Simulizi : Biashara Ya Kifo
Sehemu Ya Tano (5)
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Walisuguana kwa nguvu. Wote walidondoka chini, wakiwa katika mtindo uleule.
Kwa mara nyingine tena Malkia ndiye aliyeamua cha kufanya. Alimbana meno Inspekta Jasmine mguuni, katika ugoko. Inspekta Jasmine alipiga kelele za ghadhabu, naye alipata cha kufanya, alifanya kitendo kilekile kilichofanywa na Malkia, naye alitumia meno yake kujitetea. Kutokana na maumivu ya meno walijikuta wameachiana. Wote wakiwa wanagalagala chini kwa maumivu.
Ni Inspekta Jasmine ndiye aliyeanza kuamka, alienda kwa mwendo wa taratibu pale alipokuwa amelala Malkia. Alimkuta Malkia naye akiwa katika harakati za kuamka, teke moja tu la nguvu mbavuni lilimlaza tena Malkia. Inspekta Jasmine aliona ile ndio nafasi pekee ya kuumaliza mchezo. Aliruka juu kwa miguu yake yote miwili alikuwa kaielekeza katika kifua cha Malkia. Kilikuwa ni kitendo cha haraka, kufumba na kufumbua, lakini cha ajabu haikuifikia haraka ya Malkia, yule mwanamke hatari alijiviringisha kwa haraka na kuruhusu miguu ya Inspekta Jasmine kuukanyaga ardhi kwa nguvu. Inspekta aliumia miguu lakini alivumilia, harakaharaka alibadili maamuzi, alimpiga teke la mbavu, safari hii lilimpata lakini likiacha mguu wake ukiwa umenaswa na mikono ya Malkia.
Kilikuwa kimbembe!
Malkia aliuvuta kwa nguvu ule mguu, Inspekta Jasmine hakuweza kujizuia, alidondoka chini mzimamzima, sasa wote wawili walikuwa wamelala chini. Malkia alijisogeza pale alipolala Inspekta Jasmine, yeye alikuwa juu, Inspekta Jasmine alikuwa chini, akakamwida shingoni kwa nguvu, Inspekta jasmine nae alipeleka mikono yake pale shingoni ili kupunguza ile kasi ya roba ya Malkia. Kwa mara nyingine tena walipata nafasi ya kuangaliana, wote jasho likiwatoka, damu za puani za inspekta Jasmine ziliendelea kutoka. Waliangaliana sekunde moja sekunde iliyofuata Malkia alipiga kichwa takatifu katikati ya utosi wa Inspekta Jasmine. Kichwa kilimpata vizuri sana Inspekta jasmine, na kwa haraka katika utosi wa inspekta Jasmine lilitokea nundu.
Malkia alirudia tena kitendo kilekile.
Kipindi hicho kichwa cha Inspekta Jasmine kilikuwa kinawaka moto. Maumivu makali aliyapata, na alimuona Malkia akirudia tena kitendo kile. Alikuwa anajiandaa kumpiga tena sehemu ileile, ambapo kulikuwa na uvimbe kwa sasa. Inspekta Jasmine hakuwa tayari kuruhusu kupigwa tena sehemu ileile. Alikwepesha kidogo kichwa chake, lakini hakuweza kuzuia lisimpate hata kidogo pigo lile. Lilimkwaruza kidogo pembeni ya kichwa chake. Waliachiana, wote walikuwa wamechoka. Wote walikuwa wamelala chini, wako hoi bin taaban. Ni Malkia ndiye aliyeanza kuufunua mdomo wake.
"Nani kamuua Peter?" Sauti ilitoka kwa mbali lakini ilifika katika sikio la Jasmine.
Jasmine hakujibu, lakini kichwani kwake alikuwa na mshangao mkuu, yeye aliamini Malkia ndiye itakuwa kamuua Peter, bila shaka katika kuupoteza ushahidi. Sasa Malkia alikuwa anamuuliza kuhusu aliyemuua Peter? Bila shaka kutakuwa na mtu wa tatu anahusika katika mkasa huu, ni nani sasa?
"Nani kamuua Peter?" Malkia aliuliza tena.
Jasmine hakujibu.
Malkia alikuwa haamini kwamba Jasmine ndiye atakuwa kamuua Peter, Peter alikuwa sio mtu wa mchezo, Peter alikuwa ni moto wa kuotea mbali. Aliyemuua Peter bila shaka alikuwa mtu wa hatari sana, ni nani sasa?
Malkia aliona pale sio mahali salama, bila shaka kuna kiumbe kingine cha hatari ukiondoa Jasmine. Ndipo alipowaza kukimbia, lakini alipomfikiria Malolo alisita, alipoyafikiria maisha yake, Malkia alitoka mkukuu akimwacha Inspekta Jasmine katika mshangao mkuu...
Nusu saa baadae gari ya Polisi ilikuwa katika nyumba ya Inspekta Jasmine. Walimchukua Inspekta Jasmine aliyekuwa hoi na kumpeleka hospitali, na Malolo naye alipelekwa hospitali. Huku askari wengine watatu wakiwa wamebaki pale katika nyumba ya Inspekta Jasmine wakiilinda, wakijaribu kuitafuta pia maiti ya Peter Kissali. Zaidi ya saa tatu walifanya kazi hiyo lakini hakuna cha maana walichokipata, zaidi ya damu walizozikuta pale nje hakuna kingine chochote walichokipata, lakini bado waliendelea kukaa palepale kuilinda nyumba.
Inspekta Jasmine alikuwa bado kapigwa na butwaa akiwa juu ya kitanda cha hospitali, ingawa aliufurahia ujio wa askari lakini kulikuwa na mambo mawili yaliyomshangaza sana.
Kwanza ni nani aliyewataarifu Polisi juu ya mambo yale, yeye hakuwapigia simu polisi na hata wale aliokuwa nao alikuwa na uhakika hawajapiga simu Polisi.
Pili kwanini wale polisi walichelewa kufika mahali pale, alihisi bora hata wangewahi kufika ili wamkamate na Malkia.
Mambo hayo yalizidi kumchanganya Inspekta Jasmine akiwa juu ya kitanda cha hospitali. Alikuwa amebandikwa plasta kadhaa usoni kutokana na majeraha aliyoyapata, kila alipoyafikiria mambo yale hayakuelewa, na maiti ya Peter ilienda wapi? Hapo ndipo kulipokuwa na utata mkuu...
Malkia alikuwa njiani kuelekea katika kambi yao, njiani alikuwa na kitete haswa, moyo ulikuwa unamfukuta vibaya sana, mwili mzima ulikuwa unamuuma, alikuwa anatembea njiani huku akitetemeka, akiterereka.
Bila kujua nyuma yake kulikuwa na watu wawili, waliokuwa wanakanyaga kila mahali alipokuwa ananyanyua mguu wake. Walikuwa wanamfatilia kwa umakini mkubwa, nia yao kuona uelekeo wa Malkia ili wakaumalize mchezo, wakaimalize biashara ya kifo .
Ilikuwa Malkia akikata kona, nao wanakata kona, Malkia akisimama nao wanasimama. Malkia akigeuka nyuma wao wanajibanza. Walikuwa wanamfatilia Malkia kwa umakini mkubwa sana, nia yao kuu ilikuwa Malkia asistukie kabisa kama anafuatwa.
Hawakufanikiwa.
Ingekuwa wanamfatilia mtu mwengine tofauti na Malkia asingejua, lakini sio kwa Malkia, mwanamke imara, mwanamke mwerevu katika misheni, mwanamke mjanja sana. Haikuwa mara yake ya kwanza kufatiliwa, haikuwa mara yake ya kwanza kugundua kama alikuwa anafatiliwa.
Malkia alitambua kama anafuatwa pindi tu watu wale wawili walipoanza kumfatilia, Amini, usiamini ...Malkia aliwaona watu wale wakati wakiuhamisha mwili wa Peter Kissali pale mlangoni, na aliuona uelekeo wao pia, na aliwaona wakati wanarejea, na hiyo ndio sababu ya kukimbia ndani ya himaya ya Inspekta Jasmine, hakumkimbia Inspekta Jasmine katu, alikuwa na uwezo wa kupambana nae na kumshinda, aliwakimbia watu wale wawili aliokuwa anawatambua vizuri umahiri wao, alipaswa kuwakimbia. Lakini sasa walikuwa wanamfatilia...
Mwanzoni alipanga kuelekea nyumbani kwao, kwenye kambi yao ambao wenyewe walizoea kuiita getho. Lakini pindi alipogundua tu kwamba anafuatwa aligairi, sasa alikuwa anaelekea sokoni Mbozi badala ya getho kwake. Alipanga kwenda kuwapoteza wale majamaa wakiomfuatilia sokoni Mbozi.
Kama alidhani atawapoteza kiurahisi basi alikosea sana. Jamaa walikuwa wafatiliaji waliofudhu katika fani hiyo, fani ya ufatiliaji, na mbaya zaidi na wao waligundua kwamba Malkia aligundua kama wanamfatilia, ilikuwa akikata kulia basi na jamaa mmoja anaenda kulia na mwengine anaenda kushoto...ilikuwa ni ngumu sana kwa Malkia kuwapoteza watu wale...
Ilikuwa imepita siku tatu tangu mambo yale yapite. Malkia sasa alikuwa katika nyumba mmoja ya kifahari jijini Mbeya. Siku ya tatu alikuwa hajaliona jua, alikuwa amefungiwa katika chumba kimoja kilichokuwepo katika mtaa wa Forest.
Mbio zake za sakafuni ziliishia ukingoni, alikamatwa kwa urahisi sana na wale majamaa wawili, alikamatwa mithili ya kuku mwenye homa, hakuweza kabisa kuwakimbia watu wale wawili..
Siku ileile walimsafirisha Malkia hadi Mbeya mjini. Pamoja na kuwa na Malkia kwa siku ya tatu sasa lakini majamaa hawakukipata walichokuwa wanakitaka, hawakumbulia chochote kile, Malkia hakusema lolote lile kwa siku tatu sasa, hakutamka neno lolote, hakusema hata jina lake, alikuwa anawaangalia tu wale majamaa wawili mithili ya midoli.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Msichana nina imani bado unapenda kuishi, bado unapenda kuivuta hewa ya duniani bure.... Lakini pengine hayo nayasema mimi, pengine unatamani kufa, sasahivi ndo utatuthibitishia nadharia ipi kati ya hizo mbili ni sahihi kwako.."
"Mbona unaongea sana Mwanashera mlevi, huu sio muda wa kumsomea risala ndefu huyo mwanaharam wa kike, huu ni muda wa kumfanya atapike kila kitu, auseme ukweli.."
"Unajua Daniel Mwaseba wakati mwengine ni vyema kuwapa nafasi ya kuchagua wahalifu kabla hatujawaua, lazima wachague wenyewe kufa ama kuishi?" Mwanasheria mlevi alisema kwa sauti yake ya kilevi.
Malkia alikuwa anawaangalia tu wale watu wawili wakati wakijadiliana. Hakutishika hata kidogo na maneno yao, pamoja na kuwa na shauku ya kutaka kuwajibu kwa dharau lakini aliamua kunyamaza tu, huku moyoni mwake akicheka kicheko cha dharau...
Daniel na Mwanasheria walikuwa wanayaona yote yaliyokuwa yanapita kichwani kwa Malkia, wote walikuwa wasomi waliofudhu vyema katika taaluma ya saikolojia juu ya uhalifu, hivyo haikuwa ngumu kwao kutambua alichokuwa anawaza Malkia kwa muda ule. Walikisikia kile kicheko cha siri cha dharau toka kwa Malkia...
"Tumekulea kwa siku tatu, sasa leo utasema utake usitake!" Mwanasheria mlevi alipiga mkwara wa nguvu.
Muda uleule, wote walitoka nje wakimuacha Malkia mle chumbani peke yake.
Walimfungia mlango kwa nje.
Malkia alibaki ndani ya chumba kile peke yake, huku akijua kwamba pindi watakaporejea wakina Daniel Mwaseba patakuwa hapatoshi mle ndani.
Kwa mara nyingine tena alitafuta namna ya kutoka mle chumbani, kutoka ndani ya lile jumba lililokuwa kama kaburi kwake...
Malkia alinyanyuka toka pale alipokuwa amekaa, alielekea mlangoni, alishika kitasa cha mlango, mlango ulikuwa umefungwa!
Alikizunguka kile chumba pande zote nne, hakukuwa na nafasi hata ndogo ya kupenya, jamaa walimuweka katika chumba makini, chumba anachostahili kufungwa mtu mjanja kama yeye. Taratibu alirudi tena katika kitanda chake, alikaa kitako huku akiwaza.
'Tumejiingiza wenyewe katika mkono wa Polisi, ule mtego wetu wa kumuingiza Inspekta Jasmine katika himaya ya Malolo umefeli kizembe sana.
Alikumbuka vizuri sana kwamba ni yeye ndiye aliyeshauri mtu mmoja aende kuanzisha uhusiano wa kimapenzi na askari mpya aliyeletwa kupeleleza mauaji waliyokuwa wanayafanya wao. Jana yake waliambiwa na mkuu wao Don Genge juu ya ujio wa askari huyo wa kike. Don Genge alishauri wamuue mara moja pindi tu atakapowasili, wamuue kama walivyomuua Koplo John. Lakini Malkia alipinga wazo la bosi wake, yeye alishauri wamuweke karibu huyo askari ili kutambua mipango yote ya polisi. Don Genge alikubali mara moja huku akimsifu sana Malkia kwa wazo lake.
Laiti angejua?
Malolo naye aliliunga mkono wazo hilo, ni Peter pekee ndiye aliyelipinga wazo hilo. Lakini Peter hakusema mbele ya Don Genge lakini alikuja kuwaambia wenzake baadae kwamba wanacheza pata potea.
"Hawawezi kumleta askari lelemama, lazima wamlete askari imara, kumfatilia askari imara ni hatari sana. Bora akitua hapa mjini tu tumuue!" Malkia aliikumbuka sauti ya Peter, ambaye kwa sasa alikuwa marehemu.
"Inamaana Peter leo humuamini Malolo? Askari gani imara nchi hii anayeweza kumuua Malolo? Umemsahau Malolo? Hiyo ndio njia sahihi Peter, kuwa karibu na wale ni kuijua mipango yao yote, unaijua nguvu ya mapenzi Peter? Hiyo ndiyo itakayotusaidia katika misheni hii. Hakuna askari imara katika mapenzi, awe mwanamke au mwanaume.."
Pamoja na kukubali, lakini dhamira ndani ya moyo wake ilimsuta Peter. Hakutaka kuamini hata kidogo kwamba ile njia waliyokuwa wanaitumia ilikuwa sahihi. Hakuwa tayari hata kidogo mmoja wao kuanzisha uhusiano na askari Polisi.
Alichukua uamuzi.
Siku ya kwanza tu Malolo kuingia uhusiano na Jasmine, Peter aliamua kuufatilia uhusiano wa Malolo na Jasmine kimyakimya.
Upande wa Malkia nae alipunguza kumuamini Peter baada ya kubishia sana mipango yao, naye alianza kufatilia mienendo ya Peter kimyakimya.
Kundi hili hatari likaingia katika hali mbaya sana, hali ya kutoaminiana, hali ya kufatiliana, hali ya uwoga na wasiwasi kwa kila mmoja. Hiko ndio kilikuwa chanzo kikuu cha Inspekta Jasmine kugundua hila za watu wale siku tatu tu za mahusiano yake na Malolo.
Siku moja walikuwa wanatoka mjini na Malolo. Yeye ndiye alikuwa akiendesha gari. Hakushindwa kugundua kwamba walikuwa wanafuatwa baada ya gari yao kuingia tu barabarani.
Dakika sita baadae aligundua kitu kipya, kwamba aliyekuwa anawafuata nae alikuwa anafuatwa. Inspekta Jasmine alikuwa makini katika usukani, huku mwili ukimsisimka kama umsisimkavyo siku zote anazoingia katika hali ya hatari. Alimuangalia Malolo kwa jicho la wizi, alikuwa anasinzia. Aliamua kuucheza mchezo pekee yake bila kumshirikisha Malolo.
Aliongeza kasi ya gari yake, gari lilikimbia haswa, mshale ulisoma katika 180. Na gari za nyuma nazo zilizokuwa zinawafatilia nazo ziliongeza mwendo. Na hivyo ndivyo alivyotaka.
Baada ya kama dakika kumi za mwendo mkali, alipunguza mwendo ghafla. Zile gari hazikujiandaa kwa jambo hilo. Ziliipita gari ya Inspekta Jasmine kwa kasi. Hakuziona sura za madereva wale, ila aliliona koti alilolivaa dereva wa gari la katikati. Lilikuwa sawa na koti alilomnunulia Malolo jana yake. Hapo ndipo hisia kwamba Malolo sio mtu mzuri zilipokinasa kichwa chake.
Aliamini kwamba Malolo alikuwa anamsaliti.
Tangu kutokea kwa tukio lile Inspekta Jasmine alikuwa makini sana na nyendo za Malolo. Hisia zake zilimwambia Malolo si mtu nzuri kwake. Lakini hakutaka kumtumia mapema aliamua kumtumia Malolo ili amfikishe katika mikono ya wauaji.
Malolo na Jasmine, walikuwa wapenzi, walifanya kila kitu wanachofanya mtu na mpenzi wake, bila kujua kwamba walikuwa na dhamira tofauti ndani ya mapenzi yao.
Kama Inspekta Jasmine alidhani Malolo alikuwa amesinzia siku ile ndani ya gari basi alikuwa anajidanganya. Na kama alidhani Malolo hajaona juu ya magari yale mawili yalikuwa yanawafatilia basi alikuwa anajidanganya kabisa. Malolo aliona kila kitu. Alikuwa anaangalia kwa macho yake yote yaliyokuwa yanaendelea, na alijifanya kusinzia pale alipoangaliwa na Inspekta Jasmine tu. Na alikuwa katika mshangao mkuu kichwani mwake kutokana na watu waliokuwa wanamfatilia, alikuwa anawajua vyema. Walikuwa ni washirika wake, wenzie, marafiki zake, sasa kwanini wamfatilie?
Malkia gari yake ilikuwa ya tatu katika msafara ule. Pamoja na akili yake kumakinika na mambo waliyokuwa wanayafatilia lakini hakushindwa kutambua kwamba kulikuwa na gari nyuma yao inawafuata. Ulikuwa msafara wa watu wanne ambao ilikuwa ni ngumu sana kwa jicho la kawaida kujua kwamba wanafatiliana.
Hawa wote hawakuwa watu wa kawaida!
Lakini mchezo alioucheza Inspekta Jasmine ndio uliharibu kila kitu, mfuatano ukaharibika...
Malkia alirudi nyumbani kwake na maswali chungumzima. Alikuwa ameyajua magari mawili ya mbele, ila alikuwa na maswali lukuki juu ya gari la nyuma. Lilikuwa gari la nani?
Tangu hapo mashaka mabaya juu ya Malolo yalimuanza taratibu, alihisi Malolo anamsaliti, alihisi Malolo anawasaliti. Malkia hakumwambia mtu juu ya mashaka hayo ila akawa anampeleleza Malolo kwa siri sana.
Sekunde zikasonga, dakika zikaenda, na saa zikaja, hatimaye Ikatokea ile siku ambayo Inspekta Jasmine aligomewa sana na bosi wake na aliporudi nyumbani alienda katika nyumba ya kulala wageni ya Uchochoroni huku akimuacha mpenzi wake Jasmine kitandani. Alivyotoka tu nje ya nyumba yake, Malkia ambaye alikuwa amekaa nje ya nyumba ile kwa muda mrefu aliunga tela.
Dakika moja baadae Peter Kissali nae aliufuata msafara ule. Na zilipita sekunde kumi na tano tu mtu mwengine kabisa nae aliufuata msafara ule. Kabla ya Malolo kuamka na kwenda uelekeo uleule.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ulikuwa msafara wa watu hatari sana. Kila mmoja akiwa makini sana, hawakuwa tayari kuruhusu kosa lolote lile. Malkia alijibanza katika nyumba ya mbele ya guest ya Uchochoroni. Peter alienda nyuma ya nyumba ile ambako pia yule mtu wa tatu alienda upande huohuo. Ikatokea Peter akagundua kuna mtu anamfatilia kwa siri, naye alimvizia na kumkaba kwa nguvu, wakati huo Inspekta Jasmine akiwa juu ya ukuta akitafuta nafasi ya kutoka katika nyumba ile ya kulala wageni. Ndipo alipowaona na kwenda hadi pale.
Peter alikimbia huku yule mtu mwengine akibaki palepale, huku akidai akitaka kuchunwa ngozi na kumpa Inspekta Jasmine kitambulisho cha yule mtu. Inspekta kutokana na haraka alizokuwa nazo za kutaka kurejea nyumbani hakutaka kumdadisi sana mtu yule. Alirudi kwake mbiombio kumuwahi Malolo. Bila kujua yule jamaa nae alimfuata hadi nyumbani kwake.
Baadae Malolo nae alirejea na kumkuta Jasmine amelala kitandani. Wakati yule mtu akiwa amejibanza nyuma ya stoo ya nyumba ile.
Ule mvutano kuhusu simu ya Malolo na Ispekta Jasmine jamaa aliusikia wote. Alivyoona mvutano unazidi alimtumia Meseji mwenziwe, dakika tano baadae mwenziwe alifika, aliungana nae, sasa walikuwa watu wawili wakifatilia kila kitu kilichokuwa kinatokea ndani ya nyumba ile. Wakina Malolo walikuwa wanagombana bila kujua kwamba kuna watu walikuwa wanawasikiliza kwa nje, wanawafatilia kwa kila wanachokifanya. Wakati wapo katika dunia ya maraha ndipo mtu mwengine alipoonwa na macho ya wale watu wawili kule nje. Walimuona, walimvizia kimyakimya na walimnyamazisha kimyakimya, mtu aliyenyamazishwa alikuwa anaitwa Peter Kissali. Waliitoa maiti gizani na kuileta katikati ya mlango, huku wao wakijibanza mahali ambapo walikuwa wanauhakika walikuwa hawaonekani na mtu yeyote yule..
*****
Ndani ya chumba alichofungiwa Malkia alisikia mlango ukifunguliwa. Hawakuingia wale watu wawili wa mwanzo, safari hii aliingia askari wa kike ambaya Malkia alikuwa anamfahamu vizuri sana, kwa majina askari huyo alikuwa anaitwa Jasmine Wahab.
Inspekta Jasmine alifunga mlango kwa ndani, alimwangalia Malkia kwa jicho la hasira, jicho la 'siku ile ulinikimbia lakini leo nimekubamba'.
"Naitwa Inspekta Jasmine.." Jasmine alijitambulisha kijeuri akiwa anamsogelea Malkia.
Malkia hasira zilimpanda juu ya mwanamke yule. Alitokea kumchukia askari yule kuliko askari yeyote yule Duniani.
Hakumjibu.
"Umepata bahati ya kukutana na mimi tena. Safari hii sitaki tupambane kwa mwili, nataka tupambane kwa maneno, maneno matupu. Huna ujanja mwanamke, ujanja pekee uliobakiwa nao ni kusema ukweli, ukweli kwa kila nitakachokuuliza..." Inspekta Jasmine aliongea huku akitamba chumbani.
"Hapa umenoa dada, hutopata ukweli uutakao kamwe!" Malkia alijibu kwa kiburi.
"Nakwambia utasema leo mtoto wa kike wewe.." Sauti ya kilevi ilitoka nje ya mlango. Mlango ulikuwa umefungwa, lakini sauti ilipenya na kuyafikia masikio ya Inspekta Jasmine na Malkia.
Ilikuwa ni sauti ya Mwanasheria mlevi!
"Songelael Ntenga?" Inspekta Jasmine aliropoka. Aliikumbuka sauti hiyo kuwahi kuisikia huko Kilwa miaka kadhaa iliyopita, katika mkasa ambao mwandishi mmoja aliutungia riwaya na kuuita jina la Balaa. Inspekta Jasmine alianza kuisikia sauti hiyo kupitia katika simu na mwisho kukutana nayo moja kwa moja katika jumba la bluu...
Yeye alitolewa hospitali ya Mbozi na daktari aliyejitambulisha kwake kwamba anaitwa Dokta Yusha. Inspekta Jasmine alikuwa anafahamu vizuri sana askari yule, askari aliyeyafanya makubwa katika mkasa wa Balaa.
Dokta Yusha alimuelekeza mahali alipo adui yake, huku akipewa funguo ya chumba kile na daktari huyo. Inspekta Jasmine aliamini kwamba Dokta Yusha ndiye amefanikisha kutekwa kwa Malkia, kumbe haikuwa hivyo, ulikuwa ni mpango uliopangwa vizuri na mpelelezi mahiri nchini Tanzania, mpelelezi jasiri na mkakamavu, mpelelezi bora kabisa, anayekwenda kwa jina la Daniel Mwaseba. Mpango uliratibiwa vizuri na Mwanasheria mlevi. Waliipanga vizuri mipango yao na kuanza kufatilia kimyakimya.
Walikuja Mbozi watu watatu kutokea jijini Dar es salaam. Lengo lao kuu ni kuja kuumaliza mchezo mchafu wa watu hawa. Walimuweka Dokta Yusha hospitalini ili kuchunguza kila kitu kinavyoendelea pale hospitali. Hospitali ambayo wachunwa ngozi wote walikuwa wanafikishwa pale. Na wale majamaa wawili ndio waliokuwa wafatiliaji wa nyendo zile uraiani.
Dokta Yusha, Inspekta Jasmine alipopelekwa hospitali alimtambua na kusubiri apate nafuu ili amtwishe mambo yale aliyokuwa anayajua kwa undani wake. Baada ya kumueleza ndipo Dokta Yusha alipompa funguo, na Inspekta Jasmine alienda moja kwa moja katika chumba alichofungiwa Malkia. Sasa yupo chumbani na aliamini yupo peke yake katika nyumba ile, ndio anasikia sauti ya Mwanasheria mlevi...
Mlango ulifunguliwa kwa funguo kwa nje.
Mbele ya macho yao walikuwa wamesimama watu wawili, Daniel Mwaseba na Mwanasheria mlevi.
"Unajiita Malkia hahaha leo umekutana na Mfalme, na kwa bahati mbaya sana mimi ni Mfalme mlevii. Leo utatapika hadi visivyotapikwa" Yalikuwa ni maneno ya majigambo kutoka katika mdomo wa Malkia.
Malkia hakujibu.
"Nataka kujua jambo moja tu toka kwako..KIFO ni nani?" Mwanasheria mlevi alimuuliza huku akimwangalia usoni.
Malkia alistuka kusikia jina hilo. Sura yake ilitahayari.
Lakini alikaa kimya.
"Najua KIFO ndiye aliyefanikisha mpango wa kuiba kiti cha kifo kwa waziri mkuu. Najua kwamba Don Genge ambaye nyie mnachukua oda toka kwake alihusika katika kuiba kiti hiko. Najua wewe unamjua KIFO baada ya Peter Kissali kung'ang'ania amtambue. Najua hujui, ila nakujuza kwamba Don Genge yupo mikononi mwetu.."
"Unasemaaaaa!" Malkia aliropoka kwa nguvu.
"Nimesema hivi...Malolo pia yupo mikononi mwetu. Malolo ametueleza kila kitu kuhusu nyinyi, katueleza kila kitu kuhusu KIFO..."Mwanasheria mlevi aliendelea kueleza.
"Kumbe mshaelezwa? Sasa hapa mnataka nini? Malkia alirudia jeuri yake.
"Kwako tumefata uthibitisho tu.." Kwa mara ya kwanza Daniel aliongea kwa sauti yake ya kipole.
"Uthibitisho wa nini?" Malkia aliendeleza jeuri.
"Ni kweli mlitoka gerezani kwa rushwa? Ni kweli KIFO ni KIFO?"
"Sina majibu kwa maswali hayo"
"Utajibu" Daniel alisema huku akimsogelea Malkia pale kitandani.
"Sitojibu" Malkia aligoma.
"Humjui Daniel wewe" Mwanasheria mlevi alisema.
Daniel alimfikia Malkia. Alikuwa anatabasamu huku akiiangalia sura ya Malkia.
"KIFO ni nani?" Daniel alimuuliza huku akimwangalia usoni.
"Simjui"
"Nakuuliza kwa mara ya mwisho mwanamke, KIFO ni nani?"
Hakujibu.
Kilikuwa ni kitendo bila kuchelewa. Ngumi ya Daniel ilitua katika pua ya Malkia, muda uleule damu zilikuwa zinambubujika. Daniel alirudia tena kitendo kile, ngumi yake ya kushoto ilitua katika sikio la kushoto la Malkia. Sikio lilianza kusikia milio isiyoeleweka. Pua ilitoa damu vibaya sana. Lakini cha ajabu Malkia alikuwa anatabasamu.
Ngumi ya mkono wa kulia ilitua katika sikio la kulia la Malkia huku ngumi ya kushoto ikielekea tena puani kwa Malkia.
Lakini haikufika.
Malkia alirudi nyuma kidogo kuipisha ngumi ile huku akirusha ngumi yake kwa mkono wa kulia iliyotua vizuri katika mbavu za Inspekta Jasmine aliyekuwa kasimama pembeni.
Kivumbi!
Inspekta Jasmine alipandwa na hasira, Mwanasheria mlevi aliyeaangalia yote kwa umakini mkubwa wakati Daniel Mwaseba alikuwa anatabasamu...
Akiwa amekaa palepale kitandani Malkia alitanguliza mguu wake wa kulia mbele na kujigeuza kwa nyuma. Goti lake la mguu wa kushoto likiwa limekandamiza kitanda. Alipeleka ule mguu wake wa kulia kwa nguvu na kasi kubwa sana, watu wote watatu mguu ule uliwagusa, kila mmoja aliugulia kivyake.
Malkia alikuwa amesimama wima, kichwani mwake akizichanga karata zake vizuri na kutafuta namna ya kujiokoa katika kisanga kile. Alitumia sekunde mbili tu kuwaangalia wale watu watatu, aliamini anao uwezo wa kuwatoka. CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alitishia kama anataka kumvaa Mwanasheria mlevi halafu akanesa kidogo na kurusha teke la kinyumenyume lililomkumba kwa nguvu Inspekta Jasmine. Inspekta yule wa kike alianguka mzimamzima na kujibamiza ukutani. Malkia alipangusa damu puani kwake kwa kutumia kiganja chake kwa nyuma, akaziangalia damu, akazilamba na kuzitemea katika uso wa Daniel Mwaseba kwa kupitia mwanya wake.
Daniel alikuwa anatabasamu.
Malkia alibabaika kidogo kuliona tabasamu la Daniel Mwaseba. Sekunde ya kwanza alibabaika, sekunde iliyofuata alirusha ngumi kwa mkono wake wa kulia, Daniel Mwaseba aliiona, aliinama kidogo na kurusha ngumi ya nguvu iliyotua katika mbavu za Malkia. Malkia alinesa huku akigumia kwa maumivu. Alivyokaa sawa alikishuhudia kiganja imara cha Daniel Mwaseba kikitua shingoni mwake. Alibaki katika mshangao, shingo ilimuuma vibaya mno akishindwa hata kumeza mate yake mwenyewe. Alinyoosha mikono juu kumuomba msamaha Daniel, lakini Daniel hakumuuelewa. Alirusha teke lililoenda kuipangusa kwa nguvu ile mikono iliyokuwa kule juu, Malkia alianguka chini mzimamzima.
"Basi Daniel Utamuua!" Mwanasheria mlevi alipaza sauti.
'Bora afe" Daniel alisema huku akitabasamu.
Wakati huo Inspekta Jasmine alikuwa alijitahidi kuinuka, halikadhalika Malkia.
Malkia alikanyaga mguu wake wa kulia juu ya kitanda ili kujipa nguvu na kutengeneza pigo mujarabu kwa mguu wake wa kushoto.
Daniel Mwaseba alimkuta kasimama imara...
Alibonyea kidogo kupisha pigo lile huku akimsindikiza kwa ngumi ya nguvu ya mgongo. Ngumi iliyompeleka hadi ukutani na kujigonga kwa nguvu usoni. Moyoni mwake Malkia alikiri amekutana na kiumbe cha ajabu, lakini bado alikuwa na dhamira ya kutoroka mle ndani.
"Hebu funga pingu huyo" Daniel alisema huku akimwangalia Inspekta Jasmine. Jasmine alimsogelea Malkia kwa dhamira ya kumfunga pingu.
Hakufanikiwa.
Malkia aliinuka harakaharaka na kukinga ngumi kumkaribisha Inspekta Jasmine. Inspekta Jasmine safari hii alikuwa amesimama imara. Hakutaka kudharirika tena. Malkia alirusha ngumi iliyopanguliwa kwa ustadi mkubwa sana na Inspekta Jasmine, alirusha ngumi nyingine ambayo ilidakwa na mkono wa Inspekta. Akaunyonga ule mkono, sauti ya kama kuvunjika kwa kijiti kikavu ilisikika, mkono ulikuwa umevunjika. Malkia huku akipiga kelele alirusha ngumi kwa ule mkono mwengine, mkono wa kushoto, Malkia aliufanya vilevile. Aliuvunja tena mkono ule.
Malkia alilia kwa maumivu.
Inspekta Jasmine alimgeuza kwa nyuma na kufanikiwa kufunga pingu katika mikono iliyovunjika. Akamwacha akiwa kauegemea ukuta, akiwa kakata tamaa.
"KIFO ni nani?" Daniel Mwaseba alimuuliza huku akiwa anamsogelea.
Hakujibu.
"KIFO ni nani?" Daniel alirudia tena.
Hakujibu tena.
Daniel alitabasamu.
Inspekta Jasmine na Mwanasheria mlevi walikuwa wanawaangalia watu wale wawili na kuyasikiliza mahojiano.
"Mfanye kama Dokta Yusha alimvyomfanya Dokta Kilumba katika Balaa.." Mwanasheria mlevi alipayuka.
Daniel alimshika shingoni Malkia na kuanza kumkaba, alizidi kumkaba kwa nguvu kila sekunde zilivyosogea. Malkia alikabika haswaa. Alianza kuishiwa pumzi. Aliishiwa nguvu. Daniel alizidi kumkaba. Sasa alikuwa amemsimamisha kwa roba. Malkia akitaka kuitumia miguu yake, Mwanasheria mlevi alimuwahi. Aliirukia na kuishika kwa nguvu kwa mikono yote miwili, mkono wa kulia wa Mwanasheria mlevu umeshika mguu wa kushoto wa Malkia, mkono wa kushoto wa Mwanasheria mlevu umeshika mguu wa kulia wa Malkia.
Inspekta Jasmine alifungua begi dogo na kutoa kamba, alimrusha Mwanasheria mlevi.
Alimfunga miguu.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Sasa Malkia alikuwa hana ujanja. Alikuwa na njia moja tu kama alikuwa anataka kuendelea kuishi. Ni kusema ukweli na aliusema, aliusema ukweli wote ...
Malkia alitumia dakika thelathini kuyajibu maswali ya watu wale watatu. Baada ya mahojiano Daniel alipiga simu Polisi. Dakika kumi baadae Polisi walifika pale na kumpeleka Malkia kituoni. Huku wao wakielekea kuumaliza mchezo.
*****
Mzee Kessy alikuwa ni mzee maarufu sana nchini Tanzania. Uwekezaji wake mkubwa alioweka sehemu mbalimbali ulimfanya atambulike hata na watoto wadogo.
Ukienda katika sekta ya madini lazima utalikuta jina la mzee Kessy, ukienda katika sekta ya habari na mawasiliano huwezi kulikosa jina la mzee Kessy, alikuwa na magazeti kadhaa. Ukienda katika sekta ya elimu lazima utaambiwa juu ya shule yake kubwa aliyoijenga huko mkoani pwani, na kujitolea kuwasomesha watoto waathirika wa madawa ya kulevya na Ukimwi bure .
Katika sekta ya michezo ungesimuliwa juu ya timu yake ya mpira wa miguu iliyoibuka miaka mitatu iliyopita tu na Kuwa tishio hata katika timu kongwe.
Ilikuwa huwezi kuangalia taarifa ya habari katika kituo chochote kile ukakosa kusikia habari inayomhusu mzee Kessy. Kama sio kusaidia masikini, basi kusafirisha wagonjwa wakatibiwe nje au kutoa kiasi kikubwa cha pesa kanisani au msikitini. Kessy alikuwa mkombozi wa waTanzania masikini, mhimili wa serikali. Mara kadhaa alikuwa anaikopesha serikali pindi inapodaiwa.
Mzee Kessy alikuwa mzee Kessy kweli.
Na kubwa juu ya mzee Kessy alikuwa ni rafiki mkubwa mno na rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania, urafiki uliopelekea hata waziri mkuu pia kuwa rafiki yake.
Huo ulikuwa upande mmoja wa mzee Kessy.
*****
KIFO alikuwa ni mzee wa makamo. Mzee mwenye nusu nywele nyeupe, nusu nywele nyeusi. Nywele zikizoashiria kuwa uzee ulikuwa unamkimbilia kwa kasi sana. Alikuwa ni mzee mwenye tamaa, pamoja na kuwa na pesa za kutisha lakini siku zote bado alitamani kuendelea kuwa tajiri. Hakuridhika, hakutosheka. Hali iliyopelekea pamoja na kuwa na miradi mingi ya halali lakini pia alionelea ili kuwa tajiri zaidi kuwa na miradi haramu. Hapo ndipo alipoanzisha mpango wa Angamizo, mpango ambao kuna mwandishi mmoja aliuandikia kitabu na kukiita ANGAMIZO. Katika mpango huo KIFO alikuwa na mpango wa kuiba silaha zote katika kambi ya silaha iliyopo huko Makete, Iringa Tanzania na kwenda kuziuza Somalia. Mpango ulikwama pale tu Daniel Mwaseba alipoingilia kati.
Mbinu yake ya pili kujiongezea kipato ilikuwa ni kuanzisha mpango wa kutoa mioyo watu. Mpango huo ulifanyikia katika wilaya ya kilwa na kuleta Balaa katika wilaya hiyo kongwe nchini. Mpango huo aliamini atashinda hasa baada ya kukipata kiti cha kifo. Siri ya uwepo wa kiti hiko aliambiwa na rafiki yake waziri mkuu na kutafuta namna ya kukipata. Waziri mkuu alikuwa anamuamini sana KIFO, na hata ujio wake na Don Genge nyumbani kwake hakuutilia shaka. Kumbe ndio alienda kuibiwa kiti cha kifo.
Naam, wiki moja tu baada ya kuletwa kiti hiko kiliibwa. Ni Don Genge ndiye aluyefanikisha wizi wa kiti hicho. Toka hapo KIFO alimuamini sana Don Genge na kumpa ukuu katika misheni ya huko Kilwa. Don alipewa na vijana sita waliokuwa wanajiita Six killers. Mpango huo ulienda vizuri kabla ya kuingiliwa na vijana wanne, Mwanasheria mlevi, Inspekta Jasmine, Dokta Yusha na Daniel Mwaseba.
Vijana ambao sasahivi walikuwa nje ya geti la KIFO katika mtaa wa Mikocheni jijini Dar ea salaam...
Haikuwa kazi ndogo hadi kupata ruhsa ya kwenda kuizunguka nyumba ya KIFO kwa ajili ya kumkamata. Haikuwa kazi rahisi hata kidogo. Iliwapasa kutoka Mbozi na kwenda jijini Dar es salaam kuonana na rais mwenyewe ambaye ndiye alikuwa amiri jeshi mkuu, hiyo ni baada IGP kuogopa kutoa kibali hiko. Mbele ya rais na waziri mkuu Daniel Mwaseba aliwaeleza uhusika wa KIFO katika vifo vya raia wasio na hatia. Walikuwa na ushahidi wa sauti toka katika simu ya Don Genge. Simu ya Don iliwekwa katika mtindo wa kurekodi mazungumzo yote waliyokuwa wanaongea. Hakuna aliyeamini kwamba mzee Kessy ndiye alikuwa KIFO. Mzee akiyeheshimika sana na chama pamoja na serikali kumbe ndiye alikuwa mkuu wa mipango hasi. Ilimchukua siku tatu hadi rais kukubali mzee Kessy akamatwe. Hiyo ni baada ya kudukua mazungumzo yake na mtu mmoja akimsikitikia kufeli kwa Biashara ya kifo na kuamua kuihujumu kiuchumi serikali kisha kuipindua. Hapo ndipo vijana wale wanne walipopewa ruhsa ya kwenda kumkamata mzee Kessy na raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Daniel Mwaseba na Dokta Yusha walikuwa mbele ya nyumba ya mzee Kessy, Inspekta Jasmine na Mwanasheria mlevi walikuwa nyuma ya nyumba ya mzee Kessy, wote wakiwa wamejipanga kisawasawa kufanya uvamizi katika nyumba ambayo ilikuwa inalindwa sana.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nyuma yao kulikuwa na wanajeshi wasiopungua ishirini na silaha zao mikononi, wakiwalinda askari wale wanne katika kila hatua waliyopiga, wakiwalinda wasipate madhila yoyote. Ni Daniel Mwaseba ndiye aliyegonga geti la mzee Kessy. Waliamua kuwazubaisha kwa njia hiyo. Wakati akili za walinzi wa mzee Kessy zikiwa mbele ya mlango wa nyumba ile uliokuwa unagongwa, kule nyuma wakina Inspekta Jasmine walipata nafasi ya kuuparamia ukuta mrefu wa nyumba ile. Ulikuwa ukuta mrefu sana na mgumu kuupanda lakini Inspekta Jasmine na Mwanasheria mlevi waliupanda kirahisi sana. Sasa walikuwa katika uwanja mpana wakielekea katika mlango wa nyuma ya nyumba ile.
Kule mbele geti kubwa lilifunguliwa. Daniel alikaribishwa na mitutu mitatu ya bunduki...
Hatari!
"Karibu sana kijana, sijui tukusaidie nini?" Askari mmoja alimuuliza Daniel Mwaseba.
"Nina shida na mzee Kessy" Daniel aliongea kwa sauti yake ya kipole.
"Una miadi nae?" Yule mlinzi alimuuliza tena.
"Hapana, sina miadi naye"
"Ok waweza kutudokeza shida yako"
"Ni shida binafsi hivyo ni vyema nikamueleza mwenyewe"
"Ngoja tukamtaarifu mzee" Mlinzi alisema huku akifunga mlango.
Hakumaliza kuufunga.
Daniel Mwaseba nae alijitosa ndani sambamba na mlinzi, na nafasi ileile Dokta Yusha aliyekuwa pembeni aliitumia kujitosa ndani. Walikutana na macho ya walinzi sita yakiwashangaa kwa mshangao na bunduki zao zikiwa mbele.
Daniel alitabasamu.
"Nyi vipi? Mbona mnaingia bila ya ruhsa?"
Hawakujibu.
Walinzi wawili walikoki bunduki tayari kwa kulipua. Daniel Mwaseba na Dokta Yusha walinyoosha mikono juu. Dakika ileile waliwaona walinzi wanne wakija toka pande mbili za nyumba, wawili upande wa kulia na wawili upande wa kushoto.
Daniel alitabasamu tena huku akiwa kanyoosha mikono juu, hilo ndilo walilokuwa wanalitaka.
"Nyi ni nani, jibuni kabla hatujaziruhusu bunduki zetu ziwapasue!"
"Na KIFO mtamjibu nini?"
Waliona mstuko dhahiri Dokta Yusha alipolitaja jina hilo, wakajua na wale walinzi nao wanauelewa mchezo.
"Kwani nyinyi ni wakina nani?" Mlinzi aliyeonesha kuwa alikuwa kiongozi wao aliuliza.
"Naitwa Daniel Mwaseba..." Daniel alitamka huku mlango wa mbele wa ile nyumba ukifunguliwa. Macho yote ya walinzi yaliangalia kule mlango ni. Walimuona mzee Kessy P.A.K KIFO akiwa kasimama wima mlangoni, na taulo kiunoni, tumbo wazi, mikono juu, alikuwa analia, anadondosha machozi.
"Shusheni bunduki zenu chini" Mzee Kessy alisema kwa sauti yenye kukata tamaa.
Askari wote sita walishusha silaha zao chini. Mzee Kessy alipiga hatua nyingine mbele. Ndipo Inspekta Jasmine alipoonekana. Alikuwa kaishika imara bastola yake ikiwa imeelekea katika kisogo cha mzee Kessy. Daniel Mwaseba alitoa bastola zake mbili toka kila upande wa kiuno chake, alikuwa anawaelezea wale askari sita kwa zamu. Dokta Yusha naye alifanya hivyohivyo.
Watekaji wakageuka watekwaji.
Mwanasheria mlevi nae alitoka ndani ya nyumba. Ni yeye ndiye aliyefanya kazi ya kuwafunga pingu wahalifu wote wale, huku Daniel Mwaseba akipiga simu, wanajeshi wote waliokuwa nje waliingia ndani ya nyumba na silaha zao na kurahisisha kazi ya kuwakamata wahalifu wale.
Wiki tatu baadae habari kubwa katika vyombo vya habari ilikuwa ni juu ya hukumu waliopewa wahalifu wanne, mzee Kessy, Don Genge, Malkia na Malolo walihukumiwa kunyongwa hadi kufa katika mahakama kuu. Walipelekwa katika gereza la Segerea wakisubiri saini ya raisi ili adhabu yao itekelezwe. Raisi ambaye alikuwa rafiki mkubwa wa mzee Kessy.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Daniel Mwaseba, Dokta Yusha, Inspekta Jasmine na Mwanasheria mlevi walipewa nishani za ushindi na zawadi mbalimbali toka serikali ya jamhuri ya muunguno wa Tanzania. Huku wakipewa likizo ya mwezi mmoja na kulipiwa kila kitu ili kwenda nchini Hispania mapumzikoni.
Yote hayo Martin aliyasikia redioni na kuyasoma magazetini. Alijisemea kimoyomoyo..
"Raisi akichelewa kutia saini nitawanyonga mimi kwa mkono wangu!"
MWISHO WA RIWAYA HII KWA SEHEMU HII YA PILI...ITAENDELEA SEHEMU YA TATU MWAKANI INSHAALLAH.
Imeandikwa na Halfani Sudy
0 comments:
Post a Comment