Simulizi : Msitu Wa Solondo
Sehemu Ya Pili (2)
Golam akachuchumaa na Amata akafanya vivyo hivyo,
“Papasa kwa mkono polepole mpaka ufike ukingo wa mto kisha tumbukiza japo kidole uone maji yanaelekea wapi!”
Golam alimwambia Amata. Amata akafanya hivyo akapapasa na mara akahisi kafika mwisho wa kanjia kale na kelele za maji ziliongezeka, akaingiwa na woga mkuu, moyo wake ulikuwa unadunda kwa kasi na kijasho kumtiririka. Akayagusa yale maji yalikuwa ya moto kama yako jikoni akahisi mkono wake unavutwa upande wa kulia, akajaribu kuutoa alihisi kama kitu kimemshika mkono kinamvuta majini, nguvu zikamuishia akapiga keleleCHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Golaaaaaaaammmmmmmmm!!!”
Kishindo kikubwa kikasikika cha kitu kutumbukia majini, Golam akapiga hatua mbili mbele akaita
“Amataaaaaa!!!”
Alipoona kimya akajirusha majini akapiga mbizi maridadi, ndani yamaji yale palikuwa na mimea iliyotambaa akamuona Amata amenasa kwenye mimea hiyo akaogelea na kuanza kumsaidia akitoa kisu chake kidogo na kuanza kukata mimea ile, kila alipokata ilitoa kitu kama damu, alipofanikiwa kumtoa Amata wakaanza kuogelea kinyume na maji haikuwa kazi ndogo. Amata hakuwa mzuri kuogelea kama Golam kila mara Golam alijikuta kamuacha Amata nyuma, Golama akamshika Amata huku upande mmoja kashika kwenye ncha ya jiwe akamvuta Amata kwa nguvu zote na kumuweka mbele yake, wakaendelea kuogelea sasa Amata akiwa mbele na Golam nyuma. Amata akiwa mbele aliendelea kuogelea kwa shida kwa kuwa maji yalikuwa yanasukuma nyuma, Golam alijitahidi kumlinda Amata asije kubebwa na maji. Baada ya kuogelea kama masaa mawili hivi Amata alianza kuona maji yale yanang’aa kwa mwanga wa nje, alikuwa amechoka hata kujisogeza haikuwa rahisi, Golama alimvuta Amata na taratibu walijikuta wanafika nje ya lile pango kubwa lakini bado kasi ya maji haikuwa ndogo, Amata akahisi kitu kimemshika mguu akahangaika kujinasua akashindwa, Golam akajitahidi kumvuta lakini haikuwa rahisi wote walikuwa wamechoka sana, Amata akaponyoka kutoka katika mikono ya Golam, akahisi kuvutwa tena majini mara hii ni kwa nguvu zaidi, alihisi kama mikono ya watu imemshika miguu, alikunywa maji akajaribu kujizuia lakini ikashindikana alilegea na kukosa nguvu kabisa. Golam aliibuka nje ya mto, akarushiwa kamba na kuishika barabara akavutiwa nje
“Amata yuko wapi?”
aliulizwa, akajibu kwa ishara tu kuoneshea kuwa yuko ndani ya maji. Jiwe kubwa lililosukumwa na maji lilimgonga Amata kwenye paji la uso akachanika ngozi ya usoni damu zikaanza kumvuja kwa nguvu, mara akajikuta ameibuka nje na kunaswa kwenye miti midogo iliyo jirani na hapo, Golam akamuona Amata, wakafanya juu chini na kumnasua na kumleta nchi kavu. Wakakoka moto mkubwa ili kuwapa joto Golam na Amata, wakamsaidia Amata kutapika maji yale na kuzuia damu iliyokuwa inatoka katika jeraha lake. Amata akapoteza fahamu.
************
Msitu wa Solondo ni msitu mkubwa wenye miti mingi na wanyama wakali, ndani yake wanaishi watu wa jamii mbalimbali wenye mila tofauti za kizamani. Watu wengi waliuogopa msitu huo kutokana na kile kilichosemwa kuwa kuna miujiza mingi, uchawi na hatari za kila aina pia waliamini kuwa majini na mashetani hutokea katika msitu huo. Msitu huo ambao wakoloni wa kijerumani na kiingereza walihifadhi mali nyingi sana uliachwa katika hali hiyo hakuna hata aliyediriki kuingia baada ya kusikia kuwa wapo waliojaribu kwenda huko hawakurudi wengine waliliwa nyama na kupotelea huko. Kwa hiyo kila mtu aliogopa hata kuzungumzia. Matambiko na ibada za kijadi zilifanyika katika msitu huo, katikati ya msitu huo kulikuwa na jiwe kubwa sana jeusi ambalo kwa kuliona tu linatisha na inasemekana lilikuwa linaongea, hapo ndipo walipotolea sadaka ya damu jamii walioishi ndani ya msitu huo. Katika jiwe hilo kulikuwa na pango kubwa ambalo ndani yake kulikuwa na mapango madogomadogo mengi, jamii iliyokuwa inaishi katika msitu huo ambayo iliitwa ‘Gorino’ , gorino kwa lugha yao ilimaanisha ‘mla watu’ walikuwa wanawakamata watu wanaoingia ndani ya msitu huo na kuwaficha katika pango hilo ambalo wao waliamini lilikuwa ndio nyumba ya Mungu wao na kila walipotaka kutoa sadaka walichukuwa mmoja wa watu hao na kutoa sadaka ya damu, waliwakata vichwa na kuwatoa kafara, nyama iliyobaki ililiwa na vichwa vilining’inizwa kama mapambo ya eneo hilo hii ilikuwa ni sherehe kubwa sana ngoma zilipigwa na walicheza, hakuruhusiwa mwanamke kusogea hapo kwani waliamini mwanamke atamkasirisha mungu wao. Lakini eneo hili ambalo wakoloni walilitumia kama hifadhi ya mali zao lilikuwa ni lasiri sana kiasi kwamba hata wakazi wa huko na pembezoni hawakujua ukweli huo, madini mbalimbali yaliyohifadhiwa pangoni humo miaka ya elfu moja mia nane hamna aliyeyagusa kwa kutokujua, Msitu huo ulibaki katka hali niyo watu weupe wengi walijaribu kuingia kwa kuwa walijua ni nini kipo huko lakini nao waliishia uko huko.
**************
Amata alirudiwa na fahamu, akiwa pale chini bado alitazama juu na kuona watu watatu kati yao alimtambua Golam ambaye alichuchumaa jirani yake pembeni yake kulikuwa na mwanaume mwingine mwenye asili ya kizungu ambaye hakumjua alimuona mwanamke mwingine naye alikuwa na asili ya kizungu, Amata alizidi kuchanganyikiwa kwani hakuwajua hao wote ni akina nani, ghafla alipata mshtuko ambao ulimfanya anyanyuke ghafla na kushikwa na mshangao kwa kumuona huyu aliyesimama mbele yake sio mwingine ni Saringo. Huyu alimtambua bila kificho kwani kati ya wote huyo ndiye aliyemfahamu kwanza, Amata aliwatazama wote mmoja baada ya mwingine ila alimkazia macho sana Saringo ambaye bado alikuwa hamuelewi uhusiano wake na matukio yote haya.
“Amata, kaa chini tuongee kidogo...”
Saringo alimuomba Amata. Amata akaketi na wengine wote wakafanya hivyo. Wakiwa wamezunguka moto uliokuwa unawaka hapo alfajiri hiyo ili kuidhibiti baridi kali iliyowanyanyasa, kando yao miti mirefu na mikubwa iliwazunguka, mto mkubwa wa maji mengi yaendayo kasi ulipita eneo hilo, kelele za ndege wakubwa zilisikika.
“Hawa unaowaona ni rafiki zangu, huyu anaitwa Bw. Stephan Van Leuwen kutoka Poland na huyu ni rafiki yake kutoka German anaitwa Bi. Hellen Schurman wote ni wakufunzi katika chuo kikuu cha Heidernburg huko Ujerumani, ni wataalamu wa mambo ya kale. Huyu mwengine unamfahamu Golam, huyu ni binamu yangu mtoto wa mjomba wangu, na mimi naitwa Saringo mjukuu wa mzee Koloto.”
Saringo alitoa utambulisho huo, kisha akageukia upande wa pili
“Huyu anaitwa Amata!”
alimtambulisha kwa kifupi
“Amata Ga Imba, au mate ya Simba”
Golan aliongezea na wote wakatabasamu
Amata bado alimkazia macho binti huyu anayeitwa Saringo ambaye alionekana mkakamavu akiwa ndani ya jinsi iliyomkaa vizuri na fulana yake nyekundu ambayo kwa nje aliifunika na kishati cha buluu angavu ambacho hakufunga vifungo ila alifunga fundo kwa chini, buti kubwa nzuri ya kijeshi aliyoitupia mguuni mwake haikuwa ya kawaida. Amata bado alikuwa hajaelewa vizuri kinachondelea hapo alipomtazama yule mzungu ambaye kichwani mwake alivaa kofia kubwa kama ile ya Marlboro akiwa anavuta kiko yake, mgongoni akiwa na begi la kijeshi na mkononi akiwa na bunduki aina ya ‘rifle’, na rafiki yake wa kike mwenye macho makali daima litafuna jojo akiwa kavaa jinsi ya kaki na shati zito pia la kaki, alionekana mtaratibu na mpole kiunoni mwake alikuwa na bastola mbili kushoto na kulia. Amata aliogopa sana kwakuwa kwanza alizoea kuwaona wazungu makanisani tu na wakiwa wamevaa makanzu, alizoea kuona bunduki za kuwindia tu kama gobole ambalo hata yeye aliachiwa na marehemu baba yake. Alikuwa na mawazo mengi yaliyokuwa yakipita kichwani mwake.
“Tuko hapa kwa nia moja tu, tunakwenda ndani ya msitu wa Solondo, sisi watano na wewe tuliona unatufaa, mimi ndiye nilikutafuta kwa gharama kubwa”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Saringo alimuambia Amata. Amata akaendelea kumsikiliza kwa makini, Saringo akaendelea
“Nilikuja kijijini kwenu kumsalimia shoga yangu Chausiku ambaye unamfahamu sana, nikiwa pale ule ugomvi uliokuhusisha wewe niliuoana na nilivutiwa kwa jinsi ulivyompa mkong’oto yule bwege. Nikafuatilia mwisho wake kuona, nilipojua kuwa umekamatwa na uko polisi nikaja kukutembelea nilikuja tu kukutia hasira na si kingine lakini nilipanga wewe ufungwe nikiwa na lengo moja kuwa kule gerezani utakutana na binamu yangu Golam na kweli ikawa hivyo, Golam nilimpa kazi muda mrefu ya kutafuta mfungwa mkakamavu, mpiganaji, asiyeogopa kitu na ulivyofungwa wewe nikamwambia Golam akuchunguze, siku chache tu akanipa taarifa nzuri ya kuwa ulimpiga hata mtu ambaye wao wote wanamuogopa, ndio hapo tukasuka mpango wa kukutorosha wewe na Golam, na mpango huo tuliusuka mimi na hawa wazungu kwa kuwa sisi tulikuwa na ramani ya gereza lile, njia zote za siri ambazo wenyewe wakoloni walizitumia kuwakimbia maadui pindi wanapovamiwa.”
Saringo akakohoa kidogo na kuendelea
“Baba wa babu yangu alifanya kazi kama askari wa mkoloni na kituo chake kilikuwa hapo gerezani, wakati huo ikiwa ngome ya mjerumani kabla ya kuchukuliwa na waingereza, yeye ndiye aliiba hii ramani, yeye pamoja na wenzake ndio walikuwa wanaenda Solondo kuhifadhi vitu vingi vya wajerumani, alimpa babu yangu siri hii miaka mingi sana mpaka kwa baba yangu, baba yangu alinipa siri hii na kabla ya kufa kwake alifuatwa na watu wengi sana waliodhani kuwa yeye alikuwa anajua zaidi na amefika huko katika pango la msitu wa Solondo. Kabla hajafa alinipa mkoba wake mchafumchafu nilipoufungua ndani ndio niliona makaratasi ya kizamani na maandishi ya ajabu ajabu siyaelewi, nilihifadhi karatasi zile vizuri, na nilipokwenda masomoni Ulaya ndipo nilikutana na hawa rafiki zangu katika darasa moja, nilipojua vizuri kijerumani ndio nilipojua maana na siri nzito iliyomo katika makabrasha yale, ndio hapo tulipopanga kikosi kazi kuukabili msitu huu wa Solondo hadi tuone mwisho, tukaona wewe pia unafaa kuwepo katika kikosi kazi hiki”.
Amata alibaki ameduwaa
‘Msitu wa Solondo!’
alijiwazia aliona kama yuko katika ndoto labda ataamka lakini haikuwa hivyo.
“Saringo!”
Amata aliita na kuweka pozi kabla hajaendelea kuongea
“unaujua msitu wa Solondo au umeusoma tu kama ulivyosema?”
“Sijawahi kuingia msituni ila sasa tumeamua kwenda”
Saringo alimueleza Amata
“Msitu wa Solondo sio wa kuuchezea, tutakufa sote hakika, kuna mashetani na viumbe vya ajabu, kwa nini tuyakatishe maisha yetu tukiwa bado vijana? Kuna nini kule cha maana? Acheni upumbavu wenu. Golam ndio hii safari uliyotaka twende?”
Amata alimuuliza Golam.
“Amata! Hii ndiyo safari, usiogope zile ni hadithi tu, wazee hawakupenda twende huko lakini ni msitu tu wa kawaida. Ujue kila kona sasa unatafutwa mfungwa uliyetoroka utajificha wapi? Twende Solondo”
Golam alijibu na kutoa tabasamu lake la kuvutia ambalo daima humfanya Amata kucheka.
“Hao wazungu wanaweza kutembea kwa miguu? Maana ni safari ya siku kama saba hadi tufike.” Amata aliuliza kwa wasiwasi
“Wataweza ndio maana wamekuja.”
Saringo alijibu. Amata akatikisa kichwa kuashiria kuwa ameridhika, akanyayuka akaingia kwenye vichaka vya karibu akatokomea huko. Saringo, Golam na wenzao walibaki kumsubiri bila mafanikio.
***********
Walibaki kujadiliana tu nini cha kufanya kwa kuwa hawakujua Amata kaenda wapi na kwa nini. Wakiwa katika butwao hilo mara walisikia kelele za mnyama mwenye hasira kutoka porini wakiwa bado hawapo vizuri mnyama aina ya Ngiri alikatiza kati kati yao kwa kasi ya ajabu alimpiga, Bw Stephan alipigwa kikumbo na kudondoka vibaya kwenye mawe bunduki ikianguka upande mwingine, wengine walikimbia kila mtu upande wake wakiwa wamechanganyana hawaelewi kilichotokea. Bw Stephan aliumia sehemu ya mkono alikuwa akivuja damu. Amata akasimama mbele yao
“nauliza tena! Nyinyi mnaweza kuingia Msitu wa Solondo? Huyo ni ngiri tu mmekimbiana hivyo wengine na bunduki zenu mmeshindwa kujipanga kumshambulia, sijui kama tutarudi mi nina wasiwasi.”
Amata aliwaeleza huku akitweta.
“Amata acha ujinga!”
Saringo aling’aka
“Sio ujinga mimi nilienda porini kumkurupusha huyo mnyama ili niwapime uwezo wa kukabiliana na hatari za ghafla, maana huko msituni kuna wanyama wakali, na isitoshe kuna mashetani ambayo hata uyaoni kwa macho we utahisi unatandikwa bakora tu! Sasa itakuwaje?”
Amata aliwauliza kwa ukali
“Haya na tuanze safari mengine tutayaona uko huko!”
Saringo aliwaambia wengine.
Safari ya kuingia Msitu wa Solondo ikaanza, Golam akiwa na jisu kubwa kiunoni mwake aliongoza msafara akifuatiwa na Bw. Stephan na bunduki yake kubwa, Saringo akiwa na begi lake la kijeshi mgongoni alionesha kutembea mwendo wa kikakamavu haswa, Bi.Hellen mkimya asiye na maneno mengi aliendelea kuchapa mwendo na bastola zake kiunoni alionekana amejiandaa haswa katika safari ile ngumu. Walipita katikati ya msitu ni ndege na wadudu ndio waliokuwa wanawasindikiza, Amata akiwa na uta wake mgongoni alikuwa wa mwisho katika msafara huo ambao ulikuwa ukiongozwa na Golam hakukuwa na anayeongea kwa wakati wote huo, walikuwa wakifuata kanjia kadogo kanakoelekea milimani, ilionekana kuwa Golam alikuwa mzoefu wa eneo hilo kwa kiasi fulani ukiacha Saringo ambaye aliku na karatasi kubwa tu la khaki ambalo ndani yake kulikuwa na michoro mingi ya ajabu na isiyoeleweka. Amata akiwa hana wasiwasi nyuma ya wote alivuta hatua uku akiwa na mgagi wake mdomoni, baada ya mwendo mrefu wa kama masaa matatu hivi walifika mtoni ambako ilibidi wavuke kwenda ng’ambo ya upande wa pili, maji ya mto yalikuwa yanakwenda kwa mwendo wa wastani, maji haya yaliyochanganyika na udongo yalikuwa na rangi kama chai ya maziwa.
Wote walisimama kando ya mto huo wakiyaangalia maji kwa makini
“Inabidi tuvuke!”
Saringo aliwambia wenzake. Wote wakatazamana na kuanza kujiandaa kwa kuvuka hakuna aliyejua kina cha mto huo wala hatari yoyote iliyopo hapo, hakuna aliyeonekana kuogopa bali kila mtu alionesha ujasiri, Amata alionekana kasimama tu kana kwamba hakuwa mmoja wao katika hilo.
“Kuna kamba? Inabidi mmoja aogelee mpaka ng’ambo akafunge hiyo kamba kwenye mti ili wengine iwe rahisi kuvuka”
Amata alitoa rai. Na kila mmoja kukubaliana na wazo hilo. Stephan akatoa kamba ndefu ya kutosha Golam akajitolea kuivusha kamba hiyo. Akaichukua na kujifunga kiunoni tayari kwa kuvuka, aliyaangalia yale maji kwanza kisha akachukua podo na uta wake na kuuweka mgongoni tayari kwa kuvuka
“Naomba mnilinde”
Amata aliwaambia wenzake na kujitoma ndani ya maji aliogelea kwa ustadi sana kukatisha mto huo, maji yalikuwa magumu kwake katika kuvuka. Alikotoka wote walikuwa kimya kumuangalia Amata jinsi anavyoyakata maji japo si kwa ustadi sana wakiwa bado katika kumwangalia mara walimuona Amata akizama kabla hawajajiweka vizuri waliona mkia wa mamba mkubwa ukitokeza juu ya maji
“Mamba!!!”
Golam alipiga ukelele. Amata alibanwa mguu na mamba alijitahidi kujinasua lakini mamba yule alimzamisha tena, aliipomuibua mara ya pili alichomoa mshale mmoja kutoka katika podo lake na kumchoma mamba yule jichoni, Mamba alimuachia Amata na akajigeuza chali Amata kwa ustadi mkubwa alimchoma tena eneo la kifua mamba yule kisha akajaribu kuogelea kwa kujihami, mamba yule akajinyayua juu Bwana Stephan kwa ustadi mkubwa alimlenga na kumpiga risasi mbili eneo la tumbo mamba yule alijibwaga majini...
mfu!.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Bw Stephan akashusha bunduki yake na kushusha pumzi ndefu, Amata alifika ng’ambo na kuifunga kamba ile mtini kisa kuwapa ishara wengine kuvuka, mmoja baada ya mwingine walivuka na hatimaye wote walifanikiwa kuvuka. Bi Helen aliuangalia mguu wa Amata lakini haukupata majeraha makubwa alipohakikisha kuwa anaweza kusonga mbele basi safari ikaendelea. Giza lilianza kuunyemelea msitu
“Hapa tunaweza kulala”
Amata alilisisitiza wakakoka moto na kupumzika. Kila mtu akiwa amejilaza kwa mang’amung’amu. Saringo alilala jirani kabisa na Amata, Hellen akiwa jirani na Stephan, Golam alikuwa mbali kidogo kakaa kaegemea mti peke yake. Usiku mnene ulifika msitu wote ulitulia, moto uliendelea kuwaka polepole, Golam alinyanyukla pale alipo na kuja kwa wenzake
“Amata!”
akamuamsha Amata kwa upole Amata akaamka, Golam akamuonesha ishara ya mkono kuangalia upande wa pili, Amata aliona wasichana wawili kwenye kamfereji wakiwa kama walivyozaliwa, weupe, warembo wana nywele ndefu. Wakiwa wanatazamana macho na wasichana wale, mara wale wasichana wakaanza kuwaita kwa ishara ya mkono, Golam alichanganyikiwa akiwa kasimama wima mwili wake ukionekana wenye hitaji baada ya kukaa gerezani miaka sita bila kuona hata utupu wa mwanamke alivutiwa na wasichana wale hata kusahau kila kitu na kutamani kwenda. Amata aliwaangalia kwa makini, akili ikamrudia ghafla
‘msituni hapa wasichana hawa wametokea wapi?’.
“Golaaammmm”
Amata aliita kwa nguvu, ukelele uliowaamsha wengine, Golam aliendelea kuelekea kwa wale wasichana huku akianza kuvua nguo zake, Golam aliwafikia wale wasichana nao wakamdaka na kuanza kufanya mapenzi, kelele za mahaba zilisikika kwa nguvu hata zikageuka kuwa kelele za kutisha za wanyama wa ajabu lakini pale walipokuwepo hapakuonekana mtu tena.
**************
Amata alibaki kaweka mikono yake kichwani huku akitokwa na machozi, Saringo
Alishindwa kujizuia kulia kwa sauti na uchungu Hellen alimsaidia kumnyamazisha na kumpa moyo, Stephan alibakia akiangalia kwa mbali japo mkononi mwake alikuwa na bunduki yake kubwa lakini haikuweza kufanya chochote kwani pale walikutana na ulimwengu mwingine.
Upepo ulivuma taratibu usiku ule na moto uliendelea kuwaka taratibu, wakiwa wameuzunguka moto huo kila mmoja akiwa kimya akipanga na kupangua yaliyo kichwani mwake
“Msitu umemmeza...”
Amata alisema kwa sauti ya upole
“One down, four to go!”
Hellen aliongeza huku akirushia vijiti katika moto. Milio ya bundi na wanyama watawalao usiku vilisikika kutoka ndani kabisa ya msitu huo
“Masikini Golam!”
alisikitika Saringo, Amata akamsogeza karibu na kumbana ubavuni kwake akimpa maneno ya faraja. Hellen aliinuwa mkono wake wa kushoto na kusoma saa yake iliyokuwa bado inajizungusha kuonesha wakati unavyokwenda, ilitimu saa kumi na nusu alfajiri, akavuta begi lake na kutoa kijiguduluia kidogo na kutengeneza kahawa ambayo wote walikunywa na kuchangamka upya. Alfajiri hiyo ilikuwa tulivu, kibaridi kilipuliza kwa upole, wote wanne walianza safari ya Solondo kwa siku ya pili,
“Sasa tuwe makini zaidi maana tunazidi kuingia ndani ya msitu wa Solondo na tunakabiliwa na mauzauza mengi”
Amata aliwasisitizia wenzake huku wakiendelea kukatisha pori lile nene, walikokuwa wakienda wote hawakujui isipokua tu kadiri ya maelekezo ya mchoro wa kale ambao mara nyingi Stephan na Saringo waliusoma uliwaelekeza upande Fulani na sasa uliwaekeza kuutafuta mbuyu mkubwa ambao upo huko ndani ya msitu na kwamba kutoka mbuyu huo ndio hasa atapata maelekezo sahihi ya wapi waelekee. Waliendelea mbele huku wakitumia panga kukata manyasi marefu yaliyofanya njia hiyo kuwa ngumu kupita. Amata aliyekuwa mbele alitumia ujuzi wake wote kukata manyasi hayo ambayo kana kwamba yaliwasihi wasiendelee na safari yao ngumu. Wakiwa katika mwendo wa tabu sana dhidi ya nyasi ndefu na vichaka vya kutisha, miba mikali iliyowachoma na kuwakwangua kila upande wa miili yao lakini hawakukata tama hata kidogo, mara wakasikia mvumo kama wa wadudu wengi warukao, Amata alipoinua macho kutazama juu aliona mzinga mkubwa wa nyuki na wengi wakirandaranda huku na huko, Amata akawapa ishara wenzake kuonesha wawe watulivu dhidi ya nyuki hao wenye hasira. Helen alionekana kuchoka sana akiwa kamuegemea Stephan begani huku wakiendelea na safari yao
“Tupumzike kidogo”
Stephan aliomba kwa kutumia Kiswahili chake cha kubabaisha, jua lilikuwa ni kali mno wakaketi chini ya mti mkubwa na kupumzika wakinywa maji na mikate waliyobeba.
“Amata, inaonekana safari za msituni unazijua sana eee!?”
Saringo alimuuliza Amata
“Nilipokuwa na marehemu baba yangu tulikuwa tukienda kuwinda mara nyingi na yeye ndiye alinifundisha lugha na tabia ya msitu”
Amata akajibu huku akiendelea kula mabungo aliyoyachuma porini.
“Lugha na tabia ya msitu! Ni vitu gani hivyo?”
Saringo aliuliza kwa mshangao, akasogea karibu na Amata kana kwamba alitaka kujua vizuri juu ya maneno hayo.
“Msitu huongea Saringo, na una tabia pia kama wewe ulivyo!”
Amata alijibu
“msitu una mambo mengi sana, hatari kubwa zipo, vyakula vingi vinapatikana na pia wanyama wa kuliwa na kula binadamu wapo”
akamtazama Saringo aliyeonekena kuvutiwa na habari hiyo
“pia msitu hukwambia juu ya hatari ijayo na ya namna gani, baba yangu alinifundisha haya yote kwa kuwa yeye kalelewa msituni robo tatu ya maisha yake”
Amata alimalizia kusema.
“Ina maana wewe umeshawahi kuja huku Solondo?”
Hellen alimtupia swali Amata
“Hapana, ni mara yangu ya kwanza kuja ndani kabisa ya msitu huu, na baba yangu aliniambia nisije kujaribu kuingia maana msitu huu unaaminiwa unakula watu, sikuwahi kuelewa kauli ile lakini sasa nimeijua maana yake!”
Amata alimjibu Hellen
“Kwa vipi umeijua hiyo kauli?”
Stephan alidakia
“Golam! Golam amemezwa na msitu”
alijibu na kutikisa kichwa kuoneshwa masikitiko yake, kisha akaendelea
“tunakokwenda hatukujui lakini hatari kubwa iko mbele yetu, kwa kuwa tumeamua tuendelee, ila tusishangae tutakapopoteana huko mbele”
Amata alimalizia kauli yake na kumtolea tabasamu Hellen akageuka upande wa pili kwa kuwa daima hakupenda kumwangalia Amata usoni maana tangu alipomuaona mara ya kwanza kule mtoni mara baada ya kutoroka gerezani alijikuta moyo wake ukimpenda ghafla kijana huyu, fukara asiye na dira ya maisha lakini mzuri wa uso na siha ya kiuanaume zaidi ya hapo kwa ujasiri mkubwa alionao wa kupambana na hatari na kujitolea mhanga, hilo ni swala ambalo Hellen lilizidi kuongeza mapenzi kwa Amata tatizo tu ni kuwa pale alikuwa na mchumba wake Stephan hivyo hakuthubutu kabisa kuonesha hali hiyo, na mara nyingi Saringo alipokuwa jirani na Amata, Hellen alisumbuka sana moyoni.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Stephan aliinuka pale alipoketi na kuchukua kimkoba chake kidogo ambacho ndani yake kulikuwa na kibuyu kidogo akaenda karibu na kijito kidogo umbali wa kutupa jiwe, kijito kile kilichosongwa na mitete mingi kilikuwa na maji machache yakitembea kwa taratibu sana. Alipofika pale alichota maji na kujaza kibuyu chake, kisha akaanza kutoa nguo zake ili apate kujimwagia maji. Amata akiwa kwenye maongezi na Saringo na hellen mara Amata akanyamaza ghafla na kutaza kwenye mitete ile akamuonesha ishara saringo ya kumuomba uta wake, amata aliupokea na kujiweka vyema
“Nini Amata?”
Hellen alimuuliza
“Chatu! Nyoka mkubwa anayeweza kumeza mtu”
Amata alijibu. Hellen akajificha nyuma ya Amata, Saringo alikuwa akiangalia kwa makini lakini hakuweza kuona cha kufanya alisubiri kuona nini Amata anataka kufanya, kwa upole Amata aliweka mshale sawia katika uta wake na kuvuta kwa nguvu zake zote, mikono yake iliyojaa misuli ya nguvu ilituna na kuonesha kiasi gani nguvu alizotumia kuvuta uta huo, huku akiongea lugha isiyoeleweka akiwa ameuma meno bado hakuachia pigo lake, kilichoonekana ni jinsi tu alivyoutembeza uta huo taratibu sana kutoka upande mmoja kwenda mwingine. Kutoka ndani ya mitete ile nyoka mkubwa alifyatuka kwa spidi ya ajabu kuelekea alipo mtoni alipo Stephan, Amata aliachia uta wake na mchale uliondoka kwa spidi kali kukikabili kichwa cha nyoka yule, hamad!!
“Stephannnnnnn!!!!!”
Hellen alipiga kelele ya nguvu na Stephan alipogeuka alishuhudia joka kubwa refu lililofungua domo lake likimuelekea, mara alishuhudi kitu kikipita kwa kasi kati yake na joka lile, ulikuwa mshale wa Amata aliopigwa kwa ustadi lakini kutokana na ukelele wa Hellen Joka lile liligeukia upande ulikotoka ukelele hivyo kufanya shabaha ya Amata kuwa ya bure. Joka lile lilijivuta na kuburizika chini likijikunjakunja kuelekea walipo akina Amata, Amata alijinyanyua na kujirusha upande wa pili akimvuta Saringo wakati huo Helleni alijiinua na kujikuta amechelewa, alipigwa ngwala maridadi sana na joka lile na kupaishwa juu, kabla hajafika chini joka lili lilimdaka kwa ustadi mkubwa na kujiviringwa mwilini mwake,
likiwa linadondoka kwa kwa kasi, Amata alikuwa tayari kesha vuta uta wake na kuuwachia, shabaha ya ajabu! Mshale ule ulipenya sawasawa karibu kabisa na kichwa cha joka lile, kutokana na maumivu yale joka lile likamuachia Hellen na kudondoka chini Hellen nae akadondoka juu yake, Joka lile likajivuta tena kumkimbiza Amata, amata hakukimbia mbali bali aliuzunguka mti ule waliokuwa wamekaa huku akiweka vizuri mshale wake wa tatu alijikwaa na kuanguka vibaya, joka lile likamtia mkononi likamviriga vizuri, bahati nzuri mkono mmoja wa Amata ulikuwa nje ya mvirigo ule
“Amataaaaa....”
Saringo aliita,
Saringo aliita na kumrushia kisu ambacho Amata alikidaka kwa ustadi mkubwa na bila kuchelewa alididimiza kisu kile kwenye sehemu ya mwili wa joka hilo, joka likajiinua juu likiwa bado halijamuachia Amata, Amata alisikia mlio mkali na alichokishuhudia ni damu iliyoruka kwa matone makubwa makubwa, joka lile halikuwa na kichwa tena, likaanguka kwa mshindo mkuu, ilikuwa ni risasi kutoka AK 47 iliyopigwa kwa ustadi wa hali ya juu na Stephan na kukitawanya kichwa cha joka lile na kukichanachana vibaya.
“Nice shot!!”
Hellen alimsifu Stephan, wakakumbatiana na kubusiana kama ishara ya kupongezana. Saringo alimfuata Amata pale alipolala na kumsaidia kujitoa katika joka lile, haikuwa kazi rahisi kuukunjua mwili wa joka lile kubwa ambao kwa wakati huo ulikuwa bado umejiviriga katika mwili wa Amata. Helen na Stephan nao waliungana na Saringo katika kazi hiyo, mara wakafanikiwa na kumnasua Amata ambae uso wake ulikuwa umechafuka kwa damu ya joka lile, wakamlaza vizuri na kumuosha uso wake. Mikono laini ya Saringo ilipita usoni mwa Amata, Amata akajittikisa kidogo na kuushika mkono wa Saringo
“Nini Amata?”
saringo alimuuliza
“Mkono wako laini umenisisimua mwili...”
Saringo akatabasamu aliposikia maneno hayo ya Amata
“Usianze Amata!”
Saringo akasisitiza. Amata aliketi na kutazama vizuri huku na huku, akaokota uta na podo lake akaweka mgongoni... safari inaendelea!
Msitu ulizidi kuwa mnene mbele yao, lakini Stephan aliyekuwa na ramani ya wapi wanakokwenda alisisitiza kuelekea upande huo hata kama haukuwa na njia, walisonga mbele, panda milima, shuka, vuka mto pasua vichaka, mvua, jua vyote vilikuwa juu yao, chakula kikubwa kilikuwa ni matunda ya porini ambayo kwao walijitosheleza na kujipatia vitamini za kutosha sio mpaka akuandikie daktari.
Jioni hiyo ya siku ya tatu mvua ilikuwa kubwa sana, radi zisizo na huruma zilipasua anga lote na kulifanyia michoro ya kutisha, hapakuwa na pa kujikinga wala kujificha, wote walitota miili hata nguo zao kugandamana na miili yao, walitetemeka kwa baridi kali ya msituni hata miguu ilishindwa kutoa ushirikiano na mwili mara nyingi ilikataa kusonga mbele, hakukua na lakufanya isipokuwa ni kujivuta hivyo hivyo, walitamani jua liwake haikuwa hivyo, walipanda wakoke moto lakini kila kitu kililowana, safari ilizidi kuwa ngumu kwani msitu wote ulifunikwa na ukungu mzito hata mwanga wa tochi haukufua dafu. Amata alisimama na kugeuka nyuma akawaonea huruma wenzake maana walikuwa wakitetemeka kupita maelezo. Saringo alimuendea Amata na kumkumbatia kwa nguvu huku akitetemeka, vivyo hivyo kwa Hellen na Stephan, walivuta hatua fupifupi japo kwa shida kujitafutia mahali pa kupumzika.
“Tukae humu mpenzi!”
Amata alishtuka kidogo kusikia kauli hiyo toka kwa Saringo, alibaki kujiulizauliza maana hajawahi kuitwa mpenzi katika maisha yake. Amata alitazama na kuona pango pembezoni mwa mti kabla hajaamua cha kufanya Stephan na Hellen wakawa tayari wamejitoma ndani ya pango hilo lenye kiza,
“Amata twende!”
Saringo alisema huku akimvuta mkono kuelekea pangoni, Amata alimvuta Saringo kwa nguvu na kumkumbatia kifuani mwake, akamkazia macho Saringo alimtazama Amata usoni kwa hasira lakini hakuwa na la kusema alizungusha mikono yake mgongoni kwa Amata na kuikutanisha kisha kuegemeza kichwa chake kifuani mwa Amata. Amata alitulia kimya kwa muda akiangalia lile pango waliloingia akina Stephan
“Saringo! Unafikiri hilo ni pango? Isije kuwa mtego tu”
Amata alimuuliza Saringo
“Wenzetu wameingia wewe hutaki, Amata una nini twende!”
Saringo alisisitiza
“Saringo! Mbona hatumsikii Stephan au Hellen hata kutuita!? Nina wasiwasi hili si pango la kawaida!”
Amata aliposema maneno hayo Saringo akashtuka na kugundua kuwa ni kweli hawa viumbe wawili wangeshawaita lakini kimya yapata dakika kumi sasa, Saringo akamuachia Amata, akaokota kipande cha mti kilicho jirani hapo akakirushia ndani ya pango lile lakini hakusikia chochote hata mdondoko wa kipande cha mti, Saringo akajishika mdomo na kuanza kutoa machozi.
“Saringo! Hapa ni msituni, usilie, tulia, jikaze kama mwanamke. Kilichobaki hapa ni kutafuta cha kufanya kwa kuwa sasa tumebaki wawili wenzetu tayari msitu umewameza”
Amata alimbembeleza Saringo
“Hatuna silaha za kutosha itakuwaje kupambana na maadui?”
Saringo alimuuliza Amata. Amata akatazama podo na uta wake akajikuta kabakiwa na takribani mishale kumi na tano podoni, akatikisa kichwa akaingiza mkono kwa ndani ya suruali yake kama anayetaka kutoa dhakari ili ajisaidie, Saringo akasogea pembeni kidogo kwa hofu maana hakujua Amata anataka kufanya nini, alipotoa mkono ukatoka na bastola moja. Saringo alishangaa
“Umeipata wapi?”
Saringo alimuuliza Amata
“Alinipa Hellen nimuhifadhie”
alimjibu Saringo na kumtupia swali
“unajua kuitumia?”
“Ndio!”
Saringo akajibu huku akiichukua mikononi mwa Amata na kuigeuzageuza kisha akatikisa kichwa kuashiria amekubali, akajaribu kama analenga kitu, Amata akampatia kibox kimoja cha risasi, Saringo akakipokea na kukihifadhi vizuri...
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Stephan na Hellen waliingia kwenye kitu kama pango lakini halikuwa pango la kawaida bali ni kama shimo lakini halikuenda chini isipokuwa lilikuwa na mteremko mkali sana, hawakuweza hata kufanya lolote bali waliporomoka ndani kwa kasi ya ajabu na huku kulikuwa na giza nene kuliko giza lenyewe, waliendelea kuseleleka hakuna aliyepiga kelele kwani kati yao kila mmoja alikuwa akitahamaki. Baada ya kama dakika tano za mseleleko ule Hellen alijigonga kwenye kitu kama ukuta au jiwe na kupoteza fahamu, Stephan hakujua afanye nini maana giza ni nene, huku akiwa anavuja damu mkononi mwake kwa kuwa alichunika vibaya sehemu ya nyuma ya mkono wake, alitoa kiberiti na kuwasha angalau apate mwanga kidogo, lakini mwanga ule bado haukufua dafu kwa giza lile. Stephan aliegeme kitu kama ukuta lakini alihisi ulikuwa rafu sana alijaribu kuvuta hisia na kutega sikio lake kwa makini labda atasikia chochote ama watu kuongea au chochote, lakini hakusikia kitu, taratibu macho yalianza kupambana na giza lile na kuanza kuona japo kidogo, akiwa bado katika kutambua kilichopo ndipo aliposikia kwa mbali mtweto wa mtu anayehitaji msaada, mara moja akagundua kuwa bila shaka ni Hellen lakini hakujua upande upi hasa yupo akajaribu kuita kwa upole, lakini bado aliendelea kuusikia ule mtweto ambao kwa sasa ulikuwa wa taratibu lakini ulisikika kutokana na ukimya wa mle shimoni, alijaribu kupanda taratibu haikuwa rahisi kwa kuwa hapakuwa na pakujishikia ila tu alisaidiwa na vipande vya mawe vilivyochomoza huku na huku, mara akamfikia Hellen ambaye alikuwa amenasa kwenye jiwe fulani kumbe hakuwa mbali na pale alipoangukia Stephan, alijaribu kumnasua pale aliponasa na lile jiwe likang’oka kumbe lilishikwa tu kwa udongo, wakaporomoka nalo mpaka pale chini. Stephan alitoa mguno wa uchungu na kishindo kile kilimrudishia fahamu Hellen, Hellen aliangalia huku na huku na kumgeukia Stephan
“Tuko wapi Stephan? Amata na Saringo wako wapi?”
hellen aliuliza huku akionesha kuweweseka. Stephan alimtuliza akiwa hajui nini cha kufanya zaidi kwa wakati ule alitazama uku na huku na akagundua kuwa lile shimo lilikuwa linaendelea lakini sasa si kwa kwenda chini bali tambarare ambapo unaweza kutembea ukiwa wima, bila kupoteza muda alisimama na kumuinua Hellen, akiwa bado na bunduki yake mgongoni walianza kutembea taratibu ndani ya shimo lile wakiwa hawajui wapi wanakoelekea,Hellen alikuwa anamfuata tu akijua labda Stephan anajua chochote, waliendelea kwenda nusu wakitembea na nusu wakikimbia ili mradi wafike wanakokwenda. Hellen alianza kushikwa na woga aliushika mkono wa Stephan kwa nguvu zote akiwa anatweta kwa nguvu, mara Stephan akasimama akainama na kushika magoti yake huku akitingisha kichwa kwa masikitiko
“...tumekwisha! Hellen, sijui hata tuendako”.
Alichukua bunduki yake nakufanya kama analenga kitu lakini hakuna alicholenga akafyatua bunduki yake na ukelele wa bunduki hile ulijirudia mara nyingi kabla hakujakua kimya tena, haja yake asikie tu kama kuna mlio mwingine utakaosikika zaidi ya huo wa bunduki hiyo. Taratibu waliendelea kutembea na kutembea mwisho walichoka na njaa iliwashika wakaketi chini na kila mmoja alipitiwa na usingizi kwa muda wake.
Safari ilikuwa ngumu kwa Amata na Saringo, chakula chao kikiwa ni matunda ya mwituni na maji ya mtoni, waliendelea kwenda wakiwa hawajui hasa ni upande upi ambao wanatakiwa kuelekea.
“Nahisi tunapotea !”
Saringo alisimama na kusema huku kajishika kiuno
“Tufanyeje sasa! Tuendelee mbele labda tutajua la kufanya”
Amata akamjibu huku akimsika mkono akimaanisha safari iendelee. Saringo ambaye wakati huo alioneka uso wote kusawajika kwa uchovu alijivuta kwa hatua za taratibu na kufuata kule alikoongozwa na Amata.
“Twende mpaka tupate mahali pazuri pa kupumzika maana jioni nayo imeshakaribia”
Amata alimueleza Saringo huku wakiendelea na safari hiyo isiyo na mwisho bali yenye hatari na misukosuko mingi. Baada ya kutembea kwa muda walifika eneo moja ambalo liko wazi sana kama kiwanja cha mpira lakini ilikuwa ni katikati ya msitu, katika eneo hilo kulikuwa na nyasi nzuri za kijani fupifupi lakini katikati kulikuwa na mbuyu mkubwa sana mnene ambao juu yake ulionesha wazi kuwa kulikuwa na mibuyu iliyoning’inia, Amata alisimama kabla ya kuingia katika uwanda ule akatafakari mawili matatu, akamgeukia Saringo
“Umeona! Umeona mbuyu ule?”
alimuuliza Saringo ambaye kwa wakati huo alikuwa kamuegemea Amata begani kwa upande wa mgongo.
“Huu ni uwanja au kitu gani?”
Saringo naye alitupa swali kwa Amata,
“Hapana huu si uwanja hapa lazima kuna kitu, Stephan alitueleza kuhusu mbuyu siyo ule?”
Amata alimuuliza Saringo, kwa hamaki kubwa saringo aliutazama mbuyu ule, kikapita kimya cha dharula. Akatikisa kichwa kwa ishara kuwa amekubaliana na Amata
“Yeah utakuwa ndio wenyewe! Alisema upo katikati ya uwanja, ndiyo nimekumbuka, ndiyo utakuwa ni huu”
saringo aliongea kwa upole sana katika hali ya kushangaa.
“Mbuyu wa Shetani!!!”
Amata aliongezea kwa upole uleule
“Unasemeje Amata? Mbuyu wa Shetani?!”
Saringo alimwangalia Amata usoni na kumtupia swali lile.
“Ndiyo Saringo, ule ni mbuyu wa Shetani! Unaitwa Mbuyu Kolo... mbuyu wa maajabu, babu yangu alinisimulia mengi sana juu ya mbuyu huu”
Amata alimueleza Saringo huku akiwekaweka manyasi vizuri kwa kukaa chini.
“Saringo!”
Amata aliita taratibu na saringo alimgeukia
“Bee, Amata unasemaje?”
huku akikaa katikati ya miguu ya Amata na kumlalia kimgongo kifuani.
“Ni nini mnakitafuta huku porini? Na akina Stephan?”
Amata alimuuliza Saringo.
“Ni stori ndefu sana Amata, ndefu mno”
Saringo akashusha pumzi ndefu na kumeza mate kwa shida kutokana na ukavu wa midomo yake.
“Niambie tu, maana hapa tutalala ili kesho tujue cha kufanya, ila lazima tulale juu ya mti kuepuka wanyama wakali wenye uchu na nyama tamu yenye chumvi ya Binadamu”
Amata alimueleza hayo saringo huku mikono yake akimzungushia saringo kwa mbele kwa kuipitisha chini ya makwapa yake, alifikiri atapata upinzani kwa kitendo hicho lakini la, Saringo aliivuta na kuikutanisha juu ya kifua chake kisha akainamisha kichwa kwa nyuma na kumuangalia Amata kwa juu
“nakupenda Amata!”
alimwambia huku akitabasamu, Amata akapotezea kimtindomtindo.
“Amata! Tukimaliza safari yetu tutakuwa matajiri sana, tunakwenda Solondo kuchukua sanduku kubwa na ndani ya sanduku hilo kuna mali nyingi sana, dhahabu, almasi, yaspi, lulu za aina mbalimbali, mawe ya thamani tofauti”.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Saringo alimwambia Amata, Amata alimkazia macho saringo
“Nani aliyekwambia Saringo?! Solondo ni msitu wa kifo, msitu unaokuwa hai na kumeza kila aingiyae...”
Amata alieleza lakini saringo alimkatisha
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment