Search This Blog

Friday, 20 May 2022

DILI TATA - 1

 







    IMEANDIKWA NA : SULEIMAN KIJOGOO



    *********************************************************************************



    Simulizi : Dili Tata

    Sehemu Ya Kwanza (1)



    Wazo hili lilimjia ghafla tu pale alipokuwa akiifunika albam ya picha zake. Utambuzi kwamba anaweza wazo hili kulizalisha kwa vitendo na kuleta faida kubwa itakayomfanya kulala masikini na kuamka tajiri, ulimfanya ahisi mapigo ya moyo wake kwenda kwa kasi ya ajabu. Wazo hili lilimjia kwa nguvu na ghafla zaidi hata ya ndege za kivita zinapovamia kambi ya adui kwa mtindo wa kushitukizaCHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Akawa ameganda na albamu yake ikiwa ameshaifunga bila kuirudisha katika meza mawazo yakiwa mbali akili ikichekecha hili na lile hapa na pale kama vile Ava Find katika Compyuta inapotafuta faili linalohitajika kwa haraka

    Kupotea kwakwe mawazoni kulimfanya Chan’duu amtazame kwa muda mrefu bila kumuuliza kitu, lakini alipoona yule amtazamae haonyeshi dalili zozote kwamba anaangaliwa yeye, ikamlazimu kuvunja ukimya

    ‘Vipi baby! Mbona ghafla tu umezama katika dimbwi la mawazo?’ akauliza akikaa sawa kwenye sofa

    ‘Ahg..’ akataka kujibu lakini hakujua anataka kujibu nini, kwani hata yeye alikuwa bado hajajua anachokiwaza ni kweli anakiwaza kwa ajili ya kukifanyia kazi au ni mawazo yake ya kawaida yanayokuja na kupita kichwani kwake, yale mawazo yanayoonekana daima kama ndoto za alinacha

    Kigugumizi chake kikamfanya Chan’duu kushangaa

    ‘Ahg vipi sasa?’ ikabidi aulize kwa umakini zaidi, akiamini katika usemi kwamba, ukiona Kobe kainama basi ujue anatafakari jambo

    ‘Kuna kitu kimenijia ghafla sasa nashindwa hata kujielewa..’ akajibu na kunyamaza

    Akamuangalia bwana wake usoni kwa kutaraji kwamba, ataulizwa ni jambo gani hilo lililomfanya kutojielewa kiasi cha kumzamisha katika dimbwi la mawazo mazito. Alipoona haulizwi wala kusisitizwa kumalizia maneno yake, ikawa hana budi ila kumwaga maelezo ‘Nahisi kama nimepitiwa na wazo la maana sana lakini naona utaniona kama mjinga mno nitakapokueleza’ akasema huku akijishtukia kama kweli alichokiwaza kina maana yoyote kiasi cha kuweza kumueleza mtu mwingine na asikuone kama mtu unayeanza kuchanganyikiwa

    Pamoja na mwenyewe kujiona amewaza ujinga na atakapozungumza atadhihirisha ujinga wake, lakini Chan’duu alitaka kujua ni ujinga gani mpenzi wake anawaza kiasi cha kumtoa katika ‘mood’

    ‘Kitu gani hicho kilichokuchanganya ghafla?’ Chan’duu akang’ang’ania kuambiwa

    ‘Sikia baby! Nitakuambia kwasababu umeng’ang’ania nikuambie, lakini usinione kama naanza kuwa na mawazo ya kipumbavu’ akaonya

    ‘Wewe niambie tu’ mwanaume msimamo wake ukabaki hapo hapo

    Kujibu ilikuwa rahisi, lakini namna ya kuelezea mawazo yake ndio ikawa tatizo. Ataeleza vipi, katika ufafanuzi upi mpaka aeleweke?

    Akakaa kimya kwa sekunde kadhaa akijiuliza wapi pa kuanzia? Mawazo yakamtuma kuanza na ushahidi moja kwa moja. Akaona kuna umuhimu wa kueleza mawazo yake huku akionyesha na mifano hai. Akaifunua tena albam yake na kuikagua picha moja iliyokuwa inamuonyesha yeye na mtoto mmoja wa kike wa kihindi wakiwa ufukweni mwa bahari

    ‘Nilikuwa nafikiri… Kwa jinsi bosi wangu anavyompenda huyu mtoto wake, basi kama tukimteka, anaweza kulipia fidia ya mamilioni ya shilingi kama vile wanavyofanya katika filamu za kimafia’ akatoa maelezo yake kwa ufupi sana huku akimuangalia mtu wake kwa wasiwasi mkubwa akijua kwamba sasa ataonekana kama mtu anayeanza kudata

    Kwa jinsi Chan’duu alivyokuwa akimuangalia, dhana yake kwamba ameongea utumbo ikashika kasi. Aibu ikamvaa usoni akashindwa kusema lolote kwa sekunde kadhaa. Akataka kunyanyuka huku akiwa anasema ‘Nilikuambia yatakuwa mawazo ya kijinga..’ lakini kabla hajasimama wima na wala hajamalizia maneno yake

    Chan’duu akamshika mkono na kumshusha kwenye sofa

    ‘Una uhakika na unachokizungumza?’ Chan’duu akauliza akiwa amekaza macho

    ‘Si nimekuambia kuwa ni mawazo ya kijinga!’ akajibu akiwa sasa aibu imemvaa rasmi

    ‘Sijakuuliza kuhusu mawazo yako kama ni ya maana au ya kipumbavu, ninachotaka kujua ni kwamba unahakika kuwa bosi wako anampenda sana mtoto wake na akitekwa anaweza kulipa fidia ya mamilioni ali aachiwe?’ Chan’duu akauliza akiwa akilini mwake anaanza kuona picha za matukio asiyoyajuaCHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ‘Hilo nina hakika nalo asilimia bilioni zote, ila naona ni kitu kisichowezekana kuweza kumteka huyo mtoto’ akajibu akimuangalia bwana wake usoni akiona kuwa hapa sasa wanaanza kufanyana kama watoto wanaoanza kuwaza kiutu uzima

    Sasa ikawa zamu ya Chan’duu kuzama katika dimbi la mawazo, akishika wazo hili na kuliacha akishika wazo lile na kulitupa, akili yake ikiwa inajaribu kuumba kitu huku ikiwa haimpi njia sahihi za kuweza kulijua jambo hilo

    ‘Baby, hebu tuachane na wazo hilo la kijinga, acha nikapike chakula tule’ msichana akasema akimkamata begani bwana wake ili kupima ni vipi wazo lake limepokelewa rasmi

    ‘Hapana baby, unajua umezungumza jambo kubwa sana japo kama wewe mwenyewe hujajua. Si umesema watu wanafanya katika filamu? Sasa wewe unadhani yale matukio ya katika filamu ni matukio ya kuigiza tu? Yale ni matukio ambayo huwa yanatokea kweli katika jamii, na kwa vile hapa nchini halijawahi kutokea tukio kama hilo basi tulikifanya kwa umakini tunaweza kupiga hela mbaya. Niamini mke wangu’ Chan’duu akasema kwa kusisitiza huku akinyanyuka, sura imemuiva kama mtu aliyepigwa kibao cha kushitukiza

    Akapiga hatua na kuliendea kabati

    Akatoa fulana na kuivaa

    Akarudi kwenye sofa na kuchukua simu yake

    ‘Nakuja’ akaaga bila kusema anapokwenda huku akiwa amekunja uso akionekana kama mtu aliyepatwa na jambo zito lililomchanganya kupindukia

    Msichana akabaki akiwa ameshangaa tu akiwa hawezi kujiuliza wala kujijibu juu ya suala hili lililotokana na mawazo ya kujipitia tu kichwani. Ni vipi sasa wazo hili limeanza kujiumba na kuwa jambo la maana na lenye kuzalisha kitu kikubwa? Akajiuliza swali hili tena na tena

    Akanyanyuka na kutaka kuelekea nje lakini alipofika mlangoni alikuwa hajui alitaka kutoka ili aende wapi. Akarudi katika sofa na kuketi

    kwa kifupi alikuwa amechanganyikiwa

    Akakaa na kuanza kufikiri kwa kina ni kitu gani kilimfanya kuwaza alichowaza, na kipi bwana wake anaweza kufanya katika kuthibitisha kwamba wazo lake ni la maana na linaweza kuzalisha matokeo makubwa. Mara wazo likamjia kwamba umasikini unawafanya sasa kuanza kuwaza upumbavu. Hapa akatabasamu kwa mbali lakini akajiona kama anajicheka ujinga. Tabasamu likamtoka

    Akajiegemeza katika sofa akili yake ikiwa haiwazi hili wala lile

    Msichana huyu kwa jina anaitwa Sofia, watu wengi walikuwa wanapenda kulifupisha jina lake kwa kumuita Sofi. Ni binti wa mzee mmoja aitwaye Rahim Kulindwa mwenyeji wa mji wa Tanga. Kwa sasa ana umri wa miaka ishirini na mbili. Mrefu, mwembemba, maji ya kunde, mzuri kisura na mzuri kiumbile. Tokea afike mjini kutoka kijijini kwao Kilambo, ni mwaka wa sita sasa. Hapa Jijini Dar aliletwa na dada wa jirani yake huko kijijini kwao kwa ajili ya kuja kumsaidia kazi za nyumbani. Mama huyo baada ya mwanawe wa kike kumaliza masomo ikawa nyumbani kuna watoto wawili wa kike na kazi zikiwa hakuna. Mama huyu aliyekuwa akifanya kazi katika kampuni moja ya vifaa za ujenzi kama katibu muhtasi, aliposikia kuwa kuna nafasi ya mfanyakazi wa ndani kwa bosi wake wa kihindi, akampa nafasi hiyo Sofia. Kazini hakukuwa na mishemishe nyingi. Kikubwa kilichokuwa kinamkwaza katika kazi yake hii mpya, ni manyanyaso na matusi anayoyapata kutoka kwa bosi wake wa kike na mshahara mwembamba uliokuwa unamfanya ajibane sana ili apate hela ya kumpelekea baba yake kijijini na yeye kuweza kupata mahitaji muhimu

    Kukutana kwake na Chan’duu aliyekuwa akiishi mtaa wa pili toka anapoishi yeye maeneo ya Magomeni mikumi, ilitokana na yeye Sofi kwenda dukani kununua vitu wakati huo alipokuwa akifanya kazi kwa mama huyo aliyemtoa kijijini. Chan’duu alikuwa kijana wa mjini asiye na kazi maalumu lakini alikuwa anajitahidi kuvaa vizuri na kula vizuri huku hela ndogo ndogo zikiwa hazimpigi chenga mfukoni

    Chan’duu ndio mwanaume wa kwanza wa Sofia na kama si mtoto wa bosi wake wa kihindi aitwae Chandramuki kumtongoza kwa ahadi kemkem na kuamua kumvulia nguo, basi Chan’duu angebaki mwanaume pekee maishani mwake kwa sasa

    Mwaka jana wakati sasa akiwa na kazi ya kuweza kumfanya kujikimu baadhi ya mambo, huku akiwa bado anaishi kwa mama aliyemtoa kijijini, alimuomba Chan’duu ahamie kwake ili waanze maisha ya pamoja

    Hili Chan’duu hakulipinga hata kidogo, hasa ukizingatia kwamba mwanaume huyo aliyekuwa na miaka thelathini na mbili, alikuwa akimiliki kitanda tv meza na ndoo za maji tu.





    Sofia akatoa hela yake ya kukusanya upatu na kununua Dresingtable Deki Sofa na baadhi ya mapambo ili kuanza maisha na mwanaume wake aliyekuwa akiishi katika nyumba ya familia

    Asubuhi Sofia anaenda kazini na kurudi jioni, Chan’duu kwa kipindi hicho akiwa analala muda mwingi wa mchana akisubiri dili za mjini wakati wa usiku -dili zilizokuwa zikija kwa nadra- na kumuingizia hela kidogo kwa ajili ya mahitaji yao ya kimaisha

    Maisha yao yalikuwa si mabaya kwa maana ya kwamba walikuwa hanajimudu kula na kulala bila kudaiwa kodi, lakini ukitaja masikini nao pia walikuwa wapo katika fungu hilo

    Tokea Sofia ameanza kazi kwa muhindi huyo, kazi yake kubwa ukiacha kufanya usafi, ilikuwa ni kuhakikisha anachukua Taxi na kumfuata au kumpeleka shule mtoto wa bosi wake

    Mtoto huyu, ambaye leo ibilisi ameshawaingiza Sofi na Chan’duu mawazo ya kumteka, alikuwa anaitwa Vidya na alikuwa na umri wa miaka mitano, akisoma shule ya Chekechea st Joseph maeneo ya Upanga

    Familia hii ya kihindi ilikuwa na wanafamilia watano, baba, mama, mtoto mmoja wa kiume mwenye miaka kumi na saba, na huyu wa kike mwenye miaka mitano, na mdogo wa mama mwenye nyumba aliyekuwa akifanya kazi katika kampuni moja ya usafirishaji wa angani

    Sofia, ilikuwa ikifika muda wa saa kumi na mbili kasorobo anatoka Magomeni na kwenda Msasani ambako ndiko ilipo nyumba ya waajiri wake. Akifika humtayarisha mtoto na kumpeleka shule, akirudi ilikuwa akishirikiana na mfanyakazi mwingine wa kike-mtu mzima- kufanya usafi, kisha baada ya hapo wanakaa wakiangalia filamu hizi na zile kupitia dish lenye kuonyesha chanel zaidi ya mia moja kupitia tv ndogo ya jikoni

    Ikifika mchana alikuwa anatoka na kwenda tena shule kumfuata mtoto. Wakirudi, tayari mfanyakazi mwenzake ambaye ndie huwa anaishi na mabosi zake na kuwa mpishi na mtayarishaji wa shakula, huwa ameshandaa msosi, wanakula, anamtayarisha mtoto na kumpeleka kulala mpaka jioni mabosi wanaporudi na yeye kuwa siku yake ya kazi imekwishia hapo, anasubiri siku nyingine zikatike ili achukue mshahara wake kiduchu na kuutia kibindoni

    Japo kama familia hii ya mabosi zake haijui vizuri, kwa undani, lakini kuna sifa mbili kuu alikuwa anazijua kindakindaki

    Sifa ya kwanza, ni ubahili ulioambatana na roho mbaya wa bosi wake wa kiume, na sifa ya pili, ni kuhusu bosi wake wa kike alivyo mkali na mkorofi juu ya watu wengine na mapenzi makubwa aliyonayo mama huyo juu ya mtoto wake mdogo

    Kiundani kabisa Sofi kazi hii alikuwa inaifanya kwa sababu alikuwa hana uwezo wa kupata kazi nyingine. Kusoma hajasoma, na mtu wa kuweza kumuunganishia kibarua sehemu nyingine alikuwa hana. Mapenzi juu ya mabosi zake alikuwa hana hata chembe na wala alikuwa hajali kuwaona wanacheka ama wamenuna wanagombana au wanachekeana

    Sasa leo hii wazo hili lililompata ghafla juu ya umafia ambapo ameshauona sana katika filamu anazoziangalia kwa mabosi zake kupitia televisheni, hakuwa anawaza kabisa kwamba anaweza kusababisha hali ya huzuni na mtafaruku kwa familia ya mabosi zake

    Umasikini wake na umasikini wa familia yake kijijini sio kitu kikubwa kilichomfanya kuwaza alichokisema, ila tu jambo hili liliuvaa moyo wake ghafla na wala halikumfanya kujihisi kwamba anawaza ushetaniCHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Akakaa hapo varandani kwa muda wa masaa mawili mfululizo bila kujijua wala kunyanyuka kwenda popote mpaka usingizi ukampitia

    Kilichokuja kumgutusha usingizini ni simu yake ya mkononi kuita

    Akiwa bado ana mang’amung’amu ya usingizi, kiuvivu kabisa akapeleka mkono na kuichuka simu yake na kuiweka sikioni, lakini kipindi anaiweka tu katika sikio lake nayo ikakata

    Hakuangalia mpigaji, akashusha mkono chini ili aiweke simu chini na kuendelea kuuchapa usingizi

    Lakini kipindi ndio mkono unadondokea katika sofa tu simu ikaita tena

    Huku akihisi anasumbuliwa na kukatishwa stimu ya usingizi akasonya kidogo na kuipeleka simu sikioni

    Akaipokea bila kutazama ni nani anayepiga

    ‘Hallow’ akasema kwa sauti ya chini iliyojaa uchovu

    ‘Sasa wewe muda wote nakupigia simu hupokei maana yake nini?’ mpigaji akauliza kwa kulalamika

    ‘Ah! Hamna beby, nilikuwa sijaisikia mana umeniamsha usingizini’ akajibu akijua kwamba anongea na Chan’duu

    ‘Hujasikia wakati simu imeita zaidi ya mara nne?’ mwanaume akauliza tena kwa msisitizo

    ‘Nilikuwa nimepitiwa wangu’ akajitetea

    ‘Sasa hebu nyanyuka ujimwagie maji uvae vizuri upendeze kisha uje hapa Mwembechai katika hii Bar tunayopenda kuangalia mpira’ Chan’duu akasema kiamri

    ‘Kuna nini baby? Mimi najihisi usingizi Bwana’ akasema kwa sauti laini ili amshawishi bwana wake kuachwa aendelee kulala

    ‘We hebu acha ujinga. Nyanyuka na ufanye fasta kuna mtu anataka kuongea na wewe’

    ‘’Kuna mtu anataka kuongea na mimi? Mtu gani huyo!?’ akauliza akiwa ameshangaa

    ‘Ndio. Na fanya haraka’ Chan’duu akajibu kwa amri bila kumuainishia ni mtu gani anayetaka kwenda kuzungumza naye

    ‘Mtu gani huyo? Mbona sikumbuki kama tuna ahadi na mtu. Au kuna ndugu yako anataka kuniona?’ akang’ang’ania kuelezwa

    ‘Hapana sio ndugu yangu, ila ni jamaa yangu katika mishemishe, anataka uhakika kuhusu dili uliloniambia’

    Hapa usingizi Sofia ukamruka

    ‘We Chan’duu! Yani jambo ambalo tumelizungumza mimi na wewe tayari unatafuta watu unataka kuwaingiza? Sasa hata hatujapanga chochote unaanza kumwa siri? Mimi nilikuambia wewe ili kama inawezekana tufanye wawili sasa ..’

    ‘Baby.. Hebu acha porojo’ akamkata kauli kwa ukali ‘huyu mtu ni mzoefu katika mambo hayo japo kama si katika matukio kama hayo lakini anayajua na anaweza kuwa msaada mkubwa sana’ akamalizia na maneno ya kumtoa wasiwasi

    ‘Mh! Mbona unanitisha? Kama vipi tuachane nalo mana mimi niliongea kama utani tu’ akataka kukwepa

    ‘Sofia nimesema acha ujinga, hebu njoo huku tuongee mambo ya maana usitake kunikorofisha kabisa au kwasababu sijakutandika siku nyingi sasa unaaanza kunizoea?’ akauliza kwa ukali

    ‘Hapana baby ila..’

    ‘Hakuna ila, nakupa dakika kumi na tano iwe umeshafika’ akaamrisha na kukata simu

    Sofi akabaki na simu yake mkononi akiwa haamini kwamba Chan’duu wazo hili amelishupalia zaidi ya alivyodhani

    Akiwa anamjua mwanaume wake alivyokuwa hapendi kuchezewa, akanyanyuka na kwenda maliwatoni kuoga

    Aliporudi ndani akavaa jinz na tshat na kutoka

    Akafika barabarani akachukua bodaboda na kuanza safari

    Ilikuwa yapata saa tatu sasa za usiku

    Akaingia Mtaa wa Kwimba maeneo ya Mwembechai katika Bar aliyoelekezwa Akatoa simu yake na kupiga ili kuuliza bwana wake alipo

    ‘Njoo huku kiti moto utatuona tumejitenga pembeni kabisa huku mwisho’ akapewa maelezo

    Akamlipa dereva bodaboda na kuelekea ndani moyo wake ukimpiga vibaya sana akili yake ikiwa inajiuliza maswali yafuatayo

    Ni nani huyo atakayekuwa nyuma ya mpango huu aliouanzisha?

    Je suala hili linaweza kufanyika kweli?

    Na likafanikiwa?



    Chan’duu jambo hili mbona kalichangamkia sana wakati hajawahi kumsikia hata siku moja kuzungumzia suala la kupata hela nyingi kwa wakati mmoja, na wala hajawahi kumuona na ishara za kuweza kufanya kazi zilizokaa kijambazi jambazi?

    Akapishana na muhudumu na kupita meza za karibu

    Akasimama kidogo kuangalia pembe ya kwanza lakini hakuwaona walengwa wake

    Akaangalia pembe ya pili

    Akamuona aliyemkusudia lakini tofauti na alivyodhani, kwani alimuona Chan’duu akiwa peke yake chupa za pombe tu ndio zikiwa mwenza wa kumpa ushirikiano

    Huku akienda alipo mtu huyo moyoni alikuwa akijiuliza kama huenda bwana wake anamletea utani

    Lakini alipofika karibu na meza na kutupa macho akagundua kwamba Chan’duu hakuwa peke yake kwani kulikuwa na chupa za pombe katika upande wa pili wa meza ikiwa ni ishara kwamba kuna mtu mwingine mahala hapo inawezekana amekwenda msalani tu kujisaidia

    Akavuta kiti na kuketi

    Muhudumu alipokuja akaagiza Redbul na mtu wa jikoni kwani nyumbani alikuwa hajapika na alikuwa hana mpango huo kwa muda huu uliosonga

    ‘Ebu niambie vizuri kinachoendelea’ akadai maelezo kabla hata ya kukaa vizuri

    ‘Unajua baby kitu ulichokizungumza ni bonge la dili, lakini kama unavyoona kwamba si kitu cha mimi na wewe tu peke yetu kukikamilisha, hivyo nimechekecha akili nimeona bora tutafute patna kwa ajili ya kushuhulikia hili swala’ Chan’duu akajibu taratibu kwa kufahamisha zaidi kuliko kutoa maelezo

    ‘Kwanini unasema hivyo?’ Sofi yeye akataka maelezo zaidi

    ‘Kwanza kuna suala la wapi pa kumuhifadhi huyo mtoto tukishamteka, kisha kuna mambo yatakuja kujitokeza na nilazima tutaka msaada’

    ‘Mambo gani hayo?’

    ‘Kwasasa siwezi kukufafanulia kwani mimi kazi za kuhifadhi kago zinazotafutwa na polisi nimeshawahi kuzifanya na najua mambo yanayotokea. Kwasasa ridhika tu kwamba hii kazi tunahitaji msaada na huyu jamaa anatufaa sana’

    ‘Huyo mtu ni nani na mnajuana vipi?’ akauliza akijua kwamba sasa hakuna kurudi nyuma

    ‘Mshikaji anaitwa Mfaume lakini wengi wanapenda kumuita Kijogobwire..’

    ‘Kijogobwire?’ Sofi akadakia kwa kuuliza

    ‘Ndio jina lake la utani sijui kwanini wanamuita hivyo lakini hilo ndio jina lake maarufu’

    ‘Ehe!!’ Sofi akaitikia bila kujua anataka kuchangia nini

    ‘Huyu jamaa ninamjua kutokana na kufanyakazi za kuiba kwenye magodauni kisha mali ndio huwa tunatafutia wateja, yeye ni mzoefu wa kazi na ana sehemu nyeti ambazo tunaweza kumficha mtu wetu baada ya kumteka na kudai fidia kiulaini kabisa. Na hata tukitaka kampani yeye anaweza kututafutia watu wa kazi zaidi’

    Sofi akafikiria maelezo haya kwa kina kisha akasema

    ‘Sikia baby.. Unajua hili suala itabidi tujitahidi kulifanya sisi watatu tu kwani tukiwa wengi tunaweza kugeukana kisha ikawa balaa huko mbele’ akaonya

    ‘Usijali tutalipanga kwa umakini wa hali ya juu kisha baada ya hapo wewe mwenyewe utaona’ akajibiwaCHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ‘Enhe, na huyo bwana Kijogobwire yuko wapi?’ akauliza kwa utani

    ‘Kuna mtu anaongea naye hapo nje kidogo’

    Sasa ikabidi Chand’uu kunywa bia yake na Sofi kunywa Redbul yake kila mmoja kichwani akiwa anafikira zake

    Chan’duu akili yake ikiwa mbali akijaribu kuratibu katika kichwa chake suala zima la utekaji na ufanikishaji wake na jinsi mchezo huu watakavyoucheza kwa tahadhati kubwa

    Sofia mawazo yake yote yalikuwa juu ya Kijogobwire, akiwaza mtu huyo yukoje?

    Mawazoni mwake akamchukulia kwamba kwa vyovyote atakuwa mrefu eliyejazia mwili na kuwa kama mbeba vitu vizito huku akiwa na sura ngumu yenye kuonyesha kwamba ni mtu hatari aliyekubuhu katika kazi za wizi

    Kwa vyovyote mtu huyu mwenye umri wa miaka thelathini na tano au hata arobaini, atakuwa hata kama hana makovu makubwa lakini kovu usoni mwake hazitakosekana

    Sura yake itakuwa siyakuvutia na atakuwa mtu ambaye hacheki wala kutabasamu muda mwingi atakuwa mkimya akiwaza dili za wizi tu

    Mtu mwenye dili za wizi kiasi cha kazi hatari kama hizi kuonekana ndio anafaa kushirikishwa, kwa vyovyote hatakuwa mtu mwema wala mwenye kuvutia

    Hakuna namna nyingine mtu huyu aitwaye Kijogobwire anaweza kuwa zaidi ya hivyo alivyomfikiria yeye

    Wakati akiwa bado yuko mbali kimawazo akili yake ikimuumba Kijogobwire katika namna anayotaka yeye, mara akasikia mtu akisema

    ‘Sory nilikuwa naongea na jamaa yangu kuna dili la nguvu litaingia leo usiku’

    Sofi akanyanyua sura na kumuangalia mtu huyo aliyetoa kauli hiyo

    Cha kushangaza ni kwamba, mtu huyo aliyesema hivyo alivuta kiti na kuketi mahala ambapo Kijogobwire alitakiwa kukaa

    Mtu huyu aliyekuwa mbele ya Sofi alikuwa mweupe, mzuri kisura, si mrefu lakini si mfupi, mwembamba, aliyevalia kinadhifu, uso wake umejenga tabasamu la kuvutia na kupendeza, umri wake hauzidi miaka ishirini na nne

    ‘Sofi huyu ndio Kijogobwire’ akatambulishwa

    Wakati mshangao bado uko wazi usoni mwake kwa kumuona mtu tofauti na alivyomjenga katika mawazo yake akasikia sauti laini na nzuri kutoka kwa Kijogobwire ikisema

    ‘Niambie patna, mambo yako kama mr alivyoniambia?’

    Sofi akabaki kubabaika. Japo kama hii haikuwa salamu lakini kule kusikia sauti ya mtu huyu na kuwa tofauti na alivyodhani, kulimbabaisha mno, akajikuta akitoa mkono wake na kumpa mtu huyo kama vile amesalimiwa

    Kijogobwire akajua kwamba mwanamke huyu alitegemea kusalimiwa kwanza kisha ndio maongezi ya kazi yaanze

    Hakumuangusha, akatoa mkono wake akamkabidhi na kumsalimia

    ‘Niambie patna’ ikawa ndio salamu yake

    ‘Fresh’ ndio neno Sofi aliloweza kujibu, akili yake ikiwa katika ulaini wa mkono wa Kijogobwire

    Kitu hiki kikazidi kumbabaisha Sofi

    Mtu huyu hakuwa na alama hata moja ya kumfanya kuwa muhalifu

    Toka Sofi alipotoka nyumbani alikuwa amejenga picha kwamba mtu huyo anayetarajiwa kuwa mshirika wao atakuwa mtu hatari mwenye umbile la hatari, lakini huyu alikuwa anaonekana kama vile.. Nani?

    Mmh! Kama mwanamuziki wa kizazi kipya. Yah. Ndio. Huo ndio mfano wake. Alivyovaa na anavyoongea hana tofauti na vijana wachana mistari.

    Macho yake yanaonekana laini kama ya mtoto wa kike na manukato anayonukia ni kama anajiyarisha kwenda mtoko na demu wake. Hana dalili hata chembe ya kuwa mtu anayeweza kukamilisha mipango ya kijambazi

    ‘Sofi, huyu ndio bwana Kijogobwire. Kijogobwire, huyu ndio wife wangu anaitwa Sofia na ndio mwenye mchongo mzima’ akasikia sauti ya Chan’duu ikiwatambulisha rasmi

    ‘Nashukuru kukufahamu na usibabaike na muonekano wangu kwani hivi ndivyo watu wa kazi tunatakiwa kuwa sio unakuwa rafurafu mtu akikuona tu anaanza kukutilia shaka’ Kijogobwire akasema ili kumtoa wasiwasi ambao alikuwa ameuona katika uso wa patna wake mpya

    Lakini pamoja na kudhani kwamba Sofi ana wasiwasi tu, kuna kitu cha ziada ambacho hakukigundua kutoka kwa msichana huyo. Ni kwamba Sofi alikwishaanza kumpenda





    ‘Kama nilivyokuambia awali’ Chan’duu ikabidi kuingilia kati baada ya kuona Sofi hana maneno ya kuchangia na akiwa amebakiwa na mshangao uliochanganyika na kigugumizi

    ‘Shemeji yako hapa anafanya kazi kwa mdosi. Huyo mdosi ana mtoto wake wa kike kama miaka nane hivi..’

    ‘Miaka mitano’ Sofi hapa akadakia kusawazisha ili kujiweka sawa pia

    ‘Mitano ee?’ Chan’duu akauliza na bila kusubiri jibu akaendelea na maelezo yake

    ‘Huyo mtoto anapendwa sana na mama yake, na baba yake anapesa chafu, sasa wife anaona kama tukifanya mpango wa kumteka huyo mtoto na kudai fidia basi ndani ya siku moja tu tunalala masikini na kuamka matajiri’ Chan’duu akamalizia maongezi yake na kumuangalia Kijogobwire kama ana cha kuuliza

    Kijogobwire hakufanya haraka. Alikuwa na muda mwingi kwa ajili ya kulipima jambo hili, na aliamua kuutumia

    Akawasha sigara na kisha akamuita muhudumu

    ‘Niletee Mbuzi ubavu niongezee na bia sita’ akaagiza

    Kitu hiki kilimfanya Sofi kuzidi kumuona Kijogobwire katika mtazamo anaoutaka mwenyewe ‘Huyu ndo mwanaume bwana’ moyo wake ukamshawishi

    Muhudumu alipoondoka mazungumzo yakarejea, sasa Kijogobwire akiwa muanzaji

    ‘Malipo yangu yatakuwa kiasi gani?’ ndio neno pekee alilouliza

    Sofi na Chan’duu wakatazamana

    Hii ilikuwa kaliCHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mtu hata bado hujaanza kupanga mikakati ya kufanikisha kazi we unaanza kutaka kujua malipo?

    ‘Hivi kwanza si tuanze kupanga mikakati ya ufanikishaji wa suala kisha ndio tuanze kujua tutalipana vipi?’ Chan’duu akazungumza akimuangalia Kijogobwire usoni moja kwa moja

    ‘Hapo hakuna la kupanga, hilo ni suala dogo sana halihitaji wala kuumiza kichwa, cha msingi nikujua je hela mnayotaka kunipa inatosha kwa kazi ninayotaka kuifanya?’ akauliza tena

    Sofi na Chan’duu wakatazamana kwa mara nyingine tena

    Mbona hii sasa kasheshe. Walikuwa hawajapanga lolote achilia mbali suala la malipo

    Wakabaki kutazamana tu

    ‘Vipi patna hamjajipanga? Hamna hakika na dili lenu?’ akamuuliza Sofi huku akitabasamu

    ‘Tutakulipa robo ya fedha tutakazo lipwa’ Sofi akajibu akimuangalia Kijogobwire usoni

    Macho ya Kijogobwire yalipotua katika macho yake akajikuka akihema kwa mbali na koo kuanza kumkauka

    Ikabidi ajikaze tu

    ‘Malipo ya awali?’ Kijogobwire akauliza tena

    ‘Kwa sasa hatuna cha kukupa, tunafanya kazi kisha ndio tunalipana’ Chan’duu akaingilia kati baada ya kuona Sofi amepata kigugumizi

    ‘Haha’ Kijogobwire akacheka kidogo ‘mwanzo uliniambia hii kazi ni ya hatari lakini hatari kubwa ni hii kufanya kazi iliyokuwa haina advansi’ akajibu na kukunja sura akionyesha kwamba analetewa utani

    ‘’Sikia Kijo’ Chan’duu akaingilia kati ‘hili ni bonge la dili hata wewe mwenyewe umekiri, sasa..’

    ‘Sasa ndio nifanye kazi bila advansi?’ akadakia kwa swali ‘we si unajua kila kazi inahitaji maandalizi na mipango?’

    ‘Ndio lakini..’

    ‘Sio lakini, sula la kuteka linahitaji mambo kadhaa ya kutayarisha.. Hebu sikilizeni, tafuteni laki tano tuanze kazi’ akahitimisha

    Chan’duu na Sofi wakatazamana kwa mara nyingine huku wakiona mambo kuharibika kabla ya kuanza

    ‘Sikia Kijo..’ Sofi akasema taratibu kwa sauti laini ‘unataka laki tano, sisi hatuna, ila tuna laki mbili ambazo naamini zitatosha kuanzia kazi’

    Kijogobwire akamungalia Sofi kama vile ndio kwanza anamuona. Bwana huyu kwa wasichana naye hajambo. Ni mwepesi wa kutamani na ni mwepesi wa kutangaza fedha kwa ajili ya kununua ngono. Katika akili yake akapata wazo kwamba huyu naye anaweza kumpeleka kitandani kama vile anavyowapeleka kitandani wanawake wengi anaokutana nao. Na kwa Kijogobwire wanawake ndio starehe yake kubwa, hasa wanawake wembamba na maji ya kunde kama huyu

    Akatafakari kiasi kisha akajibu

    ‘Ok, kabla ya kusema kwamba nimekubali au nimekataa kuchukua hizo laki mbili, kwanza nataka mujue kuwa nyinyi ni wachanga sana katika kazi hizi za kimafia, bora kidogo hata Chan’duu tushawahi kupiga mishe za usiku pamoja lakini wewe mrembo unaonekana unaweza kufagia na kupika tu’ akatania

    Sofi hilo likamchekesha na Chan’duu naye akacheka pia ili kuweka mambo sawa

    ‘Ninachotaka kwanza, mujue kwamba dili hii ni Dili tata, hivyo inahitajika umakini na usahihi wa ripoti na utendaji wa wote, kutoka kwako Sofi ninachotaka kwanza unipe maelezo kamili kuhusu huyo mtoto kisha nipime kama mimi nitaweza kupanga kitu chochote juu ya utekaji au tunahitaji mbinu mbadala’

    ‘Ni kitu gani zaidi unataka kujua?’ Sofi akauliza mara tu baada ya Kijogobwire kumaliza herufi ya mwisho, sasa akiwa kazini rasmi

    ‘Mienendo mizima juu ya huyo mtoto, na baba yake ni mtu wa aina gani? Mana tusije kumteka mtoto kisha tukaingia mkenge, kama baba yake anajuana na vigogo wa serikali inamana hiyo dili ni kasheshe na hatuiwezi’

    ‘Baba yake ni mfanyabiashara wa kawaida hana uhusiano na mtu yoyote serikalini tena yeye hata askari anawaogopa, kazi yake ni uingizaji bidhaa kutoka kwao India na kuwasambazia wahindi wenzake kwa mkopo kisha baada ya muda anachukua hela zake. Ni tajiri mkubwa kwa mahesabu lakini ukimuona huwezi kudhani kwamba benki ana mabilioni ya shilingi na kwamba kariakoo ana magorofa mawili na posta gorofa moja. Watu wanasema utajiri wake ni wa kiugangauganga, kwani anavaa nguo za kawaida wakati mwingine utamkuta na kandambili na hata gari yake ya kutembelea ni ya kizamani na hata maisha anayoishi ni ya kawaida sana tofauti na hela aliyonayo. Sifa ya ubahili ndio inayomtawala zaidi’

    Wakati Sofi akiongea hayo Chan’duu alikuwa akimuangalia Kijogobwire jinsi hamu ya kunywa pombe inavyomtoka na akili yake kubebwa jumla na maelezo hayo

    Kwa vyovyote Kijogobwire amepata picha kwamba dili hili ni dili kubwa na lenye faida nzito huku utendaji wake ukiwa wa kawaida sana

    Mara akapata wazo kwamba hapa ni tofauti na alivyofikiria

    Mwanzo kabisa alidhani kuwa anahitaji mtu ambaye ana uzoefu kidogo tu na mahala sahihi pa kuweza kuificha bidhaa yao kabla ya kudai mapato, na Kijogobwire ni mtu sahihi. Lakini mwitikio wa macho na mshangao wake pale alipotajiwa kuwa baba wa mateka wao ana mabilioni ya shilingi na hana uhusiano na wakubwa wa nchi hii na hata polisi anawaogopa, kumemfanya ahisi kwamba mtu huyu ni mjanja mno na mzoefu zaidi ya inavyotakiwa. Huyu huko mbele huenda asishikike iwapo kama mambo yakinyooka na yeye kuwa mshirika sawa na si jeshi la kukodi

    Chan’duu akajikuta akitamani Kijogobwire aseme kazi isiyo na malipo mazuri ya awali haiwezi ili watafute mtu mwingine anayeweza kwenda sawa na spidi anayoitaka

    Au hata kama ikiwezekana akakubali hizo laki mbili basi amuwekee kipingamizi ambacho hatoweza kukivuka sasa na kuichukia kazi kabla ya kuianza na kujiweka pembeni kabla hakujacha

    Akajikuta akiingilia kati

    ‘Mmh, nimekumbuka..’

    Wakageuka kumuangalia.



    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ‘Ni kweli tungekupa laki mbili ya kuanzia lakini hiyo hela haitokamilika kwani pale ndani baby tumebakia na elfu themanini tu hela nyingine jana nilinunulia stoku ya chakula mana niliona mwezi huu utakuwa mgumu’ akaamua kudanganya

    Sofia macho ya mshangao na sura ya hasira vikamvaa. Ghafla akaanza kumuona Chan’duu kama mtu wa ajabu na anayeropoka vitu bila kupima wala kujiuliza

    Kwa kweli hapa kwa mwanaume huyu handsome gangstar ambaye tayari Sofi ameshaanza kumzimikia ghafla, ilikuwa si mahala pa kujifanya masikini. Sawa, hawana hela ya kusema wana hela, lakini si sehemu ya kuanza kujionyesha kwamba wao ni wanyonge dhofulhali. Hiyo itamfanya jamaa aanze kumuona Sofi kama mwanamke asiye wa kiwango chake, na hilo Sofi asingependa kuona likitokea

    Lakini ukiacha hilo kuhusu kuonekana masikini, pia kuna hili la pili. Jamaa ameshapachika tahadhari kuwa hatatia kwato au kuishika mkononi kazi ambayo haina advansi, hivyo kumtangazia kuwa hata hiyo pesa chache iliyopo imepungua na kuwa zaidi ya kiduchu, si ndio mwazo wa kumtoa ndege tunduni?

    Hapa Sofi alikuwa anachanganya

    mapenzi na kazi bila kujali kwamba yupo mbele ya mpenzi wake

    Akajikuta anataka kumkaripia bwana wake kwa maneno ya kipuuzi aliyoyatamka

    Chan’duu yeye alikuwa akimuangalia Kijo kwa jicho la kuonyesha masikitiko na kuomba radhi kwa usumbufu ili mtu huyo aseme kwamba kama unataka sadaka basi nenda msikitini au kanisani kwangu ni pesa kwanza then kibarua baadae

    Bwana na bibi wakawa wakimuangalia Kijo kwa jicho la huruma lakini kila mmoja akilini mwake akiwa na lengo lake. Bibi akitaka jamaa aseme basi nitawasubiri mpaka mtakapopata hela ya advansi ndio tujadili hili swala, au hata ikiwezekana, leteni hicho kilichopo tuanze mambo, huku bwana akitaka jamaa auteme mzigo ili atafute mtu mwingine atakaye onyesha ufuasi na sikutaka kuwa sawa

    ‘Ok. Mimi nimekubali kufanya hii kazi japo kama inaonekana hapa mwanzo haina mafao. Kitu ambacho kimenivutia ni kwamba, huko mbele tunaweza kupiga mshiko wa maana na nikafidia kila sekunde niliyotumia’ Kijo akajibu, moyoni akijiambia kwamba, hapa atapiga ndege wawili kwa jiwe moja. Ni dhahiri mwanamke huyu atalala naye na ni dhahiri alivyo mjanja kazi ikikamilika yeye ndio ataondoka na mshiko mkubwa zaidi

    Chan’duu akahisi vitu kama sindano vikimchoma tumboni. Ni kama vile amejiingiza katika janga bila kulipima

    Hakutakiwa kumuweka mtu katika msitari kabla ya kumpima uwezo wake wa kiutambuzi. Jamaa ameshaona kwamba hapa kuna pesa na hatoiacha nafasi hiyo. Sasa afanyeje? Akaamua kuleta zwengwe

    ‘Unajua Kijo, hii kazi ni kama vile haina uhakika sawasawa kwa hiyo..’ akataka kuleta maneno ya kukatisha tamaa lakini hapa Sofi akashindwa kumvumilia

    ‘Chan’duu sasa maneno gani hayo unayozungu..’

    Naye pia hakumaliza maneno Chan’duu akamdakia kwa ukali

    ‘Wewe, mwanaume akiongea kuhusu kazi basi unatakiwa kunyamaza na si kujitia kimbelembele’

    Kauli hii ikamchoma mno Sofi

    ‘Kama natakiwa kunyamaza basi poa ila itabidi mimi nisishiriki katika huu mpango’ akasema kwa hasira ili kuonyesha umuhimu wake

    Hapa wanaume wote wawili wakaona hatari iliyopo

    Huyu ndio anayejua kila kitu katika hii kazi na ndie mwenye kazi mwenyewe, sasa akijiweka pembeni si sawa na dili lenyewe kufa. Ikabidi Kijo kuingilia kati ili kuuzima moto ambao Chan’duu ameshauwasha

    ‘Naomba niongee kitu kimoja. Mimi ni mzoefu, najua jinsi ya ufanikishaji wa kazi na ukwamaji wake. Hakuna kitu kibaya katika kazi kama wahusika kuanza kugombana wenyewe kwa wenyewe. Ugomvi wa patnas, daima huifanya kazi ama kukwama au wahusika kuingia katika kasheshe isiyoteta tija, so kama hapa tuko pamoja basi inabidi tuwe pamoja pia kimaneno na kivitendo. Tukianza kukwazana amini hatutafika hata mbali mambo yataingia funza, hili ni dili tata na dili tata daima huhitaji umoja’

    Japo kama kwa Chan’duu hakukuwa na dhamira ya kumkwaza Sofi ila kutaka kuiweka kazi sehemu salama, ikabidi hapa akubali kwani ilikuwa ameshaingia mahala bila kupenda na haina namna ya kujikwamua

    ‘Unaloongea ni kweli’ mwanaume akatetea ugali

    ‘Hamna Kijo wala usiwe na shaka mimi na mr tumeshazoea kutamkiana maneno kama hivyo. Unaweza kudhani kama vile tunagombana kumbe wenyewe ndio tunaweka mambo sawa’ Sofi yeye akaamua kuyeyusha

    ‘Mh kumbe? Basi vyema. Ila kwa sasa ningependa tuende kwa staili ya kuwa wawazi zaidi kuliko hiyo staili yenu mliyozoea’

    Kauli hii ikazidi kumuweka Chan’duu katika wakati mgumu kwani mtu huyu ana akili na anasoma alama za nyakati kabla hata kitu hakijatendwa. Ni dhahiri mtu huyu amejua kwamba Sofi amezungumza hivyo ili kuweka mambo sawa, na kama amejua hilo basi hii inadhihirisha jinsi jamaa alivyo mjanja na akili za haraka. Akajikuta amenyong’onyea hana kauli

    ‘Ok, sasa tupange mipango kamili’ Kijo akasema na kuwaangalia mmoja baada ya mwingine

    ‘Hii kazi itabidi tuifanye fasta kabla watu hawajaanza kututilia shaka. Kunzia kesho, Sofi unatakiwa uchunguze mazingira ya shule anayosoma dogo yakoje, je tunaweza kupata nafasi ya kumchoropoa hapo? Na pia angalia ni vipi unaweza kuigiza na kujifanya kuchanganyikiwa iwapo kama mtoto atatekwa huku wewe unaona..’

    ‘Kuhusu kuigiza hapa umefik..’ Sofi akadakia kati ili kutaka kueleza kuwa kazi hiyo ni ndogo sana kwake lakini Kijo akampuuza na kuendelea na maelezo yake ‘Chan’duu kesho saa tano tuonane…’ akasita baada ya simu yake kuita. Akaitoa mfukoni na kuipokea

    ‘Umeshafika?’ akauliza kwenye simu ‘Ok mimi nimeshamaliza hapa nakuja baada ya dakika tano’ akakata simu

    ‘Umeona ee? Sasa kesho saa tano tukutane ili tujue ni wapi tutamuhifadhi mtu wetu na ni vipi tutadai fidia. Ok?’ akauliza huku akimalizia pombe yake katika glasi, kisha akamalizia alichokiacha ‘Na ukija usisahau kuileta hiyo elfu themanini ya kunitia stata’

    Chan’duu hakuwa tena na cha kupinga ikabidi kuitikia tu ‘Poa mzee wa kazi tutakutana kesho’

    Sofi yeye ilikuwa furaha tupuCHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ‘Ok mpenzi, kila kitu kitakwenda sawa’ akasema na kumuangalia Kijogobwire kwa jicho laini na legevu huku akimpa mkono

    ‘Usijali malkia utafurahi na mziki wangu’ Kijo akajibu na kuupokea mkono wa Sofi na kumshika katika namna ya kumpa ishara iliyomfanya binti kutabasamu kwa mbali ikiwa ni ishara kuwa ujumbe umefika na umepokelewa

    Japo kama kushikana kwao mikono hakukuwa katika kukubaliana mambo mengine zaidi ya kazi, lakini Chan’duu akahisi hapa asipokuwa makini huenda akazidiwa ujanja na mtu huyu katika kila kitu. Akachukua pombe na kuinywa kwa hasira

    ‘So, mimi nimuwahi jamaa kidogo, Sofi, Chan’duu atakuambia wapi tutakutana kesho baada ya mimi na yeye kukutana hiyo saa tano’ akamalizia bia yake ‘Bob ndio hivyo basi’ akamuaga Chan’duu na kuondoka zake huku akiacha pesa ya malipo ya vinywaji na nyama ya mbuzi aliyoagiza



    ITAENDELEA



0 comments:

Post a Comment

Blog