Search This Blog

Sunday, 22 May 2022

ISABEL NDANI YA MPANGO HASI - 4

 







    Simulizi : Isabel Ndani Ya Mpango Hasi

    Sehemu Ya Nne (4)



    Isabel aliamka kutoka katika usingizi mzito uliojalizwa ndoto mbaya na nzuri. Macho yake yalijaribu kupambana na nuru ya taa kubwa nyeupe iliyokuwa kiwaka juu tu ya uso wake, alifumbafumba macho na kujaribu kujikinga kwa mikono yake.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Muuguzi wa zamu alifika moja kwa moja na kufungua pazia lile la plastiki na kuingia ndani, kwanza alizimisha lile taa na kumuacha kwa muda. Baada ya dakika kadhaa alimsaidia kukaa vizuri, Isabel alikuwa akijishika ubavuni mwake mara kwa mara kutokana na mvunjiko wa mbavu zake kadhaa. Alijaribu kujinyanyua lakini ilikuwa ni ngumu sana kwake.

    “Endelea kupumzika Isabel” muuguzi alimueleza kwa sauti ya upole kabisa. “Samahani, nesi, nipo wapi?” Isabel aliuliza kwa tabu kidogo

    “Hapa ni Hospitali ya Muhimbili” Nesi alimjibu

    “Muhimbili! Nimefikaje hapa na lini?” Isabel alizidi kuchanganyikiwa na kumtupia maswali muuguzi yule.

    “Uliletwa hapa wiki mbili zilizopita, ulipata matatizo ulipokuwa safarini kwa treni” Muuguzi alijibu



    huku akiwa ameketi katika kitanda kilekile alicholalia Isabel. Isabel aliposikia juu ya treni picha ilirudi na kumbukumbu zikaanza kujirejesha ubongoni taratibu.

    “Mandi!” alianza kujisemea taratibu huku aking’ata kidole kimoja cha mkono wake. Mara nyingi alitamka jina hilo ‘Mandi’.

    “Njaa!” alimwambia Muuguzi. Mara tu uji uliletwa na akaanza kuubugia kwa fujo sana. Baada ya kuufakamia uji ule kwa fujo, hali yake ya tumbo haikuwa nzuri alisikia kichefuchefu cha hali ya juu, aliomba msaada ka muuguzi na moja kwa moja aliongozwa maliwato.

    Kitu kidogo cheusi kilionekana katika matapishi ya Isabel, alikitazama kwa makini hakujua mara moja ni kitu gani, baada ya kuvuta kumbukumbu ndipo akakumbuka ile memory card aliyoimeza kule kwenye treni ‘Nilijua washaichukua!’ aliipekua na kuisafisha bombani kisha akaihifadhi vizuri.



    Kamanda Amata aliingia katika wodi aliyolazwa Isabel kwa kificho, kwa kuwa alishaambiwa asijihusishe na lolote katika sakata hilo; awaachie polisi, lakini alijiapiza moyoni kuwa ni lazima ahakikishe anapata maelezo yote kutoka kwa Isabel kabla hajayatoa kwa mtu mwingine. Mara ya mwisho kuja hapo alimuaomba muuguzi kuwa endapo Isabel ataamka tu basi amjulishe mara moja kabla ya mtu mwingine, na ndivyo ilivyokuwa. Akiwa ndani ya kanzu na barakhashea, miguuni kajitupia makubanzi aliingia bila tabu katika wodi hiyo akiwapita polisi waliopo zamu, maana kila aliyeingia katika wodi hiyo ilipaswa kufanyiwa upekuzi wa kina.

    “Dakika tano tu tafadhali” WP aliyekuwa jirani ya kitanda cha Isabel alimueleza Amata, ambaye aliingia hapo kama mmoja wa ndugu. Alisimama kando ya kitanda na kumtazama Isabel, Isabel alimtazama Amata lakini hakumtambua kabisa ukizingatia hawajawahi kuonana hata siku moja, walibaki wakitazamana, Amata alitabasamu, hakuweza kuongea chochote kwani yule WP alikuwa pale, na Amata hakupenda mtu yeyote ajue juu ya mazungumzo yao.

    “Hujambo Isabel?” alimsabahi huku akimuinamia pale kitandani “Sijambo, shikamoo,”

    “Marhaba, wajisikiaje sasa?”

    “Mungu anasaidia nimeamka. Mbona mi sikufahamu, we ni nani?”

    “Huwezi kufahamu wote wanaokuja kukuona. Ila mi ni mgeni uliyemtegemea sana kuonana nae japokuwa humjui hata kwa sura” Amata alimueleza Isabel, lakini ilikuwa ngumu kwake kujitambulisha kwa uwazi kwa kuwa yule WP angeweza kusikia kwa ukaribu na picha ingeungua. Lakini Amata alipenda kusikia juu ya tukio lile kutoka kwa Isabel, hakujua mbinu gani atumie katika kulifanikisha, aliumiza kichwa kwa kuwa alijua wazi kuwa asipopata habari hiyo muda huo basi polisi wakija wataondoka na Isabel ili akapate hifadhi na kwa mahojiano.

    Mungu si Athumani, yule WP alinyanyuka na kuelekea ofisini kwa wauguzi, ni muda huo mfupi ulitosha kwa Amata kutekeleza azma yake. Aliingiza mkono ndani ya kanzu yake na kutoa kitambulisho kidogo ambacho daima huwa hakioneshi hovyo kutokana na unyeti wa kazi yake, akanong’ona.

    “Mimi Amata, nilitaka kuongea na wewe lakini naona haiwezekani. Nitashindwa kukusaidia Isabel” alirudisha kile kitambulisho mahali pake kwa haraka. Isabel alishasoma kwa haraka na kuwa na uhakika juu ya mtu huyo. Isabel alitikisa kichwa kuashiria kuwa alimuamini.

    “Niitie nesi tafadhali!” Isabel alimuomba Amata, na Amata akafanya hivyo haraka, nesi alifika pale pamoja na yule WP.

    “Nini Isabel?” nesi aliuliza “Najisikia kutapika.”

    Yule nesi alimshika mkono Isabel na kumsindikiza maliwato, kwa kuwa Isabel alikuwa hana nguvu za kutosha kutembea mwenyewe, WP alikuwa nyuma yao kuhakikisha usalama wa binti huyo.

    Baada ya muda kidogo alikuwa akirudishwa kitandani na kabla hajakifikia kitandani alisimama na kujishikia kwenye nguzo iliyo katikati ya wodi hiyo, akihema kwa shida huku kajishika mbavu zake.

    “Kaka, tunaomba utusaidie kidogo” WP alimwita Amata kutoa msaada wa kumfikisha Isabel kitandani. Amata alinyanyuka na kwenda kutoa msaada, alitaka amnyanyue Isabel, lakini Isabel alikataa akampa mkono amshike, na hapo ndipo Amata alipogundua hila ya Isabel. Kamanda Amata



    alihisi kama kitu kidogo kigumu kikikandamiza kiganja chake kutoka kile cha Isabel, alimsaidia Isabel kutembea mpaka kitandani na ye kubakia na kile kitu mkononi mwake.

    Akiwa kitandani Isabel, alimwangalia kijana huyu na kutoa tabasamu pana.

    “Naomba nipumzike, sitaki kuongea na mtu” Isabel alimueleza muuguzi, na Amata aliombwa kutoka nje ya wodi ile maalum.



    Kwa hatua za haraka haraka Amata aliiendea gari yake Toyota Altezza na kujitoma ndani. Memory card ndogo ilikuwa kiganjani mwake, aliitazama na kuigeuzageuza kisha akaihifadhi vizuri katika wallet yake, na kuondoka kuelekea nyumbani kwake moja kwa moja, ili kwanza akajue nini kilichomo ndani ya card ile.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Ton aliketi kwenye moja ya viti vilivyopo chumbani kwake, akisubiri maelekezo mengine kutoka kwa asiyemjua. Mara kwa mara aliangalia saa yake na kuona muda ulivyokuwa ukikimbia alinyanyuka na kuangalia dirishani lakini hakuna aliyemuona kuja wala kumjua aliketi na kuwasha televisheni ndogo chumbani hapo. Mara simu iliita aliinyakuwa na kubofya kidude cha kusikilizia. “Halo” aliita

    “Ok nakuja” aliijibu hiyo sauti ya upande wa pili, akaliendea kabati na kufungua, aktupa jicho lake hapa na pale na kuivuta bastola yake anayoiamini aina ya Winchester 73, akaitia kotini na kufunga mlango nyuma yake, alishuka taratibu ngazi za jingo hilo na kutokea barabarani moja kwa moja akaiende marcedec benz nyeusi iliyokuwa imesimama eneo hilo.

    Ton alikutana na watu wawili asiyowajua garini mle aliwaangalia kwa hadhari kubwa, aliyekuwa nyuma ya usukani akageuka.

    “Ton Ton, kutana na meno ya Mamba” alimueleza Ton huku akimuoneshea kijana mwingine aliyeketi kushoto kwake “ na Anaconda” alimalizia kwa kumuonesha mtu wa kiti cha nyuma. Ton alitikisa kichwa kuonesha amekubaliana nao, akawapa mikono.

    “Swahiba huyu ni Ton, mtakuwa naye katika ile opereshen, mnatakiwa muifanye kwa umakini na haraka iwezekanavyo,mambo mawili tu apatikane mzima au ikishindikana auawe” alimaliza kauli yake na kuondoa gari, Ton aliitoa bastola yake na kuiweka tayari kwa kazi na wenzake walifanya vivyo hivyo. Gari ile kwa mwendo wa kawaida ilipita mtaa wa Swahili na kuelekea taa za faya kabla ya kupita njia panda hiyo kuchukua barabara ya Umoja wa mataifa mpaka Muhimbili. “Yupo wodi maalum, ndani ya chumba hicho ni yeye, muuguzi na msaidizi mmoja,” sauti nyembamba ya kike ilisikika katika kidubwasha maalum ndani ya gari hiyo, ikatulia kidogo kisha

    ikaendelea “nje mlangoni kuna polisi wawili wenye bunduki, muwe makini sana wasilete matatizo, muda mzuri ni jioni ya saa moja mimi nitakuwa nimetoka zamu ataingia mwingine” kisha sauti ile ilikatika.

    “Mmesikia vijana?” yule dereva aliwauliza, wote wakaitikia kwa vichwa kukubali. Yule dereva aliinua mkono wake kuangalia saa ilikuwa saa kumi na mbili jioni, walipopaki gari katika maegesho ya wageni, Ton na wale wawili wakashuka na ile gari ikaondoka.

    “Mmoja ataingia kwa muuguzi kwanza wakati wawili watasubiri nje, kisha ataingia mtekaji baadaye wa mwisho atakuwa makini na askari, tutatofautisha dakika mbili kwa mtu wa kwanza na wa pili, halafu sekunde thelathini kwa mtu wa pili na wa tatu” Ton alitoa maelekezo kwa wenzake na kuonekana wako pamoja kisha wakatawanyika na kukubaliana kuanza kazi baada ya kupeana signal Fulani.





    “Surprise!” Amata alimwambia Madam S

    “Surprise ya nini?” madam S alimjibu huku akifunga faili alilokuwa akilipitia. “Nilishakwambia Kamanda, ukiwa unakuja ofisini kwangu uwe unanipa taarifa” Madam S alimueleza Amata huku akimnyooshea Amata kalamu aliyoishika mkononi.

    “Hapana, nimekuja tu kwa dharula, lakini kuna jambo zito sana nataka tuliongee, tukichelewa itakuwa balaa” Amata alimueleza madam S huku akivuta kiti na kuketi, kisha akaendelea “Kuna



    mpango mchafu, mpango hasi, kutoka nchi jirani kwa ajili yetu”, Madam S aliduwaa kumsikiliza Amata.

    “Unasema nini kamanda!?” aliuliza kwa mshangao

    “Watu wanataka kufanya mapinduzi, kama ilivyotokea huko nchi za jirani mwaka 1994 ndiyo mpango uliopo unaosukwa na haohao kwa ajili ya Tanzania” Amata alinyamaza na kumwangalia Madam S usoni.

    “Mh! Mbona unanitisha na hizo habari, we umepata wapi?” madam S alimtupia swali Amata. “Isabel” alimjibu

    “Isabel?” madam S aliuliza kwa sauti

    “Ndiyo, Isabel kanipa taarifa hii” Madam S aliposikia taarifa hiyo alinyanyuka kitini na kuiacha meza yake kisha akampa ishara Amata ya kumfuata. Walitoka nje na kuingia kwenye gari na kuondoka eneo hilo. Breki ilikuwa katika uwanja wa shule ya msingi ya jirani, wakashuka. “Umenileta huku kufanya nini?” Amata alimuuliza Madam S

    “nataka kukunulia karanga za kukaanga, hupendi?” alimjibu na kumuuliza. “Ha ha ha ha!” Amata alicheka kwa jibu hilo.

    Wakiwa wamesimama katikati ya uwanja wa shule kamanda Amata na Madam S waliabadilishana mawazo.

    “Nafikiri hapa ni sehemu salama zaidi kwa maongezi” Madam S alimueleza Amata “Ndiyo.”

    “Ok, niambiye hiyo habari na mpango wenyewe ulivyo”

    “Kuna kikundi cha watu wachache wanaoongoza mapinduzi katika Africa, na nchi zinazoendelea, na ndiyo hao waliotekeleza mapinduzi na mauaji ya kimbali katika Rwanda na Burundi, sasa wamesuka mpango huohuo kwa ajili ya Tanzania” alijikohoza kidogo na kuendelea “Sasa kabla ya kutekeleza mpango huo kuna mambo ya kuandaa mazingira, Madam hivi tunavyoongea kuna watu wameshaingia nchini na si mmoja ni kikundi kutekeleza kazi hiyo”.

    “Amata!” madam S aliita, akamshika bega Amata, “Isabel, anahusika.” “Hapana, sina uhakika kama anahusika.” Amata alimjibu Madam S

    “Yeye amejuaje yote haya? Hata akueleze wewe, na wewe mmeongea saa ngapi? Maana ulishaambiwa usijiingize katika sakata la Isabel”

    “Swali zuri Madam, nilikwenda kumtembelea jana jioni…” “Hawakukuona?” madam S alimkatisha

    “Hakuna aliyeniona, nilikwenda kikazi” Amata alijibu, madam S akacheka kidogo “Mbona unacheka?” Amata alimuuliza

    “Umenikumbusha siku ulipojifanya wewe ni padri ukavaa kanzu na stola tulipokuwa Nairobi kwenye lile sakata la ‘mauaji ya kasisi’” Amata alirudisha kicheko.

    “Nakusikiliza” Madam S akaendelea

    “Sasa nilipokuwa pale nilimuonesha kitambulisho changu Isabel, akanifahamu na akafanya ujanja Fulani akanipatia memory card bila mtu kujua, ndani ya memory card hiyo ndiyo kuna huo mpango wa mapinduzi, Mpango Hasi wameuita hivyo”, Amata akashusha pumzi kidogo na kuendelea, “Madam utakelezaji wake umeanza, kaa tayari, kifo kinachokuja ni cha kwako baada ya kile cha IGP na DCI”, alimaliza. Madam S alibaki mdomo wazi.

    “Amata, una hiyo memory hapo?”

    “Yes, Madam” Amata akatoa kijifuko kidogo cha plastiki na kumkabidhi Madam S.

    “Twende” madam alimuamuru Amata na wote wakarudi garini. Ndani ya gari madam S alifungua kijikompyuta kidogo kilichotengenezwa maalum katika dashboard ya gari hiyo, akatumbukiza memory ile na ikaanza kusoma.

    Baada ya kumaliza kuisoma, Madam S alishusha pumzi nzito na kujiweka vizuri kitini, hakuamini anachokisoma mbele yake, machozi machanga yalianza kumtoka, kwa kitambaa chake akajifuta. “Madam,” kamanda Amata aliitaCHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kamanda” Madam aliitikia, akatikisa kichwa na kuendelea “Asante Kamanda, kwa kunijulisha kifo changu, tatizo sijui watanitafutia wapi, na sijui adui yangu ni nani. Ningekufa kama kuku mwenye kideli, lakini sasa nitakufa kishujaa, ama zao ama zangu” Madam alimaliza kusema kwa



    masikitiko, akaitoa memory ile na kuirudisha katika kile kiplastiki.

    “Isabel, akachukuliwe jioni hii awekwe hospitali ya jeshi kwa mahojiano” Madam alimwambia Amata, “Na hapo yeye atatueleza kila kitu, kisha tutajua tunaanzia wapi. Sasa twende kwa waziri mwenye dhamana”, alimalizia. Kamanda Amata alikaa nyuma ya usukani wa gari ya Madam S, alipotaka kuwasha gari ile, Madam S akamshika mkono Amata.

    “Nakupenda Amata, nakupenda sana”

    “Oya, pancha hiyo!!!” kijana wa pembeni barabarani hapo aliwatahadharisha kwa ukelele. Amata na Madam S walishuka na kuangalia kweli tairi lilikuwa flat, wakatafuta uwezekano wa kulirekebisha ili waendelee na safari. Vijana walichangamkia tenda haraka haraka, lo! Mlipuko mkubwa ulitokea, gari ya Madam S ilipaishwa juu huku ikiwaka moto, hali ilikuwa ya taharuki eneo lote hilo, watu walikimbia huku na huku vilio vilisikika kila kona. Madam S alichanganyikiwa, alitaka kukimbilia kwenye gari lakini Amata alimshika na kumzuia alimvuta pembeni palipokuwa na tax na kumuingiza katika moja ya tax hizo.



    “Shit!” madam S alitamka kwa hasira, “Walitaka wanimalize namna hii, saa ngapi wameweka bomu kwenye gari yangu, saa ngapi? Nani kafanya hivi, ntamtia mkononi tu.” Madam S alishikwa na hasira kali iliyoshindwa kujificha, Amata alijaribu kumpoza kidogo.

    “Madam, tulia Madam, tuendelee na ratiba yetu kama ilivyo maadam tumepona maana kwenye orodha si umeona hata mimi nipo, wangefurahi kutumaliza pamoja” Amata alizungumza hayo huku akitoka na Madam S. Moja kwa moja safari iliishia kwa katika ofisi ya waziri wa ulinzi na jeshi la kujenga taifa. Madam S alioneka kuchanganyikiwa kabisa.

    “Vipi mbona ghafla hivyo?” aliuliza Mheshimiwa.

    “Tumenusurika kifo mheshimiwa,” Amata alimueleza waziri wa ulinzi kila kitu kama kilivyokuwa. Baada ya habari hiyo, mheshimiwa waziri alionekana kuchanganyikiwa kidogo, alitikisa kichwa chake na kumeza funda la mate.

    “Hali imekuwa mbaya, tukicheza tutakufa wote huku tunajiona. Hatua za haraka inabidi zichukuliwe, na hii memory ifike kwa Mheshimiwa Rais haraka iwezekanavyo, hakuna jinsi.”



    Waziri wa ulinzi aliitisha kikao cha dharula ofisini kwake cha wakuu wote wa vyombo vya ulinzi na usalama mchana huo. Punde tu wote walifika, Amata aliondoka kupisha kikao hicho na kurejea ofisini kwake ambako alimkuta Gina anasoma gazeti la alasiri ya siku hiyo. Amata aliingia na kuketi juu ya kiti chake, akamtazama Gina na kutikisa kichwa.

    “Tungekuwa tumekufa mimi na Madam S leo”

    “Kwa nini?” Gina aliuliza huku akimpa juice kwenye bilauri. Amata alimueleza Gina tukio hilo, Gina alionekana kuchoka kwa habari hiyo.

    “Gina, sina la kufanya hapa lazima niingie kazini bila ruhusa” Amata alimueleza Gina huku akivuta kitabu chake cha kumbukumbu na kupekua kurasa kadhaa, na kuandika vitu Fulani.

    “Gina, nashindwa nianzie wapi, naomba hata wewe uwe makini na usitembee kizembe kama kawaida yako, hakikisha muda wote unakuwa na mawasiliano na mimi ili kujua nilipo na ulipo, kimenuka mama” alipokuwa akimaliza maneno hayo, saa yake ilimfinya mkono kuashiri kuna ujumbe uliokuwa ukiingia, aliinua mkono na kubonyeza namba Fulani mara mkanda maalum ukawa unatoka ndani ya saa hiyo ukiwa na maadishi ‘tukutane shamba haraka iwezekanavyo mama anataka msaada Tena Sana Aisee’ mkanda ule uliishia hapo na kukatika, Amata alijiweka tayari. “Gina natoka, signal yetu iwe ileile, sawa?”

    “Yes Sir!” Gina alijibu kwa utani kama kawaida yake. Amata alitoka na kuelekea shamba.



    **********

    Gari ya wagonjwa ya Jeshi kutoka hospitali ya Lugalo ilifunga breki mbele ya wodi ya mifupa



    (MOI), vijana wawili waliovalia kombati za jeshi na msichana mmoja waliteremka na kuielekea wodi hiyo, jambo la kushtua! Polisi aliyekuwa lindo alionekana kwenye kiti chake akiwa hana uhai, yule kijana wa jeshi alimtazama yule polisi mwenye bunduki mkononi, kisha akapitiliza ndani akifuatiwa na mwenzake walipoingia ndani walimkuta muuguzi akiwa chali juu ya meza yake, tundu la risasi lilionekana wazi kifuani mwake. Chumba hakikuwa na mtu, walitazamana hawakujua la kufanya walitoka ndani ya chumba hicho kwa kasi na kuripoti haraka kambini, Isabel ametekwa.

    Haraka gari za polisi zilifika eneo hilo lakini habari hazikubadilika, Isabel alikuwa ametekwa. Inspekta Simbeye alijishika kiuno, hakujua nini la kufanya, aliusogelea ule mwili wa yule askari na kuuangalia kwa makini, kisha akaingia ndani ambako vijana wake walikuwa wakifanya mambo mbalimbali ya kiusalama.

    “Ina maana we hukuona yeyote aliyekuja?” Inspekta Simbeye alimuuliza daktari wa zamu jioni hiyo.

    “Hapana, mi nimetoka hapa niliacha kila kitu sawa. Nashangaa hawa jamaa wameingia saa ngapi” “Uhhhhhh” Inspekta Simbeye alishusha pumzi, kisha akausogelea mwili wa yule muuguzi, ilionekana wazi kuwa hata tukio lenyewe bado ni bichi kwa kuwa jeraha lile la risasi lilikuwa bado linavuja damu taratibu. Kazi ilikamilika na miili yote ilihifadhiwa katika chumba cha kuifadhia maiti.

    Inspekta Simbeye alikuwa kwenye lindi la mawazo ‘Isabel anaweza kufanya hili?’ alijiuliza sana kwa kuwa aliamini kuwa ulinzi aliouweka wodini hapo ulikuwa makini lakini nini kimejiri katika utekaji huo, lilikuwa swali gumu sana. Simbeye aliuangalia ule mlango mkubwa wa wodi hiyo, bado alikuwa haamini kilichotokea, mbele yake aliiona kazi jinsi itavyomuia ngumu, aliingia kwenye land cruiser ya Polisi na kuondoka.





    Kamanda Amata aliketi juu ya kochi kubwa na upande wa pili kulikuwa na Madam S, pamoja nao kulikuwa na watu wengine wawili.

    “Kamanda, mi nakwambia kwenye hili sakata Isabel lazima anahusika” Madam S alimsisitizia Amata juu ya uhusika wake katika mpango hasi,.

    “Hapana Madam, mi nafikiri ngoja aondolewe pale kisha tutaenda kuongea nae vizuri”

    “Ok! Kamanda…” Madam S alikatishwa na mlio wa simu, akainua mkono wake na kuelekeza sikioni.

    “Yes, nakusikia…” Madam S alijibishana na sauti ya upande wa pili

    “Eee? What?” aliuliza kana kwamba kuna kitu ambacho hajakielewa katika simu hiyo. Alishusha mkono wa simu taratibu na kuupachika kwenye kikalio chake, kisha akainua bilauri ya maji na kujimiminia kinywani, alikunywa kama mtu aliyekuwa na kiu ya jangwani, kisha macho yake mawili yaliyofunikwa kwa miwani yalitua kwa wale vijana wawili na kisha kwa Amata, akatikisa kichwa kuonesha masikitiko yake.

    “Isabel” alitamka.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Isabel? Kafanya nini?” Amata aliuliza

    “Isabel katoroka, na isitoshe ameuwa muuguzi na askari wa mlangoni”.

    Amata alishtushwa na habari hiyo ambayo kwake ilikuwa ngeni sana na ya kutoaminiwa, alisimama kitini na kuliendea dirisha kubwa lililopo hapo, uso wake ulianza kushikwa na taswira ya gadhabu, ‘Madam yuko sahihi, inaonekana Isabel ni mmoja wao’, kamanda Amata aligeuka na kumtazama Madam.

    “Lazima apatikane” Kamanda alijikuta akitamka maneno hayo bila mwenyewe kujua. “Kamanda, kazi imerudi mikononi mwetu kwa ushirikiano na jeshi la polisi, ila wao watafuata

    maelekezo kutoka kwetu, kazi njema vijana” Madam S alimaliza na kuelekea kwenye vyumba vya kulala.

    Kamanda Amata alitoka katika jumba lile kubwa ‘shamba’ akaingia kwenye gari yake na kutokomea.



    Tairi zake zilisimama moja kwa moja katika wodi ya mifupa, kwa mwendo wa haraka alizivuta hatua zake na kuingia kwenye lango kuu kisha moja kwa moja akingia kwenye kijivhumba cha wauguzi akawakuta watatu wameketi hapo.

    “Habari zenu wadada? Mimi ni afisa usalama” Amata alijitambulisha moja kwa moja bila kujizungusha, “poleni kwa msiba. Lakini naomba mnisaidie kitu kimoja ili kukabiliana na jambo hili”

    “Karibu sana” mmoja wa wauguzi hao alimkaribisha

    “Ningependa kuona daftari la zamu zenu, hasa wale waliokuwa wanamhudumia Isabel”

    Bila kusita muuguzi yule alivuta daftari kubwa na kuliweka mezani, Amata aliangalia orodha ya majina yale na akalifikia jina la muuguzi aliyebadilishana zamu na marehemu ‘Suzan Crispin’, alifunga lile daftari na kuwarudishia

    “Asanteni warembo” alijibu

    “Kaka tutoe hata soda basi” mmoja wa wauguzi alitamka

    Amata alitoa wallet yake na kutoa noti ya ya sh elfu kumi nma kuwapatia, kisha akaondoka zake.



    Madam S, alibaki akihangaika mawazoni mwake, moyo wake ulijawa hasira, kila mara aliapa kumsaka aliyeweka bomu kwenye gari yake, lakini alimshukuru Mungu kwa kuwa amemuokoa katika hilo. Alitafakari kwa muda mrefu akipanga na kupangua lakini picha haikuja sawa sawa. Polepole alianza kupata hisia na kujua wapi ni pa kuanzia kazi, akiwa katika mawazo hayo alipitiwa na usingizi.



    Asubuhi ya siku iliyofuata



    Madam S, aliliendea geti kubwa la gereji hiyo, akasukuma kijimlango kidogo, hakikuleta matata akaingia na moja kwa moja akafika ofisini.

    “samahani kuna kijana mmoja, jana asubuhi alinitengenezea gari yangu, nina shida nae, ile gari imekorofisha nataka akaiangalie” madam Limueleza fundi mkuu

    “Unamjua kwa jina?”

    “Hapana ila nikimuona nitamjua kwa sura”

    Madam S pamoja na yule fundi walitoka na kuingia eneo la kazi, haikuchukua muda alimtambua kijana yule, baada ya mazungumzo yote waliondoka pamoja. Madam S alipita taratibu eneo la uwanja wa Taifa.

    “Unaijua ile gari iliyochakaa pale?” alimuuliza “Hapana, ntaijuaje gari iliyoungua vile?”

    “Ok, umejibu vizuri. Gari yangu jana imelipuliwa kwa bomu kama umesikia kwenye redio au TV”, Madam akameza mate na kuendelea “Sasa nina wasiwasi mkubwa wewe ndiye uliyefanya kazi hii, ya kuweka bomu na kutaka kuniua siyo?”

    Yule kijana akaonekana kuchanganyikiwa, alikaa kimya kwa muda bila kujibu chochote. “Usiponipa ushirikiano, utalala pabaya leo”

    “Mama, utanionea tu, labda gari imelipuka kutokana na mfumo wa umeme”

    “Hapana, mimi najua aina za milipuko, lile ni bomu” Madam S alitulia kisha akaendelea “Najua si wewe, ila nambie nani unamuhisi”

    Yule kijana alibaki kimya moyo ulimuenda mbio hakujua nini cha kufanya katika hali hiyo. Alijaribu kuvuta kumbukumbu ya siku ile ili angalau ajue ni nani labda alifanya hivyo, ‘Bro Jose’, alijiwazia mwenyewe.

    “Nafikiri nimekumbuka kitu mama, kama ni yeye kuna bro mmoja tunamwita Bro Jose, mara nyingi huwa anakuja pale gereji”

    Madam S akatikisa kichwa kuashiria kuwa amekubaliana na kijana huyo. “Ok, uliona anafanya nini?”

    “Alikuja pale, akawa anaisifia gari yako, mi nikiwa narekebisa tairi, ye akawa mara anaingia ndani ya gari mara anaagalia engine”

    “Ok, zaidi ya hapo, hamna kingine?”



    “Hapana”

    “Sawa, sasa nitampataje huyo Jose?”

    “Huyu Bro Jose ni ndugu na mwenye gereji yule uliyekwenda ofisini kwake”

    Madam S, aligeuza gari na kurudi mjini, kisha alichukua simu yake ya upepo na kuongea na watu Fulani, alisimama mahali na mara land cruise yenye vioo vyeusi ilikaribiana nao, vijana wawili walishuka na kumchukua fundi gereji kutoka katika gari ya Madam S na kumuingiza kwenye ile Cruiser

    “Sikia, sikufanyii hivi kwa nia mbaya ila utajua baadae, utaenda kupumzika sehemu mpaka nitakavyokuachia” Madam S alimueleza yule kijana, na baada ya hayo “Panda kwenye gari” alimuamuru kupanda kwenye ile cruiser, akiwa ndani wale vijana walimvalisha kofia kubwa ya sox ambayo ilimfunika uso wote , na hakuona chochote kilichoendelea zaidi ya kupitiwa na usingizi mzito.





    “Umejiingiza kwenye jambo lisilokuhusu msichana!” Jomse alimueleza Isabel ambaye alikuwa hoi kwa kipigo kutoka kwa jamaa huyo.

    “Hata mkiniua, nina uhakika hamtafanikiwa, taarifa tayari zipo kwenye vyombo vya usalama na ninajivuna kwa kufanya hilo, heri mimi nife lakini niwaokoe maelfu wanaotarajiwa kufa hapo mbeleni” Isabel alizungumza kwa sauti ya kwikwi huku damu zikimtoka mdomoni, mguu wake uliokuwa umeanza kupona sasa ulitoneshwa tena kiasi kwamba hata hakuweza kusimama. Jomse alichukizwa na jibu la Isabel, alimpiga mateke mengi na mikanda ya kijeshi mpaka Isabel akapoteza fahamu kwa mara nyingine.

    “Jomse, acha hasira utamuua bure tu huyu na haitatusaidia lolote” Tonton alimwambia Jomse. “Na we usiwe kama Mandi, badala ya kufanya kazi uliyotumwa unaanzisha mambo mengine, hata nikimuuua huyu mimi napata faida gani, afe tu tutatupa maiti yake porini iliwe na mbwa” Jomse aliongea kwa hasira huku akirusha mikono yake hewani na kuondoka hapo “Muacheni afe apo hapo” aliwaeleza wengine na wote wakaondoka katika chumba hicho na kumuacha Isabel peke yake akiwa hana fahamu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ok! Tuzungumze yajayo, kazi karibu inakamilika plan A, japo kuwa jana tumemkosa yule bibi kizee (Madam S), kweli ni tukio baya kwa upande wetu. Tunapofanya kosa moja tunajiharibia wenyewe” Jomse aliwaambia vijana wake akiwemo Tonton, akawatupia macho mmoja mmoja kisha akaendelea “Jamaa wapo tayari mipakani, wanasubiri tukamilishe plan A, ili wao waanzishe plan B, lakini kumkosa yule bibi jana, naomba muwe makini sana” Jomse alimaliza na kujimiminia wine yake kinywani. Kabla hajasusha bilauri yake simu iliita mfukoni, akaitoa na kuiweka sikioni, “Yeah man” aliitikia

    “Eh! Unasema?(...), kama atarudi ni wa kumpoteza tu. We njoo huku watarudi hao” Jomse akashusha simu yake.

    “Jamaa wamemkusanya dogo kule gereji” taarifa hiyo iliwashtua wote, kila mtu alionekana kuchanganyikiwa na hilo.

    “Du! Eee sasa hapo patamu, tukamilishe mpango huu haraka iwezekanavyo” Ton alitoa rai. “Sasa ni kuwa makini zaidi, maana tayari watakuwa wameanza uchunguzi juu ya tukio lile, na hivyo kabla hawajatushtukia tuwe tumekamilisha. Ton mkabili bibi kizee ila kuwa makini, sisi watatu tumkabili Kamanda Amata, na roho yake iwe mikononi mwetu leo hii”



    Walivunja kikao na kurudi kule walikomuacha Isabel, wakamkuta bado amezirai, Jomse akachuku maji ya baridi kwenye ndoo na kummwagia.

    “Amka mpumbavu wewe, na wewe lazima ukutane na Madam Rose akutie adabu” Jomse alifoka na kumuacha Isabel akijivutavuta pale chini.

    Ton alikuwa kimya sana, fikra zake zilimfanya akose raha kabisa, aliingia kwenye gari yake tayari kuondoka



    “Ngoja nikaonane na Suzan nimpe mzigo wake narudi baadae” Tona alimuaga Jomse

    “No. Ton usiende peke yako, uko uendeko hakutabiriki,nenda na Anaconda akulinde” Jomse alitoa amri na ikafuatwa.

    Punde si punde walifika katika hotel ya Valley View, Anaconda akashuka kwanza na kuangalia uku na huko kisha akagonga kioo cha dirisha la nyuma kuashiria kitu, Ton akashuka na moja kwa moja akongoza kuelekea hotelini na Anaconda akamfuata nyuma yake.



    Tax nyeupe ilisimama nyuma kidogo ya gari ya akina Ton, mwanadada mrefu kiasi, mwenye mwili wa kawaida, aliteremka na baada ya kuiweka miwani yake vizuri, alivuta hatua taratibu kuielekea hoteli hiyo, alichukua lifti kupanda ghorofa ya nne kisha akaelekea chumba namba saba akagonga mlango kwa staili aliyoelekezwa, na mlango ukafunguliwa.

    “Karibu Suzan” Anaconda alimkaribisha “Upo peke yako?” Ton alidakia kwa swali

    Suzan alisita kidogo kujibu “Ee nipo peke yangu”

    “Ok haina haja kuchelewa, tunashukuru kwa kazi uliyotufanyia. Na ujira wako huu hapa dola za kimarekani elf moja” Ton alipomaliza kuongea hayo alimkabidhi kitita hiko Suzan, nae akakisunda katika mkoba wake. Suzan hakuamini kabisa anachokishuhudia, pesa zote hizo kwa kazi ndogo, kazi ya kumsaliti Isabel.

    “Ok. Mi naomba niende” Suzan aliaga na kusimama tayari kuondoka “Ok Suzan, be carefull” Ton alijibu na kumruhusu Suzan kuondoka.

    Suzan aliiendea tax iliyomleta na kuingia mlango wa nyuma wa gari hiyo.

    “Ingia! Ukileta fujo nakumaliza” Suzan alitazamana na domo la bastola kutoka kwa Gina, Gina hakuonesha uso wa masihara hata kidogo

    “Ingia” alirudia tena na Suzana akaingia ndani, Gina akiwa na gloves maalum mikononi aliuchukua mkoba wa Suzan huku mkono mmoja ukiwa bado umeshikilia bastola ile, aliupekua na kutoa na alipoiona simu yake aliichukua kisha akaitia kwenye kimfuko cha plastiki na kuihifashi. Suzan akatiwa pingu mikononi.

    “Haya endesha gari” “Tunaelekea wapi?” “Central police”

    Dreva aliondoa gari na kuelekea alikoagizwa. Walipofika central Suzan alishushwa na Gina akafuata nyuma yake.

    “Hifadhi huyu, naomba asihojiwe lolote mpaka mpatapo amri nyingine” Gina aliwakabidhi Suzan polisi waliopo kaunta na kisha yeye akaongoza kuelekea ofisi ya Inspekta Simbeye.

    “Kazi uliyonituma imekamilika afande” Gina aliongea kwa ukakamavu mbele ya bosi wake “Vizuri sana afande, waweza kwenda nitawasiliana na wewe nitakapokuhitaji” Inspekta Simbeye alimueleza Gina, Gina akaonesha ukakamavu wake kwa kubana mikono yake miwili kuonesha heshima, kisha akageuka na kuondoka.





    “Suzan, hebu kuwa mzalendo, tueleze, unajua Isabel alipo?” Sergeant Bizibu alimuuliza kwa upole “Jamani mimi nina mhusiano gani na Isabel? Mimi ni muhudumu wa afya, nimeingia kazini nakuta hiyo habari, mbona mnanionea?” Suzan alilalamika

    “Sikia mrembo, hapa hatujaja kukufanyia chochote kibaya, tunachotaka ni wewe kujibu maswali yetu, usitufiche kitu. Tii sheria bila shuruti, lakini ukikaidi utashurutishwa kuitii. Tueleze Isabel ametoroka au ametekwa kwa mawazo yako?”

    Suzan alitulia kidogo aliziangalia pingu zile za chuma mikononi mwake hakuamini, aliinua uso wake na kumtazama polisi huyu mwenye cheo cha sergeant aliyeketi mbele yake, aligeuka huku na huku akaona kuwa kumbe wapo wawili tu mle ndani, akajikohoza kidogo

    “Sikia afande Isabel alikuwa anaumwa sana hasa mbavu na mguu wake, lakini mimi simjui kiundani anaweza akawa ametoroka au ametekwa kwangu ni swala gumu kwa kuwa sikuwepo



    kazini na aliyekuwepo ameuawa” Suzan alijibu kisha akainamisha kichwa chake kwenye kijimeza kile kidogo kilichotengenezwa kwa chuma

    “Kwa hiyo unatuambiaje?” “Mi sijui kilichotokea”



    Baada ya mahojiano marefu kati yao, sergeant Bizibu alighairisha zoezi na kuamuru Suzan apelekwe chumba cha pili akahifadhiwe kwa muda.

    Kilikuwa ni chumba chenye giza kilichojengwa katika chini ya ardhi, Suzan aliingizwa na kukalishwa kwenye kiti maalum mikono yake ikiwa nyuma ya kiti hiko na kusikiliwa na kamba maalum, Suzan hakuona chochote zaidi ya giza nene lililokijaza chumba hicho.

    “Jamani huku ni wapi?” aliuliza kwa sauti ya kilio

    “Huku ndiyo chumbani kwako kwa muda tu” alijibiwa na WP mmojawapo aliyekuwa akimfunga vizuri katika kiti hiko kisha wakatoka na kumuacha wamemfungia mlango.



    ********

    “Amekataa kutoa ushirikiano” Inspekta Simbeye alimueleza Kamanda Amata aliyekuwa akizungushazunguash akalamu yake vidoleni.

    “Au tunamuonea?” aliuliza AmataCHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hapana haonewi mtu, huyu kwa vyovyote anahusika”

    “Inspekta, tusifanye mambo kwa hisia, anahusika vipi? Hilo ndilo la msingi. Katika pekuzi zenu kitu gani mmechukua kama kisaida polisi?”

    “Ah, tumechukua simu yake ya mkononi.”

    “Hapo umecheza, hebu lete hiyo simu tuangalie namba zilizopigwa au zilizoipigia, tunaweza kupata jibu” Amata alimaliza kwa maneno hayo.

    “Kamanda, sikuwa na wazo kama hilo, mi nilitaka kwenda kampuni ya simu kucheki rekodi za simu na meseji zake”

    “Huko mbali Inspekta, umeanza kuzeeka au?” Kamanda Amata alimtania mzee huyo wa makamu amabaye anamkumbuka sana kwa kwata alilompigisha huko CCP Moshi.

    Kamanda Amata aliifungua simu ile na sekunde kadhaa ilitoa mlio mkali na kuonesha picha ya bahasha juu ya kioo chake, akaufungua ujumbe huo…



    ‘…umefika salama, kama utahitaji msaada utuambie…’



    Ujumbe ule uliisha hivyo na hakukuwa na namba yoyote zaidi ya maandishi private number, Amata alitikisa kichwa na kuendelea kuangalia jumbe zingine, nyingi alizishuhudia za mapenzi tu ambazo hazikuwa na maana sana kwake, alipotaka kubadili kuangalia simu zilizoingia na kutoka ndipo alipouona ujumbe wa mwisho



    ‘…Valley View hotel Na. 407…’



    Amata hakuona umuhimu wake alijua itakuwa ni sehemu ya kukutania na mpenzi wake, lakini kengele za hatari ziligonga kichwani mwake, akainua mkono kwa kidole chake cha shahada akajikuna pua yake.

    “Vipi Kamanda, umegundua kitu?” Inspekta Simbeye aliuliza “Aaa mapenzi na miadi tu”

    Akampa ile simu Inspekta Simbeye aliitupia macho ile meseji, jicho lake la kushoto likamcheza, hatari! Alirudisha simu kwa Amata.

    “Kamanda, Valley View.”



    “Vipi umehisi kitu, Inspekta?” “Kabisa, bila shaka”

    “Ok, hiyo ni point namba moja, na hiyo itazaa namba mbili. Naomba nikuache Inspekta” “Hamna shida ukihitaji msaada usisite kunitafuta”



    Kamanda Amata alitoka na kuchukua tax kuelekea ofisini kwake ambako alimkuta Gina akiendelea na kazi hii na ile ilimradi siku zilienda.

    “Karibu” alimkaribisha “Asante, hamna jipya?” “Hamna”

    Amata aliketi juu ya kiti chake na kuanza kutafuna karanga zake moja baada ya nyingine huku akiandika mambo Fulani katika kitabu chake cha kumbukumbu.





    “Kamwe hamtoweza kufisha juhudi za kimataifa, mpango huu umesukwa na kusukika” Jomse alimueleza Madam S maneno hayo huku akiwa kamuelekezea domo la bastola kubwa aina ya revolver iliyofungwa kiwambo cha sauti.

    “Wewe ni nani?” Madam S aliuliza

    “Mimi ni mwanamapinduzi halisi, nipo hapa kwa kazi moja tu ya kuondoka na roho yako” aliongea kwa dharau.

    Ilikuwa ngumu kwa Madam S kujitetea mbele ya bastola hiyo ambayo haikuonesha masikhara hata kidogo, alishindwa kumtambua mtu huyu kwa kuwa alikuwa amevaa soksi kichwani kuuziba uso wake na kuruhusu macho tu kuona.

    “Umeingiaje ofisini mwangu hali milango yote nimefunga?”

    “Kama Yesu alivyoingia kwa wanafunzi wake huku milango imefungwa” alijibiwa. Madam S alipandwa na hasira kwa dharau alizozionesha huyo bwana, alimkazia jicho na kumwangalia kwa hasira.

    “Usiniangalie kama unavyomwangalia paka wako, nimeshakwambia nataka kuondoka na roho yako ili mipango mingine iende, na hapa ninavyoongea na wewe kijana wako anayejifanya mtukutu Kamanda Amata yupo matatani, tunataka tupindue nchi hii na hilo kwamwe halipingiki.”

    Madam S alishusha pumzi ndefu akimwangalia mtu yule aliyekuwa akijiamini ndani ya ofisi ya watu, akili ilimzunguka huku na huku hakujua afanye nini. Kutoka pale alipoketi Jomse alisimama taratibu, kitendo ambacho madam S alikiona ni udhaifu mkubwa, kwa wepesi ambao haukutegemewa madam S alijirusha mtindo wa tick tack na kuipiga bastola ile kutoka mikononi mwa Jomse, ilipaa juu na kugonga ceiling board, Jomse akiwa bado anashangaa akitaka kuidaka bastola, Madam S alikuwa tayari ameshatua chini, pigo moja la karate lilitua sawia katika mbavu za Jomse, maumivu yake yalimfanya apoteze muelekeo, bila kuchelewa Jomse aliachana na wazo la bastola na kumkabili Madam, patamu! Jomse kwa haraka alimtazama Madam S na kumuona jinsi alivyotulia kumkabili, bila kuchelewa Jomse alicheza Ashi Barai,(Foot sweep kick), kwa mguu wa kushoto aliupiga mguu wa madam S ambao ulikuwa umetanguliza mbele kwa kuufagia, madam S alipoteza stamina na teke la nguvu lilitua sawia kwenya sikio la madam S, mpepesuko wako ulimpeleka mpaka kwenye kabati lililokuwa limejaa mafaili na kabati lile lilishindwa kuvumilia na kuanguka palepale alipoangukia madam S, kitendo bila kuchelewa madam S alikuwa tayari kajirusha kiufundi na kuondoka eneo lile ambapo kishindo cha kabati kiliwashtua walinzi wa nje nao kwa haraka wakakimbilia ndani kuona kunani, madam S alijiviringa na kusimama karibu kabisa na kabati lake dogo upande wa pili wa meza kubwa tayari Colt 45 bastola hadimu ya kimarekani ikiwa mkononi mwake, kidole kwenye trigger kilicheza kidogo tu colt ikabanja lakini kwa haraka Jomse alishatoka eneo lile kwa sentimeta kadhaa.

    Mlango ulipigwa kikumbo na walinzi wawili wakaingia.

    “Mikono juu!” askari mmoja wa kampuni ya ulinzi alimuamuru Jomse, kosa kubwa! Jomse aliinua mikono juu wakati huo tayari alishachomoa kisu chake kidogo katika mkanda wake na kukirusha



    kwa ustadi wa hali ya juu, moja kwa moja kilitua katika koromeo la askari yule, kishindo kingine kilisikika cha bunduki kubwa na kutawanya taa kubwa iliyokuwa imesimamishwa kwenye kona, Jomse aliruka back na miguu yake ikatua katika kioo kikubwa cha dirisha na kudondoka nje, madam S na yule mlinzi mwingine walitoka haraka na kukuta tayari Jomse karuka wigo wa waya na kudandia pikipiki lake kubwa Cagiva la Kirusi, wamemkosa.

    Madam S aliificha haraka bastola yake kwenye mkanda wake maalum aliouvaa ndani ya koti lake la suti, na kurudi kule ofisini kwake, walimkuta yule mlinzi akikata roho, mauti yakamfika.

    Vitu vilikuwa shghalabaghala ofisini kwa madam S.

    “Bastard !!!” Madam S alifoka kwa hasira huku kifua chake kikipanda na kushuka, akachukua simu yake na kubofya namba za Kamanda Amata, ‘mteja unayempigia kwa sasa hapatikani, jaribu tena baadae’

    “Shit !!” aling’aka madam S na kufungua droo yake, akatoa magazine nyingine iliyojaa risasi, akatoka nje akiwa anataka kuingia kwenye gari yake, alishtushwa na sauti iliyomwita. “Madam S” alikuwa ni Inspekta Simbeye.

    “Hali ni tata Inspekta”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Unaenda wapi madam?” Inspekta aliuliza

    “Naenda kumsaka hayawani” alijibu huku akiingia kwenye gari

    “Hapana Madam subiri kidogo, akili yako itulie” Simbeye alimbembeleza madam, maana alimuona jinsi alivyopaniki na ule utu uzima, “Nipe bastola” Inspekta Simbeye alimuomba Madam bastola huku akimnyooshea mkono ishara ya kuomba, madam S alitulia kidogo.

    “Kwa kuwa ni kazi yako chukua unikabidhi baadae” madam S alimwambia Inspekta Simbeye. Madam S alipiga tena simu ya Amata bado ilikuwa haipatikani, kijasho kilimtiririka, hana la kufanya, alishuka garini na kurudi ofisini kwake, mlangoni alisipishana na mwili wa yule mlinzi ukiwa ndani ya machela na kufunikwa kitambaa cheupe, aliufunua na kumtazama kwa huruma, akafanya ishara ya msalaba na kuufunika tena.





    Kamanda Amata alifika katika kaunta ya Valley View Hotel, mwanadada mrembo alimwangalia kijana huyu mtanashati ambaye mwili wake uliojengeka vizuri ulikuwa umetulia vyema kwenye fulana yake nyeusi iliyombana na kuonesha siha yake ya kimazoezi.

    “Karibu nikusaidie tafadhali” muhudumu yule alimkaribisha Amata

    “Asante sana, nafika chumba namba 110 tafadhali” akili ya Amata ilikuwa inafanya kazi haraka, katika kitabu cha wageni pale mezani alishaona kuwa chumba namba 110 kimechukuliwa na mwanamke hivyo ingekuwa rahisi kwa mhudumu huyo kumruhusu bila shaka.

    “Sawa, subiri mtu akusindikize.” “Hapana, nitakwenda mwenyewe”

    Kwa mwendo wa haraka haraka Amata alikwea ngazi za jingo hilo mpaka ghorofa ya nne na siyo chumba alichotamka, baada ya kuzimaliza ngazi zile alifika kwenye korido ndefu iliyotandikwa zuria mororo jekundu, alitembea mpaka mlango namba 07, alisimama kidogo akaangalia huku na huku na alipoona kuna utulivu alisikiliza kidogo akagungua kuwa kuna utulivu wa hali ya juu, akachukua moja ya funguo zake na kutumbukiza kunako tundu husika, mizunguko miwili mitatu tu mlango ulilegea na taratibu Amata aliufungua na kuingia ndani kisha kuubana nyuma yake na funguo kurudisha mfukoni. Kwa hatua za hadhari akihakikisha hagongi kitu chochote alitembea taratibu na bastola yake ndogo ikiwa tayari mkononi, alisita kidogo na kurejesha akili yake chumbani mle, alisikia maji yakitiririka bafuni, aliuendea mlango wa bafuni taratibu bastola ingali tayari mkononi, kwa mkono wa kushot alitikisa kitasa cha mlango huo na mlango bila ubishi ukajiachia, maji yalikuwa yakitiririka, hakuna mtu bafuni. Amata aligundua hapo kachezwa shere, akapuuzia na kurudisha bastola yake kiunoni, lahaula! Kabla alipoiweka tu bastola yake kabla hajageuka pigo moja la haja la karate lilitua shingoni mwake, kigiza cha sekunde kadhaa kilimtawala, alijihisi kukosa nguvu lakini nuru ya mwanga ikamrejea tena, hakuona haja ya kufanya mzaha katika hilo akajiangusha chini, adui yake akaona huo ndiyo mwanya wa kufanya yake



    alimuendea Kamanda Amata pale chini kabla hajatahamaki, kamanda Amata aliinua chupa ya whisky iliyokuwa hapo chini na kumrushia adui yake usoni kwa nguvu zote, wakati adui yake akiipangua kwa ufundi chupa ile, Amata kwa mguu wake wa kulia bado akiwa chini alikanyaga kwa nguvu sehemu za siri za adui yake na kumfanya atoe mguno wa maumivu. Kwa mruko wa kisarakasi, Amata alijinyanyua na kuwa wima, ngumi nzito ilikuwa ikiuelekea uso wa Amata nae kwa mchezo wa kitoto akepa na kuudaka, bila ajizi akaukunja na kuuvunjia begani kwake, yowe la nguvu lilimtoka jamaa huyo baada ya kushuhudia mifupa ya mkono wake ikiachana, Amata aliuvuta mguu wake wa kulia na kumpita kidogo kisha kumchota mtama a nyuma na jamaa alitua chini kama mzigo na kuivunja meza ya kioo iliyokuwa hapo vipande viwili, goti la kamanda likatua juu ya tumbo la adui.

    “Tulia! Shhhhhh” Amata alimuonya jamaa kutulia huku akiwa kamshika mkono wake uliovunjika kwa mkono mmoja na mwingine kashika kipande cha chupa, “nani amekutuma?” alimsaili huku akiuzungusha taratibu ule mkono uliovunjika.

    “Aaaaaaaa, unaniumiza, ntasema ntasema..” adui alitoa yowe la uchungu “Sema!”

    “Walionituma siwajui kwa undani” huku akilia kwa uchungu “wapo wengi ila nawajua kwa uchache”

    “Wataje majina na wapo wapi?” Kamanda aliuliza kwa hasira, “Hujibu ee?” aliuzungusha mkono kwa nguvu.

    “Wapo Burundi, wapo Burundi na wengine Rwanda” alijibu “Taja majina” Amata alilazimisha

    “Aaaa nimeshakujibu tayari” alilalamika

    “Bado, na hapa mko wangapi?” Amata aliuliza nalipoona jamaa huyo hatoi ushirikiano, aliuzungusha mkono kwa ghafla, yowe la nguvu lilimtoka na Amata akubana mdomo wake kwa kiganja cha kulia baada ya kukitupa kile kipande cha chupa.

    “Tupo wengi, na wengine miongoni mwenu…” alijibu huku akianza kutupatupa miguu huku na huko, Kamanda Amata alimwangalia kwa hasira.

    “Shit!” povu lilimtoka mdomoni na macho yake yakageuka kuashiria kuwa uhai haupo tena, kimbebe.

    ‘Tupo wengi na wengine miongoni mwenu’ sentensi hii ilimjengea mwangwi Amata, hata akajikuta nguvu zinamwishia, alisimama na kumuacha huyo jamaa hapo chini, aliiendea meza iliyokuwa na computer mpakato, akapekua kwenye vidroo na kukuta business card mbalimbali akakusanya zote na kutia mfukoni, flash iliyokuwa ikining’inia katia laptop na kitabu cha kumbukumbu akavitia katika kibegi chake cha mgongoni na taratibu akauendea mlango, alichukua funguo mezani na kufunga kwa nje kisha kushuka ngazi taratibu. Alipita kaunta na moja kwa moja alifika nje kabisa, alikatiza mtaa wa kwanza wa pili na kuingia katika gari yake akaketi.

    “Uhhhhhhhh” akashusha pumzi kisha akawasha gari na kuingia barabarani akatokomea mjini.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    **********



    :: Unavyodhani ni kitu gani kitaendelea hapo??





    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog