IMEANDIKWA NA : RICHARD MWAMBE
*********************************************************************************
Simulizi : The Escrow Mission
Sehemu Ya Kwanza (1)
Dar es salaam – saa 04:10 asubuhi
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
JIJI LA DAR ES SALAAM liligubikwa na moshi mzito wa mabomu ya machozi yaliyokuwa yakirushwa na vijana wakakamavu wa fanya fujo uone ‘FFU’. Vijana wenye uchungu na hasira, macho yao yaliyojaa machozi na makamasi membamba yakiwa yanatiririka katika pua zao walikuwa wametawanyika kila kona ya eneo la Magomeni njia panda. Hapo palikuwa ni makutano ya maandamano makubwa yalioitishwa na wanaojiita wadai haki, wanaopigania haki za wananchi. Kundi kubwa lilitokea eneo la Morocco kupitia Kinondoni kwa barabara ya Kawawa mpaka Magomeni, kundi la pili lilitokea maeneo ya Kimara, Ubungo kupitia barabara ya Morogoro mpaka Magomeni na kundi la tatu lilitoke Temeke, Keko, Kigogo kupitia barabara ya Kawawa.
Magomeni palikuwa na watu wengi vijana kwa watu wazima, wanawake kwa wasichana, kila mmoja alionekana akiwa na chupa ya maji mkononi, kama si ya uhai basi ya Ndanda au Kilimanjaro, walipiga kelele wakipunga mikono yao juu wakinyanyua mabango yalioyosomeka jumbe mbalimbali. Tunataka haki yetu mojawapo lilisomeka, Tumechoka kuburuzwa lingine nalo liliandikwa hivyo, Sasa basi ! lilisomeka hivyo pia.
Kwa ujumla mabango mengi yalikuwa yakipendezesha maandamano hayo, wale wenzangu na mie waliokuwa hawataki shari walijifungia ndani na watoto wao. Waliodai haki yao walishatangaza juma zima kuwa siku hiyo itakuwa ni siku ya kile walichokiita nguvu ya umma.
Siku hiyo ya ijumaa ilianza kwa utulivu sana katika jiji la Dar es salaam, mitaa na barabara zote za kuingia mjini zilionekana kuwapo na polisi was are na wale wasiotumia sare, yote ilikuwa ni kuhakikisha hakuna maandamano yoyote ambayo yangetukia siku hiyo. Kwa kuwa na waandamanaji nao walilijua hilo, hivyo wakatumia njia nyingine kutimiza azma yao. Wakapanda madaladala kimyakimya kutoka katika maeneo yao na kuteremkia Magomeni, pale ilipangwa watajikusanya na kuandamana kuelekea jangwani ambapo watatoa yotye ya moyoni na vinywani.
Vikosi vya kulinda usalama vilivyoamriwa kuhakikisha maandamano hayo hayafanyiki vilijikuta vikipigwa chenga ya mwili. Wakapata taarifa kuwa Umati mkubwa wa watu umekusanyika katika viwanja vya shule ya msingi Magomeni tayari kwa maandamano. Polisi wakasema ama zao ama zetu na wao wakasema hapa mpaka kieleweke, jangwani tutafika.
Nusu saa baadae maandamanoi yale yakaanza yakitanguliwa na mabango na matarumbeta, wimbo uliopamba siku hiyo ulikuwa na ujumbe, ‘Hata mkituua rudisheni pesa zetu,’. Maandamano hayo yalipofika njia panda ya kwenda Jangwani pale Magomeni kwenye mataa ndipo mdai haki alionekana na mamluki vivyo hivyo. Land Rover Defender kumi na nne zilizofungwa bendera nyekundu huku na huku zilifunga njia, lakini hakukuwa na askari hata mmoja aliyekuwa amesimama ardhini, wote walikuwa ndani ya gari hizo. Lori moja kubwa lenye maji ya kuwasha nalo lilikuwapo tayari likisubiri amri ya mkubwa ili lianze kampeni yake ya kuwafanya watu wajikune mpaka ngozi ziwatoke. Kati ya gari hizo za askari na wale waandamanaji kulikuwa na utepe wa njano uliofunga njia na kufanya mpaka kati yao, ‘Police line do not cross’ Utepe huo ulisomeka hivyo.
“Tunaomba sana, ndugu wananchi, tunajua wazi kuwa mmeguswa na mnakereketwa na hayo mnayoyadai, lakini maandamano yenu si rasmi na hayaruhusiwi kisheria, hivyo tunatoa dakika kumi, za kusitisha na kila mtu arudi katika kazi za kulijenga taifa,” ilikuwa ni sauti iliyotoka katika kipaza sauti cha gari moja wapo iliyosimama mbele kuliko zote. Bado watu wale walikuwa wakizidi kusogelea pale katika utepe ule.
“Mtakapogusa utepe huo tu, maana yake mmekaidi na hapo tutatumia nguvu kuwaondoa, tunatoa tena onyo, maandamano hayo si rasmi, yasitishwe mara moja, hatupendi kutumia nguvu lakini mkitulazimisha itatubidi,” ile sauti bado ilikuwa ikiendelea kuomba suluhu kwa waandamanaji hao. Hakika hali ya amani bado ilitawala katika dakika hizo chache. Waliokuwa madirishani walikuwa wkihesabu hatua za waandamanaji waliokuwa wakizidi kusogea katika ule utepe. Kimoyomoyo watu waliojifungia ndani walikuwa wakiona nukta kwa nukta amani inayotaka kutoweka makusudi, kama ni tarakimu basi walikuwa wakihesabu kuanzia kumi, tisa, nane na kuendelea huku kauli ya mheshimiwa Fulani mkubwa na mwenye madaraka ikichukua nafasi katika vichwa vyao, ikirudisha kumbukumbu ya maneno hayo yaliloleta gumzo katika magazeti, redio, televisheni na kila aina ya mtandao, ‘Tutawapiga tu,’.
Vijana wenye hasira na uchungu wa haki yao walikuwa wakiendelea kuimba na kubeza nguvu za wanausalama hao, wakiwa wamejiandaa kwa chupa za maji ya kunawa na wengine wakiwa wanasukuma matairi ya magari huku wakiwa na mafuta ya taa na petrol wakiamini kuwa kwa maoshi wa mabomu ya machozi basi maji na moshi wa matairi vitamaliza sumu hiyo na wao wataendelea na azma yao.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Haikupita dakika tatu, kilichozaniwa kikatokea, utepe wa njano ukakatika, bendera nyekundu ikapepezwa juu. Kutoka juu ya zile defender polisi walioshikilia mitutu ya mabomu ya machozi wakafyatua takribani mabomu kumi, yakatua katikati ya kundi la watu, polisi wengine wakaruka kutoka katika yale magari, kizaazaa kikaanza.
Marungu, mateke, fimbo zilitawala, kila aliyeonekana jeuri alibebwa na kutupiwa ndani ya kalandika. Ilikuwa mshikemshike, patashika nguo kuchanika. Hakuna mzalendo aliyedindisha kifua mbele ya vijana hao waliovalia mavazi na vinyago vya kutisha, wenye marungu makubwa na vioo vizito vya kujikinga kwa mawe, wepesi wa kukimbia na kurusha mitama ambayo iliwabwaga chini waandamanaji, ‘Mtapigwa tu!’
§§§§§
Ilikuwa ni siku ambayo nchi iligubikwa na watu barabarani wakiandamana na kudai haki yao. Mwanza, maandamano yasiyo rasmi, kama yalivyopewa jina yalikuwa yakielekea viwanja vya Nyamagana. Polisi walikuwa na kazi ngumu ya kuzuia na kuyazima maandamano hayo yaliyojawa na vijana wenye jazba na uchungu, waliokuwa wakipepeza mabango mbalimbali. Hawakuogopa kitu, walijua wanachokidai.
Huko Arusha nako kazi ilikuwa ngumu kuwazuia wananchi waliokuwa wakielekea viwanja vya Unga Limited. Kama ni mabomu ya macxhozi basi yalilindima kisawasawa. Masaa matatu yalioigeuza historia ya nchi kwa kugubikwa na maandamano hayo ya kutisha. Wananchi walikuwa wakidai, wakidai nini haswa? Lilikuwa ni swali la kujiuliza kwa wote wenye akili, nani kawaambia wadai? Wakifika pale wanapotaka ama viwanja vya Jangwani, Unga Limited au Nyamagana, watamkuta wanaemtaka? Nani atawapokea kwa niaba ya serikali na kuwasikiliza hoja zao wakati maandamano yameitishwa bila Baraka za serikali. Ni maswali magumu yaliyovijaza vichwa vya walio wengi.
Kamanda wa polisi kanda ya Dar es salaam alikuwa akifuatilia taarifa zote kutoka maeneo mbalimbali ya kanda yake, aliona wazi jinsi wananchi wanavyopambana na polisi, upande mmoja ukitaka kuandamana na mwingine ukizuia maandamano. Ina maana hawa waliokua wakizuia hayo maandamano hawakua na uchungu nay ale ambayo wananchi wanayadai. Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni.
§§§§§
MADAM S alizima luninga yake iliyokuwa ikimuonesha tukio hilo moja kwa moja kutoka eneo la Magomeni, akajishika tama akitafakari hili na lile, hakuwa na uwezo wa kufanya lolote juu ya hilo lakini hata yeye kila alipotafakari aligundua baadhi ya makosa ambayo kweli wananchi waliitaji ufafanuzi na majibu ya maswali magumu yaliokuwa yakiwaumiza vichwa licha ya kupandikizwa kasumba hiyo ya kuandamana kudai wanachodai. Alivuta faili moja akalifunua, akaliweka pembeni, la pili nalo ikawa hivo hivo, Madam S hakuona anachoweza kufanya, hakuona kazi inayowezekana kufanyika, meza yake ilikuwa nyeupe, haikuwa na kabrasha lolote lile. Kwa ujumla ilikuwa siku mbaya kidogo kwa wote, yaani yeye na wale anaowaona kwenye luninga. Aliinua macho na kuitazama picha kubwa ya Baba wa Taifa, haikuwa na msaada kwake.
“Ujinga!” akajisemea kwa sauti kana kwamba anamwambia mtu wakati yuko peke yake ofisini. ‘Wananchi wamechoka? Au hawaelewi? Tunajidanganya. Akainua simu yake na kubofya namba Fulani kisha akaiweka sikioni na kusibiri.
“Yes Madam,” Kamanda Amata akaipokea simu hiyo.
“Naomba uje ofisini mara moja,” Madam S akamwita kamanda kuripoti mara moja ofisini kwake, akakirejea kiti chake na kumsubiri mtu huyo.
Haikupita muda, mara mlango wa ofisi yake ukafunguliwa, kijana shababi akaingia na kukalia kiti bila kukaribishwa.
“Ndiyo Madam, niambie!” Kamanda Amata akaanzisha mazungumzo.
“Ulikuwa wapi?” akauliza.
“Nilikuwa mitaani nikisikiliza hili na lile si unajua kwa sasa nchi yetu iko kwenye kipindi kigumu kidogo,” Kamanda akajibu.
“Sio kidogo, ni kigumu sana, haya sikiliza kuna ishu nataka nikuingize ukanusenuse uniletee majibu ya haraka,” Madam akamwambia Kamanda. Akavuta mtoto wa meza na kutoa faili moja kisha akampatia. Lilikuwa ni faili lenye kurasa chache tu, Kamanda akalipokea na kukaribishwa na maandishi ya kupendeza The ESCROW mission katika jalada lake.
“The Escrow mission?!” akauliza kwa mshangao.
“Ndiyo, nataka ulitazame kwa makini kilichomo ndani kisha tuanze hiyo mission haraka iwekanavyo,” Madam akatoa amri.wa ni ku
“Yes sir!” kamanda akajibu kwa utani kama kawaida yake.
Akaanza kulipitia kabrasha lile hatua kwa hatua huku akitazama na viambatanisho mbalimbali.
DODOMA
“Sikia hili swala limeshakuwa tata, ijapokuwa tunajipa matumaini kuwa tumewini, tusijidangaje, tumekaliwa kooni,” Bwana Matata aliwaeleza wajumbe wa kikao cha siri kilichofanyika Mkonze Inn maeneo ya nje kidogo ya mji wa Dodoma. Katikati yao kulikuwa na vinywaji vinavyoteketea bila huruma.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Bwana Matata, mimi sioni swala la kuhofia hali halisi iliyopo, waache wapige kelele, sisi tuendelee na maisha, wale hawana linguine la kusema ndio maana wanabaki kupiga kelele na kuharibu taratibu ya mambo ya wenzao, na nakuapia mwisho wao upo,” akaongeza mtu mwingine aliyejuolikana kwa jina la Kagosho.
“Ah, mnatumia nguvu sana kubishana na kufikiria, dawa ni kuwasafusha tu mmoja baada ya mwingine,” akasema mtu wa tatu.
“Kwa hiyo we unatakaje?” akauliza bwana Matata.
“Tunamwondosha, wa nini akae atusumbue sote sisi, tuache kula maisha tumtetemekee mtoto wa juzi,” Yule bwana alisisitiza. Baada ya kikao hicho kirefu kilichofuata ni maamuzi na mipango mahususi juu ya utekelezaji wa hilo.
Jopo la watu watatu waliamua kukata mzizi wa fitina kwa kila anyeonesha kimbelembele katika skata hilo. Baada ya mazungumzo marefu yaliyochukua takribani masaa manne pale Mkonze Inn kilimalizika kwa maamuzi sahihi na mazito.
§§§§§
“Sasa sikiliza, ninachotaka ufanye ni kitu kidogo tu, kuna watu watatu ambao lazima uwamalize ndani ya siku tatu tu, nitakupa picha na majina yao. Bwana Matata akafungua mkoba wake akatoa picha tatu za ukubwa wa kutosha tu, akamkabidhi huyo aliyekuwa akiongea naye.
“Tazama, hawa hapa,” akamuonesha na kumkabidhi zile picha, Yule bwana akazigeuzageuza na kujaribu kuzikariri zote.
“Ok, wako wapi wote hawa?” Yule jamaa akauliza.
“Wapo, huyu hapa anaitwa Segaratumbo, yeye amefikia katika Uwanja wa ndege Resort, huyu mwingine anaitwa Msesema yeye yupo Bahi hotel na huyu anitwa Kibanio yeye kafikia Dodoma Hotel, hawa ndio tunataka washughulikiwe kwa njia yoyote ile,” aliongea bwana Matata.
Obobo ‘bacteria’, alikuwa na muuaji aliyekodiwa kutoka Kenya kwa ajili ya kazi maalum ambayo alikuwa akikabidhiwa na bwana Matata. Alipewa kazi hiyo siku mbili nyuma na kuwasili nchini kwa ndege ya kukodi. Sasa alitakiwa kufanya kazi moja tu ya kuong’oa roho za hao aliokabidhiwa picha zao na bwana Matata. Kwake ilikuwa ni kazi ndogo tu ukizingatia kuwa anaotakiwa kuwamaliza hakuna hata mmoja mwenye ujuzi wa kujilinda.
“Ok, boss, lakini kuna jambo moja, we huoni ndani ya siku tatu kuwamaliza hawa italeta utata?” Obobo akauliza.
Bw. Matata akatulia kimya na kuona ukweli wa swala hilo, akatafakari, akawaza na kuwazua, afanyeje, ni kweli kama hao watu wote watatu wakiuawa ndani ya siku tatu italeta masali juu ya vifo vyao.
“Sasa wewe unaona tufanyeje maana kuna ishu ambayo tukizubaa hapa tunaumbuka ndani ya masaa tisini na sita,” Matata alieleza.
“Hebu nambie ishu yenyewe kinagaubaga halafu nitakwambia la kufanya,” Obobo akamwambia bwana Matata. Ijpokuwa ilikuwa ni siri lakini ilibidi amwambia ili aone mbinu gani huyo bwana anaweza kufanya katika kulimaliza hilo. Bwana Matata akamueleza Obobo kwa kifupi lakini habari iliyoeleweka bila tabu.
“Ok, nimekuelewa, sasa hapa umesema nani ana hilo kabrasha?” Obobo akauliza.
“Huyu bwana Kibanio ndio mwenye mamlaka na ana hilo kabrasha, ila sijui lipo ofisini au analala nalo hotelini,” Matata akamaliza kusema.
“Sawa hapo nimekuelewa, sasa mi nafikiri hawa wasiuawe kwa tofauti ya siku tatu ni hatari, tutaondoa mmoja kwanza usiku wa leo, hapo shughuli zenu za kikazi zitasimama kwanza kwa hiyo tutakuwa tumeongeza siku za utendaji serikalini wakati huo tunatafuta hilo kabrasha, tukishajua lilipo, tunaliiba, hatuui mtu, tunaliiba halafu yeye atakosa ushahidi, kishapo ndipo tunaua mwingine halafu tutamalizia wa mwisho nafikiri kazi iwe ya wiki mbili, hii kidogo ina afadhali kuliko siku tatu,” Obobo akatoa maelekezo.
“Hivi unafikiri kulipata hilo faili ni kazi rahisi? Je ni vipi likiwa ofisini, na ofisi ina ulinzi wa kutosha maana ofisi iko ndani ya jengo la Bunge,” Matata alionesha mashaka yake katika mbinu hiyo.
“Usijali, we si ndo umenikodi mimi? Basi kwa taarifa yako hata kama lipo Ikulu mi naondoka nalo, ukisikia ‘bacteria’ ndo mimi, na nitawakabidhi kabrasha hilo mikononi mwenu ndani ya masaa 48,” Obobo akajigamba, wakaagana na kila mmoja akachukua hamsini zake, wakiahidiana kukutana baada ya kazi ya kwanza kukamilika.
Kutoka Chako ni Chako, Obobo alikatisha barabara na kufika upande wa pili ambapo kulikuwa na tax. Akafungua mlango na kuingia katika moja ya tax hizo.
“Bahi hotel tafadhali,” Obobo akamwambia dereva tax.
“Eldu kumi tu kaka,” Yule dereva tax akamwambia Obobo. Na muda huohuo Obobo akalipa ile pesa na kuondoka na tax ile.
Bahi Hotel ilikuwa hotel kubwa sana katika barabara ya kuelekea Singida eneo linaloitwa Bahi, hotel hiyo iliyojengwa nje kidogo ya mji wa Dodoma ilikuwa na kila kitu cha kuvutia mgeni anayekuja, wahudumu warembo wenye nidhamu na heshima bila kusahau ukarimu, wote walikuwa weupe wa rangi, wembamba wa wastani na warefu kiasi, kwa mtu anayejua makabaila ya Tanzania lazima angegota kati ya Warangi, Waarusha au Wanyaturu. Obobo alifika katika hotel hiyo majira ya saa kumi jioni, akashuka na kuiendea kaunta iliyopambwa na msichana mrembo.
“Nahitaji chumba tafadhali,” akamwambia Yule mwanadada mara tu baada ya kusalimiana naye.
“Umepata,” Yule dada akamjibu Obobo huku akimtazama kichinichini, kwa jicho la wizi. Akavuta kitabu chake cha wageni na kukifungua kurasa mpya yenye fomu ya kuandikisha wageni. Obobo akatoa hati yake ya kusafiria na kuandikishwa katika kitabu hicho kisha akakabidhiwa funguo na kupewa mtu wa kumuongoza kwenda chumbani humo.
§§§§§
Kamanda Amata alilifunga lile kabrasha na kuliweka mezani kwa Madam S.
“Umeelewa?” madam S akauliza.
“Hapa kuna siju tuite wizi au ubadhilifu wa fedha, sijui tuupe jina gani, au utakatishaji wa fedha, sasa kuna hao uliowaona hapo ndio watuhumiwa kuwa wamejichotea hayo mahela lakini nataka ufanye uchunguzi wa kitaalamu ili uone nani na nani hasa wanahusika au kama lolote la zaidi, maana sasa usalama wa taifa uko mashakani kutokana na sakata hili, fanya kila kitu kwa siri kama ilivyo kawaida yetu,” Madam akamaliza. Kamanda Amata akabaki kasimama wima hajui la kufanya maana hakuelewa hata aanzie wapi katika hilo sakata.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Sasa unamtolea macho nani? Ndo tumemaliza hivyo,” Madam alifoka. Kamanda akachukua tena lile kabrasha na kutoa copy kurasa alizozihitaji kisha akaaga na kutoka ofisini, akipanga kuwa usiku wa siku hiyo afike Dodoma kwa usafiri wake binafsi. Kamanda Amata aliona ni vizuri kazi hiyo kuianzia Dodoma kabla ya sehemu yoyote ile, akidhamiria kukutana na wahusika kwa jinsi yoyote na kufuatilia nyendo zao kabla hajaanza na wengine.
§§§§§
KAMANDA Amata alianza kujipanga kwa safari yake ya kwenda Dodoma usiku wa siku hiyo, alichukua kila kinachowezekana ambacho kitamsaidia katika safari na kazi yake inayomkabili, hakuona kama kazi ya safari hii ni ngumu bali kwake ilikuwa kama kama kuua tembo kwa ubua. Aliitazama landrover defender yake ilikuwa katika hali nzuri kabisa, gari hii aliyopewa zawadi na mmoja wa rafiki zake kutoka Uingereza ilikuwa ikimpa kichaa sana Kamanda awapo barabarani.
Saa mbili usiku wa siku hiyo aliondoka zake kuelekea Dodoma, kuianza kazi aliyopewa. Njiani alikuwa akiwaza na kuwazua wapi pa kuanzia na wapi pa kumalizia.
Siku hiyo ilikuwa ni siku iliyoacha hisoria kwa Watanzania kwa jinsi walivyoweza kupigia kelele ufisadi kwa njia ya maandamano ijapokuwa walizuiwa na jeshi la polisi kila upande. Madam aliumizwa sana katika hili na moyoni mwake alikuwa akijisemea kuwa nguvu ya umma Mungu huwa ndani yake, kuna kitu ambacho anataka kuzungumza na watu wake kwa njia hiyo. Lakini baadae akajikuta kuwa hajui kamtuma Kamanda Amata Dodoma kufanaya nini.
OBOBO alitulia kwenye kibaraza kilichojengwa upande wa pili wa chumba chake. Lakini macho yake yote yalikuwa ni kuangalia wanaofika katika hotel hiyo, miwani aliyovaa ilimuwezesha kuona vizuri kabisa watu waliokuwa wakifika hotelini hapo. Obobo alikuwa akitaka kutekeleza lile alilotumwa usiku huo. Aliitazama saa yake ilikuwa yapata saa tano usiku, na alimuona huyo anayemchunga akiingia ndani mwake na kimada ambapo bila shaka ni changudoa kwa jinsi alivyovaa, alitega sikio pindi atakapotoka tu atamsikia hivyo hapo angejua afanye nini.
Bwana Msesema alikuwa na shughuli nzito na mwanmke aliyempata siku hiyo, mchaka mchaka haukuwa wa kawaida, kelele za kitanda nazoz zikajitahidi kunogesha burudani hiyo. Zikapita dakika kama kumi na tano hivi za ukimya, mara ukasikika mvutano kati ya wawili hao.
“Nilikwambia laki moja,” sauti ya kike ikasema.
“We mwanamke usiniletee nuksi mi nilisema elfu hamsini kama utapitisha usiku mzima na mimi, sasa haya masaa mawili tu unataka laki moja!?” akasikika Msesema akiunguruma kwa sauti yake ya kiume.
“Haya yaishe acha ubahili, we una minoti ya eskro halafu mi kunipa laki tu unawaka, tutaona utafika wapi na hiyo mihele yako, wizi tu umekujaa, Watanzania wanakufa nyi mnajichotea tu,” akaendelea kulalama yule mwanamke, “Haya nipeleke mimi,” akaongeza.
Kama kuna sentensi ambayo ilikuwa ikisubiriwa na Obobo basi ni hiyo, akaivuta bastola yake kubwa yenye kiwambo cha sauti, akaitia ndani ya koti lake kisha akanyanyuka na kutoka mlangoni kwake, akashika korido ya kuteremka chini, huku nyuma yake Msesema akaifuatana na yule binti anayelingana na mwanaye kiumri.
Alifika chini na kusimama pembezoni mwa ua kubwa nje ya hotel hiyo, akasubiri aone kitakachoendelea.
Msesema na kidosho wake wakaingia ndani ya V8 kubwa la kisasa wakajifungia milango na gari ile ikaondoka taratibu.
Obobo alijaribu kufikiri jinsi ya kummaliza Msesema lakini hakupenda kumdhuru binti huyo. Akatazama huku na kule na kuiona gari moja iliyokuwa haijafungwa kioo cha mbele, ‘Bingo!’ akajisemea kisha akaiendea na kuitoa lpki za milango akaketi ndani yake akafunga mkata na kuitekenya gari hiyo kwa funguo zake za bandia, akaiweka barabarani, akawa nyuma ya gari mbili na mbele kabisa ilikuwa ile ya Msesema. Wakaifuata barabara ya Bahi kuja Dodoma mjini, walipokaribia mzunguko wa kugawanya njia, Obobo akaongeza mwendo na kuchomoka kushoto. Kwa mwendo wake hakuweza kuipita ile V8 kwa jinsi ilivyokuwa ikikimbia, akajaribu kutafuta usawa mzuri akalenga tairi la mbele kwa bastola yake. Risasi iliyoachiwa haikufanya makosa, ilifumua tairi la mbele kushoto, Obobo akapunguza mwendo alipoiaona ile V8 ikiyumba na kukosa muelekeo. Msesema alijaribu kuiokoa huku na kule, alipoirudisha kwa nguvu kulia, ikamzidi nguvu, ikagonga nguzo ya taa, ikarudi barabarani ikapitiliza na kuingia kwenye ukuta wa round about ikapanda na kunyanyuka ikajibwaga juu yake ikiwa chali. Obobo akavaa sox usoni kwa haraka, akaegesha gari yake pembeni na kushuka, akaelekea katika ile V8, akachumgulia na kumku Msesema akiwa kabanwa na mkanda wa gari, akachomoa bastola yake kwa mara nyingine, akafyatua na kumpiga risasi Msesema pembeni kidogo mwa kifua chake. Obobo akatoka na kurudi garini wakati huo watu walikuwa wakija kwenye eneo la tukio ingawaje ilikuwa ni usiku. Obobo akawasha gari na kuondoka mpaka chuo cha mipango, akaiacha ile gari na kurudi akitembea kwa miguu yake miwili.
Alipohakikisha ameiacha mbali ile gari akasimamisha tax na kurudi tena mpaka pale ilipotokea ajali, akajifanya kushangaa, wakapita na kuelekea mpaka hoteli ya Bahi, Obobo akalipa pesa na kurudi chumbani kwake.
“One down two to go,” akasema kwa sauti ya chini, kisha akajipumzisha kitandani kusikiliza kinachoendelea.
Taarifa mbaya kama hizo husafiri haraka kama pepo za kusi. Haikuchukua dakika ishirini viongozi wa chama na serikali walikwishapata taarifa za ajali hiyop mbaya kila mmoja alichanganyikiwa kwa namna yake. Hakuna aliyeweza kujizuia kuangusha chozi lakini ukweli ndio ulikuwa huo, Msesema alikufa kwenye ajali ile.
Mheshimiwa Matata akapigiwa simu usiku huo na kujuzwa juu ya taarifa hiyo mbaya, alikurupuka na kukiacha kitanda akajiandaa harakaharaka na kuingia katika gari kuelekea hospitali ya serikali ya mkoa wa Dodoma. Alifika na kukutana na maswahiba zake kila mmoja akiwa anaongea lake, lililovuma zaidi ni kitendo cha kuwa na kimada ndani ya gari. Bila kuchelewa, polisi waliingia kazini kuanza kuchunguza juu ya ajali hiyo. Vilio na simanzi vilitawala, ulikuwa usiku wa majonzi.
§§§§§
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Madam S alipata taarifa hiyo majira ya saa saba usiku akiwa tayari amejilaza kitambo akiendelea kutembelewa na njozi mbalimbali zilizouburudisha ubongo wake.
Mwili ulimsisimka, akabaki kashika simu mikononi mwake kana kwamba hakuamini anachoambiwa na huyo aliyekuwa akipiga simu.
‘Itakuwaje?’ akajiwazia.
Madam S alitulia kidogo kisha akawasiliana na wanausalama wengine, kujua kinachoendelea, akapata maelezo yote ya jinsi ajali hiyo ilivyotoke. ‘Ajali,’ akajiwazia, akaanza kupata mashaka na jambo hilo, ‘lakini ajali haina kinga,’ akajipa moyo na kuendelea kulala usingizi. Madam S alikuwa akimfahamu vizuri sana bwana Msesema kutokana na wadhifa wake serikalini, alikuwa ni mtu anayependa kupigania haki ya wanyonge, kusema ukweli pale unapopindishwa, alitokea kupendwa sana na wenzake watatu ambao Watanzania waliwapa jina ‘Askari wa miamvuli,’ kutokana na tabia yao ya kuibua mambo yaliyo chini ya kapeti. Kipindi alichokufa ilikuwa ni kipindi muhimu sana kuwa na mtu huyo kwani ndiyo kwanza yeye na wenzake walikuwa wameibua uozo, ufisadi na wizi mkubwa wa mamilioni ya shilingi kama sio fedha katika akaunti maalumu ya kuhifadi fedha za mradi wa nishati.
Sakatia hilo lilikuwa kubwa kila mtu akawa analiangalia kwa jicho lake, lilisababisha malumbanoi makubwa kila mmoja kumuoneshea mkidole mwingine, wananchi nao wakaamua kuingia barabarani kuandamana juu ya hilo. ‘Tunataka fedha zetu’ kikawa kilio cha kila Mtanzania.
Madam S akakumbuka mara ya mwisho mtu huyo alipokutana naye waliongea mengi kwa kirefu lakini pia mambo mengi aliyoyaongea yalikuwa ni kama anahashiria kifo chake.
§§§§§
Kamanda Amata aliwasili Dodoma alfajiri ya siku hiyo ambayo kifo cha Msesema kilitokea, moja kwa moja akaenda na kupanga chumba Kenya Lodge, alifanikiwa kupata kimoja ijapokuwa watu wengi wa serikali walikuwa huko na inasemekeana kukiwa na shughuli yoyote ya kiserikali huwa si rahisi kupata chumba.
Kamanda Amata akaweka kila kitu vizuri katika chumba chake, vitega usalama vyote muhumu alivitega ndani ya chumba hicho kilicho ghorofa ya tatu juu. Akaagiza aletewe gazeti kisha yeye akajipumzisha kidogo kwani alikuwa na uchovu sana.
Akiwa katikati ya usingizi alisikia simu yake ikifurukuta, akainyakua, sio yenyewe, mfurukuto ule ulikuwa ukitoka katika simu yake ya siri, akaitoa na kuitazama, ‘TSA 0’ akashangaa kidogo maana simu hiyo ikiitwa moja kwa moja huwa anajua ni kazi ya hatari inamkabili. Akainyakuwa na kuiweka sikioni.
“Kuna ajali imetokea hapo, bwana Msesema amefariki dunia, hebu fuatilia unipe habari kamili,” ile simu ikakatika. Kamanda akakaa kitandani kwa muda akifikiria simu hiyo. ‘Ajali, madam anambie nifuatilie ajali, kwani mi traffic police? Any way, yeye akisema ujue kuna jambo,” akanyanyuka na kuingia maliwato, akajiswafi na kutoka. Akachagu suti nzuri kati ya alaizotembea nazo, ilikuwa suti nyeusi, aliyoitangulizia shati jeupe bila tai, miwani nyeusi iliyaficha macho yake, akatoka chumbani akiwa mtu mwingine kabisa. akazishuka ngazi na kupita katika kaunta ndogo.
“Nipe savanna moja baridi tafadhali, na toti moja ya GIN,” Kamanda akaomba.
“Umepata, sema linguine,” mhudumu wa kaunta akamwambia huku akimpatia alichohitaji. Kamanda Amata akachanganya madawa yake na kupiga tarumbeta kinywaji chote, aliposhusha glass ilikuwa tupu.
“Hilo linguine ntakwambia baadae,” akamwambia yule mhudumu na kumpa noti ya elfu kumi, “keep change mtoto mzuri,” akamwambia huku akiicha kaunta na kuondoka.
Kwa mwendo wa mguu, Amata alkatiza barabara chache na kuwasili katika lango kuu la hospitali ya mkoa wa Dodoma, alipita getini na moja kwa moja akafika eneo la chumba cha kuhifadhia maiti, baada ya kuongozwa na mhudumu wa chumba hicho, kamanda Amata aliuona mwili wa Bwana Msesema ukiwa katika mfuko maalumu.
“Naweza kuonana na uongozi wa hospitali?” aliomba Amata.
“Bila shaka, inawezekana,” yule mhudumu alimjibu na kumuongoza mpka kwa mganga mfawidhi wa hospitali hiyo.
“Karibu sana, karibu kiti,” Mganga mfawidhi Dr Chilonwa alimkaribisha kitini Kamanda Amata, naye akaketi. Baada ya kuijitambulisha kama kawaida yake.
“Nilitaka kuona kama kuna taarifa yoyote ya uchunguzi wa mwili wa bwana Msesema,” kamanda aliomba kwa Mganga mfawidhi.
“Mwili wa bwana Msesema umechunguzwa na mganga mkuu wa mkoa kwa niaba ya serikali, hivyo taarifa zote wanazo wao hapa bado hawajaleta kopi,” yule Mganga akamueleza Amata. Kwa sekunde chache kamanda Amata alichukua uamuzi wa kuonana na mganga mkuu wa mkoa ili kujua nini kimepatikana kwenye mwili huo, aliagana na Dr Chilonwa akatoka nje ya hospitali hiyo.
Usafiri wa tax ulikuwa ni usafiri mahsusi kwa Amata muda huo, kabla ya kuonana na mganga wa mkoa aliamua kwanza kuingia katika ofisi za serikali zilizojengwa katika eneo la Makole.
“Nisubiri hapa, nakuja sasa hivi,” alimwambia dereva tax na kumuachia noti ya shilingi elfu kumi, akapita getini na moja kwa moja akaingia katika ofisi mojawapo.
“Karibu kijana,” kamanda Amata alikaribisha na mwanamama aliyevaa nadhifu, suti nyeusi mbele yake juu ya meza kulikuwa na bendera mbili zikipepeza kuonesha ukuu uliotukuka wa mwanamama huyo.
“Asante mama, nimekaribia,” Kamanda aliitikia huku akiketi katika kiti kimojawapo kati ya viwili vilivyokua jirani kabisa ya meza hiyo.
“Enhe, niambie kamanda, maana ujio wako lazima una jambo, mi nakufahamu sana,” yule mama alianza mazungumzo.
“Ndiyo, mama nimekuja kukusalimia tu ni sikunyinmgi sana hatujaonana, lakini pia nakupa pole kwa kuondokewa na mmoja wa vijana wako machachri,” kamanda alitoa pole.
“Asante sana, japo hatuwezi kiupoa kwa sababu tukio lenyewe bado la moto, maana kama ulivyosikia ni ajali alipata jana usiku,” yule mama kiongozi akaeleza.
“Poleni, ni kitu ambacho mtu hakitegemei lakini basi hajali haina kinga,” Kamanda alitoa pole.
“Basi ndo hivo Kamanda, enhe niambie juu ya ujioi wako hapa,” Yule mama alimweleza Kamnda.
“Usihofu, nimepata taarifa ya huu msiba hivyo nimetumwa kuja kuwakilisha ofisi, lakini hata hivyo kusaidia uchunguzi, sasa sijui naweza kupata taarifa iliyopo ya uchunguzi juu ya kifo hichi?” kamanda akaeleza wazi tu juu ya shida yake.
“Hapa kuna taarifa mbili ambazo zote zimeingia asubuhi hii, kuna hii ya polisi nah ii ya daktari,” yule mama akampa Kamanda taarifa zote mbili. Kamanda Amata akazichukua na kuzitazama moja baada ya nyingine.
Taarifa ya polisi ilieleza tu kuwa gari ya mheshimiwa Msesema ilipoteza uelekeo baada ya tairi lake moja kupata pancha, na gari kupanda msingi wa barabara kabla ya kugonga ukuta wa round about na kupinduka matairi juu. Taarifa iliendelea kusema kuwa gari hiyo ilisota kuanzia eneo la pancha mpaka ilipoangukia kwa umbali wa mita kumi na tatu hii ikiwa na maana dereva alikuwa akiendesha kwa mwendo kasi wa kilomita katia ya 100 na 130 kwa saa.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kamanda Amata akaweka pembeni taarifa ya polisi na kuchukua ile ya kidaktari iliyoonesha vipimo mbalimbali viliyotazamwa kitaalamu. Ilisema mwili wa marehemu una majeraha machache na mikono yote miwili ilivunjika, hakuwa na jeraha baya au hakuumia mahali pabaya sana zaidi ya vioo vikali vilivyoijeruhi vibaya sura yake na bati lililomkata vibaya katika kisogo chake.
“Uhhhhh!” kamanda akashusha pumzi baada ya kusoma taarifa zile.
“Nafikiri umepata jibu,” yule mama akamwambia Kamanda. Kamanda Amata akatulia kimya hakujibu lolote, baadaye akamtazama yule mama.
“Mheshimiwa, mimi nahitaji kurudiwa kwa hizi chunguzi zote mbili, nikiwa na maana kwamba ni vizuri serikali iwe na uhakika na hili, daktari kachunguza mwili wa marehemu, sawa, lakini mwili huo kaukuta tayari ukiwa hospitali, je alichukua muda kuwaona polisi waliopima ajali? Najua hilo sio lazima sana lakini, tuyaache nitakutafuta baadae,” Kamanda alikatisha maneno yake.
“Aaaah Kamanda endelea kusema, unajua wewe ukiwa na mashaka na kitu, basi ujue hata Ikulu ina mashaka, na mimi sipendi kuharibu kazi, kwa hiyo sema utakacho,” yule mama alimruhusu Kamanda kusema.
“Ni hivi, hatuna budi kuangalia kwa makini sana hii ajali, je ni vipi kama Msesema atakuwa ameuawa?” Maneno ya Kamanda yakamfanya yule mama aduwae kwa muda.
“Hivi inawezekana?” akauliza.
“Kwa nini isiwezekane mheshimiwa? Sisi ndo tunajua mambo haya yanayopita chini ya jamvi, naomba marehemu asizikwe kwanza mpaka ofisi yangu itakapokamilisha uchunguzi,” kamanda alioa oda kama kawaida ya kazi yake.
“Sawa kamanda, kwa kuwa ni wewe na ofisi yako imeona hilo basi nitatoa tu taarifa ya kusubiria kidogo kwa shughuli za kuaga mwili ili nikupe nafasi,” Mheshimiwa akamwambia Kamanda Amata.
“Sasa hutakiwi kumwambia mtu kama tunafanya uchunguzi huu wa siri,” kamanda akamwambia mheshimiwa.
“Usijali nalijua hilo,” akajibu. Baada ya hapo wa kaagana na kila mtu akaendelea na shughuli zake za kawaida.
Kamanda Amata alipokuwa anatoka katika ofisi ya mheshimiwa, alipishana na Land Cruiser Prado iliyokuwa ikiingia ndani ya viwanja hivyo, harakaharaka alipochungulia ndani alimuona bwana Matata akiwa ametuna kwenye kiti cha kushoto mbele. Matata alipata kitu kama mshtuko alipomuona kijana yule akitoka katika eneo lile. Mbele kidogo akateremka garini na kurudi kwa mguu kuingia ofisi ya Mheshimiwa.
Kamanda Amata aliingia kwenye tax aliyokuja nayo, lakini jicho lake lilinasa kitendo cha Bwana Matata kushukia njiani na kuingia kwenye ofisi ile aliyotoka Amata.
“Nipeleke, kituo cha polisi cha kati,” kamanda akamwambi yule dereva tax. Akaitoa ile gari kwenye maegesho ya jengo la bunge na kuingia barabarani kuja Jamatini, alipopita mzunguko wa kwanza pale stendi kuu akanyoosha mpaka mzunguko wa pili na kukunja kushoto akachukua barabara ya Iringa, alipovuka reki tu akakunja kulia kuelekea alikoamuriwa.
Mbele ya kituo cha polisi wa usalama barabarani pale Dodoma, kulipambwa na magari mengi yaliyobomoka na kubondeka kwa ajali mbalimbali. Kamanda Amata alipita katikati yake na kuifikia kaunta ya kituo hicho.
“Nikusaidie nini ndugu?” polisi mmoja wa kike aliyekuwa hapo alimuuliza Kamanda Amata huku akiendelea kuandika andika kwenye likitabu lake.
“Nahitaji kumuona RTO,” kamanda akamwambia yule WP.
“Kibinafsi au kiofisi?” akauliza yule WP.
“Kuna tofauti gani kati ya hayo mawili?” kamanda akauliza.
“Hapa mtu unamuona kiofisi tu lakini kibinafsi umuone nje hukohuko,” yule WP akajibu kwa nyodo huku akiendelea kuandika na kuwasikiliza wateja wengine waliokuwa hapo.
“Ok, nimekuja kibinafsi, naomba uniitie RTO hapa nje nimuone,” Kamanda akamwambia yule WP.
“Hivi we kaka, mbona una dharau na ofisi za watu?” akauliza yule WP akiwa amefura na kuacha kuandika.
Kamanda Amata akaamua kuzunguka kaunta na kupita bila kukaribishwa akaingia mwenyewe katika ofisi ya RTO, akamkuta akiwa bize na kuchakurachakura makaratasi lukuki pale mezani mwake.
“Karibu sana kijana,” yule RTO akamkaribisha Kamanda Amata.
“Asante afande,” kamanda akashukuru na kujitambulisha.
“Sasa afande shida yangu ni moja, najua una habari za ajali iliyotokea jana, ajali ya Mheshimiwa Msesema,” kamanda akaanza.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ndyo nakusikiliza,” RTO alimjibu
“Nimeiona taarifa ya uchunguzi, sasa ninaomba nionane na askari aliyepima ajali kuna mambo nataka kumhoji na pia nilione gari lenyewe,” kamanda akatoa ombi lake. Kutokana na uzito wa kazi yake haikuwa tabu. RTO akachukua simu ya upepo na kuibofya mahala Fulani.
“PC Omari Kihondo, ripoti kwenye ofisi ya RTO haraka iwezekanavyo, ova” akairudiarudia hiyo sentensi mara kadhaa, sauti nyingi zikawa zinapishana kwenye spika ya redio hiyo.
“PC Omary Kihondo, nimekusoma mheshimiwa, ova” sauti moja ikajibu kupitia redio ile.
Dakika kumi baadae, PC Omary Kihondo alikuwa amesimama kwa ukakamavu mbele ya bosi wake.
“Nimekuita hapa, kuna huyu kiongozi kutoka serikalini, anataka akuhoji maswala machache na kuichunguza upya gari ya mheshimiwa Msesema,” RTO akamaliza. Kamanda Amata akatoka na PC Omary Kihondo wakaelekea nje.
“Ndiyo bwana Omari,” kamanda Amata akaanzisha mazungumzo wakati wakizishuka ngazi za kituo hicho kulielekea gari iliyopata ajali, “Hebu nambie, jana ulipofika eneo la ajali ulikuta hali gani kwa majeruhi?” akauliza.
“Nilifika pale kwa kuchelewa kidogo, lakini nilikuta tayari Mheshimiwa amekwishakufa alikuwa amelazwa pembeni na wasamalia wema, nilichokifanya ni kutafuta usafiri wa mwili huo kufikishwa hospitalini, hii gari inaonekana ilipanda tuta la kutenga barabara baada ya kupasuka kwa gurudumu lake, ina maana liliyumba na dereva akakosa uongozo,” PC Omary akaeleza kwa ufasaha sana jinsi alivyoipima ile ajali, kiukweli alieleza kama alivyoandika hakuongeza wala hakupunguza.
“Ningekuuliza kama marehemu alifunga mkanda, lakini umeshasema ulichelewa kufika,” kamanda akazungumza.
“Inaonekana alifunga mkanda kwa maana tazama mkanda huu umekatwa kwa kitu kama kisu au wembe, labda wakati wanamnasua,” PC Omary akajibu. Kamanda Amata akaizunguka ile gari na kutazama huku na kule, alipofika eneo la kiti cha abiria, altazama kwa makini kulikuwa na damu japokuwa sio nyingi sana lakini zilikuwepo.
“PC, kwa jinsi ulivyoikuta gari inawezekana damu za marehemu kufika kwenye kiti cha pili?” kamanda akauliza.
“Hapana na haiwezekani, kwa sababu huyu marehemu lazima ameumia wakati gari ikitua chini, hivyo kama ni damu basi nyingi ndio hizi juu kwenye paa la gari,” Omary alijibu. Kamanda Amata aliangalia vizuri, akakumbuka ripoti ya daktari kuwa marehemu kaumizwa sana sehemu ya nyuma ya kichwa chake, lakini pale aliona tu bodi lililobonyea ambalo kama ni kumuumiza mtu halitaweza kumsababishia jeraha. Baada ya kazi hiyo iliyowachukua takribani saa moja, Kamanda Amata alimshukuru PC Omar akaagana na RTO na kuondoka zake.
§§§§§
Kamanda alitoa taarifa yake ya uchunguzi kwa Mkuu wake Madam S na kumuomba kama anaweza kumtuma haraka Dr Jasmine au mwili wa Msesema upelekwe Dar es salaam, cha muhimu alichokitaka ni uchunguzi tu wa kina wa kitabibu juu ya mwili ule kutokana na utata mdogo ambao yeye ameuona na labda mganga mkuu wa mkoa hajauona. Madam S alilipokea na kumuahidi kulifanyia kazi mara moja na kumpa majibu yatakayopatikana juu ya hilo.
Kamanda Amata alitulia kimya kabisa pale alipoketi katika moja ya viti vilivyo katika baa ya Srafina pembezoni kabisa mwa reli ya kati na barabara ya Iringa, alikuwa akijaribu kutafakari hatua ya kufanya, akiwa ndani ya tafakuri hiyo mara simu yake ilitoa mlio wa taratibu sana akaipokea na kuisoma kwenye kioo ‘Mama’, akainyakuwa mara moja na kuiweka sikioni.
“Ndiyo mama…” aliitikia ile sauti ya upande ule, “…Ok, nimekupata (…) hiyo ni nzuri zaidi, oka bye,” alimaliza kuongea na ile simu, akaikata na kuirudisha katika mfuko wa ndani wa koti lake.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
§§§
Wakati Amata Ric au Kamnda Amata kama alivyozoeleka akimalizia bia yake aina ya Safari iliyokuwa chupani, tayari Dr. Jasmine, mganga wa idara maalum ya usalama wa Taifa, TSA, alikuwa akielekea uwanja wa ndege kuondoka asubuhi hiyo kuelekea Dodoma kwa kazi hiyo iliyoita maalum.
Ilimchukua dakika arobaini tu tayari alikuwa akipumulia Dodoma, makao makuu ya nchi, alipokelewa na Kamanda Amata na moja kwa moja walielekea katika hospitali ya mkoa wa Dodoma baada ya kupewa kibali na serikali cha kuendelea na uchunguzi huo
“Niambie Kamanda,” Dr. Jasmine alivunja ukimya uliokuwa baina yao wakiwa wanatembea kwa miguu yao kuelekea katika ofisi ya mganga mfawidhi wa hospitali hiyo.
“Niliona ufike, kuna mambo yananitatanisha kidogo katika taarifa ya uchunguzi na siwezi kumwambia mtu mwingine yoyote zaidi yaw ewe,” Wakati Kamanda akimaliza kuongea hayo tayari walikuwa wamekwishafika katika mlango wa ofisi ya Mganga Mkuu.
“Oh, karibu sana daktari,” yule Mganga mfawidhi akawakaribisha.
Baada ya maamkiano mafupi moja kwa moja yule mganga alimwongoza Dr. Jasmine na Kamanda Amata mpaka chumba cha uchunguzi na kuwaacha yeye mwenyewe akitoka ndani ya chumba hicho.
Dr. Jasmine na muuguzi mmoja walisaidiana kuutoa mwili wa hayati Msesema na kuulaza vizuri juu ya kitanda tupu cha chuma na Jasmine akaianza kazi yake mara moja, akichukua hiki na kile akikata hapa na pale kwa utulivu wa hali ya juu sana, wakati huo Kamanda Amata alikuwa ameketi mbali kidogo akisubiri kuona ni nini ambacho atakigundua.
Baada ya ukimya kama wa dakika arobaini na tano hivi, Dr. Jasmine alifungua kinywa chake,
“Kamanda Amata,” akaita.
“Nipe taarifa,” kamanda akaitika huku akiinuka mahali alipokuwa ameketi na kabla na kusogea pale kwa Dr. Jasmine.
“Hapa kuna utata kidogo naugundua, sijui kwa upande wako, kifo cha huyu marehemu kimetokana na nini?” alimtupia swali Amata ambaye alibaki kimya kwa nukta kadhaa.
“Ajali ya gari,” akajibu.
“Hapana, impact ya ajali na majeraha yake yasingeweza kumletea mauti huyu marehemu, kuna kitu cha ziada ninachokigundua hasa upande wake wa kichwani, huyu bwana Msesema ameuawa, tazama hapa kichwani ukiachana na majeraha ya vioo huku usoni, tazama hapa kwenye paji la uso, hili sio jeraha la kioo, nimejaribu kupitisha kitu nikaona kinazama bila ukinzani, ina maana tuntu hili limepita kwenye fuvu, (kisha wakamgeuza upande wa nyuma) unaona hii kisogoni? Hili ni jeraha lenye uwiano kabisa na lile katika paji la uso, naweza nikasema kapigwa risasi, lakini risasi gani hii?” Dr. Jasmine akamliza maneno yake kwa swali. Amata Ric au Kamanda Amata akamtazama daktari huyu makini wa usalama wa Taifa, akatikisa kichwa chake kuashiria amekubaliana na hilo.
“Well done doctor,” Kamanda Akampongeza huku akimpigapiga begani, “Hata mimi nilipata wasiwasi na hilo jeraha, sikuliona kabla lakini kwenye ripoti ya awali walisema amekufa kwa kuumizwa kisogoni nilipoenda kuchunguza gari hakuna alama yoyote ya mabaki ama ya damu au hata unywele wa kisogo isipokuwa mbonyeo hafifu wa paa la gari, nikachukua hatua ya kukuita nawe umenipa mwanga,” Amata akasogea na kwa kutumia saa yake akapiga picha za ukaribu wa jeraha lile nyuma na mbele na sura nzima ya mwili wa Msesema. Akatoka na kuketi pembeni, akafungua simu yake kubwa na kuzirusha zile picha kwa kutumia Bluetooth kutoka kwenye saa kwenda kwenye simu kisha akazituma kwa Chiba, mtalaama wa kusaka siri za kitu kwa kupitia mitandao anuai ulimwenguni. Chiba alikuwa na sifa ya kipekee ya uwezo wa kukariri mitandao mingi duniani bila kuichanganya na kupata njia ya ufumbuzi wa haraka wa jambo kwa mtandao pasina shaka.
Walipojiridhisha na uchunguzi huo, ule mwili ulirudishwa katika jokofu. Dr. Jasmine aliandika taarifa ya uchunguzi wake na akaisaini na kugonga mhuri wake maalum kisha akaitia bahashani. Zoezi hilo lote lilichukua kama masaa manne hivi kukamilika.
§§§§§CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Enhe Bwana Matata hebu tuambie maana umetuita hapa ki-kuku kuku,” aliongea Kagosho
“Leo nimemwona yule mpelelezi mtata wa serikali pale katika ofisi za zetu akitoka kwa Mheshimiwa,” Matata aliongea huku akionekana kuwa na wasiwasi.
“Kwa hiyo?” Aliuliza mjumbe wa tatu.
“Nahisi kuna kitu, wasije kugundua udhalimu huu,” Matata aliongea kwa kusema huku uso wake ukijawa na wasiwasi.
“Aaaaaa Matata hebu acha matata yako, Obobo ni profesheno katika kazi hizi, hawawezi kugundua lolote zaidi ya ajali,” alibisha Kagosho, akakohoa na kuongeza, “Yule jamaa anakuua wakati unakata roho, ni mtaalamu, sasa hapo hata wapimeje ajali ni ajali tu”.
Pumzi ndefu zikasikika kutoka katika tundu kubwa za pua ya Matata, “Mi sio mtoto, na mkumbuke niliwahi kuwa kepteni wa jeshi hapo nyuma, nayajua haya mambo, yule kijana ni intelligent, yuko smart, ukimuona katua hapa ujue Ikulu imemtuma, nina wasiwasi”.
Kimya kifupi lakini chenye mshindo mkuu kikapita kati yao, hakuna aliyeongea.
“Ngoja tuone!” alimalizia Kagosho, “Na sasa Obobo amesemaje kuhusu hao waliobakia na zile dokumenti zenyewe?” akauliza.
“Amesema ‘kazi ya pili ni kuziiba hizo dokumenti ofisini’ halafu baada ya hapo ndipo atamaliza kazi,” Matata aliwaelewesha.
Baada ya mazungumzo hayo marefu sana, waliafikiana kutulia na kutazama kinachoendelea katika shughuli hiyo ya mazishi kwanza, kusikia kama kuna tashtiti zozote zinazoweza kuvuruga mpango wao, waliachana na kila mmoja alirudi kwenye majukumu yake kwa wakati wake.
§§§§
Muda uleule kikao kile kikiendelea, huko Dar es salaama nako Madam S alikuwa na kikao kifupi na Chiba wakijadiliana juu ya taarifa ile ya Dr. Jasmine pamoja na ile ya kwanza wakichanganya na ile ya polisi ili kutanabahi ukweli uliopo. Bila shaka wote wawili waligundua kuwa marehemu kauawa kwa silaha maalum inayotumiwa na majasusi,silaha hiyo huwa na umbo la peni ambayo huweka mfukoni kama peni za kawaida, lakini ina uwezo wa kubeba risasi ndogo zenye ncha kali tatu na kufyatuliwa pindi tu aliyeishika akibofya kinibu cha juu ya peni hiyo kama mtu anayetaka kuandika, risasi yake huweza kumpanya mlengwa na kutopkea upande wa pili bila kuleta madhara ya kutisha, daima inahitaji wataalam sana kuchunguza vifo kama hivyo.
Tafutishi za Chiba zilimpa jibu hilo lisilo utata mwanamama huyu aliyeanza kufunikwa na mvi kichwani mwake.
“Chiba, hii mbona kali, ina maana sakata hilihili ndilo limfanye aondolewe maisha au kuna lingine nyuma yake?” Madam S aliuliza na Chiba alibaki kamkodolea macho akiwa hajui la kufanya.
“Na kwa nini wafanye hivyo?” akauliza kama mtu aliyegutushwa usingizini.
“Mi na wewe tutajuaje? Cha muhimu ni kumsaka muuaji yeye ndiye atatupa jibu la haya yote,” Madam akaongea huku anagonga-gonga kwenzi katika meza yake ya ofisi.
“Wanataka kupoteza ushahidi, si unajua huyu bwana Msesema na wenzake wameshikia bango lile swala la upotevu wa mabilioni!” Chiba alikazia huku akinyanyuka.
“Una uhakika Chiba au na wewe unaamua kupiaga ngumi kichakani,” Madam aliongea kwa sauti ya chini.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Vyovyote vila Madam S, itakayempete huyohuyo, watu lazima waangalie, wewe unajibebea mabilioni wakati mahospitali ahayna dawa wala vifaa tiba, mashule hayana mahabara wala madarasa yanayokidhi mahitaji, watu vijijini wanakunywa maji pamoja na ng’ombe maana hawana miundo mbinu, barabara mbovu nchi nzima, reli tangu ajenge Mjerumani miaka hiyo. Huu ungekuwa wakati muhimu wa kuboresha haya yote lakini wachache na sijui wana matumbo ya aina gani wanajikusanyia mabilioni yote hayo, uroho umewajaa,” Chiba alilalama.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment