Search This Blog

Sunday, 22 May 2022

ISABEL NDANI YA MPANGO HASI - 1

 









    IMEANDIKWA NA : RICHARD MWAMBE



    *********************************************************************************



    Simulizi : Isabel Ndani Ya Mpango Hasi

    Sehemu Ya Kwanza (1)



    Kasulu - Kigoma



    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Vumbi jekundu lilikuwa likitimka huku na kule katika eneo la stand mpya ya Kasulu, kila mtu alificha uso wake ili vumbi hilo lisije kumletea madhara yoyote, lakini watoto walionekana kuifurahia hali hiyo walikimbiakimbia kutaka kudaka makaratasi na mifuko ya nailoni iliyokuwa ikipeperushwa na vumbi hilo, kwao ilikuwa ni mchezo mzuri sana, hawakufikiri hata mara moja kuwa vumbi hilo lingeweza kuwaletea madhara au hata upofu, kwao haikuwa hivyo kwani hawakujali hata kesho ikoje.



    Katika moja ya migahawa iliyopo stand hapo palikuwa na vijana watatu walioonekana kubishana kitu fulani na kati yao ilionekana hakuna uelewano, lugha waliotumia ilikuwa si ya hapa ila ni ya nchi jirani. Vijana hao waliovalia kitanashati, suruali zilizokaa vizuri katika matumbo yao walinyanyuka kutoka katika mgahawa huo na kutoka nje kila mtu akiwa na mawazo yake, walipanda magari tofauti ya kuelekea Kigoma mjini na kuondoka eneo lile.



    Vumbi bado lilikuwa halijatulia katika eneo hilo na watoto wale walikuwa bado wanacheza wakiwa na furaha kabisa huku wengine wakiwa wameshikilia kaptula zao zisiwadondoke. Wengine wkiendelea kucheza kabumbu wakiwa na ndoto za kuwa wachezaji nyota wa dunia siku moja.

    Vumbi lile lilitenganisha dunia zilizokuwa hapo kwa wakati huo kila mmoja hakujua nini kinaendelea upande wa pili.



    Magari yaliondoka katika eneo lile kwa nyakati tofauti mengine yakielekea Kahama, mengine Manyovu, mengine Kigoma mjini basi ilimradi kila kitu kiliendelea.

    Vumbi lilitulia na hali ikawa tulivu katika eneo hilo lote, watoto wale sasa iliwabidi wabadilishe aina ya mchezo kwani ule wa kwanza haukuwa na vitendea kazi tena.



    Isabel, msichana mfupi, kibonge mwenye macho ya kuvutia, mweusi kidogo mwenye kucheka na kila amuonaye akaondoa mtandio wake usoni na kupepesa macho huku na huku na kushuhudia utulivu wa hali ya juu stendi hapo

    “Kaka samahani hakuna basi lililokuja hapa?” alimrushia swali kijana mmoja aliyekua akiuza vocha eneo hilo

    “Ha! We dada mabasi manne yamekuja na kuondoka ulikuwa wapi? Hukuyaona? Itabidi usubiri bahati nyingine” kijana yule alimjibu Isabel, Isabel alitafakari kidogo imekuwaje hakuyaona mabasi yale, kumbe alipojifunika mtandio ule kuzuia vumbi kausingizi kalimpitia ndiyo maana hakujua hata nini kiliendelea stendi hapo, alitafakari kidogo, akanyanyuka kutoka katika bench lile na kuuendea mgahawa Fulani ili apate chochote na kasha aamue afanye nini.



    Aliketi kwenye moja ya viti vya plastiki katika mgahawa huo na kuagiza soda na keki, alipokuwa akiendelea kunywa soda yake alihisi kama amekalia kitu Fulani lakini alipuuzia, baada ya muda alipitisha mkono wake kitini alipokaa na kushika kitu Fulani kisha akakitoa ili ajue ni kitu gani “mh” aliguna, alijikuta na bahasha ndogo mkononi ndani ina kitu kigumugumu hivi, baada ya kutazama uku na huku hakuna aliyemuona aliitia bahasha ile katika mkoba wake wa laptop na kumalizia soda yake. Alitoka na kupanda Toyota hiace kuelekea mjini, akiwa ndani ya daladala ile alikuwa na mawazo mengi sana, lengo lake la kurudi ni kuangalia kama kuna treni ya Dar maana mabasi yamempita kwa kuendekeza usingizi.



    Josephat Msengiyumva alivua mawani yake ya jua na kuchukua kitambaa kujifuta vumbi kidogo machoni, akiwa amejiegemeza kwenye nguzo ya umeme akiangalia mapito ya wapiti njia mfuko wake wa shati ulitikisika kidogo, akaingiza mkono na kutoa simu kuna meseji ilifika muda si mrefu ‘Mr Jomse unayo ile memory card?’ Jomse alistuka kidogo, akili iliporudi aliijibu meseji ile kuwa hana hiyo memory card. Kichwa kilimzunguka na hakujua kama swali aliloulizwa lilikuwa la mzaa au la ‘mzaa katika kazi’ alijiwazia akcheka kidogo kasha akarudisha simu sehemu yake. Mara meseji ikaingia tena ‘na jamaa anasema hana, hapa na mi sina’ . Jomse alishusha pumzi ndefu na kujiondoa pale aliposimama, akasogea pembeni pasipo na watu na kupiga simu “mbona siwaelewi nyi jamaa, kwani wa mwisho kuwa nayo nani?” Jomse aliuliza kwa ukali na baada ya kusubiri sekunde kadhaa aliendelea “ nasema hivi! Mrudi palepale kwenye mgahawa mkaangalie, msilete ujinga unafikiri mama akijua tutasema nini!? Haya nasubiri jibu!” aliwakaripia wenzake na kukata simu kwa hasira na kuirudisha mfukoni.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Jomse alijishika kichwa kuonesha amechoka ghafla.



    Memory card ndogo iliyotiwa kwenye kibahasa cheupe ilianza kuwachanganya akili vijana wale, hawakujua wafanye nini, kazi waliyopewa, maelekezo na picha zote zipo ndani ya card hiyo, shughuli pevu.



    Mathias Ndirikumana au Mandi kama anavyojulikana kikazi alikuwa wa kwanza kufika katika mgahawa ule, alipoingia moja kwamoja alitupa jicho sehemu mbalimbali za kibanda hiko kwa ufundi sana lakini hakuona dalili ya kibahasha kile

    “dada, tulipoondoka hukuona kitu chochote hapa?” alimtupia swali mama lishe yule “hapana kaka, ni kitu gain?” mama lishe alijibu na kuuliza kwa wakati mmoja

    “aaah, tumesahau bahasha na hapa tulikuwa nayo, kama umeiona niambie hata pesa nitakupatia” Mandi alimueleza yule mama ntilie ambaye alionesha wazi kuwa kitu hiko hajakiona hata kidogo. Mandi alionesha uso wa kuchanganyikiwa kila wakati alikuwa akijifuta jasho usoni, mara ashike kiuno, mara atikise kichwa.

    “Vipi umeipata?” sauti ilitokea nyuma yake, alipogeuka alikutana macho kwa macho na Tonton ambaye alifika mahali hapo muda huo

    “hapana Ton, sijaiona” alimjibu

    “ah! Huyu dada anasemaje?” Ton aliuliza

    “anasema hajaiona kabisa” Mandi alimjibu Tonton, Tonton alishikwa na hasira nakuanza kumfuata yule dada lakini alizuiliwa na mkono wenye nguvu wa Mandi

    “tulia Tonton, mbona una pupa” mandi alimtuliza Ton, na Ton alitulia na kuketi kwenye moja ya viti vilivyopo mgahawani hapo.

    “Dada! Unakumbuka mi nilikaa hapo kwenye kiti cha pepsi, nilipotoka nani alikaa?” Ton aliuliza, kwa kuwa yeye ndiye aliyekuwa na bahasha hiyo mfukoni.

    “Hapo alikaa mdada mmoja hivi, naye ameshaondoka na hiace kwenda mjini, lakini sijui kama yeye kaichukua” mama lishe alimjibu Ton, Mandi na Ton walitazamana kisha wote wakageuka kwa dada yule kabla hawajaongea lolote sauti ya mtoto iliwakatiza

    “mama! Kwani hawa wanataka nini?” mtoto yule alimuuliza mama yake,

    “wanatafuta bahasha wameipoteza” dada yule alimjibu mtoto huku akimsukuma akacheze “ah! Mi najua, alishika yule dada aliyekaa hapa, hapa kwenye hiki kiti” mtoto alieleza na kisha kukimbia kuendelea kucheza mpira na wenzake.



    “Dada huyo msichana alikaa hapa yukoje?” Ton alidakiza swali kwa dada yule.

    “Alikuwa amevaa suruali ya jeans nyeusi na tshirt nyekundu, ila sikumbuki ilikuwa imeandikwa nini ana begi jeusi la mgongoni” mama lishe aliwajibu vijana wale, bila kuchelewa Mandi na Ton waliondoka kituoni hapo na kukodi tax

    “Kigoma mjini tafadhali” Mandi alimueleza dreva tax huku akifunga mlango na kujiweka vizuri katika kiti cha nyuma. Ton alichukua simu yake na kutuma sms kwa Jomse kumueleza juu ya tukio hilo “sasa tufanyeje?” Jomse alirudisha sms ile kwa Ton, “nafikiri tujaribu kumtrace ikiwezekana



    kumpata tuchukue hiyo memory card” . Wazo lilikubaliwa na wote watatu na moja kwa moja Jomse ambaye wakati huo alikuwa mjini moja kwa moja alielekea kituo cha mabasi cha Mwanga ili kujaribu kama anaweza kumpa msichana yule na jinsi gain ya kupata memory card ile.



    Vurugu za wapiga debe na wabeba mizigo katika kituo hiko cha mabasi zilishamiri mchana ule, wanaoshuka na wanaopanda mabasi walikuwa ni wengi, Jomse alisimama karibu kabisa na kibanda cha simu, kutokana na urefu aliokuwa nao haikuwa vigumu kuwaona wote waliokuwa katika pilikapilika kituoni hapo. ‘Msichana mfupi, kavaa fulana nyekundu na suruali ya jeans nyeusi’ Jomse alijesemea moyoni maneno hayo huku akiangalia kila daladala inayoshusha abiriria katika eneo hilo.

    Mandi na Ton nao waliingia katika eneo hilo na kumshukuru dreva tax, Ton alitoa noti nyekundu moja na kumpatia kijana yule kasha wakajichanganya kuanza msako wao.

    Jomse alikuwa makini akiwa na gazeti lake mkononi alijifanya akifungua kurasa hii na ile lakini hakuwa akisoma chochote ndani ya gazeti hilo, aliang’aza macho huku na huku kuangalia kama atamuona msichana yule, huku akili yake ikizidi kuchanganyikiwa juu ya upotevu huo wa memory card, wasiwasi wake ulikuwa ni jinsi gain wataonekana wazembe kwa sababu hata kazi waliyopewa bado hawajaanza kuifanya memory card hiyo wameshaipoteza, Jomse alijua wazi kuwa Mama akisikia jambo hilo watapata shida sana kwani wataonekena wazembe kupita maelezo.

    Mandi na Ton waligawana kila mtu upande wake ili wote waweze kuona kama watampata msichana huyo, walikuwa na wasiwasi na daladala waliyoipita njiani, walijua hakika atakuwa katika hiyo, na walipanga watafanya kila hila wampate ili wapate watakacho. Toyota Hiace ya buluu iliingia kituoni hapo na kutafuta maegesho ili ishushe abiria wake, watu walikuwa wengi ndani ya gari hiyo na walianza kushuka mmoja mmoja, “muwe makini katika kufanya hili” sms iliingia katika simu ya Mandi na Tom kwa wakati mmoja “msitumie nguvu ila akili ndiyo inahitajika” sms nyingine iliingia kwa wote wawili.

    Isabel alijisikia baridi kidogo akafungua begi lake na kutoa sweta aina ya ‘kaba shingo’ na kulivaa kabla hajashuka katika gari ile, alipohakikisha limemkaa vizuri, taratibu alishuka garini nakuangalia huku na huku kisha kujichanganya na watu wengine kituoni hapo. Msichana anayekadiriwa umri wa miaka kumi nane alishuka katika daladala upande wa pili, Jomse alimgundua haraka msichana yule aliyevalia sweta jekundu na sketi nyeusi, Jomse alimkazia macho lakini alijiuliza kwa nini maelekezo aliyopewa hayakulingana na mtu mwenyewe alivyo, alimtupia jicho mara nyingine na kutoa simu yake mfukoni akaandika kitu Fulani “kwenye mitumba” meseji ziliingia kwa Mandi na Ton, mara moja walimuona msichana yule lakini wote walishangaa kuona hajavaa suruali kama walivyoelekezwa. Ton alisogea taratibu eneo la muuza mitumba ambapo binti yule alionekana akichagua vibrauz vya hapa na pale, alipomwangalia kwa makini aliona kuwa hilo ni windo tofauti na wanalolitaka, alijaribu kuangalia vizuri huku na huku kama atamuona mwingine lakini eneo lote alikuwa ni binti yule tu aliyevaa vile. “Ni huyu kweli?” Ton aliwatumia meseji Jomse na Mandi, hapo nao wakapata shaka wasije kubana mtu tofauti, waliumiza vichwa wafanyeje kwa hilo. Lakini katika eneo hilo hakukuwa na msichana yoyote aliyevaa vile walivyoelekezwa.

    Baada ya kuchagua vibrauz viwili yule msichana alinunua mfuko wa Rambo na kuweka kasha akachukua begi la mdogo wake na kuingiza humo na kulitia mgongoni safari ikaendelea. Mandi alimfuata nyuma nyuma msichana yule huku akilipigia taiming begi lile, mpango ulipangwa kiufundi sana. Mara ghafla gari aina ya Toyota mark II ilifunga breki karibu kabisa na msichana yule, Jomse alichomoza na kumvutia ndani kwa haraka kabla hatahamaki gari ile iliondoka kwa kasi. Mandi aliangalia gari ile ilivyotokomea, watu walikusanyana eneo lile kuangalia kilichotokea akina mama wakipiga kelele za msaada

    “dada!!, dada!!” mtoto mmoja wa kiume alikuwa akilia kwa uchungu pembeni mwa barabara.



    Isabel akiwa na begi lake mgongoni aliona tukio lote lilivyotokea, alipigwa na bumbuwazi alibaki kajishika mdomo, naye alijichanganya na watu wengine katika eneo hilo. Mandi alimtazama Isabel kwa makini kana kwamba kuna sehemu ambayo amekwishawahi kumuona, Isabel alipogeuka alikutana macho kwa macho na Mandi lakini hakumtilia maanani akijua tu ni moja ya wapita njia,

     CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mandi alimwita Isabel

    “we dada njoo umsaidie motto huyu” Isabel alikwenda na kumchukua mtoto yule aliyekuwa akilia sana, Isabel aliivuta sweta yake kwa juu na kumfuta machozi motto yule, Mandi akiwa bado hajaondoka eneo lile alimuona Isabel alipofanya jambo hilo na mara moja aliiona fulana ile nyekundu iliyotokeza kwa chini baada ya kulivuta sweta lile kwa juu, na lipomwangalia vizuri alimuona kweli kava jeans nyeusi, Mandi alipagawa alitoa simu yake mfukoni na kutuma meseji “Wrong number, rudi haraka namba sahihi umeiacha”, alirudisha simu mfukoni na kuanza kumfuatilia Isabel. Isabel alimkabidhi motto yule kwa askari polisi mmoja wa kike ambaye alifika eneo hilo na yeye kuendeea na safari yake.



    Mandi alikuwa bado akimwangalia Isabel wapi anakoelekea, Isabel aliangalia saa yake ya mkononi na kuona muda unamuacha alisimamisha bodaboda na kupanda kasha akampa maelekezo Fulani dereva. Mandi naye akachukua bodaboda iliyofuata na kuifunguzi ile nyingine

    “hakikisha hakupotei” Mandi alimsisitiza muendesha bodaboda. Isabel akiwa hajui kama anafuatiliwa alikuwa anawaza tu kama ataiwahi treni ambayo ilikuwa iondoke jioni hiyo kuelekea Tabora mpaka Dar huku akiwa ameshasahau juu ya ile bahasha.

    ************



    Jomse na Ton walimpekua binti yule kila kona ya mwili wake na begi lake kisha wakambana maswali mengi, lakini msichana yule alibaki kulia tu maana hakuna alichokielewa walichokuwa wakimuuliza

    “ina maana tumekosea?” Ton alimtupia swali Jomse ambaye alibaki akimkodolea macho Ton, “labda tumeshindwa kujua suruali ni ipi na sketi ni ipi!” Hapo wote walijiona hawana akili kwa hilo “simama!” Jomse alimuamuru dreva wa gari ile

    “haya binti shuka, samahani” Jomse alimpa noti ya shilingi mia tano ili apande daladala kurudi mjini.

    Simu ya Jomse illita na muda uo huo ya Ton nayo iliita

    “what!?” ilisikika sauti ya Ton na kudakiwa na Jomse kwa mshangao pia “Tufanyeje sasa?” Jomse aliuliza,

    “Tuache hapa” Ton alimwambia dreva, wakampa hela yake na akaondoka, hawakukaa hata dakika mbili defender ya polisi ilipita na kusimama mbele yao

    “Habari!” polisi mmoja aliuliza, “salama sana, za kazi” Ton alijibu

    “mmeona gari moja salon nyeupe imepita hapa kuelekea huku ?” waliuliza

    “hapana afande hatujaiona sisi ndiyo tumefika sasa hapa barabarani tunasubiri daladala” Ton alijibu, mara tax ikapita eneo hilo na Jomse akasimamisha wote wawili wakajitoma ndani na kurudi mjini.



    Jomse na Ton walifika eneo lile na kukuta hali imetulia kabisa kana kwamba hakuna kilichotokea muda mfupi uliyopita. Walishuka katika tax ile na kumlipa dereva kisha kilammoja wao akachukua njia yake maana hiyo ndiyo mbinu kubwa waliyokuwa wakiitumia. “Stesheni ya reli” meseji ya simu ilisomeka kwa Jomse na Ton mara moja kila mtu alichukua usafiri wake kuelekea stesheni.

    Mandi alihakikisha hampotezi Isabel katika macho yake, alipomuona akishuka katika bodaboda ile nay eye alikshuka kisha kutembea kwa miguu kuelekea katika jingo la stesheni ambako Isabel alielekea huko pia. Jomse na Ton walifika eneo hilo kwa tofauti ya dakika kama tano hivi na kujichanganya na wasafiri waliokuwa wakiingia ndani ya jingo hilo ili kupanda treni hiyo kuelekea pande tofauti za nchi.



    Isabel akiwa hajui lolote alipanga foleni kama ilivyo ada kwa wasafiri katika eneo hilo, alishtuka kumuona Mandi tena katika eneo hilo tena sasa akiwa anamtazama sana

    “Ooh samahani mdogo wangu, kumbe wote tunasafiri!” Mandi alimsemesha Isabel ambaye kwa wakati huo akili yake ilikuwa mbali sana akiwaza hili na kuwazua lile, Isabel alitoa tabasamu fupi na kuendelea na hamsini zake. Watu walikuwa ni wengi katika eneo hilo, kelele na shughuli nyingi ziliendelea hapo, polisi, vibaka wote waliendelea kuwindana bila kukamatana. Lango la kuingia ndani lilifunguliwa na watu wakaanza kuingia kuelekea katika mabehewa ya treni hiyo tayari kwa safari

    “Ee dada, nilikuuliza kumbe tupo wote safarini?” Isabel alimwangalia Mandi hakumjibu chochote aliendelea na safari yake kuelekea lilikosimama treni lile. Alipoona Mandi anazidi kumsumbua alijichanganya upande wa pili wa abiria wengine na kutokomea, alimuacha Mandi akimsindikiza kwa macho tu.



    Begi la Isabel lilichomolewa mikononi mwake na kijana aliyepita kwa kasi isiyoelezeka “mwizi, mwizi, mwizi kamata huyo” kelele za watu zilisikika wakati Isabel akilia kwa uchungu kwa kuibiwa begi lake ambalo ndani yake kulikuwa na laptop na vitu vyake vichache, alishindwa afanyeje alibakiwa na begi lake la mgongoni tu, Isabel alilia sana kwa kupoteza begi lake.

    Wananchi wenye hasira walimkimbiza kibaka yule ambaye alikimbia na kuruka kwenye wigo wa stesheni hapo na kuonekana akipeleka begi lile kwenye gari moja nyeusi iliyopaki eneo la nje la stesheni hiyo, lakini kabla hajafika alipigwa dafrao na mmoja wa wapita njia

    “we kijana vipi mbona huangalii?”

    “samahani bro watu tupo kazini, majanga haya!” aliongea kwa sauti ya kitejateja, kutahamaki alijikuta yuko chini akifuatiwa na kipigo kikali cha wananchi wenye hasira “ua, ua huyo, wamezidi hao!!!” sauti za watu zilipishana, mwenye jiwe, rungu, fimbo ilimradi tu kumuadhibu kiumbe huyu. Jomse na Ton waliangalia tukio zima lilivyoendelea hawakufanya chochote, polisi ndiyo walioweza kumuokoa kijana huyu aliyekuwa hatamaniki kwa damu iliyochanganyika na vumbi, Polisi yule aliokota begi lile na kumpiga Tanganyika jeki kibaka yule mpaka kituo cha polisi kilichopo stendi hapo. Mandi akifuatana na Isabel walifika katika kituo hiko kidogo na Mandi alikuwa ndiyo msemaji mkuu kueleza polisi lililotokea na kuomba ikiwezekana begi hilo akabiziwe mwenyewe, baada ya mazungumzo machache polisi walikabidhi begi lile kabla Isabel hajalichukua tayari lilikuwa mikononi mwa Mandi.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Bingo!” Ton alisikika huku akimpiga ngumi mgongoni Jomse ambaye alibaki kutabasamu tu. Ton na Jomse walikuwa wakifuatilia hatua kwa hatua kila jambo liliokuwa likitokea, walitoka pale waliposimama na kuelekea lango kuu la steshen ili kuona jinsi watakavyopata begi lile toka kwa Mandi. Isabel alimuomba Mandi lile begi “usijali twende tu, watakupora tena vibaka wa hapa mi nawajua sana ntakupa ndani ya treni” Mandi alimjibu Isabel huku akiongoza katika treni ambalo tayari lilisahawashwa na kupiga honi zake tayari kwa safari, Mandi alimnyayua Isabel na kumpandisha kwenye ngazi kisha yeye mwenyewe kufuatia huku akining’iniza begi lile kwa nje,

    Jomse na Ton waliiona trick ile

    “Oya begi hilo” bwana mmoja alimwambia Mandi na kulivutia ndani kabla Ton na Jomse hawajalifikia begi hilo. ‘Huyu mzee choko kweli’ Mandi alijisemea moyoni.

    “Kaka mi naenda daraja la tatu, naomba mkoba” Isabel alimwambia Mandi

    “usijali hata mi nipo ukohuko daraja la tatu” Mamdi alimjibu Isabel na wote wakafuatana kuelekea daraja la tatu, katika korido ya treni walipishana na watu mbalimbali waliokuwa wakitafuta vyumba vyao ili wapumzike. Isabel kila wakati aligeuka nyuma kumwangalia Mandi, aliridhika kumuona Mandi naye akiwa katika harakati za kupenyapenya kufika huko ‘kajamba nani’ . Baada ya kuvuka mabehewa kama manne hivi Isabel aligeuka kumwangalia Mandi hakumuona, Isabel alichanganyikiwa kwa mara nyingine alianza kurudi alikotoka akihema watu walikuwa wakimwangalia na kumuona kana kwamba kapungukiwa, mara alikutana na Mandi kama behewa la tatu hivi

    “Nakuja dada usiwe na wasiwasi nilikuwa naongea na rafiki zangu hapa tumepoteana miaka mingi” Mandi alimueleza Isabel kisha wakaendelea kwenda huko daraja la tatu “kaka mi naona unipe tu



    begi langu tutapoteana humu” Isabel alimueleza Mandi. Mandi alijifanya hakusikia, Isabel aliwatazama wale vijana wawili waliokuwa wakiongea na Mandi na wao pia walimtazama sana Isabel, Isabel woga ulimuingia sana hapo akaona usalama wake ni mdogo.

    Watu walikuwa wamejaa sana hata pa kuweka miguu hapakupatikana. Isabel na Mandi walijibanza kwenye kanafasi kadogo sana.

    “Binti” mandi limwita Isabel, akaendelea kumwambia “Upo confortable hapo?”

    “Nitafanyaje sasa hata kama sipo confortable?” Isabel alimjibu Mandi huku akilini mwake akijiuliza kwa nini Mandi ameling’ang’ania begi lake.

    “Huku sio kuzuri binti, twende tutafute daraja la pili huwa kuna vyumba vinakuwa wazi” Mandi alimuomba Isabel

    “Naogopa! We nenda tu utanikuta apahapa” Isabel alijibu huku akichukua begi lake kwa Mandi lakini Mandi hakumpa, aliendelea kumlazimisha waende daraja la pili.

    “Ukunihakikishia usalama wangu nitakwenda” Isabel alikubali na wakaondoka na Mandi mpaka mabehewa ya mbele, Mandi hakukosea chumba kimoja kilikuwa tupu ndani yake kuna nafasi ya watu sita.

    “Tuingie hapa tupumzike” Mandi alitoa ombi kwa Isabel, ijapokuwa Isabel alikuwa na moyo mzito kwa hilo lakini hakuwa na jinsi alimuamini sana Mandi na kumuona kama Malaika mlinzi kumbe hakujua hila yake.

    “Sawa, hamna shida” Isabel aliingia chumbani na Mandi wakaketi, Mandi alijilaza kwenye kitanda cha chini na Isabel alikaa kimya kabisa upande wa pili. Mara kwa mara Mamdi alikuwa anachati kwenye simu na watu fulani hivi. “Tupo second sleeping class namba 32” Ton alipata meseji lutoka kwa Mandi, akatabasamu na kumpa simu Jomse kisha wote wawili wakaanza kuelekea huko

    “sasa tutafanyaje kuchukua lile begi?” Ton alimuuliza Jomse

    “unakuwa kama mtoto katika kazi! Makofi mawili tu si anatuachia hilo begi” Jomse alimjibu Ton huku wakiendelea na safari yao.



    Treni ya express kama wanavyopenda kuiita ilikuwa tayari ipo katika mwendo wa kasi, ikipiga honi nyingi kuomba watu na magari viachie njia kwa kuwa yenyewe haikuwa na vituo vingi kama ile ya Oldinary. Wengine alikuwa wamelala, wengine ndani ya behewa lenye hotel wakila hiki na kile, wengine wakicheza karata ilimradi tu safari iwe fupi. Ni mtu mmoja tu ndani ya treni hii aliyekuwa hajui mpaka hapo kama atafika salama au la, akiwa ameketi katika kitanda mara mlango ukagongwa na kitasa kilionekana kukunjwa kuelekea chini, mlango ukaachia bila ubishi Jomse na Ton wakajitoma ndani kisha wakafunga mlango nyuma yao. Isabel aliona sasa amekwisha, aliogopa kuona wanaume wote wale wanakuja pale ndani nay eye ni msichana peke yake, aliwakumbuka vijana wale ‘rafiki wa Mandi’ alijisemea moyoni. Mandi aliwakaribisha na baada yamazungumzo machache aliwaomba kama wangeweza kutoka ili wakamilishe kazi yao, wote waliafiki wakanyanyuka, Mandi akanyanyuka na begi akamwita Isabel waende wote.

    “Hapana mi siendi nyie nendeni, ila kaka Mandi niachie begi langu utanikuta apa hapa” ulikuwa mtihani mgumu kwa vijana hawa Jomse akambania jicho Mandi kuwa amuachie lile begi, Mandi akampatia, Isabel alishukuru sana kulipata begi lake kichwani akiwaza kuwa wakiondoka tu nay eye abadilishe behewa aliona kuwa atakuwa salama zaidi akiwa daraja la tatu kwa kuwa linakuwa na watu wengi. Alipohakikisha kuwa mlango umefungwa alitulia kama dakika kumi akiomba Mungu kisha akainuka akiwa na begi lake moja mgongoni na lingine mkononi alijiingiza mkono katika mfuko wa jeans aliyovaa na kuikuta ile bahasha ipo hakujua ndani ina nini alitamani kufungua lakini aliona si mahali pake kwa nza atafute sehemu ya usalama, aliusogelea mlango na kushika kitasa akakikunja alipouvuta mlango alikuta mlango haufunguki, umefungwa na funguo kwa nje. Isabeli alidondoka kwa kizunguzungu akiwa hajui afanye nini alijua kuwa vijana wale lao moja labda wanataka kumbaka, alilia kwa uchungu, hakuona la kufanya zaidi ya kujirusha dirishani ‘bora nife kuliko aibu ya kubakwa’ alichungulia nje kwa kutumia dirisha lile aliona jinsi kasi ya treni ile ilivo aliogopa kwani ni vumbi na upepo mkali vilisababisha na kasi ya treni ile, cheche za moto zilionekana katika giza lile kutokana na msuguano wa vyuma vya reli na vyuma vya



    magurudumu ya gari moshi hilo. Isabel alifumba macho mara mlango ukagongwa na kujaribu kufunguliwa lakini haukufunguka Isabel alishikwa na woga mkuu ila alijifariji kwa kuwa alijua kama wangekuwa wao wenyewe si wanajua uwa wameufunga wasingeutikisa, mara akasiki chokochoko za funguo na mlango ukafunguka. Isabel uso kwa uso na afisa polisi

    “Asante Mungu umesikia sala zangu” Isabel alibwabwaja bila kujielewa

    “wamenifungia, wanataka kunibaka” aliendelea kubwabwaja, polisi yule kijana alimuangalia Isabel kwa jicho la uchu akajikuta anamtamani hivyo hakuwa na budi kumsikiliza

    “Nani anayetaka kukubaka? Yuko wapi?” polisi yule alimsaili Isabel. Isabel alimueleza polisi yule hali yote ilivyo mpaka dakika hiyo na kumuelekeza jinsi walivyo na muonekano wao.

    “Ok! Unaitwa nani mrembo?” “Naitwa Isabel.”

    “Mi naitwa konstebo Kirama au niite ‘K’, Usihofu, upo kwenye mikono salama kabisa, hakuna wa kukudhuru” polisi yule alimpa matumaini Isabel.

    “chumba namba 32 afande ova” radio call iliita katika behewa la mwisho kabisa la treni hiyo. “nimekusoma afande ova”

    “Msaada wa haraka Ova”

    “read and clear, work in progress ova”

    Mazungumzo baina ya polisi hao kwa kutumia redio zao maalum yalimfariji sana Isabel, hapo aliona umuhimu wa kuwa na vituo vya polisi kila panapohitajika.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ************

    “Sasa kale kasichana kasitusumbue ni kukasachi na kuchukua mzigo,kwa nini tupoteze muda watu tuna mambo mengi!” Jomse aliwaaeleza wenzake

    “Mandi umekaa nae muda wote umeshindwa kumlaghai? Au ulitaka ubadili mawazo” Ton alimwambia Mandi kwa utani na Mamdi akaishia kucheka.

    “Ok vijana, tupo kwenye treni cha kufanya ni kuchukua mzigo na kuteremka lakini hii ngoma haisimami mpaka Tabora” Jomse aliendelea kuzungumza

    “Tufanye hivi, tujigawe mmoja aende kwenye engine, mwingine acheki usalama na mwingine akambane yule mrembo akijifanya jeuri ni kichapo hakuna huruma tena” Ton aliongeza “Mandi wewe uende kwenye engine hakikisha unamlazimisha operator apunguze mwendo ili tukipata mzigo wetu tutambae” Jomse alimteua Mandi kwa kazi hiyo maana alijua keshamzoea Isabel kwa hiyo hatoweza kufanya kazi ipasavyo.



    Mpango ulikamilika kila mtu akachukua idara yake, haikuwa kazi kwa Mandi kufika kwa operator. Mzee Kasimu, mzee wa makamo opareta wa treni za reli ya kati kwa miaka takribani ishirini, hakika alikuwa mzoefu wa kazi yake, alistuka kumuona kijana huyu mwenye ngozi maji ya kunde, mrefu kidogo mwenye umbo la kiume hasa.

    “Kijana vipi umepotea njia?”

    “Hapana baba, mimi ni mgeni wako, Mashine yako ipo kasi sana tunaomba upunguze mwendo”

    Mandi alimuamuru operetta

    “Unasema?! We unanifundisha kazi mimi? Mbona nyie vijana wa siku hizi hamna adabu nani kwanza kakuruhusu kuingia huku?” Mzee Kasimu alifoka

    “Shhhh, mzee usilete maneno mengi, mi sio mzaramo” Mandi alimtuliza huku akimuonesha mtutu



    wa bastola

    “Haya punguza mwendo” Mandi aliamuru. Mzee Kasimu tangu azaliwe hajawahi kuona bastola alianza kutetemeka kwa hofu. Alianza kugusagusa vitufe mbalimbali kwenye dash board yake na engine ikaanza kumtii.

    “unajua kijana, sisi tunakwenda kwa muda, sasa mimi sielewi kawa nini unataka nipuinguze mwendo” Mzee Kasimu alilalama

    “Nimesema punguza mwendo, sicheki na wewe hapa” Mandi alionesha ukali kidogo. Hali ilikuwa ngumu kwa mzee Kasimu kijasho kilimtoka hata alihisi suruali inalowana bila yeye kuwa na taarifa.



    Ton aliendelea kusavey karibu kabisa na behewa alimokuwa Isabel ili aone kama kuna dalili yoyote ya askari au hatari yoyote kabla hajamruhusu Jomse kuingia katika chumba hicho. Kwa mbali aliwaona askari wawili wenye silaha wakielekea upande ule kutokea behewa la nyuma. Ton alitulia kama mtu anayefikiri jambo Fulani, korido yote ilikuwa na watu wachache sana, waliofika kwenye ule mlango na kuutikisa kidogo ulionekana umefungwa wakapita na kuendelea mbele. Ton alituma meseji kwa Jomse kumpa taarifa, Jomse akafika na kuingia mara moja akamkuta Isabel peke yake amejilaza kitandani, akaingia kwa upole na kana kwamba anataka kuiba kitu Fulani, Isabel akashtuka

    “Usishtuke mrembo! Ni mimi, nahitaji unipe mzigo wangu” Jomse alimtamkia maneno hayo Isabel ambaye kwa wakati huo alikuwa amejikunyata kitandani.

    “Mzigo gani? Mi nna mzigo wenu nyie?” Isabel alijibu huku akilia. Kabla Jomse hajatulia alijikuta akipigwa double kick kwa nyuma iliyotaka kumtolea dirishani, Jomse aligeuka na kukutana na ngumi mbili za uso, damu zilimtoka mdomoni na kuanguka chini akiwa hoi, konstebo Kirama mtoto wa Arusha aliyepitisha utoto wake huko Mererani alimtuliza Jomse kwa kipigo cha sekunde kadhaa

    “Tulia! Hivyo hivyo. Mnataka nini kwa huyu msichana” Kirama alimuuliza Jomse ambae hakuonekana kutoa ushirikiano, Kirama alimuongezea kipigo akiwa pale chini, Jomse alibaki kutambaa kila alipotaka kunyanyuka alipigwa mateke ya mbavu mpaka akapoteza nguvu kabisa. Isabel alitumia mwanya huo kutoka ndani ya chumba kile alipofika mlangoni hamad! alikumbana na Ton, Ton alijaribu kumshika lakini Isabel alimuwahi kwa kumtandika na begi lenye laptop usoni, Ton alipoteza mtandao kwa sekunde kadhaa alipozinduka hakukuwa na Isabel.

    Bila kuangalia anakokimbilia Isabel alijikuta akitokea katika behewa la mizigo, akachagua sehemu na kujibanza kutokana na ufupi wake alitosha kujipachika katikati ya mabegi na masanduku, Isabel hakujua vijana wale wanataka nini kwake, alichukua ile bahasha mfukoni mwake na kuichana kitu kidogo cheusi kikadondoka kutokana na giza katika behewa lile alitumia simu yake kumulika akakipata, alikigeuzageuza kwa makini ‘memory card’, Isabel alitikisa kichwa kuashiria kuwa sasa ameelewa nini wanachomtakia lakini alijiuliza ‘kwa nini watumie nguvu zote kwa kidude hiki si wangenieleza tu ningewapa’ Isabel aliamua kurudi katika lile behewa ili akawakabidhi hiyo card hakuona haja ya kukimbizana kwa sababu hiyo, mwanzoni alijua labda wanataka laptop yake au kumbaka, alisonya na kuendelea kuelekea behewani, ikiwa punde tu afike alisikia sauti ya kitu kama bunduki kutoka katika chumba kile, Isabel alisimama na kurudi kwa kasi kule alikotoka.

    Mlio ule uliwaamsha watu wa vyumba vingine na wakatoka kuona nini kilichotokea “Huku,”

    “hapana ni huku” walisikika wakibishana wenyewe kwa wenyewe, korido yote ilijaa watu wa behewa lile wakikimbia huku nahuku hata wengine wakinusurika kutumbukia kwenye maungio yaliyopo kati ya behewa moja na lingine, kwa mtingo uo huo Ton na Jomse walitoka ndani ya chumba kile na kujichanganya na watu lakini wao bado walikuwa wakimtafuta Isabel kwa kuwa kiu yao bado ilikuwa haijaisha mpaka watapompata, hasira juu ya msichana huyu iliwatawala kila kona ya mwili wao, na katika kujichanganya huko kila mmoja alienda upande wake kuendelea kumtafuta Isabel.



    Polisi walifika chumba namba 32 na kusukuma mlango taratibu huku mitutu ya SMG zao ikitangulia kabla yao ndani ya chumba kile, mlango ulikubali kufunguka taratibu na polisi wale



    walijitoma ndani kwa tahadhari kubwa.

    Mwili wa afande Kirama ulibaki umelala kati ya vitanda vile ukiwa ndani sare yake nadhifu ya kipolisi ukivuja damu nyingi katika ubavu wa kushoto, risasi iliharibu vibaya ubavu wa afande Kirama. Afande Benso alipiga goti moja chini huku akiweka vizuri bunduki yake mgongoni, machozi yakimlengalenga aliusogelea mwili wa afande Kirama na kuugusa shingoni na moyoni kuona kama kuna dalili ya uhai, alipougusa aligundua bado mwili huo una joto

    “machela haraka!” aliwaeleza wenzake na mara moja wakawasiliana na wengine. Dakika chache machela ilikuwa tayari imefika wakauweka mwili wa afande Kirama na kurudi nao behewa la mwisho kwa huduma ya kwanza kabla hawajaufikisa hospitalini. Watu walibaki wakiangalia yote yaliyojiri walipohojiwa na polisi juu ya tukio lile nini wanachojua walijibu tu “hatujui kitu, tumesikia mlio huo tukaanza kukimbia” lakini mioyo yao ilisema ‘sitaki ushahidi’ . wananchi katika treni ile walishindwa kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi kama kawaida ya watanzania wengi. “Jamani maelezo haya tunayohitaji yatasaidia kumpata muhalifu, sasa nyie hamtaki kutuambia kitu sasa mlitoka vyumbani kufanya nini!” afande Benso aling’aka kwa hasira na kuendeleaCHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Maisha ya mtanzania yashapotea, tunahitaji kumpata muuaji na yupo umuhumu miongoni mwenu” Watu waliokuwepo eneo lile wakatawanyika mmojammoja na kurudi vyumbani mwao, afande Benso kwa kushirikiana na polisi wengine wakafunga ule mlamgo wa namba 32 kwa utepe maalum wa njano ulioashiria hilo ni eneo la hatari liko chini ya uchunguzi wa kipolisi.

    Treni iliendelea na safari yake kwa mwendo wa kasi, watu wengine katika mabehewa mengine hawakujua hata ni kitu gani kimetokea, waliendelea na mazungumzo na kuangalia luninga zililiwapa burudani murua ya muziki wa DRC Congo.

    “Kituo cha polisi kati Tabora, tukusaidie nini” simu ilipokelewa upande wa pili huku Tabora “Koplo Kibona naripoti kutoka ndani ya treni ya reli ya kati inayotoka Kigoma kwenda Dar es salaam” Koplo Kibona alikuwa hewani akitoa taarifa ya tukio

    “Tumekusoma afande… endelea” sauti ilijibu

    “Afande Kirama amepigwa risasi na watu wasiojulikana, na watu hao tunahisi bado wapo humu ndani ya treni, hali ya afande ni mbaya tunaomba msaada wa haraka” Koplo Kibona alimaliza “Copy” sauti ilijibu na simu ikakatika.

    Koplo Kibona na afande Benso walijaribu kutafuta mawasiliano na opereta wa treni hiyo lakini simu ilikuwa inaita tu na haipokelewi. Wakaamua kwenda huko kuona kuna nini kimetokea.



    Msako mkali ulianza ndani ya treni hiyo behewa moja baada ya jingine ili kuweza kuwakamata waliofanya unyama ule, wale wote waliofanania na unyama huo walichukuliwa kwenye behewa moja na kupewa vitisho ili waseme ni nani aliyehusika. Polisi walipojaribu kupitia orodha ya wasafiri ilionekana chumba namba 32 hakikuwa na abiria aliyetumia, hivyo ilikuwa ngumu kwao kugundua ni nani alikuwa ndani humo. Vitisho vya hapa na pale, kuwafinya kidogo waliwakamata haikusaidia kitu. Ton alikaribia behewa la mizigo ambamo Isabel alijificha humo, alitembea taratibu na kwa hadhari kubwa huku akiangalia huku na kule, akapita behewa la kwanza mpaka la pili, kwa mbali aliona polisi wakija upande huo, akajibaza nyuma ya mlango kwa utulivu wa hali ya juu sana, polisi wale walipita wakiwa wanaongeea habari ile.

    Isabel kutoka pale alipojibanza aliona polisi wale walipokuwa wakija roho yake ilitamani atoke ili awape habari ile na ile memory card lakini roho nyingine ilikataa kabisa asifanye hilo ila aikabidhi katika mikono salama. Aliumiza kichwa sana kutafakari kwa nini watu wale waitafute memory card ile kwa nguvu zote, Isabel alikosa jibu alichofikiri ni kuwa treni ikisimama tu awahi kushuka na atoroke nayo ili ajue kuna nini ndani yake.

    SIKU CHACHE ZILIZOPITA

    Bujumbura Burundi

    Gari aina ya Ramborghin iliingia kwa mwendo wa taratibu katika eneo la maegesho la Motel du Afrique, mwanamama mrefu, mwembaba aliyevalia nadhifu suti yake ya bluu bahari, mawani myeusi na kofia kubwa ya kiingereza ya rangi ya bluu bahari aliteremka taratibu kwa madaha huku akitoa tabasamu lenye bashasha, mlango wa upande wa pili alishuka kijana nadhifu akiwa ndani ya



    suti nyeusi kichwani hakuwa na nywele hata kidogo alitembea polepole akimfuata mama yule kwa nyuma, alionekana kama ni mlinzi wa mwanamama huyo. Mwanamama yule ambaye tabasamu lake halikujificha muda wote, alipanda ngazi taratibu kabisa na akasimama kama sekunde tano hivi mtu mwingine mwenye asili ya kizungu lakini alionekana amekaa sana Africa kutokana na rangi ya ngozi yake alifika kwa mwanamama yule na kumpa mkono kama ishara ya kusalimiana kisha akamkaribisha ndani ya motel hile ya kifahari. Wakiwa katika meza ya duara mwanamama yule alikutana na watu kama wanne hivi na baada ya kutambulishana mmoja kwa mwingine mzungumzo yaliendelea.

    “Yeah! Ni kazi ngumu kidogo lazima ikamilike ili tupate tunachotaka” mwanamama yule alilieleza jopo lile, baada ya kupumzika kidogo na kunywa maji akaendelea

    “Au mnaona tutashindwa? Mbona mwaka ule tuliweza hapa Burundi na Rwanda, na sasa huko Uganda kaskazini kazi inaenda vizuri, kwa nini tushindwe hapa jirani, wamezubaa, wamelala” alimaliza

    “Ni kweli madam, lakini kumbuka nchi hile haiingiliki kama tunavyofikiri, kila nikijaribu kufikiri tutawezaje na kutana na vikwazo vingi” mwanaume mmoja aliongea kwa hisia

    “Security yao ipo makini sana, na isitoshe wananchi wake ni wazalendo mno, kwa hiyo tuna kazi ngumu sana mbele yetu” mjumbe mwingine alitia chumvi

    “Sasa kama tunaanza kuweka mashaka, tutaweza?” yule mzungu aliuliza

    “Wakubwa wametuma kazi na sisi tumekubali, pesa nyingi inatumika, tufanyeje?” aliuliza tena yule mzungu

    “Acheni waoga nyie wanaume. Mkutano wetu ulopita tuliona watu wa kuwafanyia kazi kwanza, ambao wao wanaweza kuwa kikwazo kwenye mpango wetu ‘Mpango hasi’ kama walivyouita, si ndiyo jamani, tukawasiliana na watu wetu waktuambia nani na nani, sasa kazi ya kwanza nikuwafutilia mbali, iwe kwa sumu, au kwa ajali, au kwa vyovyote vile ndani ya miezi sita plan A ikamilike” mwanamama yule alifoka

    Akaingiza mkono kwenye pochi yake na kutoa flash akampa yule mzungu ambaye aliingiza kwenye laptop yake ndogo na kukopi mafaili fulanifulani kisha akamrudishia. Kikao kiliendelea kwa ufupi sana na baada ya hapo wote walitawanyika kila mtu katika njia yake. Mwanamama yule alitoka ndani ya Motel ile kama kawaida akasindikizwa na kijana wake yule mkakamavu ambao muda wote alikuwa amesimama pale kwenye ngazi, aliingia kwenye gari ile na kuondoka kwa kasi kuelekea kusikojulikana.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    **************

    ITAENDELEA



0 comments:

Post a Comment

Blog