Simulizi : Siku Ya Graduation
Sehemu Ya Tatu (3)
Nikaiona Bunduki ikiwa pale pale kwenye kiti kilichopo mbele ya kitanda, nikaisogelea nikitaka kuichukuwa, akili ikakataam nikaiacha. Nikasogea mbele tena kwenye suruali yake ya jinzi aliyokuwa kaitundika kwenye msumari ukutani, nilipoigeuza upande wa pili nikaiona Bastola yake, hii sikutaka kuiacha nikaichukuwa haraka kisha nikaenda mpaka pale kitandani nikaingia chini ya kitanda, uvunguni.
kitendo cha kama sekunde kadhaa nikwasikia wakija na hatimaye wakaingi
"Funga mlango vizuri, unatakiwa kuwa makini usipende kulala bila ya kufunga mlango" Sauti ya Baunsa Ikimwambia Ntahondi. nikiwa bado chini ya uvungu wa kitanda niliiona miguu ya Baunsa ikienda mpaka usawa wa kile kiti kilichotundikwa bunduki, halafu nikaiona ile bunduki ikiwa inaning’inia usawa wa miguu yake, nikawa naomba dua zangu zote ili asiende kule alikotundika suruali yake maana angekuta hakuna Bastola yake haipo mtanange ungeanza mapema. Nikawa sasa naiona miguu ya Ntahondi ikiwa inatoka usawa wa mlangoni akarudi mpaka pale kitandani akapanda kisha akakohoa tena kwa nguvu nadhani hakujuwa kama tayari nipo ndani hivyo ilikuwa ni ishara tena ya kuniita,
nikaendelea kutulia, nikaiona sasa miguu myembamba ya Baunsa ikija mpaka kitandani naye akapanda kitandani kisha baada ya mazungumzo yao ya hapa na pale nikasikia sasa sauti za mahaba hasahasa kutoka kwa kidume.. Nikaanza kutambaa taratibu kwa Tumbo mpaka mwisho wa kitanda wakati huo nikiwa tayari nimeshaikoki Bastola, kidole cha shahada kikiwa makini kwenye kifyatulio (trigger) kwa ajili ya kufyatua risasi muda wowote.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mwanga wa chumbani ulikuwa ni hafifu mno hivyo ilikuwa ni hali nzuri kwangu kuzidi kujiamini, sasa nikatambaa tena mpaka mbele ya kitanda,nikafanya dua zangu zote kwa Mungu anipe nguvu na ujasiri wa kupambana kisha nikasimama ghafla ili nilianzishe sekeseke.. niliposimama tu jamaa akashtuka, akamwacha mwanamke, akaruka kutoka kitandani na kunirukia kwa kasi ya umeme, nikamkwepa na kumtandika teke kali lililombwaga chini, akajizoazoa na kuinuka, nikamkandamiza tena na teke kali la mbavu. Hapo sasa mpambano ukakolea, akiwa pale chini sakafuniakajibetua na kunitandika ngwara iliyonipeleka mpaka chini almanusra nivunje mkono, bahati nzuri bastolahaikunitoka mkononi. Nikajiweka sawa nikaona sina sababu ya kuuchelewesha mchezo, nikafyatua Risasi moja lakini ikamkosa. jamaa alikuwa ni mwepesi wa viungo kuliko hata nilivyotegemea, akarukia upande wa nyuma wa kitanda, nikamrushia tena risasi ya pili nayo ikamkosa, hapo sasa hali ya tafrani ilizidi kupamba mle chumbani, sasa nikawa naogopa kufyatua Risasi hovyo nikihofia kumdhuru Ntahondi ambayye nae alikuwa kitandani hapo, niikaanza kuhaha sasa maana nilijuwa ndani ya Bastola ile hapakuwa na Risasi zaidi ya tano. Hivyo kama nitazimaliza bila ya kumtandika itakuwa balaa
Ghafla nikasikia mlango wa chumbani umepigwa kwa nguvu kutokea nje, akaingia jamaa mwingine nilipogeuka kumuangalia ni nani hiyo nd’o ilikua mistake ya kwanza Baunsa alinirukia na kunipiga ngumi ya kichwa nikaenda mpaka chini, Bistola ikaniponyoka ikarukia kitandani.. nikaanza kazi mpya na ngumu ya mchezo wa ngumi na watu wawili, hali ya mwanga hafifu mle ndani ikanisaidia kidogo maana baunsa alikuwa anapiga mapigo hovyohovyo kama chizi mpaka anampiga Yule jamaa aliyeingia ambaye baadaye nilimtambuwa kuwa ni Yule mlinzi wagetini.
Mpambano ulichukuwa takribani dakika sita ndipo nilipohamia upande wa pili karibu na kitanda na haraka Ntahondi akaiwahi ile Bastola akanirushia, nilipoishika tu nikamuelekezea yule Mlinzi
"WEKA SILAHA CHINI.. CHINI HARAKA," nilifoka huku nikiwa nimemkazia macho kama nyoka, wakati huo Ntahondi alikuwa analia akiwa amesimama upande wa kiti kile chenye Bunduki, yule Mlinzi akawa bado ameshikilia vyema Bunduki yake, hataki kuiachia.. hapohapo sikumkawiza nikamdungua Risasi akaanguka chini hukuakitapatapa na akupiga kelele kali za maumivu nikadhani nimeshamuuwa kumbe sivyo. Risasi ilimpata karibu ya kifuani chake kwa juu kidogo upande wa bega la kulia.
Nkamgeukia Baunsa na kumfyatulia Risasi, LooSalale! Risasi zilikuwa zimekwisha.. Baunsa akaligundua hilo sasa ikawa kizaazaa kipya mle ndani wote macho yetu yako kwenye Bunduki ya huyu Mlinzi anayegaragara kwa maumivu ya risasi!
Ngumi zikaanza tena kwa kasi ya ajabu, kiukweli jamaa alikuwa akinizidia nguvu sana tu tatizo alikuwa kahamaki hivyo nikawa naitumia hiyo fursa kumpa mapigo ya kumshtukiza, silaha kubwailikuwa ni ngumi na mateke.. ilipotokea tumeshikana basi vichwa namno vilihusika pia. nikiwa nagalagazana naye pale sakafuni wakati huo huyu mlinzi akiendelea kulia kwa maumivu makali ya Risasi, baunsa alinizidia nguvu,akaniweka chini huku yeye akiwa juu.. akaanza kunipa makonde ya kichwa mpaka nikataka kupoteza fahamu. Kila nilivyojaribu kujinasua pale chini ilikuwa ni kazi bure, hakika jamaa alinibana, kuona hali ile Ntahondi akaja kwa kasi ya ajabu akiwa amenyanyua kiti kidogo cha chuma kilichokuwa mle chumbani na kumpiga nacho baunsa kichwani, nilimsikia akitoa mlio mkali wa maumivu kisha akaenda mpaka chini na kuanza kukoroma kama anayekata roho. Alitengana na fahamu zake
Ahsante Ntahondi, mwanamke shujaa!
Nikanyanyuka haraka na kujifuta damu zilizokuwa zikinitoka puani na maeneo ya kisogoni. nilikuwa nimepasuka baada kuanguka pale chini wakati ninakikirishana na bazazi Yule aliyesalitiwa na fahamu zake kufuatia pigo takatifu kutoka kwa mwanamke,
Hatukuwa na muda wa kupoteza tena, haraharaka tukachukuwa Bunduki zote mbili ile ya Mlinzi na ile ya baunsa iliyokuwa kwenye kiti kisha tukatoka haraka mle ndani. tukaenda mpaka Getini hapakuwa na mtu, tukafungua geti kisha tukatoka nje tukiwa hatuamini kama tumesalimika.
Tukaanza kukimbia hovyo tusijuwe tuelekeako, ni kama kuku aliyekatwa kichwa! hatukujuwa tuko wapi na tunakwenda wapi, hatukujuwa ni mkoa gani wala wilaya gani ndani ya Tanzania yenye mapori ya kutisha kama yale ukizingatia giza nene lililotanda usiku ule nd’o kabisa hatukujitambua
Sasa tunakwenda wapi? Nilijiuliza
Hatukukata tama kwa kuuogopa msitu ule ukizingatia tulichotoka kupambana nacho ni zaidi yam situ, tuliamini Mungu yu pamoja nasi, tukaendelea kukimbia kwa kwenda mbele tu.
Tulikimbia umbali mrefu sanahuku miguni tukiwa peku. majani magumu almaarufu kama Magugu yalituchanachana miguu, ikafika mahali Ntahondi akawa analia kwa maumivu huku akilalama kuwa pumzi zimemuishia hivyo asingeweza kuendelea kukimbia, nilimbembeleza kwa kumpa matumaini lakini akagoma kabisa kukimbia, Hakika alichoka sana! miguuni alikuwa akivuja damu zilizotakona na kuchomwa na visiki vikavu vya miti mle Msituni… mbaya zaidi hakukuwa na dalili hata ya Nyumba moja licha ya umbali mrefu tuliokimbi, niliendelea kumbembeleza ajikaze ili tuendelee na safari lakini ilishindikana, binti alikuwa hajiwezi,
Sasa tutafanyaje? Kama wale mabazazi watawasiliana na wenzao na kupewa msaada wanaweza kutukimbilia na kutupata, nguvu bado nilikuwa nazo lakini nisingeweza kumkimbia Ntahondi porini. Ni lazima tuondoke, lazima tukimbieCHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nikasimama, nikajifunga vizuri nguo zangu. Nikamnyanyua Ntahondi na kumbeba mgongoni. safari ikaendelea! Nilitembea kwa taabu, hofu na mashaka huku mara kadhaa nikijikwaa kwenye visiki na kuanguka.. Ntahondi alionekana kunihurumia sana lakini hakuwa na hali kabisa
Niliendelea kutembea kwa shida bila ya dalili za harufu ya msaada, mara kwa mara tulikuwa tukipumzika njiani na kuendelea na safari ndefu isiyojulika mwisho wake, Hatimaye Ntahondi akapata tena nguvu tukaanza tena kukimbia kuelekea kusikojulikana
Tuliendelea kukimbia mpaka tukafika sehemu Fulani iliyokuwa na kama mfano wa majaruba ya mpunga, hatukuweza kutambua vizuri kutokana na giza lile lililofunika anga, tukajipa moyo kuwa tunaanza kukaribia makazi ya watu, na kweli punde tukaanza kuona sasa kwa mbali vitu mfano wa nyumba, ilikuwa ni ishara nzuri kuwa tumefika kwenye makazi ya watu japo hapakwu mjini, hatukujali siye tulichokuwa tukikililia ni msaada tu kutoka kwa raia wema,
Tukayafikia maeneo yale,zilikuwa ni nyumba ndogondogo zilizoezekwa kwa nyasi, palikuwa kimya sana bila shaka watu walikua wamelala, kwa kukadiria ilikuwa ni mida ya saa tisa za usiku, tulijaribu kujadiliana kama tuwagongee wenyeji kisha wakitufungulia nd’o tujielezee kwao na kuomba msaada, tukajadiliana sana mwishowe tukakubaliana kuwa tusiwaamshe tukihofia kuwa wasingweza kumfungulia mtu wasiyemjua na hiyo pengine ingeleta madhara kwetu maana tungepigiwa hata kelele za wizi.
Tukaenda mpaka pembeni kidogo ambapo palikuwa na kibanda ambacho hakikuwa na milango, tukaingia! ilikuwa ni kama sehemu wanayoitumia kwa kupikia maana kulikuwa na majiko tu ya kienyeji yaliyofinyangwa kwa udongo pamoja na viroba kama vitano hivi vyenye mabunzi ya mahindi, tukakubaliana kuwa tulale mle jikoni mpaka asubuhi kisha wenyeji wakiamka tutawafuata na kuwaeleza tatizo letu, Hilo likapita!
Kila tulipojaribu kulala, usingizi haukupita kabisa pengine kutokana na woga tuliokuwa nao ukichagizwa na m’bu wengi waliokuwa wakifumuka kutokea kule kwenye ile mifuko ya mabunzi, walitushambulia kisawasawa!
Muda ulizidi kuyoyoma huku baridi kali ilikitupuliza, baada kama ya nusu saa hivi tukiwa mle jikoni tulisikia mlio wa pikipiki zikija kwa kasi, tukainuka na kusikiliza milio ile ilikuwa ikielekea wapi! baada ya dakika kadhaa tulikubaliana sote kua ni pikipiki na zilikuwa zikija kule tulipo.
Ni akina nani hao huku porini na pikipiki mida kama hii? Hakuna jibu
Tukataka tutoke nje na tuendelee kukimbia lakini haikuwa rahisi maana lazima tungeonekana tu, nikamshauri Ntahondi kuwa inabidi tujifiche mlemlejikoni, tuingie ndani ya ile mifuk yenye mabunzi ya mahindi tujifiche, akakubali, nikamshika mkono mpaka kwenye ile mifuko nikapuguza baadhi ya mabunzi kisha nikampakia katika kiroba kimoja huku kwa juu nikimfunika nay ale mabunzi niliyoyapunguza kisha nikakiegesha vizuri, nikamsisitiza atulie! Nami nikafanya vivyohivyo, nikakitwaa kiroba kingine kilichokuwa nyuma ya jiko la kupikia nikajipakia na kutulia, wakati huo sauti zile za pikipiki zilizidi kuja maeneo yale.. nilikuwa nikijutamajuto ya firauni. Baada ya miungurumo mikali ya pikipiki hatimaye nikasikia zikisimama maeneo yale ya kijijini
Nikasikia Sauti za watu wakiongea kwa kufokezana, sikujuwa ni kina nanii! Mara moyo wangu ulipiga sarakasi baada ya kusikia sauti niliyoifahamu fika ikifoka nje
"FUNGUA HARAKA KABLA SIJAKITIA MOTO HIKI KIBANDA CHA KUOSHEA MAITI," ilisikika ile sauti naikaendelea “…Fungua we mjumbe, hausikii?”ilikuwa ni sauti ya Yule Baunsa, nikapoteza kabisa matumaini huku nafasi yake ikichukuliwa na hofu pamoja na uwoga,
Nadhani huyo mjumbe aliyekuwaakiamriwa kufunguwa mlango alitii, maana kelele zilikoma n badala yake kukawa na mazungumzo ya kina, sikuweza kuyasikia sana ila niling’amua tu baadhi kuwa walikuwa wakitusaka. Punde nikaanza kuona mwanga wa tochi mkali ukifuatiwa na sauti za nyayo za watu wakija kule jikoni
"..Ni majambazi watatu, mmoja akiwa ni mwanamke wametuvamia kule kwenye godauni letu la nafaka.. wamemuua mlinzi wetu na mimi wamenijeruhi sana si unaona! Embu ona na huku.. tazama damu zote hizi, kama wamefika huku wakawalaghai mkawahifadhi naomba muwataje, Laa sivyo mtajutaw." Ilikua ni sauti ya yule Baunsa, sauti iliyojawa na munkar na ghdhabu, hatimaye wakaingia kule Jikoni
"Hii mifuko ni ya nini?" Aliuliza baunsa,
"Ni mabunzi tu ya mahindi.. huwa tukishayapukuchuwa nd’o tunayaweka humo kwa ajili ya kukokea moto." Nilikuwa kama niliyegandishwa kwenye friji
"Zungu hebu pekuwa humo kwenye hiyo mifuko kama hakuna kitu twende tukakaguwe na huko wanakolala."
Toba!
mwanga mkali wa tochi uliendelea kumulika ndani chumba hiki cha wazi, kisha nikasikia mlio wa mifuko ile ya Sandarusi ikitaabishwa, nikaanza kulia moyoni nikijuwa sasa tunakamatwa tena.
“Mwaga kiroba kimoja baada ya kingine, FASTAA.” Baunsa aliamuru
‘Eeh Mungu tusitiri waja wako dhaifu sisi, hakuna likushindalo wewe, tutendee miujiza, hakika wewe waweza kubadilisha jambo lolote kwa neno tu..’ Nilikuwa nikiomba kimya kimya
*******CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Niliendelea kuomba huku nikitetemeka kwa hofu, nilijuta hata kwanini tulikimbia bila ya kuhakikisha tumem 'shoot'.. ilikuwa ni hamaki tu..
Baunsa aliendelea kuongea kwa sauti ya Ukali huku nikiisikia Sauti yake sasa ikija usawa wangu. nilizidi kuingiwa na hofu lakini nilijikaza kisabuni,
"…Majambazi wanatoka mjini huko wanakuja kuuwa watu halafu wanakimbilia huku mnawaficha, na ninyi dawa yenu iko jikoni," Aliongea baunsa “..Na hakyamungu tukiwapata humu kwenu nitwakaanga kama bisi.”
“Jamani sisi hatuwezi kumficha mhalifu hata siku moja.. na kwanini hasa tufanye hivyo? Hakuna mtu humu mwetu.” Sauti ya mtu mmoja aliyeonekana na mtu mzima ililalama kujitetea kwa baunsa.. sasa nikasikia sauti ya mifuko ile ya viroba vya kule mbele ikitaabishwa kwa kupigwa, bila shaka na mateke katika kuhakiki.. wakati huo mwanga mkali wa tochi ukizidi kumulika usawa wangu.. sambamba na sauti za nyayo zao zikija upande ule na kukomea pale nilipo
Nikamsikia Baunsa akimwambia kijana aliyekuwa akivikaguwa vile voroba kuwa aachane navyo, havina watu! Kisha akamwamuru mjumbe kuwa waende wakakague na kule vyumbani mwao wanakolala,
“Lazimawapatikane usiku huuhuu.” Wakatoka nje
hali ya giza ikarejea, nilishusha Pumzi kwa nguvu, nikamshukuru Mungu japokuwa hali ilikuwa bado tete. nilikuwa nikimfikiria Ntahondi hali aliyokuwa nayo mle kwenye Kiroba alichojikunja kama mnyoo wa Amiba.
Sikujuwa huko walikokwenda walikwenda kumkagua nani! au kama waliwakagua wanakijiji wote kwa kua hawakuwa wengi sana, tuliendelea kutulia mle kwenye viroba mpaka baadaye kabisa tukasikia sauti za pikipiki zikiondoka tena kwa kasi,
baada ya dakika kama 20 nikatoka ndani ya kiroba change kisha nikaenda kumtoa na Ntahondi, tukajifuta vumbi lililokuwa kwenye viroba vile, vumbi ambalo kwa kiasi kikubwa lilikuwa tayari limeganda mwilini kutokana na damu zilizokuwa zikituvuja. Tukawa tunajadiliana tutajiokoa vipi maana sasa Wanakijiji wameshaambiwa kuwa sisi ni Majambazi na tulikuwa na Bunduki moja ambayo nayo tumeificha nyuma ya jiko hilohilo, ile bunduki nyingine bila shaka tuliiangusha njiani wakati tunakuja huku na bila shaka waliiona njiani nd’omaana wakaamua kutufuatilia maeneo ya kule huku wakiwa na hakika kabisa ya kutupata. tukafikia muafaka wa kusubiri kwanza kupambazuke ili asubuhi tujitokeze tuwaeleze ukweli tu hawa wazee wa kijijini pengine watatuelewa, japo swali kubwa tulilobaki nalo itakuwaje endapo watashindwa kutuelewa na kutuchukulia kuwa ni majambazi?
Hakuna ajuaye!
Tuliendelea kukaa mle jikoni muda mrefu tu sana. baadaye hali ikaanza kubadilika na kuwa ang'avu ikiwa ni ishara tosha kulikuwa kunaanza kupambavuka, nilipochungulia nje niliwaona wazee wawili wakionekana kujadili vitu kwa umakini mkubwa, nikamrudia Ntahondi “..Acha mimi niwawahi hawa wazee nikajaribu kujieleza kabla hapajakucha na hawajajua lolote.” Ntahondi alionekana kukosa imani kabisa na hawa wana kijiji kwakuwa wanaonesha kuingiwa na hofu ya mikwara waliyopigwa na Baunsa, Lakini ikawa haina budi tuongee nao tu ili tupatemsaada. nikamuambia Ntahondi yeye atulie tu pale pale asitoke. Nikatoka mle ndani nikiwa hoi kwa mchoko, nikaanza kuwaelekea waliko wazee wale wawili mmoja akiwa ni kitu kirefu mkononi kama vile Jambia, mwingine akiwa amejifunga shuka iliyokatiza upande mmoja wa Bega lake la kulia, Lubega!
Wazee waliposikia sauti za nyayo zangu wote waligeuka kuangalia upande ule ninaotokeahuku nikichechemea kwa maumivu. Mzee mmoja akanisemesha kwa lugha ambayo sikuielewa.. sikujuwa sasa nijubu vipi, mzee Yule akarudia tena kunisemesha kwa lugha ileile.. nikapata wazo, nikawanyooshea mikono yangu miwili kuashiria amani.
"Usiku..?" mzee mwingine alitamka neno hilo ambalo nililielewa vema, Mara nyingi vijijini ukikutana na mtu mida ya usiku na ukamtilia shaka unamuuliza 'usiku' akikujibu 'mchana' ujue anamaana ya Amani na akikujibu tofauti inaashiria hatari. hima nikamjibu "Mchana!"
Nikawaona wazee azee wale wakijiweka tayari kukabiliana na mimi, nikaendelea kuwasogelea huku mikono yangu ikiwa vilevilejuu. nilipofika karibu yao wakanistopisha, nikasimama! kisha wakanihoji kwa lugha ile ambayo sikuielewa kabisa,
"Siijui lugha hiyo," nikajibu
Yule mzee aliyejifunika shuka akanihoji sasa kwa Kiswahili
"We ni nani na unatokea wapi saa hizi?"
"Naitwa Naufal.. nina matatizo makubwa sana wazee wangu naomba mnisikilize" wote wakawa makini kunisikiliza "…Mimi niko na mwenzangu tulikuwa tumetekwa na majambazi karibu mwezi mzima chini ya himaya yao, wametutesa naktudhalilisha sana.. hatimaye usiku wa kuamkia leo tukapambana nao na kufanikiwa kuwatoroka. Tukakimbia sana ndipo tukajikuta tumetokea huku.." kabla sijamaliza kuongea yule mzee mwingine akaniwahi "..Anhaa kumbe nyie nd’o mliovamia kule kwenye Godauni la nafaka.. mmeuwa mtu huko mkakimbila huku kuja kutuletea matatizo sio?"
"Hapana wazee sisi sio wizi sisi ni raia wema kabisa tunatoka Dar es Salaam.. nikweli tulitekwa, na hata hapa sipajui ni wapi."
"huyo mwenzio yuko wapi?"
"Yuko humo ndani." nikawasontea kwa kidole kwenye lile jiko tulikokuwa tumejificha.. tukiwa tunaendelea na mahojiano Yule mzee aliyejifunga shuka akaondoka hadi upande wetu wa kulia ambako kuna nyumba zao ndogondogo, nikamsikia akiwaita watu kwa majina.. baada ya muda mfupi akarejeana kundi la vijana kama sita hivi. Walipofika hawakutaka kunisikiliza kabisa zaidi ya shutuma tu juu
"Hawa ni wezi tu.. wanatoka huko mjini na kuja kufanya uhalifu huku, wafungeni kamba tuwapeleke hukohuko Godauni walikokwenda kuvunja," aliongea kijana mmoja kati ya wale walioamshwa kule vyumbani, alionekana kuungwa mkono na wenziye,
Mwingine akakataa na kusema"Tusipoteze muda wa kuhangaika na hawa watu.. tuwachome moto tu huko shambani kisha tutawafukia hukohuko." Naye alipata walio msapoti kwa rai yake hiyo. Rai zote zikawa mbaya kwangu si kuchomwamoto wala kurejeshwa kwenye mikono ya maharamia! Nilizidi kuchanganyikiwa, wana kijiji waligoma kabisa kunisikiliza. Mara kijana mmoja akanisogelea na kunipiga sasa makofi huku akinitaka nikae chini, nikaa! kisha akaongea kwa lugha yao nisiyoifahamu, nilishuhudia kijana huyo akielekezwa kitu huku akioneshewakule jikoni, akaendakisha muda mfupi akatoka akiwa amemshika Ntahondi huku akimburuta kwa kasi. Alipomfikisha pale naye wakamshambulia kwa kichapo cha makofi kisha wakamkalisha chini pale karibu yangu,
Tukawa kama wizi kweli tuliokamatwa. wakati huo hawa wanakijiji wakibishana juu ya nini cha kufanya kufuatia rai zilizotolewa moja ni kutuchoma moto na nyingine kuturudisha kule Godauni kwa wale maharamia wa Pablo, nilikuwa nikilia huku nikijaribu kujieleza lakini hawakunielewa kabisa. wakati wakiendelea kubishana kwa fujo kuna kijana mmoja yeye akaja na kamba ngumu za katani kna kuanza kutufunga mikono kwa nyuma ya mgongo, wakatufunga na miguu, Ntahondi naye alijaribu kujitetea huku akilia kwa uchungu, haikufaa kitu!CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya majadiliano ya muda mrefu akaja Mzee mwingine hivi mwenye mvi nyingi kichwani na kwenye nyusi zake, alipofika wote wakamsogelea na kumsalimia kwa heshima sana. Inaonekana ni mzee mwenye cheo fulani pale kijijini,
"Shikamoo Mzee Ngozi." aliamkiwa na kila kijana pale kisha wakaanza kumfahamisha hali ilivyo
"Hawa nd’o wale majambazi walioenda kuvamia na kuuwa kule Godauni, sasa tulikuwa tunafikiri tu kuwapeleka kulekule walikoiba." Yule mzee akamuangalia sana Yule bwana vijana aliyekua akimpa maelezo
"Hivi una akili Timamu wew?” alifoka Mzee Ngozi, Kimya kikapita akawageukamawale wengine “Ninyi.. mna mna akili timamu? Mna uhakika gani kama hawa ni majambazi kweli? Mnakijuwa walichokiiba?" Alifoka mzee Yule huku akiwaangalia kila mmoja usoni, akaendelea “Majambazi gani wameuia kiasi hiki! na hata kama watakuwa ni majambazi kweli sasa huko mnakowapeleka ndiyo mahakamani? Ikitokea wakauawa huko halafu ikafahamika kuwa ninyi nd’o mliwapeleka kule hamwoni kuwa mtaingizwa hatiani?” Yaani nilitamani nimbebe huyu mzee furaha. kundi zima likawa kimya kabisa, hakuna aliyenyanyua kinywa chake. yule Mzee aliyekua kajifunika shuka alijaribu kumuelewesha Mzee Ngozi kwa maneno ya ushawishi lakini ilikuwa ni kazi bure, Mzee Ngozi alizidi kuwapinga kwa hoja za msingi kutokana na kila walichomueleza.
Baada ya majadiliano marefu wakafikia muafaka kuwa wapige simu Polisi watoe taarifa, Rai ya kuchomwa moto na ile ya kuturejesha kule kwenye hilo godauni ambalo wao wanaamini ni la kuhifadhia nafaka vikafa!
"Simu yangu mimi haina charge karibu wiki nzima sasa.. labda mwende hapo kwa Mzee Banzi mkamwambie namwita hapa aje na simu yake sasa hivi." Alitoa agizo mzee Ngozi, hakika likuwa ni kama Mkombozi wa maisha yetu kwa sasa,
"Wafungueni haraka hizi kamba.. mbona hamna huruma ninyi watu! angalia huyo binti mpaka mikono imeanza kuvimba jinsi mlivyomfunga hizo kamba. na nyinyi wazee wenzangu mnakosa hekma kiasi hiki kweli?" Hakuna majibu, ikawa ni hekaheka ya kutii kila amri iliyotolewa na Mzee Yule
Wakati wanatufungua kamba yule kijana alietumwa naye akawa ameshawasili akiwa na Mzee mwingine wa makamu bila shaka ndiye Mzee Banzi huyo, alipofika baada ya salamu naye akasimuliwa kila kitu kasha akaanza kuzungumza kwa ukali
"Hili suala limeanza kunishtua sasa unajua kwa maelezo yenu haya kuna kitu kimetuwama kichwani mwangu." Akatuangalia kwa muda kabla hajaendelea "..Unajua juzi alikuja mwanangu kutoka mjini japo hakukaa sana ila katika mazungumzo akaniambia kuwa huko mjini kuna kijana ameuawa, halafu kuna wengine wawili wamepotea katika mazingira ya kutatanisha na kwamba inasemekana wametekwa.. alinitajia mpaka jina la huyo Binti aliyetekwa sema tu nimelisahau. sasa isije ikawa watu wenyewe nd’o hawa!" kauli hii liwashtua wote pale, wakaangaliana kwa hofu sasa kisha Mzee Ngozi alikuwa akitikisa kichwa kuashiria kumwunga mkono mzee mwenziye "…Ngoja tumpigie simu Mwanagu atutajie jina la huyo binti aliytekwa kisha tutajuwa tu na hata kama sio huyu pia tutamtuma haraka aende kituo cha polisi akatoe taarifa kisha aje nao hao polisi mpaka hapa wawachukue ili haki ikatendeke." Akamaliza,kisha akatoa simu na kumpigia huyo mwanaye. Sote tukawa kimya kusikiliza majibu yatakayotoka ndani ya simu
"Hallow, hebu nipigie haraka Baba simu yangu haina salio," aliongea Mzee Banzi akimtaka mwanaye ampigie. Wakati tunasubiri huyo mwanaye apige simu, ndipo Mzee Ngozi akawahi kumuuliza Ntahondi
"Unaitwa nani Binti?" Nilijua lengo lilikuwa ni kumjuwa mapema kamandiye yeye ili afananishe majibu watakayopewa na huyu mtoto wao ambaye bado hatujamjua ni nani na Je ana tujua sisi au Laa,
"Naitwa Ntahondi."
Mara simu ya Mzee Banzi ikaita tena, sote tukawa kimya tukisubiri ipokelewe,
*****
"Hallow hujambo?"
"Sijambo, Shikamoo mzee.."
"Marhaba."
"Kuna nini Baba mbona asubuhi namna hii, kuna usalama kweli?"
"Usalama upo.. Hebu kwanza niambie yule Binti aliyetekwa huko mjini anaitwa nani vile?" Wote tulikuwa tumetega masikio kwenye simu ya Nokia ya Tochi, kwakuwa ilikuwa imewekwa Loud Speaker tuliyanasa mazungumzo yao kisawasawa
"Anaitwa Ntahondi, kwani kuna nini Baba?" Wote tukaangaliana usoni. Mzee Ngozi alimwangalia kwa ghadhabu yule kijana aliyekua anampa maelekezo kuwa wanataka kuturejesha kule godauni. Mzee Banzi aliendelea kuongea na simu na huyo mwanaye
"..Sasa sikia, huyo Ntahondi tuko naye hapa kijijini muda huu. ameumizwa sana na yuko na kijana mwingine hivi naye anaonekana kuumia sana maeneo ya kichwani, sasa fanya hima baba kachukuwe Polisi uje nao huku kijijini haraka."
"Baba mbona kama sikuelewi? una uhakika ni Ntahondi? na we umemjuaje?"
"Sasa hutaki? hebu ongea naye huyu hapa." Mzee Banzi akampa simu Ntahondi , nilitamani niidake miye ile simu ili nijaribu kutumia akili ya ziada kumshawishi huyo kijana ili asiende Polisi na badala yake nijaribu kumpa utaratibu wa kuwapata ndugu zetu kwanza maana nilikuwa najuwa Pablo ana nguvu sana ya pesa hivyo atakuwa kaishawanunua askari wengi tu ambao wanaoweza kutugeuka na kutupoteza kabisa ili kuficha ushahidiCHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Hallow.." Aliongea Ntahondi
"Enhee Ntahondi?"
"Ndiyo mimi, we ni nani?"
"Miye ni Oscar mlinzi hapa chuoni kwenu IFM,, Pole sana na matatizo, imekuaje sasa mpaka uko hapo?"
"Ahsante nimekufahamu, hatuwezi kuongea mengi kwa sasa ila tuko hapa kijijini kwenu tumefika baada ya kuwatoroka wale waliotuteka, naomba umfuate haraka Mwalimu Honde umpe hii habari, umwambiye atupigie simu tumpe maelekezo ya kwenda kutoa Polisi.."
“Okay poa.” Simu ikakatwa,hakika Ntahondi ni mwanamke wa aina ya kipekee maana kila hatua ananikonga nafsi. Kikapita kimya kilichofuatiwa na malumbano ya hapa na pale.
Wazee wale wakatuambia tuinuke pale chini tulipokuwa tumekalishwa kisha wakaanza kujadili kwa hofu kubwa juu ya hili tukio, Mzee Ngozi alizidi kuonekana na hekma sana mbele ya hawa wana kijiji wenziye. wakatuchukua mpaka katika nyumba iliyokuwa imejitenga mbele kidogo ya kichuguu kikubwa kilichonekana kwenda juu mpaka kuizidi urefu nyumba ile. tulipokuwa mle ndani tulijaribu kuwasimulia japo kwa mukhtasari tu mkasa huu uliotukumba, ilikuwa ni simulizi ambayo ingeweza kumkuna yeyote, Wale walionesha kuguswa sana na habari ile.
Simu ya Mzee Banzi ikaita tena tukiwa tumeshamaliza mazungumzo, akapokea
"Hallow.."
"Eeh baba, sasa tunakuja huko muda si mrefu ila msimwambie mtu yeyote hii habari kwani nasikia huyo aliyewateka ana pesa na anajuana askari wengi sana hivyo isije ikawaletea tabu hapo."
"Hakuna mtu ajuaye zaidi yetu sisi na wewe huko mjini."
"Haya hebu mpe simu huyo dada.." Mzee akamsogelea Ntahondi na kumpa simu
"Ntahondi are you oky?" ilikuwa ni Sauti ya Mwalimu Honde sasa. maskini Ntahondi akashindwa kujikaza baada ya kumsikia mwalimu wake na kuanza kulia
"NO Ntahondi Usilie sasa, tuko njiani tunakuja huko, uko na nani?"
"Niko na Naufal."
"Wewe?!are you sure?" Inaonesha Mwl Honde hakutegemea kabisa kusikia jambo lile, kabla Ntahondi hajajibu tena simu ikakatika, kuangalia hivi ilikuwa imeishiwa charge, hatukusikitika sana kwani tulikuwa tunajua sasa tuko katika mikono salama walau kwa kiasi Fulani
Tuliendelea kukaa pale kwa muda mrefu, ndhani ilikuwa ni saa nne asubuhi, kutokana na Jua lilivyokuwa likizidi kuchomoza. Punde tukaanza kusikia sauti ya gari ikija, Ntahondi masikini akasimama na kutaka kujificha akijuwa pengine ni wale mabedui wa Pablo Mwaki wanarudi tena, tulipochungulia nje tuliona gari aina ya kama ya Range Rover ikiwa imeegeshwa nje ya nyumba iliyokuwa mbali kidogo na pale tulipo, kisha wakashuka vijana watatu, wote wakiwa na Bunduki tuliamini kuwa ni askari japo walikuwa wamevalia kiraia, mara wakashuka tena wengine wawili kwa upande wa pili. nilipowaangalia vizuri niliwajua alikuwa ni Mwl Honde, na Oscar Mlinzi wa pale chuoni kwa kina Ramla na Ntahondi ambaye pia ni Mtoto wa Mzee Banzi.
Nikamsikia Mzee Banzi akimwambia Mzee Ngozi "Itakuwa wanajua tuko kule kwangu."
"Haya basi tuwasogelee." Tukasimama na kuanza kutoka nje. pamoja na Mzee Ngozi na Banzi pia tulikuwa pamoja na wale wazee wawili niliowakuta asubuhi huku Yule mmoja akiwa amevaa lubega, hawakuwa wakiongea chochote bila shaka wakijilaumu kwa kile walichotaka kutufanyia.
Tulitembea mpaka walipokuwa akina Honde, tulipowakaribia tu nikamwona Mwalimu Honde akinikimbilia kwa kasi, aliponifikia akanikumbati kwa furaha huku akitokwa na machozi, kisha akaenda kumkumbatia na Ntahondi, baada ya hapo tukaingia Ndani kwa Mzee Banzi.
Tukiwa ndani baada ya salamu ndipo akaanza kuongea Honde
"Wazee tunawashukuru sana kwanza kwa kila jitihada zenu mlizozifanya za kuhakikisha mnawatunza vijana hawa na kututafuta sisi mpaka tumefika hapa… pili tunawaomba radhi kwa kila aina ya usumbufu mlioupata tangu mlipokuwa na hawa vijana hapa kwenu." Akatulia kidogo halafu akaendelea
"Kwa harakaharaka Mimi ni naitwa Stephen Honde.. hawa wawili ni askari wa kitengo maalum cha upelelezi. Kwa kuwa kesi hii ni kubwa hivyo hatutakuwa na muda mrefu wa kukaa hapa." nilishukuru Mungu kimoyomoyo kusikia maneno haya ya Mwalimu Honde kwakuwa sasa niliamini saa ya ukombozi imewadia. Honde akanigeukia na kuniambia "..Sasa tunaondoka na kwenda moja kwa moja mpaka ofisi ndogo za upelelezi.. kule maeneo ya Posta, mtakaa pale kwa mahojiano maalum mpaka mtakapoelekezwa vinginevyo." baada ya kuongea maneno hayo Honde aliwasisitiza wazee hawa wasitoe habar ilei popote kisha akawapa pesa kama shukrani.. tukawaaga kwa ahadi kwamba tutarudi tena kuzungumza nao siku nyingine.. Wazee walishukuru sana na kuahidi kuwa watatupa ushirikiano wowote kama utahitajika na kwamba hawatoongelea chochote. Tukanyuka na kutoka nje huku wanakijiji kadhaa wakiwa wanashangaa tu. tunaingia kwenye gari kwa ajili ya Safari ya kurudi mjini.
*****
Safari ikaanza kwa kasi na mbwembwe, Tulitembea kwa umbali mrefu bila ya kuona nyumba zingine tofauti na zile za awali tulizokuwa tumehifadhiwa, sikuweza kutambua tulikuwa katika kijiji gani kwa maana sikupata hata nafasi ya kufanya hivyo kutokana na Shauku na kiu yangu ya kufika mjin, Hamu yangu kuu ni kuona na Ramla pamoja hawara yake Pablo Mwaki wakiadhirika mbele ya macho yangu kwa uovu na unyama waliotutendea,CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wakati safari ikiendelea nilikuwa nikitafakari na kujenga darasa huru kichwani mwangu kufuatia kadhia hii iliyotukumba.. japo nimepata taabu na kuteseka sana bado kuna vitu nilivichukulia kama sehemu ya darasa kubwa katika maisha yangu na katika maisha ya mtu mwngine yeyote atakayebahatika kuipata kwa kina simulizi hii. Kila nilipomwangalia Ntahondi ambaye alionekana kuwa bado hajaamini kama kwa sasa tuko kwenye mikono salama nilimfikiria mambo mengi sana.. nilianza sasa kuitambua Nguvu ya Wanawake katika baadhi ya mambo muhimu. Niliamini kuwa bila Ntahondi kamwe nisingekuwa pale muda ule, hakika Ntahondi ndiye chachu ya kusalimika kwangu.
Safari ilikuwa ndefu sana, hatimaye tukatokea katika maeneo niliyoanza kuyaelewa, ilikuwa ni wilaya ya bagamoyo iliyo katika mkoa wa pwani na hapo ndipo nikaanza kupata picha sasa ya Muelekeo wa tunapotoka na tunapoelekea
Gari ilishika kasi barabara kuu ya kuelekea jijini Dar, nilifarijika sana kuanza kuyaona mandhari ya mji ambayo sikutegemea tena kuyaona, maana kuponyoka kwa wale Maharami ilikuwa ni sawa na Ngamia kupenya kwenye Tundu la sindano
Mwl Honde kila alipojaribu kutuongelesha tulimjibu tu ili mradi tumemjibu lakini kila mtu alikuwa akiwaza yake kichwani, Katika habari ambazo sikupenda kuzisikia wa muda ule ni pamoja na hii aliyotuambia Honde kuwa kwa sasa Ramla ni mjamzito na kila mtu ameshajuwa pale chuoni, ni mimba ya Pablo.
Japo sikuwa na hamu tena ya kuwa na Ramla ila roho ilizidi kuniuma tu, sijui kwanini
Baada ya Safari Ndefu tuliingia sasa jijini Dar na moja kwa moja msafara ukaendelea kwa kasi. tukawasili maeneo ya Posta ya zamani, tukapinda upande wa kushoto ambako ndiko zlipo ofisi ndogo za upelelezi, sikujuwa kwanini zilijengwa pembeni kabisa na vituo vya polisi tulivyozoea kuviona. hapo tukakutana na kijana mmoja aliejitambulisha kwetu kama Sajent Gululi, alionekana ni mkorofi sana na alijipambanua mapema kuwa ni kijana mjuwaji sana,
Sajent Gululi alituamuru tuingie ofisini kwake huku yeye mwenyewe akitangulia ndani, kule nje tukawaacha akina Honde. tukaingia mpaka ndani! ilikuwa ni ofisi ndogo tu, hakukuwa na vitu vingi zaidi ya kabati ndogo iliyosheheni mafaili ya kazi, Meza ndogo ya mbao, na viti kadhaa visivyozidi vitano. tulipofika tu Sajent Gululi akaketi kwenye kiti chake kisha akatuashiria nasi kwa mkono wake wa kushoto tuketi..
Tukavuta viti nasi tukaketi!
Kabla ya mazungumzo yoyote akavuta droo ndogo katika meza yake na kutoa faili moja, si kubwa sana. akaliweka juu ya meza, akajipangusa mikono yake miwili mithili ya mtu anayehisi baridi, halafu akaingiza mkono kwenye mfuko wa shati lake akatoa kalamu na kuiweka juu ya meza, akaifumbata mikono yake kifuani
“Mbona unaniangalia sana kijana?” Alinisaili kwa sura iliyojaa dharau
“Sidhani kama kukuangalia ni kosa kisheria.” Jibu hili lilimfanya aniangalie tena mara mbili, akaachia tabasamu la hasira
“Nimekuwa nikiifuatilia kesi yenu kwa muda mrefu sana tangu mwanzo mpaka mwisho, nashukuru leo tumeonana nadhani mtakuwa wakweli na hamtonisumbua kabisa maana kwa kufanya hivyo mtajiongezea ugumu na uzito wa kesi hii.” Akashusha pumzi kidogo, akamtupia jicho Ntahondi kisha akarudi tena kwangu, hakuna aliyemkwepa
“Mlikuwa wapi siku zote hizi sisi tunawatafuta?”
“Tulitekwa kisha tukapelekwa porini.. tumepigwa na kuteswa sana,” Nikamjibu huku nimemkazia macho
“Mlitekwa kwa pamoja?”
“Hapana, nilitekwa kwanza mimi nikapelekwa huko kisha baadaye nd’o akatekwa Nt….” Kabla sijamalizia neno akanikatisha kwa swali la harakaharaka
“Sasa kwanini unasema mlitekwa? Una uhakika gani kuwa na Ntahondi naye alitekwa?”
“Kwa sababu naye aliletwa kule akiwa ameteswa sana mpaka amepoteza fahamu na alipozinduka dipo akanihadithia jinsi alivyotekwa.”
“Kumbe alikuhadithia! sasa unatoa wapi uhakika wa kuamini kua alitekwa kweli? Je kama huyu ana uhusiano na waliokuteka hivyo aliigiza tu ili apate data muhimu kutoka kwako kabla hawakuuwa?”
“Hakukuwa na haja ya kumleta Ntahondi ili anipeleleze huku akiwa ameteswa kiasi kile wakati mimi tayari niko chini yao wangeweza tu kunibana mpaka nikautapika ukweli wowote kama ningekuwa nao ila hawakuhitaji ukweli wowote.. Pia nakumbuka kuwa meseji aliyonitumia kunitahadharisha kuwa niwe makini huenda nikatekwa ndiyo iliyosababisha naye atekwe maana mimi muda huo nilikuwa nimeshatekwa hivyo wale watekaji wakaiona na kuanza kumfuatilia maana walijua kuwa anajua mipango yao yote.”
“Unamjua aliyekuteka?”
“Ni vijana waliotumwa na Pablo Mwaki..”
“Katika kipindi chote hicho unachodai ulitekwa ulimuona Pablo hata mara moja?”
“Hapana..” Nilipojibu tu hivyo Sajenti Gululi alipiga meza kwa nguvu huku akifoka kwa sauti
“SASA UNAMTUHUMU VIPI MTU KAKUTEKA WAKATI HATA HUKO HAKUJA KUKUONA?” Mwili wangu ulikuwa ukitetemeka kwa hasira kuona naulizwa upuuzi tu
“..Ni Kwa sababu hao walioniteka walikuwa wakiniambia kuwa sasa nimeingia kwenye himaya ya Pablo.. na hata nilipokuwa kule walikuwa wakinisisitiza nitaje kama kuna mtu yeyote anayejua kuwa nilikuwa na mgogoro na Pablo hivyo ni yeye tu ndiye aliwatuma.”
“Yaani wewe una mgogoro na Pablo? Pablo aache majukumu yake mazito ya kimaisha aingie katika mgogoro na wewe mtoto mdogo, is it Possible?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Si ajabu, ni jambo la kawaida sana hilo hasa kwenye mambo mazito yahusuyo mapenzi.”
“Mapenzi? Pablo akuteke kwa sababu ya mapenzi? Kwahiyo nd’o maana na wewe ukamwua Paschal kisa mapenzi au sio?” Nilipigwa bumbuwazi kusikia na mimi nimemuua Paschal, kwanza hata hilo jina silijui
“Mbona sikuelewi afande? Paschal nd’o nani?”
“Pumbavu! Unadhani kuna siri tena?” akaingiza mkono kwenye droo ya meza yake akatoa bahasha kubwa ya kaki, akaifungua na kutoa picha kama tatu hivi. akazibwaga pale juu ya meza huku akinikodolea macho, nilizishika picha zile huku mikono yangu ikitetemeka, jasho likinitiririka makwapani, nikashuhudia picha zikinionesha mimi nikiwa nainyanyua maiti iliyolala juu ya Dimbwi la damu, baada ya sekunde chache nilivuta taswira kichwani nikakumbuka tukio lile la mauaji ya Yule dereva teksi, nikakumbuka jinsi walivyonishurutisha niinyanyue ile maiti na hapohapo wakanipiga picha kadhaa, nikajua kumbe ule ulikuwa ni mpango wa Mwaki tu wa kuniangamiza.
Nikiwa bado natafakari nikaendelea kushtushwa na maneno ya huyu Sajent
“Umemwua kijana watu kisa mapenzi.. kisa huyu Malaya wako Ntahondi, utaozea jela kijana!”
“Mimi sijaua kaka hizo ni hila tu, tafadhali niamini.”
“Naomba usinifanye miye mtoto, nieleze kila kitu na kama utasimamia katika msimamo wako huo, nitakunyoosha wewe, nitakupa adhabu za kivita wewe mpaka utasema.. acha hayo mateso unayosingizia kuwa ulipewa huko porini hapa nitakutesa kisayansi mpaka utajuta.” Alipomaliza kunisemea maneno yake ya kuudhi akamgeukia Ntahondi na akamtupia swali
“Inakuwaje mrembo kama wewe unashiriki mauaji kisa mapenzi? Tena unakubali bwana wako dereva teksi auawe na bwege tu? Huyu Naufal si alikuwa bwana wa rafiki yako wewe? mbona Ramla hakukuuwa wewe ulipomsaliti kwa bwana wake huyu?” Sajent alionesha dhahiri kuwa anaijua vema kesi hii ila ameamua kuupindisha ukweli, pengine alifanya hivyo makusudi tu au na yeye kajazwa uongo na wafuasi wa Pablo
“Mimi sijawahi kushiriki mauaji yoyote tangu nizaliwe.”
“Hata mimba hujawahi kutoa?”
“Hiyo sio kazi yako.”
“Nani aliemuua Yule dereva?”
“Sijui.”
“Nitakuzaba vibao sasa hivi, usifikiri nacheza hapa, nani aliyemuuwa Yule dereva?”
“Acha hivyo vibao, utuuwe kabisa pengine nd’o utapewa tuzo na Pablo, si ndiye aliyekutuma!” Ntahondi kumbe naye alikuwa kaishagundua kuwa huyu afande sio Bure lazima atakuwa ametumwa tu. Sasa jibu hilo lilimtibua kabisa Sajent Gululi, akabadilika akawa kama mtu aliyemfumania mkewe,
“Okay! Viburi eeh? dawa yenu iko jikoni.” Akasimama na kutoka nje kwa hasira sana, tukabaki mimi na Ntahondi tukitazamana, hatukuwa na haja ya kuulizana kitu bali dalili za wazi zilijidhihirisha kuwa kuna mkono wa Pablo eneo lile, nilikuwa najiuliza kuwa mbona akina Honde hawaingii ndani, ila sikupata jibu! na muda Sajenti Gululi akarejea tena mle ofisini, safari hii akiwa ameandamana na vijana wengine wawili
“Nimeshaongea na mkuu wa Gereza, wachukueni muwapeleke segerea, watakaa kule kwa siku kumi na nne, watapata cha moto kule mpaka watasema ukweli wa mambo.”
“Okay Boss” Vijana wale wakatuamuru tuinuke, tukainuka na kutoka mpaka nje ambako tulikuwa na gari zao zikitusubiri, tukaingia huku tukitokomezwa maneno na Gululi, cha ajabu pale nje sikuwaona tena akina Honde na wale maofisa waliotuijia kule Porini, nilijuliza maswali mengi lakini sikuambulia jibu hata moja, haikuchukuwa muda safari ya kuelekea rumande ikaanza
Joto kali, Njaa, Mwanga hafifu, na hewa chafu vilinizidia sana mpaka nikajihisi kama kupoteza fahamu, ni Ndani ya gereza la Segerea nilipokuwa nimewekwa. Ramla naye aliswekwa ndani ya selo ya wanawake huko. Ilikuwa ni kama ndoto hivi, ladha tamu ya ukombozi kutoka chini ya mikono ya Pablo iligeuka shubiri kwangu, Chemchem za machozi zilichemka kutoka katika mboni za macho yangu na kutengeneza michirizi katika mashavu yangu.. kadri nilipoyafikiria haya matatizo yanayonikumba nilijikuta najichukia mwenyewe, niliyachukia sana maisha yangu maana kila kukicha nazidi kuteketea tu, na sasa nimeingia kwenye utata wa mauwaji ambayo sikushirikia kabisa, nilijuwa fika ni mbinu za Pablo Mwaki tu ili kuniteketeza
“We bwege unalia nini kama mtoto wa kike?” Sauti ya kijana mmoja alieykua ameketi pembeni yangu nd’o ilinitoa katika lindi la mawazo, alikuwa kidali wazi, sura yake ilikuwa na alamaalama kama vile alieyechanwa na visu hivi, sura yake mbaya mpaka niliogopa kumtupia jicho kwa mara ya pili,. Sikumjibu kitu akaendelea kunipa vitisho vyake vya kijelajela
“Unaleta uzuri jela, uliza wazuri wenzio wako huko Sero namba saba, wote wamepata waume humu, sasa na wewe umekuja selo ya wasimbe hii halafu unaleta ugwadu.. ngoja usiku ufike utaniamkia wewe.”
Nilihisi dunia yote imeniinamia, sikuwa na msaada wowote mle ndani, nikawa najiuliza kama hali ya jela nd’o ile itakuwaje kwa Ntahondi ambaye hajazoea hekaheka kabisa
Hofu kubwa iliendelea kunitawa lakini nilijipa moyo wa kishujaa, na nikajilazimisha kujivisha sura ya utata mithili yao na nikajiapiza kuwa yeyote atakayethubutu kunifanyia ubabe nitapambana naye mpaka tone la mwisho la damu yangu.
Hatimae muda wa kulala ukafika, sikujua ilikuwa ni saa ngapi maana hali ya giza mle ndani ilikuwa imetanda tangu zamani sana.
Tulihesabiwa na maaskari magereza, baada ya hapo Nyampara akahimiza sote tulale, Hatimaye nikalala Selo kwa mara ya kwanza katika historia ya maisha yangu!
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Iliniuma sana ila sikua na jinsi
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment