Simulizi : Roho Ya Paka
Sehemu Ya Tatu (3)
Zaidi ya saa moja iliyopita alipokea habari toka Zanzibar kuwa Kakakuona ambaye alitoweka ghafla, aliibuka toka katika mitaa ya mji huo akiwa amefuatana na msichana ambaye alionekana kama Nuru. Kombora aliwakumbusha waendelee kumchunguza bila kumshtua. Lakini dakika tano baadaye, alipoambiwa kuwa Kakakuona alikuwa akija Dar es Salaam kwa Sea Express na kwamba Nuru alionekana kama ambaye yuko chini ya ulinzi, aliongoza kikosi cha vijana wake wazuri, sita, ambao walikuwa tayari; wakisubiri amri yake.
Kombora alisita kuitoa amri baada ya kuona kile ambacho hakutarajia kukiona katika macho ya Kakakuona. Kitu kisichoelezeka kwa jinsi kilivyofungwa pamoja katika fungati la ukatili, dharau, unyama na dhihaka ya hali ya juu.
Kombora alishangaa alipoona kuwa Kakakuona alijua fika kuwa amezingirwa na makachero wengi, ambao walikuwa tayari kumuua mara tu wapewapo ishara, lakini bado alipita kwa kujiamini. Dharau yote hiyo ya Kakakuona ilitokana na ukweli kuwa asingekufa kabla hajamuua Nuru, jambo ambalo alifahamu kuwa yeyote duniani asingelifanya kwa urahisi.
Kwa ajili ya unyama wa mtu huyo, kwa jinsi ambavyo alikuwa anaendelea kuteketeza maisha ya watu wasio na hatia, Kombora angekuwa tayari kutoa amri avamiwe na kuuawa bila kujali ambacho kingemtokea msichana huyo.
Ndiyo, angefanya hivyo, iwapo tu msichana huyo asingekuwa Nuru.
Nuru ni mmoja kati ya wasichana wachache wenye nafasi ya pekee katika moyo Kombora. Ingawa hakupata kumwambia hivyo waziwazi, lakini aliheshimu sana mchango wake katika harakati za yule mpenzi wake Joram Kiango.
Kombora asingeweza kusahau jinsi msichana huyo alivyobadilika kutoka katika umbile laini la kike na kuwa jabali la chuma tangu aliposhirikishwa katika ule mpango wa kinyama wa kuwaua viongozi wa nchi huru za Kiafrika mjini Arusha, mkasa ambao tayari umehifadhiwa katika kitabu kinachoitwa Salamu Toka Kuzimu ambao kwa jinsi unavyotisha hata baadhi ya watu wanauchukulia kama riwaya ya kubuni.
Baada ya hapo ndipo Nuru alipoamua kuudhihirisha uanamapinduzi wake katika visa na mikasa kadha wa kadha ambavyo pia vimetolewa vitabu vinavyoitwa Tutarudi na roho zetu? Malaika wa Shetani na vinginevyo.
Kazi ya Nuru katika mikasa hiyo ilikuwa kubwa kiasi kwamba bila ya yeye pengine Joram Kiango asingekuwapo duniani leo hii.
Kombora hakuona kama inayumkinika kutoa amri msichana kama huyo afe kwa ajili ya kumwogopa Kakakuona na unyama wake. Akaendelea kuduwaa.
“Mzee… wanaondoka,” msaidizi wake aliendelea kumkumbushia.
Wakati huo Kakakuona alikuwa akimaliza kuingia katika gari la kukodi, aina ya Datsun, baada ya kumtanguliza Nuru kukaa na dereva mbele, yeye, nyuma. Dereva akiwa haelewi lolote alitia gari moto na kuondoka taratibu.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wakati gari hilo likiondoka, kijikaratasi cheupe kilidondoka toka dirisha la nyuma. Mmoja kati ya makachero wa Kombora alikiokota. Baada ya kusoma alikileta kwa Kombora huku akiwa na dalili za mshtuko mkubwa. Alimkuta Kombora akiongea katika Redio call kuwaarifu watu wake waliokuwa nje ya eneo hilo walifuate gari hilo kwa hila. Aliwapa namba za gari na rangi yake.
Kisha, aliitupa sigara yake ambayo ilikuwa imekwisha na kujiwashia nyingine.
“Ni nini?” alimuuliza askari huyo huku akipokea kipande cha karatasi.
“Ujumbe.”
“Ujumbe gani?”
Ulikuwa ujumbe mfupi ambao uliandikwa kwa peni ya wino mweusi;
Fanyeni upumbavu wa aina yoyote ile mtashangaa kuiokota maiti ya msichana huyu barabarani ikiwa na sura ya wale waliotangulia. Na sipendi kufuatwafuatwa.
Kakakuona.
Kombora aliisoma kwa mara ya pili. Kisha, akaitumbukiza katika mfuko wa koti, hasira zikichemka kichwani mwake, kutokana na dhihaka hiyo ya Kakakuona. Kombora alijikuta akizungumza peke yake kwa minong’ono, “It’s too much. Kama anajua anafuatwa ya nini kuendelea kujificha?”
Kwa sauti alikoroma, “Ok, twendeni.”
“Wapi?”
“Mfuateni,” aliamuru. “Usijali kama atafahamu kuwa anafuatwa au la,” alimwambia dereva. “Anaonekana kama anayetaka tumfuate.”
Magari mengine matatu ya polisi, yenye namba za kiraia, ambayo yaliegeshwa katika eneo hilo yalianza kuondoka moja baada ya jingine, kwa maelekezo ya Kombora kupitia Walkie talkie yake magari mawili kati ya hayo yalilipita gari la Kakakuona, ambalo lilikuwa likienda kwa mwendo wa wastani, na kulitangulia. Mbele ya safari gari moja lilichepuka kama vile halina habari na msafara huo, la pili likiendelea taratibu.
Gari la Kakakuona liliifuata Barabara ya Sokoine na lilipoifikia Barabara ya Morogoro likaifuata, jambo ambalo lilifanya gari la makachero wa Kombora lililotangulia lipitilize hadi katika mzunguko wa Mnara wa Saa ambapo lilipinda na kuingia samora hadi walipopishana na Kombora, ambaye aliwaashiria kurudi ofisini kazi yao ilichukuliwa na teksi moja yenye namba za TX ambayo ilionekana kama imechukua abiria watatu.
Kichwa cha Kombora kiliendelea kusumbuliwa na hali ya kucheza na mtu kama Kakakuona. Alijihisi kuwa yeye na askari wake wote wako katika duru wakicheza ngoma wasiyoifahamu, ngoma ambayo mpigaji hakuwa mwingine zaidi ya Kakakuona mwenyewe. Jambo hilo lilizidisha hisia za hatari kichwani mwa Kombora.
Ingekuwa rahisi sana. Kati ya magari yake yaliyotangulia, moja lingeweza kusababisha ajali ya ghafla kwa lile lililomchukua Kakakuona, papohapo, yeye na askari wake kuivamia ili kumuua Kakakuona na kujaribu kumwokoa Nuru. Ni moja kati ya mambo ambayo yamekwishafanywa sana. Hata hivyo, ilikuwa kama kamari ambayo Kombora hakuwa tayari kuicheza. Hivyo, ikabidi aendelee kustahimili, akiruhusu magari yake yaendelee kumsindikiza Kakakuona kama shujaa anayepelekwa Ikulu kuchukua wadhifa wa nchi.
***
Kwa Joram Kiango ilikuwa kazi rahisi kuliko alivyotarajia. Mara tu alipomwona Inspekta Kombora akishindwa kuchukua hatua dhidi ya Kakakuona, badala yake akianzisha msafara wa kumfuata, yeye pia alifanya hima kuliendea mojawapo ya magari mengi yaliyokuwa yakisubiri abiria nje ya stesheni.
Alichagua gari jipya, aina ya Suzuki, lenye namba za Posta, ambalo ingawa dereva alidai kuwa yuko kazini, lakini Joram hakuchelewa kugundua kuwa alikuwa akisubiri abiria yeyote ambaye angemkodi ili ampatie chochote cha kutia mfukoni.
“Una petroli ya kutosha?” alimuuliza.
“Kwani unakwenda mbali mzee?”
“Itategemea,” Joram alijibu akizunguka upande wa pili ambako alifungua mlango na kuingia ndani. “Ifuate ile. Ifuate taratibu wasijue kuwa wanafuatwa.”
Dereva huyo alionyesha wasiwasi kidogo. “Gari ile, mzee! Kwa nini tuifuate? Unajua…” alisita kidogo. Lakini alipoona kitita cha shilingi elfu tano kikiwekwa juu ya mapaja yake alionekana kubadilika kidogo.
“Wakienda mbali zaidi nitakuongeza,” Joram alisisitiza, huku akimhimiza kuondoa gari.
“Tatizo ni kwamba ile gari naijua brother,” alisema akiondoka shingo upande. “Ile ni gari ya wenyewe ile. Inatumiwa na manjagu, pamoja na kuwa na namba za kiraia. Naogopa wasije wakaniletea matatizo wakijua kuwa wanafuatwa.”
“Usijali, hawatafahamu.”
Akili ya Kakakuona ikiwa juu ya magari ya Kombora ambayo alikwishayakariri namba zake vizuri sana kichwani, hakujishughulisha na gari dogo la Posta ambalo lilionekana kwa mbali sana miongoni mwa magari mengine.
Aidha, Kombora vilevile fikra na hisia zake zote zikiwa katika gari la mbele yake, ambalo lilimchukua muuaji hatari kama Kakakuona, hangeweza kulitazama gari hilo la Posta lililokuwa nyuma yao. Hali kadhalika, ikiwa tabia ya polisi ni kufuata badala ya kufuatwa, kusaka badala ya kusakwa, wazo la kugeuka nyuma mara kwa mara halikumjia akilini kabisa. Tabia hii ilifanya kazi ya Joram na dereva wake iwe nyepesi kama ilivyokuwa.
***
Ulikuwa ni msafara usio na kona nyingi wala mizunguko mingi. Ilielekea kama Kakakuona alikuwa hana haja ya barabara nyingine zaidi ya ile ya Morogoro, Hata hivyo, walipofika Mtaa wa Jamhuri, gari hilo lilionekana likipinda kulia kuufuata mtaa huo. Gari la Kombora likafanya hivyohivyo. Joram pia akamwamuru dereva wake kuwafuata.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Njia hiyo ilikuwa na msongamano mkubwa wa magari hivyo, safari yao ilikuwa ya taratibu, jambo ambalo lilimtia hofu Kombora kuwa Kakakuona angeweza kuitumia fursa hiyo kuchepuka ghafla mahala ambapo asingekuwa mwepesi wa kuona alipoelekea.
Lakini Kakakuona hakuonekana kama mwenye haraka ya kufanya hivyo. Aliendelea na safari yake taratibu kama ambaye alikuwa na nia njema sana ya kumwongoza Kombora na msafara wake hadi alipoufikia uchochoro ambao unachepuka na kuunga mtaa huo hadi Mtaa wa Kisutu ambapo alionekana akisogea kulia na kuliingiza gari katika ukumbi wa jengo moja jipya, ambalo liliacha eneo zuri la kupaki magari chini yake kwa meta kama kumi ndani yake.
Kombora alilitazama gari hilo likipaki kwa utulivu. Alitumia dakika mbili tatu za kuduwaa, akijiuliza afanye lipi, kwa makini. Jengo hilo lenye ghorofa nne lilikuwa moja kati ya majengo mapya yaliyokuwa yakiibuka huko na huko jijini Dar es Salaam.
Vibao vya kampuni na biashara mbalimbali vilionekena katika kuta mbalimbali za jengo hili chini ya kibao kilichoandikwa Sunrise Modern Club. Kibao hiki kilimeza karibu robo ya ghorofa zima ya chini. Maandishi yake yalikuwa juu ya kioo kikubwa, kwa rangi mbalimbali ambazo usiku ziliwaka kwa namna ya kuchezacheza katika hali ya kuvutia macho. Kombora aliwahi kupita hapa mara nyingi usiku na kuvutiwa, kama watu wengine, lakini hakuwahi kuingia ndani. Kumwona Kakakuona akipaki hapo aliyakumbuka mauaji ambayo amekuwa akiyafanya katika hoteli na kumbi za starehe kama yale ya Lang’ata; akajikuta akipatwa na hisia za hatari kuliko awali.
“Liwalo na liwe,’ aliwaza. “Tunamfuata hukohuko ndani,” aliamuru, “Angalieni. La msingi ni kuyaokoa maisha ya Nuru. Hivyo, risasi za kwanza, kama itabidi, ziwe za kumvunja mabega, ili asiweze kuitumia mikono yake. Aliye kulia, alenge mkono wa …”
Kombora alilazimika kuyakatisha maongezi yake alipomwona Kakakuona akishuka huku akifuatiwa na Nuru ambaye alikumbatiwa kiuno kama wapenzi wa damu.
Walishuka harakaharaka na kuingia ndani ya jengo hilo.
Kombora, akiwaongoza askari wake wawili, pia alishuka na kumfuata. Alipolifikia gari lililokuwa likitumiwa na Kakakuona nusura atokwe na ukelele wa mshtuko, mshangao na hasira, alipomtazama dereva.
Alikuwa amelalia usukani wake akitapatapa; tundu kubwa la risasi likiwa limekifumua kichwa chake kisogoni, na kuruhusu damu nzito iliyochanganyika na ubongo iendelee kumwagika kama uji mwekundu unaomwagika toka katika birika.
“Haraka… ndani,” Kombora alinguruma akiitoa bastola yake na kutangulia ndani ya jengo hilo. Mlango uliwaongoza katika korido nyembamba iliyowafikisha katika chumba cha mapokezi, ambacho kilikuwa na makochi manne makubwa yaliyokuwa matupu. Makochi hayo yalikielekea chumba cha kioo ambamo hamkuwa na mtu. Kombora alitazama huku na huko kama anayeomba msaada. Aliiona lifti, na upande wa pili aliiona ngazi iendayo juu.
“Mmoja atumie lifti, mwingine apande kwa ngazi. Upesi. Kama nilivyosema, mkimwona msizungumze naye. Acheni risasi zizungumze. Ok?”
Wakati yule aliyeamriwa kwenda kwa miguu alipoanza kupanda ngazi harakaharaka na yule wa lifi akiita kwa kubonyeza tufe, Kombora aliitoa walkie talkie yake na kuwaamuru makachero wengine kuja mara moja. Kisha, akasogea kaunta bila kujua alihitaji nini. Kama awali alijisikia kupiga kelele, safari hii akijisikia kuzimia kwa kile ambacho alikiona chini ya meza hiyo ya kaunta.
Mzoga wa mtu ulikuwa umelala kifudifudi katika dimbwi la damu nyingi ambayo ilikuwa ikiendelea kujaa sakafuni. Dalili yoyote ya uhai haikuwamo katika umbile hilo ambalo sare alizovaa msichana huyo zilionyesha kuwa alikuwa mhudumu wa mapokezi.
Akili ya Kombora ilidumaa kwa kitambo cha robo dakika. Watu wawili, wasio na hatia, kuuawa huku yeye anashuhudia…! Aliwaza kwa uchungu. Alishindwa kuendelea kuwaza. Badala yake alikurupuka mbio kuiendea ngazi ambayo aliipanda kwa kuruka ngazi tatu tatu, bastola ikiwa imemtangulia.
***
Kwa Nuru ilikuwa kama mtu anayeshuhudia mchezo wa sinema ya kusisimua ambao yeye mwenyewe ndiye mtazamaji, wakati huohuo mwigizaji. Naam, ilikuwa kama ndoto tu; tangu alipojikuta akihama kutoka katika mikono ya yule muuaji Chongo na kuangukia katika milki ya Kakakuona. Kama kondoo, aliafiki kila alichoelekezwa. Aliafiki kuushika mkono wa muuaji huyo huku akitabasamu.
Kadhalika, aliafiki kupita kote huku akijua kabisa kuwa kila hatua anayopiga na muuaji huyo inamsogeza karibu zaidi na mauti yake mwenyewe.
Hata hivyo, ile kiu yake ya kufahamu kwa undani zaidi kiini cha mauaji haya ilikuwa sababu nyingine iliyomfanya aendelee na ukondoo huo. Aidha, ile bastola yake, ambayo aliificha vyema alipokuwa akioga bafuni ilimpa moyo na kumpa matumaini ya kupata fursa nzuri ambayo ingemwezesha kuyaokoa maisha yake mara mambo yatakapovuka kina.
Matumaini hayo yaliongezeka maradufu mara aliposhuka bandarini na kumwona Joram Kiango akimsubiri, bila ya Kakakuona kumtambua. Nuru alizidi kupata moyo.
Ilikuwa mara yake ya kwanza kumtia Joram Kiango machoni. Ile hofu yake kuwa tayari wauaji hawa wamempata ikatokomea. Ingawa hawakuongea wala kupeana ishara yoyote, lakini bado kule kumwona akiwa hai na kuyaona macho yake yaking’ara kama ilivyo kawaida yake kulimwongezea ari na kumpa matumaini makubwa ya ushindi.
Hivyo, hakuwa na hofu kubwa sana pindi walipochukua gari na kuondoka huku domo la bastola ya Kakakuona, iliyofichwa mfukoni, likiendelea kumtekenya ubavuni. Wala hakubabaika Kakakuona alipouandika ule ujumbe wa kejeli kwa Kombora, ambao ulikusudiwa kumwongezea hofu.
Lakini, mara tu baada ya gari kusimama hapa na Kakakuona kufanya kile kitendo ambacho Nuru hakukitarajia, alijikuta akiingiwa na hofu kubwa iliyochanganyika na hasira.
Ndiyo, Nuru ameshuhudia mara nyingi watu wakiuawa. Kamwe hakuwa mgeni kwa hilo. Lakini kuuawa kwa kijana huyu wa Kipemba, asiye na hatia, ambaye aliwaendesha bila hofu wala hisia zozote za hatari, kuliufanya moyo wake ukose baadhi ya mapigo yake, hasa pale alipoona kijana wa watu akianguka ghafla juu ya usukani kama mbuzi.
KAKAKUONA alitenda kitendo hicho kwa wepesi wa ajabu. Sekunde ya kwanza alitulia akiupima mwendo wa gari la Kombora lililokuwa nyuma yao. Sekunde ya pili tayari alikuwa ameua na kuirejesha bastola yake mfukoni, huku akimwamuru Nuru kutoka nje ya gari haraka.
Mshangao, kutotarajia na wepesi huo wa ajabu ulimfanya Nuru aduwae kwa hofu; kama mtazamaji asiye na uwezo wa kufanya lolote. Jambo hilo lilimuumiza sana rohoni. Kama angejua kinachokaribia kutokea angemuua Kakakuona kwanza, yeye binafsi kufa baadaye, badala ya kushuhudia kijana huyo asiye na hatia akiuawa mbele yake, kwa ajili yake.
“Fanya mzaha, kifo kitakachofuata kitakuwa chako,” Kakakuona alimwonya wakati wakiingia ndani ya jengo hilo, akiwa mtulivu.
Tabasamu laini lilitanda usoni mwake kama mtu aliyeua mbu tu. Akiwa na tabasamu hilohilo, huku kashikilia kiuno cha Nuru, alimsogelea msichana wa mapokezi. Nuru alihisi nia yake huku tayari akiwa amechelewa sana kwa nusu sekunde nzima. Wakati huo risasi ilikuwa imekwishapenya katika paji la uso mzuri wa msichana huyo.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kwa wepesi uleule aliupenyeza mkono wake ndani ya vazi lake la ndani na kuishika bastola yake. Lakini hakuwahi kuitoa. Kitako cha bastola iliyomuua msichana huyo tayari kilikuwa kimepigwa upande mmoja wa kichwa chake na kumfanya arukwe na fahamu na kupepesuka. Aliongezwa kipigo cha pili ambacho kilimmaliza kabisa. Kama ndoto, alihisi akididimia katika shimo lenye kiza na kina kirefu kisicho na mwisho.
Wakati hayo yakimtokea Nuru, kikosi cha makachero wasiopungua kumi, wakiongozwa na Inspekta Kombora walikuwa tayari wamelivamia jengo hilo, wakichungulia kila uchochoro na kuchunguza kila chumba. Wenzi wao, vijana sita machachari, walikuwa nje ya jengo wakichungulia kila kona na kila uchochoro. Wote walikuwa makini, silaha zao mikononi, tayari kwa lolote.
Inspekta Kombora alikuwa makini zaidi ya wote. Akiwa na hasira ambayo iliimeza kabisa hofu ya kifo dhidi ya muuaji huyu, aliwaongoza askari katika kila chumba, akiamuru kupekuliwa kila kabati. Kila jokofu na kila sanduku; kuchungulia kila choo na kufunua kila kitanda na kadhalika.
Bastola yake ikiwa wazi mkononi, mikunjo ya hasira tele usoni, iliwafanya wapangaji wa jengo hilo kushindwa kumwuliza lolote. Badala yake waliduwaa, wakimtazama, kama ambavyo hawakuyaamini macho yao.
Baada ya dakika kumi za kuepuka hapa na pale, Kombora na kikosi chake kizima walijikuta wamerudi tena katika ukumbi wa disko wa Sunrise huku wakitazamana kwa namna ya kukata tamaa; kila mmoja akitokwa na jasho jingi lililotokana na mbio walizozipiga katika jengo hilo.
“Haiwezekani,” Kombora alinong’ona kama anayezungumza peke yake. “Nilimwona kwa macho yangu mwenyewe akiingia katika jengo hili. Na ameua watu wawili, wasio na hatia, mbele ya macho yangu katika jengo hilihili. Haiwezekani kuwa ametoweka.”
“Kwani kuna nini mzee?” aliyeuliza ni mzee wa makamo aliyekuwa nyuma ya kaunta, ambayo alimezwa na kila aina ya pombe ipatikanayo katika sayari hii, katika karne hii. Mzee huyu pamoja na wateja wake watatu, Mhindi na waswahili wawili, ambao alikuwa akiwahudumia, walishikwa na bumbuazi walipoliona kundi la watu wenye silaha, likiuvamia ukumbi huo na kuanza kuchungulia kila mahali huku nyuso zao zikionyesha wazi kuwa walikuwa tayari kwa lolote, tayari kuua, tayari kufa.
“Kuna nini?” mmoja wao aliuliza.
Alijibiwa kwa swali la harakaharaka, “Yuko wapi?”
“Nani?”
Kombora alihisi kama anayezungumza na ukuta. Alimwacha huyo na kujishughulisha kikamilifu katika msako huu wa aina yake, ambao hakumbuki lini amewahi kuufanya tena. Baada ya kukata tamaa ndipo aliporudi chumbani humu na kujumuika na askari wake. Alimtazama mhudumu huyo wa baa na kugundua kuwa alikuwa hajui lolote, wala hakumwona mtu yeyote akiingia au kutoka.
Hivyo alimpuuza na kuwatazama wasaidizi wake, akisubiri mawaidha yao. Alipowaona kimya alizungumza tena kwa sauti dhaifu, “Haiwezekani kuwa ametoweka, lazima yumo humu ndani. Chumba gani ambacho hatujakikagua?”
“Nadhani hakuna chumba tulichokiacha mzee,” mmojawao alimjibu. “Kama yumo katika jengo hili tungekuwa tumempata…” Alisitasita maneno yake aliposhuhudia macho maangavu ya Kombora yakimtazama kwa ukali.
“Yumo humu…” alifoka. “Yuko humuhumu. Lazima apatikane leo hiihii. Ikibidi kila tofali la jengo hili lifunuliwe hadi apatikane. Mnanielewa?”
Kimya kilichofuata, baada ya kauli hiyo nzito ya Kombora, kilifuatiwa na mshindo mkubwa wa ajabu ambao ulisikika ghafla na kumeza anga nzima. Ulikuwa mshindo wa aina yake ambao Kombora hakupata kamwe kuusikia maishani mwake, mshindo ambao ulilifanya jengo hilo zima litikisike kama ambalo lilikaribia kubomoka. Mshindo ambao ulidumu kwa nusu dakika tu, nusu iliyofuata, kila kitu kilikuwa shwari kana kwamba hakuna kilichotokea.
Kombora na vijana wake walitazamana kwa mshangao.
“Ni nini hicho?” mmojawao aliuliza kwa mshangao.
Wenzake wote walimtumbulia macho.
***
Joram alipoliona gari hilo likipaki katika mtaa huo wa Kisutu, alimshauri dereva wake kupitiliza kana kwamba hana shughuli nao. Alimwelekeza dereva huyo kufuata barabara ya umoja wa wanawake, upande wa pili wa mtaa huo, ambapo alishuka na kumruhusu dereva huyo kuondoka.
Kijana huyo hakuamini, shilingi elfu tano kwa kazi ndogo kiasi hicho! Alionekana kama aliyetaka kumwambia hivyo Joram. Lakini Joram hakuonekana kama yuko tayari kwa maongezi zaidi. Alikwishashuka garini na kuliacha hatua kadhaa huku macho yake yakitazama jengo refu lenye maandishi makubwa: Kangaroo Enterprises Ltd, ambalo alihisi lilielekeana na Sunrise Club ambapo Kakakuoa alishukia.
Nia ya Joram ilikuwa kutafuta upenyo au uwezekano ambao ungemwezesha kuifikia klabu ile kwa njia ya mkato badala ya kufuata njia aliyojia.
Uwezekano ulikuwa mdogo. Jengo hilo lenye ghorofa nne lilikuwa limeungana na majengo mengine kwa ukuta mkubwa wenye chupa zilizobandikwa juu. Magari ya watumishi, wateja wa ofisi hiyo walikuwa nje badala ya ndani ambako Joram angeweza kutumia hila kuingia.
Wakati Joram akiendelea kutafakari afanye nini, hakuyaamini macho yake alipomwona mtu aliyekuwa akitoka nje ya jengo akiwa ameshikilia briefcase mkononi. Ingawa macho yake alikuwa ameyafunika kwa miwani, Joramasingeshindwa kumtambua maramoja. Alikuwa Kakakuona. Alikuwa akitembea kwa mwendo wa harakaharaka kuliendea moja ya magari yaliyopaki hapo ambalo alilifungua na kuingia. Kisha, kama aliyekumbuka jambo,Kakakuona alitoka nje ya gari hilo na kuufunga mlango. Akaanza kurudi ndani harakaharaka kama alivyokuja.
Joram Kiango hakuweza kuamini bahati yake. Ilikuwa kama mungu kamleta kwake moja kwa moja. Alikuwa na nafasi nzuri ya kumtia risasi ya kisogo. Lakini kwakuwa alimhitaji alimfuata, rohoni akijua kuwa wakati wa kukijaribu kile ambacho alikuwa akijikumbushia huko kisiwani umewadia.
Ni wakati huohuo anga lilimezwa na mlio mkubwa wa ghafla ulioitetemesha ardhi. Joram alipepesuka na kujikuta akiliegemea gari la Kakakuona. Alifanya harakaharaka kujiweka sawa ili asimpoteze muuaji huyo.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hakumwona.
Kakakuona alikuwa ametoweka mbele yake kama muujiza. Pale ambapo alikuwa hatua kumi tu aliposimama Kakakuona, palikuwa patupu bila dalili yoyote ya binadamu wala uhai. Joram alitazama huku na huko na kuambulia macho ya mshangao ya wapiti njia ambao waliduwaa, baadhi wakitetemeka kwa tukio hilo ambalo hawakuweza kulitafsiri.
“Ni kitu gani?” mpita njia mmoja aliuliza, akimtazama mwenzie ambaye kapu alilokuwa amelibeba lilikuwa limedondoka chini.
“Tetemeko la ardhi…”
“Wala!” alidakia, “Tetemeko gani lenye mlio wa kutisha kama huu.”
Walitazamana. Wakatazama huku na huko kisha wakaachana. Kila mmoja alishika njia yake.
***
“Kuna nini jamani?” Fidels Sembera, mfanyakazi wa Shirika la Maktaba ya Taifa ambayo iko katika barabara hiyo, nyumba kadhaa toka aliposimama Joram, alifoka.
“Nani anayejua?” mtu mmoja alimjibu. “Au ndio mwisho wa dunia?”
Kicheko.
***
“Nini tena hicho?” Muhidini Michuzi, mwandishi wa habari wa Daily News alimwuliza Wilson Kaigarula ambaye waliketi meza moja wakijadili jambo.
“Mwangwi.”
“Mwangi, toka wapi!”
“Labda mvuayataka kunyesha!”
“Mvua kweupe hivi!. Hata hivyo mvua za Dar es Salaam tangu lini zikaanza kunguruma?”
“Kwahiyo?”
Kisha, “Achana nayo. Tulikuwa tukisema nini vile?”
Mhindi, dereva wa daladala ambaye alikuwa akipinda kona kuiacha Umoja wa wanawake aingie Maktaba, alijikuta akisimamisha gari ghafla na kushuka chini huku akitetemeka. Aliamini kuwa amegongana au kagongwa. Alipoona gari likiwa halina dosari, huku kila mtu kaduwaa akauliza, “Nini hiko nalia?”
Hakupata jibu.
***
Jibu alikuwa nalo mtu mmoja tu, Joram Kiango. Ni yeye aliyeona na kujua kilichotokea. Kakakuona alikuwa ameuawa! Mlio uliosikika ni silaha ya aina yake, ambayo tangu ilipogundulika iliaminika kuwa ilikuwa imekwisha tumiwa mara mbili tu. Mara ya kwanza ilitumika nchini Urusi, kwa amri ya Stalin. Ilitumiwa kumwondoa duniani mjerumani mmoja ambaye alijipenyeza hadi katika jeshi la Urusi , miaka nenda miaka rudi akiiba siri mbalimbali ambazo alikusudia kuzipeleka kwao. Wakati huohuo Urusi na Ujerumani ikiwa katika vita, Stalin aliamuru bunduki hiyo itumike juu yake ikiwa pia kama sehemu za majaribio kwa silaha hiyo. Matokeo yake yaliwasisimua sana warusi.
Lakini matokeo hayo yaliwavutia pia Wamarekani ambao walifanya jitihada zote hadi baada ya miaka kumi wakawa wameiba mbinu za kuitengeneza. Na walijikuta wakilazimika kuitumia miaka saba baadaye.
Kijana mmoja aliibuka kusikojulikana na kutangaza kuwa aliwahi kufanya mapenzi ya kimwili na mke wa Rais wa Marekani ambaye alikuwa madarakani wakati huo. Alidai kuwa anamtaka Rais huyo ajiuzulu, vinginevyo angezitoa hadharani picha za video alizopiga akifanya mapenzi na mama huyo. Siku chache baada ya madai hayo, kijana huyo alipokuwa akitoka nje ya nyumba yake, alisikia akiitwa na watu waliokuwa ndani ya gari lililosimama mbele ya nyumba hiyo. Wakati akilisogelea ulisikika mlio kama huu. Ukawa mwisho wake na mwisho wa madai yake.
Silaha hii, ambayo wenyewe huiita ‘kifutio’ ilikuwa kali kiasi kwamba mara unapopokea kipigo chake unasambaratika katika vipande vidogovidogo zaidi ya milioni mbili.Matokeo yake ni kwamba hakionekani kipande cha mfupa, nyama wala tone la damu. Unakuwa umefutika katika uso wa dunia kana kwamba hukuwai kuwepo.
Ni silaha hiyo iliyotumiwa kwa Kakakuona, mbele ya macho ya Joram Kiango. Sekunde moja alikuwa hai mbele ya macho yake, sekunde iliyofuata haikuwepo hata dalili yake.
Joram alilitazama jengo hilo kwa makini. Hakuona mtu wala kitu. Yeyote Yule aliyeifyatua bunduki hiyo alitumia mfadhahiko uliowakumba. Joram pia aliamua kuitumia fursa hiyo. Alitumia funguo zake Malaya, akalifungua gari la Kakakuona na kuichukua ile briefcase yake aliyokuwa nayo mkononi. Akaurudishia mlango na kuondoka taratibu.
***
Akiwa na shahuku kubwa ya kufahamu chochote ambacho angeweza kufahamu juu ya hayati Kakakuona, Joram Kiango hakwenda mbali. Aliivuka barabara hiyo ya UWT na kuingia katika moja ya majengo ya SIDO ambayo baadhi yamepangishwa kwa watu wanayoyatumia kama ofisi.
“Naomba kwenda haja,” alimweleza mtu wa kwanza ambaye alimkuta mbele ya ofisi mojawapo, msichana mtanashati ambaye alimchekea na kisha kumwelekeza kwa mkono.
Joram aliufuata mkono huo na kujikuta katika choo ambacho bila shaka hakikuwa na mwangalizi kwa jinsi kilivyokuwa kichafu. Hata hivyo, alijifungia kwa komeo, kisha akajibanza nyuma ya mlango huo na kuanza kuishughulikia ile briefcase ya Kakakuona. Kwa mtu wa kawaida, briefcase hizi zinafunguliwa kwa namna maalumu, ingemchukua miaka kuifungua. Lakini si kwa Joram Kiango. Yeye alikuwa na mbinu zake ambazo alizitumia kucheza na namba hizo. Dakika mbili baadaye tayari ilikuwa wazi ikimchekea.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kati ya yote aliyoyategemea katika mfuko huo, kamwe hakutegemea kukuta mabunda mengi ya pesa za kigeni kiasi hicho. Kwa hesabu ya harakaharaka zilikuwa paundi za kiingereza laki moja. Zaidi ya pesa hizo ilikuwemo hati ya kusafiria yenye jina la Bruno Malapaka ambaye alielezewa kuwa raia wa Naijeria ambaye alikuwa ni mfanyabiashara. Picha ilikuwa ya Kakakuona. Chini ya vitu hivyo kulikuwa na bastola.
Joram alivitazama vitu hivyo kwa mshangao. Kwa kiasi fulani, mategemeo yake katika kuuchukua mfuko huo yalididimia. Alitegemea kupata maelezo ya kutosha ambayo yangemwezesha kufahamu mengi juu ya Kakakuona; aliajiriwa na nani, mwajiri yuko wapi, kwa nini anafanya mauaji hayo, na mengine mengi. Badala yake alichoambulia ni hati ya usafiri ambayo bila shaka yoyote ni ya bandia, bastola ambayo hakuihitaji sana na pesa ambazo bila ya Nuru kupatikana mapema, akiwa hai, kamwe zisingeweza kumfariji.
Kulifikiria kwake jina la Nuru kulimrejeshea hasira na hofu aliyokuwanayo juu ya usalama wake. Hisia zilimfanya ashuku kuwa waliomuua Kakakuona ni watu haohao waliotumwa kumkamata Nuru. Hisia zilionyesha kuwa mara baada ya Kakakuona kumfikisha Nuru mikononi mwao hawakuuona tena umuhimu wake. Hivyo, walichofanya ilikuwa kumlipa malipo waliomwahidi na kisha kumshawishi aondoke mara moja. Wakati akiondoka ndipo walipoamua kumfuta duniani kwa matumaini kuwa hakuna ambaye angeona wala kuelewa kilichotokea, jambo ambalo lingewafanya polisi waendelee kumsaka Kakakuona ambaye hayuko tena duniani hali wao wakiwa wametulia zao raha mustarehe.
Kuwa kwao na silaha hatari kama hiyo, ambayo ni wachache tu waliowahi kuisikia na uwezo wao kiuchumi, ni miongoni mwa mambo yaliyomfanya Joram azidi kuamini kuwa hawa hawakuwa watu wa kawaida. Licha ya kujizatiti kwao kwa kiwango hicho bado walikuwa wakatili kupindukia. Kitendo chao cha kumwua mtumishi wao, Kakakuona, kikatili kiasi kile, na kupuuza mamilioni ya pesa walizompa kulimfanya Joram aamini kuwa walikuwepo kwa kazi moja tu, kuua.
Hali hiyo ilimfanya ataabike sana moyoni kila alipowaza kuwa Nuru yuko mikononi mwao, mikononi mwa viumbe wasihofahamika, katili kuliko shetani mwenyewe.
‘Lazima atoke mikononi mwao… mapema iwezekanavyo…’ Joram aliwaza huku akiyasaga meno yake kwa hasira. Hata hivyo, alijirudi mara moja na kujaribu kuituliza hasira yake alipojikumbusha, kwa mara nyingine, kuwa dhamira kubwa ya watu hao, kwa kila aina ya ukatili wanaoufanya, ilikuwa kumtia uchungu na hasira, ili ashindwe kufikiri kikamilifu, jambo ambalo litamfanya akurupuke na kuangukia katika mikono yao kama kinda la ndege.
‘Lazima nitulie… nipange kila kitu kwa tuo…’ alijinong’oneza moyoni.
Akiwa ameituliza akili yake alijiuliza anafahamu nini juu ya maadui hao. Hakuna! Aliwaza kwa uchungu muda wote alikuwa akihangaika na Kakakuona ambaye sasa ni marehemu. Hivyo, alikuwa hajui chochote zaidi ya ukweli kuwa anapambana na watu wenye nguvu zote: kiuchumi, kiulinzi na kiukatili.
Chanzo pekee cha kufahamu juu ya watu hao ni katika jengo hilo la kampuni ya Kangaroo ambamo silaha iliyomwua Kakakuona ilitokea. Alijua kuwa jumba hilo au chumba katika jumba hilo kilihusika, kwa namna moja au nyingine, na mkasa huu. Ni hapo ambapo angeanzia. Hata hivyo, Joram alifahamu fika asingekurupuka na kwenda huko kwani ingekuwa sawa na kujitumbukiza wakati moto anauona, hakuwa na shaka kuwa maadui hao wanamsubiri kwa hamu.
Kwamba angehitajika kushughulika mara moja ili kumtoa Nuru katika mikono yao, hilo halikumsumbua tena. Alikuwa na uhakika kuwa Nuru alikuwa akitumiwa kama chambo cha kumfanya aharakishe kuwaendea, jambo ambalo lilimtia moyo kuwa wasingemdhuru kabla hajatokea.
‘Nitatokea… nikiwa tayari…’ aliwaza.
Wazo lake lilikatizwa kwa mlango kusukumwa kwa nguvu nyuma yake. Kitendo hicho kilifuatiwa na sauti nzito ya kiume iliyoita toka njeikiuliza, “vipi braza, bado tu?”
Ndio kwanza Joram akakumbuka kuwa alikuwa chooni. Akaitazama saa yake na kugundua kuwa alikuwa ametumia zaidi ya robo saa, akiwa amejifungia katika choo hicho cha watu. Sasa aliweza hata kusikia harufu kali ya mchanganyiko wa kinyesi na mkojo chooni humo.
Akahakikisha kuwa ameifunga briefcase hiyo kama ilivyokuwa na kutoka nje ya choo huku akijitia kufunga vifungo vya suruali yake. “samahani ndugu yangu.” Alimwambia kijana wa kiume aliyekuwa amenyoa panki, ambaye alikuwa kasimama nje ya choo hicho katika hali ya kubanwa sana na haja ndogo. “Tumbo lilikuwa likinisumbua sana,” alimlaghai.
“Shauri ya bia za Mtikila.” Kijana huyo alimjibu akiingia na kujifungia.
Joram aliduwaa hapo nje kwa muda. Kisha, akajiwashia sigara na kuipachika mdomoni. Kwa mwendo wa utulivu, alivuta hatua moja baada ya nyingine akielekea katika hoteli ya Mawenzi ambako alipanga achukue chumba na kuziifadhi zile pesa. Mengine yangefuata baadaye.
***
Wakati Joram Kiango alipokuwa ameduwaa chooni, Inspekta Kombora alikuwa pia ameduwaa robo kilomita toka hapo. Yeye aliduwaa akiwa ameliegemea gari lake kwa mgongo, katika hali ya kukata tamaa.
Hakutaka kuamini kuwa Kakakuona alimponyoka katikati kabisa ya mtego wake kama samaki katika mdomo wa mamba. Hakupenda kuamini ingawa hali iliashiria hivyo. Upekuzi wa hali ya juu kupita kiasi tayari ulikuwa umefanyika katika jengo zima.
Tayari Kombora alikuwa na malalamiko ya baadhi ya wapangaji hao, mmoja akidai kuwa alilazimishwa kutoka bafuni akiwa uchi,mwingine akidai kuwa kapigwa ngwara bila sababu; watatu wakilalamika kusukumwa na kusachiwa bila maelezo. Halikadhalika, kulikuwa na malalamiko ya kuvunjwa kwa kabati moja ambalo funguo wake ulichelewa kupatikana, kubomolewa kwa tundu la ndege, kuharibiwa kwa mafriji matatu na friza moja; kuchanwa kwa mazulia na mapazia yasiyo na idadi, n.k. yote hayo Kombora alijua yangeletwa kwake kwa maandishi. Hakujali.
Ambacho alijali, ambacho kilimtisha ni kule kutopatikana kwa dalili yoyote ya Kakakuona. Alikuwa ametoweka! Nuru akiwa mikononi mwake! Ni hilo lililomfanya Kombora aduwae, Na kwa mara ya kwanza maishani mwake alijikuta akiwa hajui la kufanya kwa dakika kadhaa.
Alipotanabai kuwa karibu vijana wake wote walikuwa wamerejea na kumzunguka kwa namna ya kusubiri maelekezo zaidi ndipo alipojiinua toka kwenye gari na kupiga hatua mbili tatu za taratibu, huku akiwaza. Mara akagundua kuwa hakujua awaze lipi zaidi. Ndipo ikamjia akilini kuwa alihitaji kupata muda wa kutuliza akili yake ili aweze kuwaza kwa makini zaidi.
“Wanne wabaki hapa na kulilinda jengo hili kwa uangalifu mkubwa kila dakika, kila upande wa nyumba uwe katika macho yenu; mpo?” alisema.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Tupo.” Msaidizi wake wa karibu alijibu
“Vizuri. Nitarudi ofisini kwa muda. Baadaye nitaleta maelekezo mapya. Bado naamini mshenzi huyu yupo humuhumu ndani. Na sitamruhusu aiachie nyumba hii akiwa hai, alisema akigeuka kuliendea gari lake.
“Hayumo mzee, kama angekuwemo hata kama angekuwa amejigeuza sisimizi tungempata. Naamini hayo…” kachero kijana aliyeyasema hayo alilazimika kusita ghafla huku akiulaani ulimi wake baada ya kuona Kombora akimgeukia na kumtupia jicho kali, ambalo lilipenya uso wake na kuunyanyasa moyo wake kiasi cha kumfanya atetemeke miguu, jicho ambalo kamwe hatalisahau.
Kombora alipanda gari na kumwamuru dereva kuelekea ofisini. Lakini kabla dereva hajalitia moto wazo jipya lilimjia. Akashuka garini na kumwita tena sajini Kangua, msaidizi wake wa karibu “Nadhani tunahaja ya kutupia macho majumba ya jirani kabla ya kuendelea na ulinzi wa nyumba hizi. Unasemaje?”
“Wazo zuri afande,” Kanguru alimjibu “Kwasababu kama angekuwa humu ndani kwa vyovyote angekuwa amepatikana.”
Walifuatana kuiendea nyumba iliyokuwa kushoto mwa jengo hilo. Lilikuwa duka kubwa, la Mhindi mmoja aliyenenepa kupita kiasi. Mhindi huyo, ambaye bila shaka yoyote alikuwa anafahamu kuwa kwa jirani kuna jambo, alijizoazoa kwa tabu na kumfuata Kombora kaunta.
“Ndio bana kuba, iko taka nini?”
Kombora alimvuta nje ya wateja na watumishi wake, ambao walitega masikio yao kwa makini ili wasikie kinachoendelea. “Tungependa kuikagua nyumba yako hii.”
“Iko kosa gani? Mimi niko fanya biashara lali bana kuba. Bana Rema iko jua ivo. Iko toa michango mingi. Iko lipa kodi pato. Iko…” alisema huku akitetemeka.
Kombora angeweza kumwacha aropoke hadi mwisho wa maelezo yake, akiwa na hakika kuwa wafanyabiashara hawa hawakosi madhambi. Lakini kwa kuwa hakuwa na nafasi hiyo alimkatiza kwa kumwambia kwa upole, “Hatuna haja na wewe wala biashara zako. Tunataka tuone kama kuna uwezekano wowote wa mtu kupenya toka jengo hilo la jirani yako kupitia hapa kwako.”
“Hakuna mitu pita hapa,” alijitetea
“Tunajua. Lakini tunataka kuwa na hakika,” Kombora alisema akianza kuingia ndani. Mhindi huyo alimzuia kwa kono lake zito lililolowa jasho.
“Hapana taka… Ngoja mimi iko piga simu kwa waziri Rema ulizia yeye. Iko subiri.”
Kauli yake ilipandisha hasira za Kombora. Aliutoa mkono huo kifuani pake kwa pigo moja la kiganjakwa mkono wake wa kushoto. “Sikia,” baadae alifoka huku kamkazia macho makali mhindi huyo, “Ukiendelea kunipotezea muda wangu nitaruhusu vijana wangu ishirini waingie humu na kuipekua nyumba hii. Na nakuhakikishia baada ya dakika ishirini tu utakuwa mahabusu kwa makosa yasiyo na idadi.”
Ukali wa Kombora ulifikisha ujumbe katika kichwa cha Mhindi huyo. Kwa unyonge, huku akijitia kutabasamu, alimpisha Kombora na kumfuata taratibu huku akisema, “Mimi iko mitu mema iko penda saidia…”
Kombora hakumsikiliza alimwita hadi uwani akifuatiwa na msaidizi wake. Huko walikutana na ukuta mnene, mrefu ambao ulikingwa na vipande vya chupa. Kombora hakuona uwezekano wa mtu kuupanda ukuta huo katika muda mfupi kama ule. Akageuka kumtazama msaidizi wake ambaye macho yake yalionekana kuwa na wazo hilohilo.
“Kwa mtu kama Kakakuona ukuta huu unapandika. Lakini apande yeye, ampandishe na mateka wake kwa nguvu, huku akiwa na bastola mkononi sio rahisi.”
Hata hivyo, Kombora na msaidizi wake, bastola zikiwatangulia, walianza ziara ya chumba hadi chumba. Mhindi huyo ambaye tayari alikuwa ameamuru kufunga duka alikuwa akiwafuata nyuma huku akitetemeka na kulalamika kwa maneno mengi ambayo Kombora aliyapuuza.
Karibu kila chumba kilikuwa na vitu mbalimbali vya thamani kubwa kama mashine za kupozea hewa, TV, deki za video, mazulia, nguo na vitu mbalimbali. Kwa jinsi Mhindi huyo alivyokuwa akitetemeka Kombora alijua fika kuwa kama angehoji mengi juu ya vitu hivyo angegundua kuwa nyingi zilikuwa mali za magendo au hazikulipiwa ushuru bandarini, au zimelipiwa nusu n.k. hata hivyo hakuwa na muda huo hadi alipofikia chumba ambacho Mhindi alitetemeka hadi kutokwa na machozi wakati Kombora akimshurutisha kukifungua.
“Iko kupa pesa milioni, sawa?” alibembeleza.
Kombora alimshika ukosi wa shati na kumsukasuka kwa hasira hadi funguo zikamtoka mkononi. Sajin kangua alizidaka na kuufungua mlango huo. Huku bastola ikimtangulia alitangulia kuingia, Kombora akimfuatia, na kumvuta mhindi huyo ambaye baada ya kuona hana hila alijikaza kisabuni na kuendea sefu la chuma lililokuwa katika kona moja ya chumba hicho. Alilifungua na kutoa mabunda ya pesa za kigeni na kumkabidhi Kombora.
“One hundred thousand dollars. Please…”
Kombora alizichukua fedha hizo na kuzikabidhi kwa msaidizi, “Yaani hata benki ya fedha za kigeni unayo katika chumba hikihiki, sio?” alimwuliza “Very well. Suala lako litamalizwa na polisi,” aliongeza akizungumza katika redio call yake na kuombwa aunganishwe na kituo kikuu cha polisi. Kilipopatikana aliwataka kuja kumchukua mtu wao mara moja.
Alipomgeukia Mhindi huyo nusura amhurumie kwa jinsi alivyolowa jasho na mkojo ambao ulikuwa ukimtoka kama mtoto hali mwenyewe hana habari. Kombora alimtazama kwa dharau na kumwacha mikononi mwa kachero wake mmoja kuwasubiri polisi. Kisha, akaongoza kutoka akiifuata nyumba ya upande wa kulia.
Nyumba hiyo haikuwasumbua. Lilikuwa jengo la ofisi ya idara moja ya serikali moja ambayo wafanyakazi wake wote tayari walikuwa wameondoka na kumwacha mlinzi ambaye hakuwa na funguo. Baada ya kutazama Kombora aliona mara moja kuwa Kakakuona hakuwa katika jengo hilo pia. Kuta zilikuwa ndefu, imara, ambazo pia zilipambwa kwa vipande vya chupa.
“Turudi ofisini,” aliamuru kwa sauti ya unyonge.
Nyumba hiyo haikuwasumbua. Lilikuwa jengo la ofisi ya Idara moja ya serikali ambayo wafanyakazi wake wote tayari walikuwa wameondoka na kumwacha mlinzi ambaye hakuwa na funguo. Baada ya kutazama Kombora aliona maramoja kuwa Kakakuona hakuwa ndani ya jengo hilo pia. Kuta zilikuwa ndefu, imara ambazo pia zilipambwa kwa vipande vya chupa.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Turudi ofisini,” aliamuru kwa sauti ya unyonge.
Wakati wakipanda magari yao walipishana na polisi wengi wenye magwanda ambao walikuwa wakimburura Yule Mhindi mwenye duka huku tayari alikuwa ametiwa pingu “Tutawaandikieni ushahidi mdogo tulionao dhidi yake.” Kombora alimwambia kiongozi wao ambaye alikuwa amesimama kwa ukakamavu mbele yake baada ya kupiga saluti ambayo Kombora aliipuuza.
Msafara wa Kombora ulitanguliwa na gari lake. Waliuacha mtaa huo na kuingia barabara ya umoja wa wanawake. Walipopinda kushoto na kuelekea hatua kadhaa Kombora alitupa macho kulia na kuliona jengo ambalo kwake limekuwa kama fumbo la aina yake, fumbo lililomtia aibu na hasira kubwa kwa kushindwa kulifumbua.
Jengo hilo lilionekana nyuma ya jengo jingine la ghorofa mbili lililobeba maandishi yaliyosomeka Kangaroo Enterprises. Kampuni hiyo ilikuwa sambamba mgongo kwa mgongo na Sunrise Modern Club. Hisia zilimfanya Kombora ashuku kuwa inawezekana kabisa Kakakuona alitorokea katika jengo hilo. Akaamuru gari lisimamishwe mara moja. Huku akimwashiria Kanguru kumfuata, alishuka na kuliendea lango la kampuni hiyo.
Mlango ulifunguliwa hata kabla hawajaugusa. Aliyeufungua alikuwa askari aliyevaa magwanda ya mgambo ambayo ilionyesha ni moja ya kazi yake kuwafungulia wageni wote mlango waingiapo na watokapo.
Ilikuwa moja ya zile ofisi nyingi ambazo unaweza kudhidharau kwa nje lakini ndani ukaziogopa. Ndio kwanza Kombora na msaidizi wake wakagundua kuwa walikuwa wamechakaa kwa jasho baada ya kujikuta katika chumba hicho cha mapokezi, chenye vioo kila upande ambavyo viliwafanya wajitazame. Chumba kilikuwa na hewa safi ambayo ilikuwa ikitokea katika vipozea hewa. Mbele yao, nyuma ya meza ya mapokezi kulikuwa na wasichana wazuri watatu. Kushoto kwao kulikuwa na msichana mwingine, nyuma ya ukuta wa kioo, ambaye alikuwa akiendelea kuwachekea huku akisema kwa mara nyingine, “Karibuni kwenye viti.”
Kombora alianza kujiona mpumbavu kwa uamuzi wake wa kuingia humo. Kati yao hakuna aliyeonekana kuwa na wasiwasi wowote juu ya lolote ambalo lilitokea nje ya ofisi hiyo.
Kakakuona hakuwa amepita hapo. Alishawishika kuketi kwenye makochi ya kuvutia chumbani humo, kutokana na uchovu aliokuwa nao.
“Kangaroo Enterprises shughuli zenu hasa ni zipi?” Alimwuliza msichana huyo ambaye alianza kupoteza tabasamu lake kutokana na jinsi alivyomwona mgeni wake.
Kabla ya kujibu msichana huyo aliinama na kuinuka huku mkono wake ukiwa umeshikilia kijitabu chenye kurasa zaidi ya ishirini zilizochapwa kwa rangi mbalimbali ndani na nje. Juu ya kijitabu hicho lilitajwa jina la kampuni hiyo na nenoCatalogue chini yake. Kombora alikipokea na kukididimiza mfukoni mwake. Msichana huyo alipoona hana walau nia ya kukitupia macho alisema kwa sauti ya kibiashara “Tuna fanya mambo mengi, tunajenga viwanda, tunasafirisha watalii, tunaagiza na kuingiza mali nje ya nchi, tuna maduka ya kubadili fedha n.k. Hii ni ofisi kuu hapa nchini. Ni tawi la kampuni ya Kangaroo yenye makao yake makuu nchini Marekani na matawi katika nchi mbalimbali za dunia” msichana huyo alieleza kwa ufasaha. Alipoona maelezo yake hayaelekei kumvutia. Kombora aliongeza harakaharaka.
“Sijui nikusaidie nini mzee wangu?”
“Naweza kumwona bosi wako?” lilikuwa jibu la Kombora
“Bosi huwa hapatikani kwa urahisi, labda ueleze shida yako ili tumwulize kama anahitaji kukuona..”
“Shida yangu ni kumwona yeye!” Kombora alijibu kwa sauti nzito iliyoonyesha madaraka. Alipomwona msichana huyo kaduwaa aligeuka na kuufuata mlango ulioandikwa Mkurugenzi Mkuu.
Akifuatana na msaidizi wake, walipanda ngazi ambazo ziliwachukua hadi ghorofa ya kwanza ambapo walijikuta ndani ya ofisi nyingine iliyojaa watu ambao pia walikuwa katika mishughuliko mingi. Alikuwepo msichana mwingine wa mapokezi. Kwa mshangao wa kombora msichana huyo aliwaelekeza kwa adabu katika chumba kilichoandikwa Mkurugenzi Mtendaji. Nje ya ofisi hiyo kulikuwa na chumba cha kusubiria chenye makochi bora zaidi, ambayo yaliizunguka meza ndogo iliyojaa makabrasha ya kujisomea. Kombora hakuketi. Aligonga mara moja mlango wa mkurugenzi na kisha kuusukuma. Ulifunguka na kumruhusu kuwa ndani ya chumba kipana nadhifu, ambacho kilinukia kila dalili ya pesa. Zulia lililotandikwa hapo sakafuni lingetosha kujenga madarasa matatu ya shule ya msingi, meza kubwa iliyokuwemo ingeweza kuwafanya ombaomba kuwa matajiri kwa miaka mitatu. Viti vilivoizunguka meza hiyo vingewafanya watoto wa mitaani wanane wasahau kuwa hawana wazazi.
Lakini vitu hivyo havikumvuta Kombora kama alivyovutwa na mtu aliyeketi nyuma ya meza hiyo pana akiwatazama. Kombora alitegemea kumkuta Mkurugenzi wa kampuni iliyonona kama hiyokuwa mtu aliyenona, mtu ambaye hakuhitaji kujitambulisha ili umtambue.
Badala yake aliyeketi nyuma ya meza hiyo alikuwa mtu wa kutisha au kutatanisha. Haikuwa rahisi kujua kama alikuwa mzungu au mwafrika kutokana na kovu kubwa jeusi ambalo lilikula nusu ya uso wake, kuharibu jicho lake moja na kuchoma robo tatu ya nywele zake kiasi cha kumfanya awe katikati ya mataifa hayo mawili.
“Yes. Sir what can l do for you?” mwenyeji huyo alimwambia Kombora ambaye tayari alikuwa ameketi mbele ya kimojawapo ya viti hivyo.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kabla hajajibu Kombora alitia mkono mfukoni mwake na kutoa moja ya kadi zake, ambazo humfanya awe na cheo kidogo kuliko kile cheo chake kamili, kile ambacho ni siri yake yeye pamoja na mkuu wa nchi. Meneja huyo alipokea kwa mkono wake wa kushoto, jambo lililomfanya Kombora aamue kuutazama mkono wa kulia na kugundua kuwa ulikuwa wa bandia ambao ulitengenezwa kwa mbao au plastiki kwa ufundi kiasi cha kufanana na ule wa kawaida.
“Vita… vita sio mchezo. Vita vya Angola ndiyo ilinifanya hivi,” alisema ghafla kana kwamba alikuwa akiyafuata macho na mawazo ya Kombora. “ Kwa hiyo wewe ndiyo Inspekta Kombora? Tumekuwa tukizisikia jitihada zako. Hongera sana.”
Kombora hakujua ni jitihada zipi hizo, na huyo bwana alizifahamu vipi, “Sijui na wewe mwenzangu unaitwa nani?” aliuliza badala yake.
“Naitwa Paul Powel. Ni mkurugenzi mwendeshaji wa kampuni hii. Sina budi kushukuru sana kutembelewa na mtu mzito kama wewe.”
Kombora alihisi kitu kama kebehi katika sauti yake. Naam, aliweza hata kuiona waziwazi katika jicho lake moja ambalo lilikuwa likimcheka ingawa mdomo wake ulikuwa hauna tabasamu lolote.
“Vizuri.” Alimjibu kwa utulivu. “Shida yetu ilikuwa ndogo sana. Kuna mtu wa hatari ambaye ametoroka jengo la jirani yenu upande wa pili wa mtaa. Tulichohitaji ni kukagua jengo zima ili tuwe na hakika kuwa hayuko humu ndani.”
Powel alicheka. “Jengo hili haliingiliki hovyo. Tuna biashara ya mamilioni hapa, hivyo tumelijenga kwa usalama wa hali ya juu. Mtu atakayeingia hapa itambidi kupitia mlangoni peke yake…”
“Hilo tunaelewa. Lakini kiutaratibu lazima tuhakikishe kwa macho yetu wenyewe, kwa usalama wenu…” Kombora alilazimika kusita ghafla alipoona pazia lililokuwa nyuma ya Powel likifunuka
taratibu na Powel mwingine kuingia ghafla kama kivuli na kuketi kwenye kiti kilichomuelekea Kombora.
Kombora alimfikiria kama Powel mwingine, kwa jinsi walivyofanana kimaumbile na kimavazi.Yeye pia alikuwa ameungua uso na sehemu mbalimbali za mikono yake. Yeye pia alikuwa na jicho moja, ingawaje lake lililoungua lilikuwa wazi nyuma ya kovu kana kwamba linaona. Badala ya mkono wa bandia yeye alikuwa na mguu mmoja wa mbao. Hilo Kombora aliligundua wakati alipoukunja kwa mikono yake yote miwili pindi akiketi chini, vinginevyo isingekuwa rahisi kugundua.
Powel aliyaona macho ya Kombora yakitembelea uso huu hadi ule kana kwamba yanadai maelezo. Kwa sauti ilelile inayocheka Powel alisema, “Watu wengi wanasema tumefanana. Wengine wanadhani tu mapacha. Lakini wanakosea sana. Hatujafanana hata kidogo. Ukishatuzoea, utagundua kuwa huyu mwenzangu ni mrefu kuliko mimi, mnene kuliko mimi.” Alipoona maelezo hayo hayajamridhisha Kombora aliongeza, “ kinachotufanya tufikiriwe ndugu ni haya masahibu yaliyotukuta, siku moja, saa moja, kwa bomu moja. Ilikuwa tufe pamoja, kwa bahati mungu alitunusuru pamoja. Tungeweza kuwa ombaomba barabarani, lakini mungu ametusaidia vilevile na kutuwezesha kuwa wafanyabiashara wakubwa duniani…”
“Hujaniambia mwenzako anaitwa nani,” Kombora alimkatiza
“Oh kweli anaitwa Philip Benjamin. Yeye ni Mkurugenzi wa Fedha” alimgeukia mwenzake huyo na kumwambia, “Philip, huyu hapa ni Inspekta Kombora bila shaka umepata kumsikia”
Philip alitikisa kichwa kukubali.
Powel aliendelea “Inspekta Kombora anadhani kuna mwizi ambaye amejificha katika jengo hili. Unadhani inawezekana Philip?”
Badala ya kujibu Philip aliangua kicheko.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Unaona Inspekta? Unapoteza muda wako bure.”
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment