Simulizi : Roho Ya Paka
Sehemu Ya Pili (2)
“Usinilazimishe kukulazimisha,” Chongo alifoka. “Mbona huna shukrani, mtu wewe? Ombi dogo kama hilo likushinde wakati unanenepa tumbo kwa mamilioni yangu?” alimaliza kwa kicheko chake cha kikohozi.
Banduka alipoona kuwa hana uwezo wa kumkana alijitia kuafiki huku akibuni mbinu zaidi ambazo aliamini zingemfanya Chongo ajute milele kumtibulia maisha yake ya amani ambayo amekuwa akiishi miaka nenda rudi.
“Nitakuhifadhi,” alimwambia, “lakini kwa masharti kwamba hutatoka nje ya nyumba hii mchana, na utakapokamatwa usithubutu kunitaja kwamba tunafahamiana. Upo?”
Chongo alipochelewa kujibu aliongeza, “Usijidanganye kuwa ushahidi ulionao utakusaidia chochote. Nina marafiki wakubwa hapa. Ukikorofisha ukamatwe elewa kuwa utakufa na ushahidi wako hata kabla hujafika mbele ya mahakama.”
Hilo lilimchekesha Chongo. Baada ya kicheko chake alisema, “Kabla sijafa mimi elewa kuwa wewe utakuwa na risasi sita kichwani mwako. Hilo nakuomba ulitie maanani. Hila yoyote itakuletea balaa. Unaiona hii?” kwa wepesi wa ajabu, bastola yake ilitolewa na kuzungushwa angani, akairusha mara mbili na kuidaka huku ikizunguka. Kisha, aliipunga kumwelekea Banduka
“Unaona?” alimuuliza. “Sina mchezo, sitaki mzaha. Na kuanzia sasa hivi ni mimi nitakayetoa amri zote katika nyumba hii hadi nitakapoondoka. Tumeelewana?”
Muda mfupi baadaye, kwa amri ya Chongo, Nuru ambaye alikuwa amelazwa nje ya mlango kwa nyuma, aliingizwa humo akiwa amebebwa na Alhaji Banduka. Nuru akiwa taabani kwa uchovu. Alijifanya mgonjwa zaidi kiasi kwamba hata alipoongea kuomba maji iliwachukua dakika mbili kumwelewa. Alipatiwa maji. Kisha, Banduka aliamriwa kuleta chakula. Ulipatikana wali mkavu kwa kahawa. Nuru alifunguliwa mkono mmoja na kutakiwa ale. Kwa jinsi alivyokuwa na njaa aliusikia wali huo kama biriani ya kuku.
“Unaweza kwenda kulala,” Banduka aliambiwa. “Nitakuhitaji kesho saa mbili. Kumbuka ukijitia akili utajuta kuzaliwa. Nenda.”
Banduka akatoka.
Chongo akaufunga mlango nyuma yake na kuutia ufunguo. Kisha akamgeukia Nuru na kusema, “Mpenzi… tupo peke yetu kama nani na nani vile?... Adamu na Hawa,” akajijibu mwenyewe. “Wapi ilikuwa vile?... Bustani ya Edeni… au sio?...”
Nuru hakujua kama ilimpasa kulia ama kucheka kwa kipande hicho cha habari. Kufanya mapenzi na dude hilo, rohoni mwake ilikuwa ni aibu na tusi lisilostahimilika. Kwa mara nyingine akafanya uamuzi kuwa ni maiti yake tu ambayo ingelala na chongo. Yeye hapana.
“Unasemaje mpenzi?” Chongo alikuwa akiendelea. “Si unajua kuwa roho yako iko mikononi mwangu? Basi uweke pia mwili wako miguuni mwangu. Ukifanya kazi nzuri naweza kukuachia roho yako. Tuna muda wa saa tatu za kusubiri. Nataka tutumie kwa kujiburudisha. Baada ya hapo nitapiga simu moja Dar es Salaam. Majibu yakiwa mazuri utatoka chumba hiki ukiwa na sura nyingine kabisa, yakiwa mabaya utatoka kama ulivyo, pengine na mtoto wetu tumboni mwako. Upo?”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nuru alimtumbulia macho, hasira zikichemka rohoni mwake.
“Sema,” Chongo alisema akimsogelea na kumminya titi. Nuru alitazama kwa makini zaidi.
Kabla hajaliwasha, alichunguza kila kitu kwa makini. Hakuona kasoro yoyote. Akaliwasha na kuliondoa kufuata Mtaa wa Samora. Macho yake yalikuwa makini. Alisimamisha gari hilo mbele ya duka moja na kuingia. Hakuona gari lolote. Alipotupa macho mbele aliona gari moja dogo jeupe likisimama, magari manne mbele yake. Alipomfikia dereva wa gari hilo, alimtazama kiujanjajanja katika kioo chake cha ndani. Akatabasamu na kumpita huku yeye pia akijitia hamwoni.
Aliendesha gari moja kwa moja hadi Mtaa wa Lumumba. Mbele ya Jengo la Ushirika. Hapo alishuka na kukiendea kikundi cha watu ambacho kilikuwa kikisubiri lifti. Yeyote aliyekuwa akimfuata Kakakuona aliamini kuwa hakuwahi kuipanda lifti hiyo kwani mara tu alipofika lifti ilifika, naye akawa mtu wa mwisho kuingia.
Alipanda hadi ghorofa ya mwisho kisha akashuka nayo hadi mwisho wa lifti hiyo ambako ni ghorofa moja zaidi chini ya ardhi. Huko aliacha lifti na kufanya haraka kuifuata ngazi ambayo inatokea upande wa pili wa jengo hilo. Huko alitembea hadi mtaa wa pili ambapo alikodi teksi iliyomfikisha Kariakoo ambako alishuka na kukodi teksi nyingine iliyompeleka Ilala.
Akaingia ofisi ya ndege za kukodi, AirTanzania, na kuomba usafiri wa haraka kwenda Zanzibar. Akitumia pesa nyingi na hati zake za bandia dakika ishirini baadaye alikuwa akielekea juu ya anga ya Zanzibar.
***
Ulikuwa usiku mrefu mno kwa Joram Kiango, usiku unaochosha na kukinaisha kupita kiasi. Kwa mtu wa vitendo kama yeye, ilikuwa kama adhabu kukesha wima, ndani ya chumba chako, kando ya kitanda chako, ukisubiri jambo ambalo halitokei.
Kucha aliyatega macho yake yakipasua kiza kuchunguza chochote ambacho kingekuwa kigeni chumbani humo. Kadhalika, masikio yake yalikuwa makini, tayari kunasa mchakacho wowote ambao angeusikia. Lakini hadi kulipopambazuka hakusikia wala kuona chochote, jambo ambalo lilimfanya ajikute akipandwa na hasira kali zaidi dhidi ya yeyote aliyekuwa akimtendea kitendo hicho, hasira ambazo kiasi zilimfanya ajione mpumbavu kwa uamuzi wake wa kuwasubiri adui hao.
Ilikuwepo haja gani ya kupoteza usiku mzima akiwa ameketi akiwasubiri badala ya kuwa mitaani akipambana nao? ‘Haiwezekani kuwa kitendo chake cha kukesha hapo bila ya kushughulika ndicho hasa walichokihitaji ili waendelee na unyama wao mitaani? Wamenifanya mpumbavu!’ aliwaza kwa uchungu na hasira. Na kwa hasira hizo alitabasamu.
Hata hivyo, hakujilaumu sana. Alijua kama siyo leo, kesho wangekuja kuhakikisha mauti yake. Na alikusudia wamkute akiwa anajua adui yake ni nani na anakusudia nini. Hivyo, asubuhi hiyo aliamua kuitumia kwa uchunguzi.
Kulipopambazuka kikamilifu, Joram akaingia bafuni kuoga. Kisha, akaliendea kabati la nguo na kutafuta moja kati ya mavazi yake ambayo humfanya asitambulike kwa urahisi wala kumtazama kwa makini. Leo alivaa kanzu nyeupe, kijikoti cheusi juu, ndala miguuni, kofia pana kichwani na miwani myeusi.
Akachukua fimbo yake ya kutembelea na kutoka nje akitumia mlango wa nyuma. Baada ya kupenya hapa na pale, aliifikia barabara kuu ambako alikodi gari lililomfikisha mjini. Huko alitafuta hoteli na kujipatia kifungua kinywa. Kutoka hapo alikwenda Mtaa wa Mkwepu kwenye duka moja ambalo wanaruhusu wapita njia kupiga simu kwa malipo. Alimwomba Mhindimwenye simu hiyo aitumie nusu saa huku akimpa shilingi elfu tano.
“Napiga hapahapa mjini zikiisha, nitaongeza,” alimwambia.
Huku akiwa na mshangao, mwenye duka huyo alipokea harakaharaka na kumpisha Joram kiti.
Polisi ni watu wanaojua sana kufumba midomo. Kujaribu kunyofoa ukweli toka katika mikono ya polisi ni kazi ngumu kama kujaribu kung’oa ulimi wa jabali. Lakini si kwa mtu kama Joram Kiango. Hadhi yake katika masuala ya mapambano ilimpatia marafiki wengi katika jeshi hilo. Aidha, alikuwa na marafiki zake wawili, watatu ambao humuuzia siri na habari mbalimbali anazohitaji, kama vile ambavyo yeye huwapa ‘tip’ wanapofuatilia masuala fulanifulani anayoyafahamu.
Akiwa na hakika kuwa mauaji ya wasichana wote wawili yalikwishagundulika na polisi, simu yake ya kwanza aliielekeza Idara ya Upelelezi ya kituo kikuu. Alikuwa na bahati ya kumpata mtu wake.
Baada ya maongezi mafupi ya mafumbo-mafumbo, Joram aliweka simu chini. Habari alizopata licha ya kuwa hazikumnufaisha sana bado zilimwongezea hasira. Mpelelezi huyo alikiri kuwa bado kuna jambo la ‘moto sana’.
Anachofahamu ni kwamba, raia watatu na askari kanzu mmoja wamekwishauawa. Ni hilo lililomsikitisha Joram Kiango. Watu zaidi wameendelea kufa wakati yeye ameketi juu ya kochi akisubiri adui ajilete. Aibu iliyoje!
Maswali yake yaliyofuata hayakupata majibu zaidi. Hivyo, Joram akakata na kupiga kwenye simu ya Kombora. “Namtaka Shoka,” aliomba.
“Hayupo”
“Yuko wapi?”
“Amehama.”
Moyo wa Joram ulidunda kwa nguvu. Hakuwa mgeni wa msamiati huo. Askari anapotamka moja kwa moja kuwa askari fulani amehama, huwa haina maana nyingine zaidi ya kufa. Yawezekana ni yeye aliyekufa kwa ajili yake? Joram alijikaza na kutaja jina la pili.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hayupo,” mtu wake wa tatu pia hakuwepo.
Wakati Joram akiwa ameduwaa, mtu aliyekuwa upande wa pili wa simu alimshangaza alipomwambia, “Au nikupe Inspekta Kombora mwenyewe Joram?”
“Ndi…yo… hapana. Labda hahitaji kuniona. Pengine wewe unaweza kunisaidia…”
“Najua Inspekta hana muda wa kukuona. Wala asingependa kukushirikisha. Hata hivyo, mimi nitakuibia siri. Suala hili ni zito na gumu. Watu wanaendelea kuteketea kwa ajili yako, wakati uko gizani. Mwiba hutokea ulikoingilia. Tunaweza kuonana wapi nikudokolee hicho tulichonacho?”
“Tukutane New Africa…”
“Hapana.”
“Embassy.”
“Haifa?”
“Wewe unadhani wapi panafaa?” Joram alimuuliza.
“Hapohapo ulipo. Dakika tano baadaye. Uko wapi?”
Joram akaeleza.
Kama walivyo vijana wote wa Inspekta Kombora, kijana huyu ambaye alimtokea Joram Kiango dakika saba baadaye, alikuwa mkakamavu, mtulivu na mstaarabu kiasi kwamba haikuwa rahisi kumshuku kuwa ni kachero. Lakini si kwa Joram. Alitambua mara tu alipoingia katika mgahawa huo, gazeti mkononi na kuketi kama wateja wengine, akimsubiri mhudumu ambaye aliagizwa kuleta soda. Joram aliiacha meza yake na kuhamia meza aliyoketi bwana huyo.
“Ningeomba kuwa mwenyeji wako,” alimnong’oneza.
Mgeni huyo alimtazama Joram kwa mshangao kidogo, mshangao ambao uligeuka kuwa tabasamu baada ya kumtambua, licha ya mavazi yake bandia.
“Vizuri. Nadhani tunaweza kuzungumza hapahapa. Au?”
“Siyo pabaya.”
“Kwanza, ningeomba unielewe kuwa kwa kuzungumza nawe navunja amri zote za kazi yangu. Jambo ambalo natarajia kuzungumza ni siri kubwa sana ambayo haikutakiwa kuyafikia masikio ya raia yeyote yule. Mzee Kombora ataninyonga kwa mkono wake kama atasikia kuwa nimekudokezea. Natumaini unanielewa.”
“Vizuri sana,” Joram alimjibu.
“Hata hivyo, kama nilivyoeleza awali, sioni umuhimu wa kutokukuhusisha. Hakuna asiyefahamu mchango wako katika kupambana na udhalimu hapa nchini na kote duniani. Zaidi, sioni kwa nini watu wasio na hatia waendelee kuuawa kinyama wakati wewe umestarehe. Sidhani kama wewe u mvivu kiasi hicho. Natumaini tutakuwa bega kwa bega kupambana naye. Sawa.”
Joram aliona kama anayepotezewa muda kwa maelezo yasiyo ya msingi. Alichohitaji ilikuwa ni kitu kidogo sana. Kuelewa makachero wanaelewa nini juu ya adui huyo, ili aanze harakati. Kulala ndani kulikuwa kumemchosha.
“Unaonaje ukikata mahubiri na kunieleza kile ulichopanga kunieleza. Huoni kama tunapoteza muda?” alimuuliza.
“Yote ambayo naweza kukueleza yako katika gazeti hili. Ambacho hakimo ni kwamba sasa hivi Kakakuona yuko Zanzibar.”
“Kakakuona?”
“Inaonekana humfahamu,” kachero huyo alieleza. “Huyo ndiye mbaya wako. Anaweza kuwa ni mtu hatari zaidi ya kifaru aliyejeruhiwa. Anaua huku ametulia kama anakunywa maji baridi. Kifo chake ni muhimu kitokee kabla hajatuathiri,” alimaliza akiinuka huku akiliacha gazeti lake mezani.
“Wazulu wa kale hawakuwa na neno ‘asante’ katika msamiati wao, wala samahani, mimi na wewe tunaishi katika dunia na kucheza na kifo. Hatuna tofauti yoyote na Wazulu hao. Hivyo, sina la kusema…” Joram alimwambia kachero huyo huku akijaribu kumpa mkono ambao ulipuuzwa.
“Hunijui, sikujui. Sawa?”
“Sawa,” alijibu akitabasamu. Kisha, akalichukua gazeti hilo na kuhamia hoteli nyingine ambako nako pia alichukua meza ya kando, isiyo na mtu. Baada ya kupata kinywaji chake alitoa nakala sita za kopi za maandishi yaliyoonekana kama yaliyotoka kwenye faili.
Alizisoma kwa makini. Dakika mbili baadaye alizichanachana huku akiwa tayari amezichora akilini.
‘Kakakuona!’ aliwaza kwa hasira. ‘Anamtaka nini? Ameibuka kutoka wapi? Nani anamtumia? Kwa nini? Kwa nini? Kwa nini?’ alifoka kimoyomoyo.
Maswali yalikuwa mengi na marefu. Majibu yalihitaji muda. Kuwasiliana na wenzake wa nje. Kuwasiliana na benki, kujadiliana na nyumba za wageni, kufuata nyayo zake zinakotokea, kuwalipa maajenti wa nje, wenye kompyuta ambazo zinaweka kumbukumbu za vitendo vya watu kama hao n.k. Yote hayo yalihitaji muda, kitu ambacho Joram hakuona kama kilikuwepo. Kilichohitajika ni kumuua Kakakuona kwanza, na kuuliza maswali baadaye.
Baada ya kuwaza hayo, alifanya haraka kwenda Air Tanzania ambako walimvunja moyo kwa kutokuwa na ndege ambayo ingeondoka muda huo isipokuwa “Saa kumi na mbili za jioni.”
Shingo upande, akageuza njia na kuifuata Sea Express.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Boti ambayo ingeondoka mapema zaidi ilikuwa ni ya saa tisa mchana, saa nne baadaye. Joram alikata tiketi yake. Kisha, akatafuta simu ambapo alipiga moja Zanzibar na ya pili Nairobi. Zote hazikuwa na majibu ya mara moja. Akaahidi kupiga tena usiku huo.
Muda wa kusubiri Joram aliuona mrefu kupita kiasi. Kila dakika iliyopita ilizidi kumtia wasiwasi. Mara kwa mara akilini ilimjia picha ya Nuru akiwa na uso kama ulioteketezwa kinyama kama nyuso alizoziona katika picha alizotumiwa, jambo ambalo lilizidi kumtia hasira na kumfanya atamani kuruka, apae hadi Zanzibar, mbele ya Kakakuona.
***
“Ndege yake inatua mzee.”
Kombora aliarifiwa katika simu, kutoka Uwanja wa Ndege Zanzibar.
“Vizuri,” alijibu.
“Anashuka. Abiria ni mmoja tu. Amebeba mkoba. Mavazi yake ni kama uliyoyaeleza. Haonekani kama mtu mwenye wasiwasi wowote. Sasa hivi amefika meza ya Uhamiaji. Tumkamate?”
“Nimesema msimsogelee hadi nitakapotoa amri nyingine. Ni mtu hatari kuliko mnavyoweza kufikiria nyie,” Kombora alifoka. Kisha akaongeza “Endelea kuniarifu kila tukio na wekeni makachero wengi waangalie kila hatua yake. Angalieni asifahamu kuwa anafuatwa. Sawa?”
“Sawa”
Baada ya muda, “Amekodi teksi. Anaelekea mjini. Magari yetu mawili ya teksi yanamfuata kwa uangalifu.” Na baadaye “Inaelekea kama anafahamu kuwa anafuatwa. Lakini yaelekea hajali.”
Dakika kumi baadaye Kombora aliarifiwa ghafla, “Ameshuka mzee! Amechoropoka ghafla sehemu za Darajani. Haonekani alipo. Yaelekea amejichanganya katikati ya watu na kuingia mitaa ya Mji Mkongwe. Tufanyeje?”
“Asipotee.” Kombora alinguruma “Makachero wote wafanye kazi ya kumtafuta ili awe chini ya miwani yenu kila dakika. Nataka kujua anafanya nini, anakutana na nani, na kadhalika, na bado naonya asisogelewe wala kushtuliwa. Sawa?”
“Sawa, Afande.”
“HUWEZI kulala na mwanamke aliyefungwa kamba mikononi na miguuni, ukafaidi, huwezi ukatamba mbele ya marafiki zako kuwa mwanamke yule nimefanya naye mapenzi, wakati alikuwa kafungwa mikono na miguu, ambapo hakukukumbatia, hakukubusu wala hakukufurahia. Ni aibu. Ni kitendo cha kihanithi.”
Nuru aliyasema hayo kwa sauti aliyoifanya dhaifu kuliko ilivyokuwa, macho yake yakimtazama Chongo kwa ulegevu huku akiruhusu tabasamu dogo kuutembelea uso huo.
Ilimgharimu kila kitu kuyatamka maneno hayo. Tangu kiumbe huyo alipoonyesha dalili za kumtaka mapenzi roho ilipasuka na akili kufadhaika. Alijisikia kulia, alijisika kucheka na alijisikia kutapika. Yote hayo hakuyafanya. Badala yake alijikaza kisabuni na kuyatamka hayo kwa nia ya kumlaghai Chongo.
Chongo hakuwa mpumbavu kwa namna ambavyo Nuru alimkadiria. Kama jibu kwa maelezo ya Nuru alikitoa kitu kile ambacho alikusudia kuwa tabasamu usoni mwake. Kisha, alimwambia, “Una hila kama kinyonga, mpenzi. Ningeweza kukukomoa zaidi kwa kunifikiria bwege kiasi hicho. Bahati mbaya muda wa kuketi chumbani humu ni mrefu mno. Siwezi kuvumilia kukuachia. Ila tu nakuomba wakati nikifanya vitu vyangu usiote kabisa kunivamia. Nitakufungua miguu. Na nitakuwa na bastola mkono mmoja.”
“Na mikono?”
“Siwezi kukufungua.”
“Nitakukumbatia vipi? Au unaniogopa? Mwanamke mmoja tu katika chumba kilichofungwa, huku una bastola mkononi! Nilidhani wewe ni mwanaume..!”
Sauti hiyo yenye dhihaka ilimwingia Chongo. Akiwa mtu ambaye hana asili ya kukubali kudharauliwa, alimwambia Nuru, “Vizuri. Nitakufungua mikono na miguu. Lakini nakuonya. Kama nia yako ni kujaribu ushangingi, kwangu sina lawama. Nitakuharibu bila kujalI kuwa nitakuuza kwa mamilioni. Upo?”
Kitu kimoja Chongo hakuelewa. Hakuelewa kuwa Nuru alikuwa ameamua kitambo kuwa alikuwa tayari kuacha maiti yake ilale na Chongo, siyo yeye! Hivyo, alitulia pindi Chongo alipokuwa akizikata kamba za miguuni na mikononi. Akatulia pia wakati nguo zake zikipambuliwa moja baada ya nyingine na kuwekwa kando ya kitanda.
Na alizidi kutulia alipolazwa chali juu ya kitanda hicho, miguu yake ikipelekwa mmoja huku mwingine kule. Kisha, bila ya kuitua bastola iliyokuwa imara mkononi mwake, Chongo akaanza kufungua vifungo vya suruali yake.
Ni kitendo hicho ambacho Nuru alikuwa akikisubiri. Aliifyatua miguu yake kama mshale, akailenga shingo ya Chongo!
Lilikuwa pigo zuri. Lakini Nuru naye alikuwa gizani. Hakuwa na habari kuwa Chongo alikitarajia kitendo hicho. Hivyo, teke hilo zuri lilipepea angani na kuikosakosa shingo hiyo iliyokusudiwa kwa nusu inchi. Wakati huohuo, Chongo aliachia ngumi nzito ambayo pia ilimkuta Nuru ameviringika kutoka kitandani na kusimama, akiwa tayari kwa lolote.
Tayari kufa.
Tayari kuua.
Ilikuwa dhahiri kuwa Chongo hakupenda kutumia bastola. Aliididimiza mfukoni na kumsogelea Nuru huku akiyumba kwa mbinu. Nuru alimsubiri. Ngumi mbili za Chongo zilimkosa Nuru, kitendo ambacho kilikuwa kosa kubwa katika maisha yake, kwani wakati huohuo vipigo vya Nuru vilimnyeshea kama mvua kiasi cha kumfanya aanguke kitandani. Nuru alipojaribu kumfuata kitandani hapo alisita baada ya kuona Chongo akiichomoa bastola yake na kumwelekezea huku akinguruma “Naua!”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mauaji yalikuwa wazi katika macho yake. Huku uso wake ukitetemeka kwa hasira na maumivu, aliilenga vizuri bastola yake. Kwa sauti nzito akasema, “Malaya mkubwa nimejaribu kukuhurumia hadi dakika hii bado unanionyesha ushangingi. Sasa sina budi kukuondoa duniani.”
Kwa mara ya kwanza maishani Nuru alijikuta hana la kufanya. Kana kwamba mwili mzima umeshikwa na ganzi alijikuta katulia kimya akiisubiri risasi!
***
Baada ya kuuacha uwanja wa ndege huku akiwa na hakika kuwa anafuatwa, Kakakuona alimwamuru dereva wa gari alilokodi kumshusha katika kundi la watu eneo la Darajani. Alipiga chenga mbili tatu za mwili na kuingia sokoni. Kutoka hapo akapenya hadi mbele ya duka mashuhuri la vitabu, ambako alijinunulia gazeti la Heko na kisha kuingia katika mgahawa mdogo ulioelekeana na duka hilo.
Akiwa katika mji huo mkongwe wenye vichochoro vingi, alikuwa na hakika kuwa amewapiga chenga ya mwili makachero waliokuwa wanamwandama. Hata hivyo, alijua hiyo ni chenga ya muda mfupi tu. Mji wa Zanzibar ulivyo mdogo, na mkongwe kiasi kwamba karibu raia wote wanafahamiana alijua baada ya saa chache atakuwa tena machoni mwao, akichunguzwa kwa kila kitendo chake. Hivyo alitaka atumie muda huo mfupi wa Uhuru kukamilisha suala la kumuua Chongo na kumtia Nuru mikononi mwake. Mengine yangefuata baadaye.
Hofu ya kukamatwa kabla ya kutimiza azma yake haikuwa na nguvu akilini mwake. Alikuwa na hakika kuwa japo polisi walikuwa wanamshuku bado hawakuwa na ushahidi wowote wa haja ambao ungemfanya asimamishwe kizimbani kwa kosa la mauaji. Na ni hilo peke yake lililowafanya wasite kumvamia wakati walipopata mwanya.
Kwa utulivu alifikiria wapi ambapo mtu kama Chongo angeweza kujichimbia. Suala la kwamba angeweza kwenda hotelini alilitupia mbali. Akiwa na “mateka” ambaye ni msichana mzuri na maarufu kama Nuru kwenda hoteli yoyote ingekuwa sawa na kwenda Central Police. Lazima atakuwa amejificha katika majumba ya majambazi wengine, ambao ni haba sana Zanzibar. Kakakuona akiwa mtu ambaye alikuwa nje ya nchi kwa muda mrefu, hakumjua jambazi hata mmoja.
Baada ya kuwaza sana alimkumbuka Alhaji Banduka. Akakumbuka kuwa aliwahi kusikia maongezi juu ya mzee huyo ambaye aliamua kubadili maisha yake kabisa na kuondokea kuwa mmoja kati ya matajiri wakubwa mjini hapo. Aliyeogelea hafi maji. Aliwaza. Banduka atamsaidia walao kwa kumwelekeza wapi aanzie kumtafuta Chongo. Alikuwa hafahamu Banduka anakaa upande gani wa kisiwa hicho.
Lakini hilo halikumsumbua. Alikuwa na hakika kuwa kama angeuliza mtu yeyote angeweza kumsaidia.
Akiwa na wazo hilo kichwani, aliuacha mgahawa huo na kujichomeka ndani zaidi ya Mji Mkongwe. Ikamshangaza zaidi kuona hoteli za kitalii zilizokuwa zikifunguliwa katika majumba hayo makuukuu. Alichagua hoteli moja ndogondogo ambamo alijipatia chumba na kulipia. Alichofanya chumbani humo ilikuwa kuyabadili mavazi yake ili aweze kuwachanganya polisi walau kidogo.
Macho yake akayafunika kwa miwani myeusi na kuweka kofia kichwani. Kisha, akazikagua silaha zake. Akatoa bastola yake ndogo na kuifutika katika mfuko wa suruali. Dakika kumi baadaye alikuwa tena mitaani, briefcase mkononi, akiuliza iliko nyumba ya Banduka.
Baada ya kuwauliza watu wawili watatu, mtoto mdogo aliamua kumpeleka. Walipenya vitongoji hivyo vya kihistoria hadi walipotokea mbele ya hoteli ya kitalii iitwayo Africa House. Kutoka hapo mtoto huyo alimwelekeza uchochoro unaoteremka ufukoni ambao ungemfikisha mbele ya nyumba aliyoihitaji, ambayo aliiona meta mia tatu toka hapo walipokuwa. Kakakuona alimshukuru kijana huyo na kuondoka.
Akiwa mbele ya nyumba hiyo alisikia sauti za minong’ono. Lakini mara tu alipogonga mlango alishangaa kusikia akijibiwa kwa ukimya wa ghafla. Akagonga tena. Kimya. Alipogonga kwa mara ya tatu alisikia sauti ya kiume ikiitika toka katika chumba kimojawapo, “Nani?”
“Mimi.”
“Wewe nani?”
Kakakuona alipochelewa kujibu alisikia hatua za mtu zikiujia mlango. Ukafunguliwa kidogo na uso wa mwanamume wa makamo kuchungulia nje.
“Nikusaidie nini?” aliulizwa.
Kakakuona hakuwahi kuhusiana sana na Banduka enzi za ujambazi. Hivyo, alikuwa hamfahamu, japo aliwahi kumwona mara mbili, tatu katika vikao vya matumizi na kuonyeshwa kwa mbali kuwa “Yule ni wetu kabisa.”
Sura hiyo haikumkaa sana akilini. Lakini hakuhitaji kutambulishwa kufahamu huyu hapa mwenyeji wake. Hata hivyo, alisita baada ya kumwona mwenyeji huyu akiwa katika hali ambayo hakuitarajia. Macho yake yalijaa wasiwasi, uso wake uliloa jasho, sauti yake ilikuwa ya mashakamashaka na kwa mbali alikuwa akitetemeka. Macho makali ya Kakakuona yaliona kitu kingine zaidi katika mkono wa Banduka, damu.
Damu mbichi! Ikilowesha kiwiko cha mkono huo na kusahaulika katika juhudi za kufutwa.
“Unataka nini?” Banduka aliuliza tena akitaka kufunga mlango.
“Nina shughuli ndani.”
“Naomba unikaribishe ndani. Mimi mgeni wako,” alisema akiuzuia mlango huo kwa mguu
“Mimi sikufahamu”
“Mimi nakufahamu. Kwani wewe si Banduka?”
Banduka alionekana kaduwaa. “Pamoja na hayo” akamwambia,
“Sina nafasi ya kupokea mgeni yeyote leo. Labda uje jioni naweza kukusikiliza.”
Kakakuona aliusukuma mlango huo na kuingia ndani. Kitendo ambacho kilimfanya Banduka apepesuke na kutaka kuanguka. Wakati anajiweka vizuri Kakakuona alikuwa akiufunga mlango kwa utulivu kabisa nyuma yake. “Kuna nini humu ndani?” alimuuliza Banduka ambaye alitokwa na macho ya hasira na mshangao.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kakakuona aliyatupa macho yake huko na huko ukumbini hapo na kuona dalili nyingi za mshughuliko usio wa kawaida. Kochi moja lilikuwa limevutwa upande, kiatu kimoja cha kiume kilikuwa juu ya kochi hilo na glasi iliyovunjika ilikuwa haijazolewa toka juu ya meza ilipovunjikia. Akapiga hatua mbili tatu kukiendea chumba ambacho aliona macho ya mwenyeji wake yakielekezwa mara kwa mara. Banduka alimfuata na kujaribu kumzuia, lakini alisukumwa kando na kupepesuka kama kishada, jambo ambalo lilimfanya apandwe na hasira na kuingiza mkono wake katika mfuko wa suruali ambamo aliificha bastola yake yenye kiwambo cha kupotezea sauti ili amwadhibu mgeni huyu “mkaidi”. Lakini hakujua kiasi gani ameondokea kuwa mzito. Hata kabla mkono huo haujatoka mfukoni alijikuta tayari yumo ndani ya kabali ngumu ya Kakakuona huku mkono huo ukinyongwa hadi bastola ilipopokonywa. Aligugumia kwa maumivu na kutapatapa, nusura pumzi imwishie kama asingeachiwa na kuanguka chini kama mzigo.
“Tatizo lako wewe huelewi kama u steki tupu,” alimsikia mgeni huyo akimwambia. “Huna uwezalo kufanya. Unaiona bastola yangu hii? Dude la uhakika. Sio hili toi lako unalochezea. Kwa hii naweza kufumua bichwa lako kwa urahisi kama kuvunja yai. Upo?”
Banduka, kinywa wazi, akitetemeka, hakuwa na la kujibu zaidi ya kutokwa na jicho la hofu; macho kayakodoa kuitazama bastola hiyo ambayo ilimlenga paji la uso.
“Nadhani unanielewa,” Kakakuona alimwambia. “Sasa niambie kuna nini nyumba hii.”
Alipochelewa kujibu Kakakuona alimwinua na kumshurutisha kutangulia katika chumba hicho alichokuwa akikiendea.
Banduka alifungua mlango na kusita mlangoni. Macho ya Kakakuona yalimpita hadi chumbani humo. Kinyume na matarajio yake alikiona chumba kikiwa kitupu ingawa kulikuwa na dalili zote za vurumai. Alimtazama Banduka kwa namna ya kudai maelezo. Macho yake yalimsaliti tena. Yalikuwa yakilitazama kabati kubwa la ukutani kiwiziwizi kwa namna ya wasiwasi. Kakakuona aliliendea kabati hilo na kulifungua.
Kama asingekuwa mzoefu wa masuala hayo angeweza kushtuka sana kwa kukabiliana ghafla na maiti ambayo ilisimama ndani ya kabati hilo, damu ikiendelea kumvuja toka katika jeraha la risasi ya kifo. Jicho pekee la marehemu huyo lilikuwa wazi, kama linalomtazama Kakakuona kwa namna ya kuomba radhi.
Kakakuona alimgeukia Banduka na kumwona jinsi alivyokuwa akitetemeka mwili mzima kama mgonjwa wa homa. Kwa kumtoa wasiwasi Kakakuona alimwambia, “Kama ni wewe uliyemuua mtu huyu umekuwa rafiki yangu. Kwa kweli nilikuja hapa kwa kazi moja tu ya kumtia risasi ya kifua. Umenitangulia.”
Kiasi Banduka alipata ahueni.
“Ni wewe uliyemuua?” Kakakuona aliuliza ghafla.
Huku akikerwa na mgeni huyo alivyotamka neno “kuua” kwa urahisi kama “kula” au “kunywa Banduka alitikisa kichwa kukubali.
“Alifuatana na mwanamke?”
“Ndiyo…”
“Mwanamke huyo ni mpenzi wangu. Mshenzi huyu alifanya kumtorosha tu. Ningemuua kwa tabu kuliko ulivyomuua wewe.”
Alisita kidogo akiitazama maiti ya Chongo ndani ya kabati hilo na kumrudia Banduka. “Ebu nieleze kila kitu. Toka mwanzo hadi mwisho,” aliamuru. “Nadhani ukiketi tutazungumza kwa urahisi zaidi.”
Banduka alijibweteka juu ya kochi. Kwa suti hafifu, alimweleza jinsi alivyoingiliwa na marehemu huyo alfajiri hiyo akiwa amefuatana na “mateka” ambaye ni mwanamke mzuri. Ili kuifanya habari yake ikubalike zaidi Banduka alilaghai kwa kueleza kuwa marehemu alitishia maisha yake kwa kumwelekezea bastola na kudai pesa.
“Kama si mwanamke huyo kupiga teke bastola hiyo na mie kuidaka sasa hivi tungekuwa marehemu badala yake. Sikukusudia kumuua.” Banduka aliongeza. “Ilikuwa katika kumtishia kwani alikuwa akiendelea kunifuata, ndipo nilipolenga na kusikia ikifyatuka.”
“Usijali. Alistahili kufa,” Kakakuona alisema na kuuliza, “Yu wapi Nuru?”
“Nuru! Nuru yupi?”Banduka alishangaa.
“Yule msichana… mpenzi wangu. Yuko wapi sasa hivi?”
Banduka alielekeza mkono wake mlango wa bafu na kusema, “Anaoga, ili kuondoa uchovu. Yaelekea amepata shida nyingi sana…” Kisha, alisita na kujiuliza huyu mgeni ni nani na ana uhusianao gani na mkasa huu wa ajabu ambao hakujua umemfikisha wapi na kuishia wapi?” alimuuliza.
“Wewe ni nani?”
Kakakuona alitabasamu na kumwambia, “Usijali kunifahamu.” Na kisha, aliongeza “Nadhani ameoga kwa muda mrefu. Mgongee mwambie mpenzi wake anamsubiri hapa nje. Una hakika hana silaha?”
Banduka aliduwaa, “Silaha…mpenzi wako…”
“Usijali. Mgongee.”
***
‘Una hakika hana silaha?’ Hilo lilitosha kabisa kumdhihirisha Nuru kuwa kifo cha Chongo kwake kilikuwa sawa na kuruka jivu na kukanyaga moto. Hakuwa na shaka tena kuwa kijana huyu mtanashati, ambaye amekuwa akimsikiliza na kumchungulia katika tundu la ufunguo, hakuwa rafiki bali adui yake mkubwa; adui ambaye bila ya shaka yoyote ndiye aliyekuwa akimtumia Chongo na marehemu wenzake wote.
Hofu, ambayo ilimtinga saa mbili zilizopita alipokata tamaa kabisa ya kuendelea kuishi mara Chongo alipomlenga bastola tayari kabisa kuifyatua, ambayo ilianza kumtoka, ilimrudia tena. Akiwa hana la kufanya Nuru alikuwa akiisubiri risasi hiyo wakati jambo ambalo hakulitarajia lilipotokea.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Picha iliyokuwa katika ukuta mmoja wa chumba hicho iliteleza ghafla na kuanguka. Papohapo bastola ambayo ilikuwa na kiwambo cha kupotezea sauti ilichungulia na kufyatuka. Risasi mbili zilimpata Chongo kifuani na kumfanya aanguke chini ambapo alitapatapa kwa muda kabla ya kukata roho.
Nuru alipotazama ilipotokea risasi hiyo aliuona uso wa Banduka ukichungulia na sauti yake kumfikia ikisema, “Usiogope, nakuja.” Baada ya muda alisikia funguo zikichomekwa katika kitasa cha mlango. Harakaharaka, Nuru aliinama na kuiokota bastola ya Chongo akaifutika katika vazi lake la ndani. Banduka alipofungua mlango na kuingia chumbani humo huku akitetemeka alimkuta Nuru kaketi juu ya kochi akimtazama marehemu.
“Nimeua. Sikutegemea kuua…” aliropoka. Kisha, kana kwamba ndio kwanza anamwona Nuru alifoka, “Msichana, huu nani wewe?? Nilikuwa nikichungulia unavopigana. Sijaona mtu akipigana kama wewe.”
“Ni hadithi ndefu, isiyo na kichwa wala miguu,” Nuru alimwambia “Nadhani kwa wakati huu ningekushauri tuwapigie simu polisi ili waje wamwondoe huyo,” alisema akielekeza mguu wake kwa marehemu.
Polisi? La! La! La! Siwezi kuwashirikisha.”
“Lakini umeua katika kujihami. Amekuvamia na angeweza kuniua mimi na wewe pia… Mimi nitakuwa shahidi,” Nuru alijaribu kumwelimisha.
“Na wakati huo nitakuwa mahabusu wanangu wakifa njaa na biashara zangu kuharibika. Polisi hapana” Alisita kidogo akiwaza. Kisha akaongeza. “Labda nikuombe unisaidie tuufiche huu mzigo ndani ya kabati, wakati nafikiria la kufanya. Baada ya hapo unaweza kwenda zako.”
Waliifanya kazi hiyo kwa tabu kuliko Nuru alivyotarajia. Kuua ni jambo moja, kubeba maiti ni jambo lingine. Kwa Nuru ilikuwa kazi ya kutisha na ilimtia kichefuchefu. Alijikaza kisabuni na kustarehe pale tu ambapo maiti hiyo ilifungiwa kikamilifu ndani ya kabati hilo.
Baada ya kazi hiyo ndiyo kwanza Nuru alijitazama na kuona alivyokuwa mchakavu. Nguo hizo chafu pia zilikuwa zimetatuka ovyo hapa na pale. Kwa jumla, nguo zilimfanya awe nusu uchi. Alimtazama Banduka kwa aibu na kumwomba msaada wa kuazimwa nguo za mkewe ili aondoke akiwa katika hali nzuri kiasi.
Bila kusita Banduka alimletea gauni moja zuri, jozi ya viatu na khanga mbili. Nuru alimshukuru na kuingia bafuni ambako alivua na kuufariji mwili wake kwa maji baridi.
Ni wakati alipomaliza kuvaa aliposikia hodi na hatimaye, kuchunguliwa na mtu huyo ambaye alikuwa akizungumza kwa kujiamini; mtu ambaye alionekana hatari zaidi.
Afanye nini? Alijiuliza. Apige kelele? Hilo alilipuuza mara moja. Yeye si msichana wa kufanya hilo. Zaidi, udadisi ulikuwa umeipiku hofu katika moyo wake. Alijisikia hamu ya kufahamu ni kina nani wanaofanya mambo haya yasiyoeleweka na kiini chake. Kujificha bafuni kusingemsaidia. Aliipapasa tena bastola yake na kuhakikisha kuwa imefichika vilivyo. Kisha, alijitazama katika kioo na kurekebisha nywele zake. Baada ya hapo alifungua mlango wa bafu na kutoka taratibu.
Picha za Nuru ambazo Kakakuona alikuwa nazo zilimdhihirishia kuwa binti huyo ni “kipande kizuri cha kazi ya sanaa ambayo mungu aliifanya kikamilifu.” Hayo aliwahi kuyasema kimoyomoyo. Hata hivyo, hakujua kuwa msichana huyu alikuwa mzuri kiasi hiki. Alimwangalia kwa mshangao tangu alipoufungua mlango na kutoka taratibu kana kwamba anafanya majaribio ya kupigwa picha za sinema. Alimtumbulia macho pia wakati alipowasogelea na kuwasalimu kwa sauti dhaifu, ambayo Kakakuona aliiona tamu. Kisha, alijikusanya na kuukumbuka wajibu wake.
“Pole sana, darling,” alimwambia.
Nuru alimtumbulia macho yake mazuri, huku akiliweka vizuri gauni lake la kuazima, ambalo alihisi linampwaya japo lilimkaa kana kwamba mshonaji alimfikiria yeye.
“Pole kwa misukosuko yote iliyokukumba. Maadamu nimefika hakuna lingine litakalotokea,” aliendelea.
Nuru hakumjibu. Hakuwa na la kumjibu, jambo ambalo lilimfanya Kakakuona ahisi kuwa anamwogopa Banduka. Hivyo, alimwomba akatayarishe chakula ili azungumze faragha na mpenzi wake.
Walipobaki peke yao, Nuru alimuuliza, “Wewe ni mmoja wao?”
“Ndiyo na hapana.”
“Una maana gani?”
“Nina maana hiyohiyo. Ndiyo, mimi ni mmojawao na hapana; mimi si mmojawao.”
Alipoona Nuru hajamwelewa aliongeza baada ya kutoa tabasamu pana, “Maana yangu ni kwamba, mimi ndiye niliyewatuma wakulete. Amri ya kufa au kuishi kwako iko mikononi mwangu. Niliwalipa vizuri sana ili wafanye kazi ndogo sana ya kukuchukua na kukuleta kwangu. Kwa bahati mbaya wamekuwa kundi kubwa la wapumbavu watupu. Wote sasa ni marehemu. Mmoja anaoza humo ndani ya kabati. Sio?”
Nuru hakumjibu.
“Wamekufa wote. Wanaume wanne. Wewe huko hai. Umetulia huna wasiwasi wowote. Ndio kwanza unatoka zako kuoga. Sivyo?”
Nuru alipochelewa kujibu Kakakuona aliongeza, “Sijui una kitu gani. Sielewi umetumia hila gani kuwaangamiza watu wote wale. Ila ninachokuarifu ni kitu kimoja. Naitwa Kakakuona. Mimi na kifo hatutofautiani sana. Nikisema kufa, lazima utakufa. Upo?”
Nuru aliamua kutomjibu.
“Napenda uelewe hivyo. Wala usidhani kuwa najipendekeza kwako. Ngoja nikuonyeshe.”
Aliinama na kuichukua briefcase yake. Akaifungua na kuipekua hadi mkono ulipotoka ukiwa umeshikilia picha ya yule msichana aliyeharibiwa uso.
“Unaona?” alisema akimkabidhi Nuru. “Unaona? Hiyo ni kazi yangu.”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ilikuwa haitazamika mara mbili. Nuru alimrudishia upesiupesi huku akijisikia kutapika.
“Hiyo ni kazi yangu,” Kakakuona alirudia akicheka. “Nafurahi kuwa umeipenda picha hiyo. Unaonaje hapo utakapojikuta na sura kama hiyo? Utafika mbele ya yule hawara yako, Joram Kiango? Si atakufa kwa uchungu?”
Kutajwa kwa jina la Joram kuliisisimua damu ya Nuru. Alijikuta akirudiwa na maswali ambayo yamekuwa yakimsumbua sana juu ya usalama wake. Alitamani amuulize mtu huyo kama wamemkamata au la. Kwa jumla, alikuwa na maswali mengi ya kumuuliza. Lakini aliamua kutumia silaha ya ukimya na utulivu ili kupambana na mtu huyo ambaye alikuwa akijaribu kupandikiza hofu katika moyo wake, mchezo ambao Nuru hakuwa mgeni nao.
“Nasikia Joram ni shujaa na ana roho ngumu. Nasikia hakutokwa hata na chozi moja baba yake alipofariki. Hivyo, bila shaka hatashtushwa na kifo chako. Lakini atakapokuona uko hai, ukiwa na sura kama hii, hatalia kweli?”
Kana kwamba anajijibu mwenyewe aliongeza harakaharaka, “ Lakini haitatokea, labda kama utakuwa mbishi. Jitahidi akija mwenyeji wetu tuwe kama mtu na mpenzi wake. Baada ya kula tutaondoka zetu kwenda Dar es Salaam, mkono kwa mkono hadikwenye chombo. Tutakaa mkono kwa mkono hadi tuendako. Ukijitia kujua umeumia. Iwe mbele ya watu, iwe mimi na wewe, upo?”
Penye wengi hapakosi mengi. Katika mkusanyiko wa wasafiri waliokuwa wakiisubiri Sea Express bandarini Dar es Salaam, ili iwapeleke Zanzibar kulikuwa na pilikapilika nyingi ambazo hazikuwa na msingi wowote. Kwa mfano, pamoja na ukweli kwamba kila msafiri alikuwa na tiketi yake mkononi, yenye namba ya kiti chake, bado kuna wale waliojifanya kuwa wana haraka zaidi ya wengine. Hawa walikuwa wakikimbia huku na huko, mizigo mikononi, na kisha hukaa katika ukingo wa kivuko tayari kuivamia meli hiyo ambayo ndio kwanza ilikuwa inatia nanga.
Milango ilipofunguliwa na abiria watokao Zanzibar kuanza kushuka taratibu abiria hawa “wenye haraka” walikuwa kikwazo kwa jinsi walivyosababisha msongamano mkubwa mlangoni hapo. Watumishi wa Bandari walifanya kazi ya ziada kuwadhibiti abiria hao ili wenzao washuke kwa utaratibu.
Kati ya abiria hao wenye haraka alikuwamo Joram Kiango. Pengine yeye alikuwa na haraka zaidi ya watu wote katika msafara huo. Lakini, kama kawaida yake haraka au shauku yake ya safari hiyo ilikuwa siri yake binafsi. Usoni alionekana mtulivu, ambaye isingekuwa rahisi kufahamu kama anasafiri, amekuja kupokea mgeni, au anasindikiza.
Aliketi juu ya kiti cha mbao, ambacho wasafiri wengi walikiacha na kusimama wima na mizigo yao. Akiwa katika mavazi yake yaliyomfanya awe mtu asiyetazamika sana, yaani kanzu ya kawaida, kijikoti juu ya kanzu hiyo, kilemba kichwani na ndevu za bandia huku kijimfuko kidogo kikiwa miguuni pake, hakuna aliyejisumbua naye.
Lakini yeye alikuwa akijisumbua na kila mtu. Macho yake yenye uzoefu yalimpitia karibu kila mtu katika umati huo. Watu wawili katika umati huo walimsumbua. Ingawa walikuwa wageni kwake, lakini macho yao na tazama yao ilimfanya Joram aone kuwa si wasafiri wa kawaida. Neno “kachero” lilikuwa wazi katika tazama yao, zungumza yao na simama yao.
Joram alihisi kuwa hawa pia wako safarini kwenda Zanzibar kumfuatilia Kakakuona, jambo ambalo halikumpendeza kwani alitamani sana ngoma hiyo aicheze peke yake. Hata hivyo, alitulia kimya, akiendelea kutazama kwa makini zaidi, aone nani mwingine yumo katika msafara huo.
Kwa uzoefu wake wa upelelezi hiyo haikuwa kazi kubwa kwake. Alifuatilia tazama ya makachero hao wawili. Kila walipoelekeza macho yao kwa hila, yeye pia aliyaelekeza huko kwa mbinu, akichunguza ishara zote.
Haukupita muda mrefu kabla Joram hajakipata hicho alichokusudia. Macho ya makachero hao yalikosea kulitazama gari moja, aina ya Toyota Land Cruiser, lililokuwa limepaki nje kidogo yabandari, ndani yake mkiwa na watu watatu. Joram Kiango alimtambua mmoja kati yao mara moja. Alikuwa Inspekta Kombora.
‘Kombora pia anakwenda Zanzibar!’ Joram alijiuliza kwa mshangao. Ndio kwanza akahisi kuwa Kakakuona ni mtu hatari sana. Awali ya hapo alimchukulia kama mtu kichaa tu, ambaye anaua watu wanyonge na kumteka mtu asiye na hatia, kama Nuru, kwa sababu zake anazozijua yeye mwenyewe, ambazo Joram Kiango hakuona kama angepata muda wa kuzifahamu kwani alichokusudia, mara tu baada ya kukutana na kichaa huyo ana kwa ana, ilikuwa kumuua kwanza, kumuuliza maswali baadaye.
Akaamua kumpuuza Kombora na makachero wake wote na kuendelea kuwasubiri abiria waliokuwa wakiendelea kushuka kutoka katika chombo hicho waishe ili awe miongoni mwa watu wa kwanza kuingia.
Kama kawaida ya abiria wa meli, ile haraka yao ya kupanda waanzapo safari, haitofautiani sana na ile ya kushuka wanapofika mwisho wa safari. Hivyo, pilikapilika zilikuwa nyingi. Joram alitulia akiwatazama abiria hao, hali fikra zake zikiwa nje kabisa ya eneo hilo. Hakuwatilia maanani watu mbalimbali waliopita mbele yake, mizigo yao mikononi.
Lakini haukupita muda kabla hajashuka abiria mmoja aliyemfanya agutuke ghafla kama aliyenaswa na waya wa umeme. Kama si mzoefu katika masuala ya upelelezi angeweza kuinuka na kumkimbilia abiria huyo. Angeweza kumkumbatia na kumbusu. Lakini si yeye. Pamoja na kushtuka kwake, pamoja na kutoyaamini macho yake, alitulia kwa utulivu kana kwamba abiria huyo ni miongoni mwa abiria wa kawaida machoni mwake; kana kwamba hamfahamu na wala hajapata kumwona maishani mwake.
Abiria huyo alikuwa msichana mzuri kupita kiasi, mwenye umbo zuri kupindukia, alilolificha katika baibui alilojitanda juu ya mavazi yake. Mkono mmoja wa abiria huyo ulikuwa umeshika briefcase ya kiume hali mkono wa pili umeshikana na ule wa kijana mmoja ambaye alionekana kama mpenzi wake. Mkono wa pili wa kijana huyo wa kiume ulikuwa ndani ya mfuko wake wa koti.
Abiria huyo wa kike hakuwa mwingine zaidi ya Nuru.
Wala Joram hakuhitaji kuambiwa kwamba mtu huyo aliyeandamana naye alikuwa mtu baki zaidi ya Kakakuona.
Kwa mtazamo wa kawaida, mtu yeyote angepata hisia kuwa abiria hao walikuwa wapenzi wawili ambao ndio kwanza wameoana, hivyo, wanatoka zao Zanzibar kusheherekea ndoa yao. Lakini kwa mtazamo wa mtu kama Joram alifahamu fika kuwa uhusiano wa kimapenzi baina ya viumbe hao wawili ulikuwa sawa na ule wa kondoo na mbwa mwitu. Joram aliona wazi kuwa Nuru alikuwa ametekwa nyara na mtu huyo. Aliona wazi vilevile kuwa mkono wa mtu huyo uliofutikwa mfukoni ulikuwa umeshikilia bastola iliyomlenga Nuru kikamilifu na asingesita kuifyatua iwapo lolote lingetokea.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Adui huyo alikuwa akitembea kwa mwendo wa kujiamini kwa kiwango kilichomshangaza Joram. Hakutarajia muuaji mwoga, kiasi cha kuua watoto wa kike wasio na hatia, angeweza kuwa na moyo sugu kiasi hicho.
Macho ya Joram yaligongana na ya Nuru. Mavazi bandia aliyoyavaa hayakuwa kipingamizi cha kumfanya Nuru asimtambue mara moja. Joram alihisi kitu kama faraja ikichepuka ghafla katika macho yake mazuri.
Hata hivyo, akili yake ilikuwa nzuri vilevile kwa kiwango ambacho kilimfanya Joram Kiango azidi kumheshimu. Zaidi ya kumtupia jicho hilo moja la kawaida kama ilivyokuwa kwa watu wengine, Nuru aliendelea na safari yake kama kawaida.
Pamoja na uduni wa mavazi yake, Joram alikuwa kamili kikazi. Isingemchukua sekunde moja kuifikia bastola yake na kuufumua ubongo wa Kakakuona. Hali kadhalika, maungo yake yalikuwa yakichemka kwa hamu ya kumfanyia mazoezi ya judo mpuuzi huyo.
Hata hivyo, kwa kuchelea kuyanadi maisha ya Nuru, hasa baada ya kukumbwa na misukosuko yote ile isiyokadirika, Joram aliamua kuacha mchezo huo uendelee kidogo.
Jambo lingine lililomfanya Joram aahirishe kumchukulia hatua muuaji huyo ni ile heshima au hadhi mpya ambayo alijikuta akimpatia muuaji huyo kutokana na kitendo chake hicho cha aina yake. Halikuwa jambo la kawaida muuaji ambaye anafahamu fika kuwa anawindwa zaidi ya kifaru mwenye kichaa, kujitokeza hadharani, mchana kweupe, akiwa na mateka ambaye ni mwanamke hatari zaidi ya nyoka aina ya swila. Hivyo, Joram alijikuta akiamua kujionea kitu kinachomtia ujeuri huo.
Kisha, akamkumbuka Kombora na makachero wake. Ndio kwanza akafahamu kuwa hawakuwa safarini, bali walikuja kwa ajili ya kumlaki mwuaji huyo kwa matumaini ya kumkamata.
Akageuka kuwatazama makachero hao. ‘Polisi ni polisi, avae magwanda asivae,’ Joram aliwaza alipoona hali ya makachero hao. Japo walijitahidi kujikaza, kana kwamba hakuna kinachoendelea, lakini hakushindwa kusoma ramani ya misukosuko katika nyuso zao.
Kila mara mikono yao ilichopoka na kupelekwa mifukoni, kuzipapasa bastola zao; miguu yao ikichezacheza kwa namna ya ukosefu wa utulivu mioyoni mwao. Mara kwa mara waliyatupa macho yao katika gari alilokuwemo Kombora kwa namna ya watu wanaosubiri amri ili wafanye jambo, amri ambayo Joram hakuona kama Kombora alikuwa tayari kuitoa kwa jinsi alivyopigwa butwaa ingawa alijifanya mtulivu; akivuta sigara yake, gazeti mkono wa pili.
Wakati huo Kakakuona na Nuru walikuwa wakimaliza ngazi na kuanza kutoka nje ya banda. Kakakuona aligeuka kumtazama mmoja kati ya makachero wa Kombora kwa namna ya kumwambia, “Nimekutambua.”
Joram alihisi kuona tabasamu la kebehi katika macho hayo.
***
Kama kuna siku ambayo Inspekta Kombora aliwahi kuhisi akili yake imeduwaa, huku fikra zake zikiwa zimedumaa, ni hii. Mwili mzima ulimlegea, mikono ikamtetemeka kwa kitu ambacho asingeweza kukipambanua kati ya hasira na aibu. Sigara ambayo aliiwasha kitambo iliendelea kuteketea mdomoni mwake.
“Mzee… anakwenda zake… Tufanye nini mzee?” mmoja kati ya wasaidizi wake, aliyekuwa kiti cha nyuma cha gari hilo alimuuliza Kombora akigeuka kumtazama, ingawa macho yake yalidhihirisha kuwa alikuwa hamwoni.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Akili yake bado ilikuwa imepaa au kuzama katika lindi refu la mshangao na kutoyaamini macho yake.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment