Search This Blog

Sunday, 22 May 2022

SALAMU KUTOKA KUZIMU - 4

 







    Simulizi : Salamu Kutoka Kuzimu

    Sehemu Ya Nne (4)



    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mtu huyu alitabasamu alipomwona Joram akirudiwa na fahamu.Tabasamu ambalo lilikuwa ni vigumu kutofautisha na kilio.



    "Naitwa Unono. nimekuokoa kutoka katika kifusu cha nyumba iliyopatwa na ajali. Unajisikiaje bwana wangu?"



    "Bwana wake hili lingemchekesha Joram Kiango. Lakini maumivu yaliyokuwa yakimsumbua hayakuwa madogo. Yakamfanya amshukuru na kuuthamini msaada wa Unono. Alijuwa kuwa bila ya unono angekuwa marehemu. "AHsante sana," akijikongoja kutamka.



    "Usijali mpenzi."



    Mpenzi! Joram aliwaza kwa hasira kidogo. Kisha alitabasamu alipojikumbusha kuwa huenda mama huyu hana akili timamu. Kwani Joram hakumbuki lini aliwahi kuitwa "Mpenzi" na mtu wa aina yake.



    Tabasamu la Joram lilimtia Unono moyo. Akacheka na kueleza kwa mnong'ono. "Nimekuleta kwa siri. Majirani wote wamelala. Hakuna anayejua kama uko humu. Kama wangejua wangekupokonya kutoka mikononi mwangu. Hakuna mtu anayependa kuniona nikipata kitu kizuri. Nawe u mzuri bwana wangu. Mzuri na mwenye afya. Nimekubeba kwa taabu kubwa sana. Baada ya muda si mrefu utapona. Utakuwa wangu. Nitakupa chochote na kila kitu utakachokitaka kutoka kwangu."



    Joram hakuwa amemsikiliza. Alikuwa ameirejesha akili yake katika tukio zima na kulitafakari. Akajikumbusha kuwa kuna mtu aliyekuwa amedhamiria kumuua. Mtu ambaye ametumia njama namna kumuua. Kwanza, akamtumia yule msichana kumpa sumu. Pili, ametumia bomu. Na ameponea chupuchupu kuuawa na bomu hilo. Pengine mtu huyu anaamini kuwa amekwishafariki. Ama asingeshindwa kuja hapa na kummaliza kwa urahisi. Kwanini mtu huyu akataka kumuua kwa vyovyote vile? Amefanya kosa gani ili aweze kuchukuwa na binaadamu mwenzake kiasi hiki? Joram hakupenda kuwindwa kama mnyama mwituni. Hasira zilimjaa. hasira zilizompa nguvu. AQkashindana na udhaifu aliousikia mwilini. Akainika kwa kujikongoja. Akajitahidi kusimama wima.



    "Una nguvu za ajabu mpenzi," Unono alisema kwa mshangaoJoram alimtazama bila kumsikia. Akilini mwake aliwaza: Ni vipi angekuwa mwinda badala ya mwindwa? Vipi angemtia mkononi mtu huyu wa hatari? Alikuwa na fursa nzuri sana kwani huyu alikwisha mtoa akilini kwa kudhania kuwa tayari amemwangamiza. Aliona kuwa isingekuwa kazi ngumu kumtia mikononi.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hata hivyo, aliuona ugumu wa Jukumu hili. Alikuwa amepoteza silaha zake zote. Alipoteza ndevu zake za bandia pamoja na kilemba chake. Begi lake lililobeba vifaa vyake muhimu lilikuwa limepotea pia. Basi, alifurahi mno kupata pochi yake kwenye kwenye mfuko wa suruali. Pochi ambayo ilisetiri mambo yake mawili muhimu, noti zake chache na picha ya adui yake. Picha ambayo alikuwa ameipiga kwa siri sana kule hotelini ambako adui yake huyu alikuwa akimwandalia kifo chake. Joram aliitazama picha kwa makini, kisha akaihifadhi, na kujilazaq kitandani akisubiri mapumziko.



    Unono, ambaye wakati huu wote alikuwa ametulia akimtazama Joram, alimfuata kitandani. Buibui amelivua tayari kusheherekea vuno lake. Weusi wa umbo lake haukupendeza hata kidogo. Lakini Unono alikuwa amedhamiria.



    "Naona umepona mpenzi," alisema

    "Tunaweza kufurahi kidogo..."



    Hili Joram hakulitegemea. Alitamani kumwachia kofi kali ambalo lingetuwa katika sura hiyo mbaya na kuirejeshea akili. Lakini kwa kuwa bado alimhitaji, hili hakulifanya. Badala yake, alizungumza kwa sauti ya udhaifu zaidi. "Baada ya kunitoa hatarini unataka kuniua hapa? Huoni kama niko hoi?"



    "Pole!"



    Usiku huo ulikuwa mgumu kwa Joram. Kwa kweli Joram alikuwa amezoea kukutana na wanawake wazuri. Lakini alikuwa hajazoea kupambana na wanawake aina ya Unono. Mwanamke mzuri anaponuna, Joram huwa anaelewa na sura yake haichukizi, na anapocheka inapendeza. Huyu akicheka inachukiza, na akinuna tazama anavyotisha! Ulikuwa usiku mgumu. Usingizi ulimpata alfajiri. Alikurupuka na kumkuta Unono yuko juu yake!



    Kulipopambazuka alitayarishiwa maji ya moto ambayo aliyaoga haraka haraka. Alipotoka bafuni alikuta Unono kaandaa chai nzito. Baada ya kuinywa aliambiwa, "Sasa hujambo. Tafadhali tulale kidogo kabla hujanikimbia kama wenzako wote."



    "Kukimbia?" Joram alihoji, akijitia kushangaa. Bado nauhitaji sana msaada wako." Akaitoa pochi yake. Ninahitaji sana msaada wako," aliongeza. "Pesa hizi ni nauli yako. Na hii hapa ni picha ya mtu ambaye nitakuomba uipeleke kwa msichana mmoja. Anwani yake ni hii..." akamweleza. "Utanisaidia mpenzi."



    Unono hakuwa amemsikiliza kwa makini. Lakini "Mpenzi" lilimfanya ayakumbuke yote aliyoelezwa kwa uhakika kabisa. Kuitwa "Mpenzi" na kijana mzuri kama huyu, aliyekuwa amemnyima usingizi usiku kucha. Hakumbuki kama kuna binadamu yeyote wa kiume aliyewahi kumuita hivyo. "Nitakusaidia kwa lolote," alimjibu.



    "Ahsante," Joram alijibu. "Jambo jingine nitakalokuomba ni la siri. Tafadhali sana usimfahamishe mtu yeyote kuwa unaishi na mtu hapa. Wala usimfahamishe mtu yeyote kuwa mtu huyu alinusurika ajali ya bomu. Tafadhali iweke vyema siri hiyo. Ningependa kuishi hapa kwa wiki nzima bila mtu yeyote kufahamu."



    Wiki! Unono hakuyaamini masikio yake. Alizidiwa na furaha. Hakuahidi tu bali aliapa kuwa asingeitoa siri hiyo hata kwa ncha ya kisu. Baada ya kujiandaa, aliaga na kutoka nje ambako alipanda basi kama alivyoelekezwa na Joram. Ndipo alipomwendea Neema na kumpa ile picha, ingawa kwa ajili ya wivu, hakueleza kikamilifu yote ambayo Joram alikuwa amemwelekeza. Wivu ambao ulimharakishia Neema Idd kifo chake.



    Baada ya Unono kuondoka, Joram pia alifuata. Aliingia mitaani ambako alinunua mavazi fulani fulani na miwani myeusi, akajibadilisha.Mtu asingeweza kumfahamu kwa urahisi, hasa mtu ambaye alikuwa na uhakika kuwa Joram Kiango alikwisha fariki. Ktoka hapo, alienda kwa Neema. Alishuku kuwa binti huyo alikuwa anachunguzwa. Aliingia katika nyumba hiyo kwa siri mno bila ya jirani yeyote kumwona. Alishangaa kutomkuta Neema ndani ingawa picha aliyoihitaji ilikuwa mezani ikiwa na maelezo yote nyuma yake. Baada ya kusubiri kwa muda, aliondoka tena kwa siri kama alivyoingia. Alirejea kwa Unono ambaye Joram alimkuta tayari kanuna na kukata tamaa. Hivyo alipomuona Joram alimrukia na kumkumbata. Lakini Joram alijitoa mikononi mwake kwa kumuomba aende kwa Neema kupata majibu. Alimpa pia maelezo mengine.



    Unono aliondoka, lakini hakurudi.



    Subira ya Joram haikuzaa matunda yoyote. Kiza kilipoingia, aliondoka hadi kwa Neema. Mbele ya nyumba hiyo alisikia maongezi ya watu juu ya ajali ya "Mwanamke kichaa, mfupi..." Ndani kwa Neema, alimkuta kalala kitandani, Kapoa kitambo.



    Kifo cha Neema kilimshtua Joram zaidi ya kitu chochote kilichowahi kutokea. Hakutegemea. Alitaka kulia ingawa hakujua kwa nini machozi hayakujitokeza machoni mwake. Neema kafa! Msichana pekee ambaye waliondokea kupendana zaidi ya dada na kaka au mtu na mkewe. Msichana ambaye daima alikuwa tayari kuhatarisha maisha yake kwa ajili yake. Binti ambaye mara nyingi ameyaokoa maisha yake. Asingeweza kusahau mchango wake katika kisa cha Najisikia Kuua Tena. Wala asingekosa kumkumbuka kila alipofikiria tukio la Dimbwi La Damu. Neema! Mtoto Mpole, msikivu, mwenye hekima. Mtoto mzuri kwa sura na umbo. Kapotea bure kwa uzuri ule katika mikono ya mtu mwenye roho ya kinyama na fikira za shetani...

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hatimaye machozi yakamtoka.



    Joram hakuwa na haja ya kuambiwa kuwa kifo hiki ni matokeo ya kazi ndogo Aliyompa Neema kupeleleza juu ya mtu au watu hawa waliokusudia kumwua. Akaaapa kuwa asingestarehe hadi amtie mikononi mtu huyu! Mikononi? Alijiuliza kwa hasira. Ndiyo, Joram hajawahi kuua. Wala leseni yake haimruhusu kuua isipokuwa katika kujitetea tu. Lakini huyu lazima amwue kwa mkono wake. Aliapa. Damu ya Neema na wote wasio na hatia waliouawa na mtu huyu lazima ilipwe. Deni la damu hulipwa kwa damu.



    "Wazimu wa hali ya juu... Wazimu wa hatari..." Kombora aliendelea kufoka kimya kimya, masaa kadhaa baada ya kuhudhuria kile kikao ambacho kiliendeshwa na Joram. Karatasi zile zilikuwa kando mbele yake, zikimtisha na kumtamanisha. "Mtu kadhamiria kuua kinyama umati mzima wa viongozi, kwa njia za kipekee ambazo si rahisi kubainika! Mtu huyu yu hai na huru mahali fulani katika Jamhuri hii! Wazimu ulioje? Hana haki ya kuendelea kuishi. Lazima afe haraka iwezekanavyo".



    Hayo Kombora alikuwa ameyasema mara nyingi usiku huu. Tangu Joram alipomwacha, alitoa amri ya kuwahifadhi 'Waheshimiwa' wote na kisha kuanza jukumu la kumsaka Proper. Kati ya karatasi alizoacha Joram, zilikuwa pia zile ambazo zilifichua makazi yake yote na majina yake mbalimbali. Hivyo makachero walitumwa sehemu mbalimbali kumsaka. Mengi ya kutisha yalibainika, lakini mtu waliyemhitaji hakupatikana. Alikuwa ametoweka kama moshi unavyopotelea hewani. Ndipo Kombora alipoelekeza juhudi zake kumtafuta Joram kwa matumaini ya kwamba angeweza kuwa na fununu ambayo ingerahisha kupatikana kwa mtu huyo. Lakini alishangaa alipoona kuwa juhudi za makachero za usiku kucha hazikufanikiwa. Sasa kulikuwa kukipambazuka bila dalili zozote za Joram kupatikana. Yeye pia alikuwa ametoweka!



    Ulikuwa usiku wa manane. Lakini Kombora hakusinzia hata kidogo. Wala hakudani kama angeweza kupitiwa na lepe la usingizi usiku wowote hadi wakati mtu huyo hatari atakapokuwa ameuawa au kutiwa mbaroni. Zilikuwa zimesalia siku chache sana kabla ya mkutano huu maalumu wa viongozi wa nchi ziliko mstari wa mbele ufanyike mjini Arusha Tanzania. Ilisemekana pia kuwa viongozi wa nchi nyingine huru za Afrika wangehudhuria mkutano huo. Na mtu huyu - lanakum - anayekusudia kuwaangamiza viongozi hawa kinyama, yuko mahali fulani katika nchi hii! Vipi Kombora angeweza kustarehe?.



    Alikuwa na wajibu. Wajibu muhimu na wa haraka kuliko wowote mwingine uliowahi kumhusu kama kiongozi wa kikosi hiki maalumu: kumpata muuaji huyu mapema iwezekanavyo. Ni hili lililomfanya aendelee kuwa ofisini hadi muda huo, akipokea simu na taarifa mbalimbali za makachero waliosambazwa kote Jijini kufanya kazi moja tu, kumpata Proper akiwa hai ama maiti.



    Hakupatikana. Saa tisa... saa kumi... na moja! bado hakukuwa na taarifa yoyote ya uhakika, jambo ambalo lilizidisha hasira na mashaka katika kichwa chake. Akaelekeza imani yake kwa makachero wa uwanja wa ndege waliodai kuwa mtu wa aina hiyo alikuwa amepanda ndege iliyoelekea mkoani Mwanza. Hata hivyo, Kombora hangeweza kukubali taarifa hiyo mara moja, hakuona kama Proper alikuwa mtu wa kukubali kushindwa hata kukimbilia Mwanza. Kombora aliamini kuwa mahali ambapo mtu mwehu kama huyo angekimbilia ni Arusha ambako angesubiri ili kujaribu kuukamilisha uendawazimu wake kwa vitendo. Hivyo akatoa amri kwa makachero kuendelea na upelelezi hadi mtu huyo apatikane.



    Mapambazuko yalifika kabla Proper hajapatikana. Baada ya kunywa vikombe viwili vya kahawa, ili kupunguza uchovu, Inspekta Kombora alijikuta akiinua simu na kuzungusha namba za nyumbani kwa Katibu Mkuu wa Wizara.



    Usiku mzima alikuwa amepingana na wazo hilo. Hakuwa mtu mwenye tabia ya kuyatupa matatizo yake kwa wakubwa. Lakini hili aliliona kuwa la hatari zaidi. Maana lingeweza kuleta madhala ya kimataifa. Hivyo, haikuwepo njia nyingine ila kuiarifu serikali mapema kabla maji hayajamwagika.



    Simu ilipokelewa na Katibu Mkuu mwenyewe. Maelezo ya simu hayakumridhisha Katibu Mkuu. Akamwamru Inspekta Kombora kufika ofisini kwake saa mbili kamili ili amuarifu taarifa hiyo barabara. Ndipo Kombora aliporejea nyumbani kwake ambako alioga, akabadili sare zake za kazi kisha akarejea ofisini kimya kimya kumweleza mama watoto wake wapi walilala. Haikuwa tabia ngeni katika kazi yake.



    "Unadhani ni kweli mtu huyu ameamua kuitekeleza ndoto yake", Katibu Mkuu alimwuliza Kombora baada ya kumsikiliza kwa makini.



    "Ndiyo mzee", Inspekta Kombora alimjibu baada ya kusita kwa muda.



    "Tazama mtu huyu alivyofauru kumuua jasusi mwenzake aliyekuwa akijificha kwa kuvaa mavazi ya kipadri. Kwa kila hali anakusudia kuendelea na ndoto yake", Inspekta Kombora alieleza kwa msisitizo.



    "Na unasema huyu kijana Joram Kiango ambaye iliaminika kuwa amekufa, aliyesaidia kufichua yote haya hajulikani aliko?", Katibu Mkuu wa Wizara aliendelea kuuliza.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kombora alikohoa kabla ya kujibu. Hajulikani mzee. Ni ajabu kuwa yeye pia alitoweka. Naamini yuko katika msako wa kumtafuta huyu ambaye amemuua pia msichana wake mpenzi Neema. Hata hivyo juhudi zake hizo za kibinafsi akiongozwa na hasira zaweza kuleta madhara.



    "Ingefaa tushirikiane..." Mara Kombora akasita baada ya kukumbuka kuwa mengine kati ya maelezo yake hayakumhusu Katibu Mkuu. Yalikuwa maelezo yake binafsi.



    "Ndiyo, ndiyo Inspekta", Katibu Mkuu alimjibu, "Sasa sijui sababu za kuniona mimi. Sidhani kama hutapenda kuniambia kuwa kikosi chako kimeshindwa kabisa hivyo unaomba msaada wa wizara nzima ifanye kazi ya kumsaka na kumtia mbaroni mwendawazimu mmoja tu".



    "Sivyo mzee", Kombora alijibu akimtazama kijana huyu kwa aibu baada ya kumwita kijana huyu 'mzee' ilihali alimzidi kijana huyu kwa umri. "Naamini tutampata... Isipokuwa niliona ni vyema kukujulisha ili ikiwezekana uishauri serikali iahirishe kikao cha wakuu wa nchi zilizo mstari wa mbele".



    "Hilo haliwezekani kabisa", Katibu Mkuu aidakia. "Kikao hiki mhimu mno. Ni kikao pekee ambacho kinaelekea kufanikisha dhamira yetu ya kuipatia Namibia Uhuru. Na kadharika tumekusudia kuratibu mbinu mpya za kuharakisha kutokomeza ubaguzi wa rangi Afrika Kusini. Aidha kikao kimeadhimia kujadili vita vya wenyewe kwa wenyewe huko Sudan na Ethiopia. Tumekusudia kukuza misingi ya muungano wa Afrika. Haya ninayokusimulia ni siri kubwa. Naratajia utayahifadhi. Nimelazimika kukueleza haya ubaini kuwa kikao hicho ni muhimu. Haiwezekani kuahirisha mkutano huu. Ni wajibu wako kumnasa mtu huyo mnayemwita Proper.



    "Fanya kila uwezavyo", Katibu Mkuu aliendelea. "Kadharika, siri ya kunusurika kwa Joram Kiango ingepaswa ilindwe vilivyo. Kijana huyu ana busara sana. Anaweza kukusaidia kumpata mtu huyo. Lakini itabidi isifahamike kabisa kuwa kijana huyu yuko hai", Katibu Mkuu akasita na kumtazama Kombora. Kisha akauliza ghafla.



    "Kwa nini kijana huyu hujamweka katika kikosi chako". Kombora akatabasamu. "Joram! Tumemwomba mara nyingi. Hataki. Ni mtu apendaye uhuru wake".



    "Na pengine mkiwa naye pamoja huenda akashindwa kufanya kazi yake", Katibu Mkuu akaongeza. "Naona njia zake za upelelezi zimo katika tapo la kipekee. Nimezisoma harakati zake magazetini na katika vitabu mbalimbali".



    "Nadhani ni kweli". Kikafuata kimya kifupi. Kombora alifahamu kuwa Katibu Mkuu alikwisha msahau na kuzama katika mawazo ya shughuli nyingine. Hivyo, aliinuka na kuaga. "Asante mzee".



    "Naamini utafanya juu chini kumpata mtu huyu Inspekta", Katibu Mkuu alimtupia neno Inspekta Kombora alipoukaribia mlango.



    "Bila shaka mzee", Inspekta Kombara alijibu, huku kichwani mwake akijiuliza angeweza kufanya nini zaidi.



    Proper alikuwa juu ya kitanda katika chumba cha mojawapo ya Hoteli nyingi za Mji wa Mwanza. Mkono wake wa kulia ulikuwa ukichezea matiti ya mischana mrembo aliyelala kando yake, mkono wa kushoto ulikuwa ukipepesa kiuno cha msicha huyu. Wote walikuwa uchi na miili yao ikitokwa jasho. Jasho liliendelea kuwatoka asubuhi hii yenye baridi kali. Jasho lililotokana na juhudi za miili yao katika kuthibitisha utaalamu na uwezo wao kimahaba.



    Huyo alikuwa msichana wa tano tangu Proper aingie mjini Mwanza na kufikia katika hoteli hii... Wawili waliotangulia, alikuwa amewaona wa kawaida tu. Zaidi ya uzuri wao wa sura na maumbile ya kuvutia, kitandani hawakuwa na la ziada. Hivyo aliwapa ujira wao na kuwaaga. Lakini huyu wa tatu, hakuonekana kama alikuwa mtu wa kuagwa kwa urahisi. Sura haikuwa nzuri sana. Wala umbile lake halikuwa kama yale ambayo huwafanya madereva wa magari waroho wasababishe ajali barabarani kwa kuwatazama. Msichana huyu alikifahamu kile alichopaswa kuwatendea wanaume. Alielewa alichokusudia Muumba wake kwa kumwezesha kuwa na viungo tofauti. Kila kitendo chake kitandani alikitenda kwa ari na nia, bila uchoyo wa aina yoyote. Kila kiungo chake mwilini alikitumia kikamilifu bila hiana. Na hakuonekana mwanafunzi katika vitendo vyake vyote.



    Ni hayo yaliyomfanya Proper ajisahau kwa kiasi fulani.



    Ni kweli kuwa aliyoyaona Mwanza hayakuwa ya kawaida. Katika Jiji la Dar es Salaam ambako aliishi sana, kupata msichana au mwanamke wa kujiburudisha haikuwa tatizo. Ziko saa za jioni, au usiku, ambazo utajitokeza mitaani na kujipitisha. Hutavuka mtaa wa tatu kabla hujapata mtu ambaye ataivunja safari yake na kuandamana nawe hadi chumbani kitandani, ambako ataondoka alfajiri na siku ya pili. Lakini si hivyo kwa muda wa Mwanza. Hapa unachotakiwa kufanya ni kujipatia chumba chako kwanza katika moja ya hoteli nyingi zilizogaa. Kaa chumbani kwako kwa utulivu. Haitapita muda mrefu kabla hujapigiwa hodi na watoto wa kike ambao watajitia kuuliza hili na lile hadi maswali yao yatakapokufanya utoe jibu litakalowafanya waangukie kitendani.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Proper pia alitulia chumbani kwake kimya akingoja hodi yake. Haja yake haikuwa kujiburudisha tu, bali alitaka kujificha, ili aonekane kama wapangaji wengine. Kama vijana ambao waliamua kuonyesha ujana wao au wazee ambao waliifurahia fursa ya kuwaasi wake zao. Ndipo alipoanza kuwakaribisha wasichana mmoja baada ya mwingine hadi alipotokea huyu, ambaye hakuonekana kama alistahili kuondoka.



    "Jina lako", Proper alimwuliza huku akihamisha mkono mmoja kutoka kiunoni na kuupeleka kichwani kwa ajili ya kuchezea nywele ndefu zilizotimuliwa kutokana na zoezi lililokuwa likiendelea kitandani hapo.



    "Sofia" msichana huyu alijibu kwa sauti ya mahaba. "Na wewe?" akaendelea kuuliza.



    "Bakari, ingawa rafiki zangu hupenda kuniita Beka", Proper alimlaghai.



    "Kwa maana hiyo nikuite Beka siyo".



    "Hapana. Niite mpenzi".



    Sofia akacheka. Na kicheko chake kilikuwa cha kupendeza.



    Baada ya muda, msichana huyu alipitiwa na usingizi. Kichwa akakiegemeza katika kifua cha Proper, mkono wake akauweka mahala fulani katika mwili wake, akawa amelala kwa utulivu mkubwa. Uso wa msichana huyu ulikuwa kama anacheka, kwa jinsi alivyokuwa amelala.



    Proper alimtazama kwa muda. Kisha alijitoa kitandani hapo kwa uangalifu bila ya kumwamsha Sofia. Akaliendea begi lake ambalo alilifungua na kulichunguza. Sehemu za kawaida zilikuwa na mavazi yake, vitambulisho vyake bandia na vikorokocho vingine. Mifuko ya siri, ambayo kama alivyotegemea, wakaguzi wa uwanja hawakuweza kuifikia, ilikuwa na silaha zake, nyaraka zake muhimu, dawa zake maalumu, na pesa nyingi. Kila kitu kilikuwa kama kawaida. Proper akakirudia kitanda ambako alikiinua kichwa cha msichana huyo taratibu na kukirejesha kifuani kwake na mkono kuuweka kama ilivyokuwa awali. Kisha akayafumba macho yake kwa namna ya utulivu.



    Lakini akilini hakuwa na utulivu wowote. Kichwa chake kilikuwa kazini kikitafakari matukio yote yaliyopita na ajali. Aliukumbuka kwa hasira mpangi wake madhubuti ambao aliuandaa kwa gharama kubwa na muda mrefu, na ulivyokaribia kumpotezea maisha. Ilimchukiza kuona kuwa waliokusudia kumwangamiza walikuwa watu wa upande wake. "Kwa ajili ya uoga", aliwaz. Uwoga usio na msingi. Uoga ule ule ambao umewafanya kwa muda mrefu watumie pesa nyingi kukamilisha mabomu ya nyuklia, lakini hadi leo hawajadhubutu kufanya majaribio walao katika nchi moja. Wapi basi haja ya kusumbua vichwa? Yeye Proper angewaonyesha. Liwalo na liwe lakini mpango wake aliouanzisha lazima atautekeleza. Peke yake na kwa mkono wake Dunia ione Ulimwengu usikie.



    Proper aliyarejesha mawazo yake kwa Inspekta Kombora na jeshi lake. Walikuwa wanafanya nini alijua kwamba, kifo cha yule Padri kiliwafungulia polisi mwanya fulani. Hata hivyo alielekeza fikra zake zote kwa kazi hii ya mwisho. Hakuna ambaye angeweza kulizuia pigo la mwisho, Pigo la kihistoria.



    Proper alimtazama Sofia usoni. Akamuona alivyolala kwa utulivu. Angetokwa na kicheko kwa kumhurumia msichana huyu alivyolala kwa utulivu bila kufahamu amelala na mtu wa aina gani. Hajui kama amelala na kifo! Alinongona kimoyomoyo. Kisha alimwamsha na kumtaka wafanye tena mapenzi. Kama kawaida, msichana alikuwa tayari. Kama kawaida yalikuwa mapenzi ambayo yaliacha kumbukumbu akilini mwao.



    "Wapi unaishi Sofia?" Proper aliuliza baada ya kukusanya pumzi kwa dakika kadhaa.



    "Kirumba, nyuma kidogo ya Uwanja wa mpira".



    "Unaishi na nani Sofia?".



    "Peke yangu", Kimya kifupi kikapita. "Kwa nini unapenda kujua?".



    Proper alipeleka ulimi wake kuchezea chuchu za Sofia kabla hajatoa jibu.



    "Kwa sababu nyingi. Kubwa ni kwamba ni kwamba sijapata kukutana na aliyeniburudisha kama wewe. Nisingependa kutengana nawe tena, kwani nikikukosa huenda nisipate mtu wa aina yako. Hivyo, nimependa nihame hapa hotelini na kuishi kwako hadi shughuli zangu zitakapokwisha hapa Mwanza, halafu twende zetu pamoja Bujumbura. Unasemaje?"



    Habari hii ilimfurahisha sana Sofia. Msichana huyu alikuwa ametoroka kwao Sengerema baada ya kupata mimba isiyokuwa na mwenyewe. Mimba hiyo iliishia chooni. Tangu siku hiyo, amekuwa mtu asiyekuwa na tumaini la kupata bwana wa kudumu. Sura yake pia, ilikuwa pingamizi kubwa. Daima mabwana aliowapata, walikuwa hawa wa 'kuokota' Mabwana waliosukumwa na uchu tu wa kuwa na mwanamke. Hali hii ilimfanya msichana huyu ajikabidhi kwa kila mwanaume bila kujali lolote, akiwatimizia kila haja bila aibu wala kinyongo. Lakini harakati zake za kuwaburudisha wanaume mara nyingi hazikumfikisha mbali. Mara kwa mara alikuwa akipewa 'kwa heri ya kuonana' na mabwana hao. Wengi waliwarudia wake zao. Wengine walikuwa wameishiwa. Na wengine walikusudia kuziponyesha pesa zao.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ndiyo Sofia akayachukulia maombi ya 'Mzee kijana' huyu kama tunu aliyonunuliwa bila ya kutazamia. Aliyaona kama mwisho wa matatizo yake na mwanzo wa maisha mapya. Alimtazama tena Proper. Hakuona dalili yoyote ya mzaha katika sura yake. Kama kweli mtu huyu alikuwa na tatizo lolote, pesa hazikuwa mojawapo. Angekubali mara moja. Hata hivyo alikumbuka hali ya chumba chake, mazingira yaliyostahili jina la pango. Ndipo alipomweleza Proper kwa sauti iliyonasihi.



    "Ningependa sana kukukaribisha kwangu. Lakini hali ya chumba kile... kwa kweli, hakifai kwa mtu kama wewe".



    Proper hakuwa mgeni kwa maisha ya wasichana wengi mjini. Alikwisha waona wengi ambao wawapo mitaani wanaonekana kama malaika kwa mavazi mazuri, lakini ukifika wanakoishi utadhani ni vijakazi. Alimsihi Sofia aondoe shaka. Alimweliezea kuhusu msingi wake wa kimaskani. Kwamba ameishi sana 'gheto' na maisha hayo anayapenda. "Nikiwa Dar hupendelea sana kutembelea sehemu za Manzese. Nikiwa Arusha makazi yangu ni Ngarenaro. Na nikiwa Moshi nastarehe zaidi nikiwa Majengo", alimhakikishia. "Sababu hiyo ndiyo iliyonifanya niishi katika hoteli hii ndogo badala ya kubwa kama Mwanza Hoteli".



    Maneno hayo yalimaliza ubishi wa Sofia. Usiku uliofuata uliwakuta Kirumba katika chumba chake.



    Chumba kilikuwa katika hali ambayo Proper aliitarajia. Raslimali za muhimu zilikuwa kitanda kikuukuu chenye godoro kukuukuu la sufi ambalo halikuwa na hadhi ya kuitwa godoro pia kulikuwa na sanduku, meza na sufuria mbili tatu zilizonuna kwa uchafu. Ambacho Proper hakutegemea ni ukarimu wa kunguni na mbu walikuwa huru katika chumba hicho. Walimlaki moja kwa moja bila kumpa fursa ya kujipumzisha.



    Yote hayo Proper alilazimika kuyastahamili eti kwa sababu amependa, kumbe ni uhitaji tu. Alikusudia kujisetili akisubiri siku kuu ili atimize lengo lake. Hakuna askari wala mpelelezi yeyote ambaye angefikiria kumtafuta pale. Alitarajia kuwa wangeweza kumsaka katika mahoteli makubwa na kwenye vitongoji vikubwa vikubwa, siyo kwa malaya wa chini kama Sofia anayeishi maeneo yaliyosahaurika.



    Siku mbili zikapita bila ya kitu chochote cha kawaida kutokea. Proper alishinda ndani akijisomea vitabu, nae Sofia alijishughulisha kutafuta vyakula na vinywaji. Sofia alikuwa akipewa pesa zilizozidi mahitaji yake ya kawaida. Proper alikuwa amemruhusu kununua mavazi mapya. Hali hii ngeni ilimuinua Sofia, akawa anapepea mfano wa kishata. Nafasi yoyote iliyojitokeza, ilitumiwa kufanya mapenzi. Sofia alijitia kila aina ya juhudu kumridhisha Proper. Lakini hakuweza kuutambua unafiki wa Proper. Akazidi kutekwa akili na vitendo vya mtu huyu. Hata hivyo sauti nyingine ilimnong'oneza atahadhari.



    Jioni ya siku ya tatu, mambo yalianza kwenda mrama. Sofia alirejea kutoka mjini na gazeti mkononi. Alimfuata Proper aliyelala chali kitandani na kumfungulia ukurasa wa tatu ambao ulikuwa na picha sita chini ya kichwa cha habari kilichosema;



    "TANGAZO LA POLISI.

    JIHADHARI NA MTU HUYU- MARA UMWONAPO IARIFU POLISI. ANATAFUTWA KWA MAUAJI YA WATU WENGI NA ANAWEZA KUUA WAKATI WOWOTE, KUWAMAKINI".



    Proper alisoma haraka haraka. Kisha alizitazama picha hizo kwa makini. Moja ilikuwa yake halisi. Zilizosalia zilikuwa picha za kuchora. Zilikuwa zimechorwa kwa namna mbalimbali kuonyesha nywele zote; nyingine ilichorwa kuonyesha madevu mengi, nyingine kavaa miwani na kadhalika. Ni moja kati ya picha hizo ambayo ilikuwa imefanana kikamilifu na sura aliyokuwa akiitumia sasa. Alijitia utulivu na kumgeukia Sofia na kumwuliza kwa upole, "Ni hii tu uliyoiona habari ya maana katika gazeti lote".



    "Hapana. Nilitaka kukuonyesha huyo mtu. Naona mmefanana naye sana".



    "Tumefanana!" Proper alijitia kushangaa. "Mimi nafanana na huyo anayetafutwa kwa mauaji? Haiwezekani".



    "Mmefanana sana Beka. Nadhani ni wewe".



    "Usiwe mjinga Sofia, mimi siwezi kuwa muuaji".



    "Kweli kabisa. Hata yule rafiki yangu aliyekuja hapa jana amesema hivyo. Labda ungesoma hapa chini uone".



    Proper alianza kusoma kifungu hicho kilichoandikwa kwa herufi za mlazo.



    Mtu huyu ni hatari sana, anatakiwa mapema mno. Zawadi nono ya shilingi laki nne itatolewa kwa mtu yeyote atakayewezesha kukamatwa kwake. Inasemekana kwa sasa yuko mjini Mwanza au mikoa ya jirani. Unaonywa tena kujihadhari naye...



    "Ni wewe Beka?", Sofia alisisitiza huku akimkazia macho.



    "Siyo mimi". Sauti ya Proper ilikuwa ya utulivu mkubwa.



    "Kwani unanionaje mimi, naweza kuwa muuaji?".



    "Hapana, lakini hiyo picha inaonyesha ni wewe".



    "Achana na picha hii. Huoni kama huyu amechorwa tu? Usiwe msichana mjinga Sofia. Mimi ni mtu ninayejiheshimu sana huko kwangu. Wasichana kama wewe, wazuri zaidi yako, ninao kama ishirini hivi ambao wanalipwa mshahara mzuri kutoka katika mfuko wangu. Na wanaume wengi wasiopungua mia, wote wako chini yangu, wote wananiheshimu. Au kwa vile niko nawe katika chumba hiki hafifu ndipo umefikia hatua ya kuniita mwuaji?".



    "Sivyo mpenzi, ila..."



    "Ila..."



    "Nina mashaka yule rafiki yangu amekwenda kutoa taarifa polisi. Laki nne siyo pesa ndogo".



    "Polisi. Akiwaleta hapa, wakinikuta mimi watanitia ndani kufunza adabu. Ondoa hofu. Sofia njoo kitandani, tujipumzishe nikudokeze jambo. Lete ulimi tufurahi".

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Sofia alisogeza shingo. Hakutarajia radi iliyompiga ghafla. Lilikuwa pigo kali jepesi ambalo lilitua katika shingo na kulivunja kabisa. Sofia hakujua kapigwa na nini. Wala hakuona ugumu wa kufa. Alianguka chini na kupapatika kwa muda, kisha akakata roho.



    Proper alifanya kazi haraka haraka. Aliuzoa mzoga wa aliyekuwa Sofia na kuulaza kitandani. Akaufunika vizuri kwa shuka. Kisha alikusanya vifaa vyake na kutoka nje. Giza lilikuwa limeanza kutanda. Hakuona haja ya kujificha kama alivyotegemea. Aliifuata polepole barabara iendayo mjini. Alipofika Mabatini, alisimamisha taksi na kuingia ndani.



    Dereva taksi alikuwa kijana wa Kiarabu mwenye ndevu nyingi. Alimsalimu Proper kwa adabu, kisha akamuuliza wapi anataka kwend. Proper hakumjibu kwa maneno bali kwa kitendo fulani. Aliudidimiza mkono wake katika begi lake na kutoa bastola yake. Aliigandamiza ubavuni mwa kijana huyo.



    "Ukifanya ujinga utapoteza maisha. Nataka wewe na gari hii mfuate matakwa yangu. Haya endesha mpaka nitakapokwambia wapi tuelekee".



    Huku akitetemeka, macho yakiwa yamemtoka, kijana huyo alilitia gari moto na kuliondoa taratibu huku mapigo ya moyo yakimwenda kasi kwa hofu.



    "It's him. It's him. That's his style" Inspekta Kombora alifoka. Kisha alijisahihisha haraka na kusema polepole; "Ndiye. Bila shaka ni yeye huyu muuaji". Macho yake yalikuwa yakiwatazama wasaidizi wake wawili ambao waliketi mbele yake kimya wakimsikiliza.



    Walikuwa wakijadili taarifa ambayo ilikuwa imewafikia muda mfupi kutoka Mwanza. Taarifa hiyo ililetwa na mtu mmoja ambaye alimgundua mtu huyo anayesakwa kwa udi na uvumba, Proper mahali alikojificha. Mtu aliyetoa siri alieleza kuwa anayetafutwa amejificha nyumbani kwa mwanamke fulani. Lakini makachero walipoivamia nyumba hiyo, waliambulia kukutana na maiti ya mwanamke aliyekutwa amelala chali kitandani. Tayari mhusika mkuu alikuwa ametoweka. Ushahidi uliopatikana ulieleza kuwa mtu huyo alimhukumu mwanamke huyo kifo baada ya kubaini kuwa amejulikana. Hakika mtu huyo ni hatari. Makachero walibaini baadhi ya vifaa vyake vya kazi na maandishi ya kijasusi. Mambo mengi yalikizonga kichwa cha Inspekta Kombora, lakini hakukata tamaa.



    "Ni yeye. Msimpe nafasi tena akaponyoka", Inspekta Kombora aliagiza huku akisisitiza. "Hakikisheni yeye au maiti yake inapatikana haraka kabla ya kesho", aliongeza huku kila baada ya nusu saa akipiga simu kuulizia maendeleo ya operesheni hiyo.



    Ilikuwa alfajiri ya siku ya pili Inspekta Kombora alipopata taarifa nyingine alipokuwa ofisini kwake ameketi na wasaidizi wake wakijadili. Taarifa mpya ilisema taksi moja aina ya Peugeo 504 ilikuwa imeokotwa katika pori la Ngara mpakani mwa nchi za Rwanda na Burundi kando ya barabara iendayo Burundi. Dereva wa gari hiyo aliokotwa akiwa hoi bin taaban mahututi. Hivyo hakuwa na chochote za kueleza alipoulizwa ilikuwaje gari hilo likaweza kuvuka vipingamizi vyote vya barabarani kutoka Sengerema, Geita, Biharamuro hadi kufika Ngara. Lakini baada ya kupatiwa matibabu, aliweza kueleza kuwa gari lake lilitekwa na mtu mmoja ambaye alikuwa akielekea Burundi. Kwamba mtu huyo alimpiga kwa dhamira ya kuua, huenda alimwacha hai kwa kukosea tu akidhani kuwa tayari ameua. Dereva huyo alipoonyeshwa picha ya Proper alimtambua mara moja.



    "Ni yeye", Inspekta Kombora alirudia tena. Lakini ni kitu gani kimempeleka huko mpakani?".



    "Ametoroka afande", mmoja wa wasaidizi wake alimjibu.



    "Amesoma alama za nyakati, ameona mambo yamezidi kimo. Akifika Bujumbura atapata usafiri ambao anaamini utamtoa nje ya Afrika mapema awezavyo".



    Inspekta Kombora alifikiri kwa muda kabla hajasema, "Labda. Hata hivyo, mimi sioni kama kwamba mtu huyu ametoroka. Sio mtu wa kukata tamaa mapema. Huyu mwendawazimu anakusudia kufanya unyama wake kwa vyovyote vile".



    "Mambo yamemzidi kimo afande, ndiyo maana anahaha kutoroka".



    "Hata hivyo, sidhani kama ana haki ya kuvuka mipaka ya nchi hii akiwa salama. Alikuwa mtu wa kufa. Na nitahakikisha kuwa Serikali ya Burundi inamtia mbaroni ili arejeshwe nchini kusubiri kitanzi chake".



    Inspekta Kombora alikuwa akiilaani bahati yake kimoyomoyo. Alijilaumu kwa kutangaza picha za mtu huyo gazetini. Ingawa hiyo ilikuwa njia yenye uhakika, lakini kwa polisi aliyehitimu, kitendo hicho huwa cha mwisho katika harakati za kumpata mtuhumiwa. Kitendo hicho mara nyingi humfanya mtuhumiwa kujianda kwa mbinu mpya. Ama, mtu kama huyo huweza kutenda uovu zaidi usiotazamika. Inspekta Kombora alifahamu kuwa kufa kwa mwanamke yule, na kuponea chupuchupu kwa dereva taksi, ni matokeo ya picha hizo zilizotokea gazetini. Inspekta Kombora alilaani baada ya kuona mpango wake umesababisha kifo cha mwanamke. Angejitakasa tu kwa kumnasa Proper au kwa kumfumua kichwa chake 'kibovu' kwa risasi. Ilimsikitisha sana.



    Aliufikia uamzi wa kuzitangaza picha hizo gazetini baada ya kuona siku ya mkutano wa wakuu wa nchi huru za Afrika ikikaribia bila mtu huyu hatari kukamatwa.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Pengine imesaidia", aliwaza. "Kwa hiyo tuseme mtu wetu kaingia Burundi?", Inspekta Kombora alisema baadaye.



    Wasaidizi wake waliokuwa wameketi kando wakimsikiliza wakatikisa vichwa kukubaliana naye.



    "Hata hivyo nataka ulinzi uzidi kuimarishwa hadi baada ya mkutano. Makachero wengi zaidi watumwe Arusha. Na msako wa mtu wetu uendelee kama awali. Sina imani na mtu mwehu kama yule hata chembe. Anaweza kuwa popote na akathubutu kufanya chochote".



    Arusha, maandalizi ya mkutano yalikuwa yamepamba moto. Zikiwa zimesalia siku chache wageni mashuhuri waanze kuwasili mjini Arusha, viongozi mbalimbali wa chama na serikali walikuwa kazini usiku na mchana. Walijitahidi kuhakikisha kwamba hakuna lolote ambalo lingeweza kuuchafua mkutano huu ambao ulikusudia kuiandika upya historia ya Afrika.



    Hoteli ya Maunt Meru iliangaliwa kwa uangalifu mkubwa. Ilipangwa tafrija zifanyike katika hoteli hii. Wajumbe wangeenda baadaye katika jengo la mikutano la kimataifa la Arusha Internation Confrence Centre (AICC) ambako wangehudhuria kikao. Usafi wa hali ya juu ulidumishwa. Maua ya aina aina yalipamba mazingira ya hoteli hii. Bendera za nchi tofauti zilipepea kuthibitisha matayarisho ya mkutano huo muhimu.



    Vinywaji na vyakula viliandaliwa kwa uangalifu mkubwa kulingana na mahitaji ya kila kiongozi na ujumbe wake. Wataalamu, wapishi na wachanganyishaji vinywaji stadi walipewa maagizo kwa tafsili. Wahudumu waliteuliwa kwa uangalifu mkubwa wakiwa tayari kutekeleza wajibu wao. Sura na maumbile yao vilizingatiwa ili kuwaridhisha na kuwasisimua washiriki wa mkutano huu.



    Kati wa wahudumu waliondaliwa kutoa huduma katika tafrija hii alikuwepo Nuru, msichana ambaye aliumbwa akaumbika. Msichana huyu aliumbwa kwa njia ambayo haingeweza kupambanuliwa kwa urahisi. Hakuwa mfupi wala mrefu, siyo mnene wala mwembamba, alikuwa kati kama aliyepimwa kwa mizani ya kipekee. Sura yake pia ilitatanisha. Umtazamapo, utashindwa kusema moja kwa moja kama ni binti wa Kiajemi, Kihindi, Chotara wa Kizungu au Bantu halisi. Mtazamo wake, mcheko wake, kuzungumza kwake, mwendo wake, kila kitu kiliwatoa jasho watazamaji wake. Baadhi ya watu walidiriki kutamka kwamba Nuru hakuwa binadamu wa kawaida. Eti alikusudiwa kuwa malaika, likatendeka kosa la kumleta duniani. Kwamba kosa kama hilo hutendeka mara moja kila baada ya miaka mia moja duniani.



    Mengi zaidi yalisemwa juu ya Nuru. Sifa hizi zilimwingia kichwani. Wengi walitamani kumchumbia lakini hakuna aliyefua dafu. Na kuna hata Masheikhe waliokuwa tayari kuwapa taraka wake zao kwa ajili ya msichana huyu. Msichana huyu akakamilisha miaka ishirini na mitano bila mume wala mchumba. Nuru hakumuona yeyote ambaye angemstahili. Wenye mapesa aliona adamu zimewalemea. Wenye vyeo serikalini, aliwaona wanafiki. Kwa muda mrefu, akaendelea tu kuwa Nuru mwenye 'kiburi' japo alicheka na watu na watu kama kawaida.



    Nuru aliajiriwa kama Katibu Mahsusi wa mmoja wa mmoja wa wakubwa katika hoteli hii ya Maunt Meru. Lakini umbo na sura yake ya kuvutia ilimfanya ateuliwe mara kwa mara, kuwahudumia wageni wa kimataifa waliofika nchini. Viongozi ni watu, hawana roho za chuma wala macho ya shaba, wanaujua uzuri wa wasichana na kuuthamini. Nuru alikuwa na uwezo wa kumsahaulisha yeyote na matatizo yake. Huwafanya viongozi anaowahudumia watabasamu kwa dhati. Sio-lile tabasamu la 'kisiasa' lililojaa uzandiki. Mwanadada huyu atoapo kinywaji hakuna anayekikataa.



    Jinsi hii Nuru alikuwa amemaliza shughuli za kutwa nzima na kuanza kujiandaa kutoka. Aliamua kufuata ngazi badala ya kutumia lifti. Alipokuwa akimaliza ngazi za ghorofa ya tatu, alikutana na kijana huyu, Duncan Adolf. Alikuwa mpangaji ambaye ameishi hotelini hapo kwa zaidi ya wiki sasa. Lakini aliondokea kuzoeana na karibu kila mtu hotelini hapo kama kazaliwa na kuishi hapo hapo. Wafanyakazi na wageni wote alizungumza nao vizuri, kila mmoja akipenda kumsikiliza. Naye Duncan alikuwa mwingi wa maongezi. Aliongea juu ya kila kitu, uchumi, vita, utamaduni, starehe na kadhalika. Alionekana kuwa na upeo mkubwa wa elimu katika kila fani.



    Ilisemekana kuwa Dancan alikuwa mzaliwa wa Uingereza ambako baba yake aliishi tangu ujana wake. Kwamba Duncan alikuwa ameamua kurudi nyumbani tazama uwezekano kuanzisha kiwanda cha utengenezaji wa vipuri vya magari. Mradi huo ungeendeshwa na Duncan mwenyewe kwa pesa zake ambazo alipewa na baba yake, ambaye ni tajiri sana nchini Uingereza. Nuru hakupata kumsikia Duncan mwenyewe akisema maneno hayo. Lakini kwa jinsi alivyomuona, mambo hayo hayangekuwa mbali na ukweli.



    Alikuwa na sura yenye dalili ya utulivu, sauti yake ikionyesha uridhivu wa moyo na mwendo wake ukionyesha uthabiti wa nia. Sifa za kijana huyu zilimvutia Nuru. Hakumbabaikia kama wanaume wengine. Walipokuwa pamoja, maongezi yake yalikuwa ya kawaida. Awali, Nuru alimchukia Dancan kwa kutoonyesha nia yoyote. Lakini baadaye alianza kumpenda na kumtamani. Alimhusudu Dancan na husuda ikazaa mapenzi. Na penzi hilo likawa la upande mmoja, likaumiza kama jeraha lisilo na dawa. Penzi lilimchoma Nuru.



    "Kwanini kijana mwerevu kama huyu hawezi kubaini kuwa nampenda?" Nuru alijiuliza kimoyomoyo.



    "Salama tu, za kwako bibie?"



    Ndipo Nuru alipong'amua kuwa alikuwa amemsalimu Duncan bila kutegemea.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Si vizuri msichana kuanza kumsalimia mvulana mara kwa mara; Nuru aliwaza akiwa na haya kidogo usoni. "Siyo mbaya", akamjibu.



    Kama kwamba macho ya Duncan yalikuwa yakimtazama kwa tabasamu; kama yanayosoma kila wazo katika fikra za Nuru. Lakini, yanaona? Nuru alijiuliza akitabasamu kidogo. Pengine yanaona! Nuru aliwaza baada ya kuona Duncan akilijibu tabasamu hilo na kumshika mkono na kusema polepole.



    "Naona ndiyo unatoka zako. Bi. Nuru. Sujui itakuwa adabu kuomba nikaribishwe nyumbani? Nimechoshwa na maisha ya hotelini usiku na mchana".



    Ingawa Nuru alifurahishwa sana na ombi hili, lakini hakulitegemea. Hata hivyo, alijikumbuka na kujibu haraka haraka: "Karibu wakati wowote, isipokuwa leo tu".



    "Kwanini isiwe leo, maana nilisoma mahala fulani ambapo Mwalimu Julius Nyerere alisema linalowezekana leo lisingoje kesho".



    "Ndio, ndiyo", Nuru alijibu. Lakini leo imekuwa ghafla mno. Itabidi nipate muda wa kujiandaa kukaribisha mgeni"...



    "Ujiandae? Humkaribishi rais wala waziri nyumbani kwako. Ni kijana mmoja asiye na hili wala lile".



    "Hata kama".



    Maongezi hayo yalikoma Duncan alicheka ghafla na kusema polepole, "Usijali, siwezi kukutembelea ghafla kiasi hicho. Tutapanga baadaye. Au sivyo?" Akauachia mkono wa Nuru na kuuhamishia begani. "Samahani sana kwa kukuchelewesha. Kesho tutazungumza kirefu. Kwa sasa nadhani tuagane".



    Baada ya kuagana na Ducun, Nuru alitelemka ngazi polepole, moyo wake ukiwa umejaa furaha na faraja. Mguso wa Duncan ulikuwa na ulioacha kitu fulani katika nafsi yake. Sauti ilikua kama kinanda kinachoburudisha fikra zake. Nuru alitamani arudi nyuma ili aendelee kumsikiliza Duncan akiwa ameshikwa mkono. Hata hivyo, alijikaza kisabuni, akamaliza ngazi na kuliendea gari lake ambalo lilikuwa likimsuburi. Alipoingia ndani ya gari, alilitia moto na kuelekea Sanawari ambako alikuwa akiishi katika moja ya nyumba za shirika la nyumba.



    Mara Nuru akamuona tena mzee yule. Alikumbuka kuwa leo ilikuwa mara ya pili kila atokapo kazini, mara ya kwanza alimuona mzee huyo akiwa amesimama upande wa pili wa barabara akimtazama. Alikuwa mzee mwenye kichwa ambacho nusu ya nywele zake zilimezwa na mvi na kidevu chenye ndevu fupi nyeusi. Kilichomfanya Nuru amtie akilini mzee huyu ni mavazi yake. Alikuwa amevaa suti nyeusi ambayo kutoka mbali ilidhihilisha kuwa ilikuwa imegharimu pesa nyingi. Nuru alimtazama mzee huyo kwa mshangao kidogo kisha alitoa ufunguo wake na kujishughulisha na kufuli. Mlango ulipofunguka, alimtazama tena mzee yule. Akashangaa kumwona akivuka barabara kumjia, mkononi akiwa na fimbo ya kutembelea ambayo ilimsaidia kuvuta mguu wake mmoja ambao ulionekana mbovu. Nuru hakudhani kama mzee huyo alikuwa akimfuata yeye, hivyo aliingia zake ndani na kujitupa chali juu ya kochi lake refu.



    "Unataka nini?" Nuru alihoji.



    "Kukuona tu. Hujui kuwa umeumbwa vizuri sana kuliko binadamu wote niliopata kuwaona".



    "Toka nje! Nani kakuruhusu kuingia kwangu?".



    "Niruhusu nikutazame mara moja zaidi. Siyo mzaha ninapokwambia kuwa uzuri wako hauna mfano wake. wazazi wako walimpa nini Mwenyezi Mungu mpaka ukazaliwa mrembo namna hii".



    Mzee huyu aliyasema haya huku akijiweka juu ya juu ya kochi lililomwelekea Nuru na kupangua mifuko yake ambamo alitoa sigara, ambayo alianza kuivuta kwa utulivu.



    Ulikuwa utulivu mkubwa ambao ulizidisha hofu na mshangao wa Nuru. Mtu huyu ni nani? Na anataka nini kwangu? Nuru alijiuliza kimoyomoyo. Zaidi ilimshangaza kwa kutofahamu kitu gani hasa kilikuwa kikiujaza moyo wake mbele ya mtu huyu ambaye alionekana mstaarabu mwenye sura iliyoficha utajiri mwingi, au cheo kikubwa sana ama vyote pamoja.



    Mgeni huyu alikuwa akiyasoma mawazo yote ya Nuru. Rohoni kicheko kikubwa kilikuwa kikichanua. Nuru angefanya nini kama angefahamu kuwa yeye hakuwa mwingine zaidi ya mtu yule ambaye Inspekta Kombora na jeshi lake lote la polisi walikuwa wakimtafuta kama chawa na kumwombea mauti kama watu waishio jangwani waombavyo mvua. Huyu hakuwa mwingine zaidi ya Proper.



    Kuwa kwake hapa aliamini kuwa ilikuwa siri yake binafsi. Tayari alikuwa amewapumbaza polisi kwa kujifanya kuwa amekimbilia nchi jirani. Bila shaka waliamini kuwa alivuka mpaka na kwenda zake Burundi baada ya kumuua yule mwanamke malaya ambaye alimhifadhi chumbani kwake. Na wataendelea kuamini kuwa yule dereva aliyeponea chupuchupu. Hawatashuku kuwa alimwacha hai ili awe shahidi ambaye angefanya kazi ya kuwarahisishia polisi kumtambua na kuwahakikishia kuwa alitorokea Burundi.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hakwenda Burundi na asingeweza kwenda Burundi. Alichofanya ilikuwa hila ya kumpumbaza Inspekta Kombora ili alegeze ulinzi mjini Arusha baada ya kudhani kuwa Proper alikuwa amekimbia. Hivyo alitafuta usafiri mwingine uliomrejesha Mwanza mjini ambako alitumia ujuzi wake usio na mashaka kujibadili. Kisha akaingia Arusha ambako tayari amejiandaa kikamilifu kwa ajili ya kazi yake. Kazi ambayo alikuwa amedhamilia kuifanya. Kazi ya kuhakikisha marais wasiopungua kumi, mawaziri wao wasiopungua hamsini na makatibu wasio na idadi wakianguka na kupoteza maisha mmoja baada ya mwingine, hadharani.



    Msichana huyu alikuwa na bahati mbaya sana. Uzuri wake ulikuwa umemponza. Ni mkono wake utakaotumika kuyateketeza maisha ya viongozi hao. Proper alikuwa amemchunguza kwa muda mrefu, baada ya kukusanya taarifa za watu wake ambao humuuzia habari. Watu ambao hawakujua kama Proper bado yuko nchini au duniani.



    Itakuwa kazi rahisi...



    "Unataka nini?" Sauti tamu ya Nuru ilimzindua Proper.



    "Kweli!", Proper akajitia mshituko. "Tafadhali usinifikirie kuwa mimi ni mzee mhuni. Kama nilivyosema awali sura yako nzuri ndiyo iliyonivutia. Haja yangu ni kukuona tu..." Nuru alifungua mdomo ili atie neno. Lakini mgeni wake alimkatiza kwa kusema.



    "USiwe na haraka bibie. Usiseme neno ambalo utalijutia baadaye. Ningependa unielewe kuwa mimi ni mzee asiye na hatia yoyote. Sina wazo lolote baya juu yako. Nakwambia ukweli ambao sipendi kusema kwa mtu yeyote. Si unaliona hili jicho langu moja? Pamoja na mguu mmoja? Basi waliniharibia mguu wangu na jicho hilo la pili. Walinifanyia ukatili mwingine ambao hausahauliki. Walinivua nguo na kuukata uume wangu".



    "Ilikuwa sauti ya kusikitisha. Sauti iliyobeba kila chembe ya majinzi na simanzi. Ikamtia Nuru hudhuni hata akajikuta akimtazama mgeni huyo kwa nia ya kumsaidia.



    "Kwa kweli ni habari ambayo sipendi kusimulia mtu yeyote. Ni msiba ambao daima nimeuhifadhi katika moyo wangu. Nimekusimulia ili tu usinifikirie kama mmoja wa wazee waroho ambao vijana mnawaita Sugar daddy. Nia yangu ni kuwa nawe kwa vipindi fulani fulani tu. Unajua mtu aliyenyang'anywa nusu ya uhai wake alivyo".



    Nuru hakujua ajibu nini. Hivyo alikaa kimya akimtazama mzee huyu kwa huruma. Mzee ambaye alitabasamu kwa namna ya kujifariji kisha akasema.



    "Isikutishe sana habari hii bibie. Ni tatizo langu binafsi ambalo nimelizoea baada ya kuwa nalo kwa zaidi ya miaka ishirini sasa. Jambo ambalo limeufanya utajiri wangu wote uwe hauna thamani yoyote. Kwani kila mtu ananishakia kwa kutoniona hata mara moja na mwanamke yeyote japo ni wengi wanaonimezea mate. Basi bibie, moja kati ya mambo ambayo nitakuomba endapo itawezekana ni safari. Ningependa kusafiri nawe kwenda nchi za Magharibi ambako kuna miradi yangu. Rafiki zangu huko wakiona na mtu kama wewe walau kwa wiki moja tu watabadili mawazo juu yangu. Unasemaje bibie?".



    Nuru aliposita na kuonyesha kutomwelewa, haraka mzee huyo alimuonyesha tabasamu na kusema, "Usijali! Sikutegemea jibu la haraka kiasi hicho".



    Kisha alianzisha maongezi ya kawaida. Nuru alijikuta akisahau hofu yake juu ya mzee huyu na kuanza kumzoea. Ikamshangaza kuona mzee huyo alivyo mwingi wa maongezi matamu.



    Baada ya muda Proper aliinuka na kuaga. Alipofika mlango alisimama na kumgeukia Nuru, "Siyo ustaarabu kuzungumza na bibi mzuri na mkarimu kama wewe kisha niondoke bila kumwachia zawadi yoyote. Hasa nikikumbuka kuwa kwa miaka ishirini iliyopita hajatokea mwanamke ambaye aliupoteza muda wake kunisikiliza".



    Mkono ulitoka mfukoni na kijisanduku kidogo ambacho alikifungua na kitoa kidani cha kuvutia. Kilikuwa kikimelemeta kwa madini ya thamani kubwa, pengine mchanganyiko wa almas, dhahabu na Tanzanite.



    "Tafadhali pokea", mzee alisema akikabidi kidani kwa Nuru.



    "Na nakuomba unifanyie hisani ya kuuvaa kuanzia leohadi hapo tutakapoagana".



    Nuru alikipokea kidani hicho na kukitazama kwa mshangao na tamaa. Hakujua alikuwa amepokea kitu gani.



    Usiku ulimkuta Nuru akiwa bado kaduwaa, hajui lipi anawaza, lipi anataka. Mkoni alikuwa kashika kile kidani cha thamani alichopewa na yule mzee tajiri. Mara kwa mara alikitazama, hali hakioni. Fikra zake zilikuwa maili kadhaa wa kadhaa nje ya chumba chake. Zilikuwa zikiitazama kwa namna ya njozi safari yake huko Ughaibuni, katika nchi kubwa kubwa na miji mashuhuri. Miji ambayo hakuwahi kuota kama angeweza kuikanyaga. Alijiona akitembea, mji baada ya mji, bega kwa bega na mzee huyo chongo na nusu kiwete. Alitarajia kuiona miji yote mizuri, alitarajia pia safari ya kusisimua na kila aina starehe ikimwandama. Lakini hakuhisi kama atapata raha katika msafara huo. Ni upungufu wa hisia hizo, uliomfanya ajiulize kama tukio la kutembelewa na mzee huyo, pamoja na lile ombi la kwenda naye nje, ilikuwa bahati au balaa.



    Ndiyo, mzee alikuwa na dalili zote za utajiri, wala hakuwa na dalili zozote za ubahili. Ni dhahiri kuwa mwisho wa safari hiyo Nuru asingeendelea kuwa Nuru yule yule kiuchumi, aliwaza. Hata hivyo bado hakujisikia kulisherehekea pendekezo hilo. Lilimtisha badala ya kumfurahisha, likambabaisha badala ya kumburudisha. Laiti pendekezo hilo lingekuwa limetolewa na yule kijana... nani vile jina lake? Duncan.



    Ni hilo lililokuwa limemfanya Nuru achanganyikiwe badala ya kufurahi. Wazo la kwamba Duncan angechukua nafasi ya mzee huyo na kumwomba chochote ama lolote. Angekuwa tayari kufuatana naye hata mwisho wa dunia. Mawazo hayo yalimfanya Nuru atokwe na machozi. Hakujua kitu gani kinamliza.



    Nuru hakuwa ametoka katika familia tajiri wala masikini. Ilikuwa familia ya kawaida kama zingine nyingi za hapa nchini. Baba yake mzazi alikuwa amefia katika kazi yake ya ualimu wa shule ya msingi huko kwao Mbeya. Mama yake alikuwa mzee ambaye hakukubali kuitwa mzee bali aliendelea kulitegemea jembe la mkono badala ya kumtegemea mwanaye Nuru, ambaye ni binti wa pekee. Elimu ya kidato cha sita na kozi mbalimbali za ukatibu mahsusi ni urithi pekee ambao hayati baba yake alikuwa kamwachia Nuru. Pesa za kuchezea na starehe za kusisimua ni vitu ambavyo Nuru hakuwa navyo. Alivikuta ukubwani. Hivyo havikumbabaisha ka ilivyo kwa wasichana wengine. Kutobabaika huko ndiko kulikomwezesha kuwa huru hadi sasa. Au, tayari angekuwa kashawishika kuwa mke wa meneja fulani au bepari fulani. Alikuwa kashinda nguvu ya tamaa.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Lakini ulikuwa ushindi usio kamili. Kwani mara kwa mara alihisi kudhulumiwa jambo kimaisha. Kwamba alikuwa hajapata haki yake katika suala la mapenzi. Kwamba hana bahati ya kufuatwa na bwana anayestahili. Mzee huyo tajiri alikuwa mmoja tu katika orodha isiyo na mwisho ya mabwana ambao humfuatafuata. Laiti Duncan angekuwemo katika orodha hiyo...



    Usiku ulipokolea, Nuru alijibwaga kitandani. Rohoni aliuomba usingizi umchukue haraka, na umfanye aote akiwa katika safari hiyo na Duncan, wakielekea popote duniani. Hakuota chochote. Tangu lini mtu akaota wakati yuko macho.



    ******************************



    "Mbona hivyo bibie, unaumwa?".



    Swali hili lilimzindua Nuru. Ingawa Duncan hakujua ugonjwa wake lakini sauti hiyo ilikuwa kama dawa iliyomfanya Nuru apone ghafla. Alimtazama msemaji kwa haya kidogo huku kitu ambacho asubuhi hiyo hakikupata kuutembelea uso wake kilijitokeza ghafla na kuchanua. Lilikuwa tabasamu zuri kama tabasamu la Nuru ilivyo.



    "Siumwi kabisa kaka Duncan", alijibu baadaye akiyaepuka macho yake. Kila mtu asubuhi hiyo alikuwa amemuuliza swali hilo. Wote aliwaambia kuwa haumwi ingawa hakuna aliyeelekea kuamini.



    "Kama huumwi basi kuna mtu amekuudhi sana. Hana haki ya kufanya hivyo. Ni nani huyo? Au siruhusiwi kuuliza au kujua?", Duncan aliendelea.



    "Wala hamna aliyeniudhi".



    "Sidhani kama ni kweli".



    "Kweli kabisa. Labda ni kwa ajili ya kukosa usingizi. Leo sikulala kabisa".



    "Ina maana kuna mtu amekukosesha usingizi. Basi sidhani kama ni haki kwa mtu yeyote kukosa usingizi. Nina haki ya kuuliza, ni nani mtu huyo?".



    Sauti ya Duncan ilikuwa ya kawaida, yenye mzaha kidogo. Hata hivyo Nuru alihisi msisitizo fulani katika sauti hiyo. Akamtazama usoni. Ndiyo, yalikuwa macho ya mtu ambaye hakupata usingizi mzuri vilevile.



    Kisha Duncan alicheka na kusema, "Nadhani ungekuja chumbani kwangu muda wa mapimziko dada Nuru. Kuna mengi ambayo ningependa kuzungumza nawe.



    Nuru aliitikia kwa kichwa.



    Alimkuta Duncan katulia juu ya kochi, mkononi kashika kitabu kinachoitwa The Day of the Fackal.



    "Karibu sana".



    "Asante", Nuru alijibu akiketi juu ya kochi la pili. "Naona unamsoma Frederick Forsyth. Watu wanasema ni mtunzi mzuri, lakini mimi hanifurahishi sana".



    "Kwanini?".



    "Sijui kwanini, Nawapenda waandishi wengine wa vitabu kama Mario Puzo, Denis Robbins na Harold Robbins zaidi yake".



    Maongezi ya vitabu yalichukua muda. Huyu akimsifu mwandishi yule, huyu akiuliza kama fulani kamsoma fulani, na kadhalika. Kisha yaliingia maongezi ya kawaida. Duncan aliuliza mengi juu ya Nuru na maisha yake. Maswali yake yalikuwa mafupi yaliyohitaji majibu marefu. Kila jibu lilielekea kumsisimua sana Duncan. Mazungumzo ya watu hawa wawili yaliibuka kama ambavyo watu waliozoeana kwa muda mrefu, bila kuzingatia chochote. Nuru aliyazungumza yale yote ambayo yalikuwa yakingojea fursa kama hii. Mara akawa akisimulia habari ya juzi na jana.



    "Mzee wa ajabu sana".



    "Yupi"."Yule wa jana. Mtu akufuate ghafla. Akuambie kuwa wewe ni mzuri sana, hii hapa zawadi yako. Akupe mkufu mzuri kama huu, na kukuahidi kwenda naye ulaya".



    Akamsimulia Duncan yote kwa urefu na mapana. Habari hii ilielekea kumvutia sana Duncan. Baada ya maswali mengine mawili matatu juu ya mzee huyo alimwomba Nuru amuonyeshe mkufu huo. Nuru akauvua na kumpatia Duncan. Aliuchunguza kwa muda mrefu, akausifia uzuri na thamani yake. Kisha Duncan aliinuka na kwenda chumba cha pili ambacho kina choo na bafu, akauacha huko na kurejea mikono mitupu.



    "Mkufu wangu umeusahau?", Nuru aliuliza.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    "Hapana nimeuacha makusudi. Unajua mimi kidogo nina wivu? Nilikuwa sina raha kabisa kuzungumza nawe nikiwa na mkufu huo mkononi. Najiona kama niliyeachwa nyuma hatua moja na huyo mzee".



    "Kwa vipi?".



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog