Search This Blog

Friday, 20 May 2022

SAA LA 25 - 4

 







    Simulizi : Saa La 25

    Sehemu Ya Nne (4)

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    € € € €

    “Kwa mujibu wa yule mama, anasema ile nyumba si yako na wala huna mali yoyote kutoka kwake.” Mwanasheria alikuwa akimueleza maneno hayo Mzee Njiku ambaye aliketi akitazamana na bwana huyo. Pembeni yake akiwa na dada na kaka yake, wote wakiwa kimya kabisa katika shauri la madai ya mali za ndugu yao mzee Njiku.

    “Ile nyumba nimeijenga mimi kwa pesa zangu, yeye hakuna alichochangia,” Mzee Njiku alisisitiza huku akigonga meza kwa pigo hafifu la mkono wake ulioishiwa afya kabisa.

    “Sikiliza Mzee, sisi tunaongozwa na sheria, na siku zote sheria hufanya kazi vizuri kadiri ya ushahidi uliopo, tumemwita yule mama amekuja hapa tukamueleza juu ya hili swala akakana kabisa kuwa wewe hukuchangia chochote katika ujenzi wa nyumba hiyo...”

    “Huyo ni muongo!” dada wa Mzee Njiku alimueleza wakili

    “Dada, mbele ya sheria kitakachokupa haki ni uthibitisho na si vinginevyo. Hivyo basi kama ninyi mnasema ile nyumba na mali zile ni za kaka yenu, wekeni uthibitisho mezani” wakili alizungumza kwa tuo huku akiwa kaegemea meza kwa mikono yake miwili, mwili wake uliojaa afya ukiwa ndani ya suti nyeusi iliyotanguliwa na shati jeupe hakuonekana kama mwenye mzaha bali alikuwa kikazi zaidi. Kwa maneno hayo Mzee Njiku akiangusha chozi mbele ya wakili.

    “Kwa pesa zangu mimi, za jasho langu, leo naambiwa eti sina nyumba wala chochote kwake” Mzee Njiku alilia kwa uchungu.

    “Mzee, mi sijasema kuwa huna nyumba, mi nimesema mbele ya sheria kitakachokupa haki ni uthibitisho. Yule mama nilivyomuita hapa alitii, na nilivyoongea nae alinieleza A mapaka Z na ushahidi anao, kaja na hati ya kiwanja, risiti za manunuzi ya vifaa vya ujenzi na hatimiliki ya nyumba kutoka serikali ya mtaa mpaka manispaa navyote ipo kwa jina lake halisi ambalo pia nimelithibitisha kupitia kitambulisho chake cha uraia na cheti cha kuzaliwa. Sasa kama na nyie mnampinga basi leteni ushahidi wenu ili sasa mjadala wetu uingie hatua nyingine” yule wakili aliwaeleza.

    “Mwanamke shetani yule. Na atakoma mi nasema, kama alikuwa hajui mimi ndio Selina Njiku, namfuata uko huko”. Dada wa Mzee Njiku aling’aka kwa hasira mbela ya yule wakili. Mahojiano yalipofanyika kwa kina kati ya wakili na Mzee Njiku ilionekana wazi kuwa Mzee Njiku hakuwa na ushahidi wowote juu ya nyumba, kiwanja wala mali yoyote katika zile alizofungulia madai kwa wakili huyo, sheria ilimbana hasa kwa kukosa ushahidi, alibaki katoa macho pima akiangalia ukutani kulikokuwa na picha ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Al - Haj Ally Hassan Mwinyi, lakini haikuwa na msaada kwake, alijiinamia chini na kushikwa na hasira lakini afanye nini, hapo ndipo alipokumbuka ujinga wote alioufanya tangu aliposikiliza ushauri wa rafiki zake ambao sasa wanaendelea na maisha yao wakati yeye anateseka na dunia, ama kweli dunia hadaa ulimwengu shujaa.

    Baada ya shauri hilo waliagana na wakili yule na kukubaliana kurudi wakati mwingine watakapokuwa tayari wamekusanya ushahidi katika hilo. Kwa kumshika huku na huku, Mzee Njiku alijikongoja kutoka nje ya ofisi hilo lakini kabla hajafika nje kabisa alijihisi kuishiwa nguvu na mara akaponyoka kutoka katika mokono ya ndugu zake hao , akaanguka chini akapoteza fahamu. Jitihada za kumpepea hazikuzaa matunda ya kurudisha fahamu za mzee huyo, hakukuwa na la kufanya walimbeba na moja kwa moja walielekea hospitalini ambako alipokelewa na kulazwa.

    Mzee Njiku alilala juu ya kitanda kile kimya kabisa, macho yake yakiwa hayataki kumtazama mtu ila yaliruhusu machozi kutoka mara kwa mara, mapigo ya moyo wake yalibadilikabadilika mara kwa mara, hayakuwa na utulivu hata kidogo, mara nyingi mawazo yake yalimrudisha nyuma na kumkumbuka nyumba ndogo wake huyo, ambaye sasa haamini yaliyomkuta hata kidogo.



    **************



    Mama Njiku alitulia kimya akimsikiliza mama Minja yote aliyokuwa akimueleza, mara kwa mara alionekana akitikisa kichwa kuonesha kama hakukubaliana na jambo Fulani.

    “Unasikia mama Minja, mi naamini kabisa kuwa maneno hayo waliyokwambia si ya kweli” alimueleza mama Minja, kisha akanywa maji yaliyokuwa katika kikombe cha plastiki na kukishisha tena mezani kisha kuendelea “mimi angenieleza tu, lakini mkasa wote kanisimulia, na sivyo walivyokwambia.”

    Mama Minja hakuwa na la kufanya waliamua kwa pamoja kutafuta mbinu ya kumsaidia mama Vituko dhidi ya janga hilo.



    Haikuwa chukuwa mud asana kufika katika kijiji hicho cha Msele kilicho karibu na Sekenke, maswali mawili matatu kwa wanakijiji tayari mama Minja alishajua ni kituo gani cha polisi ambacho Mama Vituko alikuwa amehifadhiwa.

    “Sisi ni ndugu wa mama Vituko, tumekuja kufuatilia kesi ya ndugu yetu” Mama Njiku aliongea na polisi aliyekuwa hapo.

    “Nyie ndugu zake gani?” polisi yule aliuliza kwa makini swali hilo, “Maana huyu mama hapa kijijini tunamjua vizuri sana kuwa hana ndugu wa karibu, sasa ninyi ni ndugu vipi?” aliwatupia swali lililoonekana gumu kidogo. Mama Minja na Mama Njiku walijiona wamekosea kwa hilo walibaki kutazamana.

    “Kwani ndugu ni lazima awe wa ukoo afande?” Mama Njiku alimtupia swali hilo yule polisi aliyeonakana ana shughuili nyingi za kiofisi.

    “Unajua ninyi ndo mmesema ndugu yenu, sisi hapa twawajua ndugu zake wote, lakini ninyi hatuwajui…”

    “Afande, jirani yako ndiyo nduguyo na akufaaye kwa dhiki ndiyo rafiki” mama Minja alimhasa yule afande ambaye sasa alionekana kuweka kalamu yak echini kusikiliza ngonjera za akina mama hawa wasiofanana kwa lolote.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Poleni sana, ndugu yenu amekosa mtu wa kumdhamini amerudishwa rumande” yule polisi alizungumza huku akimkazia macho mama Minja.

    “Tunaomba kuonana naye!” Mama Minja aliomba

    “Hamuwezi kuonana naye!”

    “Afande ni haki yeye kuonana na ndugu zake” Mama Minja aliendelea kusisitiza

    “Hivi we mama na kwa niaba ya Watanzania wote, haki yeni mnaijua nyie? Sasa sikilizeni, hamuwezi kumuona huyu mtu, mkitaka kumuona ni baada ya siku saba atakapopelekwa tena mahakamani.”



    Maelezo yaliyotolewa na yule askari kwa akina mama hawa yalikuwa kama msubari wa moto katyika kidonda kibichi. ‘Kwa nini tusiruhusiwe kumuona?’ ‘kosa gani hasa alilolifanya?’ maswali kama haya na mengine mengi yalipita katika kichwa cha Mama Minja, alielewa wazi kuwa hapo kuna kitu ambacho hakiend sawa katika swala hilo, haki haitendeki. Alivuta hatua chache na kulifikia gari lake, lakini moyoni alikuwa akiumia sana katika hilo, alikiangalia tena kituo kile cha polisi bila kukimaliza kisha akaingia garini pamoja na mama Njiku, wakaondoka taratibu. Mwendo mfupi tu walisimama katika eneo lililoonekana kama soko ambalo lilikuwa limechangamka sana. Wakajichanganya na kupata sehemu panapouzwa pombe za kienyeji na nyama choma wakaingia humo. Walinunua nyama kadhaa zilizochomwa na kuketi hapo wakianza kula kidogo kidogo huku wakishushia na soda.

    “Akina mama jamani hata mi mtoto wenu sijala kabisa, mnisaidie japo mia, miambili!” kijana mchafu alisimama mbele yao na kuwaomba. Mama Minja alimtupia jicho kijana huyo na kumuuliza.

    “Unataka nini, nyama?”

    “Kama ntapata na kinywaji pori mama zangu mi ntainjoi, si mnajua njaa huku kwetu”

    “Haya chukua utakacho”

    Yule kijana aliagiza nyama na lita moja ya pombe ya kienyeji.

    “Usiende mbali, kaa hapa” Mama Minja alimuita yule kijana. Muda wote mama Njiku alibaki kimya akitafuna nyama zile taratibu na kujimiminia soda yake, kichwani mwake akijiuliza maswali mengi, alishangaa sana kumuona mama Minja jinsi anavyochangamana na watu kwa muda mfupi, kumbe hakujua hila ya shoga yake huyo, alipitiwa na msemo usemao penye wengi pana mengi. Macho ya Mama Njiku mara nyingi yaligongana nay a mzee mmoja aliyekuwa akinywa pombe hapo ‘kama namfananisha’ alijisemea moyoni mara nyingi.

    “Unaitwa nani?” Mama Minja alianza kumsaili yule kijana aliyekuwa akila nyama ile kwa pupa sana alionekana wazi alikuwa na njaa ya kutosha.

    “Naitwa Mancatcher, alijibu kwa sauti yake ya majigambo huku akijimininia pombe ile kinywani.

    “Mazeli, ndiyo umetia timu na huo mkoko hapo nje ee?”

    “Ee ndiyo mimi”

    “Aisee Mkoko wa maana kweli ule!” Mancatcher alimsifia mama Minja huku akigonga naye kwa ngumi mara nyingi.

    “Sa’ nyie mazeli mmekuja huku pori kununua shamba au?” yule kijana alimuuliza mama Minja

    “Hapana! Kwani huku mna mashamba nyie?” aliuliza mama Minja

    “Mengi tu, ya dhuluma yapo, ya kiukweli utayapata. Huku ndo kila kitu mama ‘angu, kama vipi nikutafutie dalali?”

    “Hapana! Usijali” alijibu mama Minja, baada ya kunywa funda moja la soda, “nilikuja kwenye ishu ya ndugu yangu hapo mahakamani…”

    “Ana kesi?” Mancatcher alidakia kwa kumkatiza mama Minja, akiwa kamkodolea macho akaendelea “ Au ya yule mama nini?!” alimuuliza mama Minja.

    “Iyo hiyo! Nilikuwa nimekuja nimuwekee dhamana nimtoe”

    “Aaaa Mama! Huwezi kumtoa pale, pana mchezo uliochezwa pale si wa kitoto, anayefunga goli nyingi anapewa ubingwa” alikamata pande lingine la nyama na kulitafunatafuna kwa meno yake yaliyokosa mswaki muda mrefu.

    “Kwa nini unasema hivo?” mama Minja aliuliza

    “Mh! Mama yangu wewe! Watu wabaya sana duniani hapa, ndiyo maana hata Marijani aliimba, kwenye watu kumi binadamu mmoja, hakukosea mama yangu”

    Mama Minja akajiweka vizuri kwa maneno yale ili kujua kwa undani, akamuagizia lita ingine ili amchangamshe vizuri. Baada ya kupiga funda la kwanza na la pili, Mancatcher alifunguka.

    “Mama yangu yule, kaingizwa kwenye game isiyomuhusu. Yule mama, ndugu yako, alitoroka hapa kijijini kipindi kirefu kilichopita baada ya kufiwa na mumewe. Ndugu zake walitaka arithiwe kindoa halafu mali zote walimnyang’anya. Mama yule alipoona hivo akatambaa, na hakuna aliyejua. Mara huku nyuma tukaanza kusikia ametoroka kwa sababu amehusika kwenye kifo cha mumewe, wanasema kamtilia sumu mumewe ili afe yeye arithi mashamba na mali zingine.”

    Maneno yale yalimgutusha Mama Njiku kutoka katika mzubao uliompata kwa muda akimwangalia yule mzee ambaye muda wote alihisi anamfananisha, alivutiwa na habari hii na kutega sikio kwa chati, wakati huo mama Minja alikuwa akiendelea kuongea na yule kijana.

    “Unasikia mama, ndugu za mumewe huku nyuma wakapata mseti, wakauza kila kitu halafu wakazusha huo uzushi …

    Miezi kadhaa ilopita

    “Ukichukua hapa, ni mpaka kwenye mti uleeeee unaouona kule kabisa!” mzee Malombe na baadhi ya kaka wa marehemu walikuwa wakimuonesha mteja huyo ardhi aliyoachiwa mama Vituko na marehemu mumewe. Walikuwa katika hatua za mwisho za kuuza mali za marehemu pa si kujali watoto wataishi vipi. Cha kushangaza mauzo hayo yalifanyika mahali pengine na hapo shambani ilikuwa makabidhiano tu, na kila kitu kilifanyika alfajiri kwa kisingizio kwamba mchana hawatakuwepo.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Sasa mjomba, hapa kitatusumbua hati za hili shamba na nina uhakika kuwa yule mwanamke anazo” shemeji wa mama Vituko alimng’ata sikio mjomba wake mzee Malombe.

    “Hilo lisikuumize kichwa bwana mdogo, kila kitu kinanunulika, pesa ndiyo kila kitu. Tuuze hapa tupate pesa na pesa hiyo hiyo tutafanya kila kitu” Mzee Malombe alimueleza kwa utaratibu baada ya mnunuzi kuondoka “ na lazima tuhakikishe hizo karatasi zote tunazipata” alisititiza.



    Mancatcher kama anavyojiita, kijana mtukutu kijijini,polisi wote walikwishamjua utukutu wake, kibaka aliyeshindikana, usiku uliotangulia aliiba kwenye nyumba ya mchaga mmoja kijijini hapo sanduku moja alilokuta limezubaa chumbani na kuja kulitupia katika kichaka kimoja jirani kabisa na shamba hilo. Alfajiri hiyo alikuwa katika kulifungua kujua nini kapata katika wizi wake huo ndipo alipoona mtu mmoja mwenye asili ya kiburushi akiongozana na Mzee Malombe pamoja na mdogo wa Marehemu na mazungumzo yote aliyasikia mwanzo mpaka mwisho ‘zee silipendi hili!’ alijisemea moyoni akimaanisha mzee Malombe.



    Shemeji wengine wa mama Vituko walikuwa tayari wakitia heshima kwenye vilabu vya pombe kwa pesa hizo wakifurahia mafanikio, na chini chini walianza kueneza habari kuwa kaka yao aliuawa kwa sumu aliyowekewa na mkewe ili arithi mali lakini wao wanajitahidi kurejesha shamba hilo ili kuwakabidhi watoto, ilikuwa ni moja ya kujikosha tu mbele za watu.

    “Na lazima aje ajibu kesi yake kwa alichomfanyia kaka yetu” walitamba kwa maneno hayo. Kila mtu aliisubiri siku ya kufika mama Vituko, kijiji kizima walijua kuwa mama Vituko aliyatenda hayo, ni wachache wenye upeo wa kufikiri walikua tofauti na wengine.



    ******************



    Siku chache zilizopita





    “Sasa nielezeni, nyi mnatakaje?” Bw. Kilipa alikuwa akiongea na wageni wake sebuleni kwake usiku ule, simu yake aina ya Samsung Galaxy akiwa ameilaza mezani, si mbali na dirisha kubwa.

    “Sisi mheshimiwa, tunataka tumkomeshe yule mwanamke. Hawezi kujifanya mjanja kuliko sisi” Shemeji mkubwa wa Mama Vituko alikuwa akiongea na Bw. Kilipa ambaye serikali ilimpa dhamana ya kuendesha mahakama ya mwanzo kijijini hapo, hakimu.

    “Nimewaelewa. Ila kuna kitu hamjanifafanulia. Nyie mnataka huyu mama mumkomeshe kwa nini na kivipi?” aliuliza Bw Kilipa.

    “Unajua huyu mama alitoroka kama tulivyoongea vile. Sasa kutokana na urithi wa mali sisi tumechukua mashamba yote na tumeyauza kwa tajiri mmoja Mburushi. Tuna wasiwasi huyu mwanamke atatuletea shida maana hati za serekali za yale mashamba hatuzioni” walijieleza kwa mapana

    “Sasa mpaka hapo nyi ndiyo mnatakiwa mshitakiwe, kwa sababu mmenyang’anya ardhi ambayo ni ya mjane, mali ya urithi” Bw Kilipa, hakimu wa mahakama ya mwanzo aliwageuka ndugu wale.

    “Sasa mheshimiwa ndiyo maana tukaja kwako kuyaweka sawa” mzee Malombe alidakia kutoka pembeni alipoketi.

    “Sikatai, ila ninyi mnajua mnavunja sheria ya haki ya kikatiba ya Tanzania? Kinachohusiana na haki ya kumiliki mali? Kifungu namba 24 Ibara ndogo ya pili, mnajua kinasemaje?” Bw Kilipa aliwatega kwa swali. Ndugu wale walibaki kimya kabisa hawakuwa na jibu, walijisikia aibu sana, kwao waliona kuwa kila kitu kitakuwa rahisi lakini sasa waliona wazi kuwa wanagonga ukuta.

    “Sikilizeni ‘Ni marufuku kwa mtu yeyote kunyang’anywa mali yake kwa dhumuni la kutaifisha au madhumuni mengineyo bila idhini ya sheria ambayo inaweka masharti ya kutoa fidia inayostahili’, sasa ninyi hamjui kuwa mjane huyu ana haki zote za kumiliki mali za mumewe? Ambazo wamechuma wote?.” Bw Kilipa alimaliza maneno yake, huku akivuta gazeti lake la Mfanyakazi, na kuanza kulisoma huku akipiga mluzi. Mzee Malombe na vijana wake walibaki hawana cha kusema.



    Walitazamana kwa muda kama wanaoongea kitu Fulani kwa ishara za macho na kuafikiana kitu.

    “Haya, mi naona swala letu limekuwa gumu sasa, labda uturuhusu twende, tutakuja tena tuyamalize” alisema shemeji wa mama Vituko huku wakinyanyuka vitini tayari kuondoka.

    “Au ninyi mlikuwa mnasemaje maana siwaelewielewi, kuweni wazi tu vijana, ee Mzee Malombe, kuweni wazi” Hakimu, Bw Kilipa aliwasihi.

    Wageni wale walinyanyuka, wakaaga na kwenda zao. Bwana Kilipa baada ya kuwasindikiza mpaka nje alirudi ndani na kuketi kwenye kiti chake kilekile akiendelea kusoma gazeti lake la Mfanyakazi ambalo hutoka kila jumamosi.

    Alimwita mmoja wa wtoto wake wa kike na kumwambia arekebishe vitambaa katika viti vilivyokaliwa na wageni wale, ndipo binti yule alipokuta bahasha ya kaki kitini, aliichukua na kumkabidhi baba yake. Bwana Kilipa akaifungua ndani, hakuamini alichokikuta, noti nyekundu takribani thelathini zilizojipanga vyema zilionekana kwa macho ya kawaida.

    “Ha ha ha ha ha ha” alicheka huku akiruhusu tumbo lake kuchezacheza kwa furaha, ‘Haya ndiyo mambo, sio mnakuja mikono mitupu, mkono mtupu haulambwi jamani’ alijisemea moyoni, akanyanyuka kuuelekea mlango wa chumbani kwake huku akipiga mluzi na mkononi akining’iniza bahasha ile.



    Macho ya Mancatcher, yaliendelea kuwa juu ya simu ile kubwa, lakini alichelewa kuibeba kutokana na utamu wa mazungumzo ya watu wale pale sebuleni, alifuatilia kwa makini kila lililozungumzwa na walipoondoka hakuchelewa kutimiza adhma yake. Kwa kutumia fimbo yake ndefu yenye kimfuko kwa mbele alijibebe simu ile bila jasho na kutoweka nayo, ‘ndiyo maana wananiita Mancatcher’

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Yule hana lolote!” Mzee malombe aliweleza vijana wake

    “Babu, penye uzia penyeza rupia, kwisha habari yake yule, akiiona ile bahasha pale atalowa tu. Tungempa mkononi angekataa na angeweza kutugeuzia kibao”, shemeji mdogo wa Mama Vituko aliongezea huku akinyanyua kombe kubwa lililojaa kilevi na kujimiminia mdomoni. Wote wakacheka na kugonga mikono yao kwa furaha. Walijua wazi kuwa kazi haikuwa ngumu mbele ya pesa.

    “Yule mwanamke akishawekwa ndani, na lile shamba la Sekenke tunalipiga bei, mali za kaka yetu hizi. Tuuze pesa tusomeshee watoto wake”.

    Waliendelea kuitisha pombe usiku ule huku wakifurahia ushindi wao, ambao bila shaka walishajua kuwa wameshinda maana waliamini kuwa pesa ndiyo kila kitu.



    ….Mama Minja na shoga yake walishusha pumzi ndefu kila mmoja kwa wakati wake baada ya kijana huyo kumaliza kuweka mambo hadharani. Walitazamana na kubetuliana midomo.

    “Sasa we kijana,” Mama Njiku aliita, “Kesi itasomwa lini tena?” aliuliza.

    “Juma lijalo, walisema jumanne. Mje lakini sijui kama mtafanikiwa kumtoa maana ndugu zake wameshahonga hela kwa hakimu nina uhakika. Na ninyi msije mikono mitupu” Mancatcher alizungumza kwa kujiamini sana.

    “Sawa. Tumekuelewa, tutakuja siku hiyo kamilikamili” Mama Minja alimueleza Mancatcher huku akiiweka vizuri pochi yake tayari kwa safari, kabla hajanyanyuka kutoka katika kibenchi kile Mancatcher alimkatiza.

    “Sikia mama yule Pilato anapenda sana mlungula, kwa hiyo kama mko gado niwaunganishe fasta mfanye mambo siku hiyo ndugu yenu aachiwe”

    “Haina shida Man, yote tutayafanya tukija na tutakutafuta ili tuwe wote.” Mama Minja alitoa noti ya elfu tano na kumpa Mancatcher, kisha yeye na Mama Njiku waliingia garini tayari kuondoka, ndipo kioo upande wa Mama Njiku kilipogongwa na mtu kama abishae hodi. Mama Minja kwa kutumia kitufe Fulani alikishusha kioo kile taratibu mpaka nusu ya dirisha.

    “Samahani akina mama, nimevumilia nimechoka, nimeona kuuliza si ujinga,” alikuwa yule mzee aliyekuwa akimwangalia sana Mama Njiku pale kilabuni.

    “Mimi naitwa Bwana Kilaka, mwalimu mkuu mstahafu wa shule ya Mivinjeni.” Baada ya kujitambulisha hivyo, moja kwa moja Mama Njiku alimtambua mwalimu huyo, alishawahi kuwa mkuu wake wa kazi wakati alipokuwa akianza tu ualimu mara baada ya kumaliza chuo cha ualimu.

    “Shikamoo mwalimu” Mama Njiku alimsabahi huku akishuka garini.

    “Ndiyo mama, habari za siku nyingi”

    “Salama, leo tumewavamia kijijini kwenu” Mama Njiku na yule mzee waliongea mengi kidogo na kukumbushana mambo ya kazi ambayo Mama Njiku alishayasahau kabisa. Mwisho wa mazungumzo aligundua kuwa hata yule mwalimu mstahafu hajui lolote juu ya Mama Njiku kuacha kazi na aliyotendwa na mumewe.

    “Mumeo anaendeleaje lakini?” alimtupia swali ambalo lilimuumiza kiasi Fulani

    “Anaendelea vizuri, nikija juma lijalo tutaongea mengi kwa sasa ngoja niwahi” alimuaga yule mzee huku machozi yakimlengalenga. Aliingia garini na wakaondoka.

    Maswali mawili matatu kutoka kwa mama Minja yalimfanya Mama Njiku kumueleza kisa chote cha mumewe. Mama Njiku alisikiliza kwa makini huku moyoni akijisemea kuwa ‘kumbe wanaume wote ni sawa’.

    € € € €



    Zai aliiona dunia imekuwa ndogo kama yai, akiwa na bilauli yake iliyojaa mziwa mkononi alijikuta anashindwa kabisa kumaliza maziwa hayo. Akitazama mambo yanayomzunguka ambayo yametokea kwa muda usiopungua siku tano alijikuta akili inacanganika na ubongo. Aliwaza kuondoka na kurudi kwao Iringa lakini vipi kuhusu watoto wa watu, Kautipe ambaye yupo polisi na Ashura ambaye hata hajui yuko wapi. Zai aliinamisha kichwa chake na kukilaza juu ya kiganja chake cha mkono wa kulia uliosimama mezani kwa kutumia kiwiko, alishika tama. Siku hizi zote hakuweza kufanya shughuli zake za kujiuza na kubaki kuishi kwa mawazo mengi, hata wateja wake waliokuwa wakitaka huduma za nyumbani alishindwa kuwafanyia hivyo, kila mtu alimshangaa, Zai, mtoto mchangamfu, mcheshi, mwenye maneno kuntu, lakini leo hii mtulivu, mpole, asiye na maneno mengi, alisahau kuchana nywele zake. Alitafakari afanye nini kuinusuru hali hiyo lakini hakupata jibu sahihi. Aliinua bilauli yake na kujimiminia maziwa hayo, mara simu yake ikaanza kuita, ‘nani tena huyo?’ alijiuliza na kuitoa simu mkobani na kuitazama, ‘Mr Dam Dam’ ilijiandika kwenye kioo huku ikiendelea kuita, Zai aliiangaliza simu ile na mara tabasamu pana likajitokeza katikati ya sura yake yenye huzuni.

    “Hallo!” aliita kwa sauti yake ya kazi, ya kumtoa nyoka pangoni.

    “Zai, mtoto mzuri, mrembo, mtamu, mtundu wa kitandani, mmm mama upo?” sauti ya upande wa pili ilimwaga sifa zote zilizostahili na zisizostahili, zinazoonekana na zisizoonekana.

    “Niambie Dam Dam, dume langu la nguvu, linalonipa mapigo ya maana, ndani na nje ya uwanja jamani mi nipo nikuone wapi?” Zai na yeye alijibu kwa mtindo uliofanana na ule.

    “Naomba uje nyumbani leo, nahitaji huduma yako, nimeimiss sana. Nikikumbuka mambo uliyonifanyia wakati ule, kamwe sintokusahau beibi” sauti ya upande wapili iliongea

    “Hamna shida, ila leo siko vizuri sana, lakini ntakuja”

    “Haupo vizuri kivipi? Ndiyo umeingia katika mzunguko?”

    “Hapana, sipo vizuri sana kiutulivu, nina matatizo yananichanganya”

    “Usijali njoo tutayamaliza, chukua tax ntalipa”

    Zai alitoa kijikioo kidogo na kujiangalia, ndipo akagundua hakuchana nywele, akachukua kitana chake na kuziweka vyema, rangi yam domo nayo ikafanya kazi yake, nguo moja nzuri ya rafgiki yake akajitupia mwilini kisha kuiendea tax iliyokuwa imesimama hapo jirani.

    “Magomeni kota. Nyumba namba ishirini na tano” alimuamuru dereva na wote wakatokomea mjini.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Haikuchukua muda tax ilifika mahali panapotakiwa. Zai alilipana kulijongea geti kubwa la nyumba hiyo. Baada ya kubofya kengele mlango ulifunguka wenyewe nae akaingia ndani, hakuwa mgeni na nyumba hiyo ambayo amekwishafika mara kadhaa, moja kwa moja alipitiliza sebuleni na kulakiwa na mwenyeji wake Mr Dam Dam. Wakiwa juu ya kochi kubwa lililo sebuleni hapo makumbatiano hayakuwa haba na mabusu motomoto kabla hawajakokotana chumbani.

    “Darlin, nina shida mwenzio” zai alianza ubembe wake kwa mwanaume huyo

    “Sema, nakusikiliza darling, hakuna shida itakayokuwa ngumu mbele ya pesa.” Zai alimueleza Dam Dam mambo yote juu ya Kautipe kuwekwa ndani kwa kosa la kushukiwa kuwa na biashara ya bangi, lakini kila alipotaka kumjuza kuhusu Ashura roho yake ilisitasita.

    “Ok, nimekuelewa, sasa siku ya kesi wewe utamuwekea dhamana ya shilingi milioni moja, sawa?” Damdam alimueleza Zai huku akimchezea chuchu zake zilizochongoka kama mshale. Zai aliitika kwa kichwa akaona kuwa hapo moja amelimaliza na linalobaki angemshirikisha mwingine kumsaidia.

    “Nashukuru Damdam.” Zai alimshukuru mwanaume huyo na kumkumbatia, bila kusita Damdam naye alimkumbatia Zai kwa bashasha kubwa na mapenzi yao yamuda mfupi kuchukua nafasi yake juu ya kochi hilo kubwa huku wakisindikizwa kwa muziki laini uliotoka kwenye spika kubwa za kisasa ambazo Damdam alizinunua alipokuwa katika moja ya safari zake huko Uchina.



    € € € €

    “Mgonjwa wenu hali yake si nzuri, amepooza mwili, hivyo hana uwezo wa kufanya lolote kwa nguvu zake” Dakta Msola aliwaeleza ndugu wa mzee Njiku, walipokuja kumtazama hospitalini hapo. Sura za huzuni zilitawala nyuso za ndugu hawa walitazamana kwa muda bila kupata chochote cha kuongea.

    “Kwa vyovyote wamemloga” Dada wa Mzee Njiku alianza kubwabwaja kama kawaida yake huku akitoka nje ya chumba cha daktari kilichopo katika wodi hiyo.

    “Hivi wewe kwa nini unapenda kuamini uchawi?” kaka yake alimuuliza kwa hasira.

    “Mimi najua, wamemloga kaka yangu” aliendelea kusisitiza kaui yake

    “Sasa wewe mwema kwako nani?” kakaye aliuliza tena

    “Hamna mwema, wote wachawi tu. Yule mkewe wa kwanza alimloga kulipiza kisasi, na huyu nae mchawi sasa anataka kurithi mali, na hazipati”, aling’aka dada yule huku akirusharusha mikono yake kwa hasira.



    “Jamani ndugu yetu ndiyo huyo, tunamsaidiaje? Maana sasa hana hata pa kuishi” ndugu wa mzee Njiku walikusanyika kuzungumza machache juu ya mgonjwa wao. Kila mtu alikuwa mzito kutoa maamuzi ya nini cha kufanya, nani amchukue kumtunza, kila mmoja alijesemea moyoni ‘nani abebe mzigo huo’. Baada ya mawili matatu kuzungumzwa waliafikiana kumsafirisha nyumbani kijijini.

    Wakiwa katika mazungumzo hayo gari ya mama Minja ilisimama taratibu mbele ya jengo hilo la hospitali, mama Njiku, mke wa ndoa wa mzee Njiku aliteremka na moja kwa moja akamuendea shemeji yake.

    “Asante kwa ujumbe, niliupata ila nilikuwa mbali, namuomba mume wangu niondoke nae, nitamtunza mwenyewe, huyu ni mume wangu” mama Njiku alisema maneno hayo ambayo yalimgusa kila mmoja wao, wakikumbuka walivyomwita mchawi, walivyomfukuza kama mbwa na kumthamini mwanamke mwengine ambaye sasa wameona yaliyompata kaka yao. Kaka wa mzee Njiku alimwita pembeni mama Njiku na kumueleza majibu yote ya daktari bila kumficha. Mama Njiku aliyapokea majibu hayo na moja kwa moja alimuendea daktari kwa mazungumzo ya kina.

    “Licha ya kupooza, mumeo ameathirika na gonjwa la ukimwi, hivyo nizuri hata wewe kufanya vipimo kwa uhakika zaidi”, Mama Njiku hakuonekana kushtuka kwa jambo hilo kwani alilitegemea muda wowote kutokea, alitulia kimya akiwa kajishika tama, mawazo yake yalimrudisha nyuma kabisa enzi za wawili hao wakiwa katika mtafaruku mzito…



    “Sawa, mi ntaondoka ntakuacha, lakini kumbuka maradhi mume wangu, hao unaowathamini leo hujui wangapi walifanywa hivyo” Mama Njiku alikuwa akiongea huku akitoa machozi akimueleza kwa uchungu baada ya kupokea kipigo kikali kutoka kwa mumewe…



    *************





    …aligutuka aliposikia mlio wa chupa ya dawa iliyoanguka kwa bahati mbaya na kupasuka. Mama Njiku alikubali kufanya vipimo ili kuhakikisha afya yake, baada ya majibu kutoka aligundulika hakuwa na maambukizi. Alinyanyuka kutoka katika meza ile na kuingia wodini kumuona mumewe. Aliketi pembeni kabisa ya Mzee Njiku walitazamana uso kwa uso, machozi yaliwalenga wote wawili kila mmoja alijikuta ana haki ya kumsamehe mwingine. Mzee Njiku hakuwa na uwezo hata wa kuongea kutokana na hali yake, moyoni alitamani atamke japo neon moja la msamaha kwa mkewe lakini haikuwa hivyo, aliongea ndani ya moyo wake



    Nisamehe mke wangu

    Yote ni makosa yangu

    Ulifungwa moyo wangu

    Sikujua nifanyalo



    Niombee kwa wanangu

    Sahau kauli zangu

    ‘mefika safari yangu

    Ya kuuacha ulimwengu



    Enyi waume wenzangu

    Jifunzeni toka kwangu

    Niliivunja nyumba yangu

    Mapenzi yalihadaa

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Jihadhari na rafiki

    Wengi wao wanafiki

    Wabilah tawfiq

    Watakupoteza hakika



    Moyo wangu waniuma

    Kwa niloyafanya nyuma

    Sina mbele wala nyuma

    Kitandani naishia



    Ninatubu kwa Mungu

    Na kwako mke wangu

    Ndugu na watoto wangu

    Goti ninawapigia



    Mama Njiku alizidi kulia huku akiwa ameushika mkono wa mume wake ambaye sasa hakuweza kufanya lolote, Mama Njiku aliyahisi maneno hayo kutoka kwenye macho ya mumewe, aliuhisi msamaha wa nguvu na maneno mazito yaliyougusa moyo wake. Alipiga magoti sakafuni na kumtazama mumewe aliye kufani kwa ukaribu zaidi, kinywa chake kilifunguka akasema



    Laazizi mume wangu

    U mweupe moyo wangu

    Hakuna kinyongo kwangu

    Mimi nimekusamehe



    Dunia yetu mapito

    Mambo mpwitompwito

    Hilo nalo ni pito

    Mimi nimekusamehe



    Marefu pa si na ncha

    Hamna kutwa kwa kucha

    Maadam kumekucha

    Mimi nimekusamehe



    Najua unaumia

    Kwa yote yalotukia

    Ni njia ya kupitia

    Mimi nimekusamehe



    Siku zote nilijua

    Kuwa kwangu utarudia

    Mimi ni mke wandoa

    Wengine viruka njia



    Mateso nilipitia

    Gerezani kuingia

    Maisha kunichachia

    Kila kitu kupoteza



    Yote tumuachie Mungu

    Muumba nchi na mbingu

    Toka kwako na kwangu

    Maombi tumtolee



    Nakupenda mume wangu

    Kuliko wazazi wangu

    Narudisha moyo wangu

    Kwako laaziz wangu.



    Mama Njiku aliuinua mkono wa mumewe na kuubusu kisha kuukumbatia na kulia kwa machozi ya upendo. Masikini, mzee Njiku, muda wake ulikuwa umefika tamati, macho yake yalishindana na kiza kinene lakini nuru ilizidi kufifia kwa haraka, alihisi mabadiliko ya maisha yakiivamia roho yake, mara tu, roho yake ikaacha mwili, macho yakafumba akapumzika kwa amani.

    Mama Njiku alibubujikwa na machozi, alilia kwa uchungu, alitamani mumewe arudi wamalizie maisha lakini haikuwa hivyo, mauti yalikwishamfika.



    € € € €



    Kautipe alitulia kimya katika chumba cha mahabusu pale mahakama ya mwanzo ya Chang’ombe. Alijua wazi kuwa mwisho wake umefika kwa kosa lisilomhusu, atafungwa pasipo kutarajia.

    Jalada lake lilifika, kizimbani akasimama pamoja na Rasta, mahakama ikaendelea hakukuwa na utetezi, hakimu alipoitisha dhamana kama ipo, Kautipe hakuamini macho yake. Zai alijitokeza na kumuwekea dhamana Kautipe. Mambo yote ya kimahakama yalipomalizika Kautipe na Zai walitoka mahakamani na kuketi kwenye grosary moja iliyopo katika eneo hilo, waliagiza vinywaji na kunywa taratibu.

    “Pole mdogo wangu!” Zai alianzisha mazungumzo

    “Asante da Zai, mi nimekamatwa bure tu” Kautipe aliongea huku analia

    “Basi yataisha tu maadamu upo nje, tutafanya kinachowezekana” Zai alimfaraiji mwenzake.

    “Nitashukuru, mi naogopa” Kautipe aliendelea kulia

    “Usiogope we tulia tu”.

    Punde si punde gari moja nyeusi salon ilisimama eneo hilo, kioo cha mbele upande wa kulia kiliteremka taratibu, hakuwa mwingine bali Mr Damdam. Zai alijiinua na Kautipe wote wakaingia garini.

    Msichana mmoja alievalia baibui alikuwa akifuatilia nyendo zote za Zai na Kautipe kila hatua mapka walipoingia garini humo, mara tu walipoondoka na ye alichuku tax kuwafuata.

    “Fuata hiyo gari mpaka itapoishia” alimuamuru dereva, na dereva alitii amri ya mteja wake.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya kuendesha kwa muda Fulani waliiona ile gari ikiingia katika jumba Fulani eneo la Magomeni.

    “Sasa, unashuka au?” dereva aliuliza

    “Hapana nilitaka nijue tu wameenda wapi” kautipe alijibu. Wakasogea mbele kidogo, akamlipa dereva tax na yeye akachukua kiti katika duka moja la jirani hapo ili aone kitachoendelea, ‘Zai si mtu mzuri hata kidogo’ alijiwazia huku taratibu akinywa juice yake ya embe, ‘yaani alinidanganya mi nimepata kazi kumbe ananiuza kwa mwanaume, huu sio ubinadamu, nitalipiza kisasi tu. Sijui kama Kautipe atapona humo ndani’ , aliendelea kuwaza na kuwazua.



    Damdam alimwangalia Kautipe kwa jicho la huba, alivutiwa na miguu yake minene yenye afya, kiuno cha wastani kilichotulia vizuri juu matako yake ya kubinuka kidogo.

    “Zai, tuongee kidogo” Damdam alimwita Zai pembeni wakati Kautipe akiwa anaelekea katika chumba alichooneshwa.

    “Huyu ni nani kwako?”

    “Ni jirani tu huko kijijini. Alikuja kutafuta maisha yeye na mwenzake sasa ndiyo hivyo”

    “Mwenzake yuko wapi?”

    “Kwa sasa sijui maana, alitoweka ana kama wiki sasa.”

    “Sasa sikiliza Zai, mi nimekusaidia kumwekea dhamana huyo mdogo wako, unafikiri malipo gani yananistahili kwa wema wangu?” Damdam alimtega Zai kwa swali.

    Zai alikuna kichwa, alielewa Damdam anazungumza nini lakini alishindwa kujua yeye amjibu nini, alifikiri kwa muda akajikuta ndani ya mtego finyu wa panya.

    “Damdam, we unataka nini?, kama penzi nimekupa, na ukitaka tena ntakupa, zaidi ya hapo sina” Zai alijieleza huku akirembua macho yake ya mviringo.

    “Sawa kabisa, lakini unaonaje ukiniachia mdogo wako huyu, japo kwa siku tatu?” Damdam aliwasilisha ombi huku akiinua kinywaji chake na kutia kinywani.

    “Mmmm aaaaannhh ok, we utakavyo. Sasa mi utaniachaje?” Zai alijibu na kuuliza

    “Usijali mi na wewe. Kamwambie mdogo wako hali yote ilivyokuwa halafu njoo mi na wewe tumalizane” Damdam alishangilia moyoni, maana alijua kuwa ombi hilo lingekuwa na upinzani sana kwa Zai kwa kuwa Zai alikuwa mpenzi wake wa muda wa kustarehe nae kwa malipo na wakati mwingine hata kwa mkopo.

    Zai aliinuka kutoka kitini na kuvuta hatua fupifupi kuelekea kwenye chumba ambacho Kautipe alikuwa ameingia japo apate maji ya kuoga. Zai aliingia kimyakimya kwakuwa alikuta mlango huo ukiwa umeegeshwa tu, alijiegemeza ukutani akilisanifisha umbo zuri la Kautipe, macho yake yalitua katika kiuno cha kautipe ‘msichana mzuri, nahisi atanipindua’, Zai aliumia sana moyoni lakini afanyeje.

    “Kau,” aliita. Kautipe alishtuka na kuyaficha matiti yake kwa taulo maana alikuwa bado anajifuta maji na hakuwa na nguo yoyote mwilini mwake.

    “Umenishtua da Zai”

    “Usijali,” alivuta hatua chache kuelekea Kautipe alipo “Sikia mdogo wangu, huyu kaka anaitwa Damdam, ana roho nzuri sana sana sana, nilipomsimulia juu ya ishu yako, yeye ndiye akakuwekea dhamana kwa jina langu. Sasa unajua kanipa ushauri mmoja, anasema kwa kuwa wewe bado una kesi, si vizuri kurudi kule Tandika, rafiki wa Rasta wanaweza kukudhuru.” Zai alimeza funda la mate na kuendelea “Ameshauri ubaki hapa kwa siku kadhaa. Mi nimekubaliana naye nimeona ni wazo zuri, mdogo wangu kaa hapa kidogo, halafu utafaidi we acha tu” Zai alimalizia huku akitweta kwa wivu. Aligeuka mara moja na kuuelekea mlango ambao ulimsubiri apite.

    Kautipe aliketi kitandani huku akiwa kapigwa na butwaa, alijiwazia kubaki hapo siku kadhaa, kwake haikuingia sana akilini lakini pia alifurahi maana alikuwa akifikiri jinsi atakavyokuwa ndani ya jumba hilo la kifahari, lenye kila kitu ndani, kumbe hakujua nini kimejificha nyuma ya habari hiyo.

    Kwa hatua za hesabu Zai aliifikia sebule, akachukua kipimajoto chake na mtandio.

    “Vipi, waondoka?” Damdam aliuliza

    “Yap, sasa nikae nifanye nini, si ushapata mwingine” Zai alijisemesha huku akijiweka tayari kuondoka. Damdam alimuwahi na kumshika mikono.

    “Kwani vipi mpenzi? Mbona hivyo, kama ulikuwa hutaki si ungesema palepale” damdam alibembeleza

    “Hapana, malizana na huyo kwanza halafu ukimchoka nitafute” Zai aliongea huku akitoka nje ya nyumba hiyo. Damdam aliingiza mkono mfukoni na kutoa noti za elfu kumikumi kama sita hivi na kumpatia Zai.

    “Chukua hii mpenzi, ila tuonane kijiwe kesho mchana”

    Zai alipokea zile pesa na kuzifutika kwenye sidiria yake, kisha akiwa na sura yenye tabasamu aliingia kwenye tax iliyokuwa tayari imekuja kumchukua na kutokomea.



    Ashura alishusha bilauri yake iliyokuwa tupu, alimuona Zai akiondoka na tax ile. Haraka haraka alijua kinachoendelea, maana alijua kuwa lazima Kautipe kabaki na lile janaume. ‘Mwanamke shetani huyu! Keshamuuza Kau kwa Mwanaume’ alijiwazia huku hasira zikimtawala. Ashura alifikiria jinsi ya kumpata Kautipe na lengo lake akimpata tu shoga yake huyo basi wapange mpango wa kulipiza kisasi kwa Zai kwa yale aliyomfanyia ambayo sasa anayaona akimfanyia tena Kautipe, ‘dawa yake ipo’, aliinuka na kuondoka zake. Ashura alikuwa akiishi kama digidigi, hata aina mivao yake ilikuwa ya kujificha sana, muda wote alishinda na baibui akihofia asije akajulikana endapo alikuwa anatafutwa.



    € € € €



    Mjane Mama Njiku alikuwa kajiinamia akitafakari hili na lile, akiwaza na kuwazua lakini iionekana wazi kuwa hakupata jibu. Aliwaangalia watoto wake wawili na wale a mama Vituko ambao sasa wote walikuwa pale, kwake ilikuwa ni kudondosha chozi kila mara alimkumbuka sana mumewe japokuwa walikuwa wametengana ‘amekufa mapema’, alijiwazia huku akiangalia picha zake za siku ya harusi yao zilivyomkumbusha mambo mengi. Siku hiyo hakwenda kufungua mgahawa wake, alikuwa bado akiomboleza. Hata akiwa pale nyumbani kwake wateja na marafiki zake wengi walikuja kumpa pole na rambirambi pamoja nao.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Maumivu ya moyo wake yalisababishwa tu na mali alizochuma na mumewe ambazo sasa zipo mikononi mwa wengine, nyumba yao ambayo kwa asilimia kubwa ilijingwa kwa mshahara wa Mama Njiku iliuzwa na mumewe kwa ushawishi wa nyumba ndogo, mashamba na mifugo vyote viliteketezwa kwa mtindo huohuo, Mama Njiku alipoka kutumikia kifungo chake alikuta kila kitu si chao tena na hapo ndipo alipokuja mjini kuanza maisha mapya, kutoka ualimu mpaka ufagiaji barabara na sasa mama ntilie.

    Daima alikumbuka maneno ya Mama Minja ‘usiumize moyo, endelea ulipofikia’, maneno haya yalimpa faraja sana Mama Njiku na kujipa moyo wa kusonga mbele kimaisha. Alijua kuwa hakuna cha kurithi katika yote kwani nyumba ndogo ilishapiga bao kila kitu, labda kilichobaki ni mirathi tu ambayo nayo hakuwa na uhakika nayo kama ataipata au la.



    ************



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog