Search This Blog

Sunday, 22 May 2022

MWANAHARAMU WA KISIASA - 2

 







    Simulizi : Mwanaharamu Wa Kisiasa

    Sehemu Ya Pili (2)

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ndezi akakata simu, moyo wake ulikuwa kwenye furaha tele kwani alipata simu tatu za bure na hivyo mpango uliokuwepo ulikuwa ni kuziuza na fedha kufanyia mambo yake mengine. Akaondoka na Chris kwenda mitaani kabisa. Muda wote Chris alionekana kuwa na hofu, hakuamini kama yale mauaji makubwa yaliyofanywa yalifanywa na mtu kama Ndezi.

    Umri wake na matendo aliyoyafanya vilikuwa vitu viwili tofauti, alionekana kuwa na umri mdogo lakini alikuwa na roho ya chuma, hakukubali kuona akionewa, hakukubali kuona akifanyiwa jambo lolote baya.

    Walipoondoka hapo, wakaelekea katika Mtaa wa Mavizio, huko, alitaka kwenda kuziuza simu hizo. Walipofika, akaanza kuzitembeza huku na kule, alikuwa akimuonyeshea kila mtu aliyekuwa akikutana naye.

    Zilikuwa simu nzuri, baada ya kuzitembeza kwa dakika kadhaa, akasimamishwa na mwanaume mmoja ambaye naye alizitaka simu hizo kwani kwa muonekano wake zilikuwa nzuri na isingekuwa rahisi kuziacha.

    “Kiasi gani?”

    “Hii laki mbili na nyingine laki laki,” alisema Ndezi hivyo mwanaume yule kumchukua na kumpeleka sehemu ambayo ilikuwa nzuri kufanya biashara hiyo ya wizi.

    “Nakupa laki tatu zote!” alisema mwanaume huyo.

    “Umeua bendi mzazi! Niachie jiwe tatu na nusu,” alisema Ndezi.

    “Hiyo nyingi sana. Si unajua simu zenyewe za wizi hizi zimejaa magumashi, kama vipi kamatia tatu nisepe,” alisema mwanaume huyo, waliendelea kupatana bei pasipo kujua kwamba moja ya simu zile ilikuwa ikifuatiliwa.

    “Tuondoke…” alisema Chris huku akionekana kuwa na hofu, macho yake hayakutulia, yalikuwa yakiangalia huku na kule..

    “Subiri kwanza tupige mkwanja halafu tutasepa.”

    “Ila nina hofu!”

    “Ondoa hofu! Upo na komandoo,” alisema Ndezi huku akiwa na uhakika kwamba kila kitu kilikuwa salama kabisa.

    ***

    Vijana wale walikuwa na uhakika kwamba watu waliokuwa nyuma ya nyumba ile ndiyo ambao walikuwa wakihitajika na Rais Labad hivyo walichokifanya ni kwenda nyuma ya nyumba ile.

    Wakawakuta vijana watatu, baada ya vijana hao kuwaona, wakashtuka kwani hawakutegemea kuona wakifuatwa na watu kama hao ambao kwa kuwaangalia tu walionekana kuwa si watu wa utani hata kidogo.

    Wakawaweka chini ya ulinzi na kuwapokonya simu, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kuwauliza kuhusu simu hiyo, walichowaambia ni kwamba waliinunua kutoka kwa kijana mmoja aliyekuwa na mwenzake.

    “Kijana gani?”

    “Dogo fulani, alinifuata na kusema kwamba anauza simu, tena alikuwa nazo tatu ambazo zote nilizinunua,” alijitetea kijana huyo.

    “Yupo wapi?”

    “Sijajua! Ni mtoto wa mitaani, hata nilipoona anauza simu nilijua angeniuzia kwa gharama nafuu, hivyo nikamlalia,” alijitetea kijana huyo.

    Kwa kumwangalia tu ilionekana kuwa vigumu kuamini kama yeye ndiye aliyeiiba simu hiyo, alikuwa kijana mtanashati, alivalia shati jeupe na alichomekea.

    Hawakuwa wakimuhitaji yeye, waliyekuwa wakimuhitaji alikuwa kijana ambaye aliiba simu hiyo lakini pamoja na hayo, hawakutaka kumuacha, wakamchukua yeye na wenzake na kuondoka nao mahali hapo.

    Rais Labada akapewa taarifa juu ya kile kilichokuwa kimetokea, hakuamini kama kweli alishindwa kufanikisha kumpata kijana huyo ambaye aliamini kwamba alikuwa na Chris ambaye alikuwa akimtafuta kwa udi na uvumba.

    Akawaambia vijana hao wawapige picha na kuwatumia ili kuona kama walikuwa wao au si wao, alivyotumiwa picha na kuziangalia, hawakuwa wao, hakumuona Chris na hata vijana hao walionekana kuwa wasafi kwani mtu ambaye alipokea simu alikuwa mhuni sana.

    “Siyo hao!” alisema Rais Labad.

    “Kwa hiyo hawa tuwafanye nini mkuu?”

    “Waachieni ila wapokonyeni simu zote.”

    Hilo ndilo lililofanyika, halikuhitaji maswali, wakafanya kama walivyoambiwa, wakawapokonya simu na kuwaambia wapotee, wakafanya hivyo.

    Mitaani, vijana walikuwa wakihangaika huku na kule, kumpata Chris lilionekana kuwa jambo gumu, kwa kuwa alikuwa na mtandao mkubwa, Rais Labad akapeleka picha za Chris katika vituo vyote vya polisi na kuwaambia kwamba kijana huyo alitakiwa kutafutwa kimyakimya na picha zake zisitoke nje ya vituo hivyo.

    “Sawa mkuu!”

    Polisi wakaanza kumtafuta Chris mitaani, walikuwa na uhakika kwamba wangeweza kumpata kwani mbali na vituo ishirini vilivyokuwa katika Jiji la Motown, pia kulikuwa na polisi wengi ambapo kwa pamoja waliweka nguvu kwa mtu mmoja tu.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wakaachana na mambo mengi, wakaacha kuwatafuta wavuta bangi, kipindi hicho ndicho biashara haramu ilipokuwa ikifanyika kwa nguvu zote kwani polisi hawakuwa na mpango wa kuwatafuta watu hao, wao walikuwa wameweka nguvu zao kumtafuta Chris tu.

    Kila siku ilikuwa ni lazima kufikisha taarifa kwa mkuu wa kituo juu ya mahali walipofikia ambapo wao walimpigia simu Rais Labad na kumwambia kile kilichotokea.

    Rais hakuamini kama kazi ingekuwa ngumu namna ile, aliamini kwamba kumkamata Chris haikuwa kazi kubwa kwa kuwa alikuwa hapohapo Motown, sasa ugumu ulitoka wapi?

    Alikasirika! Aliendelea kuwasisitizia watu wake kwamba iwe isiwe ilikuwa ni lazima Chris apatikane kwani alijua hatari iliyokuwa mbele yake kama tu wasingehakikisha mtoto huyo anakamatwa.

    Akaagiza ulinzi uongezeke mipakani kwani alijua kwamba kwa namna moja ama nyingine Chris angeweza kuondoka nchini Matapatapa kuelekea Tanzania ambapo huko angeweza kutoa ushahidi juu ya kile kilichokuwa kimetokea.

    “Hakikisheni mipaka inaongezwa ulinzi na picha za huyo mtoto zinasambazwa huko mpaka apatinake! Mmenielewa?” alisema Rais Labad.

    “Ndiyo mkuu!”

    Hilo halikuhitaji kupoteza muda, haraka sana likafanyika, mipakani, picha zikapelekwa, ilikuwa ni lazima wamzuie Chris kama tu angetaka kutoroka nchi hiyo.

    Hakutakiwa kufika nchini Tanzania kwa kuamini kwamba kama angefika huko ilikuwa ni lazima kukutana na waandishi wa habari na hiyo kuwaambia kilichokuwa kimetokea nchini Matapatapa.

    Akaongeza vijana wake mitaani, polisi wote jicho lao likawa kumtafuta Chris, hawakujua alifanya nini wao walichokuwa wakikifanya ni kumfurahisha rais wao kwani bila kufanya hivyo waliogopa kupoteza kazi zao.

    ***

    Ndezi alikubaliana na mnunuaji na kumuuzia simu zote alizokuwa nazo, akapewa kiasi cha laki tatu na kuondoka zake huku akifurahia, hakutaka kubaki na simu zile kwa kuamini kwamba zilikuuwa tatizo kwani angeweza kutafutwa na kukamatwa kwani simu aliyokuwa amepokea, ilimtisha.

    Wakatafuta maji na kunawa, wakatafuta sehemu na kupumzika kwani walijiona kuwa na safari kubwa na bahati kubwa ajali ile haikuwa imewajeruhi kwa kuwa walikuwa katika siti za nyuma.

    Hakujua sababu iliyomfanya Rais Labad kuwatuma watu na kuwakamata, aliamini kwamba yeye hakuwa na tatizo lolote bali mtu aliyekuwa na tatizo alikuwa Chris.

    Alitaka kujua ukweli juu ya kitu kilichokuwa kikiendelea, alitaka kufahamu sababu iliyomfanya kutafutwa na mtu mzito kama Rais Labad. Akamuuliza lakini Chris hakumwambia ukweli, alimficha, kwa jinsi maongezi yake yalivyokuwa, Ndezi akahisi kwamba kulikuwa na tatizo.

    “Niambie ukweli,” alisema Ndezi.

    “Huo ndiyo ukweli! Mimi mwenyewe sijui!” alisema Chris.

    Ndezi alikasirika sana, hakukuwa na kitu alichokuwa akikichukia kama kudanganywa, alimwambia Chris amwambie ukweli vinginevyo kama alikuwa akimdanganganya na siku moja kuujua ukweli basi kungekuwa na tatizo.

    “Ni kwamba anataka kuniua!” alisema Chris.

    “Najua! Ila nisichokijua ni kwa nini anataka kukuua,” alisema Ndezi.

    “Ni kwa sababu aliwaua wazazi wangu!”

    “Wazazi gani?”

    “Wale waliouawa jana mbugani!”

    “Unamaanisha bilionea Massawe aliyeiua familia yake jana?”

    “Ndiyo huyohuyo ila hakuiua familia yake bali iliuawa na watu waliotumwa na rais huyo!” alisema Chris

    “Na wewe ndiye huyo mtoto ambaye anatafutwa kila kona?” aliuliza Ndezi.

    “Ndiyo!”

    “Duuh! Kumbe nipo na brifukesi la pesa halafu sijui. Tufanye mishe tusepe hapa Motown, kushanuka, tusepee zetu Tanzania tukachukue huo mkwanja aliouacha baba yako,” alisema Ndezi huku akionekana kuwa na furaha.

    Walikuwa na pesa, kiasi walichokuwa wamekipata waliamini kwamba kingewawezesha kufika nchini Tanzania. Kulikuwa na njia mbili za kufika huko, wangeweza kupitia mpakani auu baharini, walichochagua, kupitia mpakani ilikuwa rahisi zaidi.

    “Hapa ni kuvuka boda mwana, hakuna jingine,” alisema Ndezi.

    “Sawa.”

    Walichokifanya ni kuchukua daladala iliyokuwa ikielekea Mabweni, Kusini mwa Jiji la Motown, kilometa mia nane kutoka hapo mjini. Huko ndipo kulipokuwa na mpaka wa kuingia nchini Tanzania.

    Ndani ya daladala waliyochukua, walikuwa kimya. Kila mmoja alikuwa na mawazo yake, kwa Chris alikuwa akifikiria kufika salama nchini Tanzania lakini kwa Ndezi alichokuwa akikifikiria kilikuwa ni pesa tu.

    Kitendo cha kuwa karibu na Chris alihisi kwamba yeye ni milionea mkubwa. Hakutaka kumuacha Chris, aliambatana naye na hata kama angepata matatizo pamoja naye, alikuwa radhi lakini mwisho wa siku apate kile alichokuwa akikitaka.

    Hawakujua kwamba hata huko mpakani, kulikuwa na polisi waliokuwa wakiwatafuta kwa udi na uvumba.

    ***

    Umati wa Watanzania ulikusanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwa ajili ya kuipokea miili ya wanafamilia, Bilionea Massawe ambaye alikufa nchini Matapatapa.

    Kila mtu alionekana kuwa na huzuni, wengi walilia, hawakuamini kama kweli bilionea huyo aliiteketeza familia yake kwa kuipiga risasi na kuwamaliza.

    Mioyo yao iliuma na wengi kumlaumu kwamba hakutakiwa kufanya kitu kama kile, hata kama alikuwa na mawazo, hasira alitakiwa kuongea na watu wa ushauri na kumwambia nini cha kufanya.

    Waandishi wa habari hawakukosa uwanjani hapo, kamera zao zilikuwa mikononi kwa ajili ya kupiga picha kila kitu kilichokuwa kikiendelea mahali hapo.

    Ulionekana kuwa msiba mkubwa wa kitaifa kwani bilionea huyo alikuwa mtu wa watu, alipendwa, alikuwa na kampuni nyingi ambazo ziliwaajiri Watanzania wengi.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Viongozi wengi wa kisiasa walikuwa uwanjani hapo, bado hakukuwa na mtu aliyeamini, kila mmoja alikuwa akijiuliza kama iliwezekanaje mwanaume huyo akafanya mauaji hayo katika siku ya matembezi nje ya Tanzania badala ya kuyafanya mauaji hayo hapahapa Tanzania tena nyumbani kwake?

    Huzuni ziliendelea kuwatawala, maswali mengi yaliendelea kuwatatiza vichwani mwao. Wengi walitaka kufahamu kuhusu Chris, hakuwa miongoni mwa watu waliouawa, alikuwa wapi na kwa nini hakuuawa? Wengi walitaka kulifahamu hilo.

    Saa 4:18 asubuhi ndege iliyobeba miili ya marehemu hao ikaanza kuingia uwanja wa ndege. Vilio vilivyokuwa vikisikika mahali hapo, vikaongezeka zaidi, ndugu wengi walilia kwani hawakuwa wakiamini kama huo ndiyo ungekuwa mwisho wa kuwa na ndugu zao hao.

    Ndege ilipotua, majeneza matatu yakatolewa ndani ya ndege na kisha kuanza kusukumwa kwa vyombo vilivyokuwa na mataili kuelekea kule kulipokuwa na umati wa watu.

    Waandishi wa habari wakajisogeza kule na kuanza kupiga picha. Kilichokuwa kikiendelea mahali hapo kilimuumiza kila mmoja. Miili hiyo ikachukuliwa na kupelekwa nyumbani kwao.

    Huko, umati mkubwa wa watu ulikuwa umekusanyika nyumbani hapo, watu walitaka kuona kitu gani kilikuwa kikiendelea kama kuhuzunika, walihuzunika na kulia sana.

    “Jamani! Hivi kweli Massawe ameimaliza familia yake kweli?” aliuliza jamaa mmoja huku akionekana kutokuamini.

    “Hata mimi mwenyewe nashangaa….jinsi jamaa alivyokuwa na furaha na familia yake kweli aliwezaje kuiangamiza? Nahisi si kweli, mimi mwenzenu naanza kuhisi kitu,” alisema msichana mmoja, alionekana kuwa na huzuni mno.

    “Wewe ni kama mimi! Nahisi kuna mchongo umechezwa,” aliongezea mwanaume mwingine.

    Kila mmoja alionekana kuwa na wasiwasi, walimfahamu Massawe, alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakiipenda mno familia zao, kwenye mitandao ya kijamii na sehemu nyingine aliionyeshea kwamba ilikuwa kila kitu katika maisha yake.’

    Kitendo cha taarifa kusema kwamba yeye ndiye aliyeiua familia yake kilimshangaza kila mmoja na kuhisi kwamba kulikuwa na kitu kilichokuwa kimetokea.

    “Kuna kitu hapa.”

    “Hata mimi nahisi hivyo!”

    Hayo ndiyo maneno yaliyokuwa yakisikika msibani hapo, kila mmoja alihisi kwamba kulikuwa na mtu aliyeiangamiza familia hiyo lakini hakukuwa na mtu aliyejua kama familia hiyo iliangamizwa na Rais Labad.

    Japokuwa alikuwa na matatizo nchini kwake lakini hakukuwa na mtu aliyefahamu kama watu hao walikuwa kwenye ugomvi mkubwa. Kutokana na kile kilichotokea, kila mmoja akahisi kwamba kulikuwa na bilionea ambaye alikuwa kwenye ugomvi na marehemu na kuamua kumfanyia unyama huo.

    Polisi hawakutaka kubaki kimya, kwa kile kilichokuwa kimetokea kilikuwa kikubwa mno, ilikuwa ni lazima wafanye uchunguzi wa ndani kugundua ni kitu gani kilitokea, ni mtu gani alisababisha mauaji yale.

    Walijua kwamba kama wangetaka ushirikiano na nchi ya Matapatapa wasingeweza kuupata kwani wao ndiyo waliotangaza kwamba mwanaume huyo aliiangamiza familia yake na mwisho kujimaliza yeye mwenyewe.

    “Ni lazima tuliangalie jambo hili kwa undani, ni lazima tujue kila kitu kilichokuwa kimetokea,” alisema Kamanda Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Mwalami, alikuwa akizungumza na polisi wenzake wa kitengo cha upelelezi.

    Waliamua kuweka kikao hicho ambacho kiliwachukua dakika thelathini, mwisho kabisa wakamalizia kwa kumchagua Edson Mwalugonde, kijana machachari aende nchini MAtapatapa, kulekule kwenye Mbuga ya Kizwalinda kwa ajili ya kufanya upelelezi na kugundua ni kitu gani kilikuwa kimetokea mpaka bilionea huyo aiangamize familia yake.

    Wakati wakimchagua Edson kwa ajili ya kuchunguza juu ya vifo hivyo, hakuwepo nchini Tanzania, alikuwa nchini Uingereza akifurahia maisha baada ya kukamilisha kazi ya kupeleleza kila kitu kilichotokea katika utekwaji wa watoto wengi nchini Tanzania. Kazi hiyo aliifanya na kuimamilisha, wahusika wakakamatwa, hivyo kuelekea nchini Uingereza kwa ajili ya kupumzika.

    Alipopigiwa simu na kupewa taarifa ya kifo cha Bilionea Massawe, alichanganyikiwa, hakuamini kama bilionea huyo aliweza kuimaliza familia yake, kama watu wengine walivyohisi kwamba waliuawa ndivyo alivyohisi hata yeye mwenyewe.

    Hakutaka kuendelea kukaa nchini Uingereza, alichokifanya, kwa haraka sana akaondoka kurudi nchini Tanzania, alipofika, akapewa kazi hiyo na kuambiwa kwamba alitakiwa kuelekea huko, katika mbuga hiyo kama mtalii kutoka nchini Nigeria, hilo halikuwa tatizo, akaahidi kufanya kazi hiyo kwa uadilifu mkubwa kabisa.

    Kesho yake, saa 6:09 mchana alikuwa ndani ya ndege akielekea nchini Matapatapa. Kichwa chake kiliendelea kumfikiria Bilionea Massawe, alifahamu, mwanaume huyo alikuwa roho nzuri, aliipenda familia yake kuliko kitu chochote kile, kila alipokuwa akitafuta uwezekano wa bilionea huyo kuiteketeza familia yake, kitu hicho hakikuingia kabisa kichwani mwake.

    “Hapa kuna kitu! Sidhani kama Bilionea Massawe anaweza kuiteketeza familia yake. Nahisi kuna kitu, na nitakijua tu,” alijisemea huku ndege ikikata mawingu kuelekea nchini Matapatapa.

    Haikuchukua saa nyingi, ikafika huko. Akateremka na kukodi gari ambalo lilimpeleka mpaka katika mbuga hiyo. Ilikuwa vigumu kumgundua kama alikuwa Mtanzania, alizungumza Kiingereza kama Mnigeria, aliiga lafudhi hiyo na kila alipokuwa akizungumza, watu wengine hawakuelewa kutokana na Kiingereza chake kuwa na lafudhi ya Lugha ya Yoruba.

    “Where are from?” (Umetoka wapi?) aliuliza mhudumu wa mapokezi.,

    “Yoruba my friend,” (Yoruba rafiki yangu) alijibu Edson huku akichia tabasamu, kwa jinsi alivyoonekana, alikuwa mcheshi, mpole lakini upande wa pili, huyo jamaa alikuwa hatari hata zaidi ya Mafia.

    ****

    Safari ilikuwa ikiendelea kama kawaida, walikuwa kimya ndani ya basi, kila mtu aliyekuwa humo hakuwa na taarifa kuhusu Chris ambaye naye alikuwa safarini kuelekea nchini Tanzania.

    Walitulia kwenye viti vyao huku wakiwa kimya kabisa, kila mmoja alikuwa akifuatilia safari hiyo. Chris alitamani kufika nchini Tanzania haraka iwezekanavyo kwani aliamini kwamba huko ndipo kulikuwa sehemu salama kuishi kwa maisha yake kuliko kuishi katika nchi kama Matapatapa ambapo alikuwa akitafutwa kila kona.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kwa Ndezi, kwake alitamani kufika Tanzania kama ilivyokuwa kwa Chris, hakufika kwa sababu maisha yake hayakuwa na usalama hapo Matapatapa bali alitaka kufika huko kwa sababu ya pesa, aliamini kwamba wazazi wa Chris walimwachia pesa kwenye akaunti, hivyo naye alitaka kuzitumia.

    Baada ya saa mbili, wakafika katika Kijiji cha Mbilingu, kilikuwa kilometa tano kutoka mpakani. Walipofika hapo, abiria walioshikwa na haja walitakiwa kurudi kwani ndiyo kilikuwa kituo cha mwisho kabla ya kuingia mpakani ambapo huko wangeangaliwa vibali vyao na kisha kuruhisiwa kuingia nchini Tanzania.

    “Nakwenda chooni,” alisema Chris huku akinyanyuka kutoka kitini.

    “Poa! Utanikuta!” alisema Ndezi huku akimwangalia Chris ambaye aliondoka kuelekea nje.

    Chris alikwenda mpaka sehemu iliyokuwa na choo cha kulipia, kwa kuwa alipewa pesa kidogo na Ndezi, akaingiza mkono mfukoni na kisha kulipia, akaingia ndani na kuanza kujisaidia.

    Wakati akiwa huko, ghafla akaanza kusikia sauti za watu nje waliokuwa kama wakilalamika. Hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea, akaingiwa na hofu, harakaharaka akatoka ndani ya choo kile, alichokiona ni kundi la polisi wanne waliokuwa wakiwashusha watu kutoka garini.

    “Mmh! Kuna nini tena?” alijiuliza, polisi wote walikuwa na picha zake mikononi.

    Abiria walikuwa chini, waliambiwa wasimame mistari miwili, wakafanya hivyo na polisi hao kuanza kumwangalia mtu mmoja baada ya mwingine huku wakati mwingine wakiangalia picha, kwani kwa muonekano, hakujulikana kama alikuwa mtu mzima au kijana mdogo.

    Walipomaliza kuwaangalia, wakawaambia waingie ndani ya basi kwani mtu waliyekuwa wakimtafuta hawakuweza kumuona. Chris hakutaka kutoka nda ya choo kile, alijibanza huku akiangalia kilichokuwa kikiendelea.

    Alikuwa kwa mbali lakini aliweza kugundua kwamba picha zilizokuwa zimeshikwa zilikuwa zake na zilionekana kwa ukubwa, zilipigwa kwa mfumo wa pasipoti saizi.

    Wakati abiria wakiingia ndani ya basi, Ndezi akajiweka nyuma nyuma na kuondoka kuelekea upande mwingine, hakutaka kuondoka mahali hapo na kumuacha Chris kwani mtu huyo alikuwa muhimu sana.

    Abiria wakaingia na basi kuondoka mahali hapo. Hakukuwa na mtu aliyejali kwamba kulikuwa nafasi za watu wawili zilikuwa wazi, walichokiangalia kilikuwa ni kuwahi na kuingia nchini Tanzania.

    Basi ilipoondoka, haraka sana Chris akachomoka kule chooni na moja kwa moja kumfuata Ndezi aliyekuwa ameelekea upande wa pili.

    “Ni mimi?” aliuliza Chris.

    “Ndiyo! Wanakusaka sana wapumbavu wale. Hakuna haja ya kuingia Tanzania kupitia mpakani, ni lazima tuingie kupitia njia za panya,” alisema Ndezi.

    Hilo ndilo walilolifanya, hawakutaka kuendelea na safari ya kuelekea mpakani, ilikuwa ni lazima wafanye kila liwezekanalo kuondoka nchini humo kupitia njia za panya.

    Hawakujua hilo lingekuwaje, lingewezekanaje na wakatihitaji mtu wa kumuuliza njia za panya za kuelekea nchini Tanzania kwani waliamini kwamba ni lazima kungekuwa na wajanja waliokuwa wakifahamu njia hizo.

    “Mna kiasi gani?”

    “Kwani wewe unahitaji kiasi gani?” aliuliza Ndeezi kwa kujiamini sana.

    Jamaa huyo hakujibu kitu, kwanza akawaangalia, akawapandisha na kuwashusha, walionekana kuwa watoto wa mitaani japokuwa kwa Chris alionekana kuwa kawaida kutokana na mavazi yake ambayo hayakuwa machafu sana kama Ndezi.

    “Nipeni buku kumi,” alisema mwanaume huyo huku akiwa haamini kama vijana hao wangeweza kutoa hata shilingi elfu tano.

    Hilo halikuwa na tatizo, Ndezi akaingiza mkono mfukoni na kutoa kiasi cha shilingi elfu kumi na kumkabidhi. JAmaa akapokea na kuwaambia wamfuate kule alipokuwa akienda.

    Wakaondoka mahali hapo, safari ya kuelekea huko kwenye njia za panya za kuingia nchini Tanzania ikaanza. Walikuwa makini, walitembea porini, ilikuwa ni safari ndefu na yenye kuchosha sana mpaka walipofika sehemu iliyokuwa na mto mkubwa ambapo kwa juu yake kulikuwa na daraja.

    “Naishia hapa, nimewasindikiza sana,” alisema jamaa yule.

    “Kwa hiyo tutafikaje?” aliuliza Chris.

    “Ni rahisi, nyie nendeni na njia hiyo, moja kwa moja mpaka mtafika,” alijibu mwanaume yule.

    “Mmh!”

    “Nyie wanaume bwana! Au mnaogopa simba?”

    “Kwani kuna simba?”

    “Ndiyo! Itawabidi muwe makini sana,” alisema jamaa yule maneno yaliyomfanya kila mmoja kuogopa.

    Hawakuwa na sababu ya kusubiri mahali hapo, wakaondoka na kuendelea na safari yao. Walilivuka daraja lile lililoonekana kuwa bovu sana, walikuwa makini, walivuka na kwenda upande wa pili.

    Walikuwa porini, sehemu hiyo ilitisha kupita kawaida. Kila walipokuwa wakipiga hatua, mioyo yao ilidunda kwa nguvu kwani waliona kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wao kama tu wangekutana na mnyama mkali.

    “Hivi itakuwaje tukikutana na simba?” aliuliza Chris huku akiangalia huku na kule.

    “Sijui! Labda tutamuua simba au yeye kutuua!” alijibu Ndezi huku akimwangalia Chris.

    Waliendelea kwenda mbele mpaka kukutana na shamba kubwa la mpunga. Hiyo ilikuwa dalili iliyowaonyesha kwamba kulikuwa na makazi ya watu karibu na eneo hilo hivyo kuanza kuvuka.

    Walikuwa makini, waliangalia huku na kule kuona kama wangemuona mtu yeyote yule. Kinyume na mategemeo yao, hawakuweza kumuona mtu yeyote mpaka walipomaliza eneo la shamba hilo la mpunga na kuendelea kusonga mbele.

    Baada ya kutumia muda wa saa nne kutembea ndipo wakafika katika eneo ambalo lilikuwa na bango lililloandikwa ‘Danger’ kwa maana ya hatari huku kukiwa na alama iliyowaonyeshea kwamba hawakutakiwa kuvuka.

    Kwa kuliangalia, ni kweli lilionekana kuwa eneo la hatari. Kulikuwa na harufu kali ya mzoga, walihisi kwamba inawezekana ulikuwa mzoga wa mnyama lakini kwa jinsi harufu kali iliyokuwa ikiendelea kuzisumbua pua zao, ilionyesha mzoga huo ulikuwa ni zaidi ya mnyama wa mwituni.

    “Harufu kali sana,” alisema Ndezi huku akiziba pua yake.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wakapiga macho mbele, walichokiona, walishtuka, kulikuwa na masalia ya mwili wa binadamu, ulikuwa umegawanyika vipandevipande, mikono ilikuwa sehemu nyingine, miguu sehemu nyingine, kichwa na viungo vingine, hali iliyoonekana, iliwatisha.

    “Mmh! Kuna nini? Ameliwa na simba au?” aliuliza Chris, hakuonekana kujua kilichokuwa kimetokea.

    “Hatujui! Tuvuke twende Tanzania,” alisema Ndezi.

    “Subiri kwanza.”

    “Nisubiri nini?”

    “Unakiona hicho kibao?”

    “Ndiyo!”

    “Unajua maana ya hilo neno?”

    “Hapana!”

    “Linamaanisha hatari! Yaani sehemu tuliyokuwepo hapa ni ya hatari,” alisema Chris.

    “Sasa hatari ya nini?”

    “Sijui! Ila ni ya hatari sana,” alisema Chris.

    “Huo uoga Chris. Tuvuke!”

    Walijua kwamba kwenye njia za panya walizokuwa wakizitumia, hapo ndipo palikuwa pa kupenyea. Kitu kilichowashangaza, hawakuweza kuona mtu yeyote katika eneo hilo zaidi ya kupambana na harufu kali ambayo ilitokana na mzoga wa mtu uliokuwepo mahali hapo.

    “Ila hapa kutakuwa na tatizo…” alisema Chris.

    “Tuvuke. Kama imeandikwa tufe leo, tutakufa tu! Tuvuke,” alisema Ndezi pasipo kujua kwamba kwa kipindi hicho, sehemu za njia za panya zote kulitegeshwa mabomu ya kufukia ambayo yalilipuka baada ya kukanyagwa na watu. Hivyo wakaanza kuinua miguu kuvuka hapo kulipokuwa na mabomu ili waingie nchini Tanzania.



    Polisi hawakuacha kumtafuta Chris, walitanda mipakani, walipekua kwenye kila gari, iwe daladala, basi au hata magari ya watu binafsi lakini bado hawakuweza kumuona mtoto huyo.

    Walichanganyikiwa, hawakujua ni kitu gani walitakiwa kufanya kuhakikisha Chris anakamatwa kilazima. Kila siku waliambiwa na wakuu wao wa vituo kuhakikisha mtoto huyo anakamatwa kwani nao pia walipokea vitisho kutoka kwa Rais Labad kitu kilichomfanya kila mmoja kuwa na presha kubwa.

    “Huyu mtoto mbona nilimuona,” alisema mwanamke mmoja mara baada ya kuonyeshewa picha ya Chris.

    “Wapi?”

    “Hapahapa Mbilingu!” alijibu mwanamke huyo.

    “Kweli?”

    “Ndiyo! Alikuwa na mwenzake chokoraa!”

    Polisi yule akawaita wenzake na kuwaambia wamsikilize mwanamke yule aliyesema kwamba alimuona Chris akiwa na mwenzake. Mwanamke yule hakubadilisha maneno, aliendelea kuwaambia kwamba aliwaona na alihisi kwamba ni vijana wabaya kwani polisi walipokuwa wakipekua abiria kwenye basi moja, kijana huyo alijificha mpaka baadaye alipoungana na mwenzake.

    “Safi sana. Wameelekea wapi?”

    “Njia ile kule,” aliwaonyesha njia aliyoondokea Chris na mwenzake.

    Hakukuwa na sababu ya kuendelea kubaki mahali hapo, wakaondoka na gari lao kuelekea huko huku kila mmoja akiwa na presha kubwa. Wakawasiliana na mkubwa wao na kumwambia kile kilichotokea kwamba muda wowote ule huyo mtoto na mwenzake wangepatikana.

    Waliijua njia hiyo, walijua fika kwamba vijana hao walitaka kuvuka mpaka na kuingia nchini Tanzania ila hiyo njia waliyotaka kuitumia ilikuwa ni hatari kubwa kutokana na kuwa na mabomu mengi.

    Dereva aliendesha kwa mwendo wa kasi, mtoto huyo hakuhitajika kufa, alitakiwa kupatikana akiwa hai haraka iwezekanavyo kwani vinginevyo mambo yangekuwa mabaya kwao, na hakutakiwa kabisa kuingia nchini Tanzania.

    Waliendelea na safari yao kwa gari mpaka walipofika katika daraja lile dogo, wakateremka na kuanza kuvuka na kuliacha gari hilo mahali hapo. Walitembea na kukimbia kwa dakika tisini ndipo kwa mbali wakasikia mlio mkubwa wa bomu. Hawakujiuliza, wakapata majibu kwamba bomu hilo lilipuka kule mpakani na hivyo kijana huyo na mwenzake wangekuwa wamekufa.

    “Jamani! Amekanyaga bomu,” alisema jamaa mmoja huku akionekana kukata tamaa.

    “Ndiyo! Nilijua hilo tu! Twendeni tu tukauchukua mwili wake,” alisema jamaa mwingine, kila mmoja alikuwa na uhakika kwamba Chris alikuwa amekufa baada ya kukanyaga bomu na kulipuka huko mpakani katika njia za panya.

    ***

    Chris na Ndezi hawakujua ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea mahali hapo, hawakuwa na taarifa kwamba kulikuwa na mabomu yaliyokuwa yamechimbiwa ardhini, kila mmoja alikuwa na uhakika kwamba hiyo ilikuwa njia nyepesi ya kuwafanya kuingia nchini Tanzania na si kule katika mpaka ambao wangehitajika kuonyesha vibali vyao.

    Wakati wakitaka kuvuka, ghafla wakaanza kusikia sauti ya mtu nyuma yao ikiwaaambia kwamba hawakutakiwa kuvuka mahali hapo. Hawakujua ni kwa sababu gani, walisimama na kugeuka nyuma, mwanaume mmoja alikuwa akikimbia kuwafuta kule walipokuwa.

    “Simameni…simameniiiii…” alisema mwanaume huyo kwa sauti huku akiwakimbilia.

    Hawakujua ni kitu gani walitakiwa kufanya, hawakumjua mwanaume huyo alikuwa nani na kwa nini alikuwa akiwasimamisha, tena huku akiwakimbilia kitu kilichowafanya kuogopa.

    “Tusimame?” aliuliza Chris.

    “Haiwezekani! Tutasimama vipi sasa! Tusepetue,” alisema Ndezi huku akimshika Chris mkono tayari kwa kukimbia na kuvuka mahali pale.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kuna mabomu hapo. Kuna mabomu mtalipuka,” alisema mwanaume huyo maneno yaliyowafanya wote kuogopa kwani hawakuamini kusikika kwamba sehemu hiyo ilikuwa na mabomu.

    Walibaki huku wakitetemeka, hawakuwa na cha kufanya zaidi ya kusimama na kumsubiri mwanaume huyo ambapo baada ya kuwafikia, akawauliza mahali walipokuwa wakienda, na kwa nini walikuwa wakitumia njia hiyo.

    “Tunataka kuingia Tanzania!” alijibu Ndezi.

    “Mna hatari sana! Hii si sehemu salama hata kidogo!” alisema mwanaume huyo huku akiwaangalia kwa zamu.

    “Sehemu salama ni ipi? Na kwa nini hii si salama?” aliuliza Chris.

    “Twendeni huku,” alisema mwanaume huyo na kuwataka kumfuata.

    Hawakuwa na jinsi, walikubaliana naye na kuanza kwenda nao huko alipowaambia. Walipofika kama umbali wa hatua mia moja, mwanaume yule akachukua mawe makubwa na kuanza kuyarusha kule kulipokuwa na mabomu kwa lengo la kuwahakikishia kwamba kile alichokuwa akikizungumza kilikuwa kweli kabisa.

    “Puuuuuu!” ulisikika mlipuko mkubwa.

    Wakabaki wakishangaa, hawakuamini kama maneno ya mwanaume yule yalikuwa ya kweli mpaka pale walipohakikishiwa na kuamini kwamba sehemu ile haikuwa salama hata kidogo.

    Wakaondoka na kuelekea mbele kabisa, hawakupajua, walikuwa wakimwamini mwanaume yule kwamba angeweza kuwasaidia kwani kama mtu aliwaokoa kutoka kwenye ile sehemu iliyokuwa na mabomu, ingekuwa vigumu vipi kumuamini mtu huyo?

    Waliendelea kwenda mpaka walipofika umbali wa kilometa mbili ndipo mwanaume huyo akawaambia kwamba sehemu walipofika ilikuwa salama kuvuka na kama wangefanikiwa kupita wangeibukia katika Kijiji cha Mawimuhi kilichokuwa Horohoro nchini Tanzania.

    “Tunashukuru sana! Ila hatuna hela ya kukupa kwa msaada wako,” alisema Ndezi, alijua kabisa kwamba mwanaume huyo angehitaji pesa.

    “Wala msijali! Nimewasaidia tu!” alisema na kuwaacha, wakaondoka zake.

    Mwanaume huyo akajiona shujaa, moyo wake ukawa na furaha tele kwa kuwasaidia watoto wale. Akaondoka kurudi nyumbani kwake huku akisikia amani kubwa moyoni mwake.

    Baada ya dakika kumi, macho yake yakatua kwa watu sita waliokuwa wakija kule alipokuwa, hakujua walikuwa wakina nani lakini baada ya kufika karibu akagundua kwamba watu hao walikuwa polisi. Wakamsimamisha.

    “Ulisikia mlipuko wa bomu?” aliuliza polisi mmoja huku akimwangalia mwanaume huyo.

    “Ndiyo wakuu!”

    “Kilikuwa nini?”

    “Mimi mwenyewe sijajua wakuu!”

    “Hakuwa huyu mtoto?” aliuliza polisi mwingine huku akimuonyeshea picha ya Chris.

    “Hapana hakuwa huyo!”

    “Umejuaje kama si yeye?”

    “Kwa sababu nimetoka kuonana naye sasa hivi akiwa na rafiki yake, wanaelekea Horohoro sasa hivi,” alisema mwanaume huyo kwa kujiamini.

    “Wamekwenda njia gani?”

    “Nyoosheni moja kwa moja, watakuwa hawajafika mbali. Mkiwawahi kabla ya kuingia msituni, mtakuwa mmewafikia na mtawapata,” alisema mwanaume huyo, polisi hawakutaka kupoteza muda, wakaanza kukimbia kuelekea kule walipoambiwa waende huku wakiziweka vizuri bunduki zao. Piga ua ilikuwwa ni lazima wapatikane hata kabla hawafika hapo Horohoro.



    Ilikuwa vigumu sana kugundua kwamba Edson alikuwa mpelelezi aliyetumwa kutoka nchini Tanzania. Aliendelea kuwalaghai kwa kuongea Kiingereza kwa lafudhi ya Kabila la Yoruba nchini Nigeria na wakati ukweli alikuwa Mtanzania aliyekuwa akizungumza Kingereza kizuri tu.

    Alikuwa muongeaji. Baada ya kukaa kwa siku tatu, kila mtu hotelini alipokuwa alimjua kama mtu mcheshi ambaye hakutaka kuwa kimya, muda wote alikuwa akizungumza kama kompyuta huku akiwachekesha wafanyakazi wa hotelini hapo kitu kilichowafanya kuwa karibu naye.

    Wengi wakapenda ukaribu naye, hawakujua mwanaume huyo alikuwa mahali hapo kwa sababu gani. Alichokifanya ni kujenga ukaribu na kijana mmoja aliyeitwa Hussein ila alikuwa maarufu mahali hapo kama Joker.

    Huyo ndiye alikuwa swahiba wake, hiyo haikumaanisha kwamba hakuwa akizungumza na wengine, uchangamfu wake uliendelea kama kawaida japokuwa kwa Joker ndiye alikuwa mtu wa karibu sana.

    Huyo ndiye aliyekuwa akiongozana naye kuingia mbugani, ndiye aliyekuwa akimuonyesha sehemu za kuwinda na sehemu ambazo hawakuruhusiwa kuwinda. Edson hakuona kama jambo hilo lingewezekana kama asingetumia fedha hivyo alichokifanya ni kufungua pochi kwa kuamini kwamba angepewa kila kitu ambacho angekihitaji.

    Baada ya wiki mbili, Edson akaanza kupata mambo mengi mahali hapo kupitia Joker, aliamini kwamba asingenyimwa kitu alichokuwa akikihitaji kwani fedha alizokuwa akitumia na Joker zilikuwa nyingi kiasi cha kutosha kuufumbua mdomo wake kumwambia kila kitu.

    “Joker, are you courageous enough,” (una moyo wa ujasiri?) aliuliza Edson huku akimwangalia Joker.

    “What do you mean?” (unamaanisha nini?) aliuliza huku akimwangalia mwanaume huyo.

    “Hahah! I want to tell you something…” (nataka nikwambie kitu kimoja) alisema Edson.

    “What is it?” (kitu gani?)

    “Are you courageous enough?” (una moyo wa ujasiri?) alilirudia swali lake.

    “Yeah!”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hiyo yote ilikuwa ni kutaka kumuonyeshea mwanaume huyo kwamba kwa urafiki waliokuwa nao hakukuwa na mambo ya kufichana kabisa, kwa sababu walikuwa na ukaribu basi kila kitu walitakiwa kuambiana.

    Alimdanganya kwa kumwambia kwamba yeye alikuwa mtoto wa mchungaji nchini Nigeria, alikwenda Matapatapa kwa sababu kulikuwa na kazi kubwa aliyotakiwa kuifanya. Hapo Matapatapa kulikuwa na kazi nyingine kubwa ambayo alifika kwa ajili ya kuifanya, kazi hiyo ilikuwa ni kuchukua mzigo wa madawa ya kulevya na kuyapeleka nchini Nigeria.

    Aliendelea kumwambia kwamba baba yake aliutumia uchungaji kama kivuli, nyuma ya pazia kulikuwa na siri kubwa, biashara ya madawa ya kulevya ambayo alikuwa akiifanya kwa kipindi kirefu. Aliua watu, wale wote waliokuwa wakiwafanyia utapeli na katika kipindi hicho alifika mahali hapo kwa ajili ya kufanya mauaji.

    “Ya nani?” aliuliza Joker huku akimshangaa.

    “Kuna bilionea nilipewa taarifa anakuja hapa. Nimekuja kwa kazi moja ya kumuua lakini nashangaa mpaka sasa hivi hajafika,” alisema Edson huku akimwangalia Joker.

    “Yupi?”

    “Mwenzetu ambaye tunashirikiana kazi hii! Alitutapeli mzigo mkubwa sana,” alisema Edson.

    “Nani huyo?”

    “Ni Mtanzania, anaitwa Massawe. Nilipewa taarifa kwamba angekuja wiki hii au ijayo,” alisema Edson.

    “Massawe?”

    “Ndiyo! Mbona umeshtuka?”

    “Nimeshangaa!”

    “Kwa nini?”

    “Mbona aliuawa wiki zilizopita!” alisema Joker, alimshangaa Edson, ilikuwaje mpaka kutokufahamu jambo kama hilo.

    “Aliuawa? Kuna watu waliniwahi?”

    “Ndiyo! Aliuawa kama wiki tatu zilizopita,” alisema Joker huku akimwangalia Edson ambaye alikwenda pembeni na kuanza kujilaumu kwa kujipigapiga mikononi mwake hali iliyomuonyeshea Joker kweli mwanaume huyo alikuwa na hasira na Bilionea Massawe.

    “Hao waliomuua ni Wanaigeria?” aliuliza.

    “Hapana! Watu wa hapahapa Matapatapa!”

    “Au ndiye yule niliyesikia kwamba aliiua familia yake?”

    “Ndiye huyohuyo! Hakuwa ameiua, hiyo ni stori iliyozagaa ila ukweli ni kwamba kulikuwa na watu walimuua,” alisema mwanaume huyo kwa kujiamini.

    “Sasa kama walimuua, kwa nini hawakumuua mtoto wake mmoja?”

    “Hilo ndilo linamshangaza kila mtu. Eti aliwakimbia!”

    “Duu! Basi makubwa! Na chumba kilichofanyikia mauaji ni kipi?”

    “Namba 23! Kimefungwa kwa muda mpaka baada ya miezi sita,” alijibu Joker.

    “Sawa. Hivi kuna klabu huku twende japo kuruka majoka?” aliuliza Edson, alimtoa kabisa Joker katika stori kuhusu Bilionea Massawe.

    “Ipo Manyaranyara! Ni kali sana, mademu wakali wa kumwaga.”

    “Basi tutakwenda huko. Tule sana bata,” alisema Edson.

    Moyo wake ulifurahi, alitaka kupata uhakika juu ya kile kilichokuwa kimetokea, aliambiwa kwamba Bilionea Massawe hakuwa ameiangamiza familia yake bali aliuawa na watu kutoka hapohapo Matapatapa. Hakujua ni wakina nani walihusika katika mauaji hayo lakini alitakiwa kupambana mpaka anaupata ukweli juu ya wauaji huyo.

    “Mtoto! Yupo wapi? Ni lazima nijue mahali alipo hata kabla sijafanya kitu chochote kile,” alijisemea.

    Usiku huohuo wakaondoka kuelekea klabu. Mpaka kipindi hicho Joker hakujua kwamba mwanaume aliyekuwa naye alikuwa mpelelezi, alijifanya muuza madawa ya kulevya ambaye alifika Matapatapa kwa ajili ya kumuua Bilionea Massawe ambaye tayari alikuwa ameuawa yeye na familia yake.

    Joker alikunywa pombe, aliwakumbatia wanawake na kuwafanyia uchafu wote aliotaka kuwafanyia kwa sababu tu alikuwa na mtu aliyekuwa na fedha pembeni yake. Baada ya kucheza sana, saa nane usiku wakarudi hotelini.

    Edson hakulala, kichwa chake kiliuma na kitu pekee alichokuwa akikihitaji kipindi hicho ni kuingia ndani ya chumba namba 23 ambacho ndicho walichochukua Massawe na familia yake.

    Alitaka kupiga picha mazingira ya chumba kile, jinsi yalivyokuwa kwani ilikuwa ni lazima aone ni jinsi gani chumba kilivyokuwa mpaka mauaji yalivyotokea. Ilipofika saa tisa usiku, akagundua kwamba katika chumba alichokuwemo kulikuwa na mlango wa kuingilia darini, hiyo ilikuwa nafasi kubwa kwake kwani aliamini kwamba angefanikiwa kupanda juu basi kutumbukia ndani kusingekuwa na tatizo lolote lile.

    Hakutaka kuendelea kusubiri, usiku huohuo akasogeza meza ndogo iliyokuwa humo ndani na kisha kupanda juu. Akafanikiwa kuufungua mlango wa dari lile na kisha kuingia. Kulikuwa na giza totoro hivyo alichokifanya ni kuwasha tochi ya simu yake na kuanza kukanyaga mbao ili asiweze kugundulika.

    Kutoka chumba alichokuwepo mpaka katika chumba namba 23 hakikuwa mbali, kulikuwa na vyumba vitano katikati yao. Aliendelea kukanyaga mbao zile huku akiendelea kusogea mbele mpaka alipohakikisha kwamba tayari alikuwa amefika pale kulipokuwa na chumba kile, akatafuta mlango kwa ajili ya kuingia ndani ya chumba kile lakini bahati mbaya kwake, hakukuwa na mlango wowote ule.

    “Haiwezekani kuingia. Ni lazima nilitoboe hili dari,” alisema.

    Kazi hiyo haikutakiwa kufanyika usiku huo kwani aliamini kwamba watu wengine wangesikia na kuhoji. Kazi kama hiyo ilitakiwa kufanywa mchana hivyo piga ua ilikuwa ni lazima kuhangaika ili afanye kazi hiyo pasipo kugundulika.

    Ilipofika asubuhi, akamwambia Joker kwamba alitaka kuondoka hivyo kulikuwa na baadhi ya vitu alivyokuwa akivihitaji kwa hali na mali. Akamuagiza amtafutie msumeni mwembamba ambao ni mgumu pamoja na misumali ya nchi sita. CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hilo halikuwa na tatizo, Jiker akaondoka kwa ajili ya kumpelekea vitu hivyo. Baada ya saa moja, akaletewa, akavichukua na kukaa na vyo chumba. Ilipofika saa nne asubuhi, haraka sana akaondoka mpaka katika choo cha wafanyakazi ambacho kilikuwa humo, akaingia na kisha kulibomoa bomba, likaanza kumwaga maji hovyo.

    Aliporudi chumbani akamsikia msichana mmoja ambaye alikuwa mfanyakazi hotelini humo akikimbia kutoa taarifa ya bomba hilo ambapo haraka sana mafundi wakaitwa kwa ajili ya kufanya kazi ya kulirekebisha bomba hilo.

    Wakati mafundi walipokuwa wakigongagonga, naye akapanda juu ya dari na kuanza kuelekea kule kulipokuwa na chumba kile, alipofika, akachukua misumali, akapigilia kupata upenyo wa kupitisha msumeno wake, akafanikiwa.

    Si kwamba watu hawakusikia, walisikia lakini walihisi kwamba ni wale mafundi ndiyo waliokuwa wakisababisha hali hiyo hivyo wakapuuzia. Edson alichukua dakika kadhaa, akatoboa tundu kubwa, kabla ya kutumbukia ndani ya chumba kile, akachungulia, chumba kilikuwa shaghalabaghala, kulikuwa na michirizi ya damu, tangu mauaji yafanyike, hakukuwa na usafi wowote ule uliofanyika chumbani humo, hivyo akarukia ndani.

    “Puuu!” akatua kama komandoo na kuangalia huku na kule.



    Chris na Ndezi waliendelea kusonga mbele, walikuwa kwenye haraka na muda mwingi walikuwa wakikimbia zaidi kuliko kutembea. Ndoto zao zilikuwa ni kuingia nchini Tanzania sehemu ambayo waliamini kwamba wangekuwa salama maisha yao yote.

    Hawakujua kama walikuwa wakifuatiliwa na polisi wa nchini Matapatapa. Walitembea na baada ya dakika kadhaa, wakaanza kuingia kwenye pori kubwa ambalo hilo ndilo lingewawezesha kuingia nchini humo kwa kuamini maisha yao yangekuwa salama salmini.

    Waliendelea kusonga mbele, pori lilikuwa linatisha lakini hawakutaka kusimama njiani, waliendelea kusonga mbele mpaka walipokutana na Mto Uyomi ambapo hapo wakatulia huku wakijifikiria ni kwa namna gani wangeweza kuvuka kwani ulikuwa mto mkubwa, uliokuwa na maji mengi.

    Walitulia pembezoni mwa mto, hakukuwa na mtumbwi wowote, waliendelea kubaki mahali hapo huku wakiendelea kutafakari ni kwa jinsi gani wangeendelea na safari yao kwani pia ua ilikuwa ni lazima wasonge mbele, wasingeweza kurudi nyuma ambapo kulikuwa na hatari zaidi.

    Pale walipokuwa wakafanikiwa kuliona gogo moja kubwa likiwa pembeni, hilo likawapa matumani kwamba kama wangelichukua basi ingekuwa kazi rahisi kwao kuvuka kwa kulitumia gogo hilo. Wakalifuata ili waweze kulitupa mtoni kwani hawakutaka kupoteza muda zaidi mahali hapo.

    Wakati wamelifikia gogo hilo, wakaona bango likiwa pembeni huku kukiwa na maneno yaliyosomeka ‘Hatari! Kuna mamba wengi ndani ya mto huu’. Wakashtuka, hawakutegemea kukutana na hali kama hiyo, mapigo yao ya moyo yakaanza kuwadunda kwa nguvu na kuhisi kwamba kama wangefanya mchezo wangeweza kuliwa na mamba hao waliokuwa mtoni.

    “Kwa hiyo?” aliuliza Chris huku akimwangalia Ndezi.

    “Hapa ni kuvuka tu! Hakuna kusubiri!” alisema Ndezi.

    “Na mamba?”

    “Acha watule, ila kubaki, haiwezekani! Bora uliwe na mamba kuliko kupigwa risasi,” alisema Ndezi.

    Chris hakuwa tayari kuvuka, aliogopa, alimwambia Ndezi kwamba asingeweza kuvuka ndani ya mto huo na kuelekea ng’ambo ya pili lakini Ndezi alimwambia kwamba iwe isiwe ilikuwa ni lazima wavuke.

    Walibaki kwenye malumbano, hakukuwa na muafaka waliokuwa wameufikia, ndani ya dakika kumi za malumbano makali, wakaanza kusikia sauti za watu kutoka nyuma yao ambao walikuwa wakipiga kelele kwamba walikuwa wamewaona. Hata kabla hawajajiuliza watu hao ni wakina nani, milio ya risasi ikaanza kusikia, bahati nzuri risasi hizo ziliwakosa na kuingia mtoni.

    “Chris, turuke!” alisema Ndezi kwa harakaharaka.

    “Siwezi!”

    “Turuke Chris! Siwezi kukuacha hapa utakufa na siwezi kuelekea Tanzania bila wewe! Turuke!” alisema Ndezi huku akimshika Chris mkono.

    “Naogopa mamba….” alisema Chris lakini hata kabla hajaongeza maneno mengine, Ndezi akamsukuma Chris kwa nguvu ndani ya mto ule uliokuwa na mamba wengi.

    ****

    Polisi wale waliendelea kuelekea mbele zaidi, walikuwa na kiu kubwa ya kumpata Chris ambaye alionekana kuwa mtu hatari sana. Walipokea vitisho kutoka kwa Rais Labad ambaye aliwaambia mapema kama wasingeweza kumpata Chris basi ajira zao zingekuwa hatarini.

    Walizidi kusonga mbele kwa kuamini kwamba huko wangeweza kumpata Chris ambaye alikuwa na mwenzake wasiyemfahamu. Walimtaka, hata kama maiti yake, bado waliitaka kwa udi na uvumba.

    Waliingia katika pori lile kubwa, ilikuwa ni kazi kubwa kugundua upande waliokuwa wamekimbilia hivyo kujigawa wawiliwawili na kueleka pande tatu porini humo, wamtafute na wahakikishe anapatikana, na hata ikiwezekana wamuue na kumpeleka rais maiti yake.

    “Hata tukiipata maiti yake itakuwa sifa kwetu, ni lazima tuhakikishe anapatikana haraka iwezekanavyo,” alisema kijana mmoja huku akiiweka vizuri bastola yake.

    “Kweli kabisa. Tuhakikishe anapatikana!”

    Waliendelea kusonga mbele, baada ya kwenda kwa mwendo wa dakika ishirini wakafanikiwa kuziona alama za miguu ya kina Chris waliokuwa wameelekea mbele yao, katika njia ambayo ilikuwa na nyasinyasi mbichi na udongo uliokuwa umelowanishwa na maji.

    Vijana wawili hao wakaongeza kasi kuelekea kule kulipokuwa na alama hizo za miguu. Walipofika kama hatua mia moja kabla ya kuufikia mto wakawaona Chris na Ndezi wakiwa pembezoni mwa mto huku wakionekana kuzozana.

    “Wale pale, wale pale,” alisema jamaa mmoja.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Tuwapige risasi!” alisema mwingine na kuanza kuwarushia risasi.

    Hilo likawashtua Chris na Ndezi, waliendelea kuzozana kwa sekunde chache na hapohapo kuwaona wakitumbukia ndani ya mto huku Chris akiwa amesukumwa.

    Hawakutaka kuchelewa, nao, kwa kasi kubwa wakaanza kuelekea kule, walipofika, hawakutaka kubaki nchi kavu, nao wakaingia mtoni kwani kama wasingefanya hivyo ilimaanisha kwamba watu hao wangeweza kuvuka na kuelekea upande wa pili kitu ambacho kingekuwa vigumu sana kuwapata.

    Walionekana kama kuchelewa, hawakukiona kibao kilichoonyesha kwamba kulikuwa na mamba mtoni. Waliwaona Chris na Ndezi wakiendelea kusonga mbele. Majamaa hao walipofika katikati ya mto, tayari Chris na Ndezi wakawa wakitoka mtoni hivyo kwa haraka sana kuchukua bastola zao zilizokuwa viunoni, wakawanyooshea kwa lengo la kuwaua.

    “Tuwapige wote,” alisema jamaa mmoja, wakakoki bastola zao huku wakiwa katikati ya mto ule.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog