Simulizi : Kosa
Sehemu Ya Tatu (3)
Nakumbuka siku ya kwanza kumuona Huwaida ilikuwa ni siku ya kwanza ya mimi kukanyaga miguu yangu katika chuo kikuu cha Dar es salaam kama mwanafunzi wa mwaka wa kwanza hapo chuoni, kwenye zoezi la usajiri wa wanafunzi tulikaa mstari mmoja na yeye alikaa nyuma yangu. Nikiwa kwenye foleni hapo ujumbe mfupi wa maneno wa mtandao wa whatsapp uliingia kwenye simu yangu na ikanilazimu niufungue na niusome. Nakumbuka vizuri siku hiyo nilivaa kama hadhi ya familia ninayotoka ilivyo, uturi niliojipulizia uliashiria natoka kwenye familia ya gharama, miwani ya giza niliyovaa ilinifanya nizidi kuonekana nimependeza kutokana na kupangilia rangi za nguo nilizozivaa. Ujumbe mfupi ulioingia kwenye simu yangu ulinifanya nianze kuujibu palepale huku nikisahau kama mstsri inaenda, nikiwa naandika kwenye simu yangu aina ya Ipad mini nilihisi kuguswa na mkono wenye joto ambalo lilileta athari kidogo kwenye bega langu ambapo uligusa. Sikuhitaji stashahada au shahada ya aina yoyote katika kuutambua mkono ulionigusa ulikuwa wa jinsia gani, nilitambua wazi kama nimeguswa na mkono wa msichana na kama ningemuita mwanamke basi ningejiona namzeesha mapema. Niligeuka nyuma kumuangalia huyo mwanamke aliyenigusa na hapo moyo wangu nikahisi kama umetaka kupasuka kwa sura niliyoiona iliyonifanya niduwae sana, nilimuona msichana mrembo mrefu mwenye juba la rangi nyeusi lililomkaa vyema mwilini mwake. Binti huyu alibeba kipochi kipochi kidogo pamoja na bahasha ndogo mkononi, asili ya binti huyu ilikuwa haitofautiani na mimi kwani wote tulikuwa wasomali ila yeye alionekana kuwa na weupe kwa mbali uliomfanya azidi
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
kuonekana mrembo na kunifanya nizidi kumshangaa hadi nikavua miwani ya giza niliyokuwa nimeivaa.
"kaka foleni inatembea" Aliniambia huku akionesha tabasamu hafifu usoni mwake, mimi nilishtuka kisha nikaangalia mbele nikakuta foleni imesogea na sasa ipo mbali kidogo na mbele yangu kulikuwa na uwazi mkubwa kutokana baada ya mimi kusimama nikijibu ujumbe mfupi wa maneno mtandao wa Whatsapp.
"oooh! Sorry" Niliongea kwa mtindo wa aina yake kama mmrekani au mtanzania aliyekaa Marekani kwa muda mrefu, hapo ndipo ukawa mwanzo wetu wa kuongea hadi tunamaliza kufanya usajiri na pia nilikuja kubaini wote tunasoma kozi moja hivyo nikaona ukaribu wa zaidi ndiyo unafuatia. Siku hiyo kwa mara ya kwanza macho yangu yalitamani na moyo wangu ukahitaji kuwa kuwa na huyu binti ambaye aliniambia anaitwa Huwaida ingawa sikuwa na ujasiri wa kumwambia kwa muda huo. Maisha mapya ya chuo niliyaanza kwa kukaa katika hosteli za chuo hicho na huko ndipo nikapata marafiki wapya kutoka sehemu mbalimbali, chumba nilichopangiwa nilipata rafiki anayesoma shahada ya uhandishi wa tarakilishi (Bachelor in computer engineering) ambaye alionekana ni mjanja wa mji kuliko mimi mtoto wa kitajiri niliyekulia jijini Tanga. Faiz Faiim ndiyo jina lake huyu rafiki yangu mpya katika hosteli hii, siku ya kwanza tu kukaa katika hosteli hiyo tulitokea kuwa marafiki wakubwa kutokana na kuelewana sana kwa muda mfupi. Faiz alitokea kuwa mtu mchangamfu na mwenye kujali urafiki wangu na mimi pia nilikuwa najali urafiki wake kwangu, tulipendana kama ndugu ingawa mwenzangu alikuwa ana weusi wa kiafrika kabisa. Masomo yalipoanza kila mtu alikuwa anachukua masomo tofauti na mwenzake na muda mzuri wa kuonana ikawa ni baada ya muda wa masomo, kipindi chote hicho sikuwahi kumueleza kuhusu suala la mimi kumpenda Huwaida na wala yeye hakuwahi kunionesha mpenzi wake zaidi ya kuniambia tu kuna shemeji yangu kwake anasoma hapo chuoni kozi tofauti na yeye. Kila nilipomuambia anioneshe alinijibu muda bado na muda wa kufanya hivyo ukifika atanionesha, nakumbuka siku moja ilikuwa ni jumapili tulivu nikiwa nimepumzika chumbani nikiwa nimechoka sana. Siku hiyo Faiz aliingia chumbani akiwa na furaha sana tofauti na siku zingine, alinikuta nikiwa nimelala kifua wazi kitandani usingizi ukiwa unaninyemelea.
"Oyaaa! Amkaa babu" Faiz alinitikisa huku akiongea kwa sauti ambayo kwangu niliiona kero kutokana na usingizi nilionao.
"aaaaah! Faiz unajua jana nimechelewa kulala na leo nimewahi kuamka hebu wacha nipumzike babu" Nilimwambia Faiz huku nikijigeuza kuangalia ukutani nikimpa mgongo Faiz.
"Mwana acha uzee hebu amka saa nane mchana hii usingizi wa nini?" Faiz aliniambia huku akinigeuza kwa namna iliyonikera sana.
"Faiz acha kunizingua babu mbonji limenikaba hadi kwenye macho" Nilimwambia Faiz kwa sauti yenye kuonesha wazi kukereka na suala hilo.
"Abdul unataka kuniangusha ndugu yako wa hiyari, shemeji yako amesema anataka akuone na akujue sasa ukilala hapo si unaniwekea usiku ndugu au unataka bishosti anione mimi mduwanzi babu" Faiz aliongea na kusababisha nikurupuke kutoka kitandani huku nikisema, "usiniambie man".
"ndiyo hivyo man, sasa wewe upo tayari mwanao wa ukweli nioneksne mduwanzi mbele ya usingizi wangu" Faiz aliniambia huku akikaa kitandani kwake.
"hapana man, ngoja nikalitoe hili mbonji bafuni kisha tumuibukie" Nilimwambia Faiz huku nikiinuka kuelekea nje nikiwa na uchovu. Nilienda moja kwa moja bafuni nikaoga kisha nikarudi chumbani nikamkuta Faiz akiwa kashavaa nguo ambazo nilimnunulia kama rafiki yangu, nilivaa na mimi nikawa naonekana nimependeza kama alivyopendeza yeye.
"hapo vipi unanionaje?" Nilimuuliza Faiz huku nikikaa kama mwanamitindo wa kiume.
"hapo upo poa kabisa yaani kama unaenda kunipora tunda vile" Faiz aliongea huku akitia masihara.
"wacha zako wewe au hujioni ulivyotupia zaidi yangu man" Nilimwambia Faiz huku nikicheka kutokana na masihara.
"hamna kama hicho Abdul we upo juu hata usipotupia kivile tena utakuja kupata kisu kikali zaidi ya hicho ninachoenda kukuonesha leo" Faiz aliniambia huku akielekea mlangoni.
"wacha zako wewe hebu tujikatae nikamuone shem wangu wa ukwee" Nilimwambia huku nikimfuata Faiz ambaye tayari alikuwa ameshatoka nje. Tulifunga mlango wa chumba chetu kisha tukachukua teksi nje ya hosteli zetu, Faiz alimwambia dereva mahali pa kwenda naye akatutajia bei ambayo niliikubali bila tatizo na safari ikaanza kwenda kumuona shemeji yangu kwa rafiki yangu. Safari yetu ilifika maeneo ya Kunduchi kwenye ufukwe mwanana wa bahari ya hindi pamoja eneo la kupumzika watu, Faiz alimuamrisha dereva asimame naye akatii kisha tukampa pesa zake. Faiz alipiga simu kisha akaongea na mpenzi wake akimuuliza yupo wapi, alipokata simu aliniambia "twende".
Faiz aliniongoza hadi ndani kabisa ya sehemu hiyo ya kupumzika watu pamoja na kujipatia vinywaji, tuliingia kwenye ufukwe wenye ghorofa lililojengwa kwa ubunifu pamoja kuezekwa na paa lenye umbo la kuvutia. Muda wote huo nilikuwa nimebanwa na shauku ya kutaka kumuona shemeji yangu ambaye anapendwa sana na rafiki yangu, Faiz naye alikuwa akimwagia sifa kedekede mpenzi wake kila kukicha ili nipate shauku ya kutaka kumuona. Tulifika sehemu ambayo kulikuwa na wasichana wawili warefu na wenye asili moja wakiwa wamekaa meza moja yenye viti vinne na kusababisha viwili viwe wazi, wasichana hawa wote wawili walikuwa na asili ya kisomali na walionekana ni ndugu kutokana na kuwa na kila dalili ya kufanana ingawa mmoja alivaa kofia na miwani ya jua iliyoufunika uso wake kwa kiasi kikubwa. Walikuwa ni warembo hata kwa kuwatazama wakiwa na mavazi ya kawaida huku nywele zao wakiwa wameziacha zikiwa zinaning'inia vichwani mwao, eneo walilokaa lilikuwa ni sehemu iliyojitenga hivyo Faiz alipokuwa anawasogelea nilijua dhahiri kwamba mmojawapo ndiye atakuwa shemeji yangu.Tulipokaribia msichana mmojawapo aliyevaa miwani alisimama akaenda kumkumbatia Faiz kisha akampa busu la mdomo, alisalimiana na mimi kwa kupeana mkono kisha tukakaribishwa kwenye meza tujumuike nao. Muda huo wote sikuweza kuiona sura ya shemeji yangu ingawa hapo nilitambulishwa kisha nikatambulishwa na msichsna wa pembeni kama binamu yake.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Abdul umemuona shemeji yako, ndiye huyu" Faiz aliniambia huku akiwa amemshika mgongo shemeji yangu ambaye hakunitajia jina hadi muda huo, huyu msichana niliyetambulishwa kama shemeji naye aliikia mguso wa Faiz na akawa amejilaza kwenye kifua cha Faiz.
"Faiz nimemuona ingawa hujanitambulisha jina hadi muda huu umenitambulisha binamu yake ambaye ni Nurulayt tu" Nilimuambia Abdul kutokana na kitendo chake cha kutonitambulisha jina la mpenzi wake.
"come on Abdul yaani huyu humjui unasoma nae kozi moja chuo, au hii kofia na miwani aliyovaa ndiyo zinakufanya usimjua nini" Faiz aliongea huku akimvua kofia mpenzi wake na kupelekea niione vizuri sura ya shemeji yangu ambaye tangu mwanzo nilitamani kumuita mpenzi . Wakati naiona sura ya shemeji yangu ambaye ni Huwaida msichana ninayemhusudu kuliko kitu chochote, nilijikuta nikishindwa hata nikishindwa kumeza mate nikaanza kuhisi kuna kitu kimenikaba kooni, maumivu niliyoyapata moyoni hayaelezeki hata kitabuni zaidi ya kuishia kuyaeleza kidogo. Huwaida huyu aliyeufanya moyo wangu uwe mbioni kila nikimuona, Huwaida huyu aliyefanya nitamani kila siku kumuona, Huwaida huyu niliyekuwa sina amani nisipomuona, Huwaida huyu ninayemuwaza sana ndiyo leo hii namuita shemeji kwa mtu ambaye ni rafiki yangu ambaye anaonekana mtu kwasababu yangu sasa anamiliki msichana ambaye ni kipenzi cha moyo wangu. Maumivu niliyoyapata kwa sekunde tu nilipouona uso wake wa madaha uliopambwa na tabasamu pana likiwa linaachiwa kwa ajili ya rafiki yangu, Huwaida alionekana kutabasamu kwa tabasamu lililoniumiza mtima wangu nilipoiona sura yake baada ya kuvuliwa kofia. Faiz naye alitabasamu kutokana na mshangao niliuonesha kutokana na kumuona Huwaida, Faiz alijua kuwa mshangao ni kutokana na jambo nisilolitarajia kuwa na shemeji niliyekuwa namfahamu tangu mwanzo.
"Abdul naona umepigwa na bumbuwazi la mwaka" Faiz aliongea huku akicheka na kupelekea na mimi nicheke bila hata kuelewa nilichokuwa nakicheka ni nini na hata nilipomaliza kucheka nilibaki najishangaa mwenyewe kwa kucheka karika jambo ambalo halikuwa likinifurahisha hata kidogo.
"yaani shem kukaa hapa muda wote ulikuwa hujanitambua tu" Huwaida aliongea kwa kuniita jina ambalo lilikuwa ni mwiba mkali wa sumu unaouchoma moyo wangu na kuniachia maumivu makali yasiyovumilika kwa urahisi.
"Huwaida hilo kofia lako umefunika nusu ya uso mzima we unafikiri atakujua vipi na hiyo miwani uliyoivaa si atakujua jamaa tu" Nurulayt naye aliongea akithibitisha ugumu wa kumtambua Huwaida akiwa amevaa kofia na miwani ambavyo alivuliwa na Faiz.
"jamanii! Nimebadilika kwa lipi nikiwa navaa hivi?.... Eti Sweetie nimebadilika nini si niko vilevile tu. Si eti eh!" Huwaida aliongea huku akimchezea kidevu Faiz bila hata kutambua anaumiza moyo wangu kwa kila anachokifanya hapo muda huo kwa rafiki yangu Faiz.
"ndiyo mpenzi umebadilika sana ukiwa na mavazi hayo" Faiz aliafiki suala la kubadilika kwa Huwaida akiwa kavaa kofia pamoja na hiyo miwani.
"Mmmh! Sweetie mbona umeweza kunitambua kama nimebadilika si ungeshindwa" Huwaida aliongea kwa kudeka huku akijiacha huru zaidi katika kifua cha Faiz.
"kumbuka chuma siku zote hufuata sumaku hata sumaku iwe na muonekano wa namna gani, sasa ndiyo na mimi nitakufuata wewe hata ubadilike namna gani kwasababu wewe ni sumaku na mimi ni chuma. So usishangae mimi kukutambua kwa muonekano wa leo na sio ule mashungi" Faiz aliongea huku akimtazama Huwaida usoni na akijua anawafurahisha wanaomuona, hakutambua kama alikuwa anamuumiza rafiki yake kipenzi anayempenda sana mpenzi wake hata kabla hajajua kama ni mpenzi wake.
"mmmh! Makubwa haya tena madogo yana nafuu" Nurulayt aliongea baada ya kusikia maneno ya Faiz akimuambia Huwaida.
"bibiie! Makubwa yapi? Umbea tu muone" Huwaida aliongea huku akimtazama Nurulayt.
"umbea wapi wewe yaani mtoto umepata anayejua kubembeleza na kuchombeza na shem amepata mtu anayejua kubembelezwa na kuchombezwa, eti Abdul nadanganya?" Nurulyt aliongea kwa madaha na kupelekea Faiz na Huwaida wacheke sana.
"hudanganyi kabisaa!" Nlijilazimisha kukubaliana na maneno ya Nurulayt huku macho yangu yote yakiwa yanamtazama Huwaida hadi akaona aibu.
"Mpenzi huyu ndugu yako huyu ana maneno huyu....na wewe Abdul unampa support kabisa" Faiz aliongea huku akicheka.
"mwenzangu nahisi lao moja hawa" Huwaida naye alidakia huku akicheka akiwa amelalia kifua cha Faiz, nilipokiona kitendo hicho moyoni nilijihisi kuungua ndani kwa ndani tena kwa moto usio wa kawaida. Nilijikuta natamani hata niondoke hapo lakini nilishindwa kutokana na chakula kuwekwa muda huo huo na wahudumu wa eneo hilo, laiti ningenyanyuka na kuondoka ingeweza kuhisiwa kuna jambo limenikera. Ilinibidi nivilie tu kuka hapo kwenye kiti ambacho nilikiona kama kinanitoboa na miiba katika makalio yangu, chakula kililika hadi kikamalizika kwa ustahimilivu na uvumilivu wa kila ninachokiona. Baada ya kumaliza kula nilitamani ninyanyuke niondoke lakini Faiz na Huwaida wakaniwahi kwa kunyanyuka wakiwa wameshikana.
"Oyaa Abdul si tunaingia ndani mara moja" Faiz aliniaga huku akiwa anaelekea mahali vilipo vyumba vya kulala wageni katika hoteli, mikono yake ilizidi kuniumiza tu kila nilipoiona ikiwa ipo kiunoni mwa Huwaida. Mezani nilibaki mimi na Nurulayt tukiwa tumekaa kimya bila ya kuongea chochote, Nurulayt alikuwa makini katika kuperuzi simu yake na mimi ndiyo dimbwi la mawazo juu ya nilichokiona leo likaanza kunizamisha taratibu. Nilijikuta nikianza kumchukia Faiz kwa kuwa na msichana ambaye kwangu ni kila kitu na sikutegemea kama mtu ambaye mwenye maisha ya chini atakuja kunizidi hatua kiasi cha kuliruka bonde la kuwa peke yake na kufika katika ukingo wa pili katika bustani ya maua yenye ua ambalo nililiwekea malengo tangu mwanzo nilipoliona. Urafiki wa dhati uliokuwa kwa Faiz tangu mara ya kwanza tilipopangiwa chumba kimoja hosteli nilihisi ukianza kuyeyuka taratibu mithili ya barafu linavyoyeyuka kwenye joto, kwa mara ya kwanza moyoni mwangu niliazimia kufanya jambo lolote baya kwa Faiz ingawa alikuwa ananiona kama ndugu kwake. Nilichokuwa nafikiria muda huo ni kumpata Huwaida kwa namna yoyote na sijali lolote, yaani nilijiona natafuta shilingi(Huwaida) katikati ya majani marefu(Faiz) na sikuwa na namna nyingine ya kuipata shilingi hiyo zaidi ya kuyapinda marefu haya tena ikibidi niyakate kabisa ili kuipata shilingi ambayo kwangu ilikuwa ina thamani zaidi ya lulu marjani ya katikati ya bahari kwenye mpaka wa bahari mbili zenye maji yenye joto tofauti. Mawazo yalizidi uzito hata kiasi cha kuizuia baadhi ya milango yangu ya fahamu isiwe katika kufanya kazi inavyostahiki, kiufupi mwili wangu ulikuwepo hapo jirani na Nurulayt lakini mawazo yangu na kila kiungo changu hakikuwepo katika eneo hilo. Nilikuja kurudi katika hali ya kawaida baada ya kutingishwa na Nurulayt na hapo ndipo nikaisikia sauti yake ikiniita kama ananiamsha usingizini, nilishtuka kidogo kisha nikapangusa uso wangu kwa viganja vyangu kama nilikuwa nafuta maji usoni mwangu.
"Abdul una tatizo gani mbona hivyo?" Nurulayt aliniuliza huku akinitazama kwa udadisi mkuu usoni mwangu.
"sina tatizo nipo sawa kabisa" Nilimjibu kwa kumficha tatizo nililokuwa nalo kutokana uzito wa jambo lenyewe.
"upo sawa kivipi mbona nakuita zaidi ya mara nne huitiki mpaka nikutingishe kama umelala usingizini, unawaza nini?" Nurulayt ambaye ndiyo kwanza ninaonana naye kwa mara ya kwanza alizidi kuniuliza kwa udadisi.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"mawazo ni sehemu ya maisha ya binadamu"Nilimwambia huku nikikaa sawa kwenye kiti.
"ok yameisha sasa, Abdul naomba simu yako tafadhali" Nurulayt aliniomba simu yangu kama mtu mwenye shida sana, nilimpatia simu yangu akaandika namba zake kwenye simu akazipiga halafu akazihifadhi.
"je nimefanya vibaya?" Nurulayt aliniuliza.
"hapana hujafanya vibaya" Nilimjibu kisha tukaendelea kuongea mambo mengine tukiwa tunawasubiri Faiz na Huwaida ambao nina uhakika asilimia zote wameenda kula tunda haramu ambalo hata watu wa kwanza kuletwa duniani walilila ingawa walikatazwa na Muumba. Mnamo saa kumi na mbili jioni Faiz na Huwaida walirejea wakiwa na furaha kama walivyoondoka, tuliondoka kurudi hosteli baada ya kuagana na Huwaida pamoja na Nurulayt.
Kuanzia siku hiyo ndiyo siku ambayo chuki na wivu kwa Faiz vilichukua nafasi na mawasiliano baina yangu na Nurulayt yalizidi kuwa makubwa mpaka ikawa haipiti asubuhi bila ya kuwasiliana, nilimchukia Faiz wa kitu ambacho si kosa kwake na nilitamani kumfanya kitu chochote kibaya ili aweze kuachana n mwanamke ninayompenda. Mapenzi baina yao yalizidi kuwa makubwa na wivu kwangu ukazidi kuwa mkubwa hadi nikaazimia nifanye jambo ili niweze kumpata Huwaida, mawasiliano yangu na Nurulayt nayo yalizidi kuwa makubwa na katika mawasiliano ya siku zote alikuwa akiniambia kuhusu mpango ambao alitaka kufanya na mimi ili alipe kisasi. Nilipouliza kuhusu mpango huo hakunijibu chochote zaidi ya kuniambia niwe na subira, nakumbuka ilikuwa ni jumapili siku ambayo nilikula njama za kundi la watu wakampige Faiz hadi aachane na Huwaida. Njama hiyo ilifanikiwa kwa kumnasa Faiz akiwa yupo njiani akienda kwao kama alivyoniaga, Faiz alitekwa kama ilivyopangwa na akapigwa sana ili amuache Huwaida. Baada ya siku mbili tangu Faiz aniage alikutwa kwenye mtaro wa barabara ya Sam Nujoma akiwa hajitambui na ana majeraha mwili mzima, taarifa za kuokotwa kwake katika mtaro huo zilinifikia nikiwa nipo hosteli nikiwa nimepumzika baada ya kupigiwa simu na Huwaida ambaye alikuwa analia mfululizo. Taarifa hiyo nilivyoipata nilijifanya nimeshtuka sana na nikivaa haraka ili niwahi kutoka kuelekea hospitali ya Lugao alipopelekwa kutokana na hali ya kuwa si ya kuridhisha, nilipofungua mlango wa chumba chetu ili nitoke nilikutana uso kwa uso na Nurulayt akiwa amekasirika akiwa amesimama katikati ya mlango.
"ndiyo unajifanya una haraka siyo!" Nurulayt alinisemesha kwa ukali.
"Nur kuna ninj si unipishe njia niwahi hospitali nikamuangalie Faiz" Nilimuambia Nurulayt huku nikimtoa mlangoni lakini hakutoka mlangoni na badala yake alinisukuma ndani kisha akafunga mlango.
"eti niwahi hospitali nikamuangalie Faiz, wakati unawalipa hela Danger boys wamteke na wampige ndiyo baadae ukamuone sio" Nurulayt aliongea huku kabana pua kwa dharau akiwa ameshika kiuno mbele yangu.
"we Nur unaongea nini hivi akili zipo timamu kweli?!" Nilijikuta nikianza kujifanya sijaelewa alichoongea Nurulayt ingawa moyoni nilikuwa najiuliza huyu mwanamke kajuaje wakati ule ni mkataba wa siri na kikundi hicho cha wahalifu. Nurulayt alipoona kuwa najifanya sielewi kinachoendelea alitoa bahasha akanipatia huku akinitazama kwa macho makali, bahasha hiyo niliifungua kwa pupa na nikajikuta nimeshtuka kwa nilichokiona ndani yake.
"sema sasa huelewi kipi?"Nurulayt aliuliza huku akinitazama kwa dharau.
Nilibaki nikiwa nimechoka bila hata kufanya kazi nzito yoyote, nilizidi kuhema kwa nguvu bila hata kukimbia umbali wowote. Niliishia kumtazama Nurulayt bila kumuambia neno lolote, kwakweli sikutegemea kama suala kama hili ambalo litagunduliwa na mtu yoyote mpaka kufikia hatua ya kupigwa picha wakati nafanya makubaliano na muwakilshi wa kundi la wahalifu llilompiga Faiz. Nurulayt alipoona nababaika namna hiyo alianza kucheka kisha akazichukua picha zake kisha akaziweka Nurulayt eka kwenye bahasha. Alinitazama kwa uso uliopambwa na tabasamu kisha akaniambia, "kumbe na wewe muoga hivi".
Niliposikia maneno hayo nilibaki namtazama nikiwa sijamuelewa kitu gani anachomaanisha, alinishika mkononi hadi kitandani kwangu halafu akaketi na mimi nikaketi.
"Abdul both we have the same enemy(Abdul wote tuna adui mmoja) Nurulayt aliniambia huku uso wake ukiwa umeondokwa na tabasamu usoni na umakini ukawa umechukua nafasi yake.
"what(nini)?" Niliuliza kwa mshangao sana baada ya kusikia kauli hiyo ya Nurulayt.
"Faiz ni adui yako kwakuwa amemchukua msichana unayempenda na mimi Faiz ni adui yangu kwasababu kamuua kaka yangu huko Afrika ya kusini na akamuibia kiasi kikubwa cha madini" Nurulayt aliongea huku machozi yakimtoka machoni mwake kwa hasira sana halafu akaniegemea begani huku akisema, "Abdul ukae utambue huyo rafiki yako uliyekuwa unamhusudu mwanzo ni jambazi hatari na ana kundi kubwa la magaidi nchini Afrika ya kusini na kwingineko barani Afrika na pia ametajirika kupitia tani mojaya madini ya almasi aliyomuibia kaka yangu baada ya kumuua". Nurulayt alinieleza mambo ambayo hata sijuyaelewa na wala sikuyategemea kama Faiz huyu mtoto wa kimasikini ninayemjua kama atayafanya.
"Huwaida hatambui lolote juu ya hili na ninayetambua ni mimi niliyeenda kumtembelea kaka yangu Sabir aliyeondoka nyumbani Somalia kwenda kutafuta maisha Afrika ya kusini akiwa na mtaji mkubwa sana aliopewa na baba, kaka yangu alipokuwa anauawa nilimshuhudia kila kitu na Faiz ndiye aliyemuua ndani ya nyumba ya kaka yangu na muda huo anafanya hayo mimi nilikuwa nimejificha sehemu katika nyumba ya kaka yangu ili asinione akaniua" Nurulayt alizidi kuniambia maelezo ambayo yaliniacha kinywa wazi, Faiz huyu ninayemjua mimi kusikia ni muuaji na jambazi mkubwa.
"Nuru kwahiyo wewe ulikuwa unaishi Afrika ya kusini?" Nlimuuliza Nurulayt ili nipate maelezo yake kiupana zaidi.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"hapana sikuwa naishi Afrika ya kusini ila nilikuwa naenda kumtembelea kaka tu mara chache na hata hiyo siku aliyouawa nilikuwa nilikuwa nimekuja kumsalimia na ndiyo siku hiyo Faiz akapiga hodi nikaambiwa nijifiche" Nurulayt alizidi kunieleza huku akiwa na hasira sana.
Kusikia habari za mtu ambaye kwangu ni adui na kwake ni rafiki, nilibaki nikiwa na mshangao sana kutokana na nilivyokuwa namfikiria Faiz jinsi alivyo. Nilikuwa namuona kama mtu mchovu tu mwenye ujanja wa kawaida tu lakini sasa nilibadili fikra zangu na nikaziweka kuwa nashindana na mtu hatari na mwenye nguvu nguvu ya kunifanyia kitu chochote kibaya nilianza kumuogopa kutokana kusikia habari zske. Jambazi na muuaji ndiye ambaye fikra zangu ziliniambia napambana naye na ninahitajika nimshinde kwa namna yoyote, nilitaka kumpata Huwaida ili niwe naye na kuna mti wa mbuyu ambao mwanzo niliouona niliuona mchicha ndiyo unaonizuia kumpata na nilitakiwa kuuondoa huu mbuyu ambao ndiyo unanizuia kupata waridi la moyo wangu. Muda huo bado nilikuwa nikiyafikiria maneno ya Nurulayt, hakika nilimuona ni mwanamke atakayeweza kunirahisishia kupata kila ninachohitaji na kupata kile moyo kitakachojifariji.
"sasa hapo unataka nikusaidie sio?" Nilimuuliza Nurulayt baada ya kufikiria kwa muda mrefu.
"nisaidie na mimi nikusaidie Abdul, kifupi tusaidiane katika hili. Nataka kulipa kisasi kwa Faiz hivyo nahitaji msaada wako, unahitaji kumpata Huwaida hivyo utahitaji msaada wangu ili umpate" Nurulayt aliongea huku akinitazama usoni.
"ok, hilo linawezekana mbele ya pesa hakuna kinashindikana. Nipo tayari kukusaidia nadhani na wewe uko tayari kunisaidia" Nilimwambia Nurulayt huku nikimtazama usoni, Nurulayt aliachia tabasamu mwanana kwa kukubaliwa jambo lake na mimi.
"vizuri na hapa tunahitajika tutoe kiasi kikubwa cha pesa kwa ajili ya kumteka Faiz kwasababu tunatumia kundi la wahalifu hatari kutoka Kongo hivyo tujiandae kiuchumi" Nurulayt aliniambia baada ya kumkubalia kisha akajiachia kitandani.
"Nur kuhusu pesa hata iwe milioni mia moja we usihofu itapatikana hata leo hii" Nilimwambia Nurulayt huku nikimtazama usoni mwake.
"kiasi chote cha pesa utakipataje leo hii hata kama tunatokea familia zenye uwezo mkubwa wa pesa?" Nurulayt aliniuliza kwa mshangao.
"Hilo niachie mimi, Nadhani ni muda wa kutoka kwenda Lugalo kumuangalia yule punda" Nilimwambia Nurulayt huku nikisimama kwa ajili ya kuondoka. Nurulayt alinivuta mkono nilipotaka kuondoka kisha akanibusu ghafla kwenye papi zangu za midomo bila hata kutarajia tendo hilo, aliponiachia akanikumbatia kwa nguvu halafu akaniambia "Abdul kaa utambue na mimi ni mwanamke na nina hisia kama mwingine, nakupenda sana lakini kwa suala la kusaidiana mimi na wewe sina budi kukupeleka kwenye himaya ya Huwaida". Wakati hayo maneno Nurulayt alikuwa anahema huku akitazamana na uso wangu kwa karibu wa takribani sentimita mbili, kifua chake kichanga kilikuwa kikinipa majaribu matupu hadi muda huo. Nilijikuta nikipandwa na hisia za mapenzi na nikaanza vurugu hapo hapo hadi kitandani, baada ya saa moja wote tuliingia bafuni tukaoga kisha tukaelekea hospitali ya Lugalo kwenda kumuona mbaya wangu. Tulitumia muda mfupi na tukafanikiwa kufika katika hoapitali hiyo ya jeshi ambayo haipo mbali sana na eneo ambalo Faiz aliokotwa, Nurulayt aliniongoza hadi jirani na wodi ambayo Faiz alikuwa kalazwa ambapo tulimkuta Huwaida akiwa pembeni ya mlango kwenye dawati akiwa amejiinamia. Nilijifanya naenda kwa kasi huku nikihema hadi Huwaida akautambua ujio wangu na akanikimbilia akanikumbatia huku akilia kwa uchungu, ulaini wa mwili wake kwangu ulikuwa ni faraja tosha kwani nilihisi kama nimekumbatiwa na mpenzi wangu.
" Shem sijui Faiz wangu kawakosea nini watu hawa mpaka wamfanyie hivi" Huwaida alilalamika sana huku machozi mfululizo yakimtoka, nilimbembeleza huku nikiwa nina firaha moyoni ya kukumbatiwa naye. Baada ya kuachiana kukumbatiana tulikaa kwenye dawati tukiwa tunasubiri, baada ya muda daktari aliyevalia sare za kijeshi pamoja na koti la kitabibu alitoka ndani ya wodi aliyolazwa Faiz.
"dokta mgonjwa wetu anaendeleaje?" Nilijifanya nina wasiwasi nikamkimbilia daktari huyo nikamuuliza.
"mgonjwa wenu anaendelea vizuri ingawa hajarejewa na fahamu bado" Daktari huyo alitujibu.
"tunaweza kumuona dokta?" Huwaida aliuliza akiwa na wahka mkubwa sana.
"mnaweza mkamuona lakini baada ya saa moja" Daktari alitujibu halafu akaondoka akituacha tukiwa tumesimama vilevile kama tilivyokuwa tunamuuliza maswali, baada ya saa moja ya kusubiri hatimaye tuliruhusiwa kwenda kumuona Faiz. Wote kwa pamoja tuliingia ndani ya wodi hiyo aliyolazwa Faiz hadi kwenye kitanda chake, tulimkuta akiwa amelala na hajitambui huku dripu ya damu ikiwa inaturirika kuingia kwemye mwili wake. Usoni alikuwa ana plasta kadhaaa ambazo zilimfanya Huwaida alie kama kafiwa hadi Nurulayt akawa anafanya kazi ya kumbembeleza lakini haikufanikiwa na ikabidi atolewe nje na Nurulayt kuhofia kutokea usumbufu kwa wagonjwa wengine waliolazwa humo ndani. Wodini nilibaki mimi pekee nikiwa na namtazama Faiz nikiwa na ghadhabu kubwa nilizozificha nafsini mwangu, hadi natoka wodini humo chuki yangu kwa Faiz ndiyo ilizidi kuongezeka. Niliwakuta Nurulayt na Huwaida wakiwa wamekaa kwwnye dawati lililopo pembeni ambapo na mimi nikajiunga nao.
Baada ya wiki moja na nusu Faiz aliruhusiwa kutoka hospitali na akarudishwa nyumbani kwao Kigogo kwa ajili ya kujiuguza na huo ndiyo ukawa muda mwingine wa kupanga tukio jingine la kulifanya nikiwa mimi na Nurulayt ambaye kwangu alitokea kuwa mwanamke ninayefanya mpango mzito pamoja na kunitimizia haja za kimwili kutokana na mapenzi mazito aliyonayo kwangu. Katika kipindi hicho ndicho kipindi ambacho Faiz na alitoweka katika mazingira ya kutatanisha kwa watu wa kawaida ingawa kwetu sisi mimi na Nurulayt tulikuwa tunajua kwa kina juu ya suala hilo. Utekwaji nyara wa Faiz ulikuja kujulikana kwa familia yake ambayo ilipewa sharti gumu ambayo ilikuwa ngumu kulitimiza katika muda wa miezi minne.Huwaida alilia mpaka na na baada ya miezi minne alikata tamaa hasa alipotumiwa mkanda wa video na vijana hatari kutoka Kongo ikionesha Faiz akiuawa kikatili, mkanda huo ulikuwa gumzo jijini na hata katika bara la Afrika baada ya kunaswa na vyombo vya habari. Maelfu ya watu kutoka nchi mbalimbali walilaani kitendo kama kile cha kuuliwa mtu kikatili, lilikuwa ni tukio lililodumu kwa muda wa miezi kadhaa vichwani na hatimaye lilisahaulika kabisa. Huwaida naye alilia sana lakini alisahau kabisa tukio lile akijua ameshampoteza mwanaume anayempenda, kipindi chote hicho mimi nilikuwa karibu na Huwaida nikiwa namfariji hadi akaniona mtu muhimu katika maisha yake kwa muda huo na alikuwa akiendelea kuniita shemeji na hata darasani alikuwa ni mtu wa kukaa karibu nami kila muda. Kipindi hicho Nurulayt alikuwa akiutumia muda wake mwingi katika kunimwagia sifa ili kumfanya Huwaida azidi kunipenda, penzi ni kama pembe kwa ng'ombe halifichiki hata siku moja na hata ulikate litachipua tena na litaendelea. Penzi langu kwa Huwaida lilikuwa kama namna hiyo na nilijitahidi kulificha na hatimaye nikalidhihirisha kwa kwake tukiwa tumekaa katika mgahawa wa Samaki samaki wa Mlimani city, siku hiyo ndiyo siku ilikuwa ngumu kwa Huwaida kutokana na penzi lake kwa Faiz.
"Mh! Abdul ujue mimi nakuheshimu kama shemeji yangu hilo suala haliwezekani" Siku hiyo Huwaida aliniwekea kikwazo pale nilipomfunulia hisia zangu juu yake.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"natambua hilo suala Huwaida ulikuwa ni mpenzi wa rafiki yangu kipenzi nimetokea kukupenda tangu mara ya kwanza tunakutana pale kwenye foleni ya usajiri lakini nilipobaini ni mpenzi wa rafiki yangu kipenzi ambaye ninamuheshimu na kumpenda kama ndugu yangu wa damu niliamua kumuachia ingawa mipango ya Mungu imetokea" Nilimuambia Huwaida ambaye alionekana kuwa na aibu muda huo.
"ok, Abdul nipe muda wa kufikiria nitoe uamuzi unaostahiki" Huwaida aliniambi baada ya kujifikiria kwa muda wa dakika kadhaa, hali hiyo ilifufua matumaini katika moyo wangu wa kupata penzi nililokuwa nalipigania kwa muda mrefu. Sikutaka kabisa kumuharakisha Huwaida hivyo niliamua kumpatia muda wa kutosha wa kujifikiria nikiwa nina uhakika wa kumpata, muda huo niliuona moyo wangu umekuwa mwepesi kwa kubeba mzigo mzito kwa muda mrefu ambao hadi hapo nilikuwa nimeutua.
"ok nakupa muda wa kujifikiria nadhani utakuwa umefanya maamuzi yanayostahiki, kesho nina safari ya nje ya mji kidogo na huko nitakaa siku kadhaa. Nadhani nikirudi nitapokea jibu zuri kutoka kwako" Nilimwambia hivyo ili nimpe muda wa kutosha wa kujifikiria nikijua nitapata jibu zuri kutoka kwake, tuliongea mambo mengi tukiwa hapo na hatimaye tukaagana na kila mmojw akaondoka anapoishi.
Asubuhi iliyofuata nilisafiri kwa ndege kwa shirika la ndege la Kongo hadi jijini Brazaville katika mji wa Kongo ambayo ilikuwa ni safari ya masaa kadhaa angani, nilifanikiwa kufika Brazaville salama na nikakuta wenyeji wangu ambao nimewazoea kila siku wakiwa wananisubiri ambao walikuja na usafiri kwa ajili ya kunipeleka eneo ambalo ninaloelekea. Wenyeji wangu walinipokea kwa furaha na tukaingia katika moja ya magari mawili waliyokuja hapo katika Uwanja wa kimataifa Maya-maya kuja kunipokea, safari ilianza salama kuifuata barabara ambayo sikuwa naitambua jina kwa masaa kadhaa tukawa tumefika kwenye msitu ambao naujua kwa jina la Patte d'ioe. Tuliingia kwenye barabara ya vumbi kisha tukatembea kwa mwendo wa kilomita kama tano tukawa tumefika kwenye uzio wenye geti la nyavu ambalo linalindwa na watu wenye silaha nzito za moto, geti hilo lilifunguliwa gari ikaingia hadi ndani halafu tukatembea umbali wa kilomita moja tukawa tupo mbele ya jengo la ghorofa moja. Wenyeji wangu walishuka na mimi nikashuka na tukongozana hadi ndani ya jengo lililopo mbele yetu katika sehemu ya juu, tuliingia katika ofisi moja ya jengo hilo iliyojaa silaha za kila aina na mbele palikuwa na mtu ambaye nilikuwa nafahamiana naye sana ambaye alinichangamkia aliponiona.
"Ohooo! Somalian welcome(Ohooo! Msomaji karibu)" Mtu huyo ambaye nilimkuta alinilaki.
"Thanks , I don' have time i think you know the aim of being here(asante, sina muda nafikiri unajua dhumuni la kuwa hapa) Nilimwambia yule mtu.
"ok, follow me (sawa, nifuate)"Aliniambia huku akitoka nje ya ofisi na mimi nikamfuata, tulienda hadi chini ya ardhi ya jengo hilo kwenye chumba chenye giza ambacho kiliwashwa taa baada ya sisi kuingia ndani. Mbele yetu alionekana mtu aliyedhoofu akiwa amefungwa kwa kamba ngumu akining'inia, nilipoiona sura yake niliishia kucheka hadi yule mtu akawa ananitazama kwa hasira.
"Tanzania nzima inatambua kama wewe ni marehemu hasa baada ya kuisambaza ile video ya kutengeneza ikionesha unavyouawa kikatili, ila miongoni mwa watu wachache wanatambua kama bado upo hai unakula mateso kwa ukaidi wako Faiz" Niliongea huku nikicheka kimadharau hadi Faiz akatema mate ambayo hayakunifikia.
"Jeuri siyo kabisa, sasa nilitaka nije nikuambie kwamba Huwaida ni wangu kwa sasa na nikirejea Tanzania jua ninaenda kukaa na mwanamke aliyepaswa kuchukuliwa na mimi mtoto wa kitajiri na si wewe masikini na jambazi wa kutupwa uliye chini ya mikono ya wabaya wako. Faiz una siku nne tu za kuendelea kuishi duniani kabla hujauawa na sumu ambayo umechomwa kupitia sindano, sasa basi nataka utambue kuwa ukifa utakuwa utakuwa msosi wa fisi na tai wala mizoga huku msituni. Buriani rafiki yangu" Nilimwambia Faiz kwa dharau halafu nikamgeukia mwenyeji wangu nikamwambia " After his death, his body suppose to be food for Hyena and Vulture(baada ya kifo chake, mwili wake unatakiwa uwe chakula kwa Fisi na Tai). Nilipomaliza kuongea hivyo Faiz alianza kulia mwenyewe huku akisikitika kwa mambo yanayoenda kumkuta, nilitoka humo ndani nikiwa sina hata chembe ya huruma kwa huyu aliyekuwa akiniona kama ndugu yake hapo awali. Muda huo huo niliondoka huko porini kwa kutumia magari niliyoletwa nayo awali hadi katikati ya jiji la Brazaville, nilichukua chumba katika hoteli mojawapo katika jiji la Braazaville na nilikaa kwa siku mbili. Asubuhi ya siku ya siku ya tatu niliondoka nchini Kongo kurudi Dar es salaam na nikafanikiwa kufika salama kwa mapenzi ya anayenipa pumzi, majira ya saa nane mchana nilikuwa njiani kuelekea hosteli nikiwa sina hili wala lile. Nilikuwa nina furaha sana nikijua ninaenda kuanzisha ukurasa mpya wa mahusiano na Huwaida kwani Faiz angekufa ndani ya siku moja inayokuja, furaha yangu ilitimbukia nyongo baada ya mambo kwenda mrama tofauti na ilivyokuwa. Nilipokuwa nakaribia maeneo ya Tazara ikiwa ndani ya teksi simu yangu iliita kwa fujo na nilipoitoa kuangalia jina mpigaji nilikuta ni Nurulayt ndiye ananipigia, niliipokea na kuiweka sikioni halafu nikatulia kimya bila ya kuongea neno lolote.Taarifa aliyonipa Nurulayt ilinifanya nisems, "unasema mambo hovyo?.......kivipi?....upo wapi?...ok nakuja". Nilikata simu kisha nikamwambia dereva wa teksi, " kaka samahani kwa usumbufu, naomba unipeleke Kawe sasa hivi nitakulipa hela yote ya usumbufu huu". Yule dereva wa teksi alitii nilichomuelezaa safari ikaanza kuelekea Kawe, baada ya dakika thelathini niliwasili Kawe na nikamlipa yule hela yake kisha nikaanza kutembea kuelekea katikati ya tarafa ya kawe, nilipofika katikati ya mitaa nilienda moja kwa moja hadi kwenye geti la kiwanda ambacho kimefungwa siku zingi. Niligonga geti kwa nguvu na baada ya sekunde kadhaa Nurulayt alikuja kufungua akiwa ameonekana kuchanganyikiwa.
"vipi kuna nini?" Nilimuuliza hapohapo.
"nifuate" Nurulayt aliniambia huku akielekea ndani, nami niliingia nikafunga geti kisha nikamfuata kule alipoelekea. Nurulayt aliniongoza hadi kwenye mashine za kiwanda hicho kidogo ambacho hakitumiki, tulipofika eneo hilo Nurulayt alinionesha kwa ishara upande ambao kulikuwa na mateka mmoja aliyekuwa amefungwa kwa kamba ngumu sana.
"sikuwa na jinsi Abdul imenibidi nifanye hivi maana siri ilishavuja kwake kupitia kwa mtu asiyejulikana" Nurulayt aliniambia huku akinitazama usoni kwa huruma, taarifa hiyo ilinifanya nijihisi naelekea kupagawa kwani haikutarajiwa kutokea.
"hebu mtoe kitambaa cha mdomoni kwanza maana naona anababaika" Nilimwambia Nurulayt huku nikimtazama kwa huruma yule mtu akiyefungwa pale. Nurulayt alimtoa kitamba kile mdomoni na hapo ndipo nikaanza kulaumiwa na mateka yule.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Abdul yaani umeamua kuniulia kipenzi changu ili niwe nawe sasa kwa taarifa yako sikuhitaji shetani mkubwa wee" Alikuwa ni Huwaida akiropoka maneno hayo huku akilia kutokana na kitendo nilichomfanyia Faiz ingawa hakuonekana kujua kama Faiz yupo hai hadi muda, maneno hayo yalinishtua sana kuyasikia.
"Nuru imekuaje hebu nieleze vizuri" Nilimuuliza Nurulayt ambaye aliishia kunipatia simu ya mkononi ya Huwaida bila kuongea chochote. Niliipokea simu hiyo ambayo nilipoigusa kitufe cha kuionesha mwanga katika kioo nilikutana na barua pepe pamoja na picha mbalimbali za Faiz akiwa amelala akionekana ni mfu tayari, nilipomuangalia Nurulayt ambaye muda huo alikuwa ameshika kisu kikali kisha nikamuambia, "mfungulie" baada ya kuona Huwaida anatukana matusi mfululizo. Nurulayt alimfungulia kwa kuzikata halafu akasimama pembeni ya Huwaida huku anamtazama, macho ya dharau. Huwaida baada ya kufunguliwa alinifuata kwa kasi huku akiniita mwanaharamu, aliponikaribia alinipiga kibao kikali halafu akaokota chuma kizito akiwa anahema. Alikinyanyua kila chuma akawa ananielekezea usoni ili anipigae nacho, alikinyanyua kisha akakishusha kwa nguvu. Nilibaki nikifumba macho huku nikisubiri hukumu yangu kwa Huwaida kwa kitendo nilichomfanyia, nilijiona sina thamani tena ya kuendelea kuishi ikiwa yeye anaonesha dhahiri ananichukia na hataki hata kuiona sura yangu kuanzia muda huo. Nikiwa nasubiri hukumu yangu nilihisi kama kitu kikitoboa mfuko wa gunia kisha kimiminika kizito kikinirukia usoni, nilipofumbua macho nilijikuta nikiwa sina hata nguvu ya kusimama.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment