Search This Blog

Sunday, 22 May 2022

MWANAHARAMU WA KISIASA - 5

 







    Simulizi : Mwanaharamu Wa Kisiasa

    Sehemu Ya Tano (5)

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Ishu ya kutaka kufuta mikopo ya vyuo vikuu ndiyo ilikuwa habari ya kila kona kipindi hicho. Watu hawakuamini kile walichokisikia, wakati mwingine walihisi rais huyo alikuwa amechanganyikiwa kwani halikuwa jambo la kawaida kwa rais kama yeye kuweka uamuzi mkubwa na mgumu kama huo.

    Wanafunzi wakapigiana simu, habari hiyo iliwashtua sana, hakukuwa rais ambaye aliwahi kufanya kitendo kama hicho, walichokipanga hakikuwa kingine zaidi ya kutaka kufanya maandamano kwani kwa jambo kama hilo, haikuwa rahisi kuliachia hivihivi.

    Chris alijua kwamba lazima wanafunzi hao wangeandamana, alichokifanya ni kuwaita waandishi wa habari na kutangaza kwamba kwa mwanachuo yeyote ambaye angejitolea barabarani, ama zake ama zao.

    “Ninatoa onyo kwa watu wote waliokuwa kwenye mpango wa kuandamana, msijaribu kufanya kitu kama hicho,” alisema Chris kwa muonekano wa Rais Labad.

    Onyo hilo likaendana na kufanyika kwa mawasiliano kutoka ikulu mpaka kwa katika ofisi ya IGP na kumwambia kwamba alitakiwa kuandaa vikosi vyake kwa ajili ya kupambana na wanafunzi ambao walitaka kuandamana siku inayofuatia.

    Hilo halikuwa tatizo hata kidogo, taarifa zikatolewa katika vituo vya polisi na kisha siku inayofuata, muda ambao wanafunzi wa vyuo vikuu walikuwa wakijiandaa, tayari polisi walikuwa barabarani huku wakiwa na mabomu ya machozi.

    Wanafunzi hawakuogopa, kuogopa kulimaanisha mikopo yao kutokufika mikononi mwao, ilikuwa ni lazima wapambane, ilikuwa ni lazima waionyeshe serikali kwamba mikopo waliyokuwa wakiihitaji ilikuwa na umuhimu mkubwa katika maisha yao.

    Waliwaona polisi, tena wengine wakipiga doria lakini hawakutaka kujali, walichokifanya ni kujipanga na kisha kuingia mitaani. Waandishi wa habari kama kawaida yao hawakupitwa na chochote kile, walikuwa na kamera zao barabarani kwa ajili ya kupiga picha kila kitu ambacho kingeendelea mahali hapo.

    Wanafunzi waliendelea kujitokeza, wengine walikuwa na mabango ya kuukataa utawala wa Rais Labad ambaye kila siku aliwakandamiza watu na kufanya mambo ambayo hayakuwa yakipendwa na wananchi wengi.

    Si kwamba polisi walifurahia, wengi waliumia lakini hawakuwa na jinsi. Hawakumpenda rais wao lakini ndiye aliyekuwa na nguvu ya kuamua lipi lifanyike na lipi lisifanyike.

    “Hata mkiua hakuna shida,” alisema Chris.

    Baada ya dakika kadhaa, mabomu ya machozi yakaanza kusikika mahali hapo. Kila mmoja aliogopa, walihisi kwamba polisi walishika silaha hizo kama kuwatisha lakini baada ya kupigwa, wakagundua kwamba walikuwa siriazi kwa kile walichotaka kukifanya.

    Wanafunzi wengi waliumizwa, polisi ambao walikuwa wakipiga kisifa, wakawakamanda wanafunzi wengine na kuwapiga virungu, ndani ya dakika chache, Mji wa Motown ulionekana kuwa kama uwanja wa vita kwani kila kona mabomu ya mchozi yalikuwa yakisikika huku moshi ukitawanyika kila kona.

    Lilikuwa tukio baya, lililoumiza sana watu lakini hakukuwa na mtu aliyejali, Chris alikaa kwenye kiti chake hotelini huku akifuatilia kila kitu. Moyo wake ulikuwa na furaha tele kwani ndicho kitu alichotaka kukiona, alijua kwamba kwa jinsi alivyokuwa akifanya, hakukuwa na mtu yeyote ambaye angekuwa na mapenzi tena na Rais Labad.

    Vyombo vya habari havikukaa kimya, waandishi wengi wa habari kutoka nje ya nchi wakampa jina la Mwanaharamu wa Kisiasa kwani kile alichokuwa akikifanya hakikuwa kizuri machoni mwa watu.

    Kila mtu kutoka nje ya nchi hiyo akaichukia Matapatapa kwani haikuonekana kuwa mahali salama tena. Waandishi wa habari waliokuwa nchini humo wakawa wakipewa vitisho kwamba hawakutakiwa kuripoti kitu chochote kibaya kuhusu yeye, na hata wale waliokaidi, walitekwa na kufichwa kwa siku kadhaa kisha kuachwa.

    Chris hakutaka kuua, hakutaka kuwaua waandishi wa habari waliokuwa wakikaidi, aliogopa kudaiwa damu za watu mikononi mwake na ndiyo maana kila alipokuwa akituma watu wamteke, waliwachukua na kisha kuwapa mikwara kadhaa, waliwashikilia kwa siku kadhaa kisha kuendelea na mambo yake.

    Hali haikuwa ya amani tena, kila kona, kulikuwa na kelele za watu kumchukia rais huyo ambaye alionekana kuwa katili kuliko marais wote waliopita nchini humo. Wanadiplomasia wengi wakashinikiza rais huyo akamatwe kwani kwa kile alichokuwa amekifanya hakikuwa kitu cha uungwana kabisa.

    Hakukuwa na sheria ya kumkamata rais akiwa madarakani, walitakiwa kusubiri mpaka atakapotoka madarakani ndipo akamatwe na kisha kufikishwa katika mahakama ya kimataifa, ya kihalifu nchini Uholanzi.

    “He has to resign,” (inabidi ajiuzulu) alisikika mwandishi mmoja wa BBC aliyekuwa akitangaza kuhusu hali iliyokuwa ikiendelea nchini Matapatapa.

    Mijadala mbalimbali iliandaliwa sehemu nyingi duniani, kwenye kila mjadala, mada kubwa ilikuwa ni kumtaka Rais Labad aachie madaraka na kupisha uchaguzi. Mpaka kufikia hatua hiyo tayari Chris akajiona kuwa mshindi, akaitisha waandishi wa habari, walipokusanyika, akaagiza kitu kimoja kwamba Wazungu wote waliokuwa nchini, walitakiwa kuondoka nchini humo.

    Ulikuwa ni uamuzi wa kipumbavu mno, uliomaanisha kwamba kweli rais huyo alikuwa amchanganyikiwa. Hofu kubwa ikaingia kwa wananchi kwa kuona kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wa misaada, ndiyo ungekuwa mwisho wa kupata kila kitu kutoka kwa Wazungu.

    Chris hakutaka kujali, hicho ndicho alichokihitaji. Baada ya siku kadhaa, akamuita waziri mkuu na kumpa kazi ya kuondoka naye, alitaka kwenda barabarani kununua changudoa kwa ajili ya kulala naye hotelini.

    “Unasemaje?” aliuliza waziri mkuu ambaye mpaka katika kipindi hicho hakuwa ameachia ngazi.

    “Ninataka nikanunue changudoa mmoja.”

    “Lakini bosi!”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hilo ni agizo! Twende!” alisema Chris huku tayari ikiwa ni saa tatu usiku.

    ****

    Hawakubisha, aliwaambia kwamba hilo lilikuwa agizo na ilikuwa ni lazima lifanyie haraka sana. Dereva akajiandaa na baada ya muda, Chris mwenye muonekano wa Rais Labad, waziri mkuu wakaondoka na kuelekea walipokuwa machangudoa.

    Njiani, waziri mkuu alikuwa na maswali mengi, hakuamini yale yaliyokuwa yakitokea yalifanywa na rais ambaye alikuwa akimuheshimu na kumuona mtu wa maana mno. Alitaka mwenyewe kwenda kununua changudoa japokuwa alijua fika kwamba watu wengine wangemuona.

    Walipofika, waziri mkuu akamuagiza dereva ili aende kumfuata changudoa mmoja lakini Rais Labad akakataa, akataka kwenda mwenyewe kwani yeye ndiye aliyekuwa na uhitaji na angemchagua yeyote aliyekuwa akimtaka.

    Machangudoa wakajisogeza lilipokuwa gari lile, lilikuwa la kifahari, walijua kabisa kwamba mwanaume aliyekuwa humo alikuwa na pesa. Huku wakisubiri mlango ufunguliwe, ghafla ukafunguliwa na mwanaume mmoja kutoka.

    Watu wakamwangalia mwanaume huyo, alikuwa Rais Labad, uso wake ulikuwa kwenye tabasamu pana, machangudoa walipomuona, hawakuamini kama mwanaume huyo alikuwa Labad.

    Akawaita na kuanza kuzungumza naye, aliwaambia kwamba alitaka mwanamke mmoja wa kwenda kulala naye. Wakajipanga mstari na kuanza kuwaangalia, alichagua mwanamke mwenye wowowo kubwa na kutaka kuondoka naye.

    “Naomba nipige picha na wewe mpenzi!” alisema changudoa mmoja, alijua kwamba Rais Labad angekataa, lakini kitu cha ajabu kabisa, akakubali, si yeye tu, hata wale machangudoa wengine ambao wangependa kupiga naye picha, alikuwa tayari kufanya hivyo.

    Hilo ndilo lililomchosha zaidi waziri mkuu, aliona kabisa kwamba picha hizo zisingebaki katika simu za machangudoa hao tu bali zingesambaa mpaka katika mitandao ya kijamii. Alitamani kuwazuia lakini rais huyo alikuwa mbishi, alipokuwa akiamua kitu, hakutaka kuingiliwa na mtu yeyote yule.

    Machangudoa hao wakapiga naye picha nyingi, zingine akiwa amewashika makalio, nyingine akiwa amewapakata na mbaya zaidi nyingine alikuwa akinyonyana nao midomo. Zilikuwa picha ambaya ambazo hazikustahili hata kuwekwa kwenye magazeti.

    “Mmeridhika?” aliwauliza machangudoa hao.

    “Ndiyo bebi!” waliitikia.

    Hakuondoka bure, akachukua kiasi kikubwa cha pesa na kuwagawia huku akimchukua changudoa wake na kuelekea naye hotelini. Njiani, walikuwa wakishikana huku na kule, kila mmoja alionekana kuwa na hamu na mwenzake.

    Waziri mkuu alikuwa kimya, aliwapiga macho ya kuibia. Hakuacha kumshangaa rais huyo, kwake, alionekana kuwa kituko kikubwa kwani hakudhani kama kulikuwa na rais kama huyo duniani, rais ambaye angeweza kufanya mambo ya kijinga kama aliyokuwa ameyafanya.

    Usiku huohuo machangudoa wale wakaanza kuziweka picha zile kwenye mitandao ya kijamii. Kila mmoja alishangaa, hakuamini kile alichokuwa akikiona kwamba rais wao, mtu waliyeamini kwamba angefanya mambo mengi nchini Matapatapa ndiye aliyekuwa akifanya mambo ya kijinga namna ile.

    Walimchoka, alikuwa na matukio mengi ya ajabu, wakati mwingine walihisi kama alikuwa amechanganyikiwa, walitaka kuwa na maisha yao, hawakumtaka tena huyo rais kwani mambo aliyokuwa akiyafanya yalionekana kuwa tofauti na marais wa nchi nyingine.

    Picha zikazua gumzo, kila mtu alisema maneno yake, wengine waliponda, walimkashifu, walimsema sana, walimtukana kwani aliwashangaza, iweje rais aende sehemu ya kununua machangudoa na kununua, tena hakuridhika, akapiga nao picha za kimahaba ambazo zilimsisimua kila mwanaume aliyekuwa akiziangalia.

    Gumzo halikuwa Matapatapa tu bali hata sehemu nyingine. Kila mtu alikuwa akishangaa, mambo aliyokuwa akiyafanya rais huyo yaliwashangaza sana, hawakuamini kama kweli aliamua kufanya mambo hayo yaliyokuwa ya aibu kubwa, mambo ambayo hayakustahili hata kuzungumzwa mbele ya watoto.

    Mwenyewe hakujali, hakusikia lolote lile japokuwa watu wengi duniani walilizungumzia suala hilo. Matapatapa ikakosa kiongozi bora, Wazungu waliendelea kumlalamikia kwa kile alichokuwa amekifanya, walimsema kwenye vyombo vya habri, tena kitendo chake cha kuwafukuza katika nchi hiyo ndicho kilichowapa hasira zaidi.

    Ndani ya mwezi mmoja tu, Rais Labad akawa adui wa kila mtu, familia yake ilimchukia kwa kuwa tu aliamua kuishi hotelini ambapo alipata nafasi ya kulala na wanawake wa kila aina. Sedika aliyekuwa na matumaini ya kuolewa na Chris, matumaini yalipotea kwani Chris hakuwa akipatikana mara kwa mara na baba yake ndiyo hakutaka kabisa kuzungumza naye.

    Vyama pinzani vikapata nguvu, kwa kipindi kirefu sana vilihitaji kuichukua nchi hiyo na kuiweka mikononi mwao. Walichokifanya ni kuungana, wakatengeneza chama kimoja walichokipa jina la Mkombozi ambacho kingewafanya kuingia madarakani.

    “Lengo letu ni moja, kukiondoa chama tawala madarakani!” alisema kiongozi wa chama hicho aliyeitwa Gideon Mruru.

    Huo ndiyo ulikuwa mpango wao, asilimia tisini na nane nchini Matapatapa walikiunga mkono, hawakupenda kabisa kumuona rais huyo akiendelea kuwa madarakani, walitaka kumuona akipotea katika uso wa dunia na ikiwezekana azikwe baharini ili asikumbukwe milele yote.

    Kazi ilikuwa ni moja tu, kubadili katiba, kulikuwa na kazi kubwa ya kulishawishi bunge kubadili katiba yake kwani viongozi wengi walikuwa chama tawala ambapo walimuunga mkono kiongozi wao kwa asilimia mia moja, walichoangalia hakikuwa maslahi ya nchi, bali maslahi ya matumbo yao.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Rais Labad alifikishwa hospitalini akiwa hoi, aliona kila kitu kilichokuwa kikiendelea lakini hakuwa na la kufanya, alionekana kama mgonjwa, hakuweza kuongea vizuri. Hakuwafahamu watu hao waliokuwa wamemteka, alikiona kifo kikiwa mbele yake, hakujua sababu iliyowafanya wanaume hao kumteka na kisha wao wao kumpeleka hospitali.

    Pale hospitali, vijana wale wakazungumza na manesi na kuwaambia kwamba walitaka kumpeleka ndugu yao katika hospitali nyingine kwani hawakuwa wakiamini huduma zilizokuwa katika hospitali hiyo.

    Hilo halikuwa na tatizo, wakaruhusiwa kumchukua ila wakapewa na dawa ambazo alitakiwa kupewa. Walipotoka nje, wakakodi teksi na kuondoka mahali hapo. Kabla ya kuingia nchini Uingereza, tayari walipanga mipango yao, waliwaweka watu tayari kwa kucheza michezo yao hivyo hakukuwa na tatizo lolote lile.

    Baada ya dakika kadhaa, gari likawa linasimama nje ya jumba moja kubwa, Rais Labad akateremshwa na kuingizwa ndani ambapo baada ya kufikishwa ndani ya chumba kimoja kikubwa, akaambiwa atulie humo.

    Aliogopa, hakuonekana kuwa kwenye mikono isiyo salama, alikumbuka vizuri kwamba kulikuwa na mtu aliyekuwa na muonekano kama wake, mtu huyo alikuwa nani na kwa nini alikuwa na muonekano kama wake, na mbaya zaidi hata sauti zao hazikutofautiana.

    Akahisi kuna tatizo, akahisi kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea. Humo ndani, hakutulia, alikuwa akipiga kelele aachiwe lakini hakukuwa na mtu aliyemsikiliza, ndiyo kwanza mara kwa mara mlango ulifunguliwa na kuambiwa anyamaze.

    “I want to go home,” (nataka kwenda nyumbani) alisema Rais Labad huku akimwangalia mwanaume aliyefungua mlango.

    “Then?” (kisha?)

    “I want to see my family! Please don’t hurt them,” (nataka kuiona familia yangu! Tafadhali msiiumize) alisema Rais Labad.

    “We won’t hurt them,” (hatutowaumiza) alisema jamaa huyo.

    “Please! Let me go,” (tafadhali niacheni niondoke) alisema rais huyo, jamaa huyo hakumjibu, alichokifanya ni kuufunga mlango na kuondoka mahali hapo.

    Maisha yake yakawa ndani ya chumba kile, humo, aliletewa chakula na kupewa kila kitu alichokuwa akikihitaji. Alipelekewa magazeti, kitu pekee ambacho hakukipanda ndani ya chumba hicho kilikuwa ni kompyuta na simu tu.

    Alijua kila kitu kilichokuwa kikiendelea, alizisoma taarifa kuhusu yeye, upuuzi wote aliokuwa akiufanya Chris kupitia sura yake alikuwa akiziona katika magazeti. Aliumia, hapo ndipo alipojua sababu ya wanaume hao kumteka, hakujua walikuwa wakina nani lakini aliona kabisa kwamba lengo lao lilikuwa lilikamilika.

    “Mnanichafua! Naomba msinichafue,” alisema Rais Labad huku akimwangalia mwanaume aliyekuwa akimletea magazeti.

    “Kuchafuka na kufa bora nini?” aliuliza mwanaume huyo.

    “Naombeni mnisamehe! Msinichafue zaidi. Siwezi kwenda kununua changudoa, kwa nini mnanifanyia hivi?” aliuliza rais huyo huku akionekana kuchanganyikiwa.

    “Utamuuliza Chris!”

    “Chris?” aliuliza huku akichanganyikiwa.

    “Ndiyo!”

    “Chris gani?”

    “Uliyemtafuta usiku nz mchana umuue. Inamaana unataka kusema umemsahau bilionea Massawe uliyemuua?” aliuliza jamaa mmoja.

    Hapo ndipo kichwa chake kilipokumbuka, alikumbuka namna alivyoiangamiza familia yake kwa kuipiga risasi katika chumba cha hoteli, alikumbuka namna alivyokuwa akimtafuta kwa nguvu zote kwa lengo la kumuua ili asije kulipiza kisasi hapo baadaye.

    Pamoja na juhudi zote hizo, alishindwa kumuua, alishindwa kumzuia na mwisho wa siku mwanaume huyo alikuwa akilipiza kisasi katika njia ambayo hakuwahi kuifikiria maisha yake yote.

    “Siwezi kuwanyima mikopo wanafunzi!” alijisemea.

    Upuuzi wote uliokuwa ukifanyika Matapatapa aliuona kupitia magazeti mbalimbali, alizisoma hisia za wananchi wake dhidi yake, hiyo ilipoonekana haitoshi, akapelekewa televisheni mule ndani ili kufuatilia kila kitu.

    Habari ambazo zilishika vichwa vingi vya habari zilimhusu yeye, jinsi alivyokuwa akiiongoza nchi kipumbavu, alivyotaka kumvua nyadhifa waziri mkuu na kutaka kumuweka mkewe.

    Kila kitu kilichokuwa kikiendelea, aliumia moyoni mwake lakini hakuwa na cha kufanya, alitakiwa kukubaliana na kila kitu. Hakutoka ndani ya chumba hicho kwa miezi mitatu, aliendelea kusulubika, aliendelea kuikumbuka familia yake ambayo kila siku ilikuwa naye bega kwa bega kwa kila kitu alichokuwa akikifanya.

    “Hapana! Mimi siwezi kufanya hivi! Mimi siwezi kufanya hivi!” alisema huku akilala chini na kuanza kulia, kitu kilichomuuma zaidi ni kwamba kila kitu kilichokuwa kikitokea, kilipangwa na Chris, kijana aliyekuwa akimchukia kupita kawaida.

    ****

    Muda mwingi Kashindi alikuwa na furaha tele, hakuamini kama alikuwa amefanikiwa kwa mpango mzima aliokuwa amepanga na Chris. Kambini, kila mmoja aliona dalili za kuichukua nchi ya Matapatapa ambayo walipambana kwa miaka nenda rudi.

    Alikuwa akiwasiliana na Chris, wakati mwingine alikuwa akimwambia ni kitu gani alitakiwa kufanya. Matendo mengi yaliyokuwa yakifanyika, yaliwakera wananchi ambao kila siku walitamani kumuona rais huyo akitoka madarakani na kuchaguliwa mtu mwingine.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hawakutaka kuipindua nchi kwa nguvu kama walivyokuwa wamepanga, kitu ambacho waliona kwamba walitakiwa kufanya ni kuendelea kumtumia Chris mpaka wahakikishe kila kitu kinakuwa kama kinavyotakiwa kuwa.

    Chris aliwaambia kuhusu mipango mingi, akawaambia kwamba alitaka kuzungumza na jeshi. Ili jeshi limchukie ilitakiwa kuwapandikiza chuki kubwa dhidi yake ili hata kama Kashindi na kundi lake wangeamua kuivamia nchi hiyo wanajeshi wasiweze kuingilia kwa chochote kile.

    “Kwa hiyo tumekubaliana nipandikize chuki kwa wanajeshi?” aliuliza Chris.

    “Ndiyo!”

    “Sawa. Hakuna kitu ambacho wanajeshi wanakichukia kama kucheleweshewa mishahara yao. Nitaanza na hapo,” alisema Chris.

    Hilo lilikuwa ni suala la haraka sana, hakutaka kusubiri, siku hiyohiyo akawaita waandishi wa habari kwa lengo la kutaka kuzungumza nao. Kila mmoja aliweka sikio wazi, alijua kwamba kulikuwa na kitu kingine cha hovyo rais huyo alitaka kuzungumza kama kawaida yake.

    Watu wakajikusanya kwenye televisheni zao, wengine waliokuwa vijijini, wakajisogeza katika redio zao, walitaka kusikia kile ambacho rais huyo alitaka kuzungumza siku hiyo kwani tangu arudi kutoka Uingereza, hakuwahi kuongea jambo lolote zuri kwa wananchi wake.

    Alisimama, kila mmoja alikuwa makini kumsikiliza, kamera zilitegeshwa, watu wote walikuwa kimya kutaka kusikia kile alichotaka kuzungumza. Akasimama mbele ya watu wote kisha kunywa maji kwa lengo la kulainisha koo yake.

    Alionekana kuwa na mengi ya kutaka kuzungumza siku hiyo, alijua ni kwa jinsi gani wanajeshi wangeumia lakini hakuwa na jinsi, wakati mwingine alitakiwa kuwakasirisha kwa sababu alihitaji kuchukiwa.

    “Hivi nchi yetu kupigana vita kwa mara ya mwisho ilikuwa mwaka gani?” aliuliza swali hilo ambalo kila mtu aliyelisikia hakutegemea kama rais huyo angeuliza swali hilo.

    Watu walishangaa, walijaribu kujiuliza maana ya swali hilo, kwamba rais alimaanisha nini lakini hawakupata jibu lolote lile. Alimwangalia kila mtu aliyekusanyika katika ukumbi wa ikulu, uso wake ulikuwa kwenye tabasamu pana.

    “Mwaka 1969,” alijibu mwandishi mmoja.

    “Tena ilikuwa ni vita dhidi ya Rwanda? Si ndiyo?”

    “Ndiyo!”

    “Baada ya hapo?”

    “Hakuna!”

    Akaachia tabasamu tena, alikuwa na msumari wa moto wa kuwachoma wanajeshi, alijua kwamba wangekasirika, na hilo ndilo lilikuwa lengo lake, kwani alitaka kusambaza chuki kwa kila mtu nchini Matapatapa.

    “Sasa kuna haja gani ya kuwalipa wanajeshi mishahara mikubwa na wakati wengi wao hawajawahi kupigana vita?” aliuliza Chris.

    Kila mtu alishangaa, wanajeshi waliokuwa wakiangalia kipindi hicho, wakawaita wenzao kwa lengo la kusikiliza upuuzi ambao rais wao alikuwa akiuzungumzia, walishangaa, ilikuwaje rais akawa na ujasiri wa kusimama hadharani, tena mbele ya waandishi wa habari na kuzungumza maneno ya kipuuzi kama yale?

    “Tunawalipa wafanyakazi mishahara kwa kuwa wanafanya kazi, si ndiyo? Sasa wanajeshi hawafanyi kazi, hakuna vita, nchi ina amani, si bora tuwapeleke shambani wakalime tupate chakula!” alisema rais na kutoa tabasamu.

    “Kuanzia leo, kwanza mishahara wanayopokea ni minono mno, katika kipindi kigumu cha uchumi kama hiki, ni anasa kwa watu kama wao kupokea mishahara minono kama wanayoipokea, hivyo kama Amir Jeshi mkuu, naagiza mishahara ipunguze nusu kwa nusu,” alisema Chris na kisha kufunga mkutano wake.

    Siku hiyo ndiyo ilionekana kuwa ya hatari kuliko siku zote. Wanajeshi wakachanganyikiwa, walikuwa wakilalamika lakini hawakuwa na la kufanya. Jenerali wao alikuwa bega kwa bega na rais, alikuwa radhi kufanya kitu chochote ili kumlinda rais huyo.

    Wanajeshi hawakutaka kukaa kimya, walikuwa wakilalamika, maneno ya rais wao yaliwaumiza mno kwani hawakuamini kwamba kazi kubwa waliyokuwa wakiifanya haikuonekana kuwa kitu, haikuthaminiwa na rais wao na kuona kwamba hakukuwa na kitu kilichokuwa kikifanyika.

    Kila mtu akatoa maoni yao, hakukuwa na mtu aliyepongeza, kila mmoja alikuwa akiponda kile kilichokuwa kimezungumzwa na rais huyo. Kwenye mitandao ya kijamii hakukukalika, kila mmoja alionekana kuwa mkali kana kwamba watumiaji wote walikuwa wanajeshi.

    “Hivi huyu rais wetu ana akili kweli?” aliuliza jamaa mmoja kwenye mtandao wa Facebook, moja ya posti iliyochangiwa na watu wengi mpaka kufika elfu kumi hali iliyomfanya kijana huyo kukamatwa na jeshi la polisi.

    Kukamatwa kwa kijana huyo kutangazwa sana, wanasheria walijitokeza na kuanza kumtetea kwamba hakukuwa na haja ya kumkamata kwa kuwa hakumtukana mtu, aliuliza kama rais alikuwa na akili hivyo rais alitakiwa kujitokeza na kujibu swali kwamba alikuwa na akili au la.

    “Kwani rais katukanwa?” alihoji mwanasheria mmoja.

    “Hakutukanwa!”

    “Sasa? Basi inabidi kijana aachwe huru kwani hilo ni swali. Ilimpasa rais ajitokeze hadharani na kusema kwamba anazo akili lakini si kufanya hivi walichokifanya,” alisema mwanasheria huyo.

    Suala hulo lilizungumzwa kila kona, waandishi wa habari kutoka sehemu mbalimbali walijitokeza kumtetea kijana huyo ambaye alitakiwa kupandishwa mahakamani na kujibu mashtaka likiwemo la kumtukana rais kitu ambacho hakikuwa kweli kabisa.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Chris alikuwa ametulia hotelini, hakutaka kuwasiliana na mtu yeyote kwa kipindi hicho zaidi ya Kashindi tu ambaye kila siku waliendelea kupanga mipango ya kumuondoa Rais Labad kutoka katika nchi hiyo.

    Walifanikiwa kwa kiasi kikubwa, walikuwa na uhakika kwamba mpaka wanafikia hatua hiyo ilikuwa ni lazima rais huyo aondoke madarakani huku watu wakishangilia kwa nguvu kubwa.

    Chama pinzani ambacho kilikuwa kikitegemewa na watu wengi hakikuonekana kuwa na uwezo, ili kumuondoa rais huyo madarakani ilibidi Kashindi na jeshi lake waingie mjini Motown na kuiteka ikulu, kituo cha redio cha taifa ambapo mtangazaji alitakiwa kutangaza kwamba mapinduzi ya amani yalikuwa yamefanyika.

    Sedika hakuacha kupiga simu, kila siku alikuwa akimsumbua huku akitaka kusikia sauti ya mwanaume aliyekuwa akimpenda kuliko wanaume wote katika dunia hii. Simu yake haikupokelewa, aliumia moyoni mwake na wakati mwingine alihisi kwamba baba yake alimuua mwanaume huyo kwani alikuwa akimsumbua sana na kila siku alitaka kumuua kama alivyotaka kufanya hivyo kule uwanja wa ndege.

    “Baba atakuwa amemuua! Kwa nini amuue? Kulikuwa na kitu gani kilichokuwa kimetokea?” alijiuliza Sedika lakini hakupata jibu lolote lile.

    Moyo wake ukawa na majonzi, hakuamini kilichokuwa kimetokea, alichoamini ni kwamba mpenzi wake huyo alikuwa ameuawa. Kila siku alilia, hakukuwa na kipindi ambacho alikuwa kwenye wakati mgumu kama kipindi hicho.

    Wakati mwingine alitamani kuona kila kitu kilichokuwa kikitokea kiwe ndoto na baada ya muda mfupi aamke kutoka kitandani. Hakuwa akila kwa raha, alikosa amani kwani kila alipokuwa akimpigia simu mpenzi wake huyo, haikuwa ikipokelewa kitu kilichompa maswali mengi.

    “Au alikwenda tena Marekani? Lakini kwa nini hakuniambia? Inamaana hanipendi? Au alipata mwanamke mwingine?” alijiuliza lakini hakupata jibu lolote lile zaidi ya moyo wake kuendelea kuumia kila siku.



    Mambo hayakuwa kama yalivyotakiwa kuwa, nchi ilibadilika, wafanyabiashara walilazimishwa kulipa kodi kubwa zilizowaumiza, kila mtu alikuwa akizungumza lake, wengi waliumia.

    Wanachuo walianza masomo yao na hakukuwa na mikopo, wengi wakakasirika kusoma nchini Matapatapa kwa sababu tu rais wa nchi hiyo hakutaka jambo lolote lile kuhusu maendeleo ya nchi hiyo.

    Siku zikakatika, kila mtu nchini humo alimchukia rais huyo aliyekuwa akitawala kimabavu. Kila kona, watu walikuwa wakizungumza yao, nchi ya Matapatapa ikakosa ukaribu na nchi za jirani ikiwemo Tanzania kwa sababu tu rais huyo aliwaambia kwamba hakutaka kuona akishirikiana na nchi nyingine kwa kuwa wengine walikuwa wakimuonea wivu kutokana na madini mengi yaliyokuwepo nchini mwake.

    Njaa ikaanza kuingia nchini, wakulima hawakutaka kulima chakula cha kutosha kwa kuwa bei walipangiwa na hivyo kupata hasara kubwa. Kila kona kulikuwa ni mishemishe, hakukuwa na mtu aliyetamani kubaki ndani ya nchi hiyo.

    Wanajeshi walicharuka, walitamani kumpindua rais huyo lakini mkuu wao wa majeshi hakutaka kuona hilo likitokea kwa sababu rais huyo alikuwa rafiki yake wa karibu sana.

    “Kwa hiyo tufanye nini?” aliuliza mwajeshi mmoja.

    “Hatujui! Hapa ni lazima tuanze na mkuu wa majeshi, tuzungumze naye, msoto umeingia kambini, tutakuwa wazembe sana kama tu tutaacha jambo kama hili litokee,” alisema mwanajeshi mmoja.

    Walikubaliana kwamba ilikuwa ni lazima kupambana, hakukuwa na muda wa kusubiri kwani kasiri walivyokuwa wavumilivu ndivyo walivyokuwa wakipata shida zaidi. Walimwambia mkuu wao kuhusu hali iliyokuwa ikiendelea na alimfuata rais na kumwambia ukweli lakini rais huyo hakutaka kusikia, na ndiyo kwamba alimwambia mkuu wa majeshi kwamba asijali kwani kama ni pesa, zingejazwa kwenye akaunti yake.

    Wakati hayo yote yakiendelea, Rais Labad alikuwa amehifadhiwa nje ya nchi, alitakiwa kusafirishwa mpaka nchini Matapatapa. Alikuwa akilia tu, kila kitu kilichokuwa kikiendelea, alikuwa akikiona tu.

    Ndege ya rais ikatumwa mpaka nchini Uingereza ambapo akapandishwa na kuanza kupelekwa nchini humo huku taarifa zikisema kwamba alikuwa ndugu wa rais huyo ambaye alikuwa hoi kutokana na kusumbuliwa kwa ugonjwa wa ini.

    Wafanyakazi wa kwenye ndege hawakugundua kitu chochote kwani kabla ya kupandishwa ndege, rais huyo alichomwa sindano ya usingizi, wakati safari ikiwa imeanza, alikuwa amelala na mpaka anafikishwa nchini Matapatapa, bado hakuwa amerudi katika hali yake ya kawaida.

    “Amefika!” alisema jamaa mmoja, alikuwa akizungumza na rais kwenye simu.

    “Sawa. Nitakuja kumchukua. Muwekeni sehemu nzuri,” aligiza Chris.

    Hilo likafanyika, akapelekwa katika nyumba nyingine iliyokuwa hapohapo Motown. Wote waliokuwa wakifanya kazi na Chris hawakujua kama mtu waliyekwenda kumpokea ndiye alikuwa rais wa nchi hiyo.

    Ilipofika majira ya saa moja usiku, Rais Labad akarudiwa na fahamu, akayafumbua macho yake na kuangalia huku na kule. Alikuwa kitandani, alifungwa kamba, alijaribu kupiga kelele lakini ilishindikana kwani mdomoni alikuwa na gundu ya karatasi.

    Baada ya saa moja, mlango ukafunguliwa, watu watatu wakaingia wakitangulizana na Chris aliyekuwa na muonekano wake. Rais Labad alimshangaa Chris, hakujua mwanaume huyo alikuwa nani na kwa nini alikuwa akifanya hayo yote.

    “Kwa nini mnafanya haya yote? Kwa nini lakini?’ aliuliza rais Labad huku akimwangalia Chris mwenye muonekano wake.

    “Kwa sababu uliwaua wazazi wangu, ulimuua na dada yangu pia,” alisema Chris huku akimwangalia rais huyo.

    “Mimi?”

    “Ndiyo!”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hapana! Sikuwahi kufanya hivyo!”

    “Unakumbuka nini ninapokwambia kuhusu Mbuga ya Wanyama ya Kizwalinda?” aliuliza Chris huku akimwangalia mwanaume huyo.

    Rais Labad akabaki kimya, mawazo yake yakaanza kurudi nyuma na kukumbuka kuhusu mbuga hiyo. Hakuwa mwendaji wa huko na kila kitu alichokuwa akikifikiria na kukumbuka kilikuwa cha kawaida sana.

    “Sijakuelewa unamaanisha nini!” alisema rais huyo.

    “Unakumbuka nini kuhusu Massawe?’ aliuliza Chris.

    Hapo ndipo Rais Labad akaanza kukumbuka kila kitu, akakumbuka jinsi alivyomuua bilionea huyo na familia yake lakini kulikuwa na mtu mmoja tu ambaye alibaki, naye alikuwa Chris ambaye mpaka kipindi hicho hakujua mahali alipokuwa.

    “Unatakiwa kujuta sana kwa kutokumuua Chris tangu zamani,” alisema Chris na kusimama.

    Rais Labad akabaki akitetemeka, akagundua kwamba mtu aliyekuwa akizungumza naye alikuwa Chris. Alilia, alihuzunika na kujuta kwa kutokumuua mwanaume huyo ambaye leo alisimama mbele yake akizungumza mambo mengi, tena akimkumbusha ubaya ambao aliufanya miaka mingi iliyopita.

    “Chris…wewe ni Chris?” aliuliza huku akionekana kupagawa.

    “Ndiyo maana nimekwambia kwamba unatakiwa kujuta kwa kutokumuua mtu huyo,” alisema Chris.

    “Naomba usiniue! Bado ninahitaji kukaa na familia yangu,” alisema Rais Labad.

    “Sikuwahi kufikiria kukuua, ninataka nikutie aibu, nataka uione dunia chungu. Utatoka madarakani, na utatoka kwa aibu kubwa,” alisema Chris huku akimwangalia Rais Labad.

    “Naomba unisamehe!”

    “Yaani mimi kutokukua ni msamaha tosha. Umeiteketeza familia yangu ambayo nilikuwa naitegemea, umechukua kila kitu mikononi mwangu, kama kweli ningetaka kukua si ningekuua! Kwa nini nisikuue? Hii ni kwa sababu nimekusamehe na ndiyo maana nimeona bora nikutie aibu,” alisema Chris.

    Hakutaka kubaki hotelini hapo, akaondoka na kurudi katika hoteli aliyokuwa ameishi kwa kipindi kirefu. Alipofika, akachukua simu na kumpigia Sedika ambaye alimtaka kufika hotelini hapo kwa ajili ya kuzungumza.

    Msichana huyo hakuchukua muda mrefu akafika ndani ya hoteli hiyo. Alimwangalia mwanaume aliyekuwa mbele yake, alikuwa baba yake. Kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kusimama kisha kumkumbatia, alimkumbuka, alitamani kuzungumza naye lakini kila alipokuwa akimpigia simu, mara nyingi hakuwa akipokea.

    “Nini kinaendelea?” aliuliza Sedika huku akimwangalia mtu aliyeamini kwamba alikuwa baba yake.

    “Hakuna chochote!”

    “Mbona unatoa maamuzi ambayo hakukuwa na mtu aliyeyategemea? Nini kimetokea?” aliuliza Sedika huku akimwangalia.

    “Nimeamua!”

    “Umesoma magazeti ya leo?”

    “Hapana!”

    “Utafunguliwa kesi kama utatoka madarakani!”

    “Wapi?”

    “Mahakama ya The Hague, kwenye utawala wako umeua watu wengi sana, wameweka maovu yako yote. Kumbe ulitaka kumuua Chris kwa sababu uliiua familia yake?” aliuliza Sedika huku akionekana kuanza kubadilika.

    “Nani kakwambia?”

    “Nimesoma kwenye gazeti. Yote yameandikwa, hakuna hata moja lililoachwa! Baba! Kwa nini ulifanya hivi? Kwa nini umejichafua kiasi hiki?” aliuliza Sedika huku akimwangalia usoni.

    “Ni tamaa!”

    “Ndiyo iliyokufanya uwaue wazazi wa Chris?”

    “Naomba unisamehe na ndiyo maana nimeruhusu muoane na Chris, naomba unisamehe binti yangu,” alisema.

    Sedika alikuwa akilia, moyo wake ulimuuma mno, hicho ndicho kilichomfanya kuhisi kwamba hata kupungua nguvu kwa uhusiano wake na Chris ni kwa sababu ya hilo lililokuwa limetokea.

    Kosa alilifanya baba yake lakini lilimuumiza mno moyoni mwake, akajiona yeye kuwa mhusika mkubwa kwa kile kilichokuwa kimetokea. Hakutaka kubaki hotelini hapo, akaondoka zake huku akilia kama mtoto.

    Chris akabaki hotelini, hapohapo akampigia simu Kashindi na kumwambia kwamba nchi hiyo ilitakiwa kupinduliwa haraka iwezekanavyo, na wale watu waliokuwa hotelini wakimshikilia Rais Labad walitakiwa kumvua sura yake ya bandia na kumwacha humohumo hotelini pasipo kumwambia chochote kile.

    Hilo halikuwa tatizo, kitu cha kwanza kabisa walichotakiwa kukifanya ni kuwasiliana na mkuu wa majeshi pamoja na wanajeshi wengine wenye vyeo kwa lengo la kuwalaghai na hatimaye wakubaliane nao.

    Hilo halikuonekana kuwa tatizo, Rais Labad alichukiwa kila kona, kila mmoja aliona hiyo ndiyo ilikuwa nafasi ya kumuondoa rais huyo madarakani. Kitu cha kwanza kabisa kilichofanyika ni kuanza kufanya mipango.



    Ilikuwa ni lazima Kashindi na watu wake wafanye kila linalowezekana kuhakikisha Rais Labad anatoka madarakani haraka sana. Kitu cha kwanza walichokifanya ni kuweka ukaribu na wanajeshi ambao walitakiwa kuwa kama walivyokuwa na si kuzuia kufanyika kwa mapinduzi.

    Hilo halikuwa tatizo, japokuwa Mkuu wa Majeshi, Jenerali Boniphace Semwaga alikuwa upande wa Rais Labad lakini wakati huo alitakiwa kuangalia kundi la wanajeshi lilikuwa wapi. Alijiona kuwa mpinzani, kama angemzuia Kashindi na watu wake kufanya mapinduzi ilimaanisha kwamba alipingana na wenzake na alikuwa tayari kuona wakiteseka na kulia kila siku.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wakakubaliana kwamba Matapatapa ilikuwa ni lazima ipinduliwe kama ambavyo ilitakiwa kuwa. Hakukuwa na watu waliojua kitu kilichokuwa kikiendelea, wakati wakiendelea kulia maumivu yaliyosababishwa na mtu waliyejua kwamba alikuwa Rais Labad kumbe upande wa pili waasi walikuwa wakijipanga.

    Hawakutumia nguvu kuingia Motown, ili watu wajue kwamba fujo zilikuwa zimeingia mitaani, risasi kadhaa zikapigwa hewani, wanajeshi kumi na tano wakawa wanaelekea kule kulipokuwa na ikulu, walinzi waliokuwa wakilinda, wakapigwa risasi za miguu kwani katika mapinduzi hayo hakutakiwa kuuawa mtu yeyote yule.

    Wakaingia ikulu, Kashindi akaelekea ilipokuwa ofisi ya rais na kisha kukaa miguu ikiwa juu kabisa. Walifanikiwa, hawakutumia nguvu. Mtangazaji wa redio ya Taifa, Bwana Abdul Maweni akaambiwa awatangazie wananchi kwamba nchi hiyo ilikuwa imepinduliwa kijeshi, akafanya hivyo kitu kilichowafanya watu wote kushangilia.

    “Serikali ya Rais Labad imepinduliwa na Jeshi la msituni la Movement of 40 People au M40P lililo chini ya Mpiganaji wa msituni, Kashindi,” alisema Bwana Maweni.

    Kelele zilisikika kila kona nchini Matapatapa, hakukuwa na watu walioamini kama kiongozi huyo, rais asiyependwa na watu wengi, rais aliyejilimbikizia madaraka hatimaye alikuwa amepinduliwa.

    Watu wengi wakajitokeza barabarani na kuanza kuimba nyimbo nyingi za uhuru, hawakuamini kama kweli rais huyo alikuwa amepinduliwa na hatimaye kiongozi wa msituni, Kashindi ambaye alipambana miaka mingi kuingia madarakani.

    Matumaini yakarudi, taarifa za mapinduzi hayo zikatangazwa kila kona na kwa kuwa kulikuwa na matumizi makubwa na ya haraka ya mitandao ya kijamii, ndani ya nusu saa tu dunia nzima ikajua kile kilichokuwa kimetokea nchini Matapatapa.

    Kashindi akasimama dirishani ndani ya ofisi yake ikulu, nyuma yake walikuwepo vijana wake waliokuwa na bunduki, hakuamini kama alifanikiwa kuipindua serikali hiyo. Kwa kipindi kirefu alitamani kuwa rais wa nchi hiyo, alitamani kuona akiingia madarakani ili aiendeleze nchi hiyo kwani ilikuwa imeanguka vibaya.

    “Mkuu! Kuna watu humu!” alisema mwanaume mmoja, alikuwa amekimbia kule kwenye ofisi na kumwambia kwamba ndani ya ikulu hiyo kulikuwa na watu.

    “Wapi?” aliuliza huku akikoki bunduki yake.

    Wakaanza kuelekea kulipokuwa na watu hao, wakafika nje ya mlango wa chumba kimoja, wakafungua na kuingia ndani. Wakamkuta Sedika akiwa na mama yake, walikuwa wamekumbatiana huku wakilia.

    Waliomba msamaha wasiuawe, walikuwa na hofu kubwa kiasi kwamba hata Kashindi alipowaangalia, aliwaonea huruma. Hao hawakuwa na kosa, mtu ambaye alifanya makosa makubwa alikuwa rais wa nchi hiyo, Labad ambaye walimshikilia pasipo watu kufahamu.

    “Tunaomba mtusamehe! Tunaomba msituue,” alisema Sedika huku akilia.

    “Hatuna mpango wa kuwaua! Nyie si watu wabaya. Sedika, Chris alituambia kila kitu. Alituambia jinsi baba yako alivyowaua wazazi wake. Msijali. Nyie si watu wabaya hata kidogo, hatutowafukuza, hatutowafilisi, tulikuwa tunataka kuionyeshea dunia kwamba hakuna kitu kinachoshindikana chini ya jua,” alisema Kashindi.

    Sedika na mama yake wakachukuliwa na kutolewa ndani ya jengo hilo. Walihakikishiwa usalama wa maisha yao hivyo wakahifadhiwa sehemu ambayo ilionekana kuwa salama kabisa na wasingeweza kupata bughudhi yoyote ile.

    Upande wa pili wakati mapinduzi yakiwa yamefanyika, vijana waliokuwa na Rais Labad wakamchukua huku akiwa na sura ya bandia na kisha kumpeleka ufukweni ambapo huko wakamuweka ndani ya boti moja ya kifahari kisha kuchukua kamera zao na kuanza kupiga huku tayari wakiwa wamemvua sura ya bandia na kubaki na sura yake.

    “Ni lazima tutengeneze habari kwamba alikuwa akitoroka,” alisema mwanaume mmoja.

    Hivyo ndivyo walivyofanya, wanajeshi wakaonekana wakiingia ndani ya boti ile huku wakiwa na bunduki zao, wakati kila kitu kikiendelea, wengine walikuwa na kamera, kazi yao ilikuwa ni kupiga picha za video na kawaida.

    Walipoingia, wakamtoa na kutoka naye mpaka nje. Picha ziliendelea kupigwa kama kawaida. Picha zile, hapohapo zikawekwa katika mitandao ya kijamii na kudai kwamba baada ya kupinduliwa, alikuwa safarini akitorokea nchini Kenya kwa kuogopa kufikishwa katika vyombo vya sheria.

    Kukamatwa kwake ikaonekana kama siku ya uhuru, kila kona watu walikuwa wakishangilia wengi wakiwa na mabango yaliyoonyesha kuchoshwa na uongozi wa rais huyo.

    Picha iliyokuwa imetengenezwa, hakukuwa na mtu aliyejua, hakukuwa na mtu aliyehisi kwamba kila kitu kilichokuwa kimetokea kilikuwa kama maigizo fulani ya televisheni. Matapatapa ikapata uhuru kwa mara ya pili, rais ambaye alikuwa ameiharibu na kuipa umasikini mkubwa hatimaye ikarudi mikononi mwa watu wengine.

    Kule alipokuwa, Chris akavua sura yake ya bandia na kila kitu, akaiweka kwenye kiboksi kisha kufungua dirisha la chumba hicho na kuteremka kwa kutumia bomba huku akiwa na kiboksi kilichokuwa na sura ile ya bandia, na kwa kuwa ilikuwa ni usiku, hakuonekana, akashuka kwa bomba hilo mpaka chini, nyuma ya hoteli hiyo ambapo akaunganisha kwenda mbele ya hoteli ile, akaondoka huku akiwaacha walinzi wakiwa mlangoni wakiendelea kulinda kama kawaida.

    Taarifa za kukamatwa kwa Rais Labad akiwa ndani ya boti akitorokea nchini Kenya ndizo zilizowashtua walinzi waliokuwa wakilinda hotelini. Hawakutaka kubaki nje, wakaingia ndani kwani waliamini kwamba rais huyo alikuwa ndani ya hoteli hiyo na si kule alipokuwa amekamatwa.

    Wakaingia ndani, wenyewe walishangaa, hawakujua ni kwa namna gani mwanaume huyo alitoka ndani ya chumba kile. Hakukuwa na sehemu iliyotobolewa, wakaelekea dirishani na kuchungulia, hakukuonyesha kabisa kama mwanaume huyo alitokea kupitia hapo dirishani.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Walichanganyikiwa, hawakujua ni kitu gani kilitokea na ilikuwaje rais huyo akaamua kutoroka chumbani na wakati alijua kwamba walikuwa na jukumu la kumlinda kwa kila kitu.

    Hawakutaka kubaki mahali hapo, kama rais huyo alikamatwa ilimaanisha hata wao pia walikuwa kwenye hatari ya kukamatwa hivyo walichokifanya ni kuondoka mahali hapo kwa kujificha.

    Wakati hayo yote yakiendelea, bado watu walitaka kujua zaidi kuhusu Rais Labad, alikuwa amefumbwa mdomo kwani walijua kwamba kama wasingefanya hivyo ilikuwa ni lazima kusema kwa kupiga kelele kwamba yule mtu aliyekuwa amejifanya yeye, hakuwa yeye bali alikuwa ametekwa.

    Akapelekwa katika kituo kikuu cha polisi hapo Motown ambapo kila mtu, hasa waandishi wa habari walitaka kujua ni kitu gani kingetokea hapo, kama kupelekwa mahakamani kwa makosa aliyokuwa ameyafanya au la.

    “He wasn’t me…he wasn’t me…” (sikuwa mimi….sikuwa mimi…) alisema huku akiwa ndani ya sero.

    Hakukuwa na mtu aliyemsikiliza muda huo, kila mmoja alikuwa na uhakika kwamba rais ambaye alikuwa akifanya maamuzi ya kipumbavu alikuwa yeye. Alitakiwa kusubiri huko mpaka baada ya siku kadhaa ambapo barua ikaandikwa kutoka katika mahakama ya kihalifu ya The Hague iliyokuwa nchini Uholanzi ambapo alitakiwa kupelekwa huko kwa ajili ya kushtakiwa.

    Hilo hakulipinga, ilikuwa ni lazima apelekwe kwenda huko kwa kusikiliza kesi iliyokuwa ikimkabili ya kuua watu kipindi cha nyuma kisa tu walikuwa wakiandamana.

    Kesi hiyo iliunguruma kwa takribani miezi mitatu na ndipo hukumu ikatolewa kwamba anatakiwa kufungwa kifungo cha maisha gerezani. Hiyo ilikuwa taarifa nzuri japokuwa watu wengi wa Matapatapa walitaka kuona rais huyo akihukumiwa kifo kwa kuwaua ndugu zao ambao hawakuwa na hatia yoyote ile.

    Moyo wa Chris ukaridhika, akasikia amani moyoni mwake. Hicho ndicho kitu alichotamani sana kukisikia. Alijua kwamba mwanaume huyo aliwaua wazazi wake na dada yake lakini hakutaka kuua kama kisasi, akaiachia mahakama ifanye kile kilichoonekana kuwa sahihi.

    Matapatapa ikaingia katika uongozi mwingine. Kashindi alifurahi mno. Kwa kuwa Chris alitumia muda mwingi kuishi nchini Matapatapa, akaamua kuchukua uraia wa nchi hiyo ambapo baada ya uchaguzi kufanyika, akachaguliwa na kuwa mbunge, nafasi ambayo ilimpeleka mpaka kuwa waziri wa maliasili.

    Kwa kipindi chote hicho familia ya Labad ilikuwa ikishikiliwa, hawakutakiwa kuwa huru kabisa kwani waliamini kwamba raia wenye hasira kali wangeweza kuwafanyia vitendo vya kikatili mitaani hivyo walichofanya ni kuwahifadhi ndani.

    Chris hakuwa ameonana na Sedika, alitamani kuonana naye lakini hilo lilikuwa gumu, Kashindi alimzuia mpaka pale ambapo mambo yangekuwa yametulia ndipo angekwenda kuonana naye.

    Hilo halikuwa tatizo kwani baada ya siku kadhaa, akamfuata msichana huyo na kuonana naye. Alitaka kuzungumza naye, hakumficha, alimwambia kila kitu kilichokuwa kimetokea tangu mwanzo japokuwa alikumbuka kwamba alimwambia kuhusu uovu wa baba yake.

    Sedika hakutaka kujali kuhusu baba yake, aliumia kwa kuwa alikuwa baba yake lakini maisha yake yalibadilika kwani kwa jinsi mzee wake alivyokuwa akiishi, akiikandamiza Matapatapa kwa ajili ya manufaa yake, hata yeye aliumia.

    Kashindi akakaa madarakani, viongozi wote waliokuwa wameiba fedha kwa staili yoyote ile, wakafikishwa mahakamani na kupekewa gerezani huku mali zao zikistahifishwa na serikali.

    Lilikuwa pigo kubwa kwa viongozi hao wa chama tawala. Ili maisha yawe mazuri, chama cha Labad kikafutwa, Matapatapa mpya ikaanza kujengwa huku wanafunzi wakipata mikono, wanajeshi wakiongezewa mishahara na mashirika ya nje ya nchi yakiitwa kwa ajili ya kuwekeza huku ajira mbalimbali zikitolewa serikalini.

    “Nataka nikuoe!” alisema Chris huku akimwangalia Sedika.

    “Unioe mimi?”

    “Ndiyo! Kwani kuna hatari?”

    “Unafikiri watu watapenda kumuona waziri akimuoa mtoto wa Labad?” aliuliza Sedika.

    “Kwani wanaoa wao au mimi?”

    “Ni wewe lakini….”

    “Hakuna cha lakini! Ngoja nianze kukuposti kwenye mitandao ya kijamii!” alisema Chris.

    Alikuwa akipendwa kuliko wabunge wote. Alikuwa kijana makini, aliyefanya kazi zake kwa kujiamini sana. Kila alipokuwa, alikuwa akiitwa, alithaminiwa, alionekana kuwa shujaa mkubwa kwani Rais Kashindi aliwaambia wananchi kwamba mtu aliyechangia kwa kiasi kikubwa kumuondoa madarakani Rais Labad alikuwa Chris japokuwa hakusema alichangiaje.

    Kitendo chake cha kumposti Sedika kwenye Mtandao wa Instagram kiliwashtua watu wengi, hawakuamini kama mtu huyo angemuweka msichana huyo katika akaunti yake.

    Mbali na kuweka picha ya msichana huyo, alisindikizia na maneno mengi yaliyoonyesha mapenzi makubwa kwa msichana huyo, aliwaambia watu kwamba alianza uhusiano wa kimapenzi na msichana huyo kwa kipindi kirefu mno hivyo kila mtu alitakiwa kulifahamu hilo.

    Hakuishia hapo, aliandika jinsi alivyonusurika kutekwa uwanja wa ndege, bila msichana huyo, angetekwa na kuuawa. Kidogo watu wakamuuelewa, wakamsifia Sedika kwa kuyaokoa maisha ya shujaa wao japokuwa baba yake ndiye aliyekuwa amehusika katika kila kitu.

    Upendo ukaanza kurudi, kwa Sedika ilikuwa ni furaha tele kwani kabla aliamini kwamba chuki ya wananchi hao ingeendelea kudumu mioyoni mwao miaka yote hiyo.

    Baada ya miezi minne, tena baada ya kuposti picha zaidi ya hamsini, hatimaye wawili hao wakaoana katika kanisa la Living Water huku rafiki yake wa muda mrefu ambaye alikuwa kamanda wa majeshi, Ndezi akisimamia harusi hiyo kubwa.

    “Umekomaa sana mwamba. Ila mchuchu mkali kinoma. Sipati picha juu ya sita kwa sita utakavyorukaruka,” alisema Ndezi kwa sauti ndogo ya kunong’oneza iliyomfanya Chris kuanza kucheka.

    “Hahaha!”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kwichi kwichi kwichi…” alisema Ndezi kwa kumaanisha mlio wa kitanda.

    Walicheka pamoja, harusi ikafungwa na usiku wa siku hiyo kukafanyika sherehe kubwa hapo Motown na hatimaye wawili hao kuanza maisha kama mume na mke.

    Mfumo wa vyama ukawekwa upya, kukawa na uchaguzi ambapo wananchi hawakutaka kumchagua kiongozi mwingine zaidi ya Kashindi ambaye alikuwa kiongozi mzuri, aliyewasikiliza watu na kufanya kila kitu kilichotakiwa kufanywa na kiongozi bora.

    Uchumi ukapanda, watu wakawa na fedha, hakukuwa na shida ya maji wala umeme. Maisha yalibadilika, walimu wakalipwa vizuri, kwa kipindi hicho, kila kitu kiliendelea kuwa kama kilivyokuwa kabla ya utawala wa Labad.

    Kila kitu kilichopita, kikabaki kuwa historia.



    MWISHO



0 comments:

Post a Comment

Blog