IMEANDIKWA NA : BEN R. MTOBWA
*********************************************************************************
Sehemu Ya Kwanza
(1)
POLISI…kikosi cha
kumi na mbili…Inspekta Kombora anaongea. Nani
mwenzangu?”
Kwa muda kukawa kimya. Kombora
alisikiliza kupumua kwa dalili ya hofu katika chombo cha simu kutoka upande wa
pili. “Nani mwenzangu?” akaongeza nguvu
kidogo.
“Ni Kombora mwenyewe anayeongea?” iliuliza
sauti hiyo yenye wasiwasi kutoka upande wa
pili.
“Ni mimi, nani
mwenzangu?”
“Ndiye! Mkuu wa kituo hicho
sio?”
“Ndiye,
tu…”
“Sikiliza Inspekta,” sauti ilidakia na
kunong’ona harakaharaka, “Nina tatizo zito sana. Sijui kama utaweza
kunisaidia.”
“Nadhani tunaweza. Tutajie tatizo
lako na jina lako ili tujadiliane.”
“Jina sitaji,”
iliongeza sauti hiyo, “Na tatizo lenyewe ni zito sana, siyo mzaha. Najisikia
kuua mtu Inspekta. Najisikia kuua. Na ni lazima niue. Waweza kunisaidia
Inspekta?”
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kuua!” Kombora
aliropoka. Katika matatizo yote, hilo kamwe hakulitegemea. Ni rahisi mtu kupiga
simu polisi na kusema “mtu anataka kuniua.” Ni rahisi pia mtu kudai “nilimwona
fulani akiua” lakini “nataka kuua” lilikuwa jipya kwa Inspekta
Kombora.
Angeweza kulichukulia suala hilo kwa
mzaha; kwamba ni chizi au mlevi mmoja ambaye ameamua kuwasisimua polisi lakini
uchizi au ulevi haukuwemo kabisa katika sauti hiyo. Ilikuwa sauti dhaifu
iliyojua kipi inasema. Kwa muda Kombora aliduwaa akiwa hajua lipi amjibu mtu
huyo.
“Upo Inspekta?” ilihoji
sauti.
“Nipo ndugu yangu,” Kombora alijibu kwa
unyonge.
“Mbona kimya? Huna msaada
wowote?”
“Ninao. Sikia rafiki yangu, njoo zako
hapa mara moja ili tukae na kulijadili tatizo. Naamini
tutakusaidia.”
“Hilo sifanyi Inspekta. Nikija huna
uwezalo kufanya zaidi ya kunitia ndani, na mimi nauhitaji uhuru wangu. Kama huna
msaada mwingine…”
“Ninao. Ni hivi, u nani jina
lako?...Uko wapi?...Na unayetaka kumuua ni nani…Kwa
nini?...Haloo!...Haloo!...”
Haikumchukua muda
Kombora kung’amua kuwa alikuwa akizungumza katika simu iliyokatwa. Kwa muda
aliendel;ea kuduwaa, simu mkononi, macho kayakodoa kutazama ukuta uliokuwa mbele
yake, akiwaza mengi. Kisha alitua simu na kuinuka. Mara akakumbuka kuwa hakujua
anakotaka kwenda. Akaketi na kutikisa kichwa kwa wingi wa mawazo mazito
yaliyomjaa
ghafla.
********
KITENGE
alizinduka kutoka usingizini kwa kugutuka kidogo. Hakujua kilichomwamsha ghafla
hivyo. Akatazama huku na huko kama anayejaribu kutafuta kitu hicho kilichomfanya
auache usingizi wake ambao haukuwa na ndoto
yoyote.
Mara mlango ukagongwa tena, ndipo
alipokumbuka kuwa kilichomwamsha ni mlio wa mlngo huo. Kwa dalili za uchovu
aliinuka kutoka kitandani na kuvuta taulo iliyokuwa juu ya kiti, akaitanda
kiunoni, kisha aliuendea mlango na
kuufungua.
Mlango huu ulimfikisha ukumbini ambapo
alipita kuuendea mlango mkubwa, macho yake yakiipitia saa ya ukutani ambayo
ilidai kuwa ni saa kumi na mbili kasoro dakika nne, jambo ambalo lilimshangaza
mno, kuona ugeni wa alfajiri kama hiyo.
Alifungua
mlango; aliyesimama hapo nje alikuwa ni mwanamke ambaye Kitenge, baada ya
kumtazama kwa muda, alimkumbuka. Alikuwa ni Machozi Rashidi. Mwanamke ambaye
alipokuwa msichana waliishi jirani na Kitenge wakihusiana kwa njia mbalimbali
katika harakati za maisha baina ya wasichana na
wavulana.
Kitenge hakujua kama ilimpasa
kumkaribisha au la. Kwa kila hali huyu hakuwa yule Machozi ambaye Kitenge
alimfahamu wakati ule. Huyu, wakati ulikuwa umemwathiri sana na kumtenga mno na
Kitenge kiasi cha kumfanya aionee aibu kila dakika ambayo aliendelea kusimama
naye hapo mlangoni.
Hakuwa mwanamke wa haja hata
kidogo. Kama aliwahi kuwa mzuri, Kitenge hakuiona dalili yoyote ya uzuri
iliyosalia katika sura hiyo. Sasa ilikuwa sura kavu, yenye mikwaruzo mingi,
macho mekundu kwa athari ya kitu kama gongo au bangi, nywele nyekundu, kavu
zenye dalili zote za kutoonja aina yoyote ya mafuta. na mwili mzima ulikuwa na
mikwaruzo juu ya ngozi hiyo kavu na ilikuwa dhahiri kuwa mwanamke huyu aliishi
kwenye mazingira yasiyofaa. Ngozi hiyo ilifunikwa na mavazi hafifu ambayo pamoja
na kuwa dhaifu yalikuwa yamechanika hapa na
pale.
“Haunikaribishi Boni?” aliuliza mwanamke
huyo. Sauti yake pia ilikuwa tishio jingine, haikuwa ya mwanamke hata kidogo,
wala haikumfaa mwanamume. Boni lilikuwa jina la utotoni la Kitenge ambalo sasa
lilikuwa limetoweka kabisa baada ya majina mengine kuibuka, majina ambayo
yalifungamana na hadhi yake mpya. Kwani sasa Boni alikuwa mwandishi maarufu wa
vitabu.
Ghafla jina hilo likamkumbusha uhusiano
wa kimapenzi aliokuwanao awali na kiumbe
huyu.
“Ingia,”
alimwambia.
Mwanamke huyo aliingia ndani na
kufuata moja ya makochi sita yaliyopangwa kistaarabu katika ukumbi huo.
Alitazama kila upande akihusudu hiki na kuvutiwa na kile. Kisha akamtupia
Kitenge macho yake mabaya. “Hongera,” akakoroma kwa sauti hiyo ya
kuchukiza.
“Kwa?”
“Vitabu
vyako. Hukujua kuwa hata sisi washamba ambao hatukusoma tungeweza kuviona?
Ulidhani kuwa tusingeona hata picha nyuma ya vitabu hivyo? Ama hujui kuwa hata
redioni vinaongelewa? Pamoja na hayo, ningependa kukujulisha kuwa ingawa
sikusoma sana, naweza kuelewa waandishi wanasema nini katika magazeti yao.
Karibu wote wanakusifu. Hongera tena
Boni.”
Kitenge hakujua kwamba ilimpasa kufurahi au
kuchukia kwa sifa hizo. Kusifiwa halikuwa jambo geni kwake. Tangu alipotoa
kitabu chake cha kwanza, MACHOZI YA DAMU, kupata sifa lilikuwa jambo la kawaida.
Kitabu cha pili, KIFO USONI, kilimzidishia sifa kemkem, cha tatu na ambacho ni
kama cha mwisho katika vitabu vilivyokwishatolewa; ALIKUFA ANACHEKA, kilifanya
sifa zitapakae pembe zote kiasi cha kumtia katika mashaka ya kukosa nafasi ya
kufikiria vitabu vingine.
Kila alikopita
aliandamwa na ‘hongera’, yeyote aliyemfahamu alimtupia tabasamu. Waandishi wa
habari walimtaka picha na mahojiano mara kwa mara. Katika baa moja aliwahi kuona
maandishi yanayosema ‘Kondokondo Kitenge zaidi…’ na kadhalika. Hata katika basi
ilikuwa ni jambo la kawaida kukuta kikundi cha watu kikizijadili sifa
zake.
Naam, kusifiwa kwake sasa lilikuwa jambo la
kawaida. Lakini sifa hizi za alfajiri, kutoka kwa mama huyu ‘aliyechoka’ kwa
sauti yake ambayo licha ya kuchakaa, ilidhihirisha kitu kama kebehi, unafiki au
uadui katika sifa hizo, zilimfanya ghafla ahisi jambo lisilo la kawaida katika
nafsi yake. Wasiwasi ukamwingia rohoni. Wasiwasi ambao nafsi yake ilipokonywa na
hasira, akajikaza kisabuni kumtazama mama huyo huku akisema, “ Nadhani hukuja
asubuhi yote hii kwa ajili ya kunisifu. Niwie radhi, kama huna zaidi, nenda zako
ili nijiandae kwenda zangu kazini.”
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Machozi akacheka.
Kicheko chake kilikuwa kitu kingine cha kutisha, na kilikuwa mbali kabisa na
kicheko cha mwanamke, na karibu zaidi na kile cha
shetani.
“Nilitegemea hutasema hayo,” alisema.
“Najua umekuwa mtu mkubwa na tajiri sasa. Umetoa nakala elfu ngapi hadi sasa?
Haikosi una akiba ya milioni benki. Mungu akujalie,” akacheka tena. Bila
kusubiri jibu la Kitenge, aliongeza, “Ndiyo nimekuja kukusifu, kwani hukumbuki
kuwa mimi ni mpenzi wako? Hukumbuki kuwa uliniahidi kuwa bila mimi usingeishi?
Kwamba lazima tungeoana tu. Hukumbuki?”
Kitenge
aliduwaa, hakujua mwanamke huyu anaelekea wapi katika maongezi hayo. Hivyo
akaamua kunyamaza
akimtazama.
Baada ya kicheko
kingine Machozi aliongeza, “Nimekuja mpenzi, nimekuja kukukumbusha ahadi hiyo,
kama umesahau. Nyumba yako hii nimeitafuta mwaka mzima, leo ndiyo nimeipata.
Nimefika nyumbani, kwa hiyo wewe nenda zako kazini utanikuta mkeo nimekuandalia
kila kitu. Au ulianza kusahau mapenzi yetu hadi ukaoa mke
mwingine?”
Bado Kitenge aliamini Machozi alikuwa
akimkebehi, hakuwa amesema alilokusudia. Hata hivyo tayari alianza kupandwa na
hasira, huku akiificha hasira hiyo katika sauti yake alisema, “Sikia Machozi,
mimi sina muda wa kupoteza. Kama umechanganyikiwa nenda mahala ukazungumze yote
unayotaka kuzungumza. Hapa sipo kabisa. Sasa inuka utoke
zako.”
“Kweli mpenzi tuseme umesahau ahadi zako
zote?”
“Toka…”
“….
umesahau barua zako tamu…”
“…uende zako
haraka!”
“….zenye kila neno la mapenzi na ahadi za
kuishi pamoja?”
“Nasema
toka!”
“Pamoja na jinsi nilivyokupenda nikajitoa
kwako mwili na roho? Umesahau kweli mara hii?
Siamini!”
Ana wazimu mwanamke huyu? Kitenge
alijiuliza. Mapenzi!
Mapenzi gani hayo ambayo hakumbuki? Kwa kadri ya
kumbukumbu zake, neno ‘nakupenda’ wakati huo lilikuwa moja ya michezo ya kawaida
mongoni mwa watoto. Angeweza kumwambia yeyote wakati wowote ‘wewe ni wangu wa
heri na shari,’ kadhalika angeweza kusikiliza jibu lolote la msichana yeyote na
kumwamini.
Halikuwa jambo la ajabu mtu kumwambia
mtu ‘nikila sishibi kwa ajili yako’ au ‘usiku silali’. Karibu kila mvulana
alikuwa na faili kubwa la barua za mapenzi. Barua hizo zilikuwa zikiandikwa kwa
ufundi au kunakiliwa kutoka vitabuni huku zikiwa zimenakshiwa kwa maua ya
kuvutia pamoja na kupambwa kwa harufu ya poda. Machozi alikuwa na akili gani
hadi leo hii kuendelea kuamini mambo kama
hayo?
Mchezo wa mapenzi, vichakani na hata
nyumbani ni jambo lililokuwa la kawaida pia. Ingawa Kitenge hakuwa mpenzi sana
wa mchezo huo, lakini Machozi alikuwa mmoja tu katika orodha ndefu ya wasichana
aliowahi kufanya nao mapenzi.
Yalitokea,
yakatoweka. Yeye Kitenge baada ya kufaulu darasa la saba, akiwa mtoto pekee
aliyetoka katika kijiji hicho cha Mayange, wilayani Kasulu, alijibidiisha zaidi
katika masomo yake. Kila aliporudi likizo wasichana wote walimlaki kwa furaha na
kuridhia lolote alilotaka; Machozi akiwa
mmojawao.
Alipohitimu kidato cha sita na kupata
kazi hapa Dar es Salaam, alikata mguu kijijini hapo. Hakuwa na muda wa kutosha
kumfikisha huko mara kwa mara kutokana na shida ya usafiri. Huu ulikuwa mwaka
wake wa sita tangu alipofika huko kwa mara ya mwisho. Likizo ya mwaka huu
alikuwa akijiandaa au kutarajia kuwa angeenda. Katika mapya na mageni yote
aliyotarajia kuyakuta huko nyumbani, hili hakulitarajia
kabisa.
“Unatoka katika nyumba hii au hutoki?”
aliuliza ghafla.
Machozi hakumjibu haraka.
Alitazama huku na huko kisha akasema, “Nikisema sitoki nadhani utaniitia mgambo.
Vizuri sana. Sasa nitasema dhamira ya safari yangu hii; ilikuwa ni kukupa
hongera, ndiyo, lakini si hongera ya mafanikio ya kuandika kwako vitabu. Ni
hongera kwa kufanikiwa kwako kuniharibia maisha yangu. Kwa kunidanganya hata
nikadanganyika na kuamini kuwa ulikuwa wanipenda kumbe la. Haukuishia hapo,
ukanijaza mimba na kisha ukaikana. Hongera sana
Boni.”
Ndipo Kitenge alipokumbuka kuwa aliwahi
kupata barua moja kutoka kwa baba au mmoja wa wadogo zake ambaye alidai kuwa
amemtia mimba msichana mmoja. Ati aende akamuoe! Wakati huo, Kitenge alikuwa
ndiyo kwanza anaanza kazi. Wazo la kuoa, na hasa kumuoa mtu kama huyo, lilikuwa
nje ya ratiba yake a maisha. Hivyo suala hilo alilipuuza. Hakumbuki kuwa aliwahi
kujibu barua hiyo. Kumbe ilikuwa kweli? Yaweza kuwa kweli?
Alijiuliza.
“Nikikuruhusu kusema utaanza kuikana
mimba hiyo. Waweza hata kudai kuwa hukuwahi kufanya nami mapenzi japo ni wewe
uliyeniharibia ubikira. Napenda kukufahamisha kuwa mwanao alikuwa msichana.
Nilimtupa katika mapipa ya takataka za hospitali ya Maweni. Kama walimwokota
akiwa hai au maiti, sijui. Sikujali. Najua na wewe hujali wala usingejali.”
Machozi akanyamaza akimtazama Kitenge kuona hadithi yake ilimwingia
vyema.
Alipomwona akitoa macho ya mshangao
aliongeza: “Usiseme unasikitika, najua una moyo wa jiwe kama mimi. Ingawa mimi
sikuzaliwa na moyo huo, nimeupata ukubwani kwa haki kabisa ingawa nikiiambia
hivyo jamii haitanielewa.”
Akasita kidogo na
kuendelea, “Ninachotaka kueleza ni taabu niliyoipitia baada ya kumtupa mtoto
huyo. Njaa ilinifanya niangukie mikononi mwa mwanamume mwingine. Huyu, tangu
awali nilijua ananilaghai, lakini sikuwa na njia ya kumzuia asinitie mimba
nyingine. Alipogundua nina mimba aliniepuka, ikabidi niteseke sana kutunza mimba
hiyo bila mafanikio. Mwisho, niliamua kumeza dawa za kuitoa. Ilitoka kwa taabu,
nami niliponea chupuchupu. Nilipopata nafuu zawadi yangu ilikuwa kifungo cha
miaka mitatu.
“Majuzi tu ndiyo nimetoka jela.
Maisha yangu yamekuwa mpira usio na thamani. Unaochezwa na kila mwanaume
atakaye. Nadhalilishwa, naonewa na kufanywa kiumbe duni asiye na haki ya kuwa
hai. Yote hayo ni kwa ajili yako Boni. Ni wewe uliyenivuta katika mkondo huu
ukahakikisha siwezi kutoka.”
“Mimi!” Kitenge
aliropoka akiwa hajui la kufanya.
“Wewe!” Machozi
alijibu. Sauti yake haikuwa ya kebehi tena, wala haikujali kuweka furaha ya
kinafiki. Ilikuwa wazi ikitangaza kulipiza kisasi na
uadui.
“Wewe!” aliongeza, “Na nilichokuja
kukuambia si kukuomba unioe au unipe pesa za kutumia, la. Nimekuja kukuambia
kuwa nakuchukia. Ninakuchukia kama ninavyomchukia shetani. Sasa hivi, mimi ni
kama maiti ambaye hajaanza kunuka tu. Sina mbele wala nyuma. Lakini kabla
sijaoza nitahakikisha na wewe unalipa gharama za madhambi yako. Lazima twende
wote ahera Mungu akatuamulie nani mwenye haki. Nitakuua Boni. Tena kwa mkono
wangu huu!” Aliutikisa mkono huo huku akiinuka na kuanza
kutoka.
Mlangoni aligeuka na kuanza kumtazama
Kitenge. “Kwa heri,” alisema, Tutakapoonana tena, ujue ndiyo mwisho wa uhai
wako.” Akatoka na kutoweka.
Kitenge alibaki akiduwaa juu ya kiti
chake. Aliyemzindua ni mama mwenye nyumba, kikongwe ambaye huwa hapitwi na neno
lolote humo au nyumba za jirani. Alibisha hodi na kusimama
mlangoni.
“Baba, mwanamke huyo ni nani?”
aliuliza.
“Simfahamu. Nadhani ni mwendawazimu,”
Kitenge alilaghai akiinuka na kuelekea bafuni.
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Anasema
anakufahamu.... jihadhari baba,” sauti ya Bi mkubwa huyo
ilimfuata.
Hakujishughulisha
kumjibu.
*****
ASUBUHI
hiyo, Kitenge alikuwa mtu wa kwanza kuwasili ofisini. Milango yote ilikuwa
imefungwa. Akatumia funguo zake za akiba kufungua na kuingia hadi katika ofisi
yake. Alikuwa na maandishi yaliyochorwa kisanii kabisa, juu ya kipande cha ubao
kilichowekwa juu ya meza yake yaliyosema, KONDOKONDO KITENGE, MANAGING
DIRECTOR-BLACK POWER PUBLISHERS. Zamani maandishi haya yalikuwa yakimvutia sana
na aliyatazama mara kwa mara. Si sasa ambapo aliweza kushinda ofisini humo macho
yake yalitazama na kuona kila kitu isipokuwa maandishi
hayo.
Hii ilikuwa ofisi yake. Ofisi ya kampuni
ambayo alikuwa ameianzisha miaka miwili iliyopita, kushughulikia vitabu vyake na
vya wandishi wengine ambavyo vilionekana vyafaa. Wazo la kuanzisha kampuni hii
lilikuwa limemjia baada ya kuona alivyowatajirisha wachapishaji wake wa awali,
huku yeye akimegewa kidogo kutoka katika faida hiyo kubwa, wakati huohuo
wakichelewesha uchapishaji wa vitabu vyake bila sababu ya
kuridhisha.
Kitabu chake cha kwanza ambacho
alikiandika akiwa shuleni kilikuwa kimesubiri miaka minne ndipo kikatolewa. Cha
pili kiliwahi sana, miaka miwili! Tangu alipoanzisha kampuni hii mambo yalianza
kumwendea vyema, ingawa yapo matatizo kadhaa yaliyomkwamisha hapa na pale.
Alifurahi kupambana nayo mwenyewe badala ya mtu mwingine
kumpigania.
Tatizo kubwa ambalo lilimtisha ni lile
la kuona kama aliyeelekea kuishiwa na ule uwezo wake wa uandishi. Tangu
alipobeba mzigo huo wa Ukurugenzi Utendaji, mtiririko wa mawazo yake ulipungua
kasi. Na alipojikongoja hadi kumaliza kitabu washauri wake walidai kuwa hakifai
kutolewa. Kwamba kingemvunjia hadhi yake. Ati mambo mengi yalikuwa marudio ya
vitabu vya waandishi wengine, hasa wa
magharibi.
Jambo hilo lilimtia hofu sana, kuona
akielekea katika hatari ya kuishia vitabu vitatu tu ilhali alidhamiria kutoa
vitabu vingi kama kina James Hadley Chase, Shabani Robert, Ngugi wa Thiong’o na
wengi wengine. Aibu ilioje! Mara kadhaa alijiuliza kama alitumia busara kuamua
kuwa mchapishaji badala ya kuacha wachapishaji wake waendelee kushughulikia
miswada yake, yeye akishughulikia mawazo
mapya.
Akiwaza hayo Kitenge alikuwa ameketi juu ya
kiti chake, hafahamu wala hajaamua lipi aanze katika shughuli nyingi alizoacha
jana. Kulikuwa na mengi ya kufanya. Kuna ule muswada wa kusoma, miswada miwili
ya kusahihisha lugha, mmoja wa kumrudishia mtunzi afanye marekebisho, madai ya
fedha katika maduka ya vitabu, kuwasukuma wachapaji waliokwamisha vitabu viwili
vya hadithi za watoto na kadhalika. Mengi. Hakujua lipi aanze kushughulikia na
lipi liahirishwe tena.
Mara, mawazo yake
yakaikumbuka tena ziara ya alfajiri ya yule mwanamke, Machozi. Ana nini? Wazimu
au upungufu wa akili? Madai yake yana ukweli kiasi gani? Na hata kama yana
ukweli wowote, si yamhitaji mtu mwendawazimu sana kuyafuatilia madai ya aina
hiyo! Ati ulinitia mimba miaka mingapi iliyopita, kwa hiyo tangu leo mimi mkeo!
Ati nitakuua kwa kuwa ni wewe uliyeniharibia maisha
yangu!
Wazimu ulioje! Kitenge akaangua kicheko.
Hakujua kama alikuwa akimcheka Machozi alivyochakaa au madai yake
yasiyokubalika.
*****
KAMA
kawaida Rusia alikuwa katika moja ya mavazi yake ya thamani zaidi ya mshahara
wake, nywele kazitia mafuta au madawa yaliyozifanya zifanane na za Kizungu, kama
si chotara. Ni sura yake tu ambayo Kitenge aliona hairidhishi. Hakumbuki kwa
nini alimwajiri mtu mwenye sura kama hiyo kuwa karani wake mahususi.
Kilichomshangaza ni wale watu wakubwa ambao huja mara kwa mara na magari yao
kumchukua msichana huyu kwa chakula cha
mchana.
Hakujua nini wanaona cha haja katika sura
hii. Hawaioni kasoro yoyote? Wakati mwingine alijiona pengine ni yeye mwenye
kasoro. Kwani hajawahi kumpenda msichana yeyote kwa dhati. Wote aliotembea nao,
na anaotamani kutembea nao, huwatoa kasoro kemkem. Jambo ambalo limemfanya hadi
leo hii kutokuwa na mke.
“Naona unaendelea
kucheka, vipi? Au tayari umepata hadithi mpya kichwani? Najua wewe huridhishwi
na chochote zaidi ya hadithi,” Rusia
aliendelea.
Mara wazo likamwingia Kitenge; kweli!
Tukio la leo asubuhi baina yake na Machozi ni hadithi nzuri sana! Hadithi ya
mapenzi! Mapenzi ambayo yatageuka kuwa chuki. Hata jina la riwaya sasa lilielea
kichwani mwake. Ataiita MAPENZI HUCHUJA. Naam, itakuwa hadithi nzuri. Mwisho?
Akajiuliza. Uweje mwisho wake? Machozi alipendekeza mauaji, yeye ataangalia
mwisho wa kuridhisha. Akacheka tena.
Safari hii
kicheko kilimtia Rusia mashaka. “Mwenzangu! Nadhani tumwite daktari. Tangu
nilipoingia husemi lolote, hufanyi lolote zaidi ya kucheka. Sema tumwite kama
unaona mambo si ya kawaida,” alisisitiza bila mzaha
wowote.
“Usiwe juha we mwanamke,” Kitenge alimjibu
akiukunja uso wake. “Siku nikianza wazimu itakuwa ni kwa hasira si furaha. Na
katika ofisi hii hatatoka mtu. Nitavunjavunja kila kitu na kila mtu, huyo
daktari atakayenisogelea ataadhirika.”
Wote
wakacheka.
“Basi tuombe Mungu
isitokee.”
“Wala haitokei. Hata shetani ni mwoga,
anaangalia wapi aelekeze pepo wake mchafu.”
Baada
ya maongezi hayo walizama katika shughuli zao. Kitenge alikuwa hajafanya lolote
mhudumu alipomtaka radhi ili afagie. Akaamua kutoka nje kabisa. Ofisi yao ambayo
ilikuwa katika Mtaa wa Samora, haikuwa mbali sana na Hoteli ya Salamander.
Kitenge alivuka huku akiendelea kuitayarisha hadithi yake mpya kichwani. Akataka
kuiandika mara moja, lakini roho nyingine ikamzuia na kumshauri aitafiti vyema
na kuipamba kabla hajaitia katika maandishi.
Aliporejea ofisini, Rusia
alimtambulisha kwa mgeni ambaye hakuwa mgeni sana machoni mwa
Kitenge.
“Bwana Bazile Ramadhani, mwenye ule muswada ambao bado
tunautafuta. Nimemwambia aje kesho, lakini mwenyewe anadai anataka kuzungumza na
wewe.”
Kitenge akaukumbuka muswada huo, ulikuwa
mmoja kati ya ile miswada ambayo huwezi kuitilia maanani. Ulikusudiwa kuwa
hadithi ya upelelezi, lakini ilivyoandikwa si hadithi ya upelelezi, isipokuwa
mtiririko wa mauaji ya kikatili yanayotokea bila sababu za kuridhisha. Muswada
huo ulimfanya Kitenge kumfikiria mwandishi kama mtu mwenye hasira dhidi ya
ulimwengu wote, mtu atakayefurahi sana endapo lolote lingetukia kuharibvu dunia
na vyote vilivyomo.
Ni kama mtu ambaye alidhani
au kuamini maisha yanamwonea na binadamu wote wanamchukia, hivyo akaondokea
kumchukia kila mtu ikiwa ni pamoja na yeye mwenyewe. Kwa kuwa hana silaha wala
uwezo wa kuiangamiza dunia, ndipo akaandika kitabu hicho ambacho binadamu
wanateketezwa ovyo na mhusika wake mkuu kujiua mwishoni. Sababu ya vifo vyao
haionekani, sababu ya kujiua kwake haikutajwa. Nje ya hayo, muswada huo
uliandikwa kwa mtindo usioleweka na lugha isiyotamanika. Kitenge hakumbuki
alivyofaulu kuusoma mpaka mwisho.
Kitenge
akamgeukia mwandishi huyo na kumtazama. Naam, uso wake ulidhihirisha yote, macho
yake yalisema kila kitu. Ni mtu aliyetaabika akakata tamaa. Tazama uso
ulivyojikunja! Tazama macho yanavyotangaza uadui! Tazama tabasamu lake
lilivyoficha chuki! Kitenge akajikuta
akimwogopa.
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ndivyo, bwana
Ramadhani,” alisema kwa jitihada. “Muswada wako kama alivyokwambia dada huyu,
haujafikia kiwango. Unahitaji marekebisho mengi. Kwa kuwa hapa tunayo miswada
mingi mno si rahisi kufahamu wapi uliwekwa. Pengine tumeutuma kwa wasomaji wa
nje. Mpe muda aendelee kuutafuta.”
“Sina muda
zaidi bwana Kitenge,” sauti yake ilikuwa na hasira kama macho yake. “Hujui taabu
kiasi gani nilipata hata kuukamilisha. Bado huo ni wa nne, yote imo mikononi mwa
wachapishaji. Na jibu ni hilohilo, ‘ngoja.’ Tafadhali leo hii nitoke na muswada
wangu. Jana nilipiga simu nikiwaambia niukute, leo mnasema kesho. Nisipoupata
leo kwa kweli utajilaumu Kitenge.”
Kitenge na
Rusia wakatazamana. “Ya nini maneno yote hayo?” alihoji Kitenge baada ya kucheka
kidogo. “Unadhani tuna haja gani ya kukaa na muswada wa aina ile? Mara tu
utakapopatikana utapewa.”
“Nitapewa?” Ramadahani
alidakia akiinuka, Kitenge akashangaa kuona alivyo mrefu mwenye mwili mkubwa.
Fedha au chakula zaidi kingeweza kumfanya awe pande la mwanamume zaidi ya
alivyokuwa.
“Nitapewa!” alinguruma tena. “Wadhani
sifahamu kitu gani kinatokea? Usijidanganye bwana Kitenge, nafahamu vizuri sana
kuwa muswada huo umeubadili jina na kufanya umeutunga wewe. Najua kuwa sasa
hivi, uko KIUTA ambako unachapwa.”
“Nini?” Kitenge
aliuliza kwa mshangao akimgeukia Rusia. Wakaangua
kicheko.
“Chekeni, ndiyo. Lakini kaeni mkijua kuwa
hicho ni kicheko chenu cha mwisho pamoja. Nisipoupata muswada wangu kesho
nitahakikisha mmoja wenu anachekea kuzimu, naapa!” Akamgeukia Rusia na kuongeza,
“Nakupa hadi saa nane niwe nimeupata, vinginevyo mtajilaumu.” Akageuka na kuanza
kuondoka.
Kitenge akamwahi kumshika mkono, “Ngoja
bwana Rama,” alimweleza, “Hivi unafahamu
usemalo?”
“Nafahamu.”
“Kwamba
nimeubadili muswada wako uonekane kuwa nimeutunga
mimi?”
“Ndiyo.”
“Ni
nani huyo aliyekupa wazo la kipumbavu kama
hilo?”
Ramadhani hakujibu. Si kwamba hakutaka
kujibu bali hakuwa na jibu halisi. Alijua na kuamini kuwa Kitenge aliubadili
muswada huo. Alikuwa na hakika, hakika ambayo ilimtatanisha yeye binafsi kila
alipojiuliza ni wapi alikoipata. Anachokumbuka vyema ni kitu kama maongezi
ambayo aliyasikia baina ya watu wawili wafanyao kazi KIUTA wakisema wameletewa
muswada wa mtu anayeitwa Bazile Ramadhani watayarishe na kubadili jina la mtunzi
kuwa Kitenge.
Watu hao walisema kuwa muswada huo
utamtajirisha sana Kitenge. Kwamba kama wangekuwa wao, wangeamua kuua kuliko
kuacha Kitenge asifike na kujitajirisha kwa jasho lao. Ramadhani hakumbuki pia
kama aliwajibu chochote watu hao, anachokumbuka vyema ni nadhiri aliyoweka ya
kujiua au kumuua Kitenge endapo muswada huo usingepatikana. Hilo alilidhamiria
akizingatia taabu alizokwishazipata katika harakati zake za uandishi wa
vitabu.
Kama utunzi huwaletea watu wengine faraja,
yeye ulimzalia simanzi. Kama wengine huwapa utajiri, kwake ulimfanya fukara
zaidi. Alikuwa ameanza kutunga tangu akiwa shuleni, muda wake wote wa mapumziko
aliutumia kuandika. Senti zake zote za matumizi ziliishia kununua kalamu,
karatasi na stempu za kusafirishia. Akawa hana
rafiki.
Wenzake wote walimdharau wakimwita
mwendawazimu. La kusikitisha zaidi ni jinsi miswada yake ilivyorudishwa na
wachapishaji wakidai ‘haieleweki’ wala hana ‘fununu’ juu ya mtunzi. Hakukata
tamaa. Alipokuwa sekondari vitabu vilianza kutoa ‘picha’ ya kutamanika.
Wachapishaji walianza kumtia moyo kwa kumwelekeza hapa na pale. Halafu miswada
ikaanza kupotea. Kila alipotuma haukurudi. Barua za madai hazikusaidia. Ofisi za
wachapishaji wengine hata hazikujulikana kama kweli zipo, alizitafuta bila
mafanikio. Miswada mingi ikatoweka!
Huu aliompa
Kitenge ulikuwa wa nne kati ya zile zilizokuwa mikononi mwa wachapishaji.
Aliupenda na kuuthamini kuliko yote. Hakudiriki kuutuma kwa posta, bali
aliupeleka kwa mkono baada ya kuitafuta ofisi hii kwa siku kadhaa. Matumaini
yalikuwa yamezidi baada ya kumwona Kitenge, mtunzi mashuhuri, akitabasamu baada
ya kusoma sehemu kadhaa siku ile alipouleta. Leo aambiwe hauonekani, wakati ana
uhakika uko mitamboni! La asingevumilia, lazima huu uwe ama mwanzo wa faraja
zake ama mwisho wa mateso yake!
“Nani alinipa wazo
hilo?” alijibu Kitenge kwa swali jingine. “Sina haja ya kumtaja,” akalaghai.
“Ninalokutaka uelewe ni kuwa njama zako ziko hadharni. Ukiendelea nazo utapoteza
bure maisha yako. Saa nane nitarudi hapa. Tafadhali nikute muswada wangu,
vinginevyo, kichwa chako halali yangu.”
Akatoka
na kuufunga mlango kwa nguvu.
Rusia akajaribu
kucheka kicheko ambacho alikikatiza ghafla baada ya kuhisi kuwa hakikuwa na
ladha yoyote ya kicheko. Kadhalika macho ya Kitenge ambayo yalimtazama kwa namna
ambayo hakupata kuiona huko mbeleni, ilikuwa sababu nyingine iliyomkatisha
kicheko hicho.
“Usijali bosi, ana
wazimu…”
“Labda,” Kitenge alidakia, “Suala ni watu
wangapi wenye wazimu watakaonisumbua asubuhi ya leo? Nisipoangalia
wataniambukiza wazimu wao.” Alipoona Rusia akipanua mdomo kuuliza swali,
aliongeza harakaharaka, “Hatuhitaji watu wenye wazimu katika ofisi hii. Jitahidi
kutafuta muswada wake umpatie. Usisahau kumwonya asilete kazi yake nyingine
hapa.”
Baada ya maneno hayo alitoka
nje.
*****
HUKO nje
Kitenge hakujua aende wapi. Moyo haukumpa kwenda kokote. Kurudi ofisini roho
ilikataa vilevile. Kwa muda aliduwaa hapo nje ya ofisi yake akitazama pande
zote. Mara, akajikuta akiifuata miguu ambayo ilianza safari bila idhini yake.
Ilimwongoza hadi Coffee Bar, chini ya Telephone
House.
Hapo aliwakuta baadhi ya rafiki zake ambao
walimkaribisha kwa kahawa ambayo aliinywa japo hakushiriki katika maongezi.
Baada ya kitambo, alijikuta kabaki peke yake. Miguu ikamchukua tena hadi British
Library ambamo alishika kitabu hiki na kile na kukodolea macho maandishi, lakini
akiwa haoni chochote.
Mawazo yake yalikuwa
yakitatanishwa na siku kama ya leo kwake. Wazimu? Alikuwa akijiuliza. Ramadhani
pia ana wazimu? Na vipi kisa chake, si kinatosha kuwa hadithi nzuri? Hadithi ya
mtunzi aliyechanganyikiwa, ambaye baada ya kushindwa kuitumia vyema kalamu yake
anatumia ulimi wake kwa vitisho. Naam, ni hdithi nzuri. Ataiunganisha na tukio
la Machozi. Atawafanya wote wahusika wakuu. Mwisho wa hadithi? Swali hilo
alilipuuza tena. Atapata mwisho wa kuridhisha baada ya hadithi
kuanza.
Mara akasikia furaha ikimjia tele moyoni.
Pengine alicheka kwa nguvu, kwani aliwaona watu kadhaa waliokuwa wakisoma kimya
wakiinua macho kumtazama. Akatua mezani kitabu alichokuwa nacho mkononi na
kutoka nje.
Akaifuata tena Barabara ya Samora
hadi alipoifikia sanamu ya askari. Hapo alielekea baharini akiiendea hoteli ya
New Africa. Hotelini hapo alipata kiti katika meza iliyokuwa imekaliwa na
Wazungu watatu, mmoja akiwa mwanamke. Akaagiza bia nne aina ya Safari,
akiwakaribisha wale Wazungu. Walipokataa alizinywa zote moja baada ya nyingine.
Baada ya hizo aliagiza whisky. Jinsi alivyokunywa harakaharaka, haukupita muda
akawa hajiwezi.
Mmoja kati ya Wazungu hao
akamwinamia na kumnong’oneza: “Excuse me sir, i think you have taken too much.
Can’t you switch off and go back home?”
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kitenge alimkosa
kofi hafifu huku akisema, “Go to hell.”
Wazungu
hao wakaondoka na kuhamia meza nyingine. Aliendelea kunywa. Kisha usingizi
ukamchukua, akainamia meza na kujilaza kwa
starehe.
Alipoinuka alijikongoja kuendea teksi.
Dereva akamsaidia kuingia baada ya kuuliza anakoishi. Kitenge aliitazama kwa
taabu saa yake ambayo ilisema ni saa mbili za usiku kasoro dakika kadhaa.
“Magomeni Mapipa Mtaa wa Kiyumba namba kumi na mbili,” alijibu kilevi huku
akilala tena.
Kilichomzindua tena ni dereva ambaye
alimsukasuka kumwamsha. Walikuwa wamewasili. Akajikongoja kuingia ndani, nusura
amgonge mama mwenye nyumba ambaye alikuwa kasimama mlangoni akimtazama kwa
mshangao kwani alikuwa hajawahi kumwona Kitenge akilewa kiasi hicho. Kitenge
alifungua mlango kwa shida, alipoingia hadi chumbani hakujishughulisha kuwasha
taa wala kuvua viatu. Alijibwaga kitandani na kuanza
kukoroma.
Ilikuwa usiku wa manane alipokurupuka
ghafla kwa maumivu makali ambayo yalipenya kifuani mwake. Mkono wenye nguvu
ulimkandamiza asiweze kuinuka kutoka kitandani hapo. Mkono wa pili ulimziba
mdomo hata akashindwa kutoa sauti. Pigo la pili lilipenya hadi moyoni, Kitenge
akahisi maumivu yakipungua na badala yake akimezwa na usingizi mzito wenye kiza
cha kutisha. Usingizi ambao ulimfanya asisikie chochote kisu kilipopenya kwa
mara ya tatu katika kifua
chake.
*********
“SEMA
kama mwanamume, sajini Abdala!” InspeKta Kombora alifoka, macho kayatoa.
“Zungumza lugha ya kiaskari; amekufa au
ameuawa?”
“Ameuawa afande,”Abdalla alisema akitua
faili lililokuwa kwapani mwake. “Taarifa kamili ya kifo na mauaji yake utaipata
katika faili hilo.”
Kombora alipokea faili na
kulitupia jicho la haraka haraka. Kisha alitazama saa yake ambayo mshale wa
dakika ulikuwa juu ya kumi na mbili, wa saa ukiwa juu ya nane. Ghafla, aliinua
uso wake na kumtazama sajini Abdala. Macho yake yalitulia kwa muda juu ya uso
huo wenye macho maangavu, yakateleza hadi juu ya kifua chake kipana na
kiwiliwili kirefu ambacho kilitoa picha ya
ukakamavu.
Ingawa alimtazama kijana huyo ni macho
tu yalikuwa yakimwona. Kifikra alikuwa mbali akifikiria kifo hiki na kujaribu
kulinganisha na simu ile aliyoipokea jana kutoka kwa mtu asiyejulikana. Mtu
ambaye alidai anajisikia kuua mtu. Sauti hiyo ikiwa haina chembe yoyote ya mzaha
ilikuwa imemfanya Kombora ashinde kutwa nzima ya jana akiwa na hofu ya kupokea
habari mbaya.
Usiku ulipoingia hofu hiyo
ilimzidi, kwani mara nyingi ni usiku ambapo waovu hutenda maovu yao. Hakupata
usingizi kikamilifu, kila dakika alitegemea simu ambayo ingemfahamisha maafa.
Hivyo kulipopambazuka bila habari hiyo kumfikia, alianza kufarijika akidhani
kuwa pengine aliipa uzito usiostahili ile sauti; yawezekana ni mlevi au mpungufu
wa akili na hata mtu mzima kabisa ambaye alikuwa na muda wa kuchezea akaamua
kuutumia kwa kuwasisimua polisi, lakini mawazo hayo yalimtoka Kombora mara
alipopokea simu ya kumjulisha kifo hicho alipokuwa akijiandaa kuja
kazini.
“Nani aliyeuawa?” alinguruma katika chombo
cha
simu.
“Kitenge.”
“Kitenge!
Tuna vitenge madukani sajini?”
“Kondokondo Kitenge
afande. Yule mtunzi mashuhuri wa hadithi za ujambazi na
upelelezi.”
“Alaa!”
Alifahamishwa
kwa ufupi maafa hayo yalivyotokea. Ndipo akaharakisha kuja ofisini ambako
alikabidhiwa faili la mkasa huo ambalo bado alikuwa kaduwaa nalo kabla hajaanza
kulisoma.
“Ungelisoma haraka mzee,” sajini Abdalla
alimzindua, “Kuna mengi ambayo hayajaanza kutekelezwa, yanayoisubiri idhini
yako. Kwa maoni yangu, muuaji hayuko mbali, tutamtia mikononi mara
moja.”
Kombora akayateremsha macho yake mezani na
kuanza kupekua faili hilo. Hakujishughulisha kuipokea saluti ya Abdala,
alipokuwa akiondoka. Badala yake, kama kwa kumtupia aliongeza, “Usiende mbali.
Nitakuona mara baada ya hii,” alisema.
Aliisoma
kwa makini. Hakukuwa na mengi zaidi ya aliyokwisha simuliwa. Marehemu alikuwa
ameuawa kwa kisu baina ya saa nne na saa nane usiku. Maiti yake ilikutwa chali
juu ya kitanda. Kwa mujibu wa daktari, marehemu alikuwa amelewa sana kabla ya
kufa, hivyo hakufanya vurugu yoyote kabla ya kukata
roho.
Ripoti ya wataalamu wa vidole inadai haimo
alama yoyote ya vidole zaidi ya zile za marehemu mwenyewe. Jambo ambalo
linaonyesha kuwa muuaji au wauaji walivaa glovu maalumu kwenye mikono yao kabla
ya kugusa kitu chochote humo ndani. Silaha iliyotumiwa haikuonekana. Taarifa
iliongeza kwamba, aliyearifu polisi ni mmoja wa wapangaji ambaye aliarifiwa na
bi kizee mwenye nyumba aliyeigundua maiti
alfajiri.
Kilichomsisimua Kombora katika ripoti
hiyo ni madai ya bi kizee huyo kwa makachero kwamba anamfahamu muuaji, ati ni
mwanamke ambaye alidai kwa sauti na kuapa kuwa angemuua Kitenge. Hilo Kombora
hakulitegemea.
Kwanza hakutegemea ufumbuzi uje
kwa urahisi namna hiyo; pili hakudhani kuwa muuaji angetukia kuwa mwanamke.
Sauti iliyompigia simu ilikuwa ya kiume. Aliamini kuwa ni mwenye sauti hiyo
ambaye alielekea kuwa muuaji. Hivyo aliinua simu yake na kumtaka opereta amwitie
sajini
Abdala.
“Afande.”
“Sajini.
Unaonaje kesi hii, waweza kuyaamini maneno ya huyu
mama?”
“Hadi dakika tano zilizopita nilikuwa
nikiyaamini afande…”
“Sikia Abdala,” Kombora
akamkatiza kwa ukali, “Hatuna muda wala nafasi ya kuzungumza kwa mafumbo. Katika
ripoti yako mwenyewe unadai kuwa silaha ya mauaji haikupatikana. Hilo peke yake
linatosha kukufahamisha kuwa muuaji bado ana nia au uwezo wa kufanya unyama
mwingine kwa silaha ileile au nyingine, wakati wowote. Hatutaki jambo hili
litokee. Sasa, haya mambo ya kuamini ripoti yako mwenyewe dakika tano zilizopita
yanaingiaje katika swali langu?”
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Sajini Abdala,
akiwa mtu anayemfahamu vyema ofisa wake, hasa katika masuala ya aina hii, kuwa
hapendi mzaha wala maneno mengi, alitabasamu kwa uficho, kisha akamjibu mara
moja.
“Nilichotaka kusema ni hivi afande, taarifa
hiyo ya mama mwenye nyumba alinipa mimi mwenyewe asubuhi ya leo. Alikuwa na
hakika na kile anachosema. Nikaelekea kumwamini, hasa baada ya kusema kuwa mama
huyo anayeshukiwa anayo kila dalili ya ulevi wa gongo na bangi. Mlevi wa vitu
hivyo anaweza kufanya lolote afande, hasa anapoondokea kuamini kuwa ni wewe
uliyemfanya yeye aishie kuwa mlevi hali wewe unainuka
kimaisha.”
“Sawa,” Kombora alijibu. “Na baada ya
dakika hizo tano?”
“Baada ya dakika tano, siyo
kwamba simwamini kabisa, ila nimechanganyikiwa tu. Nilikuwa nikipiga simu katika
ofisi ya marehemu kuwafahamisha maafa haya. Katibu wake mahsusi akaropoka kuwa,
alitegemea jambo hilo. Nilipomuuliza kwa vipi, akaniambia kuwa anamfahamu hata
muuaji kwa jina na sura. Nilipomuuliza kama mtu huyo ni mwanamke, alikanusha na
kudai kuwa ni mwanamume, mtunzi wa vitabu. Kwamba mtu huyo alifika ofisini hapo
na kuahidi kumuua Kitenge. Unaona ilivyo vigumu mzee? Wauaji wawili, marehemu
mmoja! Kila shahidi ana imani na ushahidi
wake.”
“Kweli inatatiza,” lilikuwa jibu la Kombora
baada ya kuwaza sana. Kisha akaongeza, “Nitapenda kuonana na hawa mashahidi mara
moja. Andaa gari twende kwanza huko nyumbani kwake halafu tutamwona huyo karani
wake ofisini.”
“Timamu
afande.”
Dakika chache baadaye walikuwa ndani ya
Land Rover wakielekea Magomeni Mapipa. Walipoufikia Mtaa wa Kiyungi
hawakuhangaika kuipata nyumba waliyoihitaji. Nje kulikuwa na watu wengi
waliozungumza hili na
lile.
Kombora
na Abdala waliupenya umati huo kwa urahisi, kwani watu wenyewe walijitenga
kuwapisha. Ndani walikuta umati mwingine ambao ulimzunguka mama mwenye nyumba
aliyekuwa akiendelea kueleza kwa sauti yenye shauku kubwa. Kombora aliwataka
radhi majirani hao na kumchukua mama katika chumba cha
marehemu.
“Sijisikii kabisa kuingia chumba hiki
baba, kinatisha,” alisema bibi huyo huku
akiingia.
“Usijali mama. Hamna litakalotokea,”
Kombora alijibu bila kumtazama. Macho yake yalikuwa yakitazama kila upande. Kama
ilivyosema taarifa, haikuonekana dalili yoyote ya kuashiria mauaji katika chumba
hicho. Kila kitu kilikuwa katika hali inayostahili. Ni shuka moja tu yenye damu
iliyosaliti siri hiyo. Shuka nyingine bila shaka zilikuwa zimechukuliwa na
polisi kwa uchunguzi zaidi. Kisha Kombora aliyarejesha macho yake kumtazama
kizee ambaye alikuwa akisema.
“Wamekuja hapa
wenzako baba. Wanauliza mengi ambayo hayana maana. Muuaji najua ni yule mwanamke
tu. Sauti yake inaonyesha wazi alikuwa akisema kweli. Kama angekuwa mwingine,
lazima angeiba kitu chochote humu ndani. Yule hakuwa na nia ya chochote bali
kumuua tu."
“Kweli mama,” alijibu Kombora.
“Unaweza kumfahamu iwapo utamwona tena?”
“Bila
shaka. Hata wewe baba, ukimwona japo hujawahi kumwona utamjua tu. Ana sura ya
kutisha sana.”
“Unadhani tunaweza kumpata wapi
bibi?” aliongeza Abdala.
“Mjukuu wangu, usiniambie
hujui wanakopatikana walevi wa gongo. Darisalama hii ni kubwa, ndiyo, lakini
nyie mnajua wapi na wapi mnaweza kumpata mwanamke
yule.”
Kombora alitabasamu kwa haya kidogo kabla
hajajibu, “Kweli mama, tutampata hivi karibuni. Unasema ulisikia marehemu
akimwita Machozi sio?”
“Ndiyo baba, nitafurahi
mkimkamata. Aweza kuua tena yule.”
“Tutamkamata
bibi.”
Yakafuata maswali mengine ya kawaida.
Ilimshangaza Kombora kuona bibi huyo alivyokuwa hodari wa kujibu maswali ambayo
yangeweza kuwatatanisha wasomi na vijana. Walipotosheka walimshukuru na kumuaga.
Wakatia moto gari na kurudi
mjini.
*******
OFISI
ya BLACK POWER PUBLISHERS ilikuwa kimya kupindukia Kombora na Abdala
walipoingia. Waliwakuta vijana wawili wa kiume wameinamia meza zao, na msichana
ambaye mikono yake ililalia mashine ya chapa. Kombora aliyaona machozi
yakimlengalenga msichana huyo pindi alipoinua uso
kumtazama.
“Karibuni,” mmoja kati ya vijana wale alitamka
polepole.
“Asante,” maofisa hao walijibu
wakijiketisha juu ya viti vilivyokuwa
wazi.
Yalifuata maongezi mafupi, Kombora akihoji
juu ya hili na kutaka kujua juu ya lile. Mengi yalimsaidia ingawa ni machache
yaliyopata nafasi katika daftari lake. Mengi yalikuwa yaleyale ambayo
alikwishaambiwa kabla. Aliporidhika, alimgeukia msichana huyo ambaye alikuwa
akijibu kwa nadra sana na kumwita, “Tafadhali bibie. Bibi Rusia kwa jina
sio?”
“Ndiyo.”
“Nadhani
ni wewe mwenye ufunguo juu ya suala hili. Nina maana kuwa, ni ushahidi wako
ambao utatuwezesha kumtia mkononi huyu muuaji mapema zaidi. Unasema una uhakika
kuwa huyu kijana anayeitwa Bazile Ramadhani ndiye aliyemuua bwana
Kitenge?”
“Naamini hakuna mwingine,” alijibu bila
kuwatazama.
“Kwa
nini?”
“Mwenyewe alisema hivyo. Zaidi ya kusema
anaonyesha kuwa ni mtu katili. Aliporudi mara ya pili nilipomjulisha kuwa
muswada wake bado ulikuwa haujapatikana alitoa macho na kukimbilia katika chumba
cha marehemu. Kama angemkuta naamini angemuua papohapo. Kwa bahati nzuri
hakuwepo. Hata hivyo...” akasita na kufuta machozi yaliyomtoka
ghafla.
“Pole dada,” alitamka
Abdala.
“Ulikuwa unahusu nini huo muswada wake?”
Kombora alihoji.
“Mauaji tu, yaelekea ni mtu
anayependa sana mauaji?”
“Na unafikiri umekwenda
wapi?”
“Muswada huo sio? Kwa kweli hata mimi
nashangaa. Iko hapa miswada iliyoletwa miaka miwili iliyopita. Huo wake
hatujakaa nao miezi minne, hauonekani. Kama ungekuwa wa kuvutia, tungesema
mwenzetu mmoja kauchukua nyumbani kwake akausome. Kila aliyejaribu kuusoma
alikata tamaa.”
Kombora akamshukuru na kuongeza,
“Waweza kutusaidia vipi kumpata mtu huyu,
Rusia?”
“Sidhani
kama…”
“Huna barua yake yoyote yenye anuani
yake?”
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Zipo nyingi.
Alikuwa akiandika kila mara. Barua nyingine hata tulichoka kuzisoma. Nakumbuka
iko moja ambayo aliiambatanisha na picha yake. Eti iwekwe nyuma ya
kitabu.”
“Itafute
tafadhali.”
Baada ya upekuzi mfupi katika
majalada, Rusia alimkabidhi Inspekta Kombora barua tatu, moja ikiwa na picha.
Kombora aliitazama picha hiyo kwa makini.
Akiwa
mtu mzoefu wa kusoma picha za wahalifu alimwona Bazile vilivyo: kijana mwenye
ndevu changa, umri baina ya miaka ishirini na mbili hadi ishirini na sita, sura
yenye busara ingawa ilibeba macho yaliyokuwa yakitangaza mengi na hayakuwa na
ladha ya maisha wala uangavu wowote, na ni kama ambayo yalikuwa yakinong’oneza
kwa huzuni: “nimeonewa jamani.”
“Ndiyo, huyu
anaweza kuwa muuaji,” aliwaza Kombora, huku akimpa Abdala picha hiyo. Akafunua
barua kusoma anuani. Ilikuwa rahisi kuliko alivyotarajia. Anuani zote zilitaja
sanduku la kazini pale TEGRY. Kiwanda cha kutengenezea vifaa vya
plastiki.
“Tunashukuru sana dada,”Kombora aliaga
ghafla akiinuka. “Nadhani sasa tuondoke tukawahi shughuli
nyingine.”
“Asante mzee,” alijibu msichana huyo
akiinuka kuwatazama kikamilifu kwa mara ya kwanza. Macho yake hayakuchelewa sana
juu ya umbo la makamo la Inspekta Kombora, ambalo nywele zilianza kumezwa na
mvi, uso ukiingiliwa na mikunjo. Lakini macho hayo yalikawia katika umbo lenye
kiasi kikubwa cha ujana la Sajini Abdala. Sura ikiwa nzuri na umbo la
mwanamichezo, Sajini Abdala alipendeza vyema katika magwanda yake ya kipolisi
machoni mwa Rusia.
“Karibuni
tena.”
“Asante bibie,” Abdala
alijibu.
Walipofika katika ofisi yao walianza
maongezi yenye lengo la majadiliano. Kila mmoja alitaka wazo la
mwenziwe.
“Nadhani mwenye nafasi nzuri ya kuua ni
huyu mwanamke Inspekta. Yeye ndiye aliyefika nyumbani kwa marehemu. Pia bado
anaongozwa na nguvu za bangi na gongo. Simwamini mtu yeyote anayetumia vileo
hivyo.”
“Kwa
hiyo?”
“ Kwa hiyo, napendekeza uturuhusu tumsake
huyu mama. Tukiwatuma vijana huko katika mageto ya Luhanga, Buguruni, Kigamboni,
Kawe, Tandale na kote nadhani atapatikana tu. Sidhani kama yuko nje ya jiji hili
mara hii.”
Kombora hakujibu mara moja. Yeye
alimshakia zaidi huyu mtunzi, Bazile. Sauti katika simu ile haikuwa ya kike.
Wala hakuona kama mwanamke huyu mlevi wa gongo angekuwa na haja ya kumwandaa na
kumpigia simu polisi kama hadithi ile ya Simu ya
Kifo.
Hata hivyo, bado aliona umuhimu wa kuwapata
wote wawili mapema iwezekanavyo. Yawezekana kuwa mtunzi yule hahusiki.
Yawezekana vilevile kuwa yeyote kati yao hahusiki! Aliwaza ghafla kwa hofu.
Jambo ambalo litaongeza uzito katika jukumu
hili.
*****HAYA, INSPEKTA KOMBORA YUKO KAZINI
AKIMSAKA MUUAJI HUKU AKISHIRIKIANA NA SAJINI ABDALA. NI KIPI KITAKACHOFUATA?
FUATILIA RIWAYA HII KALI
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment