Search This Blog

Sunday, 22 May 2022

TAHARUKI - 3

 







    Simulizi : Taharuki

    Sehemu Ya Tatu (3)



    WIBO akamkabidhi Scola gari dogo la kifahari, aina ya Ford Munstang, lenye milango miwili, na kumwambia aende nalo. Na kweli baada ya kujiswafi na kuvalia vizuri, mrembo Scola alipanda lie gari na kuutoka mtaa ule, kuelekea London Hilton Hotel, ambayo ilikuwa mbali na pale alipokuwa anaishi Wibo Eze. Scola alikuwa mwenyeji sana ndani ya jiji la London , hivyo barabara zake hazikumsumbua.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Akaendesha gari hadi alipofika kwenye hoteli ile, ambapo akalipaki gari katika eneo la maegesho, halafu akashuka na kelekea ndani ya hoteli ile. Akapanda lifti iliyomfikisha juu alikopanga chumba Frank Mumba, na baada ya kuufikia mlango wa chumba kile, akaugoga na kuingia ndani, ambako alimkuta Frank akimsubiri kwa hamu ndani ya chumba hicho, kiasi kwamba alipoingia tu, Frank alimpokea kwa mabusu mazito kana kwamba walikuwa wamezoeana kwa muda mrefu sana .



    “Oh, karibu Scola...” Frank akamwambia huku akizidi kumkumbatia!



    “Ahsante Frank...” Scola naye akasema huku akijiachia kwake.

    Hatimaye, Scola alikaa kwenye kiti kilichokuwa pale, halafu wakaanza kuongea maongezi yaliyohusu maisha kwa ujumla. Na muda wote huo walikuwa wakinywa vinywaji, ambavyo vilikuwa kwenye friji dogo lililokuwa mle chumbani.



    Halafu baadaye, walijikuta wamezama katika mapenzi mazito na kuishia kujitupa katika kile kitanda kikubwa, na kilichoendelea kilikuwa ni kitu kingine kabisa. Kwani sekunde kadhaa, wote walikuwa kama walivyozaliwa, na Frank akahisi mikono laini ya Scola ikiendelea kumpapasa taratibu mgongoni.



    Hakika Frank alijisemea moyoni mwake kwamba mwanadada yule wa Kinijeria alikuwa ni moto wa kuotea mbali katika masuala ya mapenzi, na hatua nyingine ilichofuata pale kilikuwa ni mapenzi motomoto baina yao wawili hadi walipofikia kilele cha mapenzi yao pamoja. Raha kutoka kwa Scola ikapenya katika mishipa ya damu ya Frank, na raha kutoka kwake, ikapenya katika mishipa ya damu ya Scola Eze!



    Kila mmoja alimng’ang’ania mwenzake kwa takriban dakika tano, halafu wakaachana na kuelekea ndani ya bafu lilokuwa mle mle ndani kwenda kuoga. Baada ya kumaliza kuoga, walirudi chumbani na kuvalia nguo zao, wakionyesha kuwa na nyuso za furaha.



    “Scola Eze,” Frank akasema.



    “Unasemaje Frank Mumba?”



    “Habu naomba unieleze mpenzi…”



    “Nikueleze nini?”



    “Napenda kujua, kaka yako, Wibo Eze, anafanya kazi gani hapa London. Samahani sana kama itakuwa nimekuudhi.”



    “Bila samahani, hujaniudhi hata chembe,” Scola akasema na kuendelea. “Kaka yangu, Wibo Eze, ni mfanyabiashara maarufu sana hapa London, anayemiliki kampuni kubwa sana inayojihusisha na vito vya thamani, madini pamoja na mapambo aghali yanayotokana na vito hivyo.”



    “Ni kweli,” Frank akasema na kuendelea. “Anaonekana ni mtu mashuhuri aliyejiimarisha sana jijini London .”



    “Hakuna tajiri asiyemjua Wibo hapa London …” Scola aliendelea kusema huku akimwagia sifa kaka yake.



    “Je, anauza almasi pia?”



    “Ndiyo, kaka yangu ni mmoja wa wanunuzi wakubwa wa almasi kutoka nchini Angola .”



    “Mh!” Frank akaguna bila Scola kusikia.



    Ile ilikuwa ni baada ya Scola kusema kuwa Wibo alikuwa akijishughulisha na biashara ya almasi. Frank akashuku kuwa Wibo Eze alikuwa ni mtu wa kumtilia mashaka kwa sababu mkufu ule uliokuwa umeibwa, ulikuwa na asili ya nchini Angola .



    “Wakati mwingine…” Scola aliendelea kusema. “Mara nyingi kaka yangu hufanya safari za kwenda Angola . Na siyo huko peke yake tu, bali amekuwa akizuru maeneo ya Lobito , Huambo, Bihe na Kabinda…”



    “Huwa anakwenda yeye mwenyewe?”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mh,” Scola akaguna na kuendelea. “Mbona unadodosa sana kuhusu kaka yangu? Kwani vipi mwanaume wewe?”



    “Kibaya ni nini mpenzi wangu…hutaki nimfahamu shemeji yangu?” Frank akamwuliza tu.



    “Kumfahamu siyo vibaya.”



    “Basi, nimevutiwa mno na kaka yako. Anaonekana ni mtu aliyejaa hekima na maarifa.”



    “ Kama ni hivyo, nashukuru...”



    Baada ya kukaa kwa muda mle chumbani, Frank na Scola wakaamua kutoka, kwani bahati ile ya kuwa na kimwana mrembo kama Scola, aliona kuwa ni vyema watoke na kwenda na kwenda kuvinjari kidogo katika mitaa ya jiji la London . Hivyo basi, wote wakashuka chini kutoka ghorofani, halafu wakapanda lile gari la kifahari, Ford Munstang, lenye milango miwili. Scola akaliondoa kwa mwendo wastani kuliingiza barabarani.



    Frank na Scola walitembelea sehemu mashuhuri kama vile, mtaa wa maduka wa Oxford , Hampton Court na mto Thames . Baadaye wakakamilisha mizunguko yao ya kuzunguka katika mitaa ya London na kuingia ndani ya mgahawa wa Covent Garden , ambapo walijipatia chakula na vinywaji baridi.



    Baada ya kumaliza kula, Frank akawa ametosheka na kumwambia Scola amrudishe hotelini, hasa ukizingatia alikuwa na miadi ya kukutana na mpelelezi mwenzake, Brown Lambert. Scola akamrudisha mpaka London Hilton Hotel alipofikia. Wakaagana kwa kupigana mabusu kabla Frank hajashuka garini. Walipomaliza kuagana, ndipo Frank aliposhuka na kuelekea hotelini. Scola akamuangalia kwa takriban dakika mbili, halafu akaliondoa gari lile, wakati Frank alipokuwa akiingia ndani ya hoteli.

    Akapanda lifti kuelekea juu katika chumba chake namba 222…



    *********



    Awali kabla ya hapo, wakati mwanadada, Scola na Frank Mumba, walipokuwa wamekwenda kustarehe katika viunga vya mji wa London, Wibo Eze, kaka yake Scola, alikuwa amekaa kikao maalum na watu watatu, ndani ya chumba cha faragha. Walikuwa ni wanaume watatu, watu wa shoka, wenye asili ya ki-afrika, waliokuwa wamejazia maumbile yaliyoshupaa. Alikuwa amewaita pale kwa kazi maalum ya kumfuatilia mpelelezi, Frank Mumba.



    Muda wote, mbele ya meza ndogo ya kioo, ilioyokuwa mbele yao , ilikuwa imesheheni vinywaji, pombe kali aina ya wiski, waliyokuwa wakinywa, na huku wakipanga mikakati iliyowakabili. Kisha, Wibo Eze aliwaangalia kwa zamu wale watu watatu waliojulikana kwa majina ya, Kim, Rodge na Mark.



    Halafu akawaambia kwa sauti ndogo lakini yenye msisitizo: “Nimewaiteni hapa kwa ajili ya kazi ile maalum...”



    “Sawa mkuu...” Kim akasema kwa niaba ya wenzake.



    “Ni kwamba mtu wetu, mpelelezi wa Kimataifa, Frank Mumba, ameshafika hapa London . Amefikia kwenye hoteli ya Hilton, chumba namba 222. Hivyo basi, jiandaeni, muende mkamkamate na kuhakikisha mnamfikisha katika sehemu husika, ndani ya ngome yetu ya mateso. Sijui mnanipata?”



    “Tunakupata bosi,” Kim akasema.



    “Tuko na wewe,” Rodger naye akasema.



    “Tuko tayari kwa kazi…” akamaliza Mark.



    “ Kama mko tayari, basi chukueni silaha zenu muondoke haraka! Nataka mumlete hapa akiwa hai au maiti yake!” Wibo Eze alisema kwa msisitizo!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Vijana, Mark, Rodger na Kim wakanyanyuka na kuondoka pale chumbani. Wakamwacha Wibo amekaa, akiendelea na utaratibu wake mwingine, pengine na kusubiri taarifa kwa wale aliokuwa amewatuma. Vijana wale walipotokea nje, walipanda gari aina ya Ranger Rover, dereva akiwa Kim. Akaliondoa gari kuelekea Hilton Hotel.



    Baada ya mwendo wa robo saa, walifika hotelini, na kulipaki gari sehemu ya maegesho nje ya hoteli, ambapo palikuwa na magari mengine. Kabla ya kushuka, wakaangaza macho yao pande zote kama kulikuwa na adui. Alipohakikisha hakuna adui, wakashuka na kuelekea kule hotelini kwa mwendo wa kawaida, hadi walipoingia na kuifikia lifti inayopandisha wateja juu vyumbani.



    Kim akabonyeza batani na mlango ukafunguka, na wote wakaingia ndani na kupandisha juu katika chumba namba 222, hadi walipofika. Baada ya kufika, kama kawaida walikuta sehemu yote kukiwa kimya kabisa, kwani hakukuwa na pilikapilika za watu waliokuwa wanapita. Kwa haraka wakauendea mlango ule huku wakiwa wamejiandaa kwa chochote kitakachotokea, ingawa walishajua kwamba Frank hakuwepo mle chumbani, alikuwa ameondoka na mwanadada, Scola, kwenda kwenye starehe. Rodger akautoa ufunguo wa bandia na kuufungua ule mlango, na chumba kikawapokea kwa kishindo kukiwa kimya.



    Hivyo basi, wote wakaingia wakiwa na tahadhari, ambapo walianza kupekua kila sehemu ndani ya chumba kile, ambapo walichokikuta mle ndani, ni begi la nguo za Frank, mzigo wa pekee aliokuwa nao, ukiachilia silaha, bastola, ambayo alikuwa anatembea nayo. Wakalivamia begi ile na kulifungua, halafu wakawa wanalipekua kwa tahadhari, lakini hawakupata chochote cha maana ambacho kingewasaidia.



    Baada ya kukosa chochote, wakavamia kitandani, ambapo walifunua godoro lakini ikawa ni vilevile. Pia, wakapekua ndani ya kabati la nguo lililokuwa limejengewa ukutani, lakini hawakupata kitu chochote! Hata hivyo hawakukata tamaa.



    Wakapanga kumsubiri mlemle ndani ili waweze kumtia mbaroni.Wakaamua kuingia ndani ya bafu lililokwa mle chumbani, ukizingatia walishaambiwa ni lazima warudi na Frank akiwa hai au maiti!

    Baada ya kuingia ndani ya bafu, wakajificha, wakijua kuwa ni lazima Frank Mumba angerudi muda siyo mrefu baada ya kumaliza starehe na mwanadada, Scola Eze, ambaye alitumika kama chambo cha kumnasa mtu wao waliyekuwa wamemfuatilia kuianzia mbali!





    *******

    Frank Mumba alipoingia ndani ya chumba namba 222 alichokuwa amefikia, machale yalianza kumcheza baada ya kugundua vitu ndani ya chumba kile havikukaa kama alivyokuwa ameviacha. Aligundua kuwa vilikuwa vimepekuliwa kwa ustadi wa hali ya juu, na mtu mwenye ujuzi katika taaluma ya ujasusi na upelelezi!

    Ni hatari sana !



    Frank akavuta pumzi ndefu na kuzishusha, akitafakari. Halafu akakiendea kitanda ili akae na kutafakari cha kufanya, lakini akashtukia akivamiwa kwa teke zito lililomsomba juu na kumfanya adondoke juu ya zulia lililokuwepo sakafuni. Akili yake ikavurugika kwa muda, punde alipokuwa akijaribu kunyanyuka ili akabiliane na yule mtu aliyemvamia!



    “Tafadhali kijana, tulia kama ulivyo na utii amri yetu!” Sauti nzito ya Kim, mmoja wa watu wenye umbile la miraba minne ilimwamrisha!



    “Oh, imekuwaje tena?” Frank akawauliza!



    “Kufanya kinyume cha maagizo yetu itakuwa ni kujihalalishia tiketi ya kwenda kuzimu mara moja!” Sauti nzito ya Kim iliendelea kumwambia.



    “Mh, jamani, imekuwaje? Ni hatari sasa!” Frank akajiasemea moyoni, huku akiiweka akili yake vizuri!



    “Toa chochote ulichokuwa nacho na ukitupe chini!” Kim aliendelea kumwambia, huku wale wengine, Rodger na Mark wakimwangalia kwa hasira kali! Walikuwa wameshika viuno vyao kusubiri amri ya kumsulubu itolewe na Kim, kiongozi wao!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Na kweli Frank Mumba alikuwa na bastola aliyokuwa ameichimbia kibindoni. Akaitoa na kuiweka chini juu ya zulia, halafu akanyoosha mikono yake juu. Kwa muda wote ule, Frank hakuweza kuwatambua watu wale ni akina nani, kwa vile walikuwa wamevalia mavazi yaliyokuwa yamefunika nyuso zao na kuacha matundu ya macho tu, mavazi yenyewe yakiwa meusi mithili ya kitambaa cha kaniki!



    “Sasa utafuata amri yetu!” Kim akaendelea kumwambia.



    “Hivi mnajua kuwa sijawaelewa mpaka sasa?” Frank akawauliza watu hao katili!



    “Usiwe na wasiwasi, utatuelewa tu, punde tutakapofika sehemu husika!”



    “Sehemu gani tena hiyo, na kwa kosa gani?”



    “Twende uongoze njia kuelekea mahali tutakapotaka sisi!” Sauti ile ya Kim iliendelea kumuamrisha.



    Frank Mumba hakubisha, akaendelea kutii, kwani asingeweza kukabiliana nao kwa ghafla, ilibidi ajipange kwanza. Hatimaye wakamtoa ndani ya chumba kile, huku wamemwekea bastola hadi walipofika kwenye lifti. Batani zikabonyezwa na mlango ukafunguka, wakaingia na lifti ikashuka chini. Baada ya dakika mbili tu, wakawa wameshafika chini, katika ghorofa ya mwanzo.



    Mlango ukafunguka, nao wakaondoka naye hadi kwenye sehemu ya maegesh ya magari, ambapo kulikuwa na gari lao aina ya Ranger Rover.



    Wakamuamrisha Frank aingie ndani ya hilo gari, naye akaingia na gari likaondolewa kwa mwendo wa kasi bila kuelewa anapelekwa wapi!



    Kwani baada ya Frank kuingia garini, walimfunga kitambaa cha uso na kumfanya asiweze kuona. Walisafiri kwa mwendo mrefu kiasi usiku ule, hatimaye gari likafika mahali ambapo Frank alipewa amri ya kushuka haraka na kuelekezwa kuingia ndani ya nyumba moja na kufikishiwa katika chumba. Wakamfungua kile kitambaa usoni na kumfanya aweze kuona tena kama mwanzo.



    Sehemu ile aliyopelekwa ilikuwa ni nyumba ya kifahari, ambayo ilionyesha kama makazi ya mtu mwenye uwezo wa kifedha. Hata hivyo hawakutulia ndani ya chumba kile, bali waliendelea kumuongoza kuelekea katika vyumba vingine vilivyokuwa ndani ya nyumba ile.



    Baada ya kutembea na kuingia ndani ya vyumba kadhaa vya nyumba ile, sauti nzito ya Rodger, ikamuamuru aelekee vyumba vya upande wa kushoto, akafuata na kuingia chumba namba sifuri mlangoni bila kusita, akifuata maagizo yao .



    Wakajikuta wakiwa ndani ya chumba kilichokuwa na mashine za ajabu ambazo hata kwa Frank Mumba kwa uzoefu wake, aligundua kwamba ilikuwa ni sehemu iliyotengwa maalum ya kutesea watu. Katika mashine hizo, Frank aliweza kuona matone ta damu mbichi ambayo hakuweza kujua ni ya nani, lakini akagundua kuwa lazima itakuwa ni ya binadamu, watu walioteswa saa chache zilizopita katika chumba kile kabla yeye hajafikishwa pale!



    Hakika Frank alijiona kama mtu aliyekuwa ndotoni baada ya kushtukiwa siku ile ya pili tu aliyoingia jijini London . Au mwanadada mrembo, Scola Eze atakuwa amemuuza kwa watu wale katili? Lakini mbona muda siyo mrefu alikuwa ametoka kujirusha na kimwana huyo? Frank alijiuliza bila kupata jibu! Na pia muda ule hakujua mpelelezi mwenzake, Bw. Brown Lambert alikuwa wapi, kwani walikuwa bado hawajawasiliana wakutane muda gani, ili waianze kazi yao ya upelelezi.



    Yeye Frank na Brown, walitakiwa wakutane kwa siri sana , ukizingatia ni watu wengi waliokuwa wanautafuta mkufu ule wa thamani, na pia wale walioupora wakijitahidi wasijulikane. Ni lazima wamwage hata damu, ilimradi wasijulikane! Hakika ilikuwa ni hekeheka nzito! Na kitu kingine kilichomuumiza, ni kwamba hakuwa na mawasiliano na mtu yeyote, kwani vifaa vyake pamoja na simu zilikuwa mikononi mwa watu wale waliomteke nyara.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Basi, ilimbidi awe mpole, na kusubiri kitakachoendelea ili akabiliane nacho! Ukweli ni kwamba Frank hakuwa mtu wa kukata tamaa haraka sana , mafunzo magumu ya kikomandoo yalimsaidia sana kumweka katika hali ya uvumilivu wakati anapokuwa katika shida kama ile!



    “Keti kwenye kiti na ujibu maswali yetu kwa ufasaha, na kadri nitakavyokuuliza!” Sauti nzito yu Rodger iliendelea kumwambia Frank.



    “Hakuna shaka…” Frank akasema kwa kujiamini. Halafu akakaa kwenye kiti kimoja kilichokuwa katikati ya chumba kile.

    Ghafla taa ya mle ndani ilizimwa na kukawa giza totoro. Halafu wakawasha mashine iliyokuwa na kurunzi yenye mwanga mkali sana , ambao ulimmulika moja kwa moja Frank Mumba usoni, kiasi cha kushindwa kuona kitu chochote kilichokuwa pembeni yake. Na hata wale watu waliokuwa wanamlinda, hakuweza kuwaona zaidi ya kusikia sauti tu iliyokuwa inamhoji!



    “Ndiyo Frank Mumba, mpelelezi shupavu kutoka Afrika Mashariki, habari za Tanzania ?” Sauti nzito ya Rodger ilimwambia Frank, kiasi kwamba alishindwa kufahamu watu wale wamelijulia wapi jina lake? Na wamejuaje kama ametokea nchini Tanzania ?

    “Nyie ni akina nani, na mnataka nini kutoka kwangu?” Frank akawauliza.



    “Hupaswi kutufahamu sisi ni akina nani. Ila wewe fahamu wazi kwamba tunazo taarifa kwamba mpelelezi, Brown Lambert amekuleta hapa London kufuatilia juu ya watu walioiba mkufu wa thamani kubwa kutoka kwenye kasri la Malkia…” sauti ile ya Rodger ikanyamaza kidogo ili kumpa nafasi Frank aweze kumwelewa!



    “…Pia, Frank Mumba, unapaswa kujua kuwa sisi si watoto wadogo wa kuchezewa akili, mtu wetu alipanda ndege na wewe katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dare s Salaam mpaka hapa London . Hivyo mazungumzo yako na Bw. Brown yalisikia kwenye simu kabla hujaondoka Tanzania .



    Pia, tunapenda kukupa pole kwani unajitaabisha bure, mkufu ule hauko hapa London . Ni kwamba uko mbali sana , wasipoweza kwenda watu wa aina yako na kurejea ukiwa hai!”



    Sauti ile ya Rodger ilitulia na kuacha maelezo yake yakimuacha Frank Mumba akiwa amechanganyikiwa baada ya kugundua alikuwa mikononi mwa watu hatari kuliko alivyotegemea!



    “Sasa nyie mnanitaka nifanye nini?” Frank akawauliza wale watu waliomteka kutoka hotelini na kumfikisha katika jumba lao la mateso.



    “Tunataka ufe, kwa sababu chumba hiki tulichokuleta ni namba sifuri, ikiwa na maana hakuna kitu hapa, hakuna uhai! Hiki ni chumba ambacho huletwa watu ambao wameshahukumiwa kifo, na kuanzia sasa anza kusali sala zako za mwisho, kwani muda siyo mrefu utaungana na wafu kuzimu!” Sauti ile nzito ya Rodger iliendelea kutoa hotuba ya kutisha!



    “Hii ni hatari sasa!” Frank Mumba akasema moyoni!



    “Maadam umefika katika ngome ya wagumu, huna budi kutulia!” Rodger akamwambia Frank. Halafu akaiendea swichi iliyokuwa pale ukutani, ili awashe taa ya mle ndani.



    Hata hivyo, kabla mkono wake haujaifikia swichi ile, Frank Mumba aliamua kuutumia mwanya ule na kurusha mateke mawili mfulilizo kuwawahi, Mark na Kim, waliokuwa na bastola mikononi mwao. Wote wawili wakadondoka kwa kishindo! Na hatua nyingine iliyofuata ni kumuwahi Rodger ambaye alikuwa bado ameshangaa. Akamkusanya na kumbamiza ukutani na kudondokea ile taa ya kurunzi ambayo ilizimika!

    Frank Mumba akaiendea ile swichi na kuiwasha ile taa ya umeme, na chumba kizima kikawa na mwanga wa kutosha. Baada ya taa kuwaka, ndipo Frank alipoweza kuwaona adui zake mmoja baada ya mwingine. Silaha zilikuwa zimetapakaa sakafuni. Mapambano makali ya mikono yakaanza, ambapo Rodger alirusha teke la mzunguko, ambali lilimpata Frank na kumfanya apepesuke, lakini akajiweka sawa na kuanza kuwashambulia kwa mtindo wa kareti, ambapo baada ya muda aligundua kuwa watu wale hawakuwa mahiri katika kucheza karate. Walikuwa watu wa kutumia silaha tu! CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Dakika tano tu tokea Frank aanze kuwashambulia kwa karate, midomo yao ilikuwa inavuja damu. Akawashushia vipigo mfululizo vilivyowapelekea wote watatu wadondoke chini kwa kishindo na kupoteza fahamu. Hakika kilikuwa na kitendo cha haraka sana , kiasi kwamba Frank aliutumia mwanya huo kutoroka ili adui zake wasijue alipo punde watakapopata fahamu. Haraka, akaichukua ile bastola yake aliyokuwa ameisalimisha na kuiweka chini katika zulia, akaiweka kibindoni. Akatoka nje ya nyumba ile ya kifahari, ambapo alilikuta lile gari aina ya Ranger Rover, lililokuwa limepaki pale nje.

    Frank akaufungua mlango ambao ulikuwa haujafungwa, hivyo akaufungua mlango na kuingia ndani. Ufunguo wa gari ulikuwa kwenye swichi unaning’iania. Bila kupoteza muda, akalitia moto na kuliondoa kwa mwendo wa kasi, kuelekea katikati ya jiji la London . Na kwa vile hakuwa mgeni, aligundua kuwa barabara aliyokuwa ameikamata ilikuwa ni ya Kingsway Aveue 345. Ilikuwa ni barabara kubwa iliyoruhusu kuendesha kwa kasi kubwa. Baada ya kuiacha barabara ile, akaifuata nyingine, ambayo alikuwa na uhakika ingeweza kumfikisha London Hilton Hotel, alipokuwa amefikia kabla ya kutekwa na watu wale hatari, ambao muda siyo mrefu walitaka kumtoa uhai wake!

    Ili kuwakwepa adui zake, Frank Mumba alilitelekeza lile gari, Ranger Rover, jirani na bustani ya Haide Park , umbali wa mita mia moja kutoka ilipo hoteli ile maarufu. Usiku ule jiji la London lilikuwa kimya, naye baada ya kushuka garini, akaanza kutembea kwa miguu kuifuata barabara ndogo iliyokuwa imezungukwa na miti pande zote na kufanya kuwe na giza kiasi, mpaka alipofika hotelini. Nje ya hoteli palikuwa na taa zilizokuwa zinawaka kwa kutoa mwanga hafifu usioumiza macho, kitu ambacho kilimfurahisha Frank.

    Ingawa kulikuwa na walinzi sehemu ya nje ya hoteli, lakini hakuna aliyemhoji kwa kuingia usiku ule, kwani hapakuwa na mashati yoyote ya kuingia pale hotelini. Akapanda lifti hadi ilipomfikisha juu alikopanga chumba namba 222. Akakiendea chumba kile kwa haraka na kuuchukua mzigo wake na pengine amtaarifu, mpelelezi mwenzake, Brown Lambert, kilichokuwa kimemsibu usiku ule ikiwa ndiyo kwanza walitaka kupanga mikakati yao ya kuanza upelelezi…

    *******

    Scola Eze hakujua kilichokuwa kinaendelea mara baada ya kumshusha Frank Mumba, nje ya hoteli ya London Hilton, walipokuwa wametoka kwenye mizunguko ya starehe. Kwani baada ya kumshusha, yeye aliendelea na safari yake kuelekea nyumbani kwa kaka yake, Wibo Eze, ili kujua kilichokuwa kinaendelea ukizingatia alikuwa na hamu kubwa ya kuhakikisha Frank anapotezwa katika uso wa dunia.

    Baada ya Scola kufika tu, akamkuta kaka yake amekaa kwenye sofa akitafakari. Mbele yake runinga kubwa ilikuwa inaendelea na matangazo yake, lakini yeye hakuonyesha kuijali kabisa. Basi, Wibo alipomwona Scola akiingia pale sebuleni tu, ndipo aliposhtuka na kuondoka katika lindi lile la mawazo. Akamwangalia na kumwuliza kwa sauti ndogo iliyokauka:

    “Vipi dada, umesharudi?”

    “Ndiyo, nimerudi…”

    “Frank yuko wapi?”

    “Yuko hotelini nilikomwacha…”

    “Basi vizuri…” Wibo akasema na kuongeza. “Basi watamkuta…”

    “Kina nani watamkuta?”

    “Mbona unaniuliza maswali ya kipuuzi?”

    “Upuuzi kivipi kaka?”

    “Ndiyo! Kwani hujui kama Frank anatakiwa auawe? Nimewatuma watu wangu wa kazi wakamshughulikie!”

    “Kweli?” Scola akauliza.

    Wibo Eze hakumjibu zaidi ya kumwangalia tu!

    Mapigo yake ya moyo yakaongezdeka mara dufu, kwani hakutegemea kama Wibo Eze angechukuwa uamuzi kama ule, hasa ukizingatia yeye alishampenda Frank Mumba tokea siku ya kwanza alipomwona, ingawa alitakiwa afanye juu chini kwa kuchunguza nyendo za Frank.

    Uzalendo ukamshinda Scola, hivyo akaona kuwa ule ulikuwa ni muda muafaka wa kuonana na Frank, na amsaidie kuokoka katika janga lile la kutisha. Basi, baada ya kumaliza kuongea na kaka yake, Wibo Eze, Scola akapitiliza hadi upande wa pili wa nyumba kulikokuwa na mlango mwingine unaotokeza nje sehemu ya uani.

    Baada ya kutokea kule, akaliendea gari, ambalo alikuwa amelipaki baada ya kutoka kumsindikiza Frank hotelini. Akafungua mlango na kupanda bila kaka yake kushtuka. Akalitia moto na kulindoa kwa mwendo wa wastani kumfuata Frank. Wibo aliyekuwa bado amechanganyikiwa, hakujua kama Scola alikuwa ameondoka.

    Alipofika pale hotelini, Scola alipaki gari na kushuka haraka, halafu akaingia mle ndani huku nusu akitembea na nusu akikimbia hadi alipoifikia lifti. Akabonyeza batani na liti ikafunguka na kwa haraka akajitoma ndani yake na kuanza kupandisha juu, kilipo chumba alichopanga Frank! Alipofika tu, akakiendea chumba kile huku mapigo ya moyo wake yakipiga kwa kasi, kwani alihisi hali ya hatari!

    ******** CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Frank Mumba alipoufikia mlango wa chumba wa chumba chake, alishangaa baada ya kumkuta Scola Eze amesimama akonekana kama mtu mwenye wasiwasi sana ! Mwili mzima ulikuwa ukimtetemeka!

    “Haloo Frank!” Scola akasema huku akimkumbatia.

    “Scola!” Frank akasema huku akimwangalia. “Siamini macho yangu!”

    “Kwa nini?”

    “Unafanya nini hapa hotelini usiku huu wa manane?”:

    “Ninazo habari njema!”

    “Habari njema zipi?” Frank akamwuliza.

    “Nimekuja kukuokoa!”

    “Umekuja kuniokoa?”

    “Ndiyo, chukua kila kilicho chako uhame hapa hotelini! Twende!”

    “Hivi unavyoniona ndiyo narejea Scola. Nilikuwa nimetekwa nyara na watu wasiojulikana, hakika ningekuwa maiti saa hizi!”

    “Oh, pole sana Frank, ninawajua waliokuteka. Niamini na usiogope tafadhali…”

    “Unamaanisha nini?”

    “Mimi nimeshakupenda,” Scola akasisitiza na kuendelea. “Siko upande wao, ndiyo maana nataka nikuokoe. Tuondoke na mambo yote tutaongea mbele kwa mbele, hali ni mbaya!”

    “Aisee, kaka yako ni mtu hatari sana !” Frank akamwambia Scola waziwazi baada ya kuwa amegundua kuwa mhusika mkuu alikuwa ni Wibo Eze na si mwingine kama walivyoeleza watu wale waliomteka. Hata hivyo Frank akaufungua mlango wa chumba na wote wakaingia mle ndani, lakini hawakukaa zaidi ya kuendelea kusimama na kuendelea na maongezi yao .

    “Ni kweli mwanzoni nilikuwa upande wake, lakini kwa sasa siko upande wao tena. Nimewasaliti na sasa nataka nikuokoe wewe…niamini!”

    “Sawa Scola kama ni kweli…” Frank Mumba akamwambia Scola, ikiwa wakati huo amesimama katikati ya chumba, akiuangalia mzigo wake, begi la nguo, ambao ndiyo mzigo pekee aliokuwa nao ukiacha ile bastola aliyokuwa ameichimbia kibindoni baada ya kuinusuru kutoka kwa adui wale waliokuwa wamemteka nyara.

    Frank aliuchukuwa mzigo wake, begi, halafu wakatoka huku wameongozana na Scola. Wakapanda lifti iliyowashusha chini, na wakati huo kukiwa kumetulia sana . Baada ya kufika kule chini, Frank alikuwa bado hajapanga kuwa waelekee wapi. Hata hivyo walipolifikia gari la Scola, wakapanda na Scola akaliondoa kwa mwendo wa kasi.



    “Tunaelekea wapi?” Frank akamwuliza huku akimwangalia kwa hofu na mashaka! Alimwona ni mtu wa hatari!

    “Tunakwenda kwenye nyumba ya siri, iliyoko sehemu salama…” Scola akamwambia huku akiendelea kuendesha gari kwa mwendo ule wa kasi kwa kuufuata mtaa wa High Halborn, ambao kwa muda ule haukuwa na magari yaliyokuwa yanapita.

    “Una uhakika na unachokisema Scola?” Frank akamuuliza!

    “Nina uhakika…tambua kuwa ninakuokoa!” Scola akamwambia huku ameangalia mbele.

    “Haya, nakusikiliza…”

    Hatimaye wakafika kwenye nyumba moja iliyokuwa katika mtaa ule, ambapo Scola aliliingiza gari hadi ndani kwa kupitia getini. Ni geti ambalo lilikuwa halijafungwa na wala hakukuwa na mlinzi. Baada ya kuliingiza gari, akalipaki mbele ya nyumba ile iliyokuwa imezungukwa na uzio wa michongoma pande zote, na pia kulikuwa na miti mingi iliyokuwa ndani ya uzio ule, kiasi cha kufanya kuwe na giza kiasi lilifanya taa ya nje ifunikwe mwanga wake.

    Wote wawili wakashuka na kuelekea ndani ya nyumba hiyo, ambapo Scola aliufungua mlango kwa kutumia ufunguo aliokuwa nao, halafu wakaingia hadi walipofika katika sebule nadhifu iliyokuwa imesheheni samani za gharama. Lakini kulikuwa kumepooza sana na kuonyesha hakukuwa na mtu yeyote aliyekuwa anaishi mle ndani, kwani hata harufu ya utupu ilinukia. Hata hivyo, Frank hakupenda kuhoji sana kwa muda ule, zaidi ya kwenda kujikalia kwenye kochi na kuvuta pumzi ndefu.

    “Karibu sana Frank…” Scola akamwambia huku naye akijikalia kwenye kochi sambamba na Frank.

    “Oh, nimekaribia…lakini bado nimechanganyikiwa!” Frank akamwambia huku akimuangalia kwa hadhari kidogo!

    “Usihofu Frank…umefika sehemu salama…” Scola akamwambia na kuongeza. “Nimeamua kuwasaliti…”

    “Hebu nieleze vizuri…maana mpaka sasa niko kizani!”

    “Nilikuwa upande wao, nikimsaidia kaka yangu Wibo Eze, ambaye alikuwa ananilipa vizuri sana .”

    “Ina maana na wewe ni mmoja wao?”

    “Ndiyo, nilikuwa mmoja wao…”

    “Na sasa je?” CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nimeamua kujitoa nikusaidie. Ni kama nilivyokwambia tokea mwanzo kuwa nimekupenda!”

    “Aisee? Na safari yangu ya kuja huku London ulikuwa unaifahamu?”

    “Ndiyo, nilikuwa naijua tangu Dar es Salaam , Tanzania . Na mimi ndiyo nilikuwa nakufuatilia, na si kweli kwamba nina shangazi yangu katika Ubalozi wa Nigeria nchini Tanzania . Hata hivyo nimejikuta nikikupenda ghafla na kuamua kwamba tupambane na kundi hili lililouiba mkufu kutoka ndani ya kasri ya kifalme!” Scola alisema na kuonekana kuwa alikuwa anajua mambo mengi sana , kitu ambacho kilimsisimua sana Frank!

    “Kumbe ni Wibo Eze, kaka yako ndiye aliyehusika na wizi huo wa mkufu?” Frank akamuuliza huku ameshika kichwa chake!

    “Ndiyo, ni yeye, akiwa ameshirikiana na mtu mwingine, tajiri wa Kikongoman, aitwaye Mokili wa Ngenge, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, anayeishi jijini Paris , Ufaransa. Lakini waliohusika zaidi kuuiba mkufu huo ndani ya kasri ile, ni watu wawili, Edmond Balle na Hamis Kengwa, kwa kushirikiana na kaka yangu, hapa London …”

    “Sasa walitumia njia gani mpaka wakafanikiwa kuingia ndani ya kasri ile bila kuonekana?”

    “Ni washirikina. Walitumia nguvu za giza na kuweza kuingia bila kuonekana na walinzi waliokuwa wanalinda, ukweli ni kwamba mpango huo ulikuwa umepangwa muda mrefu sana na pia kugharimu fedha nyingi sana !”

    “Baada ya kufanikiwa kuupora hu mkufu, wameupeleka wapi?”

    “Wameshausafirisha kwa ndege, kumpelekea Mokili wa Ngenge, kule Ufaransa. Mpaka tunavyoongea na wewe, watakuwa wameshafika na hata kumkabidhi mkufu huo.”

    “Sasa, kaka yako, Wibo Eze na Mokili Ngenge, walikuwa wametumwa na nani kuifanya kazi hiyo ya kupata mkufu huo? Na ni wa kazi gani?”

    “Mkufu huo unahitajiwa na Bilionea mmoja wa Kireno, aitwaye, Miguel da Silver, anayeishi nchini Angola , ambaye anauhitaji mkufu huo kwa sababu anazozijua mwenyewe.”

    “Mokili wa Ngenge anaishi sehemu gani katika jiji la Paris , kwa sababu unasema ni mtu maarufu sana …”

    “Mokili wa Ngenge ni mtu tajiri na anayejulikana sana . Anaishi katika mtaa wa Mtakatifu Dennis, ambapo makazi yake yanalindwa kwa muda wa saa 24 na walinzi waliopitia mafunzo makali, pamoja na mitambo. Basi, mtu huyo ni rafiki mkubwa wa kaka yangu, Wibo Eze!”

    “Nashukuru kwa kunifungua macho. Umenipatia mwanga, hivyo sina budi kumfuatilia hukohuko!”

    “Fanya hivyo. Lakini mimi nitabaki ili kaka yangu, Wibo Eze asinishtukie kuwa nimewauza kwenu.”

    “Utafanya hivyo, lakini tuwe tunawasiliana.”

    “Hakuna shaka,” Scola akasema huku akionyesha alikuwa na moyo wa kumsaidia Frank Mumba.

    Baada ya kumaliza maongezi yao , wakakumbatiana kwa muda huku mapigo yao ya moyo yakipiga kwa kasi na kuhitaji kitu fulani cha ziada. Lakini ule haukuwa muda wake. Walipomaliza kukumbatiana, wakaachiana na Scola akabaki akimwangalia Frank kwa nukta kadhaa kana kwamba alikuwa anamsikitikia kijana mzuri kama yule, kujiingiza katika kazi za hatari ambazo ni kuhatarisha maisha yake muda wote!

    Hata hivyo bila kupoteza muda, Scola akamuaga Frank, ambapo walitoka hadi nje ya nyumba ile ambapo gari lilikuwa limepaki. Akiwa katika hali ya unyonge, Scola akapanda garini na kuliondoa kurudi nyumbani kwa kaka yake, Wibo Eze, mtaa wa Porche Terrace, wakati huo ikiwa imetimu saa 11:40 kwa saa za Uingereza. Baada ya Scola kuondoka, ndipo Frank alipoamua la kufanya. Ni kumjulisha mpelelezi mwenzake, Bw. Brown Lambert!

    ********

    Kengele ya hatari iligonga kichwani mwa Wibo Eze, tokea alipokuwa amebaki pale nyumbani kwake. Kwani alipojaribu kupiga namba za simu ya mkononi ya Kim, mtu ambaye alimpa kazi ya kwenda kumteka nyara, Frank Mumba, iliita bila kupokelewa kwa muda wa dakika tatu hivi. Hata hivyo, ilipopokelewa tena, upande wa pili, Kim aliongea kitu ambacho kisichoeleweka, na kuonyesha alikuwa kwenye matatizo makubwa kwa jinsi alivyokuwa anahema!

    Kumbe wakati ule ndiyo walikuwa wakipambana na Frank Mumba, ambaye alifanikiwa kuwashinda na kutokomea gizani na gari lao, kurudi Hilton Hotel, alikopanga chumba. Hivyo basi, Wibo hakuchelewa, akatoka nje na kupanda gari lake jingine , aina ya Opel, na haraka sana akalitia moto na kuliondoa kwa kasi kuelekea katika nyumba ile iliyokuwa maficho yao ya kutesea watu wanaowahisi kuingilia mambo yao . Ni nyumba ambayo haikuwa mbali sana , ni kama kilo meta tatu hivi kutoka pale.

    Alitumia dakika kumi tu kufika hasa ukizingatia hakukuwa na usumbufu wowote wa magari barabarani. Akalipaki gari na kushuka hata bila kulifunga mlango, na kuuendea mlango wa kuingilia mle ndani, ambao ulikuwa wazi. Wibo akachomoa bastola yake na kuanza kuingia kwa tahadhari kubwa huku mtutu wa bastola ameuelekeza juu, na pia akitembea kiupande kwa kutanguliza mguu mmoja mmoja, wa kulia na wa kushoto.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog