IMEANDIKWA NA : NYEMO CHILONGANI
*********************************************************************************
Sehemu Ya Kwanza (1)
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“I want him dead,” (ninataka afe mara moja)
“Okey! Sir! Do you want us to kill his family too?” (Sawa! Mkuu! Unataka tuimalize na familia yake pia?)
“Yes! Just kill them all,” (ndiyo! Waue wote)
“Okey! No problem. Give us the time we are going to make you smile,” (sawa! Hakuna tatizo. Tutakupa tabasamu) alisema kijana mmoja.
Yalikuwa ni mazungumzo yaliyokuwa yakifanyika kwa njia ya simu kati ya rais wa nchi ya Matapatapa, Bwana Salim Labad na vijana wake aliokuwa amewatuma kwa ajili ya kummaliza mtu mmoja na familia yake.
Hayakuwa mazungumzo marefu sana, ndani ya sekunde chake, wakamaliza na hatimaye kilichokuwa kikisubiriwa kilikuwa ni mauaji hayo kufanyika na rais huyo kupewa taarifa kwa kila kitu kilichokuwa kimefanyika.
Huo ulikuwa mwaka wa kwanza wa Rais Labad kukalia nchi ya Matapatapa. Alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakipendwa ambao watu waliaminika kwamba kama wangekuwa viongozi wa nchi hiyo basi ilikuwa ni lazima nchi hiyo ipae kiuchumi kutokana na biashara kubwa aliyokuwa akiifanya mtu huyo.
Hakuwa mwanasiasa, alikuwa mfanyabiashara mkubwa, alifanya biashara sehemu mbalimbali duniani. Alijijengea heshima, alipata kila kitu alichokihitaji katika maisha yake, na kitu pekee alichokihitaji ambacho hakuwa akikipata kilikuwa ni saluti tu kutoka kwa polisi na wanajeshi.
Hakutaka kuwa mbunge, hakutaka kuwa mwenyekiti wa chama bali kitu alichokihitaji kilikuwa ni urais tu. Alitumia kiasi kikubwa cha fedha kwenye chama chake mpaka kumpitisha. Alihonga kadiri alivyoweza na hatimaye kufanikiwa kuwa rais wa nchi hiyo.
Kutokana na sura yake ya kipole aliyokuwa nayo, wananchi wengi wakampenda na wengine kumfananisha na malaika huku mabango mitaani yakisema kwamba malaika alipewa nchi hiyo hivyo watu walitakiwa kusubiri neema.
Kabla ya kuwa rais wa nchi hiyo, Labad alikuwa mfanyabiashara mkubwa, aliyekuwa na migodi mingi ya dhahabu, alipendwa kwa sababu tu alikuwa mtu wa watu, kila alipokanyaga kulionekana kuwa na neema kubwa.
Aliwapenda wananchi wenzake, alikuwa tayari kufanya kitu chochote katika maisha yake lakini mwisho wa siku apate alichokuwa akikihitaji. Alitumia sehemu kubwa ya utajiri wake kwa watu wengine, masikini na watoto wa mitaani kitu kilichomfanya kupendwa kila siku.
Machoni alionekana mtu, alionekana kuwa mwema lakini maisha yake ya upande wa pili alikuwa mtu mbaya, katili, aliyewanyanyasa wanawake kingono kwa kufanya nao kilazima hasa baada ya kuwatuma vijana wake kwenda kuwanunua.
Alikuwa msambazaji mkubwa wa madawa ya kulevya, aliwatumia vijana wengi kusafirisha madawa hayo kwenda nchi mbalimbali duniani kama China, Pakistan na nchi nyingine nyingi.
Hakukuwa na mtu aliyeyaona maovu yake, kila alipoangaliwa, watu walimuona kuwa malaika ambaye alishushwa duniani kwa ajili ya kuwafurahisha na kuwaletea neema watu wote.
Japokuwa alikuwa na utajiri mkubwa lakini maisha yake hayakuwa na raha. Kila siku alikuwa mkimya, hakuwa mzungumzaji sana, moyo wake ulijaza kisasi kikubwa ambacho kila siku kilikuwa kikimfurukuta moyoni mwake.
Alikuwa kwenye ugomvi mzito na bilionea kutoka nchini Tanzania, Bwana Fredrick Massawe. Bifu hilo lililodumu kwa miaka mitano, lilisababishwa na upinzani wa biashara uliokuwa kati yao.
Japokuwa alikuwa raia wa Matapatapata lakini Labad hakutaka biashara zake ziishie nchini Matapatapa, alichokifanya ni kuzitawanya kwenda mpaka nchini Tanzania ambapo huko alitaka kuanzisha biashara ya kusambaza saruji, mabati na chokaa lakini kabla ya kufanya hivyo alitakiwa afuatilie taratibu zote, apate kibali kihalali kitu ambacho hakutaka kabisa kukifanya kwani aliamini kwamba kwa pesa alizokuwa nazo, zingemrahisishia kila kitu.
Serikali ya Tanzania ikamuwekea kizuizi kwa kumlazimisha kufanya kile alichotakiwa kukifanya. Hakutaka kufanya hivyo kwani aliamini angetozwa kodi kubwa, akakataa na hivyo kurudi nchini kwake na ndani ya wiki hiyohiyo, zile biashara zote alizotaka kuzifanya, zikaanza kufanywa na bilionea Massawe.
Hilo likawa kosa kubwa, Labad akaumia moyoni kwa kuhisi kwamba serikali ya Tanzania ilimuwekea vizuizi kwa sababu ya Massawe na ndiyo maana alipoamua kuondoka mwanaume huyo akachukua tenda hiyo. Moyo wake ukawaka kwa hasira. Hakutaka kukubali, hakutaka kumuacha Massawe akaishi, alichoamua ni kumuua, hivyo akaanza kupanga vijana wake.
Kumpata haikuwa kazi nyepesi, alihangaika kwa miaka yote hiyo, alipambana lakini hakufanikiwa. Massawe alikuwa na ulinzi mkubwa, kila alipokuwa, alikuwa na wanaume kama watano waliokuwa na bastola, mbali na vijana hao, pia kulikuwa na wengine ambao hawakuwa wakigundulika, wote hao walikuwa wakimlinda yeye.
“Nitamuua tu siku moja, haiwezekani nishindwe na wakati nishawahi kuua watu wenye ulinzi mkubwa zaidi yake,” alisema Labad huku akionekana kuwa na hasira kubwa.
Mpaka anapata urais wa nchi hiyo bado alikuwa akihangaika kumuua mwanaume huyo, alishindwa, moyo wake ulimuuma na siku ambayo aliambiwa kwamba Massawe na familia yake walitembelea katika Mbuga ya Wanyama ya Kizwalinda iliyokuwa hapo Matapatapa, akapanga kumuua katika kipindi hichohicho.
“Una uhakika ni yeye?” aliuliza huku akionekana kushtuka.
“Siwezi kumchanganya mkuu! Ni yeye!”
“Nashukuru!”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alipewa taarifa na askari wa mbugani ambao alikuwa amewaweka kuhakikisha kote anakuwa na ulinzi, kutokusemwa kwa mabaya aliyokuwa akiyafanya. Alipopewa taarifa kwamba mwanaume huyo alikuwa kwenye mbuga hizo akawasiliana na vijana wake na kuwaambia wafanye kila linalowezekana mpaka kuhakikisha mwanaume huyo na familia yake wanauawa kinyama kama kulipa kisasi.
****
“Sina amani mke wangu…” ilisikika sauti ya bilionea Massawe.
“Kwa nini mume wangu? Mbona unanitisha hivyo?”
“Sijajua! Ila sina amani kabisa.”
“Hapana ! Inawezekana kuna kitu! Hebu tusali kwanza,” alisema mke wake, Lydia aliyekuwa kitandani pamoja naye na hivyo kushikana mikono kuanza kusali.
Moyo wa bilionea Massawe ulikuwa mzito, hakuwa na furaha, moyo wake ulisononeka mno kana kwamba kulikuwa na kitu kilichokuwa kikienda kutokea. Alimwangalia mke wake, hakufurahia, walikuwa na safari ya kuelekea Matapatapa kwa ajili ya kutembelea mbuga ya wanyama lakini kila alipokumbuka safari hiyo, alikosa amani.,
Hakujua ni kitu gani kilikuwa kinakwenda kutokea. Aliamua kumshirikisha mkewe na kumwambia alichokuwa akijihisi moyoni mwake na hivyo kumwambia kwamba walitakiwa kusali.
Walifanya hivyo, mpaka sala inakwisha bado moyo wake ulikuwa vilevile. Alishindwa kuelewa sababu gani alikuwa katika hali hiyo.
“Mpigie simu daktari aje mara moja,” alisema Massawe.
Daktari wa familia akapigiwa simu na kufika nyumbani hapo. Alimpima Massawe kwa kuhisi labda alikuwa akiumwa lakini kitu cha ajabu kabisa, hakuwa na tatizo lolote lile.
“Huna tatizo lolote!”
“Kweli?”
“Ndiyo! Nimeangalia Malaria, typhord na magonjwa mengine, huna tatizo, hata presha yako ipo vizuri kabisa,” alisema daktari huyo wa familia.
“Sawa. Nashukuru!”
Usiku mzima hakuwa na amani moyoni mwake, alishindwa kulala, alikuwa na mawazo mno na kitu alichokuwa akikifikiria kilikuwa ni safari ya kuelekea nchini Matapatapa tu.
Alihisi kwamba angepata tatizo kwenye safari hiyo, alijaribu kumwambia mkewe waahirishe safari, ili kama itawezekana waende siku nyingine lakini mkewe hakukubaliana naye kwani alijua fika kwamba mumewe alikuwa bize mno na kama angekubaliana naye, kupata muda kama huo kufurahia na familia yake ingekuwa ngumu kupatikana.
“Haiwezekani! Ikishindikana kipindi hiki, utaniambia unakwenda Marekani, mara Uingereza au Kongo! Hebu tumalizane na jambo hili mume wangu,” alisema mkewe kwa sauti ya upole iliyoonyesha kwamba alikuwa na hamu kubwa ya kuwa na mumewe katika safari hiyo.
“Basi sawa. Waandae watoto kabisa.”
Hilo halikuwa tatizo, Lydia akawaanda watoto wao mapacha waliokuwa na miaka kumi na tano, Christopher na Christina kwa ajili ya safari ambayo ilitarajiwa kufanyika siku inayofuata.
Siku ya safari ilipofika, wakajiandaa na saa 4:12 asubuhi safari ya kwenda huko kwa kutumia ndege yao binafsi ikaanza. Kila mmoja akaonekana kuwa na furaha, ndani ya ndege walizungumza mambo mengi, walitaniana sana.
Ilipofika saa 5:25 ndege ikaanza kutua kwenye kiwanja kidogo cha ndege kilichokuwa katika Mbuga ya Wanyama ya Kizwalinda ambapo wakapokelewa na kupelekwa katika hoteli ya kifahari iliyokuwa hapohapo mbugani.
“Mungu ni mwema. Tutaitumia siku nzima kuzunguka mbugani, na kesho tutarudi nchini Tanzania,” alisema MAssawe huku akionekana kuwa na furaha tele.
“Ninashukuru kwa kuniheshimu mume wangu! Nina furaha sana kuwa pamoja nawe katika mbuga hii,” alisema mke wake huku uso wake ukionyesha kuwa na furaha tele.
Hawakujua kama siku hiyo ndiyo walitakiwa kuuawa na tayari wauaji walikuwa njiani kutekeleza azma yao.
Vijana watatu walikuwa njiani wakielekea katika Mbuga ya Wanyama ya Kizwalinda kwa ajili ya kutekeleza mauaji waliyokuwa wameambiwa. Walikuwa na mabegi yao na ndani ya mabegi hayo walikuwa na bastola ambazo wangezitumia kuimaliza familia hiyo.
Walionekana kuwa na hamu ya kufanya mauaji hayo kwani ni kazi ambayo walipewa na rais wa nchi hiyo ambaye alitaka kuona lile alilokuwa ameliagiza likifanyika kwa haraka sana pasipo watu wengine kugundua kitu chochote kile.
Hawakuchukua muda mrefu wakafika mbugani hapo ambapo moja kwa moja wakachukua vyumba katika hoteli ileile na kujifanya kwamba ni Wamarekani waliofika mahali hapo kwa ajili ya kutembelea mbuga hiyo.
Kuwagundua ilikuwa ngumu kwani hata kwa jinsi walivyokuwa wakiongea, waliongea kama Wamarekani. Hawakuishia hapo bali hata fedha zao walitumia dola, yote hiyo ilikuwa ni kuwazuga wahudumu wa hoteli hiyo kwamba walikuwa Wamarekani waliofika hapo kwa ajili ya utalii.
Chumbani, wakaanza kupanga ni kwa namna gani wangeweza kufanikisha mpango wao. Kabla ya yote ilibidi wachunguze kwa makini ili wajue mahali ilipokuwa familia hiyo, hilo wala halikuwa tatizo kwani walimuita mhudumu mmoja na kumwambia kwamba walifika hotelini hapo kwa ajili ya kuonana na bilionea Massawe kutoka Tanzania.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“He is here,” (yupo hapa) alisema mhudumu kwa uchangamfu huku akiachia tabasamu pana, hakuishia hapo bali alimwambia mpaka vyumba walivyochukua yeye na familia yake.
“Thank you! Have the great day,” (nashukuru sana! Uwe na siku njema)
Wakarudi katika chumba kimoja walichokuwa wakipanga mipango yao na kutulia huko. Ilikuwa ni lazima kuhakikisha siku hiyo bilionea huyo na familia yake wanauawa kwani hawakuwa na siku zaidi ya mbili kukaa ndani ya hoteli hiyo.
Walipanga kufanya mauaji hayo usiku, muda ambao kila mtu atakuwa amelala. Mchana, walipokuwa wakienda katika matembezi yao ya kuona wanyama, walikuwa ndani ya gari moja na familia ya mzee huyo, hawakutaka kuua kwani idadi kubwa ya watu iliwaogopesha na mbaya zaidi kulikuwa na askari wa wanyamapori waliokuwa na bunduki.
“Tuwaue hapahapa ndani?” aliuliza jamaa mmoja kwa sauti ya kunong’oneza.
“Hapana! Tusubiri kwanza.”
“Ila hii ni nafasi yetu kubwa.”
“Najua! Ila hatutakiwi kugundulika. Usiwe na presha,” alisema jamaa mmoja.
Wakatulia, hawakutaka kuonyesha presha yoyote mpaka aliporudi hotelini ambapo saa mbili usiku, walikuwa wakiwafuatilia watu hao, jinsi walivyokuwa wakinywa juisi kwenye mgahawa hotelini hapo kama familia na mpaka walipokwenda chumbani.
Walifika huko na kutulia, haikuwa usiku sana hivyo kabla ya Chis na Tina hawajakwenda chumbani kwao walikaa chumbani humo na kuzungumza kama familia. Kila mmoja alionekana kuwa na furaha tele, mkewe, ndiye aliyeonekana kufurahi zaidi kwani alimuondoa hofu mume wake kwamba safari hiyo isingekuwa na hatari yoyote ile, na kweli walikwenda, walitalii mpaka walipokuwa wakijiandaa kurudi, hakukuwa na jambo baya lolote lile.
“Nilikwambia! Hakuna baya lolote,” alisema mke wa Bilionea Massawe.
Wakati wakiwa wanazungumza humo ndani, Chris akasimama na kwenda chooni kujisaidia huku wengine wakiendelea kukaa chumbani hapo wakizungumza mawili matatu huku mazungumzo hayo yakishushiwa kwa kahawa tamu iliyokuwa moja ya huduma zilizokuwa zikipatikana humo.
Wakati wakiendelea kuzungumza, ghafla walisikia kama kitu kikiwa kimeanguka kwa nje, si kimoja, kama viwili. Hawakujua ni vitu gani, walihisi kulikuwa na kitu kumbe walinzi wao wawili waliokuwa wamesimama nje ya chumba hicho walipigwa risasi na wanaume wale ambao waliamua kuifanya kazi hiyo usiku huohuo.
Bilionea Massawe akashtukia kitu, harakaharaka akasimama na kwenda kuufungua mlango kwa ufunguo, hata kabla hajarudi kukaa kwenye kitanda, akashtuka kuona kitasa kikitekenywa kwa lengo la kufunguliwa.
“Who are you?” (wewe ni nani?) aliuliza Bilionea Massawe.
“Open the door,” (fungua mlango!)
“I ask you, who the hell are you?” (nimeuliza, wewe ni nani?) aliuliza Bilionea Massawe
Kila mtu ndani ya chumba hicho alikuwa akitetemeka, waliviona vifo vyao mbele yao, walitamani kukimbia lakini hakukuwa na sehemu nyingine ya kukimbilia zaidi ya kubaki ndani ya chumba hicho.
Wanaume waliokuwa nje ya chumba kile waliendelea kusisitiza kwamba wafunguliwe mlango lakini Bilionea Massawe na familia yake hawakutaka kabisa kuufungua hivyo watu hao kuanza kuuvunja.
Hawakutumia nguvu kubwa, mlango ukavunjika na kuingia ndani. Tina na mama yake walikuwa wakipiga kelele za kuomba msaada lakini hakukuwa na watu waliowasikia.
“Naombeni msituue,” alisema Bilionea Massawe huku akipiga magoti.
“Hilo utakwenda kumwambia Mungu! Sisi tumetumwa ni lazima tuzichukue roho zenu,” alisema mwanaume mmoja huku akikiweka vizuri kiwambo cha kuzuia mlio wa risasi kusikika.
“Tunaomba mtusamehe…” alisema Bilionea Massawe.
“Hilo ungemwambia Rais Salim Labad hata kabla hatujaingia ndani ya chumba hiki.
Hawakutaka maelezo zaidi, hawakutaka maswali walichokifanya kilikuwa ni kuwamiminia risasi watu hao, damu zikatapakaa chumbani, hawakuwaonea huruma hata kidogo, walikwenda ndani ya chumba hicho kwa kazi moja tu ya kufanya mauaji hivyo ilikuwa ni lazima kuhakikisha watu hao wanakufa kama walivyotakiwa kufa.
Walipomaliza, wakatoka nje ya chumba kile. Hakukuwa na mpangaji yeyote aliyetoka, walisikia mlango ukivunjwa, na walipotoka kwenye korido waliiona miili ya walinzi wakiwa chini huku damu zikiwatoka na hivyo kujua kwamba kulikuwa na hatari, wakajifungia vilivyo vyumbani mwao.
Wakatoka nje, hata kabla ya kuondoka, kitu cha kwanza kilikuwa ni kumpigia simu Rais Labad na kumwambia kwamba kazi aliyokuwa amewatuma waliikamilisha kwa asilimia mia moja.
“Safi sana. Mmekumbuka kuimaliza na familia yake?” aliuliza rais kwenye simu.
“Ndiyo bosi!”
“Safi! Rudini mjini! Nilitaka nimalize kizazi chake chote, yaani watoto wake wasizae kuendeleza kizazi na ndiyo maana hata wao nilitaka muwamalize,” alisema Rais Labad huku sauti yake tu ikisikika kama mtu aliyekuwa na furaha tele.
“Watoto wake?”
“Ndiyo!”
“Kwani si ana mtoto mmoja wa kike?”
“Hapana! Anao wawili!”
“Mbona sisi tumemkuta mmoja?”
“Hapana! Wanatakiwa wawe wawili. Rudini ndani ya chumba mkamtafute na yeye mmuue,” aliagiza Rais Labad, harakaharaka vijana hao wakaanza kurudi ndani ya chumba hicho kwa ajili ya kumuua mtoto mmoja aliyebaki ambaye walikuwa na uhakika kwamba alikuwa chooni au chini ya uvungu wa kitanda amejificha.
**** CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Chris alikuwa chooni akijisaidia. Moyo wake ulikuwa na hofu tele, pale alipokuwa palikuwa ni mbugani na kwa jinsi choo kile kilivyokuwa kimejengwa kwa kuweka dirisha kubwa kidogo bila nondo akahisi kwamba angeweza kuvamiwa na mnyama mkali kule alipokuwa japokuwa lilikuwa juu.
Hakuwa na hili wala lile, kichwa chake kilikuwa kikifikiria mambo mengi hasa juu ya safari hiyo waliyokuwa wameifanya na wazazi wake.
Akiwa huko chooni, akaanza kusikia sauti ya mtu akigonga mlango kwa fujo. Hakujua walikuwa wakinanani lakini watu hao walitaka kufunguliwa mlango lakini pia alimsikia baba yake akijibizana nao kwa kuwauliza walikuwa wakina nani, watu hao hawakujibu zaidi ya kuhitaji kufunguliwa mlango tu.
Wala hazikupita sekunde nyingi, mlango ukafunguliwa, kwa masikio yake akawasikia watu hao wakimwambia baba yake kwamba wlaikuja kumuua kwa sababu walikuwa wametumwa na Rais Labad.
Aliyasikia yote hayo akiwa chooni mpaka pale wazazi wake na dada yake, Tina walipopigwa risasi, akasikia watu hao wakitoka ndani kwenda nje. Hakutaka kubaki ndani ya chooni, harakaharaka akatoka, alichokiona, miili ya wazazi wake ilikuwa sakafuni wametulia huku damu zikiwatoka, moyo wake ulimuuma sana, hakuamini kama kweli siku hiyo ndiyo ilikuwa ya mwisho kuzungumza na wazazi wake.
Akaziinamia maiti zile, alilia mno lakini hata kabla hajajua ni kitu gani alitakiwa kufanya, akasikia vishindo vya watu kutoka ukumbini. Akaogopa, akahisi kwamba walikuwa watu walewale, alichokifanya ni kukimbilia chooni.
“Mungu nisaidie,” alisema Chris, hapohapo akaufunga mlango wa chooni.
“Kama uvunguni hayupo, kamwangalieni chooni! Kumbukeni kwamba huyu mtoto naye ni muhimu sana kufa usiku huu,” alimsikia mwanaume mmoja. Hapohapo akasikia vishindo vya mtu akielekea kule kulipokuwa na chooni, akakishika kitasa na kukitekenya kwa lengo la kuufungua mlango.
“Buum…Buum…Buum…” aliyasikia mapigo yake ya moyo yakidunda kwa nguvu na kwa kasi mno kwani alikiona kifo kikiwa mbele yake.
Watu wale waliokuwa nje ya choo kile wakaendelea kukitekenya kitasa cha mlango ule kwa lengo la kuufungua lakini haukufunguka kitu kilichowaganya kugundua kwamba mtoto huyo alikuwa ndani ya choo hicho na ilikuwa ni lazima kumuua.
Mule alipokuwa Chris hakutaka kubaki hivihivi tu bali alichokifanya ni kuanza kupanda juu kwa lengo la kutoka kupitia kidirisha kile. Hilo lilifanikiwa bila tatizo lolote lile na kwa jinsi dirisha lile lilivyokuwa kubwa kidogo bila kuwa na nondo zaidi ya wavu, akatoa wavu harakaharaka na kisha kuliparamia na kutokea upande wa pili.
Hakubaki mahali hapo. Ilikuwa ni usiku mbugani lakini aliona ilikuwa ni afadhali kuuawa na wanyama wakali kuliko kuuawa kwa bunduki kama ilivyokuwa kwa wazazi wake.
Alikimbilia mbugani, hakutaka kusimama, alikuwa akilia, hakuamini kama huo ndiyo ulikuwa mwisho wa kuwaona wazazi wake waliouawa kwa kupigwa risasi chumbani.
Hakuwaona wauaji lakini alisikia vilivyo kwamba walitumwa na Rais Labad. Alimfahamu rais huyo, alikuwa kiongozi wa juu kabisa nchini humo, Matapatapa. Alikimbia mpaka akaanza kuingia mbugani zaidi, akaanza kusikia milio ya fisi waliokuwa wakilia, akaogopa, alichokifanya ni kusonga mbele, hakutaka kusimama hata kidogo.
“Mungu! Naomba unisaidie,” alisema Chris huku akiendelea kusonga mbele.
Alikimbia mpaka alipofika katika eneo lililokuwa na mti mkubwa, hakutaka kusubiri, harakaharaka akapanda juu na kutulia huko. Mawazo juu ya wazazi wake na familia yake hayakupungua, muda wote alikuwa akiwakumbuka na moyo wake kumuuma sana kwani hakuamini kama kweli walikuwa wameuawa huku akisikia.
Wakati akiwa huko mtini, ghafla kwa mbali akawasikia watu wakija kule alipokuwa huku wakiongea kwa sauti. Walikuwa wakilalamikiana kwamba ilikuwaje mpaka hawakufanikiwa kumpata na kumuua na wakati walikuwa na nafasi kubwa ya kufanya hivyo.
Akaingiwa na hofu kwa kugundua kwamba watu hao waliokuwa wakizungumza walikuwa walewale ambao walivamia chumbani na kufanya mauaji kwa familia yake.
Walipofika chini ya mti ule, wakapumzika kwani walimtafuta kila kona lakini hawakuweza kumpata, na hawakuwa radhi kumpa taarifa Rais Labad pasipo kukamilisha mauaji ya Chris ambaye hawakuwa wakijua kama alikuwa juu ya mti ule waliokuwa wamekaa chini yake.
“Ni lazima tumuue. Hivi unafikiri rais akisikia kwamba hatukumuua atachukua hatua gani? Ni lazima tumuue,” alisema jamaa mmoja kwa sauti kubwa huku Chris akiwasikia.
“Si una tochi hapo?”
“Hapana! Ipo kwenye gari,” alijibu jamaa mmoja.
Akaondoka na kwenda kuchukua gari. Kila kitu kilichokuwa kikiendelea mahali hapo, askari wa wanyamapori walikuwa wakiangalia tu lakini hawakuingilia kwani kila kitu waliambiwa na kupewa onyo kwamba hawakutakiwa kuzungumza chochote kile.
Jamaa aliporudi na gari, wakachukua tochi kwa ajili ya kumtafuta Chris huku wakiwa na uhakika kwamba bado angekuwa ndani ya mbuga hiyo kwani kwa wakati huo hakukuwa na basi lolote lililopita kuelekea mjini.
“Hebu mulika juu ya mti huu, inawezekana dogo akawa amepanda huko,” alisema jamaa mmoja na mwenzake kuanza kumulika juu ya ule mti aliokuwepo Chris.
Walimulika lakini hawakuona kitu chochote kile. Chris alijificha vilivyo, kila mwanga ulipomulika huko, alijificha upande wa pili na hivyo kutokuonekana.
Wanaume hao wakaondoka mahali hapo na kuelekea mbele zaidi. Hawakutaka kurudi mjini pasipo kumpata Chris ambaye hawakujua alikuwa wapi. Walizunguka na kuzunguka lakini hawakufanikiwa kumuona kitu kilichowachanganya mno.
*** CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Rais Labad alitulia kwenye kiti chake sebuleni, macho yake yalikuwa kwenye simu yake iliyokuwa juu ya meza. Alitaka kusikia kile kilichokuwa kikiendelea kuhusu Chris ambapo aliwaambia vijana aliowatuma kwamba ni lazima wamuue kama kukamilisha mpango wake wa kuiangamiza familia nzima ya Bilionea Massawe.
Muda ulizidi kwenda, dakika zilikatika lakini hakufanikiwa kupokea simu yoyote ile, moyo wake ulikuwa na presha kubwa, hakutulia, muda wote macho yake yalikuwa katika simu ile ambayo ilikuwa kimya kabisa kitu kilichomfanya kuwa na presha kubwa.
Hakutaka kutulia, wakati mwingine alisimama na kuzunguka huku na kule, alionekana kuwa mwingi wa presha kwani kama vijana wake wasingefanikiwa kumuua Chris basi angekuwa kwenye hali mbaya kwani mtoto huyo angeweza kutoa taarifa kwa polisi na hivyo kuingizwa matatani.
Hakulala, alikesha usiku mzima, mara kwa mara mkewe alimfuata sebuleni hapo na kumwambia kuhusu kulala lakini Labad hakukubali, hakutaka kuona akilala na wakati hajajua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea kule mbugani.
Ilipofika saa kumi alfajiri, akachoka kuvumilia, akanyanyua siku yake na kuwapigia vijana hao. Simu ikaita, haikuita sana ikapokelewa na sauti ya mwanaume mmoja kusikika ambapo akamwambia kwamba hawakufanikiwa kumuua Chris.
“Kwa nini?”
“Alikimbia!”
“Yaani mmeshindwa kumuua mtoto! Hivi inakuwaje mnaua watu wazima halafu mnamkosa mtoto?” aliuliza kwa hasira, kwa jinsi alivyoonekana tu, alikuwa amechanganikiwa.
“Mkuu! Ila tunaendelea kumtafuta. Amekimbilia mbugani, nina uhakika kwamba hata kama hatutompata, ataliwa na simba,” alisema kijana huyo.
Rais Labad hakutaka kuendelea kuwasikiliza wanaume hao, alichokifanya ni kukata simu na kutulia kwenye kochi. Hakusikia hata lepe la usingizi, mpaka inaingia saa kumi na mbili asubuhi hakuwa amepokea taarifa ya kupatikana kwa mtoto Chris.
Alichokifanya ni kuwapigia simu maaskari wa wanyamapori na kuwaambia kwamba walitakiwa kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha Chris anapatikana kwani vijana wake walimwambia kuwa alikimbilia mbugani, hivyo piga ua ilikuwa ni lazima wampate.
“Hakuna shida!”
“Pekueni kwenye mabasi yote yanayopita mbugani! Ikitokea akipita salama, nitawaua wote,” alisema Rais Labad, kwa jinsi alivyochanganyikiwa, alikuwa na uhuru wa kumwambia mtu yeyote kile alichotaka kumwambia kama kuhakikisha alichokitaka kinafanikiwa.
Askari wa wanyamapori hawakutaka kuchelewa, maagizo waliyopewa walitakiwa kuyafanyia kazi haraka sana hivyo kuanza harakati za kumtafuta Chris kana kwamba walikuwa wakiwatafuta majangili mbugani.
Walisimamisha kila basi lililokuwa likitaka kutoka mbugani kwani waliamini kwamba inawezekana Chris alikuwa ndani ya mabasi hayo kwa ajili ya kutoroka mbugani humo.
Wakati msako huo ukiendelea kwa nguvu zote, tayari taarifa ya kifo cha Bilionea Massawe na familia yake zikasikika, watu waliogopa, hawakujua kitu gani kilikuwa kimetokea mpaka mauaji hayo kutokea huku polisi wa wanyamapori wakiwa hukohuko, askari wa hoteli hiyo walikuwa huko hotelini.
Kitu kilichoshangaza, hakukuwa na askari yeyote aliyetiwa hatihani kwani walijua kwamba mpago mzima ulichezwa na mkubwa wa nchi hiyo wakafunga midomo yao.
“Bilionea Massawe aliamua kujiua, aliiua familia yake kabla ya kujiua,” alisema msemaji wa mbuga hiyo.
Kauli yake ilizua utata mkubwa, hawakuamini kama bilionea huyo angeweza kujiua kirahisi namna hiyo kwani kama kweli alikuwa amejiua, bila shaka angemuua Chris kwani naye pia walikuwa naye katika safari hiyo.
Hilo ndilo waliloambiwa, halikubadilika kitu. Dunia nzima ilitakiwa kukubaliana na ukweli huo kwamba bilionea huyo aliiua familia yake na yeye kujipiga risasi.
“Inawezekana kweli?” aliuliza jamaa mmoja.
“Labda kwa sababu hawa mabilionea wana mambo yao,” alisema jamaa mwingine.
“Sasa mtu unakuwa na pesa, halafu unaiua familia yako! Si bora tu ungefanya kitu kingine,” alisema jamaa mwingine kwa majonzi, mpaka muda huo hakukuwa na mtu aliyejua ukweli juu ya kilichokuwa kimetokea.
Chris alikuwa juu ya mti, usiku mzima hakutaka kulala, alikesha akilia tu. Wauaji wale walioliacha gari lao wakalirudia na kuondoka zao pasipo kumpata mtoto huyo aliyevisumbua vichwa vyao.
Kule mtini alipokuwa, Chris alikuwa akilia, bado kichwa chake kiliifikiria familia yake, hakuamini kile alichokiona kwamba wazazi wake waliuawa kwa kupigwa risasi.
Hakulala, ilipofika saa kumi na moja asubuhi akateremka na kuanza kutembea mbugani. Hakuogopa wanyama wakali, wakati mwingine alitamani kuona akiuawa kwani hakujua ni kwa namna gani angeendelea kuishi pasipo kuwa na wazazi wake.
Alimkumbuka dada yake, Tina. Moyo wake ulimuuma mno kila alipomfikiria. Hakuamini kama wangeweza kutendewa unyama mkubwa kiasi kile, aliumia, alilia na kulia lakini hakukuwa na kilichobadilika, ukweli ulibaki palepale kwamba hakuwa na familia, wote waliuawa vibaya ndani ya chumba cha hoteli.
Aliendelea kusonga mbele, alipokuwa akiwaona wanyama wakali kwa mbali, alijificha kichakani, na walipoondoka aliendelea na safari yake. Hakujua alipokuwa akienda, alichokitaka ni kusonga mbele tu.
Alitembea mpaka alipofika sehemu ambayo kwa mbali aliliona basi likija kwa mwendo wa taratibu. Hakutaka kusimama alipokuwa, akaanza kutembea harakaharaka kuelekea kule kulipokuwa na barabara na kusimama.
Alihitaji msaada, hakujua ni kwa namna gani angeweza kutoka salama ndani ya mbuga hiyo. Aliposimama, akapunga mkono kulitaka gari hilo kusimama. Kila mtu aliyemuona Chris pale mbugani alishangaa, hakuamini kama kungekuwa na mtu, tena mtoto kama yeye ambaye angediriki kuwa kwenye mbuga hiyo iliyokuwa na wanyama wakali.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Dereva akasimamisha gari na kondakta kumtaka kuingia ndani haraka sana. Kila mmoja alimshangaa, walimwangalia, waliona akiwa analia tu na walipomuuliza aliwaambia kwamba wazazi wake walimuacha mbugani na hakujua ni mahali gani walipokuwa.
“Ni hatari sana! Hivi wazazi wanawezaje kumuacha mtoto peke yake katika mbuga yenye wanyama wakali kama hawa?” alihoji jamaa mmoja.
“Kuna watu wana roho mbaya sana. Unaweza kukuta mwanaume kagundua huyu mtoto siyo wake, akaamua kumuacha mbugani ili aliwe na wanyama wakali,” alisema dereva huku akiendesha gari hilo kwa mwendo wa 50 ambao walitakiwa kuutumia wawapo mbugani.
Hakukuwa na mtu aliyegundua kwamba mtoto waliyekuwa wamempakia alikuwa Chris, ilikuwa ni asubuhi sana hata matangazo juu ya msako wake hayakuwa yametolewa. Waliendelea na safari mpaka kufanikiwa kutoka salama ndani ya mbuga hiyo.
Safari iliendelea, basi lilipomaliza mbuga hiyo na kuingia katika Jiji la Motown, Chris akateremka huku akiwashukuru watu hao kwa wema mkubwa waliomfanyia kwani hakika kama wasingekuwa wao basi angeweza kufa pale mbugani.
Akaondoka. Hakujua ni mahali gani alipotakiwa kwenda. Hakuwahi kufika Matapatapa, hiyo ilikuwa mara yake ya kwanza, alibaki mjini huku akiwa anazungukazunguka, hakujua ni mahali gani alipotakiwa kwenda.
Ilipofika saa nane mchana huku akiwa mitaani akakutana na kijana mmoja, alikuwa mchafu, macho ya kijanjajanja, alipomuona Chris, hapohapo akamfuata.
“Wewe nani?” aliuliza kijana huyo huku akimwangalia Chris, hakuishia kumwangalia bali akaanza kumzunguka kana kwamba alikuwa akimchunguza.
“Chris…” alijibu huku akitetemeka.
“Mtoto wa kishua?”
“Hapana!”
“Mbona umependeza? Mbona msafi sana? Wewe utakuwa mtoto wa kishua,” alisema kijana huyo huku akiendelea kumwangalia Chris.
Chris hakujibu kitu, kila alipomwangalia kijana yule, kwake alionekana kuwa mtu mwenye roho mbaya kwani kiunoni mwake alikuwa na kisu, alikichomeka na kukifunika na shati lake lililokuwa limechanika, kwa kutumia matundu ya shati, Chris aliweza kukiona.
Kijana huyo hakuzungumza sana, akaondoka mahali hapo. Chris aliendelea kubaki mitaani, hakujua ni mahali gani alitakiwa kwenda kwani kote humo alikuwa mgeni, kila kitu alichokuwa akikiona, kwake kilionekana kuwa kigeni.
Ilipofika saa moja usiku, kijana yule akamrudia tena, akahisi kwamba Chris alikuwa na tatizo kwani kama alivyomkuta mtaani mchana, hata usiku alikuwa hukohuko.
Akazungumza naye na kumtaka kumfuata alipokuwa akienda, safari yao ndogo iliishia katika sehemu moja iliyokuwa na mapipa mengi ambayo ndani yake kulikuwa na takataka zilizokuwa zikiungua moto huku pembeni kuwa na watoto wengine wa mitaani waliokuwa wakiota moto na wengine kujifunika na magunia.
“Hawa ni washikaji zangu,” alisema mtoto huyo aliyejulikana kwa jina la Ndezi.
Hayo ndiyo yalikuwa makazi yake mapya, hakukuwa na sehemu nyingine ya kwenda, alitamani kurudi nchini Tanzania lakini ilishindikana kwani hakuwa na kiasi chochote cha fedha.
Moyo wake uliumia sana, usiku wa siku hiyo hakulala kwa amani, kila wakati alikuwa akishtuka, sauti za wazazi wake wakiomba msamaha zilijirudia kichwani mwake, zilimuumiza sana huku hasira kali ikianza kumpanda dhidi ya rais wa nchi hiyo kwani aliamini kwamba ndiye mtu aliyefanya mipango kuuawa kwa wazazi wake.
“Kuna siku nitamuua kama kulipa kisasi, siwezi kumuacha hivihivi,” alisema Chris huku akiwa na hasira kali, siku hiyo aliendelea kulala usingizi wa mang’amung’amu mpaka asubuhi.
****
Msako wa kimyakimya ulikuwa ukiendelea, maaskari wa mbugani waliendelea kumtafuta Chris pasipo mafanikio yoyote yale. Vichwa vyao viliuma mno, hawakujua mahali alipokuwa kijana huyo kwani kwenye kila basi walilokuwa wakilipekua, waliambulia patupu, hawakujua kama kijana huyo alipita asubuhi sana kuelekea Motown.
Walipoona kwamba mbugani alikosekana, wakahisi kwamba mtoto huyo alikuwa amekimbilia Motown hivyo vijana kutumwa huko na kuambiwa kwamba walitakiwa kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha kwamba mtu huyo anapatikana na kuuawa.
Vijana wenye hasira, walioshika maagizo ya rais wakaingia Motown na kuanza kumtafuta Chris, walizunguka sehemu mbalimbali lakini hawakufanikiwa kumuona kitu kilichowafanya kuhisi labda aliliwa na wanyama wakali kule mbugani.
“Hayupo! Tumemkosa, hivi yupo hai kweli?” aliuliza kijana mmoja, alikuwa amechanganyikiwa, hakujua kama kweli walimkosa Chris.
“Haiwezekani tumkose. Kama kweli aliliwa na wanyamapori, basi ilikuwa ni lazima askari wa mbugani wajue hilo, wangeona hata mifupa yake,” alisema kijana mwingine na hivyo kuendelea kumtafuta Chris.
Hawakuchoka, lakini hawakuweza kumpata, walikuwa wakihangaika, siku hiyo ilipita, hawakuwa wamemuona, wakawasiliana na Rais Labad na kumwambia kile kilichokuwa kikiendelea, rais alikasirika, akawaagiza kwamba wafanye kila liwezekanalo kuhakikisha mtu huyo anapatikana kwani waliamini kwamba bado alikuwa nchini Matapatapa.
“Hakikisheni mnampata,” alisema Rais Labad kwa hasira.
“Haina shida mkuu!”
“Nawapeni siku mbili tu! Hakikisheni mnampata, vinginevyo bora niwape kazi watu wengine na nyie niwaue,” alisema Rais Labad kwa hasira.
Vijana zaidi ya hamsini wakaongezeka, wengine wakaambiwa kwamba walitakiwa kwenda kumtafuta katika mbuga ya wanyama ya Kizwalinda lakini wengine walitakiwa kwenda katika Jiji la Motown kuhakikisha wanamtafuta kila kona.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hilo likafanyika, zaidi ya vijana ishirini wakashushwa katika Jiji la Motown na kuanza kumtafuta. Chris alikuwa mtu muhimu, alivisumbua vichwa vyao, Rais Labad alikuwa na mawazo tele, moyo wake uliuma sana kwani aliamini kwamba kama asingehakikisha mtoto huyo anapatikana basi hapo baadaye maisha yake yangekuwa ya hatari zaidi.
Wakati akiwa na mawazo tele kuhusu Chris, akapigiwa simu na kuambiwa kwamba mtoto huyo alionekana mitaani hapo Motown huku akiwa pamoja na watoto wa mitaani.
“Una uhakika ni yeye?” aliuliza Rais Labad huku akionekana kutokuamini.
“Ni yeye mkuu!”
“Kweli?”
“Ndiyo!”
“Hebu mpigeni picha ya siri mnitumie,” aliagiza.
Vijana hao walimuona Chris akiwa na watoto wengine wa mitaani, walipomwangalia, alionekana kuwa na hofu kubwa, kila wakati alikuwa akiangalia huku na kule na muda mwingi alionekana kuwa na huzuni tele.
Alichokifanya kijana mmoja ni kuchukua simu yake yenye uwezo mkubwa kisha kumpiga picha na kumtumia Rais Labad ambapo baada ya kuiangalia, akagundua kwamba alikuwa Chris.
“Ndiye yeye! Muueni haraka sana,” alisema rais.
“Hapahapa?”
“Hapana! Hapo ni noma! Mtekeni na mkamuulie mafichoni,” alisema Rais Labad na vijana hao kumwambia kwamba jamboo hilo lingefanyika haraka sana na hivyo kumfuata kwa lengo la kumteka.
Chris alikuwa mitaani na watoto wenzake, hakuwa na marafiki, mtu ambaye alikuwa naye kila alipokuwa alikuwa Ndezi tu ambaye kila wakati yeye ndiye aliytemwambia twende huku au kule, yeye ndiye aliyemkutanisha na watoto wengine na kumtambulisha.
Maisha hayo yalimuumiza mno, hakuamini kama katika safari ya kuelekea nchini Matapatapa na familia yake angejikuta akiwa mitaani huku akitafuta maisha. Kwa wakati huo, hakukuwa na mtu aliyejua kama Chris alikuwa mitaani, kwa Tanzania, walipata taarifa kwamba Bilionea Massawe aliiua familia yake lakini hawakujua mahali alipokuwa Chris kwa wakati huo.
“Chris! Unapokuwa kwenye tatizo ni lazima upambane kiume,” alisema Ndezi huku akimwangalia Chris.
“Kivipi?”
“Kuna ubabe mkubwa sana huku mtaani. Unaweza kupata pesa halafu kuna wajinga flani wakakufuata na kutaka kuchukua pesa zako, hivyo ni lazima upambane,” alisema Ndezi huku akimwangalia Chris.
“Kwa kupigana?”
“Hapana! Unaweza kupambana kwa kisu au hata bisibisi,” alisema Ndezi maneno yaliyomfanya Chris kushtuka kwani katika maisha yake hakuhisi kama ingetokea siku angeweza kuchukua kisu na kupambana na watu wengine.
Walikuwa wakizunguka huku na kule, walionekana kama watoto wa mitaani lakini kwa Chris alionekana kuwa tofauti na wenzake. Mavazi yake yalikuwa masafi na muda mwingi hakuwa mtu wa kuomba pesa kama ilivyokuwa kwa wenzake.
Saa zilikatika, mpaka vijana wa Rais Labad wanamuona mitaani hakuwa akijua, hakuwafuatilia kwani aliamini kwamba kwa kile kilichotokea mbugani, kisingeweza kuendelea mpaka mitaani.
“Tumfuateni!” alisema kijana mmoja, alikuwa akimwangalia Chris aliyekuwa na Ndezi katika Soko Kuu la Motown ambapo kulikuwa na idadi kubwa ya watu.
“Tusubiri mpaka atoke ndani ya soko!”
“Tunachelewa!”
“Ila tukimfuata, watu wengine watahisi vipi? Tena na hii hali ya watoto kutekwa na kuuawa si ndiyo itatuletea msala?” alihoji jamaa mmoja, alionekana kuwa na wasiwasi mkubwa.
Wenzake hawakutaka kumsikiliza, walijiona wao kuwa sahihi kuliko hata yeye, walichokifanya ni kuteremka kutoka ndani ya gari na kuanza kumfuata Chris aliyeendelea kuwa na Ndezi, walipomfikia, wakamsimamisha.
“Dogo mambo vipi?” aliuliza jamaa mmoja.
Chris hakujibu, alisimama na kuanza kuwaangalia watu hao, hakuwafahamu, alihisi labda wanaweza kuwa wale wanaume waliokuwa hotelini lakini hawakuwa wao, hakujua walihitaji nini, alisimama pamoja na Ndezi huku wakiwaangalia kwa mshtuko.
“Tuna kazi tunataka utusaidie,” alisema jamaa mmoja huku akimwangalia Chris.
“Kazi gani bro?” aliingilia Ndezi.
“Siyo wewe! Tunataka atusaidie huyu.”
“Mimi ndiye meneja wake, bila mimi haendi sehemu,” alisema Ndezi huku akiwaangalia wanaume hao nyusoni mwao.
Alikuwa kijana wa mitaani, mhuni asiyeogopa kitu chochote kile, kwa jinsi mtazamo alioutumia kuwaangalia wanaume hao ulionyesha kabisa kwamba hakuwa mtu wa mchezo hata kidogo.
Walichokifanya ni kuwaambia wawafuate kule walipokuwa wakielekea kwenye gari ambapo ndipo waliposema kwamba kulikuwa na mizigo, walipofika na kuufungua mlango, wakawaingiza wote na kisha kuufunga mlango.
“Tulieni humo ndani,” alisema mwanaume mmoja kwa sauti ya ukali, tena ya kibabe hasa.
Ndezi hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea mahali hapo lakini kwa Chris akagundua kwamba inawezekana watu hao walikuwa miongoni mwa wale vijana waliokwenda hotelini mule na kuwaua wazazi wake.
Akaingia na hofu na kuona kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wake, akaanza kulia. Ndezi alikuwa kimya, aliwaangalia watu hao, waliwaweka nyuma ya gari lile huku huko wakiwa na mwanaume mmoja na wengine wawili wakiwa mbele. CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Gari lilikuwa likiondoka kutoka ndani ya soko lile, kutokana na umati mkubwa wa watu, gari liliendeshwa kwa mwendo wa taratibu sana mpaka walipofika nje ya soko lile na ndipo dereva alipoongeza mwendo kuelekea kulipokuwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Motown.
“Oya! Tunakwenda wapi huku?” aliuliza Ndezi huku akiwaangalia watu hao, hakujua kitu chochote kile, kwake, walionekana kuwa watekaji ambao waliwachukua kwa ajili ya kwenda kuwaua.
“Nyamaza nyambafu we’,” alisema jamaa waliyekuwa naye katika viti vya nyuma.
“Nitanyamazaje na wakati nataka kujua tunakwenda wapi,” alisema Ndezi lakini hata kabla hajakaa vizuri akashtukia akipigwa kibao kimoja cha nguvu shavuni mwake.
“Nimekwambia nyamazaaa…” alisema mwanaume ambaye walikuwa naye nyumba ya gari lile.
Ndezi akanyamaza, moyo wake ukajawa na hasira, hakuamini kama alipigwa kibao kizito namna ile, kwake, ile ilionekana kuwa dharau kubwa, hakuamini kama kungekuwa na mtu ambaye angediriki kumzaba kibao namna ile.
Mwanaume mmoja miongoni mwa wale waliokuwa mbele ya ile gari akampigia simu Rais Labad kwa ajili ya kumpa taarifa kwamba walifanikiwa kumpata Chris na muda huo walikuwa njiani kuelekea sehemu walipotakiwa kumuulia.
“Safi sana, muueni haraka iwezekanavyo halafu mwili wake muuzike porini,” alisikika kwenye simu kwa sauti ambayo watu wote ndani ya lile gari waliisikia.
Ndezi akajiangalia kwenye kiuno chake, kisu chake kilikuwa mahali hapo, alihisi kwamba safari hiyo ilikuwa mbaya na kama asingefanya jambo moja basi wangeweza kupelekwa sehemu na kuuawa.
Alichokifanya kwa haraka sana ni kukitoa kisu chake kisha kumchoma mwanaume walioyekuwa naye nyuma ya gari lile, hakumchoma mara moja, kwa haraka sana akamchoma mara tatu na kisha kuhamia kwa wanaume waliokuwa mbele ya gari.
Alianza na aliyekaa upande wa kushoto, akamchoma mara mbili kisu cha shingo, wakati dereva akigundua hilo na kutaka kumpokonya kisu kile, akashtukia naye akichomwa kisu cha shingo mara mbili tena kwa haraka sana.
Damu zikaanza kumtoka, akahisi kwamba mwili wake ukiishiwa nguvu, mikono yake ikaacha usukani na hapohapo gari likaacha njia na kuanza kuelekea bondeni kwa kasi kubwa.
“Jifunge mkanda,” alisema Ndezi na Chris kufanya hivyo harakaharaka.
Gari likaelekea bongeni ambapo huko likagonga mti mmoja mkubwa, likapinduka na wote wawili kuanza kuugulia maumivu mule garini walipokuwa.
“Chris…Chris….upo hai?” ailuliza Ndezi huku akimwangalia Chris aiyekuwa akitokwa na damu kwenye paji la uso.
“Nipo hai…koh koh koh,” alisema Chris na kukohoa mfululizo.
Hawakutaka kubaki mule, wakaanza kutoka. Ndezi hakutaka kukubali, alihisi kabisa kwamba watu wale walikuwa na pesa mifukoni hivyo akaanza kuwapekua.
Akawakuta na kiasi kikubwa cha fedha, akachukua simu zao na kuondoka katika eneo la tukio haraka sana kwani hawakutaka mtu yeyote awaone mahali hapo.
Wakati wakiwa njiani, ghafla simu moja ikaanza kuita, harakaharaka akaichukua na kuangalia kwenye kioo, jina aliloliona lilisomeka ‘Rais Labad’ akamuonyeshea Chris.
“Huyu amewaua wazazi wangu na dada yangu,” alisema Chris huku akionekana kuwa na hasira kali.
“Kumbe! Sasa wewe mtoto wa mbunge au?” aliuliza Ndezi.
“Pokea kwanza!”
Ndezi akaipokea simu ile na sauti ya Rais Labad ikaanza kusikika kutoka upande wa pili. Kitu cha kwanza kabisa alichouliza kilikuwa ni kazi yake aliyokuwa amewapa, je Chris alikuwa amekwishauawa na mwili wake kuzikwa au bado?
“Bado hajauawa kwa sababu tumewaua wao,” alijibu Ndezi huku akibadilisha sauti yake na kutaka isikike kama mtu mzima.
“Wewe nani?”
“Mshikaji mmoja hivi mtata.”
“Umepata wapi simu hii?” CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nimewachukulia kisela. Ishu ni kwamba wana wamepata mzinga huku barabarani, kama vipi njooni mchukue miili yao ila kuanzia sasa usipige simu hii kwani ndani ya saa moja itakuwa imeuzwa kwa mtu mwingine kabisa,” alisema Ndezi.
“Wewe ni nani?”
“Daah! Rais unayumba sana! Nimekwambia msela flani hivi mtata lakini hunielewi! Wewe njoo uchukue maiti zako,” alisema Ndezi, hakutaka kuendelea kuongea, hapohapo akakata simu, akaizima, akatoa laini kisha kuiweka mfukoni na kuondoka mahali hapo akiwa na Chris aliyekuwa hoi, na muda wote alionekana kumuogopa Ndezi kwani hakuwahi kumuona mtu aliyekuwa na ushujaa wa kuwaua watu watatu kwa tukio moja kama alivyofanya ndani ya gari lile.
Rais Labad alichanganyikiwa, hakujua ni kitu gani alitakiwa kufanya, alipoambiwa kwamba baadhi ya vijana wake walikuwa wameuawa, alihisi moyo wake ukipata hasira kali ambayo hakuwahi kuipata katika maisha yake.
Kitu kilichomkasirisha zaidi kilikuwa ni simu aliyozungumza na mtu asiyemjua. Aliongea kihuni, maneno ya kejeli ambayo yaliufanya mwili wake utetemeke na kijasho chembamba kumtoka.
Hakutaka kukubali, alitaka kumuangamiza Chris kabla ya kuwaambia watu ukweli wa kile kilichokuwa kimetokea, akawapigia simu vijana wake wengine na kuwaambia kilichokuwa kimetokea, na kama ingewezekana basi waondoke kwenda kule kulipotokea ajali hiyo na kuangalia ni kitu gani kilitokea na wafanye juu chini, kama wahanga hawajafa, basi wawaue.
“Sawa mkuu!”
Hakutaka kuishia hapo, alijua kwamba kulikuwa na kazi kubwa kumpata Chris kwani mpaka hapo tu tayari aliona akisumbuka kumpata, akajua kwamba kama kweli gari lilipata ajali, basi inawezekana yule mtu aliyezungumza naye kwenye simu alikuwa rafiki wa Chris au mtu yeyote ambaye alikuwa akijua mahali Chris alipokuwa, hivyo mtu wa kwanza kabisa ilikuwa ni kumtafuta huyo mtu.
Akawapigia simu watu wa mitandao ya simu na kuwaambia kilichokuwa kimetokea, alitaka kujua mahali simu hiyo ilipokuwa, hata kama laini ya simu ingetolewa, aliamini kwamba bado simu hiyo ingeweza kufanya kazi, hivyo alihitaji kujua mahali ilipokuwa.
Hilo halikuwa tatizo, watu wa mitandao wakaingia kwenye kompyuta zao na kuanza kufanya kazi zao. Haikuwa kazi kubwa, kwa kuwa laini ya simu hiyo ilitumika katika simu iliyoibwa, wakaweza kuinasa mpaka mahali ilipokuwa hivyo kumpa taarifa.
“Mkuu! Tumeweza kuinasa simu yenyewe,” alisema kijana mmoja.
“Safi sana! Nitataka kijana mmoja aje, aongozane na vijana wangu mpaka mahali ambapo simu hiyo ilipokuwa,” alisema Rais Labad.
“Hakuna shida!”
Rais hakutulia, muda wote alikuwa akizunguka huku na kule, alichanganyikiwa, mtu aliyekuwa akimuumiza kichwa kwa wakati huo alikuwa Chris ambaye hakujua alikuwa mahali gani.
Alitaka kuficha siri juu ya kila kitu kilichotokea, kitendo cha kijana huyo kutokupatikana kilimaanisha kwamba angekuwa kwenye wakati mgumu sana, alitaka kuona akiuawa haraka iwezekanavyo ili kuifanya ile siri iendelee kuwa siri milele na milele.
Baada ya saa kadhaa vijana watatu wakafika mahali hapo, wakapewa vijana ambao walitakiwa kutangulizana nao kwa ajili ya kuifuatilia simu hiyo kwani ilikuwa ni lazima kumpata mtu aliyekuwa nayo kwa kuhisi kwamba ndiye aliyesababisha ajali au aliliona tukio hilo tangu mwanzo hivyo alikuwa mtu muhimu wa kutoa ushahidi.
Wakaondoka, yeye akabaki ikulu akiendelea kusikilizia kile kilichokuwa kikiendelea. Hakutulia, wakati mwingine hata simu za mawaziri hakuwa akizipokea kwani kile alichokuwa akikisubiria kilikuwa muhimu kuliko simu hizo.
Vijana wale kwa kutumia msaada wa GPRS wakaweza kuinasa simu hiyo. Ilionyesha kwamba ilikuwa katika Mtaa wa Mavizio ambao ulikuwa pembeni kidogo ya Mji wa Motown, mtaa uliokuwa uswahili ambapo kulikuwa na matuki makubwa yaliyokuwa yakitokea kila siku.
“We got him,” (tumemnasa) alisema jamaa mmoja, alikuwa akiwaambia wenzake kumaanisha kwamba GPRS ilisoma mahali alipokuwa mtu huyo.
Wakaanza kumfuatilia, haikuwa kazi nyepesi kwani hapo walipokuwa walitakiwa kuendelea na safari mpaka huko Mavizio kwa ajili ya kuonana na mtu huyo. Huko, walitakiwa kuwa wapole, walijua dhahiri matukio yaliyokuwa yakitokea huko hayakuwa ya kawaida, wanawake walibakwa, watu waliuawa, kulikuwa na matukio mengi yaliyokuwa yakitokea.
Hawakuchukua muda wakafika Mavizio, wakateremka kutoka garini na kuanza kufuatilia simu hiyo ilipokuwa ikionekana kwenye kifaa kidogo walichokuwa nacho. Kulikuwa na ugumu kwani kuifikia ilikuwa ni kupita katika vichochoro vingi, walikutana na wahuni lakini hawakuogopa kwani walikuwa na bastola ambazo zilionekana kama ulinzi kwao.
“Ipo kule mbele, tunaikaribia,” alisema jamaa mmoja wa mtandao wa simu.
Waliendelea kwenda mbele, watu walikuwa wakiwaangalia, kwa jinsi walivyoonekana, hawakuonekana kuwa watu wa kawaida hata kidogo, wengi walihisi kwamba walikuwa polisi waliokuja kumkamata mtu ila hawakutaka tu kuvaa sare. Waliogopwa, kila walipopita, wahuni wengine waliokuwa na bangi mikononi wakaingia ndani kujificha.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ni hapo nyuma,” alisema mwanaume mmoja, walikuwa wamekwishafika sehemu husika, kilichobaki ni kwenda mahali hapo kwani walizisikia sauti za watu wakizungumza kuhusu simu, wakajua ndiyo sehemu yenyewe.
****
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment