Simulizi : Najisikia Kuua Tena
Sehemu Ya Nne
(4)
SAUTI hiyo ilimzindua
Joram. Akamwacha muuaji huyo aliyelala kama mzoga na kumsogelea mtu huyo
aliyekuwa akijaribu kuinuka ili ainue tena jisu na kummaliza adui yake. Joram
hakuwa na haja ya kuambiwa kuwa mtu huyo ni Dismas
Komba!
“Asante kwa kuokoa maisha yangu Bwana
Dismas,” alimweleza haraka haraka. “Unadhani kwa nini walitaka kukuua?”
aliuliza.
“Wamekwishaniua…Nakufa…” Komba
aliendelea kulalamika.
“Wewe sio
mmojawao?”
“Mimi ni adui yao
mkubwa.”
“Wewe ni
nani?”
“Huwezi kunifahamu. Kwa jina ni Joram
Kiango.”
“Joram! Nakujua sana…” Komba alisema kwa
juhudi kubwa. “Joram! Walinitesa sana…Laiti wangeniua…nilikuwa sina hali siku
zote. Nikienda huku nakutana nao. Nikikaa hapa usiku wanafika na kuniadhibu kwa
vitisho na mateso. Wameniua…” akaanza tena
kulalamika.
Ingawa nuru ilikuwa hafifu, ikitoka
katika mshumaa uliowekwa kwenye kona moja ya chumba, lakini ilitosha Joram kuona
katika macho yake Dismas Komba kuwa uhai ulikuwa ukimtoka harakaharaka. Hakuwa
na muda wa kuishi zaidi.
“Sema haraka,” Joram
alimhimiza. "Dismas kwa nini walitaka kukuua?”
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Wameniua tayari…
nakufa…”
“Kitu gani wanadai kutoka
kwako?”
“Wa…wame…wa…” Komba akaishiwa na uwezo wa
kuzungumza. Alichofanya ni kuinua mkono kwa udhaifu akiuelekeza katika pembe
moja ya chumba. Joram aliufuata mkono huo na kuona unaelekea debe lililokuwa
hapo. Akaliendea na kuchungulia.
Alilakiwa na
harufu kali ya kinyesi cha haja kubwa na ndogo ambacho kilikuwepo ndani ya debe
hilo. Akarudisha macho ya kutoelewa kwa Komba. Akaona kakazana kuelekeza kidole
papohapo, akajitahidi kutamka neno ambalo halikutamkika. Joram akahisi kuwa
lazima kama kuna chochote alikuwa kaficha haikuwepo nafasi ambayo isingeweza
kufikiriwa zaidi ya hapo. Hivyo akazidi kupekuapekua kando ya
debe.
Akaliinua. Chini yake akakuta bahasha
iliyofurika karatasi. Akaitwaa na kumgeukia Komba. Alimwona akitabasamu kisha
kuanguka kwa nyuma. Mara akaanza kutapatapa kwa maumivu pindi roho ikimtoka.
Joram alikimbia na kujaribu kumshika, haikusaidia. Tayari, Komba alilala kwa
utulivu katika usingizi usio na mwisho.
Joram
hakuona lipi zaidi angeweza kulifanya kuokoa maisha ya mtu huyo. Akaiendea
swichi ya taa ya umeme na kuiwasha, haikuwaka. Hivyo akaichomoa tochi yake yenye
ukubwa wa kalamu na kuiwasha. Nuru ilitoka kumwezesha kusoma neno moja tu ambalo
liliandikwa juu ya bahasha hiyo USIFUNGUE.
Joram
hakumtii yeyote aliyeandika neno hilo, akaifungua na kutoa karatasi ndefu ambayo
iliandikwa kwa mashine ya aina yake kwa lugha ya Kiingereza, maneno ambayo
tafsiri yake ilisema:
…NI DHAHIRI KUWA NJAMA ZETU
ZA KUCHANGIA HALI NGUMU YA KIUCHUMIAMBAYO ILIKUWA IKIIKABILI NCHI HII HAZIKULETA
MATUNDA TULIYOYAHITAJI, YAANI KUWAFANYA WANANCHI WAENDE KINYUME NA UTARATIBU WAO
NA KULETA GHASIA AMBAYO TUNGEINGILIA KATI NA KULETA UTAWALA WETU. NI WAZI KABISA
KUWA WAMEWAELEWA VIONGOZI WAO NA WAKO NAO BEGA KWA BEGA KUJENGA UPYA UCHUMI WAO.
BAADA YA MUDA MFUPI, NJAMA ZETU ZA KUCHANGIA HALI HII NGUMU
ZITAJULIKANA.
NA HAPO WANANCHI WATAKAPOAMKA NA
KUPATA MOYO MPYA AMBAO SI KWAMBA UTAWAFANYA WASHINDE VITA VYA KIUCHUMI TU BALI
WATAENDELEA KUIAMINI NA KUITEGEMEA KABISA SIASA YA UJAMAA NA KUJITEGEMEA. HAPO
NDOTO ZETU ZA KUUWEKA UTAWALA MIKONONI MWETU KATIKA NCHI HII ZITAKUWA
ZIMEKWISHA.
NAAMINI INAFAHAMIKA WAZI KUWA, NCHI
HII NI KAMA NURU AMBAYO AFRIKA NZIMA INAIFUATA. UKOMBOZI WA NCHI ZOTE ZA KUSINI
AMBAZO ZILIKUWA HAZIJAPATA UHURU WAKE NA ZINAZOENDELEA KUUPATA UMETOKANA NA
MSIMAMO WA NCHI HII.
BAYA ZAIDI NI UHURU WA
KIUCHUMI AMBAO NCHI HII INAONGOZA MAPAMBANO. MARA ITAKAPOJIIMARISHA KIUCHUMI
NCHI YA SIASA YA UJAMAA, NCHI ZOTE ZITAONA NURU NA KUIFUATA HILO LITALETA
MUUNGANO WA AFRIKA. HATUTAKI MAMBO HAYO YATOKEE LEO WALA KESHO. INASIKITISHA
KUWA PAMOJA NA HALI KUWA NGUMU YANAELEKEA
KUTOKEA.
KWA HIYO UAMUZI ULIOFIKIWA NA TWAA,
WADHAMINI WETU NI KUUCHUKUA UTAWALA HUU KIMABAVU. YATAFANYIKA MAPINDUZI YA
SILAHA. HATUJALI KUMWAGIKA DAMU WALA MAAFA, MAADAMU TUMESHINDA. WATU
TULIOWAANDAA HUKO JESHINI, KATIKA BARAZA LA MAWAZIRI, NDANI YA CHAMA, KATIKA
MASHIRIKA YA UMMA NA VYUO VIKUU WATASAIDIA KUULAGHAI UMMA ILI UTUUNGE MKONO.
VILEVILE WANANCHI WATAPAKWA MAFUTA KWA MGONGO WA CHUPA KWA KULETEWA VITU ADIMU
KAMA SUKARI, SABUNI, MAFUTA, NGUO NA KADHALIKA. WATAAMBIWA KUWA HAYO NI MATUNDA
YA UTAWALA MPYA.
WATAFURAHI. BAADA YA HAPO MAMBO
YATABADILIKA. UBEPARI UTARUDI MTINDO MMOJA. HATAKUWEPO YEYOTE MWENYE AMRI YA
KUUPINGA UTAWALA WETU.
MPAKA SASA MASHARTI BADO NI
YALEYALE ; KUWAPA WADHAMINI KISIWA KIMOJA ILI WAFANYE KAMA KITUO CHAO CHA
UTAFITI WA SILAHA. WANANCHI WOTE WATAHAMISHIWA HADI KISIWA KINGINE ILI
KUWARUHUSU KUANZA BIASHARA ZOZOTE ZA KIUCHUMI BILA MASHARTI, KUWASHUKURU KUTEUA
AU KUPENDEKEZA VIONGOZI WANAOWATAKA NA MENGINE
YATAKAYOJITOKEZA.
KWA SASA BADO VIONGOZI NI
WALEWALE AMBAO WALITAJWA KATIKA KIKAO
KILICHOPITA;
TOP KOLOTO – RAIS WA
NCHI
MOTO MATATA – MAKAMU WA RAIS
BOMBO MTORO – WAZIRI WA
MAMBO YA NCHI ZA NJE
CHEMA CHITIME – WAZIRI WA HABARI
JOE
KILEO – WAZIRI WA ULINZI.
WALIOSALIA WATATEULIWA
KUTOKA KATIKA ORODHA YA WANACHAMA WETU WALIOKO KATIKA NAFASI KUBWA
SERIKALINI.
Taarifa hii ni ya
mwisho itakayofanyika kwa siri kubwa kiasi hiki. Wakati wowote katika wiki mbili
zijazo mambo yatapamba moto. Watu wetu wataarifiwa kwa dharura ili kuanza mambo.
Ndipo maji yatakatwa kwa siku kadhaa kuwalegeza wananchi, vyombo vya habari
vitatoa habari za ajabuajabu zenye nia ya kuwachukiza wananchi dhidi ya Serikali
yao, kisha siku hiyo umeme utakatika ghafla na mapambano kuanza. Itakuwa rahisi
sana. Wachache watatiwa pingu, wachache watauawa na kutakapopambazuka utawala
utakuwa mpya.
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/-
Joram alimaliza
kuisoma karatasi hiyo huku akitetemeka kidogo. Haikuwa na mzaha hata chembe
ingawa aliamini kuwa iliandikwa na watu wenye wazimu na tamaa ya madaraka ya
uroho wa utajiri wa haraka haraka. Kama alivyokuwa amehisi kitambo, zilikuwepo
njama kubwa zaidi ya ile iliyofikiriwa na polisi ya mwandishi aliyechanganyikiwa
–Bazile – kupata kichaa na kuanza kuua ovyo. Mauaji hayo yalipangwa tu,
yakitumia jina la Bazile ili yaendelee kufanyika kwa siri bila wahusika kuhisi
lolote. Na kiini cha mauaji pengine kilikuwa hiki cha kuficha siri hii ambayo
kwa namna moja au nyingine iliondokea kuifikia mikono ya watu
wasiohusika.
Mara Joram akagutuka na kumsogelea
yule adui aliyekuwa akipambana naye muda mfupi uliopita. Alikuwa amekumbuka kuwa
sura yake haikuwa ngeni machoni mwake. Akainama na kummulika usoni kwa kurunzi
lake. Naam, sura ilikuwa ile ile ambayo si yeye tu bali karibu kila mtu
aliifahamu na kuiogopa. Sura ya mtu yuleyule ambaye alikuwa akihitajiwa sana na
polisi. Yule mtunzi wa vitabu vya mauaji na ambaye aliondoka kuwa muuaji mkubwa;
Bazile Ramadhani.
Ugunduzi huu ungeweza
kuwafurahisha polisi, kwani mtu hatari sana alikuwa amenaswa. Lakini kwa Joram
Kiango, kunaswa kwa Bazile hakungeweza kumpa furaha hata chembe: Taarifa ya
njama za mapinduzi ilikuwa mfukoni ikimkodolea macho. Hakuona vipi Bazile
aliweza kuingia katika kikundi hicho na vile aliondokea kuwa hodari kwa
mauaji.
Kwa kweli alikuwa haamini kuwa muuaji ni
Bazile. Na kama alikuwa huyo, kulingana na madai au ushahidi wa polisi hasa kwa
kifo cha Kitenge yule mtoaji vitabu, basi Joram aliamini ni kifo hicho tu
ambacho angeweza kukifanya. Vifo vingine alihisi kuwa ziko njama za mtu au watu
wengine. Lakini leo kashuhudia mwenyewe, na anaye mkononi Bazile huyohuyo,
muuaji, anaweza vipi kuendelea kukanusha? Akazidi kumtazama
vizuri.
Akaingiza mikono yake mifukoni na kutoa
silaha za kijasusi ambazo hutumiwa na majasusi wa hali ya juu sana. Vitu kama
vikopo vyenye sumu za kulevya, vidonge viwezavyo kuua kwa muda mfupi sana,
bastola ndogo, kitambulisho na kadhalika. Vyote hivyo Joram alivitia mfukoni
mwake. Kisha akarudisha macho yake juu ya uso wa Bazile kwa
mshangao.
Macho yake yalikuwa wazi yakimtazama
kwa ujeuri na kutokujali. Hayakuwa macho ambayo Joram alimtegemea mwandishi huyo
kuwa nayo. Akaupeleka mkono wake kuupapasa uso huo. Mara Joram akaangua kicheko.
Alipoutoa tena mkono wake ulikuwa umeshikilia ngozi ya uso wa Bazile ambao
uling’oka kwa taabu. Uliobaki badala ya uso huo ulikuwa uso mweupe wa mtu mwenye
sura mbaya. Uso wa jasusi lenye moyo wa mnyama ambalo bila
shaka
lilikuwa limekodiwa kufanya mauaji
hayo.
“Kill me” lilimwamuru
Joram jitu hilo.
“Who are you?” Joram
alimuuliza.
“Just kill
me.”
Joram akaokota tambara chafu na kulididimiza
katika domo la jitu hilo ili lisiendelee kusema. Kisha akahakikisha kamba
alizotumia kulifunga jitu hilo zilitosha. Akaongeza nyingine na kutoa kila kifaa
mwilini mwa jitu hilo. Aliporidhika, alitoka chumbani na kuufunga mlango vizuri
akiwa na hakika kuwa jasusi huyo asingepata mwanya wowote wa
kutoroka.
Saa yake ilidai ni zaidi ya saa nane za
usiku. Bado alikuwa na saa nne ili aendelee na harakati zake za kumaliza
upelelezi huo.
Akaamua kusubiri papohapo akimlinda mateka wake.
Alitumia funguo zake ‘malaya’ kuingia chumba cha pili ambako alikuta kitanda
kizuri kikimsubiri. Akajilaza. Usingizi haukumjia. Akijua kwamba chumba cha pili
kina muuaji hatari na maiti ya mtu, mawazo hayakuweza
kutulia.
Zaidi, alishindwa kulala kwa jinsi fikara
zilivyokuwa zikimpita kichwani juu ya barua hiyo ya siri aliyokuwa nayo.
Alifahamu kagundua siri kubwa. Lakini bado alifahamu kuwa hajagundua lolote
dhidi ya watu hao wanaokusudia kuichukua nchi. Ilikuwa wazo kuwa majina hayo
yalikuwa bandia tu. Hakuwa na muda wa kujisumbua kumtesa mateka wake mzungu ili
amwambie.
Kwani, kwa kadri anavyowafahamu majasusi
hao, hawawezi kutamka lolote. Hata hivyo, Joram alijua lipo ambalo angefanya
kesho ili kuweza kupata walao njia ambayo ingemwezesha kuwafahamu watu hao
waliochoshwa na amani. Kiasi pia alijiuliza juu ya Bazile. Kama muuaji alikuwa
akiutumia uso wake, yeye mwenyewe yuko wapi? Pengine naye kauawa na kuzikwa kwa
siri?
Mapambazuko! Joram aliyasubiri kwa hamu
kubwa mapambazuko ili apate majibu ya maswali hayo na mengi
mengine.
*****
KULIPOPAMBAZUKA, Joram
aliwachungulia maiti na mateka na kuona wako katika hali ile ile ya usiku.
Akawafungia tena na kuamua kuwaacha katika hali hiyo. “Maadam nyumba inaogopwa
kuwa ina mkosi au majini, wanaweza kuendelea kukaa humu walau kwa saa sita bila
kuonekana,” alijisemea akihifadhi vizuri vifaa vyake vyote alivyopata katika
nyumba hiyo. Akakiendea kivuko ambako alikuwa miongoni kwa abiria wa kwanza.
Upande wa pili alitembea kwa mguu hadi kituoni ambako alipanda basi
lililompeleka uwanja wa ndege.
Wafanyakazi
walikuwa ndio bado wanawasili na mabasi yao. Joram alitazama hadi alipomwona
yule binti aliyempa orodha ya wasafiri wa ndege aliyoihitaji jana. Binti huyo
alimtazama kwa macho ya kufahamiana na
tabasamu.
“Mbona mapema hivyo?”
alihoji.
“Kuna kitu nilisahau kuuliza jana,” Joram
alihoji na kuongeza,
“Tafadhali jaribu kukumbuka kama uliona tukio
lolote la ajabu au ambalo halikuwa na kawaida siku
ile?”
“Ipi?”
“Ile
waliposafiri watu hawa,” akamwonyesha orodha ya majina yao.
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Msichana huyo
alijaribu kuwaza sana. mara akakumbuka
jambo.
“Nakumbuka yuko mzee mmoja kati yao ambaye
alitujia katoa macho pima na kudai kuwa begi lake limeibwa, mikononi alikuwa na
begi lingine aina ileile ya suitcase. Tulipomuuliza hiyo kapata wapi alisema
ameikuta badala yake. Tukamwelekeza kwenda chumba ambacho begi hilo lingeweza
kufunguliwa ili ijulikane nani mwenyewe. Alienda huko. Aliporudi huko alikuwa
akicheka na kutuambia kuwa begi lilikuwa lake isipokuwa lilikwaruzwa kidogo
ndipo akalisahau.”
“Unamfahamu mtu
huyo?”
“Sana. huwa anasafiri mara kwa mara. Jina
lake ni Kwame. Nasikia ana kampuni yake
binafsi.”
Joram hakuweza kujizuia kuonyesha furaha
aliyoipata baada ya kusikia hayo. Tayari alikuwa na shilingi mia mbili mfukoni
akimpa binti huyo huku akisema, “Umenisaidia sana
mpenzi.”
“Sioni nimekusaidia
vipi.”
“Utaona baadaye,” Joram alisema akiondoka
kuendea teksi zilizosimama kando yao zikiwasubiri
abiria.
Hisia zake za awali juu ya kuhusika kwa
Kwame kwa njia fulani katika njama hizi sasa zilikuwa zimethibitika. Kupotelewa
na mfuko, Joram alifahamu ni jambo lililotokea. Pengine marehemu Komba
aliuchukua mfuko huo kwa kukosea, pengine alikusudia. Kwame bada ya kugundua
hayo, akijua kuwa kuna siri kubwa ambayo hakupenda ijulikane, alichanganyikiwa
na kuwapigia kelele wahudumu.
Lakini baada ya
kufikiri zaidi ndipo alibuni uongo kwa kudai kuwa mfuko ni wake kwa matumaini ya
kumfahamu mwenye mfuko huo kwa kusoma hati ambazo zingekuwepo ndani ya mfuko
huo.
Ni njia hiyo iliyomwezesha kumpata marehemu
Komba. Pengine, hata kuchelewa kumuua kulitokana na hofu yao ya kutojua iliko
barua ile ya siri. Naye Komba yaelekea alikuwa mgumu wa kuitoa kwa kufahamu kuwa
mara waipatapo, wasingesita kummaliza.
Wakati wakiwaza hayo, Joram
alikuwa ndani ya gari akielekea mjini. Teksi ilimfikisha nyumbani kwake ambako
alioga vizuri, akavaa mavazi yaliyomstahili na kuweka mifukoni vitu
alivyovihitaji, kisha alitoka kwenda
ofisini.
Neema alimlaki na maswali mengi. Joram
alijibu machache tu akimwahidi kuwa baada ya saa chache atajibu yote. Kisha,
aliandika kadi moja ya ‘express’ na kumwomba Neema aipeleke Posta. Aliporudi,
Joram alimpa maelekezo mengine ambayo yalimfanya Neema atoe macho kwa shauku na
tamaa akijua kuwa mambo yameanza.
Joram
aliitazama saa yake, kisha akajistarehesha juu ya meza akisoma gazeti la Daily
News ambalo lilikuwa na habari za kuchekesha chini ya kichwa cha habari: BAZILE
MUUAJI HATARI YU HAI BADO
Joram aliisoma habari
iliyofuata kama hadithi kisha akalitupa juu ya meza na kuendelea kusubiri,
sigara zikiungua mdomoni mwake moja baada ya
nyingine.
*****
Kwame,
kwa mara ya kwanza tangu alipoanza harakati zake alijikuta katika hali ya
wasiwasi na mashaka makubwa. Kwa mbali, moyoni mwake, hofu ilikuwa iitishia
kuutawala hasa kwa hisia zilizokuwa zikimnong’oneza kuwa mambo yameanza
kumwendea mrama. Rohoni alipata wazo lililomshawishi kutoroka nchini mara moja,
aende kokote duniani ambapo angeishi kwa starehe akitumia utajiri wake mkubwa.
Wazo hilo alilipinga kwa kujikumbusha mara kadhaa kuwa hiyo dalili ya uoga wa
kike.
Mashaka hayo yalikuwa yamemnyima usingizi usiku kucha tangu
alipoarifiwa kuwa Joram Kiango alikuwa ametoweka baada ya kumshambulia mmoja
kati ya watu aliowaamini waliokabidhiwa jukumu la kumlinda. Ingawa alikuwa na
uhakikia kuwa Joram bado alikuwa hajui lolote la haja, lakini alimshakia sana
hasa kwa kujua kuwa, iwapo angefika Kigamboni na kumsikia Komba angeweza
kugundua mengi ya hatari. Kwa hofu hiyo, baada ya Joram kutoweka, ndipo akaamua
Komba auawe mara moja bila kujali tena kupatikana kwa zile nyaraka za siri
ambazo Komba alizipata kwa ajali na kuzing’ang’ania kama roho
yake.
Mtu aliyetumwa kuua, Kaburu Vosgan Bon alikuwa mtu mwenye hakika
na kazi yake. Kwame hakuwa na shaka naye, hasa kwa kukumbuka alivyokwisha fanya
mauaji yote kwa ukamilifu chini ya kivuli cha yule kijana mtunzi, Bazile
Ramadhani, kiasi cha polisi na taifa zimakuendelea kuamini kuwa muuaji si
mwingine zaidi ya kijana huyo.
Hata hivyo, hofu ilianza kumshika
baada ya kuona mapambazuko yakifika kabla ya kupewa taarifa juu ya kazi
hiyo.Pengine alifanya makosa kuondoa makachero wote waliokuwa wakimlinda
Kombaili Bon afanye kazi yake vyema? Yawezekana Bon amekwama kwa njia moja au
nyingine? Hata hivyo, alifarijik kidogo baada ya kukumbuka kuwa pantone hufungwa
saa fulani za usiku hadi alfajiri ya siku ya pili, hivyo yangewezekana baada ya
kuua, Bon ameshin dwa kuvuka na angetokea kama kawaida kesho yake. Yawezekana?
Bon ni mtu wa kushindwa kupata ngalawa au hata kuogelea hata alale mahala penye
hatari kiasi hicho?
Ni hayo yalimtia Kwame mashaka, ingawa alipotoka
asubuhi na kwenda kzini kwake alikuwa katika hali ya kawaida. Aliwasalimu
wafanyakazi wengine na kumpita katibu wake mahsusi hadi ofisini mwake ambamo
aliketi juu ya kiti akijiuliza lipi afanye katika hali kama hiyo. Kabla hajajua
la kufanya katibu wake alimjia akiwa na barua mkononi yenye bahasha
iliyobandikwa kijikaratasi cha ‘express’ yaani haraka. Aliipokea kwa mashaka na
kuitazama kwa makini kabla hajagundua kuwa bahasha hiyo ni ile ile ambayo
ilikuwa imehifadhi nyaraka za siri alizokuwa akizitafuta sana kutoka kwa
Komba.
“Umeipata wapi hii?” alihoji hafla alipoikumbuka bahasha
hiyo.
“Imeletwa na mtu wa posta asubuhi hii hii.”
“Vizuri
unaweza kwenda.”
Binti huyo malipoondoka Kwame aliifungua haraka
haraka na kutoa kadi ambayo iliyavuta macho yake kwa hofu kubwa .ilikuwa
imeandikwa:
Bwana Kwame, nadhani bado una ndoto za kuendelea na
mipango yako michafu ya kuleta maafa katika nchi hii. Kama bado unayo,
nakushauri uiache tangu dakika hii. Nimekwisha kufahamu wewe pamoja na wenzako
wote. Ninachokushauri ni nyie wenyewe kujitoa serikalini na kuomba radhi. Iwapo
itafika saa sita kabla hamjafanya hivyo nitachukua hatua mabzo zitakuonyesha
kuwa sina mzaha hata chembe.
Kwame alisoma mara kadhaa kabla
hajayaamini macho.Alipojikuta akiwajibika kuyaamini, alijisikia akitetemeka
ghafla. Hakuwa na uwezo wa kueendelea kukanusha kuwa tayari siri imemfikia mtu
hatari kama Joram. Hakujua ilitokea vipi hadi siri hiyo akaipata. Wala hakuwa na
nafasi ya kujua hayo kwa sasa. Alichotaka sasa ni kupata ufumbuzi kabla ya saa
sita, awe amemfanya Joram marehemu, siri irudi katika milki ya siri na harakati
ziendelee kama zilivyopangwa.
Hilo halikuwa jukumu
rahisi.
Hivyo aliinua simu na kuwapigia washirika wake ili kuwatane
hapo ofisini haraka iwezekanavyo. Simu ya pili iliwaamuru wasaidizi wake wa
idara ya mauaji wahakikishe kabla ya saa sita za mchanawawe wamempata Joram
Kiango na kumuua. Alisistiza kuwa kazi hiyo lazima ifanyike haraka, mahala
popote na kwa njia yoyote.
Baada ya simu hizo, alitulia kwa muda
akiwaza wa uchungu uwezekeano wa kufa kwa Jorm bila ya kuwepo kwa muuaji
aliyekubuhu-Bon, ambaye hadi sasa hakujulikana aliko. Yaweza kuwa amekamatwa na
kuuawa na Joram? Alijiuliza. Pengine…
Mlango wake wa siri sakafuni
ukatoa alama ya kudai kufunguliwa. Akabonyeza kidude ambacho kiliufungua. Mtu
mmoja akapanda ngazi na kuingia chumbani. Wakasalimiana kimya kimya. Baada ya
muda walifuata watu wengine kwa njia hiyo hiyo. Nyuso zao zilionyesha wasiwasi,
hivyo walisalimiana bila uchangamfu wowote, huku kila mmoja akiketi juu ya
kimojawapo ya viti vilivyomzunguka Kwame. Walipokamilika Kwame alimtahadharisha
katibu wake kuwa asingependa kusumbuliwa na mtu yeyote. Kisha akawatazama wageni
wake kwa macho yaliyoonyesha kuchanganyikiwa, hajui wapi aanzie
kueleza.
“Nadhani tulikubaliana kuwa tusikutane tena katika hali kama
hii hadi mambo yatakapoonyesha kuwa nchi iko mikononi mwetu,” mmoja kati ya
wageni hao alisema alipoona Kwame ameduwaa. Kwa hali hiyo nadhani Bwana Kwame
angetueleza haraka kisa cha mwito huu ili tuondoke hapa.”
Wenzake
wakatikisa vichwa kumuunga mkono.
“Ni juu ya waraka huu,” Kwame
alisema akiwapa ile kadi. Waliisoma na kisha kutazamana kwa hofu kubwa.CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nilisema zamani
kuwa singewezekana…” mmoja alisema ghafla.
“Hata mimi,” alidakia
mwingine.
“Kwa hiyo?” mwingine akaropoka.
“Tusubiri
kitanzi,” jibu lilitolewa.
Yakafuata mengi. Kila mmoja akisema hili na
lile. Hawa wakifokeana, huyu akilalamika, yule akjilaumu na kadhalika. Kisha
Kwame alifanikiwa kuwanyamazisha kwa kusema, “Jamani, tusiwe kama watoto.
Nimekuiteni ili tupate jawabu la pamoja. Joram ni mtu mmoja tu, kijana mdogo
sana, ambaye hwei kushinda kundi hili pamoja na jeshi letu la siri
lililojengeka. Kisha kafanya ujinga wa kutuarifu kwanza na kutupa muda wa
kutosha. Bado tuna saa mbili. Zinatosha kabisa kumpata Joram na kumweka
kaburini.
“Labda humfahamu
Joram, bwana Kwame,” alidakia mwingine..
“Mimi namjua vizuri sana. ni
kijana mdogo lakini anajua anachokifanya. Tusijidanganye…”
Kwame
akamkatiza kwa hasira. “Uoga siyo dawa,” aliongeza,” sisi ni wanaume. Tunajua
kabisa tusingeweza kutegemea utajiri mkubwa na vyeo vinono bila kutaabika
kidogo. Bsuala la Joram ni tatizo dogo tu kati ya mengi yawezayo kutokea.
Nilichotaka kupendekeza ni kuharakisha mambo yetu. Leo hii tukamilishe mipango,
usiku mapinduzi yatokee, kesho sisi tulio hapa tuwe baraza lipya la mawaziri.
Mnasemaje?”
“Joram jee?” alihoji mtu.
“Suala lake niachieni
mimi. Hadi saa sita atakuwa safarini akielekea walikohamia babu zake. La muhimu
ni sisi wenyewe. Tukubaliane moja. Tukitoka hapa kila mmoja akafanye jukumu lake
haraka. Mnasemaje jamani? Angalieni hii ni nafasi yetu ya pekee ya kula
nchi.”
Kabla hajajibiwa simu kutoka kwa katibu wake ilimfikia Kwame.
Alii9nua chombo cha kusikilizia na kuunguruma ndani yake, “Nimesem sitaki
usumbufu. Una nini kichwani wewe msichana?”
“Kumradhi mzee. Kuna mtu
mwenye haja kubwa kukuona. Anasema jina lake ni Von.”
“Nani? Von!
Mwambie aingie mara moja.”
Macho yake yalielekea mlangoni kumsubiri
mgeni huyo. Aliingia taratibu bila haraka yoyote mikono mifukoni, macho yake
yakimtazma kila mgeni kabla hayajamrudia Kwame ambaye kama wenzake wote alikuwa
katika hali ya mshangao na mashaka mashaka. Mashaka ambayo yalitokana hasa na
mgeni huyo kuwa katika sura ya Bazile Ramadhani, mtu ambaye alisadikiwa kuwa yu
muuaji na aliyekuwa akitafutwa sana na kila mtu.
“Bon!” Kwame alifoka
kwa Kiingereza. “Unawezaje kutebea hadharani mchana huu katika sura
hiyo?”
“Usijali, siyo rahisi kujulikana.”
Sauti yake ilizidi
kumtia Kwame mashaka. “Bon?” aliuliza tena.
“Ni wewe Bon! Ulikuwa wapi
muda wote huu?”
Akajibiwa kwa tabasamu. Mikono ikatolewa mfukoni na
kuelekea mdomoni ikiwa na sigara. Ilikuwa mikono ya mtu mweusi.
“Wewe
sio Bon!” Kwame alifoka ghafla.
“Ndiyo.”
“Wewe ni
nani?”
“Unataka kujua mimi ni nani? Ni rafiki yako
mpenzi.
“Labda nitoe dude hili usoni unione vizuri.” Dude lilipotolewa
kiufundi uso uliotulia mbele yao ukitabasamu ulikuwa wa Joram
Kiango.
“Joram!” wote waliropoka kwa hofu na
mshangao.
“Ndiye,” aliwajibu kwa dhihaka.
“Joram,” Kwame
alifoka tena. Very well. Umejileta mwenyewe. Hutatoka humu ukiwa
hai.”
Joram hakuonyesha kushtushwa na vitisho vya Kwame. Aliendelea
kuivuta sigara yake, huku akiwatazama kwa makini. Nadhani tufahamiane vizuri
ndugu zangu. Sipendi sana tabia ya kutumia majina ya bandia. Nani kati yenu
anayejiita Top Koloto?” aliwahoji.
Alimuona mmoja akigutuka na wawili
kumtazama mwezi wao jambo ambalo lilimfanya Joram amfahamu mara
moja.
“Na Moto Matata?”
Wakazidi kugutuka. Joram akaangua
kicheko. “Sikieni waheshimiwa,” akasema. “Hasa mheshimiwa Joe Kileo ambaye
naamini u kiongozi wa kikundi hiki,” alikuwa akimtazama Kwame.
“Najua
hii ni jumuia ya watu wenye njaa kali ya utajiri na kiu kubwa ya vyeo. Najua
nyote hamtosheki na mlichonacho na kamwe hamtatosheka na lolote mtakalopata.
Wengi wenu mmebahatika kuwemo katika madaraka makubwa, lakini hii ndiyo zwadi ya
kwanza toka kwenu kwa nchi na wananchi; kupanga njama ambazo zimedhamiria kuleta
umwagaji wa damu na kisha nchi iangukie mikononi mwenu. Iwe kama shamba lenu,
wananchi wote wakiwa watumwa badala ya watu huru katika nchi huru. Waheshimiwa,”
alipunguza hasira kutoka katika hali ya hasira na na kuwa ya huruma
zaidi.
“Hamwoni aibu kwa uchafu wa vitendo vyenu?”
Hutuba
yake ilikuwa imewafanya wote waduwae.walipopata nafasi ya kujikumbuka baada ya
kuulizwa swali hilo, walitazamana kwa kutojua la kujibu. Kisha Kwame akafoka
ghafla.
“Tusibabaishwe. Tusibabaishwe na kijana huyu mwenye hila kama
knyonga.” Akainuka na kusogea mbele hatua moja akiendelea kusema, “Dakika chache
kabla hajaingia hapa tulikuwa tukijadili kifo chake. Hatujabadili utaratibu huo.
Atakuwa marehemu muda mfupi ujao.” Akageuza sauti kuwa amri. “Haya wote nendeni
mkaendelee na mopango, huyu niachieni mimi.”
Umati ukaanza kuinuka.
Joram akagutuka kidogo. Kama kawaida yake kujileta kwake haikuwa moja kati ya
njia zake za kuwadhihaki adui zake tu. La hasha, nia ilikuwa ni kupata hakika
juu ya kuhusika kwa Kwame ktika mpango ule wa mapinduzi – jambo ambalo tayari
alikuwa amelipata – pamoja na kutaka kuwafahamu wote wengine ambao walikuwemo
katika njama hizo. Kwani baada ya kutuma warakaule aliamini Kwame asingesita
kuita wenzi wakeili wajadiliane kabla haujawadia muda aliotishia. Na ndipo
akaingia ofisini huko mapema zaidi ili awafumanie kama alivyowafumania. Hakuwa
amekuja mikono mitupu. Silaha zake muhimu zote zilikuwa tayari katika sehemu
zake za siri. Zaidi kamera yake ndogo ya siri ilikuwa ikiendelea kupiga picha za
umati huo hali kinasa sauti kkiendelea kunasa yote yaliyokuwa yakisemwa. Hivyo,
ushujaa wa Kwame kiasi ulimtisha. Alihitaji muda zaidi ilia pate ushahidi zaidi
kisha aondoke na kupata msaada wa polisi kuwanasa. Maadamu hakuwa tayri kwa
hilo, aliona heri abadili mbinu na kuwaambia.
“Bado. Msiondoke kabla.
Hamjafahamu kwa nini niko hapa na nije peke yangu badala ya kuongozana na polisi
ambao wangewatieni pingu kesho muwe vizimbani na kesho kutwa mahabusu mkisubiri
kitanzi.”
“Hatuna muda wa kukusikia…” Kwame alizidi kufoka. “Umejileta
mbele ya mauti na hutatoka kwa miguu yako mwenyewe. Haya wote ondokeni
mkaendelee na mipango yetu. Fanyeni haraka.”
“Msiondoke,” Joram
akaamuru. “Angalieni, huyu anataka kuwaponza. Nilikuwa na nia njema kwenu nyote,
nikizingatia kuwa nyote mna hadhi serikalini kiasi kuwa endapo mambo haya
yatajulikana itakuwa aibu mno kwenu.” Alipoona wametulia kumsikiliza, aliongeza,
“Kwa hali hiyo, nia ya kuja kwangu ilikuwa kuwashaurini kwa amani muache ndoto
hizo. Na endapo mmedhamiria, mimi nipeni chochote ili nikae kimya. Milioni moja
zinanitosha. Najua mnazo, au siyo
Kwame?
Kwame alianza
kubadilika, uso ukichukiza na macho kutisha, “Una wazimu,” alinguruma. “Huna
utakachopata zaidi ya zawadi ya kifo. Nazifahamu sana hila zako za kitoto.
Kwangu umekwama bwana mdogo.”
Joram akatabasamu, “Kwa hiyo uko tayari
niipeleke siri polisi? Yuko mtu ambaye nimempa jukumu la kupeleka mambo haya
polizi na kumtaka awaambie waje hapa mara moja endapo dakika kumi zaidi zitapita
kabla sijamfikia hapo anaponisubiri.”
Kwa mshangao, Joram alimwona
Kwame akiangua kicheko. “Polisi? Watafanya nini? Najua huo ni uongo lakini hata
wakija hawatagundu lolote. Watakachofanya ni kuizoa maiti yako. Pindi
watakaposubiri kesho kupata ushahidi, nchi itakuwa mikononi mwetu.” Kwame
akawageukia wenzake. “Hamjaondoka tu? Tafadhalini ondokeni na mkatimize wajibu
wenu bila hofu.”
Hayo Joram hakuyategemea. Lakini hakuduwaa kuwaza.
“Hakuna atakayeondoka,” alifoka ghafla. Walipomtazama walijikuta wakitazamana na
bastola yake ambayo aliishika kishujaa, “Wote mtaketi chini na kuwasubiri
polisi.”
Wenzi wa Kwame waliduwaa, hata hivyo walipata moyo
walipotazama na kuona naye kashika bastola iliyokuwa ikimwelekea Joram huku
akicheka na kusema, “Kinda anapoamua kucheza na chatu asitegemee fadhila. Haya
nendeni mmoja mmoja, huyu niachieni mimi.”
“Atakayethubutu kuondoka,
risasi yangu halali yake,” Joram alionya.
“Msiogope vitisho vyake,”
Kwame aliongeza. “Kama mnavyomfahamu, yeye ni mtundu tu, lakini yu mwoga mno wa
kuua. Nendeni.”
“Aondoke mtu…” Joram alifoka tena. Lakini sauti yake
ilikatizwa na king’ora chenye sauti kali ambacho kililia ghafla mezani mwa
Kwame. Kikafuatwa na sauti ya watu waliokuwa wakisema
haraka.
“Inspekta Kombora hapa. Kikosi cha kumi na mbili…”
…
“Kombora? Sikieni, kuna mauaji yanafanyika katika ofisi ya Snow Fund. Nendeni
haraka mtawapata wauaji.”
“Wapi? Snow… haya… tunaondoka mara
moja…”
Wote wakazidi kuchanganyikiwa. Joram aliwatazama kwa kebehi.
Lakini, alipomgeukia Kwame, aliambulia kuona akibonyeza kidude fulani na chumba
kumezwa na giza Ghafla. Mlio wa bastola ukasikika. Joram alijtupa sakafuni na
kutambaa kutoka alipokuwa. Mra akasikia harufu ya aina fulani ya marashi
ikimfikia ghafla. Papo hapo usingizi mzito ukammeza na kumteka. Kama ndoto,
alisikia ubishi mkali ukiendelea kwa sauti za wasiwasi, huyu akisema hili na
huyu lile.
“Tumuue.”
“Nasema hapana. Mwacheni alale.
Anajitia kujua. Hivyo atafurahi sana atakapoamka baada ya saa ishirini nan ne na
kuona bendera mpya ikipepea.”
“Tumuue…”
“Nasema
hapana.”
Kisha alisikia hodi kwa mbali. “Hodi… fungua…” huku mikono
inayotetemeka ikijatribu kumbeba na kushindwa. “Polisi… funguia…” ikaendelea
kusikika. Joram hakusikia lolote zaidi.
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
*****
Bazile
Ramadhani aliibuka kutoka katika kitu kama ndoto au usingizi mzito ambao ulikuwa
umemmeza kwa muda mrefu ambao hakuweza kukadiria. Usingizi ambao ulikuwa
umemwanza kwa namna isiyoelezeka tangu usiku wa siku ile ambayo alimwendea
Kitenge ofisini kwake kumpa maneno ya hasira kwa ajili ya muswada wake
alioupenda kuliko yote. Kumpa yale maneno makali ambayo hata hakumbuki wapi
alipata uwezo wa kuyaropoka.
Alipofika nyumbani aliendelea na shughuli
zake kama kawaida. Usiku alipanda kitandani na kujilaza. Usingizi uliomchukua
ulikuwa na tofauti kubwa na ule aliouzoea. Ulikuwa mzito mno. Ndoto zake zikiwa
kama jinamizi. Mara, alihisi kubebwa na kupakiwa kama gunia. Mara, alihisi
akilazwa juu ya meza kubwa huku uso wake ukipimwa na jitu lenye madevu. Mara,
alihisi kusikia watu wakipanga au kujadili kifo na mazishi yake na mengi mengine
ya kutisha.
Hakuwa na uwezop wa kuamka wala kufumbua macho isipokuwa
leo baada ya kuhisi na kisha kuona mtu akimdunga sindano. Alijikuta akiwa katika
chumba ambacho hakupata kukiona maishani.
“Ni.. nini? Niko wapi?”
alihoji kidhaifu.
Mtu aliyekuwa akimhudumia alimtazama kwa macho
makali na kumwamuru ainuke, “Pita hapa uende huko,” aliambiwa.
“Wapi?”
Bazile alihoji kwa udhaifu huku akijikongoja kuinuka.
“Fanya haraka!”
alifokewa.
“Kama kondoo aliinuka na kufuata mlango alikoelekezwa.
Baada ya kupita milango na vyumba kadhaa, aliamriwa kusimama.
“Geuka
huku.”
Alipogeuka alikutana na risasi ya bastola isiyo na mlio ambayo
ilimfanya ausahau udhaifu wake na kupaa juu. Alipotua chini tena alikuwa chali,
damu nzito zikimvuja huku akiwa tena kamezwa na na aina nyingine ya usingizi
ambao haukuwa na ndoto wala hisia.
*****
“Fungua,” Kombora
alifoka tena. “Polisi hapa,” aliongeza akiitazama saa yake. Dakika tatu zilikuwa
zimepita tangu alipowasili hapo na kuwakuta askari wa doria wakiendelea kuugonga
mlango wa ofisi ya Kwame
“Mnadhani kuna nini kinachofanyika humo
ndani?” aliwahijo.
“Hatujui mzee. Hatusikii
chochote.”
“Msichana anayekaa hapa
mmemkuta?”
“Hatukumkuta.”
“Okay, tutavunja mlango. Nitaita
kwa mara ya mwisho… FUNGUA!” akafoka.
“Mara mlango ukafunguka
polepole. Kwame alitokeza akitetemeka mwili mzima isipokuwa macho yake tu.
Kombora hakuyaona kuwa na dalili yoyote ya hofu. Aliwatazama kwa mshangao na
shukrani.
“Karibu,” aliwaambia akiwapisha
mlangoni.
Walipoingia macho yao yalidakwa na mizoga ya binadamu wawili
waliolala juu ya sakafu. Mmoja akiwa kalala chali bastola mkononi. Wa pili
ambaye ilikuwa dhahiri alikuwa marehemu alikuwa chali, sura yake ikitazama
angani. Kombora na wasaidizi wake sita walimtazama marehemu huyo mara moja na
kisha kutazamana.
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment