Simulizi : Dili Tata
Sehemu Ya Nne (4)
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kijogobwire alipotoka hapo akapita sehemu mbili tatu anazozijua mwenyewe kama alivyosema na kutayarisha vitu vyake muhimu anavyotaka kuhusu suala la kesho nafsini kwake akijua wazi kwamba hapa kuna mchezo anachezewa. Ni kipi kilimfanya mdosi kubadili mawazo ghafla masaa machache tu baada ya kupinga alichoambiwa? Kwa vyovyote amewasiliana na polisi kama vile ambavyo mtu yoyote angefanya baada ya kupata maelezo mepesi kama aliyoyapata yeye kutoka kwa mtu asiyejua kazi yake kama Chan’duu.
Kwa vyovyote huu ni mtego wa polisi na ni uzembe wa Chan’duu. Sasa ataucheza huu mcheo kama Chan’duu na muhindi walivyoamua. Atawapiga chenga polisi na kuhahikisha linakuwa funzo kwa familia ya Mazarkhan na atampiga chenga Chan’duu na akileta za kuleta atamrambisha arzi. Hakuna msalie mtume katika wakati wa kupata milioni zaidi ya mia moja. Wazo kwamba zitakuwa zaidi ya milioni mia moja likamfanya kuwaza zaidi kwanini ziwe mia moja? Kwa nini zisiwe zote mia mbili? Kwanini asimpige pia changa la macho na Sofi. Ndio.. Hela hii atakayoikusanya hatampa mtu yoyote. Atakachokifanya ni kumshirikisha Sofi mpaka mwisho kwani kumgeuka sasa itakuwa mtihani mkubwa kwake, kwani akimpoteza kabla ya mtoto kupatikana itazusha maswali na hapo panaweza kumkwamisha katika zoezi la kukimbia na hela yake kwani kuna watu walishawahi kumuona na Chan’duu na kuna watu wanajua kwamba Chan’duu na Sofi ni damu damu
Kumpoteza Chan’duu hakuna atakaye patwa na wasiwasi kwani wengi wa watu wanajua kuwa jamaa ni mission-town na kuna siku yatamfika, hivyo yakimfika hakuna atakayeingiwa na shaka. Halafu akapata wazo kwamba, haina haja hata ya kukimbia wala kumpoteza Sofi kwani si hatari. Akisha mzulumu, mwanamke huyo hawezi kumchoma kwani itamlazimu kurudi kibaruani kwake na kujifanya atakuwa makini sana huko mbele juu ya suala la kumlea mtoto huku akiugulia maumivu ya kuingizwa mjini.
Alipokubaliana na wazo hili akapita kumalizia mambo yake mpaka saa tano na nusu usiku akapitia mgahawani kuchukua chakula na vinywaji kwa ajili ya washirika wake na kurudi kambini
Alipofunguliwa geti na kuingia ndani akamkuta Chan’duu akiwa yuko ukumbini macho, akionekana kukonda kwa simu moja tu na sura yake kuwa kama mzee kwa mawazo yaliomtawala huku Sofi akiwa ndani amelala
‘Vipi bob’ akamsalimia
‘Poa wangu. Vipi mishe zimekwenda?’ akauliza huku akitia huruma
‘Usikonde mtu wangu kesho saa sita mchana utakuwa na utajiri wa milioni sabini mikononi mwako’
‘Kweli?’ akauliza akiwa amechangamka haamini alichoelezwa
‘Kabisa. Sisi wanaume tutachukua sabini sabini na mwanamke atapata sitini’ akamuhakikishia kimagumashi
‘Dah? Nakuamini mwanangu. Na naomba unisamehe kwa kutaka kuharibu dili’ akaomba huku akionyesha sura ya majuto na kutia huruma
‘Usikonde huu ni mwanzo tu tunakokwenda tutaanzisha mtandao hatari kila mwenzi tunafanya tukio na kuingiza mamilioni’ akazidi kumdanganya
Neno hili lilimfanya Chan’duu kuchangamka sana
‘Sasa kamuite Sofi ili tule tulale tusubirie hiyo kesho’ akamuamrisha
Chanduu akanyanyuka na kuelekea katika chumba alicholala Sofi kama vile mtumwa anavyokwenda mahala alipoagizwa na bwana wake
Akachukua dakika kadhaa na kurudi akiwa peke yake. Kijogobwire alipomuangalia akajua kwamba huko hakuchangamkiwa pamoja na kujigongagonga kwake
‘Vipi?’
‘Anakuja’
Wakakaa kumsubiri
Ilichukua kama dakika tano ndipo Sofi akatoka akiwa amevaa khanga chini juu akiwa amevaa kiblauzi kinachoonyesha maziwa yake yaliosimama usoni akiwa amejiremba kwa mbali. Katika kivazi hicho na jinsi alivyojipodoa alipendeza kama vile mke aliyekuwa anajua kwamba mumewe anarudi na anatakiwa amkute katika hali ya kuvutia na kushawishi.
Mavazi aliyovaa ni mavazi ambayo alikuwa anayavaa katika mtindo wa kumtega Chan’duu na kumpagawisha wakati ule mapenzi yao yalipokuwa motomoto. Kijogobwire alipomuona Sofi moyo wake ulilainika na kujikuta akipata faraja na uchovu aliokuwa nao wote kupotea. Jinsi sofi alivyokuwa akija kwa mikogo na jinsi alivyotokelezea huku ukichanganya kwamba sasa hivi anammiliki yeye baada ya kumzidi maarifa Chan’duu, kulimfanya ajione kama vile yuko katika jumba la ufalme mtawala akiwa yeye akioga mito ya maziwa na kula kuku kwa mirija. Mfano wa jinsi alivyokuwa anajihisi kwa kweli hakuna. Kifupi ni kwamba mwanaume alikuwa anajiona zaidi ya bonge la bwana
Kama Kijo alikuwa anajihisi raha nafsini basi kwa Sofi ilikuwa zaidi ya hapo kwani muda mwingi alikuwa na mawazo juu ya mpango mzima ulivyo huku akiwa anamfikiria Kj kwa namna mbali mbali. Hakuna kitu ambacho kiliupoza moyo wake zaidi ya Chan’duu kumuambia kwamba Kj amerudi na kila kitu kiko safiCHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alipoamka aliona hapa anatakiwa kujiweka sawa kwa ajili ya bwana ili kupalilia upendo na alifanikiwa sana katika hilo kwani kweli alimchanganya mwanaume Kijo
Hata Chan’duu naye kutokana na hali aliyokuwa nayo sasa alipomuona sofi anavyokuja alijihisi nafsi yake kwenda taratibu uchu kumzidi na tamaa kuongezeka
‘Mambo K’ akamsalimia Kj kwa kifupi tabasamu kwa mbali likiwa mdomoni mwake
‘Poa. Keti’ akamuitikia na kumpa kiti akae huku yeye akikaa katika bench alilokuwa amekalia Chan
‘Sasa patna kila kitu kiko sawa. Hapa tule tulale kesho tuchangamkie milioni mia mbili’ akasema na kufungua mfuko aliokuja nao na kutoa chakula alichokuja nacho
‘Umeshapanga kila kitu vizuri?’ Sofi akahoji akiwa na hakika kuwa anachokisema mtu wake ni kitu cha kweli ila aliuliza tu kupata kufanya mazungumzo yaendelee
‘Kila kitu kiko pouwa’ akajibu huku akipokea bia aliyopewa na Sofi na kuiweka pembeni na kuanza kunawa kwa maji aliyoyashika kwa mkono mwingine ‘Kwanza tule, kisha sofi utalala chumba kile kile ulichotoka, mimi nitalala chumba cha mbele huku nyumba kubwa, Chanduu utalala chumba kile pale karibu na chumba cha Sofi’ akapanga huku moyoni akiwa na yake. Madhumuni yake alikuwa anayajua mwenyewe lakini Chan’duu alifarijika sana kuona kwamba pamoja na kuwa atalala peke yake lakini na Kijo naye atakuwa peke yake hivyo hapa hakuna namna ya kuzidiwa ujanja na huko mbele ataanza kubembeleza ili amrudishe mbuzi zizini
Wakati wa kula kwa vile Kijo alikuwa anataka kuhakikisha kwamba Chanduu anajua kwamba yeye ni mtu wa mjini huku kwa wakati huo huo Sofi akijua kwamba yeye ni mtu mzoefu na anayeijua pesa huku akiwa anaujua vizuri mji na watu wake akaanza kutoa hadithi zinazomuhusu kuhusu shuhuli mbali mbali alizoshiriki na kuwa zinamuingizia hela ya matanuzi huku kila mwisho wa maelezo akisifia kazi hii ilivyokuja wakati muafaka na hela ya kutakata
Baada ya chakula Sofi akasafisha takataka za mabaki ya chakula na vinywaji na kwenda kuviweka sehemu ya kutupia taka. Aliporudi akakaa kwa muda akisikiliza hadithi za kuvutia kuhusu Kj na maisha yake ya ki-mission town. Saa saba ikawakuta hapo mazungumzo yamekolea na vinywaji kuwapa kampani
‘So, nahisi muda umevuta sana sasa tukalale tusubiri kesho kuyatia mikononi majihela, ila nawaomba msikose usingizi. Sawa?’ akasema huku akicheka akimuangalia Sofi usoni
‘Mh, sijui kama mi usingizi utakuja. Sijawahi kukamata milioni, je zikiwa tano si nina haki ya kukosa usingizi?’ akatania huku akicheka, kwa macho laini akimuangalia Kj kama kumpa mualiko wa kuungana naye chumbani kwake
‘Mi naenda kulala’ Chanduu akasema akiona kwamba anapuuzwa. Lakini pamoja na kuaga hakuondoka mpaka akahakikisha kila mmoja anaondoka kuingia chumbani kwake
Kijo alipoingia chumbani kwake tu akachukua simu yake na kumtumia ujumbe Sofi ‘Usifunge mlango nakuja tutale wote mpenzi’
Alipokwisha utuma ujumbe huo akavua nguo alizovaa na kubadilisha na traksuit. Akafanya mazoezi kwa muda wa nusu saa na kuingia maliwatoni kujimwagia maji. Alipokwisha fanya usafi, kama kawaida yake, akajipodoa kidogo na kujipulizia manukato. Akavaa suruali nyepesi na fulana laini akatoka na kufunga mlango wake na kwa mwendo wa taratibu akaingia katika chumba alicholala Sofi na kuufunga mlango kwa komeo
……….
Japo kama usiku mzima hakulala kutokana na kuwa katika purukushani za kujistarehesha katika mwili wa mtoto aliyekuwa na hamu ya kukutana kimwili, lakini saa kumi na mbili akaamka na kurudi chumbani kwake. Ni kawaida kwake baadhi ya siku kulaa kwa masaa mawili iwapo kama siku ya pili kuna kazi anataka kuifanya hivyo kukesha kwa muda mwingi wa usiku haikuwa tatizo hata chembe kwake
Akaingia chumbani kwake na kuvaa pensi na kurudi uwani kufanya mazoezi mawazo yake yote yakiwa katika namna ya kuweza kuwachenga askari kwanza na kumchenga Chan’duu hapo baadae. Alikuwa anajua kwamba hili ni suala dogo sana hapa mwanzo, suala kubwa ni pale atakapokuwa katika wakati wakuikusanya hela rasmi
Alipomaliza mazoezi akaingia ndani na kuoga. Alipotoka akakuta Chan’duu naye ameshatoka kisha akafuatiwa na sofi. Wakatenga chai lakini si Sofi wala Chan’duu waliokuwa na uwezo wa kunywa chai hiyo. Kila mmoja mawazo yake yakiwa katika tukio lijalo tu
Baada ya hapo mipango ikaanza
‘Ok. Sasa iko hivi. Hapa tutatoka mimi na Chan’duu, kuna taxi inakuja na yule dereva wetu wa siku ile, tutapanda na kwenda sehemu ya tukio tukiwa na mtoto ndani yake. Sofi utatusubiri hapa hapa pamoja na dogo, sawa?’
‘Ok. Kuweni makini mi nasubiri zigo la mahela tu’ akawaambia
Ilipofika taxi dogo akaifungulia ikaingia ndani. Kijo akiwa amejiziba uso akaingia ndani katika chumba alichokuwapo mtoto na kukaa kwa muda kidogo
Alipotoka alikuwa amembeba mtoto aliyekuwa amelala bada ya kumpa vidonge vya usingizi
Wakatoka Kijo mbele upande wa dereva Chan’duu nyuma akiwa na mtoto
Wakati wanatoka kwa siri Sofi akampungia busu Kj kama ishara ya kumtakia kazi njema. Kj akatabasamu na safari ikaanza
Ndani ya gari hakukuwa na maelezo mengi kimya kilitawala zaidi, Kijo akijua kwamba maelezo aliyompa dereva yatafuatwa kwa umakini kama alivyoyatoa. Walipofika maeneo ya Posta wakatafuta maegesho na kupaki. Ikiwa yapata saa tano kasoro sasa, akaiwasha simu na kumpigia Mazarkhan
‘Uko wapi?’ akamuuliza bila salamu wala kugisagisa
‘Mimi iko feri apa’ Mazar akajibu kwa sauti ya kujiamini
‘Vizuri, subiri hapo hapo’ akakata simu na kuizima
‘Sasa Jorg, sisi acha twende tukifika nitakutumia meseji utaiwasha hii simu na kumuambia mdosi akuelekeze alipo kisha utanitumia meseji kuniambia alivyokujibu kisha mimi nitakupa maelekezo mengine’ akamuambia jamaa huku akichukua miwani yake ya jua na kuivaa
‘Usijali Kijo, ila itabidi hii kazi ikiisha unione tena kidogo maana naona kama inampunga mnene’ akasema Jorg huku anacheka
‘Aa wewe, tulia kwanza’ Kj akasema na kumtaka Chanduu ateremke katika gari
‘Mtoto je?’ Chan’duu akahoji
‘Usijali mtoto atakuja kwenye gari sisi tunachukua bodaboda mkapa Feri kuhahikikisha kwanza je mtu wetu hakuja na maaskari wengi kiasi cha kutuzidi ujanja’ akamjibu huku akifunga mlango wa gari
‘Nini? Inamana kuna askari’ Chan’duu akahoji huku akiwa ameshituka sana
‘Ndio itakuwa kaja na askari kwani wewe si ndo ulivyotaka? Si nilikuambia usiwasiliane naye? We unadhani alipokupigia simu na kukubali alikuwa keke yake. Usijifanye mjanja kwa kazi usizozijua’ akamuambia kama vile anampa tahadhari kuwa kikiharibika basi naye hana chake
‘Basi wewe nenda mimi nitakuja na gari ikiwa kila kitu kiko sawa’ Chanduu akajibu akitaka kufungua mlango wa gari na kurudi ndani
‘Hebu acha …’ Kijo akasema kwa hasira akitumia lugha ya matusi huku akiwa amemshika shati
Jinsi alivyomshika kuna watu walikuwa wanapita wakataka kusimama ili kuona kama kuna ugomvi
Akamuachia na kushusha hasira akijua kwamba hapa akilikoroga tu na kukatwa kwa bahati mbaya basi wameumia
‘We twende kila kitu nimekipanga vizuri’ akasema taratibu lakini akiwa amekaza sura
Ikawa haina budi ila Chan’duu kukubali
Wakachukua bodaboda kila mtu yake. Wakafika fery
Walipofika Kijogobwire akawalipa watu wa boda boda. Walipoondoka tu akatoa simu yake mfukoni na kumtumia ujumbe Jorg kumuambia awashe simu kisha amuulize mdosi ni wapi alipo halafu amtumie ujumbe kumfahamisha majibu aliyotoaCHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya hapo wakaingia soko la samaki na kujifanya kutafuta mboga
Baada ya dakika tano simu yake ikapokea ujumbe uliomfahamisha kwamba mdosi anasema amepaki gari yake katika maegesho ya taxi karibu na lango la kuingia katika pantoni. ‘Gari yake ni aina ya ford ina vioo vyeupe namba ya usajili ni T 517’ ndio maelekezo ya ziada aliyopewa
Alipousoma ujumbe huo akatoka yeye na Chan’duu wake taratibu mpaka karibu na mahala hapo. Akiwa wanajifanya kushanga bahari kama watalii wa ndani, akaangalia gari aliyoelekezwa. Akamuona mtu wake. Akatoa simu yake na kumtumia ujumbe Jorg kumuambia ampige Mazarkhan amuamrishe aingie kwenye pantone kisha hapo atapewa maelekezo mengine
Wakati akiwa anasubiri majibu kutoka kwa Jorg akili yake ilikuwa inacheza akijua hapa sasa ndipo atajua, je kweli muhindi ana maaskari alioambatana nao au yuko peke yake? Je ana mabegi yaliojaa wekundu wa msimbazi au makaratasi yalio kama bosheni ya kumkamatisha mtu?
Baada ya muda kidogo akamuona mdosi akiishika simu yake na kuzungumza mawili matatu na kukata simu, lakini baada ya kufanya hivyo kwanza hakuingia katika gari alinyanyua mkono wake kama vile anaangalia saa kisha akatingisha kichwa kukubali muda aliouona kwenye saa yake
Hapa Kijo hata hakutaka kujua ni nini Jorg atamuambia. Alijua kwamba alichokifanya mr Mazar ni ishara ya kuwaeleza watu alionao kwamba sasa anaelekea katika sehemu husika. Akapata hakika kwamba huu ni mtego
Akasuburi na kumuangalia mdosi ambaye aliingia katika gari lakini bila kuiondoa. Akakaa kama dakika mbili hivi kwa makini bila kumpa mtu wasiwasi kama anapeleleza, akiangalia je Mazar ataondoa gari au kuna mtu anamsubiri. Mara akaona gari moja iliyokuwa na vioo vyeusi ikipita na mr Mazar kuunganisha katika msafara huo. Akatulia tuli
Ikapita kama dakika moja nyingine akaona gari mbili zilizoongozana zikiingia mahala hapo. Katika hali ya kijicho pembe akawaona watu kadhaa wakitoka sehemu moja ya mgahawa uliopo hapo feri. Watu hawa walikuwa kama timu ya mpira inayokwenda katika mechi upande wa Kigamboni. Akajua kwamba hapo kuna maaskari si chini ya thelathini wameshazunguka eneo
‘Twenzetu’ akamuambia Chan’duu na kuanza kupiga hatua kurudi katika Jengo la Samaki
‘Vipi?’ Chan’duu akahoji akiwa hana anachokijua
‘Kuna askari kama mia hivi wametuzunguka lakini hawatujui’
Kusikia neno askari mia na wametuzunguka, bado kidogo Chan’duu atoke mbio, kama si Kijo kumdaka ghafla basi angehisiwa kuwa ni mwizi anakimbia baada ya kupora
‘We tulia askari wenyewe wako kwenye boti sio huku’ akamuambia huku akimminya mkono
‘Tembea taratibu bila wasiwasi’ akamuambia akimuachia mkono huku akiangalia kwa siri kushoto na kulia
Walipofika sokoni Kijo akamuambia Chan’duu
‘Chukua boda boda tukutane kambini. Usipite sehemu yoyote, sawa?’
‘Ok’ akajibu akiwa bado haamini kama yuko huru
Kijo akatoa elfu ishirini na kumkabidhi.
Chan’duu alipoondoka tu naye akachuka bodaboda kurudi Posta alipomuacha Jorg
Alipofika akaingia kwenye gari na safari ikaanza
‘Mdosi kama nilivyokuambia mwanzo, amekwenda kweli polisi, so nipeleke Mwenge kwenye kambi yangu mpya, baada ya siku tatu nitakupigia kukuambia nini tufanye, na usikonde utapata mgao utaridhika
…………….
Wakati wanaume wakiwa wako katika zoezi aliloambiwa kwamba litakuwa ni la ukusanyaji wa fedha, Sofi alibaki ndani akiangalia filamu za kibongo ili kupoteza mawazo lakini haikusaidia. Kila wakati akawa akitoka nje kuchungulia au kumuuliza dogo kama jamaa wanaonekana kurejea. Alipokuwa chumbani kila mara alikuwa akiangalia simu yake ili kuona kwamba Kj atampigia na kumpa taarifa ya kufanikiwa kwa jambo lao. Alipata mshituko baada ya kusikia geti linafunguliwa na alipotoka nje mbio kuona ni nani anaingia, au ndio kwamba ndio wanaume wanarudi mzigoni akakuta ni Chand’uu akiwa peke yake akionekana kuchoka na mawazo kumtawala.
‘Kimetokea nini?’ akauliza wasiwasi ukiwa umemjaaa na hali ya taharuki ikiwa imemtwala
‘Yule muhindi mshenzi sana amejaza maaskari kila kona bado kidogo nikamatwe’
‘Nini? Inamaana umekimbia na kumuacha mwenzio kwenye balaa’ Sofi akauliza kwa ukali
‘Hapana, wote tumewahi kutoroka kabla ya kunaswa’
‘Sasa K yuko wapi?’ akauliza akishusha pumzi
‘Amesema mimi nitangulie hapa’
‘Amesema utangulie hapa?’ Sofi akauliza kwa mshangao na wasiwasi
‘Ndio yeye anakuja’ mwanaume akajibu, akitaka kuulizia maji ya kunywa apoze koo
‘Umeona sasa ubishi na upumbavu wako? Umeshaharibu kila kitu’ Sofi akasema akiwa amechanganyikiwa
‘Sasa unanilaumu nini? Kwani kimeharibika kipi? Si mtoto bado tunaye?’
‘Tunae? Tunaye yuko wapi?’ akauliza Sofi kwa hasira
‘Si anaye Kijo!’
‘Asiporudi?’
‘Nini? Nilazima atarudi’
‘Wewe unawajua mishentown au unawasikia tu? Yani mpaka leo bado uko mlugaluga tu..’
Chan’duu kauli hii ni kama ilimzindua na kujua kwamba maneno ya Sofi ni ukweli mtupu
Akajihisi maini yakimkoroga. Akajua kwamba hapa wameshadhulumiwa na hawana ujanja. Hawawezi kumtafuta Kj na hawawezi kumchoma. Kama wangelikuwa na sehemu ya kukimbilia hiyo ingelikuwa sawa lakini kumchoma mtu na bado wako hapa hapa Dar haiwezekani
‘Unaona sasa ujinga wako? Tumeshaingizwa mjini. Si ulikuwa unasema Tukigeukana… Tukigeukana.. Sasa tumeshageukwa utafanya nini wewe mpumbavu? Utafanya nini?’ Sofi akauliza kwa hasira akitamani kumpiga kibao Chan’duu
‘Nakuul..’ akataka kutamka tena maneno mengine lakini kabla hata hajamalizia neno lake akakatishwa kauli na kijana mlinda nyumba
‘Samahani nimepigiwa simu na braza Kijo anasema kila mtu aondoke hapa hapako salama atawapigia simu kuwaambia mkutane wapi’CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kauli hii ikawafanya kuganda tu kama masanamu
Kijana wa Kijo, aliyekuwa ameganda naye anawasikiliza -akiwa ameshapewa maelezo na anajua kinachoendelea juu ya bosi wake- aliopoona anacheleweshewa muda akaingilia kati
‘Fanyeni basi tukimbie kabla wazee hawajavamia’ akawaambia akionyesha hataki utani
Chan’duu na Sofi kuona hivyo kila mmoja akaelekea katika chumba chake na kuchukua kilicho chake. Muda wote huo Sofi akiwa anajiuliza inawezekana kweli kwamba Kijo amewageuka au ni kweli kuwa hapa si mahala salama baada ya Chan’duu kulikoroga? Jibu alilopata, kila akikumbuka jinsi alivyokuwa katika mikono ya K jana usiku, walivyokuwa wakifanya hababa na jinsi walivyokuwa kama pea, aliona dhahiri kuwa hapa hawajageukwa ila ni kweli kamba mambo yameharibika. Lakini je hayo mambo yameharibikaje? Je hawawezi kushitukiwa?. Kila akikumbuka maneno ya Kijogobwire kwamba amepanga mambo katika namna ambayo hakuna mtu yoyote anayeweza kushtukia, basi alijipa moyo kwamba hakuna baya ilitakalo tokea
Walipokwisha kusanya kila kilicho chao kwa tahadhari wakatoka na kuelekea katika kituo cha daladala cha Bi Zakaria na kuchukua daladala ili kurudi nyumbani Magomeni.
Kama Chan’duu na Sofi wakati huu wangetumia mtego kidogo tu basi wangeshitukia kwamba hapa kuna mchezo wanachezewa, kwani yule kijana aliwavizia wanakata mitaa tu, akajifanya kukimbia anapopajua mwenyewe kumbe akarudi kule kule kambini kuendelea na mambo yake akiwa tayari ameshatekeleza magizo aliyopewa
…..…
Kwa bahati mbaya daladala waliyopanda Chan’duu na mwanamke wake ilikuwa imeshaanza kujaa watu hivyo hawakupata kiti cha kukaa wawili. Chanduu akapata kiti nyuma ya dereva na Sofi akakaa kiti nyuma ya Chan’duu. Toka wanapanda daladala Chan’duu ilikuwa bado yuko mbali kimawazo, akiwaza ni vipi alijitia ushujaa wa kutaka kusimamia mchezo huu asiokuwa na ujuzi nao mpaka sasa bado kidogo muda huu awe polisi. Kama si ujuzi wa Kijo basi sasa hivi angelikuwa ananyea debe. Lakini pia inakuwaje umri alionao na ujanja wote wa mjini anakubali kudhulumiwa na mtoto mdogo laini laini kama Kijo? Hilo haliwezekani, ni lazima atazame ni jinsi gani atarudisha mambo katika msitari
Akanyanyua macho na kutazama mbele ili aone sasa wako wapi mana tokea wanatoka Mwananyamala ni foleni mapaka saa hapa walipo. Alipoona kwamba sasa wapo kwa Komakoma akataka kurejesha macho chini na kuendelea na mawazo yake ya kupanga jinsi ya kumsaka Kijo, lakini wakati anarudisha macho chini akajikuta bila kupenda anaangalia katika kioo cha dereva na kwa bahati akaiona sura ya Sofi.
Kule kumuona Sofi ni kama kulimgutusha kwamba muda wote anajiwazia yeye tu bila hata kuwaza ni kipi kingetokea kwa mtoto wa watu. Chan’duu kwa jinsi alivyokuwa anampenda na kumkubali Sofi japo kama siku mbili hizi anajifanya mjuaji lakini asingeweza kamwe kumtaja na kuunganisha katika kesi hii kama angekamatwa. Alikuwa ameshaapa kwamba hata iweje yuko tayari kuona anaozea jela lakini kamwe katu hatomuunganisha binti huyu mrembo na kesi hii. Akatupa macho vizuri katika kioo ili amuangalie kwa kuibia na kumtathmini urembo na uzuri wake katika kipindi hiki cha matatizo. Wakati alipomuangalia vizuri akamuona kama anatabasamu. Akajiuliza inamaana amegundua kwamba anamuangailia au?
Lakini alipomuangalia vizuri akaona kama vile anachezea simu. Kwanza alidhani huenda labda akawa anaangalia saa lakini ule utulivu wa kusoma na kutulia kisha vidole vyake kufanya kazi ya kuandika akajua kwamba anachat na mtu
Anachat na nani wa kuweza kumfanya atabasamu katika wakati huu mgumu? Akajiuliza
Katika wakati huu ambao mambo yanaonekana magumu sofi anaonekana wala hajali kiasi cha kuweza kuchat na marafiki zake? Hakuamini
Kisha mara akamuona Sofi kama ananyanyua shingo ili kuangalia mbele. Mwanaume akazuga kuangalia pembeni ili Sofi asijue kama alikuwa anamtazama. Kwa kutumia jicho pembe akajua kwamba Sofi alikuwa anamuangalia yeye ili kuona kama hajastukiwa kuwa anachat na mtu. Alipoona haangaliwi akarudisha umakini wake katika simu. Hapa Chan’duu akaona kuna jambo lakini wakati bado anamchunguza Sofi mara kuna abiria aliyekuwa katika upande wa pili wa kiti akanyanyuka ili ateremke na Sofi baada ya kuona hivyo akaenda kukikalia kiti hicho kilichokuwa mbali na Chanduu
Hapo mwanaume akarudi katika mawazo ya kujiuliza ni nani hasa aliyekuwa akichat naye?
Daladala ilipofika Magomeni Mikumi wakateremka
Sasa ilikuwa yapata saa nane na nusu. Kwa vile walikuwa hawajala na huku Sofi akisema anajihisi vibaya hawezi kwenda kupika ikabidi waingie kwenye mmoja wa mgahawa na kupata chakula
Walipomaliza wakaondoka na kurudi nyumbani
Nyumba hii ya urithi ya kina Chan’duu ilikuwa na pande tatu tofauti zenye kujitegemea na wao walikuwa na pande moja yenye chumba varanda jiko na choo, hivyo walipoingia hakuna aliyewaona
Walipofika ndani tu Chan’duu akaingia msalani moja kwa moja kwenda kuoga. Alipomaliza akachukua maji na kumuwekea Sofi ili naye akaoge. Aliporudi chumbani akachukua taulo na kumkabidhi Sofi na kumtaka avue nguo alizovaa ili akajimwagie maji. Sofi hakuwa na mpango huo lakini katika wakati huu ambao Chanduu hajui kinachoendelea akaona haina haja ya kumbishia. Akavua nguo zake na kuzivingirisha na kuziweka mbali kama vile kuna kitu anataka Chan’duu asikigundue katika nguo hizo. Akatoka na kuingia chooni. Chanduu wakati wote huo alikuwa anamchungulia Sofi anavyokwenda chooni akiwa anamvizia kama vile Paka afanyavyo anapomnyatia PanyaCHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alipoona Sofi anaingia chooni akazifuata nguo na kuzitapanya. Akaitoa simu ya Sofi na kutaka kufungua upande wa ujumbe. Katika hali ya kushituka akaona kwamba Sofi leo hii simu yake ameweka password
Chan’duu akajua hapa kuna kitu
Sasa afanyeje kabla mwenyewe hajatoka chooni? Akapiga hesabu za haraka haraka
Akaizima simu na kuitoa laini
Akafungua simu yake na kutoa laini pia
Akaingiza laini ya simu ya Sofi katika simu yake
Akaiwasha
Akaingia katika hifadhi za meseji zilizotumwa. La kushangaza hakukuta hata meseji moja iliyotumwa leo. Akashika kichwa na kujiuliza bila kupata jibu. Akarudisha umakini wake katika meseji zilizotumwa jana. Akakuta meseji ambazo ilikuwa Sofi anachat na marakiki zake wawili, mmoja akiitwa Fursana na mwingine Wajna
Akaona hapa hakuna cha maana laini wakati anataka kuizima simu ili kuchomoa laini akaona arudi tena nyuma katika meseji za jana. Mara akakutana na meseji moja chini iliyokuwa na jina la Kijo
Akaifungua
Meseji ilikuwa imetumwa jana usiku wa saa nne na iliandikwa ‘Usifunge mlango nakuja mpenzi’
Chan’duu akajihisi mate ya moto mwili kuanza kupata joto na hasira kumjaa
Yaani bado kidogo simu zimdondoke
Hapa sasa ameshapata ushahidi kwamba kumbe wawili hawa wanamcheza shere. Kumbe ile jana ilikuwa wanamfanya mjinga kumuambia akalale wakati kumbe mwanaume Kijo alikwenda kulala na Sofi? Sasa hapa hakubali katu. Ataanza na mjinga huyu kisha Kijo atamtambua
Lakini wakati akiwaza hayo mara moja kuna kitu kikamjia ghafla mawazoni na kumtaka kutokuchukua uamuzi wa jazba
Ilivyo ni kwamba, kwa vyovyote Kijogobwire anataka kuwasaliti na kwa vyovyote atakuwa yuko na Sofi upande mmoja. Kwa vyovyote baada ya siku mbili Sofi atamshauri hili suala waliache Kijo amalize mambo yake kila mtu aishi kwa amani kwani kumchoma Kj itakuwa balaa kwao pia
Sasa kwa vile amebahatika kugundua siri hii katika wakati huu muafaka basi haina haja ya kuchukua uamuzi mkubwa. Anachotakiwa kukifanya sasa ni kuucheza huu mchezo katika staili yake peke yake
Sasa ni muda muafaka wa kujiuliza pale alipokuwa akisema Tukigeukana.. Tukigeukana.. alikuwa anamaanisha atafanya nini? Na kama alikuwa hana hakika na atakachokifanya sasa ni muda mufaka wa kufikia uamuzi na kuutekeleza kwa kasi sahihi
Akaizima simu na kuitoa laini na kuirudisha katika simu ya Sofi. Akairududisha sehemu ilipokuwa na nguo kuziweka kama zilivyo. Kwa vile bado alikuwa na hasira alijua wazi kwamba Sofi akitoka chooni basi anaweza hata kumzibua makofi. Akaona hapa ni kutoka na kwenda kunyoosha miguu kidogo katika kujipanga zaidi na mipangilio yake
Akatoka hapo taratibu kwa mguu na kupitia njia ya vichochoroni ili asikutane na marfiki zake na kuanza kumzingua. Akatokea mtaa wa Magomeni mwembechai katika Bar ya Makuti. Akaingia ndani na kutafuta meza ya pembeni akajitenga. Akaagiza bia baridi na sigara nane. Taratibu akaanza kunywa huku akivuta sigara na pia akivuta mawazo taratibu katika kuratibu shambulio kali zaidi la kufanya juu ya maadui zake hawa wawili
Alipowafikiria tu watu hao akajikuta hasira kubwa ikiuvaa moyo wake kiasi cha kuhisi kichwa kumuuma. Akajikuta akijiambia moyoni kwamba cha kufanya ni kuwaua tu hakuna kingine. Kuwanyofoa roho ndio kitu sahihi. Wakati alipowaza hivyo akagundua kwamba anajidanganya hana uwezo hata wa kuua kuku achilia mbali binaadamu. Akaanza kujichukia kwa kujiona dhaifu kiasi cha kushindwa kuchukua uamuzi huo aliouona muafaka
Kisha akaona mawazo hayo ni ya kijinga kwani anajikatisha tamaa badala ya kujipa moyo na kutafuta ufumbuzi wa kipi cha kufanya
‘Fikiria kwa pozi’ akili yake ikamshauri ‘katika wakati huu wa ajabu kwa bahati umeweza kuitumia akili yako ya kimachale machale kugundua kama jamaa wanakuzunguka, sasa si muda wa kutumia jazba’ akajiambia
Wazo alilolikubali kwa asilimia zote
Hapo ndipo wazo jipya lilipokuja na kuanza kuchukua sura. Akaliwaza na kuliunga mkono wazo hilo jipya. Kama wao waliamua kumsaliti basi na yeye awasaliti tu.
Akatabasamu kwa fikira hizo sahihi
Cha kufanya ni kuchukua namba ya mama wa mtoto na kumtaka ampatie milioni ishirini na tano kama mwenyewe alivyokuwa amepanga kabla kisha atamuambia wapi atampata mtoto wake. Kwa kweli hajui mtoto alipo ila atakachokifanya ni kuwataja wahusika wenye mtoto
Lakini kabla ya kufanya hivyo anatakiwa kuhakikisha kwamba tayari ameshajiandaa kukimbia mji na kukimbilia Afrika kusini kisha brazil kopakabana kwa watoto wa mchanganyiko wa kireno na amerika kusini.
Akawaza na kuwazua kwa kirefu juu ya plan yake hii na ilipomkaa akaagiza tena chupa kadhaa za pombe ili alewe tilalila usiku asiweze kabisa kumtazama Sofi na asubuhi akishaoga tu atoke kwa ajili ya kwenda kutayarisha mipango yake ya afrika kusini na kisha kumpigia simu mama wa kidosi ili kumpa maneno
Akakaa hapo mpaka saa saba na nusu kisha akarudi nyumbani
Kwa kweli hakumbuki hasa alifikia vipi nyumbani na alikutana na nani njiani kwani alikuwa yuko mtungi sana kiasi cha asubuhi kujikuta akiamka peke yake kitandani. Kwa kweli hata hakumbuki kama aliporudi alimkuta Sofi au alikuwa yuko kwa bwana wake mpya ambaye si muda mrefu atajua kumjuaCHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alipoamka akafanya usafi na ilipotimu saa tano akatoka bila kujali kwamba Sofi amerudi au la
Cha kwanza alikwenda mpaka Magomeni kondoa kwa mshikaji wake mmoja na kumpa mchongo wa safari. Kwa bahati nzuri akamkuta mtu huyo naye alikuwa na mawazo hayo hayo. Alipokuwa na uhakika na safari akatoka na kwenda mpaka sehemu ambayo wanauza laini za simu na kununua laini mpya. Akiwa hapo katika hali ya kushanga Sofi akampigia simu.
Akaitazama mpaka ikakata huku hasira zikiwa zimemjaa. Ilipokata ikaita tena. Ikaita na tena. Ilipofika mara tano akaona Sofi hana mpango wa kutopiga mpaka apokelewe. Akaipokea
‘Halow’ akasema kwa sauti ya kawaida
‘Vipi babii naona jana umerudi umelewa tilalila na leo mapema tu umetoka?’ akauliza Sofi kwa sauti ya kilaghai
‘Hamna babii mambo tu, unajua ilikuwa napoteza mawazo tu lakini leo nitarudi mapema na kila kitu kiko sawa’
‘Ok, basi babii wangu usijali mbona kuzulumiwa ni jambo la kawaida tu’
Chan’duu akauma meno kwa hasira bado kidogo aropoke lakini akajikamata wakati muafaka ‘Ok’ akajibu kwa kifupi na kukata simu
Ni jambo la kawaida ee? Mbona utajua muda si mrefu. Akajiambia maneno hayo kwa kujidai
Alipotoka na hapo akaenda sehemu na kununua vocha ya shilingi elfu mbili. Akajiunga katika namna ya kupata dakika nyingi za kuongea kisha akjitenga mahala tulivu sana pasipo na fujo wala ukaribu wa watu. Namba kwake haikuwa tabu kwani Sofi namba za watu wote muhimu aliwahi kumpatia ili kama siku kukiwa na tatizo basi aweze kuwasiliana nao. Chan’duu huwa akiandika namba hana kawaida ya kuzifuta kama vile wanavyofanya baadhi ya watu. Kuna watu kama ukiwapa namba zako akiona kipindi humpigii basi huwa anaidiliti. Chan’duu hakuwa mfuasi wa tabia hii ya ajabu
Mwanaume akatafuta namba iliyoandikwa namba ya bosi wa mke wangu na kwenda hewani
Iliita mpaka ilipokaribia kukatika ikapokelewa
‘Hellow’ sauti ya kike ikasikilikana
‘Naonge..’ sauti Chan’duu ikamkwama. Akaokohoa kidogo kuirekebisha
‘Hellow akasikia tena mtu akiita
‘Hallow, naongea na Msr Mazarkhan’
‘Ndio nani wewe?’
‘Aa mimi naitwa Chinga ndio mtu aliyemteka mwanao..’
‘What? Iko wewe ndio nataka pesa ili patia mwanangu?’ mama wa kihindi akauliza kwa shauku na sauti ya juu
‘Sikiliza mama..’
‘Ndio baba iko sikiliza’ akamkatisha tena kwa shauku
‘Mimi nataka milioni ishirini na tano tu nikupatie mwanao’
‘Sema baba lini nataka iyo hela na wapi?’
‘Iyo hela naitaka kesho saa nne za asubuhi maeneo ya Kigogo jangwani’
‘Iko mimi panajua iyo sehemu’
‘Haina haja ya kuja mwenyewe mtume mtu aje na gari akifika maeneo ya Kigogo jangwani nitamfahamisha wapi pa kunipata kisha nitakuambia wapi utamkuta mwanao’
‘Hapana shaka baba iko wewe kesho saa tano pata iyo pesa kisha mimi pata mwanangu, ondoa shaka babatoto akuna shiriki ivo akuna polisi sogea’ mama akatoa uhakika
Mh, mambo yanakwenda vizuri zaidi ya alivyotarajia
‘Usijali mama mimi ni mtu makini sasa hivi nitazima simu ila nitakupigia kesho ili kukuambia kama nimeshafika’
Akasema na kukata simu
Dah? Hakuweza kuamini kama kumbe suala lenyewe ni jepesi kuliko kumsukuma mlevi. Kama angejua tokea mwanzo kuwa mambo haya ni mepesi kama hivi asingemshirikisha yule mshenzi aliyempokonya mwanamke wake na sasa anapanga kumzulumu na dili lake
Akatoka hapo kama kawaida akapitia bar ili kupata moja moto moja baridi na kuua muda ili asikutane na Sofi msaliti
Kama sasa hivi yuko kwa bwana wake sawa au kama leo atajifanya kumpoza pia haina shaka
Akabaki hapo bar mpaka ilipotimu saa kumi na moja za jioni ujumbe kutokwa kwa Sofi ukaingia katika simu yake
‘Samahani babii rafiki yangu Jamila kwao kuna matatizo hivyo ameniomba niende nikamsaidie nitalala huko huko’ ujumbe huu akausoma na kisha akatabamu. We nenda kwa bwana wako kamalizie siku zako za mwisho mwisho na mbona utajuta!. Akajihakikishia
Alipoona kwamba hatamkuta adui yake akaondoka na kurudi nyumbani
Alipofika japo kama ilikuwa mapema lakini akaamua kulala
Asubuhi ya saa moja tu akakurupuka na kufanya usafi. Aliporudi ndani akajianda na kuichomoa simu yake aliyoichomeka kwenye chaji usiku mzima ili isilete sababu ya kuja kumzimikia katika muda ambao ndio anakusanya mapato yake ya kumuendesha kimaisha huko nchi ya watu
Akili yake ikamuaminisha uamuzi wake aliofikia kwamba atakapoingiza milioni hiyo ishirini na tano basi cha kwanza kabisa atakwenda kukodi gesti maeneo ya kariakoo kisha kuanza taratibu za kutafuta usafiri
………….
Chan’duu alikuwa na mipangilio yake lakini na Sofi na mwanaume Kijogobwire nao walikuwa na mipangilio yao pia. Leo kama ilivyo jana watu hawa wamelala pamoja katika gesti moja maeneo ya Ubungo. Katika vichwa vya watu hawa kila mmoja alikuwa na mawazo yake
Bi Sofi kichwa chake kilikuwa kimejaa mawazo ya ndoto za maisha bora yenye furaha ya mbele yanayoonekana kutaka kujaCHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Tokea pale alipotoka katika nyumba waliyokuwa wamejificha pale maeneo ya Mwananyamala na kisha kuchukua dalaladala kwa ajili ya kurudi Magomeni akili yake ilikuwa inajaribu kujiuliza juu ya msimamo wa Kj. Alipokuwa katika gari katika hali ya kustaajabisha akapokea ujumbe kwa njia simu kutoka kwa mwanaume Kijo iliyoanza na neno ‘Vipi mke wangu uko mahala poa tuchat kidogo?’
Kilichofuatiwa hapo ni kuwasiliana kwa njia ya ujumbe, maneno mengi ikiwa ni kufarijiwa kwamba asiwe na wasiwasi kuwa mambo yatakuwa sawa na ni kwa watu wawili tu kwani mpaka sasa mwanaume anapanga mipango thabiti ya kuweza kumtoa Chan’duu katika dili huku wakiwa na hakika kwamba hawezi kuwaletea usumbufu huko mbele ya safari
Pale alipofika nyumbani na kwenda kujimwagia maji alitoka chooni na kukuta Chan’duu hayupo, alishukuru kwani alikuwa na hakika kuwa sasa Chan’duu ni kero kwake na asingeweza kukaa naye hata dakika moja bila kugombana hasa baada ya kuutibua mpango wa kuingiza mamilioni ya shilingi. Kuona Chan’duu hayupo akampigia simu Kj na kumuomba aende akamuone ili atulize nafsi yake na kwa vile Kj alikuwa anashida naye basi akampa ruhusa ya kufanya hivyo na kumuelekeza hapa Ubungo kwenye gest iitwayo Kula taratibu. Penzi alilopata jana kutoka kwa mwanaume huyu anayefanya kitendo kwa kujinafasi tofauti na Chan’duu anayetaka aridhishwe yeye tu, kulimfanya Sofi atoke hapa saa nne za subuhi ili kwenda kumuaga Chan’duu kwa njia ya uongo kwamba anakwenda kwa rafiki yake kuna matatizo. Kutokumkuta Chan’duu pia ilikuwa furaha yake kwani kwa kweli kama angemuambia uongo na Chan’duu kuleta ubishi basi angempasulia ukweli kwamba kuanzia sasa hana chake kila kitu ni mali ya mwanaume Kijogobwire. Sasa hakuwa na sasababu yoyote ya kumuheshimu au kumuogopa Chan’duu hasa baada ya kuhakikishiwa kwamba Chan’duu atazibwa mdomo na hatoweza katu kuvujisha siri. Sofi ambaye mpaka sasa alikuwa anamuona Kj kama malaika, alijua kwamba kitakachofanyika katika kumziba mdomo Chan’duu ama ni kumtisha kwamba akijaribu kusema kitu basi watatumia hela kumuweka pabaya au watampa mgao wake na kumtaka akae kimya. Kitu ambacho Sofi hakukijua ni kwamba Kj alikuwa amepanga hatua kubwa mara dufu kuliko alizokuwa akifikiria mwanamke huyu
Kwa Kijo kulikuwa na mawazo manne mazito. Mawazo ambayo alikuwa anajaribu kuyaumba na kuyapatia ufumbuzi ili kuyafanyia kazi haraka iwezekanavyo.
Kwanza awali ya yote alikuwa anawaza na kupanga jinsi ya ukusanyaji wa shilingi milioni mia mbili kutoka kwa mdosi bila kuwapo kwa kikwazo chochote. Hapa wazo lake likapanuka na kufikia muafaka kwamba kitendo cha mdosi kwenda polisi kitakuwa kimeleta faida kubwa kwa upande wake kwani jambo hili litamfanya kupandisha bei ya bidhaa yake. Sasa itakuwa ni milioni mia tatu kwani ana hakika wa muhindi kuzilipa. Kule kumuonyesha kwamba yeye aligundua mpango mzima wa polisi kutamfanya muhindi kujua kwamba anacheza na moto na akibisha utamuunguza. Hatua ya kwanza atakayoipiga kesho ni kuchukua nguo ya juu ya mtoto na kuipaka damu kidogo ya kuku na kuituma kwa mama mtoto kwa ajili ya kumuonya kwamba iwapo kama mumewe ataleta tena za kuleta basi watampelekea kipande cha mkono ili kumuonyesha kwamba asipofuata masharti basi mtoto atauawa. Kipande kicho cha nguo kitambatana na maelezo kwamba sasa dau rasmi ni milioni mia tatu na zinatakiwa kulipwa wiki ijayo katika mahala ambao patatajwa baadae. Wazo hili likapanuka kwa kufikiria kwamba itakuwa muhimu sana kumpiga mtoto picha za kuisindikiza salamu. Wazo hili likamfanya atabasamu kwani lilikuwa muafaka na makini. Akageuza upande wa pili wa shilingi. Kuna suala la nani wa kumshirikisha katika kulifanikisha suala hili. Kwanza Jorg. Jorg ni mtu muafaka sana katika dili hizi lakini pekee hatoshi. Je ni nani wa kuweza kumuamini kupiga naye dili la hatari la kuingiza mabegi yalioja manoti katika gari kisha yeye umpe milioni moja na asitele ujanja. Hili ni suala la kumuumiza kichwa lakini atakaa na kulifikiria baadae ili ajue jinsi ya kuweza kumchagua mtu muafaka na mahala muafaka wa kuipeleka hela yake na wakati muafaka wa kuweza kuitumia. Suala la tatu ni kuhusu Chan’duu. Ni hakika na dhahiri kwamba hata kama Chan’duu atakuwa bwege na muoga vipi akiona amedhulumiwa dili lake na kisha mwanamke wake hawezi kukubali katu. Japo kama akiwachoma bado na yeye atadondokea shimo hilo hilo lakini anaweza kuamua kujitoa muhanga ili mradi kulipiza kisasi. Sasa ni lazima Chan’duu anyamazishwe. Na hakuna kumnyamazisha zaidi ya kumuondoa duniani. Tokea jana amesha mpekenyua Sofi jinsi ya kuweza kujua mienendo ya Chan’duu li kumtumia wazee wa kazi na kumuondoa katika ulimwengu. Atakachokifanya si Sofi wala mtu mwingine atakaye gundua kwamba Chan’duu ameuawa kwa makusudi. Kila mtu atadhani kama Chan’duu hakujiua basi itakuwa ameuawa na vibaka baada ya kujifanya mbishi na kupambana wakati wa kuporwa mali zake. Jambo la nne ambalo ndio kubwa zaidi na zito lakini ambalo mwanaume Kijo analiona jepesi la kawaida ni kuhusu hitimisho la mchezo huu. Nalo ni kuhusu Sofi mwenyewe. Siku mbili hizi amejitahidi sana kuwa karibu na Sofi ili kuweza kumtumia katika kulikamilisha dili hili. Hakuna mtu wa kumuogopa kama mwanamke pale utakapo mtibua. Mwanamke ukimuudhi atakachokifanya kama akiamua, basi huwezi amini. Ni bora mwanaume mara nyingine anaweza kusema kwa hasira nitafanya kitu lakini baadae akaghairi, lakini si mwanamke. Mwanamke akipania na kuamua ujue utaumia. Sasa kwa vile tamaa imeshamuingia Kj kwamba zigo la hela hawezi kabisa kuona analigawa kwa mtu mwingine yoyote iwe Sofi au hata mama na baba yake mzazi, sasa kilichopo ni kuhakisha na Sofi naye anatoweka kama vile atakavyotoweka Chan’duu. Kikubwa ambacho alikuwa anakifanya sasa Kijo ni kuwa na Sofi ili kuhahikisha kwamba anamsaidia katika suala zima la kuhakisha hela inapatikana na baada ya hapo atakachokifanya ni kumuua kama atakavyo muua bwana wake. Tena kwa hakika kifo cha Sofi kitakuja na faida kubwa sana kwani atafanya kila kinachowezekana kuhakikisha inatambulika kwamba Sofi ndio alisuka mpango wa utekaji na upatikanaji wa pesa lakini kwa bahati mbaya naye yamemkuta. Baada ya jamii kujua tu hapo ndio atakapomtoa uhai. Wazo hili akaona halijakaa sawa. Ni vipi ataweza kumuuza Sofi kisha kumuua halafu bado askari wasigundue kwamba hakuna mtu mwingine juu ya mpango huu.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/ Akakaa akichekecha kichwa kisha katika kuona kama vile anarudi nyuma akaamua mipango kuigeuza vaisvesa. Mwanaume akaona kuna umuhimnu mkubwa sasa wa kumrudisha Chan’duu kundini mpaka mwisho wa mchezo halafu sasa siku ya mwisho ya ukusanyaji pesa ambayo mtu atakaye kwenda kuuchukua mzigo huo atakuwa Chan’duu ndio afanye makeke. Watakapokutana sehemu ya mgao ndio atawaua Sofi na Chan’duu kwa pamoja katika namna ya kuonyesha kwamba wamevamiwa na majambazi waliokuwa wanajua mpango wao. Wazo hili pia likawa halijakaa sawa. Ni vipi atapanga kitu kitakachofanya Chan’duu na Sofi kuwa watuhumiwa wa mkasa huu kipindi wameshauawa na bado kusiwepo na namna ya kumuunganisha mtu aliyewaua na kukimbia na hela. Yeye bado hajafikia uwezo wa kupanga mipango mizito kama hiyo, hapa sasa atahitaji mtu mzoefu atakaye muahidi milioni kumi kama atampa muafaka wa mipango yake
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment