IMEANDIKWA NA : AHMED MUSSA MNIACHI
*********************************************************************************
Sehemu Ya Kwanza (1)
Niliwasili Dar es salaam saa tisa na nusu alasiri, ilikuwa ni mapema zaidi kuliko nilivyotarajia. Mvua ambayo ilinyesha masaa kadhaa yaliyopita ilisaidia kupunguza vumbi ingawa ilisababisha fukuto la joto kuzidi.
Watu walikuwa wametawanyika ovyo pale kituo kikuu cha mabasi Ubungo kana kwamba ni siafu walioangukiwa na kaa la moto. Miongoni mwao walikuwa ni abiria ambao wanasafiri huku wengine wakiwasili. Pia walikuwepo wapiga debe ambao walileta kero kubwa kwa abiria.
Bonge alinionya kuwa nisipitie sehemu nyingine kabla ya kumfikishia mzigo wake. Pia alinitisha kuwa iwapo sitatekeleza maagizo yake, basi asingenipa malipo yangu kwa kazi ya kusafirisha mzigo ule. Vile vile alinikumbusha kuhusu ile picha ambayo ilikuwa inaniweka katika wakati mgumu. Ni picha ambayo leo inanifanya niwe mtumwa inanifanya pia nishindwe kuamua iwapo nitekeleze au nisitekeleze kile nitakachotumwa. Ndiyo ni hii picha ambayo imenifanya nijikute nakuwa mtumwa wa Bonge, huku nikitekeleza maagizo yake kana kwamba yeye ni rimoti na mimi ni runinga.
. Sifahamu kama kuna nguvu ya ziada kutoka nje ya nafsi yangu ilinituma kufanya uamuzi huo wa aina yake; Kuvunja maagizo ya mtu kama Bonge halikuwa jambo la kawaida. Pengine chuki yangu juu ya Bonge ilinipa ujasiri wa kufanya hayo yote, lakini pia inawezekana ni ujasiri wa nafsi yangu ambao nimetunukiwa na Muumba.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ilikuwa siku ya tatu toka nikabidhiwe begi lile. Sikujua kilichokuwamo ndani yake ingawa hisia zilinituma kuwa huenda ni almasi au dhahabu. Nilijikuta nikianza kuingiwa na mashaka kwani nilitishwa kuwa iwapo nitathubutu kufungua tu basi adhabu yangu itakuwa kifo!
“Hivi kweli nikiufikisha huu mzigo nitaweza kuepukana na hicho kifo?” Lilikuwa ni swali gumu ambalo nilijiuliza bila kupata jibu.
Lazima nifungue kwani Martin na Bonge watajuaje kuwa mzigo umefunguliwa?
Nilipofika chumbani nikalitua begi lile kitandani, moyo wangu ulikuwa unaenda mbio kama mtoto aliyemuona daktari akiwa na sindano mkononi. Martin alikuwa miongoni mwa watu ambao niliwafikiria sana kila liliponijia wazo la kufungua begi, huyu ndiye aliyenitisha zaidi, jinsi alivyo!
Ana umbo kubwa lenye misuli iliyojengeka kama mnyanyua vitu vizito, macho yake ni makubwa kama kurunzi huku uso wake ukipambwa na kovu kubwa lililopita katikati ya uso wake likionyesha kila dalili kuwa kilikuwa kidonda kikubwa ambacho kilishonwa kwa nyuzi kadhaa kabla ya kuwa kovu la kutisha. Kwa jinsi alivyo alitosha kabisa kumnyamazisha mtoto anaelia kwa neno moja, huyo Martin anakuja, labda awe hajawahi kumuona.
Pale alipokuwa ananitazama nilikuwa sijamkosea chochote lakini alikuwa anatisha kama yule nyoka anayeshambulia kwa kurusha mate ya sumu. Macho yake yalionesha wazi dalili zote za mtu muovu kama si muuaji kamili, ni bora kusimuliwa kuliko kukutana na mtu kama huyo usiku. swali kubwa nililo jiuliza lilikuwa atanifanya nini akigundua kuwa nimefungua ule mzigo? Iwapo alikuwa ananitazama kwa sura ambayo kwake ilikuwa ya upole lakini kijasho chembamba kilinitoka, vipi nikutane naye siku ambayo amekasirika? Halafu ajue kuwa maagizo waliyonipa nimeyavunja, nini kitatokea?
Bila shaka atanifanya kama alivyofanyiwa yule mwanamke kule guest. Nilikuwa sijawahi kuona mtu aliyeuwawa kikatili namna ile. Taswira yake ilinijia kichwani mara kwa mara, mwili ulisisimka na kufanya vipele vidogovidogo kama mtu anayehisi baridi kali.
Maskini Merina, Mungu amlaze mahali pema peponi.
Shauku yangu ya kutaka kujua kuhusu mzigo ule ilisababishwa na vitisho vya Martin na Bonge. Adhabu ya kifo kwa kufungua mzigo tu? Woga niliokuwa nao ulimezwa kabisa na hamu ya kujua kilichomo ndani yake, na sasa nilikuwa nimeamua kuchagua kufuata maelekezo ya nafsi yangu na si yale ya Bonge.
Laiti wasingenionya kiasi kile nisingekuwa na wazo lolote juu ya mzigo wao. Ningeufikisha kama walivyotarajia bila hata kuwa na chembe ya wazo juu ya kutaka kujua kilichomo ndani.
Kwa mara nyingine nikalikazia macho begi lile jeusi, lilikuwa kama refarii katika maisha yangu. Nifungue niishi kwa mashaka au niache niishi kwa amani. Kwangu lilikuwa jambo zito sana kwani sijawahi kubeba kitu ambacho sikifahamu.
Jambo moja ambalo lilinikosesha raha ni kuwa iwapo sitafungua basi nitakuwa na fumbo moyoni, fumbo ambalo sitaweza kulifumbua maisha yangu yote. Nakumbuka sana nilipokuwa mwanafunzi jinsi nilivyoumiza kichwa kwenye mafumbo. Nilikuwa sikubali kushindwa. Lakini kwa mara ya kwanza leo nakabiliana na fumbo ambalo gharama ya kufumbua kwake ni kifo.
Nikubali kushindwa?
Kweli nilikuwa naelekea kushindwa. Lakini kwa nini nishindwe?
Nikiwa mtaalamu wa mafumbo nilikuwa na kazi mbili, kwanza mzigo halafu uhai wangu. Lengo lilikuwa ni kujua kuhusu ule mzigo bila kupata matatizo, yaani nilitaka kuuwa ndege wawili kwa jiwe moja.
Nikatabasamu huku nikiwa nalitazama vizuri begi lile ambalo niliahidiwa pesa nyingi kwa kulifikisha kwa muhusika bila kuvunja masharti. Fedha nilizoahidiwa sijawahi kufikiria hata siku moja kuwa ipo siku nitakuja kuzihesabu achilia mbali kuzimiliki.
Kwanini kusafirisha lile begi kutoka Mwanza nilipwe pesa zote hizo? Kutatua fumbo lile kwangu lilikuwa jambo kubwa kuliko zawadi ambayo ningepewa na bonge huku fumbo likiendelea kubaki kama maisha ya kaburini ambayo maiti tu ndiye anayejua yalivyo.
Haiwezekani! Lazima begi lifunguliwe.
Kabla sijafungua nikapata wazo muruwa kabisa. Nikatabasamu, Lilikuwa wazo kabambe sana. Nilitaka niue ndege wawili kwa jiwe moja. Nilidhamiria kulifumbua fumbo lile bila kupata matatizo yoyote. Nilianza kujihisi kuwa mshindi ingawa bado niliendelea kujionya juu ya hatari ninayokabiliana nayo. Bonge hajawahi kuliona lile begi likoje kwani lilionekana wazi kuwa ni jipya, hii ilinifanya niamini kuwa wazo langu litakuwa muruwa.
Kabla sijafanya lolote nikakaa kitandani kwanza kisha nikaegemea ukuta nikavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha, taratibu zikaanza kunijia fikra juu ya mambo ya ajabu ambayo yanatokea katika maisha yangu.
Muda huu mfupi ambao nilikaa hapo uliweza kunifanya niyatazame maisha yangu kama mtu anayetazama filamu ndefu ya kusisimua. Nilikuwa kama mtu ninayejitazama mwenyewe kwenye kioo. Ilikuwa kana kwamba ninajisimulia kitu fulani. Kabla sijaendelea naomba nikusimulie mwanzo wa yote mpaka kufikia hapa, kwanza ingekuwa vema unifahamu mimi ni nani?……
***
Naitwa Kajuna Daudi Kazakamba, ni mtoto wa kwanza katika familia yenye watoto watatu, mimi na wadogo zangu wawili wote wa kike Koku na Waridi………
***
Baadhi ya watu wanaoishi Dar es salaam wana akili za ajabu sana. Hawapendi kuishi maeneo yenye nafasi na hewa nzuri. Hupenda sehemu zenye misongamano ya watu na hususani zile zilizoko kando ya barabara. Mfano mzuri maeneo kama Kinondoni na Manzese. Hilo ndilo jambo lililomfanya baba yangu kununua kiwanja eneo ambalo liko karibu na barabara. Madhara yake yalikuwa makubwa kwa baba na familia kwa ujumla.
Ikiwa ni miaka kumi na mitano toka ajenge nyumba hiyo akapokea barua kutoka serikalini ikimtaka kuhama eneo hilo. Katika barua hiyo serikali ilidai kuwa baba amejenga katika eneo ambalo linatambuliwa kisheria kuwa ni hifadhi ya barabara. Kwa masikitiko makubwa kabisa nikashuhudia nyumba yetu ikibomolewa. Hakuna fidia iliyotolewa ingawa vyombo vya habari vikiwanukuu viongozi husika vilitoa taarifa kuwa waathirika wote wamelipwa fidia zao.
Ukawa mwanzo mpya wa maisha ya kupanga na kuhamahama, mpaka pale baba alipojenga nyumba nyingine Mwananyamala baada ya kupata fedha zake za mafao kutoka shirika la reli Tanzania ambako alifanyia kazi. Fedha hizi zilipatikana kwa mbinde, iliwalazimu wazee kuandamana na kulala barabarani wakati wa kudai mafao hayo. Wakati mwingine polisi walilazimika kutumia nguvu za ziada kuwadhibiti wazee hao.
Fedha zote za kiinua mgongo ziliishia kwenye ujenzi wa nyumba hiyo. Mwaka huo nilikuwa kidato cha sita shule ya sekondari Tambaza. Mapema mwaka uliofuata nikahitimu masomo yangu.
Kama zilivyo hadithi za watoto wengine wanaotoka kwenye familia kama zetu hapo ndio ikawa tamati sikuweza kuendelea.
Nikaanza kutangatanga kutafuta maisha. Nikahama Mwananyamala kwa wazazi wangu nikahamia Yombo buza. Huko nilihama nyumba kadhaa hatimaye nikapata sehemu ambayo nilikaa muda mrefu kuliko nyumba nyingine.
Chumba kimoja, kitanda, ndoo na vyombo vidogo vidogo vilikuwa vinaonesha taswira halisi ya maisha yangu. Ulikuwa mkusanyiko usiovutia ndani ya chumba hicho cha kupanga, hakukuwa na tofauti kubwa na sehemu inayouziwa pombe za kienyeji. Niliridhika kuishi maisha hayo kuliko kumuongezea baba mzigo, kwani biashara yake kubwa kipindi hicho ilikuwa ni samaki ambao alikuwa anawauza katika mitaa ya Mwananyamala na Kinondoni, pale inapotokea hali ya hewa si nzuri alikuwa anachoma mahindi na kuyauza. Baba yangu hakuwa mtu anayependa kukaa bila kazi mwenyewe alijisifu kwa kusema yeye ni zao la Tanu Youth league.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
***
Ilikuwa saa 12.37 jioni. Nilivua sare zangu za kazi nikazitia kwenye boksi. Nikachagua nguo safi kutoka kwenye kamba ya nguo. Kamba hiyo niliifunga kwenye misumari ambayo niliigongea ukutani. Baadhi ya wenye nyumba hawapendi mtindo huu wa kutoboa ovyo nyumba zao kwa misumari. Nyumba niliyoishi haikuwa na masharti kama hayo, vyumba vyote vilikuwa vimetobolewa kwa misumari. Kimsingi ulikuwa ni uharibifu ambao wakati mwingine uliweza hata kusababisha nyufa ndio maana baadhi ya wenye nyumba walikuwa hawaridhishwi na hilo. Sisi tulikuwa na bahati kwani mwenye nyumba alikuwa mlevi hivyo wewe fanya lolote lakini siku ikifika mpe chake akalewe.
Hakuwa na uchungu sana na nyumba yake labda kwa kuwa ni nyumba ya urithi. Nilikuwa naamini kuwa kitu ambacho mtu hukipata bila kukitolea jasho mara nyingi hakionei uchungu na wala hakithamini kama kile ambacho amekifanyia kazi.
Niliitazama kalenda ya kampuni ambayo nilikuwa nafanyia kazi, nikagundua kuwa ilikuwa ni ya miaka miwili iliyopita. Niliziangalia kwa hasira picha za watu ambao walikuwa wanacheka kwenye kalenda ile. Walikuwa na matumbo makubwa ambayo bila shaka yalikuwa yanawapa shida wakati wa kupumua na kulala. Hivi hawa wanakumbuka kweli kuwa kuna watu wanapata shida duniani au wanajali matumbo yao tu? Kwenye picha ile kulikuwa na Watanzania wenye asili ya kiasia na wale weusi kama sisi.
Nikaitazama tena kwa uchungu kalenda ile. Kalenda mpya zilikuwa zinatoka kila mwaka, ili uweze kupata kalenda hizo ulitakiwa kuwabembeleza waajiri waweze kukupatia. Wengi wao walikuwa ni watu wenye majivuno. Sikuwa na muda wa kumbembeleza mtu, kazi yenyewe sikuipenda, tatizo kubwa sikuwa na kazi nyingine ya kufanya. Kilichonikera zaidi kazi zenyewe hazikuwa za kila siku huku siku nenda rudi tukiendelea kuwa vibarua.
Tulikuwa tunarushiwa vikaratasi ambavyo vimekunjwa, ukifungua unakuta idadi ya siku utakazofanya kazi kwa mwezi pamoja na malipo utakayolipwa. Ilikuwa ni kampuni inayojishughulisha na utengenezaji wa juisi za aina mbalimbali, biskuti na mikate. Ilikuwa ni miongoni mwa makampuni yanayosifika sana kwa kusamehewa kodi. Nilipata kusikia tetesi kuwa ni ya shemeji yake kigogo mkubwa wa wizara ya viwanda na biashara. Roho iliniuma sana, Mungu ametuzawadia sote hii nchi, lakini kuna watu wanaoifanya kuwa mali yao. Hawa ni wale ambao hata sheria haifanyi kazi upande wao.
Nilizikagua tena zile nguo nikaridhika kuwa ni safi. Nikavaa shati jeupe, suruali nyeusi na viatu vyeusi. Sikusahau kufunga tai siku hiyo. Nikaonekana kama mmoja wa wafanyakazi wa benki kwa nguo nilizozinunua kwa mmachinga. Nikazikagua nywele zangu, hazikuhitaji kitana kuzichana. Nikachukua brashi, nikaanza kupitisha kichwani huku nikijiangalia kwenye kioo kidogo.
***
Sikuwa mpenzi wa kumbi za starehe lakini siku hiyo niliamua kusafisha macho. Nguo zile zilikuwa zinanipendeza sana ilibidi mtu afanye kazi ya ziada kugundua kuwa zote nilikuwa nimenunua kwa wamachinga mitaani.
Jioni ile nilikuwa nazunguka maeneo mbalimbali ya mji bila mpangilio maalum. Hakuna nilichokuwa natafuta, labda ilikuwa ni furaha ya malipo yangu kibaruani. Siku hiyo mifuko yangu ilikuwa imenona kwa noti za kitanzania . Mwisho nikafika sehemu ambayo nilihitaji kupumzika. Nilikuwa nimechagua baa moja iliyoko maeneo ya Tabata Mawenzi. Ni sehemu ambayo inasifiwa kwa utulivu. Nililijuwa hilo kupitia kwa baadhi ya vibarua wenzangu wanaoishi maeneo hayo.
Nikakaa kwenye kona ya kushoto ya baa. Vitu vingi mle ndani vilikuwa vigeni kwangu. Mazingira ya mle ndani yalikuwa ni ya aina yake. Kuna vitu ilikuwa ndio kwanza naviona humu ndani. Kubwa ilikuwa ni staili ya mavazi, hasa yale ya wanawake. Wengi walikuwa wamevaa mavazi ambayo yaliruhusu mapaja yao kuwa nje, nilimeza mate. Kwa upande wa wanaume walikuwa na mavazi yao ya siku zote, ya kawaida. Sijui kwanini nilipokuwa kwenye kundi la watu nililaumu sana mavazi haya ya kina dada, leo niko peke yangu najikuta nikivutiwa na mavazi haya, tena nilitamani ufupi wa sketi zao ungezidishwa ingawa kimsingi zilikuwa zimefika mwisho.
Labda ni unafiki.
Hii ndio baa bwana, starehe nyingi zinapatikana huku. Mapaja ya hawa watoto wa kike yalinifanya nipagawe kabisa. Siku nyingi nilikuwa sijaona mambo ya namna hii kwani toka nianze hivyo vibarua mara nyingi nilikuwa nashinda nyumbani. Moyo ulikuwa unaenda mbio kila nilipokuwa ninatizama vitu adimu namna hii, nilihisi kubanwa na pumzi kutokana na kuwatazama viumbe hawa.
Kona ya kulia ya baa ile kulikuwa na meza kubwa ambayo ilikuwa imefunikwa kwa zulia la kijani. Meza hii ilikuwa imewekwa vishimo sita, vitatu kila upande. Katikati kulikuwa na mipira midogo yenye rangi tofauti tofauti. Wazee kwa vijana niliwaona wakishindana kuipiga ile mipira kwa kuiingiza kwenye vile vitundu. Walifurahi na kushangilia lakini nilikuwa sijui kabisa nini maana ya mchezo ule ambao baadaye nilikuja kugundua kuwa unaitwa ‘pool’. Kwani siku zile ulikuwa ndio kwanza unaanza kupata umaarufu nchini.
“Kaka nikusaidie nini?” Nilishtushwa na sauti ya kike, nikageuka. Duh, huwezi kuamini! Nilishindwa kutofautisha muhudumu wa baa na mfanyakazi wa benki. Mwanamke mrembo alikuwa amesimama mbele yangu. Alikuwa na uso wa duara ambao ulisanifiwa vizuri na mola muweza kwa ngozi laini nyeusi ambayo haikuhitaji vipodozi vikali. Macho yake yalikuwa makubwa kiasi cha kuyafanya mapigo ya moyo wangu kuongezeka pale alipokuwa ananitazama. Umbo lake lilikuwa ni lile ambalo linajulikana kama namba nane. Nilimshangaa mrembo huyu ambaye hakuwa na nyongeza zaidi ya urembo wa asili.
“Inakuwaje mwanamke mrembo kama huyu anafanya kazi baa!” Niliwaza.
“Naomba pepsi baridi tafadhali!” Yule dada alinitazama kwa mshangao kidogo. Bila shaka ni kutokana na kujisahau na kumshangaa wazi wazi. Sio siri alikuwa anavutia. Akatabasamu kidogo kisha kwa sauti ileile ya kuvutia akaongea.
“ Naomba ulipe kwanza tafadhali ” alisema huku akinyoosha mkono wake wa kulia. Nikampatia noti ambayo tayari nilishaiweka kwenye mfuko wa shati.
Aliporudi alikuwa amebeba sinia likiwa na pepsi na karatasi laini ikiwa ndani ya glasi. Akanikabidhi chenji yangu
Niliwaona watu wengi wakinywa vinywaji vyao taratibu, kwa kuwa nilikuwa na kiu sikuupenda utaratibu ule. Nikajimiminia pepsi yangu kwenye glasi, nikanywa ile soda funda tatu za nguvu. Ndani ya dakika moja na nusu glasi ikawa tupu. Nikamalizia soda kidogo ambayo ilibaki kwenye chupa. Ile soda ilikuwa tamu mno! labda kwa kuwa nilikuwa nakunywa mara moja moja. Sikuwa na uwezo wa kununua soda kila siku, kwa mshahara gani!? Hata pale nilipokuwa nyumbani kwa wazazi wangu bado soda kilikuwa kitu adimu. Soda ilikuwa haipatikani mpaka ushikwe na homa tena baada ya kudeka sana na kukataa vyakula mbalimbali ndipo utaletewa, pia soda ilipatikana siku za sikukukuu; Hapo familia nzima itakunywa soda.
Nilimalizia funda la mwisho huku nikiusikilizia ule ubaridi ulivyokuwa unashuka kooni na kunipa raha na faraja. Angalau uliweza kunisahaulisha ugumu wa kazi za vibarua vya viwandani. Nilitamani hali ile ingekuwa kila siku, lakini zilikuwa ni ndoto na mawazo ya masikini ambaye kutwa haachi kuwaza kupata fedha za ghafla na ndoto zilizojaa bahati nasibu ya kuokota kiroba cha noti au dhahabu.
Ghafla, akaingia mwanamke ambaye alivuta hisia za wanaume wengi. Kila mwanaume aliyegeuka kumwangalia aligandisha jicho lake kwa sekunde kadhaa kisha akarudisha jicho mahala pake. Wengi walikuwa na wapenzi wao mle ndani hivyo walijifanya kama hawajaona chochote kumbe walikuwa wanazuga tu. Niliona mmoja akipigwa kibao na mtu niliyehisi kuwa ni mkewe baada ya kugandisha jicho lake kwa muda mrefu zaidi. Nikacheka! Kwani yule mtu alikuwa na umri ambao ungemfanya awe anakaribia kustaafu serikalini au ameshastaafu karibuni.
Sikujishugulisha sana na yule mwanamke, nilijua wazi hakuwa katika daraja langu. Sikupenda macho yauumize moyo wangu. Nikamgeukia tena yule muhudumu, alikuwa anahudumia wateja wengine. Nikaendelea kumkazia macho ili akigeuka nimwite kwa ishara ya mkono. Baada ya dakika chache akageuka nikamwashiria kwa mkono kuwa nahitaji huduma. Nilimpenda sana muhudumu huyu. Sura yake ilikuwa na kila dalili ya upole na busara. Ndio maana sikutaka kumwita muhudumu mwingine.
“Samahani kaka naweza kukaa hapa” Sauti ya kike ilinishtua na kunifanya niache kumtazama yule muhudumu.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kaa tu dada, hakuna mtu hapo” Nilimjibu huku kwa mbali nikihisi mapigo ya moyo yakiongeza kasi yake. Nilijitahidi kupambana ili nisiruhusu hali hiyo.
Alikuwa ni yule mwanamke ambaye kwa dakika kadhaa nahisi alibadilisha mapigo ya mioyo ya baadhi ya wanaume mle ndani. Sikubabaika, wala sikuruhusu moyo wangu ushtuke zaidi. Nahisi wengi mle baa walitamani bahati ile ingekuwa upande wao, kukaa meza moja na yule mrembo kwao lilikuwa jambo kubwa sana. Wengine walilaani kwa nini walikuja na wapenzi wao mle ndani. Wakati natafakari kuhusu yule Msichana nikamuona muhudumu akiisogelea meza yangu.
“Naomba Pepsi nyingine tafadhali” Nilitamka baada ya kumuona amesimama mbele yangu kwa heshima, Sijui kama ilikuwa ni heshima kweli au ndio zile heshima za baa za kijana kuitwa mzee.
“Naomba unipatie Redbull!” Aliongea yule dada kwa sauti ambayo ilikuwa na mikwaruzo kiasi.
Yule muhudumu akaondoa chupa na glasi ya kwanza bila kusema lolote. Dakika mbili baadaye akarudi na vitu tulivyoagiza. Yule mwanamke alianza kunywa kinywaji chake taratibu. Alionekana mwenye mawazo mengi. Hata kile kinywaji alionekana kujilazimisha. Kisha akanigeukia kwa aibu kwani alikuwa hajanisalimia.
“Habari yako kaka!” alinisalimia kwa sauti ya upole na uungwana.
“Salama dada!”. Nilijibu huku nikiwa sina uhakika kama sauti yangu ilikuwa
imetoka vizuri, kwani mapigo ya moyo wangu yalikuwa yanaenda kasi sana. Sijui kwanini huyu dada alikuja kwenye meza hii, alinivurugia kabisa amani niliyokuwa nayo kwani nilianza kupotelewa na ule ujasiri niliojisifu kuwa nao. Alivuruga hata mfumo wangu wa kawaida wa mawazo. Sikupenda aendelee kukaa pale lakini nilikuwa sina jinsi.
Kitu kimoja kilikuwa wazi katika macho ya yule dada, hakuwa na furaha. Hili lilinipa udadisi sana. Nilitaka kumuuliza lakini moyo ukasita.
Nikaamua kuachana nae. Nikaendelea kutembeza macho yangu ndani ya ukumbi ule wa kisasa. Watu walikuwa wametulia kwenye viti vyao wakinywa vinywaji tofauti tofauti.
“Siwezi! Nasema siwezi……!” Nilishtushwa na sauti ya yule dada. Tukakutanisha macho. Hapo ndipo nilipogundua kuwa yule dada alikuwa na tatizo. Hata hivyo bahati ilikuwa upande wake, wengi mle ndani hawakuweza kumsikia. Sauti yake ilimezwa na sauti nzito ya muziki mnene uliokuwa unapigwa mle ndani.
Kitendo kile cha kuongea kwa sauti kali mbele yangu kikamfanya ajisikie aibu.
Hakuchelewa akainuka kwenye kiti na kuondoka. Akawa anasindikizwa na macho ya wanaume wenye uchu wa fisi.
***
Muda ulikuwa umeenda sana. Ilikuwa ni saa sita na nusu usiku muda uliotangazwa na serikali wa kufunga baa ulikuwa umefika. Watu walianza kupungua taratibu. Nilikunywa pepsi tatu tu lakini nilikaa pale karibu masaa matano. Wakati nataka kuinuka ndipo nikagundua kuwa yule dada alikuwa amesahau kipochi chake pale mezani. Sikujiuliza nilikichukua nikakiweka mfukoni.
Nilikaa muda mrefu mle baa kwani walionekana kutozingatia onyo la serikali la kufunga baa saa sita kamili, nikaamua kuondoka. Kabla sijaondoka nilitamani sana kuonana na yule dada ambaye mara zote alikuwa ananihudumia. Nikatembeza macho yangu huku na huko bila mafanikio. Sikutaka kuongea nae chochote. Nilitamani kuingalia tena miguu yake illiyojaa vizuri, sikumuona.
Nilipofika getini ndipo nikamuona yule dada. Alikuwa amevaa mavazi mengine. Alikuwa amevaa sketi ndefu nyeusi, blauzi nyeupe ya mikono mirefu pia alikuwa amezifunika nywele zake zilizosukwa mtindo wa rasta ya majongoo kwa kilemba cha kijani. Nilijiuliza amebadilisha nguo zile muda gani. Nikamsogelea.
“Habari yako dada!.” Nilimsalimia huku nikipanga namna ya kuanzisha maongezi.
“poa!” Alinijibu kwa mkato huku akiniremburia macho. Alionekana kama anasubiri kupewa taarifa fulani. Nilitishika, lakini nikapiga moyo konde. Nilikuwa sijiamini kabisa kwani hata pale nilipokuwa nataka kuongea nilihisi kubanwa na pumzi.
“Samahani sister, nina maongezi kidogo na wewe.” Niliongea huku nikijitahidi kuficha woga niliokuwa nao.Hata hivyo sikujua kama niliyoongea yamesikika au yametoka kwa ufasaha. Nilijihisi kama niliyekosea, hata lugha niliyotumia niliona kuwa si sahihi. Nilihisi kuwa ili kuweza kuwanasa kiurahisi viumbe hawa basi kulikuwa na umuhimu wa kuchanganya na lugha za kigeni hususani kiingereza, sikuamini kama kiswahili peke yake kinaweza kutosha kumnasa mrembo yule. Hata hivyo nilikuwa nimetawaliwa na hofu ya kuongea kiingereza kwa kuchelea kuvurunda kwa kuongea kiingereza kibovu. Hapa nilimkumbuka sana mwalimu wangu wa kiingereza Chambuso ambaye alikuwa anapenda kutukejeli kwa kutuambia kuwa kiingereza chetu ni kibovu, eti “You know…..” ni nyingi. Kweli huyu mwalimu alichangia kunifanya nikose kujiamini .
“Oh! Pole kakaangu, muda umeenda sana halafu nimechoka tafuta muda kesho tuongee” hapo nilishusha pumzi kwani angalau aliniweka kwenye nafasi nzuri ya kujiandaa. Nilianza kuhisi ushindi ndani ya nafsi yangu. Mambo mengine haya yana wataalamu wake, mimi si mtaalamu kiasi hicho, hata hivyo nilianza kuhisi ushujaa kwenye nafsi yangu, ule woga ambao ulinivaa hapo mwanzo uliyeyuka nikajihisi furaha kana kwamba nimezaliwa upya.
“Kama utakuja naomba ufike upande ule kule wa kaunta, kisha uliza sister Betty!” Alinitazama akatabasamu. Tabasamu lake lilikuwa kama mkuki wenye ncha kali kwenye moyo wangu. Nikahisi kama moyo wangu unataka kusimama. Nikaingiwa na kitu ambacho nilishindwa kutafsiri ni kana kwamba moyo ulimwaga sumu fulani kwenye mwili wangu.
Tukatazamana. Kuna kitu kilikuwa kinapita kwenye macho yetu au sijui kwenye macho yangu tu.
Mpaka kufikia hapa napenda ufahamu kuwa Sikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamke yeyote Yule lakini kwa mara ya kwanza moyo wangu unaangukia kwa muuza baa ‘Bar maid’ . Nilimpenda si utani.
***CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilifika nyumbani saa 7.30 usiku. Eneo lote lilikuwa kimya kabisa. Sikutaka watu wajue muda niliorudi, kwani haijatokea hata siku moja ambayo nimechelewa kiasi kile.
Kwa kuhofia kugundulika, nikautumbukiza ufunguo kwenye kitasa kwa namna ya kunyenyekea sana. Hata pale nilipokuwa natekenya kitasa ili kifunguke bado nilihofia kubainika. Mlango ukafunguka bila makelele, nikaingia ndani huku nikiwa na furaha baada ya kufanikiwa kuingia bila ya kubainika kwa yeyote.
Nilijilaza kitandani. Sikuhitaji hata kuoga kutokana na kibaridi kilichokuwa kinapiga siku ile. Hata hivyo umbali wa kutoka chumbani hadi bafuni nao ulinifanya nisite kwenda kuoga. Wakati nafsi yangu ikikataa kwenda kuoga, mawazo mengine yalikuwa yanapita kichwani kwangu. Nilikumbuka jinsi siku ile nilivyotumia fedha bila utaratibu. Kwa kipato changu kukodi taksi kutoka Tabata hadi Buza ni ubadhirifu mkubwa.
“Aa mara moja moja sio mbaya” Niliwaza na kujifariji mwenyewe.
Mawazo yangu yakarudi kwa Betty. Bado nilishangaa kwanini aliamua kufanya kazi ya uhudumu wa baa. Alikuwa msichana aliyeumbika kwelikweli. Macho makubwa yasiyohitaji kungumanga ili aweze kurembua. Uso wake ulikuwa wa duara, mashavu yenye vishimo vidogo ambavyo unaweza kuviona kwa urahisi pindi anapotabasamu au kucheka. Kilichonimaliza zaidi katika sura yake ni mwanya.
Ee bwana eeh! nilikuwa sijaona mwanya mzuri kama ule. Ulikuwa ni mwanya wa kuvutia. Haukuwa mwanya wa kuchongwa, ulikuwa wenyewe wa kutunukiwa na Muumba. Nilikuwa dhaifu kwenye aina hii ya maumbile. Mwanya na vile vishimo vidogo vinavyoonekana mashavuni pindi mtu anapotabasamu. Sijui vinaitwaje vile… Nilitumia muda mrefu kumfikiria yule mwanamke hadi pale usingizi uliponichukua.
Miale ya jua ilinipiga usoni, nikashtuka kutoka usingizini. Moja kwa moja nikaelekeza macho yangu ukutani. Saa yangu kuukuu ilinionesha kuwa ni saa 2.37. Nikainua macho nikitafuta wapi nilikovulia suruali yangu usiku. Nilikuwa nimeiweka juu ya kiti. Nilitaka kuchukua fedha ambazo zilibakia mfukoni. Nikatembea huku nikipiga mwayo mrefu wa mtu aliyetoka usingizini. Nilipoishika ile suruali nikashtushwa na mtetemeko mdogo uliofanywa na ile suruali.
“Ni nyoka kwenye suruali yangu?” Nilijiuliza huku nikianza kutawaliwa na hofu.
Bado suruali iliendelea kutikisika huku ikitoa kitu kama mngurumo mdogo na kunifanya nitamani kukimbia . Nikapiga moyo konde na kuinyanyua ile suruari, ikaacha! Sikujua ni nini kiliifanya ile suruali itikisike yenyewe kwani baada ya kuiinua iliacha kabisa. Nikiwa nimetawaliwa na woga, niliendelea kuikagua ile suruali. Nilikuwa nafanya hayo yote huku nikiwa nimeiweka sawa miguu yangu ili iwapo kitatokea kitu cha hatari niweze kutimua mbio.
Nikaanza kuingiza mikono katika mfuko mmoja baada ya mwingine. Hapo ndipo nilipobaini kitu ambacho kilinishangaza. Nilishasahau kabisa kuwa niliokota kipochi ambacho yule dada alikisahau pale baa. Ndani ya kipochi kulikuwa na simu ambayo haikuwa na mlio. Ilikuwa imewekwa muito wa mtikisiko ‘Vibration’ . Nikatabasamu baada ya ugunduzi huo mdogo kisha nikashusha pumzi na kupotelewa na hofu ambayo ilinitawala muda mfupi uliopita.
Nikaitoa ile simu kwenye kile kipochi. Ilikuwa simu kubwa kwa umbo. Jina lake lilikuwa geni katika macho yangu. LG maandishi hayo mafupi ndiyo yaliyoinadi simu hiyo katika ulimwengu wa watumiaji wa simu. Moja kwa moja nikabonyeza kwenye menyu ya simu. Sehemu ya kwanza iliyonivutia kufungua ni ile ya meseji. Watu wengi wana udhaifu wa kupenda kufungua maeneo hayo hata kama hawajaruhusiwa. Ni eneo hatari sana kwani wakati mwingine hutunza siri za mmiliki wa simu.
Nikabofya kitufe ambacho kilinionesha maeneo mengi ya kufungua. Nikavutiwa na inbox yaani sehemu ya ujumbe ambao mwenye simu ametumiwa, nikafungua.
Ujumbe niliokutana nao ulinitisha kidogo, pia jina la mtumaji lilinishangaza, Kimeo. Nilikuwa sijawahi kusikia mtu anaitwa Kimeo labda baadhi ya watu ambao huhifadhi majina ya mafundi simu kwa kuwaita vimeo, lakini si jina rasmi la mtu.
“Bila Shaka ni jina la kizushi.” Nilijisemea ndani ya nafsi yangu.
Mwanamke tekeleza maagizo yetu la sivyo………………….
Ujumbe ulikuwa hivyo na mtumaji alikuwa Kimeo. Nikafungua meseji ya pili. Hii ilikuwa na ujumbe mrefu kidogo kuliko ile ya kwanza. Please, usikose kufika. Zingatia kuwa zawadi nono ya fedha, nyumba pamoja na gari inakusubiri. Ukifanikiwa kumuua Pili. Nikajikuta napatwa na mshtuko baada ya kusoma ujumbe huo.
Meseji zilizoko kwenye in box zilikuwa zimeisha. Nikafungua sent items yaani ile sehemu inayoonesha ujumbe uliokwishatumwa, ‘sent items empy’ lilikuja neno hilo pale nilipojaribu kufungua, nikafungua sehemu imeandikwa outbox, Kulikuwa na meseji ambayo kama ile ya kwanza nayo ilinitisha kidogo. Kilichonisisimua zaidi ni tarehe ya ile meseji. Ilikuwa ni tarehe ya siku ile ambayo tulikutana na yule mwanamke mwenye kipochi kule baa.
“Yaani ni meseji ya jana?!” Nilijiuliza kwa mshangao, kisha nikarudia kuisoma ile meseji.
Samahani sana mpenzi wangu, sina imani ndani ya moyo wangu. Namuogopa sana yule Bonge. Bonge ataniua tu. Kesho njoo Tabata Kisukuru. ZAWADI GUEST HOUSE chumba no. 7 saa 12 jioni. Lazima nitoroke haraka iwezekanavyo na hali jinsi ilivyo siwezi kulala nyumbani.usikose mpenzi wangu .Ni mimi nikupendaye Merina Dismas.
Kwa mfumo wa ile simu ni kwamba ile meseji ilikuwa imehifadhiwa kwenye simu haikutumwa kokote.
Alitaka kumtumia nani? Nilijiuliza.
Nilitanabahi kuwa najiuliza maswali ya kijinga kwani ni wazi kuwa alikuwa anahitaji kuonana na mpenzi wake ambaye kwa muda huo nisingeweza kumfahamu.
Moyo wangu ulikuwa na hamu ya kujua ni nini kilikuwa kinamfanya yule dada ambaye kupitia meseji nilifahamu jina lake kuwa ni Merina, atake kutoroka mji. Ilikuwa ni siku nzuri kwangu, siku ya Jumapili. Siku hiyo na Jumamosi zilikuwa ni siku za mapumziko kwangu hivyo niliamua kufuatilia suala lile. Sikujua, nasema sikujua, Laiti ningejua mapema kuwa umbeya ule wa aina yake ungezusha matatizo makubwa sidhani kama ningethubutu kufanya nilichofanya.
Kuna kitu kimoja ambacho mpaka hii leo kinanishangaza. Kwa tabia yangu ya asili huwa sipendi kufuatilia mambo ya watu. Kilichonishangaza ni nini kilinisukuma kutaka kujua mengi kuhusu yule dada. Kimsingi ni mambo ambayo yalikuwa hayanihusu. Lakini kitendo kile cha siku moja tu, kimejenga mambo ambayo hayataweza kusahaulika. Yatabaki kwenye historia kama kumbukumbu ya aina yake, naamini kuwa hata kama nitakufa ni vigumu kufutika.
***
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Saa 7.30 niliwasili maeneo ya Nyumba ya kulala wageni iitwayo ZAWADI pale Tabata Kisukuru. Sikupata shida sana kuuliza wapi iliko nyumba hiyo, sidhani kama ni sahihi kuita nyumba ya kulala wageni. Najiuliza usahihi wa nyumba hizi zinazoitwa za kulala wageni kwa sababu kila nilipochunguza daftari ambazo husajili wageni basi wengi utakuta wanatoka Dar es salaam wanakwenda Dar es salaam.
Niliposhuka kwenye daladala pale Tabata Kisukuru maarufu kwa Swai, nikaona kibao ambacho kilikuwa na maandishi yaliyonielekeza kule nilikotaka kwenda. Nilifuata maelekezo ya kile kibao. Nyumba hiyo haikuwa mbali sana na kituo cha magari kisukuru. Nilifika kwa Swai nikaenda mbele kidogo, nikaliona kanisa dogo ambalo limejengwa juu ya muinuko upande wa kulia. Nikafuata kijia kidogo ambacho kilikuwa kinaelekea upande wa kushoto. Nilipotembea kama hatua kumi nikaiona ile nyumba.
Kabla hujafika kwenye ile nyumba yaani hatua kama kumi kutoka pale ilipo nyumba ile kuna banda la mkaanga chips, niliamua kwanza kwenda ili nipate mlo kabla sijaenda kuchukua chumba.
“Habari yako!” Nilimsalimia muuza chips
“Poa kaka mkubwa, karibu sana.”
“Ahsante, naomba uniwekee chips moja.”
“Chips mayai au kavu?”
“Naomba na mayai kama inawezekana niwekee matatu”
“Usijali mkubwa.” Alinijibu huku akifanya haraka kuvunja mayai.
Nilikaa pale kwa dakika kadhaa huku nikijaribu kujiuliza kama nilikuwa sahihi kwa uamuzi wangu wa kuja huku. Upande mwingine nilianza kujikosoa huku upande mwingine udadisi wa ule ujumbe wa simu ukinihimiza kutorudi nyuma. Baada ya dakika chache mlo wangu ulikuwa tayari.
“Naweza kupata soda?”
“Nipe hela nikuchukulie hapo kwenye kioski.”
“Nichukulie Mirinda nyeusi.” Niliongea huku nikimpatia noti ya shilingi elfu moja.
Baada ya dakika chache akarudi akiwa na ile soda niliyomuagiza. Nikala chips huku nikinywa soda yangu taratibu. Baada ya kumaliza mlo nikanawa na kufuta mikono yangu kwa leso yangu kisha nikaelekea kule nilikokusudia baada ya kuhakikisha kuwa nimelipa kiasi anachodai muuza chips.
Ilikuwa ni nyumba yenye vyumba takribani ishirini. Ilikuwa imejificha kidogo, Kama si kile kibao nisingeweza kufika. Mfukoni nilikuwa nimebakiwa na elfu thelathini tu baada ya kula zile chips. Sikuwa na akiba nyingine zaidi ya hiyo. Nilihisi kuwa gharama za kulala pale huenda zikalingana na hela niliyokuwa nayo.
Potelea mbali.
Nilifika mapokezi, kulikuwa na kidirisha kidogo ambacho kilikuwa na kiubao kidogo ambacho kilitokea kwa mbele kidogo kama kikofia. Pembeni ya kile kidirisha kulikuwa na sofa zuri lililovikwa kitambaa ambacho kinafanana na ngozi ya chui kwa jinsi kilivyonakshiwa maua yake. Nikakaa pale kwenye sofa karibu kabisa na kile kidirisha ambacho kiliandikwa RECEPTION Msichana mweusi mwenye nywele ndefu ambazo alizibana kwa kibanio kwa nyuma akanipokea.
“Karibu kaka.”
“Ahsante habari za kazi.”
“Nzuri, karibu sana.” Alinijibu huku akitabasamu.
“ Nahitaji chumba aunt”. Nilimwambia baada ya kusalimiana.
“Vyumba vipo. Sijui unataka vya uani au vya ndani?”
“ Kama inawezekana naomba chumba namba 7”
“Kwanini umechagua namba hiyo?”
“Ndivyo nilivyoelekezwa na mnajimu, kuwa hiyo ndiyo namba yangu ya bahati”
Yule dada akacheka kabla ya kunijibu.
“Hicho kimeshachukuliwa, tena kimelipiwa toka jana asubuhi lakini mwenyewe amefika leo.”
“Haya nipe angalau kinachokaribiana na hicho”
“ Labda namba 18 maana vinatazamana”
Nilifurahi sana, ingawa sikutaka kumuonesha yule muhudumu furaha yangu.
“Shilingi ngapi?”
“Elfu tano kulala, Mapumziko mafupi elfu tatu” Alinijibu huku nikiwa nimeingiza mkono mfukoni.
Nililipa huku nikiwa nafurahia gharama ile ndogo. Aliandika kwenye daftari lake la kusajili wageni. Wakati wa kuweka sahihi yangu ndipo nikapata mwanya wa kuchungulia jina la yule mwanamke. Kumbe alikuwa anaitwa Merina. Nikakumbuka jina lile lililoko kwenye simu Merina Dismas. Nikajiona mshindi kwa kukamilisha hatua ile.
***
Ilikuwa yapata saa 3.18 usiku. Nilizima taa ambayo niliona inaleta joto nikawasha ya rangi, iliyokuwa na mwanga hafifu kwani ile swichi ambayo ilikuwa inaning’inia pale kitandani ilikuwa na uwezo wa kuchagua aina ya taa unayotaka kutumia kama ni ile ya mwanga wa kawaida au ile nyingine ambayo mwanga wake ulikuwa hafifu wa rangi ya kijani. Halafu nikachomeka vizuri chandarua, nikajitupa kitandani. Huku nikilitazama pangaboi lilivyokuwa linazunguka na kuleta upepo ambao ulinifariji.
Nilikaa kimya kwa muda usiojulikana nikitafakari juu ya yule mwanamke. Nilianza kujutia hamu yangu ya kutaka kujua mambo yasiyonihusu. Lakini kama mtu anataka kuuwawa kwanini isinihusu? mimi ni raia mwema nina wajibu wa kutoa msaada. Nikaanza kuwakumbuka watu wa kubuni ambao walikuwa wahusika wakuu kwenye riwaya mbalimbali jinsi walivyofanya mambo makubwa kwa ajili ya kuokoa wengine. Walinivutia sana ingawa kimsingi ilikuwa ni tafsiri tu ya mawazo ya mwandishi. Ndani yake nilikutana na mashujaa wa kufikirika ambao walilitetea taifa kwa nguvu zao zote, walikuwa ni wazalendo wa kweli. Ilisisimua sana hata ikasababisha msomaji ajione kuwa ndiye yeye huyo shujaa wa kufikirika. Lakini ukweli unabaki wazi kuwa mashujaa hao wa kufikirika ni tafsiri ya mashujaa halisi kama Mkwawa, Kinjekitile na wegineo.
Lengo langu lilikuwa ni kumsubiri mpenzi wake yule mwanamke. Nilipanga kuwa atakapoingia nitavizia mlangoni ili nisikie wanazungumza nini. Mpaka wakati huo nilikuwa nafanya mambo hayo bila kujua hasara au faida yake.Nashindwa kujua kwa nini nilijiingiza kwenye umbea kama ule. Labda nilikuwa nasukumwa na nguvu fulani ambayo sikuifahamu. Kwa kifupi nilikuwa kama mtu ambaye nina dalili za matatizo ya kiakili. Wakati nikiendelea kuwaza usingizi nao haukufanya ajizi, ukaniondoa kwenye dunia halisi na kunipeleka kwenye dunia ya ndoto. Nikawa nje kabisa ya chumba kile nikimiliki magunia ya fedha.Ah! ndoto bwana…….
***
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ghafla,nikashtuka kutoka usingizini.Kuna kitu kilinishtua,.“Lazima kuna kitu” Niliwaza.Kwanza nilihisi kuwa mlango wangu umegongwa.Mwanzo nilifikiri ni ndoto.Lakini baadaye nikasikia sauti za viatu vya watu waliokuwa wanatembea kwenye korido.Kilichonishtua ni muundo wa gesti ile kwani kila chumba kilikuwa na choo na bafu.Saa nane za usiku hao watu wanatafuta nini? Balaa likaanzia hapo. Nilitembea kwa kunyata hadi mlangoni.Nikauvuta ufunguo kwa tahadhari kubwa ili usiweze kuleta makelele. Kumbe nililala bila kufunga mlango.Kujisahau namna hii ni hatari sana.Lakini muda huo sikuwa na fursa ya kuufunga tena mlango ule kwani ningejaribu ningewashtua wale jamaa. Nilikuwa natetemeka kiasi cha kuhisi kubanwa na haja ndogo.Niliganda pale mlangoni kwa dakika kadhaa. Kwa kutumia Tundu la funguo niliweza kuona viwiliwili vya watu waliokuwa wanatembea kwenye korido.Walikuwa wamevaa makoti makubwa kama yale yanayovaliwa na polisi.Walikuwa wanatoka upande mmoja na kurudi upande mwingine.Utembeaji ule ulikuwa unanitia hofu kwani nilihisi kuwa wanataka kufanya jambo baya. Baada ya sekunde chache nikagundua kilichokuwa kinaendelea. Nilimuona mmoja akiwa anachungulia kwenye tundu la ufunguo chumba alicholala yule mwanamke. Wanataka nini na wamejuaje kama yupo huku? Wale watu waliokuwa wanatembea kwenye korido waliendelea na utaratibu wao ule ambao ulinitisha,kuna wakati niliona kama wanataka kufungua mlango wa chumba changu.Mapigo ya moyo wangu yalikuwa yanaenda mbio sana kutokana na hofu niliyokuwa nayo. Nilijihisi kubanwa na haja ndogo lakini nikmaingiwa na hofu kwani niliona kuwa iwapo nitafungua mlango wa kule chooni watanisikia. Hatimaye walifanikiwa kufungua mlango.Hapo mapigo ya moyo wangu yaliongezeka maradufu. Niliona kundi lote likiingia mle chumbani.Sina uhakika kama kuna mtu alikuwa amesalia.Kwa makadirio ya chini walikuwa watano.Moyo wangu ulikuwa unaenda kasi zaidi nilipomuona yule mtu wa mwisho akiwa na bisu kubwa lenye mpini mweusi. Nilihamanika kijasho chembamba kikaanza kunitoka. Baada ya muda usiozidi robo saa wale watu wakatoka mle chumbani.Nikaamua kwenda ili nijue kama yule Mwanamke yuko salama. Huku mapigo ya moyo wangu yakienda kasi nilitoka chumbani kwangu na kuuendea mlango wa Chumba namba 7.Huku mikono yangu ikitetemeka nilishika kishikio cha kitasa nikakifungua taratibu.Mlango ukafunguka.Chumba kilikuwa na giza,nikapapasa ukutani nikaipata swichi.Nikawasha. Nilichokiona ilikuwa ni moja ya kumbukumbu mbaya katika maisha yangu. Nilijihisi kuishiwa na nguvu kwa hofu niliyokuwa nayo. Kijasho chembamba kiliendelea kunitoka, maungio ya miguu yalikuwa kama yameingiwa na ganzi hali iliyonifanya nipige magoti karibu na kile kitanda. Mwili wa Merina ulikuwa kama alivyozaliwa.Sikuwa na shaka kuwa alianza kubakwa kabla kisu kikali hakijafanya kazi yake.Alikuwa amechomwa kisu tumboni na kusababisha utumbo utoke nje, pia bisu kubwa jeusi lilikuwa limezama kwenye titi la kulia.Mdomoni alikuwa amejazwa matambara,bila shaka ilikuwa ni kumzuia asipige kelele.Pamoja na kisu hicho kuzama hadi pale ulipoishia mpini,bado kulikuwa na dalili za uhai. Nikamsogelea Merina ili nimfungue na kumpa msaada zaidi. Kitu cha kwanza ilikuwa ni kumuondoa matambara ambayo alijazwa mdomoni. Baada ya kuondoa yale matambara akakohoa kwa nguvu na kuanza kuhema. Damu zilianza kumtoka mdomoni na puani. “On…n…ndoka..wa..takuuu..wataku..ua…”. Kwa sauti ndogo yenye kila dalili ya mauti Merina alisisitiza. Nilimtazama bila kumjibu huku machozi yakinilengalenga. “ Kwani umewafanya nini?” Nilimuuliza swali hilo nikionesha kuipuuza kauli yake ya kuondoka”. “Sii ..siri..ii….go..oh, mh nakufa ondoka …..wata….yukk kaaa…ssspill” Hakumaliza kauli yake,alikuwa anaongea vitu ambavyo vilikuwa havieleweki tena.Hatimaye akakata kauli. Mwili wangu ulikuwa umelowa kwa jasho. Niliutazama ukuta wa chumba kile jinsi ulivyochafuka kwa damu ambazo bila shaka ziliruka baada ya kuchomwa kisu. Harufu ya damu ilikuwa inanuka.Nikaishika maiti ya Merina bila kutarajia.Huyu binti alikuwa jasiri kweli hata mwisho wa uhai wake bado alikuwa na moyo wa kumtahadharisha kiumbe mwenzake.Alikuwa anataka kusema neno lakini hatima yake ilikuwa imefika.Tayari alikuwa ameuacha ulimwengu huu ulimwengu wenye kila aina ya vituko. Ulimwengu wa dhulma,dhambi na ufisadi. Nikajikuta nikiwa nimeshikilia kisu ambacho kilikuwa kimezama katika kifua cha Merina,nilijisikia uchungu kana kwamba nilikuwa nafahamiana na Merina miaka mingi iliyopita. Ghafla,nikashtushwa na mwanga mkali ambao ulikuwa kama tochi iliyowashwa ghafla na kuzimwa.Nilipogeuka nikawaona watu wawili. Mmoja alikuwa ameshika kamera na yule mwingine alikuwa na bastola mkononi. Nilikosa la kufanya. Nilikuwa nimepatikana, jamaa alikuwa amenipiga picha.Picha mbaya kabisa. Mkono mmoja nilikuwa nimeshika bega la kushoto la Merina huku ule mwingine nikiwa nimeshika kisu ambacho kilikuwa kimezama kwenye titi la kulia. Ee bwanaee! ilikuwa si mchezo yaani ile picha kama itafika mbele ya jaji ambaye si makini au amekula rushwa ni kitanzi tu.Swali la haraka lilipita kichwani kwangu huu ni mtego? Balaa. Wale jamaa walinitazama bila kusema lolote wakaondoka.Huku nikiwa nimetawaliwa na hofu nikatoka ndani ya kile chumba na kurudi chumbani kwangu nikiwa nimechanganyikiwa kabisa. Ghafla kengele ya tahadhari ikalia kichwani kwangu.Sasa nilianza kuiona wazi jela ikinukia. Kwanza jamaa walinipiga picha,halafu kuna alama za vidole ambazo nimeziacha kwenye kisu. Sikuwa na wazo zaidi ya kutoroka.Nikae nifanye nini wakati kuisaidia polisi ni adhabu kamili ambayo inamtosha mhalifu yeyote. Sijui kwanini sikukumbuka taratibu za polisi za kuchunguza alama za vidole. Nikatoka mbio kuelekea Mapokezi.Nilishangaa kwani msichana wa mapokezi alikuwa anakoroma tena mkoromo ambao ulisikika nje ya chumba kile. Nikaona bora niingie kule mapokezi ili aweze kunifungulia mlango niondoke.Nilifahamu wazi kuwa angetaka kujua kilichotokea mpaka niondoke muda huo lakini sikujali kwani nilijiandaa kumjibu kutokana na aina yoyote ya swali atakalouliza. ......Nikagonga mlango kama mara tatu hivi lakini mlango haukufunguliwa.Nikajaribu kukinyonga kile kitasa, kumbe mlango ulikuwa haujafungwa kwa funguo.Nilipoingia mle chumbani ndipo nilipokutana na tukio lingine la aina yake,msichana wa mapokezi alikuwa anakoroma huku povu likimtoka mdomoni, haukuwa mkoromo wa kawaida ulikuwa MKOROMO WA MAUTI. Sikutaka kupoteza muda tena kama mara ya kwanza,nikapiga hatua za haraka haraka kuuendea mlango wa kutokea nje.Bahati ilikuwa upande wangu,bila shaka wale jamaa hawakufunga na funguo ule mlango. ‘Nitatoka?’ Swali hilo ndilo nililojiuliza kwa wakati huo *********
Saa 9.37 usiku,nilivuka bonde la mto msimbazi. Bonde hili liko maeneo ya Barakuda tabata chang’ombe.Nilijikuta nikiyaingia maji ambayo yalifika nusu muundi.Sikujali hali ile ambayo ilisababisha suruali yangu ilowe.Jambo la muhimu kwangu lilikuwa kujinusuru na mikono ya dola na wale jamaa ambao sikufahamu ni kina nani. Saa 9.54 nilikuwa maeneo ya viwandani.Nikavuka barabara na kutokea kituo cha Jet. Hapo hofu ikapungua kwani nilijua nikifika Lumo nitakuwa kwenye amani zaidi. Nikiwa eneo la Jet nikawaona watu wanne wakinifuata kwa kasi, moyo ulitoa mlipuko wa hofu.Nikaanza kutimua mbio kama mtu anayeshiriki mbio za mita fupi.Kila nilipofikiria adhabu ya kunyongwa nilijikuta nikiongeza mbio. Jamaa waliendelea kunifukuza, jambo la ajabu ni jinsi walivyokuwa wananifukuza kimya kimya. Nikaamua kuongeza mbio bila kugeuka. Nilipofika maeneo ya Kigilagila nikapunuza mwendo na kugeuka nyuma. Nikagundua jamaa nilikuwa nimewaacha mbali sana. Lakini baada ya kuwatazama vizuri nikagundua kuwa walikuwa ni vibaka. Nikasonya kabla ya kuanza kutembea taratibu kwani jamaa walionekana kuchoka kabisa na kusimama,bila shaka walikuwa wameshangazwa na kasi yangu ambayo haikuwa ya kawaida kwao. Saa 10.22 nilikuwa mbele ya mlango wa chumba changu. Angalau niliweza kushusha pumzi.Haikuwa mara yangu ya kwanza kuona maiti. Lakini ajabu ni taswira ya maiti ile kujirudia kichwani mara nyingi na kunikosesha usingizi. Pia niliwaza sana juu ya yule dada wa mapokezi,kwa vyovyote vile nilijua wazi kuwa yule dada hatofika asubuhi,nilijiuliza ni vipi wateja watahamanika baada ya kukutana na tukio lile la aina yake,pia nilivuta hisia jinsi watakavyopata msukosuko katika adhabu isiyo rasmi iliyopewa jina la kuisaidia polisi.Huku nikiendelea kuwaza hatimaye nikaamua kujifunika shuka,baada ya dakika kadhaa,hatimaye nikapata usingizi. Haukuwa usingizi mzuri,ulikuwa ni usingizi wa mang’amung’amu.Mara kadhaa niliota nikiwa mbele ya jaji kujibu tuhuma za mauaji.Wakati mwingine niliota babu akinipokea ndani ya kaburi.IIi mradi niliandamwa na ndoto za ajabu ajabu.Ndoto ya mwisho ninayoikumbuka sana ni ile ya watu wenye makoti makubwa wakinikimbiza huku kila mmoja akiwa na kisu chenye mpini mweusi mkononi………. *********CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Niliamka saa 5.30.Nikabaini kuwa nilikuwa nimelala bila kuvua suruali yangu ambayo ilikuwa imelowa kwani nilipovuka pale mto msimbazi nyuma ya Barakuda sikukumbuka hata kukunja nguo.Afadhali hilo la kulala na nguo iliyolowa balaa zaidi ni kulala na viatu! Kimsingi matatizo yote nilikuwa nimejitakia.Sikuwa na sababu yoyote ya kufuatilia mambo kama Polisi.Lakini najua sana kilichoniponza,kupenda kusoma riwaya za upelelezi. Riwaya hizi mara nyingi zilinisisimua na kunifanya nijihisi kama mimi ndio muhusika mkuu.Mara nyingi nilitamani kufanya kazi idara ya Usalama wa Taifa,pia nilitamani kuwa kachero. Nakusudia wale askari polisi ambao hawavai sare kama wengine.Nilihisi kuwa ninaweza. Lakini ilikuwa ngumu kupata nafasi hizo,kama huna ndugu huko uwe na pesa na kama huna pesa……we ulie tu. Nilitazama juu kana kwamba kuna kitu nilikuwa natafuta huko.Ukweli ni kwamba dali ile ilikuwa dhaifu sana mbele ya Fikra zangu.Fikra zangu ziliweza kupenya dali ile kama mwanga unavyopenya kwenye dirisha la kioo.Hamu ya kwenda kazini iliniishia. “Niende wapi?”, ni swali ambalo nilijiuliza nikakosa jibu. Na ile picha niliyopigwa? Duh!Nilihisi tumbo likinguruma baada ya kuikumbuka ile picha.Sijui kwanini wale jamaa walinipiga picha bila kuongea lolote.Bila shaka walikuwa na ajenda ya siri, ni ajenda gani? hilo ndilo swali lililoutesa moyo wangu. Nikaamua kuyapuuza mawazo ya ile picha. Nikamkumbuka Betty,yule muhudumu wa Baa ambaye nilitokea kumpenda sana. Pamoja na purukushani nyingi katika maisha,kwenye uwanja wa mapenzi sikuwa mzoefu.Hivyo kila nilipokumbuka kukutana na Betty,kidogo niliingiwa na hofu.Niliwashangaa wale watu majasiri sijui niwaiteje yaani anaweza kukutana na binti kwenye siti ya gari na ndani ya nusu safari wakawa wapenzi ********
Siku hii niliamua kuwatembelea baadhi ya rafiki zangu waishio Mwananyamala.Nikiwa kwenye daladala ndipo nilipokutana na kile ambacho sikukitarajia kwa muda huo. “Vipi tena?” Niliuliza baada ya kuona askari wengi barabarani.Yaani gari lilikuwa haliwezi kupita eneo la Tazara bila kukaguliwa. “Kuna jamaa,kaua watu huko Tabata, leo kila kwenye makutano ya barabara kuna askari. “Aah,kwa hiyo mpaka wamalize kukagua magari yote hayo?” Niliuliza huku nikianza kuingiwa na woga. “Ina maana wakimuona huyo muuaji watamjua?” Aliuliza abiria mwingine ambaye alikuwa amekaa siti ya jirani yangu. “Itakuwa hivyo mbona siku zingine hawasimamishi?” Abiria mwingine akajibu. “Sasa kama walimuona si wangemkamata muda huohuo?” “Labda aliahidi kufanya hivyo kabla?” Majibizano ya abiria yaliendelea na sasa nilikuwa siwasikii tena kwani akili yangu ilikuwa inawaza ni jinsi gani nitajinasua katika zoezi lile. “Aah,wanataka kutuchelewesha hawa,nifungulie nianze mdogo mdogo.” Nilimwambia konda ambaye alinielewa na kunifungulia mlango kisha nikashuka. Nikatembea taratibu lakini kwa tahadhari kubwa huku nikiwapita askari ambao hawakujishugulisha kunitazama. Ingawa niliwapita salama lakini nilikuwa na hisia kuwa kuna askari anakuja au wanakuja nyuma yangu,hali hiyo ikanifanya nijione kama ninayerudi nyuma badala ya kwenda mbele.Nilihisi kama mwili unataka kuishiwa nguvu.Kila kitu kilikuwa kimebadilika katika maisha yangu, furaha yangu ilipotea na nafasi yake ikachukuliwa na hofu na mashaka.Ni wakati kama huu ambao watu tuliomsahau Mungu huwa tunamkumbuka sana tena kwa imani hasa. Nilijilazimisha kila nilipowaona askari kutowakwepa na kuelekea upande waliopo ili kuwaondolea hofu juu yangu,kwa hilo nilifanikiwa sana kwani askari walikuwa wamejishugulisha na watu wa kwenye magari. Nilitembea hadi Buguruni sheli hapo nikakona na kufuata kichochoro ambacho kinaenda kwa Mnyamani. Safari yangu ya kurudi nilikotoka ilinifikisha Vingunguti eneo la kiembe mbuzi ambako niliamua kufuata reli ambayo ilinifikisha nyuma ya viwanda vilivyoko Kipawa.Nikafuata kichochoro kinachotokea barabarani,nikavuka barabara na kutokea eneo la Jet club ambapo nilipanda gari kurejea nyumbani.
*****
Ilikuwa ni jioni ya Jumatatu tulivu. Haikuwa siku ambayo tulikubaliana kukutana na Betty lakini sikuwa na jinsi kwani nilimuhitaji kwa udi na uvumba. Siku ile ya kwanza kumuona nilivaa kama afisa fulani serikalini au sehemu ambazo pesa si tatizo. Jumatatu hii nilikuwa nimevaa Fulana Nyeusi na suruari ya jeans ya bluu. Niliingia ndani ya ile baa nikaanza kumtafuta Betty kwa macho, sikumuona. Wateja walikuwa wachache kwa sababu ilikuwa ni siku ya kazi lakini sikuweza kumuona.
Nikaamua kuhamishia macho yangu kwa wacheza pool. Nilifurahi jinsi walivyokuwa wanaigonga mipira ile na kuiingiza kwenye vishimo vidogo. Kitu kimoja tu walikuwa wananikera, walipenda sana kutumia lugha ya matusi. Pamoja na kutumia lugha hiyo mbaya lakini hakuna aliyekasirika, wenyewe waliona kuwa jambo la kawaida kwani hata mtu aliyesifia kitu aliisindikiza sifa hiyo kwa tusi kali mengine yakiwa ya nguoni.
Nikaachana na wacheza pool nikaanza kuzungusha macho yangu huku na kule. Muda mfupi baadae mmoja wa wahudumu wa baa alikuwa amesimama mbele yangu. “Nikusaidie nini kaka” alisema huku akiwa ameibana sauti kama anayeongelea puani. Nikamtazama kidogo kwa jicho la kutathmini. Bado alikuwa hajamfikia Betty kwa uzuri wake.
“Naomba pepsi baridi tafadhali.” Nilimjibu huku nikiwa nimemkazia macho angalau ajisikie kuwa nimemjali. Nilikuwa na uwezo wa kuvunja mawe makubwa na kubeba mzigo mzito wa mawe lakini kukabiliana na hawa viumbe ilikuwa ni zaidi ya huo mzigo wa mawe.
Muda mfupi baada ya kuhudumiwa nikamuona Betty akiingia. Alikuwa ameshika gazeti mkononi. Tulikutanisha macho yetu. Kidogo nilimuona akibabaika, bila shaka alikuwa anajaribu kuvuta kumbukumbu ya sura yangu, wapi aliniona. Hilo lilikuwa swali ambalo nahisi lilipita kichwani mwake. Siku hiyo hakuwa amevaa sare. Nikamwita kwa ishara ya mkono. Akaja akakaa, sikuwa na hofu tena kama ilivyokuwa siku ya kwanza.
“Habari yako Betty.” Nilimsalimia kwa ujasiri huku nikitabasamu.
“nzuri!” alijibu kwa mkato huku akionesha wazi mshangao jinsi nilivyoweza kufahamu jina lake.
“Utakunywa nini?” Nilimuuliza huku nikiendelea kushangaa jinsi alivyoumbika. “Ahsante sijisikii kunywa kitu cha baridi.” Alinijibu huku akitabasamu. Niliinamisha kichwa changu mezani nikitafakari namna ya kuanzisha maongezi.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
”Nikununulie bia ya moto?”
“Hapana, nahitaji kitu cha moto kama chai au maziwa.” Alinijibu, nikatumia nafasi hiyo kumuuliza swali.
“Unanikumbuka?” lilikuwa swali langu la kwanza.
“ Sura yako si ngeni sana, naona kama nilishawahi kukuona mahali” Jibu lake kidogo lilinifariji.
“Nilikuja hapa juzi, tukapanga kukutana jana lakini…………” Sikumaliza nilichotaka kuongea.
“ Aah, sawa. Sasa nimekumbuka. Samahani sana jana nilikuwa off hata hivyo nilikuwa nimesahau kabisa!” Hiyo nikaiona fursa nzuri kwangu.
“Jana nimekaa sana hapa mpaka wakati wa kufunga baa ndipo nikaondoka!” Nilikuwa namuongopea yule mwanamke.
“Enhe, lete story.” Aliongea kwa upole na uchangamfu kitu ambacho sikukitarajia. Nikakohoa ili kuiweka sawa sauti yangu.
Nikapatwa na mshtuko baada ya kukiona kichwa cha habari ambacho kilikuwa kwenye gazeti ambalo alikuwa amelishika Betty mkononi. MAUAJI YATIKISA TABATA. Sikuthubutu kuomba lile gazeti kwani kichwa cha habari tu nilijisikia kubanwa na haja ndogo vipi niisome habari mzima halafu nikute picha yangu……. Sikutaka kudhihirisha mshtuko wangu kwa Betty. Lile gazeti kwa kiasi fulani lilikuwa limenipunguzia nguvu na ujasiri wa kuongea na Betty.
“Betty, sina maneno mengi ya kuongea isipokuwa ni neno moja tu; Hilo ndilo limenifanya nifunge safari kutoka nilikotoka hadi hapa. Kwa kifupi nakupenda.” Nilishusha pumzi na kumkazia macho Betty.
“Sijakuelewa bro, kwanza hata jina sijakufahamu, kwa kifupi hatufahamiani vizuri!”
Nikajisikia aibu baada ya kutanabahi kuwa nilikuwa nimeanza mazungumzo yale bila umakini. Kidogo nikajisikia Vibaya ingawa nilipiga moyo konde na kutaka kuendeleza mazungumzo yale. Kisha akaendelea kuongea“usijali sana, mimi naitwa Betina Samson Masawe, nimezaliwa wilaya ya Moshi mkoa wa Kilimanjaro. Elimu yangu ni kidato cha nne. Sina mtoto, sina mume wala sina mchumba na sihitaji mume wala mchumba.” Alimaliza kwa kauli ambayo ilikuwa kama mkuki kwenye moyo wangu. Nilimtazama tena Betty, nikainamisha uso wangu chini kwani alianza kunipa wakati mgumu kutokana na kauli yake hiyo.
“Kwa nini hutaki mume ina maana hutaolewa” Nilimuuliza.
“Utapeli wao ndio unao nifanya nitamani zaidi kuwa peke yangu!” Alinijibu kwa upole lakini akionesha kutokuwa na mzaha na kauli yake.
“Utapeli upi?” Nilimuuliza kwa sauti iliyokata tamaa.
“Kama huu ambao unauleta wewe sasa, eti unanipenda, mimi baamedi?”
“Una uhakika kuwa naongopa?”
“Kwa asilimia mia moja” Alinijibu kwa msisitizo. Nikamtazama Betty kwa hasira kidogo kwani sikupenda kuitwa tapeli.
“Narudia, sitaki mwanaume hivyo hata wewe sikutaki labda kama unataka kuwa kaka yangu wa hiyari, leo unanitaka kesho unitangaze vijiweni kuwa malaya eti kisa kuuza baa.”
Nilishindwa kuvumilia maneno makali ya Betty, nikainuka na kutaka kuondoka. Nilikuwa nimeshapiga hatua mbili nikamsikia Betty akiniita.
“Bro…Mbona unaondoka?” Aliniuliza Betty kwa sauti ileile ya upole.
“Nimekata tamaa.” Nilimjibu kwa hasira.
“ Kwa hiyo hata kuagana hatuagani!”
“Kwa heri.” Nilimjibu huku nikiwa nimemkazia jicho la hasira.
“Kwaherii, yaani leo niandike kwenye diary yangu nilikutana na mtu hakunitambulisha jina wala nini….. kaniita na kuniambia eti ananipenda kisha kwa heri!” Naye aliongea huku akionesha hasira na dharau kwa jinsi nilivyokosa ustaarabu.
Nikaamua kuituliza hasira yangu la sivyo tusingeelewana. “Betty..” Nilianza huku nikiwa nimesimama nyuma ya kiti ambacho nilikalia.
“Kwanza naomba samahani kwa kutokukufahamisha jina langu. Naitwa Kajuna Kazakamba. Elimu yangu ni kidato cha sita. Sina kazi. Sijaoa wala sina mchumba. Nahitaji mke, nakuhitaji wewe.” Nilimaliza na kumtazama Betty huku hasira zangu zikiwa zimepungua.
“Mimi ni baamedi, inakuwaje unihitaji mimi hujawaona wengine ambao ni tofauti na mimi huko unakotoka?” Lilikuwa swali gumu kidogo.
“Hakuna tatizo kwangu kama unaweza kujiheshimu katika kazi yako hiyo, kwa jinsi nilivyokuona naamini unajiheshimu.” Betty alikuwa kama anayepingana na akili yake akubali au akatae.
“ Ah, hapana Kajuna siwezi na sitaki mwanaume anivurugie maisha yangu, Kwa heri.” Aliinuka kwenye kiti na kuanza kuondoka. Hakuweza kukatisha pale niliposimama nikaudaka mkono wake wa kushoto. Alikuwa anahangaika kutaka kujinasua kwenye mikono yangu. Sikumpa nafasi, kwa kutumia mkono wangu wenye nguvu nikambana. “Kaju…niachiee” alikuwa analalamika kwa sauti ndogo lakini yenye hasira. Nikazungusha mikono yangu mgongoni kwake. Nikamvutia kifuani kwangu kwa nguvu nikamkumbatia.
Bahati ilikuwa upande wangu kwani wakati huo spika zilikuwa zinatoa sauti kubwa ya muziki laini ulioimbwa na Shania Twain Your still the one. Yeyote aliyetuona alijua kuwa tunacheza muziki huo. Nikawa nalazimisha kukutanisha ndimi zetu. Ndimi zikakutana. Nikaitoa mikono yangu, alikuwa anahema kweli kweli. Ajabu, alikuwa amekilaza kichwa chake kwenye bega langu la kulia. Nikaanza kumpapasa mgongoni kwa namna ambayo ilimfanya asisimke na kuniganda safari hii ikiwa kwa hiyari yake.
“Kajuna, Ilove you”.Kwa sauti iliyojaa kitetemeshi alitamka Betty na kunifanya nihisi kuwa niko ndotoni. Alikuwa hana ujanja tena, kijana nilikuwa nimeshinda ‘gemu’.
“Twende nyumbani!” niliongea kwa sauti ndogo ya kubembeleza.
“Twende kwetu”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Wapi?”
“Si mbali” alinijibu. Nikamfuata kama kondoo anayeenda kuchinjwa……..
***
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment