Search This Blog

Sunday, 22 May 2022

THE LAST SUMMER IN TANZANIA - 1

 





    IMEANDIKWA NA : NYEMO CHILONGANI



    *********************************************************************************



    Simulizi : The Last Summer In Tanzania

    Sehemu Ya Kwanza (1)

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Matangazo yalikuwa yamebandikwa kila kona ndani ya Jiji la Dar es Salaam yaliyokuwa yakihusu ujio wa mjasiriamali mkubwa, Potter Mickey aliyejulikana duniani kote kutokana na mafundisho yenye nguvu ya kuwafanya watu kujishughulisha na biashara na mwisho wa siku kufanikiwa.

    Huyu alikuwa mjasiriamali mwenye nguvu kubwa ya ushawishi, mjasiriamali aliyejitengenezea jina kubwa duniani kote kutokana na masomo yake yaliyoleta mabadiliko makubwa katika jamii.

    Mickey alikuwa miongoni mwa watu mashuhuri duniani, kazi yake kubwa ilikuwa ni kuwahamasisha watu wengi kuweka nguvu kubwa katika biashara na hatimae kufanikiwa kwa kiasi kikubwa.

    Japokuwa alikuwa Mmarekani lakini hakuwa mtu wa kutulia tu nchini mwake, leo alikuwa Afrika Kusini, wiki ijayo Uingereza, mara Urusi na sehemu nyingine duniani zikiwepo nchi za Kiarabu.

    Ingawa lilikuwa ni jambo gumu kwa Waarabu kuwaruhusu Wamarekani kuingia nchini mwao kiholela lakini kwa bwana Mickey lilikuwa jambo jepesi sana, kila alipotaka kuingia katika nchi hizo zilizokuwa katika Umoja Waarabu wa Emirate, aliruhusiwa bila tatizo lolote lile.

    Alizunguka kuanzia Dubai, Fujairah, Abu Dhabi, Ajman na sehemu nyingine katika nchi zilizokuwa katika umoja wa Kiarabu wa Emirate, huko kote alikuwa akihubiri kuhusiana na namna ambavyo mtu anaweza kufanya ili kufanikiwa katika biashara zake.

    Mbali na nchi hizo, pia Mickey alitembelea nchi zilizokuwa Asia kama Iran, Iraq, China na sehemu nyingine, kote huko bado alikuwa akihubiri kuhusu ujasiriamali katika kufanikiwa.

    Mickey alipendwa, mahubiri yake yalimfurahisha kila mtu aliyekuwa akimsikiliza, mara kwa mara alikuwa akipokea mialiko kutoka katika nchi za Kiarabu, wote walikuwa wakinufaishwa na mahubiri yake na hivyo kuyatumia katika biashara zao za mafuta.

    Baada ya kuzunguka katika nchi za Kiarabu kwa kipindi kirefu, bwana Mickey akahama na kuhamia barani Ulaya, kama kawaida yake bado mahubiri yake yalikuwa gumzo kwa kila mtu aliyeyasikia.

    Aliendelea kuwasisitizia watu kwamba paundi moja waliyokuwa nayo ambayo ilikuwa ni kiasi kidogo cha fedha kingeweza kuyabadilisha maisha yao na kuwagawia mabilioni ya paundi.

    Kwa maneno yake ya harakaharaka, ilionekana kuwa ngumu sana lakini alipokuwa akifafanua namna ambavyo hiyo paundi moja ilivyotakiwa kutumika na kuzalisha mabilioni, kila mtu alibaki akishangaa na kukubaliana naye.

    “This is the man of God,” (Huyu ni mtu wa Mungu) alisikika jamaa mmoja akiwaambia wenzake.

    “Yes! His words change me positively from one step to another” (Ndiyo! Maneno yake yamenibadilisha kutoka hatua moja kwenda nyingine) alisema jamaa mwingine.

    Kila alipokwenda, Mickey aliacha sifa kubwa, watu walikuwa wakimpenda huku wengi wakimuita mhamasishaji wa utajiri kwa masikini bila kuwa na ubaguzi wowote ule. Sifa zake hizo ndizo zilizomfanya kupokea mialiko mingi katika nchi nyingine nyingi.

    Kila alipokuwa akienda, aliongozana na mkewe, Elizabeth ambaye alionekana kuwa mtu muhimu kuliko wengine. Kupitia mafundisho yake, akajikuta akijiingizia kiasi kikubwa cha fedha, vitabu vya ujasiriamali kama Think like A Businessman, Walking With Success vilimuingizia fedha nyingi ambazo alizitumia kuwasaidia watu waliokuwa na matatizo mbalimbali kama umasikini na wagonjwa.

    Baada ya kuzunguka duniani kwa kipindi kirefu, akahitaji muda wa kupumzika, akili yake ilichoka, hakutaka tena kusafiri na kwenda sehemu nyingine kufanya mafundisho yake, kwa wakati huo, alihitaji kuipumzisha akili yake tu.

    Kichwa chake kikalifikiria Bara la Afrika, sehemu ambayo ilikuwa na vivutio vingi. Alichokifanya ni kufungua kompyuta yake ili kuangalia ni nchi gani alitakiwa kwenda kwa ajili ya mapumziko hasa katika majira ya joto kama hayo, akaichagua nchi ya Tanzania.

    “We are going to Tanzania once again” (Tunakwenda Tanzania kwa mara nyingine) alisema Mickey, alikuwa akimwambia mke wake, Elizabeth.

    “What am I suppose to do?” (Natakiwa kufanya nini?) aliuliza Elizabeth.

    “You have to tell Victor that we are going to meet with him there,” (Unatakiwa kumwambia Victor kwamba tunakwenda kukutana naye huko) alisema bwana Mickey.

    “No problem.” (Hakuna tatizo)CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Victor alikuwa mtoto wao aliyekuwa akisoma katika Chuo cha Mississippi nchini Marekani. Kama alivyokuwa baba yake, hata naye alikuwa akisomea mambo ya biashara ili baadae aje kuwa mfanyabiashara mzuri na mhamasishaji kuhusu ujasiriamali.

    Uwezo wake chuoni haukuwa mdogo, Victor alikuwa akifaulu sana masomo yake, alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakifanya vizuri kabisa katika masomo yote. Kila siku alikuwa akitumia dakika ishirini kuwaambia wanachuo wengine ni kwa namna gani walitakiwa kuyabadilisha maisha yao na mwisho wa siku kuwa mabilionea.

    Kama alivyokuwa baba yake, naye alitokea kupendwa na kuwa mhubiri mzuri kuhusu mambo ya biashara kiasi kwamba wanachuo wengine walisema kwamba Victor alikuwa zaidi ya baba yake.

    Ingawa alipanga kuja Tanzania kupumzika na mkewe lakini mara baada ya maprofesa wa Chuo Kikuu kusikia kwamba bwana Mickey alikuwa akija ndani ya nchi hiyo, wakaandaa tamasha lake kwa ajili ya mafundisho ya ujasiriamali kwa ajili ya wanachuo wa chuo hicho.

    “Kuna kazi nimepewa,” alisema bwana Mickey.

    “Kazi gani?”

    “Natakiwa kwenda kuwafundishi wanachuo kuhusu ujasiriamali.”

    “Wapi? Uarabuni kama kawaida?”

    “Hapana. Hukohuko Tanzania tunapokwenda.”

    “Mmmh! Lakini hiki si ndiyo kipindi chetu cha mapumziko mpenzi!”

    “Najua hilo, lakini haina jinsi, sijawahi kufundisha nchini Tanzania, mara nyingi tumekuwa tukienda kule na kupumzika, naomba uniruhusu tu nifanye kitu kama hicho,” alisema Mickey kwa sauti ya upole.

    “Mpenziiiiiii...”

    “Naomba uniruhusu, siku mbili tu.”

    “Lakini kw.....”

    “Si zaidi ya siku mbili mpenzi, naomba uwape nafasi watu wengine nao watajirike.”

    “Sawa. Ila niahidi, siku mbili!”

    “Nakuahidi.”

    Mickey akamsogelea mke wake, Elizabeth na kumkumbatia. Alikuwa akifanya mambo mengi katika maisha yake lakini mengi aliyokuwa akiyafanya, ilikuwa ni lazima kumshirikisha mkewe. Alimpenda mwanamke huyo, alimthamini na kumjali kwa kila kitu.

    Ingawa alikuwa na ndugu, marafiki lakini mke wake ndiye alikuwa kila kitu, kila nchi aliyokwenda kufundisha ilikuwa ni lazima aende na mke wake huyo aliyekuwa mtu muhimu kuliko watu wote katika maisha yake.

    Baada ya wiki moja safari ya kwenda nchini Tanzania ikaanza. Ndani ya ndege, kila mmoja alionekana kuwa na furaha, kila wakati walikuwa wakikumbatiana tu, hakukuwa na kitu ambacho kwao kilionekana kuwa cha thamani kama kuwa karibu.

    Waliishi pamoja kwa miaka thethini na tano, walizoeana na mapenzi yao kukua kadiri siku zilivyozidi kwenda mbele, hawakuwa watu wa kugombana mara kwa mara, kila mmoja alipokuwa akifanya kosa, alikubali kwamba alikosea na aliomba msamaha.

    Baada ya wiki moja, safari ya kuelekea nchini Tanzania ikaanza. Ilikuwa ni safari ndefu na yenye kuchosha lakini baada ya masaa ishirini na tano, ndege ya Shirika la Ndege la American Airlines ilikuwa ikitua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.

    Hali ya hewa ilikuwa ni ya joto sana, kwa kuwa safari hiyo ilihusiana na ufundishaji wa ujasiriamali chuoni, maprofesa walikuwa uwanjani hapo kwa ajili ya kuwapokea. Mapokezi yalifanyika vizuri, walipoona kila kitu kimekamilika, wakawachukua na kuelekea hotelini kwa ajili ya mapumziko kabla ya kuanza kwa semina ya ujasiriamali iliyokuwa ikitangazwa sehemu zote jijini Dar es Salaam kwa kubandika matangazo mbalimbali.

    **** CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wanachuo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam walikuwa wamejiandaa kwa ajili ya kusikiliza mafundisho juu ya namna ya kuwa bilionea kutoka kwa mhamasishaji mashuhuri aliyekuwa akifanya ziara zake mbalimbali duniani, bwana Potter Mickey.

    Kila mmoja alikuwa na kiu ya kufanikiwa, kitendo cha kuambiwa kwamba shilingi elfu moja waliyonayo inaweza kuwafanya kutajirika na kuwa na mabilioni ya shilingi, kuliwachanganya watu.

    Siku iliyofuata, wanafunzi wengi walikuwa wamekusanyika katika Jengo la Nkurumah kwa ajili ya kumsikiliza mhamasishaji huyo aliyetarajiwa kuingia chuoni hapo muda mchache ujao.

    Idadi hiyo kubwa ya watu waliokuwa wamekusanyika ndani ya jengo hilo, liliufanya ukumbi huo kuwa mdogo kwani si wanachuo peke yao waliokuwa mahali hapo bali hata watu wengine kutoka sehemu nyingine walikuwa ndani ya jengo hilo.

    Vitabu vyake vya ujasiriamali vya bwana Mickey viliendelea kuuzwa ukumbini, kila mtu alitaka kuwa navyo, kutoa shilingi elfu ishirini kwa ajili ya kuwa na vitabu hivyo viwili wala haikuonekana kuwa tatizo hata kidogo.

    Baada ya dakika thelathini, bwana Mickey akafika chuoni hapo huku akiwa na mkewe. Watu wakaanza kushangilia, kuonekana tu ndani ya chuo hicho, tayari watu wakapata matumaini mapya, wale wasiokuwa na fedha wakajiona kuanza kupata utajiri.

    “Daah! Huyu jamaa ni noma sana, unajua nilianza kufuatilia mafundisho yake kwa njia ya vitabu toka mwaka juzi, jamaa anatisha, amenifanya na mimi kuwa mtu miongoni mwa watu kwa kuwa na biashara nyingi,” alisikika mwanachuo mmoja, alikuwa kijana lakini mwenye biashara nyingi.

    “Kumbe ulipata ujuzi kutoka kwa huyu jamaa?” aliuliza mwanachuo mmoja.

    “Ndiyo! Yaani ukimsikiliza na kuvisoma vitabu vyake, utapenda.”

    “Hebu ngoja na mimi nimsikilize, naweza kupata kitu,” alisema jamaa huyo.

    Siku hiyo, watu walijifunza mambo mengi kuhusiana na biashara, kila neno alilokuwa akilizungumza bwana Mickey, lilionekana kuwa msingi mkubwa kwa wanachuo waliokusanyika mahali hapo.

    Alijua kuzungumza na watu, kadiri alivyoendelea kuongea na ndivyo ambavyo watu walitamani aendelee kuzungumza zaidi na zaidi. Alionekana ni mtu mwenye mafanikio makubwa ambaye alikuwa akitaka kuwaona watu wakifanikiwa na kuwa mamilionea wakubwa duniani.

    Hakutaka kuwaona watu wakiwa masikini, aliamini kwamba kila mtu duniani alikuwa na uwezo mkubwa wa kupata fedha kwa kufanya biashara, hivyo nafasi hiyo alikuwa akiitumia vilivyo kwa kuwaambia watu ni kwa namna gani walitakiwa kuanza na kiasi kidogo cha fedha walichokuwa nacho.

    Siku hiyo, kila mtu akaonekana kumuelewa bwana Mickey ambaye alikuwa akizungumza hatua kwa hatua kama ambavyo mtu anaweza kumuhadithia mtoto mdogo kitu fulani. Baada ya kufanya semina hiyo kwa saa moja na nusu, akamaliza na kuomba kuondoka.

    “Nitakwenda kuwa tajiri, nipe miaka miwili,” alisema mwanachuo mmoja.

    “Mawazo yako ni kama mimi, pia nitakwenda kuwa tajiri mkubwa,” alisema jamaa mwingine.

    Maneno yake yakawatia watu hamasa, kila mmoja alijiona kuwa na uwezo mkubwa wa kufanya biashara na kufanikiwa na mwisho wa siku kuwa mfanyabiashara mkubwa nchini, yaani ilikuwa ni sawa na mtu aliyeangalia filamu za mapigano za kina Jackie Chan na mwisho wa picha, akitoka nje kujiona kuwa na uwezo wa kupigana kama mcheza filamu huyo.

    Siku hiyo bwana Mickey na mkewe wakarudi hotelini ambapo wakafanya mambo yao na kujiandaa kwa ajili ya siku ya pili na ya mwisho ya semina hiyo iliyotakiwa kufanyika palepale chuoni ili waendelee na ishu zao za mapumziko kama walivyotarajia.

    Siku hiyo ilipofika, bwana Mickey akaonekana kuwa tofauti kabisa, hakuwa na furaha kama siku iliyopita, kila wakati alionekana mtu wa mawazo kupita kawaida kitu kilichomtia hofu mke wake, bi Elizabeth.

    “Kuna nini?”

    “Hakuna kitu mke wangu!”

    “Hapana, niambie kuna nini, umebadilika sana!”

    “Sijajua kwa nini, lakini kiukweli hakuna kitu, endapo kungekuwa na kitu, nisingeweza kukuficha mke wangu!” alisema bwana Mickey.

    Japokuwa aliambiwa na mume wake kwamba hakukuwa na kitu chochote kibaya lakini moyo wake haukuonekana kuridhika hata kidogo, naye akajikuta akiingia katika huzuni.

    “Unakumbuka kwamba Victor anaingia leo usiku?” aliuliza bi Elizabeth.

    “Yeah! Nakumbuka sana kipenzi. Tutakwenda kumpokea na vitu vingine viendelee, kwanza tumalize hii semina,” alisema bwana Mickey.

    Siku hiyo ya pili na ya mwisho ndiyo ilionekana kuwa balaa. Watu walifurika mara mbili ya siku iliyopita, zaidi ya watu elfu moja walihitaji kumsikia mhamasishaji huyo kutoka nchini Marekani.

    Ukumbi wa Nkurumah ukawa mdogo kiasi kwamba kwa haraka sehemu ikabadilishwa na kupelekwa katika uwanja wa mpira chuoni hapo ili kila mtu apate nafasi ya kumsikiliza mtu huyo.

    “Hapa poa sasa, hewa safi na ukitaka hata juu ya mti unakaa, full kujiachia tu,” alisema jamaa mmoja.

    Kutokana na sehemu hiyo kuwa na miti mingi, wapo wanachuo ambao walipanda juu ya miti na kuanza kumsikiliza bwana Mickey aliyekuwa akiongea kwa uchungu wa kuwataka watu watoke pale walipokuwa na kusonga mbele.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Siku hiyo alizungumza mambo mengi ambayo yote yalionekana kuwa faida kwa kila mtu aliyekuwa akimsikiliza.

    “One day my father gave me fifty cent that changed my life forever. I know, it is very difficult to believe me but let me tell you what I did. I asked myself abo.....” (Siku moja baba yangu alinipa senti hamsini iliyobadilisha maisha yangu milele. Najua ni vigumu mno kuniamini lakini acha nikwambie kile nilichokifanya. Nilijiuliza kuh....) alisema bwana Mickey lakini hata kabla hajamaliza sentensi yake, ukasikika mlio wa risasi mahali hapo.

    “Paaaaaa.....” mlio mkubwa wa risasi ukasikika, bwana Mickey akaangua chini, damu zikaanza kumtoka kichwani kwake, kama alivyokuwa ameanguka, aliishia hivyohivyo na hakuweza kuutingisha mwili wake.

    Watu waliokuwa mahali hapo, mara baada ya kusikia mlio wa risasi ile, wakaanza kukimbia hovyo, wale waliokuwa juu ya miti, ghafla wakajikuta wakiwa chini bila kujua wameshukaje na kuanza kukimbia.

    Lilikuwa ni moja ya tukio lililoogopesha, mlio wa risasi uliokuwa umesikia, haukuonekana kuwa wa kawaida, ulikuwa na sauti kubwa kiasi kwamba baadhi ya watu walihisi kwamba lilikuwa bomu.

    Kila mmoja akakimbia na ni bi Elizabeth peke yake ndiye aliyekuwa amebaki mahali hapo, aliuhisi mwili wake ukiwa umepigwa ganzi, picha aliyokuwa akiiona kwamba mume wake alikuwa chini, damu zilikuwa zikimtoka kichwani baada ya risasi kupenya kwenye paji la uso wake na kutokea nyuma, ilikuwa ni moja ya picha yenye kutisha ambayo hakuwahi kuiona maishani mwake.

    Hapohapo akaanza kumkimbilia mume wake pale chini, hakukuwa na wa kumsaidia, kila mtu alikuwa amekimbia kuyaokoa maisha yake.

    “Mickey...Mickey...please wake up, dont’t leave me alone, wake up my husband...wake up and look at me....” (Mickey...Mickey...tafadhali amka, usiniache peke yangu, amka mume wangu...amka na uniangalie...) alisema bi Elizabeth huku akilia kama mtoto.

    Aliushika mwili wa mume wake pale chini, hakuwa akiamini kile kilichokuwa kimetokea, wakati mwingine alifikiri kwamba alikuwa ndotoni na baada ya dakika chache angeamka na kujikuta akiwa kitandani, chumbani na mumewe lakini ukweli ulibaki palepale kwamba hakuwa kwenye maisha ya njozi, kila kilichokuwa kikitokea, kilitokea katika maisha halisi.

    Baada ya dakika tano kuona kwamba kila kitu kilikuwa shwari, wale watu waliokuwa wamekimbia wakaanza kujikusanya mahali hapo ili kuona ni kitu gani kilikuwa kimetokea.

    Bi Elizabeth alikuwa jukwaani, bado alikuwa ameushika mwili wa mume wake huku akilia kama mtoto, muda wote alikuwa akimtaka aamke kwani hakuwa akiamini kama alikuwa amefariki dunia.

    “Kuna nini?” aliuliza jamaa mmoja, alikuwa akiangalia huku na kule, hakuwa akijiamini.

    “Mmmh! Sijui, mimi nilisikia paaa, baada ya hapo nikajikuta nipo barabarani,” alisema jamaa mwingine.

    “Hivi ilikuwa risasi au bomu?”

    “Mmmh! Wala sijui!”

    Bi Elizabeth alikuwa akiendelea kulia, moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali, bado hakuwa akiamini kile kilichokuwa kimetokea, kila aliyekuwa akimwangalia mahali hapo, alimuonea huruma, wala hazikupita dakika nyingi, akaanguka chini na kupoteza fahamu, hakujua ni kitu gani kiliendelea baada ya hapo.

    ****

    Mwili wa bwana Mickey ulikuwa chini, damu zilikuwa zimetapakaa katika jukwaa lile, watu walibaki wakishangaa tu kana kwamba hawakuwa wakifahamu ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea mahali hapo.

    Maprofesa wakapiga hatua mpaka katika jukwaa lile, pembeni ya mwili wa bwana Mickey kulikuwa na mke wake ambaye alipoteza fahamu kutokana na mshtuko mkubwa alioupata baada ya kushuhudia mume wake kipenzi akiwa amepigwa risasi mbele ya macho yake.

    Gari la mtu binafsi likasogezwa na kumchukua bi Elizabeth na kuondoka naye huku wakiuacha mwili wa bwana Mickey palepale ulipokuwa. Ndani ya dakika kadhaa, polisi wakafika na baadhi ya watu kutoka katika kitengo cha upelelezi, walichokifanya ni kuupiga picha mwili ule na kuchukua vipimo vyote ambavyo walitakiwa kuvichukua, baada ya hapo, wakauchukua na kuondoka nao.



    Ilikuwa ni taarifa iliyoshtua mno, hakukuwa na mtu aliyeamini kama kweli mhamasishaji huyo kutoka nchini Marekani alikuwa ameuawa nchini Tanzania. Taarifa hizo ziliendelea kusambazwa na ndani ya kipindi kichache tu, dunia nzima ikafahamu kile kilichokuwa kimetokea katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

    Dunia nzima ikaanza kuilalamikia Tanzania kwa kutokuwa makini katika kudumisha ulinzi wa nchi yao, kitendo kilichokuwa kimetokea kilimsikitisha kila mtu na kuendelea kuilaumu nchi hiyo.

    Marekani haikutaka kukaa kimya, wakatoa tamko ambalo walitaka litelekezwe mara moja na nchi ya Tanzania kwamba muuaji aliyemuua bwana Mickey anapatikana na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

    “Kimenuka!”

    “Kuna nini?”

    “Umewasikia wakina Obama huko?”

    “Wamesemaje?”

    “Wamesema wanataka kumjua muuaji, sijui kama ataweza kupatikana.”

    Tamko la Marekani walilokuwa wamelitoa likaanza kuwa gumzo, kila mtu alilizungumzia kitu ambacho kwa kiasi kikubwa kikaleta hofu katika serikali ya Tanzania. Magazeti yakaandika sana kuhusu agizo hilo lililotakiwa kufanyiwa kazi mara moja na ripoti kutolewa.

    “Mmesikia kilichosemwa?” aliuliza kamanda wa jeshi la polisi, bwana Kizota.

    “Tumesikia.”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Tunahitaji kumpata huyu mtu, iwe isiwe, ni lazima apatikane. Naliacha jukumu hili kwenu, nataka ndani ya siku mbili, muuaji ajulikane, na ndani ya wiki moja, muuaji huyo apatikane! Mmenielewa?” aliuliza kamanda Kizota.

    “Tumekuelewa mkuu.”

    Taarifa zikapelekwa mpaka katika kitengo cha upelelezi, TISS (Tanzania Internal Security Service) ambapo huko wakaandaa watu wawili kwa ajili ya kupeleleza na kujua ni mahali gani mtu huyo alipokuwa.

    Mtu mmoja miongoni mwa wale waliokuwa wamechaguliwa aliitwa Martin Subian, alipewa jukumu la kumjua mtu huyo, alikuwa akiishi wapi na mtu wa pili ambaye naye alichaguliwa katika jukumu hilo la kumtafuta muuaji alikuwa ni Mathias Jonathan, kazi yake kubwa ilikuwa ni kumpata mtu huyo na kumtia nguvuni.

    Siku iliyofuata, asubuhi na mapema Martin akaanza safari ya kuelekea chuo kikuu kwa lengo la kupata taarifa zote zilizokuwa zikimhusu mtu huyo, alikuwa nani, alikuwa katika eneo gani alipokuwa akimpiga risasi bwana Mickey na kwa nini alifanya hivyo.

    Alipofika chuoni, moja kwa moja akaunganisha mpaka kwa Professa Ahmed Mitimingi na kuanza kuzungumza naye. Kwa kumwangalia Martin, hakuonekana kama alikuwa kijana shupavu, mwenye nguvu, alionekana kuwa hohehahe ambaye hata kama ungemuona basi ungeweza kusema kwamba una uwezo mkubwa wa kupambana naye na ukampiga.

    “Ninaitwa Martin Subian kutoka TISS,” alisema Martin huku akitoa kitambulisho chake na kumkabidhi Professa Mitimingi. Akakichukua na kukiangalia, aliporidhika, akamtaka kuendelea kuzungumza.

    “Ninataka kufahamu eneo alilouliwa bwana Mickey,” alisema Martin.

    “Hakuna tatizo, twende.”

    Wawili hao wakainuka na kutoka nje, hakukuwa na mtu aliyegundua kwamba mtu aliyekuwa akiongozana na Profesa Mitimingi alikuwa mtu hatari kwa kupambana na watu hata kama walikuwa watano.

    Alionekana nadhifu, suti nyeusi lakini kiunoni alikuwa na bunduki iliyofichwa ambapo kama hali ingechafuka bunduki hiyo ingeingia katika matumizi wakati wowote ule. Hawakuchukua muda mrefu, wakafika uwanjani hapo.

    “Hapa ndipo alipouawa.”

    “Sawa. Jukwaa lilikuwa wapi na aligeukia wapi?” aliuliza Martin.

    “Twende nikupeleke jukwaa lilipokuwa.”

    Wakaendelea kupiga hatua mpaka sehemu kulipowekwa jukwaa lile, bado alama za vyuma vilivyokuwa vimechimbwa kwa chini zilionekana. Martin akasimama sehemu ile na kuangalia upande ambao bwana Mickey alikuwa akiangalia.

    Muda wote huo Martin alikuwa kimya, alikuwa akiangalia huku na kule huku akionekana kujifikiria kitu. Kichwa chake kikianza kuivuta picha ya bwana Mickey, aliikumbuka vilivyo kwamba risasi ilipenya katika paji lake la uso na kutokea kichogoni.

    Alisimama usawa mzuri na kuanza kuangalia sehemu ambayo ilikuwa ni nyepesi kwa mpigaji kupiga risasi ile.

    “Bunduki iliyotumika ni Rifle yenye uwezo mkubwa wa kumpiga hata mtu aliyekuwa umbali wa mita mia mbili, ni bunduki iliyotengenezwa nchini Urusi ambayo mara nyingi hutumiwa na watu watunguaji wajulikanao kama snipers,” alisema Martin huku akiangalia kila kona maeneo hayo.

    “Umejuaje?”

    “Hakuna bunduki inayoweza kupiga umbali mrefu kama Rifle, hii ni bunduki iliyotengenezwa mahususi kwa ajili ya maadui wanaokaa kwa umbali mkubwa, na hii ndiyo iliyotumika mahali hapa,” alijibu Martin.

    “Kulikuwa na watu wengi mahali hapa, sasa inawezekana vipi mpigaji kuwa karibu na mlengwa?”

    “Mpigaji alikuwa mbali na ndiyo maana nilisema alitumia bunduki hii kwa kuwa ilikuwa na uwezo wa kupiga kitu kilichokuwa hata umbali wa mita mia mbili. Kama bwana Mickey alisimama hapa na kupigwa risasi upande huu, ina maana mpiga alisimama kule,” alisema Martin.

    “Mmh! Huku kote kulijaa watu!”

    “Najua, atakuwa alisimama kule porini. Unapaona?”

    “Napaona, ila sidhani.”

    “Twende nikuonyeshee.”

    Wakatoka mahali hapo na kuelekea katika kichaka kilichokuwa umbali wa mia mia moja. Baadhi ya wanachuo walikuwa wakiwaangalia tu. Kila walipokuwa wakipiga hatua, waliwafuatilia kwa ukaribu pasipo kujulikana.

    Prosefa Mitimingi na Martin wakafika katika kichaka kile kile kidogo na kuingia ndani. Martin akasimama na kuanza kuangalia kule kulipowekwa jukwaa, alipaangalia kwa umakini, alipoona amekosea, akasimama pembeni kidogo, alipoona hajakaa sawa, akaelekea pembeni kidogo mpaka alipojiona amekaa sawa na sehemu ile aliyosimama bwana Mickey kule jukwaani.

    “Mpigaji alikuwa mahali hapa,” alisema Martin maneno yaliyomfanya Profesa Mitimingi kushtuka.

    “Umejuaje?”

    “Subiri.”

    Martin akainama chini na kuanza kuyaangalia majani vizuri. Hali ya utofauti ilionekana katika majani yale. Majani ya upande mwingine yalikuwa yamesimama lakini majani ya pale alipokuwa ameinama yalikuwa yamelala kuonyesha kwamba kulikuwa na mtu aliyalalia.

    “Unaona...majani yamelala, kuna mtu alikuwa mahali hapa, bila shaka ndiye huyo muuaji,” alisema Martin.

    “Mmmh.”

    “Subiri.”

    Martin akaanza kutafuta kitu mahali pale, hakutulia, kila wakati alikuwa akipekua huku na kule, alionekana kuwa bize kupita kawaida. Wala haukuchukua muda mrefu, akakuta ganda la risasi likiwa mahali hapo, akalichukua na kuanza kuliangalia, Professa Mitimingi alikuwa kimya akimwangalia.

    “Nini hicho?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hili ni ganda la risasi, lisome lilivyoandikwa,” alisema Martin huku akimpa ganda lile na kuliangalia, liliandikwa Rifle 07T, bunduki kali iliyotoka nchini Urusi.

    Kila kitu alichokuwa akikisema Martin mahali pale, Professa Mitimingi alikuwa akishangaa na kujikuta akimkubali kijana huyo kwamba alitoka TISS. Waliendelea kukaa kule huku akiambiwa vitu vingi, baada ya hapo, wakarudi ofisini.

    “Nadhani nimekuonyeshea mengi na kukufundisha mengi, nahitaji kitu kimoja kutoka kwako,” alisema Martin.

    “Kitu gani?”

    “Kumjua mtu aliyepiga risasi hiyo.”

    “Mmmh! Ni vigumu kufahamu.”

    “Ulikuwepo wakati wa tukio?”

    “Ndiyo! Nilikuwepo.”

    “Hukumuona?”

    “Hapana, sikumuona.”

    “Hapana! Hebu vuta kumbukumbu, kumbuka vizuri, kumbuka kuanzia mwanzo mpaka mwisho,” alisema Martin.

    “Kweli sikuweza kumuona.”

    “Hapana. Hebu jaribu kukumbuka, vuta picha, kumbuka kuhusu kichaka kile, jaribu kukumbuka, nahisi nitapata picha. Kumbuka vizuri.”

    Profesa Mitimingi akabaki kimya, ni kweli alijitahidi kuvuta picha zaidi, kila alipokuwa akikumbuka, hakukumbuka kumuona mtu kama huyo.

    “Unasema ulikuwa jukwaani?”

    “Ndiyo!”

    “Hebu kumbuka vizuri, hakuna mtu aliyekwenda kule kichakani? Kumbuka, vuta kumbukumbu,” alisema Martin.

    Prosessa akabaki kimya, alionekana kujifikiria kitu. Alijitahidi kukumbuka kila kitu kilichotokea siku ile katika uwanja ule. Alivuta kumbukumbu, alizivuta zaidi na zaidi mpaka akaonekana kushtuka.

    “Mmmh!” alibaki akiguna.

    “Niambie umekumbuka nini.”

    “Kuna mtu alikwenda katika pori lile kukojoa, namkumbuka sana, alikuwa akiishikashika zipu ya suruali yake, mgongoni alibeba begi,” alisema Professa.

    “Unamfahamu mtu huyo?”

    “Mmmh! Hapana.”

    “Bado! Jaribu kukumbuka.”

    “No! Kuna mtu nilimuona akielekea kule, lakini sikuwa nikimfahamu kabisa, nilipomuona akiishikashika zipu ya suruali yake, niligundua kwamba alitaka kukojoa, nilitaka kumtuma mtu akamwambie kwamba hairuhusiwi kukojoa vichakani, sasa sijui kwa nini nilipuuzia,” alisema Professa Mitimingi.

    “Umesema alibeba begi, alibeba begi rangi gani?”

    “Lilikuwa jekundu, sikumbuki lilikuwa la aina gani.”

    “Sawa. Kidogo maelezo yako yanaweza kufaa. Alivaa nguo za aina gani?’

    “Nakumbuka ilikuwa jinzi nyeusi na fulana nyekundu.”

    “Hivyo tu?”

    “Hapana, alikuwa na kofia nyeupe,” alijibu professa.

    “Sawa.

    Professa akabaki akijiuliza, ni kwa jinsi gani Martin alikuwa amemwambia akumbuke kitu fulani mpaka kumfahamu mtu aliyeingia ndani ya kichaka kile na wakati hakuwa akikumbuka kitu chochote kile, mpaka hapo, alijipa uhakika kwamba mtu aliyesimama mbele yake alikuwa hatari sana na hakuwa na mchezo hata kidogo.

    “Umejuaje kama ningeweza kukumbuka?”

    “Hakuna siri. Kwenye tukio lolote linalotokea jukwaani, wale watu waliokaa mbele ambao wanawaona watu wengi, ni lazima muuaji au mtu aliyefanya tukio fulani walikuwa wakimuona ila walimpuuzia, ndiyo inavyotokea kila siku. Hata ukimfuata mtu mwingine aliyekuwa jukwaani siku ile, atakwambia kwamba alimuona ila alipuuzia na ndicho kilichotokea kwako!” alisema Martin.

    “Mmmh! Ni hatari sana. Kwa hiyo nini kinafuata?”

    “Kumtafuita mtu huyo aliyevalia jinzi nyeusi, begi jekundu na kofia nyeupe.”

    “Tunampataje?”

    “Ni kazi nyepesi sana. Ila jua huyo mtu si Mtanzania.”

    “Mmmh!”

    “Ndiyo. Kwa sisi Watanzania hakuna mtu anayeweza kuitumia Rifle vizuri mpaka awe komandoo, ni moja ya bunduki zinazosumbua sana. Kama umeona mtu kaitumia na mpigo mmoja tu aliweza kumuua mhusika, jua huyo si Mtanzania, atakuwa mtu wa nje ya Tanzania, na kama ni Mtanzania, jua kwamba atakuwa komandoo kitu ambacho hakiniingii akilini,” alisema Martin.

    “Mmmh! Sasa utampata vipi?”

    “Ni kitu chepesi sana, kama kumsukuma mlevi mlimani, usiwe na wasiwasi, nataka kuonana na rais wa chuo hiki,” alisema Martin.

    “Unadhani atakusaidia?”

    “Ndiyo. Asilimia mia moja.”

    “Hakuna tatizo.”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ilikuwa saa 11 jioni, Ndege ya Shirika la Ndege la British Airlines ilikuwa ikitua katika Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere uliokuwa jijini Dar es Salaam. Ndege hiyo iliposimama, abiria wakaanza kuteremka na miongoni mwa abiria hao alikuwepo Victor, mtoto wa marehemu Mickey.

    Victor akaanza kupiga hatua kuelekea katika sehemu ya jengo la uwanja huo na kisha kuelekea katika sehemu ya kuchunguzia mizigo, akaliacha begi lake na lilipopita katika mashine maalumu ya kuchunguzia mizigo na kuonekana hakuwa na tatizo lolote lile, akalichukua na kuondoka nalo.

    Mwendo wake ulikuwa ni wa taratibu, alipofika nje ya jengo hilo, akachukua teksi na kuondoka nayo kuelekea hotelini. Kichwa chake kilikuwa na mawazo lukuki, kila alipokuwa akiwafikiria wazazi wake, hakupata jibu.

    Alikumbuka kuwa walimwambia kwamba wangewasiliana katika kipindi atakachokuwa ameshuka kutoka kwenye ndege lakini kitu cha ajabu, kila alipokuwa akiwapigia simu, hawakuwa wakipatikana.

    Hakujua ni kitu gani kilichokuwa kimetokea, lakini hakutaka kujipa kazi kubwa ya kufikiria sana, yote hayo, hakuona kama kulikuwa na tatizo lolote lile, alikuwa na uhakika kwamba angewasiliana nao.

    “Where to, my brother?” (Unaelekea wapi kaka yangu?) aliuliza dereva teksi kwa lugha ya kihuni.

    “Take me to Serena Hotel,” (Nipeleke katika Hoteli ya Serena) alisema Victor, dereva akapiga gia na kuanza kuelekea huko.

    Walichukua dakika arobaini mpaka kufika katika hoteli hiyo ambapo Victor akateremka na kuanza kuelekea katika sehemu ya mapokezi, akalipia kiasi cha fedha kilichohitajika, akapanda lifti na kuanza kuelekea katika chumba alichoelekezwa.

    Kila wakati kichwa chake kilikuwa kikiwafikiria wazazi wake, baada ya simu zao kutokupokelewa kwa kipindi kirefu, sasa hivi hazikuwa zikipatikana kabisa. Alichokifanya ni kupumzika kwa kuamini kwamba baadae angeweza kuwatafuta kwa mara nyingine.

    Ilipofika saa kumi na mbili jioni, akasikia simu yake ikiwa imelia mlio mfupi uliomaanisha kwamba kuna ‘breaking news’ ilikuwa imetumwa kutoka katika Kituo cha Habari cha CNN ambacho alikuwa amejiunga nacho.

    Hakutaka kuifuata simu yake, alibaki kitandani pale huku akionekana kuwa mwingi wa mawazo. Baada ya kuhisi kwamba kulikuwa na umuhimu wa kuiona habari hiyo ilihusu nini, akaamka na kuanza kuifuata simu yake, alipoifikia, akaichukua na kukiangalia kioo cha simu hiyo.

    ‘POTTER MICKEY HAS BEEN KILLED IN TANZANIA’ (POTTER MICKEY AUAWA NCHINI TANZANIA) ilisema sehemu ya taarifa hiyo huku ikiwa imeambatanishwa na picha ya bwana Mickey.

    Victor akahisi kutetemeka, hakuamini kile alichokuwa akikisoma, akaliangalia jina lile vizuri, aliporidhika nalo, akayaamisha macho yake na kutazama picha iliyokuwa imeambatanishwa na taarifa ile, alikuwa baba yake mzazi.

    Moyo wake ukashindwa kuvumilia, ghafla, machozi yakaanza kumbubujika mashavuni, hakutaka kuendelea kubaki mahali hapo, akatoka chumbani mule.

    Hoteli ilikuwa na lifti lakini hakutaka kuitumia, aliona kama zingemchelewesha, alichokifanya ni kuanza kuteremsha ngazi, tena kwa kasi. Mwendo wake ulikuwa wa harakaharaka, alijiona akichelewa kufika chini, moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali kwani hakutegemea kupokea taarifa kama ile aliyokuwa ameipokea.

    Alipofika chini, hakutaka kusimama, akatoka nje ya hoteli hiyo na kuifuata moja ya teksi zilizokuwa eno hilo na moja kwa moja kuingia.

    “Take me to University of Dar es Salaam,” (Nipeleke katika Chuo cha Dar es Salaam)

    “Thirty thousand shillings bro,” (Shilingi elfu thelathini kaka)

    “No problem” (Hakuna tatizo) alisema Victor.

    Bado alionekana kuchanganyikiwa, kichwa chake kilimzunguka na kujiona akikaribia kuwa kichaa, taarifa aliyokuwa ameipata kwamba baba yake kipenzi alikuwa ameuawa ilikuwa imemchanganya mno.

    Hawakuchukua muda mrefu wakafika katika eneo la chuo hicho. Katika kila kona watu walikuwa wakilizungumzia tukio hilo ambalo halikuwahi kutokea kabla chuoni hapo. Hakujua amuulize nani, akajikuta akipiga hatua mpaka katika Jengo la Utawala na kupandisha juu.

    “Samahani,” alisema Victor, alikuwa amemsimamisha mwanachuo mmoja.

    “Bila samahani.”

    “Nimepata taarifa kuna mtu alipigwa risasi leo hii mahali hapa, ni kweli?”

    “Ndiyo! Kuna Mzungu alikuja kwa ajili ya masomo ya ujasiriamali, bahati mbaya kapigwa risasi,” alijibu jamaa yule.

    “Kapigwa risasi wapi?”

    “Hapa kichwani.”

    “Hapana, namaanisha eneo gani.”

    “Kule uwanjani.”

    “Unaweza kunipeleka?”

    “Hakuna tatizo. Twende!”

    Wakaanza kuondoka mahali hapo, bado Victor alionekana kutokuwa sawa. Mwendo wao ulikuwa wa harakaharaka, bado watu walikuwa wakilizungumzia tukio lile lililotokea kipindi kifupi kilichopita. Walipofika uwanjani, kwa haraka Victor akaanza kukimbia kuelekea katika jukwaa lile, bado damu zilikuwa mahali pale, alipofika katika eneo hilo, akajikuta akipiga magoti na kuanza kulia.

    Wanachuo wote wakaanza kumwangalia, alionekana kuwa na majonzi kupita kawaida, kwa muonekano wake, kila mmoja akagundua kwamba mtu huyo alikuwa na undugu na marehemu Mickey lakini hawakujua kama alikuwa mtoto wake.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wanachuo waliokuwa mbali wakaanza kumsogelea, walipomfikia, wakamzunguka na kuanza kumwangalia vizuri.

    “Pole sana...” alijikuta akisema mwanachuo mmoja.

    Victor hakuitikia kitu, alichokifanya, ni kuondoka mahali hapo huku akionekana kuwa na hasira mno.

    Alichokifanya Victor ni kuwauliza wanachuo kuhusu tukio zima lilivyokuwa. Alipohadithiwa, akawaomba wampeleke katika hospitali aliyolazwa mama yake, baadhi ya wanachuo wakampeleka huko huku moyo wake ukiwa na machungu mno.

    “Nitampata tu muuaji, nitampata tu,” alisema Victor huku akiuma meno yake kwa hasira.

    ****

    “Ninahitaji kufahamu kitu kimoja, kuna wanafunzi wangapi kutoka nje ya nchi?” aliuliza Martin huku akimkazia macho rais wa chuo hicho, Ibrahim.

    “Wapo wengi sana.”

    “Wangapi?”

    “Kwa kweli idadi yao kamili siifahamu.”

    “Sawa. Kuna mwanafunzi mmoja namtafuta.”

    “Yupi?”

    “Mwanachuo anayependa kubeba begi jekundu na kupendelea kuvaa kofia nyeupe, unamfahamu?”

    “Mhh! Wapo wengi wanaovaa hivyo.”

    “Lakini bahati nzuri si kwa wenyeji.”

    “Kivipi?”

    “Kuna mgeni mmoja alikuwa akipendelea kubeba begi hilo na kuvaa kofia hiyo, haumfahamu?”

    “Kiukweli simfahamu.”

    “Sawa.”

    Martin hakutaka kupoteza muda ndani ya ofisi ya rais huyo, alichokifanya ni kuaga na kuondoka. Kichwa chake kilikuwa na mawazo lukuki, alijua fika kwamba mbele yake kulikuwa na mtihani mkubwa lakini hakutaka kuona akikubali kushindwa kirahisi, alichokifanya kwa wakati huo ni kuwasiliana na mkuu wa TISS na kumwambia kile kilichokuwa kimeendelea.

    “Rudi, kuna jambo jingine la maana tutalifanya, hili ni siri na hakuna mwanachuo yeyote anayelifahamu, muuaji tutampata tu,” alisema mkuu wa TISS, Bwana Godson Materu.

    “Sawa.”

    Martin akarudi mpaka ofisini kwake huku akiwa na ripoti kamili juu ya kile kilichokuwa kimeendelea. Hakujisikia furaha, hakufurahia kujiona akishindwa kazi aliyopewa na wakuu wake kuifanya, kutokumpata muuaji siku hiyo kulimhuzunisha kiasi kwamba hata kula hakuweza kula.

    “Usijali, hii ni kazi kubwa, wewe ishia hapa, huku kulipobakia, tumuachie Mathias,” alisema bwana Materu.

    “Mkuu!”

    “Unasemaje?”

    “Samahani kama nitakuwa nakuingilia kazi yako!”

    “Usijali, kuna nini?”

    “Nimeanza kuifanya hii kazi kwa kipindi kirefu mno, naomba unipe jukumu la kuianza kazi ya kumtafuta huyu muuaji, najua ni kazi ngumu lakini nakuahidi kwamba nitaikamilisha, haijalishi ni kipindi kirefu namna gani nitachukua,” alisema Martin.

    “Una uhakika utaiweza?”

    “Nakuahidi hilo. Huu ni mwanzo na ndiyo maana umekuwa mgumu sana kwangu, ila nakuahidi nitaiweza.”

    “Sawa. Sisi tutakusaidia kuipata picha ya muuaji, baada ya hapo, kumtafuta na kumtia nguvuni itakuwa kazi yako!”

    “Nitashukuru mkuu. Vipi kuhusu Wamarekani?’

    “Hali imekuwa mbaya, wamechachamaa mno, sikuwahi kuwaona wakichachamaa kiasi hiki, mbaya zaidi, hata majasusi wao wa CIA wameingilia kati kwa kusema kwamba kama tumeshindwa kumpata muuaji kwa uzembe wetu, waje kuifanya kazi hiyo wao wenyewe.”

    “Hakuna kitu kama hicho, hatujashindwa, wakiwaambieni tena, waambie kwamba kijana wenu yupo kazini, ndani ya kipindi kichache, muuaji atapatikana.”

    “Nakuamini, ila kama ukishindwa?”

    “Nakuahidi sitoshindwa, nitataka kuifanya kazi hii kwa uwezo mkubwa,” alisema Martin.

    Hakutaka kuona kazi hiyo ikipotea bure huku akiwa ameshindwa kumpata muuaji huyo. Alikuwa tayari kufanya kitu chochote kile lakini mwisho wa siku muuaji huyo apatikane.

    Alijua kwamba lilikuwa jambo gumu mno kupatikana lakini moyo wake ulimwambia kwamba alikuwa na uwezo mkubwa sana wa kumpata muuaji huyo hivyo asonge mbele zaidi.

    Hiyo ikawa furaha kwake, aliuamini uwezo wake, alitaka kuikamilisha kazi hiyo kwa kipindi kifupi kijacho, ila kabla hajaingia kazini kwa kazi maalumu, akataka kuonana na mke wa marehemu, Elizaberth, hapo ndipo alipoona kufaa kuanzia, aliamini kupitia mwanamke huyo, angeweza kugundua mambo mengi.

    “Huyu ndiye wa kwanza kuonana naye, ngoja nimfuate hospitalini,” alisema Martin huku akiwa amepania kuifanya kazi hiyo kwa uaminifu mkubwa.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Victor alibaki akiwa na majonzi tele, alifika hospitalini lakini akazuiliwa kuingia ndani kumuona mama yake ambaye aliambiwa kwamba alipoteza fahamu mara baada ya kifo cha mume wake. Moyo wake ulikuwa kwenye maumivu mazito yasiyoweza kusimulika.

    Alibaki kitini huku akimuomba Mungu kwamba kila kitu kilichokuwa kikitokea kiwe ndoto na si maisha halisi aliyokuwa akiishi duniani. Hakuweza kubadilisha kitu, ukweli uliendelea kubaki palepale kwamba baba yake alikuwa ameuawa.

    “Niambie nini kinaendelea,” Victor alimwambia daktari wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dk. Kimario.

    “Subiri kwanza.”

    “Nitasubiri vipi na wakati sijajua hali anayoendelea nayo mama, niambie kwanza,” alisema Victor.

    “Subiri, usiwe na presha.”

    Ikambidi Victor awe mpole kitini. Kama kulia, alikuwa amelia kwa kipindi kirefu lakini hakukuwa na kitu chochote kilichobadilika, kuna wakati alimuomba Mungu kwamba ilikuwa ni bora na yeye amchukue kama amemchukua baba yake lakini kuna kipindi alimuomba Mungu kutokufanya hivyo mpaka atakapomkamata muuaji wa baba yake.

    Aliendelea kubaki kitini pale mpaka ilipofika saa tatu usiku alipoambiwa kwamba alikuwa na mgeni aliyetaka kumuona na kuzungumza naye mawili matatu, hakupinga, akakubali kuonana naye.

    Mgeni huyo alikuwa Martin, alifika hapo, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumpa pole kwa kila kitu kilichokuwa kimetokea, baada ya hapo akaanza kuzungumza naye.

    “Ninataka kumuona mama yako,” alisema Martin.

    “Bado hawaruhusu mtu yeyote kuingia ndani, wewe nani?” aliuliza Victor.

    “Ninaitwa Martin.”

    “Unahusika na nini na kwa nini unataka kumuona mama yangu?” aliuliza Victor.

    “Ninahitaji kusaidia.”

    “Kusaidia nini?”

    “Kumkamata muuaji.”

    “Hilo niachie mimi, nitamkamata tu.”

    “Umkamate wewe?”

    “Unanionaje? Acha, nitamkamata kwa mkono wangu, na nitamuua kama kisasi kwa baba yangu,:” alisema Victor.

    “Naomba nikuulize swali moja.”

    “Uliza.”

    “Hivi unajua kwa nini baba yako aliuawa?”

    “Hapana.”

    “Nahisi kuna kitu, sijajua kimeanzia wapi ila nahisi kuna kitu.”

    “Kitu gani?”

    “Hapo ndipo upelelezi wangu utakapoanzia, tukifanikiwa kujua sababu, basi muuaji atapatikana, hatuwezi kumpata muuaji kabla ya kujua sababu iliyopelekea kifo chake,” alisema Martin.

    Martin alijaribu kuzungumza na Victor na kumwambia mipango yake kabambe ambayo alikuwa njiani kuifanya. Hakutaka kumficha japokuwa hakuruhusiwa kufanya hivyo. Mtu pekee ambaye angewezesha kukamatwa kwa muuaji huyo alikuwa Victor na mama yake.

    Kichwa chake kilimwambia kwamba kulikuwa na kitu ambacho kilipelekea kifo cha bwana Mickey kwani alimini kwamba hakukuwa na mtu ambaye angeamua kufanya mauaji tu bila kuwa na sababu.

    Mbali na hivyo, akaanza kumfikiria bosi wake ambaye alimwambia kwamba angempa mwanzo wa kuanzia kazi yake. Ugumu mkubwa ulikuwa mbele yake, japokuwa alifika mahali hapo kwa ajili ya kuhitaji msaada lakini kuna kipindi alifikiria kwamba hiyo haikutosha, kulikuwa na sehemu nyingine ya kuanzia.

    Waliendelea kusubiri mpaka bi Elizabeth aliposhtuka kutoka katika usingizi wa kifo. Akaanza kuangalia huku na kule, hakujua ni mahali gani alipokuwa lakini baada ya kuona dripu ya maji ikining’inia juu yake, akagundua kwamba mahali alipokuwa kulikuwa ni hospitali.

    “Mickey!” alijikuta akiita.

    Hapo ndipo kumbukumbu zake zilipoanza kurudi, akaanza kukumbuka kila kitu kilichokuwa kimetokea toka mume wake kipenzi alipopigwa risasi mbele ya macho yake na kufariki dunia.

    Kila kitu kilichokuwa kikijirudia kichwani mwake kilikuwa kama filamu aliyokuwa akiitazama mbele yake, hakuamini kama mume wake ambaye alikuwa akimpenda, leo hii hakuwa naye, alikuwa ameuawa katika kifo kibaya cha kupigwa risasi.

    Kikaanza kilio cha kwikwi na mwisho wa siku kulia kwa sauti kubwa. Maumivu ya moyo wake hayakupungua, kadiri muda ulivyozidi kwenda mbele na kukumbuka kile kilichokuwa kimetokea, aliendelea kuumia zaidi.

    Baada ya dakika kadhaa, mlango ukafunguliwa na Dk. Kimario kuingia huku akiwa ametangulizana na watu wawili, mmoja alikuwa mtoto wake, Victor na mtu mwingine hakuwa akimfahamu. Alipomuona Victor tu, akaanza kulia.

    Mtoto wake alimkumbusha marehemu mume wake, walifanana kwa kila kitu kiasi kwamba kadiri alivyokuwa akimtazama, alimkumbuka mume wake zaidi.

    “Victor...bab...a ya...ko wam...emu...ua...” alisema bi Elizabeth huku akilia kama mtoto.

    “Nyamaza mama, tutampata muuaji tu,” alisema Victor, naye machozi yakaanza kumtoka kwa mara nyingine tena.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hakukuwa na wa kumbembeleza mwenzake, kila mmoja alikuwa akilia kwa uchungu mkubwa. Martin alibaki akiwaangalia, japokuwa alikuwa mwanaume shupavu mwenye moyo wa kikatili, naye akajikuta akibubujikwa na machozi, picha aliyokuwa akiiona ilimtia uchungu mno.

    “Ni lazima nimpate muuaji,” alijisemea Martin.

    Wala hakukaa sana mahali hapo, simu yake ya mkononi ikaanza kusikika ikiita, alichokifanya ni kutoka ndani ya chumba kile na kuelekea nje, mpigaji alikuwa bosi wake, bwana Godson ambaye akamtaka afike moja kwa moja mpaka ofisini kwake, hivyo akaaga na kuahidi atarudi kesho.

    Hakuchukua muda mrefu, akafika ofisini hapo ambapo moja kwa moja akaanza kuelekea katika chumba cha bosi wake ambaye akamuweka kitini.

    “Kila kitu tumekamilisha, muuaji amejulikana, kazi kwako kwenda kumkamata,” alisema bwana Godson.

    “Mmmh! Muuaji amepatikana?”

    “Ndiyo! Picha yake hii hapa,” alisema bwana Godson na kumpa picha ambayo Martin akaanza kuiangalia vizuri, akaonyesha mshtuko.

    “Haiwezekani!”

    “Ndiyo hivyo! Huyo ndiye muuaji wetu. Hakikisha anapatikana.”

    “Lakini bosi, kweli Gideon anaweza kuwa muuaji?”

    “Ndiyo! Hakikisha anapatikana.”

    “Lakini unakumbuka kwamba huyu ni kipofu?”

    “Najua hilo.”

    “Sasa toka lini kipofu akaua tena kwa kumlenga mtu na bunduki akiwa mbali?”

    “Hata sisi hatufahamu, cha msingi mtafute, kuna mengi ya kufahamu. Tunataka kujua zaidi huyu ni nani na kwa nini aliua. Usiuangalie upofu wake, kesho rudi chuoni ukamtafute, ukimkamata, mtie nguvuni,” alisema bwana Godson, Martin akaondoka huku akionekana kuchanganyikiwa, kumkamata kipofu na kumleta mbele ya chombo cha sheria, kwake ilionekana kuwa kitu kigumu, ila kwa sababu aliambiwa afanye hivyo, hakuwa na ubishi.

    “Nitamkamata hiyo kesho, tena kwa sababu ni kipofu, hakuna tatizo,” alisema Martin huku akiondoka mahali hapo kurudi nyumbani kwake, kwani tayari ilikwishatimia saa teno usiku.



    Wanachuo kutoka sehemu mbalimbali duniani walikuwa wakivutiwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kutokana na elimu bora iliyokuwa ikitolewa. Sifa mbalimbali za chuo hicho kuanzia mandhari na vitu vingine ikiwepo elimu bora ndivyo vilivyowakusanya watu wengi kutoka sehemu mbalimbali na kuja kusoma katika chuo hicho.

    Kulikuwa na wanachuo kutoka Afrika Kusini, Malawi, Msumbiji na sehemu nyingine, na si nchi hizo tu bali hata wanachuo kutoka katika baadhi ya nchi za Ulaya walikuwa wakija chuoni hapo kwa ajili ya kupokea elimu bora.

    Kutokana na wingi mkubwa wa watu waliokuwa wakikusanyika chuoni hapo tena kutoka katika nchi mbalimbali, serikali ya Tanzania ikaanza kuhofia, ikaogopa kuingiliwa na kukifanya chuo hicho kuwa mlango wa ugaidi ambao ungeweza kutokea nchini hapa na hivyo kufanya uamuzi wa kuweka kamera ndogo zijulikanazo kama CCTV kwa ajili ya kuangalia kila kitu kilichokuwa kikiendelea chuoni hapo.

    Kamera hizo za siri zilikuwa na kazi moja, kuangalia mandhari ya chuo hizo sehemu mbalimbali bila mtu yeyote kufahamu.

    Kamera pekee zilizokuwa zikionekana zilikuwa zile zilizowekwa madarasani ambapo wanachuo wengi wakafikiri kwamba zilikuwa zikiwachunguza kila walipokuwa wakifanya mitihani kitu ambacho hakikuwa sahihi.

    Katika sehemu kama kwenye miti, sehemu za kulia vyakula, vituoni na sehemu nyingine, kuliwekwa kamera ndogo zilizokuwa na nguvu ambazo hazikuwa zikionekana kwa wanachuo chuoni hapo na hata maprofesa hawakuwa wakikijua hicho.

    Kamera zilifungwa usiku na asubuhi iliyofuata, kila kitu kilikuwa hewani. Picha zilizokuwa zikionekana chuoni hapo, zilikwenda moja kwa moja katika kompyuta za TISS zilizokuwa makao makuu na kuanza kukifuatilia chuo hicho na kuangalia mipango yote iliuyokuwa ikifanywa na wanachuo bila kujua.

    Walifahamu mengi, kupitia kamera hizo, wakabaini wanachuo wengi waliokuwa wakifanya mapenzi porini na hata mabwenini, kila uchafu uliokuwa ukifanyika chuoni, walikuwa wakiuona lakini hawakutaka kujali, kile walichokuwa wakikitaka ni kuhakikisha kwamba ulinzi unakuwa wa kutosha.

    Siku zikaendelea kukatika, wanachuo wengi kutoka katika nchi mbalimbali waliendelea kumiminika chuoni hapo. Baada ya kipindi cha muda mrefu toka kamera ziwekwe chuoni hapo kisiri, akahamia mwanachuo mmoja kutoka Malawi, mwanachuo aliyewachanganya watu wengi, mwanachuo wa kiume aliyekuwa kipofu, huyu aliitwa Gideon Mutinyama.

    Watu wakaanza kujiuliza maswali mengi kuhusiana na kipofu huyo aliyekuwa na uwezo wa hali ya juu. Kila alipokuwa akikaa, pembeni kulikuwa na fimbo yake huku macho yake yakiwa yamefunikwa na miwani miyeusi ya jua.

    Hakusoma vitabu vya kawaida, vitabu vyake vilikuwa ni vile vilivyokuwa vikitumiwa na vipofu ambavyo havikuandikwa kitu chochote zaidi ya kuwekwa nukta tu. Watu walimshangaa Gideon, hakuwa mtu wa kupiga stori na watu lakini baada ya kuishi kwa kipindi cha miezi minne, akajikuta akiwa rafiki wa watu wengi.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Uwezo wake wa darasani haukuwa mdogo, kila mwanachuo akagundua kwamba mwanafunzi huyu alikuwa genius kwani katika kila somo alilokuwa akisomea, ilikuwa ni lazima kupata alama A katika kila mtihani.

    “Huyu Gideon ni mtu hatari sana, nasikia kakimbiza vibaya mpaka Professa Abdul ameona noma,” alisikika kijana mmoja.

    “Acha masihara.”

    “Ndiyo hivyo kaka.”

    “Si ndiye huyu kipofu! Au kuna Gideon mwingine?”

    “Ndiye huyohuyo.”

    “Mmmh!”

    “Yaani ni noma, kila mtu anashangaa, sasa angalia vitabu vyake, nukta, nukta, nukta, hakuna herufi hata moja, ni nukta nukta na nukta,” alisema jamaa huyo.

    Bado uwezo wake ulikuwa gumzo chuoni, watu wengi wakawa wakifika chuoni hapo, kitu cha kwanza kilikuwa ni kuomba kukutana na kijana huyo aliyekuwa akimshangaza kila mtu.

    Alishinda na miwani huku fimbo ikiwa mkononi mwake na hata mara mojamoja alipokuwa akivua miwani yake, macho yake yalionyesha wazi kwamba alikuwa kipofu jambo lililowafanya watu wengi kumuonea huruma kutokana na hali aliyokuwa nayo.

    Gideon akajikuta akianza kupata umaarufu, upofu wake ukamfanya kuanza kujulikana, katika kila kona ndani ya Jiji la Dar es Salaam walikuwa wakimzungumzia, vyombo vya habari vikamtangaza sana huku watu wakitumia nguvu zao nyingi kuandika mambo mengi kuhusu yeye katika mitandao ya kijamii.

    Siku ziliendelea kukatika, bado wanachuo hawakuweza kugundua kwamba chuo kizima kilikuwa kimewekwa kamera ndogo ambazo zilikuwa ngumu kuonekana kwa mtu yeyote yule.

    Hakukuwa na mtu aliyekuwa akifahamu kuhusu uwepo wa kamera zile ndani ya chuo kile kwani hata professa Mitimingi ambaye alikuwa akikiongoza chuo hicho kwa wakati huo hakuwa akifahamu kitu chochote, yaani alikuwa kama wengine.

    “Samahani....” ilisikika sauti ya msichana mmoja, kwa muonekano alikuwa binti mrembo ambaye sura yake ilipendezeshwa na tabasamu pana. Alikuwa akiongea na Gideon.

    “Bila samahani...” alisema Gideon huku akiangalia juu, kwa mtazamo wake ulivyokuwa, ungegundua kwamba mtu huyo alikuwa kipofu.

    “Naweza kukaa na wewe na kuzungumza pamoja?”

    “Usijali, bila shaka wewe ni Juliet.

    “Waooo! Umenijuaje?”

    “Sauti yako haiwezi kunipotea.”

    “Ila hatukuwahi kuongea hata siku moja!”

    “Lakini huwa ninakusikia ukiongea na marafiki zako! Hongera kwa kupendeza,” alisema Gideon.

    “Hahaha! Nimependeza! Sasa wewe kipofu umenionaje?”

    “Huwa tunaishi kwa hisia, tunaweza kugundua kitu chochote kile kuanzia rangi, muonekano, minong’ono na vingine vingi,” alijibu Gideon huku akipapasa huku na kule kutafuta fimbo yake.

    Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa ukaribu wa watu hao wawili, Juliet akaanza kuwa na Gideon huku kila wakati akimshikia fimbo yake hasa kila alipotaka kumuongoza barabarani.

    Wawili hawa wakazua gumzo, msichana Juliet alikuwa kila kitu kwa Gideon, siku ambayo kijana huyo hakuisikia sauti ya msichana huyo, hakuwa na raha, alipenda kila wakati awe karibu naye jambo lililoonekana kumfurahisha sana Juliet.

    Kupitia Juliet, watu ndiyo wakajua historia ya maisha ya Gideon, historia iliyomhuzunisha kila mtu kwamba katika kipindi ambacho mvulana huyo alizaliwa, alikuwa akiona kama watu wengine lakini alipofikisha umri wa miaka kumi, akamwagiwa sumu kali machoni mwake na mwanamke aliyekuwa akiishi naye na kumuita mama wa kambo.

    Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa upofu wake, watu hawakuamini kama kweli kulikuwa na wanawake waliokuwa na roho mbaya kama alivyokuwa mwanamke huyo. Japokuwa alikuwa kipofu, baadae ikagundulika kwamba Gideon alikuwa na uwezo mkubwa wa kufikiria na kufanya maamuzi yake, au kwa kifupi aliitwa genius.

    Shuleni akawa mwiba, watu waliutambua uwezo wake kwa kiasi kikubwa. Kila mwalimu aliyekuwa akimfundisha alifurahia kupata mwanafunzi kama huyo ambaye alikuwa msaada mkubwa hata kwa wanafunzi wengine.

    “Ikawaje baada ya hapo?” aliuliza Juliet.

    “Nikaamua kumchukia mama wa kambo, aliyabadilisha maisha yangu kwa kiasi kikubwa, sikuweza kumuona kwani ilikuwa ni lazima nimuue kwa kile alichonifanyia,” alisema Gideon.

    Mambo yote hayo Juliet alikuwa amehadithiwa na kijana huyo aliyemwambia ilikuwa ni lazima iwe siri lakini Juliet hakuweza kukubali, kila alipokuwa akikaa, siri ile ilikuwa ikimfurukuta moyoni mwake na mwisho wa siku kujikuta akiizungumza kwa marafiki zake.

    “Halafu eti mnasema nyie wanawake mna roho nzuri, si mmemsikia mwenzenu amemuharibia mtoto wa watu maisha yake, kumbe mimi kuwachukia nyie wapumbavu sawasawa tu,” alisema mwanachuo mmoja.

    “Hiyo ni hulka ya mtu, haimaanishi kwamba wanawake wote wapo hivyo,” alisikika msichana mmoja.

    Huyo ndiye alikuwa Gideon, kijana kipofu aliyemshangaza kila mtu chuoni hapo, kijana genius aliyekuwa akiongoza katika kila somo. Leo hii, bila kujua kitu chochote, mpelelezi Martin anaambiwa kwamba mtu aliyemuua mhamasishaji wa ujasiriamali kutoka Marekani, Potter Mickey kwa kumpiga risasi ya kichwa alikuwa Gideon.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Moyo wake haukuamini, alimfahamu Giodeon kuwa kama kijana kipofu, ilikuwaje ashike bunduki ya Rifle kwenye umbali wa mita zaidi ya hamsini na kisha kumlenga nayo mhamasishaji huyo wa ujasiriamali, kila alipofikiria, alikosa jibu, ila hakutaka kupuuzia, alitakiwa kufanya kama alivyoambiwa afanye, ilikuwa ni lazima arudi chuoni hapo na kumkamata Gideon.

    “Sawa, ngoja niwaridhishe nirudi chuoni, ila, mmh! Sidhani kamaa kipofu yule aliweza kufanya mauaji hayo,” alisema Martin.



    ITAENDELEA



0 comments:

Post a Comment

Blog