Search This Blog

Friday, 20 May 2022

BIASHARA YA KIFO - 1

 











    IMEANDIKWA NA : HALFANI SUDY



    *********************************************************************************



    Simulizi : Biashara Ya Kifo

    Sehemu Ya Kwanza (1)



    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hali ya hewa ilikuwa tulivu katika jiji la Dar es salaam. Hakukuwa na mvua wala hakukuwa na jua kali lichomalo kama ilivyozoeleka.

    Mvua iliyoonyesha asubuhi ya siku hiyo iliifanya jiji la Dar es salaam kupoa kabisa.



    Katika mtaa wa Posta, mahali maarufu sana katika jiji la Dar es salaam kulikuwa na pilikapilika za watu kama kawaida. Huyu anaenda huku, yule anarudi kule.



    Daladala mbalimbali zilikuwa zinaingia na kutoka stendi ya Posta kama ilivyo ada.

    Kelele za wapiga debe zilishamiri, kwa wanaojua mahali waendako zilikuwa ni kelele zisizo na manufaa, kwa wasiokujua waendako zilikuwa kelele zenye faida sana kwao. Kelele za wapiga debe zilikuwa msaada mkubwa sana kwao kuwaelekeza waendako.



    Martin Hisia alikuwa ni mmoja kati ya abiria wengi waliosimama katika kituo cha daladala. Alikuwa makini akiliangalia kila gari litokalo na kuingia katika kituo cha daladala.



    Martin alikuwa amesimama akiwa ameegemea mojawapo ya nguzo za mti zilizokuwepo pale kituoni. Alikuwa amevaa suruali ya jeans na shati la jeans. Mavazi aliyokuwa anayapenda sana hasa akiwa na kazi maalum, kazi maalum kama iliyopo mbele yake.

    Kichwani alikuwa amevaa kofia pana aina ya pama. Kofia isiyoruhusu sura yake kuonekana kwa urahisi, huku macho yake yakiwa yamefichwa nyuma ya miwani kubwa meusi.

    Miguuni alikuwa amevaa raba nyepesi, raba nyeusi aina ya Nike. Viatu alivyoviamini sana hasa awapo na kazi maalum. Viatu vinavyomruhusu kufanya atakavyo...



    Mita kama ishirini toka pale mahali alipokuwa amesimama Martin kulikuwa na mtu. Mtu aliyekuwa amevaa nguo zilizokuwa zimepoteza rangi yake halisi. Jamaa hakuwa na viatu miguuni, huku mgongoni akiwa amebeba furushi kubwa jeusi, furushi lenye rangi sawa na nguo zake, rangi sawa na ngozi ya mwili wake.

    Akiwa katika hali ya uchizi nyuma ya Martin lakini jamaa alikuwa anampigia hesabu Martin, akifikiria namna sahihi ya kumvamia na kumfanya alichokuwa anataka kumfanya.



    Martin alikuwa hatulizi macho yake. Dakika hii akiangalia kulia dakika inayofuata anaangalia upande wa kushoto. Akauweka mkono wake usawa wa kifua. Alitumia dakika mbili kuiangalia saa yake ya mkononi. Macho yalimtoka pima!



    "Saa saba na dakika saba!" Martin aliropoka kwa nguvu.



    Harakaharaka alibofya simu yake upande wa meseji zilizoingia. Meseji ya kwanza iliyokuwa inaonekana katika kioo aliifungua.



    "Kama unataka kujua chanzo cha hayo yote nikukute kituo cha mabasi ya Posta saa saba kamili. Usipitilize hata dakika moja...

    @ Biashara ya Kifo"



    Na sasa alikuwa ameshapitiliza dakika saba mbele.



    "Lakini nilifika saa sita na nusu hapa, labda yeye nd'o amepitiliza" Martin alisema kimoyomoyo huku akiushusha mkono wake wenye saa chini.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Yule jamaa mwenye muonekano wa uchizi alitabasamu kidogo. Tabasamu hadhimu litokalo pale anapowazidi watu akili. Huwa anafurahia sana hali hiyo, hali ya yeye kuwa mjanja kuliko wengine. Jamaa alifungua furushi lake la kiuwendawazimu, akatoa matambara mengi machafu, aliendelea kuyatoa huku akiimba wimbo wake usioeleweka. Akatoa matakataka mengi sana, mwishowe akatoa kitabu. Kilikuwa kitabu kipya cheusi, alikigeuza nyuma, alitulia kama dakika mbili kukiangalia, akafunua katikati ya kitabu. Maandishi juu ya jalada yalionwa na macho yasiyoruhusiwa kuyaona maandishi yale.



    Lilikuwa limeandikwa "Biashara ya Kifo!"



    Wakati yule mwendawazimu anafunua katikati ya kitabu ndio wakati uleule Martin aligeuka nyuma kutafuta kitu chochote akichokitafuta. Ndipo alikutana na maandishi yaliyomstua sana. Mwili ulimzizima ulimsisimka, ubaridi wa hofu ulimnasa, midomo ilimtetemeka.

    Martin aligeuka nyuma mzimamzima. Mwili wake ukiwa umeelekea palepale alipokuwa amekaa yule mwendawazimu.

    Akaanza kupiga hatua kumfuata....



    Mwendawazimu alikuwa makini akikiangalia kitabu chake. Palepale alipokuwa alikuwa anamuona Martin akimfata kupitia tobo dogo alilolitoboa katikati ya kitabu.

    Alitabasamu tena.



    Martin aliendelea kusogea eneo alilokuwepo yule jamaa. Alipiga hatua za harakaharaka ili kumuwahi.



    Njiani aligongana na dada mmoja. Begi dogo la dada lilidondoka chini. Kwa kasi Martin aliokota lile begi huku akimuomba msamaha yule dada. Kilikuwa ni kitendo kilichodumu kwa nusu dakika tu. Baada ya kuagana na yule dada Martin aliendelea na safari yake. Kwa mwendawazimu.

    Alipoangalia tena mahali alipokaa mwendawazimu awali.

    Mwendawazimu aliyeshika kitabu cha riwaya ya biashara ya mauti hakuwepo!



    Martin alisimama wima akiwa haamini macho yake. Harakaharaka aliangalia pande zote, ni kweli jamaa hakuwepo.

    Martin hakuamini.



    Muda uleule alihisi kichwa kizito sana. Alijisikia kizunguzungu, aliona umati wa watu Posta ulikuwa unazunguka kwa fujo. Macho yalimuwia mazito sana. Miguu ilimuisha nguvu. Macho yake mwenyewe yalimshinda kuyafumbua, yakawa yanajifunga taratibu.

    Alianguka chini kama mzigo.



    Hatua kama ishirini mbele yule dada aliyegumiana na Martin alikuwa anatabasamu. Aliitupa pembeni sindano yenye sumu aliyofanikiwa kumkwaruza nayo Martin mkononi.



    Mwendawazimu yeye alipita upande wa kushoto huku wakiwa wamepanga kukutana na yule mwanamke maeneo ya Faya ili kupanga vizuri mipango yao. Wote kwa pamoja waliamini yule jamaa hatokuwa hai kwa kuwa walifanikiwa kumchoma na sindano yenye sumu.



    Kumbe haikuwa kama walivyodhani. Martin aliiona ile sindano aliyokuwa kaishika yule dada waliyegumiana. Alijaribu kuikwepa lakini hakuweza, pamoja na jitihada zake za kuikwepa ilimkwaruza kidogo mkononi. Aliagana nae kwa amani kumbe alikuwa na lake moyoni, na alikuwa kashamkariri yule dada. Aliamua kuachana na yule Dada ili kumuwahi mwendawazimu. Bila kutegemea aliwapoteza wote wawili na yeye alirukwa na fahamu...



    *****



    Huko Faya, Peter Kissali na Malkia walikutana. Wote walikuwa na tabasamu tele katika nyuso zao. Walihisi wamefanikiwa kumuua Martin Hisia, na kuufutilia mbali ushahidi kuwa walikuwa wanamiliki biashara ya kifo.



    Martin sasa alikuwa hospitali. Wasamaria wema walimbeba pale Posta na kumpeleka hospitali. Sasa alikuwa hajitambui huku madaktari wakihangaika kuirudisha sawa hali ya Martin.



    *****



    ***Usiku uliopita***



    Martin Hisia alikuwa katika baa ya Tegeta by night akipata vinywaji na makulaji. Alikuwa katika meza ya peke yake, juu ya meza kulikuwa na bia nusu aina ya safari na sahani nyeupe yenye maua mekundu iliyojaa vibanzi na nyama ya kuku wa kisasa. Martin alikuwa anakula huku akiangaza huku na kule. Hakuna alichokuwa anakitafuta ama kukihofia, ilikuwa ni mazoea tu ya kufanya tathmini ya hali ya usalama sehemu yoyote ile anapokuwepo. Baada ya kuridhika aliichukua ile chupa ya bia na kupiga funda refu, wakati bado chupa kaishikilia kwa mkono wake wa kulia, mkono wa kushoto alimuita mhudumu. Mhudumu akaja mbiombio na trei lake mkononi. Kwa kutumia ule mkono wa kushoto alimuonesha vidole viwili, mhudumu alielewa.

    Akaondoka.



    Kabla Mhudumu hajarejea alipata mgeni mpya. Alikuwa mwanamke mrefu mwembamba, alikuwa mweupe mithili ya Chuchu Hans. Alikuwa amevaa gauni refu jeupe, huku mkononi akiwa ameshika begi dogo la mkononi. Alikaa katika kiti sambamba na Martin bila kukaribishwa.

    Martin alibaki amemkodolea macho.



    "Naitwa Sophia" Mwanamke alijitambulisha bila kuulizwa.



    Martin hakujibu, bado alikuwa anamwangalia kwa makini yule mwanamke aliyejitambulisha kwa jina la Sophia.



    "Naitwa Sophia" Alirudia tena.



    "Naitwa Abeid" Martin alidanganya.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Nafahamu umenidanganya jina, lakini hilo sitaki tulijadili kwa sasa. Kilichonifanya nikuvamie katika meza yako ni kutaka kukwambia kwamba hauko salama"



    Martin alikaa vizuri kitini. Pamoja na makelele ya muziki pale baa lakini aliyasikia na kuyaelewa vizuri sana maelezo ya mwanamke aliyejitambulisha kwa jina la Sophia.



    "Siko salama kivipi?" Martin aliuliza kwa taharuki.



    Sophia alitabasamu, alipenda ile hofu aliyoipeleka kwa Martin.



    "Anatabasamu" Ni maneno yaliyopita kichwani mwa Martin.



    "Hauko salama Martin Hisia. Wakina Malolo wako nje ya gereza. Wakina Peter Kissali wako huru mtaani. Na wana kusaka mithili ya almasi, wanamsaka Binunu, wanamsaka Brown..."



    "We ni nani hasa?" Martin aliuliza kwa ukali.



    "Nipe namba yako ya simu nitakupigia. Yatupasa tukutane mahali pengine palipotulia, nikueleze vizuri, kuna mengi wamefanya wale washenzi gerezani"



    "0674 395733..." Martin alitaja namba yake ya simu na Sophia kuiandika katika simu yake.

    Walipeana mikono ya kuagana. Sophia aliufata mlango wa kutokea nje ya Tegeta by night.

    Martin hakutaka kumuacha hivihivi yule mwanamke wa ajabu. Aliamua kumfatilia. Alinyanyuka na kumfata nje. Alisimama katikati ya mlango wa kutokea nje, aliangaza huku na kule.



    Sophia hakuwepo!



    Madaktari walijitahidi kurudisha hali ya Martin sawa. Kitanda alichokuwa kalazwa Martin kilikuwa kimezungukwa na watu wanne makini, wataalam wa afya.



    Kulikuwa na madaktari wawili waliokuwa wamevalia mavazi safi ya kidaktari juu ya mashati yao ya kawaida, chini walikuwa wamevaa suruali za kitambaa nyeusi. Kifaa cha kupimia mapigo ya moyo kikiwa kinaning'inia shingoni. Huku puani wakiwa wameziba puani. Mkononi walikuwa wamevaa 'gloves' safi nyeupe.



    Manesi wao walikuwa wamevaa magauni safi meupe, jasho likiwatiririka kutokana na majukumu yao ya kutumwa mara kwa mara. Kachukua hiki, kapeleke kile.



    Kwa mara nyingine tena daktari mmoja alipima tena mapigo ya moyo ya Martin, bado mapigo ya moyo yalikuwa chini sana. Dripu ya maji ilikuwa inaingia taratibu mwilini mwake huku kifaa cha kumsaidia kupumua kikiwa kimekaa vizuri katika matundu ya pua zake.



    Ama hakika hali ilikuwa tete kwa Martin, kiasi kidogo cha sumu kilichokuwa kimemuingia mwilini kilikuwa kinamuadhibu vya kutosha. Ilikuwa sumu kali sana lakini kwa bahati nzuri haikumuingia kwa kiasi kikubwa sana kama watiaji walivyodhamiria.



    Upande wa pili



    Malolo na Malkia walikuwa katika nyumba ya kulala wageni mitaa ya Magomeni. Walikuwa wamekaa kitandani huku wametandaza karatasi kubwa jeupe juu ya kitanda. Wote walikuwa na kalamu mkononi wakiwa tayari kuichora ile karatasi nyeupe.



    "Tumefanikiwa kumuua Martin, hii ni nzuri sana kwetu, kwakuwa inatuongezea wigo wa kufanya hii kazi iliyopo mbele yetu kwa umakini. Sasa lazima tumtafute Richard popote alipo. Ni zamu ya Richard kufa kisha tuifanye kazi aliyotutuma Don Genge."



    Malolo hakujibu kitu, alichukua kalamu yake na kuandika jina la Martin katika ile karatasi, aliliangalia kwa muda na kuweka alama ya X mbele yake.

    Kisha akaliandika jina la Richard na kuliwekea alama ya kuuliza (?).



    Mara simu ya Malkia iliita, aliipokea baada ya kuliangalia kidogo jina lililopo katika skrini.



    "Nambie Mwendawazimu?" Malkia alisema baada tu ya kuipokea simu.



    "Nimefanikiwa Malkia" Sauti ilisema.



    "Umemuona Richard? Kweli wewe jamaa ni Genius"

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Tena ninaye hapa" sauti ilisema kwa kujiamini. Bila shaka kwa kuridhika na sifa alizopewa.



    "Acha mas'hara Peter?". Malkia alisema kwa nguvu.



    "Nakwambia Rich ninae hapa nipe maelekezo yako nimfanyaje?"



    "Mpeleke kuzimu mara moja" Malkia alisema.

    Simu ikakata.



    Peter alionana na Richard kwa bahati mbaya tu maeneo ya Magomeni. Alimfatilia kwa siri na kufanikiwa kuiona nyumba aliyoingia Richard. Sasa Richard alikuwa ndani, Peter alikuwa nje. Ndipo alipopiga simu kwa Malkia.

    Na sasa ameruhusiwa kumuua.



    Taratibu Peter alielekea getini kwa Richard..



    Alifika hadi getini. Alipiga mahesabu ya harakaharaka ili kujua namna ya kuingia ndani kwa Richard. Hakupata namna sahihi ya kuweza kuingia mle ndani zaidi ya kugonga mlango. Alisogea hadi getini kabisa. Akajipapasa kiunoni, bastola mbili toka kila upande wa kiuno chake zilimpa jeuri.

    Mwanaume akagonga mlango!



    Richard alikuwa yuko sebuleni kwake akiwa katingwa na mawazo. Alikuwa na dili la pesa na Martin siku hiyo, lakini cha kushangaza Martin alikuwa hapatikani kwenye simu yake saa kadhaa sasa.



    Ndipo ilipotimu saa nane mchana aliamua kumfata Martin nyumbani kwake. Nako hakumkuta. Aliamua kurejea nyumbani kwake, njiani ndipo alipoonwa na Peter Kissali na kuanza kufuatwa. Kutokana na wingi wa mawazo Richard hakuwa makini kabisa kuweza kutambua kama alikuwa anafuatwa. Alifatana na mwindaji hatari hadi nyumbani kwake.



    "Ngo ngo ngo.." Mlango wa geti la Richard ulikuwa unagongwa. Richard alisikia mlio wa mlango akiwa kajituliza sofani.



    "Martin! " Aliropoka kwa nguvu.

    Alinyanyuka sofani na kuelekea nje kwenda kufungua geti, huku moyoni mwake akijua Martin ndo mgongaji.

    Laiti angejua....



    Bila kufikiria mara mbili Richard alifungua kimlango kidogo cha geti ili Martin aweze kuingia.

    Lilikuwa kosa!

    Mguu wa kulia wa mwanaume ulikita kwa nguvu katika kifua chake. Richard hakuwa amejiandaa kabisa na shambulio hilo, lilikuwa shambulio la kustukiza kama ziara za Magufuli. Richard aliyumba kwa nguvu na kwenda kujigonga katika kibanda kidogo kilichojengwa maalum kwa ajili ya mlinzi. Peter hakutaka kumpa nafasi ya kujipanga Richard, alirusha ngumi tatu za harakaharaka na zote zilitua bara'bara katika kifua cha Richard. Pumzi zilimbana, alijaribu kukooa, damu ziliambatana na mate pamoja na makohozi. Peter alirusha teke la nguvu lililotua vizuri tumboni kwa Richard. Akamsogelea kwa kasi na kumkaba shingoni, Richard alijaribu kuitoa mikono ya Peter, lilikuwa kosa lengine. Kichwa cha Peter kilitua katika mdomo wa Richard. Alimchana vibaya sana. Richard alilia kama mtoto mdogo.



    Ulikuwa uvamizi wa ghafla ambao Richard hakujua sababu yake. Hakuwa katika misheni kwa wakati huo, kwahiyo hakuwa na wasiwasi wowote katika mienendo yake. Adui zake wa mwisho walikuwa wale aliopambana nao katika operesheni ya Mkanda wa Siri. Aliamini kwamba hakuwa na maadui kwa sasa kwakuwa maadui wote aliopambana katika ile operesheni walikuwa wamefungwa kifungo cha maisha.



    Adui watoke wapi? Wakati ndio kwanza alikuwa katika maandalizi ya operesheni mpya na Martin Hisia.

    Pamoja na yote hayo lakini ilimpasa kupambana. Maana mbele yake kulikuwa na mtu aliyekuwa amedhamiria kumuua.



    Bado Peter alikuwa amemkaba shingoni Richard huku akimbamiza kwa nguvu ukutani. Maumivu akiyoyapata Richard yalikuwa hayana mfano, alijitahidi kujitutumua ili kutoka katika mikono ya yule jamaa mvamizi lakini wapi, jamaa alikuwa na nguvu pasi na kifani.

    Peter hakutaka kufanya kosa lolote lile, alinyanyua mguu wake wa kulia kimo cha mbuzi, na kuurudisha chini kwa nguvu, alifanikiwa, alimkanyaga Richard vibaya sana mguuni. Yowe la uchungu lililoambatana na damu lilimtoka.



    "Nakuua..!" Peter alisema kwa ghadhabu.



    Alirusha kichwa kingine cha nguvu kama kile cha awali.

    Safari hii, Richard alikiona.

    Kwa kasi ya haraka alikikwepa kwa kuelekeza kichwa chake upande wa kulia. Kichwa cha Peter kilikutana ana kwa ana na ukuta wenye vinundu.

    Alilia kwa fadhaa.

    Richard aliona ile ndio nafasi pekee ya kulitumia kosa la mvamizi wake. Alirusha ngumi kwa mkono wa kulia, ngumi iliyotua vizuri sana katika mbavu za Peter. Peter alipiga magoti bila kutaka akiwa kazishikilia mbavu zake kwa mikono. Alivyonyanyuka alikuwa ameshika kitu kingine mkononi.



    Bastola!



    Richard akaona mambo sasa yamekuwa magumu. Alinyoosha mikono yake juu kwa tahadhari kubwa sana.



    Jamaa alimuelekezea bastola katikati ya paji la uso wake. Richard alikuwa anatafuta namna ya kujiokoa. Lakini alichelewa.

    Risasi toka katika bastola ya Peter ilitua katika paji la uso la Richard! Huku mikono yake ikiwa juu alidondoka kinyumenyume na kisogo chake kikitangulia kufika ardhini.

    Alikuwa amekufa!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Peter alitoa simu yake mkononi na kumpigia Malkia. Alipewa maagizo ya kuikagua nyumba ya Richard kuona kama kuna lolote watakalolipata.

    Kwa mwendo wa tahadhari, bastola ikiwa kaitanguliza mbele aliingia katika nyumba ya Richard.



    *****



    Huko hospitali hali ya Martin Hisia bado ilikuwa si nzuri. Ingawa sasa alikuwa anapumua bila mashine lakini bado fahamu zake zilikuwa hazijarejea.

    Martin Hisia alikuwa hana fahamu wakati rafiki yake kipenzi akiuwawa nyumbani kwake. Mzimu mbaya waliofurahi kuushinda katika operesheni ngumu kabisa ya Mkanda wa Siri sasa ulikuwa umerejea. Tena umerejea kwa nguvu zote na ukiwa na hamu ya kulipa kisasi.



    Chanzo Cha Haya Yote.



    Martin Hisia, Brown, Binunu na Richard waliingia katika vita ya akili kupambana na wakina Malolo, Malkia na Peter ili kuupata Mkanda wa siri miaka mitatu iliyopita. Ni Mkanda uliokuwa na siri za mahali ambapo kulikuwa na madini pamoja na kiwanda cha madawa ya kulevya cha Chifu. Mwishowe kwa kushirikiana na wanajeshi wakina Martin walifanikiwa kuirudisha mali ya Serikali mikononi mwa Serikali. Na kusababisha wakina Malkia kufungwa kifungo cha maisha jela....



    Maisha ya gerezani hayakuwa magumu sana kwa kina Malkia. Wote walikuwa ni watu waliozoea shurba na mateso. Maisha ya jela kwao yalikuwa laini sana zaidi ya maisha magumu waliyopitia. Wakina Malolo walikuwa watemi siku ya kwanza tu kuingia gerezani kwa upande wa wanaume. Malkia alikuwa moto siku ya kwanza tu kuingia katika gereza upande wa wanawake.

    Hakuna aliyewatisha. Walikuwa wanatumikia kifungo cha maisha lakini wote waliamini ipo siku isiyo na jina watatoka kwa njia yoyote ile. Waliamua kutulia gerezani ili kuweka mipango yao sawa...



    Mbozi, jijini Mbeya.



    Mbozi ni miongoni mwa mji maarufu katika mkoa wa Mbeya. Pamoja na mambo mengi mazuri, lakini Mbozi ilikuwa inavuma sana kwa tabia ya uchunaji ngozi za binadamu.



    Ngozi za binadamu zilikuwa dili bila ya kujulikana ngozi hizo zinatumika kwa kazi gani. Amani ilitoweka Mbozi kutokana na biashara hiyo haramu, biashara ambayo kwa kiasi kikubwa ilihusishwa na imani za kishirikina.



    Ni mwaka sasa tangu mtu aitwaye Don Genge awasili katika mji wa Mbozi.

    Don Genge alikuwa ni jambazi sugu aliyevuma sana miaka mitatu iliyopita. Don Genge alipeleka kizazaa kikubwa sana Kilwa miaka hiyo na kutokomea kusikojulika.



    Don Genge kwa kushirikiana na mtandao wa wahalifu wa kimataifa walikuwa na mkataba wa kupeleka mioyo ya binadamu. Mioyo ambayo ilikuwa inatumika kutengenezea sumu ghali na hatari zaidi duniani. Sumu ya proxine. Biashara hiyo haramu ya mioyo ilimfanya Don awe wakala wa kupeleka mioyo. Huku mkurugenzi wa biashara hiyo nchini akiwa ni mtu aliyejulikana kwa jina la Kifo.



    Siku Ile Ilikuwa Hivi.



    Baada ya kambi ya kundi hatari la Six killers kuvamiwa na askari, wakiongozwa na mpelelezi mahiri nchini Tanzania, Daniel Mwaseba. Don Genge aliruka soti kinyumenyume na kuingia ndani ya nyumba yao. Alipofika ndani alisimama wima na kugeuka kwa haraka. Akili yake ilifanya kazi harakaharaka. Akili ilimwambia aende chumba cha tatu upande wa kushoto. Alikimbia mbio na kuingia chumbani. Huko ndani alikuwa anatazamana na kitanda kidogo na kabati la chuma lililowekwa ukutani. Kwa haraka alilifungua kabati na kujitosa ndani yake.



    Lile kabati la chuma kwa nje lilionekana ni kabati la kawaida. Lakini ukweli lile halikuwa kabati. Lilikuwa ni zaidi ya kabati. Kabati la kazi.



    Don alivyoingia mle ndani alivuta kamba ndogo ya bluu iliyekuwepo juu ya kabati lile. Kwa ndani kabati lilifunguka tena. Alijitosa ndani mzimamzima.



    Lile kabati lilikuwa njia. Njia ya siri kuweza kumtoa nje ya nyumba ile iwapo mambo yatakuwa magumu. Kama hali ilivyo sasa. Ulikuwa ni mlango ambao Don Genge pekee ndio alikuwa anaufaham. Alipofika kwa ndani alivuta kikamba kingine cha rangi nyeusi kwa juu, ambacho kiliruhusu kabati kujifunga.

    Kule kwa ndani alikutana na njia ndefu iliyokuwa inamtoa katika nyumba ile ambayo ilikuwa imevamiwa na mpelelezi mahiri Daniel Mwaseba na wenzake.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wakati wakina Daniel Mwaseba wakiingia ndani ya nyumba ile kupekua, Don Genge alikuwa anafungua mfuniko wa chuma ili kuweza kutoka shimoni. Hiyo ilikuwa karibu na pwani ya Jimbiza.



    Alivyotoka shimoni. Alichukua simu yake na kumpigia Kifo. Alimueleza kila kitu jinsi mambo yalivyoharibika. Saa moja baadae alikuwa juu ya ndege binafsi akielekea jijini Dar es salaam. Huku akiwaacha washirika wake toka kundi la Six killers wakiwa chini ya mikono ya dola.



    Don alijichimbia miezi tisa mifichoni ili mambo aliyoyasababisha yapoe. Alikuwa anapata kila kitu katika moja la jumba la kifahari lililokuwa linamilikiwa na Kifo. Na katika kipindi hiko chote ambacho Don alikuwa mafichoni, Tanzania ilikuwa salama.

    Mpaka hivi juzi tu ndipo lilipotokea tukio la hatari baada ya mtu mmoja kuchunwa ngozi huko Mbozi.



    Ilikuwa ni muendelezo wa mipango haramu ya Don Genge kwa kushirikiana na Kifo kupata pesa. Walikuwa tayari kufanya lolote lile ili kuweza kupata pesa. Kuua kwao lilikuwa jambo dogo sana. Kuua kikatili ilikuwa ni burudani nzuri sana kwao.



    Katika kufanya hayo, Don Genge alihitaji washirika. Sasa hakuhitaji huduma ya Six killers ambao walionesha udhaifu mkubwa sana katika misheni ya awali. Katika utafiti wake ndipo alisikia habari kuhusu Malkia na genge lake na vurugu lao katika Mkanda wa siri. Aliridhika na uwezo wao wa nguvu na akili. Don Genge alitafuta namna ya kuwatoa wakina Malkia gerezani ili aje kushirikiana nao katika biashara ya kifo..





    Haikuwa kazi rahisi hata kidogo. Maana kabla ya kuwatoa wakina Malkia ilimpasa kumtafuta mtu wa kuweza kuongea nao ili kuona kama wako tayari kushirikiana na Don Genge uraiani.



    Huyo mtu ilimpasa kwenda gerezani ili kuweza kuongea nao wakina Malkia.

    Waelewane, kisha wawatoe.



    Baada ya kuwaza na kuwazua, kichwani kwa Don Genge lilikuja jina moja tu, Devil.

    Devil alikuwa kijana hatari sana katika misheni za kijasusi.



    Baada ya kuongea na Devil, wiki tatu baadae wakina Malkia walikuwa nje ya gereza. Devil alitumia pesa, akili na bastola ili kufanikisha wakina Malkia wawe nje ya gereza.



    Devil alitumia pesa zaidi ya milioni ishirini. Alitumia akili kuwashawishi wakina Malkia wakubaliane nao na mpango wao haramu.



    Devil Ilimpasa kufanya kosa ili afungwe kuwa karibu na wakina Malkia. Aliwaambia wakamuelewa.

    Risasi toka bastola ya Devil ziliua askari wapatao kumi na sita, na kuacha taharuki kubwa sana gerezani. Wakina Malkia na Devil walitoka nje ya gereza usiku wa manane, huku Devil akiwa ameahidiwa milioni hamsini.

    Lakini hakuzipata!



    Don Genge hakuona sababu ya kutoa hela zake bure ilhali watu akiowahitaji walikuwa mbele yake. Pia alijua kumpa hela Devil na kumuacha hai ni kufanya siri zao kuwa sio siri tena. Alimuua Devil kwa siri na kumfukia nyuma ya nyumba yake. Hakuuona umuhimu tena wa kuwa na Devil. Na safari hii alikuwa makini kuliko wakati wowote ule. Hakutaka kuruhusu kufanya kosa lolote, ndio maana aliamua kuwachukua watu makini.



    Kazi ya kwanza ya kuchuna ngozi ya mtu Don Genge alifanya kwa mkono wake. Hiyo ili kuondoa dhana kwa wakina Malkia labda yeye haiwezi kazi. Na leo hii Don Genge alikuwa mbele ya wakina Malkia akiwapa kazi ya kufanya.



    Don Genge alikuwa mbele ya meza. Alikuwa anatazamana na watu watatu. Malkia akiwa katikati, upande wa kushoto wa Malkia alikuwa amekaa Malolo, na upande wa kulia kwake kulikuwa na Peter Mwendawazimu. Wote macho yao yalikuwa kwa Don Genge. Walikuwa kimya wakimsikiliza bosi wao mpya.



    "Naitwa Don, Don Genge. Nitakuwa mkuu wenu katika misheni hii. Najua kijana Devil ameshawaambia nini tunakusudia kufanya toka mpo gerezani.

    Lakini kwa kifupi, tunahitajika kuwa makini sana katika misheni hii, kutokuwa makini ni kuikaribisha hatari". Don Genge alinyamaza, aliwaangalia wale washirika wote, wote walionesha umakini mkubwa kumsikiliza.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Aliendelea " Malkia. Nimesikia sifa zako nyingi katika medani, sifa zake katika operesheni mbalimbali. Uwezo wako huo katika sifa nilizozisikia ndizo zimekufanya uwe huru leo. Kwa ajili ya kuja kupambana. Kufanya kazi. Kufanya biashara. Biashara ya kifo. Nakuamini sana Malkia usiniangushe" Don Genge alisema kwa nguvu macho yakiwa kwa Malkia.



    Sasa sura yake aliigeuzia kwa Peter



    "Peter Kissali Mwendawazimu, najua wewe ni kichwa sana. Uko vizuri sana katika kupanga mambo, uko vizuri katika kuitumia akili yako. Wewe ni genius, na mipango kama hii inahitaji mageneniuos kama wewe. Kwa kutumia akili zako naomba tuifanye hii misheni na kuikamilisha"



    Sasa alimwangalia Malolo huku akiongea " Malolo, naujua uwezo wako katika mapambano. Najua na hii biashara itahitajika mapambano. Mapambano ya nguvu. Najua mauaji niliyoyafanya juzi yatawasogeza wambea kadhaa hapa, akiwemo Daniel Mwaseba. Malolo upo huru mahsusi kwa ajili ya kuitoa roho ya Daniel Mwaseba. Na naamini utafanikisha hilo"



    "Bila shaka mkuu" Malolo alijibu kwa kujiamini.



    Don Genge aliongea " Safi sana Malolo. Sasa tufanye hii kazi jamani. Ni kazi ya mwaka mmoja tu ambayo na uhakika tukiimaliza itawaacha wote kuwa mabilionea. Hamtakuwa na haja ya kusaka pesa tena katika maisha yenu, mtakuwa na pesa za kutumia hadi mnakufa"



    Wote watatu walitabasamu. Wote walikuwa wapenda pesa, na walikuwa wametajiwa pesa za kutosha. Iliwalazimu kutabasamu.



    "Kuna yeyote mwenye maoni, swali, dukuduku, ama ushauri? Wakati ni huu" Don Genge aliuliza huku akihangaika kuitoa sigara yake mfukoni.



    Mimi nina swali dogo tu, lakini muhimu katika operesheni yoyote ile, je kuna zana za kutosha kuifanya hii kazi?" Malkia aliuliza huku akimwangalia Don Genge.



    "Tuna zana za kutosha. Tuna kila kila kitu kinachoweza kutufanya tufanye hii kazi kwa asilimia mia moja. Tuna silaha nyingi, tena za kisasa. Tuna Proxine za kutosha, ambazo tone moja tu huruhusu ngozi kuvuka mwilini mithili ya kanzu. Tuna magari mengi ya kutupeleka hapa na pale, ndege binafsi. Tuna rasilimali watu makini ambao ni nyinyi. Hatuwezi kujitetea kwa kushindwa hii kazi eti kutokana na kutokuwa na zana" Don Genge alielezea kwa kirefu.



    Wote waliitikia kwa kichwa.



    "Swali lengine?" Don Genge aliwauliza tena.



    "Mimi nina ushauri. Yatupasa kuongeza watu ili kuweza kuifanya hii kazi kwa haraka na ufanisi. Ngozi elfu kumi zinazohitajika ni nyingi sana. Kwa wastani yatupasa tuue watu ishirini na saba kwa siku. Ni watu wengi sana hao. Maana hapo kwa sisi watatu kila mmoja yampasa kuua watu tisa kwa siku. Its not easy task Don. Nashauri tuongeze watu" Peter alieleza.



    "Kuongeza watu sio tatizo, tatizo ni kuwapata watu wanaojua kufanya kazi hii kwa ufanisi mkubwa kama nyinyi. Kama mnao hao watu, nipeni sifa zao nione kama tunaweza kuwajumuisha katika operesheni hii. Ila ni lazima wajue namna ya kutunza siri na kufanya kazi bara'bara " Don Genge alijibu.



    Wote watatu waliangaliana usoni. Walikaa kimya, ishara kwamba hawakuwa na mtu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    TWENDENI TU...TUUSOME HUU MCHEZO..



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog