Search This Blog

Sunday, 22 May 2022

UCHU - 1

 





    IMEANDIKWA NA : ARISTABLUS ELVIS MUSIBA (A.E MUSIBA)



    *********************************************************************************



    Simulizi : Uchu

    Sehemu Ya Kwanza (1)

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ARUSHA



    Christopher Temu, ambaye Jumapili hii nyumbani kwake Arusha, alikuwa amefikiwa na ugeni mkubwa kutoka Umoja wa wanaharakati wa Afrika (Pan African Movement PAM) kutoka sehemu mbalimbali za Afrika. Temu alikuwa mwanachama wa chama hicho.



    Hii haikuwa mara ya kwanza kwa watu hawa kukutana nyumbani kwa Temu kwani watatu kati yao walikaa nyumbani kwake kwa muda usiopungua miezi sita. Mnamo mwaka 1992 na 1993 walihudhuria mkutano uliofanyika Arusha kuvisuruhisha vikundi mbalimbali vilivyokuwa vikipambana katika mgogoro wa nchi ya Rwanda, ili mgogoro huo umalizike kwa njia ya amani



    Kikundi hiki cha PAM. ambacho kilikuwa kinahudhuria kama kikundi cha wapenda amani wa Afrika. Kilikuwa kinaweka shinikizo kwa kila upande uliokuwa unahusika na mgogoro huo ili umalizike kwa amani. PAM ilianzishwa mwanzoni mwa karne ya 19 ikiwa na lengo la kupambana na utumwa, ukoloni mkongwe, ukoloni mamboleo, kupigania haki ya watu weusi na kuhakikisha kuwa waafrika wanaweza kupambanua mambo yao wenyewe.



    Hivyo, mara hii kikao kilichokuwa kinafanyika nyumbani kwa Temu kilikuwa cha kutathmini juhudi zote zilizofanywa kuumaliza mgogoro wa Rwanda kwa amani, lakini bila mafanikio. Wakiwa wamekaa kwenye bustani nzuri iliyokuwa nyuma ya nyumba hii iliyojengwa kisasa. Ikiwa kwenye barabara ya Njiro kwenye kilima kidogo ikiuangalia mji wa Arusha kwa upande wa Kijenge. Mkutano uliendelea mchana huu wa saa kumi alasiri huku bia aina ya safari na ndafu, iliyokuwa inachomwa hapohapo kwenye jiko la mkaa vikiendelea kuwa viburudisho vya wageni hawa.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Ndugu zangu. Fundisho kwa Rwanda ni fundisho kwetu sote, na sisi tukiwa tumejitolea kuona Afrika inajikomboa na kujitawala kwa amani ni lazima tukae chini kulitafakari swala zima la Rwanda tuone makosa yalitokea wapi, na kwanini hali ilifikia hapo ilipofikia na watu zaidi ya milioni moja kuteketea bila Afrika wala dunia kufanya chochote", Jackson Musoke kutoka Uganda ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa PAM Kanda ya Afrika Mashariki alieleza.



    "Ni kweli kabisa maneno uliyosema, lakini mimi nafikiri wakati mkutano wa amani ulipokuwa unaendelea hapa Arusha. Ukweli wa mambo Rwanda ulikuwa haufahamiki. Na hivyo maamuzi mengi yaliyofanyika hayakuzingatia hali halisi ya mambo ilivyokuwa Rwanda wakati huo. Na ningependa niseme kuwa hata hivi sasa tunavyokaa hapa hali halisi na ukweli wa mambo Rwanda bado haujulikani. Ndio maana Jumuia ya Kimataifa, Umoja wa Mataifa, Umoja wa Nchi Huru za Afrika bado wanafanya maamuzi ambayo yanazidi kuleta matatizo nchini humo, na kuifanya serikali ya sasa iyumbe katika kutekeleza shughuri zake za kuleta amani iliyo ya kweli katika nchi hiyo", Alfred Kimani kutoka Kenya aliongezea.



    "Sasa tutafanya nini ili huo ukweli wa mambo uweze kujulikana na matatizo yaliyo mengi katika nchi hiyo yaweze kutatuliwa?", Temu aliuliza.



    "Mimi nafikiri tuunde tume ya uchunguzi, ikafanye uchunguzi, ichimbe chanzo cha matatizo Rwanda toka kabla ya uhuru mpaka sasa, na kujaribu kuelewa kabisa tatizo ni nini na nani anahusika na matatzo kwani mimi siamini kuwa tatizo hasa ni kabila tu. Miaka yote tumefikiria hivyo na kujaribu kumaliza tofauti za kikabila lakini mambo bado yako pale pale", Abdul Abakutsi toka Nigeria alijibu.



    "Vilevile, kama tatizo ni la kikabila, lazima uchunguzi ufanyike ili ipatikane namna ya kulitatua tatizo hilo maana hatuwezi kukaa tu na kusema kwa sababu ni tatizo la kikabila, basi halina ufumbuzi", Lukaka Makwega kutoka Zambia aliongeza.



    "Tulipokuwa hapa kwa ajili ya mkutano wa amani, ilionekana kwamba serikali tawala ndiyo iliyokuwa inachochea ukabila. Swali hapa ni kwanini serikali inachochea ukabila?. Ni kwa sababu inataka kubaki madarakani kwa njia ya gawa utawale au Rais alikuwa na sera za kikabila yeye mwenyewe au kulikuwa na kitu kingine kilichokuwa kinachochea hali hii, maana kinachotisha zaidi ni jinsi mauaji hayo yalivyotokea. Inaonekana kuwa dakika ishirini tu baada ya ndege ilikuwa imemchukua Rais kutunguliwa mauaji yalianza sehemu zote. Hii inaonyesha mauaji yamepangwa kabla. Ina maana ilijulikana kuwa Rais atauawa siku hiyo?. Na kama Rais ndiye aliyepanga mauaji haya, je alijuwa kuwa atauawa, na kwa hiyo akapanga akiuawa alipiziwe kisasi?. Na kama alijuwa atauawa kwani alirudi na ile ndege! Mimi vilevile naanza kukubaliana na wenzangu kuwa huenda kuna mambo zaidi yasiyojulikana ambayo yanaleta matatizo nchini humo. Nami naamini kuwa mambo hayo yakifichuliwa ufumbuzi wa matatizo ya ndugu zetu hao utapatikana haraka", Charles Malisa wa Tanzania alichangia.



    "Kuna kitu kingine nilichokisema mwanzoni ambacho kinatisha sana. Jumuia ya Kimataifa haikufanya kitu chochote pamoja na kuona jinsi watu walivyokuwa wakiuawa kinyama. Majeshi ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa yalikuwepo. Na Jeshi la Ufaransa lilikuwemo nchini humo wakati wa mauaji. Nchi kama Marekani ambazo zimejitokeza kama Polisi wa dunia, vilevile haikushtuka. Na kila mtu anakubali kuwa haya yalikuwa mauaji ya kikatili yaliyopangwa kuliko yale ya Hitler aliyowaua Wayahudi. Kwanini hali ilibaki hivi! Na nchi za kiafrika nazo zilikaa tu zikiangalia kabila moja ndani ya nchi ya kiafrika likiangamizwa kabisa ili lisiwepo tena. Jamani hapa kuna sababu na kuna jambo ambalo halieleweki. Uchunguzi ni kitu cha lazima", Musoke alisisitiza.



    "Abakutsi ametoa ushauri wa kuunda tume ya uchunguzi, sijui ni tume ya watu wa namna gani anayozungumzia, maana nchi yenyewe ya Rwanda bado iko katika hali ya kivita bado wanauana. Serikali ya sasa bado haina uwezo wa kudhibiti hali ya usalama katika nchi hiyo. Mambo yote bado shagalabagala. Tukisema watu kama sisi twende huko kufanya uchunguzi hakika hatutaambulia kitu kama si kutafuta kuuawa. Uchunguzi ni muhimu lakini lazima tufikirie uchunguzi huu ufanywe namna gani", Makwega alishauri.



    Watu wote waliohudhuria kikao hiki walinyamaza kimya wakitafakari kwa kina kuhusu uzito wa suala hili nyeti.



    "Lete ndafu na utuongeze vinywaji, tunatakari huku tukilegeza makoo", Temu alimwagiza mtumishi wake. Bia baridi aina ya Safari zikaletwa na mabwana hawa wakaendelea kulegeza makoo na kutafuna ndafu, huku wote wakitafakari mazungumzo yao kwa makini.



    Baada ya kimya kirefu Abakotsi alivunja kimya hicho. "Huenda ikawa ni lazima tuunde kikosi cha siri cha upelelezi, kipeleleze kwa sirisiri halafu kituletee taarifa maana serikali zetu zinao vijana wanaoweza kufanya upelelezi kama huo na ukazaa matunda. Kama bwana Makwega alivyosema, tume ya kawaida haiwezi kuambulia kitu, kwani mambo ni magumu huko. Nia yetu ni kupata ufumbuzi na si kupeleka watu wakauawe. Mnasemaje jamani?".

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Hapo umenena, hiyo ndio njia pekee ya kuweza kuingia ndani na kupeleleza kiini cha matatizo hayo. Mimi nakuunga mkono ila tutaiomba serikali gani itupe msaada huo?. Nyinyi wenyewe mliona jinsi serikali zetu zilivyonyamaza na kuacha kana kwamba hazikujua kuwa mauaji yalikuwa yakifanyika Rwanda", Makwega alinena.



    "Wote tunakubaliana kuwa njia nzuri ya kupata kiini cha matatizo yaliyosababisha hali ya Rwanda ikafikia pale ni kutuma kikosi cha upelelezi?", Musoke aliuliza.



    "Ndiyo", wote walijibu kwa pamoja.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Basi, tuahirishe mkutano kwa leo, tuonane hapa kesho mchana saa kama hizi ili niweze kuwasiliana na watu fulani fulani ambao naamini wanaweza kutusaidia bila kugongana na serikali zetu", Musoke alisema.



    Nyuso za wajumbe, ambazo kwa muda mrefu zilikuwa zikionyesha wasiwasi, zilikunjuka na kuonyesha furaha. Ndipo wote walipokumbuka kuwa Musoke ndiye aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Upelelezi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kabla haijavunjika. Hivyo, alijuana na wakuu wa idara hizi katika Afrika Mashariki, na alisemekana hadi sasa alikuwa akiombwa ushauri wa kiupelelezi mara kwa mara.



    Baada ya kumaliza vinywaji vyao, wote waliondoka kuelekea kwenye hoteli zao walikofikia. Usiku ule Musoke aliporudi hotelini kwake, pale Mount Meru, aliwapigia simu rafiki zake, yaani wakurugenzi wa upelelezi wa Kenya, Uganda na Tanzania. Alizungumza nao kidiplomasia na kila mmoja alimuomba ushauri na kumweleza sababu za kufanya hivyo. La kusikitisha ni kwamba, kwa vile yeye alikuwa sasa anaongoza chombo ambacho si cha kiserikali, serikali zisingeweza kumsaidia mtu au kikundi cha watu, kwa vile ingeshindwa kujieleza iwapo mkasa wowote wa kiupelelezi ungetokea.



    Hilo ndilo lililokuwa jibu la kila mkurugenzi wa upelelezi. Wote waliomba samahani kwa hilo kwani walimheshimu sana, lakini ilikuwa nje ya masharti yao ya kazi, hasa wakati huu ambapo siasa za nchi hizi ni kutoingilia mambo ya ndani ya nchi zingine!



    Swala hili lilimkasilisha sana Musoke. Wakati wenzao katika PAM wanapigania Afrika iwe moja, wengine wanadai eti ni kuingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine!



    "Ole wetu Afrika", Musoke alijililia. Ni wakati alipokaribia kukata tamaa, baada ya kufikiri sana namna ya kuweza kufanya ndipo alipomkumbuka Mzee mmoja mstaafu. Alifikiri huyu angeweza kumtatulia shida yake kwani ni Mzee aliyeisaidia sana Afrika, hasa wakati wa ukombozi wa nchi zilizo kusini mwa Afrika. Yeye alijuana na wapelelezi wengi na maamuzi yake yalikuwa ya pekee, na ndiye aliyekuwa kitovu cha ukombozi Kusini mwa Afrika. Mpaka leo wengi walimjua kwa jina la "Chifu" tu.



    Musoke aliangalia ndani ya kitabu chake cha simu, akaipata namba ya Chifu ya nyumbani na kumpigia simu.



    Alipoangalia saa ilikuwa yapata saa tano usiku.



    "Hallo", alisikia sauti ya Chifu, ikiwa na nguvu kama ya kijana wa miaka thelathini.



    "Mzee, shikamoo, Musoke hapa".



    "Marahaba Musoke, habari za siku nyingi, nini kinakufaya unipigie simu saa hizi?".



    "Umekasirika Mzee?".



    "Hapana, shauku".



    "Bado tu uko vilevile, utafikiri hujastaafu?".



    "Mwili ndio unastaafu lakini nafsi huwa haistaafu maana nafsi haizeeki isipokuwa mwili".



    "Ahsante nitazingatia, huo ushauri, maana nami naitwa mzee sasa na nafsi yangu imeanza kukubali".



    "Hapana usiruhusu kabisa. Haya, lete habari zinazokufanya umpigie simu mzee kama mimi saa hizi kwanza uko wapi?".



    "Niko Arusha".



    "Aha, nilifikiri uko Kampala".



    "Niko Arusha, Chifu". Ilikuwa ukimwita Chifu mara moja anajuwa kazi imeanza.



    "Haya lete hizo habari".



    Musoke alimweleza habari zote toka mwanzo mpaka mwisho. Pia alimweleza jinsi idara za upelelezi za serikali zilivyokataa kumsaidia kwa kitu nyeti kama hiki.



    "Pole sana", Chifu alimjibu baada ya kuyasikia yote.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Tatizo lako ni kubwa, la kuangaliwa kwa makini sana. Mimi mwenyewe nimekuwa nikishangazwa sana na mambo yalivyo Rwanda. Enzi zetu sisi tusingeruhusu hali kama hiyo itokee, wewe mwenyewe unajuwa msimamo wetu ulivyokuwa".



    "Ndio Chifu, lakini serikali zetu za sasa kila mtu eti na nchi yake, eti hiyo ndio wanaiita demokrasia", Musoke alijibu.



    Wakati wanazungumza kwenye simu mawazo ya Chifu yalikuwa yanakwenda kama Kompyuta kutafuta nani angeweza kumsaidia Musoke na Chama chake cha PAM katika azma yao ya kutafuta kiini cha matatizo ya Rwanda. Chifu mwenyewe alikuwa mwana PAM, na aliamini Umoja katika Afrika.



    "Jack", Musoke alishituka kusikia Chifu akimuita kwa jina lake la kwanza. Hii ilikuwa na maana amekwisha pata jawabu. "Nafikiri nitakupatia ufumbuzi wa tatizo lako. Mtu mmoja tu katika Afrika hii ambaye anaweza kuifanya kazi yako. Hivi sasa ameacha kazi za kiserikali maana ameowa na anafanya shughuli zake. Lakini kutokana na imani yake katika Umoja wa Afrika anaweza akaifanya kazi hii, huna haja ya kuwa na kikosi, maana yeye pekee ni kikosi. Nitazungumza naye, nipe namba yako ya simu na chumba chako; nitakupigia simu kesho asubuhi".



    "Ahsante Chifu, nilijuwa wewe ndiye utakayenimalizia matatizo yangu", Musoke alijibu kisha akampa namba ya simu ya pale hotelini na namba ya chumba. Alipomaliza tu akasikia simu ikikatwa. Akajuwa tayari Mzee yuko kazini.



    Chifu alipokata simu ya Musoke, alipiga simu nyingine.



    "Hallo".

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Chifu".



    "Aha shikamoo".



    "Marahaba, tuonane kusho asubuhi, tutastafutahi pamoja pale Kili, kama kawaida.



    "Sawa Mzee, kesho", Chifu alijibiwa.



    "Kesho, ahsante", Chifu alijibu na kukata simu.



    KAZI KWAKO



    "Umesikia George Foreman amerudi ulingoni na kutwaa ubingwa", Chifu aliuliza.



    "Sikusikia tu, nimeona kwenye televisheni".



    "Basi na wewe nataka urudi ulingoni", Chifu anasema kwa tabasamu huku akiupaka mkate wake siagi.



    "Mimi! mimi nimeoa na mke wangu ana mimba. Mchezo huo sifanyi, sifanyi ng'o".



    Chifu anaangua kicheko kiasi cha kuwafanya watu wote ndani ya chumba cha mkutano wamwangalie.



    "Kwani mimi sijui umeoa! Kwani mimi sijui mke wako ana mimba! Najua, lakini nakutaka ulingoni tena. Kwani George Foreman hana mke, hana watoto, mbona karudi ulingoni", Chifu aliendelea kusema kwa kebehi.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Huenda alikuwa anataka pesa, huenda alikuwa anatafuta sifa, mimi sitaki vitu vyote hivyo, sirudi ng'o", Chifu alielezwa kwa busara.



    "Sikiliza nikueleze kwanza. Mimi ndiye niliyekuruhusu uache kazi na kukushauri uoe na nisingependa uharibu ndoa yako. Najua unampenda sana mkeo, sasa nasema nisikilize kwa makini nikueleze, kama utakataa itanibidi niingie mimi mwenyewe ulingoni", Chifu alijibu kwa masikitiko kiasi cha kumfanya mwenzake apoe hasira zake.



    "Chifu, hebu nieleze kuna nini? Kitu cha maana namna hiyo, kiasi cha kusema utafanya kazi hiyo mimi nisipokubali? Unajua mimi siwezi kukuruhusu wewe kufanya hivyo.



    "Basi sikiliza".



    Ilimchukua Chifu saa nzima kumweleza suala la Rwanda na jinsi msimamo wa PAM ulivyohusiana pamoja na vipengele vingine vingi ambavyo hata akina Musoke wasingeweza kumweleza maana hawavijui.



    "Unafikiri Serikali ya sasa ya huko haiwezi kufanya kazi hiyo", Chifu aliulizwa.



    "Haiwezi. Inahitaji ujuzi wa hali ya juu kufanya kazi hiyo, katika hali ya machafuko namna ile, maana hata wao hawajui nani ni nani katika nchi yao. Hawamwamini mtu yeyote na wao hawaaminiki vilevile na kuweza kupata habari za kina kama zinavyotakiwa, unahitajika ujuzi wa juu sana. Na katika Afrika nzima kama si wewe basi itanibidi mimi mwalimu wako nikaifanye.



    "Umenipa mtihani mkubwa sana. Unafikiri kazi kama hii inaweza kuchukua muda gani?".

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Chifu alipoulizwa swali hili, moyo wake ilitulia akijuwa kazi itafanywa.



    "Inategemea na wewe mwenywe, wiki moja au mbili, mwezi yote yategemea wewe. Kwani Pepe atajifungua lini?".



    "Bado ana miezi miwili".



    "Nakutakia heri. Nafikiri utamaliza kazi kabla ya hapo. Tafadhali, hafadhari iwe kitu cha kwanza kwako maana huko kuna hatari nyingi, usifanye mchezo kama unataka kumwona mtoto wako", Chifu sasa alikuwa amebadilika na kumwasa mwenzake.



    "Nikifa utamlea wewe", Alijibu.



    "Sasa nina miaka sabini, nitamlea miaka mingapi mie", Chifu alijibu.



    "Wewe ndiye uliyetaka, shauri yako, damu yangu itakuwa juu ya kichwa chako".



    "Pole sana. Ndege ya Shirika la Ndege Tanzania inaondoka saa tano na nusu kwenda Kilimanjaro. Tiketi hii hapa, umepatiwa nafasi kwenye ndage hiyo. Musoke mtaonana uwanja wa ndege, atakuja kukupokea, si unamfahamu?".



    "Ndio, namfahamu".



    "Haya kwa heri. Ukirudi toka Arusha, kabla ya kwenda Kigali, njoo unione nitakuwa tayari na taarifa za kukusaidia kule".



    "Asante, nitafanya hivyo.



    Chifu alilipa wakaondoka.



    Ilikuwa saa tatu na nusu Chifu alipompigia simu Jack Musoke kule Arusha.



    "Naam Chifu. Nilikuwa nasubiri huku kiroho kinanidunda. Haya nipashe".



    "Willy Gamba ndiye mtu wako, mpokee uwanja wa ndege saa sita na nusu mchana".



    Musoke alipigwa na butwa. Hakuweza kujibu kwa ajili ya furaha na msisimko. Hata Chifu alipokata simu hakusikia. Utafikiri kapigwa na radi.



    "Willy Gamba! Willy Gamba! Jamani huyu Chifu nitamfanyia nini kwa kumleta willy Gamba! Mungu anatupenda sana Waafrika maana sasa kazi itafanyika", Musoke alijisemea kama kichaa.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya kuachana na Chifu, Willy Gamba alikwenda tena kwenye ofisi za Shirika la Ndege Tanzania ATC kujua kama kutakuwa na ndege ya kurudi siku ile ile jioni, maana Chifu alimkatia tiketi ya kurudi kesho yake jioni ambayo hakuiafiki. Alitaka arudi siku ile ile.



    "Kuna ndege toka Kilimanjaro jioni", Willy alimuuliza kimwana mmoja kati ya vimwana walikuwa kwenye kaunta wakiwashughulikia wateja.



    "Hakuna ndege jioni, kuna inayoondoka saa tano na nusu hapa na kuondoka kule saa saba na dakika kumi basi', yule kimwana alijibu huku akimrembulia macho.



    "Hakuna ndege ya shirika lingine lolote?".



    "Hakuna, labda uchukuwe ya kukodi huko Tanzanair", kimwana alijibu kwa kebehi akijuwa kuwa Willy hawezi kumudu gharama za kukodi ndege.



    "Unaweza kunifanyia mpango ili hiyo ndege inichukuwe uwanja wa ndege wa Kilimanjaro saa kumi na mbili jioni?", Willy aliuliza katika hali ya kuomba.



    "Sisi haturuhusiwi, sisi tunahusika na kuuza tiketi za ATC tu", yule kimwana alijibu kwa wasiwasi. Willy alitoa kadi yake, na kumweleza. "Mimi ni mteja wenu mzuri sana. Nenda hapo Tanzanair kanikodishie, nitamtuma katibu mahsusi wangu, atakuja kukuona mkalipe na kwa kufanya kazi hiyo na wewe utapata chochote kwani hakuna kazi ya bure siku hizi. Wewe unaitwa nani?".



    Akiwa amepigwa na butwa yule msichana alijibu. "Naitwa Mariam".



    "Oke, Mariam fanya hiyo kazi kungali mapema, mimi naenda uwanjani kuwahi ndege yenu ya saa tano. Katibu wangu anaitwa Dudu, atakuja kumaliza mambo ya malipo na wewe".



    Kabla Mariam hajaanza kulalamika Willy alikuwa amekwisha nyanyuka na kuondoka.



    "Wanaume wengine utafikiri wana dawa. Huyu mwanaume kanitia butwa, sasa itanibidi nifanye hiyo kazi yake; nimeshindwa hata kupata mwanya wa kukataa", Mariam alimweleza mwenzake aliyekuwa amekaa karibu naye.



    "Hukuona macho yake! Akikuangalia tu roho inadunda, hiyo ndiyo dawa yake, ni mwanaume anayevutia sana, ana sumaku ya kiume, mwanamke hawezi kumkatalia kitu naye anajuwa hivyo", Husna alimjibu Mariam.



    Mariam aliondoka na kwenda kumtafutia Willy ndege huku kiroho chake kinarukaruka. "Sijui nitamwona tena yule mwanaume, kaniachia kadi yake, ngoja nitamtafuta", Mariam alifikiri huku akielekea ofisi za Tanzanair.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Willy Gamba alipofika ofisini kwake kwenye jengo la Sukari, Mtaa wa Ohio, ilikuwa saa nne na robo. Dudu aliangalia saa yake na kumwangalia Bosi wake kwa macho ya kumshitaki kuwa kachelewa.



    "Shikamoo bosi", Dudu alimsalimia Willy.



    "Marahaba, najuwa umeninunia kwani sikuwahi kutimiza miadi na wateja.



    "Kumbe unajuwa, na ukafanya makusudi", Dudu alijibu.



    "Siyo makusudi, ila ndiyo sababu kuna usemi kuwa, bosi hachelewi kazini, huwa amepita kwenye shughuli kadhaa wa kadha, nami nilipita kwenye shughuli kadha wa kadha. Sasa sikiliza, mimi naondoka kwenda Arusha kwa ndege ya ATC saa tano unusu, nina muda mfupi sana. Kumetokea dharura. Nataka nirudi leo jioni, maana dharura hii inaweza kunifanya nisafiri kwa muda wa wiki kadhaa nje ya nchi. Kwa vile ATC hawana ndege kutoka Kilimanjaro jioni, nimemuomba msichana mmoja aitwaye Mariam pale kwenye ofisi ya mauzo ya ATC anifanyie mpango wa ndege ndogo ya kukodi ya Tanzanair. Hivyo, uende ulipie na ndege iwe kwenye uwanja wa ndege wa Arusha saa kumi na mbili jioni, umeelewa?".



    "Nimeelewa bosi, naona kweli dharura, mpaka kukodi ndege, nani atalipia gharama hizi bosi?".



    "Nina mteja ambaye atalipia", Willy alijibu.



    Dudu alikwisha fanya kazi na Willy kwenye ofisi yao hii ya watu wawili kwa muda wa miaka mitatu. Hivyo alikwisha mwelewa vizuri Willy na alifurahi sana kufanya kazi na mtu sifa na mwenye roho nzuri kama Willy. Hata siku moja hakupata ugonjwa wa moyo toka kwa bosi wake huyu. Alikuwa mtu tofauti sana na watu wengine ambao Dudu aliwahi kufanya nao kazi.



    Baada ya kuacha kazi serikali, ambako alifanya kazi kama mpelelezi, na akawa mpelelezi wa kutegemewa si Tanzania tu bali Afrika nzima, Willy Gamba aliamua kuanzisha ofisi yake binafsi ya upelelezi, hasa iliyohusu mambo ya Bima. Aliamua kuacha kazi akiwa na umri mdogo wa miaka 42 tu. Kwa vile alitaka aoe kwani kazi yake serikalini ilimfanya asafiri sana nje, kitu ambacho kilimfanya asioe maana ndoa yake ingekuwa ya wasiwasi. Hivyo aliomba na kwa shingo upande na baada ya malumbano ya muda mrefu na waajiri wake huku akisaidiwa na Chifu ambaye alikuwa Bosi wake kabla hajastaafu, alikubaliwa kuacha kazi. Ndipo baada ya kuacha kazi, akamwoa mchumba wake ambaye alikuwa amesubiri kwa muda mrefu huku akimvumilia kwa safari zake nyingi.



    Huyu mchumba wake aliitwa Pepe. Pepe alikuwa mtoto wa watu, msichana aliyeumbika, mzuri wa sura na tabia, na kwa uzoefu wake mwingi kwa wasichana, Willy aliamua lazima amwoe Pepe na kila wakati alimwambia mama yake ambaye kila siku alikuwa akimpigia kelele aoe, na asipomuoa Pepe basi hataoa tena.



    Mama yake Willy alikuwa na wasiwasi sana na Pepe, kutokana na jinsi mtoto yule alivyokuwa mzuri wa sura. Alifikiri kuwa msichana mzuri kiasi kile hawezi kuwa mke wa nyumbani kwani lazima atakuwa na maringo. Lakini Mama yake Willy alikuwa kakosea kabisa. Huyu msichana alikuwa amelelewa kwao, wazazi wake walimlea kwa kumtayarisha ili aje awe mke wa mtu. Walimsomesha vizuri mpaka chuo kikuu, lakini walihakikisha kuwa Pepe anapata mafunzo ya namna ya kuishi na watu na maisha ya ndoa yanapewa kipaumbele. Na kweli pamoja na uzuri usioelezeka wa maumbile ya Pepe, tabia yake ilikuwa nzuri isiyoweza kuelezewa vilevile. Hii ndio inaonyesha kuwa tabia ya mtu haitokani na maumbile yake, bali zaidi inatokana na malezi.



    Hivyo, baada ya kuacha kazi, Willy alifanya vitu viwili kwa mara moja. Alianzisha ofisi yake binafsi na akamwoa Pepe. Na hii miaka yao mitatu ya ndoa ilikuwa miaka mitamu iliyojaa kila aina ya raha, starehe na mapenzi yasiyo kifani. Kila mtu aliyewaona na kujuwa walivyokuwa wanaishi, aliwaonea wivu.



    Dudu naye aliajiriwa na Willy alipofungua tu ofisi yake, Chifu ndiye aliyemtafutia mfanyakazi huyu. Hivyo hata ofisini kwake kazi zilifanyika vizuri na kwa uelewano mkubwa. Kweli Willy alikuwa hatoka nje ya Tanzania kikazi, ila tu kwa mapumziko ambayo alisafiri pamoja na Pepe wakitalii nchi nyingi sana, na kumwonyesha dunia ilivyo.



    "Kama ndege inaondoka saa tano na nusu itabidi uwahi maana siku hizi msururu wa magari kwenye barabara ya Nyerere ni hatari".



    "Kweli kabisa, niitie taksi, AVIS, na uwaeleze waje wanipokee jioni, kama yule dereva wao Ismail yupo ningependa aje yeye".



    Ofisi za AVIS zilikuwa ofisi mpya jijini Dar es Salaam na haikuwa mbali na ofisi za Willy. Tangu ianzishwe ilikuwa na uhusiano wa karibu na ofisi ya Willy vilevile meneja wao walikuwa rafiki wa Willy.



    "Pepe ana habari", Dudu aliuliza baada ya kuagiza taksi.



    "Hajui, na ndio maana ningependa nirudi jioni ili kama nitasafiri nje ya nchi nijuwe nitamwelezaje. Na maelezo ili yaeleweke usiku ndio mzuri, hasa mkiwa ndani ya shuka".



    "Au vipi", Dudu alidakia.



    "Hivyo akipiga simu mwambie nitachelewa kurudi nyumbani, huenda hadi saa mbili usiku. Pale shuleni kwao kama kawaida ya Dar es Salaam, simu bado haifanyi kazi".

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Nitamweleza baba, usiwe na wasiwasi".



    Taksi ilifika. Willy akachukua mkoba wake tayari kuelekea uwanja wa ndege.



    "Shikamoo", Ismail alimwamkia Willy.



    "Marahaba Ismail, maana sasa abiria tayari wana 'check-in' fanya kila njia sitaki kuachwa na ndege hii".



    "Inaondoka saa ngapi?".



    "Saa tano u-nusu".



    "Dakika hamsini zimebaki, utawahi acha mimi nifanye kazi yangu", Ismail alimjibu Willy wakaondoka. 



    Kweli Ismail aliijuwa kazi yake maana walipotoka kwenye jengo la Sukari aliingia Mtaa wa Ohio ili kukwepa msururu wa magari, akaingia Barabara ya Titi Mohamed, alipofika Mnazi Mmoja akaingia Mtaa wa Uhuru, halafu Lumbumba na kisha Mtaa wa Lindi tukatokea Ilala na kushika tena Mtaa wa Uhuru, tukaingia Barabara ya Nelson Mandela. Ndipo akashika Barabara ya Nyerere kwenye taa za Tazara, na ndani ya dakika ishirini tulikuwa Uwanja wa Ndege.



    "Asante Ismail", Willy aklimshukuru na kumkabidhi shilingi elfu moja kama asante. "Usisahau jioni?".



    "Nimeshaelezwa mzee, utanikutwa nakusubiri".



    Willy alijulikana sana na wafanyakazi wa ATC na Dahaco, kwenye kaunta ya kujiandikisha kabla ya kuondoka na kwa vile alikuwa na mkoba wake tu walimchukuwa mara moja na kulipia kodi ya kiwanja na kuelekea chumba cha kuondokea.



    Ndege ya Shirika la Ndege Tanzania ATC iliondoka Dar es Salaam saa tano na nusu kamili. Willy alikuwa na tiketi ya daraja la kwanza, na alipoingia ndani ya ndege akitafuta mahali pa kukaa alimwona mwalimu wake, mzee Petro Magoti, akimchekea.



    "Njoo ukae hapa Willy, habari za siku nyingi?".



    "Nzuri, shikamoo", Willy alijibu huku akiuweka mkoba wake chini ya kiti chake.



    "Marahaba, nimefurahi kukuona baada ya miaka kama mitatu hivi".



    "Asante mwalimu, unajuwa nilikwambia wakati tulipoonana Mwanza kuwa nilikuwa natarajia kuacha kazi ya kuajiriwa ili nijiajiri mwenyewe, sasa tayari nimefanya hivyo. Na pia sasa nimeoa.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Aha, hongera, nimefurahi sana nikisikia wanafunzi wangu mkiendelea vizuri", Mzee Magoti alijibu.



    Mzee Magoti alikuwa Mkuu wa Shule ya Sekondari ambako Willy alisoma. Kwa vile Willy alikuwa na akili nyingi sana darasani, walimu wengi walimpenda sana na kumheshimu. Hata wakati matokeo ya mtihani wa Cambridge wa darasa la kumi na mbili yalipotoka Willy alipata ushindi wa juu kuliko mwanafunzi mwingine yeyote katika Afrika Mashariki na hivyo kuiletea shule ya Mwalimu Magoti heshima kubwa. Kutokana na matokeo hayo mazuri hata Mwalimu Magoti alipandishwa cheo hata kushika nyadhifa mbalimbali katika Wizara ya Elimu hadi kufikia kuwa Kamishna wa Elimu. Na alipostaafu walimu walimchagua kuwa Mwenyekiti wa Chama chao kama miaka miwili iliyopita.



    "Nimekusikia ukiunguruma kwenye magazeti kuhusu matatizo ya walimu", Willy alimzungumzia.



    Ndege ilikuwa inaweka speed ili iruke. Hivyo kama ilivyo kwa abiria wengi wakati huu kila mtu hunyamaza kimya akingojea ndege ipae ndipo waendelee na mazungumzo.



    "Ndio kijana wangu, hali ni mbaya sana mashuleni mpaka sasa walimu wana mgomo baridi. Watoto hawasomi kabisa,  shule ambazo zinasemekana zinasoma, hasa zile za Sekondari, mwalimu anaweza kuingia darasani mara moja kwa wiki. Sasa utasema huku ni kusoma kweli, si hatari kwa maendeleo ya hawa vijana wetu ambao watakuwa viongozi wetu wa baadaye", Magoti alijibu.



    "Lakini mzee, wewe ukiwa kiongozi wa walimu si uzungumze nao waelewe athari za kufanya hivyo kwa taifa hili", Willy alimshauri.



    "Bwana mdogo, wewe unaweza kumshauri mtu mwenye njaa! Walimu hawa wote wana njaa, ndicho kilio chao. Mishahara ya serikali wewe mwenyewe unaijuwa. Na kutokana na kupanda kwa gharama za maisha, mshahara wa mwalimu wa kawaida anaweza kuutumia kwa siku tatu tu katika mwezi na ukaisha, je, siku ishirini na saba afanyeje?", Mzee Magoti aliuliza.



    "Lakini mzee hii inahusu watu wote walioajiriwa serikalini. Wote mishahara yao haitoshi", Willy alijibu.



    "Ahaa, sasa unasema. Yote hii inategemea unyeti wa kazi. Ili watu wajiongezee kipato wanahangaika na kufanya shughuli nyingine. Sasa hivi ukienda kwenye maofisi mengi ya serikali hukuti watu, ukiuliza katoka nje kikazi. Kweli kikazi, maana anakwenda kufanya kazi kwenye miradi yake binafsi, iwe kwenda kukamua ng'ombe wake maziwa au kuwatafutia majani, au iwe kwenda kununua bia kwenye kampuni ya bia ili apeleke kwenye kiduka chake pale nyumbani, yote wanasema kaenda nje kikazi. Sasa kwa mwalimu hahitaji kutoka. Mimi nimekuwa mwalimu karibu maisha yangu yote, ualimu ni kazi ambayo unahitaji saa ishirini na nne, siyo kazi unayoweza ukafanya na kazi nyingine, hutaweza kuifanya sawasawa, Saa hii unafundisha. saa hii unasahihisha kazi za wanafunzi, saa hii unatayarisha masomo kwa ajili ya kesho. Kweli kazi ya ualimu ni nyeti inayohitaji muda wako wote. Sasa walimu nao wanapofanya kama wafanyakazi wengine na kuwa na miradi matokeo yake ndio hayo! wanafunzi hawafundishwi", Mzee Magoti alieleza.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mhudumu wa ndani ya ndege alifika na kuwauliza watakunywa nini.



    "Mimi chai", Mzee Magoti alijibu.



    "Na mimi chai", Willy naye pia alijibu.



    "Msingependelea bia au pombe nyingine kali", yule msichana aliendelea kuwashawishi.



    "Hapana ni mapema mno", Mzee Magoti alijibu huku Willy akitingisha kichwa kukubaliana naye.



    Hata kama Willy angependa bia lakini haikuwa heshima mbele ya mzee aliyemheshimu kama huyu kufanya hivyo.



    "Haya, chai yenu inatengenezwa.



    "Asante", walijibu, tena kwa pamoja. Kisha wakaendelea na mazungumzo yao.



    "Sasa Mzee Magoti, si mmeieleza serikali na serikali inajuwa tatizo hili, na athari zake kwa taifa hili! Maana hawa vijana ndio taifa la kesho, na kama hawasomi ina maana karibuni tu tutakuwa na taifa la wajinga. Yaani wakati dunia inaingia kwenye karne ya ishirini na moja, elimu ndio kitu muhimu kwa taifa lolote, ili liweze kwenda sambamba na mataifa mengine katika sayansi na teknolojia: kama maneno unayosema ni kweli basi tuko hatarini", Willy alieleza mawazo yake kwa Mzee Magoti.



    "Maneno yako ni kweli kabisa kijana. Na hiki ndicho tunachopigia kelele sisi mpaka sasa hatuelewani na viongozi wakifikiri tunajaribu kuwachochea wananchi. Lakini viongozi wetu hawajali kabisa. Jibu lao kila siku ni kwamba hali ya uchumi ni mbaya, na serikali haina fedha. Lakini sababu kubwa kwa nini hawajali. ni kwa sababu wao na marafiki zao hawaathiriki na tatizo hili walimu hapa nchini, maana wao wanasomesha watoto wao nje. Hivyo hawajali kama watoto hawasomeshwi: wa kwao wanasoma nje na katika shule za hali ya juu", Mzee Magoti alijibu kwa uchungu sana.



    "Mzee Magoti umegusa kitu cha hatari sana. Yaani viongozi wetu wamekuwa na ubinafsi. Kwa vile wao wana pesa, basi wanapeleka watoto wao nje na hawajali nini kinawapata watoto wa wakulima na wafanyakazi, ambao hawana uwezo wa kupeleka watoto wao nje".



    "Barabara kabisa Willy, lakini zaidi ya hapo wanajenga tabaka la watawala na watawaliwa. Kwa vile watoto wa wakulima na wafanyakazi ambao ndio wengi katika nchi hii, watapata elimu duni, basi hawa watoto wa viongozi na matajiri ambao ni kama asilimia (2%) ya idadi ya watoto wote wa nchi hii, watarudi na elimu nzuri na hivyo ndivyo watakavyoshika madaraka hapo baadaye maana wao watakuwa wamesoma vizuri, na kama ulivyosema ndivyo wataenda sambamba na mataifa mengine. Hii ni hatari kubwa kwa taifa hili", Mzee Magoti alijibu tena kwa uchungu.

     

    "Ina maana viongozi wetu wanaiachia hali hii ya kushuka kwa kiwango cha elimu nchini kwa makusudi kabisa ili wawape watoto wao na wa matajiri nafasi ya kuendelea kuiongoza nchi hii, na kuwanyima watoto wa watu wa kawaida nafasi hii! Kama hii ni kweli, basi tunaelekea kubaya, maana katika nchi hii tangu uhuru watoto wa watu wa kawaida, ambao ndio sisi, serikali ilitupa nafasi nzuri na kutusaidia ili tuinuke na tuweze kuliondoa taifa katika ujinga na kuweza kuinua taifa na familia zetu kutoka katika hali duni", Willy alieleza.



    "Nchi imegeuka, ubinafsi umetawala roho za viongozi wetu, wanajifikiria wao tu. Si viongozi wa wananchi tena, ila wanatafuta uongozi kwa faida yao wenyewe. Hata ukiangalia ni viongozi wachache sana kwa sasa ambao sio matajiri. Wanaingia katika uongozi wakiwa hawana kitu, lakini baada ya muda mfupi unawakuta wamejilimbikizia mali. Afadhali wangefanya hivyo halafu wakaendelea kuwasaidia wananchi ili na wao hali zao ziinuke, la hasha, sera zao ni za kuwadidimiza wananchi wawe masikini pamoja na vizazi vyao ili wasiwe na sauti kabisa. Sauti wanataka ibaki yao na vizazi vyao ili wabaki madarakani kama vile wafalme.



    "Sikilizeni... tunakaribia kutua kwenye uwanja wa ndege wa Kilimanjaro. Mabibi na mabwana, inuweni viti vyenu wima, fungeni mikanda yenu ya viti tayari kwa kutua", sauti ya msichana ilisema.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Mzee, basi nitakutafuta ili unielimishe zaidi kuhusu mambo yalivyo katika nchi yetu hii kwa sasa, maana kwa muda mfupi huu nimeelimika kwa kiasi fulani", Willy alimweleza Mzee Magoti maana ndege ilikuwa inaelekea kutua na hivyo wasingekuwa na muda wa kuzungumza zaidi.



    Mzee Magoti alitoa kadi yake yenye anwani na simu.



    "Basi ukirudi Dar es Salaam, nipigie simu tuonane".



    "Asante Mzee".



    Ndege ilipogusa chini wote wakawa kimya mpaka iliposimama kabisa.



    "Haya kwe heri Mzee Magoti", Willy alimpa mkono. Akachukuwa mkoba wake na akawa wa kwanza kutoka. Alipoiangalia saa yake ilikuwa saa sita na nusu mchana .



    Willy aliposhuka kutoka ndani ya ndege, alimkuta Musoke anamsubiri.



    "Shikamoo".



    "Marahaba, habari za siku nyingi, haujabadirika bado, ila umetia uzito kidogo", Musoke alimweleza Willy.



    "Asante, unajua nimeoa, sasa mapochopocho yananimaliza". Wote walicheka na kuelekea kwenye gari ambalo lilikuwa la kukodi lakini Mzee Musoke alikuwa analiendesha mwenyewe.



    "Nimefurahi sana umekubali wito".



    "Unajua tena Chifu, ni vigumu sana kumkatalia kitu, hasa anachokiamini yeye kuwa ni kitu muhimu".



    "Najua, lakini lazima nikushukuru", Musoke alijibu huku kiroho kikizidi kumdunda kwa furaha kwa kuwa na uhakika kuwa Willy yuko naye tayari kwenda kutekeleza kazi hii nyeti, ambayo inaweza kuleta ufumbuzi mkubwa kwa mataifa ya Afrika.



    TAFUTA UKWELI



    Ilikuwa yapata saa saba unusu. Musoke na Willy walipofika nyumbani kwa Temu. Walimkuta Temu akitembeatembea mbele ya nyumba yake katika bustani huku ameweka mikono yake nyuma. Kwa vile nyumba ilikuwa juu kwenye kilima, na wao walimwona kabla hajawaona mpaka walipopiga honi ya gari ili kufunguliwa lango la mbele. Alipoona ni gari la kukodi la Musoke, mara moja alikimbia na kulifungua lile lango hata askari wake anayelinda nyumba yake hakuwahi mbio za mzee huyu. Hii yote ilionyesha shauku aliyokuwa nayo Temu juu ya suala hili la Rwanda.



    "Shikamoo", Willy alimshalimia.



    "Marahaba, karibu".



    Temu alipeana nao mikono na wote na kuwakaribisha kule uani kwenye bustani ya nyumba.



    "Wengine?", Musoke aliuliza.



    "Saa nane watafika".



    "Vizuri".



    Walipokuwa wameketi kule uawani kwenye kivuli kizuri cha miti, Musoke alitumia nafasi hiyo kuwafahamisha.



    "Bwana Temu, huyu ni kijana wetu, anaitwa Willy Gamba, sasa hivi anafanyakazi za kujitegemea, lakini alikuwa kwenye idara ya upelelezi ya Tanzania kabla hajaamua kuacha kazi ili ajitegemee. Yeye ameombwa na marafiki zetu wengine aje atusaidie kwenye hili tatizo letu", Musoke alieleza huku Temu akionekana kushikwa na butwaa.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Na bwana Gamba, huyu ni mzee Temu na ndiye Mkuu wa PAM upande wa Tanzania.



    Willy aliinuka na kumpa Temu mkono.



    "Mimi siamini macho na masikio yangu", Temu aliendelea kuonyesha kama mtu aliyeshituka sana. "Hivi kweli Willy Gamba yupo! na ni wewe! Hivi ni kweli baba yangu, ni kweli. Mimi siku zote husikia habari za Willy Gamba na huamini kuwa ni hadithi tu, maana mambo ambayo ameyafanya wakati wa ukombozi wa nchi zilizo kusini mwa Afrika tulifikiri ni propaganda tu ya kamati ya ukombozi ya OAU. Kumbe mtu mwenyewe upo na ni kweli. Eehe, ama kweli kuishi kwingi kuona mengi. Basi bwana Musoke, kazi yetu itafanikiwa", Temu alieleza.



    "Huyu kijana wetu Mwenyezi Mungu amemjaalia uwezo mkubwa sana katika kazi hii ya upelelezi. Hakuna mtu unayeweza kumlinganisha naye hapa Afrika, sijui huko Ulaya, lakini hata majasusi wa huko Ulaya ndiye aliyekuwa akiyakomesha wakati wote huo. Kwa kweli hata mimi niliposikia amekubali na ni yeye anayekuja basi roho yangu ilitulia, najuwa tutafanikiwa. Hivi kwanini wamekukubalia kustaafu mapema hivi?", Musoke alimuuliza Willy lakini kabla ya kujibu, mhudumu wa pale nyumbani alifika na kutaka kujuwa watakunywa nini.



    "Bwana Gamba unataka kunywa nini?, kunywa kitu kidogo, maana huko ndani wanatengeneza chochote cha mchana, sisi wachaga ndizi ndicho chakula chetu, sijui wewe utapendelea?", Temu aliuliza.



    "Kinywaji naomba klabu soda, na nitafurahia sana macharari", Willy alijibu huku Temu akicheka na kufurahi kusikia macharari.



    "Kumbe unayajuwa eeh basi baba yangu tutakula hayo maana wanaandaa. Na wewe mzee Musoke?".



    "Mimi nitakunywa ki-wiski kidogo, unajuwa sisi wazee lazima ushituwe damu kidogo upate joto".



    "Sawa kabisa, nenda kalete haraka", Temu alimwagiza mhudumu wake.



    "Ehe Willy, kwanini umeruhusiwa kustaafu mapema hivi?, au kwa sababu ya Afrika Kusini kupata uhuru?", Musoke aliuliza tena.



    "Hapana, mimi niliomba kustaafu ili niweze kuoa na kuanza maisha ya kifamilia maana kazi hii haifai kama umeoa na una familia. Sasa hivi nimeoa na mke wangu ni mjamzito. Na hata kazi hii nimekubali tu, kwanza kwa sababu na mimi nimeumwa sana na hali hii ya mauaji ya Rwanda na pili kwa sababu Chifu alisema nisipokwenda mimi atakwenda yeye. Na unajuwa bwana Musoke, mimi nisingependa hata kidogo kuruhusu kitu kama hicho".



    "Ni kweli kazi hii inahitaji kuweka mawazo yako pamoja, usiwe na fikira zingine, lakini ndivyo hivyo, taifa bado linakuhitaji mara kwa mara kama hivi, ingawaje si sana kama ulivyokuwa jikoni", Musoke alikubaliana na Willy. Mara wakaona wenzao wengine wanaingia na wote wakasimama kuwasalimia.



    Temu alichukuwa nafasi ya kuwafahamishe wenzake kwa Willy Gamba. "Hawa ni wana PAM kutoka sehemu mbalimbali za Afrika. Na wamekuja kwa ajili ya kikao hiki cha kutathimini jinsi mambo yalivyokuwa huko Rwanda. Huyu ni bwana Kimani kutoka Kenya, huyo ni Abakusi toka Nigeria, huyu ni Makwega toka Zambia na huyu kijana mwenzio ni Malisa kutoka hapa hapa Tanzania". Kisha akageuka na kumgusa Willy. "Na huyu ndiye mgeni tuliyemtarajia kwa ajili ya kazi yetu. Bwana Willy Gamba.



    Kimani na Malisa waliwahi kusikia habari zake nao walishikwa na mshangao kama wa Temu. Musoko alitumia nafasi hiyo kunong'ona na Abakusi na Makwega kuwaeleza Willy Gamba hasa alikuwa mtu wa sifa za namna gani. Bila hata kusema mengi, alipoeleza kazi zake mbili alizofanya na kuutingisha ulimwengu kwa kuwazuia majasusi wa Afrika Kusini tayari wote wakamtambua na kupigwa na butwaa vilevile.



    "Wakati mwingine binadamu akili inashindwa kuamini kitu. Mimi nilisikia jinsi mpelelezi wa Afrika alivyoyaangamiza majasusi kule Kinsasa, Zaire, na nikaamini kuwa zilikuwa hadithi tu. Sasa namuona hapa mtu mwenyewe, akili inashindwa kuamini. Inashangaza", Abakusi alisema.



    "Kama Willy Gamba ndiye huyu kijana, basi mambo yetu yameiva", Makwega naye alinena na kutokwa na wasiwasi aliokuwa nao usiku.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Bila kupoteza muda mkutano uliendelea huku wakipata huduma za vinywaji na chakula.



    "Nafikiri wasiwasi wetu wote sasa umepungua baada ya kumpata kijana huyu?", Musoke alisema kama vile akitoa maoni ya mkutano.



    Wote walitingisha vichwa kama ishara ya kukubali.



    Kwa vile kijana huyu yuko hapa, tumpe maelezo tunataka atufanyie nini. Nafikiri mimi niendelee na kama mtu ataona nimepwelea mahala naomba asisite kuongezea, sawa".



    "Sawa", wote walimjibu mzee Musoke.



    "Bwana Willy, wewe mwenyewe naami unazo habari nyingi kuhusu matukio ya Rwanda. Ila sisi, kama wana PAM tungetaka tupate undani zaidi wa mambo yalivyotokea huko Rwanda mpaka yakafikia yalipofikia na watu zaidi ya milioni moja katika nchi ya watu milioni tano kuteketezwa kwa siku kadhaa tu. Kitu hiki kinatisha na kama hakiwezi kuangaliwa kwa undani na kuthibitiwa inaweza kutokea tena si Rwanda tu bali hata mahali pengine Afrika. Sijui unanielewa?", Musoke alimuuliza Willy.



    "Nakuelewa, ila nataka nijie ni nini hasa mnataka mimi nifanye maana kule sasa kuna serikali ya RPF, kuna mashirika ya kimataifa, kuna mashirika yanayotetea haki za binadamu, mnafikiri mimi nitafanya nini zaidi ya watu hawa na wenye uwezo na mapesa mengi nyuma yao, maana na wao wanachunguza kwa kina maovu yaliyotendeka Rwanda", Willy alisema akitaka ufafanuzi zaidi.



    "Sawa bwana Gamba, kitu tunachotaka sisi ni uchunguzi wetu wenyewe. Hawa watu wengine wote wanaweza kuwa na nia zao tofauti. Serikali ya RPF ni mhusika kwa kiasi fulani. hatuwezi kupata ukweli asilimia mia toka kwao. Mashirika ya kimataifa yenyewe yanaweza kuwa na ajenda tofauti, tena wanaweza kutoa ripoti kutokana na ajenda yao. Wanaotetea haki za binadamu nao wana mtazamo wao kwa maana ya kuonyesha kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa haki za binadamu Rwanda. Sisi tunataka uende zaidi ya pale, ujue kama haki za binadamu zilikiukwa, na kwa nini zilikiukwa, lazima kuna sababu. Mauajiyaliyotokea nini kiini chake, maana yanaonekana yalikuwa yamepangwa toka mapema. Na vilevile kwanini Afrika na dunia kwa ujumla, ikiwa kimya pamoja na nchi jirani kama Uganda, Tanzania, Zaire na Burundi hazikufanya chochote kuzuia mauaji haya. Tukishajuwa chanzo na sababu zilizofanya mpaka binadamu akafikia kuwa mbaya kuliko mnyama, nafikiri tutakuwa tumejifunza; na hili fundisho litatusaidia kuweka mkakati wa kuzuia kitu kama hicho kitakapotokea. Vilevile tujue namna ya kukidhibiti kabla hakijaleta maafa makubwa kama haya", Musoke alijibu.



    "Oke, nimeelewa nini mnataka, nitajitahidi niweze kuchimbua mambo uliyoyataja hapo ili nipate vyanzo vyake", Willy alijibu.



    "Lakini haitakuwa kazi lahisi, lazima uwe macho maana ukweli wa mambo haya unaweza kuwa na athari nyingi kwa watu mbalimbali ndani ya Rwanda na pengineko duniani. Kwa hiyo ikijulikana kuwa kuna mtu anatafuta ukweli na ikaonekana kuwa ataupata, basi ujuwe masiha yako yanaweza kuwa hatarini maana mpaka sasa tunaamini kuna watu wanajaribu kufukia ukweli usijulikane. Na hawa watu watakuwa watu hatari. Tafadhali, hadhari ni lazima", Abakusi alimwasa Willy.



    "Nitalitazama hilo", Willy alijibu na kuendelea, "Na malipo yangu yatalipwaje, maana sasa ni mfanyabiashara na si mfanyakazi wa serikali tena. Kazi hii nimeichukua binafsi".



    "Malipo utalipwa na PAM. Kwa ajili ya kazi hii PAM iliwaomba michango wafanyabiashara wa kiafrika ambao wanaunga mkono msimamo wa PAM na wametoa michango mizuri sana na tukitoka hapa tutapitia hotelini kwangu nikupatie malipo yako. Sijui utahitaji kiasi gani?", Musoke aliuliza.



    "Mimi vilevile, kama nilivyosema, naunga mkono madhumuni ya PAM, kwani ni mpaka pale Mwafrika atakapojitambua kuwa lazima azungumze na Waafrika wenzake kupambana na ukoloni mambo leo ndipo atakapokuwa amejikomboa kutoka katika umasikini, ujinga na maradh. Kwa jinsi hiyo na mimi nikiwa mshabiki wa PAM nitaomba nilipwe gharama zangu tu nitakazotumia, lakini utaalamu wangu nautoa bure".



    Makofi na kupeana mikono ya shukrani vilisikika.



    "Sijui hii kazi unafikiri itachukuwa muda gani?", Kimani aliuliza.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Mimi nitawafanyia kazi, nipeni muda", Willy alijibu.



    "Wiki mbili?", Makwega aliuliza pia.



    "Nitajitahidi".



    "Basi tuonane hapa baada ya wiki mbili", Musoke aliagiza.



    "Sawa".



    "Lakini Willy Gamba atakuwa anawasiliana na mimi Kampala kwa kila hatua atakayofikia. Kama ikionekana kazi inakuwa bado baada ya hizo wiki mbili, nitawajulisha", Musoke alieleza.



    "Sawa".



    "Haya, asanteni sana wazee, tutaonana Mwenyezi Mungu akitujaalia baada ya wiki mbili. Sasa hivi ngoja niende na mzee Musoke akanikamilishie masuala ya mapesa", Willy aliaga huku akiwachekesha.



    "Nilitaka kusahau. Tumekupatia nafasi ya kulala Impala, ukienda tu pale mapokezi watakupa funguo, tumelipia kila kitu, kazi kwako. Sijui kama utahitaji usafiri kesho kukupeleka uwanja wa ndege?", Temu alieleza na kuuliza.



    "Hapana, nitajitegemea kwenda uwanja wa ndege".



    Musoke alipoangalia saa ilikuwa saa kumi na nusu. Willy alipewa mkono wa heri na wajumbe wa PAM huku kila mmoja akimwombea mafanikio na usalama. Willy aliupokea mkono huo wa heri huku naye kimoyomoyo akiomba sala zao ziwe pamoja naye, kwani hawa walikuwa watu wenye roho za ubinadamu, ambao walikuwa wakitumia muda wao kujaribu kuwasaidia wengine bila malipo ya aina yoyote. Kweli Mungu awabariki.



    Musoke na Willy aliondoka, wakaelekea Maunt Meru.



    "Kesho umesema ndege saa ngapi?", Musoke alimwuliza Willy.



    "Saa tatu asubuhi".



    "Nije nikupeleke?".



    "Hapana, nina marafiki wengi hapa watanipeleka".



    "Na leo jioni tunaweza kula pamoja?", Musoke alimkaribisha chakula cha usiku.



    "Hapana, nitakwenda kwa dada yangu jioni, alifiwa na mjukuu wake na nilikuwa sijapata nafasi ya kumsalimia na hii ndio nafasi pekee niliyopata".



    "Umeua ndege wawili kwa jiwe moja".



    "Bila shaka", Willy alijibu huku akijuwa kabisa kuwa angeondoka jioni ile. Willy kama kawaida yake, aliendelea kuonyesha kama angelala Arusha. Hii inaonyesha jinsi ambavyo Willy hamwamini mtu yeyote mara akishakuwa kazini.



    "Huwezi kujuwa, kikulacho ki nguoni mwako, uzoefu wa siku nyingi umenifundisha", Willy alijisemea moyoni.



    Walipofika Hoteli ya Mount Meru, walikwenda chumbani kwa Musoke na kuanza kuelezana tena. Kwa vile Musoke naye alikuwa na uzoefu wa siku nyingi na kazi ya upelelezi alijuwa Willy angetaka nini.



    "Bwana Gamba, unajuwa kazi hii inaweza ikawa ngumu na ya hatari kuliko hata jinsi tunavyotegemea. Hivyo, jitayarishe kwa yote, nadhani unanielewa?", Musoke alimwuliza.



    "Nakuelewa sana, kazi hii naichukulia uzito uleule wa kawaida, sintaipuuza hata chembe. Kwa kawaida uzoefu umenionyesha kuwa kwa kawaida kazi rahisi ndio hugeuka kuwa ngumu sana".

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Vizuri, mimi ninao wenyeji kule Rwanda, ambao nafikiri wanaweza kukusaidia kupata fununu za awali", Musoke alisema na kufungua mkoba wake na kutoa kitabu chake cha anuani. "Yuko rafiki yangu ambaye kwa miaka amekuwa akiipinga siasa ya chama cha MRND. Yeye ni mwanajeshi. Alikuwa kamanda katika jeshi la kumlinda Rais, lakini kwa vile hakukubaliana na sera yao, aliacha na kuanza kwa siri kueneza habari kwa vyombo vinavyotetea haki za binadamu jinsi serikali ya Rwanda ilivyokuwa inavunja haki za binadamu nchini humo. Wakati Rais alipouawa Aprili 6, 1994, yeye alikuwa Nairobi kuonana na Katibu wa Chama cha kutetea Haki za Binadamu ulimwenguni. Hata hivyo, huku nyuma mke wake na watoto wake sita na wapwa wake wawili, wote waliuawa tarehe 7, Aprili. Hii ina maana angekuwepo Kigali na yey vilevile leo angekuwa marehemu. Anakaa Kimihurura nyumba namba 168. Simu yake kwa bahati ni moja ya chache zinazofanyakazi sasa hivi na ni namba 50486. Yeye ni Mhutu.



    "Umeishazungumza naye?", Willy aliuliza.



    "Nitazubumza naye, tuna uelewano mzuri, na yeye anajuwa mengi kwa watu wachache waliokuwa wanaipinga serikali waliobaki. Na ujuwe huyu mtu alikuwa karibu sana na serikali ya Rwanda, na huenda karibu sana na Rais mpaka kufikia kuwa kamanda wa jeshi lake. Hivyo, anajuwa serikali ilivyoondolewa madarakani na RPF vizuri sana, na ndio sababu vilevile kumtafuta ili kumuua ili kuua ukweli wa mambo".



    "Vizuri, nikifika Rwanda nitamtafuta kama nitamhitaji".



    "Tumekupangia kwenye hoteli iitwayo Des Mille Collines. Hoteli hii ni maarufu maana wakati wa mauaji watu wengi, hasa wa mataifa ya nje, walijificha hapa na hivyo hata wanyarwanda waliokuwa wanatafuta ili kuuawa kati ya walionusurika ni wale waliobahatika kufika hoteli hapo. Hivyo, nayo itakupa fursa nzuri kupata fununu mbalimbali.



    Vilevile ningependa umwone Padre mmoja ambaye tunafahamiana na yeye alinusurika kimiujiza baada ya mapadri, maburuda , watawa na watu wote waliokuwa kwenye kituo hicho cha dini kiitwacho Centre Christus, kuuawa na Wahutu wenye siasa kali. Padri huyu anaitwa Jean Marie Karangwa. Utapata mengi toka kwake vilevile".



    "Bado yuko kwenye kituo hicho?", Willy aliuliza.



    "Ndio yupo, na anajaribu kukianzisha upya. Na wa mwisho ambaye ningependa umwone ikiwa unahitaji msaada, maana huwezi kujuwa, unaweza kuwa kwenye hatari ambayo inahitaji msaada wa kiserikali, hasa kijeshi. Huyu ni rafiki yangu saana, tumekaa naye jirani mjini Kampala na ni mmoja wa makamanda wa RPF, mtu shupavu kama wewe na msomi kama wewe na kijana wa rika lako. Naamini mkionana mtashibana tu. ana roho safi sana. Anaitwa Col Thomas Rwivanga, namba yake ya simu 60314".



    "Asante, nikihitaji msaada wake nitamtafuta", Willy alijibu.



    "Utaondoka lini na kwa njia gani?", Musoke aliuliza.



    "Mimi kesho kutwa nitakutafuta Kampala nikiwa Kigali kukujulisha nimefika".



    Musoke hakuuliza zaidi maana alielewa maana yake. Kisha akatoa bahasha kubwa iliyokuwa na pesa za dola za Kimarekani. Idadi yake haikuzungumzwa, lakini bila shaka ilikuwa maelfu ya madola.



    Baada ya kumpa mzigo huo walisimama na kuagana.



    "Haya, nakutakia safari njema na kazi njema. Nakuombea heri", Musoke alimshika mkono akionyesha uchungu kidogo.



    "Asante sana, tuombe Mungu", Willy alijibu na kuondoka.



    Willy alipoachana na Musoke alikodi teksi pale nje ya Mount Meru Hotel na kuelekea Impala. Alipofika Impala alijitambulisha. "Naamini nina nafasi ya chumba hapa, naitwa Willy Gamba.



    Msichana wa mapokezi aliangalia kwenye orodha yake ya majina kisha akaliona jina la Willy Gamba.



    "Ndio baba, chumba 212", alijibu huku akitoa funguo na kumkabidhi.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Una mizigo?".



    "Hapana, huu mkoba wangu una kila kitu".



    "Kila kitu?".



    "Kila kitu nakuambia, utashangaa nikiufungua, mrembo zaidi yako atatokea".



    Yule msichana akacheka na Willy akapandisha ngazi.  Alikifungua chumba na kukuta kidogo lakini kizuri sana. Aliangalia saa yake akaona ilikuwa saa kumi na mbili kasoro robo.



    Alikwenda kitandani akatoa blanketi,  akaliweka pembeni na kufunua shuka na kutengeneza kama kwamba kulikuwa na mtu aliyelala pale.  Kisha, akauweka ufunguo kwenye kufuli la mlango kwa ndani, akachukua mkoba wake.  Akafungua mlango na kuurudisha bila kuufunga na funguo kwa vile aliziacha ndani makusudi na kutelemka chini.  Alipoangalia pale mapokezi na kuona wapokeaji wapo shughulini,  alichepuka na kutoka nje. Akelekea kwenye maegesho ya teksi na kukodi teksi kuelekea uwanja wa ndege wa Arusha.



    Ilikuwa yapata saa kumi na mbili na robo alipofika uwanja wa ndege na kukuta ndege imeshatua tayari. Rubani wa ndege alimfuata na kumpokea mkoba wake.



    "Habari za jioni?", Rubani alimshalimia.



    "Za jioni nzuri asante".



    "Huna mzigo zaidi?".



    Sina,  ni huo huo".



    Rubani aliufungua mlango wa ndege hii ya Tanzanair,  aina ya Cessina Mark 4, na kumkaribisha abiria wake huyu mmoja, ambaye walikaa pamoja kwenye viti vya mbele, na kisha akawasha injini  za ndege, na kuruka.



    Baada ya Musoke na Willy Gamba kuondoka nyumbani kwa Temu, kila mtu alitawanyika kuelekea kwenye hoteli yake.



    Malisa aliyekuja kwenye mkutano huo akitokea Dar es Salaam, alikuwa amefikia Hoteli ya Sabasaba. Alijulikana sana katika kundi la wasomi na kiserikali alikuwa mmoja wa watu waliokuwa mstari wa mbele katika kupigania kuwepo Umoja wa Afrika. Hata maafisa wa ngazi za juu serikalini mara nyingi walitafuta ushauri kwake kila walipotaka kuzungumzia swala la Umoja wa Afrika.



    Malisa alikuwa msomi na Mhadhili wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika kitivo cha Sayansi ya Jamii. Mara hii alipokuwa anakuja kwenye mkutano huu Arusha, Afisa mmoja wa ngazi za juu kabisa serikalini alimwomba amweleze mazungumzo na makubaliano ya mkutano wao, kwani serikali ilipenda kujuwa mambo gani PAM inafikiria kuhusu tatizo la Rwanda ili serikali nayo iweze kusaidia. Huyu Afisa wa serikali alimpa namba zake za simu za nyumbani na kumwomba ampigie baada tu ya mkutano.



    Malisa alipofika Hotelini tu, ikawa yapata saa kumi na mbili na robo, alichukua ufunguo wa chumba chake mapokezi na kueleka chumbani. Alipofika chumbani alimwomba opereta wa simu pale hotelini ampatie simu ya Dar es Salaam na kumpa namba.



    "Subiri kidogo nitakuita", opereta alimwambia.



    "Haya asante, lakini nifanyie haraka maana nataka kutoka nina miadi", Malisa alimwomba opereta.



    "Sasa hivi", aliambiwa.



    Baada ya muda si mrefu simu iliita chumbani kwa Malisa.



    "Hallo".



    "Namba yako ya Dar es Salaam inaita", opereta alijibu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Haya asante", na akaunganishwa na namba hiyo ya Dar es Salaam ambayo iliendelea kuita.



    "Hallo", mtu aliitikia baada ya muda kidogo.



    "Hapa ni Arusha, mzee yupo?", Malisa aliuliza.



    "Yupo, subiri".



    Na baada ya muda kidogo akasikia, "Hallo, nani mwenzangu?".



    "Malisa hapa, shikamoo".



    "Marahaba, habari ya huko?".



    "Salama".



    "Vipi mkutano".



    "Tumemaliza".



    "Ehee, hebu nipe maazimio yenu kwani wazee huku wana shauku ya kusikia".



    "Haya tega sikio nikueleze, mambo ni mazuri sana", Malisa alijibu na kumweleza mambo yote tokea mwanzo mpaka mwisho.



    "Hizo ni habari njema", yule afisa alijibu na kuendelea. "Willy Gamba ni kijana wetu na ni mtu shupavu. Kwa hakika ataifanikisha hiyo kazi. Na mimi nitawaeleza wazee naamini wataridhika na hatua mliyochukuwa. Mnajua sisi kama serikali ni vigumu kuchukua hatua yoyote dhidi ya nchi nyingine, lakini nyinyi mkiwa umoja usio wa kiserikali mnaweza kutusaidia sana kwa mambo kama haya. Willy amefikia wapi?".



    "Yuko hoteli ya Impala chumba namba 212. Huenda mzee si vizuri kumpigia simu sasa hivi tu atashituka", Malisa alijibu.



    "Na kweli, ingawa ni kijana wetu basi tuache nyinyi muendelee nae. Asante sana kwa kazi nzuri, na mwanzo mzuri, watu wenye uchungu na Afrika kama nyinyi ndio mtakaoisogeza Afrika mbele katika kuleta maendeleo wakati tukielekea katika karne ya sayansi na teknolojia. Asante sana", yule afisa wa serikali alijibu na kukata simu.



    Bila kujua alichokuwa amefanya, Malisa alifurahi sana kusikia sifa alizozitoa mtu huyu mashuhuri katika serikali ya Tanzania, kwa umoja wao. Minongono mingi jijini Dar es Salaam ilikuwa ni kwamba afisa huyu, ambaye watu wengi walipenda kumwita kwa kifupi tu kama 'JKS' alitegemewa kugombea Urais baada ya muda wa Rais wa sasa kumalizika.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya kukata simu ya Malisa tu, JKS alipiga simu nyingine. Mara hii ilikuwa simu ya masafa marefu, alipga Paris, Ufaransa. Na mara moja ikaitikiwa.



    "Hallo, naomba kuzungumza na Jean Yves Francois".



    "Subiri kidogo", alijibiwa.



    "Hallo Francois, nani anaita?".



    "Yaani huwezi kutambua sauti".



    "Ah JKS. Ehe, nipe habari".



    "Habari nzuri, sijui wewe huko?".



    "Huku salama, tunasubiri tu kwa hamu kusikia Umoja wa Mataifa mahakama ya mauaji ya Rwanda ianze lini".



    "Nasikia itaanza miezi minne ijayo huko Arusha".



    "Aha, majina?", Jean aliuliza.



    "Majina ni yaleyale mpaka sasa".



    "Kwa hiyo upande wa watu wetu hakuna aliyeguswa?".



    "Bado kabisa, ila kumetokea hali ambayo inaweza kutuletea madhara".



    "Hali gani?", Jean alihoji kwa shauku.



    "Unakumbuka niliwahi kukueleza juu ya chama kiitwacho kwa kifupi PAM?", alimwuliza.



    "Nakikumbuka na nimekitafiti vilevile kujua msimamo wake. Wanachama wake wanapigania umoja wa waafrika ili kuleta haraka uhuru wa watu weusi dhidi ya ukoloni mambo leo, ili watu weusi waweze kujiamulia mambo yao wenyewe. Na vilevile walikuwa mojawapo ya makundi yaliyotoa shinikizo katika mkutano wa Arusha ili mgogoro wa Rwanda umalizike kwa njia ya amani. Hata mkutano wa Algers, walikuwepo wawakilishi wao, niliwaona maana nilikuwepo. Haya sema watu kama hawa wanaweza kuleta madhara gani?", Jean aliuliza.



    "Wanaweza kuleta madhara makubwa sana", JKS alimjibu na kisha akaanza kueleza kwa kirefu jinsi Malisa alivyomweleza, na hatua ambazo tayari zilikuwa zimechukuliwa.



    "Huyu Willy Gamba ni hatari, anaweza kuchambua kila kitu mpaka akafikia ukweli unaweza kukugusa hata wewe", JKS aliasa.



    "Lililopo ni kuzuia asiende", Jean alijibu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    "Tutamzuia vipi na hayuko chini yetu?", JKS aliuliza.



    "Mbona huelewi, kwani maiti inasafiri?".



    "Aha, sasa nimekuelewa, lakini hiyo ni kazi kubwa", JKS alijibu.



    "Hiyo ni kazi ndogo kabisa, si umeeleza kuwa mtu wako ameeleza kuwa leo huyo Willy Gamba analala Arusha. Hotel ya Impala na chumba amekupa namba zake, au sikukuelewa vizuri?", Jean aliuliza.



    "Ni sawa kabisa, alinipa kila habari bila kuelewa maana yake, na mimi aliponieleza sikuelewa habari hiyo itakuwa muhimu", JKS alijibu.



    "Hiyo ilikuwa muhimu sana. Unakumbuka kuwa tuna watu wetu kule Arusha, ambao walikuwa wasafiri na Rais aliyeuawa, lakini kwa ajili ya ujumbe wa Rais wa Burundi hawakwenda na wapo kule Arusha kama wageni wa serikali yako?", Jean aliuliza katika hali ya kukumbusha.



    "Hao! hata juzi nilizungumza na kiongozi wao maana alikuwa ametokea Ngala kwenda makambi ya wakimbizi wa Rwanda kwa ajili ya kuwachukuwa vijana kumi muhimu ambao waliingia Tanzania baada ya kufunga kazi kule Rwanda. Alikuwa anataka msaada wangu kwa ajili ya makazi, nami nimewafanyia mpango katika nyumba za mashirika ya serikali pale Arusha na sasa wako salama salimini", JKS alijibu.



    "Hiyo ni kazi nzuri sana. Kwa kazi hiyo na kwa habari ulizonipa leo, nitapeleka dola za kimarekani elfu ishirini kwenye akaunti yako kule Uswisi, kufika kesho jioni pesa zitakuwa zimeingia. Na kama kazi hii ya usiku ikifanikiwa dola zingine elfu ishirini zitapelekwa", Jean alimweleza JKS.



    "Asante sana, nami nitafanya kazi kwa upande wangu. Nitampigia simu kiongozi wao hapo Arusha, Bwana Phillipe Habimana, atume vijana wawili waimalize hiyo kazi. Umeshatoa agizo, na agizo lako litatimizwa", JKS alijigamba.



    "Oke, vizuri; unajuwa vijana wetu wana ujuzi wa hali ya juu, na swala la kuua kwako si swala tena la maana wameishaua sana kiasi kwamba kuua kwao sasa ni sawa na kunywa chai", Jean alijibu huku akiangua kicheko cha kejeli.



    "Tena sana, juzi tu kwenye kambi huko Ngala wamemaliza kuua vikaragosi vinavyojipendekeza kwenye serikali mpya, kwa kuwashawishi wakimbizi waanze kurudi ili ionekane serikali ya sasa imeshaleta amani na usalama Rwanda ili iweze kuungwa mkono na jumuia za kimataifa. Ni baada tu ya kumaliza hiyo kazi ndipo Phillipe alipokwenda kuwachukuwa kwa msaada wangu. Hivyo, nikiwaagiza leo, hakika huyu Willy ajihesabu ni marehemu maana bado wana mori kabisa", JKS alijibu.



    "Haya basi, nipigie simu kesho, baada ya kumaliza hiyo kazi. Na kama ukisikia habari zingine zozote, fanya kama kawaida na mimi nitafanya kama kawaida yangu", Jean alijibu na kukata simu.



    Jean na JKS walikuwa wanafahamiana yapata miaka mitano sasa. Uhusiano wao ulianza wakati JKS alipokuwa na wadhifa wa kuamua juu ya ununuzi wa silaha mbalimbali zilizokuwa zinahitajiwa na serikali ya Tanzania. Jean Yvers Francois alikuwa kijana bado yapata miaka therathini na minane, na alikuwa tayari mfanyabiashara maarufu sana duniani. Alikuwa akifanya biashara ya kuuza silaha katika nchi zinazoendelea, na alimudu sana kupata biashara hiyo kwa urahisi kwa vile watu wengi walisema kuwa alikuwa mtoto wa kiongozi wa ngazi za juu kabisa katika serikali ya Ufaransa.



    Kwa kutumia wadhifa wa baba yake na umaarufu aliokuwa nao baba yake katika nchi zinazoendelea, kijana huyu hakukosa biashara hii ya silaha na biashara nyinginezo zilizokuwa zikipita mbele yake. Lakini vilevile alinong'onwa kuwa, kijana huyu alijua kuwazawadia waliompa biashara, hasa viongozi wa ngazi za juu katika nchi za Kiafrika. Kutokana na sifa hii ya kutoa asilimia kumi na zawadi zingine, kijana huyu alikuwa akitafutwa na biashara badala ya yeye kuzitafuta hata ikasemekana kwamba viongozi fulanifulani wa nchi za Kiafrika iliwabidi wazungumze naye kwanza kabla hawajatoa maamuzi yoyote muhimu ya kibiashara.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Kwa hiyo, wakati JKS alipoagizwa na serikali ya Tanzania kutoa zabuni ya kisiri kwa makampuni yanayotengeneza silaha, mara moja alimtafuta Jean, maana viongozi wenzake walishawahi kumweleza kama angetaka kunufaika na wenzake pia wanufaike basi Jean ndiye  alikuwa mtu wa kuwasiliana naye. Ingawa wakati huo walikuwa hawafahamiani, lakini JKS alikuwa tayari ana anuani ya Jean kutoka kwa rafiki zake. Hivyo hakusita, akawasiliana naye. Ni baada ya kuwasiliana naye na kufanya biashara ya kwanza ndipo urafiki wa karibu sana ulipoanza kati yao.



    Kwa vile Ufaransa ilikuwa na uhusiano wa karibu sana wa kiserikali na serikali ya Rwanda, Jean alijikuta ana uhusiano wa karibu sana na uongozi wa serikali ya nchi hiyo kuliko ilivyokuwa serikali za nchi nyingine za Kiafrika alizokuwa akifanya nazo biashara. Inasemekana kuwa, kwa njia moja ama nyingine, Jean ndiye aliyekuwa mshauri mkuu wa uongozi huo na hakuna uamuzi wowote uliofanyika bila yeye kuhusishwa. Kiuchumi, Jean alimiliki njia zote muhimu za uchumi wa Rwanda kwani uongozi wa serikali ya Rwanda ulimpa uwezo wa kufanya biashara yoyote aliyoitaka nchini humo, na uongozi huo ulinufaika kwa kujilimbikizia mali, na kumwachia anyonye jasho la wananchi wa Rwanda kwa kununua mazao yao yote kwa bei rahisi na kuwauzia bidhaa kwa bei ghali.



    Kwa jinsi hii Rwanda ilimtajirisha Jean na viongozi wa serikali isivyo kifani. Na ndio sababu wakati wa mkutano wa kusuruhisha pande zote za mgogoro wa Rwanda mjini Arusha, Jean alikuwepo. Inasemekana alimtumia sana JKS kujaribu kuipotosha serikali ya Tanzania ili isione ukweli wa mambo ulivyokuwa Rwanda kutokana na urafiki wao wa karibu uliotokana na kupeana bakshishi.



    Baada ya Jean kukata simu, JKS alitafuta kitabu chake cha simu na kutafuta simu ya Phillipe Habimana kule Arusha. Baada ya kuipata alimpigia simu.



    "Hallo Habimana".



    "Habari za leo", JKS alijibu na mara moja Phillipe akaitambua sauti.



    "Nzuri mzee, shikamoo".



    "Marahaba, sikiliza kwa makini, nina kazi nataka vijana wako wakaifanye usiku huu, tafadhali sitaki makosa ya namna yoyote yafanyike kwani yanaweza kuleta madhara kwa suala lenu zima. Nimeshazungumza na Jean.



    JKS alitoa maagizo yake kwa kirefu na akamalizia.



    "Narudia tena, mtu huyu ni hatari sana; vijana wako wasifanye mzaha wakafikiria ni mtu wa kawaida, si wa kawaida, hadhari yote ichukuliwe".

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    "Hamna matatizo mzee, hesabu kazi imekwisha, tuonane kwenye msiba wa Willy Gamba", Phillipe alijigamba.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog