Simulizi : Najisikia Kuua Tena
Sehemu Ya Tatu
(3)
BAADA
ya kuyafahamu hayo, yeye kama Joram Kiango angekuwa tayari kufuata njia zake
ambazo zingemfikisha hadi kisogoni au usoni pa muuaji huyo. Joram, angependa
zaidi kukutana naye uso kwa uso, aupime na kuushuhudia kwa macho yake ujabali wa
mtu huyo aliyeondokea kuwa jitu kwa muda mfupi
tu.
Akiwa na uhakika na mbinu zake, pamoja na
matumaini juu ya njia atakazopitia ambazo ni kinyume na zile za polisi,
alijisikia furaha kana kwamba tayari kamtia adui huyo mikononi mwa sheria.
Akaitupa sigara yake katika kasha la taka na kutoka nje akipiga
mluzi.
*****
BAADA ya kuwaona tena
rafiki zake ambao humuuzia habari za siri kutoka polisi na kupata anuani za
marehemu wato, alirudisha gari lake nyumbani kwake Ilala na kuanza kutumia ‘Dala
Dala’ kwenda hapa na pale.
Safari yake ya kwanza
iliishia Mapipa ambako alionana na mama aliyekuwa amempangisha marehemu Kitenge.
Alizungumza naye mengi ambayo alidhani au kuamini kuwa polisi wasingekumbuka au
kujishughulisha kuuliza. “mwenendo wa marehemu siku chache kabla ya kifo…”
“Wageni au rafiki zake wa karibuni.” “Tabia na maongezi yao….’ Na kadhalika.
Pia, alihoji sana juu ya Yule mwanamke ambaye alidai au kutishia kumuua
marehemu. Majibu aliyoyapata aliona kama hayakuwa na msaada mkubwa. Bibi huyu
alikuwa kama mtu aliyechanganyikiwa sana baada ya kuwa na kila hakika kuwa
aliyemuua Kitenge ni Yule ‘malaya’ kisha vifo vya aina na vya kutisha mno
vikaendelea kutokea.
“Yawezekana kuwa muuaji wa
kitenge ni Yule mama. Huyu mwingine pengine anaitumia nafasi hiyo ili kutimiza
dhamira yake tu,” Joram alimshauri.
“Yawezekana
baba. Haya mambo kwa kweli yanatisha, yaweza hata kunitia wazimu kwa jinsi
ninavyoyafikiria na kuwajibika kujibu maswali magumu kutwa kucha. Nadhani
utaniwia radhi nipumzike baba.”
“Bila shaka bibi,”
aliitikia Joram akiinuka na kumshukuru mama huyo. Kutoka hapo alienda mtaa wa
india ambako alikutana na mke wa marehemu Wamangi. Jorah alimkuta mjane
kajiinamia huku mkononi kashika gazeti ambalo baada ya Joram kulitupia macho
alifahamu kuwa lilikuwa na habari za mauaji hayo. Baada ya kumsalimu na kumpa
pole mama huyo, Joram aliwataka radhi jirani wawili ambao waliketi kando ya mama
huyo, wakimfariji kwa kuwepo kwao pale. Watu hao wakaondoka na kumwacha Joram na
mama huyo ambaye alianza kutokwa na
machozi.
“Usilie mama,” Joram alimfariji, macho
yake yakilikagua umbo la mama huyo na kuona kuwa umri wake wa kati ya miaka
thelathini na arobaini ulikuwa haujauathiri sana uzuri ambao ni dhahiri uliwahi
kuwepo katika umbo hilo nene lenye ngozi laini
nyekundu.
Macho ya mama huyo yalikuwa malegevu,
pengine yaliashiria ulegevu wa moyo, pengine ulegevu wa mapenzi. Joram akiwa
mzoefu wa mitazamo hiyo hakubabaika bali alianza kumtupia maswali kwa sauti yake
nzuri.
“Nadhani polisi wamekuuliza mara nyingi
swali hili mama, lakini naomba si majibu bali maoni yako juu ya mtu ambaye
anaweza kuwa kamuua mumeo. Yaani kufuatana na taarifa juu ya kifo hiki
inaonyesha muuaji ni mtu ambaye ama anaifahamu sana nyumba hii, ama alidhamiria
kwa hali na mali kumuua mumeo. Vinginevyo, asingepanda ngazi zote hizi na
kuthubutu kuua hali na wewe umo kitandani. Unadhani ni nani
mama?”
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Muuaji? Na huyu
hapa aliyetajwa gazetini? Baba unauliza swali gani hilo? Kama unahaja ya msaada
ni kumsaka huyu mtu ili apatikane haraka,” mama huyo alijibu kwa
udhaifu.
“Nina maana,” Joram alitamka baada ya kumpa mama huyo moja ya
tabasamu zake ambazo humsaidia mbele ya wanawake kupata akitakacho, “….nilikuwa
na maana kuwa mtu huyo Bazile anaweza kuwa anafahamiana na mumeo au kuifahamu
nyumba hii kiasi cha kufanya yote yale bila vikwazo? Yaani, kama nia yake ni
kuua tu, kwa nini asivizie walevi huko manzese na buguruni? Kwa nini afanye kila
njia kumuua mumeo?”
“Hata mimi nashangaa,” mjane
alijibu. “Nadhani hiyo ndiyo kazi yenu kama
wapelelezi.”
“Ni kweli,” Joram alijibu akitabasamu
tena, “Lakini tunahitaji msaada wako pia mama. Kwa mfano, juu ya kifo
kilichotokea, wewe na mumeo mlilala kitandani kama kawaida
siyo?”
“Ndiyo.”
“Ulipoamka
ukajikuta bafuni, ukiwa umefungwa kamba mikononi na miguuni, mumeo akiwa
kachinjwa…” Joram alilazimika kusita mama lipoangua kilio. “Unadhani yawezekana
katika usingizi wako wa kawaida mtu akufunge kamba na kukubeba hadi bafuni hali
hujaamka tu?”
“Nimesema mara nyingi kwa polisi
kuwa mtu huyo alitumia uchawi. Nashangaa walivyonicheka. Haijawahi kunitokea
kamwe nikalala usingizi wa aina hiyo. Wala sifahamu mangapi mtu huyo alinitendea
baada na kabla ya hapo.” Akaangua kilio tena kwa sauti
ndogo.
“Una hakika kuwa haukuwa usingizi wa
kawaida?”
“Kila hakika. Unajua mume wangu alikuwa
ndiyo bado karejea toka Zanzibar ambako aliishi huko kwa miezi miwili na zaidi
kwa shughuli za kikazi. Sidhani kama nina hakika ya kusema haya, lakini sina
budi kukuambia kuwa kila arejeapo toka safari za mbali tulikuwa tukirejewa na
ujana wetu. Tulilala na kukesha huku tumekumbatiana , kila mmoja kiwa hataki
kumwacha mwenziwe.
Fikiria basi, katika hali kama hiyo, nani mwenye
uwezo wa kututenganisha bila uwezo wa mazingaombwe? Zaidi nashangaa kwa nini
hamtaki kuamini kuwa uchawi ulitumika. Wangapi wameibiwa kwa njia
hiyo?”
Joram aliendelea kuhoji madhumuni ya
safari hiyo ya Zanzibar ilikuwa lini , hali ya mume baada ya kutoka huko na
mengi mengine. Majibu akiyopata yalikuwa ya kawaida kiasi cha kumfanya ashindwe
kuona kama alikuwa akiendelea mbele au nyuma katika upelelezi wake. Hata hivyo
alinukuu mengi katika daftari lake kisha akamshukuru mama huyo na
kuaga.
Baada ya hapo Joram alipanda basi ambalo
lilimfikisha katika kituo cha mabasi cha Mkwajuni, Kinondoni. Akasoma namba ya
mtaa na nyumba ya marehemu Jugeni Kawamba. Joram hakuwa na matumaini mengi ya
kumkuta mtu katika nyumba hiyo, hasa baada ya kuarifiwa kuwa marehemu alikuwa
akiishi peke yake. Lakini alifurahi kukuta watu watatu jamii ya marehemu,wakiwa
wamehamia hapo kulinda nyumba.
Walimkaribisha kwa
huzuni huku macho yao yakimuuliza ni nani na anahitaji nini. Kama kawaida yake
alijieleza kwa hila kisha kuanza kuwatupia maswali ambayo walibabaika
kuyajibu.
Alipoona msaada wao ni mdogo kwa jinsi
ambavyo hawakuwa wakiishi na marehemu, aliinuka na kuaga. Kabla hajainua mguu
kuondoka macho yake yalidakwa na ganda la tiketi ya ndege ya ATC iliyokuwa
imeanguka chini ya meza. Akainama
kuiokota.
Alipoisoma ilimsisimua zaidi. Ilikuwa
ya kutoka Zanzibar, ikiwa na tarehe ileile aliyoitaja mjane wa marehemu Wamangi
mume wake alipotoka Zanzibar.
“Kumradhi marehemu
alikwenda kufanya nini Zanzibar?” aliwahoji akimtazama mmojawao , mwanamume
mwenye ndevu nyingi kinyume cha wenzake japo walionekana wana umri mkubwa zaidi
yake.
“Alikuwa wapi? Zanzibar? Kijana huyo
alimhoji Joram badala ya kumjibu.
“Kufanya nini?”
mwingine aliongeza.
Joram akagundua kuwa hakukuwa
na habari zozote za karibuni kuhusu marehemu ndugu yao. Akaondoka zake polepole
baada ya kuwashukuru kwa mara nyingine. Nje ya nyumba alilihifadhi ganda hilo
mfukoni huku akiingia katika teksi iliyosimama mbele yake
ghafla.
“Airport,” alisema bila kumtazama dereva.
Alikuwa akitazama saa yake ambayo ilidai ni saa tisa kasoro dakika kadhaa.
“Tafadhali tupitie hapo Mapipa Mtaa wa Kiyungi,”
aliongeza.
“Bila tafadhali,” dereva alisema huku
akiigeuza gari yake kiufundi na kutia mwendo kufuata Barabara ya Morocco.
Walipowasili nyumbani kwa marehemu Kitenge ,Joram alifanya haraka kuingia ndani
ambako alipokewa na bi kizee kwa
mshangao.
“Kumradhi
mama, nimerudi tena baada ya kupata swali moja la muhimu. Nilitaka kufahamu kama
marehemu aliwahi kufanya safari yoyote ya Zanzibar hivi karibuni. Kwa ndege au
meli.”
“Siwezi kufahamu baba. Watu hapa mjini
wanaweza kufanya lolote bila mtu wa chumba cha pili kufahamu. Na kama ni safari
ya ndege si anaweza kwenda na kurudi bila watu kujua? Nasikia ni safari ya
dakika kumi tu. Pengine …”
“Ahsante mama,” Joram
alimshukuru akiondoka harakaharaka.
“Tafadhali
endesha gari kama mwanamume,”alimweleza dereva. “Kama hujiamini acha niendeshe
mwenyewe.”
Dereva alitabasamu na kumwambia, “
Utachoka mwenyewe.”
Naam, Joram alikubali kuwa
wapo vijana wanaojua kukimbiza gari.
Baada ya
dakika chache tu gari ilikuwa tayari imewasili uwanja wa ndege wa Dar es
Salaam.
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nisubiri,
tafadhari “ alisema akimpa mqalipo yake. Kisha akaenda katika chumba cha
kuhudumia wasafiri ambako alikuta watu wengi wakihudumiwa. Akaingia upande wa
watumishi na kujieleza vizuri kwa mhudumu mmoja wa kike ambaye alionekana
kuvutiwa na tabasamu la Joram pamoja na sura yake zaidi ya maombi yake. Hata
hivyo baada ya muda mfupi tayari alikuwa kamkabidhi Joram orodha kamili ya
abiria wote waliosafiri katika ndege aliyoitaka Joram, siku hiyohiyo tarehe 17
Machi 1984 saa ya kuondoka Zanzibar ikiwa kumi na moja kamili za jioni
.”Niliwahudumia mimi,” alisema kwa furaha.
Safari
hiyo ilikuwa imefanyika katika ndege ndogo aina ya Twin Otter. Abiria walikuwa
watano: majina ya wasafiri yalikuwa kama ifuatavyo:
J. Kawamba-S.L.P
71701 Dar es Salaam
B. Kwame-S.L.P 6142 Dar es Salaam
F.
Wamangi-S.L.P 4700 Dar es Salaam
D. Kombo-S.L.P 41421Dar es
Salaam
K.Key- S.L.P 1600010 Dar es
Salaam
Joram Kiango aliyanukuu majina hayo na
kumshukuru msichana huyo. Baada ya kumtupia maneno mawili matatu ya ahadi za
kukutana katika madisko ambazo alijua zisingetekelezwa na upande wowote,
aliondoka harakaharaka.
Kichwani alikuwa na mawazo
mengi. Hakuwa na uhakika kama anachofanya ni kitu cha maana chenye manufaa
katika upelelezi wake. Hata hivyo damu ilikuwa ikimsisimka kwa kushuku jambo
katika safari au orodha hiyo. Tangu alipogundua majina ya marehemu wawili
waliokufa usiku mmoja yakiwa katika orodha ya safari moja, alijikuta akihisi
kuwa lipo jambo fulani katika safari ambalo laweza kuwa kisa au mkasa wa vifo
vyao.
Lakini alikuwa akirudiwa na mashaka kwa
kuona majina mawili tu. Jina la Bazile ambaye alikuwa mshukiwa wa kwanza katika
mauaji yaliyokuwa yakiendelea lilikuwa halimo. Pia jina la Kitenge – marehemu wa
kwanza – lilikuwa halimo. Yawezekana kuwa alikuwa anaupoteza bure muda wake?
Alijiuliza alipokuwa akijikumbusha msorokoto uliokuwa katika kesi au mauaji
hayo: Kwanza yule mwanamke anayedai kwamba alimuua Kitenge, pili, Bazile
Ramadhani anayeaminika kuwa muuaji na anaendelea kupigia simu polisi kuwa ataua
tena. Aidha, yote hayo yalishangaza. Yakoje mambo
haya?
Joram akaamua kutosumbua kichwa chake hadi
atakapopata nafasi ya kufahamu na ikiwezekana kujadiliana na abiria waliosalia
ambao angeweza kuwapata.
Nje ya jengo la huduma za
wasafiri, Joram aliingia katika kibanda cha simu na kujipatia kitabu cha orodha
za masanduku ya posta.
Akakipekua haraka haraka kutafuta anuani za
abiria wale watatu ambao alikuwa hawafahamu. Anuani ya K. Key haikumsumbua sana.
Mara moja aligundua kuwa haikuwepo katika orodha ya namba za masanduku. Ilikuwa
imekosewa au imebuniwa. Kwa nini? Hakuwa na muda wa kujibu. Akaamua kutafuta
anuani nyingine. Ya D. Kombo ilikuwa ya kazini kwake Kamata, na B. Kwame
ilisemwa Snow Fund.
Mara moja Kiango akalikumbuka
jina pamoja na kukumbuka ilipo ofisi yake. Akatoka kibandani hima na kukimbilia
kituo cha teksi.
Gari lililomleta kwanza lilikuwa limeondoka kitambo.
Akavamia jingine na akamwamuru dereva aichukue mbio iwezekanavyo kumfikisha
mjini. Dereva hakuwa mbaya, ingawa Joram hakuridhika
naye.
Saa kumi na moja kamili walikuwa mbele ya
kituo cha mabasi ya Kamata. Joram akamtaka radhi dereva, akateremka na kuingia
ofisini. Karani mwanamume akamtazama kwa
makini.
“Tafadhali, nataka kumwona ndugu D.
Komba,” Joram alisema.
“Komba? Dismas Komba?”
alihoji kijana huyo. “Leo siku ya ngapi sijui hajafika kazini. Watu wengi mno
wanamtafuta. Hatujui kwa nini haonekani. Pengine kapata kazi nyingine, pengine
amerusha mali za watu huko mitaani na
kutoweka.”
“Yaani hamna taarifa yoyote juu yake,”
Joram alifoka kwa mshangao na hofu ambayo ilianza
kumpanda.
“Hatuna
taarifa...”
“Mnajua wapi
anakoishi?”
“Hakuna
anayejua...”
“Hakuna! Ofisi hii nzima hakuna
anayejua?” Joram alifoka ghafla.
Sauti yake
ilikuwa kali yenye amri ikamfanya kijana huyo kuinua uso kutoka katika majalada
yaliyokuwa mbele na kumtazama Joram kwa makini zaidi. Ndiyo kwanza akayaona
macho yake yalivyodhamiria na paji la uso lilivyokunjamana. Kwa muda kijana huyo
aliduwaa. Joram, alipoona hivyo akamtia moyo kwa kucheka kidogo, kisha akaongeza
kwa sauti laini kiasi.
“Sikia kaka, tuna shida
kubwa ya kumpata haraka. Huwezi kufahamu mtu yeyote anayeweza kutuelekeza
kwake?”
“Wewe ni CID?” alihoji kijana
huyo.
“La, ni mgeni wake
tu.”
Kijana huyo alionekana kutokuliamini jibu la
Joram. Hata hivyo, alitoka ili kuwaona wenzake ambao wangeweza kumpa habari
hizo. Aliporejea alikuwa na kipande cha karatasi chenye anuani ya Komba ambayo
alidai anaishi Kigamboni hatua kadhaa kutoka Kivukoni. Joram alimshukuru na
kutoka akiitazama saa yake ambayo ilisema dakika chache mbele ya saa kumi na
moja.
“Kigamboni,” alimweleza dereva
wake.
Walipita Barabara ya Nkurumah na kuifuata
hadi mnara wa saa ambapo walifuata Mtaa wa Railway hadi Sokoine Drive.
Msongamano wa magari ulivyokuwa mkubwa ilibidi gari liende polepole, kwa mwendo
ambao ulimchukiza sana Joram Kiango.
Lakini baada
ya muda alitabasamu alipoona ofisi ya makao makuu ya Snow Fund ikiwa wazi mbele
yake. Mara moja akamwamuru dereva kusimamisha gari kando, akateremka na kufuata
mlango wa ofisi
hiyo.
“Kumradhi
kwa kuchelewa kwangu,” alimwambia askari mgambo aliyesimama mlkangoni tayari
kumzuia. “Nina miadi ya kuonana na bwana
Kwame.”
“Saa hizi?” alihoji mgambo huyo. “Tulikuwa
tukifunga. Tumechelewa kidogo...”
“Unazidi
kuchelewesha. Atakufukuza kazi kwa kuniweka hapa muda mrefu,” Joram
alitishia.
Mgambo huyo akatabasamu kidogo kuficha
hofu iliyomwingia,
“Pita hapa,” akaelekeza. “Uende moja kwa moja hadi
mlango ule utamwona katibu wake umweleze shida yako. Sijui kama atakuruhusu.
Wafanyakazi wote wamekwishatoka.”
Joram alimwacha
akiendelea kusema. Alipofika chumba hicho aligonga na kufungua mlango. Macho ya
msichana mwenye dalili zote za uanamji yakampokea kwa mshangao. “Unataka nini
saa hizi?” aliuliza alipomwona Joram akijiweka vizuri
kitini.
“Samahani mpenzi,” alisema akiachia moja
ya zile tabasamu zake. “Nina ahadi ya kuonana na Bwana
Kwame.”
“Hana miadi ya kuonana na mtu yeyote leo.
Isitoshe saa zimekwisha,” msichana alimjibu.
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ni kweli dada
yangu. Lakini mwambie kuwa kuna mgeni wake anayetaka kuzungumza naye jambo
muhimu.”
“Jambo
gani?”
“Mwambie ni juu ya safari yake ya Zanzibar
majuzi.”
“Imefanya
nini?”
Joram akachoka na upuuzi wa katibu huyo.
“Sikia sister, kama huwezi kumwambia leta simu nizungumze naye mwenyewe,”
alisema huku tayari amevamia mkono wa simu. Binti huyo akaupokonya mkono na
kubonyeza kidude kilichomuunga na bosi wake.
“Jina
lako nani?” akamuuliza Joram.
“Wananiita Kalulu
bin Kalulumanga.”
“Nani?”
Joram akarudia
jina hilo la bandia. Baada ya maswali mengi kiasi aliruhusiwa kwenda.
Ikamshangaza Joram kuona ilivyokuwa safari ndefu kumfikia ‘bosi’ huyo.
Ilimlazimu kupita vyumba vidogovidogo zaidi ya vitatu ambavyo havikuwa na
chochote zaidi ya taa za umeme ambazo zilitoa nuru kali sana. Mjenzi wa aina
gani huyu asiye na wazo lolote la kiuchumi kiasi cha kujenga hivi?” alijiuliza
Joram. Alipofikia mlango wa Kwame aliukuta ukiwa
wazi.
Macho makali yaliyofunikwa na miwani mieusi
yalimlaki. Macho ya Kwame ambaye alikuwa kaketi nyuma ya meza pana iliyozingirwa
na viti kadha wa kadha, mfano wa chumba cha
mikutano.
Kwame alikuwa kavaa suti ya kijivu
ambayo ilimkubali vyema na kuoana na umbo lake refu, nene lenye nguvu. Ofisi
nzima ilikuwa katika hali ya kuvutia, mapambo ya aina mbalimbali, vinyago vya
aina aina na vitu vingine ambavyo Joram hakuweza kuvifahamu vikiwa vimepangwa
vyema kabisa, macho ya Joram yalitambaa kwa muda juu ya vitu hivyo kama ambaye
hakusikia Kwame akiuliza kwa mara ya
pili;
“Unataka nini
kijana?”
“Ofisi hii nzuri sana bwana Kwame,”
lilikuwa jibu la Joram.
“Nadhani hukuja hapa kuisifu ofisi yangu. Sema
unachotaka kisha uende zako. Nina shida za muhimu ambazo zimeniweka hapa hadi
saa hizi.”
“Usijali. Mimi pia sina muda wa
kuchezea,” Joram alimjibu.
“Nimekuja kwa nia njema kwako. Nadhani
unafahamu mauaji ambayo yanaendelea
kutokea?”
Mauaji gani? Haya ya huyu mtu mwehu
ambaye anaendelea kuua ovyo? Hiyo ni kazi ya polisi. Wewe ni nani hadi unifuate
kuyajadili? Nami nahusika vipi?”
Jorah
hakujishughulisha na kuyajibu maswali ya Kwame. Badala yake aliongeza swali
lingine, “Unamfahamu kijana huyo muuaji
mzee?”
“Kumfahamu vipi?” Kwame alihoji
akimchunguza Joram kwa makini zaidi. “Namfahamu kupitia magazetini, toka
alipojitokeza kuwa muuaji,” akaongeza.
“Hujamwona
ana kwa ana kabla ya hapo? Huku
Zanzibar…”
“Sijamwona kabisa. Wala sitaki
kumwona,” alidakia. “Suala la Zanzibar linahusika vipi na mjadala
huu?”
“Ndiyo. Umegusa dhamira kubwa Kwame.
Nimekuja hapa kukutahadharisha maisha yako yapo mashakani. Muuaji huyu anaua
watu wote mliosafiri katika ndege moja tarehe 17 Machi kutoka Zanzibar. Wawili
wameshakufa. Bado wewe na wenzako wawili.”
“Upuuzi
ulioje? Nani aliyekwambia hayo?”
“Nani aniambie?
Nimefanya uchunguzi na kuona. Dakika yoyote muuaji anaweza kukufikia wewe au
yeyote kati yenu. Ushirikiano wako ni muhimu mno bwana Kwame.
Ni…”
“We ni nani?” Kwame alikatiza
tena.
“Kwa jina ni Kalulu, kama nilivyokwambia.
Swali lako halina maana kwa sasa tunachotaka ni maelezo yoyote uliyonayo juu ya
safari hiyo, yepi yaliyotokea ambayo yangeweza kuleta kitu kama hiki. Vilevile
naomba uniambie yukoje msafiri mwenzenu aliyejiita K.
Key.”
Joram aliona tahayari katika macho ya Kwame
mara alipolitaja jina hilo. Hapana alikosea. Lilikuwepo tabasamu usoni mwake!
Tabasamu la dharau au kebehi! Nyuma ya tabasamu hilo macho ya nafsi ya Joram
yalisoma kitu kingine kabisa. Kitu ambacho ni kinyume na
tabasamu.
“Sikia kijana,” alisema Kwame baadaye.
“Sina muda wa kupoteza hapa. Wala sina jibu lolote la kumpa C.I.D au wewe, kwani
nikiwa safarini sijishughulishi na jambo lolote la mtu yeyote zaidi ya shughuli
zangu. Zaidi, siamini kama una lolote la ukweli katika maongezi yako. Yaelekea
wewe kama si punguani wa akili u mhuni mwenye nia nyingine nje ya madai yako.
Kwa hiyo. Kabla sijakuitia polisi, inuka uondoke zako haraka. Na angalia usirudi
hapa tena.”
“Joram akacheka, “Yaelekea unajua
mengi bwana Kwame,” akamwambia. “Shukrani kwa kunionyesha hali hiyo. Nakwenda na
nitarudi nikiwa na jambo ambalo litakusisimua zaidi.”
Akainuka.
“Na kama madai yako ni ya kweli, huoni
kuwa unakitafuta kifo kwa miguu yako mwenyewe? Ungali kijana sana bwana mdogo.
Kifo chako hakiwezi kunifurahisha hata
kidogo.”
Lilikuwa kama onyo la kidugu. Lakini
masikioni mwa Joram akiyatazama macho ya Kwame ambayo yalikuwa na udugu,
lilikuwa tishio kali ambalo lilikusudiwa kumfanya aache harakati zake zote.
Jambo ambalo lilimfanya Joram atabasamu tena kwa namna ya kumweleza Kwame:
“Nimekuelewa,” lakini hakusema hilo.
“Nakushukuru
tena ndugu Kwame, tutaonana…” akageuka na kuvuta hatua kuelekea
mlangoni.”
******
“So
this is Joram Kiango” Kwame alinon’gona akitazama picha tatu ambazo zilifotolewa
na mashine yake maalumu pindi Joram alipoondoka. Ilikuwa baada ya kulinganisha
picha hizo na zile kadhaa za Joram ambazo hutokea gazetini, zilizohifadhiwa
katika mafaili yenye habari zake na watu wengine ambao Kwame aliona haja ya
kuhifadhi harakati zao.
Alizitazama picha hizo kwa
makini, akihusudu uangavu wa macho ya Joram ambao ulidhihirisha busara na
ubishi. Kadhalika alivutiwa na umbo lake refu lililokaa kiriadha, Joram Kiango!
Akanong’ona tena akizidi kutabasamu. “Well…" akasita akiukunja ghafla uso
wake.
***
*** *** *** *** **
ALIKUWA amelikumbuka lile
pendekezo la mmoja wa wanakamati wenzake ambaye alitaka Joram auawe au kufanyiwa
njama za kumfungisha jela kwa muda pindi harakati zao
zikiendelea.
Kwamba angeweza kuingilia kati na
kuharibu mipango yao yote kwa ukatili zaidi ya polisi. Lakini yeye Kwame
alilidharau pendekezo hilo kwani kwa kadri alivyomfahamu Joram alimwona kama
kijana mtundu tu, play boy, ambaye huingilia harakati za kitoto na kufanikiwa
kuziharibu; si hizi ambazo zilikuwa zikifanywa na wasomi waliokubuhu katika fani
ya ujasusi huku hatua zote na za ziada zikiwa zimechukuliwa kuweka
siri.
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hivyo,
ilimshangaza sana kuona Joram amemfikia na kuuliza maswali ambayo
yalimdhihirishia kuwa alikuwa hajapata picha yoyote dhidi ya mipango yao. Kuja
kwake hadi mbele yake ilikuwa kubahatisha tu kama wasemavyo Waingereza ‘a shoot
in the dark’.
Hata hivyo, Joram hakuwa mtu wa
kuruhusiwa zake vivi hivi. Aweza kuwa hajui lolote lakini pengine ameona kitu
katikka mambo nya Kwame. Hastahili kupewa mwanya wa kufikiri lolote. Akainua
mkono wake na kubonyeza kidude fulani kilichowekwa kwa siri nyuma ya meza yake.
Mara sauti ikasikika ikitokea katika kijisanduku kilichokuwa mezani
kikisema:
“Number two here. On duty
sir,”
‘Vizuri,” Kwame alimjibu. “Umemwona mtu
aliyetoka humu ndani sasa hivi?”
“Nimemwona
mzee.”
“Ni mtu hatari. Nataka afuatwe na
kuangaliwa kila anachokusudia kufanya. Asiruhusiwe kuongea na watu hatari ambao
orodha yao unayo. Sawa?”
“Bila shaka
mzee.”
“Huenda nikayahitaji maisha yake wakati
wowote baada ya uchunguzi wangu. Nitapenda kazi ifanyike vizuri sana. Afe kwa
ajali ya gari, kizunguzungu au maradhi yoyote ambayo hayatamshangaza yeyote.
Sawa?”
“Bila shaka,
mzee.”
“Well.”
*****
NJE
ya nyumba hiyo, Joram alisita mlangoni akijaribu kuyaunga maandishi yote
aliyoyasoma katika sura ya Kwame ili aupate kikamilifu ujumbe uliokuwemo.
Haikuwa rahisi.
Mambo yote yalikuwa nusu nusu
kiasi cha kutokupata ujumbe kamili. Alichoweza kufanya ni kupata hisia tu. Hisia
ambazo zilimfanya amshuku Kwame kwa jambo moja au
lingine.
Alimshuku hasa kwa hotuba zake ambazo
zilidhamiria kumtisha., Kwa nini atishwe? Na ilikuwa vipi hata maongezi yake na
Kwame yawe kwa maana ya uadui badala ya urafiki? Lazima lilikuwepo jambo. Na
lazima afahamu ni lipi jambo hilo.
Wazo au mawazo
hayo yakamtia shauku hata akajikuta kajawa na hamu kubwa ya kuendelea na
upelelezi wake. Kwa hatua ndefu ndefu akaliacha eneo la ofisi hiyo na kuliendea
gari aliloacha likimsubiri. Rohoni akihisi kama anayetoka makaburini au kuzimu
na kurejea katika dunia hai.
"Twende zetu
brother,” Joram alimweleza dereva ambaye alikuwa kainamia usukani akifikiri au
kusinzia.
“Kwa nini? Tunaenda
Kigamboni?”
“Kweli! Nilikuwa naanza kusahau,”
alijibu akitia gari moto kuiondoa polepole. Msongamano wa magari uliwafanya
wapoteze dakika kadhaa kabla ya kupata mwanya wa kurejea
barabarani.
Walipoupata na kuanza kuifuata
Sokoine Drive, Joram bila kujua kisa cha hofu yake, alijikuta akitazama kila
pande kuhakikisha kama halikuwepo gari lolote linalowafuata. Baada ya kusoma
kitu kile kisichoelezeka katika macho ya Kwame hakutaka ifahamike na yeyote wapi
anakoelekea. Hakuona kama ilikuwepo gari yoyote inayowafuata katika msafara
uliokuwa nyuma yao.
Hata hivyo, alimshauri dereva
kuiacha Sokoine Drive na kuifuata Samora Avenue akipitia Barabara ya Makunganya.
Ni hapo alipoona gari moja iliyokuwa mbele yao ikisita kidogo. Kisha iliendelea
na safari. Ilikuwa Datsun yenye namba ambazo Joram hakuweza kuzisoma
kikamilifu.
Akiwa katika barabara hiyo ya Samora
mbele ya jengo la Kitega Uchumi, Joram aliona gari ile ya Datsun ikitokea mbele
yao kasi na kuwapita baada ya dereva kumtupia Joram jicho la haraka haraka.
Ndipo Joram alipopatwa na hakika ya kufuatwa
huko.
Akamwamuru dereva kusimama, akamlipa na
kumtaka aondoke.
“Kwa nini ndugu? Si tunaenda
Kigamboni?” alihoji dereva huyo kwa
mshangao.
“Nimebadili mawazo. Nitaenda siku
nyingine.”
“Pamoja na hayo ndugu, itakuaje
nikuache ovyo namna hii? Si bora nikufikishe nyumbani
kabisa.”
“Usijali.”
Baada
ya kufanikiwa kumwondoa dereva huyo, Joram aliingia katika jengo hilo na kupanda
kwa lifti hadi ghorofa ya tano ambapo aliacha lifti na kusimama kando ya dirisha
akichungulia chini. Haikumchukua muda kabla hajaiona ile Datsun ileile ikirudi
polepole na dereva wake kutoka nje na kutazama huku na
huko.
Ilikuwa dhahiri kuwa alimwona Joram
alipoachana na ile teksi. Ilikuwa dhahiri pia kuwa mtu au watu hao walimhitaji
Joram binafsi, si dereva wa gari ile.
Baada ya
kupata hakika hiyo, Joram aliteremka chini na kutoka njeya jumba hilo kwa mwendo
wa kawaida, kama ambaye hakujua kuwa kuna mtu anayemsubiri. Joram alipita kando
ya gari hiyo bila kuitazama na kuanza kurudi katikati ya jiji. Mara tu
alipoipita, Dutsun ilitiwa moto na kuendelea na safari kama gari yoyote isio na
shughuli na Joram. Lakini jambo hilo halikumpumbaza Joram hata kidogo. Badala
yake ilikuwa ushahidi mwingine ambao ulimtia hakika kuwa anapambana na timu
kubwa inayojua wajibu wao. Kwani kuondoka kwa dereva huyo kulimaanisha kuwa huko
aendako Joram alikuweko mtu au watu ambao wangeendelea na jukumu la
kumfuata.
Hayo yalimfanya Joram acheke rohoni.
Kadhalika damu ilimchemka na akili yake kuchangamka. Alihisi kuwa tayari
ameingia katika mapambano. Ingawa alikuwa hajawafahamu adui zake, bado
alifarijika kwa kuona adui hao tayari wameujua uwezo wake ndipo wakachukua hatua
hizo za kumfuatafuata wajue lipi anafanya. Lipi zaidi angehitaji zaidi ya hilo
kupata hakika kuwa alikuwa amegundua jambo fulani katika upelelezi wake dhidi ya
vifo vya kina Kitenge? Sasa alichohitaji Joram kilikuwa kitu kimoja tu; kumjua
adui huyo. Baada ya kumfahamu, isingemchukua muda kufahamu kiini cha mauaji hayo
yote.
Kwa Joram Kiango kumjua mtu anayemfuata
halikuwa tatizo. Alichofanya ni kuendelea kutembea polepole huku akiwa na hakika
kuwa anafuatwa. Alipofikia sanamu ya askari, alipanda kufuata Barabara ya
Maktaba.
Alisita kidogo mbele ya maktaba ya
Wafaransa akitazama picha zilizowekwa ukutani, kisha aliendelea. Akapinda kona
kuifuata Barabara ya Jamhuri. Baada ya kuifuata kidogo, aliacha barabara na
kufuata uchocho mdogo wenye giza.
Hapo alijificha
akichungulia barabarani. Haikuchukua muda kabla hajamwona mtu mrefu mwenye
dalili zote za tabia ya kutumia nguvu akifika hapo na kutazamatazama. Mtu huyo
alisita, kisha akajitoma kuufuata uchochoro huo. Alitembea kwa tahadhari na
uangalifu.
“Unanitafuta mimi ndugu?” Sauti ya
Joram ilimgutusha mtu huyo. Kabla hajajua afanye nini alipokea pigo la judo
ambalo lilimtua vyema shingoni. Akalalamika na kuanza kuanguka. Lakini Joram
alimdaka na kumweka chini kistaarabu huku akimzindua kwa ngumi ya uso. Mtu huyo
alijaribu kujitetea lakini pigo lingine la Joramu usoni mwake lilimlegeza
kabisa. Akakoroma kwa maumivu huku akiruhusu damu kumtoka kinywani na
puani.
“Hiyo ni kukufahamisha kuwa sipendi
kufuatwafuatwa,” Joram alimweleza kwa kebehi. “Sasa nataka uniambie mara moja
nani amekutumeni kunifuata?” jitu hilo liliguna tu. Joram akalizawadia pigo
lingine ambalo lilifanya lilalamike na kusema kwa
udhaifu.
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Utaniua
bure. Mimi simjui mkubwa wangu. Napewa amri na mtu mmoja anayeitwa Kauzibe bin
Kaubandike. Nasikia naye pia si mkubwa wala hatumjui mkubwa
wetu.”
“Mnapewa amri gani?” Joram alizidi
kusaili.
“Amri ya kufanya lolote, hata kuua
ikibidi. Tunachojali ni pesa ambazo ni
nyingi.”
“Leo pia kawapeni amri ya
kunifuata?”
“Ndiyo.”
“Saa
ngapi?”
“Muda mfupi uliopita. Ilikuwa amri ya
haraka sana.”
“Ilisemaje amri
hiyo?”
“Tulipewa picha zako. Tukaambiwa usivuke
kwenda Kigamboni.ukilazimisha kufanya hivyo tukuue. Hivyo endapo ungelazimisha
ukiwa ndani ya gari ile ajali ingetukia. Na ingekuwa muujiza kama
ungepona.”
“Mko
wangapi?”
“Tuko wengi sana, lakini hatufahamiani.
Sasa hivi watafika hapa endapo nitachelewa.’
Joram
alijua huo ni ukweli ambao pia ulikusudiwa kuwa tishio kwake. Akaikagua mifuko
ya mateka wake na kupata bastola ambayo aliipachika mfukoni mwake na
vitambulisho vya uongo ambavyo
alivichana.
“Unasikia wewe,” alifoka baadaye.
“Mwambie yeyote huyo unayemwita bosi wako kuwa sipendi mzaha wa kufuatwa.
Ningeweza kumwonyesha kuwa sipendi tabia hiyo kwa kukufanya wewe maiti, aiokote
kesho, maadamu wewe mtumwa nimekusamehe. Mwambie akithubutu tena kufanya hivyo
atapata salamu za Joram Kiango.”
Jina hilo
lilimfanya yule mtu agutuke na kutoa macho ya mshangao na kutokuamini. “Nani…
Joram…” Joram hakumjibu, aliondoka zake polepole lakini kwa hadhari
zaidi.
Dakika kadhaa baadaye, hakuwa Joram Kiango
yuleyule tena. Alikuwa mtu mwingine aliyebadilika kimavazi kiasi cha kuweza
kumchanganya mtu yeyote. Sasa alivaa suti yake nyeusi, tai nyeusi, shati jeusi
na kofia nyeusi. Kitu pekee cheupe mwilini mwake kilikuwa ni kitambaa cheupe
alichofunga shingoni.
Kitambaa ambacho kukiondoa
hapo kungemfanya aonekane kivuli au sehemu ya kiza ambacho kilitanda kwa silaha
zake ambazo ni pamoja na bastola, visu, nyembe, tochi yenye ukubwa wa kalamu na
dawa ambazo humsaidia katika shughuli zake.
Akiwa
karidhika na hali yake, aliyaacha makazi yake, sehemu za Ilala na kukiendea
kituo cha basi ambapo alijiunga na watu waliokuwa wakisubiri usafiri wa kwenda
mjini kufunga siku kwa starehe za dansi, sinema na
vinywaji.
Hayo yalikuwa yakitokea dakika arobaini
na tano tu baada ya Joram kumwacha mahututi yule jambazi aliyekuwa akimnyemelea
katika vichochoro vya Mtaa wa Jamhuri. Alikuwa amesafiri harakaharaka,
akisaidiwa na usiku ambao ulianza kutawala na kumficha asionwe na gaidi mwingine
na kuweza kusumbuliwa pindi akienda
kwake.
Alipofika nyumbani alipiga simu ya haraka
kwa katibu wake kumjulisha hali ilivyo, kisha hima akaanza kubadili mavazi na
baadaye kujitokeza mitaani akiwa kama alivyo. Sura ikionyesha utulivu, mavazi
yakitangaza starehe hali rohoni kabeba furushi la mashaka na taharuki kwa
kufikiria jukumu lililokuwa mbele yake.
Hofu yake
haikuwa juu ya maisha yake, ingawa kwa mujibu wa taarifa ya yule jambazi
aliyepambana naye dakika chache zilizopita, alifahamu kuwa anaelekea eneo la
hatari sana. Hasa, hofu yake ilikuwa juu ya maisha au usalama wa mtu aliyekuwa
akimfuata; Dismas Komba. Aliamini kwamba yupo mashakani. Moyo ulimshawishi
kufanya haraka sana ili kujaribu kumtoa katika hatari
hiyo.
Lilitokea basi lielekealo Posta, Joram
alikuwa mtu wa kwanza kulidandia. Na lilipowasili aliwatangulia wote kuteremka.
Akafanya haraka kuchukua teksi ambayo ilimfikisha Ferry ambako alijiunga na
wavuvi pamoja na watu wengine waliokuwa wakinunua samaki. Alijitia mteja wa
kawaida lakini macho yake yalikuwa kazini yakisoma sura za watu kuangalia kama
alikuwepo yeyote kati ya maadui ambao walipewa jukumu la kutokumruhusu kufika
Kigamboni. Aliporidhika na nyuso hizo alimshawishi mvuvi mmoja, kijana ambaye
alikubali kumvusha hadi upande wa pili kwa shilingi hamsini akitumia ngalawa
yake.
Joram alimsaidia kijana huyo kwa kupiga
kasia kwa namna ambayo ilimchekesha sana kijana huyo kwa jinsi asivyofahamu kazi
hiyo. “Acha tu mzee,” alisema kijana huyo. Kisha alibadili sauti katika kicheko
chake na kukifanya kiwe cha kitu kama dharau ama mshangao. Kicheko hicho
kilifuatwa na swali lililodai, “Yaonyesha u tajiri sana
mzee?”
“Kwa nini? Alihoji
Joram.
“Watu wenye fedha ndogo kama mimi si rahisi
kukodi mtumbwi. Pantoni iko pale na inachukua watu bure kwa haraka na usalama
zaidi.”
Ikawa zamu ya Joram kucheka. Kijana huyu
hakujua kuwa alikuwa ameepuka pantoni hiyo kwa hadhari akijua kuwa kama kuna
ulinzi wowote dhidi yake, haikuwepo sehemu nzuri zaidi ya hapo kivukoni. Hivyo,
alikuwa akiepuka kuonekana na jicho ambalo halikustahili kumwona hasa kwa wakati
huo. Lakini alimjibu kijana huyo kwa kumlaghai, “Siku nyingi mno sijasafiri
katika chombo kidogo kama hiki. Hizo shilingi hamsini nilizokupa ni kati ya mia
nilizozipata katika bahati nasibu. Hazikuwa katika
bajeti.”
“Kwa nini basi usingekuja mchana? Saa
mbili u nusu za usiku! Utafaidi nini?”
“Safari ya
usiku naipenda zaidi.”
Walipowasili upande wa pili
nje kabisa na kituo cha kawaida, Joram alimshukuru kijana huyu na kisha kuanza
safari ya kuingia Kigamboni. Akiyafuata maelekezo ya yule mtumishi wa Kamata
alifikia nyumba ambayo alidhani ingekuwa ya Komba. Lakini mara baada ya kuuliza
kwa mtoto aliyeketi nje ya nyumba hiyo aligundua kwamba
aliikosea.
“Ni ile pale. Si yule Komba wa
Kamata?”
“Ndiye.”
“Ile
pale.”
Joram alipoanza kuondoka ili aiendee,
mtoto huyo alimzuia kwa kusema, “Unakwenda pale mzee? Hapafikiki siku hizi. Hasa
usiku kama huu!”
“Kwa
nini?”
“Pana miujiza sana. Mambo ya ajabu
yanatokea katika nyumba ile. Nadhani kuna jinsi au
majini.”
“Kwani vipi bwana
mdogo?”
“Mengi yanatukia pale. Wapangaji wote
wamehama. Amebaki Dismas peke yake. Inasemekana kwamba anajifungi achumbani
usiku na mchana. Bila shaka kati ya kesho na keshokutwa atakuwa
chizi.”
Joram akajikuta akizidiwa na hamu ya
kuyaelewa maongezi hayo. “Kijana, nieleze vizuri nikuelewe. Unataka kusema
kwamba kuna mambo ya ajabu ajabu yanatokea katika nyumba ile? Kama yapi? Nieleze
hatua kwa hatua.”
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ni habari ngumu
kueleweka. Watu wanadai kuwa kabeba jini kutoka Unguja alikokwenda hivi
karibuni. Tangu alipotoka huko mambo yake hayaeleweki. Siku ya kwanza aliporudi,
alikuwa katika hali ya kawaida. Usiku huo alisikika akilia na kunyamaza ghafla.
Jirani aliyeamka na kumwendea alirudi mbio akilia ati kapigwa kama jiwe tumboni
na mtu asiyeonekana. Asubuhi waliomwona Dismas walidai kuwa alikuwa kachubuka
usoni na damu ikiwa imekaukia puani. Yasemekana alitoka ili aende mjini,
akaingia katika pantoni na kuvuka ng’ambo, lakini aliporudi alirudi nalo huku
akitetemeka.
“Ni hapo alipoanza tabia ya
kujifungia ndani. Yasemekana pia kuwa wapangaji hao waliohama walikuwa wamelala
ndani lakini walipoamka alfajiri walijikuta wamelala nje, uchi wa mnyama, hali
vitu vyao humo ndani vikiwa vimetapanywa ovyo ovyo. Hata sisi watoto ambao
tumekuwa tukicheza mbele ya nyumba hiyo tumeacha baada ya mwenzetu mmoja usiku
wa juzi kutoweka ghafla na kuokotwa baada ya muda mrefu kalala ufukoni.
Alipoulizwa kilichomfanya alale huko na vipi alienda huko hakuwa na jibu zaidi
ya kushangaa tu.”
“Ni hadithi nzuri,” Joram
alimjibu akitabasamu.
“Siyo hadithi. Yametokea na
yanaendelea kutokea…”
Joram hakuwa na nafasi ya
kumsikiliza zaidi. Mawazo yake tayari yalikuwa kazini yakiifikiria taarifa hiyo.
Macho yake pia yalikuwa yakipambana na kiza kujaribu kutazama eneo la nyumba
hiyo ambayo kiasi ilijitenga na nyumba nyingine kutokana na utaratibu
usioridhisha wa mjenzi au mpimaji. Nyumba hiyo ilizungukwa na kichaka kikubwa
cha miti au maua yasiyo katika utaratibu
mzuri.
Kwa
mtu kama Joram ilikuwa ni rahisi kuhisi kichaka hicho kingeweza kuwa hifadhi
nzuri ya mtu au watu waliodhamiria kumtendea Dismas Komba jambo fulani, si kama
walivyodhani watu wengine kuwa ni majini yaliyofanya yote hayo. Joram alimshuku
pia kuwa kile kitendo cha watoto na majirani kilidhamiriwa kuwaweka watu wote
mbali ya eneo hilo ili wapate nafasi nzuri ya kuendelea na harakati zao.
Harakati ambazo zilikusudiwa kupoteza maisha ya Komba. Kwa
nini?
Hakuwa na nafasi ya kujijibu maswali hayo.
Damu ilikuwa ikimchemka na moyo kumwenda mbio huku nafsi ikimshawishi kufanya
haraka kabla halijatukia lolote baya zaidi kwa
Komba.
Hata hivyo, baada ya kumshukuru mtoto huyo
kwa sauti ambayo haikuonyesha kuwa kaamini lolote kati ya hayo, aliondoka zake
polepole akielekea upande mwingine. Mikono yake ilikuwa shingoni kuondoa kile
kitambaa cheupe. Mara akawa kama kivuli. Ili kupima kama alikuwa katika hali ya
kuridhisha alipiga hatua mbili nje ya barabara na
kusimama.
Watu wengi walipita bila ya kumwona.
Mara alitokea mzee, kafutana na binti mwenye umri wa mjukuu wake. Walikuwa
wakizungumza mambo ambayo yalimshangaza Joram kupita kiasi. Walipomkaribia zaidi
walisimama na kuendelea na maongezi yao.
Nusura
atokwe na kicheko kwa kusikiliza utongozaji huo wa kizamani mno. Lakini
alijikuta akishindwa kustahimili kuondoka pindi maongezi hayo yalipopamba moto
na kubadilika kuwa mahaba kwa mtindo ambao Joram hakutarajia kuwa binti mdogo
kama huyo angediriki kumtendea babu wa kiasi
hicho.
Aliondoka kwa kunyata akiifuata nyumba ya
Dismas Komba. Alipoikaribia alitafuta nafasi nzuri katika kichaka cha maua na
kuketi chini akisubiri.
Alisubiri sana. Kusubiri
ikiwa miongoni mwa shughuli zake hakukinai kuketi hapo, akivumilia mirija ya mbu
huku macho yake ambayo yalikwishazoea giza yakiwa wazi kutazama lolote. Nia yake
ilikuwa ifike saa saba au nane ya usiku ndipo aendelee na safari yake hadi
katika nyumba ambamo alikusudia kuonana na Komba. Kwenda papara baada ya kusikia
‘hadithi’ ya yule kijana juu ya nyumba hiyo isingetofautiana na nondo aendavyo
katika moto kwa tamaa ya mwanga.
Joram
alipoitazama tena saa yake na kuona ikikaribia saa sita za usiku, alianza
kujiandaa kuisogelea nyumba hiyo. Nia yake ikiwa ashughulikie dirisha moja au
mlango na kuingia ndani ambako angehitaji kupata hakika kama sehemu ya kiza
ikichezacheza hatua kadhaa mbele yake. Baada ya kutazama kwa makini aliona
dalili za kiumbe hai, kikitembea polepole kuiendea nyumba hiyohiyo. Alikuwa mtu!
Kavaa mavazi mieusi kama yake. Macho ya Joram yaliongeza juhudi kutazama kama
mtu huyo alikuwa peke yake. Hakuona dalili ya mtu mwingine. Ndipo Joram
alipouinua mguu mmoja baada ya mwingine kwa hadhari na utulivu kama kivuli
akimfuata.
Mtu huyo alipoufikia mlango hakuchelewa
sana kuushughulikia, ukafunguka polepole naye akaingia huku akiufunga. Joram
alimpa dakika mbili, tatu kisha akausogelea mlango na kuujaribu. Haukuwa
umefungwa. Akaufungua na kunyata ndani huku masikio yake yakiwa wazi, mkono wake
ukiipapasa bastola yake.
Humo ndani kulikuwa na
kiza ambacho kilitisha mno. Nuru hafifu sana ilionekana kwa shida kutoka chumba
kimoja. Joram alikifuata chumba hicho na kutega sikio lake katika tundu la
ufunguo akisikiliza. Haikuwepo haja ya kusikiliza kwa makini kiasi
hicho.
Sauti ya mtu au watu wanaogombana kidhaifu
ilimfikia kwa urahisi. Mmoja alikuwa akisema, “Wapi? Usiposema nitakuua…”
Mwingine alilalamika tu.
“Nitakuua kweli,” ilidai
tena sauti hiyo nzito zaidi. Ikafuatwa na malalamiko ya maumivu
makali.
Joram hakustahimili zaidi. Akaufungua
mlango kimyakimya kwa haraka zaidi na kujitoma ndani. Aliingia wakati mzuri sana
wa kuwa shahidi aliyeshuhudia jisu kali na refu likiingia katika kifua cha mtu
aliyelala juu ya sakafu.
Pigo la pili Joram
alilizuia kwa kumpiga muuaji huyo judo ya shingo. Hakuwa amelipiga vizuri pigo
hilo, kwani badala ya mtu huyo kuzirai kama alivyotarajia Joram, alishangaa
kumwona akiinuka na kumtazama Joram kwa macho makali yenye mshangao. Joram
akaachia pigo jingine. Hili lilimwingia mtu huyo, lakini halikumtosheleza.
Alichofanya ni kupepesuka kidogo tu na kuinuka tena akimjia Joram huku kajiandaa
tayari. Joram akaona kuwa alikuwa kakukutana na mtu hatari kwa
judo.
Akajiandaa vyema zaidi. Mt huyo alimjia
Joram, mikono yake iliyotapakaa damu ikiwa imetangulia. Joram alimwepuka nsa
kurusha kung fu ambayo ilikwepwa na kufuatwa na karate ambayo ilimkubali Joram
ubavuni. Kabla hajakaa vyema pigo la pili lilimtua
shingoni.
Joram alitamani kuuzamisha mkono wake
mfukoni ili apate bastola yake, lakini alihisi hiyo ni dalili ya woga na bado
alifurahia nafasi hiyo ya kuupima uwezo wake kijudo. Hata hivyo alijutia uamuzi
wake huo baada ya dakika kadhaa za mapambano na kujikuta katupwa chali, mikono
ya jitu hilo ikitambaa kooni ili kumkaba. Joram alijitahidi kurusha mateke na
mikono, haikusaidia.
Mikono ya mtu huyo
ilikwishapata koromeo lake na sasa ilianza kumkaba kwa nguvu kana kwamba ni
vidole vya chuma. Macho yakaanza kumtoka Joram kwa hofu. Lakini macho hayo
yalibadilika na kutazama kwa faraja pindi alipoona yule mtu aliye sakafuni
akijikongoja kuinuka na kuchomoa jisu kutoka kifuani mwake na kukididimiza
mgongoni mwa adui aliyemkalia kifuani.
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Lilikuwa pigo dhifu
mno lakini lilimfanya mtu huyo kumsahau Joram na kugeuka nyuma. Joram aliitumia
nafasi hiyo kuachia pigo zito la mwisho. Pigo ambalo lilitimiza wajibu wake.
Muuaji akaanguka sakafuni. Joram akamwahi kwa kumtia kamba za miguuni na
mikononi haraka haraka. Kisha akamwinamia na kumtazama
vizuri.
“Mama.”
Sauti
hiyo ilimzindua Joram. Akamwacha muuaji huyo aliyelala kama mzoga na kumsogelea
mtu huyo aliyekuwa akijaribu kuinuka ili ainue tena jisu na kummaliza adui yake.
Joram hakuwa na haja ya kuambiwa kuwa mtu huyo ni Dismas
Komba!
“Asante kwa kuokoa maisha yangu Bwana
Dismas,” alimweleza haraka haraka. “Unadhani kwa nini walitaka kukuua?”
aliuliza.
“Wamekwishaniua…Nakufa…” Komba
aliendelea kulalamika.
“Wewe sio
mmojawao?”
“Mimi ni adui yao
mkubwa.”
“Wewe ni
nani?”
“Huwezi kunifahamu. Kwa jina ni Joram
Kiango.”
“Joram! Nakujua sana…” Komba alisema kwa
juhudi kubwa. “Joram! Walinitesa sana…Laiti wangeniua…nilikuwa sina hali siku
zote. Nikienda huku nakutana nao. Nikikaa hapa usiku wanafika na kuniadhibu kwa
vitisho na mateso. Wameniua…” akaanza tena
kulalamika.
Ingawa nuru ilikuwa hafifu, ikitoka
katika mshumaa uliowekwa kwenye kona moja ya chumba, lakini ilitosha Joram kuona
katika macho yake Dismas Komba kuwa uhai ulikuwa ukimtoka harakaharaka. Hakuwa
na muda wa kuishi zaidi.
*****JORAM ANAKUMBANA NA
KASHKASH KUBWA KATIKA HARAKATI ZAKE. HAPA KAKUTANA NA DISMAS KOMBA, LAKINI
ANAMWONA KUWA HANA MUDA MREFU WA KUISHI. JE, NI KIPI KITAFUATA? FUATILIA RIWAYA
HII KALI I
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment