Simulizi : Mzigo
Sehemu Ya Pili (2)
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Miezi mitatu ya mapenzi yangu na Betty ilikuwa imepita salama bila misukosuko, hata zile habari za mauaji ya kule Kisukuru zilipotea kama upepo . Betty alikuwa anaendelea na kazi yake ya baa. Alikuwa mwanamke mwenye msimamo thabiti. Hakuyumbishwa na yeyote. Pamoja na usumbufu mkubwa alioupata kutoka kwa wanaume wenye fedha, bado alinithamini na kunijali.
Ikatokea siku miongoni mwa siku ambazo ni ngumu kuzisahau katika maisha yangu. Siku hiyo ndio ilikuwa mwanzo wa kubadilika mfumo wa maisha yangu. Huo ndio ulikuwa mwanzo wa kipindi kigumu kabisa katika historia yangu ambachi sifikirii kama kitakuja kutokea tena.
Ilikuwa ni Jumamosi kama zilivyo jumamosi nyingine. Tofauti ni kwamba siku hiyo niliamua kupumzika nyumbani. Siku hiyo sikuwa na ahadi ya kukutana na mpenzi wangu Betty. Hivyo niliamua kuitumia siku hiyo kwa kazi ndogo ndogo za nyumbani. Kutokana na uchovu wa kazi ngumu za vibarua vya juma zima niliamua kurudi tena kitandani baada ya kumaliza kazi zangu.
Wakati usingizi ukianza kunichukua nikasikia mlango unagongwa. Nikainuka kitandani na kwenda kufungua. Nilipofungua mlango, nikashtuka kidogo kwani mtu niliyemuona alikuwa mgeni kabisa machoni mwangu. Licha ya ugeni wa mtu yule bado sikuona kama nina hadhi ya kutembelewa naye. Alikuwa pandikizi la mtu ambaye kama hufahamu jina lake unaweza kumwita Bonge. Alikuwa ananukia manukato yaliyomtofautisha na mtu mwenye kipato cha kawaida kwenye jamii. Alikuwa na uso wa duara huku akiwa amenyoa ndevu zake kwa mtindo wa ‘O’ ukijulikana zaidi kwa jina la ‘Timberland’ . Alikuwa amevaa suti ya kijivu ambayo bila shaka ilikuwa ni ya gharama kubwa. Miguuni alivaa viatu vyeusi ambavyo viling’arishwa vema kwa dawa. Alikuwa anapendeza.
Amefuata nini?
“Habari yako bwana Kajuna.” Alinisalimia na kunizidishia mshangao. Kwani alikuwa kama mtu anayenifahamu siku nyingi.
“nzuri, karibu ngoja nikuchukulie stuli.” Niliwahi kumzuia ili asije kuingia ndani, niliogopa mtu mzima nitaadhirika.
“Hapana siwezi kukaa kwa sasa isipokuwa nina mazungumzo machache, kama hutajali naomba unifuate tukaongelee kule kwenye gari langu.” Aliongea huku akinyoosha kidole kule liliko gari lake. Lilikuwa Toyota Landcruiser nyeupe.
“Hakuna tatizo” Nilimjibu huku tukielekea kule liliko gari lake. Majirani walikuwa wananitazama kwa jicho la husuda wakati naondoka na Bonge kuelekea kule kwenye gari. Walikuwa wananong’ona, sikujua ni kitu gani kiliwafanya wanong’one.
Jambo usilolijua!
“Ndugu Kajuna nafikiri hii ni mara yetu ya kwanza kukutana mimi na wewe.” Alitulia kidogo na kunikazia macho. Kisha akaendelea. “Mimi ni mgeni kwako lakini wewe si mgeni kwangu, nakufahamu sana Kajuna.” Sikutaka kujiuliza sana kwani moyo ulikuwa unaenda mbio sana pia sikuona sababu ya kuumiza kichwa kwa kujiuliza mwenyewe wakati nina uhakika wa kupata majibu kutoka kwa mtu huyo ambaye alikuwa mbele yangu yaani nilikuwa sioni haja ya kuandikia mate wakati wino upo.
Nilianza kuhisi kuwa huenda huyu mtu ni polisi. Nilikuwa nimesahau kabisa tukio la kule Zawadi guest house lakini sasa nilianza kuileta picha ya tukio lile katika nafsi yangu. Nilichanganyikiwa ile mbaya. Yule jamaa alikuwa hatari sana kwani muda wote alikuwa kama anayesoma mawazo yangu.
“Usiwe na wasiwasi Kajuna, nimekuja na habari njema kwako. Habari hizi zitabadilisha kabisa maisha yako wewe na Betty. Lililo muhimu kwako ni kunisikiliza kwa makinini kile nitakachokueleza” Akatulia tena na kunikazia macho. Alizidi kunichanganya kwani badala ya kupunguza aliongeza maswali ambayo ilikuwa ni vigumu kuyajibu. “Kamfahamu vipi Betty?” Nilijiuliza huku nikihisi tumbo langu likichafuka na kunguruma. Nilimkazia macho kwa hamu ya kutaka kujua nini alitaka kuongea. Naye kama aliyekusudia kunitia umakini akatulia kwa dakika mbili.
“Utakuwa tajiri tena tajiri mkubwa kama utatekeleza kazi nitakayokupa”. Akatulia tena kama mwanzo.
“Mimi niwe tajiri!”Niliwaza huku upande mwingine nikiona kama ninayefanyiwa dhihaka.
“Safari hii hutakiwi kuua mtu kama ulivyofanya kule guest, itakuwa kazi nyepesi sana.” Niligwaya baada ya kusikia kauli ile. Nilitamani arudie tena maana nilikuwa kama sijamuelewa vizuri.
“ Au unabisha kuwa hujaua mtu wewe!” akaingiza mkono mfukoni akatoa kitu ambacho kwa wakati huo nilikitarajia sana, PICHA! Ilikuwa ni picha ya lile tukio la yule mwanamke. Mandhari ya ile picha ilinitisha sana. Nilikuwa muuaji kamili kwa mujibu wa picha ile.
“Samahani sana kwa kukukumbusha kitu cha kuogofya kama hiki, lakini hii nakuonesha kuwa sina nia mbaya na wewe maana mimi ni ofisa wa polisi hivyo ningetaka kukuweka ndani ningekuweka siku nyingi!” Akatulia tena. Huwezi kuamini jamaa aliniteka kabisa kwani nilikuwa tayari kwa lolote ili mradi ile picha asiipeleke kunakohusika. Kisha akaendelea.
“ Lengo la kukufuata tunataka kukutuma, si kazi ya bure. Malipo makubwa yatafuata baada ya kukamilisha kazi yetu!”
Wanataka kunituma, wao kina nani wanataka kunituma nini na wapi? yalikuwa maswali yaliopita haraka sana kichwani mwangu. Safari hii Jamaa hakuruhusu niwe na muda mwingi wa kujiuliza.
“unatakiwa kwenda Mwanza, huko kuna mzigo ambao jukumu lako ni kuufikisha salama Dar. Malipo yako ni dola elfu hamsini. Jambo la muhimu ni kutekeleza masharti utakayo pewa, ukivunja masharti utasababisha matatizo makubwa kwani zile picha bado tunazo, pia unatakiwa ufahamu kuwa mimi ndiye niliyekabidhiwa jukumu la upelelezi wa mauaji ya Muhudumu wa gesti na yule binti ambaye ulimuua kwa kumchoma kisu.” Akaingiza mkono mfukoni akatoa kitita cha noti. Zilikuwa noti za shilingi elfu kumikumi. Sikujua zilikuwa shilingi ngapi kwani baada ya kunikabidhi niliziweka mfukoni
“ Jiandae kwa safari, safari yako itakuwa keshokutwa Jumatatu.” Yule jamaa alikuwa amemaliza maongezi, akaingia ndani ya gari na kuliondoa kwa kasi.
Nilibaki nimeduwaa nikilitizama gari lile lilivyokuwa linatokomea kwenye barabara ya vumbi. Nilisimama pale kwa dakika kadhaa huku nikiwa nimechanganyikiwa nisijue la kufanya.
Nikarudi nyumbani na kukuta kina mama wakiwa makundi makundi. Kumbe muda wote wakati naongea na yule jamaa wao walikuwa hawajatoka pale wakinikazia macho, umbea tu ndio uliowashugulisha hata wakaacha kazi zao.
Walinisindikiza kwa macho hata pale nilipokuwa naingia chumbani kwangu. Hali hii ilinikera sana kwani kuna ajabu gani mimi kutembelewa na mtu kama yule.
***CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Tamaa ya fedha ilinifanya nisifikirie sana kuhusu kukataa au kukubali kwenda kuchukua huo mzigo. Nilikata shauri kukubali kwani siku niliyokutana na Bonge alinipa shilingi milioni moja ambazo hazikuwa na masharti wala makubaliano. Sijawahi kuzishika pesa hizo hivyo ilikuwa ni furaha kubwa kwangu. Mwanza tu! Kufuata mzigo ambao sikutakiwa hata kujua ndani yake ulikuwa na nini. Bora niuage umaskini mapema.
Siku iliyofuata Bonge alikuja nyumbani saa saba usiku. Nilishangazwa sana na ujio huu. Lakini tamaa ya fedha ilikuwa imenishika kiasi cha kuweza kusahau ile picha. Nakumbuka siku hii Bonge alikuja akiwa ‘sirias’ sana. Niliingiwa na hofu kubwa kwani alinitisha.
“ Kajuna kesho ndio siku ya safari zingatia maagizo yangu. Jambo la kwanza utakaporudi kutoka Mwanza hutakiwi kupitia sehemu yoyote mpaka uufikishe mzigo mikononi mwangu. Sharti la pili hutakiwi kufungua huo mzigo, narudia hutakiwi kufungua huo mzigo. Naomba uelewe wazi kuwa picha zako za mauaji tunazo. Pia napenda ufahamu kuwa kama utavunja sharti la Kwanza basi adhabu yako itakuwa ni kukosa malipo na kama utavunja sharti la pili basi si kingine zaidi ya Kifo.”
Aliongea bila kuonesha chembe ya mzaha hata kidogo. Niliogopa sana, nikaanza kuhisi chuki juu ya huyu jamaa. Sijui kwanini huyu jamaa hata pale alipokuwa anaongea taratibu nilimuogopa sana. Nilishindwa kumuangalia machoni kwani nilihisi moyo ukienda mbio sana.
Nitoroke? Nilijiuliza. Wazo lolote nililokuwa nalo lilivurugwa na tamaa ya fedha. Kiasi alichoniahidi Bonge kilikuwa kikubwa mno. Nilikubali, nilikubali masharti yote ya Bonge, pesa bwana… kila kitu pesa!
***
Napenda sana kusafiri. Lakini safari hii ya Mwanza sikuifurahia. Ninaposafiri huwa napenda kushangaa hili na lile hasa misitu wanyama na kadhalika. Safari hii ilikuwa ni ndefu kwangu kuliko urefu wake wa kawaida. Ingawa nilikuwa dirishani bado nilikuwa sielewi nini kilikuwa kinaendelea huko nje. Dola elfu hamsini si mchezo, zilinitoa jasho kweli kweli. Mpaka kufikia hapo sikuwa na mawazo mengi juu ya huo mzigo. Nilichohitaji ni pesa, pesa tu na si kingine. Nilijikuta nikijenga na kubomoa kwenye kichwa changu. Nilijenga nyumba nzuri ya vigae Kinondoni nikaibomoa, nikajenga, nikajenga…… ili mradi nikajenga nyumba nyingi tu za kufikirika.
Safari ya Basi kwenda Mwanza ni ndefu sana. Lakini urefu huo ulizidishwa mara mbili na fikra zangu. Niliwatazama abiria wenzangu, wengi walikuwa wamelala. Nikatoa karatasi ambayo ilikuwa na maelezo jinsi nitakavyokutana na Martin ambaye atakuwa mwenyeji wangu huko Mwanza. Yaweza kuwa wanataka kumdhulumu huyo Martin hivyo ili kupoteza ushahidi ndo wameamua kunituma mimi.
Masaa kadhaa baadae nami nikasalimu amri kwa kuungana na abiria wenzangu, nikalala. Sijui usingizi wangu ulichukua Muda gani lakini niliposhtuka tayari tulikuwa tumeingia Mwanza. Niliteremka kwenye gari lile ambalo hata sikuwa na muda wa kujua ni nani mmiliki wake.
***
Saa 7.30 mchana niliwasili Mwanza. Nilipokelewa na baridi kali. Abiria wengi walitoa nguo mbali mbali ambazo zingewakinga na baridi yakiwemo makoti na majaketi. Sikuwa na ufahamu na hali ya kijiografia ya jiji la Mwanza. Lakini niliipenda sana hali hii ya hewa. Wakati nikiendelea kuwaza ghafla nikaguswa begani. Nilipogeuka nikamuona kijana mrefu ambaye alikuwa amesimama nyuma yangu, tukasalimiana. Kisha akanielekeza kwenye gari ndogo aina ya Toyota carina.
“Bila shaka wewe ndiye mgeni wa Mr. Martin.”
“Ndiyo mimi.” Nilimjibu kisha tukaingia kwenye gari alilokuja nalo.
“Karibu sana Mwanza, nimetumwa kuja kukuchukua na kukupeleka nyumbani kwake”
“Ahsante.”
“Hii ni mara yako ya kwanza kuja Mwanza?”
“Ndiyo” Nilimjibu kwa mkato huku akiwa anakata kona kuingia katika mtaa ambao sikuufahamu.
“Mimi naitwa Masanja nimetumwa na Mr.Martin kuja kukuchukua!” Aliongea kwa lafudhi ya kisukuma.
Tuliendelea kukona hapa na pale nashindwa kuelezea mitaa hii kwani Siifahamu mitaa ya Mwanza ingawa nilikuja kuambiwa baadae kuwa maeneo hayo yanaitwa Nyakato.
“Umefahamu vipi kuwa mimi ndie mgeni mwenyewe?”Nilimuuliza ili kuvunja ukimya ulioanza kutawala kwenye gari.
“picha yako!” Alinijibu na kunifanya nisikie tumbo likinguruma. Sijui ni picha ya aina gani huyu jamaa alikuwa anaizungumzia. Kama ni ile niliyopigwa kule gesti basi ni balaa kubwa. Jibu lake lilinifanya nikose hamu ya mazungumzo kwa kuhofia kukumbushwa mkasa ule wa aina yake.
Gari ilifunga breki mbele ya Nyumba moja kubwa ambayo ilikuwa imezungushiwa ukuta wa tofali za kuchoma. Lango likafunguliwa baada ya kupiga honi mara tatu. Gari ikapaki mbele ya bustani ndogo ya maua.
“Tumefika.” Alisikika Masanja huku akifungua mlango wa upande wake, nami nikafungua upande wangu nikashuka.
“Huyu ndiye mgeni wa Martin ambaye nilimfuata.” Alimuelekeza yule mtu aliyetufungulia geti.
“Kwaheri ndugu, jukumu langu lilikuwa ni kukufikisha hapa.” Masanja aliongea huku akiingia kwenye gari lake.
Nikasalimiana na yule mtu aliyetufungulia lango. Akanielekeza kwa ishara niingie ndani.
“ Mr. Martin amefuata mzigo Shinyanga hivyo utamsubiri hapa mpaka kesho atakaporudi”. Niliitikia kwa kichwa huku nikijitupa pale kwenye sofa. Nilikuwa nimechoka sana. Yule mtu ambaye bila shaka alikuwa ni mlinzi alikuja na kunielekeza chumba cha kwenda kupumzika. Nikaingia ndani ya chumba hicho. Kabla sijapumzika akaja
“Ebwana kama utahitaji chakula naomba unifahamishe.”
“Sawa.” Nilimjibu kwa mkato kwani sikujisikia kula kwa muda huo.
Niliikagua mandhari ya Chumba kile. Kilikuwa ni chumba kikubwa kizuri,kikiwa na bafu na choo. Zaidi ya zulia zuri la hariri na kitanda cha futi sita kwa sita hakukuwa na kitu kingine mle ndani. Nikaingia kule bafuni, baada ya kuoga nikarudi chumbani.Nikajilaza kitandani, usingizi ukanichukua.
***
Kutokana na uchovu wa safari nililala kwa masaa kadhaa pale chumbani. Ghafla! Nikashtuka kutoka usingizini. Kuna watu walikuwa wanaongea. Niliwasikia vizuri, Bila shaka walikuwa wamesimama kwenye korido karibu na chumba changu.
“Vipi mzigo wa mheshimiwa tayari?” Aliuliza mmoja.
“Uko tayari, nimeupata kutoka Shinyanga maeneo ya Mwadui tena mzigo safi kabisa” Ilijibu sauti nyingine.
“Kwa hiyo kesho utamkabidhi jamaa ausafirishe”
“No, jamaa tutamkabidhi kesho lakini atasafiri nao kesho kutwa!”
“Huoni hatari kama atalala hapa kesho?”
“Nishamchukulia chumba gesti hata hivyo sikuwa na uhakika wa kupata mapema mzigo ndio maana nikakata tiketi ya kesho kutwa” .
Kwa akili ya haraka nikajua kuwa pengine huo mzigo ni almasi kwa sababu nilisikia kuwa umetoka Mwadui. Nikatabasamu kwa furaha. CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kumbe ndio maana bonge alinionya kuwa nisifungue mzigo! Alijua iwapo nitafungua nitaingiwa na tamaa” Niliwaza. Wakati nikiwaza hivyo nilisikia milango ya vyumba viwili tofauti ikifunguliwa. Nikajuwa wale jamaa watakuwa wameenda kulala.
Usiku ule sikupata usingizi mawazo yangu yalikuwa juu ya mzigo. Ni mzigo gani? Kwanini uwe na masharti magumu kwa kuusafirisha tu, kama thamani yake ni kubwa kwanini wasiusafirishe wenyewe? Kama hauna thamani kwanini wakubali kutumia gharama zote hizo. Maswali yalikuwa magumu pia yaliniumiza sana kichwa. Nilikuwa nashindwa hata kuhisi undani wa jambo lile.
Wakati nikiendelea kuwaza juu ya mzigo nikapata wazo. Wazo hilo nililiona kuwa zuri. Bonge alinionya kuwa nisipitie sehemu yoyote kabla sijampelekea mzigo wake. “Huu mzigo itakuwa wameupata kwa njia zisizo halali, kwa hiyo si mbaya hata mimi nikiuchukuwa”. Niliwaza. Almasi kutoka Mwadui niziache nichekwe? Haiwezekani. Dawa ya moto ni moto kama wao wamefanya dhulma kuupata huo mzigo basi si vibaya hata mimi nikiwadhulumu.
***
Saa 1.05 nilikuwa mbele ya Martin. Tofauti na nilivyotarajia, Martin alikuwa pandikizi la mtu mwenye sura ya kutisha. Macho yake yalikuwa mekundu. Bila shaka alikuwa mvutaji mzuri wa bangi. Alikuwa amevaa fulana ya mikono mifupi ambayo iliruhusu misuli yake iliyojengeka kimazoezi kuonekana. Katika mikono yake alikuwa na michoro ya nge, nyoka na mingine ambayo nilishindwa kuilewa. Kama ungemtazama machoni lazima ungekubaliana na mimi kuwa ni muuaji. Hakuhitajika mtaalamu wa saikolojia kulitambua hilo. Hata pale alipokuwa anaongea hakuonesha mzaha hata kidogo. Nakuambia huyu jamaa alikuwa anatisha si mchezo hata kama ungekuwa na mtoto analia ukamtisha kumpeleka kwake huyo mtoto angenyamaza.
“Bwana Kajuna karibu sana! ” alianza baada ya kusalimiana.
“Ahsante!” Nilijibu huku nikishangazwa na karibu hiyo ambayo ni wazi haikutoka moyoni.
Unafiki tu.
Hapo alijitahidi kuonesha upole na uungwana lakini hakufanikiwa alitisha tu, tena sana. Alikuwa kama chui anayemchekea mbuzi ili kumzubaisha, hakuna mbuzi atakayetambua kicheko cha chui. Akicheka anachekea nyama akikasirika anajiandaa kuvamia, tafsiri itabaki kuwa hivyo daima katika maisha ya mbuzi.
“Mimi ndio Martin kama ulivyoelezwa na bosi. Mzigo ulioambiwa uko tayari nitakukabidhi dakika kumi zijazo. Tafadhali usisahau maelekezo yetu. Aliongea kwa sauti ndogo yenye amri kali. “Kama utathubutu kuvunja maelekezo……., tena ole wako ufungue mzigo lazima nikuue kwa mkono wangu, tena si kukuua tu! Bali nitakuua kifo kibaya sana. Narudia, kitakuwa kifo kibaya sana.” Aliongea kwa msisitizo mpaka nikaingiwa na hofu. Eeh, angalau sasa alianza kujionesha dhahiri jinsi alivyo. Sikujibu lolote lakini mpaka kufikia hapo hamu yangu yangu ya kufungua ule mzigo ilikuwa imeisha. Hata awe nani kwa vitisho ya Martin lazima angetii tu. Nilihisi joto kali kutokana na hofu. Dakika chache za vitisho kutoka kwa Martin zilitosha kabisa kuifanya dakika moja ionekane kuwa saa nzima.
***
Mzigo ukaletwa. Lilikuwa begi jeusi la kawaida. Halikuwa tofauti na yale mabegi yanayouzwa pale Karume Dar es salaam kwa wauza mitumba. Nikatabasam kimoyomoyo. Nilianza kuhisi ushindi fulani ndani ya nafsi yangu.Nikakabidhiwa begi na Martin Kisha tukaingia kwenye gari lilelile lililonileta. Wazo likanijia, wakati naingia ndani ya lile gari nikasoma namba zake nikazikariri kichwani. Nilipoingia kwenye gari nikaziandika kwenye note book yangu. Tukaondoka kuelekea ‘guest’. Saa tatu na robo tulikuwa mbele ya jengo lile la kifahari ambalo lilikuwa katika mtaa ambao nilifahamishwa kuwa unaitwa Kirumba.
Martin alikuwa amemaliza kazi yake, akaniacha peke yangu pale ‘guest’. Akaondoka baada ya kuhakikisha kuwa amenikabidhi tikiti ya gari ambalo lilikuwa linaondoka kesho. Akili yangu ilikuwa inafanya kazi haraka kuliko uwezo wake kawaida.
Kwa kiasi fulani hili lilinishangaza.Nikachukua begi langu na kuondoka pale ‘guest’. “Anko vipi mbona unaondoka?” Aliniuliza dada wa mapokezi “Nimepata simu ya msiba hivyo siwezi kulala hapa!” Nilimjibu huku nikiwa nimeshapiga hatua kadhaa kuuendea mlango wa kutokea nje.Bado aliendelea kuongea lakini sikumuelewa,akili yangu yote ilikuwa juu ya mzigo na safari yangu. Teksi chache zilikuwa zimeegeshwa nje ya ‘guest’ hii. Nikaisogelea moja ya teksi zile. “ Sema bosi unaenda?” aliniuliza mmoja wa madereva wa teksi.Nikaitikia kwa kichwa. “Naomba uniwahishe kokote ninakoweza kupata magari yanayokwenda Dar”nilisema huku nikiwa tayari nimeshakaa siti ya nyuma. “Duh! Saa hizi utapata lakini siti za nyuma” “Hakuna shida ninachotaka ni kusafiri leo hata kama itakuwa ni lori la samaki niko tayari!” “ Nahisi Saibaba halijaondoka!” alisema huku akikoleza mwendo wa gari yake.Baada ya dakika kumi na tano tulikuwa Kituo kidogo cha magari yanayoelekea Dar. “ Shilingi ngapi?” “Elfu tano Mkubwa”. Nikachomoa noti ya shilingi elfu tano nikampa. Mungu alisikia maombi yangu.Nilipofika tu,dada mmoja akanifuata. “Kaka samahani kama unasafiri nina tiketi yangu naiuza tena ni D 5 yaani dirishani,mimi nimeahirisha safari mpaka kesho” Alisema yule dada kabla hata ya kusalimiana. “ Unaonje tukibadilishana tiketi,mimi nikupe ya kesho!” “Nitashukuru sana kaka yangu maana kuna mizigo muhimu nimesahau.” Mchezo ulikuwa umekwisha,lengo lilikuwa limetimia.Ni kama Mungu aliamua kunisaidia.Moyo wangu ulitawaliwa na furaha nikajihisi amani zaidi. Tikiti aliyonipa ilikuwa ni ya basi la Mwanza Coach.Safari yetu ikaanza saa sita kamili. Kama ni mawazo basi safari hii nilikuwa na mawazo zaidi kuliko ile ya kwanza.Ule mzigo ulinishughulisha sana. Kuna nini ndani ya ule mzigo. ”Ngoja nifike Dar nitaamua nini cha kufanya” Niliwaza. Lakini upande mwingine nilikuwa nasikia sauti ambayo ilikuwa inanionya,watu wenye vitisho namna ile kweli wataniacha hai nikishafikisha huo mzigo wao,kwanini walimuua yule mwanamke?Maswali hayo yalizidi kunitisha lakini yakiniongezea ujasiri wa kuvunja masharti. ******** Niliwasili Dar es salaam saa tisa na nusu alasiri.Hii ilikuwa ni mapema zaidi kuliko nilivyotarajia.Safari yetu ilichukua siku tatu.Watu walikuwa wametawanyika hovyo pale kituo kikuu cha mabasi cha Ubungo. Walikuwa kama siafu walioangukiwa na kaa la moto.Miongoni mwao walikuwa nia abiria ambao wanasafiri huku wengine wakiwasili.Pia walikuwepo wapiga debe ambao walileta kero kubwa kwa abiria. Bonge alinionya kuwa nisipitie sehemu nyingine kabla ya kumfikishia mzigo wake.Pia alinionya kuwa iwapo sitatekeleza maagizo yake,basi asingenipa malipo yangu kwa kazi ya kusafirisha mzigo ule.Vile vile alinikumbusha kuhusu ile picha ya hatari.Ni picha yangu ambayo ilikuwa inaniweka katika wakati mgumu.Ni picha ambayo leo inanifanya niwe mtumwa. Kwa sababu ambazo mpaka leo sijazielewa nikaamua kuvunja maagizo yake kwa kupitia nyumbani kwangu Yombo Buza.Sifahamu kama kuna nguvu ya ziada kutoka nje ya nafsi yangu ilinituma kufanya uamuzi huo wa aina yake. Kuvunja maagizo ya mtu kama Bonge halikuwa jambo la kwaida. Ilikuwa ni siku ya tatu toka nikabidhiwe begi lile.Sikujua kilichomo ndani yake ingawa hisia zilinituma kuwa huenda ni almasi.Kidogo nikaanza kuingiwa na mashaka kwani nilionywa kuwa iwapo nitathubutu kufungua tu,basi adhabu yangu itakuwa ni kifo! “Hivi kweli nikiufikisha huu mzigo nitaweza kuepukana na hicho kifo?” Lilikuwa ni swali gumu ambalo nilijiuliza bila kupata majibu. Lazima nifungue kwani Martin na Bonge watajuaje kuwa mzigo umefunguliwa? Nilipofika chumbani nikalitua begi lile kitandani.Moyo ulikuwa unaenda mbio kama mtoto aliyemuona daktari akiwa na sindano mkononi. Nilimfikiria sana Martin.Huyu ndiye aliyenitisha zaidi,jinsi alivyo!Ana umbo kubwa lenye misuli iliyojengeka kama mnyanyua vitu vizito,macho yake ni makubwa kama kurunzi huku uso wake ukipambwa na kovu kubwa lililopita katikati ya uso wake. Kwa jinsi alivyo alitosha kabisa kumnyamazisha mtoto anaelia kwa neno moja, huyo Martin anakuja! Pale alipokuwa ananitizama nilikuwa sijamkosea chochote lakini alikuwa anatisha kama nyoka anayetaka kumrukia mtu.Macho yake yalionesha wazi dalili zote za mtu mwovu kama si muuaji kamili. Atanifanya nini akigundua kuwa nimefungua ule mzigo? Iwapo alikuwa ananitazama kwa sura ambayo kwake ilikuwa ya upole lakini nilibanwa na haja ndogo,vipi nikutane naye siku ambayo amekasirika?Ndo ajue sasa maagizo waliyonipa nimeyavunja, atanifanya nini? Bila shaka atanifanya kama alivyofanyiwa yule mwanamke kule guest. Sijawahi kuona mtu aliyeuwawa.Maiti ambazo nimewahi kuziona kwa macho yangu ni za ajali ya gari. Taswira yake ilinijia kichwani mara kwa mara.Mwili ulisisimka na kufanya vipele vidogovidogo kama mtu anayehisi baridi kali. Maskini Merina,Mungu amlaze mahali pema peponi. Amin. Shauku yangu ya kutaka kujua kuhusu mzigo ule ilisababishwa na vitisho vya Martin na Bonge.Adhabu ya kifo kwa kufungua mzigo tu! Balaa Laiti wasingenionya kiasi kile basi nisingekuwa na wazo lolote juu ya mzigo ule. Ningeufikisha kama walivyotarajia bila hata kuwa na chembe ya wazo juu ya mzigo wao. Nikalikazia macho begi lile jeusi.Lilikuwa kama refarii katika maisha yangu. Nifungue niishi kwa mashaka au niache niishi kwa amani. Kitu kimoja ambacho kilinikosesha raha ni kuwa iwapo sitafungua basi nitakuwa na fumbo moyoni,fumbo ambalo sitaweza kulifumbua maisha yangu yote.Nakumbuka hata nilipokuwa mwanafunzi niliumiza sana kichwa kwenye mafumbo.Nilikuwa sikubali kushindwa.Kwa mara ya kwanza leo nakabiliana na fumbo,fumbo ambalo kufumbua kwake ni kifo. Nikubali kushindwa? Kweli nilikuwa naelekea kushindwa. Lakini kwa nini nishindwe!? Nikiwa mtaalamu wa mafumbo nilikuwa na kazi mbili,kwanza mzigo halafu uhai wangu.Lengo lilikuwa ni kujua kuhusu ule mzigo bila kupata matatizo. Nikatabasamu huku nikiwa nalitazama vizuri begi lile ambalo niliahidiwa pesa nyingi kwa kulifikisha kwa muhusika bila kuvunja masharti.Fedha nilizo ahidiwa sijawahi kufikiria hata siku moja kuwa nitakuja nizitie mikononi. Kwanini kulisafirisha lile begi kutoka Mwanza nilipwe pesa zote hizo?Kutatua fumbo lile kwangu lilikuwa jambo kubwa kuliko zawadi ambayo ningepewa na bonge huku fumbo likiendelea kubaki kama maisha ya kaburini ambayo maiti tu ndiye anayejua yalivyo. Haiwezekani!Lazima begi lifunguliwe. Kabla sijafungua nikapata wazo.Nikatabasamu. Lilikuwa wazo kabambe. Nilitaka niue ndege wawili kwa jiwe moja. Nilidhamiria kulifumbua fumbo lile bila kuniletea matatizo. Nilianza kujihisi kuwa mshindi ingawa bado niliendelea kujionya. *********CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/ Kama nilivyoeleza lile begi halikuwa na tofauti na yale Mabegi yanayouzwa pale Karume.Kwa akili ya Bonge ningewasili Dar Jioni ya siku iliyofuata.Hivyo nilikuwa huru kutekeleza malengo yangu mapema zaidi. Nyumba niliyokuwa naishi haikuwa mbali sana na Kituo cha magari Buza Kanisani. Ilinichukua dakika takribani kumi kutoka nyumbani hadi kituoni.Nilipofika nikapanda bajaji ambalo lilikuwa linaenda kituo maarufu ambacho kinajulikana kama mwisho wa lami.Siku za nyuma hapo ndio ulikuwa mwisho wa lami kama unatokea Lumo,lakini sasa lami ilikuwa imevuka hapo. Jina halijabadilika. Nikiwa ndani ya bajaji nilikuwa nafikiria jinsi nitakavyotumia fedha za mauzo ya almasi ambazo zipo kwenye begi. ”Ni matanuzi tu si kingine!” niliwaza. Ukweli ni kwamba sikuwa na uhakika ni mzigo gani ambao ulikuwa kwenye lile begi lakini sikuwa na shaka kuwa thamani yake ilikuwa kubwa sana.Dola elfu hamsini kwa kufuata mzigo tu, unafikiri mzigo kama huo utakuwa na thamani gani? Tena mtu anakupa milioni moja zisizo na maelezo wala masharti. Bajaji lilikuwa limefika eneo maarufu la mwisho wa lami. Nikamlipa dereva wa bajaji hela yake.Nikapanda daladala kutoka Mwisho wa lami hadi Lumo.Mpaka hapo naomba uelewe wazi kuwa nilikuwa na fedha za kutosha ambazo sijawahi kuzishika maishani mwangu.Fedha hizo ni zile nilizopewa na Bonge.Kwani nilipozihesabu zilikuwa shilingi milioni moja. Nilikuwa sijawahi kushika kiasi kikubwa cha fedha kama hicho katika maisha yangu. Lakini thamani ya zile fedha niliiona kuwa ndogo sana kila nilipoufikiria ule mzigo. Nilijua kuwa miezi mitatu ijayo nitakuwa tajiri mkubwa sana.Ajabu!Nilikuwa nawaza mtaa ambao utanifaa baada ya kupata fedha zangu. Nilikuwa nimeshaamua akilini mwangu kuutorosha ule mzigo,tatizo lilikuwa ni mbinu gani salama ya kuutorosha mzigo ule. Nilitaka kutafuta mbinu ambayo haitamshtua Bonge mapema.Labda agundue wakati nitakapofika sokoni Nairobi,maana nasikia huko ndiko waliko wanunuzi wakubwa wa madini. Nilifika kituo cha teksi Lumo. Moyo ulikuwa unaenda mbio sana,nilikuwa nimeshavunja sharti la kwanza.Nilikuwa nakaribia kuvunja sharti la pili tena kwa staili mbaya zaidi kuliko alivyotarajia muonyaji. Potelea mbali! “Vipi boss! tunaenda wapi?” Dereva teksi aliniuliza baada ya kuona nimeingia kimya kimya kwenye gari lake bila kumueleza lolote.Hapa nilianza kuona hali ya hatari niliyokuwa nakabiliana nayo,akili yangu haikuwa katika hali ya kawaida kwani nilikuwa nimeingia kwenye gari bila kujijua.Nilikuwa nimezidiwa na mawazo kiasi ambacho mwili ulikosa mawasiliano mazuri na akili. “ Nipeleke Karume tafadhali” “Vipi boss unapenda muziki?” aliniuliza huku akikata kona kona kutoka kituo cha teksi na kuingia barabara inayoelekea kariakoo. “Poa tu!” Nilimjibu kwa mkatao lakini kimsingi sikuhitaji aina yoyote ya burudani kwa wakati huo. Muziki mzuri uliokuwa unatoka kwenye gari lile haukuweza kuniliwaza hata kidogo.Ulikuwa muziki wa siku nyingi ambao uliimbwa na Washirika Tanzania stars watunjatanjata. Tulipofika maeneo ya Tazara tukaiacha Bara bara ya Pugu ambayo sasa inajulikana kama barabara ya Mwalimu Nyerere tukaingia barabara ya Mandela.Sikuipenda sana tabia hii ya kupachika karibu kila kitu jina la Mwalimu Nyerere.Ingekuwa bora kama mambo mengi yangefanywa kwa kuiga tabia zake na aina ya uongozi wake.Mimi sio mwanasiasa lakini kitu kimoja kinanifanya nimheshimu na kumthamini Mwalimu,Mwalimu alithamini rasilimali zetu. Mwalimu hakupenda tabia ya kujilimbikizia mali hovyo,Wakati wa mwalimu hakukuwa na misamiati ya ajabu kama; Mafisadi papa,mafisadi nyangumi na mafisadi nini sijui……. Wakati bado naendelea kuwaza dereva akasimamisha gari kwenye kituo cha mafuta cha Buguruni.Akajaza mafuta,kisha akaiondoa teksi kwa kasi.Akafuata barabara ya uhuru. Tulifika Karume Saa 11.47. Nikachagua saizi ya begi nililolitaka.Dereva wa teksi nilishamwambia anisubiri,hivyo nilipolipata lile begi nikaingia kwenye teksi tukarudi Lumo.Tulipofika Lumo nikamwamrisha dereva anipeleke Buza kanisani. “Shilingi ngapi?” nilimuuliza baada ya kufika. “Elfu ishirini bosi!” Alijibu huku akitikisatikisa funguo za gari lake kama mtu anayesubiri upinzani kutoka kwangu tuanze mabishano. “Poa nisubiri!” Nilimjibu huku nikilipeleka begi lile ndani. Nilipofika ndani nikaliacha lile begi ambalo nimetoka nalo Karume kisha nikachukua lile ambalo nilitakiwa kumfikishia Bonge. Hapo nilishaamua kufanya ujanja wa kubadilisha mzigo. Nilipotoka nilikuwa na begi lingine kama lile tulilotoka nalo Karume.Tofauti na madereva teksi walio wengi huyu hakuwa mwongeaji. Muda mwingi alikuwa kimya na alionesha kuwa mtu makini.Tabia yake hii ilinivutia na kunifanya niwe na hamu ya kuongozana nae kila nilikokwenda.Lakini kitu kimoja hakikufichika kwenye sura yake,alikuwa mtu mwenye dalili za huzuni hakuwa na furaha.Hata ule uchangamfu mdogo aliouonesha kwangu ulikuwa wa kulazimisha. “Tuna safari nyingine bosi?” Aliniuliza baada ya kuona nikiingia na begi kwenye gari. Niliitikia kwa kichwa. “wapi?” aliuliza tena kwa mkato. “Mbagala charambe!” nilimjibu kwa mkato. Nilichomoa noti mbili za shilingi elfu kumi nikampa. Hayo yalikuwa ni malipo ya mizunguko ambayo tulikwishaifanya.
********* Kama ilivyo ada,baadhi ya watanzania wenye kipato hupenda kuibatiza majina mabaya au ya dharau mitaa ya watu wenye kipato duni. Hili lilikuwa miongoni mwa maeneo ambayo huitwa Uswahilini.Sijui kwanini watu wenye kipato wanapenda kuyapachika maeneo haya kwa majina dharau kama hayo.Uswahilini sio jina baya tatizo ni kusudio la hao waitaji,kimsingi huwa wanakusudia kuwa ni maeneo ya chini ambayo watu waliostaarabika hawastahili kuishi.Ni wazi kuwa watu hawa wamerithi kasumba ya wakoloni ya kudharau watu weusi,kitu kimoja watu hawa hawajagundua.Laiti wangejua kuwa wao ni watumwa na nafsi zao zimehiyari utumwa kuliko uungwana wasingethubutu!Kwanini wasiwe watumwa wakati hawa ndio wale waliohiyari kuwa mbwa ulaya kuliko binadamu Afrika?Heri babu zetu waliingia mikataba ya ulaghai bila kujua kuliko wao waliohiyari kuutumikia uhayawani huko ulaya na kupoteza utu wao ambao thamani yake ni kubwa. Nyumba za maeneo haya zilikuwa zimejengwa bila kufuata utaratibu.Zilikuwa zinaonesha taswira halisi ya Mtanzania wa hali ya chini. Mtanzania ambaye ni vigumu kukamilisha milo mitatu kwa siku.Hata watoto ambao ungekutana nao mitaa hii wangekuwa ni tafsiri tosha kwa yeyote yule kujua kuwa maeneo haya ni ya watu wa hali ya chini. Niliteremka kwenye teksi nikamuashiria dereva anisubiri. Alionekana kuniamini. Akanisubiri wakati naingia kwenye vichochoro vya Mtaa wa Charambe magengeni. Ghafla! Nikamuona mzee wa makamo ambaye alikuwa ananifuata kwa hatua za haraka. “Aah,mjomba huyo,Karibu sana!” Alikuwa ni mjomba’angu Mzee Francis Kipupwe.Ni kaka wa mama yangu mzazi.Akanishika mkono na kuutikisa kwa furaha huku akinitembeza kwa kasi kuelekea kule iliko nyumba yake. “ Haya mjomba habari za siku tele!”alinisalimia kwa furaha huku akionesha wazi kufurahishwa na ujio wangu. “Salama mjomba shikamoo.” “Marhaba!” Akaingia ndani na kunitolea stuli chakavu. “Haya mjomba kwanini umetupa jongoo na mti wake!?”. Nilijichekesha chekesha kabla ya kumjibu. “Si unajua mjomba,maisha yamekuwa magumu sana.” “Sawa lakini siku hizi kuna mitandao kwanini hata simu hutaki kutupigia? “ “Nisamehe mjomba nitajirekebisha!” Nilimeza mate kisha nikaendelea “Kwa leo naomba unisamehe mjomba sina muda wa kupoteza nina kazi muhimu ambayo inabidi niifanye,naomba tu hili begi langu niliache hapa kwako nitalifuata Kesho kutwa Mungu akipenda.” “Hakuna shida mjomba!”. Kitendo cha kuacha begi langu kilionekana kumfurahisha sana mjomba. Nikaingiza mkono mfukoni nikatoa noti za shilingi elfu kumi kumi,nikahesabu noti tano.Wakati nahesabu nilimuona mjomba akiwa amezikodolea macho yenye uchu.Nikampatia shilingi elfu Hamsini.Ni kawaida ya mjomba kupenda kucheka lakini siku hiyo alicheka akapitiliza.Niliweza kuyaona hata meno yake ya mwisho. Nikarudi kwa dereva wa teksi. “ Vipi shwari?” aliniuliza. “Shwari twen’zetu!”. Tuliingia kwenye gari tukaondoka. Dereva teksi alinifurahisha sana kwani hirimu yetu ilikuwa moja halafu alikuwa mtu makini sio mropokaji. “Samahani muda mwingi wa safari yetu tumekuwa tunatembea bila kufahamiana hata majina” nilisema kisha nikamtambulisha jina langu. “Naitwa Omari Kisilani,Pale kijiweni najulikana zaidi kama Ommy Kiss au Mjeda” “Kwanini unaitwa Mjeda!” “Nimewahi kufanya kazi jeshini miaka miwili nikaamua kuacha”sikutaka kuhoji kwanini aliacha kazi hiyo kwani kila mtu ana namna yake anavyopenda kuishi. “Ok,nahitaji kwenda Mwananyamala!” “Poa.” Alinijibu ******** Saa 3.30 Tuliondoka maeneo ya Mwananyamala ambako nilienda kuwasalimia wazazi na wadogo zangu.Wote niliwakuta wakiwa wazima. Niliondoka nyumbani nikiwa na huzuni sana.Sikuwa na uhakika kama nitaweza kuwaona tena ndugu zangu. Nilikuwa katika mikono ya mauti muda huo.Sikujua hatma yangu.Niliitazama tena tena nyumba ya baba yangu nikajikuta nikitiririkwa na machozi. Gari lilifika kwenye kona tukaiacha nyumba ile sikuweza kuiona tena nyumba yetu.Nilikuwa nasikia uchungu kweli kweli. Kimsingi safari yangu ilikuwa ni kwenda kuaga. Niliwakumbuka rafiki zangu mbalimbali ambao nilikuwa nikicheza nao maeneo yale. “Rafiki yangu mkubwa Bundu Mayala yeye alikuwa amebahatika kuajiriwa katika benki ya CRDB tawi la Lumumba akiwa dirishani sijui ndio keshia au nani vile … Lakini bahati iko upande wake maana tumemaliza wote kidato cha sita na yeye hajasomea kozi yoyote kama mimi.” Hayo yalikuwa ni mawazo tu ambayo yalikuwa yanapita kichwani mwangu. Niliwaza mambo mengi mengine yakiwa ni ya utotoni,nilimkumbuka sana shangazi yangu mama Douglas,alikuwa ameiacha dunia wakati nampenda huenda kifo ikawa sababu ya kukutana naye.Sijui kama watu waliokufa wanakutana au ndio wale wanaogeuka mizimu na kusumbua watu,sijui kama kweli kuna mizimu maana huwa naiona kwenye filamu tu!Lakini kwanini niwaze zaidi kifo? Ah! Siko tayari kufa,sijajiandaa nimejiandaa kuishi. ********
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Tulifika Tabata Kisukuru saa 4.19. Betty Alikuwa amepanga mbele kidogo ya kituo cha Kimanga mwisho. Alikuwa karibu kabisa na Mazda bar. “Twende mpaka mtaa wa nyuma pale Mazda bar” Nilimuelekeza Ommy ambaye pamoja na kupata mteja wa kutwa bado hakuonekana mwenye furaha.Tulipofika nyumbani kwa Betty nikamuashiria Ommy anisubiri nje.Akalaza kichwa chake kwenye usukani,ni wazi alikuwa ameniamini alijua siwezi kutoroka. Nikaingia chumbani kwa Betty baada ya kubisha hodi dakika kadhaa,pamoja na upole uliokuwa katika sura ya Betty lakini hakuweza kunificha hasira aliyokuwa nayo. Kwa makusudi mazima niliamua Betty awe mtu wa mwisho kutokana na uzito na umuhimu wake.Mwanamke mpole mwenye mapenzi ya kweli ua la moyo wangu. Nikatabasamu licha ya hasira alizokuwa nazo. “Ulikuwa wapi siku nne mfululizo hatujaonana?”. Alianza kuuliza kabla hata ya salamu. “Usiwe na haraka mpenzi nina mambo mazito ya kukueleza.” “Haya lete huo uongo wako maana nilishasema mapenzi siku hizi yamejaa utapeli!” alisema Betty kwa hasira huku akinisogezea kiti cha plastiki.Tukakutanisha macho yetu. Sikuweza kuvumilia machozi yalianza kunitoka.Betty ndiye mpenzi wangu wa pekee.Sijawahi kuwa na mpenzi kabla ya Betty.Kama walikuwepo basi ni michezo ya mimi Baba wewe Mama. Kwa kifupi nilikuwa nimetulia. Nilimtazama kwa jicho la huzuni kwa sababu sikuwa na uhakika kama nitaweza kumuona tena Betty.Aliniona nikiwa na majonzi akanisogelea nakuanza kunifuta machozi kwa kanga yake. “Betty sina uhakika kama baada ya kesho tutaweza kuonana tena na wewe……..”Nilimkazia macho Bety ambaye alionekana kushtushwa sana na kauli yangu,hasira zake zote zikaisha.Akawa na shauku kubwa ya kutaka kujua nini kimetokea.Nikamueleza kila kitu mpaka safari ya Mwanza lakini sikumweleza wapi nimeuficha ule mzigo. Alinitazama kwa jicho lililojaa udadisi huku akikosa la kuongea.Niliona machozi yakitiririka kwenye mashavu yake kama maji ya chem chem kwenye miamba. Alikuwa na majonzi makubwa mpaka nikajuta kwa nini nilimueleza ukweli.Nikasimama kisha nikamsogelea nikampiga mabusu mfululizo. “ Kwanini siku zote hukunieleza mambo mazito kama hayo?” “Ni tukio la juzi tu ningekueleza lini?” “Huyo Mwanamke aliyeuwawa gesti kauwawa juzi?” “Ni tukio ambalo lilitokea kabla hatujawa wapenzi!” “Lakini kulikuwa na umuhimu wa kunieleza”aliongea huku akiendelea kutokwa na machozi! “ “Samahani kwa hilo mpenzi,yaliyopita si ndwele” niliendelea kujitetea “Sawa sasa kwanini usiwape huo mzigo wao?” “Sina uhakika kama nikiwapa wataniacha hai” “Na usipowapa?” “Nina uhakika wataniua wakinitia mikononi mwao” “Basi bora uwape uepukane nao!” “Sikiliza mpenzi huu ni mchezo wa kifo,hainiingii akilini kwa wauaji wakubwa kama wale kukubali kunilipa dola elfu hamsini eti kwa kusafirisha mzigo tu!” “Kwa hiyo unaamua vipi?” “Nitawapelekea mzigo feki ili hata wakiniua tukose wote” Nikamuona Betty akiitikia kwa kichwa kukubaliana na mimi. “Iwapo watakulipa hali ya kuwa umewapa mzigo feki utafanyaje?” “Nina uhakika hawatanilipa kwani muonekano wao umejaa unafiki mkubwa!” “Betty,mi nafikiri hatuna muda zaidi wa kupoteza tutaonana Mungu akipenda.” Niliamua kumuaga baada ya kuona muda mrefu tukitazamana kwa hisia za majonzi na si mapenzi kama ilivyo kawaida yetu. “Kajuna mpenzi,unaonaje tukiwa wote katika kila hatua yako!” “Betty,sipendi nikusababishie matatizo huu ni mchezo hatari kuhusika kwako kunaweza kuzalisha mambo mengine mabaya zaidi,bora uniache peke yangu niicheze hii ngoma na si vinginevyo.” Nilipojibu hivyo nikainuka na kuuendea mlango. Kabla sijaondoka Betty akaniita kwa sauti ndogo. “Kajuna mpenzi.” Nikageuka akanivuta kwake kisha akanikumbatia. Akanikumbatia kwa nguvu sana. “Kajuna,naamini kuwa una mapenzi ya kweli kwangu,naamini kuwa uko nami kwa kila hali,kitendo cha kuniamini na kuniambia siri hii nzito ni imani kubwa uliyo nayo kwangu sina cha kukushauri fanya unaloona kuwa bora niko nyuma yako kwa moyo wangu wot…….” Alimaliza kwa kilio. “Betty naomba nikuahidi kuwa iwapo huu mchezo nitaumaliza salama basi nitaanzisha safari mpya katika maisha yangu,nakusudia kufunga pingu za maisha wewe ndio chaguo langu,wewe ndio………” sikuweza kuongea chochote nilichokusudia machozi yalikuwa yanadondoka kama matone ya mvua,Donge lilikuwa limenishika kooni nikajikuta nikiendelea kumkumbatia Betty kwa hisia kali. Ommy alikuwa ametulia kwenye usukani huku akiwa hana wasiwasi kabisa. Alikuwa mpole lakini mwenye huzuni. Nilishindwa kujua huzuni ya Ommy inatokana na nini. Nilikuwa nashindwa kumuuliza kwani kuna mambo mengi ambayo hata yeye angeweza kuniuliza lakini hakufanya hivyo.Tabia yake hii ndio ilionitisha na kunifanya hata mimi nisithubutu kuuliza. ********* Saa 6.39 nilifika nyumbani kwangu Yombo buza. Nilikuwa nimechoka sana. Sikuweza kufanya jambo lolote zaidi ya kulala Ikiwa ni baada ya kula Chips kwenye baa iliyokuwa karibu kabisa na nyumbani kwangu. Niliamka saa 11 Alfajiri. Ilikuwa ni siku ya ahadi.Siku ngumu kuliko zote zilizowahi kutokea katika maisha yangu. “ Lakini kwa nini nipeleke mzigo,si nitoroke nao tu?” Niliwaza.Wazo la kutoroka liliondoka haraka akilini kwangu,kwa sababu sikuwa na uhakika kama ule mzigo ulikuwa na kitu chenye manufaa kwangu.Hivyo ilikuwa lazima kwanza nizipate dola elfu hamsini nilizoahidiwa na Bonge ndipo nitoroke.Siwezi kutoroka na mzigo ambao sijajua una nini ndani yake.Isije kuwa ni madawa ya kulevya.Itakuwa ni balaa zito maana sitajua wapi kwa kuuza.Pia sikutamani kabisa kujihusisha na biashara hiyo ambayo inapigwa vita dunia nzima.
********* Muda wa siku moja ulinitosha kumtambua Ommy kuwa ni mtu anayenifaa sana.Nilipofika Lumo madereva teksi wakaanza kunigombea.Sikuwajali,nikaanza kutembeza macho yangu huku na kule hadi nilipomuona,kumbe alikuwa amesimama karibu na gari lake huku akinyoosha mkono ili nimuone. “Ah! Ommy mteja wako huyo sijui mwenzetu una kizizi maana sisi wengine toka asubuhi lakini mwenzetu hicho kichwa cha tatu!” Alilalamika mmoja wa madereva tax. Ommy hakumjibu badala yake akacheka na kuingia kwenye gari. “vipi bosi wangu!” “Shwari Ommy,leo naomba unipeleke Ubungo.” “Pia nitakuomba ufanye kazi nyingine ya ziada lakini usijali nitakulipa tu.” “wewe tena bosi wangu…… usiwe na wasiwasi tuko pamoja.”Alinijibu huku akitekenya swichi ya gari lake. “Enhee.”Akanishtua baada ya kuona bado sijamueleza hiyo kazi ya ziada niliyomuomba kuifanya. “Tukifika Ubungo nitaomba ufuatilie nyendo zangu bila mtu yeyote kufahamu!” “Hapo sijaelewa bosi!” “Ni hivi,kuna mtu atakuja kunisubiri ubungo.Anajua kuwa naingia kutokea Mwanza leo nikiwa na huu mzigo wake” nilimwonesha lile begi jeusi. “Kutokana na makubaliano yetu jamaa inabidi anilipe kiasi fulani cha pesa kwa sababu huu mzigo nilioubeba ni almasi,hivyo naomba ufuatilie nyendo zetu ili kama ana nia ya kunidhulumu utoe taarifa polisi.” “Hapo nimekupata mkubwa,hii ngoma nzito inabidi tuicheze kikomando!” Alitamka Ommy na kunifanya nitabasamu. “Lakini kwanini usitafute sehemu salama kwa ajili ya biashara yenu hiyo” “Hakuna sehemu salama kwenye mambo ya fedha kwa sasa,hata huyo polisi anaweza kukugeuka akiona noti.” Alitikisa kichwa kukubaliana na kauli yangu. Tuliiacha barabara ya Pugu tukaingia Lumumba,hofu ikaanza kunitawala upya kwani nilijua wazi kuwa tulikuwa tunaitafuta Ubungo. “Sikiliza bosi saa hizi ni mapema sana unaonaje badala ya kusubiri hapa Ubungo tukajivuta hadi vijiji vya jirani huko utapanda gari ambalo huyo muheshimiwa atajua kuwa unatoka Mwanza” “Duh,Ommy una akili sana hiyo plani yako ni sahihi halafu wewe utanisubiri pale Ubungo” “sawa!” ********* Kitu kimoja nieleze wazi,maelezo yangu kwa Ommy yalianza kunitia hofu,Kiasi fulani nilijutia kitendo changu cha kumsimulia kuhusu almasi kwani niliogopa asije kunigeuka kwa tamaa ya pesa.Hii ilitokana na tetesi kuwa kuna baadhi ya madereva wa teksi hushirikiana na majambazi. Tulifika safari yetu salama. Hatukwenda mbali sana, tulikuwa mwanzo tu wa jiji la Dar-es-salaam.Saa 1.07 gari la Shabib liliingia ndani ya jijila Dar es salaam.Mapigo ya moyo wangu yaliongeza kasi yake.Nilisimama kando ya Barabara nikajaribu kusimamisha lakini Dereva alionekana kunipuuza na kuongeza mwendo.Nikahisi kuwa alikuwa na wasiwasi kuwa anasimamishwa na majambazi.Kosa tulilolifanya ni gari la Ommy ambalo lilipaki kando ya barabara.Lakini lilipofika mbele kidogo likasimama. Nikalikimbilia. “Samahani muheshimiwa naomba unifikishe hapo Ubungo Terminal Gari yetu imetuharibikia!” “Panda haraka basi usitucheleweshe!”alilalamika konda huku akionekana wazi kukerwa na kitendo changu.Tulipofika makao makuu ya Tanesco nikaliona gari la Ommy likikatisha kwa kasi.Nikashusha pumzi kwa faraja,kwani mpaka wakati huo mtu wangu wa karibu alikuwa Ommy.Ingawa sikumueleza siri ile lakini Ommy alitoa ushirikiano kwa moyo mmoja. Mapigo ya moyo wangu yaliongeza kasi yake kama ndege inayotaka kupaa.Kukutana na Bonge halikuwa jambo la mchezo.Ni wazi kuwa nilikuwa nacheza na kifo. Nilipokumbuka ile picha hofu yangu ikaongezeka.Hapa nataka nikueleze siri ambayo ilinifanya niamue kuwasaliti na kuvunja maagizo yao.Ni kweli sikuwa na uhakika kama kwenye lile begi kuna almasi au kitu kingine ingawa nilikuwa ingawa hisia zangu kwa asilimia kubwa nilihisi kuwa zile ni almasi au kitu kingine chenye thamani kubwa.Kumbuka kuwa picha yangu walikuwa nayo,hivyo walikuwa wanayaweka maisha yangu katika himaya yao. Kwani sikujua baada ya huu mzigo nini kingefuata,Kwa ufupi niliogopa sana kugeuzwa mtumwa wao.Pamoja na hayo yote nilianza kuingiwa na wasi wasi wa kulipwa dola elfu hamsini walizoniahidi.Ilikuwa haiingii akilini kwa watu ambao wananitishia kifo waje kunipa kiasi kikubwa cha fedha kama kile.Ndio maana nilimuomba Ommy afuatilie nyendo zangu.Kama wasingekuwa na ile picha ya tukio la kule Tabata ningewatoroka.Lakini ile picha ilikuwa kama mbu aliyeingia ndani ya chandarua hana kwa kutokea. Kuna wakati niliwaza kutoroka ili liwalo na liwe lakini wazo hilo lilipotea haraka sana.Nilikuwa kwenye mtafaruku mkubwa na nafsi yangu kwani nilikuwa nawaza mambo huku nikikubaliana nayo kwa upande mmoja lakini kwa upande mwingine nikiyakataa.Mkanganyiko huu mkubwa wa mawazo uliniumiza kichwa. Sikutamani kabisa kukutana na Bonge lakini nilikuwa sina ujanja.Ni mtu ambaye alikuwa ananitisha sana kila nilipomkumbuka.Zaidi nilimuogopa Martin kwani kwa upande wangu alikuwa anatisha kuliko kifo chenyewe. Kuna watu kule kukutana nao tayari inakuwa ni adhabu. *********
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Gari liliingia kituo kikuu cha Mabasi ubungo saa 1.28,Nikateremka kwenye basi lile na kuongoza kule abiria wengine walikokuwa wanaelekea.Nilikuwa naangaza macho huku na huko kama nitaweza kumuona Bonge lakini sikumuona.Nikatembea kwenye milango ya kutokea. Moyo ulikuwa unaenda kasi ajabu.Nilikuwa nahisi joto kali sana,lakini hali ya hewa ilikuwa ya kawaida kabisa. Tumbo liliunguruma hali niliyoitafsiri kuwa ilitokana na woga. Ilikuwa kama niliyegusa waya wa umeme,mshtuko nilioupata ulikuwa mkubwa sana baada ya kumuona Bonge akiwa amesimama karibu kabisa na milango ya kutokea. Akanipokea lile begi jeusi huku akiwa amekunja uso.Hakuonesha dalili yoyote ya furaha baada ya kumkabidhi mzigo.Tukaenda moja kwa moja kule alikoegesha gari lake.Tukaingia kwenye gari yake Toyota Rav4.Safari ikaanza huku nikiwa sijui wapi tunaelekea.Safari yetu ilitawaliwa na ukimya. Ukimya wake ukaanza kunitia hofu. Hivi kweli huyu mtu atanilipa fedha zangu katika hali kama hii?Niliwaza huku nikijaribu kupoteza mawazo kwa kuangalia hili na lile nje.Vile vile nilikuwa najiuliza kama kweli ile picha yangu nitarudishiwa mwenyewe baada ya kuwakabidhi mzigo wao.Lakini kwa kiasi kikubwa nilikuwa nawazia zawadi mbaya kabisa ambayo hawa jamaa wangenipa,sidhani kama kuna kitu ningezawadiwa zaidi ya kifo.Kitu kimoja kilinifariji,nitakapokufa sote tutakuwa tumekosa.Wataukosa mzigo nitaukosa uhai lakini safari ni moja mimi nitatangulia wao watafuata nyuma. Tumeumbwa kwa mavumbi tutarudi mavumbini. Tulifika maeneo ya Mtoni mtongani huku bado sijaelewa hatima ya safari yetu kwani mpaka kufikia hapo nilikuwa sijaongea lolote na Bonge.Alikuwa amekunja uso kama mtu aliyelazimishwa kula ndimu. Bado safari ilikuwa inaendelea.Tulipofika maeneo ya Rangi tatu tukanyoosha kufuata barabara iliyokuwa inaelekea Kongowe.Hapo hofu yangu ikaongezeka maana tulikuwa tunaanza kuelekea nje ya jiji.Bado niliendelea kujuta. Hivi kwanini sikumueleza baba yangu juu ya mkasa huu?Hilo ndilo swali lililoanza kukitesa kichwa changu.Kitu kimoja kilinifanya nishindwe kumwambia baba,angeshangaa sana kusikia mkasa wenyewe ulikoanzia,pia angenigombeza kama ningemwambia jinsi nilivyomfuatilia yule mwanamke kule ‘guest’, “Ah! Bora niicheze mwenyewe hii ngoma nione mwisho wake” niliwaza. Tukafika maeneo ya mpakani.Hapo kulikuwa na kibao ambacho kiliandikwa Karibu wilaya ya Mkuranga nikajua kuwa sasa tumeingia mkoa wa pwani.Hapa hatukwenda mbali tukakata kushoto na kuiacha kulia shule ya sekondari ya St. Matthews.Tukafuata kichochoro ambacho kilitufikisha eneo ambalo nyumba zake nyingi zilikuwa mpya huku nyingine zikiwa bado Hazijamalizika ujenzi wake.Gari likasimama mbele ya nyumba moja kubwa.Kitu kimoja kilinishangaza,nyumba hii ilifanana sana na ile niliyoiona Mwanza. Nilikuwa najiuliza kama zilikuwa zinamilikiwa na mtu mmoja au vinginevyo.Mawazo yangu yakakatishwa na Msukumo wa Lango lile.Lango lilifunguliwa kwa kusukuma upande wa kulia,Lilikuwa limewekewa magurudumu maalum ya chuma.Gari likaingia ndani na kusimama kwenye sehemu maalum ya kuegesha magari.Hapa naomba uelewe kuwa ni katika sehemu ambayo nilikuwa nakaribia kupoteza fahamu kwa hofu niliyokuwa nayo.Jasho lilinitoka pia nilihisi joto kali sana.Tumbo liliunguruma na kufanya mvurugiko usiokuwa wa kawaida.Huu mzigo ulinitia mashaka sana.Mzigo feki! Itakuwaje akifungua mbele yangu.Nilishaonywa kutopitia sehemu yoyote kabla ya kukabidhi mzigo,nilishaonywa kutofungua mzigo.Ajabu! Nilikuwa nimefanya zaidi ya vile nilivyo onywa.Mzigo nimebadilisha na malipo nayataka. Kweli nilikuwa kwenye mdomo wa mauti. “ Karibu mkuu!” Sauti ya mmoja wa vijana aliyetokea ndani ya jengo lile ilisikika. Akatikisa kichwa bila kuongea lolote.Nami nikamfuata Bonge bila kusita.Swali moja nilikuwa najiuliza nini kitatokea iwapo atafungua mzigo mbele yangu.Bila shaka kwa mshtuko atakao upata ataniua papo hapo.Hapa lazima nijipongeze kwani nilijitahidi kuficha hofu niliyokuwa nayo mbele ya Bonge. Nilijifanya niko kawaida lakini ukweli ni kwamba nafsi ya mtu ni kichaka kwani haja ndogo zilikuwa zinakaribia kuniadhiri kwa hofu niliyokuwa nayo.Nikarudisha mawazo yangu kwa Betty. “Sawa sasa kwanini usiwape huo mzigo wao?”sauti yake ilijirudia kichwani kwangu wakati ule ananionya kuhusu mzigo.Nilikuwa kwenye mkanganyiko mkubwa sana. Nilikaribishwa katika sebule kubwa ambayo ilikuwa na samani ambazo bila shaka hazikununuliwa kwa fedha za kitanzania. Ilikuwa ni sebule iliyotimia,samani za gharama ziliipamba sebule hii na kuifanya mandhari yake isitofautiane sana na ikulu. Kutokana na hofu niliyokuwa nayo nilishindwa kuisanifu vema sebule ile.Kila nilichokuwa naangalia sikuweza kukimaliza kwani kilikatishwa na mkanganyiko wa mawazo niliokuwa nao. Dakika tano nilizokaa pale niliziona kama saa kumi. Kulikuwa na kiyoyozi kina fanya kazi lakini kilishindwa kabisa kupoza joto la mwili wangu ambalo lilipanda kweli kweli. Baada ya dakika chache nikamuona Bonge akiingia na begi jeusi sebuleni.Hapo nashindwa hata kuelezea hofu niliyokuwa nayo kwani nilijua saa yoyote atafungua mzigo. Sikuweza kukadiria ukubwa wa balaa litakalojitokeza hapo. Akaanza kufungua zipu za lile begi.Muda huo nilikuwa natamani sana ardhi inimeze. Mungu mkubwa!Kumbe halikuwa lile begi nililokuja nalo. Ndani ya begi hili kulikuwa na vitu tofauti kabisa. Kulikuwa na ‘Briefcase’ mbili ndogo moja nyekundu nyingine nyeusi,akachukua ‘Briefcase’ nyeusi akanikabidhi.Kama alivyoupokea mzigo wangu nami nikapokea mzigo wake bila kuufungua.Akaingiza mkono mfukoni na kutoa simu na kuanza kuongea. “Hallow,mzigo umewasili salama lakini bado magugu hayajang’olewa!” Baada ya mtu wa upande wa pili kuongea Bonge akajibu. “Magugu tumeyawekea sumu nafikiri yataisha baada ya muda si mrefu,tutalima vizuri shamba letu.” Akacheka na kukata simu. Namshukuru Mungu hapa ndipo nilipouona umuhimu wa kusoma masomo ya fasihi nikiwa shuleni.Mimi ndio nilikuwa magugu yenyewe na ni wazi kuwa lengo lao lilikuwa ni kuniua Kutokana na hali yangu duni Bonge hakuweza kubaini kuwa nilikuwa tajiri wa kupambanua mambo.Nilielewa wazi kuwa lengo lao lilikuwa ni kuniua. Angeniua vipi?Nikahisi kuwa sumu anayoisema pengine kaniwekea watu waje kunivamia.Nikatoka nikiwa na Lile ‘briefcase’ mkononi.Hofu ilikuwa imeshanitoka kwani sasa nilijua wazi kuwa napambana na kifo hivyo sikutakiwa kuwa mwoga tena.Bonge hakuwa na ujanja wa kuongea mafumbo mbele yangu.Nilikuwa na kazi moja tu! Nilitakiwa kuwa makini na safari yangu kwani kifo kilikuwa kinanifuata.Hofu yangu ilipungua kidogo nilipomkumbuka Ommy.Nilijua atakuwa ananisubiri huko nje kwani Bonge hajui kama nina usafiri huko.Nikatembea taratibu kuelekea barabarani.Nilipotokea barabarani nikakuta kuna foleni.Magari yalikuwa yanaenda taratibu. Sikumuona Ommy.Hili nalo likanitisha kidogo.Nikaanza kutembea kwa miguu kuelekea kituo cha daladala cha Kongowe. Moyo wangu ulikuwa tayari kwa lolote.Nikatembea kwa umakini wa hali ya juu nikijaribu kuangalia balaa litatokea upande upi.Kwa mbali nililiona gari la Ommy likinifuata taratibu.Umakini huu wa Ommy ulinifurahisha sana. Dakika chache baadae nikaiona foleni ikiyeyuka nafikiri,nikagundua kuwa kuna gari lilikuwa limezimika katikati ya barabara na sasa lilikuwa limewaka. Ghafla,gari ndogo iliipita kwa kasi gari ya Ommy.Ikafunga Breki za ghafla mbele yangu. Watu wawili ambao wote walikuwa na Bastola wakanifuata kwa kasi huku wakiwa wameninyooshea bastola. “Lete hilo ‘Briefcase’” Alisema mmoja wa wale watu kwa sauti yenye amri,mbele ya bastola,mbele ya watu wasio na mzaha sikufanya ubishi nikawapa walichotaka. “Wametumwa?”Hilo lilikuwa swali la kwanza lililopita kichwani kwangu. Ommy akaongeza kasi ya baada ya kuliona tukio lile. Giza lilikuwa limeshaingia lakini aliweza kuona vizuri kila kilichokuwa kinaendelea kutokana na mwanga ulioletwa na taa za magari mbalimbali.Akafunga breki mbele yangu na kunifungulia mlango kwa haraka nami nikajitoma ndani. “Mwanangu tusikubali hawawezi kutunyang’anya fedha kikondoo namna hii!” Alifoka Ommy huku akishindwa kudhibiti hasira zake.Aliliondoa gari kwa kasi,akaanza kulitafuta lile Nissan patrol .Nilikuwa nimechukia vibaya sana.Dakika chache nilikuwa naota utajiri dakika chache ndoto ikafutika. Nilikuwa na hasira sana. Bahati ilikuwa upande wetu,wale jamaa hawakuweza kugundua kuwa walikuwa wanafuatwa.Walipofika maeneo ya Mtongani wakaingia barabara iliyokuwa inaelekea Kijichi kupitia kwa Buruda. Tukaendelea kuwafuata kimyakimya.Wakasimama maeneo ya Mbagala kuu karibu na kituo maarufu kwa fundi redio. Bila shaka hapa walikuwa wanataka kuangalia kilichokuwemo kwenye ‘briefcase’. “Tulia Kajuna wana bastola hao watakuua”.Aliniambia Ommy huku akinizuia kwa mkono wake nisiteremke kwenye Gari,alionekana kurudiwa na umakini wake kwa kutambua hatari iliyoko mbele yetu.Tulikuwa tumesimamisha gari letu kama hatua Thelathini kutoka pale waliposimama. Ingawa nilikuwa mbali kwa kutumia taa yao ya ndani niliweza kuwaona vizuri wale jamaa wakihangaika kufungua lile ‘briefcase’ mmoja alionekana wazi akicheka kwa furaha.Roho iliniuma sana.Nikaanza kuhisi kuwa huenda ni njama za Bonge kutaka kunidhulumu.Nikazidi kumchukia! Ghafla!nikashuhudia tukio ambalo sikulitarajia.Lilikuwa ni tukio la kutisha na kushangaza mno kwani halikuwa jambo nililolitarajia.Moyo ulienda kasi lakini nilijikaza kiume na kuendelea kukazia macho eneo la tukio.Watu walikimbia hovyo na kujikuta wakigongana kila mmoja akijaribu kuokoa maisha yake.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kudadekii….Walikutegeshea bomu mshikaji sio mapene wala nini!”Alitamka Ommy kwa kihoro. Ulikuwa ni mlipuko mkubwa ambao bila shaka ulikuja baada ya wale jamaa kufungua ‘Briefcase’. Nililishuhudia lile gari likirushwa juu na kutawanywa vipande vipande,pia niliweza kuona kichwa cha mtu kikiwa kimerushwa juu na kutua chini.Duh,kifo kibaya kama hiki nilikiona kwenye filamu za hollywood tu na niliamini kuwa ni jambo ambalo haliwezi kutokea.Vioo vilitawanyika ardhini huku vingine vikiwa na athari ya damu na kuleta taswira ya kutisha.Mkono na vidole ni miongoni mwa vitu nilivyoviona vikiwa vimejitenga na mwili na kuangukia senti meta chache kutoka pale lilipo gari. Baada ya hapo ukafuata moto ambao ulikuwa unawaka kuteketeza kabisa masalia ya gari lile.Hapo ndipo nilipoelewa maana ya fumbo la Bonge kuwa angeng’oa magugu baada ya muda mfupi kwani alikuwa ameyawekea sumu yale magugu.Likanitoka tusi zito la nguoni bila kutarajia. “Unafikiri huu ndio mwisho?”Aliniuliza Ommy “Hapana Ommy huu ndio mwanzo!” “Mwanzo wa nini sasa!” Aliuliza Ommy kwa mshangao. “Mwanzo wa vita!” “Na nani?”Sikumjibu baada ya kuona maswali yake yanakuja mfululizo.Kwa upande mwingine nilijipongeza kuwapa mzigo tofauti na ule walioutarajia. Sasa ngoma droo kama walivyoimba waswahili wa bongo!Niliwaza huku nikikuna kichwa.Kumbe ndio maana akili ilikuwa inakataa kabisa kuuacha ule mzigo bila kufungua! Nilistaajabia mwenyewe maamuzi yangu ingawa upande mwingine nilianza kujilaumu kwani kama si msaada wa wale vibaka sijui majambazi hata mimi nisingefikiria zaidi ya kuufungua ule mzigo bila tahadhari.Lakini hata hivyo ni tahadhari gani ningeichukua hali ya kuwa sina ujuzi wowote wa mambo ya milipuko.Ningekufa tu tena kama bwege Fulani vile. “Twenzetu mshikaji kimeo hicho,tusipoangalia tutaisaidia polisi muda mfupi ujao”Akanishtua Ommy baada yakuona watu wakianza kurudi na kulizunguka eneo la tukio kama ilivyo kawaida yao. Tukageuza gari kurudi tulikotoka. Nikageuka nakuutazama moto ulivyokuwa unaivisha viungo vya majambazi wale! “Mtego wa panya,ameingia asiyekuwemo!”Nilisema huku nikimshuhudia Ommy akiongeza kasi ya gari. “Afadhali wale wajinga wameramba garasa katika mchezo usiowahusu!” Aliendelea kuropoka Ommy. Toka nimfahamu hakuna siku niliyomuona Ommy kuwa na maneno mengi tena mengine ya kihuni kama hii.Kiasi fulani nilimuona akiwa kasahau kabisa huzuni ambayo ilikuwa kwenye sura yake toka siku ya kwanza niliyokutana naye. Alionekana kuvutiwa na kuchangamshwa na mlipuko ule kana kwamba ni burudani fulani ingawa alificha udadisi mkubwa kwenye nafsi yake. Nilijua lazima ataniuliza tu! Tulipofika Maeneo ya kituo cha Buruda tukapishana na gari tatu za polisi ambazo bila shaka zilikuwa zinaelekea eneo la tukio. Hatua chache mbele yetu kulikuwa na gari kubwa la jeshi nalo lilikuwa linaelekea eneo la tukio.Eneo hili la tukio ndio lilelile ambalo lilitokea milipuko ya mabomu ambayo yalitikisa jiji la Dar es salaam.Hivyo wanajeshi walikuwa wanaelekea eneo la tukio kwa kuhisi kuwa huenda ni yale mabomu yao. Mlipuko haukuwa mkubwa sana kiasi cha kuleta askari wengi namna ile,tatizo labda ni maelezo ya watu waliotoa taarifa.Kuna uwezekano mkubwa wa kutoa maelezo kuwa yale mabomu yameanza kulipuka tena. Taarifa kama hiyo isingeweza kupuuziwa na vyombo vya usalama kwani ni kama mtu aliyeng’atwa na nyoka angeshtushwa hata na uzi mwembamba wa kushonea nguo. ******** Tulifika Lumo sasa 6.15.Nikashusha pumzi baada ya kubaini kuwa niko eneo ambalo kwa kiasi fulani ni salama kwangu. “Hivi kwanini hawa jamaa wakufanyie hivi?”Aliuliza Ommy huku akipunguza mwendo wa gari. Nikamtazama Ommy kabla ya kumjibu.Mpaka kufikia hapo Ommy alikuwa ni msaada mkubwa kwangu. “Sikiliza Ommy,Ukweli nimekuwa nikikuongopea juu ya tukio zima.” Nikaanza kumuelezea tukio lote bila kumficha. Jambo la kustaajabisha ni kuwa baada ya simulizi yangu hiyo nilimuona Ommy akitokwa na machozi. Nikashangaa sana kwani sikujua nini kilikuwa kimemgusa katika tukio hilo ingawa kimsingi lilikuwa ni tukio la kusikitisha. “Vipi Ommy nini kinakuliza?” Nilimuuliza kwa huruma. “Umenikumbusha majonzi Kajuna,huyo mwanamke aliyeuwawa gesti alikuwa mpenzi wangu.Tulipendana mapenzi ya dhati kabisa sasa sijui nini kilimpeleka huko gesti,nahisi alikuwa ananisaliti ndo wahuni wakamuua huko huko.” “La!……Hapana Ommy,tatizo lilisababishwa na ujumbe ambao aliutuma kwenye simu,nahisi haukukufikia!” “Simu ipi?” aliuliza Ommy huku akionesha kutoelewa nini nilichokusudia.. “Ommy nafikiri haya mambo tunatakiwa kuongea usiku huu huu kwani niko kwenye wakati mgumu sina uhakika kama siku ya kesho nitaimaliza nikiwa hai” Nilimtazama Ommy ambaye niliona mshtuko na umakini kwenye uso wake baada ya kumdokeza mambo yale ya kutisha. Alikuwa na majonzi mara mbili,kwanza alihisi kusalitiwa na mpenzi wake pili kifo cha mpenzi wake. Nilielewa wazi kuwa Ommy alikuwa hanielewi hivyo nilimuomba twende nyumbani kwangu nikampe kitu ambacho kingemfanya anielewe. Tukaanza safari ya kutoka Lumo hadi Buza.tulipofika nikaingia ndani,nikachukua simu ya marehemu Merina.Kisha nikampa Ommy akawa anasoma meseji akaanza kutokwa machozi zaidi. Ghafla kama aliyezinduka kutoka usingizini akanishika bega. “Kajuna,hapa kwako si sehemu salama tena,Chukua kila kilicho chako tuondoke.Hawa watu wakigundua kuwa mzigo uliowapa ni feki lazima watarudi kuja kuutafuta huku kwako” Ndipo nikabaini uwezo mkubwa wa kufikiri aliokuwa nao Ommy kwani sikufikiria kitu kama hicho kabla kwa namna Fulani nikajikuta nikizidi kuwa na imani na Ommy katika wakati ule mgumu.Nikarudi ndani haraka sana nikachukua begi langu maana ndilo nililoliona muhimu kwa wakati huo. Nikakimbia kuelekea kule aliko Ommy. “Sikiliza Ommy,litoe gari maeneo haya kisha ‘upaki’ sehemu ambayo ni salama halafu tujaribu kuangalia kama kuna yeyote atakayekuja” nilimshauri naye hakupinga akakubaliana nami. Tukalificha gari umbali wa kilomita moja kutoka nyumbani kwangu kisha tukarudi nyuma kushuhudia kama kuna lolote litakaloendelea. Mpaka saa 10.12 alfajiri hakuna lililotokea tukaamua kuondoka kwenye maficho yetu na kuliendea gari kule tulikoegesha. Tukaondoka kuelekea nyumbani kwa Ommy.Wakati tunaenda ndipo Ommy akaanza kunisimulia kisa cha mpenzi wake.Haikuwa hadithi ndefu ilikuwa ni hadithi fupi ya kushangaza,kustaajabisha na kusikitisha. “Merina alikuwa ni Katibu muhtasi katika Kampuni ya kusindika ngozi,Kulikuwa na mfanyakazi mwenzie wa kike ambaye alikuwa anaitwa Pili.Huyu Pili alikuwa ni rafiki mkubwa wa Merina.Siku moja Pili alikuja na habari za kutisha kwa Merina.Alimsimulia kuwa kuna Watu wanajishugulisha na biashara ya ngozi za binadamu pale kiwandani.Alipotaka kumsimulia akatokea mmoja wa wahusika ‘story’ ikakatishwa.Baada ya hapo Mpenzi wangu akawa anafuatwa na watu mbalimbali akiwemo huyo Bonge ambaye aliniambia hakuwa mfanyakazi kiwandani hapo.Walimwahidi pesa nyingi kwa kazi ya kumuua Pili.Alipewa vidonge ambavyo vilikuwa ni sumu kali sana lakini alikataa katakata.Huyo Bonge ndiye aliyekuwa anamfuatilia zaidi.Zikapita siku tatu sijamuona wala kupata mawasiliano yake,Siku ya nne nikapata taarifa za kuuwawa kwa Merina.”Alikuwa amemaliza hadithi yake. “Huyo Pili yuko wapi sasa!” “Pili alikufa Siku moja kabla ya kifo cha Merina,Inasemekana alikufa ghafla bila hata kuugua” “Ooh my God,walimuua bila shaka!” “Na ndio maana mpenzi wangu aliamua kuukimbia mji lakini bahati haikuwa yake!”Alipofika hapo nikamuona akianza kutoa tena machozi. “Hicho kiwanda cha ngozi kinaitwaje?” “Kinaitwa NAI COMPANY l.t.d yaani NEW ASIAN INVESTORS” Nilitikisa kichwa kuonesha kukifahamu kiwanda hicho lakini nilikuwa sifahamu walikuwa wakijishughulisha na usindikaji wa ngozi. “Unaonaje tukienda kutoa taarifa Polisi?” Aliniuliza. “We!Usithubutu kwa sasa.Kumbuka kuwa wale watu wana picha yangu nafikiri ni bora tuwafuatilie kimya kimya kwa sababu kwa akili zao nitakuwa nimekufa kwa lile bomu au nimetoroka” Ommy akaonekana kukubaliana nami. Ommy Alikuwa anaishi maeneo ya Makangarawe karibu na kituo kidogo cha Polisi.Alikuwa amejenga nyumba ndogo ya vyumba vitatu.Ni eneo ambalo kiasi fulani lilikuwa tulivu kuliko kule kwetu.Alikuwa anaishi peke yake. Akanionesha sehemu ya kulala.Baada ya kuoga nikaingia chumbani.Ajabu sikupata usingizi,nilikuwa najiuliza maswali mengi ambayo hayakuwa na majibu.Kwanini kazi ya kumuua atumwe Merina wakati wenyewe waliiweza. “Huenda walitaka likishatokea watafute namna ya kumuweka kwenye himaya yao kama walivyonifanyia mimi kule Tabata”. Hayo yalikuwa ni mawazo yangu,kimsingi nilikuwa sina jibu sahihi.Hata hivyo niligundua kitu,hawa jamaa wakikuahidi zawadi basi kinachofuata ni kifo na si vinginevyo.Ndiyo lazima kifo kinaniwinda sasa na Mzigo wao tu ndio utakaochelewesha kifo change. Nilikuwa najiuliza kwa nini hawa watu waliamua kutumia ubabe kunituma mzigo wao.Kama ule mzigo ulikuwa na thamani kubwa kwanini wasiuchukue wenyewe?Au walishajua kuwa sina ujanja kwa kuwa wana picha yangu ambayo inaonesha kuwa mimi ndiye muuaji wa Merina? Bado nilikuwa sina jibu la maswali yote hayo.Likaja swali ambalo lilikuwa gumu kuliko yote.Hivi hawa watu ni kina nani na wanataka nini? Ni magaidi?Swali hilo lilinikosesha raha,shauku ya kuufungua ule mzigo ikaongezeka.Kama ule mzigo hauna thamani kwanini Bonge alinipa milioni moja ambayo haikuwa sehemu ya malipo yangu na kwanini wametumia gharama kubwa kunitegea bomu baada ya kuwafikishia mzigo wao. Bado swali lilikuwa pale pale ule mzigo ni mzigo gani? Mawazo yangu yakahamia kwa Betty.“Kama nitamaliza salama matatizo haya lazima nifunge ndoa na Betty.Yeye ndiye liwazo na ua langu la moyo”niliwaza.Ukweli ni kwamba muda huo nilikuwa nahitaji sana faraja kutoka kwa Betty.Wakati nikiendelea kuwaza taratibu usingizi ukanichukua.Haukuwa usingizi nzuri,ndoto za milipuko ya mabomu na mauaji makubwa zilikuwa zimetawala. Mara kadhaa niliota nikifukuzwa na watu wenye silaha huku wakinikosakosa risasi kdhaaa.Pia kuna wakati nilijikuta nikiwa katika mikono ya polisi tayari kujibu maswali kwa kosa la mauaji. ******** Niliamka saa 4.15.Nilikuwa na uchovu mwingi,nikaenda sebuleni nikamkuta Ommy akiwa amekaa kwenye kiti. Alionekana mwenye mawazo mengi sana.Hali hiyo ilimfanya asitambue ujio wangu pale sebuleni.Ukutani alikuwa amepachika picha yake kubwa akiwa amekumbatiana na Merina.Merina alikuwa amerudi mavumbini kule tulikotoka,njia ambayo kila mmoja ataiendea. “Unafikiri ni muda muafaka sasa kwenda kufungua mzigo?” Nilimshtua kutoka kwenye lindi la mawazo.Aliinua macho yake na kunitazama,Macho yake yalikuwa yanalengwa lengwa na machozi. “Kajuna…..” aliniita kisha akatulia kidogo kabla ya kuendelea. “….. Inabidi nifanye kila niwezalo kumlipia kisasi mpenzi wangu!” Alitamka Ommy kwa uchungu. “Sawa lakini mpaka uwafahamu waliohusika vipi kuhusu mzigo,tuufungue?”. “Tusiwe na haraka na huo mzigo,kwanza tuangalie usalama wako lazima ujue kuwa maisha yako yapo hatarini.” Niliukubali ushauri wake nikawa nafikiria nini cha kufanya. “Hivi huyo Pili alikuwa na mume?” Nilianza kumsaili. “Pili yupi?” “Yule uliyenieleza kuwa alikuwa rafiki wa Mpenzi wako!” “Hapana.”Alijibu kwa mkato. “Alikuwa anaishi wapi?” “Ilala Shariff shamba alikuwa anakaa na mdogo wake wa kike ambaye anaitwa Debora” “wewe unaifahamu nyumba aliyokuwa anaishi?” “Hata majirani zake wananifahamu!” “Mimi nafikiri tuanzie huko nyumbani kwa Pili” Nilimweleza akanitazama kwa mshangao. “Huko tutaenda kufanya nini!?” Aliniuza Ommy kwa mshangao. “ Lazima tuanze kumtafuta adui yetu kuanzia huko!” Ommy akanitazama kwa mshangao wa wazi kisha akakubaliana nami kwa shingo upande. “ Kuna ‘stationery’ hapa jirani” Nilimuuliza. “Ndiyo!” “Nahitaji passport size yako!” Jamaa alikuwa ananishangaa kweli kweli.Nikafungua kwenye begi langu nikatoa picha yangu ya mkato ‘Passport size’ Nikachukua na ile ya Ommy nikaenda nazo Kule ‘stationey’.Ommy alikuwa ameshaelewa nilichokuwa nafanya.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment