Simulizi : Uchu
Sehemu Ya Tano (5)
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ilikuwa saa nne na nusu usiku, wakati Jean na kundi lake walipoondoka Kibumba kuelekea Goma.
"Hakika nimeridhika na ari ya wanajeshi wetu na uwezo mkubwa wa vikosi vyetu, pia nimefurahishwa sana na aina ya silaha tulizonazo, hii inaonyesha ni jinsi gani tumedhamilia kufanya kweli", Jean alisema kwa kujiamini.
"Nilikwambia toka mwanzo kuwa ukifika na kuona lazima utaamua tuingie vitani, kwani hakuna sababu wala haja ya kusubiri, vita vianze moja kwa moja, tuchukue madaraka", Col. Gatabazi alitamba huku Jean akitingisha kichwa kukubaliana nae.
"Twendeni Goma tukafanye maamuzi. Sijui kwa upande wa wenzangu, lakini mimi nafikiri tuanze mashambulizi alfajiri na mapema ila kwanza tukamate vikosi vya hapa Gisenyi kabla ya jua kuchomoza, maana adui hajui nguvu zetu, sisi nguvu yake tunaijua", Jean alishauri, wote kwa pamoja wakakubaliana.
"Mimi niko tayari wakati wowote, hata sasa vijana wangu wako tayari, uamuzi wenu tu ndio unasubiliwa", Col. Gatabazi alijibu.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Haya twendeni Goma tukafanye uamuzi mara moja", Jean alijibu wakaondoka haraka kuelekea Goma.
Ilipofika saa tano kamili za usiku, Willy Gamba na Bibiane walikuwa tayari wamewasili Kibumba. Bibiane alizijua vizuri njia za vichochoro za sehemu hii. Hivyo, walifika bila tatizo lolote. Bibiane alimuonyesha Willy sehemu yalipo maghala makubwa ya silaha ambayo baada ya Willy kuyaona, alitaka waanzishe mapambano dhidi ya watu wakiwa kwenye maghala hayo kwani aliamini hapo ndipo nguvu kubwa ya Akazu ilikuwa imewekwa.
"Sehemu hii inalindwa sana", Bibiane alimwambia Willy baada ya kutoka kwenye msitu na kuona kambi kubwa ya kijeshi ambayo ilimshangaza hata Willy.
"Walijenga lini kambi kubwa ya jeshi kama hii?", Willy aliuliza kwa mshangao.
"Hapa kulikuwa na kambi ya jeshi la Zaire, na Akazu walipewa kambi hii baada ya matukio makubwa ya Rwanda, na mara moja wakaleta vifaa vyao vya kivita na kuifanya kuwa kambi ya jeshi ya kisasa kabisa. Ina kila kitu kama unavyoona, taa, maji, mawasiliano, yaani kuna kila kitu cha kisasa nakwambia. Hata maafisa wa mashirika ya kimataifa yanayoshughulikia wakimbizi wanapotokea hapa kwa bahati mbaya wanaamini ni kambi ya jeshi la Zaire, maana kambi za wakimbizi ziko kilomita moja tu kutoka hapa upande ule wa kilima, hata wakiuliza basi huambiwa kuwa hii ni kambi ya jeshi la Zaire, na raia hawaruhusiwi kabisa kusogea karibu na kambi hii", Bibiane alimwambia Willy, ambaye wakati huo alikuwa ameshikwa na mshangao.
"Maghala ya silaha ni yapi?", Willy alihoji huku akichungulia kuangalia vizuri kambi hii akitumia kiona mbali. Bibiane alitumia nafasi hiyo kumwelekeza kila kitu. Kwa vile kambi ilikuwa ikiwaka taa utafikiri mchana waliweza kuona kila kitu vizuri kabisa.
"Kambi hii yote imezungukwa na seng'enge yenye umeme wenye nguvu kubwa unaoweza kumuua hata tembo haraka kama inzi, yaani ukigusa tu unakaushwa kwa umeme kama nyama", Bibiane alieleza.
Willy aliamua kwanza walifiche gari la jeshi walilokuwa wakitumia kwenye msitu ule, wakachukua mizigo yao ya kazi na kasha wakatafuta njia ya siri kwa ajili ya kuingia pale kambini.
"Hii kambi inaweza kuwa na askari kama wangapi kwa kukisia kwako?", Willy alimuuliza Bibiane.
"Eeeh… wanafika elfu tano na zaidi, wenye mafunzo ya juu sana, wale askari wa kikosi cha Rais wako hapa pia na askari wenye ujuzi mkubwa. Kuna makomandoo waliofuzu vizuri kama mia tano, halafu kuna askari wa kawaida wenye mafunzo mazuri vilevile zaidi ya elfu nne na mia tano. Hivyo, kuna askari kama elfu kumi hapa, na ndilo tegemeo kubwa la Akazu kurudi madarakani. Lakini kusema kweli wanaweza kushika tena madaraka, ukichukulia ari, uwezo na vifaa vya kijeshi walivyo navyo", Bibiane alimweleza Willy.
KKwa kweli kambi hii ilikuwa kubwa sana kiasi cha kumtia hofu Willy Gamba, kwani hakutegemea kabisa kukutana na kambi kubwa ya adui yenye idadi kubwa ya askari kama hii.
"Hebu nipe muda nifikiri kabla ya kujitumbukia huko", Willy alimwambia Bibiane.
"Hatuna muda Willy, hatuna muda kabisa kabisa, lazima ufahamu kuwa tunatafutwa na adui, na wakihisi tuko huku hakika tumekwisha", Bibiane alilalamika wakati Willy akimwangalia tu bila kusema kitu.
Baada ya Willy kutafakari kwa dakika kadhaa alilazimika kumwambia Bibiane. "Nikisema nahitaji muda wa kufikiri nina maana dakika tano tu, lakini niwe peke yangu, naamini sasa umenielewa?", Willy alimwambia Bibiane huku akielekea kwenye kichaka kilichokuwa hatua chache kutoka walipokuwa wamesimama.
"Kumbe unaamini uchawi, wewe unakwenda kuloga, mimi nifanyeje sasa?", Bibiane alimkebehi Willy.
"Jifanyie lolote kwa imani yako", Willy alijibu huku akipotelea kwenye kichaka. Inasemekana katika hali kama hii ya hatari Willy husali sana akimuomba Mungu. Baada ya dakika kadhaa Willy alirudi alimkuta Bibiane akiwa amebeba silaha za kiasi chake akiwa tayari kwa kusonga mbele kwa ajili ya mapambano dhidi ya jeshi la Akazu.
"Ehe, sema sasa tunasonga mbele ama tunarudi nyuma kumsubiri Col. Rwivanga?", Bibiane aliuliza.
"Tunaendelea", Willy alijibu kwa mkato huku akitoa vifaa vyake vya kazi kwenye mkoba wake.
Willy alibeba silaha na vifaa vilivyokuwa vimebaki, na kwa hadhari kabisa wakaanza kuelekea kwenye ile seng'enge yenye umeme.
"Mara nyingi ulinzi si mkali sana upande wa ua kwa kuwa wanaamini hakuna kitu kinachoweza kuzipenya hizi seng'enge bila kufa kwa umeme, maana kila siku wanyama wanakutwa wamejikaanga wenyewe. Vilevile, kitu chochote kinachokaribia mita moja ishara inaonekana kwenye chumba maalum kinachodhibiti usalama wa kambi hii kama kuna kitu kinasogelea seng'enge mara moja hatua za haraka za usalama wa kambi zinachukuliwa.
"Yote haya yamefanywa lini?", Willy alitaka kujua.
"Sababu ya pesa Willy, pesa, askari wa kukodishwa kutoka Afrika Kusini ndio wameleta vifaa na teknolojia hii iliyopo hapa kambini. Tukifanikiwa utajionea mwenyewe", Bibiane alidokeza.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Walipokuwa mita kumi kutoka usawa wa seng'enge walisimama na Willy alitoa kifaa maalum kwenye mkoba wake. "Tutapita chini ya seng'enge, baada ya kuchimba handaki".
"Itatakiwa liwe mita mbili kwenda chini, vinginevyo tutakaushwa kama mikaa", Bibiane alisema huku akionyesha wasiwasi.
"Hili bomu", Willy alisema akiwa ameshika bomu dogo lenye ukubwa wa yai la kuku. "Lina uwezo wa kuchimba handaki la urefu wa mita kumi na upana wa mita tatu, na kina cha mita tatu unasemaje?".
"Sikupingi, kwa teknolojia ya sasa hata mimi nimeona maajabu mengi katika vifaa vya vita, teknolojia imeendelea sana. Haya chimba tuone".
Willy alishika kisu na kuanza kuchimba shimo la mita moja kwenda chini, kisha akawasha lile bomu na kulitumbukiza pale shimoni na kulifukia.
"Litalipuka baada ya nusu dakika turudi nyuma haraka tulale chini".
"Halitasikika baada ya kulipuka?".
"Hapana, bomu hili limetengenezwa mahususi kwa ajili ya matumizi kama haya, ili kuziba mlio ndio sababu tunalizika chini ya ardhi", Willy alimwambia Bibiane na kumtoa hofu.
Baada ya nusu dakika bomu lile lililipuka na kutoma sauti kidogo, hii yote ilitokana na kazi ya Willy na kukatokea handaki zuri kwa ajili ya wao kupita bila kikwazo.
"Bwana, hakika kazi yako nimeipenda, sasa tuingie ndani tukafanye kazi iliyotuleta, kikwazo hiki ndicho kilikuwa kinanipa wasiwasi mkubwa", Bibiane alisema wakati wakiingia ndani ya handaki ili wapite kwa ajili ya kuwakabiri wanajeshi zaidi ya elfu kumi ndani ya kambi yao.
Nkubana na wale askari watatu walifika mpakani yapata saa tano na robo usiku. Walishangaa kukuta moja ya magari yao halipo na wale madereva wa magari hayo pia hawaonekani. Kwanza walifikiri huenda baada ya wao kuchelewa wale askari waliona waondoke, lakini askari mmoja aliona damu mahali gari moja lilikuwa limeegeshwa.
"Hebu angalieni vizuri huenda Willy Gamba kafika hapa na kufanya uharibifu tena", Nkubana alieleza huku mikono yake ikiwa imeshika nyonga.
Wakati Nkubana na askari wake wakitafakari, ndipo mmoja wa wale askari alipoona maiti za wale madareva wa magari zikiwa zimetupwa nyuma ya ua palepale kituoni.
"Shenzi kabisa huyu ni WIlly Gamba alikuwa hapa, na kachukua hata gari pamoja na sare zetu. Mtu huyu ni mshenzi sana, ole wake nikimuona sintangoja kumpeleka kwa Jean, nitamuua mwenyewe keshanisumbua sana. Twende haraka Kibumba, lazima atakuwa ameelekea huko", Nkubana aliwaamru askari wake.
Walitafuta funguo za magari haya na kwa bahati nzuri. gari moja lilikuwa na funguo zilizoachwa ndani. Hivyo wakaliwasha gari hilo na kwa kasi kubwa wakaondoka kuelekea Kibumba, wakiamini kuwa watamkuta Willy huko.
...............................................................................................................
IX
Mapigano makali kati ya kikosi cha Luteni Nyamboma na jeshi la Meja Kasubuga yaliendelea kwa kila upande kutumia mbinu kuukabiri upande mwingine. Kwa muda wa saa moja na nusu, Luteni Nyamboma hakurudi nyuma, lakini alikuwa amewapoteza askari wake wapatao kumi na watano, lakini nao pia walikuwa wamefanikiwa kuwaua askari zaidi ya arobaini wa jeshi la Meja Kasubuga. Luteni Nyamboma alipoona anaelemewa na risasi zinamwishia aliwaamru askari wake waliobaki kurudi nyuma ili wakimbilie mpakani ambako waliamini kuwa wangepata msaada zaidi.
Walirudi nyuma kwa hadhari na walipoona sasa wanaweza kukimbia ili kuwatoroka wanajeshi wa jeshi la Meja Kasubuga walifanya hivyo. Meja Kasubuga alimru jeshi lake liwafukuze na kuwakamata. yeye mwenyewe alirudi ofisini kwake ili aweze kupeleka habari Makao Makuu Kigali kueleza mambo yaliyokuwa yametokea. Col. Rwivanga ndiye aliyepokea simu na alipoangalia saa yake ilikuwa saa tano usiku.
"Afande, tumevamiwa hapa na jeshi la Intarahamwe na Wahutu wenye msimamo mkali, tumepoteza askari kama arobaini hivi, lakini tumefanikiwa kumrudisha adui nyuma, amekimbilia mpakani mwa zaire", Meja Kasubuga alimweleza Col. Rwivanga na kisha kueleza kwa kirefu mapigano yalivyokuwa.
"Hivyo, inaonekana hao ni askari wenye ujuzi mkubwa?", Col. Rwivanga aliuliza.
"Sana afande, mpaka mimi nimeshangaa, nafikiri fununu tulizonazo kuwa kuna kambi kubwa ya mafunzo yenye wakufunzi wenye utaalamu wa hali ya juu kuhusu mambo ya kijeshi ni kweli kabisa".
"Willy yuko wapi?".
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Katika prukushani hii Willy na mwenzake wamechomoka, naamini wamekwishavuka mpaka. Huyu mtu ataleta kasheshe kubwa, nadhani niruhusu sasa mimi na kikosi changu tuvuke mpaka ili tuwasaidie, maana alitaka kwenda Kibumba na huko ndiko kunasemekana kuna jeshi zima la Intarahamwe. Kwa vyovyote hawezi kurudi, kwani taarifa za siri tulizonazo kama ni kweli kuna askari zaidi ya elfu kumi katika kambi hiyo, na wakimbizi wote katika sehemu hiyo wamepewa mafunzo ya hali ya juu ya kijeshi. Kwani wale wakimbizi wanaokataa kushiriki mafunzo ya kijeshi wanauawa, elewa kuwa kuna wakimbizi zaidi ya laki moja wanaume, achilia mbali wanawake na watoto. Hivyo, Willy yuko katika hatari kubwa, huenda hakujua vizuri nguvu ya adui", Meja Kasubuga alimwambia Col. Rwivanga.
"Wewe fanya kazi moja kwanza, wafukuze hao wavamizi mpaka mpakani, wakivuka mpaka wewe na jeshi lako msivuke, mtusubiri hapo hapo mpakani. Mimi, Meja Tom Kabalisa wa Banyamlenge na Bwana Mpinda wa vikosi vya vyama vinavyopinga serikali ya Zaire tutakuja usiku huu kwa helkopita, naamini saa nane usiku tutakuwa tumefika hapo mpakani, msivuke mpaka tufike", Col. Rwivanga aliagiza.
"Sawa afande, mimi naendelea na mapambano, jeshi langu sasa linaelekea mpakani hivi sasa. Mkifika helkopita itue ile sehemu ya kawaida, tutakuwa tumeimalisha ulinzi eneo hilo, nitawasubiri", Meja Kasubuga alisema.
"Asante na kwaheri, msifanye chochote kwanza", Col. Rwivanga alisisitiza na palepale akajiweka tayari kisha akatoka kwenda kuwafuata akina Mpinda na Kabalisa kwa ajili ya kuelekea kwenye uwanja wa mapambano.
Willy na Bibiane walitambaa chini kwa chini kama nyoka na hatmaye wakayafikia majengo yaliyokuwa upande wa pili kutoka sehemu waliyotokea.
"Haya ni maghala ya kuhifadhia silaha, ni makubwa sana yana silaha nyingi za kisasa na vifaa vya kila aina vya kijeshi, zikiwemo silaha mpya za kisasa kabisa kwa ajili ya vita", Bibiane alieleza.
"Itabidi tuingie ndani kwanza ndio tutajua cha kufanya", Willy alieleza.
"Mlango uko upande ule kabisa, yaani unatazamana na majengo ya upande ule kabisa, ambako ndiko kuna ofisi na nyumba za kulala askari. Ulinzi upande ule ni mkali sana na lango la upande ule linafunguliwa kwa chombo maalumu ambacho kinahifadhiwa kwa mmoja wa makamanda wa juu wa jeshi lao", Bibiane alieleza.
"Kuta za maghala haya zimejengwa kwa teknolojia gani, au wametumia nini kujenga, tofali za simenti ama mabati?", Willy aliuliza.
"Kampuni moja ya Afrika Kusini iitwayo Super Frame ndiyo iliyojenga maghala haya pamoja na mabanda yote unayoyaona tena kwa muda wa mwezi mmoja tu. Kila kitu kililetwa hapa kwa helkopita kubwa zilizokodishwa kutoka Urusi na hapa waliunganisha tu hizi kuta na kuezeka. Wakati wa joto kuta zake zinaleta ubaridi na wakati wa ubaridi kuta hizi zinaleta joto, hivyo sijui zimetengenezwa kwa teknolojia gani?", Bibiane alijibu.
"Nimeelewa, baada ya hayo maelezo yako, teknolojia hii imetoka Marekani na inatumika kwa kujenga nyumba za gharama nafuu, lakini zenye kudumu kwa muda mrefu hata zaidi ya matofali ya saruji", Willy alijibu.
"Wewe kuna kitu usichokijua katika Ulimwengu huu", Bibiane alitania kisha akaendelea. "Sasa tunafanyaje Bwana kujua?".
"Utaona, sasa hivi tutaingia ndani", Willy alijibu kisha akafungua na kupekua kwenye mkoba wake, akatoa kifaa kimoja kilichofanana na kalamu lakini hiki ni kinene kidogo. alikifungua akatoa mfuniko wa mbele na kukifungua tena nyuma, baada ya kukifungua zilitoka betri mbili ndogo sana, Willy akazikagua kuona kama ziko sawa, kisha akazirudisha.
"Haya, rudi nyuma hiki chombo kinatoa miale aina ya leza bimu na hii miale ina nguvu za ajabu na miale hii inakata huu ukuta utadhani kisu ndani ya siagi, rudi nyuma yangu kabisa", Willy alisema Bibiane akarudi nyuma kwa hofu.
"Nasubiri kuona", Bibiane alitania.
"Subiri utaona japokuwa umeingiwa na hofu, lakini usiogope maana hapa hakuna ujanja zaidi ya kumuomba Mungu".
Willy alisukuma nyuma ya kile chombo kama mtu anavyosukuma kalamu wakati anataka kuandika, na mara moja miale myekundu ilijitokeza Willy akaielekeza kwenye ukuta na taratibu alikata saizi ya mlango sehemu ile walipokuwa, alipomaliza akakizima kile kifaa chake.
"Mbona hujakata chochote?", Bibiane aliuliza.
"Subiri kidogo, hii ni sawa na sayansi inayotumiwa na madaktari siku hizi kupasua mwili wa binadamu, wewe uko wapi mama, wenzio twaelekea karne ya ishirini na moja, karne ya sayansi na teknolojia wewe bado upoupo tu. Siku hizi mtu anafanyiwa opresheni, anapasuliwa tumbo, halafu baada ya saa moja anarudi nyumbani mwenyewe na haoni sehemu iliyopasuliwa", Willy alimkoga Bibiane aliyekuwa anashangaa.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Willy aliiangalia saa yake kisha akaufungua mkoba wake akatoa kitu kama bawaba kisha akaipachika kwenye ukuta kikanasa.
"Hiyo ni sumaku?", Bibiane alihoji.
"Ndiyo, inashika kitu chochote hata kama ni mbao".
"Ama kweli wewe mkali Willy, sikutegemea kabisa".
"Au vipi", Willy alijibu. Huku akiitumia ile bawaba alivuta taratibu na ile sehemu ikachomoka na kuacha uwazi wenye ukubwa wa mlango.
Willy na Bibiane walijikuta wanaangalia ndani ya ghala kubwa sana lililojaa silaha.
"Ingia sasa, mbona kama umepigwa na radi!" Willy alimweleza Bibiane.
"Bado nashangaa, hakika mambo uliyonionyesha ama kweli ujuzi huzidiana", Bibiane alijibu huku akiingia ndani ya ghala la silaha.
Willy akitumia chombo kingine kwa kukishikanisha na ile bawaba, ile bawaba ilitoka akaiweka upande mwingine wa kipande cha ukuta alichokuwa amekata, kisha na yeye alipoingia ndani ghala alivuta kile kipande cha ukuta kwa nguvu zake zote na kukipachika mahali pale tena. Mtu yeyote angepita pale kwa macho tu bila darubini asingejua kuwa pale pamekatwa. Bibiane hakuna na neno la kusema isipokuwa kuangalia ile sehemu tu.
"Wewe ni mkali kwelikweli", Bibiane alirudia kusema.
"Kwa mambo mengi si hili tu", Willy alisema kwa kumwemwesa.
wakiwa ndani Willy alishangaa kuona ghala kubwa sana la silaha. Kwa vile taa zilikuwa zikiwaka kwa ndani hawakuamini macho yao. Hata Bibiane hakujuwa kuwa Akazu walikuwa wamejiimarisha kiasi hiki. Mara ya mwisho Bibiane kufika hapa ilikuwa kama miezi mitatu iliyopita na katika hii miezi mitatu silaha nyingi, yakiwemo makombora ya masafa marefu na mafupi, vifaru, ndege aina ya MIG 21 na 23. mizinga, magari ya kivita, helkopita za kivita zilikwishaletwa eneo hili! Hakika ilikuwa ajabu na kweli.
"Hawa watu wanajipanga kupigana na Rwanda tu ama nchi nyingine jirani?", Willy aliuliza kwa mshangao.
"Nia yao ni kupigana na serikali ya Rwanda basi, hakuna kingine", Bibiane alijibu na kuongeza. "ila wanataka kuyapiga majeshi ya RPF kipigo kitakatifu, wasijejaribu tena mara baada ya kufukuzwa Rwanda".
"Fedha za kununulia vifaa hivi vyote watakuwa wamepata wapi?", Willy aliuliza.
"Miaka yote hii unafikiri walikuwa wakifanya nini?, wamewaibia wananchi mali zao zote. Akazu na Jean ni matajiri ajabu. Wana uhusiano na Rais wa Zaire na kiongozi wa waasi wa UNITA kule Angola. Almasi za Angola na Zaire dalali wake ni Jean. Sasa wewe fikiria wana utajiri wa kiasi gani?", Bibiane alijibu.
"He, sasa nimekuelewa mama".
"Kila kitu kilipangwa kwa ustadi wa hali ya juu. Hii ingewezekana kuchukua silaha zao kwa kutumia muda mfupi sana kwama wangeshambuliwa. Willy aliamini kuwa hii kweli ilikuwa kazi ya askari wa kukodishwa kwani hakika hili lilikuwa ghala la silaha lililotayarishwa na kupangwa na watu wenye ujuzi wa juu sana.
Willy na Bibiane walitembea kwa hadhari lakini kwa haraka wakijificha ndani ya vivuli vya zile silaha. Waliziangalia silaha hisi kiasi kwamba walianza kusahau kilichowaleta hapa.
"Unayaona makombora haya Willy", Bibiane alimwonyesha Willy makombora yaliyotengenezwa Urusi. Kisha akaendelea. "Haya makombora ni aina ya SAM 16 yalitekwa na majeshi ya Ufaransa wakati wa vita vya Ghuba, Februari 1991 na kupelekwa kwenye maghala ya silaha huko Ufaransa lakini kutokana na mahusiano wa karibu kati ya Jean na viongozi w ngazi za juu wa Ufaransa waliamua kumuuzia Jean makombora hayo. Katika makombora haya yamo yaliyotumika kuipiga ndege iliyokuwa imewabeba marais wa Rwanda na Burudi Aprili 6, 1994. Ni Jean na Akazu ndio waliamru rais auawe kwa sababu alikuwa ameanza kwenda kinyume na maagizo yao wakati wa mkutano wa Arusha, nakumbuka niliwahi kukueleza".
"Kama ndivyo, basi hawa Akazu na Jean ni wabaya kwelikweli, sasa naamini", Willy alisema huku hasira zikimpanda dhidi ya watu hawa.
"Lililobaki sasa ni kuziteketeza silaha hizi zote, naamini kuwa jeuri na nguvu ya Jean na Akazu tutakuwa tumeimaliza", Bibiane alieleza.
"Mkuki wa nguruwe, kwa binadamu mchungu, itabidi sasa tutumie yale mabomu yako aliyokuletea Jean, maana kazi kama hii ndio saizi yake", Willy alishauri.
"Unafikiri kwanini nilisema tuyachukue, nilijua. Kwanza ni madogo, na pili yana nguvu kubwa ya ajabu. Ghala kubwa kama hili, matano au sita yanaliteketeza kabisa na hakibaki kitu. Hili senduku linatosha kuiteketeza Kigali nzima. Nia ya Akazu ilikuwa wakishindwa mpango huu basi waiteketeze Kigali nzima na vyote vilivyomo bila kujali maisha ya watu", Bibiane alieleza.
Willy alimwangalia Bibiane kwa jicho kali, baada ya kutafakari akaelewa kwanini Willy alibadilika vile, ikamlazimu Bibiane kubadili maneno. "Haya tuyatege, nafikiri ulikuwa unasoma maelezo sasa unajua nini cha kufanya".
"Bila shaka", Willy alijibu sasa akiwa makini tayari kwa kazi. Kwa hesabu zake alitega mabomu ambayo alihakikisha angeteketeza kila kitu ndani ya lile ghala. Bila kushitukiwa walitoka kwa kupitia sehemu ileile na kisha wakairudishia ile sehemu ya ukuta kiasi kuwa hakuna ambaye angefikiria kuwa kuna mtu aliyewahi kupitia pale.
"Umesema kama ukitumia hii saa ya kulipua haya mabomu unatakiwa kuwa umbali gani, nina maana haya mabomu tuliyotega", Bibiane aliuliza huku wakiambaa na ukuta kuelekea kwenye mabweni ya kulala askari.
"Umbali usizidi kilomiota moja", Willy alijibu.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nkubana aliamua kuwasiliana na Col. Gatabazi kwa simu ya upepo. Alipompata alikuwa tayari amewasili Goma na walikuwa wameanza mkutano. Nkubana alieleza kwa kirefu yote yaliyotokea na kisha akashauri. "Huyu Willy Gamba hajui nguvu zetu. Hivyo, ameamua kwenda kujinyonga huko Kibumba, mimi naelekea huko kwenda kuongeza nguvu na kuwashitua makamanda wetu ili tumkamate kabla hajaleta kasheshe zake".
"Sawa, fanya hivyo, Jean anahitaji kumuona akiwa hai", Col. Gatabazi alikubaliana na Nkubana na kumweleza shabaha ya bosi wao Jean.
"Vilevile nitazungumza na makamanda hapa ili waniruhusu tupeleke jeshi mpakani kumsaidia Luteni Nyamboma kudhibiti mpaka wa Zaire, mpaka hapo amri ya kuishambulia Rwanda itakapotoka. Sisi tuko tayari, naamini uamzi utatoka haraka ili kazi ianze alfajiri ya leo. Hebu ngoja kidogo usizime radio yako", Col. Gatabazi aliwaeleza wenzake mambo yalivyokuwa Gisenyi na jinsi ambavyo Nkubana alikuwa akihisi kuwa Willy ameelekea Kibumba. Mara moja Jean alisimama baada ya kusikia habari hii ya Willy kuelekea Kibumba. Haraka alichukua radio na kutoa maagizo kwa Nkubana.
"Sikia, sisi tunakuja huko sasa hivi, tutakuja kwa ndege yangu na mimi nitaondoka. Sasa hivi bado tunawasiliana na Kamanda Bazimaziki awahi uwanja wa ndege. Waeleze wakiwakamata Willy na Bibiane wasiwaue kwanza mpaka tufike, hao ni halali yangu", Jean alitoa amri.
"Unafikiri ni busara sisi viongozi wa juu kwenda huko?", Anatoile kabuga alihoji.
"Bila shaka, huko ndiko yaliko majeshi yetu na ndiko tutakapotoa amri", Jean alieleza msimamo wake.
"Mimi pia nafikiri tuwe pale wakati wanajeshi wanaelezwa kukaa tayari kwa ajili ya kuanza vita alfajiri, hii itawaongezea mori", Jenerali Kasongo alijibu.
"Na mimi nimefurahi sana kwa uamzi huo, kuanzia sasa ofisi yetu kubwa ya kuratibu shughuli za vita itakuwa hukohuko Kibumba, maana ndiko kwenye vifaa vyote, sioni sisi tutafanya nini hapa wakati kila kitu chetu kiko kule", Col. Gatabazi alieleza kwa sauti ya juu.
"Sawa, wengi wape", Kabuga alijibu.
Kisha wakawasiliana na Col. Marcel Bizimaki, ambaye ni Kamanda wa jeshi la Akazu wakitumia njia ya simu ya satellite, wakamweleza kuwa wote walikuwa wanarudi hapo tena, kwa ajili ya kutoa mwongozo na ruksa ya kuanza mapambano dhidi ya adui alfajiri ile. Vilevile, alielezwa aweke vikosi vyake vyote kwenye tahadhari ili waweze kumsaka na kumkamata Willy Gamba akiwa hai.
"Karibuni, nitawapokea na nitawaweka kwenye nyumba ya mkufunzi wetu mkuu. Kamanda Moris ambayo ina ulinzi mkali pia inalindwa na mitambo ya kisasa ya usalama. Na mtakapokuwa pale kwake itakuwa rahisi kwenu kuona kwa macho jinsi majeshi yetu yanavyosonga mbele kupitia mitambo ya kisasa kabisa", Col. Bizimaziki alitamba.
Kundi zima liliondoka kuelekea uwanja wa ndege, likiwa tayari kuelekea Kibumba, ambako kuna umbali usiozidi dakika kumi kwa ndege, Jean alifikiria kuwa ni vizuri kuwa na ndege yake karibu, ikiwa kwa bahati mbaya kikatokea kitu na kutakiwa kuondoka ghafla na kujisalimisha aweze kufanya hivyo kwa ndege yake. Wakati wanaelekea uwanja wa ndege. Co. Gatabazi aliwasiliana tena na Nkubana.
"Uko wapi sasa?".
"Nimekwisha kuwasili Kibumba na sasa naelekea kwenye lango kuu la kuingilia ndani, nimewasiliana nao kwa radio wananisubiri", Nkubana alimweleza Col Gatabazi.
"Sawa, kazi yako kubwa ni kumkamata huyo Willy na kikaragosi chake huyo Bibiane na uwalete kule mlimani ilipo nyumba ya Kamanda Moris, sisi tutakuwa huku muda si mrefu", Col. Gatabazi aliagiza.
"Nitafanya hivyo afande. Mara hii kaingia mkenge yeye mwenyewe", Nkubana alijibu.
"Lakini mtu huyu ni hatari sana, naomba umwambie Kamanda Bizimaziki mchukue tahadhari kubwa sana. Hata tulipofika sitaki makosa yatokee", Col. Gatabazi alisisitiza.
"Sawa afande, tutafanya hivyo, lakini mtu mmoja na mwanamke mmoja wanaweza kufanya nini mahali kwenye kambi kubwa ya jeshi kama Kibumba?", Nkubana alihoji.
"Wewe chukua hadhari ya hali ya juu huyu mtu si wa kawaida", Col. Gatabazi alisisitiza na kuzima radio.
Nkubana alifahamu kuwa viongozi wake walikuwa na mashaka na Willy, lakini Nkubana yeye hakuna na wasiwasi. Aliamini kuwa huu ndio ulikuwa mwisho wa Willy Gamba. Ulinzi na uwezo wa kambi ya Kibumba ulikuwa mkali mno, kiasi kwamba ilikuwa vigumu sana kwa mtu mmoja kuingia na kutoka salama. Gari lilisimama na kumwondoa Nkubana katika mawazo yake. Walikuwa wamefika kwenye lango kuu na kusimama kama ilivyo sheria ya kusimama na kukaguliwa kabla ya kuingia ndani ya ngome hii.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nkubana alipoangalia saa yake ilikuwa yapata saa sita na nusu usiku.
"Saa ngapi sasa?" Bibiane alimwuliza Willy Gamba.
"Imefika saa sita na nusu sasa", Willy aliMjibu.
Walikuwa tayari wana saa moja ndani ya kambi hii ya kijeshi na bado walikuwa hawajapata tatizo lolote. Sasa ndio walikuwa wanaanza kutega mabomu kwenye bweni la mwisho ili baada ya hapo kama itawezekana watafute namna ya kutoka nje, kwani mabomu waliyokuwa wameyatega na kuyaprogramu kwa saa ya Willy ili kuyalipuwa lazima wawe mbali, maana yalikuwa na uwezo wa kuharibu kambi nzima na vitu vyote vilivyomo kama yangefanya kazi kama ilivyotarajiwa. Wakati wanafikiri hivi, ghafla taa za kiwanja cha ndege zikawashwa.
"Aha, kumbe ule ni uwanja wa ndege!" Willy alinong'ona.
"Ndio, unafikiri zile ndege za kijeshi zinaruka kutokea wapi!", Bibiane ambaye naye hapo awali alikuwa hajui uwanja ulikuwa wapi, alijibu.
"Kwanini wanawashwa taa wakati huu?", Willy alijiuliza.
Wakiwa wameduwazwa na kitendo hiki na wakiwa sasa wameondoka kwenye ukuta wa bweni la mwisho na kujibanza kwenye kivuli cha lori kubwa la jeshi lililokuwa limeegeshwa pale, Bibiane alijibu. "Huenda ndege za kivita zinatolewa ili zikashambulie mahali ama ndege ya Jean inataka kutua".
"Nafikiri hilo la pili ni sawa. Hii itakuwa raha sana mimi kukutana uso kwa uso na huyu bwana yako", Willy alikejeli Bibiane akafadhaika.
"Si bwana yangu tena, bwana yangu ni wewe Willy, maana wewe ndiyo uko na mimi sasa, sema, fanya kila unachotaka nifanye", Bibiane alijibu kwa sauti ya mahaba. Willy alimwangalia, kisha akamshika na kumbusu.
Mara wakasikia king'ola na askari wakatoka na kuanza kuelekea kwenye kiwanja cha ndege.
"Hapa kuna hatari, nafikiri wametushitukia", Willy alisema huku ile kengere yake ya hadhari ikilia kichwani mwake. Kisha akaendelea. "Kinachotokea hapa ni sisi kutoka ndani ya kambi hii. Wataanza kutusaka sasa hivi".
Mara tena wakasikia mwungurumo wa ndege na magari sita aina ya Landrover ya wazi yakiwa yamebeba askari yakielekea karibu na uwanja, yalipokaribia yakasimama. Kisha, yakafika magari mengine mawili aina ya Landcruiser GX nayo yakasimama pale vilevile kusubiri ile ndege itue. Pale kwenye uwanja mkubwa, vikosi vya askari vilizidi kujipanga kwa ajili ya mapokezi.
Ile ndege ilipotua watu wanne walitoka ndani ya Landcuiser zilizokuwa zimesimama kando na kusogea karibu ili kuilaki ile ndege. Wakiwa bado wamefichwa na kivuli cha lile Lori walitumia viona mbali vyao na kuwaangalia kwa makini wale watu waliotoka kwenye yale magari.
"Yule aliyetangulia ni Col. Marcel Bazimaziki, huyu ndiye kamanda mkuu wa majeshi yote ya Akazu. huyo wa kushoto ni Kapten Nkubana aliyekutoroka Kigali, ndiye aliyetumwa kuniua, kumbe naye keshafika huku. Wa kulia ni kamanda Morris huyu ni mkuu wa vikosi vya kukodiwa ambavyo vinafundisha majeshi ya Akazu. Huyu wa nyuma simfahamu".
Ndege ilisimama na milango ikafunguliwa na watu wakaanza kutoka. Jean ndiye alikuwa wa kwanza kutoka ndani ya ndege hii.
"Aha huyu ndiye Jean nafikiri?", Willy aliuliza.
"Bila shaka huyo ndiye Jean, ambaye ndiye mzizi wa fitina katika Rwanda. na yule anayemfuatia ni Anatoile Kabuga, huyo ndiye kiongozi wa Akazu, anayefuata ni Jenerali Kasongo, kamanda wa majeshi ya Rais wa Zaire, rafiki mkubwa wa Jean, anayetokea sasa pale mlangoni ni Col. Gatabazi na huyo anayetokea mwisho simfahamu, maana sijawahi kumuona", Bibiane alieleza.
"Asante, sijui bila wewe ingekuwaje, umefanya kazi yangu iwe rahisi kiasi fulani".
"Ni kweli, lakini ungetumia njia nyingine, wewe si wa kushindwa jambo".
Baada ya kutoka ndani ya ndege, kundi la Jean liliingia ndani ya zile Landcruiser wakaondoka huku wakisindikizwa askari kwa ulinzi mkali.
"Unadhani watakuwa wanaelekea wapi sasa?", Willy alimuuliza Bibiane.
"Sijui, nilitegemea huenda wanataka kuzungumza na vikosi vilivyofanya gwaride pale uwanjani, lakini wameondoka moja kwa moja kuelekea upande ambao ndiko kuna lango kuu. Huenda wanakwenda kupumzika kwa kamanda Morris, nyumba na ofisi ya kamanda Morris iko juu ya hicho kilima, huwezi kuona ukiwa hapa kwa vile kumefichika kwa miti", Bibiane alieleza.
Kati ya magari yaliyobeba askari moja halikuendelea na msafara isipokuwa lilielekea kwenye gwaride. Gari hilo lilipofika hapo lilisimama na watu waliotoka ndani walikuwa Nkubana na askari wengine watano. Kisha Nkubana akaanza kuhutubia hilo gwarinde na kikosi kimoja wapo kikapiga hatua moja mbele na vingine vikatawanyika. Willy na Bibiane hawakuelewa nini kilikuwa kinaendelea.
"Lililopo ni sisi kuondoka hapa kambini haraka iwezekanavyo. Vinginevyo tutakamatwa hata kabla hatujamaliza kazi iliyotuleta", Willy alieleza.
"Mimi bila kummaliza huyu Jean siendi kokote ng'o", Bibiane alijibu kwa hasira.
"Lazima ufahamu kuwa hatuwezi kukabiliana na watu wote hawa, lazima kutumia akili ya ziada, wewe unajua katika kazi yetu hii swala ni kuendelea kuishi; lazima uhakikishe unajilinda ili ubaki salama. Hapa tukitaka kuanza mapambano ni sawa na kujinyonga sisi wenyewe. Pili ili tuweze kulipua mabomu tuliyotega ni lazima tutoke nje kabisa ya eneo hili, la sivyo sisi pia tutakuwa tumejiteketeza pamoja na adui", Willy alimuasa Bibiane kisha wakaona wale askari wa kikosi wanakabidhiwa silaha na kuelekea kwenye seng'enge ya ua wa kambi.
"Ehe, umeona kazi hiyo, hawa jamaa wanategemea tutakuja hapa, lakini hawajui kama tumeingia ndani na kazi imefanyika", Willy alieleza.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Lakini wakifika pale tulipoingilia lazima watajuwa tuko ndani", Bibiane alijibu.
"Ndio sababu nikasema tutafute njia tutoke humu ndani", Willy alisisitiza.
Wakati wote Willy alikuwa akipanga mbinu za kuweza kutoka ndani ya kambi hii wakiwa salama.
"Hebu nifuate tuangalie hali ikoje upande wa lango kuu", Willy alimwambia Bibiane.
"Kule hatuwezi kupita, afadhari tuwahi palepale mahali tulipotumia mwanzo", Bibiane alisema na Willy akamuunga mkono na kuona alikuwa na mawazo sahihi hivyo, haraka haraka wakaelekea sehemu waliyokuwa wameingilia, huku askari wa doria wakizidi kujipanga na kupewa silaha ili kuzidi kujipanga kando ya ua huu wa seng'enge wakiwa tayari kulinda kambi yao. Ile tembetembea ya hawa askari kiasi fulani iliwasaidia sana akina Willy na Bibiane kutobainika mapema kwani walikuwa wamevaa mavazi ya kijeshi kama wale askari. Nkubana na watu wake waliweka ulinzi mkali upande la lango kuu wakiamini kuwa Willy angeweza kujaribu kuingia pale kambini kwa kutumia lango kuu.
Hakuna askari wala kiongozi katka kikosi chicho aliyefikiri kuwa adui wangeweza kupitia sehemu nyingine yoyote kwani waliamini kwamba hakuna kitu ambacho kingeweza kupita ua ulioizunguka kambi hii. Hivyo, hata hawakuweka askari kuzunguka ua ilikuwa ni kwa hadhari tu. Kumbe kitu ambacho hawakujua ni kwamba teknolojia yotote inaweza kushindwa na teknolojia nyingine yenye maarifa ya juu zaidi. Willy alikuwa ndani na tayari alikuwa ametega mabomu kila upande.
Huyu Willy Gamba lazima atakuwa kaingia hapa, hatujui kapita njia ipi na yuko sehemu gani?", Nkubana alimwambia Col. Gatabazi kwa njia ya radio.
"Haiwezekani, hakikisha kwanza", Col. Gatabazi alijibu kwa hofu.
"Hakika ni yeye Willy Gamba, tumekuta sehemu imechimbwa chini ya ua mita kama tatu hivi kwenda chini, hata hatujui imetumika nini kuchimba ardhi. Kwa maana hiyo, tumeanzisha operesheni kali ya kumsaka ndani na nje ya kambi, japokuwa hatuna uhakika kama bado yuko ndani ama ametoka. Hakika mtu huyu ni hatari sana, itabidi kuongeza ulinzi katika eneo hilo hususan mahali mlipo, nitatuma askari zaidi kuimarisha ulinzi hapo", Nkubana aliahidi.
"Kuna madhara yoyote kafanya huyo Willy", Col. Gatabazi alihoji kwa wasiwasi.
"Mpaka sasa hakuna, tumekagua sehemu zote ni salama isipokuwa hapa kwenye ua palipochimbwa ardhi, ni sehemu hii tu".
"Nani kagundua eneo hilo limechimbwa na muda gani umepita toka hali hiyo itokee", Col. Gatabazi aliuliza tena kwa shauku.
"Niko hapa katika eneo husika afande", Nkubana alijibu. Baada ya ukimya wa sekunde kadhaa akaendelea. "Askari wetu mmoja wa doria aliyepangwa kulinda eneo hili la ua anasema haiwezi kuwa zaidi ya dakika kumi na tano hivi zilizopita. Nafikiri bado hajaingia ndani, anasubiri ama ameona ndege wakati mnaingia, anaweza kuwa anajipanga kujaribu kuanzisha mashambulizi. Ujue yuko pamoja na Bibiane ambaye anaijua sehemu hii vizuri sana".
"Bibiane anataka kulipa kisasi, kwa hiyo lazima watakuwa wanaelekea hapa baada ya kuona tumetua kwa ndege, ongeza ulinzi, nafikiri umebashiri sawasawa", Col. Gatabazi alijibu.
Baada ya kuzungumza na Nkubana kwa radio, Col. Gatabazi aliwafahamisha wenzake kuhusu maelezo ya Nkubana. "Huyu mtu ni hatari sana, lazima atakuwa anaelekea hapa, nimeagiza ulinzi uongezwe zaidi. Nia yake ni kutuangamiza sisi kwani Bibiane atakuwa amemweleza yote kuhusu uongozi wetu. Naomba wote tuwe katika hadhari, huyu mtu ananitia wasiwasi maana anaonekana amepania ni mjuzi na haogopi kitu. Watu wa aina hii ni hatari sana", Col. Gatabazi alieleza.
"Hapa hawezi kuingia, ajaribu aone moto, hii itasaidia kumkamata kirahisi maana nyumba hii inalindwa na mitambo maalumu ya kisasa, kuna kamera zimetegwa eneo hili. Na tunaweza kuona sehemu zote zinazoizunguka nyumba hii kwa mara moja, kwenye chumba chetu kuna vifaa vya kuangalia usalama wa nyumba hii, kuna televisheni nne ambazo zinaangalia mzunguko wa eneo hili kwa umbali wa kilomita moja. Hii ina maana hata sehemu ya upande huu wa kambi tunaona. Halafu pale kambini kuna mitambo kama hii, sijui imekuwaje hawakuweza kumuona!", Kamanda Morris alieleza kwa mshangao.
"Hebu twende kwenye hicho chumba chako", Jean ambaye pia alianza kuingiwa na hofu, alieleza. Wakaelekea kwenye chumba cha mawasiliano na usalama wa kambi hiyo.
Walipoingia ndani ya chumba hiki waliwakuta askari kama sita hivi waliokuwa wakisimamia kuendesha ile mitambo ya ulinzi mle ndani. Wakiwa ndani waliweza kuona picha za maeneo yote yaliyozunguka ile nyumba, waliwaona pia askari waliokuwa wakilinda eneo hilo. Kwa kweli, kulikuwa na askari wengi kila mahali wakiwa tayari kupambana na adui kwa njia yoyote. Kupitia mitambo hiyo waliweza kuwaona askari wengine zaidi wakiongezeka na kujipanga kwa ulinzi zaidi.
Kwa vile kambi hii inao komandoo zaidi ya mia tano waliofuzu vizuri mafunzo yao, hii ilimpa jeuri Jean na Col. Gatabazi kuwa na imani kuwa hakuna adui anayeweza kuleta rabsha mbele ya vijana hao ambao pia walikuwa sehemu ya ulinzi wakati huo.
"Kukitokea kitu chochote cha hatari, sisi tutakuwa wa kwanza kukiona hata kabla ya askari wa hapo nje hawajakiona. Tumeweka taa kali za ulinzi ili eneo hili lionekane kama mchana na kamera zetu zichukue picha kwa ufasaha zaidi", Kamanda Morris aliwaeleza na kufanya wageni wake waridhike na maelezo hayo na kuamini kuwa hakuna madhara.
"Lakini ikitokea bahati njema Willy Gamba akamatwe, huyu atakuwa mfungwa mikononi mwangu, msimuue tafadhari, nileteeni hapa nimle nyama taratibu. Nasisikia kuonja nyama yake", Jean aliagiza.
"Na Bibiane?", Col. Gatabazi aliuliza huku akimwangalia Jean.
"Huyu nitapenda kufanya naye mapenzi kwa mara ya mwisho kabla hajaenda ahera", Jean alijibu huku uso wake ukionyesha uovu wa ajabu na mate yakimjaa mdomoni.
"Huyu mtu ni mgonjwa", Col. Gatabazi alijisemea moyoni.
"Tunaweza kuendelea na mkutano", Jean aliagiza baada ya kujiridhisha na hali ya usalama wa kambi, wakarudi kwenye chumba cha mkutano walikokuwa Kamanda Morris, Bizimaziki na wataalamu wengine wa kijeshi waliokodishwa, waliendelea kuwaeleza jinsi mipango ya mashambulizi ilivyokuwa imepangwa.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Meza moja ilikuwa na ramani ya nchi za Zaire, Rwanda na Burundi na baadhi ya nchi zote za maziwa makuu zikitumiwa kuonyesha jinsi ambavyo jeshi la Akazu lilivyojiandaa kusonga mbele katika kuivamia Rwanda, wakitumia askari wa miguu, magari ya kisasa ya kivita, vifaru, makombora ya masafa mafupi na marefu pamoja na ndege za kivita, yote ni kuivamia nchi hiyo kijeshi.
Wakiwa ndani ya kambi hii, Willy na Bibiane walijificha kwenye vichaka vilivyokuwa kando ya njia ambayo magari ya jeshi yalikuwa yanapita kuelekea kwenye jumba analoishi Kamanda Morris.
Walikuwa wamefanikiwa kuvuka kizuizi cha kwanza kutoka kambini bila kushitukiwa, na moja kwa moja walitumia vichaka kujificha huku wakiua askari waliokuwa wakilinda maeneo hayo, mpaka wakafika sehemu hii wakitafuta nafasi nzuri ya kuishambulia nyumba ya Kamanda Morris ili waweze kuukabiri uongozi wa juu wa Akazu.
"Ikitokea gari lisilo na askari wengi nyuma au hata likiwa na askari wawili ama watatu tulivamie na kulifanya letu ili tulitumie litupeleke kule juu bila kuwashtua walinzi. Kwa vile tumevaa sare zao tunaweza kujaribu kuingia mpaka ndani bila shida ndipo tuanze mapambano, kama tutakuwa bado hatujashitukiwa", Willy alimwambia Bibiane.
"Kama nilivyowahi kukwambia nyumba hii inalindwa kwa mitambo maalumu ya kisasa. Nje kuna kamera nne zinazopeleka picha kwenye televisheni ndani ya chumba cha udhibiti wa mitambo, ambamo kuna askari wanaangalia mitambo hii kwa zamu, kwa saa ishirini na nne kila kinachotokea nje kinaonekana kwenye televisheni hizi, kamera hizi ninafanya kazi katika mzunguko wa kilomita moja kutoka eneo la kambi. Vilevile ndani ya chumba hicho kuna vifaa vya kisasa kwa ajili ya kunanasa sauti na mazungumzo yoyote ya radio kwa radio kwa umbali wa zaidi ya kilomita mia moja. Pia wanaweza kunasa picha zinazoletwa kwa rada kama kuna kitu kinaruka sehemu hii. Hivyo, tukijaribu kufanya chochote lazima tutaonekana moja kwa moja", Bibiane alimuasa Willy.
Baada ya kutafakari kwa sekunde kadhaa, Willy alitoa kile kitochi chake chenye miali ya leza akampatia Bibiane.
"Sikia, mimi ninacho kingine, kama tutafanikiwa kuikaribia ile nyumba tutagawana njia, wewe utaelekea mashariki mimi nitapita magharibi, kitu cha kwanza kabisa ni kuua zile kamera za upande wako kwa kutumia miali ya chombo hiki. Ukiwasha tu na kuelekeza miali hii kwenye hizo kamera basi zinakufa papohapo, hazifanyi kazi tena. Harafu unaweza kukitumia haraka kukata ukuta kama tulivyofanya wakati tunaingia kwenye maghala ya silaha, Pia unaweza kukitumia chombo hiki kupofua mtu yeyeto macho. Tukifanikiwa kuifikia ile nyumba basi tuivamie na kuanza mapambano, hapo ndipo kuna kufa ama kupona. Jean na wenzake ama sisi. Tukifanikiwa tutaonana ndani, nataka umuonyeshe Jean mafunzo yote aliyokupeleka ulihitimu vizuri na unao iwezo mkubwa wa kutumia nafasi kama ulivyofundishwa".
Wakati Willy bado anaeleza waliona gari aina ya Landrover la jeshi linakuja, nyuma ya gari hilo kulikuwa na askari wawili waliokuwa wamesimama wakiwa wamevalia mavazi ya kijeshi kama wao.
"Gari hilo, kazi kwako Bibiane", Willy alitoa amri, na gari lilipokaribia wote walilirukia kwa nyuma na kuingia ndani bila kutoa kishindo. Wale askari wawili walikuwa wakizungumza huku wakiangalia mbele. Willy alimuonyesha ishara Bibiane, na kwa kutumia vipaji vyao vya karate, waliwavamia wale askari na kuwaua palepale na kisha kuwainamisha chini ndani ya lile gari bila kutoa kishindo cha kuwashitua wale waliokuwa mbele ya gari. Wakawalaza vizuri na kuwafunika kwa turubai lililokuwa ndani ya lile gari.
Kisha wakajifanya ndio wale askari kwani walivaa kofia za chuma za wale askari waliowaua. Gari lilipopunguza mwendo na kusimama, Willy alitoa ishara wote wakaruka na kuelekea pande mbili tofauti. Bibiane akaelekea kulia, Willy kushoto. Kwa vile wote walikuwa wamevaa nguo za kijeshi kama wale askari wengine, hakuna aliyewashitukia. Willy aliongoza kwenye ile nyumba bila wasiwasi huku akipigiana saluti na askari wengine wa pale. Alipofika karibu kabisa na nyumba ile aliona ile kamera. Wakati Willy anaiona ile kamera ya upande huu wa kushoto, Bibiane naye alikuwa akijipenyeza upande wa kulia, akaiona ile kamera wa upande wake.
Kama vile walivyoambizana, wote walitoa zile tochi zao zenye miali ya leza na kuzielekeza kwenye kamera hizo. Macho ndani ya zile kamera yalikufa palepale na kukatisha mawasiliano ya kutuma picha za pande zote mbili kwenye televisheni. Na baada ya kufanya hivyo tu Willy alijipenyeza na kwenda kuitafuta ile kamera ya upande wa kusini.
Mle ndani ya chumba maalumu kilichokuwa na mitambo walishituka baada ya televisheni zinazopokea picha kutoka kulia na kushoto kushindwa kutuma picha.
"Tumeingiliwa, hii si bure", Kiongozi wa wale askari waliokuwa wakiendesha mitambo ndani ya chumba alisema na kwenda kumweleza Kamanda Morris. Kamanda Morris na wenzake walikuwa katikati ya mkutano wakati yule askari alipofungua mlango na kuingia ndani.
"Kuna nini?". Kamanda Morris alimuuliza kwa shauku huku kundi zima likisimama kumwangalia yule askari kwa taharuki.
"Televisheni zote za kulia na kushoto hazileti picha, inawezekana zimeharibiwa", yule askari alisema.
"Tayari yuko hapa", Col. Gatabazi alijibu na kuinuka kutoka kwenye kiti. Kabla mtu mwingine hajasema lolote, mlango ulifunguliwa na askari mwingine kutoka chumba cha kingine mitambo nae akaingia na kueleza. "Sasa kamera zote hazileti picha".
Kundi zima la Akazu na mamluki wao wakaingiwa na hofu.
"Huyu mtu ameweza kufika mpaka kutuingilia hivi kwa namna gani, Nyinyi hamna ulinzi wa kutosha hapa", Jean alifoka kwa hasira huku akionyesha hofu.
"Usitahayali Jean, lazima ufurahi kuwa mtu wetu kajileta mwenyewe na hataweza kuondoka hapa akiwa hai", Col. Gatabazi alijibu huku akielekea mlangoni na kwenda nje akifuatiwa na Kamanda Morris.
"Twende zetu tukamsake, mambo yameiva sasa", Col. Gatabazi alimwambia Kamanda Morris.
Nkubana ambaye naye alikuwa amefika kwenye eneo la nyumba hii akiwa anahisi Willy na Bibiane wangekuwa wamefika, alizunguka eneo hili kwa hadhari kubwa huku akiwachunguza kwa makini kila askari waliokuwa karibu yake, aliwaangalia machoni mwake. Kutokana na kitendo cha pale mpakani alijuwa kuwa Willy na Bibiane walikuwa wamevaa sare za jeshi sawa na wao. Wakati Bibiane anapiga miali ya leza kuua ile kamera ya kusini Nkubana alikuwa karibu nae kabisa lakini alikuwa bado hajamtambua. Ile miale ilipotoka kwenye tochi ya Bibiane na kuunguza jicho la kamera likatoa mwanga wa kati baada ya sekunde kadhaa jicho lake likaungua.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nkubana alisitushwa na mwanga uliotokea na kuua kamera. Akamwangalia Bibiane na macho yao yalipokutana mara moja wakatambuana. Kama umeme Nkubana alitoa bastola yake kiunoni ili awahi kummalize Bibiane. Bila hata kufikiri kuwa Bibiane alikuwa fundi zaidi, alimuelekezea ile mionzi ya leza machoni na palepale akajitupa chini kukwepa risasi, Nkubana alipiga risasi hovyo kwani alikuwa amekwisha pofuka macho na kupiga makelele, "Bibiane huyu hapa kanipofua macho".
Risasi zote alizorusha Nkubana hazikumpata Bibiane ambaye alijiviringisha na kuinuka mahali penye mlango ambao Col. Gatabazi na Kamanda Morris walikuwa wanaufungua ili kutoka nje, baada ya kumsikia Nkubana akipiga kelele. Hivyo, mlango ulipofunguliwa tu, Bibiane alijitupa pale mlangoni na kuwakumba Col. Gatabazi na Kamanda Morris, kitu ambacho hawakukitegemea na wote wakaangukia ndani huku wakifuatiwa na risasi zilizoelekezwa kwa Bibiane.
"Acheni acheni kupiga risasi, mtaleta madhara makubwa", Ofisa mmoja wa jeshi la Akazu aliamru baada ya kuona kilichotokea. Bibiane ndiye aliyekuwa wa kwanza kuinuka na alipoinuka huku katoa Bastola yake, askari mmoja aliyekuwa analinda mle ndani alimpiga kichwani kwa kitako cha bunduki; Bibiane alianguka chini na kuzirai.
Jean, aliyekuwa anaangalia yaliyokuwa yanatokea huku akiwa amezugukwa na kundi la viongozi wa Akazu na marafiki zake wa jeshi la Zaire, aliagiza, "Msimuue. Nasema mpelekeni bafuni mmwagieni maji. Kwanza mfungeni kamba, sikujua mtoto huyu ni hatari kiasi hiki. Kumbe sikupoteza fedha zangu bure nilipompeleka kwenye mafunzo ya kijeshi. Nilikuwa nasikia sifa zake tu leo nimemuona mwenyewe akiwa kazini, nimefarijika sana".
Col. Gatabazi na Kamanda Morris sasa walikuwa wamesimama huku wakiwa na hasira ya kutaka kummaliza Bibiane.
"Wewe huna akili nzuri kweli, huyu mwanamke ni mtu hatari halafu unasema umefarijika, huyu ni mtu wa kuuawa sasa hivi si mtu wa kusubiri". Col. Gatabazi alihamaki.
"Poa, Col. tulikubaliana kuwa kabla sijamuua ni lazima nifanye naye mapenzi mara ya mwisho. Hakuna mwanamke aliyewahi kuniridhisha kimwili kama huyu. Ngoja azinduke halafu nitimize ahadi yangu ndipo nitakuachia umuue", Jean alieleza.
Willy aliposikia purukushani na milio ya risasi upande ule wa kusini na kelele alizopiga Nkubana alijua kuwa kwa Bibiane mambo tayari yameharibika. Alitumia hii vurugu na yeye akakimbilia ule upande wa kusini. Alipofika akamuona mtu anataka kubebwa ili aingizwe ndani, alikuwa haoni na hakujua yule ndiye alikuwa mtu aliyepambana na Bibiane na kupofuliwa macho. Kwa vile nia ya Willy ilikuwa kuingia ndani na kuwaangamiza viongozi wa Akazu, aliona amepata upenyo wa kuweza kufanya hivyo. Huku akijifanya kama mmoja wa askari wa pale, aliwahi na kumuondoa askari aliyekuwa anataka kumbeba Nkubana kumpeleka ndani na kumuonyesha ishara ambayo yule askari hakuelewa lakini akafikiri huenda yule ni askari mwenzake ndiye aliyeamriwa kufanya vile.
Willy alimshika Nkubana kiunoni na kumweleza. "Afande ngoja nikuongoze ndani ukapumzike, huyu mshenzi Willy atatutambua leo".
"Nia aibu kwangu, mimi Nkubana kufanywa hivi na mwanamke, mimi nia yangu ilikuwa kumuangamiza kabisa Willy kwa mikono yangu, nasikia uchungu sana", ndipo Willy alipotambua kuwa huyu aliyekuwa amemshika alikuwa Nkubana. Alifurahishwa sana na kazi ya Bibiane.
"Usihofu Afande, tutakulipizia, hapa huyo Willy kafika, atawezaje kutoka hapa, huyu mtu ni mwendawazimu. wakati Willy akieleza hayo walikuwa wamefika mlangoni na kuingia ndani ya sebule kubwa ya nyumba hiyo.
Bila kuhisi kuwa huyu aliyekuwa akimuongoza Nkubana alikuwa ni Willy Gamba, Col. Gatabazi alimweleza.
"Mkarishe pale kwenye kiti, halafu askari toka haraka mkamsake huyo Willy Gamba".
"Ndio Afande", Willy alijibu huku akielekea kwenye pembe nyingine ya ile sebule kulipokuwa na makochi. Wakati huo Willy alimsikia Kamanda Morris akitoa amri kwenye kipaza sauti kuwa askari wote walioko pale wapange mstari mara moja kuizunguka nyumba na kila mmoja amnong'oneze afisa wake lile neno la siri wanalotumia wakati wa usiku. Wakati huo huo Willy aliliona kundi la Akazu na Jean likizunguka meza na mmoja wao kutamka, "Nafikiri tuyaamrishe majeshi yetu yaanze kusogea, tunapoteza muda kwa huyu Willy, mtu mmoja asitupotezee muda hata kama ni hodari atakua wangapi, sanasana hawazidi mia, ndio atakuwa amefanya nini?", Kabuga alieleza.
"Namuunga mkono bwana Kabuga. Askari wachache wabaki wamshughulikie huyo Willy, wengine waanze kuelekea mpakani, huku kusubirisubiri kunaweza kutuletea madhara. Tumeshaona tuko tayari kabisa, hakuna wakati tumekuwa tayari kama wakati huu", Col. Gatabazi alieleza.
"Oke, nami nakubali, kwanza huyu Bibiane kesha fufuka?", Jean aliuliza.
Willy alikuwa amekwisha mkalisha Nkubana huku akili yake ikipiga hesabu za haraka namna ya kuwateka hawa Akazu na vibaraka wao.
"Wewe askari njoo hapa, na wewe uninong'oneze neno la siri tunalitumia usiku", Kamanda Morris alimwita Willy wakati alipotaka kutoka nje. Willy alikuwa hajui hilo neno la siri, hivyo mtego huo ulikuwa umemnasa. Karibu na Kamanda Morris alikuwepo Jean akaagiza chumba cha mitambo askari wamlete Bibiane aweze kuulizwa alipo Bibiane.
"Willy alimsogelea Kamanda Morris na ghafla alimrukia Jean na kumkaba na kuvuta kwenye ukuta, bastola kichwani kwa Jean na kusema, Jean huna haja ya kumtafuta Willy, niko hapa. Kundi zina lilisimama huku askari wote wakiwa wamepigwa na butwaa. Kamanda Morris, Jenerali Kasongo, Meja Masamba, wale askari wa kukodiwa na hata Nkubana, japo alikuwa kipofu walitoa bastola zao.
"Msifanye mchezo wowote, wekeni silaha zenu zote hapo kwenye meza, mkifanya mzaha huyu bwana yenu Jean atakuwa historia nitamwangamiza", Willy Gamba alieleza kwa ukali. Wote walijua hatari. "Na mtu asisogee hapa wala asiondoke humu ndani. Ila wamlete Bibiabe", Willy aliendelea kuamru.
"Fanyeni anavyosema", Jean alieleza huku akitetemeka huku mkojo ukimtoka chapachapa.
Kamanda Morris alitaka kutoka ili kwenda kumleta Bibiane, lakini Willy alikataa, "Mtu hatoki huku ndani, nimesema kwa lugha inayoeleweka, umenipata wewe Kaburu".
"Kampuni yenu ya mamluki naijua safari hii mmeingia hasara, mmetengeneza faida kubwa katika biashara hii, lakini leo nasema tena, safari hii mmeingia hasara".
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kamanda Morris alimwagiza askari mmoja amlete Bibiane, ambaye alikuwa tayari amepata fahamu. Na Kamanda Morris akawa amesema na neno moja ambalo Willy hakulielewa. "Umesema nini wewe kibaraka?", Willy alihoji huku macho yake yakionekana mekundu.
"Nimeita mwisho jina la yule askari", Kamanda Morris alijibu. Lakini Willy machale yalimcheza. Wakati bado anafikiria lile neno aliwahi kulisikia wapi, ghafla ukuta aliokuwa ameuegemea ukapitishwa umeme na yeye akamsukuma Jean upande mwingine na kuruka nyuma ya makochi.
Nguvu ya ule umeme ilikuwa kubwa kiasi cha kumfanya Willy kupoteza fahamu baada ya kuanguka chini. Kamanda Morris alikuwa amejiwekea usalama wa kila aina na alikuwa amemzidi Willy maarifa, mara moja kila mmoja alichukua silaha yake, na Bibiane kabla hajafanya lolote alikuwa ameshikiliwa vizuri na askari watatu.
"Mfungeni kwenye hicho kiti, sasa tutamla nyama vizuri", Col. Gatabazi aliagiza. Bwana Kabuga akiwa bado anatetemeka kwa kuwa mambo kama haya yalitokea kama miujiza alidai arudi kwenye ndege ili waondoke eneo hilo.
"Hapana, kaa uone maana ya utawala", Jean alijibu baada ya kuinuka kutoka mahali alipokuwa amedondoka na macho ya chuku akiwa ameyaelekeza kwa Bibiane aliyekuwa anafungwa kwenye kiti. Kisha, akamwendea Bibiane na kumnasa kibao, akisema "Mbio za sakafuni huishia ukiongoni, janja yako kwisha. Lakini kabla mwisho wako haujafika niliahidi nitafanya mapenzi na wewe kwa mara ya mwisho".
"Utawahi, kwani na wewe unadinda", Bibiane alijibu.
Jean alimnasa tena kibao na kusema, "Umesahau nilivyokuwa nakunyanyasa kitandani".
"Wewe ni mgonjwa na huu ndio mwisho wako", Bibiane alijibu kwa dharau.
"Unachekesha, huu ndio mwanzo wangu na mwisho wako", Jean alijibu na kugeuka nyuma, kwani wakati mawazo yake yakiwa kwa Bibiane, Kamanda Moris alileta kifaa cha umeme na kumfunga Willy kwenye kiti na kumtingishatingisha ili azinduke.
"Willy alipozinduka tu, Jean alikuwa wa kwanza kumfikia na kuanza kumpiga vibaya sana mpaka Willy akaanza kutoa damu puani.
"Wewe mwanaume gani, mpaka mwanaume mwenzako afungwe ndio umpige, si umfungue tuone nani mwanaume hapa, kati yako Jean na Willy", Bibiane alisema kwa dharau.
"Ngoja amalize hasira zake, huyu mshenzi hatufanyia mambo mabaya sana", Col. Gabatazi alidakia huku akisogea na kumchakaza Willy kwa makofi yaliyomfanya azirai tena.
"Basi inatosha, kabla hajala umeme nataka nimpe maneno yake. Nikimaliza kusema Kamanda Morris fanya kazi yako. Huyu tayari tumemhukumu kifo, na atakufa si kwa risasi bali kwa umeme, kama wahalifu waliohukumiwa kunyongwa kule Marekani.
"Kufa si tatizo, kila mtu atakufa", Willy alisema baada ya kuzinduka na kuongeza, "Ila hata mkitumaliza leo, lakini hamfiki popote".
"Wewe ni mwehu, sisi tuna jeshi la kuikamata Rwanda chini ya wiki moja, unasema nini mwehu wewe, utapata habari utakapokuwa ahera", Col. Gatabazi alitamba.
"Wewe ndiye nani", Willy aliuliza.
"Mimi ndiye Col. Gatabazi".
"Nijulishe basi kwa wengine maana kata anayehukumiwa kifo hujui majaji waliomhukumu", Willy alihoji akiwa na maana ya kuvuta muda kama kuna njia nyingine ya kujiokoa aweze kufanya hivyo.
"Huyu hapa ni Anatoire Kabuga, ndiye kiongozi wa Akazu. Najua unafahamu Akazu ni nini. Wale rafiki zetu toka jeshi la Zaire. Anayeingiza ni Col. Marcel Bizimaziki, ambaye ni kamanda wa Akazu anayesaidiwa na huyu mzungu. Kamanda Morris kutoka kampuni ya kijeshi ya Afrika Kusini. Na waheshimiwa huyu ndiye adui yetu namba moja Willy Gamba, kutoka Tanzania lakini na yeye tuna habari kuwa kazi hii anaifanya kwa kukodishwa. Hivyo, hawakilishi msimamo wa Tanzania hata kidogo katika suala hili; yeye na Kamanda Morris hawana tofauti na huyu Bibiane ni msalti kama mnavyomjua. Niliwahi kumshawishi Jean kuwa karibu sana na mwanamke akajua siri zake ni balaa kwani wao fikira zao zinatoka chini na si juu kichwani. Si watu hawa, lakini hakunisikia, sasa ona madhara aliyotufanyia", Col. Gatabazi alilalamika.
"Kazi na dawa, bila kuwa karibu na mwanamke mzuri anayekupa mapenzi vizuri huwezi kufikiri sawasawa, usisahau Col. Gatabazi hata sisi tumenufaika sana na huyu kiupmbe, mimi binafsi nilikuwa na bahati ya kufaidi mwili wake hivyo usinionee wivu, ngoja nikafaidi mara ya mwisho", Jean alijibu. Akimuonyesha ishara askari aliyekuwa karibu amfungue kamba ili ampeleke chumbani. Willy sasa fahamu zake zilikuwa zimerudi na akili yake ilikuwa ikifanya kazi ya ziada namna ya kuponyoka toka ndani ya balaa hii.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Aliona azidi kununua muda kidogo wa kuomba.
"Huenda nimefanya yote haya bila kujua undani wa suala zima hili, kwa sababu kwa akili ya mtu yeyote haya mauaji mliyofanya na kuyatekeleza yanafanya akili isikubali maana yalikuwa ya kikatili na kunyama. Kabla sijanyongwa naweza angalau kuelezwa sababu zilizowafanya mkatekeleza mauaji mabaya ya aina hii ambayo ni ya kipekee baada ya Dikteta Hitler?".
Wakati Willy anamuuliza Col. Gatabazi, Jean na Kamanda Morris walikuwana wananong'onezana na Kamanda Bizimaziki ili askari waondoke kuelekea mpakani. Willy, huku macho yakifunguka kwa shida kutokana na kipigo aliweza kuwaona jinsi wanavyonong'onezana na vilevile akaweza kuona jinsi Bibiane anavyofunguliwa kamba kutoka kwenye kiti na kupelekwa kwenye mlango uliokuwa ukielekea chumbani. Aida, alihisi Jean alikuwa anataka kufanya nini. Yote haya yalifanyika wakati Willy akiongeza kasi ya kuwaza jinsi ya kujinasua ili aweze kukamilisha kazi yake iliyomfikisha haba badala ya kukata tamaa.
Acha mimi nimjibu, wewe endelea na shughuli inayotusubiri, ambayo ni muhimu zaidi. Nimefurahi kuona kuwa huyu Willy anataka kujua sababu na sababu nitazitoa mimi", Anatoile Kabuga, Kiongozi wa Akazi, alijibu huku akiangalia saa yake iliyoonyesha kuwa ilikuwa saa nane na nusu usiku.
Meja Kasubuga alipigana vikali na jeshi la Luteni Nyamboma na kufanikiwa kuwazidi nguvu na hivyo askari wa jeshi hilo walilazimika kukimbilia mpakani. Luteni Nyamboma alikuwa amepoteza askari wengi sana, walipfika mpakani wakitegemea kumkuta Nkubana ili awaongezee nguvu ya askari warudi kuendeza mapambano, lakini hakumkuta Nkubana. Hivyo, Luteni Nyamboma akaamua kuelekea Kibumba na masalia ya askari wa kikosi chake waliobaki. Luteni Nyamboma alipoangalia saa yake ilikuwa saa nane usiku. Walitumia magari waliyoyakuta pale mpakani, Luteni Nyambona na askari wake waliondoka kuelekea Kibumba.
Hata hivyo, Luteni Nyamboma alilazimika kuwaacha askari wa jeshi la Zaire pale mpakani kwa ajili ya ulinzi ili baada ya kazi ya Gisenyi Luteni Nyamboma awafuiate Kibumba.
Meja Kasubuga alipofika mpakani aliyaona magari yanaondoka kasi eneo la mpakani. Meja Kasubuga akagundua kuwa magari yale yalikuwa yakielekea Kibumba. Asingekuwa ameamriwa na Col. Rwivanga awasubiri pale mpakani hakika Meja Kasubuga angeyafuata magari yaliyoondoka na kikosi kile. Baada ya kufika mpakani, jeshi la Meja Kasubuga lilifanikiwa kukitwaa kikosi cha jeshi la Zaire kilichokuwa kikiwasaida wanajeshi la Intarahamwe na hii ikawa ngome ya jeshi lake kwa muda.
Kikosi hiki kilichokuwa mpakani mwa Zaire na Rwanda kilikuwa kimejijenga vizuri kivita, kikiwasaidia wanajeshi wa Intarahamwe na kundi la Akazu lililokuwa likifanya jitihada ya kuivamia serikali ya RPF ili kutwaa madaraka ya kuiongoza Rwanda kijeshi.
Baada ya kuhakikisha usalama wa eneo hili, Meja Kasubuga alielekea sehemu iliyoandaliwa, ambayo Col. Rwivanga alimweleza kuwa angetua hapo kwa Helikopta akiwa na kiongozi wa kikundi cha Banyamulenge na kiongozi wa vikosi vya vyama vinavyoipinga serikali ya Zaire. Meja Kasubuga alipoangalia saa yake ilikuwa saa nane na dakika kumi. Muda ambao Col. Rwivanga aliahidi kuwa atafika Gisenyi. Hivyo, Meja Kasubuga na kikosi chake wakaamua kusubiri.
Col. Rwivanga alikuwa na matumaini makubwa na kikosi cha Meja Kasubuga, hivyo baada ya kuondoka Kigali kwa Helikopta ya jeshi, walisafiri moja kwa moja usiku huo kuelekea Gisenyi. Col. Rwivanga hakuwa na papala wakati wote alikuwa akitafakari jambo kabla ya kulifanyia kazi. Alikuwa mmoja wa maofisa wa jeshi walioheshimiwa na kutegemewa sana na serikali ya Rwanda. Alikuwa mtu mwadilifu asiyependa kuisalti nchi yake, kutokana na msimamo wake dhabiti aliogopwa sana na vibaraka hususan wanaotaka kuigawa Afrika.
Alikuwa akijitosheleza kiulinzi, kutokana na hali hiyo nyumba yake haikuwekewa ulinzi kutoka jeshini, kama ilivyo kwa maofisa wengine wa ngazi za juu kama yeye. Alikuwa mmoja wa makomandoo wa jeshi waliofuzu vizuri mafunzo yake, lakini kutokana na cheo chake jeshini alibaki kuwa ofisa wa jeshi aliyeheshimiwa sana. Alikuwa mpole asiyependa makuu, alikuwa na subira, hata ukimchoma kidole machoni hatakufanya kitu. Lakini akilazimika kuchukuzwa na upuuzi alifanya kitu ambacho hakuna awezaye kuamini, hakuwa na mchezo tena. Huyo ndiye Col. Thomas Rwivanga, Afisa wa jeshi mwandamizi.
Anatoile Kabuga alimwangalia Willy kwa jicho baya sana, alimuona kuwa ndiye kikwazo na adui wao namba moja kwa kuwachelewesha Inyenzi na washirika wao kushika madaraka ya nchi ya Rwanda. Hata hivyo aliamini kuwa hakuna mtu mwingine zaidi ya Willy atakayeweza kupena na kuingia katika ngome yao.
"Nitakupa historia kidogo", Anatoile Kabuga alianza kumweleza Willy Gamba. "Willy Gamba, lazima ufahamu kuwa sehemu hii ya Maziwa Makuu katika Afrika watu wa kwanza wa asili ni wabantu. Wabantu ndio walioishi eneo hili la Maziwa Makuu kwa karne nyingi sana tena wakiishi kwa raha mstarehe bila migogoro wala matatizo mpaka walipokuja watu wenye asili ya Kihemetiki ambao baada ya kufika eneo hili walianza kuleta chokocoko, vita wakitokea Kaskazini na Mashariki mwa Afrika. Kwa ufupi, Watutsi wamo kwenye kundi hilo. Tangu wafike katika sehemu hii amani imekosekana kabisa. Karne mbili zilizopita walianza kuweka Ufalme wao katika eneo hili baada ya vita vikali na wabantu wa sehemu hii na kuwashinda. Waliweka wafalme wao waliowaita wafalme wa Kihima ambao walitawala kutoka Bahari ya Hindi mpaka Atlantiki, sehemu ambayo sasa ni Zaire, Rwanda, Burundi, Tanzania, Uganda na Kenya", alinyamaza kidogo kisha akaendelea.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Willy Gamba. Nitakueleza kwa kifupi sana maana hatuna muda wa kupoteza. Lakini kwa sababu wao walikuwa wachache na wakawa wanaendeleza utawala wa mabavu na unyanyasaji kwa wabantu ambao ndio waliokuwa wengi, hali inayoendelea mpaka sasa, mapigano ya kuukataa utawala huo yaliendelea sehemu zote, hatmaye ufalme huo ukaangushwa katika sehemu zingine na kubaki sehemu ambayo sasa ni Rwanda na Buurundi. Na hali hii iliendelea mpaka wakati wa Ukoloni ambapo katika Rwanda utawala wa ukandamizazi wa Watutsi dhidi ya Wahutu na wabantu ambao ndio wengi katika Rwanda, uliendelea. Miaka yote hii mpaka vita vya pili vya dunia Watutsi wachache waliendelea kutawala na kuwanyanyasa Wahutu wakihakikisha kuwa hawapati elimu, madaraka na hata mali. Ni mpaka juzi tu, mwaka 1957, Wahutu walipojikomboa na kushika madaraka, na hawa Inyenzi wakakimbilia nchi jirani ikiwemo Tanzania. Wakati wa utawala wetu tulijaribu sana kuwaweka karibu lakini siyo wote waliotaka kutawaliwa na walio wengi sababu wao walijiona wana hadhi ya juu kuliko sisi. Vilevile, waliapa kuwa lazima watatafuta njia mbadala warudi kututawala maana sisi ni watumwa wao. Na kwa taarifa yako kila Mtutsi anamuona kila Mbatu kama mtumwa wake. Ndivyo wanavyokuona wewe hata kama unawasaidia kwa sababu wewe ni Mbantu na ndivyo wanavyoniona hata mimi. Sasa basi tatizo kubwa lilikuja wakati nchi jirani ilipopata kiongozi mwenye asili hiyohiyo ya Kitutsi, na akawa na nguvu na akaahidi kuwasaidia Wahutu ili wautoe utawala wa wabantu katika Rwanda, Yaani watu wenye asili ya Kitutsi tu ndio watawale sehemu hii ya maziwa makuu ikiwemo Zaire, Rwanda, Burundi, Tanzania, Uganda na Kenya. Sisi tulipopata habari hizi tukajua eneo lote hili la maziwa makuu halitapata amani ikiwa hawa Watutsi wanazidi kuzaliana na kuwa wengi eneo hili. Njia pekee ya kuleta amani ni kuhakikisha mmewaua waume, wake kwa watoto, ili kuua kabisa nguvu yao. Leo hawa tusipowaangamiza nakueleza wewe Willy Gamba, Tanzania haitakuwa na amani na wala Zaire, Uganda na Kenya hawana amani maana hawa wana asili ya kujipanua. Ni watu hatari ajabu, na kama mngejuwa kuwa hawa ni watu wa kuteketezwa kabisa hata mmoja asionekane katika sehemu hii".
"Ngoja nikukata kauli, umesema watu wengi katika eneo hili la maziwa makuu ni wabantu, hawa Watutsi wachache watatawala vipi", Willy aliuliza huku akisogeza vidole vya mkono wake wa kulia kujaribu kama vingeweza kuifikia saa yake aliyovaa mkono wa kushoto.
"Unasema nini, tunavyozungumza nani anatawala Rwanda, Burundi na Uganda, watu wengi katika nchi hizi ni watu gani, sisi wabantu, sasa nini kitawashinda kutawala Zaire, Tanzania na Kenya kama wameweza katika nchi hizo, njia pekee ni kuwateketeza ili waishe, wasiendelee kutunyanyasa na kuleta vita vya mara kwa mara katika eneo letu. Hawa na Wayahudi hawana tofauti. Ngoja nikwambie Willy Gamba, hawa Watutsi hata kama ukiona Mtutsi amezaa na wewe lazima atatembea na Mtutsi mwenzie ili azae Mtutsi, kazi yako wewe itakuwa ni kukuza damu isiyokuwa yako. Na wamehakikisha wanawake wao wamesambaa dunia nzima, lakini kila mwanamke wa Kitutsi ahakikishe mahali alipo anapewa mimba na Mtutsi mwenzie tu. Huku wanawake wao kusambaa ni njia mojawapo ya kujipanua ili waweze kufanya kampeni yao kwa kuhurumiwa na mataifa mengine. Hivyo, mauaji haya tuliyofanya ni kwa niaba ya wabantu wote na sasa hivi tuko tayari kuurudisha utawala wetu Rwanda na Burundi ili heshima ya mbantu katika eneo hili ipatikane. Baada ya kuichukua tena Rwanda mara hii tutataka viongozi wote katika eneo hili waelewe ukweli huo na watuunge mkono kuwatokomeza Watutsi hawa. Vinginevyo nakwambia Willy Gamba watatawala tena sehemu yote hii, la sivyo hakuna amani katika eneo hili. Vita vitaendelea kwa miaka mingi. Sisi Akazu ndio tumaini pekee la sehemu hii, bila sisi kesho tawala zote za sehemu hii zinazotawaliwa na wabantu zitatikiswa na kumalizwa. Hivyo, wewe Willy ni msaliti, unawasalti wabantu kwa kuwasaidia Inyenzi ili waweze kutawala ardhi halali ya wabantu. ndio sababu tumekuhukumu kifo. Na, wote wawe wabantu au taifa lingine, wakibainika wanasaidia Inyenzi lazima wauawe. Na sasa wewe utauawa ili Akazu ifanye kazi yake ya kuwakomboa wabantu", Kabuga alisema kwa sauti nzito iliyoashiria hasira ya ajabu ambayo kila mtu pale ndani alihisi kapagawa.
"Yote hayo uliyoyasema yanaweza kuwa na ukweli mwingi tu, lakini ukweli huwa hautoi uhalali wa kuangamiza kabila zima. Hii ni kinyume na haki za binadamu. Njia nyingine itafutwe kuwadhiti na si kuwaangamiza", Willy alijibu huku kidole chake cha karibu na gumba kwenye mkono wa kulia kikiwa kimefika kwenye ufunguo wa saa yake na kukandamiza ufunguo wa saa na kusubiri kuona kifo chake ama kifo cha jeshi la Akazu.
"Unasema haki za binadamu, sisi wabantu hatuna haki mbona............", Kabuga hakumaliza sentensi yake teknolojia ilianza kufanya kazi yake.
Col. Rwivanga, Mpinda na Meja Tom Kabalisa waliwasili mpakani mwa nchi za Rwanda na Zaire katika sehemu waliyokuwa wamekubaliana na Meja Kasubuga mnamo saa nane na dakika arobaini usiku.
Hali ya usalama ilikuwa imeimalishwa katika eneo hili, ambapo vijana wa Meja Kasubuga walikuwa makini kwa kila jambo, baada ya Helikopta ya jeshi la Rwanda waliyosafiri hadi mpakani kutua, Col. Rwivanga alikuwa wa kwanza kushuka akifuatiwa na Mpinda, kasha Meja Kabalisa.
"Mambo yakoje hapa", Col. Rwivanga alimuuliza Meja kasubuga wakati wakisalimiana baada ya heshima ya kijeshi.
Meja Kasubuga alieleza kwa urefu jinsi mapambano yalivyokuwa, kisha akamalizia, "Huyu Willy atakuwa kauawa kule Kibumba maana kajipeleka mahali ambapo panatakiwa vikosi vyote husika, huyu Willy ingawaje Afande unamsema ni hatari lakini hana akili ya tahadhari, angesubiri twende wote, ndipo angeweza kuwa msaada kwetu maana maiti haina msaada wowote.
"Nakubaliana na wewe lakini yule ni mtu mwenye maisha mengi, unaweza kumuona kaibuka", Col. Rwinga alisema wote wakacheka kwa utani huo.
"Kweli, akiibuka tena atakuwa mtu wa maisha mengi", Meja Tom Kabalisa wa Banyamulenge alijibu kwani na yeye alijua nguvu za Intarahamwe kule Kibumba na ndio sababu alikuwa hajathubutu kufanya lolote. Kisha akaendelea. "Col. Rwivanga, nafikiri sasa tumweleze Meja Kasubuga mipango ikoje ili....", Kabla Meja Kabalisa hajamaliza kusema sentesi yake, mripuko mkubwa usio kifani ulisikika mpaka huko walikokuwa.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Ooh Willy Gamba, kweli u-hatari", Meja Kasubuga aligwaya.
Wakati huo Jean alikuwa ameanza kumvua nguo Bibiane ili atimize ahadi yake kama alivyoahidi kuwa atafanya nae mapenzi kabla ya kumuua, wakati akikaribia kutimiza ahadi yake, ghafla mlipuko mkubwa ulitokea eneo hilo na kuleta hofu, palepale nyumba ile ikasambaratika vipande. Bahati nzuri nyumba hii ilikuwa imetengenezwa kwa mbao tupu ili likitokea tatizo kama hili Kamanda Morris asihatarishe maisha yake.
Kwa vile Bibiane alikuwa akiutegemea mlipuko kama huo, ulipotokea tu hakuzirai kama wengine. Alizitupa mbao zilizomwangukia mwilini mwake, akainuka na kuanza kumsaka Willy ambaye wakati huo alikuwa amefungwa kwenye kiti pale ukumbini. Kumbe mlipuko ulipotokea kile kiti kilirushwa pamoja na Willy Gamba mpaka nje kwenye bustani. Bibiane aliangalia huku na huko kwa tahadhari kubwa, maana watu wote walikuwa wamelala chini kwa hofu. Vilio vilisikika eneo lote la kambi hii mara akamuona Willy Gamba na kiti chake akiwa nusu amezirai.
Milipuko ile iliendelea kuleta hofu na kusababisha mwanga mkubwa katika eneo lote. Milio na mwanga ilionekana na kusikika mpaka Goma, Gisenyi na sehemu nyingine kwani sasa mizinga na makombora nayo nayo yalianza kulipuka bila mpangilio na kusababisha Jean na wenzake kupatwa na taharuki. Bibiane alitoa kisu chake kidogo alichokuwa amekifika kwenye nywele zake, akiwa tayari kabisa kummaliza Jean. Na kwa kutumia hiki kisu alifanikiwa kuzikata kamba alizokuwa amefungwa Willy Gamba kisha akamtingisha hadi Willy akapata fahamu. Baada ya Willy kuzinduka Bibiane akamshika mkono. Willy alisimama wakakimbia kuelekea sehemu ile ya Magharibi ya kambi mahali ambapo kulikuwa na mstu mkubwa.
Walipokimbia kama mita hamsini hivi Bibiane alitoa bomu la kurusha kwa mkono akalitupa kwenye ile nyuma kisha wakajitupa chini. Bomu hilo liliporipuka likasambaratisha eneo hilo halikubakiza mtu wala kitu kilichokuwa ndani ya nyumba hii au mita thelathini kuzunguka nyumba hii. Wakati wanaelekea kwenye ule mstu mabomu, mizinga na makombora yaliyokuwa ndani ya maghala makubwa ya kuhifadhia silaha yaliendelea kuripuka yenyewe.
"Kazi ipo Willy, wamelikoroga acha walinywe sasa", Bibiane alisema kwa kebehi.
"Kazi yenyewe si kidogo, wamelala matajiri wataamka masikini", Willy alijibu wakiwa wemeingia kwenye msitu.
"Naona sasa tumechoka, kazi hii inatosha kabisa kwa siku moja ya leo", Willy alieleza wakiwa wametokeza kwenye sehemu ya majani mazuri chini ya mbaramwezi. "Hapa panafaa kupuzika, au vipi", Willy aliuliza.
"Hapa tumetafutiwa na Mwenyezi Mungu ili tupumzike baada ya hii kasheshe. Nilikuwa natamani ufike muda nipate mahali ambapo dunia itakuwa mimi na wewe tu. Na mahali hapo ni hapa, yaani mimi, wewe, mbaramwezi, nyota, malaika na Mungu", Bibiane alieleza.
Willy alivua gwanda lake la juu akatandika chini kwenye majani, Bibiane akavua pia na kusema. "Hili tutajifunika".
Willy akamwinua na kumbeba mikononi kisha akambusu na kumlaza juu ya gwanda lake.
KAMPALA
JKS aliamka mapema asubuhi huku roho yake ikiwa na furaha nyingi sana. Sasa hivi alikuwa akielekea benki kwa ajili ya kuchukua pesa zake. Hisia za urais wa Tanzania zilimjia katika mawazo yake, akatamani kuwa kiongozi wa Tanzania ili atimize ndoto yake ya kuwa mheshimiwa rais wa Tanzania.
Baada ya kustafutahi kwa chai nzito, alipiga simu kwenye benki yake hapo Geneva na kuuliza mahali ilipo. Baada ya kupata maelekezo sehemu na mtaa ambao benki ipo, alipiga simu mapokezi na kumuomba mhudumu amletee teksi saa tatu kamili ili impeleke benki.
Baada ya kujiweka sawa, alitelemka chini taratibu ilikuwa majira ya saa tatu kamili, akiwa amebeba mkoba wake wa ngozi ya mamba mkononi aliokuwa amepewa kama zawadi na rafiki yake Jean.
Alipofika chini alikuta teksi inamsubiri mbele ya hoteli. Alifungua mlango wa nyuma kama VIP akaingia, akampa dereva anuani ya benki, baada ya kuthibitisha ni eneo gari dereva aliondoa gari huku mawazo ya JKS yakiwa juu ya baraza lake la mawaziri baada ya kuukwaa urais.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Jean alikuwa amempa jina la meneja wa benki na kumweleza kuwa akifika benki amwone meneja huyo. Alipofika benki alitelemka na kumwambia mwenye teksi amsubiri akaingia ndani ya benki na kuelekea mapokezi. alimwonyesha yule msichana wa mapokezi jina la meneja. Asubuhi ile meneja alikuwa bado hana watu wengi, hivyo akamkaribisha vizuri sana.
"Karibu Mheshimiwa, nikusaidie nini?", meneja wa benki aliuliza JKS baada ya kuingia ofisini kwake.
"Asante", JKS alijibu na kutoa bahasha yenye maelezo yake yote. Meneja aliipokea kwa tabasmu na kuifungua bahasha na kuanza kusoma. Alivuta Kompyuta yake na kuanza kushughulika. Meneja, akiwa anatabasamu tena alimgeukia JKS na kumweleza, "Samahani, hii akaunti imefungwa jana na aliyeifunga ametoa pesa zote na kusema mtu yeyote akifika hapa kuuliza juu ya akaunti mwenye kitambulisho namba hii, aelezwe kuwa akaunti hiyo imefungwa maana mkataba umeisha. Samahani sana mheshimiwa, nina wateja wengine wananisubiri".
JKS alichanganyikiwa. Aliinuka, mara akamuona yule meneja wa benki anakuwa mkubwa zaidi na yeye JKS anakuwa mdogo na chumba kinazidi kuwa kidogo, akasikia anakosa pumzi halafu giza nene likamuingia mara akaanguka chini na kupoteza fahamu.
Ilikuwa yapata saa moja asubuhi Willy aliposhituka kutoka usingizini baada ya kuota ndoto mbaya ya vita ambayo aliota Bibiane akipigwa risasi sita kifuani na kupoteza maisha, alipotaka kupiga kelele alishituka kutoka usingizini, akamwona Bibiane amemlalia kifuani wakiwa kitandani akakumbuka kuwa kumbe walikuwa Hoteli ya Sheraton, iliyoko mjini Kampala, baada ya kuletwa hapa jana jioni kwa ndege ya serikali ya Rwanda baada ya kuchukuliwa na helikopita ya jeshi ya akina Col. Rwivanga kutoka kule porini Kibumba walikolala baada ya usiku wa kasheshe walipofanikiwa kuiteketeza ngome ya Akazu. Taratibu Willy alimwondoa Bibiane kwenye kifua chake na kumlaza kwenye mto. Alichukua chombo cha kuwashia televisheni ili kusikia taarifa ya habari ya saa moja.
Baada ya kuwasha televisheni mtangazaji alisoma taarifa ifuatayo.
"Zaire. Vikosi vya wapinzani wa serikali ya Zaire, vikiongozwa na mpinzani mkuu Bwana Mpinda vimeanzisha mapigano makali dhidi ya serikali hiyo vikisaidiwa na vikosi vya waasi wa kabila la Banyamulenge vikiongozwa na Meja Tom Kabalisa Mubanyamulenge, aliyeasi kutoka jeshi la Zaire. Bwana Mpinda amekaririwa na vyombo vya habari kuwa nia yao ni kuuondoa utawala wa kidikteta wa serikali iliyoko madarakani Kinshansa. Wamejigamba wakisema usiku wa kuamkia jana walishambulia kambi kubwa ya kivita iliyoko Kibumba, karibu na Goma na kuteketeza silaha nyingi, vikiwemo vifaru, ndege za kivita, mizinga mkibwa na midogo na kuua askari wapatao elfu kumi".
"Pamoja na kwamba habari hizi hazijathibitishwa na vyombo vingine vya habari vya ndani na nje, raia wa sehemu hiyo wamethibitisha kutokea kwa milipuko mkubwa ya ajabu ambayo hawajawahi kuisikia katika kambi hiyo. Na wanasema wanajeshi karibu wote na silaha zilizokuwa kwenye kambi hiyo zimeteketezwa kwa milipuko hiyo iliyosikika mpaka Gisenyi na Goma".
"Habari zilizotufikia hivi punde katika chumba chetu cha habari zinasema waasi tayari wamekamata miji wa Goma na Bukavu na bado wanasonga mbele kuchukua maeneo mengine. Vilevile, kuna habari ambazo hazijathibitishwa kuwa vikosi hivyo vya wapinzani vinasaidiwa na vikosi vya jeshi la RPF la Rwanda".
"Hii ina maana kuwa wapinzani wamekusudia kuung'oa utawala wa sasa ambao umedumu madarakani kwa zaidi ya miaka thelethini sasa ambao wameupachika jina kuwa utawala wa mabavu, unyanyasaji uliojaa rushwa na udikteta. Bado hakuna taarifa yoyote ya kukanusha habari hizo kutoka kwa serikali ya Zaire, mji Kinshansa".
"Na huko Jijini Dar es Salaam, Tanzania kuna habari kuwa waziri wa ngazi ya juu nchini humo kwa jina maarufu la JKS amefariki dunia akiwa katika benki moja huko Geneva, Uswisi baada ya kupatwa na shinikizo la damu. Kiongozi huyo aliondoka nchini Tanzania siku mbili zilizopita na kuelekea London kwa ajili ya matibabu ya moyo, bado haijabainika kwa nini alikwenda Geneva, na alifuata nini kwenye benki hiyo. Waziri huyo ndiye aliyekuwa akitegemewa kuwania urais wa Tanzania baada ya rais wa sasa kumaliza muda wake".
Willy alitabasamu baada ya taarifa hii iliyonoga. Kisha, akachukua simu na kumpigia Mzee Musoke na kumwomba waonane mchana kama walivyokuwa wamepanga wakati akiwa mjini Kigali ili ampatie ripoti ya kazi yake aliyoifanya kwa mafanikio.
"Nimefarijika kusikia kazi yako kwenye taarifa ya habari ya asubuhi hii, wewe ni mwanaume wa shoka", Musoke alimsifu Willy.
"Asante mzee, tutaonana hiyo saa nane", Willy alimjibu Musoke na kukata simu. Kisha akapiga simu nyingine.
"Pepe mpenzi".
"Uko wapi", Pepe aliuliza.
""Niko Kampala narudi kesho".
"Ooh Mungu wangu, toka umeondoka sijapata usingizi. Njoo mume wangu nina hamu sana na wewe, nakupenda sana".
"Na mimi zaidi, kesho mama, kwaheri", Willy akakata simu.
Bibiane alikuwa akisikia lakini alijifanya kama hamsikii alimgeukia Willy na kusema. "Uko wapi Willy?, njoo ulale, najua siku yangu ni leo tu, hivyo lazima niitumie siku hii kikamilifu".
"Katika nafsi yangu hupenda mtu anayeelewa mambo kama wewe", Willy alijibu huku akirudi ndani ya shuka na kumkumbatia Bibiane.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
MWISHO wa HADITHI YA UCHU
0 comments:
Post a Comment