Search This Blog

Sunday, 22 May 2022

TUTARUDI NA ROHO ZETU? - 5

 







    Simulizi : Tutarudi Na Roho Zetu?

    Sehemu Ya Tano (5)



    iLIPOISHIA TOLEO LILILOPITA...

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Sasa kazi ya kutega vigololi ikiwa imekwisha, Joram alimtazama Nuru na kumnong’oneza, “Awamu iliyobaki ni yangu peke yangu. Ni lazima niingie katika mtambo wao na kuulipua. Nikiweza kuulipua kabla ya madhara tuliyoandaa katika jiji hili kutokea litakuwa jambo jema sana. Nikishindwa, mioto itakapoanza nenda pale ambapo nimekuonyesha katika ramani ukanisubiri.”

    “Hatuwezi kwenda wote?”

    “Haiwezekani. Tumelijadili hilo mara nyingi sana.”

    Wakakubaliana.





    ****SASA ENDELEA****



    Kisha Joram akajiingiza miongoni mwa watu waliokuwa wakipita katika mitaa hiyo, akielekea ilikomwelekeza ramani yake. Mwendo wake ulikuwa wa haraka na uhakika, ingawa alifahamu kikamilifu ulinzi mkali uliozunguka mtambo huo. Matumaini ya kurudi yalikuwa ndoto isiyo na hakika. Hakujali. Asingejali kufa, endapo tu kifo hicho kingetokea baada ya kufanikiwa kutega mabomu yake katika mtambo huo. Aliamini kuwa Nuru asingeshindwa kurudi Tanzania katika msukosuko mkubwa utakaoutokea mji huu, saa mbili na nusu baadaye.

    Nuru alimwacha Joram na kuondoka kwa hatua chache. Mara tu alipoamini kuwa asingegeuka tena kumtazama, alianza kumfuata. Hakujua kuwa yeye pia alifuatwa na watu wanne wenye silaha kali mkononi na mioyo yenye hofu na hasira dhidi yake.



    *****SURA YA KUMI*****



    MKOBA wake wenye silaha zake zote ukiwa umetulia mkononi, kwa utulivu na uhakika kama mzigo wowote ambao haukuchukua chochote cha haja, Joram alipiga hatua moja baada ya nyingine katika mitaa ya mji mkuu wa Afrika Kusini. Alipishana na wengi akiandamana na wengi wenye misafara yao.

    Kitu fulani katika damu yake kilimnong’oneza kuwa anafuatwa. Hilo halikumshangaza. Tangu alipoachana na Nuru alifahamu fika kuwa angepinga ushauri wake wa kumsubiri pale alipomwelekeza hadi atakapoimaliza awamu hii ya mwisho ambayo ilikuwa ya hatari mno. Akiwa ameshangazwa na ushujaa wa msichana huyu, jinsi alivyokuwa tayari kuihatarisha roho yake kwa hiari, aliamini kabisa kuwa asingekubali kuikosa fursa hii ya mwisho, fursa ambayo endapo ingefanikiwa isingefutika katika kurasa za matukio muhimu ya kihistoria duniani.

    Hivyo, hakujishughulisha kugeuka nyuma, kwa hofu ya kuwafanya makachero, ambao aliamini wamezagaa kote mitaani wakimtafuta, kumshuku. Badala yake aliendelea na safari yake huku akitafuta nafasi na wasaa ambao ungemwezesha kumtia Nuru chenga ya mwili. Hakuumaliza mtaa huo kabla fursa hiyo haijajitokeza. Katika kona ya mtaa huo Joram alikuta mahala palipokuwa na ajali ya magari matatu yaliyogongana.

    Watu wengi walikuwa wamejazana kuitazama ajali hiyo. Kati yao, Joram aliweza kuona nyuso za watu wenye dalili ya ukachero na uaskari. Hakuwajali. Badala yake alijitia mmoja kati ya raia waliokuwa wakiitazama miili ya madereva wawili ambao hawakuwa na dalili ya uhai.

    Aliitumia fursa hiyo kutoa kofia mfukoni na kuivaa kichwani, pamoja na kuyafunika macho yake kwa miwani ya jua. Kisha akajipenyeza katika kundi hilo na kutokea tayari akiwa amemchanganya Nuru. Hivyo, akaendelea na safari yake, mluzi mdomoni, tabasamu usoni na hadhari moyoni.

    Baada ya mitaa kadhaa aliumaliza mji. Kwa mbali, aliliona jengo lenye mtambo aliokuwa akiuhitaji. Ili kuthibitisha alitumia hila kuitazama ramani yake. Hakuwa amekosea. Akaendelea na safari yake akianza kujikumbusha kwa mara nyingine hila ambazo aliziandaa ili zimwezeshe kufanikisha jukumu lililokuwa mbele yake. Hakuwa amekosea. CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Akaendelea na safari yake akianza kujikumbusha kwa mara nyingine hila ambazo aliziandaa ili zimwezeshe kufanikisha jukumu lililokuwa mbele yake. Moyoni alijua kabisa kuwa alikuwa akikaribia mbele ya domo la mauti lililo wazi. Kuingia ulikuwa wajibu wake, lakini kutoka kinywani humo akiwa hai ni jambo ambalo hakuwa na hakika nalo.

    Hakuogopa. Lakini kutokuogopa hakukumfanya astahimili kujikuta akitokwa na sala ndefu kimoyomoyo, jambo ambalo hakumbuki kwa mara ya mwisho alilifanya lini.



    ********

    “Bado yuko mbele yetu mzee…” Taarifa ilimfikia Von Iron ambaye alitulia katika ofisi yake, mara kwa mara akitazama saa yake ya mkononi. “… Tufanyeje mzee? Tumuue?...” sauti iliendelea.

    “Nimesema mwacheni,” Von alinguruma katika walkie talkie iliyokuwa mbele yake. “Mfuateni hadi mtakapopata nafasi nzuri mumkamate. Tunamtaka hai.”

    “Anaelekea kuwa anaweza kuleta madhara, mzee. Anaweza kuwa na silaha…” sauti iliendelea.

    “Unataka kuniambia kuwa wanaume wanne mnashindwa kumkamata malaya mmoja tu wa Kiafrika?”

    “Sivyo, mzee. Lakini…”

    “Lakini nini? Mnachotakiwa kufanya ni kumleta hapa akiwa hai, ili atueleze wapi alikotorokea Joram Kiango. Mkishindwa kufanya hivyo nadhani hamtashangaa kwa lolote litakalowapateni.” Alimaliza na kufunga redio hiyo.

    Taarifa ya kuonekana kwa Nuru ilimfikia nusu saa iliyopita. Fununu iliyosaidia kupatikana kwake ililetwa na mtu aliyefia hospitali baada ya kuruka dirishani kwa maumivu ya kisu. Kabla ya kukata roho mtu huyo alifaulu kutamka kuwa aliuawa na msichana wa kizungu mwenye lafudhi ya Kiafrika. Wakagundua kuwa mafanikio yote ya Joram yalitokana na hila ya kujifanya mzungu.

    Ndipo wakuelekeza upelelezi kwa namna nyingine. Na haukupita muda kabla hajatiliwa mashaka msichana huyu ambaye alikuwa akitembea mitaani kwa namna ambayo si ya kawaida kwa wasichana, asubuhi kama hiyo. Mtu alimsogelea. Akamsalimu. Majibu aliyopata yaliutia kasoro uzungu wake kutokana na lafudhi. Mwingine alimkaribia.

    Akajitia kukosea na kuugonga mkoba wake, kisha aliinama mbiombio kumsaidia kuuokota. Alishangazwa na wepesi wa msichana huyo katika kuuokota mkoba huo. Alimtazama vizuri zaidi. Akaona dalili ya Uzungu bandia katika uso na mwili wake. Ndipo akaandamwa, bila ya yeye kufahamu, dakika yoyote akiwa tayari kupigwa risasi, endapo Iron angeafiki…

    Iron hakuwa tayari kuafikiana na makachero hao waliojaa hasira na uchu wa kumuua Nuru. Hakuafiki kwa kuwa yeye pia alijawa na uchu moyoni, uchu wa kumpata Nuru akiwa hai, uchu wa kuonja kile ambacho aliambulia kukishuhudia kwa macho tu. Ndiyo, kufa, Nuru alikuwa hana budi. Lakini angeweza kufa baadaye. Hakuiona sababu yoyote ya kufanya haraka.

    “Bosi tumeamua kumnasa…” taarifa ziliendelea kumfikia.

    “Mkamateni.”

    Mara zikasikika purukushaniu katika chombo hicho. Zilifuatiwa na milio ya risasi tatu. Moyo wa Iron ulidunda kwa hofu. Asingevumilia endapo msafara wa risasi hizo ungeishia katika mwili wa Nuru kabla…

    “Bosi amemjeruhi mtu wetu… turuhusu tummalize…”

    “Nasema mleteni akiwa hai,” Iron alinguruma.

    *******



    Mara chombo cha mawasiliano kikazimwa. Dakika chache baadaye mlango wa ofisi ya Iron ulifunguka na kumruhusu msichana ambaye alikuwa akisukumwa kwa mitutu ya bastola nne kuingia chumbani humo huku akipepesuka. Alikuwa hai. Lakini jeraha la kisu katika mkono wake wa kulia, kuchubuka shavuni, na uvimbe usoni, vilidhihirisha kuwa aliupigania uhai wake kwa gharama kubwa.

    “Ameua watu wawili,” kiongozi wa msafara huo alieleza.

    “Atajuta…” lilikuwa jibu pekee la Iron.

    “Amegoma katakata kuelekeza alikojificha mwenzake.”

    “Ataeleza.”

    Makachero hao walishangazwa kiasi na tabia hiyo mpya ya kiongozi wao. Hakuwa Von Iron waliyemfahamu. Von Iron waliyemfahamu angekuwa wa kwanza kutamka kwa ukali “ua.” Na endapo kifo kisingetokea mapema Von Iron waliyemfahamu angeshuhudia ukatili wa hali ya juu ukitendeka katika mwili wa msichana huyo jeuri aliyetisha, hasa jinsi ngozi yake ya bandia iliyobanduka hapa na pale kwa purukushani na kufanya mabaka ya ngozi yake asilia yajitokeze kwa namna ya kuchekesha na kutisha kiasi.

    “Sikieni,” Von aliwaamuru. “Huyu niachieni mimi. Nitajua la kumfanya. Fanyeni hivi, endeleeni kumtafuta Joram Kiango. Mkimpata namtaka vilevile. Hai au maiti. Sawa?”

    “Sawa, bosi,” waliafiki wakitoka mmojammoja, baada ya kutazamana tena kwa mshangao.

    Walipobaki peke yao Von Iron alikiacha kiti chake na kumsogelea Nuru. Akamkazia macho yake makali. Mara alilazimika kuyainamisha macho hayo mara moja baada ya kuona kitu ambacho hakupata kukiona katika macho ya msichana yeyote, kitu kisichoelezeka kwa ukamilifu, kitu kama nuru ya aina yake ambacho kilifunua mapazia fulani na kuacha barabara ndefu inayoelekea kusikojulikana; kilichomfanya Joram ayaepuke macho hayo ni zile hisia za kutatanisha ambazo zilimjia ghafla zikimfanya ajihisi kama anayeifuata barabara hiyo akielekea huko ambako hakujulikana, katika dunia nyingine inayotatanisha.

    “Una habari kuwa maisha yako yamo mikononi mwangu?” Von Iron aliuliza.

    Hakupata jibu, jambo ambalo lilimfanya ainue tena macho na kumtazama Nuru.

    Ile nuru ya kutisha aliyoiona awali katika macho hayo haikuwepo tena. Badala yake alikutana na macho yaleyale aliyoyategemea, macho aliyotamani kuyaona, macho ya msichana, yenye dalili zote za usichana. Mara akawakumbuka marehemu wazazi wake. Akakumbuka kuwa ni kitu fulani katika maumbo ya msichana mweusi kama huyu ambacho kiliwafanya waondoke duniani kwa aibu na uchungu, kitu ambacho Von alikuwa akikitamani ili akione au kukionja. Leo ilikuwa fursa ya kipekee. Atamtumia msichana huyu kumfunulia siri hiyo, kisha angemwua.

    “Una habari kuwa maisha yako yamo mikononi mwangu?” alilirudia swali lake.



    Bado Nuru hakumjibu. Aliendelelea kusimama paleplae alipokuwa, uchovu ukimsumbua, maumivu yakimtesa. Moyoni hasira kali ilikuwa ikichemka dhidi ya watu hawa. Hakuwa na shaka kuwa maisha yake yalikuwa ukingoni. Lakini si hilo lililomtia hasira. Hasa alisikitika kwa kule kuona kuwa amekamatwa kabla ya kazi ya mwisho kukamilika. Japo alikuwa na hakika kuwa Joram alikuwa hajakamatwa, lakini aliamini kuwa ingekuwa haki yake kushirikiana na Joram bega kwa bega katika awamu ya mwisho kama walivyofanya katika ile ya awali. Kiasi, vilevile, alikuwa akijiuliza kama hakuwa amefanya makosa kwenda kinyume cha matakwa ya Joram na kumfuata kwa siri badala ya kumsubiri kama alivyoamriwa. Alijuwa wazi kuwa ni kitendo hicho ambacho kilimtia mashakani.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hata hivyo, hakuwa na hofu kubwa sana juu ya maisha yake. Hakuamini kuwa kifo kilikuwa karibu kiasi hicho. Mipango waliyoiandaa ilimtia hakika kuwa ingetokea fursa nzuri ambayo ingempa mwanya wa kutoroka hadi nchi jirani za mstari wa mbele. Imani hiyo ilijengeka katika moyo wake mara alipojikuta amezungukwa na askari wenye silaha, lakini wakiwa hawana dalili ya kuzitumia silaha hizo dhidi yake. Hata baada ya kutoa bastola yake na kuwaua wawili kati yao walifyatua silaha zao kwa dhamira ya kumtisha tu; akajua kuwa walimtaka hai ili wamlazimishe kutoa siri fulani. Hivyo, hata alipozidiwa nguvu, baada ya kuvamiwa na kupigwa sana, hakuwa na shaka sana.

    Na hasa huyu mtu mnene anayeonekana kama kiongozi wao. Huyu ambaye tamaa ya kimwili ilikuwa wazi katika macho yake. Kosa analofanya huyu la kumtamani lingeweza kabisa kusaidia kuyaokoa maisha yake na ya Joram Kiango. Alichohitaji ni muda kidogo.

    Suala hili la kupendwa au kuhitajiwa kimapenzi halikumshangaza. Kwa kweli, alilitegemea. Joram alikuwa amemfafanulia hilo pia walipokuwa wakijiandaa kuingia nchini humu. Alimweleza kwa lugha ya kishairi akisema “Katika silaha zote za mwanamke uzuri unazitangulia.” Akamweleza kinagaubaga nini la kufanya. Hata walipokuwa wakifanya mapenzi kitandani, kabla ya Joram kutumia hila ya kuharibu kile chombo chao cha kutazamia alimnong’oneza, “Tutafanya kila kitu. Najuwa wanatutazama, usione haya. Nataka tuwatie homa ili endapo watatukamata, watamani kuyashuhudia waliyoyaona kwa vitendo. Nafasi ambayo natumaini hutashindwa kuitumia.”

    Haya, sasa nafasi hiyo imetokea… Nuru alijiambia kimoyomoyo. Akayainua macho yake, akayalegeza kidogo, akiruhusu tabasamu dogo. “Najua kuwa ninakufa…” alimjibu Iron kwa sauti ndogo ambayo masikioni mwa mwanaume ilitosha kuanzisha kongamano fulani baina ya mwili na damu.

    Kufa huna budi! Iron alisema rohoni… utakufa kifo kibaya. Lakini itakuwa baada!... kwa mdomo alisema, “Nimesema maisha yako yamo mikononi mwangu. Vitendo vyenu vilikuwa vuya kinyama mno. Pamoja na kupokelewa vizuri katika nchi hii na kuahidiwa kuishi kwa amani na starehe, bado mmediriki kufanya mambo yasiyoeleweka. Mnapita kuua watu wasio na hatia bila sababu yoyote. Naamini huo ni ushauri wa huyu mwendawazimu uliyefuatana naye. Unafahamu alikokimbilia?”

    “Sifahamu…”

    “Amekutoroka,” Iron alidakia. “Amekutoroka. Bila shaka hivi sasa anajaribu kuitoroka nchi. Hafiki mbali. Dakika yoyote ataletwa hapa akiwa hai au maiti,” alimaliza akimkazia macho Nuru. Macho yake yalikumbuka alichohitaji. Akazisahau hasira zake dhidi ya Joram na kumnong’oneza Nuru kwa sauti ambayo kwake ilijaa upendo. “Suala lako ni tofauti bi mdogo. Una nafasi nzuri ya kusamehewa madhambi hayo iwapo tu… iwapo…”

    Mara Iron alijikuta hajui lipi zaidi amwambie Nuru. Hakuwa hodari wa kutongoza. Ingawa alisoma riwaya nyingi za mapenzi, lakini ilikuwa vigumu sana kila alipotamani kuyaweka aliyoyasoma katika vitendo. Sababu moja kati ya nyingi zilizomfanya hadi leo awe hana mke ni hiyo ya kutojua kuwakabili wanawake wote aliowahitaji walikuwa kama wanaomdhihaki kwa kusubiri aseme nini. Wale ambao hakuwataka ndio waliojileta kwake kwa urahisi. Alipolewa hakubabaika kuwalaki. Lakini leo, kichwani akiwa hana hata tone moja la pombe, hakuona vipi ampate Nuru. Akaduwaa akimtazama.

    Nuru aliuhisi unyonge huo. Akaamua kusubiri.

    Nusu dakika ilipotea kabla ya Iron kujua aseme nini. Kisha alikumbuka kuwa alikuwa na akiba nzuri ya vinywaji vikali. Akafungua kabati na kutoa chupa moja ya John Walker ambayo aliimimina katika glasi. Alimkaribisha Nuru ambaye alikataa. Akaimimina tumboni mwake. Glasi ya pili ilimchangamsha. Akarudisha vifaa hivyo katika kabati na kumsogelea Nuru na kumgusa bega huku akinong’ona kwa sauti ambayo kichwani mwake alihisi imejaa mahaba. “Wewe ni msichana mzuri sana wa Kiafrika. Sijapata kumwona mwingine wa aina yako.” Mkono wake ukagusa pale ambapo ngozi ya bandia ya Uzungu aliyoivaa Nuru ilikuwa imebandukabanduka kwa purukushani. Akaishika na kuibandua. Gundi nyepesi iliyotumiwa kuiambatanisha ngozi hiyo ya nailoni na mwili iliacha mabaka meupe. Lakini nyuma ya mabaka hayo ulijitokeza uso mzuri, uso asilia wa Nuru. “Wewe ni mzuri kama ulivyo. Huhitaji kabisa ngozi hii,” Iron alisema akizidi kuzibandua ngozi sehemu za mapajani.

    Sasa aliyesimama mbele yake hakuwa tena yule msichana wa Kizungu. Alikuwa msichana wa Kiafrika, msichana mzuri, ambaye kwa muda, uzuri wake ulimpumbaza kaburu Iron. Kisha tamaa ikamzidi nguvu, mikono yake ikapoteza utulivu na kuanza ziara kutambaa katika mwili wa Nuru. Mara ulimi wake ukaanza kudai njia katika kinywa cha Nuru, huku akitweta kwa nguvu na kunong’ona maneno ambayo Nuru hakuyaelewa. Hakutofautiana na sokwe mweupe aliyeonjeshwa asali.

    Kila kitendo cha Von kilizidisha hasira katika moyo wa Nuru. Mikono hiyo ilipoyafikia matiti yake na kuyachezea, akahisi kama aliyeguswa na kinyaa ulimi ulipokuwa ukibishana na meno yake ukitafuta mwanya wa kuingia mdomoni mwake, aliona kichefuchefu. Ambacho alitamani kufanya ni kutumia fursa hiyo kuachia pigo ambalo lingeondoa uhai kisha kutafuta fursa ya kutoroka. Hata hivyo, hakuthubutu kufanya hivyo kwa kuchelea kuharibu mambo. Hakukoma kuitazama saa kubwa iliyokuwa ukutani. Kila dakika iliyopita alikuwa akisheherekea kimoyomoyo. Sasa ilikuwa imebaki kama saa moja tu kabla ya mitego waliyoitega kufyatuka. Wakati huo asingekosa mwanya wa kutoroka. Kabla ya hapo alihitaji kuubembeleza muda kwa bei yoyote.. isingemgharimu chochote kuendelea kuliruhusu jitu nene liendelee kujipumbaza katika mwili wake. Mara moja mbili akaguna na kutetemeka kwa namna ya kumfanya aonekane kama aliyeshikwa na ashiki.

    Kitendo hicho kilichochea wazimu wa Iron. Mara akapambua mavazi ya Nuru. Mikono yake iliyokuwa ikitetetemeka iligombana na vifungo vya mavazi huku akizidi kunong’ona hili na lile. “Sikiliza…” Nuru alimweleza akiushika mkono wake na kuutoa mapajani mwake huku akimfinyafinya. “Hapa ni ofisini. Mtu yeyote anaweza kuingia…”

    “Hii ni ofisi yangu,” Von alikoroma. “Hamna anayeweza kuingia bila ruhusa yangu.”

    “Sio vizuri.”

    “Tafadhali…” kisha Von alijilaumu kwa kutamka neno hilo. Vipi amtafadhalishe mtu mweusi? Zaidi, mtu ambaye roho yake iko katika mikono yake. Akaupeleka mkono wake wa pili katikati ya mapaja ya Nuru kwa nguvu kidogo. Nuru aliyabana mapaja yake. Ni hapo Von alipokumbuka kuwa isingekuwa kazi ndogo kumtenda msichana huyu bila hiari. Hakuwa amezisahau zile picha za sinema ambazo huonyesha jasho linavyowatoka watu wanaojaribu kunajisi. Wala asingesahau yaliyosemwa katika kile kitabu cha mapenzi alichowahi kusoma, “… hicho ni kitu pekee ambacho mwanamke ana mamlaka nacho… kitu pekee anachoweza kujivunia… rasilimali yake pekee…” hivyo, akajikuta akilazimika kutumia njia nyingine. “Una habari kuwa maisha yako yamo mikononi mwangu? Dakika yoyote nitakayosema ufe utakuwa marehemu. Najaribu kukuokoa kwa kuwa sioni kama unastahili kufa mapema kiasi hiki,” alimweleza Nuru.

    “Nitajuaje kama hunidanganyi? Nitajuaje kama baada ya kumaliza shida zako hutaniua?” Nuru alisema akimlegezea macho.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nakuhakikishia kuwa utakwenda zako kwa amani na furaha kokote unakotaka kwenda.” Von alipoona hajaaminika kikamilifu alimwacha Nuru kwa muda na kuliendea kabati ambalo alilifungua na kutoa bahasha kubwa. Ndani ya bahasha hiyo mlikuwa na pesa nyingi za nchi mbalimbali. “Hizi ni pesa zenu. Ni miongoni mwa vitu vyenu mlivyonyang’anywa mlipofika hapa. Sasa hivi nakukabidhi pesa hizi ukae nazo ili utakapoondoka zako ukaishi popote unapotaka.” Alimpa Nuru na kuziweka katika mfuko wake. Alikuwa akicheka kimoyomoyo akifahamu kuwa mara baada ya kuimaliza hamu yake na kumwua Nuru angezirejesha fedha hizo katika himaya yake. “Sasa tunaweza kuendelea,” alisema akianza upya kuchezea mwili wa Nuru.

    Nuru hakumzuia mara moja. Alikuwa hajafahamu atumie hila ipi kumchelewesha tena. Safari hiyo kilichomwokoa Nuru ni king’ora kilichotoa mlio wa aina ya paka aliyekabwa koo katika moja ya mitambo ya Von. Sauti hiyo ilimfanya Von aruke hadi kwenye simu ambako aliichukua na kusikiliza kwa makini. Sauti nyembamba ilisema kwa wasiwasi, “Bosi, inaelekea kuna jambo la hatari katika mtambo maalumu. King’ora cha hadhari kimekuwa kikilia kwa muda mrefu. Simu za walinzi wetu huko hazipokelewi.”

    “Impossible,” Von alifoka. “Unataka kuniambia kuwa maafa yanayotokea mjini yanaweza kuhamia huko nje ya mji?”

    “Inaelekea, mzee. Kwa sababu huyu mtu anayeitwa Joram haelezeki. Aweza kuwa huko sasa hivi.”

    “Impossible,” alifoka tena. “Na kama kweli kaenda huko, basi kajipeleka mwenyewe kaburini.” Von alisita kidogo. Kisha aliongeza, “Sikia. Andaa helikopta yangu na dereva. Nataka kufika huko mara moja. Nataka kushuhudia kwa macho yangu mwenyewe mtu huyo anayejiita Joram Kiango anavyosulubiwa.

    ***

    Huko angani Nuru aliziona vizuri kabisa maiti nne za askari wa Makaburu zilizovalia magwanda na silaha zao mikononi. Zilikuwa zimelala sakafuni mbele ya lango kubwa la chuma ambalo lilizunguka ua wa seng’enge uliozunguka jumba kubwa. Helikopta ililizunguka jengo hilo mara tatu, Von akitazama kwa darubini huku na kule. Aliporidhika alimwamuru rubani kutua kando ya ua huo katika kichaka kilichoutenga mtambo huo na mji.

    Kutoka mjini hadi hapa, ilikuwa safari ya dakika mbili tatu tu. Kabla ya kuanza safari hiyo Von alitupiana maneno makali na msaidizi wake ambaye alishangazwa na uamuzi wa Von kumpeleka Nuru huko. Alimwambia, “Sikubali kabisa. Nadhani ni wewe mwenyewe uliyeweka sharia ya kupigwa risasi mtu yeyote atakayekaribia mtambo ule, awe raia wa nchi au mgeni. Vipi aende huyu ambaye tunamhisi kuwa ni mwenzi wake ambaye amefika huko kufanya mashambulizi?”

    “Huyu ni mateka wangu,” Von alimjibu. “Bado nina mengi ya kumsaili. Zaidi ya hayo, kama kweli Joram yuko huko tutamtumia huyu kumfanya Joram asithubutu kuendelea na chochote anachoota kichwani mwake.”

    “Bado sikubali,” msaidizi huyo alieleza. “Nimeandaa kikosi cha askari wanne ambao ungefuatana nao huko. Kadhalika, nilikuwa nikisubiri amri yako ili nitumie askari wengine hamsini kwa gari. Inaelekea yote niliyofanya ni bure.”

    “Ni bure kabisa,” Von alimjibu. “Unajua kabisa kuwa mtambo ule unalindwa katika hali isiyo na shaka kabisa. Hata kama atafanikiwa kuingia ndani hawezi kabisa kufanya madhara yoyote. Baada ya juhudi zake zote ataambulia kufa tu. Hivyo, nakushauri urudi na hao askari wako uliowaandaa. Nitakwenda mimi, huyu mateka na dereva tu. Sawa?”

    Msaidizi huyo alimtazama Von kwa hasira ya mshangao. Alizithamini sana hekima zake katika masuala yote ya kiusalama katika nchi hii miaka yote aliyokuwa naye. Lakini vitendo vyake saa chache zilizopita vilimchanganya kabisa. Vilikuwa vitendo ambavyo havikubaliki. Yeye, kama mtu wa pili katika usalama wa utawala huu, hakuona kama alistahili kumtii Von hata kwa hilo. Hivyo, alimtupia jicho la hasira na kumwambia, “Kwa mara ya kwanza nitafanya kinyume cha matakwa yako.”

    “Na kwa mara ya kwanza nakuambia kuwa… kuwa… hufai kufanya kazi chini yangu. Baada ya suala hili nitaangalia suala lako,” Von alisema akimsukumiza Nuru katika helikopta na kumwamuru rubani kuondoka.

    Hata hivyo, rohoni alikuwa na mashaka kwa uamuzi wake huu. Alijua kabisa kuwa alikuwa akifanya kosa kubwa kufuatana na Nuru huko aendako. Hata hivyo, alifahamu fika kuwa hii ilikuwa nafasi yake pekee ya kufanya naye mapenzi na baadaye kumwua. Kimojawapo cha vyumba kadhaa katika jengo la mtambo huu kilikuwa chumba maalumu cha faraja kwa ajili yake na wakubwa wachache sana. Chumba hicho kilikuwa na mitambo ya televisheni, ambayo ilitumia nguvu ya setilaiti yao hiyo iliyoko angani kuitazama miji mbalimbali ya Afrika kinaganaga. Vilevile kulikuwa na chombo maalumu ambacho kinaweza kutazama shughuli zote zinazofanyika katika chumba hicho. Mara kwa mara Von hujifungia humo na kutazama utendaji kazi wahandisi bila ya wao kuwa na habari. Mhandisi mmoja aliwahi kupoteza kazi na maisha yake baada ya kushukiwa na Von kuwa alikuwa na dhamira mbaya kwa mtambo huu. Hivyo, kifo chake machoni mwa watu wengi kilionekana kama ajali tu iliyosababishwa na dereva mlevi kugonga mtu anayetembea kando ya barabara katika mitaa ya Johanesburg. Leo Von alitegemea kukitumia chumba hicho kujistarehesha na mwili wa Nuru kabla ya kutulia na kuanza kuangalia kwa furaha watu wanavyoteketea kwa moto katika miji ya Dar es Salaam, Lagos, Lusaka, Harare na kwingineko.

    Furaha iliyokuwa ikichemka katika fikra za Von iliingia nyongo mara baada ya helikopta yake kupita juu ya jengo hilo na kushuhudia walinzi wake walivyolala ovyo wakiwa maiti. Hivyo, akamtupia Nuru jicho la chuki. Tamaa aliyokuwanayo dhidi yake ilianza kuyeyuka na nafasi yake kuchukuliwa na hasira kali. Alitamani ammalize papo hapo na kuyasahau yote aliyokuwa akiyawaza juu yake. Hata hivyo, wazo jingine lilimjia akilini. Nuru alionekana katili sana ambaye haogopi kifo kama wanawake wengine anaowafahamu. Hata hivyo, anaweza kufa baada ya kutaabika sana. Hakuna mateso ambayo yatamtaabisha zaidi ya kushuhudia kifo cha mpenzi wake, Joram Kiango. Akiwa na hakika kabisa kuwa Joram alikuwa maala fulani katika jengo hilo akifa au kusubiri kifo, Von alitoa bastola yake na kuigongagonga katika kisogo cha Nuru. “Twende,” alimwamuru, baada ya kumtaka rubani asubiri katika helikopta.

    Nuru alitelemka na kufuata maelekezo ya Von. Waliipita miili ya marehemu waliolala ovyo, damu ikivuja kutoka katika majeraha ya risasi miilini mwao.

    Von alimshangaa Joram, peke yake, aliwezaje kuwaangamiza askari wengi kiasi hicho bila wao kufanya lolote. Lakini haikumshangaza Nuru hata kidogo. Wala Nuru hakuhitaji kusimuliwa. Akiwa mtu anayemfahamu Joram na hila zake nyingi alijua kuwa alitumia njia moja au nyingine kuwafikia askari hao waliojiamini kwa silaha zao aina ya machine gun. Baada ya hapo alitoa hati zake za bandia kuwaonyesha askari hao, hati ambazo zilifungwa kinamna kiasi cha kuhifadhi hewa ya sumu ambayo, bila shaka, iliwafanya askari kulewa ghafla na hivyo, kuwaua mmoja baada ya mwingine haikuwa kazi ngumu.

    Kilichomshangaza Nuru ni kutofahamu Joram alikuwa akifanya nini muda wote huo katika eneo la hatari kama hilo. Alikadiria kuwa dakika tano zingetosha kabisa kuuteketeza mtambo huo na kutoweka. Na kwa mujibu wa ramani yao ndani ya kiwanda hicho hamkuwa na ulinzi wowote zaidi. Vipi asitokee na kummaliza mtu huyu mnene ili waondoke zao?

    Von hakumpa nafasi ya kuwaza zaidi. Alikuwa akimsumbua mbele kwa mtutu wa bastola yake harakaharaka. Nuru hakuwa mzito wa kuelewa kuwa Von alikuwa akimtangulia kwa dhamira ya kumfanya ngao endapo lolote lingetukia kinyume na mategemeo yake.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya kukagua vyumba mbalimbali wakafika katika chumba cha Von. Ukiondoa makochi na kabati lililojengwa ukutani chumba hicho hakikutofautiana na maabara au studio ya aina yake machoni mwa Nuru. Mashine na mitambo mingi ilikuwa imepangwa kwa tafsiri fulani, kuta zikiwa screen zilizopangwa katika hali ya kupokea habari mbalimbali. Von aliisogelea mashine moja ambayo machoni mwa Nuru ilikuwa kama kompyuta na kubonyeza swichi ainaaina. Kioo katika ukuta mmoja kilipata uhai na kuanza kuonyesha mambo ya ajabuajabu. Baada ya hali kutulia Nuru aliona kuwa walikuwa wakitazama chumba baada ya chumba katika jengo hilo. Kilitokea chumba ambacho kilikuwa na mitambo mingi ya kutisha. Chumbani humo Nuru aliwaona wahandisi watatu waliokuwa makini wakichapa kazi ya kuongoza mitambo bila dalili yoyote kuwa mambo yanakwenda mrama. Hilo lilimfurahisha sana Von. Akaangua kicheko kwa furaha. Ni yeye aliyependekeza kuwa kwa usalama wa mitambo ishara za hatari zisiwafikie wahandisi hao, wasije wakapata hofu na kusababisha setilaiti iliyoko angani kukosa uongozi wa ardhini, jambo ambalo lingeweza kusababisha maafa na hasara isiyokadirika. Kwa jinsi jengo hilo lilivyoandaliwa Von alikuwa na hakika kabisa kuwa ingemhitaji binadamu mwenye moyo wa malaika kuwafikia wahandisi hao na kuuharibu mtambo huo. Joram hakuwa na moyo huo. Ni hilo lililomtia nguvu. Sasa ameamini kuwa hakukosea. Kwa muda, aliwatazama wahandisi hao wanavyoshughulikia. Wakijua kuwa leo ilikuwa siku ya kazi kubwa walifanya kila kitu kwa juhudi na umakini wa hali ya juu. Kisha Von alibonyeza sehemu nyingine. Chumba hicho kikahama na vyumba vingine kuanza kupita katika kioo.

    “Nataka tumwone mpenzi wako anavyokufa au alipofia,” alimweleza, tabasamu la kifedhuli likiyasindikiza maneno yake. “Keti tafadhali. Keti ili uone kwa starehe.”



    *****SURA YA KUMI NA MOJA*****



    KIOO kilionyesha vyumba mbalimbali ambavyo vilijitokeza na kupita. Kila chumba kilikuwa na vitu mbalimbali vilivyoyavuta macho ya Nuru. Lakini ilielekea kuwa havikuwa vyumba Von alivyovihitaji. Aliuendesha mtambo huo harakaharaka kwa kubonyeza kidude hiki na kile kama karani anayepiga chapa. Mara kilitokea chumba ambacho Von alikuwa akikitafuta. Katika chumba hicho, ambacho kilionekana kidogo, walikuwemo watu wawili waliokuwa wakipigana. Mmoja hakuwa mtu bali jitu. Lilikuwa pande la mwanamume, refu, nene, jeusi lenye magumi manene na macho ya kutisha. Lilikuwa likipigana kwa maguvu yote katika hali ambayo ilionyesha kuwa lilikusudia kuua kwa mikono. Jitu hili halikuwa na dalili yoyote ya uchovu wala maumivu yoyote. Kinyume kabisa cha mtu wa pili ambaye lilikuwa likipambana naye. Huyu alikuwa kijana wa kizungu, mwenye dalili zote za ushujaa na ufundi wa kupigana ngumi na karate. Lakini ufundi wake haukuwa na dalili yoyote ya kuonyesha kulishinda jitu hili kwani tayari kijana huyo alikuwa akivuja damu hapa na pale katika majeraha ya kutisha, huku akiwa na dalili za uchovu mkubwa.

    “Unaona?” Von alisema akicheka. “Mpenzi wako yuko mashakani. Wakati wowote ataaga dunia. Hajatokea binadamu aliyewahi kumshinda Toto na kukivuka chumba kile akiwa hai.”

    “Kwanza Nuru hakuelewa. Kisha akaelewa. Kijana wa kizungu aliyekuwa akipambana na jitu hilo la kutisha hakuwa mwingine zaidi ya Joram Kiango, akiwa bado katika hali ya Uzungu bandia. Moyo ulimdunda Nuru kwa hasira kuona akiwa ameketi hapa, juu ya kiti cha starehe, hali Joram anateseka peke yake. Akamgeukia Von kutazama uwezekano wa kumwua na kwenda kumsaidia Joram Kiango. Alikutana na macho makali ya Von ambayo yalimtazama katika hali ya kuyasoma mawazo yake kinaganaga. Bastola yake ilikuwa imara mkononi, ikimwelekea Nuru kifuani. Nuru hakuwa na la kufanya zaidi ya kuyarejesha macho yake katika screen na kulitazama pambano hilo lilivyokuwa likiendelea. Kichwani alikuwa akijiuliza kwa mshangao ni jitu la aina gani hili, kubwa kupindukia, jeusi kupindukia lenya nguvu kupindukia ambalo, badala ya kutumia maguvu hayo kupambana na utawala dhalimu wa makaburu bado, linawatetea kiasi hiki?

    Alijilazimisha kutulia na kuendelea kulitazama pambano hilo la kutisha. Joram alibadili mbinu mbalimbali, akikwepa kiufundi karibu kila konde lililotupwa na jitu hilo, pamoja na kulipachika makonde mazito. Lakini haikusaidia. Joram hakuweza kupita chumba hicho kukiendea chumba cha pili ambako angeifikia mitambo aliyokusudia kuilipua. Kwa muda, Nuru alimwona Joram kama mtu aliyekata tamaa, akifikiria kuitumia bastola yake ambayo bila shaka ingewaweka tayari wahandisi aliokuwa akiwanyatia au kurudi alikotoka. Hapana, alimwona vizuri zaidi. Joram alikuwa akiwaza kwa makini huku akilitazama jitu hilo ambalo lilitulia kimya, likimsubiri kwa utulivu kama ambalo halikuwa na uhusiano wowote na matukio yote yaliyokuwa yakitendeka. Baada ya kulitazama sana jitu hilo Joram alifuta jasho na damu iliyojaa usoni mwake na kutamka maneno fulani ambayo hayakuwafikia Nuru na Von. Alitamka neno jingine.

    Jitu hilo lilitulia kama lililosikia lugha yoyote ya dunia. Joram alipolisogelea hatua moja lilikaa tayari kwa mapambano. Aliposogea hatua ya pili lilirusha ngumi nyingi mfululizo. Joram akarudi nyuma na kuangua kicheko. Kicheko chake kilipokelewa na Von Iron ambaye alikuwa akilitazama pambano hilo kwa furaha. “Naanza kumheshimu mpenzi wako. Tayari amegundua kuwa hapigani na binadamu wa kawaida.”

    Nuru alijikuta akijiuma mdomo kwa hasira. Kwa nini muda wote huo alikuwa hajagundua hilo? Joram alikuwa hapambani na binadamu. Alikuwa akipambana na jitu lililoundwa kwa mkono wa binadamu katika umbo la binadamu, yaani robot. Aliwahi kusikia kuwa matajiri wengi wamekwishaanza tabia ya kuyaweka madude haya kama walinzi wao badala ya binadamu wa kawaida ambaye hutokea siku akakukimbia au kukugeuka.

    “Sasa tuone atafanya nini,” Von alikuwa akisema.

    Nuru aliyafuata macho yake kumtazama Joram ambaye alionekana akiacha kujisumbua kupambana na jitu hilo na kuchungulia kwa makini, alifunua hiki na kile. Pilikapilika zake hizo zilimwezesha kufunua mahala ambapo kulikuwa na waya ainaaina hadi alipoona jitu hilo likijiweka sawa kama askari katika gwaride. Kisha lilianguka kifudifudi.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nuru alishangilia kimoyomoyo. Kwa mshangao alimwona Von akishangilia vilevile. “Ana akili. Amegundua kuwa dude hilo linaendeshwa kwa nguvu ya sumaku ya umeme ambayo mitambo yake iko pale alipofunua. Ana akili…” Von alisema katika hali hiyo ya kushangilia. Alizidi kucheka. Nuru alizidi kushangaa kwa kutomwelewa hadi alipoongeza, “Ana akili ndiyo. Lakini zitamsaidia nini? Kwa kweli, jitu lile lina huruma sana. Muda wote huu lilikuwa likimrudisha kwa makonde ili asiende kujiua mwenyewe. Sasa mtazame. Ona mpenzi wako anavyojiua… Ona…”

    Roho ikiwa juu Nuru, hakuwa na la kufanya zaidi ya kutazama. Alimwona Joram akitazama saa yake na kuanza mwendo wa haraka kukiendea chumba alichokuwa akikihitaji. Mwendo wake ulikuwa wa hadhari na uhakika, macho yakiwa wazi, mikono tayari kwa lolote ambalo lingetukia. Mara aliufikia mlango wa mwisho, uliomtenga na lengo lake. Alinyoosha mkono na kugusa kitasa. Papo hapo ardhi miguuni mwake ilifunuka na Joram kudidimia ghafla. Juhudi zake za kushika kando hazikuzaa matunda yoyote. Ardhi ilijifunika kama ilivyokuwa na Joram kupotea kama ndoto iliyofikia ukingoni.

    “Tayari…” Von alichekelea.

    Nuru alijikuta yuko wima mbele ya Von akinyoosha mikono kumpiga huku akifoka, “Yuko wapi Joram? Sema yko wapi?...”

    Pigo la kitako cha bastola ambalo lilitua barabara kichwani mwake lilimpoteza fahamu. Fahamu zilipomrudia alikuwa amelazwa chali juu ya kochi alilolikalia awali. Alikuwa uchi kama alivyozaliwa, mavazi yake yaliyochakaa yakiwa yametupwa kando. Von alikuwa kaketi palepale alipokuwa, sigara mdomoni. Macho yake yalimtazama Nuru kwa namna ya mtu aliyekuwa ameikata kiu yake ya muda mrefu. Nuru alimtazama kisha akajitazama na kuona alivyochafuka. Hakustahimili. Aliinuka na kumwendea Von kwa nia ya pambano jingine. Lakini hakumfikia. Hatua mbili alizozipiga zilimfanya ashindwe kuendelea na badala yake kuanguka sakafuni. Hata hivyo, mdomo haukuwa na udhaifu kiasi hicho.

    “Wewe ni mshenzi kuliko washenzi wote niliopata kuwaona,” alifoka. “Mwanaume hayawani… Haya unasubiri nini? Niue kama ulivyomwua Joram. Niue…”





    Von alitabasamu kifedhuli. Kitendo cha mapenzi ambacho kilimchukua dakika moja, Nuru akiwa hana fahamu, kiliupa moyo wake faraja kubwa. Hakutegemea. Mara akawa ameelewa kisa cha baba yake kupoteza maisha kwa ajili ya msichana mweusi. Hata hivyo, baada ya kuionja ladha aliyohitaji sana alianza kuiona athari ya kumwacha kiumbe huyo aendelee kuwa hai. Mapambano aliyoyaona baina ya Joram na robot yalikuwa yanatosha kabisa kumwonyesha watu hawa walivyo wapiganaji wasiokata tamaa. Joram amekwisha, lakini huyu japo ni mwanamke yungali hai, na anaweza kufanya lolote. Kifo cha haraka alichokidai kilikuwa halali yake kabisa.

    Hata hivyo, angehitaji kumwona akifa kwa mateso zaidi. Angependa kuona tena anavyotaabika kushuhudia mji wao mashuhuri wa Dar es Salaam unavyoteketea. Angependa kuuona uso wake ukijaa hofu na majonzi kama ulivyofanya wakati Joram alipokuwa akiadhibiwa na robot Toto, na hasa pale alipodidimia ardhini.

    “Ungependa kufa sasa hivi au baadaye kidogo?” aliuliza bila mzaha wowote katika sauti yake. “Saa moja na dakika chache baadaye kioo, ambacho kilikuwa kikionyesha mchezo wa ngumi baina ya mpenzi wake na Toto, kitaonyesha mchezo wa kupendeza zaidi. Jiji lenu la Dar es Salaam na miji mbalimbali ya Tanzania na nchi nyinginezo, litapata sura mpya, sura ya kupendeza. Natumaini ungependa kuliona hilo pia kabla hujafa ili upate habari ambayo utamsimulia Joram huko kuzimu alikotangulia.”

    Nuru, nguvu na fahamu zikizidi kumrejea, aliufurahia uamuzi wa Von. Aliyakumbuka maneno fulani ya Joram, kati ya mengi aliyokuwa akimpa, aliposema: katika mambo haya, kila dakika ambayo inaweza kukuweka hai zaidi inunue kwa bei yoyote. Aliamua kuafikiana na Von. Wazo hilo hasa lilimjia baada ya kukumbuka kuwa, kama walichofanya ni kitu chenye uhakika, dakika chache kuanzia sasa jiji la Johanesburg litakuwa mashakani na Von atakuwa akisema mengine. Nafasi kama hiyo itakapowadia asingeshindwa kuitumia.

    Hivyo, alijifanya mnyonge zaidi. Akajiweka kitini hapo katika hali iliyotosha kumsumbua mwanamume yeyote. Von alikwisha timiza Fula yake ya kimwili kwa Nuru. Hata hivyo, Nuru alijua fika kwamba, kutokana na tabia ya roho ya Fula ya mwanaume; dakika chache baadaye angerudiwa na Fula ileile kwa kiwango kikubwa zaidi.

    “Wewe ni mshenzi…” alimchokoza tena ili atazamwe wakati huohuo akiyalegeza macho yake na kuzidi kujiweka juu ya kochi kinamna fulani.



    *********

    Kitu hiki ambacho asili kiliwekwa baina ya mwanaume na mwanamke, kitu ambacho hakielezekai kikamilifu kwa maneno, kilitimiza wajibu wake. Nuru alibaini kuwa Von na ukatili wake, pamoja na kuamini kwake kuwa ametosheka na kukinai, alianza upya kutaabika. Macho yake hayakuweza tena kutulia, mikono yake ilikuwa haikai pamoja. Alihangaika, akienda hapa na pale na kushika hiki na kile. Tahamaki akawa ameketi kochi moja na Nuru, mkono wake mmoja ukikosa kochi na kuangukia juu ya paja nono la Nuru.

    “Wewe ni mtu mbaya sana,” Nuru alisema, sauti ikiwa laini, huku akijitia kusogea kando kidogo.

    “Sikiliza…”

    Nuru alijitia kumsikiliza. Alichofanya hasa ilikuwa kuupima uwezekano wa kumzidi Von maarifa aikwapue bastola yake ambayo ilikuwa imara kama hirizi katika mkono wake wa pili.

    Von hakuwa mgeni kwa silaha hii ambayo ilikuwa ikitumiwa na Nuru. Alifahamu fika kuwa msichana huyu alikuwa akitumia mbinu ili ayaokoe maisha yake. Lakini kufahamu huko hakukukata shauku yake ya kutamani tena. Alitamani tena, kwa mara ya mwisho. Nuru angefanya nini? Kama kuna kisu basi Nuru alikuwa ameshika makali yake yeye akiwa ameshikilia mpini. Hata hivyo, alijua kuwa anacheza mchezo hatari, anacheza na nyoka. Haikuwa busara kuchezea roho kando ya shimo la mauti lililowazi kiasi hicho. Ni hilo ambalo lilimfanya aendelee kuishikilia bastola kama roho yake.

    Wakati huo Von alikwishaibonyeza mitambo yake ambayo alisema ingemwezesha kuiona setilaiti hiyo ikishuka taratibu toka angani na kuiendea anga ya Tanzania ambapo ingesubiri muda uliopangwa kabla ya kuanza kuachia dhoruba za hewa ambayo ingezusha moto wa kutisha. Katika kioo hicho waliweza kuyaona mawingu mazitomazito yakipita katika kioo. Kisha dude la ajabu likajitokeza. Lilikuwa kubwa, jeusi lenye muundo wa ndege aina ya kunguru. Lilikuwa likisafiri kwa mwendo mkali sana kama linaloifuata televisheni hiyo.

    Von aliinuka ghafla huku ameshikwa na mshangao. Aliiendea meza iliyokuwa na chombo chenye vidude vingi alivyokuwa akivibonyeza na kuvikagua kwa makini. Alibonyezabonyeza na kutazama tena katika kioo. Alikuwa kama ambaye hakuyaamini macho yake kuliona dude hilo likizidi kusogea. Mara jiji la johanesburg likajitokeza katika kioo hicho, majumba fulanifulani makubwa yakitoa nuru nyekundu kama gari linaloonyesha linaelekea upande upi. Nuru hiyo ilipokelewa au kujibiwa na dalili hiyo ya moto kutoka katika domo la chombo hicho ambacho sasa kilikuwa kikielea juu ya mji.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nuru aliyaelewa majumba yote hayo ambayo yalionyesha alama za moto. Ni yale ambayo yeye na Joram walifanikisha kutega vile vigololi walivyovipata kutoka kwa hayati Chonde. Akaitazama saa yake. Ilikuwa ikikaribia muda uleule ambao Joram alikuwa ameviandaa vidude vile kufanya kazi. Alitamani apige ukulele wa furaha. Tangu walipoanza harakati hizo hakuwa na hakika kama walikuwa wakifanya kitu chenye uhakika. Wala hakumwona Joram kuwa na hakika hiyo, pamoja na kufunua majitabu mengi ambayo yalikaribiua kumtia wazimu. Kumbe alijua anachokifanya! Ndoto yake imetukia kuwa kweli.

    Wakati Nuru akifanya sherehe hiyo moyoni, Von alikuwa akitaabika kichwani. Hakuelewa kinachotokea. Dalili zilizojitokeza zilikuwa za kutisha kabisa, zisizokubalika. Ilionyesha kuwa wakati wowote mji wa Johanesburg ungekuwa ukiwaka moto, Johannesburg badala ya Dar es Salaam, aliwaza kwa hasira. Haikuwepo njia nyingine ya kufanya zaidi ya kuamuru setilaiti hiyo iharibiwe na kuanguka. Si kitu ikiangukia mji na kuua watu kadhaa. Heri nusu shari kuliko shari kamili. Ni hilo alilokusudia kufanya, kuinua simu na kuwapa wahandisi amri hiyo.

    Hilo pia hakuweza kulifanya. Alijikuta akitazamwa na bastola yake mwenyewe, ambayo alihisahau kando alipokuwa akihangaika na mitambo. Bastola ilikuwa imara mikononi mwa Nuru, macho yake yasiyo na mzaha yakitangaza shari. “Pokea chako, mwuaji mkubwa,” Nuru alinong’ona akifyatua bastola.

    Kwanza Von hakusikia maumivu. Alihisi kitu kikipenya kifuani na kuupapasa moyo wake. Kisha alisikia moyo ukiwaka moto. Akahisi kifo. Alipiga ukelele wa nguvu akichupa kumwendea Nuru mikono yake ikiwa wazi, tayari kumkaba koo. Lakini Nuru alimwepuka kwa urahisi na kumwongezea risasi nyingine ambayo ilimfumua fuvu la kichwa chake. Akadondoka chini na kulala kwa utulivu kama nguruwe aliyechunwa kwa maji ya moto.

    Nuru aliyatazama matokeo ya kazi yake harakaharaka. Akaibusu bastola hiyo. Kisha akafanya haraka kujivika mavazi yake. Baada ya hapo alikimbilia kabati la Von ambalo alilifunua na kuanza kupekuapekua harakaharaka. Alipata alichokitaka. Ilikuwa ramani ya jengo hilo, ikiwa tofauti na ile waliyoitumia awali. Aliisoma himahima, kwa makini, kisha akaiweka mfukoni na kuuendea ukuta ambao ulikuwa na funguo nyingi. Akazichukua na kuziweka katika mfuko wake. Kisha, bastola ikimtangulia, alitoka chumbani humo mbio kama miguu yake ilivyoweza kumruhusu.



    *********

    Kuanguka umbali wa zaidi ya mita ishirini kutoka angani hadi juu ya sakafu ngumu sio mchezo. Bila ya uhodari wake wa karate na sarakasi, kama Joram asingefikia kichwa basi angefikia mgongo na kuvunjikavunjika. Lakini alijitahidi kusahau uchovu na maumivu makali aliyokuwanayo, akaikusanya akili yake pamoja na kubingirika. Hata hivyo, fahamu zilimtoka kwa dakika kadhaa.

    Uhai ulipomrudia alifungua macho yake kwa taabu na kutazama pande zote. Aligutuka kujikuta akiwa amelala katikati ya mizoga mingi ya binadamu, baadhi ikiwa mifupamifupa, baadhi ikiwa imevimbiana, mingine ikiwa imeoza kabisa. Mara akapatwa na harufu kali ya kutisha, harufu ambayo iliambatana na mainzi mengi manene ya kutisha, ambayo yalikuwa yakirukaruka katika hali ya kushangilia mawindo haya rahisi. Licha ya mainzi hayo Joram aliwaona panya wakubwa mithili ya paka waliokuwa wakifanya karamu katika miili ya binadamu hao. Panya mmoja alikuwa akipita kumzunguka Joram huku akimtazama kwa namna ambayo ilionyesha kuwa alitamani kuanza kumla akiwa hai bado.





    Moyo ulimdunda Joram. Ingawa hakujua au kupata kuhisi hofu katika moyo wake lakini kitu fulani kilimpanda moyoni na kumtia hasira na kichefuchefu. Alihisi kama aliyeruka jivu na kukanyaga moto. Kama kufa kwa nini afe kifo kibaya kama hiki? Afe huku anaona? Huku analiwa na panya? Kwa nini asingeruhusu lile dude limwue?

    Kisha alijikaza kiume na kujikongoja kusimama wima. Ilikuwa baada ya kujikumbusha ule usemi wake wa mara kwa mara kuwa “Binadamu hufa kwa uzee, hufa kwa ajali, hufa kwa maradhi. Lakini kuna binadamu ambao hufa kwa uvivu vilevile, hasa katika shughuli hizi za upelelezi.” Wazo hilo lilimtuma aanze kutembeatembea humo akitafuta mwanya ambao ungeweza kumtoa nje ya kaburi hilo.

    Alizitazama kuta na kugundua kuwa zilijengwa kwa chuma cha pua, zikiwa kama chumba kirefu chenye upana wa mita kumi kwa ishirini. Akatazama juu, akiangalia uwezekano wa kupanda hadi huko alikoangukia. Ilikuwa ndoto nyingine. Ukuta ulikuwa laini mithili ya kioo ambacho kingemshinda hata paka.

    Afanye nini? Aketi kukisubiri kifo? Alijiuliza. Hapana, lazima ajitahidi kutafuta mwanya. Lazima kuna mahala pengine penye mlango unaotumiwa kuwaleta watu hawa kusubiri kifo. Akaendelea kutembea akiiruka mizoga na wakati mwingine kulazimika kukanyaga mifupa. Mainzi na panya vilimwongezea msukosuko kwa kukimbia hapa na pale, bila ya shaka kwa mshangao wa kuona mlo wao ukitembea ovyoovyo kwenda huko na huku.

    Joram alichunguza kila ukuta kwa makini. Hatimaye, aliufikia ukuta uliokuwa na mlango wa chuma uliofungwa kwa nje. Alijaribu kuutingisha mlango huo bila ya mafanikio. Ulikuwa mlango imara kama ukuta huo. Akautia mkono wake mfukoni na kuitoa bastola yake ambayo aliilenga mlangoni na kuifyatua. Risasi iliugonga na kuanguka ardhini kama gololi. Hata bomu lisingeubomoa mlango huo, jambo lililomfanya Joram aduwae kwa mara nyingine akifikiri la kufanya.

    Mara macho yake yakavutwa na maiti moja iliyokuwa ikitikisika. Akaisogelea na kuitazama kwa makini. Naam, ilikuwa na uhai mdogo mwilini mwake. Miguu yake ilikuwa imekatwa na Joram aliona vilevile kuwa jicho lake moja lilikuwa limeng’olewa. Huyu alikuwa mtu mweupe, kinyume cha wengi ambao walikuwa weusi. Bila ya shaka alikuwa Mrusi.

    “Pole,” Joram alimwambia.

    “Wewe ni nani?” mtu huyo aliuliza kwa udhaifu.

    “Itakusaidia nini kunifahamu?” Joram alimjibu. “Unakaribia kufa.”

    Mtu huyo alicheka kidogo kabla ya kujikongoja kusema polepole, “Kweli. Haiwezi kunisaidia chochote. Hata hivyo, naona wewe utakufa kabla yangu. Mwenzio hii siku ya kumi na nne bado naishi.”

    Joram hakuona kama kuna umuhimu wowote wa kuendelea kumsikiliza mtu huyo aliyekaribia kukata roho. Lakini hakukuwa na jambo muhimu la kufanya na akaendelea kumsikiliza. Haikuchukua muda kabla hajafahamu kuwa Mrusi huyo alikuwa mmoja kati ya watu wengi waliokuwa wakiuawa kinyama baada ya kushukiwa kuwa walikuwa wakifanya upelelezi dhidi ya utawala wa makaburu.

    Pango hili lilichimbwa maalumu kwa ajili ya kuwaangamiza watu hao kwa siri baada ya mateso mengi. Wengi waliachwa na kufa kwa majeraha waliyoyapata, lakini adhabu kubwa iliyowaangamiza ilikuwa njaa.

    “Usishanagae,” aliambiwa. “Ni njia pekee ya kutuwezesha kuishi.” Alipomwona Joram akizidi kushangaa aliongeza, “Au unaogopa kula maiti? Sikia, unaweza kunila nikiwa hai. Sina dalili ya kupona. Na ninavyokuona unaonyesha kuwa tuko pamoja katika kupambana na utawala huo haramu. Unaweza kunila ukaishi kwa wiki moja zaidi, pengine mwujiza utatokea nawe ukapona na kuendelea na pambano. Usiogope wala usinishukuru. Wala sitaki kujua wewe ni nani. Haitanisaidia.”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Joram aliona kama angerukwa na akili endapo angeendelea kuketi hapo akimsikiliza mtu huyo ambaye ilikuwa dhahiri kuwa uhai mdogo aliobakiwa nao ulikuwa mdomoni mwake tu. Akaondoka hapo taratibu na kuurudia mlango huo ambao alitulia tena akiutazama kwa makini.

    Bado hakujua angeweza kufanya nini kuufungua. Ingehitaji mwujiza. Harufu ya maiti hizo, kelele za panya na mainzi yaliyokuwa yakishangilia bahati zao, vilizidi kumsumbua. Joram alijua kuwa harufu na usumbufu huo vingemwua kabla hajasikia njaa.

    Aliutazama tena mlango kwa uchungu na hasira. Akatamani apige magoti na kumwomba Mungu ili afanye mwujiza mlango ufunguke. Hilo hakufanya. Ingekuwa unafiki kwani hakuwa amemwomba Mungu walao kwa kumshukuru kwa miaka mingi sasa. Vipi amkumbuke wakati wa shida? Na vipi ategemee mwujiza mkubwa kiasi hicho wakati enzi ya miujiza ilikwishapita? Hii ilikuwa enzi nyingine, enzi ya kutumia akili na nguvu.

    Bado hakuona kama alikuwa na lolote ambalo angeweza kulifanya kujitoa katika gereza hilo kwani kwa kila hali alijiona kama aliyefikia mwisho wa msafara wake kimaisha. Kwa mara ya kwanza alilaani bahati yake.

    Si kwa hofu wala uchungu aliyoipata katika gereza hilo ambalo halikutofautiana na kuzikwa hai. Hasa alijilaumu kwa kuikosa fursa ya kujionea kwa macho yake mwenyewe utawala wa makaburu na raia wake watakavyotaabika pindi mitego aliyoitega itakapofyatuka na silaha ambayo waliiandaa kuwateketeza watu wasio na hatia itakapowageukia. Joram, kama alivyo, hakuna ambacho kingemsisimua zaidi ya hilo. Aone macho ya mshangao yanavyowatoka wakubwa wa utawala na machozi yaliyochanganyika na kamasi yanavyowatiririka juu ya mashavu yao meupe. Aone majumba yao makubwa waliyoyajenga kwa jasho la wanyonge yakiteketea na kubomoka kama milima ya barafu. Na hatimaye, aone setilaiti yao ikianguka katikati ya mji wao baada ya mitambo inayoiweka angani kulipuliwa. Ndiyo.

    Ni hayo tu aliyoyahitaji Joram. Ni hayo ambayo yalimfanya ayahatarishe maisha yake kwa muda wote huu na hata kumwaga damu isiyo na hatia, ili, afanikishe dhamira yake. Hayo, kuyashuhudia kwa macho yake kungempendeza zaidi ya pesa na kumsisimua zaidi ya starehe. Kwa nini amekuwa hana bahati hiyo? Alijiuliza.

    Kisha alimkumbuka Nuru. Kiasi hofu ikamrudia alipojiuliza kama atafanikiwa kunusurika katika mapambano haya. Alikuwa amempa maelekezo yote muhimu na kusisitiza wakati gani aanze safari ya kutoroka zake endapo asingemwona.

    Bila shaka hakuna hatakayehangaika kumtafuta msichana mmoja ambaye hana tofauti na wasichana wengine wakati mamia ya watu yakiungua, maelfu yakikimbia kwa fujo na mamilioni yakiwa yamepigwa na butwaa, wakati majumba na viwanda vitakuwa vikiteketea kwa moto mkali ambao mfano wake haujapata kutokea katika historia ya nchi hii na dunia kwa ujumla, wakati chombo kisichoonekana kwa macho ya nguvu ya kawaida kitakuwa kikielea angani; na baadaye kuanguka; nguvu yake inayokifanya kielee angani na za madini inayokifanya kutoonekana zikiwa zimekwisha.

    Hapana, Joram hakuona kama Nuru angeshindwa kuitumia fursa hiyo. Bila shaka baada ya kumchanganya kwa hila alipokuwa akimfuata, atayafuata maelezo yote.

    Joram asingejisamehe endapo lolote lingemtukia msichana yule na kumpotezea maisha. Licha ya kwamba uzuri wa Nuru haukustahili kuharibiwa kwa mkono wa Kaburu yeyote katili, ushujaa wake ulikuwa nguzo ambayo Joram aliitegemea sana. Yote aliyoyatenda, hekima na juhudi za Nuru zilimsaidia. Mungu msaidie arudi salama, alimwombea.



    Utulivu aliokuwa nao pindi akiwaza hayo ulimfanya panya mmoja amrukie kifuani na kujaribu kumwuma. Joram alimkwepa na kuliachia teke dhaifu ambalo panya alilikwepa vilevile. Hata hivyo, panya huyo alimfanya ayatoe mawazo yake nje na kuyarudisha katika pango hilo la mauti. Harufu mbaya ya binadamu waliooza ikamrudia tena akilini na moyoni. Akajisikia kutapika lakini akajikaza kisabuni.

    Kisha alikumbuka kumtupia jicho jingine yule Mrusi. Akashangaa kuona kundi dogo la panya likiwa juu ya uso wake, wakimla. Kwanza alishangaa, kisha akaelewa. Mrusi huyo alikuwa amekata roho! Kichefuchefu kikamrudia tena Joram. Alitamani afumbe macho asiendelee kuona ukatili wa panya hao kumla mtu ambaye dakika chache walikuwa wakizungumza naye, mtu ambaye bila shaka ni mwema sana. Vinginevyo angewezaje kujitolea aliwe akiwa hai? Joram aliuliza.

    Ghafla mwujiza ulitokea.

    Joram aliuona mlango ukitikisika na hatimaye kufunguka. Yeyote ambaye angeingia Joram alitegemea kumlazimisha ama amwue kwa risasi ama amtoe chumbani humo. Hivyo, alisubiri kwa hamu akitazama kwa makini tayari kwa lolote, heri au shari.

    Bastola ilichungulia ikiwa katika mkono wa kike. Ilifuatwa na uso mzuri, wenye jasho na damu. Uso wa Nuru.

    “Joram?” alipiga ukelele wa furaha mara alipomwona Joram kasimama kando akimtazama.

    “Naweza kuyaamini macho yangu?” Joram alimwuliza akiwa bado amesimama palepale. “Wewe ni Nuru kweli au malaika?” aliongeza.

    Hakupata muda wa kujibiwa. Tayari Nuru alikuwa kifuani mwake kamkumbatia kwa nguvu huku akilia kwa sauti ndogo. Wakati ikimpambazukia Joram kikamilifu kuwa haikuwa ndoto – huyu alikuwa Nuru halisi aliyekuja kumwokoa – alianza kuinua mikono yake ili naye amkumbatie. Lakini Nuru tayari alikuwa amejitoa mikononi mwake na kumvuta nje harakaharaka huku akisema, “Twende zetu. Wakati umewadia.”

    Joram alimfuata kikondoo.

    Wakiwa nje baada ya kupigwa na hewa safi, fahamu zilimrudia Joram kikamilifu. Saa yake ilikuwa imevunjwa katika mapambano na jitu lile, aliitazama ya Nuru na kuelewa kwa nini aliambiwa wakati umewadia. Uhai ukamrudia mara moja rohoni, ingawa kimwili alikuwa bado dhaifu. “Niambie Nuru tafadhali. Niambie, mitego tuliyoitega haijafyatuka tu? Mji haujaungua?”

    Badala ya kumjibu Nuru alimwambia, “Sikiliza.”

    Kwa mbali mjini kulikuwa na kelele nyingi za hofu. Vilio na milipuko ya kutisha ilisikika kutoka katika kila upande. Walisikiliza kwa nusu dakika, kisha Joram alitabasamu na kusema polepole, “Nadhani inatosha. Wanakufa wenye hatia na wasio na hatia. Sasa iliyobaki ni ile kazi moja ya mwisho. Kuulipua huu mtambo.”

    Alimshika Nuru mkono na kuanza kukiendea tena chumba cha mitambo. Nuru, akiwa na ramani halisi ya jengo hilo, alimshauri Joram wapitie wapi. Dakika mbili baadaye tayari walikuwa wamewasili katika chumba hicho.

    Wahandisi watatu walikuwa chumbani humo, jasho likiwatoka kwa mshughuliko wa kutoelewa kinachotokea, hawakuweza kuwaona Joram na Nuru walioingia ghafla. Walipotanabahi walikuwa wakitazamana na bastola mbili. Wakaduwaa. Mshangao wao ulikoma pale risasi za mfululizo zilipopenya katika miili yao na kuwafanya waangukiane, damu zikiwavuja.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Joram aliikimbilia mitambo hiyo na kuanza kuikoroga kama alivyokusudia. Alipotosheka aliyatoa mabomu yake ya mkono na kuyatega sehemu mbalimbali za mtambo huo. Mara tu alipomaliza alimshika Nuru mkono na kutoka naye mbio.

    Nje ya jengo, kwa mbali, waliona moto mkali uliokuwa ukipaa angani kwa namna ya kutisha. Kisha waliona kitu kingine cha kutisha. Kundi la askari wenye silaha likija mbio kiwandani huko.

    Joram aliduwaa kidogo, akijiuliza wafanye nini. Kurudi ndani isingewezekana kwani jumba hilo pia lingelipuka wakati wowote. Na kukimbia ingewachukua hatua chache kabla ya kukamatwa na risasi za askari hao. Lakini Nuru, alijua la kufanya. Alimwongoza Joram katika upenyo alioutumia na Von hadi nje ya uwa ambako walipiga mbio wakitegemea kumkuta rubani akiwemo, ili wamlazimishe kwa bastola kuendeshwa kutoka nchini humo. Hakuwemo. Bila shaka “miujiza” iliyokuwa ikitokea ilimtia kiwewe hata akaondoka zake, au alikimbilia familia yake kwa matumaini ya kuiokoa. Hivyo, kiasi Nuru alikata tamaa. Lakini Joram alimrejesha matumaini alipomwamuru kupanda mara moja. Wakaingia.

    Joram alikuwa na ujuzi wa nadharia juu ya kuendesha helikopta. Alilazimika kujikumbusha ujuzi huo kwa vitendo, jambo ambalo liliwagharimu zaidi ya dakika mbili. Wakati huo askari walikwishawaona na kuanza kuwafuata kwa nguvu zaidi.

    Askari mmoja aliamua kutokimbia, badala yake aliilenga bunduki yake na kuiandaa kupiga.

    Wakati huohuo jambo jingine la kushangaza lilitokea. Jumba hilo, ambalo lilikuwa hifadhi ya mitambo haramu lililipuka kwa mshindo mkubwa. Moto wa kutisha ulipanda juu na kusambaa kote.

    Wakati askari hao walipokuwa wakitazama hilo, pia kwa mshangao, helikopta ilikuwa angani. Walipokumbuka kupiga risasi ilikuwa ikigeuzwa kuelekea Botwasana.



    *****SURA YA KUMI NA MBILI*****



    “… NA kama anafanya mauaji hayo kulipiza kisasi dhidi ya maafa ambayo utawala huu utayafanya katika nchi hii saa chache zijazo, bado si kitendo cha kujivunia sana, kwani haitasaidia kitu,” Kombora alinong’ona. Alikuwa akisema peke yake, akiwa kimya katika ofisi yake.

    Hayo yalimtoka mara baada ya kutazama televisheni na kusikia habari za kutatanisha kutoka BBC, bila shaka zikiwa zimekuja kutoka Afrika Kusini bila hiyari ya utawala huo, kwamba Joram alikuwa ametoweka kutoka katika jumba alilowekwa nchini humo. Kwamba mauaji ya ajabuajabu dhidi ya makaburu katika nchi hiyo yalitokea usiku huo. Na kwamba kulikuwa na mashaka kuwa mwuaji au wauaji hao hawakuwa wengine zaidi ya Joram na Kiango na yule msichana anayefuatana naye, Nuru.

    Habari hizo, zikiwa zimewasili pindi vyombo vyote vya habari nzito zaidi ya hiyo zilipokelewa kama habari ndogo na kupuuzwa mara moja. Kwa wananchi wa Tanzania na nchi nyingine ambazo zilikuwa mashakani zikisubiri maafa makubwa kwa hofu na mashaka makubwa, walizipokea kwa shangwe na vigelegele kwa dakika mbili tatu, dakika zilizofuata ikawa imesahauliwa. Hofu ikachukua nafasi yake. Wakaendelea kusubiri, kusubiri kifo.

    Waumini wa dini walikisubiri kifo katika makanisa na misikitini. Wakristo walichubuka magoti kwa sala ndefu zilizoambatana na vilio. Waislamu walivunjika migongo kwa kwenda rakaa huku wakimlilia Mola. Wasiomjua Mola walikisubiri kwa namana mbalimbali. Wako waliotulia kwa utulivu, wako waliopiga kelele na kuna wachache ambao waliamua kufa wakiwa wamelewa; hivyo, chochote walichokuwa nacho walikitumia kununulia pombe. Watoto ambao walipata hisia fulani kutokana na tofauti katika tabia za wazazi wao walitulia kimya, kwa mara ya kwanza maishani mwao wakionja ladha ya hofu. Hata wanyama wanaofugwa, kama kuku, mbwa, mbuzi na ng’ombe hawakuwa katika hali ya kawaida kwani ilikuwa siku yao ya kwanza ambayo hawakushuhudia binadamu akila mayai, kuchinja mbuzi wala kumkamua ng’ombe.

    Jeshi liliwekwa katika hali ya hadhari, tayari kwa lolote ambalo lingeweza kutukia. Lakini kwa vile madhara hayo yalikuwa hayafahamiki yangetokea upande upi, na silaha ipi ingeweza kuyazuia, ilikuwa dhahiri kuwa jeshi hilo lisingeleta upinzani wowote. Ilikuwa kama waliowekwa tayari kusubiri kifo.

    Rais na mawaziri wake, pamoja na viongozi wa ngazi za juu katika Chama walijiinamia juu ya viti vyao vya Ikulu. Mengi yalikuwa yamesemwa, mengi yalifanywa, lakini halikuwepo lolote lililoelekea kuwa kipingamizi kwa maafa yaliyokuwa yakiendelea dakika baada ya dakika. Wao pia ilikuwa kana kwamba waliamua kusubiri kifo kwa pamoja. Mara kwa mara walitazama saa zao kisha wakatazamana. Kisha kiongozi mmoja aliinuka baada ya kumnong’oneza jirani yake kuwa anakwenda haja. Hakurudi. Mwingine aliondoka taratibu kwa madai hayohayo. Yeye pia hakurudi. Yuko ambaye alikwenda moja kwa moja msikitini. Kuna aliyekwenda kanisani. Mwingine alikwenda nyumbani ambako aliungana na familia yake, kusubiri kifo.





    Tahamaki Rais alijikuta kabaki na Waziri wake Mkuu. Walitazamana kwa muda, kisha mmoja aliyaepuka macho ya mwenziwe, wakizitazama saa zao. Zilisalia dakika tano tu. Wakatazamana tena. Wakazitazama tena saa zao. Dakika tatu… Dakika mbili… mmoja alimsika mwenziwe akiguna. Mwingine aliinuka akiwa kaloa jasho ambalo hakufahamu lilivyoishinda air conditioner ambayo ilikuwa ikifanya kazi kikamilifu. Kisha aliketi tena na kuyafumba macho yake.

    Dakika moja…



    ******

    Dakika yoyote kuanzia sasa! Kombora aliwaza akitoka dirishani alikokuwa akichungulia na kukirudia kiti chake. Alikuwa ameamua lolote ambalo lingetukia limkute katika ofisi yake. Hakuiona haja ya ya kutaabika wala kwenda kushuhudia maisha yanavyowatoka wanawe endapo nyumba yake ingetukia kuwa moja kati ya nyumba zisizo na bahati.

    Mara mawazo ambayo hakutaka yamjie akilini yakamtoka. Mawazo ya upweke, unyonge na msiba mkubwa, mawazo ambayo yalikuwa yakimfunulia hali ambayo angekuwa nayo endapo ingetukia yeye kuwa mmoja kati ya wale watakaosalimika na familia yake nzima kuteketea. Angeishi vipi bila ya mama watoto wake, yule mwanamke mpole ambaye hajaacha kumwonea haya kwa kiwango kilekile walipokuwa wachumba hadi leo ambapo wamekuwa pamoja zaidi ya miaka thelathini. Angeishi vipi bila ya watoto wake wanne, mmoja akiwa mwanamume ambaye amehitimu Chuo Kikuu na kuajiriwa mwaka jana na wale wa kike ambao wote wameolewa na kumpatia wajukuu watano? Maisha yangekuwa vipi endapo yote hayo yangebadilika ghafla kwa ajili ya ukatili wa utawala dhalimu wa weupe wachache huko kusini?

    Kisha alikumbuka saa yake. Dakika kumi zilikuwa zimepita! Hakuyaamini macho yake. Akayainua na kupiga hatua mbili tatu kuliendea dirisha. Akachungulia chini. Mitaa yote ya Dar es Salaam ilikuwa imetulia kabisa. Kelele ndogo zilisikika kwa mbali kutoka katika viwanda kadhaa ambavyo vilikuwa vikiendelea na kazi. Kombora aliirudia meza yake na kuketi. Masikio yake yalikuwa wazi yakisubiri kwa hofu kudaka mlio wowote wa mashaka ambao ungesikika. Macho pia yalikuwa wazi yakitazama angani kupitia dirishani.

    Dakika ishirini!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Wakati wo…” alitaka kutamka. Sauti yake ilikatizwa na ukelele wa ghafla ambao ulivuma ghafla katika anga. Bila ya kutegemea aliyafumba macho yake kwa nguvu na kutamani kuweka vidole masikioni ili asisikie zaidi. Kelele ziliendelea kwa mvumo mkubwa zaidi. Hisia zilimfanya Kombora adhani kuwa zilikuwa kelele za kushangilia badala ya vilio na maombolezo kama alivyotarajia. Akasikiliza kwa makini zaidi. Naam. Watu walikuwa wakipiga vigelegele na kucheka kwa nguvu.

    Watu wote!

    Kama waliopatwa na wazimu!

    Dakika moja baadaye Kombora alikuwa miongoni mwa watu wengine katika chumba cha habari, ghorofa ya mwisho. Askari hao walikuwa wakitokwa na machozi ya furaha huku wakisikiliza redio BBC ambayo ilikuwa ikiendelea na taarifa.

    …hadi sasa inaaminia kuwa utawala wa Afrika Kusini haujafanikiwa kuuzima moto huu mkali ambao unateketeza majumba mbalimbali ya mjini johanesburg. Kadhalika, haijafahamika watu wangapi wamefariki na wangapi ni majeruhi japo inaaminika kuwa idadi hiyo itakuwa kubwa sana.

    Kadhalika, mtambo wa siri ambao ulikuwa umejengwa na utawala huo ukiendesha setilaiti ya aina yake, isiyoonekana kwa macho, umelipuliwa na wahandisi wake wote kuteketea. Inasemekana kuwa baada ya mtambo huo kulipuka chombo hicho cha ajabu kimeanguka katikati ya mji wa Johanesburg na kusababisha madhara makubwa kwa maisha na mali za wananchi. Kadhalika, inaaminika kwamba afya za wananchi katika mji huo zitakuwa mashakani kutokana na nguvu ya nyuklia zilizoshirikishwa katika kukiunda chombo hicho. Kwa kila hali inaonyesha dhahiri kuwa Joram Kiango alishirikiana na mwenzi wake, yule msichana mzuri, Nuru, wameshiriki kwa njia moja au nyingine katika kufanya haya yaliyofanyika huko Afrika Kusini. Na endapo wasingekifanya walichokifanya dakika hii Afrika nzima ingekuwa katika msiba kwani kulikuwa na mipango ya mtambo huo kuzishambulia nchi zote za mstari wa mbele kwa pamoja…

    Kombora hakustahimili. Machozi mengi yalimtoka na kuteleza juu ya mashavu yake, machozi ya furaha. Joram Kiango tena! Kwa mara nyingine ameliokoa taifa lake na Afrika nzima kuepuka kipigo cha kikatili ambacho kisingesahaulika. Joram, ambaye alimfikiria vibaya kwa kutoweka kwake na pesa nyingi za umma ambazo amezichezea duniani kote.

    Ghafla, ikampambazukia Kombora. Joram hakuwa ameziiba zile pesa. Alizichukua kwa mtindo ule ili ionekane kama ameziiba ili azitumie kwa shughuli hii pamoja na kuaminika kama msaliti mara aingiapo nchini Afrika Kusini. Angeweza kuchukua hata zote! Kombora aliwaza. Angeweza kuzitumia apendavyo! Kijana huyu ni nani kama sio malaika aliyeletwa kuishi kama binadamu kwa manufaa ya binadamu wengine?

    Kombora alirejea ofisini kwake. Mara tu alipoketi simu zilianza kumsumbua. Nyingi zilikuwa za waandishi wa habari zikiuliza hili na lile. Swali kubwa lilikuwa kutaka kujua kama kweli ni Joram Kiango aliyeifanya kazi hiyo ambayo majeshi yote ya nchi za Kiafrika yasingeweza kufanya. Zaidi walitaka kujua Joram yuko wapi.

    Simu ambayo ilimsumbua Kombora kuliko zote ni ile iliyotoka Ikulu. Alizungumza na Rais mwenyewe. “Tunamtaka haraka kijana huyu ndugu Kombora. Kuna tuzo maalumu ya ushujaa ambayo inamsubiri…”

    Kwa kadri Kombora alivyomfahamu Joram, hakuamini kama angepatikana kwa urahisi kiasi hicho, na hasa kujitokeza aipokee tuzo hiyo hadharani.

    Siku mbili baadaye uhai ulilirudia jiji la Dar es Salaam kama kawaida. Pilikapilika za mitaani, viwandani na maofisini ziliendelea mtindo mmoja. Kila uso ulikuwa na furaha, tabasamu likiwa karibukaribu. Jina la Joram lilikuwa katika fikra za kila mmoja. Ambao hawakupata kumfahamu waliuliza huyu Joram ni nani?

    “Humfahamu?” waliulizwa huku wakitazamwa kama wapumbavu.

    Tawi la Benki ya City Drive lilikuwa na uhai vilevile. Wateja wengi walifurika kama kawaida wakiweka au kuchukua pesa, kuangalia hesabu zao na shughuli nyingine mbalimbali. Pilikapilika hizo ziliwafanya wasimtazame zaidi ya kawaida mzee huyu aliyevaa kanzu nyeupe na koti jeusi, ambaye alikuwa na nywele na ndevu nyingi nyeupe kwa wingi wa mvi. Mkononi alikuwa na mfuko mnene wa ngozi. Aliwapita wateja wote, akipokea shikamoo zake hadi chumbani kwa meneja ambaye alimpokea kwa heshima zote, kwani haikuwa mara kwa mara kutembelewa na watu wenye umri kama huo.

    “Marahaba,” Babu huyo aliitikia. “Wewe ndiye meneja mwenyewe?”

    “Ndiye.”

    “Ndiyo wewe uliyeibiwa zile pesa za kigeni?”

    “Ni mimi, mzee.”

    “Basi huu hapa mzigo wako,” mzee huyo alisema akifungua mfuko huo na kutoa mabunda ya noti. Pesa za kigeni na shilingi chache za Tanzania. “Nimetumwa na kijana mmoja anayesema anaitwa Joram nikuletee. Amesema nikuombe radhi sana kwa kuzichukua. Alikusudia kuzitumia kwa safari yake lakini alipata pesa nyingine kutoka kwa jasusi moja ambalo alilikamata kule New Africa Hotel. Hivyo, alizitumia pesa zile badala ya hizi. Hata hivyo, amesema zimepungua kidogo atalipa…”

    Meneja alikuwa hamsikilizi kwa makini. Mshangao ulikuwa umemshika. Alimtazama mzee huyo kwa muda kisha aliinama na kuanza kuzihesabu kwa mabunda. Katika hesabu ya harakaharaka zilipungua dola mia mbili. Akazirudisha katika mfuko wake na kuinua uso ili amshukuru mzee na kumwambia la kufanya. Hakumwona. Mzee alikuwa ameondoka bila ya kuaga alipokuwa kainamia meza.

    Meneja huyo aliduwaa. Kisha alikumbuka la kufanya. Akauchukua mfuko huo wa pesa na kuondoka nao hadi katika gari lake. Akalitia moto hadi katika ofisi ya Kombora ambako alimwona moja kwa moja na kumsimulia mkasa mzima.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “My God,” Kombora alifoka. “Aliyezileta pesa hizo kwako hakuwa mzee. Alikuwa kijana sana, Joram Kiango mwenyewe!”

    Meneja huyo alizidi kushangaa. “Mbona alikuwa mzee, Inspekta? Hata sauti yake ilionyesha…”

    “Huyo ni Joram,” Kombora alimkatiza. “Ametumia moja ya mbinu zake ili asipatikane na kupewa heshima yake. Amejifanya mkongwe kama alivyofanya katika mkasa ule ulioitwa Salamu Toka Kuzimu.” Kombora alijiinamia kwa muda. “Tulimhitaji sana,” alisema kama aliyemsahau Meneja huyo wa Benki na badala yake kujizungumzia peke yake. “Anahitajika. Kumtafuta haitasaidia kitu. Kwa jinsi ninavyomfahamu hatajitokeza hivi karibuni hadi hapo mchango wake utakaposahauliaka, au litakapotokea suala jingine linalohitaji ushujaa."



    ***MWISHO*****

0 comments:

Post a Comment

Blog