Search This Blog

Sunday, 22 May 2022

MSALITI ASAKWE - 2

 







    Simulizi : Msaliti Asakwe

    Sehemu Ya Pili (2)



    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    BAADA ya kutoka Biharamulo, wakaendelea na safari kuelekea Mwanza. Vijana, Jean, Pierre na France wakawa wanawasiliana kwa simu zao za mkononi na Bw. Paul Rugoye, aliyekuwa jijini Mwanza, kuwapokea. Hakika yote yalizidi kumchanganya utingo Cosmas! Akayaweka rohoni! Lakini akipanga kuwa ni lazima aje kuyalipua baadaye itakapobidi.



    Dereva akaendelea kuendesha gari huku akipangua gea moja baada ya nyingine. Hakuwa na mawazo mengine zaidi ya kuwazia safari yake afike salama akiwa na wale watu alioambiwa awachukuwe, na mara nyingine alikuwa akivuta sigara na kupulizia moshi nje ya dirisha.





    *******

    Usafiri wa kwenda jijini Arusha ulikuwa umeshaandaliwa na Paul Rugoye, ambaye aliamua kuwafuata yeye mwenyewe. Kwa kutumia gari lake jipya kabisa aina ya Ranger Rover Vogue Sports, ambalo alikuwa amelinunua hivi karibuni kwa kiasi kikubwa cha fedha. Akiwa ni dereva mzuri wa gari, aliondoka Arusha na kusafiri kuelekea Mwanza, ambapo alitumia saa chache tu kufika kwa vile hakuwa na sababu zozote za kumfanya awe anasimama njiani. Alikuwa amejikamilisha kwa kila kitu.



    Hivyo baada ya Paul Rugoye kufika jijini Mwanza, alipanga kwenye hoteli nadhifu ya Rizano, iliyoko katika Barabara ya Nyerere, ambayo ni sehemu waliyokubaliana kukutana, ambapo pia mmiliki wa hoteli hiyo walikuwa wanafahamiana wakiwa wote ni wafanyabiashara wakubwa. Yeye Paul alikuwa amefika pale siku mbili zilizopita huku akifanya mawasiliano na watu wake, wakiwa katika safari nzima ya kutokea nchini Rwanda hadi Mwanza.



    Gari lile Mitsubishi Fuso lilifika jijini Mwanza salama. Baada ya kufika, vijana, wakashuka na kuagana na dereva, Anton Mjivumi, pamoja na utingo wake, Cosmas, kwa kuwafikisha salama.



    Walimkuta Paul Rugoye akiwasubiri kwa gari lake, sehemu ile ya Nyamagana walipofika na kulipaki lile lori. Bila kupotez\a muda, wote wakaingia kwenye gari la Paul wakiwa na mizigo yao yote iliyokuwa na vitu hatari. Safari ikaanza palepale, dereva akiwa ni Paul, kwani hakupenda kumpa kazi ile mtu yeyote, kwa kuhofia kushtukiwa. Hakuna jasusi anayemwamini mtu kirahisi! Ndivyo alivyokuwa yeye!



    “Habari za safari jamani…” Paul Rugoye akawaambia punde tu baada ya kupanda ndani ya gari.



    “Safari siyo mbaya sana mkuu!” Jean akasema.



    “Lakini tushukuru Mungu ametufikisha salama bila matatizo...” akadakia Pierre .



    “Kwa nini unasema hivyo?’ Paul akauliza huku akimwangalia Jean.



    “Ilikuwa ngumu na yenye mashaka!”



    “Mashaka kama yapi?”



    “Juu ya wale watu waliotufikisha hapa!”



    “Una maana dereva na utingo wake?”



    “Ndiyo.”



    “Wamefanya nini?”



    “Mimi binafsi, nina wasiwasi na yule utingo wa lile gari tulilokuwa timepanda. Kwa sababu muda wote alikuwa anatuangalia sana , kana kwamba anatuchunguza!”



    “Hata mimi nilikuwa na wasiwasi naye sana …” akaongeza Pierre .



    “Anaweza kutuchoma yule. Na kwa mbinu zangu za kijasusi simwamini!” France naye akadakia kwa msisitizo!



    “Aisee…basi ingebidi auawe!” Paul akasema na kuendelea.



    “Mbona hamkusema mapema mpaka tumeondoka?”



    “Lakini tumechelewa!” Akasema Jean.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    “Tuendelee na safari…” France akadakia.

    Safari ikaendelea…



    Ilikuwa ni safari ndefu, huku wakiipita mikoa ya Shinyanga, Tabora, Singida na hatimaye walipofika jijini Arusha kunako majira ya saa saba za usiku. Hawakupenda kulala njiani kwa kuhofia usalama wa watu wale, ukizingatia walikuwa watu wa hatari waliokuwa na silaha. Baada ya kufika,wakafikia kwenye nyumba ya Paul Rugoye iliyoko eneo la Kijenge.



    Ni nyumba iliyotumika kuhifadhi magari yake, na pia kama gereji, ambapo haikuwa rahisi kwa mtu yeyote kugundua kama kulikuwa na watu waliofikia pale, kwa sababu ilikuwa imezungukwa na uzio madhubuti wa michongoma.



    Kwa kuficha uovu wake, mbali na nyumba iliyokuwa Kijenge, Paul alikuwa anamiliki nyumba nyingine ya kifahari iliyo eneo la Sakina, sehemu alipokuwa anaishi na familia yake. Hivyo basi, vijana, Pierre , Jean na France wakafikia ndani ya nyumba ile na kukabidhiwa vyumba maalum vya kupumzika ili kuondoa uchovu wa safari ile ndefu.



    Lakini kabla ya kupumzika, wakiwa ni watu wa kazi, wakaanza kuzichambua silaha zao na kuzifanyia usafi!



    Ama kweli vijana wale walikuwa wamejindaa vya kutosha, kiasi cha kuweza kupambana na vyombo vya dola. Walipomaliza kuweka kila kitu sawa, wakalala kuutafuta usingizi ili kesho yake waanze kazi rasmi!





    ********

    Ndani ya jiji la Mwanza hali ilikuwa tofauti kidogo, kwani utingo wa gari aina ya Mitsubishi Fuso, Cosmas Kishoka, lililiowasafirisha vijana, Jean, Pierre na France, kutoka Rusumo mpaka jijini Mwanza, hakuwa na imani zaidi ya kuwa na wasiwasi nao. Hata baada ya kushuka na kupanda gari jingine aina ya Ranger Rover, na kupotea machoni mwao, roho yake ilikuwa bado ikimuhimiza kufanya jambo. Ni kujua watu wale walikuwa na agenda gani ya siri!



    Akiwa na dereva wake, Anton Mjivumi, walikwenda kulipaki gari lao eneo la Nyamagana, jirani na Uwanja wa Mpira wa Miguu wa Nyamagana, halafu wakaagana kila mmoja akaelekea nyumbani kwake kupumzika. Ni baada ya kutoka safari ile ya mashaka, ambayo kila mmoja hakujua ina siri gani ndani yake kutokana na kulipwa fedha nyingi.



    Basi jioni yake ilimkuta utingo Cosmas akiwa ndani ya baa ya Florida Inn, iliyoko mtaa wa Kaluta, alipokwenda kujiburudisha kwa kujipatia bia moja mbili tatu, ikiwa ni baa aliyoizoea sana , pamoja na kukutana na marafiki.



    Cosmas aliendelea kunywa taratibu na jamaa zake huku wakiongea maongezi ya kimaisha kwa ujumla,au hata masuala mengine ya ujana kwa kiasi fulani. Hata hivyo Cosmas akajikuta akielezea juu ya ile safari yao ya kutoka Rusumo, Ngara, hadi pale jijini Mwanza, wakiwa na wale watu watatu, ambapo yeye aliwaita wa ajabu ajabu. Alieleza kirefu huku wenzake wakimuuliza maswali kadhaa kutikana na watu hao waliotoka nchini Rwanda kwa njia ya siri!



    Mmoja kati ya watu hao, aliokluwa anakunywa nao, ni kijana mtanashati, Frank Mbuga. Huyu hakuna mtu aliyekuwa anajua anafanya kazi gani, zaidi ya kumwona akitanua.



    Ni kwamba alikuwa ni Afisa Usalama wa Taifa, ambaye alianza kuzichekecha habari zile na kuziona zilikuwa na umuhimu wa hali ya juu kiusalama juu ya watu wale. Kwa vile walikuwa wanafahamiana, Frank akamwomba Cosmas wakutane faragha, ili wazungumze suala lile. Cosmas hakubisha, wakatoka nje ya baa ile na kusimama sehemu ya kupaki magari, kando ya barabara mtaa wa Kaluta.



    “Samahani Cosmas kwa kukutoa huku nje…” Frank akamwambia.



    “Ah, usijali sana braza, ni mambo ya kawaida tu,” Cosmas akasema huku akiwa na hamu ya kutaka kujua alichomwitia.



    “Unajua wewe na mimi tumefahamiana kwa muda mrefu sasa…”

    “Ni kweli kabisa…”



    “Na kazi ninayoifanya unaifahamu.”



    “Ndiyo…nasikia nasikia ni Afisa Usalama wa Taifa kama sijakosea…”



    “Hujakosea!” Mbuga akamwambia na kuendelea. “Ndiyo maana nikakuita hapa nje ili unisaidie jambo moja muhimu sana.”



    “Jambo gani hilo ?”



    “Ni juu ya ile habari uliyokuwa unasimulia mle ndani kuhusu wale watu watatu mliotoka nao kule Rusumo, Ngara, na kuja nao hapa Mwanza…” akasema Frank Mbuga.



    “Oh, kumbe ni jambo hilo …niulize tu.”



    “Vizuri sana . Hivi wale watu watatu unaohisi ni Wanyarwanda ni kweli?”



    “Ndiyo. Nahisi hivyo kutokana na lugha waliyokuwa wanaongea,



    “Cosmas akasema na kuendelea. “Ni kinyarwanda na kifaransa, na hiyo nilijua kwa sababu mimi kikabila ni Muha wa Kigoma. Hivyo lugha waliyoongea inafanana na ya kwetu!”



    “Mliwachukuwa sehemu gani?”



    “Tuliwachukuwa eneo la mpakani, Rusumo, kama kilometa tatu hivi kutoka mpakani.”



    “Ina maana mliwapa lifti?”



    “Hatukuwapa lifti, bali dereva wa gari letu ndiye aliyekodiwa na mtu mmoja tajiri, wa Arusha, ili awachukuwe na kuwafikisha hapa Mwanza. Sisi tulikuwa tumetokea nchini Rwanda kupeleka mzigo wa mchele kutoka Kahama, ambazo ndizo shughuli zetu.”



    “Unamfahamu huyo mtu aliyemkodi dereva wako?” Frank akaendelea kumuuliza.



    “Kwa kweli simfahamu…lakini ni tajiri kutoka jijini Mwanza. Baada ya kufika hapa Mwanza, wakapanda gari jingine aina ya Ranger Rover, ambayo ni ya kampuni ya kuhudumia watalii kwa jinsi nilivyoiona. Walipopanda tu wakaondoka mara moja bila kuongea lolote la ziada…”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Je, wakati wakiwa ndani ya gari lenu uliwaona wakifanya nini mpaka ukawatilia mashaka?”



    “Niliwasikia wakiongea lugha yao , ambayo mimi naifahamu. Na mara nyingine wakisoma ramani ya mji wa Arusha, na pia walikuwa na mizigo, mabegi kila mmoja na la kwake!”



    “Makubwa!” Frank akasema. “Mimi nawatilia masghaka watu hao! Ni kwa nini waingie hapa nchini kinyemela bila kufuata utaratibu?”



    “Ndiyo maana na mimi nikawa na wasiwasi mkubwa!”



    “Basi, nashukuru sana Cosmas, itabidi nizifanyie kazi habari hizi!”

    Baada ya kumaliza mazungumzo yao wakarudi ndani ya baa na kuendelea na vinywaji. Frank akawa ameyahifadhi yote kichwani mwake, hakupenda kufanya mzaha. Aliona ni vyema habari zile azifikishe Makao Makuu ya Usalama wa Taifa, jijini Dar es Salaam, ili waweze kuchukuwa tahadhari na watu wale, ambapo hata yeye hakujua waliingia nchini kwa madhumuni gani! Hivyo Frank hakuendelea kukaa pale Florida Baa, bali aliaga na kuondoka akiwa amepanga ni lazima atoe taarifa usiku uleule bila kuchelewa!



    Ndiyo. Aliamua kumpigia simu Mkuu wa Usalama wa Taifa, Brigedia Matias Lubisi, ili awe na taarifa hizo mapema iwezekanavyo ukiwa ndiyo utaratibu wao wa kufikishiana kila taarifa wanazozipata. Baada ya kutoka nje, Frank akaliendea gari lake aina ya Toyota Sprinter, lililokuwa sehemu ya maegesho.



    Akapanda na kuondoka katika ofisi zao za Mwanza, ambazo ziko ufukweni mwa Ziwa Victoria , mkabala na Bandari ya Mwanza na siyo mbali sana na Makao Makuu ya Polisi, Mwanza, na Kituo Kikuu cha Polisi. Ni ofisi zilizoko katika jengo la kizamani la ghorofa tatu, lililojengwa kando ya majabali makubwa ya mawe yaliyofanya mandhari ya sehemu ile ivutie na kuonekana kama yalipangwa.



    Frank alipofika akalipaki gari lake na kushuka. Halafu akaelekea ndani ya jengo lile na kupandisha ngazi hadi katika ghorofa ya pili ilipo ofisi yake. Alipoufungua mlango tu, akapokewa na ukimya wa pekee kwa usiku ule hadi alipokaa kwenye kiti chake.



    Mbele yake palikuwa na simu mbili, moja ya mawasiliano ya ndani tu, na ile nyingine ya kutoka nje. Kwa vile alikuwa ameamua kumtafuta mkuu wake, akachukuwa mkonga wa simu na kumpigia ukizingatia sehemu ile ndiyo aliyoiona bora zaidi.



    “Haloo…Matias Lubisi anaongea…” Brigedia Lubisi akaipokea.



    “Mkuu…ni mimi Frank Mbuga…naongea kutoka jijini Mwanza.”



    “Oh, Mbuga…habari za huko?”



    “Habari ni nzuri mkuu...”



    “Ndiyo, naona umenipigia simu muda huu, bila shaka kuna chochote!”



    “Ndiyo mkuu, nimekupigia simu usiku huu, ili nikujulishe taarifa muhimu ambazo nimezinyaka hapa Mwanza.”



    “Ni taarifa gani hizo?”



    “Nimekutana na kijana mmoja, ambaye ni utingo wa magari makubwa ya mizigo...” Frank akamwambia yote aliyoelezwa na kijana Cosmas. Halafu akamalizia:



    “Hivyo basi, kuna watu watatu wameingia hapa nchini wakitokea nchini Rwanda ambao hawajulikani wamekuja kufanya nini!”



    “Nashukuru sana kwa kunipa taarifa hizo, tutazifanyia kuanzia kesho!” Brigedia Matias Lubisi akasema baada ya kumwelewa vizuri Frank Mbuga.



    “Haya mkuu…usiku mwema!” Akamaliza Frank.



    Hakika roho yake ilisuuzika baada ya kuzifikisha habari zile muhimu!





    ********



    Brigedia Matias Lubisi, Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, alikuwa amekaa zaidi ya nusu saa ndani ya ofisi yake asubuhi ile. Alikuwa akitafakari jambo lile zito ambalo lilitakiwa kufanyiwa ufumbuzi wa kina na kwa haraka ukizingatia alikuwa ni kiungo muhimu katika idara ile. Ni kuhusu ile simu aliyopigiwa usiku wa jana kutoka jijini Mwanza, na Frank Mbuga. Kwa upande wake aliona kuwa taarifa ile siyo ya kupuuza, hivyo akaona ni vyema atayarishe vijana wake wa kazi aliokuwa anawaamini iliwafuatilie kadhia ile jijini Arusha!



    Ingawa siku ile ilikuwa ni ya Jumamosi, na ni ya mapumziko, ilimbidi Brigedia Matias Lubisi kwenda ofisini kuweza kupanga mikakati ya kazi ile. Pia, alimtaarifu Katibu Muhtasi wake, Bi. Mary, aweze kufika kazini kutokana na dharura ile. Naye hakupinga akafika ofisini kama kawaida na kusubiri maelekezo. Hakika Bi. Mary alikuwa mwanamke shupavu, aliyekuwa akikutana na misukosuko mingi hasa zinapotokea kazi za dharura kama zile ambapo inabidi awepo kazini. Tuseme alikuwa mtu mzoefu sana ambaye hakuchoka wala kukata tamaa!



    Alikuwa mwajibikaji!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Brigedia Matias Lubisi alikuwa mtu mchapakazi ambaye hakupenda kupitwa na taarifa zozote anazopata, ambazo zinaweza kuhatarisha Usalama wa Taifa kwa ujumla. Yeye alichaguliwa kujiunga na idara ile baada ya kupitia mafunzo maalum ya kijeshi, na pia kulitumikia Jeshi la Wananchi wa Tanzania .



    Ni baada ya utendaji wake mzuri ndipo alipohamishiwa katika idara ile. Ingawa alikuwa na umri wa miaka 53 lakini alionekana bado kijana kutokana na kuutunza mwili wake kwa kufanya mazoezi mara kwa mara. Kitu uzembe kilikuwa mwiko kwake!



    Kwa muda wote aliokuwa amekaa pale ofisini, aliamua kumteua kijana James Upele, kuifanya kazi ile ya kufuatilia taarifa zile, akishirikiana na mwanadada, Sajini Sofia Mlanzi. Hao ni wapelelezi mashuhuri aliowaamini! Hivyo hakupoteza muda akabonyeza namba kumpigia Luteni James, ambapo alimpata:



    “Mkuu…Luteni James hapa…” upande wa pili ukasema.



    “Lubisi hapa…habari za asubuhi.”



    “Nzuri mkuu…naomba maelekezo…”



    “Maelekezo ni kwamba nakuhitaji ofisini muda huu…na kama una ratiba nyingine kwa sasa uiache kwanza, kwani kuna jambo la dharura limetokea, unanipata?”



    “Nimekupata Mkuu na hapa niko timamu!” Luteni James akasema kwa nidhamu ya hali ya kikazi.



    “Usikawie tafadhali!” Brigedia Matias Lubisi akasisitiza na kukata simu.

    Baada ya kutoa maelekezo yale, Brigedia Matias Lubis akabaki ndani ta ofisi yake akimsubiri James, na pengine akiliwazwa na runinga iliyokuwa kwenye kona, ambayo ilikuwa ikiendelea na matangazo yake.



    Ofisi za Idara ya Usalama wa Taifa ziko eneo la Upanga, Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, jijini Dar es Salaam , ikiwa ni sehemu tulivu sana . Ni ndani ya jumba la ghorofa nne, ambalo kwa mtu wa kawaida asingeweza kujua kama ilikuwa ni ofisi zaidi ya makazi ya mtu. Basi, ofisi ya Brigedia Matiasi Lubisi ilikuwa katika ghorofa ya tatu.



    ********

    Hakuna kitu kilichomchanganya Luteni James kama kile, kwani mipango yake aliyokuwa amepanga kwa siku ile ya Jumamosi ilikuwa imeharibika, baada ya kuitwa na mkuu wake wa kazi. Siku hiyo ya aina yake, James alikuwa na ahadi ya kukutana na mchumba wake, Diana, mwanadada mrembo wa kutamanisha, ambapo walikuwa wamepanga kwenda kustarehe katika ufukwe wa Coco , Oysterbay, baada ya kutengana kwa muda mrefu ukizingatia alikuwa masomoni.



    Basi, siku hiyo, kijana huyo mtanashati, Luteni James alikuwa na raha ya pekee, sasa mpango mzima umetibuka. Ni Diana Msofe, msichana mwenye umri wa miaka 26, kwa muda mrefu alikuwa anasoma kwenye Chuo Kikuu cha Sokoine, Morogoro, akisomea Uchumi. Kwa hivyo ulikuwa ni muda muafaka wa kustarehe, kubadilishana mawazo, pia kukumbushana mengi ya zamani, na kupanga mipango ya kufunga ndoa.



    Baada ya kupigiwa simu, Luteni James aliingia maliwatoni kuoga, na alipomaliza akarudi chumbani na kuvalia nadhifu. Kisha akatoka nje ya nyumba yake aliyokuwa anaishi eneo la Oysterbay. Akaliendea gari lake aina ya Toyota Civa, lililokuwa ndani ya banda na kuondoka nalo kuelekea ofisini. Haikumchukuwa muda mrefu akafika ofisini na kuliegesha sehemu ya maegesho. Kwa ujumla sehemu yote ilikuwa kimya kabisa, ukizingatia ilikuwa siku ya Jumamosi. Akashuka na kuliendea lile jengo la ofisi na kupandisha ngazi kuelekea katika ghorofa ya tatu.



    Luteni James alifika kwenye ofisi ya Katibu Muhtasi, Bi. Mary, ambayo ilikuwa ni ya mwanzo kabla hujafika kwa mkuu wao, Brigedia Matias Lubisi. Ndani ya ofisi ile akamkuta akichapa kazi kwenye kompyuta, na alipoinua kichwa chake akamwona ni James akiingia kwa hatua za taraibu. Akaacha kuchapa na kumwambia: “Karibu James…”



    “Ahsante…za saa hizi dada Mary…” James akasema.



    “Nzuri kaka James…karibu.”



    “Natumaini bosi yupo…”



    “Ndiyo, anakusubiri…”



    Luteni James akagonga mlango na kuingia ndani ya ofisi ya Brigedia Matias Lubisi. Akamkuta amekaa katika kiti cha mzunguko akimsubiri yeye, na kama kawaida akamsabahi na kukaa kwenye kiti kilichokuwa mbele yake wakawa wanatazamana.



    “Karibu James...” Brigedia Matias Lubisi akamwambia huku akimwangalia kupitia chini ya miwani yake aliyovaa.



    “Ahsante mkuu...” Luteni James akasema anagali bado amesimama.



    “Keti tafadhali...”



    Luteni James akavuta kiti na kukaa wakitazamaba sambamba na mkuu wake.



    “Usishangae kukuita ghafla ofisini James...”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hapana, siwezi kushangaa, hiyo ni moja ya kazi zetu...”



    “Vizuri sana , basi, kuna jambo muhimu nataka kukueleza. Ndiyo maana nikakuita Jumamosi hii ya leo.”



    “Ndiyo mkuu…nakusikiliza…”



    Brigedia Matias Lubisi akamweleza yote Luteni James, juu ya kazi ile ya kufuatilia watu wale, kwa mujibu wa simu aliyokuwa amepiga Frank Mbuga, kutoka jijini Mwanza.



    Halafu akamalizia kwa kusema: “…Sasa nakutuma kazi hiyo ya kufuatilia watu hao walioingia hapa nchini kinyume cha utaratibu, ambao wametokea nchini Rwanda , kupitia njia za panya, mpakani Rusumo, Ngara, kuelekea Arusha. Sisi tukiwa ndiyo tunashughulika na Idara ya Usalama wa Taifa, ni budi kulifuatilia jambo hili kwa kina. Inawezekana ikawa ni vinara wa magenge ya uhalifu waliojipenyeza kuja kufanya hujuma kadhaa ndani ya nchi yetu yenye Amani na utulivu!”



    Brigedia Matias akameza mate na kuendelea: “Safari ya kwenda Arusha mtaongozana na Sajini Sofia Mlanzi, ambaye naye yuko njiani kuja hapa ofisini. Kwa hivyo unatakiwa ujiandae, na kuhusu masurufu ya safari yanaandaliwa na ofisi ya fedha, na mhasibu nimeshamtaarifu, sijui umenipata?”



    “Nakupata mkuu…” Luteni James akasema na kuendelea. “Tena nimefurahi baada ya kunishirikisha na Sajini Sofia . Sofia ni askari mzuri aliyenisaidia katika operesheni nyingi sana . Ukweli ni kwamba nimeridhika!”



    “Nashukuru kwa hilo . Basi, usafiri wa ndege utakuwepo, ambao ni wa ndege ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania . Mtakapofika Arusha mtapokewa na Meja Bombe, ambaye atawapa maelekezo yote. Pia, mtakuwa chini yake mtakapokuwa pale Arusha. Hivyo nawatakia safari njema, isipokuwa tuwe tunawasiliana mara kwa mara kwa kila hatua zinavyokwenda. Na hiyo ni kwa ajili ya usalama zaidi!” Akamaliza Brigedia Matias Lubisi.



    “Ndiyo mkuu…yote nimeyasikia. Kilichobaki ni utekelezaji tu,” Luteni James akamaliza, kisha akamuaga mkuu wake na kuelekea ofisini kwake.



    Baada ya kuingia ofisini na kukaa tu mwanadada, Sajini Sofia Mlanzi akagonga mlango na kuingia. Moja kwa moja akaelekea kwenye kiti kimojawapo na kukaa huku akionyesha sura ya tabasamu kama kawaida yake.



    “Ndiyo mkuu…kumekucha…” Sajini Sofia akamwambia.



    “Na kweli kweli kumekucha Sofia ….natumaini na wewe umekurupushwa kama mimi.”



    “Ni kweli nikumekurupushwa…”



    “Basi ndiyo hivyo, si unajua ndiyo tulikuwa tunajiandaa kwa kuianza wikiendi? Tena mbaya zaidi nilikuwa na miadi ya kukutana na mchumba wangu, Diana, tukapunge upepo ufukwe wa Coco , Oysterbay. Si unajua kwamba hatujaonana naye muda mrefu?” Luteni James akamwambia Sajini Sofia.

    “Oh, pole sana mkuu…”



    “Nimeshapoa…tupange mipango yetu ya safari…” Luteni James akasema huku akimwangalia Sofia kwa makini, akiamini kwamba kweli alikuwa mwanamke wa shoka aliyepangwa naye kazi.



    Ni mwanamke mrembo aliyeumbika kike kwa kila kiungo chake. Alichaguliwa kujiunga na Idara ya Usalama wa Taifa baada ya kumaliza mafunzo maalum ya kijeshi. Kielimu alikuwa amehitimu kidato cha sita katika moja ya shule za Sekondari hapa nchini. Yeye hakuwa mwanamke legelege, alikuwa mkali katika mapigano ya aina mbalimbali aliyofundishwa chuoni. Kiumri alikuwa na umri wa miaka 28 hivi, akiwa bado hajaolewa!



    Ndiyo. Luteni James aliridhika kuwa naye!



    Kwa upande wa Luteni James Upele, alikuwa bado kijana, mwenye umri wa miaka 35 hivi, ambapo alichaguliwa kujiunga na idara ile baada ya kufanya vizuri katika mafunzo ya kijeshi, pia alikuwa na elimu ya kidato cha sita. Mbali ya hayo alikuwa mkali katika sanaa ya mapigano kama , Judo na Kareti, na utumiaji wa silaha za kila aina. Alikamilika katika kila idara kiasi cha kufanya awe bidhaa muhimu sana.



    Luteni James na Sajini Sofia wakapanga mipango yao ya safari ya kwenda Arusha hapo kesho yake. Wakaagana na kuahidiana kukutana kesho yake. Hata hivyo, James hakwenda nyumbani kwake kwa ajili ya maandalizi, isipokuwa aliamua kuelekea Kinondoni Mkwajuni, nyumbani kwa mchumba wake, Diana Msofe, kwani walikuwa wameahidiana kukutana jioni ile ya Jumamosi.



    Ni Jumamosi ya aina yake!



    ********

    Saa nane za mchana, Luteni James alisimamisha gari nje ya nyumba ndogo iliyokarabatiwa vizuri. Ni moja kati ya nyumba zilizokuwa za Shirika la Nyumba la Taifa zilizouzwa, ambapo ndipo alipokuwa anaishi Diana Msofe. Baada ya kushuka garini akaelekea ndani ya nyumba ile, ambapo mlangoni alikutana na Diana aliyekuwa anakwenda kumpokea.



    “Oh, karibu sana James…” Diana akasema huku akimwewesa.



    “Ahsante sana Diana…” James akasema huku akitabasamu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nilifikiri hutatokea kwa vile ahadi yetu haikuwa muda huu.”



    “Ni kweli Diana…” James akasema huku akiingia pale sebuleni na kukaa katika kochi dogo.



    “Kulikoni?” Akauliza Diana.



    “Kilichonifanya nichelewe, ni kwamba wakati wanajiandaa kuja huku, nikaitwa na Bosi wangu, mzee Matias Lubisi…”



    “Mh, Jumamosi hii?”



    “Ndiyo hivyo tena…ni kazi!”



    “Aisee…kuna nini tena?” Diana akauliza huku akianza kuwa na wasiwasi.



    “Ni mambo ya kikazi tu. Ninasafiri kwenda Arusha kama unavyojua kazi zetu…”



    “Ina maana hata miadi yetu ya leo ndiyo basi tena…haitowezekana?”



    “Itabidi iwe hivyo mpenzi. Vumilia tu, nitarudi na kukutana tena.”



    “Ni sawa…na hiyo ni moja ya shughuli za kikazi,” Diana akasema huku akimkumbatia James.



    “Nashukuru umeelewa hilo …” James akamwambia huku akimfuata machozi mchumba wake Diana.



    Ingawa Diana hakuifurahia safari ile, James hakujali sana . Ilikuwa ni wajibu wake na nilazima atekeleze. Basi kilichofuata pale, Diana akamtayarishia chakula kizuri ambacho walikula wote kama wapenzi wawili, kisha wakaendelea kunywa vinywaji laini huku wakiongea hili na lile, hadi ilipotimu saa tatu za usiku, ndipo James alipoondoka kwenda kujitayarisha kwa safari ya kwenda Arusha.



    Baada ya kufika nyumbani kwake, Oysterbay, James akaanza kupanga nguo zake chache na kuziweka ndani ya begi, na pia akachukuwa vifaa vidogo vya upelelezi, pamoja na bastola yake ambavyo vyote alivihifadhi vizuri. Alipomaliza kupanga kila kitu, James akaingia bafuni na kujimwagia maji ya baridi. Alipomaliza akaingia chumbani kwake kulala, kuutafuta usingizi uliokuwa mbali…



    ********

    Ndani ya jiji la Arusha, kwenye nyumba ya Paul Rugoye, eneo la Kijenge, vijana watatu, Jean, Pierre na France, walikuwa wameamka asubuhi na mapema ikiwa ni siku ya pili yake tokea wafike pale. Baada ya kuamka wakafanya mazoezi ya viungo katika sehemu ya nyuma ya nyumba ile, ambapo ilikuwa siyo rahisi kuonekana, ikiwa ni mahali ambapo walionyeshwa na mwenyeji wao Paul Rugoye, kabla hajaondoka usiku, kuelekea nyumbani kwake, Sakina, na kuahidiana kukutana asubuhi tayari kwa kupanga mikakati ya kazi inayowakabili.

    Baada ya kumaliza kufanya mazoezi yao , wakaingia bafuni na kuoga, katika mabafu yaliyokuwa mlemle ndani. Wakati wote huo Paul alikuwa ameshafika kutoka nyumbani kwake, akakuta vijana wake wameshamaliza kuoga, na wanamsubiri yeye ili awape maelekezo zaidi. Vijana wote watatu walikuwa wamekaa katika chumba kimoja kilichokuwa kama ukumbi mdogo na mbele yao pakiwa na runinga kubwa wakiangalia, na pia walikuwa wakifungua kinywa kwa chai nzito na mapochopocho waliyoletewa na Paul asubuhi ile.

    Kamwe, Paul hakupenda vijana wale waonekane nje na mtu yeyote zaidi ya mlinzi mmoja wa pale, aliyekuwa ameshapewa karipio kali kwamba asieleze chochote anachokiona ndani ya nyumba ile, zaidi ya kunyamaza. Baada ya kumaliza kufungua kinywa, ndipo Paul na vijana wake wakaamua kukaa kikao ili kupanga cha kufanya, yeye Paul akiwa ndiye kiongozi na mwenyeji wao jijini Arusha.

    “Ndiyo ndugu zangu…natumaini mambo shwari sasa…”

    “Mambo ni shwari. Tunachosubiri ni kazi tu!” Kijana Pierre akasema.

    “Ni kweli, tupe kazi!” Akadakia Jean.

    “Tupe kazi!” Akaongeza France .

    “Hakika mnanipa moyo kuwa mna hari ya kazi. Sasa tupange cha kufanya. Kazi yenyewe itaanza leo jioni, na mpangilio wake utakuwa kama ifuatavyo. Mimi nitaondoka na wewe Pierre kuelekea eneo la Njiro, ambapo ndipo walipopewa hifadhi watu wetu tunaowatafuta, Roman, Teobale na Laurent. Hivyo basi, nyie France na Jean mtasubiri humu ndani kama watu wa akiba, sisi tutaenda kuifanya kazi hiyo ukizingatia mimi ni mwenyeji na mtu tajiri na ninayejulikana, siyo rahisi kushtukiwa wala kutiliwa mashaka. Sijui mnanipata?”

    “Mpango wako ni mzuri kama unavyosema. Na kiusalama siyo vizuri tukaongozana wote,” Kijana Pierre akasema.

    “Hakuna tatizo,” Jean naye akasema.

    “Ulivyopanga ni sawa mkuu!” Akaongeza France . “Tuko kwa ajili ya kazi!”

    “Ni vizuri sana kama mmenielewa,” Paul Rugoye akamaliza kusema.

    Halafu wakaendelea kupanga mikakati yao huku wakipitia vielelezo muhimu, na pengine walikuwa wakisafisha silaha zao walizotoka nazo nchini Rwanda , na kuzipangilia katika mpango unaotakiwa. Baada ya kumaliza wakabaki wakiangalia runinga angalau kupoteza muda, ukizingatia walikuwa na muda mrefu sana wa kukaa ndani ya nyumba ile kwa kukwepa kuonekana!



    ********

    Hali ya hewa ilikuwa ni shwari huku kijua cha asubuhi kimechomoza upande wa Mashariki mwa jiji la Dar es Salaam . Kwenye Uwanja wa Ndege wa Jeshi la Anga, Ukonga, ndege ndogo aina ya ‘Twin Otter’, ilikuwa imepaki tayari kwa safari ya kwenda Arusha. Kando yake alionekana Rubani Mkuu akiikagua ndege ile sehemu zote kwa kuizunguka na Msaidizi wake naye alikuwa akimfuatilia kwa makini. Asubuhi hiyo iliwakuta Luteni James na Sajini Sofia wakiwa pale uwanjani tayari kwa safari ya kwenda Arusha katika kazi ile maalum. Baada ya muda wakapanda ndani ya ndege pamoja na abiria wengine na rubani akaiwasha na kuiondoa kwa mwendo wa taratibu kuelekea katika barabara yake ya kurukia, na pia akiwasiliana na waongoza ndege waliokuwa katika chumba cha mawasiliano.

    Halafu akaongeza mwendo na kuipeleka kwa kasi na hatimaye kuirusha angani kuelekea Arusha. Wakati wote huo, James na Sofia walikuwa kimya kabisa hadi ndege ile ilipotulia angani. Hata hivyo haikuwa safari ya kuchosha sana hadi walipofika Arusha na kutua salama katika uwanja wa ndege wa Arusha. Pale wakapokewa na Meja Bombe, aliyefika pale kwa gari aina ya Land Rover 110 ya Idara ya Usalama wa Taifa, pamoja na dereva, kijana Peter. Peter akaenda kuwapokea ile mizigo yao baada kushuka ndani ya ndege ile ya jeshi. Wote wane wakapanda ndani ya gari na kuondoka kuelekea katikati ya jiji, walipokuwa wametayarishiwa vyumba vya kulala, na pia kupitia ofisini ili kupanga mikakati ya kazi ile.

    Dereva akaliondoa gari na kuelekea moja kwa moja hadi katika ofisi za Idara ya Usalama wa Taifa zilizoko Barabara ya Boma, katikati ya jiji la Arusha. Baada ya kufika, dereva akaliingiza gari kwa kupitia getini kwa kuifuata barabara ndogo ya kokoto iliyozungukwa na miti pande zote kuelekea katika jengo la ofisi ile iliyokuwa umbali wa mita thelethini kutoka getini. Kama yalivyo majengo yaliyojengwa zamani, lilikuwa ni jengo la ghorofa moja lililojificha kwa kuzungukwa na miti ya aina mbalimbali iliyofanya mandhari ya pale ipendeze. Isitoshe palikuwa na waya uliokuwa na seng’enge.

    Kwa ujumla eneo lote lilikuwa kimya kabisa, hasa ukizingatia ilikuwa siku ya Jumapili. Baada ya dereva kulipaki gari, wakashuka na kuelekea katika ofisi ya Meja Bombe, iliyokuwa katika sehemu ya chini, tayari kwa kupanga mikakati ya kazi. Wakakaa katika viti vilivyokuwa mbele ya meza ya Bombe na kuanza kumsikiliza.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Karibuni Arusha…” Meja Bombe akawaambia.

    “Ahsante mkuu!” Luteni James akasema.

    “Ahsante Mkuu…” naye Sajini Sofia akasema.

    “Ni matumaini yangu nyote mnaelewa kilichowaleta hapa Arusha…”

    “Ndiyo mkuu, tunaelewa. Ni majukumu ya kazi!” James akasema.

    “Basi, ndiyo kama mlivyosikia. Ni kwamba kuna watu wameingia hapa Arusha kinyemela bila kujulikana, hivyo inawabidi kufanya upelelezi wa kina, ukizingatia hatuwafahamu watu hao, na sehemu walipofikia. Cha muhimu ni kuwa makini sana huku mkijua kwamba mnapambana na watu msiowajua. Ili nisiwachoshe mpaka muda wa kupumzika, napenda kukutaarifu James, kuwa umepangiwa kufikia nyumba ya wageni ya Serena Inn …” akanyamaza kidogo huku akiwaangalia.

    “Kila kitu kimeshalipiwa. Wewe Sofia utafikia katika hoteli ya Victoria Villa, iliyoko mtaa wa Bondeni, na mtakapotoka hapa, dereva atawapeleka…” Meja Bombe akamaliza kusema.

    James na Sofia wakamwelewa. Halafu wakaondoka kuelekea katika hoteli waliyopangiwa ili kupumzika na kujiandaa kwa kazi ile nzito!

    ********

    Jioni ya siku ile, majira ya saa mbili za usiku, Paul na Pierre walikuwa wameshajiandaa vya kutosha, tayari kwa safari ya kwenda eneo la Njiro. Walivalia nadhifu, mavazi maalum, ambayo kwa mtu wa kawaida angeona kama ni suti, kumbe ni nguo zilizokuwwa zimebeba silaha ndani yake, kama bastola zilizosheni risasi, sumu kali, visu maalum vya kijasusi, na hata mikasi ya kukatia waya. Ni vifaa ambavyo hutumiwa mara nyingi na Majasusi!

    Hatimaye wakapanda gari dogo aina ya Toyota Corolla, ambalo ni kati ya magari kadhaa aliyokuwa anamiliki Paul. Baada ya kupanda, wakaondoka ndani ya makazi yale, dereva akiwa ni yeye mwenyewe. Ndani ya nyumba waliachwa Jean na France, wakisubiri kuletewa taarifa za upelelezi ule. Kama kawaida eneo lile la Kijenge Maghorofani palikuwa kimya kwa muda ule, hasa ukuizingatia ni sehemu waliyokuwa wanakaa watu wastaarabu, hivyo Paul akaendesha gari kuelekea Njiro, ambapo hapakuwa mbali sana . Ni umbali wa kilometa nne na nusu hivi kutoka Kijenge.

    Dakika ishirini baadaye wakafika Njiro, huku giza lilishaingia, hivyo wakalipaki gari lao katika maegesho nje ya baa moja wakionekana kama watu wa kawaida tu waliokwenda kustarehe. Eneo lile la Njiro lilikuwa limejengeka sana , huku sehemu kubwa ikiwa ni ya kibiashara hususan grosari nyingi za kuuza pombe. Basi, ili kuvunga wasijulikane nia yao , walizunguka na kuingia katika baa mojawapo na kunywa bia mbili tatu katika kuvuta muda.

    Tena walikaa sehemu iliyokuwa na giza , kuepuka Pierre asitambuliwe, na muda wote waliokaa, walikuwa wakiangalia saa zao, kusubiri muda muafaka ufike hawakupenda kufanya kazi za kubabaisha. Ni hadi ilipotimu saa tatu za usiku, ndipo Paul na Pierre walipotoka ndani ya baa ile, ambapo wateja walikuwa ni wachache. Wakajifanya kama wanaliendea gari lao, halafu wakalipita na kuufuata uchochoro mmoja uliotokeza upande wa pili wa maduka na uzio wa nyumba za Umoja wa Mataifa, sehemu ambayo haikuwa na taa nyingi za ulinzi na kufanya pawe na giza kiasi.



    Kwa usiku ule walionekana kama watu waungwana wakitazama zile nyumba zilizokuwa zimezungukwa na uzio imara wenye urefu wa futi saba kwenda juu. Ili wasijulikane nia yao , wakapitiliza hadi mwisho wa nyumba zile. Wakiwa katika mwendo wa kawaida, wakafika katika sehemu iliyokuwa na mti mkubwa wa mwembe uliokuwa umefungamana na kusababisha giza . Paul na Pierre wakasimama pale kwa muda sambamba na mti ule. Wakawa wanachunguza bila kuonekena na mtu yeyote, kwa vile walikuwa wamevalia suti nyeusi zilizofanana na giza . Wakasimama kwa muda, hadi Bw.Paul aliposema kwa sauti ndogo:

    “ Pierre …”

    “Mkuu!”

    “Sasa tupange la kufanya!”

    “Ni jambo la maana…”

    “Sasa wewe utaingia ndani…”

    “Hakuna tatizo…nitaingia ingawa kuna ulinzi mkali!”

    “Ni sawa Pierre , jitahidi. Mimi nakusubiri hapa nje, ukichelewa sana nakufuata!”

    “Hakuna shaka!” Pierre akasema halafu akapiga hatuia mbili ili ajiandae kuuruka ule uzio. Ni uzio ambao kwa mtu kama yeye haukumpa shida kwani alikuwa mtu wa mazoezi.

    Baada ya kuuruka uzio, Pierre akatua ndani bila kutoa kishindo. Sehemu ile aliyotua ilikuwa imezungukwa na miti mingi iliyosababisha vivuli vya giza , ambavyo vilimsaidia sana Pierre aweze kunyata kuelekea katika nyumba zile. Na katikati yake ndipo ilipokuwa ile nyumba maalum, walipowekwa wale vijana, Roman, Teobale na Laurent. Kwa muda wote walikuwa chini ya ulinzi mkali wakilindwa usiku na mchana na walinzi maalum. Ndani ya nyumba ile palikuwa na nafasi ya kutosha iliyowatosheleza, ikiwa na kila kitu muhimu kama vile, simu, runinga na samani zilizohitajika kwa ujumla.

    Hatimaye Pierree alifanikiwa kuifikia ile nyumba bila kuonekana na mlinzi yoyote, kwani alikuwa anatumia ujuzi wa hali ya juu. Akaanza kuchunguza ndani ndani, lakini hakuweza kuona chochote au hata mtu; kwani milango ilikuwa imefungwa. Pierre akasimama kwa muda bila kufanya papara, kisha akamwona mlinzi mmoja akizunguka upande wa pili bila kumwona yeye sehemu ile aliyobanisha sambamba na ukuta. Mlinzi yule aliyekuwa na koti jeusi, kofia na buti za kijeshi, akampita tu bila kumwona. Hivyo hakumkawiza, Pierre akakusanya nguvu lililompata sawia mlinzi!

    Mlinzi yule akaachia mguno mdogo akaanguka chini na kupoteza fahamu kabisa. Na dakika chache akakata roho. Pierre akaisogeza ile maiti na kuisukumia katika giza lililokuwa katika bustani za maua . Tukio lile lilikuwa limefanyika haraka sana bila mlinzi mwingine kugundua. Lakini wakati Pierre amesimama pale, akijiandaa kusonga mbele, akasikia sauti za nyayo za mlinzi mwingine aliyekuwa akimsogelea. Naye akampita bila kujua kwamba Pierre salikuwa mawindoni. Ile kumpita tu, akamrukia mlinzi yule na kumkaba ipasavyo na pia kuondoka naye ili wakamhoji kule nje ya uzio alikomwacha Paul.

    Pierre akaondoka naye huku akiwakwepa walinzi wengine, hadi alipofika kwenye uzio ule wa michongoma. Kwa kutumia nguvu akamrusha mlinzi nje ya uzio, ambako alipokelewa na Paul, ambaye alimlaza chini ya ule mti mkubwa wa mwembe. Pierre naye akauruka uzio na kumwendea mlinzi aliyekuwa na Paul, wakati naye alikuwa amechanganyikiwa bila kujua kilichokuwa kinaendelea; kwani baada ya kuachwa apate kupumua vizuri, aliweza kuwaona watu wawili wamemdhibiti huku wakimwonyesha bastola kumtaka asifanye fujo ya aina yoyote!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Sisi ni watu wa kazi! Tunataka utujibu maswali tutakayokuuliza!” Pierre akamwambia baada ya kumwinamia pale alipolazwa yule mlinzi.

    “Nyie watu wa kazi?” Mlinzi yule naye akauliza huku macho yamemtoka pima!

    “Mh, mbona siwaelewi?”

    “Basi utatuelewa!” Pierre akamwambia. Halafu akamshindilia ngumi ya nguvu iliyompata barabara kwenye taya la upande wa kulia kiasi cha kutoa mlio wa kuvunjika!

    “Mh, Ooohps!” Mlinzi yule akaguna baada ya kipigo kile! Ama kweli alikiona kifo kinamnyemelea!

    “Wewe ni mlinzi?” Pierre akamuuliza tena!

    “Ndiyo…mimi ni mlinzi…”

    “Vizuri. Tunajua kwamba kuna vijana watatu waliotokea nchini Rwanda wamefikia hapa, je, ni kweli?”

    “Inawewzekana…ni kitu kama hicho.”

    “Tuambie wanakaa nyumba gani?”

    “Mh,” Mlinzi yule akaguna na kuendelea. “Kwani wanawahusu nini jamani? Sipaswi kuwaambia!”

    “Hebu tujibu, na siyo kutuuliza maswali sisi! Nilishakuonya!”

    “Sasa nitawajibu nini wakati mimi sikuelewi? Kwani nyie akina nani mnaniuliza tena kibabe?”

    “Hupaswi kujua!”

    “Basi na mimi sijui!”

    “Unaleta jeuri sivyo? Sasa mimi nakuua!” Pierre akamwambia mlinzi yule na kumwekea bastola kichwani mwake kwa kuukandamiza kwa nguvu!

    “Mama yangu!” Mlinzi akasema

    “Haya, sema!” Pierre akasisitiza!

    “Oh, ngoja niseme!”

    “Ni kweli kwamba…” mlinzi yule akaanza kusema kwa sauti ndogo. Lakini kabla hajaendelea zaidi, gari moja likatokea na kuelekea katika upande waliokuwa wao huku likimulika taa zenye mwanga mkali. Sehemu ile palikuwa na barabara ndogo iliyokuwa inakatiza kutoka katika nyumba ile, kitu ambacho tokea mwanzo, Paul na Pierre hawakugundua!

    “Mh, imekuwaje tena?” Pierre akauliza huku akisitisha zoezi lile huku akimdhibiti yule mlinzi kwa kumvutia nyuma ya mti ule wa mti wa mwembe!

    “Ni gari linakuja huku! Ni bora tujifiche nyuma ya huu mti…atatuharibia kazi!”

    Lile gari lililokuwa kama linapitiliza, likapunguza mwendo na kuwafuata pale walipokuwa, Paul na Pierre, wakiwa na mlinzi. Wala gari halikupunguza mwanga wa taa zake, kuashiria kuwa dereva yule alikuwa amewaona na kuwashtukia baada ya kumbana mlinzi aliyekuwa amevaa sare za kazi.

    “Tumeshtukiwa Pierre!” Paul akamwambia huku amekamata bastola!

    “Ni kweli!” Akadakia Pierre!

    “Sasa tufanyeje?”

    “Tummalize huyu dereva kwani atatuharibia kazi!”

    “Na huyu mlinzi je?”

    “Mmalize vilevile!”

    “Sawa…” Pierre akasema na kuikamata shingo ya mlinzi ambayo ilivunjika!

    “Hik!” Mlinzi akaguna na kukata roho!

    “Ok, sasa mshughulikieni huyo dereva!”

    Pierre akaikamata vyema bastola yake na kuielekeza kwenye lile gari lililokuwa limesimama pale likiwamulika. Akafyetua risasi mbili ambazo zilimpata dereva, ambaye aliguna na kufa palepale huku akiuachia usukukani na kulalia kiti, na damu nyingi kumtoka katika jeraha la risasi zilizompata kichwani!

    Baada ya mauaji yale, Paul na Pierre wakaondoka haraka sana kwa kuufuata uchochoro ule waliokuja nao. Wakaliendea gari lao katika sehemu ile walikoliacha, na kuondoka kurudi katika maficho yao Kijenge, wakati huo ikiwa imetimu saa tano za usiku. Hata hivyo Paul na Pierre hawakutegemea kama wangekumbana na kizuizi kile kilichowaharibia kazi yao ya upelelezi dhidi ya wasaliti wao!



    ********

    Alikuwa ni kijana Deo Mshanaki, dereva gari aina ya Toyota Land Cruiser, la Umoja wa Mataifa, aliyeuawa baada ya kuwashtukia Paul Rugoye na Pierre, wakiwa wamebanisha chini ya mti wa mwembe. Hivyo basi, purukushani zile ziliwashtua wakazi wa eneo lile na kuwafanya wakimbilie, na kulikuta tukio lile la mauaji ya dereva na wale walinzi wawili waliokuwa wanalinda katika zile nyumba za Umoja wa Mataifa.

    Haraka sana wakapiga simu polisi kujulisha tukio lile la kinyama. Baada ya dakika kumi na tano hivi, askari polisi wakafika pale wakiwa na magari mawili aina ya Toyota Land Cruiser wakiwa wamejizatiti kwa silaha. Pia, walikuwepo askari wengine wa Kikosi cha Mbwa, na wataalam wa picha, milipuko na alama za vidole. Wote wakashuka ndani ya gari na kulizingira eneo lile, ingawa waliotenda kosa lile walikuwa wameshaondoka kitambo!

    Katika msafara ule walikuwepo viongozi wa polisi wa ngazi za juu, na pia makachero, ambao walianza kufanya uchunguzi katika maeneo mengi. Wakaokota yale maganda ya risasi mawili, yaliyofyetuliwa na Pierre na kumuua Deo. Wakachukuwa maiti ya mlinzi aliyeuawa kule ndani na kufichwa katika bustani ya maua , halafu wakaiunganisha na ile ya yule mlinzi mwingine aliyeuawa kule nje na kuachwa chini ya mwembe. Basi, maiti zote tatu zikachukuliwa na kupelekwa katika Hospitali ya Mount Meru kuhifadhiwa.

    Usiku mzima askari polisi walifanya msako wa nguvu huku wakitumia mbwa wa Polisi, lakini haukusaidia kitu, kwani watuhumiwa wale walitumia usafiri wa gari. Ni hadi palipokucha, ikiwa ni siku ya Jumatatu. Hali ilikuwa ni mbaya katika jiji la Arusha, kiasi cha kuwashtua watu wengi sana . Haikujulikana kama watu wale walikuwa na maana gani, na kwa sababu gani. Mkuu wa Upelelezi akateua makachero kadhaa kufanya upelelezi dhidi ya mauaji yale, ambapo kiini chake kilikuwa hakijajulikana na Jeshi la Polisi. Wakauanza upelelezi wao eneo loa Njiro.

    Jiji la Arusha halikukalika! Hali ya hatari ikanukia sehemu zote, hasa katika vitongoji, ambapo ulifanyika msako wa nguvu wa askari wa Jeshi la Polisi. Walioambulia kadhia ile ni walevi ni walevi na wauzaji wa pombe haramu za gongo na bhangi, ambao hawakuhusika na tukio lile kabisa. Wengi walikuwa ni vijana wa kijiweni, waliosombwa kwa wingi na kuzijaza mahabusu za polisi. Lakini si Paul Rugoye na vijana wake, Jean, Pierre na France waliohisiwa kufanya mauaji yale, kwani walikuwa wamejichimbia katika maficho ndani ya nyumba iliyoko Kijenge, wakiendelea kupanga mipango iliyowakabili.

    Ilikuwa ni lazima waimalize kwa njia yoyote ile!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mauaji ya wale walinzi wawili, na dereva, Deo, yalitokea usiku ule, ikiwa wapelelezi wale mahiri wa Idara ya Usalama wa Taifa, Luteni James na Sajini Sofia, wamewasili jijini Arusha. Ukweli ni kwamba yaliwashtua sana kiasi cha kujua ni kazi ya watu wale watatu waliotokea nchini Rwanda , ambao walikuwa wanawafuatilia!

    Kazi ilikuwepo!



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog