Simulizi : Najisikia Kuua Tena
Sehemu Ya Pili
(2)
KOMBORA hakujibu mara
moja. Yeye alimshakia zaidi huyu mtunzi, Bazile. Sauti katika simu ile haikuwa
ya kike. Wala hakuona kama mwanamke huyu mlevi wa gongo angekuwa na haja ya
kumwandaa na kumpigia simu polisi kama hadithi ile ya Simu ya
Kifo.
Hata hivyo, bado aliona umuhimu wa kuwapata
wote wawili mapema iwezekanavyo. Yawezekana kuwa mtunzi yule hahusiki.
Yawezekana vilevile kuwa yeyote kati yao hahusiki! Aliwaza ghafla kwa hofu.
Jambo ambalo litaongeza uzito katika jukumu
hili.
Kwa kawaida kesi hii isingemjia yeye Kombora
au kikosi chake moja kwa moja. Ingekuwa kesi ya kushughulikiwa na vituo vya
kawaida vya polisi. Kikosi hiki cha kumi na mbili kilikuwa chini ya idara
maalumu inayoshughulikia masuala makubwa ya mauaji katika jiji hili. Kesi ambayo
ilielekea kuwashinda polisi wa kawaida au yenye masuala yanayokanganya au hujuma
za kiuchumi na kisiasa ndiyo iliyokuwa ikiletwa
hapa.
Hii haikuwa kubwa kiasi hicho. Lakini
alikuwa ameipokea na kuiomba toka majuzi alipopata simu ile inayodai mauaji.
Alihisi muuaji huyo anamhitaji yeye. Ndipo akawaarifu polisi kumletea kesi
yoyote ya mauaji ambayo ingetokea katika saa ishirini na
nne.
Hata hivyo, hakuwa amemgusia yeyote juu ya
simu ile. Wala hakuwa tayari kumgusia Sajini Abdala suala hilo. Hivyo alimwambia
kwa sauti ya amri akisema, “Vizuri sajini. Nawahitaji haraka hawa wawili.
Machozi na huyu Bazile. Nafahamu wajua lipi utafanya ili wapatikane kabla ya
kesho.”
“Bila shaka
afande.”
******
ULIKUWA
ni usiku mbaya mno kwa walevi wa pombe haramu, hasa wanawake. Kote
kulikofahamika au kushukiwa kuwa maskani ya walevi hao kulizingirwa na vijana wa
polisi na JKT wenye kiu kubwa ya kuupima ujana wao. Wengi walikamatwa na
kusukwasukwa kwa makofi na mabuti ya vijana wa polisi. Waliochukuliwa moja kwa
moja walichukuliwa, walionusurika walinusurika. Mamia waliyosalia walichujwa
hata wakasalia kina Machozi arobaini. Ni hao waliofikishwa kituo cha polisi.
Huko pia walichekechwa hadi waliposalia watatu waliofanana kwa sura na tabia. Ni
katika watatu hao alipopatikana Machozi
aliyetakiwa.
“Wewe unasema umekamatwa Luhanga
sio?”
“Ndiyo.”
“Ulikuwa
ukifanya nini?”
“Kwani vijana wako walikwambia
nini bwana askari? Nilikuwa nikinywa na kustarehe. Sina jambo lingine la
kufanya.”
“Hujui kwamba gongo ni haramu kidini na
kisheria?”
“Mangapi ni haramu na yanafanywa?
Siachi gongo kwa taarifa yako! Bia haitengenezwi kwa ajili yangu wala watu wa
aina yangu!”
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Sajini Abdala
akamkazia macho. Pamoja na uzoefu wake wa kutazamana na wahalifu wa kila aina,
lakini macho ya huyu yalimtisha. Yalikuwa ya kila hali ya ulevi na wazimu.
Yalitangaza waziwazi kuwa ‘lolote laweza kutokea’. Baada ya misukosuko yote ya
vijana wa polisi ambayo iliacha ushahidi wa jeraha dogo katika mdomo wa mama
huyo na ngeu katika paji lake la uso, macho hayo hayakuonyesha athari yoyote.
Yalikuwa imara yakimtazama sajini huyo na askari wote kwa dharau, kebehi na
kutojali.
“Unamfahamu Kondokondo Kitenge?” Abdala
alifoka ghafla.
“Mara ngapi nikwambie kwamba
namfahamu?” Machozi alirudisha.
“Ni nani
wako?”
“Mara ngapi nikwambie kwamba ni baba watoto
wangu?”
Ni majibu hayo aliyokuwa kayatoa tangu
aanze kuhojiwa suala hilo. Kilichomshangaza Abdala ni jinsi mama huyo
alivyozungumza kwa uhakika kama aliyeamini
anachokizungumza.
“Sikia wewe mwanamke,”
alinguruma Abdala. “Uko hapa si kwa mzaha ila ni suala gumu mno kwako. Hivyo
nataka uache majibu ya kilevi. Unijibu kikamilifu. Sawa? Kwa taarifa yako,
Kondokondo Kitenge amekufa. Ameuawa usiku wa jana!” Abdala alisita akiutazama
uso wa Machozi kuona vipi ujumbe huo
ungemwingia.
Kama alitarajia kuona mshangao au
hofu katika uso huo, lolote kati ya hayo halikutokea. Machozi alikuwa vilevile
kama mama aliyearifiwa kifo cha panya au kifaranga. “Umesema kweli askari?”
Alihoji polepole. “Amekufa kweli?”
“Amekufa.
Ameuawa usiku wa jana. Waweza kutuambia ni nani
kamuua?”
Ndipo kitu cha kutisha kikatokea katika
uso wa Machozi. Tabasamu. Lilikuwa la kutisha kuliko tabasamu lolte la
mwanadamu. Abdala alililinganisha na lile la sokwe alilowahi kuliona katika
hifadhi za wanyama. Baada ya tabasamu hilo Machozi aliropoka kwa sauti ya
juu.
“Amekufa sio! Ameuawa….sikupata kupokea
habari njema kuliko hiyo katika maisha yangu bwana polisi. .. ndiyo, namjua
aliyemuua. Ni mimi mwenyewe. Nimemuua kwa mkono huu!” Akaupunga mkono wake wa
kulia angani.
Sajini Abdala akaduwaa. Akawageukia
wenzake ambao walikuwa katika mshangao pia. Hakuna aliyetarajia jibu rahisi kama
hilo. Hivyo, badala ya kulikubali kama walivyotaka, wakajikuta wakilitilia
shaka.
“Nadhani dada yangu hujui unalosema. Huna
habari kuwa suala hili linaweza kukufanya ule kitanzi?” alisema askari
mmoja.
“Najua! Na nitaingia kitanzini kwa furaha
maadamu nimemuua!”
“Ulimuua
lini?”
“Jana
usiku.”
“Saa
ngapi?”
“Sikumbuki vizuri, sijawahi kuwa na
saa.”
“Ulitumia silaha
gani?”
“Kisu!”
Askari
wakatazamana tena. Kisha walibadili mtindo na kuanza kumuuliza mfululizo.
Walishangaa kukuta mama huyo akisimama imara akiendelea kudai: “Nimemuua…
Nimemuua.”
Taarifa hiyo ilipopelekwa kwa Inspekta
Kombora nusura imtie wazimu. Alimsikiliza Sajini Abdala kwa makini kisha akakuna
kichwa huku kainamia meza. Kisha alikuna macho akitazama dari. Aliporudisha
macho hayo mbele yake yalikuwa yamejaa
maswali.
“Unadhani anasema ukweli
sajini?”
“Nani, mwanamke huyo sio? Hilo ndilo
tatizo lenyewe afande. Ni vigumu kukataa au kukubali kuwa anasema ukweli.
Mwenyewe kang’ang’ania hivyo.”
“Achana na maneno
ya mlevi,” alidai Kombora. “Kinachotakiwa ni ukweli. Waruhusu vijana maalumu kwa
shughuli za aina hiyo wafanye kazi yao hadi watakapohakikisha kuwa kama hasemi,
anautapika ukweli huo. Sawa?”
“Sawa,
afande.”
Kilichomfanya Kombora achanganyikiwe ni
hiyo taarifa nyingine aliyoipata kwa sajini aliyepewa jukumu la kumpata Bazile
Ramadhani, mtunzi ambaye Kombora alimshuku zaidi katika mauaji haya. Sajini huyo
alirejesha majibu kwa ‘radio call’ ambayo yalimtisha
Kombora.
Kwamba alipoenda Barabara ya Pugu kwenye
kiwanda cha TEGRY ambako Bazile alikuwa akifanya kazi, aliarifiwa na wakubwa
wake kuwa alikuwa hajafika kazini hapo siku mbili nzima. Baada ya kuhangaika
sana, walimpata msichana mmoja ambaye alisemekana kuwa alikuwa rafiki wa
Bazile.
Ni huyo aliyewaongoza hadi Kigamboni
ambako Bazile alipanga chumba. Huko pia walikuta chumba kitupu. Jirani zake
walidai kuwa ‘ametoweka ‘ tangu majuzi. Hakuna aliyefahamu alikoenda. Hakuna
aliyeagwa.
Ni hilo lililomtia Kombora mashaka
zaidi. Aweza kuwa popote. Aweza kuua tena wakati wowote. Hivyo, alimwamuru
sajini huyo kuendelea na upelelezi juu ya tabia na mwenendo wa mtu
huyo.
Maongezi hayo Kombora aliyasikiza moja kwa moja katika ‘radio
call’ hiyo.
“Bi nani sijui
mwenzangu.”
“Mimi sio? Naitwa
Ashura.”
“Ndiyo, bi Ashura. Waweza kutusaidiaje
ili kumpata mapema huyu rafiki yako? Aweza kuwa kaenda
wapi?”
“Kwanza ningeomba nisieleweke moja kwa moja
mimi ni mpenzi wake Bazile, bwana askari. Niwie radhi kwa hilo lakini ndio
ukweli wenyewe. Niliondokea kumpenda lakini hapendeki. Hana muda wa mapenzi. Na
hata maongezi hajui. Ukitaka kumsikia akizungumza lazima uongelee vitabu. Mimi
mambo ya vitabu siyajui. Hivyo nilikuwa kama najilazimisha kwake tu. Mara kwa
mara muwapo pamoja utamkuta kakusahau kabisa yuko maili elfu moja katika dunia
ya peke yake. Hivyo kuhusu swali lako siwezi kulijibu. Hakuwahi kuniamini katika
masuala yoyote ya maisha yake isipokuwa ya vitabu
tu.”
“Ahsante
sana. sasa dada Ashura, unadhani Bazile aweza kuua mtu?” kicheko laini cha
msichana yule kikamfikia Kombora.
“Kuua! Bazile!
Siamini. Kwa kuwa anaandika vitabu vya mauaji siyo? Kwa kweli sijapata kuona mtu
mwoga au mstaarabu kama yeye. Hajapata kumtukana mtu, hajapata kumpiga mtu kofi,
ataanzaje kuua? Ebu bwana askari, kweli mnamtafuta kwa nini? Eti mnamshuku kaua
mtu?
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kuua au kuuawa.
Hajaonekana siku mbili. Unadhani habari hiyo ni njema? Chumbani kwake kila kitu
kimo, isipokuwa yeye tu.”
“Kweli
kabisa!”
Baba mwenye nyumba naye alikuwa na
yake.
“Kuua siyo? Japo ni mtulivu, mimi nadhani
anaweza kabisa. Mtoto hakai nje na wenzake kuongea. Kutwa nzima chumbani.
Ukimuuliza nini anafanya atadai anasoma. Ukichungulia utamwona kainamia meza
anaandika. Hachoki kuandika. Nadhani alikuwa na aina fulani ya wazimu. Yaweza
kumtuma kufanya lolote.”
Hayo ndiyo yaliyokisumbua
kichwa cha Kombora. Kafa mtu mmoja. Washukiwa wawili ambao hawafahamiani wala
kuishi pamoja. Mmoja anadai kuwa kaua, wa pili haonekani aliko. Angewezaje
kulipeleka mbele suala hilo likiwa katika utatanishi mzito kama
huo?
La muhimu lilikua kupatikana huyo Bazile.
Akiwa katika milki ya polisi, Kombora angeweza kufarijika zaidi na kufahamu
namna ya kutatua msongamano huo. Hakujua vipi na lini Bazile angeingia
mkononi.
Simu ikalia. Kombora akainyakua na
kuiweka sikioni akinguruma. “Inspekta Kombora
hapa.”
“Kombora! Rafiki yangu Kombora
siyo?”
Haikuwa sauti ngeni masikioni mwa Kombora.
Ilikuwa ileile ambayo alihitaji kumpata mwenyewe. Naam, sauti ileile ambayo
sasa, Kombora hakuitarajia, akishuku mwenyewe tayari yu ahera. Hakujua kama
ilimpasa kuisikiliza au la. Hakujua ajibu nini
zaidi.
Maadamu chombo cha kusikilizia bado
kilikuwa sikioni, aliendelea kumsikiliza.
“Mbona
kimya rafiki yangu Inspekta? Upo? Sikia ndugu yangu najisikia kuua mtu mwingine.
Waweza kunisaidia?”
“Wewe! Ni wewe Bazile
Ramadhani?” aliuliza Kombora kiasi
akitetemeka.
“Umelipataje jina langu mapema hivyo
Inspekta? Kumbe u hodari kiasi hicho? Ndiyo ni mimi. Kwa heri
Inspekta.”
“Sikiliza….” Tayari simu
ilikatwa.
Kombora aliduwaa nusu dakika. Katika
nusu nyingine alikuwa alikuwa akimngurumia opereta kuchunguza ilikotoka simu
hiyo.
Jibu halikumfariji. Simu ilipigwa kutoka
katika vibanda vya simu vilivyoko huko Forodhani. Simu ya wazi ambayo mtu yeyote
wakati wowote anaweza kupiga.
Hata hivyo hakusita
kutuma makachero hao. Hakutokea yeyote aliyekuwa tayari kueleza sura na umbile
la mtu au watu walomtangulia kutumia simu. Pamoja na watu wote waliokuwa hapo
kuonyeshwa picha ya Bazile, jibu la haja
halikupatikana.
*********
IWAPO
Kombora alikuwa akisubiri habari za kifo kimoja, basi alikosea sana. Usiku huo
walikufa watu wawili. Wa kwanza alikuwa Fambo
Wamangi.
Kama ilivyo kawaida ya kifo, kilimtokea
bila kutarajia. Kutwa nzima alikuwa ameshinda katika ofisi yake alikuwa
akiendelea na shughl zake za kila siku. Alikuwa meneja-masilahi katika kampuni
ya Enterprise.
Kampuni hii ilishughulikia
biashara za aina zote na mataifa mbalimbali. Wote waliomwona siku hiyo
walishangazwa na jinsi alivyokuwa mchangamfu na mcheshi zaidi ya kawaida
yake.
Baada ya kazi, alirejea nyumbani kwake
ambapo alicheza na wanawe, akacheka na mkewe na kutaniana sana na jirani zake.
Saa mbili za usiku alitoka na mmoja wa jirani hao kwenda baa ya jirani ambapo
walipata chupa mbili mbili zilizomfanya Wamangi azidi kuchangamka. Kisha
walirejea nyumbani. Wamangi akakiendea kitanda ambako alikuwa ‘mtundu’ kama siku
zile za ujana wao, jambo ambalo lilimfurahisha sana mama watoto wake. Usingizi
uliwakuta katika hali hiyo ukawachukua na kuwahamisha hadi katika milki
nyingine, ya ndoto na starehe.
“Nilipoamka
nilijikuta bafuni,” yalikuwa maelezo ya mama huyo kesho yake. “Nilikuwa
nimefungwa kamba mkononi na kitambaa mdomoni. Nikajitahidi hata kamba hizo
zikafunguka. Nikarejea chumbani ambako niliyoyakuta yalikuwa hayatazamiki. Mume
wangu mpenzi alikuwa kalala chali kitandani, uchi kama alivyolala usiku wa jana,
mwili wake mzima ukiwa umelowa damu nzito ambayo ilikuwa ikiendelea kutiririka
kutoka katika jeraha baya mno la kisu au sime lililokuwa wazi kifuani. Sikuweza
kutazama mara mbili. Sikuweza kupiga kelele. Nadhani nilianguka na kuzirai kwani
nilipopata fahamu tena nyumba nzima ilijaa watu, askari na jirani ambao walikuwa
wakinihudumia.”
Kifo hicho ni katika Mtaa wa
India, jengo la Abdulkar lenye ghorofa nne. Marehemu alikuwa akiishi katika
ghorofa hiyo ya nne pamoja na jirani ambao ni familia mbili za Kiafrika na tano
za Kihindi. Ni mmoja kati ya jirani hao aliyeipigia simu polisi alfajiri baada
ya kusikia watoto watatu wa marehemu wakilia kwa nguvu bila msaada wowote wa
wazazi wao. Alipochungulia na kuwaona wazazi katika hali hiyo, alidhani wote
walikuwa wamekufa, hivyo aliiambia polisi, “Bana na bibi ake yote
kafa.”
Kifo cha pili kilikuwa kimetokea kilomita
kadha wa kadhaa nje ya wilaya hii ya Ilala. Hicho kilitokea huko Kinondoni
Mkwajuni. Marehemu kama bwana Jugeni Kawamba, kama Wamangi kutwa nzima ilikuwa
ya kawaida kwake.
Kwa muda wa miezi kadhaa,
Kawamba hakuwa na kazi. Hivi alikuwa kamrejesha mama watoto wake pamoja na
wanawe wote kwao katika vijiji vya Wilaya ya Mbulu mkoani Arusha, ili aweze
kuyakabili maisha pindi akiendelea na msako wa kutafuta
kazi.
Akiwa mtu aliyepitia madaraka makubwa,
yenye marupurupu ya kutosha, maisha ya kuishiwa yalimtatiza mno. Ingawa hakuwa
kaishiwa kiasi cha kukosa pesa ya matumizi, lakini kule kuona akiba yake ya
benki ikielekea kumezwa kabisa bila matumaini ya kuongeza chochote juu ya akiba
hiyo siku za usoni kulimtia hofu.
Hivyo alikata
makundi ya urafiki wa matumizi na kuwa mtu wa kutulia nyumbani
akijisomea.
Usiku huo usingizi ulimtoka kabisa.
Japo alijituliza kitandani macho kayafunga na kujaribu kubembeleza usingizi,
haukukubali kabisa. Mawazo yalikuwa yakimrejesha kuitazama hali yake kiuchumi
inakoelekea. Haikuridhisha. Mara akaanza kuijutia safari yake ya majuzi
aliposafiri kwa ndege kwenda na kurudi Zanzibar ambako aliitwa kwenda kufanya
mahojiano ya ijara. Labda asingesafiri kwa ndege, meli ingetosha!
Aliwaza.
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mara alihisi
kuinamiwa na dude refu jeusi na alipojaribu kufumbua macho yalizibwa kwa mkono
wenye nguvu kama chuma. Juhudi zake zote za kuutoa mkono huo hazikufua dafu.
Alipojaribu kurusha teke lilidakwa kwa mkono mwingine. Dakka hiyohiyo jisu kali
lilipenya kifuani kwake kwa maumivu makali. Hakuwahi kupiga kelele, kwani mkono
uliokuwa usoni ulihamia mdomoni kuuziba. Pigo la pili lilimmaliza. La tatu
hakulisikia kabisa.
Akiwa mtu anayeishi peke yake
katika nyumba hiyo ambayo hata alikuwa hajamaliza mkopo wake aliopewa na THB,
ilichukua muda kabla maiti yake haijagunduliwa. Ni kijana muuza magazeti ambaye
aliigundua. Kijana huyo akiwa na mkataba wa kumletea magazeti kila siku, asubuhi
hiyo pia alimfikia.
Akashangaa kuona mlango ukiwa
wazi alfajiri yote hiyo jambo ambalo halikuwa la kawaida katika nyumba hiyo.
Hivyo aliamua kuchungulia. Mlango wa chumbani pia ulikuwa
wazi.
Macho yalipofika chumbani humo yalivutwa na
damu kavu ambayo ilitapakaa sakafuni, kitandani akiwa kalala mzee Kawamba,
jeraha kubwa likicheka kifuani mwake. Akitetemeka, kijana huyo aliwaita jirani
ambao walijua la
kufanya.
****
“HAIWEZEKANI.
Hawezi kuvumiliwa zaidi. Lazima yeye au maiti yake ipatikane katika muda wa saa
ishirini na nne zijazo.
“Unasikia Sajini Abdala?” alifoka Inspekta
Kombora, macho kayatoa kwa ukali na hasira.
Mbele
yake kulikuwa na majalada lukuki. Jalada la Machozi ambalo lilikusanya habari
zake zote na kutokuacha mwanya wowote unaomuunga na kifo cha Kitenge japo
mwenyewe aliendelea kudai hivyo licha ya mateso ili aseme
ukweli.
Jalada la marehemu Wamangi na Kawamba
lilionyesha mienendo yao ya kutwa nzima pamoja na shughuli zao za nyuma. Hayo
pamoja na maandishi mengine, yalifurika mbele ya Kombora yakimdai atulie na
kuyasoma. Hakujisikia kusoma
chochote.
Hakujisikia kutulia. Alitamani apate
uwezo wa kupaa, aruke hadi mbele ya Bazile popote alipo ammiminie risasi zote
zilizokuwepo katika bastola yake. Ni hilo tu
alilohitaji.
“Lazima afe,”
akaongeza.
“Ni kweli afande. Ni mtu hatari mno
kuendelea kuishi nje ya kuta za magereza. Tatizo ni jinsi alivyoondokea kuwa
hodari mno pamoja na mitego yote ya polisi usiku na mchana, bado anawakwepa na
kutimiza nia yake,” alijibu Sajini Abdala aliyekuwa kaketi mbele ya
Kombora.
“Mimi pia hilo linanishangaza,” Kombora
alimuunga mkono.
“Nilivyoichunguza historia yake ya nyuma inaonyesha
kuwa aliwahi kupitia JKT. Pengine ni hilo linalompa uwezo wa kutushinda ujanja.
Bila hivyo, ningeweza kupendekeza kuwa anasaidiwa na mtu au
watu.”
“Kweli mzee, kwa mfano alivyoua siku ya
leo. Ameweza kuua hapa mjini kisha akasafiri hadi Kinondoni ambako ameua tena.
Utadhani kuna mtu anayemsaidia kwa
usafiri.”
“Aweza kuwa anatumia mabasi ya abiria.
Akiwa kakificha kisu chake vyema, kondakta na abiria wanamwona kama mtu wa
kawaida tu. Nimejaribu kutazama uwezekano wa mtu yeyote kumsaidia sikuona. Yeye
ni kichaa aliyepata kichaa hicho baada ya utunzi kuiathiri akili yake na vitabu
vyake visivyoeleweka kudharauliwa na watoaji. Amepata wazimu. Nani
atakayemsaidia mwendawazimu kama huyo? Angeweza kusaidiwa na mwehu mwenzake
Machozi, lakini katika uchunguzi inaonyesha kuwa hawafahamiani kabisa. Na bado
Machozi tunaye ndani. Hapana sajini, tusisumbue vichwa vyetu kutafuta mambo
yasiyo ya muhimu. La muhimu ni kumpata huyu Bazilw kwanza. Endapo baada ya
kupatikana kwake vifo vitaendelea, ndipo tutaanza msako
mpya.”
“Ndiyo
afande.”
“Na kuhusu picha yake, peleka katika
magazeti yote. Tangaza kuwa yeye ni mtu hatari ambaye anatakiwa hai au maiti
mapema mno. Yeyote atakayemwona aiarifu polisi mara moja.
Sawa?”
“Lakini afande...” Abdala akasita tena
kidogo kabla ya kuendelea. “Suala hili naona unalipa uzito mno. Ni rahisi sana
kutoa maelekezo yasiyoridhisha endapo utakuwa katika hali uliyonayo siku hizi.
Tangu kisa hiki kilipoanza sijakuona ukivuta; jana nzima hukunywa hata chai; leo
pia naona huna wazo la kutia chochote. Licha ya hayo, uso wako umegeuka kabisa
utadhani mtu anayefuata katika orodha ya vifo hivi ni wewe. Kwa nini afande?
Huoni kuwa ni hatari kwako? Nadhani hii ni kesi ya kawaida kama nyingine nyingi
ambazo tumezitatua kwa njia ya kawaida. Isikutishe
sana...”
“Isinitishe!” Kombora alifoka. Kisha
alijirudi na kujaribu kutabasamu, lakini tabasamu halikutokea. Akamtazama Abdala
kwa huzuni huku akiwaza: Huyu hajui. Hafahamu kuwa napata simu za muuaji kila
kabla ya mauaji hayo. Naweza kustarehe vipi, mimi kama kiongozi wa polisi, hali
muuaji ananikebehi kwa siku kabla ya kumwaga damu isiyo na
hatia?
“Hapana sajini,” akajibu. “Kama ni mzaha
tutaufanya baada ya kumtia Bazile katika mikono yetu. Kwa sasa jambo muhimu ni
kumpata tu. Sawa?”
“Bila shaka atapatikana
afande.”
“Sawa.”
*******
“...ATAPATIKANA
afande....sawa...” Brown Kwame akafunga chombo chake na kumgeukia mwenzake
aliyeketi upande wa pili wa meza. Wakaangua
kicheko.
“Umeona Chenja?” alimuuliza mwenzake.
“Hakuna lolote watakalozungumza hapo kituoni kwao ambalo linapita bila
kulisikia. Nafahamu kila mpango wao kabla hawajaanza kuutekeleza. Kwa hiyo, kaa
ukijua kuwa hakula chochote wala lolote litakalotukwamisha. Moto tuliouwasha
umeshashika mbuga nzima. Hawawezi kuuzima. Acha waendelee kujua adui yao ni yule
bwana mdogo Bazile. Napenda waendelee kuamini hivyo. Watakapogutuka itakuwa ‘too
late’ kwao. Sisi tutakuwa tumemaliza kazi
yetu.”
“Kwa kweli watu hawa ni wazembe kuliko
nilivyotegemea,” Chenja alisema. Kama ilivyo kawaida yake, alisema huku
akipapasa tumbo lake ambalo lilichomoza nje ya kifua chake. “Hadi sasa wanaamini
kuwa adui yao ni Bazile?”
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Na bado
nitawafanya wazidi kuamini hivyo,” Kwame alijibu kwa majivuno. “Huu ni mpango wa
kimataifa bwana Chenja. Mbinu zilizotumika ni za kitaalamu ambazo mtu yeyote
mwenye akili za kawaida lazima ahadaike tu. Leo nitawaonyesha adui yao. Bazile
atawatembelea. Nataka kumfurahisha zaidi rafiki yangu
Kombora.”
“Angalia usi-over
do.”
“Hakuna litakalotokea. Bado kifo kimoja tu,
baada ya hapo amri iko mikononi mwetu, nchi miguuni mwetu. Utaona bwana Chenja.
Subiri kidogo tu.”
“Sawa, sasa nadhani niende
zangu. Ni hatari kukawia hapa.”
“Hakuna mahala
penye usalama kama hapa. Mtu yeyote anayevuka geti hapa ndani namwona vizuri.
Silaha zilizotegwa katika chumba hiki zimepangwa kwa namna ambayo mtu kwa
kawaida haoni na zaweza kumteketeza wakati wowote nitakapo. Zaidi ya hayo,
vyumba vya jirani wapo walinzi waliohitimu kuua na kuadhibu endapo nitatoa amri
hiyo. Licha ya yote hayo, ulikoingia wewe watu wanadhani uko maliwatoni. Hakuna
anayejua siri ya mlango huo. Hatufanyi mzaha hata kidogo bwana Chenja.
Tumedhamiria. Na kwa kuwa tuko ukingoni hatuna lolote la kuhofia. Hata hivyo
bora uende
zako.”
“Kwaheri."
Kwame
alibonyeza dude fulani, sakafu ya chini ya meza ikafunuka na kuachia mwanya
wenye ngazi inayoingia ardhini. Chenja aliaga tena na kisha kuifuata ngazi hiyo.
Alitokea katika nyumba moja upande wa pili wa mtaa. Nyumba hiyo siku zote ikiwa
haina watu wengi, isipokuwa wachache ambao walijua wanachokifanya, ilikuwa
rahisi kwa Chenja kutoka nje ya mlango huo ulioandikwa GUEST LAVATORY bila
kuonekana na kuingia katika gari lake ambalo lilimrejesha kazini
kwake.
Kwame
aliendelea kutulia juu ya meza yake akitabasamu. Kila kitu kilikuwa kikimwendea
kama ilivyokusudiwa. Furaha ilioje!
Machoni mwa
serikali na mbele ya kila mtu, Brown Kwame alikuwa yuleyule, mtu mfupi, mnene,
kidevu kilichofunikwa na ndevu nyingi zilizozunguka uso mpana wenye macho
maangavu, mtu ambaye siku zote alionekana mtanashati kwa suti za nje na viatu
ambavyo vilitengenezwa kwa matakwa yake binafsi katika viwanda
mashuhuri.
Mtu huyu kikazi alikuwa Mkurugenzi
Mtendaji wa kampuni mashuhuri iliyoitwa Snow Fund ambayo ilishughulikia mambo
mengi yakiwa pamoja na huduma za usafiri kwa watalii, uuzaji wa vinyago nchi za
nje, uwakala wa uingizaji na usafirishaji wa bidhaa na kadhalika. Ofisi hii
ilikuwa ikifanya kazi vyema na wafanyakazi wake walikuwa wakiridhika kabisa
kimshahara.
Ni hiyo picha ya nje iliyokuwa wazi
machoni mwa wengi. Hata wafanyakazi wote wa matawini na hapa makao makuu
walikuwa na picha hiyohiyo. Kwame alipenda iendelee kuwa katika hali hiyo.
Hakupenda upande wa pili uonekane, hadi hapo baadaye
kidogo.
Katika upande huu wa pili, Kwame hakuwa
Kwame, bali alikuwa
Joe Kileo, mwakilishi wa kampuni moja kubwa ya
kijasusi kutoka nchi za Magharibi. Kampuni ambayo ilikuwa ikiendesha shughuli
nyingi za hatari katika nchi kubwa na ndogo kuhujumu tawala na uchumi ili
zielekee upande wautakao kwa manufaa yao na nchi
zao.
Shirika hilo la ujasusi, licha ya kumlipa
Kwame fedha nyingi za kigeni, ndilo lililompa mtaji mnene ambao aliutumia
kufungua kampuni hii. Haja yao haikuwa faida wala huduma kwa jamii, bali ilikuwa
kupata fursa nzuri ambayo iliwawezesha kukutana na watu wao waliojifanya watalii
kuingiza silaha, dawa hatari na vitu vingine ambavyo vilikusudiwa kutumiwa siku
za usoni.
Tayari walikuwa wamefanya mengi maovu.
Bado walikusudia kufanya mengi. Wakiwa katika kuyaandaa hayo ambayo walikusudia
kuyafanya ‘pigo la mwisho’, ndipo Kwame alipomwona kijana yule Bazile Ramadhani
akimjia ofisini kwa mwendo wa haya haya na miswada mitatu mikononi, akiomba
msaada wa kusaidiwa kuchapishiwa vitabu.
Kwame
akajitia huruma, akampa ushauri wa kuwaona wachapishaji. Kijana huyo akamweleza
jinsi alivyokata tamaa kwa wachapishaji hao. Kwame akazidi kumhurumia. Kumbe Joe
Kileo, kama alivyojulikana kwa washiriki wake, alikuwa amepata. Alifurahia sana
kimo cha kijana huyu, hasa urefu wake ulivyosadifu na kupatana na matakwa
yake.
Njama alizokuwa ameinjika zilikuwa kwenye
hatari ya kuvuja-sasa eti Muumba kamwonyesha njia. Hivyo aliwaamuru makachero
wake ambao walimfuata Bazile kwa siri hadi kwake ambako walitekeleza jukumu
walilopewa la kufanya waamini kwamba kaibiwa muswada kwa kumlaza kwa dawa zao za
kitaalamu na kuanza maongezi hayo yaliyomfanya aamini. Kisha waliingia ofisi ya
Kitenge usiku na kuiba muswada huo; ndipo yakafuata yote ambayo yalikuwa
yakiendelea kutukia. Yote ambayo yalikuwa yakizungusha kichwa au ubongo wa
Inspekta Kombora na wenzake wote kwa namna alivyokusudia kabisa
Kwame.
Jambo lingine la kutia moyo ambalo lilizuka
bila kutarajiwa katika wakati unaostahili ni lile la kujitokeza yule mwanamke
malaya, Machozi na madai yake ya ‘kumuua’ Kitenge. Hayo Kwame alikuwa
ameyasikiliza katika chombo chake kilichonasa kila maongezi yanayofanyika katika
ofisi ya Kombora.
Kwanza yalimshangaza kisha
yakamfanya acheke kwa furaha. Ilikuwa nyongeza nyingine juu ya mtafaruku
uliokuwa umepangwa kumsumbua Kombora na polisi wote wasiweze kupata walao wazo
ambalo lingewaelekeza kulikokuwa na
ukweli.
Lingine ni jinsi Kitenge alivyolewa usiku
ule hata wasipate haja ya kutumia dawa zao za kulevya. Bahati ilioje. Polisi
wangeendelea kumsaka muuaji wa bandia katika sehemu ambazo hayupo hali yeye
Kwame na kikosi chake wakiwacheka na kuendelea na harakati zao pasi ya aina
yoyote ya hofu.
Kwame alitabasamu tena,
alijipongeza kwa jinsi mambo yalivyokuwa yakimwendea kwa utaratibu na bahati
kubwa. Kisha aliitazama saa yake ya mkono, akainuka na kumpitia katibu wake
ambaye alikuwa kainamia mashine ya chapa akichapa
barua.
“Natoka kidogo,” alisema na kuendelea na
safari yake bila kusubiri jibu. Je, alielekea Kituo cha Polisi namba kumi na
mbili.
Kituoni aliomba kumwona Kombora. Alimkuta
akiwa kachakaa uso kwa mikunjo ya hasira na mshughuliko. Nusura Kwame acheke au
kumpa pole. Lakini alijifanya hajui lolote linalotokea. Badala yake alimsalimu
Kombora kirafiki na kujikaribisha juu ya kiti
kilichomwelekea.
Hawakuwa wageni kwa kila mmoja,
ingawa kazi zao zilikuwa zikiwanyima fursa ya kufahamiana zaidi. Mara mbili,
tatu wamekutana katika baa au tafrija fulani, mara kadhaa wameonana kikazi Kwame
akileta malalamiko au matakwa fulani fulani ya kampuni
yake.
Kwa Kombora, Kwame alikuwa mtu wa
kuheshimiwa, ambaye ‘amebahatika’ kupata wadhifa mnono wenye nafasi zote za
kutumia. Wadhifa ambao ulimruhusu kusafiri kokote kule nje ya nchi bila hofu ya
wanawe kulala njaa. Kinyume na yeye ambaye kazi yake ilikuwa kulinda masilahi ya
nchi na watu wengine usiku na mchana sehemu za hatari ambazo dakika yoyote
waweza kupoteza maisha. Kazi ambayo malipo hayakuwa ya kuridhisha sana kulingana
na uzito wa jukumu.
Hata hivyo, Kombora aliipenda
sana kazi yake. Aliona furaha mno kuona matajiri wa matajiri na maskini maisha
yao yakiwa mikononi mwake na kuutegemea msaada wake. Ilikuwa tamu zaidi ya
utajiri kuona baba mzima mwenye umri zaidi ya baba yake akikulilia ili umwokoe
kutokana na ‘mtu’ au ‘jambazi’ ambalo linakusudia kumuua. Wadhifa
ulioje!
“Ndiyo bwana Kwame, unaendeleaje huko Snow
Fund?”
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/-
“Vizuri
tu.”
Kwame alipoona Kombora akimtazama kwa macho
yanayomuuliza shida yake aliongeza, “Nilichofuata ni kukueleza juu ya lile suala
lililonileta majuzi.”
“Suala
la?”
“Wizi wa shilingi elfu
moja.”
“Alaa!” Kombora akakumbuka. Lilikuwa moja
kati ya masuala madogo ambayo kwa kawaida hayashughulikiwi na ofisi hii. Zaidi
ilimshangaza kuona Kwame na ukurugenzi wake aking’oka toka ofisini na kuja kutoa
ripoti juu ya wizi mdogo kama huo. Kwa nini asipige walao simu? Alikuwa
amejiuliza siku hiyo.
Hakujua kuwa ni siku hiyo
ndiyo Kwame alipoleta chombo chake kidogo chenye ukubwa wa gololi na kukipachika
kwa hila sehemu fulani kwenye meza ya Kombora. Chombo ambacho kilikuwa kikinasa
na kupeperusha maongezi yote yaliyokuwa yakifanyika katika ofisi
hii.
“Kwa kweli ndugu Kwame,
suala lako bado…”
“Ndiyo, ndiyo Inspekta,” Kwame
alikatiza. “Nilichofuata ni kukuomba ufute kesi hiyo. Nilikosea kuileta mbele
yako. Ulikuwa wizi mdogo mno. Kuufanya ufahamike itakuwa kuwatangazia
wafanyakazi wote wenye nia ya wizi kuthubutu kufanya hivyo. Watakuwa wameona
kuwa Snow Fund si imara kama wanavyodhani.”
“Siyo
vibaya ndugu Kwame. Hata hivyo endapo tutampata mwizi hatutasita kumfungulia
mashtaka.”
“Vizuri,” Kwame alijibu akiinuka. “Kwa
heri Inspekta.”
“Karibu tena bwana
Kwame.”
Nje ya kituo kicheko kingine kilimtoka
Kwame. Hata hivyo, hakukiruhusu kitoke nje. Alichekea
tumboni.
*****
USIKU huo, kama mwingine
wowote, tangu mauaji yalipoanza kutokea, jiji la Dar es Salaam na vitongoji
vyake lilifurika askari polisi na JKT ambao walikuwa makini wakilinda doria.
Kila mlinzi alikuwa na picha ya Bazile akilini na rohoni. Picha ambayo ilikuwa
imetangazwa na kusambazwa kote kwa juhudi kubwa. Walevi, wachawi, wazinzi na
wote wenye maradhi ya kutembea usiku walitaabika sana usiku
huo.
Kila mmoja alihojiwa na kutazamwa sana
akilinganishwa na picha ya Bazile. Wale ambao waliondokea kufanana naye walao
kidogo walitaabika zaidi kwa maswali ya mdomo na vitendo. Baadhi waliendelea na
safari zao baada ya kupitia vituo vya polisi.
Mtu
aliyehitajika hakuonekana. Polisi mmoja alikuwa kajibanza kwenye uchochoro wa
Mtaa wa Nkurumah. Hakuwa usingizini wala hakusikia kusinzia. Hata hivyo,
alitahamaki akipatwa na kitu kama kizunguzungu au usingizi wa ghafla.
Alipojaribu kupambana na hali hiyo alisikia kishindo kutoka kwa nyuma yake.
Pindi akigeuka alikutana na pigo la judo ambalo lilitua shingoni mwake na
kumlainisha. Akaanguka chali, silaha ikimtoka mkononi na kudakwa na jitu lenye
mavazi meusi. Jitu hilo lilimwinua na kumsogezea askari huyo uso wake
likisema:
“Natumaini
wanifahamu.”
Askari huyo hakujua ajibu nini. Uso
huo haukuwa mwingine zaidi ya ule wa Bazile Ramadhani. Uso wa mtu katili ambaye
alikuwa tayari kuua wakati wowote. Huku akitetemeka, askari huyo alijaribu
kujitetea, lakini aliambulia pigo jingine ambalo lilizidi kumlegeza
viungo.
“Naona wanifahamu,” liliongeza jitu hilo
likiutia mkono wake mfukoni na kuuchomoa ukiwa umeshikilia jisu refu ambalo
licha ya kiza kilichotanda katika uchochoro huo, lilimeremeta. “Hiki ni kisu
kilichowaua wote. Kingeweza kukuua wewe pia endapo kingehitaji. Hata hivyo
nitakuacha hai, nakuhitaji. Nataka upeleke salamu kwa rafiki yang mpendwa Mkwaju
Kombora.”
Polisi huyo hakuwahi kusikia yote.
Alikuwa hajifai kwa kutetemeka, kutetemeka ambako kulikoma na nafsi yake
kuchukuliwa na mshtuko mkubwa pindi kisu hicho kilipopita ghafla kifuani na
kuacha jeraha kubwa kwa alama ya msalaba. Maumivu hayo makali pamoja na mshtuko
vilimfanya aruke na kuanguka sakafuni ambako alitulia kwa dakika nzima kama
anayesikiliza ili afahamu kama yungali duniani au tayari kawasili kuzimu. Akiwa
katika hali hiyo alisikia kwa dhiki kubwa sauti ya jitu hilo iliyosikika
ikicheka na kisha kusema, “Mpe Kombora salamu
tafadhali.”
Fahamu zilipomrudia vyema, askari huyo
alijikuta yu peke yake, damu zikimvuja na kuiharibu sare yake. Silaha yake
ilikuwa imetupwa hatua chache kando yake. Akajitahidi kuinuka na kuiokota silaha
hiyo. Kisha alikumbuka kupuliza kipenga ambacho kiliwaleta askari wote karibu na
alipokuwa. Baada ya kuona mkasa huo, askari walijitoma mbio huku na huko
wakisaka na kusakanya kila pande ya eneo hilo. Hawakuona
chochote.
Wakati huohuo, Inspekta alikuwa
akiamshwa kutoka katika usimgizi ambao ulikuwa ndiyo kwanza anaupata baada ya
saa sita za kufanya doria jijini na baadaye kuduwaa chali kitandani akifikiri
kwa nguvu. Simu ilikuwa imemfuata nyumbani baada ya kupigwa kituoni baada ya
kuunganishwa.
“Kombora hapa, nani
mwenzangu?”
“Inspekta Kombora? Ni mimi rafiki yako
kipenzi…”
Kombora asingeweza kuisahau sauti hii.
Ilikuwa ya yuleyule adui yake mkubwa katika orodha ya maadui zake wote walioko
hai. Hakupenda kuisikia sauti hii. Lakini bado pia alipenda kuisikia ili ajue
lipi mwendawazimu huyu alikusudia kutenda.
“…wako.
Nimeona nikufahamishe mwenyewe kuwa nimekutumia salamu za upendo kwa mkono kwa
mmoja wa askari zako. Utafurahi sana kumwona Inspekta. Anavutia kwa rangi
nyekundu na kidani cha aina yake alichovaa
kifuani.”
Kombora hakuwa na hamu ya kuendelea
kusikiliza sauti hiyo. Sauti ambayo sasa ilikuwa ikisikika masikioni mwake kama
mwito wa mauti yenyewe utokao kuzimu moja kwa moja. Hata hivyo, aliendelea
kusikiliza. Haja haikuwa kumsikia bali kuwapa fursa makachero wake ili waifuate
simu. Alikwishatoa siri ya simu baina yake na muuaji huyo na kuweka wataalamu
tayari kujua simu inatoka wapi na kuwaashiria vijana ambao waliandaliwa kutoa
ishara kwa askari wa doria katika eneo hilo ambao waliruhusiwa kuua chochote
watakachokikuta kikipiga simu hiyo. Uzoefu wake kikazi ulimfanya Kombora ajue
kwamba vijana hao walikuwa kazini wakisikiliza simu hiyo a kutimiza wajibu
wao.
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Inspekta?”
“Nipo.”
“Mbona
kimya rafiki yangu?”
“Hujajibu
chochote.”
“Juu ya
nini?”
“Salamu zangu. Zaidi ya salamu ni kwamba
najisikia kuua mtu mwingine. Unasemaje?”
“Unataka
nisemeje? Nikupigie magoti kukusihi usiue? Niwezalo kusema ni ukae ukijua kuwa
nitakutia mbaroni. Na utajuta kuzaliwa. Pamoja na hayo, bado nakushauri kuwa
ujitokeze mwenyewe. Upo uwezekano wa kukusamehe,” Kombora alimaliza huku
akijiuliza kama hajavuka kiwango kiasi cha kumtoa mtu huyo kwenye simu mapema
kabla watu wake hawajamfikia.
“Inspekta! Mbona
maelezo mengi mno?”
“Siyo mengi, ningeweza kueleza
mengi zaidi…”
“Inspekta. Uko peke yako kwenye
simu?” alidakia mtu huyo.
“Ndiyo. Nitakuwa na nani
tena?”
“Uongo. Unajaribu kupata nilipo kwa simu.
Hongera kwa juhudi zako na pole kwa kazi yako isiyo na
matunda.”
“Sivyo…sikia…” ilikuwa kazi bure.
Kicheko kilisikika upande wa pili kikifuatwa na kukatwa simu. Kilichobaki katika
masikio ya Kombora ni kicheko ambacho kilitisha na kuchukiza mfano wa kicheko
cha mauti
yenyewe.
*****
HABARI
mbaya husafiri haraka sana kuliko habari njema. Hii ya mauaji ilienea haraka
mara mbili zaidi ya kawaida. Licha ya picha ile ambayo ilitokea magazetini na
maandishi ya waandishi ambayo yalieleza kwa ufupi chini ya vichwa vya habari:
“MUUAJI HATARI AZUKA JIJINI” na la Kiingereza lililodai “THE MURDERER STILL AT
LARGE”, bado kuna mengi yaliyosemwa baina ya mtu na mtu mitaani. Huyu alisema
hivi na yule akaongezea lake ikawa habari pana ya kutisha kuliko
ilivyokuwa.
Kama watu wengine, Joram Kiango akiwa
mkazi wa jijini Dar es Salaam, alipokea habari hiyo kwa njia zote. Aliwasikiliza
wambeya wa mitaani, akayasoma magazeti yote na kisha kuulizia vizuri kwa
miongoni mwa rafiki zake walioko katika Jeshi la Polisi. Baada ya kuipata
kikamilifu na kuona jinsi polisi walivyokuwa wakitapatapa katika hali ya kukata
tamaa, alitabasamu.
Kwa Joram, tabasamu hili
halikuwa la furaha ya kusikia watu wasio na hatia wanateketea pasi sababu,
hasha. Kwake, tabasamu hili huwa dalili ya shauku. Shauku kubwa ambayo humjia na
kumteka kikamilifu kila litokeapo tukio la kutisha na kusikitisha kama hili
ambalo huhitaji mtu shujaa kulitatua. Moja kwa moja Joram hujihisi kama mtu huyo
na kujitupa katika duru la mapambano kwa mbinu zake ambazo humfanya aponee
chupuchupu, huku katatua au kuweka hadharani siri za hatari ambazo polisi huwa
wamefikia hatua ya kukata tamaa.
Hakuna asiyemjua
Joram Kiango. Ni yule kijana mrefu, mwenye maungo yenye nguvu na sura nzuri
ambaye wakati wote huwa mchangamfu. Yule kijana mwenye ofisi yake inayoitwa
Private Investigator ambayo hushughulikia upelelezi wa aina mbalimbali toka kwa
wateja ambao huwa kampuni au mashirika yenye haja ya kujua jambo fulani, watu
binafsi wanaohitaji kutatuliwa hili na lile na yeye anapojisikia haja au njaa ya
kusaidia polisi katika shughuli zao za kila
siku.
Kijana huyu mwenye umri usiozidi miaka
ishirini na sita ni juzi tu aliporejea kutoka Marekani ambako alikuwa akiishi na
wazazi wake wanaoishi huko. Ni huko ambako Joram alipata moyo wa kishujaa baada
ya kukua miongoni mwa watoto weusi na kuona walivyokuwa wakinyanyaswa na wenzao
weupe.
Ingawa alipata elimu nzuri lakini mara
baada ya elimu hiyo alijiunga na vikundi vya wahuni weusi waliokuwa wakisumbua
sana Jeshi la Polisi. Waliiba na kupigana wakiharibu na kusumbua katika maduka
na benki. Baada ya hapo Joram alijiunga na CID na kufanya kazi nzuri, lakini
ghafla akaacha kazi baada ya kujiona kakamilika kimwili, kifikra na
kimtazamo.
Ndipo akaja Dar es Salaam ambako
alifanya mengi, yaliyoipendeza polisi kabla hajapatiwa kibali cha kufungua ofisi
hii.
Machache kati ya aliyoyafanya yaliwavuta waandishi hata
wakayaandikia vitabu na kuviita DIMBWI LA DAMU na LAZIMA
UFE…
Alitabasamu tena akalitupa gazeti na
kumtazama Neema Idd katibu wake ambaye pia alikuwa
akimtazama.
“Unajua
Neema…”
“Usiniambie. Najua kila kitu. Macho yako
yanaonyesha kuwa unataka kujiingiza katika mambo haya. Sijui umelogwa mwenzangu.
Labda hukusikia juu ya yule polisi aliyepewa salamu za kumpa Kombora?” Neema
alimaliza.
“Yule bwege? Mtu una bunduki mkononi
kama siyo uzembe ni nini hata mtu mwenye kisu akuchanje kifuani?” Joram alijibu
akicheka.
“Siyo kuchanjwa Joram! Amejeruhiwa
vibaya sana.”
“Pamoja na hayo,” kisha sauti ya
Joram ikabadilika na mzaha ukatoweka kabisa. “Jambo linalonishangaza katika
suala hili ni huyu mwandishi Bazile! Imekuwaje akawa hodari ghafla kiasi
hiki?
Vipi awe mjanja wa kuepuka mitego yote ya
polisi, shujaa kiasi cha kumkabili polisi mwenye silaha na kumpa salamu za
jeraha kifuani na wakati huohuo akimdhihaki mkuu wa polisi kwa simu za kashfa
mara kwa mara? Hamu yangu ni kujua alivyopata uwezo huo kwanza, kisha nitajua
namna ya kumtia mikononi.”
“Yaani umeshaanza
kazi?”
“Bila shaka. Sina haki ya kustarehe hali
mtu yuko hai na ameahidi kumwaga damu nyingine zisizo na hatia. La, Joram Kiango
si mvivu kiasi hicho mama.”
Neema hakuwa na la
zaidi. Kwa kadri anavyomfahamu, Joram kamwe hatastarehe tena, tayari kazama
kichwa na miguu katika dimbwi la mkasa huo. Kumshauri kusingesaidia. Hata hivyo
alimwambia neno lilelile ambalo amemwambia mara
nyingi:
“Angalia Joram.
Jihadhari.”
“Hakuna anayemfahamu Joram Kiango
zaidi yako Neema. Ninayo nafasi nzuri ya kumtia muuaji mkononi kwani kama
ujuavyo, adui huyo kajizatiti kukabiliana na jeshi la polisi, hana habari ya mtu
mmoja anayejiita Joram. Huoni kama hiyo ni nafasi nzuri ya kumfumania?”
alimalizia akiwasha sigara na kuanza kuivuta kwa
utulivu.
Katika utulivu huo, alikuwa akipambana
vikali na tamaa ambayo ilikuwa ikimshawishi ainuke na kuanza uchunguzi juu ya
mkasa huo. Tamaa ambayo aliishinda nguvu baada ya kujikumbusha tena na tena kuwa
alikuwa hajajiandaa kikamilifu kuweza kusimama kiume dhidi ya muuaji au mauaji
mazito kama hayo, mauaji ambayo sasa yalikuwa yamewashinda polisi
kuyakabili.
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kujitumbukiza kiholela ingekuwa sawa na kumwalika muuaji ampe yeye Joram salamu ambazo safari hii zingeelekezwa si kwa Kombora bali ahera. Naye Joram hakuwa tayari kwenda huko mapema kiasi hiki.
Kujitumbukiza kiholela ingekuwa sawa na kumwalika muuaji ampe yeye Joram salamu ambazo safari hii zingeelekezwa si kwa Kombora bali ahera. Naye Joram hakuwa tayari kwenda huko mapema kiasi hiki.
Hivyo alijituliza akiwaza
yapi ameyafahamu tayari dhidi ya muuaji huyo, mangapi polisi imefanya katika
juhudi zao za kumtia mbaroni, kiasi gani wamefanikiwa na vipi wamefeli.
Kadhalika alihitaji kujua mangapi yanafahamika juu ya marehemu, mangapi
hayafahamiki na yapi yalistahili
kufahamika.
Baada ya kuyafahamu hayo, yeye kama
Joram Kiango angekuwa tayari kufuata njia zake ambazo zingemfikisha hadi
kisogoni au usoni pa muuaji huyo. Joram, angependa zaidi kukutana naye uso kwa
uso, aupime na kuushuhudia kwa macho yake ujabali wa mtu huyo aliyeondokea kuwa
jitu kwa muda mfupi tu.
Akiwa na uhakika na mbinu
zake, pamoja na matumaini juu ya njia atakazopitia ambazo ni kinyume na zile za
polisi, alijisikia furaha kana kwamba tayari kamtia adui huyo mikononi mwa
sheria. Akaitupa sigara yake katika kasha la taka na kutoka nje akipiga
mluzi.
*****JORAM KAAMUA KUINGIA KAZINI KUMSAKA
HUYU ANAYETUMA SALAMU ZA MAUAJI. NI KIPI KITAFUATA? FUATILIA RIWAYA HII
KALI
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment