Simulizi : The Last Summer In Tanzania
Sehemu Ya Tatu (3)
Bwana Timoth alikuwa amekaa kitini mwake, alionekana kuwa na mawazo mengi, kitendo cha binti mrembo, Rebecca kuchukuliwa na mwanaume mwingine kilimuumiza mno.
Kichwa chake kilimuuma, aliwatuma watu kwa ajili ya kumuua mtu aliyekuwa amemchukua msichana huyo, Mathias, lakini mpaka katika kipindi hicho, hakupata taarifa zozote kama mchakato mzima ulifanikiwa au la.
Aliambiwa kwamba mpaka saa tisa usiku kila kitu kingekuwa kimekamilika, yaani Mathias aliyejulikana kwa jina la Kenneth au Young Bilionaire angekuwa kashauawa.
Hiyo ilikuwa ni saa kumi na moja alfajiri. Kila alipokuwa akiangalia simu yake kuona kama kijana wake, Matata alikuwa akimpigia simu, alikuwa kimya, hakukuwa na simu yoyote iliyongia.
“Kuna nini? Mbona kimya?” alijiuliza pasipo kupata jibu.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hakutaka kulala, alikesha usiku mzima kwa ajili ya kufuatilia kile kilichokuwa kikiendelea. Alijaribu kuchukua simu yake na kumpigia Matata, simu ilikuwa ikiita lakini haikupokelewa, baada ya saa chache, ikawa haipatikani.
Akashuka kutoka kitandani na kuelekea sebuleni, kwa muonekano aliokuwa nao tu ulionyeshea ni namna gani alikuwa na mawazo tele.
Sebuleni hapo, akalifuata kochi na kutulia. Akachukua simu yake na kuanza kupiga tena, simu haikuwa ikipatikana.
Kwa sababu alikuwa na mawazo tele, alichokifanya ni kuifuata televisheni na kuiwasha. Ilipofika saa moja kamili, taarifa ya habari ikaanza kusomwa katika Kituo cha Televisheni cha MBC (Malawi Broadcast Co-operation).
Taarifa ya kwanza kabisa kusikika ilikuwa ni ya mauaji yaliyotekea katika Msitu wa Mushibwaha alfajiri ya kuamkia siku hiyo. Hakuonekana kushtuka sana lakini mara baada ya picha za maiti kuonekana, bwana Timoth akapigwa na mshtuko mkubwa.
Hakuamini kama vijana wake aliowatuma kwa ajili ya kumuua Mathias walikuwa wameuawa kinyama huku miili yao ikiwa imetobolewa kwa risasi kadhaa.
Hakuamini kile alichokuwa anakiona, akainuka kutoka kochini na kuisogelea televisheni ile, kile alichokiona kwa mbali na kukihisi kwamba ndicho chenyewe, hakikubadilka, kilikuwa kilekile.
“Matata...” alijikuta akilisema kwa mshtuko.
Hapo, akachanganyikiwa zaidi, walikuwa ni vijana pekee aliokuwa akiwategemea kufanya kazi zake kipindi chote, katika kila kazi alizokuwa akiwatuma, walizifanya kwa mafanikio makubwa ambayo yalimjengea kuwaamini zaidi.
Leo hii, vijana hao aliokuwa akiwategemea, walikuwa wameuawa vibaya msituni mara baada ya kuwatuma kumuua mtu aliyemchukua msichana mrembo, Rebecca.
“Hapana! Haiwezekani vijana wangu kuuawa!” alisema bwana Timoth pasipo kujua alikuwa akitaka kumuua mtu wa aina gani. Japokuwa Mathias alikuwa mwanaume tajiri, lakini undani wa maisha yake, hakuwa tajiri kama alivyokuwa bali alikuwa mpelelezi mwenye ujuzi wa kutumia bunduki na uwezo mkubwa wa kupigana na watu hata kama walikuwa kumi.
****
Gari ya kifahari, Lamboghin ilikuwa ikiegeshwa katika sehemu ya maegesho ya Kituo Kikuu cha Polisi hapo Lilongwe. Polisi wote waliokuwa nje, wakabaki wakilishangaa gari lile kwani lilikuwa ni miongoni mwa magari ya kifahari yanayovuma duniani.
Mlango wa gari hilo ukafunguliwa na Rebecca kuteremka, polisi wote wakapigwa na mshangao, si kwamba hawakumfahamu msichana huyo, walimfahamu lakini siku hiyo alionekana kuwa mrembo haswa.
Japokuwa ilikuwa ni usiku sana lakini kulikuwa na baadhi ya polisi waliokuwa mahali hapo, kwa mwendo wa madaha lakini wenye haraka akaanza kupiga hatua kuelekea katika mlango wa kuingia ndani ya jengo la kituo hicho.
Polisi waliokuwa nje ya jengo la kituo kile, walibaki wakimwangalia kwa macho ya matamanio, Rebecca hakutaka kujali, hakuwasalimia zaidi ya kwenda mpaka kaunta ya kituo hicho.
“Kuna nini Rebecca, mbona harakaharaka huku ukihema kwa nguvu?”aliuliza mmoja wa polisi waliokuwa kaunta.
“Mpenzi wangu ametekwa,” alisema Rebecca huku akilia.
“Unasemaje?” aliuliza polisi mmoja huku akionekana kutokuamini alichokisikia.
“Kenneth ametekwa.....!!” alisema Rebecca na kuanza kulia kwa sauti kubwa.
“Hebu subiri kwanza, vuta pumzi,” alisema polisi mwingine.
Rebecca akatulia, japokuwa hakuongea kitu chochote lakini bado aliendelea kulia, kila alipokuwa akikumbuka namna ambavyo mpenzi wake, Mathias alivyokuwa ametekwa na watu wasiojulikana na kupelekwa pasipojulikana, aliumia kupita kawaida.
“Aya hebu tueleze, nani ametekwa?”
“Mpenzi wangu!”
“Nani? Bilionea?”
“Ndiyo!”
“Ilikuwaje?”
“Kuna watu walikuja kutuvamia.”
“Muda gani?”
“Dakika kadhaa zilizopita.”
“Hivi ilikuwaje mpaka watu hao wakaja kuwavamia? Tena bila sababu?” aliuliza polisi mwingine.
Hapo ndipo Rebecca alipoanza kusimulia kila kitu kilichokuwa kimetokea, toka walipoingia ndani ya klabu mpaka walipotoka na mpenzi wake kutekwa waliposimamisha gari katika Makutano ya Barabara za Ilukweza na St. Joseph kulipokuwa na mataa.
Kwa sababu polisi walijua kwamba mtu aliyekuwa ametekwa alikuwa tajiri mkubwa, alichokifanya ni kujikusanya, wakachukua bunduki zao, wakaingia ndani ya gari lao na kuondoka huku wakiwa na Rebecca garini humo.
Safari yao iliishia katika makutano ya barabara hizo, walibaki wakiangalia huku na kule kana kwamba waliambiwa watu hao walikuwa wamejificha mahali hapo.
“Walielekea wapi?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Walielekea kule,” alijibu Rebecca huku akiinyooshea barabara iliyokuwa ikielekea upande wa Kaskazini.
Walichokifanya ni kuelekea kule walipoambiwa kwamba watekaji wale walielekea. Barabara ilikuwa tupu, hakukuwa na magari yaliyokuwa yakipita, walijaribu kuangalia huku na kule, hawakufanikiwa kumuona mtu yeyote yule.
“Tunatoka nje ya mji sasa, kweli tunaweza kuwapata?” aliuliza mmoja wa polisi wale, mkononi akiwa na bunduki yake.
“Huku tunajipoteza, tukienda kule, tunatoka nje ya Lilongwe, nadhani ni vigumu kufuatilia, cha msingi itatubidi tuanze msako kesho asubuhi,” alishauri mkuu wa polisi wale.
Hakukuwa na aliyebisha, kwa sababu kiongozi wao ndiye aliyeshauri hayo, wengine wakabaki wakiuunga mkono ushauri wake. Wakarudi huku wakiamua kuanza msako rasmi kesho yake.
*****
Gari likuwa likiendeshwa kwa kasi kuelekea katika Msitu wa Mushibwaha uliokuwa kilometa mia sabini kutoka katika Jiji la Lilongwe. Ulikuwa msitu mkubwa ambao mara nyingi watu waliokuwa wakifanya mauaji walikwenda kutupa miili ndani ya msitu huo.
Hakukuwa na simba wala chui, wanyama wengi waliokuwa wakipatikana ndani ya msitu huo walikuwa wale wanaokula majani tu. Ukubwa wa msitu huo ulikuwa ni kilomita mia tatu, kulikuwa na idadi kubwa ya miti mirefu ambayo mara nyingi watu wanaohusika na utengenezaji mbao walifika msituni hapo na kukata miti kadhaa kwa ajili ya matumizi hayo ya kutengeneza mbao.
Kwa sababu mauaji yalikuwa yameshamiri sana ndani ya msitu huo, serikali ikaamua kuweka ulinzi mkubwa lakini wala haikusaidia kwani polisi waliokuwa wakipewa majukumu hayo, walikuwa wakihongwa fedha kidogo na kuwaruhusu wahuni au wauaji kuingia msituni humo.
Msitu ukachafuka, damu zikatapakaa, kulikuwa na sehemu nyingi zilizokuwa zikitoa harufu mbaya ya miili ya watu au damu. Watu wakakatazwa kungia msituni humo kwani hali haikuonekana kuwa ya amani hata kidogo.
Gari lile liliendeshwa kwa kasi mpaka kuingia ndani ya msitu huo, hakukuwa na mtu aliyewaona kwa sababu ilikuwa ni usiku sana. Garini, waliendelea kumpiga makofi Mathias hata kabla ya kumuua.
“Ni lazima tukuue, haiwezekani utoke Tanzania halafu uje hapa na urukie wanawake wa watu,” alisema jamaa mmoja.
“Kosa langu ni nini?” aliuliza Mathias, alikuwa akijiamini kupita kawaida.
“Kutembea na mke wa mtu!”
“Kwani Rebecca aliolewa?”
“Hebu fumba mdomo wako, maswali ya nini.”
“Paaaaaa...” lilisikika kofi moja, lilitua usoni mwa Mathias. Hakuugulia maumivu, alikuwa kimya ila sura yake ilionyesha kwamba alikuwa na hasira mno.
Walipofika sehemu ambayo waliiona kufaa, wakateremka na kumshusha. Walikuwa vijana watatu huku kila mmoja akiwa na bunduki yake mkononi, kila mmoja aliikoki tayari kwa kumyatulia risasi Mathias aliyekuwa mbele yao.
Hawakujua ni kitu gani kilitokea na wala hawakujua ni kasi ya aina gani aliyokuwa nayo Mathias, ghafla, jamaa mmoja akajikuta akipigwa teke kali la mbavuni, mmoja wa wale vijana wawili waliobaki akashtuka na kutaka kufyatua akishikwa mkono wake ulioshika bunduki na kupelekwa begani na kuvunjwa kwa staili ya aina yake.
“Aauugghh...!” alipiga kelele jamaa huyo.
Yule mmoja aliyebakia, akaona usalama wake ni kumfyatulia risasi Mathias lakini cha ajabu alipofyatua risasi zile, akajikuta akimpiga mwenzake kwani alifanywa kuwa kama kinga na Mathias.
Likatoka teke moja takatifu lililotua shingoni mwa yule jamaa, kama mzigo, akajikuta akianguka chini kwani alipigwa sehemu iliyokuwa na mishipa mingi ya damu iliyoaanza kuvilia kwa ndani.
Haikuwa kazi kubwa, alitumia muda wa dakika moja tu kuwaweka chini wote. Jamaa yule aliyekuwa amevunjwa mkono bado alikuwa akiugulia maumivu pale chini, alichokifanya Mathias, akachukua bunduki na kuwamiminia risasi za kifua, alipomaliza, akaingia garini na kuondoka zake huku akiiacha miili ile msituni pale.
Polisi wakaanza kufanya upelelezi juu ya miili ile waliyoikuta katika msitu ule ikiwa imetobolewa na risasi kadhaa. Wakaanza kufanya msako ndani ya msitu huo kwa kuona kwamba wangeweza kuwaona watu waliowaua lakini waliambulia patupu, walichokifanya ni kuichukua na kuondoka nayo.
Uchunguzi wao haukuisha, kila walipoiangalia miili ile, ilikuwa ni ya watu waliokuwa wakiongoza kwa uharifu na fujo katika Jiji la Lulongwe. Walishukuru Mungu kuona watu ambao waliwashindwa kwa kipindi kirefu wakiwa wameuawa kwani wao walijaribu kufanya hivyo kwa miaka kadhaa lakini walishindwa.
Magazeti yalipotoa taarifa juu ya vifo vya watu hao akiwepo Matata aliyekuwa akiongoza kwa uharifu, watu wakanyoosha mikono yao juu kama ishara ya kumshukuru Mungu kwa kuona kwamba inawezekana ule uharifu uliokuwa ukifanyika mara kwa mara ungepungua.
Upande wa pili, usiku uliopita, Mathias alikuwa akitembea kuelekea nyumbani kwake. Hakuonekana kuwa na wasiwasi hata mara moja, japokuwa damu zilikuwa zimelichafua shati lake lakini hakutaka kujali, alichokuwa akikihitaji kwa wakati huo ni kufika nyumbani tu.
Alifika nyumbani baada ya saa moja, akaingia ndani na kutulia kochini. Alikaa mahali hapo kwa saa moja na ndipo mpenzi wake, Rebecca akaingia. Kitu cha kwanza, hakuamini kama yule aliyekuwa akimwangalia alikuwa mpenzi wake au la, akabaki akimshangaa.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alimuacha katika makutano ya barabara alipokuwa ametekwa na watu asiowafahamu ambao waliondoka naye kuelekea pasipojulikana, sasa kwa nini katika kipindi hicho alikuwa mahali hapo? Kila alipokuwa akijiuliza, alikosa jibu.
“Kenneth! Is tha you?” (Kenneth! Ni wewe?) aliuliza Rebecca huku akionekana kutokuamini.
“It is me! Where have you been?” (Ni mimi! Ulikuwa wapi?) aliuliza Mathias.
“I went to police station, I had to report what happened, are you okey?” (Nilikwenda kituoni kutoa taarifa kilichotokea, upo salama?) alijibu Rebecca.
“I’m okey! Just give me a hug,” (Nipo salama, hebu nikumbatie) alisema Mathias.
Rebecca hakutaka kujivunga, alichokifanya ni kumsogelea Mathias na kumkumbatia. Moyo wake ulijawa na furaha tele lakini wakati mwingine alikuwa akijiuliza maswali mengi yaliyomfanya mpenzi wake kuwa nyumbani hapo na wakati alikuwa ametekwa na kupelekwa kusipojulikana.
Maswali hayakuishia hapo, kila alipokuwa akiziangalia damu zilizochafua shati lake, alibaki akitetemeka na kuhofia kwa kuona kwamba mpenzi wake huyo alikuwa amejeruhiwa na watu wale.
“Kuna mengi ya kukuuliza,” alisema Rebecca huku akijitoa kifuani mwa Mathias.
“Uliza tu.”
“Ilikuwaje? Mbona una damu halafu unasema hawakukujeruhi?”
“Ni habari ndefu, jua kwamba nilipambana nao!”
“Ulipambana nao?”
“Ndiyo! Huwa sipendi kupambana na watu, ila ilibidi iwe hivyo!”
“Mmmh! Una nguvu kweli?”
“Unanionaje? Mtoto wa mama?”
“Sidhani, nahisi kuna kingine, ukiniambia kwamba ulipambana nao, nahisi unanidanganya tu!” alisema Rebecca, kwa mbali tabasamu likaanza kujengeka usoni mwake.
Walikumbatiana kwa mara nyingine tena na kisha kuelekea chumbani. Hakukuwa na mtu aliyelala, kila mmoja alikuwa na hamu ya mwenzake hivyo wakabaki utupu huku wakikumbatiana na sauti ya kitanda tu kusikika usiku kucha.
Asubuhi iliyofuata, taarifa ya habari ilionyesha kwamba kulikuwa na vijana ambao waliuawa ndani ya Msitu wa Mushibwaha. Hapo ndipo Rebecca alipoamini kwamba mpenzi wake alikuwa nyuma ya kila kitu kwani baadhi ya vijana ambao waliuawa siku hiyo ambao aliwaona katika televisheni, aliwafahamu kwani ndiyo waliokuwa wakiongoza kwa vurugu na mauaji hapo Lilongwe.
****
Moyo wake uliendelea kumuuma, hakuamini kama vijana wake walikuwa wameuawa na mtu mmoja ambaye wala hakuufahamu uwezo wake. Hasira zake zikawaka, hakutaka kusikia kitu kingine chochote zaidi ya kummaliza Mathias kwa mkono wake.
Hakujua ni kwa jinsi gani angeanza kummaliza lakini alichokuwa akikiona, msichana Rebecca ndiye ambaye angemsaidia katika kukamilisha mauaji hayo aliyokuwa ameyapania.
Alichokifanya ni kuchukua simu yake na kuanza kuzungumza na msichana huyo, kitu cha kwanza kabisa alichokifanya ni kumuomba msamaha kwa kile kilichokuwa kimetokea miezi tisa iliyopita. Rebecca akawa muelewa, kwa kuwa mzee huyo alikuja kwa lengo la kumuomba msamaha, akakubaliana naye.
“Hakuna tatizo, nimekusamehe, na si kwamba nimekusamehe sasa hivi, toka kitambo tu,” alisema Rebecca.
“Nashukuru sana. Naomba nikukaribishe kwenye sherehe kesho,” alisema bwana Timoth.
“Sherehe gani?”
“Natimiza miaka sitini, ningependa uwe mgeni mwalika katika sherehe hiyo,” alisema mzee huyo.
“Sawa, hakuna tatizo, ila sitoweza kuja peke yangu.”
“Unataka kuja na nani?”
“Mpenzi wangu.”
“Sawa, usijali, uwepo wako ni muhimu zaidi.”
“Sawa, itafanyika saa ngapi?”
“Saa sita mchana.”
“Mmmh! Mbona mchana?”
“Mimi ni mzee, siwezi kufanya sherehe usiku, ninachoka mno,” alijitetea bwana Timoth.
“Sawa. Tutakuja.”
Furaha ya bwana Timoth ikawa kubwa, lengo lake la kumuua Mathias likaonekana kwenda kukamilika, kitu alichokifanya ni kuandaa mikakati ni kwa jinsi gani zoezi lake lingefanyika mchana wa siku inayofuata.
Kitu cha kwanza kilichomjia kichwani mwake ni kwamba ilikuwa lazima amuue Mathias kwa kumuwekea sumu kwenye juisi, sumu ambayo ingechukua siku mbili mwilini mwake na ndiyo imletee madhara makubwa na hatimae kumuua kabisa.
Akawaandaa vijana wake ambao walitakiwa kuwaleta watu kadhaa ambao hawakuwa wageni rasmi bali watu waliotakiwa kuonekana kama wageni katika sherehe hiyo. Kila kitu kilipokamilika, akaandaa vinywaji na kununua sumu iitwayo Sporthimus, sumu iliyoweza kuua baada ya siku tatu kuingia mwilini mwa binadamu.
“Itafaa, nitamuwekea kwenye kinywaji,” alisema bwana Timoth huku akionekana kuwa na furaha tele. Usiku huo ukawa wa raha kwake kwa kuona kwamba angekwenda kukamilisha kile alichokitaka kesho yake.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Saa 5:30 asubuhi, magari ya wageni bandia yakaanza kuonekana nje ya jengo la bwana Timoth, muda wote geti lilikuwa wazi hivyo kulifanya kila gari lililofika nje ya jengo hilo moja kwa moja kuingia ndani. Kila mgeni aliyeteremka, alikuwa amevalia suti kali huku pembeni akiwa na binti mrembo.
Kwa muonekano tu, kila mtu aliyekuwa akiingia ndani ya jumba hilo alionekana kuwa na pesa nyingi, hawakuwa na mionekano ya shida, walionekana kuwa watu wenye fedha na ilikuwa ngumu kugundua kwamba watu hao walipangwa kuingia ndani ya jumba hilo, lengo kubwa likiwa ni kuwazuga Rebecca na Mathias.
Saa 5:43 asubuhi, gari la kifahari, Lamboghin ilikuwa ikisimama nje ya jengo hilo, japokuwa mtaa wa Livingstone ulikuwa ukikaliwa na watu waliokuwa na fedha nyingi lakini hiyo haikutosha kutokuliangalia gari hilo kwa ukaribu zaidi.
Ilikuwa gari ndogo ya watu wawili tu ambapo milango yake ilikuwa ikifunguka kwa kwenda juu huku ikiwa imeshuka sana, kwa jinsi muundo wake ulivyokuwa, gari hiyo haikustahili kuendeshwa kwenye barabara za Tanzania kutokana na matuta yaliyokuwepo.
Mara baada ya milango kufunguliwa, Mathias na Rebecca wakaanza kuteremka, kila mmoja aliyekuwa ndani ya eneo la nyumba hiyo akabaki akiwaangalia tu, walionekana kupendeza kupita kawaida.
Mathias alikuwa amevalia suti nyeusi, huku ndani kukiwa na kikoi cheusi kulichokuwa nje ya shati jeupe lenye tai nyekundu, miguuni alikuwa amevalia moka nyeusi zilizopewa jina la ‘Four angle’
Kwa Rebecca, alivalia gauni lake refu la rangi ya pinki lililokuwa na mpasuko mpaka pajani na kulifanya paja lake jeupe kuonekana kwa ukaribu zaidi, paja lisilokuwa na doa hata moja, paja lililofananishwa na mwanamuziki mrembo kutoka nchini humo aliyejulikana kwa jina la Khadija ambaye alijipa jina la Dida.
Mbali na gauni hilo, chini alikuwa amevalia viatu vyake vilivyokuwa na kisigino kirefu vilivyokuwa na rangi ya pinki huku vikiwa na michirizi miyeusi kwa mbali, kichwani, alizifunga nywele zake vilivyo kama wanavyofunga wanawake wa Kiafrika waishio nchini Marekani.
Uso hakuuacha hivi hivi, aliupendezesha kwa miwani yake ya kike iliyokuwa na rangi ya pinki kwa mbali na masikio yake yaliwekewa hereni kubwa zilizomfanya kuvutia zaidi.
Ukiachana na mkoba wake wa bei mbaya, Rebecca alionekana kuvutia, kila mwanamke aliyekuwa ndani ya jumba lile alibaki akimshangaa, alionekana kuwa mwanamke wa kisasa.
Walitembea mpaka katika sehemu iliyokuwa na mkusanyiko wa wageni wengine na kuanza kumsalimia mmoja baada ya mwingine. Walikuwa wakinukia vizuri, manukato ya The Prince waliyokuwa wamejipulizia yalitoa harufu nzuri iliyopagawisha pua za watu wote mahali hapo.
“Tunavyoangaliwa, mpaka najisikia noma,” alisema Mathias huku akijifanya kusikia aibu.
“Hahaha! Hata wewe unasikia aibu?”
“Ndiyo! Ila umependeza sana, sijutii kuwa na msichana mzuri kama wewe,” alisema Mathias huku akionekana kuwa na furaha isiyo kifani.
“Asante mpezi, ila hata wewe umependeza mno, hakika sijuti kuwa na mtu kama wewe,” alisema Rebecca.
Mapenzi yaliwateka sana lakini kila siku Mathias alijitahidi kujificha, hakutaka kumuonyeshea msichana huyo kwamba alikuwa mpelelezi na aliletwa nchini humo kwa kuwa alikuwa katika kazi kubwa ya kumtafuta muuaji aliyefanya mauaji nchini Tanzania, Gideon.
Sherehe ikaanza huku kila mmoja akiwa na furaha, baada ya mhusika, bwana Timoth kuwakaribisha wageni, akaanza kuzungumza maneno kadhaa na baada ya kuridhika, akaruhusu vinywaji vipitishwe kwa watu ili waendelee kunywa huku yeye akiendelea kuzungumza.
Vijana walioonekana kuwa shapu, waliovalia mavazi yenye kuvutia, wakatokea mahali hapo huku wakiwa na vyombo vilivyokuwa na glasi zilizokuwa na juisi na kisha kuanza kuwapitishia watu.
Kijana ambaye alikuwa amepewa jukumu la kuwagawia juisi Mathias na Rebecca, akaanza kupiga hatua za harakaharaka kuwapelekea vinywaji vile, chombo chake kilikuwa na glasi mbili na hakutaka kumpa mtu yeyote glasi zile, aliendelea kupiga hatua mpaka alipowafikia, akawapa glasi zile, tena kwa nidhamu kubwa.
“Asante,” walisema kwa pamoja huku Mathias akishika ile glasi yenye sumu pasipo kujua kama juisi iliyokuwa ndani ya ile glasi, ilikuwa na sumu.
“Cheeers baby...!” alisema Mathias huku akiwa kwenye uso wenye tabasamu pana.
“Cheers...!” aliitikia Rebecca.
Wote wakaanza kuzipeleka glasi zile midomoni mwao.
****
Bado Martin aliendelea kuigiza kama kichaa mitaani, watu waliendelea kumshangaa kila siku. Hakukuwa na mtu aliyemsogelea tena, bado alionekana kuwa kichaa mwenye hasira ambaye muda wowote ule alikuwa radhi kumchapa mtu yeyote kwa fimbo aliyokuwa akitembea nayo.
Katika kila sehemu aliyokuwepo, bunduki yake ilikuwa kiunoni mwake, alikuwa katika kazi nzito ambayo ingeweza kumchukua kipindi kirefu mpaka kukamilika.
Siku ziliendelea kwenda mbele huku kichaa huyo akiendelea kupata umaarufu kila siku. Alijulikana zaidi ya meya wa jiji hilo na makao yake makuu kama kawaida ilikuwa jalalani.
Aliendelea kufuatilia kila kitu kilichokuwa kikiendelea, japokuwa jeshi la polisi nchini Malawi lilikuwa na kitengo chao cha upelelezi lakini hakukuwa na mtu aliyeweza kugundua kama mtu waliyemuona kila siku kwamba ni kichaa, alikuwa mpelelezi kutoka nchini Tanzania.
Alizunguka kwa kipindi kirefu ndani ya jiji hilo, kila alipokuwa akiamka, alikuwa mjini lakini kuna kipindi akaamua kubadilisha mazingira, alitaka kutembea mitaani zaidi kwa kuamini kwamba huko angeweza kumuona Gideon.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alianzia kwenye mitaa ya uswahili, alizunguka sana na hata wakati mwingine watoto kumuimba kama kichaa, hakujali, alijifanya kichaa mwenye hasira.
Katika kila sehemu aliyokuwa akipita, alikuwa akiangalia vizuri. Alizunguka kwa zaidi ya mitaa mitano ya uswahilini lakini hakuambulia kitu. Baada ya kuona kwamba hakuweza kufanikiwa, alichokifanya ni kuanza kuelekea katika mitaa ya uzunguni.
Huko, mitaa ilikuwa kimya sana, majengo makubwa na ya kifahari yalikuwa kwa wingi. Alizunguka katika mitaa mingi na mwisho wa siku akajikuta akiwa katika Mtaa wa Livingstone.
Mtaa huu ulionekana kuwa tofauti, kulikuwa na msururu wa magari yaliyokuwa yakiingia katika jumba moja la kifahari, hakujua jumba lile lilikuwa la nani kwani magari yote yaliyokuwa yakiingia, yalikuwa ya kifahari mno.
Huku akiendelea kuyaangalia magari yale, ghafla akaliona gari alilokuwa akilifahamu kabisa, ilikuwa Lamboghin ya rangi ya nyekundu ambayo alipewa Mathias kwa ajili ya kufanikisha kazi zake.
Hakutaka kufuatilia sana kwani alijua kwamba mwenzake naye alikuwa kwenye mchakato wa kuhakikisha kwamba kazi waliyokuwa wamepewa inafanikiwa kwa asilimia mia moja.
Aliendelea kusonga mbele, wakati amekata kona na kuingia katiba barabara nyingine ya vumbi iliyokuwa imezungukwa na majumba ya kifahari, akakutana na kundi la wanawake waliokuwa wamekusanyika sehemu moja huku wakionekana kama wamekizunguka kitu.
Alitamani kuuliza ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea mahali hapo lakini haikuwezekana kuwa hivyo kwani bado alijulikana kama mwanaume kichaa.
Hapo, shombo kali ya samaki ikaanza kuzisumbua pua zake na kupata jibu la moja kwa moja kwamba kundi lile la watu waliokuwa wamesimama mbele ya meza hiyo walikuwa wakichagua samaki kwa ajili ya matumizi nyumbani kwao.
“Jamani kichaa anakuja, atatuchapa,” alisema mwanamke mmoja, alionekana kuwa na hofu moyoni mwake.
Sauti ya mwanamke huyo ikawashtua wengine, walipogeuka, macho yao yakagongana na macho ya kichaa yule aliyekuwa akija huku fimbo ikiwa mkononi mwake.
Mmoja baada ya mwingine wakaanza kuondoka mahali hapo, walimfahamu kichaa huyo, alikuwa mkorofi ambaye angeweza kukuchapa fimbo wakati wowote ule tena pasipo kumfanya kitu chochote, wakaanza kutawanyika.
Ndani ya sekunde thelathini, hakukuwa na mnunuaji yeyote mbele ya meza ile zaidi ya muuza samaki aliyejulikana kwa jina la Mutombo tu. Macho ya Martin yalipotua usoni kwa Gideon, kwanza akashtuka, akaanza kumwangalia vizuri usoni.
Japokuwa aliiangalia sura hiyo siku moja tu tena katika kipindi ambacho alikuwa akitaka kuja nchini Malawi, lakini aliikumbuka vizuri sura ile, ilikuwa ni ya yule mtu aliyejitambulisha kwa jina la Gideon ambaye alijifanya kipofu na kumuua mjasiriamali, Potter Mickey nchini Tanzania.
Kwa jinsi alivyokuwa amemkodolea macho, kwa kiasi fulani Gideon akaonekana kushtuka, akaanza kuwa na wasiwasi juu ya kichaa yule aliyekuwa akimwangalia, akajiandaa kuchukua bunduki yake iliyokuwa chini ya meza.
Alichokifanya Martin ni kuanza kumsogelea Gideon kwa mwendo ambao ulizidi kumtia mashaka, alipoifikia meza ile huku mkono wa Gideon ukiwa chini ya meza tayari kwa kuchukua bunduki yake, Martin akachukua samaki mmoja na kuanza kukimbia naye, yote hiyo ilikuwa ni kucheza na akili ya Gideon ili aone kwamba alikuwa kichaa kweli.
Kwa kitendo kile alichokuwa amekifanya, Gideon akashusha pumzi, akajiona mjinga kwa kutaka kuchomoa bunduki yake chini ya meza na wakati mtu mwenyewe alikuwa kichaa na alimsogelea kwa ajili ya kuchukua samaki tu.
Martin aliendelea kwenda mbele huku mkononi akiwa na samaki yule, wanawake mbalimbali walikuwa wakimwangalia huku kila mmoja akimshangaa.
Martin alitembea mpaka katika geti la kuingilia katika jumba la kifahari la bwana Timoth na kuanza kugonga kifujofujo, lengo lake kubwa likiwa ni kutaka kuonana na Mathias ambaye alikuwa ndani ya jumba hilo, alitaka kumpa taarifa kwamba mtu waliyekuwa wakimtafuta kwa kipindi kirefu alikuwa katika mtaa huo, hivyo walitakiwa kumkamata.
“Ngoo..ngoo..ngoo..” aliendelea kuligonga geti lile, kila mtu aliyesikia, akazichukia kelele zile kwani ndiyo kwanza sherehe ilikuwa imeanza ndani ya jengo lile la kifahari.
Kelele za mlango ule ndizo zilizowashtua watu waliokuwa ndani ya eneo la jumba lile la kifahari la bwana Timoth ambao walikuwa wakiendelea na sherehe kama kawaida yao.
Kitendo cha Mathias kupeleka glasi yake mdomoni, hata kabla hajainywa juisi ile, mlango ukaanza kugongwa kwa fujo, kelele zikawa nyingi kutoka getini na kumfanya kusitisha zoezi lake la kunywa juisi ile.
Alichokifanya mmoja wa walinzi akaelekea getini pale, akalifungua geti ili kuona ni nani alikuwa akiugonga mlango huo kwa fujo, ghafla, akajikuta akivamiwa na Martin kichaa, akaingia ndani.
Kila mmoja akabaki na mshangao, hawakuamini kama yule kichaa aliyepata umaarufu kwa kipindi kirefu alikuwa ameingia ndani ya jumba lile, wanawake wakaanza kukimbia kwani kila mmoja alimuogopa.
Japokuwa alikuwa akimfahamu Martin, alichokifanya Mathias, naye akajifanya kumuogopa, akaanza kurudi nyuma kwa lengo la kutaka kujificha. Alipoyagonganisha macho yake na Martin, akapewa ishara moja ambayo hakukuwa na mtu aliyeweza kuiona mahali pale, ishara iliyomwambia kwamba asimame kwa kuwa kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ameonekana?” hilo lilikuwa swali la kwanza alilojiuliza.
Martin akawa anaichezesha fimbo yake mkononi, akaanza kumsogelea Mathias mahali pale aliposimama na kuwafanya watu wote kuogopa kwamba angeweza kuchapwa na kichaa yule.
Huku akiwa amesogelewa, Martin akatoa ishara nyingine, ishara za siri ambazo hakukuwa na mtu yeyote aliyeelewa zaidi ya watu wa usalama wa taifa, ishara iliyomwambia kwamba ilikuwa ni lazima amkimbize.
Huku akiwa amemuelewa kabisa, Martin akachukua ile fimbo yake na kumchapa Mathias na kisha kuanza kukimbia kutoka nje. Mathias akajifanya kuwa na hasira, akatoka mbio na kuanza kumkimbiza Martin, hakukuwa na mtu yeyote aliyeelewa, naye Mathias akaonekana kama kichaa kwa kuwa alikuwa akimkimbiza kichaa.
“Kenneth...Kenneth....” aliita Rebecca lakini alikuwa amekwishachelewa, tayari wawili hao walitoka nje ya jengo hilo huku Mathias akiwa nyuma akimkimbiza Martin.
Kelele alizokuwa akizipiga Martin ndizo zilizowafanya watu wengi washangae, walikuwa wakijiuliza sababu ya Martin kukimbizwa na Mathias lakini hawakupata jibu, nao wakamchukulia kama Mathias alikuwa kichaa, na kama hakuwa kichaa, basi alikuwa amechokozwa na kichaa yule.
Mbio zao walikuwa wakielekea kule kulipokuwa na meza ile ya samaki ya Gideon ambaye alikuwa akiendelea kuuza samaki wake. Wakati wakiwa njiani, wanawake waliokuwa wamezunguka meza ile wakaanza kukimbia huku kila mmoja akimshangaa Mathias kwa kitendo chake cha kumkimbiza Martin kichaa.
Gideon hakuelewa kilichokuwa kikiendelea, alibaki akiwashangaa tu huku naye akiwa na swali kwamba ilikuwaje Mathias amkimbize kichaa yule lakini kitu alichokielewa, ni kwa sababu kichaa yule alikuwa mtata, basi ilikuwa ni lazima alimchokoza mtu huyo na ndiyo maana alikuwa akikimbizwa.
“Tutakimbia mpaka wapi? Mbona bado sijaelewa kinachoendelea? Huyo mtu mwenyewe yupo wapi?’ Mathias alikuwa akijiuliza maswali mfululizo pasipo kupata jibu.
Huku wakiwa wamefika karibu na ile meza ya samaki, Martin akaifuata na kuivamia, Gideon alitaka kuizuia lakini akashindwa, meza ikaanguka, samaki wote wakawa chini.
Hata kabla hajajua nini cha kufanya, akashtuka kuona mdomo wa bunduki iliyoshikwa na Martin kichaa ukimwangalia. Kuona hivyo, naye Mathias akatoa bunduki yake na kumnyooshea Gideon, kila mtu aliyekuwa akiliangalia tukio lile, akapigwa na mshangao.
Kichaa Martin kuwa na bunduki! Watu wote waliokuwa wakilishuhudia tukio hilo, wakapigwa na butwaa!
Gideon alibaki kimya, alikuwa akiwaangalia watu waliomzunguka, aliwagundua kwamba hawakuwa watu wa mchezo hata mara moja na walionekana kuwa na nguvu, ujanja, kujua mapigano hata zaidi yake, alichokifanya ni kuwa mpole tu.
Bado watu walikuwa wakiwaangalia, hawakuwa wakiwaelewa wale walikuwa wakina nani na walihitaji nini mpaka kumnyooshea bunduki muuza samaki.
Kitu ambacho kiliwashangaza watu zaidi ni kichaa Martin kushika bunduki na kumnyooshea Gideon. Wala hazikupita sekunde nyingi, Rebecca na watu wengine ambao walikuwa katika sherehe ile wakafika mahali hapo, hata wao walionekana kushangaa.
“Kuna nini mpenzi?” aliuliza Rebecca huku akimsogelea mpenzi wake, Mathias.
“Usinisogelee, baki hukohuko,” alisema Mathias huku akionekana kumaanisha kile alichokuwa akikizungumza.
Hakuwa na sura ya upole kama ile iliyozoeleka kila siku, leo hii, tena katika tukio kama hili, Mathias alionekana kuwa tofauti kabisa, hakuonekana kuwa na utani hata mara moja.
Kivutio zaidi mahali hapo kilikuwa ni Martin, yule kichaa aliyekuwa akivuma nchini Malawi, kitendo chake cha kushika bunduki bado kilizua maswali mengi.
Alichokifanya Martin, akamsogela Gideon huku Mathias akiwa na bunduki mkononi na kisha kumfunga pingu mkono mmoja huku mwingine akijifunga yeye na kuondoka mahali hapo.
Simu zikapigwa nchini Tanzania na kuwaambia kuhusu mafanikio makubwa yaliyokuwa yamepatikana katika ukamatwaji wa Gideon nchini Malawi, kwa haraka sana, ndege ya kijeshi ikatumwa mpaka nchini Malawi na kisha kupandishwa na kupelekwa nchini Tanzania.
Walipofika, hawakutaka kupoteza muda, moja kwa moja akapelekwa sehemu husika kwa ajili ya kuhojiwa kabla ya kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya mauaji yaliyokuwa yakimkabili.
Usiku wa siku hiyo, taarifa zikaanza kutangazwa kwamba yule mwanaume aliyemuua bwana Mickey chuoni zikaanza kutangazwa katika vyombo mbalimbali vya habari hasa redio na televisheni.
Kutokana na maendeleo makubwa ya teknolojia, watu walizipata taarifa hizo kwa haraka sana, kila mtu aliijua taarifa hiyo kuhusu kukamatwa kwa muuaji huyo aliyekuwa akitafutwa kimyakimya.
“Kuna barua pepe nimetumiwa kutoka nchini Marekani,” alisema Materu, mkuu wa kitengo cha Usalama wa Taifa.
“Inasemaje?”
“Wamekiri kwamba wao ndiye waliyemtuma kijana huyo kumuua bwana Mickey!”
“Mmmh! Kwa nini sasa?”
“Hatujui!”
“Sawa. Kisha wamesemaje?”
“Kwamba tumuachie huru kwani huyo ni mtu wao!”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kivipi? Yaani naye ni jasusi?”
“Ndiyo!”
“Hapana! Haiwezekani kuwa kirahisi namna hiyo,”
Kila mmoja alibaki katika hali ya sintofahamu, barua pepe iliyotumwa kutoka nchini Marekani tena ndani ya Shirika la Kijasusi la CIA iliwashtua mno.
Hawakuamini kama kwa kipindi chote hicho walikuwa wakifanya kazi ya kumtafuta muuaji ambaye naye alikuwa jasusi kama jinsi walivyokuwa. Walipokea maombi yote ya Marekani lakini kumuachia Gideon huru likaonekana kuwa jambo gumu sana, hawakutaka kukubaliana nalo.
Waliendelea kumshikilia mpaka pale ambapo CIA ilipotuma mwakilishi wake nchini Tanzania kwa ajili ya kulizungumzia jambo hilo.
Bwana Mendez, mwakilishi kutoka nchini Marekani katika Shirika la Ujasusi la CIA akafika nchini Tanzania na moja kwa moja kwenda katika Jengo la Usalama wa Taifa kwa ajili ya kulizungumzia suala lao.
Huko, aliwaambia kila kitu kilichokuwa kikiendelea na hata mauaji ambayo yalifanyika, yalitakiwa kufanyika miaka mitatu nyuma lakini kutokana na uzoefu aliokuwa nao bwana Mickey, hakuweza kuuawa kipindi hicho.
“Kwa hiyo mkaamua kumleta mtu wenu nchini Tanzania katika chuo kikuu ili kukamilisha kazi yenu?” aliuliza bwana Materu, walikuwa wamekaa katika chumba kikubwa cha kukutania kwa ajili ya mikutano, walikuwepo na viongozi wengine.
“Ndiyo! Hiyo ni sababu iliyotufanya tumtume mtu ili asigundue.”
“Sawa. Sasa mlijua vipi kama angekuja nchini Tanzania? Na kwa nini iwe Tanzania na isiwe uarabuni?” aliuliza bwana Materu.
“Tofauti na Afrika, angeshtukia na lingekuwa suala gumu sana. Mickey hakuwa mtu wa kawaida, alikuwa mtu wa juu mwenye uwezo mkubwa sana, akili nyingi, bila kufanya hivi, angeweza kutuletea balaa hapo baadae kwani alivunja sharti letu kubwa, hivyo alitakiwa kuuawa,” alisema bwana Mendez.
“Tumekuelewa, ila ni kwa nini mlimuua bwana Mickey?” aliuliza Materu.
Bwana Mendez akakaa kimya kwa muda, akaanza kumwangalia kila mtu aliyesimama mahali pale, alionekana kama alikuwa akiwachunguza, aliporidhika, akayahamisha macho yake na kuiangalia saa yake aliyoivaa.
Swali hilo likaanza kuyarudisha mawazo yake nyuma kabisa, toka alipoanza kazi katika shirika hilo la kijasusi na mpaka alipokutana na bwana Mickey ambaye kwa kipindi hicho alikuwa kijana mdogo.
Alikumbuka mengi, mwisho wa siku, akashusha pumzi ndefu.
“Unaweza kutuambia sababu ya nyie kumuua bwana Mickey? Hata kama kuna vizuizi vya wewe kutuambiwa, hebu tuweke wazi,” alisema bwana Materu.
Mendez hakuzungumza kitu, alibaki kimya huku akionekana kama mtu aliyekuwa akifikiria jambo fulani. Alikaa katika hali hiyo kwa sekunde kadhaa kisha kushusha pumzi ndefu na kuachia tabasamu la mbali lililoonekana kuwa na mashaka.
Aliwaangalia watu waliokuwa ndani ya chumba kile, walionekana kuwa watu makini sana lakini kwa jinsi alivyokuwa akijiamini, kuna kipindi kingine aliwaona kuwa watu wa kawaida mno, alichokifanya, akaipeleka mikono yake mezani, mkono wake mmoja ulikuwa na tattoo kubwa iliyosomeka ‘Merciless’ (Isiyo na huruma)
“Historia ya maisha ya bwana Mickey inaanzia mbali sana,” alisema Mendez.
“Tunajua, unaweza kutuambia yote kisha na sisi tutafanya uamuzi wetu,” alisema Materu.
“Hakuna tatizo, historia yenyewe ipo hivi…..” alisema bwana Mendez na kuanza kusimulia historia ndefu ya bwana Mickey, mengi yaliyokuwa yametokea huko nyuma mpaka Marekani kuamua kumtuma mtu amuue. Kila mtu alikuwa kimya akimsikiliza.
Kilikuwa ni kipindi cha baridi kali jijini New York, theluji zilitapakaa katika kila kona ndani ya jiji hilo hali iliyopelekea barabara zote za lami kutokuonekana kabisa kitu kilichopelekea halmashauri ya Jiji hilo kuleta magari kadhaa kwa ajili ya kuziondoa theluji hizo barabarani.
Mazingira yalikuwa mabovu, viwanja vya mpira, tenesi, NFL na vinginevyo vikatawaliwa na theluji hiyo iliyoonekana kila kona. Watu wakavaa makoti makubwa huku baadhi yao wakiwa na miamvuli kwani theluji iliyokuwa ikiendelea kudondoka, ilimkera kila mtu.
Huo ulikuwa mwezi wa saba, kipindi ambacho huwa na baridi kali nchini Marekani, waliokuwa wakicheza michezo ya kuteleza katika barafu, hicho kilikuwa kipindi chao na mashindano kadhaa kuanzishwa.
Mtoto wa miaka kumi na tano alikuwa amejikunyata karibu na pipa la takataka lililokuwa likiwaka moto, alikuwa akisikia baridi kali, koti kubwa alilokuwa amelivaa lililokuwa limechakaa mno, likaonekana kutoumsaidia kabisa.
Meno yake yalikuwa yakigongana, kila alipokuwa akizungumza au kupumua, moshi fulani ulitoka mdomoni mwake kwani kulikuwa na baridi kali mno.
Hakukuwa na mtu aliyemjali, wapitanjia wengi waliokuwa wakipita mahali alipokuwa, walikuwa wakimwangalia na kumpuuza, japokuwa alikuwa ameweka chombo kidogo mbele yake kwa ajili ya kupata msaada wa fedha kama ambavyo anafanya kila siku, siku hiyo ikaonekana kuwa gundu kwake.
Aliyatamani maisha mazuri, hakutaka kuendelea kuishi katika maisha hayo hata siku moja, alihitaji kuwa na magari ya kifahari, kuwa na nyumba kubwa na nzuri, kuwa na kiasi kikubwa cha fedha katika akaunti yake, lakini kwa jinsi hali aliyokuwa nayo, kila kitu kikaonekana kuwa ndoto ya mchana.
Kila alipokuwa akiyaona magari yaliyokuwa yakipita katika barabara nyingi ikiwepo St. Joseph Hill 34W, moyoni alijisikia kuwa na maumivu makali kiasi kwamba kuna wakati alimlaumu Mungu, aliona kama amemtenga na kuwapendelea watu wengine.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baba yake alifariki kwa ugonjwa wa kansa ya damu miaka miwili iliyopita katika Hospitali ya Lauren Medical Center iliyokuwa jijini Washington DC huku mama yake akimkimbia kwa sababu tu hakuwa na maisha mazuri hata kidogo na aliogopa kuwa na majukumu mengi lakini mbali na hilo, ukweli ni kwamba alipata mwanaume mwingine na kumwambia kwamba hakuolewa na wala hakuwa na mtoto yeyote yule.
Hakujua wapi pa kwenda, baada ya kukaa kwa kipindi cha miezi kadhaa huku akila na kulala mitaani, hapo ndipo alipoamua kujiunga rasmi na kundi la watoto wa mitaani jijini New York waliojipa jina la Outcast (Watengwa).
Hilo lilikuwa kundi kubwa la watoto wa mitaani na wa watu wasiojiweza ambao waliishi ndani ya jiji hilo huku muda wao mwingi wakiutumia kushinda karibu na mapipa yao machafu huku wakiwa wameyawasha moto kutafuta joto.
Hakukuwa na mtu aliyekuwa akipita mitaa hiyo kwani pamoja na kuwaomba watu fedha lakini kundi hilo la watoto hao ndilo lililoongoza kwa unyang’anyi mkubwa.
Kutembea na visu viunoni lilikuwa jambo la kawaida mno, kutokana na upatikanaji bunduki kuwa mwepesi nchini Marekani, baada ya muda nao wakajikuta wakimiliki bunduki.
Maisha hayo ndiyo aliyoamua kuishi, hakutaka kuondoka jijini humo kwani ndiyo sehemu pekee iliyokuwa ikimpa chakula na kiasi fulani cha fedha kwa ajili ya kuyaendesha maisha yake.
Hakuwa msafi wala hakuwa na fedha lakini kijana huyo alionekana kuwa tofauti na wengine katika kundi hilo. Uwezo wake kichwani wa kufafanua vitu na hata kutoa njia mbalimbali ambazo zingewawezesha kupata fedha zilikuwa kubwa kiasi kwamba kila mmoja alionekana kumshangaa.
Kwa hilo, akajikuta akipendwa na kila mtu, kila aliyetaka ushauri, alimpatia huku akiwasisitizia vijana wenzake wa kundi hilo kufanya jambo jingine zuri mbali na kuiba na kutumia fedha shaghalabaghala.
Ili kuonyesha mfano kwa wengine, kiasi kidogo cha fedha alizokuwa akigaiwa mara baada ya kuomba mitaani au hata kupora, alikuwa akizifungulia biashara lakini ugumu ulikuja pale alipokuwa akizihifadhi, wenzake walikuwa wakimuibia na hivyo biashara zake ndogondogo kufa.
“Do you see these New Yorkers?” (Unawaona hawa Wa New Yorkers?) aliuliza kijana huyo, alikuwa akiwazungumzia watu waliokuwa wakiishi jijini New York.
“Yes! What the hell with them?” (Ndiyo! Wana nini?)
“They have got lot of money, so, we have to take it from them,” (Wana fedha nyingi mno, kwa hiyo tunatakiwa kuzichukua kutoka kwao)
“How can we rob them? We are only two people, can we be able to take it from them? What if they have guns! Don’t you see they will shoot us down?” (Tutaweza vipi kuwapora? Tupo wawili tu, tutaweza kuzichukua kutoka kwao kweli? Je kama wana bunduki! Hauoni kama wanaweza kutufyatulia risasi?) aliuliza Sam, mmoja wa watoto wa mitaani.
Hapo ndipo kijana huyo alipoanza kufafanua kwamba maana yake haikuwa kushika bunduki au kisu na kuwavamia bali walitakiwa kufanya jambo ambalo lingewafanya watu hao wote kutoa fedha mifukoni mwao na kuwagawia kwa kununua vitu watakavyokuwa wakiviuza.
Hiyo ikaonekana kuwa akili nzuri lakini ilihitaji fedha kwa ajili ya kuanzisha biashara hizo. Walikuwa na umri mdogo hivyo upatikanaji wa fedha haukuwa rahisi kama kwa watu wengine.
Walichokifanya ni kujaribu kwenda katika hoteli kubwa mbalimbali kwa ajili ya kuomba kazi ili waweze kupata fedha za kufanya biashara ambazo walikuwa wamezipanga.
Siku ya kwenda huko, wote wawili, kijana huyo na rafiki yake Sam wakaamua kuvalia vizuri na kwenda katika Mghahawa wa McDonald uliokuwa katikati ya Jiji la New York, walipofika huko, waliomba kazi ndogondogo za kufagia na kusafisha vioo lakini hawakuweza kukubaliwa kwani hawakuwa wamefuata utaratibu wa kuomba kazi.
“Kwanza kaandikeni barua,” ilisikika sauti ya bosi wa mghahawa huo.
“Ila kazi zipo?” aliuliza kijana huyo.
“Bado sijajua, ila mkituma barua, siku zikitokea tutawashtua,” alisema bosi huyo.
Hakukuwa na muda wa kuendelea kubaki mahali hapo, walichokifanya, tena huku baridi likiendelea kuwapiga ni kuondoka mahali hapo na kurudi mitaani. Nguo safi walizozivaa siku hiyo zikaonekana kutokuwasaidia kabisa.
Hayo ndiyo yalikuwa maisha yao mitaani, kila siku walikuwa wakijaribu kwenda sehemu mbalimbali kutafuta kazi lakini hawakuweza kufanikiwa. Siku zikaendelea kukatika mpaka mtoto huyo alipokuja kukutana na msichana mzuri, msichana mrembo ambaye kwa kumwangalia, hata kama alikuwa mdogo lakini alionekana kuvutia sana, huyu aliitwa Elizabeth Kenz, binti mrembo aliyekuwa na asili ya Ujerumani.
“What is your name?” (Unaitwa nani?) aliuliza Elizabeth.
“My name is Potter Mickey from Harlem,” (Naitwa Potter Mickey kutoka Harlem) alisema Mickey huku akiutaja mtaa waliokuwa wakiishi watu masikini hapo New York.
“Harlem! Ooh My God! I’ve never expected to meet someone from Harlem, you look handsome,” (Harlem! Ooh Mungu wangu! Sikutegemea kukutana na mtu anayetokea Harlem, unaonekana mzuri mno) alisema Elizabeth huku akionyesha tabasamu pana.
Huo ndiyo ukawa mwanzo wa wawili hao kukutana. Japokuwa walikuwa na umri chini ya miaka kumi na nane lakini bado walionyeshana mapenzi ya dhati. Kila mmoja akatokea kumpenda mwenzake, walithaminiana lakini hakukuwa na mtu aliyekuwa radhi kumwambia mwenzake jinsi alivyokuwa akijisikia moyoni mwake.
Elizabeth alitoka katika familia ya kitajiri, alikutana na Mickey katika kipindi alichokuwa amekwenda maktaba na baba yake. Kwa kumtazama tu, hakuonekana kuwa na fedha, alionekana kujaa shida kwani hata muonekano wake, ulikuwa ni wa kimasikini sana.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kila mmoja akaanza kumuonea aibu mwenzake, hakukuwa na aliyekuwa na uwezo wa kumwangalia mwenzake machoni kwa zaidi ya dakika moja, wote wawili walikuwa wakijisikia aibu.
Wazazi wa Elizabeth wakamfahamu Mickey kama rafiki wa binti yao hivyo wakati mwingine walikuwa wakimpa nafasi ya kuja nyumbani hapo, kukaa na binti yao na kisha usiku kuondoka, alipokuwa akiondoka, hakukuwa na mtu aliyegundua kwamba Mickey alikwenda mitaani, kulala karibu na mapipa yaliyowashwa moto, maumivu yote hayo ya maisha yalibaki kuwa siri yake, hata Elizabeth, hakutaka kumwambia. Umasikini ulimtesa mno!
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment