake ilizivuruga hisia zangu. Nguo zake zilizombana kiasi zililichora vyema umbo lake refu chakaramu lenye kiuno chembamba lakini imara kilichoshikilia minofu ya mapaja yake iliyokaza kutoka na ratiba nzuri ya mazoezi. Begani alikuwa amening’iniza mkoba mzuri wa rangi nyekundu wa thamani ya hesabu ya bodaboda kwa wiki mbili.
“Karibu ndani kachero”. Nikamkaribisha Hidaya wakati alipozuga kuitazama saa yake ya mkononi akipambana na aibu ya kiutu uzima wakati nilipoduwaa kumtazama. Hidaya hakunijibu badala yake akatafuna bazooka yake mdomoni huku akitabasamu kisha akaingia ndani. Harufu nzuri ya manukato aliyojipulizia ikaleta uhai wa pua yangu wakati kinipita pale mlangoni. Kabla ya kufunga mlango nikatoka nje na kuchungulia huku na kule, sikumuona mtu yeyote hivyo nikaingia ndani na kufunga mlango. Bastola yangu nikaisunda kiunoni kisha nikavua shati na kulitupa kwenye kochi pale sebuleni. Nilipogeuka kumtazama Hidaya nikamuona kuwa alikuwa akinitazama kifuani kwa kificho, nikaamua kumezea.
“Mh! Tibba, pole sana kwa masaibu yaliyokukuta”. Hidaya akaongea kwa upole huku akionesha masikitiko.
“Kama siyo Mungu pengine tusingeonana tena hapa duniani”. Nikaongea huku nikitabasamu kisha nikamshika mkono Hidaya na kumkokota taratibu tukielekea chumbani kitandani kwani nisingeweza kuendelea kusimama wala kuketi kwene kochi pale sebuleni kwa vile nilivyokuwa nikijisikia kizunguzungu. Kitendo cha kumshika mkono Hidaya nikahisi kumfurahisha kwa vile tabasamu lake lilivyochanua usoni hata hivyo sikutia neno badala yake nilipofika kitandani nikajilaza taratibu na kuegemeza kichwa changu kwenye mto na kujifunika kwa blanketi hadi kiunoni. Hidaya pembeni ya kitanda huku akinitazama kwa huruma.
“Mh! kama kazi yenyewe ndiyo hivi ni afadhali ukaiacha Tibba”
“Sasa nikiiacha nani ataifanya wakati kila mtu anaogopa kifo?”
“Sasa huoni namna unavyosurubika hivyo, kila sehemu ina kiraka mwilini utasema nanasi”
“We acha tu Hidaya, warembo wakiniona kwa nje nikiwa nimenyuka viwalo vyangu wanababaika na uzuri sasa shida inakuja pale ninapovua nguo wengine hadi huniomba msamaha kwa woga kwa jinsi mwili wangu ilivyo na makovu ya kutisha”
“Khe! Haraka ya kuvua nguo ya nini tena si ungekuwa unavulia gizani hadi kukipambazuka unakuwa ushamaliza ya kwako”. Manano ya Hidaya yakatupelekea sote tuangue kicheko mle ndani.
“Mh! ushaanza maneno yako yasiyochosha”. Nikamwambia Hidaya huku nikitabasamu.
“Wacha tu niseme ukweli Tibba labda utanielewa”. Hidaya akaongea huku akiendelea kucheka.
“Mh! huna lolote umbea tu umekutawala”. Nikaongea na hapo wote tukaangua tena kicheko. Ukimya kidogo ukapita mle ndani huku kila mmoja akionekana kuzama kwenye tafakuri yake. Hidaya akaw wa kwanza kuutowesha ukimya ule.
“Vipi kuna tetesi zozote juu ya balozi?”
“Bado ni tetesi tu lakini zinapaswa kufanyiwa kazi”. Nikaongea kwa utulivu baada ya Hidaya kuyarudisha tena mawazo yangu mle ndani kisha nikaanza kumhadithia juu ya mambo yaliyojili tangu siku ile tulipoachana huku nikimsimulia mikasa yote hadi nilivyokamtwa na wale maafisa wa SNR. Nikaendelea kumueleza namna nilivyoteswa na mambo yote niliyoyaona kwenye zile selo za kutisha na maongezi niliyoyafanya na Kepteni Amadou Coulibary Sidibe kabla hajauwawa kwa kuchomwa moto. Bila kusahau namna nilivyofanikiwa kutoroka wakati nilipokuwa nikisafirishwa kupelekwa gereza la Muramvya kwa mahojiano zaidi na maafisa wa jeshi. Nilipomaliza kusimulia Hidaya alikuwa akinitazama kama kiumbe cha ajabu kutoka sayari nyingine dhahiri akionekana kuogopa misukosuko ile.
“Pole sana Tibba”
“Nishapoa”
“Unadhani balozi anaweza akawa ameshikiliwa kwenye hizo selo za SNR?”
“Sidhani”
“Kipi kinachokupelekea ufikirie hivyo?”. Hidaya akaniuliza baada ya kitambo kifupi cha ukimya.
“Nina imani kuwa kama balozi angekuwa kwenye zile selo za SNR ningefahamu tu kupitia mahojiano na wale maafisa lakini hakukuwa na kiashiria chochote”
“Sasa balozi atakuwa wapi?”
“Huwenda akawa nje ya mipaka ya nchi hii”
“Nini kinachokupelekea ufikirie hivyo?”
“Sijui ni kwanini lakini ni kama hisia zangu zinanituma hivyo”. Kitambo kifupi cha ukimya kikafuatia mle ndani na nilimpotazama Hidaya nikamuona kuwa alikuwa amezama kwenye tafakuri, mwishowe akavunja ukimya.
“Sasa nini kinachofuatia baada ya hapa?”
“Nahitaji kuelekea kisiwani Madagascar”
“Madagascar…?”. Hidaya akaniuliza kwa mshangao kama ambaye hakunisikia vizuri.
“Ndiyo sehemu pekee yenye matumaini katika mkasa huu”
“Lakini afya yako bado haijaimarika vizuri”. Hidaya akaongea kwa upole huku akinitazama kwa huruma.
“Nitakaa hapa kwa siku kadhaa hadi hapo afya yangu itakapoonesha matumaini kabla ya kuanza safari ya kuelekea kisiwani Madagascar”
“Lakini hapa siyo mahali salama Tibba”
“Ni kweli lakini hii ndiyo sehemu pekee yenye nafuu ya usalama”
“Nani atakayekuhudumia?”
“Veronica”. Nikaongea kwa kujiamini na hapo Hidaya akabetua mabega yake kwa kebehi.
“Mh! kweli Veronica kakulisha limbwata maana akili yako yote ipo kwake”. Hidaya akaongea huku akiuvuta mdomo.
“Wivu tu unakusumbua”. Nikaongea kwa kujiamini na hivyo kumpelekea Hidaya aachie msonyo wa nguvu na kisha kuniuliza.
“Veronica yuko wapi wifi yangu nimsalimie?”
“Huweza amini yaani tangu nilipofika hapa jana usiku sijamuona wala kuwasiliana naye”. Nikamwambia Hidaya na kuanza kumuelezea juu ya ule ugeni nilioukuta mle ndani usiku wa jana. Nilipomaliza simulizi langu sura ya Hidaya ilionesha mashaka.
“Tibba huwezi kukaa hapa wakati mwenyeji wako hujui yuko wapi. Ni afadhali ukakae nyumbani kwangu”. Hidaya akaongea huku akinitazama.
“Veronica akirudi je?”
“Yeye si yupo tu ukija muda wowote utamkuta. Mh! hata kama ndiyo mapenzi mubashara lakini kaka yangu umetekwa”
“Bora nitekwe na Veronica kuliko kutekwa na maafisa wa SNR”. Sote tukaangua kicheko.
“Kweli yaelekea wamekunyoosha vilivyo”
“Yaani we acha tu Hidaya”. Ukimya mdogo ukafuatia tena mle ndani huku kila mmoja akizama kwenye tafakuri yake. Mara nikakumbuka kitu na kumuuliza Hidaya.
“Uliwasiliana na chifu?”
“Ndiyo, hata leo asubuhi nimezungumza naye kwa simu. Sote tulikuwa na mashaka juu ya ukimya wako na hiyo ndiyo iliyokuwa ajenda kwenye maongezi yetu”
“Utakapowasiliana naye tena mwambie kuwa mimi nipo salama mengine nitazungumza naye mimi mwenyewe”
“Ondoa shaka”
Maongezi baina yangu na Hidaya yalendelea pale chumbani huku tukipeana habari juu ya mambo yalivyokuwa pale Burundi. Hidaya akanieleza namna alivyosumbuana na maafisa wa usalama wa Burundi baada ya lile nilikuwa nikilitumia kukutwa nje ya viunga vya maegesho ya magari vya Le Tulip Hôtel Africaine. Akaendelea kunieleza namna alivyowashinda kw hoja baada ya kukosekana kwa ushahidi wa kutosha. Kwa kweli nilifurahi sana kwa vile Hidaya msichana mjanja. Nakwambia chifu hakukosea kumleta Hidaya pale Burundi.
Baada ya maongezi marefu hatimaye Hidaya akaendelea jikoni na kuniandalia taftahi ya chai ya maziwa ya unga na mayai ya kuchemsha aliyakuta kwenye treyi jikoni. Ilipofika mchana Hidaya akaniaga kuwa anaendelea kazini kwa vile asubuhi alikuwa hajaingia huku akiniahidi kuwa angerudi usiku kunichukua twende nyumbani kwake kama Veronica angekuwa bado hajarudi. Hatimaye tukaagana huku nikifurahi kupata muda mrefu zaidi wa kuendelea kupumzika pale kitandani kwani kichwa bado kilikuwa kikinigonga na mwili wangu haukuwa sawa. Nikiwa pale kitandani mawazo yangu hakwenda mbali na Veronica na kadili muda ulivyokuwa ukizidi kusogea ndivyo mbegu ya wivu wa penzi dhidi ya Veronica ilivyokuwa ikizidi kuchipua moyoni mwangu.
_____
Saa moja usiku ilipotimu bila dalili zozote za kuonekana kwa Veronica mle ndani Hidaya akafika kunichukua na kunipeleka nyumbani kwake eneo la Avenue de l’Imprimerie sehemu kulipokuwa na makazi ya wafanyakazi wengi wa taasisi za kimataifa kama UN, UNHCR, WHO, Amnesty International, Humani Right Watch na taasisi nyingine zenye taswira ya kisomi. Hidaya alikuwa akiishi peke yake katika nyumba namba 25 katika floo ya pili ya jengo la ghorofa sita. Nyumba hiyo ilikuwa kubwa ya kuweza kuchukua familia. Ilikuwa ni nyumba kubwa yenye vyumba yenye vitatu, sebule kubwa yenye kila thamani za kisasa yakiwemo makochi mazuri ya ngozi ya sofa, runinga pana kutani na madirisha makubwa yenye kupitisha hewa safi. Mbele ya sebule ile kulikuwa na ukumbi wa kulia chakula wenye meza moja iliyozungukwa na viti sita. Kwa kweli ilikuwa ni nyumba nzuri ya kupendeza na yenye hadhi ya kukaliwa na afisa yeyote wa serikali mwenye cheo cha juu. Hata hivyo pamoja na ukubwa wa nyumba ile lakini Hidaya akiishi peke yake.
Tulipofika Hidaya akanikaribisha kwenye chumba kimoja kilichokuwa kwenye kona mwisho wa korido ambapo humo ndani kulikuwa na kitanda kikubwa cha futi sita kwa sita, kabati kubwa la nguo ukutani na sehemu ya maliwato inayojitegemea huku anikiambia kuwa yale ndiyo yangekuwa makazi yangu pale siku nitakapoondoka jijini Bujumbura. Nikamshukuru sana Hidaya na wakati nikiingia bafuni kuoga Hidaya akaniaga kuwa alikuwa akielekea jikoni kutayarisha chakula. Nilipotoka kuoga nikabadili nguo na kuelekea sebuleni kwenye ukumbi wa chakula huko nikamkuta Hidaya akinisubiri huku tayari ameandaa wali wa samaki, mchemsho wa ndizi matoke na utumbo wa ng’ombe, juisi ya parachichi na machungwa pamoja na maji baridi kutoka kwenye jokofu. Hidaya alikuwa msichana fundi wa kupika na kwa kweli nilimuomba Mungu nipate mwanamke fundi wa kupika kama yeye. Kilikuwa chakula kitamu sana ambacho sikuweza kukumbuka kuwa mara ya mwisho kula chakula kitamu namna ile ilikuwa wapi.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Usiku ulikuwa tulivu mno na manyunyu hafifu ya mvua yalikuwa yameanza kuanguka kwenye paa la nyumba ile. Usiku ule uzuri wa Hidaya ulikuwa umevunja rekodi kutokana na vazi alilolivaa. Hidaya alikuwa amevaa nguo nyepesi nyeupe ya kulalia iliyolichora vizuri umbo lake matata, ingawa alivaa sweta refu lakini halikufanikiwa kuificha nguo yake nyekundu ya ndani. Macho yalikuwa yakinitazama kiwiziwizi, mdomo wake ulikuwa ukinisubiri na akili yake haikuonekana kuzama kwenye kile chakula pale mezani badala yake alikuwa akila taratibu kwa kupekua pekua chakula kwenye sahani, mkono wake mmoja shingoni huku akinitazama kila mara na kutabasamu. Uzoefu wangu kwa wasichana warembo wa aina yake ukaniacha njia panda.
Kumbe wakati tulipokuwa tukipata mlo pale mezani Hidaya tayari alikuwa amewasiliana na daktari mmoja wa kitanzania aliyekuwa akifahamiana naye ilia je kunifanyia matibabu pale nyumbani. Hivyo tulipomaliza kupata chakula yule daktari tayari alikuwa amefika hivyo nikapumzika kidogo kisha sote tukaelekea chumbani ambapo yule daktari alianza kunifanyia tiba ikiwemo kuondoa zile bandeji na pamba mgongoni, kusafisha vidonda vyangu vyote...
MWISHO
0 comments:
Post a Comment