Simulizi : Kikosi Cha Kisasi
Sehemu Ya Tano (5)
"Bwana Chitalu, sijui kama una habari kuwa mfanyakazi wetu mmoja aliyekuwa anafanyakazi hapo mapokezi aitwaye Mwadi ameuawa?" Meneja aliuliza.
Willy alionyesha sura ya kushtuka sana na kushangaa kiasi kwamba hata polisi walidanganyika.
"Sina habari", alijibu taratibu kabisa.
"Basi hawa mabwana wana maswali machache ya kukuuliza. Usiwe na wasiwasi kwani wapangaji wetu wote inabidi waulizwe. Wewe mwenyewe unajua wakati kitendo kama hiki kikitokea lazima mambo kama haya yatokee". Meneja alijaribu kumtuliza.
"Hamna taabu", alijibu Willy kwa unyonge.
Polisi mmoja alitoa daftari tayari kwa kuandika malezo na mwingine akajitayarisha kwa kuuliza.
"Bwana Chitalu kama alivyokueleza Meneja, maswali yetu ni jambo la kawaida tatizo kama hili linapotokea, hivi unaombwa kueleza ukweli mtupu", yule polisi alimweleza.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
""Hamna wasiwasi", Willy alijibu.
"Bwana Chitalu umefika hapa mjini lini?" Polisi aliuliza.
"Jumatatu", alijibu Willy.
"Ni mara yako ya ngapi kufika mjini Kinshasa?"
"Mara ya tatu", alijibu Willy.
"Huyu msichana Mwadi ulikuwa unamfahamu?"
"Ndiyo", alijibu Willy.
"Kwa muda gani umemfahamu?"
"Toka Jumatatu", alijibu.
"Je mmewahi kuwa na uhusiano wowote toka siku hiyo?"
"Ndiyo", alijibu Willy.
"Uhusiano wa namna gani?"
"Uhusiano wa kawaida tu wa mwanamke na mwanaume", alijibu Willy.
"Je, umewahi kufika kwake ama kwenda naye mahali popote?"
"Ndiyo", alijibu Willy.
"Lini na wapi mlitembelea?"
"Juzi usiku na tulitembelea Parafifi baa", Willy alijibu.
"Je jana jioni mlionana?"
"Hapana", Willy alijibu.
"Unaweza kutueleza jana kiasi cha saa kumi na moja jioni mpaka leo asubuhi ulikuwa wapi?"
"Nilikuwa nimekaribishwa mahali", alijibu.
"Mahali gani?"
"Kwa msichana mmoja," alijibu.
"Unaweza kututajia jina la huyo msichana?" Willy alisita kidogo kisha akasema, "Anaitwa Ntumba Akanda".
"Anakaa wapi?"
"Anakaa huko Matonge barabara ya Inzia nyumba nambari 26B ", Willy alijibu.
"Anafanya kazi?"
"Ndiyo."
"Wapi?"
"STK uwanja wa ndege", alijibu Willy.
"Una maana jioni yote ulikuwa huko na hukuondoka hata mara moja mpaka asubuhi?"
"Ndiyo", alijibu Willy.
"Una lolote unaloweza kutueleza juu ya mauaji ya Mwadi?"
"Nimesikitika sana", alijibu Willy.
Yule polisi aliyekuwa anauliza maswali alimwangalia mwenzake na mwenzake naye akaonekana kuwa hakuwa na swali zaidi.
"Asante sana bwana Chitalu. Tunalokuomba ni kwamba usiondoke hapa mjini bila kupasha habari kituo cha polisi cha 'Brigede Mobile'. Vile vile tunakuomba usihame kutoka hoteli hapa mpaka sisi tuwe tumepata habari", yule polisi alimweleza.
"Hamna wasiwasi", Willy alijibu.
"Unaweza kwenda".
"Asanteni sana," aliaga Willy na kutoka nje.
Wale polisi walichukua simu na kupiga moja kwa moja STK uwanja wa ndege. Walimuulizia Ntumba na walipompata walimuuliza kama alikuwa anamfahamu Willy Chitalu. Baada ya mazungumzo marefu aliwathibitishia kuwa alikuwa na Willy tokea saa kumi na moja jioni mpaka asubuhi. Waliridhika wakaondoka.
Willy alipoondoka ndani ya ofisi ya meneja aliitwa na kijana aliyekuwa mapokezi.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Kuna msichana mmoja anaitwa Tete amekupigia simu zaidi ya mara nne, anasema umpigie," yule kijana alimweleza. Willy alimpa simu ya Tete na kumwambia. "Ukimpata niletee simu chumbani kwangu", Willy alipoingia chumbani kwake alikuta chumba chake kimepekuliwa kwa ustadi sana kiasi cha kwamba mtu wa kawaida asingeweza kujua. Aliangalia vitu vyake akakuta vyote salama. Yeye naye akakipekua kile chumba kuona kama wangeweza kuwa wameacha chombo chochote cha kunasa sauti hakukuta kitu. Mara kengere ya simu iliita.
"Hallo", Willy aliita.
"Zungumza na Tete", yule kijana wa mapokezi alimwambia.
"Hallo, Willy hapa".
"Tete, habari yako?" Tete alijibu kwa sauti ya chini sana.
"Nzuri, je wewe?" Willy aliuliza.
"Bado moyo wangu mzito sana kwa ajili ya kifo cha Mwadi," Willy alijibu.
"Tafadhali sana tuonane saa sita. Sasa hivi ni saa sita kasoro dakika ishirini, tafadhali fanya kila njia tuonane nina jambo la lazima," Tete alisema kwa sauti ya wasiwasi.
"Wapi?" Willy aliuliza.
"Mahali popote utakapoona pana usalama hata kama ni hapo hotelini kwako", Tete alijibu.
Willy alifikiria nini msichana huyu alikuwa anamtakia lakini, hakupata jibu. Alifikiria huenda akina Muteba walikuwa wamemuwekea mtego lakini akaamua ajaribu bahati yake. Hata yeye alikuwa na haja ya kuzungumza na msichana huyu lakini si kwa namna hii.
"Fanya hivi, ukitoka njoo na gari lako moja kwa moja na barabara ya 30 Juin halafu ingia kwenye maegesho ya Banque Comerciale Zairose, mimi nitakukuta hapo, sawa?" Willy alieleza.
"Sawa, saa sita", alijibu Tete.
"Saa sita", alijibu Willy huku Tete akiwa tayari ameisha kata simu. Baada ya kuweka simu chini, Willy alibadilisha nguo zake haraka haraka, halafu akatelemka chini mbio mbio. Aliingia ndani ya gari lake, akaondoka kuelekea kwenye ofisi za Agence Sozidime. Willy aliposimamisha gari lake katikati ya magari yaliyokuwa kwenye maegesho ya Cine Rac ilikuwa saa sita kasoro dakika tano.
Alitoka ndani ya gari na kuelekea upande mwingine wa barabara ambapo alibana kwenye sehemu ambapo alikuwa anaona moja kwa moja ndani ya lango la ofisi za Sozidime. Hakuwa hata hajajibanza vizuri alipomuona Tete akiwa anatoka ndani, akaingia ndani ya gari lake, akawasha moto na kuondoka. Mlinzi wa pale alimfungulia lango na gari la Tete likapita.
Willy alisubiri kuona kama kulikuwa na gari lolote linamfuata Tete. Lakini hakuona dalili. Alikimbia mpaka kwenye gari lake na kuondoka kwa mwendo mkali alimfuata Tete. Ni kwenye barabara ya 30 Juin alipomuona, alimfuata pole pole mpaka walipofika B.C.Z. Tete akaingia kwenye maegesho ya pale kama Willy alivyokuwa ameagiza. Willy huku akiwa amehakikisha kuwa hakukuwa na mtu aliyekuwa anawafuata naye aliingia kwenye maegesho ya B.C.Z. akafunga gari lake akafuata pale Tete alipokuwa ameegesha. Alipofika kwenye gari la Tete alimwambia.
"Sogea huko, mimi nitaendesha," Tete alisogea kwenye kiti cha abiria, Willy aliingia kwenye kiti cha dereva akawasha gari moto, wakaondoka.
"Mbona umeacha gari lako?" Tete alimuuliza.
"Napenda sana kuendesha gari aina ya sports", alitania Willy.
"Tunakwenda wapi sasa?" Tete aliuliza.
"Mahali penye usalama kama ulivyokuwa umesema", Willy alijibu. Willy alikuwa amekata shauri kuwa, mahali penye usalama pa kuweza kuzungumza na Tete palikuwa nyumbani kwa Robert tu, potelea mbali kama angegundua maficho yao, lakini alitumaini ya kwamba lilikuwa ni jambo la busara.
Walifika nyumbani kwa Robert na kukuta hakuna mtu. Willy alifungua gereji na kulificha gari la Tete ndani kwani alitegemea gari la msichana kama Tete lazima lingekuwa linafahamika mjini. Alimkaribisha ndani, akatayarisha kinywaji kwa ajili yao wote.
"Hapa ni nyumbani kwa nani?" Tete aliuliza.
"Kwa rafiki yangu" Willy alijibu.
"Mbona jana hukurudi nyumbani kwangu kama ulivyoahidi?" Tete aliuliza.
"Shughuli zilinizidi", Willy alijibu.
"Kwanza nataka kutoa shukrani zangu kwa kumlipizia rafiki yangu Mwadi kisasi", alisema Tete.
"Umejuaje kama nililipiza?" Willy aliuliza.
"Si uliniambia kuwa ungelipiza, na nikapata habari toka kwa Muteba kuwa Kabeya ameuawa hivi nikajua umelipiza," Tete alijibu.
"Muteba alikueleza saa ngapi?" Willy aliuliza.
"Alikuja nyumbani kwangu kiasi cha saa kumi za asubuhi. Kwanza tuache hayo tafadhali Willy nataka unieleze bila kunificha chochote wewe ni nani na uko hapa Kinshasa kwa ajili gani, halafu na mimi nitakueleza mambo ambayo ninaamini yatakuwa na manufaa kwako. Mpaka sasa hivi ninauza maisha yangu kwa ajili yako, tafadhali usinifiche", Tete alisema.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Kwanini ujitolee kuuza maisha yako kwa ajili yangu?" Willy alimuuliza.
"Kwa sababu ile ile ambayo ilimfanya Mwadi auze maisha yake kwa ajili yako. Mwadi alikuwa rafiki yangu mpenzi sana, hivi niko tayari kuendeleza chochote alichoacha bila kumaliza," Tete alieleza.
"Mimi nitakuamini namna gani kukueleza mambo hayo unayotaka kuyajua?" Aliuliza Willy.
"Nafikiri itabidi uniamini au kama huniamini ubahatishe kuniamini, maana nadhani kama nilivyokueleza kuwa nina habari zinazoweza kuwa na manufaa," Tete alijibu.
"Wewe unaaminije kuwa niliyokueleza ni ya kweli?" Willy aliuliza.
"Mimi ninaamini lazima mtu kama wewe si wa kusema uongo," alijibu Tete.
Willy aliamua kujitosa na kumweleza msichana huyu kila kitu na ikiwa kama alikuwa ametumiwa kuja kumdadisi, hayo yalikuwa mambo ya kawaida katika kazi hivi angeweza kuyakabiri bila taabu.
"Nimeridhika Tete, hivi nitakueleza kwa kirefu. Mimi jina langu hasa ninaitwa Willy Gamba na kazi yangu mimi ni mpelelezi." Willy alimweleza. Tete alimwangalia kwa macho makavu bila kuonyesha mshangao wowote. Akiwa anavutwa na uzuri na ukali wa macho ya msichana huyu. Willy alimweleza kwa ufasaha kabisa mambo yaliyokuwa yamemleta hapa pamoja na wenzake na mambo yote waliyokuwa wameyafanya mpaka wakati huo. "Ulitaka kujua sasa umeshajua, nimekueleza kila kitu sikuacha kitu," Willy alimalizia.
"Sasa nimeelewa, nimeelewa kabisa kwanini mambo yako namna ile ofisini kwetu. Nilikuwa naona mambo mengi ya ajabu ajabu lakini sikuwa ninajua yana maana gani. Umenifumbua macho, nimekuwa kama kipofu ambaye amefumbuliwa macho. Wamekuwa wananitumia kwa mambo mengi bila mimi kujua," alieleza Tete akiwa kama anazungumza ndotoni.
"Uliniambia kuwa ungenieleza mambo ambayo yangekuwa na manufaa kwangu, nieleze".
"Mambo mengi umeshayaelewa kutokana na ulivyonieleza. Ni kweli kabisa kuwa Kampuni yetu inashughulika na mambo ya kijasusi sasa nimeona kwanini mambo yako hivyo. Mkurugenzi wetu anaitwa Fernand Barbier anajiita kuwa ni Mbelgiji lakini ni kaburu. Huyu Mkurugenzi wa 'Gereji Du Peuple', Pierre Simonard naye si Mbelgiji ni kaburu hata Jean Vergeance. Mambo haya niliwahi kuelezwa na Muteba siku moja wakati mapenzi yetu yalipokuwa moto sana. Nilimuuliza hawa wazungu alifahamiana fahamiana nao namna gani akanieleza kuwa alikuwa ameonana nao huku Afrika Kusini alipokwenda huko na askari wa kukodiwa baada ya kupigana na askari hao upande wa majeshi ya Tshombe huko jimbo la Shaba", Tete alinyamaza kidogo kuvuta pumzi kisha akaendelea.
"Nilipomuuliza kwa nini wanajiita kuwa ni Wabelgiji, alisema kuwa ingekuwa vigumu kwa makaburu kufanya biashara katika nchi huru ya Kiafrika kufuatana na siasa ya nchi za Kiafrika. Hii ndiyo alitoa kama sababu kwa nini watu hawa walikuwa wanatumia uraia wa bandia. Yule Maximilian leo uliyekuja kumuona, naye si Mbelgiji bali ni Mfaransa. Mpaka sasa nashindwa kujua kwa nini anatumia uraia bandia, Kwani Wafaransa hawakataliwi katika Afrika na wako chungu nzima hapa Zaire kwa shughuli mbali mbali", Tete alitua tena kuvuta pumzi kisha akaendelea.
"Huyu Max kama tunavyomuita aliwahi kunieleza mwenyewe akijitapa mbele yangu kuwa si Mbelgiji bali ni Mfaransa kamili." Tete alimwangalia machoni Willy, akasita kidogo kama kama kwamba anaona haya kueleza alichotaka kueleza, kisha akaangalia sehemu nyingine akaendelea. "Max ananipenda sana mimi, amekuwa ananitongoza kwa muda mrefu sana. Anamchukia sana Muteba kwa ajili yangu mimi. Katika kutaka kujionyesha alivyo na thamani kuliko Muteba na hawa watu wengine, amekuwa ananieleza mambo mengi sana. Anasema amewahi kuwa Meneja katika jeshi la Ufaransa kabla hajaweza kupewa kazi mbali mbali katika nchi mbali mbali zenye uhusiano na Ufaransa. Wakati fulani Fernand alikwenda Ulaya kwa likizo yeye akabaki ndiye Mkuu wa ofisi yetu. Siku moja Lucie alikuwa anaumwa mimi nikawa nafanya kazi ofisini kwake ilipofika saa za kufunga ofisi aliniambia nisiondoke kuna kazi. Wafanyakazi wengine wote waliondoka tukabaki mimi na yeye tu. Kisha akafunga milango ya kutokea nje ya ofisi akanijia nimfuate." Tete alitabasamu kidogo kisha akaendelea.
"Nilimfuata ingawaje kwa woga sana lakini nilitaka nijue nini nia yake. Tulienda mpaka kwenye ofisi ya Fernand akafungua tukaingia ndani akafunga. Akiwa sasa amenishika mkono tulienda mpaka kwenye ukuta ambao ulikuwa nyuma ya meza ya Fernand. Alinieleza kuwa nisiogope kwani alitaka kunionyesha milango inayoenda kwenye chumba cha siri ambako ndiko tungeweza kufanya mazungumzo yetu. Alienda kwenye pembe ya ukuta wa nyuma kulikuwa na kidude akakibonyeza mara ukuta ukaachana na kuwepo na mlango. Kumbe ukuta huo ulikuwa wa bandia ulikuwa wa mbao. Chini ya mlango kulikuwa na ngazi zinatelemka chini, aliwasha taa za kwenye ndazi hizi, na tulipokuwa kwenye uchochoro wa ngazi hizi za kutelemka chini alibonyeza kidude kingine, ukuta ule ukarudi sawa sawa. Tulitelemka chini tukakuta mlango akaufungua tukaingia ndani ya chumba kimoja kizuri ajabu, kilikuwa na kila kitu. Kitanda kikubwa, makochi mazuri, barafu, jiko la umeme, kusema kweli chumba hiki kilikuwa na kila kitu mtu anaweza kuhitaji. Vile vile mlikuwa na makabati mawili makubwa ya chuma. Max alinionya kabisa kuwa nisimweleze mtu yeyote juu ya chumba hiki na akasema ni yeye na Fernand tuu waliokuwa wanajua juu ya chumba hiki na kwamba mimi ndiye nilikuwa mtu wa tatu," Tete alimwangalia Willy, kisha akaendelea. "Kusema kweli Willy sijawahi kumwambia mtu ila ni wewe leo. Nilipomuuliza kwa nini iliwabidi wawe na nyumba ya namna hii, alijibu kuwa kwa ajili ya usala wao yakitokea machafuko, kwani Zaire ni nchi yenye machafuko mara kwa mara.
Nilimuuliza chumba kama hiki kilikuwa na usalama gani. Akaniambia kuwa nyumba hii ilikuwa ya Jenerali mmoja wa jeshi la Kibelgiji ambaye alijijengea kwa usalama wake wakati wa msukosuko. Alisema Jenereli huyo alikuwa amekitengenezea chumba hiki mlango ambao ulikuwa unatokea sehemu nyingine kabisa. Alienda kwenye sehemu nyingine ya ukuta akabonyeza kidude kama kile alichokuwa amebonyeza ofisini kwa Fernand mara ukuta ukaachana na nikajikuta naangalia ndani ya uchochoro wenye giza kubwa. Akaniambia kuwa uchochoro huu ulikuwa unatokea nyuma ya lile jumba refu liitwalo' Galleries Presidentielles', na kulikuwa na taa ndani ya uchochoro huu. Max alinieleza yote haya ili niweze kumtia maana kusudi niweze kumtimizia haja zake. Wanaume wana matatizo sana," Tete alinyamaza na kumwangalia Willy, lakini Willy aliendelea kumwangalia katika hali ile ile, "Sasa leo ndiyo nimejua kwa nini Sozidime ina ofisi za namna ile. Nimekubaliana kabisa Willy, ile ni ofisi ya majasusi ndiyo sababu iko vile", Tete aliendelea.
Maelezo yote haya yalimwingia Willy kama nyali za moto. Alijiona mtu mwenye bahati sana katika safari hii kwani alikuwa ameweza kupata habari za muhimu sana bila matatizo makubwa. "Je umewahi kwenda kuona pale kwenye uchochoro huo unapotokea?" Willy aliuliza.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Kwa bahati nimewahi. Nilitaka kuhakikisha kama maneno ya Max ni kweli kwani mimi sikuamini kama kungeweza kujengwa njia ya chini kwa chini mpaka mahali pale aliposema. Hivyo siku moja nilimtania na kumwambia kuwa alikuwa ni mwongo, ilikuwa haiwezekani kuwa na njia ya namna hiyo. Kwa vile alikuwa hataki kuniacha hata mara moja alinipeleka pale mahali na kunithibitishia kwa hivi ninapafahamu. Pamefunikwa na mfuniko kama ule unaofunika mashimo ya vyoo, lakini unaingia sawa sawa pale kwenye shimo la mlango na kufungwa kwa funguo," Tete alijibu.
"Kwa hiyo na mimi utanionyesha hapo mahali?" Willy aliuliza.
"Bila wasiwasi", Tete alijibu.
"Endelea na maelezo yako", Willy alimwambia.
"Sasa tukiacha hayo mambo ya zamani, nataka kukueleza kuwa wao wameishagundua kuwa wewe si willy Chitalu bali Willy Gamba mpelelezi hatari sana," Tete alieleza.
"Wamejuaje?" Willy aliuliza.
"Zilikuja habari kwa telex, kutoka kwa hao wateja wao leo asubuhi zilizokuwa zinakuelezea wewe. Nilizipokea mimi lakini kama kawaida huwa zinafumbwa fumbwa zikiwa zinazungumzia mambo ya spea. lakini nilieleza kwa sababu niliona majina yako yote kwenye hiyo Telex. Nilipompelekea karatasi hiyo Max, alinieleza ya kwamba wewe ulikuwa mtu hatari sana katika mambo ya biashara na akanishukuru sana kwa kuweza kukufahamisha kwake", Tete alijibu.
"Ahaa," aliitikia Willy.
"Kisa hasa kilichonifanya nikate shauri kukuona na kuzungumza na wewe kinatokana na maneno aliyonieleza alipokuja leo asubuhi nyumbani kwangu. Muteba huwa haji kwangu wakati wa saa kama zile ila anapokuwa anakerwa na kitu.
Alikuja akionekana amechoka kabisa na akiwa amepoteza hata rangi ya sura yake. Aliniambia kuwa umemuua Kabeya na Charles na kwamba ulikuwa umelipua magereji yao yote isipokuwa gereji la Pierre. Alikulaani vikali sana na akaniapia kwamba lazima atakuua. Alinieleza pia kuwa Mwadi aliuawa na Kabeya sababu za kuficha siri zako na akanionya kuwa kama mimi ninajua kitu chochote juu yako ni afadhali niseme, maana kweli toka tufahamiane na Muteba sijamwona katika hali ile, na niliogopa hata kumuuliza swali lolote. Alilala kwa muda wa saa moja tu akaamka na kuondoka na kuaniambia tuonane naye mchana.
Maelezo haya yalinifanya nifikiri vitu viwili, cha kwanza wewe si mfanyabiashara kama ulivyosema, na pili kuwa Muteba naye alikuwa si mfanyabiashara tu kama alivyokuwa anafahamika ila alikuwa amejiingiza katika jambo fulani la kijambazi na wale wazungu na ndiyo sababu alikuwa katika hali aliyokuwamo. Tokea asubuhi nilikuwa nafikiria niwe upande upi, na baada ya kufikiria sana nikaona ikiwa Mwadi alikuwa anakufichia siri yako na kujitolea kufa basi wewe hukuwa mtu mbaya, Maana Mwadi ninamfahamu sana alikuwa msichana aliyejisitahi sana na hakuwa na uhusiano na watu hovyo hovyo. Hata mimi aliwahi kunionya juu ya urafiki wangu na Muteba, kwani alisema Muteba hakuwa anatembea na kundi zuri. Hivyo nikaona nikuone ili niweze kuwa na msimamo," Tete alimalizia na kuvuta pumzi ndefu.
"Sasa umepata msimamo?"Willy alimuuliza.
"Ndiyo, nina msimamo kamili tokea sasa mimi niko upande wako. Nitaanzia pale marehemu rafiki yangu alipoachia", alijibu Tete huku machozi yanamtoka.
Willy aliyekuwa amekaa karibu naye alimsogelea akatoa kitambaa akaanza kumfuta machozi. Tete alipitisha mikono yake mabegani kwa Willy na wakaanza kupeana busu moto moto, "Kazi na dawa", Willy alibwabwata.
Ilikuwa saa nne unusu juu ya alama Willy aliposimamisha gari lake mbele ya ofisi za O.A.U. Robert naye alikuwa tayari ameishatelemka pale chini, alipomuona Willy anaegesha gari alimfuata.
"Ingia twende", Willy alimwambia.
"Gari langu niliache?" Robert aliuliza.
"Liache", Willy alimjibu. Robert aliingia ndani ya gari wakaondoka.
"Vipi umeweza kufaulu kumuona Kadima?" Willy aliuliza.
"Ndiyo nimefanikiwa", Robert alijibu.
"Sasa twende tubane mahali pale Wizarani kwao tumsubiri, akitelemka tu, tumteke nyara, ili tukamuulize vizuri," Willy alishauri.
"Lakini pale Wizarani pana watu wengi, kumteka nyara patakuwa na kazi," Robert alieleza.
"Si kitu tutafanya kila mbinu hata ikibidi tufanye ghasia ili tumchukue tutafanya," Willy alijibu.
"Vipi mambo yako, yameenda namna gani?" Robert alimuuliza.
Willy alimweleza mambo yote yaliyotokea tangu alipofika Hoteli Memling na vile vile akamweleza juu ya mazungumzo yake na Tete. Alieleza yote haya wakiwa wameegesha gari lao kwenye nafasi ambayo walikuwa wanauona mlango wa mbele wa Wizara ya mambo ya nchi za nje, na kuhakikisha kuwa kila mtu aliyetoka ndani wanamuona.
"Msichana huyu ameenda ofisini kwake lakini atakuja huko nyumbani kwako baada tu ya kutoka kazini," Willy alimalizia kueleza.
"Hii sasa imeleta picha yote ya mambo ilivyo. Ninaweza kusema bila kusita kuwa huyu Maximillian ni jasusi wa Shirika la Ujasusi la Ufaransa 'SCEPE' maana SCEPE, BOSS na CIA zinafanya kazi zao kwa pamoja katika Afrika. Mimi kila siku nasema ningekuwa rais wa nchi yoyote huru ya Afrika lazima ningepiga kelele nchi za Afrika zisiwe na uhusiano wowote na Ufaransa." Alisisitiza Robert.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Siasa ni kitu kingine, utakuta Mkuu wa nchi hii ana sababu zake za kuhusiana na nchi fulani na Mkuu wa nchi nyingine ana sababu zake za kuhusiana na nchi nyingine ili mradi kila mtu apate maslahi yake. Umasikini wa nchi za kiafrika ndio tatizo kubwa linalozifanya zisiwe na msimamo thabiti wa kisiasa." Willy alieleza. Ilikuwa imeishatimia saa tisa na nusu lakini Kadima alikuwa bado hajatokea. Watu walikuwa wanatoka lakini Kadima alikuwa hajatokea.
"Vipi huyu mtu hakuja nini?" Willy aliuliza.
"Habari nilizopata na ni za uhakika ni kwamba yupo ndani ya mkutano. Huenda mkutano haujaisha", Robert alijibu.
Mara watu wawili walitokea wakiwa wamebeba mikoba yao. "Huyo wa upande wa kushoto ndiye Kadima," Robert alimweleza Willy.
"Twende," Willy alimweleza Robert. Walitelemka kama watu wa kawaida tu, wakaelekea kwenye maegesho ya magari hapo Wizarani huku wanajifanya kama kwamba wana mazungumzo kati yao. Kadima alisimama akizungumza na yule mwenzie. Willy na Robert nao walisimama.
"Nenda ukalete gari sehemu hii. Atakapomaliza mazungumzo yake mimi nitamfuata." Willy alimweleza Robert.
Kadima aliagana na yule mwenzake na kila mtu akaelekea kwenye gari lake. Willy alimkatisha na kuonana naye kabla hajafika kwenye gari lake.
"Bwana Kadima nafikiri," Willy alimsemesha.
"Ndiyo kijana nikusaidie nini?" Kadima alijibu baada ya kumwangalia Willy na kumuona kijana muungawana kabisa.
"Ningependa kuzungumza nawe kidogo", alisema Willy na wakati ule ule Robert akasimamisha gari pembeni mwao. Willy alitoa bastola yake alikokuwa ameificha na akamwamrisha Kadima. "Ingia ndani ya gari na usipige kelele kwa usalama wako."
Kadima ambaye tokea azaliwe alikuwa hajawahi kuonyeshwa bastola au silaha ya aina yoyote alikuwa karibia azimie. Bila kusema neno aliingia ndani ya gari na Willy akaingia pembeni mwake Robert akaondoa gari. Waliondoka naye moja kwa moja mpaka nyumbani kwa Robert. Njiani kila mtu alikuwa kimya. Kadima ambaye mawazo yake yalikuwa yakizunguka huku na kule ili kujua kwa nini ametekwa alikaa amezubaa kabisa. Walipofika nyumbani kwa Robert walimteremsha na kumuingiza ndani ambako walimkaribisha kitini. Robert alienda akachukua glasi tatu akaweka barafu halafu akaweka kinywaji na kuwakaribisha. Kadima alishangaa sana kujikuta ameletwa ndani ya nyumba nzuri na vile vile alijua nyumba za mtaa huu zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya maafisa wa vyeo vya juu nchini na mabalozi. Alizidi pia kushangazwa na vijana hawa walioonekana waungwana sana. Woga wake kwa ujumla ulipungua.
"Bwana Kadima samahani sana kwa jinsi tulivyokuchukua kwa sababu hakukuwa na njia nyingine. Mimi naitwa Willy na mwenzangu anaitwa Robert. Ndugu Robert ni Katibu Mwenezi katika ofisi ya OAU iliyoko mjini hapa huenda utakuwa umewahi kumsikia kwani kazi zako na zake zinakaribiana", Willy alimfahamisha.
"Sijawahi kumwona", Kadima alijibu kwa mkato.
"Tuna maswali machache ambayo tungependa kukuuliza na tungeomba usitudanganye maana sisi tayari tunaelewa mambo mengi. Usishangae ukikuta tunabadilika na kuwa watu wabaya", Willy alimwekea mikwala.
"Wewe ni nani? Maana umesema jina lako tu hukujieleza wewe ni nani?" Kadima aliuliza.
"Mimi utanijua muda si mrefu", Willy alijibu.
"Haya kama ni maswali ninayoyajua nitayajibu kama siyajui sitaweza." Kadima alieleza.
"Vizuri. Wewe ndiye unashughulika na mambo ya Ukombozi wa Kusini mwa Afrika Wizarani kwenu", Willy aliuliza.
"Ndiyo", alijibu Kadima.
"Siku chache zilizopita Mkuu mmoja wa vyama vya wapigania Uhuru Kusini mwa Afrika aliuawa mjini hapa sijui kama una habari hizi?" Willy aliuliza.
Jasho jembamba na baridi lilimtoka Kadima. Sasa ndipo alikuwa amegundua kwa nini amekamatwa na kuletwa hapa kwani asubuhi ile alikuwa amepata habari kutoka kwa Fernand wa Agence Sozidime kuwa kulikuwa na wasiwasi wa mambo, lakini alikuwa amemweleza ya kuwa wangezungumza baadaye.
"Siku za mwizi ni thelathini na tisa ya arobaini unakamatwa", Kadima alifikiria.
Willy alihisi kuwa Kadima alikuwa amegutuka kutokana na swali hili kwa vile aliliona jasho lililomtoka na jnisi mikono yake ilivyotetemeka kiasi cha kutoweza kushika glasi.
"Habari hizo ninazo, na hivi leo nimetoka mjini Lusaka kupeleka mizigo ya marehemu." Kadima alijibu taratibu.
"Kifo cha marehemu ni miongoni kati ya vifo vingi ambavyo vimetokea kwa wapigania uhuru katika nchi kadhaa za Afrika. Na kifo hiki ni cha pili katika Kinshasa kwa muda huu wewe ukishughulikia idara hiyo katika Wizara ya mambo ya nchi za nje. Sijui unaweza kutueleza ni nini chanzo cha mauaji haya?" Willy alimuuliza huku amemkazia macho.
"Siwezi kujua, polisi na idara ya upelelezi ndio wanajua," Kadima alijibu.
"Bwana Kadima sina haja ya kupoteza muda wako mwingi, hivi sina haja ya kuzunguka, au kusumbuana na huku mambo yanaeleweka waziwazi. Hivi nataka utueleze uhusiano ulionao kati yako na Mkurugenzi wa Kampuni ya Sozidime Agence au wenye magereji ya G.A.D. Papadimitriou, Baninga na Du Peuple", Willy alimuuliza.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kadima alitetemeka kabisa, alitambua kuwa huu ndio ulikuwa mwisho wake na kwa sababu hakuwa mtu aliyezoea matatizo hivi hakuwa mtu mwenye moyo mgumu. Siku moja aliwahi kujifikiria kuwa kupenda pesa kulikuwa kunampeleka mbali. Alianza kukumbuka miaka mitatu iliyopita simu ya Pierre Simonard ambaye alikuwa ameunda urafiki kutokana na kupeleka gari lake kwenye gereji yake. Pierre alimuomba waonane Hoteli Intercintinental jioni hiyo kama yeye akikubali. Jioni ile walipoonana, Pierre alikuja na mtu mwingine aliyemjulisha kwake kuwa alikuwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Agence Sozidime.
Ni jioni hiyo ambapo uhusiano kati yake na Fernand ulipoanza. Na tokea hapo ndipo walipomshawishi na kumfanya kibaraka wao wa kuweza kuwapasha habari zote juu ya wapigania uhuru. Alikuwa amelipwa pesa nyingi sana na sasa hivi alikuwa kati ya maafisa tajiri sana katika Zaire. Alikuwa na pesa chungu nzima huko Geneva, na alikuwa na majumba na hoteli kubwa huko Paris. Sasa leo maji yalikuwa yamemfika shingoni, kwa sababu alikuwa hajui watu hawa wanajua kiasi gani, na kwa sababu alikuwa anaogopa kufa, na kwa vile alitambua vijana hawa lazima ni wapelelezi aliamua kuwaeleza ukweli. Lakini kabla ya hapo alitaka kujua ki ukweli huyu kijana ni nani.
"Kijana umeniuliza swali la maana kabisa. Lakini kabla sijakujibu naomba kitu kimoja unieleze wewe ni nani na unawakilisha nini. Halafu mimi nitakueleza kila kitu bila kuficha. Nimechoka kukaa na mzigo huu, moyoni mwangu, na kama wewe ndiye mtu mwenyewe unayefaa nikueleze nitakueleza. Lakini kwanza nieleze wewe ni nani?" Kadima alieleza. Willy alijua mtu huyu alikuwa anazungumza ukweli na alijua ataeleza ukweli akijibiwa swali lake. Maana Willy alikua ameishaona watu wengi wa namna hii kutambua kama mtu huyu atasema ukweli au vipi. Hivyo Willy aliamua kumweleza yeye ni nani, na alikuwa amekuja hapa kufanya nini. Vile vile alimweleza mambo juu juu ya kuonyesha kuwa tayari walikuwa wamepata habari za kutosha juu ya 'WP' kwa hivi Kadima kuficha kusema ukweli kusingemsaidia neno.
"Lo poleni sana, sasa nisikilizeni kwa makini, nikimaliza kueleza mnaweza kunifanya lolote", Alianza Kadima. Kadima alieleza tokea siku ile Pierre alipomfahamisha kwa Fernand mpaka tukio hili la Mongo. "Mimi nimewasaliti ndugu zangu shauri ya pesa. Na katika nchi hii tuko wengi. Hiki kikundi cha 'WP' kimeotesha mizizi mirefu katika nchi hii na ina vibaraka wengi sana. Jambo hili limewezekana katika nchi kwa kufuatana na siasa ya nchi hii. Viongozi wote wa nchi hii wako tayari kufanya lolote ili kujaza tumbo lao. Mimi nimekuwa hivyo ingawaje jambo hili limekuwa linanikera moyoni. Sasa mnaweza kunifanya mnavyotaka mimi nimetubu yote niliyoyafanya nayajutia", Kadima alimalizia machozi yanamtoka.
"Lo masikini Afrika", Robert alilalamika.
"Tamaa ya viongozi ndiyo inaiangamiza Afrika. Mpaka hapo tutakapopata viongozi wenye kuipenda Afrika kwa dhati na siyo matumbo yao ndipo Afrika itakapoendelea", Willy alisikitika.
"Ni viongozi wachache wanaoipenda Afrika kwa dhati" Kadima alithibitisha.
"Kwa sasa hivi bwana Kadima utakaa hapa mbapa hapo tutakapokuruhusu. Tutakupa mwanya upige simu nyumbani kwako uwaeleze umepata safari ya ghafla. Tutakata shauri juu yako baadaye", Willy alimweleza Kadima.
Kadima ambaye roho yake ilikuwa imechoka kabisa alijibu, "Lolote mtakaloniambia, nitafanya ili mradi tu mtakapomaliza kazi zenu mnisikilize mambo yangu, Fernand na Pierre ni watu wabaya sana ndio wamenifanya mimi nikatumbukia katika maovu haya, mkiwakamata wapeni salamu zangu", Willy alimuongoza katika chumba kimojawapo baada ya kupiga simu na kumfungia ndani. Chumba hiki kilikuwa kidogo na dirisha dogo ambalo Kadima asingeweza kupita.
Robert alimwita Willy akamweleza, "Unajua nilitaka kusahau, Nilipata habari kutoka kwa Chifu anaeleza kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ukombozi ya OAU anaingia mjini hapa leo jioni. Ameeleza sisi tuendelee kama kawaida yeye anakuja na mipango kamili."
"Ahaa vizuri, kama akitutaka atatujulisha, nafikiri Chifu atakuwa amemweleza jinsi ya kutupata. Sasa hivi tuwangojee akina Ozu, tupange mipango ya leo jioni". Willy alieleza.
Pierre na wenzake walikuwa wamekutana tena mchana huu kama walivyokuwa wameahidi.
"Nilipokwenda kuonana na Mkurugenzi huko Sozidime wakati nilipowaacha hapa nilipata habari nzuri sana kutoka BOSs. Boss imeamua kuwa baada ya kuhakikisha kuwa tumewateketeza wapelelezi hawa wa Afrika tutaruhusiwa kustaafu na kuchangua nchi yoyote tunayotaka kwenda kuishi kazi tuliyoifanya ni nzuri ya kutosha," Pierre aliwaeleza wenzake kwa tabasamu kwa mara ya kwanza tangu wafahamiane. Pierre siku zote alikuwa mtu ambaye hatabasamu wala hacheki. Kisha aliendelea. "Tayari Mkurugenzi ameishatufanyia mipango ya usafiri kiasi kwamba tukimaliza shughuli hii iliyobaki tunaondoka bila kuchelewa kwani wakati mwingine itatubidi kuondoka mjini hapa kwa haraka.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Kwa hivi jamani tuwateketeze wapelelezi hawa mapema ndiyo itakuwa raha yetu," Pierre aliwaeleza. Kila mmoja wao waliingiwa na mawazo ya kupanga wapi pa kwenda. Muteba alimfikiria Tete.
"Sijui kama Tete atakuwa tayari kuondoka na mimi, nitaenda kumshawishi nikitoka hapa," Muteba aliwaza.
Jean naye alikuwa na haja ya kwenda kukaa Ufaransa na alikuwa siku zote anaota kwenda kuishi huko. Aliamua kuwa angemchukua Lucie aende naye kwani walikuwa wanapendana sana.
Papa yeye alikuwa anafikiria kwenda Hong Kong, kwa vile alikuwa amejiwekea pesa nyingi sana katika benki za nchi za nje basi alikuwa hana wasiwasi. Alifikiria kuwa kweli muda ulikuwa umefika kwake kustaafu ili akafaidi utajiri aliokuwa amejiwekea.
Pierre yeye alikuwa na mipango ya kwenda Marekani ambako alikuwa na marafiki aliokuwa amefanya nao kazi wakati walipokuwa amepelekwa C.I.A. kufanya kazi kwa muda, ambao sasa amestaafu.
"Loo mpango mzuri sana. Hii kazi iliyobaki ni kidogo sana naamini tutaimaliza usiku wa leo", Papa alieleza. Kisha walianza kupanga namna watakavyoweka ulinzi wao tayari kwa kuwakabili adui zao.
"Tuna walinzi wapatao thelathini ambao ni wazuri sana sidhani tutapata matatizo yoyote hasa ikiwa sisi wenyewe ndiyo tunawaongoza. Lililobaki ni kutayarisha silaha za kutosha," Pierre alishauri.
Mara kengere ya simu ililia, Pierre aliangalia saa yake ilikuwa saa tisa na nusu, akaondoka kwenda kuijibu. Alisikiliza mara moja akajibu kwa sauti. "Tunakuja", akakata simu. Wenzie wote walimkodolea macho kwani nywele zake zilisimama.
"Vipi?" Muteba aliuliza.
"Vijana wetu wamewaona Kofi na Ozu wanaingia Hoteli Intercontinental hivi wanaomba msaada. Naamini hawatategemea kuwashambulia mchana na mbele za watu, Hivyo twende sisi wenyewe, nafikiri hii ndiyo nafasi nzuri sana," Pierre alishauri.
"Lo, tusiipoteze nafasi hii," alijibu Muteba akasimama tayari kwenda kwenye mapambano. Kundi zima la watu wanne, wakiwa ni majasusi wenye ujuzi wa hali ya juu waliondoka.
Kofi na Ozu baada ya kuchukua plani yote ya gereji Du Peuple, pamoja na maelezo yote waliyoyataka tayari kwa mashambulizi ya jioni. Waliondoka na kuelekea Hoteli Regna ambako Ozu alikuwa amefikia. Ozu alibadilisha nguo na kuchukua silaha zingine alizokuwa amezitayarisha kwa mapambano zaidi.
Chakula cha mchana walipatia hapa hapa, na baada ya hapo waliondoka kuelekea Hoteli Intercontinental ili Kofi naye akajiweke tayari kwa ajili ya jioni.
Ilikuwa saa tisa na nusu walipoingia Hoteli Intercontinental baada ya kuridhika kuwa hakuna mtu aliyekuwa amewafuata. Lakini kwa bahati mbaya vijana wa 'WP' waliokuwa wakiwangojea hapo Hoteli Intercontinental walipowaona bila wao kujua. Ozu alienda kwenye bar wakati Kofi alipanda juu kwenda kubadilisha nguo zake. Ilikuwa saa kumi kasoro dakika kumi Kofi alipompitia Ozu kwenye bar. "Niko tayari kabisa, twende zetu tukawawahi Willy na Robert wasije wakatungoja sana. Maana tulikubaliana kuonana saa kumi", Kofi alimweleza Ozu.
"Twende zetu," alijibu Ozu. Ozu alilipa bia yake na wakaondoka.
Nje ya Hoteli Intercontinental kundi la 'WP' lilikuwa limekaa tayari likiwasubiri, Pierre na Jean pamoja na vijana wao wawili walingojea kwenye mlango unaotokea pembeni mwa hoteli upande wa barabara ya 8E Armie. Papa na Muteba pamoja na vijana watatu walingojea kwenye mlango wa mbele, Makundi haya mawili yalikuwa kila moja likiwa linajifanya linashughulikia gari lililoharibika na kwa jinsi hii hakuna mtu aliyewajali. Pierre, Jean, Papa na Muteba walibaki wamekaa ndani ya gari tayari tayari huku vijana wao wakijifanya kushughulika.
Kofi na Ozu walikata shauri kutokea mlango wa mbele bila kujua kuwa wanangojewa, walitembea katika tahadhari yao ya kawaida tu. Walipotokea mlangoni waliangaza kwa mara moja. Na wakati huo huo Papa na Muteba walibonyezwa kuwa tayari walikuwa wameshatoka nje. Papa na Muteba waliruka mara moja na kupiga risasi. Ozu aliwaona mara moja wakati Kofi aliangaza sehemu nyingine, hivi Ozu akapiga kelele "Kofi" yeye akajitupa nyuma ya gari wakati ule ule risasi zikamiminika pale alipokuwa amesimama. Kofi aliposhituliwa na Ozu aliruka kama umeme kwa bahati mbaya risasi zikampata kifuani na kuanguka ndani ya mlango wa hoteli na kujiviringisha mle ndani. Ozu alipiga risasi kuwazuia wale watu, lakini waliruka ndani ya gari na kuondoka mwendo mkali sana. Ozu alisimama akakimbia ndani ya hoteli ambako watu wote walikuwa wamelala chini kwa kuogopa risasi na huku kelele za vilio zikisikika huku na huko. Alienda akamwangalia Kofi akakuta tayari ameishakata roho. Alikuwa amechanwa na risasi kifuani kwani watu wale walikuwa wametumia 'Sub Machine Gun'
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Kofi Kofi," Ozu aliita huku machozi yanamtoka. Watu walikusanyika na simu ikapigwa polisi.
"Sijaona kitu kama hiki kwa muda mrefu sana hapa Kinshasa. Kumshambulia mtu mchana mchana mbele ya watu wengi namna hii na mbele ya hoteli kubwa namna hii," mtu mmoja katika hilo kundi alilalamika.
"Tena aliyekuwa na bunduki ile kubwa alikuwa Mhindi", mtoto mmoja mdogo alisema, lakini mama yake akamfinya na kumvuta kutoka hapo. Kwa sababu ya uchungu mwingi. Ozu hakujua la kufanya ila alijua hawezi kufanya jambo lolote kwa sasa ila kwenda kuwaarifu akina Willy tayari kwa mapambano na watu hawa. Vile vile kama polisi watamkuta hapo wangepoteza muda mwingi wa kumuuliza maswali. Hivi aliangalia mwili wa Kofi akasema moyoni. "Kofi umekuwa kama mdogo wangu tangu tulipofahamiana, Mungu yupo damu yako haitamwagika bure. Nitahakikisha," kisha akapotea ndani ya kundi lililokuwa pale kama umeme. Pierre na kundi lake walirudi gerji Du Peuple na furaha kubwa sana kwa sababu walijua wamepunguza adui mmoja hivyo upinzani jioni yake ungekuwa kidogo sana.
"Watu wawili kwa watu thelathini, hawatuwezi" Papa alidiriki kusema.
Ilikuwa saa kumi na nusu Ozu alipowasiri nyumbani kwa Robert. Alipoingia aliwakuta Willy, Robert pamoja na msichana mmoja mzuri sana ambaye alitambua kuwa msichana huyu atakuwa ndiye Tete. Alimwangalia Willy na Robert machozi yalianza kumtoka tena, mara Willy na Robert wakatambua kuwa Kofi ameuawa. Robert alikimbia akaweka Whiski ndani ya glasi akampa Ozu ambaye alikuwa bado machozi yanammiminika.
"Tueleze imetokea vipi?" Willy alimwambia.
Ozu alikunywa glasi yote ya Whiski kwa mara moja halafu akawaeleza ilivyotokea, "Kofi amekufa mbele ya macho yangu mimi ninaona hivi hivi, Watu hawa ni wanyama watakufa kwa mkono wangu, Mungu anisaidie," Ozu alimalizia machozi yalianza kumtoka tena.
Willy alitambua uchungu Ozu aliokuwa nao akamwambia, "Ozu, hata sisi jambo hili limetushitua sana, sasa lililopo ni kutulia na kupanga jinsi ya kupambana na watu hawa," Willy alieleza taratibu.
Tete aliyekuwa amekaa pembeni kidogo alimwambia Ozu na ghafla naye akaanza kulia. Jambo hili lilimshitua Ozu na kumfanya atulie na kuelekea maliwatoni.
Mimi sasa namchukia Muteba na wenzake kiasi ambacho sijawahi kumchukia mtu maishani mwangu. Tokea sasa mimi nitachukua nafasi ya Kofi," Tete alisema bila kutania.
"Kazi hiyo haikufai mama, kazi uliyokwishafanya inatosha kabisa "Willy alimjibu.
"Mimi najua kitu nitakachowasaidieni. Mimi ni dereva stadi sijui kama kati yenu kuna dereva kama mimi. tafadhali sana msiniache mtakapokwenda kwenye mapambano ya leo. Tafadhali naomba mniridhishe nafsi yangu. Kule kuwaendesha tu nitajiona nimelipa deni kubwa kwa Mwadi, maana ni mimi niliyefanya akina Muteba wamfahamu. Hivyo Willy mpenzi usiniache," Tete aliomba akaanza kulia tena.
Ozu aliporudi kutoka maliwatoni alikuwa na hali nzuri kidogo. Alipofika alianza kuwaeleza plani yote ya gereji Du Peuple na jinsi alivyokuwa amefikiria wanaweza kuiingilia.
"Hata wakiwa watu hamsini, tukiwashambulia hivi tunaweza tukawapenya, ili mradi tu, tuwe na silaha za kutosha. Mimi naona 'machine gun' na bastola tulizonazo zinatosha kabisa," alimalizia Ozu. Willy naye alimwelezea Ozu juu ya Kadima. "Na jambo jingine ni kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ukombozi ataingia hapa usiku", Willy alimweleza.
"Nafikiri atafika wakati unaofaa kabisa, maana leo mimi nataka kuona mwisho wa watu hawa," Ozu alisisitiza. Waliendelea na mipango ya siku ile na mwishowe hata ombi la Tete lilikubaliwa.
"Yeye anazifahamu ofisi za Sozidime vizuri sana hivi anaweza kuwa wa msaada sana kwetu ingawaje ni jambo la hatari", Ozu alisema.
"Mimi siogopi hata kidogo hiyo hatari nataka niipate. Mimi naomba mnihesabu kama mmoja wenu," Tete alizidi kuomba. Baada ya kukubaliwa. Willy na Tete waliondoka kwenda chumbani ambako Willy alikuwa analala. Huko alitoa silaha zake huku akiwa anaongea na Tete, alizitia mafuta. Robert na Ozu nao walishughulikia silaha zao kuziweka tayari.
USHINDI NI DHAHIRI
I
Ilikuwa saa nne za usiku na hapo gereji Du Peuple huko Limete kulikuwa na pilika pilika nyingi sana. Kundi zima la 'WP' lilikuwa limewasili isipokuwa Muteba. Pierre alizunguka kila sehemu kukagua ulinzi ulivyokuwa umepangwa. Alikuta kila mtu ameshika nafasi yake. Baada ya kuridhika na ulinzi uliopangwa alirudi ofisini mwake ambamo Jean na Papa walikuwa wanamsubiri.
"Muteba amepatwa na maafa ama vipi?" Pierre aliuliza.
"Sijui, Patron, alikuwa ameniambia kuwa atakuwa hapa kabla ya saa tatu lakini ninashangaa mpaka sasa bado hajafika," Alijibu Papa. Alipomaliza kusema hivyo tu walisikia mlango unagongwa halafu ukafunguliwa na Muteba akaingia. Wote wakapumua walipomuona. Muteba alikuwa amechelewa kwa sababu alipokuwa ameachana na wenzake baada ya shambulio lile la Hoteli Intercontinental, alienda moja kwa moja nyumbani kwake na kubadili nguo. Baada ya kubadilisha nguo aliondoka kwenda nyumbani kwa Tete ambako alitarajia kumweleza mipango ya kuondoka naye kama BOSS ilivyokuwa imewaletea habari. Alipofika nyumbani kwa Tete hakumkuta. Akaanza kumtafuta kila mahali alipofikiria kuwepo asiweze kumuona. Jambo hili lilikuwa karibu limtia Muteba wazimu. Alitumia zaidi ya masaa manne akimtafuta Tete bila kumuona kabisa mwishowe akajikuta ameishachelewa kufika gereji Du Peuple kama alivyokuwa anatakiwa ndipo akaondoka na kuja moja kwa moja gereji Du Peuple.
Wenzake walipomwangalia walijua kulikuwa na kitu kinamsumbua rohoni. "Vipi, mbona hivi?" Pierre alimuuliza bila kuficha jinsi alivyokuwa amemtafuta Tete. "Sahau hayo mambo ya mwanamke tukimaliza shughuli hii salama, mambo haya yatanyooka tu. Bila shaka anashughuli zake" Pierre alimshauri.
"Huenda huyu Willy amemkamata baada ya kujua kwa kikamilifu juu ya uhusiano wangu na wake", Muteba alilalamika.
"Achana na mawazo hayo, sasa hivi tuna kazi muhimu kuliko kufikiria matatizo ya mwanamke." Pierre alisema kwa ukali. Muteba alijigundua kuwa alikuwa kweli amefanya kosa la kikazi kuwa na mawazo mengine wakati mbele yao kuna kazi muhimu kabisa. Hivi alijisahihisha akasema. "Samahani Patroni, tuendelee".
Pierre alieleza tena ulinzi ulivyokuwa umepangwa na wote wakaridhika nao kabisa. "Vijana tayari, wameishashika sehemu zao," alisema akimwangalia Muteba.
"Nimewaona wakati naingia, hakika ulinzi umepangwa vizuri kabisa". Muteba alikubaliana. Papa ataongoza ulinzi wa mbele, Jean utaongoza wa nyuma na Muteba utaongoza sehemu zilizobaki," Pierre aliwaeleza. "Sasa twendeni wote tukakague sehemu zenu, na ikiwa kuna marekebisho turekebishe halafu tuwangojee washenzi hawa kama watathubutu kuja," Pierre alieleza.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Willy na Robert ambao walikuwa wameondoka jioni ile na kuelekea mjini walirudi kiasi cha saa tatu na kumkuta Tete na Ozu wakiwa wameishatengeneza chakula. Willy alikuwa amepitia hotelini kwake ambako alichukua vifaa fulani fulani ambavyo vilikuwa vya lazima katika shughuli ya usiku huo. Pamoja na silaha zaidi alizokuwa amechukua, alichukua na fulana mbili ambazo zilikuwa haziingiwi na risasi. Fulana hizi Willy alikuwa mara kwa mara anazitumia alipokuwa karibu kukabili pambano kali sana. Na mara nyingi zilikuwa zimemsaidia, hivi alikuwa akisafiri nazo mara kwa mara. Fulana hizi zilikuwa ni zawadi alizokuwa amepewa na Mkuu wa kikosi cha Scotland Yard wa huko Uingereza alikokuwa amepelekwa kwa mafunzo ya miezi sita na kujitokeza kuwa mtu aliyefuzu vizuri kuliko watu wote waliokuwa wamepitia kwenye kikosi hicho cha mafunzo. Kwa furaha ya Mkuu wa kikosi hicho alimpa fulana hizo kama zawadi.
Robert alikuwa amemwacha Willy Hoteli kwake akijitayarisha, na yeye akaenda nyumbani kwa rafiki yake yule aliyekuwa Afisa wa juu katika Shirika la Upelelezi la Zaire C.N.D. Alimkuta huyu rafiki yake na wakazungumza vitu vya manufaa kati yao. Akiwa na furaha kubwa baada ya kuwa na mazungumzo yaliyofanikiwa kati yake na huyu rafiki yake alirudi hoteli Memling akampitia Willy na bila kumueleza Willy wapi alikuwa ameenda, walirudi nyumbani.
"Chakula tayari", Tete aliwaeleza.
"Ooh, safi sana mimi nina njaa sana", Robert alidai.
"Vipi Bwana Kadima mmempa chakula?" Willy aliuliza.
"Tayari kabisa", Ozu alijibu. Walikaa kwenye meza wakala chakula cha jioni ambacho kilikuwa kimepikwa vizuri sana. Wakati wakila Tete alieleza."
"Wakati mmeondoka alikuja msichana mmoja hapa anaitwa Ebebe, alikuwa anamtafuta Robert. Tulimwambia Robert ametoka amsubiri lakini hakutaka, akaondoka akaenda zake. Alionekana amechukia".
..."Shauri yake nitamwona kesho. Rafiki yangu sana, lakini ana wivu mwingi." Robert alieleza.
"Nafikiri alipomkuta Tete anapika alifikiri kuwa amepinduliwa serikali yake ya hapa nyumbani," Willy alitania wote wakacheka.
"Hasa alipoona mapinduzi yenyewe yamefanywa na msichana chuma namna hii", aliongeza Ozu. Walipomaliza kula walianza kujiandaa.
"Tunasubiri tukashambulie sehemu hii usiku, ili kama watakuwa wanatusubiri wawe wameshakata tamaa na kuchoka. Unajua mtu wa kawaida tu kuwa katika hali ya tahadhari kwa muda usiopungua masaa manne ni vigumu sana", Willy aliwaeleza.
"Hizo ndiyo saa zenyewe, wengine watakuwa wameanza kusinziasinzia. Hata mimi zamani kabla sijazoea, nilikuwa na ubovu huo", alieleza Ozu.
Willy alitoa fulana zake ndani ya mfuko akaeleza. "Hapa ninazo fulana hizi mbili ambazo haziingiwi risasi. Sasa kati yenu sijui nani atachukua moja,"
"Mpe Robert mimi sina taabu," Ozu aliamua.
"Hapana mpe Ozu. Mimi nina ujuzi wa hali ya juu sana katika karate na kung fu, sitahitaji kabisa fulana hiyo. Na kwa taarifa yenu ni mara chache, natumia silaha, mpaka iwe lazima sana," Robert alieleza. Willy alikubaliana na Robert kwani alikuwa amemuona siku ile walipopambana na akina Mulumba.
"Ozu chukua hii. Wewe una ujuzi mwingi katika kutumia bunduki hasa hizi kubwa kubwa hivyo naamini utahitaji". Willy alimshauri.
"Huenda tumpatie dereva wetu." Ozu alisema huku anamwangalia Tete.
"Wacha matani, mimi sina haja nayo", Tete alijibu kwa ukali.
"Wengi wape," alijibu Ozu na kuichukua ile fulana.
"Sasa ni saa nne twendani tukapumzike lakini saa nane tuwe tumejiweka tayari kwa kuondoka hapa." Willy alishauri. Kila mmoja alienda chumbani kwake, Willy na Tete wakaandamana chumbani kwa Willy. "Tete unajua unachukua mzigo mzito sana usiokuwa kiasi chako," Willy alimweleza Tete.
"Wewe niache, mimi mwenyewe ndiye nimekata shauri na wala sikushawishiwa na mtu yeyote. Tuzungumzie jambo jingine Willy, jambo hili tuliache hivyo lilivyo, mimi nitakwenda pamoja nanyi," Tete alijibu kwa ukali, Willy bado alikuwa hajakuwa na imani kabisa na msichana huyu. Maana yeye Willy huwa hawaamini sana wasichana wenye sura nzuri kwani kila wakati mambo yao hayaeleweki. Lakini hata hivyo aliamua kuyaacha mambo yalivyo aangalie huko mbele ya safari.
Ilipotimia saa nane simu ililia ofisi kwa Pierre. "Hallo", aliitikia alipoinua simu.
"Fernand hapa, vipi mambo bado?" Aliuliza Mkurugenzi.
"Bado, huenda hawatakuja na kama hawatakuja watakuwa wamvuruga mambo maana mimi nimechoka. Kama tutamaliza shughuli hii mimi kesho nitaondoka." Pierre alieleza kwa unyonge.
"Usiwe na wasiwasi mambo yote yako tayari, ukimaliza shughuli za hapo tu njoo moja kwa moja hapa ofisini, mimi nipo tu mpaka mwisho", alijibu Fernand na kukata simu.
Pierre aliangalia tena saa yake, akiwa na mashaka makubwa kama mambo yangekwenda kama walivyopanga. Wenzake nao ambao walikuwa nje na vijana wao walikuwa nao wamechoka. Kwani walikuwa sasa wamesimama wakisubiri zaidi ya masaa manne. Wale vijana wengi walikuwa wameanza kusinzia sinzia. Kwa ujumla jeshi zima lilikuwa limeshikwa na uchovu, na mawazo ya kwamba "Hakuna kitu" ndiyo yalikuwa yamewajaa wote.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ilikuwa saa tisa kasoro robo wakati KIKOSI CHA KISASI kilipokuwa tayari kuondoka nyumbani kwa Robert ili kuelekea Limete. Kila mtu alivaa mvao wa kazi. Tete naye alivaa dingirizi na T'shati, na akaweka jaketi juu. Miguuni alivaa raba na nywele zake akawa amezifunga, kwa ujumla alionenana mmoja wao kabisa. "Loo utafikiri tunaenda kuteka ndege nyara. Kwa kawaida wateka nyara wasichana wa Kipalestina huwa ni wazuri sana kama Tete" Ozu alitania.
"Na wewe na maneno yako". Robert alijibu na kuingia stoo. Aliporudi alikuwa na kamba akampatia Willy. Ilikuwa kamba ndefu. Willy akaikata akampa Robert kipande akamwambia aiweke wataondoka nayo. Willy alienda akafungua mlango wa chumba ambamo Kadima alikuwa amelala. Alimkuta Kadima amelala akamwamsha.
"Samahani Bwana Kadima itabidi nikufunge kwa usalama wako," Willy alimwambia. Kadima alimwangalia tu bila kumjibu, Willy akamfungia kwenye kitanda. Alimfunga miguu na mikono kwa ustadi kabisa, "Samahani sana", Willy alimwambia tena Kadima na kuondoka, na kuufunga mlango vizuri kabisa. "Sasa twende zetu," Willy aliwaambia wenzake. Wakiwa wameweka silaha zao tayari walipanda ndani ya gari Willy alilokuwa akitumia. Tete akapiga moto na kuondoka pale nyumbani kwa Robert kama risasi.
"Tete ukifika Limete kwenye barabara ya P.E Lumumba ingia barabara ya tisa inayoingia viwandani, nenda moja kwa moja na usimamishe gari mbele kidogo na Kampuni ya BISCO, sisi tutatelemka hapo. Wewe utarudi mpaka kwenye njia ndogo inayounganisha mabarabara yanayoingia viwandani, na egesha gari mbele ya nyumba ya pili kutoka barabara ya nane. Nyumba hii wenyewe wamekwenda Brazzaville na haina mlinzi bali lango lake limefungwa. Wewe utaegesha gari mbele ya lango la nyumba hiyo na nina imani hakuna mtu atakutilia mashaka yoyote. Utatungoja hapo ukiwa tayari tayari, kama itapita zaidi ya saa moja na nusu hujaona hata mmoja wetu, jua mambo yameharibika ondoa gari uende zako. Lakini nina imani nusu saa itatutosha. Umenielewa?" Willy aliuliza.
"Nimeelewa hamna wasiwasi kabisa" Tete alimjibu kwa sauti kavu kabisa.
Kutokana na taarifa Ozu aliyokuwa ameleta, kampuni ya Bisco ambayo hutengeneza biscuti inafanya kazi masaa ishirini na nne. Na inafanyakazi kwa zamu na kwa bahati kulikuwa na zamu iliyokuwa inaingia saa tisa za usiku. Kufuatana na taarifa hii ndiyo sababu walikuwa wameamua kushukia mbele ya Kampuni hii ili ionekane kama kwamba gari ile ilikuwa imeleta watu wa zamu. Jengo la gereji Du Peuple likuwa jengo la tatu mkono wa kushoto kwenye barabara ya tisa kama unatoka barabara ya Patrice Emiry Lumumba. Kulikuwa na majengo mengine matatu makubwa kabla hujafika kwenye jengo la kampuni ya BISCO kutoka gereji Du Peuple.
Tete ambaye aliwadhihirishia abiria wake kuwa alikuwa dereva stadi sana aliongoza gari kama alivyokuwa ameelezwa. Alipofika kwenye kona ya P.E. Lumumba na barabara ya tisa. alionyesha taa na kuingia barabara ya tisa. Alivuta gari katika mwendo mkali sana na kusimama mbele kidodo ya Kampuni ya BISCO. Alimvuta kidogo Willy aliyekuwa amekaa naye kwenye viti vya mbele ya gari na kumbusu haraka haraka. "Bahati njema aliwaambia kwa ujumla huku akiwarushia busu".
"Na wewe vile vile," Ozu alijibu kwa niaba ya wenzake. Vijana wa Kikosi cha Kisasi wakatelemka kuelekea kwenye mapambano ambayo yangeamua mwisho wa kazi yao unakuwa vipi. Tete aliondoa gari lake, huku watu wote walioona mwendo wake wakahisi kuwa alikuwa taksi dereva aliyekuwa ameleta wafanyakazi wa BISCO waliokuwa wamechelewa zamu. Wazo hili ndilo lilimpata hata Papa aliyeliona gari hili na kulishuku lakini baada ya kusimama mbele ya kampuni ya
Bisco akaondoa wasiwasi wake.
Baada ya kutelemka tu Willy na wenzake walipotelea ndani ya uchochoro uliokuwa ukipita kati ya BISCO na jengo lililokuwa linafuata. Kulikuwa na giza katika uchochoro huu lakini kwa vile Ozu alikuwa amepita aliwaongoza. Walienda mpaka wakatokea kwenye uchochoro uliokuwa nyuma ya majengo haya yaliyokuwa yanatazama barabara ya nane. Walipokaribia jengo la gereji Du Peuple kwa nyuma, walianza kutembea kwa kunyata na katika tahadhari kubwa.
"Sii" Robert aliyekuwa mbele aliwasimamisha wenzake, "Nimeona mtu amepita", aliwanong'oneza, "Nisubirini" Robert alienda akinjongwajongwa, na alipofika kwenye pembe ya mwisho ya jengo jirani na gereji Du Peuple alisimama. Alianganza akaona kuna walinzi watatu kwenye ukuta uliokuwa umepakana na jengo hili jingine na walikuwa wanazungumza. Walikuwa hatua chache tuu na alipokuwa. Alipoangalia juu ya ngome ya ukuta uliozunguka gereji Du Peuple aliona kulikuwa na walinzi wanatembea kwa juu. Mmoja alitembea juu ya ukuta wa nyuma na mmoja kwenye ukuta wa pembe ya upande waliyokuwa. Alipokwisha kuona mambo haya alirudi pale wenzake walipokuwa akawaeleza.
"Kwa hiyo hawa wanaozungumza nafikiri ndiyo walinzi wa nje". Willy alisema.
"Sawa kabisa", Robert alikubaliana, "Na ninafikiria kuna mlinzi mwingine juu ya ukuta wa upande mwingine lakini amezuiwa na paa la nyumba hatuwezi kumuona", aliongeza wote watatu wakiwa wamefichwa na kivuli cha majengo haya walinyata mpaka kwenye pembe ya mwisho ya kutokea gereji Du Peuple. Wale walinzi waliokuwa wanazungumza walimaliza na wakamuacha mmoja wao anaelekea mbele ya jengo. Watu hawa walipitia karibu kabisa na pale akina Robert walipokuwa wamejibanza.
"Hawa watu hawaji tunasumbuka bure, mle ndani watu wameishachoka wanasinzia ovyo", mmoja wao alisema.
"Hata mimi najisikia kuchoka kabisa katika siku hizi tatu sijalala vizuri", yule mwenzake alijibu na wakaendelea. Walipoenda hatua chache kidogo Robert alinyata mpaka kwenye ukuta wa ngome bila kuwagutua walinzi hawa. Aliangalia juu akamuona yule mlinzi aliyekuwa juu ya ukuta alikuwa amekwenda upande mwingine, hivyo hakuwa na wasiwasi wa kuonekana.
Wale walinzi wawili walisimama, mmoja wao akamuomba mwenzake sigara Robert alichukua hii nafasi wakati mawazo yao yako kwenye sigara akawanyatia. Yule mmoja alitoa sigara akampa mwenzake na akatoa kiberiti ili kumwashia sigara. Robert alikuwa ameishafika bila wao kujua, akatoa kiberiti chake haraka akamwashia yule mlinzi aliyekuwa tayari ameweka sigara yake mdomoni akingojea moto. Yule mlinzi mwingine aliyekuwa amewasha kiberiti akagutuka, moto mwingine unatoka wapi. Walipotaka kugeuka tu Robert akawapiga karate wote wawili kwa mara moja na pigo alilokuwa ametoa lilikuwa kali sana akiwa amewapiga shingoni, wote walianguka chini na kufa pale pale bila kelele.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Aliangalia tena juu ya ukuta yule mlinzi wa juu alikuwa haonekani. Akawafanyia ishara wenzake wamfuate. Wakiwa wamezuiwa na kivuli cha majengo waliruka mpaka nyuma ya majengo ya gereji Du Peuple ambako Robert alikuwa bila kuonwa na walinzi wa pembeni kwao. Waliwavuta hawa watu wakawalaza chini ya ua wa michongoma mtu asiweze kuwaona kwa urahisi. Willy alimuona yule mlinzi wa juu ya ukuta wa upande ule wa nyuma akirudi akiwabonyeza wenzake ambao walijibanza. Ozu alijificha chini ya michongoma. Robert na Willy wakajifanya kama kwamba wao ndio wale walinzi waliokuwa wameuawa. Kwa vile wote walivaa nguo nyeusi nyeusi ilikuwa vigumu kutambuana usiku namna hii. Yule mlinzi wa juu hakuweza kuwatilia mashaka kwani aliamini ni wenzake.
Yule mlinzi alipokaribia Robert alimwita kwa kumfanyia, "Sii" yule mlinzi alikuja akauliza, "Unasemaje?"
"Inama nikueleze", Robert alimwambia akawa anajua ni mwenzake akadanganyika akainama. Robert aliruka kama umeme akampiga karate ya katikati ya paji la uso na kumpasua kabisa. na wakati huo huo alimvuta wakamdaka na kumlaza chini akiwa ameisha kufa. Naye alikufa bila kelele. Upesi upesi wakampandisha Ozu akachukua nafasi ya yule mlinzi, akaanza kulinda sehemu hii ya nyuma. Kitendo hiki kilifanyika bila kufahamika ndani ya ngome.
Willy alizunguka mpaka pembe nyingine akakuta hakuna mlinzi wa chini ila yule wa juu ya ukuta alikuwepo. Willy alikohoa yule mlinzi wa juu aliyekuwa anaangalia upande mwingine akageuka, akampungia mkono. Akiwa anafikiri kuwa ni yule mwenzake alikuja. Ozu aliyekuwa tayari akijifanya kulinda sehemu hii ya nyuma aliona ishara ya Willy akajua Willy alikuwa anataka kufanya nini, hivi naye akasogea upande ule. Yule mlinzi akiwa na uhakika na uhakika kuwa wote walikuwa walinzi wenzake alikuja mbio mbio. Alipofika pale Willy alipokuwa amesimama Ozu naye akawa amefika. "Huyu anasemaje", yule mlinzi alimuuliza Ozu.
"Inama msikilize," Ozu alimweleza kwa sauti ya chini chini. Alipoinama tuu Ozu alimkata mkono wa shingo na kumtua chini. Robert alikuja wakamficha. Robert akampandisha Willy kwenye ukuta akachukua nafasi ya huyu mtu.
Ozu alimfuata yule mlinzi wa chini wa upande ule waliokuwa wametokea. Mlinzi huyu alikuwa amesimama tu karibu na kona ya kwenda upande wa nyuma. "Hallo" Ozu alimwita kwa sauti ya chini chini, yule mlinzi akaangalia juu. Ozu akamuonyesha ishara kuwa anaitwa kule nyuma. Robert alikuwa amebana kabisa kwenye kona akiwa anaona mambo yote yaliyokuwa yanafanyika. Yule mlinzi naye akiwa hana wasiwasi wowote akijua kuwa hawa ni walinzi wenzake alienda haraka haraka. Alipojitokeza tu kwenye kona Robert alimrukia akamkaba kabari mpaka akamuua na kumvuta mpaka pale wenzake walipokuwa wamelazwa.
Ozu akamuonyesha ishara Willy kuwa amebaki mmoja. Bila kujua nini kinatokea yule mlinzi wa juu ya ukuta wa upande ule waliotokea alikuwa anaendelea na shughuli zake za ulinzi bila wasiwasi. Robert alijifanya kuwa yeye ni mlinzi wa chini wa upande ule alimwendea akamwita, "Sii" Yule mlinzi alipogeuka kumwangalia alimuonyesha ishara amfuate nyuma. Yule mlinzi akiwa hana wasiwasi naye alimfuata. Alipofika kule kwenye ukuta wa nyuma Ozu naye alikuwa yuko tayari. "Inameni niwaeleze". Robert aliwaambia wote. Ozu alijifanya anainama na yule mlinzi naye akadanganyika akainama. Ozu akamkata mkono wa shingo na kulivunja, akamsukumia Robert akamdaka na kumvuta chini. Kisha Ozu akainama akampa Robert mkono akapanda na yeye juu ya ngome.
Willy ambaye alikuwa ameishazunguka na kuona jinsi ulinzi ndani ya gereji ulivyokuwa alipita kwa wenzake akiwaeleza huku wakijifanya kama kwamba wanabadilishana sehemu, "Sehemu ambayo bado wako macho ni kule mbele, sehemu hizi zote wengine wamelala na wengine wanasinziasinzia." Willy alimnong'oneza Robert.
"Basi mimi ninatelemka kwa huku nyuma. Nitajaribu kushambulia kwa kadri niwezavyo nikitumia mikono yangu, nyinyi muwe tayari kunichunga kama watagutuka," Robert alisema.
"Kuna walinzi karibu ishirini humu ndani," Willy alimweleza. Kisha Willy aliendelea akamweleza Ozu. Walipokuwa wameshika nafasi sawa sawa na kuweza kumchunga. Robert kama nyani alitumbukia ndani ya gereji kwa nyuma bila kishindo. Jean ambaye alikuwa analinda sehemu ya nyuma pamoja na vijana wapatao sita alikuwa amelala ndani ya gari moja bovu, na akiwa amewaamrisha vijana wake kumwamsha kukitokea tatizo lolote. Alikuwa amekaa macho, mpaka saa tisa lakini akawa amekata tamaa kuwa hawa watu hawawezi kuja tena. Na kwa vile alikuwa hajalala vizuri kwa muda wa siku tatu alisikia usingizi mzito sana.
Ilikuwa sasa imepita miaka mingi bila Jean kujiweka katika hali ya kuweza kukabili hali ya namna hii. Zamani alipokuwa hajaletwa Zaire angeweza kukaa hata juma moja bila kulala asichoke kama alivyokuwa amechoka siku hii, Hivto Robert alipotumbukia ndani Jean alikuwa amelala kabisa.
Baada ya Robert kutumbukia ndani aliwanyatia walinzi wawili waliokuwa wameegemea kwenye gari, aliwatokea nyuma akawapiga karate za katikati ya vichwa vyao wakafa pale pale kwani alivipasua kabisa. Akatoa ishara kwa Willy kuwa ameua wawili. Kisha akamuona mlinzi mmoja anatokea sehemu ya kushoto kwake akajiegemeza kwenye gari kama mmoja wao, na kutoa sigara. Yule mlinzi alipomuana alimfuata akidhani ni mwenzake akamwomba sigara. Robert akampa halafu akatoa kiberiti kumwashia, na akatelemsha kiberiti chini. Yule mlinzi alipotelemsha mdomo chini ili kuwasha sigara. Robert alimkata mkono wa shingo na kulivunja. Akamchukua taratibu akamuegemeza kwenye gari. Alipozunguka kutokea ule upande wa kushoto, Willy alimfanyia ishara kkumuonyesha kuwa kuna watu ndani ya gari alilokuwa karibu kulipita. Alichungulia ndani akakuta kuna walinzi wawili wamelala, alifungua malngo taratibu kabisa akatoa bastola yake yenye sailensa akawapiga risasi kimya kimya.
Ni wakati alipokuwa amemaliza kuwaua hawa ndipo mlinzi mwingine aliyekuwa amelala ndani ya gari ambapo Robert alikuwa amewaegemeza wale watu wawili aliokuwa amewaua kwanza alipoamka. Kufungua mlango, alipojitokeza na kuwagusa wale wenzake aliokuwa anafikiri wamelala akakuta wamekufa. Kwa hifu akafyatua risasi ovyo. Gereji nzima ikawa katika vurugu, Walinzi waliokuwa wamelala wakaanza kukimbia ovyo, hii iliwapa nafasi nzuri Willy na Ozu kujua ni wapi washambulie. Ozu alirukia ndani katikati ya kikundi kilichokuwa kinaongozwa na Papa na akaanza kushambulia. Willy naye alirukia katikati ya gereji ambako Muteba ndiko alikuwa akiongoza. Robert akabaki kule kule kwenye kikundi cha Jean.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Jean aligutushwa na mlio wa bunduki, akaamka na kupiga kelele, "Shambulia shambulia", Robert aliwahi kumpiga risasi yule kijana aliyekuwa anapiga risasi na kutahadharisha gereji nzima. Jean alijikuta hana mtu ila yeye peke yake kwa upande huu. Robert alimuona, akamsubiri kwani alikuwa anakwenda ovyo katika woga mkuu. Kisha akakata shauri kurukia kwenye ukuta na kujitupa nje. Robert alihisi mawazo yake, na kwa vile alikuwa ameelekeza mgongo wake kwa Robert, Robert alimnyemelea akapiga bastoka kutoka mikononi mwa Jean, Jean kwa hofu aligeuka akajikuta uso kwa uso na Robert.
"Nitakuua kwa mikono yangu kulipiza vifo vya wazalendo wa Afrika ambao umewaua". Robert alimtishia Jean naye alikuwa mjuzi sana wa karate, hivi hakusita kuzianzisha moja kwa moja akifikiri Robert hakuwa na ujuzi kiasi chake. Jean alipeleka pigo la kwanza akapoteza la pili akapoteza la tatu akapoteza, akabadilisha. Robert alikuwa anatabasamu. Jean alipobadilisha alikuja na ufundi wa hali ya juu sana. Mapigo haya yalimpata Robert na kumpandisha mori. Robert alimwingilia Jean kwa Kung fu ya hali ya juu kabisa ambayo Jean alikuwa hajawahi kuona. Robert alimpiga Jean mapigo matatu mfululizo. Jean akaona hamwezi akageuka kutaka kukimbia. Robert akamvuta shati, akamgeuza na kumpiga mapigo mengine matatu ya haraka haraka. Jean alijaribu kwa kadri ya ujuzi wake lakini wapi. Jean aliruka juu ya gari, halafu akamrukia Robert. Robert akamkwepa halafu yeye Robert akamrukia Jean akampiga teke kali kali ajabu kifuani, likamuua Jean pale pale.
Willy aliporukia ndani ya gereji alikuwa ameshikiria 'machine gun'. Aliwaua walinzi kama mchezo maana walikuwa wanapigana bila mpango, Muteba alipoona walinzi wake wanakwisha alichukua 'machine gun' akaanza kushambulia yeye mwenyewe. Alikumbuka ujuzi wake aliokuwa ameupata vitani na katika makambi ya mafunzo ya BOSS, Willy akiwa anadonga huku anaruka hapa na pale aliwaua walinzi wa Muteba wote. Ikawa wamebaki yeye na Muteba.
Ozu naye alishambulia vibaya sana kundi la Papa. Hili ndilo kundi lililokuwa kali sana. Lakini Ozu alipigana kwa ujuzi wa hali ya juu, Akitumia magari kama ngao yake aliua mmoja mmoja akitumia bastola. Walipoanza kutumia bunduki kubwa na yeye akakamata 'machine gun' na hapa ndipo hakuwakawiza, akawa amebaki yeye na Papa. Pierre aliyekuwa anachungulia mapigano yalivyokuwa yanakwenda, aliogopa alipoona walinzi wake walivyokuwa wameteketezwa. Hivyo akatambua kuwa mwisho wa mapigano haya ungekuwa mbaya.
Alirudi ofisini kwake haraka haraka akachukua mkoba wake aliokuwa ametayarisha, akachukua bastola yake akaijaza risasi aoaktoka ndani ya ile ofisi. Alipofika nje ya ofisi alikuta mapambano kati ya Muteba na Willy. Ozu na Papa yanaendelea, Robert alikuwa naye ndiyo anaondoka nyuma ya ofisi baada ya pambanp lake na Jean. Hivi Pierre aliweza kukimbia bila upinzani mkubwa. Wote waliokuwa wanapambana walimuona lakini hawakuwa na nafasi ya kumfanyia lolote. Hivyo alipata nafasi ya kuondoka gereji Du Peuple salama. Ozu alipokumbuka sura ya Papa wakati anampiga Kofi risasi alijawa na hasira na uchungu mpya hasa ALIPOTAMBUA KUWA MTU HUYU NDIYE ALIYEKUWA ANAPIGANA naye sasa.
"Papadimitriu?" Ozu aliita. Papa hakujibu ila alitupa risasi nyingi pale sauti ilipokuwa inatokea. "Mchana umemuua ndugu yangu Kofi nikikuona sasa utalipa, utalipa madeni yote". Ozu alimpigia kelele. Ghafla Ozu aliruka juu ya gari, Papa akamimina pale risasi nyingi. Ozu aliruka tena kabla na kumuwahi na kuupiga mkono wake risasi, bunduki ikaanguka upande. Papa aliinuka na kujaribu kuirukia tena bunduki yake Ozu akampiga risasi ya kiuno akaanguka chini na kupiga kelele. Ozu alimfuata mpaka pale chini. "Umeua watu wengi sana katika maisha yako, watu wasio na makosa. sasa mimi ninawalipizia wote. Nitakupiga risasi tatu kifuani, kumlipizia ndugu yangu Kofi, na zile zitakazofuata ni kuwalipizia ndugu zangu wana mapinduzi wa Afrika uliowaua", Ozu alimsomea risala.
"Nisamehe...," kabla hajamaliza Ozu alimpiga risasi zaidi ya kumi.
Willy na Muteba walipambana vikali sana. Muteba alitumia ujuzi wake wote aliokuwa nao, lakini alimkuta Willy yuko tayari kabisa. Willy alitupa 'machine gun' akachukua bastola. Muteba aling'ang'ania 'machine gun' lakini Willy aliruka hapa na pale kumhangaisha mpaka risasi zikamuishia, hapo ndipo Willy aliporuka mpaka pale Muteba alipokuwa kabla hajachukua silaha nyingine, Muteba alisimama wakaangalia na Willy ana kwa ana. "Wewe ndiye Willy Gamba?" Muteba alimuuliza.
"Ndiyo mimi, na wewe ndiye Muteba Kalonzo?" Willy naye alimuuliza.
"Tete yuko wapi?" Muteba alimuuliza Willy.
"Yupo hapo nje ndani ya gari langu". Willy alimjibu taratibu huku bastola imemlenga Muteba kifuani.
"Umemkamata kwa nguvu?" Muteba alisema.
"Amenitafuta kwa hiari yake. Hana nafasi na watu waovu kama wewe" Willy alimtibua Muteba, jambo hili lilimtia uchungu akapandisha mori. Kama umeme aliruka na kupiga teke bastola ikatoka mikononi mwa Willy.
"Mwongo..." alipiga kelele. Hapo hapo alichomoa bastola yake nyingine kwa upesi sana na kupiga risasi pale Willy alipokuwa lakini Willy naye alikuwa ameisharuka kabla risasi hazijatua pale. Akiwa ameruka kabla hajatua chini alichomoa bastola yake nyingine akampiga Muteba risasi iliyompata katikati ya paji la uso na kumuua. Willy aliangalia chini akajiviringisha aliposimama akamuona Robert amesimama karibu naye akiwa ameshikilia bastola.
"Umemuwahi vizuri sana, sikutegemea, mimi nilikuwa tayari tayari", Robert alimweleza Willy.
"Asante sana, mtu huyu alikuwa hatari sana," Willy alijibu. Ozu alikuja anakimbia.
"Tayari?" aliuliza. Wenzake walimjibu tayari. Wote walitoka pale mbio kwani walitegemea polisi kufika wakati wowote. Walipofika pale Tete alipokuwa ameegesha gari walipanda Willy akasema. "Moja kwa moja SOZIDIME".
Tete ambaye alikuwa anawasubiri kwa wasiwasi sana alifurahi kuwaona wote wamerudi salama. Alitia gari moto na kuondoka kuelekea sehemu za Gombe. "Nimeona gari la Pierre linaelekea mjini", Tete aliwaeleza.
"Ndiyo hata sisi tumemuona", Willy alimjibu. Tete alienda na kusimamisha gari pale "CINE RAC' "Sasa utatusubiri hapa," Willy alimweleza Tete, wakatelemka wote watatu.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Robert utatupandisha sisi turuke juu ya michongoma tukiisha ingia ndani tutakufungulia wewe lango", Willy alimweleza Robert. Walienda kwenye uchochoro uliokuwa unatenganisha Cine Rac na ua wa Sozidime. Walipofika pembeni mwa ua huu wa michongoma Robert alimpandisha kwanza Willy ambaye alirukia ndani ya ua wa ofisi hii na kuwa tayari kwa pambano lolote. Kisha Robert alimpandisha Ozu na wote wawili wakawa wametumbukia ndani. Kwa mshangao wao walikuta ile ofisi shwari kabisa na hakukuwa na dalili ya kuwepo mtu. Lakini hata hivyo walikaa tayari tayari na walitembea katika tahadhari kubwa. Robert alizungukia kwenye lango Willy akamfungulia,
"Inaonekana hakuna mtu hapa lakini wanaweza kuwa wamefanya mtego, hivyo wewe Robert utabaki umejibanza nje, wakati sisi tutakapoingia ndani, kama lolote likitokea unajua la kufanya", Willy alimweleza Robert.
"Sawa", Robert alijibu. Robert alinjongwajongwa na kubana kwenye ukuta wa ile. Willy na Ozu walenda kwenye mlango wa mbele. Willy akatoa funguo zake malaya na kuanza kufungua huku Ozu akiwa tayari tayari analinda kwa lolote. Lakini kinyume na walivyotegemea, walifungua mlango ule bila kupambana na kitu chochote. Waliingia ndani wakarudisha mlango na wakajikuta wako mapokezi ya ile ofisi mahali ambapo Willy alipokuwa amefika.
Ghafla taa zikawaka, na wakajikuta wote wanaangalia ndani ya midomo ya bunduki ya watu wanne waliokuwa wamewalenga huku wamelala chini.
"Tupeni silaha zenu", walielezwa. Kuona walivyokuwa wamesakamwa walitupa silaha zao. Mmoja wa wale watu alisimama akaanza kuwapekua na kuwanyang'anya silaha zilizobaki. Mara Max akatokea.
"Oh Willy, mbona umekuja namna hii, wafanyabiashara hawavuji ndani ya maofisi ya watu, karibuni", Max alisema huku akitabasamu. "Haya tembeeni", waliamrishwa na mlinzi mmoja aliyekuwa ameshikilia 'machine gun'. Willy na Ozu walijua hapa wasingeweza kuanza lolote ila kufuata amri ili waweze kununua muda, kwani walikuwa wamejiingiza ndani ya mtego wao wenyewe kama wajinga.
"Lukamba, nenda ukafunge lile lango na kufuli na fikiri watu tulio kuwa tunawangojea wamefika," Maxx alimwamru Lukambo akiwa ameshika silaha yake sawa sawa alifungua mlango na kutoka nje. Willy na Ozu waliongozwa huku wanamfuata Max.
Robert aliona mambo yote yalivyotokea. Hivyo Lukamba alipotoka nje Robert alimvizia. Lukamba akiwa anaenda bila wasiwasi Robert alimnyemelea na alipofika pale langoni Robert alimkaba kabali kwa nyuma na kumuua halafu akamlaza chini. Robert alifungua lile lango akakimbia mpaka pale Tete alipokuwa ameegesha gari. Alitoa kikaratasi kilichokuwa na jina na anuani akampa Tete halafu akamweleza. "Nenda pale kwenye kibanda cha simu kiko hapo kwenye kona ya upande ule wa Cine Rac. Mpigie huyu Umba Kitete ni rafiki yangu, na ni afisa wa C.N.D. mwambie Robert anasema mambo tayari, aje hapa Sozidime na atakukuta wewe na wewe utaingia naye ndani, afanye haraka maana mambo tayari. Yeye anaelewa nilikuwa nimezungumza naye wakati tulipokuacha na Ozu, tukaondoka na Willy saa zile zajioni. Hivi utamkuta yuko tayari, fanya haraka".
"Usiwe na wasiwasi", Tete alijibu, Robert aliweka bastola yake sawa sawa haraka haraka akarudi ndani ya ua wa Sozidime akajifanya yeye ndiye Lukomba. Kwa vile Max na watu wake walikuwa wanajua kuna Willy na Ozu tu, hivyo walipowakamata wale wawili walijua hakuna mtu mwingine. Jambo hili lilimpa faida sana Robert kuingilia ofisi za Sozidime bila kipingamizi kikubwa.
Willy na Ozu waliongozwa mpaka ofisini kwa Fernand ambako Max alifungua ule mlango wa siri, na kuwatelemsha kuelekea chumba cha siri. Jambo hili halikuwashangaza sababu walikuwa na habari nalo kabla. Max aliwaongoza mpaka katika chumba cha siri ambako walimkuta Pierre na Fernand wamekaa wanakunywa kahawa.
"Nimewaleta hawa watu ambao wametupa taabu nyingi sana." Max aliwaambia Fernand na Pierre.
"Ohooo, karibu Willy Gamba pamoja na Kapteni Petit Osei, nashukuru sana kuwaona. Lazima nitoe heko zangu kwenu kwani kazi yenu mmeitekeleza vizuri sana ingawaje hamtaweza kuimaliza kabisa. Kwani hapa ndipo mmefika mwisho wenu," alijigamba Fernand halafu akatoa kicheko cha dharau kisha akaendelea; "Nchi huru za Kiafrika, nchi huru za Kiafrika... zitaweza nini?"
"Haziwezi kamwe," alijibu Pierre.
"Unajua bwana Gamba mimi nasikitika sana kuwaueni vijana shupavu na jasiri kama nyinyi, lakini itabidi nifanye hivyo maana hiyo ni amri kutoka kwa wakubwa zangu. Lakini kabla sijawaueni nitawaeleza kwanini nchi za Kiafrika hazitaweza kamwe kuishinda Afrika Kusini", alinyamaza kidogo kupitisha mate halafu akaendelea.
"Nchi za Kiafrika hazina umoja. Nchi za Kiafrika viongozi wake wengi ni watu wapenda pesa wala siyo viongozi wanaopenda nchi zao kwa dhati, OAU ikipiga kelele Afrika Kusini iwekewe vikwazo vya uchumi na jambo hili likipitishwa kwenye kikao cha viongozi wa nchi huru za Kiafrika, kesho yake viongozi wengine wanatupigia simu na kutuambia tusijali hayo yaliyopitishwa, hiyo ilikuwa ni siasa tu. Uhusiano wetu utaendelea hapo hapo ulipokuwa. Kwa hivyo nchi za Kiafrika zinakosa umoja na hili ndilo tatizo lake kubwa. Kwa mfano utakuta BOSS inasaidia viongozi wengi wa nchi huru za Kiafrika wasiweze kuangushwa. Wewe unafikiri mtu uliyemsaidia namna hiyo ukimuomba msaada wa kukupa siri za OAU atakataa. Kwa taarifa yenu BOSS itasonga milele, na itaendeleza shughuli zake bila shida katika Afrika. Hao wapigania uhuru tutahakikisha tutawateketeza, kiasi mlichotuchafulia sisi hatukijali ni kama mtu aliyejikwaa tu na kuumiza kidole. Lakini akishakiangalia na kukifunga anaendelea na safari yake." Fernand aliangua tena kicheko.
"Lakini ujuwe siku zaja, wapo vijana wanamapinduzi wa Kiafrika ambao watateketeza kabisa udhalimu wa makaburu na Afrika nzima itakuwa huru. Kitu ambacho lazima ujuwe ni kwamba utafika wakati vijana wa Afrika watakuwa wamekandamizwa sana na hawatakubali lazima watafanya mapinduzi makubwa ambayo yataangusha serikali zote za vibaraka, na kuua ukoloni mamboleo na kujenga serikali za kizalendo. Mapambano bado yanaendelea, ushindi ni dhahiri", Willy alizungumza kishujaa kabisa.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Wapige risasi hawa, wananieleza siasa inayonuka, ambayo sitaki kui..." kabla Fernand hajamaliza kusema, mlango wa hiki chumba ulifunguliwa ghafla na Robert akajitupa ndani bastola mbili mkononi na kuwashambulia walinzi wa Fernand ambao walishituliwa bila kutegemea, hivi hawakuwa tayari kwa tukio. Kule kufunguliwa tu mlango Willy na Ozu waliruka upande mwingine, na kumpa Robert nafasi ya kuwapiga risasi wale walinzi. Bastola za hawa walinzi zilidondoka na moja ikarukia karibu na Willy alipokuwa akaidaka na kumsaidia Robert katika mashambulizi ambayo yalichukua chini ya nusu dakika na kuweza kuwa wameua walinzi wote pamoja na Max. Pierre alikuwa amejeruhiwa sana, Fernand ndiye alikuwa mzima akiwa anatetemeka ovyo.
"Vijana wa C.N.D. watafika sasa hivi. Tete atakuja nao", Robert alisema huku Willy na Ozu wanamwangalia kwa mshangao mkubwa. Willy alimwendea Fernand akamfunga mikono na miguu na akamweleza, "Huu ndio mwanzo wa kuwasafisha majasusi wa nchi zinazopinga maendeleo ya Muafrika, wewe ndiwe utakuwa mfano". Ozu alimwendea Pierre lakini alikuwa mahututi sana lakini akatambua kuwa angeweza kufa dakika yoyote.
"Muteba, Jean na Papa wamekufa sasa wewe", alimweleza. Willy alifungua mkoba wa Fernand uliokuwa pale kwenye meza, na ndani yake akakuta makaratasi yenye habari za kijasusi zilizonaswa katika nchi nyingi za Kiafrika. "Karatasi hizi ndizo zitakuwa kielelezo", Willy alisema. Mara wakasikia nyayo zinateremka ndazi. Haraka haraka Tete akiwa anaongoza msafara wa watu sita aliingia.
"Oh Willy nilifikiri tutakuta mambo yameshaharibika", Tete alisema akamrukia Willy, akaning'inia shingoni mwake na kumbusu.
"Kazi na dawa", Ozu aliwatania.
"Kazi imekwisha. Bwana Umba huyu mtu wako. Mfuko huu umejaa karatasi ambazo ni vielelezo. Nyumbani kwangu kuna shahidi mwingine twende ukamchukue. Hadithi kamili nitakueleza baadaye", Robert alimweleza Umba afisa wa juu wa C.N.D.
Huko sehemu za Nsele ambayo ni sehemu inayotumiwa na wakazi wa Kinshasa kwenda kupumzika wakati wa siku za mapumziko, na ambayo iko kando kando ya mto Congo. Jumapili hii palijaa watu. Sehemu hii ambayo iko kilomita 60 kutoka Kinshasa ni sehemu nzuri sana. Katika watu waliokuwa wamefika hapa kulikuwa na kundi la wavulana watatu na wasichana watatu ambao walivutia sana watu wengine kwa jinsi walivyokuwa.
Siku tatu baada ya kusafisha kikundi cha 'WP' Willy na wenzake walikuwa wanapumzika hapa Nsele. Willy akiwa katika nguo za kuogelea alilala kando kando ya bwawa la kuogelea lililoko sehemu hii linaloitwa 'Bassin Olympic' na huku Tete ambaye naye alikuwa katika nguo za kuogelea, alijilaza ubavuni mwake huku akimpapasa kifuani kwa mkono laini wakiota jua. Mara Ozi akiwa ameshikana mikono na Ntumba na Robert akiwa amemshikilia Ebebe kiunoni na wote wakiwa katika nguo za kuogelea walikuja mpaka pale Willy na Tete walipokuwa wamelala. Ozu akiwa amebeba gazeti mkononi.
"Willy umeshaona gazeti la 'Salongo' leo" Ozu alimuuliza.
"Bado", Willy alijibu.
"Haya soma habari hizi hapa", Ozu alimuonyesha. Willy alichukua gazeti, yeye na Tete wakaanza kulisoma. Lilikuwa limeandikwa kama ifuatavyo.
"Wapelelezi wa OAU juzi usiku waligundua na kuteketeza maofisi yaliyokuwa yanatumiwa na majasusi wa Shirika la Ujasusi la Afrika Kusini 'BOSS'. Ofisi hizi ambazo zilikuwa mjini hapa zilijidai ni za biashara na kumbe za majasusi zimeteketezwa kabisa na wapelelezi hao. Hili limekuwa onyo kali sana kwa Afrika Kusini kuacha mbinu zake za kishenzi inazotumia katika Afrika huru.
Wakati huo huo Mwenyekiti wa Kamati ya Ukombozi ya OAU, ambaye naye yuko mjini hapa tokea juzi amezitaka serikali zote za Kiafrika zenye mikataba na uhusiano wowote na Afrika Kusini kuvunja mara moja mikataba hiyo vinginevyo afadhali zijitoe katika umoja wa nchi huru za Kiafrika, ili harakati za Ukombozi wa Kusini mwa Afrika ziweze kupata nguvu kamili. Na huko Algiers Algeria. Umoja wa Chama cha umoja wa vijana wa Afrika (PAYM) ambacho kina makao yake makuu nchini humo, kimeitisha maandamano kwenye ofisi zake zote zilizoko katika nchi mbali mbali za Kiafrika ya kuzitaka nchi za Kiafrika zenye uhusiano wa kiuchumi na Afrika Kusini kuvunja uhusiano na nchi hiyo baada ya kugundulika mbinu zake", gazeti hilo lilieleza. Willy aliweka gazeti kando.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Tutaenda wote Dar es Salaam?" Tete alimuulza Willy alipomuona amemaliza kusoma gazeti. Willy aliwaangalia wenzake waliokuwa wamesimama kando wakingojea atoe maelezo yake juu ya habari zilizoandikwa kwenye gazeti hilo lakini akainuka na kumlalia Tete kifuani akamjibu. "Tutaangalia", huku akimbusu.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment