Search This Blog

Friday, 20 May 2022

MZIGO - 3

 







    Simulizi : Mzigo

    Sehemu Ya Tatu (3)

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

     “Sasa nipeleke kwa mchonga mihuri!” Ommy alikuwa hoi jinsi akili yagu ilivyokuwa inafanya kazi haraka. “Lakini kitambulisho cha usalama wa Taifa kina maandishi ya chuma kwenye gamba lake wewe utapata wapi hilo gamba!” “Mtu professional kama wewe unaweza kufahamu hilo lakini kule ninakokusudia najua hawafahamu lolote lile!” Akacheka bila kuongeza neno lolote zaidi ya kutikisa kichwa. ********* Saa 10.30 tulikuwa maeneo ya Ilala Sharif shamba. Ommy alinielekeza nyumba aliyokuwa anaishi Pili. Nikavuka barabara na kuifuata nyumba ile ambayo ilikuwa ndani kidogo. Ilikuwa ni nyumba yenye rangi ya bluu ambayo ilipauka sana.Ni wazi kuwa nyumba hii ilijengwa wakati Tanzania haijapata uhuru au miaka ya mwanzo ya uhuru.Ilikuwa imezungushiwa uzio wa bati ambazo zilibadilika rangi na kuwa rangi isiyo rasmi ambayo ilifanana na udongo kutokana na kutu.Nikauendea mlango ambao ulitengenezwa kwa bati la debe la mafuta ya KORIE.Baada ya Kubisha hodi mara tatu mama mtu mzima akaja kunifungulia.Alikuwa ni mama ambaye umri ulianza kumpungia mkono. “Bibi shikamoo”nilimsalimia kwa heshima za kibantu. “Marahaba mwanangu hujambo!” “Sijambo bibi,samahani hapa ndio nyumbani kwa marehemu Pili” Nilimuuliza. “Ndio hapa mwanangu tena mdogo wake amefika sasa hivi alikuwa huko kazini kwake,chumba chake hicho hapo!”. Alinijibu yule mama huku akinionesha kwa kidole chake cha shahada kile chumba,moja kwa moja nikaelekea Kule alikonielekeza.Kilikuwa chumba cha nje.Nikabisha hodi. Mlango ukafunguliwa,msichana mwenye sura ya kuvutia akafungua mlango.Akasimama mlangoni akitaka lililonileta nimweleze palepale bila kuingia ndani. Alikuwa amesimama mlangoni huku akiwa amefungua nusu ule mlango mkono wa kulia alikuwa amemshika kitabu maarufu cha riwaya kinachoitwa MJELEDI.Niligeuka na kumtazama yule bibi alikuwa ameingia ndani.Yule msichana alionekana kunitazama kwa hasira kitu ambacho kilinishangaza kidogo. “Habari yako!” “Nzuri nikusaidie nini?” aliniuliza kwa jazba. “Nina maongezi na wewe kama inawezekana tafadhali naomba unikaribishe ndani!” “Sikiliza wewe,mimi kuuza baa haina maana kuwa nauza mwili.Please naomba mambo yote yaishie kule kule baa hapa ni nyumbani nahitaji kupumzika nahitaji kuheshimiwa.Narudia tena mimi nauza baa siuzi mwili.” “Umemaliza?”nilimuuliza kwa sauti yenye utulivu mkubwa. “Ondoka,nasema ondoka unanipotezea muda wa kusoma kitabu changu!” Sikusema neno lolote nikafanya kitu ambacho hakukitarajia.Nikamsukumia ndani kwa ghafla!Akayumba na kuangukia kwenye zulia ambalo lilikuwa mle ndani. Nikafunga mlango kwa haraka sana.Akataka kupiga kelele kwani nahisi alidhani kuwa lengo langu ni kumbaka.Kwa haraka sana nikatoa kitambulisho changu cha kugushi ‘feki’ nikamrushia pale alipolala.Nilikuwa mtulivu huku nikionesha kujiamini sana. Kitambulisho kile kilionesha kuwa ni Afisa mwandamizi wa idara ya Usalama wa Taifa.Nikamuona akinitazama kwa macho yaliyojaa mshangao. “Uko tayari kutoa ushirikiano kwangu?”nilimuuliza kwa sauti ya upole.Akaitikia kwa kichwa huku akiona aibu kwa mambo aliyonifanyia. Nilijipongeza moyoni kwa kutengeneza kitambulisho hiki.Nilikuwa nimetengeneza vitambulisho viwili kimoja kilikuwa cha Ommy.Nilifanya hivyo baada ya kugushi mihuri ya ofisi ya Rais. “Naomba tuanze na jina lako!” “Naitwa Deborah Boimanda” alinijibu huku akitetemeke. “Marehemu pili alikuwa nani kwako?”Nilimuuliza kwa sauti iliyojaa utulivu mkubwa. “Alikuwa dada yangu wa mama mmoja” “Mlikuwa mnalala wote chumba kimoja!” “Ndio tena chumba chenyewe ndio hiki!” “Marehemu alikuwa na mume au mpenzi?” “Hapana…ah,alikuwa naye lakini ni hizi siku za mwisho za uhai wake” “Unaweza kujua nini kilimuua Dada yako!” “Hapana ninachokumbuka alikuwa analalamika kizunguzungu akaanza kutoa povu mdomoni hatimaye akafa nikiwa nimempakata.” Akaanza kutokwa na machozi. Nikamuacha mpaka nilipomuona akiwa amerejewa na utulivu. “Hiyo hali ya kizunguzungu ilimuanzia hapa nyumbani?” “Hapana ilianza muda mfupi baada ya kurudi kutoka kwa mpenzi wake” “Unamfahamu vizuri huyo mpenzi wake?” “Ndiyo anaitwa Masudi alikuwa anafanyakazi kampuni moja na dada!” “Kwa nini unasema alikuwa anafanya kazi ina maana ameacha?” “Hapana na yeye ni marehemu kwa sasa!” Nilishtuka lakini sikutaka Debora agundue. “Alikuwa mgonjwa?” “Hapana,nasikia alijiua baada ya kifo cha dada.” Nikashusha pumzi na bila kutegemea nikajikuta nakaa pale kitandani.Siku nyingi nilikuwa natamani kusoma kitabu kile cha MJELEDI kwani kilikuwa gumzo mitaani na watu walikuwa wanakitafuta kila kona bila mafanikio kutokana na nakala zilizotolewa kuisha mapema.Ni kitabu cha kusisimua ambacho kiliteka hisia za wapenzi mbalimbali wa riwaya Afrika mashariki. Hata hivyo kutokana na mawazo na mkanganyiko wa mambo niliokuwa nao sikutamani hata kidogo kusoma kitabu hicho kwa wakati huo ingawa niliweka azma ya kuja kuazima kitabu hicho pale mambo yatakapoisha salama. “Ahsante kwa maelezo yako,tafadhali naomba usimueleze yeyote kuwa umekutana na mtu kama mimi” akaitikia kwa kichwa.Nikakiacha kile kitabu kitandani kisha nikaondoka mle ndani. ********* Nilirudi kwa Ommy nikamkuta akiwa ameshikilia usukani. Akawasha gari tukaondoka. “Enhe lete story” alianza Ommy tukiwa tumeshaingia barabara ya kawawa. “Duh,hii ishu nzito rafiki yangu inaonekana mzunguko wake ni mrefu” “Kwanini?” “Nahisi Pili kauwawa na mtu ambaye alijifanya mpenzi wake,tena na yeye alikuwa anafanya kazi kiwanda kile kile cha ngozi!” “Sasa Ugumu uko wapi hapo?” “Huyu mpenzi wake yuko nyuma ya wauaji!” “Una maana gani?” “Nilichogundua ni kuwa wauaji hawapendi kufanya kazi yao wenyewe wanapenda kupitia kwa watu fulani kwa hiyo hata huyo aliyejifanya mpenzi wake hana analoelewa zaidi ya kurubuniwa pesa kwa kazi hiyo tena cha kushangaza hata yeye kauwawa.” “Unafikiri ni kwanini wamemuua?” “Wanataka kuwachanganya Polisi na yeyote atakayejaribu kuchunguza mauaji hayo.” “Kivipi?” “Pale yeyote atakapogundua kuwa fulani ni muuaji bado atakutana na changamoto ya muuaji kauwawa kwa hiyo hatajua kwanini muuaji kaua!” Kisha nikamsimulia mahojiano yangu na Debora. “Niambie ukweli Kajuna hivi hujawahi kuwa askari wewe!?” Aliniuliza kwa mshangao. “Siwezi kukuficha rafiki yangu!” “kama ni hivyo una akili ya ajabu maana mbinu zote ulizotumia ni za kiaskari sijui kwanini serikali haijawaona watu kama wewe.” Nikatabasamu bila kuongea lolote. Baada ya nusu saa tukafika nyumbani kwa Ommy,Njaa ilikuwa imeanza kunishika.Nikachukua kiasi cha fedha nikampa Ommy ili ajaze mafuta kwenye gari na nyingine anunulie chakula.Ilikuwa ni saa 12.33 nikajilaza kitandani nikapitiwa na usingizi.Saa mbili na nusu Ommy akaniamsha.Alikuwa amenunua Chips mayai na soda.Njaa ilinifanya niuvamie mlo huo kwa pupa.Baada ya kushiba nikajinyoosha kiuvivu. “Unafikiri kuna haja ya kuyafikisha Polisi haya mambo?” Nilimuuliza Ommy.“Hapana! Sasa nakubaliana na ushauri wako wa mwanzo,unajua tatizo la hawa polisi wetu ukipeleka ishu kama hii wataanza na wewe halafu utafuata mlolongo wa watu ambao hawana hatia mpaka waje kuachiwa watakuwa wamesota sana halafu mtuhumiwa atakuwa hajapatikana na watautangazia umma kuwa wanaendelea na upelelezi mkali na kuwathibitishia kuwa watamtia hatiani mtuhumiwa.” Nikafurahi baada ya kugundua kuwa Ommy ameanza kuelewa mpango wangu. “Nafikiri huu ni wakati muafaka wa kumtembelea Betty” Nilisema huku nikimuangalia Ommy ambaye alionekana kukubaliana na mawazo yangu. Nikaingia chumbani. Nikachagua nguo ambazo niliona zitanifaa kwa usiku huo.Niliamua kuvaa suruali nyeusi ya jeans na fulana rangi ya udongo huku nikimalizia kwa raba za rangi ya udongo miguuni . Akafunga mlango tukaingia ndani ya gari lake na kuondoka. “unajua kesho ni lazima tuufungue ule mzigo?” Nilisema huku nikimkazia macho Ommy. “Hata mimi nina shauku kubwa ya kutaka kujua lile begi lina nini ndani yake.” “Bila shaka itakuwa ni almasi ”.Nilitamka kwa kujiamini. ********** CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/Saa nne kasorobo (3.45) tuliwasili Tabata Kimanga,tukavuka daraja dogo lililokuwa mbele ya Mazda bar kisha tukasimamisha gari hatua kumi kutoka pale ilipo nyumba ya mpenzi wangu Betty.Nilitembea taratibu kuelekea pale kilipo chumba chake. Kwa mbali niliweza kusikia sauti ya muziki kutoka Redioni.Taa ilikuwa inawaka jambo lililonipa matumaini kuwa mwenyewe yupo.“Hodi! …”Kimya.Nikabisha hodi kama mara tatu lakini nililakiwa na ukimya uleule. Betty alikuwa anakaa vyumba vya uwani lakini hata nyumba kubwa ilikuwa kimya kabisa.Haikuwa kawaida kwa nyumba hiyo kukosa watu. “Leo kuna nini?” niliwaza. Nikagonga kwa nguvu kidogo. Mambo yalikuwa yale yale.Nikaamua kujaribu kufungua kitasa cha mlango ule,ukafunguka. Kwanza nilipokelewa na harufu nzito ambayo haikuwa ya kawaida pili nikashtushwa na mtawanyiko wa vitu mle chumbani,viti vingine vilikuwa vimepinduliwa.Nguo zilikuwa zimetawanywa huku na huko.Ni wazi kwamba kulikuwa na vurugu hapo ndani.Nilianza kuingiwa na hofu ya kuwa kuna jambo si la kawaida limetokea,nilihisi kuwa huenda Betty ametekwa.Nilikosea sana kwani sekunde chache baadae nilifumbuka macho na kufahamu nini kimetokea humo ndani. Mshtuko nilioupata haukuwa wa kawaida.Kama nilifikiri kuwa Merina ndiye mtu aliyeuwawa kikatili basi nilikuwa nimekosea. Nilichokiona nilitamani iwe ndoto.Hayakuwa mauaji ya kawaida.Mauaji ambayo hayakufanywa na binadamu mwenye akili timamu. Mwendawazimu tena zaidi ya mwendawazimu.Nilikosa nguvu nikaegemea ukuta huku nikiendelea kuangalia kitu ambacho nilitamani iwe ni ndoto tu.Haikuwa ndoto lilikuwa tukio la kweli ambalo kama utasimuliwa unaweza kusema ni simulizi zinazotoka kwenye filamu za kusisimua hususani za Wanaijeria. Kichwa cha Betty kilikuwa kimekatwa kikawekwa Mezani, mikono na miguu nayo ilikuwa imekatwa na kupangwa mezani kama wanavyofanya wauzaji wa nyama za kuku. Utumbo ulikuwa umetolewa na kuwekwa kitandani. Kitanda chote kilikuwa kimelowa damu.Yeyote aliyefanya hivyo alikuwa amedhamiria kuleta maudhi makubwa kabisa. Nilitetemeka kwa hasira. “Ole wao hawa mbwa!” niliwaza.Nilizunguka kwa hasira huku nikipiga ngumi ukuta.Naweza kusema katika kumbukumbu zangu hakuna siku mbaya katika maisha yangu kama siku hiyo na sidhani kama itakuja kutokea siku kama hiyo.Amewakosea nini?Kwanini makosa yangu yawe mateso kwa mtu mwingine?Niliikumbuka sana siku niliyokutana na Betty pale baa.Alikataa,akakataa… Nikambembeleza,nikambembeleza kwa maneno ya uungwana. Maskini sikujua kuwa uhusiano wangu ungemponza kiasi hiki.Bora ningekutana naye baada ya mkasa huu.Nilijiuliza swali moja ambalo lilinitisha na kuniongezea hofu.NANI ATAFUATA? Bila kujitambua nilikuwa nazunguka zunguka mle ndani kwa muda wa dakika tano.Nilikuwa nahisi kichefuchefu,mwili wote ulikuwa wa baridi.Hofu ilikuwa imenitawala. Nilikuwa nimechanganyikiwa vibaya,nikasikia sauti ya Ommy. “Vipi mshikaji mbona unapoteza muda?” “Ingia!” Nilimwambia kwa sauti iliyojaa utulivu. Akaingia. “Haa! My God,they killed her”(Mungu wangu wamemuua). Akashtuka huku akiwa ameziba mdomo.Ommy aligwaya vibaya sana.Kwa dakika kadhaa alikuwa ametumbua macho kwa mshangao. “Twenzetu Kajuna hii ni kesi nzito!”.Wakati nataka kuondoka nikauona ujumbe wa karatasi ambao nilihisi umeachwa na wauaji. Sikutaka kupoteza muda,nikaichukua ile karatasi na kuiweka mfukoni.Kabla sijatoka mle ndani nikaanza kuhisi kichefuchefu kikizidi. Nikaanza kusikia maumivu ya kichwa ghafla.Ommy hakutaka kuruhusu hali hiyo akanishika mkono kwa nguvu na kuanza kukimbia. Nikajikuta nikikimbia bila kutaka. “Kimbia kijana Polisi watakuja hapa muda si mrefu!”. Tukaingia ndani ya gari kisha akaliondoa kwa kasi.Baada ya dakika kama tano tukakutana na gari aina ya 110 defender likiwa na askari wapatao watano.Wote walikuwa na silaha.Ommy aliongeza kasi ya gari kitendo kilichonifanya niwe na hofu zaidi. “Ulijuaje kama askari watafika? Nilimuuliza kwa mshangao. “Mazingira ya ile nyumba yanaonesha kuwa wanaishi watu wa familia tofauti haiwezekani wote wawe wameondoka ni hofu tu ndo imewakimbiza pale na ni lazima watoe taarifa Polisi”.Alijibu huku akiendelea kuongeza mwendo wa gari lile.Spidi ilikuwa inatisha mpaka wakati fulani nilihisi kuwa tutaingia kwenye mtaro.Kutokana na kasi ile niliogopa kuendelea kumsemesha kwani angekosea kitu kidogo tu sidhani kama tungesalimika. Ule mwendo ungeweza hata kuwashawishi askari wa usalama barabarani kulitilia mashaka gari letu.





    ********* Jua lilipochomoza tu,Kitu cha kwanza ilikuwa ni kukusanya magazeti ya siku ile. Magazeti mengi yalikuwa na vichwa ambavyo viliyafanya yauzike kwa siku ile.DAR YATIKISWA KWA MAUAJI MENGINE YA KUTISHA.Baadhi ya magazeti yalijinadi.Nilikuwa najua wazi kuwa hakuna jipya nikachukua gazeti na kuanza kusoma.Kama nilivyotarajia zilikuwa ni habari za Mauaji ya Betty.Mwisho habari ilimalizia kwa kusema Polisi wanaendelea na uchunguzi mkali. Nikatulia kidogo nikitafakari tukio la jana.Kwa namna fulani nilianza kujishangaa mwenyewe,nilishaanza kuzoea matukio ya kutisha kwani katika hali ya kawaida tukio la Betty lingeniumiza sana kichwa lakini nikajikuta likinizidishia hasira na kutamani kukutana tena na Bonge. Sikuwa na woga tena mbele ya Bonge,nilitamani aingie kwenye anga zangu nimuonyeshe kazi.Nilikuwa na hasira kiasi ambacho mtu angekuwa karibu yangu angeweza kusikia jinsi nilivyokuwa nasaga meno. “Ole wake,ipo siku tu!….” Niliwaza. Wakati nikiwa kwenye mawazo hayo mazito ndipo nikakumbuka kile kikaratasi ambacho nilikichukua eneo la tukio.Huku nikianza kurudiwa na woga ambao ulishapotea nikaanza kukisoma kile kikaratasi. …..Tunajua uko hai makosa yalifanyika,uliandaliwa kifo kitamu tena cha heshima.Ni raha ilioje kutangazwa kuwa umekufa kwa bomu,je! Huoni kuwa huo ni ujasiri? Umekataa kifo kile…safari hii tunataka kukusamehe lililo muhimu kwako ili kupata msamaha tunaomba mzigo wetu….La sivyo tutakuuwa kinyama kuliko alivyouwawa huyo malaya wako.Pia lazima ukumbuke kuwa picha yako tunayo tunaweza kukuweka matatizoni.Mtemi. Niliusoma tena ule ujumbe, nikatikisa kichwa. “Eti watanisamehe!” Nilijikuta nikisema kwa sauti na kumshangaza Ommy ambaye alikuwa anaingia kutoka bafuni. “Watakusamehe kina nani!?” Sikumjibu nikampa kile kikaratasi asome mwenyewe. Akakisoma,alipomaliza nikamuona akitikisa kichwa. “Wendawazimu kamili, uwape mzigo wakuache hai!?” Alisema Ommy huku akiwa amekunja sura. “Kifo cha heshima,kifo ambacho kingetawanya viungo vyangu huku wao wakicheka na kula kuku!” Nilitamka kwa sauti iliyojaa utulivu. Walinishangaza sana hawa viumbe ambao niliwatoa katika kundi la binadamu. Vyovyote ambavyo ungeweza kuwaita kinyume cha binadamu na malaika kwangu ilikuwa sahihi. Ukiwaita mbwa sawa, ukiwaita nguruwe sawa ukiwaita……..jina lolote lile ambalo litawatoa katika kundi la binadamu wastaarabu wao liliwastahili. “Leo wapi?” Aliuliza Ommy. “Leo ilikuwa siku ya kufungua mzigo” Nilimjibu nikamuaona ananitazama kwa mshangao. “Unasema ilikuwa siku ya kufungua Mzigo ina maana hatufungui tena?” “Mzigo utafunguliwa lakini sioni sababu ya kufungua leo wakati bado tuko kwenye majonzi ya kifo cha Betty. Sitaki nisherehekee wakati mbele yangu kuna tatizo kubwa kiasi hiki.” “Sawa wazo lako ni zuri,kwa hiyo leo tutafanya nini?” “Leo tuna mambo mawili Ommy,kwanza nahitaji kuonana na Debora pili nataka kufika eneo la msiba ili niweze kujua nini kinaendelea.” “Ina maana unataka kuhudhuria mazishi!” “Hapana Ommy,Ingawa majirani walikuwa wananifahamu lakini ndugu wa marehemu hawanifahamu.” “Sasa utaenda kufanya nini huko?” “Nataka kujua kilichotokea kama itawezekana.” “Unataka kuhoji watu msibani?” “La,nataka kujaribu kama naweza kupata fununu kutoka kwa waombolezaji.” “Na huko kwa Debora?” “Huko lazima niende kwani kuna mengi nataka kujua kutoka kwa yule binti!” “Ok,twenzetu.” ********* Watu walikuwa wengi pale msibani.Ndugu jamaa na marafiki walikusanyika kwa wingi,kingine ambacho kilisababisha kuvuta zaidi watu bila shaka ni aina ya tukio lililosababisha kifo.Mauaji yalikuwa ya aina yake,mtu kukatwa kiungo kimoja kimoja halikuwa jambo la kawaida. Dakika tano zilipita tukiwa ndani ya gari.Sikuthubutu kuteremka kwani niliona kuwa ni hatari kwangu kama wangeniona watu ambao walikuwa wanafahamu uhusiano wangu na Betty.Sijui ni kwanini ujasiri wa kwenda pale msibani uliniishia ghafla. “Kajuna!” “Sema Ommy!” “Tutaganda hapa mpaka saa ngapi?” “Mi nafikiri kuna umuhimu wewe uende kule ukajue ukweli wa mambo,kwani kila ninavyowaza nahisi kama kuna hatari inaniandama!” Ommy akashuka garini na kuelekea kule msibani,pale nilipokaa nilijitahidi kuinama ili macho ya watu yasinifikie. Nilikaa pale kwa muda wa nusu saa nikimsubiri Ommy ambaye alishapotea katika macho yangu baada ya kujichanganya kwenye umati ule wa watu.Mara moja moja niliinua kichwa na kuchungulia kule msibani lakini sikumuona Ommy. Nilishangaa baada ya kuona nusu saa inamalizika bila ya kumuona Ommy. Niliamua kujilaza kwenye siti,sikutaka kusumbua tena kichwa changu kujiuliza mambo yanayokuja. “Oyaa vipi tena unalala!” “Sijalala nimeamua kuificha sura yangu si unajua anaweza kutokea mtu anayenifahamu nikaibua mambo mengine?” “Vipi una ripoti?” “Ripoti si mzuri.” “Kivipi?” Niliuliza huku kwa mara nyingine kijasho chembamba kikianza kunitoka. “Unatakiwa kuendelea kujificha zaidi kuliko mwanzo.” “Mhhhh!” Nilishusha pumzi nikamuangalia Ommy ambaye alikuwa anaonesha kutaka kuendelea kuongea. Kisha akaendelea. “Eti wewe ndio mtuhumiwa namba moja wa mauaji yale!” Tumbo lilishika joto ghafla baada ya kusikia kauli hiyo. Nikaganda bila kuongea lolote huku nikihisi kama midomo yangu imekauka.” “Inawezekana vipi?” Kwa sauti iliyokauka yenye mikwaruzo nilijikuta nikijikakamua na kuuliza swali hilo. “Inasemekana mara ya mwisho ulipoondoka kuna uwezekano mkubwa kuwa mligombana na ndio maana baada ya wewe kuondoka Betty hakuwa na furaha mpaka kifo kilipomkuta!” “Duh,bila shaka ni baada ya kumsimulia mkasa wangu!” “Sawa lakini kwa majirani hilo hawakulitambua na ndio maana wameripoti kuwa huenda yale mauaji yalikuwa ni ya wivu wa kimapenzi!” “Duh huu msala sasa na kwa jinsi ninavyowafahamu polisi hawana dogo hizo taarifa watazishikia bango utafikiri wamethibitisha!” “Lakini ni vizuri tumefahamu hatari iliyoko mbele yako.” “Na ndio maana nilihitaji kuja huku.” ********* Jua lilikuwa linawapungia mkono wakazi wa jiji la Dar es salaam,giza nalo lilikuwa linapiga hodi na kuwafanya baadhi ya wakazi wa jiji hili kuwa katika hekaheka tofauti.Wako ambao huo ndio ulikuwa muda wao wa kuanza shughuli huku wengine wakiwa wanarejea mapumzikoni baada ya kumaliza harakati zao za kimaisha. Palepale ambapo tulisimama siku iliyopita ndipo tuliposimama siku hii pia.Kama ilivyokuwa na siku hii pia nilimuacha Ommy kwenye gari nikaelekea nyumbani kwa Debora. Nilitembea haraka na kwa kujiamini sana kwani jua lilikuwa limepotea na hivyo nilifanikiwa kusitirika kwa kigiza chepesi ambacho kilianza kutawala.Sikugonga kama nilivyofanya siku ya kwanza kwani nilikuta ule mlango wa bati la KORIE ukiwa wazi. Kutoka nyumba kubwa nilikuwa nasikia muziki wa taarabu ulioimbwa na marehemu Issa Matona. Sauti ya kiutu uzima ilisikika kwa mbali ikifuatisha wimbo huo.Taa ilikuwa inawaka chumbani kwa Debora.Kwa kuwa kazi zake ni za usiku nilihisi kuwa saa hizo atakuwa anajiandaa kuondoka. Niliposogea mlangoni nikashtuka baada ya kusikia mtu akifoka. “Usitake kuongopa chochote wewe mbwa sema,Kajuna alifuata nini hapa kwako?” “Mimi simfahamu huyo Kajuna.” Niliisikia sauti ya Debora ikiwa yenye kwikwi kwa kilio “Uhai wako uko mikononi mwangu,ili uweze kunusurika unatakiwa kuwa mkweli,yule mtu aliyeingia hapa kwako jana alifuata nini?” Kikapita kimya kirefu bila kujibiwa chochote. Nikaangaza macho pale uani nikayaona matofali ambayo yalikuwa yamepangwa sehemu moja.Yalikuwa mengi kiasi bila shaka.Nikajitwisha moja nakusogea pale mlangoni. “Sasa kwa kuwa hutaki kusema nitakupa kile unachohitaji.” “Nis..s..sameh…. mimi simjui yul…….” Hakuwahi kumaliza kauli yake niliuusukuma mlango kwa nguvu na kuingia ndani. Yule mtu akiwa ameduwazwa na uvamizi huo wa ghafla alishindwa kufanya lolote licha ya kuwa na bastola mkononi.Niliitumia Fursa hiyo kwa kumpiga kwa tofali lile zito kichwani.Nilitumia nguvu zangu zote nikamshushia kwa nguvu katikati ya paji lake la uso. “Mungu wangu…umeua kaka nitafanya nini mimi?” Alianza kulia yule binti. “Shhhiiiiiiiiiii!” Nilimtuliza kwa kuweka kidole cha shahada katikati ya mdomo wangu. Niliufunga mlango haraka kisha nikamkazia macho makali. “Tuna maiti humu ndani na muda si mrefu unaweza kuwa kwenye mikono yas polisi,lazima ujue kuwa wewe utakuwa mtuhumiwa namba moja uko tayari?” Alionesha mshtuko zaidi nilipotoa kauli hiyo lakini hakujibu kitu. “Nimekusaidia nimemuua mtu aliyetaka kukuua au ulipenda ufe wewe?” Alikataa kwa kutingisha kichwa. “Sikia we mwanamke,Chukua kilicho muhimu kwako haraka sana kwani kuendelea kukaa hapa ni hatari kwako.” “Niende wapi?” “Nifuate!” Akili yake ilionekana kutulia kidogo,akakusanya vitu ambavyo aliona kuwa muhimu kwake akaviweka kwenye begi kubwa. Tukaondoka kuelekea kule aliko Ommy huku tukisaidiana kushika begi lile kubwa. “Aaah,Shemeji!” Alishtuka Debora baada ya kumuona Ommy ndani ya gari. “Vipi na huyu?” Aliuliza Ommy huku akionesha mshangao wa wazi baada ya kuona nimeongozana na Deborah tena akiwa na begi lake. “Mkuu tuondoke haraka kwani nimeua mtu huko ndani.” “Umeua?” Aliuliza Ommy huku akichochea moto kwenye gari. “Ilibidi!” Nilimjibu kwa mkato.Nikamsimulia Ommy kilichotokea kisha nikampa maelekezo tuelekee Ubungo. “Kuna nini Ubungo?” “Ni huyu binti hatakiwi tena ndani ya Dar kwani usalama wake bado uko hatarini!” “Sasa utampeleka wapi?” “Yeye mwenyewe atasema.” “Shemeji….unatakiwa kusafiri utaenda wapi kwani ni lazima uondoke ndani ya jiji!” “Musoma kwa mama.” Alijibu Deborah huku machozi yakitiririka kwenye macho yake. “Yule mtu aliyetaka kukuua unamfahamu?” “Nilikuwa namuonaona tu huko nje.” “Umeanza kumuona lini!” “kama sikosei nimeanza kumuona maeneo ya jirani na nyumbani akiuza kahawa baada ya kifo cha dada!” “Mh,hawa jamaa wana mpango gani?” Aliuliza Ommy. “Inashangaza maana kila kona wameweka mtu,bila shaka ni watu hatari sana.” Niliongea huku nikihesabu fedha kwa ajili ya nauli ya Debora. Tulifika Ubumgo saa 3.02,bahati ilikuwa upande wetu kwani tulipata nafasi kwenye gari ambalo lilikuwa linaondoka siku ya pili. ******** CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/Nilijisikia tofauti kidogo kila nilipowaza kufungua mzigo.Niliwaza iwapo nitakuta almasi ambazo nilikuwa nazifikiria basi lazima niitafute familia ya Betty kokote iliko ili niwape sehemu ya malipo ambayo ingemstahiki Betty au sehemu ya rambirambi yangu. Oh,maskini Betty umeniacha.Saa 2.15 tulifika maeneo ya Charambe magengeni.Nilimwacha Ommy pale nilipomwacha siku ya kwanza wakati napeleka ule mzigo kwa mjomba.Kama kawaida nikaanza kutembea taratibu kufuata vichochoro vinavyotokea kwa mjomba Kipupwe. “Ooh! karibu mjomba,karibu sana!” Ingawa alinichangamkia niliuona wazi mshangao ambao ulikuwa kwenye macho yake. “Vipi mjomba ulikuwa unaumwa!?” aliniuliza kwa mshangao. “Kwani vipi mjomba,mbona niko kawaida?” “hapana,mjomba ingawa nimekuona siku chache zilizopita lakini leo nakuona umebadilika,Kuna tatizo?” “Hapana ni kazi ngumu tu mjomba!” nilimjibu huku nikikaa kwenye kigoda. “Haya,habari za siku mbili tatu” “salama mjomba shikamoo!” “Marhaba mama yako hajambo?”Aliniuliza huku akifunga vizuri msuli wake kiunoni. “Toka nimemuona ile siku niliyokuja hapa sijamuona tena!”Nilimjibu huku nikitamani amalize mapema maswali yake nichukue begi langu. “Mjomba nimefuata lile begi!” “Ah!hapa ni kwako mjomba ingia tu uchukue!” “Nikaingia ndani,nikawasha kibatari nikaingia chumba ambacho nilihisi kuwa begi limewekwa huko.Wakati natoka nikakutana na mke wa mjomba mlangoni. “ooh! Kajuna Mwanangu unataka kuondoka bila hata kunisalimia!”Alisikika mke wa mjomba akiongea kwa sauti ya kulalamika kana kwamba nilikuwa namdharau. “Samahani shangazi si unajua maisha yanatupeleka puta,hatuna hata muda wa kukaa mahali nusu saa”. Nilimjibu huku nikiwa na hofu ya kukalishwa na kuendelea kucheleweshwa.Nashukuru shangazi hakuwa na maongezi mengi. Nikabeba begi langu na kuondoka kuelekea kule aliko Ommy.Kwa mbali tuliweza kusikia kama harufu fulani ya kitu kilichooza kikitoka kwenye lile begi.Haikuwa harufu kali sana lakini haikutofautiana sana na nyama iliyokaa siku mbili tatu kwenye friji. “Labda ni dawa za kuhifadhia Almasi!” Niliwaza.Mpaka kufikia hapo naomba niweke wazi kuwa mapigo yangu ya moyo yaliongezeka maradufu.Kijasho chembamba kilikuwa kinanitoka nilikuwa kama mtu anayesubiri kupewa taarifa za mgonjwa anayepumulia mashine. “Huu mzigo umenisababishia matatizo mengi sana una nini ndani yake?” Hicho ndicho kilichonipa hofu zaidi. “Kajuna,unajua nauogopa sana huo mzigo hasa kutokana na mambo mengi yanayojitokeza!”. Nilitabasamu baada ya kugundua kuwa kumbe Ommy naye alikuwa na hisia kama zangu. “Yaani jinsi moyo unavyopiga kwa nguvu nahisi kama unataka kuchomoka!” alisema Ommy na kunifanya nicheke. Aliwasha gari akaliondoa kwa mwendo wa kawaida. ********* Tulikuwa tumepanga kufungua ule mzigo baada ya kumaliza kula.Kwani kama ule mzigo ungekuwa na almasi ambazo tulisadiki kuwa zimo basi tusingeweza kula kwa furaha ambayo tungekuwa nayo. Tulitazamana na Ommy kana kwamba tulikuwa tunaambiana fungua wewe.Nililitazama tena lile begi nikapiga moyo konde. “Naomba kisu!” nilisema kwa sauti ambayo hata Ommy alibaini kuwa ilikuwa na kitetemeshi.Akanipa kisha akasimama kando. “Fungua!” Nilisema huku nikimpa kile kisu. “Hapana Kajuna moyo wangu una hofu kweli siwezi!” Niliona wazi Ommy akipotelewa na ujasiri.Kweli alikuwa hataki kabisa kufungua lile begi.Tukabaki tukitazamana kwa dakika kadhaa.Mzigo huu una nini? Hilo pia lilisababisha hofu.Hakuna aliyekuwa tayari kuchukua jukumu la kufungua mzigo huo.Kingine kilichonifanya ni hofu ni kumbukumbu ya lile Briefcase hawa watu ni vichaa kamili wanaweza kuweka hata bomu kwenye mzigo huu. Nikaamua liwalo na liwe tu wakati wa kufungua begi ulikuwa umefika.Begi lilikuwa limefungwa kwa kufuli ndogo la shaba.Kwa kutumia kisu nikatanua sehemu ambayo ilishikilia vishikio vya zipu.Kikawa kimebaki kishikio cha upande mmoja huku kile kingine kikining’inia kwenye kufuli.Mzigo ukafunguliwa! Chochote kilichohifadhiwa kilikuwa kimefunikwa kwa kitambaa cheusi ambacho kilikuwa juu yake. Nikakitazama kile kitambaa halafu kwa mikono inayotetemeka nikafunua. Huwezi kuamini!Nasema huwezi kuamini…..Hata kama ungesimuliwa bado ungekipa shida kichwa chako kutafakari ni kwa namna gani jambo hilo linaweza kuwa na ukweli.Akili ya kawaida ingekataa.Oh,huu ndio MZIGO ambao umenitesa na kuniweka njia panda,huu ndio mzigo ambao umesababisha uhai wa mpenzi wangu kukatishwa,MZIGO umenipa majonzi………….Ah! MZIGO.







    Si mimi wala Ommy,sote tulikuwa tumeacha midomo yetu wazi.Ni vigumu kuamini lakini zilipita dakika kumi tukiwa tumeukodolea macho mzigo ule.Baada ya hapo zilifuata dakika tano nyingine ambazo tulikuwa tunatazamana bila kusema neno lolote. “Si mchezo babaake!”Ommy alivunja ukimya.Sikusema neno lolote badala yake nilikaa kwenye kiti nikashika tama. Ilikuwa haiingii akilini kabisa kuwa siku zote nilikuwa natembea na mzigo wa ajabu namna ile.Mzigo ambao umenitesa na kuniingiza kwenye misukosuko mizito. Mzigo ambao kama ningekutwa nao nilikuwa sina ujanja wa kukwepa hukumu ya kifo kwani aliyekutwa na ngozi ndiye mwizi wa mbuzi. Kama ningenusurika basi ingechukua muda mrefu kubainika kuwa sijahusika.Mpaka hapo ningekuwa nimepoteza muda mwingi gerezani. Kwa moyo wenye ujasiri niliinuka kwenye kiti nikauendea ule mzigo.Nikawa naukagua vizuri. Hapa niliweza kubaini kuwa binadamu amefikia kiwango cha ushenzi zaidi ya mnyama.Mnyama mara nyingi hufanya mambo kwa mipaka lakini kwa hili binadamu alikuwa amevuka mpaka.Ndani ya lile begi kulikuwa na miguu miwili na mikono miwili ya Albino,yote ikiwa ni ya kulia,nilihamanika vibaya sana. Kwa makadirio ya haraka viungo hivyo vilikuwa ni vya watoto wenye umri wa kati ya miaka tisa na kumi na nne. “This is too much…” Aliropoka tena Ommy huku akiwa ameshika kiuno kwa mikono yote miwili. “Unafikiri kuna haja ya kuripoti Polisi!?” Niliuliza huku bado nikiwa nastaajabia mzigo ule. “Uko tayari kuwa mshukiwa namba moja?”Aliniuliza huku akiwa amenikazia macho kwa mshangao.Niligwaya. “Unafikiri hili tukio linamaanisha nini?” Nilimuuliza tena. “Mwisho wa dunia!” “Kwa vipi?” “Huyu au hawa watu wangekuwa wanataka pesa si bora wangefanya uporaji Benki kuliko haya waliyoyafanya na hii si tabia yetu Watanzania” “Nafikiri kuimarishwa kwa ulinzi kwenye Mabenki ndio maana wameshindwa!” “Hapana usiniambie hawa watu wana matatizo ya fedha nafikiri kuna kitu kimejificha hapa!” “Kwanini?” “Unajua haya mauaji ya Albino yanapofanyika hawa watu wanatumia gharama kubwa hili linanifanya nijiulize wanataka nini zaidi?” “Ukiuliza hivyo utakuwa unarudi kwenye jibu lako, hii ni dalili ya mwisho wa dunia!” “Pamoja na kuwa ni dalili ya mwisho wa dunia sikutegemea kitu hicho kifanywe na Mtanzania!” Alijibu Ommy huku akiwa bado ameshika kiuno. “Unafikiri tufanye nini sasa?” aliniuliza Ommy. “Mimi nafikiri tufuatilie mkasa huu kwa tahadhali kubwa pale tutakaposhindwa tutaomba msaada Polisi!” “Yaah!Kwa hilo nafikiri uko sahihi kwani si ajabu kukuta baadhi ya polisi wanahusika.” ********* Saa 1.09 tulikuwa maeneo ya Yombo Buza.Tuliegesha gari Buza kwa Lulenge halafu tukaanza kutembea kwa miguu kuelekea Buza Kanisani.Kulikuwa na Umbali wa Kilomita Moja na nusu. Jinsi tulivyokuwa tunatembea hakuna aliyeweza kugundua kuwa safari yetu ilikuwa moja. Tulipokariba Ommy akasimama kwenye Mkorosho akanipa ishara iliyonifahamisha kuwa yeye atanisubiri hapo. Nikatembea taratibu kuelekea nyumbani. Nilipofika wapangaji wenzangu walikuwa vyumbani mwao wakiangalia kipindi cha vichekesho ambacho hurushwa na moja ya runinga za hapa nchini.Niliishukuru Mungu maana kama ningewakuta nje wangeanza kuuliza hili na lile kitu ambacho sikutaka kabisa kitokee. Nikafungua mlango nikaingia ndani kisha nikawasha taa. Nilichokiona nilikuwa nimekitarajia.Chumba changu kilikuwa kimepekuliwa.Kila kitu kilikuwa kimetawanywa mle ndani.Nikamshukuru mungu ambaye aliniongoza kukutana na Ommy kwani kwa kumbukumbu zangu Ommy ndiye aliyenishawishi nisilale nyumbani kwangu. Nikaangalia mle ndani sikuona kitu cha umuhimu zaidi ya uhakika kuwa wale jamaa walifika.Nilikiangalia chumba changu kwa uchungu,machozi yalianza kunitoka na kujihisi unyonge kila nilipokitazama kile chumba kwani kilinirejeshea kumbukumbu ya mpenzi wangu Betty yaani amekufa hata hajui naishi wapi!Nilijua siku moja Betty atakuja kuwa mama watoto wangu. Tungekaa hapa siku chache kabla ya kutafuta makazi mengine.Bado kidonda cha uchungu wa kifo cha kikatili cha Betty ulikuwa kwenye nafsi yangu. Nikafunga mlango kimya kimya ili majirani wasigundue ujio wangu.Nikaangalia huku na huko sikuona mtu nikanza kuondoka kumfuata Ommy pale nilipomwacha,sikumkuta! Kidogo nikaanza kuingiwa na hofu.Si kawaida ya Ommy kuvuruga utaratibu.Sikutaka kujiuliza zaidi nikaendelea kupiga hatua kuelekea kwa Lulenge.Ingawa ilikuwa ni usiku kichochro nilichokuwa napita kilikuwa na giza zaidi kwa sababu ya miti iliyokuwa imelizunguka eneo hilo. Sikutembea hatua zaidi ya kumi nikashtushwa na sauti kali iliyojaa amri. “Tafadhali simama na usithubutu kugeuka,sipendi nikulipue kabla muda wako haujafika!” Ilikuwa ni sauti ambayo haina hata chembe ya mzaha.Nikaanza kuongozwa kikondoo huku nikiwa na uhakika kuwa kama Ommy hajauwawa basi atakuwa ametekwa.Kiasi fulani nikaanza kujilaumu kwanini tukio lile nilikuwa sijaripoti polisi mapema. Tukatembea hadi sehemu ambayo wale jamaa walikuwa wamepaki gari. Lilikuwa ni gari la kizamani aina ya Toyota Corrola,tulipolifikia nikamkuta mtu ambaye alinifungulia mlango wa mbele kwenye siti ya abiria kisha watu wawili wakakaa siti ya nyuma huku wakipiga mikwara mizito. Dereva alikuwa ni mtu mfupi mwenye mapele mapele usoni.Macho yake yalikuwa mekundu na alionesha kuwa hakutoka kuvuta bangi muda mrefu kwani alikuwa ananuka harufu ya bangi. Nikamtazama mara mbili,sura yake haikuwa ngeni. Nilijaribu kuvuta kumbukumbu hatimaye nikamkumbuka.Ni huyu ndiye aliyetufungulia lango siku niliyopeleka mzigo feki kwa Bonge. “Hivi hawa wamemfanya nini Omari!” Niliwaza nikiwa na ghadhabu iliyochanganyika na hofu.Gari liliondolewa kwa kasi sana.Tukapitia barabara ya vumbi inayoelekea Abiola.Hata kama ungekuwa na wazo la kuruka kwenye gari kwa kasi hiyo usingethubutu.Ilikuwa ni ‘spidi’ kubwa ambayo ilimshangaza yeyote aliyeliona gari hilo.Wengi walilitilia mashaka.Lakini hakuna hata aliyejaribu kutoa taarifa polisi. Tulipofika katika mteremko mkali ambao uko karibu na reli ya Tandika likatokea tukio la ghafla.Nikasikia kishindo kikubwa kama mlipuko. “Mshenzi…anatuuaaaa….”nilimsikia dereva akilalamika huku akimalizia kwa matusi ya nguoni,bila kuelewa kilichotokea nikaliona gari likiacha barabara na kuserereka kuelekea bondeni. ‘Buuuuu….’ Kilikuwa ni kishindo kikubwa ambacho kilinifanya nifumbe macho. Nikajiona nazama kwenye kiza kizito sana. “Sijui ndio kufa kwenyewe….” Niliwaza hatimaye nikapotelea kwenye hicho kiza halafu sikukumbuka kitu tena baada ya hapo. ********* CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/Nilifumbua macho nikakutana na mwanga mkali ambao uliumiza macho yangu.Nikafumba tena. Chumba kilikuwa na harufu kali ya Dawa.Nikafumbua tena macho yangu,nilishindwa kujua kama niko ndotoni au niko katika mazingira gani.Nilipoangalia vizuri mle ndani nikagundua kuwa niko hospitali. “Mbona sina tatizo lolote la Afya” nilijiuliza huku bado nikiendelea kushangaa mandhari ile.Kuna wakati mtu unaweza kuota na ukajuwa kuwa uko ndotoni,basi nilifikiri kuwa ndio wakati huu. “Hii sio ndoto ni kweli kabisa!” Niliwaza. “Kama ni hospitali nimefikaje,au nina kifafa,mbona sina kumbukumbu ya kitu kama hicho au kimeanza ukubwani!?” Nilijiuliza maswali mengi ambayo hayakuwa na majibu. Nikajaribu kuzungusha macho yangu mle ndani,hapo nikaanza kusikia maumivu makali ya kichwa.Nikajaribu kunyanyuka hapo ndipo nilipopatwa na mshangao zaidi. Mkono wangu wa kulia ulikuwa umefungwa Pingu. “Hii ajabu kweli!Hivi hapa ni Polisi magereza au hospitali?” Bado mlolongo wa maswali uliendelea kuongezeka.Nilipoangalia vizuri kumbe nilikuwa nimetundikiwa chupa ya damu.Nikawa najitahidi kuvuta kumbukumbu kwanini niko pale.Nikaanza kukumbuka safari yangu ya Mwanza. “Hivi nilisharudi Mwanza au bado niko Mwanza?”Nikatulia nikikumbuka kipande hicho cha Mwanza. “Kwani jamaa alishakata tikiti ya kurudia?”Nikakumbuka jinsi nilivyoagana na Martin. Kipande cha Mwanza kikapita. Ikaja kumbukumbu ya kuuwawa kwa mpenzi wangu Betty nikashtuka nikataka kuamka,nikakutana na Maumivu makali ya kichwa yakanifanya niendelee kutulia kitandani. Hatimaye ikanijia kumbukumbu ya lile tukio la kuanguka na gari pale karibu na reli ya Tandika.Nikawa nimeipata kumbukumbu ya kile kilichotokea.Sasa ilikuwaje nikaletwa Hospitali tena nikiwa nimefungwa pingu hicho kilikuwa ni kitendawili ambacho kiko nje ya uwezo wangu. Hivi kweli nilipona mbona kama nilishakufa? Wakati bado niko kwenye lindi la mawazo nikauona mlango wa chumba kile ukifunguliwa.Mpaka kufikia hapo nilikuwa sina uhakika kama ile ni wodi au chumba cha kawaida ambacho kina mkusanyiko wa vifaa vya hospitali.Akaingia muuguzi ambaye alikuwa amevaa sare nyeupe. “Ooh!umeamka ashukuriwe Mungu wa mbinguni” aliongea yule mama ambaye umri wake katika kazi ulikuwa unaelekea ukingoni. “ Mwanangu pole sana kwa matatizo.Najua ni shetani tu ndo’ alikuteka mpaka ukaingia kwenye ujambazi,lakini bado nafasi unayo kwani Bwana anakuita…… Bwana asema……” Chochote alichoongea sikuweza kusikia kwani alinishtua mno eti shetani ndo alikuteka ukaingia kwenye ujambazi! Ina maana mimi ni jambazi? Nilitishika kidogo kwani ni wazi kuwa niko kwenye mikono ya Polisi. Angalau nilikuwa sehemu ambayo ina usalama kidogo kuliko ningeangukia kwenye mikono ya Bonge na kundi lake.Lazima wangeniadhibu.Lakini hata huku niliko kama nitakuwa nimefikishwa kwa kutumia ushahidi wa ile picha bado niko hatarini. Sijui kama yule mama aliongea mpaka mwisho au alikatisha maongezi yake kwani fikra zangu zilikuwa mbali sana.Ninachokumbuka ni kusikia tu baadhi ya maneno kama Matayo…Wakorintho na wengine sijui nani vile….Eee! Nimekumbuka Waefeso lakini sijui alizungumzia nini zaidi. Bila shaka alikuwa ananihubiria kitu fulani akijua kuwa mimi ni jambazi. Sikumsikia,sikumsikiliza. Hata jinsi alivyoondoka mle ndani sijui. Baada ya muda kidogo nikasikia mlango ukifunguliwa tena.Pamoja na maumivu niliyokuwa nayo nikageuza kichwa ili kujua ni nani alikuwa anaingia.Moyo ukanipiga “Paaaa…” alikuwa ni mzee Kazakamba yaani baba yangu mzazi,alikuwa ameongozana na mama yangu mzazi. Walikuwa wamesindikizwa na askari wa jeshi la polisi ambaye bila shaka alikuwa amekaa nje akinilinda nisitoroke. Duh!Kwangu lilikuwa jambo la kustaajabisha yaani mimi nimekuwa mtuhumiwa kwa lipi?Mbona sina kumbukumbu ya tukio baya ambalo lilistahili hata kukaa gerezani kwa siku kadhaa. Nikakumbuka kitu PICHA,moyo ukalipuka tena “Paaaaa!” Kweli nilikuwa kitanzini.Na sasa baba yangu mzazi kaja kuniona kama nani mtuhumiwa mgonjwa au………….vyovyote vile hakuna zuri kwangu kwanza kajuaje? “Mwanao ni mtu hatari sana mzee,anahusika na mauaji ya watu wengi yanayoendelea hapa mjini!” Alisema yule askari huku akiwa amesimama kiubabe ubabe.Nilimwangalia baba usoni,machozi yalikuwa yanamlengalenga.Kwa upande wa mama yeye alikuwa analia kabisa. “Baba…”nikafanikiwa kutoa sauti.Kwa kuwa nilikuwa naongea kwa sauti ndogo akanisogelea. “Niamini baba...mimi ni mwanao niombeeni kwa Mungu kwani sina hatia na hii kesi naamini nitashinda tu. ” Niliongea huku nikiwa nimefumba macho kwani mwanga ulikuwa unaniumiza kichwa.Baba akanitazama kwa huruma kisha akajikakamua na kuuliza. “Hivi ilikuwaje Kajuna Mwanangu?” Baba aliniuliza kwa sauti yenye majonzi “Ni habari ndefu sana inahitaji muda kuelezea!”Kabla sijaendelea na maongezi yule askari akaingilia kati. “Mzee mimi nimekufanyia uungwana tu,kimsingi huyu haruhusiwi kuongea na mtu mwingine zaidi ya Polisi na daktari!” Alisema yule askari huku akifungua mlango na kuwataka wale wazee wawili waondoke.Nilimuona mama akifuta machozi kwa kitenge chake.Nilihisi kitu fulani kikiwa kimenishika kooni,lilikuwa ni donge la uchungu,mama analia baba analia naonewa mimi.





    ******** Ilikuwa ni siku ya tatu nikiwa katika hospitali ile ambayo hata jina sikuifahamu.Kila aliyeingia alikuwa hana muda wa kusikiliza shida yangu. Nilikuwa nachukiwa na askari na wauguzi.Wakati mwingine wauguzi walikuwa wakilalamika kwa nini kazi ya kuhudumia majambazi wapewe wao.Wapo waliotamka wazi kuwa eti bora askari wangenimaliza moja kwa moja kuliko kuwaletea usumbufu.Niliumia sana moyoni.Hivi hawa hawajui kabisa kuwa kesi nyingine huwa zinajitokeza kwa makosa tu!Mbona kuna watu wamechomwa moto kwa kudhaniwa kuwa ni wezi.Hujafa hujaumbika bwana,hawakuwa na haki ya kuninyanyasa kiasi kile.Kwa upande mwingine hawa wauguzi walipendeza zaidi kuwa askari kuliko hivi walivyo.Nakumbuka siku zile nikiwa mdogo muuguzi akinichoma sindano atanipa pole,atanibebembeleza,ata…. Ili mradi atanifanyia kila lenye kuleta faraja.Hawa wauguzi gani ambao huwasimanga hata kina mama wajawazito wakati wa kujifungua!Sina kwa kutolea malalamiko yangu ningewaambia wauguzi jirekebisheni muwe kama wale wa zamani au sijui hawa tulio nao ndio wale wanaoingia kazini kwa migongo ya ndugu zao? Wakati nikiendelea kuwaza akaingia askari mwingine. Nilikuwa nimeshapata nafuu.Yule askari akanijia pale kitandani akaongea kwa sauti ya kunong’ona. “Kijana usalama wako uko katika mambo mawili tu.Moja ni kufunga mdomo na la pili ni kurudisha mzigo!La sivyo utafute majibu ya kumridhisha Jaji kuwa hujaua mwanamke kule gesti picha yako tunayo na nakala nyingine iko polisi!" Lilikuwa kama pigo kali la radi. “Huyu nae yumo!?”. Nilichanganyikiwa vibaya sana. Nilikuwa najua nipo kwenye mikono salama kumbe ni wafuasi wa bonge.Yaani bora angetaja kitu kingine chochote kuliko habari ya picha. Ghafla,mlango ukafunguliwa. Akaingia askari mwingine ambaye aliduwaa kwa dakika kadhaa baada ya kumuona askari mwenzake ambaye hakuwa kwenye ratiba na pengine alikuwa hamfahamu kabisa.Ajabu!Yule askari alionekana kushtushwa na ujio wa askari mwenzake. Nikauona mkono wa kulia wa yule afande wa kwanza ukitafuta kitu kwenye mfuko wake. Mungu wangu! Bastola. Jamaa alichomoa bastola bila kushtukiwa na askari wa pili. “Nooo!” Niliropoka kwa kihoro baada ya kukiona kidole cha shahada cha yule askari wa kwanza kikiwa kimeelekea kwenye kitasa cha kufyatulia risasi!” “Paaaa! paaa….” Mlio wa risasi mbili mfululizo uliwashtua watu pale hospitali.Jamaa alikuwa ameelekeza bastola kwangu.Nilikuwa nakiona kifo wazi wazi.Nikataka kuruka kitandani,lakini pingu ikanishika barabara kwani ilikuwa imefungiwa kwenye moja ya pembe za kitanda kile cha chuma.Badala yake nikapiga mwereka mkubwa kitanda kikaniangukia na kunifunika.Nikasikia risasi nyingine tatu ambazo zilikilenga kitanda kile. Sikuwa na uhakika kama risasi zilikuwa zimenipata au la!Kwani maumivu yalikuwa makali kutokana na kuangukiwa na kitanda halafu kutonesha majeraha ambayo yalikuwa yameanza kupona. Nje kulikuwa na balaa kubwa. Kwa kelele nilizokuwa nasikia nahisi hata wagonjwa waliacha vitanda vyao na kuanza kukimbia.Wakati nikiwa bado nimefunikwa na kile kitanda nikasikia milipuko mingine ya risasi. Maumivu yalikuwa makali lakini nikajikaza kiume na kujiinua pale chini. Duh! Ilikuwa inatisha.Nilimuona yule askari akitapatapa kwenye dimbwi la damu. Alikuwa anarusha miguu huku na huko kwa uchungu wa kifo.Baada ya dakika chache nikamshuhudia yule askari akikodoa macho ukodoaji ambao si wa kawaida. Alikuwa amekufa! “Duh!Huu sasa msala mpya,Askari ameuwawa kwa bastola mbele yangu nitaeleweka kwele?”Niliwaza huku nikiwa na wasiwasi wa kuongezewa idadi ya mashtaka yanayo nikabili. ******** Ukimya ulikuwa umetawala katika korido hii.Nilikuwa nimefungwa kitambaa usoni.Nilijua kabisa eneo hilo ni korido lakini sikujua ni sehemu gani.Nilikuwa na uhakika kuwa niko ghorofani nikipelekwa chumba hiki na kile bila kuambiwa lolote. Nikaingizwa katika chumba ambacho nafikiri walikusudia kunifikisha,wakanifungua kitambaa. Kulikuwa na watu watano ambao nyuso zao zililikuwa na mikunjo ya hasira kama mtu anayekula kitu kichungu.Kwa mtazamo wa haraka niliwatambua kuwa ni askari,lakini nahisi walikuwa ni askari maalum.Chumba hiki kilinitisha sana kilikuwa na vitu vingi vya ajabu ajabu. Vitu nilivyovitambua ndivyo vilivyonifanya niingiwe na hofu. Kulikuwa na visu,mikasi, nyundo na kiti ambacho nilikitambua mara moja kuwa kimetegeshwa nguvu za umeme, maalum kwa kuadhibu wahalifu. Nilikifahamu kiti hiki kupitia filamu za kizungu,nilikuwa naona jinsi watu walivyokuwa wanateswa kwa kiti hicho kwenye filamu hizo.Askari wote walikuwa wananitazama kwa macho makali bila kuongea neno lolote.Moyo ulikuwa unaenda mbio ajabu!Askari mmoja akanielekeza kwa kidole niende kukaa kwenye kile kiti cha umeme. “Vipi bado?” aliuliza askari mmoja. “Tunamsubiri afande Edwin,si unajua yeye ndo’ mtaalamu wa mambo kama haya hata akiwa bubu ataongea tu!” Duh! Niligwaya baada ya kusikia kauli hiyo lakini nikapiga moyo konde. Nikarejesha mawazo yangu nyuma.Nikakumbuka tukio la kuuwawa askari pale Muhimbili.Nilikuja kugundua kuwa ni hospitali ya Muhimbili ile siku ambayo madaktari walithibitisha kuwa Afya yangu ni nzuri hivyo kuwaruhusu askari kunichukua. Kilichonishangaza ni msafara wa magari mawili yaliyokuwa na askari lukuki tena wenye silaha! Kana kwamba haitoshi nilikuwa nimefungwa pingu mikononi na miguuni.Tena nikapigwa na butwaa baada ya kuliona kundi kubwa la watu likiwa nje huku wakifanya purukushani za kutaka kuniona.Wapiga picha nao hawakuwa nyuma,sijui kama walikuwa ni wapiga picha wa magazeti au wale wa kawaida.Lakini kitu kimoja niliweza kukibaini kutoka kwenye kundi hili la watu.Bila shaka nilikuwa ni mtu ambaye nimefanya tukio ambalo limetikisa jiji la Dar es salaam.Mle wodini sikupata fursa ya kusoma habari wala kusikiliza taarifa ya habari hivyo nilikuwa sijui nini kinaendelea huko nje. Nikachukuliwa hadi kituo cha polisi Temeke pale Chang’ombe.Nikafungiwa bila kuambiwa wala kuhojiwa chochote kwa muda wa siku tatu. Halafu ndio ikafika siku hii ya leo ambayo nimefungwa kitambaa na kuondolewa pale Temeke kwa gari hadi huku ambako sikufahamu. “Hivi nimeletwa huku kwa kosa gani?” niliuliza baada ya kuona hakuna ninachoelewa. Askari wakanitazama bila kunijibu kisha wakaendelea na maongezi yao.Kutokana na mawazo sikuweza kujua walichokuwa wanaongea. Kitendo cha kunidharau na kuendelea na maongezi yao kilinifanya niwe na hasira.Wakati nikiwa kwenye bahari hiyo ya mchanganyiko wa mawazo nikauona mlango wa chumba kile ukifunguliwa.Watu wawili waliovaa suti na tai ambao bila shaka nao walikuwa ni askari wakaingia. Wakakaa kwenye viti. “Vipi mbona hamjaanza kazi?” aliuliza mmoja wa wale walioingia. “Ah,mtu mwenyewe kama ni huyu hatuoni sababu ya kufanywa na watu mia kazi ndogo kama hii!” Dharau? “Tulijua hii kazi anaweza kuimaliza afande Edwin hata akiwa peke yake” Ukimya ukatawala ndani ya chumba kile hakuna aliyeongea baada ya kauli ile ambayo kwa upande wangu niliiona kuwa ni ya dharau kubwa “ Vipi afande mko tayari?” aliuliza mmoja wa askari wale. Akaitikia kwa kichwa.Wale askari wengine wakaondoka mle ndani wakabaki wale wenye suti.Wakanifunga kwa mikanda maalumu pale kwenye kiti cha umeme. Nikamuona mmoja wa askari wale akivua koti.Akafungua tai,akavua shati lake jeupe. Akawa amebaki na fulana ya ndani tu. “Kijana tunataka majibu mazuri kwa maswali yote tutakayokuuliza sawa?” alianza yule ambaye bado alikuwa kwenye vazi lake la suti. “Jina lako ni nani?”. Alianza kuuliza huku akizunguka zunguka kiti nilichokalia. “Kajuna Daudi Kazakamba” “Kajuna Daudi Kazakamba!” akayakariri yale maneno huku akiandika kwenye kidaftari chake kidogo. “Kabila lako?” “Mhaya!” “Una uhakika?” “Ndiyo!” “Mimi naitwa Rutashobya nataka tuongee kihaya ili nithibitishe kauli yako uko tayari?” “Hapana!” “Kwanini?” “Nimezaliwa na kukulia hapa hapa Dar es salaam.” “Unataka kuniambia hata bibi yako hujawahi kumuona?” “Nimewahi kumuona kwani nilikuwa naenda na kukaa wiki moja tu!” “Hapa Dar es salaam unafanya kazi gani?” “Sina kazi maalum!” “ndio maana umeamua kuwa muuaji?” “katika maisha yangu sijawahi kuua hata mbuzi!” ‘Paaaa….’ Jamaa akanizaba kibao kikali ambacho kilinifanya nione vimulimuli fulani kama nyota vile. Kilikuwa kibao cha haja cha mtu aliyeshiba. “Tulianza vizuri lakini sasa unaanza kuharibu!” Sikumjibu nikamtazama bila kuongea chochote. “Ninachotaka kujua si kama uliua au hukuua.Kwa nini unaua watu na kuleta hofu hapa mjini?” lilikuwa swali lililoniingia kama ncha ya kisu katikati ya moyo wangu. Sikujibu hadi niliposhtushwa na kofi lingine safari hii likiwa la upande wa kulia.Shavu lilikuwa kama lililomwagiwa mafuta ya moto kwa ukali wake. “Narudia kwanini unaua hovyo na kusababisha hofu hapa mjini?” “Afande nikuambie mara ngapi kuwa si mtu tu! Sijawahi kuuwa hata mbuzi.” Afande akashikwa na jazba akanishika sehemu za siri,akanibinya kwa nguvu kule sehemu… sehemu.Maumivu yalikuwa makali nikajikuta nikitokwa na matusi ya nguoni. “Nataka uniambie kwa nini unaua?”. Nikamtazama yule afande kwa hasira. “Hivi uliniona wakati naua?” Nilimuuliza kwa jazba. “Afande Edwin naomba hiyo picha!”.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/ Sikushtuka ni kama niliyetarajia.Ilikuwa ile ile picha ya Merina. Niliitazama ile picha kwa umakini mkubwa kisha nikatikisa kichwa. “Hii picha ni ya nani?” aliniuliza huku akiendelea kukizunguka kiti changu. “Ni yangu!” “Unafanya nini hapo?” “Nimeshika kisu huku nikiwa na uchungu kwa kifo kile!” “Kwa nini uue halafu usikie uchungu!” “Nasema sijaua!” “Umesema picha ni yako halafu unasema hujaua tukuelewe vipi?” “Hapo nimeshika kisu afande na kama unaitazama vizuri hiyo picha huo mkono hauonyeshi dalili yoyote ya kuchomoa au kukandamiza hicho kisu uwe unatumia akili mambo mengine!” Nilifoka “pumbavu!umeua hujaua!” Ilikuwa ni sauti kali ya yule askari aliyeitwa Edwin. “We huna akili nimeshaongea mara nyingi kuwa sijaua kwanini uendelee kuniuliza?” Nilimjibu huku nikiwa na hofu kwani nilimuona akiiendea ile swichi ambayo inaleta umeme kwenye kile kiti. Akaiwasha.Siwezi kusimulia kwani sina kitu cha kufananisha na maumivu niliyoyasikia. Sekunde ishirini zilikuwa kama siku saba. “Haya sema umeua hujaua?” alirudia swali. “Niseme mara ngapi sijaua,ukitaka fanya lolote lakini ukweli ni huo!” Niliongea kwa kujiamini huku nikiwa tayari kuendelea na adhabu ile. “Narudia,umeua hujaua?” “Kamuulize mama yako!” Niliamua kuongeza jeuri. “Lete koleo!” Aliagiza Edwin ambaye alikuwa katili kuliko yule wa kwanza. Akaubana mdomo wangu kwa mkono wake wa kulia kisha akaingiza ile koleo mdomoni.Akalibana jino moja kwa nguvu sana. “naomba uwe mkweli vinginevyo leo nahamisha meno yote mdomoni ubaki kama pakacha!” “Naomba ukubali umeua hujaua!” Nikakaa kimya nikifikiria ukubwa wa adhabu ya kung’olewa jino.Usifanye mchezo na polisi,bora uwasikie redioni tu! Hapo nikawa na mawazo mengi ajabu.Nilimfikiria sana Ommy.Yuko wapi? Huko aliko anafanya nini? Hivi alipotea vipi siku ile ambayo nilitekwa?” Nikashtuka baada ya kumuona yule askari katili akichukua bendeji tayari kwa kung’oa jino. “ Jiandae kuingia kwenye ulimwengu mpya wa vibogoyo!” Lilikuwa ni tangazo lenye kuleta hasira.Nikamtazama bila kuongea lolote.Mapigo ya moyo yalikuwa yameongeza kasi yake,kung’olewa jino bila ganzi si jambo la mchezo. Chochote alichotaka kufanya Hakuwahi.Mlango ukagongwa akasitisha zoezi lake.Akaenda kufungua mlango. “Mkuu anamuhitaji mtuhumiwa!” alikuwa ni askari wa kike ambaye kama wale wengine hakuwa na sare. “Bahati yako!” aliongea yule askari katili huku akionesha wazi kukerwa na wito ule ambao ni wazi ulikuwa umevuruga burudani yake. Yaani watu wengine sijui wameumbwaje!Huyu jamaa nilivyomtazama tu nilijua kuwa matendo yake haya alikuwa anasikia raha.Bila shaka alikuwa anavimba kichwa zaidi pale anaposifiwa. Nilimchukia! Mpenda sifa!





     Nikafunguliwa pale kwenye kiti.Kisha nikafungwa tena kitambaa usoni.Sijui hata maana ya kitendo kile,nilikuwa naogopwa tofauti na vile nilivyo.Lakini sijui kama nilikuwa naogopwa au hawa jamaa walikuwa wanaigiza. Nilikuwa nashindwa kuelewa inakuwaje polisi ambaye kasomea kazi yake ameshindwa kugundua kuwa ile picha hainihusishi moja kwa moja na mauaji.Kwanini asiulizwe aliyepiga ilikuwaje akanipiga picha katika mazingira kama yale halafu asitoe taarifa mapema.Swali hilo lilinifanya niutilie mashaka uwezo wa askari wale.Kama uwezo wanao kweli basi watakuwa wanahusika na wanajua siri yote.Ni hapa ndipo nilipowaza jinsi ajira ya jeshi la polisi inavyotolewa. Kwa nini wasichague watu ambao wana uwezo wa kufikiri? Badala yake kumekuwa na utaratibu mbovu wa kuwaingiza watoto wa maafande.Pia upande mwingine nilikuwa nauchukia huu utaratibu wa kutaka watu warefu tu!wako watu wengine ni warefu kwa maumbo lakini akili zao ni fupi.Pia wapo ambao ni kinyume chake hawa ni wafupi wenye akili ndefu.Si kila kitu kinahitaji nguvu au mbio! Mambo mengine yanahitaji uwezo mkubwa wa kufikiri.Jeshi letu linakosa watu makini wa kuwahoji wahalifu kutokana na utaratibu huu mbovu. “Mwanangu amemaliza…….hana kazi!” “Mlete kuna nafasi zinatolewa na jeshi la polisi zitatangazwa wiki ijayo!” Hivi ndivyo walivyopeana. Tukaingia kwenye chumba kingine kile kitambaa kikafunguliwa tena.Nilikuwa kwenye chumba kingine kipana,kizuri.Kwa mandhari ya chumba kile nafikiri ni ukumbi mdogo wa mikutano.Mbele yangu kulikuwa na watu wawili ambao walionekana kunawiri kwa madaraka waliyokuwa nayo.Mmoja alikuwa mnene huku akiwa na kitambi kikubwa ambacho kilikuwa kimegusa meza iliyokuwa mbele yake,alikuwa amevaa sare ya kipolisi ambayo ilikuwa na nyota tatu begani Yule mwingine alikuwa na umbo gumu kuelezea kama ni mnene au mwembamba lakini ilikuwa ni rahisi kuelezea kimo chake,alikuwa mrefu.Alikuwa amevaa shati la bluu,suruali nyeusi na viatu vyeusi.Alikuwa anapendeza sana.Sikuona dalili ya ukatili kwa mtu huyu ambaye nilihisi kuwa ni askari.Sikuwa na uhakika lakini kwa kuwa alikuwa mazingira haya nilihisi ni mmoja wao. “Samahani bwana Manyika nahitaji kuongea na huyu mtu Faragha!” “Usiwe na wasiwasi Mr.Mtuvu Viko vyumba maalum kwa kazi kama hiyo!” Tukaondoka bila kufungwa tena kitambaa. Tukaingia kwenye chumba ambacho kilikuwa na maandishi MAHOJIANO MAALUM.Tukaingia kwenye chumba hicho ambacho kilikuwa na viti vinne,meza moja na mtungi mkubwa wa maua.Ukutani kulikuwa na picha mbalimbali za wakuu wa jeshi la polisi wa mikoa mbalimbali na ile ya Rais wa kwanza wa jamhuri ya muungano wa Tanzania. “Naitwa Jerrome Mtuvu,natokea idara ya Usalama wa Taifa makao makuu,ni mkuu wa kitengo cha operesheni maalum!" huyu alikuwa anaongea kwa utulivu mno hali ambayo ilinifanya niwe makini zaidi. “Unavuta sigara!” aliniuliza huku akiingiza mkono mfukoni “hapana!” Nikamwona anachomoa sigara ambayo mpaka leo sijaifahamu kwani ilikuwa pana kuliko zile nilizozoea. Akawasha na kuanza kuvuta. “Samahani kijana,sina njia nyingine kwani siwezi kuanza lolote kabla ya kuvuta kidogo.” Akawa anavuta huku anautazama moshi unavyopotelea hewani.Huyu alionesha ustaarabu wa hali ya juu tofauti na matarajio yangu ingawa kitendo chake cha kuvuta sigara mbele yangu kilinifanya nimtilie mashaka kidogo. Mawazo yangu yakarudi kwa Edwin,sijawahi kuona mtu katili kama yule yaani aning’oe meno kwa koleo. Duh! angening’oa sijui ningekuwa mgeni wa nani?Watu wengine wanapenda sifa za ajabu!” Mawazo yangu yakarudi kwa Betty,ua la moyo wangu lilikuwa limechanua na kunyauka ghafla.Ilinitia uchungu sana eti kwa sababu yangu Betty amekufa. “Usijali mpenzi nitakulipia kisasi nikishindwa nitakufuata !” Niliwaza. “Kama sikosei unaitwa Kajuna Kazakamba!” “Ndiyo” “tafadhali naomba uwe mkweli naomba unileze chanzo cha mauaji yote haya!” “Akatulia kidogo na kunikazia macho. Nikaanza kumsimulia kuanzia mwanzo hadi mwisho huku nikificha habari za Ommy!” “Sawa nimekuelewa kijana,nahitaji kukusaidia,kwa kuanzia leo nitakutoa hapa polisi lakini naomba unithibitishie haya ndiyo utakayoeleza mahakamani?” “Ndiyo na yako mengi zaidi ambayo nikitoa ushahidi lazima hawa watu wachukuliwe hatua kali!” “Umesema huo mzigo uko wapi?” ” kuna mahali nimeuficha ili uwe ushahidi baadae!” “Unafikiri utakusaidia vipi huo ushahidi?” “Utasaidia kufuatilia chanzo cha mauaji kwa kujua aliyeuwawa alikuwa anaishi wapi nani kanikabidhi huo mzigo na je kuna alama ya vidole aliacha?” Akatulia na kuangalia simu yake nikamuona akibofya bofya. Mara,mlango ukafunguliwa. Akanishtua yule aliyeingia. Alikuwa ni waziri wa bunge na usimamizi wa vikao vya serikali. Alikaa kwenye kiti kivivuvivu baada ya kuhakikisha mlango umefungwa. “Vipi mmefikia wapi maana naona mambo yanazidi kuharibika!” “Usijali mzee mtaro utafunikwa tu!” “Umejaa takataka au unataka kuufunika tu!” “Tena unatakataka za sumu!” “Duh!” aliguna Mheshimiwa waziri.Kama si kuwa waziri yale maneno yao yangenitia hofu sana. “Hivi unafikiri ni ushahidi gani utautoa kuweza kukuokoa kwenye tuhuma hizi mzito?” “Ninazo picha za wahusika kwani matukio mengine nilikuwa napiga picha bila wenyewe kufahamu!” Niliongopa “Hizo picha ziko wapi?” Ziko sehemu salama kwani hakuna anayeweza kuzifikia huko ziliko.” Nilimuona muheshimiwa waziri akiniangalia kwa macho yaliyojaa hofu.Nikaanza kumtilia mashaka mheshimiwa huyu nikaamua kuongezea msumari wa moto. “Pia kuna picha nimemuachia mtu fulani ili aujulishe umma wa Watanzania nini kilitokea iwapo nitakufa kabla sijapata fursa ya kuweka mambo bayana.” Ulikuwa ni msumari wa moto kweli kwani nilianza kuona kijasho chembamba kikimtoka waziri. “Unaweza kuwataja baadhi ya hao watu?” Waziri ambaye alionekana kuchanganyikiwa akalazimika kuniuliza. “Wengi wao ni watu maarufu na wazito katika nchi hii kwa hiyo bora tusubiri mahakamani!”. Sasa nilipata uhakika waziri hakuwa mtu mzuri kwani hofu yake ilikuwa bayana. Hata yule aliyejitambulisha kuwa ni afisa usalama nilimuona akiwa na hofu iliyofichika. Baada ya muda nikaondolewa mle chumbani nikapelekwa chumba kingine. Nikafungiwa huko.Ubaya wa jengo hili ilikuwa ni vigumu sana kujua kama ni usiku au mchana.Ni taa tu ndizo zilizoniwezesha kuona.Toka niingie kwenye jengo hili sijawahi kuuona mwanga wa jua.Kwani kila chumba nilichoingia hakikuwa na madirisha,ni viyoyozi tu ndivyo vilivyosaidia kuifanya hali ya hewa iwe mzuri. Mpaka leo ninapoandika huu mkasa bado sijagundua nilikuwa ndani ya jengo lipi. Baada ya kukaa masaa kadhaa mara mlango ukafunguliwa. Askari wawili wakaingia wakanifunga tena kitambaa kilekile kisha nikatolewa ndani.Jinsi tulivyokuwa tunatembea nilijua wazi kuwa tulikuwa tunashuka kutoka ghorofani.Kama ni msaada kwanini nifungwe kitambaa usoni,huu usiri ni wanini? Maswali hayo na mengineyo yaliendelea kunitesa. Nikaongozwa kuingia ndani ya gari bila kufunguliwa kitambaa.Baada ya mwendo wa masaa kadhaa nikasikia sauti “mfungue!” Ee bwana eeh! Almanusura nipoteze fahamu kwa kihoro,huwezi kuamini,nilipofunguliwa kitambaa nikajikuta nikiwa mbele ya nyumba ile ambayo nilileta mzigo. Nilichanganyikiwa vibaya! Nilihisi miguu ikigongana gongana.Mbele yangu nilimwona yule aliyejitambulisha kwangu kwa jina la Jerrome Mtuvu akiwa ametangulia.Nyuma yangu kulikuwa na watu watatu wenye bastola. Nikageuka! Duh,kama kuna siku nilitamani sana ardhi inimeze nididimie basi ni siku hii.Nyuma yangu kulikuwa na watu wa mwisho kabisa ambao nilitamani kukutana nao katika Maisha yangu. Nilimwona yule mtu mwenye kila dalili ya muuaji mzoefu yaani Martin,hakuwa Martin mwingine ni bali yuleyule aliyenikabidhi mzigo kule Mwanza,katikati alikuwa ni yule askari alieuwa askari wengine kule Muhimbili ‘askari feki’ na mwisho kabisa alikuwa yule jamaa aliyenipiga picha kule Tabata. Sikuonadalili yoyote ya kunusurika safari hii. Nilikuwa katika mikono ya kifo.Ommy hayupo,nashukuru sikumtaja mbele ya yule mnafiki aliyekuwa ananihoji. Eti Jerrome Mtuvu afisa wa idara ya usalama wa Taifa kitengo cha Operesheni maalum,mpumbavu mkubwa. Waombe Mungu nisiwatie mikononi.Sina bunduki lakini hata upanga au kisu nitashindwa kutumia?Lakini sijui kama nitatoka hai hapa! ********* CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/Niliingizwa kwenye chumba kizuri ambacho kilikuwa na kila kitu muhimu kwa matumizi ya binadamu ndani. Kuta zake zilikuwa zimepakwa rangi ya maziwa huku kwa chini kukiwa na ufito wa rangi ya udongo. Kulikuwa na kabati kubwa lililotengenezwa kwa alminium kabati hili liliwekwa karibu kabisa na mlango.Kwenye kona nyingine ya chumba hiki kulikuwa na Jokofu zuri refu la rangi ya fedha. Nilifungua friji nikakuta matunda,juisi,mikate na vitu tofauti. Sikutaka kujiuliza nikaanza kuishambulia milo mbalimbali ambayo ilikuwa ndani ya lile friji. Nilipohakikisha kuwa nimeshiba nikaanza kukagua chumba kile kama kuna uwezekano wa kutoka. Nikagundua kuwa uwezekano ulikuwa mdogo.Mbaya zaidi kama ningekutana na walinzi ningepambana nao vipi? Ukubwa wa hatari iliyopo mbele yangu nilikuja kuuona baada ya kugundua kuwa kuna kiongozi mkubwa anahusika.Waziri! Waziri na viungo vya albino wapi na wapi! Hili la waziri kuhusiana na hawa watu lilinichanganya sana. Mwanzo wakati anaongea na yule mnafiki Jerrome alikuwa anaongea mafumbo ambayo nilishindwa kuyatafsiri kwa sababu ilikuwa ni vigumu kuamini kama waziri ambaye yuko mstari wa mbele kutetea maslahi ya wananchi anaweza kufanya mambo ya ajabu namna ile.Sasa huyu naona anafaa kuitwa mnafiki.Ndiyo huyu ni mnafiki kamili,halafu yule Jerry.. Yule…yule ah! Atabaki kuwa Jerry afisa usalama wa kughushi.Hivi yule anapoomba kura huwa anatumia maneno gani kuwashawishi wapiga kura? Ni yeye huyu ambaye hutoa hutuba za kusisimua akiwasisitizia wabunge jinsi serikali itakavyopambana na majanga mbalimbali likiwemo la mauaji ya Albino, Mnafiki mkubwa kabisa. “Lakini kwa nini hawa watu wamekuwa wakarimu kwangu?Au ndiyo maisha ya binadamu na mbuzi? Atamtafutia majani kokote yaliko lakini mwisho wa siku ni kitoweo,lazima atamchinja tu. Nikapata wazo! Ilikuwa ni lazima nifanye kitu la sivyo siwezi kuokoka. Nikatabasamu,lilikuwa wazo zuri ajabu! Unajua mawazo mengine yanakuja katika wakati ambao ni muhimu mno.Hapa lazima nikiri kuwa mambo mengine huwa ni msaada wa Mungu. “Ahimidiwe Bwana,Bwana wa mbingu na ardhi.Unastahili sifa ee Mola wetu….” Nilikuwa namtukuza Mungu wangu kwa nguvu zote lakini moyoni nikiwa na lengo la kumbembeleza Mola wangu anipe mbinu zaidi.Kipindi hiki cha matatizo nilijikuta nikimuweka karibu sana Mungu lakini kabla ya hapo nyumba za ibada kwangu zilikuwa kama kituo cha polisi.









     Nilifungua friji nikatoa chupa ambayo ilikuwa na kinywaji ambacho sikukifahamu.Sikuwa na muda wa kusoma maandishi ya chupa ile. Nikakipiga chini kikapasuka.Nikashika kile kipande cha chupa ambacho kilibaki mkononi.Moyo ulikuwa unaenda mbio sikuwa na uhakika kama mbinu nilizokuwa nazifikiria kwa wakati huo ni sahihi.Nikapanda dirishani,mikono yangu ilikuwa imefikia kwenye ubao wa dari ‘ceilingboard’ nikaanza kujaribu kupapatua.Kazi ilikuwa ngumu kwa sababu nilikuwa na kazi mbili mkono mmoja ulikuwa umeshika dari huku mwingine nikijaribu kuharibu ubao ule. Nilishindwa kabisa kufanikisha zoezi langu.Nilianza kufikiria mbinu za ziada za kufanikisha nafasi ile ya mwisho kwangu kuweza kujiokoa. “Nimekwisha!” Niliwaza.Wakati nikiendelea kuwaza nitaifikia vipi ile dari nikasikia mlio wa viatu.Kuna mtu alikuwa anakuja.Kama alikuwa anakuja kwangu basi nilikuwa sina la kufanya.Nilisikia uchungu sana,nilijua wazi kuwa iwapo hawa jamaa wataniua basi maiti yangu isingeonekana tena. Nilihuzunika sana,nilimfikiria zaidi mama yangu. Angejisikiaje kuishi bila kujua kama mwanae niko hai au nimekufa. “Eeee, Mungu nisaidie na uniokoe mja wako mkosefu!” Niliwaza. Kumbe yule mtu alikuwa anapita,bila shaka alikuwa anakagua usalama mle ndani. Nikashusha pumzi.Ilimradi nilikuwa natapatapa kutafuta namna ya kujiokoa.Nikapata wazo jingine,nikazima swichi inayopeleka umeme kwenye friji.Nikalisogeza friji karibu na dirisha. Nikapanda juu ya friji. Nikaigusa vizuri ile ‘ceilingboard’ nikaisukuma kwa nguvu.Nikahisi misumari inaanza kuachia mbao ndogo ndogo zilizoshikia ubao ule. ‘Ta! ta! ta……’ Nilikuwa nasikia raha misumari ilipokuwa inatoa sauti ya kujiachia. Ghafla! Nikasikia hatua za mtu aliyevaa buti zikija kule nilikokuwa nimefungiwa.Nikaruka haraka juu ya friji,kwa kuwa sikuvaa viatu sikutoa kishindo ambacho kingemshtua yeyote aliyeko nje. Mlango ukafunguliwa.Alikuwa ni Martin,Martin muuaji,Martin ambaye kanipa mzigo unaonitesa mpaka leo.Viungo vya albino!Tena huku akisisitiza safari hii nimepata mzigo safi kutoka Mwadui,huyu ni zaidi ya mnyama. “Mungu wangu! Sijui itakuwaje akiona sehemu ya dari ambayo imepapatuliwa.” Niliwaza huku nikiwa na hofu kubwa sana.Sikupenda kabisa yule ibilisi agundue kilichofanyika. “Na hii friji imefuata nini huku?” aliongea Martin kwa hasira. “Angalia bwana mdogo ujanja wowote utakaojaribu ujue unaharakisha kifo chako.” Akasogeza lile friji mahali pake.Mungu mkubwa,hakuinua macho kutazama juu.Akafunga mlango kwa funguo.Nikashusha pumzi kwa nguvu zaidi kuliko mwanzo.Sauti ya viatu vyake ikapotea masikioni mwangu,nikajua ameshafika mbali. Nikaanza tena harakati zangu za kujinusuru Sikuwa na muda wa kupoteza,nikapanda kwenye ukingo wa dirisha kisha nikasukuma kwa juu ile sehemu ya ubao ambayo bado ilikuwa imeng’ang’ania pale kwenye dari. Nikashuka chini nikachukua kipande cha chupa ambayo niliipasua nikakiweka mfuko wa nyuma wa suruali yangu ya ‘jeans’.Nikavua fulana yangu nyeusi ambayo ilikuwa inanuka kutokana na kutofanyiwa usafi siku nyingi. Kwa ujumla nguo zangu zote zilikuwa zinanuka.Sikumbuki ni lini nilioga au kufua nguo zangu.Hata kama kile chumba kilikuwa na bafu lakini sikujisikia kabisa kuoga. Nikapanda kule darini,Oh! nashukuru Mungu ingawa kulikuwa na ukuta lakini ukuta ule ulitenganisha vyumba vya upande wa kulia na kushoto tu.Hivyo niliweza kutembea upande huu wa kulia kadri ya uwezo wangu.Kule juu nilikuwa kama kipofu kutokana na giza,nilikuwa nimeshaamua kujaribu bahati yangu kwani kuendelea kukaa pale na kusubiri kitu ambacho sikijui ni wehu kamili. Baada ya hatua kadhaa kule juu nikafika sehemu ambayo niliweza kusikia kilio cha mtu kwa chini,nahisi nilikuwa kwenye usawa wa chumba kingine. “Mhh! mmh! mmh!.....” kilikuwa kilio cha mtu ambaye ni wazi alikuwa anaugulia maumivu.Nikakanyaga kwa nguvu sehemu ile ya dari.Pakabomoka bila utaratibu. Nikaangukia chumbani huku nikifanya kishindo ambacho kingemshtua yeyote aliyeko nje ya chumba hicho.Chumba kilikuwa na giza ingawa niliweza kukiona kitanda kikiwa na mtu ambaye sikuweza kumtambua. “kuna nini tena!” nilisikia sauti kutoka nje ya chumba. Nikasikia funguo zikiingizwa kwenye tundu la kitasa.Sikuwa na muda wa kujiuliza nini cha kufanya nilikuwa nimeshayakoroga ilikuwa lazima niyanywe.Nikajibanza kando ya ule mlango,nikachomoa kile kipande cha chupa. Moyo wa ujasiri ulikuwa umeniingia.Naomba nieleze wazi kuwa muda huu nilimkumbuka sana Betty,hivyo hasira zilizidi.Ilikuwa ni fursa yangu ya kumlipizia kisasi. Nilishaamua kuingia kwenye mchezo wa kifo.Ilikuwa ama zangu ama zao.Alipofungua mlango akawa anaenda upande ambao ulikuwa na swichi,sijui ujasiri ulitoka wapi nilijikuta nikimrukia na kuanza kudidimiza kile chupa kooni kwake.Haikuwa rahisi kama nilivyofikiri,Jamaa alikuwa na nguvu kweli kweli hakukubali kufa kikondoo.Ingawa kulikuwa na giza lakini niligundua alichotaka kufanya.Alikuwa anaingiza mkono mfukoni ili atoe bastola.Ajabu!Nikamuona analegea na kuanguka chini kabla ya kutoa bastola yake.Nikawasha taa.Duh!Ile chupa hatari kweli,yaani damu zilizomwagika pale sakafuni huwezi kuamini.Alikuwa maiti!.Nikatabasamu kabla ya kukigeukia kitanda.Kama ungeniona wakati huo lazima ungekimbia nilikuwa nanuka damu,hofu ilikuwa imenikimbia kabisa sikuwa kajuna wa kawaida.Sura na moyo wangu vilivaa kwa muda vazi la ukatili na hasira. Nilipigwa na butwaa pale nilipoangalia kitandani.Mwanamke alikuwa amelazwa kitandani huku akiwa amefungwa mikono na miguu.Kikubwa kilichonishtua nilifikiri ni Mchina lakini nilipomwangalia vizuri zaidi ndipo nilipogundua kuwa ni mwanamke mwenye ulemavu wa ngozi yaani albino.Duh huu sasa unyama yaani binti nzuri kama huyu amehifadhiwa kama bidhaa ya dukani.Roho iliniuma sana. “Hawa watu sijui wana roho za aina gani?” nilijiuliza huku nikimwangalia kwa makini mwanamke yule ambaye kama angekuwa anasoma basi angekuwa mwaka wa kwanza au wa pili chuo kikuu yaani bado alikuwa mbichi. Alikuwa amefungwa plasta mdomoni,bila shaka hawakutaka apige kelele.Sikutaka kuanza na huyu mwanamke,nikarudi kule kwa yule jamaa aliyeanguka.Kiunoni alikuwa na kisu kikubwa chenye mpini mweusi,nikakichukua kile kisu na bastola ambayo ilikuwa kwenye mfuko wa kushoto wa suruali yake.Nilikitazama mara mbili kile kisu ama kwa hakika kilifanana sana na kile kisu kilichotumika kufanyia mauaji ya Merina kule Tabata.Kisu kilinirudishia tena kumbukumbu ya lile tukio,kwa dakika kadhaa nilikuwa nimeduwaa nikikikodolea macho kile kisu. Nikamgeukia yule binti albino aliyelala kitandani.Nikamfungua kamba alizokuwa amefungwa kisha nikatoa ile plasta aliyofungwa mdomoni. “Niacheee!” alianza kufoka kwa sauti kali na ya hofu. “Shiiiiiiiii!”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    nikaweka kidole cha shahada katikati ya mdomo kumuashiria anyamaze.Akanirushia ngumi nikawahi kuudaka mkono wake. “Una kichaa wee mwanamke!” Nilimfokea.Kidogo nikamuona ametulia alianza kunielewa. “Vipi Dula mbona unachelewa!” sauti kutoka nje ilinizindua na kunifanya nijiweke tayari.Nikamuashiria mwanamke akae kitandani.Nikaruka kidimbwi cha damu nikaenda kusimama palepale niliposimama mwanzo.Akafungua mlango, akaingia. “Aah!We mwanamke,umemfanya nini Dula!” alifoka bila kufikiria huku akichomoa bastola yake kijingajinga.Hakuwahi! nilimrukia nikapitisha kisu katikati ya shingo yake,nikakata kwa nguvu zangu zote koo lake,akatapatapa hadi alipokata roho.Chumba kilikuwa kinanuka damu. “Wewe nani?!’’ aliniuliza yule mwanamke kwa mshangao uliochanganyika na woga.Kwanza sikumjibu nikachomoa kile kisu kutoka katika mwili wa yule jamaa.Nikafuta damu kwa kutumia suruali yake kisha nikamgeukia yule mwanamke. “Naitwa Kajuna sijui wewe unaitwa nani?” “Johari,na umefikaje huku?” “Sikiliza Johari hatuna muda wa kuendelea kuulizana hili na lile la msingi ni kutafuta namna ya kutoka humu ndani!” “Mimi sitaki kutoka humu ndani!” “Kwa nini!” “Maisha yangu yamekosa thamani halisi nimekuwa kama bidhaa kila ninakoenda naitwa dili bora nife kuliko kuishi kwa mashaka!” “hapana Johari yatupasa kuondoka,bado kuna watu wana roho nyeupe tena nyeupe kama theluji wanakuhitaji” “Hapana Kajuna nashukuru kwa kunijali lakini naomba uniache, waje wanichinje wanifanyie kafara sijui madudu gani niache……..” alianza kulia huku akiwa hataki kabisa kujaribu bahati ile ya kujiokoa. “Lakini kwa nini unakuwa mbishi we mwanamke!” “Kama baba yangu mzazi amethubutu kuniuza kwa hawa jamaa unafikiri nani atanithamini!” “Mwanamke twende utakufa hayo maneno tutayachambua baadae!”



    ITAENDELEA



0 comments:

Post a Comment

Blog