Simulizi : Hati Feki
Sehemu Ya Nne (4)
NAJUA Aminata lakini lazima tuanze hili jambo mapema kabla hawajagundua mipango mingine hivyo ni lazima nikutane na Max mara moja ili tujue tutawafanyaje,” John alimhakikishia Aminata juu ya hilo.
“Sawa mpenzi lakini nahofia sana maisha yetu, na mi sitakuacha tutaenda wote kila mahali ukifa na mimi nife hapo hapo,” Aminata alimfariji John.
“Aminata, nimekumbuka kitu,” alisema John.
“Kitu gani tena mpenzi?” Aminata aliuliza.
“Mi naona ungeliacha hili suala kwetu sisi. Sitaki mtoto wetu apate shida ya kuwa bila ya wazazi. Nakuomba usiende. Tuachie mimi na Max. Najua tutaweza,” John alijaribu kumshawishi Aminata ili asijihusishe na mpambano ambao alitaka kufanya na Max na Antony bila ya kuwashirikisha wengine.
“Siwezi John, sitakaa kwa hofu juu yako, isitoshe huu mpango ni wa kwetu pia. Unakumbuka ni Mosses pia aliyewaua wazazi wangu na ndugu zangu? Mi sitaweza John. Isitoshe nna hasira sana na huyo Mosses. Najua hajui alilolifanya kwa wazazi wangu limeniuma kiasi gani. Sitakubali nimwone akiendelea kutanua wakati mi nna hasira na maumivu moyoni. Lazima nipambane nao. Bora nife na hata ukinkatalia John.”
“Lakini Aminata, huoni tukipotea wote mtoto atapata shida?”
“Kweli John lakini mi sitaweza kukaa mwenyewe kusubiri kama hutaki kwenda na mimi nitakufuata,” Aminata alimkaripia John kumzuia asijaribu kumwacha kila aendapo.
“Aminata unajua kwamba hili sio jambo la kufanyia mzaha? Wewe unajua tuna mtoto, mimi nikifa unadhani ataishije maisha ya kuwakosa baba na mama? Mimi najua nitaweza pamoja na Max na Antony. Naomba nikuwakilishe maana jambo hapa ni kummaliza Mosses.”
“John kwani hata nisipoenda maisha yangu yatakuwa hatarini kwa vile wameshajua mimi ni mke wako, hivyo popote watakaponiona watataka kunikamata,” Aminata alimwambia John.
“Ila sitakuwa na wewe, nitakupa ramani ya kila tunapokwenda ili kama tukizidiwa utusaidie. Sawa mpenzi.”
“Sawa mpenzi.”
Saa nane na nusu usiku wote walikuwa wamekwisha lala. Asubuhi John alikuwa ndiye wa kwanza kuamka na kwenda moja kwa moja hadi sehemu ya mapokezi kwa lengo la kupiga simu. Alitaka kuwasiliana na Max. alitaka kumjulisha kule walipo ili aweze kuwafuata na gari.
Simu iliitikiwa na Max ambaye alionekana kushtuliwa toka usingizini pasipo kuamini kwamba aliyempigia alikuwa ni John.
“Haloo Max mimi John, njoo mshikaji wangu, hapa Mainland Hotel mida hii niko na Aminata. Siko fresh mshikaji wangu njoo na nguo za kubadilisha, mwambie shemeji aje na nguo amsaidie Aminata tuweze kutoka hapa. Tafadhali naomba usimjulishe mtu yeyote juu ya hili ila we njoo mengine nitakuambia tukishafika kwako. Naomba pia uje na pesa ya kulipia tupo gesti na chakula,” wakati huo Max yeye alikuwa akimsikiliza John kwa makini zaidi ili ajue nini cha kufanya.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Sawa kaka nimekupata, nipe muda kidogo nitakuwa hapo na shemeji,” Max alifanya kama alivyotakiwa, alimwambia kila alichosikia Michelle ambaye alipatwa na woga. Waliharakisha asubuhi hiyohiyo mapema na kuwafuata walipo.
Walikuwa wamepaki gari nje ya Mainland Hotel tayari kumchukua John na Aminata. Alifika pamoja na Michelle ambaye walikaa pamoja kwa kipindi kirefu bila ya kufunga ndoa.
Michelle alitoka na mzigo wa nguo katika begi na kufuatana na Max mpaka ndani sehemu ya mapokezi, waliulizia na kuruhusiwa kuingia. John na Aminata walikuwa wako chumba namba 143.
Max na Michelle waligonga na kufunguliwa na John.
“Haa! John ni nini nkilichokusibu hivyo shemeji yangu?” Michelle ndiye aliyekuwa wa kwanza kuhoji mara tu baada ya kuingia ndani.
“Karibuni, Max na Shemeji Michelle, is a long story my friends naomba kwanza tuondoke hapa nitawapa kisa kizima huko kwako. Nadhani umekuja na ule mzigo niliokuagiza Max?” alihoji John baada ya kuwaomba wakazungumzie jambo hilo nyumbani.
“Bila shaka John tumekuja nao huo hapo kwa shemeji yako,”
Mishelle aliukabidhi ule mzigo wa nguo kwa John. Wakati huo Aminata alikuwa ameingia bafuni kuoga tayari kwa safari ya kurudi nyumbani. Wakati John akiwa anawakaribisha Max na Michelle.
“Aminata pole sana japo sijajua lolote ila hali halisi inaonyesha hamkuwa katika hali yenye ushwari,” aliamka Max kutoka katika kiti alichokuwa amekaa kumsalimia Aminata.
“Kwani John hajawaelezea yaliyotokea shemeji?” alihoji Aminata.
“We mjeshi gani unataitiwa,” Max aliyemfahamu vizuri Aminata alimtania.
“We acha tu Max, hali ilivyokuwa si mchezo. Kwani hujaelezewa bado na John.
“Hapana Aminata ila ameahidi kutusimulia pindi tutakapofika nyumbani kwangu,” John na Aminata walikuwa tayari wameshavaa, John alichukua kiasi cha pesa alicholetewa na Max.
Alilipia gharama zote za hoteli kuanzia malazi na chakula. Waliondoka hotelini hapo saa mbili asubuhi kuelekea nyumbani kwa Max.
Waliingia moja kwa moja hadi sebule kubwa aliyoitumia Max wakati wa mazungumzo na wageni wake. Michelle aliamka mara moja kwenda kutengeneza chai.
“Naitamani hiyo stori shemeji naombeni niweke chai kwanza ndiyo uanze kusimulia,” Michelle alimsihi shemeji yake John. John, Max na Aminata waliangua vicheko baada ya kuona Michelle akihaha kutaka stori isianze.
Baada ya dakika tano Michelle alikuwa tayari ameshaandaa chai na wote wakiwa wameshakaribishwa na kuanza kunywa.
“Haya shemeji ruksa sasa, ila samahani sana kwa kukuchelewesha japo sijui kama inanihusu mimi,” Michelle alimsihi shemeji yake John. Michelle alikuwa ni mcheshi sana na aliyependa kufurahi saa zote, alionekana ni mchangamfu wakati wote. Hiyo ndiyo sababu hasa iliyomfanya Max kuvutiwa na binti huyo ambaye kwa sura alikuwa ni mzuri wa aina yake.
“Eebwana ilikuwaje kaka mbona sielewi?” Max aliuliza kwa shauku la kutaka kujua ni nini kilichowapata John na Aminata.
“Dah! Kaka kazi yetu tunayoifanya bila ujasiri umekwisha. Tulijikuta tumezungukwa na kundi la watu. Tumepigwa hapo tukafungwa vitambaa na sijui tulipelekwa wapi,” John alisimulia kisa kizima hadi walipofanikiwa kuwaua wale askari wa Mosses na kutoroka.
Walikaa kimya kama dakika mbili huku kila mmoja akitafakari kutafta namna ilivyokuwa. John alakuwa akiwaangalia huku akiangaliana na Aminata ambaye alionekana kufurahishwa sana na uwepo wa John katika maisha yake. John alitabasamu na kuendelea.
“Isitoshe, wale jamaa kumbe wameungana tena wawili… mmoja ndo yule aliyechukua mgodi wa mzee kwa hati feki tukafanikiwa kuukomboa.”
“Si ndo wao nawafatilia kuhusu kuulipua,” Max alidakia kwani ndiyo kazi aliyopewa aitekeleze.
“Nadhani itakuwa ni wao maana wana kisa na sisi. Antony tutampata wapi wakati huu?” anatakiwa kuwa na sisi kwani kipindi kile alikuja tukafanikisha.”
“Kwani alirudi Nairobi?”
“Ndiyo, na sasa itabidi aje tena,” John alisema huku akichukua kikombe cha chai na kubwia kidogo. John aliendelea kusema.
“Sikuwahi fikiria kutekwa kirahisi namna ile, inaelekea wale jamaa walilifanya mipango yao siku nyingi kuhakikisha kwamba wanatuangamiza, ila walipata wapi picha yangu? Au ya Antony ile?” John aliuliza swali ambalo hakuna aliyejua jibu lake.
“Unajua ni nini John? Max alianza kumwambia John. Mi nadhani hao jamaa watakuwa wameweka makachero wa kutufuatilia pamoja na kuifuatilia serikali ni nini wanafanya pamoja na wewe, si unajua mzee wako alikuwa karibu sana na serikali,” John alitikisa kichwa kuonyesha kwamba amekubaliana na jambo ambalo Max alikuwa amelizungumza.
“Na tena hao hao makachero ndio watakuwa wamewapa hiyo picha yako, inawezekana pia picha yangu watakuwa nayo. Kwani hawajakuonyesha picha za watu wanaowatafuta?” wote walibaki kimya kutafakari nini cha kufanya juu ya watu hao. Vikombe vya chai vilinyanyuliwa na kila mmoja alikunywa kidogo na kurudisha.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hiyo ni katika kufikiria cha kufanya.
“Ebwana kaka kwani watu hao waliwapeleka wapi?” aliuliza Max ambaye bado alikuwa anashauku ya kujua kwamba kina John walipelekwa wapi..
“Dah! Kaka sehemu tuliyoingizwa hata siijui, ila inaonekana ni bonge la jumba alilomiliki yule mkubwa wao ila sijui ipo pande zipi. Inabidi kaka tufanye mpango wa kujua wapi hilo jumba lilipo ili tuweze pia kufanikisha kazi yetu. Mikakati tutaipanga wenyewe, tumtafute Antony kabla ya kuijulisha serikali juu ya mkasa huu kwani serikali imetupa kazi hivyo haipaswi kuonyesha kama tumeshindwa, nna uhakika hii kazi ni ndogo sana,” alimaliza John huku akitikisa kichwa kuonyesha kazi anayoenda kuifanya ni ndogo sana.
“Shemeji ilikuwaje ukaweza kuwatoroka hao jamaa pamoja na wifi yangu?” Michelle ambaye alikuwa na hamu ya kujua stori nzima aliona kwamba hajaridhika na hicho kidogo alichosema John na hivyo alihoji zaidi ili kupewa uhondo zaidi.
“Shemeji, hiyo ilikuwa ni sehemu ya kazi yangu, hata wifi yako hakuamini kitu kilichotokea, sikuwa tayari kupoteza maisha yangu mikononi mwa wale washenzi hivyo ilikuwa ni lazima nitumie mbinu nizijuazo hadi tukapona. Wifi yako alikuwa kashakataa tamaa lakini kilio chake nilikisikiia na hivyo ilinibidi nichukue hatua na kuwafundisha adabu washenzi wale,” John alikuwa anaongea huku akimwangalia Michelle ambaye alikuwa akisikiliza kwa makini na kwa huruma kwa kile kilichotokea.
“Ni wapumbavu sana kwani niliwalaghai wanifungue kamba ili niweze kuagana na mke wangu, hawakujua kwamba ile ilikuwa mbinu mojawapo ambayo hawajawahi kukutana nayo milele hadi mauti yao yalivyowafika siku hiyo. Nilipambana na mmoja nikahakikisha namnyang’aya silaha kisha nikaiwahi na kuwafyatulia risasi wale wawili waliobaki. Hivyo tukapata nafasi ya kuondoka eneo hilo. Nilichukua silaha zao zote na kutoweka nazo.
John alimaliza huku wote wakicheka kwa furaha ya kuwa pamoja baada ya kipindi kifupi cha kutekwa kwa John na Aminata.
“Dah! Poleni sana, kaka umeonyesha jinsi ulivyokomaa na mafunzo tuliyopewa kipindi kile, unakumbuka watu arubaini waliondolewa kwa ajili ya kushindwa zoezi lile jepesi tuu la kumsoma adui amekaaje. Watu kama hao wangekuwa wameshakufa siku nyingi. Ila kaka hongera sana,” Max alimsifia John huku wote wakicheka kwa furaha.
Alimwona John ni mwenye kupokea mafunzo na kuyaelewa haraka kwani hata Aminata alipomfundisha pamoja na Antony walichukua muda mrefu mpaka kumaliza mafunzo. Hata Aminata alishangaa kuona wakielewa mafunzo haraka. Alijua ni kwa sababu ya haraka yao ya kutaka kulipiza kisasi cha mauaji ya baba yao kuchuku mgodi wao.
“Shemu, sasa nimeambiwa nisiende, unadhani wawili mtaweza?” Aminata aliuliza huku akinyanyua kikombe cha chai na kunywa. John alisimama na kukaa karibu na Max. alipatwa na aibu baada ya Aminata kusem vile. Hali hiyo ilimfanya Aminata aelewe kwamba anataka kumwambia kuhusu kubaki kwake wasiende pamoja. John alitaka kuongea jambo na Max huku Aminata akimwangalia kwa jinsi alivyokuwa akimsogeleahuku Max akiwa tayari kumsikiliza John.
“Max nadhani sasa tumtafute Antony ili tufanye mipango,” John alimsihi Max kuonesha kuwa alikuwa na shauku ya kupambana na adui zao.
“Ni kweli, na mbona tumeshalizungumzia hilo, Max alisema huku akimwangalia Aminata na kuhisi kwamba kulikuwa kuna jambo linaloendelea baina ya John na Aminata.
“Nitampigia simu aje, nadhani mipango tutaifanyia nyumbani kwangu kesho jioni,” John alisema huku akijaribu kumsisitiza Max kwamba ana nia ya kuwasiliana na Antony ilia je.
“Kwani Antony alisema hatakuja mwanzo?”
“Hapana,” alijibu John.
“Basi mpigie simu ili tuanze hii ishu mara moja,” Max alisema huku John akijitayarisha kumwambia jambo ambalo alijua ni lazima angebembeleza ili Max amwelewe.
“Aminata nataka akae na shemu ili sisi tuende, najua ni kazi yake lakini kwa sasa naomba akae kwanza pembeni tuende mi na wewe,” John ambaye alikuwa amekaa karibu zaidi na Max alimwambia kwa sauti ya chini.
“Kwa nini tusiende naye, unajua anajua mbinu nyingi sana, tuwe naye bana,” Max alimsihi John.
“Hapana, nimemwambia kuwa tunaye mtoto na likitokea baya atatukosa wote. Nimeonelea yeye abaki afu tuende mimi na wewe na Antony.”
“Mi sijajua, kwani yeye alisemaje?”
“Alikataa kabisa, naomba umshauri basi.”
“Mi kukushauri ntakushauri twende naye kwani najua Aminata ni komandoo, anaweza kupambana na matukio mengi ameweza kwa nini hili ashindwe na tena tuko wengi, labda Michelle ndo siwezi nikamwambia aende maana hajui lolote, ila Aminata mi naomba tuwe naye. Kumbuka ni mwalimu wako na anajua zaidi haya mambo.”
“Dah, ila kama ni hivyo tutamwelekeza tulipokwama atusaidie.” John alionekana kutokufurahia kwenda pamoja na mke wake, Aminata. Alitafuta njia yoyote itakayomfanya asiende ili awe karibu na mtoto wao.
“Sawa kama atakuja tu kama msaada. Mi nadhani wawili tukiongezeka na Antony tutaweza.”
“Basi watabaki hapa kwako.”
Max alikuwa anaishi maeneo ya Kijenge. Aliishi pamoja na Mishelle japo hawakuwa wamefunga ndoa.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kwa kuhofia maisha yao kwa kipindi walichokuwa wakiugulia maumivu waliyoypata baada ya kuwekwa nguvuni na Mosses, John na Aminata ilibidi washinde na kulala nyumbani kwa John mpaka kwa kipindi hicho. Habari za kutekwa kwao zilienea sehemu nyingi. Waandishi wa habari na viongozi walifika na kuwatakia hali.
Waliwaeleza ya kwamba hawakujua walipopelekwa wala nani aliyefanya unyama ule. Hivyo hawakutaka polisi wafuatilie ili wao wakamilishe lengo lao baada ya kubaini kwamba baadhi ya viongozi walikuwa wakiwasaidia Steve na Mosses katika harakati zao za kufanya uhalifu kwa masilahi yao na viongozi.
Ni katika kikao ambacho kilikuwa kikizungumzia masuala ya ulinzi na amani nchini. Maofisa usalama wote walikuwepo wakiwemo Max, John na Aminata. John na Aminata walishangaa kuwaona Steve na Mosses ambao hawakuwa wahusika. Max ambaye alikuwa hajawajua alielezwa na John na Aminata.
Yaliyoongelewa huko yalikuwa ni yale yale ya askari kulinda raia na mali zao. Hawakusikia lolote kuhusu uhalifu unaoendelea. Walihisi jamaa wameshaongea na waziri wa ulinzi ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika kikao hicho na ambaye ndiye aliyesisitiza ulinzi wa askari kwa raia.
“Bado… hajaongea kitu kabisa… sijasikia akizungumzia lolote kuhusu uhalifu mkubwa unaoendelea kuumiza watu. Na wahalifu wenyewe wapo hapa hapa na wao wanasikiliza,” Aminata aliwaka akiwaambia John na Max ambao walikuwa wamesimama wakimsikiliza waziri wa Ulinzi.
“Huyu mtu aliteuliwa na rais kimakosa, hafai kuwepo….., dawa za kulevya zimepitishwa mara ngapi hapa… ulinzi upi kwa raia wakati raia na mali zao wanalia hawajui pa kukimbilia. Leo anasisitiza badala ya kuwakamata hao wanaojifanya wajuaji alafu ndio rafiki zake,” Max alisema huku akiitikiwa na Hancy kwa kutikisa kichwa chake.
Hawakuendelea tena kukaa pale. Max na John walianza kutoka nje. Aminata alikuwa akiangaliana sana na Mosses ambaye alikuwa ameshikilia glasi ya wine akiwa amesimama pembeni ya Steve. Alishtuka sana baada ya kugundua yule alikuwa ni Aminata na hivyo aliita walinzi wake na kusimama nao karibu.furaha yote ilimwondoka akawa hajui la kufanya. Hakumweleza Steve hadi pale waliporudi katika jumba lake ndipo alipomsmulia kisa kizima.
“Sasa kwa nini wakusumbue hivyo, tuwatafuteni na tuhakikishe tunawapoteza, alisema Steve kwa kufoka. Tukio ambalo liliendeshwa wiki moja baadaye kwa kuwateka John na Aminata wakati wakiwa njiani kuelekea kwa Aminata kupumzika.
*****
Ni baada ya kula chakula cha jioni ndipo Max akalikumbuka gari la Aminata ambalo baada ya kutekwa liliachwa palepale barabarani. Habari zilipomfikia Max aliamua kufuatilia na kulipata gari lile na kulipeleka kituo cha polisi kwa ajili ya usalama.
“Shemeji sidhani hata kama unalikumbuka gari lako?” Max
alichokoza Aminata ambaye alisahau kabisa kuhusu gari lake walilolitumia kabla ya kutekwa.
“Sidhani kama nilishawahi kulifikiria tangu tutekwe, kikubwa kilikuwa ni juu ya maisha yetu na nashukuru tupo hai,” Aminata alimjibu kuonyesha kuwa hakujali sana anasa zaidi ya uhai wake. Huku akicheka aliomba aelezwe kuhusu gari lake.
“Gari lako shemeji nililikuta Barabara ya Barakuda nikalipeleka polisi kwa usalama zaidi. Nilikuwa njiani kuja kwako kuangalia kama John alikuwa huko baada ya simu yake kuwa haipatikani. Ukilihitaji tutaongozana kwenda kulitoa huko,” alimaliza Max.
Baada ya maongezi yao ya muda mrefu Max aliwakaribisha wageni wake John na Aminata katika chumba cha kulala na yeye na Michelle wakaongozana kwenda kulala.
*****
Asubuhi ya siku inayofuata John na Max walielekea ofisini kwa Max tayari kukutana na Antony ambaye alikuwa amesharudi nchini akitokea nchini Kenya ambako alikuwa amerudi kwa ajili ya biashara zake. Safari hii hakuwa zaidi akijihusisha na biashara bali alikuwa anatafuta zana za kufanyia kazi. Kazi moja tu ambayo baada ya kuambiwa na John kwamba Mosses alikuwa hai na kwamba walitekwa sasa alijua ni lazima wammalize.
Aliamu kurudi akiwa tayari kwa mapambano n kwenda kukutana na kina John na Max ili kupanga mikakati ya kupambana na maadui zao. Walifika ofisini saa mbili asubuhi na kumkuta Antony akiwasubiri nje na gari lake. John alifurahi kumwona pacha wake. Alijua yuko tayari kupambana.
John aliendelea kuzungumza na Max na Antony juu ya yaliyotokea. Walimweleza Antony kila kitu juu ya mipango yao. Alifanya hivyo ili waweze kuwa tayari katika kuhakikisha wanapata njia ya kukabiliana na maadui zao.
“Safari hii tusiwakawize, najua wapo wengi sana hasa baada ya kuniteka, nilikutana na kundi kubwa. Sasa itabidi tuichukue hii nchi kwa muda watu watatu, tunavamia Mererani tunashambulia migodi afu tutajua tu jengo lao lilipo. Sawa?” Max alisema akiwapa mbinu John na Antony.
“Sawa sawa,” John na Antony waliitikia kuonyesha wako tayari kupambana.
Max alianza kugawa majukumu kwao.
“Antony,” aliita Max.
“Ndio mkuu,” aliitikia Antony huku akimwangalia Mx kwa kuwa tayari kusikia ambacho alikuwa anataka kumwambia.
“Wewe utatumia ile Range Rover nyeusi yenye mitambo mingine ya mawasiliano,” Antony alikabidhiwa Range Rover iliyokamilika mitambo ya kuweza kuwasiliana nao. Gari lake alitakiwa na Max aliache kwani siku zote Max alitumia Range Rover kwani lilikuwa na teknolojia ya mawasiliano iliyokuwa anawajulisha askari wenzake taarifa za aliko na pia wakiwasiliana.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Aliunganisha mawasiliano ya kwenye gari na simu ya John nay a kwake ili popote atakapokuwa waweze kuwasiliana na Antony ambaye ndiye atakayekuwa akilitumia lile gari.
“Nadhani tumemalizana Antony,” Max alimkabidhi antony funguo huku Antony akimwangalia. Alimwona ni mtu aliyejua mbinu nyingi sana katika kupambana na hivyo alijua watashinda tu.
“I think we should start tonight if possible kabla hawajashtukia mipango. Nimeshajua mavazi yao, wale jamaa wanapenda mavazi meusi na miwani meusi, wanatumia gari nyingi zenye rangi ya maziwa na nyingi ni Mini Bus, hivyo Antony utatumia ile Range kuzunguka nayo na kutufahamisha walipo. Ila itakuwa vizuri kama tungejua jengo lao ili tuweze kuwavamia,” John alitoa wazo ambalo Max aliliafiki.
“Kweli John, ni vizuri tukajua wapi wanakotokea ili tujue tunaanzia wapi, nashauri Antony afanye utaratibu kwanza wa kuweza kufika huko kwa kuwafuatilia mpaka watakapoishia,” Max alitoa pendekezo ambalo hata Antony mwenyewe aliafiki na kuona kuwa hilo ndo la msingi zaidi.
Mi nitawafatilia kwanza nikishajua wanaingia wapi nitawashtua then mtanifuata, au sio?” alihoji Antony. Wote walikubali na kuonyesha ishara ya ushindi mapema kwani kila mmoja aliamini mwenzake anaweza kazi.
*****
Saa kumi na mbili jioni, Antony anaondoka na gari kuelekea Mererani. Anawaacha John na Max ambao walikuwa wakimfuata taratibu ili asije akakwama. Mpango wao wa kwenda kulipua mgodi wao kama hatua ya kwanza ya kujua mahali lilipokuwa jingo lile.
Saa mbili na nusu usiku walikuwa wamefika. Hali ilikuwa ni shwari na hivyo, Max alitoka na mabomu mawili ya kutegwa na kwenda moja kwa moja hadi katika uzio. Alitumia mbinu zake kuingia ndani. Alifanikiwa kufika hadi eneo la kuingilia machimboni na kuyatega yale mabomu mawili kisha akaondoka.
Wakiwa kwenye gari wakisogea mbali kidogo la lilipokuwa lango kubwa la kuingilia katika mgodi wa Steve. Max alimwonyesha Antony kifaa cha kulipulia na kubonyeza.
Mlipuko mkubwa ulitokea katika mgodi. Eneo zima likawa halikaliki kwani watu walikimbia ovyo. Dakika chache baadaye Antony alilipua bomu la pili na hivyo kupelekea wasiwasi zaidi uliowafanya baadhi ya wachimbaji kukimbia na kutokomea mbali. Waliamini kwamba wameshinda mpango wao wa kwanza katika kuonyesha kwamba wataweza kuwafikia kiurahisi.
Askari baadhi, walikimbilia gari na kuanza kuondoka wakielekea eneo lilipokuwa jengo lile. Hawakujua kwamba Antony alikuwa akiwafuata nyuma. Aliwafuata hadi alipoona wakiingia. Alishangaa sana kwani hakuona njia bali aliona kichaka. Magari yaliingia kichakani huko. Aliyafuata hadi alipofikia kile kichaka.
Alisimama kwa muda huku akisoma ramani ya magari yalipokuwa yakielekea hadi yalipoishia ambapo aliona lango kubwa likifunguliwa na magari yale kuingia.
Max na John walikuwa wakisubiri mawasiliano na Antony. Waliwasiliana na Antony kujua alipofikia.
“Nimefanikiwa kujua ngome yao ilipo John, inaelekea si rahisi kuingia lakini tukimteka mmoja wao itakuwa rahisi,” alisema Antony ambaye alikuwa njiani kuwafuata wenzake waliokuwa wakimsubiri ndani ya nyumba moja lililoko kule Mererani.
“Utatukuta palepale pa mwanzo tulipokutana,” alisema John wakati akiwasiliana na Antony. “Sawa kwa kuwa nimeshapajua….tusiwaache wale jamaa kwani wataleta maafa makubwa sana, inaelekea ni mtandao mkubwa kiasi cha baadaye kutishia amani ya nchi,” alisema Antony.
“Ni kweli Antony, inabidi tufanye mikakati ya kuwavamia kwa mbinu kali, njoo hapa utatupata,” alisema John.
Antony alifika na kuwaeleza yote waliyoyakuta huko. Waliamua kurudi kwanza mjini kabla hawajarudi tena Mererani kwa ajili ya kushambulia na kufanya lile ambalo walidhamiria kulifanya katika kupambana na uhalifu.
*****
Siku nmbili baadaye John, Antony, Aminata pamoja na Max walikuwa wameshagundua mpango wa Bosi Steve wa kwenda katika mkutano ambao uliwahusisha wafanya biashara wakubwa.
Max alitoa wazo la kwenda huko kuhudhuria ili kujua kitakachoongelewa ikiwa ni pamoja na kumwona Steve na kumtisha. Walikubaliana wafanye hivyo ikiwa ni pamoja na kumteka Steve ili waweze kuwadhibiti na kuwadhoofisha askari wa Mosses Ndula na Mosses mwenyewe.
“Jamani kama tunavyojua leo wanapanga kuingia The Hall City Garden kwa ajili ya mkutano wa wafanyabiashara wakubwa nadhani mpango wetu tutaukamilisha wa kumteka Steve.
Tuanzeni kujipanga namna ya kufanikisha mpango wetu ili tusije tukakose,” Max alisema huku wote wakiwa wanamsikiliza.
“Kweli, inabidi tujipange kabisa ili tusishindwe, tunaweza tukawa tumerahisisha sana kazi. Sasa iweje?” aliuliza Aminata ambaye alikuwa pembeni ya John wakimsikiliza Max.
“Sasa itabidi Antony uwahi ukumbini ili usome mchezo mzima kisha utatusubiri nyuma ya jengo hilo ukiwa tayari umeliweka gari katika mazingira mazuri,” alisema Max.
“Sawa mkuu,” aliitikia Antony huku Max akiendelea kutoa maelezo ya nini kifanyike.
“Mimi na John tutaingia ukumbini alafu Aminata atakuja pale kama mgeni. Wakiwa wanamshangaa pasipo ya sisi kuonekana itakuwa ni njia rahisi ya sisi kumkamata,”
“kweli, ila na mimi nitakuwa makini maana wanajua sehemu nyingi za mikutano huwa tunaingia wote,” alisema Aminata huku akimwangalia Max ambaye alikuwa akitikisa kichwa chake kuonyesha kwamba amekubaliana na mawazo yake.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Antony aliwaacha John na Max na kuondoka kwa ajili ya kufanya maandalizi kwani mkutano wa wafanyabiashara hao ulikuwa uanze majira ya saa kumi na nusu jioni.
Alifika na kuangalia hali ilivyokuwa kasha kuwataarifu wenzake. Wahudumu walikuwa wakipitapita kugawa vinywaji kwa watu ambao walikuwa wakisubiri mkutano kuanza.
“Tumefanikiwa kuingia, Max sasa kazi ni moja tu kuhakikisha Steve anakuwa mikononi mwetu,” alisema John. Waliwasiliana na Antony kuhakikisha kwamba ameshaegesha gari lake nyuma ya ukumbi kwani wana kila sababu ya kufanikisha mpango wao.
Ilikuwa ni zamu ya Bosi Steve kuwasili katika ukumbini ambapo alisindikizwa na Mosses Ndula pamoja na askari wanne waliovalia suti nyeusi na miwani nyeusi kuonyesha kuwa walikuwa makini sana na kazi yao.
Wakati bosi Steve akiingia chumba cha mikutano, Antony aliwasiliana na John, alimjulisha juu ya kuwasili kwa Steve na hivyo John alielekea upande wa mlango wa kutokea wa nyuma ya jengo ili kuhakikisha kuwa unakuwa wazi. Wageni wote walisimama wakati MC akizungumza machache kukaribisha wageni ili mkutano uanze.
Max alikuwa akiangalia nyendo zao huku akimwangalia zaidi Steve ambaye alikuwa mwenye furaha sana. Mhudumu alipitisha glass za wine na Steve aliichukua moja na kuanza kunywa.
Wakati mkutano unaendelea Bosi Steve alitoka na kuelekea maliwatoni. Alimhakikishia Mosses Ndula kuwa atarudi kwani Mosses Ndula alimsihi kuongozana na mlinzi mmoja.
“Usijali ndugu nitarudi mara moja, unakumbuka kabla ya safari ya huku tulikunywa wine nyingine nyumbani kwangu hivyo nahisi haja ndogo, kabla mkutano haujaanza vizuri naona ni bora nikatoe haja ndogo ili niweze kufuatilia, nitatumia dakika tano tu,” alisema Bosi Steve kabla ya kuondoka.
Max alimwona akielekea maliwato. Alihakikisha hamuachi baada ya kuona akiwa mwenyewe bila msindikizaji.
Max mara moja alifika eneo la maliwato kumsubiri Steve aingie. Aliwasiliana na John ili aweze kuzuia watu kuingia eneo hilo na badala yake awashauri watumie maliwato nyingine. Wakati huo hakukuwa na watu wakiingia maliwatoni huko na hivyo ilikuwa ni nafasi nzuri ya Max na John kufanikisha mpango wao.
Haikuchukua muda Bosi Steve aliingia, Max alisubiri hadi amemaliza na kuchomoa bastola yake na kumnyooshea Steve. Bosi Steve alishtuka kusikia sauti ya Max ikimwambia.
“Usijiguse na simama hapo hapo kama ulivyo,” kabla ya kugeuka kumwangalia aliyetoa sauti hiyo alipigwa ngumi na kuzirai. Max aliwasiliana na John kwamba kashamteka hivyo wajitayarishe kuondoka.
Antony alifungua mlango wa gari na kulisogeza mpaka karibu na mlango wa kutokea na hivyo ilimchukua Max dakika mbili kumfikisha Steve ndani ya gari hali ya kuwa amezirai.
Walifika katika nyumba moja kuukuu iliyoko maeneo ya Mianzini wakiwa wameshamteka Bosi Steve. Nyumba hiyo haikuwa inatumiwa na mtu yeyote. Ilikuwa ni saa moja na nusu usiku.
Baada ya Steve kuzinduka John alikuwa amesimama mbele yake. Alishtuka kumwona John.
*****
Ukumbini Mosses Ndula na Askari wake walikuwa wakimtafuta Bosi Steve bila ya mafanikio. Waliamua kutoka na kuelekea nje ya ukumbi wakidhani atakuwa huko kwani hata simu yake haikupatikana. Walizunguka kila mahali nje ya hoteli wakijua labda anavuta sigara sehemu.
“Atakuwa ametekwa, hivyo wasiliana na kikosi cha anga ili kuzunguka na helikopta kujua watekaji,” Mosses Ndula alimwambia mmoja wa askarti wake ili aweze kuwasiliana na askari wa kikosi cha anga waanze kazi ya kumtafuta Bosi Steve mara moja.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment