Simulizi : Uchu
Sehemu Ya Nne (4)
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kwa kutumia pesa, Jean aliweza kuwakamata wakuu wa nchi nyingi duniani, hasa katika Afrika na Asia, lakini vilevile viongozi wa ngazi za juu katika serikali za nchi za Ulaya. Alipata kila alichokitaka kwa kutumia pesa. Hivyo, simu ilipolia alijua analetewa habari njema za kuuawa kwa Bibiane na Willy Gamba maana alikuwa amesema alikuwa amesema wakishauawa aelezwe. Kila alipopewa taarifa ya kuuawa kwa mtu alipata faraja ndani ya moyo wake, Ndio sababu maelfu ya Watutsi walipouawa alisikia raha isiyo kifani. Hakika mtu huyu alikuwa mgonjwa, tena mgonjwa sana!.
"Jean", aliitikia kwenye simu.
"Col. Gatabazi hapa".
"Sema Col. Gatabazi".
"Kazi imeharibika".
"Nini?".
"Kazi imeharibika. Vijana wote wameuawa. Bibiane yuko hai na ameokolewa na Willy Gamba. mimi na Nkubana tunaondoka kwenda Kibunda, hatuna muda maana wakati wowote wataanza kutusaka, afadhari tuyaandae majeshi yetu tayari kwa vita", Col. Gatabazi alimwambia Jean.
"Ilikuwaje", Jean aliuliza kwa sauti ya kukata tamaa. Col. Gatabazi alimweleza kwa ufupi kama Nkubazi alivyomweleza.
"Basi tuonane kesho Goma, saa tisa mchana nitakuwa huko, natarajiwa kuja na ndege yangu, lakini nitampitia rafiki yetu Kinshasa", Jean alieleza na kukata simu kabla hata Col. Gatabazi hajajibu kitu.
Jean alipokata simu ya Col. Gatabazi, alitumia muda huo kupiga simu Zambia, Zaire, Afrika Kusini, Angola, Kenya na kumalizia Tanzania.
"Umenipata JKS?", Jean alimuuliza JKS baada ya kumweleza yote yaliyotokea na maelekezo mengine huku JKS akipatwa na shinikizo la damu.
"Nimekupata", JKS alijibu kwa sauti ya kutetemeka.
Bibiane alipomaliza kuoga alimkuta Willy amemtengea kikombe.
"Kahawa au chai?"
"Kahawa."
Willy alimmiminia kahawa na alipotaka kumwekea sukari Bibiane alikataa.
"Bila sukari," alisema.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kwa mara ya kwanza vilevile Bibiane alimuangalia Willy vizuri na kumuona mwanaume mzuri sana, na alipofikiria namna alivyowasambaratisha akina Xavier na kundi lao, mwili wake mara moja ulisisimuka. Halafu, palepale akamfikiria Jean na jinsi alivyompenda na kumfanyia kila kitu lakini akaamua kumuua. Hasira ilimpanda sana, na akaapa kiroho kuwa kwa vile yupo hai atalipiza kisasi.
"Unafikiri nini?" Willy alimwuliza Bibiane.
"Ahera."
"Umeshapona sasa?".
"Xavier alisema mimi na wewe tutaonana ahera baada ya masaa machache, akili yangu inafikiri huenda tupo ahera." wote walicheka.
"Uko tayari kuzungumza lolote," Willy alimuuliza Bibiane huku sauti yake ikiwa imebadilika ghafla na kuwa sauti yenye uzito fulani.
"Niko tayari, nimekuambia kila unachotaka," Bibiane alijibu kwa sauti ya mahaba.
"Wewe ni nani?" Willy alimwuliza.
"Mimi naitwa Bibiane Habyarimana, ni Mnyarwanda, na wewe?".
Willy alishtuka namna alivyo mjibu na kuzidi kuimarisha hisia zake kuwa huyu msichana vilevile alikuwa si mtu wa hivihivi ila alikuwa mtaalamu katika nyanja kama yake. Mara ya kwanza alipohisi, ilikuwa jinsi alivyojirusha nyuma ya kochi pale nyumbani kwake baada ya yeye kuwapiga risasi wale watu wawili, na alivyochupa dirishani kumfuata Xavier. Kwanza alifikiri alikuwa na mafunzo ya kijeshi tu, lakini kutokana na jinsi ya majibizano yao aligundua alikuwa na utaalamu zaidi.
"Willy Gamba, Mtanzania," alijibu na wote wakaangaliana kama wanapimana saizi. "Ningependa nijue historia yako nzima, na usinifiche kitu, mpaka kufikia uhusiano wako na hawa wauaji na hasa huyu aliyekuhukumu kifo bwana Jean", Willy alimwambia Bibiane.
"Nimeshatoa kauli yangu kuwa nitakueleza kila kitu unachotaka niseme. Hivyo, usiwe na wasiwasi nitakueleza, ila itabidi uwe na subira maana ni hadithi ndefu", Bibiane alijibu.
Bibiane alimweleza Willy kwa kirefu maisha yake ya utoto, maisha ya shule, juu ya baba yake na mama yake na akaendelea, "Mwaka nilipoanza kazi baada ya kuhitimu digirii ya kwanza ya lugha katika Chuo Kikuu cha Kigali, wazazi wangu wote wawili walikufa kwa ajali. Nilikuwa nimeanza kazi Wizara ya Mambo ya Nje kama mkalimani.
"Inasemekana kuwa wazazi wangu hawakufa kwa ajali ya kawaida ila waliuawa na vikaragosi vya Watutsi ambao walifikiri kuwa baba yangu alikuwa ndugu yake na Rais. Hivyo waliwaua wazazi wangu ili kumkomoa Rais. Kitendo hicho kiliniuma sana nikawachukia sana Watutsi", Bibiane alieleza.
"Pole sana", Willy alisema kwa sauti ya huruma.
"Kwa kunisikitikia kutokana na yaliyowakuta wazazi wangu, serikali ikanihamishia ofisi ya Rais, huko ndiko nilipokutana na Jean Yves Francois, yeye ni Mfaransa anaishi Paris lakini alikuwa rafiki kipenzi na Rais. Tulionana naye nyumbani kwa Rais ambako alikaribishwa na tulianza urafiki siku hiyohiyo", Bibiane alieleza Willy huku akimwangalia kwa jicho la kuiba.
"Huyu Jean Yves Francois ndiye aliyekufundisha ujasusi?", Willy alimuuliza.
"Umejuaje?".
"Nimehisi".
"Jean ni mfanyabiashara na alikuwa akifanya biashara na kundi la marafiki wa Rais pamoja na familia ya Rais, wakati mimi nafahamiana naye serikali ilikuwa imeanza kuwa na matatizo kwani Watutsi waliokuwa humu ndani na nje, nchini kwenu na Uganda walikuwa wakipigana ili waiangushe serikali. Jean ndiye aliyekuwa akimsaidia Rais kwa kumjenga kijeshi, kiusalama na kiutawala. Huyu Jean ana utajiri usio kifani, kwani ndiye anayezifadhili serikali na wakuu wengi wa nchi za Afrika. Kwa vile mimi pia nilikuwa kwenye himaya yake alinipeleka kwenye mafunzo ya kiusalama sehemu mbalimbali duniani".
"Na ukahitimu vizuri", Willy alidakia.
"Vizuri sana".
"Ehee, endelea".
"Si ni wewe unanikatisha".
"Huu utajiri aliupataje?", Willy aliuliza.
"Sijui mwenyewe ameupataje, ila anashughulika na mambo ya silaha. Hapa alikuwa analeta silaha, halafu anachukua chai yote na kahawa inayolimwa katika nchi. Hili suala ni moja ya malalamiko mengi ya wananchi maana Jean ndiye aliyekuwa akipanga bei anayotaka, na hakukuwa na mtu wa kusema kitu, maana alikuwa akifanya biashara na Rais na kundi lake, lililokuwa likiitwa Akazu. Kusema kweli Jean na hilo kundi la Akazu ndio waliokuwa wanatawala na si baraza la mawaziri au Bunge", Bibiane aliendelea huku sasa Willy akimsikiliza kwa makini zaidi.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Huoni kuwa hiyo haikuwa sawa?", Willy aliuliza.
"Mimi ningefanya nini, nilibaki kufanya kila nilichoagizwa kama ilivyokuwa kwa wengine wengi maana sasa hii ndio ilikuwa namna ya maisha. Ama uko na Akazu, vinginevyo hupati kitu cha aina yoyote, iwe mali, elimu au kazi ya aina yoyote Rwanda".
"Kwa hiyo rushwa ndio ilitawala utawala uliopita?", Willy aliuliza.
"Inategemea unavyotafasiri rushwa", Bibiane alijibu huku akiwa kama haelewi anasema nini.
"Rushwa ni pale vyombo vya serikali vinaposhindwa kufanya kazi zake, kwa sababu hiyo kushindwa kutoa haki kwa wananchi wake, na kuwafanya wananchi wengi wapoteze imani, utu, uhuru na maadili kwa serikali yao kwani wote sasa huishi kama wanyama ambapo mwenye nguvu na pesa ndiye anayepata anachohitaji", Bibiane alisema.
"Hivyo ndivyo, maana nchi inakosa maendeleo kwani mapato yote ya nchi badala ya kuendeleza watu wote huingia kwenye mifuko ya watu wachache. Na kama ulivyosema uhalali wa serikali kama chombo cha watu unakwisha, badala yale wale wanaofaidika ndio wanakuwa na nguvu zaidi ya serikali yenyewe", Willy alitafasiri rushwa.
"Kwa tafasiri hiyo nakubali kuwa rushwa ndiyo imetawala. Na sasa Watutsi na Wahutu walipoanza kudai demokrasia isingewezekana maana Jean na Akazu hawakutaka kusikia kitu kama hicho kwa vile kingeweza kuingila maslahi yao. Na ndio sababu Watutsi walipokazana na kusikia eti wako tayari hata kupigana na Akazu, kwa kufadhiliwa na Jean, walianza kulifundisha jeshi la wahutu lililoitwa Intarahamwe ili liweze kuwadhibiti Watutsi wa ndani na nje ya Rwanda".
"Kwa hiyo huyu bwanako Jean ndiye alikuwa Rais hapa?".
"Si hapa tu, mimi najuwa nchi nyingi ambako amewakamata wakuu wa nchi na viongozi wa ngazi za juu serikalini na anawajaza mapesa kila wakati".
"Huoni kuwa yeye ndiye ananufaika zaidi, maana anajaza mapesa watu wachache lakini yeye anachukuwa mali za wananchi wengi", Willy alijaribu kumwelimisha Bibiane.
"Najuwa, maana hata huko kwenu Tanzania pia amewakamata wakubwa, ndio sababu nchi yenu imekuwa ikisita juu ya suala hili la Rwanda".
Willy alisitushwa na taarifa hii lakini hakutaka kujionyesha maana kweli msimamo wa serikali ya Tanzania ulikuwa unalegalega kabla na hata baada ya mauaji.
"Ina maana maamzi yoyote ilikuwa lazima Jean akubaliane nao?".
"Ndiyo, na mapesa yalitembea sana kuhusu swala hili na viongozi wengi wamenufaika. Unafikiri kama swala hili lingefanyiwa maamuzi mapema mauaji yangetokea!", Bibiane alimwambia Willy kwa njia ya kushangaza.
"Kwa hiyo huyu Jean ndiye aliamru mauaji haya?".
"Baada ya Rais kuonekana kwamba angekubali mkataba wa Arusha. Jean na Akazu walikasirika sana maana hawakutaka, kama nilivyosema mwanzo, kugawana madaraka na mtu mwingine. Hii ingegusa maslahi yao. Kwa hiyo, kwanza ndio waliamru Rais auawe na pili tayari walikuwa wamewatayarisha na kuwahamasisha Wahutu kuwamaliza Watutsi wote asibaki mtu ili wajihakikishie uwezo wa kutawala milele. Mpango ulikuwa kwamba hata kama jeshi la RPF la Watutsi lingeshinda jeshi lao lazima baada ya kuchukuwa nchi wangeshindwa kutawala maana wangemtawala nani huku Watutsi wote wakiwa wameshauawa, waliobaki ni Wahutu watupu ambao hawawaungi mkono. Hivyo, ingewachukuwa siku chache kuuangusha na kuutokomeza kabisa utawala wa RPF. Hii ingebaki nchi ya Wahutu chini ya utawala wa Jean na Akazu.
Bibiane alipofika hapa ndipo Willy alipoanza kuelewa kwa undani mambo yalivyokuwa. Kumbe mauaji yote haya yalitokana na watu wachache kutaka kulinda maslahi yao ya kunyonya mali ya wananchi, na kutumia hiyo mali kuweza kuwachochea wananchi kuuana!.
Kwa mara ya kwanza Willy aliona jinsi ambavyo nchi zote za Afrika zilivyo hatarini kutokana na rushwa. Kwa vile viongozi wa nchi hizi kuabudu rushwa, hivyo Willy akaamini kuwa tukio kama la Rwanda kumbe linaweza kutokea mahali pengine katika Afrika!.
"Baada ya RPF kushinda na mipango ya Jean kushindwa, wana mikakati gani sasa?", Willy alihoji.
"Kama nilivyosema hawajashindwa. Wewe ndiye umeingilia ndani ya mipango yao, kuna mpango kabambe wa kuisambaratisha serikali ya RPF kutokea jimbo la Kivu, Zaire. Akazu wamekuwa wakiliimarisha jeshi lao katika makambi ya wakimbizi kule Goma na Bukavu, Zaire, huku Jean akiwatumia rafiki zake kutoka Afrika Kusini hasa waliowahi kuwa katika idara ya ujasusi ya makaburu, alikokuwa akinunua silaha na kuzipitishia Angola ya UNITA, Zaire na Zambia kwa kutumia viongozi wa ngazi za juu za serikali za nchi hizo ambao wako kwenye orodha ya malipo kutoka kwa Jean. Kwa hiyo mambo bdo sana Willy, vita ndio sasa karibu vitaanza".
"yaani dunia inafikiri kuwa kambi zilizoko Zaire ni za wakimbizi kumbe ni kambi za jeshi".
"Ni kambi za jeshi na serikali ya Zaire inajua na ndio inayosaidia hata mafunzo. Hata katika kambi zilizoko kwenu Tanzania kuna wanajeshi wa jeshi la zamani na Intarahamwe, na kuna watu wazito katika serikali yenu ambao wanalipwa na huyu Jean ili kuwasaidia hawa watu, kwa hiyo hili si dogo. Kama ulivyosema pesa ni kitu kibaya sana, watu hawaoni tena madhara ya mauaji yaliyotokea bali wanaona pesa tu".
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Swala la rushwa ni swala linalohujumu haki za binadamu, yapaswa lichukuliwe hatua kimataifa katika uzito huo wa haki za binadamu", Willy alijibu kwa hasira.
Bibiane alikaa kimya bila kujibu kitu.
"Wewe ulikuwa uwasaidie vipi Jean na Akazu katika kutekeleza huu mpango wao wa kuivamia tena Rwanda", Willy aliuliza.
"Usije ukanipeleka kwenye mahakama ya mauaji ya Arusha maana mauaji yale sikuyajuwa pia sikushiriki, nilikuwa Nairobi nikitokea kwenye mkutano Arusha. Ila juu ya hili la sasa Jean amekuwa akinituma kupashana habari kati ya kambi za wakimbizi ambazo ni kambi za jeshi lao huko Zaire, yeye na Akazu. Vilevile kuna wanajeshi na viongozi wa RPF ambao tayari wamenunuliwa na wako upande wa Akazu, mmoja wao ndiye anayetarajiwa kuchukua madaraka mara tu jeshi la Akazu litakapotwaa madaraka tena".
Willy hakuamini masikio yake kuwa tayari hata ndani ya RPF kuna wasaliti.
Mara moja Willy alielewa jinsi alivyotaka kuuawa na akagudua kuwa kweli kama anavyosema Bibiane kuna kiongozi wa juu na karibu sana katika serikali ya Tanzania amabye anamtumikia Jean na kundi la Akazu.
"Utasaidia kunipa majina ya watu wote unaowajuwa kuwa wanahusika, maana hiyo ndio njia pekee tunaweza kulikosha jina lako", Willy alimuasa Bibiane.
"Swala la Jean kunisaliti mimi, na kunihukumu kifo, bila kujali yote niliyomtendea kwa hali na mali ikiwa pamoja na kumpa mwili wangu auchezee atakavyo, na jinsi nilivyojitoa kumstarehesha. Willy mimi niko upande wako, kama uko tayari kupambana nao nihesabu na mimi. Jean akishaambiwa kuwa umenichukua ninavyomjua atataka apambane na wewe yeye mwenyewe, ikifika hapo niachie mimi. Majina na mipango yao yote ni juu yako na uongozi wa RPF mjuwe la kufanya kwani jeshi la Akazu, likisaidiwa na viongozi wa nchi kadhaa ambao ni marafiki na Jean watakuwa tayari kuingilia kati. Ni lazima liwahiwe mapema kabla halijajiimarisha sawasawa", Bibiane alieleza.
"Nafikiri swala la vita si letu, ni la serikali ya Rwanda na RPF, mimi nipe hayo majina na kutokea hapo ndipo nitajua kama kazi yangu imeisha au ndio kwanza inaanza", Willy alieleza taratibu.
Bila kuwa ameandika mahali popote, Bibiane alitoa kichwani jina hadi jina akianza na kundi la Akazu mpaka viongozi wa nchi mbalimbali wanaolipwa na Jean huku Willy akiyaandika chini kwa mshangao mkubwa, kwani watu waliokuwa wanatarajiwa wengi wao ni viongozi wanaoheshimika Afrika na kote duniani. Alishangaa zaidi Bibiane alipotaja jina la yule waliyekuwa wakimwita JKS wa Tanzania.
"JKS, hii imenishangaza sana, maana huyu ndiye anayetegemewa kugombea urais wa Tanzania katika uchaguzi mkuu unaokuja," Willy alimweleza Bibiane.
"Najua kabisa, na tayari Jean ameshamtengea mamilioni ya dola za Kimarekani zitakazo msaidia katika kampeni hiyo ya uchaguzi kuusaka urais. Nia ya Jean ni kuwa na marais vibaraka kote Afrika ili yeye na wenzake huko Ulaya, waweze kufanya vile wanavyotaka katika nchi hizi. Jean anaongoza kundi la wafanyabiashara wakubwa wanaomiliki makampuni makubwa ya kimataifa. Na nia yao ni kuhakikisha kuwa Afrika inakuwa soko lao tu, na hata siku moja Afrika isisimame kiuchumi. Ingawaje nchi zao zinapigia kelele rushwa, lakini nchi hizohizo ndizo zinazoyasaidia makampuni makubwa kwa madogo kutoa rushwa kwa nchi zinazoendelea, maana makampuni hayo yakitoa hongo, hongo hii huchukuliwa kama gharama na kutolewa kwenye kodi ya mapato. Hii yote inaonyesha unafiki wa nchi za magharibi, na kila wakati Jean alikuwa akinieleza kuwa kelele zote hizi kuhusu rushwa, demokrasia na soko huria ni kelele za kinafiki tu, lakini huku nyuma katika vikao vya viongozi wa nchi za magharibi ni kuchochea rushwa. Wanajuwa kuwa rushwa ikiisha Afrika basi demokrasia na soko huria vitashamiri na hivyo uchumi wa nchi hizo utakua haraka sana, kitu ambacho hawataki kitokee. Jean anasema, rushwa ndiyo sera inayotumiwa kuendeleza umaskini katika nchi za Afrika ili nchi zilizo endelea ziendelee kuitawala Afrika kiuchumi. Kwa hiyo, iwapo JKS ataitawala Tanzania rushwa itazidi mara dufu, na kutokana na fedha alizotengewa na Jean lazima atashinda, kwani kila walipoweka mtu wao hajawahi kushindwa uchaguzi", Bibiane alieleza.
Sasa Willy alikuwa na picha kamili namna JKS alivyokuwa anahusika na swala zima la Rwanda. na sababu za Tanzania kutokuwa na msimamo dhabiti juu ya swala hili na kuweza kuyumbisha mikutano kule Arusha kiasi cha kutofikia maamzi kwa muda mrefu maana swala hili la Rwanda kwa muda mrefu lilikuwa chini ya Tanzania kwa muda mrefu na JKS alikuwa mmojawapo wa viongozi walioonyesha kuchoshwa na mauaji ya Rwanda. Na alifanya hivyo kwa shinikizo la Jean aliyekuwa akimlipa pesa nyingi na uchu wake wa kutaka madaraka kwa njia ya ruswa ili aweze kuyatumia kwa faida yake na kujinifaisha yeye na rafiki zake. Na ni hii rushwa iliyowanyima Wanyarwanda haki yao mpaka kufikia hatua ya kuuawa vibaya namna ile kweli ni aibu! Aibu sana kwa Afrika nzima.
"Vizazi vijavyo vitakapoyasoma na kuyaelewa matukio haya, hakika hawataamini, watajuwa sisi wote tulikuwa wendawazimu kabisa, kwani ni sisi wote ndio tulioachia hali hii ikafikia hapo ilipo, kwa kuwapa walarushwa madaraka kwa gharama ndogo ya kuuza kura zetu na wao kutumia madaraka tuliyowapa kwa malipo ya fedha kidogo, lazima wayatumie kutuangamiza", Willy alisema kwa uchungu huku akikuna kichwa chake.
Mara moja Willy alimkumbuka Malisa wa Arusha, aliyekuwa mshauri wa JKS katika masuala ya uhusiano wa Kimataifa kabla hajarudi Chuo Kikuu. Hivyo basi, alijuwa Malisa ndiye aliyemweleza JKS kuhusu msimamo na mipango ya PAM na kuteuliwa kwa Willy kufuatilia jambo hili. Willy aliamini kuwa JKS ndiye aliyetoa taarifa za safari ya Rwanda kwa Jean na kundi lake na ndi sababu ndege aliyopanda ikapigwa kabla ya kutua uwanja wa ndege wa Kigali.
"Kwa hiyo JKS ndiye aliyotoa habari zangu zote kwa Jean?", Willy aliuliza kwa shauku.
"Ndio, na ndio sababu Col. Gatabazi aliamru ndege hiyo ipigwe kabla ya kutua uwanja wa ndege, lakini kwa bahati na umahiri wako ukawaponyoka", Bibiane alijibu huku akimwemwesa. Mara mlango wa mbele ukafunguliwa na Col. Gatabazi akaingia ndani.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Willy alipoangalia saa yake ilikuwa yapata saa tisa usiku. Wote walisimama, na Willy akawatambulisha.
"Pole Kanali, leo tumepata mgeni na anaitwa Bibiane, na Bibiane huyu ndiye mwenyeji wetu. Col. Rwivanga, kiongozi katika serikali mpya ya RPF".
"Nashukuru kumfahamu", Col. Rwivanga alijibu.
"Nami nimefurahi kukuona leo, nimekuwa nikisikia sifa zako nyingi kwa muda mrefu, toka kwa Col. Gatabazi kuwa wewe ni mpiganaji hodari, hongera", Bibiane alijibu kwa tabasamu akimwangalia Col. Rwivanga.
"Asante kwa sifa hizo zilizotoka katika kinywa cha msichana mrembo kama wewe", Col. Rwivanga alijibu akaendelea, "Ehe, imekuwaje Willy, hebu nipe habari kamili, maana kazi tumeiona kwa Bibiane, sasa halafu ikawaje hivi", Col. Rwivanga alionekana kuwa wasiwasi na Bibiane.
"Mimi naomba nikalale ili mzungumze vizuri, nionyeshe chumba cha kulala", Bibiane aliomba.
Willy na Col. Rwivanga aliangaliana na Willy ndiye alikuwa wa kwanza kujibu, "Kwa vile nyumba hii ina vyumba viwili tu vya kulala, basi kalale chumbani kwangu, maana tayari hata kuoga umeoga huko. Mimi nitalala hapa sebuleni kwenye kochi hamna taabu".
"Asante", Bibiane aliwaaga na kuelekea chumbani huku wote wakimwangalia. Kisha wakatazamana na kutabasamu.
"Ehe, hebu nipe mambo".
Willy alichukua muda mrefu kumweleza mambo yalivyotokea na mambo mengine yote aliyoelezwa na Bibiane. Col. Rwivanga akasimama na kumshika mkono Willy kwa hatua aliyofikia haraka na kwa umakini mkubwa.
Baada ya Col. Gatabazi kuvaa nguo vizuri, walichukua silaha mbalimbali na fedha zilizokuwa pale ndani. Wote walivaa mavazi ya kijeshi na kutumia gari ndogo aina ya MB 230E, ambalo awali Nkubana alikuwa amepewa na Col. Gatabazi kwa ajili ya Operesheni ya usiku. Gari hii ni mojawapo ya magari yaliyokuwa yameachwa na viongozi wa serikali iliopita, baada ya kukimbia mji wa Kigali, wakati RPF inaingia madarakani.
Nkubana alikaa kwenye usukukani kwa ajili ya kuendesha gari, Col. Gatabazi akakaa upande wa kulia, maana gari hili lilikuwa na usukani upande wa kushoto.
"Aha, kumbe gari limejaa mafuta kwenye tenki".
"Ndio, nilijaza kwa sababu kama hizihizi kama dharura itatokea", Col. Gatabazi alijibu.
"Tuchukue njia gani?", Nkubana aliuliza.
"Najua sasa hivi wataanza kututafuta. Hivyo, twende na barabara kubwa iendayo Ruhengeri. Kwa vile bado mawasiliano ni shida kati ya vikosi, tunaweza kupata bahati tukafika Gisenyi kabla habari zetu hazijaenea. Kwa vile vikosi vya RPF vinanifahamu na kuniheshimu njiani hatutaulizwa wala kupata tatizo lolote, watajua kuwa niko kazini. Kwa hiyo tutumie barabara kubwa mpaka Ruhengeri, halafu moja kwa moja mpaka Gisenyi, halafu tutavuka mpaka na kuingia Goma. Upande ule Jean ameshafanya mipango, hatutakuwa na shida. Nimemweleza amweleze Mkuu wetu wa Majeshi Col. Marcel Bazimaziki atukute mpakani"Col. Gatabazi alieleza.
"Sasa hivi ni saa sita na robo, itatuchukua masaa kama manne kwa gari hii, kwa hiyo saa kumi na moja alfajiri tutakuwa Goma?", Nkubana aliuliza huku akitia gea na kuondoa gari kwa kasi kuelekea Goma.
Baada ya Jean kumweleza JKS mambo yote yaliyokea Kigali, palepale JKS usingizi ulimtoka. Aliona na kuamini kuwa huo ndio ulikuwa mwisho wake. Ndoto zake za kuwa Rais wa Tanzania zilianza kuyeyuka mfano wa seluji. Hakujua afanye nini. Aliamini kuwa Willy Gamba akipata habari zake kuwa yuko kwenye mtandao wa kuisaliti Afrika haitamchukua zaidi ya siku mbili kabla mambo yake hayajabainika na kuanikwa hadharani.
JKS alimjua vizuri Willy Gamba alivyokuwa makini na hodari katika kufanya kazi zake. Alifikiri asubiri Willy arudi kwanza nchini ndio amkabiri yeye mwenyewe au aieleze serikali ya Tanzania kilichokuwa kinafanyika Rwanda. Aliona kashifa kubwa inakuja mbele yake. Ingawaje Rais wa sasa wa Tanzania alikuwa rafiki yake mkubwa, lakini ingekuwa vigumu sana kuizuia kashifa hii, maana vyombo vya habari vingemmaliza kabisa. Kisha, akakumbuka kuwa alikuwa na mapesa mengi ambayo Jean alimwekea kwenye akaunti zake katika mabenki ya huko Uswisi na Cyprus.
Baada ya kutafakari kwa muda mrefu huku jasho jembamba likimtoka. JKS akaamini kuwa mapesa hayo yangeweza kuzuia kashifa hii kwa kuwanunua wamiliki wote wa vyombo vya habari Tanzania kama Radio, magazeti na taasisi zingine kama polisi, usalama wa Taifa na idara zingine nyeti za serikali ambazo zingeonekana kumletea madhara kwenye safari yake ya kuelekea Ikulu.
"Watanzania karibu wote wana njaa, nitawanunua kwa mapesa tu. Hapo ndipo Willy atajuwa jeuri na nguvu ya pesa. Hakuna mtu atakayemsikiliza tena Willy Gamba, mimi nitaendelea na mambo yangu bila hofu. Uchu wangu wa kuwa Rais wa Tanzania utafanikiwa", JKS alijisemea mwenyewe huku akiwa amelala mfano wa mtu aliyeko katika usingizi mnono akiota ndoto.
Hivyo, baada ya kutafakari hili na lile kwa mapana na marefu, JKS aliamua kuwa atamfuata Rais ili amuombe ruhusa na kusafiri kwenda Ulaya kwa ajili ya kuangaliwa afya yake kwa madaktari wake walioko Uingereza, na angemwambia daktari mkuu wa Hospitali ya Muhimbili atoe ushauri wa haraka. Akiwa amejiwekea malengo kuwa akifika Ulaya akusanye mapesa yake halafu ndipo ajue kitu cha kumfanyia Willy Gamba aliyemwona mchawi wa safari yake ya kuelekea Ikulu ya Tanzania.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
JKS aliamini kuwa akiwa na mapesa mkononi, ataweza kufanya chochote atakavyo. Akapiga moyo konde, akamkumbuka tena Willy Gamba moyo wake ukapata maumivu makali, akahisi mtu huyu ni mchawi. Hata hivyo akaapa kuwa hatarudi nyuma.
GISENYI
Ilikuwa yapata saa kumi na mbili alfajiri wakati Willy Gamba na Bibiane walipokuwa wakiondoka nyumbani kwa Bibiane kuelekea Goma, nchini Zaire. Baada ya Bibiane kwenda kulala usiku na kumwacha Willy akimpa habari Col. Rwivanga kuhusu yote aliyoelezwa na Bibiane, usiku, uleule Willy na Col. Rwivanga waliamua kwenda haraka kumkamata Col. Gatabazi nyumbani kwake, baada ya kuchunguzi wa kina waligudua kuwa nyumba hiyo imefungwa na hakuna mtu. Mara moja Col. Rwivanga akahisi kuwa Col. Gatabazi alikuwa ameelekea kwenye majeshi yake huko Kibumba karibu na Goma kama ambavyo walikuwa wameelezwa na Bibiane. Hivyo, waliafikiana kuwa asubuhi na mapema Willy aondoke na Bibiane kwenda Goma, kuwasaka Col. Gatabazi, Nkubana na Jean.
Wakati huo Col. Rwivanga alikuwa akijiandaa kwenda kutoa taarifa za uhalifu huo kwa serikali ya RPF ili iandae jeshi la kushambulia sehemu ya Kibumba na kuliangamiza jeshi la Akazu pamoja na Jean kabla halijaishambulia Rwanda tena. Hivyo, Willy Gamba na Col. Rwivanga walirudi nyumbani na Willy akatafuta usingizi wa saa moja kwa ajili ya kujiweka sawa. Ilipofika saa kumi na moja alifajiri Willy alimuamsha Bibiane ili waanze safari.
Willy akilipokuwa akijipumzisha, Col. Rwivanga alitoka usiku huo kwenda kumwona mkuu wa shirika la Msalaba Mwekundu ambaye alikuwa rafiki yake na kumwomba gari. Col. Rwivanga alipewa gari ya Msalaba Mwekundu aina ya Toyota Land Cruser GX ambalo alipanga Willy na Bibiane walitumie kwenda mpakani kwenye kambi ya wakimbizi ya Kibumba. Vilevile Col. Rwivanga aliwatanguliza vijana wake watatu askari wa kikosi maalumu cha upelelezi kutoka jeshi la RPF ili wawahi kufika Gisenyi na kutoa taarifa za Col. Gatabazi kwa makamanda wa RPF walioko Gisenyi. Pia alituma taarifa ya siri kwa Meja Tom Kabarisa, kiongozi wa waasi wa Banyamulenge kikundi kilichokuwa kikipigana kupinga serikali ya Zaire, kilichokuwa na makao makuu yake sehemu za milimani, karibu na mji wa Goma. Hawa Banyamulenge walikuwa ni watu wa asili wa Kitutsi ambao walihamia miaka mingi eneo hili na Mashariki mwa Zaire kutokana na misukosuko ya muda mrefu ndani ya Rwanda.
Kwa muda mrefu watu hawa waliishi kama wananchi wa Zaire, lakini miaka ya hivi karibuni serikali ya Zaire ilianza kuwabagua kiasi cha kuwanyima haki hata ya kupiga kura na kisha kuwataka wahame maeneo waliyokuwa wakiishi ndani ya Zaire ili warudi kwao Rwanda. Lakini walikataa katakata kutii amri hii ya serikali ya Zaire na kuanzisha kikundi chao cha wapiganaji ili kiweze kulinda maslahi yao. Kikundi hiki kilikuwa na mahusiano mazuri na maofisa wa jeshi la RPF. Wakati na baada ya mauaji ya Watutsi na Wahutu kukimbilia eneo hili la Ziwa Kivu, uhusiano wa Banyamulenge na uongozi wa RPF uliimarika zaidi kwa sababu za kiusalama kwa pande zote mbili.
"Mimi niko tayari kwa safari, lakini naomba tupite pale nyumbani kwangu ili nipate nguo za safari ya namna hii na nyenzo nyingine ambazo zinaweza kutusaidia katika safari yetu", Bibiane ambaye alikuwa ametokea chumbani na kujiegemeza kwenye ukuta alisema.
Willy na Col. Rwivanga waliokuwa wanapanga mikakati huku wameupa mgongo ule upande wa chumba waligeuka na kumwangalia. Alfajiri hii Bibiane alionekana mrembo hata zaidi ya jana yake.
Willy na Col. Rwivanga walitazamana tena na kutabasamu huku macho ya Col. Rwivanga yakimweleza Willy kuwa. "Haya kazi unayo".
"Mmenisikia?", Bibiane aliuliza tena.
"Sawa", Willy alijibu kisha kama amekumbuka kitu akahoji, "Lakini sijui kama pale kwako tutaweza kuruhusiwa kuingia".
"Tutaenda wote", Col. Rwivanga alijibu.
Kisha Col. Rwivanga alimmalizia Willy maelezo na mipango yote, wakaondoka kuelekea nyumbani kwa Bibiane.
Kwa vile kulikuwa bado hakujapambazuka, walipofika nyumbani kwa Bibiane ilibidi Col. Rwivanga atoke na kujitambulisha kwa askari wapatao wanne waliokuwa wamejitokeza baada ya kusikia mwungurumo wa gari. Kisha lango la mbele lilifunguliwa wakaingiza gari ndani. Baada ya maelezo mengine mafupi, Bibiane aliruhusiwa kuingia ndani.
"Karibuni", Bibiane aliwakaribisha Willy na Col. Rwivanga ndani.
Bibiane aliingia chumbani na kuwaacha Col. Rwivanga na Willy sebuleni. Nyumba ilikuwa bado kabisa haijakaguliwa. Hivyo, kila kitu kilikuwa kimebaki kama kilivyokuwa isipokuwa maiti za wale tu ndizo zilikuwa zimeondolewa.
"Willy njoo", Bibiane alimwita Willy chumbani kwake. Willy na Col. Rwivanga waliangalia na kutabasamu, baada ya sekunde kadhaa Col. Rwivanga alimuonyesha Willy ishara aende chumbani kama alivyoitwa.
Willy alipoingia chumbani alimkuta Bibiane anavaa suluali lakini sehemu ya juu yote ilikuwa bado iko wazi yaani hajavaa kitu hata sidiria.
"Hatuna muda wa kukaa hapa hivyo itabidi unisaidie vitu vingine ili tuweze kuondoka mapema", Bibiane alimwambia Willy ambaye alikuwa kama amepigwa na butwaa. Hakika msichana huyu alikuwa mzuri, umbo lake jinsi alivyoumbika hutaamini kama alizaliwa kutoka tumboni kwa mwanamke isipokuwa alishushwa kutoka juu. Hakukuwa na maelezo ya kutosha kueleza urembo wa msichana huyu bali ujitahidi kumtafuta ili uthibitishe mwenyewe kama Willy alivyojionea.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Usinitie majaribioni", Willy alisema huku akirudisha mlango.
"Aaa mshirika, mapigo yangu nikitaka utayaweza?. Kazi kwanza mambo mengine baadaye. Nimekuita kwa sababu hatuna muda wa kukaa hapa nataka kukuonyesha kitu", Bibiane alisogea kwenye ukuta akabonyeza sehemu na ukuta ule ukafunguka. Willy alishangazwa kuona kumbe ule haukuwa ukuta isipokuwa kabati la siri lililojificha likiwa na zana mbalimbali za kazi za kisasa kabisa.
"Pale mwisho kuna makasha mawili makubwa yameandikwa 'hatari', yatoe", Bibiane alimwambia Willy huku akichukua sidiria na kuendelea kuvaa.
Willy aliyatoa na kuyaweka chini.
"Fungua", alisema huku akiendelea kuvaa. Willy alipofungua alikuta ni mabomu aina ambayo hakuwahi kuyaona wala kuyatumia kabisa.
"Haya ni mabomu aina ya teknolojia ya kisasa kabisa, ambayo Jean aliniletea siku chache tu zilizopita, akanielekeza niyahifadhi mpaka nitakapopata maelekezo zaidi. Lakini yule mtu wa DOSE aliyeleta silaha hizi alinieleza jinsi zinavyotumika na kweli ni aina ya mabumu ya kisasa na hatari sana", Bibiane alieleza huku akivaa viatu na kutengeneza nywele zake. Alimweleza Willy jinsi mabomu hayo yanavyofanya kazi na kumalizia. "Hayo mabomu mawili yana uwezo wa kulipua nusu ya mji wa Kigali, na kwa kutumia saa hii ninayokupa unaweza kulipua mji wa Kigali huku umeketi mahali unakunywa chai.
"Ili mradi tu usiwe umetega na nyumba yako au ya majirani zako", Willy alitania na wote wakacheka.
Willy alikubaliana na Bibiane kuwa waende na makasha yote mawili, maana kutokana na maelezo ya Bibiane, Jean na Akazu walikuwa wameandaa jeshi kamili kwa ajili ya kuivamia Rwanda, wakiwa na silaha kali na za kisasa kutoka Ufaransa na Afrika Kusini, huku wakitumia kisingizio cha wakimbizi. Kisha Bibiane alitoa bastola nne, mbili zikiwa ndogondogo sana alizoziweka kwenye mkoba na mbili kubwa alizomkabidhi Willy, vilevile alichukua risasi nyingi sana.
"Nafikiri sasa tuko tayari", Bibiane alisema huku akimsaidia Willy kubeba kasha moja na mfuko wake wa nguo.
"Ehe, vipi huko ndani?", Col. Rwivanga aliuliza.
Kabla Willy hajajibu Bibiane alijibu."Salama kabisa".
Wote wakacheka, kisha kwa kifupi, Willy akamweleza Col. Rwivanga kuhusu kilichokuwa ndani ya yale makasha waliyotoka nayo ndani.
Baada ya hapo, Willy na Bibiane waliingia ndani ya gari na kumtakia Col. Rwivanga heri ya kuonana, kisha wakaanza safari ambayo hawakuwa na uhakika kama mambo yangeendaje huko.
"Mungu awe pamoja nanyi, naamini atawasaidia", Col. Rwivanga aliwaaga, askari waliokuwa wakilinda nyumba ile waliwafungulia lango wakatoka na kutokomea kuelekea Kibunda.
Ilipofika saa nne asubuhi JKS alikuwa tayari ameshapata kibali kutoka kwa Rais ili aweze kwenda Uingereza kwa matibabu. Daktari alikuwa ameiandikia serikali barua kufanya haraka na kila njia JKS aondoke siku ileile kwani alihisi kuendelea kusubiri kungeweza kumletea shinikizo la damu lenye nguvu kubwa ambalo huenda wao wasingeweza kumsaidia kabisa.
Ni barua hii ya Daktari iliyomfanya Rais akubali kutoa kibali harakaharaka na kuamru kuwa ifikapo jioni ile JKS awe ameondoka kwenda Uingereza kwa matibabu. Hadi saa saba mchana Wizara ya Afya ilikuwa imefanya mipango yote na ikawa wamempatia usafiri kuondoka na ndege ya shirika la ndege la Uingereza usiku ule.
JKS alikataa kusindikizwa na maofisa wa serikali kwa kisingizio kuwa atapokelewa na watoto wake walioko mjini London, Uingereza ambao alisema watamwangalia kwa karibu zaidi wakati wa matibabu yake. Bila watu kujua, alifanya mipango yake mwenyewe ili usiku uleule aweze kuunganisha ndege kwenda hadi Geneva, Uswisi, kitu ambacho alifanikiwa. "Hakika Willy Gamba hataniweza, nikirudi na mapesa yote yale, hakika naamini ataiona dunia na ardhi ya Tanzania chungu", JKS alijisemea mwenyewe huku mapigo ya moyo yakimwenda mbio.
.............................................................................................................................
III
Wakati Willy na Bibiane wanaondoka Kigali kuelekea Goma, saa kumi na mbili asubuhi. Col. Gatabazi na Nkubana walikuwa wanapokelewa na Col. Marcel Bazimaziki na kikundi cha wanajeshi wa jeshi la Zaire kikiongozwa na Meja Massamba kwenye mpaka wa nchi hizo za Rwanda na Zaire.
"Pole sana na safari, ulipokaribia kufika Gisenye natumaini umepita ile njia yetu na nadhani hukupata shida", Col. Bazimaziki aliwasalimia kuwapa wageni wake mkono huku kila kikundi cha askari kikijiweka sawa kutoa heshima kwa gwaride rasmi lililoandaliwa kwa ajili ya Col. Gatabazi ambaye kama walivyokuwa wameelekezwa kuwa baada ya muda si mrefu ndiye atakuwa kiongozi wa Rwanda.
"Safari ilikuwa safi kabisa na hizi Benz ni gari imara sana ha hata kile kinjia tulichopita hatukupata taabu sana. Asante kwa kutuma mtu wa kutuongoza, maana tungeweza kubabaika kufika hapa", Col. Gatabazi alijibu.
"Jean tulizungumza kwenye simu yetu aliyoleta hivi karibuni ya Satellite. Sasa mawasiliano ni mazuri sana kati yake na sisi. Hata kabla ya kuja kukupokea tulizungumza nae, alikuwa akielekea uwanja wa ndege, nae tayari amepanda ndege na imeondoka Paris tangu saa kumi na mbili.
"Anatumia ndege yake ile ya Falcon, atakuwa hapa saa kumi na mbili jioni, maana atapitia Kinshasa kuonana na viongozi wa serikali kule, mkutano utafanyika uwanja wa ndege ili waweke msimamo, halafu watakuja na Jenerali Kasongo ili kuangalia hali pamoja na wewe mwenyewe ukiwepo ili mkiridhika na hali kazi ianze", Col. Bizimaziki alieleza na kisha Col. Gatabazi akaelekea kwenye gwaride ili apokee heshima zake kutoka kwa kikundi cha wanajeshi wa Zaire.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya kupokea heshima na kukagua gwaride. Col. Gatabazi na wenyeji wake waliamua kuondoka kuelekea Kibumba kwanza na kisha jioni ndio waelekee Goma kwenda kuonana na Jean na maofisa wengine wa juu.
"Acheni hilo gari hapa mpakani, hakuna matatizo askari wa jeshi la Zaire wapo wataliangalia maana kule kwenye makambi lazima kwenda na magari ya jeshi la Zaire ndio idara na taasisi za Kimataifa zinazoshughurikia wakimbizi haziwezi kushituka", Col. Bizimaziki alieleza.
"Sawa, vipi minong'ono kwamba watu wetu wanajitayarisha kuishambulia tena Rwanda huku wakitumia kinga ya wakimbizi?", Col. Gatabazi aliuliza.
"Usijali kabisa kuhusu hilo, serikali ya Zaire itakanusha vikali huku sisi tumetia pamba masikioni. Na kama ujuavyo kiongozi wa baraza la Akazu, Anatoile Kabuga. Alitusihi tusisikilize propagada za vyombo hivi isipokuwa tujiimarishe kijeshi tayari kwa kuikomboa nchi yetu kutoka kwa wavamizi wa Kitutsi. Kwanza nilitaka kusahau, vilevile Bwana Kabuga anakuja pamoja na Jean ili maamuzi yaweze kufanyika, ameeleza kuwa mjumbe mwingine wa Akazu ambaye anaweza kufika ni John Ngeze ambaye sasa yuko Afrika Kusini, lakini ameambiwa apande ndege ya shirika la ndege la Afrika Kusini inayoingia mjini Kinshasa saa sita na kama akiwahi atawasubiri pale uwanjani na wao wakiwahi watamsubiri|.
"Lo, kumbe tutakuwa na mkutano mkubwa", Col. Gatabazi alinena.
"Wakati umefika kwa wewe Col. Gatabazi kuchukua nchi kutoka mikononi mwa wavamizi wa Kitutsi. Siri zote za adui yetu unazijua, nguvu ya RPF yote unaijua, ya kijeshi na kisiasa. Sasa nini kitazuia?, wao hawajui nguvu yetu wanafikiri tunacheza. Utaenda sasa hivi kujionea mwenyewe salaha za kisasa, magari, vifaru. Tuna silaha ambazo zina uwezo wa kupiga masafa marefu hadi kilomita mia mbili, na kuna mafunzo makali yanayoendelea kutoka kwa askari wale tuliowakodi kutoka Afrika Kusini na wana kazi kubwa na vijana wetu wana ari kubwa maana wanajua tusiposhika nchi tena maisha yao yako hatarini. Ni kweli kama ulivyosikia wakimbizi tumewazuia kurudi ili siku tutakapoamua kuanza kazi ndiyo siku ambayo wakimbizi wote wanaume tutaandamana nao. Wakirudi wakati huu uhalali wa kuivamia tena Rwanda hatutakuwa nao. Hii vurugu ya wakimbizi kwanza inaficha mambo yote tunayoyafanya, pili itatupa uhalali na nguvu za kuvamia. Rafiki zetu wote watasema. "mlitaka wafanye nini, yaani mamilioni ya watu yabaki kuwa wakimbizi nje ya nchi yao", Col. Bazimaziki alieleza, kisha wakaelekea kwenye kambi.
Walipofika huko kambini walitumia muda mrefu kuangalia aina mbalimbali za silaha za kisasa kabisa, mafunzo makali ya kijeshi, ari ya vijana wa Kihutu, hasa wale Intarahamwe waliotaka siku hiyohiyo kwenda kuvamia Inyenzi na kurejesha madaraka yao. Kutokana na aina ya silaha walizonazo na mafunzo waliyokuwa wakipata na moto waliokuwa nao wa kutaka kupigana na adui. Col. Gatabazi aliamini kabisa kuwa wakisaidiwa na Wahutu waliokuwa ndani ya Rwanda ushindi ulikuwa wao asilimia mia. Col. Gatabazi alipandwa na mori akatamani kama vita vingeanza saa ile. Kisha, wakaondoka kuelekea Goma.
Ilikuwa saa kumi na moja na nusu jioni, Jeana na wenzake walipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Goma. Baada ya kuwasiliwa, walipokelewa na Col. Gatabazi aliyesindikizwa na askari wake. Jean aliwasili akiwa pamoja na kiongozi wa Akazu, Bwana Anatoile Kabuga, Bwana John Ngeze, ambaye ni Mjumbe wa Baraza la Akazu, Jenerali Kasongo, ambaye ni mshauri wa Rais wa Zaire, Meja Karongo, Mkuu wa kikosi cha jeshi linalomlinda Rais wa Zaire, Bwa, George Karikutis, ambaye ni dalali wa mamluki aliyefanya mipango yote ya kuwawezesha Jean na wenzake wa Akazu kupata askari wa kukodi.
Baada ya kuwasili uwanja wa ndege walipelekwa moja kwa moja hadi Ikulu, ambako Rais alitoa kibali Jean na wenzake wafikie kwenye jumba hilo. Ikulu hii ilikuwa ya kifahari sana. Ili uweze kuelewa kwa kifupi, vyoo, bafu na vyumba vya kulala alivyokuwa akitumia Rais vilijengwa kwa vito vya dhahabu tupu. Sasa naamini utakuwa umeelewa maana yake. Karibu na Ikulu hii kulikuwa na Jumba jingine kubwa ambalo Majemedari wa jeshi wa ngazi za juu walikuwa wakifikia. Ndani ya jumba hilo ambalo pia lilikuwa la kifahari sana, ndimo alipofikia Col. Gatabazi na wenzake. Kisha, wakaenda kukaa kwenye sebule ya kifahari ajabu. Wasichana warembo sana wapatao kumi hivi walijitokeza kwa ajili ya kutoa huduma, wakiwa wamevaa kaputula fupi, matiti nje, yaani asilimia tisini walikuwa uchi.
"Hivi ndivyo mzee anavyoishi hapa duniani Jean, hapa panaweza kuwa peponi ukitaka. Mzee ameyafanya maisha yake hapa duniani kuwa sehemu ya peponi. Hivyo, na wewe onja pepo kidogo ukiwa hapa", Jenerali Kasongo alimweleza Jean, ambaye wakati huo alikuwa akitikisa kichwa, maana pamoja na utajiri wake mkubwa usio kifani alikuwa hajawahi kukalia viti na meza za kahawa vilivyotengenezwa kwa dhahabu tupu, ukiacha sehemu za kukaa ambazo zilivishwa kwa ngozi ambazo hata yeye hakuwahi kuziona kabisa duniani.
Huku wale wasichana wakiendelea kuwahudumia, kila mmoja alikuwa amejichagulia mrembo wa kumhudumia, wakileta vinywaji vya kila aina vilivyokuwa ndani ya jumba hilo. Baada ya muda mazungumza yalianza.
"Ehe, hebu Nkubana tueleze ilikuwaje hata huyu Willy Gamba akachafua mipango yetu namna hii, maana inaniuma sana kufikia hatua ya Bibiane kuwa mikononi na mshenzi huyu. Hebu tueleze", Jean aliuliza kwa hasira.
Huku akitetemeka Nkubana alieleza jinsi mambo yalivyokuwa huku wote wakimsikiliza kwa makini sana, kisha akamalizia kwa kusema, "Tulichukua tahadhali ya kila aina, lakini nafikiri huyu Willy Gamba alikuwa na bahati kuliko sisi. Katika biashara kama hii yetu, wakati mwingine ni bahati tu inaweza kukusaidia", Nkubana alijitetea.
"Unafikiri huyu mtu ana mipango gani sasa?", Jenerali Kasongo aliuliza.
"Sijui, lakini naamini Bibiane anaweza kumleta huku. Hizi ni hisia zangu, maana Bibiane atakuwa na uchungu wa kutaka kulipiza kisasi na siri zetu zote anazijua. Hivyo, atataka amtumie Willy Gamba baada ya kuona umahiri wake, alipize kisasi", Nkubana alijibu.
"Mbona hiyo itakuwa raha, maana nitaua ndege wawili kwa jiwe moja, Col. Bazimaziki na Meja Massamba, moja ya kazi zenu ni kuweka kikosi imara chenye wapiganaji jasiri cha kuweza kuwakamata hawa watu wawili, nataka Nkubana akiongoze kikosi hicho, Nkubana, ukiweza kuwakamata usiwaue hao ni halali yangu. Nataka niwafanyie kitu ambacho wakiwa ahera wasinisahau milele", Jean aliamru.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Sawa bosi", Nkubana alijibu hku Col. Bazimaziki na Meja Massamba wakiitikia kwa vichwa vyao.
"Ratiba ikoje?", Jean alimuuliza Col. Gatabazi.
"Nafikiri kwanza twendeni wote tukaangalie hali ya vikosi vyetu ilivyo, hasa hapa Kibumba, maana mtapata mwanga baada ya kuona jinsi tulivyojiandaa tayari kwa vita. Tumetuma habari kwa vikosi vyetu vingine vilivyoko karibu na Bukavu, navyo vijiweke tayari. Ile simu moja kati ya simu nne za Satellite ulizoleta tuliwapelekea na sasa tunawasiliana vizuri sana kati ya hapa na sehemu zingine zote ambako kuna vikosi vyetu, lakini kwa kuwa nguvu yetu kubwa iko hapa nafikiri twende mara moja Kibumba mkajionee wenyewe, kwani ni kilomita thelathini tu kutoka hapa Goma. Halafu tukirudi tutakula chakula hapa na baadaye kidogo tutaanza mkutano wetu. Mimi naamini kuwa mkishaona kama nilivyoona mimi mkutano wa leo utaruhusu tuanze uvamizi leoleo", Col. Gatabazi alimalizia.
Wote walikubaliana naye. Kabla hawajaondoka alichukua simu ya Satellite akapiga simu Tanzania. Nia yake ilikuwa kumpata JKS ili ampatie habari za wakati ule kuhusu nyendo za Willy Gamba kama alikuwa amezipata kutoka kwenye vyanzo vyake vya habari. Kwa mshangao alipata habari kutoka kwa mke wa JKS kuwa alikuwa ameumwa ghafla na kuondoka jioni ile Tanzania kuelekea Uingereza kwa ajili ya matibabu. Na mama huyo alieleza kuwa mumewe aliondoka kwa ndege ya shirika la ndege la Uingereza. Mara moja Jean alihisi kuna tatizo. huku akitingisha kichwa huku wengine wakimwangalia kwa kustaajabu, Jean aliwaambia wenzake wote wamsubiri nje.
Walipotoka nje Jean alipiga simu zingine tatu zilizomchukua dakika kama kumi hivi na baada ya kuzipiga aliagua kicheko kwa sauti mpaka askari aliyekuwa karibu akashangaa akifikiri kuwa huyu mzungu alianza kupata uchizi kwa kucheka peke yake hivi. Jean alipoangalia saa yake ilikuwa yapata saa moja na nusu jioni, hivyo aliungana na wenzake wakaondoka kuelekea Kibumba.
Mjini Kigali baada ya Willy Gamba na Bibiane kuondoka wakielekea mpakani mwa Zaire, Col. Rwivanga alikwenda moja kwa moja kuonana na Mkuu wa Majeshi mnamo saa mbili, akamweleza yote aliyoyapata kutoka kwa Willy kutokana na maelezo ya msichana mrembo Bibiane.
"Kamanda, hali ni mbaya, tusipofanya haraka tunaweza kuvamiwa," Col. Rwivanga alimuasa Mkuu wa Majeshi.
"Sasa tunafanyaje?" Mkuu wa Majeshi, Jenerali Bunyenyezi, alimuuliza Col. Rwivanga.
"Nafikiri mpigie simu Rais aitishe kikao cha Baraza la Mawaziri na makamanda wa vikosi vyote haraka ili tuliangalie swala hili kwa undani zaidi, maana tukifanya mchezo hawa Interahamwe wanaweza kutuvamia, wamepania sana kufanya hivyo, wanaweza kutuvamia, silaha wanazo tena kali na za kisasa, mafunzo wanapewa na askari wa kukodi, maana wapiganaji wao hawana njia nyingine ila kupigana tu ili warudi. Wamekataza hata wakimbizi halali wanawake kwa watoto wasirudi Rwanda kwa hiari yao ili wawatumie katika uvamizi huu. Kamanda, hii ni hatari na ni hatari sana lazima uamuzi upatikane leo", Col. Rwivanga alishauri.
Jenerali Bunyenyezi alimpigia simu Mkuu wa nchi, nae aliposikia uzito wa swala lenyewe aliamua kuitisha mkutano saa sita na nusu ili watu wote wanaohusika waweze kuwepo maana swala hili lilikuwa na maana ya kuanzisha vita dhidi ya Interahamwe waliokuwa mpakani mwa Zaire na Rwanda.
Baada ya Col. Rwivanga kuona umuhimu wa mkutano huu aliwasiliana na Col. Tom Kabalisa, Kiongozi wa Banyamulenge, Baada tu ya kuwasiliana na Mkuu wa Majeshi kwa njia ya simu ya Satellite ambayo serikali ya Rwanda ilikuwa imewapa kurahisisha mawasiliano na kumweleza ajitayarishe kuja Kigali kwenye mkutano muhimu na kwamba angemtumia helikopta ya kumchukua awe Gisenyi saa nne na watu wasiozidi watatu wa ngazi za juu katika uongozi wao wanaoweza kufanya maamuzi. Kwa miezi mingi Col. Tom Kabalisa alikuwa anasubiri huo muda hivyo alifurahi sana kupata habari hizi.
Baada ya kupata habari hizi walikubaliana kuitisha mkutano wa dharura mnamo saa sita na nusu mchana. Rais alipiga simu tena kwa Jenerali Bunyenyezi na kumwambia afike ofisini kwake haraka akiwa pamoja na kiongozi wa upinzani wa Zaire, aliyekuwa akiunganisha vyama vyote vya upinzani na ambaye askari wake waliwahi kupigana vita bega kwa bega na majeshi ya RPF, wakati wa mapambano dhidi ya Serikali ya Rwanda ili wapate uzoefu kutoka kwao. Bwana Mpinda ambaye nae alikuwa mjini Kigali kwa mazungumzo.
Haikuchukua zaidi ya saa moja wote walifika ofisini kwa Rais.
"Bwana Mpinda karibu sana. Nimekuita pamoja na Kamanda hapa ili tuzungumze kama uliyonieleza juzi, maana naona hali imegeuka, sasa inakupendelea wewe", Rais alicheka kidogo na wote wakatabasamu.
"Asante sana Mheshimiwa Rais, nashukuru Mungu, kama umegeuza uamuzi wako na uko tayari kutuunga mkono sisi", Mpinda alijibu.
"Kama nilivyosema naona hali inakupendelea, kuna mambo ambayo yametokea na kuashiria tulifikirie kwa makini ombi lako. Askari wako wote bado wako kwenye ardhi ya Rwanda?", Rais aliuliza.
"Hapana Mheshimiwa, wengine wengi bado wapo lakini baadhi yao wamevuka wapo mpakani, wakisaidia kufundisha jeshi la Wabanyamulenge", Mpinda alimwambia Rais.
"Kamanda Bunyenyezi, nataka basi ufanye mpango na kiongozi wa Banyamulenge nae awepo kwenye mkutano wa saa sita na nusu", Rais aliagiza.
"Na hilo tumelifikiria, na Col. Rwivanga ameshatuma Helikopita kwenda kumchukua", Kamanda Bunyenyezi alijibu.
"Oh, vizuri sana. Sasa bwana Mpinda unakaribishwa kwenye kikao saa sita na nusu, na naomba ujieleze vizuri, na kama ukiweza kuwashawishi mawaziri na makamanda wangu, basi utakuwa umefanikiwa. Hii ni nafasi nzuri sana kwako kwani na sisi sasa tunalazimika kutumia mpango wako ili nasi tukidhi lengo letu. Hivyo, kazi kwako kukishawishi kikao kama kweli una mipango thabiti ya kuweza kufanya kazi", Rais alimalizia.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Mheshimiwa Rais, naenda kukaa na makamanda wangu, na kwa vile viongozi wa Banyamulenge nao watakuwepo na wako upande wenu na wetu, basi naamini nitaweza kukiridhisha kikao kuwa tuko tayari kufanya kweli", Mpinda alijibu.
"Haya Bwana Mpinda kwa heri. Kamanda Bunyenyezi, wewe ngoja kidogo".
Walimtoa nje Bwana Mpinda na wakamrudisha kwenye nyumba ya wageni ya Serikali alikokuwa amefikia na makamanda wake. Rais na makamanda wake walipobaki nyuma, walitafakari swala zima kwa undani. Wakaangalia jinsi ambavyo wangeweza kufaidika kwa kuwatumia wapinzani wa Serikali ya Zaire ili waweze kutimiza lengo lao kuwaondoa Intarahamwe na Wahutu wote wenye siasa kali pale mpakani kwao ili wasije wakaivamia Rwanda, huku bila kulaumiwa na Jumuia ya Kimataifa kuwa wamevamia nchi nyingine na kuwaua wakimbizi.
"Nafikiri hii ndio nafasi yetu ya pekee kumaliza tatizo hili. Kwa hiyo, inabidi tulieleze kwenye mkutano vizuri", Kamanda Bunyenyezi alieleza.
"Je, hawa wapinzani na waasi wa Banyamulenge wakishindwa, itakuwaje? si siri itavuja?", Rais aliuliza.
"Hilo litakuwa jambo jingine, sisi tutakuwa tumetimiza lengo letu na tutakuwa tumewaondoa na kuwamaliza kabisa hawa Intarahamwe karibu na mipaka yetu. Tutakuwa tumewatokomeza mstuni huko Zaire. Shida na wasiwasi kwetu vitakuwa vimemalizika kabisa. Kazi yako itabaki kujenga nchi na si kupigana tena", Kamanda Bunyenyezi alijibu.
"Kweli, sasa tumepata kisingizio; Mungu yuko pamoja nasi, maana chochote tungefanya serikali ya Zaire na Jumuia ya Kimataifa visingetupa nafasi. Basi nenda kajitayarishe, Mkutano utakuwa mgumu sana, maana najua mawaziri wengi itakuwa vigumu kukubali", Rais alijibu.
"Asante Mheshimiwa Rais, nafikiri watatuelewa kwa sababu hii ni kwa faida ya Taifa la Wanyarwanda ambalo limeteseka sana, lazima wananchi wapate muda wa kupumua na si vita kila siku", Kamanda Bunyenyezi alijibu na kueondoka kwenda kujitayarisha.
Mpinda alipofika kwenye nyumba aliyokuwa amefikia, aliteremka haraka kutoka ndani ya gari na kuingia ndani ya nyumba hii, akawagongea wenzake waliokuwa ndani ya vyumba, akiwataka kwenye mkutano pale sebuleni.
Alifikiria na kuona kwamba Mwenyezi Mungu alikuwa ameyajibu maombi yake. Hii ilikuwa nafasi aliyoisubiri kwa muda mrefu sana. Na yeye vilevile kama wenzake wa Rwanda aliona nafasi hii ilikuwa inazifaa pande zote tatu zilizokuwa zinahusika kwenye harakati hizi za mapambano. Kati ya wote waliokuwa katika sakata hilo, alijiona ndiye mwenye fursa ya kufaidika zaidi ingawaje Serikali ya Rwanda ndio ingefaidika zaidi kwa kuhakikisha kuwa haina mgogoro au wasiwasi wa kushambuliwa na Wahutu wenye msimamo mkali chini ya wanamgambo wa Intarahamwe na Banyamulenge ambao nao wangefaidika kwa kutobuguziwa tena na Serikali ya Zaire, na wangeendelea na maisha yao raha mstarehe.
Makamanda hawa walipokusanyika pale sebuleni Mpinda aliwaeleza kila kitu jinsi mambo yalivyokuwa wamejipa.
"Tunachotakiwa kufanya ni kukishawishi na kukikahakikishia kikao cha Serikali ya Rwanda na viongozi wa Banyamulenge kuwa tutakapoanzisha vita hii ni kweli uwezo wa kushinda tunao?. Pande zote zimekubali kuwa sababu tunayo na nia tunayo, swala hapa ni uwezo, wakiridhika kuwa uwezo upo, basi mambo tayari", Mpanda aliwaeleza wenzake.
"Mkuu, wala tusipoteze muda wa kufikiri, sisi tumekuwa hapa tukijaribu kuwashawishi siku zote, tusingekuwa na uhakika na uwezo wetu kivita tusingekuja kuomba watuunge mkono, uwezo tunao. Nenda kawaeleze kwa uhakika kama watatoa msaada kidogo tu, basi nchi yetu tumeikomboa kutoka kwenye mikono ya utawala wa Kidikteta na kifashisti", Col. Mkengeri, mmoja wa makamanda wa wapinzani wa serikali ya Zaire alijibu. Wenzake wote walitingisha vichwa kukubali maneno yake.
"Azimio, tunakwenda wote kushiriki kikao hicho", Mpinda alijibu.
Willy Gamba na Bibiane walisafiri salama kutoka Kigali mpaka Gisenyi bila kukutana na kituko cha aina yoyote Barabarani. Lile gari lenye alama ya Msalaba Mwekundu liliwafanya wasafiri bila kupata usumbufu na habari zilikuwa zimetumwa mapema na wale askari watatu waliotumwa kutangulia mbeke ili lile gari la maofisa wa Msalaba Mwekundu lisibugudhiwe.
Walipofika Ruhengeri walipumzika huku kila mmoja wao akili yake ikifanya kazi jinsi ya kukabiliana na jambo lililokuwa mbele yao.
Baada ya mapumziko ya saa moja hivi, Willy na Bibiane waliendelea na safari yao na kuwasili Gisenyi saa nane za mchana. Moja kwa moja walikwenda Hoteli Meridien-Izuba, ambako walipanga kuonana na maofisa ambao Col. Rwivanga alikuwa amewapasha habari waonane nao na wawape habari kamili kuhusu uhalifu unaofanywa huko Gisenyi na Kibumba, ili kama walikuwa wamebahatisha kupata habari zozote wazipate hapo.
Meridien Hoteli Izuza ilikuwa moja ya hoteli nzuri sana ingawa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Rwanda vilikuwa vimeiathiri kidogo hoteli hii, lakini ilibaki kuwa safi pamoja na misukosuko ilivyokuwa sehemu hii. Ikiwa kwenye ufukwe wa Ziwa Kivu, mpakani mwa Zaire, huku kwa mbali ukiangalia milima ya volkano ya Virunga, kweli Meridien-Izuda palikuwa mahali pazuri sana pa kupumzika.
"Umepapenda hapa?", Bibiane alimuuliza Willy Gamba.
"Mbona wewe unapenda kusoma mawazo yangu?", Willy aliuliza.
"Ubaya uko wapi Willy, fikiri kama tungekuwa tunakuja hapa kwa ajili ya mapumziko na si hii kazi ya hatari, huoni kuwa ingekuwa raha sana, mimi naona tungestarehe sana", Bibiane alijibu.
Huku akitabasamu Bibiane alitoa mkoba wake ndani ya gari huku Willy akijibu. "Sawa mama umeshinda".
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya gari la Msalaba Mwekundu lililokuwa likitumiwa na Willy na Bibiane kusimama, askari wanne walielekea kwenye gari hilo, walipofika karibu mmoja wao moja kwa moja akauliza. "Natumaini nyinyi ni Bwana na Bibi George Mambo wa Msalaba Mwekundu kutoka Makao Makuu Nairobi?".
"Bila shaka", Willy alijibu bila kusita huku Bibiane amejikausha utafikiri kweli alikuwa mke wake, baada ya kutambulishwa vile, Willy alitambua kuwa huyu mwanamke alikuwa kweli amefundishwa vizuri mambo ya upelelezi maana Willy hakumweleza mapema jinsi ambavyo wale askari wangetambulishwa hapa. Kazi yote hii ilikuwa imefanywa na Col. Rwivanga.
"Kamanda Kasubuga anawasubiri pale ofisini kwake", yule askari alimweleza Willy Gamba.
"Twende", Willy alimweleza Bibiane.
"Hapana, wewe nenda tu, mimi nitakusubiri hapa", Bibiane alijibu na Willy akaelewa maana na sababu ya Bibiane kubaki pale, akafurahi moyoni kuwa kweli alikuwa amepata mshirika katika kazi.
Kamanda Kasubuga alikuwa mtu mwenye rika la Willy na baada ya Willy kuingia ofisini kwake aliinuka kwenye kiti alichokuwa amekaa akisoma faili moja hivi, huku akitabasamu akamlaki Willy.
"Karibu sana", Kamanda Kasubuga alimkaribisha Willy.
"Asante", Willy alijibu huku wakishikana mikono na Kamanda Kasubuga alimwonyesha ishara yule askari aliyemleta Willy awape faragha kidogo, yaani aondoke awaache peke yao.
Baada ya yule askari kutoka Kasubuga alisema, Lo! Bwana Willy Gamba ni wewe huyu, Sifa zako na wewe mwenyewe hufanani. Col. Rwivanga amenieleza yote na mimi nikamweleza kuwa nimekusikia sana nilipokuwa Tanzania. Mimi nimefanya kazi na Jeshi la Tanzania na vyeo vyangu vyote mpaka hiki cha umeja nimevipata nikiwa Tanzania".
"Alaa! nashukuru sana", Willy alijibu na kuketi kwenye kiti.
"Oke, bila kupoteza wakati, habari kutoka kwa kijana wetu ambaye juzi tu tumeweza kumnunua kutoka katika jeshi la Zaire linalolinda mpaka na sisi zinaeleza kuwa leo hii yapata saa kumi na mbili na nusu asubuhi waliwasili watu wawili upande ule wa Zaire na kupokelewa kwa heshima zote za kijeshi na kisha wakaondoka kuelekea kwenye makambi ya wakimbizi kule Kibumba. Baada ya maelezo ya jinsi wale watu walivyofanana tulielewa mara moja kuwa mmoja wao alikuwa Col. Gatabazi. Hivyo, Col. Gatabazi kafika na yuko Kibumba", Meja Kasubuga alieleza.
"Hizo ni bahari njema sana, sasa ngoja na sisi tupumzike halafu giza likiingia na sisi tutakwenda Kibumba", Willy alijibu huku Meja Kasubuga akimwemwesa.
"Sawa mzee, ila tumewawekea chumba kimoja maana ni mimi tu ninajua wewe ni nani, hawa askari wengine wote wanajua kweli wewe ni afisa wa Msalaba Mwekundu na kwamba kwa vile unajua utakaa Rwanda kwa muda mrefu umekuja na mke wako", Meja Kasubuga alimweleza Willy.
"Hapa taabu", Willy alijibu kwa mkato.
"Safari ya Kibumba, tumeagizwa na Mkuu wetu kuwa tufuatane, maana siku zote nimetaka kuvuka na kikosi changu cha hapa lakini nimekuwa nakatazwa, lakini leo nimeamriwa tufuatane wote, sijui safari itakuwa saa ngapi?".
"Sijui, tutaangalia wakati huo si na wewe unakaa hapa hapa hotelini?".
"Ndiyo mzee, niko chumba namba 110, nyie mtakuwa nambari 220 kwenye vyumba vinavyofuata".
"Sawa", Willy alijibu na kuaga. Aliporudi pale kwenye gari alimkuta Bibiane anapiga soga na wale askari.
"Tupelekeni chumba namba 220", Willy aliwaeleza wale askari.
Askari mmoja aliingia ndani ya gari baada ya kushusha mizigo yao, akawapeleka kwenye banda lililokuwa na chumba nambari 220. Yule askari alipoondoka Bibiane akasema, "Kwa vile kuna kitanda kimoja tu wewe utalala ng'ambo ile na mimi ng'ambo hii".
"Lo, kumbe ulikuwa unajidai bure, sasa umeanza masharti".
"Si tulisema kazi kwanza?", Bibiane alijibu huku akifunga mlango kwa funguo na kuanza kuvua nguo huku akiendelea kusema, "mimi nitaoga kwanza.
"Sawa mama", Willy alijibu huku mawazo yake yakiwa tayari yameanza kupanga mipango ya usiku ule. "Tukimaliza wote kuoga tuitishe chakula kidogo halafu tupumzike angalau kwa masaa mawili ndipo safari ya Kibumba ianze", Willy alimwambia Bibiane.
"Amri itatoka kwako baba, mimi kazi yangu ni kutii amri tu", Bibiane alijibu huku sasa akiwa amevua nguo zote pale kitandani.
Meja Kasubuga baada ya kuachana na Willy Gamba, alimtafuta Col. Rwivanga akitumia simu ya Satellite na kumweleza kuwa Willy alikuwa amefika salama na kwamba Willy na Bibiane walipanga kuelekea Kibumba usiku uleule.
Col. Rwivanga alifurahi kupata simu ya Meja Kasubuga lakini akakataa Willy na mwenzake wasiondoke, "Hapana mwambie Willy na mwenzake wasiondoke mpaka kesho, kuna mabadiliko ya mipango ya kazi huku, waambie wapumzike tu hakuna tatizo. Meja Tom Kabalisa atakuja kumuona Willy kesho asubuhi, nami nitafika huko kesho asubuhi. Hivyo, mambo yote tutapanga kesho baada ya sisi kufika huko".
"Nimekusoma, nitamweleza kuhusu taarifa hii afande".
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kasubuga aliona si vyema kumweleza Willy wakati ule, bali amwache mpaka baadaye ili apumzike kidogo, lakini muda si mrefu alikuja askari mmoja na kusema kuwa wale wageni wa Msalaba Mwekundu walikuwa wakihitaji chakula. Meja Kasubuka akaona huo ulikuwa muda mwafaka vilevile kuwaeleza kuhusu maagizo kutoka kwa Col. Rwivanga. Hivyo, akaamua yeye mwenyewe ndiye awapelekee chakula kitakapokuwa tayari ili awaeleza kama alivyoagizwa.
"Chakula kilipokuwa tayari Meja Kasubuga aliwapelekea yeye mwenyewe na kuwaeleza kuhusu maagizo aliyopewa kutoka kwa Col. Rwivanga.
"Sawa tumekusikia", Willy alijibu bila kuonyesha kama alikuwa na maana gani au alipanga kufanya nini usiku ule.
KASHESHE
Ilikuwa yapata saa tatu na nusu usiku wakati Willy na Bibiane walipokuwa wakijiandaa kuelekea Kibumba, walivalia sare za Msalaba Mwekundu huku wakiwa wamebeba silaha mbalimbali ndani ya mifuko ya nguo na mikoba waliyokuwa wamebeba yenye alama ya Msalaba Mwekundu. Walibeba silaha zote za hatari yakiwemo mabomu ya kisasa yaliyotolewa na Bibiane.
Willy alikuwa amevaa saa iliyoendana na yale mabomu akiwa tayari kuyatumia wakati wowote wakati wa safari yao. Walipofika kwenye gari na kufungua mlango ili waweke mikoba yao tayari kwa safari, mara moja Meja Kasubuga alijitokeza akitoka gizani akiwa ameshika bastola yake mkononi akawauliza. "Mnakwenda wapi Willy, hamkusikia maagizo ya Col. Rwivanga kwamba msifanye chochote wala msiende Kibumba mpaka mtakapowasiliana nae kesho, haraka ya nini Willy?, mimi sintaruhusu muondoke".
"Sisi hatuendi Kibumba Meja, tuko hapa hapa sehemu ya mpakani ili kufanya utafiti wa hali ya usalama katika maeneo hayo", Willy alijibu.
"Siamini, huenda mnataka kuvunja amri ili mvuke mpaka, hilo sintaruhusu na nimeamru kikosi changu hapa kiwazuie msiondoke hapa hotelini mpaka hiyo asubuhi, mimi nina amri zangu. Willy naomba tafadhali rudini ndani tusije tukavunjiana heshima kwa kuwakamata na kuwaweka chini ya ulinzi mpaka Col. Rwivanga atakapofika hapa", Meja Kasubuga alionya.
Willy na Bibiane waliangaliana, maana wao walikuwa wameamua kuendelea na kazi yao usiku ule. Hawakuona sababu ya kusubiri kesho yake kwani wao walikuwa na mipango yao tofauti ambayo haikuwahusu akina Col. Rwivanga. Nia yao ilikuwa kuwasaka Col. Gatabazi, Nkubana na Jean. Wakati lengo la Col. Rwivanga na jeshi la RPF ilikuwa kuliangamiza jeshi zima la Akazu.
"Naona kama hutuamini Meja, hakuna tatizo tutarudi ndani tukalale", Willy alijibu kwa sauti ya unyonge sana.
"Samahani bwana Willy, mimi natii amri niliyopewa na wakubwa wangu wala msijaribu kunitoroka maana hiyo haiwe.....", kabla hajamaliza kusema sentensi hiyo, milio ya bunduki aina ya AK 47 ilisikika upande mwingine wa hoteli.
"Tumeingiliwa", Meja Kasubuka alisema huku akikimbia kuelekea sehemu ulipotokea mlipuko huku akitoa amri kwa wanajeshi wake kujitokeza tayari kwa mapambano dhidi ya wavamizi.
II
Wakati Jean na wenzake wanatoka Goma kuelekea Kibumba saa moja na nusu ya jioni ile, Nkubana akiwa na kikosi cha askari shupavu wenye mafunzo thabiti wapatao thelathini hivi, walielekea mpakani kutafuta habari za Willy na Bibiane, kwani walikuwa na hisia kuwa lazima wangewatafuta kwa vile Bibiane aliijua mipango yao yote.
Nia ya Nkubana ilikuwa kupeleleza ili amuwahi Willy kabla Willy hajawawahi, maana hii ndio sheria ya mchezo wao huu. Nkubana na kikosi chake walipofika mpakani upande wa Zaire ilikuwa yapata saa mbili na nusu na ndipo walipoelezwa na vikaragosi wao waliokuwa wamejipenyeza ndani ya vikosi vya jeshi la RPF pale Gisenyi kuwa mtu mgeni aliyekuwa amefikia pale Meridien Hotel alikuwa ofisa wa Msalaba Mwekundu na mkewe.
"Huyo mkewe alifananaje?", Nkubana aliuliza kwa shauku.
"Afande, ni mwanamke mrembo ajabu, utanisamehe afande lakini kusema kweli nilipomwangalia yule mwanamke mara moja nilizini afande, ni mzuri sanasana chotara yule?", askari alijibu huku mawazo yake yakiwa yamerudi kwa yule mwanamke na kuanza kumfikiria huku mwili wake unasisimka.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hata Nkubana alipokuwa anakieleza kile kikosi chake. "Watu wetu wamefika yafaa tupange mipango madhubuti tuwashambulie na kuwakamata hai kama bosi alivyoagiza", yule askari hakusikia kabisa mpaka Nkubana alipomshitua tena. Wewe vipi, una tatizo la kifafa", maana alianza kutetemeka.
"Hapana afande, hapana, nafikiri ukame umetuathiri sana mawazo".
"Ukame gani, wewe ni mwehu nini?, hetu tufahamishe huyu jamaa na mkewe wanakaa upande upi pale hotelini?".
Yule askari alieleza kila kitu kwa ufasaha jinsi hotelini ilivyo na akawaelekeza namna ya kuingia mpaka kwenye chumba walichofikia akina Willy bila kushukiwa na askari wa RPF waliokuwa wakilinda eneo hilo.
"Inapofika saa tatu mara nyingi askari wengi wanaondoka kuelekea mpakani na wale wanaobaki mara nyingi wanakuwa upande wa Ziwa. Hivyo itabidi tuvuke mpaka kabla ya saa tatu na nitawaonyesha sehemu salama ya kupita, halafu tutajibanza sehemu mpaka hapo askari wengi watakapotawanyika kuelekea kwenye malindo ya usiku halafu ndipo tutavamia kwani askari watakaobaki tutaweza kuwamudu", yule kikaragosi alielekeza.
"Maelezo yako ni safi sana, unafikiri kutakuwa na askari kama wangapi, yaani watakaokuwa wamebaki kwa ajili ya kulinda hoteli?", Nkubana alihoji.
"Hawawezi kuzidi hamsini pamoja na mimi, maana leo ni zamu yangu kulinda hoteli", yule askari alieleza.
"Ulikuwa ulinde upande gani?", Nkubana aliuliza kwa shauku.
"Unande ule niliokueleza kuwa tutapita halafu tujibanze maana askari anayelinda sehemu hiyo ni mtu wetu, anajuwa kila kitu", yule askari alibainisha.
Nkubana alimwangalia kwa makini yule askari na akaridhika kuwa alisema ukweli na akamwamini.
"Kwanza nenda na askari wangu mmoja mkavinjari, halafu mrudi. Kama kila kitu kiko tayari na mambo shwari ndipo tutaanza kazi", Nkubana aliwatuma ili kuwa na uhakika wa mambo na kuthibitisha maneno ya yule askari alivyoeleza. Baada ya wale askari wawili kuondoka. Nkubana alibaki akiwaweka sawa askari wake tayari kwa kuishambulia hoteli ya Meridien-Izuda ili waweze kuwakamata Willy na Bibiane.
Wale askari waliporudi na kumweleza Nkubana kuwa mambo yalikuwa shwari na vilevile kupata habari kuwa yule mtu wa Msalaba Mwekundu na mke wake walikuwa wamelala baada ya safari ndefu habari hizi zilimfurahisha sana Nkubana, akafikiri kuwa angeweza kumteka Willy na Bibiane wakiwa wamelala na huenda wakiwa wanafanya mapenzi. Alisikia hasira inampanda na palepale akakiamru kikosi chake. "Haya sasa tunakwenda kazini".
Willy aliangaliana na Bibiane. "Unasemaje tuwasaidie hawa ama vipi?", Bibiane aliuliza.
"Hapana tuendelee na mipango yetu. Hii imekuwa bahati nzuri kwetu, naamini Meja Kasubuga ana uwezo wa kuukabiri uvamizi huu, na nahisi walengwa wa uvamizi huu ni sisi tunatafutwa, huenda kikosi cha Col. Gatabazi kimesikia ama kuhisi kuwa tuko hapa. Wakati wao wanatusaka hii itatupa nafasi nzuri, kwanza kumtoroka Meja Kasubuga na pili kuendelea na mipango yetu. Panda gari twende zetu Kibumba tukawasake hawa majahiri", Willy alieleza huku wakipanda gari na kuondoka kwa kasi kuelekea Kibumba.
IV
Wakati kikosi cha Nkubana kikisonga mbele kuelekea hoteli Meridien-Izuda kilishitukiwa na askari mmoja wa doria ambaye baada ya kusikia nyayo za watu zisizo za kawaida akapanda juu ya mti na kuchungulia chini ya kjinjia kilichotelemka kutoka mlimani kuelekea hotelini. Akisaidiwa na mbalamwezi askari hjuyu aliweza kukiona kikundi cha askari kadhaa kikielekea hotelini hapo, baada ya kuthibitisha kuwa walikuwa askari wa adui na jinsi walivyokuwa wakisonga mbele kwa tahadhari kubwa huku silaha zao zikiwa zimewekwa tayari kwa mashambulizi.
Huyu askari wa doria alitelemka kwenye mti haraka haraka na kimya ili asiwagutue wale wavamizi waliokuwa hatua kumi tu karibu na ule mti na kwa kutumia uzoefu wa sehemu ile alikimbia kwa kutumia njia za mkato na kwenda kutoa taarifa kwa kikosi kilichokuwa kwenye maandalizi ya kuondoka kuelekea mpakani kisiondoke kwani kulikuwa na uvamizi.
"Kuna kikosi cha adui kinaweza kutushambulia sasa hivi, kimetumia kichochoro namba tatu na kitafika hapa sasa hivi, askari huyo alimweleza Mkuu wa kikosi hicho Sajenti Ibrahim.
"Oke, wewe kimbia kwa Afande Kasubuga umweleze wakati sisi tunaelekea huko kuwasimamisha mpaka tupate msaada", Sajenti Ibrahim aliamru na palepale akawaamru askari wake waweke silaha zao tayari na kusonga mbele kuelekea kichochoro namba tatu. Njia zote zilizokuwa zinaelekea kwenye hoteli hii zilipewa namba ili iwe rahisi kuzitambua kwani zilikuwa nyingi. Yule askari wa doria alikimbia mpaka ofisini kwa Meja Kasubuga lakini hakumkuta, kwani ndio wakati Meja Kasubuga alikuwa amewasimamisha Willy na Bibiane wasiondoke, na kabla hajajuwa ampate wapi na yeye alisikia milio ya bunduki akajuwa tayari mapambano yameanza.
Sajenti Ibrahim na kikosi chake walifanikiwa kuwaona wale askari wavamizi wakisonga mbele kuelekea hotelini na kwa vile hakujuwa walikuwa na nguvu kiasi gani aliamru askari wake waanze kushambulia hata bila kulenga shabaha kwa uhakika ili kuwatia kiwewe. Na kweli hii ilimshitua Nkubana kwani hakutegemea kukutana na upinzani haraka kiasi hicho kutokana na maelezo ya yule askari muasi.
"Luteni Nyamboma", Nkubana alimwita msaidizi wake, "Wewe endelea kukabiliana na hawa adui zetu ili mimi na askari watano tuweze kupata mwanya wa kwenda kumkamata Willy. Fanya mashambulizi makubwa ili askari wote wafikiri kuwa wanashambuliwa na kikosi kikubwa ili wote waje upande huu na sisi tupate urahisi pale Willy alipo".
"Sawa, nimekusoma Kamanda", Nyamboma alijibu.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nkubana aliwachagua askari watano wazuri pamoja na yule kikaragosi wao. "Wewe tupeleke chumba cha yule mtu, tumia uzoefu wako wa hapa".
"Sawa afande, yule askari alijibu huku akitetemeka maana alistaajabu namna walivyokuwa wamebainika na kuonekana kwa adui mapema namna ile.
Mapigano makali yalianza na, kama Nkubana alivyotaka, askari wengi wa kambi ile walielekea upande wa mapigano kuongeza nguvu wakiongozwa na kiongozi wao Meja Kasubuga. Nkubana na askari wake hawakupata kikwazo mpaka walipofika kwenye chumba alichopangiwa Willy.
Baada ya Nkubana kushuhudia umahiri wa Willy Kigali, hakutaka kufanya makosa tena. Aliwapanga askari wake vizuri na kwa hadhari kubwa, walipofika kwenye chumba cha Willy na kwa amri moja wakaupiga mlango kwa nguvu zao zote na askari wawili wakaingia na mlango ndani ya kile chumba. Chumbani hawakumkuta mtu isipokuwa mikoba miwili iliyokuwa na nguo, Nkubana akautambua mkoba mmoja kuwa ulikuwa wa Bibiane, maana alipata kuuona pale sebuleni kwa Bibiane mjini Kigali.
"Watakuwa wapi hawa?", Nkubana alihoji, kisha akaendelea. "Wanaweza kuwa wamejiunga na askari wa hapa wanaopigana na kikosi chetu au wamevuka mpaka".
Yule askari kikaragosi alikuwa ametoka nje na akarudi na kusema. "Gari lao halipo, nafikiri wamekimbia mapigano".
Nkubana aliposikia hivyo woga ulimwingia kwani alijua mtu huyu amevuka mpaka. "Itatubini na sisi tuvuke mpaka sasa hivi. Wao wameondoka na gari sisi itabidi twende kwa miguu sasa", Nkubana aliamru huku ule upande wa mapigano makali yalikuwa yakiendelea.
"Itabidi turudi kuongeza nguvu", askari mmoja alishauri.
"Hapana, Luteni Nyambona ana ujuzi wa kutosha, akiona amezidiwa atarudi nyuma na kukimbilia mpakani. Huu ni wakati mzuri kwetu kuondoka kuwafuata hawa washenzi", Nkubana alijibu huku wakiondoka kuelekea mpakani.
V
Usiku ule Willy na Bibiane walipokuwa wakielekea kwenye mpaka wa Rwanda na Zaire, mbalamwezi iling'aa sana na kuyaonyesha mandhari safi ya milima ya Volkano ya Virunga.
Milima hii ilijulikana toka zama za kale, ambapo hata Wagiliki wa zamani waliizungumzia sana milima hii wakiita milima ya mwezi. "Sasa wewe mwenyewe unaweza kuona kwanini waliita hivyo", Willy alimsimulia Bibiane.
"Inaonekana wewe umesoma sana historia", Bibiane alieleza.
"Unajuwa kitu chochote hakiwezi kuwa kitu bila historia. Ili uijue dunia hii lazima ujue historia. Hata binadamu hawezi kuwa binadamu kama hana historia. Ndio maana mimi nikikwambia naitwa Willy, lazima utaniuliza Willy nani, nitakujibu Willy Gamba. Halafu utataka kujuwa baba yangu anatoka wapi halafu nitakwambia. Hii yote ni kutaka kujua historia yangu ili uweze kujua namna utakavyoniweka. Hata nchi. Nchi isiyokuwa na historia si nchi. Haiwezi kuwa na maendeleo. Sijui kama umenielewa vizuri mpaka hapo?", Willy alijibu na kuhoji.
"Nimekuelewa vizuri sana Willy. Kwa muda huu mfupi nitakaokuwa na wewe hakika nitajifunza mambo mengi", Bibiane alimwambia Willy.
"Sasa walikuwa wanakaribia sana mpakani, na Bibiane akasema.
"Tukivuka mpaka tu, lazima tutakutana na kikosi cha jeshi la Zaire, Unasemaje?".
"Unazijuwa njia nyingine tunazoweza kukwepa mambo ya mpakani?", Willy aliuliza.
"Ndiyo Willy, na ndio sababu nimesema hivyo, hapo mbele utakata kulia nitakuonyesha njia ya siri wanayotumia wapelelezi wa Akazu, lakini tuwe na tahadhari kubwa. Willy akakata kulia baada ya mwendo wa dakika kadhaa mara njia iliisha. Kukawa na njia ya majani tu. "Endelea tu. Ukikata tena kushoto. Tutakuwa tayari tuko Zaire. ni kilomita kama moja tu kutoka hapa", Bibiane alimwambia Willy, baada ya kutembea mwendo wa kilomita moja na baada ya kupita sehemu ya miti mingi walitokea mahali pa wazi na upande wa kushoto wakaona taa zinawaka.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Pale ndio mpakani upande wa Zaire na ile ni kambi ya jeshi la Zaire", Bibiane alieleza.
"Tunaweza kupata magari ya jeshi pale?", Willy alimuuliza Bibiabe.
"Lazima. Unataka tukaibe gari moja la jeshi?", Bibiane alihoji.
"Unasoma sana mawazo yangu. Tusiibe, tukachukue tu?", Willy alijibu na kuendelea. "Ili tusije tukatia shirika la Msalaba Mwekundu dosari, yafaa tusiwe na gari lao kwenye uwanja wa mapambano. Hapa tutapata mahali pazuri pa kulificha halafu tukachukue gari la jeshi la Zaire. Itakuwa vilevile vigumu kusimamishwa na askari hovyohovyo".
"Je kuhusu nguo itakuwaje?", Bibiane alihoji tena kwa shauku.
"Kuhusu nguo tutawavua askari walioko mpakani". Willy alisema huku Bibiane akicheka sana.
"Wewe una mambo. Mbona naanza kusikia raha, usiku huu naona itakuwa kasheshe tupu", Bibiane alinena.
Walitafuta sehemu iliyokuwa na msitu wakalificha gari la Msalaba Mwekundu na kuitoa mizigo yao. Gari lilifichika vizuri sana kiasi kwamba ingekuwa vigumu mtu kuligundua mara moja.
"Tutalipitia kabla jua halijachomoza", Willy alinena.
"Kama tukiwa hai", Bibiane alijibu.
"Ili uweze kubaki hai fikiri kuwa utakuwa hai. Na ukiwa hai ukifikiri utakufa. Utakufa tu", Willy alifafanua.
"Sawa bosi. Tutarudi hapa kwenye gari letu tukiwa hai", Bibiane alisema.
"Mawazo safi kabisa", Willy aliongeza. Wakiwa wamebeba silaha zao na kila kitu walichohitaji kwa mapambano usiku ule walianza kuinyemelea ile kambi ya jeshi mpakani Zaire. Walipofika pale kituoni waliyaona magari matatu ya jeshi aina ya Landrover ya wazi nyuma yakiwa yameegeshwa. Walipoangalia vizuri waliwaona askari watatu. Kila mmoja akiwa ameegemea kwenye gari lake.
"Hao watakuwa madereva wa hayo magari", Bibiane alibobota kwa sauti ya chini.
"Hata mimi nafikiri hivyo, nahisi yalikuwa yamewachukua wale askari walioshambulia kule Meridiane hoteli, maana inaonekana hawa askari wanaosubiri watu", Willy alijibu.
Kwa vile yale magari yalikuwa karibu na ua wa michongoma na pale mahali. Willy alifikiri namna ya kuwashambulia bila ya kuwagutusha watu wengine pale kikosini. Mara akawaona askari wote wanakuja kuzungumza na yule askari aliyekuwa kwenye gari la mwisho karibu kabisa na ua.
"Bibiane kazi kwako, hapohapo wewe mshambulie yule wa kushoto. Mimi nitamalizana na wale wawili. Wa kati na kulia", Willy aliagiza huku hawa askari wakiwa sasa wameegemea kwenye magari yao huku wameipa visogo sehemu ile waliyokuwa wamejibanza akina Willy.
"Wale tutumie bastola zenye kizibo tusipoteze muda", Bibiane alishauri.
"Hapata, tunahitaji kila risasi tuliyonayo isipotee bure, pale ambapo tunaweza kulinda risasi nashauri tutumie njia nyingine, au unaogopa hutaweza kumkaba sawasawa?", Willy alimuuliza Bibiane.
"La, hasha! naweza sana Willy na wewe mwenyewe utanishuhudia leo; haya twende", Bibiane aliamru.
Huku wakitambaa chini kama nyoka, waliwanyemelea wale askari. walipofika usawa wa gari la kwanza Willy alisema. "Sasa", wote wawaili walirukia na bila kuwapa nafasi hata ya kushituka, Willy aliwapiga wawili karate kwenye vichwa akitumia mikono yake miwili na kupasua vichwa vyao palepale. Bibiane alimrukia yule wa kushoto na kumbana shingo na kisha kuikata kwa mikono yake. Hawa askari waliuawa kama kondoo. Hawakutoa upinzani wa aina yoyote, huenda kwa vile hawakutegemea kushambuliwa kama lile mahali pale. Kisha walizivuta maiti zao mpaka nyuma ya ua, wakawavua zile sare za jeshi na kuzivaa haraka haraka. Bibiane alichekelea sana maana zilikuwa kubwa. Hata hivyo akazifungafunga zikamwenea hivyohivyo.
"Utaweza kukimbia ama kupigana na adui ukiwa na magwanda haya?", Willy alimuuliza Bibiane huku akicheka.
"Tena ndio mazuri zaidi hasa kwa judo na karate", Bibiane alijibu.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Willy na Bibiane walibeba mizigo yao na kisha wakachungulia ndani ya magari na kukuta la gari la katikati likiwa na funguo. Waliweka mizigo yao ndani na kuliwasha na kisha kuondoka. Walipoangalia saa ilikuwa yapata saa nne na nusu usiku. Waliondoka bila mtu yeyote pale kuhisi kitu. "Moja kwa moja Kibumba", Bibiane alisema.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment