Search This Blog

Sunday 22 May 2022

MSAKO WA MWANAHARAMU - 4

 







    Silimulizi : Msako Wa Mwanaharamu

    Sehemu Ya Nne (4)



    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    “Minde, nahitaji kuondoka sasa, nitakuja kukusalimia tena,” akamuaga lakini ilikuwa ngumu kwa Minde kumruhusu Amata kutoka pale, alimbembeleza akae japo siku moja zaidi lakini Amata alijua wazi kuwa kwa vyovyote wenzake watakuwa wakimtafuta. Akaichukua saa yake sasa hii ilikuwa ya mwisho kuitoa katika ule mfuko, akaizungusha mahala fulani na kutazama kwenye kioo, kisha akamtazama Minde.



    “Hapa ni Bagamoyo?”



    “Ndiyo”



    Baada ya kama saa tatu hivi, Minde alimruhusu Amata kuondoka kwa minajiri ya kuonana tena, Amata akaagana na wale wazee na kuanza kufuata barabara taratibu kuelekea barabara kubwa ambapo angepata usafiri wowote.







    MASAKI – saa 1:30 usiku



    MADAM S alisimamisha gari ndani ya uwa wa nyumba yake na kuruhusu lile lango lijifunge lenyewe nyuma yake. Aliposhuka garini akavuta hatua kuelekea mlango mkubwa wa kuingilia ndani huku akitumia simu yake ya mkononi kuzima kengele za hatari ambazo huziacha zikifanya kazi kama yeye hayupo. Akaufungua mlango na kuingia ndani alipouelekeza mkono wake kuwasha taa, taa zikawaka zenyewe na sebule yote ikang’azwa na mwanga wa kupendeza.



    Madam S alipigwa na mshangao, akabaki akikodoa macho huku mkono wa kuume ukiwa tayari na bastola kiganjani.



    “Amani iwe nawe!” sauti ya Amata ikasikika.



    “Uhhhhh! Siku nyingine utakuja kufa wewe, kwanza ulikuwa wapi?” Madam S akaanza kufoka huku akishusha pumzi ndefu.



    “Nilikuwa kuzimu, na sasa nimefufuka katika wafu,” Amata akajibu.



    “Shiiiit! Mzima wewe? Au mzuka!”



    “Njoo unipapase maana mzuka hauna mifupa wala nyama,” Amata akajibu.



    “Oh! No, hebu ujinga wako…”



    Madam S akainua simu yake na kubofya tarakimu fulani fulani kisha akaweka sikioni na kusungumza na mtu wa upande wa pili.



    “Hello (…) sawa, njoo haraka nyumbani kwangu,” alipomaliza hayo akakata simu.

    Moja kwa moja akakiendea kiti kilicho mbele kinachotazamana na mgeni wake huyo huku bado bastola yake ikiwa mkononi.



    “Ina maana bado hujaamini kama ni mimi?” Amata akauliza kwa mashaka.



    “Watu ni wataalam huweza kujigeuza vyovyote watakavyo…” Madam akajibu huku sura yake bado ikionesha shaka kuu, “kweli wewe ni Amata?” akamuuliza tena.



    “Ndiyo Madam!”



    “Jina lako lingine…”



    “Mr. Spark!”



    “Lingine…”



    “Inspekta Jaffary…”

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Na ulilotumia Arusha kwa Abiseilim…”



    “Jaffari Makono…”



    “State of Living…”



    “Living of state!”



    “Good!” Madam akaafiki na kuirudishia usalama bastola yake kisha akaitia katika pochi. Hatua nne nyingine zikamfikisha katika jokofu, akatoa pombe kali na bilauri tatu, akaja nazo mezani na kuketi, akajimiminia na kumpatia Kamanda kisha akajiegemeza kitini na kumtazama kijana huyo kwa makini.



    “Nini kilikupata Amata, na ulikuwa wapi?” akauliza. Amata akainua fulana yake aliyoivaa na kumuonesha Madam S jeraha la risasi kwenye nyama za ubavu wake. Lilikuwa jeraha bichi kabisa lililoonesha dalili zote ya kuwa bado linahitaji tiba ya kitaalamu.



    “Shiiiit! Risasi?”



    “Ndiyo!” akajibu na kunyamaza kwa sekunde kadhaa, akavaa fulana yake na kuinua bilauri iliyojaa pombe, akapiga funda moja la maana kisha akaitua mezani kwa kishindo.



    “Sifi tena kama hii haijaniua,” akajibu huku akifunika na kumwacha Madam S akiwa kinywa wazi kisha Amata akamsimulia kila kilichomsibu.



    Hadithi ile ya kuogofya ilimfanya Selina atahayari, mara kadhaa alionekana akifinya macho, mara nyingine akishtuka na kadhalika. Hakuamini jinsi ambavyo kijana wake amepona katika hali isiyoelezeka.



    “Tumshukuru huyo mwanadada aliyekupatia tiba ya mitishamba, si tungeshakukosa!” Madam akamwambia.



    “Hata wale wazee pia ambao wameniokota, washukuriwe…”



    “Of coz!” Madam akamwambia a kutulia huku akiitazama simu yake, kisha akamtazama tena Amata.



    “Kamanda Amata, nilishatakiwa kutangaza kifo chako lakini nilikataa na kuwahakikishia kuwa upo hai kwa sababu najua wazi kuwa ni Mungu atakayeichukua roho yako lakini si binadamu mwingine awaye yote,” Madam akaeleza.



    “Umenea sawa, vipi kuhusu Scoba?” Amata akauliza maana hakuwa akijua chochote kuhusu mtu huyo.



    “Scoba tulimpata usiku wa siku hiyohiyo, sasa ni mzima na anaendelea vyema, hataki kabisa kusikia habari za kuwa wewe umekufa,”



    “Yuko wapi?”



    “Shamba. Bado yuko shamba na hatuwezi kumwacha hadharani, tuliliweka hivyo ili kuhakikisha kuwa tumekupata kama si wewe basi mwili wako,” Madam akaeleza.



    “Nipo hai, na ninaishi kwa mara nyingine tena, je; mlifanya lolote kwa kumsaka Pancho?”



    “Hapana kamanda, tuliliacha kama lilivyo, tuliona kwanza tuhakikishe habari ya wewe kisha ndiyo tujue kama ni kuweka matanga au kama ni kufanya sherehe…”



    “Fanya sherehe…” Amata akadakiza kusema.



    “Mpenzi wako Gina hana raha kabisa kwani hata yeye ana huzuni na kifo chako,” Madam S akaendelea kuzungumza na Amata juu ya tukio hilo lililowapa mshtuko mkubwa na kuwafanya kiasi fulani kutikisika.



    Wakati huohuo honi za gari zikasikika getini Madam S akabonya swichi maalumu iliyowekwa ukutani na kuruhusu geti hilo kufunguka. Gari dogo aina ya RAV 4 likaingia ndani. Amata akasimama pale alipo na kulitazama gari hilo likiingia taratibu.



    Jasmine! Akawaza na kurudi kitini.



    Hali ya Jasmine ilikuwa ileile pindi tu alipoingia nyumbani kwa Madam S, alipatwa na mshtuko alipomuona Amata pale kitini.



    “Ni wewe? Amata nooo!!!!” akapagawa na kumkumbatia kwa nguvu hapo hapo kitini, “sijui Gina atafurahi kiasi gani akikuona, maana nahisi karibu anarukwa na akili kwa kukukosa…” akalalama. Baada ya mazungumzo ya kina, Amata alimwonesha Jasmine lile jeraha ubavuni mwake. Naye kama daktari akalitazama kwa mbali na alipoona hawezi kujua vyema ukubwa wa jeraha hilo akachukua mipira ya mikono na kuivaa, kisha akalitomasa taratibu kila upande.



    “Asssss!!!! Taratibu bwana!” Amata akagugumia maumivu.



    “Nilitaka nijue linauma kiasi gani, risasi au kitu gani?” akahoji.



    “Risasi!” Amata akajibu wakati Jasmine akitulia kwenye stuli.



    “Inabidi tusafishe,” akamwambia.



    “No, nina dawa nimepaka hapo, huo weusi sio uchafu,” akamjibu.



    “Risasi wameitoa? Lazima nijue…”



    “Mi sijui, nilipostuka nimejikuta nagangwa tu!”



    “Good, lazima tufike Shamba ili niweze kutazama kwa Ultra Sound, nijwe na uhakika kama imetoka au bado ipo,” Dkt. Jasmine akamwambia Amata.



    “Sawa dokta! Utahitaji kunichoma sindano?”



    “Sindano muhimu, yaani ushujaa wote huo unaogopa sindano?”



    “Sindano ni sindano mama!!!”



    “Ok, hata hivyo inabidi sasa kwenda pamoja Shamba tukaweke mikakati yetu vizuri hakuna kulala,” Madam aliwaeleza vijana wake na wote wakajipanga kuondoka. Chiba na Gina nao wakapewa taarifa za kufika huko usiku huo

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Usiku huohuo…

    SHAMBA



              Madam S, Amata na Jasmine walikuwa kundi la kwanza kuwasili katika afisi hizo za siri. Moja kwa moja walimfikisha Amata katika chumba chao kidogo ambacho kwacho uganguzi wote na utabibu hufayika. Kilisheheni mitambo tiba ya kisasa ambayo ingeweza kuwekwa kwenye hospitali kubwa lakini hapa iliwekwa kwa kazi maalumu. Amata akafikishwa ndani ya chumba hiki na kutakiwa kulala juu ya kitanda ambacho juu yake kulifungwa taa kubwa yenye mwanga mkali pamoja na vifaa vingine.



    Akiwa hana fulana wala suruali isipokuwa nguo maalum aliyotakiwa kuvaa, alitulia kimya kitandani. Jasmine akawasha mtambo huo na kuweza kufuatilia kila kilichoonekana katika luninga yake pale ukutani. Baada kama ya dakika tano za kumulika huku na huku akakipachika kidubwasha ‘Transducer Probe’  kile mahala pake. Akashusha pumzi na kumtazama Madam S.



    “Vipi?” Madam akauliza.



    “Hamna kitu, risasi kama ilikuwepo basi wameshaitoa kwa njia yao, na kinachonishangaza ni kuwa hili jeraha liko vizuri tu kwa ndani kasoro hapa nje tu, na panaonekana kuwa panaendelea vizuri, kweli hizi dawa za shamba zina nguvu,” Jasmine akamwambia Madam S.



    “Haya kaa!” Amata akaambiwa naye akakaa juu ya kile kitanda.



    “Unajisikiaje sasa?” Madam S akamuuliza.



    “Niko poa, unaweza kuingia kazini?”



    “Kama kawaida, na ni lazima nimtie mkononi huyu Premji anayejiita Pancho!” Amata akajibu.



    “Noooo! Hauna budi kupumzika kwa saa sabini na mbili kabla ya mikiki mingine haijaanza…” Jasmine akamwambia.



    “Sawa dokta…”



    *    *    *



    Chiba na Gina waliingia katika jumba hilo kwa nyakati tafauti na kujikuta ndani wakiwa hawajui nani na nani wamekwishafika. Kwa jinsi jumba hilo lilivyojengwa kwa ndani, huwa ni vigumu kutambua nani kaingia na yuko wapi. Kila mmoja alikuwa na chumba chake kilichokuwa na kila kitu na angeweza kukaa humo hata mwezi pasi na kutoka nje. Zaidi ya hapo kulikuwa na chumba cha mikutano, chumba cha mazoezi ‘GYM’, baa ndogo, jiko, na afisi tafauti. Kama ukikaa katika afisi ya Chiba ungeweza kujua wote waliongia ndani ya nyumba hii kwani ni yeye tu anayeweza kuona kwenye kamera za usalama milango yote ya kuingili humo ndani na maeneo mengine. Iliitwa SAFE HOUSE kwa sababu inaweza kumficha mtu na asionekane katika jamii kwa muda usiojulikana. Kulikuwa na sehemu ya kuhojia wahalifu, ikiwa imesheheni kila zana ya kutesea, kulikuwa na chumba cha matibabu na maegesho ya magari ndani kwa ndani. Kwa ujumla jumba hili lilikuwa na sehemu kubwa mbili yaani ‘ground floor’ na ‘underground floor’. Ground Floor ilikuwa ni nyumba ya kawaida sana ambayo wageni wote waliokuja kwa siri walifikia hapo. Underground floor ndiyo ilikuwa na hayo makolokolo yote, na mlango wa kuingilia ilikuwa ni siri yao. Mhalifu yeyote aliyefikishwa hapo aliondolewa sox ya usoni pindi afikapo katika chumba cha mahojiano na si zaidi ya hapo. Lakini ‘Shahidi’ alifikishwa katika ‘ground floor’ na mambo yake yalifanyikia hapo. Hakuna aliyekuja katika jumba hili macho wazi zaidi ya TSA, hata Mheshimiwa Rais akitaka kufika hapa lazima afichwe sura yake asione wapi anakwenda.



    Kikazi iliitwa Safe House na kimaisha waliita Shamba.



                Madam S na Kamanda Amata wakapanda ghorofa ya juu kutoka shimoni ili kukutana na wapendwa wao. Ilikuwa furaha ya aina yake walipokutana tena na Kamanda Amata, kila mmoja alikuwa na hamu ya kutaka kujua hasa ni nini kilimsibu mwenzi wao huyo hata kutoweka kwa siku hizo tatu kama sio nne. Gina ndiye haswa aliyeonekana kuchanganyikiwa zaidi kwa kumwona Amata hakuamini kabisa kwani alishajua mtu amekufa alikuwa akisubiri tu taarifa ya kiofisi.



    “Mmefurahi sana ee?” Madam S akawauliza.



    “Ndiyo maana yake, hii ni furaha ya kukutana pamoja maana tulikwishachanganyikiwa,” Chiba akaeleza.



    “Ok basi sherehe iishe na sasa tuangalie kazi,”



    Wote wakaketi vitini katika meza yenye umbo la yai huku wakimwacha madam S upande wa peke yake kama kiongozi.



    “Hatutakiwi kuchelewa kwani adui yetu anaweza kututoroka na tusimwone tena,” ilikuwa ni sentensi ya kwanza katika kufungua kikao hicho kutoka kwa Madam S. Na wote wakatikisa vichwa.



    “Tunapaswa kuingia kazini, tukamsake huyu mwanaharamu, tumtie nguvuni, hastahili kuishi nje ya gereza,” akaendelea kuongea mara hii akionekana wazi kuwa ana hasira moyoni mwake.



    “Sawa Madam, sasa tunajipangaje kwa maana bila shaka pale walipodunguliwa Scoba na Amata ndipo kwenye makazi ya mtu huyo ijapokuwa hapajaonekana wazi,” Chiba akaeleza wasiwasi wake.



    “Ndio, msako huu utafanyika katika eneo hil…”



    “Ina maana mpaka sasa Pancho atakuwepo bado? Nina wasiwasi atakuwa keshaondoka nchi hii,” Gina alimkata kauli Madam S.



    “Yupo hajaondoka, tulidhibiti njia zote za kutokea nje ya nchi kuanzia viwanja vya ndege, bandari mpaka stendi za mabasi na hasa kule mipakani, kila basi linapekuliwa kwa umakini na kila abiria anafanyiwa uchunguzi wa kina kwani anaweza kujibadilisha sura na akaondoka. Kwa jinsi hiyo hatujapata jibu kama amekamatwa,” Chiba alieleza.



    “Kwa hiyo yupo,” Scoba akaeleza.



    “Kamanda Amata ana jeraha yampasa kupumzika kwani hawezi mikikimikiki kwa sasa,”



    Jasmine aliliambia jopo, ndipo na wengine wakapata kujua kuwa Amata alikuwa amejeruhiwa.

    Wote wakageuka kumtazama kwa huruma.



    “Alikwambia nani, hii show tunaingia wote jukwaani na lazima mtu huyo akamatwe ndani ya saa 24 kutoka sasa. Hata kama ni kukodi vifaru, tutakodi na kuchimbua eneo lote lile,” Amata akawajibu.



    “Ndio maana nakupenda mpenzi,” Gina akamalizia.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Art of War,” Kamanda akamwambia Gina huku akimtazama usoni kisha wote wakacheka.

    Simu ya mkononi ya Madam S ikaita, akaitazama kwenye kioo na kukunja sura kisha akawatuliza kwa ishara ya mkono na kuiweka sikioni ile simu wakati huo Chiba akiwa tayari keshapachika kifaa chake cha kurekodi sauti hiyo.



    “…na kwa sababu mnajifanya mnajua, sasa sikilizeni redio usiku huu mtaelewa kuwa sitaki kutaniwa…”



    Na ile simu ikakatika baada ya sauti hiyo ya mkoromo kukoroma sikioni mwa Madam S. Private number! Akawaza Madam S na kuishusha taratibu.



    Sura ya Kamanda Amata ikabadilika na kuwa sura ya kazi, akatazamana na Madam S wasipate jibu wakatia huo, Chiba aliondoka na simu ya Madam S na kuingia katika chumba chake cha kazi kuifanyia uchunguzi simu hiyo ilipigwa kutoka uelekeo gani.



    “Pancho Panchilio au kibaraka wake, hawezi kuwa mwingine, atapatikana tu,” Chiba akajibu.



    “Hawana maisha marefu, Sun Tzu ametufundisha kwenye Art Of War ‘If the enemy leaves  door open, you must rush in…’” (Kama adui ameacha mlango wazi, fanya hima kuingia) Amata akasema huku akijiweka vyema kitini, “adui yetu kaacha mlango wazi, tusichelewe!” akamalizia. Madam S akatikisa kichwa na kumtazama Gina.



    “Gina, fanya kazi niliyokupa sasa,” akamwambia binti huyo. Gina naye hakuchelewa akasimama na kuondoka katika chumba hicho.





    Saa 7 Usiku…



    Hali ya hewa ya Jiji la Dar ilikuwa tulivu kabisa, giza nene lisilo na mbalamwezi lilitawala wakati Gina akiegesha gari lake eneo la Upanga katika barabara ya Ally Hassan Mwinyi, karibu kabisa na hoteli ya Palm Beach. Kamanda Amata akiwa ameketi upande wa kushoto katika kiti cha abiria, aliiweka vizuri bastola yake tayari kwa lolote.



    “Vipi?” Gina akauliza.



    “Sina utani na mtu sasa hivi,” Amata akamjibu Gina, kisha wakateremka garini, “vijana wako wapi?” akauliza.



    “Wameshafika tayari wapo kwenye pozisheni zao,” Gina akajibu. Kisha wakavuta hatua kuielekea hoteli hiyo ambayo siku hiyo ya wikiendi watu walijazana kwa starehe mbalimbali.



    *   *   *



    KAMBA SEBULE alikuwa akifurahia maisha ndani ya ukumbi mkubwa uliokuwa na michezo mbalimbali ya kujipatia pesa. Akiwa na walinzi wake binafsi, alijumuika pamoja na wengine wengi waliokuwa hapo kutafuna maisha. Si kwamba walifanya hivyo kwa sababu ya ukata ili wajipatie pesa ya kujikimu, la, walikuwa na ukwasi wa kutosha, walijumuika ili kuzichezea na si kucheza. Furaha haikuweza kujificha katika nyuso za wote waliozunguka eneo hilo huku wadada warembo wakitumbuiza kwa muziki uliokuwa ukipigwa mubashara kutoka jukwaani, wakicheza kwa minenguo ya Kikongo huku wakiwa wamevalia nusu utupu. Mijanaume yenye uchu ilikuwa imezunguka jukwaa hilo lililojengwa juu kidogo na kutazama wadada hao wakifanya mambo yao hadharani, macho yakiwatoka pima kana kwamba wakitazamacho kitaanguka ili wakigombanie.



    Kamba Sebule, kigogo wa serikali, aliendelea kuburudika na rafiki zake waliofanana na yeye kiuchumi, waliokuwa wakicheza ‘poker’ na wakati mwingine ‘Lucky Wheel’ na kufurahia pesa waliyokuwa wakiivuna. Mmoja wa walinzi wake alionekana kuchezwa na machale kidogo, akatoa kitu kama picha katika mfuko wake wa shati na kuiangalia kwa sekunde kadhaa kisha akairudisha mfukoni, na kumwinamia Kamba Sebule, akamnong’oneza kitu.

    *    *    *



    Gina na Amata walijichanganya ndani ya ukumbi huo, wakipenyapenya katia ya watu wengi waliokuwa wakienda huku na kule na macho yao yakifanya kazi ya ziada ya kutazama huyu ni nani na nani ni huyu.



    “Nahisi wametugundua,” Gina akamwambia Amata.



    “Ndiyo nimeona, yule mtu inaonekana ana picha ya mmoja wetu, kwa nini katembea nayo?



    Lazima tuipate na tujue kaipataje,” Kamanda Amata akamwambia Gina.



    “Wanatutazama,” Gina akamwambia Amata.



    “Ndiyo, ondoka nenda chooni, wakija nami nakuja hukohuko,” Amata akatoa maelekezo na Gina akayafuata bila kuhoji. Akavuta hatua kuelekea chooni, kama alivyofikiria Amata ndivyo ilivyokuwa.



    Daima akili zetu zipo namna hii! Amata akajiambia kisha akendelea kuweka jicho lake kwa watu hao. Yule mlinzi mmoja akambonyeza mwenzake na wote wawili wakatoka kuelekea kule chooni wakamwacha Kamba Sebule na mlinzi mwingine mmoja, wakiahidi kuwa wanarudi muda tu. Kamanda Amata naye akajinyanyua taratibu na kuelekea upande uleule.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Gina aliingia katika choo cha wanawake, ndani ya kichumba kidogo, akafungua maji na kusimama kando, dakika moja ikapita, akafunga maji, akajiweka tayari huku akipiga mruzi na kufuatisha wimbo uliokuwa ukisikika kutoka ukumbini. Akafungua mlango kutoka nje na ndipo alipokutana na vijana hao. Gina akajifanya kupita katikati yao kama hajui kinachoendelea.

    Mmoja wa wale walinzi akamzuia kwa kifua chake kipana asipite, Gina hakuuliza wala hakupoteza muda, alimsukuma kando akadakwa na Kamanda Amata kwa nyuma. Amata akamgeuza na kumpiga kichwa kisha akamdaka kolomeo kwa kono lake la kulia na kumfanya mtu huyo aanze kutapatapa kutafuta pumzi.



    Gina aligeuka ghafla na kumchapa ngumi nzito yule wa nyuma yake, nae akajibu shambulizi lakini Gina alikanyaga mguu wake ukutani na kuepa shambulizi hilo, alipotua chini alimpa pigo moja la karate lililompata barabara na kumwacha akiweweweseka alipotulia alijikuta mbele ya domo la bastola ya mwanamke huyo. Kamanada Amata aliendelea kumbana kolomeo yule jamaa mwingine huku akimhoji.



    “Nani bosi wako?” Amata akauliza.



    “Kamba, Ka-ka-mmmbbba!” akajibu kwa tabu huku akianza kulegea.



    “Makazi ya Kamba yako wapi?”



    “U-pa-ngggga!”



    “Ofisi yake iko wapi?”



    “Mtaa wa Ka-ka-lu-ttttaaaa namba 25!” akajibu na kuanza kutapatapa kwa nguvu.

    Yule jamaa aliyetazamana na domo la bastola ya Gina akajaribu kutafuta mbinu ya kujiokoa wakati huo nje ya choo hicho walisikika watu wakiingia kujisaidia. Gina akashusha bastola yake na kuifutika kiunoni, kosa. Yule jamaa akarusha ngumi iliyompata Gina usoni na kumyumbisha kiasi fulani. Ngumi ya pili Gina akaudaka mkono na kuuzungusha kwa nguvu.



    “Aaaaaiiiiigggghhhh!” akatoa yowe la uchungu, huku mifupa ya mkono ikiachana, akamrudisha mbele na kumpiga futi la kwenye korodani kabla hajajibwaga chini na kujipigiza kwenye sinki la kunawia maji na kutulia sakafuni akikoroma. Kamanda Amata akafungua mlango wakatoka na Gina na kuwaacha watu wakitukana na kusonya huku wakiingia ndani kujisaidia.



    “Mama majambaziiiiiiiii!” ilisikika sauti ya kike ikipiga yowe kutoka chooni.



    Pameharibika! Kamanda akawaza na moja kwa moja akamshika mkono Gina na kurudi ukumbini, hali ya taharuki ikaugubika ukumbi huo, walinzi wa hoteli wakaingia kuangalia kulikoni.



    “Ita vijana,” Kamanda akamwambia Gina, naye akachomoa simu yake ya upepo na kuwaita waingie.  Moja kwa moja walisimama kwenye ile meza ya ‘poker’.



    “Upo chini ya ulinzi, Kamba Sebule,” Gina alimwambia huku Kamanda Amata akiwa kasimama pembeni, bado kulikuwa hakujatulia. Mheshimiwa huyo alitulia kimya macho yake yakiwa juu ya ile meza yakiangalia karata zilizopangwa juu yake.



    “Wewe ni nani, na una mamlaka gani ya kuniambia mimi hayo?” Kamba akauliza bila kugeuka.



    “Tii sheria bila shuruti, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiyo iliyonipa malaka hayo,” Gina akaunguruma.



    “We mtoto wa kike hivi ushawahi kuzaliwa? Hujui I ni sawa na baba yako mzazi?” Kamba akalalama.



    “Kamba Sebule sitaki kutumia nguvu kwani nimekuja na nguvu kubwa kuliko unavyofikiri,”

    Kamba Sebule akageuka taratibu na kukutana na sura ya Kamanda Amata, hakuamini kama ni mtu kweli au mzimu. Akarudisha macho kwa Gina na kukutana na sura ya mwanamke mrembo lakini isiyoonesha hata chembe ya tabasamu. Akatanabahi kwa vijana walioingia ndani ya ukumbi kwa dakika moja iliyofuata, walikuwa na nyama za kimazoezi, fulana zilizowabana zilidhihirisha hilo.



    “Huna adabu msichana!” Kamba akaunguruma na kuchomoa simu yake lakini kabla hajaiweka sikioni ilinyakuliwa na Amata, na alipotaka kuleta tabu Gina alimtandika pigo moja uso na kumrudisha mezani akiwa hoi.



    “Tia pingu!” akawaambia vijana wa polisi nao wakatekeleza na kuondoka naye.







    05

    “Kijiji chote kimeteketezwa kwa moto!” Mkuu wa nchi alisikika akiongea kwa kututumka, mbele yake alikuwa Madam S amesimama.



    “Huyo ni shetani! Lazima utawala wake usambaratishwe na watenda mema,” Madam akajibu.



    “Sikiliza Sellina,” akasimama kwa msisitizo, “Nahitaji uchunguzi wa siri na ikiwezekana huyu mtu akamatwe,” akasisitiza.



    “Najua wajibu wangu mheshimiwa, mzuie Waziri wa Mambo ya ndani asitumie nguvuy kubwa, acha mimi nikafanye kazi, ikifika wakati wa kuhitaji vijana wake nitakwambia, ila kwa sasa waache wale wa Bagamoyo kwa kuwa ni eneo lao, naondoka sasa,” akamaliza Madam S na kutoka mle ofisini.



    Akiwa ndani ya gari yake akampigia Amata na Gina wakutane ofisi ndogo, akaitazama saa yake tayari ilitimu saa 4 usiku.



    Kweli kazi za serikali ni za kujitolea, watu wamelala sisi tunahangaika! Akawaza mwenyewe huku akiliacha lango la Ikulu na kuelekea afisini kwake.







    KITUO CHA POLISI CHA SULENDER BRIDGE



    “Bagamoyo, Ba- ba –gamo-yo koh! koh! koh!” Kamba Sebule aliongea mengi baada ya kipigo cha polisi kukolea mwilini mwake kwa amri ya Kamanda Amata.



    “Bagamoyo kubwa, sehemu gani?” Kamanda akauliza.



    “Si nime-wa-jib…”



    Mkanda wa jeshi ukatua mgongoni mwake na kumletea maumivu makali.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Unafikiri tunacheza hapa? Tuambie ni kijiji au ni sehemu gani?” mmoja wa polisi aliuliza.



    “Kisi-wa-wa-ni, Kale-b-be” mwishowe akatamka ijapokuwa kwa tabu kidogo.



    Kamanda Amata akatikisa kichwa juu chini huku akimtazama Gina. Simu yake ikaanza kufurukuta mfukoni akaitoa na kutazama ‘Madam S’ ilijiandika juu ya kioo, akaingiza tarakimu fungushi na kuiweka sikioni.



    “Tukutane wodini haraka mama anaumwa Tena Sana Aisee,” ilikuwa ni ujumbe wa sauti aliyoutuma. Akageuka na kumtazama Gina, kisha akarudisha macho kwa wale vijana wa polisi.



    “Sasa muhifadhini huyu mpaka nitakapowapa amri nyingine, sisi tunatoka,” akawaambia wakati wakiondoka na kuingia garini.

    *    *    *



    OFISINI NDOGO



    Ndani ya ofisi hiyo Madam S alikutana na vijana wake wote watano, aliwapa ujumbe aliyoupata kutoka Ikulu ambako kama kawaida yake alikwenda kupeleka ripoti ya siku. Kwa harakaharaka alionekana hayuko sawa kwani alikuwa akifanya vitu na kuongea kwa harakaharaka.



    “Kijiji cha Kitopeni kimevamiwa na kuchomwa moto huku raia wakipigwa vibaya leo jioni hii,” madam aliongea harakaharaka huku akiwa kasimama wima.



    “Kitopeni Bagamoyo?” Gina alidaka kwa swali.



    “Ndiyo!”



    Wakatazamana kisha wakarudisha macho kwa Madam S, hakuna aliyekuwa na swali wala  kuongea ila ndani ya macho yao kulibaki na mshangao wa dhahiri kabisa. Walikijua kijiji huki vema kwa sababu ndipo walipomuokota Scoba majuma kadhaa nyuma.



    “Kitopeni ndo wapi?” Amata aliuliza.



    “Ni usawa ule ambao ndege yenu ilidunguliwa,” akajibiwa na Madam S.



    “Bila shaka ni wao, haina kupoteza muda TSA Kazini,” Chiba alisema huku akinyanyuka na kuungwa mkono na wenzake.



    “Bila shaka, nimezuia polisi wa huku kufika kule kwanza nataka sisi tuingie kwanza ili tufanye uchunguzi wa awali ambao kwetu ni uchunguzi wa msingi wa kumjua mhalifu,” madam S aliwaambia kisha kila mmoja akaanza kuchukua kinachomfaa katika stoo iliyojengwa ndani humo.



    “Kamanda Amata, una jeraha, halijapona, ni vyema usifanye mikiki mikiki yoyote ile,” Jasmine alimwambia Amata.



    “Hapana, wacha niende, kama ni Pancho basi mara hii hatakiwi kuishi, huu ni uhalifu mkubwa sana haijawahi kutokea kwenye historia ya nchi hii,” Amata akaunguruma.



    Dakika kumi zilizofuata, Land Cruiser V8 ilifuatana na Range Rover zote zikielekea Kitopeni, ndani yake kulikuwamo na hao vijana watano. Gari ya kwanza alikuwapo Amata, Chiba na Gina ambaye aliukamata usukani na ile ya nyuma alikuwamo Jasmine na Scoba pamoja na Madam S. mwendo waliokuwa wakipita nao ulikuwa si wa kawaida. Kama wananchi walizoea kuishangaa misafara ya viongozi kwa mwendo kasi basi hii ilikuwa funga kazi ila hakuweza kuona kwa sbabu tayari ilikuwa usiku.



    Kila mmoja alikuwa akiwaza lake kichwani, ukimya ulikuwa ukitawala kila nukta katika gari hilo ambalo Chiba alikuwa akiliongoza.

    KIJIJI CHA KITOPENI



    Usiku huu ni moshi na vilio ndivyo vilivyosikika katika eneo hilo.



    Haya mambo nilikuwa nayaona kwenye filamu tu kumbe yapo hata huku siku hizi! Amata akawaza huku akiendelea kula karanga zilizokuwa ndani ya chupa ndogo.



    “Na we na makaranga yako!” Gina akaalalama.



    “Makaranga jina la mtu!” Amata akajibu huku akiendelea na shughuli yake. Muda kidogo wakaegesha magari yao na kuteremka chini, darubini vifuani mwao, bastola viunoni. Walikuwa tayari kwa lolote.



    Wananchi wa kitopeni walikuwa wamejikusanya pamoja, wengine wakiomboleza vifo wengine wakiwa hawana makazi na wengine maumivu makali ya majeraha waliyoyapata katika shambulio hilo.



    TSA waliteremka kutoka katika magari yao na kuanza kufanya chunguzi zao za hapa na pale kwa kuhoji na kutazama hali halisi ya eneo hilo.



    “Mnasema hao watu walikuwa wangapi?” Amata alimuuliza mmoja wa wanakijiji aliyeonekana kujishughulisha sana kuwasaidia wenzake.



    “Walikuwa kama kumi au kumi na tano walikuja wakitokea mashambani huku,” yule kijana alieleza.



    “Tuliwaona wanaibuka kule baharini sisi tukakimbia,” mmoja wa watoto aliyekuwa hapo alisema. Kamanda Amata akiwa na Chiba na Madam S walisikiliza maelezo ya wahanga wote walioweza kuongea, kisha wakaitana pembeni.



    “Sikia Chiba na Amata hawa bila shaka wamekuja kwa kupiga mbizi,” Madam aliwaambia.



    “Kwa maana hiyo hawa jamaa wanaweza kuwa na makazi eneo hilihili,” Chiba akaongeza.



    “Kisiwa cha Kalebbe,” Kamanda akawaambia kisha wakamwita tena yule kijana na kumwomba awatajie majina ya visiwa vilivyo karibu na eneo hilo. Akawatajia kwa majina na kuwaonesha kisiwa hicho cha Kalebbe ambacho kilikuwa katikati ya visiwa vingine.



    “Mnafikiri pale atakuwa anaishi mtu? Sio rahisi kisiwa kile kule ndio kuna mtu kajenga nyumba yake ndogo,” yule jamaa akaonesha kisiwa ambacho kina jengo la kawaida tu na lilionekana vizuri kwa darubini walizokuwa wakitumia vijana hawa.



    “Ok,” Madam akaitikia na kumwacha yule kijana kuondoka.



    “Madam, baada ya kumbana yule Kamba Sebule kule polisi kasema wana maskani yao kisiwa cha Kalebbe, so nafikiri sasa ni kuanza uchunguzi wa kisiwa hicho mara moja. Cha muhimu hapa tuache polisi wafanye kazi na sisi tuondoke tukajipange vyema, wasijue kama tumeingia hapa,” Kamanda akatoa maelekezo.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Sawa, twendeni tukapige kambi Hoteli ya Ocean Breeze, na afisi yetu itahamia hapo mpaka kieleweke…” Madam akawaambia na wote wakaingia kwenye gari na kuondoka huku wakiacha polisi wakiendelea na nyajibu zao.

    HOTELI YA OCEAN BREEZE – BAGAMOYO



    Ni hoteli kubwa ya kifahari, iliyojengwa kandokando ya Bahari ya Hindi. Jingo hili lenye ghorofa sita lilizungukwa na miti mirefu na mizuri sana iliyotengeneza kivuli kinene wakati wa jua. Usiku huo Madam S na vijana wake waliwasili tayari kwa malazi ya siku hiyo. Katika meza ya mapokezi kila mmoja akajitambulisha kwa jina la bandia na kuchukua vyumba kwa mapumziko huku akili yao ikiwa kazini kwa muda wote.



    Kijua cha asubuhi kilipochomoza pande za Mashariki kilimkuta Amata na Gina nje kwenye kibaraza cha ghorofa ya nne ya hoteli hiyo ambayo ilitazamana na Bahari ya Hindi na hapo ndipo wakagundua kuwa ipo karibu na bandari ya mji huo mkongwe, Pumbuji ya zamani, Bagamoyo ya sasa. Pembeni ya meza yao kulikuwa na darubini kubwa ‘Oberwerk’, yenye nguvu, ilikuwa na urefu wa inchi 24  iliyosimamishwa kwenye stendi madhubuti. Huku wakiburudika na kinywaji lakini akili zao zilikuwa katika kisiwa cha Kalebbe ambapo ndipo hasa walipoamini adui wao alipo. Juu ya meza hiyo hiyo kulikuwa na karatasi ambayo kwayo walikuwa wakiandika vitu fulanifulani wanavyovielewa wao.



    “Tutaingiaje pale?” Gina aliuliza.



    “Simple tu, ama tutasubiri giza la leo au twende kibabe mchana huu. Ila wazo zuri ni kuuchukua mchana huu na kukichunguza kisiwa kile ili tujue in and out, si ajabu tukapata njia nyepesi sana ya kufika pale kuliko tunavyofikiri”.



    Gina akatazama saa yake ilikuwa tayari saa tatu za asubuhi, jua linazidi kwenda juu na joto nalo likiendelea kushika hatamu. Simu ya Amata ikaita pale mezani.



    “…hello… Madam!” akaipokea.



    “…vipi kamanda, kuna lolote huko?”



    “…yeah, tunaangalia bado lakini hatujapata ufumbuzi ila taratibu tutapata,”

    “…ok, kazi njema, niko na vijana hapa. Tunawaomba mfanye kazi tu na si vinginevyo,” kisha wote wakacheka.



    Amata akainuka na kuingia chumbani akachukua simu na kupiga mapokezi akomba kuletewa vinywaji. Dakika tatu baadae, kijana aliyevalia nadhifu kabisa, nguo za kitamaduni akaleta vinywaji hivyo mpaka pale walipoketi.



    “Asante sana,” Kamanda akamshukuru.



    “We unaitwa nani?” akamwuliza.



    “Naitwa  Nassoro,”



    “Nassoro unajua kisiwa cha Kalebbe?” Kamanda akauliza. Nassoro akamtazama kwanza kabla ya kujibu swali hilo.



    “We cha nini?” akajibu kwa swali.



    “Aaaaah! Usiwe kama Watanzania wengine kwa kujibu swali kwa swali. Napenda kwenda kukitembele kama utanipa maelezo zaidi juu yake, au kama mna vipeperushi vyake,”



    “Kile ni kisiwa cha mashetani, watu huwa hawaendi kule,” Nassoro akajibu kwa kifupi.



    “Nahitaji kwenda,” Kamanda akamwambia Nassoro.



    “Sawa, karibu sana, si nimekwambia kisiwa cha mashetani, hivyo huwa yanaenda mashetani tu,” Nassoro akajibu na kuondoka.



    Gina na Amata wakatazamana. Anajua kitu huyu! kila mmoja akawaza sawa na mwenzake. Amata akainua mkono na kubofya saa yake hapa na pale kisha akaisogeza karibu na kinywa chake.



    “…muweke jichoni, amevaa shati la kitenge na suruali nyeusi na kofia ya kitenge, ni mwenyeji wa hapa tulipo…”



    “…copy…” Chiba akajibu kwa njia ileile.



    Mara kwa mara Gina alikuwa akisimama na kuiendea ile darubini na kuchungulia ndani yake kuona kama kuna lolote geni, na alipomaliza kuchungulia alibonyeza kidubwasha fulani na kupiga picha ya hicho anachokiona, na ile taswira ilisafiri mpaka kwa Chiba kwenye mashine ndogo mfano wa simu na wao waliweza kuitazama vizuri na kuangalia kama kuna mabadiliko yoyote.

    Mara hiyo saa ya Kamanda Amata ikaanza kumfinya, akaitazama kwenye kioo na kubofya mahala fulani kisha akapachika kifaa chake sikioni na kusikiliza.



    “…yuko jichoni, kaingia mapokezi, anatumia simu ya mezani…” Chiba akamwambia Amata.



    “Sawa! Jaribu kudukua chochote katika hilo…”



    Chiba akaondoa ukurasa wa juu katika chombo chake hicho na kupachika vizuri vifaa vya masikioni, akabofys hapa na pale juu ya kioo na kujaribu kutafuta mawimbi ya simu hiyo kama ataweza kuyapata.



    “…. ko wawili, wanatumia darubini kubwa kutazama kisiwa (…) hapana sijui kabisa (…) sawa sawa, nitahakikisha hilo!”



    Chiba aliweza kukamata mawasiliano ya simu hiyo kwa urahisi sana tafauti na alivyofikiria, akatikisa kichwa na kumtumia taarifa Amata kwa njia ya simu yao.



    “…tegemea ugeni…” Amata akamwambia.



    Wakakata mawasiliano, Amata akarudisha macho kwa Gina.



    “Vipi?” Gina akauliza.



    “Poa,” Amata akajibu na kusimama, akavuta hatua chache kuingia chumbani, akauelekea mkoba wake na kuchomoa bastola moja, akaijaza risasi za kutosha. Nyuma yake akahisi kama kuna mtu kasimama, akahisi mikono ikigusa mabegani, hakugeuka kwani ulaini wa mikono hiyo alishajua ni nani anayemgusa.



    “Vipi ushaanza kufikiri kuua!”



    “Akili yangu tayari ishaanza kuzunguka, nahisi kutokea hatari ndani ya muda mfupi ujao, jiweke tayari nawe pia,” akamwambia Gina na kumgeukia. Gina akaweka mikono yake kiunoni mwa Amata.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nimemiss!” akamwambia.



    “Sio wakati wake, au na wewe ni mmoja wao unataka kunilaghai kwa mapenzi?” Kamanda akajibu na kujitoa katika himaya ya Gina.



    “Ningekuwa mmoja wao ningeshawateketeza nyote mpaka sasa, hujui kama sdui mbaya ni yule aliye miongoni mwako?” Gina akamwambia huku akimwachia kijana huyo kama alivyotaka. Amata akaipachika bastola yake kiunoni “mwanamke unamaneno wewe ka mtoto wa Kizaramo,” akasema huku akiiendea ile darubini, akaweka macho yake pale na kutazama tena. Mara hii kitu kipya kikaonekana, kwa mbali aliona kitu cheupe katikati ya bahari.



    Nini kile! akajiuliza na kukiweka vizuri katika muonekano sawa. Boti, ilikuwa ni boti iliyoonekana kuja kwa kasi na kutimua maji hayo kuyafanya kuwa meupe, akabonyeza kile kitufe na kupiga ile picha. Akaendelea kuangalia ile boti iliyokuwa ikisogea kwa kasi, sasa aliweza kuiona vizuri, ndani yake kulikuwa na watu watatu, wanaume wawili, waliovaa nguo nyeupe za kisasa, mmoja alikuwa akiongoza boti hiyo na mwingine alikuwa nyuma kabisa. Katikati yao kulikuwa na mwanadada mrembo sana aliyeketi kwenye kiti na bilauri iliyojaa kinywaji, akabonyeza tena kile kitufe na kuisafirisha ile picha.

    *    *    *



    Kifaa kile cha Chiba kikatoa ukelele hafifu, akakinyakuwa na kutazama, picha.



    “Ugeni kama ulivyotabiriwa,” Chiba akamwambia Madam S huku akimpa kile kimashine ambacho kilimwezesha kuona zile picha vizuri. Muda huohuo akamwona yule kijana akitoka katika chumba fulani na kuelekea nje, Madam S akamwita kwa mruzi, kijana akageuka na kusogea pale mezani.



    “Nahitaji vinywaji kijana,” akamwambia.



    “Oh! Samahani kuna mgeni nampokea hapo gatini naomba nikuitie mhudumu mwingine,” Nassoro akajibu. Madam S akamshika mkono kwa nguvu na kumkazia macho.



    “Kwa nini unataka kupoteza bahati kijana,” akamwangalia juu mpaka chini.

    Nassoro akajikuta njia panda, akashindwa kuamua, alijuwa wazi kuwa kumkatalia huyu mama kama mteja haiwezekani na kutokwenda kumpokea huyo mgeni nako ni jambo linguine lisilowezekana.



    “Ok, niitie mtu mwingine,” Madam akamwambia na kumwacha. Nassoro akaenda na kumwita mwhudumu mwingine wa kike ili amsikilize Madam. Yule mwanadada akaifikia meza waliyoketi Madam S na Chiba.



    “Samahani, huyo anayekuja huko ni mgeni gani?” akamwuliza yule mhudumu badala ya kumuagiza vinywaji.



    “Malkia, Malkia wa Kalebbe!”



    “Malkia?” Madam akauliza na wakati huohuo yule mwanadada aliyejulikana kama malkia akaingia akiwa anafuatana na Nassoro na moja kwa moja akaenda kuketi kwenye meza iliyopambwa maua mazuri kabisa. Kulikuwa na siti mbili moja ikabakia wazi. Vazi alilovaa mwanadada huyo ndiyo kilikuwa kivutio kingine, alivaa bikini nyeupe na juu yake akavaa vazi lingiine jeupe jepesi kabisa lililokuwa wazi sehemu ya mbele na kuruhusu mwili wake kuonekana.



    Nassoro akasogeza vinywaji pamoja na kibweta cha kuwekea jivu la sigara, huyo malkia mwenye mwili wa kisichana zaidi aliketi na kukunja nne huku akiwashiwa sigara na kijana huyo na kuanza kuvuta taratibu.



    Madam S akamtumia ujumbe Kamanda Amata juu ya huo ugeni. Haikupita dakika moja, Kamanda Amata akajitokeza kutoka katika ngazi na kuvuta hatua fupifupi kuielekea ile meza. Akiwa ndani ya suti nadhifu nyeupe, shati jeupe na tai nyeusi.







    *    *    *



    “Bila shaka hautajiuliza mengi kwa mimi kuketi mbele ya mwanamke mrembo kama wewe, Malkia wa Kalebbe, hakika Mungu anajua kuumba kwa maana jinsi ulivyo hakuna mwanaume rijali atakayepita mbele yako bila kujikwaa hata kama sakafu ni ya marumaru,” Amata akaanza swaga na kuketi huku akichukua matunda madogo ya strawberry na kuyatia kinywani kisha kuyatafuna taratibu.



    Mwanamke huyo alijikuta akiangua kicheko cha mwaka kwa maneno hayo matamu na ya kufurahisha. Hakuwahi kukaliwa mbele na kijana asiye na hadhi kama huyu, hili ndilo haswa lililomfanya acheke.



    “Hakika kuna wanaume wameumbwa kufurahisha wanawake, lo, ulifikiri nini kuzungumza yote hayo?” akauliza huku bado akiendelea kucheka. Nassoro, mhudumu mahsusi wa malkia huyo akawasili pale mezani na kumtaka radhi Amata kuiacha meza ile.



    “Oh, asante Nassoro, lakini mwache, mwache kanifurahisha sana huyu, mpe kinywaji tafadhali,” malkia akamwambia Nassoro naye akafanya hivyo. Ingawa juu ya meza ile kulikuwa na kinywaji ambacho bado kilijaa pomoni, lakini Amata aliletewa kinywaji kingine kabisa, kikawekwa mezani na kumiminwa kwenye bilauri safi, akaiinua na kuipunga hewani kisha yule malkia naye akafanya hivyo wakagonga cheers kwa afya.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nitasikia raha sana nikikunywesha japo kidogo,” Amata aliendelea na ubembe wake.



    “Oh! No! kinywaji ni kwa ajili yako, enjoy little puppy!” akamwambia, Amata akaiinua na kukinywa chote kisha akaishusha ile bilauri mezani.



    “Waoh, you are so strong man,” (wewe ni jasiri)



    “Yes I am,” (ndiyo) Amata akajibu.



    “Mmmmh you are smart!” Yule mwanamke akaendelea kumsifu Amata.



    “Kawaida yangu!” akamjibu.



    “Hebu nambie huko Dar, unafanya kazi gani?” akahoji.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog