Simulizi : Njama
Sehemu Ya Tano (5)
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilitoka ndani ya jengo hili upesi upesi. Nilipofika nje nikaona niko kwenye mabohari ya Chang'ombe. Bohari hii ilikuwa imezungukwa na ua wa matofali. Nilivua joho jekundu nikapanda ua nikatokea katika uchochoro nikaanza kukimbia. Nilikadilia kuwa ilikuwa yapata saa kumi na moja. Nilipofika mbele ya bohari nilikuta ni mali ya Kampuni moja ya matairi ya magari iitwayo "Trans World Tyres", kwa sababu sikutaka kufanya uchunguzi zaidi kutokana na hali niliyokuwemo niliona teksi nikaipungia ikasimama na kumwamuru dereva anipeleke Independence Avenue haraka.
"Ohuu. Bosi umetokea wapi?". Linda aliuliza huku akitoa pumzi ndefu ya kuonyesha wasi wasi aliokuwa nao umemtoka.
"Nimetoka mahabusu".
"Pole sana bosi".
"Usinipe pole sasa hivi, mapambano bado kabisa yanaendelea, utanipa pole nikiweza kumaliza mapambano haya kwa usalama. Eddy yuko wapi?".
"Yuko katika shughuli za kujaribu kukutafuta apate kujua uliko. Lakini kila baada ya muda mchache anauliza hapa".
"Akipiga tena simu mwambie arudi haraka. Je Sherriff yuko wapi?".
"Wote wako pamoja".
"Haya kaniletee Sandwich za nyama ya kuku na niwekee glasi ya whiski ofisini kwangu. ninakwenda kunawa kidogo".
Baada ya kumaliza kunawa niliingia ofisini kwangu na kuanza kunywa whiski na Sandwich alizokuwa ameleta Linda.
"Chifu yuko?", niliuliza.
"Amesema muonane saa moja bila kukosa", Linda alijibu.
Mara simu ililia ofisini kwa Linda. Linda akashika simu yangu iliyokuwa imeunganishwa na yake. Alibonyeza kidude kimoja baada ya kuinua mkono wa simu.
"Hello nani hapo?", Linda aliuliza".
"Oh Eddy, rudi hapa haraka Bosi yuko hapa. Yuko hai kabisa ameketi kwenye kiti chake anakunywa whiski"....
"Haya asanhte", Linda aliweka simu huku akicheka.
"Nakwambia bosi ungesikia sauti ya Eddy niliposema uko hapa. utafikiri mtu aliyekwamwa na mwiba wa samaki".
Simu iliita tena ofisini kwa Linda na Linda akachukua simu.
"Hello nani hapo?", Linda aliuliza. "Ehe Unasemaje Issack... Eddy bado hajafika hapa, lakini atafika muda si mrefu, na kama una habari muhimu Bosi yuko hapa". "Oke, njoo haraka sana", Linda alijibu na kukata simu.
"Vijana wa Eddy aliokuwa amewasambaza, huyu Issack na mwenziwe ndio walikuwa na jukumu la kuangalia mienendo ya Sikazwe", alisema Linda.
"Ghafla mlango wa ofisi yangu ulifunguliwa, Sherriff, Eddy na Zabibu wakaingia ndani.
"Pole sana Bosi, sisi tulijua kwa uhakika kuwa utakuwa msambweni", Eddy alitoa pole.
Linda na Zabibu waliangaliana kwa jicho baya. Inaonekana Linda hakunda Zabibu kuja ofisini kwa bosi wake.
"Huyu anakuja kufanya nini, si afadhali angalikaa nyumbani, akawaachia wanaume hawa kazi hii. Mara nyingine kutembea na wanawake katika mapambano kama haya kunaweza kuleta mkosi".
"Mimi sina mkosi. Pilipili usiyokuwa inakuwashia nini?. Shughulika na mambo yako dada na mimi nitashughulika na yangu, usinijue kabisa", alijibu Zabibu kwa hasira.
"Haya basi yaacheni hayo mambo ya kitoto hapa tuko kazini. Sitaki kusikia uchafu mwingine wowote", niliwaonya.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilianza kuwaeleza yaliyonipata toka mwanzo mpaka mwisho. Nilipomaliza kuzungumza tu Issack akaingia.
"Ehe tupe maelezo", Eddy alimdai.
"Nitaanza toka jana usiku kwa faida ya wale ambao hawakupata habari hizo toka mwanzo. Sikazwe tulianza kumwona mnamo saa tisa za usiku akitokea barabara ya Bagamoyo. Alielekea moja kwa moja nyumbani kwake na hakutoka tena mpaka saa sita za mchana. Mnamo saa sita hivi aliondoka akaenda kula chakula cha mchana. Aliporudi mnamo saa saba hivi alikuja na lori dogo tani tatu likimfuata nyuma. Alifungua mlango na kuanza kutoa mizigo iliyofungwa kama mtu anayehama. Baada ya kujaza gari hili, liliondoka na nikamwambia Ismail alifuate. Ismail aliporudi alisema mizigo hiyo imetelemshwa kwenye bandari ndogo yaani pale ngalawa na meli ndogo ndogo zinapopakia mizigo yao.
"Yaani mizigo hiyo ilikuwa imefungwa kisafari?'.
"Ndio".
"Haya endelea".
"Kiasi cha saa tisa hivi walikuja watu wawili ndani ya gari, mmoja Mzungu mwingine mwafrika. Walikaa kama dakika tano tu wakaondoka. Nilimwambia Ismail awafuate. Walielekea barabara ya Bagamoyo, Ismail aliporudi alisema watu hawa waliingia barabara ya Kilimani na kuingia nyumba moja inayotazamana na Hosteli ya Tazara. Sikazwe hakutoka. Mnamo saa kumi na moja hivi alikuja mtu mwingine na gari akazungumza nae mlangoni. Maneno aliyosema yalionyesha kumkasirisha Sikazwe maana alimsukuma, na yule mtu haraka haraka akaingia ndani ya gari na kuondoka....
"Ismail alimfuata huyu mtu lakini mtu huyu aliingia Estiennes Hoteli na kuanza kunywa pombe, hivyo akamwacha akarudi. Wakati natoka Sikazwe alikuwa bado yuko ndani lakini nafikiri atatoka maana alichukua debe la mafuta ya petrol akajaza gari lake".
"Kazi nzuri umefanya".
"Asante", alijibu kwa furaha sana.
"Eddy nitayarishie gari, hapana Issack nitatumia gari lako mimi na wewe tutakwenda kumfuata Sikazwe, popote atakapokwenda. Sherriff Eddy na wengine mnisubiri hapa hapa nitarudi ila mjitayarishe kwa usiku wa kazi", niliwaeleza lakini niliona wanashangaa.
Kabla hawajaanza kusema mengi nilimwambia Linda. "Mwambie Chifu anisubiri kidogo nikichelewa kufika saa moja".
Nikatoka nje pamoja na Issack nikawaacha wamepigwa na butaa.
Niliangalia saa yangu ilikuwa saa kumi na mbili na dakika tano na kwa majira ya wakati huu ya Dar es Salaam giza lilikuwa limeingia. Tulipofika kwa Sikazwe tu tulimwona naye anafungua mlango wa gari akaweka mkoba wake ndani, kisha akaingia na kuwasha gari moto. Sisi tuliegesha gari letu kama watu wanaopunga hewa pwani saa za jioni kwani vile vile kulikuwa na magari mengine. Alipoondoka tu Sikazwe sisi taratibu tulimfuata.
Mimi ninapomfuata mtu hata awe na ujuzi wa namna gani hawezi kunitambua. Sikazwe alituongoza mpaka kwenye nyumba hii ambayo Issack alisema ilikuwa karibu na Hosteli ya tazara. Alipiga honi mbele ya lango kubwa. Tukaona askari anakuja kumfungulia akaingia ndani. Majibwa mawili makubwa yaliandamana na askari huyu. Sisi tulienda na kuegesha gari letu mbele ya baa ya Hosteli ya Tazara. Mtu yeyote angedhani tuko humo katika baa, tunakunywa.
"Unayo bastola yenye seilensa?", nilimwuliza Issack.
"Ndiyo".
"Nipe. Wewe ningoje hapa lakini uwe katika tahadhari kitu chochote kikitokea njoo haraka, umenielewa.
"Hamna wasiwasi bosi".
"Kazi ninayokwenda kuifanya ni ndogo ila majibu ndio yananipa wasiwasi".
"Nakutakia kheri, bosi".
"Nafikiri nitaihitaji".
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Niliondoka na kwenda kwenye nyumba ile. Mbwa walikuwa wanabweka kila gari linapopita mbele ya ile nyumba. Niliona hii itanisaidia maana hata wakibweka halitakuwa jambo la ajabu. Niliangalia wapi upepe unatoka nikaona ulikuwa unatoka mashariki kwenda magharibi, hivi nikaamua kuingia nyumba hii kutoka magharibi kuzuia mbwa wasije wakaninusa. Nyumba ilikuwa imezungushiwa ua wenye seng'eng'e zenye miba upatao urefu wa futi sita kwenda juu. Kati ya mafunzo yangu makubwa kuruka ilikuwa mojawapo. Nilikuwa naweza kuruka futi saba wakati mwingine nane. Hivyo nilirudi nyuma nikaruka juu ya seng'eng'e na kutumbukia ndani ya ua bila kishindo maana nilitanguliza mabega.
Nilikumbuka kuwa kibao nje la lango kubwa kilikuwa kimeandikwa jina la Tony Harrison, hivi nilijua huyu ndiye mwakilishi wa Euro-Afro. Zabibu aliwahi kunieleza habari hizi. Walivyokuwa wanahusiana na Sikazwe ndicho nilikuwa nimekuja kutafuta. Kwanza ilinibidi nitoe kikwazo kimoja yaani askari mlinzi na mbwa. Nilisikia mbwa wanabweka mbele ya nyumba, hivyo nilijibanza kwenye ukuta wa upande huu wa magharibi halafu nikanyata pole pole mpaka kwenye kona ya ukuta na mbele. Nilichungulia nikaona askari mlinzi pamoja na mbwa wake wawili. Nilikohoa yule askari akastuka akaangaza huku na huko asione kitu maana mimi nilikuwa nimeganda kama kupe kwenye ukuta. Ili kuridhisha mashaka yake alikuja upande niliokuwa akifuatana na mbwa. Alikuwa na bunduki mkononi, kwa umbo lake nikajua ni 'SAR'.
Alipofika karibu kabisa na mimi niliona mbwa wanainua mikia nikajua tayari wameninusa. Nililenga bastola yangu nikawaua wale mbwa kwa kuwapiga katikati ya vichwa kwa upesi sana kwamba yule askari alishangaa kuona mbwa wanaanguka hata bila kubweka. Alipogeuka na kuniona tayari alikuwa amechelewa, nilimrukia nikamkaba kabali taratibu mpaka alipokufa bila kutoa sauti. Nilivuta mizoga ya majibwa haya na maiti ya yule askari na kuyaweka kando ya ua upande wa magharibi kwenye seng'eng'e. Nikiwa nimeridhika na hatua yangu ya kwanza. Sasa nilichukua hatua ya pili.
Nilianza kuzunguka nyumba kwa nyuma nikielekea mashariki. Sikwenda mwendo mrefu kabla sijafika mahali nilipokuwa ninapahitaji. Nilikuwa nimefika nje ya sebule na dirisha la nyumba lilikuwa wazi, na nikasikia mazungumzo ya huko ndani kama nami niko pale pale. Hivyo nilibana tena kwenye ukuta nikaanza kusikiliza mazungumzo.
"Lakini Tonny, mimi nimrjitshidi sana lakini huyu mdudu Gamba na kundi lake amewaua watu wangu wengi sana. Fikiria Shuta na Mlambo wameuawa. Nadhani nisingejitahidi zaidi ya hapo. Lakini hata hivyo bado nina watu wa kutosha kutekeleza kazi hii. Usiku huu huu itakwisha, usiwe na shaka.
Hii ilikuwa sauti ya Sikazwe.
"Sawa Ray, lakini naona ungejitahidi zaidi ya hapo maana lazima ile meli ndogo iondoke saa tisa za usiku ili kuwahi meli yetu ya Euro-Afro Mtwara usiku wa kesho. Tayari rubani wa meli hiyo ana habari na mpango wa kutoa mizigo ndani ya meli ndogo (scooner) na kuingiza katika meli hiyo huko Mtwara haina uangalizi sana kama bandari ya Dar es Salaam", Tonny alisema.
"Vizuri mimi nitajitahidi, tayari mizigo yote imefungwa vizuri, imebaki kusafirisha tu kwenda kwenye bandari ya meli ndogo".
"Nimepata habari kuwa unangojewa kwa shangwe na wakuu wa serikali ya Afrika Kusini. Nimewaeleza mipango yote, na wao wako tayari kuzungumza na chama chako ili damu isimwagike Nchini. Wamefurahi sana kwa kazi yetu ya kuweza kuziiba silaha za hatari ambazo zingeua wananchi wa Afrika Kusini bure, kumbe mnaweza kufikia maafikiano ya kubadilisha siasa ya Serikali ya Afrika Kusini kwa mazungumzo", Tonny Harrison alieleza.
"Na mimi nimeona ni wenda wazimu kuendeleza vita dhidi ya Afrika Kusini kwa njia ya mapambano.Lakini bado chama cha PLF kitaendeleza mapambano. Chimalamo ni mtu mwenye nia ya kuuza ubaguzi wa rangi kwa mapambano na mtutu". Sikazwe alionya.
"Si wewe unajua vitu vyao vyote na namba ya askari wao na mafunzo waliyopata askari wao pamoja na silaha walizonazo.
"Ndiyo, najua kila mbinu ya jeshi lake maana mwaka jana Kamati ya Ukombozi ya OAU ilitaka kutuunganisha. Hivyo tulipewa fursa ya kuelezana kikamilifu hali ya mali ya kila Chama kwa mwenzake. Tulikuwa wote tumekubali kuungana tukaelezana siri zote za vyama vyetu. Ni wakati tu tulipokuja na maoni ya namna ya kuweza kufikia hali ya kubadili siasa ya ubaguzi bila kumwaga damu, ndipo nilipokataa tena mpango huo wa kuunganisha vyama. Nilidai kuwa siasa ya Chama cha PLF na chama changu zilikuwa na tofauti za kimsingi ambazo hatukuweza kukubaliana. Huu ulikuwa uongo lakini ulikubalika ikaonekana tuendelee hivi tulivyo ili mradi wote tuna nia moja kwa hivyo siri zote za PLF ninazo.
"Kwa hiyo siri zote za PLF unazijua na kwa sababu wewe umejiunga na serikali ya Afrika Kusini itakuwa rahisi sana kuwateketeza wapigania uhuru wa PLF wasijaribu tena. Yaani litakuwa pigo kubwa kiasi kuwa kuweza kuimarisha chama chao kianze mapambano tena, lazima itawachukua muda mrefu, na wakati huo Ray utakuwa uanatawala pamoja na wazungu huko Afrika Kusini". Sikazwe alitoa kicheko.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Msiwe na wasiwasi mimi nitakuwa nao bega kwa bega kuleta hali nzuri katika Afrika Kusini na nitakuwa mstari wa mbele kupinga harakati za ukombozi ambazo wakati huo zitakuwa hazina maana".
"Kesho ndiyo siku kubwa kwako utakapoingia Pretoria na kuwekewa zulia jekundu", Tonny alisema kwa sauti ya kejeli.
Bila kutambua ile kejeli Sikazwe alijibu. "Ninaisubiri kwa hamu sana. Magari yale yaliyofanya kazi tayari yamebadilishwa rangi za jeshi la Tanzania. Kwa hiyo saa nne inaweza kupitia Intercontinental Motors na kuyachukua ili kubeba ile mizigo toka bohari mpaka bandari ndogo".
"Tayari Max ameisha waarifu, au siyo ?', Tonny aliuliza.
Niliinuka taratibu kumwangalia huyu Max nikamtambua; ni yule aliyetukimbia kule kwenye uwanja wa Saba Saba.
"Mara hii nitakupata", nilijisemea moyoni maana mara moja alinikumbusha Veronika.
"Ndiyo, gari ziko tayari", Max alijibu.
"Oke mimi ninakwenda kijitayarisha saa tatu unusu ndipo nitatoka nyumbani kwangu kuelekea kwenye shughuli.
"Je kuna wasiwasi wowote?", aliuliza Tonny.
"Hamna taabu, tayari watu wa Forodha wanajua tunapeleka spea za magari Mtwara na tumeisha zungumza nao vizuri hamna taabu".
"Lakini usimsahau Gamba na wenzake", Tonny alikumbusha.
"Usiwe na wasiwasi nina askari zaidi ya mia ambao wamefundishwa mafunzo ya juu hapa hapa Tanzania. Kama Gamba na wenzake wanataka kifo vema, na waje watuingilie watakiona kilichomtoa kanga manyoya shingoni".
"Oke nakutakia upakuzi mwema".
"Max, kwa sababu wewe ndiye kiongozi wa meli hii ndogo uwe macho kusije kukatokea kosa", Tonny alimwonya.
"Wewe unanijua sifanyi kosa mara mbili", alijigamba Max.
"Haya Sikazwe nafikiri saa tisa na nusu tutaonana hapa sitalala nitakusubiri".
"Usiwe na shaka", alijibu Sikazwe huku akisimama.
"Lo, nipe tiketi yangu ya ndege kabisa".
"Chukua hii hapa imelipiwa na serikali yako unakokwenda kuwa kati ya watu wakubwa watakaoongoza nchi yenye nguvu kuzidi zote katika Afrika".
Sikazwe na Max walimwaga wakafungua mlango wakatoka nje. Tonny Harrison alibaki ameketi kwenye kiti. Kwa vile nilikuwa na wasiwasi kuwa wangeshangaa kutomwona askari mlinzi na mbwa wake, nilitoka pale dirishani nikazunguka mbele. Kwa bahati nzuri hawakushughulika kumwita askari, ila Max alikwenda akafungua mlango, Sikazwe akapitisha gari langoni, halafu Max akarudisha mlango na kuingia ndani ya gari wakaondoka.
Mimi nikaona nimepata wakati mzuri wa kuzungumza na Tonny Harrison. Nilipoangalia saa yangu nikaona ni saa moja na nusu. Saa mbili zilikuwa zinatosha kumaliza shughuli zangu na Tonny Harrison kabla sijamfuata Sikazwe hapo saa tatu na nusu. Nilifungua mlango taratibu maana ulikuwa umerudishiwa tu bila kufungwa kwa ufunguo. Nikiwa na bastola mkononi niliingia sebuleni na kumkuta Tonny Harrison ameinamia meza anasoma faili.
"Habari za kazi Tonny Harrison?".
Harrison aligeuka na kujikuta anaangalia katikati ya mdomo wa mtutu wa bastola. Pale pale aligeuka sura. Kwanza ikawa ya manjano kisha ikageuka ikawa nyekundu kama mtu aliyechapwa kofi usoni. Unajua hawa wenzetu weupe akichapwa kofi muruwa uso hugeuka na kuwa mwekundu. Alitaka kutamka neno akashindwa. Niliona alikuwa hategemei kabisa maisha mwake kukutana na wakati kama huu ambao alijikuta anatazama mdomo wa kifo.
"Habari gani?. Au umekuwa bubu?".
Nilisogea taratibu huku bastola yangu ikiwa imemlenga katikati ya uso wake. Kwa kigugumizi alijibu. "Nzuri....".
"Telemka hapo kwenye meza njoo tukae hapa kwenye makochi nina mazungumzo ya maana na wewe kabla sijaondoka".
Bila kusita aliinuka kwenye kiti na kwenda kukaa kwenye kochi. Wakati wote huu mdomo wa bastola haukumwachia hata chembe ya nafasi. Nilikwenda pale mezani alipokuwa ameacha faili nikalichukua. Nilikaa upande mwingine wa makochi tukawa tunaangaliana ana kwa ana.
"Bwana Harrison natumaini tumewahi kuonana?".
"Ndiyo, nafikiri tulionana kwenye tafrija iliyoandaliwa na Lion Club Hotelini Kilimanjaro".
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nikaweka bastola yangu kwenye paja huku macho yangu yakiwa yanamwangalia kwa makini.
"Na si mara moja au mbili?".
"Nafikiri ni mara nyingi".
"Nasikitika kusema kwamba leo sikuja kwenye tafrija ila nimekuja kuzungumza nawe kwa ajili ya suala la hatari ambalo wewe unalijua vizuri zaidi.
Faili niliyoichukua kwenye meza ilikuwa imeandikwa "SIRI" halafu kichwa cha faili kiliitwa "OPERESHENI HUJUMA". Mara moja nikajua katika faili hili ndimo kulikuwa na maelezo yote ya jinsi tukio hili lilivyofanywa na hawa majahiri. Ule ulikuwa ni ushindi thabiti hivyo niliweka faili kwenye mapaja yangu.
"Sina haja ya kujitambulisha kwako kuwa sasa hivi nimekuja kukuona kama nani, kwa sababu natambua unaelewa, au sivyo".
Ndiyo".
"Bila kupoteza muda ningependa kujua, bwana Harrison, wazo la kuziiba silaha za wapigania uhuru mkiwatumia wapigania uhuru wenyewe limetoka kwa Makaburu au kwa mataifa ya Magharibi?".
"Kwanza kabla sijajibu swali lako nataka kutoa mshangao wangu kwako jinsi ambavyo umeweza kupeleleza na kugundua jambo hili ambalo lilitayarishwa kwa mbinu za hali ya juu. Mimi ningependa unieleze kwanza jinsi ulivyoweza kupeleleza mpaka kunifikia mimi kitu ambacho sikutegemea kabisa. Nafikiri baada ya hapo unaweza kunifanya unavyotaka kwani hili faili uliloshika lina kila kitu. Sina hata haya ya kukueleza mengi; yote utayakuta humo".
Mpaka sasa nilishatambua kuwa Harrison hakuwa mtu mwenye ujuzi wowote katika mambo ya kijasusi ila alikuwa ametumiwa tu kwa sababu ndiye mtu pekee ambaye angeweza kutekeleza jambo hili bila kushukiwa, na kweli kwa muda wa miezi sita alikuwa amefaulu kutotambulikana.
"Sawa, bwana Harrison. Nafikiri nitaanzia toka mwanzo ninavyofikiri ndivyo mambo yalivyokuwa mpaka kufikia hali hii.
"Mnamo miezi sita iliyopita Rais wa Chama cha wapigania uhuru kiitwacho PLF, Ndugu Cicil Chimalamo, alitembelea Urusi kwa nia ya kutafuta msaada wa kijeshi; yaani silaha kwa ajili ya mapambano yaliyokuwa yameanza dhidi ya serikali ya Afrika Kusini.
"Kwa vile Ndugu Chimalamo alikuwa na habari zote kuhusu nguvu za kijeshi za serikali ya Afrika Kusini ilizonazo alitoa maombi yake kwa serikali ya Urusi ili aweze kupatiwa msaada wa silaha za kisasa walizonazo Makaburu. Ombi hili la Ndugu Chimalamo lilikubaliwa na serikali ya Urusi na akaahidiwa kupatiwa silaha hizi katika muda wa miezi sita. Na kwamba katika muda huo silaha hizi zitakuwa zimewasili Dar es Salaam".
Akiniangalia kwa makini, nilitoa pakiti yangu ya sigara ya aina ya Tropicana, nikatoa sigara mbili, moja nikampa na nyingine nikavuta mwenyewe, kisha nikaendelea.
"Kwa kutokana na mbinu za kisasa za kijasusi za mashirika ya kijasusi ya nchi za Magharibi habari hizi zilinaswa. Ziliponaswa habari hizi ndipo nchi za Magharibi zilipopasha habari serikali ya Makaburu tishio lililokuwa linakuja dhidi yao. Hapo ndipo serikali ya Makaburu ilipokaa chini na kufikiri nini la kufanya. Uamuzi wa Makaburu ukawa wa kufanya ujahiri huu ndilo lilikuwa tatizo. Lakini baada ya kulishughulikia suala hili ambalo nafikiri walitupiwa wakuu wa shirika la ujasusi, yaani "BOSI", walifikiria mbinu za hali ya juu na kuamua kuwa kwa kutumia mbinu hizi wangeweza kufaulu kuziteka silaha hizi kabla hazijafika mikononi mwa wapigania uhuru. Bashiri yangu ni sawa na vipi?'.
"Mpaka sasa hujakosea kitu", alijibu.
"Makaburu ni wajanja sana na wanawajua wakuu wa vyama vya wapigania uhuru vizuri sana. Hivyo waliamua kumtumia mkuu mmoja wa wapigania uhuru ambaye walikuwa wanajua kuwa hakuwa na msimamo kamili, kwa vile walimjua alikuwa hapiganii hasa ukombozi wa waafrika wanaoonewa huko Afrika Kusini bali alikuwa akipigana ili apate cheo. Ukubwa na kujaza tumbo lake ndio ilikuwa nia yake. Hivyo waliamua kumtumia bwana Ray Sikazwe wa Chama cha SANP, ambaye ndiye alipatikana na sifa hizi walizozitaka. Walipofikia hapa kilichokuwa kimebaki ni namna gani watamwingia na kuweza kumridhisha kweli akisaidiana nao katika kuhujumu vyama vingine angepata kila alichokitaka. Hapa ndipo walipohitaji msaada wa nchi za Magharibi na hapo ndipo wewe Harrison ulipoingizwa katika njama hizi".
Nilinyamaza kidogo kiasi chs kupitisha mate.
"Kampuni yenu ya Euro-Afro ni kampuni kubwa sana, na ina rasilimali nyingi katika Afrika Kusini. Inamiliki madini ya maangamizi, chromiumu na platinumu katika Afrika Kusini. Na Afrika Kusini ndiyo nchi pekee isiyo ya kikomunisti inayotoa madini haya ambayo yanahitajika sana katika viwanda vya nchi za Magharibi. Hivyo serikali ya Makaburu ilizungumza na nchi za Magharibi zizungumze na kampuni yenu ikiwa na kisingizio kuwa kama wapigania uhuru hawa wakipata silaha hizi si serikali ya makaburu tu itaangamia, bali nchi za Magharibi zilizo na rasilimali zao nchini humo nazo zitapoteza mali zao. Kwa hivyo swala hili lilikuwa muhimu kwa nchi za Magharibi kama ilivyo kwa serikali ya Makaburu.
"Kwa vile Kampuni yenu inamiliki makampuni mengi katika nchi mbalimbali za kiafrika na mojawapo ikiwa ni Tanzania, hivyo ilionekana ndiyo kampuni pekee ambayo ingeweza kusaidia katika suala hili. Hivyo wakubwa wako waliarifiwa juu ya suala hili na hatari zake kama halitaweza kushughulikiwa haraka na kwa kikamilifu. Kwani hatari hii isingekuwa kwa Afrika Kusini tu ila pia Kampuni hii ya Kibepari ingeweza kupoteza mali zake zote ikiwa wazalendo watashinda vita vya ukombozi. Kutokana na sababu hizi wakubwa zako walikubaliana na Makaburu kuwa kulikuwa na haja ya kushirikiana ili kulinda maslahi ya Makaburu na nchi za Magharibi. Hapo ndipo ulipopashwa habari namna utakavyoshughulikia suala hili. Mpaka hapo maelezo yangu ni sawa au vipi?'.
"Sijui ulijuaje?, endelea maana nashangaa sana jinsi Afrika huru ilivyoendelea katika upelelezi".
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Habari zilipokufikia pamoja na plani yote ndipo ulipomwita bwana Ray Sikazwe na kumweleza kama ulivyoelekezwa. Ndipo ulipomdanganya kuwa serikali ya Makaburu iko tayari kufanya mazungumzo na chama chake ili wafikie uhuru wa walio wengi kwa mazungumzo bila mapambano, ila kwanza atimize sharti moja. Sharti hilo ni kusaidiana kati ya majasusi wa "BOSI" ambao wataingia Tanzania kama wanachama wa chama chake na kundi lake la wapigania uhuru lililokwisha kufundishwa mbinu za vita katika kuziteka silaha za chama cha PLF ambazo zilikuwa zikitegemewa kuwasili mjini Dar es Salaam mnamo miezi sita hivi".
"Kwani unadhani Makaburu hawawezi kutafuta suluhisho la namna hii, baada ya kutambua kuwa umefika sasa wakati wa kuanza kuwachukulia waafrika kama binadamu wenzao?", Harrison aliuliza.
"Mimi najibu kuwa baso, kwani kama nia yao ingekuwa hiyo wasingetaka suluhisho na chama kimoja tu na kwa siri, wangeliutangazia ulimwengu na kuomba vyama vyote vinavyohusika na tatizo la Afrika kusini vishiriki vyote kwa ujumla bila sharti lolote, la hasha, Harrison. Hizi zilikuwa mbinu tu za kuhujumu harakati za mapambano ya chama cha PLF ambacho kinaendelea na mapambano makali dhidi ya serikali ya Makaburu".
"Sawa nafikiri umenipa msingi wa mambo kama yalivyopangwa na serikali ya Afrika Kusini ikisaidiwa na nchi za Magharibi ambao ndio sisi. Lakini tulifaulu katika kuziteka nyara silaha hizi bila tatizo, je umekuja kugundua ni nani wanahusika?, ingawaje juzi tulipata habari kuwa wewe ni mpelelezi hatari lakini hatukuamini ungeweza kugundua kitu".
"Nitakueleza sasa. Nilipoanza upelelezi wangu siku ya kwanza tu niliona mwanga kwani mlikuwa mmefanya kosa. Kosa lenyewe lilikuwa ni kumwua kiki. Nilipokuta Kiki amekufa, tulianza kuchunguza habari zake tukakuta mambo yote aliyokuwa ameeleza juu yake si kweli, hivyo tukagundua alikuwa jasusi wa Makaburu waliokuwa wamefaulu kumweka katika ofisi ya za kamati ya Ukombozi ya OAU, na ni yeye aliyeweza kufanikisha jambo hili".
"Na mlijuaje kuwa mimi na sikazwe tunahusika?".
"Kosa jingine. Sikazwe nilipomwuliza kama anamfahamu Kiki alisema aliwahi kumwona mara moja tu wakati alipofika ofisini kwake na kumpeleka kwenye kamati ya Ukombozi ya OAU ili wamsaidie kazi. Sasa tulipofahamu kuwa Kiki alikuwa na rafiki msichana aitwae Zabibu nilimtafuta.
"Nilipofika kwake wakati mmemtuma mtu wa kwenda kumwua nikamkomboa. Yeye huyu binti alinieleza kuwa Sikazwe alikuwa rafiki mpenzi wa Kiki pamoja na wewe. Hii ilidhihilisha kuwa Sikazwe alisema uongo hivyo mara moja nikaanza kumhisi kuwa yumo katika mpango huu. Nilipojua kuwa kati ya makampuni yaliyo chini ya Euro-Afro ni pamoja na Intercontinental Motors ambao ni wakala wa magari ya "Benzi" nchini hapa nikawa na uhakika kabisa wewe unahusika. Maana magari yaliyotumiwa yalikuwa maloli makubwa ya aina ya Benzi ambayo ni sawa na yanayotumiwa na jeshi letu. Na magari yote ya jeshi kwa siku ile yameweza kufahamika yalikuwa wapi. Hivyo ikaacha sababu moja tu magari yaliyobeba zile silaha yalitoka kwenye kampuni yenu ya Intercontenental Motors ya jeshi pamoja na kuyaweka namba za bandia. Juu ya mavazi ya kijeshi wapigania uhuru wengi wanayo hivyo, hilo halikuwa tatizo kwenu. Una swali jingine?".
"Nafikiri umenielewesha vya kutosha na ninakupa hongera kwani kweli wewe ni mpelelezi maarufu si Afrika tu ila Ulimwengu mzima. Maswali mengine niliyokuwa nayo nimekwishajua majibu yake baada ya kuzungumza na wewe na kuamini mimi mwenyewe kuwa wewe huwezekani".
Ghafla mlango ulifunguliwa na Issack akaingia bastola mkononi.
"Karibu Issack samahani kwa kuchelewa nilikuwa na Bwana Tonny Harrison hapa ambaye ni mwakilishi wa kampuni ya Euro-Afro ambaye ndiye alikuwa kiongozi wa tukio la bandarini".
Niliangalia saa yangu nikaona ni saa mbili.
"SWali na mwisho Harrison, silaha mmezificha wapi?".
"Sikazwe ndiye anajua, na kama umeweza kufikia hapa sidhani utashindwa hatua ya mwisho".
"Haya simama twende zetu. Issack kalete gari hapo mbele ya mlango".
Issack alitoka na Harrison bila matatizo alisimama na kuangalia sebule na vitu vilivyokuwemo kwa huzuni. Alitangulia mimi nikafuata nyuma. Nilipofika mlangoni nilizima taa, nikawa na faili kwapani na bastola ikiwa imemlenga Harrison. Nilirudisha mlango na kuelekea kwenye lango.
"Askari na mbwa wangu wako wapi?", Harrison aliuliza tulipofika kwenye lango.
"Sasa hivi wako sehemu ambayo mimi na wewe hatujafika lakini siku moja tutafika".
Issack alikuwa ameegesha gari mbele ya lango, Harrison alifunga mlango wa nyuma mimi nikamfuata na kukaa naye.
"Kwa usalama wako usijaribu kitu chochote", nilimweleza huku Issack anaondoa gari.
"Mimi hata bastola sijui kuinua, watu hawa waliniahidi ulinzi mkali na kwamba ingekuwa vigumu operesheni hii kushindwa. Kumbe wameniuza. Usiwe na wasiwasi na mimi, sijui mbinu yoyote mbele ya bastola".
Nikajua wakati wake wa kusema ukweli umefika.
"Vipi bosi?", Issack aliuliza.
"Kituo cha usalama kwa watu kama hawa".
Issack kwa sababu alielewa ni kituo gani cha usalama alikwenda moja kwa moja na kupiga honi tulipofika kwenye lango. Mlinzi alikuja akafungua lango sisi wote wawili tukatoa vitambulisho vyetu. Akastuka mara moja na kuturuhusu kuingia. Nilimwongoza Harrison mpaka kwenye ofisi ya kituo hiki cha usalama.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilipofika nilimkuta afisa wa zamu nikatoa kitambulisho changu, naye akastuka.
"Ndio Mzee".
"Huyu mtu awekwe chini ya ulinzi mkali mpaka utakapopata maelezo tena".
Niliomba kitambulisho chake nikachukua jina, namba na cheo chake.
Alikuwa na cheo kikubwa. Kisha nilirudi ndani ya gari.
"Moja kwa moja ofisini, maana saa tatu na nusu ndipo kazi kubwa ya kukata na shoka inaanza".
"UHURU UTALETWA KWA MTUTU TU"
Tulipoingia ofisini tulikuta wanatusubiri kwa hamu.
"Chifu anataka kukuona", Eddy alinieleza.
"Mwambie Maselina haiwezekani, nitamwona baadaye. Sasa hivi hakuna nafasi maana tukichelewa hapa mambo yote yatakuwa yameharibika. Mwambie asitoke ofisini mpaka saa sita. Asipotuona ajue basi makubwa yametupata, akituona ajue tumerudi na ushindi. Umesikia Linda?".
"Nimesikia".
"Sherriff, Eddy na Isaack mko tayari kwenda kwenye uwanja wa mapambano", niliwauliza.
"Bila wasiwasi", walijibu kwa pamoja.
"Na mimi?", Zabibu aliuliza.
"Wewe utabaki hapa na Linda. Tutaonana saa sita kama tukiwa salama.
"Mimi nataka twende wote, kama ni kufa tukafe wote"
"Kwanini unataka ukafe naye kwani yeye ni nani wako", Linda alimuuliza kwa ukali.
"Acheni upuuzi, nyinyi bakini hapa, haya mambo ya kuleteana haraha, mtatupa mkosi bure".
"Twendeni zetu", niliwaeleza wenzangu nasi tukaondoka ndani ya ofisi na kuingia ndani ya gari.
Eddy ndiye alichukua usukani na Isaack akaa naye mbele. Mimi na Sherriff tulikaa nyuma.
"Twende moja kwa moja nyumbani kwangu tukachukue silaha zaidi. Halafu tutapita nyumbani kwa Eddy kuchukua silaha tulizoacha kule. Tuna saa moja ya kujitayarisha kabla ya kuingia kwenye uwanja wa mapambano.
"Itabidi tutoke kwa Eddy mnamo saa tatu na nusu. Hii itatupa nafasi ya kuwa nje ya nyumba ya Sikazwe saa tatu na nusu. Maana ndipo yeye ataondoka kuelekea huko walikoziweka silaha".
"Kisha niliwaeleza mazungumzo yote niliyoyasikia kati ya Harrison, Sikazwe na Max.
Kwa hiyo tutakuwa watu wanne tukikabiriana na zaidi ya watu mia", Isaack alisema kwa mshangao.
"Ndiyo sababu watu kama sisi tunaitwa ni hatari. Siku moja Isaack utakapokuwa komando kama mimi utakuwa na uwezo wa kukabiliana na maadui mia peke yako. Kwa hiyo mimi naona kama ni afadhali sana kama tuko watu wanne dhidi ya watu mia. Tukitumia hamasa na maadili na moyo wa kimapinduzi sina shaka Mungu atatusaidia na tutashinda na kufichua hizi njama za Makaburu na mabeberu ya jumuia ya ulimwengu", niliwatia moyo.
"Nikiwa niko na wewe bosi, huna sina wasiwasi wowote", Eddy alisema.
"Hata mimi", Sherriff aliongeza.
"Kama ni hivyo, hata mimi ninafurahi kuwa nina jeshi lililohai na kamanda wake".
"Kutokana na ulivyoeleza komredi, watu hawa walikuwa wamepanga kuzichukua silaha hizi kwa meli ndogo kama spea ziendazo Mtwara", Sherriff alieleza.
"Sawa'.
"Baada ya kufika Mtwara wangefanya nini?", aliuliza.
"Swali zuri. Watu hawa walikuwa wamejitayarisha vizuri sana. Hili kampuni kubwa la Euro-Afro lina meli zake. Meli yake moja itakuwa inapakua mizigo Mtwara kuingia kesho. Hivyo walikuwa wamepanga kutoa silaha hizi kwenye hii meli ndogo na kuzipakia katika meli kubwa ambayo ingelikwenda kuzitelemsha Afrika Kusini...
"Mipango yote hii iko ndani ya faili nililompa Linda ampelekee Chifu. Meli hiyo ingekuwa inangojwa bandari ya East London kutelemsha zana hizi. Sikazwe angeondoka kesho kwa ndege akidai anakwenda Botswana lakini angekwenda Pretoria ambako mimi nafikiri wangemtia ndani mana nia yao haikuwa kufanya kama walivyomdanganya ila tu walitaka awasaidie kuziiba silaha kwa sababu ilikuwa rahisi kwake".
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Kwa hiyo mpaka sasa Sikazwe anakazana bure tu", Isaack alisema huku akicheka.
"Wajinga ndio waliwao", Eddy alijibu. Tulifika nyumbani kwangu, nikabadilisha mavazi kuvaa mavazi ya kikazi yaani koti na suruali yenye mifuko mingi ili kuweza kubeba silaha za kutosha.
Baada ya hapo tukaelekea kwa Eddy ambako tulijitayarisha kwa kikamilifu. Kwa bahati nzuri tulikuwa na majoho mekundu matano tuliyoyateka kwa hawa majahili. Kila mtu alichukua joho moja, maana hii ingetusaidia kuwaingilia wakidhani ni wenzao. Tulipata vile vile kofia tatu ambazo niliwagawia wenzangu. Nakwambia tulipojaribu kuvaa tulifanana na wao kabisa. Hivyo tulichoomba ni kuwa tukute bado hawajabadili mvao wao unaowatambulisha. Baada ya kuona kila kitu kimekamilika tulijiandaa kuondoka huku roho zetu zikipiga haraka haraka.
II
Ilikuwa saa tatu na dakika ishirini tulipoegesha gari yetu kando kando ya bahari huku tukiangalia nyumba ya Sikazwe. Tulimsubiri aanze safari yake hapo saa tatu na nusu. Gari lake lilikuwepo hivyo tuliamini yupo.
Saa tatu na nusu kamili kama alivyosema tuliona mlango wa mbele wa nyumba unafunguliwa Max ndiye alitoka kwanza akiwa amevalia joho jekundu na kofia. Roho yangua ilijawa na furaha. Baada ya muda kidogo Sikazwe akiwa amevaa suti nyeupe alitoka akafunga mlango, halafu wote wawili wakaingia ndani ya gari. Max ndiye aliyeingia upande wa dereva. Sikazwe akaa kwenye viti vya nyuma.
"Lo Sikazwe ameanza kupata heshima ya "VIP", Sherriff alisema na wote tukacheka.
"Yule aliyetoka kwanza alikuwa Max; anaonekana ndiye Kamanda wa jeshi hili la majahili, na haikosi ndiye aliyekwenda bandarini kama Meja Paul Liboi", niliwaeleza
"Bila shaka", alijibu Sherriff.
"Hamna taabu bosi".
Gari la Sikazwe liliondoka na kuingia Kenyatta Drive. Tulingoja mpaka lilipofika kwenye kona ya Barabara ya Bagamoyo ndipo tukamfuata. Nakwambia mimi nikimfuata mtu hata awe na ujuzi wa namna gani hawezi kutambua. Tulifuatana moja kwa moja wakashika barabara ya Upanga, halafu wakaingia barabara ya Azikiwe kisha wakaingia Azania Front na kutokea City Drive. Muda wote huu sisi tuliwafuata taratibu.
Kisha walishika barabara inayopita kwenye ofisi za usalama barabarani nikajua wanaelekea Kurasini. Nilishangaa kwanini hawakupita Intercontinental Motors kama walivyokuwa wamepanga, lakini nilihisi wamebadilisha mipango.
Walipovuka tu ofisi za polisi wa usalama barabarani, walisimama. Mara mtu akatokea kwenye kijinjia akaja na kuzungumza nao. Mimi niliwapita kasi mpaka kwenye mzunguko wa barabara hii na barabara ya Kilwa, Nikazungukia kulia na kuingia Railway Clab na kutoka. Sisi tukawa kama tunatokea mtaa wa Gerezani. Niliendesha polepole na mara nikawaona wanatokeza kuelekea barabara ya Kilwa nasi, tukawafuata.
Tulipofika kwenye njia panda ya Kilwa na barabara iendayo kwenye ofisi za Mamlaka ya Bandari ya Tanzania wao walichukua njia iendayo kwenye ofisi za Mamlaka ya Bandri.
"Nafikiri wamezificha Shimo la Udongo", alisema Isaack.
"La hasha, mbele ya ofisi za NOTCO na UDA kuna bohari la Intercontinental Motors, kwa hiyo bila shaka ndiko wanakokwenda", alisema Eddy.
"Sawa kabisa Eddy, umenitoa usingizini, saa zote hizi nafikiria wapi wameficha silaha hizi kumbe sehemu yenyewe iki wazi kabisa", Sasa sikiwa na haja ya kuwafuata karibu karibu. Tuliwaacha wakaenda mpaka wakapotea kwani sisi tuliingia ofisi za Mamlaka ya Bandari, na tulipoona wamepotea ndipo sisi tukatoka.
Bohari ya Intercontinental Motors lilikuwa nyuma ya mabohari ya kampuni ya NOTCO. Hivyo niliegesha kwenye ofisi za NOTCO. Mlinzi wa hapa alikuja kutuuliza. Mimi niliona huyu anaweza kuleta kidamisi hivyo alipoinamisha kichwa kwenye gari nilimpiga ngumi ya uso ambayo ingemfanya alale kwa muda wa masaa kama manne hivi kabla hajapata fahamu. Kisha wote tulitelemka na kumbeba na kumpandisha kwenye lori moja lililokuwa limejaa mizigo.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Haya mabohari ya NOTCO yana walinzi hivyo itabidi tuzunguke tutokee upande wa barabara ya Kilwa ili kuepusha rabusha kabla hatujafika maana jinsi tulivyo watu wanaweza kufikiri sisi ni majambazi", Eddy alitoa ombi.
"Hapana, sasa hivi bado mapema hata tukionana nao watafikiri ni walinzi wa usalama tu. Ili tuwe kwenye hali ya usalama zaidi lazima wote tuwafanye wakalale kwa muda".
"Nami nilikuwa nafikiri hivyo maana wakisikia mapambano yatakapoanza wanaweza kuja kujiunga na kufa bure, au kupiga simu polisi wakaja kutuingilia kabla hatujafunga kazi sawasawa.
Hivyo rafiki zangu walinzi wote wa sehemu hii walilazwa usingizi wa masaa, sio wa NOTCO tu ila wa UDA, Shirika la Usagishaji na ofisi zote za karibu. Tulipoona kazi hii ndogo tumeimaliza tuliondoka hapo na kuelekea kwenye uwanja wa mapambano.
Tulitoka kwenye kichochoro kimoja kati ya mabohari ya sehemu hii na kujikuta uso kwa uso na bohari ya intercontinental Motors. Tulikuta nje kuna malori matatu yanapakiwa kwa pamoja. Kulikuwa na watu wasiopungua ishirini, walikuwa wanapakia mizigo kwa kupeana. Tuliona gari la Sikazwe lakini yeye hakuwemo, hali hii ilitujulisha kuwa yumo ndani.
Penbeni kidogo ya magari haya kulikuwa na walinzi. Walikuwa hatua kama ishirini kutoka kwenye magari yaliyokuwa yanapakia kwa kila upande; baadhi yao walikuwa wamejibanza kwenye ukuta wa mabohari haya na mengine wote wakiwa na bunduki mkononi. Habari nzuri wote walivaa majoho mekundu na kofia. Nilihisi kuwa kulikuwa na askari wasiopungua ishirini hapa nje.
"Nafikiri wote mmeona ulinzi ulivyo. Kitu ninachotaka ni kufanya mashambulizi kimya kwanza mpaka tutakapolazimika kuwashambuliwa watu wa ndani. Kwa upande huu giza linatusaidia hivyo walinzi wa huku haitakuwa taabu kuwapata. kuna walinzi kama sita waliobana upande huu. Mimi na Isaack tutashambulia kushoto, Nyinyi Sherriff na Eddy mtashambulia upande wa kulia. Nawatakia kheri".
Tulipeana mikono kimya kimya kwani hatukujua nini kitatokea. Mimi nilikuwa wa kwanza kujitokeza kwenye michongoma na kubana kwenye huu ukuta wa bohari jingine. Kama hatua tatu kulikuwa na mlinzi anavuta sigara huku macho yake yakiwa kwenye gari. Nilimsogelea kimya kimya. Nilipokuwa karibu kabisa nilimsemesha.
"Sijui watamaliza saa ngapi kupakia, mimi najisikia kuchoka".
"Sijui hata..." Aligeuza uso kunijibu, nikamkata karate ya shingo upesi upesi na kumlaza chini. Nikamwashiria Isaack alipojitokeza nikamwona Eddy naye ananyata kwenda upande wa kulia. Nilimnyooshea kidole kimoja kumweleza mmoja tayari nimepata. Yeye akanitolea alama ya vidole ya V kuonyesha ushindi.
"Wewe Isaack simama hapa hapa uwe kama wewe ndiye mlinzi wa hapa, mpaka nitakapokuonyesha ishara nyingine".
"Sawa", alijibu.
Mlinzi mwingine alikuwa hatua kumi hivi na hakujua nini kimetokea. Kwa vile nilikuwa nimevaa kama yeye alifikiri mimi ni mwenzake hivyo nilikwenda tu kama mmoja wao mpaka nilipomfikia.
"Vipi kuna wasiwasi wote?", nilimwuliza.
Aliinua kichwa.
"Hakuna....."
Kabla hajamaliza nilimkata karate ya katikati ya kichwa akafa palepale. Nilimwegemeza vizuri kwenye ukuta nikamwacha kama mtu aliye hai.
Nilimwunulia Isaack vidole viwili na yeye akawainulia Eddy na Sherriff ambao sasa nilikuwa siwaoni. Kumbe Eddy na Sherriff walikuwa wameenda kwa haraka zaidi, maana Isaack alinionyesha vidole vitatu kuonyesha wenzetu tayari walikuwa wameua watatu.
Hii ilinitia moyo sana. Upakiaji uliendelea bila wasiwasi. Mtu wa mwisho kwa upande huu alikuwa amebana kwenye kona kabisa ya ukuta wa bohari hii. Nilimwendea huku nikiwasha sigara. Na yeye alipoiona aliweka bunduki yake chini akatoa sigara.
"Sina moto afadhali umepita huku", aliniambia.
Mimi niliwasha kiberiti akaimana ili kuwasha sigara. Palepale nikamkata karate ya shingo. Bila hata kukoroma akakata roho. Nikamwegemeza ukutani halafu nikamfanyia ishara Isaack aje.
"Sawa wewe utasimama hapa mimi nawafuata walinzi wale watatu waliosimama mbele ya magari. Kama watashtuka mimi nitajitupa chini wewe wawahi". Halafu nikatoa funguo za gari.
"Pita hapa kichochoroni panda gari mpaka ofisini mwambie Chifu aje pamoja na Mkuu wa Polisi pamoja na askari watakaokuja kulinda na kuzihifadhi zana hizi baada ya mapambano. Umenielewa?".
"Sana. Nakutakia kheri".
Nilianza kutembea kuelekea kwa wale watu. Kabla hata sijafika nilisikia mlio wa 'SMG' kwa upande wa akina Sherriff. Nikajua mambo yameiva. Nikainua SMG yangu na kuwateketeza hawa walinzi waliokuwa mbele ya magari. Isaack hakupata hata muda wa kupiga risasi ila nilimwona anaingia uchochoroni na kupotea. Mimi niliruka juu ya gari lililokuwa karibu, nikakuta watu wanne walikuwa wanapanga masanduki ya silaha.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Kumetokea nini?", niliwauliza.
Wote waligeuka na kuniangalia. Pale pale nikawaachia risasi za kuwaua kisha nikaruka chini. Milio ya bunduki ilifanya watu wote watoke ndani ya bohari na kusambaratika hovyo. Watu wote waliokuwa hapa juu walikuwa wamesharuka chini. Niliweka sanduku moja kama kinga nikaanza kutungua mtu mmoja mmoja na bastola yangu nyenye sailensa.
Kwa vile hawakusikia mlio kutoka sehemu yangu watu walipiga risasi zao kuelekea upande kwa upande wa akina Sherriff. Nilipoangalia juu ya lile gari jingine nilimwona sherriff ameseimama juu na kuwashambulia adui kwa namna ya ajabu.
Nilimfanyia ishara akaiona na yeye akanifanyia ishara ya kuonyesha kuwa Eddy alikuwa chini anajaribu kuingia ndani. Kuona hivyo nilimfanyia ishara kuwa na mimi nakwenda ndani hivyo atuchunge wote. Tulikuwa tumeuwa idadi kubwa ya askari waliokuwa wamebaki ni wachache tu.
Niliruka chini huku nikiachia risasi ovyo hata niliweza kufika kwenye ukuta wa bohari lao. Nilitupa SMG nikajitupa kwenye mlango na kujiviringisha mpaka ndani ya bohari na kama umeme nikarukia nyuma ya sanduku kubwa na kuanza kujaza risasi bastola yangu. Huko nje nilisikia bado Sherriff anaendelea kumimina risasi ili kuwazuia wasitoke nje.
Nilipoinuka niliona kama kumebaki watu kumi tu ndani; wengine wote tulikuwa tumewateketeza. Nilimwona Eddy anaviringisha na kuingia ndani. Wale watu walimwona na kabla hawajapiga risasi niliwahi wawili, wengine wote wakarudi kujificha nyuma ya masanduku.
Eddy aliruka mpaka nilipokuwa.
"Asante bosi umeniponya",
"Usinishukru ndio sababu tuko wote. Kwanza kazi mliyoifanya wewe na Sherriff sikuitegemea. Kazi imekuwa rahis kabisa".
"Kuna watu kama wangapi humu ndani?".
"Hawazidi kumi, na wote wako upande wa mashariki. Nafikiri wanamlinda Sikazwe na Max".
Huko nje kulikuwa kimya; Tukajua Sherriff anasubiri sasa kashi kashi kutoka kwetu.
"Sasa Eddy lazima tuwafanyie ujanja ili tuwapunguze. Mimi nitasimama juu ya hili sanduku ili niwadanganye. Walivyo wajinga walinzi wao watainuka ili wanipige risasi. Mimi nikiita tu jina kaa tayari na hii SMG yako kisha anza kumimina risasi. Mimi nitakuwa nimeisharuka kitambo, hivyo utawapata kama mchezo. Usiogopea kuwa unaweza kuniumiza ninakuhakikishia kuwa nitakuwa sipo".
"Lolote usemalo bosi", Eddy alijibu huku anatayarisha bunduki yake.
Niliinuka kama umeme juu ya sanduku nikawaona wote mara moja.
Nikaita
"Sikazwe?".
Hapo hapo kama umeme nikaruka nyuma ya sanduku jingine. Walinzi wanne wainuka ili kunitupia risasi huku wakiwa wamejitokeza hadi vifua. Eddy alimimina risasi na kuwashindilia wote risasi katikati ya vifua vyao wakafa pale pale. Nilimwonyesha Eddy vidole kuwa wamebaki watatu, kwani nilipokuwa nimeruka juu ya sanduku niliona wako watu saba.
"Gamba, nilisikia sauti ya Sikazwe anaita.
"Unasemaje?", nilimwuliza.
"Naomba tuzungumze, vita umeshinda.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Sawa Sikazwe, lazima ujuwe kuwa ukombozi wa Afrika Kusini utaletwa kwa mtutu wa bunduki tu, si mazungumzo.
"Walinidanganya".
"Hawakukudanganya, shida yako ni kwamba wewe ni kibaraka; yaani unapenda cheo kuliko watu wako. Matokeo yake ndiyo haya. Hata Makaburu wafanye njama za namna gani, mwisho wake wazalendo watashinda.
Wakati tukijibishana na Sikazwe, Eddy alikuwa anatambaa chini kuelekea pale walipokuwa.
"Tafadhali tuzungumze?", aliomba.
"Umechelewa, maana umeshaipaka matope Afrika, hivyo tutakupeleka mbele ya wanamapinduzi wa Afrika ndio watakao kuhukumu".
"Huwezi kunichukua hai".
Kumbe wakati huu tunajibishana Max naye na askari mwingine walikuwa wamejivuta karibu kabisa na mimi. Ghafla nikahisi kuna kitu karibu nami.
"Bosi", Eddy aliita ambaye pia alikuwa amewaona.
Kusikia tu hivyo niliruka pale nilipokuwa na wakati huo nikawaona Max na yule kijana mwingine karibu kabisa na mimi wameinua bastola tayari kufyatua. Nilijiviringisha hewani namna ambayo hata wao walishangaa risasi zao zote zikanikosa, wakati ule ule nikaachia za kwangu nikawapata wote nao wakaanguka chini.
Sikazwe aliinuka akasimama juu ya sanduku akachukua bastola akataka kujipiga risasi. Bastola tatu zililia kwa wakati mmoja na kuupiga mkono wake. Kumbe Sherriff nae alikuwa amefika mlangoni na kuona kitendo alichotaka kukifanya akakizuia. Eddy nae aliona akazuia wakati na mimi niliona nikazuia asijipige risasi.
"Bado tunakutaka Sikazwe ukiwa hai ili ukajibu maswali ya wanamapinduzi na wapenda maendeleo ya Afrika", nilimwambia huku bado anashangaa jinsi risasi tatu zikitoka pande tofauti zilivyoweza kupiga kiganja chake tu.
Mara tunasikia usiku mzima umejaa kelele za milio ya magari ya polisi.
"Chifu yuko njiani", niliwaambia wenzangu ambao sasa tulikuwa tumemzunguka Sikazwe.
Lo, Bosi ile jiviringisha uliyotoa pale hewani sijaona hata ndani ya sinema", Eddy alinisifu.
"Mimi nilichoka kabisa; sasa naamini yote niliyoelewa. Nilifikiri mengine wanakuongezea", Sherriff alisema.
"Kuwa komandoo siyo mchezo", niliwajibu nikatabasamu.
Milio wa tahadhali ya magari ya polisi ulisogea kabisa.
"Ndio sababu sikumwona Isaack", Eddy alisema.
"Ndio sababu", nilijibu.
Tulisikia milango ya magari inafungwa kwa nguvu. Mara tukamwona Chifu na Mkuu wa Polisi wanaingia.
"Karibu Chifu, kazi imekwisha. Na mtu wenu huyu hapa na mwingine nafikiri tayari una habari naye. Ndani ya malori hapo nje kumejaa silaha, na zingine zimo humu. Mkienda bandari ndogo (dhow wharf) mtakuta meli ndogo iliyotayarishwa kwa ajili ya kusafirisha silaha hizi, sisi hatuna zaidi", nilimweleza kwa niaba ya wenzangu.
"Kazi nzuri vijana, mmeokoa jina la Tanzania, na mmeitoa Afrika katika aibu", Chifu alijibu huku wakitupa mikono ya pongezi.
Mkuu wa polisi alitoa pingu akamfunga Sikazwe huku sura yake ikionyesha ukali.
Mara nikamwona Zabibu anakuja anakimbia akifuatiwa nyuma na Isaack. Niliwakonyeza Sherriff na Eddy, tukatoka pale haraka haraka tukawaacha Chifu na wenzake wanamshughulikia Sikazwe.
"Oh mpenzi Willy", Zabibu alinirukia shingoni.
"Hamna taabu wote tu wazima", nilimjibu.
"Ashukuriwe Mungu", Zabibu alijibu.
"Isaack gari liko wapi?".
"Oh Bosi, linakusubiri wewe".
"Twendeni zetu, acheni wazee hao wafanye shughuli zao sisi yetu tumemaliza", niliwaeleza wenzangu.
Sherriff, Eddy, Isaack, Zabibu na mimi tuliondoka na kwenda kwenye gari letu huku askari polisi tuliowapita wakitushangaa na kutupigia saluti. Tuliingia ndani ya gari letu, huku gari moja la polisi lenye mlio wa tahadhali limetutangulia.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Je unajua tunakwenda wapi?", aliuliza.
"Sijui lakini nafikiri imebidi tupewe heshima ya 'VIP' Isaack alijubu.
Mara gari nyingine ya polisi ikatusindikiza kwa nyuma.
"Lo, utafikiri Marais", Sherriff alitania.
"Mara moja kwa miaka si mbaya", nilijibu.
"Mimi mnitelemshe kwa Margaret", Sherriff alisema.
"Ala, mipango imeshafanywa nini?", niliuliza.
"Oh, mwenzangu siku nyingi", Eddy alijibu.
"Sawa baba, kazi na dawa", nilijibu huku nikimbusu Zabibu.
Nilipoangalia saa yangu nikaona ilikuwa yapata saa sita kasoro robo.
Ilikuwa asubuhi ya Jumapili. Jua lilichomoza kutokea baharini huku miali yake ya asubuhi ikichukua rangi ya maji ya bahari na kuipitisha kwenye vioo vya chumba changu cha kulala. Mwanga huu ulimmulika Zabibu usoni ambaye alikuwa bado amelala. Hakika mwanga huu wa asubuhi ulimfanya azidi kupendeza. Asubuhi vile vile kulikuwa na upepo baridi uliotoka baharini na kutufikia sehemu hizi za Upanga. Kwa kifupi ilikuwa asubuhi njema ambayo sitaisahau.
Niliangalia saa yangu nikaona inapata saa moja kasoro dakika tatu. Nilinyanyuka na kufungua radio ili kusikia taarifa ya habari ya saa moja. Kunyanyuka kwangu kulimwamusha Zabibu ambaye alinitolea tabasamu la kukata na shoka. Na mimi nikamrudishia lile la pekee ambalo huwa nalitoa kwa nadra sana.
"Tusikilize taarifa ya habari", nilimwambia.
Baada ya mlio wa tindo sauti ya kike ikasema.
"Sasa ni saa moja kamili". Halafu ikafuatiwa ya kiume.
"Ifuatayo ni taarifa ya habari kutoka Radio Tanzania Dar es Salaam msomaji Godfrey Chalamila. Kwanza habari kwa ufupi. Majasusi wawili walioshiriki katika njama za kuiba silaha za chama cha PLF bandarini wamekamatwa.
Mwili wa msichana mwanamapinduzi Veronika Amadu aliyeuawa katika harakati za kufichua njama za wizi wa silaha utasafirishwa kwenda Freetown, Sierra Leone.
Serikali imetaifisha makampuni yote yaliyokuwa chini ya Kampuni la kibepari la Euro-Afro.
Habari kamili; Wapelelezi shupavu wa Afrika jana usiku waliwakamata majasusi wawili na kuuwa wengine wengi na kuzikomboa silaha na kuzikomboa silaha za chama cha PLF zilizokuwa zimetekwa na majasusi waliokuwa wakiifanyia kazi Afrika Kusini. Majasusi hawa ni Ray Sikazwe, aliyekuwa rais wa chama cha SANP na Tonny Harrison aliyekuwa mwakilishi wa kampuni ya Euro-Afro.
Serikali imetamka kuwa watu hawa watafikishwa mahakamani siku ya Jumatatu kujibu mashitaka ya ujasusi na hujuma. Wakati huo huo kamati ya ukombozi ya OAU imelaani njama hizi za Makaburu na kusema kuwa lazima Makaburu wajue kuwa Afrika iko macho na haiko tayari kuchezewa. Taarifa hiyo iliendelea kusema kuwa chama cha PLF kitaongeza harakati za mapambano huko Afrika Kusini ambayo ndiyo njia pekee ya kuweza kupata uhuru wa walio wengi. Vile vile taarifa hiyo imesema kutakuwa na kikao cha kamati ndogo ya siasa mjini Dar es Salaam ili kutafuta njia ya kuviunganisha vyama vyote vya ukombozi vya Afrika Kusini, ili moto wa mapambano uweze kuwaka zaidi.
Mwili wa mwanamapinduzi shupavu hayati Veronika Amadu aliyeuawa katika harakati za kupambana na majasusi wa Makaburu ili kukomboa silaha zilizokuwa zimeibiwa bandarini utasafirishwa kwenda MJINI Freetown, Sierra Leon ambako ndiko kwao. Serikali imetoa ndege aina ya Boeng 737 ambayo itachukua na ujumbe wa kijeshi utakaosindikiza maiti hiyo pamoja na wanamapinduzi wengine. Imefahamika toka mjini Freetown kuwa mwanamapinduzi huyu atazikwa kwa heshima zote za kijeshi. Vyama vya wanamapinduzi na wapenda maendeleo duniani kote vimesema vitapeleka wawakilishi wao kwenye mazishi ya shujaa huyo.
Serikali imetaifisha makampuni yote yaliyokuwa chini ya kampuni ya kibepari ya Euro-Afro, kwa kile ilichokiita "Kujihusisha kwa kampuni hiyo na serikali ya Makaburu ili kupiga vita harakati za ukombozi. Hakuna fidia itakayotolewa. Na huo ndio mwisho wa taarifa ya habari".
Nilifunga radio baada ya taarifa ya habari maana ilinikumbusha Veronika.
"Utakwenda kwenye mazishi?", Zabibu aliuliza.
"Ndio".
"Tutakwenda wote?".
"Hamna taabu. Mambo yatatengenezwa.
TAMATI
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
BILA SHAKA UMEVUTIWA NA HADITHI HII YA UPELELEZI WA WIZI WA SILAHA ZA WAPIGANIA UHURU WA AFRIKA KUSINI, KAZI HII IMEFANYWA NA HAYATI E.A. MUSIBA AKITUMIA JINA LA WILLY GAMBA KAMA MPELELEZI HATARI WA AFRIKA.
0 comments:
Post a Comment