Search This Blog

Sunday, 22 May 2022

KIKOMO - 3

 







    Simulizi : Kikomo

    Sehemu Ya Tatu (3)





    Nikaanza kukimbiza gari huku nakwepa magari na risasi huyu msichana wa Kihindi aliponiona ninavyoendesha akashangaa sana akainuka na kuangalia.



    "Lala chini wanatutupia risasi, watakuua".



    "Wewe fanya nini, ile natupa risasi ni polisi?"



    "Siyo polisi wewe tulia nitakueleza".



    Sasa walikuwa wanalikaribia saana hili haliwezi kupambana na Benz lakini nilijitahidi mbele nikaona kivuko cha reli karibu na daraja la kidaru. Na wakati huo huo nikaona gari moshi linakaribia saana kukata barabara kusimama ilikuwa haiwezekani. Maana Ole na wenzake wangenimaliza nikapata wazo.



    "Fungua mlango na uwe tayari kwa kuruka, mimi nikisema tutaruka wote nitafanya maarifa usiumie".



    "Wewe gari moshi itaua sisi ona iko karibu, aa bana simama sisi kufa".

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Fungua mlango, nasema shika maagizo yangu".



    Aliponiangalia usoni akafuata maagizo, tulipogusa reli tu na gari moshi likagusa barabara.



    "Sasa".



    "Gari langu waka moto", alisema huku akilia huyo msichana wa Kihindi.



    Tulikuwa tumeweza kuruka na kuangukia kwenye mtaro mrefu kiasi. Tuliona kwa juu moshi unatoka, nilipochungulia nikaona gari linawaka moto wa ajabu na watu wanakimbia ovyo kwenda kuangalia.



    "Inuka twende, sitaki mtu atuone".



    "Enda wapi?"



    "Nyumbani kwenu, nataka kwenda kulipa gari lako".



    Aliniangalia kwa mshangao mkubwa.



    "Utaweza?"



    "Wewe twende".



    Wakati tunainuka watu wengi walikuwa wameishajaa hapo na nikasikia gari la wazimamoto linapiga kelele. Hii ilitupa muda mzuri wa kuondoka bila ya kuonekana.



    "Wewe pana fuata mimi, mimi onyesha wewe jumbani yetu halafu wewe iko kuja".



    "Nyumba iko wapi?"



    "Wewe jua Butiama Hoteli?"



    "Ndiyo".



    "Jumba ya pili yake. Mimi tangulia wewe takuta nasubiri pana toroka kaka taua mimi, kama wewe iko toroka".



    "Nitawasili, lazima nitakuja".



    "Wewe mtu ya ajabu sana. Haya mimi nangulia ee".



    "Haya".



    Alitangulia akaenda zake. Mimi nikazubaazubaa hapo kidogo.



    "Vipi pana nini pale mbona watu wengi?" Nilimuuliza kijana mmoja aliyekuwa anatoka kwenye hiyo ajali.



    "Loo, afadhali ukajionee mwenyewe. Lo, ama kweli watu wengine wanakufa kifo kibaya sana. Gari moshi limegongana na gari dogo . Hilo gari dogo limevutwa likasagwasagwa na linaungua vibaya sana. Nasikia kulikuwamo mtu mwanamke mmoja wote wamekufa humo na vile gari lile linavyoungua hata mfupa hawauoni".



    "Lo, hii ni ajali kweli. Watu wengine wana bahati mbaya kweli. Mtu mwingine anasema huyo mtu alikuwa jambazi anafukuzwa na askari kanzu lakini alipogonga tu na kuona amekufa lile gari la askari kanzu likakata kona na kukimbia. Nafikiri hao wanaogopa kuulizwa maana siku hizi siyo kama siku za ukoloni bwana".



    "Walikuwa askari kweli?"



    "Ndiyo mtu mmoja alivyokuwa anasema. Sijui kama ni kweli. Anasema magari yalikuwa yanakwenda mbio kweli. Nenda ukajionee mwenyewe".



    "Asante", nilimshukru na kuondokana naye.



    Kumbe Ole na wenzake walikuwa wanafikiri nimekufa? Hiyo ilinipa nafasi nzuri sasa ya kuwashtusha.



    Niliondoka hapo nilipokuwa nimesimama na kuelekea kwa yule msichana wa Kihindi. Nilimkuta ameegemea mlangoni.



    "Karibu".



    "Ahsante".



    "Hii ndiyo mtu nasema. Hii ndiyo kaka yangu Patel Jalali. Mimi kwisha sema kila kitu", alinijulisha kwa nduguye.



    "Habari yako?", nilimsalimu.



    "Juli, iko", alijibu kwa shingo upande huku amevimba kweli kweli.



    Niliingia ndani nikasimama.



    "Joo ndani sisi jungumja", alisema msichana huyu.



    Tuliongozana wote watatu tukamuacha mfanyakazi wa Kiafrika dukani. Tulipoingia sebuleni tukakaa.



    "We nani? Ni wewe fanya! Sisi taka ita polisi lakini Jasmini iko nakataa nasema kwanza wewe kuja halafu eleza".



    "Mimi naitwa Willy Gamba." Nilitoa kitambulisho changu na kumpatia, aliposoma tu alipigwa na bumbuazi.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Mjee basi sisi hapana sumbua wewe sahau," alisema huku akitetemeka na kumuonyesha kitambulisho Jasmini.



    Jasmini alipokiangalia naye akashtuka.



    "Sasa sikilizeni. Kaeni kimya, msizungumze na mtu yeyote juu ya habari hii. Mkizungumza mtajua nini kitawapata. Gari mlinunua shilingi ngapi?"



    "Hapana hapana lipa. Sisi iko nasaidia serikali, sisi iko furahi tu. Sisi nyamaza kimya hapana sema hata neno moja".



    "Lazima ilipwe, Jasmini sema shilingi ngapi?" niliuliza kwa msisitizo huku natabasamu.



    "Zaidi ya elfu thelathini".



    "Safi, nipe simu".



    Waliponisogezea simu nikapiga Dar es Salaam kwa Chifu, wakati nangoja simu Patel akaenda dukani.



    "Wewe taondoka leo?" Jasmini aliniuliza.



    "Ndiyo".



    "Hapana usiondoke, wewe mtu shujaa. Wewe kaa kidogo hapa", alisema na huku akitaka kulia.



    "Lazima niende Mwanza, kazi bado".



    "Baba yetu iko Mwanza, mimi nitakuja huko. Wapi mimi ona wewe? Mimi ondoka leo hii hii wewe wakati iko ondoka".



    Nilipoona kubishana naye ni kazi bure nikafichua.



    "Mwanza Hoteli".



    Akatabasamu. Wakati huo huo simu ikalia.



    "Hallo wapi hapo Willy?"



    "Ulijuaje ni mimi?"



    "Nilibuni".



    "Nipe Chifu".



    "Subiri".



    "Hallo, hallo Mark, habari za huko? Nilikuwa na wasiwasi".



    "Si nzuri kwani kuna malipo. Tengeneza hundi ya shilingi elfu thelathini kwa jina la Jasmini Halal S.L.P 12 Shinyanga utume haraka.   



    Nilinyoosha mkono Jasmini aondoke, akaondoka.



    "Lo, na wewe kwa kuhonga pesa zote hizo kwa bibi. Pesa za serikali tena kwa bibi wa Kihindi," alisema kiutani. Kisha nikaanza kumweleza habari yote mpaka dakika hiyo.



    "Lo, kweli kuna kazi kubwa. Jana baada ya mkutano tu Mkuu wa Polisi na Waziri wa Mambo ya Ndani waliitwa kwenda Lusaka, Zambia kuhudhuria mkutano. Kwa hiyo mambo yote ya polisi amekabidhiwa Kamishna Mkuu wa Polisi ambaye ndiye Kaimu wake." alinielza.



    "Kwa hiyo toka jana habari zote anazo".



    "Ndiyo".



    "Nipe namba zake za simu".



    "Jina lake ni Oswald Mengi. Si unamfahamu?"



    "Ndiyo, nimewahi kumuona wakati wa kesi moja".



    "Nimemtuma George toka asubuhi na mapema, nafikiri tayari yuko Mwanza".



    "Asante sana".



    "Haya asante, kazana Mungu atakusaidia tu. Hapo ulipofikia hakuna hata mtu aliyewahi kupafika. Asante kwaheri."



    Niliweka simu chini. Roho yangu ilifurahi kusikia George anakuja maana kazi ya wawili ni wawili. George alikuwa mtu wa nne kutoka kwangu, lakini nilikuwa nimemwamini sana. Ikiwa Sammy hayupo nilipendelea yeye kuliko Patrick ambaye ni wa juu yake. Alikuwa bado kijana sana, kijana mwenye umri wa miaka ishirini na mitatu. Lakini kwa hudo na karate hata mimi nilikuwa simfikii. Hivi alifaa sana kwenye misukosuko kama hii. Niliinuka nikamwita Jasmini.



    "Mimi nakwenda".



    "Haya sisi onana Mwanza jioni. Sawa bila shaka. Chunga ee, pana ile jangiri ua wewe".



    "Nitajichunga".



    "Kwaheri ee".CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    "Oke".



    Nilimuaga Patel nikaondoka kwenda zangu. Ilikuwa saa sita hivi. Kwa vile gari langu lilikuwa limegongwa ilinibidi nitafute njia ya kwenda Mwanza ambako ningepata gari jingine. Nilikuwa sina njia bali kupanda gari la abiria au kuomba msaada kwa watu wenye magari waendao Mwanza. Wakati bado ningali katika fikra hizo nikaona gari linakuja na wazungu wawili, mwanamume na mwanamke. Nikawasimamisha.



    "Naomba msaada gari langu limeharibika nakwenda Mwanza".



    "Twende, sisi tunakwenda Musoma".



    "Asante sana".



    Niliingia akaweka gari moto".



    "Wewe unakaa Mwanza?"



    "Hapana, Dar es Salaam".



    "Sisi tunakaa Musoma. Tunakaa Bukiroba Mision. Sisi tunaeneza habari za Mungu. Wewe ni Mksto?"



    "Ndiyo".



    Dini gani?"



    "Protestanti".



    Tulipovuka tu Shinyanga akalichochea moto gari.



    "Lazima tuwe Mwanza kabla ya saa nane, tunamuwahi mtu", alieleza huyo mzungu mwanamume.



    "Safi, mbona kiswahili chako kizuri sana?"



    "Aaa. Lazima mimi nimekaa hapa nchini miaka zaidi ya thelathini.



    "Ama kweli".



    Kwa vile nilikuwa nimechoka sana nilijiweka vizuri nikasinzia.



    "Amka tumefika", alinishtua huyo mzungu.



    Nilipofumbua macho nikaona kweli tumefika Mwanza, tena mbele ya Mwanza Hoteli.



    "Sisi tutakaa hapa," walinieleza.



    "Mimi nimepanga hapa pia".



    "Tumekuleta mpaka nyumbani. Hivi hatuulizani majina. Wewe ni nani?"



    "Mimi naitwa Mark Buhulula".



    "Ala, kutoka Ntuzu?"



    "Ndiyo"



    "Sisi ni Bwana na Bibi Jackson Filton toka Marekani.



    "Nimefurahi sana mmenisaidia".



    "Si kitu. Yesu anasema ukimsaidia mtu mwenye shida umemsaidia yeye, kwa hiyo ni wajibu".



    "Asante, kwaherini".



    Tuliagana.



    Nilikata shauri kwenda chumbani kwangu nikapige simu ili nipate gari jingine. Wakati napita sehemu ya baa nikamwona msichana lakini sikukumbuka nilimuona wapi. Alikuwa msichana mzuri sana, mwembamba lakini mwenye siha. Nilikuwa nimekwishamuona lakini wapi ndiyo nilikuwa nimeshindwa kukumbuka. Nilikata shauri nipande chumbani nipige simu halafu nirudi upesi huenda kwa bahati ningepata habari wapi nimemuona.



    Wakati ninapanda nilipokaribia chumba changu nikapata fikra ghafla kichwani. Niliweka bastola yangu taratibu nikanyemelea chumba changu. Nilitazama huku na huku kama kuna mtu lakini sikuona mtu. Nilipokuwa karibu sana na chumba nikasikia sauti zinazungumza ndani na watu wanacheka. Niliposikiliza kwa makini nikasikia mtu anasema. "Sijui kaziweka wapi?"



    Na mwingine akasema. "Tukipata hii mali ya serikali kweli mimi nitawacheka kweli kweli. Walete almasi yenye thamani kubwa nanma hiyo iporwe. Willy Gamba kesha kufa na sasa huko Delux na George naye atakuwa ameisha kufa, ama kweli mwaka huu serikali itatukoma.



    Niliposikia habari za George gadhabu ikanipanda, bastola mkononi nikarudi nyuma kidogo na kwenda kimgongo mgongo kwa nguvu zote hadi kuugonga mlango. Mlango ulikuwa wazi hivyo nikaangukia ndani. Nao walishtuka mno wasijue la kufanya ghafla. Wakati huo huo nikawawahi watu wawili kwa risasi na kukawa patashika na hao ambao niliwakosa. Mmoja aliupiga mkono wangu kwa teke nayo bastola ikaponyoka, akanitwanga konde la haja. Hii inaniongezea hasira yangu vibaya sana.



    Kabla sijasimama sawasawa akanitia teke la ubavuni mpaka chini. Aliponirukia nikamkwepa, Hapo nikajua kwamba kweli nimepambana na mtu na ilinibidi sasa niamue kupambana sawasawa.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alitupa shoto lake nikalikwepa na hapohapo nikalishika hilo shoto na kwa njia ya judo nikamwinua juu na kumtupa chini. Aliposimama tu nikampiga karate mpaka chini. Nikamngojea tena asimame. Kumbe yeye alikuwa ameona bastola imedondoka karibu yake. Akaichukua, lakini kabla hajafyatua nikampiga teke.



    Aliposimama tena alitupa ngumi nyingine. Nikaihepa na hapo hapo huo mkono wake wa kulia nikaupiga karate ukavunjika. Ulipovunjika nikamtwanga tena ngumi ya shingoni akaanguka chini taabani. Wengine walikuwa wamekimbia kasoro hao wawili niliowapata kwa risasi. Alipozirai nikamvuta mpaka kwenye bafu nikammwagia maji. Alipozinduka nikaushika huo mkono wake uliovunjika nikaanza kumuuliza.



    "Nani amemfuata George?"



    "Sijui", alijibu pole pole.



    Nikaupinda huo mkono akasikia maumivu makali.



    "Ole na watu wengine wanne".



    "Mmejuaje amekuja?"





    Nikaupinda tena huo mkono.



    "Ole ndiye aliyekuwa na habari zote na pia ndiye aliyetuambia kuwa wewe umekufa".



    "Mlikuja kufanya nini humu? Nani aliwaeleza nilikuja na almasi?"



    "Ole".



    "Nani aliyewaambia mimi ni Willy Gamba?"



    "Ole".



    Nilichukua kitako cha bunduki niliyoikuta humo ndani, nikamtwanga huyu mtu na kuhakikisha kuwa hataweza kuamka bila ya msaada. Halafu nikachukua bastola mbili nikazijaza risasi nikafunga mlango. Hapo chini nilimtafuta yule msichana yule mrembo lakini alikuwa ametoweka. Nikataka shauri kukodi teksi inipeleke kwenye Hoteli ya Delux.



    "Kuna nini?" Dereva aliniuliza.



    "Wewe nipeleke haraka iwezekanavyo".



    Hakuuliza tena. Akawasha gari na kuondoka kasi. Baada ya dakika chache tukawa Delux, nikamlipa haki yake. Nilipoingia hotelini nilimuuliza mpokezi wa wageni kama alikuwepo mgeni wangu aitwaye George Chikaka toka Dar es Salaam.



    "Yupo nambari 132 orofa ya kwanza".



    "Asante".



    Nilipanda ngazi kwa kukimbia. Nilitafuta chumba nambari 132 nikakiona. Nikanyata mpaka hapo nje, nikatega sikio. Nikasikia sauti ya Ole ikisema. "Sema umekuja na nani? Nakupa sekunde moja usipojibu utajua nitakufanya nini mbwa wee! Kafa Willy itakuwa wewe".



    Nikashika bastola mbili mkononi nikaupiga teke mlango nikaingia ndani. Nikalenga bastola.



    "Sijafa bado. Ole nipo na nitaendelea kuishi". Ndani kulikuwa na maiti tatu nikajua George walikuwa wamemshinda kwa taabu. Waliokuwa wamebaki ni Ole na mtu wake mmoja pamoja na George ambaye alikuwa amepigwa kiasi cha kufa wakati wowote.



    "Tupa bastola yako chini". niliamrisha.



    Walipokuwa wanataka kuweka chini bastola zao huyo mtu mmoja wa Ole akainua bastola yake kijanja lakini nikawahi kumuona na kumuwahi na kumpiga risasi akafa papo hapo.



    "Ole, tayari umenisumbua kiasi cha kutosha na wewe pamoja na kundi lako lote mtalipa maisha ya watu wote mliowaua toka Jack Mbile mpaka George ambaye sasa amezirai na nimeamua kupambana na nyinyi ana kwa ana. Nani mkubwa wenu?"



    "Sijui na wala usijidumbue kuniuliza. Mimi nilijua umekufa imekuwaje?"



    "Unaleta utani?".



    Niliweka bastola moja mfukoni nikamsogelea kusudi nimtwange, lakini kabla hata sijamfikia niliona macho yake kwa chati yanaangalia kwenye mlango na mara hiyo nikajua kuna kitu. Niliruka chini wakati tu risasi ilipopita hapo nilipokuwa nimesimama na wakati huo huo nikaachika risasi zikampata huyo mtu aliyetaka kuniua. Huku Ole alikuwa tayari akanirukia na kupiga teke bastola yangu, ikaanguka mbali lakini alikuwa amechelewa, mtu wake alikuwa amepatwa na risasi akaanguka na kufa. Ikawa kikiri mimi na Ole, tayari kwa mapambano.



    Nilimrukia Ole kwa konde la shingoni akalikwepa na kunitandika konde la shingo nikayumba.



    "Utanitambua leo", alisema na mimi sikujibu.



    Alifululiza ngumi kama nne zikitoka kama umeme na zote zikanipata mpaka damu zikanitoka puani. Hiyo damu ikanisisimua.



    Alitupa ngumi mbili tena mfululizo nikazikwepa na hapo hapo nikampiga konde la kifua akateteleka. Kabla hajajiweka sawa nikamtupia makonde mawili ya nguvu zangu zote kwenye kichwa akaanguka chini. Nikamrukia kumpiga teke la tumboni, akawahi kunishika na kunisukuma kwa nguvu nikaanguka chini.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Akanirukia hapo chini, yeye juu mimi chini. Akaanza kuninyuka. Kuona hivi nikatumia ujuzi wangu wa judo. Nikajipinda, miguu yangu ikamkaba shingoni akapiga ukelele. Nikiwa tayari nimesimama na kabla yeye hajasimama vizuri nikampiga teke la mguu na nikauvunja, akalia.



    "Aaa umenivunja mguu, niache inatosha".



    "Haijatosha, nimekwambia lazima ulipe mateso ya rafiki zangu waliyoyapata".



    Akajaribu kukimbia kwa mguu mmoja, nikaupiga ngwala huo mguu wa pili akaanguka chini kwa uchungu mwingi. Akalia.



    "Basi imetosha".



    Nilimwendea nikampiga teke la ubavu, nikaona amedhoofika kabisa. Nikaushika huo mguu uliovunjika, nikaanza kuunyonga.



    "Aaa niache, niache! Niue tu kuliko kunitesa hivi".



    "Nilifikiri wewe ni jasiri huwezi kusikia uchungu. Watu wote hao uliowaua uliwatia maumivu makali kabla hujawaua ulifikri wao si watu? Mkuki kwa nguruwe kwa binadamu mchungu. Utajua sasa".



    Niliupinda tena mguu.



    "Nani mtu wenu MWadui?"



    Kwa uchungu akajibu.



    "Watu wengi wa Mwadui wako kwenye orodha ya mshahara wa Pweke.



    "Niambie jina la mtu mmoja mkubwa ambaye naye yuko kwenye hiyo orodha.



    "Sikui".



    Nikaupinda tena mguu.



    "Aaa kweli sijui, Pweke ndiye anayewajua. Mimi ni mkubwa wa usalama wa kundi tu, sijui watu wanaoshughulika na wizi ila polisi wengi, afisa usalama na maafisa wengine wa juu nasikia pia wapo kwenye hiyo orodha".



    "Pweke ana wenzake Shinyanga, Arusha, Mwanza, Musoma, Nairobu na Kampala, wote wako saba, nipe majiba yao.



    Nikamuongezea maumivu. Hapo akaeleza.



    "Busy yuko hapa Mwanza, Jonston Mwita yuko Musoma, Mashaka Athuman yuko Arusha, Shinyanga sijui mwingine ila ni huyo huyo Pweke, Nairobi Samweli Gichuki, Kampala ni Tom Omandili na Dar es Salaam sijawahi kumuona lakini nasikia yupo."



    "Nani mzee?"



    "Kweli huyo simjui. Anayemjua katika kundi zima ni Pweke peke yake na hao wenzake hawamjua na wala hata hawajawahi kumuona.



    Nikaamini maneno yake.



    "Ulijuaje juu yangu na George?"



    Niliambiwa na Pweke">



    Kabla hajamaliza mlango ulisukumwa mimi nikaruka kando. Huyo jamaa aliyesukuma mlango akaachia risasi, zikamwingia Ole na kumuua. Mimi nikaachia risasi na kumuua vile vile. Nilipomwangalia George nikaona bado hajakata roho, nikarudisha mlango nikatelemka chini. Kufika mapokezi kijana wa mapokezi aliponiona nakuja akaanza kukimbia. Sikuwa na muda wa kuanza kumfuata ingawa ilionyesha kuwa hii Delux ilikuwa na uhusiano na haya majambazi. Nilipata teksi hapo nje ya Delux.



    "Posta haraka sana".



    "Shilingi kumi".



    "Wewe twende, pesa siyo shida".



    Aliondoa gari kwa kasi sana.



    "Mswahili bwana anaweza kuingia ndani ya gari kiofisa bila kuuliza nauli, ukimfikisha aendako na ukimwambia nauli anaanza kubishana tena", alieleza dereva wa teksi.



    "Inafuatana na mtu mwenyewe alivyo".



    Wakati ninajibu tukawa tunafika posta. Nilitoa shilingi ishirini nikampa.



    "Weka inayobaki".



    Alhamndulilahi. Mungu akusaidie", dereva alishukuru.





    Nilikimbia moja kwa moja mpaka kwenye simu, nikaweka senti hamsini.



    "Sekou Toure Hospitali! Nikusaidie nini?" Opereta alijibu.



    "Nipe daktari Makuyu".



    "Subiri".



    Daktari Makuyu alikuwa na mahusiano makubwa sana na idara yetu na aliletwa Mwanza kama daktari wa kawaida, lakini kiini hasa aliletwa kusaidia watu wa idara yetu, iwapo kuna matatizo na kuweza kutunza siri".



    "Daktari Makuyu hapa".



    "Gamba".



    "Lo! Habari zako nimezisikia".



    "Sawa, sasa fanya mbinu. George ana hali mbaya sana Delux Hoteli chumba nambari 132. Hali yake ni mbaya sana fanya haraka.



    "Vema".



    Akakata simu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wengi tulimpenda sana Makuyu kwa namna alivyokuwa anafanya kazi. Kazi kwake ilikuwa kazi, si mchezo.



    Nikapiga tena simu.



    "Polisi Stesheni hapa", niliitikiwa.



    "Nipe SSP Mwinyimkuu".



    Subiri.



    Nilingoja kidogo. baadaye sauti ikasikika.



    "Mwinyimkuu".



    "Ndani ya Mwanza Hoteli chumba nambari 230 kuna maiti na chumba nambari 132 Delux Hoteli kuna maiti vile vile. La kufanya utajua wewe mwenyewe. Pili mna mzigo humo uchukue ukae nao. Nitakupigia tena".



    "Wewe nani?"



    "Frend".



    Nikaweka simu kabla hajajibu.



    Nikazungusha nambari zingine za simu.



    "Mahfudh yupo?"



    Ndiyo".



    "Nipe niseme naye"



    Subiri.



    Pakawa kimya kwa muda.



    "Mahfudh hapa".



    "Gamba".



    "Lini uko huku?"



    "Siku mbili hivi. Nipe Dar es Salaam upesi iwezekanavyo".



    "Subiri".



    "Mahfudh naye alikuwa amewekwa maalumu hapa Mwanza kwa nyakati kama hizi.



    "Halo zungumza nao," Opereta aliniarifu.



    "Maselina hujambo?".



    "Nini wewe. Njoo upesi sisi huku tumekuota".



    "Nipe Chifu".



    "Subiri".



    Kisha nikasika sauti ya Chifu.



    "Lete ripoti Gamba?"



    "Watu wafuatao wawekwe chini ya ulinzi kwa usalama wa uchumi wa nchi hii. Jonston Mwita wa Musoma, Mashaka Athumani wa Arusha, Samweli Gichuki wa Nairobi na Tom Omandile wa Kampala. Watu hawa watafutwe wawekwe chini ya ulinzi mpaka baadaye. George yuko mahututi sijui kama atapona. Mtume Patrick sasa hivi kwa ndege mpaka Shinyanga halafu saa mbili jioni tuonane Maganzo".



    Nilimweleza na mengine yote kwa muhtasari.



    "Oke, nitamweleza Kamishna Mkuu wa Polisi ashughulikie habari hii. Nitaomba ndege ya serikali Patrick atakuwa Maganzo saa mbili".



    "Sawa, atanikuta Maswa Bar".



    "Oke, kwaheri"



    Akakata simu.



    Nilipomaliza kupiga simu nilijisikia mchovu na njaa iliniuma sana. Saa ilionyesha ni saa kumi na moja. Nilikuwa sina muda mrefu maana ilinibidi kwenda Maganzo nikamtafute Pweke ambaye ndiye aliyekuwa kiini cha kiunganisho cha wizi na ujambazi wote uliohusika na wizi wa almasi kutoka mwadui na kuuzwa kwa magendo Afrika Mashariki nzima. Niliingia kwenye mkahawa mmoja, nikanunua chakula cha kukaangwa na nikaomba wanifungie. Nilitafuta teksi ya kwenda Maganzo kwa haraka iwezekanavyo.



    "Mbona shati lako lina damu kidogo nyuma umejiumiza?" Dereva wa teksi aliniuliza.



    "Nashugulika na biashara ya nyama na huko nakwenda sehemu za Shinyanga kutafuta ng'ombe."



    "Kazi ya fedha nyingi hiyo, nasikia."



    "Wapi bwana, tunajaribu hivi hivi, tutafanya nini?"



    Tukaendelea kimya. Baadae nikafungua kimfuko changu. Nikaanza kula chakula changu. baada ya hapo nikasinzia kwani nilikuwa nimechoka sana. Hatimaye dereva akanitikisa, nikaamuka.



    "Halo, halo tumefika. Nilikwambia hii ni ndege, angalia sasa"



    Na kweli huyu kijana alikuwa ameendesha kwa kasi sana maana ilikuwa saa kumi na mbili na nusu.



    "Nipeleke Maswa bar".



    "Hiyo bar ina vipande kweli kweli vya watoto, ukicheza nao si ajabu pesa yako ya kununua ng'ombe ikaisha kabla ya kwenda mnadani kesho asubuhi."



    "Niko macho"



    Baada ya kufika Maswa Bar nilimlipa dereva haki yake.



    "Asanter sana. Sasa mimi narudi zangu Mwanza. Ukirudi nitafute tupige maji kidogo. Mimi kituo changu ni pale sokoni."

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Bila ya shaka"



    Niliingia ndani ya bar. Nikatafuta meza moja nikakaa.



    "Salama wewe bwana?"



    Niligeuka nikaona ni yule yule mwanamke aliyekuwa amenipatia chumba siku ya nyuma yake.



    "Salama Hujambo? Kwanza nipe ndovu baridi sana"



    "Huu ubaridi unatosha?"



    "Oooo sana tena."



    "Mbona Hukuonekana tena?"



    "Bwana we nilipata matatizo fuLani fuLani"



    Kitu kilichonishangaza ni kwamba, bar ilikuwa imejaa watu kama kawaida, kama kwamba hakuna kitu kigeni kilichotokea ndani ya bar hii. Hii inanihakikishia kwamba hakuna habari yoyote iliyotokeza nje.



    "Na leo unataka chumba?" niliulizwa na mpokea wageni.



    "Ndiyo"



    "Leo nafasi si kama za jana na juzi"



    "Chumba cha mtu mmoja naweza kupata?"



    "Ndiyo, bila ya wasiwasi, shilingi thelathini, nipe halafu nitakutafutia chumba chenye kitanda safi kabisa".



    "Nitashukuru sana"



    Nilitoa noti mbili za shilingi ishirini.



    "Zitakazobaki kunywa soda"



    "Asante sana" alijibu huku akiondoka kwenda kaunta.



    Nilikunywa bia yangu kwa utulivu kabisa. Nikafikilia mambo chungu nzima. Nilikata shauri nisifanye kitu chochote mpaka Patrick atakapofika maana hali ilivyokuwa sasa ilikuwa mbaya sana na kuikabili peke yangu ingeweza kuleta balaa. Hata hivyo nilihisi kwamba mpaka sasa nilikuwa nimefanikiwa kiasi kikubwa sana, maana nilikuwa nimeshapata fununu za ujambazi huu, kiasi kilichobaki ni kutafuta shina. Matawi ya ujambazi nilikuwa nimeanza kuyakata. Yalikuwa ni matawi machache makubwa makubwa pamoja na shina ndivyo vilivyokuwa vimebaki. Nilijua kuwa kuling'oa shina haikuwa kazi rahisi, kwa hivi ilibidi nipange mambo vizuri na ndiyo sababu ilinibidi nimngoje Patrick maana wawili ni wawili.



    "Njoo uone chumba chako aliniita huyo mama.



    "Ngoja nimalize bia yangu."



    "Twende nayo mimi nitakuchukulia"



    "Haya twende"



    Alinichukulia bia tukaelekea chumbani. Chumba kilikuwa kifinyu lakini kusema kweli kilikuwa na kitanda kizuri na kikubwa. Nilikagua dari nikaliona imara maana nilikataa mambo ya siku iliyopita yasinitokee tena.



    "Chumba hiki unakionaje?"



    "Safi sana"



    "Kitanda je?"



    "Safi kabisa"



    "Lakini kinafaa kuwa na mwenzi wa kuongea naye."



    "Bila shaka sina haja ya kwenda mbali ili mradi wewe upo. unasemaje?"



    "Aka babu, Mimi bwana wangu leo anakuja kunichukua. jana ndipo ungenipata maana alikuwa Mwanza lakini leo karudi".



    "Kwani huwezi kumkacha?"





    "Loo, nimkache shauri yako! Waswahii husema usiache mbachao kwa mswala upitao. Yule bwana ananifaa. Ananilipia kodi ya nyumba, ananunua chakula na analipa maziwa ya mtoto. Leo nikimkacha kwa kukufuata wewe, utanipa tuseme shilingi ishirini, hata mia, halafu kesho asubuhi huyo unakwenda zako. Nani atanilipia kodi ya nyumba, maana bwana wangu atakuwa naye kisha nikacha"



    "Sawa bibi umeshinda. Nitapata wasio na wao"



    "Bila ya shaka utapata, kijana nadhifu kama wewe utakosaje?



    Ulipoingia tu kwenye baa kila mwanmamke mle ndani alikuwa anakukodolea macho. Unafikiri asingekuwa huyu mlipa kodi ningekuachia? Ng'oo".



    "Naenda kukoga".

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Haya, utanikuta ndani ya baa".



    Ilikuwa yapata saa moja nilipomaliza kukoga. Shati langu nililifua hapo penye damu, halafu nikapakausha kwa kupanyonga na taulo nikalivaa. Sasa nilikuwa najisikia vizuri zaidi baada ya kukoga. Nikakata shauri kwenda baa nikamsubiri Patrick.



    Nilipoingia ndani ya baa moyo wangu ulishituka kidogo. Nilipotazama huku na huku nilimuona yule msichana ambaye nilikuwa nimemuona Mwanza Hoteli mchana. Alikuwa amekaa peke yake akinywa. Alinitazama na macho yetu yakapambana akainamisha kichwa. Alikuwa msichana mzuri nikakata shauri kumsogelea.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog