Sehemu Ya Tano
(5)
“Fungua,”
Kombora alifoka tena. “Polisi hapa,” aliongeza akiitazama saa yake. Dakika tatu
zilikuwa zimepita tangu alipowasili hapo na kuwakuta askari wa doria wakiendelea
kuugonga mlango wa ofisi ya Kwame
“Mnadhani kuna nini kinachofanyika
humo ndani?” aliwahijo.
“Hatujui mzee. Hatusikii
chochote.”
“Msichana anayekaa hapa
mmemkuta?”
“Hatukumkuta.”
“Okay, tutavunja mlango. Nitaita
kwa mara ya mwisho… FUNGUA!” akafoka.
“Mara mlango ukafunguka
polepole. Kwame alitokeza akitetemeka mwili mzima isipokuwa macho yake tu.
Kombora hakuyaona kuwa na dalili yoyote ya hofu. Aliwatazama kwa mshangao na
shukrani.
“Karibu,” aliwaambia akiwapisha
mlangoni.
Walipoingia macho yao yalidakwa na mizoga ya binadamu wawili
waliolala juu ya sakafu. Mmoja akiwa kalala chali bastola mkononi. Wa pili
ambaye ilikuwa dhahiri alikuwa marehemu alikuwa chali, sura yake ikitazama
angani. Kombora na wasaidizi wake sita walimtazama marehemu huyo mara moja na
kisha kutazamana.
“Bazile Ramadhani!” mmoja wao
akajaliwa kutamka.
“Ni Bazile siyo? Ule muuaji anayeua ovyo? Basi Mola
asifiwe kwa kufa kwake. Angeweza kuniua au kumuua huyo kijana hapo,” alitamka
Kwame kwa namna ya furaha.
“Kombora alimtazama kijana huyo na kumwona
akipumua polepole. Akainama na kumgeuza uso. Mara alijikuta kashtuka akiwageukia
wenzake kwa macho ya kutokuamini.
“Kati yenu hakuna anayemfahamu mtu
huyu?” aliwahoji.
Watu hao walimtazama mtu huyo na kumrudushia Kombora
macho ya mshangao. “Huyu si Joram Kiango mzee?” mmoja wao
alijibu.
“Joram Kiango!” Kwame alifoka tena. “Yule kijna wa C.I.D? La
haula! Angeweza kufa mbele ya macho yangu kama asingeweza kutumia vyema bastola
yake.”
“Joram sio C.I.D,” Kwame aliambiwa. “ Ni kijana mwenye ofisi
yake ya upelelezi, ambaye amefanya mengi kulisaidia taifa.” Kombora alisita,
kisha akamgeukia Kwame, “Ndiyo ndugu Kwame. Nadhani waweza kutufunua macho na
kutueleza kinachotokea katika ofisi hii.”
Kwame akiwa katika hali ile
ile ya kuchanganyikiwa ingawa macho yake yakiwa maangavukinyume cha hali yake,
alisema kwa sauti ya utulivu, “Sidhani kama kuna mengi ya kueleza bwana
inspekta. Nilikuwa nikiendelea na shughuli zangu kama kawaida, dakika chache tu
zilizopita, mara akatokea bwana huyo mmnayemwita Joram na kuingia huku mbio.
Kabla sijamuuliza lolote marehemu huyo naye akaingia. Wakavaana na kupigana kwa
muda. Joram alipoelekea kuzidiwa aliitoa bastola na kuifyatua. Muda mfupi nanyi
mnaingia.” Alipoona Kombora hajaridhika aliongeza, “Ni hayo tu bwana
Kombora.”
“Hayo tu? Hujasema lolote juu ya simu. Umepiga baada au
kabla? Kombora alihoji.
“Simu! Simu ipi?”
“Simu iliyotuleta
hapa.”
“Siifahamu simu hiyo. Yaani mmepata simu? Basi bila shaka hyo
ni katibu wangu. Nadhani aliona pindi wakiingia ndipo
akakupigia.
“Yuko wapi?”
“Sijamwona tangu alipoanza haya.
Nadhani mara tu baada ya simu hiyo kukufikia amekimbia. Nakuambia bwana ilikuwa
hali ya kutisha kweli. Nilichanganyikiwa…”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kombora akamkatiza
kwa kuuliza, “ Wakati wote wa mapambano wewe hukuweza kufanya lolote? Umeshindwa
walao kuinua simu kama alivyofanya karani wako?”
Haikuwa hali ya
kawaida inspekta. Nakuambia nilichanganyikiwa…”
Huonekani kama mtu
uliyechanganyiokiwa kiasi hicho! Kombora aliwaza, nusura ayatamke. Wala hakuona
kama Kwame alikuwa mtu mwenye asili ya kushtushwa na jambo lolote kiasi cha
kushindwa kujua la kufanya. Hata hivyo, hayo hayakuwa na nafasikubwa katika
fikra za Kombora. Alikufa na mengi kichwani.
Sana alilitazama suala la
mauaji hatimaye kifo cha muuaji na kuhisi tamati yake haimridhishi kama
alivyotegemea. Hakuna alichopenda zaidi ya kifo cha Bazile. Na angependa zaidi
kama fursa ya kukifumua chake kwa risasi angekuwa kaipata yeye. Lakini bado
angeridhika zaidi kama tukio hilo lingetukia kwa namna nyingine. Namna
iliyoridhisha zaidi.
Jana tu alikuwa kaanza kupata mawazo mapya juu ya
mauaji hayo. Ilikuwa baada ya kuufuata ushauri wa msaidizi wake na kuikusanya
pamoja akili yake katika kulishughulikia suala hilo. Alikuwa amemfikiria Bazile
Ramadhani kama alivyo: kijana mwandishi chipukizi asiye na mengi ya ajabu, vipi
aondokee kuwa hodari wa kuua kiasi cha kumkabili askari mwenye silaha na
kumjeruhi? Zaidi, vipia askari huyo baada ya kuhojiwa sana bado anang’ang’ania
kuwa alipoteza fahamu zake pindi akifanyiwa ukatili? Ingawa askari huyo
alithibitisha kuwa mtu huyo alikuwa Bazile, bado Kombora alisisitiza hata alama
za vidole zikachukuliwa kutoka katia uso huo ili zilinganishwe na alama
nyingine. Lakini matokeo yalikuwa ya kutatanisha zaidi. Hazikupatikana alama
zozote katika sehemu zote ambazo askari huyo alistahili kuwa ameguswa na Bazile.
Yaelekea zilifutwa kwa uangalifu na alikuwa kavaa glovu. Hilo lilimshangaza
Kombora. Kwa nini afiche alama hizo naye alikuwa akijitangaza mara kwa mara kwa
simu? Mara Kombora akawa na mawazo mapya juu ya mauaji hayo. Alihisi kuwa kuna
jambo zaidi ya wazimu wa mwandishi huyu. Vinginevyo, Kombora hakuona vipi kijana
huyo angeendelea kutaabisha jiji huku akiepuka kila kikwazo ambacho polisi
walijaribu kumwekea.
Hayo yalikuwa mawazo tu. Lakini yaligeuka kuwa
mashaka. Mashaka ambayo yalijiimarisha kichwani mwake hata akiziruhusu fikra
zake kutambaa huku na huko akitafuta uwezekano wa Bazile kushirikiana na watu
wengine. Kwa nini? Ni ipi sababu ya mauaji hayo? Kuna uhusiano gani baina ya
marehemu wote? Mara akapata wazo ambalo lilimshtua sana. yawezekana lipo jambazi
au majambazi ambayo yalikuwa yakiitumia sura ya kivuli cha Bazile?
Alijiuliza.
Yawezekana kabisa katika dunia hii iliyopiga hatua ndefu
katika ndefu katika sayansi na teknolojia, lolote lawez kufanyika. Bazile aweza
kuwa kofia tu ambayo imefunika mengi.
Mengi? Yepi? Kombora akajiuliza
kwa hofu. Mara moja akamwita msaidizi wake na kumtaka achukue jukumu la haraka
kujaribu kupata habari, mienendo, vitendo na uhusiano baina ya marehemu wote.
Alisisitiza kuwa kazi hiyo ni muhimu na ipewe umuhimu zaidi ya lile jukumu la
kumsaka Bazile.
Pindi Kombora akiwa ofisini kuisubiri taarifa hiyo
ndipo ikamfikia simu hii ambayo ilimwita hadi hapa na kumkuta Bazile akiwa
marehemu. Ni Bazile yuleyule. Si sura ya bandia wala mtu mwingine zaidi yake. Na
inasemekana kafa pindi akikusudia kuua tena. Kumuua Joram Kiango. Joram ambaye
mchango wake ni mkubwa mno katika harakati za kijambazi. Yawezekana kuwa Joram
pia alikuwa akimsaka muuaji huyu? Na yawezekana huu ukawa mwisho wa kisa hiki
cha kikatili? Hakutakuwepo na kusimama mahakamani kumsikia Bazile akikiri au
kukanusha mauaji haya.?
Kombora angeweza kuwaza mengi zaidi. Lakini
hakuiona sababu yoyote ya kuendelea kuusumbua ubongo wake pindi Joram alikuwa
hai. Baada ya sindano moja tu ya daktari atazinduka na kutoa maelezo
kamili.
“Well!”
“Well?” Kwame alihoji.
Kombora
akagundua kuwa alikuwa ameropoka. Akamtazama Kwame kwa macho yenye maswali mengi
lakini hakuuliza chochote.
Na awaze apendavyo! Kwame alijinong’oneza
kimoyomoyo. Awaze anavyotaka. Asingeweza kuutengua ushahidi aliouandaa hata kama
ni askari mwenye shahada ngapi.
Hadithi nzuri ilioje. Hadithi
isiyopingika kabisa…. Kwame aliendelea kuwaza. Bazile Ramadhani, mwandishi,
kapata wazimu. Kamuua mchapishaji wake. Damu ikampanda kichwani, akachemka kuua
ovyo. Mara kupambana na Joram Kiango. Ramadhani kazidiwa na kuuawa na Joram.
Polisi wenyewe ni mashahidi. Wamemkuta muuaji anakufa. Nani aikatae hadithi. Na
ataikataa kwa misingi ipi pindi hakuna anayejua
ukweli?
*****
Ukweli ulikuwa siri yake
Kwame na wachache ambao hawawezi kufunua midomo yao na kuitoa. Hakuna mwingine
anayefahamu kuwa muuaji si Bazile ila hilo kundi lake ambalo dakika chache tu
limetoweka na kumwachia yeye, Kwame fursa ya kutia risasi katika mwili wa
Bazile. Wala hakuna atakayefahamu kuwa mauaji ya Kitenge, mchapishaji,
yalipangwa ili kuwapotezea askari lengo la kuwafanya polisi wazidi kuamini kuwa
muuaji ni Bazile Ramadhani. Na kwamba Fambo Wamangi na Jugeni Kawamba walikuwa
wameuawa bila hatia yoyote. Kosa lao kubwa ilikuwa kusafiri katika ndege moja na
Kwame alipotoka visiwani kukamilisha mipango ya kuuza kisiwa. Ilionekana kuwa
wao wangeweza kuwa daraja la kuwafanya wapelelezi kumfikia Kwame au walao
kushuku jambo endapo kifo cha Dismas Komba kingetukia.
Ni Komba tu
aliyetakwa. Na ni yeye aliyekuwa na hatia ingawa yeye pia alipata hatia hiyo kwa
ajali. Akiwa uwanja wa ndege baada ya kutua kutoka Zanzibar, alikosea na
kuchukua suitcase ya Kwame badala ya yake. Alipofika nyumbani aliifungua na
kukutana na kile ambacho macho yake hayakutakiwa kuona. Kabla hajajua la kufanya
kwa siri hiyo, wafuasi walishapeleleza anakoishi na kumwandama kwa hadhari huku
wakimtesa kwa mbinu aina aina ili arejeshe bahashahiyo yenye siri. Naye akijua
mara tu aitoapo watamuua ndipo akaing’ang’ania kwa udi na uvumba. Jambo ambalo
halikuyaokoa maisha yake, kwani Bon alikuwa ametimiza wajibu
wake.
Nani atayajua yote hayo? Kwame alijiuliza kwa kiburi. Zaidi,
nani atayajua katika muda mfupi uliosalia?
Huyu askari mkuu hapa
haonekani mjinga, lakini hana nafasi ya kuunga vipande vyote vya matukio na
kupata pande zima la kisa na ushahidi wake wakati unaofaa. Joram? Joram yuko
usingizini na ataendelea kulala hadi kesho. Atakapoamka kujua hakutamsaidia yeye
wala mtu yeyote, itakuwa….
Kwame alilazimika kusita alipomsikia
Kombora akitoa amri ambayo hakuitegemea.
“Unasemaje inspekta? Apelekwe
Muhimbili? Ya nini kusumbuka. Nimekwisha mpigia daktari wa kampuni yangu aje
mara moja kumpa huduma ya kwanza,” Kwame alisema.
“Daktari wako?”
Kombora akauliza akitazama, “Umempigia lini simu hiyo?”
Muda mfupi
kabla yenu.”
“Nadhani ulisema kuwa hujapiga simu
yoyote.”
“Nilipiga. Atafika wakati wowote, kama una msaada wa haja
bwana inspekta nadhani msaada huo ungekuwa kuiondoa maiti hii mbele yangu. Ofisi
hii si jumba la maiti. Suala la Joram niachie mimi. Ameyaokoa maisha yangu.
Ningeweza kufa.”
“Joram hatatibiwa hapa,” sauti kali ya kike ilitamka
ghafla. Wote wakageuka kumtazama msemaji. Alikuwa msichana mwenye umo na sura
nzuri ambaye aliingia ghafla baada ya kubishana sana na askari wa
mlangoni.
Kombora alimfahamu kwa sura na jina. “Neema!”
akaita.
“Ni mimi inspekta. Ni mimi niliyekupigia simu kama
nilivyoelekezwa na Joram,” akaongeza akiinama kumgusa Joram ambaye alilala kwa
utulivu mkubwa. “Inspekta, Joram hawezi kutibiwa hapa. Tena ningeomba apelekwe
Muhimbili mapema iwezekanavyo.”
“Kwa nini? Daktari wangui…” Kwame
alijaribu kusema. Alikatizwa na Kombora ambaye alifoka kwa
Kiingereza.
“Shut up!” akawageukia wasaidizi wake na kuwaamuru
wamchukue Joram mara
moja.
*******
Fahamu zilipomrejea, Joram
alifumbua macho polepole na kuyafumba mara moja kwa kushindwa kustahimilinuru
ambayo aliona kali mno. Alipoyafumbua tena, alifaulu kutazama pande zote. Kitu
cha kwanza alichokiona ilikuwa kofia ya kipolisi, ilikuwa juu ya kichwa cha mtu
mwenye mavazi ya kipolisi aliyesimama kando akimtazama. Huyo alikuwa mmoja kati
ya polisi wane waliokuwa chumbani humo silaha mikononi. Kisha, Joram aliweza
kuwaona daktari na nesi ambao walikuwa wakimhudumia.
Baada ya kutazama
sana aligundua kuwa alikuwa katika chumba maalumu katika hospitali ya Muhimbili.
Joram akiwa mtu asiye na mazoea ya kufika hospitali kwa miaka, hilo
lilimshangaza sana.
“Nini kinatokea? Niko hapa kwa nini?”
akauliza.
“Pole sana bwana Kiango,” daktari alimjibu. “Pumzika kidogo
umsubiri inspekta Kombora ambaye yuko nje akisubiri kuzungumza nawe. Kabla
hajafika huruhusiwi kuzungumza lolote.”
“Kwa nini?” Joram alihoji.
Lakini mara akarudiwa na matukio yote ya muda mfupi uliopita. Akakumbuka kuwa
alikuwa mbele ya umati wa wauaji wenye dhamira ya kumwaga damu na kupoteza uhuru
wa wananchi usiku wa leo. Akakumbuka pia kuwa katika juhudi zake za kuwazuia
ndipo alinusa harufu ambayo bila shaka ilitoka katika mitambo ya Kwame, ikamtia
usingizi. Baada ya hapo, hakusikia lolote isipokuwa hisia tu, kama ndoto
alisikia majadiliano ya haraka haraka kwa sauti za hofu baina ya watu hao
waliochanganyikiwa. Yaliyofuata hakuyafahamu.CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ndiyo!” akafoka
ghafla akiitazam saa yake na kuona ikikaribia saa nane mchana. “Yuko wapi
Kombora?” akawageukia askari, “Mwiteni haraka.”
Haikuwepo haja ya
kumwita. Wakatri huo huo, Kombora aliingia. Baada ya kupokea saluti kutoka kwa
askari hao akawataka wasubiri nje. Daktari na msaidizi wake pia waliombwa
kutoka.
“Ndiyo bwana Joram. Kwanza nikupe pole kwa yote yaliyokupata.
Kisha nitakuomba unifafanulie kwa niaba ya jeshi zima la polisi kitu gani
kinachotokea,” alisema akiketi kitandani.
“Kitu kinachotokea? Nadhani
sijakuelewa vizuri inspekta,” Joram alimjibu. Alipoona upinzani katika macho ya
Kombora aliongeza haraka, “Sivyo. Nina maana kuwa nitapenda kufahamu yepi
unafahamu na yepi yamenifanya niwe hapa Muhimbili chini ya ulinzi mkali wa
polisi badala ya kuwa mahala fulani huko ahera au peponi. Ilikuaje hata ukafaulu
kuniokoa.
“Yametokea mengi zaidi ya kukuokoa Joram,” Kombora alisema
akitoa sigara na kumpa Joram moja. “Mengi mno. Nikianza mwanzo ni kwamba
nilipokea simu kutoka kwa msichana wako, kama alivyodai yeye, kuwa mtu anauawa
katika ofisi ya Kwame. Nikaenda mara moja na kukuta wewe umezirai na bastola
ambayo imemuua yule mtu tuliyekuwa tukimsaka kama kunguni, Bazile
Ramadhani.”
Bazile amekufa!
Umemwona!...” Joram alihoji kwa mshangao.
“Ndiyo. Kwani hukumuua
wewe?”
“Mimi!”
Kombora akatikisa kichwa na kuendelea, “Hilo
ni lingine katika mengi ya kutatanisha katika mkasa huu. Lingine ni matokeo
yaliyotokea pindi tukikuleta hapa. Ulikuwa kwenye gari aina ya Landrover
iliyokuwa ikiendeshwa na askari wangu. Msichana wako alikuwa katika hiyo gari
pia. Gari hiyo ilipokuwa imalize barabara ya Morogoro iingie mtaa wa Umoja wa
Mataifa iligongwa makusudi kabisa na gari nyingine aina ya Landrover. Wewe kwa
kuwa ulikuwa umelazwa kwenye kiti hukudhurika. Dereva wangu ameumia kidogo.
Lakini msichana wako….”
“Neema! Tafadhali Inspekta! Usiniambie kuwa
Neema amekufa!” Joram alidakia.
“Hakufa,
ila…”
“Ila?”
“Ametoweka.”
“metoweka? Sijakuelewa
Inspekta.”
“Kwa kweli ni tukio la kutatanisha. Mimi nimefika katika
eneo la dakika nne tu baada. Nimekuta watu wakishughulika. Nikaambiwa kuwa teksi
moja imejitolea kumchukua Neema na dereva wa gari iliyogonga ambaye hakuumia
sana. kwamba imewaleta hapa hospitali. Lakini tumeshakagua hospitali nzima bila
dalili yoyote ya Neema wala huyo dereva.
“Jambo la kutisha zaidi ni
barua hii fupi ambayo imeokotwa katika chumba hiki pindi ukitibiwa. Imeandikwa
jina lako.”
Joram akaipokea na kuifunua. Iliandikwa kwa mashine, wino
mwekundu ikisema;
Mpendwa
Joram,
Nakuonya usifunue mdomo kwa yeyote kusema lolote. Vinginevyo
kesho utaamka hapo kitandani na maiti ya mpenzi wako.
Rafikio Joe
Kileo.
Baada ya kuisoma Joram alimgeukia Kombora.
Ingawa alijitahidi kuficha mshtuko alioupata kwa habari hiyo, hakufanikiwa
kumfanya Inspekta Kombora asihisi mteremo katika sauti yake aliposema, “Endelea
mzee.”
“Nadhani sina zaidi,” Kombora alimjibu. “Labda naweza kusema
kuwa nina mashaka na mtu anayeitwa Kwame. Vitendo na maneno yake vinaonyesha
kuwa anajua mengi kuhusu mkasa huu. Kifo cha Bazile bado kinatatanisha. Barua
hiyo kwako inaongeza uzito katika mashaka yangu.kwa ajili hiyo, nimewapa
wapelelezi kadhaa kazi ya kuchunguza mienendo ya Kwame na kuniletea taarifa mara
kwa mara. Inashangaza ripoti zote zinaposema yuko katika hali ya kawaida na
anaendelea n shughuli zake kama kawaida baada ya kutoka mara moja kwenda
Salamander ambapo amepata kahawa na kuzungumza na watu wachache juu ya ‘mkasa’
katika ofisi yake. Sasa hivi inasemekana yuko ofisini mwake kama kawaida ingawa
katibu wake hajapatikana.”
Hayo yalizidi kumfumbua Joram macho.
Akaipata picha kamili ya yote yaliyokuwa yametukia. Akaelewa kuwa baada ya
jaribio la Kwame la kumuua kwa gari kukwama, aliona hatari ya Joram kueleza
polisi ukweli na ndipo akamteka Neema na kuleta waraka huu ili kumtisha
asiendelee na mipango yake hatari.
“Hivyo ndugu Joram,” Kombora
alikuwa akiendelea kueleza, “Kadri n inavyokufahamu, natumaini hutakuwa tayari
kutii waraka huo ambao unakusudia kuwaweka mapenzi mbele ya jambo la hatari kama
hili. Utakkuwa mwanamume kama ulivyo na kueleza kwangu yote unayofahamu ili
tushirikiane kuyaokoa maisha ya mpenzi wako pamoja na…”
“Neema si
mpenzi wangu,” Joram alitamani kufoka hivyo, lakini alijizzuia. Ingemchukua muda
mrefu mno kumfanya Kombora na watu wengine waelewe kuwa uhusiano wake na Neema
ulikuwa wa kikazi tu. Muda ambao hakuwa nao kabisa. Kwa sasa, alifikiria jinsi
Kwame alivyokuwa akiendelea na mipango yake bila hofu yoyote akiamini kuwa iwapo
majasusi wake walifaulu kuleta barua hiyo kwa siri wasingeshindwa kumuua. Bila
shaka walidharau wakijua kuwa muda waliokuwa nao ungetosha kuwawezesha kutawala
nchi. Aliwaza pia kuwa huenda wameacha vifaa vyao ambavyo sasa vinapeperusha
kila neno linalotamkwa chumbani humu hadi masikioni mwa Kwame kama
alivyowafanyia polisi. Hivyo, Joram alimkatiza Kombora kwa kumjibu akisema ,
“siwezi kutishwa na kijibarua kama hicho Inspekta. Wewe wanifahamu vyema. Kwa
bahati mbaya sifahamu lolote kinyume cha ukweli ulivyo.”
“Ukweli upi?”
Kombora alihoji kwa mshangao. “Unataka kusema kuwa ni wewe uliyemuua
Bazile?”
“Oh, Yes,” Joram alidakia.
“Hatukufahamu kama
muuaji Jopram.”
“Kwa hiyo tangu leo mmenifahamu kuwa sishindi kutumia
bastola yangu kwa muuaji kama yule. Kama unataka kunitia kizimbani kwa kosa hili
niambie.”
Kombora akaonekana kuchanganyikiwa, “Acha uoga Joram.
Mapenzi…”
“Tafadhali Inspekta. Suala la mapenzi yangu na Neema
halikuhusu,” alijitia mkali.
Wakati huo mikono ya Joram ilitambaa
polepole mwilini mwake akipapasa alikoficha silaha zake za siri, kamera ndogo
pamoja na kanda ya kunasia sauti. Akatabasamu kwa furaha kuona vitu hivyo pamoja
na misukosuko yote, vilikuwa salama katika mifuko yake ya
siri.
Akavitoa na kumpa Kombora huku akimfanyia ishara ya kutokusema
lolote. Kombora alivitazama kwa mshangao, lakini akavifahamu mara moja na
kuvidaka kwa furaha.
“Kwa hivyo bwana Kombora maadamu nimepata nafuu
naomba uniruhusu nijipumzishe. Kama maswali nitayajibu kesho. Siwezi kuihama
nchi usiku mmoja.”
Kombora , akiwa kamwelewa Joram, alijitia kubisha
kidogo.
“Mpenzi wako?”
“Suala lake niachie mwenyewe. Kesho
nitampata.”
“Sikujua kuwa u mwoga hivyo Joram. Lakini sina budi
kukwambia kwamba tuna mashaka. Polisi itafanya kila njia kupata ukweli. Nawe
utahesabiwa kuwa mwenye hatia kwa kuficha habari.”
“Kesho Inspekta,
tafadhali,” Joram alijibu akiinuka na kutoka. Ndiyo kwanza akagundua
alivyodhoofika. Mwendo wake ulikuwa wa kujikongoja hadi nje ya chumba ambapo
alisimama kwa muda akikusnya
nguvu.
*****
“Umesikia?” Kwame
alitabasamu, macho yake ambayo dakika chache nyuma yalimtazama mwezi wake kwa
hasira ya kutisha kidoo yalikuwa yameisahau hasira hiyo, ingawa yaliendelea
kutoa nuru ya kuogofya. “Umesikia mwenyewe Joram akikiri kuwa amemuua Bazile.
Hawezi kuwa mjinga na kukubali kumpoteza msichana mzuri kama yule kwa ajili ya
mabadiliko tu ya serikali. Atakachoofanya ni kuwazungusha hadi kesho. Na kesho
hiyo…”
“Simwamini hata chembe kijana yule. Ana akili za ajabuajabu,”
mwezi wake alikanusha. “Aweza kuwa sasa hivi anabuni jambo lingine la kututia
mikononi.”
Kwame akaukunja uso wake, “Uoga wa aina hiyo siupendi
kabisa bwana Matata,” alifoka. “Kama huniamini wala kuwaamini wataalamu,
matajiri na watu mashuhuri walioandaa mipango yote hii, tamka mara moja ili
tukuondoe katika mipango yetu. Na nafikiri sina haja ya kukumbusha adhabu ya mtu
anayevunja kiapo cha hatari kama hiki.”
“Siyo hivyo bwana Kileo.
Ila…”
“Ila nini?” alifoka tena. Kisha akaishusha sauti yake akisema,
“Joram yumo mikononi mwetu. I kwa kuwa tunaye msichana wake, bali pia makachero
kadhaa wako nyuma yake. Wakati wowote watakapoarifu kuwa anaelekea kwenda
kinyume cha matakwa yangu atakula risasi. Kumwachia hadi sasa ni pamoja na hamu
yangu ya kutaka kuona hayo machachari yake hapo kesho wakati tutakapokuwa Ikulu,
nchi itakapokuwa chini ya miguu yetu.”
Kimya kifupi
kikafuata.
“Kwa hiyo, bwana Matata, sikuiona kabisa sababu yaw ewe
kurejea hapa kwa ajili ya kule kusita tu ati Joram amenusurika katika ajali ya
gari. Nakupa amri ya mwisho kuondoka hapa. Na nakuomba tusionane tena hadi kesho
tutakapokutana Ikulukuapishwa kama baraza lipya la mawaziri na baadaye katika
ukumbi wa Karimjee au Kilimanjaro Hoteli kwa tafrija maalumu.
Sawa?”
“Sawa bwana…”
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
******
MOTO
Matata alipowasili katika jengo la wizara yake, alilisahau mara moja jina hilo
na kuendelea katika jina lake halisi na hadhi yake katika wizara hii. Kama mtu
mkubwa, alitumia lifti maalumu ambayo ilimfikisha ghorofa ya nane ilikokuwa
ofisi yake.
Akautumia mlango wa pili kuingia
ofisini mwake ambamo alijibwatika juu ya kiti na kuitazama saa yake. Ilisema saa
nane na dakika ishirini. Saa kadha wa kadha zilisalia kabla ya kutokea jambo
ambalo lingebadili historia ya nchi.
Matata
alihofia sana muda huo wa kusubiri. Hakuwa na hakika kama anastahili kuendelea
na mipango yake au atoroke nchini mara moja kama roho ilivyokuwa ikimshawishi.
“Utajiri hauji kwa starehe”… alijikumbusha kwa taabu maneno ya
Kwame.
Kuyakumbuka huko kukamtia moyo hata
kicheko kikamtoka na akasahau ndoto mbaya zilizomwandama usiku wa jana akijiona
yuko kitanzini huku umati wa watu ukimcheka na
kumsimanga.
“Ndoto au woga tu,” aliwaza. “Kesho
ni siku nyingine. Nitakuwa mtu mwingine; tajiri na mwenye matumaini na nafasi ya
kuwa tajiri na tajiri tena..”
Simu iliyomuunga na
katibu wake ikakoroma ghafla. Akaiinua na kulitaja jina
lake.
“Umerudi
mzee?”
“Ndiyo Salome, lakini sijisikii vizuri,
hivyo sitapenda kusumbuliwa kwa matatizo madogo
madogo.”
“Nimeelewa mzee, ila kuna huyu kijana
hapa. Anadai kuwa ni lazima akuone kwa hali yoyote. Anasema mnafahamiana na
kwamba ana hakika utafurahi kumwona.”
“Amekutajia
jina lake?”
“Ndiyo. Anajiita Joram
Kiango.”
“Nani?” Bwana mkubwa alinguruma katika
simu kiasi cha kuyaumiza masikio ya katibu wake. Hakujua afanye nini. Hakujua
kama alistahili kumwona au la. Akabaki kaduwaa na simu mkononi hana uwezo wa
kumjibu Salome ambaye aliendelea kuongea upande wa
pili.
Joram alimkuta katika hali
hiyo.
“Nadhani nitasamehewa kwa kuingia kabla ya
kibali chako mzee,” Joram alisema kwa sauti yake tulivu akijiweka kitini bila
kusubiri kukaribishwa. Nimeona nikutembelee mapema ili nishirikiane nawe
kujadili maisha yako ya baadaye. Unasemaje
mzee?”
Jibu halikusikika hivyo Joram aliendelea,
“Kitendo chako na wachache wenye nyadhifa kadha wa kadha serikalini, ambao
mmethubutu kula njama dhidi ya taifa lenu, taifa changa, ambalo linakutegemeeni
ninyi kuliokoa, ni kitendo cha aibu kubwa mno. Ni kitendo ambacho hakistahili
kuyafikia masikio ya taifa hili ambalo lilikutegemea sana hata likakupa wadhifa
muhimu kama huu.
Hivyo nilichofuata hapa ni
kukushauri tuondoke pamoja hadi Ikulu kwa mtukufu Rais ambako utakiri madhambi
yako yote na kumwachia jukumu la
kuamua.
“Usijidanganye kuwa ndoto yenu yaweza kuwa
kweli,” Joram aliendelea. “Orodha yenu, picha zenu, maongezi yenu ya asubuhi ya
leo na njama zenu zote sasa hivi ziko mikononi mwa wanaohusika. Kuchelewa
kujitoa kutakufanya uaibike zaidi. La muhimu ni kwenda mwenyewe mbele ya Baba wa
Taifa ambako utatubu na kukiri yote bila kusahau kuwa unahusika kwa kila hali
katika mauaji ya watu wengi wasio na hatia.”
Bwana
mkubwa huyo alishindwa kujibu lolote, walao kumtazama Joram usoni. Baada ya muda
mrefu alinong’ona kwa sauti ya aibu akisema, “Siwezi. Siwezi kumtazama Rais wala
raia yeyote usoni. Tafadhali nenda zako nifikirie la
kufanya.”
“Fikiria bila kusahau kwamba mpango
umeharibika,” Joram alisema akiinuka na kutoka nje. Akamuaga katibu na kutoka
hadi mbele ya lifti ambapo alibonyeza kidude cha kuteremkia. Lifti ilipofika,
aliteremka hadi chini.
Mlango wa lifti
ulipofunguka masikio ya Joram na abiria wote waliotoka ndani ya lifti hiyo
yalidakwa na kelele za ghafla zilizotoka katika umati uliokuwa ukijaa haraka
haraka chini ya jengo hilo la wizara. Joram akawa mmoja kati ya watu
waliokimbilia sehemu hiyo kutazama kinachotokea. Lilikuwa jambo la kutisha
kuliko alivyotarajia. ‘Bwana mkubwa’ ambaye alikuwa akiongea naye muda mfupi tu
uliopita alikuwa kalala chali akivuja damu nzito kutoka katika majeraha ya
kutisha ya kichwa kilichoonekana kufumuka, miguu iliyovunjika na kiuno ambacho
kilionekana kuvunjika kabisa.
“Nimemwona akijitupa
mwenyewe toka dirishani,” alidai mtu mmoja.
“Mimi
pia…”
Joram akaitazama saa yake na kuondoka mahala
hapo kwa mwendo wa haraka. Mbele kidogo, alipungia teksi na kumweleza dereva
wapi alihitaji kupelekwa. Ilimfikisha kwa muda mzuri. Joram akateremka na
kuiendea ofisi aliyoihitaji ambamo aliomba kuonana na ‘Afande mkubwa
zaidi’.
Akaelekezwa ofisi
yake.
Alimkuta afande huyo kabadilika kabisa kwa
magwanda ya kijeshi yenye nyota nyingi mabegani kinyume kabisa cha yale ya
kiraia aliyovaa katika mkutano wao wa siri. Afande huyo alimtazama Joram mara
moja na kujikuta akishikwa na hofu kubwa.
Ghafla,
akasahau furaha aliyokuwa nayo muda mfupi alipokuwa akiwaza kesho itakavyokuwa
siku tofauti mno kwake. Siku ambayo itamkaribisha katika dunia ya kutumia bila
hofu ya kuishiwa, dunia ya kumchukua msichana yeyote amtakaye bila kuogopa
sheria wala wazazi wake, dunia ya yeye kuwa na amri juu ya kuishi na kufa kwa
mtu yeyote katika nchi hii. Naam, dunia itakayomweka hadharani, kila mtu
akimtetemekea. Alikuwa akisubiri saa zitimie ili atimize wajibu wake
kuikaribisha dunia hiyo.
Katika muda huo wa
kusubiri, hakutarajia kabisa kuonana na
kijana huyu aliyeketi mbele
yake akivuta sigara na kutabasamu kisirisiri.
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nani wewe? Na
wataka nini hapa?” akajitia
kuuliza.
“Tunafahamiana sana afande. Nadhani
huwezi kusahau kuwa muda mfupi uliopita tulikuwa wote katika mkutano fulani. Kwa
jina naitwa Joram Kiango.”
“Sikufahamu wala
siufahamu mkutano huo.”
Labda,” Joram alijibu.
“Lakini naamini utaufahamu vizuri. Baada ya muda mfupi polisi watakapokutia
pingu na kukuhifadhi hadi kesho ambapo picha yako na wenzako mkiwa mkutanoni
zitakapotolewa gazetini na maongezi yenu kusikika katika Redio Tanzania. Ama
hufahamu kilichonileta mbele yenu ilikuwa kupata picha
hizo?
“U mtu hatari usiye na shukrani hata
chembe,” Joram alifoka. “Wadhifa ulionao ni mzito. Mamilioni ya Watanzania
wangeweza kuumudu wadhifa huo lakini taifa limekukabidhi wewe. Ili ulilinde. Ili
uwe mstari wa mbele kulinda silaha na masilahi yake. Lakini wewe unageuza silaha
walizokupa wao kuwaangamiza. Unashiriki katika mikataba ya kupokonya masilahi
yao. Huoni aibu kuuza wananchi. Aibu ilioje! Kwa kweli hustahili
kuishi.”
Afande huyo akainua uso kumtazama Joram
kwa hasira, “Toka nje bwana mdogo,” akafoka. “Toka, vinginevyo
nitakudhuru!”
“Lazima nikueleze kwanza
nilichokusudia…”
“Toka. Toka!”
akafoka.
“… Kwamba taifa hili si zizi la ng’ombe
ambalo mtu yeyote anaweza kuligeuza rasilimali yake kwa faida yake binafsi na
mabwana
zake.”
“Toka!”
“Na…”
“Toka!”
Safari hii ‘afande’ alikuwa na bastola mkononi. Bastola aliyotoa ndani ya mtoto
wa meza. Ilimwelekea Joram kifuani. “Toka vinginevyo
nitakuua!”
Sauti yake iliwavuta wengi. Wakaja na
kuduwaa mlangoni wakiwa hawayaamini macho yao mkubwa kaielekeza bastola kwa raia
ambaye alionekana hana hatia wala hofu.
“Kifo
change kitaongeza uzito wa madhambi yenu juu ya damu
nyingi zisizo na
hatia ambazo mmemwaga. Hakitaleta mabadiliko yoyote wala kufanikisha mipango
yenu ya kishetani…”
Mara mlipuko wa bastola
ukasikika. Kila mtu alifumba macho kwa miali ya mlipuko huo. Walipoyafunua,
walimwona bwana mkubwa kasahau kiti chake na kukaa chini, kainamisha kichwa
ambacho kilikuwa kimefumuka kwa risasi hiyo. Bado, mkono wake uliishikilia
bastola hiyo iliyotimiza wajibu.
Umati ulipiga
kelele za hofu na mshangao. Joram aliacha umati huo katika hali hiyo na kutoka
nje ambako alipata shida kidogo kupata usafiri. Watu wote walikuwa wakikimbilia
kufuata mlipuko huo. Joram akapishana nao hadi nje ya jengo hilo ambako
alijipatia usafiri.
Safari ilimfikisha katika
wizara nyingine. Akaifuata ofisi ya mtu mkubwa moja kwa moja na kuomba
kumwona.
“Huwezi kumwona mtu,” katibu alidai.
“Amepata habari mbaya. Hana hali nzuri kuweza kuonana na mtu
yeyote.”
“Habari
ipi?”
“Ya kifo. Bwana mkubwa serikalini kafa na
alikuwa rafiki yake mkubwa.”
Joram akashangaa
habari zinavyosafiri haraka haraka. Ni hicho alichohitaji. Genge hilo hatari
lifahamu kuwa limefahamika na limevunjika. Mipango yao isiweze kuendelea. Joram
akatabasamu huku huku akigeuka ili aondoke zake. Lakini mara hamu ya kuuona uso
wa mtu mkubwa baada ya habari njema kama hiyo ikamshika.
Akamgeukia
katibu wake na kumwambia: “Nataka kumwona. Ni lazima nimwone. Siwezi kuondoka
bila kumfariji. Mimi ni rafiki yake pia.”
Alipoona
achelewa kuruhusiwa, alijielekeza mlangoni na kuuendea. Akagonga mara moja na
kuufungua. Alimkuta bwana mkubwa kasimama nyuma ya meza mkono wake ukizungusha
namba za simu, mkono wa pili ukiwa umeshika shavu. Mkono uliokuwa kwenye simu
ulisita ghafla mara macho yake yalipokutana na yale ya Joram ambaye alikuwa
akitabasamu.
“Pole
mzee.”
“Nani wewe? Joram!” mtu mkubwa alifoka.
“Tafadhali toka nje ya ofisi yangu.”
“Ndiyo,”
Joram alijibu. “Lakini si kabla ya kukumbusha kuwa wenzako wametangulia kwa
heshima kidogo. Hawatawajibika kutazamana na umati ambao utajaa mahakamani
kukutazama kwa mshangao wewe na wenzako pindi mkijibu maswali ya Jaji Mkuu. Wala
hawataning’inia juu ya kitanzi na kufa polepole huku wakijutia uroho wao na
utovu wa shukrani ambao wamekufanyeni kuwa fisi mbele ya kondoo badala ya
wachungaji. Aibu iliyoje kuwa na kiu ya utajiri kiasi hicho, pole tena mtu
mkubwa.”
Mtu huyo alimtazama Joram kwa macho yenye
mchanganyiko wa hasira na aibu. Kisha aliutia mkono wake katika mfuko wa koti na
kutoa pakiti ya vidonge vidogo vidogo vya usingizi ambavyo alivimimina mkononi
na kuvitupia kinywani. Alivyohakikisha amevimeza alimtazama tena Joram na
kusema, “Siwezi kukubali kuitazama jamii….siwezi…” macho yake yakaanza
kubadilika.
Akajibwatika chini akisahau kiti na
kuketi sakafuni huku akijaribu kuyafumbua macho yake kwa juhudi kubwa.
Hakufaulu. Mara akayafumba na kutulia.
Joram
alifahamu kuwa huo ulikuwa usingizi ambao usingeisha. “Kifo cha amani kuliko
alivyostahili,” aliwaza akitoka zake polepole na kumtupia katibu ‘kwa heri’ bila
kumtazama usoni.
Nje ya jengo hilo Joram alisita
na kuwaza kwa furaha. Nusu ya kazi ilikuwa imekwisha. Mizizi mingi
ilikwishang’olewa. Uliosalia ni ule mzizi wa shina; mzizi wa fitina; Kwame au
Joe Kileo. Huyu alikuwa mtu hatari na bado alikuwa na Neema tayari kumdhuru
endapo angejua mambo yanamwendea kombo.
Hivyo,
alihitajiwa kupatikana haraka, katika hali ya uangalifu zaidi. Hali ambayo Joram
alihitajika kuwa mkamilifu kwa kila hali. Kwa bahati baya hakuwa na silaha
zozote za haja mfukoni zaidi ya visu kadhaa vilivyohifadhiwa katika mfuko wa
siri. Lakini kwa ajili ya haja kubwa ya kumpota Neema akiwa hai bado, Joram
alijikuta ndani ya teksi akielekea jengo la Snow
Fund.
Gari liliposimama, Joram alijikuta akiruka
nje na kutazamana na Inspekta Mkwaju Kombora ana kwa ana. Kombora alikuwa na
bastola wazi mkononi, nyuma yake, askari sita wenye bunduki aina ya Sub-Mashine
Gun wakimfuata kwa uangalifu.
“Joram,” Kombora
alimwita kwa nguvu alipomwona. “Umekuwa wapi muda wote huu? Kijana, nasikitika
muda hautoshi kuweza kuzungumza mengi. Lakini kwa ufupi tu safari hii
ulichogundua ni kitu kizito ambacho kingeifanya nchi hii igeuke dimbwi la damu
ama iwe zizi ambalo mchungaji ni fisi mwenye
njaa.”
“Nami nasikitika pia Inspekta kuwa
umegundua mapema kuliko nilivyotaka,” Joram akamjibu. “Ningependa kukamilisha
kazi hii peke yangu kwa faida ya watu ambao wengi wao wana vyeo vikubwa
serikalini. Nilikuwa nikiwaonea aibu au huruma kuwafanya wasimame mbele ya
wananchi waliowaamini madaraka hayo na kukiri madhambi yao. Kwa bahati
umeniwahi.
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hata hivyo, wengi
wameshafuata njia inayowastahili. Wamejiua wenyewe. Utapata taarifa kamili baada
ya muda mfupi.
“Kadhalika, huko Kigamboni iko
nyumba moja ambamo amelala marehemu asiye na hatia, Komba ambaye ndiye hasa
aliyesaidia siri hii ya hatari kutoka nje. Ameuawa na jambazi hatari ambalo bado
liko hai katika nyumba hiyohiyo. Nimelifunga vizuri. Halina nafasi ya kutoroka.
Mara tu upatapo nafasi, nitapenda kupata askari ambao nitawaelekeza katika
nyumba hiyo. Napenda Bon afe kwa kitanzi.”
“Kwa
nini Joram?” Komba alifoka. “Kwa nini hukusema mapema? Anaweza kutoroka!” Kisha
akajisahihisha kwa kusema polepole, “Kweli haikuwepo nafasi. Tuombe Mungu
nimkute hai. Atajuta kuzaliwa. Sasa ni kumwingilia huyu kiongozi wao,
Kwame.”
“Kwame ni mtu hatari sana,” Joram
alikumbusha tena. “Na bado anaye Neema mikononi mwake. Bila shaka yuko katika
jengo hilihili. Nadhani utahakikisha usalama wa Neema
Inspekta.”
“Usitie
shaka.”
“Wakaanza kuingia ndani wakiwapita
wafanyakazi wa ofisi hiyo ambao kwa muda mrefu, walikuwa wamechanganyikiwa kwa
matukio ya kutisha ambayo yalikuwa yakiitokea ofisi hii kutwa nzima. Waliduwaa
juu ya viti vyao au wima wakimtazama Kombora, Joram na askari wote ambao
waliingia na kuiendea ofisi ya mkurugenzi
mtendaji.
“Hana nafasi ya kutoroka,” Kombora
alimnong’oneza Joram. “Jumba hili limezingirwa kila upande. Askari wengine wako
juu ya paa. Sijui atatokea wapi.”
“Usisahau
usalama wa Neema Inspekta,” Joram aliasa tena. “Kwa kweli kazi hii ningependa
kuifanya mwenyewe. Sina imani sana na askari
wako…”
Kombota alimkatiza Joram kwa kumwambia,
“Neema atatoka salama. Askari wote wameonywa waangalie sana risasi zao zisimguse
msichana wako walao unywele. Natumaini watafanya kazi nzuri. Nimechagua wale
ambao ni hodari kwa shabaha tu.”
Wakaifikia ofisi
ya Kwame. Waligonga mara kadhaa bila jibu. Kombora akaita kwa nguvu ingawa
alijua mlango huo ulikuwa maalumu kwa kutokuruhusu sauti kutoka nje. Alipochoka
alielekeza bastola yake katika kitasa na kuifyatua. Risasi ya .45 maalumu kwa
polisi haikusita kutimiza wajibu.
Chumba
walikikuta kitupu, Kombora akatoa macho ya mshangao. Lakini Joram alizunguka
nyuma ya meza na kuchungulia hapa kisha pale, mara sakafu ikafunguka na kuacha
mwanya wenye ngazi iliyoelekea chini. Kombora akawa wa kwanza kuifuata. Joram
alifuatia akifuatiwa na askari.
Huko chini
walijikuta katika ukumbi wenye vyumba vingi vyumba vyote vilikuwa vimefungwa.
Risasi ya bastola ya Kombora ikavifungua vyote. Waligundua mengi; akiba ya
silaha, nyaraka za siri na dawa aina aina. Ni katika chumba cha mwisho ndimo
walipopata kitu walichokuwa wakihitaji. Walimkuta Kwame kashika bastola mkononi
mbele ya msichana aliyeketishwa sakafuni, nusu uchi kwa jinsi mavazi yake
yalivyotatuka katika hali ya kuadhibiwa
sana.
“Neema!” Joram alipiga
kelele.
“Neema, ndiyo,” Kwame aliwajibu
akitabasamu kifedhuli. “Ni mpenzi wako. Lakini endapo unampenda, waambie rafiki
zako wote pamoja na mkubwa wao anayejiita Inspekta warudi walipotoka haraka.
Mimi na wewe pamoja na mpenzi wetu tutaondoka pamoja hadi nje ya jiji ambapo
nitawapeni uhuru wenu nami nichukue uhuru
wangu.”
Kwame alichukua uamuzi huo baada ya kupata
taarifa ikimfahamisha kuwa Joram alikuwa ametoweka machoni mwa walinzi wake.
Taarifa hiyo ilifuatwa na vifo vya washiriki wenzake pamoja na kuambiwa kuwa
askari walikuwa wakiizingira ofisi yake ndipo akawa hana njia zaidi ya
hiyo.
Kombora akamgeukia Joram kwa mshangao.
Alitarajia madhara, lakini hakutarajia madhara hayo yawe katika hali hiyo.
Hakutarajia kumkuta Kwame akiwa na bastola mkononi akimtazama msichana asiye na
hatia na ambaye ametoa mchango madhubuti kuiokoa nchi katika madhara ya mtu
huyo. Msichana mzuri, Neema Iddi. Wakati huohuo, hakuwa tayari kuacha mtu huyo
anusurike mbele ya macho yake mwenyewe hasa baada ya kuziona picha alizofotoa
Joram pamoja na kusikiliza kanda ambayo ilinasa mengi yanayotosha kuwa ushahidi
kamili dhidi ya watu hawa waovu.
“Labda hunifahamu
vyema Inspekta,” Kwame alimjibu baada ya tabasamu lingine la kebehi. “Mwambie,
Joram. Mwambie mimi ni nani. Nadhani wewe wanifahamu zaidi
yake.”
“Nakufahamu sana,” Kombora alijibu. “Wewe
ni jasusi mkubwa uliyepewa jukumu la kuharibu siasa na uchumi wa nchi kwa njia
yoyote. Umefanikiwa kuwalaghai watu kadhaa kwa vishawishi vya kishetani na
kupanga kuangusha utawala halali wa nchi hii usiku wa
leo.”
“Kumbe wafahamu…” Kwame
alijibu.
“Kwa bahati mbaya bwana Kwame au Joe
Kileo mipango yako yote imeharibika. Utakachofanya ni kujitoa kwetu ili uwekwe
mahabusu kusubiri hukumu kwa makosa yako yasiyohesabika. Umemwaga damu zisizo na
hatia umethubutu kula njama dhidi ya nchi na wananchi. Umesababisha fujo na
ghasia. Kwa kweli unastahili kula kitanzi Kwame. Ni hapo mabwana zako
watakapofahamu kuwa nchi hii si uwanja wa mpira ambapo wanaweza kutegemea
wapendavyo,” Kombora aliendelea kufoka.
“Kumbe
wanifahamu Kombora!” Kwame alijibu akitabasamu kifedhuli. “Kwa bahati mbaya
siwezi kushikwa nanyi. Nitaondoka na msichana huyu hadi nje ambako nitaamua wapi
nielekee. Mkinilazimisha nitakubali kufa, lakini si kabla ya kuhakikisha bastola
hii inaifumua sura nzuri ya msichana huyu. Nadhani hutapenda kushuhudia hilo
mtakatifu Inspekta Kombora. Na Joram? Utafurahi mpenzi wako asulubiwe mbele
yako?”
Wote walikubali kuchanganyikiwa. Joram
alisaga meno kwa hasira. Lakini hakuona lipi afanye lipi aseme katika hali hiyo.
Ingawa bastola ya Kwame ilikuwa ikimwelekea Neema, lakini macho na mawazo yake
yalikuwa kwa umati huo uliomzunguka silaha zao zikimtazama kwa
uchu.
Hivyo, hakuona wala kutarajia pindi Neema
alipoinuka na kuachia pigo kali ka karate ambalo lilifanya bastola hiyo ipae
angani. Wakati huo bastola zote zilifyatuka na risasi saba kuuteketeza uso na
kifua cha Kwame. Alikufa kabla hajatua chini. Hakuwa na haja ya
kupapatika!
“Neema!” Joram aliita kwa nguvu
akimkimbilia na kumwinua pindi alipoanguka kwa mshindo wa bastola. Alikuwa hai…
hakuwa na jeraha….
“Neema!” Joram aliita tena
akimkumbatia kwa
nguvu.
****MWISHO****
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
*****HUO NDIO
MWISHO WA RIWAYA YA MAREHEMU BEN R. MTOBWA ILIYOCHAPWA KITABU KWA MARA YA KWANZA
MWAKA 1984. IMECHAPWA HAPA 'TUNGO ZETU' KATIKA KUUENZI MCHANGO WAKE MKUBWA WA
FASIHI KWA JAMII YA KITANZANIA NA HATA AFRIKA MASHARIKI KWA JUMLA. TAREHE 9,
NOVEMBA, 2008 NDIPO GWIJI HUYU ALIPOIAGA
DUNIA.
TUNASHUKURU KWA KUWA PAMOJA TANGU MWANZO
HADI MWISHO.****
0 comments:
Post a Comment